Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi (8 total)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
(a) Je, Serikali inasafirisha nje ya nchi mbao na magogo kiasi gani kwa mwaka?
(b) Je, ni nchi gani inaongoza kwa kununua mbao na magogo kutoka Tanzania?
(c) Je, ni fedha za kigeni kiasi gani zimepatikana kutokana na mauzo ya magogo na mbao nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka 2010 - 2015?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 50 ya Kanuni za Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, inakataza usafirishaji wa magogo kwenda nje ya nchi. Aidha, Kanuni hiyo hairuhusu uuzaji nchi za nje wa mbao zenye unene unaozidi inchi sita. Kanuni hii na sheria vinaweka zuio ili kutoa fursa ya kukuza viwanda vya ndani ya nchi na ajira kwa Watanzania katika kupasua mbao na utengenezaji wa samani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya mita za ujazo 333,404.91 za mbao chini ya inchi sita ziliuzwa na kusafirishwa kwenda nchi za nje.
Aidha, kwa mujibu wa takwimu nchi ya India inaongoza kwa kununua mbao kutoka Tanzania ambapo katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya meta za ujazo 210,968.07 zilisafirishwa kwenda India, ikifuatiwa na nchi ya China ambayo ilinunua mita za ujazo 68,337.04.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya fedha zilizopatikana ni shilingi 269,985,300,000 kutokana na mauzo ya mbao nchi za nje. Aidha, hakuna kiasi cha fedha kilichopatikana kutokana na mauzo ya magogo kwa kuwa biashara ya magogo kwa mujibu wa sheria haikufanyika.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI) aliuliza:-
Sekta ya maliasili na utalii ni rasilimali inayobeba uchumi wa Tanzania, ikitumika vizuri kwa uendelevu, italeta maendeleo katika jamii na uchumi wa nchi kwa ujumla:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanza kuipa kipaumbele sekta ya utalii?
(b) Je, ni lini Serikali itaboresha mazingira ya kazi ya askari wanyamapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sekta ya maliasili na utalii inatoa mchango mkubwa na kubeba uchumi wa Tanzania. Kwa mfano, sekta hii imechangia takribani asilimia 25 ya fedha zote za kigeni nchini katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo yaani 2012/2013 – 2014/2015 na hivyo kuchangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Utalii imechangia pia katika ajira nchini ambapo takribani ajira 500,000 za moja kwa moja ambayo ni takribani asilimia 11 ya ajira zote na ajira takribani 1,000,000 zisizo za moja kwa moja zimetolewa. Aidha, sekta hii imeendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, elimu, mawasiliano, burudani usafirishaji na uzalishaji wa huduma mbalimbali kwa watalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mipango ya uendelezaji wa sekta ya utalii kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021 na mipango ya kila mwaka wa fedha. Kwa ujumla mipango ya uendelezaji wa sekta inajumuisha utunzaji na uboreshaji wa vivutio vya utalii vilivyopo, uainishaji na uboreshaji wa vituo vipya vya utalii, uboreshaji wa miundombinu ya utalii, uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa watalii na kwa umuhimu wa pekee kuongeza mbinu na jitihada za kutangaza utalii wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa upande mwingine Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutekeleza programu na miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya utalii. Kwa mfano, kwa kipindi cha mwaka 2017 – 2022, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia itatekeleza mradi wa kuboresha utalii Ukanda wa Kusini mwa Tanzania kwa gharama ya takribani Dola za Kimarekani zisizopungua milioni mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa na ngumu inayofanywa na Askari Wanyamapori wanapotekeleza majukumu yao ya kutoa ulinzi na kusimamia uhifadhi kwa ujumla wa wanyamapori hususani kupambana na ujangili. Aidha, kuanzia mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali imejipanga kuboresha mazingira ya kazi ya Askari Wanyamapori sambamba na watumishi wengine ambapo kwa upande wa Askari Wanyamapori, upatikanaji wa vitendea kazi, uboreshaji wa stahili zao na usimamizi bora zaidi wa utendaji kazi ni miongoni mwa malengo ya Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA). Mamlaka hii imeanzishwa tarehe 16 Oktoba, 2015 ili ifanye kazi sambamba na Mamlaka ya Ngorongoro na TANAPA katika kutekeleza lengo kuu la udhibiti wa ujangili nchini.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
(a) Je, ni wanafunzi wangapi walifuzu kwa kiwango cha Diploma na Digrii katika Sekta za Sanaa na Ubunifu, Habari, Teknolojia na Sayansi, Elimu ya Afya kwa Mwaka 2010-2015?
(b) Je, Serikali imefanya tathmini katika maeneo ya utumishi yenye uhaba wa taaluma tajwa hapo juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi waliofuzu kwa kiwango cha stashahada kwa kipindi cha kati ya mwaka 2010 hadi 2015 katika sekta za Sanaa na Ubunifu (Fine and Perfoming Arts) ni 254, Habari yaani waandishi ni 1,565, Teknolojia ya Sayansi ni 12,538 na Elimu ya Afya ni 14,177, jumla walikuwa 28,534. Aidha, kwa upande wa wanafunzi waliofuzu kwa kiwango cha shahada kwa kipindi tajwa, takwimu zinaonesha kuwa katika sekta za Sanaa na Ubunifu ni 136, Habari 2020, Teknolojia na Sayansi ni 11,953 na Elimu ya Afya ni 5,043 ambapo jumla yao walikuwa ni 17,334
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba inaeleweka kuna upungufu wa wataalam katika baadhi ya fani, kama vile Uandishi wa Habari, Afya, Ualimu wa masomo ya Sayansi, Uandishi wa Teknolojia na Gesi, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tayari imeandaa Andiko(Concept Note) kwa lengo la kufanya tathmini ya kina katika sekta mbalimbali, zikiwemo zilizotajwa kwenye kipengele (a) cha swali la msingi ili kuainisha mahitaji na upungufu wa Rasilimali watu, kiidadi na kiujuzi katika Utumishi wa Umma na hatimaye kuweza kuandaa mkakati wa namna ya kushughulikia upungufu utakaoonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati utakaoandaliwa ambao unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2016/2017 utaiwezesha Serikali kuwa na matumizi mazuri ya Rasilimali iliyopo ili kufikia Malengo na Mipango ya Taifa ya Maendeleo.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
Sekta ya Uvuvi ni muhimu kwa uchumi wa nchi, sekta hii ikiwezeshwa ina uwezo angalau kufikisha shilingi bilioni 12 kama kipato kwa mwaka:-
Je, ni lini na kwa vipi Serikali itaipa kipaumbele Sekta ya Uvuvi nchini ili kuboresha utendaji na kuongezea nchi kipato?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha Sekta ya Uvuvi ili iweze kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa kupitia mikakati na mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira bora ya uwekezaji. Aidha, kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Uvuvi, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuboresha miundombinu ya uvuvi, ikiwemo bandari ya uvuvi na kuimarisha ubora na usalama wa samaki na mazao ya uvuvi yanayosafirishwa nje ya nchi. Katika mwaka wa fedha 2015/ 2016, Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Uvuvi ilikusanya maduhuli kiasi cha shilingi bilioni 19 ambayo ni zaidi ya asilimia 100 ya lengo la bilioni 18 ilizokuwa imepangiwa kukusanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeandaa kanuni za kusimamia uvuvi katika Bahari Kuu ya Tanzania ambapo zimetoa fursa kwa meli kubwa za uvuvi zinazovua bahari kuu kushusha samaki katika Bandari ya Dar es Salaam (Gati Na. 6) na Zanzibar (Gati Na. 3). Aidha, samaki wanaovuliwa bila kukusudiwa (by-catch) watashushwa katika bandari hizo ambapo itatochea uzalishaji wa samaki nchini, ukusanyaji wa maduhuli, upatikanaji wa ajira na kuongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeanza mapitio ya Mpango Kabambe wa Uvuvi (Fisheries Master Plan) wa mwaka 2015 kwa lengo la kutoa mwongozo wa utekelezaji wa mpango ili kuchangia katika kuongeza usalama wa chakula, lishe, ajira, kuchangia uchumi wa nchi pamoja na kuongeza pato la Taifa. Aidha, Sekta ya Uvuvi imepewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Kilimo awamu ya pili (ASDP II) ambayo utekelezaji wake unaanza mwaka 2017/2018 hadi 2022/2023.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI Aliuliza:-
Suala la mabadiliko ya tabianchi ni mtambuka na linagusa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Je, ni mashirika ya umma mangapi yamepokea ruzuku kutoka Wizara/Idara au kwa wafadhili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita? Je, nini madhumuni ya ruzuku hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mashirika ya umma yanayopata ruzuku kutoka kwenye Wizara, Idara au wafadhili.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye kipengele (a), haiwezekani kuelezea madhumuni ya ruzuku ambayo haitolewi.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
Kwa kuwa Serikali kupitia Idara ya Misitu ina jukumu la kutathmini rasilimali zake ikiwemo miti:-
• Je, Wizara inatekeleza kwa kiwango gani katika kufanya tathmini za idara zake kuangalia athari za magonjwa ya miti?
• Je, nchi inazo ekari ngapi za mioto ya asili na iliyopandwa?
• Je, hadi sasa ni ekari ngapi za miti zimekatwa kwa ajili ya mbao na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Namba 14 ya Mwaka 2002, shughuli zote za utafiti za kitaalam kuhusiana na magonjwa ya miti na athari zake hutekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Taasisi hii hufanya utafiti wa utambuzi wa aina ya magonjwa, ukubwa wa matatizo na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua kutegemeana na uzito wa matokeo ya utafiti husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya Tathmini ya Rasilimali Misitu (NAFORMA) iliyotolewa mwaka 2015 inaonesha kuwa nchi yetu ina misitu yenye hekta milioni 48.1 ambapo misitu ya asili ni hekta 47.528, sawa na asilimia 98.8 na misitu ya kupandwa ni hekta 572,000, sawa na asilimia tu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa sana bila kujali aina ya uharibifu wa misitu ambapo kiasi cha ekari 372,000 za misitu huangamizwa kila mwaka nchini. Aidha, takwimu zinaonesha kwamba ili kurejesha hali ya misitu nchini katika viwango vyake vya kawaida, kiasi cha jumla ya ekari 185,000, sawa na jumla ya miti milioni 230 kinahitajika kupandwa kila mwaka kwa kipindi cha miaka 17.
MHE. DKT IMMACULATA S SEMESI aliuliza:-
Kwa ujumla Serikali haiwatumii ipasavyo wanazuoni kama watafiti, hasa katika eneo la tafiti ya sayansi kwa kukuza sekta ya viwanda:-
Je, ni kwa nini vyuo vikuu vya Serikali havipati fungu kwa ajili ya tafiti ili kutoa suluhisho mbalimbali na miongozo ya kimaendeleo yenye misingi ya tafiti kisayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hutenga fedha kwa ajili ya tafiti kupitia Mfuko wa Taifa ya Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) unaoratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Mfuko huu upo ili kuhakikisha maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanapatikana ambayo ni pamoja na tafiti kufanyika kulingana na vipaumble vya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha kwa ajili ya tafiti kutoka kwenye Mfuko huu hutumiwa kwa utafiti wa ndani ya nchi wakiwemo wanazuoni kwa njia ya ushindani. Aidha pamoja na Wanazuoni kupata fedha za kufanya tafiti kupitia Mfuko wa MTUSATE, washirika wa maendeleo kama vile Serikali za Sweden na Norway hufadhili shule za utafiti kwa kupeleka fedha za utafiti moja kwa moja katika vyuo vikuu mbalimbali kama vile Chuo Kiuu cha Dar es Salam, Chuo cha Ardhi na Chuo cha Tiba ya Afya Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa MTUSATE imefadhili miradi 102 ambayo ilitekelezwa na Taasisi mbalimbali za utafiti za vyuo vikuu vya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Kati ya miradi hiyo vyuo vikuu vilitekeleza jumla ya miradi 48 iliyofadhiliwa kwa njia ya ushindani ambayo imegharimu jumla ya shilingi bilioni 4.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya vyuo vikuu hivyo ni pamoja na Chuo Kiuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kiuu cha Dar es Salam (UDSM), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba, Taasisi ya Syansi na Teknolojia ya Nenson Mandela, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salam na chuo Kikuu Dodoma (UDOM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya tafiti zilizofanywa na Wanazuoni zimeonekana kuwa ni tafiti zenye tija katika maendeleo ya uchumi wa viwanda. Baadhi ya matokeo ya tafiti hizo ni pamoja na utengenezaji wa chanjo mseto ya kuku inayostahimili joto ya kukinga magonjwa matatu (mdondo, ndui na mafua) iliyofanywa na SUA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kugunduliwa kwa mbinu bora za kuzalisha vifaranga vya kaa iliyofanya na SUZA, kugunduliwa kwa vifaa kusafishia maji kwa matumizi kwa matumizi majumbani iliyofanya na Taasisi ya Nenson Mandela; usindikaji wa ngozi na mazao ya mifugo ambayo imewezesha kuanzisha kwa mitaala ya astashahada na shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Sokoine iliyofanywa na SUA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna udhibiti wa magonjwa yanayiharibu mazao ili kuleta uhakika wa chakula na kuondoa umaskini iliyofanyiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salam; pamoja na udhibiti wa uharibu wa mazao unaofanywa na panya kwa kutumia mkojo wa paka iliyofanyika na SUA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa wanazuoni wanafanya tafiti zenye tija Serikali imesaidia uazishwaji wa vituo mahiri (African Center over Excellence) vinne kupitia Benki ya Afrika ambapo takribani shilingi bilioni hamsini zimewekezwa kuendeleza utafiti katika Chuo Kiku cha Kilimo cha Sokoine na Taasisi ya Teknolojia ya Nelsoni Mandela.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-

Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”; lakini kumekuwa na kiwango cha juu cha matukio na kesi zinazohusu kuvunjwa kwa haki za kiraia kwa kufanywa na vyombo vya dola:-

(a) Je, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015 ni kesi ngapi zimefunguliwa Mahakamani kuhusu madhara yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia, na huchukua muda gani hadi kutolewa hukumu?

(b) Je, kesi hizo zimekuwa zikigharamiwa kwa kiasi gani kutoka Mfuko wa Fedha za Umma tangu mwaka 2010 – 2015?

(c) Je, Serikali inafanya jitihada gani kuhakikisha wananchi wake pamoja na vyombo vya usalama wanapata elimu ya uraia?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora haijafungua kesi yoyote Mahakamani kuhusu madhara yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia. Tume imekuwa ikipokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu dhidi ya vyombo vya dola na kuyashughulikia kwa kufanya uchunguzi wa kawaida, usikilizwaji hadharani na kufanya usuluhishi na upatanishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbinu hizi zimeonekana kuwa na mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi haki yao wanayostahili, hivyo kutokuwa na umuhimu wa kufungua mashauri Mahakamani. Ikumbukwe kuwa ufunguaji wa mashauri Mahakamani ni hatua ya mwisho iwapo njia nyingine zote zimeshindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza, kwa kuwa Tume haijawahi kufungua kesi yoyote ya haki za binadamu katika Mahakama zetu kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015, hivyo basi, hakuna gharama zozote za ufunguaji wa mashauri Mahakamani zinazohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imefanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wananchi pamoja na vyombo vya usalama wanapata elimu ya uraia. Jitihada hizo ni pamoja na kuelimisha Umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, mikutano, maadhimisho, machapisho na warsha mbalimbali katika kipindi cha 2010 hadi 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vipeperushi na vijitabu 40,638, makala 18,300 za Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu, majarida yaliyowekwa kwenye tovuti ya Tume ni matano, vipindi vya redio na televisheni ni 115 na kufanya mikutano na wananchi kuhusu haki za binadamu na hasa katika kumiliki ardhi kwenye mikoa 21 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi sasa, jitihada hizi zimeendelea kufanywa na Wizara yangu Waheshimiwa Wabunge na Bunge hili kwa ujumla kwamba haki zitakuwa zinatendeka na kwamba tunaendelea kubuni mbinu na mikakati mbalimbali itakayowezesha kuendelea kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo.