Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph Michael Mkundi (33 total)

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe masikitiko yangu kwamba Serikali haina takwimu sahihi ili kuweka kumbukumbu vizuri, Ukerewe tuna zahanati 29 na vituo vya afya vitatu. Kwa kuwa, suala la kupatikana kwa wataalam kwenye kituo cha afya cha Bwisya limekuwa ni la muda mrefu, niiombe sasa Wizara au Serikali kwa ujumla itoe commitment kwa sababu akinamama wengi sana wanapoteza maisha kwenye eneo lile, lini hasa ufumbuzi wa tatizo hilo utapatikana na kituo hiki kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Ukerewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri miaka miwili iliyopita ilijitahidi kujenga kituo cha afya cha Nakatunguru ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, lakini kituo hiki bado hakijaanza. Je, Serikali sasa iko tayari kutoa vifaa na wataalam ili kituo hiki kiweze kuanza kutoa huduma na kwa maana hiyo kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni wazi tunaelewa jiografia ya Ukerewe kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema katika jibu langu la awali ni kweli, jiografia ya Ukerewe ina changamoto kubwa sana na Ukerewe tunaifananisha na Rufiji ambapo kuna deltas mbalimbali kiasi kwamba huduma za kijamii zinakuwa ni ngumu. Mheshimiwa Mbunge najua kwamba, siyo huduma ya afya peke yake, hata huduma ya elimu ina changamoto kubwa katika visiwa vile. Kwa hiyo, Serikali ina kila sababu ya kuangalia ni jinsi gani tunaweka kipaumbele katika visiwa vya Ukerewe ili hali ya kiafya iendelee vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la upatikanaji wa wataalam, naomba nikwambie kwamba sasa hivi tuko katika mchakato na siyo muda mrefu sana tutaajiri wataalam. Niwashukuru sana watu wa Ukerewe. Katika ile hospitali ya Nansio kuna vijana watano pale ambao ni Madaktari graduates wanajitolea na baada ya mawasiliano wameonesha wazi kwamba wale vijana wanataka kubaki kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie hili kwanza, kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tutakapokwenda katika mchakato wa kuwapeleka wale Madaktari watano tutahakikisha wanabaki kule Ukerewe kwa ajili ya huduma ya afya. Kwa hiyo, mchakato wa upatikanaji wa Madaktari tunaufanya kabla hatujatoka katika Bunge hili, wataalam hao watakuwa wameshakwenda siyo Ukerewe peke yake, isipokuwa na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amesema kuna changamoto katika zahanati inayojengwa Nyakatungu. Naomba nimwambie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nitakuwa na hamu sana mara baada ya Bunge hili, niweze kufika Ukerewe nijue jiografia ya Ukerewe na kupanga mikakati tukiwa field kule, kuona tutafanyaje kutatua tatizo la afya la watu wa Ukerewe. Itanipa faida kubwa zaidi siyo afya peke yake, nitaangalia hata sekta ya elimu ambayo siku moja nimeona katika TV watoto wanavuka na boti kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kupata huduma ya elimu.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Baada ya MV Butiama kusita kufanya shughuli zake pale kulikuwa na meli ya MV Clarius ambayo nayo imesimama kufanya kazi na kuna taarifa kwamba itatengenezwa na watu wa MSCL ili iendelee kufanya shughuli zake lakini meli hii imekuwa chakavu, inahitaji matengenezo makubwa. Sasa kwa kuwa wenye jukumu la kutengeneza ni MSCL wenyewe lakini wanatatizo kubwa sana la fedha. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuna haja ya kuwasaidia hawa MSCL kwa kuwapa fedha za kutosha ikiwepo pamoja na pesa za OC ili waweze sasa kutengeneza meli hii iweze kufanya kazi katika mazingira mazuri ikizingatiwa ni ya muda mrefu na katika hali halisi ya sasa kumsafirisha abiria kwa saa tatu majini akiwa amekalia viti vya mbao si kitu kizuri sana?
Swali la pili; ratiba za meli kutoka Mwanza kwenda Ukerewe zina mahusiano ya moja kwa moja na ratiba za vivuko vingine. Kwa mfano, Kivuko cha MV Nyerere kutoka Mgolola kwenda Ukala sasa kumekuwa na matatizo ya kutowiana kwa ratiba kiasi kwamba wasafiri wanakaa muda mrefu. Kwa mfano, akifika Nansio anakaa kwa saa tano ili apate usafiri mwingine wa kumpeleka kisiwa cha Ukala. Je, Serikali haioni sababu za msingi za kuainisha ratiba ya vivuko hivi ili kuondoa gharama kubwa ambazo wasafiri wanazipata wanapokuwa safarini? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza, nakubaliana naye kwamba kuna haja ya kuwaongezea uwezo wa kifedha ikiwa ni pamoja na fedha za OC ili MSCL waweze kutekeleza wajibu wao na hasa katika kuikarabati meli hii ya MV Clarius.
Kwa upande wa pili, ratiba nimepokea ombi lake, nitawasiliana na taasisi hizi mbili zinazohusika, TEMESA pamoja na MSCL waangalie kama kuna uwezekano wa kurekebisha ratiba zao, lakini kwa mazingira ninayoyafahamu, tukirekebisha kutakuwa na tatizo vilevile la kuwasumbua wale wa Ukala wakakaa muda mrefu sana kusubiri MV Clarius ifike, ilete abiria. Tutaangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kutafuta njia nyingine kuweza hili kuliweka sawa ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo mbili za kivuko pamoja na Meli.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Tatizo la
mawasiliano ni kubwa sana kwenye Visiwa vya Ukerewe, hususan kwenye
maeneo ya Bwasa, Kata ya Igala na maeneo ya Bukiko, Kata ya Bukiko. Sasa je,
Serikali iko tayari kutumia wataalam wake kufanya utafiti na kusaidia upatikanaji
wa mawasiliano kwenye maeneo haya ya visiwa vya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko
tayari. Naomba tu nitoe kauli kwamba Mfuko wetu wa Mawasiliano kwa wote
(UCSAF) waifanye kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Jumapili tulikuwa na semina inayohusu mambo ya utalii, na kwenye jarida hili kulikuwa na taarifa ambazo zilikuwa na upungufu juu ya vivutio hivi. Sasa Je, Waziri yuko tayari kutembelea visiwa vya Ukerewe na kushuhudia vivutio hivi ili awe Balozi mzuri na mwenye taarifa zilizo sahihi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, suala la ukuzaji
na uendelezaji wa vivutio hivi mbali na kuvitangaza inategemea zaidi ubora wa miundombinu ya kuvifikia vivutio hivi; na kwa kuwa Halmashauri zetu hazina uwezo wa kutosha wa kuboresha miundombinu hii, sasa Serikali iko tayari kuboresha miundombinu ya kufikia vivutio hivi hasa Jiwe linalocheza la Nyaburebeka la Kisiwani Ukara? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari kabisa kutembelea vivutio hivyo pamoja na Mbunge, Mheshimiwa Mkundi bila wasiwasi wowote na tutapanga safari hiyo mwezi Agosti mwaka huu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vivutio vyote vya utalii vinakuwa vizuri zaidi kama vinafikika na raia na watalii wanaotaka kuvitembelea. Wakati tutakapotembelea tutafanya tathmini ya vivutio hivyo na kuona ni namna gani juhudi hizi zitakamilika ili vivutio hivyo vifikike.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Ukerewe inaundwa na visiwa na kwa kuwa yanapotokea matatizo ya dharura kiafya inakuwa kazi ngumu sana kuwawahisha wagonjwa kupata huduma ya ziada.
Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kutoa ambulance boat kuweza kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wa Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshiniwa Mwenyekiti, najua kwamba tulipeleka ambulance kule ya kawaida katika kipindi cha kati, lakini na mahitaji ya kwamba watu wa Ukerewe wapate ambulance boat, naomba Serikali tuchukue kwa mawazo yenu mapana. Kama Mbunge anavyofahamu tuliongea naye private kwamba tutafika Ukerewe baada ya Bunge hili, tukifika kule tutajadiliana kwa mapana na pamoja nini tutawasaidia wananchi wa Ukerewe. Pia jambo hili tutaangalia jinsi gani tuliweke katika kipaumbele kama Serikali kwa kuweka mawazo ya pamoja kwa upana wake.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo nyingi katika hizi zilizoondolewa si zile zinazomgusa moja kwa moja mvuvi. Wavuvi husasan katika Ziwa Victoria, wanasumbuliwa sana na leseni kwa mfano wanazopaswa kulipa wanapotoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine, kuna ushuru wa uvuvi kwa mfano, na tozo nyingine za SUMATRA na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu nyingi katika hizi ziko chini ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003, Serikali sasa haioni sababu ya msingi kabisa kuleta sheria hii Bungeni ili Bunge liweze kuipitia na kuifanyia marekebisho?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa taarifa nilizonazo Mheshimiwa Waziri wewe ni mtaalam mbobezi kwenye eneo hili la uvuvi na unatoka kwenye eneo la wavuvi, kwa hiyo unaujua vizuri uvuvi na kwa sababu matatizo mengi ya wavuvi, hususan eneo la Ukerewe yanazungumzika, je, uko tayari sasa Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili tuweze kuandamana kwenda katika Visiwa vya Ukerewe upate fursa ya kuzungumza na wavuvi na kusikiliza kero zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anasema kwamba tozo nyingi zilizofutwa sizo zile ambazo ni kero hasa inayowasumbua wavuvi na akatuomba kuleta mabadiliko ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tu kwamba matakwa yake haya tunayachukua na tayari Serikali ipo katika mpango wa kuboresha moja ya Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003, Sheria Na. 22 na kupitia kanuni mbalimbali ambazo zitakwenda kuboresha kwa maana ya tozo hizi zilizofutwa, sawa na majibu yangu ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nimhakikishie; hizi tozo, hasa ile ya movement permit iliyofutwa ilikuwa ni kero kubwa kwa wavuvi wetu na ndiyo maana Serikali hii ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Jospeh Magufuli ikaona iifutilie mbali. Na nataka nimhakikishie ya kwamba kilichobaki ni usimamizi wa kuhakikisha movement permit haiendelei kutozwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni la kwenda Ukerewe; ni kweli mimi ni mvuvi na uvuvi ni maisha yetu. Nataka nimhakikishie rafiki yangu ya kwamba tutafika Ukerewe kwenda kuzungumza na wavuvi na kwenda kuwatoa majaka roho yote yanayowasumbua. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, maeneo ya Kakelege na eneo la uwanja wa ndege Kata ya Nkilizia yapo katikati ya mji wa Nansio. Lakini maeneo haya yamerukwa na huduma ya umeme, jambo linalofanya wananchi wa maeneo haya waone kama wametengwa. na Mheshimiwa Waziri nimekuwa namuwasilishia tatizo hili mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu nataka kujua Serikali imefikia hatua ipi kuhakikisha kwamba maeneo haya yaliyo katikati ya mji wa Nansio yote yanapata huduma za umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika maelezo yangu ya awali Serikali inatekeleza mradi pia wa densification ambao sasa hivi Awamu ya Kwanza na ni kwa Mikoa sita. Baada ya kukamilika kwa mikoa hiyo Serikali itaendelea pamoja na wafadhili wa Norway kutekeleza awamu ya pili. Nia ya mradi huu ni kusambaza umeme katika maeneo kaya, vitongoji na taasisi za umma zilizorukwa. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Awamu ya Pili ya mradi huu itafikiwa katika maeneo ambayo ameyataja.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Matatizo ya upungufu wa Madaktari, watumishi wengine wa afya na vifaa tiba yaliyoko hospitali ya Mkoa wa Geita ni sawa kabisa na yale yaliyoko kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, Hospitali ya Nansio. Serikali iko tayari sasa kuangalia visiwa vya Ukerewe kwa upendeleo maalum na kutusaidia kuondoa tatizo hili ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto visiwa vya Ukerewe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli. Mheshimiwa Mbunge anakiri kwamba, nilipata fursa ya kwenda na tuliweza kufika mpaka kule Ukerewe na ni kweli changamoto ya afya katika visiwa vile imekuwa ni kubwa zaidi. Ndiyo maana katika vipaumbele vyetu sasa hivi hata ukiangalia idadi ya Madaktari ambao juzi tu tumewaajiri, tumeajiri Madaktari takribani 2,058, tumepeleka vijana kule kwa ajili ya kusaidia suala la changamoto inazozipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna fedha vilevile tunaenda kuboresha kile kituo cha afya kama alivyopendekeza Mheshimiwa Mbunge na hatutasita kuendelea. Tunafanya juhudi ya kutosha hasa kwa sababu tunajua kwamba eneo la Ukerewe lazima tuboreshe miundombinu ili hata watumishi tunaowapeleka kule wawe na hamasa ya kufanya kazi baada ya kuboresha mazingira yao. Kwa hiyo, jukumu hili tumelichukua sisi Serikali kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi wa Ukerewe.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mkanganyiko katika utaratibu wa upatikanaji wa vitambulisho kwa wazee ili waweze kupata huduma za afya ambapo baadhi ya maeneo wazee hawa wamekuwa wanatakiwa kuchangia baadhi ya gharama.
Sasa Serikali inaweza kutoa kauli ni upi wajibu wa halmashauri na upi wajibu wa wazee hawa ili waweze kupata vitambulisho ili wapate huduma za afya bure? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni agizo la Serikali kwamba Halmashauri zitoe vitambulisho vya wazee ili waweze kutambulika kirahisi wanapokwenda kutafuta matibabu ya afya. Na hii inaendana na Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inasema kwamba wazee watapata matibabu bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho hivi vinapaswa vitolewe bure kwa sababu halmshauri zinagharamia. Inawezekana kwamba zile gharama ndogondogo kama upigaji wa picha ambazo wanatakiwa wazee nao wazigharamie ambayo sio gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapenda kusema tu kwamba gharama ya kitambulisho ni bure na Halmashauri zinatakiwa zigharamie hilo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na posho za Madiwani, Wenyeviti ya Vijiji na Vitongoji kuwa ndogo, lakini bado halmashauri nyingi zimekuwa zinawakopa viongozi hawa posho hizi kiasi kwamba wana muda mrefu hawalipwi. Sasa Serikali iko tayari kutoa kauli yenye muda maalum kuhakikisha kwamba viongozi hawa wanalipwa madeni yao ya posho zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, juzi nilipokea concern kutoka Buchosa kwamba Madiwani wamekopwa takribani miezi minane, hili halikubaliki hata kidogo. Wakati mwingine utagundua kwamba ni uzembe tu wa usimamizi nzuri. Watu wanafanya collection lakini wakati mwingine katika suala la kuwalipa Madiwani wanaona kama ni hisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitoe maelekezo kwamba halmashauri mbalimbali tunafanya makusanyo, makusanyo yale yanakusanywa na Madiwani ndio wanaofanya maamuzi, lazima mwende mkalipe posho za Madiwani kwa kadri iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani wanafanya kazi kubwa lakini posho zao hazilipwi na wakati huo huo shughuli nyingine zinaendelea ambazo Madiwani hao ndio waliosimamia kupata fedha hizo, haitokubalika. Tutaenda kufuatilia halmashauri moja hadi nyingine. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tuta-cross check na halmashauri mbalimbali ambazo kwa makusudi kabisa wamekataa kuwalipa madiwani either kwa kiburi au kwa jambo lingine lolote.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa kukosa fedha za kuendeshea shughuli za Mabaraza ya Ardhi ya Kata ni kichocheo kikubwa sana cha rushwa kinachopelekea wananchi wengi kunyimwa haki zao za msingi. Sasa Serikali haioni sababu na umuhimu sasa itoe ruzuku kwa Mabaraza haya ili yaweze kuendesha shughuli zake na kuondoa uwezekano wa kuchukua rushwa? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa kesi kubwa nyingi sana kuja kuziangalia hata maamuzi mengine yanakuwa yanasababishwa na baadhi ya wale ambao wako katika Mabaraza ya Kata. Wakati mwingine inaonekana kwamba mtu aliyenacho ndiyo huyo ambaye haki inamwendea, hili ndiyo maana Serikali ilikuwa inafanya tathimini kwa kina sana kuangalia nini kifanyike katika suala zima katika uendeshaji wa Baraza la Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Mheshimiwa Mbunge tunalichukua lakini kuna mchakato mpana tunaufanya kuona jinsi gani tutaboresha haya Mabaraza ya Kata yaweze kufanya kazi vizuri zaidi kulinganisha na hivi sasa kwa sababu haki nyingi za watu zinapotea kwa sababu haki haisimamiwi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wazo hili tunalichukua, lakini tunajumuisha miongoni mwa mambo ya kufanya restructuring tuifanyeje, lengo kubwa la Mabaraza hayo yaweze kufanya vizuri, kwa hiyo, ni wazo zuri tunalichukua kama Serikali kulifanyia kazi kwa mpango.
MHE. MICHAEL J. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inakiri kwamba Ukerewe ni moja kati ya maeneo ambayo watumishi wake wanafanyakazi katika mazingira magumu na kwa kuwa huduma za elimu na afya visiwani Ukerewe hususan kwenye Visiwa vya Ilugwa, Ukara, Bwilo na kwingineko zinaadhirika sana na changamoto zinazowakabili watumishi kwenye maeneo haya.
Je, Serikali iko tayari kutoa fedha na kuwezesha sera hii ya malipo ya mishahara na motisha katika utumishi wa umma kuanza kutekelezwa ili kuokoa maisha na mazingira ya wakazi wa visiwa hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwanzoni mwa mwaka huu Serikali ilisambaza walimu kwenye Halmashauri zetu hasa walimu wa sayansi lakini kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa walimu hawa kuishi katika mazingira magumu sana kwa sababu ya kutolipwa stahiki zao. Je, nini kauli ya Serikali juu ya tatizo hili? Nashukuru sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NAUTWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli ukiangalia si tu kwamba wananchi wa Ukerewe wanaadhirika kutokana na ukosefu wa huduma za elimu na afya, lakini hata watumishi wenyewe walio katika mazingira magumu pia huduma ya elimu katika eneo lile na afya inapokuwa si nzuri inawafanya pia na wenyewe wasivutiwe kufanya kazi katika maeneo hayo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeiona changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kwa ujumla wake mwongozo huu haujaanza kutekelezwa lakini kupitia Bajeti ya Serikali na kupitia bajeti za Halmashauri ambazo zimepitishwa wameshaanza kutekeleza maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu pamoja na afya.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba tutaendelea kulifanyia kazi kama Serikali kutoa msisitizo ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yanayokabiliwa na changamoto hizi basi yanaweza kutengewa fedha za bajeti za kutosha ili kuweza kutekeleza sera hii.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusiana na walimu wa sayansi na hesabu walipangiwa vituo mwaka huu, kwamba hawajalipwa stahiki zao. Kwa kweli ni jambo ambalo limetusikitisha, na haswa ukizingatia katika Halmashauri moja unakuta mtu amepangiwa walimu 12 tu, inakuwaje Halmashauri inashindwa kuwahudumia kwa watumishi wake wapya waliopangiwa katika kituo kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, niseme kupitia hadhara hii natoa tamko au agizo kwa Halmashauri zote zilizopokea walimu wapya wa sayansi na hesabu lakini pia zilizopokea wataalam wa maabara za sayansi zihakikishe ndani ya siku saba zimewalipa watumishi hao stahiki zao zote. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ukerewe ni wazalishaji wakubwa wa matunda hasa machungwa na nanasi. Lakini wananchi wa Ukerewe wamekuwa hawafaidiki sana na matunda haya kwa sababu sehemu kubwa ya matunda imekuwa ikiharibika kwa sababu ya kukosa soko.
Je, Serikali iko tayari kusaidia upatikanaji wa kiwanda cha kusindika matunda haya ili wananchi wa Ukerewe wapate soko la uhakika wa matunda yao?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba bado tunayo changamoto katika usindikaji wa matunda. Na katika mtazamo wetu Tanzania tunajipanga zaidi katika huu ukuzaji wa viwanda hasa katika eneo la kilimo na manasi pamoja na machungwa ni mazao mojawapo ambayo yana changamoto. Jambo ambalo tunaliona sasa hivi ni kwamba iko haja ya kuunganisha taasisi zetu hasa katika kukuza teknolojia zitakazowezesha matunda yanapokuwa yamezalishwa, yasiharibike kiurahisi na kuyaongezea thamani.
Lakini vilevile nikuombe Mheshimiwa Mbunge ukiwa ni sehemu ya uhamasishaji pamoja na Serikali kuendelea kuwahamasisha wadau binafsi kwa ajili ya kuwekeza viwanda katika eneo hilo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara nyingi za mikoa sasa zimeshajengwa na kuna tatizo kubwa sana la barabara Wilayani na vijijini; na TARURA wamepewa jukumu la kujenga barabara hizi, lakini pesa wanazozipata bado hazitoshi. Serikali sasa haioni sababu za msingi za kubadili formula ya ugawaji wa pesa kati ya TANROADS na TARURA ili kuongeza percentage ya pesa zinazoenda TARURA? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kati ya Lugezi na Kisorya kuna kivuko ambacho ni mbadala wa daraja, lakini katika kivuko kile kuna tatizo kubwa la utozaji wa nauli, hususan mizigo ambayo inaleta kero sana kwa wananchi kwa mizigo iliyo chini ya kilo 20. Inategemea busara ya mtozaji kama kilo moja atatoza kiasi gani? Kilo mbili kiasi gani?
Sasa Serikali haioni sababu kuweka kiwango maalum, kwa mfano, chini ya kilo 20 wananchi wasitozwe tozo zozote za nauli ya mizigo ili kuondoa migogoro ambayo imekuwa inajitokeza mara kwa mara kati ya vivuko vya Kisorya na Lugenzi na Bugorora na Ukara? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunaendelea na ujenzi wa barabara na kipaumbele kilikuwa kwenye barabara kuu. Barabara kuu zina urefu wa zaidi ya kilometa 8,000 na kwa sasa hivi tumeshavuka nusu ya urefu huo. Kwa maana hiyo, sasa ni fursa ambayo itawezesha Serikali kuelekeza fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza barabara ambazo zinaunganisha mikoa na hatimaye pia kwenda kuunganisha barabara ambazo ziko chini ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba utambue hivyo, pamoja na wapiga kura wa Ukerewe kwamba tumejipanga vizuri. Mara baada ya kukamilisha sehemu kubwa ya barabara kuu, nguvu kubwa ya Serikali itaelekezwa katika eneo la barabara ambazo ziko kwenye Mikoa na Wilaya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwamba tunachukua hatua gani kwa ajili ya gharama ya kivuko hiki cha MV Ujenzi?
Mheshimiwa Spika, ninatambua, nasi upande wa Serikali tumelichukua hili, lakini tumeshaanza kufanya utafiti wa kuhakikisha kwamba suala la bei hii ya vivuko tunaliangalia kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, iko hoja kwamba gharama ya ubebaji wa mizigo iko chini kwenye baadhi ya maeneo, lakini yako maeneo yanaonesha kwamba gharama ni kubwa. Kwa maana hiyo sasa, tunafanya utafiti ili tuweze kuja na bei ambayo itakuwa rafiki kwa watumiaji wa vivuko hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Ukerewe tuvute subira. Nawaomba na wenzetu wa upande wa TEMESA waharakishe hili zoezi la kufanya utafiti ili tuweze kuchukua hatua ambayo itafanya usafiri huu uwe rafiki kwa watumiaji wa vivuko. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa zoezi hili la kuzuia uvuvi haramu linatumiwa sasa na vikosi vya doria kunyanyasa, kudhalilisha na kupora wananchi hasa wavuvi kwenye Visiwa vya Ukerewe kwa kuwadai pesa na malipo mbalimbali yasiyo halali. Nataka kujua Serikali iko tayari kutoa kauli kuzuia unyanyasaji huo lakini na Mheshimiwa Waziri kufika Ukerewe kukaa na wavuvi na kupata ushahidi wa haya yaliyotokea ili Serikali iweze kuchukua hatua kwa wahusika? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe. Naomba kusema kwamba kama kuna changamoto yoyote ambapo watendaji wetu kwa namna ile wameenda kinyume na misingi na taratibu tulizowapa, watendaji wetu wote wanapoenda doria wanapewa mwongozo wa makosa gani ambayo yanatakiwa kuchukuliwa hatua na kwa kiasi gani. Mheshimiwa Mbunge kama anayo hiyo orodha ya watu ambao anasema kwamba hawakutendewa haki atuletee sisi tutalishughulikia mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mimi kwenda Ukerewe…
MHE. JOSEPH MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mahakama ya Mwanzo ya Bukindo, Bukonyo na Ukara zina hali mbaya sana kimiundombinu, achilia mbali upungufu wa watumishi. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira haya ili haki ya wananchi wa Visiwa vya Ukerewe iweze kupatikana kwa haraka?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wilaya ya Ukerewe, imepangiwa kujengewa Mahakama ya Mwanzo katika eneo la Ilangala katika mwaka wa fedha unaoanza sasa wa 2018/2019.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo ambapo shughuli nyingi za uvuvi zinafanyika kunapatikana athari za kijamii za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kama ilivyo kwenye maeneo zinapofanyika shughuli za uchimbaji wa madini ambapo maeneo yanayozunguka migodi hii yanapata mrahaba kama sehemu fulani ya ku-recover athari hizi.
Je, Serikali haioni sababu sasa sheria hii iweze kutumika kwenye maeneo ambako shughuli za uvuvi zinafanyika na kusababisha athari mbalimbali za kijamii kwa ajili ya ku-recover sehemu ya athari hizi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameulizia suala la kupata service levy kutokana na uvuvi katika Ziwa Victoria. Naomba niseme tu suala la uvuvi haliko katika Sheria ya Madini ambayo tunaisimamia sisi. Nadhani ni vema Mheshimiwa Mbunge akaifuatilia Sheria ya Serikali za Mitaa kuona kama kuna stahiki ambayo unaweza ukaipata kutokana na masuala ya uvuvi. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa baada ya operesheni nyavu zinazotumika sasa ni mbovu sana, hazina kiwango na wala hazistahili kutumika kwa uvuvi, zinawatia hasara sana watumiaji. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kupata nyavu zinazostahili, zinazoweza kukabiliana na mazingira ya Maziwa Viktoria, Tanganyika na mengineyo ili wavuvi wetu mbali na kupata hasara za kuchomewa nyavu wasiendelee kupata hasara za kununua nyavu kila siku chache zinapokuwa zinapita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, juu ya suala linalohusu ubora wa nyavu, ni kweli Wizara yangu imepokea malalamiko kutoka kwa wavuvi kutoka pande zote za nchi yetu hasa wavuvi wa Ziwa Viktoria na tumekwenda kujiridhisha. Tupo katika utaratibu wa kuendelea kufanya tathmini ya hali hii. Nataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tunashirikiana vyema na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya kuweza kupata viwango halisi vya ubora wa nyavu zetu zinazozalishwa nchini.
Mheshimiwa Spika, pale itakapobainika kwamba liko tatizo juu ya ubora huu, la kwanza tutawataka ama tunawataka wazalishaji wetu waongeze viwango vyao vya ubora, lakini ikibidi sisi kama Wizara tuko tayari kutafuta mpango mwingine wa kuweza kuwanusuru wananchi wetu ili waweze kuendelea na shughuli hii ya uvuvi bila ya tatizo lolote.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa fursa ya kuulizwa maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na umuhimu wa huduma za ugani na upatikanaji wa pembejeo lakini bado huduma hizi haziwafikii wananchi kwenye maeneo ya chini kule ambako ndiko kwenye uzalishaji. Nini sasa mkakati wa Serikali ili kuondoa tatizo hili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo kwa zao la pamba, zao la muhogo ambalo limekuwa muhimu sana kwa wananchi wa Visiwa vya Ukerewe kiuchumi, lakini hata kwa chakula limekuwa linakabiliwa na matatizo mengi sana ya magonjwa, lakini hata tatizo la ardhi kwenye eneo la Visiwa vya Ukerewe. Je, Serikali ina mkakati wowote wa kutuma timu ya wataalam kufanya utafiti ili basi Visiwa vya Ukerewe vitumie ardhi yake hii ndogo kwa tija zaidi katika kuzalisha zao hili la muhogo? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kujibu maswali la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kuhusu mikakati ya Serikali tuliyo nayo kwa ajili ya pembejeo na Maafisa Ugani. Kwanza tumezielekeza Halmashauri zote nchi ni kutenga asilimia 20 ya mapato yao ya ndani kwa maagizo ya Serikali kupitia Waziri Mkuu kwa ajili ya kupeleka kwenye sekta ya kilimo ili Maafisa Ugani hawa waweze kuwezeshwa kwa ajili ya kuwafikia wakulia kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, viongozi wote wa Serikali katika ngazi mbalimbali, hasa wale wanaosimamia sekta ya kilimo tumewaambia lazima washiriki katika kilimo ili mashamba yao pia yaweze kuwa mfano kwa wakulima wale ambao wapo wanazunguka. Tunafahamu pia kwamba tuna upungufu mkubwa wa Maafisa Ugani nchini, mahitaji ni zaidi ya 20,000 lakini tulio nao ni 6,800. Tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Utumishi kwa ajili ya kuongeza Maafisa Ugani nchi nzima ili wawafikie wakulima wetu kwa ajili ya kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu zao la muhogo kukubali kule Ukerewe pamoja na vituo vyetu vya utafiti, tuko tayari kama Serikali na tunawaagiza kituo chetu cha utafiti cha pale Ukiruguru, Mwanza pamoja na Ilonga kufika maeneo hayo ya Ukerewe kwa ajili ya kufanya utafiti wa udongo kuona namna gani zao hili linaweza kulimwa katika Visiwa Vya Ukerewe.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa takwimu zinaonesha ni takribani asilimia 30 tu ya akina mama wajawazito ndio wanaohudhuria kliniki.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa akina mama wajawazito ili wahudhurie kliniki na waweze kuepuka matatizo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; umbali kutoka mahali ambapo akina mama wajawazito wanapata huduma ni moja kati ya sababu zinazosababisha matatizo hayo. Kwa mfano, kwenye Jimbo la Ukerewe ambalo linaundwa na visiwa vingi, Visiwa kama Zeru, Kamasi, Bulubi, Gana vyote vile vinatumia zahanati moja.
Sasa kama Serikali ilivyofanya kwa Kituo cha Bwisya, tunashukuru, je, Serikali iko tayari kushirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Afya ili ama kituo hiki cha Kamasi kiweze kupandishwa na kupata pesa za kutengeneza miundombinu kuweza kutoa huduma zilizo bora kwa kina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu za hali ya utoaji huduma za afya mwaka 2015 akina mama ambao wanakwenda kliniki angalau mara moja tuko asilimia 90, lakini tunataraji kina mama waende kliniki angalau mara nne katika kipindi chao cha ujauzito, na sasa hivi tuko kwenye zaidi ya asilimia 60 katika kiwango cha kitaifa. Kwa hiyo, rai yangu bado naendelea kutoa kwa wanawake wote wajawazito katika nchi yetu kuhakikisha kwamba wanapokuwa wajawazito angalau kufika katika vituo vyetu vya kutolea (Anti-Natal Clinic) angalau mara nne ili iweze kuwasaidia kupata ushauri na jinsi gani bora ya kuweza kuhudumia ujauzito waliokuwa nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameongelea suala la umbali. Serikali inatambua hilo na tumekuwa tunaendelea kuboresha huduma za afya na hivi vituo 208 ambavyo tumeviboresha hivi karibuni na kuweza kutoa huduma nzuri za ujauzito na upasuaji pamoja na kujifungulia ni moja ya mkakati wa Serikali. Kuna mkakati wa kuongeza Hospitali za Rufaa za Wilaya, tuna mkakati wa kuongeza Hospitali za Rufaa za Mikoa na kadri tutakapokuwa tunaona mahitaji katika hivyo visiwa vingine vya Ukerewe ambavyo umevisema hatutasita kukaa na wenzetu wa TAMISEMI na kuangalia jinsi gani ya kuboresha huduma katika maeneo hayo husika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mradi wa maji wa Bukindo, Kagunguli Visiwani Ukerewe unatekelezwa kwa ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais na kusimamia na MWAUWASA. Mradi ule kwa sehemu kubwa umekamilika lakini haujaanza kutoa huduma kwa sababu ya kukosa pesa za kuunganisha umeme. Je, Serikali iko tayari kuwasiliana na MWAUWASA ili waweze kusaidia uunganishaji umeme mradi huo uweze kutoa huduma uweze kuwasaidia wananchi wa Kata za Bukindo, Kagunguli na Mtungulu ambao watafaidika na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari kufanya mawasiliano na Mkurugenzi wa MWAUWASA na ikatakapobidi tufanye jambo hili la haraka ili wananchi wake waweze kupata umeme ili mradi uweze kutekelezeka na wananchi waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. MICHAEL J. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali bado kuna matatizo makubwa sana kwenye utendaji katika ngazi hizi za chini zinazotokana na ama na kutokuelewa wajibu wa kila upande katika kusimamia utendaji kwenye maeneo haya. Je, bado Serikali haioni sababu ya msingi kabisa kutoa elimu pamoja na majibu haya yaliyotolewa bado kuna tatizo kubwa sana kwenye usimamizi hasa nyakati za uchaguzi ambapo kumekuwa na migogoro mingi inayotokana na watendaji wanaosimamia chaguzi hizi kufanya au kutoa maamuzi kulingana na maelekezo yanayokuwa yametolewa na viongozi wa juu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na migogoro hii, Serikali haioni kwamba kuna sababu ya msingi kabisa kutokana na mapendekezo ya Katiba iliyopendekezwa kuwepo na umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ili kuondoa kabisa migogoro hii inayotokea nyakati za uchaguzi kwenye ngazi mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimhakikishie kwanza uzoefu wangu kwamba kati ya mwaka 1996 mpaka mwaka 2000 mwenyewe nilikuwa Ofisa Mtendaji wa Kata, kwa hiyo nina uzoefu mkubwa na kile ninachokielezea na kata yenyewe ilikuwa ni Kata ya Manzese pale Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chaguzi za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa sheria na kama atatokea Msimamizi Msaidizi yeyote akatenda kinyume cha sheria, mdau yeyote anao uhuru wa kulalamika katika vyombo vinavyohusika ikiwemo kulalamika kwa Msimamizi wa Uchaguzi na hatua zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya watu ambao wanatenda kinyume cha utaratibu wa sheria ya uchaguzi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, ameuliza kwamba kuna mapendekezo kwenye Katiba iliyopendekezwa. Sasa kwa sababu Katiba iliyopendekezwa bado hatua zake hazijakamilika, nashauri Bunge lako Tukufu kwamba tusiwahishe mambo, tusubiri kwanza huo mjadala wa Katiba Mpya Iliyopendekezwa ukamilike na mambo yaingizwe kwenye sheria basi hapo tutatekeleza baada ya sheria kuwa imekamilika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Kwanza nishukuru kwa majibu yenye kutia matumaini ya Serikali kupitia kwa Naibu Waziri. Lakini kwa kuwa usanifu wa awali ulionesha chanzo cha maji kwa ajili ya miradi hii ambacho sasa si cha kuaminika, Serikali sasa iko tayari kupitia usanifu ule ili chanzo cha maji kwa ajili ya mradi huu ukiwa ni Ziwa Victoria?

Swali la pili, kwa sababu mbali na Bonde hili la Miyogwezi, kuna Bonde la Bugolola lakini na maeneo mengine ambayo ni potential kwa ajili ya uzalishaji wa chakula kwenye Visiwa vya Ukerewe. Lakini yote haya tunaweza tukayatumia kwa ufanisi kama Mheshimiwa Waziri anaweza kufika pale akapitia na tukaweza kufanya maamuzi yenye maslahi.

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuandamana na mimi ili tuweze kufika katika Visiwa vya Ukerewe tuweze kupitia mambo haya? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyotumia muda mwingi kufuatilia na kuwapigania watu wake wa Ukerewe.

Pili, nimesikiliza ushauri wake na kwa niaba ya Serikali tunauchukua ushauri huo na nichukue nafasi hii kuwaelekeza Wahandisi wetu wa Kanda ya Umwaliaji, Kanda ya Mwanza kufika Ukerewe kuanza uchambuzi wa awali kuangalia hiko chanzo kipya na cha zamani ili kuja kutushauri kitaalam kuutekeleza mradi huo upya.

Swali lake la pili, kutaka kwamba kwenda kuambatana na mimi kufika katika eneo hili, Mheshimiwa Mbunge niko tayari baada ya Bunge hili likimalizika tarehe 8 Februari tuoanane ili tupange siku gani tunaweza kutembelea huko maeneo yake.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Tatizo la kukatika kwa umeme limekuwa linajitokeza sana kwenye Visiwa vya Ukerewe hali inayoathiri shughuli za kiuchumi na hasa shughuli za utoaji wa huduma za afya kwenye hospitali yetu ya Wilaya ya Nansio.

Ningependa kupata kauli ya Serikali, ni mkakati gani uliopo kuondoa tatizo hili na kufanya Visiwa vya Ukerewe vipate umeme bila shida ya kukatikakatika kwa umeme kwenye maeneo hayo. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi Mbunge wa Ukerewe kupitia Chama cha Mapinduzi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge aliwasilisha hilo leo asubuhi kwamba kuna tatizo hilo katika Visiwa vya Ukerewe na hapa nilipo nishatoa maelekezo kwamba kwa sababu umeme wa Ukerewe unatokea katika maeneo ya Bunda na kwa changamoto ambayo nimeipata hivi asubuhi baada ya kuwasiliana na Meneja kwamba kuna tatizo la changamoto ya nguzo, ndiyo maana Serikali imefanya maamuzi ya kuhama sasa itumie nguzo za zege.

Kwa hiyo, tumetoa maelekezo ifanyike utafiti wa kina changamoto ni nini ili ifanyiwe kazi, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kutoka hapa tufanye mazungumzo ili kuweza kumpa mikakati ambayo Serikali imepanga. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nitumie fursa hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake na nimshukuru kwa ushirikiano ambao amekuwa anautoa kwa masuala ya uvuvi. Nina maswali mawili ya nyongeza; la kwanza uvuvi wa dagaa wanavuliwa kwa kuchotwa, kwa hiyo isitegemee kwamba wategemee dagaa wale wanase kwenye nyavu, ndio maana ni muhimu angalau matundu yake yawe madogo kidogo. Sasa kwa kuwa dagaa wanaopatikana Ziwa Victoria hawatofautiana sana na dagaa wanaopatikana Bahari ya Hindi na natambua kuna mchakato wa kufanya utafiti kwenye Bahari ya Hindi ili dagaa wanaovuliwa kwenye Bahari ya Hindi wavuliwe kwa nyavu za milimita sita na kuendelea. Je, Serikali haioni sababu sambamba na utafiti utakaofanyika Bahari ya Hindi ufanyike vilevile na uvuvi utakaofanyika Ziwa victoria kwa dagaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wavuvi wa Ukerewe wa samaki aina ya gogogo au ngere wanapata bugudha sana wakati wanavua samaki wale kwa kisingizio kwamba sheria hairuhusu, lakini mazingira ya uvuvi wa samaki wale na aina yake ni tofauti sana na samaki wengine. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa tamko ili wavuvi wa ngere kwenye Visiwa vya Ukerewe na maeneo mengine wasibughudhiwe ili wafanye shughuli zao za uvuvi wa samaki hawa bila shida yoyote. Nashukuru sana?
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mkundi na timu ya Waheshimiwa Wabunge katika eneo la Ziwa Victoria kwa namna ambavyo mara kadhaa wamekuwa wakisimamia maslahi mapana ya wapigakura wa eneo hili ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za nchi yetu kupitia sekta hii ya uvuvi. Sasa swali la kwanza la Mheshimiwa Mkundi linahusu juu ya ya Serikali kuwa tayari kufanya utafiti katika eneo la Ziwa Victoria kama ambavyo tunafanya utafiti kwenye maji ya bahari ili kuweza kuruhusu nyavu ya chini ya milimita nane kuweza kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kuwa, kwa upande wa bahari bahari zilizokuwa zikitumika ni milimita 10 na zimekubalika kuonekana na maoni ya wadau kuwa milimita 10 zimeshindwa kukamata dagaa na ndio maana Serikali tukaielekeza Taasisi yetu ya Utafiti (TAFIRI) kufanya utafiti na kujiridhisha ya kwamba tufanye mabadiliko ya kanuni kwa haraka ili ikiwezekana tuweze kutumia nyavu za milimita nane ili kuweza kuwabnufaisha wavuvi wa upande wa bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa rai hii ya kutaka tutumie njia hiyo ya utafiti kwa upande wa Ziwa Victoria, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mkundi na Waheshimiwa Wabunge wote wavuvi wa kutoka Ziwa Victoria tunaichukua rai hiyo na tutawaelekeza TAFIRI waweze kufanya utafiti na kuweza kujiridhisha bila ya kuathiri sekta hii ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mkundi linahusu uvuvi wa samaki aina ya gogogo, ngere na ningu. Samaki hawa ni samaki wenye kupendwa sana katika eneo la Ziwa Victoria naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge katika mabadiliko ya kanuni tunayoyafanya hivi sasa tumezingatia kwamba tufanye makubaliano ya kuweza kupitisha kanuni rasmi sasa ya kuweza kuvua na kutumia rasilimali hii ya samaki hawa aina ya gogogo, ningu na ngere ambao wameonekana katika kanuni zilizopita kuwa hawakutajwa moja kwa moja. Naomba niwahakikishie wavuvi wote wa eneo la Ziwa Victoria Serikali inalifanyia kazi jambo hili na muda si mrefu watapata matokeo ili waweze ku-enjoy na kufurahia rasilimali za Taifa lao.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini ukweli ni kwamba pamoja na maelekezo yanayoelekezwa kule chini, viongozi hawa wa Mitaa na Vijiji, Vitongoji hawalipwi posho zao; na kwa kuwa Serikali kwa namba ya viongozi hawa kuwa kubwa inashindwa kuongeza posho zao:-

Serikali haioni umefika wakati sasa kufikiria uwezekano wa kuwalipa kiwango fulani cha pesa viongozi hawa pale wanapomaliza muda wao wa Uongozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona Waheshimiwa Wabunge wanazungumzia posho za Madiwani na posho za Wenyeviti wa Mitaa; naomba nitumie nafasi hii kusema tu kwamba wakati tunamalizia hoja yetu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, suala la posho za Madiwani zile ambazo zilikuwa zimezungumzwa, Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo kwa Madiwani wote wa Halmashauri watapata Waraka wa maelekezo kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuondoa sintofahamu ya posho za Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali alilouliza Mheshimiwa Mkundi, tulipokee; ni kweli kwamba Wenyeviti wa Mitaa baada ya kustaafu kuna kiwango cha fedha wanapaswa kulipwa. Sasa maoni ya Mbunge ni kwamba tuangalie namna ya kuongeza kiwango hiki (lump sum amount) kama watasema ni shilingi 500,000/= au shilingi 1,000,000/= kwa mkupuo itaweza kuwasaidia. Jambo hili tunalipokea, tunalifanyika kazi, kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu, tutalitekeleza kwa sababu ni jambo jema kwa ajili ya viongozi wenzetu hawa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Baada ya ajali ya Kivuko cha MV Nyerere tarehe 20 Septemba, mwaka jana pale Ukala, Serikali iliahidi kutengeneza kivuko kipya kwa ajili ya kusaidia wananchi eneo lile. Hivi sasa kuna kivuko cha muda cha MV Sabasaba ambacho kimekuwa na changamoto nyingi sana. Nataka kujua kutoka Wizara, ni hatua ipi imefikiwa ya ujenzi wa kivuko kipya kitakachofanya kazi kati ya Bugolora na Ukara? Nashukuru.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ile ajali Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshatangaza tenda na Mkandarasi amepatikana na mkataba umeshasainiwa na sasa hivi tunaendelea kununua engine haraka ili kitakapokamilika kifungwe, lakini pamoja na Kivuko cha Nyamisati, Mafia.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kumekuwa na tatizo kubwa sana la kukatika kwa umeme wakati mwingine kwa siku nzima au hata zaidi ya siku kwenye visiwa vya UKerewe kila wakati mvua inaponyesha. Ningeomba Mheshimiwa Waziri awaambie wananchi wa Ukerewe ni lini tatizo hili litakoma ili wafurahie huduma ya umeme kama yalivyo maeneo mengine nashukuru sana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo la Ukerewe kwa mwezi mmoja uliopita umeme ulikuwa umekatika sana umesababishwa na sababu moja tu, wavuvi wanaovua kutoka eneo la Kisolia ambapo ni mwanzo wa kuingilia kutoka Bunda kuelekea Lugenzi wamekuwa mara nyingi sana wakikata nyaya wakati wa uvuvi. Lakini nyaya zile zimekuwa zikitikiswa pia wakati wa mvua inapoambatana na upepo, kwa hiyo, ni kweli maeneo ya Ukerewe yamekuwa yakipata changamoto kwa kukatika kwa umeme kipindi hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua tulizochukua kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge na wananzegwa wananchi wa Ukerewe ni kwamba kwanza tumeanza kujenga kebo ya kutoka Kisolia kwenda Lugenzi ambapo ni kilomita nne na tume-commit shilingi bilioni 375 na ujenzi umeanza tutafunga kebo tutaipitisha juu ili wavuvi waache kuzigusa na hivyo kutakuwa na umeme muhimu sana kwa maeneo hili. Kwa hiyo, wananchi wa Ukerewe wavumilie kipindi cha wiki mbili zinazofuata mradi utakamilika ili umeme uwe ni uhakika zaidi kwa maeneo ya UKerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipe nafasi kidogo kwa sababu ni suala la Ukerewe nitoe tangazo kwa wananchi sio wa Ukerewe peke yake ingawa Mheshimiwa Mbunge hajaliuliza, kumekuwa na changamoto kwa wananchi wa Ukerewe hasa watumiaji wadogo wa umeme kutozwa shilingi 2500 kwa unit kinyume na utaratibu na sheria ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe tangazo kwa wananchi wa Ukerewe wasikubali kutoa shilingi 1000 kwa unit kwa sababu wananchi wote wa Ukerewe ni sawa na Watanzania wengine ambao wanatumia unit 75 ambao wanatakiwa walipe shilingi 100 per unit badala ya 2500 per unit.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe tangazo hili Mheshimiwa Mbunge anifikishie, lakini nimuombe Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe alisimamie na Meneja wa TANESCO alisimamie ili mwananchi yoyote atakayepatikana akitozwa hivyo kupitia kwa mkandarasi basi atoe taarifa mara moja na Serikali ichukue hatua dhidi ya watu ambao sio wazalendo kwa kitendo hicho ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini napongeza vile vile hatua zilizofikiwa za kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na kwamba utafiti bado unaendelea, lakini tatizo la msingi tayari limepatikana kwamba kuna kiwango kidogo cha mboji, lakini pH vilevile ya udongo wa Ukerewe iko chini. Sasa swali langi, Wizara iko tayari kuijumuisha Ukerewe katika maeneo yanayopata ruzuku za pembejeo itakayoambatana na ushauri wa aina ya mazao yanayopaswa kulimwa kwenye maeneo yetu ya Ukerewe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Ukerewe tuna fursa kubwa sana ya matunda, lakini tatizo kubwa, matunda yetu yamekuwa yanaharibika kwa kukosa soko. Tumejitahidi kupata wawekezaji kwa ajili ya kujenga viwanda, lakini tumekuwa tunakwama ama kutokana na kiwango cha malighafi inayozalishwa au aina ya matunda tunayoyazalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iko tayari kuwasaidia wananchi wa Ukerewe ambao wanalima matunda ili aina ya matunda yanayotakiwa iweze kulimwa, lakini sambamba na hilo, kusaidia kuwepo kwa kiwanda cha kusindika matunda haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mkundi kwa kazi kubwa anayofanya Jimboni kwake. Kuhusu suala la kupewa ruzuku kama ni special case, suala la ruzuku kwenye mbolea, hatuwezi kutoa commitment kama Serikali kwamba tutawapa watu wa Wilaya ya Ukerewe peke yao. Suala la ruzuku ama mabadiliko ya sera juu ya suala la kutoa ruzuku katika Sekta ya Kilimo, litatazamwa kwa ujumla wake kwa kuwa sasa hivi Wizara inapitia upya Sera yetu ya Kilimo ya Mwaka 2013 ili kuona mahitaji na namna gani tunaweza kutatua changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua za awali, tunaendelea kusisitiza wananchi wa Wilaya ya Ukerewe, watumie mbolea za minjingu na mbolea nyingine ambazo zinaweza kuongeza uzalishaji katika eneo lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la matunda, siyo suala la Ukerewe peke yake, mazao yote ya horticulture sasa hivi kama Wizara tunafanya baseline study ya kuangalia ni namna gani tunaweza kufanya zoning ya kila eneo ili tuweze kutambua ni mazao gani ya high value yatokanayo na horticulture yanaweza kuzalishwa. Wizara sasa hivi iko katika hatua za awali kuangalia ni namna gani sekta ya horticulture inaweza kupewa kipaumbele na namna gani mazao ya matunda na mboga mboga yanaweza kupewa kipaumbele kama zao la muhimu kwa ajili ya export katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwaombe Waheshimiwa Wabunge watupe muda, kabla ya mwaka wa fedha ujao tuta-unveil Sera ya Wizara ambayo itafanya diversification katika sekta nzima ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri limeonesha wavuvi na wadau 520 wamepata elimu hiyo lakini pamoja na kuwapa elimu watu hawa 520 hakuna mfumo rasmi unaoweza kusaidia hii elimu waliyoipata ku-disseminate kuwafikia wadau wengine ambao ni sehemu kubwa ya wakazi wa Jimbo la Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka jana alitembelea Jimbo la Buchosa akatumia mfumo mzuri sana kutoa elimu kwa wavuvi wa eneo lile. Swali la kwanza, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuja Ukerewe ili kwa pamoja tushirikiane kuwapa elimu wadau wetu hawa wavuvi waweze kujua hasa nini kinachopaswa kufanyika kwenye eneo la uvuvi kuwaondolea adhabu wanazopata bila kuwa na elimu ya msingi kujua wajibu wao ni upi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hatua iliyofikiwa na kikundi hiki cha Bugasiga ni nzuri na ilipelekea kupata mkopo wa shilingi milioni 250 na nina kila sababu ya kuipongeza Serikali kuwezesha jambo hili. Changamoto zilizopo ni kwamba mkopo huu unatolewa kwa ushirika unaolazimisha sasa dhamana inayotakiwa iwe ni kwa mtu mmojammoja na matokeo yake sasa mkopo unaonekana kama ni wa mtu mmoja na sio ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali kwa nini isitengeneze mfumo kwamba wadau hawa kupitia ushirika wapewe mikopo lakini sasa wao wenyewe waunde SACCOS ili SACCOS zile zikopeshe mdau mmoja mmoja na wawajibike kwa SACCOS halafu SACCOS ndio iwajibike kwenye ushirika? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukrani kwa Mheshimiwa Mbunge kutupongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri tuliyoifanya katika eneo la Kanda ya Ziwa ya kutoa elimu na akatolea mfano wa Jimbo la Buchosa ambalo hivi sasa tunacho Chama cha Ushirika cha Zilagula Fisheries Cooperative ambacho na chenyewe kimeomba mkopo wa shilingi milioni 300 na kitakwenda kupata kupitia TADB lakini na vyama vingine takribani milioni 50 kila chama shilingi milioni 10. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi la utoaji elimu ni endelevu na sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tupo tayari tutakwenda Ukerewe mara tu baada ya kuahirishwa kwa Bunge hili kwenda kutoa elimu ile kwa wavuvi wa pale Ukerewe ili waweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili linahusu juu ya mfumo wa mikopo kupitia ushirika na SACCOS. Naomba tulichukue wazo lake hili ni ushauri mzuri ambapo Wizara tutaufanyia kazi. Kwa kuwa tayari tunalo Dawati letu la Sekta Binafsi linalofanya kazi nzuri sana ya kuratibu mikopo hii na kuratibu namna ya kuweza kuwasaidia vyama vya ushirika, nataka nimhakikishie kwamba ushauri huu tunauchukua na tunakwenda kuufanyia kazi kwa maslahi mapana ya wadau wetu wa uvuvi ili waweze kusonga mbele. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Jimboni Ukerewe mwaka jana tarehe 5 Septemba, 2018, alitoa maelekezo ya ujenzi wa km 14 za lami kutoka Lugeze - Nansio mjini. Nataka kujua ni hatua ipi imefikiwa ili ujenzi huo uweze kuanza? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii ameifuatilia muda mrefu na matokeo yake niseme kwamba usanifu wa barabara hii umeshaanza ukikamilika tutajenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na matatizo makubwa ya kijiografia yaliyoko katika Visiwa vya Ukerewe yanayoathiri utoaji wa huduma za afya lakini tuna madaktari 3 pekee kati ya 10 wanaotakiwa, tuna waganga wasaidizi 5 pekee kati ya 43 wanaotakiwa na tuna wauguzi 80 pekee kati ya 289 wanaotakiwa. Nini kauli ya Serikali wanayoweza kuwaambia wananchi wa Ukerewe juu ya kuboresha huduma za afya kwa kutoa wahudumu wa afya kiasi kinachotakiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yana upungufu mkubwa wa watumishi, wakati tunaajiri hao 550 tutazingatia. Naamini na Ukerewe nao hatutawasahau, ipo nia kubwa kuhakikisha kwamba tunapunguza hilo pengo la upungufu wa watumishi. Naomba nimhakikishie Mbunge tutazingatia katika mgao.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza maswali ya nyoneza. Kwanza nipongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nitakuwa na maswali mawili, la kwanza kwa mujibu wa maelezo ya waziri, Wizara inafungua Ofisi za Kanda Mwanza pale zikijumuisha Idara ya Utalii pamoja na kodi ya utalii, lakini kuna taarifa kwamba TANAPA imegawa shughuli zake Kikanda, na moja ya Kanda hizo ni Kanda ya Kaskazini Magharibi na kwa mujibu wa taarifa tulizonazo ni kwamba uongozi wa bodi umeelekeza Ofisi za Kanda ziwe Bunda eneo ambalo ni jarani sana na Serengeti. Lakini ili kusaidia ukuzaji wa utalii kwenye maeneo ya Ukerewe, Saanane, Lubondo nakadhalika. Ni kwa nini Ofisi za TANAPA za Kanda hizi, Kanda ya Kaskazini Magharibi isiwe Mwanza ziliko Ofisi za Utalii pamoja na Bodi ya Utalii badala yake zipelekwe Bunda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kama Mheshimiwa Waziri alivyosema Wizara tayari imetambua uwepo wa vivutio vya utalii na sasa inahitaji kuviendeleza na kuvitangaza. Sasa ili kufanikisha hili ni kwa nini wizara sasa isiwekeze pesa pale Ukerewe kwa ajili ya maandalizi ya miundombinu lakini pamoja na ku-train wadau mbalimbali wakiwemo hizi local groups ambazo zimekuwa zikibainisha vivutio hivi ili kama maandalizi sasa ya kukuza na kutangaza utalii ulioko kwenye Visiwa vya Ukerewe? Nashukuru sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru kwa pongezi zake, kwa wizara ambazo amezitoa na kulidhika na majibu yake ya maswali ya msingi. Lakini Mheshimiwa Mkundi ameomba kufahamu kwamba TANAPA katika juhudi za kuboresha shughuli za kukuza na kusimamia uhifadhi na utalii wamefungua Ofisi Kaskazini Magharibi, lakini Ofisi hiyo wameipeleka Bunda badala ya Mwanza na ameshauri kwa nini Ofisi hiyo isikae Mwanza ambapo kuna Ofisi za TTB na Ofisi za utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge nitawasiliana na TANAPA na kuona sababu za msingi zilizowapeleka Bunda, lakini ninaamini kwamba ushauri wake ni wa msingi kwa sababu Mwanza bado ni kitovu cha Kanda ya Ziwa ambapo ingelikuwa rahisi zaidi kuwahudumia wateja kuliko Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wake wa pili swali langu la msingi limejibu kwamba baada ya kuziimarisha vituo hivi vyote vya mali kale tunajielekeza sasa kwenye kushirikiana na taasisi zetu mbalimbali ambazo tutazikabidhi kwenye maeneo mengi ili ziweze kuviambatanisha vituo hivi pamoja vivutio mbalimbali vya utalii kama nilivyosema Saanane na Lubondo. Kwa hiyo, nimuhakikkishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya vituo ambavyo tutahakikisha kwamba vinapata pesa kwa ajili ya uendelezaji na kwa ajili ya kuviimarisha itakuwa ni Ukerewe ili kuhakikisha kwamba Kisiwa cha Kirewe kinatumika kama Kisiwa cha utalii katika Ziwa Victoria.