Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Katani Ahmadi Katani (8 total)

MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi wa Kata za Mnyawa, Nanhyanga, Nambahu, Kitama na Nguja ambao wameanza kujenga vituo vya afya kwa nguvu zao wenyewe kwa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmad Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi ulioanza katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya Mahuta, ambapo ujenzi na upanuzi umekamilika na kituo kinatoa huduma ikiwemo ya upasuaji wa dharura.

Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Tandahimba shilingi milioni 150 kwa ajili ya kumalizia maboma ya zahanati nne za Miuta, Chikongo, Mnazi Mmoja na Mabamba. Vilevile, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya zahanati na shilingi milioni 500 zitatengwa katika mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Kitama.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi kwa kutenga fedha za kukamilisha maboma ya zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa awamu vikiwemo vituo vya afya katika Kata za Nanhyanga, Nambahu, Kitama na Nguja.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Mawasiliano ya Simu yenye usikivu katika Kata ya Litehu, Ngunja na Mkwiti Wilayani Tandahimba?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani Mbunge wa Tandahimba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi saba katika kata sita za Jimbo la Tandahimba kupitia Mradi wa Awamu ya nne na tano . Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Chaume, Mdimba Mnyoma, Mkoreha katika Kijiji cha Chikongo, Ngunja. Kuna miradi miwili mmoja uko Kijiji cha Ngunja na mwingine Namindondi Juu, lakini katika Kata ya Mihambwe, na Namikupa utekelezaji wa mradi uliopo katika hizo Kata unaendelea.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado kuna maeneo mengi ya Jimbo la Tandahimba ambayo yana changamoto za mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano imevifanyia tathmini vijiji vya Kata za Litehu, Ngunja na Mkwiti katika Jimbo hilo.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba zinaingizwa katikazabuni ya mradi wa mipakani na kanda maalumu ya Kanda Maaalum awamu ya sita yaani Border and Special Zone Phase six Mradi huu unatarajiwa kutangazwa kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Uhamiaji katika Kijiji cha Chikongo kilichopo Kata ya Moreha Wilayani Tandahimba ambacho huduma ya Visa kwa Watanzania waendao Msumbiji hutolewa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chikongo ni eneo lilioko pembezoni mwa Mto Ruvuma katika Wilaya ya Tandahimba ambayo kwa upande wa Msumbiji inapakana na Wilaya ya Nangale. Kwa sasa huduma za uhamiaji katika Kijiji cha Chikongo zinapatikana kupitia ofisi ya Uhamiaji ya Wilaya ya Tandahimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji itafanya mashauriano na nchi ya Msumbiji kuanzisha kituo cha uhamiaji katika eneo la Kijiji cha Chikongo kilichopo katika Wilaya ya Tandahimba ili kuendelea kutoa huduma kwa Watanzania waendao nchini Msumbiji.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawalipa wakulima wa Korosho fedha zao walizofanya biashara msimu wa 2017/2018 na iliyokuwa Benki ya Covenant iliyofungwa kabla ya wakulima hawajatoa fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni iliyokuwa Benki ya Covenant mnamo tarehe 4 Januari, 2018 kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuifutia leseni, Benki Kuu iliiteua Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kuwa mfilisi wa Benki hiyo kwa mujibu wa sheria. Kuanzia mwezi Machi, 2018, Bodi ya Bima ya Amana ilianza zoezi la kulipa fidia ya Bima ya Amana ya kiasi kisichozidi shilingi 1,500,000 kwa wateja waliostahili kulipwa Bima ya Amana wakiwemo wakulima wa korosho wa Wilaya ya Tandahimba na zoezi hilo bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia hiyo.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Desemba, 2021, jumla ya shilingi 332,715,894.00 zililipwa kwa wakulima wa korosho 1,078 kati ya wakulima 1,346 wa Wilaya ya Tandahimba waliokuwa na amana katika Benki ya Covenant. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 98 ya kiasi cha shilingi 337,992,095.00 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia katika Kituo cha Tandahimba.

Mheshimiwa Spika, aidha, Bodi ya Bima ya Amana inaendelea na zoezi la ufilisi wa Benki hiyo kwa kukusanya mali na madeni ya Benki hiyo ili kupata fedha za kuwalipa wateja waliokuwa na amana zinazozidi shilingi 1,500,000 ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za Benki hiyo. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa maji wa Mkwiti utakamilika ili kupunguza tatizo la maji katika Kata ya Mangombya, Mkwiti na Litehu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mradi wa maji wa Mkwiti utakaohudumia Kata za Mangombya, Mkwiti na Litehu zenye jumla ya vijiji 16. Mradi huu unatekelezwa kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza na ya pili zimekamilika na ilihusisha ujenzi wa bomba kuu lenye urefu wa kilometa 13 na ufungaji wa pampu kwenye chanzo. Utekelezaji wa awamu ya tatu na ya nne unaendelea na umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022. Kazi zinazofanyika ni pamoja na ujenzi wa matanki sita yenye jumla ya ujazo wa lita 300,000, ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilomita 89 na ujenzi wa vioski 48 vya kuchotea maji. Ahsante.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha kumalizia ujenzi wa sekondari zilizojengwa na wananchi Kata za Mnchimbwe, Kwanyama na Litehu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmadi Katani, Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wananchi katika kuibua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule. Serikali imeendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kumalizia miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka wa Fedha wa 2020/2021, Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba kupitia mapato ya ndani ilitoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya umaliziaji wa Shule ya Sekondari ya Kwanyama. Mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali illipeleka shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Litehu kupitia mradi wa SEQUIP na Mwaka wa Fedha 2022/2023, shilingi milioni 250 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mndumbwe. Aidha, Shule za Sekondari katika Kata za Mnchimbwe, Kwanyama na Litehu zimekamilika, zimesajiliwa na tayari zinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za umaliziaji wa maboma ya shule katika halmashauri zote nchini kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi utaanza?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza toka Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameniteua kumsaidia katika jukumu la Waziri wa Ujenzi, kwa kibali chako naomba kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini. Namwahidi Mheshimiwa Rais sitomwangusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Mhandisi Godfrey Kasekenya, kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais. Namwahidi Mheshimiwa Rais, tutafanya kazi kwa bidii tutapambana na kudhibiti rushwa hasa kwenye maeneo ya mikataba, manunuzi na usimamizi wa miradi ili dhamira ya Mheshimiwa Rais na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi uende vyema kama tulivyowaahidi Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi yenye urefu wa kilometa 210 unatekelezwa kwa awamu ambapo ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa kilomita 50 umekamilika kwa kutumia fedha za ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sehemu ya Mnivata – Newala - Masasi yenye urefu wa kilomita 160, mikataba miwili ya ujenzi chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesainiwa tarehe 21 Juni, 2023, kwa sehemu za Mnivata – Mitesa yenye urefu wa kilomita 100 na Mitesa – Masasi yenye urefu wa kilomita 60 pamoja na ujenzi wa Daraja la Mwiti. Kwa sasa Makandarasi wa sehemu zote mbili wapo katika hatua za maandalizi ya kuanza ujenzi, ahsante sana.
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu yenye usikivu katika Kata za Litehu, Ngonja na Mkwiti Wilayani Tandahimba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmadi Katani, Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vijiji vilivyopo katika Kata za Mkwiti, Litehu na Ngonja vitafanyiwa tathmini kujua mahitaji halisi ya huduma ya mawasiliano na hatimaye kuingizwa katika orodha ya miradi ya Serikali itakayotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.