Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi (37 total)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kumekuwa na uvunaji holela wa mikoko katika eneo la Rufiji na mikoko hii ikiwa inasafirishwa kwenda Zanzibar kwa kutumia bandari bubu. Je, Serikali inajua kuhusu suala hili na je, itachukua hatua gani?
Swali la pili, kumekuwa kuna uvunaji na utoaji holela wa mbao au mazao ya misitu katika maeneo ambayo hayana hata hiyo management plan au strategy ya uvunaji wa rasilimali hii. Je, Serikali ina mpango gani kupambana na hii hali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya maliasili na utalii kwa ujumla viko vitendo ambavyo kwa ujumla wake vinaitwa ujangili na ujangili hauishii kwa wanyamapori tu peke yake na bidhaa zao, ujangili pia unahusisha bidhaa za misitu na misitu yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo vyote ambavyo vimekuwa vikifanyika vya ujangili ni kinyume cha sheria na Wizara au Serikali kwa ujumla imejipanga vizuri zaidi sasa hivi kuweza kudhibiti vitendo vyote vya ujangili kwa kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yanayohusika, kuboresha vikosi vya askari na kuwawezesha askari kuwa na vitendea kazi bora zaidi katika kufuatilia vitendo vya ujangili na kuchukua hatua mara moja.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali la nyongeza au ni ushauri kwa Wizara husika. Mafuriko mengi yanayotokea sasa hivi ni kwamba miundombinu au zile njia za maji zimejaa michanga, pamoja na mabwawa yale ambayo ni reserves za mafuriko nazo zimeharibika. Sasa naishauri Serikali, Wizara husika hiyo ya mazingira, pamoja na Wizara ya Maji wawe na mkakati maalum wa kudhibiti zile njia za maji wachimbe zile drainage pattern za mito au/na mabwawa ili ku-conserve au ku-protect mafuriko yasitokee. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea ushauri wake mzuri na ambao tunaendelea kuufanyia kazi siku hadi siku, lakini nitoe wito kwa Wabunge wote, kushiriki siku ya usafi. Inapofika tarehe ya usafi, Waheshimiwa Wabunge wote na viongozi wote lazima tuwe kielelezo kwa wananchi kushiriki usafi huu. Tutashiriki kuzibua hiyo mitaro, kufagia na tutashiriki kuhakikisha kwamba kila eneo linakuwa safi na salama.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, kuna uhusiano chanya kati ya elimu na maendeleo katika sekta za kijamii na kiuchumi; je, ni lini Serikali au Wizara itaona umuhimu wa ku-link elimu na maendeleo ya Taifa letu au katika mipango ya maendeleo ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuwa, tayari Serikali imeshachelewa kutathmini; je, tuna upungufu wa aina gani au tunahitaji watu wenye elimu ya aina gani ili kuleta maendeleo katika sekta fulani? Wameji-commit kwamba mpaka mwisho wa mwaka huu wa fedha watakuwa tayari wamekamilisha huo mkakati.
Je, huu mkakati watau-link vipi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kimsingi Serikali inatambua mahusiano kati ya elimu inayotolewa na ustawi wa jamii au katika kuleta maendeleo. Ndiyo maana msisitizo uliopo sasa hivi ni kuhakikisha kuwa, course zote zinazoanzishwa hasa katika vyuo vyetu, ni zile zinazojitahidi kujibu changamoto zilizopo katika jamii zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo basi, baada ya kukamilisha mpango huu ambao umeandaliwa, unaoangalia kwa kina sasa kwa jinsi ambavyo Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano lakini pia Dira yetu ya Taifa ya mwaka 2020 - 2025, kwamba tunataka kwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Katika uchumi wa viwanda tutahitaji wataalam mbalimbali watakaoendesha viwanda vyetu, vilevile katika hao watakaoendesha viwanda tunategemea humo kutakuwa na mambo ya aina mbalimbali. Kwa mfano, afya zetu ili hao watumishi waweze kufanya kazi zao vizuri. Pia tunategemea kupunguza madhara kwa akinamama waweze kujifungua salama. Kwa hiyo, kutokana na matatizo kama hayo, ndiyo maana hata sisi sasa mitaala yetu lazima ijibu changamoto ambazo zipo katika jamii.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kuna tatizo pia la mipaka kati ya TFS na vijiji Wilayani Kondoa; vijiji vya Mnenia, Masanga, Itolowe na Kasese ambapo beacon za TFS zimeingilia katika mashamba ya wanavijiji hawa. Sasa ningependa kujua Serikali ina mkakati gani au ni lini itarekebisha tatizo hili ambalo linawaacha wanavijiji hawa njia panda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia akisema kwamba katika vijiji alivyovitaja beacons za TFS kwa kauli yake zimeingia katika mashamba ya wananchi kwenye vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kwamba hii
ndio sababu tumeunda kamati maalum kwa sababu kusema tu moja kwa moja kwamba beacons zimeingia kwenye maeneo ya mashamba ya watu bila kuangalia kwamba upo
uwezekano mashamba ya watu yameingia ndani ya maeneo ya hifadhi haitakuwa sahihi katika hatua hii. Kwa hiyo, tuipe nafasi Serikali iweze kuendelea kufanya kazi ya kwenda kufanya utafiti wa kwenye site wa kuangalia uhalisia ulivyo tukipima kwamba ni kipi kimeingia upande upi lakini wakati huo huo tukiangalia zaidi maslahi ya hifadhi ambayo ndio priority kwa Taifa.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, japo nia ya Serikali ni njema kurasimisha ardhi kwenye maeneo ambayo hayajapimwa,
lakini kuna concern kwamba tunakuwa tunaendeleza squatters, maeneo ya wazi ambapo miundombinu inakuja
kuwa challenge. Sasa badaye mnapotaka ku-implement mambo ya mipango miji au ramani zetu tulizonazo kutakuwa kuna gharama tena husika za kubomolea watu. Je, Serikali nimezingatia hili? Asante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachozungumza nadhani kama nimejibu vizuri, ulinisikiliza wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Allan, si nia ya Serikali kuona kwamba miji inaendelea kuharibika kwa kuendeleza squatter na ndiyo maana nimewaomba Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wote ni Wajumbe wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri zetu, pale ambapo Serikali imeanza kufanya zoezi la urasimishaji katika maeneo ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha kwamba wanasimamia maeneo yao ili kusiwe na muendelezo wa ujenzi holela. Kwa sababu zoezi hili linapaswa kusimamiwa na Halmashauri zenyewe husika, Wizara sio rahisi kushuka kila maeneo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli zoezi tunalifanya na inaonekana ni zuri, lakini tusingependa kuona ujenzi holela
unaendelezwa. Sasa ujenzi huu utasimama pale ambapo kila halmashauri itawajibika katika eneo lake kuhakikisha inakuwa na michoro ya mipango miji kwenye maeneo yao na kusimamia zoezi la ujenzi holela lisiendelee katika maeneo yao. Tukifanya hivyo, miji yetu itakuwa salama na itakuwa inapendeza.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nilitegemea Wizara itaonesha angalau trend ya mapato kutoka kwenye shughuli za uvuvi angalau miaka mitano au kumi tuone kwamba inaendaje, ila wametoa tu mfano kwa mwaka wa 2015/2016. Ukiangalia mapato kutoka uvuvi 2016/2017 huu mwaka uliokwisha, walikuwa na pungufu almost shilingi bilioni tisa kwa sababu walipata tu shilingi bilioni 10. Sasa Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuamka na kuweka vipaumbele katika Sekta hii ya Uvuvi ili kujiongezea mapato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mfano tu, bajeti ya maendeleo inayotengwa katika Sekta ya Uvuvi, mwaka 2016 na mwaka huu 2017 ni sifuri. Kwa hiyo, ina maana shughuli za doria, mikakati ya kujenga Bandari ya Uvuvi au kuboresha Bandari ya Uvuvi haipo, kujikita zaidi katika kuongeza mapato katika deep sea fisheries, haipo; hii mikakati yote haipo; zaidi kuna project moja tu ya SWIOFish ndiyo ambayo imesimama ambapo fedha zake kutoka World Bank ni za mikopo. Sasa Serikali haioni kwamba hawako fair kwa wavuvi, shughuli za uvuvi na yenyewe pia inajinyima mapato ambayo yangetuletea maendeleo katika nchi yetu?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba Sekta ya Uvuvi imepewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ASDP II na katika Programu hii, yote anayoyazungumzia Mheshimiwa Mbunge, yamo. Ni programu itakayoanza mwaka huu wa fedha mpaka mwaka 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwamba haoni mikakati yoyote ya kuendeleza sekta hii ya uvuvi; mkakati lazima utengenezewe mazingira ili uweze kutekelezwa. Kwa hiyo, tusingeweza kupanga mambo ya uvuvi wa bahari kuu bila kuwa na legal framework ambayo inatuwezesha kutekeleza yale tunayotaka kufanya. Kwa hiyo, tulichoanza nacho ni kubadilisha kanuni za uvuvi wa bahari kuu ili sasa yale tutakayopanga kuyafanya, yaweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kusisitiza hapa kwamba akisoma kanuni na natumaini ameshazisoma; ataona wazi kwa vipi sasa hivi tutabadilisha sana sura ya Sekta ya Uvuvi wa bahari kuu hapa nchini na manufaa yataanza kuonekana. Sasa hivi tunapozungumza, wavuvi wa bahari kuu ambao wameomba kukata leseni kwa masharti mapya wapo wengi, wamekwishafika 30 na kadhaa hivi. Kwa hiyo, tuanze tu kutegemea kwamba manufaa makubwa ya uvuvi yataonekana hapa nchini na hicho kinachoitwa blue economy utakishuhudia kinatokea hivi karibuni.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kilometa 180 tu kutoka hapa kuelekea Kondoa – Irangi kuna malikale nzuri, kuna michoro ya mapangoni na miundombinu ya barabara imeimarika. Sasa nataka kujua Wizara hii husika itatengeneza vipi yale mazingira ya kule ili kuimarisha utalii pamoja na mafunzo katika mapango ya michoro ya kale Kondoa – Irangi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vivutio vyote vya utalii ambavyo vinaangukia kwenye eneo la heritage tourism vyote tumefanya utaratibu wa kuviorodhesha halafu baadaye tunavisajili. Kuvisajili maana yake ni pamoja na kuangalia viwango vyake vya ubora na kuona kama kweli vinakidhi haja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa tumepokea taarifa hizo kutoka kwenye Wilaya mbalimbali, baadaye hatua inayofuata ni kuvitembelea na kuvihakiki.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa kuna changamoto lukuki katika Sekta ya Uvuvi na kwa kuwa wavuvi hao wameongezeka mara dufu zaidi ya asilimia 90 kwa miaka 10 iliyopita pamoja na vyombo wanavyotumia, lakini haviendi sambamba na nini wanachokipata.
Serikali haioni sasa ijikite kwenye ku-promote acquaculture na mariculture kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Uvuvi nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Sware ametabahari sana katika masuala ya uvuvi, kwa hiyo, anafahamu fika kwamba katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili, moja kati ya masuala ambayo yametiliwa mkazo sana ni namna gani ya kujenga uwezo wa wavuvi na Watanzania wengi kushiriki katika ufugaji wa viumbe kwenye maji katika maana ya acquaculture.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba acquaculture ndiyo hasa tunakoelekea tunavyozungumzia kuhusu blue economy. Kwa hiyo, ni kweli kama alivyosema, lakini ni kweli kwamba tumewekea mkakati. Tunataka ikiwezekana kila Halmashauri iwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba wananchi wanafuga samaki, badala ya kuendelea kutumia rasilimali tulizonazo za uvuvi ambazo kwa kiasi kikubwa zimepatwa na changamoto kutokana uvuvi usio endelevu.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ahsante kwa majibu Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, napenda kujua Serikali imefikia hatua gani kwenye kulipa fidia au kuboresha mazingira ya wanakijiji wa Uvinje vis-a-vis TANAPA?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kwa vijiji vile vinavyozunguka au vilivyo ndani ya Saadani kuona vinashirikishwaje katika shughuli za kitalii ili kudumisha au kuboresha uchumi wao? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu fidia kwenye vijiji alivyovitaja. Kwa kuwa hadi nasimama hapa bado nilikuwa sijapata taarifa zilizokamilika kuhusiana na madai hayo, nimuahidi nikitoka hapa anipe kwa ufafanuzi vijiji hivyo ni vipi na kwa nini vinastahili fidia ili niweze kuangalia tumefikia katika hatua gani pale Wizarani kuweza kukamilisha utaratibu huo wa kuwalipa fidia ikiwa watakuwa wanastahili kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la namna gani Wizara au Serikali inashirikisha vijiji vinavyozunguka maeneo ya Hifadhi ya Saadani katika masuala ya kuendeleza vivutio, utaratibu wetu kwa kawaida ni kwamba kila wakati tunapofikiria kuanzisha mradi, wadau wa kwanza kabisa na hii nimeisema hata katika swali la msingi, kwamba uendelezaji wa vivutio katika hifadhi zote unashirikisha jamii zinazozunguka katika maeneo ya hifadhi na Serikali pamoja na mashirika binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kwa upande wa vijiji alivyovitaja katika Hifadhi hii ya Saadani tumeweza kuwashirikisha kwa mujibu wa taratibu tulizonazo lakini kama ana mawazo ya kuweza kuipatia Serikali ili tuweze kuboresha zaidi namna ya kuweza kushirikisha wananchi hawa au wadau hawa wanaoishi kwenye maeneo ambayo ni jirani na hifadhi basi tupo tayari kupokea ushauri huo tuweze kuboresha zaidi taratibu zinazotumika katika kuboresha vivutio kwenye maeneo ya hifadhi.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: MheshimiwaMwenyekiti, nashukuru. Nimepata masikitiko makubwa sana kutika kwenye Wizara husika ambayo inasimamia shughuli za mazingira nchini. Kwa kuwa Wizara hii ndio iliyoshikilia au inaongoza Sheria yetu ya Mazingira ya mwaka 2014; na kwa kuwa Wizara hii ndio iliyoshikilia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi; na kwa kuwa ni Wizara hii ambayo inasimamia Mfuko wa Mazingira Nchini; na kwa kuwa ni Wizara hii ambayo ina fedha kutoka mashirika mbalimbali nchini na duniani kote inayosimamia shughuli zote za mazingira nchini, inanijibu kwamba haitoi, haihangaiki, haina chochote, hamna jibu linalohusu shughuli za kusimamia fedha za ku- address issues za climate change nchini na tunaona dhahiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yameleta madhara makubwa, majira ya mvua hayajulikani, kuna ukame, na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kujua, hii Wizara ipo au haipo? Na kama ipo, mbona imenyamazia kimya issue ya mabadiliko ya tabianchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninamheshimu sana Dkt. Sware ambaye Ph.D yake ameisoma kule Stockholm, Sweden, Masters yake ameichukulia Norway, namheshimu sana, lakini kwa sababu anashindwa kutofautisha kati ya maneno mawili ambayo ni rahisi sana, yeye ameuliza swali la ruzuku na ruzuku kwa kiingereza kwa faida yako Dokta tunaita subsidies, lakini kuna kitu kingine tunaita misaada, misaada ni grants.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama yeye ameuliza ruzuku, ndio nimemjibu sisi hatuna ruzuku. Lakini haya aliyoyasema leo kama angejiongeza akauliza hayo, kwa faida ya Watanzania, kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na nchi yetu mpaka leo kuanzia tarehe 6 mpaka 17 wako Bonn, Ujerumani wanashiriki mkutano mkubwa wa kimataifa kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Na sisi Tanzania ni nchi wanachama ambao tulisaini Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kule Mjini Paris na tunayo mifuko ifuatayo ambayo sisi tunakabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa kwanza unaitwa Adaptation Fund, yani kwa maana kwamba ni mfuko wa kuhimuli mabadiliko ya tabianchi. Mfuko wa pili, unaitwa ni Least Developed Countries Fund, yaani kwa maana Mfuko wa Nchi Maskini Duniani. Na mfuko mwingine ni GEFT ambao ni Global Environmental Facility. Mfuko mwingine ni Mfuko wa Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumepata grants hizi ambazo sasa tunapambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi maeneo mbalimbali hapa nchini. Tuna mradi mkubwa sana ambao Ocean Road pale kwa sababu kina cha bahari kimeongezeka tunajenga ukuta mkubwa wa kilometa moja, ili kingo za bahari zisije zikasombwa na kuharibu makazi ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni tunajenga ukuta mkubwa ili kudhibiti kingo zisiendelee kubomoka. Vilevile kupitia grants hizo kule Rufiji tunarudishia mikoko ambayo ilikuwa imekatwa na mradi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Zanzibar Kisiwapanza, kule Zanzibar Kisakasaka pamoja na Kilimani mifuko hiyo inaendelea. Kule Pangani tunajenga ukuta pamoja na kurudishia mikoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Bagamoyo tunajenga visiwa 28 kwa wananchi wa Bagamoyo, zikiwepo na sekondari mbili mojawapo inaitwa Kinganya ambayo ni ya Mheshimiwa Dkt. Kawambwa. Mifuko hiyo, tunaitumia kwa ajili ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa wananchi wengi wanahamasika na ufugaji wa samaki na kwa kuwa kuna uchache wa mbegu bora ya samaki na kusababisha samaki kutoka nje kuagizwa hasa mbegu za sato na hii inaweza kuwa hatarishi kwa samaki wetu asilia nchini. Napenda kujua Serikali inajipanga vipi kuboresha na kuwekeza katika tafiti mahsusi za uzalishaji wa mbegu bora za vifaranga wa samaki na pia kuboresha maeneo mahsusi, hizi hatcheries za uzalishaji wa vifaranga vya samaki nchini. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inahamasisha katika ufugaji wa samaki na tunazo taasisi zetu za utafiti mathalani TAFIRI na vituo vyetu vya uzalishaji wa vifaranga vya samaki kama kile kituo chetu kilichoko pale Morogoro Kingolwira. Vituo hivi vimejipanga vyema, vina vifaranga wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wafugaji wote wa samaki wawe tayari sasa kuweza kwenda katika vituo vyetu vilivyopo katika zones mbalimbali, kimojawapo hiki cha zone ya Mashariki hapa Morogoro kwenda kuchukua vifaranga bora kabisa na wataweza kufanya ufugaji huu wa samaki na kujipatia kipato na lishe wao wenyewe bila wasiwasi wowote.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuwa hii hospitali ya Wilaya ya Kondoa inahudumia Halmashauri tatu; na kwa kuwa imepata ufinyu mdogo sana wa bajeti na kuleta changamoto katika madawa na vifaa tiba. Sasa Serikali inaona lini wakati inafikiria kuwapatia watu wa Chemba hospitali yao, hospitali hii ikaongezewa bajeti ili kuweza kuhudumia vyema Wilaya hizi tatu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kondoa changamoto ni kubwa na ndiyo maana ukiangalia kuna Majimbo matatu tofauti ambayo ni Chemba, Kondoa Vijijini na Kondoa Mjini lakini hospitali inayotumika sasa hivi ni Hospitali ile ya Kondoa na ukiangalia population mpaka watu wengine kutoka katika wilaya especially kama Wilaya ya Hanang’ walioko mpakani wengine wanakuja hapa Kondoa.
Kwa hiyo, jambo hili ni kubwa na tumeliona ndiyo maana katika mpango wetu wa bajeti wa mwaka huu sasa hasa ukiangalia basket fund tumebadilisha utaratibu wa basket fund tumeongeza bajeti katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuangalia ni jinsi gani tutafanya ili wananchi wapate huduma. Hata hivyo tumetoa maelekezo maeneo mbalimbali, kwa mfano tuna Halmashauri ya Kondoa Mji na Halmashauri ya Kondoa Vijijini lakini hospitali ni moja. Nimewahitaji Wakurugenzi wa maeneo yale waangalie katika suala zima la basket fund katika Halmashauri ambapo ile hospitali iko na jinsi gani kufanya kwa kuweka utaratibu wa kusaidia ile hospitali angalau kwa hali ya sasa iweze kufanya vizuri kwa sababu wananchi wote wanaohudumiwa ni watu kutoka maeneo hayo ambapo ni hospitali yetu lazima tutakuja kuweka nguvu wananchi wapate huduma nzuri. Kwa hiyo, nikushukuru sana Serikali inaifanyia kazi jambo hili.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nataka kuongeza kwenye swali la Mheshimiwa Sware.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kugawanya fedha kwa ajili ya dawa, vifaa na vifaa tiba tunazingatia vigezo vikuu vitatu. Kigezo cha kwanza ni idadi ya walengwa wanaopewa huduma katika hospitali hiyo (service population) ambapo inachukua asilimia 70, kigezo cha pili ni hali ya umaskini katika eneo husika ambacho kinabeba asilimia 15 na kigezo cha tatu ni hali ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano. Kwa hiyo, nilikuwa namuomba Mheshimiwa Sware Halmashauri hizi tatu ambazo zinatumia Hospitali ya Wilaya ya Kondoa wakae pamoja watuletee mapendekezo yao Wizara ya Afya kwamba hospitali hii inahudumia Halmashauri tatu na sisi tutazingatia katika kuwaongezea bajeti ya dawa. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa tunaona dhahiri kwamba kilimo kinazidi kurudi nyuma badala ya kusonga mbele, na kwa kuwa tumekuwa sasa wakulima hasa wale wa vijijini wanategemea mbegu za kununua na sio mbegu za asili na mbegu hizi zinaenda sambamba na upatikanaji wa mbolea. Siku hizi kuna mbolea ya kulimia, kuvunia na kadhalika, wakati kilimo cha zamani cha asili tulikuwa tunatumia mfano, mbolea za samadi na mbegu zenye ubora.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudi nyuma na kujitathmini kwamba tunakoenda siko, tuangalie zile system za zamani za kilimo ziboreshwe zaidi ili wakulima wapate manufaa ya mazao yao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI,VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ushauri ambao ameutoa na kama Serikali tumeuchukua.
Katika mpango wa Serikali katika huu mfumo mpya unaokuja wa bulk procurement Serikali itaagiza kwa wingi mbolea ya kupandia ambayo ni DIP na mbolea ya kukuzia ambayo ni urea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea nyinginezo kwa maana ya NPK, MOP, SA na Bio fertilizers na folia zile za maji, hizi zitakuja katika utaratibu wa kawaida. Vilevile ndani ya Wizara ya Kilimo yupo Wakala wa Mbegu ambaye kazi yake ni udhibiti wa mbegu bora ambaye ni ASA na yeye tutamtumia ili wakulima wetu wafanye kilimo chenye tija.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi hata ho wa maeneo ya Rufiji na maeneo mengine wanaojishughulisha kwa mambo ya uvuvi wametengeneza Beach Management Units na hizi BMUs zina uongozi. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa Wizara ya Kilimo pamoja na Halmshauri husika wakawa wanaviongezea nguvu hizi Beach Managementi Units kwa kuwasaidia kielimu hata na masuala ya kifedha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema vikundi vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika mwambao au tunaziita Beach Management Units ni kweli imekuwa ni fursa ambayo inaweza ikatumika katika kutoa elimu, lakini vilevile kutoa misaada mbalimbali ambayo inaweza ikawasaidia wavuvi kufanya shughuli za uvuvi katika utaratibu ambao ni endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wowote ambao Serikali imetoa elimu tumetumia sana Beach Management Unit, Serikali ndiyo imesaidia kuzianzisha lakini niendelee kumsihi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kujaribu kuhimiza Halmashauri zao ambao kimsingi wao wanakaa kwenye Baraza la Madiwani kuendelea kutoa elimu kwa kupitia Beach Management Units lakini vilevile kuhakikisha kwamba tunatenga raslimali kwenye halmashauri zetu ili hiyo elimu iweze kutolewa kwa urahisi zaidi.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa kuwa Naibu Waziri naye amekiri kwamba mito mingi ni ya misimu na kwamba wakati wa mvua tunapata mafuriko na wakati wa kiangazi ni ukame. Sasa Wizara inaonaje ikajikita katika shughuli za kukinga maji ya mvua kuyahifadhi ili yaweze kutumika kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na shughuli nyingine za kimaendeleo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na jitihada za kuhakikisha tunakinga maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya binadamu majumbani lakini pia na umwagiliaji kwa kujenga mabwawa na tumeshaelekeza kila halmashauri kila mwaka ihakikishe inatenga fedha na kufanya utafiti bwawa moja ili ikiwezekana kila halmashauri ijenge bwawa moja kila mwaka. Na pia tumeelekeza halmashauri wanapopitisha ramani za nyumba basi wahakikishe kwamba wanaweka na utaratibu wa kuvuna maji kutoka katika mapaa ya nyumba kama inavyofanyika maeneo mengine.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa tunajua umuhimu wa misitu na miti na kazi zake katika jamii na katika ekolojia, ni vizuri tukajua kwamba afya ya miti au misitu yetu ikoje. Sasa kwa kuwa kuna changamoto ya kibajeti kwenye Idara hizi za Tafiti za Misitu, napenda kujua Wizara inajipangaje ili kuweza kuweka sawa tathmini ya hali ya misitu nchini in terms za afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kujua kwamba, Wizara inaweka mikakati gani madhubuti ili kuweza kuondokana na changamoto ya upotevu wa misitu kutokana na kukata miti ovyo au uvunaji holela wa miti? Sasa Serikali inajipangaje kujua ni aina gani ya miti na idadi ya miti inapangwa sehemu gani na inashirikishaje jamii ili zoezi hili liwe na manufaa na endelevu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, Wizara imejipangaje katika kuangalia afya ya miti? Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, chini ya Taasisi ya TAFORI ambayo ni mahususi kabisa kwa ajili ya kufanya tafiti, Serikali inafuatilia hali ya misitu nchini kwa namna ambayo ni endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wote tunaangalia misitu yetu inaendaje ili kuweza kubaini matatizo yanayoweza kutishia uharibifu wa misitu kutokana na magonjwa na changamoto nyingine zinazohusiana na afya ya miti kwa mfululizo ambao, kwa kuwa ni endelevu, changamoto zinazoonekana zinashughulikiwa mara tu zinapogundulika huko kwenye misitu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inawezekana kupitia jitihada mbalimbali ambazo ni za Serikali kwa maana ya kupitia bajeti za ndani. Pia kwa sababu suala la uharibifu wa mazingira, masuala ya maendeleo endelevu; haya ni masuala yanayotazamwa na dunia nzima kwa pamoja kwa sababu uharibifu wa mazingira unaathiri dunia yote kwa pamoja. Kwa hiyo, kupitia taasisi mbalimbali ambazo zina maslahi katika kuhakikisha kwamba kuna maendeleo endelevu na utunzaji wa misitu unakuwepo, Taasisi hii ya TAFORI mara kwa mara kwa kupitia maombi mbalimbali inapata support ya kibajeti na kuweza kukamilisha majukumu hayo.
Meshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, napenda kusema kwamba tunao Mkakati wa Taifa wa Kupanda na Kutunza Miti. Hapo awali tumekuwa tukielekeza nguvu kwenye kupanda miti peke yake, lakini sasa baada ya kuona kwamba baada ya kupanda miti bila kufuatilia utunzaji wake na kuhakikisha kwamba inakua, tunapoteza asilimia kubwa sana ya miti ambayo tumetumia rasilimali nyingi sana katika kuipanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mkakati huu wa Taifa wa sasa hivi unaopita katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuanzia mwaka 2016 mpaka mwaka 2020, Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwa ndiyo inayoongoza, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Asasi za Kiraia, Washirika wa Maendeleo pamoja na Sekta Binafsi, wote katika mkakati huu wamegawana majukumu ya kuhakikisha kwamba tunafanya jitihada za kufikia lengo hili ambalo nimelisema hapo awali la kuweza kufikia upandaji wa miti 1,075,000 kila mwaka katika muda wa miaka 17.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya muda mfupi misitu yetu itakuwa katika hali yake ya afya ya kawaida.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, ningependa kupata majibu ya Serikali, kwa nini sekta hii ya uvuvi nchini iko nyuma sana au haikui kabisa ukilinganisha tu na nchi jirani zetu za Kenya na Uganda ilhali sisi tuna maeneo makubwa zaidi ya rasilimali maji nchini na wavuvi wengi wa kutosha. Sasa kwa nini tunasababisha kwamba sekta hii ya uvuvi iko chini sana kiasi ambacho tunaagiza samaki kutoka nje wakati rasilimali tunazo, wavuvi tunao, ili kukuza uchumi wa hawa wavuvi husika pamoja na uchumi wa nchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali zuri sana la mwalimu wangu Dkt. Semesi Sware. Anauliza ni kwa nini sekta ya aquaculture (ufugaji wa samaki) bado iko chini Tanzania ukilinganisha na nchi jirani za Kenya na Uganda. Ni kweli, Uganda wanazalisha tani za samaki zisizopungua 30,000 na Kenya wanazalisha tani zisizopungua 25,000, sisi tuko chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waganda waliweka mkakati mzuri wa cage farming na uzalishaji wa kambale, lakini vilevile Wakenya waliweka mkakati mzuri wa kuhakikisha kwamba Serikali yao inapeleka nguvu ya kutosha katika county zote nchini kwao ili kuhakikisha wanajenga vizimba na mabwawa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Sware na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba mkakati wa Wizara yetu ya Mifugo na uvuvi tunataka tufike mahali huko. Nataka niwahakikishie ya kwamba tayari tumeanza kazi hiyo. Idara yetu ya Aquaculture zipo sheria ambazo zilikuwa zinasababisha tusiende mbele kama nilivyotangulia kusema katika jibu langu la msingi; ambazo tayari tunakwenda kuzifanyia marekebisho. Ninaamini baada ya kufanya mabadiliko hayo yote, na kwa mkakati ambao tunao kama Wizara tutatoka na kwenda mbali sana katika sekta hii ya uzalishaji ya aquaculture. Ninashukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT IMMACULATA S SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, nina maswali mawili ya ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa inafahamika kwamba vyuo vikuu ni chachu ya maendeleo kwa sababu wanazalisha hawa wataalam na wanavumbua au wanaleta suluhisho katika shughuli mbalimbali. Swali lilivyojibiwa kwa upande MTUSATE linaonesha kwamba MTUSATE wameshafadhili miradi 102, kati ya hiyo miradi 44 kutoka vyuo vikuu na shilingi bilioni 4.6 ndio zilizotumika. Hata hivyo, kwa bahati mbaya haiku-indicate ni muda gani. Je kipindi cha miaka 10, 20 au 30 kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya hizi ya elimu ya vyuo Vikuu na issue za tafiti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni kuhusu utengaji wa fedha na upatikanaji wa fedha ambazo zinaelekezwa COSTECH. Mwaka wa fedha 2017/2018 zilitengwa bilioni 13.6, kati ya hizo bilioni bilioni tatu ni fedha za nje. Mwaka huu unaokuja wa fedha zimetengwa bilioni 9.5 kutoka kwenye mfuko wa ndani. Viwango hivi vya fedha ni vidogo sana lakini ningependa kujua kati ya hizi fedha zinazotengwa zinazowafikia COSTECH ni kiasi gani ili ziweze kushuka kwenye hivi vyuo vikuu husika kwa ajili ya tafiti? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo nimezungumzia kwamba tayari zimeshatolewa kwa ajili ya vyuo vikuu kwa ajili ya utafiti ni fedha ambazo zimetengwa kuanzia mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, kwamba ni kiasi gani ambacho kimeshatolea COSTECH ni suala la takwimu, naahaidi nitakapotoka hapa nitampatia takwimu sahihi Mheshimiwa Dkt. Sware.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Watanzania wanawake watatu kati ya kumi na mwanaume mmoja kati ya kumi wamekuwa waki-experience hii kunyanyaswa kijinsia, kikatili (sexual abuse). Idadi hii inaweza ikawa kubwa zaidi kwa sababu moja, watu wengi hawatoi taarifa, sasa Serikali imekuja na mikakati mbalimbali ya kurekebisha hili, lakini tatizo sugu ni kwamba taarifa hazifiki kwenye mamlaka husika. Sasa Serikali itakuja lini na mkakati mahususi wa kuhakikisha kwamba taarifa zinapelekwa kwenye mamlaka husika ili tatizo hili lipate ufumbuzi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiangalia kabla hatujazindua mpango mkakati tulikuwa tuna changamoto ya utoaji wa taarifa. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, matukio kama haya yalikuwa yanafanywa na watu wako karibu sana na familia. Sasa ukiangalia takwimu zetu kuanzia baada ya kuzindua mpango mkakati wetu, utoaji wa taarifa wa matukio umezidi kuongezeka. Hili linaweza likamaanisha mambo mawili; moja, matukio yanaongezeka, lakini pili, linaweza likawa linamaanisha kwamba utoaji wa taarifa umeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutoa rai kwa jamii kwamba vyombo vya dola viko imara na tunashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi. Pia nitoe rai kwa wananchi kwamba badala ya kumalizana na masuala haya ya udhalilishaji wa kijinsia majumbani, twende kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Wabunge wa Viti Maalum uwakilishi wao uko kimkoa, lakini sasa Wabunge hawa wa Viti Maalum wamekuwa wakipata changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yao ya Kibunge hususan katika kufanya mikutano ya hadhara. Sasa ni nini kauli ya Serikali katika hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mikutano ya hadhara linahusisha idara nyingi, ikiwemo Idara ya Polisi ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kwamba kama kuna mawasiliano mazuri kati ya Wabunge wa Viti Maalum na mamlaka zinazohusika, wakiwemo Wabunge wa Majimbo, hakuna matatizo yoyote. Inawezekana ukaandaliwa mkutano, hasa Mbunge wa Jimbo anaweza akaandaa mkutano ambao vilevile utahutubiwa na Mbunge wa Viti Maalum kwenye eneo lake. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikidhibiti nyavu haramu kwa kuzichoma, lakini tunajua kwamba uchomaji wa nyavu hizi za plastic huleta madhara makubwa sana kwa afya za binadamu kwa sababu uchomaji wa plastic huachilia sumu kali sana aina ya dioxin ambayo inaweza ikaleta madhara makubwa sana kwenye ini, figo, moyo na magonjwa mengine kwa binaadamu. Kwa nini Serikali isitafute mikakati mingine mahsusi inayotunza mazingira katika kudhibiti hizi nyavu haramu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mwalimu wangu Mheshimiwa Dkt. Semesi Sware ambaye amenifundisha, pamoja na mengine Sheria za Uvuvi za Mwaka 2003, Na.22 pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Sheria ya Uvuvi inaeleza wazi kwamba ukikamata nyavu haramu ni kuteketeza. Sasa katika uteketezaji ndiyo yeye anasema tutafute njia nyingine siyo ile ya kuchoma moto kwa sababu ukichoma moto ule moshi unakwenda kuathiri wanaadamu. Mimi nadhani tutalichukua jambo lake hili na tutalifanyia mkakati mzuri wa kuhakikisha wakati tunachoma basi ule moshi usiende kuathiri watu wengine wanaozunguka jamii ile. Ahsante.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Spika, wakulima wa mwani sasa hivi wanapata shida kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa sababu ya ule mfumo wa ukulima unafanyika katika maji mafupi, mazao yale ya mwani mengi yamekuwa yakifa kwa sababu ya joto la maji na mchanga. Napenda kujua nini mkakati wa Serikali kuwawezesha wakulima hawa ambao wengi wao ni wanawake waweze kufanikiwa katika kilimo hiki ukiangalia sasa hivi wanapata tatizo la mabadiliko ya tabianchi uzalishaji wa mazao yao unashuka chini? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mwalimu wangu Mheshimiwa Dkt. Sware Semesi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kutokana na mabadiliko ya tabianchi kilimo cha mwani ambacho kilikuwa kikifanyika katika maji mafupi sasa kinawalazimisha wakulima wa mwani wasogee na waende katika maji marefu. Je, mkakati wetu ni nini kuwasaidia akina mama hawa ambao wana vifaa duni vya kuwapeleka katika haya maji marefu. Mojawapo ya mkakati ni kusisitiza na kupatikana kwa zile kamba, tunayo teknolojia ya kamba za kisasa za kufunga mwani ule ili uweze kuwa imara zaidi na upate ubora zaidi. Pili, ni kuwapa vyombo kwa maana ya boti ama mashine za kuwasaidia kuweza kufika walau kina kirefu kidogo. Kwa hivyo, huu ndiyo mkakati wetu na tayari Serikali tunazo mashine za kukopesha vikundi vya wavuvi, ikiwemo wakulima wa mwani. Kwa hivyo, Wabunge wote tunayo kazi ya kuvileta Wizarani vile vikundi vyetu ili tuweze kuwakopesha kile tulichonacho ili waweze kusogea katika hayo maji marefu zaidi. Ahsante.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa upatikanaji wa maji safi na salama huathiri afya, muda wa uzalishaji na hivyo huathiri uchumi wa kaya au jamii kwa ujumla. Sasa Serikali yetu tunajua dhahiri kuna changamoto ya maji nchini.
Je, mnajua kwamba bila kutatua changamoto ya maji nchini hatutakaa kufikia lengo la uchumi wa kati 2020/ 2025? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwa maana ya kwamba tunatambua sasa hivi nchi yetu inaenda katika nchi ya viwanda kwa maana ya uchumi wa kati na tunajua kabisa maji ni rasilimali muhimu sana na maji hayana mbadala sio kama chai ukikosa chai labda utakunywa uji. Tunajua viwanda vinahitaji maji, wananchi wanahitaji maji, kwa hiyo tutaongeza jitihada kubwa sana katika kukarabati, kujenga na kuunda miradi mikubwa katika kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji na tuwe na vyanzo vya kutosha ili mwisho wa siku azma iweze kutimilika. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, moja ya sababu inayosababisha mabadiliko ya tabianchi ni uharibifu wa mazingira kwa ukataji miti. Kwa kuwa hapa nchini ukataji miti uko kwa juu sana kwa sababu watu wengi tunategemea nishati ya kuni au mkaa kwa ajili ya mapishi nyumbani na shughuli nyinginezo. Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba huu uharibifu wa mazingira kwa kutumia nishati hizi ambazo zinapunguza idadi ya miti nchini inakuwa imepunguzwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, majibu ya Serikali inaonesha kwamba wale wachafuzi wa mazingira kupitia viwanda hutozwa faini au baadhi kufungiwa. Serikali haioni kwamba inafaa iwe na mikakati mahsusi ya kudhibiti viwanda hivi kuangalia miundombinu yake kabla haijaanza kazi kwamba haitakuwa inaharibu mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwa nishati mbadala na sisi tumekuwa tukisisitiza na tumeanza mkakati huo na tumeshirikisha na ndugu zetu wa TFS sasa wanatoa miti ambayo inahimili ukame na wanatenga maeneo maalum kwa ajili ya kuvunwa na maeneo maalum kwa ajili ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia swali la pili namna ya kudhibiti wamiliki wa viwanda, kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba tutaendelea kuzingatia sheria ileile. Niwaombe wamiliki wa viwanda wajue kabisa kwamba wanao wajibu wa kuyatunza mazingira na wanao wajibu wa ku-treat yale maji ambayo yanaleta zile taka hatarishi. Ahsante sana.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikipokea fedha mbalimbali kutoka kwa wafadhili ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kila mwaka. Miaka miwili iliyopita walikabidhiwa takribani shilingi bilioni 224 kwa ajili ya shughuli hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anaongelea kuhusu mikakati; je, kuna utekelezeji wowote wa mikakati hii ya kuhusisha mabadiliko ya tabianchi na kuboresha kilimo chetu kwa kutumia hizi fedha za wafadhili ambazo zinagusa hususan mabadiliko ya tabianchi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Sware ni mwanamazingira na ni kweli anafahamu kabisa kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais tumekuwa tukipata fedha ambazo zinasaidia miradi mbalimbali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Amesema sasa mbali na mikakati, fedha hizi namna gani tunazi-link.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie kwamba mojawapo ya miradi ambayo tumeihusianisha na hiki kilimo kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ukienda kule Rufiji tayari katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji tulikuwa tunatekeleza mradi ukiwa ni pamoja na kupanda mikoko na kuwawezesha wananchi wahimili mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo cha mboga pamoja na matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ukienda kule Pemba Kisiwa Panza mbali na kujenga ukuta, vilevile tulikuwa tunawasaidia wananchi waweze kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo cha mboga na matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo sasa hivi tuna Mikoa kama Tabora, Singida, Kagera, Morogoro, Tanga ambako tayari tunatekeleza miradi mbalimbali ya kutumia fedha hizi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wakulima wa namna wanavyoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatumia zile fedha katika kilimo cha mboga pamoja na matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni pamoja pia na Bonde la Kihansi kule Kilombero, vilevile tumeweza kutoa fedha ili wananchi wahimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo katika lile mbonde.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Sware kwamba siyo mikakati tu ambayo Serikali inaishia, ni pamoja na fedha hizi. Tumetoa fedha nyingine shilingi milioni 200 sasa ambazo zinapeleka maji kule Shinyanga na yale maji yatatumika pia katika kusaidia umwagiliaji kwenye kilimo. Hiyo ni katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Napenda kujua kwa nini Serikali haijikiti katika kuviimarisha Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi yaani BMU’s ili kuweza kuwa na uhakika wa uendelevu wa usimamizi wa rasilimali hizi na wenye kuleta tija? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, BMUs zipo kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na.22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake lakini pia inatambulika na Sheria ya Ugatuaji wa Madaraka kwa maana ya D by D. Sisi tunaendelea kuzitumia BMUs na katika maboresho yetu ya sheria ambayo tunayategemea kuingia katika mwaka huu tutahakikisha kwamba tunazipa nguvu zaidi na mwongozo zaidi ili BMUs ziweze kufanya kazi vile ambavyo inatakiwa kwa sababu BMUs ni mali ya wananchi wenyewe.
MHE. DKT. IMMACULATA S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Jimbo la Kondoa la Vijijini pia lina uhaba wa mkubwa wa mabwawa na yale yaliyopo yanahitaji ukarabati mkubwa hususan katika bwawa la Kisaki ambalo linahudumia mifugo na wanadamu.
Sasa Serikali ina mpango gani pia wa kuweka jicho la ziada katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya Maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imekuwa ikichimba mabwawa na hata visima virefu katika maeneo yenye ukame mkubwa sana. Labda nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kushirikiana na wafadhili wetu, tutaangalia namna ya kuweza kuondoa tatizo hilo na kuwachimbia mabwawa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni ianze kujitathmini kwa upya aina za adhabu zinazotolewa kwa wanafunzi wetu kwa sababu adhabu hizi mara nyingi huwa zinadhalilisha na zinaleta madhara ya kisaikolojia na katika mwili. Sasa ni bora Serikali itathmini kwa upya hizi adhabu hata kama ni kiboko kinatolewa sehemu gani, unakuta adhabu mtoto anaambiwa azomewe mbele ya darasa, achapwe mbele ya darasa tayari unamu-affect kisaikolojia na mwili wake. Kwa hiyo, tuangalie na tutathmini hizi adhabu ni katika kujenga na sio kumbomoa yule mwanafunzi. Kuna umuhimu wa kujitathmini hizi adhabu tunazowapa wanafunzi, ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niongelee hili suala. Kwanza niseme kwamba suala la utoaji wa viboko lengo lake si kuongeza ufaulu, adhabu inakuwa inarekebisha nidhamu au dosari ambayo imejitokeza. Kwa hiyo, tutofautishe haya mambo ya kurekebisha nidhamu na suala la ufaulu. Suala la adhabu linatolewa pale mtu anapoenda kinyume na taratibu.

Mimi ningependa kuchukua nafasi hii, kuwahimiza wanafunzi wote nchini kufanya utii wa sheria bila shuruti, kwa sababu watakapotii sheria hakutakuwa na sababu ya wao kupewa adhabu. Lakini pale ambapo inakuwa ni lazima mwanafunzi apewe adhabu kwa sababu hajatii sheria zilizowekwa, ni muhimu sana kwa walimu kuhakikisha kwamba wanazingatia taratibu ambazo zimewekwa na mwalimu yeyote ambae anakwenda kinyume na zile taratibu za kuadhibu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Mheshimiwa Upendo Peneza bado ana maswali mawili ya nyongeza kutokana na majibu ya Serikali. Swali la kwanza, nauliza kwamba, japokuwa Serikali imeondoa baadhi ya kodi katika uzalishaji wa taulo za kike lakini bado bei ya taulo hizo iko juu sana. Sasa Serikali ina mkakati gani wa kusimamia bei hii kushuka ili kufikia wale walengwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anauliza, sasa kama Serikali imeshindwa kusimamia kushuka kwa bei za hizi taulo japokuwa wameondoa baadhi ya kodi, je, haioni kwamba iendeleze tu kodi zile za awali lakini kodi hii ikusanywe na iwe ringfenced ili kuweza kununulia hizi taulo za kike na kuzigawa bure shuleni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Sware Semesi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nianze na swali lake la pili ambapo amesema kama Serikali imeshindwa kusimamia kushuka kwa bei; naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taifa letu kwa ujumla tupo katika soko huru kwa bidhaa zote, kwa hiyo sio kwamba Serikali imeshindwa kusimamia kushuka kwa bei, hapana, haijashindwa na ndiyo maana sasa hivi baada ya kuondoa kodi ile kwenye bidhaa hii Serikali imeendelea kupokea maoni mbalimbali ya wananchi wetu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuweka bidhaa hii kuwa ringfenced Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali, lakini kuna changamoto ya kusema kwamba kodi inayotozwa specific kwenye bidhaa hii iwekwe kwa ajili ya wanafunzi hawa kwa sababu yapo makundi mengine ambayo kodi zinatozwa kwenye bidhaa zinazotumika specifically na makundi kadhaa, kwa hiyo tutatengeneza ombwe la kila kundi kuja kuomba kodi inayotozwa kwenye makundi hayo waweze kupewa wao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kama nilivyosema inaendelea kufanya utafiti, tumekwenda nchini Afrika Kusini, Botswana na Kenya kujifunza nini wanafanya. Wenzetu waliondoa kodi hizi na wakagundua kwamba haiwezi kuleta matokeo chanya kama ambavyo yamekuwa ni majibu ya Serikali yetu ndani ya Bunge lako Tukufu. Kinachotakiwa kufanyika ni kubuni njia nyingine ya kuhakikisha watoto wetu wa kike wanapatiwa bidhaa hizi lakini bila kui-attach na kodi au tozo zozote zinazotozwa kwenye bidhaa hii kwa sababu tumejiridhisha kwamba unapoondoa kodi wanaonufaika ni wazalishaji kwa sababu tuko kwenye soko huria.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, kwamba ni mkakati gani kama Serikali tunaweka; nimesema sasa hivi tunaendelea kufanya tafiti mbalimbali ambapo tutakapojiridhisha na options ambazo zitaleta matokeo chanya kwa pande zote mbili watoto wetu wa kike na Serikali yetu, basi tutakuja na option hiyo ndani ya Bunge lako Tukufu ili tuweze kuwasaidia watoto wetu.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majibu niliyoletewa na Serikali ni dhahiri kuwa suala hili bado halijawekewa mkazo na bado wananchi wanapata shida wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola. Sasa Serikali haioni ni wakati sasa wa kujifanyia tathmini mahususi na kuja na mikakati thabiti ili wananchi wa Taifa hili wapate kuwa na kusimamia haki zao? Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tathmini ni muhimu na ni endelevu. Wizara yangu inaendelea kufanya hivyo na kusisitiza kwamba Tume ya Haki za Binadamu inafanya hiyo. Pia ninapenda kusisitiza kwamba suala la haki za binadamu lazima iwe ni sehemu ya utamaduni wa Taifa; na kuifanya ni sehemu ya utamaduni wa Taifa itabidi tutengeneze mkakati wa somo la Haki za Binadamu liingie katika mitaala ya shule zetu zote na katika ngazi zote. Somo la Haki za Binadamu na Utawala Bora liwe ni sehemu ya lazima kwa mafunzo yote ya vyombo vyetu vya usalama. Kama ni ulinzi, kama ni Polisi, Usalama wa Taifa au Uhamiaji, iwe ni sehemu muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Askari wetu wanaoshiriki katika vikosi vya kulinda amani duniani huwa wanapewa kozi ya haki za binadamu kwa wiki sita na Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa na Taasisi mbalimbali za Kimataifa ziko tayari kuisaidia Tanzania kuweka Chuo cha Haki za Binadamu ambacho kitatengeneza mitaala katika shule mbalimbali. Hiyo nimehakikishiwa na ninadhani inaweza kutokea tukishachukua maamuzi. Watu wako tayari kutusaidia ili haki za binadamu na utawala bora iwe ni sehemu ya utamaduni wa Taifa hili.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kumekuwa na ongezeko kubwa sana hususan katika haya magonjwa yasiyoambukizwa kama saratani. Kuna shida kubwa sana ya kutambua magonjwa haya mpaka zinakuwa dalili au zile hatua za mwisho sana. Sasa Serikali haioni imefika wakati wa kuja na mkakati mahususi kwa kutoa elimu kujua hizo symptoms na kuboresha huduma katika vituo vyetu vya afya ili kuweza kutoa diagnosis inayotakiwa mapema? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Sware kama lifuatavyo; na ameuliza swali moja zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyektii, ni kweli kansa nyingi ambazo tunaziona katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya zinakuja katika hatua za mwisho sana, na hili yote ni suala tu la elimu na hususan saratani ya shingo ya uzazi ambayo inawaathiri wanawake wengi sana. Wengi wanakuja katika hatua ya tatu na ya nne ambazo ni hatua za mwisho sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama Serikali tumeendelea kutoa elimu katika masuala haya magonjwa ya saratani, na tumeendelea vilevile kuhakikisha kwamba huduma za msingi za utambuzi tunazitoa na tunazitoa bure. Katika vituo vyetu vya afya utambuzi wa sarakani ya shingo ya uzazi tunazitoa hizi huduma bure, na mashine za Clio therapy tumeziwekeza sana kwa ajili ya matibabu ya awali ya saratani za shingo za kizazi, zipo.

Mheshimiwa mwenyekiti, na tumekwenda mbali, sasa hivi tunatoa chanjo ya kukinga saratani dhidi ya shingo ya kizazi. Kusudio letu ni kwamba takriban watoto mabinti 650,000 walio kati ya miaka tisa mpaka 14 tuweze kuwafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tumeendelea kuboresha huduma zetu za matibabu ya saratani. Pale ocean road tumefunga linear accelerator ambayo inaifanya Hospitali yetu ya Ocean Road kuwa hospitali ya kisasa kabisa katika matibabu ya mgonjwa wa kionzi. Vilevile tutafunga mashine ya PET scan ambayo itaifanya sasa Taasisi yetu iwe ni taasisi ya kisasa sana katika matibabu ya kansa ndani ya dunia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaendelea kuboresha huduma hizi za matibabu ya saratani kule Bugando, wanatoa dawa lakini vile vile watatoa huduma za mionzi. Pia tunaendelea kuboresha kule KCMC ili waweze kutoa huduma za dawa na vile vile matibabu ya mionzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mikakati ya Serikali ipo na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kufika katika vituo vya afya na kufanya uchunguzi na utambuzi wa ugonjwa wa kansa mapema iwezekanavyo.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala la mmomonyoko wa udongo ni kubwa na lipo dhahiri kabisa, ukiona mkusanyiko wa udongo na mchanga katika mapito ya njia za maji za mito. Kumekuwa pia na uchimbaji holela wa michanga hii, inazidi kuvunwa au pia vina vya maji vinakuwa vifupi na nyakati za mvua basi husababisha mafuriko. Wizara husika ina mkakati gani kuleta suluhisho katika suala hili ambalo ni muhimu sana na lina effect kubwa sana katika mazingira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Sware.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane naye kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mmomonyoko wa ardhi hasa kwenye maeneo ambayo kuna mapito ya maji. Eneo hili kwa kweli nikiri kabisa tumeendelea kulifanyia kazi na limekuwa na changamoto kubwa. Mkakati uliopo ni kuhakikisha maeneo yote haya kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri wanatupa taarifa zilizo rasmi ili kutengeneza miradi ya kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa tukitoa maelekezo kwenye Halmashauri husika ili kukabiliana na maeneo ambayo yanahitaji kupata ufumbuzi wa muda mfupi lakini yale ya muda mrefu Wizarani tunapata taarifa na tunachukua hatua stahiki.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi. Kwa kuwa ukatili wa kijinsia huathiri watu mbalimbali kisaikolojia na huathiri; afya ya akili na kwa kuwa ukishaathirika kisaikolojia afya ya akili inaleta kutokuzalisha vizuri kama ni shughuli za kutuletea uchumi au watoto ku-perform darasani kwa hiyo unakuwa na taifa ambalo halipo sawasawa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wale wanaoathirika kisaikolojia au afya ya akili wanakosa kupata huduma stahiki kwa sababu kuna changamoto ya gharama tiba na pia watalamu ambao wanafanya hizi shughuli za counseling wapo wachache nchini; sasa Serikali haioni ni muda muafaka wa kufanya tathmini wa hali hii na jinsi ya kuweza kuwapatia huduma wananchi wake stahiki inavyotakiwa kwa gharama ambayo wanaweza wakaimudu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sware Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli hathari moja wapo ya ukatili wa kijinsia ni kuweka makovu ya kisaikolojia kwa watu wengi na napelekea baadhi ya watu hata kushindwa kufanya vizuri katika masomo, kushindwa kujenga mahusiano na watu wengine, kuwa na tabia ya kuwa na hasira na vitu vingi ambavyo vinamwathiri mtu kisaikolojia. Ni kweli hili tatizo linazidi kukuwa na sisi kama Serikali kupitia mpango wetu wa MTAKUWA tumeainisha baadhi ya mikakati ambayo tunaiweka katika kudhibiti hali hiyo. Tunatambua kwamba ni kweli tuna changamoto hii ya wigo wa ushauri nasaha kwa hawa wahanga na gharama za matibabu kwa hawa wahanga wa ukatili wa kijinsia. Tutafanya hiyo tathmini na kuangalia jinsi gani sasa ya kuweza kutoa huduma nzuri kwa hawa wahanga wa ukatili wa kijinsia.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, ukatili wa Wanyama uko katika jamii zetu, hususani pale kwenye masuala ya migogoro unapokuta hifadhi na wanaovamia hifadhi, basi Wanyama wale unakuta wanapigwa risasi ama wanakatwa mapanga, na pia tunauona ukatili huu katika usafirishaji unapokuta idadi kubwa ya Wanyama hawa wakisafirishwa kwa masafa marefu na wakiwa wamebanwa sana katika yale magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitendo hata cha kuwapandisha kwenye yale magari na kuwashusha ng’ombe wale au Wanyama wale wanakuwa wanapigwa, sasa Serikali inajipangaje katika kusimamia hili kimatendo kwamba dhuluma hizi na ukatili huu kwa Wanyama unakuwa umeisha, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni juu ya ukatili unaofanywa wakati mifugo inapokuwa imekamatwa, katika hifadhi na maeneo mengine, Wizara imeliona jambo hili na nataka nilihakikishie Bunge kuwa Sheria ipo ya haki za Wanyama. Mfugo unapokamatwa, unazo haki zake lazima wapate maji, lazima wapate malisho na watazamwe na hata ikiwezekana wapate na chanjo pia vilevile.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukiwasisitiza wale wote wanaokamata mifugo waweze kutekeleza matakwa haya ya Sheria lakini kwa kukazia, tumeona kwa safari hii tunakwenda kuiboresha zaidi Sheria yetu ya Mifugo ya haki za Wanyama, ili hawa wanaokamata kiholela holela ni lazima wahakikishe kuwa siyo kila mtu anaweza akakamata tu anavyojisikia kukamata.

Mheshimiwa Spika, ni lazima watu wetu wanaohusika na tasnia ya haki za Wanyama, kwa maana ya Maafisa Mifugo kote nchini, waweze kushirikishwa, ili haki za Wanyama wale ziweze kutekelezwa ipasavyo, na jambo la pili ni hili linalohusu mrundikano katika magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba jambo hili linafanywa sana, na wafanyabiashara wetu, lakini labda nikueleze jambo moja na nilieleze Bunge lako Tukufu wafanyabiashara wale huwa tunawasimamisha katika magari, na wakati mwingine tunawauliza kwa nini mnawarundika ng’ombe namna hii, sasa majibu yao ya haraka ambayo watakujibu ni kwamba ng’ombe ukiwaacha bila ya kusimama wakawa wameshikana hivi, mmoja akikaa chini, mathalani, ng’ombe huyo hawezi kufika salama anapokwenda ni lazima atakufa, kwa sababu ya kukanyagwa na wenzake.

Mheshimiwa Spika, sasa haya yote tumeyaona na ndiyo maana tukasema kwamba ni muhimu tuweze kuirekebisha ile Sheria. Na ndiyo maana unaweza ukaona wakati mmoja tulipoona kuwa ng’ombe hawa wanajazwa sana Sheria yetu ya barabara ilileta kidogo sintofahamu miongoni mwa wafanyabiashara wa ng’ombe kwa sababu walitakiwa wahakikishe wale ng’ombe wanapokuwa kwenye magari wasitingishike.

Mheshimiwa Spika, na maana yake wanapotingishika, katika Sheria inaleta tabu kwa upande wa ulinzi wa miundombinu yetu, na hili wamefanya kwa sababu wasitingishike kwa kuona kuwa wanawekwa wengi, sasa unaweza ukaona kwamba tunao wajibu kweli kabisa wa kuangalia Sheria zetu na kuziboresha na naomba niliahidi Bunge lako kwamba hili tunalifanyia kazi na tunatoa wito kwa wale wote wanaosafirisha mifugo wazingatie haki za Mifugo, na siyo kuwapeleka katika uholela.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, juu ya hili suala la ukamataji holela wa Mifugo na jinsi kama Mheshimiwa Mbunge alivyoliuliza.

Mheshimiwa Spika, nataka kuongezea tu kwamba kwa hivi karibuni baadhi ya Watendaji wa Serikali wamekuwa wakiwaona hata Mifugo na wenyewe ni wahalifu, hawa ni viumbe hai wana mahitaji yao ya msingi ya maji, wana mahitaji yao ya msingi ya malisho, wana mahitaji yao ya msingi ya chanjo na tiba.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, hata wanapokamatwa si wahalifu katika namna yoyote katika makosa yoyote ambayo yanamuhusu mmliki wa mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya kuona hivyo kwamba ukamataji sasa kila Afisa wa Serikali anakamata Mifugo tukaamua kama alivyosema Naibu Waziri kuboresha Kanuni za Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya mwaka 2008 na Sheria ya magonjwa ya Mifugo Na. 17 ya mwaka 2003, ambapo marekebisho ya Kanuni ya hizi, yatakuwa tayari ifikapo tarehe 01 mwezi wa saba, ili kuweza kushughulika na hawa Watendaji wa Serikali ambao wamegeuza wameleta manyanyaso makubwa sana kwa Mifugo na Mifugo mingi imekuwa ikifa, ikiwa imeshikiliwa kwa sababu zisizojulikana. Lakini vilevile, kuwaeleza Watanzania wajue kwamba katika raslimali za Taifa, Mifugo ni raslimali ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa vyovyote vile unapofanya, vyovyote vile unavyofanya unaharibu kama Mifugo ikifa ikiwa imeshikiliwa maana yake kwamba raslimali ya Taifa imekufa ikiwa imeshikiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala hili tunalifanya kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba ifikapo tarehe 1 mwezi wa saba, hawa tutashukughulika nao, Watendaji ambao wamekuwa wakitoa kisingizio cha kwamba, natekeleza Sheria anasahau kwamba hata mifugo hawa nao wana Sheria zao zinazowalinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatutakubali tena kama Serikali ifikapo tarehe moja mwezi wa saba badala ya huyu Afisa ambaye anasema kwamba anatumia mgongo wa Sheria tutawashughulikia wao kama individual na wala siyo Serikali tena. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Mheshimiwa Ruth Mollel, bado ana maswali amwili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ni moja na Serikali Kuu alikasimu baadhi ya madaraka yake katika Serikali za Mitaa, basi Serikali Kuu haina budi kusimamia na kuratibu shughuli mbalimbali za Serikali za Mitaa. Serikali haioni ni vyema sasa kusimamia na kutoa maelekezo mahususi katika Serikali za Mitaa katika kujikita kupanga ili tujue kwamba matumizi ya ardhi ni nani anatumia nini kwa ajili ya shughuli za kiuchumi?

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kuwa Serikali Kuu imechukua vyanzo vikuu vya mapato katika Serikali za Mitaa, Serikali Kuu haioni sasa ni muhimu ku-ring fence fedha fulani kwa ajili ya shughuli mahususi za kuratibu shughuli za upangaji wa matumizi ya ardhi? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli Wizara ya Ardhi ina wajibu ya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ardhi Na. 5 na utekelezaji wa Sheria ya Mipango Miji zote zinahusiana na mambo ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunafanya hivyo, tunatoa mwongozo wa kusimamia na kupitia wataalam wetu waliopo kila Halmashauri wanashiriki, kwa sababu kazi hii inasimamiwa na wataalam wa Sekta ya Ardhi ambao wako katika kila wilaya. Ndiyo maana imewezesha leo hii Wilaya hiyo ya Mkuranga anayoiulizia swali, Mheshimiwa Ulega, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, ni shahidi, vijiji 21 tayari vimeshafanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mafunzo ambayo Wizara tumeyatoa na uwezeshaji tulioufanya katika Wilaya ya Mkuranga, wale viongozi, Madiwani pamoja na watendahi wa Sekta ya Ardhi wa Mkuranga wameweza kujiongeza wenyewe kutekeleza wajibu wao na kwenda kufanya sasa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 21. Kwa hiyo, kazi hiyo ndiyo tunayofanya.

Mheshimiwa Spika, la pili ni fedha. Sisi kama Wizara, hata kwenye bajeti yangu kesho mtaona, tumekuwa tunapanga fedha kusaidia kazi hii tunayofanya. Leo kwa mfano tunapanga matumizi bora ya ardhi na kupanga na kupima kila kipande cha ardhi. Tumeanza Mkoa wa Morogoro katika wilaya tatu. Namwalika mwuliza swali siku moja katika Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ifakara ili aje uone kazi inayofanywa.

Mheshimiwa Spika, tumeanza mpango mwingine ambao tunakamilisha sasa wa kutaka kupanga na kupima kila kipande cha ardhi nchi nzima. Sasa huo ndiyo mpango wa Serikali Kuu kwa uwezo wa Serikali Kuu. Kwa hiyo, yote mawili tunafanya; hatuwezi kuwaacha wenye jukumu lao wasifanye, lakini Serikali Kuu nayo imekuwa ikishiriki katika kufanya kazi hii tukijua kwamba tuna wajibu wa kufanya hivyo.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa vifo vingi vya wamama wakati wa kujifungua hutokana na kukosa huduma na ufuatiliaji katika hatua mbalimbali za ujauzito, sasa basi Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kurasimisha hao Community Health Workers au watoa huduma katika jamii kwa mambo ya afya ili waweze kupewa mori, kuelimishwa na ili kuwawezesha wanajamii hususan akina mama wajawazito ili kupunguza vifo vya wamama wajawazito? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MADINI (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Semesi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Community Health Workers wanapewa elimu pana. Tumeanza kwenye masuala ya UKIMWI, lakini vilevile kwenye masuala ya afya ya uzazi na afya ya lishe kwa watoto. Hii elimu inatolewa kwa hawa Community Health Workers ili waweze kutoa elimu kwa wananchi, watoe elimu kwa wanavijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ni kwamba sasa hivi mkakati mkubwa ambao tunafanya katika Wizara hii ya Afya ni kuhakikisha kwamba hata wale ambao ni Waganga wa Jadi na wenyewe wanapewa elimu waelezwe vihatarishi, wapewe elimu kuweza kutambua hali ya hatari ambayo inaweza kusababisha mtu kupata kifo kutokana na uzembe fulani, kwa mfano, kupungukiwa na damu, masuala hayo ya ujauzito, wanapewa ile elimu ambayo ni kujua kabisa hali hatarishi kwamba katika hali kama hii mgonjwa huyu anatakiwa apewe huduma fulani, lakini hali fulani ikizidi, basi mgonjwa huyu apelekwe hospitali aweze kupata huduma zaidi. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi, Mheshimiwa Bulaya ana swali la nyongeza, Mheshimiwa Bulaya anasema kwamba mkandarasi anayehusika na mradi huu kwa miaka kumi na moja sasa hajatimiza/hajakamilisha Mradi huu na 2017 Mheshimiwa Waziri Mkuu na 2018 Mheshimiwa Rais walitoa tamko juu ya mkandarasi huyu apate kuwekewa nguvu ili aweze kumaliza mradi huu.

Sasa nini hatma ya Mkandarasi huyu ambaye bado yuko site ili mradi huo uweze kukamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nirudi sasa Mkoa wa Dodoma hata Mkoa wa Dodoma kuna maeneo mengi tuna shida ya maji, hususani katika Jimbo la Kibakwe, watu wa Jimbo la Kibakwe wana shida sana na maji safi na salama. Sasa ni lini Serikali itawaangalia wananchi hao ili kuweza kuimarisha afya zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri, lakini kikubwa tukiri kwamba huu mradi ulitekelezwa umechukua muda mrefu na hii yote inatokana kwa baadhi ya miradi kupewa wakandarasi wababaishaji, lakini sisi kama viongozi wa Wizara tumefatilia mradi ule na tumeongeza nguvu yetu kubwa sana katika kuhakikisha mradi ule unakamilika.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa umeshafikia asilimia 92 na tunaendelea kuongeza nguvu katika kuhakikisha mradi ule unakamilika ili wananchi wa Bunda waweze kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu eneo hili la Dodoma la Kibakwe, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji na Umwagiliaji tumeliona hilo, nataka tumuagize Mhandisi wa Maji aone namna sasa ya kufanya mradi haraka ili kuhakikisha wananchi wa Kibakwe wanaweza kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa katika kuhakikisha Mji huu wa Dodoma unaondokana na tatizo la maji, tuna ujenzi huu wa Bwawa la Farkwa, na tupo katika hatua ya utafutaji wa fedha tunaamini upatikanaji utakapokuwa umepatikana Mradi ule utatatua kabisa tatizo la maji katika Mji huu wa Dodoma, ahsante sana.