Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Grace Sindato Kiwelu (11 total)

MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Mheshimiwa Waziri hospitali yetu ya Wilaya ya Siha haina wodi ya watoto wala ya wazazi na hii inasababisha msongamano mkubwa sana katika hospitali yetu ya Mkoa ya Mawenzi.
Je, ni lini fedha hizo zitatoka ili ujenzi huo uanze mara moja?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, sikumsikia amesema hospitali ipi?
MHE. GRACE S. KIWELU: Hospitali ya Wilaya ya Siha.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki nisiamini kwamba kweli hakuna wodi kwa ajili ya watoto na wazazi na kama kweli hakuna basi ni jambo ambalo linahitaji udharura wa hali yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango mingi ya vipaumbele katika sekta mbalimbali za huduma za jamii inapangwa kenye Halmashauri zetu. Kwa hivyo, tutajaribu kuona ni kwa namna gani wamepanga vipaumbele vyao na kwa sababu bajeti ya Wizara yangu imeshapitishwa na kwa maana ya Halmashauri zote nchini, basi tuweze kuona tunaweza tukaanza na hivi ambavyo ni muhimu zaidi katika sekta ya afya, kwa sababu kweli ni jambo gumu kidogo kuonekana kwamba hakuna wodi kwa ajili ya watoto na wazazi katika hospitali ambayo ina hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, nitalichukulia very seriously na kulishughulikia jambo hilo.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda kuuliza ni lini wodi ya wazazi katika Hospitali yetu ya Mkoa ya Mawenzi itakamilika kwa sababu imejengwa kwa zaidi ya miaka mitano na inakuwa ni kero kwa wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukamilika kwa wodi ya wazazi katika hospitali ya Mawenzi, Moshi ni suala la kipaumbele kwenye Serikali ya Awamu ya Tano. Wiki takribani tatu zilizopita nilifika pale na kuona hatua ya ujenzi iliyofikiwa na tukashauriana na uongozi wa hospitali ile na kukubaliana kwamba kwa mwaka huu wa fedha waombe wapewe bajeti maalum kwa ajili ya kukamilisha sehemu ya jengo hilo ambayo itatoa huduma kwa akina mama wajawazito na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile watumie mikopo inayopatikana kwenye taasisi mbalimbali za kifedha ili wakamilishe ujenzi huo mara moja sasa hivi kuliko kusubiria huu utaratibu wa kutumia bajeti. Tayari wameanza mchakato huo kupitia Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Said Meck Sadick kwa kufanya mazungumzo na Benki ya TIB.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, bado hayajaridhisha. Nchini kwetu safari za ndani ni ghali kuliko safari za kwenda nje ya nchi. Hii imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wetu. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kushirikiana na mamlaka hiyo ili kuweka kiwango maalum kisizidi hiyo bei kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, tuliamua na kupitia Bunge hili kwamba turuhusu ushindani na ndivyo tulivyofanya. Kupanga viwango kwa mamlaka zetu maana yake ni kutoka katika kile tulichoamua awali na mimi sina matatizo kama Bunge hili na Serikali kwa ujumla itaamua.
Kwa maoni yangu ni vema ngoja tuimarishe Shirika letu la Ndege la Air Tanzania na mnafahamu tumeanza kuliimarisha, litaingiza ushindani mkubwa na mimi nina uhakika hao sasa hivi ambao wamepanga viwango vya juu watalazimika kuvishusha ama kuondoka katika biashara hiyo na kuliacha shirika letu likitamba. (Makofi)
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti katika hospitali yetu ya Wilaya ya Siha hatuna hatuna jokofu na imekuwa inaleta usumbufu sana kwenye kuhifadhi miili ya marehemu wetu.
Je, ni lini Serikali itatuletea jokofu kupunguza upungufu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Hospitali ya Siha takribani wiki sita zilizopita nilikuwa pale Siha na namshukuru sana Mbunge tulikuwepo pamoja na
tulitembelea hospitali ile na kipindi kilichopita hapa nilitoa maelekezo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyofika pale Siha,
kutokana na changamoto tuliyobaini pale, kwamba tumepeleka fedha lakini matumizi yale ya fedha tumeona hayaelekezwi sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kabla ya jokofu kuanza kuna suala zima la fedha tulizozipeleka pale lazima zitumike vizuri na tumeshatoa maelekezo hayo. Lengo letu ni kwamba lile jengo, floor ya juu iweze kukamilika vizuri lakini hatuachi hapo kwa sababu changamoto kubwa ya pale lazima tuhakikishe hospitali ile inafanya kazi vizuri na Serikali
itaweka nguvu za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishapeleka zaidi ya milioni 250, inafanya kazi lakini suala la jokofu litakuwa ni kipaumbele chetu ili kuhakikisha, lengo kubwa hospitali ile inafanya vizuri kwa wananchi wa Siha.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Timu yetu ya Serengeti imeendelea kufanya vizuri huko ilipo, ningependa kujua Serikali imetenga kiasi gani, kwa ajili ya kuisaidia timu yetu hii ili iweze kufanya vizuri na kurudi na kombe hapa nchini? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza sana Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana. Ninataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba timu hii ya Serengeti haijaibuka tu, tumeanza nayo miaka mitatu iliyopita, kwa kushindanisha vijana wa chini ya umri wa miaka kumi na tano, tukapata timu bora, tumeilea hiyo timu na kuhakikisha kwamba inashiriki kwenye mashindano ya kimataifa kabla ya hizi mechi 22 ambayo haijapata kutokea toka historia ya nchi hii, yote hii huu ni uwezeshaji na uwekezaji wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nisisitize kwamba figure kamili yaani ni kiasi gani tumetumia kama Serikali tutaiandaa tumpe Mheshimiwa Mbunge, lakini Serikali imejitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba timu hii inatuletea ushindi katika mashindano haya. (Makofi)
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, askari wanaoishi uraiani huwa wanapewa shilingi 40,000 kwa ajili ya pango. Shilingi 40,000 hii ni kwa ajili ya room moja, maji, umeme na familia hizi wana watoto.
Je, Serikali haioni umuhimu a kuongeza kiasi hiki cha fedha, ili askari wetu wanaporudi kupumzika nyumbani waweze kupumzika vizuri bila kelele za watoto?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Grace kwa swali alilolileta. Niseme tu jambo alilolisemea ni kilio cha askari na hata nilipozunguka maeneoe mengi nimekutananacho na Mheshimiwa Rais tayari alishatuelekeza tufanye upya uchambuzi wa masuala mengi yanayohusu stahiki za askari pamoja na sheria zinazo-govern utaratibu mzima wa taasisi hizi za majeshi yaliyoko ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani na hiyo ni moja ya kitu ambacho tutakiangalia yakiwepo na mengine ambayo yanashusha morali ya kazi ya askari wetu. (Makofi)
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Naibu Waziri amesema Kamati ya Kitaifa iliyoundwa, ninapenda kujua ni lini Kamati hiyo itakamilisha taarifa hiyo na kuileta ndani ya Bunge ili matatizo hayo yaweze kukoma?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba Kamati ya Kitaifa ambayo ilikuwa inashirikisha zaidi ya Wizara tano iliundwa kupitia maeneo mbalimbali na kupitia nchi nzima kuona migogoro ambayo iko katika maeneo mbalimbali. Kamati hiyo imeshatoa tayari matokeo ya awali ambayo yamebainisha kila kitu ni maeneo gani ambayo yapo kwenye matatizo, baadhi ya maeneo ambayo yamebainishwa ni pamoja na vijiji 366 viko ndani ya hifadhi.
Kwa hiyo, basi juzi tumekaa na hiyo Kamati imetoa tena draft nyingine tumetoa maelekezo ni imani yangu ndani ya kipindi cha miezi miwili, Kamati hiyo itakamilisha kabisa hiyo taarifa na itawasilishwa kwa Waheshimiwa Wabunge na kutoa taarifa kamili.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro imekuwa kwenye ujenzi wa wodi ya wazazi zaidi ya miaka mitano sasa na wodi hiyo haijakamilika na kusababisha gharama za ujenzi kuongezeka. Je, ni lini Serikali itatoa pesa za kutosha kukamilisha wodi hiyo ya wazazi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda nitoe ahadi kwamba tutawasiliana ndani ya Serikali ili tuweze kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Mbunge katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali kwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Rombo limekuwa na tatizo kubwa sana la mawasiliano hasa katika kata zilizoko mpakani na ukanda wa juu na Mbunge wa Jimbo hili amekuwa akiuliza maswali mara kwa mara. Je, ni lini tatizo hili litamalizika katika Jimbo hilo la Rombo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Kiwelu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo Jimbo la Rombo tu maeneo ya mpakani ni karibu majimbo yote ambayo yako mipakani Tanzania kuna tatizo la mwingiliano wa mawasiliano ya simu kutoka nchi jirani. Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekwishawaagiza watoa huduma kwanza kwenda kuongea na majirani zao watoa huduma wa nchi jirani kurekebisha changamoto iliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kulikuwa na utaratibu ambao wenzetu nchi jirani walikuwa wameukiuka ambapo tunaendelea kuufanyia kazi. Sasa hivi eneo la Rombo wako Vodacom na Halotel kwa ajili ya kurekebisha tatizo hil. Eneo la Musoma (Tarime) tumewapeleka Airtel na Tigo kwa ajili ya kurekebisha tatizo hilo. Maeneo ya Bukoba na Kigoma tumewapeleka tena watoa huduma wengine kwa ajili ya kurekebisha tatizo hilo.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya Same - Kisiwani - Mkomazi ilishafanyiwa usanifu na umekamilika na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa ili kuondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi wa Jimbo la Same na majimbo mengine yanayoweza kutumia barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Kiwelu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Serikali inayo mpango wa kujenga barabara hii kutoka Same
- Kisiwani - Mkomazi lakini pia tutakwenda mpaka kule Mkinga ili iweze kwenda mpaka Tanga. Ni kweli usanifu ulishafanyika, sasa hivi Serikali inafanya mapitio ili tuweze kwenda kwenye hatua ya manunuzi, sasa hivi Mkandarasi Mshauri anaendelea na kazi katika mwaka huu wa fedha ili kufanya review ya barabara hii ili tuweze kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira tukamilishe zoezi hili. Pamoja na hayo tumeweka mpango katika mwaka wa fedha unaokuja kwa maana ya kwamba kidogo kidogo kuna sehemu ambayo tutaanza kujenga kwa kiwango cha lami. Ahsante sana.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi, Kituo cha Afya cha Pasua kilichopo Manispaa ya Moshi nacho kina tatizo la ultrasound, lakini pamoja na mortuary. Je, ni lini Serikali itapeleka ultrasound na kujenga hicho chumba cha kuhifadhindugu zetu waliotangulia mbele ya haki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa majibu katika swali la msingi, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo vituo vya afya vinajengwa, vinakuwa ni vituo vya afya ambavyo vinakamilika kwa maana ya kuwa na watalaamu lakini pia kuwa na vifaa vya kutosha.

Mheshimiwa Spika, sasa katika swali lake anaongelea Kituo cha Afya ambacho kinaitwa Pasua kiko Moshi na anasema kuna haja ya kuwepo mortuary lakini pia na uwepo wa ultrasound. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hakuna kituo cha afya hata kimoja ambacho tungependa kikawa kituo cha afya nusu, tungependa vituo vya afya vyote vikamilike, ni vizuri tukaelezana tatizo ni nini na hasa ukizingatia kwamba, hata kwa Halmashauri ya Moshi, mapato yake ya ndani yapo ya kutosha kabisa. Kwa hiyo, ni suala tu la mipango tujue nini kifanyike kwa haraka ili wananchi waweze kupata huduma hizo.