Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King (12 total)

MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. DKT. NORMAN A. SIGALLA KING) aliuliza:-
Je, ni lini Mkoa wa Njombe utaunganishwa na Mkoa wa Mbeya kilomita 205 kutoka Njombe – Makete – Isionje - Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Njombe – Makete – Kikondo - Isionje (Mbeya) yenye urefu wa kilometa 205.6 ni barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Njombe kwa sehemu ya kilometa 183.4 kutoka Njombe hadi Kikondo na sehemu iliyobaki ya kilometa 22.2 kutoka Kikondo hadi Isionje inasimamiwa na TANROADS Mkoa wa Mbeya. Ili kutekeleza azma ya kuunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Mbeya, Serikali itatekeleza ujenzi wa mradi wa barabara ya Njombe – Makete – Isionje - Mbeya kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo kwa sehemu ya Njombe – Ndulamo - Makete, yenye urefu wa kilometa 109.4 umefanyika na kukamilika mwezi Machi, 2014. Aidha, Serikali inafanya maandalizi ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya Makete – Kikondo - Isionje yenye urefu wa kilometa 96.2.
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njombe – Ndulamo - Makete, yenye urefu wa kilometa 109.4 unatarajiwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2016/17.
MHE. DEO K. SANGA (K.n.y. MHE. PROF. NORMAN A. S. KING) aliuliza:-
Shamba la Mifugo la Kitulo lililoko Wilaya ya Makete lilianzishwa kwa madhumuni ya kuwezesha wananchi kupata ndama na maziwa kwa ajili ya kukuza uchumi wao, lakini cha kusikitisha, uzalishaji wa ng‟ombe katika shamba hilo kwa sasa umepungua sana kutokana na Serikali kushindwa kusaidia kuimarisha shamba hilo:-
Je, Serikali inafanya jitihada gani kuimarisha shamba hilo ili liweze kusaidia wananchi wa Makete na Mikoa ya jirani kupata ng‟ombe na kukuza uchumi wao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la kuzalisha mifugo la Kitulo ni kati ya mashamba matano ya kuzalisha mifugo yanayomilikiwa na kuendeshwa na Wizara kwa lengo la kuzalisha mifugo bora kwa ajili ya kuwauzia wafugaji kwa bei nafuu. Shamba hili huzalisha ng‟ombe wa maziwa aina ya Friesian pamoja na maziwa, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016, jumla ya mitamba 365 na madume bora 515 yalizalishwa na kuuzwa kwa wafugaji katika Mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa na Ruvuma. Kati ya mitamba hiyo, 40 iliuzwa kwa wafugaji wa Wilaya ya Makete.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kipindi hicho jumla ya lita 1,963,241 zilizalishwa katika shamba hili na kuuzwa. Shamba hili pia linaendelea kutumika kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na wafugaji kutoka vijiji jirani vikiwemo vya Wilaya ya Makete. Katika kipindi hicho, wanafunzi 930 kutoka vyuo mbalimbali vya mifugo hapa nchini na wastani wa wafugaji 250 walipata mafunzo ya vitendo kupitia shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuliimarisha na kuliendeleza shamba hili kwa kuboresha miundombinu ya shamba ikiwepo maeneo ya malisho kwa kupanda na kuwekea mbolea hekta 500 za malisho, kukarabati kilometa 15 za mfumo wa maji, kukarabati na kuweka umeme nyumba 13 za watumishi, kuongeza ubora wa ng‟ombe waliozalishwa na kununua madume bora ya Friesian 12 na kutumia teknolojia ya uhimilishaji wa mbegu zilizotengenezwa kijinsi, kununua mitambo na mashine ikiwa ni pamoja na mashine moja ya kukamulia na tenki moja la kubeba maziwa, magari mawili pamoja na trekta mbili na vifaa vyake kwa ajili ya kuboresha na kurahisisha kazi za shamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hizi zimetekelezwa kwa kutumia fedha zinazozalishwa shambani kila mwaka na zinazotolewa kupitia bajeti ya Wizara. Katika mwaka wa fedha, 2016/2017 jumla ya shilingi milioni 105 zitakazozalishwa shambani na zilizotengwa kupitia bajeti ya Wizara zimepangwa kutumika katika kuimarisha na kuendeleza shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawahamasisha wananchi wa Makete kutumia huduma ya uhimilishaji ili waweze kuzalisha ndama bora kutokana na mifugo yao wenyewe.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING aliuliza:-
Hifadhi ya Kitulo ni muhimu sana kwa Taifa lakini mpaka sasa TANAPA haijaweka miundombinu ya hoteli na barabara ili kuwezesha watalii wanaokwenda Kitulo wawe na mahali pa kukaa:-
(a) Je, ni lini Serikali itawezesha ujenzi wa hoteli ya kitalii katika Tarafa ya Matamba?
(b) Je, ni lini Serikali itawezesha ujenzi wa barabara ya Chimala – Matamba – Kitulo ili kuinua utalii katika Hifadhi ya Kitulo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla, Mbunge wa Makete, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Kitulo inasimamiwa kwa kufuata mpango wa jumla (General Management Plan) wa miaka 10 ulioandaliwa mwaka 2008. Mpango huo umetoa fursa ya kujenga lodge ya vitanda 50 ndani ya hifadhi. Kulingana na taratibu za Hifadhi za Taifa, ujenzi wa huduma za malazi ya aina hiyo hufanywa na sekta binafsi. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele katika kutangaza fursa za utalii, hivyo kuvutia uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya hoteli ili kuboresha shughuli za utalii katika eneo la magharibi na kusini mwa Tanzania ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Barabara ya Chimala – Matanda – Kitulo ni sehemu ya mipango ya Serikali ya kuendeleza na kusimamia miundombinu inayoelekea kwenye maeneo yenye fursa za kiuchumi. Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili kuweka kipaumbele katika ujenzi wa barabara zinazoelekea kwenye maeneo yenye vivutio vya utalii zikiwemo za Chimala – Matamba – Kitulo ambayo ni muhimu kwa Hifadhi ya Kitulo, lakini vilevile Iringa – Tungamalenga – Ruaha mahsusi na muhimu kwa Hifadhi ya Ruaha na nyinginezo kwa kiwango cha lami ili kuchochea maendeleo ya utalii.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING) aliuliza:-
Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya ya Makete hakina mabweni hivyo kunufaisha kata moja tu wakati watoto wanaotoka Tarafa za Matamba, Ikuwo, Magoma, Bulongwa, Ukwama na Kata za Lupila na Tandala hawawezi kunufaika na Chuo hicho kwa sababu ya umbali uliopo.
Je, ni lini Serikali itakipa chuo kipaumbele cha kujengewa mabweni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi 250,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika Chuo cha VETA cha Makete. Mkandarasi Tanzania Building Agency (TBA) anategemewa kuanza ujenzi kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2017 baada ya kukamilisha hatua za kusaini mkataba.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING aliuliza:-
Utafiti uliofanywa na Serikali unaonesha kuwa Mto Lumakali unaozalisha maji katika Wilaya ya Makete unaweza kuzalisha megawatts 640 za umeme na hasa ikizingatiwa kuwa Wilaya ya Makete inapata mvua kwa miezi nane (8) kwa mwaka:-
Je, ni lini ujenzi wa bwawa ambao ni mpango wa Serikali wa tangu mwaka 2005 utaanza ili kusaidia kujenga uchumi wa kudumu huko Makete, Mkoa wa Njombe na Mbeya kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu uliofanyika mwaka 2012 kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ulibainisha kuwepo uwezekano wa kuzalisha umeme wa nguvu za maji wa megawati 222 katika eneo la Mwakauta kwenye Maporomoko ya Mto Rumakali. Juhudi mbalimbali zimefanywa na Serikali ikiwemo kuingia mikataba mbalimbali ya Makubaliano ya Awali ya uendelezaji wa Mradi huu kwa kushirikisha Kampuni mbalimbali za nje za JSC ya Urusi pamoja na kampuni ya China. Kampuni hizo hazikuweza kutekeleza mradi huo kutokana na gharama kuwa kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na taratibu za kumpata mshauri mwelekezi kwa ajili ya kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mbia wa ujenzi wa mradi huo. Kazi ya kumpata mbia itakamilika mwezi Juni mwaka huu wa 2017 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka 2019 na utakamilika mwaka 2026. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 936.
MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y MHE. PROF. NORMAN A. S. KING) aliuliza:-
Pamoja na juhudi nzuri zinazofanywa na Serikali kupeleka umeme vijijini:-
Je, ni lini Vijiji 86 vya Wilaya ya Makete hususani Tarafa ya Ukwama, Lupalilo, Ikuwa, Matamba na Bulogwa watapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini kupitia REA awamu ya tatu iliyoanza mwezi Machi, 2017. Utekelezaji wa mradi huu utakamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya mradi huu itajumuisha kufikisha umeme katika vijiji vyote vilivyobaki, vitongoji vyote, Taasisi zote za umma na maeneo ya pembezoni. Vijiji 28 kati ya vijiji 86 vya Wilaya ya Makete vilipatiwa umeme kupitia mradi wa REA II uliokamilika mwezi Desemba, 2016. Vijiji 58 na vitongoji vyake ikiwa ni pamoja na Bulongwa, Lupalilo, Matamba, Ikuwa na Ukwama vitapelekewa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu ulioanza mwezi Juni, mwaka huu ambao pia utakamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 29 vilivyobaki, itajumuisha kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 47.5, ufungaji wa transfoma 18, pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,439. Mradi huu utakamilika mwezi Machi, 2019 na utagharimu shilingi bilioni 4.54.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING aliuliza:-
Mwaka 2013 Serikali ilianza kutekeleza mradi wa maji wa Kata za Kinyika na Matamba katika Wilaya ya Makete lakini mradi huo haukufanikiwa kutokana na Serikali kutoa maelekezo ya kulaza mabomba ya inchi 2.5 na 4 badala ya inchi 8 kwenye mradi wa kilometa 18; mradi wa maji wa Tarafa za Magoma na Bulongwa ulijengwa muda mrefu wakati idadi ya watu ikiwa ndogo lakini sasa idadi ya watu na matumizi vimeongezeka.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Tarafa ya Matamba?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Tarafa ya Bulongwa ili Kata za Bulongwa, Kipagalo na Luwumbu ziweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Kata ya Matamba na Kinyika unaosambaza huduma za maji kwenye vijiji tisa ulianza kujengwa mwaka 2007 na ulikamilika mwaka 2014. Kabla ya ujenzi kuanza usanifu wa mradi huo ulilazimika kubadilishwa ili kutumia bomba la inchi 4, 2 na 1.5 badala ya bomba la inchi 8 kulingana na fedha zilizokuwepo kwani gharama za mradi kwa usanifu wa awali zilikuwa kubwa zaidi. Kutokana na ongezeko la watu kutoka 12,019 mwaka 2007 hadi 17,686 kwa sasa mradi huo haukidhi mahitaji. Ili kukidhi mahitaji Serikali inakamilisha usanifu wa mradi utakaotoa maji Mto Misi ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza mwaka 2018/2019.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mradi wa maji Bulongwa na Magoma unaohudumia vijiji 14 uliojengwa mwaka 1984 haukukidhi mahitaji ya sasa na miundombinu yake ni chakavu. Serikali imeanza ukarabati wa mradi ambapo hadi sasa bomba jipya kwa umbali wa kilometa nne limelazwa na linahudumia Vijiji vya Unyangogo, Iniho na Mwakauta. Mchakato wa kumpata mkandarasi atakayetekeleza awamu ya pili ya ukarabati huo unaendelea ili kukarabati bomba kwa umbali wa kilometa mbili. Ukarabati wa mradi mzima unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2018.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING) aliuliza:-
Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya ya Makete hakina mabweni hivyo kunufaisha kata moja tu wakati watoto wanaotoka Tarafa za Matamba, Ikuwo, Magoma, Bulongwa, Ukwama na Kata za Lupila na Tandala hawawezi kunufaika na Chuo hicho kwa sababu ya umbali uliopo.
Je, ni lini Serikali itakipa chuo kipaumbele cha kujengewa mabweni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi 250,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika Chuo cha VETA cha Makete. Mkandarasi Tanzania Building Agency (TBA) anategemewa kuanza ujenzi kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2017 baada ya kukamilisha hatua za kusaini mkataba.
MHE. PROF. NORMAN S. KING aliuliza:-
Hifadhi ya Kitulo iliyoko Mkoa wa Njombe, Wilaya ya Makete ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu na ni hifadhi ya kipekee katika Afrika kwa sababu ina aina tofauti ya maua zaidi ya 120.
Je, ni lini TANAPA kwa kushirikiana na TANROADS itaona umuhimu wa kujenga kwa lami barabara ya kutoka Chimala – Matamba – Kitulo – Makete ili kurahisisha uingiaji wa watalii kwenye mbuga hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba, kujenga barabara ya Chimala – Matamba – Kitulo kwa kiwango cha lami ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na hasa jamii zitakazotumia barabara hiyo ikiwa ni pamoja na hifadhi ya Kitulo. Napenda kuchukua fursa hii kumwarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa hivi sasa Wizara yangu ina mchakato wa kuboresha miundombinu ya barabara, utalii na utawala kwenye hifadhi zetu, mojawapo ikiwa ni Hifadhi ya Kitulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la ujenzi wa barabara zilizo nje ya hifadhi ni jukumu la Halmashauri za maeneo husika ikishirikiana na TANROADS. Kutokana na hali halisi ya mapato ya Shirika la Hifadhi ya Taifa, Hifadhi ya Taifa haina uwezo wa kuchangia ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hiyo, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili barabara hiyo iwekwe kwenye mpango wa ujenzi wa lami. (Makofi)
MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING aliuliza:-
Mwaka 2016 - 2018 bei ya zao la mahindi ambayo ndiyo nguvu ya uchumi kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imeshuka sana hadi kufikia shilingi 2000 kwa debe kwenye baadhi ya Wilaya kama Ludewa na Makete.
• Je, ni lini Serikali itaongeza fedha NFRA ili mahindi yanayozalishwa yanunuliwe na kuwapa ahueni wananchi?
• Je, ni lini Serikali kupitia NFRA itajenga maghala katika kila Halmashauri ili kurahishisha uhifadhi wa mahindi na mazao mengine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge na kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama naomba nilitumie Bunge lako tukufu kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyoionesha kwangu kuniamini kama naweza kutoa mchango wangu kumsaidia katika sekta hii ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mheshimiwa Spika kwa miaka mitatu niliyokaa hapa Bungeni jinsi alivyonihamisha kwenye Kamati tatu kuanzia Kamati ya Sheria Ndogo, Kamati ya PAC na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii imenipa uzoefu wa kutosha kufahamu shughuli za Serikali na Bunge kwa ujumla. Pia niwashukuru wajumbe wa Kamati hizo zote wakiongozwa na wenyeviti na makamu Wenyeviti hasa nikianza na ile ya Kamati ya Sheria Ndogo Mzee wangu Chenge nimekuja PAC Mama Kaboyoka na Kamati ya Ardhi ndugu yangu Nape na Wabunge wote wa Kamati hizo walinipa ushirikiano wa kutosha katika majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kwa uvumilivu na ushirikiano wanaonipa hasa kwa wakati huu niliokuwa mbali nao kwenye kutimiza majukumu yangu ya kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nimshukuru mke wangu mpenzi na familia yangu, Bi. Husna Abbas Mgumba kwa uvumilivu na ushirikiano wa karibu sana wanaonipa na ushauri wake kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo na shukrani hizo, nianze kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge na kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Jimbo la Makete lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa nafaka hususan mahindi ili kuiwezesha NFRA kutekeleza jukumu la kununua na kuhifadhi akiba ya chakula. Pamoja na ruzuku ya Serikali, wakala hutumia vyanzo vyake vingine vya mapato kugharamia ununuzi wa nafaka ambazo hununuliwa kutoka kwenye maeneo yenye ziada katika uzalishaji wa chakula kupitia vikundi au vyama vya wakulima. Aidha, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hauna uwezo wa kununua mahindi yote yanayozalishwa nchini bali inatekeleza na jukumu la kununua na kuhifadhi akiba ya chakula cha taifa kwa kuzingatia bajeti inayototengwa na Serikali na vyanzo vingine vya mapato kwa lengo la kuhakikisha usalama wa chakula ili kukubaliana na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mikakati ya kutafuta masoko kwa ajili ya mazao ya wakulima ikiwemo mahindi kwa kuondoa zuio la kuuza mahindi nje ya nchi, kuongeza bajeti ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa ajili ya ununuzi wa mazao na kuongeza uwezo wa Wakala wa Kuhifadhi Nafaka kutoka tani 251,000 hadi kufikia tani 501,000 ifikapo mwaka 2019/2020. Aidha, mikakati mingine ni kuongeza matumizi ya mahindi kwa kuyaongezea thamani ili kuuza unga na pumba pamoja na kuliingiza zao la mahindi katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuongeza wigo wa masoko ya mazao ya kilimo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa maghala 15 katika Halmashauri za mikoa ya Mwaza, Manyara, Singida, Kigoma, Simiyu, Tanga na Tabora. Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) unajenga maghala na vihenge vya kisasa katika Halmashauri za Shinyanga, Babati, Makambako, Sumbawanga, Mpanda, Mbozi, Dodoma na Songea ambayo ni makao makuu ya kanda zetu saba yenye uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 250,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika mradi wa kudhibiti sumukuvu jumla ya maghala 14 yatajengwa katika Mikoa ya Songwe, Dodoma, Manyara, Tabora, Kigoma, Mtwara, Ruvuma, Mwanza, Geita na Simiyu. Aidha, Wizara itakamilisha ukarabati wa maghala 33 kwa ajili ya hifadhi ya mahindi katika Halmashauri za Wilaya za Mlele, Nsimbo, Songea na Njombe pamoja na kuandaa mpango wa ukarabati na ujenzi wa maghala kwa nchi nzima. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI (K.n.y. MHE. PROF. NORMAN A. S. KING) aliuliza:-

Ili kuboresha utalii katika Hifadhi ya Kitulo, Serikali iliahidi kupeleka wanyama wasio wakali yaani pundamilia 25, lakini mpaka sasa bado wanyama hao hawajapelekwa licha ya Serikali kuahidi kuwa itatekeleza mwezi Mei na Juni mwaka 2018.

(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?

(b) Je, ni lini Serikali itaongeza aina ya wanyama kama vile paa na swala?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norman Adamson Sigalla, Mbunge wa Makete, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishatekeleza ahadi ya kupeleka Wanyamapori wasio wakali katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo mnamo mwezi Oktoba, 2018 ambapo pundamilia 24 walihamishwa katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kupelekwa Kitulo. Zaoezi lilifanyika mwezi Oktoba kipindi ambacho hali ya hewa ya Hifadhi ya Taifa ya Kitulo inafanana na hali ya hewa ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuongeza pundamilia wengine 26 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwenda Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, kufikia mwisho wa mwaka 2019/2020. Lengo ni kupandisha idadi ya pundamilia katika Hifadhi ya Kitulo kufikia 50. Pia sambamba na hilo kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali inatarajia kupeleka katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo wanyamapori wengine aina ya swala pala wapatao 50 na kuro wapatao 30.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING) aliuliza:-

Kumekuwa na maandalizi ya kuzalisha umeme katika Mto Lumakali uliopo Balogwa Makete na ni miaka 11 sasa wananchi wanaendelea kusubiri ambapo mwaka 2015/2016 Serikali ilitoa kauli kwamba ujenzi huo ungeanza mwaka 2017.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga bwawa hilo kwa ajili ya kuzalisha umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla, Mbunge wa Makete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kuzalisha umeme katika mto Lumakali unahusisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 222 na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 220 kutoka eneo patakapojengwa mitambo ya kuzalisha umeme Lumakali hadi Kituo cha Kupooza umeme cha Mbeya. Jumla ya gharama za mradi inakadiliwa kuwa Dola za Marekani milioni 388.22.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Lumakali ulifanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 1998. Kwa sasa Mshauri Mwelekezi wa Mradi anakamilisha mapitio ili kuboresha Upembuzi Yakinifu uliofanyika mwaka 1998 na kazi hiyo itakamilika Mwezi Machi, 2020. Utekelezaji wa Mradi huu utaanza Mwezi Januari, 2021 na kukamlisha mwezi Juni, 2023.