Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Grace Victor Tendega (18 total)

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kuwa REA III imeanza Machi, 2017. Kwa kuwa wananchi katika vijiji hivyo vya Wangama, Ikuvilo, Tagamenda, Lupembelwasenga pamoja na Lyamgungwe ni wakulima na wanajihusisha na kilimo cha umwagiliaji na kuna wawekezaji ambao wameonesha nia ya kujenga viwanda na tunasema tunahitaji Tanzania ya viwanda lakini umeme haupo. Naomba commitment ya Serikali ni lini watapata umeme kwa sababu imekuwa ni muda mrefu kutopatiwa umeme katika maeneo hayo ili wanufaike na viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika kipengele
cha kwanza majibu ya Waziri ni tofauti kabisa na hali halisi ya eneo hilo la Malulumo kwa sababu mimi natokea eneo hilo na wanasema utekelezaji umefanyika kwa 90%. Je, Waziri yuko tayari kuongozana na mimi akaone huo utekelezaji wa 90% uliopo maeneo yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na swali la pili, niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Grace kwenda kwenye eneo lake ili kuangalia utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Grace tukimaliza Bunge tu mguu mmoja mimi na wewe Iringa tukamalize kazi hiyo, lakini kwa ruhusa yako Mwenyekiti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Grace na Wabunge wote wa Mkoa wa Iringa kwa jinsi ambavyo wanafuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme. Niwahakikishie kwamba tarehe 21 Machi, 2017 tulizindua rasmi utekelezaji wa Mradi wa Umeme Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Iringa na eneo la Iliwa kwa Mheshimiwa Mwamoto ndipo tulipofanyia uzinduzi kwa niaba ya mkoa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie kabisa Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Iringa pamoja na Mufindi, Kilolo, Njombe, tumeshawakabidhi wakandarasi wawili, NACROI na NAMIS na wameshaanza utekelezaji wa kazi hiyo. Kwa hiyo, kuanzia Machi tumeshaanza kutekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji ambavyo amevitaja Mheshimiwa Grace vya Wangama, Lupembelwasenga, Tagamenda na Mseke pamoja na vijiji vingine ambavyo amevitaja na kwa Mheshimiwa Mwamoto vitapatiwa umeme katika awamu hii ya mradi. Nimeenda kwa Mheshimiwa Mwamoto na Waheshimiwa Wabunge wengine, nimeenda Nang’uruwe, Kihesa Mgagao na huko tumeshawapelekea umeme. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba utekelezaji wa mradi huu umeanza na utakamilika mwaka 2020/2021.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nitoe masikitiko makubwa sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, ambapo tarehe 8 Juni, 2016 niliuliza swali kuhusu vijiji na kata hizo hizo na aliyekuwa Naibu Waziri na sasa ni Waziri mwenye dhamana TAMISEMI alinipa majibu ambayo yalikuwa yanaeleza kwamba vijiji hivyo vimetengewa bajeti ya shilingi milioni 49.5 ambayo itatekelezwa mwaka 2016/2017. Mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea, ni Bunge hili hili ambalo linatoa majibu hayo na leo tena nimepewa asilimia hiyohiyo 49.5 kwamba itatekelezwa 2018/2019. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa wananchi hawa, toka mwaka 1995 mpaka leo ni upembuzi yakinifu unafanyika, ni lini hawa wananchi watapata maji? (Makofi)
MheshimiwaMwenyekiti, swali la pili, ni kwa nini hawakufanya upembuzi wa kina wakati bajeti ilitengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, ni kweli kwamba usanifu wa kina haukufanyika ule wa zamani, lakini kwa sasa tunatarajia usanifu kina utafanyika mwaka 2018/2019 kwa ajili ya utekelezaji wa kumaliza kabisa matatizo ya maji kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ambalo lilikuwa ndiyo la kwanza, ni kwamba kazi ambazo zimefanyika kuanzia 2016 mpaka Desemba, 2017 nimesema hapa kwamba tumejenga visima sita katika Kata za Magulilwa, Luhota, Maboga na Mgama. Hii kazi imefanyika na taarifa hizi zimetoka kule kule kwenye Halmashauri yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taarifa za kina zaidi namuomba sana tushirikiane naye baada ya kikao hiki ili tuweze kushauriana vizuri namna bora ya kuhakikisha kwamba tunamaliza matatizo ya wananchi kwenye maeneo hayo.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kabisa yanaonyesha jinsi ambavyo walimu wetu wamekuwa wakikosa nyumba za kuishi, walimu wa sekondari 52,000 hawana mahala pa kuishi na walimu 130,300 wa shule za msingi hawana nyumba za kuishi. Tumesema tunataka kuwa na elimu bora katika nchi yetu na hatufahamu walimu wanaishi wapi.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka sasa wa kuamuru Jeshi la Polisi liweze kujenga nyumba hizi za walimu kama walivyofanya kwa Mererani kuzuia ile migodi yetu, tatizo hili ili liweze kuisha kwa haraka?
Swali la pili, walimu wamekuwa wakikosa udhamini katika mabenki mbalimbali kwa kutokuwa na mali za kudhaminiwa na taasisi alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri ni hizo ambazo huwezi kudhaminiwa kama huna dhamana ya vitu visivyohamishika kama viwanja, magari na vitu vingine na tunatambua hali za walimu wetu zilivyo.
Je, sasa Serikali haioni haja kwamba ni wakati muafaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iweze kuwa dhamana kwa walimu wetu wakati bado wakiwa kazini na siyo baada ya kustaafu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nisisitize kwamba katika jibu langu la msingi ile takwimu niliyoitaja kwa faida ya Bunge lako tukufu haikumaanisha kwamba walimu hao hawana makazi kabisa. Nimesema kwamba walimu hao wanaishi katika aidha, nyumba za kupanga au nyumba zao binafsi, hilo ndilo jibu langu la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ya swali lake kwamba kwa nini Serikali isiamuru Jeshi la Polisi kujenga nyumba za walimu nchi nzima, hilo ninaomba sana majeshi yetu yana kazi zake maalum ambayo yamepewa kufanya na waliojenga ukuta wa Mererani siyo Jeshi la Polisi ni Kitengo cha Ujenzi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Tumekuwa tukiwapa kazi nyingi sana, SUMA JKT kujenga nyumba za walimu kujenga nyumba za walimu katika mahali pengi. Hata kwake kule Iringa tumewapa sehemu nyingi tu SUMA JKT kujenga nyumba na tutaendelea kuwapa mikataba ya kujenga nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kwamba ujenzi wa nyumba ambao unafanywa na Serikali utaendelea kuwa kidogo kidogo kwa sababu unategemea sana bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, napenda nimuondoe wasiwasi kuhusu dhamana. Karibu mabenki yote na taasisi zote zinazokopesha hakuna dhamana zaidi ya mshahara wa mtumishi. Kinachotakiwa tu ni kwamba mtumishi asiwe anadaiwa mikopo mingine hilo ndiyo jambo la msingi, kama mtumishi hadaiwi mikopo mingine anao uwezo wa kukopa na ataamua mwenyewe, je, akope kwa kurejesha miaka mitatu au akope kwa kurejesha miaka 10 au akope kwa kurejesha miaka 25 ni yeye mwenyewe katika makubaliano ya fomu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuwasisitiza watumishi wote nchi nzima na Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wako chini yangu nataka niwaambie kwamba mikopo hiyo ya watumishi ipo, waingie makubaliano maalum na hizo taasisi na mabenki ili kusudi watumishi waweze kukopesha waweze kujenga nyumba zao binafsi. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Ibofwe uko Mkoani Iringa ambao unahudumia vijiji 10. Nilikwishauliza swali la msingi nikajibiwa kwamba shilingi milioni 49 zitatolewa baada ya kutoka certificate. Certificate ilishatolewa pesa hazijapatikana toka mwaka jana, naomba kujua ni lini pesa hizo zitatolewa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitumie nafasi hii kumjibu Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa maji ni uhai na sisi kama Wizara ya Maji hatupo tayari kupoteza uhai wa wana Iringa, namuomba Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge tukae na wataalam wetu tuangalie namna ya kuzipeleka fedha hizo wananchi wapate maji.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nasikitika Waziri anavyojibu, anaingiza suala la Mbunge wa Jimbo wakati mimi niliuliza swali langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, majibu ya Waziri hayajaniridhisha kabisa. Kuna vijiji vya Kimala, Idete, Uluti, Nyamuhanga, Ibofwee na Itimb. na vingine ambavyo sijavitaja wanajihusisha sana na kilimo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzalisha zao la mbao, ambayo yote haya yanahitaji mawasiliano kwa ajili ya kupata soko. Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa wananchi hawa wanapata mawasiliano ili waweze kuuza mazao yao na kupata masoko wanayoyahitaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Waziri amesema minara hiyo imejengwa na inatoa huduma kama kawaida, yuko tayari twende akaone hiyo minara anayosema inatoa huduma ili ahakikishe mwenyewe kwamba huduma hiyo haipatikani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Tendega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuondoe masikitiko kwa sababu hizi shughuli tunazifanya kwa kuwa tunazijua na tumeshatembelea na kufanya survey ya kutosha nchi nzima kujua maeneo gani yana shida ya mawasiliano critical na eneo gani ambalo lina shida ya mawasiliano ya kawaida ambayo yanahitaji kuongezewa coverage na ni maeneo gani ambayo yana shida za mawasiliano kwa vipindi tu vifupi kutokana na kufungiwa solar badala ya umeme wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujibu maswali yake kuhusu eneo la Kimala, Kidete na vijiji vinavyohusiana, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya ziara baada ya Bunge hili la bajeti kwenye maeneo yote pamoja na maeneo ya Kata nzima ya Kising’a najua kuna changamoto za mawasiliano, lakini nitafanya ziara kwenye Kata ya Mahenge, maeneo ya Magana na Ilindi ambako kuna shida kabisa ya mawasiliano, vilevile nitafanya ziara kwenye Kata ya Ibumu kwenye Kijiji cha Ilambo kuangalia kuhusu changamoto ya mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nitakuwa tayari kuongozana naye pamoja na Mbunge wa Jimbo kuangalia maeneo hayo. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda Serikali isikwepe wajibu wake wa kuhudumia watu wasiojiweza. Natambua kabisa kuwa kuna walemavu wenye uwezo lakini watu wengi wenye ulemavu wana matatizo mengi; kuna wale ambao ni yatima, kuna wengine ambao wametelekezwa na kuna wengine ambao kaya zao ni maskini sana. Ni kwa nini Serikali isiwajibike kuwahudumia watu hawa wenye ulemavu hasa kwa kuwatambua na pili kuwapatia bima ya afya bure? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema wagonjwa kuna wagonjwa wengi sana wa msamaha ambao wako katika hospitali zetu. Sawa wako wagonjwa wengi lakini ni lini Serikali sasa itatekeleza wajibu wake wa kutoa ruzuku katika hospitali zetu za mikoa au hospitali zetu za rufaa kwa sababu hawa wagonjwa ambapo wengine ni watu wenye ulemavu, watoto umri chini ya miaka mitano na wazee wanakwenda katika hospitali hizi kutibiwa na hizi hospitali zinakuwa na watu wengi ambao wanatakiwa kupata vifaatiba na vitendanishi? Ni lini Serikali itatoa ruzuku katika hospitali zetu ili ziweze kujikimu na kutoa huduma bora? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kutoa huduma za afya na haijawahi kusitisha kutoa huduma ya afya kutokana na sababu eti kwamba mtu anashindwa kugharamia matibabu. Hilo lipo vizuri ndani ya Sera yetu ya Afya na kuna makundi ambayo tumeyaainisha katika sera ambapo watu wanapata matibabu bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la walemavu kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, si kila mlemavu hana uwezo wa kupata matibabu, nataka niweke msisitizo. Ndiyo maana nimesema katika Sera hii Mpya tutaweka utaratibu mzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya sasa kati ya asilimia 60 - 70 ya wagonjwa ambao wanafika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya wanapata matibabu bure. Sasa hivi tunataka tuweke mfumo mzuri na kuhuisha na mifumo mingine kama ile ya TASAF kuhakikisha kwamba tunawatambua tu wale ambao kweli hawana uwezo na wanahitaji kupata matibabu. Tutakapokuja na huu utaratibu wa bima ya afya kwa wananchi wote tutakuwa na kundi dogo sana ambalo limebaki ambalo litakuwa linagharamiwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza kwa nini Serikali haipeleki ruzuku. Nimthibitishie Mheshimiwa
Mbunge na bahati nzuri naye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na analijua na hivi karibuni tumetoa taarifa ya utekelezaji ya nusu mwaka, Serikali inapelekea mishahara hatujashindwa kupeleka mishahara, dawa na hela ya uendeshaji. Hakuna hospitali ya rufaa ya mkoa ambayo haijapata huduma zote hizo ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna vyanzo vingi vya mapato ndani ya hospitali. Pamoja na ruzuku ya Serikali tuna fedha za papo kwa papo, fedha za bima na nyingine zinapata basket fund. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ninapozungumza watoto njiti nina maana wanazaliwa kabla ya miezi tisa haijatimia:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; dawa ya kusaidia mtoto ili aheme vizuri inayoitwa surfactant inauzwa shilingi laki sita kwa dozi moja na inategemea hali ya mtoto ambayo amezaliwanayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama una mtoto mmoja shilingi laki sita, kama umejifungua watoto wawili ni shilingi 1,200,000/=. Na watoto walio wengi wanatoka katika familia zenye hali duni na kipato cha hali ya chini, kama wanashindwa tu kwenda nao kliniki itakuwa na hii shilingi laki sita. Je, sasa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, dawa hizi zinatolewa bure, ili kunusuru maisha ya watoto hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba, likizo ni siku 84 kwa mtoto mmoja na siku 100 kwa watoto mapacha, lakini hawa ni watoto njiti. Kama amejifungua kabla ya miezi tisa tusema miezi saba ina maana kuna miezi miwili ambayo iko kabla ya miezi ile tisa. Sasa je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, wazazi wote wawili, baba na mama, wanapata likizo yenye malipo kwa miezi hiyo iliyopo kabla ili waweze kutunza hawa watoto njiti? Asante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Grace tendega kwa swali lake zuri. Na nianze kwa kutoa tafsiri ya mtoto njiti, watoto njiti wako katika makundi mawili; kuna wale ambao wamezaliwa kabla ya wiki 37 na kuna wale ambao wanazaliwa na uzito mdogo kuliko ule ambao tunatarajia, kwa maana ya kilo 2.5 kwa hiyo, wote hawa tunawaweka katika group hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, watoto ambao wanazaliwa njiti mara nyingi wanazaliwa na changamoto mbalimbali, hususan wale ambao wamezaliwa kabla ya umri wa wiki 37. Na moja ya changamoto ambayo wanayo ni matatizo ya kupumua, mapafu yanakuwa hayajakomaa na wanahitaji dawa ambayo ni surfactant kukomaza yale mapafu. Na nikiri kweli, gharama za surfactant ni kubwa na sisi kama Seriakali tumeliona hilo, tunajaribu kuliangalia utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, tunatoa afua kwa akinamama ambao wamezaa watoto njiti. Hatutaweza kuitoa bure, lakini tutaweka utaratibu ambao unaweza ukapunguza gharama katika utaratibu ambao tunao sasa hivi wa kuagiza dawa moja kwa moja kutoka viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linahusiana na kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa wazazi ambao wana watoto njiti:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, watoto njiti wanazaliwa wakiwa na changamoto nyingi pamoja na matatizo ya kupumua, wengine wanazaliwa na viungo bado havijakomaa, ikiwa ni pamoja na ubongo na wengine wanaweza wakapata matatizo mengine endapo hawatapata matunzo ya karibu. Lakini jiwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, sasa hivi kwa mujibu wa teknolojia watoto ambao wanazaliwa hata akiwa na wiki 22 kwa maana ya miezi mitano, wana uwezo mzuri sana wa kuweza kukua na kuishi vizuri. Na mtoto ambaye ameweza kuzaliwa na…

MWENYEKITI: Muda, muda.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalotaka kulisema kwa kifupi tu kwamba, Serikali inaweza ikaliangalia suala hili kwa maana ya kuwa, pale kama mtoto ana matatizo mzazi anaweza akawa anapewa ruhusa kwa mujibu wa kanuni na taratibu ambazo tunazo.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona, barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Wilaya ya Kilolo kilometa 133 ambayo kuna kipande cha Jimbo la Kalenga napo kuna changamoto ya barabara mvua zimenyesha barabara nyingi zinakuwa hazipitiki vizuri wananchi wanapata adha na mazao yao yanashindwa na ni ahadi ya Rais ambayo alitoa kwamba kufikia 2020 itakuwa imetengenezwa.

Ni lini sasa Serikali itahakikisha barabara hii inatengenezwa na wananchi wanapita bila matatizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba kipindi hiki tumepata mvua myingi sana na uharibifu wa miundombinu umekuwa ni mkubwa sana, sisi
kama Seriikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunakwenda kufanya urejeshaji wa miundombinu hii. Niseme tu kilometa 4217 hadi Desemba zimekuwa na hali mbaya hizi ndiyo barabara katika nchi tunaendelea na uratibu nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira tumeshatambua maeneo yote yenye shida na tunahitaji fedha za ziada kwenda kufanya marejesho ya miundombinu ya barabara.

Kwa hiyo, wananchi wavute subira sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na wenzetu upande wa Serikali za Mitaa kwa maana TARURA tunafanya uratibu wa pamoja ili tuhakikishe kwamba tunaenda kufanya uridhishaji maeneo mbalimbali ya nchi maeneo ambayo yameharibiwa na mvua, ahsante sana. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona pamoja na ukosefu wa nyumba za walimu katika Jimbo la Kalenga ni mwaka wa nne sasa walimu hawa hawajapandishwa madaraja na wamekuwa wakipata adha kubwa sana katika masuala hayo ya nyumba.

Ni lini sasa Serikali itawapandisha madaraja walimu hawa ili waweze kuongeza morale katika utendaji kazi wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tuna malalamiko mbalimbali mengi ya walimu katika maeneo mbalimbali ya nchi wakionesha kukerwa na kutopandishwa madaraja.

Niwaombe pia katika jambo hili pia kwa sababu ya mchakato wa kupandisha madaraja unaanzia kule ngazi ya halmashauri zetu ambako kila Mbunge pale yupo, mchakato unaanzia pale ngazi ile inaenda kwa Afisa Utumishi inakuja kwa Mkurugenzi mpaka maeneo mengine. Tupeane taarifa tumeshatoa maelekezo tumekutana walimu wote na mawakilishi wao kwa maana Maafisa Elimu wa Wilaya na Mikoa na Wakurugenzi na Makatibu Tawala, juzi walikuwa hapa Dodoma, tukaagiza kwamba tupate taarifa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu unakuta, mwalimu yupo kwenye halmashauri yako Mheshimiwa Mbunge, lakini mwenzake yeye kapanda mara ya kwanza, mara ya mwisho 2013 mpaka leo hajapanda, lakini kuna wengine wamekuwa wakipandishwa. Kwa hiyo, tukipata taarifa mahusui katika maeneo haya tutazifanyiakazi haraka sana. Walimu wanalalamika na wanakwazwa, tungependa tuwaondolee adha, yale mambo ambayo yapo ndani ya uwezo tuyaondoe ili tuondoe kero kwa walimu wetu waendelee kufundisha kwa moyo. Ahsante sana.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nasikitika sana swali langu halijajibiwa kama nilivyokuwa nimeuliza. Katika majibu ya Naibu Waziri anasema kwamba wao wametenga zaidi ya ekari 217 ambazo ziko katika mikoa mbalimbali lakini hajaainisha ni mikoa ipi na wilaya zipi makambi hayo yapo ili tuweze kujua kwa sababu sisi ndiyo wawakilishi wa hao vijana na tunawaona jinsi ambavyo wanapata adha huko tuliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema kwamba kuna programu mbalimbali na mazingira ambayo wamewawezesha, ni program zipi na mazingira yepi ambayo wameyaweka ili hawa vijana tukawaona wanafanya kazi. Amekiri kabisa hakuna hata sensa waliokwisha kuifanya ya kufahamu ni vijana wangapi ambao wanafanya kazi hizo mchana na usiku kwa maana ya kwamba hakuna wanachokijua kuhusu vijana wetu na tunawaona wakiwa wako na hali ngumu na hawana ajira na ajira hazijapatikana. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Victor Tendega (Viti Maalum), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lake la kwanza amehoji kwa nini hatujaainisha maeneo yote ya ekari 217,882 ambayo yametengwa. Katika utaratibu wa uwasilishaji wa majibu nimetoa majibu ya jumla kuonyesha ekeri zilizotengwa lakini bado hii haizuii Mheshimiwa Mbunge kupata taarifa ya maeneo ambayo yametengwa. Kupitia TAMISEMI tutawasilisha orodha ya maeneo yote haya ambayo yametengwa ili Waheshimiwa Wabunge pia wafahamu ardhi ambayo imetengwa kwa ajili ya shughuli za vijana kwa ajili ya kilimo, viwanda na ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili anahoji kuhusu program ambazo tunaziendesha. Ofisi ya Waziri Mkuu kwa 2016/2021 tunaendesha Programu Maalum ya Ukuzaji Ujuzi Vijana yenye lengo la kuwafikia vijana milioni 4.4 kwa mwaka 2021 ili vijana hawa wapate ujuzi waweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ameomba azisikie program, kwa ruhusa yako naomba nimtajie chache tu ili ibaki kwenye kumbukumbu sahihi za Bunge hili. Program ya kwanza ambayo tunaifanya inaitwa RPL (Recognition of Prior Learning), ni mfumo wa Urasimishaji wa Ujuzi kwa vijana wenye ujuzi ambao hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo ya ufundi. Ukienda leo mtaani kuna vijana wanajua kupaka rangi au kutengeneza magari lakini hawajawahi kusoma VETA wala Don Bosco. Serikali inachokifanya inarasimisha ujuzi wao na kuwapatia vyeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Program ya Greenhouse ambapo kila wilaya tunawafikia vijana 100 katika awamu ya kwanza. Mpaka sasa nchi nzima tumeshafikia vijana 18,800. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Program ya Mafunzo ya Ufundi kupitia vyuo vya Don Bosco na vyuo shirikishi. Takribani vijana 8,800 katika awamu ya kwanza wamenufaika na tunaendelea na awamu ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna program ambayo inaendeshwa DIT Mwanza ya Viatu na Bidhaa za Ngozi ambako vijana wanapata mafunzo na kuweza kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, program ziko nyingi sana kwa sababu ya muda, naomba niishie hapa lakini Mheshimiwa Mbunge atapata taarifa zaidi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri tena ya kina kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuongeza jambo dogo tu, Mheshimiwa Tendega amelalamika hapa kwamba hakuna chochote kinachofanyika na haelewi chochote. Ili kumsaidia zaidi Mheshimiwa Mbunge akumbuke kwamba kila tunapopitisha bajeti za Serikali kila Wizara inaeleza program zote zitakazofanyiwa kazi kwenye bajeti ya Serikali.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuliweka suala hili, vizuri namwomba Mheshimiwa Tendega arejee kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hizo program zote, utekelezaji wake kwenye ripoti ya Kamati upo na mambo yote yaliyofanyika yako wazi na yanaeleweka. Kwa hiyo, hatujaficha na siyo kwamba hakuna kinachojulikana. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Ruaha National Park Iringa ni ahadi ambayo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Nne na Awamu ya Tano na mpaka sasa ni upembuzi yakinifu tu unaendelea kwa miaka yote hiyo kumi na tano. Ni lini sasa barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ili kusaidia wale watalii wanaokwenda kule waweze kwenda kwa ufasaha? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara anayoizungumza inaitwa jina Iringa - Msembe (km 104). Barabara hiyo ilikuwa imewekwa kwenye mafungu mawili; moja ni la ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli ambao tumeshatangaza tenda na mkandarasi amepatikana wakati wowote tutasaini mkataba. Hizi km 104 tayari tumeshamaliza mpaka usanifu wa kina na tumeomba fedha kutoka Benki ya Dunia. Kwa hiyo, wananchi wa Iringa, tena ndiyo nimeoa kule, shemeji zangu wale, wala asiwe na wasiwasi barabara ile inajengwa.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Barabara ya kutoka Iringa Mjini kuelekea Ruaha National Park ambayo ni Jimbo la Kalenga imekuwa ni changamoto na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano. Ni lini sasa barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile itajengwa pamoja na Uwanja wa Ndege wa Nduli na itajengwa kupitia fedha za Benki ya Dunia, taratibu za kupata hizo fedha zinaendelea itakapokamilika mradi utaanza.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu hii ya Twiga Stars ni timu ambayo imeweza kushinda michezo mingi nje ya nchi na ni timu ambayo kwa kweli ina makombe mengi kushinda hata makombe mengine ambayo yapo ya timu zingine za wanaume zilizopo hapa Tanzania. Sasa Serikali haioni haja sasa ya kuwatambua, kuwathamini na kuwekeza katika timu hii ya wanawake ili hawa wanawake waweze kupata ajira ndani na nje ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, michezo ni ajira na soka hili la wanawake limekuwa ni ajira sasa hivi. Tunaona watoto wengi wa kike wamependa michezo. Kule Kalenga sasa hivi nikienda badala ya watoto wa kiume kuomba mipira ni wasichana wanaomba mipira kwa ajili ya kucheza soka la wanawake na tunaona nchi za Ujerumani, Japan na West Africa nchi zao zimewekeza na timu za wanawake zimeweza kushinda katika soka kombe la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali ina mkakati gani wa muda mrefu wa kujenga academy za soka la wanawake hata kwa kila kanda ili kuwawezesha hawa wanawake wakajengewa vipaji na kwa sababu michezo ni ajira. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri lakini nikianza na swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kwamba mpango wa Serikali ni nini katika kuwekeza kwenye Timu ya Twiga Stars?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba ni kweli Timu ya Twiga Stars imekuwa ikifanya vizuri sana kwa miaka mingi na kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge umesema, kufanya vizuri kwa Timu ya Twiga Stars maana yake Serikali imefanya uwekezaji mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nikuhakikishie kwamba kama ambavyo tumekuwa tukifanya uwekezaji katika Timu ya Twiga Stars, tunaahidi kwamba tutaendelea kufanya uwekezaji zaidi ili timu hii ifanye vizuri lakini si Timu ya Twiga Stars peke yake ni pamoja na timu nyingine kwa sababu tunazo timu nyingi sana ambazo zinafanya vizuri na ni timu za wanawake ikiwemo timu ya Kilimanjaro Queens inafanya vizuri lakini pia tunayo timu nyingine ya Mlandizi Queens pamoja na timu zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uwekezaji ni mpango ambao kama Serikali tunao na tunaendelea kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lako la pili ambalo umetaka kujua kwamba Serikali tuna mpango gani katika kujenga academy. Nikuhakikishie kwamba sisi kama Serikali tumekuwa tukihamasisha sana kwa sababu tunatambua kwamba hatuwezi kuwa na timu kubwa za kitaifa kama hatujawekeza kwenye kujenga academy ambazo zitalea vijana. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tumekuwa tukitoa hamasa kwanza kwa wadau kwa mashirikisho lakini vilevile hata kwa Waheshimiwa Wabunge tuweze kushirikiana katika kuhakikisha kwamba tunajenga academy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie fursa hii kuwapongeza wadau wote ambao wameshirikiana na Serikali lakini wameunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga academy ikiwepo academy ya kule Kaitaba lakini tunayo academy ya pale Filbert Bayi pamoja na wadau wengine ambao wanafanya kazi vizuri katika kuhakikisha kwamba tunawekeza katika kuwakuza vijana wetu ili siku moja tuweze kuja kuwa na timu ambazo ni bora zaidi. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Waziri yameonesha kweli Kiswahili kimekua, lakini nchi ya Afrika Kusini wanafundisha Kiswahili na walitupa tender kama Tanzania ili tuweze kuwaandaa walimu wa kuwapeleka katika nchi ile. Lakini mpaka sasa hakuna jambo hilo limetekelezeka na hata nchi ya Kenya sasa wametupiku wamepeleka kule.

Je, Tanzania ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwamba wana walimu wa kutosha wa kuwapeleka nchi hizo? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie kwamba Serikali au nchi yetu ya Tanzania inao walimu wa kutosha wa Kiswahili ambao ni wabobezi, kwa hiyo suala la upungufu wa walimu wa kutosha ambao wanaweza kwenda kufanya kazi katika nchi za nje hamna tatizo lolote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la nchi kuamua kwamba inafanya kazi na nani hilo ni suala la hiyari ya nchi yenyewe, lakini kama Tanzania tuko tayari kupeleka walimu wetu wa Kiswahili mahali popote katika dunia hii kwa sababu tunao walimu wa kutosha mahiri na Serikali inaendelea kuimarisha ufundishaji wa somo la Kiswahili kwa sababu kama ambavyo tumeona lugha ya Kiswahili imeendelea kuheshimika na imeendelea kutumika sehemu mbalimbali katika Afrika na hata nje ya Bara la Afrika. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Waziri naomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, afya ni jambo la msingi sana, Serikali ilikuwa imeshauri kwamba kila halmashauri iweze kutenga asilimia nne, wanawake; nne, vijana; na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu ili waweze angalau kujimudu kiuchumi, lakini halmashauri nyingi zimeshindwa kutenga fedha hizo kwa sababu vyanzo vingi vya mapato vimekwenda Serikali Kuu ikiwemo halmashauri yangu ninayotoka mimi ya Iringa DC. Swali la kwanza, je, Serikali sasa ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba hawa watu wenye ulemavu wanapata matibabu bila vikwazo ikiwemo wale wenye bima unakuta hata wakiwa katika bima vifaa tiba kama sun screen lotion inakuwa ni shida, haipatikani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini sasa Serikali italeta huo Muswada wa Bima ya Afya kwa Watu Wote (Universal Health Coverage) ili tuupitishe na watu hawa wenye ulemavu waweze kupata huduma hii ya afya bila matatizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali tuliweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunatenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na asilimia mbili kwa ajili ya walemavu na hili ni takwa kwa kila halmashauri ambalo wanapaswa wazingatie na kuhakikisha kwamba hii mikopo inafika na inapatikana pasipo kuwa na riba.

Mheshimiwa Spika, nikiongelea suala la matibabu, hakuna mwananchi ambaye anahitaji matibabu atayakosa kwa sababu ya hali yake ya maumbile. Kwa hiyo hilo nataka niliweke wazi na sisi kama Serikali tutaendelea kutoa matibabu kwa walemavu ambao wanastahili kwa mujibu wa taratibu ambazo tunazo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameongelea ni lini Serikali italeta Muswada wa mabadiliko ya sheria ama sheria inayohusiana na bima ya afya kwa wananchi wote, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge mpango wetu sisi Serikali ni kuleta katika Bunge la Septemba.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililopo katika Jimbo la Mbulu Vijijini ni sawa kabisa na changamoto iliyoko katika Jimbo la Kalenga. Kata ya Kihanga, Ulanga, Ifunda katika Vijiji vya Mibikimitali na Kata ya Mgama iliyoko katika Vijiji vya Lupembewasenga, kuna changamoto ya mawasiliano.

Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kawaida?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto tuliyonayo kwa sasa, labda nitoe maelezo kidogo. Ni kwamba kuna baadhi ya sehemu ambazo mawasiliano au minara ilipelekwa ambapo uhitaji wake inawezekana walikuwa watu 5,000 ambao walikuwa wanaweza kutumia huduma hiyo. Kwa sababu ya ongezeko la watu katika eneo husika, kwa hiyo, ile minara yetu inashindwa kuwa na uwezo wa kuhudumia watu wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, kwa kugundua hilo, tumeagiza mobile operator wote wafanye tathmini, wafanye research za kutosha ili waongeze uwekezaji katika maeneo hayo, aidha kwa kuongeza minara au kwa kuongeza capacity katika minara ambayo tayari ipo katika maeneo husika ili kuhakikisha kwamba wananchi wote wanafikiwa na mawasiliano hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa sehemu za kujisubiria akina mama hasa wajawazito. Tumesema katika sera kwamba tutakuwa na Vituo vya Afya katika kila Kata na Zahanati katika kila kijiji; lakini katika Jimbo la Kalenga hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Akina mama wakijifungulia njiani wanatozwa Sh.50,000/= mpaka Sh.70,000/=. Ni lini Serikali itajenga majengo ya kujisubiria katika Jimbo hili la Kalenga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini kauli ya Serikali kuhusu hizo tozo ambazo zinatozwa kwa akina mama ambao pia ni walipa kodi katika nchi hii na Serikali ndiyo yenye changamoto ya kutojenga hivyo Vituo vya Afya? (Maikofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Tendega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunahitaji kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga kwa kuboresha miundombinu ya huduma za afya. Ni kweli kwamba miradi ya ujenzi wa majengo ya kujisubiria kwa maana ya maternity waiting homes, imekuwa ni kipaumbele cha Serikali. Hata hivyo, majengo hayo yanajengwa ili kupunguza umbali wa wajawazito kufika kwenye Vituo vya Huduma za Afya. Kwa hiyo, ili ujenge majengo haya ni lazima uwe na Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Spika, sasa kupanga ni kuchagua. Ndiyo maana Serikali imepanga kwanza kujenga kwa wingi Vituo vya Afya ili viwe karibu zaidi na makazi ya wananchi na tuweze sasa, yale maeneo ambayo yana umbali mkubwa, kuweka mpango wa pili wa kuanza kujenga majengo ya kujisubiria wajawazito. Haitakuwa na tija sana ukiwekeza kujenga majengo ya kujisubiria wananchi sehemu ambayo ina umbali mkubwa sana kutoka kwenye vituo vya huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kipaumbele namba moja ni lazima uwe na kituo, ndiyo maana yale majengo yanajengwa karibu na kituo. Ndiyo maana katika miaka hii mitano tumejenga vituo vingi na tunaendelea na ujenzi wa vituo hivyo ili kusogeza huduma kwa wananchi, hatimaye tutakuja kujenga sasa majengo ya kusubiria wajawazito. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipaumbele hicho bado kipo, lakini tunaboresha kwanza vituo na baadaye tutakenda kwenye awamu wa ujenzi wa majengo ya kujisubiria.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kauli ya Serikali kuhusu tozo, Serikali haijatoa maelekezo yoyote kwa watendaji na watoa huduma kutoza faini kwa wajawazito wanaojifungulia majumbani.

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ni wajibu wa watumishi katika vituo vya huduma kutoa elimu na kuhamasisha wajawazito kuona umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya huduma badala ya kuwalipisha faini wakijifungulia nje ya vituo vya huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea kusimamia jambo hilo. Naomba nitoe wito kwa watendaji wote kuzingatia jukumu lao la kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujifungua katika vituo vya huduma.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Iringa Mjini kupitia Jimbo la Kalenga kwenda Kilolo kilometa 133 ambayo ina madaraja ni barabara ambayo ilikuwa ni ahadi ya hayati Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, alipofika pale akatoa ahadi hiyo, ni miaka mitano sasa imepita haijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lini Serikali itaijenga barabara hii ili angalau kumuenzi hayati kwasababu alienda akaona wananchi wa kule wanavyohangaika katika kuuza mazao yao kwenda katika sehemu mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii yenye urefu wa km. 133 iliyoko Mkoani Iringa na ambayo ni ahadi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Hayati, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli naomba nimhakikishie kwamba Serikali haitaacha ahadi zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais. Nataka nimhakikishie kwamba barabara zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais ikiwa ni pamoja na hiyo zitajengwa kwa kiwango cha lami awamu kwa awamu. Ahsante.