Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Charles John Tizeba (49 total)

MHE. MARIAM N. KISANGI: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Pamoja na juhudi za Serikali za kuboresha Soko la Samaki la Feri, naipongeza sana Serikali kwa kuwapa hata majiko ya gesi pale katika Soko la Samaki la Feri, mimi kama Mbunge wa Dar es Salaam napongeza.
Kwa kuwa utoaji wa leseni za uvuvi imekuwa ni kero kubwa sana kwa wavuvi kwani wanatakiwa kulipia leseni za uvivi kila wanapotoka sehemu moja kwenda nyingine.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwaondoshea wananchi kero hiyo ya kulipia leseni za uvuvi kwa kila wanapoenda kuvua?
Swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Kigamboni na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla umezungukwa na Babari Kuu, na kwa kuwa wavuvi wa Mkoa wa Dar es Salaam, hawana mipango yoyote ya kuboreshewa mazingira ya kazi yao ya uvuvi na Serikali.
Je, Serikali imejipanga vipi kuwasaidia wavuvi wa Kigamboni na Dar es Salaam kwa ujumla katika kuboresha kazi yao ya uvuvi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kisangi kwa maswali mazuri, kuhusu swali la leseni kutozwa kila wanapovuka mpaka mmoja kwenda mwingine, jambo hili linahusisha Wizara zaidi ya moja, Wizara ya Kilimo tumeandaa waraka ambao tunategemea tutakaa pamoja na wenzetu wa TAMISEMI na wa Wizara ya Fedha, tunategemea jambo hili lipate ratiba hapa kabla ya Wizara ya Fedha ku-table Finance Bill, ili kuweza kukubaliana kuhusu mambo haya ya leseni ambazo zinatozwa kwa wingi, hili jambo linaendana sambamba na makato yanayotozwa kwa wazalishaji wetu wa sekta hizi. Hili ni agizo la Mheshimiwa Rais la kuhakikisha kwamba Watanzania wanaofanya kazi zao wanapata tija kutokana na shughuli hizo wanazozifanya kwa kuwaondolea makato mengi wanayoyapata kutokana na vyanzo mbalimbali kukata kutoka kwenye shughuli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwaboreshea mazingira, moja ya mazingira linahusiana na hili alilolisemea la makato, Wizara tumepanga baada ya Bunge hili kukutana na Wavuvi wanaovua katika Jimbo lake na Waheshimiwa Wabunge, tutawakaribisha ili tuweze kupokea mapendekezo yao kuhusu mazingira ambayo tutayaboresha.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kijiji cha Kipili, Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa, tulikuwa na Chuo cha Uvuvi, na kulikuwa na generator na cold room, lakini bahati mbaya awamu zilizokuja ikageuzwa ikawa secondary school na uvuvi ukaisha, na sisi watu wa mwambao tunategemea sana uvuvi, hasa mwambao wa Ziwa Tanganyika, na hakuna Chuo:-
Je, ni lini Serikali itakirudisha Chuo cha Uvuvi cha Kipili ili kusaidia wavuvi wetu wa mwambao wa Ziwa Tanganyika?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala alilolisema Mheshimiwa Keissy, Serikali ilikuwa na nia njema kufuatana na mahitaji la kupanua elimu, ikafanya mabadiliko hayo, lakini kwa kuzingatia kwamba Jimbo la Mheshimiwa Keissy wananchi wake wanategemea uchumi wa uvuvi, sisi pamoja na TAMISEMI tutashirikiana kuangalia utaratibu mpya wa kuweza kurejesha utaratibu wa kuwa na chuo ambacho kitasaidia vijana wetu kuweza kujifunza na kuweza kumudu kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili litaendana pia na mpango wa Wizara ya Elimu na Ufundi, ambao unahusisha vyuo vya VETA katika kila Wilaya ili tuweze kupata wanafunzi wengi ambao watafanya kazi kwa utalaam zaidi. Hili jambo linaenda sambamba na Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso wa Jimbo la Pangani ambaye alishaongelea kwamba wananchi wake pia wanahitaji sana kufufuliwa kwa chuo ambacho uchumi mkubwa wa Pangani wa vijana unategemea uvuvi.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, masoko ya tumbaku yanayumba au kwa lugha nyepesi yanasuasua kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Bodi ya Tumbaku ambayo ndiyo inapaswa kulipa wale ma-classifiers wanaopanga tumbaku lakini pia na kuajiri ma-classifiers. Je, Serikali katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, imeiongezea Bodi ya Tumbaku kiasi gani ili ifanye kazi ipasavyo masoko yaende kama inavyopaswa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inafahamu kwamba makato mbalimbali yako kwenye pembejeo lakini pia katika bei anayopangiwa mkulima kodi ni nyingi. Lini Serikali itakuja hapa na orodha ya kodi ambazo zimeondolewa ili mkulima apate mapato anayostahili?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba masoko ya tumbaku yanayumba na siyo kwamba yanayumba Tanzania peke yake bali yanayumba dunia nzima mahali tumbaku inakozalishwa kwa sababu ya bei ya tumbaku kidunia imeshuka. Kwa hivyo, hilo jambo linasababisha hata soko letu hapa ndani na lenyewe liyumbe hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ni hiyo, lakini sababu zingine ni hizi za kwetu za ndani kama hivyo Bodi yenyewe kutokuwa na pesa za kutosha kuendesha shughuli zake kikamilifu. Ndiyo maana mwaka wa fedha uliopita pamoja na kwamba walikuwa wanapata ruzuku ya Serikali kuendesha Bodi yao, ukaanzishwa huo ushuru kwa wanaosafirisha nje tumbaku ili kuisaidia kukidhi mahitaji yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili kwamba kodi ni nyingi ni kweli kodi ni nyingi kama nilivyosema katika jibu langu la msingi. Ndiyo maana Serikali imechukua hatua hii ya kuunda Kamati ya Makatibu Wakuu wapitie hizi kodi za mazao yote siyo zao la tumbaku peke yake ili kuona zile kodi ambazo ni kero na ambazo zinaweza zikafutwa au kuondolewa mara moja ziondolewe na zile ambazo zitakuwa zinaathiri bajeti za Halmashauri zetu au Serikali Kuu basi hizi zitakuja kufutwa katika mwaka wa fedha ujao.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba na mimi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wakulima wa eneo langu Manyoni Mashariki eneo la Makuru, Heka na Mkwese wana kilio kikubwa sana cha mapunjo ya bei ya tumbaku kutokana na hawa wapangaji wa madaraja (classifiers) kutokuwa waaminifu na pia kutokana na utitiri/wingi wa madaraja ya tumbaku, yapo 72. Waziri anatoa tamko gani kusimamia hawa classifiers vizuri kwa maana ya kutoa elimu kwa wakulima?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, ni lini Serikali…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtuka swali la nyongeza huwa ni moja, Mheshimiwa Waziri.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Naomba majibu tafadhali.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wako classifiers ambao siyo waaminifu, lakini katika kumwajiri mtu huwezi ukajua mara moja kwamba huyu siyo mwaminifu ni mpaka pale anapoingia kazini ndiyo tabia zake za hovyo hovyo zinaanza kuonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na Wizara ilichokifanya sasa hivi ipo katika utaratibu na imekwishatoa idhini au kibali cha ajira kwa Bodi ya Tumbaku iajiri classifiers wengine 35 katika mwaka huu wa fedha unaokwisha ili kuongeza idadi ya classifiers hawa wafike kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jambo ambalo limekuwa linasababisha kufanya vitu ambavyo siyo vya kiadilifu katika kukagua madaraja ya tumbaku ni kwa sababu classifier wanakuwa wachache, anahitajika maeneo mengi kwa hivyo anaanza kutumia ule uhaba wao kufanya mambo ya kuomba kitu hiki au kingine. Kwa maana hiyo, hawa watakapokuwa wameajiriwa tunatarajia kwamba angalau hilo zoezi la kutambua madaraja ya tumbaku litakwenda bila vikwazo au tabia hizo za kuomba rushwa kwa wenye tumbaku.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama lilivyo swali la msingi, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wakati yupo kwenye kampeni aliahidi kuondoa tozo mbalimbali ambazo zinamdidimiza mkulima wa kahawa. Mpaka sasa Serikali bado haijaondoa hizo tozo. Je, Serikali ipo tayari kuwaruhusu wananchi wale wanaolima kahawa waweze kuuza kahawa sehemu nyingine ambapo watapata bei nzuri?
shimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi Watanzania kwamba huu msururu wa kodi utatafutiwa utaratibu wa kuziondoa zile ambazo hazistahili kutozwa au zenye kuleta kero kwa wananchi. Pamoja na nia hiyo nzuri ya Mheshimiwa Rais bado mazao haya tunayahitaji hapa nchini. Serikali hii imeweka kipaumbele cha kuwa nchi ya viwanda na hivi viwanda vitahitaji malighafi ipatikane hapa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, halitakuwa jambo la busara leo tukisema kwa sababu tuna tatizo hili la kodi ndogo ndogo zenye kero, basi tuachie malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu ianze kuuzwa nje. Utaratibu tunaoufanya ni kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kwamba bei zinakuwa nzuri na masoko yanakuwa mazuri ili kutowapa shida wananchi wakati wa kuuza mazao yao.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sababu kubwa ya ukosefu wa elimu kwa wakulima ni uchache wa Maafisa Ugani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Ugani kwa kila kijiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa wakulima wa kahawa hupeleka kahawa zao nchi jirani kufuata bei nzuri. Je, Serikali ina mpango gani kuongeza bei ya kahawa ili wananchi hawa wasipeleke nchi jirani?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba tuna upungufu wa Maafisa Ugani 6,022, hii ni idadi kubwa. Vilevile kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Serikali inasomesha Maafisa Ugani hawa zaidi sasa katika vyuo vyetu ili kukabiliana na huu uhaba ambao upo na vibali vya kuwaajiri vinaendelea kutolewa. Kwa hivyo, hivyo hivyo tunakwenda kukabiliana na huo upungufu na nina uhakika baada ya miaka michache ijayo kama nia ilivyo ya Serikali na Mheshimiwa Mbunge, kila kijiji kitakuwa na Maafisa Ugani wanaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kahawa kuruhusiwa kuuzwa nje ya nchi, nikijibu swali lililotangulia nimesema kwamba kahawa hatutakubali iende nje kwa sababu tunavyo viwanda vya kuhudumiwa hapa hapa nchini. Hii kahawa bei yake itakuwa nzuri tukiondokana na msururu wa kodi hizo ndogo ndogo zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la kahawa leo tunapozungumza hapa lina kodi 26, ni kodi nyingi sana na ndiyo maana tunafanya sasa uchambuzi ndani ya Serikali ili kuona hizo kodi ambazo kwa kweli zinastahili kuondolewa, ziondolewe ili kuwapa wakulima unafuu. Kwa sababu kodi zikitozwa wanunuzi hawalipi wao, zinahamishiwa kwa muuzaji wa kahawa ambaye ni mkulima. Kwa hivyo, tukizipunguza hata kwa wanunuzi na watu wengine, mwisho wa siku atakayenufaika ni mkulima kwa sababu kodi hizo zitakuwa zimepungua na bei ya kahawa zitakuwa zimepanda.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazao mengi ya biashara tunategemea sana soko la nje ambalo lina ushindani mkubwa kuzingatia nchi nyingi zinalima mazao hayo na wakati mwingine wakulima wanalima kutokana na mazoea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kitengo cha Utafiti wa Masoko hayo ili kujua mahitaji halisi ya soko la dunia kuliko kama sasa ufuta umeshuka mpaka Sh.1,500 kutoka bei ya mwaka jana ya Sh. 3,000? Nataka kujua tu Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kitengo hicho cha Utafiti wa Masoko Ulimwenguni ili kutoa habari nchini kwa wakulima kulima mazao kutokana mahitaji ya soko badala ya kulima mazao kwa mazoea.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mazao yetu mengi kwa sasa bado yanategemea masoko ya nchi za nje, lakini naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba takribani kila zao kubwa la biashara linalo Bodi na hizo zina Vitengo vya Utafiti wa Masoko. Kwa hivyo, labda tu tutumie nafasi hii kuvikumbusha hivyo vitengo kwamba wanao wajibu wa kufanya huo utafiti na kufikisha habari wanayoipata kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hapa ninaloliona ni pale ambapo bodi na hivyo vitengo wanapokuwa na habari kuhusu soko kuanguka au kupanda wakaacha kufikisha habari hiyo kwa wadau wao ambao ni wakulima. Kwa hivyo, niwakumbushe tu katika bodi na taasisi hizi zinazohusika na utafiti wahakikishe kwamba hicho wanachokibaini na kukijua kuhusu masoko ya haya mazao basi kwa haraka iwezekanavyo wafikishe habari hiyo kwa wahusika kwa maana ya wakulima na wafanyabiashara wa mazao hayo.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, nataka kumuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali haijawekeza kikamilifu katika sekta ya uvuvi na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kodi zinazotozwa wavuvi ni nyingi sana na zisizokuwa na mpangilio. Nataka nitolee mfano wa Mafia ambapo Wilaya hiyo imesema kwamba kila boti itakayokuwa inaingia pale inatozwa shilingi milioni tano; whether wamevua au hawajavua. Je, Serikali itakuwa tayari katika bajeti ijayo kutuletea majibu ya kina katika Finance Act kuhakikisha kwamba kodi hizi zote zimehuishwa na zile kodi ambazo ni kero kufutwa? Swali la kwanza hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika ardhi ya Kigamboni tulikuwa na taasisi inaitwa TAFICO (Tanzania Fishing Company) ina majengo na ilikuwa inafanya kazi ya uvuvi pale Kigamboni. Majengo yale yapo pale mpaka sasa hivi hayafanyi kazi yoyote. Je, Serikali itakuwa tayari kubadilisha majengo ya taasisi ile kuwa kiwanda cha kuchakata samaki ili kuongeza ajira na kuongeza thamani ya mazao ya bahari?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, hizi kodi kama nilivyosema kwenye maswali yaliyotangulia na katika swali hili, zipo nyingi na kwa kweli Mheshimiwa Rais alikwishatoa maelekezo kwamba ni lazima zipitiwe upya na hizo ambazo zinastahili kuondolewa kwa sababu zina kero mbalimbali ziondolewe siyo kwenye mazao ya uvuvi peke yake, lakini kama nilivyosema awali hata kwenye mazao ya kilimo pia. Kwa hivyo, kodi zile ambazo zitaondolewa na zisiwe na madhara yoyote ya kibajeti baada ya ile Kamati kukamilisha kazi yake zitaondolewa na zile ambazo zitakuwa na madhara ya kibajeti hizo zitasubiri sasa utaratibu wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni wazo na mimi nalichukua, nitakwenda kuzungumza na wenzangu katika Wizara na Serikali kuona pendekezo hili la Mheshimiwa Dkt. Ndugulile linaweza kutekelezwa namna gani.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Ziwa Tanganyika tuna Halmashauri tano na kila Halmashauri ina licence yake na mvuvi anakata licence, lakini anapotaka kuhama kwenda Halmashauri nyingine hata kama licence yake haijakwisha muda lazima alipie licence upya kwenye Halmashauri anayokwenda. Je, ni lini Serikali itaondoa kero hii kwa wavuvi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema hapo awali kwamba ziko tozo ambazo zimekuwa ni chanzo cha mapato ya Halmashauri mbalimbali na moja ya vyanzo hivi vya mapato kwa Halmashauri zetu ni leseni. Bahati mbaya sana kwa kanuni tulizonazo na Sheria ya Uvuvi iliyopo leseni hizi za Halmashauri zimekuwa za maeneo ya Halmashauri husika yaani hazihamishiki na ndiyo maana kumekuwa na huu usumbufu kwa wavuvi kwamba leseni zinazotolewa na Halmashauri ya Sikonge haiwezi kwenda kutumika katika Halmashauri ya Urambo, hili ndilo limekuwa changamoto. Nimpe tu faraja Mheshimiwa Mbunge kwamba hili nalo liko katika mambo ambayo yanaangaliwa na hiyo Tume ya Taifa ya Makatibu Wakuu inayopitia upya hizi kodi ambazo zimekuwa kero kwa wananchi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naomba niulize swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uvuvi ni kazi inayozalisha ajira hapa nchini. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo ambacho kitasaidia kusomesha wavuvi tukaweza kupata tija katika nchi yetu?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli uvuvi ni shughuli ambayo inahitaji ujuzi fulani kama ilivyo kilimo na shughuli nyingine zote za uzalishaji. Ili kupeleka maarifa kwa wananchi kwanza Serikali inavyo vyuo kadhaa vya uvuvi. Vyuo hivi vinatumika kufundisha wataalam ambao wao sasa kama Maafisa Ugani wanapelekwa katika vijiji na halmashauri zetu ili maarifa hayo waliyonayo wayafikishe kwa wavuvi mbalimbali wanaofanya shughuli hizo. Itakuwa vigumu sana wavuvi wote nchini kuwapeleka kwenye vyuo lakini Maafisa wetu wa Ugani kwa maana ya Maafisa Uvuvi katika halmashauri zetu mbalimbali wao ndiyo wanaopaswa kufikisha maarifa ya uvuvi kwa wavuvi ili waweze kuvua kwa tija.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Uvuvi katika bahari na katika maziwa makubwa unafanyika usiku na mchana, lakini uvuvi katika Mto Koga kule Sikonge unafanyika mchana tu usiku Serikali inakataza. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, ni kwa nini Sikonge tu ndiko uvuvi unakatazwa usiku wakati ndiyo kuna samaki wengi? Ahsante sana.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Sikonge nimekaa miaka mitano kama Mkuu wa Wilaya na kwa hivyo hiki anachokisema nakifahamu vizuri sana. Ni kweli kwamba uvuvi katika mito na mto huo bahati mbaya eneo ambalo uvuvi unafanyika ni ndani ya hifadhi. Kwa hivyo, ili kuzuia shughuli ambazo si za kivuvi wakati wa usiku ndiyo maana imepigwa marufuku kufanya uvuvi usiku katika eneo hilo. Pia katika Mto huo Koga uvuvi pia unafanywa kwa msimu, wakati ule ambako shughuli za uwindaji katika hifadhi hiyo haziruhusiwi na uvuvi pia unazuiwa ili kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana kwa ajili ya msimu unaofuata.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Tizeba kwa kuchaguliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na pia kumshukuru kwa majibu mazuri sana pamoja na kwamba ameanza kazi leo. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa zao la mwani limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwemo kutofahamika kwa zao lenyewe lakini vilevile kukosa soko, pembejeo na hivyo kufanya wakulima wa mwani na hasa wanawake kuhangaika kutafuta masoko na pembejeo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha zao hili la mwani linaongezewa thamani kwa kujenga viwanda katika maeneo yote yanayozunguka ukanda wa bahari ili zao hili lilete tija kwa wanawake na hasa ikizingatiwa kwamba zao hili limekuwa linachukuliwa tu na Wachina na soko lake liko China, Korea na maeneo mengine? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vikundi vya ujasiriamali kwa asilimia kubwa vimekuwa vikitegemea mabenki ya kibiashara ambayo kwa kweli riba yao imekuwa kubwa sana na hivyo kufanya vikundi vya wanawake na vijana kushindwa kabisa kumudu kwenda kukopa katika mabenki hayo. Serikali ina mkakati gani kupitia upya mabenki yote na vyombo vyote vya fedha ili kuangalia hizi riba zinazotozwa na kulinganisha na hali halisi ilivyo ili wanawake na vijana waweze kunufaika na mabenki haya? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa sasa hili zao la mwani soko lake siyo zuri sana hapa nchini. Kama alivyosema yeye mwenyewe, wakulima wa mwani wanauza kwa makampuni ya kutoka huko Korea, China na India.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sababu kubwa ya msingi ya kutoongeza thamani ya zao hili hapa hapa nchini ni uzalishaji mdogo ambao uko katika zao hili kwa sasa. Ili uzalishaji uweze kuwa na tija kwa mwekezaji mwenye kiwanda kwa uchache zinahitajika tani 12,000 kwa mwaka au zaidi, ndiyo mtu akiwekeza kwenye kiwanda cha kuchakata mwani anaweza kupata faida. Sasa hivi uzalishaji tulionao ni tani 600 tu kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana sasa Serikali, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kupitia huu mradi wa SWIOFish tunajipanga kupitia vikundi vya uzalishaji wa mwani ili viweze kupatiwa mikopo. Nitoe wito kupitia nafasi hii kwamba Halmashauri zote ambazo ziko katika Ukanda wa Pwani watie jitihada kubwa katika kuviorodhesha hivi vikundi ili hizi fedha ambazo zinatolewa na Benki ya Dunia ziweze kutumika vizuri kwa vikundi hivyo vya akina mama na hata wasio akina mama kwa sababu zao hili siyo kwa ajili ya akina mama na vijana peke yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko fedha ambazo Serikali imeshapata kutoka Benki ya Dunia, Dola za Kimarekani milioni 36. Dola za Marekani milioni 17 zitatumika kwa Tanzania Bara na Dola milioni 11 zitatumika kwa Tanzania Zanzibar na Dola milioni 8 hivi zitatumiwa na taasisi zinazohudumia utafiti katika eneo hili la uzalishaji viumbe katika Ukanda wetu wa Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujibu swali lake la pili la nyongeza, hivi vikundi vijiorodheshe. Hizi fedha hasa ndiyo zimelenga kuwakomboa hawa watu wa vikundi kuondokana na mikopo ambayo siyo rafiki sana wakati mwingine kutoka kwenye taasisi za fedha kwa sababu, watapewa msaada wa pembejeo, ruzuku za dawa na vitu vingine ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji wao. Tutakapofika tani 12,000 au zaidi, watu wengi wanayo nia ya kuwekeza katika viwanda hapa nchini vya kuchakata hizi mwani na ndiyo hapo sasa hata thamani ya hili zao itaweza kuongezeka.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Na mimi siridhiki kabisa na majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, mazingira ya ushindani yanayosemwa kwanza hajawekewa mazingira mazuri ya ushindani na nauli kwa tunaosafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam mara kwa mara, nauli kwa mfano za Shirika la FastJet, wanapoaihirisha safari wewe abiria hawakulipi na ukichelewa ndege unalipa zaidi ya nauli. Je, TCAA na Mheshimiwa Waziri wanalijua hili na kama wanalijua wana mpango gani wa kuliondoa? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, alivyoliweka ndivyo hivyo lilivyo. Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) na sisi kama nchi mwanachama tunao wajibu wa kufuata taratibu za Kimataifa za usafiri wa anga. Moja ya taratibu zilizopo katika IATA ni kwamba ushindani ndiyo utatawala bei za tiketi katika usaifirishaji wa anga. Lakini ushindani huo umewekewa masharti, ikitokezea kwamba route iliyokuwa na ushindani sasa ushindani huo umekwisha kumetokeza monopoly ya msafirishaji mmoja; sheria za IATA na kwa maana hiyo sheria zetu za usafiri wa anga zinairuhusu mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa anga kuweka ukomo wa bei kwa huyo msafirishaji ambaye anayo monopoly wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie case ya Fast Jet na route za Mwanza au Songwe. Ni kweli kwamba hizi route ya Dar es Salaam – Mwanza imekuwa inaendeshwa kwa ushindani kwa sababu zipo scheduled flights za kampuni zaidi ya moja. Precision Air bado wameendelea kuwa wana-operate kati ya Dar es Salaam na Mwanza ingawa siyo kwa frequency kubwa kama ilivyo ya FastJet. Na jambo hili limesababishia sana usumbufu kule mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa anga kwa sababu linawafanya washindwe kuingia saa kwenye hiyo hatua ya kuwawekea ukomo FastJet wa nauli kwa sababu bado route inaonekana ina ushindani, kwamba Precision Air wapo wana-operate kwenye hiyo route.
Mheshimiwa Spika, lakini ikifika mahali kwamba Precision Air wamesimamisha kabisa safari zao za Dar es Salaam kwenda Mwanza basi mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa anga itakuwa ina uwezo wa kisheria sasa wa kuweka ukomo wa bei kwa msafirishaji aliyebaki kwenye route hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na pili usafiri wa ndani wa kawaida kimataifa bado huwa hauwezi kulinganishwa na usafiri wa nje kwa maana ya kuangalia umbali, hii ni practice ya dunia nzima ndivyo ilivyo, sio Tanzania pekee tu.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa Dar es Salaam – Dodoma; Dar es Salaam – Dodoma ndege zinazokuja ni ndege ndogo na hizi ndege ili iweze kuja na kurudi kwa faida lazima bei per seat iwe ni kubwa kidogo kuliko ndege kubwa zaidi ambayo ingefanya route ya namna hii. Ndiyo maana sasa hivi upanuzi huu wa uwanja wa Dodoma ndege za size kubwa zikianza kuja kwa vyovyote vile bei za kusafiri kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma kwa ndege zitashuka sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Mkoa wa Geita, hususan Jimbo la Bukombe mwaka wa jana walivyogawiwa mbegu na pembejeo mbegu zile hazikuota, na waliahidiwa kupewa fidia, hawakupewa na sasa wanaogawa mbegu ni wale wale waliowatia hasara mwaka jana. Je, Serikali inawahakikishiaje wale wananchi, kama zile mbegu hazitaota ni nani ataingia gharama ya kuwafidia?
Swali la pili, asilimia kubwa ya Jimbo la Geita vijijini linategemea sana uvuvi. Kumekuwa na operation nyingi sana za kukamata wavuvi na mitego midogo midogo, na kuchoma mitego yao kwa Wakuu wa Wilaya.
Je, Serikali inafanya operation lini kwenye viwanda vinavyotengeneza, vinafahamika na makontena yanayoingia, badala ya kwenda kuwasumbua wale wavuvi maskini?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika misimu miwili ya nyuma mfulilizo kuna baadhi ya mbegu ambazo ziligawanywa na Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba kupitia ginneries mbalimbali ambazo hazikuota na hasa mbegu ambazo hazikuota ni zile ambazo zilikuwa zimenyonyolewa nyuzi. Utaratibu ulifanyika wa kujua ni nani aliyekuwa amefanya kosa kwa sababu batch hizo hizo kuna maeneo ziliota vizuri na kuna maeneo mengine hazikuota vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wataalam waliingia katika kutafiti ni kutu gani kimesababisha mbegu ambazo zimezalishwa sehemu moja, maeneo mengine siziote na maeneo mengine ziote. Ziko sababu mbalimbali, zingine zikiwemo za upandaji usiokuwa sahihi wa mbegu hizo, lakini ziko pia mbegu ambazo zilibainika kwamba wakati zinanyonyolewa wauzaji wa hiyo pamba walikuwa wamezimwagia maji ili kuongeza uzito wa pamba yao, kudanganya katika ununuzi na hivyo kuzifanya zipoteze ubora hata wakati zinanyonyolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni complex ili kujua ukweli kwamba kosa ni la msambazaji au ni la aliyezinyonyoa au ni la mkulima aliyeuza mbegu ambayo ilikuwa imemwagiwa maji. Tutakapokuwa tumejiridhisha exactly nani aliyefanya jambo hilo ni nani, huyo ndiye tutakaye mchukulia hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu operations zinazoendelea nchi nzima kwenye uvuvi, kwanza hili swali siyo mahali pake, lakini nitalijibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi haramu tutaushambulia na kupigana nao vita popote utakapojitokeza na kwa namna zote. Kwa hiyo, hatukomei katika kukamata wavuvi wenye nyavu, isipokuwa tunakwenda kwa wazalishaji, wasambazaji na waingizaji wa hizo zana haramu nchini. Ndiyo maana umeona tumekamata viwanda wanazalisha nyavu haramu, malori ya wanaosafirisha, tumeingia kwenye maduka mahali zinakouzwa na tunawakamata wavuvi wenyewe wanaotumia hizo zana haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kwenda hatua zaidi, kwamba sasa tunaanzisha utaratibu wa kwenda na mashua huko huko ziwani, tutawahukumu huko huko, wale tutakaowakuta wanatumia zana haramu. Na humu barabarani kama agizo lilivyo la Mkuu wa nchi, tukikukamta hata wewe una malori tunakushitaki na ku-confiscate kila kitu ulichonacho.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pia pamoja na Serikali kutoa maelekezo kwa TIC kuhusu kunadi fursa hiyo kwa wawekezaji kuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Tabora lakini wawekezaji wa Philip Morris wanaozalisha sigara duniani wanatarajia kuja kujenga kiwanda hiki mkoani Morogoro. Pamoja na kwamba Serikali kupitia Halmashauri yetu ya Nzega, Tabora Manispaa na Wilaya ya Uyui tulishatoa maeneo kwa ajili ya kiwanda hiki kuja kujengwa Tabora, lakini bado tunasikia Philip Morris wanakuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Morogoro.
Je, Serikali haioni kwamba haiwatendei haki wana Tabora ambao ndiyo watoka jasho wakubwa katika zao hili la tumbaku? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili, Serikali imekiri asali bora na nyingi inazalishwa katika Mkoa wa Tabora hususani katika Jimbo la Igalula. Kwa nini Serikali kwa makusudi makubwa kabisa isingesaidia uongezaji wa thamani wa zao hili la asali kwa maana ya kupata utaalamu na packaging ili kusaidia kipato cha wana Igalula na nchi kwa ujumla? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WIZARA YA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ntimizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Kampuni ya Philip Morris wamekwishaanza ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya tumbaku pale Morogoro. Wawekezaji wanazo sababu na vigezo wanavyovitumia katika kuchagua maeneo ya mahali gani wawekeze. Kazi ya Serikali mara zote imekuwa ni kuwashawishi na kuwashauri lakini hatufiki mahali tukawalazimisha kama wao wanaamini kwamba sehemu fulani ndipo patakapowapa tija katika uwekezaji wao. Kwa hivyo, Philip Morris pamoja na kushauriwa kwamba wakajenge kiwanda hicho Tabora wao waliamua kuendelea kuwekeza hapo Morogoro. Tukiwalazimisha wanaweza wakaamua kwenda kujenga kiwanda hicho nchi nyingine ambayo pia inazalisha tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kuona hilo, Chama Kikuu cha Ushirika cha Tumbaku Mkoa wa Tabora (WETCU) katika mkutano wao mkuu waliamua kwamba na wao wawekeze kwenye kiwanda cha kuongeza thamani tumbaku. Mpaka leo wamekwishapata eneo kule Urambo na limepimwa. Sasa hivi wanafanya tathmini ili walipe fidia kwa wananchi walioko pale. Wakishawaondoa wale wananchi walio kwenye eneo hilo, ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani katika mkoa wa Tabora Wilaya ya Urambo utaanza kufanyika mara moja kupitia Chama hiki cha Msingi cha Ushirika cha WETCU.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Ntimizi lilihusu wananchi kueleweshwa namna bora ya kusindika na kufungasha asali. Hili jambo linaendelea, viko vikundi na kupitia Halmashauri vikundi hivi vimekuwa vinaendelea kupatiwa mafunzo ya namna hii na SIDO Mkoa wa Tabora na wao wamekuwa wakijihusisha na hili jambo la kuwafundisha wananchi namna bora ya usindikaji wa asali ili iweze kuwa na ushindani katika soko la ndani na soko la Kimataifa.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, wanawake wa Tanzania kwa kiwango kikubwa walio wengi ndiyo wakulima; na kwa kuwa wanawake wa Tanzania hawana fursa za kiuchumi zitakazowafanya wafikie Benki hii ya Wakulima kwa sababu ya kukosa dhamana. Napenda kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanawake wengi ambao ni wakulima waishio vijijini wanafikia fursa hii ya kupata mikopo katika Benki ya Wakulima kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wanawake wengi wa Tanzania ndiyo wanaojihusisha katika kilimo hapa nchini. Serikali kwa kutambua hilo imeweka mipango mbalimbali ikiwemo ukopeshaji wa vikundi vya akinamama katika uzalishaji kupitia Halmashauri zao lakini pia tunatoa kipaumbele katika Mfuko wa Pembejeo. Wanawake wanaokwenda kukopa katika Mfuko wa Pembejeo wanapata kipaumbele kwa sababu wao wanafahamika ndiyo wanaoshiriki zaidi katika shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio Benki ya Kilimo tu inayotoa mikopo katika sekta ya kilimo, benki nne hapa nchini kwa sasa zinatoa fedha katika shughuli za kilimo. Utoaji wa fedha hizi hauko katika shughuli yenyewe ya kilimo tu, isipokuwa benki zinatoa fedha katika mnyororo mzima wa thamani katika kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Benki ya NMB mwaka huu pekee wa fedha imetenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya shughuli za kilimo na akinamama wana kipaumbele. Masharti ya mikopo katika benki ambazo tumezungumza nazo za NMB, Commercial Bank of Africa, CRDB, wote wamepunguza masharti katika mikopo ya kilimo ili kuwawezesha Watanzania wengi na hasa wale wasio na dhamana kuweza kupata mikopo hii kwa urahisi.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mheshimiwa Rais kabla ya Mei Mosi alitoa kauli akiwa Hai kwamba anaondoa kero ndogo ndogo za ushuru ambazo wanalipishwa watu ambao wanafanya biashara ndogo ndogo, akina mama pamoja na vijana.
Swali langu ni kuwa kauli hii ya Rais ililenga kuondoa
kero ya huu ushuru ndogo ndogo katika Halmashauri ya Hai peke yake au katika masoko yote Tanzania nzima likiwemo Soko la Buzogwe, soko kubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Soko la Mpanda Hoteli na masoko madogo yote yaliyoko katika Mkoa wa Katavi? Kauli hii pia inawalenga watu wa Mkoa wa Katavi?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nilitaka kufahamu, kumekuwa na wawekezaji ambao wamekuwa wakienda kuihadaa Serikali kuomba maeneo kwa ajili ya uwekezaji, ikiwepo katika Kata ya Kekese ambako kuna mwekezaji ambaye alichukua eneo zaidi ya eka 1,000 akiwahadaa wananchi kwamba anahitaji kuwapatia ajira. Lakini mpaka sasa shamba lile analitumia kwa manufaa yake binafsi, hakuna ajira zozote alizotengeneza katika hilo shamba lililopo katika Kata ya Kekese, Manispaa ya Mpanda. Nini tamko la Serikali kumuwajibisha mwekezaji huyu kwa sababu anatumia pesa za wananchi na watu wa Katavi, vijana pamoja na akina mama wanahangaika hawaelewi nini cha kufanya?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli suala la ushuru na tozo ndogo ndogo limekuwa kero ya muda mrefu kwa wakulima wa nchi hii na Rais alikwishatoa maelekezo kuanzia wakati wa kampeni na katika mikutano mbalimbali kwamba, Serikali iangalie namna ya kupunguza, kama si kuondoa kabisa shuru tozo na hizi ambazo zinashumbua wananchi na zitaondolewa sio kwahalmashauri moja moja kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa avute subira ya siku chache sana zijazo hazizidi 13 atasikia kwa kiwango gani Serikali itafutilia mbali tozo na ushuru mwingi sana ambao unasumbua wananchi mbalimbali. Tunadhamiria kufanya hivyo na tuseme tu kwamba nina hakika kila mtu atafurahi jinsi tutakavyokuwa tumeshughulikia hili tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kwa upande wa mashamba ambayo wawekezaji mbalimbali wameyachukua kwa lengo la kuyaendeleza halafu hawayaendelezi uko utaratibu unaofanywa na Wizara yetu ya Kilimo ya Ardhi, mashamba haya yanafuatiliwa na wale wote ambao hawatekelezi masharti yale yaliyo katika mikataba yao. Mashamba haya yako katika hatua mbalimbali, mengine yameshachukuliwa yamefutwa, mengine yanaendelea kufanyiwa utaratibu wa kuyafuta ili yarejeshwe kwa wananchi au mikononi mwa Serikali.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka Serikalini, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sheria inawataka wavuvi wanaovua katika Ziwa Victoria wakiwemo wavuvi wa Mkoa wa Mwanza kutumia nyavu za inchi sita hadi saba ambazo hazikidhi mahitaji ya uvuvi katika maji ya kina kirefu. Je, Serikali ina mpango gani ya kupitia upya Sheria ya Uvuvi ya mwaka 1973, sheria ambayo ilitungwa kabla hata samaki aina ya sangara hawajapandizwa ndani ya Ziwa Victoria na kuwa imepitwa na wakati? (Makofi)
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri na Mbunge wangu wa Jimbo la Buchosa, ni lini utakuwa tayari kuja Mkoani Mwanza kukaa na wadau ili kuweza kusikiliza kero zao na changamoto zinazowakumba katika uvuvi ndani ya Ziwa Victoria? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Namba 22 na maboresho ya kanuni zake kama yalivyofanywa imeweka aina za nyavu ambazo zinaruhusiwa kutumika katika maji baridi, kwa maana ndani ya maziwa yetu; na aina za nyavu ambazo zinaruhusiwa kutumika katika uvuvi baharini. Sasa utafiti ambao umefanywa na wataalamu wetu kwa muda mrefu ulibaini kwamba nyavu zenye matundu size ya chini ya inchi sita zinasababisha uvuvi kutokuwa endelevu ndani ya maziwa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii imezingatia pia
aina za samaki waliomo Ziwani na imewekwa ili kuhakikisha kwamba samaki aina kadhaa hawatoweki na aina nyingine wanaendelea kuzaana kwa ajili ya matumizi ya wavuvi wenyewe na watu wengine wanaohusika na suala hili la uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokifanya, mimi binafsi nimeshakutana na wavuvi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine, siyo mara moja, mara kadhaa na mara ya mwisho tulichokubaliana ni kwamba utafiti wa pamoja ufanyike tena kuangalia mesh size na lile suala la kuunganisha nyavu yaani double tatu, double tisa na kadhalika, ili tuweze kujua kwa kushirikiana ni njia gani sahihi ya kuendesha uvuvi katika Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukutana na hawa wavuvi, mimi nakutana nao kila mara ninapokuwa Jimboni. Ahsante sana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri katika swali la msingi (b); katika bajeti ya mwaka 2014/2015 Serikali ilisema ilizalisha vifaranga milioni 20 na kuwapa wafugaji wa samaki ili kuweza kuzalisha samaki. Sasa katika bajeti ya mwaka 2015/2016 na 2016/2017 ingawa haijaja, sijasikia Serikali ikisema tena kwamba wamepeleka vifaranga vingapi vya samaki kwa ajili ya wakulima. Je, mpango ule uli-fail ndio ikawa haikuja tena au ulifanikiwa? Kama ulifanikiwa ni kwa kiasi gani?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa nchi yetu wa kuzalisha vifaranga vya samaki umeongezeka sana hasa baada ya sekta binafsi kuingia katika biashara hii ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki. Sasa hivi Morogoro, Dar es Salaam, Mkuranga na Mwanza kuna uwezo mkubwa tu wa watu binafsi kuzalisha vifaranga vya samaki hadi kufikia vifaranga milioni karibu 36. Kwa hiyo, tunaendelea tu kuhimiza na kutoa elimu kwa watu wenye nia ya kujiingiza katika biashara hii ya uzalishaji wa vifaranga waendelee kufanya hivyo ili kukidhi mahitaji makubwa ambayo yanazidi kuongezeka hapa nchini.(Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ni mpango wa Serikali kuanzisha Vyuo vya VETA katika kila Wilaya: Je, kuna mkakati gani wa kuanzisha mkondo wa kilimo na uvuvi katika kila Chuo cha VETA kinachoanzishwa kwenye Wilaya zetu ili kuongeza Maafisa Ugani hawa wa kilimo na uvuvi ambao wanaweza kufanya kazi kwenye vijiji vyetu na kuinua kilimo chetu na uvuvi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la Mheshimiwa Ishengoma ni zuri sana. Nitaiagiza mamlaka yetu ya FETA iwasiliane na VETA kuona ni namna gani wanaweza kushirikiana katika kutekeleza wazo lake. (Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Najielekeza hapo kwenye wavuvi. Kwa kuwa wavuvi katika Ziwa Victoria nyavu wanazotumia wanazinunua madukani na Serikali ipo na bandari ipo; Serikali ituambie ni lini itayafunga yale maduka yanayouza nyavu zisizotakiwa kuvuliwa na lini itaweza kuleta sheria hapa Bungeni kuzuia viwanda vinavyozalisha nyavu zinazosababishia wavuvi hasara? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Jumuiya anapomuuliza mdhamini wake inakuwa shida kidogo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupambana na uvuvi haramu kwa ujumla, Serikali sasa hivi inachokifanya, inashambulia maeneo yote, yaani hatuendi kwa wavuvi peke yao, tunamchukulia hatua yeyote aliyeko katika ule mnyororo wa thamani wa uvuvi kwa maana kwamba mzalishaji wa zana haramu, msambazaji, mtunzaji, mhifadhi na yeyote. Kwa hiyo, anayeuza akipatikana anachukuliwa hatua kama mhalifu mwingine yeyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tumekwenda hatua zaidi hata ya kudhibiti uingizwaji wa nyavu nchini, acha wenye viwanda ambao tunawakagua mara kwa mara na kwa kweli mwenye kiwanda hapa nchini akipatikana anazalisha nyavu zisizoruhusiwa tunachukua leseni yake na kufunga kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunakagua hata uingizaji, kwa sababu wako watu wanaagiza nyavu kutoka nchi za nje kwa kisingizio kwamba zinapita Tanzania zinakwenda nchi nyingine, lakini baada ya kuwa wamesha-clear pale bandarini, wanafanya maarifa hizi nyavu zikifika mpakani Tunduma au pengine, zinarudi nchini. Kwa hiyo, hata hawa sasa hivi tunashughulika nao, tunahakikisha wanatoka nje ya mipaka yetu na hizo nyavu zao. Tukimkamata tunamchukulia hatua kama sheria inavyotaka.(Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nilitegemea Wizara itaonesha angalau trend ya mapato kutoka kwenye shughuli za uvuvi angalau miaka mitano au kumi tuone kwamba inaendaje, ila wametoa tu mfano kwa mwaka wa 2015/2016. Ukiangalia mapato kutoka uvuvi 2016/2017 huu mwaka uliokwisha, walikuwa na pungufu almost shilingi bilioni tisa kwa sababu walipata tu shilingi bilioni 10. Sasa Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuamka na kuweka vipaumbele katika Sekta hii ya Uvuvi ili kujiongezea mapato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mfano tu, bajeti ya maendeleo inayotengwa katika Sekta ya Uvuvi, mwaka 2016 na mwaka huu 2017 ni sifuri. Kwa hiyo, ina maana shughuli za doria, mikakati ya kujenga Bandari ya Uvuvi au kuboresha Bandari ya Uvuvi haipo, kujikita zaidi katika kuongeza mapato katika deep sea fisheries, haipo; hii mikakati yote haipo; zaidi kuna project moja tu ya SWIOFish ndiyo ambayo imesimama ambapo fedha zake kutoka World Bank ni za mikopo. Sasa Serikali haioni kwamba hawako fair kwa wavuvi, shughuli za uvuvi na yenyewe pia inajinyima mapato ambayo yangetuletea maendeleo katika nchi yetu?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba Sekta ya Uvuvi imepewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ASDP II na katika Programu hii, yote anayoyazungumzia Mheshimiwa Mbunge, yamo. Ni programu itakayoanza mwaka huu wa fedha mpaka mwaka 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwamba haoni mikakati yoyote ya kuendeleza sekta hii ya uvuvi; mkakati lazima utengenezewe mazingira ili uweze kutekelezwa. Kwa hiyo, tusingeweza kupanga mambo ya uvuvi wa bahari kuu bila kuwa na legal framework ambayo inatuwezesha kutekeleza yale tunayotaka kufanya. Kwa hiyo, tulichoanza nacho ni kubadilisha kanuni za uvuvi wa bahari kuu ili sasa yale tutakayopanga kuyafanya, yaweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kusisitiza hapa kwamba akisoma kanuni na natumaini ameshazisoma; ataona wazi kwa vipi sasa hivi tutabadilisha sana sura ya Sekta ya Uvuvi wa bahari kuu hapa nchini na manufaa yataanza kuonekana. Sasa hivi tunapozungumza, wavuvi wa bahari kuu ambao wameomba kukata leseni kwa masharti mapya wapo wengi, wamekwishafika 30 na kadhaa hivi. Kwa hiyo, tuanze tu kutegemea kwamba manufaa makubwa ya uvuvi yataonekana hapa nchini na hicho kinachoitwa blue economy utakishuhudia kinatokea hivi karibuni.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri aliyoyajibu hata asiyoulizwa, maana yake kaulizwa ng’ombe wa maziwa tu kuku hatoi maziwa. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza kuna viwanda vingi vinavyozalisha maziwa hapa nchini, na kwa idadi ya maziwa ya pakiti tuliyonayo ndani ya nchi hii yanazidi mara tano au sita ya lita hizi alizozitaja. Je Mheshimiwa Waziri anataka kutuaminisha kwamba maziwa haya ya pakiti yanayozalishwa nchini ni zile tetesi kwamba ni unga unaotoka India unakuja kuzalisha maziwa hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili amesema wanategemea kuzalisha lita bilioni 3.8 ifikapo mwaka 2021/2022 ni kati ya miaka sita kuanzia leo. Mheshimiwa Waziri kuna miujiza gani ambayo mtaifanya kama Wizara muweze kuzalisha lita bilioni 1.7 katika kipindi hiki cha miaka sita? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba yako maziwa yanayozalishwa hapa nchini yanayotokana na unga wa maziwa na pia ni ukweli kwamba siyo maziwa yote yaliyo kwenye paketi ni yanatokana na huo unga wa maziwa. Wako wazalishaji wanaotumia unga wa maziwa kuzalisha maziwa ya paketi lakini pia wako wazalishaji wanaotumia maziwa ya paketi wanaotumia maziwa ya asili ya moja kwa moja. Viko viwanda vyetu wasindikaji wa maziwa huko Iringa na Tanga hawa hawatumii unga katika kuzalisha maziwa ya paketi ambayo yanauzwa hapa nchini. Lakini viwanda kama vya Bakhresa yeye anatumia unga katika kuzalisha baadhi ya maziwa anayotoa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili tutatumia muujiza gani kufikia hizo lita bilioni 3.8 muujiza ni ule tuliousema katika jibu letu la msingi kwamba combination ya hizo measures ya uzalishaji wa mbari safi, koo safi za mifugo uhimilishaji na uongezaji wa huduma katika mashamba yaliyopo na urasimishaji wa wavunaji wa maziwa katika vijiji vyetu huko, utatufikisha kwenye hili lengo letu la lita bilioni 3.8.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, katika ngo’mbe milioni 28 ni ng’ombe 700,000 tu wanaozalisha maziwa, hii inatokana na wafugaji kutokuwa na watetezi katika nchi wakiwemo wafugaji wa Iragua. Je, Wizara sasa iko tayari kuhakikisha wafugaji hawanyanyaswi na watu wa maliasili? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Serikali itahakikisha kwamba wafugaji nchini hawanyanyaswi na mtendaji yeyote wa Serikali na inapotokea tukapata ushahidi kwamba mtendaji yeyote wa Serikali amekiuka maadili ya kazi, basi Serikali haitasita kuchukua hatua mara moja.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa pembejeo za ruzuku hazitoshelezi mahitaji yote ya zao la korosho, Serikali inampango gani sasa zile pembejeo zingine ambazo mkulima atahitaji azipate sokoni kuagiza kwa pamoja (bulk purchase) kama itakavyofanya mbolea katika msimu huu kwa mwaka 2017/2018?
Swali la pili, ni ukweli usiopingika kwamba korosho mwaka huu imeingiza fedha nyingi sana za kigeni ni zao ambalo linaongoza, je, Benki ya Maendeleo ya Wakulima Tanzania ni lini itafungua tawi Mkoani Mtwara ili iweze kuwahudumia wakulima wa korosho wa Mikoa ya Mtwara na Lindi. Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, pembejeo hasa ya korosho ambayo inatumika zaidi ni hiyo sulphur na sulphur dust imekuwa ikiagizwa kutegemea na fedha ambayo imekuwa inapatikana katika ule Mfuko wa WAKFU wakati ule wa uendelezaji wa zao la korosho, pamoja na ile iliyokuwa inaagizwa kwa ruzuku na kuuzwa kwa wakulima kwa asilimia 50 bado wafanyabiashara binafsi walikuwa wanaagiza hii sulphur na kuiuza kwa wakulima ambao walikuwa hawapati fursa ya kununua ile inayoletwa kwa ruzuku ya Serikali. Kwa hivyo, sasa hivi tulichokifanya kwanza tumeongeza volume ya kuagiza kutoka tani 13,000 zilizoagizwa katika msimu uliopita mpaka tani 18,000 mwaka huu na lengo letu ni kwamba kwa msimu ujao wa korosho tutaongeza kutoka tani 18,000 mpaka tani 25,000 ambazo zinahitajika kwa ajili ya wakulima maeneo yote nchini.
Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao umekuwa unatumika ni uleule ambao tunau–introduce sasa kwenye mbolea ni wa bulk importation, umetusaidia sana katika kushusha bei ya sulphur dust yenyewe.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini TADB itafungua tawi huko Mtwara, nadhani mipango ipo na tulisema katika hotuba yetu ya bajeti kwamba, kwa kuanzia TADB wanataka wafungue matawi katika Kanda Saba hapa nchini, tulizitaja na jinsi kadri mtaji wao unavyoongezeka wataendelea kufungua matawi katika maeneo mengine nchini.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa gharamba za uzalishaji wa korosho za wabanguaji wa ndani wadogo na wakubwa ni kubwa pamoja na korosho yenyewe kuzalisha, na kwa kuwa wabanguaji wadogo na wakubwa wanashindanishwa kupata korosho kama malighafi katika mnada wa stakabadhi ghalani pamoja na wabanguaji kutoka nchi za nje kutoka India na Vietinam ambao wanapata ruzuku.
Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuwawezesha wabanguaji wadogo na wakubwa waliowekeza nchini, kupata korosho kama malighafi katika minada hapa nchini ili kutoa ajira na kuongeza thamani korosho zetu. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge ndilo eneo mojawapo ambalo Serikali inalifanyia kazi kwa umakini sana, kwa sababu ni katika eneo hili ambako au tutaendelea kusafirisha korosho ghafi kwenda nje au tutatengeneza utaratibu ambao korosho itabanguliwa nchini na kusafirishwa ikiwa imebanguliwa.
Mheshimiwa Spika, suala la soko, ndio msingi wa kwanza wa kujua, mbangue muuze iliyobanguliwa au muuze ambayo haijabanguliwa. Kwa sababu soko la korosho liko sensitive sana na ubora wa korosho yenyewe, mnaweza mkatumbukia kwenye ubanguaji, halafu mkaishia kukaa na korosho yenu mkakosa mnunuzi na wakulima wataathirika zaidi ama mkabangua nchini kwa utaratibu ambao unawezekana mkashindana kwenye soko, kwa hivyo mkatengeneza hizo ajira anazozisema hapa nchini na mkauza korosho mkapata soko kuuza korosho nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, ziko nchi ambazo wameweka utaratibu wa upendeleo, kwanza, kwa kuwaruhusu wabanguaji wa ndani wanunue katika masoko na baada ya kununua ndio wanaruhusu wanunuzi kutoka nje waingie na wao kununua, yote haya tunayatafakari na tutakuja na jawabu ambalo litakuwa kwa vyovyote haliwaweki katika uwezekano wa kukosa soko wakulima, pia tuwe na uwezo wa kubangua korosho wenyewe hapa nchini ili twende na yote mawili bila kuathiri jambo moja au lingine. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kuna mambo mengine Serikali haitakiwi hata iyaseme, kwa sababu yanaitia Serikali aibu. Wavuvi wanasema wanawafahamu, ni Waganda. Sasa ni kitu rahisi, kwa nini Serikali isikae na wavuvi, wavuvi wakasaidia kuwa- identify hawa watu? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Selasini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hizi kwamba kuna majambazi kutoka mje ya nchi wanavamia wavuvi huko ziwani, hata mimi nimepata kuzisikia, lakini baada ya kufanya verification kwa kuongea na wavuvi wenyewe, mimi naongea nao wengi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea na wavuvi wenyewe hasa katika visiwa vya huku Mara, kilichothibitika ni kwamba ni Watanzania hawa hawa ambao wanajifanya kwamba ni wageni wanapoenda kwenye visiwa jirani kwa kujifanya wanaongea lugha ambayo kama siyo Kiswahili sawa sawa. Ajenda ya kwamba ni majambazi kutoka sijui nchi za jirani, siyo sahihi. Hawa watu wanafahamika na tumeshatoa taarifa kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza wawatafute kwa sababu at least identity zao sasa zinafahamika. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kwenye taarifa ya habari ITV kulikuwa kuna kauli kwamba kuna uingizaji wa mbegu fake nchini. Kama kauli hii ina ukweli ni hatari sana kwani inamdhulumu mkulima ananunua mbegu akidhani ni mbegu yenye ubora lakini mbegu hii inakuwa ni feki matokeo yake anapanda havuni anachokitegemea.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu kauli hii ambayo ilitoka ITV jana usiku kwenye taarifa ya habari? Nashukuru.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi nimeiona hiyo kauli au statement iliyotolewa na kituo cha televisheni cha ITV kwamba nilikiri nchini hapa mbegu inayotumika kwa wakulima ni mbegu fake. Naomba nitoe ufafanuzi wa hilo jambo kwamba sikusema hivyo na jambo hilo lililotangazwa halina ukweli wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokisema ni kwamba wakulima wengi nchini bado wanatumia mbegu hafifu na kwa hivyo uzalishaji wao bado uko duni kwa sababu ya matumizi ya mbegu hizo na si kusema kwamba wanatumia mbegu feki. Kwa hivyo, niwaombe tu wenzetu wa kituo hicho cha televisheni wafanye hayo marekebisho ya kauli yangu. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema kwamba Serikali inachokisema ni kwamba bado yako matumizi ya mbegu hafifu kwa wingi hapa nchini na hiyo inatusababishia uzalishaji hafifu na si vinginevyo.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; swali langu kipengele cha (a) lilikuwa liko straight forward niliomba kwamba Serikali iongeze ardhi ya wakulima wadogo toka hekta 3,000 mpaka hekta 23,000, lakini kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri bado hakutoa jibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa swali langu ilikuwa ni ardhi iliyotengwa kwa ajili ya wakulima wadogo ni ndogo, naiomba Serikali iongeze. Je, ni nini kauli ya Serikali katika suala hili kuongeza ardhi hiyo kutoka hekta 3,000 kwenda 23,000? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sSwali la pili; kwa kuwa, katika jibu la Serikali limesema imetenga ardhi ya ukubwa wa hekta 3,000 kwa ajili ya wakulima wadogo wa vijiji vinavyozunguka shamba hili la Mkulazi kwa maana ya Vijiji vya Kidunda, Chanyumbu, Usungura, Mkulazi katika Kata ya Mkulazi na Kijiji cha Kwaba katika Kata ya Matuli; na kwa kuwa, mradi huu ni miongoni mwa miradi mitano ya kielelezo ya Kitaifa, manufaa yake inawanufaisha Watanzania wengi. Je, Serikali itatenga ardhi kiasi gani kwa ajili ya wananchi wengine nje ya vijiji hivi vitano wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili washiriki katika mradi huu wa wakulima wadogo. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ombi lake la kwamba ardhi ile iongezwe mpaka hekta 23,000 kwa ajili ya wakulima wadogo, naomba nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli katika majadiliano ambayo yanaendelea kati ya NSSF na PPF ambao hasa ndio wanaomiliki Mkulazi Holdings tayari kuna mwelekeo kwamba ardhi ile itaongezeka ili wakulima wadogo waweze kuongezeka kwa wingi zaidi. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba tayari hilo linafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na swali lake la pili ni kwamba huu ni mradi wa Kitaifa na hivyo ingekuwa vema kama vijana na wananchi wengine Watanzania wakaweza kunufaika. Nimhakikishie kwamba tayari Ofisi ya Waziri Mkuu ya Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu wameweka mkakati wa kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi watanufaika katika mradi huo na watatengewa blocks pamoja na kupatiwa mafunzo ili waweze kushiriki vizuri katika kilimo cha miwa, vijana wale watatoka nchi nzima siyo Morogoro peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari kuna huo mpango wa kuhakikisha vijana wengi wanashiriki zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba vijana wanapata elimu nzuri ya namna ya kuotesha miwa na kushiriki katika value chain nzima ya zao la miwa. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza na mimi nitoe shukrani kwa Mwenyezi Mungu kukujalia wewe kurudi hapa katika hali ya afya na uzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nyoyo zetu zimefurahika na nafsi zetu zimeburudika kukuona tena katika kiti chako. Karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri; Tanzania kila mwaka tunakuwa na upungufu wa sukari kutokana na uzalishaji mdogo wa viwanda, lakini zipo taarifa za uhakika kwamba Kiwanda cha Kagera Sugar kimekuwa kikisafirisha sukari kupeleka Uganda kila mwaka.
Je, ni kwa nini sukari haitoshi katika soko la nchi yetu na Kiwanda cha Kagera Sugar kinaruhusiwa kuuza Uganda lakini Zanzibar haitoshi kwa Zanzibar, lakini hairuhusiwi kuleta Tanzania Bara? Kwa nini?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza na mimi niungane na wengine kukupongeza na kukutakia afya njema sana na karibu tena katika Bunge letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba ni kwamba suala la sukari na biashara yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki linayo protocol maalum. Protocol hiyo inaelekeza kwamba bidhaa hii haiwezi kuhama kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine bila makubaliano kwanza kupitia katika Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Ndiyo maana hata sukari ikizalishwa namna gani Kenya au Uganda au Tanzania haiwezi kwa kirahisi tu kuvuka mipaka wa Tanzania kwenda au kutoka nje ya nchi hii.
Mheshimiwa Spika, kadri tulivyo na kumbukumbu, Serikali hii hajawahi kumpa kibali Kagera Sugar kupeleka sukari nje ya nchi. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mkoa wa Singida unastawisha sana zao la alizeti na wananchi wa Mkoa wa Singida wameelewa sana dhana ya viwanda. Sasa tatizo linakuja kwenye zao la alizeti kwa sababu Serikali haijaweka msisitizo katika kuleta ruzuku ya mbegu ili zao lile lilimwe kwa wingi kukidhi viwanda vinavyojengwa Mkoani Singida. Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mkakati mahsusi wa zao la alizeti ambao mkakati huo pamoja na mambo mengine umelenga kwanza kuongeza uzalishaji wa alizeti hapa nchini na usindikaji wa mazao yanayotokana na alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu kwa kuanzia umeanza kwanza na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa mbegu bora za alizeti unakuwa na utoshelevu. Tumeshapata sasa aina nne za alizeti variety mpya ambayo tija (productivity) yake ni kubwa kuliko mbegu hizi ambazo au variety hizi ambazo tumekuwa tunatumia hapa nchini kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ni kweli kwamba kwa miaka ya nyuma mbegu ya alizeti ilikuwa haitoshi, mbegu yenye ubora lakini sasa mbegu inayoweza kutoa mafuta megi zaidi na katika kiwango kidogo imeshapatikana, ni variety hizo nne na zitaanza kusambazwa kwa wakulima hapa nchini.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Mtemi. Wilaya ya Kakonko mwaka jana ilipata shida kubwa ya mbolea mpaka nikadiriki kumpigia Waziri wa Kilimo juu ya ukosefu wa mbolea katika Wilaya ya Kakonko. Tatizo hili lilitokana na wale suppliers ambao hawakuwa na uwezo kabisa wa kununua mbolea na kuiuza kwa bei elekezi kwa sababu ilikuwa inatoka mbali. Nataka Waziri, tena bila kumumunya maneno, anihakikishie kama wananchi wa Kakonko watapata mbolea mwaka huu bila usumbufu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa niaba ya Waziri Wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba tu nimhakikishie rafiki yangu Mheshimiwa Kasuku Bilago kwamba mfumo huu ambao tunataka kuwasiminisha Wabunge wote utampa huo uhakika anaoutaka. Naomba nimhakikishie kwamba mbolea itapatikana kwa wakati wote nchini.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulikubaliana na Mheshimiwa Waziri na Wabunge wote wa Mkoa wa Lindi kwamba zao la ufuta mwaka huu litanunuliwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, lakini mpaka hivi sasa tunapozungumza hakuna mipango ama mikakati yoyote ambayo tayari Serikali wameshaiweka tuanze kununua kwa stakabadhi ghalani na ufuta upo tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba commitment ya Mheshimiwa Waziri, kwamba tunakwenda na stakabadhi ghalani ama tunatumia mfumo wa kawaida ili wakulima sasa waache kuyumba kuona kwamba mfumo gani utatumika mwaka huu? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuli-commit kwamba msimu huu tutajitahidi kadri iwezekanavyo tuweze kuanza kuuza au kununua ufuta kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na maandalizi yanaendelea na hivi kesho tutakuwa na kikao cha Wakuu wa Mikoa yote inayozalisha ufuta ili tuone maandalizi yamefika kiasi gani na tuweze kutangaza rasmi lini tunaanzisha mfumo huu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mwaka jana mahindi yalishuka bei sana kutokana na Serikali kufunga mipaka hivyo kuwasababishia wananchi hasara kubwa sana kutoka bei waliyouza mahindi awali shilingi 20,000 wakauza shilingi 3,500.
Je, Serikali ipo tayari sasa mwaka huu kuhakikisha kwamba haifungi mipaka ili wananchi waweze kuuza mahindi kwa bei nzuri? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si kweli kwamba Serikali ndiyo inasababisha mahindi yashuke bei bali ni kwa sababu mahindi ni mengi yamezalishwa across region yote wamezalisha vizuri msimu uliopita lakini kwa sababu hili jambo linahitaji umakini katika kulishughulikia majibu mazuri tutayatoa katika hotuba yetu ya bajeti.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Tanzania ni nchi pekee ambayo mwakilishi wa nchi akifungwa, Waziri anakuja anashangilia Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu lilikuwa relevant kwenye msimu wa 2016/2017 na limechelewa. Lakini naomba niishukuru Wizara kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu huu wa 2018/2019 katika Kata za Ihanamilo, Nyanguku na Bulela nilimjulisha Mheshimiwa Waziri kwamba limekuwepo tatizo la pamba kurefuka na hazitoi matunda. Kutokana na sababu hiyo wakulima katika maeneo hayo wameshindwa kufahamu kama utafiti huu wa mbegu za pamba ulikuwa universal katika nchi nzima.
Sasa swali langu ni lini Wizara itatuma wataalam kwenda katika maeneo hayo ili tuweze kufahamu sababu za kwa nini pamba hiyo imerefuka tu na imeshindwa kuzaa matunda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wakulima katika maeneo yao walikopeshwa pembejeo na msimu wa ununuzi wa pamba umeanza na uzalishaji ulikuwa mbaya na ni lazima wakatwe, ni nini kauli ya Serikali katika suala hilo? Nashukuru.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kusema kweli kwamba swali lenyewe la msingi lilikuwa limepitwa na wakati kwa sababu katika msimu huu hatukuwa na ushahidi wa mahali popote kwamba mbegu tuliyoisambaza ilishindwa kuota, taarifa tuliyokuwa nayo ni kwamba imeota vizuri maeneo yote na kwa hiyo namshukuru sana kwa uungwana wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika maswali yake ya nyongeza, ni kweli taarifa kwamba pamba imerefuka kuliko ilivyotarajiwa ipo maeneo mengi, na tumewatuma tayari watafiti wetu wa Chuo cha Ukiriguru kwenda maeneo mbalimbali kujionea wenyewe na kutafiti ni sababu gani inayosababisha pamba ile irefuke. Suala ambalo kwa tafiti ya awali wamesema ni kuongezeka kwa mvua, mvua imenyesha nyingi kuliko ilivyokuwa kawaida kwa hiyo pamba imerefuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukosa vitumba, yapo maeneo ambako viuadudu vilichelewa kufika na wakulima wa maeneo hayo hawakuwa wamepulizia kwa wakati kwa hiyo vitumba vingi vikawa vimekwishaharibiwa na ndiyo maana huenda pamba ile inarefuka. Wale ambao hawakuvuna vizuri, tusubiri kwanza kwa sababu sasa hivi baada ya mvua kuanza kupungua pamba nyingine bado iko inatoa matunda na huenda pia mavuno yao yakawa mazuri tu bila tatizo lolote ingawa tayari watafiti wetu wako maeneo mbalimbali wanafuatilia jambo hili.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa lengo la Serikali ni kumuwezesha mkulima huyu wa pamba ili aweze kupata thamani ya pamba yake na kwa kuwa pamba hii imekuwa na gharama kubwa sana kwa mkulima kutokana na bidhaa ya pamba inayoingizwa kutoka nje. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka zuio la makusudi ili pamba inayozalishwa hapa nchini itumike kuzalisha bidhaa za pamba hapa nchini?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezekano huo upo kama mazingira ya matumizi ya pamba hapa ndani yatakuwa mazuri yanayoweza kutumia pamba yote inayozalishwa hapa nchini. Kwa sasa hivi uwezo wa kutumia pamba yote tunayozalisha hapa nchini ni mdogo na kwa hiyo wafanyabiashara wanalazimika kupeleka hii pamba nje ya nchi, ndiyo maana sasa hivi tunafanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda kuhakikisha kwamba viwanda vya kutengeneza nguo, viwanda vya kutengeneza bidhaa za pamba vinajengwa hapa nchini ili soko la ndani liwe kubwa kuliko soko la nje kwa bidhaa zinazotokana na pamba.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba kupata kauli ya Wizara juu ya ubora wa sulphur ambayo safari hii wakulima wetu wa zao la korosho watakwenda kupata. Ukirejea ripoti ya CAG msimu wa mwaka jana sulphur ambayo imesambazwa kwa sehemu kubwa ubora wake ulikuwa na mashaka makubwa sana; naomba Mheshimiwa Waziri atoe kauli, safari hii sulphur iko katika kiwango gani? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sulphur ni kiuatilifu kinachotumika kwenye zao la korosho na taratibu za uingizaji wa sulphur hapa nchini ziko kwa mujibu wa sheria. Tunacho chombo chetu cha TPRI cha kuhakiki ubora wa sulphur kabla ya kuruhusu sulphur hiyo kuingia hapa nchini. Kwa hiyo naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara kupitia TPRI inajitahidi kuhakikisha kwamba sulphur inayoingizwa nchini ina ubora unaokubalika.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na watendaji wote wa Kilimo, wanajitahidi sana kuokoa zao la pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kabla sijauliza, nisahihishe tu kwenye Hansard kwamba hakuna Jimbo linaitwa Bunda Vijijini. Kuna Jimbo linaitwa Bunda. Kwa hiyo kwenye Hansard kusomeke kuna Jimbo linaitwa Bunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa wakulima wa pamba na kwa kuwa katika jibu la msingi Naibu Waziri amesema kuna watu walikopa pamba na kuna vikundi vilifanya mkataba na wana makampuni kukopa pamba, sasa hili tamko la Serikali la kukata shilingi moja kwa kila mkulima ili kulipia pembejeo na hata yule ambaye hakukopa, ni la nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali imejiandaa vipi sasa kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza kutokana na miongozo yake ya mara kwa mara ambayo haijawa na maandalizi? Kwa mfano, kuna suala la wakulima kufungua akaunti, kuna suala la pamba kununuliwa na ushirika au na watu binafsi kwa maana ya ushirika kununua pamba, kuna suala la kwamba ushirika hauna fedha ya kununulia pamba, sijui ni watu binafsi watatoa kwenye ushirika; Serikali imejiandaa vipi sasa kukabiliana na matatizo haya ambayo watu watayapata kutokana na miongozo yake hii mifupi? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi. Pia nampongeza Mheshimiwa Getere kwa maswali haya ya muhimu sana katika tasnia ya pamba. Nianze na swali lake la nyongeza la kwanza kuhusu fedha; shilingi moja moja aliyoisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pembejeo waliyopata wakulima wengi walio katika mkataba ni lazima ilejeshwe na utaratibu wa kuirejesha ile pesa ni kwa makato kutokana na mauzo yao. Hiyo fedha inayokatwa siyo tu kwamba itafanya kazi ya kurejesha pembejeo waliyopata, lakini ili twende vizuri katika msimu ujao tunapaswa kuwa na fedha ya kuanzia kwa ajili ya kupata pembejeo hizo hizo ambazo wakulima watapata. Ndiyo maana Serikali imeshatamka kwamba msimu ujao wakulima wa pamba kote nchini hawatakopeshwa au pembejeo kwa maana ya dawa au mbegu za pamba. Watapata bure na hii inatokana na hii fedha ambayo wanakatwa sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza, siyo kwamba Serikali imesema ushirika utanunua pamba ya wakulima, kwa sababu wakulima wenyewe ndiyo ushirika. Kwa hiyo, kitakachofanya sasa hivi na kinachofanyika ni ushirika unakusanya pamba ya wanachama wake halafu wanunuzi wanaenda kununua kwenye ushirika huo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Kati ya wakulima wanaopata taabu kwa kulaliwa bei na watu ambao hawana soko la uhakika ni wakulima wa pamba. Kwa sababu wanunuzi wengi wanalangua na wanapanga bei wanayoitaka wao na mwisho wa siku wakulima wanapata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, ni lini Serikali itawatafutia wakulima wa pamba soko la uhakika ili na wenyewe waweze kunufaika na kilimo cha pamba? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nitofautiane kidogo sana na Mheshimiwa Bulaya kuhusu uhakika wa soko. Soko la pamba ni la uhakika na hatujawahi kuwa na tatizo la kuuza pamba nchini. Pamba ni bidhaa inayouzwa na nchi nyingi duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, soko la Tanzania haliwezi kuwa tofauti na Soko la Dunia la Pamba. Majadiliano yanapofanyika kati ya wadau na wauzaji, ni zao pekee ambalo kwa msingi wadau wanajadiliana na wanunuzi, wanafikia muafaka wa bei. Hii inakuwa pegged kwenye bei ya pamba katika Soko la Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bei inayopatikana siyo kwamba inawalalia wakulima, lakini pia inawapa faida wafanyabiashara na wakulima wanapata haki yao kutegemea na soko la dunia lilivyo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Suala hili ni nyeti sana na sijui kwa muda tulionao kama unatosha kulizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri anasema pamba itauzwa kwa kukusanywa na Vyama vya Ushirika vilivyoko kwenye maeneo yetu, makampuni wataenda wanunue pamba hapo. Tunajua wote ushirika kwenye nchi yetu hali yake ilivyokuwa na sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza swali, nisirefushe maneno, je, Serikali imejiandaa kwa namna gani kuhakikisha kwamba huu ushirika tunaouzungumza uko imara na kwamba utahakikisha mkulima hapotezi pamba yake na bei ya pamba inapanda kulingana na mahitaji?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ni kweli ushirika kwa miaka ya nyuma hapa umekuwa na tatizo sana hasa ushirika wa zao la pamba. Siyo siri kwamba wakulima wengi wa pamba walipoteza pesa zao kutokana na viongozi wa Ushirika ambao hawakuwa waaminifu na hivyo kupelekea Serikali wakati ule kuruhusu watu binafsi kuingia katika kununua pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ndaki na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tumefanya jitihada kubwa sana kwanza za kuhakikisha kwamba viongozi waliochaguliwa katika Vvyama vya Msingi vya Wakulima wa Pamba safari hii ni wale viongozi waadilifu ambao hawatachezea pesa za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoa rai kwa Viongozi wa Ushirika katika Vyama vya Msingi nchini kote kwamba yule anayetaka kuonja sumu kwa kuiba pesa ya wakulima wa pamba afanye hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na matatizo ya ushirika yaliyokuwapo, lakini lengo la Serikali ni kuhakisha kwamba ushirika utaimarika, wizi katika ushirika utakoma na wakulima wapate sauti ya pamoja kupitia ushirika. (Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi, naomba kuuliza Wizara ya Kilimo hapo. Kwa kuwa wakulima wa kahawa ni sawasawa na wakulima wa pamba. Wakulima wa pamba wamewaruhusu waliofanya biashara ya mkataba waweze kuendelea na shughuli hiyo, lakini wakulima wa kahawa katika nchi wa mkataba hawazidi watano mpaka sita. Kwa nini Wizara inakuwa double standard, msimu umeanza sasa hivi wiki ya pili watu hawa hawataki kuwapa kibali cha kuweza kukusanya kahawa kwa sababu ni biashara yao. Naomba tujue hawa haki yao wanaipata wapi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, utaratibu tuliouweka sasa hivi lengo lake la kwanza ni kuhakikisha kwamba wakulima wanapata malipo stahiki kwa jasho lao. Mfumo tuliokuwa nao sasa hivi kwa kiwango kikubwa ulikuwa hautoi malipo stahiki kwa jasho la wakulima na moja ya njia zilizotumika kuwanyima haki wakulima ilikuwa ni mfumo wa kununua kahawa kwa kulipa advance kutoka kwa wafanyabiashara na hasa katika Mkoa ambako Mheshimiwa Bulembo anatoka maarufu kwa jina la Butura. Ili kukabiliana na Butura, lazima kuweka mfumo unaofafana maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, jana nilisema hapa ndani wakati nachangia hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali kwamba pale ambapo mikataba hiyo iliingiwa officially kwamba kuna mkataba na mamlaka za Serikali zinatambua mikataba hiyo kama ilivyo kwenye pamba, pamba mtu haingii mkataba mtu na mtu mmoja, mikataba hiyo inaingiwa kupitia mamlaka za Serikali, kama wako wakulima wa kahawa ambao wameingia mikataba kwa njia hiyo, nilielekeza kwamba wapeleke habari hiyo haraka Bodi ya Kahawa ili waweze kupata utaratibu wa kuuza kahawa kwa mtu waliyeingia naye mkataba.
Mheshimiwa Spika, ile mikataba ya kuingia kienyeji ndiyo utaratibu uliokuwa unasababisha watu kupoteza haki yao na jasho lao kwa kuuza kwa watu ambao wanawapa malipo kidogo kwa kahawa ya bei kubwa.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwanza KACOFA iko kwenye Kata yangu, Organic iko Kalinze ambako ni Kata yangu. Kwa masikitiko makubwa Waziri anasema kesi iko Mahakamani, si kweli hakuna kesi Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, kilichotokea, KACOFA walipeleka Kahawa na hawa Organic-Kalinze walipeleka Kahawa. Kile kiwanda kilipouza Kahawa ile kikawalipa KACOFA, hakikuwalipa Kalinze Organic. Kalinze Organic walipoanza kufuatilia pesa zao wamefanya usuluhishi Wizarani na Bodi ya Kahawa mwisho wake Kiwanda kikasema kitawalipa, naomba nitoe maelezo haya; kitawalipa Organic taratibu.
Mheshimiwa Spika, toka mwaka 2011 kiwanda kile ambacho kilikubali kuanza kuwalipa watu wa Kalinze Organic, kwamba tutawalipa taratibu mpaka leo hakijalipa. Waziri anakuja leo hapa anasema suala lipo kwa Attorney General wakati wameshakubaliana waanze kuwalipa taratibu.
Mheshimiwa Spika, swali langu; naomba Wizara isimamie watu wa Kalinze Organic waweze kulipwa fedha zao kwa sababu makosa haya yamefanywa na kiwanda kile cha Moshi.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi alivyojibu hili swali la msingi la Mheshimiwa Albert Obama. Jambo hili ni la siku nyingi na hatua za awali kama anavyozisema Mheshimiwa Serukamba ni kweli zilichukuliwa namna hiyo. Kosa lililofanyika ni ku-identify nani anatakiwa kulipwa baada ya yule kupeleka ile kahawa kule mnadani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Bodi ya Kahawa ilivyopokea yale malipo ikapeleka kwa mtu ambaye alitajwa na mtu aliyeleta kahawa kwamba ndiye beneficiary wa hiyo kahawa; kwa hivyo wakamlipa na wale watu wakapokea pesa isiyo yao na wakaitumia.
Mheshimiwa Spika, baadaye ilipoonekana kwamba wamepokea pesa isiyo yao na wametumia, kwanza wakatakiwa wasuluhishwe tu amicably, wakaitwa, wakakiri kwamba watalipa msimu utakaofuata, kwamba watakapouza kahawa msimu unaofuata watalipa hilo deni. Wale waliokuwa wanadai Mheshimiwa Serukamba wakakubaliana na hiyo position, kwamba watapewa pesa yao msimu utakaofuata.
Mheshimiwa Spika, msimu uliofuata wale mabwana wa KACOFA hawakupeleka kahawa, kwa hivyo sasa kukawa na default ya makubaliano hayo; na baada ya hapo ndipo taratibu zikaanza. Nikiri tu kwamba jambo hili lilienda polepole lakini sisi safari hii tulichokifanya tumelipeleka kwenye vyombo vya uchunguzi kwanza tujiridhishe kwa nini walitumia hela ambayo si yao at a time wakati ya kwao walishalipwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, humu ndani kuna jinai katikati ya hili jambo, kwamba mtu amekuta benki fedha ambayo si kwake lakini bila kuuliza benki hela hii imetoka wapi, ameitumia, Sheria za Fedha ziko wazi, umeona! Sasa katika hatua hiyo ndiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali atatushauri sasa hivi tuendelee na hatua gani.
Mheshimiwa Spika, kama atatushauri tuwapeleke Mahakamani ili wale viongozi wa ule Ushirika waweze kuchukuliwa hatua wachukuliwe hatua, kwa sababu as we speak hawa hela ya kuwalipa wale wenzao mara moja, kwamba tungewaambia leteni hizi pesa tuwalipe wale ambao wanastahiki ya kupata hizo pesa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Sasa hivi ni kipindi cha msimu wa kahawa. Vyama vya Ushirika vimeshindwa kuwahudumia wananchi kupata maturubai ya kuvunia Kahawa na hii kahawa inaendelea kukaukia Mashambani, wananchi wamekosa msaada. Hata hivyo, hata wale ambao wamepata maturubai, maturubai haya hayana viwango yanachanika hovyo. Ni hatua zipi za dharura ambazo zitachukuliwa ili kunusuru zao hili na mkulima aweze kulifaidi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na matatizo sana katika suala zima la Vyama vyetu vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika na ndiyo maana kama Serikali tunasema kwamba, tuko katika mikakati ya kuhakikisha tunafufua, tunaimarisha na kuboresha Vyama vya Ushirika.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo kutokana na swali lake hili la msingi katika Jimbo lake la Kyerwa, kwamba mpaka sasa hivi kunasuasua, naomba nichukue fursa hii kuagiza Chama Kikuu cha Ushirika cha Kyerwa kuanzia leo wahakikishe kabisa kwamba, zoezi zima la mazao ya kahawa katika Jimbo la Kyerwa wanafanya kazi yao kwa ubunifu, wanafanya kazi yao kwa utii, wanafanyakazi yao kwa weledi, wanafanyakazi yao kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, lakini na mimi kama Naibu Waziri nikitoka hapa Bungeni ninaahidi kuwapigia Vyama Vikuu vya Ushirika vile AMCOS pale Kyerwa nikishirikiana na Mrajisi wangu kuhakikisha kwamba jambo hili halijirudii na linaweza kufanikiwa kwa uhakika. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa zao la mchikichi linafanana na zao la nazi; na kwa kuwa watu wa Pwani wanategemea sana zao la nazi; kwa kipindi kirefu zao hilo limekumbwa na ugonjwa ambapo minazi inanyauka na Serikali iliahidi kufanya utafiti. Je, utafiti huo umefikia wapi na kuna mkakati gani wa kuhakikisha zao hilo litafufuliwa upya? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Naomba nimjibu Mheshimiwa Zaynab Vulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyauko ni ugonjwa ambao unakumba mazao mengi na mbinu iliyopo mpaka sasa ya kukabiliana na mnyauko ambayo inaeleweka ni kwa kufanya usafi (sterilization). Mbinu hii imekuwa ikiandamana na hasara na vimelea hawa kuendelea kubaki kwenye maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasayansi sasa hivi duniani wanaelekea kwenye mbinu nyingine bio-control ambapo enzymes zinazalishwa kwa ajili ya kimelea mahsusi kilichosababisha mnyauko kwenye zao au mmea fulani. Utafiti huu umeendelea kufanyika katika vituo vyetu vya utafiti na sasa hivi tuko katika hatua ya kujenga kiwanda cha kuzalisha hivi vimelea (enzymes) zitakazokabiliana na aina mbalimbali ya minyauko katika mimea yetu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Bodi ya Mazao Mchanganyiko iko imara na haijatetereka. Naomba kuuliza kwa nini wakati tunaingiza zao la ufuta kwenye stakabadhi ghalani wasimamizi wakapewa Bodi ya Maghala badala ya Bodi ya Mazao Mchanganyiko?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Kuchauka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Bodi kununua mazao na mfumo wa kuuza ni vitu viwili tofauti. Hata hiyo Bodi ya Mazao Mchanganyiko ikitaka kununua zao linalouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, itabidi na wao waende wakanunue huko kwenye huo mfumo. Siyo kwamba Bodi ya Mazao Mchanganyiko maana yake ni mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, Bodi na yenyewe itashiriki kununua kama wanunuzi wengine walivyo kwa kwenda kununua kwenye mfumo huo wa stakabadhi ghalani. Kwa hivyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge asichanganye haya mambo, Bodi hii itafanya biashara ya kununua mazao na kuuza kwa kushindana na wafanyabiashara binafsi na watu wengine katika mazao mbalimbali.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali kuhusu ununuzi wa pamba, Mkoa mzima wa Mara, Wilaya za Serengeti, Bunda, Musoma Vijijini na maeneo mengine mpaka sasa hawajaanza kununua pamba. Tuliomba hapa kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo kwamba mtindo uliokuwa unatumika zamani wa kununua pamba uendelee kuliko huu wa kulazimisha mwananchi atembee kutoka Kilometa ngapi akafungue akaunti benki jambo hili limekuwa gumu kwa wananchi.
Kwa hiyo, naomba kuuliza ni lini pamba itaanza kununuliwa Mkoa wa Mara?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu wa pamba ulifunguliwa tarehe 1 Mei na ununuzi unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kutegemeana na upatikanaji wa pamba ulivyo. Pamba haikomai kwa mara moja nchi nzima, inakomaa tofauti kulingana na ukanda wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi ununuzi katika Mkoa wa Mara umeshaanza, nimezungumza leo asubuhi na Mkuu wa Mkoa. Tatizo lililoko Mara ni wale wanaohusika kununua wanawatapeli wananchi kwamba akilipa taslimu anapewa Sh.800 badala ya Sh.1,100 bei iliyotangazwa ya kununua pamba msimu huu. Sasa hivi maelekezo yapo, watafutwe wanaofanya huo udanganyifu ili wananchi wapate haki yao kwa mauzo halali wanayoyafanya.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Naibu Waziri anafanya kazi nzuri, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa butura ulikuwa unamsaidia sana mkulima wa kahawa Mkoa wa Kagera kupunguza ukali wa maisha wakati anasubiri kuvuna kahawa shambani. Je, Serikali imejipangaje kumsaidia huyu mkulima baada ya kuzuia uuzaji wa butura? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, butura ni mfumo ambao wakulima wamekuwa wanauza mazao kabla hawajavuna na ni mfumo ambao umewanyonya kwa miaka mingi. Ndiyo, walikuwa wanapata fedha lakini fedha wanayopata hailingani na thamani ya mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, ni mfumo ambao sasa hivi Serikali inahakikisha kwamba hautaendelea. Badala yake Vyama vya Ushirika vimeshawishiwa na tunavisaidia kuweka utaratibu ambao utakuwa unaweza kuwawezesha wakulima wenye shida ndogondogo badala ya kuuza mazao kwa bei za chini sana ambazo wananyonywa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa swali zima limejikita kwenye mambo ya pembejeo; na kwa kuwa wakulima wengi sana wa mazao kama ya pamba, muhogo, chai na hata korosho, wamekumbwa na tatizo la wadudu waharibifu. Kwa mfano, wakulima wa pamba na wakulima wa mahindi wanasumbuliwa na yule fall armyworm wakulima wa muhogo wanasumbuliwa na cassava mealybug.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni nini mkakati wa Serikali kumwondolea adha mkulima ambaye anajitahidi kulima sana lakini anasumbuliwa na hawa wadudu au viwavijeshi ambao ni waharibifu zaidi? Nataka tamko la Serikali.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. American fall army worm wameonekana kwa mara ya kwanza nchini mwaka jana. Jitihada ya Serikali iliyofanyika ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha elimu inawafikia wakulima wote namna ya kukabiliana na hawa wadudu. Kwa hivyo, tulichokifanya ni kueneza hii elimu lakini na kufanya utafiti wa haraka kubaini ni aina gani ya dawa inayoweza kuuwa hawa wadudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa hiyo tumekwishaitangaza ili mwananchi akiona mazao yake yanashambuliwa atumie dawa hiyo kuuwa hawa wadudu. Tunafanya hivyohivyo na kwa visumbufu vingine vya mimea.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mheshimiwa Ngombale na siyo Mheshimiwa Katani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mwaka huu ilijielekeza kwamba sisi wa zao la ufuta tutatumia Stakabadhi Ghalani…
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mheshimiwa Vedasto Ngombale sio Mheshimiwa Katani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Katani hayupo kwa leo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru baada kuwa sasa umetambua jina langu vizuri. Ninachosema ni kwamba Serikali ilielekeza mwaka huu katika zao la ufuta utaratibu wa manunuzi utafanyika katika Mfumo wa Stakabadhi Ghalani na kwamba mikoa yote inayolima ufuta itatakiwa kuingia katika mfumo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ninavyozungumza ufuta umeshakuwa tayari na kuna baadhi ya mikoa tayari wameshaanza kuuza katika mfumo holela na Serikali iko kimya haijasema chochote. Naomba kufahamu, je, tutaingia katika mfumo wa Stakabadhi Ghalani au tutaendelea katika utaratibu ule ambao tulikuwa tumeufanya mwaka jana? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli kwamba, ufuta ni moja ya zao ambalo Serikali ilidhani na inatarajia kuliweka kwenye Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, lakini ili uingie kwenye huo mfumo yako maandalizi ya msingi ambayo lazima yafanyike vinginevyo mfumo hautafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachofanya sasa hivi tunakamilisha hayo maandalizi, tutakuwa na mkutano wa wakuu wa mikoa yote inayolima ufuta ili tujiridhishe kwamba maandalizi hayo yako in place tuweze kuanzisha mfumo wenyewe.