Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joram Ismael Hongoli (11 total)

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Serikali Awamu ya Nne ilianzisha utaratibu wa mbolea za ruzuku ili kuwasaidia wakulima wasio na uwezo wa kununua pembejeo waweze kuzipata na kuboresha kilimo:-
(a) Je, Serikali haioni kama inapoteza fedha nyingi kusambaza pembejeo hizo kupitia mawakala ambao mahali pengine hupeleka mbolea kidogo au wanawasainisha wakulima vocha bila kuwapa mbolea kwa kuwapatia shilingi 5,000 - Shilingi 10,000 na baadaye kurejesha mbolea mahali pengine;
(b) Je, kwa nini Serikali isisambaze mbolea hizo kupitia Kamati za Ulinzi na Uslama kuliko hao Mawakala ambao siyo waaminifu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa wako baadhi ya mawakala na watumishi wa Serikali wasiowaaminifu ambao huwarubuni wakulima ili kukiuka utaratibu wa utoaji wa ruzuku uliowekwa kwa manufaa ya mawakala na watumishi wao. Wizara yangu inafanya ufuatiliaji wa karibu na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika hao kwani huwakosesha wakulima pembejeo na hivyo kudumaza maendeleo ya sekta kilimo nchini. Aidha, ili kuondoka na mfumo huu Wizara yangu imeunda kikosi kazi cha kupitia gharama za uzalishaji na uagizaji wa pembejeo nchini ili kama kuna uwezekano kuondoa baadhi ya tozo na kodi ili kufanya pembejeo hizo zipatikane kwa bei nafuu. Sambamba na hilo viwanda vya kuzalisha mbolea vinatarajiwa kujengwa hapa nchini katika Wilaya za Kilwa na Kibaha, mategemeo yetu ni kuwa uzalishaji utakapoanza bei ya mbolea itakuwa nafuu kwa wakulima wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, usambazaji wa mbolea za ruzuku umekuwa ukifanywa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali. Makampuni ndiyo yenye mitaji na dhamana ya kuuza pembejeo hizo kwenye mpango wa ruzuku. Serikali inatoa vocha kwa mkulima ambayo ni hati punguzo ya kupunguzia mkulima makali ya bei ya pembejeo. Kwa utaratibu wa sasa Kamati za Pembejeo za Wilaya chini ya Uenyekiti wa Wakuu wa Wilaya, zimepewa jukumu la kusimamia mgawo na usambazaji wa pembejeo katika maeneo yao. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wamekuwa wakialikwa katika vikao vya Kamati ya Pembejeo za Wilaya ili kusaidia katika mikakati ya kudhibiti upotevu na ubadhirifu wa vocha za pembejeo.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Ilani ya CCM iliahidi kutengeneza barabara ya kutoka Njombe - Lupembe - Madeke - Morogoro - kwa lami katika mwaka 2015/2016:-
Je, ni lini barabara hiyo itaanza kutengenezwa hasa ikizingatiwa kuwa imebaki miezi mitano katika mwaka wa fedha 2015/2016?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika ni kweli kuwa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 imeweka katika mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kibena – Lupembe - Madeke.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara TANROADS, imeshaanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Njombe (Kibena) – Lupembe - Madeke yenye urefu wa kilometa 126.2 kwa kiwango cha lami. Maandalizi haya yalianza kwa kusaini mkataba kati ya TANROADS na Mhandisi Mshauri M/S Howard Humphreys (T) Limited kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo. Kazi ya usanifu ilikamilika mwezi Machi 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 503.55, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njombe – Lupembe - Madeke unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Uchumi wa wananchi wa Jimbo la Lupembe na Tarafa ya Lupembe unategemea biashara ya chai lakini kwa muda mrefu sasa wananchi wanataabika kupata soko la chai yao kwa sababu ya kufungwa kwa Kiwanda cha Chai cha Igombola - Lupembe mwaka 2009; na kwa kuwa kiwanda hicho kilikuwa cha wananchi lakini baadaye Serikali ikampata mwekezaji baada ya wananchi kushindwa kukiendesha lakini ukatokea mgogoro kati ya mwekezaji na wananchi ambao umesababisha hasara kubwa kwa wananchi, mwekazaji na Serikali pia.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro huo ili Serikali iweze kunufaika na kiwanda hicho kupitia tozo ya kodi, ajira na kadhalika na wananchi waweze kuuza chai yao kwenye kiwanda hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji wa Kampuni ya Dhow Mercantile East Africa Limited alishinda kesi dhidi ya Muungano wa Vyama vya Ushirika Lupembe (MUVYULU) iliyoamuliwa ilipe fidia inayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 28 pamoja na gharama za kuendesha kesi hiyo. Hata hivyo, MUVYULU walikata rufaa na hivyo kesi hiyo bado ipo mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inasubiri maamuzi ya kesi iliyoko mahakamani kupitia uongozi wa Mkoa, Serikali iliomba Mufindi Tea and Coffee Limited kuangalia uwezekano wa kujenga Kiwanda cha Chai katika Tarafa ya Lupembe ili kuwezesha wakulima wa chai wa eneo hilo kuuza majani ya chai. Mufindi Tea and Coffee Limited ilitekeleza ombi hilo na kuunda Kampuni iitwayo Ikanga Company Limited na kujenga kiwanda katika eneo hilo na kilianza kufanyakazi mwezi Agosti, 2013 na kuzinduliwa rasmi mwezi Novemba 2013 na Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Kupitia kiwanda hicho sasa, wakulima wa Lupembe wanauza chai katika kiwanda hicho na kutoa ajira katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Ikanga imeingia makubaliano na wakulima wa Lupembe kwa kuwapatia pembejeo na huduma za ugani ili kuweza kuzalisha chai yenye ubora mfumo ambao Serikali imekuwa ikiusisitiza katika kuendeleza uzalishaji wa mazo ya kilimo. Mwaka 2016 kampuni ya Dhow Mercantile East Africa Limited ilifanya ukarabati katika Kiwanda cha Lupembe ili kiweze kufanya kazi tena.
Hata hivyo, Serikali kupitia Bodi ya Chai imefanya ukaguzi na kugundua kasoro kuhusu hali ya kiwanda hivyo ilitoa leseni ya muda wa majaribio wa miezi mitatu kwa mwekezaji huyo ili kumpa muda wa kurekebisha kasoro zilizodhihirika. Baada ya mwekezaji kumaliza muda wa majaribio Bodi imemuongezea muda wa leseni kwa mwaka mmoja baada ya kujiridhisha na utendaji wake.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilianzishwa mwaka 1982, lakini mpaka leo hii haina Hospitali ya Wilaya na ina Vituo vitatu vya Afya:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kuviwezesha Vituo hivi vya Afya kutoa huduma ndogo ya upasuaji ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto pamoja na wananchi wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismail Hongoli, Mbunge wa Lupembe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi milioni 82.0 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Njombe na itaanza kwa jengo la wagonjwa wa nje, yaani OPD. Fedha hizo bado hazijatolewa kutoka HAZINA.
(b) Mheshimiwa Spika, ukarabati wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya cha Lupembe umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 21.0 kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Vile vile, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 36.0 kwa ajili ya kukarabati chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya cha Kichiwa.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Waathirika wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamekuwa wakipoteza maisha haraka zaidi kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za matibabu.
Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi, vifaa tiba
na dawa katika kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Njombe ilitengewa bajeti ya shilingi 295,000,000 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo mpaka Machi, 2017 tayari shilingi 87,000,000 zilipelekwa na kuelekezwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya afya. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri hiyo imetengewa bajeti ya shilingi 433,000,000 sawa na ongezeko la asilimia 47. Vilevile Serikali imeongeza fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya kutoka shilingi milioni 259.4 zilizotengwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi shilingi milioni 306.2 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 18. Fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Halmashauri inatakiwa kutumia makusanyo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana pamoja na dawa katika vituo vinavyotoa huduma ya afya. Serikali itaendelea kuongeza fedha kila mwaka na kushirikiana na wananchi ili kuimarisha huduma za afya Wilayani Njombe na Tanzania kwa ujumla.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Dawa zinazotolewa na MSD zimekuwa zikichelewa sana kupelekwa kwenye Halmashauri na hivyo kusababisha baadhi ya dawa kupelekwa zikiwa zimekaribia kuisha muda wake wa matumizi hali inayozisababishia Halmashauri gharama kubwa za utekelezaji.
Je, ni kwa nini gharama za uteketezaji wa dawa hizo zigharamiwe na Halmashauri badala ya MSD ambayo inachelewa kuzipeleka?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismail Hongoli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu wa usambazaji wa moja kwa moja wa dawa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma (direct delivery) unaofanywa na Bohari ya Dawa (MSD). Kwa mujibu wa utaratibu huu, Kamati za Afya za vituo husika hupokea na kuhakiki kila dawa iliyopokelewa kituoni hapo kama inavyoonyeshwa kwenye hati ya madai. Hati hiyo huonyesha gharama za dawa pamoja na muda wa dawa kuisha matumizi yake.
Mheshimiwa Spika, endapo Kamati ya afya ya kituo haitaridhika na kupokea dawa kwa sababu yeyote ile muhimu ikiwa ni pamoja na kuharibika au dawa kuwa na muda mfupi kwa matumizi, kituo hutakiwa kujaza fomu namba saba ili kurudisha bidhaa iliyokataliwa moja kwa moja Bohari ya Dawa ambapo gharama ya dawa husika hurejeshwa kwenye akaunti ya kituo husika.
Mheshimiwa Spika, taarifa za usambazaji wa dawa na vifaa tiba kutoka MSD katika Halmashauri ya Njombe kwa mwaka 2016/2017 hazionyeshi uwepo wa dawa zilizosambazwa zikiwa na muda mfupi wa matumizi. Hivyo, MSD haipaswi kugharamia uteketezaji wa dawa zilizokwisha muda wa matumizi katika Halmashauri ya Njombe kwa kuwa jukumu la uteketezaji ni la Halmashauri husika.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nitumie Bunge lako Tukufu kuzitaka Halmashauri zote nchini kuzingatia vyema taratibu za kupokea, kuhifadhi na matumizi ya dawa.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Lupembe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni ya muda mrefu na tulishaomba na kufanya maandalizi ya kuwa na Kidato cha Tano kwa Mchepuo wa CBG.
Je, ni lini Serikali itaanzisha Kidato cha Tano katika
Shule hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Lupembe ni miongoni mwa shule mpya 22 ambazo zimeombewa kibali Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili iweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano katika mwaka 2017. Hivyo, shule hiyo itaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano baada ya kupatikana kwa kibali kilichoombwa kufuatia ukaguzi wa miundombinu ya shule iliyofanyika.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Katika Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Njombe, Tarafa ya Lupembe, hususan Kijiji cha Madeke kinazalisha matunda aina ya nanasi, parachichi na matunda mengine, lakini hakuna soko la matunda hayo na hii ni kutokana na kutokuwa na kiwanda kikubwa cha matunda.
• Je, Serikali inasaidiaje upatikanaji wa masoko ya mazao hayo?
• Je, ni lini Serikali italeta kiwanda katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismail Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) wakati wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyomalizika mwezi Julai, 2017 iliwaunganisha wakulima wa nanasi, parachichi na matunda mengine ambao wana uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 6,000 kwa mwaka na kampuni ya Tomoni Farms Limited iliyopo Jijini Dar es Salaam. Mwakilishi wa Kampuni ya Tomoni na mwakilishi wa Kikundi cha Wakulima wa Matunda kutoka Kijiji cha Madeke walitiliana saini ya mkataba usiofungani wa kununua wastani wa tani 3,000 za matunda kwa mwaka zenye thamani ya shilingi bilioni 1.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tomoni Farms Limited ni kampuni kubwa inayonunua matunda na mbogamboga kutoka kwa wakulima mbalimbali nchini. Aidha, wakulima hao pia wameunganishwa na wanunuzi wa matunda kutoka nchi za uarabuni kwa ajili ya soko la nje.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya kusindika matunda katika eneo hili, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imeanzisha kiwanda kidogo cha kukausha chips za nanazi. Kiwanda hiki kinamilikiwa na wanakijiji wa Madeke kupitia mradi uliobuniwa na mpango wa maendeleo wa kilimo wa wilaya (District Agriculture Development Plans – DADPS), hata hivyo kiwanda hiki bado hakikidhi mahitaji ya usindikaji wa zao hili na jitihada zimeendelea kufanyika, ili kupata wawekezaji, hususan katika Kijiji cha Madeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo katika kijiji hicho ni kukosekana kwa umeme. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilishawaandikia barua TANESCO kuweka katika mipango yao kufikisha umeme katika Kijiji cha Madeke, ili uwekezaji uweze kufanyika na vilevile nimefuatilia hata REA watafikia kijiji hicho.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali isiingize kwenye mitaala ya elimu somo la umuhimu wa kulipa kodi ili lifundishwe kuanzia shule ya msingi ili wananchi wapate uelewa wa kodi na waweze kufurahia kulipa kodi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya mlipa kodi katika kumjengea mwananchi tabia, mwenendo na mazoea ya kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa letu. Wizara yangu kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania ndiyo yenye jukumu la kubuni, kuandaa na kuboresha mitaala ya elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeona umuhimu wa kuingiza elimu ya mlipa kodi kwenye mitaala ya elimu nchini ili kuwajengea Watanzania tabia, mwenendo na mazoea ya kuwa na utamaduni wa kulipa kodi. Katika somo la uraia na maadili kuanzia darasa la III na kuendelea, mtaala umelenga kumjengea na kumuandaa mwanafunzi kuwa mwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku, kuiheshimu na kuithamini jamii yake na kuwa mwadilifu na mzalendo ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya kitaifa ikiwemo kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kutokana na umuhimu wa kuwajengea vijana tabia kuhusu elimu ya mlipa kodi, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kushirikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaendelea kuboresha elimu hii ili isisitizwe na kuwekewa mkazo katika mitaala ya elimu kuanzia elimu ya msingi.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-

Madeni ya Halmashauri hususan mikopo ya vijana na wanawake ya miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2016 yamekuwa hayalipiki kutokana na Halmashauri nyingi kutokuwa na mapato ya kutosha kuendesha Halmashauri hizo hasa miradi ya maendeleo.

Je, ni kwa nini madeni hayo yasifutwe ili kuondoa hoja za ukaguzi kwenye Halmashauri hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikitoa fedha za mikopo kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali. Katika kipindi chote cha utekelezaji hakukuwa na sheria kwa ajili ya kusimamia utengaji na utoaji fedha hizo na kusababisha kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya fedha ambazo hazikutolewa kwa walengwa katika kipindi husika na kusababisha hoja za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutungwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Fedha hizo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inakusudia kuyafuta malimbikizo hayo kama ilivyoelekezwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kazi ya kuhakiki takwimu, kubaini kiasi ambacho kimelimbikizwa katika Halmashauri zote nchini inaendelea na Mara tu itakapokamilika, taratibu za kufuta malimbikizo hayo zitafanyika. Aidha, kwa sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI inazisimamia kwa karibu Halmashauri ili kuhakikisha zinatoa fedha hizo kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-

Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yamekuwa ni chanzo cha migogoro badala ya kutatua migogoro.

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kutoa mafunzo ya muda mfupi ili waweze kumudu majukumu yao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaraza ya Kata ni vyombo vya kisheria vya utatuzi wa migogoro katika ngazi ya chini ya jamii vyenye nguvu ya kisheria katika kutatua migogoro ya wananchi. Mabaraza hayo yaliyoanzishwa mwaka 1985 kwa Sheria ya Mabaraza ya Kata, Sura ya Namba 206 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika utekelezaji wa majukumu yake, baadhi ya Mabaraza yamekuwa na changamoto za kiutendaji zinazotokana na uelewa mdogo wa masuala ya kisheria kwa wajumbe, maadili na kutofahamu mipaka ya majukumu yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilitoa mafunzo kwa Wanasheria wa Halmashauri kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Mabaraza ya Kata. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo ilitoa mafunzo kwa Wakurugenzi na Wanasheria wa Halmashauri. Mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa mafunzo kwa Mabaraza hayo kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.