Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King (7 total)

MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa tatizo la maji la Kilindi linafanana sana na tatizo la maji la Jimbo la Makete na upo mradi ambao ulikuwa unatekelezwa na Serikali kwenye Kata ya Matamba na Tandala. Nini tamko la Serikali juu ya ukamilishaji wa mradi huo, kwa sababu mpaka sasa hivi maji hayatoki maeneo yale ambayo yalitakiwa yatoke? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kwamba mradi wa maji wa Matamba umekamilika lakini maji hayatoki. Bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeipitisha tumeelekeza kwamba kwanza tukamilishe miradi ambayo ilikuwa inaendelea kabla hatujaingia kwenye miradi mipya. Pia bajeti imeelekeza, miradi ambayo imekamilika, lakini maji hayatoki, basi tuhakikishe kwamba tunafanya utafiti kwa nini maji hayatoki na kama chanzo hakitoshi, basi tutafute chanzo kingine kuhakikisha kwamba miundombinu iliyowekwa inatoa maji na wananchi wapate maji.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, naogopa majibu kama haya yasije yakarudiwa mwakani. Kwanza, nini kauli ya Serikali kufanya commitment ya ujenzi hasa wa barabara hii? Kwa sababu nafahamu Hifadhi za Ngorongoro, Manyara na Serengeti zina sifa kubwa kwa sababu ya miundombinu kuwa imeboreshwa na hasa ya barabara.
Pili, sambamba na hilo, Pori la Mpanga Kipengere, mipaka imerekebishwa kiasi kwamba inaumiza Kata za Ikuo, Kigala, Mfumbi, hivyo kusumbua wananchi kiasi kwamba hakuna hata eneo la kujenga miundombinu. Nini kauli ya Serikali kuhusu hili? Kwa sababu upande wa TAMISEMI najua wameshalishughulikia. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Profesa Norman King juu ya uwepo wa uwezekano wa kurudiwa kwa jibu nililolitoa leo. Nia njema ya Serikali kwanza ni kuhakikisha kwamba Hifadhi ya Kitulo inaboresha au Serikali inaboresha utalii kwenye Hifadhi ya Kitulo, siyo kwa faida ya Kitulo peke yake na wananchi wa Kata tulizozitaja na Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, lakini pia kwa ajili ya Taifa zima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Kitulo tunaiboresha kwanza kwa kuboresha miundombinu ya ndani ambako tayari tumeboresha barabara za ndani na mageti ya kuingia ndani ya hifadhi, nyumba za wafanyakazi pamoja na ofisi. Pia tumeboresha upatikanaji wa bidhaa za utalii. Kwa sasa hivi hifadhi hii ni maarufu kwa ajili ya maua na hali ya miinuko (terrain) ya pale na hali ya hewa ambayo inafanana tu na nchi nyingine za Ulaya tofauti na hapa kwa maana ya baridi ya muda mrefu na vitu vya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tayari tunataka kurudisha wanyama ambao walikuwepo zamani lakini baadaye kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujangili, wanyama hao wametoweka. Sasa tuna mpango wa kurudisha tena wanyama wakiwemo pundamilia, swala na nyumbu ili kuweza kuifanya hifadhi hii iweze kupanda hadhi, tuweze kupata watalii zaidi, ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza utalii kwenye eneo la kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba ni nia ya Serikali na kwa kweli tumepania kuweza kupandisha hadhi ya utalii, siyo kwa Kitulo peke yake, bali kwa utalii wa eneo la Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili; Mpanga Kipengere ni mojawapo ya maeneo ambayo tuna migogoro ya mipaka, lakini nataka kusema kwamba kama ilivyo kwa maeneo mengine kadhaa ambayo tumekwisha yaorodhesha, yanaendelea kushughulikiwa na Tume Maalum ya Serikali ambayo tumeiunda ya kushughulikia migogoro ya namna hii. Nafikiri tuwape muda mfupi tu ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii ilipata changamoto mbalimbali, mojawapo ikiwa ni ya kifedha, lakini sasa hivi tumetatua changamoto hiyo ya kifedha, wapo kazini na wanakwenda kwa kasi ili kuweza kutatua migogoro inayofanana na huu ambao uko pale Mpanga Kipengere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ziada tu namwomba Mheshimiwa Mbunge, baada ya session hii nikutane naye ili niweze kupata details za status ya Mpanga Kipengere ili niweze kuwashauri wale ambao wanaendelea na kazi hii kwa maana ya Kamati ya Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri yanayoleta matumaini. Hata hivyo, nina maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mradi huu ulitegemewa kuzalisha umeme na wananchi wote wa Tanzania kunufaika, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme kwenye vijiji 76 ambavyo havina umeme Wilaya ya Makete? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itakamilisha upelekaji wa umeme kwenye vitongoji ambavyo havikupata umeme Awamu ya Kwanza ya REA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Profesa anavyotupa ushirikiano katika jimbo lake na awali ya yote nimhakikishie vijiji vyake 76 vitapata umeme kwenye Awamu ya Tatu ya REA inayoanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa vijiji vilivyobaki vitapelekewa umeme, katika majibu yetu ya kila siku tumekuwa tukisema Mradi wa REA Awamu ya Tatu umeanza tangu mwezi Machi, 2017 na vijiji vyote vilivyosalia pamoja na vya Mheshimiwa Profesa King vya Makete pamoja na maeneo mengine vitapelekewa umeme kati ya mwaka huu wa 2017 hadi 2020. Kwa hiyo, Mheshimiwa Profesa, vijiji vyake vyote vitapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua sana Kata za Mang’oto, Lupende, Kambata na Mabacha pamoja na maeneo mengine ambayo anayataja yatapatiwa umeme katika awamu hii. Vilevile vitongoji na taasisi zake za umma vitapatiwa umeme na mradi huo ni mmoja umeshaanza, tumezindua kwa Mkoa wa Iringa na Njombe kwa Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo na kwake wameshaanza, naambiwa wiki ijayo watafika kwa Mheshimiwa Profesa.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na pia natambua kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikifanya kazi nzuri kwenye suala maji. Nina maswali mawili ya nyongeza.(Makofi)
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni kweli kabisa kwamba tangu mradi huu uanze, wananchi wa Matamba, Nakinyika, Itundu na Mlondwe hawajawahi pata maji hayo. Nini kauli ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inakamilisha mradi huo?
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Tarafa hii ya Matamba pia linafanana sana kwenye Kata za Tandala, Mang’oto pamoja na Ukwama; nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba pia Kata hizi tatu zinapata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Norman Sigalla, nimefanya ziara kule na hilo tatizo nililikuta, kwamba mradi umetekelezwa lakini wananchi hawapati maji, lakini pia wananchi wameongezeka na tukakubaliana. Tumetengeneza mpango ambao utakuwa na gharama ya zaidi ya bilioni nne, na tutatekeleza miradi katika eneo lake katika hiki kipindi cha miaka miwili iliyobaki kwenda mwaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Norman Sigalla, amesimamia Halmashauri, andiko wameleta, tunakamilisha kulifanyia kazi ili utekelezaji uendelee. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Norman Sigalla pamoja na wananchi wa Matamba na Kinyika kwamba Serikali ya CCM itahakikisha ikifika 2020 wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. PROF. NORMAN S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kidogo kwa sababu, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 51 iko bayana, barabara hii imetajwa kwamba ni muhimnu iwekwe kiwango cha lami. Ni lini Serikali itapeleka nguvu kuhakikisha kwamba hili linatekelezwa ili kuboresha miundombinu hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mwaka 2017 Serikali ilikuwa imeahidi kupeleka wanyama kwenye hifadhi hii ili kuongeza vivutio kwenye Hifadhi ya Kitulo. Ni lini mpango wa kupeleka wanyama wasio wakali, ukiacha simba, kwenye hifadhi hii utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu maswali hayo naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya, lakini pia nimpongeze kwa jitihada kwamba sasa hivi anaenda kuoa na amesambaza kadi. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge wamchangie ili akamilike, aendelee kufanya kazi vizuri. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hii barabara iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, lakini naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge tu kwamba hivi sasa barabara ambayo inawekwa lami ni ile ambayo inatoka Njombe hadi Makete, inawekwa lami sasa hivi na bado kuna barabara nyingine ya kutoka Isonje – Makete mpaka Mbeya, nayo iko kwenye feasibility study. Hii barabara ya tatu itakuja kuunganishwa na hizi barabara nyingine mbili ambazo nimezisema na ninaamini kabisa hali itakuwa ni nzuri na Mheshimiwa Mbunge utafurahia baada ya hilo suala kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu ni lini wanyama wale ambao tuliahidi kwamba tutawapeleka katika Hifadhi yetu ya Kitulo, Serikali ina mpango wa kupeleka wanyama 25. Ili kuhamisha wanyama kutoka hifadhi moja kwenda hifadhi nyingine kuna taratibu za kisheria ambazo ni lazima zikamilike. Hivi sasa zimeshakamilika na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii amesharidhia wanyama 25 wahamishiwe katika Hifadhi yetu ya Kitulo kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naamini baada ya muda mfupi utawaona hao wanyama.
MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina swali moja tu la nyongeza.
Kwa kuwa maeneo yote yaliyotajwa kwa ajili ya ujenzi wa maghala hazijatajwa sehemu zile ambazo tunajua zinazalisha mahindi kwa wingi ikiwemo Wilaya ya Makete, nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi wa ghala Makete?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuwatetea wananchi wake na kunihimiza kufika Makambako tarehe 3 mwezi huu kwenda kuangalia hali ya ununuzi wa mahindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia jibu langu la msingi niliyataja maeneo mbalimbali ambayo Serikali inakwenda kujenga maghala ya kuhifadhia mahindi kuanzia ya Halmashauri mpaka ya wakala wetu wa hifadhi. Moja ya sehemu hiyo ni Makambako; Makambako ni Makao Makuu ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inajumuisha Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya pamoja na Songwe. Eneo analotoka Mheshimiwa Mbunge ni Makete, ni eneo la Mkoa wa Njombe na ni sehemu ya hii Makambako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili eneo la Makambako ndiyo tunakwenda kujenga ghala kubwa kuliko sehemu yoyote Tanzania; maghala haya matatu tunayoenda kujenga yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 kwa mwaka. Maana yake tukiongeza na uwezo wa sasa wa ghala lile tani 39,000 tutakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 99,000. Hii maana yake maeneo ya mikoa yote hiyo miwili hususani Mkoa wa Njombe ambako lipo Makao Makuu na Wilaya ya Makete tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mahindi kwa mwaka ujao Desemba. (Makofi)
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Makete tumekwenda pale na Waziri kutembelea kile kituo tukaona kwamba idadi ya ng‟ombe wanaotakiwa kuwepo pale ni 4,000 lakini sasa hivi wako ng‟ombe 750 tu. Ni Lini Serikali itapeleka ng‟ombe wa kuzaliana Kitulo? Ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa majibu yaliyokuwa yakiendelea Mheshimiwa Naibu Waziri na swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na Kituo cha Kitulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namuunga mkono kabisa kwamba Kituo chetu cha Kitulo ndiyo Kituo pekee cha uzalishaji wa Ng‟ombe wa maziwa bora hapa nchini kwetu, na ni kweli kabisa kwamba idadi ya Mifugo imepungua kwenye lile shamba letu; na kama yeye mwenyewe alivyosema hivi karibuni nilikuwa kwenye ziara katika eneo hilo.

Nataka tu nimhakikishie kwamba tunakamilisha mipango ya kuhakikisha kwamba shamba letu hilo tunaliboresha upya kuanzia uoteshaji wa nyasi katika shamba lenyewe pamoja na miundombinu mingine iliyochakaa. Vilevile kuhakikisha kwamba ng‟ombe wanarejeshwa mle, kwa maana ya kuongeza idadi ya ng‟ombe, ili iendane na ukubwa wa eneo na mahitaji ya wananchi ambao kwa sasa wanahitaji mitamba mingi sana kila sehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tukuhakikishie kwamba ujio wangu ule ndiyo ilikuwa mipango ya kuanza kununua ng‟ombe wengine na kujaza kwenye hilo shamba lakini na kuhakikisha kwamba mahitaji ya wananchi wa Tanzania wanaohitaji mitamba bora kutoka Kitulo wanaipata mitamba hiyo.