Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Susan Alphonce Kolimba (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua nafasi hii ya kipekee kama wenzangu walivyotangulia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake madhubuti na makini unaoendelea kugusa sio tu Watanzania bali mfano wa kuigwa katika nchi na Bara zima la Afrika na dunia kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza kipekee Mheshimiwa Balozi Dkt. Agustino Philip Mahiga, Waziri wangu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa uongozi makini na kuhakikisha tunapata ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara anayoiongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uongozi wake ndani ya Bunge hili. Aidha, napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa namna wanavyoliongoza Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Andrew John Chenge; Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan na Mheshimiwa Najma Murtaza, wewe Mheshimiwa Giga kwa kuchaguliwa kuwa Wenyeviti na kwa namna mlivyoonesha uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge hili katika kipindi hiki. Pia nawashukuru sana Wabunge wenzangu kwa ushirikiano wao wanaoendelea kunipa. Nawaombea kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yao hapa Bungeni na kwenye majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwa namna ya pekee kuwashukuru sana wananchi wenzangu na wanawake wote wa Mkoa wa Njombe na kwa kipekee Jumuiya ya Wanawake Tanzania, Mkoa wa Njombe kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mbunge wa Viti Maalum katika Mkoa huo na kwa imani kubwa walionipa na wanaoendelea kuonesha kwangu. Nitaendelea kuwa nao karibu na kushirikiana nao kuleta maendeleo makubwa zaidi na naahidi kuwa sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru sana familia yangu ikiongozwa na mume wangu mpendwa Dkt. George Yesse Mrikaria kwa uvumilivu wao kwangu na kwa namna inavyonisaidia na kuniunga mkono katika majukumu yangu. Aidha, shukrani za dhati ziende kwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, viongozi, watendaji, wasaidizi wangu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ushauri na msaada wao katika utekelezaji wa majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo sasa nianze kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwanza nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii. Ni dhahiri kwamba michango yao itatusaidia sana katika kufanikisha shughuli za Wizara na kuimarisha ufanisi wa watendaji. Tunashukuru michango yote iliyoletwa kwa maandishi, ni michango karibu ya watu 50 na wale ambao wamezungumza moja kwa moja tunawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kujibu hoja za mzungumzaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani na nitazungumzia baadhi ya vitu na vingine Mheshimiwa Waziri wangu atamalizia. Kwenye suala lililozungumzwa kwamba ni chombo gani hasa kinachotumika kama kiunganishi kati ya Balozi zetu na Wizara nyingine ili Mabalozi hawa waweze kujua na kujifunza mambo mengi mazuri yanayofanywa katika Wizara mbalimbali na lile la namna gani wananchi wanaweza kupata ripoti za Balozi mbalimbali kwa njia rahisi ili wahamasike katika kutafuta fursa za kiuchumi katika nchi hizo zenye uwakilishi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni fupi, hili ni jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wao kazi yao kubwa ni kuratibu shughuli hizo. Hata Waraka unaolalamikiwa na Waziri Kivuli wa Wizara yangu unatokana na wajibu wa Wizara yetu hii lakini unalenga na unasimamia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utaratibu uliotolewa na Wizara kuwataka Mabalozi kutoa taarifa Wizarani na kadhalika na kadhalika ambazo zimezungumzwa katika Kambi ya Upinzani kwenye taarifa yao, naomba nitoe maelezo haya kwa kirefu ili yaeleweke ili baadaye labda kila mtu apate ufahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu unaolalamikiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani unarejea Waraka wa Rais Namba Mbili (2) ambao ulitolewa mwaka 1964 na unatoa muongozo kuhusu utaratibu wa mawasiliano kati ya Taasisi za Serikali na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao na Mashirika ya Kimataifa hapa nchini. Utaratibu huo si mpya na wala haujaanza kutumika Awamu hii ya Tano ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli bali umekuwa ukitumika tangu mwaka huo 1964 kwa lengo la kuwa na utaratibu mahususi unaotakiwa kufuatwa ili kuweka mtiririko mzuri wa Mawasiliano baina ya Serikali na Taasisi tajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya waraka huo, Mabalozi hawatakiwi kuomba ruhusua kama ilivyoelezwa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani bali hutakiwa kutoa taarifa ya maombi yao ya miadi au safari za nje za kituo chao cha kazi, yaani kama ni Dar es salaam, ili kutoa fursa ya Wizara ya Mambo ya Nje ambao ndiyo wasimamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na kumbukumbu kuhusu miadi hiyo na kuratibu. Uratibu huo haupo Tanzania peke yake, bali hufanyika katika nchi zote duniani na kuwawezesha Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa kuwafikia kwa wepesi viongozi na taasisi mbalimbali za kiserikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuviwezesha vyombo vya Ulinzi na usalama kuhakikisha usalama wa Mabalozi hao katika nchi hiyo husika wawapo mikoani au sehemu nyingine yoyote. Hivyo Waraka huo wa Kibalozi, unatajwa katika maelezo ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara yetu ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa Wizara kuwakumbusha Mabalozi na taasisi za Serikali kuhusu wajibu wao katika Mawasiliano husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu waraka huo ulipotolewa, Mabalozi wameendelea kufanya kazi zao vizuri kama kawaida na hatujawahi sisi kama Wizara kupata malalamiko yoyote kutoka kwa Mabalozi hao wala taasisi hizo; na wala hawajawahi kuhamishwa kwa sababu waraka huo ni sehemu tu ya utekelezaji wa sheria ile inayohusiana na mahusiano ya kidiplomasia iliyotungwa mwaka 1963. Hivyo napenda kutoa wito kwa watumishi wote wa Serikali pamoja na taasisi zake, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waendelee kuzingatia waraka huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea, katika taarifa ile ya Kambi ya Upinzani, ilitumia tu sehemu moja na ikasema tu na ikataja article ile ya 41, lakini nataka niwasomee hapa, naomba kwa ruhusa yako Mheshimiwa Mwenyekiti, niweze kutoa quotation hiyo. Katika section ya pili ya article hiyo ya 41 inasema:
“All officials business with receiving state in entrusted to the mission of the same state shall be conducted with or through the minister of foreign affairs of the receiving state or such other ministry as be agreed. Kwa hiyo, waraka ule ni supplement tu ya hii sheria ambayo hata wao wanaitambua. Niliona nitoe maelezo haya yaeleweke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala la remitence kutoka diaspora. Ni kweli hatuna hesabu kamili ya remitence zote zinazofanywa lakini katika taasisi ambazo sisi tumezifanyia kazi, taasisi kama ya CRDB, Bank ya Watu wa Zanzibar, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Mitaji (UTT), tunachojua ni kwamba kwa mchango wa diaspora so far kuanzia mwaka wa 2013 mpaka 2015 katika Taasisi hizo tunajua kwamba diaspora wamechangia karibu milioni 26.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kujibu hilo, niende kwenye suala la visa kutoka nje ya Tanzania. Kuna suala ambalo limeulizwa kwamba Uingereza wanatoa visa zao kule Pretoria-South Africa na Canada wanatolea Nairobi, Australia wanatolea Nairobi na kadhalika na kadhalika. Tunasema hivi, ili kubana matumizi, nchi mbalimbali duniani zikiwemo zilizotajwa hapo juu, zimeweka mfumo wa kuweza ku-centralize huduma zao za utoaji wa visa na hizi zinaratibiwa kutokana na wao kwa matakwa yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama Tanzania hatuwezi kuwalazimisha wao kufuata utaratibu wa kwetu ila tunaweza tu kushauriana nao na kuwashawishi. Kwa hiyo, ule mtindo wa kutoa visa labda kwa Watanzania kupata visa zao kupitia South Africa, sisi tunajua kwamba hawaendi lakini wana process wao wenyewe na wao wameamua kutolea visa South Africa hatuwezi kuwalazimisha. Hata hivyo, tuahidi tu, kwa sababu sisi ni Wizara ambayo inajali mahusiano na taratibu, tutajaribu kuendelea kuwashawishi ili jambo hilo lifanywe kama lilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushiriki wa Ubalozi wetu Washington katika msiba wa Mtanzania aliyeuawa Houston-Marekani Marehemu Andrew Sanga. Ubalozi ulishiriki kwa kuhudhuria ibada na kutoa rambirambi kupitia Jumuiya yetu ya Watanzania wanaoishi Houston. Aidha, Ubalozi uliwakilishwa na Afisa wetu wa Ubalozi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kutokuwepo kwa Balozi kwa Washington katika msiba ule siku ile ni kwamba Balozi huyo alikuwa anamwakilisha Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli katika Kongamano la Watanzania lililofanyika Dallas-Marekani. Hata hivyo, kama nilivyosema kwamba, Balozi alimtuma Afisa wa Ubalozi kumwakilisha katika msiba huo, kwa hiyo nataka kuweka taarifa hii wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vigezo vya kufungua Ubalozi. Niseme tu kwamba, kwa mujibu wa article namba 5 ya Mkataba wa Vienna kuhusu mahusiano ya Ki-consular ya mwaka 1963, ziko sababu kadhaa zinazoweza kuchochea kufunguliwa kwa Ofisi za Ubalozi. Baadhi ya sababu ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuongezeka kwa wigo wa mahusiano kati ya Tanzania na nchi husika;
(ii) Kuongeza wigo wa kuendeleza mahusiano ya Kibiashara, Kiuchumi, Kiutamaduni; na
(iii) Ni kuwa na fursa ya kuwahudumia Watanzania waliopo katika nchi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoona kwamba katika nchi hizo tunao Watanzania kwa hiyo, hiyo inatusukuma sisi kuhakikisha kwamba tunaweka Ubalozi sehemu husika na vile vile kuwa na Wawakilishi katika nchi husika ili kukuza uhusiano wetu na nchi inayohusika. Ili kwenda sambamba na vigezo hivyo, kwa kuwa hatuwezi kufungua Balozi kila sehemu na uwezo kama mlivyojua kwamba bajeti ni ndogo; lakini kwa mwaka huu na katika mpangilio na Mkakati wa Wizara tumeweka katika balozi ambazo tunategemea labda tutazifungua tukipata pesa baada ya kufungua ile ya Quwait mwaka huu. Katika mkakati huo, tukipata pesa, tumepanga kufungua Ubalozi Qatar, Uturuki, Korea ya Kusini, Israel, Namibia na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali inavyowashughulikia Raia wa Tanzania waliopo Magerezani. Wakati kuna swali ambalo limeuliza kuhusu Maafisa Uhamiaji wanafanya kazi gani katika Balozi zetu? Moja ya kazi ambazo wanazifanya ni kuhakikisha kwamba wanaweza kwenda kuwatembelea wafungwa hao wanapokuwa gerezani na kujua matatizo waliyokuwa nayo na kutoa utatuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Balozi za Tanzania zina utaratibu wa kuwatembelea raia wa Tanzania waliopo gerezani. Utaratibu huo unafanywa kwenye balozi zetu za China, India, Japan na sehemu nyingine ambazo tunazo balozi zetu. Pale ambapo tunasikia na tunapogundua kwamba tunao Watanzania kwenye magereza hayo hufanya hivyo kwa sababu ni moja ya wajibu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wafungwa kuja kutumikia vifungo nyumbani, utaratibu huo upo. Nchi yetu imeingia kwenye mikataba ya kubadilishana wafungwa, lakini vilevile katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunayo sheria ambayo tumekubaliana kwamba inapotokea kuna mfungwa anayetoka Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda na sasa Sudan ya Kusini basi tuna utaratibu wa kubadilishana na practice hiyo ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kuhusu hoja kutokana na mwelekeo wa dunia ulivyo hivi sasa kuhusu uhusiano na ushirikiano wa Kimataifa, Serikali kupitia Chuo cha Kidiplomasia, iweke mitaala ambayo itazalisha wataalam wengi wa fani ya diplomasia kiuchumi. Aidha, Chuo kitawanye na kujipanua kuandaa mafunzo ya Kidiplomasia. Maelezo yetu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kuanzisha Sera ya Mambo ya Nje inayotilia msisitizo wa Kidiplomasia ya Kiuchumi, Chuo kimeandaa mitaala maalum kufundisha Diplomasia ya Uchumi na tayari Chuo chetu kinatoa shahada ya Uzamili katika Diplomasia ya Uchumi; na Maafisa wa mambo ya nje wote walioko Tanzania na wale ambao wako katika balozi zetu nje ya nchi, wote wamepata mafunzo hayo; na moja ya kigezo ambacho kinamfanya aweze kutoka nje ya Tanzania ni pamoja na kupata mafunzo hayo. Aidha, mipango ya baadaye ni kuongeza mafunzo katika ngazi ya Cheti, Stashahada na Shahada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kutoa fedha kwenye balozi zetu nje ili kueneza sera ya diplomasia ya uchumi ambayo itaongeza uwekezaji na Watalii. Fedha za matumizi Ubalozini hutengwa kulingana na ukomo wa bajeti na hutolewa na Hazina kwa mwaka hadi mwaka. Tutaendelea kuwashawishi Bunge hili pamoja na Hazina kuhakikisha kwamba ukomo huo wa bajeti unakuwa ni mkubwa ili kuhakikisha kwamba tunawawezesha vijana wetu au watumishi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kuelekeza fedha ubalozini kwa ajili ya kuwarejesha maafisa wetu waliomaliza muda wao katika balozi, aidha, Wizara iangalie uwezekano wa kuacha kutoa barua kwa maafisa kurejea nyumbani kwa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo kabla ya fedha hiyo haijatoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo ni kwamba, ni kweli kwamba kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa mambo ya nje, ni lazima maafisa wa mambo ya nje warudi nchini kila baada ya miaka minne ili kubadilishana na Maafisa wengine. Changamoto kubwa inayotukabili katika Wizara yetu katika kutekeleza kanuni hiyo, ni ufinyu wa bajeti, ambayo nimekwishaizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa taarifa tu, kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara imerejesha Mabalozi watano, watumishi tisa na wengine kumaliza muda wao wa kufanya kazi Ubalozini. Mabalozi hao wamerejeshwa kutoka katika Balozi zetu za Tanzania Rome, Tokyo na maelezo zaidi mtayapata tutakapokuwa tunawapa majedwali ya majibu ya hoja zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hoja binafsi. Mheshimiwa Job Lusinde alikuwa amejaribu kutuuliza, tunazingatia umuhimu wa Chuo cha Diplomasia katika kuwajengea uwezo viongozi wake na Wanadiplomasia? Je, Serikali imetenga fedha kiasi gani kwa ajili ya kuwawezesha Chuo hicho kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Tunasema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Chuo kimetengewa kiasi cha bilioni 3.1, kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi milioni 882.2 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Shilingi bilioni 2.2 ni kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi, mengine mtayaona katika sub votes zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Masele Steven, ameuliza Wizara imejipangaje ili kuhakikisha uwezekano unaoongezeka kwenye sekta za kilimo, biashara na viwanda kama ilivyo katika Sekta ya Madini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Wizara imekuwa ikitumia mahusiano mazuri tuliyonayo na nchi nyingine kuvutia uwekezaji hapa nchini. Hii inafanyika kupitia itifaki ya soko la pamoja, kutumia balozi zetu mbalimbali huko nje ya nchi, viongozi wetu kwenye nchi mbalimbali, ziara za viongozi mbalimbali wanaotembelea katika nchi hizo na kadhalika; lakini maelezo zaidi mtayapata pale tutakapokuja kuwaletea majibu katika jedwali la hoja mlizoziulizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala la Wabunge wa Afrika Mashariki. Naomba nitoe tu taarifa kuwa mara tu baada ya uchaguzi wa Wabunge wale ambao sasa hivi wanafanya kazi katika Bunge lile, Wizara iliitisha kikao baina ya Wabunge wa Afrika Mashariki, Ofisi ya Bunge na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kujadiliana namna bora ya kuwawezesha Waheshimiwa Wabunge wa EALA kufanya kazi kwa ufanisi na bila kero. Yote aliyoyasema Mheshimiwa Msigwa yalijadiliwa na kutolewa uamuzi na wao wanafahamu hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara zote, Wizara wanapokuwa wanaanza session zozote aidha Dar es Salaam au Arusha tunafanya nao vikao wanapoanza au wanapomaliza ili kuwapa mikakati. Niwaeleze tu, sisi tunapokwenda katika vikao vile, viwe ni vikao vya Bunge la Afrika Mashariki ama vikao vya Mabaraza ya Mawaziri tunakwenda na position ya Tanzania na inashauriwa na wale ambao nyinyi mnaowaita Mabalozi wa nyumba kumi kumi na matokeo ya kazi zao za taaluma na ujuzi zimeonekana. Ushindi wa bomba la mafuta la kutoka Tanga kwenda Uganda, hilo pia ni fundisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mtu ambaye anaweza kuwasaidia katika utafiti, tunae yuko Wizarani na wanajua. Vile vile nisisitize tu, Mheshimiwa Waziri wa Sheria aliposema kwamba hawa Wabunge makao yao ni Arusha, lakini unaposema kwamba tuwatafutie ofisi, ofisi Dar es salaam ziliwekwa. Vile vile hawa watu mfahamu kwamba ni Wabunge wanaotoka katika Majimbo tofauti. Kuna wanaotoka Dar es Salaam, Dodoma, Mara na Zanzibar. Sasa, unaposema watafutiwe ofisi centre yao iko wapi? Sisi tumeendelea na tutaendelea na wao wanajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshiriki katika ku-coordinate mambo yao yote, wanapotafuta maelezo wanapewa, wanapohitaji kukusanya wadau tunafanya na Wizara hii itaendelea kufanya hivyo kwa sababu tumepokea jukumu hili kama viongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kufuatia uchaguzi wa Burundi 2015 na ule wa Uganda Februari, 2016, makundi ya wanasiasa, wanaharakati wa haki za binadamu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, lakini nitakwenda kwenye hotuba iliyotolewa na Kambi ya Upinzani katika ukurasa ule wa 14 ambapo walikuwa wanazungumzia suala la usalama wa mipaka ya nchi na hasa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa ifuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2014 tarehe 20 mpaka tarehe 21 Machi, mkutano wa kwanza ambao unasimamiwa na jopo la Marais wastaafu watatu ulifanyika. Nataka tu nitoe status kwa sababu swali lao linaulizia status, lakini sitaweza kuwaambia yale ambayo yanazungumzwa ndani ya jopo lile kwa sababu bado linaendelea na linatoa taarifa kwenye ngazi maalum inayohusika lakini sio mahali ambapo ni pa wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kulikumbusha na kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba mahusiano ya Tanzania na Malawi yako vizuri, ninyi ni mashahidi na yako vizuri kwa ushahidi wa kwamba sisi kama Wizara ya Mambo ya Nje na kwa niaba ya Serikali tumeweza kufanya mikutano na Malawi kwa pamoja na yapo vizuri katika mahusiano ya kiuchumi na kijamii na ninyi ni mashahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda katika suala la mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa, niseme tu kwamba, mgogoro ule ulisitishwa mwaka 2014 na sababu ya kusitishwa mgogoro ule ni kwamba Malawi ilikuwa unaingia kwenye uchaguzi mwezi Julai na kwa hiyo, Mwenyekiti wa jopo lile la usuluhishi akaona kwamba ni hekima Malawi wangekuwa hawana nafasi ya kuweza kuhudhuria vikao vile kwa hiyo, wakasitisha. Ilipofika mwaka 2015, Tanzania iliingia pia kwenye uchaguzi Mkuu, kwa hiyo, Mwenyekiti wa jopo pia alisitisha mazungmzo ya kujadili usuluhishi wa mgogoro huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi nchi zote hizi haziko kwenye uchaguzi na utaratibu sasa hivi unafanyika ili kuweza kuendelea na mazungumzo haya katika mwaka huu. Kwa sasa hivi Mwenyekiti wa jopo hili anajaribu ku-consult na wadau watakaohusika katika Mkutano huu ili kuweza kuendelea na mazungumzo ya usuluhishi. Hiyo ndiyo status ya mgogoro huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, naomba sana kwa Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania kwa ujumla wake, diplomasia iachwe ifanye kazi yake. Tunapokuwa tunaiingilia kwa kuangalia labda mitandao au nani kasema nini, nasema kwa niaba ya Wizara yangu kwamba jambo hili linashughulikiwa na lipo katika mikono ya jopo na tuiache diplomasia ifanye kazi yake. Hii ni kwa nia njema tu, kwa sababu tunapokuwa tunashabikia kuchukua maneno yanayosemwa huku, sisi tunasema kutoka kwenye Ofisi husika kwamba usuluhishi wa jambo hili unaendelea na hivi karibuni mtaambiwa lini watakapo- consult kwamba wadau watakuwa na nafasi kwa siku gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mipaka; kuna Kamati ambayo inaendelea kufanya kazi yake, lakini kama mnavyojua kwamba mpaka wa Ziwa Nyasa bado haujaweza kupata usuluhishi wa kusema kwamba mpaka unapitia wapi mpaka hapo usuluhishi utakapokuwa umekwisha, jopo litakapomaliza kazi yake ndipo mpaka wa Ziwa Nyasa utakapokuwa umesemwa. Kwa hiyo, siwezi kuzungumzia suala la mpaka kama lilivyoandikwa kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye hotuba ile ile ya Kambi ya Upinzani, katika ule ukurasa wa 15, Kambi ya Upinzani inauliza ni nini hatima ya mgogoro huu? Hivi kweli tunaweza tukatoa jibu saa hizi, kama mgogoro huu unaendelea kujadiliwa na usuluhishi wake unaendelea! Wawe na subira, Kamati hiyo na jopo litakapomaliza kazi yake, ndipo tutakapojua kwamba lini tutapata jibu na mwisho wa mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono hoja hii.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ruhusa yako na kwa heshima kubwa niweze kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu, hoja ya kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika kuchangia hoja hii, nitachangia hoja ambazo zimetolewa na baadhi ya Wabunge kuhusu hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza ilitolewa na Mheshimiwa Kanali Mstaafu Masoud Ally Khamis ambaye alikuwa anaitaka Serikali iweke mkazo katika kusimamia alama za mipaka kwani tayari kumekuwa na tuhuma za kuondoa alama hizo katika mipaka ya Sirari na maeneo mengineyo. Naomba nitoe maelezo juu ya utekelezaji wa Serikali juu ya hoja ambayo imetolewa na Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la urekebishwaji wa mipaka ya nchi linafanyika kupitia mazungumzo baina ya nchi na nchi. Tayari Serikali imekwishaanza majadiliano na nchi ambazo zinapakana nazo na hivi karibuni nafikiri mmesikia, Tanzania ilifanya majadiliano na Serikali ya Uganda kuhusu mpaka katika Mkoa wa Kagera ambayo yameshakamilika na hatua inayofuata sasa ni kujenga na kuimarisha alama za mpaka ule. Aidha, Serikali inajiandaa kupitia upya mpaka wa nchi hizi mbili hasa kwenye upande ule wa ziwani kati ya Tanzania na Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa upande wa mpaka wetu wa nchi ya kwetu pamoja na Kenya, mazungumzo yalishakamilika na tayari Serikali imeshatoa mchango wake katika kugharamia, kujenga na kuziimarisha alama za mipakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, kwa upande wa nchi za Malawi, majadiliano bado yanaendelea. Kama mlivyosikia mara ya mwisho, Tanzania pamoja na Malawi waliitwa na lile jopo la Marais Wastaafu kule Kusini ili kujadili suala la mpaka wa Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa tofauti zozote zinazojitokeza kati ya nchi na nchi na hasa zinazohusu masuala ya mipaka, zitakuwa zinaendelea kusuluhishwa kwa njia ya mazungumzo na kwa amani kwa faida ya pande zote mbili kwa sababu hawa ni majirani zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya pili ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Kanali Mstaafu Masoud Ally Khamis. Hoja hii ilikuwa inahusu Ibara ile ya 12 (e) ya Itifaki inayozitaka nchi wanachama kushirikiana katika kukabiliana na wahamiaji haramu. Niseme tu kwamba nchi yetu imekuwa ikipokea wahamiaji haramu kutoka nchi za Eritrea na Ethiopia wanaokwenda Afrika Kusini, ambapo tatizo ambalo kwa Tanzania tumeshalisikia mara nyingi na limekuwa ni changamoto; Serikali ihakikishe kuwa nchi ya Kenya haiwaruhusu watu hao kupitia kuja kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kwa kusaini Itifaki hii, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watatumia mikakati ambayo iko ndani ya Itifaki na kuhakikisha kwamba hivi vyanzo na njia kuu na Vituo vya Wahamiaji haramu ambavyo vipo kwa sasa hivi, vitaondolewa kwa kupitia Itifaki hii ambayo sasa hivi tunairidhia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge nawaomba sana tuweze kuiunga mkono Itifaki hii ipite ili mikakati iliyowekwa na Serikali na kwa kupitia Itifaki hii, changamoto hii ambayo inapatikana kwenye nchi yetu na nchi za jirani itakuwa imekwisha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema, kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua nafasi hii ya kipekee, kama wenzangu walionitangulia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake madhubuti na makini unaoendelea kugusa si tu Watanzania, bali mfano wa kuigwa katika nchi za Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza sana na kipekee Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa uongozi wake makini na kuhakikisha tunapata ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara anayoiongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uongozi wake ndani ya Bunge hili. Aidha, napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Spika na Naibu Spika na kwa namna wanavyoongoza Bunge hili. Pia nampongeza Mheshimiwa Andrew John Chenge, wewe Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu na Mheshimiwa Najma Murtaza Giga kwa namna mnavyoweza kuonesha uwezo wenu mkubwa wa kuliongoza Bunge hili katika kipindi hiki. Pia nawashukuru sana Wabunge wenzangu wote kwa ushirikiano wao wanaoendelea kunipa, nawaombea kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yao hapa Bungeni na kwenye majimbo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wananchi wenzangu na wanawake wote wa Mkoa wa Njombe na kwa kipekee Jumuiya ya Wanawake Tanzania, Mkoa wa Njombe kwa imani kubwa waliyonipa na wanayoendelea kuonesha kwangu.

Nitaendelea kuwa nao karibu na kushirikiana nao kuleta maendeleo makubwa zaidi na naahidi kuwa sitawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru sana familia yangu, ikiongozwa na mume wangu mpendwa Dkt. George Yesse Mrikariya, kwa uvumilivu wao kwangu na kwa namna inavyonisaidia na kuniunga mkono katika majukumu yangu. Aidha, shukrani za dhati ziende kwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, viongozi, watendaji, wasaidizi wangu, Mabalozi, Wakurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ushauri na msaada wao katika utekelezaji wa majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, sasa nianze kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwanza nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na ni dhahiri kwamba michango yao itatusaidia sana katika kufanikisha shughuli za Wizara na kuimarisha ufanisi na utendaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kwa kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani na zitakazobakia Mheshimiwa Waziri ataendelea kuzijibu. Kambi ya Upinzani ilikuwa inataka kujua juu ya mpango mkakati wa Wizara na kama Wizara ina Mpango Mkakati wowote kuhusu utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mipango ya maendeleo ya Serikali ambayo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2020-2025 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano hususan Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 mpaka 2020/2021, unaojikita kwenye uchumi wa viwanda ambao utaiwezesha nchi yetu kufika katika uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mipango hiyo imekuwa ikiendana na mipango ya maendeleo ya Kikanda na Kimataifa kama vile Mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa 2013/2014 - 2017/2018; Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC); Regional Indicative Strategic Development Plan (RISDP) wa 2005-2020; Agenda 2063 na Umoja wa Afrika pamoja na Mpango wa Maendeleo Endelevu wa 2030 wa Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mipango hii, Wizara imekuwa ikivutia uwekezaji, biashara na utalii na misaada kutoka nchi mbalimbali kupitia makongamano ya biashara ya uwekezaji na kushawishi wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza nchini na kutangaza fursa zilizopo nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo utalii, kilimo, madini, nishati na kadhalika. Ninyi wenyewe mmekwishakuona wawekezaji mbalimbali wamekuja Mikoa kama ya Pwani, Singida na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani pia ilikuwa inataka tueleze kinaga ubaga hadi sasa kupitia diplomasia ya uchumi inavyoweza kujitangazia fursa zilizopo nchini kupitia Balozi zake kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kigeni, kuimarisha uhusiano wa kibiashara na mataifa mengine sambamba na kukuza sekta ya utalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema ikaeleweka kuwa Sera ya Mambo ya Nje ni mwendelezo wa sera zote iliyojiwekea Serikali katika kujiletea maendeleo. Hivyo utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje unahusisha Wizara, taasisi zote za umma na sekta binafsi pamoja na wadau wengine ikiwemo Bunge hili. Maneno haya yalisemwa pia mwaka jana tukimweleza Waziri Kivuli wa Wizara hii lakini naona swali limajirudia vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu kubwa la Wizara yangu limekuwa siku zote ni kusimamia, kuratibu na kurahisisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita kwenye diplomasia ya uchumi. Ni ukweli ulio wazi kuwa Wizara yangu hulifanikisha jukumu hili kwa kushirikiana na Wizara na taasisi zote pamoja na sekta binafsi. Hii inatokana na kuwa Wizara hii inahusika na masuala mtambuka ya Wizara tofauti kama vile kilimo, utalii, biashara, madini, elimu, afya na sekta nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa zilizopo nchini zinatangazwa na Balozi zetu ikiwa ni sehemu ya majukumu yao ya ubalozi. Balozi hizi huhudhuria makongamano ya uchumi, biashara, kilimo, elimu na kushiriki katika mialiko ya sekta hizo, hivyo, kupata fursa nzuri ya kuzitangaza fursa zilizopo nchini sambamba na kuweza kuvutia uwekezaji wa kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia majukumu ya Wizara na Sera yetu ya Mambo ya Nje pamoja na vipaumbele vya Taifa letu, Wizara iliandaa Kitabu Maalum (Ambassadors Handbook 2008) kinachoainisha majukumu ya msingi ya Balozi mbalimbali katika maeneo wanayowakilisha nchi yetu. Lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba Balozi hizi zinadumu kwenye malengo ya Sera ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo kwenye diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani pia waliuliza swali kwamba ni kigezo gani wanatumia kuwateua Mabalozi na kwa nini inaonekana kwamba uteuzi wa Mabalozi hao unazingatia zaidi u-CCM na itikadi ya chama hicho badala ya kuzingatia zaidi utaalam, uzoefu, umahiri na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe kuwa suala la uteuzi wa Mabalozi liko kwenye mamlaka ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na viongozi wengine mbalimbali ikiwemo Wizara. Uteuzi wa Mabalozi tangu na baada ya Uhuru umehusisha watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na kutoka Wizara na taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi kwa kuzingatia taaluma, uzoefu, weledi na uchapakazi wao. Ni busara hizo Marais wote watano wamekuwa wanateua Mabalozi kutoka kada za Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wasaidizi, viongozi wa Kitaifa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa hatutendi haki kama tutahitimisha kwa kusema kuwa viongozi wote hawa hawana sifa za kuwa Mabalozi baada ya kulitumikia Taifa kwenye nyadhifa mbalimbali muhimu kama hizo. Aidha, uteuzi umekuwa unazingatia matakwa ya eneo la uwakilishi kwa mfano utaona kabisa Mabalozi kutoka kada ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama wanapelekwa sehemu zile zenye hitajio la aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa na kada yeyote ndani na nje ya Wizara hufanyika hapa nchini kwa kutumia vyombo vyetu vya nje na ndani kwa kulipiwa na Serikali yenyewe au nafasi hizo kutolewa na nchi na mashirika wahisani. Ni kwa msingi huo Wizara yangu inatumia kikamilifu fursa zote zinazojitokeza nje na ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo Kambi ya Upinzani pia waliuliza kwamba Wizara kwa muda mrefu sasa imeshindwa kutoa mafunzo ya diplomasia ya uchumi kwa maafisa wake badala yake kutegemea ufadhili kutoka nje na marafiki. Naona hii ni dhana potofu na tulikwishaizungumzia katika bajeti ya mwaka jana na nilifikiri labda pengine Waziri Kivuli ameelewa lakini naona niendelee kutoa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Chuo chake cha Diplomasia kilichopo Kurasini imekuwa ikitoa mafunzo ya Diplomasia ya Uchumi mara kwa mara kwa watumishi wa Wizara yangu na wadau wengine ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi duniani. Kwa Maafisa wa Mambo ya Nje ni lazima kujiunga na chuo hicho kama mojawapo ya sharti ya kupandishwa cheo. Aidha, Wizara pia imekuwa ikiwapeleka maafisa wake kuongeza ujuzi zaidi ya Diplomasia ya Uchumi kwenye nchi za China, Japan, Misri, Afrika Kusini, Uswis, Marekani, Urusi pamoja na nchi zingine kupitia bajeti yake na ufadhili wa nchi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutafuta fursa za mafunzo nje ya nchi ni moja ya utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi kwenye eneo la elimu. Aidha, chuo kimeandaa kozi fupi na ndefu za diplomasia ya uchumi kwa Waheshimiwa Wabunge na tayari chuo kimepeleka ombi kwa Wabunge Wateule wa Bunge la Afrika Mashariki walioteuliwa hivi karibuni ili nao waweze kushiriki katika kozi hiyo. Itakuwa ni upotofu kusema kwamba Wizara haijajipanga na haijatekeleza maelekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu naomba kuweka kumbukumbu sawa kwa takwimu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 watumishi 77 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi na wa kati na watumishi 14 wamehudhuria mafunzo ya muda mrefu ya Shahada ya Umahiri kupitia fedha za ndani na za wafadhili. Hivyo basi, mafunzo haya hayategemei ufadhili kutoka nchi marafiki peke yake kwa kuwa Wizara imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya mafunzo haya kila mwaka na ukiangalia katika kila kitengo kuna bajeti ambayo inaonesha kwamba kuna mafunzo ya ndani na mafunzo ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Waziri Kivuli wa Wizara hii amesema hapa kwamba kwa miaka ya nyuma tumefundisha tu watu 32. Nataka niweke taarifa sawa, ile ilikuwa ni mwaka 2015/2016 ndiyo walikuwa wamefundishwa watu 32. Ili uweze kuelewa ni lazima ijue kwamba idadi ya watumishi ndani ya Wizara ile wapo wangapi na wangapi wanafundishwa kwanza, lazima waende kwa mpango. Huwezi ukapeleka wote 300 wakaenda shule wakati pengine hitajio ni watu 12, kwa hiyo, ni mipango mikakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo Kambi ya Upinzani wameulizia ilikuwa ni kwamba Wizara imechukua hatua gani katika kuvutia wawekezaji wakubwa kwenye sekta kilimo ambao asilimia 75 ya Watanzania wameajiriwa kwenye kilimo duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo awali, Wizara yangu ndiyo inayosimamia na kuratibu masuala ya mahusiano kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani na mashirika ya Kimataifa. Kwa hiyo, tuna jukumu la kuratibu Wizara na taasisi nyingine kwenye masuala haya. Wizara imekuwa inatangaza fursa za uwekezaji na kuvutia wawekezaji kwenye sekta zote na siyo kilimo peke yake. Lazima ieleweke hiyo kwanza, mahitaji ni mengi ni lazima tuyashughulikie kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kupitia ushiriki wa Mikutano ya Kimataifa, ziara za viongozi, makongamano ya kibiashara na uwekezaji, mikutano ya Tume ya Pamoja ya Kudumu pamoja na shughuli za kila siku za Mabalozi na Wizara yangu kwa ujumla huvutia wawekezaji kwenye miradi mikubwa ya kilimo katika kukuza sekta hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia kwa nchi za Afrika uliofanyika Dar es Salaam Mei, 2010, Tanzania ilichaguliwa kutumia Ushoroba wa Kati (Central Corridor) kuanzia Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) katika kuendeleza sekta ya kilimo. Ushoroba huu ulishindanishwa na nchi nyingine za Kiafrika na ukaibuka kuwa mshindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia SAGCOT, Tanzania imefanikiwa kuvutia makampuni makubwa kuja kuwekeza kwenye sekta ya kilimo nchini. Kwa sasa SAGCOT inaratibu miradi mbalimbali ya makampuni yasiyopungua 100. Miongoni mwa hayo, makampuni 80 yameshafanya uwekezaji na mengine yanaendelea kuwekeza. Makampuni 36 yameandika barua ya kukusudia kuwekeza na makampuni 20 yamefanya ubia wa kimkakati kwenye kuzalisha mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile uwekezaji unaokadiriwa kuwa wa thamani ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.2 umefanyika. Kwa mfano, mradi wa Shamba la Chai Iringa na Njombe (Unilever); mradi wa uzalishaji wa mchele Kilombero Plantantion (Morogoro); mradi wa kununua mbolea kwa wingi na kuifungasha hapa hapa nchini chini ya kampuni ya YARA; mradi wa maziwa

Asas Dairies (Iringa); mradi wa mbegu za viazi, Mtanga Food Limited (Iringa na Njombe) na mradi wa chakula cha kuku na uuzaji wa vifaranga, Silverland Tanzania Ltd (Iringa) ambapo mimi nashangaa na yeye anatoka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo inatarajia kuwaondoa kwenye umaskini wakulima wengi. Mpaka sasa zaidi ya Dola za Marekani 250,000,000 zinaendelea kuwekezwa kwenye uzalishaji wa mahindi, chai, viazi, soya, nyanya pamoja na huduma zingine za pembejeo. Haya ni matunda ya uratibu wa Wizara yangu katika kuvutia wawekezaji. Utasema kwamba akili ndogo inaongoza kubwa au kubwa inaongoza ndogo, ipi ni kubwa na ipi ni ndogo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Kimataifa kama vile FAO, IFAD, WFP pamoja na nchi marafiki imefanikisha misaada katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini. Kwa mfano, IFAD imetoa msaada wa Dola za Marekani milioni 10 na mkopo wenye masharti nafuu na jumla ya Dola za Marekani milioni 56.6 kwa ajili ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utashangaa nimechukua muda mrefu, Waziri wangu amenituma niongelee hilo tu na yeye atasema machache, mengine tutayajibu kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada gani zinafanywa na Wizara katika kuchangamkia fursa za uchumi badala ya kusubiri nchi rafiki ambazo zenyewe zina ajenda zao. Wizara imeendelea kutafuta fursa za uchumi kwa kushirikiana na Wizara na taasisi zote za Serikali pamoja na sekta binafsi kupitia makongamano ya biashara na uwekezaji, mikutano ya kimataifa, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano na mikutano ya ujirani mwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, fursa zilizopo nchini zinatangazwa na Balozi zetu ikiwa ni sehemu mojawapo ya majukumu yake. Balozi hizo huudhuria makongamano, biashara, kilimo, elimu na kushiriki kwenye mialiko ya sekta hizo kwenye maeneo ya uwakilishi na hivyo kupata muda mrefu wa kuzingatia fursa zilizopo nchini sambamba na kuvutia uwekezaji wa kigeni. Hivyo, siyo kweli kwamba Wizara haichangamkii fursa za kiuchumi na badala yake kusubiri nchi rafiki zije. Huu ni mkakati, unaweza ukawaita wakaja na mkazungumza, mkamaliza mikakati yenu, lakini vilevile ukawafuata na tumefanya hivyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uzima na kuweza kusimama mbele yako na kuchangia katika hoja hii ambayo Waziri wangu ameiwasilisha leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii ya kipekee kama wenzangu walionitangulia kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake madhubuti. Vilevile nimpongeze pia Waziri wangu ambaye nafanya naye kazi kwa karibu kwa kazi nzuri anayoifanya kuitetea Tanzania kuisemea, kujenga mahusiano kati ya nchi mbalimbali na kuhakikisha kwamba diplomasia ya kiuchumi inatekelezwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa sababu ya muda nimshukuru kwa namna ya kipekee mume wangu mpendwa Dkt. George Ayese Mrikalia kwa uvumilivu wao kwangu pamoja na familia yangu watoto wawili wanajua kwamba nimepewa kazi na mimi nimekubali, tutapambana mpaka kieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba niende moja kwa moja kwenye hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge najua kwamba hatutaweza kuzijibu hoja zote, lakini tunaahidi kwamba kwa niaba ya Wizara tutaweza kuzijibu kwa maandishi na kuzikabidhi kwao. Nikienda kwenye hoja ambazo zilikuwa zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge hasa kwenye Kamati nitajibu tu baadhi ya hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna suala la Kamati kutushauri kuhusu kuandaa sera ya Taifa ya diaspora. Nasema kwamba Wizara imeunda timu mahususi ili kufanikisha uandaaji wa sera hii ya Taifa ya diaspora itakayoainisha mikakati na kutoa mwongozo kuhusu ushiriki wa diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi. Timu hiyo tayari imekwishaanza hatua za awali za maandalizi ya sera hiyo. Pia Wizara imetenga fedha kwa mwaka huu kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa ajili ya zoezi hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu kuongeza kasi ya kukamilisha mchakato wa sera mpya yaani Revise Foreign Policy, niseme tu kwamba Wizara imekamilisha kuandaa rasimu ya Sera hiyo Mpya ya Mambo ya Nje ya Tanzania, lakini hatua inayofuata sasa ni kuandaa mkakati wa utekelezaji ambao pamoja na rasimu ya sera hiyo vitawasilishwa kwa wadau kwa maana ya Serikali na sekta binafsi ili kupata maoni yao na Wizara imetenga fedha kwa ajili ya zoezi hili ya bajeti ya 2018/2019 kwa ajili ya kukamilisha sera hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruke kidogo niende kwa Mheshimiwa Masoud ambaye alizungumzia kuhusu wale wafungwa 11 ambao wako kwenye gereza lile la BEO kule Msumbiji niseme tu nimeshakwisha wasiliana na Mbunge wao ambaye alikuwa anafuatilia hilo na tumewasiliana na Balozi wetu kule Msumbiji. Alimtuma Afisa kwenda kuangalia wiki mbili zilizopita, pia juzi alienda yeye mwenyewe na anasema tu kwamba anasubiria taratibu za kimahakama watakavyomaliza process za kuandaa kila kitu tutakuwa tunaendelea kumtaarifu Mbunge husika na kuhakikisha kwamba maslahi ya wale Watanzania yanalindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Masoud kwa kuhakikisha kwamba anafuatilia masuala ya Watanzania wakiwemo Watanzania ambao yeye ni Mbunge wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikienda kwenye suala lingine ambalo pia limetolewa na Kamati kwa kushauri Wizara ambalo linahusu kuhusu upatikanaji wa fedha za ujenzi wa majengo ya ubalozi na makazi katika Balozi zetu. Suala hili limekwishaongelewa sana kwenye hotuba ya
Mheshimiwa Waziri na mikakati tuliyokuwa nayo mkakati wa kwanza wa miaka 15 ambao ulikuwa ulioanza mwaka wa fedha 2002/2003 mpaka mwaka wa fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sasa hivi tumetengeneza mkakati mpya ambapo tumejaribu kuangalia kuhakikisha kwamba suala la kutengeneza mkakati wa upatikanaji wa fedha na ujenzi pamoja na ukarabati wa Balozi zetu zilizoko nje unafanyika kwa haraka iwezekanavyo. Tutaendelea kulisimamia hilo na kufuatilia kwenye Wizara ya Fedha na kwa vile Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ni Serikali basi nadhani Mungu atatusaidia na tutaweza kufikia mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie uwezekano wa kuziruhusu Balozi kubakiza angalau asilimia 40 ya makusanyo kwa maana ya maduhuli ili ziwezeshe kutekeleza majukumu yao kwenye Balozi husika; hili suala ni la kanuni na sheria. Tutajaribu kuangalia kukaa pamoja na Wizara ya Fedha na kupata ushauri wao wa kitaalam na kama sheria zitakuwa zinaruhusu basi sisi tuko tayari kupokea ushauri wa Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni wasikivu kama mnavyoona, tumetekeleza yale ambayo tumefanya, mmesema tufungue Counsel tumefungua, mmesema tufungue Balozi Cuba, tumefungua; lakini mmesema kwamba tuhakikishe jengo letu la Maputo linajengwa na kukarabatiwa na watu wanahamia, tumefanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja ya Waziri wangu. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nichangie hoja ya Kamati inayotusimamia ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Balozi Adadi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa kuwasilisha kwa ufasaha Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati yake hususan masuala yaliyotekelezwa na Wizara yangu katika kipindi cha Januari 2016 hadi Januari 2017. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutambua na kushukuru mchango wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati katika kipindi chote ambapo wamewezesha Wizara yangu kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi na weledi. Wizara yangu kwa kuzingatia ushauri na miongozo ya Kamati yetu katika kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017, imeweza kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake pamoja na malengo yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 kwa kiwango kikubwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yamewezekana kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Wizara, Kamati yetu, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Wizara ya Fedha, Wizara za kisekta, taasisi za Serikali na sekta binafsi. Ni dhamira ya Wizara yangu kuendelea kutekeleza dhima ya Hapa Kazi Tu kwa ufanisi na weledi ili kuwezesha nchi yetu kufikia maelengo na matarajio yake ya uchumi wa viwanda. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa shukrani zangu, naomba sasa kuchangia baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge na mapendekezo ya Kamati na ambayo yameletwa katika Wizara yangu. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ilikuwa ni mapendekezo ya Kamati ambapo ilikuwa inashauri kwamba Serikali itoe fedha zinazotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyoidhinishwa na Bunge ili kufanikisha azma ya Serikali kuhusiana na miradi. Ushauri huu umepokelewa na Wizara yangu na itaendelea kupeleka fedha katika miradi ya maendeleo iliyopangwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napenda tu kutoa taarifa kwa Bunge lako Tukufu kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ilitengewe kiasi cha shilingi bilioni nane kwa ajili ya bajeti ya maendeleo na hadi kufikia Februari, 2017 Wizara imepokea kiasi cha shilingi bilioni 3.4 ambayo ni sawa na asilimia 43.62. Kiasi cha shilingi bilioni 2.1 zimepelekwa Ubalozi wa Stockholm (Sweden) na shilingi bilioni 1.3 zimepelekwa Maputo, Msumbiji. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kukosekana kwa Balozi Ndogo na Uwakilishi wa Heshima kwenye baadhi ya miji yenye fursa nyingi za kiuchumi kunaathiri malengo ya Serikali ya kukuza uchumi wa nchi kupitia diplomasia ya uchumi, hilo sisi tunalipokea na tunakubaliana na jinsi Kamati ilivyoelekeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nitoe tu status ya sasa hivi kwamba Mheshimiwa Rais ameweza kuruhusu kufungua balozi sita mpya ambazo ni katika Miji ya Doha (Qatar), Ankara (Uturuki), Tel Aviv (Israel), Seoul (Korea Kusini), Khartoum (Sudan) na Algeria (Algiers). Aidha, Serikali inatemegea kufungua consular zifuatazo ambazo ni za Balozi Ndogo katika Miji ya Lubumbashi - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lagos - Nigeria na Guangzhou - China. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la tatu ambalo lilikuwa linahusu APRM Tanzania kutokuwa na hadhi ya kisheria yaani kwa Kiingereza legal entity. Tunaweza kusema tu kwamba Wizara pamoja na taasisi hii ya APRMtulishawasilisha nyaraka katika Ofisi ya AG naye ameipitia na kwa sasa hivi imepelekwa katika Wizara ya Utumishi ili na wao waweze kuichambua na kuangalia upangaji wa muundo wa taasisi hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malimbikizo ya michango ya uanachama wa Tanzania katika Taasisi ya APRM ya Afrika kwamba yanapunguza hadhi ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa, Wizara inatambua umuhimu wa kulipa kwa wakati michango katika mashirika mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama. Wizara imekwishawasilisha orodha ya michango inayotakiwa kulipwa kwa ajili ya kutatua changamoto ambayo imetajwa na Kamati na sisi kama Wizara tutaendelea kufuatilia Hazina kuhusu ulipaji wa michango hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine linalohusu APRM kutoa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu faida zake. Hili sisi tunapokea mchango wa Kamati na ushauri wake na tutaufanyia kazi na tutahakikisha katika bajeti inayokuja ya mwaka 2017/2018 tuweke hilo ili tuweze kusimamia vizuri jambo hilo. Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ufinyu wa bajeti ya matumizi ya kawaida, ya maendeleo, kunachangia Chuo cha Diplomasia kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hali inayoweza kusababisha chuo hicho kufutwa na usajili wa NACTE. Tunachoweza kusema ni kwamba Serikali inaendelea kuongeza bajeti ya Chuo cha Diplomasia ili kukidhi mahitaji ya NACTE. Pamoja na juhudi hizo kwa taarifa napenda kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara kwa kupitia mahusiano yake mazuri na nchi rafiki imeingia makubaliano na nchi ya Kuwait ili kukiwezesha chuo katika nyanja ya kukijengea uwezo hususani…
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu mengine nitawasilisha. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. DKT. SUSAN A. KOLIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupewa nafasi ya kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu. Moja kwa moja kama wenzagu waliotangulia, naomba niunge mkono taarifa zote mbili zilizotolewa mbele yetu na maoni na maazimio ya Kamati hizo zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyoongea Mheshimiwa Timotheo, Mbunge, jirani yangu, narudi pale pale kwenye suala la uhuru. Tunapozungumzia suala la haki ya uhuru kwa raia yeyote wa Tanzania, tunazungumzia suala ambalo liko ndani ya Katiba yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Timotheo alipozungumzia kuhusu suala la haki na uhuru, pia alitukumbusha kwamba tunapodai uhuru lazima pia tujue kwamba tunatakiwa kuwa na wajibu. Ukimsikiliza mzungumzaji, Mheshimiwa Mbunge Lema, alipokuwa anazungumza alitukumbusha sisi wote kama Wabunge wa Upinzani na wa Chama Tawala kwamba tunapozungumza kwamba watu wengine wako Magerezani, maana yake ni kwamba tukumbuke kwamba nasi pia tutakwenda Magarezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hoja yake na dhana yake naitafsiri kwamba Mheshimiwa Lema anakubali kabisa utendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu inasimama kwenye haki na wajibu. Pale ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaposimamia suala la uhuru, haki na wajibu, maana yake ni kwamba pale inapoona mwananchi au raia yeyote wa Tanzania anavunja sheria, ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba nakubaliana na Mheshimiwa Lema anaposisitiza kwamba sisi wote tuwajibike, tusimamie sheria, tuzifuate na tuzitekeleze. Sheria hizi ni msumeno, inaweza ikakata upande wowote na hatuwezi kusema kwamba pale wanapowekwa Magerezani labda wanachama wanaotokana na Chama cha Mapinduzi maana yake ni sahihi; lakini wanapoguswa wanachama wanaotokana na vyama vingine maana yake sheria inavunjwa au Katiba inavunjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba nizungumzie kuhusu utendaji wa Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake. Tumeona katika Kamati, Wizara hii imejipanga vizuri na hasa kwa kuanzisha vile vyombo vipya ambavyo vimewekewa utaratibu. Kitu ambacho nimekipenda zaidi ni pale ambapo Taasisi mpya ambazo zimeanzishwa ndani ya Wizara hii ya Katiba na Sheria zinapoweka utaratibu wa mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kitendo cha Wizara ya Katiba na Sheria cha kuanzisha zile Mahakama za kielektroniki, nafikiri ni wazo zuri kwa sababu litakuwa linasaidia kupunguza msongamano wa uendeshaji wa mashtaka madogo madogo yaliyopo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndani ya Kamati, tumepata taarifa ya jinsi Wizara ya Katiba na Sheria ilivyojipanga vizuri katika kujenga capacity ya watumishi watakaojiriwa katika Taasisi hizi mpya na kule katika Wizara zao. Ninachoshauri, Wizara iweze kutumia nafasi waliyonayo ya kuhakikisha kwamba katika kila mwaka waweke mpangokazi wa kuhakikisha kwamba wanajenga uzoefu na ujuzi kwa wafanyakazi na watumishi watakaoajiriwa na wale ambao wanafanya kazi katika Ofisi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Wizara pia iweze kutumia vizuri zile scholarships ambazo zinatolewa na Mataifa mbalimbali rafiki ili kuwajengea uwezo na hasa practice katika Taasisi hizi mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono ushauri uliotolewa pia na Kamati Ndogo ya Sheria Ndogo ya Bunge ambayo pia imejaribu kuangalia upungufu unatotokana na sheria ndogo ndogo zinazotungwa katika Taasisi, kwenye Wilaya au Ofisi za Kiserikali. Katika upungufu huo, tunaungana nao kwamba utaratibu uwekwe vizuri, pale ambapo Taasisi au Ofisi zinapotunga hizi Kanuni, zihakikishe kwamba zinatengeneza mpangokazi wa kuhakikisha kwamba kabla hazijatolewa kwa matumizi, zinapitiwa vizuri na kuhakikisha kwamba hazikiuki masharti yaliyowekwa kwenye sheria na Katiba ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe kutoka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, nitaendelea kuishauri Serikali na kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao bila kuvunja sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kutoa mawazo kwamba pale ambapo sheria au sheria ndogo zinapotungwa, waweze kuwajulisha watumiaji, wadau wanaotumia hizo sheria ndogo ili waweze kuzitumia sheria hizi bila kuzivunja na kupata mataizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa taarifa hizi zote mbili. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. SUSAN A. KOLIMBA: Mheshimiwa Spika, naomba kuipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa juhudi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha wanatatua changamoto zinazojitokeza katika sekta hii muhimu kwa taifa, sekta ya kilimo; ikiwemo utafutaji wa masoko kwa mazao ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizi naomba kuishauri Serikali kutafuta masoko ya mazao ndani na nje ya nchi yetu. Mazao hayo ni pamoja na zao kama mahindi, viazi, maparachichi, mananasi matunda mengine kama maembe, apples, nk yanayolimwa katika Mkoa wetu wa Njombe.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali (Wizara ya Kilimo) kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya TAMISEMI ili kufanya utafiti katika Mikoa ili kujua wapi wamezalisha zao gani kwa wingi na mikoa ipi ina uhitaji wa zao hilo. Kwa mfano Njombe wanazalisha mahindi kwa wingi na mara nyingi wakulima wanavuna wanapata changamoto kubwa ya kuuza mahindi hayo ilhali kuna mikoa au wilaya nyingine zina uhitaji mkubwa wa chakula kama mahindi, maharage n.k. Kwa mfano mwaka jana Wilaya ya Longido walikuwa na uhitaji mkubwa wa chakula ikiwemo wananchi wa wilaya ya Ludewa/Njombe walikuwa na mahindi ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, Masoko Nje ya Nchi. Naipongeza Serikali kwa kupata masoko ya nje ya nchi. Kuna baadhi ya mazao kama mihogo, maparachichi n.k; naendelea kuishauri Serikali kuitumia Wizara ya Mambo ya Nje kupitia mabalozi walioko ndani na nje ya nchi ili kuweza kupata masoko ya maparachichi, mahindi, maharage na viazi; nchi kama vile Sudan Kusini, nchi za Falme za Kiarabu, nchi za SADC na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa Pembejeo. Naomba kuipongeza Serikali kuweka mikakati ya upatikanaji wa pembejeo ikiwemo mbegu, mbolea na viuatilifu vilivyowafikia wakulima kwa wakati. Niishauri na kuiomba Serikali kuhakikisha mbegu bora ikiwemo mbegu za mahindi, viazi mviringo, maharage na maparachichi kwa Mkoa wa Njombe vinasambazwa kwa wakati na kusimamiwa vizuri ili kuwafikia wakulima kwa wakati sahihi.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali/Wizara kwa kutoa mafunzo ya uongozi wa mbolea kwa maafisa kilimo kutoka Mkoa wa Njombe ili kuweza kuleta tija katika kilimo. Naomba Wizara itoe mafunzo kwa wafanyabiashara wa mbolea wa Njombe kama ilivyofanya katika mikoa mingine.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Wizara hii.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. DKT. SUSAN A. KOLIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu kwa Taifa langu katika Bunge lako hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijatoa mchango wangu wa jumla ninaomba kwanza niseme kwamba ninaunga mkono hoja iliyowekwa mezani. Ninaposema kwamba, ninaunga mkono hoja iliyowekwa mezani, sababu za kuiunga mkono ninazo. Labda watu tujiulize kwamba muswada huu wale wanaoupinga kwa masaa mawili na wanaukubali baada ya masaa matatu, wanatafuta nini ndani ya muswada huu? Na wao ni akina nani? Ni wananchi, ni wazalendo au ni watu wa aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nimeshaona sasa ni mara ya pili watu wanapinga muswada huu, lakini wakati huo huo wanauunga mkono wanasema kwamba muswada huu ni mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kabla sijaenda kwenye ya kwangu ninaomba kwanza nijaribu kuuweka sawa ukweli. Wakati Kiongozi wa Kambi ya Upinzani anawasilisha hoja/taarifa yake kutoka kwenye chama chake, Mheshimiwa Ester Bulaya, nilikuwa ninashangaa sana kwa sababu mambo mengi ambayo alikuwa anayazungumza ni mambo ambayo Serikali pamoja na Kamati ya Katiba na Sheria kwa ujumla wao, kwa uzalendo wao na kwa uyakinifu wao wameyaona kabisa kwamba haya yanapingana na Katiba na yatolewe na yamekubalika. Sasa unapokuwa unazungumza kitu ambacho kimekwishatolewa halafu uko ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wengine Wananchi wako huko nje wanakusikiliza inakuwa si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niende moja kwa moja kwenye hoja. Muswada huu ulioletwa katika Bunge lako tukufu, ukiuona kwa macho ya kizalendo ni muswada ambao unakwenda kutatua changamoto tulizonazo katika uendeshaji wa vyama vya siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivi kwa sababu watu wengi waliokuwa wanachangia, wadau na baadhi ya Wabunge ndani ya Bunge hili na baadhi ya taarifa wanasema Msajili wa Vyama vya Siasa amepewa majukumu makubwa sana au mamlaka makubwa saa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na wengine wamejaribu kuzungumza kwamba huyu Msajili wa Vyama vya Siasa amepewa mamlaka mpaka ya kuingilia vyama, lakini nadhani wangeusoma muswada huu vizuri wangeweza kuelewa; kwa sababu tangu sheria ya kuendesha vyama vya siasa ilipotengenezwa mwaka ule wa 1992 mabadiliko kama saba yametokea na kila mabadiliko yalipotokea na mimi nilipofuatilia historia nimeona kabisa kwamba, lengo la Serikali ilikuwa ni kujenga demokrasia iliyo makini na kwa ajili ya watu wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tukija kwenye muswada huu ukiyaangalia marekebisho mengi ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo yamefanywa kwa kipindi cha kama mara saba, lakini hayakuweza kuweka bayana na kuainisha majukumu halisia ya msajili wa vyama vha siasa, lakini muswada huu umefanya kazi hiyo. Kwa hiyo mtu anapokuwa anaupinga mimi ninamshanga, kwa sababu kwa kuweka bayana majukumu ya msajili wa vyama vya siasa yanamfanya msajili wa vyama vya siasa aweze kuongozwa na kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi na vilevile kujenga demokrasia makini na kuvilea vyama vya siasa ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini ninasema kwamba, mimi ninaunga mkono muswada huu, muswada huu kwanza unaorodhesha majukumu ya msajili wa vyama vya siasa na yako bayana na hii inamsaidia kufanya good governance kwa sababu atakuwa haendi nje ya utaratibu uliowekwa ndani ya sheria, sasa kama mtu anapinga hilo mimi simwelewi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili inaweka muongozo mzuri wa mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa na vyama vya siasa ndani ya vyama vyao vya siasa kwa kuangalia wanatakiwa kutengeneza sera za namna gani na utaratibu gani wa kuviendesha vyama vyao vya siasa. Mimi ninashangaa sana pale ninapoona baadhi ya ya Wabunge au baadhi ya wadau wanapopinga kwamba vyama hivi vya siasa vinapotengeneza sera zao na majukumu yao na shughuli zao za kuendesha vyama vyao vya siasa hivi vyama visihakikishe kwamba muungano wetu unakuwepo, au umoja unakuwepo, au utu unakuwepo, au uzalendo unakuwepo na haya yote yameelekezwa katika kifungu kile cha 3 cha muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niende katika kifungu kingine ambacho kinaangalia utawala bora. Ni kile ambacho kinatoa mamlaka au kinaelekeza kwamba, katika vyama vya siasa, kiongozi yeyote wa chama cha siasa hataweza kuwa mjumbe katika Bodi ya Wadhamini na hiyo ni good governance kwa sababu, wale watakuwa wanakisimamia chama, lakini kama akiwa ni kiongozi wa chama cha siasa ndio ambaye anakuwa kwenye bodi ya udhamini inakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niende katika kifungu ambacho kinazungumzia kinaweka makatazo kwenye vyama vya siasa. Vyama vya siasa ni vyama vya siasa, lakini vyama vya siasa haviwezi kuwa vyama vya ulinzi. Nimeona watu wamezungumzia sana kuhusu suala la vikundi vya ulinzi kuwepo katika vyama vya siasa. Mimi nafikiri hekima itutume kwamba kwenye suala la ulinzi tuwachie majeshi, tuachie vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake. Hatuwezi kuchanganya masuala ya chama cha siasa kuwa masuala ya ulinzi, ni aidha uchague wewe ufanye kazi ya kuunda vikundi vya ulinzi kama kampuni za ulinzi au uwe chama cha siasa. Sasa muswada huu unaweka wazi na sisi kama Kamati tumependekeza kwamba pale ambapo vyama vya siasa vitahitaji ulinzi nchi ipo, Serikali ipo na chama kitalindwa kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni kuhusu ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa. Mimi bado naendelea kukubaliana na hoja hii ya Serikali iliyowekwa kuhusu kuhakikisha kwamba ukaguzi na kudhibiti ruzuku ambazo zinatolewa na Serikali kwenye vyama vya Siasa, inaangaliwa vizuri na inasimamiwa na jinsi itakavyokuwa inatumika. Nakubaliana na kifungu hiki kama Kamati yetu ilivyokuwa imetoa mapendekezo kwamba kibaki kama kilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nizungumzie suala la Msajili wa Vyama vya Siasa kusimamia utaratibu wa uchaguzi kwenye vyama vyetu vya siasa. Mimi sioni kama ni tatizo, kwa sababu yeye anapokuja kwenye kusimamia utaratibu unaofanywa na vyama vya siasa hana maana kwamba atakwenda kumpandikiza kiongozi ndani ya chama husika, yeye anaangalia Katiba yako inasemaje? Imefuata Kanuni? Imefuata Katiba ya nchi na utaratibu uliowekwa? Tunapopotosha kusema kwamba Msajili anapokwenda kuhakikisha kwamba utaratibu umefuatwa, maana yake ameingilia na amepandikiza au amechagua viongozi kwenye chama husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala ambalo limezungumzwa kwenye taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani na Waziri Kivuli wa Wizara hii ya sekta, amesema kwamba kuna mambo mengi yapo ndani ya Muswada huu ambao yanakinzana na Katiba. Naomba nimtaarifu rasmi, sisi ndani ya Kamati ya Katiba na Sheria tumepitia vifungu vyote na tumejadili. Kama Mwenyekiti wangu alivyosema, tumejadili na kuviondoa vifungu vyote ambavyo vilikuwa vinakinzana na Katiba. Kwa hiyo, unaposema kwamba bado vipo, ni kwamba unapotosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo linapotoshwa ni la kuhusu pale mwanachama wa chama cha siasa anapofanya kosa na hatua zinapochukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, upotoshaji unaofanywa hapa ni kusema kwamba Msajili anamfuta chama. Hapana. Msajili hata kwenye jedwali na hata kwenye mapendekezo yetu tumesema kwamba utaratibu utafuata kama ulivyowekwa kwenye chama usika, ila Msajili atakachokuwa amefanya ni kukitaarifu chama juu ya kosa alilolifanya mwanachama husika ili wao wachukue hatua ya kum-suspend.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale ambapo chama cha siasa kitashindwa, bado atawaandikia kwa sababu hapa inaonekana kama hawapewi nafasi ya kujieleza; bado watamwandikia na kumkumbusha kuhusu hilo. Wakishindwa kabisa, basi hatua nyingine za sheria ya nchi yetu itachukua nafasi yake.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naangalia kile kifungu cha 8(c) ambacho kinazungumzia kuhusu chama cha siasa kutunza kumbukumbu za Wajumbe na vikao vya chama husika ili pale ambapo Msajili wa Vyama vya Siasa atakapohitaji taarifa, waweze kumpa. Mimi sioni kama ni jambo baya, ni jambo zuri tu kwa sababu ni lazima ajue kama chama hiki je, bado ni hai au kimekufa? Atajuaje kama hawezi kupewa hiyo register?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilinde, Wajumbe wako wananisumbua sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Susan Kolimba. Ahsante sana.

MHE. DKT. SUSAN A. KOLIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)