Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Grace Victor Tendega (13 total)

MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-
Katika miaka ya 1990, Wilaya ya Iringa Vijijini kulikuwa na mradi wa usambazaji wa maji kwa kutumia chanzo cha maji ya Mto Mtitu ili kuondokana na adha ya maji inayowakumba wananchi wa Iringa Vijijini; juhudi za kufanya upembuzi yakinifu zilifanyika ili kuweza kusambaza maji kwa gravity kwenye vijiji vyote vya Kata za Maguliwa, Luhota, Mseke, Ifunda, Mgama na Maboga:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha mradi huu ili kuweza kuondoa tatizo la maji kwa wananchi wa Kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, imepanga kufanya usanifu wa kina wa mradi mkubwa wa maji ambao utahusisha vijiji vya Kata za Ngawila, Luhota, Mseke, Ifunda, Mgama na Lugonga. Lengo ni kubaini uwezo wa chanzo cha Mto Mtitu katika kuhudumia maeneo hayo yote. Kazi hiyo imepangwa kufanyika katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo zimetengwa Shilingi milioni 49.5. Mradi huo utakapokamilika, jumla ya vijiji 17 vyenye wakazi wapatao 36,397 vitanufaika.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-
Mojawapo ya jukumu la Serikali katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma na waathirika kupatiwa huduma za matibabu kulingana na masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo ndiyo hufadhili huduma hizo kwa takribani 100%.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizo zinaendelea kutolewa hata kama msaada kutoka Shirika la Afya Duniani utatetereka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba huduma za elimu kwa umma na matibabu kwa waathirika wa UKIMWI zinaendelea kutolewa hata pale misaada ya hisani itakapopungua, Serikali tayari imeanzisha Mfuko wa UKIMWI kupitia marekebisho ya Sheria ya UKIMWI Namba 6 ya mwaka 2015 kwa madhumuni ya kuratibu ukusanyaji fedha za kudhibiti UKIMWI nchini. Hata hivyo, Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) na bajeti za kila mwaka inaendelea kuhakikisha huduma kwa waishio na VVU na elimu kwa wananchi kuhusu UKIMWI inakuwa ajenda muhimu katika nchi yetu.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Tagamenda Substation ni kituo kikubwa kati ya vituo vinavyosafirisha umeme wa Gridi ya Taifa kwani kinapokea umeme kutoka Mtera, Kidatu na Kihansi, lakini vijiji vya Tagamenda, Ikuvilo na Wangama vinavyozunguka kituo hicho havina huduma ya umeme ingawa ndivyo vinalinda kituo hicho.
(a) Je, ni kwa nini Serikali inashindwa kutoa huduma
ya umeme katika vijiji vinavyozunguka kituo hicho?
(b) Je, ni sababu gani zinazofanya vijiji hivyo kukosa kupatiwa huduma hata ya umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitongoji cha Malulumo
Kijiji cha Tegamenda kiliwekwa katika Mpango wa kupatiwa umeme kupitia Shirika la Umeme TANESCO katika mwaka 2015/2016. Kazi hiyo ilianza Mei, 2016 na inakamilika Juni, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za kupeleka umeme katika Kitongoji hicho zimejumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa umeme wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa moja; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 1.4; ufungaji wa transfoma moja pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 70. Kazi hii imekamilika kwa asilimia 90 na inagharimu shilingi bilioni 93.1.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu umeanza nchi nzima tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele-mradi vitatu vya densification, grid extension pamoja na off-grid renewable vinavyolenga kuongeza wigo wa umeme katika vijiji vyote nchini, vitongoji vyote vilivyobaki, taasisi za umma na maeneo ya pembezoni ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na visiwa. Vijiji vya Ivukilo, Wangama pamoja na maeneo mengine ya kijiji cha Tagamenda vimewekwa katika utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu wa Densification na Grid Extenson utakaokamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 10.3; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 9.7; ufungaji wa transfoma tatu pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 300. Gharama ya kazi hii ni shilingi bilioni 14.45.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Upembuzi yakinifu wa kutumia chanzo cha maji cha Mto Ibofwe ili kumaliza tatizo la maji katika Kata za Magulilwa, Luhota, Mseke, Ifunda, Mgama na Maboga ulifanyika kati ya mwaka 1995 – 2000 chini ya usimamizi wa Mbunge wakati huo, Mheshimiwa George Mlawa na bajeti ya utekelezaji wake kupitishwa na Bunge hili ili uwe katika kipindi cha mwaka 2000-2005/2005-2010.
Je, ni tatizo gani lililofanya mradi huo usikamilike na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka wakati Bunge lilikwishapitisha bajeti ya mradi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa kutumia chanzo cha Mto Ibofwe ulifanyiwa usanifu wa awali miaka ya 1990 lakini haukufanyiwa usanifu wa kina (detailed design) ambao ungebaini mahitaji na gharama halisi za kutengeneza mradi huo ndiyo maana haukutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwapatia huduma ya maji wananchi wa Kata za Maboga, Lumuli, Isupilo na Itengulinyi, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji unaogharimu shilingi bilioni 2.18 utakaonufaisha wakazi 6,914 katika maeneo hayo. Mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2013/2014 ulisimama utekelezaji wake mwaka 2015 kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 umetengewa shilingi milioni 800 na unatarajiwa kukamilika Desemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kati ya Julai 2016 na Desemba 2017, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imechimba visima sita katika Kata za Magulilo kisima kimoja, Luhota visima vitatu, Maboga kisima kimoja na Mgama kisima kimoja vinavyohudumia wananchi 1,600. Idadi ya visima kwenye kata hizo tangu miaka ya 1990 hadi sasa imefikia visima 41 vinavyohudumia wakazi 8,200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwaka huu 2017/2018, jumla ya shilingi 410,000,000 zimetengwa kutekeleza miradi ya maji ya Izazi - Mnadani, Migoli - Mtera, Malinzanga, Isupilo – Lumweli – Itengulinyi - Magunga na Mfyome. Mpango wa muda mrefu wa Serikali ni kufanya usanifu wa kina (detailed design) ili hatimaye tutumie chanzo cha Mto Ibofwe kumaliza kabisa matatizo ya maji kwenye maeneo hayo. Usanifu wa kina utafanyika mwaka 2018/2019 kwa gharama ya shilingi milioni 49.56 ambazo ziko kwenye mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018/2019 endapo Bunge litaridhia.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Kuna uhaba wa nyumba za kuishi walimu licha ya juhudi za wananchi kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari; walimu hao pia wanahitaji kujenga nyumba zao wenyewe za kudumu.
Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kutoa mikopo kwa walimu ili wajenge nyumba zao binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa upo uhaba wa nyumba za walimu katika shule za msingi na sekondari ndiyo maana imekuwa ikijitahidi kila mwaka kujenga nyumba za walimu. Katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 Serikali kwa kushirikiana na wananchi, imekamilisha ujenzi wa nyumba 274 za walimu na hivyo kufikisha idadi ya nyumba 14,640 kati ya nyumba 67,711 zinazohitajika kwenye shule za sekondari. Aidha, nyumba 290 za walimu zimejengwa kwenye shule za msingi na hivyo kufikisha idadi ya nyumba 45,638 kati ya nyumba 175,930 zinazohitajika. Takwimu hizo zinabainisha kwamba familia za walimu 52,071 katika shule za sekondari na familia za walimu 130,300 kwenye shule za msingi zinaishi kwenye nyumba za kupanga au nyumba zao binafsi. Ni wazi kwamba mahitaji ya nyumba za walimu ni makubwa mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kuendelea kuweka kipaumbele cha kujenga nyumba za walimu za kuishi familia mbili, nne au sita ambazo ni za gharama nafuu kulinganisha na gharama za kujenga nyumba za kuishi familia moja. Kipaumbele cha juu kitaendelea kuwekwa kwenye maeneo yenye mazingira magumu ya kupata nyumba za kupanga hasa maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa mikopo kwa ajili ya Walimu kujenga nyumba zao binafsi ni kama ulivyo kwa watumishi wengine wa Serikali, ambapo mtumishi anaruhusiwa kukopa kwenye taasisi au benki yenye mkataba maalum na mwajiri kwa kujaza fomu ili akatwe marejesho ya mkopo kutoka kwenye mshahara ambapo makato ya mkopo hayatakiwi kuzidi theluthi mbili ya mshahara na mkopo wote kulipwa kwa kipindi cha kati ya miezi 36 (miaka mitatu) hadi miezi 300 (miaka 25) kulingana na masharti ya taasisi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa taasisi zinazotoa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa Serikali wakiwemo walimu ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kampuni ya Nyumba za Watumishi (Watumishi Housing Company), Benki ya Afrika (Bank of Africa – BOA) kupitia mpango wake wa WEZESHA, mabenki kadhaa mengine kama NMB, CRDB, Azania na kadhalika na kampuni nyingine kama vile T-Mortgage yanayolenga zaidi kuwakopesha watumishi wa kipato cha chini na cha kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili watumishi wakiwemo walimu wapate mikopo ya kujenga nyumba binafsi kwenye maeneo watakayochagua wao, inatakiwa Wakurugenzi wa Halmashauri wawasiliane na taasisi zinazokopesha ili waingie makubaliano maalum yatakayowawezesha watumishi wa Halmashauri wanaotaka mikopo ya kujenga nyumba binafsi wakiwemo walimu kupata mkopo.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Katika nchi yetu kuna kampuni za simu zenye ushindani mkubwa lakini katika Jimbo la Kilolo, hasa maeneo ya Kimala, Kidabaga, hayana mawasiliano ya simu:-
Je, ni lini Serikali itazishawishi kampuni za simu kusimika minara yao kwenye maeneo ambayo hayana mtandao wa mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iliainisha Kata ya Kimala na Kidabaga kwa ajili ya kupelekewa huduma za mawasiliano kupitia Kampuni ya Mawasiliano ya Halotel. Tayari Halotel imejenga mnara eneo la Kimala na mnara huo umeanza kutoa huduma tangu tarehe 17 Septemba, 2016. Halotel ni kampuni pekee inayotoa huduma za mawasiliano katika eneo hilo la Kimala. Vilevile Halotel imejenga mnara katika eneo la Kidabaga ambao pia, umeanza kutoa huduma tangu tarehe 9 Mei, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana wakati swali hili linaletwa na Mheshimiwa Mbunge, labda siku hiyo kulikuwa hakuna mawasiliano eneo hilo, lakini kuna barua ambayo nimeletewa na Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Mheshimiwa Venance Mwamoto, ambayo inaeleza maeneo tofauti kabisa ambayo hayana mawasiliano tofauti na aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. Hata hivyo, Wizara itawatuma wataalam wake kwenda kuangalia maeneo hayo kama kuna changamoto yoyote ili tuangalie uwezekano wa kuongeza coverage katika maeneo hayo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-
Kesi za dawa za kulevya na upelelezi vimekuwa vikichukua muda mrefu sana na kusababisha wakati mwingine ushahidi kupotea na watuhumiwa kuachwa huru baada ya upelelezi kukamilika:-
Je, kwa nini Serikali isianzishe Mahakama za Dawa za Kulevya kwenye Viwanja vya Ndege, Bandari na mipakani ili watuhumiwa wafikishwe Mahakamani punde tu ushahidi ukiwa mikononi kama zifanyavyo nchi nyingine ikiwemo India?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba wa Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uanzishwaji wa mahakama katika kushughulikia aina fulani ya makosa, ni suala la kisheria linalohitaji ushirikishwaji mkubwa wa wadau wote husika wa haki jinai (criminal justice). Kwa kutambua hilo, Serikali imeshaanza mazungumzo ya awali na wadau hao wa haki jinai, ukiwemo mhimili wa Mahakama ili kuona uwezekano wa kusikiliza mashauri ya watuhumiwa wa dawa za kulevya wanaokamatwa katika maeneo ya viwanja vya ndege, bandarini na maeneo mengine ya mipaka ya nchi, kwa kutumia Mahakama zinazotembea (mobile courts).
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wawe na subira wakati Serikali ikijadiliana na wadau wa haki jinai kuhusiana na suala hilo.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Sera ya Afya imebainisha makundi yenye msamaha wa matibabu ambayo ni wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea, watoto chini ya miaka 5, watoto wanaoishi na TB na UKIMWI:-

Je, ni lini Serikali itaweka Watu wenye Ulemavu kuwa miongoni mwa watu wanaohitaji msamaha wa gharama za matibabu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mhesimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imefanya mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 na kuandaa mapendekezo ya Sera mpya ya Afya. Katika mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 changamoto mbalimbali za matibabu kwa makundi ya msamaha ziliibuliwa na watoa huduma pamoja na watumiaji huduma hizo. Moja ya changamoto iliyojitokeza ni hospitali zetu kuwa na wagonjwa wengi wa msamaha na hivyo kushindwa kuboresha huduma za afya. Kutokana na changamoto hiyo ya kuwa na makundi mengi ya msamaha, Wizara iliona ni vyema ikaboresha utaratibu wa msamaha kwa kuhakikisha kuwa watu wasio na uwezo tu ndiyo wanaopatiwa msamaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mapendekezo ya Sera mpya na Afya kila mwananchi mwenye uwezo atapaswa kugharamia huduma za afya. Sera pendekezwa inaainisha njia mahsusi zitakazowezesha Serikali kubaini wananchi wote wenye uwezo ili waweze kuchangia gharama kabla ya kupokea huduma, kwani ni wazi kuwa si kila mlemavu ana kipato duni. Hivyo, wananchi watakaothibitika katika maeneo yao kuwa hawana uwezo wa kuchangia wakiwemo walemavu wataendelea kupatiwa matibabu bila kuchangia gharama za matibabu. Aidha, Serikali inatambua changamoto ya uchangiaji wa huduma za afya na inaandaa utaratibu wa bima ya afya kwa Watanzania wote ikiwa ni pamoja na kundi la walemavu.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo watoto wengi njiti huzaliwa na akinamama wanaojifungua watoto hao njiti wengi wao ni waajiriwa ambao hupata changamoto ya likizo ya uzazi inayotosha kwa malezi ya awali ya watoto hao njiti:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha akinamama hao wanaongezewa likizo ya uzazi?

(b) Akinamama hao wanapojifungua pia, hupata changamoto ya vifaa kama vile vifaa vya kukamulia maziwa, dawa na gharama za matibabu; Je, Serikali imejipangaje kuwasaidia gharama za vifaa hivyo?

(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kudumu wa kutokomeza suala la akinamama kuzaa watoto njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Kazi ya Mwaka 2004, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 inaelekeza kuwa mama aliyejifungua mtoto mmoja apewe likizo ya malipo ya siku 84 na siku 100 kwa mama aliyejifungua watoo pacha, sheria hiyo pia imeweka wazi kuwa mama anayenyonyesha anatakiwa kupewa saa mbili kwa siku, ili apate muda wa kunyonyesha. Serikali haina muda wa kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa sasa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza sera ya Afya ya Mwaka 2007 ya Kutoa Huduma Bila Maipo kwa Makundi Maalum wakiwepo akinama wajawazito na mwongozo wa uchangiaji unaeleza wazi kuwa, kundi hili halipaswi kugharamia huduma za afya pale wanapohitaji. Hivyo, basi, Wizara inafanya juhudi kubwa katika kuboresha huduma kwa akinamama wajawazito, hususan, wanapojifungua kwa kutumia njia mbalimbali. Kwa sasa Wizara inatekeleza Mpango wa Pili wa kuboresha afya ya uzazi na mtoto, yaani One Plan II ya mwaka 2016 mpaka 2020 ambapo imeweka vipaumbele mahususi vya kuboresha afya ya watoto wachanga ikiwemo watoto njiti nchini. Kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 Wizara imetenga fedha bilioni 22.5 kwa ajili ya huduma ya mama wajawazito na katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 inatarajia kuomba idhini ya Bunge kutumia fedha kiasi cha bilioni 29.5 kwa ajili ya kundi hili na hivyo hakuna akinamama wanaojifungua wanaoripotiwa kukosa huduma za dawa na vifaa tiba kabla na baada ya kujifungua katika vituo vya Serikali.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kujikita katoka afua mbalimbali kwa lengo la kudhibiti visababishi vya kuzaliwa watoto njiti, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha akinamama wajawazito wanaanza kliniki mapema mara tu wanapohizi kuwa na ujauzito, kuhudhuria kliniki ipasavyo, ili kuchunguza na kutibiwa magonjwa mbalimbali, ikiwa yatabainika kwa kuzingatia vilevile ushauri wa lishe n.k. Afua nyingingine zinazolenga kuokoa maisha ya watoto wachanga kama vile uanzishwaji wa vyumba maalum vya matunzo na matibabu ya watoto wachanga, kwa maana ya neonatal care units, sambamba na upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, kwa ajili ya watoto wachanga ikiwemo watoto njiti.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa tarehe 15/03/2016 Mhe. Rais alitoa agizo la kuwakamata vijana wote watakaokutwa wakicheza mchezo wa “pool table” na kuwapeleka kambini wakalime:-

(a) Je, Serikali imeandaa kambi ngapi na kujua huduma za kujikimu kwa vijana hao wakati watakapokuwa wakiendelea na shughuli za kilimo na kipindi cha kusubiri mavuno yao?

(b) Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ili kuondokana na wimbi la vijana kuzurura na kushinda bila kufanya kazi?

(c) Je, Serikali imefanya sensa na kujua ni vijana wangapi wanaofanya kazi usiku na kupumzika mchana au mchana na kupumzika usiku ili kubaini wazururaji wa mchana na wanaocheza “pool table” mchana kwa sababu ya kukosa ajira?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kuzuia vijana kucheza “pool table” wakati wa kazi umelenga kusisitiza na kuimarisha dhana na tabia ya kila mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi katika sekta mbalimbali za kiuchumi ili kuchangia kukuza pato la Taifa na kupunguza umaskini. Katika kuhakikisha kwamba vijana wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, Serikali kupitia Tawala za Mikoa na Wilaya imetenga maeneo maalum ya uzalishaji mali kwa vijana ambapo jumla ya ekari 217,882 zimeelekezwa katika kukidhi mahitaji ya shughuli za kilimo, ufugaji, viwanda na biashara ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa Vituo vya Maendeleo ya Vijana na Majengo ya Viwanda “Industrial Sheds” umesaidia kuwapa mafunzo vijana na kuwajengea uwezo wa kuongeza thamani katika mazao ya kilimo.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kuwa vijana, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ifuatayo:-

(i) Kuwajengea vijana ujuzi kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini ili vijana kutumia ujuzi wa mafunzo mbalimbali kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Kwa mwaka huu wa fedha, Serikali inatekeleza mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi ambapo jumla ya vijana 49,265 watanufaika.

(ii) Kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini ili kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususani kilimo, ufugaji, madini na viwanda.

(iii) Utekelezaji wa dhana ya local content katika miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali katika maeneo ya uchukuzi, nishati na miundombinu ya barabara na reli.

(iv) Kuwezesha vikundi vya vijana kupitia zabuni za manunuzi ya ndani kwenye kila Halmashauri za Manispaa na Wilaya nchini Tanzania kupitia Akaunti Maalum kama mabadiliko ya mwaka 2016 ya Sheria ya PPRA yanavyoelekeza.

(v) Uwezeshwaji kiuchumi kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mikopo ya asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imelipokea wazo la kujua vijana wanaofanya kazi usiku na wanaofanya kazi mchana. Hivyo suala hili litawasilishwa katika Mamlaka ya Takwimu ili lizingatiwe katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-

Walimu wenye weledi wa kuwafundisha Watu Wenye Ulemavu ni wachache sana nchini.

Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha Walimu hao ni wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-

Mheshimimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Walimu wenye taaluma ya Elimu Maalum. Changamoto hii ina sababishwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wenye ulemavu kutokana na mabadiliko chanya ya kimtazamo na uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimimiwa Spika, mahitaji ya Walimu wa Elimu Maalum nchini ni Walimu 8,882 katika shule maalum na vitengo vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum 706. Hadi kufikia Disemba 2018 Walimu 5,556 wenye taalum ya Elimu Maalum ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada walihitimu katika Vyuo mbalimbali nchini vikiwemo Chuo cha Ualimu Patandi na Chuo Kikuu Dodoma.

Mheshimimiwa Spika, Serikali imekamilika upanuzi wa Chuo cha Ualimu Patandi ili kukiongezea uwezo wa kudahili. Pia Chuo kimeanzisha kozi ya Elimu Maalum katika ngazi ya Astashahada kwa Walimu tarajali kwa mwaka wa masomo 2018/2019. Hatua hii itaongeza idadi ya Walimu wanaojiunga na mafunzo ya Ualimu wa Elimu Maalum ili kupunguza changamoto ya Walimu wenye taaluma ya Elimu Maalum wanaohitajika nchini.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Watu wenye ulemavu wamekuwa wakipata adha kubwa katika kupata matibabu ikiwemo kukosa fedha kwa ajili ya matibabu:-

Je, ni lini Serikali itahakikisha inawapatia bima ya afya watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 na kuandaa mapendekezo ya Sera mpya ya Afya. Katika mapitio ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007, changamoto mbalimbali za matibabu kwa makundi ya msamaha ziliibuliwa na watoa huduma pamoja na watumiaji wa huduma hizo. Moja ya changamoto iliyojitokeza ni hospitali zetu kuwa na wagonjwa wengi wa misamaha na hivyo kushindwa kuboresha huduma za afya. Kutokana na changamoto hiyo ya kuwa na makundi mengi ya msamaha, Wizara iliona ni vyema ikaboresha utaratibu wa misamaha kwa kuhakikisha kuwa wananchi wasio na uwezo tu ndio wanaopatiwa msamaha.

Mheshimiwa Spika, katika mapendekezo ya Sera mpya ya Afya kila mwananchi mwenye uwezo atapaswa kugharamia huduma za afya. Sera pendekezwa inaainisha njia mahsusi zitakazowezesha Serikali kubaini wananchi wote wenye uwezo ili waweze kuchangia gharama kabla ya kupokea huduma, kwani ni wazi kuwa si kila mlemavu ana kipato duni. Hivyo, wananchi watakaothibitika katika maeneo yao kuwa hawana uwezo wa kuchangia ikiwemo walemavu, wataendelea kupatiwa matibabu bila kuchangia gharama za matibabu.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inatambua changamoto za uchangiaji wa huduma za afya na inaandaa utaratibu wa bima ya afya kwa Watanzania wote ikiwa ni pamoja na kundi la walemavu.
MHE. GRACE V. TENDEGA Aliuliza:-

Akina mama wajawazito wamekuwa wakitozwa fedha kuanzia shilingi 50,000/= hadi 70,000/= wasipojifungulia katika Vituo vya Afya hasa katika Jimbo la Kalenga; huku vituo hivyo vikiwa mbali na maeneo wanayoishi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga maeneo ya kusubiri kujifungua katika Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, majengo ya wajawazito kujisubiria yanalenga kupunguza umbali kwa wajawazito kufika kwenye vituo vya huduma za afya pindi wanapokaribia kujifungua. Lengo likiwa ni kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyosababishwa na umbali kutoka katika vituo vya kutolea huduma.

Meshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hii, Serikali imeendelea kujenga vituo vya huduma za afya kote nchini na kujenga Hospitali za Halmashauri 102, Vituo vya Afya 487 na Zahanati 1,198 katika kipindi cha Novemba, 2015 hadi Septemba, 2020. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 67; shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali 67 za Halmashauri na shilingi bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya za Halmashauri. Kiasi cha shilingi bilioni 27.5 pia kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati 555.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya nchini kote, umepunguza umbali kwa wananchi kuvifikia vituo vya huduma za afya na hivyo viashiria vya huduma na vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 11,000 mwaka 2015 hadi 3,000 mwaka 2020. Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya huduma za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.