Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Charles John Tizeba (21 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa na mimi naomba niseme moja kwa moja kwamba, naunga mkono hoja ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuunga mkono niseme tu kwamba Kilimo, Mifugo na Uvuvi karibu Wabunge zaidi ya 60 wamezungumzia mambo mbali mbali; na kwa manufaa ya muda, naomba nizungumzie tu machache katika hayo ambayo kwa wingi zaidi yamezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nizungumzie tu suala la sukari kwamba sukari ipo nchini. Sukari ipo nchini na inaendelea kuletwa, sasa hivi tunachokifanya ni kusimamia vizuri usambazaji wa hii sukari ili ifike maeneo yale ambayo tulihisi kwamba yanaanza kuwa na upungufu na tumewaomba Wakuu wa Mikoa wasimamie vizuri zoezi hili la upelekaji wa sukari hasa kwenye Wilaya ambazo ziko mbali na Makao Makuu ya Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lililozungumziwa sana kwa hisia na Waheshimiwa Wabunge, ni kodi nyingi zilizoko kwenye mazao ya kilimo, uvuvi, na ufugaji. Hizi kodi kwanza Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi Watanzania kwamba zitafanyiwa kazi, na kwa kadri itakavyowezekana, zitapungunzwa au kuondolewa. Bajeti hii imekwishaanza, ziko aina za kodi ambazo Waziri wa Fedha katika hotuba yake alipendekeza ziondolewe; na sasa hizo hazitakuwapo kwenye pamba, kahawa, korosho, ziko kodi ambazo tayari zimekwisha ondolewa na kwenye tumbaku pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo hili jambo linaendelewa kufanyiwa kazi, Serikali imeunda Tume ya Makatibu Wakuu, nilikwisha sema kwenye kujibu maswali ya Wabunge hapa, kwamba Kamati hiyo inaendelea kuzipitia, na kodi zile ambazo zitaonekana hazina madhara katika bajeti hii na bajeti za Halmashauri, zitaondolewa mara moja kadri ya mapendekezo yanavyokuja; na zile ambazo zitakuwa na effect kwenye bajeti hii, basi tutasubiri tuziondoe muda muafaka kwenye bajeti ya mwaka kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeanza msimu wa pamba. Pamba msimu utazinduliwa kesho huko Mkoa wa Geita, katika kijiji cha Nyang‟hwale, naomba sana kwanza bei elekezi nzuri ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote mbili, wanunuzi na wakulima wa pamba itatajwa kesho. Lakini niombe kutumia muda huu kuwaomba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wa maeneo inakozalishwa pamba, wasimamie vizuri masoko, wananchi wasipunjwe kwenye mizani, kwa sababu wako wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, wanabana mizani kuwaibia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme na upande mwingine, kwamba wako wakulima wasiokuwa waungwana, wanaochakachua pamba kwa maji na michanga ili wapate uzito zaidi na kwa kufanya hivyo wanaharibu ubora wa pamba yetu, kwa hivyo wanapunguza thamani yake katika soko la dunia. Wote hawa niwaombe sana Wakuu wa Mikoa, hakikisheni mnatumia uwezo wa kisheria mlionao kudhibiti vitendo vya namna hii pande zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao lingine linaloleta shida sana katika usimamizi na uendeshaji wake ni tumbaku. Tumbaku umekuwa wimbo, vyama vya msingi vinakufa na wafanyabiashara makampuni ya tumbaku yanaendelea kunufanika na kupata faida. Sasa bahati mbaya sana hapa katikati utaratibu ulilegezwa wakaingizwa na wakulima binafsi na associations katika tasnia hii ya tumbaku. Matokeo yake imekuwa ni vyama vingi vya ushirika kudorora au kufa kabisa, kwa sababu hawa independent farmers na associations hizi, zingine hazina mashamba lakini wana tumbaku wanauza sokoni. Sasa tutahakikisha hili jambo haliendelei tena, maelekezo yalikwisha kutolewa wasisajiliwe upya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naangalia uwezekano wa kupunguza madaraja ya tumbaku. Madaraja ya tumbaku yako 67, haiwezekani. Wakulima hawajui, tumbaku ikisindikwa haitoki na madaraja 67, kwa nini katika kuuza iwe na madaraja 67. Hili jambo tunalifanyia kazi na kwa kweli nadhani tutayapunguza ili yawe yale yanayotambulika kwa wananchi na wakulima; kwamba madaraja ni matano, basi yabaki kuwa matano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya wafugaji na wakulima. Hili jambo ukilitazama na chimbuko lake ni ukosefu wa malisho na maji kwa wafugaji, kwa hivyo wanalazimika kuhama kwenda kuvamia maeneo ambayo hayakuwa yamelengwa kwa ajili ya ufugaji. Sasa tunachokifanya tutarajie kwamba kwanza tutapitia upya mgawanyo wa Ranchi zote za Taifa, ili kujua wale waliopewa kweli walikuwa wanastahili; na hicho walichopewa kukifanya huko kama wamekifanya, kwa sababu kilichobainika katika ziara za viongozi wetu, ni kwamba mtu alipewa kipande cha Ranchi, badala ya kufuga yeye mwenyewe anakitumia kuwakodisha wenyeji wa eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii haikuwa nia ya Serikali kwamba iwagawie watu maeneo haya kwa ajili ya kukodisha, kwa hivyo tunaangalia upya, yule aliyeshindwa kutimiza masharti aliyokuwa amepewa tutawanyanganya ili wananchi waweze kugawiwa maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa wameombwa waainishe maeneo mapya, yanayowezekana kufanyia malisho na ufugaji wa ng‟ombe, ili tuweze kupanua maeneo haya; kwa sababu yako maeneo hayatumiki vizuri, sasa haya yakibainika mkoa kwa mkoa tunaweza tukawathibiti wafugaji wetu katika maeneo ya Mikoa yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kusema naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa na mimi naomba niseme moja kwa moja kwamba, naunga mkono hoja ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuunga mkono niseme tu kwamba Kilimo, Mifugo na Uvuvi karibu Wabunge zaidi ya 60 wamezungumzia mambo mbali mbali; na kwa manufaa ya muda, naomba nizungumzie tu machache katika hayo ambayo kwa wingi zaidi yamezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nizungumzie tu suala la sukari kwamba sukari ipo nchini. Sukari ipo nchini na inaendelea kuletwa, sasa hivi tunachokifanya ni kusimamia vizuri usambazaji wa hii sukari ili ifike maeneo yale ambayo tulihisi kwamba yanaanza kuwa na upungufu na tumewaomba Wakuu wa Mikoa wasimamie vizuri zoezi hili la upelekaji wa sukari hasa kwenye Wilaya ambazo ziko mbali na Makao Makuu ya Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lililozungumziwa sana kwa hisia na Waheshimiwa Wabunge, ni kodi nyingi zilizoko kwenye mazao ya kilimo, uvuvi, na ufugaji. Hizi kodi kwanza Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi Watanzania kwamba zitafanyiwa kazi, na kwa kadri itakavyowezekana, zitapungunzwa au kuondolewa. Bajeti hii imekwishaanza, ziko aina za kodi ambazo Waziri wa Fedha katika hotuba yake alipendekeza ziondolewe; na sasa hizo hazitakuwapo kwenye pamba, kahawa, korosho, ziko kodi ambazo tayari zimekwisha ondolewa na kwenye tumbaku pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo hili jambo linaendelewa kufanyiwa kazi, Serikali imeunda Tume ya Makatibu Wakuu, nilikwisha sema kwenye kujibu maswali ya Wabunge hapa, kwamba Kamati hiyo inaendelea kuzipitia, na kodi zile ambazo zitaonekana hazina madhara katika bajeti hii na bajeti za Halmashauri, zitaondolewa mara moja kadri ya mapendekezo yanavyokuja; na zile ambazo zitakuwa na effect kwenye bajeti hii, basi tutasubiri tuziondoe muda muafaka kwenye bajeti ya mwaka kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeanza msimu wa pamba. Pamba msimu utazinduliwa kesho huko Mkoa wa Geita, katika kijiji cha Nyang‟hwale, naomba sana kwanza bei elekezi nzuri ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote mbili, wanunuzi na wakulima wa pamba itatajwa kesho. Lakini niombe kutumia muda huu kuwaomba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wa maeneo inakozalishwa pamba, wasimamie vizuri masoko, wananchi wasipunjwe kwenye mizani, kwa sababu wako wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, wanabana mizani kuwaibia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme na upande mwingine, kwamba wako wakulima wasiokuwa waungwana, wanaochakachua pamba kwa maji na michanga ili wapate uzito zaidi na kwa kufanya hivyo wanaharibu ubora wa pamba yetu, kwa hivyo wanapunguza thamani yake katika soko la dunia. Wote hawa niwaombe sana Wakuu wa Mikoa, hakikisheni mnatumia uwezo wa kisheria mlionao kudhibiti vitendo vya namna hii pande zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao lingine linaloleta shida sana katika usimamizi na uendeshaji wake ni tumbaku. Tumbaku umekuwa wimbo, vyama vya msingi vinakufa na wafanyabiashara makampuni ya tumbaku yanaendelea kunufanika na kupata faida. Sasa bahati mbaya sana hapa katikati utaratibu ulilegezwa wakaingizwa na wakulima binafsi na associations katika tasnia hii ya tumbaku. Matokeo yake imekuwa ni vyama vingi vya ushirika kudorora au kufa kabisa, kwa sababu hawa independent farmers na associations hizi, zingine hazina mashamba lakini wana tumbaku wanauza sokoni. Sasa tutahakikisha hili jambo haliendelei tena, maelekezo yalikwisha kutolewa wasisajiliwe upya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naangalia uwezekano wa kupunguza madaraja ya tumbaku. Madaraja ya tumbaku yako 67, haiwezekani. Wakulima hawajui, tumbaku ikisindikwa haitoki na madaraja 67, kwa nini katika kuuza iwe na madaraja 67. Hili jambo tunalifanyia kazi na kwa kweli nadhani tutayapunguza ili yawe yale yanayotambulika kwa wananchi na wakulima; kwamba madaraja ni matano, basi yabaki kuwa matano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya wafugaji na wakulima. Hili jambo ukilitazama na chimbuko lake ni ukosefu wa malisho na maji kwa wafugaji, kwa hivyo wanalazimika kuhama kwenda kuvamia maeneo ambayo hayakuwa yamelengwa kwa ajili ya ufugaji. Sasa tunachokifanya tutarajie kwamba kwanza tutapitia upya mgawanyo wa Ranchi zote za Taifa, ili kujua wale waliopewa kweli walikuwa wanastahili; na hicho walichopewa kukifanya huko kama wamekifanya, kwa sababu kilichobainika katika ziara za viongozi wetu, ni kwamba mtu alipewa kipande cha Ranchi, badala ya kufuga yeye mwenyewe anakitumia kuwakodisha wenyeji wa eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii haikuwa nia ya Serikali kwamba iwagawie watu maeneo haya kwa ajili ya kukodisha, kwa hivyo tunaangalia upya, yule aliyeshindwa kutimiza masharti aliyokuwa amepewa tutawanyanganya ili wananchi waweze kugawiwa maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa wameombwa waainishe maeneo mapya, yanayowezekana kufanyia malisho na ufugaji wa ng‟ombe, ili tuweze kupanua maeneo haya; kwa sababu yako maeneo hayatumiki vizuri, sasa haya yakibainika mkoa kwa mkoa tunaweza tukawathibiti wafugaji wetu katika maeneo ya Mikoa yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kusema naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami kwa kuanzia niishukuru sana Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa taarifa nzuri ambayo kwa ukweli imegusa maeneo yote muhimu ambayo wao wana wajibu wa kuyasimamia na kutoa ushauri kwa Serikali. Nawashukuru sana tumefanya kazi vizuri na niseme tu mapema kwamba yote ambayo wamependekeza na kutolea ushauri tumeyachukua, mengine tutayafanyia kazi mara moja na mengine ambayo yanahitaji muda tutaendelea kuyafanyia kazi kadri muda utakavyokuwa unakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza mambo mengi na kwa hisia sana. Hisia hizo zinaonesha ni kwa kiasi gani wanaguswa wao na wananchi wanaowawakilisha na haya mambo ambayo wameyazungumzia. Kilimo katika tafsiri yake pana kinamgusa kila mtu na kwa hivyo haishangazi na kwa kweli lazima utegemee mjadala utakaokuwa unahusu kilimo uwe na sura hii. Mimi mwenyewe ningeshangaa kama mjadala wa Kamati hii ungekuwa na sura tofauti na hii niliyoiona hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, niombe nizungumzie tu mambo machache ambayo mwenzangu Mheshimiwa Ole-Nasha hakuyagusa. Nianze na suala la tozo. Suala la tozo limekwishatolewa kauli na Mkuu wa nchi kwamba zote zile ambazo ni za hovyo hovyo na zenye usumbufu Serikali izifanyie kazi na iziondoe. Ziko tozo ambazo hazikuwa na madhara ya kibajeti katika mazao tumeziondoa, kwenye korosho, tumbaku, pamba tumezifuta. Ziko tozo ambazo zilikuwa na madhara ya kibajeti kama tungezifuta mara moja.
Kwa hivyo, hizi zinafanyiwa kazi iko Kamati ya Serikali ya Makatibu Wakuu wanaendelea kufanyia kazi na kwa kweli tutakapoingia katika bajeti hii ya mwaka huu tozo nyingi mtaona zitakuwa zimeondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo hizi haziathiri tu bei za mazao na mambo mengine lakini ziko tozo pia zinazoathiri kilimo ambazo haziko kwenye mazao. Waheshimiwa hapa wamezungumzia gharama kubwa ya pembejeo, mbolea tu inazo tozo 14 mbalimbali. Kwa hiyo, tunavyozungumzia kushusha gharama ya pembejeo pamoja na hatua zingine ambazo tumejipanga kuzichukua, lakini itabidi pia tuangalie katika hizi tozo zilizopo kwenye mbolea ili mjumuiko wa hatua hizo utuhakikishie kwamba mbolea itashuka bei kiasi kwamba wakulima na watumiaji wengine wa pembejeo wataweza kumudu bei bila wakati mwingine kulazimika kuweka ruzuku katika pembejeo hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Haonga analiona hilo, kwamba tunao uwezekano wa kufika mahali tukaondoa ruzuku kwenye pembejeo kama tutaweza kushusha bei zake katika levels ambazo mkulima wa kawaida anaweza kuzimudu. Hatua kadhaa zinachukuliwa, moja, ni kama alivyosema kununua moja kwa moja kwa wazalishaji wa hizi pembejeo. Tumefanya hivi mwaka huu na kwa kweli mbolea imeshuka bei kwa wastani wa asilimia karibu 28. Tutaendelea kuchukua hatua zingine za kupunguza kodi hizi, lakini pia kuna mazungumzo mazuri sasa hivi ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza sulphur hapa hapa nchini. Tukifanikiwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba hata bei ya sulphur tunayoinunua sasa hivi kwa bei kubwa huko nje na yenyewe itashuka bei. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie haraka haraka suala la mbegu. Mbegu ni tatizo kweli, bado utoshelevu wetu wa mbegu bora uko kwenye asilimia 40 Kitaifa, kwa hivyo asilimia 60 bado tunaagiza nje. Mbegu inayozalishwa hapa ndani ina changamoto moja kubwa kwamba inatozwa kodi wakati mbegu zinazoagizwa nje ya nchi hazitozwi kodi. Hata mimi haiingii akilini, ni kwa sababu kwa kufanya hivyo, mbegu inayozalishwa Tanzania inakosa ushindani lakini inakuwa inakatisha tamaa kwa wazalishaji wa ndani kuzalisha zaidi kwa sababu hata wakizalisha mbegu inayotoka nje inakuwa na ushindani zaidi kuliko ya hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo tutalitazama katika Serikali na kwa kweli nadhani ni jambo ambalo tunaweza tukaliondoa tu mara moja ili kuwapa motisha wazalishaji wa ndani wa mbegu tuweze kujitosheleza. Wakala wetu wa Mbegu wa Taifa nimekwishawapa maelekezo, mashamba yote ambayo wameyatunza yamekuwa mapori, wawape watu wenye uwezo wa kutuzalishia mbegu waingie nao mikataba kwa masharti ambayo yatakuwa yanawawezesha wale watu kuzalisha bila kupata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la fedha katika Wizara ya Kilimo. Kamati imeona kweli kwamba bajeti iliyokwishatolewa mpaka sasa ni kidogo, labda nitoe taarifa kwamba kilimo kinapata fedha nyingi nje ya mfumo wa bajeti ya Serikali. Leo tunavyozungumza, fedha iliyoingia katika kilimo kupitia vyanzo tofauti na bajeti ya Serikali iko kwenye tune ya shilingi trilioni 1.7, hii si hela kidogo katika kilimo cha nchi hii. Tunapata fedha nyingi kwenye kilimo nje ya mfumo wa bajeti kupitia mashirika mbalimbali kwenye SAGCOT na kadhalika. Bill & Melinda Gates Foundation peke yake imeingiza Tanzania dola milioni 700 ambazo zimeelekezwa kwenye kilimo, wacha World Bank, AGRA na wengine. Kwa hiyo, kilimo kwa maana ya bajeti ambayo inapita kwenye Wizara ni fedha inayoonekana si nyingi sana lakini fedha nyingine inakwenda kwenye Halmashauri lakini wafadhili wengi wanapeleka moja kwa moja kwenye programu na miradi mbalimbali ya kilimo inayotekelezwa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza na taasisi za fedha, zimekubali pia sasa kuanza kukopesha, kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kilimo. NMB peke yake wametenga mwaka huu wa fedha shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kukopesha miradi ya kilimo na shughuli zingine zinazohusiana na kilimo. Kwa hiyo, tukitumia hizi fursa vizuri kilimo chetu kitasonga mbele.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Hoja ya Bajeti ya Serikali iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kwa kusema tu kwamba naunga mkono hoja na baada ya kuunga mkono hoja niseme pia kwamba bajeti hii imeitendea haki sana sekta ya kilimo nchini. Ninaposema sekta ya kilimo ni kwa maana ya sekta ya kilimo, mazao, mifugo na uvuvi na pia sekta ya ushirika hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tozo, pamoja na kwamba wako walioonekana kama hawaridhiki na ufutaji wa tozo na kodi mbalimbali katika kilimo, lakini sisi tunaovaa kiatu ndio tunajua kilikuwa kinatubana kiasi gani, na kwa maana hiyo tunatarajia kwamba tozo na kodi mbalimbali ambazo zimeondolewa zitaongeza tija katika kilimo, lakini pia zitaweka mazingira mazuri ya wadau wote wa kilimo ku- participate (kushiriki) bila kukwazwa na mazingira hayo ya kodi na ushuru mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, wakulima wamekuwa wakilalamikia tozo hizo na wafanyabiashara na watu wengine katika minyororo ya thamani na wao pia wamekuwa wanalalamikia tozo hizo. Kwa hiyo, tumeziondoa na Serikali imekubali kuziondoa na kuzifuta baadhi yake, nyingine kuzipunguza ili kuhakikisha kwamba wote wananufaika, win-win situation; Serikali ibakie na mambo yake ikinufaika lakini na wananchi pia wapate nafuu na kunufaika na jitihada wanazofanya katika mashamba na maeneo mengine ya uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba baada ya hayo tutaona mabadiliko ya bei ya mazao yetu ya biashara, lakini pia tutaona uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka, tutaona ufugaji ukipata nafuu zaidi baada ya kuondoa kodi hizi na tumeweka mazingira yanayovutia uwekezaji sasa katika mifugo. Eneo hili limekuwa halipati uwekezaji mzuri kwa sababu ya tozo na ada mbalimbali zilizokuwepo.

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba tunaendelea kama Wizara na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba upatikanaji wa pembejeo unakuwa kwa wakati na kwa bei ambayo wakulima wanaweza kumudu. Hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo zilizokuwako katika uingizaji na usambazaji wa mbolea na viuatilifu. Vilevile tunaendelea na mchakato wa uagizaji wa baadhi ya mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba mwishowe bei tutakayoiweka itakuwa inahimilika, wananchi wanaweza kuimudu na kwa hivyo ituwezeshe kuongeza uzalishaji katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, Programu ya Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) imekamilika maandalizi yake na tumefanya mambo kadhaa. Pamoja na mambo tuliyoyafanya ni kutoa Mwongozo wa Kilimo, pia Mwongozo wa Ufugaji.

Mheshimiwa Spika, katika programu hii suala la umwagiliaji limepewa kipaumbele, na safari hii umwagiliaji tunaoufikiria kuuwekea msisitizo mkubwa ni umwagiliaji wa mazao makuu ya chakula. Kwa muda mrefu umwagiliaji umekuwa katika maeneo ya mpunga na mbogamboga, lakini sasa katika awamu hii ya Programu ya Kilimo ya Pili tunataka kwenda kwenye zao kubwa la chakula nchini ambalo ni mahindi. Umwagiliaji ufanyike pia katika uzalishaji wa mahindi ili kujihakikishia usalama wa chakula na uzalishaji wa muda wote ambao hautuletei mashaka.

Mheshimiwa Spika, niombe kutumia nafasi hii kuwatangazia wananchi kwamba sasa hivi maeneo mengi nchini wanavuna, lakini niwaombe sana baada ya kufanya mavuno hayo utumiaji wa chakula chao uwe wa makini kwa sababu hali ya hewa katika nchi zinazotuzunguka haikuwa nzuri na kwa hiyo, kutakuwa na mahitaji makubwa ya kununua chakula kutoka Tanzania kwenda nchi za nje. Wananchi hawazuiliwi kuuza lakini wanashauriwa wauze na kujiwekea akiba ya kuwatosha.

Mheshimiwa Spika, narudia kusema naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha tena kukutana jioni hii tukiwa na afya njema thabiti kabisa, ili tujadili yale ambayo yamezungumzwa kwa kipindi cha takribani siku tatu wakati Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakijadili mapendekezo ya mapato na matumizi ya Wizara yetu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utangulizi nimshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, Wajumbe wote wa Kamati yetu, vilevile nimshukuru Mheshimiwa Cecilia Paresso Mbunge wa Viti maalum aliyewasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa niaba ya Msemaji Rasmi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt. Emmaculate Sware. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, niwashukuru Wabunge wote waliochangia katika hoja hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwa kutambua umuhimu mkubwa wa hoja hii Wabunge wengi wamejitokeza kuchangia, kutoa maoni na ushauri hali ambayo binafsi imenipa faraja kubwa kwani michango hiyo itasaidia katika utekelezaji wa mikakati ya kuendeleza sekta ya kilimo mifugo na uvuvi na ni ushahidi tosha kwamba kilimo mifugo na uvuvi ni sekta muhimu kwa ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Wabunge takribani 134 wamechangia kwa kauli na maandishi wakati tukijadili makadirio ya matumizi ya Wizara yangu. Kati ya hao Wabunge 87 walichangia kwa kauli na Wabunge 47 kwa maandishi. Kwa hali hiyo Wabunge hawa ni wengi sana na hivyo kwa dakika hizi arobaini sidhani kama naweza kuwataja wote na kujibu hoja ya kila mmoja, haitakuwa rahisi kwangu kufanya hivyo na kwa hivyo ntajitahidi kujibu kwa ujumla mambo makubwa yaliyojitokeza katika michango hii. Napenda pia niwahakikishie kwamba Waheshimiwa Wabunge yote mliyojadili mliyochangia, mliyohoji tutajitahidi kuyajibu kwa maandishi na kuwapatia kabla hatujamaliza mkutano huu wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba sasa uniruhusu nijibu baadhi ya hoja zilizojitokeza katika mjadala wa hotuba kama ifuatavyo; Nitaanza na hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji halafu nitazungumzia machache yaliyojitokeza katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge karibu wote waliochangia wamezungumzia jambo hili la bajeti ndogo ya Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi. bajeti ya Sekta hii haiko yote katika Wizara yangu ili labda ndio nianze kwanza nalo ili tuelewane vizuri Waheshimiwa Wabunge, bajeti kubwa iko maeneo mengine nje ya hii Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara mtambuka zinazojihusisha na mambo ya kilimo kubwa kabisa ya kwanza ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kule mipango yote karibia ya utekelezaji wa shughuli za kilimo inafanyikia TAMISEMI katika Halmashauri zetu Waheshimiwa Wabunge, Wizara inajihusisha zaidi na sera na miongozo ya Kitaifa, lakini utekelezaji unafanyika kule kwenye grassroot ambako haya mambo yanasimamiwa na Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ziko Wizara zingine kwa mfano Wizara ya Miundombinu, Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, hawa nao wanafanya kazi ambazo zinahusu kilimo ingawa sio moja kwa moja. Kwa hivyo, ukilichukulia katika ujumla huo mpana utaona kwamba sekta hizi tatu kilimo mifugo na uvuvi siyo kwamba zimepata bajeti ndogo kihivyo isipokuwa tu ile inayoonekana katika Wizara yetu ya Kilimo ndiyo kwa mtazamo unaweza ukaona kwamba ni bajeti kidogo. Halmashauri jumla ya bajeti yake inayohusu sekta hizi tatu ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili zipo taasisi zetu karibia 11 ama 12 ambazo zinakusanya maduhuli ni taasisi za umma na zinajihusisha na mambo haya haya ya kilimo, mifugo na uvuvi ambazo maduhuli yale hayaji katika bajeti kuu ya Serikali wana-retain na kutumia moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache, niseme tu hizi taasisi hizi zinakusanya na kutumia katika sekta za kilimo jumla ya shilingi karibia bilioni 260. Hizi ukiziongeza katika ile bajeti ya kwetu ya moja kwa moja kwa sababu ni taasisi ambazo ziko chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ukiziongeza hizi utaona kwamba kutoka kwenye karibu 400 ile tunakwenda kwenye 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu kuna fedha nyingi ambayo inaingia katika miradi ya kilimo, mifugo na uvuvi nje kabisa ya utaratibu wa bajeti ya Serikali. Ziko taasisi nyingi za wabia wetu wa maendeleo ambao wanachangia sana katika kilimo lakini siyo kupitia mfumo wa bajeti ya Serikali. Hata hivyo, jambo la kuzingatia tu ni kwamba hawa wote hawa ushiriki wao katika miradi mbalimbali wanayoiendesha unakuwa na baraka za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni approach tu ndiyo ina- differ, kule kwenye afya wana basket wanayochangia, kwa hivyo zinaonekana zimepitia kwenye mfumo wetu wa bajeti wa Serikali, lakini kwenye kilimo wanakwenda wame-opt kwenda na kwa sababu wana complement kazi inayofanywa na Serikali hatuna sababu ya kufinyana nao. Kwa hivyo, tunawaacha watekeleze hayo majukumu ambayo otherwise ingebidi Serikali itenge bajeti hapa kwenda kufanya hayo majukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo tu, katika mwaka 2015/2016, kwa ujumla wadau wetu wa maendeleo walichangia trilioni moja na bilioni 730 katika kilimo direct, wakati bajeti yetu ya Serikali kwa ujumla ilikuwa trilioni 1.001, wenzetu wakachangia trilioni 1.73; ukizijumlisha hizi ni karibia trilioni 2.7, ni fedha nyingi kuliko Wizara nyingine yoyote iliyopata mchango wa namna hiyo katika bajeti ya mwaka uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka tu kusema kwa maneno haya ni kwamba fedha inayokuwa directed kwenye kilimo ni nyingi, katika mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao mpaka hapa ninapozungumza leo commitment za fedha hizi zinaendelea kutoka, lakini mpaka ninavyozungumza sasa hivi fedha kutoka kwa wadau wetu wengine nje ya mfumo wa bajeti wamesha-disburse karibu bilioni 400. Kwa hivyo, hizi ni fedha ambazo zimeingia kwenye kilimo kupitia programs mbalimbali ambazo wadau wetu tunashirikiana nao katika kukuza na kuimarisha kilimo chetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tusipate wasiwasi kwamba kilimo kinakuwa under funded na kadhalika. Nasema kilimo ni kipaumbele hakuna asiyejua na mmesema vizuri hapa kwamba bila kilimo viwanda na nini vitakuwa tabu sana ku-achieve, yes itakuwa vigumu sana ku-achieve! Hata hivyo, hata ukiwa na priority maana yake ni kwamba utakataa misaada, utakataa ziada eti kwa sababu jambo hilo unaloshughulikia wewe kwako ni kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo. Taifa la Israel kipaumbele namba moja chao ni usalama, security of that country is priority number one, ulinzi bajeti yao ya ulinzi pamoja na kwamba ndiyo concern, ndiyo priority number one Taifa la Israel, bajeti yao ya ulinzi wanapata msaada kutoka Marekani. Mwaka jana tu wamepata msaada wa bilioni 38 dola wakati wao bajeti yao ya ndani ilikuwa imetenga bilioni 4.6. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba wameondokana na kufanya suala la ulinzi kuwa kipaumbele namba moja. Kwa hivyo, hata sisi wakati tuna bajeti tunaangalia pia kwamba wenzetu wanaotuunga mkono katika kilimo commitment yao ni kiasi gani ili tuweze kufanya rational distribution ya resource tuliyonayo ya ndani. Kwa hivyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge hili suala lisitusumbue sana kwamba kwa nini asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nielezee hapa asilimia tatu ambayo inasemwa kwamba kwa mwaka mzima bajeti ya Fungu 43 iliyotolewa ni asilimia 3.8. Ni kweli mpaka tunaandika hivi vitabu pesa iliyokuwa imetolea ni shilingi bilioni kama 3.4 ambayo ukiipigia hesabu inakuwa asilimia tatu, lakini ni asilimia tatu yaa shilingi bilioni 101 ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya mradi mmoja tu, mradi wa kujenga vihenge (silos) na hivi tunavyozungumza majadiliano almost yamekamilika na Serikali ya Poland ambako hizi fedha sasa zitapatikana dola karibu milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa hivyo vihenge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, huenda wakati Waziri wa fedha anakuja kusoma bajeti yake hapa performance ya hiyo miradi ya maendeleo kwenye bajeti commitment ya Serikali inaweza kuwa imeshafika kwenye asilimia 98. Ndugu zangu ile asilimia tatu inayoonekana kwa sababu tusingesema uwongo, mchakato ulikuwa haujakamilika, lakini tuna hakika sasa kila lililohitajika ili tukamilishe upatikanaji wa hizo fedha kutoka Serikali ya Poland tumekwishafanya, zitapatikana, vihenge vitajengwa na kwa hivyo utekelezaji wa bajeti yetu ya maendeleo utakuwa umekwenda kwenye asilimia kubwa sana kuliko inavyoonekana kwenye maandishi yetu sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwa hisia ni hili suala la tozo tulizoziondoa. Nimesikitika kweli jana kuona baada ya kelele zote za wananchi wa nchi hii kuhusu tozo, kero zinazowasababishia kutonufaika na jitihada zao, baadhi ya wenzetu hapa ndani wamesimama wakibeza eti kwamba hili tulilolifanya ni jambo baya halina manufaa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo msemaji mzuri sana wa exchange hizi za mambo ya humu ndani, lakini itoshe tu kusema kwamba mambo ambayo ni serious kama haya tunatakiwa kuacha hizi politics za ajabu. Hapa tunazungumzia maisha na well being ya Watanzania. Watu wanalalamika anapeleka ng’ombe mnadani hajauza, anatozwa kodi ya makanyagio, halafu sisi tukae tuache kodi ya hivyo eti kwa sababu kuna mtu hapa anadhani kwamba tuko tunatafuta sifa, hatutafuti sifa! Sisi tunashughulikia matatizo ya wananchi, matatizo ya kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia mdogo wangu Mheshimiwa David Silinde asubuhi hapa, anasema kodi hizi zimewalenga middle men hazijawalenga wakulima, hivi Tanzania hizi kodi tunaziweka kwa ubaguzi? Hizi kodi zinawaathiri wote katika mnyororo wa thamani, kodi hizi zinamuathiri kila mmoja kwenye mnyororo wa thamani. Mkulima akilima kama hakuna mnunuzi kilimo chake hakina manufaa, mnunuzi akiwapo bila mkulima, uchuuzi wake hauna manufaa, wote wanategemeana. Kama watu wana mazao lakini hakuna msindikaji, mazao yale yatapoteza thamani. Kwa hivyo, tulichokifanya tumeangalia mnyororo mzima wa thamani na namna hizi kodi zinavyowa-affect mmoja mmoja kwenye mnyororo huo wa thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuondosha kwa hizi kodi hakukulenga kundi moja tu la Watanzania, kumelenga Watanzania wote ambao wanakuwa affected na hizi kodi, wafanyabiashara, wakulima wasindikaji na wengine. Nitatoa mfano mdogo ili tuwe na ufahamu unaofanana. Kwenye tumbaku au tuseme kwenye mbegu ili mfanyabiashara mzalishaji wa mbegu aweze kuzalisha mbegu alitakiwa kuwa na mtaji wa tozo tu wa milioni 60, dola 20,000 kwa ajili ya kusajiliwa kama mzalishaji wa mbegu na dola 10,000 za kusajili mbegu anayotaka kuzalisha hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huyu ni mfanyabiashara anazalisha mbegu auze kwa wakulima, ukimuachia hii kodi ibaki maana yake mbegu atakayozalisha lazima aweke ndani yake hizi gharama. Akiweka ndani yake hizi gharama bei ya mbegu inapanda, bei ya mbegu ikipanda
anayeathirika na kushindwa kuinunua ni mkulima. Kwa hivyo, tunalazimika kuondoa hizo kodi kwa yule ili finally mkulima apate mbegu kwa bei rahisi aongeze uzalishaji, akiongeza uzalishaji Halmashauri zetu zinatoza cess na tunapanga mipango mingine ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu ndugu zangu siyo kwamba watu walilala wakaamka usingizini wakaanza kufuta moja, mbili, tatu, nne, tano, sita, saba. Ndiyo maana kodi ambazo tumeona zina uhusiano wa moja kwa moja na kuongeza uzalishaji, kusimamia mazao yaendelee kuwepo na kadhalika hizo hatujazigusa, tumeziacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine mdogo, kwamba tumeondoa eti kodi ya vifungashio vya korosho, kwa hivyo hili jambo litawanufaisha wanaoingiza magunia yale ndani. Jamani wanaoingiza hayo magunia ni Vyama vya Msingi vya Wakulima, korosho ikitoka kule kwenye primary societies haiendi kwenye malori kama mchanga imebebwa, inawekwa kwenye hivyo vifungashio inaingizwa kwenye ghala na hapo kila mtu ndiyo anajua, hiii ya kwangu, hii ya nani na nani by weight and everything.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoondoa hii tozo maana yake ni kwamba hawa wakulima waliokuwa wanalazimika kulipa kodi kwa ajili ya magunia yale sasa hawatalipa hiyo hela inabaki kwao. Nilikuwa napiga hesabu, kwa hilo moja tu la tozo ya magunia saving itakayokuwepo kwa wakulima wa korosho msimu unaokuja, bilioni 11. Sasa hizi siyo hela ndogo zikibaki kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tumeondoa VAT kwenye mashudu ya pamba. Mtu anaweza akadhani kwamba tumewasaidia ginner’s siyo kweli! Ginners hawa katika mjengeko wa bei wanayonunua pamba kwa wakulima wanaweka mle ile VAT kama cost. Kwa hivyo, bei ya pamba kama ilikuwa iwe Sh.1,100/= kwa kilo moja wanaondoa shilingi karibu mia moja wanasema hii tutarudisha Serikalini kama kodi. Sasa hivi tunachofanya hiyo ikiondoka maana yake hiyo mia moja itabaki kwa mkulima, itamjengea uwezo wa kulima zaidi, itamjengea uwezo wa kununua dawa na uwezo wa kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo niombe jamani ndugu zangu, haya mambo serious namna hii, tusi-relate nayo kimzaha mzaha kama tulivyoona wenzetu wanajaribu kufanya hapa ndani. Nawashukuru sana wote ambao mmetuunga mkono kwenye hili jambo, tutakuwa makini, tutaangalia impact yake. Haya ni mambo siyo static, tutaangalia impact yake katika tasnia nzima, yale yatakayohitaji adjustment tutafanya adjustment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la ununuzi wa pamoja, uingizaji wa pamoja wa mbolea. Nashukuru sana kwamba Bunge limetuunga mkono Serikali katika hili jambo nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Maangalizo yenu yote kabisa tumeyachukua, yako maangalizo ambayo mmeyasema ni ya msingi tumeyachukua. Tutahakikisha wakati tunatekeleza hili jambo tunakuwa makini na hayo maeneo ambayo mmetupa angalizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni la kuhujumiwa kwa sababu wako ambao watapoteza katika huu mchakato na kwa hivyo kama watakuwa wanapoteza wakipata uwezekano wa kuzuia tusifanikiwe watajaribu na tumeona attempt ilikuwepo na wote ninyi ni mashahidi. Kwa hivyo hayo maeneo ya hivyo tutakuwa makini nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe wasiwasi wakulima wa nchi hii kwamba fall back position sijui niisemeje kwa Kiswahili. Kwamba jambo hili likipata tatizo lolote kwa mfano, namna ya kufikisha mbolea kwa wananchi kwa wakati kwa msimu huu tunayo. Nawaomba sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mtu asidhani kwamba tunakwenda kwenye jambo blindly kwamba ikitokea something unforeseen basi sisi ndiyo tutakuwa tumeporomoka hatujui la kufanya, wakulima wamekosa mbolea na kadhalika, hapana! Fallback position ipo, siyo jambo la mjadala wa hapa ndani, lakini naomba tu muamini kwamba fallback position ipo.

Mheshimiwa Mweyekiti, ndiyo maana tumeanza kwa uangalifu na aina mbili tu za mbolea. Tumeanza na aina mbili kwa makusudi kabisa, sio kwa bahati mbaya, kwa makusudi! Kwamba uwezekano wa kuli-perfect hil jambo asilimia 100 tunasema who knows! Kitu chochote kinaweza kutokea huko tunakoagiza na nini, sasa tunafanyaje; kwa hivyo tumejiwekea na sisi hizo tahadhari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia nafasi hii kwa ruhusa yako kuwaonya hao ambao wanajaribu kutuvuta shati. Sisi dhamira yetu ni kuhakikisha gharama za uzalishaji katika kilimo zinashuka, watu hawaoni faida ya kulima kwa sababu margins zinakuwa ndogo sana, mtu anahangaika na tumbaku miezi tisa faida anayokuja kupata two, three percent. Sasa hiki tunachokifanya tunahangaika angalau hiyo faida iongezeke basi kutoka kwenye hizo three percent ifike angalau kwenye ten, fifteen percent. Tutalisimamia kwelikweli hili jambo. Kanuni hizi ziko strict kweli kweli, mtu yeyote akiingia hapo katikati atakiona cha mtema kuni. (Makofi

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahamasishe Watanzania kwamba kilimo sasa hivi kitalipa. Wale ambao wamekuwa wanadhani kwamba kilimo hakitalipa, nataka niwaambie leo kwamba kilimo kitalipa, awe ni mkulima, awe ni mfanyakazi wa kuajiriwa, ardhi Tanzania ipo, hebu twende tulime. Tukilima kwanza unakuwa umejihakikishia kama ni umelima mazao ya chakula utakuwa na chakula chako mwenyewe hulazimiki kwenda sokoni, kama utakuwa ni mkulima utapata chakula chako lakini utalazimika kupeleka ziada sokoni. Kwa hivyo tunashusha, tunapunguza hizi gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uki-combine measure hii ya bulk purchase ya pamoja na hizi tozo na kodi mbalimbali ambazo tunaondoa kwenye pembejeo kwa vyovyote vile mbolea itashuka bei na huenda katika bajeti yetu hii hapa tunayoomba iko fedha ambayo tumeiomba Bunge lituidhinishie kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Tukifanya vizuri mwaka huu katika huu mfumo yawezekana kabisa mwaka kesho Serikali ikaja hapa bila maombi ya ruzuku kwenye pembejeo kwa sababu pembejeo itakuwa sasa ni rahisi inapatikana na kila Mtanzania anaweza kumudu kununua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni mbegu. Ni kweli kwamba utoshelevu wetu wa mbegu inayozalishwa hapa nchini bado uko chini, tuko asilimia 35 ya mahitaji. Hili jambo niliongelee kwa kujibu pia hoja ya kwamba hatuweki malengo yanayopimika katika mipango yetu. Jamani, tunayo mipango ya muda wa kati na muda mrefu, mipango ya muda wa kati tunaitekeleza kupitia bajeti za mwaka mmoja mmoja halafu finally tunakuwa na mpango wa muda mrefu wa miaka mitano au kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuondokane na hali hii ya udhaifu wa upatikanaji wa mbegu bora hapa nchini kulikuwa na tatizo kubwa sana la kisheria. Utaratibu tuliokuwa nao ulikuwa haumwezeshi mzalishaji wa mbegu kuzalisha hapa nchini aina nyingi za mbegu kwa tija au akapata faida mwisho wa siku. Faida hiyo ilikuwa inamezwa katika sheria na kanuni tulizokuwa nazo. Kwa hivyo, hatua ya kwanza siyo kuanzisha mashamba, hatua ya kwanza lazima iwe ku-adress tatizo linalozaa mengine (root cause).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tumeanza na hilo, tumeanza na kurekebisha sheria na kanuni za mbegu ili sasa tukishaweka mazingira mazuri kwa wazalishaji waingie kwenye uzalishaji kwa sababu suala la uzalishaji yeyote atakayeona sasa hiyo fursa iko nzuri kwake anaingia kwenye uzalishaji. Tutoke kwenye huu mtindo ambao mbegu inazalishwa Kenya, Zambia tunakuja kuuziwa Watanzania kama vile sisi hatuna ardhi hapa ya kuzalisha mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tumeanza na sheria. Tumefuta tozo za ovyo ovyo zilizokuwako kwenye uzalishaji wa mbegu, tumepunguza masharti ya muda na mlolongo ule tumeu-short circuit wa kupata vibali ili mtu uanze uzalishaji wa mbegu. Kwa hivyo, kwa combination ya hizi measures, tuna hakika mwaka kesho tutaona investment zaidi kwenye suala la uzalishaji wa mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mbegu moja imepigiwa kelele hapa ndani, naomba na yenyewe niitolee ufafanuzi, mbegu ya pamba UK91 ni ya tangu mwaka 1991, leo ina miaka 26 imepitwa na wakati, imechoka na mimi nasema ni kweli. Yaani aliye-observe namna hiyo ame-observe vizuri kabisa UK91 ni mbegu ya zamani, uzalishaji wake umeshuka chini lakini hata uhimilivu wa visumbufu wa hii mbegu sasa na wenyewe uko chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana ndani ya Serikali na tumeweka proramu ambayo tumeanza kuitekeleza mwaka huu na tumejiwekea lengo, wale wanaosema hatuweki malengo, tunaweka! Tumejiwekea lengo kwamba inapofika msimu wa kilimo wa 2019 tutakuwa na utoshelevu wa mbegu mpya aina ya UKM08 kwa nchi nzima. Hatutakubali tena mkulima yeyote wa pamba Tanzania apande pamba ya UK91.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu peke yake tumepanda hectares 80,000 katika Wilaya tatu, Wilaya ya Igunga, Wilaya ya Nzega na Wilaya ya Meatu. Tumepanda hectares 80,000 za UKM08 na tuna-control isije ika-mix na UK91 na tutapata kama tani 8,000 ya mbegu na baada ya hapo katika msimu unaofuata wa 2018 tukipanda mbegu ile tani 8,000 tutakwenda kwenye tani 14,000/15,000 ambayo ndiyo mahitaji ya nchi nzima kwenye aina hii ya mbegu ya UKM08. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ndugu zangu wakulima wa pamba naomba niwahakikishie tu kwamba, hili jambo tutalisimamia kikamilifu na mwaka 2018 wakulima wote wa pamba tunatarajia kabisa watakuwa na mbegu mpya ya UKM08. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wafanyabiashara wanajaribu kuingiza mbegu feki, dawa feki na kadhalika.

Jambo la kusema hapa kwa kifupi tu ni kwamba ni lazima tuimarishe usimamizi, haya mambo ya feki na nini, dawa yake ni usimamizi. Tunapoimarisha usimamizi maana yake hatutoi mwanya kwa mtu kuchomekea mbegu au dawa ambayo sio sahihi. Tumechukua hatua, stern measures kweli kweli kwa Watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wana-collude na wafanyabiashara kuingiza mbegu na dawa mbaya ambazo zinawaathiri wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza kwa makini sana Mheshimiwa Maige akilalamikia wale waliopewa mbegu ya pamba miaka mitatau iliyopita wakapanda haikuota halafu mamlaka mbalimbali za Serikali zikaanza kutupiana mpira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo kwa sababu lina utaalam ndani yake huwezi kulirukia kusema kwamba ni TOSK au TPRI au ni nani waliotufanyia foul katika hili. Kwa hivyo, tutakapojiridhisha kwamba ni nani hasa culprit katika hili tutamchukulia hatua tu. Hata kama uwezo wake wa kifedha utakuwa hauwezi kuwa-compensate wale wakulima lakini tutamfunga, tutamfanyia chochote ili iwe fundisho kwa wengine kwamba uki-temper na mambo ya wananchi Serikali ipo itakuona na itakuchukulia hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la uvuvi wa bahari kuu na mchango wa uvuvi kwa ujumla. Mheshimiwa Abdallah Ulega amesema kwa maneno mazuri sana kwamba blue economy Tanzania ni kama haipo, haipo kwa sababu tulikuwa na kanuni legelege. Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka, alitumwa Mheshimiwa Mama Tibaijuka kwenda UN kwenda kuomba hiyo EZ tukafanikiwa kwenye hilo jambo, lakini tangu tupate hiyo EZ nchi kama nchi kwa mwaka tumekuwa tunaambulia shilingi bilioni sita. Huu udhaifu ulikuwa katika kanuni tulizotunga wenyewe. Nchi zote zinazofanya uvuvi wa bahari kuu, majirani zetu hawa wamekuwa wanatushangaa, hivi Tanzania hawa wakoje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa nafanya majadiliano na kampuni kutoka Spain kampuni 29 zinazofanya uvuvi bahari kuu walikuja kuniona wanahoji hizi kanuni kwa nini ziko hivi. Siku hiyo tunafanya hayo mazungumzo, South Africa walikuwa tempted kumleta Waziri wao wa Uvuvi aje kusikiliza kama tuta-yield/bow kwenye hoja za hawa watu. Mimi nikamwambia wewe kaa tu huko, tuko imara, tunajua tulichokifanya. Tume-research, tumeangalia best practice ya wenzetu wanafanyaje na sisi tumeji-peg katika mambo ambayo yanatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali by catch siyo mali ya aliyevua, mvuvi anaomba license ya aina ya samaki, tunampa license ya kuvuna huyo jodari basi, akikamata samaki mwingine huyo hakuwa ameruhusiwa na wala hajakata license kuvuna yule na ile ni rasilimali ya Watanzania. Tunachosema kwenye Kanuni zetu, hiyo rasilimali uliyokamata ambayo siyo ya kwako ambayo tumekuruhusu kuvuna leta. Tunazungumza modality ya compensation ya mafuta na kadhalika, lakini tumeweka suala la uhakiki wa volumes au tonnage wanazovuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani mtu akivua samaki kule akishakata license ile dola 50,000 miezi sita, anavua kiasi chochote atakachopata sisi hatuambulii chochote. Tulichokomea ni hiyo dola 50,000. Sasa hivi tumesema hii nayo ni maliasili kama zingine, zitalipiwa pia mrabaha na kwa maana hiyo tutapeleka observers wetu, wakajue bwana huyu kavuna kiasi gani kwa hivyo mrabaha wetu kiasi gani. Katika hizo alizovuna kwenda nazo huko anakoenda sawa, zile zisizostahili ngapi tuletee hapa Watanzania wapate samaki kwa bei nafuu tuongeze lishe kwa watu wetu na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna multiply effect kubwa sana. Meli zile zitakapoleta ile by catch watakuja kununua chakula, kuweka maji, wataweka mafuta, watalipia sijui nini. Kwa hivyo, uchumi utanufaika siyo kwa samaki tu lakini uchumi utanufaika hata kwa mambo mengine zaidi ya hao samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka sharti la kuwa na Mabaharia Watanzania. Activity hii inafanyika ndani ya eneo letu la nchi, si ndiyo? Ni kama mtu aje aweke kiwanda hapa halafu asilimia 100 ya wafanyakazi ni watu wa nje tutakubaliana na jambo la hivyo? Kwa hivyo ile meli inapokuja kufanya activity ya mwaka mzima Tanzania, tunasema na Watanzania wa-participate lazima kuwe na local content Mheshimiwa Ngwali! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako vijana hapa wanasoma vyuo vyetu hapa wanamaliza halafu wanatushangaa tu, kwamba watu wanatoka huko watokao, China, Indonesia na Taiwan wanakuja wanafanya shughuli ya uvuvi hapa, Tanzania hakuna hata Baharia mmoja huko ndani, hakuna kila kitu tumewaacha wanasomba wanavyotaka, mimi nasema jamani niacheni jamani niacheni nishughulikie hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati akiwa Waziri wa Uvuvi alikamata tani 290 tu ya meli iliyokuwa inafanya uvuvi haramu pale. Tani ile 290 ilisambaa Magereza yote Dar es Salaam, Morogoro mpaka Tanga. Sasa kwa wastani hesabu na wataalam wetu wanasema, ukivua tani moja at least asilimia 20 ni by catch, wanakamata kule zaidi ya tani 20,000, tani elfu ngapi. Kwa hivyo, tunatarajia tu hata ile by catch itakuja hapa maelfu ya tani.

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika, kwanza kabisa nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Hoja ya Bajeti ya Serikali iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kwa kusema tu kwamba naunga mkono hoja na baada ya kuunga mkono hoja niseme pia kwamba bajeti hii imeitendea haki sana sekta ya kilimo nchini. Ninaposema sekta ya kilimo ni kwa maana ya sekta ya kilimo, mazao, mifugo na uvuvi na pia sekta ya ushirika hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tozo, pamoja na kwamba wako walioonekana kama hawaridhiki na ufutaji wa tozo na kodi mbalimbali katika kilimo, lakini sisi tunaovaa kiatu ndio tunajua kilikuwa kinatubana kiasi gani, na kwa maana hiyo tunatarajia kwamba tozo na kodi mbalimbali ambazo zimeondolewa zitaongeza tija katika kilimo, lakini pia zitaweka mazingira mazuri ya wadau wote wa kilimo ku- participate (kushiriki) bila kukwazwa na mazingira hayo ya kodi na ushuru mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, wakulima wamekuwa wakilalamikia tozo hizo na wafanyabiashara na watu wengine katika minyororo ya thamani na wao pia wamekuwa wanalalamikia tozo hizo. Kwa hiyo, tumeziondoa na Serikali imekubali kuziondoa na kuzifuta baadhi yake, nyingine kuzipunguza ili kuhakikisha kwamba wote wananufaika, win-win situation; Serikali ibakie na mambo yake ikinufaika lakini na wananchi pia wapate nafuu na kunufaika na jitihada wanazofanya katika mashamba na maeneo mengine ya uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba baada ya hayo tutaona mabadiliko ya bei ya mazao yetu ya biashara, lakini pia tutaona uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka, tutaona ufugaji ukipata nafuu zaidi baada ya kuondoa kodi hizi na tumeweka mazingira yanayovutia uwekezaji sasa katika mifugo. Eneo hili limekuwa halipati uwekezaji mzuri kwa sababu ya tozo na ada mbalimbali zilizokuwepo.

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba tunaendelea kama Wizara na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba upatikanaji wa pembejeo unakuwa kwa wakati na kwa bei ambayo wakulima wanaweza kumudu. Hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo zilizokuwako katika uingizaji na usambazaji wa mbolea na viuatilifu. Vilevile tunaendelea na mchakato wa uagizaji wa baadhi ya mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba mwishowe bei tutakayoiweka itakuwa inahimilika, wananchi wanaweza kuimudu na kwa hivyo ituwezeshe kuongeza uzalishaji katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, Programu ya Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) imekamilika maandalizi yake na tumefanya mambo kadhaa. Pamoja na mambo tuliyoyafanya ni kutoa Mwongozo wa Kilimo, pia Mwongozo wa Ufugaji.

Mheshimiwa Spika, katika programu hii suala la umwagiliaji limepewa kipaumbele, na safari hii umwagiliaji tunaoufikiria kuuwekea msisitizo mkubwa ni umwagiliaji wa mazao makuu ya chakula. Kwa muda mrefu umwagiliaji umekuwa katika maeneo ya mpunga na mbogamboga, lakini sasa katika awamu hii ya Programu ya Kilimo ya Pili tunataka kwenda kwenye zao kubwa la chakula nchini ambalo ni mahindi. Umwagiliaji ufanyike pia katika uzalishaji wa mahindi ili kujihakikishia usalama wa chakula na uzalishaji wa muda wote ambao hautuletei mashaka.

Mheshimiwa Spika, niombe kutumia nafasi hii kuwatangazia wananchi kwamba sasa hivi maeneo mengi nchini wanavuna, lakini niwaombe sana baada ya kufanya mavuno hayo utumiaji wa chakula chao uwe wa makini kwa sababu hali ya hewa katika nchi zinazotuzunguka haikuwa nzuri na kwa hiyo, kutakuwa na mahitaji makubwa ya kununua chakula kutoka Tanzania kwenda nchi za nje.

Wananchi hawazuiliwi kuuza lakini wanashauriwa wauze na kujiwekea akiba ya kuwatosha.

Mheshimiwa Spika, narudia kusema naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kusimamia sekta ya kilimo hapa nchini. Pia niwashukuru sana viongozi wetu wakuu wa Serikali, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa uongozi wao wanaonipa ili kutekeleza majukumu yangu sawasawa. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniletea Msaidizi katika shughuli Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa naamini kwamba tutafanya kazi vizuri kwa matarajio ya waliotuteua na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa kuleta huu mpango ambao kwa kweli unatoa dira ya namna uchumi wa pamoja unavyoweza kwenda na tukafikia hilo lengo letu la kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe kutumia nafasi hii kuishukuru sana Kamati ya Kilimo, Mifugo, Maji na Uvuvi kwa sababu wamekuwa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu yetu. Wametushauri na tumesikiliza ushauri wao, wametuelekeza na tumetekeleza maelekezo yao. Pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia kwa namna moja au nyingine kuhusu mambo ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati yetu, ratiba ya Bunge iliyokuwa imetolewa ilikuwa tuanze kuwasilisha taarifa za Wizara tarehe 30 mwezi uliopita, lakini kwa unyeti wa jambo la mahindi, Kamati ilituita mapema zaidi tarehe 25 ili tujadili suala la mahindi kwa udharura. Wapo wananchi wana mahindi, hawawezi kuyauza kwa sababu ya bei kushuka na kwa hivyo wanashindwa kuingia katika cycle nyingine ya kilimo kwa sababu hawana fedha kwa ajili ya pembejeo na maandalizi ya mashamba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kutokana na mjadala katika Kamati, ndipo Serikali tulisikia na tukachukua pia hatua za kidharura tukaelekeza Wakala wetu wa Mazao (NFRA) waanze tena kwenda kununua katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa, tukajipiga piga pesa ikapatikana ya kuanzia na tunaendelea ku-mobilize funds ili waendelee kununua katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi wapo wameanza manunuzi katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma lakini pesa tena tulikuwa tunazungumza na Waziri wa Fedha nyingine imepatikana sasa wataanza pia kununua katika Mkoa wa Rukwa na baadae wataingia katika Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, hizi ni hatua ambazo tulizichukua kwa udharura ule ili kuhakikisha kwamba angalau fedha inaanza kupatikana kwa wananchi waweze kuingia katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tathmini tumebaini pia kwamba mahindi yaliyopo kwa wananchi ni mengi sana na watu kwenye maeneo haya wasipopata soko la uhakika wengine hiyo fedha ambayo inatolewa na Serikali kupitia Wakala wake inaweza isiwafikie kabisa. Kwa hiyo, Serikali imeamua kwamba itawaruhusu wafanyabiashara waweze kupeleka mazao nje ya nchi, hasa mahindi ili kutengeneza soko na kuchangamsha bei kwa wafanyabiashara na wakulima wa zao hili la mahindi hapa nchini. Tunaomba tu kwamba viongozi wote tushirikiane kuhakikisha kwamba taratibu za kawaida za uondoshaji wa mazao nje ya nchi zinafuatwa ili kulinda mipaka yetu na kulinda usalama wa chakula hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote nchini kuacha mara moja tabia ya kuzuia mazao kutoka katika mikoa yao kwenda mikoa mingine au kutoka katika wilaya zao kwenda wilaya zingine. Tanzania ni moja na tungependa bidhaa ziweze kusafiri kutoka sehemu moja ya nchi kwenda sehemu nyingine ya nchi bila vikwazo vyovyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia Wabunge wote wanaotoka maeneo yanayolima tumbaku kwa jinsi ambavyo wameshughulikia suala la ukosefu wa soko la zao hili kwa umakini na kuguswa sana. Serikali ilikwishaliona hili tatizo mapema la kwamba tumbaku imezalishwa zaidi ya mikataba iliyokuwepo na wanunuzi wetu wa kawaida wa hapa ndani, kwa hivyo tulianza mchakato wa kutafuta wanunuzi wa hii tumbaku ya ziada walioko ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada kubwa zimefanyika na mpaka hapa tunapozungumza sasa zipo kampuni za ndani ya hapa ya nchi walio tayari kununua hiyo tumbaku. Zipo kampuni pia ambazo zimeonyesha mwelekeo kutoka nje ya nchi ambao pia wapo tayari kununua hii tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie pia nafasi hii kuiagiza Bodi ya Tumbaku ifanye mazungumzo na makampuni yote yaliyo tayari kununua tumbaku hii ya ziada, ifikapo kesho mchana wawe wamekwishanipa taarifa ya kampuni gani inaunua wapi kiasi gani ili hii tumbaku iliyopo kwa wananchi isiendelee kuharibika kwa kutunzwa vibaya hasa ukizingatia kwamba sasa hivi tupo kwenye msimu wa mvua na inaweza kunyeshewa na kupoteza ubora wake.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutarajie tu kwamba zoezi hili litakwenda vizuri, wanunuzi watapatikana wataichukua hii tumbaku nasi tutajipanga vizuri sasa kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa soko hili la tumbaku kwa kuingiza wanunuzi wengi zaidi wa tumbaku kuliko tulionao hivi sasa. Kwa hiyo, mazungumzo yanaendelea na nchi mbalimbali ambazo zina interest ya kununua tumbaku yetu na Inshallah Mungu akitujaalia tutapata wanunuzi wengi zaidi katika msimu ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti ilizungumzia suala la upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Ni kweli hili limekuwa tatizo kwa wakulima wetu hapa nchini kwa miaka mingi. Pembejeo inafika mahali na hasa pale tulipokuwa na mfumo wa ruzuku, pembejeo ya ruzuku inafika kwenye eneo msimu umekwisha mbolea na mbegu ndio zinafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, sasa hivi tunafanya mpango hapa nchini kupitia wizara yetu ambapo tutahakikisha kwamba mbolea inakuwepo maeneo yote wakati wote. Hili tunalifanya kupitia huu utaratibu wa uagizaji wambolea kwa pamoja, mbolea itakuwa inaendelea kuagizwa bila kujali msimu wa kilimo ili kuhakikisha kwamba ipo madukani muda wote na mwananchi akiihitaji anakwenda ananunua anafanya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la kuamini kwamba kilimo ama pembejeo zinahitajika wakati wa mvua peke yake sio sahihi, kwa sababu wapo pia wananchi ambao wanafanya kilimo cha umwagiliaji, kwa hiyo, wao hawasubiri msimu ule mvua, wanaendelea na kilimo chao muda wote. Kwa hiyo, sasa tumeanzisha huu utaratibu ambao utakuwa unatuhakikisha kwamba madukani iko mbolea na inayohimilika kwa maana ya bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la bei limekuwa ni tatizo au changamoto kwa wakulima wetu kwamba wengi wamekuwa hawawezi kumudu bei ya mbolea hizi. Sasa tulichokifanya tumeanzisha huo utaratibu ambao unatuhakikishia kushuka kwa bei ya hizi mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tena kutumia fursa hii kuwakumbusha wadau wote wahakikishe kwamba bei elekezi kwa aina mbili za mbolea tulizoanza nazo katika mfumo huu yaani mbolea ya kupandia DAP na mbolea ya kukuzia Urea bei elekezi zinazingatiwa kwenye maeneo yote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatahadharishe wafanyabiashara ambao hawataki uaminifu, wanaoendelea kuuza bei elekezi katika maduka ya jumla ya Mikoani na Wilayani kwamba jambo hilo ni kuvunja sheria, kwa sababu wao katika maduka ya jumla wanatakiwa wauze kwa bei chini ya bei elekezi ili bei elekezi imfikie mwananchi kijijini ambaye ananunua mbolea na kwenda shambani. Bei elekezi siyo katika maduka ya jumla isipokuwa bei elekezi ni ya wakulima anayenunua na kwenda shambani. Kwa hivyo, viongozi wote wa mikoa simamieni hili jambo, viongozi wote wa wilaya wasimamie hili jambo ili wananchi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge na tumeona ni vema na sisi tulitolee maoni ni kuhusu uboreshaji wa lililokuwa Shirika letu la Usagaji la Taifa (National Milling Corporation). Niseme tu kwamba sasa hivi iliyokuwa NMC iko chini ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na bodi hii imekwishaanza kazi. Ilianzishwa mwaka 2009 lakini utekelezaji wa majukumu yake umeanza mwaka 2013 na sasa hivi wanasaga na kununua mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasaga mahindi katika kinu cha Iringa na katika msimu huu mwanzo walikwisha nunua tani 2,300 za mahindi lakini sasa hivi wamepata pesa, mkopo kutoka Shirika letu la Hifadhi ya Taifa (NSSF) shilingi bilioni 8.9 na tumewaelekeza kwamba waendelee na ununuzi wa mahindi katika maeneo haya ambayo yana uzalishaji mkubwa ili kuondoa hiyo stress ya bei katika soko la mahindi. Pia wanafanya jitihada za ku-possess mali zao zote ambazo wamepewa kwa mujibu wa sheria ili waweze sasa kufanya biashara kama ambavyo inatarajiwa kutoka kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisigongewe kengele ya pili, naomba nikome hapo. Nisisitize tu kwamba ni ruhusa sasa kusafirisha mahindi kwenda nje ya nchi na taratibu tu za kawaida zifuatwe, pia ifikapo kesho mchana suala la tumbaku ya ziada liwe limekwishapata suluhu kwa maana ya kwamba mnunuzi gani ananunua kiasi gani, wapi niwe nimekwishafahamishwa ili keshokutwa kama ni ununuzi kuanza uanze mara moja bila kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninaomba nimjibu Mzee wangu, Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa tulizalisha kwa utoshelevu wa asilimia 123. Kama ulivyosikia katika maelezo yangu sasa hivi yapo maeneo yenye ziada nchini, kule bei ziko chini, wananchi wanalalamika hawana pa kuuza mahindi kiasi kwamba tumefikia turuhusu watu kupeleka mahindi nje ya nchi. Lakini yapo maeneo na kwa tathmini yetu, mikoa kama 11 itakuwa na utoshelevu wa chini ya kiwango na kwa hiyo tunaendelea kuwaomba wafanyabiashara nchini wachukue mahindi kule ambapo yapo ya ziada wapeleke kwenye maeneo haya ambayo hayana utoshelevu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitumie tu tena nafasi hii labda kulisemea hili, kwamba wafanyabiashara nchini na wakala zetu za Serikali wanaonunua watachukua mahindi maeneo haya yenye ziada na kwenda kuyauza kwenye maeneo ambayo yana upungufu ikiwamo pia Jimbo lake la Mpwapwa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kutupa nafasi kutoa maelezo kuhusu hoja ambazo zimetolewa na Kamati na Wabunge ambao wamechangia taarifa za Kamati zilizowasilishwa leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru sana Kamati yetu kwamba tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana, wametushauri mambo mengi na katika ushauri wao yako ambayo tuliyaacha na tukachukua ushauri kuufanyia kazi. Kwa hiyo, katika mapendekezo yaliyotolewa na Kamati kimsingi yote yanakubalika na tutaenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumzie mambo manne na kama muda utatosha nitazungumzia na lingine la tano, lakini nataka nizungumzie suala la masoko ya mazao, lakini pia tunavyokabiliana na wadudu na visumbufu vya mimea, jambo la uagizaji wa mbolea kwa pamoja na tatizo la uchakachuaji wa korosho iliyosafirishwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na tatizo la masoko ya mazao. Nimewasikiliza kwa uzuri sana Waheshimiwa Wabunge waliozungumzia ukosefu wa soko la mazao hasa mahindi na mbaazi. Lakini pia nimemsikia Mheshimiwa Maige akizungumzia suala la ukosefu wa soko la tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli haya mazao kama yalivyo mazao mengine ambayo pia hayakuzungumziwa hapa ndani. Masoko yake siyo mazuri sana. Na masoko haya siyo mazuri kwa mazao yanayozalishwa Tanzania tu, labda hili ndiyo naomba tuelewane vizuri. Ni hata wazalishaji walio nje ya Tanzania wanakabiliwa na tatizo hili hili la masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Tanzania mahindi yameshuka bei mpaka shilingi 5,000 kwa debe, jirani zetu Zambia debe la mahindi liko shilingi 2,600; Malawi debe liko shilingi 3,100. Mwaka juzi mahindi yalipanda bei sana kwa sababu nchi zote zilizotuzunguka hawakuwa na uzalishaji kwa hivyo soko likabaki chanzo cha mahindi kikabaki ni Tanzania peke yake.

Kwa hiyo, suala sasa hivi la uwezekano wa kupandisha bei ya mahindi wakati majirani zetu wote wanayo mahindi yanayowatosha halipo. Misimu inatofautiana, kwa hiyo wanavyozalisha na wao hawawi tena na sababu ya kuja kwetu ndivyo hivyo hivyo ilivyotokea kwa mbaazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, traditional soko la mbaazi la Tanzania ilikuwa ni India na wazalishaji wameendelea kuzalisha na wakiuza huko India miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala la Waziri Mkuu wa India alipokuja hapa akazungumza yes watu waliamasika wakazalisha zaidi na kwa sababu bei ya msimu iliyotangulia ilikuwa kubwa uzalishaji ukaongezeka watu wakaenda benki, wakachukua pesa ili wazalishe mbaazi kwa ahadi kwamba watapata soko la uhakika ambalo wamelizoea, India imezuia. Kwa hiyo, soko la mbaazi la India limesabaisha ku-distort soko la mbaazi la ndani ya Tanzania, na hapa namshukuru sana Mheshimiwa Mgumba amelieleza vizuri tatizo la commodities zile, lakini pia nimfahamishe kwamba nchi ya India walisaini mkataba na Mozambique wa kununua mbaazi sisi waka-deal dull kumbe wakichungulia uzalishaji wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji wao ulipokuwa mzuri kuliko walivyotarajia wakaweka mguu chini hawakutaka kusaini mkataba wa makubaliano na kule Mozambique ambako waliingia mkataba wamenunua tani 135,000 ya mbaazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo masoko ya mazao twende kwenye tumbaku, tumbaku inazalishwa kwa mkataba.

Tumbaku inazalishwa kwa mkataba, baada ya mabishano ya bei kwenye Tobacco Council...

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimwia Gekul sijui niikatae kwa sababu bila maelezo ya kilichotokea tutazungumza nini hapa. Sidhani kama hata ni utaratibu mzuri, lakini anyway ndiyo Bunge lenyewe lilivyo. Kwa hiyo, masoko haya...

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala tu la uelewa kwa sababu ukielewa kwamba tuna misimu tofauti na kwa hiyo sisi uzalishaji wetu unatangulia na wengine unafuata huwezi ukaacha mahali ambako soko la ndani haliko regulated kwa sababu ya nanilii... Historia ya mwaka jana nadhani iko bado live kabisa kwenye vichwa vya Wabunge. Tulienda tukakubaliana kwamba tuache mahindi yaende nje baada ya miezi miwili Bunge hili hili ndiyo likaanza kusema kwamba…

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mwakajoka kwamba utafiti tunafanya na utafiti tuliokwishaufanya hatua tutakazochukua mwaka huu zitakuwa tofauti sana na hatua ambazo tumekuwa tumechukua miaka ya nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa hiyo, utafiti tulioufanya tutachukua hatua tofauti na hizi ambazo zinatufikisha kuvutana na Serikali na Wabunge. Soko la kahawa la Tanzania limeendelea kuwa duni kwa sababu ya mazingira ya kodi ambayo tunayo Tanzania ukilinganisha na nchi zinazozalisha kahawa…

KUHUSU UTARATIBU . . .

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika tu kwamba Mheshimiwa Heche anasema nimepotosha Bunge, ninachokisema ni ukweli na ukweli huu kama haumpendezeshi masikio bahati mbaya. Mazao haya yana sheria iliyotungwa na Bunge. Kwa hiyo, hatuwezi tukaicha sheria tukaenda na mambo ambayo hayana utaratibu. Kupeleka tumbaku Kenya kuna hitaji utaratibu wa sheria, utoroshaji wa tumbaku ni uvunjaji wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nazungumzia habari ya masoko ya mazao, commodity markets ziko volatile dunia nzima na siyo Tanzania peke yake kwa hiyo ikitokea hizi fluctuation za bei fluctuation za nini siyo kwa sababu nchi hii ni Tanzania, hili ni jambo ambalo sasa hivi lina affect dunia nzima uliza nchi yoyote bei za mazao zimeporomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tunavyokabiliana na wadudu. Ni kweli suala la worms lilijitokeza mwaka jana na sisi tulitoa taarifa kwa umma namna ya kuwatambua na namna ya kudhibiti wadudu hawa. Bahati mbaya sana wadudu hawa wamekuwa wanafanana na wale viwavijeshi tuliowazoea, kwa hiyo, watu wakadhani kwamba wataporomwosha tu na mvua ikinyesha, hawakuchukua hatua. Serikali ilichukua hatua ya kupita mikoa yote ambayo ilikwishaonekana wadudu hawa wapo, kutoa mafunzo na kuelekeza wananchi namna ya kukabiliana na ...worms, lakini wameendelea kuzaana hivi hivi. Sasa hivi kuanzia wiki wiki hii tutapeleka dawa kwenye Halmashauri ambazo Mikoa yote imekuwa-affected na hawa wadudu ili halmashauri zigawe hizi dawa kwa Wananchi wapulize kwenye mashamba yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo liko kwenye pamba kuna wadudu, funza na utitiri, wamekuwa wanashambulia pamba lakini tuseme tuu kwamba dawa imekwishapatikana fedha tuliyokuwa tunahitaji tumepata dawa imenunuliwa inaendelea kusambazwa na Bodi ya Pamba, nilikuwa huko mwenyewe jana, kwa hiyo, tatizo hili nalo tutakabiliana nalo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo wale kwelea kwelea wanaoharibu mazao Shinyanga na Simiyu, upuliziaji kwa ndege utaanza lakini pia dawa kwa ajili ya panya walioko kwenye maeneo ya Handeni, Morogoro, Ifakara, Mlimba na Chalinze na kwenyewe dawa imepatikana tutapeleka kule, ili Halmashauri zikasimamie uteketezaji wa hawa panya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala la mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja. Huu mfumo una tatizo la msingi la kwamba unanyang’anya faida kwa baadhi ya wafanyabiashara waliozoea kupata faida kubwa. Kwa hiyo, lazima yatengenezwe mazingira ya kuonesha kwamba mfumo huu haufanyi kazi vizuri na sisi tunachokifanya ni kukabiliana na hayo ambayo yanajitokeza, wakati tunatekeleza mfumo wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekti, Kamati imesema kwamba lengo halikufikiwa; jibu ni ndiyo na hapana kwa sababu yako maeneo ambayo bei ilikuwa kubwa sana mbolea tuliyoiagiza kwa ile awamu ya kwanza ilikuwa ya bei ya chini kulinganisha na bei iliyokuwapo kwenye maeneo hayo. Sasa hivi bei ya Urea imepanda katika soko la dunia hatuzalishi wenyewe Urea hapa kwa hivyo awamu ya pili ilipoagizwa imekutana na bei iliyopanda. Hata hivyo, control tunazoziweka ndio zinatuhakikishia kwamba mkulima hatauziwa kwa bei ya kinyang’anyi, tunaweka mechanisim ambayo itamhakikishia mkulima ananunua kwa bei himilivu, tukiacha hivi hivi ndio mfuko unakwenda mpaka shilingi 80,000; 90,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo suala la BPS limekutana na changamoto ya ufikishaji wa mbolea kwenye maeneo ya vijijini ambako miundombinu ya barabara iliharibika usafirishaji ukapanda bei. Kwa hiyo, wafanyabiashara wakawa wanashindwa kusafirisha na kuuza kwa bei elekezi na sisi tulichukua hatua mara moja tukawaambia kuwa mikoa wafanye tathmini ya gharama halisi ili waweze ku-adjust gharama za kutoka kwenye Wilaya kwenda huko vijijini na jambo hilo limefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni habari ya korosho na uchakachuaji uliotokea. Taarifa tulizonazo, tatizo katika korosho halikuanza mwaka huu, limeanza mwaka jana kwa wafanyabiashara wa kutoka Vietnam.
Uchakachuaji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kwa kuanza kabisa niseme naunga mkono haja.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuunga mkono hoja naomba kwa haraka nitoe ufafanuzi wa baadhi ya michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo inagusa sekta ya kilimo na kwa muktadha huo nitazungumzia korosho, kahawa, pamba, ufuta, mfumo wa uingizaji wa mbolea kwa pamoja na soko la nafaka kama muda utakuwa unatosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwanza jambo la korosho katika namna mbili, moja ni kwa namna gani tumejipanga kuhakikisha kwamba kiatilifu aina ya surphur kinapatikana kwa wakulima wa korosho nchini. Mpaka hivi sasa ninapozungumza Serikali imekwishatoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kulipia advance ya suppliers wa sulphur kwa maeneo yanayozalisha korosho. Fedha hizi imelipwa Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) ambao wao wataingiza tani 8,000; na sasa hivi wanayo order ya tani 5,000 ambayo itafika mapema mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambasamba na TFC Kampuni ya Bajuta pia imeshapewa zabuni ya kuingiza hiyo sulpha tani 10,000 na wataingiza tani 5,000 mwishoni mwa mwezi huu, tani 5,000 zingine zitaingizwa na kampuni ya dunia mwanzoni mwa mwezi wa tano au katikati ya mwezi wa tano. Kwa hivyo mpaka kufiia tarehe 15 Mei tuna uhakika tutakuwa na tani zisizopungua 15,000 ambazo hizi tutazitumia kwa maeneo ya Lindi ambako ndiko mwanzo kabisa wa upuliziaji unatakiwa kuwapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitoe taarifa tu kwamba ziko tani 4,000 sasa hivi nchini zilizomilikiwa na kampuni ya Expo Trading na tunafanya mazungumzo nao kuhusu bei ili tukikubaliana bei nayo ianze kugaiwa kwa wakulima hasa katika yale maeneo ambayo yanahitaji dawa hiyo haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla Serikali kupitia vyama vya ushirika itaagiza jumla ya tani 35,000 ya sulphur mwaka huu, na tuna hakika kiasi hicho cha sulphur kitawatosha wakulima kwa nini tunajiingiza kuagiza hizi sulphur sasa hivi, hii yote ni kutaka kudhibiti bei ya sulphur ili wakulima waweze kupata nafuu wanapokuwa wananunua dawa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la muhimu hapa nitoe tu taarifa kwamba sulphur mwaka huu kwa wakulima itauzwa na itauzwa kwa bei itakayokuwa controlled na Serikali, na ndio maana tunashiriki katika uagizaji wake ili tuje tuhakikishe kwamba bei itakayouzwa hii sulphur itakuwa inahimilika kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kwa wananchi waliouza korosho zao msimu uliopita na sasa hivi hawajalipwa. Moja ya sababu ya wananchi hawa kutolipwa ni mkanganyiko uliotokea baada ya kuwashawishi wafungue akaunti ili malipo yafanyike moja kwa moja benki. Wengine badala ya kufungua wao akaunti waliwabebesha ndugu na marafiki zao na hivyo wale walioingiziwa pesa kwenye akaunti zao kugoma kuwalipa wakulima hawa. Lakini lilitokea tatizo la Benki ya Covenant kufungwa ambayo vyama 14 vya msingi vilikuwa vinapitishia pesa katika benki ile. Sasa jambo hili ni la kisheria kwa hivyo suala la Benki Kuu na ile benki linaendelea kufanyiwa kazi na litakapokuwa limetatuliwa wakulima hawa watapewa fedha zao na wala hazitapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwa haraka suala la masoko na namna ya kuuza kahawa na pamba kwa msimu wa mwaka huu. Serikali imeamua kusimamia ushirika wa nchi hii ili wakulima waweze kunufaika. Utaratibu uliokuwepo wa kuuza kahawa umekuwa hauna manufaa kwa wakulima walio wengi, lakini umewanufaisha zaidi watu wa katikati yaani watu wanaonunua na kuuza na si wakulima wenyewe. Neno linaitwa butura kwa watu wa Ziwa Magharibi wanafahamu maana yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwananchi analima kahawa, anapatwa na tatizo kidogo la shilingi 200,000; mtu mwenye pesa anakuja anampa shilingi 200,000 halafu anamuandikisha mkataba wa shilingi milioni tano na kusema hizo milioni tano wasipozilipa mpaka mwezi wa sita nyumba yake inauzwa; na kwa vile mwananchi huyu anakuwa na shida analazimika kuchukua hizo pesa kwa masharti ya kihalifu namna ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali imeona namna bora ya kuwasimamia wananchi hawa maskini kuwa ni kusababisha wauze kahawa yao kupitia mfumo rasmi mfumo wa ushirika. Kwa namna hii na nimesikiliza sana maoni ya Waheshimiwa Wabunge kwamba tutengeneze utaratibu ambao watau wenye shida kama hao katikati ya ushirika huo waweze kupata msaada. Ni kweli, Mbinga utaratibu huu unafanyika vizuri, vyama vya wakulima vya Mbinga vinao utaratibu ambao mwananchi akiwa na shida wanao mfumo wa kumsaidia na kwa hivyo tunapeleka huo uzoefu wa Mbinga katika maeneo mengine ili wananchi wa kule wasilazimike kuingia kwenye utaratibu ule usiokuwa na manufaa kwao isipokuwa wapitie ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo la wauzaji wa kahawa moja kwa moja nchi za nje yaani direct export. Wauzaji wa namna hii sio wengi, kimsingi ni wale wenye mashamba makubwa ambayo ni kama asilimia 10 au tisa ya uzalishaji mzima hapa nchini. Sasa watu wa namna hii wamekuwa wanauza moja kwa moja na katika kuuza moja kwa moja hatupati takwimu sahihi za mauzo yao. Hawa pia ndio wamekuwa wanafanya hiyo kitu inaitwa butura, wananunua kwa wakulima, wana-aggregate halafu wanauza nje moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kahawa hata kama imethibitishwa (satisfied) kwa ubora fulani ipeleke mnadani ili wanunuzi wengine pia wakaijue. Tunapofanya hivi tunazuia price transfer kwa sababu uuzaji wa moja kwa moja ambao hauwezi kudhibitiwa na bodi unakuwa unatoa mwanya mtu kutengeneza bei ya chini kwa sister company ili alipe kodi isiyostahili halafu fedha inayobaki anakwenda kukutana nayo huko nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo la utayari wa ushirika kusimamia mfumo huu, tunalifanyia kazi, vyama vya ushirika vyenye matatizo tumesha vibaini na tunazungumza na mabenki kuona namna ambavyo navyo vinaweza vikapata fedha kwa ajili ya kulipa advance ambayo wamekuwa wanawalipa wakulima wao miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kule KCU juzi ilisemekana KCU wametangaza bei ya shilingi 1,000 kwa kilo moja ya kahawa. Naomba nitoe taarifa rasmi kwamba jambo hilo sio kweli, wao walikuwa wanafanya bajeti ya chama chao cha msingi kwamba wachukue kiasi gani benki kwa ajili ya kuwa-advance wakulima kabla ya kupeleka kahawa ile mnadani na kamwe ile si bei ya kahawa ambayo wanatakuwa wananunua kutoka kwa wakulima wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamba pia tutauza kwa utaratibu huu huu, na tutapita na tunaendelea kupita maeneo yote ya pamba kujiridhisha kwamba vyama vya msingi vya wakulima wa pamba vipo in place na kama havipo basi uchaguzi ufanyike. Angalizo letu ni kwmaba wananchi wachague viongozi waadilifu wasije wakatumia kuchaguliwa kwao kwenda kuwaibia wananchi kama walivyozoea miaka ya nyuma. Nitahadharishe wale wanaogombea uongozi wa vyama hivi vya wakulima kwa lengo la kwenda kuuza wako mwili wao nusu uko jela, nusu uko bado mtaani kwa sababu hatutakuwa na huruma na mtu yeyote atakayejaribu kuiba mali ya wananchi kwa kisingizio chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la mfumo wa uingizaji wa pembejeo nchini. Katika hili tutafanya seminar ya Bunge zima kuelezea mfumo huu unafanyaje kazi.

Naomba Waheshimiwa Wabunge muwe na subira tutawapitisha katika mfumo huu ili uelewa uwe wa pamoja na tuko tayari kusikiliza maoni yenu pale mnapoona kwamba jambo hili haliendi salama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kusimamia mjadala huu na kunipa fursa ya kuhitimisha hoja niliyoitoa jana asubuhi kwa kutoa maelezo kuhusu masuala mbalimbali yaliyojitokeza na yaliyozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kutoa maelezo kuhusu hoja hizo ni vyema niwatambue Wabunge wote waliochangia kwa maandishi na kwa kuongea. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 117 wamechangia hoja hii, kati yao Wabunge 62 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge 54 wamechangia kwa maandishi. (Makofi)

Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu ya maandishi na kwa kuzungumza na kimsingi mmetoa hoja nzuri sana zenye malengo ya kuimarisha utelezaji wa majuku katika Wizara yangu. Hii inaonesha ni namna gani Wabunge wako tayari kutoa michango yao ya kimawazo kwa ajili ya kuendeleza sekta muhimu ya kilimo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango iliyotolewa ni mingi sana. Ni ukweli pia kwamba muda niliopewa hauwezi kukidhi kujibu hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, naomba mtambue kwamba michango yote iliyotolewa ninaithamini sana na Serikali kwa ujumla kama mlivyosikia inaithamini sana na tutaifanyia kazi kwa umakini ili kuendeleza sekta hii ya kilimo. Majibu ya hoja zote yataandaliwa kimaandishi na Waheshimiwa Wabunge mtapatiwa kabla Bunge hili halijahitimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kujibu hoja jumla zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Nianze na hoja za Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeishauri Serikali kuongeza bajeti ya kilimo. Ni kweli bajeti ya kilimo kama bajeti za Wizara zingine nyingi hazitoshi. Ukipewa unconstrained budget ni matrilioni ya pesa kwa kila bajeti, lakini kwa sababu ya resource envelope yetu tuliyonayo bajeti zetu karibu Wizara zote Waheshimiwa Wabunge zinaminywa, ndiyo maana kila Wizara imewekewa ukomo wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wizara ya Kilimo haitekelezi majukumu ya kilimo yote yenyewe peke yake. Muundo wa Serikali yetu Waheshimiwa Wabunge umegawanya kilimo kitekelezwe katika Wizara nyingine kadhaa. TAMISEMI ndio watekelezaji wa shughuli za kilimo kwa asilimia 80 kwa sabau miradi yote ya wananchi ya kilimo iko katika mipango ya maendeleo ya kilimo ya Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kilimo kwa muundo wa Serikali yetu Waheshimiwa Wabunge kinatekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Shughuli yote ya umwagiliaji; na nimewasikia humu Waheshimiwa Wabunge mkisema kwamba kilimo cha uhakika ni kile cha umwagiliaji na mimi nakiri, lakini kwa muundo wa Serikali yetu shughuli hiyo ya umwagiliaji inasimamiwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Tuna suala la masoko kwa mazao ya kilimo, ni sehemu ya shughuli za kilimo, hili nalo halisimamiwi na Wizara ya Kilimo, linasimamiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mambo ya maghala, mambo ya marketing ya masoko hili na lenyewe limewekwa kwenye Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mamlaka ya maghala nchini iko Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, hata wale wanaosimamia minada ya korosho hawako chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna shughuli zingine zinatekelezwa moja kwa moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Miradi ya kujenga uwezo inatekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tulikuwa na programu kubwa tu Waheshimiwa Wabunge ya MIVARF mnafahamu, hii imesimamiwa chini ya Ofisi ya Waziri, Uratibu na Sera, wamejenga barabara, masoko, wameweka viwanda vidogo vidogo vya kusindika. Yote haya ni sehemu ya kilimo cha nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wizara hii kimsingi ina mambo mawili makubwa, sera ya kilimo na uratibu wa kilimo chenyewe. Katika uratibu kuna mambo ya research, kuna mambo ya back stopping yaani kutoa msaada wa kiufundi pale unapohitajika. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge hili jambo la kwamba hela iliyopelekwa kwenye kilimo ni kidogo sana, ndiyo ni kidogo wala hilo si jambo la kubishania, lakini pia lazima tukumbuke kwamba kilimo hiki hiki tunachokizungumza kinasimamiwa pia na Wizara nyingine za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye jambo la Malabo au The Maputo Declaration. Azimio la Maputo linazungumzia kilimo kwa tafsiri ya FAO, halizungumzii kilimo kwa tafsiri ya Wizara moja ya Serikali hii, linazungumzia kilimo kwa tafsiri ya Shirika la Chakula Duniani yaani kilimo kwa tafsiri ya FAO ni kilimo cha mazao, kilimo uvuvi, kilimo mifugo, kilimo ushirika na kilimo misitu. Sasa ukichanganyna haya mambo matano unaona kwamba hilo tunalolisema asimilia kumi, asilimia sita au kumi kuelekea asimilia kumi halipo zoomed yaani siyo la kilimo mazao peke yake na ushirika ambalo linasimamiwa na Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Waheshimiwa Waheshimiwa Wabunge tunawendelea kukokotoa, na nadhani Waziri wa Fedha atakapokuwa anahitimisha, atakapokuja na bajeti ataonesha sasa maeneo yote haya niliyoyataja yatakuwa yamewekewa au yametengewa kiasi gani cha fedha na hapo ndipo tutatazama sasa kwa tafsiri hiyo pana ya kilimo ni kwamba tumeelekeza kule fedha kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo mazao na ushirika peke yake, haiwezi ikatengewa asilimia kumi ya bajeti Waheshimiwa Wabunge hapana, kilimo kinachojumuisha mifugo, uvuvi, ushirika, misitu na mazao hicho ndicho Malabo au The Maputo Declaration kinachohitaji kitengewe angalau tufike kwenye asilimia kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imeishauri Serikali kuongeza kasi ya kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuzalisha mbolea hapa nchini na kujenga viwanda. Ni kweli hili wala siyo suala la kubishana, huu ushauri wa Kamati tunaupokea moja kwa moja asilimia mia moja kwa sababu leo tunahangaika, mara vocha, mara BPS, mara sijui nini hii yote ni kwa sababu uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi ni mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Taifa tungekuwa tunazalisha mbolea haya mambo ya bei tungekuwa tuna fix wenyewe kwa sababu ni kitu product inayozalishwa hapa ndani, haya mambo ya ifike wapi, siku gani tungekuwa tunafanya haraka tu, lakini kwa sababu uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi ni wa chini kabisa ndiyo maana leo bado tuko katika tafrani hii ya mifumo ya namna gani tuwasaidie wakulima na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge ni rahisi sana nchi inayozalisha mbolea ndani ya nchi yake kuweka ruzuku kwenye hivyo viwanda vinavyozalisha hiyo mboela na mbolea ikawa rahisi au kuweka resume ya kodi ambayo inawezesha mbolea kuwa ya bei ya chini kuliko mbolea unayoagiza kutoka nje. Mbolea unayoagiza kutoka ni lazima uingie kwenye mfuko uchukue kule fedha ya kigeni uagize mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaribu ruzuku na vocha, Waheshimiwa Wabunge ninyi wenyewe ni mashahidi, nilikuwa naongea na Mheshimiwa Flatei hapa ananiambia kule kwao utaraibu wa vocha ulikuwa ni miujiza, kijiji kizima wanasainishwa vocha halafu hata mfuko mmoja hauendi watu wanaenda NMB wanapiga pesa, kilimo hakibadiliki ingawa kwenye hesabu ya matumizi ya fedha inaonekana mbolea kubwa imepelekwa kule. Sasa hii yote ni matokeo kwa sabau wenyewe hatujawa na uzalishaji wetu wa ndani wa mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nifurahi tu kuwaambia kwamba ujenzi wa kiwanda cha mbolea kule Kilwa sasa angalau unatia matumaini. Yale mabishano na mazungumzo yaliyokuwapo kuhusu bei ya gesi itakuwa kiasi gani, wauzie bei kama mtumiaji wa nyumbani au wauziwe ile gesi kama malighafi, hilo jambo sasa limemazika na kwa hiyo hatua inayofuata ni wao kuanza ujenzi wa kiwanda. Hata hivyo kule Mtwara Kampuni nyingine pia ya Kijerumani na yenyewe kwa makubaliano hayo hayo taaraifa ya tariff gesi na wao wame- commit wataanza ujenzi wa kiwanda. Kiwanda chetu cha Minjingu pale Arusha kinazo sura mbili. Mwanzo walianza na mbolea ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameisema haikufanya vizuri na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie watu hawa walijirekebisha wakafanya utafiti wamepeleka kwenye Taasisi za Utafiti (Seriani), kule utafiti umefanyika. Jambo moja lililopo mbolea ya Minjingu inabidi ufanye kwanza utafiti wa udogo kabla ya kwenda kuitumia. Hili jambo tunalitafutia na tumepata mwarobaini wake, tumepata msaada wa magari mawili yanayotembea na maabara ya kufanya analysis ya udongo. Haya magari tutayapata ndani miezi miwili ijayo, yatazunguka kijiji kwa kijiji nchini, yatapima udongo ule ni wa aina gani, na kwa hiyo recommendation ya aina gani ya mbolea inafaa kwa kijiji gani, inafaa kwa mkoa gani, wilaya gani, sasa habari hiyo tutakuwa nayo. Kwa hiyo mambo ya kupeleka DAP nchi nzima holela, kupeleka UREA nchi nzima holela, tutaachana nayo hivi karibuni, tutakuwa sasa tunajua kwa uhakika kwamba mbolea hii ukiipeleka Kanda ya Ziwa acidity kule iko kubwa sana haitafanya kazi. Hivyo kitu cha kufanya tuwashauri wananchi waweke chokaa (lime) kwanza ili tunapopeleka hii mbolea iwe na manufaa kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu niseme jambo moja hapa ndani ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wanaweza kuwa hawalifahamu. Matumizi ya mbolea niseme tu ya kukuzia UREA tunayotumia sasa hivi nchini hapa, hii mbolea ukiitumia katika maeneo ambako tindikali imekwishafikia ile wataalam wanaita PH-5 unapoteza mavuno yako kwa asilimia 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mkoa wa Njombe hata wakiongeza matumizi ya mbolea ya UREA mara mbili bado mavuno yao hayawezi kuongeza kwa asilimia 30 kwa sababu ardhi ya eneo lile kwa kiwango kikubwa tindikali iko ya juu sana kiasi kwamba mbolea ikiwekwa inatengeneza ukame usiokuwa asilia yaani ukame ambao ni artificial, mizizi hairefuki ya mazao kwenda chini kuchukua virutubisho. Kwa hiyo uzalishaji unakuwa wa chini hata kama matumizi ya mbolea yanakuwa yameongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ndiyo maana tumekwenda kwenye hatua ya kutafuta haya magari. Mwaka 2017 mnafahamu watafiti wetu waliuwawa hapa Dodoma kwa sababu walikwenda wenyewe wenyewe tu vijijini wanachokonoa chokonoa udongo, wakatuhumiwa kwamba labda ni majambazi, wakapigwa wakachomwa moto. Sasa tumetafuta nyenzo (mobile laboratory) magari mawili yatazunguka nchini, yatapima udongo na kwa hivyo tutakuwa na uhakika wa aina ya mbolea na mahitaji ya wananchi kila eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imeshauri kuwa ni vyema ununuzi wa mbolea kwa pamoja ufanyike mara tatu au mara nne kwa mwaka kadri itakavyowezekana. Mimi nakubaliana na maoni haya ya kamati, lakini nitoe tu angalizo kwa sababu tumefanya hili jambo, tumeyaona mapungufu na changamoto zilizopo. Wakati ule tumewapitisha kwenye semina Waheshimiwa Wabunge tulisema kwamba bei ya mbolea kwenye Soko la Dunia inabadilika sana. Bei ya Mbolea kwenye Soko la Dunia jamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wahindi (India) na Brazil wanapoingia kwenye msimu wa kilimo mahitaji ya mblea duniani yanapanda, kwa hiyo na bei pia na yenyewe inapanda kwenye soko la dunia. Sasa tukitangaza zabuni yetu hapa katika kipindi hicho kwa vyovyote vile tutakwenda kukutana na bei kubwa. Halafu mwezi mmoja uliopita labda ulikuwa umewatangazia watu bei elekezi 47, unakwenda unakutana na bei kwenye bulk nyingine inayofuata inayokupeleka kwenye 55; sasa ile inakuwa inawachanganya watu. Wanaona kama vile mfumo huu haueleweki, kwa nini mwezi fulani bei ilikuwa hii, mwezi mwingine bei ilikuwa hii, hii sasa manufaa yako wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tunachokifanya tunavizia pale ambako bei ya mbolea katika Soko la Dunia iko katika minimum kabisa ndipo sasa tumesema tunatangaza na tunanunua ya mwaka mzima ili ikishaingia mbolea inakuwa na bei moja mwaka mzima kuliko hii ya
kununua mara nyingi nyingi, tukinunua mara nyingi nyingi bei haitakuwa moja mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunapoagiza kiwango kikubwa sana hata wauzaji wanapunguza bei, lakini tunapoagiza tani 29,000, tani 30,000, wauzaji wanaona hawa ni kama reja reja tu kwa hiyo wanatuuzia kwa bei ambayo ni ya rejareja. Kwa hiyo tunavyojipanga sasa hivi tunataka tutangaze zabuni na tunajua bei itashuka kwenye mwezi wa sita, itakuwa ndiyo iko chini kabisa duniani, tutaagiza hiyo mbolea itakayokuwa inatutosha mwaka mzima na tukishafanya hivyo Waheshimiwa Wabunge tatizo tutakalokutana nalo tu ni namna ya kuisambaza, kuifikisha vijijini na hili ndiyo tunajipanga nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge suala la kuingiza nchini mbolea si tatizo. Tatizo tulilonalo changamoto kubwa ni namna ya kuisambaza, kuifikisha huko vijijini. Tumejiwekea mkakati na hili naomba support yenu kwamba tutatumia nyenzo na mamlaka zote za Serikali. Tunayo Kampuni ya Mbolea ya Serikali wana warehouses mikoa na wilaya zote, hawa tutawapelekea kwanza mbolea huko. Wafanyabiashara wanaoshiriki katika mfumo huu tumewawekea sharti jipya kwamba ili ushiriki kwenye kuagiza ile mbolea tani 200,000 au 300,000 lazima uwe na mtandao wa kugawanya mbolea kwa eneo la nchi lisilopungua asilimia 60 ili mmoja tu akichukua ile amount aliyo-commit kuuza tunajua kwamba at least 60 percent ya nchi atakuwa amefikisha mbolea, sasa wakiwa watatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na jambo lingine katika hii issue ya mbolea wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kupeleka mbolea maeneo yanayotumia mbolea maeneo yanayotumia mbolea kwa wingi tu, kule ambako matumizi ya mbolea ni kiodgo hawaendi kabisa. Ndiyo maana utakuta eneo kama Kakonko kwa rafiki yangu Mheshimiwa Bilago, akipeleka anapeleka tani moja na akifika kule anaipandisha bei sana kwa sababu anajua hiyo mbolea itakaa miezi nane au miezi tisa haijanunuliwa, and that’s a business sense, wala mtu wa namna hii huwezi ukamlaumu atakuwa na storage charges, atakuwa analipa walinzi, atakuwa analipa nani, sasa akiweka bei ya chini badaa ya miezi tisa mfuko ule utakuwa bado unauzika kwa elfu ngapi hiyo? Atapata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachokifanya, ili tumpe leseni ya kuwa muuzaji mkubwa wa mbolea, tutawalazimisha wawe pia na maeneo ya kuuzia mbolea kwenye maeneo hayo ya namna hiyo ili tusiwe na pocket yoyote nchini ambako eti mkulima akihitaji mbolea hawezi kupata. Kwa sababu atakuwa anauza mbolea nyingi kwenye maeneo ya matumizi makubwa, hiyo itakuwa inafidia hata kule anakouza mifuko 10 au 20 kwa mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Kamati imetushauri ni kwamba minada ya kahawa iongezwe, na sisi tunasema minada ya kahawa itaongezwa, lakini kwa sababu tumeanza commodity exchange sisi Serikali tulikuwa tunadhani kwamba kahawa yetu ianze kuuzwa kwenye TMX, ianze kuuzwa kwenye commodity exchange. Infrastructure ya kahawa ya kuuza kahawa kwa mnada iko tofauti kidogo na ile flow ya commodity exchange. Kwa hiyo nimeshaelekeza kwamba TMX waende wakakodi ile facility iliyopo pale Bodi ya Kahawa-Moshi ili wao wawe ndio wanafanyia hiyo commodity marketing pale pale kuanzia Moshi, lakini isiwe tena huu mnada wa kahawa kama tuliouzoea ambako niseme tu ukweli kateli zilikuwepo kule, watu wanapanga bei nje ya mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwaingiza wakulima wa kahawa kwenye commodity exchange kahawa yao itakuwa inajulikana tu duniani huko. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wanaotoka kwenye maeneo ya kahawa, kwamba kahawa ikishaanza kuuzwa kwenye commodity exchange habari hii ya ushirika ita-collapse tu yenyewe, yaani hakutakuwa na haja ya kutumia nguvu sana kuzungumza ushirika gani una nini, unakwenda kwa nani, No, kwa sababu suala lile ni la kimtandao wa dunia nzima kwa hivyo ushirika wamekwenda wao, imeenda AMCOS au imeenda union it doesn’t real make a big difference, watu watakwenda pale, kahawa yao itajulikana duniani kote, watauza, watagawana pesa, mambo yatakuwa mazuri.

Waheshimiwa Wabunge, sasa naomba hoja zingine za Kamati pia tutazijibu kwa maandishi. Naomba nizungumzie mambo ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwa hisia sana, naamini tukiwa na uelewa mzuri kwenye hili jambo na tukaweka commitment ya Serikali basi nina uhakika tutakwenda tu vizuri na Mungu atatusaidia.

Mheshimiwa mwenyekiti, nianze tu na hili jambo la soko la mahindi hapa nchini. Kwa kweli, naomba tu niwambie ukweli, mimi ni mkulima, naomba niwaambie huu ukweli kabisa yaani usiokuwa na mawenge mawenge, mimi nalima. Nalima mtama, nalima vitunguu na nalima mahindi. Hii adha na mimi inanipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lwenge hapa jana alipochangia alisema tunalima wote na mtama umetushika. Wamo humu Waheshimiwa chungu mzima waliolima na wao hawajauza mpaka leo. Wako wakulima wa vitunguu Singida kwa Mheshimiwa Monko, wako wakulima wa vitunguu hapa Kilolo kwa Mheshimiwa Mwamoto, wanalima mwisho wa siku hakuna soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu Waheshimiwa Wabunge mnisikilize vizuri kwa unyenyekevu sana nalisema hili jambo, seasonality, kilimo chetu ni cha kutegemea mvua kwa asilimia kubwa. Kilimo cha vitunguu kwa maeneo mengi huku nacho ni cha msimu, mvua ikiwa inanyesha huwezi kulima. Kwa hiyo, watu wanalima mvua hakuna au watu wanalima mvua ikiwa inanyesha. Kwa hiyo, watu wakiwa wanalima kwa pamoja si ndiyo? Watavuna kwa pamoja, mahitaji yanashuka, the low of demand and supply ina-setting, na kwa sababu hatuna miundombinu ya kutosha ya uhifadhi wa mavuno yetu tunajikuta tumeingia kwenye hasara, tunajikuta tumeingia kwenye kuuza kwa bei za kutupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kama tungekuwa na miundombinu mizuri ya kuhifadhi, natoa mfano tu wa nyanya, mwaka jana watu wamelima nyanya nyingi sana hapa Dumila, hakuna storage facilities. Sasa hivi wanalima Parachichi nyingi tu Njombe, hakuna pack house. Kwa hiyo wakulima hawa wakivuna, akiona mazao yake yanaelekea kuoza ndugu zangu atauza tu kwa bei ya hovyo hovyo. Si kwamba mimi Tizeba nafurahia haya mambo. Kwa hiyo, Serikali tunachokifanya tunajitahidi ku-overcome hii situation, tunajitahidi sana ku-overcome hii situation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyotajwa hapa ni ya Serikali, bajeti iliyosomwa hapa ni ya Serikali, tofauti sana niseme kwa mfano na Wizara ya Afya ambao wadau wetu wa maendeleo wanapeleka fedha kwenye basket, si ndiyo? Sisi wadau wetu wameamua kwenda moja kwa moja ku- address issues kule. Tunayo programu na ADB ambayo itatengeneza complex ya kilimo kuanzia uzalishaji mpaka usindikaji na tayari timu ipo inafanya kazi, tumeshakubaliana na ndiyo maana Rais wa Benki ya Afrika alikuwa Tanzania hivi juzi, amefanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais, wameshakubalaiana, timu ya wataalam nilikuwa nayo ofisi siku kabla ya jana, hili jambo tunaendelea nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari hii ya watu kuzalisha nyanya, anauza tenga shilingi 2,000 au mwisho wa siku unapita anakwambia chukua na wewe kawapikie watoto wako si sawa. Kwa hiyo, lazima tutafute suluhisho la haya mambo, one step ni Agro processing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge benki zetu za biashara; NMB, CRDB na Bank of Africa tumekwishafanya mazungumzo, wamekubali watakuwa wanatoa pesa kila mwaka kwa ajili ya kuingiza fedha kwenye value addition yaani kwamba mkulima akishalima, wananchi wengine ambao hawalimi, wa-takeover kwenye huo mnyororo wa thamani wale off takers wapate pesa, wanunue, wapeleke kwa wasindikaji, wasindikaji wasindike, wapeleke kwenye masoko na bidhaa zetu zikisindikwa masoko yake yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania leo, niwape mfano tu, juzi hapa ndani hapa debate kubwa kabisa ya mafuta ya kula, si ndiyo? Tunaagiza crude palm oil tani 600,000; lakini tuki-process mahindi tu kuyakamua na kupata corn oil, namshukuru sana Mheshimiwa Sokombi alilisema hili jambo. Tuki-process corn oil inaweza ikachukua nusu ya mahindi yanayolimwa hapa nchini na bado mafuta yake yasitoshe kwa matumizi hapa ndani. Kwa hiyo hizi benki zime-commit kwamba zitatoa fedha kwa Watanzania wanaotaka kufanya hiyo shughuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wafugaji wanahangaika na mifugo, kwa nini hatuwi na feed loads tukatuma mahindi yaliyokamuliwa yakatolewa mafuta, tukachanganya na soya tukapata chakula cha mifugo kizuri tu kabisa? Tumeanzisha programu ya uzalishaji wa soya nchini, Clinton Foundation wanatusaidia lakini pia tumeweka kwenye mipango yetu kwamba tuta-enhance uzalishaji wa Soya nchini ili tuanzishe utengenezaji wa chakula cha mifugo. Inawezekana watu wale ambao wanasumbuka na mazao yao wakapata masoko ya ndani hapa hapa kwa kuongeza thamani na tukafanya vizuri tu sana katika suala la masoko.

Lakini jambo lingine la masoko Waheshimiwa Wabunge, ziko nchi ambazo tuko jirani nazo lakini kwa hali ilivyo katika nchi zao hawawezi kuzalisha. Burundi, Sudan ya Kusini, Kenya nusu ya nchi hawawezi kuzalisha, hawa tunataka sasa wawe ndiyo soko letu. Kwa hiyo, nilikuwa ninazungumza hapa kwamba taasisi zetu za Serikali na za watu binafsi zichangamkie hizi fursa. Bodi yetu ya nafaka na mazao mchanganyiko; mimi nachelea sana kusema kwamba NFRA ndiyo ita-spearhead suala la biashara ya mahindi, hapana, wale wana jukumu lao la kisheria la strategic reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili lilianzisha chombo kwa ajili ya shughuli hiyo ya biashara ya mazao. Kuna ule mkopo ambao niliwambiwa hapa ume-stack, hapana, mkopo ule utapatikana, hawajajidhatiti sana kwa hiyo huwezi kuwarushia bilioni mia moja. Hizo fedha walizopewa na NSSF watazipata, wataendeleza sasa shughuli ya kununua na kuuza mazao. Tulichokifanya, tunataka tuwatume waende Sudan, si wao ndiyo kazi yao kufanya biashara ya mazao? Tunataka tuwatiume waende Sudan ya Kusini, waende huko Mauritius, huko liko soko la mbaazi, waende wakazungumze na Wahindi wa Mauritus wakubali kununua mbaazi yetu, hela wanapata, kwa hiyo, wakishapata hizi pesa waanze biashara. Kibaya ni kuwaanzishia pesa nyingi ambazo hawatakuwa na uwezo wa kuzitumia halafu waishie kupanga matumizi ya kuzimaliza. Kwa hiyo, tuombe tu kwamba suala la biashara ya nafaka, wenye mandate ya kisheria wapo na sisi mtusukume tu kuhakikisha kwamba wanafanya kweli hiyo biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi na mazao yao, nimesema katika hotuba yangu na inavyoelekea haikueleweka sawa sawa. Hakutakuwa na kizuizi kwa mtu yoyote kuuza mazao yake nje. (Makofi)

Narudia tena, hakutakuwa na kizuizi kwa mtu yoyote kuuza m azao yake nje. Angalizo tu, wakulima wasiuze kila kitu mpaka cha kula wenyewe, uzeni. Yale mambo ya mpakani pale mtakutana na Afisa TRA atakwambia una kiasi gani humu ili aweke record unatoka na nini basi, uzeni tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maeneo yanayofanya vibaya katika kuvuna chakula, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge msisahau kwamba si kila sehemu ya nchi yetu wanavuna vizuri, yako maeneo Tanzania ambayo hayavuni vizuri na sisi kama Serikali hatuwezi kufumbia macho hilo jambo. Kuna mchangiaji mmoja amesema vizuri tu, suala la usalam wa chakula ni suala la usalama wa nchi. Ni vigumu sana Waheshimiwa Wabunge, hata kambi hii naomba mnielewe vizuri, ni vigumu sana kutawala watu au kuongoza taifa lenye watu wenye njaa, ni vigumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo NFRA itafanya hiyo shughuli ya kuhakikisha kwamba chakula cha dharura kinapatikana kwenye maeneo ambayo kisheria yatathibitika kwamba yanahitaji msaada wa chakula. Utaratibu tulioweka ni kwamba wata-maintain presence kwenye maeneo hayo, kwa sababu gani; mazao yaliyonunuliwa mwaka juzi, shelf life yake ni miaka mitatu kwahiyo lazima yatoke whether kuna dharura au hakuna dharura. si ndiyo? Sasa yake yatakayokuwa yana-approach shelf life yake kwisha tutayapelekea tu kwenye maeneo haya ambapo uzalishaji wao sio mzuri ili wananchi waendele kununua kwa bei himilivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na huu ndio mpango ambao nadhani utatutoa hata kwenye haya mabishano, mahindi yaende nje, au yasiende nje, mahinda acha yaende, ngano acha iende, mchele acha uende, chochote, as long as hatutafikia hali kwamba sasa eti nchi haina chakula halafu tena, kama ndugu yangu Mheshimiwa Zuberi siku moja alivyosema kwamba nchi imebakiza chakula cha siku tatu. Hiyo ndio situation ambayo tutajitahidi tu kama Serikali tusifikie hapo. Hakuna namna tunaweza tukasema eti tumefanya fanya mambo leo tumefikia nchi tuna chakula cha nane au saba. Vinginevyo niwatoe hofu Waheshimiwa kwamba wananchi watakaozalisha wanaruhusa tu ya kupeleka chakula chao huko nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa kwa hisia sana ni hili la uingizaji wa mbolea kwa pamoja. Nimeshalizungumza na kwa hivyo sitaki kulirudia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na wachangiaji ni hili la pamba. Pamba ndugu zangu, kwanza niweke clarification ya moja kwa moja. Ushirika hawanunui pamba, kwa hiyo Mheshimiwa Kiswaga, Mheshimiwa Ndassa, Mheshimiwa Mashimba, Mheshimiwa Njalu na wengine wote wanaozungumza hili jambo kwa mtazamo huo niwafahamishe tu kwamba ushirika kwa sasa, unless wana hela zao wenyewe, maana yake sheria haiwazuii kununua, unles wana hela zao wenyewe lakini hawatanunua eti watanunua pamba kwa fedha ya wafanyabishara, hili jambo halipo. Hili jambo ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ushirika ambayo Bunge hili limepitisha haizuii ushirika kununua pamba na ushirika umekuwa ukinunua pamba miaka yote Nyanza na SHIRECU ni washirika wale, lakini kwa msimu huu hawana fedha ya kununua pamba. Suala lililokuwa limezungumzwa hapa ni kwamba wawaweke pamoja wakulima wao na hili jambo Waheshimiwa Wabunge lilitokana na kilio cha wanunuzi wa pamba pia, walisema kwamba wanatumia gharama kubwa sana kuweka utitiri wa wale mawakala huko kwenye maeneo ya huko vijijini, wakaweka figure ya watumishi 22,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kutafakari pamoja nao ikaonekana labda inawezekana watu katika ushirika wao waka-aggregate halafu ninyi mkaenda kununua. Lakini inavyoonekana imani bado haipo ya kuwapa washirika hawa pesa. Kwa hiyo kama nilivyosema kwenye taarifa yangu na vyombo vya habari, watu wa ushirika wawaache wanunuzi waende na hela zao, wakakae pale, wapime pamba wao waweke record kwamba wakulima wao wameuza kiasi gani, wawaandalie maghala, wakute pamba iko kwenye maghala wawakodishie nyumba kama zinakodishwa huko vijijini, wawatengenezee mazingira ambayo wanunuzi wetu hawatasumbuka kununua pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachokisema niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, kwamba hela italiwa, itaenda kufanya nini, no, hela haitaliwa. Serikali yote, kuanzia Wakuu wa Mikoa nchi nzima huko pamba inakolimwa, Wakuu wa Wilaya, Wakurungezi wa Halmashauri wanaochukua cess kutoka kwa wakulima hawa ni lazima wawepo huko pamba inakouzwa kujiridhisha kwamba utaratibu unakwenda ambako si mkulima au mfanyabiashara anayepata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo tutalisimamia Waheshimiwa Wabunge, si kwamba ni kitu impossible, kinawezekana, tutawasimamia. Msitie mashaka sana na dhamira ya Serikali, tumesema tutasimamia tutawasimamia, ushirika ule wa wizi ule hatuna namna ya kujiridhisha kwamba tumeukomesha kama hatuanzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuna-fear of the unknown. Walishatuibia tunajua na namna walivyokuwa wanaiba, tukaja hapa Bungeni tukarekebisha sheria, sasa hivi wanafungwa. Zamani hakuna mtu alikuwa anaiba Nyanza anafungwa, sasa hivi jaribu kuchukua kitu cha Nyanza uone utakakoishia. Nimesikia hapa mchangiaji mmoja anasema huko TANECU sijui wapi wameiba pesa, wameiba pesa na watafungwa tu, si wameiba pesa? Imethibitika wameiba? Sheria tunayo mkono kwa nini tusiwapate hawa? Tutawapata watafungwa na kufilisiwa mali zao, ndicho kinakachofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mmoja Mkuu wa Mkoa wa Mara alisemaje, tunapenda kweli mtu ajaribu kuibia wakulima ili aone tutakachomfanyia. Hata mimi natamani nimpate mmoja atakayeenda kudokoa hela ya pamba aone, tumtoe mfano, kwani kuna tatizo gani kumtoa mfano? Tunamtoa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeiti, na jambo la pili kwenye pamba Waheshimiwa ni ile shilingi 100. Shilingi 100 ndugu zangu mtakumbuka tu Bunge lililopita hapa wakati wa kupulizia dawa Waheshimiwa Wabunge wote mnaotoka maeneo ya pamba mlikuwa mnadai viuatilifu vimechelewa, viuatilifu hakuna, jamani Wizara inafanyaje, pamba inakufa, pamba inakufa. Tumechukua hatua extra ordinary kupata hivyo viuatilifu, tumenunua chupa milioni saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Serikali ilikuwa bilioni tatu kwa viuatilifu vya mazao yote. Pamba tu iliyozalishwa kwa wingi namna hii msimu huu ilikuwa inahitaji viuatilifu vya bilioni 30. Sasa tungejifunga kwenye bajeti ya Serikali leo tungekuwa na pamba ambayo tunazungumzia? Tumeenda tumezungumza na benki yetu ya kilimo imetoa LC kwa makampuni ya kuagiza dawa, wameagiza dawa hiyo ni commitment ya benki, imetoa pesa zake sasa italipwaje hiyo pesa? Bajeti ya Serikali ilikuwa shilingi bilioni tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunahitaji pesa kutoka kwa waliotumia hiyo dawa ili tuilipe benki iliyotukomboa. Nataka niipongeze sana Benki ya Kilimo, kwa hili wametusaidia kweli kweli. Kwa sababu wangejielekeza na wao kama benki ya biashara nyingine yoyote wakasema tunataka collateral tunataka nini…, leo pamba ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tunayoizungumza isingekuwapo. Sasa tunataka pesa ya kuwalipa, Mheshimiwa Kiswaga shilingi 30 walikatwa wakulima mwaka jana ndiyo, makadirio ya zao ilikuwa ni tani laki moja, mwaka huu tumekwenda tani laki sita, mwaka kesho dhamira yetu ni tani milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaweza kweli tukatoka kwenye shilingi 30 ya kuhudumia tani 100,000 tukaenda kwenye shilingi 60 ya kuhudumia tani milioni moja. Tunahitaji fedha na tuwe nayo mapema ili kuwaandalia wakulima mazingira ya kulima. Hakuna itakayempendeza hapa ikifika mweziJanuari, mwaka kesho hakuna dawa ya pamba nchini, nani atafurahi wakulima? Wetu tunawafahamu kutoa fedha mfuko kwenda kununua bomba ni issue. Kwa hiyo, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge, 30 zitatumika kulipa deni na hizo bilioni 20 tutaziweka tena benki kama cash cover ili watukopeshe fedha nyingi zaidi. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge, wakulima wanaelewa sana dhamira ya Serikali. Naomba niwahakikishie, mimi nilikuwa Igunga wakati tunazindua msimu, Mheshimiwa Kafumu ni shahidi yangu. Tulipoeleza haya wananchi walipiga makofi kwa sababu wanakuwa na uhakika. Si wananchi wetu wote wanao uwezo wa kutunza fedha kusubiria kuwekeza tena katika kilimo, lazima Serikali ichukue nafasi yake. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hii hela haiendi kulipa madeni ya nyuma, sijui ya iliyokuwa mfuko wa pamba. Haiendi kulipa hayo, huko bado hatujaelewana nao nani alisababisha hayo madeni. Tunataka tumjue huyo alipeleka wapi hizo fedha. Kwa hiyo, hii pesa inakwenda kwenye hayo mambo matatu mbegu, dawa na mabomba, na kuna hela kidogo sana ambayo pia ni lazima tuipeleke kwa ajili ya watafiti wetu wa pale Ukiriguru. Vinginevyo hii hela inarudi kwa wakulima wenyewe kwa manufaa yao itasimamiwa na Bodi ya Pamba. Bodi ya Pamba ni chombo cha Serikali. Wanatumia fedha kwa kanuni za fedha za Serikali, akidokoa fedha tunaye. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge niombe sana mniruhusu tu niendelee na hiki kilimo, mipango si mibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo moja tu lingine labda ambalo kwa haraka haraka kwa ruhusa yako, naomba niwatoe hofu Wabunge wa eneo la kati hapa la nchi yetu. Ilisemekana kwamba korosho hapa haifai kulimwa na kadhalika. Watafiti wetu na tunao ushahidi, tulikuwa tumeomba mngeweza kuona kwenye screen pale jinsi korosho inavyostawi vizuri Mkoa huu wa Dodoma na Mkoa wa Singida. Korosho inastawi vizuri Kongwa kiasi kwamba inazaa mara mbili kwa mwaka. Hiyo ni korosho inayozalishwa huko Singida. Nimuombe tu mdogo wangu na swahiba wangu Mheshimiwa Ditopile anielewe tu kwamba mimi nina wataalamu waliobobea, a center of excellency ya korosho duniani iko Tanzania, dunia nzima wanakuja kujifunza kwetu korosho. Sasa tusiwakatishe tamaa watafiti wetu, wanafanya vizuri na nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru sana, wanachokifanya ndicho hicho wanachostahili kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho inastawi Singida, korosho inastawi Dodoma na hii tunawapa option wakulima wetu, wakilima mtama hali ya hewa ikawa mbaya wawe na pa kuangia, angalau kwenye korosho. Wakilima mahindi yakakauka wawe na angalau na kilo mia moja za kuuza waende sokoni wanunue mahindi. Tusiwaache tu kwamba wakilima zao moja likashindikana basi wao ni watu wa kwenda kupiga hodi kwa Mkuu wa Wilaya kuomba pesa au kuomba mahindi ya msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja iliyo mbele ya Bunge lako Tukufu. Nitumie nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Buchosa, kwa kunirudisha tena katika chombo hiki cha uwakilishi hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze na kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya. Binadamu sifa yake kubwa ya kwanza ni kushukuru kwa jambo linalofanyika vizuri; lakini itakuwa ni udhaifu mkubwa sana pale ambako jambo unaliona linafanyika vizuri unajitoa fahamu, unapewa dakika 10 za kuchangia hapa ndani, wewe unaanza kurusha maneno mabaya tu, like waliokutoa huko kukuleta hapa; moja ya ajenda ilikuwa ni kukutuma uje kutukana.
Waheshimiwa Wabunge, hebu tutimize wajibu wetu juzi Attorney General hapa akizungumzia habari hii ya live coverage ya Bunge na kadhalika; alisema hebu kwanza tujiongoze na wajibu wetu tu wa Kibunge wa kawaida and then haya mambo mengine yata-follow in place. Ndugu zangu Mabunge yaliyopita wengi walizungumza sana humu wakahutubia Taifa sana. Halafu leo hawamo wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeomba sana tushiriki mijadala hii pale kwenye kuwezekana kukosoa, tukosoane ni kweli; lakini tusiendeleze drama zile za kutafuta umaarufu kupitia runinga na mambo ya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako makelele haya ya television na kadhalika, Mheshimiwa Nape amejitahidi sana kulielezea hili jambo. Nataka niwape hadithi tu ndogo siku tunatambulishwa, niko katika Kamati ya Huduma za Jamii, siku tunatambulishwa, Kamati hii na Wizara msemaji mmoja wa upande huo huko, akasema yeye hakumbuki mara ya mwisho yeye na familia yake wame-tune TBC lini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikamtazama yule bwana nikamuuliza hivi wewe utaratibu huu unadhani ni sifa? Nashangaa juzi kabadilisha, baniani mbaya… Samahani bwana baniani uliyemo humu; kabadilisha utaratibu, baniani mbaya huyo TBC sasa amekuwa dawa. Anamtaka humu ndani kwa udi na uvumba. Guys! mnaweza mkafanya unafiki, lakini huu unapitiliza.
falsafa ya Wachina kwamba ukiona Wapinzani umefanya jambo wanapiga yowe kanyagia hapo hapo. Ukiona unafanya jambo wanakupongeza kwa kweli hilo achana nalo haraka sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu, haya mnayoyafanya kanyagieni hapo hapo. Ukiona wana shift position hawa ujue mambo yamewakaa vibaya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine utakuwa katika maeneo mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni katika Sheria ya Mfuko wa Barabara. Sheria hii sasa ina miaka kama 17 hivi tangu ianze kutumika, lakini kuna mambo mengi yamebadilika hapa tangu sheria hii ianze kutumika na kwa kweli dhana iliyokuwa wakati ule kwamba Serikali za Mitaa hazikuwa na uwezo mzuri wa kusimamia hizo fedha, haiku valid tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Shabiby asubuhi, wakati akichangia akipendekeza utazamwe upya mgawanyo wa hizo fedha, asilimia 30 kwa 70; kama ilivyo sasa inazisababisha halmashauri na hasa sisi Wabunge wengi kuomba barabara zilizo chini ya halmashauri zipandishwe hadhi kuwa barabara za mikoa. Sasa hili tunaweza kuepukana nalo, kwa sababu hatuwezi kuendelea hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, naomba tulitazame hili jambo, tukiendelea hivi eventualy barabara zote zitakuwa za mikoa siyo? Kwa sababu kila mwaka tunaendelea ku-upgrade. Kwa hiyo, nadhani kwamba tufike mahali sasa tukubaliane, ile percentage inavyogawanywa, ibadilishwe ili kuzifanya Halmashauri na zenyewe ziwe na fedha za kutosha kufanya matengenezo yanayokidhi; huko huko katika Halmashauri bila kung‟ang‟ana kuzipandisha hadhi kuzifanya barabara za Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo andiko ambalo nitamkabidhi Waziri wa Ujenzi, ili aweze kuona ni kwa namna gani tunaweza kuhama kutoka kule bila kuathiri kiwango cha ubora wa matengenezo ya barabara za mikoa na barabara kuu. Tukilifanya hili tutakuwa tumefanya service kwa pande zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki niamini kwamba wako wahandisi wabaya katika Halmashauri zetu na wako Wahandisi wazuri katika Wakala wa Barabara wa Taifa. Wote hao wanasoma vyuo hivyo hivyo; tunachokiona tu hapa ni uwajibikaji na kiasi cha pesa ambazo mtu anakuwanacho katika ku-effect hizi kazi. Kwa hiyo, tuki-address haya mambo mawili nadhani tutaliondoa hili wingu na wimbi la kuomba barabara hizi kupandishwa hadhi kutoka barabara za Wilaya kwenda kuwa barabara za Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka kuchangia ni miradi ya maendeleo inayoanzishwa katika Halmashauri zetu. Ukitazama na Waheshimiwa Wabunge, watakuwa mashahidi; miradi mingi miaka mitatu, miwili iliyopita ilianzishwa kule, lakini katika bajeti zinazofuata miradi hii haipati tena pesa. Kwa hiyo, imebaki tu katikati na mfano mmoja wa haraka kabisa ni hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Hospitali imeanza kujengwa mwaka juzi ilipata bajeti katika Serikali, mwaka jana haikupata pesa, mwaka huu wa fedha unaomalizika haikupata pesa.Lakini sasa Mheshimiwa Waziri mmeanzisha miradi mingine ya aina hiyo hiyo wakati hii iliyotangulia haijakamilika. Niombe sana hebu tu take stock kwanza ya miradi ambayo imekwishaanza ya aina inayofanana. Tuweke utaratibu wa kuikamilisha hiyo kabla hatujaingia kwenye kuanzisha miradi mingine mipya ya aina hiyo hiyo baada ya kukamilisha iliyokuwa imetangulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililogusiwa pia asubuhi; kilimo, sasa sina hakika kama ni uvivu wa watendaji wetu katika TAMISEMI kule, lakini utaona mgawanyo wa fedha ambao umewekwa katika Wilaya mbalimbali inashangaza kidogo. Ameusema vizuri sana Mheshimiwa Shabiby; Dar es Salaam wilaya tatu zina milioni 360 hivi, mkoa mkubwa kwa kilimo kama Geita una milioni 143; hii si sahihi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hatujafika mwisho wa mchakato huu wa kuunda bajeti; hebu warekebishe hili jambo ili mipango hii i-reflect ukweli ulioko huko site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, vinginevyo tunakuwa sasa tunatanguliza toroli mbele ya punda halafu ni jambo ambalo si zuri sana. Wakati sisi humu tunaweza kuona na kufanyia marekebisho haya mambo. Niombe tu kwamba kwenye eneo hilo la kilimo litazameni sana fedha zilivyogawanywa na kama inawezekana mfanye mabadiliko haraka kabla hatujasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la mwisho; ni elimu. Elimu…
MHE. DKT. CHARLES J. TIZABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu. Kwa sababu za wazi kabisa nitajikita katika sekta ya ujenzi na mawasiliano na ile sekta nyingine nitai-skip kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kupongeza Baraza zima la Mawaziri, mmeanza vizuri sana na kwa kweli fikisheni salamu zetu kwa Mheshimiwa Rais kwamba anaendelea kufanya vizuri na ninyi mnaomsaidia tunawaombea kila lililo la kheri. Kwa kutambua kwamba hii ndiyo bajeti yenu ya kwanza basi sisi wenzenu tuna matumaini makubwa sana na ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekipitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri na kwa kweli kwa kiwango kikubwa kimekaa vizuri sana, kime-capture maeneo mengi muhimu na ya msingi. Wasiwasi wangu tu ni kama yote yaliyoandikwa yatatekelezwa kama yalivyoandikwa. Kwa sababu limekuwepo tatizo la muda mrefu tu kwamba mpango huu tunaupitisha ukiwa mzuri sana lakini utekelezaji ukianza mambo mengi yale yaliyoandikwa yanaachwa yanatekelezwa mengine pia ambayo hata hayakuwa yameandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati natafiti kwa nini hili linatokea, nimejifunza tu kwamba katika ile Appropriation Act tunayoipitisha hapa, kipengele kile cha sita (6) kinatoa mwanya kwa Waziri mwenye mamlaka kufanya mabadiliko au kuhamisha pesa, wataalam wa haya mambo wanaita budget leakage. Napenda sana niseme haya Mheshimiwa Dkt. Mpango akiwa hapa kwa sababu yeye hasa ndiye mwenye kuweza kuruhusu hizi leakages kutokea. Nina hakika leakages zisingekuwepo katika bajeti hakuna Mbunge angekuwa analalamika sana hapa kwa sababu mambo tunapitisha wote na kwa hiyo tungekuwa tunatumaini yatatekelezwa kama tulivyoyapitsha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda ifike wakati tukiangalie hicho kipengele cha sita (6), tukipe masharti ili mabadiliko hayo ya fedha kutolewa fungu moja kwenda lingine yafanyike, basi ziwepo sababu za msingi na kama inawezekana angalau Kamati ya Bunge ya Bajeti iwe imeridhia mabadiliko hayo. Kwa namna hii, tutakuwa tumezuia sana au tume-ring fence mpango mzima kama tunavyokuwa tumeupitisha hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuzungumzia ni Road Fund, lakini naomba nianze na barabara yangu. Mheshimiwa Mbarawa, hii barabara siyo ya kwangu tu, inaanzia mkoa wa Geita inaishia Mwanza. Kwa vigezo vya kiuchumi na kadhalika vyote inakidhi na kwa umuhimu huo ndiyo maana ipo katika Ilani. Mimi nisiseme mengi, nikuombe tu Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha anipe commitment, mwaka huu potelea mbali, lakini naomba commitment ya mwaka kesho na anipe kwa maandishi mzee siyo kwa mdomo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili eneo la Road Fund, katika kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu nilitoa maoni kwamba umefika wakati Sheria ile ya Road Fund iangaliwe upya. Yakatolewa majibu hapa kwamba Serikali inaangalia utaratibu wa kuanzisha kitu kinachoitwa Tanzania Rural Roads Agency lakini kwenye kitabu humu hakuna. Kama kwenye mpango wa mwaka huu hauzungumzii chochote kuhusu hiyo agency kuanzishwa basi tuangalie kwanza tulichonacho tukifanyie marekebisho ili malalamishi ya Wabunge kuhusu barabara za vijiji na za wilaya kutokuwa na appropriate funding liishe. Leo tukiendelea hivi kwa matumaini ya Tanzania Rural Roads Agency kuanzishwa, sisi tunaokaa katika vijiji huko tutaendeea kuathirika kwa matumaini. Tubadilishe hii sheria, mgawanyo uwe mwingine, itakapanzishwa hiyo agency basi ita-fit in katika hili ambalo tutakuwa tumelianzisha na kulifanyia mabadiliko sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge katika majimbo ya vijijini, ninyi mnajua suala la fedha ya barabara zetu kwenye Halmashauri ilivyo kidogo. Tunaendelea kuomba barabara zipandishwe hadhi, zitapandishwa hadhi ngapi? Suala ni kupeleka hela huko huko barabara zinakotengenezwa na siyo kuomba zipandishwe hadhi. Mmoja alikuwa anasema sijui kuna barabara elfu kumi na tatu na mia ngapi zinasubiri kupandishwa hadhi, halafu mwaka kesho tena elfu ishirini na ngapi, mwisho wake nini? Kwa hiyo, niombe sana suala hili la ama kubadilisha Sheria ya Mfuko wa Barabara au kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini basi tuambiwe haya yote yapo katika hatua gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia hicho kitabu, barabara inayoanzia Sengerema – Nyehunge - Nkome imepewa fedha za matengenezo katika sections mbalimbali. Nimestaajabu sana kipande cha Sengerema - Nyamazugo hakimo! Tutatengeneza barabara hii kwa style gani kwamba kipande hicho kisipopata matengenezo barabara hii haipitiki na kipande hicho ni kibaya kweli, Mheshimiwa Ngeleja anajua, hakina fedha. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, niende kwenye vivuko. Ukurasa wa 211, Mheshimiwa Waziri fungua uone pale, zimetengwa fedha za kununua vivuko viwili, kimoja Kigamboni na kingine Busisi. Hata hivyo, juzi tu mmezindua daraja la Kigamboni, ndani ya kitabu hiki mmetenga fedha shilingi milioni 800 na zaidi za kuanzisha usanifu kwa ajili ya daraja la Busisi, sasa unafanya lipi? Mara unaendelea kununua vivuko pale Kigamboni huku daraja limeanza kufanya kazi. Wale watu wanatoza pale, tusiwa-sabotage kwa kuendelea kununua vivuko huku. Busisi tunataka daraja pale, habari ya kununua ferry mpaka ije ikamilike na daraja umeanza kujenga, why? Maana ferry hii siyo kibiriti kwamba utakwenda dukani utanunua kesho, utaanza tena na yenyewe michoro kuja kufikia kuipata na daraja umeanza kujenga.
Mheshimwa Mwenyekiti, nataka mliangalie upya suala hilo ili zile fedha za Busisi mpeleke Kome. Pale Kome kivuko kile sasa hivi ni kidogo na hakifai, wanapandisha huku na huku, SUMATRA hawataki kufanya kazi yao vizuri tu, wangeshakizuia kile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni gharama za ujenzi wa barabara. Naomba tu nitoe ushauri katika hili, Mheshimiwa Waziri, hebu zitazame upya. Pamoja na Sheria ya Manunuzi isiyofaa lakini nadhani zimekuwa exaggerated sana. Haiwezekani hapa Tanzania ndiyo tunajenga barabara zenye gharama kubwa kuliko dunia nzima, why? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, DSTV, Star times, Azam na kadhalika, hawa watu wawekeeni sheria ya kuwabana. Jamani ukinunua airtime ni mpaka uongee ndiyo fedha yako itumike, lakini kwa hawa watu wa ving‟amuzi ukilipa hata usifungue mwisho wa mwezi fedha imekwisha. Imekwenda wapi na mimi sijafungulia king‟amuzi? Software za ku-bill zipo, kwa nini hawa watu wa ving‟amuzi hawawekewi hizo taratibu? Tuombe tu, kwa sababu watu wanalalamikia mengine lakini na hili eneo, TCRA mko hapa mnasikiliza, kitu gani kigumu kuwaambia hawa mtu akiwasha decoder ndiyo ianze kusoma matumizi ya fedha yake? Mna mgao huko, sidhani kama mna mgao huko, basi tusaidieni tu wafunge na wao software hiyo ambayo mtu akianza kutumia king‟amuzi chao ndiyo kweli aanze kuwa billed lakini vinginevyo jamani inatuumiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unalipia DSTV Dodoma hapa mnakaa wiki mbili ukiondoka ukija kurudi hiyo ilishakwisha uanze tena kulipa upya, utakuwa na hela kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nitachangia katika maeneo mawili, nitachangia kuhusu sera ya uhifadhi na baadaye nitachangia katika migogoro ya wafugaji na Serikali.
Mheshimiwa Menyekiti, sera ya uhifadhi shirikishi ni sera nzuri sana. Ukiisoma utaona ni kwa namna gani sera ile inavyozingatia maslahi ya wananchi katika uhifadhi wa maliasili za aina zote. Lakini kuna tatizo kubwa sana katika utekelezaji wa hii sera, kwa sababu sheria na kanuni zilizotungwa kuhusiana na hii sera hazitoi nafuu yoyote kwa wananchi, zimeegemea upande mmoja na nitatoa mifano kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, uhifadhi shirikishi wa misitu, utakuta msitu wa Serikali au shamba la miti liko eneo fulani. Wananchi kwa mujibu wa sheria wanalazimika kushiriki katika kuhakikisha kwamba shamba lile la Serikali haliungui moto, halihujumiwi, haliibiwi, halifanywi nini kadhalika na kadhalika. Lakini inapofika muda wa kunufaika na hilo shamba hao wananchi waliokuwa wakiambiwa hayo yote hawaonekani kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo nilikuwa namuuliza hapa Mheshimiwa Kigola wa Mufindi, kwamba hivi huko Mufindi ndugu yangu wananchi wa vijiji vyako shule zao madawati yamo? Jibu hapana!
Mnafaidikaje? Ananiambia kuna baadhi ya vijiji wanapata pata kimgao kidogo hakitoshi hata kuezeka nyumba tano, kumi za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa nimuombe sana Waziri, nilimsikia juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwa huko Kusini, nilisikia vyombo vya habari sasa sijui kama ni kweli na nitaomba sana athibitishe hili jambo kwamba sasa Wizara imeelekeza ugawaji wa quater zile za kuvuna katika mashamba haya ya Serikali ushirikishe pia vijiji viliyo katika maeneo hayo, yaani ya Serikali za Vijiji zilizo katika maeneo hayo. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri katika ku-close hotuba yako mtupe basi huo uhakika tusije kutoka hapa tunaamini tuliyasikia kwenye vyombo vya habari kumbe si hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili uko kwangu inasikitisha sana, Msitu wa Buhindi uko pale, unaomba Mbunge au Halmashauri mpate mgao wa miti ili muondoe tatizo la madawati, mnapewa cubic meter 100. Cubic meter 100 hizo Mheshimiwa Waziri hatupati bure tunapewa kama mfanyabiashara wa mbao, tunaambiwa na zenyewe tuzilipie. Sasa muanze kupitisha mchango kwa wananchi ili kulipia cubic meter 100 kwenye shamba la umma. Haya mambo yako chini ya uwezo wa Mheshimiwa Waziri, hayahitaji sheria, ayafute tu.
Mheshimiwa Mwenyekti, wananchi wale ndio wanaoutunza ule msitu, sasa iweje tena ikifika wakati wa kuvuna wanaambiwa walipie fedha ili kupata miti kadhaa pale kwa ajili ya kujengea darasa la umma, kujengea zahanati ya umma, kujengea nyumba ya mwalimu ya umma? Nikuombe sana, lakini pia msemaji mmoja amewasifia TFS kwa kukusanya sana mapato, nadhani yuko kule bwana kwanye kambi ile kule. Nakubaliana naye kabisa wenzetu wale wanajua kweli kukusanya, lakini sasa wanakusanyaje? Swali la pili hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka miwili iliyopita kwa mfano katika hifadhi za Serikali hizi ambazo kulikuwa na wananchi wanafanya shughuli zao mbalimbali, kwa ruhusa ya TFS watu hawa walikuwa wanatozwa kiasi kidogo tu cha kuwa kule ndani shilingi 64,000 kwa mwaka. Hawa watu walioko kule wanaganga njaa hakuna matajiri kule. Baadaye ghafla imetungwa kanuni nina hakika sio wewe Mheshimiwa Maghembe, atakuwa aliyekutangulia. Imetungwa kanuni watu hawa wanatakiwa walipie shilingi 74,000 kwa square meter moja. Sasa fikiria huyu mtu, mvuvi, na hili nadhani Mheshimiwa Mwigulu unafahamu tulishakuambia, mvuvi anazo kodi zingine 13 tofauti, lakini hata makazi tu kwenye eneo anakofanyia kazi anaambiwa alipe shilingi 74,000 kwa square meter moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mvuvi wa dagaa anahitaji eneo la kuanikia dagaa. Sasa lile linapigiwa na lenyewe hesabu, square meter moja shilingi 74,000 mtu kama ana square meter 20 shilingi milioni moja sijui kiasi gani uko. Watu wanatozwa mpaka shilingi milioni tano, wale maskini wale wanaambiwa walipe shilingi milioni tano hutaki toka, Sasa haya mambo siyo mazuri sana na nimemuomba Mheshimiwa Waziri kwa kweli liko ndani ya uwezo wako, hili unaweza kulifuta mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hili la migogoro ya wafugaji na Serikali, mimi nasema mgogoro wa wafugaji na Serikali na si mgogoro wa wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri Serikali yote iko hapa, hivi tafsiri ya ufugaji wa kisasa kwa leo ni ipi? Maana tunaambiwa kuchunga ni vibaya kwa hiyo, wafugaji wapunguze mifugo yao kwa sababu wanachunga. Lakini yule anayegawiwa ranchi pale Kitengule au wapi, huyo anaonekana na mfugaji mzuri kwa sababu amekatiwa kipande cha ardhi na mifugo yake iko mle ndani. Be it 300, 1,000 kwa sababu ina kipande cha ardhi amegawiwa huyu ni mfugaji mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule ambaye hajagawiwa kipande rasmi na Serikali ni mchungaji, ni mtu mbaya, apunguze mifugo yake. Niombe sana tupate kwanza tafsiri ya ufugaji uliokuwa mzuri, ni ule wa ng‟ombe ndani ya banda unakata manyasi unaweka au namna gani. Lakini tatizo langu sio tu hapo, tatizo ni sera yenyewe ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya mifugo haikwenda mbali ikaitazama mifugo hii wakati wa majanga, sisi binadamu tumejiwekea kinga kwenye mazao kwa sababu tunakula sisi, kwamba ikitokea jua likawaka sana wananchi wakaacha kuvuna kwa vile ni binadamu basi tulianzisha NRFA na kadhalika. Utaratibu upo ulionyooka wa kuhakikisha watu hawafi njaa, mbona hatuweki utaratibu wa mifugo kuhakikisha haifi njaa? Mifugo si tunaihitaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu ya muda Mheshimiwa Waziri, haitoshi hapa mimi nikaelezea mimi ninachokifikiria chote, nitakuomba tu kabla ya kesho jioni tafuta muda hata wa dakika 20 tuzungumze niseme ninachokifikiria kuhusu hili jambo. Tunaweza kabisa katika Awamu hii ya Tano tukaweka nyuma suala la migogoro ya Serikali na wafugaji kwa sababu uwezekano huo upo na Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kumaliza tatizo la hivi, wako wengine wameshafanya na hawana habari tena na migogoro ya hifadhi na vitu vya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanakuandama tu, Maghembe na migogoro ya wafugaji, si lako hili ni mtambuka mno. Linahitaji ushirikishwaji wa Serikali nzima ili kuhakikisha kwamba tatizo hili linakwisha kabisa na miaka ijayo wananchi waendelee kufanya ufugaji usiokuwa na shida na kilimo kisichokuwa na shida; kwa sababu issue inayosumbua wafugaji ni pale mifugo yao inapokosa malisho basi. Mifugo kama ina malisho huwezi kumuona Msukuma anatoka Meatu anakwenda Sumbawanga…
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwa sababu ya muda, mengine niliyopanga kusema nitaya-skip na nijikite katika mambo matatu hivi ambayo naamini kwamba yana umuhimu mkubwa Serikali kuyapima na kuona kama inaweza kuyafanyia kazi kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, moja, ume-pre-empty mazungumzo niliyotaka kufanya ya Bandari ya Bagamoyo, lakini kwa vile na wewe uliamua kuchangia siyo mbaya. Bandari hii ndiyo itakayokuwa pekee ya kupokea mzigo utakaosafirishwa na SGR, Dar es Salaam haina huo uwezo. Amesema vizuri sana Mheshimiwa Ally Saleh kule, Bandari ya Dar es Salaam tutake, tusitake, hata tuki-dredge namna gani pale Magogoni, turning base inayoweza kupatikana haiwezi ku-accommodate post panamas na forth na fifth generation ya meli zinazotengenezwa sasa, lakini Bagamoyo ndiyo ilikuwa jibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya mambo yaangaliwe upya tu, yaani tusifike mahali tukalikatia tamaa hili jambo. Naishauri Serikali yangu na naipenda, wafanye kuangalia upya suala la Bagamoyo haraka iwezekanavyo kwa sababu tutakamilisha ile SGR, hatutakuwa na mahali pa kushushia mzigo, tutaonekana kituko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni Mfuko wa Barabara; Mfuko wa Barabara wameusema wengi katika kuchangia hotuba ya TAMISEMI, lakini mahali penyewe ni hapa kwa sababu Act ya Mfuko wa Barabara ipo chini ya Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na ule mgawanyo wa 70 kwa 30 umepitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitasema neno moja tu, mtu akiwa na matatizo ya mishipa ya damu, mishipa mikubwa huwa hai-clot/haipati obstructions, inayopata obstructions ni mishipa midogo midogo (arteries) na hiyo ndiyo husababisha kifo. Sasa sisi tuki-concentrate sana na barabara kuu tukasahau kwamba barabara kuu hazina maana kama barabara ndogo hazifikishi watu na mizigo kwenye barabara kuu na lenyewe hili tunakosea. Iangaliwe upya tu, waangalie kwamba kama sasa ni 50 au 60, 40 lakini kuna kila haja ya kuongeza fedha kwa upande wa TARURA; sasa hivi ilivyo TARURA haiwezi ku-function. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, nataka kuzungumzia watoa huduma wanaitwa DSTV. DSTV hawa wanatoa huduma kama ving’amuzi vingine, wanatoa huduma kama kampuni za simu, kama umeme na kadhalika. Software ya kumfanya mtu aliyelipia atumie kadiri anavyolipia zipo lakini ndugu zetu hawa wao wana-charge kwa mwezi, ukishalipia ile subscription hata ukafunga king’amuzi, baada ya mwezi ukienda kimekwisha unatakiwa ulipe tena. Sasa mimi sitaki kuuita wizi kwa sababu tunalipa kwa halali, lakini huo ni wizi. Hizi simu tuna-recharge vocha, mbona wao hawatuambii uki-recharge baada ya siku 5 imekwisha automatically, wao kitu gani kinashindikana kwamba nikiwa nimezima king’amuzi maana yake mita haisomi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nimemaliza hayo, naomba nizungumzie jimbo langu kidogo. Ukurasa wa 300 katika kitabu cha hotuba ya Waziri, imetajwa barabara ya Sengerema- Nyehunge-Kahunda. Hii barabara natarajia inapaswa kufanyiwa upgrading na siyo feasibility study na detailed design, namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie hayo maneno yaliyo kwenye mabano yanatofautiana na uhalisia uliopo kwa sababu hiyo hatua ya feasibility study na detailed design imekwishapita na huku ameweka katika miradi kwa hiyo, hawawezi kurudia mradi huo ambao tayari umekwishakamilika. Naamini ni typo tu, kinachotakiwa hapa kuwepo na naomba hili katika kuhitimisha anifafanulie yaani anihakikishie kwamba ni upgrading na siyo habari ya feasibility study na detail design. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho; naomba kuzungumzia vivuko; nimesoma kitabu vipo vivuko vinajengwa, lakini kuna kivuko cha Kome – Nyakalilo, zimeenda tume mbalimbali pale. Sitaki na mimi kubashiri vifo, ndugu yangu Mheshimiwa Mkundi alibashiri ajali kule Ukara na ikatokea, sasa mimi hayo maneno sitaki kuyasema, itoshe tu kusema kwamba hicho kivuko hakitoshi watu ni wengi. Kome leo ina watu karibia 120,000 wanavushwa na kivuko cha tani 35, ukiuliza kwa nini kivuko kingine hakijengwi? Fedha hakuna, fedha tunayozungumzia ni shilingi bilioni mbili au tatu, watu pale wakiteketea sijui nani ataulizwa.

Mheshimiwa Spika, nilimweleza Mheshimiwa Kamwelwe tulipokuwa Ukara kwamba hicho kivuko hakifai, Mheshimiwa Kwandikwa amefika mwenyewe; tume iliyoundwa na Serikali baada ya MV Nyerere kuzama imefika pale Nyakalilo, nimeshangaa kweli kwamba humu ndani hakuna mazungumzo ya eneo hilo, halafu nikisimama kupinga bajeti nionekane mkorofi? (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia naomba nifanye declaration ya mambo matatu. La kwanza nimezaliwa nimekuwa na sasa nazeeka katika uvuvi, ufugaji na ukulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, nimebahatika sana kwa fadhira za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini declaration ya tatu Jimbo ninalotoka mimi, asilimia 90 ya wakazi wa jimbo hilo ni wavuvi na asilimia 10 ni wafugaji. Kwa hiyo, haya ninayoyasema na ninayopanga kuyasema yanatokana na hiyo background ambayo nimeitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na sekta ya mifugo, hotuba ya Waziri nzuri, imejaribu kugusa changamoto ambazo wafugaji wa nchi hii wanapitia, lakini nishauri tu jambo moja, kama mtu ambaye pia nimewahi kukaa kwenye dawati alilopo. Suala la masoko ya masoko ya mazao ya mifugo, haliishii katika kujenga viwanda, kwa sababu hata vile vichache tulivyonavyo, uuzaji wa mazao hayo unakuwa wa tabu kwa sababu ya jambo moja, kwamba, eneo kubwa la ufugaji wa nchi hii halijawa huru kutokana na maradhi mbalimbali ya mifugo, hasa, homa ya mapafu na ile east cost fever. Haya maradhi mawili yanazuia uuzaji nje wa nyama ya Tanzania na namna pekee ya kuondokana na hili jambo, hiki kikwazo ni kwa kufanya chanjo kuwa ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya wafugaji kuchanja kwa hiari ndiyo inatufanya tuendelee kuwa kwenye hicho kibano, kwamba bado nchi yenu siyo disease free kwa hiyo, hatuwezi kupokea nyama yenu. Leo Jumuiya nzima ya Ulaya haipokei nyama kutoka Tanzania, Marekani haipokei nyama kutoka Tanzania na huko ndiko kwenye soko lenye bei kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, katika mazao ya mifugo ni hili la ngozi, nimesoma takwimu zilizopo katika kitabu cha hotuba ya Waziri, tunachinja ng’ombe wengi, lakini ngozi haitusaidii chochote, hasa wafugaji. Kwa nini haitusaidii, ile export levy iliyowekwa ya asilimia 80, wachakataji hawaitaki, kwa hiyo, hawalipi, lakini on the other side wakulima hawauzi ngozi! Sasa is a zero sum issue, mimi sijui kama Waziri wa Fedha ananisikiliza, hili jambo tunaishia na zero sum issue kwamba, wachakataji hawaji kununua hiyo ngozi na wakulima wafugaji hawana pa kuuza hiyo ngozi, kwa hiyo, ngozi yote inabaki ya kutupa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tunataka ku- protect au ku-discourage export ya ngozi, tufanye hivyo tutakapokuwa tumekwishajipanga, tuna viwanda vyetu vya kuchakata. Kwa hiyo, tuvilinde kwa kuweka masharti magumu ya kuondoa ngozi ghafi nje ya nchi. Vinginevyo, tunapoteza tu pande zote, viwanda havijengwi, ngozi haziuzwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ninaloomba kuzungumzia leo, ni uvuvi wa Bahari Kuu. Huu uvuvi nao umekuwa kizunguzungu, nikiri kwamba nilifanya marekebisho makubwa ya kanuni, yameanza kutekelezwa baadhi na mengine hayajaanza kutekelezwa. Leo nilikuwa nazumgumza na Naibu Waziri wa Fedha, mpaka asubuhi ya leo, nchi hii, mwaka mzima, hatujaingiza hata senti tano inayotokana na uvuvi wa Bahari Kuu, sasa maana yake nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetunga sheria ili zitufanye tupoteze mapato au tumetunga sheria na kanuni ili zituingizie mapato? Naomba sana jambo hili lifanyiwe tafakari, ushuru ule wa mrabaha wa 0.4 dola kwa kilo moja, wadau wetu waliukataa. Tukakaa miezi minane bila ku-issue leseni hata moja, mpaka tulipo-rethink, tukasema hapana, hebu tuigawe hii issue, miezi sita wasilipe na miezi sita walipe, wakaja wavuvi 51 wakakata leseni. Sasa hili jambo lisipoangaliwa tunaendelea hivihivi kupoteza mapato wakati samaki wanapita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba samaki siyo kama dhahabu, kwamba iko kwenye shimo fulani Bulyang’hulu, haitoki pale milele na milele kama hujaigusa. Hawa samaki wanatembea, leo wako Mozambique, leo wako Tanzania, kesho wako Kenya, kesho kutwa wako Djibouti. Kwa hiyo, ukisema kwamba tunatunza maliasili hii sijui maliasili, hii siyo maliasili iliyo stagnant pale mahali, wanapita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, as we are speaking, hapo Djibouti na Kenya kuna meli zaidi ya 300, wanaendelea kusubiria samaki waki-cross Tanzania, wanavua. Sisi tunasema tunataka asilimia ngapi sijui, dola 0.4 kwa kilo moja ili tupate mrabaha. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, alitazame hili, Zanzibar wanalia, Zanzibar wanalia, huko natoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hili la operations zinazoendelea katika maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Zitto amelizungumzia kidogo, lakini mimi naomba nilizungumzie kwa mantiki ile kwamba asilimia 90 ya wakazi ya jimbo langu ni wavuvi. Naunga mkono, asilimia mia moja kufanyika kwa hizo operations kwa wavuvi haramu, hilo naunga mkono kabisa, lakini siungi mkono kabisa, operations hizi kufanyika bila kzingatia sheria za nchi zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kinachofanyika sasa hivi, mtu anakutwa amevunja Sheria ya Uvuvi, anapigwa faini za Sheria ya Mazingira na anayepiga faini hizo za Sheria ya Mazingira wala siyo Afisa Mazingira aliyesajiriwa. Nilizungumza na Mheshimiwa Makamba, nikamuuliza, hivi maafisa wako hawa, watumikaje katika kumkamata mtu na nyavu halafu akapigwa adhabu ya Sheria ya Mazingira, akasema hili haliruhusiwi na nikaenda kwenye sheria, ni kweli, hata Afisa Mazingira, siyo kila Afisa Mazingira anaruhusiwa kutoza faini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea ukienda leo, amekutwa na nyavu double mbili, double tatu, anapigwa faini ya shilingi milioni mbili. Ukiuliza, Sheria ya Mazingira, inahusika vipi na kiwango cha nyavu, hii Sheria ya Uvuvi ambayo faini yake haizidi shilingi laki mbili au kifungo cha miezi sita, lakini unakuta mtu amepigwa faini ya shilingi milioni mbili, milioni tatu. Sasa baya zaidi, Mheshimiwa Waziri, Maafisa wake hao, huo umekuwa ndiyo mwanya mkubwa wa rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si vizuri sana kumtaja mtu asiyekuwa ndani ya hili Bunge, si vizuri sana, kanuni zetu zinatuomba tuwe na tahadhali kuwataja watu wasiokuwa ndani ya Bunge, lakini yuko bwana mmoja, kiongozi wa shuguli hii ya operation kule Sengerema, ondokana naye huyo. Alikuwepo Ukerewe wa aina hiyo wakamhamishia kwa Mheshimiwa Zitto kule, sasa Mheshimiwa Zitto leo tayari anapiga kelele. Sasa huyu aliyeko Sengerema Mheshimiwa Mpina, amtoe tu, maafisa wako wengi sana wanaoweza kufanya kazi kwa uungwana bila kupaka Serikali picha mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anamkuta mtu kakatiwa leseni na Halamshauri, mwandikaji wa leseni hiyo ni mtumishi wa Halmashauri, kakosea herufi moja kwenye jina, anamchukulia mitumbwi yake, anachukua engine anakwenda compound kule, anadai milioni moja faini kwa sababu ya jina la mtu limekosewa herufi moja! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, okay, nikawaambia basi anapowatoza hizo faini awaandikie na stakabadhi. Stakabadhi haandiki, kwa sababu anajua akiandika stakabadhi ya faini ya milioni moja kwa jina kukosewa atakuwa amevunja sheria, anachukua fedha hizi anaweka mfukoni. Sasa mimi sijui huyu ni mwizi au ni mla rushwa, vyovyote vile, lakini ni mtu anayevunja sheria za nchi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tizeba.

MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona umenikatili. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyo mbele ya Bunge lako tukufu. Kwanza nianze kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na watumishi wote katika Wizara hii ya Fedha na Mipango kwa sababu kwa ukweli wanajitahidi. Wanajitahidi, hilo halina shaka kwa sababu makusanyo yameongezeka na miradi inatekelezwa. Niseme tu kwa ufupi kwamba huko Buchosa tunaona mambo yanaenda. Makao makuu yetu ya Halmashauri yanajengwa, Hospitali ya Jimbo au ya Halmashauri inajengwa na miradi mingine ya vituo vya afya na kadhalika inatekelezwa vizuri. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukurani hizi naomba niseme mambo ya jumla matatu au manne yafuatayo; moja, ni lile la uamuzi wa Serikali kuruhusu wananchi kuingia bandarini, kila anayeenda kutuma au kupokea mzigo. Hili jambo nimuombe sana Waziri wa Fedha alitazame upya. Huko nyuma bandari yetu iligubikwa na wizi, msongamano, urasimu, rushwa na kadhalika, kuna kitu kinaitwa port community wakakaa, wakafikia makubaliano kwamba watu wote wanaokuwa na mizigo ya kutuma au kupokea kuzagaa mle bandarini ni moja ya visababishi vya watu kuiba kuombaomba fedha zisizokuwa na utaratibu kwa sababu wengi wanakwenda kule hawaelewi hata abc za utoaji wa mizigo huko bandarini. Nafahamu jana aliongea kwa sauti sana Mheshimiwa Gulamali, lakini naomba tu niendelee kumshawishi Waziri kwamba hili jambo litazameni upya, sio kila mtu anaweza kufungua kompyuta akaona TANCIS inavyofanya kazi akaacha kupeleka usumbufu kwa maafisa wa bandari na TRA walioko kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo kuna ugumu sana wa watu kufungua kampuni hizi za clearing and forwarding, ni kama vile kuna kakundi kanajihakikishia monopoly ya hiyo kazi, lakini hizi kampuni zingekuwa nyingi za kutosha wala hizo gharama Mheshimiwa Mpango unazozisema zisingekuwa kubwa hivyo kwa sababu competition ingekuwa kubwa ya kupata wateja and therefore bei za huduma ile zingeshuka.

Kwa hiyo, zitazame tena, tusirudi tena kule bandari yetu hiaminiki, mzigo ukaanza kuhama. Leo tuko kwenye ushindani mkubwa, tuko kwenye ushindani mkubwa na Msumbiji, Kenya, Angola na Namibia. Kwa hiyo tukifanya tu jambo lolote la kuifanya tena bandari yetu ionekane sio competitive tunakuwa tunajiharibia wenyewe. Tuyatazame vizuri haya maamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niombe sana Serikali, nimesikiliza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakiwasilisha bajeti sikuusikia uwanja wa ndege wa Mwanza ukizungumziwa. Haiwezekani jamani, ilikuwa ujengwe wakati wa Mwandosya akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, sijui kilichotokea, mimi sitaki kwenda huko, lakini ukajengwa wa Songwe, Mwanza tupo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio kwamba ninakunanihii wewe, hapana, lakini ilikuwa ujengwe Mwanza ukajengwa Songwe tukakaa kimya, kote ni Tanzania. Sasa tunaomba na wa Mwanza ukamilike kwa sababu sio hela nyingi kihivyo kwamba Taifa litafilisika Mwanza tukiwa na terminal nzuri pale kama mahali pengine zilivyo. Ni mji mkubwa pili hapa nchini, kwa nini usipate sifa na heshima unaostahili?

MHE. FRANK. G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taaarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tizeba kuna Taarifa. Mheshimiwa Mwakajoka.

T A A R I F A

MHE. FRANK. G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimkumbushe tu kaka yangu Mheshimiwa Tizeba pale anazungumzia kwamba eti Songwe walikaa kimya, lakini ukumbuke kwamba juzi tu Chato kuna uwanja mkubwa kabisa unajengwa pale, kwa hiyo mambo yanaenda vizuri si ndiyo? (Kicheko)

MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Naibu Spika, unajua Mwakajoka nakuheshimu kwa hiyo sitakujibu. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tizeba unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa hiyo sijaipokea kwa sababu anajua sio Taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa uamuzi wake kabisa na hapa shukurani za pekee ziende kwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kujenga daraja la kati ya Busisi na Kigongo. Huo utakuwa ukombozi mkubwa sana kwa watu wa Kanda ya Magharibi. Leo watu wakitoka Dar es Salaam wale wanaokwenda Kagera wanalazimika kupitia Kahama na kwingineko, lakini lile daraja likikamilika ile njia itakuwa saa 24 watu wanasafiri, maisha yatakuwa murua. Tuombe Mungu tu kwamba daraja hili likamilike mambo ya Watanzania yaende kuwa, na nadhani litakuwa la kwanza la aina yake hapa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru pia Serikali kwa uamuzi wa kujenga meli ndani ya Ziwa Victoria. Kimekuwa kilio cha watu wa Ziwa Victoria.

Ombi langu Mheshimiwa Kwandikwa, ile meli ikikamilika ile sijui mbili zile, zile ndogo ndogo zianze kuhudumia watu wa visiwani. Kuna visiwa vingi katika Jimbo la Buchosa, kuna visiwa vingi Jimbo la Geita, kuna visiwa vingi Jimbo la Muleba, kuna visiwa vingi Jimbo la Bukoba Vijijini. Sasa hizi meli zilizopo leo, Butiama, Clarias na kadhalika tunaomba zianze kuhudumia hivyo visiwa, zisije tena na zenyewe zikabaki pale kwenda ile ile route ya Bukoba – Mwanza wakati kuna Watanzania chungu nzima kwenye visiwa kule wanasumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende jambo Iingine la uvuvi. Asubuhi Mheshimiwa Serukamba amezungumza kidogo, naomba nisisitize hili jambo. Bado yako masharti magumu sana kuwafanya Watanzania wafuge samaki majini. Naomba ni-declare interest katika hili, ninafanya hiyo shughuli, kwa hiyo ninajua ugumu uliopo kwa mwananchi wa kawaida kufika mahali akapata leseni zote ili aweze kufanya ufugaji wa samaki majini. Masharti bado ni magumu sana. Vibali vya NEMC shilingi milioni 20, huyo Mtanzania wa kawaida ili apate kibali cha shilingi milioni 20 yuko wapi? Hujazungumzia kodi zilizoko katika vifaa vya kutengeneza cage zenyewe. (Makofi)

Kwa hiyo, niombe sana haya mambo yatazameni punguzeni hizi kodi, haya masharti, wezesheni wananchi wafanye shughuli za kujiletea kipato. Leo ziwani kule samaki wa kuzaana tu wenyewe hivi ni shida, Mheshimiwa Mabula amesema hapa viwanda vinafungwa kwa sababu uvuvi ule sio endelevu. Njia bora ya kuwa na uvuvi endelevu ni kufuga samaki. Vietnam na kadhalika wote wanafuga samaki na wana-export samaki kwa mabilioni ya dola na sisi tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la jumla ni hili la madeni ya watumishi wa Serikali. Jamani jiwekeni kwenye miguu ya hao walimu, wahudumu, wakunga, sijui watu gani ambaye anadai shilingi 200,000 miaka mitatu au minne. Lakini hilo moja la watumishi, wako watumishi wa umma wa ngazi za vijiji, madiwani na vitongoji, hawa nao wanateseka sana, halmashauri hazina pesa za kukata hizo asilimia 10 kuwapeleka kule. Kwa nini inakuwa vigumu kufikiria kuwapa na wao kamshahara, mimi nakaita kamshahara vyovyote vile lakini ya uhakika. Kuna halmashauri leo Madiwani hawajalipwa posho zao zile za mwezi miezi 10. Wanapata wapi nguvu za kufanya kazi vizuri hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mambo ya Buchosa na hakika kama kumbukumbu yangu hainipotoshi ndiyo Halmashauri pekee isiyo na hata sentimeta moja ya lami. Kama yumo Mbunge mwingine humu Halmashauri yake haina hata sentimeta moja ya lami anyooshe mkono. Acha bwana wewe, Mpanda Mjini imejaa, acha! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tena hili jambo la barabara ya Sengerema – Kahunda, niliongea wakati wa bajeti ya Ujenzi na Uchukuzi yameandikwa maneno sio sahihi, kitabu kile haijulikani kimerekebishwa, Mheshimiwa Kwandikwa namuona Engineer Kamwelwe hayupo. Fanyeni kila mnaloweza hili jambo likae sawasawa. Nikipinga bajeti sitakuwa nimekosea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kivuko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Spika, nyavu za kuvulia dagaa milimita sita zimezuiliwa Tanzania lakini Kenya na Uganda zinatumika bila kuhojiwa na Ziwa Victoria ni lile lile. Jambo hili si sawa, litazamwe upya.

Mheshimiwa Spika, operations zinazofanyika hazipati maelekezo ya awali ya AG. Ni vyema Mwanasheria Mkuu wa Serikali akatoa maelekezo mahsusi kwa watendaji hawa ili utekelezaji wa sheria ufanyike bila kuonea wananchi. Kwa mfano, makosa ya uvuvi kutolewa adhabu za mazingira, rushwa na wizi wa waziwazi unafanyika.

Mheshimiwa Spika, ufugaji wa samaki kwa vizimba umegubikwa bado na urasimu mkubwa. Leseni ni nyingi, masharti ni magumu sana kwa wananchi wa kawaida. Hivi kwanini zana za kutengenezea vizimba hazipo/haziruhusiwi hapa nchini? Wizara inaniapa vibali kuagiza toka Kenya mara kwa mara, hii ni aibu. Utaratibu ufanyike, wawepo wauzaji maalum wa zana hizi.

Mheshimiwa Spika, Soko la Samaki la Nyakarilo hadi leo halijafunguliwa. Naomba katika kuhitimisha hoja itangazwe kufunguliwa kwa soko hilo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote niipongeze Serikali kwa kazi kubwa na nzuri sana inayofanyika ya kutuletea maendeleo Watanzania. Nimpongeze Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa uongozi wa kizalendo usio mfano wa kuiongoza nchi yetu. Nimpongeze pia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru na kumpongeza sana rafiki na kiongozi wangu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ya kusimamia shughuli za Serikali. Kazi inaonekana, huduma zinaonekana, maendeleo yanaonekana na hilo hakuna ubishi.

Mheshimiwa Spika, Niipongeze sana Serikali kwa maendeleo makubwa ambayo yamepatikana katika jimbo langu la Buchosa. Mambo ni mengi haina sababu ya kuyataja katika mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo ningependa kutoa ushauri kwa Serikali ni kuhusu urahisishaji wa namna ya kufanya biashara hapa nchini. Katika eneo hilo bado yako mambo ambayo yanasumbua wafanyabiashara. Blue print inabidi ifanyiwe kazi kwa nguvu zaidi. Kuna taasisi za udhibiti bado zinasumbua wafanyabiashara badala ya kuwawezesha na kuwasimamia.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, wa Mwaka 2016
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha katika hatua hii ya mwisho ya mjadala wa Muswada wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (The Tanzania Agricultural Institute Act, 2016).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, kwa masikitiko makubwa naomba kuchukua fursa hii kutoa pole kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera, Mwanza na maeneo mengine ya jirani kwa maafa yaliyotokea kutokana na tetemeko la ardhi lililosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa miundombinu pamoja na makazi yao. Namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na awajalie mioyo ya subira katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa naomba kuishukuru na kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge Viti Maalum, kwa michango na ushauri wao ambao umechangia kuboresha Miswada hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipende kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Semesi Sware, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Miswada ya TARI na TAFIRI. Niwashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao ambayo kwa kweli imeimarisha sana maudhui ya Miswada hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Miswada hii miwili ambayo imechangiwa kwa pamoja imechangiwa na jumla ya Wabunge 38 kwa kuongea ambapo Wabunge wanne wamechangia kwa maandishi. Kwa sababu ya muda na Kanuni zetu, naomba orodha ya Waheshimiwa hawa nisiwataje lakini iwe sehemu ya maelezo yangu haya. Napenda kuwahakikishia kwamba michango yao tumeipokea na tumeizingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mchoyo wa fadhila, nichukue muda huu kumshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ndugu yangu Mheshimiwa George Masaju, kwa msaada mkubwa alioutoa sasa hivi. Pia, nimshukuru Mhandisi Mheshimiwa Stella Manyanya, Naibu Waziri, kwa mchango wake mzuri katika maeneo ambayo yanahusu eneo analolisimamia. Vilevile nimshukuru sana Naibu Waziri Mheshimiwa William Ole-Nasha, kwa ufafanuzi alioutoa katika Muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako napenda sasa kujibu hoja za Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na michango ya baadhi ya Wabunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Namba 7 ya mwaka 1986 inayoanzisha Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambayo imeweka sharti la kuelekeza fedha zote katika Mfuko wa COSTECH, Wajumbe walitaka kufahamu kama fedha za utafiti katika sekta ya kilimo zitaelekezwa katika Mfuko huo na nini athari zake katika ufanisi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba sheria hiyo inasema hivyo na Mfuko wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia (National Fund for Advancement of Science and Technology) upo ili wanaofanya utafiti na kuendeleza uvumbuzi wa teknolojia waweze kutuma maombi ya kuzipata kwa kutumia vigezo vilivyoainishwa na Tume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kinachofanyika ni rahisi sana kwamba utaratibu wa kupata fedha kwenye Mfuko huu ni wa ushindani, kwa hivyo watafiti mbalimbali across the board wanachotakiwa kufanya ni kuandika maandiko ambapo vipaumbele katika Bodi pale COSTECH vimeainishwa na anayekuwa ame-qualify vizuri then anapata fedha kwa ajili ya kuendeshea utafiti wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hilo halizuii mamlaka za tafiti ku-source fedha kutoka maeneo mengine. Wanaweza wakapata fedha kutoka kwingine kokote na hili ndilo limezingatiwa katika Muswada huu kwa kukubali maoni ya Kamati kuanzisha Mfuko wa Utafiti ndani ya TARI. Kwa hivyo, tunapoanzisha TARI na kuwawekea uwezo wa kuanzisha Mfuko kwa ajili ya utafiti then ile fedha inayopatikana kule COSTECH itakuwa tu ni nyongeza ya hicho ambacho wanaweza kukusanya wao wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, Wajumbe katika Kamati walitaka kufahamu utaratibu utakaotumika kwa taasisi nyingine za elimu ya juu zinazofanya utafiti wa masuala ya kilimo. Taasisi zote za elimu ya juu zinazofanya utafiti wa masuala ya kilimo zitaendelea na shughuli hizo na hazitazuiwa na sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, uwepo wa TARI utawawezesha watafiti katika taasisi hizo kufanya kwa mashirikiano na maelewano na watafiti katika centres zetu hizi ambazo zitakuwa chini ya TARI kwa kuzingatia vipaumbele vya Kitaifa ambavyo vitakuwa vimeainishwa na TARI. Kwa hivyo, kama alivyosema Mheshimiwa Mhandisi Manyanya hili halipingani isipokuwa lina-complement na kuweka utaratibu ambao sasa utafanya duplication activities kwenye taasisi mbalimbali isitokee tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, kama watakumbuka nilivyokuwa nawasilisha hoja hili ndilo tulisema moja ya matokeo makubwa ya Muswada huu utakapopitishwa ni hilo kwamba sasa angalau kinachofanyika kwenye kila center kifahamike centrally na kusije kukawa na duplication ya activities.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Waheshimiwa Wabunge walitaka kujiridhisha endapo sheria inayoanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo haitaongeza ukiritimba katika utafiti. Kama nilivyosema hili jambo haliwezi kutokea isipokuwa tu ni kwamba coordination ndiyo itakuwa streamlined. Badala ya kuwa tu watu wanafanya utafiti chaotically kama ilivyokuwa awali sasa watakuwa coordinated hasa katika hii tasnia ya kilimo kwa kuhusisha na taasisi nyingine za utafiti kama vyuo vikuu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waheshimiwa Wabunge walitaka kufahamu utaratibu utakaotumika kuhakikisha fedha kwa ajili ya utafiti wa kilimo zinapatikana. Nimekwishasema COSTECH Fund ni moja ya sources lakini baada ya ku-introduce Mfuko wa Utafiti kwenye taasisi then watakuwa na uwezo wa kupata fedha kutoka maeneo mengine na kwa kweli hizo zitakuwa ni nyongeza tu. Jambo lingine ni suala la Serikali kujitahidi kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana ili tufikie lengo letu lile la percent moja ya GDP tuwe tunaielekeza kwenye utafiti across the board kwa maana ya taasisi zote zinazohusika na utafiti ziweze kupata fedha ya kutosha katika kuendesha shughuli zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo mambo yalizungumzwa na Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Muswada huu wa Taasisi ya Kilimo. Wenzetu wa upande wa pili wametaka kujua kifungu cha 3(3) na (5) cha sheria kinalenga kuzuia mtu, shirika, taasisi, ameshasema Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye mambo ya mashtaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walitaka Mwenyekiti wa Bodi ateuliwe kutoka miongoni mwa Wajumbe wa Bodi. Mwenyekiti wa Bodi ni sehemu ya Wajumbe wa Bodi lakini utaratibu wa kumpata Mwenyekiti ndiyo huo sheria inataka ateuliwe na mkuu wa nchi, kwa nini? Kwa sababu hiki ni chombo kikubwa sana kinachoshikilia maslahi ya Taifa zima. Nadhani ni matakwa ya Kikatiba pia kwamba viongozi wa namna hii wateuliwe na Mheshimiwa Rais. Hata hivyo, upatikanaji wake katika kanuni tutakazoziandaa utaweka sifa za huyo Mwenyekiti. Kwa hiyo, kabla ya Rais kufanya uteuzi atakuwa amejielekeza kwenye sifa ambazo zimetajwa katika sheria kwamba Mwenyekiti angalau awe na sifa zifuatazo ili aweze kuteuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nadhani pia namjibu Mbunge aliyechangia mwisho hapa ambaye alisema kwamba Wenyeviti hawa wanateuliwa ambao hawana kabisa mwelekeo wa aina yoyote na taasisi au bodi wanazokwenda kuziongoza, hapana! This time around kanuni itataja sifa za yule mtu anayeweza kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi kama ambavyo zinataja mtu anayetakiwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ya Mkurugenzi ishindaniwe kwa sifa, hili nadhani Mheshimiwa Naibu Waziri ameshalisema. Ushindani ni lazima kwa ngazi ya awali kabla ya majina kadhaa kupelekwa kwa Mheshimiwa Rais mwenye mamlaka ya uteuzi kufanya jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani pia wametaka muda wa watendaji kuhudumu ungewekwa wazi ili kuondoa tabia ya watendaji kukaa muda mrefu katika nafasi zao. Hili jambo naomba tulielewe vizuri, watendaji wa hizi taasisi (centers) hizi ambazo sasa zinakuja kuwekwa kwa pamoja chini ya TARI ni watumishi walioajiriwa na Serikali kwa masharti ya kudumu na pensheni. Hapa wataingizwa kwa sheria hii lakini siyo kwamba wanaenda kuajiriwa upya, hawa wanaingia huku lakini ajira zao zinaendelea na masharti yao ni permanent and pensionable.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, hatuwezi tukaweka sharti humu linaloweka ukomo wa ajira yao, ukomo wa ajira yao itakuwa ni either kutimiza miaka 60 kwa kustaafu kwa kawaida au kufukuzwa kazi kama watakuwa wamefikia hatua hiyo. Kwa sasa hivi kwa sababu sheria inawaingiza tu kwa ujumla kwenye utumishi wa taasisi hatuwezi kuwabadilishia masharti ya ajira kwa sababu hizi sio ajira mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka watendaji wa vituo wasiteuliwe bali wapatikane kwa ushindani. Ni kweli kabla ya kuteua watendaji wakuu wa vituo itazingatia taratibu za ajira na kwa njia ya ushindani. Vituo hivi vinasimamiwa na Bodi, tunaamini kwamba Bodi itatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelezo kwa Waheshimiwa Wabunge ambao walichangia hili jambo kwa kuzungumza. Mheshimiwa Jitu Soni amechangia passionately na Mheshimiwa mmoja hapa jina nimelisahau, waliuliza kwa nini vyuo vikuu visichukue hii dhamana ya utafiti badala ya kutengeneza taasisi tofauti na hivi vyuo vikuu tulivyonavyo. Ni kweli, hii mifumo yote miwili inatekelezwa duniani na kama mlikuwa mmesikiliza vizuri katika uwasilishaji wangu wa hoja nilitaja nchi zaidi ya tano ambazo zinatumia utaratibu huu wa utafiti katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, hutegemea nchi na nchi inaona iende na utaratibu gani wa utafiti kwa kuhusisha vyuo vikuu na institutes ambazo hizi hasihusiki na mafundisho ya aina yoyote wao wanajikita tu kwenye utafiti. Muundo tunaoupendekeza ni huu ambao unatumika katika nchi zingine ambazo zinafanya vizuri tu na wala hazifanyi vibaya kwa kulinganisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la mtu anayetaka kufanya usajili anaweza kukataliwa au haonyeshwi fursa ya rufaa. Ni kweli maoni haya tumeyapokea kwamba lazima katika kanuni tutengeneze utaratibu ambao utamfanya mtu ambaye amepeleka maombi ya kufanya utafiti endapo atazungushwa au kukataliwa, basi uwepo utaratibu wa kukata rufaa ili aweze kupata haki ya kufanya utafiti na asitengenezewe mizengwe na sheria yenyewe. Kwa hiyo, hili jambo tumelichukua na kwa kweli tutalifanyia kazi katika kanuni kuweka utaratibu ambao rufaa zitakuwa zinakubalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sakaya alisema kwamba Muswada katika kifungu cha 35 umeainisha kuwa Waziri peke yake ndiyo mamlaka ya mwisho. Mheshimiwa Naibu Waziri amelitolea maoni hapa kwamba administratively ndiyo Waziri anakuwa wa mwisho lakini bado mwananchi yaani aggrieved person ana kuwa ana uhuru wa kutafuta haki yake hiyo Mahakamani au katika vyombo vingine vilivyopo vya kutoa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la masoko na lenyewe limezungumziwa kwa hisia kubwa sana hapa ndani. Baada ya kutambua kwamba lipo tatizo la soko, zipo taasisi nyingi za Kiserikali zinazojihusisha na utafutaji wa masoko wa bidhaa kwa ujumla. Wizara ya Viwanda na Biashara inalo hilo jukumu la msingi la kutafuta masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na kujua kwamba zipo mamlaka zingine za Kiserikali za kushughulikia masoko bado tumeona umuhimu wa kuliweka hili jambo kwenye moja ya majukumu ya taasisi hii ili na wao wajihusishe na utafutaji wa masoko. Kwa hivyo, hiyo habari ya nyanya zinakosa wanunuzi na mazao mengine yanakosa wanunuzi pamoja na jitihada zilizopo kwenye taasisi zingine tumeiongezea hii Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na yenyewe iwe na jukumu la kutafiti juu ya masoko kwa ajili ya bidhaa za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limezungumzwa kwamba Muswada hauoneshi ni kwa vipi taasisi za kilimo za watu binafsi zinaweza kufanya utafiti. Nadhani aliyesema hivi hakuwa amesoma vizuri, Muswada unaruhusu watu binafsi na watafiti binafsi kufanya utafiti isipokuwa tu kwamba hayo maeneo ya utafiti wanayotaka kufanya waende wakayasajili kwenye taasisi. Pia kwa sheria ya COSTECH ilivyo wanapaswa kwenda kusajili maeneo yale ya utafiti wanayotaka kufanya kule COSTECH.
Wote mnafahamu mtu anaweza akawa anafanya utafiti kwa ajili ya kupata academic qualification, sasa kama hawatatakiwa kwenda kusajili mtu anaweza tu akachukua utafiti wa mtu mwingine akabadilisha title akaenda aka-publish kule ikaonekana ni wake. Kwa hili la kwenda kuwasajili then inaweka kama governor ya mtu kuweza kufanya udanganyifu katika mambo haya ambayo kwa kweli baadaye yana-attract vitu vingi ikiwa ni pamoja na intellectual properties na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia katika hoja hii ya Serikali ya Muswada wa Fedha ulio mbele yetu. Kwanza kabisa naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuunga mkono hoja, naomba nitoe ufafanuzi na namna gani tunafikiria tunaweza kuendesha kilimo chetu hapa nchini kwa usahihi na uhakika mzuri zaidi utakaozingatia maslahi mapana ya wakulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020 inataja bayana kwamba mfumo wa ushirika ndiyo utakaotumika vizuri katika kuhakikisha kwamba kilimo kinastawi na wakulima wananufaika. Ndiyo maana utaona jitihada kubwa imewekwa kuhakikisha kwamba ushirika unafufuka na mambo ya ovyo ovyo yaliyokuwepo katika ushirika yanakoma.

Mheshimiwa Spika, ushirika unatarajiwa sasa ujengwe kwa namna mpya na katika hili, mabadiliko ya Sheria Na.6 ya Ushirika yaliyofanyika, yalikuwa yamelenga kuhakikisha kwamba takwa hili la Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala linatekelezwa na sisi tumeanza kulitekeleza kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, tumefanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa ununuzi na uuzaji wa mazao hapa nchini. Katika kufanya mabadiliko hayo, pia tunatarajia na tumekwishaanza kwamba hata uhudumiaji wa kilimo wa mwananchi mmoja mmoja katika kilimo utafanyika kwa kiasi kikubwa kupitia mfumo wa ushirika. Ndiyo maana leo tumeweka utaratibu wa kuuza kahawa na pamba kupitia ushirika. Pia tunahimiza wakulima wa chai nchini wauze kupitia ushirika.

Mheshimiwa Spika, pia tumbaku hapa nchini inalimwa na kuhudumiwa yote kupitia ushirika. Eneo moja pia ambalo sasa mkazo utaendelea kuwekwa ni kuhakikisha kwamba huduma kwa wakulima wa korosho, mauzo ya korosho na mambo mengine yote yanahusu hili zao pia na yenyewe yatapitia ushirika.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunafikiria pia kuingiza mazao mengine yanayokuwa makubwa sana kama vile ufuta na mengineyo ili na yenyewe ianze kuhudumiwa kupitia ushirika.

Mheshimiwa Spika, ni katika mkakati huu, Soko la Mazao (Commodity Exchange), sasa hivi litaanza rasmi, maelekezo yamekwishatolewa ili hata uuzaji wa mazao mengine ambayo hayajwa na ushirika bado yaweze kuuzwa kupitia soko hilo na tutawashawishi wananchi wawe wanaweka kwa pamoja ili volume inayoingia katika Commodity Exchange iwe ni kubwa ku-attract wanunuzi waweze kununua mazao haya. Kwa hiyo, chai, tumbaku, korosho, pamba, alizeti na mazao mengine yote tuna-advocate kwamba yahudumiwe kupitia ushirika.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa tunavyozungumza mfumo huu wa ushirika na mfumo wa stakabadhi ghalani umeanza kufanya vizuri pia katika mazao mengine. Juzi tumeanzisha mfumo huu kwa zao la ufuta, wako waliosema wao hawajajiandaa lakini wengi waliosema wamejiandaa na wakaingia, tumeyaona mafanikio makubwa baada ya minada miwili mitatu ya mwanzo. Ufuta uliokuwa unauzwa kwa bei ya chini sana ya Sh.1,400 na Sh.1,500 kwa kilo moja. Minada miwili ya kwanza imeutoa kwenye Sh.2,710 mpaka Sh.2,840. Mnada wa tatu utakaofanyika Jumapili wiki hii, tunatarajia huenda ukaipeleka bei ya ufuta kwa kilo moja kufika kwenye Sh.3,000.

Mheshimiwa Spika, Dodoma hapa sehemu ya barafu pale, ufuta umefika Sh.2,700 na kwa sababu una-respond kwenye soko linaloendeshwa kwenye stakabadhi huko Mikoa ya Lindi na maeneo fulani ya Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, sasa namna gani tutahudumia mazao yote haya, mazao makuu yetu haya na yanayojitokeza kwa sababu tunaposema mazao makuu, labda naomba tueleweke vizuri Waheshimiwa Wabunge, siyo kwamba zao lingine hata likitokeza kukua au kupata demand kubwa na likazalishwa kwa wingi tutali-exclude kwenye utaratibu mzima wa Serikali. Mazao yale yalianza, lakini mengine hayazuiwi kuingia na hayazuiwi kuingia kutegemea na eneo la uzalishaji na kule yanakohitajika kuuzwa.

Mheshimiwa Spika, leo huwezi kuamini kwamba ufuta umepata demand kubwa na unazalishwa kwa wingi zaidi kuliko chai, tumbaku na kahawa. Kwa hivyo, kwa eneo la uzalishaji wa hili zao, hilo tayari ni zao la kipaumbele, huduma kwa mazao ya namna hii, itabidi tuendelee kusisitiza kwamba ni ushirika ndiyo itakuwa vehicle ya kuhudumia na kuuza mazao ya namna hii.

Mheshimiwa Spika, leo kwa mfano, kupitia Ushirika katika mikoa inayozalisha korosho sulphur ya maji karibu lita 320,000 zimekwishasambazwa kwa wakulima. Vinginevyo jambo hili lisingewezekana, kilichofanyika tu ni kwamba Bodi imezungumza na Vyama vya Ushirika vya Msingi na Vyama Vikuu, wametoa mahitaji yao na mahitaji yao yale tumeingia katika contract na supplies na wale supplier wamepeleka, sasa huduma inakwenda kwa wakulima moja kwa moja bila ujanja katikati hapa. Kwa hivyo, tunatarajia katika pembejeo zingine tutafanya hivyo hivyo, kwamba huduma, kama ni sulphur, kama ni nini, tutapitishia kwenye ushirika kuwahudumia wakulima.

Mheshimiwa Spika, wakulima kupitia vyama vyao vya msingi vitatoa mahitaji yao, Bodi za Mazao haya zitazungumza na vyama, watakubaliana utaratibu wa kupata mitaji na kadhalika na Serikali ipo, pale ambako itakuwa inahitajika kupeleka fedha kutegemea na mahitaji yaliyoletwa na wakulima kupitia vyama vyao, Serikali itafanya namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, niombe sana Waheshimiwa Wabunge, wasiwasi huu unaojengeka usitufanye tuondoke kwenye mkakati ambao utatuwezesha kuhudumia mazao yote kwa namna moja na kwa uhakika. Kwa sababu ni kupitia Ushirika ndiyo Serikali tunaweza kuwa na uhakika kwamba hili jambo kweli lina-represent interest za wananchi wote kwa upana wake na siyo watu wachache kunufaika katika mnyororo mzima wa thamani.

Mheshimiwa Spika, pia niombe kutumia nafasi hii kusema kwamba uhakiki wa miche ya korosho iliyozalishwa lengo letu ilikuwa kuzalisha mikorosho miche milioni kumi, uhakiki umefanyika, tumekwishafika Mikoa ya Kusini tumemaliza sasa tutaingia Morogoro, Pwani, Dodoma na Tabora, miche milioni nane na laki mbili imehakikiwa na waliozalisha kwa utaratibu usiokuwa na kona kona, fedha yao itatolewa na Serikali na wao watalipwa fedha yao.

Mheshimiwa Spika, fedha kwa ajili ya utafiti katika vyuo vyetu, kama nilivyosema juzi shilingi bilioni tatu zimekwishatolewa ili ikaendelee kuhudumia shughuli za utafiti katika zao letu. Jambo la msingi kubwa hapa ni kwamba shughuli za utafiti, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na itakuwa kupitia sasa Taasisi hii, ndiyo taasisi zote za utafiti tunazo sita kwa sasa katika Kanda zetu Sita zitahudumiwa kupitia umbrella organization yao inayoitwa TARI.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa hatujapata Mwenyekiti wa TARI, Mheshimiwa Rais amekwisha mteua Mwenyekiti wa TARI, Mtendaji Mkuu yupo, establishment imekwisharidhiwa tayari na Wizara ya Utumishi Ofisi ya Rais, kwa hivyo sasa tuna- take off, TARI watahudumiwa kupitia vyanzo vya Serikali, lakini Sheria waliyoipitisha inawaruhusu pia wao kuwa na mapato yao ya ndani yasiyotegemea Serikali.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunasisitiza kwamba, hivi vyuo vitumie capability waliyonayo kuzalisha fedha, wasibaki kufanya utafiti ambao hauunganiki na uzalishaji na hiyo ni fursa kwa wao kuweza kutengeneza fedha na kupunguza utegemezi kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Spika, kidogo tu, kwamba mnada wa jana wa ufuta Kibiti, bei ya kilo moja imefika Sh.3,100.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushuru sana
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.8) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu, lakini pia nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa uwasilishwaji mahiri sana. Bila kwenda mbali naomba niseme hali niliyonayo kwamba najiuliza nitachangia vipi kwa sababu wakati fulani nilisimamia sheria hizi na leo nalazimika kuzizungumzia kwa upande mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo napenda nilichangie ni hili la suspension za Local Governments watakapoonekana wameshindwa kusimamia shughuli za uvuvi. Nilikuwa naangalia definition ya Local Government katika context hii, nimeshindwa kuelewa ni wale watumishi individual au ni mamlaka nzima ya Halmashauri inayozungumziwa? Kama ni suala la mtumishi moja moja, sina tatizo nalo kwamba yule akikosea wanaweza wakam-suspend na niungane na Mheshimiwa Mkundi kwamba suspension ile ifanyike baada ya consultation na TAMISEMI, isije ikawa sasa watumishi walio katika mamlaka nyingine wanapewa adhabu na mamlaka nyingine ambayo haiwaajiri wao ninaelewa usimamizi wa professional ethics uko katika Wizara ya Kisekta, lakini suala la kinidhamu linapohusu lazima mwenye kumwajiri yule ndiye atoe mamlaka ya kum-suspend. Kama ni ku-suspend Halmashauri nzima kwa ujumla kwamba isijihusishe tena na usimamizi wa uvuvi, naona hapa tunakwenda ndivyo sivyo. Hili ni suala la Kikatiba, mamlaka za mitaa haziwezi zikawa zinanyang‟anywa mamlaka zake kirahisi rahisi namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, ni hizi adhabu zinazopendekezwa, ni kweli uvuvi haramu si jambo jema, hakuna mtu anaweza kushabikia uvivu haramu. Hakuna mtu anaweza kushabikia, mimi tatizo langu katika mapendekezo haya la kwanza ni kufananisha makosa. Wako watu wanavua kwa pamoja kama vikundi, lakini wakikamatwa kwa mujibu wa sheria hii watahukumiwa mmoja mmoja. Pili, makosa yanayofanywa na mchuuzi hayawezi kamwe yakalinganishwa na mvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaoishi kwa asilimia 90 tukitegemea uvuvi, wananchi wengi shughuli zao ni za uvuvi na biashara zinazohusiana na uvuvi. Sasa kuna mambo ambayo lazima tuwe makini sana, hivi mama wa kawaida na sikuona kama iko provided for kwenye hii sheria, hiyo exception. Samaki hali ya hewa ikibadilika wanakufa tu wanaelea, siyo lazima wamevuliwa na mtu na watu hawazuiliwi kuokota samaki wa hivi. Akikutwa ameokota anawauza kwa mujibu wa sheria hii, mama au kijana yeyote atakuwa amevunja sheria na anatakiwa afungwe miaka isiyopungua miwili au faini kati ya shilingi milioni 10 mpaka milioni 50. Hili halifanani na ukweli wa nchi hii. Niombe sana hizi adhabu ziwe graduated, watu wenye makosa makubwa katika uvuvi na yanafahamika, wale kweli tunaweza kwenda nao kwenye adhabu hizo za milioni 10 au ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wanaofanya petty offences, petty! Sasa zote zimejumlishwa zimewekwa kwenye kapu moja. Sidhani mtu anayeiibia nchi hii bilioni 100, bilioni 50 ni mwizi ndiyo, lakini hafananishwi na mwizi aliyeiba shilingi 20,000 kwenye mfuko wa mtu ndugu zangu. Hata adhabu humu tumeziweka tofauti yule mwingine tumemweka kwenye kundi la uhujumu uchumi na hawa wengine wameachwa ni wezi tu wadogo wadogo ambao kila siku Mheshimiwa Rais anawaachia baada ya kukaa jela miezi miwili, mitatu wanaambiwa wamepata msamaha wa Mheshimiwa Rais wanatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku tulivyoliweka linavyoletwa hili pendekezo adhabu hizi zimekwenda tu kama vile makosa haya yanafanana, aliyefanya kuuza furu watano atahukumiwa milioni 10 mpaka 50 na aliyefanya kuvua makokoro, kumwaga sumu majini na yeye atahukumiwa milioni 10 mpaka milioni 50, hili haliko sawa. Limewekwa hivyo, sasa linaleta mashaka kwamba ni mitego ya rushwa kwa sababu latitude ya adhabu inavyokuwa kubwa namna hii inampa mtu anayetoa hukumu kishawishi cha ku-negotiate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria mtu amekamatwa ana gunia la dagaa wa size ndogo, kwa mujibu wa sheria inavyopendekezwa huyu amefanya kosa ambalo atastahili adhabu ya kati ya milioni 10 mpaka milioni 50. Hivi kinamzuia nini huyo prosecuting officer kumwambia hebu tu-negotiate hapa au yule anayesikiliza hili shauri kusema tu-negotiate badala ya milioni 50 nikwambie leta milioni tano nikuachie, nikupige faini ya milioni ngapi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hili jambo liangaliwe upya, liangaliwe upya kabisa. Nimekusikia unasema tulete schedules of amendment lakini bahati mbaya sijui kama muda unatutosha sasa kufanya hivyo. (Makofi)