Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joseph Michael Mkundi (15 total)

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Wilaya ya Ukerewe inajumuisha visiwa 38 na kati ya hivyo, visiwa 15 hutumika kwa makazi ya kudumu lakini huduma za kijamiii hasa afya siyo nzuri:-
(a) Je, Serikali inachukua hatua zipi za makusudi za kunusuru maisha ya watu hasa akinamama wajawazito na watoto wanaokufa kutokana na ukosefu wa huduma bora za afya katika visiwa hivyo?
(b) Je, ni lini Maabara katika kituo cha afya Bwisya katika Kisiwa cha Ukara itakamilika na kupewa wataalam ili kutoa huduma ya upasuaji kunusuru maisha ya wananchi wa kisiwa hicho na visiwa vya jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya utoaji wa huduma za afya Ukerewe zinatokana na jiografia ya eneo lenyewe kuwa linazungukwa na maji. Kwa kutambua hali hiyo, Serikali imejenga Hospitali ya Wilaya katika kisiwa cha Nansio, vituo vya afya viwili na zahanati 17. Hata hivyo, Serikali inatambua bado zipo changamoto ambazo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi kupitia bajeti za Halmashauri kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa wananchi wa kisiwa hiki hupelekewa huduma za afya kwa njia ya mkoba pamoja na kliniki ambazo huratibiwa na Madaktari pamoja na Wauguzi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto, Serikali imejenga jengo la upasuaji katika kituo cha afya cha Bwisya. Tayari kituo hicho kimepatiwa Daktari Msaidizi na Mtaalam wa dawa za usingizi ili kuanza huduma za upasuaji. Changamoto inayoendelea kushughulikiwa ni upatikanaji wa vifaa na nishati ya umeme na maji ambapo mpaka sasa shughuli za kuweka umeme katika kituo hiki zinaendelea.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI (K. n. y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Ni zaidi ya miaka mitano sasa tangu Meli ya MV Butiama isitishe huduma zake katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Nansio (Ukerewe) hali inayosababisha shida na usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa Ukerewe.
(a) Je, ni lini meli hiyo ya MV Butiama itatengenezwa na kuendelea kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta meli mpya sasa ikizingatiwa kuwa meli ya MV Clarius imechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, meli ya MV Butiama ambayo ilikuwa inatoa huduma ya usafiri majini kati ya bandari ya Mwanza na bandari ya Nansio - Ukerewe ilisitisha huduma hiyo mwaka 2010 baada ya engine yake kupata uharibifu mkubwa na kukatika muhimili wake (crankshaft). Kufuatia uharibifu huo tathmini ilifanyika na kubaini kuwa injini hiyo isingefaa tena kutumika kwa ajili ya usafirishaji wa aibiria na mizigo na kwamba inabidi iununuliwe engine mpya pamoja na gear box yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ya huduma za meli MSCL ilikamilisha mchakato wa kupata engine stahiki kwa ajili ya meli hiyo na gharama elekezi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli imetenga kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya matengenezo ya meli ya MV Butiama. Aidha, kulingana na tathmini iliyofanyika matengenezo ya meli hiyo yanategemewa kukamilika ndani ya miezi wa kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mipango thabiti ya kujenga meli mpya zitakazotoa huduma ya usafiri na usafirishaji katika Ziwa Victoria na maziwa mengine makuu ya Tanganyika na Nyasa. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi bilioni 21.0 ikiwa malipo ya awali ya asilimia 50 kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria.
MHE. JOHN W. HECHE (K.n.y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Ni miaka mitatu sasa tangu barabara ya Bunda – Kisorya - Nansio iwekwe katika mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami lakini ujenzi huo unasuasua tu.
(a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika?
(b) Je, Serikali ina kauli gani juu ya ujenzi wa daraja kati ya Kisorya (Bunda) na Lugezi (Ukerewe)?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nyamuswa (Bunda) - Kisorya - Nansio yenye urefu wa kilometa121.9 inaunganisha Mikoa ya Mara na Mwanza.
Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika awamu ya tatu; Nyamuswa - Bunda - Bulamba (kilometa 55); Bulamba – Kisorya (kilometa 51) na Kosorya - Nansio (kilometa 15.9) ikihusisha pia ujenzi wa daraja kubwa kati ya Kisorya na Lugezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hii umekamilika isipokuwa sehemu ya Kisorya - Nansio (kilometa 15.9). Ujenzi wa kiwango cha lami umeanza kutekelezwa Disemba 2013 kwa sehemu ya Bulamba - Kisorya (kilometa 51) na unaendelea. Hadi sasa ujenzi wa sehemu hii ya barabara umekamilika kwa asilimia 14. Hata hivyo, ujenzi wake umekuwa ukisuasua kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya mkandarasi. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha ili kukamilisha ujenzi wa barabara hii.Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeanza mipango ya ujenzi wa daraja kati ya Kisorya na Lugezi linalounganisha Mikoa ya Mara na Mwanza ambayo imekamilisha upembuzi yakinifu na kwa sasa usanifu wa kina unaendelea.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Ni zaidi ya miaka mitano sasa tangu Meli ya MV Butiama isitishe huduma zake katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Nansio (Ukerewe) hali inayosababisha shida na usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa Ukerewe.
(a) Je, ni lini meli hiyo ya MV Butiama itatengenezwa na kuendelea kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta meli mpya hasa ikizingatiwa kuwa meli ya MV Clarius imechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.6 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ili kufanya matengenezo makubwa ya meli ya MV Butiama iliyositisha kutoa huduma zake tangu mwaka 2010 kutokana na hitilafu kubwa ya injini zake. Zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo zilikwishatangazwa na sasa kazi ya uchambuzi wa kina inaendelea. Matarajio yetu ni mkandarasi kuanza ukarabati huo mwezi Machi, 2017 na kumaliza mwezi Novemba, 2017 (b) Kuhusu mpango wa kujenga meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuimarisha huduma ya usafiri wa majini katika eneo hilo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI alijibu:-
Kisiwa cha Ukerewe kina vivutio vingi vya utalii vinavyoweza kuiingizia nchi yetu pesa nyingi za kigeni vikiwemo mapango ya Handebezyo, Makazi ya Mtemi Rukumbuzya, Jiwe linalocheza la Nyaburebeka huko Ukara na kadhalika.
Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuimarisha na kujenga mazingira na kuvitumia vivutio hivyo ili kuongeza pato la Taifa na wananchi wa Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sura ya Nne aya ya 4.2.7 ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 - 2020/2021) unasisitiza pamoja na mambo mengine upanuzi wa wigo wa vivutio vya utalii na utalii utokanao na vivutio vya urithi wa utamaduni (The heritage tourism)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kuzihusisha Halmashauri husika inakamilisha orodha ya vivutio vyote vya utalii ikiwa ni pamoja na vivutio vya malikale nchini ili kuweka utaratibu wa kuvisajili, kuviboresha na hatimaye kuvitangaza na kuviuza kwa watalii wa ndani na wa nje. Zoezi hili linatengemea kukamilika mwaka wa 2017/2018. Vivutio vya mapango ya Handebezyo, Makazi ya Mtemi Rukumbuzya na Jiwe linalocheza la Nyaburebeka vilivyoko katika kisiwa cha Ukara katika Halmashauri ya Ukerewe ni miongoni mwa vivutio hivyo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Serikali imeondoa tozo mbalimbali zilizokuwa kero kwa wananchi katika sekta ya uvuvi lakini bado kuna mkanganyiko ni tozo zipi zimefutwa na zipi zinaendelea.
(a) Je, Serikali inaweza kuainisha aina ya tozo zilizoondolewa katika sekta ya uvuvi?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa mwongozo kwa watendaji wa Halmashauri juu ya mabadiliko hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na kutekeleza Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuweka mazingira mzuri katika kuwezesha wavuvi na wawekezaji kuendesha biashara ya uvuvi kwa ufanisi.
Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 katika hotuba yake alielekeza kupitia na kuangalia tozo zote ambazo ni kero kwa wananchi ili ziondolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inaelekeza kuwezesha wavuvi wadogo kwa kuwaondolea kero mbalimbali zikiwemo tozo zisizo na tija. Ili kutekeleza maelekezo haya, wizara yangu katika Bunge la Bajeti ya mwaka 2017/2018 ilitangaza kuondoa ada na tozo mbalimbali ambazo zilionekana kuwa kero katika sekta ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada na tozo zilizoondolewa katika sekta ya uvuvi ni kama ifuatavyo:-
• ushuru wa kaa hai (waliozalishwa na kunenepeshwa) wanaouzwa kwenda nje ya nchi.
• Tozo ya cheti cha afya baada ya kukagua mazao ya uvuvi shilingi 30,000.
• Ada ya ukaguzi wa kina wa kiwanda/ghala kila robo mwaka shilingi 100,000.
• Tozo ya usafirishaji samaki yaani movement permit kuanzia kilo 101 hadi kilo 1000 shilingi 5,000; kilo 1001 hadi kilo 5000 ni shilingi 10,000; kilo 5001 hadi kilo 9999 shilingi 30,000; zaidi 10,000 na zaidi shilingi 50,000.
• Ada ya usajili wa chombo cha uvuvi chini ya mita 11 kwa wavuvi wadogo shilingi 20,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha mabadiliko ya tozo katika sekta ya uvuvi inatekelezwa na watendaji wa Halmashauri, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wizara ya TAMISEMI imeshatoa maelekezo kwa Halmashauri husika kusitisha mara moja tozo ambazo zimefutwa na Serikali. Aidha, Wizara Wizara inafanya marekebisho katika Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 ili kuendana na mabadiliko hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kupitia Halmashauri zetu kuhakikisha kuwa maagizo haya kuhusu tozo zilizoondolewa na Serikali yanatekelezwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Watumishi walio maeneo ya pembezoni mwa nchi ikiwemo Wilaya ya Ukerewe wanafanya kazi katika mazingira magumu, mfano walimu wa watumishi wa afya.
Je, Serkali ina mpango gani wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa maeneo ya pembezoni?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba watumishi walio katika Halmashauri zilizo katika maeneo ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Ukerewe hufanya kazi katika mazingira magumu na upungufu mkubwa wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010 Serikali ilipitisha Sera ya Malipo ya Mishahara na Motisha katika utumishi wa umma ambayo miongoni mwa malengo yake mahsusi ni kuwavutia, kuwapa motisha na kuwabakiza watumishi katika utumishi wa umma. Lengo ni kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi katika Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza sera hii mwaka 2012/2013 Halmashauri 33 za Wilaya, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ziliwezeshwa kuandaa miongozo ya kutoa motisha kwa watumishi wake. Kutokana na zoezi hilo Halmashauri 29 ziliandaa na kuwasilisha katika ofisi yangu miongozo iliyoabainisha aina za motisha zinazohitajika kwa ajili ya watumishi wake. Utekelezaji wa miongozo hiyo kwa Halmashauri zote 29 ulikadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 331.087 kwa mwaka, ambapo kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 314.372 kilihitajika kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni 16.761 kilihitajitaka kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miongozo hii ulitarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2013/2014. Hata hivyo, utekelezaji wa miongozo hii haujaanza kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Uwepo wa mawasiliano ya uhakika kati ya Visiwa vya Ukerewe na Mkoa wa Mara ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe na hatua kadhaa zimeshachukuliwa kuhakikisha daraja kati ya Lugezi na Kisorya linajengwa. Je, ni hatua ipi inachukuliwa na Serikali kuhakikisha daraja hilo linajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali, naomba uniruhusu nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumshukuru Mungu kwa kukurejesha na afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha mawasiliano kati ya visiwa vya Ukerewe na mikoa mingine, imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara yote ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya – Nansio (Ukerewe) yenye urefu wa kilometa 118.
Aidha, usanifu umejumuisha madaraja mawili ya Lugezi yenye urefu wa mita 600 na mita 450 yanayounganisha Kisorya na Nansio pamoja na maandalizi ya nyaraka za zabuni. Kazi ya usanifu imekamilika na ujenzi kwa kiwango cha lami kati ya Bulamba hadi Kisorya katika barabara hii unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo, pamoja na madaraja mawili kati ya Kisorya na Nansio ili kuunganisha Kisiwa cha Ukerewe na Mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza.
MHE. PAULINE P. GEKUL (K.n.y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka umeme katika Vijiji vya Kakerege na Nkilizya vilivyopo Nansio Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Nkilizya kina vitongoji saba (7) na kati ya vitongoji hivyo vitatu (3) vya Magereza, Kenonzo na Lwocho, vilipata umeme mwaka 2005 kupitia utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme Nansio Wilayani Ukerewe kutoka Wilaya ya Bunda ambapo wateja 60 waliunganishiwa umeme. Vitongoji viwili (2) vya Namalebe na Chamatuli vilipatiwa umeme mwaka 2012 kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na jumla ya wateja 47 wameunganishiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, vitongoji vingine viwili (2) vya Mumakeke na Bubange vya Kijiji cha Nkilizya visivyokuwa na umeme, pamoja na Kijiji cha Kakerege vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa kwa sasa. Kupitia utekelezaji wa mradi huu, jumla ya vijiji 35 katika Wilaya ya Ukerewe vitapatiwa umeme. Kampuni ya Nipo Group Limited aliyepewa kazi za Mradi wa REA III katika Mkoa wa Mwanza anaendelea na utekelezaji mradi huo na mradi unatarajiwa kukamilika Juni, 2019.
Mheshimiwa Spika, kazi za Mradi wa REA III Ukerewe zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 78.32; njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 156; ufungaji wa transfoma 78 za KVA 50 na 100; pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 2,640. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 9.28.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Nansio) inakabiliwa na msongamano wa Wagonjwa; Mwaka 2002 Halmashauri ya Wilaya ilitumia zaidi ya shilingi milioni 200 kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Nakutunguru kama njia ya kupunguza msongamano huo. Hata hivyo, ujenzi huu haujakamilika kutokana na ukosefu wa fedha:-
Je, Serikali ipo tayari kuondoa upungufu uliopo ili Kituo hicho kianze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kupitia fedha za Ruzuku ya Maendeleo kwa Serikali za Mitaa yaani (Local Government Development Grant) mwaka 2012 kwa ajili ya kuanza kwa awamu wa kituo cha Afya Nakatunguru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo hilo OPD ulikamilika mwezi Aprili, 2015 na lilizinduliwa rasmi tarehe 18 Februari, 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Mpaka sasa kituo hiki kinafanya kazi kwa kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) na huduma za Mama, Baba na Mtoto (Reproduction and Child Health (RCH).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa Fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imeidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi wa Kituo hiki. Kwa sasa Serikali ipo katika awamu ya nne ya utekelezaji wa mpango wa ukarabati wa Vituo vya Afya nchini, hivyo tutakiingiza Kituo cha Afya Nakutunguru katika awamu zijazo ili kuhahakisha kinakamilika na kutoa huduma zote ikiwemo huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji wa Miyogwezi uliopo katika Kijiji cha Igongo, Ukerewe ni tarajio kubwa la suluhu ya upungufu wa chakula, zaidi ya miaka mitano sasa toka kufanyika uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 700 bado mradi huo umetelekezwa:-

(a) Je, kwa nini Serikali imetelekeza mradi huo?

(b) Je, nini kauli ya Serikali kuhusu uendelezwaji wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali haijautelekeza Mradi wa Kilimo cha Umwagilia wa Miyogwezi, bali mradi huo umesimama kutokana na muda wa utekelezaji wa mradi wa DASIP uliokuwa unafadhili mradi huo kumalizika kabla ya Mradi wa Miyogwezi haujakamilika. Mradi wa Miyogwezi ulitekelezwa kupitia mradi wa District Agriculture Sector Investment Project yaani (DASIP) ambao jumla ya shilingi 695,784,852.50 zilitumika. Utekelezaji wa mradi huo ulihusisha ujenzi wa mabanio mawili na mifereji mikuu yenye urefu wa kilometa 3.15 ambapo kilometa 1.1 zilisakafiwa. Ujenzi wa mabanio mawili katika mto wa kudumu yaani perennial river wa Miyogwezi na katika mto wa msimu wa Mriti. Hadi kukamilika kwa muda wa Mradi wa DASIP mwezi Disemba, 2013 ujenzi wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 76. Aidha, uendelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na Serikali kujipa muda wa kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa miradi yote ya DASIP ili kupima ufanisi wake ulivyotekelezwa.

(b) Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mradi wa Miyogwezi na miradi mingine ya umwagiliaji nchini inakamilika, Serikali imekamilisha mapitio ya mpango kabambe wa umwagiliaji wa mwaka 2002 kwa kuzingatia mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali maji yaani (Integrated Water Resource Management) ili kubaini maeneo yanayofaa kwa uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji yakiwemo mabwawa, visima vifupi na virefu vya chini vya ardhini, pamoja na hali ya skimu zote za umwagiliaji nchini.

Mheshimiwa Spika, mapitio ya mpango huo pia yamebaini miradi yote ya umwagiliaji ambayo haifanyi kazi na ambayo ujenzi wake haujakamilika katika kipindi kilichopita ikiwemo Mradi wa Miyogwezi. Aidha, Mradi wa Umwagiliaji wa Miyogwezi ni miongoni mwa miradi ya umwagiliaji itakayotekelezwa katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2023.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na.22 ya mwaka 2003, Dagaa wanapaswa kuvuliwa kwa wavu wenye matundu mm 8 – mm10, lakini sheria hii haijazingatia aina tofauti za dagaa:-

Je, kwa nini Serikali isifanye utafiti utakaoainisha matumizi ya nyavu kutegemea aina ya dagaa wanaopatikana kwenye Ziwa husika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina jukumu la kulinda, kuhifadhi na kuendeleza na kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi hapa nchini zinavunwa kwa busara ili ziwe endelevu kwa manufaa ya kiuchumi, kijamii na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria na kanuni zinazosimamia uvuvi nchini zinalenga uvuvi unaofanyika uwe endelevu ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) hufanya tafiti ili kubaini athari za matumizi ya dhana na mbinu mbalimbali za uvuvi kwa rasilimali za uvuvi na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 66(1)(k) cha Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 kinaeleza kuwa nyavu za dagaa zenye ukubwa wa machi chini ya milimita nane zimakatazwa kutumika kwa uvuvi wa dagaa katika maji baridi ikiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Aidha, tafiti zilizofanyika katika Ziwa victoria zinaonesha kuwa aina moja tu ya dagaa anayejulikana kwa jina la kitaalam Rastrineobola argentea. Utafiti pia unaonesha nyavu zenye macho kuanzia milimita nane zikitumika kuvua dagaa hawa Ziwa Victoria zitavua dagaa waliopevuka na matumizi ya nyavu zenye matundu chini ya milimita nane zikitumika zitavua dagaa wachanga na hii itaathiri uvuvi wa dagaa katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Uvuvi na Kanuni zake imezingatia aina ya dagaa katika maji baridi na maji bahari. Aidha, TAFIRI itafanya utafiti ikiridhika kuna haja ya kufanya hivyo katika Ziwa Victoria kuhusiana na uvuvi wa dagaa. Serikali inaendelea kusisitiza wavuvi kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Kutokana na ufinyu wa ardhi na ongezeko la watu kwenye visiwa vya Ukerewe, pamoja na ardhi kutokuwa na rutuba, kumesababisha Kilimo kisicho na tija:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya utafiti wa kisayansi ili kuwashauri wananchi wa Ukerewe aina ya mazao yanayopaswa kulimwa na jinsi ya kutumia eneo dogo la ardhi kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ni kufanya utafiti wa tabaka na afya ya udongo katika kanda zote saba za kiikolojia za kilimo nchini, ikiwemo kanda ya Mwanza. Utafiti huo wa kisayansi unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo mbalimbali pamoja na kubaini mimea na mazao yanayostawi kwenye udongo husika ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Ukerewe ambayo wananchi wengi hulima mihogo, mpunga, mtama, mahindi, viazi vitamu na machungwa, utafiti wa awali unaonyesha kwamba, udongo wake una mboji kiasi kidogo cha asilimia 1.3 ukilinganisha na kiwango cha asilimia 2.5 ambacho ndicho kiwango cha mboji katika udongo wenye rutuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile utafiti umeonyesha kwamba kiwango cha tindikali kwa maana ya pH ni 5.4 ukilinganisha na pH ya 6.6, kiwango ambacho kinafaa kwa mimea ya kufyonza virutubisho kutoka kwenye udongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa kiasi hicho cha tindikali katika maeneo hayo kunaashiria kwamba kuna upungufu wa virutibisho vya nitrogen, phosphorus, potassium, sulphur, calcium na magnesium. Aidha, kulingana na matokeo hayo, inashauriwa kutumia mbolea zenye virutubisho vya nitrogen, potassium, phosphorus, sulphur, calcium na magnesium, ambazo ni pamoja na Minjingu, mazao ya ramila, samadi na CAN, UREA na DAP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sampuli za udogo zimechukuliwa katika kanda na mkoa mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Mwanza unaojumuisha Wilaya ya Ukerewe kwa lengo la kubaini viwango vya virutubisho vilivyopo katika sampuli hizo ambapo kwa sasa tathmini ya kina inaendelea kufanyika katika maabara ya TARI, Selian.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kukamilika kwa tathmini hiyo kutasaidia kushauri wakulima kuweka viwango vya mbolea vinavyohitajika kulingana na virutubisho stahiki kwa mazao husika na aina ya mazao na yanayopaswa kulimwa katika maeneo husika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, ni vikundi au wavuvi wangapi katika Kisiwa cha Ukerewe wamepewa elimu na mitaji ili waweze kufanya uvuvi wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa wavuvi wa Kisiwa cha Ukerewe juu ya uvuvi endelevu, matumizi ya zana na mbinu bora za uvuvi zinazokubalika kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na madhara yatokanayo na uvuvi haramu. Lengo la elimu hiyo ni kuwawezesha wavuvi wadogo wa kisiwa cha Ukerewe kufanya uvuvi endelevu na hivyo kunufaika na rasilimali za uvuvi zilizopo katika maeneo yao. Zaidi ya wavuvi wadogo na wadau wengine wa uvuvi wapatao 520 kutoka visiwa vya Ghana, Kunene, Lyegoba na Hamukoko katika Halmashauri ya Kisiwa cha Ukerewe walipatiwa elimu hiyo kwa njia ya mikutano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kuwezesha wavuvi kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kununua zana bora za uvuvi wakiwemo wavuvi wa Kisiwa cha Ukerewe. Ili kuwezesha wavuvi kunufaika na fursa hiyo, Serikali imeendelea kuwahamasisha wavuvi wadogo nchini wakiwemo wa Kisiwa cha Ukerewe, kuunda na kujiunga katika Vikundi vya Ushirika vya Wavuvi na Vyama vya Akiba na Mikopo ili kuwasaidia wavuvi kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Aidha, hadi sasa jumla ya shilingi million 250 zipo katika hatua ya mwisho ya kutolewa kwa wavuvi wa Kisiwa cha Ukerewe kama mkopo kupitia Chama cha Ushirika cha Bugasiga kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhamasishaji huo umewezesha kuanzishwa kwa Chama cha Ushirika cha Wavuvi katika Kisiwa cha Ukerewe, visiwa vidogo vya Ghana, Kunene, Lyegoba na Hamukoko ambacho kipo katika hatua za usajili. Uanzishwaji wa chama hiki utawezesha wavuvi kutoka Kisiwa cha Ukerewe kupata mikopo kwa urahisi kutoka Taasisi za Kifedha na hivyo kufanya uvuvi wenye tija.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Visiwa vya Ukerewe bado havitumiki ipasavyo kama eneo mahsusi kiutalii ingawa vimo vivutio vingi vya utalii ikiwemo jiwe linalocheza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na vikundi kama vile vya mila na desturi Ukerewe (KUMIDEU) katika kukitangaza Kisiwa cha Ukerewe kama eneo la utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua kuwa Ukerewe ni miongoni mwa Visiwa vichache nchini vyenye rasilimali mbalimbali ikiwemo fukwe nzuri, utalii wa utamaduni pamoja na jiwe linalocheza. Vivutio hivi kwa miaka ya hivi karibuni vimekuwa vikivutia wageni wengi kutembelea maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wizara inaendelea na zoezi la kuainisha vivutio vya utalii kwa dhumuni la kuviendeleza pamoja na kuvitangaza. Katika mwaka wa Fedha wa 2019/2020 tunatarajia kutekeleza zoezi hilo hilo katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza. Kazi hiyo hutekelezwa kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa, Wilaya, Vijiji na wadau wa Sekta ya Utalii katika maeneo hayo, hivyo nimjulishe Mheshimiwa Mbunge, zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa katika Mkoa wa Mwanza, Wataalam wangu watapita katika Kisiwa cha Ukerewe ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na kikundi cha Mila na Desturi cha Ukerewe cha (KUMIDEU)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hilo ni juhudi za makusudi za Wizara yangu za kupanua wigo wa mazao ya utalii kwa kubainisha vivutio vya utalii wa asili sehemu mbalimbali nchini. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa kusimamia na kuendeleza Sekta ya Utalii Kanda ya Ziwa, Wizara ilifungua Ofisi ya Kanda iliyohusisha Idara ya Utalii na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika Jiji la Mwanza. Lengo likiwa ni kusogeza kwa karibu huduma kwa wadau wa Sekta ya Utalii walio katika Kanda ya Ziwa na maeneo jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake za kuhakikisha Sekta ya Utalii inazidi kuendelea na kukua hususani katika Kisiwa cha Ukerewe na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla. Ifahamike kwamba Sekta ya Utalii ni Mtambuka na hivyo kazi ya uendelezaji sekta hii inahitaji juhudi za pamoja za wadau wa Sekta hii, Umma na Binasfsi. Hivyo, Wizara yangu itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa Sekta ya Utalii kuendeleza utalii nchini ahsante.