Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula (5 total)

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, kwanza niruhusu nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa ambayo nimeipata kuja kuuliza swali hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kubwa kwa kuniamini, nimefanya kazi na nimetua kijiti kwa Mheshimiwa Silaa na niko tayari kutoa ushirikiano wakati wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina swali la nyongeza. Kwanza natambua kwamba Serikali imeweka katika bejeti yake kuongeza chanzo kingine cha maji katika Jiji la Mwanza, hususan Manispaa ya Ilemela kutokana na changamoto kubwa ya maji katika mji ule: Je, ni lini utekelezaji wa mradi huo wa chanzo kipya cha maji utaanza kutekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula Mbunge wa Ilemela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nipende kumpongeza kwa sababu suala hili amesha lileta mara kadhaa katika ofisi zetu na niseme tu jitihada zako zimesababisha Mheshimiwa Waziri Jumaa Hamidu Aweso kukuletea Mkurugenzi wa mamlaka mpya mwanamama, mchapakazi. Jitihada zako zimesababisha kuileta task force ya wataalam kuona kwamba Mwanza sasa inaenda kupata suluhu.

Mheshimiwa Spika, chanzo hiki kipya Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula naomba nikupe amani kwamba kadri wataalam wetu watakapo kamilisha kazi waliyopewa na Mheshimiwa Waziri Jumaa Hamidu Aweso, chanzo hiki mara moja kinakwenda kufanyiwa kazi ndani ya mwaka huu wa fedha.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, wamejenga barabara ya kilometa 2.5 ya breweries kwa kiwango cha lami kwa kilometa 1.7 na kimebaki kipande kidogo cha mita 750. Je, ni lini watakamilisha ujenzi huo kwa maana sasa ujenzi umesimama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nitakaa na Mheshimiwa Mabula kuona ni namna gani ambavyo Serikali inaweza ikaliratibu hili na kukamilisha kipande hiki cha barabara ambacho kimesalia kwa kuwasiliana na Meneja wa TARURA, Mkoa wa Mwanza na Meneja wa TARURA, Wilaya ya Ilemela kuona ni kiasi gani kinahitajika ili kuweza kukamilisha ahadi hiyo.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Naibu Waziri, kwanza kwa kuwashukuru namna ambavyo wanatatua kero ya maji katika Jiji la Mwanza hususani Wilaya ya Ilemela. Wamekuja na mkakati wa matokeo ya muda mfupi, wameanza kusambaza sim tank katika maeneo yenye changamoto.

SPIKA: Swali Mheshimiwa, mmesimama Wabunge wengi.

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba walishafanya survey katika maeneo ambyo wanaweza kuchimba visima kwa ajili ya ku-save maji hapo;

Je, ni lini visima vitajengwa katika Kata ya Kayenze Mtaa wa Lutongo ambako tayari feasibility study imeshafanyika na maji yalipatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Angeline Mabula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeshafanya survey na baadhi ya maeneo katika vijiji hivyo alivyovitaja tumepata maji. Katika eneo la kata aliyoitaja tumepata maji kidogo lakini maji hayo tutahakikisha tutayatumia kujenga vichotea maji vichache ili wananchi wale waweze kupata huduma ya maji.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninashukuru kwa kunipa fursa na mimi niulize swali la nyongeza. Kwanza, ninashukuru kwa huduma tuliyoipata miundombinu katika Ziwa Victoria. Wilaya ya Ilemela asilimia 87 ni eneo la maji, na wanawake na vijana wengi wanashughulika na mazao ya samaki hususani dagaa lakini miundombinu yao ya kukausha samaki si mizuri hasa kwa afya ya binadamu. Ni lini Wizara itasaidia kuweka miundombinu kwa ajili ya kukausha samaki kwa wafanyabiashara hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema kwamba Serikali imeshaanza na katika Ziwa Victoria tumeshaanza kuwasaidia Wavuvi namna ya kuvua zile samaki lakini pia kuhifadhi samaki. Hili wazo la Mheshimiwa Mbunge tumelichukua tutakwenda kulifanyia kazi kuwasidia Wavuvi wakanda ya ziwa. (Makofi)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Ilemela katika kuunga mkono uwekezaji ilitenga eneo la ekari 52 katika eneo la Nyamungoro, eneo lenye miundombinu yote; maji, barabara na liko kwenye main road ya kwenda Musoma kwa ajili ya kuweka industrial park na tayari andiko lilishafika katika Ofisi za Serikali; ni lini mradi huu utatekelezwa ili tuongeze ajira na kukuza TEHAMA kwa watu wa Mwanza na ukizingatia ni ukanda wa maziwa makuu ni hub katika eneo hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, maendeleo ya Industrial Park tunafanya pamoja na Wizara ya Viwanda, ipo chini ya EPZA. Nalifahamu hili eneo na nilishafika na tayari lipo katika Taasisi yetu ya EPZA wakilifanyia kazi, linaenda kwenye bodi na baada ya hapo tutalitolea maelekezo maalum kwamba ni lini hasa ratiba itatoka ya utekelezaji. Naamini katika mpango na bajeti ambao tutawasilisha kwenye Mkutano ujao, tutaeleza mpango maalum kuhusu Industrial Park ya Manispaa ambayo Mheshimiwa Angeline Mabula ameieleza.