Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Charles John Tizeba (10 total)

MHE. MARIAM N. KISANGI (k.n.y MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE) aliuliza:-
Hapo zamani kulikuwa na Shirika la Uvuvi la TAFICO lenye Makao Makuu yake Kigamboni ambalo lilikufa kutokana na uendeshaji mbovu:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua shirika hilo?
(b) Je, Serikali imejipanga vipi kusimamia deep fishing ili iweze kunufaika na mapato yatokanayo na uvuvi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) lilianzishwa mwaka 1974, lengo likiwa ni kuendesha shuguli za uvuvi kibiashara. Aidha, mwaka 1996 TAFICO iliwekwa chini ya iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa ajili ya utaratibu wa ubinafsishaji. Mwaka 2005 TAFICO iliondolewa kwenye orodha ya Mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa na kurejeshwa Wizarani kuendeleza ubinafsishaji wake. Hata hivyo, mwaka 2007 Baraza la Mawaziri lilisitisha uuzwaji wa TAFICO na kuelekeza kuwa mali zisizohamishika ikiwemo ardhi zibaki kwa ajili ya matumizi ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inaendela na mpango wa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), ikiwa ni pamoja na kuwasilisha mapendekezo ya Baraza la Mawaziri kwa hatua husika.
(b) Mheshimwia Naibu Spika, ili kusimamia mapato yatokanayo na uvuvi katika ukanda wa uchumi wa bahari, Serikali zetu mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja zilianzisha Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority) kupitia Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu Na. 1 ya mwaka 1998 na marekebisho ya mwaka 2007. Taasisi hii ina jukumu la kusimamia uvuvi katika eneo la Uchumi la Bahari Kuu, ikiwemo utoaji wa leseni kwa meli za kigeni na za ndani zinazovua kwenye ukanda huo. Aidha, mamlaka inaendelea kufanya doria za anga na kuhuisha mfumo wa kufuatilia meli, kufuatilia vyombo vya uvuvi baharini (Vessel Monitoring System) ili taasisi iweze kudhibiti wanaovua bila kulipa leseni. Pia Serikali inaendelea na taratibu za kuwezesha ujenzi wa bandari ya uvuvi ambayo itawezesha meli za kigeni zinazovua bahari kuu kutia nanga hapa nchini na hivyo kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania pamoja na Pato la Taifa kwa ujumla.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Baadhi ya mambo ambayo yanamkosesha mkulima wa tumbaku mapato stahiki ni pamoja na tozo za pembejeo zinazoingizwa nchini na kuzifanya kuwa ghali, kuwepo wanunuzi wachache wa tumbaku na hivyo kudumaza ushindani wa bei na uwezo mdogo wa kifedha wa Bodi ya Tumbaku:-
(a) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuondoa utitiri wa tozo za pembejeo?
(b) Je, hadi sasa Serikali imevutia wanunuzi wangapi kutoka China na kwingineko?
(c) Je, kuanzia msimu wa 2016/2017 Serikali imeiongezea Bodi ya Tumbaku kiasi gani cha fedha katika bajeti yake ili iendeshe masoko ya tumbaku kwa ufanisi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na bei kubwa ya pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi, Serikali imeunda Timu ya Kitaifa kupitia kodi na tozo mbalimbali katika pembejeo hizi ili kuona uwezekano wa kuzipunguza au kuziondoa kabisa. Kazi hii itakapokamilika, wananchi watafahamishwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku bado inaendelea na mazungumzo na baadhi ya wanunuzi wa tumbaku kutoka China na Kampuni ya Sunshine kutoka China imeonesha nia ya kuwekeza katika ununuzi wa tumbaku nchini na imeshakamilisha taratibu zote hapa nchini. Kwa sasa kampuni hii inafuatilia kibali cha kuingiza tumbaku ya Tanzania nchini China. Katika hatua nyingine ya kuongeza ushindani katika soko la tumbaku, kampuni ya Japan Tobacco International imeanza ununuzi wa tumbaku msimu uliopita na imeongeza ushindani katika biashara ya tumbaku.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti, Bodi ya Tumbaku imekuwa ikipata fedha kidogo kutoka Serikalini ambazo hazikidhi mahitaji ya Bodi kuendesha shughuli zake ikiwa ni pamoja na zoezi muhimu la masoko. Kutokana na hali hiyo, msimu wa mwaka 2014/2015, wadau walichangia uendeshaji wa masoko ya tumbaku, lakini kwa sasa Bodi ya Tumbaku inatumia fedha zinazotokana na ada ya export permit inayolipwa na makampuni ya usafirishaji tumbaku nje ambayo ni asilimia 0.025 ya thamani ya tumbaku inayosafirishwa. Fedha hizi kwa sasa ndizo zinazosaidia Bodi kuendesha shughuli zake ikiwa ni pamoja na jukumu la kuendesha masoko.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA (K.n.y MHE. SAVELINA S. MWIJAGE) aliuliza:-
Pamoja na Serikali kuwa na mipango mizuri kwa wananchi wake lakini mipango hiyo baadhi yake haitekelezwi; wakulima wengi nchini wanalima bila ya kuwa na elimu ya kilimo na hivyo kushindwa kulima baadhi ya mazao ya biashara na chakula kama vile ndizi, kahawa, mahindi, maharage, karanga na kadhalika:-
(a) Je, Serikali itawasaidiaje wakulima hao ili wanufaike na kilimo pamoja na mazao yao kwa chakula na biashara?
(b) Je, Serikali ina mipango gani juu ya utoaji wa elimu kwa wakulima ili wafaidike na kilimo chao?
WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kutoa elimu kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija kwa mazao wanayoyalima. Hatua mbalimbali zinachukuliwa kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kutosha. Mathalani mwaka 2006, Wizara yangu ilianzisha mpango wa kuimarisha huduma za ugani baada ya kubaini kuwa walikuwemo Maafisa Ugani 3,379 tu ukilinganisha na mahitaji ya Maafisa Ugani 15,022.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilichukua hatua kwa kuwasomesha vijana wengi zaidi kwenye vyuo vya kilimo na kuajiri Maafisa Ugani 5,377 na hivyo kufanya jumla ya wataalam kuwa 8,756 kwa sasa ambao wanaendelea kutoa elimu ya kanuni za kilimo bora kwa wakulima. Hata hivyo, bado kuna upungufu wa Maafisa Ugani 6,266 ambao Serikali itaendelea kuajiri kadri fedha itakapokuwa inapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya inaendelea kueneza matumizi ya Vyuo vya Rasilimali za Kilimo vya Kata (Ward Agricultural Resource Centers) ambapo jumla ya vituo 322 vimejengwa katika halmashauri 106 kwenye mikoa 20. Kati ya hivyo, vituo 224 vimekamilika na vinafanya kazi ya kutoa mafunzo kwa wakulima na wafugaji, mashamba ya majaribio, kutoa huduma kwa wafugaji na matumizi ya zana za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wizara inaandaa na kurusha vipindi vya redio kuhusu kanuni za kilimo bora kupitia Redio ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Mwaka wa 2015/2016 jumla ya vipindi 122 vilirushwa ambapo vipindi 52 vilirushwa kupitia TBC Taifa na vipindi 70 vilirushwa kupitia redio binafsi za jamii. Maonesho ya kilimo yanayofanyika kila mwaka kitaifa na katika kanda mbalimbali za kilimo hutumika kama njia mojawapo ya kuwapatia wakulima elimu ya kanuni za kilimo bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu, naomba kuchukua nafasi hii kuziomba Halmashauri zote nchini kukamilisha, kuviwezesha na kuvisimamia Vituo vya Rasilimali za Kilimo vya Kata ili viweze kutoa huduma za kanuni za kilimo bora kwa wakulima kwa mazao mbalimbali wanayoyazalisha.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Sekta ya Uvuvi hapa Tanzania inaajiri wananchi wengi lakini wavuvi hawanufaiki kutokana na changamoto mbalimbali:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupitia mlundikano wa leseni kwani kuna aina nyingi sana za leseni, kwa mfano, leseni ya chombo, leseni ya mvuvi, leseni ya aina ya samaki, leseni ya eneo la uvuvi na kadhalika?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wavuvi nyenzo za uvuvi ili waondokane na uvuvi haramu?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba ni kweli sekta ya uvuvi ina wananchi wengi wanaojihusisha na uvuvi moja kwa moja na wengine wanaojihusisha na shuguli mbalimbali za sekta hii ya uvuvi. Sekta ya Uvuvi husimamiwa na Sheria ya Uvuvi Na. 22 na Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009. Kwa mujibu wa sheria hii, kuna leseni ya chombo, leseni ya uvuvi na leseni ya aina ya samaki.
Pia Mamlaka ya Kusimamia Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) nao hutoa cheti cha usalama wa chombo. Aidha, Jeshi la Zima Moto na Uokoaji linataka kila chombo cha uvuvi kiwe na chombo cha kuzimia moto (fire extinguisher). Pia Mamlaka za Mtaa (Serikali za Mitaa) nazo zimetunga sheria ndogo ndogo kuhusiana na masuala ya uvuvi kama njia mojawapo ya kuongeza mapato katika maeneo yao. Hata hivyo, kwa sasa Serikali inapitia upya leseni na tozo zenye kero kwa wananchi ili kuona uwezekano wa kuzipunguza au kuzifuta ili kuwanufaisha wavuvi. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kwa wavuvi juu ya athari zitokanazo na uvuvi haramu hususani kwa kutumia mabomu, sumu na zana zisizoruhusiwa kisheria. Aidha, Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika (outboard engines), nyuzi za kushonea nyavu (twines), nyavu za uvuvi na vifungashio ili kupunguza gharama za zana na vyombo vya uvuvi.
Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya nyavu na zana za uvuvi ambapo hadi sasa viwanda viwili vya kutengeneza nyavu vya Imara Fishnet (Dar es Salaam) na Fanaka Fishnet (Mwanza) na viwanda vinne vya kutengeneza boti za kisasa vya Yutch Club, Sam and Anzai Company Limited, Seahorse Company Limited vya Dar es Salaam na Pasiansi Songoro Marine (Mwanza) vimekwishajengwa.
Vilevile Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo ambapo jumla ya shilingi milioni 400 zilitolewa kama ruzuku ya zana za uvuvi na Serikali ilichangia asilimia 40 na mvuvi alichangia asilimia 60 na kupitia utaratibu huu injini za boti 73,000 zilinunuliwa.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha viwanda vya kusindika samaki na mazao ya uvuvi ili kuyaongezea thamani mazao hayo. Jumla ya maghala 84 ya kuhifadhi mazao ya uvuvi na viwanda 48 vya kuchakata mazao ya uvuvi vimejengwa. Viwanda hivyo vipo katika maeneo yafuatayo: Ukanda wa Pwani kuna viwanda 36; Ziwa Victoria kuna viwanda 11 na Ziwa Tanganyika kuna kiwanda kimoja. Pia Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu njia bora za uchakataji na uhifadhi wa samaki na mazao yake kwa viwanda na maghala hayo ili kulinda soko la ndani na nje ya nchi.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Zao la mwani limekuwa ni ukombozi kwa vikundi vya akina mama katika mwambao wa Pwani:-
(a) Ni lini Serikali itavipatia mtaji vikundi vya wanawake wa kilimo cha mwani ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 12,000 hadi 20,000 kwa mwaka?
(b) Ni lini Serikali itawapatia nyenzo na utaalam ili vikundi vya wanawake na vijana viweze kuzalisha chaza, walulu, kaa, kamba na pweza?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kabla sijajibu swali, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa imani yao kwangu katika kuniteua kuongoza Wizara hii nyeti ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, sasa basi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba zao la mwani limekuwa chanzo cha mapato kwa akina mama wanaoishi katika Ukanda wa Pwani lakini hata hivyo kuna changamoto za upatikanaji wa mitaji na nyenzo za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imehamasisha wakulima wa mwani zaidi ya 3,000 kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka kwenye taasisi za kifedha, kama vile Benki ya Kilimo. Vikundi vilivyopo hivi sasa ni Msichoke kilichoko Bagamoyo, Maliwazano na Kijiru vilivyoko Mkinga, Jibondo kilichoko Mafia, Mikocheni, Ushongo na Mkwaja vilivyoko Pangani, Naumbu na Mkungu vilivyoko Mtwara Mjini. Vilevile Umoja wa Wakulima wa Mwani umeanzishwa mwaka 2013 ili uweze kuwa kiunganishi kati ya taasisi za kifedha na wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuwahamasisha wakulima kujiunga katika vikundi na kuvisajili. Aidha, Serikali itawezesha wakulima zaidi ya 1,200 kwa kuwapatia mtaji kwa njia ya VICOBA kupitia mradi wa SWIOFish unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ili kuongeza uzalishaji.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiwapatia elimu, nyenzo na utaalam wazalishaji wa lulu, kaa na kamba mti kupitia mradi wa Marine and Coastal Environment Management Project ulioisha mwaka 2012. Vikundi vifuatavyo vimewezeshwa na mradi huo:-
(i) Vikundi vya ulimaji wa mwani cha Msichoke kilichoko Bagamoyo, Maliwazano na Kijiru vya Mkinga, Mikocheni, Ushonga na Mkwaja vya Pangani, Jibondo kilichoko Mafia;
(ii) Vikundi vya unenepeshaji wa kaa vya Nyamisati - Rufiji, Kipumbwi -Pangani;
(iii) Vikundi vya utengenezaji wa lulu vya Akili Kichwa kilichoko Mtwara Mjini;
(iv) Vikundi vya ufugaji samaki aina ya mwatiko ni Naumbu na Mkungu vilivyoko Mtwara Vijijini na Tangazo - Mtwara Vijijini; na
(v) Vikundi vya ufugaji wa kambamti ni Mpafu - Mkuranga na Machui - Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali itaendelea kutoa elimu na ruzuku kwa wakuzaji wa viumbe kwenye maji kwa kupitia bajeti ya Serikali na mradi wa SWIOFish na hivyo kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-
Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020 iliahidi kuimarisha huduma za ugani na mafunzo kwa kuongeza udahili wa Maafisa Ugani wa Uvuvi kutoka 1200 hadi 2500 kwa mwaka ili kuwepo Maafisa Ugani kwa ngazi ya kata na kuimarisha huduma za uvuvi na ufugaji samaki.
(a) Je, ni lini mkakati wa utekelezaji wa suala hili ambao utatoa ajira nyingi kwa vijana utaanza?
(b) Je, kuna mkakati gani wa kuzishirikisha Halmashauri nyingi katika kuhamasisha uchimbaji wa mabwawa na ufugaji wa samaki hasa katika maeneo yenye ukame ili kuongeza lishe bora na pia ajira kwa vijana?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kuongeza za udahili ili kuongeza Maafisa Ugani wa Uvuvi ulianza kwa Wizara kuimarisha Wakala wa Elimu ya Mafunzo na Uvuvi (FETA) katika Kampasi zake za Mbegani (Bagamoyo), Nyegezi (Mwanza), Kibirizi (Kigoma), Mwanza South (Mwanza). Vilevile ili kuongeza udahili wa wanafunzi Serikali itakamilisha ujenzi wa kampasi za Mkindani (Mtwara), Gabimori (Rorya) ifikapo mwaka 2019 ambapo kwa ujumla vyuo vyote vitadahili wanafunzi 2,200 kwa mwaka ukilinganisha na wanafunzi 1,200 wanaodahiliwa kwa mwaka hivi sasa. Vyuo hivyo vinazalisha wataalam wa uvuvi katika ngazi ya Astashahada na Stashahada ambapo hupata ajira Serikalini, sekta binafsi na wengine hujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa imechimba visima virefu 101 kwa ajili ya kujaza maji kwenye mabwawa ya kufugia samaki na malambo 1,381 kwa ajili ya kunyweshea mifugo ambayo pia hupandikizwa samaki. Mabwawa hayo yamechimbwa katika Halmashauri mbalimbali nchini hususan maeneo kame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu wa kuwezesha ufugaji wa samaki unafanywa kupitia mkakati wa kuendeleza ufugaji katika sekta ya uvuvi 2010. Mkakati wa Taifa wa kuendeleza ufugaji wa samaki na viumbe wengine kwenye maji wa 2009 na Mpango Mkuu wa Sekta ya Uvuvi wa mwaka 2002 (The Fisheries Master Plan, 2002).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mkakati wa ufugaji wa samaki umepewa kipaumbele katika mpango wa kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP-2) utakaoanza hivi karibuni. Mikakati yote inatekelezwa chini ya Mpango wa D by D, yaani Ugatuaji wa Madaraka ambapo utekelezaji wake unafanywa kwa ushirikiano na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara inatafiti na na kusambaza teknolojia rahisi za ufugaji wa samaki ili kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika ufugaji wa samaki kwa kuongeza ajira, lishe na kipato nchini ikiwemo wananchi wanaoishi kwenye maeneo kame.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
Sekta ya Uvuvi ni muhimu kwa uchumi wa nchi, sekta hii ikiwezeshwa ina uwezo angalau kufikisha shilingi bilioni 12 kama kipato kwa mwaka:-
Je, ni lini na kwa vipi Serikali itaipa kipaumbele Sekta ya Uvuvi nchini ili kuboresha utendaji na kuongezea nchi kipato?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha Sekta ya Uvuvi ili iweze kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa kupitia mikakati na mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira bora ya uwekezaji. Aidha, kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Uvuvi, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuboresha miundombinu ya uvuvi, ikiwemo bandari ya uvuvi na kuimarisha ubora na usalama wa samaki na mazao ya uvuvi yanayosafirishwa nje ya nchi. Katika mwaka wa fedha 2015/ 2016, Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Uvuvi ilikusanya maduhuli kiasi cha shilingi bilioni 19 ambayo ni zaidi ya asilimia 100 ya lengo la bilioni 18 ilizokuwa imepangiwa kukusanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeandaa kanuni za kusimamia uvuvi katika Bahari Kuu ya Tanzania ambapo zimetoa fursa kwa meli kubwa za uvuvi zinazovua bahari kuu kushusha samaki katika Bandari ya Dar es Salaam (Gati Na. 6) na Zanzibar (Gati Na. 3). Aidha, samaki wanaovuliwa bila kukusudiwa (by-catch) watashushwa katika bandari hizo ambapo itatochea uzalishaji wa samaki nchini, ukusanyaji wa maduhuli, upatikanaji wa ajira na kuongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeanza mapitio ya Mpango Kabambe wa Uvuvi (Fisheries Master Plan) wa mwaka 2015 kwa lengo la kutoa mwongozo wa utekelezaji wa mpango ili kuchangia katika kuongeza usalama wa chakula, lishe, ajira, kuchangia uchumi wa nchi pamoja na kuongeza pato la Taifa. Aidha, Sekta ya Uvuvi imepewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Kilimo awamu ya pili (ASDP II) ambayo utekelezaji wake unaanza mwaka 2017/2018 hadi 2022/2023.
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA aliuliza:-
Kwa muda mrefu miembe imeendelea kushambuliwa na nzi na kuoza, minazi nayo hushambuliwa na ugonjwa wa kukauka na migomba hushambuliwa na ugonjwa wa mnyauko:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondokana na magonjwa hayo ili wananchi wazidi kufaidika na matunda ya mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Morogoro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara imetunga mwongozo wa mafunzo ya udhibiti shirikishi wa inzi waharibifu wa maembe bila kuathiri afya ya mlaji. Hadi sasa Wizara imetoa mafunzo kwa Maafisa Kilimo 117 na vikundi 19 vya wakulima kutoka Mikoa tisa ya Dar es salaam, Iringa, Lindi, Mbeya, Morogoro, Pwani, Ruvuma, Tabora na Tanga. Maafisa hao walipatiwa nyenzo na mwongozo.
Mheshimiwa Spika, Chama cha Wakulima wa maembe walipewa Starter Kit ili wawe mfano kwa wakulima wengine. Kiasi cha lita 560 za methyl eugenol au kivutia wadudu zimeingizwa nchini na zinaendelea kusambazwa katika mikoa hiyo. Wizara inaendelea na utafiti wa udhibiti wa nzi huyu kwa njia ya kibaiologia kwa kutumia mdudu maji moto katika vijiji vya Visiga na Kibamba Mkoani Pwani.
Mheshimiwa Spika, utafiti wa minazi uliofanyika kwa miaka 25 umegundua kuwa minazi yote hushambuliwa na ugonjwa wa kunyong’onyea (Lethal Dieback) kwa viwango tofauti. Moja ya mikakati muhimu ya kuudhibiti ugonjwa huu ni kupanda aina ya minazi yenye ukinzani au ustahimilivu wa ugonjwa huu. Utafiti umegundua aina ya minazi ya East African Tall, Mwambani, Vuo na Songosongo hustahimili ugonjwa huo.
Mheshimiwa Spika, mbegu hizi za minazi yenye ukinzani zinazalishwa katika shamba la mbegu la Chambezi Bagamoyo na zinauzwa kwa bei nafuu kwa wakulima, ni Sh.2,000/= kwa mche. Wizara inaendelea kuboresha utafiti wa zao hili ikiwa ni pamoja na kukijengea uwezo Kituo cha Utafiti cha Mikocheni na watafiti wa zao hilo.
Mheshimiwa Spika, zao la migomba ni muhimu sana katika maisha na uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Kagera. Wizara imeweka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Maruku ili kusogeza huduma hii kwa wananchi wa mkoa huu. Kazi za utafiti zilizofanyika kwa mwaka 2016/2017 Mkoani Kagera ni pamoja na usambazaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali, kanuni bora za uzalishaji ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea, mbinu za kupambana na magonjwa na wadudu waharibifu.
Mheshimiwa Spika, kiasi cha miche ya migomba 390,000 ilisambazwa kwa wakulima wa mkoa huo. Aidha, kila Wilaya Mkoani Kagera imeanzisha vitalu vya kuzalisha miche ya migomba. Pia kitalu mama cha miche ya migomba kipo katika kituo cha utafiti Maruku chenye uwezo wa kuzalisha miche 5,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, utafiti umethibitisha kuwa ugonjwa wa unyanjano unaweza kudhibitiwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji zao hilo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbegu bora na safi, kutoa ua dume baada ya mkungu kutungwa, kutumia vifaa safi katika shamba la migomba, kuepuka kuchunga mifugo kama mbuzi katika shamba la migomba, vile vile kung’oa migomba iliyougua mara moja.
Mheshimiwa Spika, ili kutokomeza ugonjwa wa unyanjano ni lazima jamii ishiriki kikamilifu kwa pamoja kama ilivyoelekezwa katika Kampeni ya Tokomeza Unyanjano ya mwaka 2013. Maeneo yaliyozingatia kampeni hii yalifanikiwa kupunguza ugonjwa huu kutoka asilimia 90 hadi asilimia 10. Baadhi ya vijiji na wilaya zimefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu kwa asilimia 100. Wizara inashauri Halmashauri za Wilaya kutumia sheria ndogondogo kudhibiti magonjwa ya mazao ili kupata kilimo chenye tija.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. MBAROUK SALIM ALI) aliuliza:-
Tanzania pamoja na kuwa na mifugo mingi bado kuna uhaba mkubwa wa maziwa.
Je, Tanzania ina ng’ombe na mbuzi wangapi wa maziwa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubailiana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya mifugo lakini bado kuna upungufu wa maziwa ambapo takwimu za makadirio za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa kuna jumla ya ng’ombe milioni 28.4, mbuzi milioni 16.7, kondoo milioni tano, nguruwe milioni 1.9, kuku wa asili milioni na kuku wa kisasa milioni 34.5. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya lita bilioni 2.09 za maziwa zilizalishwa na unywaji wa maziwa kwa mtu kwa mwaka ulifikia lita 47, ikilinganishwa lita 200 zinazopendekezwa na Shirika la Chakula Dunian (FAO).
Mheshimiwa Spika, kati ya ng’ombe milioni 28.4, ng’ombe rasmi wa maziwa ni 782,995 tu sawa na asilimia tatu ya ng’ombe wote. Aidha, kati ya mbuzi milioni 16.7 ni mbuzi rasmi takribani 50,000 ndiyo wa maziwa ambao ni asilimia 0.3 ya mbuzi wote.
Mheshimiwa Spika, zipo jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na Serikali ili kukabiliana na upungufu wa maziwa hapa nchini. Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha mashamba ya kuzalisha mifugo ya Serikali (Livestock Multiplication Units) ili kuongeza idadi ya ng’ombe wenye uwezo wa kuzalisha maziwa kwa wingi.
Aidha, Serikali imeanzisha vituo vya uhimilishaji katika Kanda Sita hapa nchini ambazo ni Kanda ya Ziwa - Mwanza, Kanda ya Magharibi - Katavi, Kanda ya Kati - Dodoma, Kanda ya Mashariki - Kibaha, Kanda ya Kusini - Lindi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini – Mbeya, kwa lengo la kutoa huduma ya uhimilishaji wa ng’ombe wa maziwa walioko kwenye maeneo hayo pamoja na ng’ombe wa asili ili kuzalisha idadi kubwa ya ng’ombe wa maziwa. Jitihada hizi zitawezesha idadi ya ng’ombe wa maziwa kufikia milioni 2.9 ifikapo mwaka 2021/2022 ambao pamoja na ng’ombe wa asili wataweza kuzalisha lita bilioni 3. 8 za maziwa.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo kuwekeza katika uzalishaji wa mitamba ya maziwa na mashamba ya ng’ombe wa maziwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa hapa nchini.
MHE. ABBDALAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za kuzalisha korosho zinazosababishwa na pembejeo kuuzwa kwa bei ya juu.
Je Serikali ina mpango wa kutoa mikopo midogo midogo kwa wakulima wa korosho ili waweze kumudu gharama hizo?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima ikiwemo ruzuku ya kununua viuatilifu vya zao la korosho. Lengo la kutoa ruzuku hizo ni pamoja na kuwapunguzia wakulima gharama ya bei ya soko ya pembejeo hizo ambazo zinachangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoa ruzuku ya pembejeo, Serikali pia imeanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumiwa kuuzia korosho, utaratibu ambao umesaidia kupata soko la uhakika na kuongeza bei ya korosho kutoka shilingi 2,900 kwa kilo moja msimu wa mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi 4,000 kwa kilo moja msimu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, kupitia Tume ya Ushirika, Serikali imeandelea kuwahimiza wakulima kujiunga kwenye vyama vya ushirika na vikundi vya wakulima ili kurahisisha kupata mikopo itakayo wawezesha kumudu gharama za uzalishaji. Aidha, mwaka 2015 Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ambayo inatoa mikopo ya muda mfupi miaka miwili, muda wa kati miaka miwili hadi mitano na muda mrefu miaka mitano hadi miaka 15 kwa wakulima, kwa riba nafuu ya kati ya asilimia nane hadi asilimia 12. Benki hii imeendelea kutoa elimu ya mikopo kwa wakulima, kwa hali hiyo napenda kuwashauri wakulima kote nchini kupitia vyama vya ushirika na vikundi kutumia fursa hiyo.