Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joram Ismael Hongoli (47 total)

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Je ni lini sasa Serikali itaanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara yanayotokana na hii mifuko ya plastiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, tunaanza leo kutoa elimu ya uzingatiaji wa matumizi ya mifuko ya plastiki, wananchi waweze kuzingatia hilo, Sheria na kanuni hii yetu ya 2015 kwamba matumizi ya plastiki ambayo yanayoruhusiwa ni yale tu yenye makroni 50. Kwa hiyo, ni jukumu la Bunge hili na Wabunge wote, wadau wote na wazalishaji na wenye viwanda kuchukua jukumu na kuhakikisha kwamba plastiki zinazozalishwa ni zile tu zenye makroni 50 ambazo ndizo zimeruhusiwa na Kanuni, zaidi ya hapo hairusiwi na haikubaliki na watu watakaoenda kinyume watachukuliwa hatua kali za kisheria, tutachukua hatua kali kwenye viwanda ambavyo vitazalisha zaidi ya kiwango hiki kilichoruhusiwa ikiwa ni pamoja na kufunga kabisa viwanda hivyo. Hatutaruhusu matumizi hayo kwa namna yoyote yatumike nchini. Kwa hiyo, ni jukumu la Bunge hili, ni jukumu la wananchi wote, kuelewa kwamba plastiki iliyoruhusiwa ni ile yenye makroni 50 peke yake.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na maswali mawili.
Swali la kwanza, kwa kuwa vocha hizi zimekuwa zikichelewa kuwafikia wakulima na wakati mwingine zimefika wakati wakulima wameshapanda mazao yao au wameshakuzia mazao yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba mbolea hizi zinafika mapema ili kabla hawajaanza maandalizi ya mashamba haya ikiwezekana ziwe zimeshafika?
La pili, kwa kuwa mbolea hizi za ruzuku zimekuwa zikitolewa kwa wakulima wa mazao ya chakula pekee, Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa mbolea za ruzuku kwa wakulima wadogo hasa wa mazao ya biashara kama vile chai ili waweze kuongeza uzalishaji na hatimaye waweze kuongeza kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kwamba kwa utaratibu wa sasa pembejeo zinachelewa sana kwa wakulima, nimfahamishe tu Mheshimiwa mbunge kwamba katika mwaka ujao wa fedha Wizara yangu inaubadilisha utaratibu mzima wa kupeleka ruzuku kwa wananchi. Kwa hiyo, tunategemea kwamba changamoto kama hizi kuhusu ucheleweshaji wa pembejeo hautatokea tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusu mpango wa Serikali wa kutoa ruzuku kwa pembejeo kwa ajili ya wakulima wote zaidi tu ya wale wanaofanya kilimo cha mazao ya chakula hususan mahindi na mpunga. Nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba ruzuku ya pembejeo hutolewa vilevile katika mazao mengine ikiwemo kwa mfano Korosho, Pamba, Kahawa, kwa kutumia taratibu za mifuko kwa ajili ya mazao hayo na vilevile kuna utaratibu wa kuhakikisha kwamba pembejeo vilevile zinatolewa katika zao la chai. Kwa hiyo, utaratibu huu vilevile unatayarishwa na Mheshimiwa Mbunge atapata taarifa pindi itakapokamilika.
MHE. JORAM ISMAEL HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Lupembe, Kata ya Kidegembye tuna tatizo kubwa sana la umeme hasa tatizo la low voltage. Transformer iliyopo pale haiwezi kuzalisha umeme wa kutosha na hivyo kutoweza kusambaza umeme sehemu nyingi na wananchi wa pale hawawezi kufanya shughuli za kiuchumi kama vile welding na shughuli nyingine za kusaga nafaka. Je, ni nini kauli ya Serikali kutatua tatizo hili? Maana nimewaona watu wa TANESCO muda mrefu lakini mpaka leo hii tatizo hilo bado lipo.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama mlivyoona katika maeneo mengi, sasa hivi bado tunaendelea na harakati ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa Kilovolt 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Wizara yetu ina jumla ya miradi 42 sasa. Kati ya miradi 42, miradi 16 ni kwa ajili ya uzalishaji umeme wa gesi pamoja na usambazji wake; lakini miradi 11 ni kwa ajili ya miradi ya maji na kusambaza umeme wa maji. Miradi mingine minane ni kwa ajili ya vyanzo vingine na miradi saba ni rasmi kwa ajili ya usambazaji umeme mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukisema sana kwamba kuanzia sasa Wakandarasi wako site na kazi kubwa hasa maeneo ya Iringa, Njombe Dodoma, Sumbawanga na mengine, tunaanza sasa mradi wa kusafirisha umeme wa Kilovolt 400. Kazi ya mradi huu kuongeza nguvu kubwa ili umeme sasa usiwe unakatikakatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa sasa hivi tunatumia umeme wa low voltage, lakini tutakapokamilisha miradi hii mwaka 2018/2019 low voltage sasa itakuwa imekwisha kwa sababu itakuwa na umeme mkubwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wa Njombe pamoja na maeneo ya Lupembe na mengine ni kuhakikishie kwamba taratibu wa umeme kukatika zinachangiwa pia sasa na low voltage lakini kwa sababu tuna umeme mkubwa gharama hizo pia zitashuka lakini na umeme utakuwa haukatiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kama nilivyosema, maeneo mengine umeme unakatika siyo kwa sababu ya low voltage tu, ni kwa sababu ya miundombinu kuwa mibovu. Sehemu ya miundombinu ni pamoja na transformer.
Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge, mmepitisha Sheria ya Manunuzi na tumeshasema, kuanzia sasa transformer tutakuwa tunanunua hapa nchini kwa sababu shirika letu na kampuni yetu ya TANELEC sasa itakuwa na uwezo wa kutosha wa kutengeneza transformer na Serikali itanunua, kwa hiyo, matatizo ya transformer yatarekebika na kupunguza kabisa tatizo la kukatika kwa umeme.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, naomba Mheshimiwa Waziri aweze kunithibitishia juu ya kuanza ujenzi huo kwa mwaka 2016/2017, kwa kuwa kwenye vitabu vya bajeti sijaona bajeti iliyotengwa au fedha iliyotengwa kwa ajili ya barabara hiyo.
Swali la pili, barabara ya Lupembe kwa sasa hivi imefungwa, magari yote yanayoanzia tani kumi na kuendelea hayaruhusiwi kuingia, wakati wananchi wa Lupembe, hasa kata nane, wanategemea barabara hii kusafirisha mbao, wanategemea barabara hii kusafirisha nguzo na vifaa vya ujenzi kama mchanga na tofali, sasa hivi imefungwa hawawezi kusafirisha, hivyo kuathiri uchumi wa wananchi hawa. Naomba Serikali iniambie, ni utaratibu gani ambao itauweka kwa sasa hivi ambapo tunasubiri ujenzi wa barabara hii ili wananchi wasiendelee kuathirika kwa uchumi wao?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwa swali lake dogo la kwanza, naomba asubiri hotuba ya Waziri wangu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili apate tafsiri sahihi ya randama ambayo ameiangalia. Namhakikishia ujenzi huo unaanza mwaka 2016/2017 kama tulivyoeleza katika jibu la swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuharibika na kukatika kwa barabara hiyo, naomba nichukue fursa hii kuwakumbusha tena TANROADS mikoani wote pamoja na Chief wao, kuhakikisha kwamba barabara zote ambazo zimekatika kutokana na mvua kubwa iliyopita zinafunguliwa, wasimamie suala hilo ili wananchi waendelee kupata huduma ya usafiri na maisha yaendelee kama kawaida.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa shule zetu nyingi bado zinaendelea na utaratibu wa matumizi ya vitabu vingi vya kiada; na kwa kuwa vitabu hivi vimekuwa vikitofautiana kwenye baadhi ya maudhui yaliyomo kwenye vitabu hivi na kuleta mkanganyiko kwa wanafunzi. Je, lini sasa Serikali itaanza kutekeleza utaratibu wa kutumia kitabu kimoja nchi nzima ili kuleta usawa na kuondoa mkanganyiko wa wananfunzi hao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa baada ya Serikali pamoja na wananchi kugundua kwamba kuna vitabu vingi ambavyo vinatumika mashuleni kiasi cha kushindwa kutoa mwelekeo halisi hasa katika usimamiaji wa maarifa yanayopatikana, Serikali iliamua kwamba kuwe na vitabu vya kiada na ziada, mpaka sasa imekuwa inasimamia katika zoezi hilo la upatikanaji wa hivyo vitabu kadri ya fedha tunavyozipata. Hivyo naamini tukishakuwa tumekamilisha hali hiyo ya kuwa na vitabu ambavyo ni vya aina tofauti tofauti itaondoka.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule hizi za bweni zimekuwa zikipelekewa fedha shilingi 1,500 kwa siku kwa mwanafunzi. Je, nilitaka kujua ni lini Serikali itaongeza hizi fedha ili shule zetu za bweni zisifungwe mapema na kuchelewa kufunguliwa ili watoto wapate muda mwingi wa kusoma wakiwa shuleni? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, anachozungumzia ni unit cost ya chakula kwa mwanafunzi, na concern hii nadhani Wabunge wengi walikuwa wameelezea kusema na hii rate ya shilingi 1,500 ni ndogo. Unit cost siyo kwa ajili ya chakula peke yake isipokuwa kwa ajili ya mchakato mzima wa elimu, jambo hili watalamu wetu sasa hivi wanalifanyia kazi pale litakapokamilika tutaangalia ni jinsi gani kama kuna uwezekano kupandisha gharama hii kidogo ili mtoto apate lishe ya kutosha ya kuweza kumfanikisha aweze kupata masomo vizuri. Kwa sababu tunajua kwamba suala la lishe ni jambo la msingi sana kujenga akili ya mtoto.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ni kwamba jambo hili tunalifanyia kazi sasa hivi kuangalia unit cost kwa shilingi 1,500 ni kweli tutafanyaje sasa na iende mpaka kiasi gani kwa kuangalia uwezo wa Serikali kwa muda muafaka.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wanafunzi hawa wa awali pia ni elimu ambayo ni msingi na sehemu nyingi wamekuwa wakifundishwa na Walimu waliosomea kufundisha wanafunzi wa shule za msingi na kuna baadhi ya maeneo wamekuwa wakifundishwa na Walimu ambao hawajapata mafunzo. Sasa kwa kuwa tuna chuo ambacho kinatoa Walimu, au tuna vyuo ambavyo vinatoa Walimu wa shule za awali, ni kwa nini Serikali isiajiri Walimu wa shule za awali katika shule zote nchini ili waweze kufundisha vizuri kwa sababu hawa wana mafunzo maalum kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Walimu wa elimu ya awali wanahitaji kuwa na mafunzo maalum, lakini napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Walimu wote wanaofundisha shule za msingi wanakuwa na course ya lazima ambayo inahusiana na ufundishaji wa elimu ya awali. Kwa hiyo, kwa sasa hivi ambapo wale walimu ambao wamefanya kama course maalum (specialization) hawapo wa kutosha, bado Walimu wa shule za msingi wana uwezo wa kufundisha kwa sababu ni somo la lazima kila Mwalimu wa shule ya msingi lazima achukue somo la elimu ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumfahamisha Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, sasa hivi tayari Serikali imepanua wigo wa utoaji wa mafunzo ya elimu ya awali kwa Walimu na sasa hivi tuna vyuo tisa ambavyo vinatoa mafunzo na Walimu hawa watahitimu mwaka 2018, ndipo watakamilisha masomo yao.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Lupembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Moshi Mjini na maeneo mengine ndilo ambalo lipo katika Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Naomba kujua ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Lupembe kwa kuwa hatuna hospitali katika jimbo na halmashauri ile. Tuna vituo vya afya viwili tu na wananchi wengi wanasafiri umbali mrefu zaidi ya kilomita 80 kwenda kutafuta hospitali. Kwa hiyo, ni lini sasa Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya katika eneo la Matembwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, analozungumza Mbunge ni kweli, ule Mkoa wa Njombe ni mpya na nilipofika pale katika Hospitali ya Kibena nimekuta changamoto nyingi kwa sababu watu wote wanakuja katika Hospitali ya Kibena hata wa kutoka maeneo ya Mheshimiwa Mbunge ambapo imekuwa ni kero kubwa sana na nashukuru na Wizara ya Afya vilevile kupitia viongozi wake wakuu walifika pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kufanya katika eneo lile kunakuwa na Hospitali ya Wilaya, nadhani sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumelisikia hili lakini nimsihi Mheshimiwa Mbunge mchakato wa ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya uanzie kwao kwa sababu kuna suala la kutenga eneo na kuweka kipaumbele hiki cha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Tukifanya hivyo na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI hatutasita kushirikiana na wananchi na viongozi katika eneo hilo kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana jana Kamati ya Bajeti ilikutana na Wizara yetu na Wizara ya Afya, lengo kubwa ni kuweka mipango kabambe ya kusaidia suala hili ili wananchi wote wapate huduma nzuri. Katika mipango hii kabambe inayokuja sasa naamini kwamba Mheshimiwa Mbunge akijipanga vizuri katika Jimbo lake na najua kwamba amejipanga vizuri sana, tutahakikisha kwamba hii mipango ya pamoja inakwenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumetoa maelekezo kupitia kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri 181 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waainishe maboma ambayo hayajamaliziwa na changamoto mbalimbali ili Bunge hili lije katika mpango mkakati wa huduma ya afya katika ujenzi wa miundombinu. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge waanze kufanya ile needs analysis na kutenga eneo kwa ajili hiyo na tutaona ni jinsi gani tutashirikiana katika ujenzi wa hospitali hiyo.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nitoe shukrani kwa Serikali kwa jitihada ambazo imeendelea kuzichukua kwa ajili ya kunusuru uchumi wa Lupembe. Kwa namna ya pekee, nimpongeze Waziri wa kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kufanya ziara Lupembe na ni Waziri pekee aliyekuja Lupembe kwenye Jimbo langu kwa kutembelea hivi viwanda vyote viwili. Pamoja na shukrani hizo, nina swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mgogoro huu umedumu kwa muda mrefu sana na umekuwa ukienda mahakamani bila mafanikio au suluhu ya kudumu. Ni kwa nini sasa Serikali isichukue hatua ya kuwakutanisha wakulima pamoja na mwekezaji ili kuweza kupata suluhu ya kudumu?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada anazofanya kurekebisha mgogoro ulioko pale Lupembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utatuzi wa mzozo ule wa Lupembe nadhani unakaribia mwisho kwa maana kwamba mwekezaji yule sasa yuko tayari kulegeza masharti aliyokuwa ameyaweka kwa kile chama cha MUVYULU na tumekwishazungumza naye. Kwa hiyo, nitoe wito tu pia kwa MUVYULU na wao kutong‟ang‟ania mambo ambayo mahakama imeamua siyo kwa kuwapa wao ushindi. Kwa hivyo, wakikubali kwamba watoe na kupokea (give and take) hili jambo litapata muafaka mara moja kwa sababu kimsingi wananchi hawana nia na huo mgogoro isipokuwa ni mmiliki na wale MUVYULU ndiyo wanaendesha mvutano na hivyo kuwafanya wananchi wapate hasara ya kutokuwa na viwanda viwili vinavyofanya kazi kwa mara moja.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kuna watumishi ambao walipandishwa daraja kama alivyosema muuliza swali wa kwanza, na kupokea mshahara mpya mwaka jana; na kisha hiyo mishahara ikasitishwa na sasa hivi watumishi hawa ambao ni walimu na watumishi wa afya kuna baadhi yao wameshastaafu, na wengine wanatarajia kustaafu miezi ijayo hii.
Je, Serikali itatumia hesabu gani katika ku-calculate, itatumia mshahara upi? Ule wa zamani au mshahara mpya katika kukokotoa kile kiinua mgongo cha mwisho? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa watumishi ambao walikuwa wameingia katika utumishi wa umma, halafu baadaye wakaambiwa warudi nyumbani, tumeshawarudisha watumishi 421 na kwa sasa tayari wameshalipwa takribani watumishi 379, 42 tumewarudishia waajiri wao ili waweze kukamilisha baadhi ya taratibu za ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja yake ya pili kwamba unakuta wengine wameshastaafu, lakini ni kiwango gani kitatumika katika kukokotoa mafao yao? Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wote wanaosikiliza, kwa wale ambao wanastaafu wanapewa kipaumbele miezi miwili kabla ya tarehe ya kustaafu mishahara yao inarekebishwa na watakuwa wamepata katika cheo stahiki ili waweze kutokuathirika na mafao.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Ahsante sana Mheshimiwa Spika. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa sasa tutakuwa na huduma ya upasuaji mdogo katika Kituo cha Afya Lupembe na hatimaye Kichiwa ili kuboresha huduma ya madawa kwa kuwa dawa ni tatizo: Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua duka la dawa kwa maana ya MSD katika Kituo cha Afya Lupembe na baadaye Kichiwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza lazima nikiri kwamba harakati za Mbunge huyu na watu wa Mkoa wa Njombe kwa ujumla wake tutajitahidi kuziunga mkono. Lengo kubwa ni Mkoa mpya wa Njombe uweze kupata huduma ya afya. Ndiyo maana hata Waziri wangu Mkuu juzi juzi alikuwepo kule kwa ajili ya mipango ya kimkakati katika Mkoa ule mpya.
Mheshimiwa Spika, suala zima la ujenzi wa duka la madawa katika vituo hivyo, siwezi kukiri kwamba katika hivyo Vituo vya Afya tutafanyaje, lakini kwa sababu pale tuna hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa ambayo inajengwa sasa hivi, tutafanya mpango mkakati tufanyeje katika eneo lile tupate duka maalum la MSD. Nia ya Serikali ni watu wa ukanda ule waweze kupata dawa kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba niwahimize Waheshimiwa Wabunge wote, kwa sababu sasa hivi tunaelekeza fedha nyingi sana katika Halmashauri na nashukuru sana, juzi juzi karibu kila Mbunge hapa amepata orodha ya idadi ya fedha kwa ajili ya madawa katika eneo lake, sasa ni kuona jinsi gani twende tukazisimamie.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nilisema katika siku za nyuma kwamba, tumeelekeza fedha nyingi za basket fund ambazo fedha zile lengo lake ni kwamba one third nikwa ajili ya ununuzi wa madawa na vifaa tiba. Naomba tukasimamie tutatue kero za madawa kwa wananchi wetu, kwa sababu tukifanya hivi, naamini Watanzania wote watafarijika kupata dawa bora katika maeneo yao kwa sababu Serikali sasa hivi imepeleka fedha nyingi sana katika Sekta ya Afya.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa dawa za kurefusha maisha kwa waathirika hawa wa UKIMWI zimekuwa zikitolewa kwenye vituo vya afya na kwenye zahanati chache. Kwa nini sasa Serikali isitoe huduma hizi kwenye zahanati zote ili kuwapunguzia wananchi hawa ambao wameathirika kutembea umbali mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, waathirika hawa
au hawa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wanaoishi vijijini sehemu kubwa ndiyo waathirika pia kwa maana ya umaskini. Kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wa kuwakopesha waathirika hawa kwenye vikundi mikopo midogo midogo ili waweze kupata fedha waweze kufanya shughuli ndogo ndogo kama vile kilimo, kufuga na bustani ili kuwainua kiuchumi au kuweza kupata fedha za kuweza kujikimu kwa maana ya kuwasaidia kuishi vizuri kwa kupata mahitaji madogo madogo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, concern ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ikiwezekana hizi dawa zitolewa katika zahanati zote, naomba niseme sasa hivi tumeanzisha zile center maalum na tutambue kwanza zoezi hili lilipoanza tulikuwa tunafanya katika Hospitali za Wilaya lakini tuka-scale up hii programu sasa imeenda katika vituo vya afya mpaka zahanati.
Kwa hiyo, tunachukua hoja hii ya msingi lengo kubwa ikiwa ni jinsi gani tutafanya tuwasaidie wananchi wetu waweze kupata huduma kwa karibu.
Kwa hiyo, tutashirikiana na wenzetu Wizara ya Afya, kuangalia tufanyeje mambo yetu ya kisera ili wananchi wetu wa Tanzania ambao wameathirika na janga la UKIMWI waweze kupata tiba kwa maeneo ya karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amesema kwamba hawa waathirika wengi wao ni maskini, ni kweli na ndiyo maana ukiangalia mipango ya Serikali hivi sasa hata ule mpango wa TASAF, lengo kubwa ni zile kaya maskini ambazo upatikanaji wa fedha inakuwa ni tatizo tunaziingiza katika mpango wa TASAF ziweze kupata fedha kuweza kujikimu katika maisha yao.
Hata hivyo, nizielekeze Halmashauri zote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa vile tunakuwa na mpango maalum wa kuziwezesha familia zetu hasa za wanawake na vijana ambapo asilimia tano ni kwa vijana na asilimia tano ni kwa wanawake, tuangalie kama tuna watu ambao wameathirika basi familia hizi tuzipe kipaumbele katika suala zima la mikopo ili waweze kushiriki katika suala la uchumi ili kujikomboa na umaskini.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali ya nyongeza.
Tatizo la mawasiliano lililopo Lulindi linafanana na
tatizo lililopo katika jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Katika Halmashauri tuna kata nne ambazo hazina mawasiliano kata za Ninga, Ikondo, Ukalawa na Mfiriga hakuna minara na hakuna mawasiliano, je, ni lini Serikali itajenga minara katika kata hizi ili wananchi waweze kupata mawasiliano kwa kuwa inawaathiri kiuchumi kutokana na kutokuwepo mawasiliano? Naomba majibu ya Serikali. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kila kijiji Tanzania kinafikishiwa mawasiliano. Na ndio dhamira ya kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Kwa hiyo, nikuhakikishe Mheshimiwa Mbunge tutayafikisha mawasiliano katika maeneo hayo uliyoyataja mara tutakapopata fedha za kutuwezesha kufikisha mawasiliano maeneo haya.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wadogowadogo
wa miti ambayo inazalisha mbao na kuni wa Mkoa wa Njombe na maeneo mengine ya Mkoa wa Iringa wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa sana wanapovuna mbao zao na kutaka kupeleka sokoni. Wakifika Iringa wanakutana na kodi nyingine au wanakutana na utaratibu mwingine kwamba lazima wawe na risiti za EFD wakati hao wakulima wamevuna mazao haya kwenye shamba lao, na wamepata kibali cha kuvuna na kodi nyingine wameishatoa, lakini wanaambiwa wawe na risiti ya EFD na hawana mashine. Wasipokuwa na risiti ya EFD wanaambiwa watoe faini ya shilingi milioni moja. (Makofi)
Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu mzuri wa kuweza kuondoa hii kero ambayo imekuwa tatizo kubwa sana kwa wakulima wetu hususani wa Lupembe na maeneo mengine wanaosafirisha mbao zao kwenda sokoni Dar es Salaam? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi na Mheshimiwa Mbunge kama atakumbuka nimekaa naye kujadili tatizo hili na tayari nimeshaelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia jambo hili, ni risiti za aina gani zinazodaiwa Iringa tu.
Kwa hiyo, naahidi kwamba hili linafanyiwa kazi, nami nilimuahidi Mheshimiwa Mbunge nikimaliza kipindi hiki cha bajeti nitakwenda Iringa kushughulikia tatizo hili. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina Mahakama moja iliyopo Lupembe na Mahakama hii jengo lake ni chakavu sana na ina nyufa nyingi, lakini pia ipo kwenye hifadhi ya barabara. Tayari wananchi wameshatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama hii? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, maadam wameshapata ardhi na wameshachukua hatua za mwanzo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nijue taratibu nyingine zinazostahili kufuatwa ili tukamilishe jambo hilo na Mahakama iweze kuanza kujengwa mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nipate taarifa hizo ili nami nizifikishe kwa Mtendaji wa Mahakama halafu tuone tunafanya vipi kwa sababu tayari maandalizi ya awali ya kiwanja na naamini kina hati; kama ni hivyo, basi hatua zinazofuata zitakuwa ni rahisi zaidi.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Upungufu wa walimu umekuwa mkubwa sana kwenye Halmashauri za Wilaya ukilinganisha na Halmashauri za Mji. Je, ni lini Serikali itaweka mgawanyo sawa kwa walimu katika hizi shule zetu za msingi ili kuwe na usawa katika ufaulu wa wanafunzi? Maana yake ilivyo sasa hivi, kuna inequalities. Ukiangalia shule za mjini zinafaulisha vizuri zaidi kuliko za vijijini.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, suala la mgawanyo wa walimu lina mambo mengi, kuna scenario ambayo ipo na hapa tulitoa maelekezo mara kadhaa. Utakuta katika Halmashauri moja hiyo hiyo, walimu wamefika, lakini walimu wengi wanabakia katika vituo vya mijini na hii utakuja kuona sehemu ya vijijini kule walimu wanakuwa hawapo. Ndiyo maana sasa hivi TAMISEMI tunaangalia kwamba kila mikoa tupeleke idadi ya walimu na kila Halmashauri tupeleke idadi ya walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, napenda kutoa maelekezo mengine tena hapa kwamba Maafisa Elimu wote wa Wilaya wahakikishe wanafanya ile distribution ya walimu katika maeneo mbalimbali, wasiwaache walimu katika kituo kimoja cha mjini. Jambo hilo limejitokeza pale Mbeya. Nilipofika Mbeya, shule moja pale mjini ina walimu mpaka wanabadilishana vipindi, lakini shule nyingine ina walimu wawili peke yake. Hili jambo haliwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni agizo kwa Maafisa Elimu wote wa Wilaya katika Halmashauri zote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wahakikishe wanafanya re-distribution ya Ualimu katika maeneo. Lengo ni kwamba hata kule vijijini walimu waweze kuwepo wanafunzi wapate taaluma inayokusudiwa.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa swali la nyongeza, ninalo moja tu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe haina Hospitali ya Wilaya na ina kituo kimoja kikubwa sana cha afya ambacho wananchi wengi wanatibiwa pale na kituo hiki kipo umbali wa takribani kilometa 80 kutoka Njombe mjini mpaka kule Lupembe.
Je, Serikali haioni kama inaweza ikatoa au ikafungua duka la dawa pale Lupembe ili iwe rahisi kwa wananchi kupata dawa kuliko kusafiri umbali mrefu pale dawa zinapokosekana kwenda Kibena ambapo inatarajiwa kufunguliwa duka la dawa lakini bado halijafunguliwa? Ahsante.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, suala la kufungua maduka ya dawa, tumelirudisha kwa Halmashauri husika kwa sababu moja ya vyanzo vikubwa vya mapato katika hospitali ni kutoka mauzo ya dawa. Kwa hiyo, suala hili ni Halmashauri yenyewe ya Njombe kuweka fedha kidogo kwa ajili ya kufungua au kuanzisha duka la dawa.
Mheshimiwa Spika, sisi tupo tayari kumsaidia kupitia MSD endapo wataweka miundombinu ya kuanzisha duka la dawa tupo tayari kuwakopesha dawa zenye thamani mpaka ya shilingi milioni 50 ili wananchi wa Halmashauri ya Njombe waweze kupata dawa bila changamoto zozote, ahsante.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe
ni moja ya Halmashauri ambayo haina Hospitali ya Wilaya na tuna vituo vya afya vinne, kituo cha afya kimoja cha Lupembe ni cha zamani, hivi karibuni tumefungua chumba cha upasuaji tayari operation zinaendelea pale. Tuna Kituo cha Kichiwa ambacho tunatarajia pia tuwe na theater ili kuwahudumia akina mama wasitembee umbali mrefu kwenda Kibena.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kujenga au kuanzisha chumba cha upasuaji ili akina Mama katika Kituo cha Afya cha Kichiwa ili akina Mama wasisafiri umbali mrefu kwenda hospitali ya Kibena ambayo ipo mbali sana na wanapoishi ambapo Jimbo la Lupembe lipo. Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA
NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kituo cha afya cha Kichiwa kumbukumbu zangu katika programu yetu ya vile vituo vya afya vya kwanza 172, katika vituo vile kuna fedha ambazo tulipata kutoka Canada, fedha zile zimeshaendelea katika maeneo mbalimbali na baadhi ya vituo sasa hivi wameshafika level ya renta, lakini kuna zile fedha kutoka World Bank ni kwamba upelekaji wake wa fedha utakamilika ndani ya wiki hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba wananchi wako watarajie kwamba jinsi gani waweze kushiriki kazi lakini fedha zile tutatumia force account. Niwasihi hasa viongozi wetu huko katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, zile fedha zinapokuja lazima wazisimamie vizuri tupate value or money na wananchi waweze kupata huduma. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, tuna shule moja ya Matembwe ambapo watoto wenye ulemavu tofauti tofauti wanasoma pale na tuliomba vifaa vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi kutoka Wizarani au Serikali lakini mpaka sasa bado hatujapata. Nataka kujua ni lini Serikali italeta vifaa kwa ajili ya kuwawezesha watoto wale waweze kupata elimu vizuri, kwa kuwa vifaa sasa hivi hawana? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka uliopita 2016/2017, tulitoa vifaa kwa shule 213 za msingi na shule 22 za sekondari. Mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya kununua vifaa. Naomba Mheshimiwa Mbunge aongozane nami nikitoka leo Bungeni ili anieleze mazingira ya shule yake tuweze kuweka kwenye utaratibu wa kugawa vifaa katika bajeti ya mwaka huu.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe lina vyanzo vingi sana vya maji, lakini vijiji vyake vingi havina maji. Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata za Ikuna, Ninga, Kichiwa, Kidegembye, Lupembe, Matembwe, Mtwango na Igongolwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza. Waheshimiwa Wabunge katika Halmashauri ambazo zimetumia fedha vizuri kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ni pamoja na Halmashauri ya Lupembe, ilitumia fedha zote ambazo zilikuwa zimetengwa na tukawaongezea nyingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi hiyo tutahakikisha tunatenga fedha zaidi, ili vijiji vingine vyote vilivyobaki vipate maji.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina vijiji 12 tu ambavyo vimepata umeme wa REA, lakini vijiji 22 bado havijaingizwa kwenye mpango huu wa REA III. Naomba kujua ni lini sasa Serikali itaingiza hivi vijiji 22 vyote ili waweze kupata umeme wa REA? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Hongoli kwamba vijiji vyake 22 vilivyosalia vyote vitaingizwa kwa Awamu ya Tatu round ya pili ambavyo vinahusika vijiji 4,314. Kama ambavyo nimejielekeza tangu mwanzo, lengo la Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha vijiji vilivyosalia 7,873 vyote vinafikiwa na miundombinu ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu hii tumeanza na vijiji 3,559 vinasalia vijiji 4.314. Kwa hiyo, ndani yake kuna vijiji 22,000 vya Jimbo lake la Njombe. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wote, Serikali ya Awamu ya Tano inaenda kufanya mapinduzi ya nishati vijiji vyote. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibena – Lupembe – Madeke, kilometa 126 ni barabara pekee ambayo inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro kupitia Mlimba. Barabara hii mwaka wa fedha 2016/2017 ilitengewa fedha, mwaka 2017/2018 ilitengewa fedha lakini mpaka leo hii haijaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Nataka kupata kauli ya Serikali, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuweza kuokoa uchumi unaopotea kule Lupembe na Mkoa mzima wa Njombe kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hongoli kwa sababu amekuwa akiifuatilia sana hii barabara, na hii barabara ni muhimu sana inapita sehemu ambazo zina uzalishaji mkubwa lakini pia ni kiungo kikubwa cha wananchi wa Njombe na wananchi wa Morogoro, na tumezungumza juu ya ujenzi wa hiyo barabara, barabara hii imeshasanifiwa. Kwa hiyo niseme ujenzi wa kiwango cha lami umeshaanza kwa sababu baada ya usanifu wa barabara hizo ndiyo harakati za kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, kwa vile barabara hii ilikuwa imetengewa fedha na Serikali ilikuwa inaendelea kupata fedha mara tu fedha zikipatikana ujenzi wa barabara hii utaanza mara moja. Naomba tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Njombe wawe na matumaini, wawe na imani na Serikali, inatafuta fedha na itaendelea kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na niliambie tu Bunge lako Tukufu kwamba kila mwezi tunatumia fedah nyingi sana kulipa certificates zinazotoka, takribani bilioni 80 zinalipwa kila mwezi, kwa hiyo hii ni ushuhuda kwamba Serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha kila wakati, kila siku barabara tunaendelea kuziboresha na kuzijenga. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa shule nyingi zimekuwa na matatizo ya kutokuwa na Walimu hasa shule zile za A-level zenye michepuo ya sayansi. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba shule hizi ambazo zina michepuo ya sayansi zinakuwa na Walimu wa kutosha ili wanafunzi hawa waweze kusoma vizuri na kuweza kumudu masomo yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa imekuwa ni kawaida kwa shule za Serikali kuongeza tahasusi kwenye shule hizi za A-level ambavyo huenda sambamba na ongezeko la wanafunzi. Katika shule hizi za A-level utakuta wanafunzi ni wengi na miundombinu haitoshi ukilinganisha na idadi ya wanafunzi. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba ongezeko la wanafunzi linaenda sambamba na ongezeko la miundombinu kwa maana ya madarasa, mabweni na miundombinu mingine? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto ya Walimu hasa wa sayansi katika shule zetu na ndiyo maana hapa katikati tuliomba kibali kutoka Ofisi ya Rais, Utumishi na tulipata kibali cha kuajiri Walimu na Walimu wale sasa hivi tumewaajiri kuwapeleka sehemu mbalimbali. Hata hivyo, bado hatujaweza ku-fill hiyo gaps yote iliyonanii na hii ni kutokana na jinsi hali ilivyo huko katika soko.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tutaendelea kufanya kila liwezekanalo, hivi sasa tuko katika mchakato kwa lengo kwamba tukipata wale Walimu wengine ambao maombi yao yalikuwa hayajakamilika vizuri, tuweze kuongeza kupeleka katika shule zetu ili tupate Walimu wa sayansi kwa ajili ya kufundisha vijana wetu wanaojiunga na kidato cha tano na cha sita.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili kuhusu suala zima la miundombinu, ni kweli tumeliona hilo ndiyo maana ukiangalia hivi sasa hata wanafunzi waliofaulu na kukidhi vigezo hatukuweza kuwachagua wote kutokana na suala la miundombinu, wengine tutawachagua katika second selection.
Mheshimiwa Spika, Serikali sasa hivi imeweza kufanya harakati na kupata takribani shilingi bilioni 21 ili kuweka miundombinu katika shule zipatazo 85, ambazo tunajua tukifanya hivi itasaidia sana kuhakikisha vijana wetu watafika shuleni na kusoma katika mazingira salama na mwisho wa siku waweze kupata elimu bora kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyokusudia.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wadogowadogo wa miti ambayo inazalisha mbao na kuni wa Mkoa wa Njombe na maeneo mengine ya Mkoa wa Iringa wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa sana wanapovuna mbao zao na kutaka kupeleka sokoni. Wakifika Iringa wanakutana na kodi nyingine au wanakutana na utaratibu mwingine kwamba lazima wawe na risiti za EFD wakati hao wakulima wamevuna mazao haya kwenye shamba lao, na wamepata kibali cha kuvuna na kodi nyingine wameishatoa, lakini wanaambiwa wawe na risiti ya EFD na hawana mashine. Wasipokuwa na risiti ya EFD wanaambiwa watoe faini ya shilingi milioni moja. (Makofi)
Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu mzuri wa kuweza kuondoa hii kero ambayo imekuwa tatizo kubwa sana kwa wakulima wetu hususani wa Lupembe na maeneo mengine wanaosafirisha mbao zao kwenda sokoni Dar es Salaam? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi na Mheshimiwa Mbunge kama atakumbuka nimekaa naye kujadili tatizo hili na tayari nimeshaelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia jambo hili, ni risiti za aina gani zinazodaiwa Iringa tu.
Kwa hiyo, naahidi kwamba hili linafanyiwa kazi, nami nilimuahidi Mheshimiwa Mbunge nikimaliza kipindi hiki cha bajeti nitakwenda Iringa kushughulikia tatizo hili. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina Mahakama moja iliyopo Lupembe na Mahakama hii jengo lake ni chakavu sana na ina nyufa nyingi, lakini pia ipo kwenye hifadhi ya barabara. Tayari wananchi wameshatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama hii? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, maadam wameshapata ardhi na wameshachukua hatua za mwanzo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nijue taratibu nyingine zinazostahili kufuatwa ili tukamilishe jambo hilo na Mahakama iweze kuanza kujengwa mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nipate taarifa hizo ili nami nizifikishe kwa Mtendaji wa Mahakama halafu tuone tunafanya vipi kwa sababu tayari maandalizi ya awali ya kiwanja na naamini kina hati; kama ni hivyo, basi hatua zinazofuata zitakuwa ni rahisi zaidi.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki kilinunuliwa kwa shilingi milioni 100 mwaka 2013 na mwaka huo huo Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu alifungua hiki kiwanda na tangu alipofungua mpaka leo hii hakijazalisha hata tani moja. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Bisahara na Uwekezaji atakaa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ili waweze kupeleka umeme haraka kwa kuwa, tatizo ni nishati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili pia ni lini sasa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ataongozana na mimi kwenda Madeke kujionea mwenyewe jinsi wananchi wale wanavyopoteza fedha nyingi/mabilioni ya fedha, kutokana na kukosa soko la kuuza haya mananasi na matunda mengine? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Hongoli kwa jitihada kubwa anayoifanya katika kufuatilia kiwanda hiki na tija kwa wakulima wa matunda ya eneo hilo, lakini vilevile nichukue nafasi hii ya pekee kabisa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa jitihada kubwa ambayo anaifanya katika kuhakikisha kwamba, umeme unapelekwa hasa katika maeneo ambayo tunatarajia kuwa na uzalishaji mkubwa na kuongea thamani katika matunda na eneo hili tayari tumeshafanya hayo mazungumzo.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba, ni rai yangu kwa wadau wengi kuona kwamba, umeme wa REA unaoombwa katika vijiji kweli uwe na tija na hivi tufanye uzalishaji kwa sababu gharama za kupeleka umeme katika maeneo hayo ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, suala la kuongozana hiyo itakuwa ni bahati ya pili kwa sababu, bahati ya kwanza tayari Mheshimiwa Waziri wangu mwezi huu ulioisha wa tatu alishaenda mpaka Njombe na amejionea hali halisi na vilevile tunategemea kujenga shades kwa ajili ya viwanda vidogo pale Njombe.
Kwa hiyo, mimi sina taabu nitaenda, nakubali kwenda huko. Ahsante.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina Mahakama ya Lupembe ambayo ni Mahakama ya muda mrefu sana, jengo lile lilijengwa na wakoloni na mpaka sasa hivi karibu linaanguka. Tayari tulishaleta mihtasari ya kuomba ujenzi wa Mahakama eneo lingine ambalo tayari wananchi wameshatoa na nimeshaandika barua ya kuomba. Nataka kujua ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hii ambayo sio muda mrefu itaanguka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu yote ya awali ya kwamba Serikali inayo dhamira ya dhati ya kwanza kabisa kuhakikisha kwamba wilaya nyingi zinapata Mahakama za Wilaya pamoja na Mahakama za Mwanzo vilevile na kufanya ukarabati wa majengo chakavu ya zamani.
Kwa hiyo, nimuahidi tu kwamba maombi yao yameshawasilishwa Wizarani, tunaendelea kuyafanyia kazi, pindi pale fedha zitakapopatikana basi tutawasiliana na mamlaka husika ili tuone namna bora ya kuweza kufanikisha ujenzi wa Mahakama hiyo katika Wilaya ya Njombe pia.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri kwa kujibu maswali vizuri lakini pia nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wengi hawana uelewa wa kulipa kodi, wanapoenda dukani kununua bidhaa wanalipa gharama ya zile bidhaa lakini pia wanalipa na Value Added Tax (VAT) asilimia 18 na wauzaji wakati mwingine hawawapi risiti na mwisho wa siku kodi hii ambayo wananchi wanalipa inapotoea. Je, ni lini sasa Wizara ya Elimu itaiagiza Taasisi ya Elimu (TET) kwa kushirikiana na TRA ili waanze kufanya kazi ya kuboresha mitaala hii ili Serikali isipoteze kodi kupitia wananchi kutokuwa na uelewa lakini pia na wauzaji wa hizi bidhaa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa mlipa kodi, TRA kwa sasa wanaendesha zoezi hilo nchi nzima. Kwenye shule zetu nyingi wameanzisha club za kodi ambazo pamoja na mambo mengine wanafunzi wanaelezwa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ili kufanya sasa kodi iwe ni kitu ambacho kinafahamika zaidi, Wizara yangu iko tayari kushirikiana na TRA kuboresha mitaala iliyopo ili kuendelea kuwajengea vijana wetu ufahamu na umuhimu wa kuwa wazalendo ikiwa ni pamoja na kulipa kodi. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kinipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya njia ya kupunguza maambukizi ya UKIMWI ni kuhakikisha kwamba vituo vya utoaji wa huduma vinakuwa jirani na wananchi. Kwenye maeneo ya vijijini vituo vya afya vipo mbali na zahanati maeneo mengi hazitoi huduma hizi za kupima,lakini pia utoaji wa dawa.
Je, ni lini Serikali itaagiza au itaweka utaratibu rasmi kuhakikisha kwamba vituo vya afya na zahanati zote zinatoa huduma ya upimaji, lakini pia zinatoa huduma za ARV? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali la Mheshimiwa Hongoli. Sisi kama Serikali mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba ifikapo 2030 tumeweza kufikia asilimia 90 ya Watanzania tunaowapima, asilimia 90 ya wale ambao tumewapima tunawaanzishia dawa na asilimia 90 ya wale ambao tumewaanzishia dawa tuweze kufubaza virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ambayo tumekuja nayo tumeendelea kupanua wigo wa vituo vyetu vya kutolea huduma hizi za ugonjwa wa UKIMWI. Lakini tumeanzisha mkakati wa kuwa na kitu kinaitwa outreach, watoa huduma wetu wa afya kwenda kule katika maeneo ambapo hakuna huduma za kuweza kuweza kutoa huduma hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaendelea kuhamasisha Watanzania kwa utaratibu ambao tunaenda nao sasa badala ya kutoa dawa za mwezi mmoja mmoja tumeongeza sasa tu kwa wale wagonjwa ambao wako stable sasa hivi tunatoa dawa za miezi mitatu mitatu na yote haya ni mikakati ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma hizi zinawafikia wananchi wengi iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, lina vituo vya afya vinne na kati ya vituo hivyo tumeanza kutoa huduma ya theater kwenye kituo kimoja cha Lupembe kwa kupitia fedha za ndani lakini pia michango ya wananchi na Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo mengine kwenye kituo hiki na kituo kimojawapo ambacho tumeomba cha Kichiwa, kiweze kupata huduma ya theater na kukamilisha majengo yale ya Lupembe kwa kuwa tumeomba muda mrefu na hatujapata fedha yoyote? Tumekosa shilingi milioni 500, tumekosa shilingi milioni 400 na vituo vyote hivi havina hata gari la wagonjwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukamilisha majengo, Serikali inatambua kwamba yapo majengo mengi sana ambayo yameanzishwa kwa nguvu za wananchi na vilevile kwa uwezo wa Halmashauri na bado hayajakamilika. Nazidi kutoa wito kwamba naomba sana Halmashauri zote nchini ziweke kipaumbele cha kwanza kabisa kumalizia majengo ambayo yameanzishwa. Pale ambapo fedha yoyote ya ruzuku au fedha ya ndani inapokuwa imepatikana, basi waweke kipaumbele sana kukamilisha majengo. Kuhusu gari la wagonjwa naomba tuendelee kuwasiliana na ofisi yetu ili tuweze kukamilisha kazi hiyo.
MHE. JORAM A. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la umeme lililopo Wilaya ya Kagera linafanana kabisa na tatizo la umeme mradi ule wa Makambako - Songea. Ule mradi umepita katika Kata tatu; Kata ya Kichiwa, Kata ya Igongoro na Kata ya Ikuna. Kwenye maeneo hayo kuna baadhi ya maeneo yana huduma muhimu kama shule, zahanati na vituo vya afya umeme haujapelekwa huko. Nini kauli ya Serikali kwa mkandarasi aliyesambaza umeme kwenye maeneo haya, kuhakikisha kwamba umeme unaenda kwenye maeneo yenye huduma muhimu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika mradi unaoendelea Makambako - Songea kwa kweli tunarajia mwezi Septemba mradi ule utakamilika na kuzinduliwa rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayoendelea ya kusambaza umeme katika maeneo ambayo yameainisha, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa miradi hii ya kupeleka umeme vijiji ipo ya aina mbalimbali, kuna mradi wa Makambako - Songea ambao unalenga vijiji 121, lakini sambamba na hilo kuna mradi ambao unaendelea wa densification kwa maeneo ya Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu, densification ya awamu ya kwanza ina vijiji kama 305 na mradi umekamilika umefikia asilimia 98.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maeneo ambayo hajasalia kama ambavyo tunafahamu mradi wa REA Awamu ya Tatu unaendelea na maeneo yale na maelekezo yetu kama Serikali, tumesema taasisi za umma iwe shule, iwe zahanati, iwe miradi ya maji na taasisi zote kwamba kipaumbele kwa wakandarasi waelekeze kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Serikali tunaendelea kusisitiza hayo maelekezo na yaendelee kutekelezwa na Wakandarasi wote. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli kwa awamu inayoendelea, changamoto hizi hazitakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina Vituo vya Afya vinne vya Kichiwa, Lupembe, Sovi na Matembwe. Katika vituo hivi vyote hakuna gari hata moja la wagonjwa, ni lini Serikali itatuletea gari la wagonjwa kwa ajili ya vituo hivi ukizingatia kwamba Kituo cha Lupembe tunafanya operesheni lakini hatuna gari? Inapotokea tatizo la watoto njiti, inakuwa ni shida sana kuwakimbiza Kibena, zaidi ya kilometa 80. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la ndugu yangu Mheshimiwa Hongoli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia njema ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma za afya zinasogezwa na hasa maeneo ambayo ni mbali kuwe na gari kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa. Pia ni ukweli usiopingika kwamba uhitaji ni mkubwa na ndiyo maana tumekuwa tukitoa magari kwa kadri yanavyopatikana na uwezo wa kibajeti unavyoruhusu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadri fursa itakavyopatikana, tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba kule Lupembe ambako ni mbali nako gari inapatikana.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wakulima wa zao la chai, hasa wakulima wadogowadogo wamekuwa wakinunua pembejeo kwa bei ya juu sana. Ni lini Serikali itatoa mbolea ya ruzuku, kwa maana ya pembejeo ya ruzuku kwa wakulima hawa wadogo kama ilivyo kwenye mazao mengine ya korosho na pamba, ili waweze kupata faida kutokana na kilimo hiki cha chai? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwaambie kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wote, msimu huu tumeamua kwamba hakutakuwa na bei yoyote ya ruzuku kwenye mbolea. Ndiyo maana hata kwenye sulphur ambayo ilikuwa inatolewa kwa ruzuku, safari hii tumeamua kwamba na yenyewe iwe inauzwa.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nianze kuishukuru sana Serikali kwa hatua iliyochukua kuhakikisha kwamba wanapeleka wanyama hawa pundamilia na swala ili kuongeza utalii katika eneo lile la Kitulo. Hata hivyo, nina swali dogo la nyongeza tu kwamba pamoja na hao ambao wanapeleka kwa kuwa wanyama kama twiga huwa wanaweza wakachangamana na wanyama hawa ambao wametajwa pundamilia na swala. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wanyama wengine nje ya hawa swala ama twiga ili waweze kuvutia watalii kwa kuwa watalii wengi wanapenda kuona twiga katika eneo lile?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo pia niulize Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba barabara angalau inayoenda kwenye ile mbuga za wanyama ile barabara ya Chimala – Matamba inakuwa katika hali nzuri muda wote ili kuweza kuvutia utalii katika eneo lile? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Norman Sigalla, amefanya juhudi kubwa kuhamasisha Wizara kupeleka wanyama kwenye hii Hifadhi na lengo kubwa ni kujaribu kufungua Hifadhi hii ili iweze kuvutia Watalii. Pia nimpongeze kwa kweli kwa kusimama imara kuhakikisha kwamba hili zoezi linakamilika mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba twiga, swala na pala wanaweza kuishi katika mazingira ambayo yanafanana, lakini kabla ya kupeleka wanyama kwenye Hifadhi ya Kitulo, Taasisi yetu ya TAWIRI ilifanya utafiti na kujiridhisha kwamba wanyama hawa wanaweza kuishi katika maeneo hayo na kwamba ikolojia zinafanana. Kwa hiyo ili tuweze kupeleka Twiga nitawaagiza watu wa TAWIRI waweze kufanya utafiti na kuona kwamba wanyama hawa wakipelekwa katika Hifadhi ya Kitulo wanaweza kuishi na hawatakuwa na madhara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali lake la pili, ni kweli kwamba ili watalii waweze kufika maeneo ya utalii na kwenye maeneo ya Hifadhi, taasisi zetu zimekuwa siku zote zikitengeneza miundombinu kuruhusu watalii kuweza kufika maeneo hayo kirahisi. Maeneo ambayo tunayatengeneza ni yale ambayo kimsingi yako chini ya usimamizi wa Wizara yetu. Kwa hiyo nimhakikishie tu kwamba barabara zote ambazo ziko chini ya usimamizi wetu tutazitengeneza kuhakikisha kwamba tunahamasisha utalii katika Hifadhi ya Kitulo.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe tuliomba fedha kwa ajili ya vituo vya afya hasa ikizingatiwa kwamba hatujapata hata kituo kimoja mpaka leo na tuliomba kwa ajili ya Kituo cha Afya Kichiwa ili kiweze kutoa huduma ya upasuaji lakini pia Kituo cha Afya cha Lupembe ambapo tumejenga huduma ya upasuaji kupitia mapato ya halmashauri na tumejenga jengo dogo la akina mama kupitia mchango wa Mbunge na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka kujua ni lini Serikali italeta hizo fedha kama zilivyopelekwa kwenye halmashauri nyingine na sisi Jimbo la Lupembe tuweze kupata angalau zile shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuwa na vituo angalau viwili vitakavyotoka huduma ya upasuaji? Sasa hivi akina mama wanapata shida sana na wanatembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, katika maeneo ambayo hatukujenga kituo cha afya ni pamoja na Jimboni kwake Mheshimiwa kule Lupembe. Mheshimiwa hajataja kuwa miongoni mwa wilaya ambazo zinakwenda kujengewa hospitali za wilaya ni pamoja na wilayani kwake. Pia amewahi kupata fursa ya kuongea na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana akamuahidi kwamba ikipatikana fursa ya kupata vituo hata viwili au kimoja, hatutasahau kituo chake. Naomba wananchi waendelee kuunga mkono Serikali, tumeahidi, tutatekeleza.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Zamani tulikuwa na shule za msingi ambazo zilikuwa zinatoa mafunzo ya ufundi, lakini pia, tulikuwa na sekondari za ufundi. Je, ni kwa nini sasa Wizara isizifufue zile shule angalau kila kata iwe na shule moja ambayo inatoa mafunzo ya ufundi, ili kuwawezesha vijana ambao hawajafanikiwa kwenda sekondari kupata stadi na mwisho wakaweza kujiajiri na vilevile tukateua sekondari katika kila tarafa sekondari moja iwe sekondari ya ufundi, ili vijana wanaokosa kuendelea na kidato cha tano waweze kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kuna haja ya kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali na ndio maana Serikali inajaribu kwa kuanzia kujenga vyuo, lakini badaye tutaangalia uwezekano wa kurudi kwenye shule za sekondari na shule za msingi ambazo ni za ufundi. Kwa sasa zipo shule baadhi za sekondari ambazo zinatoa ufundi vilevile.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina swali moja la nyongeza. Pamoja na kwamba Serikali imejibu vizuri, nawapongeza sana; na uamuzi unaokuja wa kufuta madeni ni mzuri sana, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati hizi fedha zinakopesha huko nyuma, kuna baadhi ya Halmashauri zilipeleka fedha kidogo; pamoja na kwamba hazikupeleka zote, lakini fedha hizi wale waliokopeshwa au vikundi vilikopeshwa vimekuwa vikisuasua sana katika kulipa hizi fedha. Mfano Halmashuri ya Wilaya ya Njombe kabla, tulikuwa Halmshauri moja upande wa Wanging’ombe na Makambako. Baada ya kugawanya hizi Halmashuri, zile fedha zilizokopeshwa kwenye vikundi vya Halmashauri nyingine, kwa mfano, Wanging’ombe na Makambako, imekuwa ni vigumu sana kurejesha na wamekuwa wakisuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali kwa vile vikundi ambavyo vilikopeshwa na sasa wanasuasua kurejesha au hawarejeshi kabisa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru kwa pongezi ambazo ametoa na kwa hatua ambazo Serikali inachukua kufuta madeni na malimbikizo haya. Naomba nitoe maelekezo kwamba hizi fedha hazikuwa sadaka, wala zawadi. Hii ilikuwa ni mikopo; na dawa ya kukopa ni kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaelekeze Wakurugenzi wote nchini walipo na wale Maafisa Ustawi wa Jamii na Mikoa, Wilaya na Kata, vile vikundi ambavyo vilipewa fedha hii ya Serikali kwa ajili ya kujiendeleza na kuboresha maisha yao, ni muhimu warejeshe fedha hizi na waweke time frame baada ya muda fulani fedha irejeshwe. Kwa sababu makusudi ya Serikali ilikuwa, kikundi kimoja kikikopeshwa kikaboresha maisha yake, wakirejesha na wengine zaidi wanaendelea kukopeshwa ili waweze kuyaboresha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sanakwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe haina Afisa Ardhi Mteule na tuna mpango wa kupima ardhi katika maeneo yetu.

Je, ni lini Serikali italeta mtaalam kwa maana ya Afisa Ardhi Mteule ili kuweza kusaidia kupima ardhi lakini pia kutatua migogoro iliyopo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati najibu swali nyongeza la Mheshimiwa Yosepher, nimesema utaratibu unafanyika sasa tutaweza kuwatawanya wataalam wetu kama walivyo, lakini kwa sasa naomba tu waendelee kumtumia huyo Afisa Ardhi Mteule ambaye alikuwa kazi yote kutoka kwenye halmashauri jirani ya jimbo lake ili tuweze kuendelea. Hii kazi itakamilika muda si mrefu, naomba tu Waheshimiwa Wabunge tuvumiliane kwa sababu kazi ya kuwapanga itachukua muda kwa sababu yakutaka kujua taaluma zao na uhitaji wa kila halmashauri.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina vituo vinne lakini haijawahi kupata fedha kwa ajili ya uboreshaji wa vituo hivi na jiografia ya Jimbo lile ni mbaya sana. Tunashuruku kwamba mmetupatia Hospitali ya Wilaya lakini wananchi wanataka kujua ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Njombe itapata fedha kwa ajili ya uboreshaji wa Vituo vya Afya vya Kichiwa, Sovi, Lupembe na Ikuna ambacho ujenzi wake karibia unakamilika? Naomba tupate majibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naomba nimpongeza Mheshimiwa Hongoli kwa vile nafahamu wazi na yeye anafahamu mpaka jana takribani saa tatu na nusu usiku tulikuwa tunaongea naye kuhusu suala zima la sekta ya afya. Hii inaonyesha jinsi gani anajali wananchi wake na kufuatilia masuala ya afya. Ndiyo maana katika awamu ya kwanza tulimpatia Hospitali ya Wilaya na najua katika mpango wa bajeti ya mwaka huu tumemtengea Kituo kimoja cha Afya lakini bado hali siyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ni commitment yetu sisi Serikali na Mungu akijalia huenda kabla hata mwezi Julai haujafika, tutafanya kila liwezekanalo tukupatie Kituo kingine cha Afya bora zaidi ili wananchi wa Jimbo lile la Njombe DC waweze kupata huduma vizuri.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima na wanaishi maeneo ya vijijini. Hawa wafanyabiashara aliowataja Mheshimiwa Naibu Waziri wenye makampuni wanaonunua mbolea hizi, wamekuwa wakinunua na kuziweka mjini na inawapasa wakulima sasa watoke vijijini kwenda kununua hizo mbolea mjini kitu ambacho kimekuwa kikiwasababishia gharama za mbolea kupanda sana? Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba mbolea hizi zinapatikana kwenya Kata au Tarafa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe tuna maghala na maeneo mengi ya Njombe kuna maghala kwenye Kata hizi. Je, Serikali ina mpango gani ili kuhakikisha hawa wafanyabiashara wanapeleka mbolea hizi kwenye Kata ili gharama za usafirishaji ziweze kupungua kwa wakulima? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Hongoli, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wakulima wengi wanaishi vijijini na kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tumeshayaelekeza makampuni yote yanayoingiza mbolea hapa nchini na wasambazaji wawe na mawakala kila Mkoa
na Wilaya na pia wawe maghala ili kuwezesha mbolea hizi zinapoingia Dar es Salaam kufika kwenye mikoa yote inayotumia mbolea kwa wingi. Pia tumevielekeza Vyama vya Msingi vya Ushirika na Vyama Vikuu, kuwa mawakala kwa ajili ya usambazaji wa mbolea kwenye Kata na Vijiji katika Mikoa na Wilaya zinazolima mazao mbalimbali.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina vituo vinne na kimoja kipo kwenye ujenzi lakini vituo vyote hivi havina vifaa muhimu kama vile Ultra sound na X-ray machines pamoja na kwamba tunatoa huduma ya upasuaji katika Kituo cha Lupembe.

Je, ni lini Serikali italeta vifaa hivi muhimu sana kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waweze kupima baadhi ya vipimo kwenye hivi vituo vya afya? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kabisa, kama kuna Wabunge ambao wanafuatilia masuala ya afya kwenye majimbo yao, ni pamoja na Mheshimiwa Hongoli na hivi karibuni alikuja ofisini na tukakubaliana. Amepata fursa ya Kituo cha Afya cha Kichiwa kinajengwa na naomba uniruhusu, ifike mahali nitaleta orodha ya jinsi ambavyo Serikali imefanya commitment na fedha ambazo tumeshalipa MSD, kinachosubiriwa ni vifaa kupelekwa. Kama ambavyo nimekuwa nikijibu kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha vituo vya afya vyote ambavyo vinajengwa vinapatiwa vifaa ili vitumike kama ambavyo tumekusudia.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa swali la nyongeza Mkoa wa Njombe ni moja ya Mikoa yenye hali ya hewa nzuri ambayo inaruhusu ng‟ombe wa maziwa kuweza kustawi na kuzalisha maziwa ya kutosha. Je, ni nini Mkakati wa Wizara kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Njombe ambao wanapenda kufuga wanapata ng‟ombe bora wa kisasa ili uzalishaji uongezeke na pia ili Viwanda viweze kupata malighafi za kutosha? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkakati wa Serikali katika kuhakikisha tunaongeza idadi ya ng‟ombe katika Mkoa wa Njombe. Majibu ya msingi na majibu ya ziada yaliyojibiwa na Mheshimiwa Waziri yameeleza wazi juu ya Mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya mitamba katika mashamba yetu ya Serikali likiwemo Shamba la Kitulo lililopo katika Mkoa huo wa Njombe; pia vilevile shamba letu la sao hill lililoko pale Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati hii kwa pamoja, pamoja na mikakati mingine ya kuanzisha makambi ya uhimilishaji wa ng‟ombe mikoani, ambao tunaendelea nao hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini ya kuongeza mbali ama breed za kisasa za ng‟ombe watakaotuletea tija zaidi inayokwenda sambasamba na kutuhakikishia kufikia katika lengo la kuwa na ng‟ombe wa maziwa wa kutosha nchini kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa tuna takribani ng‟ombe milioni moja wa maziwa wazuri; na mkakati wetu ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2021/2022 tuwe na jumla ya ng‟ombe milioni nne watakao kuwa ng‟ombe wazuri wa maziwa kwa ajili ya uzalishaji mkubwa wa maziwa na kuingiza katika viwanda vyetu.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina vituo vinne ambavyo vinafanya kazi lakini vichakavu. Pia wananchi kupitia mapato ya ndani na wananchi wenyewe tumejenga kituo cha afya cha Ikuna. Sasa katika hivi vituo vya zamani Kituo cha Kichiwa, Sovi, Matembwe na Lupembe ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya kukarabati na kuongeza majengo ili wananchi wa Lupembe waweze kupata huduma kama ilivyo maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kutoa majibu katika swali la msingi. Katika maeneo ambayo tumetenga fedha ili kuhakikisha kwamba huduma ya afya inaboreshwa ni pamoja na jimbo la Mheshimiwa Mbunge na atakumbuka kwamba katika vituo vya afya vya kuboreshwa ni pamoja na Kichiwa ambacho ametaja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kadri fedha ya kwanza itakavyopatikana eneo la kwanza kupangiwa fedha itakuwa na kituo chake kwa sababu yeye amekuwa mstaarabu sana na amekuwa akifuatilia sana suala hili.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina shule tatu zenye Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita; Shule ya Lupembe Sekondari, Magilu Sekondari na Itipingi Sekondari. Katika shule hizi zote kuna uhaba mkubwa sana wa vyumba vya madarasa na mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye shule moja hii ya Itipingi wananchi wameshaanza kujenga bweni moja ambalo sasa hivi limefikia kwenye hatua ya lenta: Je, Serikali ipo tayari kutoa fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hawa ili waweze kukamilisha mabweni na hawa vijana waweze kuishi katika mazingira mazuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi na wadau mbalimbali wamejenga maboma mengi katika maeneo yao ya Shule za Sekondari na Msingi, kwa maana ya maboma ya shule lakini pia na maboma ya kujenga mabwalo na mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa fedha uliopita tumetoa shilingi bilioni 29.9 kukamilisha maboma ya nchi nzima zaidi ya maboma 2,900. Naomba niwaahidi mwaka huu pia, kwenye bajeti ambayo nimesema kwenye jibu langu la msingi tumetenga shilingi bilioni 58.2, pamoja na mambo mengine fedha hiyo imejumuishwa na fedha ya kwenda kukamilisha maboma, mabweni, mabwalo, nyumba za walimu lakini pia na matundu ya vyoo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutie moyo kwamba wakati ukifika wa kusambaza hizo fedha tutaendelea kuwa tunawasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, fedha zinapoenda katika maeneo yenu, ni muhimu mkapendekeza maeneo ya vipaumbele. Tumepeleka fedha ya kukamilisha maboma, lakini fedha nyingine zimerudishwa kwa sababu kuna shule zimepelekewa kumbe hazikuwa na maboma. Fedha ambayo inapelekwa na Serikali ni kukamilisha maboma na siyo kuanza ngazi ya msingi mpaka kwenye lenta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la ngongeza.

Tatizo la umeme lililopo Kibamba linafanana kabisa na tatizo la umeme lililopo katika Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Tuna vijiji 22 havina umeme, lakini tangu Januari, 2019 mkandarasi wa REA amesambaza umeme katika vijiji viwili kwenye vijiji hivyo viwili amesambaza kitongoji kimojakimoja. Kwa hiyo, nini kauli ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba hivi vijiji 22 vinapelekewa umeme na kuhakikisha kwamba mkandarasi huyu anasambaza umeme kwa kasi ili vijiji vyote 22 viweze kupata umeme? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hongoli atakuwa shahidi, tulifanya ziara pamoja naye katika jimbo lake na nimpongeze kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini nataka nimthibitishie mkandarasi JV Mufindi anaendelea na kazi, lakini nataka niwathibitishie Wabunge wote kwa sababu yapo maswali mengi ya Mradi wa REA, kwamba Mradi wa REA bado mudo upo, inatarajiwa ikamilike Juni, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama Wizara Mhesimiwa Waziri wa Nishati ametoa maelekezo, miradi ikamilike ifikapo Septemba, 2019. Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kumsimamia mkandarsi kwa karibu na ukizingatia sasa hivi wakandarasi karibu wote wameshafanikiwa kupata vifaa vyote vya mradi. Kwa hiyo, nimtoe hofu tu kwamba vijiji 22 vitakalika na kasha tutaanza tena REA Awamu ya III mzunguko wa pili kwa vijiji vyake vyote vilivyosalia, ili kulifanya jimbo lake ifikapo 2021 yote iwe imemeremeta. Ahsante sana.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la makazi holela sehemu nyingi linasababishwa na kukosa wataalam wa kupanga, kupima na hatimaye kutoa hati. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe hatuna Afisa Ardhi wala hatuna Afisa Mpima, tuliyenaye pale ni afisa tu ni kama technician. Je ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Njombe itapata Afisa Ardhi ili aweze kutusaidia katika kupanga na kupima na baadaye kutoa hati? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu Mbunge wa Njombe la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maswali haya bila shaka yananipunguzia muda wa kujadili kesho pengine utapungua utakuwa siku moja, maana ni haya haya ambayo nitasema kesho.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama ulivyosema mwenye tunao upungufu wa Maafisa Ardhi na katika speech yangu nimetoa uwiano ikama inasema nini lakini tulionao ni wangapi. Nataka kukuhakikishia zoezi hili litapunguza makali kidogo mwezi wa Saba ambapo Wizara yangu sasa itaanza kupanga upya hawa maafisa, wanahamishwa na kupangwa na Wizara yangu, kwa sababu tumegundua siyo kwamba ikama ilikuwa inasababisha lakini upangaji ulikuwa hauzingatii mahitaji. Ukienda Mkoa wa Mwanza kwa mfano Wilaya za Nyamagana na Ilemela unakuta kuna Maafisa Ardhi themanini lakini Njombe hakuna hata mtu mmoja. Kwa sababu tatizo ni kwamba wale wapangaji pengine pale walipokuwa wanasimamiwa hawakuwa na fani zinazofanana nao, kwa hiyo walikuwa hawajui fani gani ipangwe namna gani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka niwahakikishie Wabunge wote mwezi wa Saba tutawapanga hawa hawa wachache, lakini tutajitahidi angalau kila wilaya iwe na afisa angalau wa taaluma moja ya ardhi aweze kuwepo. Nazijua baadhi ya wilaya ambazo hazina hata mtu mmoja wa sekta nzima ya ardhi ambayo ina vitengo vitano, hawawezi kufanya shughuli.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi lako tutalitekeleza mwezi wa Saba na la Waheshimiwa Wabunge, tutawapanga upya na Njombe, tatizo la Njombe Afisa Ardhi alikuwa mtendaji mzuri sana nimempandisha cheo amekuwa Kamishna Msaidizi. Kwa hiyo nitampelekea mtu mwingine baada ya hapo na Waheshimiwa Wabunge wote wenye swali kama hili watusubiri mwezi wa Saba Mungu akipenda tumeamua kuwapanga upya, nitawaita hapa kwanza niwaelekeze lakini tutawapanga upya ili angalau kila wilaya tuwe na afisa anayeweza kufanya kazi fulani.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la kuingiliwa katika maamuzi ya kesi na wanasiasa hasa kwenye maeneo ya vijijini na hivyo kuathiri yale maamuzi.

Je, Serikali inatoa maelekezo gani kwa maeneo hayo ya vijijini ambako kumekuwa na mwingiliano wa viongozi wa kisiasa hasa Madiwani?

Lakini pili kumekuwa na tatizo kubwa la Mabaraza haya kutokuwa na vifaa vya kufanyia kazi, lakini kutokuwa na ofisi, posho za kuweza kujilipa na mwisho wa siku imekuwa wakiona yule anayedaiwa au anayehukumiwa ndiyo mwenye uwezo, wanaangalia nani mwenye uwezo basi wanamu-award ili waweze kupata hizo fedha na mwisho wa siku waweze kujilipa au kuweza kununua hivyo vifaa?

Je, ni nani mwenye wajibu wa kutoa hivi vifaa na kutoa hizi posho lakini pia na ofisi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni hatua gani zinachukuliwa dhidi ya wanasiasa ambao wanaingilia mambo hayo ya uendeshaji wa Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza kwenye jibu langu la msingi, haya mambo ni mambo ya kisheria ya tangu mwaka 1985 na yamefanyiwa marejeo mwaka 2002 wale Wajumbe wa Mabaraza ya Kata ni Wajumbe ambao wanatoka kwenye Kata husika kwa hiyo lazima uwe mkazi wa Kata husika kama siyo mkazi hupaswi kuingia katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili la kuangalia wakati unapata Wajumbe wa Uendeshaji wa Mabaraza ya Kata, ni lazima hao watu wasiwe na tuhuma zozote za jinai na makosa mbalimbali kwa lugha nyingine lazima wawe ni waadilifu katika eneo lile, lakini majina haya ambayo yanaombwa yanapaswa kubandikwa kwenye notice za matangazo ili kama kuna mwananchi ana pingamizi dhidi ya mtu yeyote mjumbe aliyeomba aondolewe, lakini hakuna nafasi kabisa ya kiongozi wa kisiasa kuingilia kwa sababu kuna Kamati ya Ward DC inapendekeza majina kwa maana ya maoni, lakini uteuzi wa mwisho wa wajumbe hawa unafanywa na Halmashauri akiwepo Mwanasheria wa Halmashauri na Mkurugenzi na viongozi wengine, na ikiwezekana Mkuu wa Wilaya anaingia katika eneo hilo kwa maana ya kufanya consultation.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mujibu wa sheria hakuna namna ya kuingilia, lakini kama kuna eneo ambalo viongozi wa kisiasa wanaingilia hayo ndiyo maeneo tunayohitaji kupata taarifa ili tuweze kuchukua hatua na kutoa maelekezo na kuendesha vizuri katika maeneo hayo bila kuingiza siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni vitendea kazi ambayo inapelekea pia maamuzi ambayo yameyumbishwa kulingana labda na vipato na kuangalia nani amepeleka kesi katika eneo hili. Ni kweli kwamba tumepata pia maneno maeneo mbalimbali wanakosa vitendea kazi, lakini haya Mabaraza yanasimamiwa na Wakurugenzi wa Utendaji wa Halmashauri na Wanasheria wa Halmashauri na ndiyo maana baada ya kuchaguliwa wanapaswa waende watoe semina na mafunzo, lakini Bajeti za Halmashauri lazima ziwe na kipengele ambacho kinasaidia uendeshaji wa Mabaraza haya ya Kata na hata fedha ambazo wanapanga kwa mfano kesi imeamuliwa kutoka eneo moja ofisini kwenda kuangalia mahali ambapo kuna malalamiko inabidi gharama ile iwe ni gharama iwe ni gharama ya kawaida kabisa ndogo ambayo mtu wa kawaida ataifanya, na lengo la Mabaraza haya ni kupunguza umbali wa kuwafanya wananchi kutoka kwenye Kata yake kwenda kwenye Mahakama za mwanzo na Wilaya, lakini vilevile kuwasaidia watu wa kawaida kabisa ngazi ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nielekeze Wakurugenzi Watendaji na Wanasheria katika Halmashauri zetu kama kuna maeneo kuna malalamiko makubwa na watu wanakuwa charged gharama kubwa, naomba wachukue hatua ili tuweze kusimamia, tuweke viwango vya kawaida kabisa ambavyo mtu wa kawaida anaweza kufanya, lakini mwisho isije ikatokea hata siku moja kwa sababu kuna mtu ana malalamiko yake na kwa sababu hana uwezo wa kifedha asisikilizwe hili litakuwa ni kosa kwa viongozi wetu ambao wanasimamia katika eneo lile na itakuwa inaenda kinyume kabisa na maelekezo ya Baraza na Uanzishwaji wa Baraza la Usuluhishi wa Kata, nakushukuru sana.