Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. William Mganga Ngeleja (2 total)

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuongezea maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Moja, kwa kuwa eneo la Nyamikoma kihistoria lilikuwa na gati, gati hilo lilikuwa linatumika kusafirisha marobota ya pamba kuyapeleka Kisumu nchini Kenya, enzi zile wakati kilimo cha pamba kipo juu. Napenda kusikia kauli ya Serikali kama katika mazingira hayo bado kunahitajika utafiti wa kijiografia ambao Mheshimiwa Naibu Waziri ameuzungumza ukilinganisha na maeneo mengine ambako hakuna gati? Pili, eneo la Nyamikoma linafanana na maeneo mengi ya mwambao wa Kanda ya Ziwa au Maziwa Makuu kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa mfano, Magu Ginnery, Nasa Ginnery, Mwabagole Ginnery pale Misungwi, Sengerema Buyagu Ginnery ambako ndiko ninakotoka pamoja na Buchosa – Nyakarilo. Napenda kujua kama katika mpango huo ambao Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Oktoba watakamilisha ramani zinazohitajika.
Je, anatoa kauli gani za matumaini kwa wananchi
wa maeneo haya ambako pia wanatarajia magati yajengwe ili kuboresha zao la pamba ambapo kwa sasa hivi Serikali imewekeza nguvu nyingi katika kufufua viwanda na hasa viwanda ambavyo vinategemea rasilimali ya hapa nchini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakubaliana nae kwamba Gati la Nyamikoma lilikuwepo toka zamani, lakini taarifa tunazozikusanya sasa hivi tunataka tupate picha kamili kwa sasa ya maeneo ya magati yote na bandari zote ili hatimae tujue tupange vipi vipaumbele vyetu katika uendelezaji wa magati na bandari hizo. Kwa hiyo, pamoja na kwamba ilikuwepo na unafahamu kwamba matumizi yake yamepungua sana itaingia katika mpango huo na bahati nzuri kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba kazi hiyo tunatarajia kuikamilisha mwishoni mwa Oktoba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili; maeneo yote aliyoyataja yapo katika mpango kabambe wa kupitiwa kuandaa hizo taarifa za GIS na baadaye kuja kuamua maeneo gani tuanze, maeneo gani tufuatie katika gati zote na bandari zote kwenye Maziwa yote Makuu; Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, nimhakikishie kwamba wananchi wa maeneo yake na maeneo mengine aliyoyataja tutahakikisha kwamba tunayapitia na tunapata taarifa kamili zitakazotuwezesha kuamua wapi tuanze na wapi tufuatie.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa ufafanuzi wa swali ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Kemirembe lakini nilitaka tu kupata commitment ya Serikali kwa sababu kwa kuwa ombi letu la Halmashauri ya Sengerema la huo mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Serikali lipo Serikalini kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Je, ni lini Serikali itaunganisha nguvu na Halmashauri ya Sengerema kutekeleza mradi huu kwa sababu ombi letu lipo pale na Serikali inafahamu? Nachotaka kujua sasa hivi ni lini Serikali itatuwezesha kupitia kasma ambayo tumeiomba ukijumlisha na kasma ambayo tumeitenga sisi Sengerema ili tutekeleze mradi huo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itafanya jambo hilo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndiyo maana nimesema katika commitment yetu katika bajeti inayokuja tumetenga shilingi bilioni 251.18 ambapo katika fedha hizo miongoni mwa mambo tunayoenda kufanya ni suala zima la ujenzi wa vituo vya afya na hospitali katika maeneo mbalimbali. Nina uhakika Sengerema waliweka jambo hili kama priority yao katika mpango wa Halmashauri basi halina shaka tutashirikiana na ofisi yetu ya TAMISEMI lengo kubwa ikiwa ni wananchi kupata huduma ya afya.