Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Katani Ahmadi Katani (31 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhuhanah Wataala kwa kunipa afya njema nikawa miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitakuwa mchoyo wa fadhila na shukrani zangu za dhati kabisa kama nitashindwa kuwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Tandahimba ambao wamenichagua kwa asilimia 57 nikawa Mbunge wa kwanza Tanzania kutangazwa, nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye Mapendekezo ya Mpango, ukienda ukurasa ule wa kumi yamezunguzwa sana mambo ya maji. Jambo la ajabu kwangu mie Tandahimba kunakozungumzwa maji ambapo kuna vyanzo vya maji vya kutosha, Serikali kama ingekuwa makini tusingeendelea kuimba wimbo wa maji leo hapa. Maana kwenye Jimbo langu sisi tupo mpakani mwa Msumbiji na Tanzania na tuna mpaka wa Tanzania na Msumbiji ni Mto Ruvuma. Jambo ambalo kama Serikali ingekuwa makini tusingekaa hapa watu wa Mtwara tukazungumza habari ya maji. Niiombe Serikali kupitia suala hili la bajeti, waone kabisa kuna kila sababu ya kuona Mkoa wa Mtwara hatuwezi kurudi tena tukazungumza suala la maji na maji yamejaa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndugu zangu wamezungumza suala la kuboresha kilimo. Tunapozungumza kuboresha suala la kilimo tunazungumza na suala la barabara pia. Tumezungumza 2014 ukitoa dhahabu ni korosho ambayo imeingiza Taifa bilioni 647.9. Ukitoka Mtwara kwenda Tandaimba, Newala, Nanyamba ambapo ndiyo wazalishaji wakubwa wa korosho hizi hawana lami kwa miaka 54 ya CCM bado mnasema mna mipango mizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara ya Fedha niombe Mawaziri wenye dhamana wawafikirie wakulima hawa wa korosho ambao wanaleta pato kubwa la Taifa lakini bado ukasafiri kwa masaa sita, saba kwenda sehemu yenye umbali wa kilometa 95 kama Jimboni kwangu Tandahimba kutoka Mtwara Mjini kwenda Tandahimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu waliotangulia wamezungumza sana suala la bandari. Nimeona mipango ya kuandaa bandari mpya ya Mbegani sijui wapi huko, nyingine ya Tanga, lakini bandari yenye kina kirefu Tanzania na Afrika Mashariki ni bandari ya Mtwara. Umezungumzwa mpango wa kujenga magati manne, lakini kwenye ule mpango limezungumzwa gati moja tu lenye urefu wa mita 300, lakini halijaelezwa lini lile gati litajegwa. Niiombe Serikali watakapokuja na mpango sasa wawaambie wana Mtwara gati hilo la mita 300 litajengwa lini na litakwisha lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema Mtwara tuna fursa kubwa kama Serikali itakuwa inaona umuhimu huu. Leo unakwenda Uchina unakwenda nchi za Ulaya ukitafuta bandari, bandari ya Mtwara yenye kina kirefu haipo kwenye ramani. Sasa Serikali hii ya CCM bado mnajivuna, mnazungumza suala la viwanda na gesi tunayo Mtwara mtajengaje viwanda vya korosho Tandahimba ambapo umeme wenyewe haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo REA phase II iliyozungumziwa mpaka leo ukija sehemu zenye uzalishaji umeme bado haupo. Napata shida sana, tunapozungumza suala la viwanda wakati sehemu yenye umeme bado wananchi wake hawana umeme, lakini mnazungumza kupeleka viwanda, unapelekaje viwanda sehemu ambayo haina umeme? Sasa niombe muwe makini sana mnapoleta mipango hii, na mara zote CCM mmekuwa wazuri sana wa ku-plan, ni wazuri sana wa ku-plan, implementation ndiyo shida. Sasa ninaiomba Serikali ya CCM kama ina nia njema, yale mliyoyaweka kwenye mpango myatekeleze. Vinginevyo sisi tuna take off 2020, tunachukua nchi hii kabisa. Haya wala siyo masihara mimi kwangu kule nimeshawapiga, Madiwani nimeshachukua kila kitu nimezoa zoa pale. Tunajiandaa kuisafisha CCM 2020, Mtwara kama hamkuleta mambo mazuri kule, kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumza suala la umeme, ambalo nimekuja kuzungumza hapa, tulipata shida, sisi ndiyo tulipigana, tulipigwa tukakaa jela wakati tunaitetea gesi, lakini watu wa Mtwara hawakuwa na shida ya Serikali kutoa gesi Mtwara kwenda Dar es Salaam, watu wa Mtwara walikuwa wanatetea maslahi ya watu wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama leo bomba limekwenda Dar es Saalam kilometa 542 ,lakini Mkoa wa Mtwara kuna watu hawana umeme. Wakilalamika mnataka wasilalamike, wakilalamika mnawapiga, sasa Serikali imekuwa ni ya kupiga piga tu hovyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezungumza suala la elimu hapa, wakati mnazungumza suala la elimu tumepongeza Mpango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Magufuli, suala la elimu bure, lakini vitu vya ajabu, kama Rais amesema elimu bure iweje leo mtoto anakwenda hospitali kupima anaambiwa atoe pesa na ndiyo kauli ya Rais. Kama Rais amesema bure vyombo vyake vingine kama ni suala la kupima mwanafunzi aende apimwe bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, joining instruction nayo ni shida wakienda Mahakamani wanatakiwa watoe pesa sasa hata kwa vitu vidogo hivi! Hata kwa vitu vidogo hivi! Hebu msaidieni Rais Magufuli huyu aonekane alichokisema kina maana ya bure kweli. Tusikae hapa kuzungumza bure watoto wanaenda hospitali tu wanaambia elfu tano ya vipimo, mwanafunzi anakwenda Mahakamani anaambiwa shilingi elfu tano ili aandikiwe sijui kitu gani sijui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niiombe Serikali hii kama ina dhamira njema kama ilivyozungumza tuone haya mambo mnaweza kuyarekebisha, lakini mlizungumza vitu vizito, wenzangu wakazungumza suala la airport ya Mtwara. Ukisoma hotuba ya Rais kuna maeneo yanaonekana airport ya Mtwara, uwanja umekarabatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Waziri mwenye dhamana kama utapata fursa njoo Mtwara, ile airport tunayozungumza kwamba imekarabatiwa ndege ikitua ni balaa. Utafikiri unatua kwenye maporomoko, sijaona uwanja wa ndege wa namna hiyo wa ovyo. Mataa hakuna sasa akina Dangote watakuja asubuhi tukiwa na mambo ya dharura ya usiku inakuwaje! Ndiyo maana hata Mawaziri hamji Mtwara usiku kwa sababu hakuna facility airport pale, taa hakuna mmezibeba taa zile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nione kama mna dhamira njema ya kuleta viwanda mnavyosema, kuboresha miundombinu mnayosema. Hebu wafakirieni watu wa Mtwara kwa namna nyingine sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu limezungumzwa suala la elimu kwa maana ya VETA nataka niizungumzie VETA kidogo, kwa maana ya viwanda mnavyosema, viwanda na Vyuo Vikuu. Kwangu pale kuna kata moja ya Mahuta, kuna majengo pale yaliyoachwa na Umoja wa Wazazi Tanzania. Kuna majengo yanayotosha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama una shida ya majengo ya VETA njoo tukukabidhi Mahuta pale ili watu wa Tandahimba wapate fursa ya kuwa na VETA ili iwasaidie watu wa Newala, Masasi, Nanyamba watapata fursa kwa sababu majengo tayari tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, mchango wangu ulikuwa huu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia nami naomba tu kuwapa maelezo ndugu zangu hao wa upande wa pili kwa maana ya chama tawala, kama Mheshimiwa Kingu na Kaka yangu Mheshimiwa Ulega pale; Serikali hii ya Awamu Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, siyo ukipiga piga maneno ndiyo anakupa Uwaziri, hakupi Uwaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote ukiwaangalia waliopewa Uwaziri, Unaibu Waziri, ni watu makini, wametulia, siyo maneno maneno ya siasa. Sasa kama mnataka Uwaziri kwa namna hiyo, Uwaziri huo haupo na bahati nzuri hakuna reshuffle, nimenusa! Kwa hiyo, mnapokuja hapa, muwe na hoja za msingi za kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikubaliane na wewe Mheshimiwa Kingu, sisi Wapinzani tutasema na Serikali ndiyo inatekeleza. Kwa hiyo, unaposema hatuna alternative, sisi hatuko kwenye mamlaka. Kweli hatuna alternative! Tutashauri tu. Nyie wenye mamlaka ndiyo mna wajibu sasa tunayoyashauri kuyafanya au kutoyafanya. Sitarajii tukija kwenye Wizara nyingine mtapiga ngonjera hapa na kwaya zenu za vyama vya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye michango yangu kuhusu Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji:-

Mheshimiwa Waziri, sisi watu wa Mtwara na Lindi mara nyingi nasema tumesahaulika sana. Nikikukumbusha Mtwara na Lindi tulikuwa na viwanda vya kubangua korosho takribani 11. Pale Newala Mjini tulikuwa na viwanda viwili, Mtama tulikuwa na kiwanda kimoja, Masasi tulikuwa na kiwanda kimoja, Lindi tulikuwa na kiwanda kimoja, lakini viwanda hivi tunavyozungumza, Serikali ya Awamu ya Tatu, ilivibinafsisha viwanda hivi na baadaye ikaja kuviuza viwanda hivi kwa bei chee. Wengine waliouziwa wamekuja kufanya ma-godown viwanda vya kubangua korosho; lakini wengine ni watumishi wa Serikali. Unaona ni dili lilifanywa! Nami naamini Mheshimiwa Waziri yuko makini na Serikali hii ya Awamu ya Tano iko makini, mtakwenda kuvichukua viwanda vile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Newala pale, vile viwanda viwili, bei iliyouziwa haifiki shilingi milioni 300, viwanda viwili! Hebu tukimaliza Bunge hili Mheshimiwa Waziri aende ufuatilie haya ninalomwambia. Sasa wanataka tuwe na Tanzania ya viwanda, viwanda ambavyo Mwalimu Nyerere alifanya kazi kubwa; akaona Kusini kuna fursa ya kuweka viwanda vya kubangua korosho kwa ajili ya kuongeza thamani. Leo korosho tunai-export mpaka inatoa ajira. Wahindi wanakuja kununua korosho hapa, Vietnam wanakuja kuchukua korosho hapa, tuna-export ajira zinakwenda India pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda India, wale Wahindi wanaofanya kazi ya kubangua korosho kazi ambazo Wamakonde wanaweza. Bahati nzuri viwanda vya kubangua korosho havihitaji mitaji mikubwa kama watu wanavyofikiri. Nami nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, watu wanakuwa hawamwelewi, lakini mimi namwelewa kweli kweli!

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilimtumia memo moja nikawa naulizia suala la kiwanda cha sabuni, alinipa alternative. Kweli nilipokwenda Kibaha pale, ile thamani aliyoniambia nimeikuta iko hivyo hivyo, shilingi milioni nane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu walitaka kuleta kiwanda cha kubangua korosho chenye thamani ya shilingi bilioni 37, hata India hakuna kiwanda cha namna hiyo. Sasa fursa ya viwanda vile ambavyo vimechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tatu kwa bahati mbaya, najua kwa bahari mbaya; kuna watu wapiga dili na kuna watu wanakuja kwa ajili ya kazi; nami naamini Mheshimiwa Waziri umekuja kwa ajili ya kazi. Twende kule maeneo ya Kusini uone viwanda vile vilitolewaje na namna gani tunaweza kuvirudisha ili sisi wakulima wa korosho sasa tunufaike na viwanda vile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka kwangu Kitama, Kijiji nilichozaliwa ukaenda Kijiji jirani cha Miuta, palikuwa na kiwanda pale cha NDC; kile kiwanda kimekufa. Ukija Kitama ambapo mimi nipo, pana kiwanda cha kubangua korosho pale, kile kiwanda kinahitaji mtaji mdogo wa kuongezewa. Nasi kwenye korosho umeona taarifa; kwa kupitia Export Levy tumekusanya kwa taarifa ya Serikali mpaka mwezi wa Pili mwaka huu zaidi ya shilingi bilioni 980.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa ya sasa, tumekusanya zaidi ya shilingi trilioni moja kwenye korosho. Sasa pesa zile za Export Levy kwa sababu zinakaa tu, uangaliwe utaratibu aidha, hata kwa kupitia SIDO, watu wakopeshwe pesa wajenge viwanda vidogo kule.

Mheshimiwa Waziri, Mtwara Mjini pale eneo lile la Mikindani kulikuwa na viwanda pale. Zamani wakati mimi nakua, palikuwa na Kiwanda cha Mashua, Mikindani pale. Vile vile palikuwa na kiwanda cha Coca Cola Mikindani pale. Viwanda vie vimepotea na wala hatujui vimepoteaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati Mheshimiwa Waziri anafanya majumuisho, nataka ajaribu kunipa maelezo, vile viwanda vimetekwa, vimekwenda wapi? Maana havipo! Ilikuwa fursa kubwa kwa watu wa Mtwara- Mikindani na maeneo ya Uwanda wa Pwani kwenda kununua vifaa vya uvuvi pale kwa sababu kulikuwa na viwanda pale. Leo tunapozungumza, hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshauri Mheshimiwa Waziri, kwa nafasi yake, najua anaweza; leo wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji wakubwa kama Bakhresa anatengeneza juice. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge, juice bora kabisa yenye Vitamin C ambayo haina shaka kabisa, inatokana na Mabibo ya Korosho. Sasa Mheshimiwa Waziri amshauri mwekezaji yule mkubwa aje Tandahimba pale na Halmashauri inaweza ikampa eneo tu la kutosha aweke kiwanda pale atengeneze juice ya matunda na Waheshimiwa Wabunge wapate vitamin ya kutosha hapa kwa ajili ya mustakabali wa afya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, japo kuna wakati walikuja wawekezaji kadhaa na nimwombe Mheshimiwa Waziri ili alifuatilie, ajaribu kuwasiliana na Profesa Aba Mpesha aliyepo Marekani. Wapo wawekezaji wazuri na najua ana mawasiliano nao mazuri, wako tayari kuja kujenga viwanda vya kubangua korosho Tandahimba, lakini kuna watu wanaleta chenga pale katikati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwamini Mheshimiwa Waziri, ni mtu muhimu sana na mara zote huwa nawaambia, mkiwa mnafanya mambo mazuri Watanzania wakayaona, watawapongezeni. Kwa mfano, Kusini ambako viwanda hatuna, barabara hakuna, kila kitu hatuna; umeme shida, maji balaa! Mtakaa mkitegemea CCM mtachaguliwa kwa matatizo haya? Hebu mje mmalize haya matatizo kwanza; myamalize haya mambo! Msije mkafanya Kusini kama scraper.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazungumzaji wamezungumza hapa, wakati tunazungumza hata suala la reli ile ya kutoka Liganga, ni stori tu. Stori hizi siyo kwamba zimeanza kwenye Serikali yenu. Nimesoma bajeti kipindi cha Awamu ya Nne, kuanzia 2010 historia hiyo ipo kwenye makabrasha; 2011/2012 ipo kweye makabrasha; 2012/2013 ipo kwenye makabrasha; 2014/2015 kwenye makabrasha; mwaka jana (2016/2017) tumepiga makabrasha kwenye Wizara hii; mwaka huu, tumeizungumza tena. Ile ilikuwa inatoa fursa kwa watu wa Kusini kule kote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Mtwara ingefunguka kwa kiwango kikubwa. Mikoa hii ya Kusini; Mbeya, Ruvuma, Njombe, watu wangefanya kazi na ajira hizi ambazo leo Tanzania ambako kuna bahati mbaya kwamba watu wake hawaajiriwi, eti kwa sababu hawawezi Kiingereza, lakini ukienda Dangote pana Wachina sijui 700 na hawajui Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya viwanda, kwanza huu utaratibu huu wa Kiingereza, wakija Wachina wasiojua Kiingereza wanaajiriwa na Kiswahili hawajui, wanaajiriwa; Watanzania wenyewe wanakosa fursa kwa vitu vya ajabu ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana, mimi namwamini sana Mheshimiwa Mwijage, nakuamini sana. Namwomba sana aone mambo haya anayafanyia kazi kwa uzuri ili at least watu wa Tandahimba na wenyewe wakipata kiwanda cha juice pale, wakipata viwanda vidogo vile ambavyo Profesa Aba Mpesha, tayari ana wawekezaji mkononi, watu wale watapandisha thamani ya korosho zao, watapandisha thamani ya mabibo, yale ambayo badala ya kuanika tukapika gongo, tutakunywa juice watu mkapata vitamin C na mambo yakaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono hoja ya baadhi ya wachangiaji waliotaka tuongeze tozo kwenye mafuta kwenye jambo hili la maji. Hata hivyo nisikitike sana wakati nasoma hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, nimeona alichokifanya mwaka huu ni ku-copy na ku-paste tu kwenye Mradi wa Maji wa Makonde. Kile kilichoandikwa mwaka jana ndicho alichokiandika leo, na pesa zenyewe zinazozungumzwa ni pesa za kutoka kwenye Basket Fund.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tume-fail na jambo hili la Mradi wa Makonde na kumbuka mradi huu Mheshimiwa Waziri unahudumia Wilaya takribani nne, majimbo matano ya Newala, Tandahimba, Nanyamba, Newala Vijijini, ni mradi huu tunaozungumza. Mwaka jana mmeweka bajeti hii ya Euro milioni 87 ambazo mlisema mnakopa kutoka India, lakini mwaka huu mlichokiandika mwaka jana ndicho mlichokiandika mwaka huu. Watu wetu watatuamini vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana mwaka jana tumewaeleza Serikali imetenga dola bilioni 87 ambazo hazijatekeleza chochote kile. Mwaka huu tunarudi Majimboni mwezi wa saba tunakwenda kuwapa scenario ile ile ya mwaka wa jana, wanataka kutuamini nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Rais alivyokuja Jimboni kwangu Tandahimba miongoni mwa ahadi alizokuwa ameahidi ni pamoja na kuona kwamba Watanzania wanaondokana kabisa na tatizo la maji. Mheshimiwa Naibu Waziri umefika Tandahimba, vizuri sana, umeona unapofika mwezi wa sita, wa saba, ndoo moja ya maji mpaka shilingi 2,000 hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amefika Tandahimba, Tandahimba hakuna tatizo la vyanzo vya maji, Mto Ruvuma ni kilometa 15 tu kutoka Wilayani lakini kuna kata ambazo ni kilomita 8 tu kutoka Mto Ruvuma maji yamejaa. Ukienda kata za Mihambwe, Mchichira, Mahuta, Kitama pamoja na Tandahimba Mjini kote kuna vyanzo vya maji, lakini watu wake hawana maji. Ukiangalia hotuba yako hii vizuri, hii uliyoiandika, mijini mmetengenezea pesa za kwenda kule tena pesa za ndani. Mijini ambako matatizo ya maji si makubwa kama vijinini. Lakini kwenye mradi ule wa Makonde mmetenga shilingi bilioni moja. Tena fedha za nje hizo hizo kwa ajili ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule una zaidi ya miaka 30, miundombinu yake imechakaa, na Mheshimiwa Naibu Waziri unajua. Pesa zenyewe tunazotengea ni hizo hizo za nje. Sasa kuna u-serious kweli kwa watu wale wa Kusini, watu wale wa mradi wa Makonde kweli kupata maji? Sasa mje mtusaidie hapa, mnapopeleka maji mijini ambako at least asilimia 72 wana maji vijijini kule, mimi jimbo langu lina kata 31 katika majimbo makubwa kabisa, na umbali kutoka kata moja na nyingine ni umbali wa kilomita 15 kilometa 16, watu wana shida ya maji.

Mheshimiwa Mwneyekiti, mimi naomba tena ikiwezekana tunapomaliza bajeti Mheshimiwa Waziri uje mwenyewe uone kutoka Mkwiti kwenda Tandahimba watu hawana maji watatembea umbali gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kata za Luagalo, Chaume pamoja na Nambahu kuna shida ya maji; kila unakotembea Tandahimba kuna shida ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana mnapotengeneza bajeti hizi nadhani watu wa nishati walifikiria mpango mbadala wa nishati vijijini (REA), na ninyi watu wa maji sasa tuwe na jambo la mbadala la maji, vijijini kwa sababu ndiyo sehemu ambako kuna waathirika wakubwa wa tatizo la maji. Badala ya kukaa hapa tunazungumza vitu vingine suala la maji liwe priority kwa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ni waombe tu walizungumza wazungumzaji hapa wakizungumza kwenye mafuta. Mimi niombe watu wanakunya bia kweli kweli; bia zinanyweka kweli kweli, tusitegemee chanzo kimoja tu cha mafuta kwenye kule tuweke shilingi shilingi mia, mia au shilingi mia mbili kule ili itusaidie mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niendee kusikitika sana; bajeti ya mwaka jana ambayo imetekelezwa kwa kiwango kidogo sana na bajeti hii ya mwaka huu ina utofauti mkubwa sana na mimi napata shida na sijui Waheshimiwa Wabunge wenzangu wanaposhauri hili jambo kwamba tuongeze bajeti; kama ya mwaka jana tulishindwa kuitimiza mwaka huu tukasema tuongeze, mimi nidhani bajeti hii iliyokuwepo sasa tuone vyanzo vyake vya pesa vinakamilika na tusitegemee vyanzo vya kutoka nje.

Haya tuliyoyaomba kwenye mafuta, kama alivyozungumza Mheshimiwa Mwenyekiti wakati alipotoa ufafanuzi mwanzo kuhusu suala la maji kwamba mtakapokaa kwenye kile kikao cha bajeti mtakapokuja hapa na majumuhisho basi tuone kwenye mafuta tumeongeza shilingi mia kwenye bia tumeongeza shilingi mia mbili. Tuongeze ongeze ili tatizo la maji Tanzania liwe limekwisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jana nilikutumia ki-note hapa kidogo, ki-memo nikiwa naomba ili tuwasaidie Wizara tulisaidie Taifa, sisi tumeomba Mamlaka ya Maji Tandahimba kwa vyanzo vya maji tulivyokuwa na mapato yetu haya ya korosho na ikitokea na Serikali ikakubali kutupa asilimia tano ya bei ya soko maana yake ni kwamba tunaweza tukaisaidia Serikali Tandahimba kukawa hakuna tatizo la maji. Sasa niombe tu barua zetu kwa sababu tumeshapeleka TAMISEMI kama ulivyoniambia kwamba nipeleke TAMISEMI, tulishapeleka na walitupa majibu kwamba wameshaleta dokezo kwenu; kwa hiyo tatizo liko kwenye Wizara yako; ukaangalie makabirasha yako vizuri. Kama Tandahimba tutapata Mamlaka ya Maji tukapokuja mwaka kesho kutwa hapa tutakuwa tunazungumza lugha nyingine nzuri kidogo kwenye jambo la maji. Vilevile niendelee kukuomba Mheshimiwa Waziri Tandahimba pale nishukuru sana ulitupa pesa ambazo zingeweza kusaidia kuweka mashine ya pump pale Tandahimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bahati mbaya nyingine kubwa mmetupa engineer wa maji wa Wilaya tuliyokuwa naye miaka zaidi ya tisa hakuna maji Tandahimba na mambo mengine ya ajabu sana tumewahi kumpa pesa mpaka za Halmashauri pale kuweza kujenga pump pale maji hayatoki. Watu wa utumishi walimpa transfer ya kumwondoa Tandahimba aende sehemu nyingine kwa sababu ana muda mrefu, lakini mmefanya lobbing mmerudisha tena pale, yaani maana yake mnamleta engineer ambaye mnajua hawezi kusimamia mambo ya maji, mnamuacha pale tuendelee kupata shida watu wa Tandahimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nakuambia Mheshimiwa Waziri kuwa engineer yule mliyemleta tukimaliza Bunge mkiendelea kumuacha pale na sisi hatuna maji tutamwondoa sisi kwa maandamano makubwa kabisa. Nazungumza kwenye Bunge hili, tutamwondoa kabisa kabisa. Haitawezekana anapewa pesa; kuna mradi wa maji amekuja Naibu Waziri wa TAMISEMI; Mheshimiwa Selemani Jafo, unazinduliwa mradi wa maji ambao inatoka hewa badala ya maji, na manasema mradi umekamilika. Mradi unakamilikaje ikiwa maji hakuna na mnauzindua na mnasema tumekabidhi mradi tayari na ikiwa mamiolioni ya fedha Watanzania mmelipa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja Mheshimiwa Selemani Jafo pale Mahuta, amezindua mradi ule wa maji wa Mkupete, umezinduliwa mradi hewa, watu wa Mkupete hawana maji, hata Mheshimiwa Waziri ukija mradi ule mmetumia mamilioni ya pesa maji hayatoki. Bado mnataka engineer yule tukae naye, anazindua miradi ambayo haina maji na viongozi mnakuja na mnasema mradi umezinduliwa, maji hakuna tunakaa na engineer kama yule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunahitaji engineer ambaye atatoa matokeo chanya ya maji. Hata ukatuletea profesa na ma-degree manne matano saba mkasema huyu ndiye professor wa maji na maji hatuyapati. Sisi wana Tandahimba tunasema huyu ni profesa uchwara tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji mtuletee mtu anayetupa maji na si kutuletea vyeti tu na vyeti vyenyewe ni vya hewa na tunaona balaa lake hili. Kwa hiyo, tunahitaji mtu mwenye capacity ya kule maji. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kule kwetu uje, ile sehemu imekuwa ni sehemu ya mwisho kwenye kila jambo. Barabara mwaka jana mmeona walivyotufanyia, wametenga kilometa 50 mpaka leo tunapozungumza tunapozungumza ni story. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa isiwe watu wa Kusini ni watu wa story tu, tumeshateseka kwa muda mrefu kusini tulishasahauliwa muda mrefu, kwa hiyo kwenye priority ya mambo haya, mnaposema maji tengeni maji pelekeni Kusini ili na sisi tujione ni Watanzania na tuna haki sawa na Watanzania wengine badala ya kutupa miradi tunarudi majimboni tunaisifia Serikali, maana unavyoleta kabrasha hili ninapokwenda mimi ninawasomea wananchi pale. Nasema safari hii bwana Serikali imetenga dola bilioni 87 saba kwa ajili ya maji, watu wanashangilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na bahati mbaya Makamu wa Rais alikuja Tandahimba mwaka wa jana akawahakikishia watu wa Tandahimba kwamba tumepata pesa mtapata maji, maji hakuna. Haya mnayoyafanya ndiyo kaburi la Chama cha Mapinduzi maka 2020 haya. Haya mnayoyafanya haya msije mkaleta mabomu, watu hawana maji hawawezi kuchagua CCM wakati haitekelezi mahitaji yake, hawawezi, msije mkatafuta labda akina Nape wanasema hivi sijui
…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kukushukuru kwa kunichagua lakini na mimi nichangie hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa namna ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kupunguza makato kwa wakulima lakini bado napata shida sana. Wakati Serikali inakusanya asilimia 15 mfano kwenye zao la korosho kama ushuru wa Serikali ile export levy, kwa bei ya mwaka jana ambapo tumeuza korosho kwa shilingi 2,990 tozo tu ya Serikali inakuwa ni shilingi 448.5. Leo tunasema tunataka kumsaidia mkulima huyu kwa kupunguza tozo lakini kuna tozo kubwa hii ya Serikali ambayo matumizi yake yamekuwa ni holela sana wakati mwingine hayana maelezo ambayo yanajitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kuangalia mgawo wa export levy ambayo tunaipata kutoka Serikalini unakutana na asilimia tano inakwenda mkoani pamoja na wilayani ambayo wanatumia tu Wakuu wa Mikoa bila kujali maslahi ya wakulima wenyewe, kuna asilimia 20 ya ubanguaji inakwenda huko. Ukiangalia asilimia 20 ya ubanguaji Serikali hii ya CCM miaka ya 1970 na 1980 mlikopa fedha nyingi sana kutoka Japan na Italy, mkajenga viwanda vya ubanguaji wa korosho Mtwara, Lindi, Newala, Tandahimba lakini leo vile viwanda mmeviuza kwa bei chee, bei isiyoelezeka na bado tunaendelea kulipa deni kwa Wajapan hawa. Sasa kama mna nia njema, leo mnakata asilimia 20 kwa ajili ya ubanguaji wakati viwanda mmegawana wenyewe, mimi sioni u-serious wa Serikali hii ya CCM na msipoangalia tuna take off mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na suala wenzangu wamelizungumza sana, la vyama vya ushirika. Kwangu Tandahimba ambayo ndio wazalishaji wakubwa wa zao la korosho hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kumekuwa na mfumo mbovu wa Wizara ya Kilimo, katikati yake kuna Bodi ya Leseni pale ambao ndiyo wanawapa leseni waendesha maghala, leo ukija Wilaya ya Tandahimba wakulima wanadai zaidi ya shilingi bilioni saba kutokana na upotevu wa korosho zao kwenye maghala, lakini Serikali hii ndiyo inatoa dhamana kwa waendesha maghala. Mwendesha ghala anapewa ghala lenye thamani ya shilingi bilioni 15 za korosho za wakulima lakini security yake ni shilingi milioni arobaini. Kwa hiyo, korosho ya mkulima inapopotea hakuna anayeweza kumfidia kwa sababu hata dhamana ambayo ameweka yule warehouse operator ni ndogo kuliko korosho zinazopotea na Serikali hakuna hatua inayochukua kwa watu hawa. Mimi niombe wakati mnafanya windup ya mambo yenu, tuone namna gani wakulima wa korosho ambao wanaendelea kudai wanaweza wakafidiwa na Serikali kwa niaba ya warehouse operator walioko kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmekuwa na mipango mizuri ya Serikali yenu, lakini utekelezaji wa mambo ni mbovu. Mmeendelea kuwasomesha watoto wa Kitanzania kwa ngazi ya cheti kwenye vyuo vyetu vya kilimo vya Naliendele na Ilonga pale Morogoro, kuanzia mwaka 2010 mpaka 2013 lakini vijana wale wako mtaani wakati vijijini na kwenye kata hatuna Maafisa Kilimo, mnakaa mnasema mnataka kukiinua kilimo. Tuna vijana zaidi ya 4,000 wako mtaani wametumia fedha za Serikali, vyuo vile mmewasomesha bure wale vijana kwa ngazi ya vyeti, diploma lakini mwisho hawana ajira halafu tunakaa tunalalamika hatuna wataalam wa kilimo, mko serious kweli Serikali ya CCM?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri mwenye dhamana muone namna gani wale vijana ambao wamekaa muda mrefu mtaani mnawasaidia kuwapa ajira kwa ajili ya kwenda kusimamia sekta ya kilimo kama kweli tuna dhamira njema ya kulitoa Taifa hapa lilipo kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza suala la vyama vya ushirika, hata sheria mnazozitunga, kama mlivyofanya mambo ya uteuzi wa Mawaziri wakawa hawana instrument hata kwenye ushirika mambo yako hivyo hivyo. Mmetunga sheria mkataka makatibu wa vyama vya msingi angalau wawe kidato cha nne, lakini Tanzania nzima makatibu hawa wa vyama msingi ni wa darasa la saba hata hesabu hawawezi. Tuna vijana ambao wamemaliza kidato cha nne kwenye shule za kata mlizoanzisha wanaweza kunyambua hesabu hizi, mmewaacha mtaani kwa ajili ya kuwa na watu ambao wanakibeba Chama cha Mapinduzi. Maana wakati mwingine pesa hizi zinapotea kwa ajili ya watu mnaowaweka kwa ajili ya kusaidia CCM. Sasa watumieni wasomi hawa ambao wamemaliza kwenye shule hizi za kata ambazo mmezianzisha wawasaidie kwenye sekta hii ya ushirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu Tandahimba leo ukija kwenye ushirika hata watu mnaoweka kwenye ushirika hawa Warajisi ni miongoni mwa wala rushwa wakubwa, kabisa. Chama cha ushirika ambacho hakina uwezo wa kukusanya hata tani 50 lakini kinasajiliwa kutokana na mianya mikubwa ya rushwa. Mfanye tathmini na mje Mtwara, tutawaambieni na tutawatajia na majina. Kwa sababu unapokisajili chama kwa rushwa kwa kutumia shilingi milioni 10, 15 ambapo fedha zenyewe wanachukua kwa riba, mtu anachukua milioni 10 kwa milioni 20 kwa ajili ya kusajili chama cha ushirika lakini anakusanya tani 50 ushuru wake haumtoshi kulipa deni mwisho wa siku mkulima anakatwa pesa yake kwa sababu pesa inaingia kwenye chama cha msingi.
Niiombe Serikali na niishauri Wizara kama mna dhamira ya dhati muangalie sana jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe Wizara ya Kilimo, kuna suala la asilimia tano ya ushuru wa halmashauri. Ukisoma sheria wanasema ile asilimia tano tutaipata kutokana na market price lakini la ajabu leo sisi hatupati asilimia tano kutokana na market price. Wilaya kama ya kwangu ya Tandahimba mngekuwa mnatupa asilimia tano kutokana na market price kuna uwezekano mkubwa hata matatizo ya barabara tungeweza kutatua wenyewe. Hizi pesa mnazowapa Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya hebu turejesheeni halmashauri ili tuendeleze Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, sitaunga mkono hoja mpaka nione majibu haya ya msingi na mambo haya mmeyaweka sawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru, nikiendelea kwa yale aliyoachia ndugu yangu Khatib, ninalo jambo la kuzungumza juu ya Jeshi la Polisi. Page ya 12 wamezungumzia suala la kuboresha Mfumo wa Upelelezi wa suala la kesi za jinai. Hili jambo ni jambo jema sana kama mfumo utafanya kazi inavyopaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo yanaleta mkanganyiko sana. Tarehe 8 Agosti, 2015 Jimboni kwangu Tandahimba wamechukuliwa watu takriban tisa. Watu wenyewe wengi wao ni Masheikh. Bahati mbaya wamepelekwa Dar es Salaam wameingizwa kwenye kesi ya mauaji tena kesi yenyewe Polisi wanafika pale Oysterbay wanauliza watu hawa tuwape kesi gani. Ndiyo maana mpaka leo kesi ipo mahakamani ushahidi mpaka leo haujakamilika. Haujakamilika kwa sababu yaliyofanyika ni uonevu unaotokana na jeshi la polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano yupo mtu anaitwa Mbaraka, Mbaraka tarehe ambayo amebambikiwa kwenye kesi ile ya mauaji ya Ikwiriri, hatupendi kuona Polisi wakiuliwa, Mbaraka alikuwa kwenye kikao cha TANEKU Newala, siku ya pili ameshiriki kikao cha kamati ya shule, amelala kwenye msiba, lakini unamkamata mtu unamwambia kwamba amehusika kwenye kesi ya mauaji ya Ikwiriri. Huu ni uonevu wa Jeshi la Polisi ambao hauna mfano kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ya ajabu kwa jeshi tunalolitegemea. Naamini IGP Kamanda Sirro anafanya kazi nzuri kwenye kudhibiti uhalifu. Kwenye kuonea watu hawa ambao hawana hatia ni mambo ya ajabu sana, wanalidhalilisha Jeshi letu la Polisi bila sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu leo wana miaka takribani mitatu au minne na kesi zao zilishawahi kwenda kwa Waziri aliyekuwa wa Sheria kipindi hicho akasema anashughulikia, lakini mpaka leo watu hawa wanakwenda mahakamani wanarudi, ushahidi bado haujakamilika. Ni lini ushahidi utakamilika? Wanawapaje v ifungo Watanzania ambao hawana hatia kwa sababu ushahidi haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana, Jeshi la Polisi tunalolitegemea, wanapoamua kufanya kazi zao wafanye kwa weledi. Nami naamini kabisa Jeshi la Polisi wapo watu wana uzoefu, wana uzoefu na upelelezi. Hizi tamaa za fedha, maana matukio haya kwa Mtwara yamekuwa yanafanyika kwa ajili ya tamaa ya fedha. Wapo watu wameuawa, wapo watu wakitoa fedha milioni mbili, milioni tatu wanaachiwa, kama kweli wangekuwa wauaji wasingewaachia basi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, leo wiki ya pili wamekamatwa watu wangu Tandahimba kule, Kijiji cha Mihambwe. Tandahimba mpaka wetu wa Tandahimba na Msumbiji ni Mto Ruvuma. Tandahimba hakuna tembo, Tandahimba hakuna mali hizo zinazosemwa watu wale wamepelekwa polisi inasemekana kwamba wanauza meno ya tembo. Meno ya tembo Tandahimba yanatoka wapi? Maana siyo Liwale Tandahimba, mwisho wa siku wanatoa 2,500,000 hawana kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo Jeshi la Polisi wanajidhalilisha bila sababu za msingi. Hata hivyo, inawezekana haya mambo yanafanyika kwa sababu ya vipato vidogo vya Jeshi letu la Polisi. Kama wangekuwa wanawapa mafao yanayofanana, nadhani wasingekuwa na tamaa na fedha hizi ndogo ndogo hizi. Kwa hiyo, niwaombe sana kwenye kuboresha maslahi ya jeshi la Polisi labda watafanya kazi kwa weledi, basi waone namna gani wanapata maslahi yaliyo bora ili watu wetu waweze kufanyiwa mambo yao kwa utu na kwa kutumia haki za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la udhibiti wa uhalifu nchini; nimpongeze IGP na jeshi lake kwa sasa suala la uhalifu limepungua kwa asilimia 90. Mimi nilipongeze sana Jeshi la Polisi nchini. Hata hivyo, kwenye matukio haya wapo wezi ambao wanaiba pikipiki Dar es Salaam, wanapeleka Mtwara, wanapeleka maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zile pikipiki wanatengeneza kadi feki unapotoa pikipiki Dar es Salaam ina kadi feki ukapeleka Ngara, mtu wa Ngara hawezi kubaini kadi feki. Anauziwa pikipiki yenye kadi feki ambayo ukiangalia document zinaonesha zinafanana na mwisho wa siku anakamatwa mtu wa Ngara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, operation yao wanayofanya kwa ajili ya wezi hawa, naamini kabisa kwamba IGP Sirro wanaweza wakawabaini watu hawa ambao wengi wao wanatoka Dar es Salaam na wizi mkubwa wa pikipiki unafanyika Dar es Salaam. Badala ya kwenda kukamata watu wetu ambao wanateswa mwishoni japo wanasema na waliowauzia pikipiki akina nani? Hata hivyo, wanashindwa kuwakamata waliouza pikipiki wanakwenda kwa watu wa hali ya chini wale, badala ya kuchukua pikipiki wazi-hold, wale watu na wenyewe wanaendelea kuwatesa bila sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye suala la mipaka, kwenye Idara za Mheshimiwa Waziri kwa maana ya Wizara yake ya Mambo ya Ndani afadhali Jeshi la Polisi wana vitendea kazi vya kutosha, japo havitoshi kwa kiwango hicho kinachoridhisha, lakini wapo watu wanafanya kazi kubwa ndugu zetu wa uhamiaji. , maeneo ya mipakani ambapo watu wa uhamiaji wapo hawana vitendea kazi, hawana magari, lakini hata OC zao hawazipeleki, watafanyaje kazi watu hawa wa Idara hii ya Uhamiaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mtwara wanajua tunapakana na Mto Ruvuma pale. Watu wa Uhamiaji ni watu ambao wanapaswa wawe na magari kwa ajili doria na vitu vingine kule, lakini leo hawana magari; lakini OC hizi za milioni moja moja tunazosema wakienda kuangalia Uhamiaji wamepeleka lini wataona aibu wenyewe. Waende wakaangalie wataona aibu wenyewe! Wawapelekee OC hizi waweze kufanya kazi kwa ufasaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye kuboresha maslahi ya ndugu zetu hawa wa Uhamiaji ambao wanafanya kazi kubwa sana. Wanafanya kazi kweli kweli, amepata kuzungumza Mzee Ally Keissy pale kwamba zamani kulikuwa na passport zinapatikana kwa raia ambao hata sio Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu wanatoka Burundi wanafanya ujanja ujanja wanapita Tanzania wanapata documents, wanaenda South Africa ndio wanauza madawa ya kulevya akikamatwa kwa sababu ana document ya Tanzania, anaonekana ni Mtanzania. Uhalifu huu umefanywa katika maeneo mengi wakitajwa Watanzania kumbe sio Watanzania ni Wanyarwanda wengine ni Warundi, wanafanya matukio haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuimarisha mifumo hii, Idara yetu ya Uhamiaji ni lazima waipe nguvu ya kutosha, waweze kufanya kazi zao vizuri ili tuweze kuimarisha mazingira haya na kuondoa maneno yanayotajwa Tanzania kumbe sio Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumwambia tatizo la Askari wetu wa Usalama Barabarani hususan Tandahimba, lakini hata alipokwenda Waziri Mkuu wananchi wameweza kuonesha mabango pale. Jeshi la Polisi Usalama wa Barabarani kuna tatizo gan? Kwa nini askari wa usalama barabarani apige mtu viboko ndio sheria inavyotaka, ndiyo PGO ilivyoandikwa ndani humo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa yametokea matukio ya Tandahimba zaidi ya matatu au manne hata akisema Mheshimiwa Waziri tuondoke au IGP twende atakuta vijana wamepata ajali kwa sababu DTO anachomeka gari yake anamchomekea bodaboda na sio mara moja au mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yametokea matukio zaidi ya mara tatu, mara nne, kwa ajili ya ustahimilivu ya watu kuheshimu Serikali, vinginevyo wangeamua kuchukua sheria mkononi, wao kwa sababu wana silaha za moto wanasema wananchi ndio wenye matatizo, kumbe matatizo mengine yanazalishwa na Jeshi la Polisi lenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Tandahimba tatizo kubwa ni DTO peke yake, askari wengine wa usalama barabarani wanafanya kazi kwa weledi, yeye ndiyo anafanya matukio haya ya ovyo na siyo mara moja au mara mbili, Mheshimiwa Mwigulu nimeshamwambia zaidi ya mara tatu jambo hili. Waziri Mkuu amekwenda kwenye ziara Tandahimba amekutana na mabango, bahati mbaya mimi sikuwepo nilikuwa Ubelgiji huko, amekutana na mabango watu wakilalamikia hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama wanampenda sana DTO wambadilishe hata kituo wachukue Mheshimiwa Mwigulu wapeleke kwake pale, akawafanyie watu wake aone uchungu atakaoupata. Atajua wapiga kura wake wakipigwa, mtu amekosa kuvaa helmet kweli amefanya kosa ni sahihi apigwe viboko na DTO? Ni sahihi achomekewe gari na DTO? Kwa nini DTO wa Tandahimba avunje sheria na Jeshi la Polisi lipo, Waziri anajua bado tunaendelea kukaa naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi bwana ni wanadamu kweli kweli na tuna utu kweli kweli, wakati mwingine ukionewa sana utakapoamua kunyanyua mguu, aliyenyanyua mguu ataonekana mkorofi. Hatutaki watu wa Tandahimba tufike huko. Najua wana busara za kutosha, IGP yupo anasikia, Waziri nimemweleza jambo hili zaidi ya mara tatu, lakini wameendelea kumwacha yule bwana, aidha kuna jambo wanalitengeneza Tandahimba, aidha utokee ugomvi baina ya polisi na raia kwa sababu wana bunduki wapige watu wa Tandahimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana mtu mmoja asisababishe amani ya watu wa Tandahimba wote. Miaka miwili mfululizo Tandahimba hatufanyi biashara kwa uhuru pale. Watu wanakwenda Newala ambako kuna unafuu Traffic hawatumii nguvu kubwa wanakwenda kununua bidhaa kule, tunaiacha Tandahimba ikididimia pale kwa ajili ya mtu mmoja ambaye anafanya watu washindwe kuingia Tandahimba kwa kutofuata sheria.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. KATANI A. KATANI. Mheshimiwa Spika, nikushukuru na niombe tu kwa namna unavyoendesha mjadala kwa siku ya leo ingewezekana ungekalia kiti siku zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo la maji linalozungumzwa ni tatizo la kitaifa, na kaka yangu Mheshimiwa Chikota wakati anachangia amejaribu kuzungumzia Mradi wa Maji wa Makonde, mradi ambao uliasisiwa mwaka 1953 katika Wilaya ya Newala, mwaka 1953 ilikuwa bado haijawa Wilaya maana Wilaya ya Newala imepatikana mwaka 1954 Mzee unajua. Mradi huu wakati unasisiwa ulikuwa unahudumia wakazi 82,000 tu; leo tunapozungumza Newala kuna watu zaidi ya 205,000, Tandahimba kuna watu zaidi ya 227,000. Nanyamaba ambako mradi unatakiwa uende kunazaidi ya watu zaidi ya 60,000.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ukiangalia mradi huu kwa sasa, unahudumia watu zaidi ya laki saba. Hata hivyo mradi huu ukiuangalia kwenye bajeti, kuanzia mwaka 2016/17, 2017/2018 na mbaya zaidi tarehe 10 Septemba, 2016, mimi nilikuwa na Makamu wa Rais Tandahimba pale, amewaambia watu wa Mtwara kwa maana ya Newala, Tandahimba na Nanyamba kwamba Serikali imetenga shilingi bilioni 170 kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Makonde.

Mheshimwa Spika, mpaka leo hii tunapozungumza ukiangalia kwenye makabrasha fedha iliyotengwa mwaka huu 2018/2019 ni shilingi bilioni moja. Sasa kuna majibu gani kwa wapiga kura wale wa maeneo ya Mtwara? Kuna maelezo gani ambayo yatawafanya watu wale waiamini Serikali ya CCM? Na tatizo la maji ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, nimewahi kumwandikia barua, message zaidi ya tatu au nne Mheshimiwa Waziri, lakini mara ya mwisho hata Naibu Waziri nimewahi kumwambia, kwangu Tandhimba kuna Mradi wa Maji ya Mkwiti ambo unatekelezwa kwenye lot nne; lot ya kwanza mwaka 2016/2017 mkandarasi ameshasaini mkataba na tayari ameshapeleka bomba zenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 1.4, advance payment hajapata, ameandika certificate ya pili ya kuomba shilingi bilioni 1.1 hajapata, Mheshimiwa Spika, tunaingia kwenye bajeti nyengine wakati mkandarasi ameshapeleka vifaa tayari lakini yeye hajalipwa hata advance payment na ukiusoma mkataba baina ya Mkandarasi na Halmashauri, advance payment inapaswa ndani ya siku 28, leo tunaozungumza toka mwezi Februari fedha hii haijatoka.

Mheshimiwa Spika, sasa sijui Waziri wa Fedha, maana niliuliza watu wa Wizara ya Maji wanasema taratibu zote zishakwenda Wizara ya Fedha, sasa sijui Wizara ya Fedha inauwezo ya kupata fedha ya kujenga viwanja vya ndege bila ya kutoka kwenye bajeti, ya kununua ndege bila ya kuwepo kwenye bajeti lakini hawana uwezo wa kulipwa fedha ya maji ambayo ipo kwenye bajeti, sijui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii sijui watu tunawaonea aibu Wizara ya Fedha, lakini kuna mambo mengi wanakwamisha ambayo hayana msingi kabisa. Wana uwezo wa kutafuta fedha za maneuver kwa kutengeneza vitu ambavyo haviko kwenye bajeti vya kwenye bajeti hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona mwaka jana Wizara ya Maji asilimia 22 tu ya fedha za maendeleo ndizo zimeenda; lakini ipo miradi zilitengwa pesa shilingi bilioni 35 zilmelipwa pesa zaidi ya shilingi bilioni 42. Kumbe mijitu hii ina pesa za kutosha kwa nini kwenye miradi ya maendeleo kama ya maji ambayo ndio uhai wa Mtanzania zisiende fedha hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana, dada yangu Ashatu Mheshimiwa Waziri sijui ametukimbia hapa, alitakiwa hapa alitakiwa awepo mwenyewe, kwa sababu yeye ndio mshauri wa mambo ya fedha kwa Rais na kwa Baraza la Mawaziri. Atuambie kama mna fedha za kufanya mambo mengine, lakini hamna fedha za kutatua tatizo la maji ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mtu alikuwa anachangia kwa kujipendekeza, mimi sijui kama Wabunge tuko Serious na Taifa letu, mtu anazungumza suala la bomba la maji mita 400? Mheshimiwa Waziri umefika Tandahimba, ukitoka Mkwiti kwenda Tandahimba kilometa 61 niambie wapi uliliona bomba? Halafu uniambie mita 400?

Mheshimiwa Spika, kilometa 61 mpaka unafika Wilayani hakuna bomba, anakuja mtu wa CCM anasema maji mita 400; mita 1000 hakuna bomba utazungumza mita 400? Tuwaonee huruma akina mama hawa, tuwaonee huruma Watanzania hawa kila anayesimama anazungumza wazi kabisa kwamba bila ya maji hakuna kinachoweza kuendelea, hivyo viwanda tunayoyasema kama bila ya maji hakuna viwanda, hili Bunge tunalolisema kama hatukuoga maji hatuwezi kuingia Bungeni, mbuzi tunaofunga, ng’ombe tunaofuga kama hawakunywa maji watakufa tu.

Mheshimiwa Spika, niombe sana nyie watu wa fedha mnakwamisha mambo mengi sana. Huyu mkandrasi wa kwangu sasa tunataingia mwaka 2018/2019 fedha ya mwaka 2017/2018 hajapata mpaka leo. Sasa hatimaye tutamlalamikia nani? kama fedha hajapewa na amepeleka bomba za shilingi bilioni 1.4 ziko site. Maana si wakandarasi wababaishaji yeye bomba ameshapeleka site, advance payment hajapata, hizo fedha za certificate ya shilingi bilioni 1.1 hajapewa. Kwa hiyo tatizo liko kwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Spika, Sasa kwa sababu jambo la maji umeliona ni jambo la msingi sana, moja mimi siwezi kuunga mkono hoja ya bajeti ya Wizara hii na ninaamini Wabunge wote kwenye shughuri pevu itatokea kwenye Wizara ya Maji, mimi ninaamini hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo miradi ambayo nataka Mheshimiwa Waziri ikiwezekana mtusaidie, ipo miradi mnapeleka fedha mnakwenda kuzindua, mfano Mahuta pale, tulienda na Mheshimiwa Selemani Jafo akiwa Naibu Waziri, akaenda kuzindua Mradi wa Maji wa Mkupete ambao fedha zake zimeshalipwa. Ule mradi umezinduliwa mwaka 2016 mpaka leo tone la maji hakuna na mradi umezinduliwa, hizi fedha mnazopeleka mnapeleka kwa ajili gani? Kama mradi umekamilika na umezinduliwa na maji hakuna huu mradi unakwenda kwa nini?

Mheshimiwa Spika, hebu mtuambie miradi inaenda kwa nini? Mnasema imekalimika lakini maji watu hawapati huduma nini maana ya kukamilika? Tuambieni maana ya kukamilka kwa mradi, umeleta mradi unasema mradi umekamilika. Mradi huo hauna tofauti ukienda Mahea kuna mradi mwengine, kuna miradi wa Mahuta mmepeleka zaidi ya shilingi milioni 86, lakini miradi hii yote imekamilika lakini watu hawapati maji.

Sasa mtuambie mnaposema mradi umekamilika maana yake ni kukamilika tu kuona aidha mmejenga mabomba mmeweka mabwawa au kukamilika Watanzania wapate amaji? Tunaomba sana mtupe ufafanuzi wa jambo hili kwa uzuri sana.

Mheshimiwa Spika, lakini bahati mbaya ukilisoma book lenu hili Mtwara tuna bahati mbaya sana. Katika mikoa ambayo bajeti ya maji ni ndogo, ni mkoa wa Mtwara. Tatizo la Mtwara ni nini? Miradi mnayotupa hewa, tunaozungumza wamakonde fedha hakuna, Kaka yangu Chikota amezungumzia mradi wa Ruvuma fedha mpaka sasa hakuna. Tuna tatizo gani watu wa Mtwara?

Mheshimiwa Spika, mimi nilidhani Mheshimiwa Rais alivyokuwa amezungumza watu wa Kusini, alijua kwamba Kusini tumeachwa nyuma kwa muda mrefu na tutapewa priority sasa kwa kuona kwamba vitu vya msingi vinavyokuja basi Kusini lazima tuwapelekee na wao waone wananufaika na matunda ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mnajua wakati anatoa taarifa Mheshimiwa wa Liwale amezungumza, zipo fedha za wakulima haohao wa korosho zaidi ya shilingi bilioni 250 na kitu zimekwenda kwenye matumizi yasiyoeleweka, lakini watu wake hawana maji. Watu wa Mtwara wanachangia pato
kubwa kwenye Taifa hili. Kwa miaka hii miwili/mitatu mfululizo ukiangalia trends ya Mtwara kutoka kwenye zao la Korosho hawakuwa watu wa kulilia maji leo, hata siku moja.

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana, tumekuwa na ngonjera, mimi tangu nakua nimemkuta Mbunge wa kwanza ninayemjua, Mzee Nandonde, kila niliposikiliza hotuba yake alizungumzia suala ya maji, akaja Mzee Lutavi alizungumzia suala la maji, amekuja ndugu yangu Njwayo akazungumzia suala la maji, napita mimi nazungumzia suala la maji. (Makofi)

Mheshemiwa Spika, ebu nyie ndugu zetu wa CCM, mnisaidie jambo kubwa sana; kwenye mazingira yetu ya taifa letu kitu gani tutaweka kipaumbele kama si maji? Katika vitu vyote tulivyokuwa navyo maji nadhani ni jambo la msingi kuliko kitu kingine chochote. Kwa hiyo tuweke priority kwenye maji kwanza halafu tufanye mambo mengine; na tunauwezo kuamua tukasema kwamba mwaka huu baadhi ya bajeti fulani zisinde tuitekeleze bajeti ya maji…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka nianze kuchangia ripoti iliyotolewa hapa na Ndugu zetu wa PAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimu wa pamba wa mwaka 2019/2020 Serikali kama kawaida yake ilifanya yale ambayo yalifanywa kwenye msimu wa korosho mwaka 2019/2020. Bodi ya Pamba imekwenda kutengeneza deni la zaidi ya shilingi bilioni 102.5. Bodi ya Pamba kwa maelekezo ya Serikali ya kwamba wanunuzi wanunue tu pamba Serikali itawafidia, wanunuzi tu peke yake wanadai zaidi ya shilingi bilioni 21, lakini wazabuni wetu wa pembejeo, wazalendo, Watanzania wa ndani wanadai zaidi ya shilingi bilioni 80 na ilitamkwa la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka hapa kwenye korosho mlivyofanya maamuzi hivyo hivyo kwamba Serikali iende ikanunue korosho kule, madeni kwenye Serikali hii bado ni makubwa. Leo PAC wamesema hapa na walitoa mapendekezo ambayo mpaka leo watu hawa hawajalipwa. Nini kinataka kutokea? Projection yako Mheshimiwa Bashe Waziri wa Kilimo ya kwamba mwaka 2025 unakwenda kuzalisha pamba tani Milioni Moja, Mheshimiwa Katani nipo hapa! Ukizalisha hata tani Laki Saba mimi na Ubunge wangu nikakae Tandahimba kule. Ukizalisha tani Laki Saba nikakae Tandahimba kule nilime korosho. Hakuna projection ya hovyo namna hii! Wazabuni hamjawalipa fedha, benki ambako mnasema kwamba agricultural input mnakopesha single digit ya asilimia tisa, mnakopesha fedha kwa zaidi ya asilimia 14. Unasema unaenda kumsaidia mkulima! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mnasimama watu hapa, mimi nashangaa mnasema mnawasemea wakulima, mnalalamika bei imepanda, bei imepanda, bei ya vyakula iliyopanda mbona mkulima wa korosho ameuza korosho shilingi 1,700 hakuna aliyemtetea hapa, sijasikia! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima gani Wabunge wenzangu mnayemtetea, mnamtetea mlaji au mkulima? Hebu tujiangalie Wabunge wa Vijijini hapa. Nani anamtetea mkulima? Yupi anamtetea mkulima? Tunauza mazao bei ya chini kule ya mashambani, wanaoleta mchele Mjini hao ni wafanyabiashara tu! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamtetea mlaji hapa...

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa Kaka yangu Mheshimiwa Katani hapa kuwa ni kweli kwamba mkulima anatakiwa kulindwa, lakini sasa alindwe ahakikishe anauzwa kwa bei ambayo anapata faida. Nikupe tu taarifa kwamba kule kijijini kwetu Nyabiromo - Tarime debe la mahindi ni shilingi 10,000 ambalo halijakobolewa wala kusagwa, huku au ukienda mtaani au ukiuliza hapa Dodoma ni kati ya shilingi 22,000 mpaka Shilingi 28,000. Sasa huyo mkulima wa kule umemtetea vipi? Debe la mahindi ina maana kwenye kusafirisha tu ndiyo shilingi 15,000 difference?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Katani.

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake inaongezea nyama kwamba kweli mkulima kule hakuna anayemtetea, ndicho anachokisema na anathibitisha kile ninachokisema, nakushukuru sana na naipokea taarifa kwamba wakulima wa nchi hakuna wanaowatetea kwa kauli ya Mbunge pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwanza Wizara ya Fedha mpo hapa, hapa mnaposema single digit kwenye bidhaa hizi za kilimo, pembejeo na vitu vingine muende mkasimamie. Waziri wa Kilimo Bashe uende ukasimamie, hayo maporojo yako utakuwa na vision kubwa na utakuwa na mission kubwa kwa trend tunayokwenda nayo huwezi kufanikiwa nakuambia kaka yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hapa mwaka 2025 ukipata tani laki saba za pamba mimi Katani nabaki Tandahimba na Ubunge wangu nauacha huko huko, nakuhakikishia leo hapa, kwa trend hii tunayokwenda nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninyi Wabunge wenzangu mmewahi kulima kweli au ninyi mnadhani garden mzoweka nyumbani kwenu ndiyo kilimo kile? Umeweka maua kidogo na nini, mnadhani ndiyo kilimo kile? Rudini mashambani sisi tunakotoka wakulima mkajaribu kulima, mtamtetea mkulima kwa uchungu kuliko haya tunayoyafanya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashe hii itakwenda kukutafuna, mission na vision zako ziko vizuri sana, lakini kama hutakuwa na mkakati thabiti kwa sababu fedha huna, hapo unakaa unajitetea hela zinakuja, zinakuja ziko wapi? Wakulima watalalamika hawa! Ziko wapi? Ziko wapi zinakokuja, ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mnatudanganya watu wazima hapa mfumo, mfumo, miezi Sita hakuna cha mfumo hakuna cha nini! Hela hatuna, semeni! Mfumo! Mnatudanganya mfumo. Waziri hapa anafanya kazi kubwa, maminara mpaka Kilimanjaro huko, mfumo upi? Mkatudanganya mfumo! Tuambieni ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuambieni ukweli, tunataka tumsaidie Mama, kila anayesimama anaona kazi inayofanywa na Mheshimiwa Rais, lakini ninyi wasaidizi wake, fanyeni tathmini ya kina. Mimi nawaambia, fanyeni tathmini ya kina tunakwenda wapi! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo unapaswa umwambie mtu mdogo sana, Mheshimiwa Mwigulu Kaka yangu na rafiki yangu, umetutukana Wabunge sana. Mimi nakuambia! umetutukana Wabunge sana, unapaswa ukae, utafakari, hapa hakuna anayeweza kujadili waganga wa kienyeji hapa, hamna, hamna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya tunayojadili ni maisha ya Watanzania na tumeletwa Bungeni tuwasaidie Watanzania, hata wananchi wa Iramba kule wanataka uwasaidie Watanzania wa Taifa hili. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Kuhusu Utaratibu.

NAIBU SPIKA: Kuhusu Utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika....

NAIBU SPIKA: Kanuni?

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 71 na kama utaruhusu nisome.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maslahi ya muda ninaomba Mbunge anapochangia, Kanuni yetu inazuia kusema jambo la uwongo. Sasa Mheshimiwa Mbunge anapo-generalize kwamba mimi nimewatukana Wabunge, hiyo ni allegation kubwa sana ambayo Bunge lako haliruhusu na mimi nisingeweza kutukana Wabunge na Kiti kikiwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa heshima zote ningemuomba Mbunge anapochangia pamoja na hoja kubwa aliyokuwa anaijenga, aepuka generalization kama ambavyo amejaribu ku-twist ili kuweza kuweka uhalali wa hoja anayoiweka.

NAIBU SPIKA: Haya Kanuni zetu zinasema kabisa kuwa Kiti kitaamua kuhusu Utaratibu au kuhusu Mwongozo kujibu hapo hapo au baadae. Kwa hivyo, baadae tutakaa na wahusika wa Sekretarieti ya Bunge kutazama maneno ya Mheshimiwa Mbunge anayoyasema. Mheshimiwa Mbunge endelea. (Makofi)

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nakuambia jambo la wakulima, nikasema Wabunge wote hapa kwenye nyumba zetu tumeweka gardens, wasiwasi wangu tunadhani ndiyo ukulima wenyewe gardens zile. Umewaka palm nyumbani kwako, umeweka sijui maua ya rose, sijui umeweka vitu gani! Tujaribu hata hekari mbili, mbili kila Mbunge na tuweke azimio hapa na kila Mbunge awe na heka mbili kule anakotoka muone adha ya wakulima wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe sana Wabunge wenzangu, tuweke azimio hapa kila Mbunge awe na heka mbili, maana hapa wengi tunakaa na tunazungumza hapa, tunakaa Mijini tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima ambaye Dada yangu Mheshimiwa Matiko alikuwa anamsema, anazungumza kile nilichokuwa nakisema cha kuwa anapata bei ndogo na hakuna anayemsemea. Korosho hapa nimesema hapa mwaka huu, average ya korosho tuliyouza bei ya juu haizidi shilingi 2,500.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kuangalia gharama tunazozitumia na bei anayopewa mkulima, hakuna siku tumekaa mkulima amepata bei ndogo, Bunge likakaa hapa kujadili wakulima kwa nini wanapata bei ndogo. Leo walaji sisi tunaokuja kununua mchele pale Majengo Sokoni, wananunua mchele Dar es Salaam ndiyo tunakaa leo, bei imepanda, bei imepanda! Tunapotaka kumsaidia mkulima tumsemee mkulima hata pale anapouza bei ndogo ndiyo tutaonekana wazalendo wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kaka yangu Bashe nikukumbushe tena kwenye kilimo na hili nishauri sana, ile export levy tuliyoipitisha uje na mabadiliko hapa, yote irudi kwenye tasnia ya korosho, yote. Utapona, utapona! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana mmeagiza pembejeo zenye zaidi ya thamani ya Shilingi Bilioni 98, lakini kukusanya fedha zenu zote hata ukichukua na export levy zote, ukasema ulipe wazabuni, una deni la Shilingi Bilioni 10, piga hesabu zako utaona, piga hesabu zako utaona! (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na ninakushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi.
Nami niungane na watangulizi wangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi kubwa anazozifanya kuhakikisha kwamba Tanzania wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri na timu yake yote Katibu Mkuu, Naibu Waziri, Mkurugenzi wa RUWASA bahati njema sana watu hawa wamepata fursa ya kufika maeneo yetu ya Mkoa wa Mtwara hususani kwenye mradi wa maji ya Makonde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwe miongoni mwa watu ambao kesho watashika shilingi ya wizara hii mimi Katani kwa haya yafuatayo; tarehe 16 Septemba, 2016 Rais wa sasa akiwa Makamu wa Rais alifika Tandahimba, kwenye mpango wa bajeti ya 2015/2016 mradi wa maji wa Makonde uliwekwa na kwenye maelezo ya mpango ule ilikuwa ni kupata fedha kutoka Benki ya India ambayo leo ukisoma bajeti hii ya Wizara ya Maji inaonekana tayari Wakandarasi wanakwenda kutekeleza mradi wa maji wa Miji 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana kitabu cha Wizara ya Maji cha 2017/2018 mradi huu wa maji wa Makonde uliwekwa hata ukienda kutafuta taarifa zake hatukupata fedha, 2018/2019 mradi wa Makonde ukawekwa tena tukiwa tunaaminishwa kwamba mradi huu utatekelezwa itakapopatikana fedha za kutoka Exim Bank ya India.

Mwaka 2019/2020 ukawekwa tena, 2020/2021 ukawekwa tena, leo 2022/2023 ukienda ule ukurasa wa 55 mradi huu umewekwa juu unaonekana kwamba ni mradi wa Miji 28 lakini kwenye Miji 28 imegawiwa miradi ya Miji 24 ambayo inakwenda kunufaika na mkopo ule kutoka Exim Bank ya India, hii miradi minne ambayo ni mradi wa Makonde, mradi wa Songwe wanasema fedha zinatokana na mapato ya ndani, lakini ukisoma hakuna kifungu kinachoonyesha hizo fedha zimetengwa wapi, maana yake hapa nina wasiwasi sana sisi watu wa Mtwara na watu wa Lindi tuna bahati mbaya kwenye miradi yote ya maendeleo, kazi yetu ni kuwekewa mipango lakini haitekelezwi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelia barabara hapa kila tunapokuja tunawekewa kwenye mpango kwenye utekelezaji hakuna kitu, ndiyo kinachoonekana kwenye bajeti hii ya maji ya ndugu yangu Aweso. Mheshimiwa Aweso ambaye amefika Mtwara ameona adha ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Tandahimba leo maji yananunuliwa Shilingi 1,000 mpaka Shiingi 2,000 lakini kwenye bajeti hii watu hapa ambao tayari walishakuwa na miradi ya Bilioni 300, Bilioni 400 wanaendelea kuongezewa fedha Lindi na Mtwara hakuna kinachoonekana, kwani sisi ni watu wa Msumbiji au ni Watanzania kama Watanzania wengine ambao wanapata keki ya Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelikosea nini Taifa hili, tukienda kwenye barabara shida, tukija kwenye maji shida, tukija kwenye umeme shida, watu wa Lindi na Mtwara tumekosea nini Taifa hili au mipaka aliyogawa mzungu mnatufanya sisi ni watu wa Msumbiji siyo Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Samia alikuja mwenyewe Tandahimba alizungumza juu ya mradi huu leo mnapata fedha Bank ya Exim kutoka India mradi huu mmeutoa mnasema ni mradi wa mapato ya ndani! Tumeona barabara kilometa 50 tu zile mlisema mapato ya ndani tumejenga miaka mitano na mradi huu maana yake mnataka tujenge miaka mia tatu sasa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwenye jambo la maji watu wa Mtwara na Lindi tumeachwa nyuma kuliko watu wengine wowote, kila anayesimama hapa anasema mimi nimepata bilioni moja, bilioni nne, bilioni tano, bilioni 50, bilioni 300, Lindi na Mtwara hizo fedha ziko wapi Mheshimiwa Waziri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitarajia ujio wa Waziri kule, ukaona mradi wa maji Makonde umekuja na Katibu Mkuu, ameona mradi wa maji wa Makonde, amekuja Mkurugenzi wa RUWASA mmeona adha na matatizo ya watu wa Lindi na Mtwara, nilitarajia kwenye bajeti hii tungeona kuna trilioni moja inaenda Lindi na Mtwara kutatua changamoto za maji, bahati mbaya sana mnapeleka matrilioni mnatoa maji Ziwa Victoria yanakuja mpaka Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tandahimba, Newala, Nanyamba, Mtwara, Liwale tuna Mto Ruvuma hauzidi kilomita 100 watu wote hawana maji safi na salama, mtuambie Wizara mna mkakati gani, mna dhamira gani na watu wa kusini au sisi mmetuondoa kwenye Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu vinasikitisha sana, kila tunaposimama hapa kuzungumza bajeti za Lindi na Mtwara ni malalamiko tu, kaeni fikirieni Mikoa ambayo ilisahaulika basi, angalau mpeleke fedha na sisi tujione kwamba na sisi keki ya Taifa hili tunagawana kwa mgawanyo ambao watu wengine wanapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wote waliochangia hapa mtu akisema anasema kwangu nilipata mradi wa maji Bilioni Nne, leo nimepewa Bilioni 10 mwingine bilioni 15 Lindi na Mtwara hatuna hiyo miradi tumekosea nini, Mheshimiwa Waziri umekuja mwenyewe kule siyo kwamba hujayaona umeyaona! Kamati, Katibu wa Chama alivyokuja na Sekretarieti yake aliagiza Katibu Mkuu aje akaja mmejionea, mnataka kutupa wakati mgumu 2025 kwa jambo la maji Lindi na Mtwara, mnataka kutupeleka kwenye wakati mgumu, Mama anaupiga mwingi Mheshimiwa Waziri unaupiga mwingi lakini hili la maji Lindi na Mtwara Mzee wangu mimi kesho nashika shilingi hapa, kama hakuna mambo yanayokwenda kuonekana kwamba Lindi na Mtwara tumeingizwa mimi ni wa kwanza kushika shilingi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuone reflection ya keki ya Taifa mnayoitaja sehemu nyingine ambazo walikuwa na miradi ya maji mnaendelea kuilundika, tuone sasa mradi wa maji wa Makonde ambao mwenyewe umefika umeona uchakavu wake, umeona shida zake, Mtendaji Mkuu wa Wizara hii Katibu Mkuu amefika ameona shida zake, mnakuja kwenye bajeti ya Wizara ya Maji mnatupa sarakasi za abunuasi, mmeandika vizuri, jambo ambalo liko kwenye mpango kwa miaka sita, Mheshimiwa Aweso mimi na wewe tukiwa hapa kila bajeti ya maji mnasema mradi huu wa Makonde tunapata fedha Exim Bank, leo mnaleta Wakandarasi mmeondoa Makonde mradi ambao ulikuwa mwanzo mnasema huu utatekelezwa kwa fedha za ndani, tunayo mifano ya fedha za ndani ndugu zangu, miradi tunayotekeleza kwa fedha za ndani tunayo mifano hatutaki turudi huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuomba Mheshimiwa Waziri umepata fursa mwenyewe ya kufika Lindi na Mtwara, tuone sasa mnapokaa kuweka vizuri bajeti yetu hii ili iende sawa, tuone mradi wa maji wa Makonde ambao unakwenda kuwasaidia watu wa Mtwara, Newala, Nanyamba, Nikitangali ipo kwenye mpango wananchi hawa wakapate maji safi na salama. Nikuombe sana sisi watu wa Kusini tumekuwa nyuma kwa muda mrefu, tunayo historia kwa sababu ya vita ya Msumbiji mkatuacha sawa, watu wamejikomboa ni wakati wetu sasa wakufikiria kwamba wenzetu walitenga maeneo yao kusaidia kusaidia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika sasa watu wamejikomboa, hao watu wapate huduma za msingi ikiwepo maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana hili jambo mliangalie kwa uhakika wa hali ya juu sana. Ndugu zangu Bungeni hapa mnaona kila akisimama mtu wa Lindi na Mtwara ni malalamiko, kila Wizara tutakayosimama Lindi na Mtwara tunalalamika, wenzetu wanapongeza, mimi nitakupongeza kwa sababu Waziri unajua shida ya maji iliyokuwepo, lakini nitashika shilingi kama sikuona mradi wa maji wa Makonde una bajeti mahsusi inayoenda kumuondoa ndoo Mama wa Tandahimba, mama wa Newala, Mama wa Kitangali, Mama Nanyamba, Mama wa Masasi, Mama Ruangwa, japo wenzetu wa Ruangwa wana visima kidogo lakini wanahitaji maji safi na salama, hawana maji ya bomba mazuri hawa pia! Mzee hawezi kusema tu kwa sababu ndiyo mwenyewe kakalia Kiti lakini wanahitaji maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda Liwale huko balaa tupu! Nenda Liwale kwa Mheshimiwa Kuchauka ukaangalie balaa la Lindi na Mtwara, nenda Nachingwea kaangalie balaa la maji Lindi na Mtwara, Lindi na Mtwara kuna nini Serikali msichofikiria, msichotuonea huruma watu sisi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana tumeonewa sana kwenye Taifa hili, kwenye miradi ya maendeleo tumeonewa sana, ufike wakati mnapokaa kwenye bajeti sasa muangalie Mikoa ya Kusini angalau tunataka tuwe kama Kilimanjaro, tunataka tuwe kama Arusha, nenda Arusha leo kila Kijiji mabomba yanapasuka..

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Katani, umeeleweka. Nimekuongezea muda mrefu; tunakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunichagua leo, lakini na mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye bajeti yake kwenye suala la barabara ya kutoka Mtwara kwenda Nanyamba - Tandahimba - Newala - Masasi wametenga pesa pale, lakini jambo hili kwa Mkoa wa Mtwara sio la kwanza. Ukisoma bajeti iliyopita ya Wizara ya Ujenzi walitenga pesa, lakini barabara haikujengwa. Sasa msije mkaendelea kutupa ngulai tukawa na matumaini mnatenga, mwisho wa siku hakuna utekelezaji; hili ni jambo la hatari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2005 Mzee wangu kipenzi, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu, wakati anaomba kura kwa watu wa Mtwara aliwaahidi kuwajengea barabara hii kwa kiwango cha lami. Mwaka 2010 karudi tena akawaahidi kuwajengea barabara hii kwa kiwango cha lami, lakini hata Rais mpendwa sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja Jimboni kwangu Tandahimba ameahidi kujenga kilometa zote 210 kwa kiwango cha lami. Leo mmekuja mmetenga kilometa 50, kwenye pesa mliyotengea ni shilingi bilioni 20. Mimi sijui kama kuna u-serious kweli wa kuijenga hii barabara yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii ndiyo barabara ambayo nimeizungumzia; Wilaya yangu ya Tandahimba, Wilaya ya Newala, Mtwara Mjini, Vijijini ndio wazalishaji wakubwa wa zao la korosho. Hebu leo jiulize Mheshimiwa Waziri kutoka Mtwara Mjini kwenda Tandahimba Jimboni kwangu ni kilometa 95, lakini unatembea kwa saa saba kutoka Mtwara Mjini. Yaani ukitoka Mtwara kwenda Dar es Salam utafika mapema Dar es Salaam kuliko Mtwara kwenda Jimboni kwangu Tandahimba. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, hii pesa mliyoiweka basi muwe na nia ya dhati kabisa ya kuona barabara hii mnaanza kuijenga angalau kwa kilometa hizo mlizozitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Barabara ya Ulinzi ipo pale na barabara hii ni muhimu sana. Jambo ambalo nataka nikukumbushe Mheshimiwa Waziri, mwezi wa 12 wakati wananchi wa Jimbo la Tandahimba wamekwama Mto Ruvuma askari wetu walitumia boti kwenda Tandahimba kwa saa 12, lakini walipofika Tandahimba walishindwa kwenda hata barabara ya Ulinzi haipitiki. Mwisho wa siku wale watu wa Tandahimba wameokolewa na boti la kutoka Msumbuji, hii ni aibu kwa Taifa letu. Nione sasa Wizara yako inajipanga vizuri kuziona barabara zile za Mtwara mnazifanyia mambo mazuri sana. Mkumbuke kwamba Mkoa wa Mtwara ulisahaulika kwa kuona kwamba sehemu ile ni sehemu ambayo mlikuwa mmewaweka watu waliokuwa wanapigania uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wameshapata uhuru tayari, mkishinda washaurini na watu wa Msumbiji wawaongezeeni pesa kwa sababu mliwaweka Mtwara ili mtuwekee lami watu wa Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Bandari ya Mtwara. Bandari hii ni fursa kubwa kwa uchumi wa Mtwara na kwa Taifa hili la Tanzania. Kama leo Bandari ya Mtwara ingekuwa inafanya kazi vizuri hata leo msingesafirisha maroli haya ya GSM mnapakia saruji kutoka Mtwara kuleta Dar es Salaam kwa gharama kubwa. Leo Bandari ya Mtwara ingekuwa inafanya vizuri watu wa Mtwara wangefanya biashara kubwa na watu wa Comoro ambao wana njaa, na sisi ni wakulima wazuri tu. Bandari ya Mtwara ingekuwa imewezeshwa vizuri leo watu wa Zanzibar tungekuwa tunapata fursa ya kukimbia kwenda Zanzibar, lakini ingekuwa ni fursa ya biashara baina ya nchi hizi za Malawi ambazo hawana bandari na wanatumia gharama kubwa sana kusafirisha mizigo yao kwenda sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmetenga pesa ya kujenga gati moja, lakini wakati tunasoma Mpango tulizungumza suala la magati manne. Niwaombe hata hako kagati kamoja mlikokasema basi tuone sasa kanajengwa kweli, badala ya blah blah ambazo haziwanufaishi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona bajeti ya suala la uwanja wa ndege wa Mtwara na nimeona mmetenga fungu pale, lakini jambo ambalo nataka nikukumbushe bajeti ya mwaka uliopita mlitenga shilingi milioni 500, sijui ile shilingi milioni 500 imekwenda wapi? Sasa watu wa Mtwara tusije tukaendelea kudanganywa. Niombe Serikali hii ina nia njema, na mimi naamini Waziri una nia njema, wakati ukiwa Wizara ya Mawasiliano ulifanya mambo mengi mazuri, nione haya uliyoyaandika unayafanya kweli ili tuone maendeleo ya nchi hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo hili la nyumba za Serikali. Hili ni jambo la ajabu na ni la hatari sana, wenzangu walizungumza. Wenzangu wamezungumza hapa, na haya mambo msipochukulia serious wazee wangu wenye kumbukumbu za dhati mtaikumbuka miaka ya 1970, nchi ya Kenya Rais akiwa Mzee Jomo Kenyatta, alifanya mambo kama tunayofanya kwenye Taifa hili la Tanzania. Uuzaji wa nyumba hizi yalifanywa Kenya kwenye ardhi ya Wakenya leo mwanae anakuja kukiri mapungufu ya miaka ya 1970 iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isomeni sheria ile mliyoiandaa wenyewe. Ukisoma Sheria ile ya Executive Agency Act namba 30 ya mwaka 1997 iko wazi, mmeipa TBA mamlaka kubwa ya kuuza, kujenga upya, kukarabati na kugawa zile nyumba zenye class A, B na C, lakini mkiangalia kwenye mambo haya ya TBA kama mtafuatilia mtaona namna wenyewe mlivyofanya na mnahusika, wenyewe mnajijua, sio jambo la siri hili. Wazee wangu mpo muda mrefu mnajua kwenye mambo yale. Sasa hizi ni pesa za Watanzania ambazo zinatumiwa kwa maslahi ya watu wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena nikuombe Mheshimiwa Waziri, suala hili la TBA uwe serious, ndani yake ukisoma magazeti yale ya zamani wapo watu wazito wa Taifa hili wanajua mambo haya. Wameingilia mamlaka ya TBA bila sababu za msingi. Tuone sasa mnakuwa serious kwa ajili ya Watanzania na muone Taifa hili la Tanzania ni la watu wote, wala tusikae hapa kwa ajili ya mambo ya vyama kama watu wa CUF, wa CHADEMA, wa CCM wanazungumza jambo kwa interest ya Taifa hili, tuwaunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isionekane tu Upinzani unapoleta hoja hamuwi serious na hoja ya Upinzani, na Wapinzani pia CCM wakileta hoja tusione hoja zao si za msingi, kwa ajili ya Taifa hili ni lazima tuzungumze lugha moja, tuizungumze Tanzania moja, tuone Watanzania wananufaika na rasilimali zao badala ya kukaa hapa tunapiga ngonjera tu. Watu wanasimama hapa wanapiga mangonjera tu, mnataja majina ya viongozi waliopita, fanyeni kazi sasa huu ndio wakati wa kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikwambie Mheshimiwa Waziri naumia sana, binafsi niseme na ni-declare interest. Pande hizi za CCM, CUF, CHADEMA nani mnakaa mnakuja hapa mnawataja viongozi waliopita. Andaeni mikakati yenu kama hi mliyoileta leo, tekelezeni ya kwenu achaneni na kuzungumza mambo yaliyopita, kama mnashindwa kuchunguza fanyeni hayo mnayoyakusudia sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana na niendelee kukuomba sana; barabara hii ya kutoka Mtwara kwenda Tandahimba kama kuna sehemu kwa kudokoadokoa hebu waone Wamakonde hawa. Zamani mlikuwa mnasema Wamakonde sio watu, sisi ni watu tena majabali kweli kweli! mtuone kwamba, tupo kwenye Taifa hili. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Binafsi napata ukakasi mkubwa wa jambo hili hususan hii fedha ya korosho ambayo tunaizungumza. Shida kubwa ninayoipata kwa sababu hii fedha tumeizungumza sheria ambayo ipo na kwa miaka sita mfululizo hizi fedha zimekuwa zikienda kule na zikiwa zinafanya kazi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka hii miwili ndiyo kimetokea kizungumkuti hiki ambacho kimekuja kuleta sheria hii ambayo tunatakiwa kufanya mabadiliko. Hii inanipa shida, kama maelezo yanayotolewa na Serikali ndivyo yalivyo, wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali anasema, aliyazungumza mambo mengi zikiwemo kanuni na vitu vingine, lakini ukijiuliza haya mambo nani aliyakosea? Ni wakulima wale tunaotaka kuwapa adhabu leo, au ni sisi watunga sheria au ni wasimamizi wa Serikali ambao ndio walipaswa kutunga hizo kanuni? Sijapata majibu yaliyo sahihi sana, dhamira ya Serikali kwenye jambo hili ni ipi?

Mheshimiwa Spika, nasikitika sana, amezungumza ndugu yangu Mheshimiwa Mwambe, alipokuwepo Katibu wa Fedha, Mheshimiwa Doto aliyazungumzia matumizi mabaya yaliyofanywa na Bodi pamoja na Mfuko. Tumezungumza hapa kwamba ripoti ya CAG imesema ubadhirifu unaonekana. Kwa nini kama kuna ubadhirifu, wasichukuliwe hatua wale wanaohusika? Mara kadhaa tumeona Serikali ikichukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwanzo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesimama hapa, akavunja Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho, tukapiga makofi wote. Haikupita muda, akaondolewa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho wa kwanza, Ndugu Mfaume, tukaona Serikali inachukua hatua. Haukupita muda akaondolewa aliye-act Ukurugenzi wa pili juzi, Mheshimiwa Jarufu akaondolewa, tukaona Serikali imechukua hatua. Kuna ukakasi gani kama majibu haya ya Serikali yanayokinzana, maana mmoja anasema tatizo ni kanuni, mwingine anasema kuna matumizi mabovu ya fedha. Lipi tulibebe sisi wawakilishi kuwaambia watu wetu kule? Tunapata shida kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la sheria ambalo tumelizungumza hapa, sheria ambayo imetungwa na Bunge. Kama kuna tatizo kwenye sheria, nani alikosea? Sasa kama ndiyo wameleta amendment, ni sawa, lakini je, fedha zile za miaka miwili ziendelee kubaki? Kule Mtwara Bodi ya Korosho inadaiwa miche. Miche ambayo imepandwa Kongwa na Mpwapwa, wanaoizalisha ni wakulima wadogo, ambao hata leo Spika ukienda au ukiunda Tume iende kule; hata Mheshimiwa Dkt. Mpango analijua hili vizuri, amepeleka watu wake kufanya utafiti. Kama kutakuwa na upungufu ni tofauti ya hiyo miche.

Mheshimiwa Spika, Bodi labda inasema Sh.20,000/=, lakini ukienda utakuta labda ni Sh.19,000/=, lakini utakuta kweli kuna madeni ya msingi ambayo wanapaswa kulipwa wakulima na ndio wazalishaji wa miche ile. Hiyo miche ya korosho tunayozungumza, haizalishwi na mtu gani, ni wakulima. Ukienda Tandahimba, kuna vikundi vya wakulima wanazalisha miti, ukienda Naliendele, kuna vikundi vya wakulima wanazalisha hiyo miche.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 zimegaiwa pembejeo na Serikali bure. Waliogawa pembejeo wanadai fedha zile. Tunapozichukua zile fedha, hawa watu wanalipwa fedha kutoka wapi? Kama nia njema ya Serikali ipo hivyo, kwenye amendment yangu, nimeleta mapendekezo. Naona kabisa inawezekana Serikali ina nia njema kutafuta vyanzo vya mapato. Nikasema kwenye sheria ile badala ya kufuta, basi wachukue hamsini wao na sisi tubaki na hamsini ili korosho ziweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi jirani ya Msumbiji kwa miaka 11 sasa wakulima wa zao la korosho wanapewa dawa bure, wanapewa viuatilifu bure. Kwa nini tusiende kujifunza? Sasa kama wakulima wameandaa MoU wakakubali wenyewe kwamba tunaweza kukubali kupata fedha kwa namna hii, fedha zinapatikana, hata zile tulizokubaliana, tulizotungia sheria nazo zinakuwa ni matatizo. Shida iko wapi kwenye jambo hili? Nadhani itumike busara sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme wazi kabisa hakuna Mbunge wa Kusini anayetetea fedha hizi kwa maslahi ya Kusini. Kuna maneno yanazungumzwa hapa ambayo wakati mwingine hayana ushahidi.

Mheshimiwa Spika, labda hukuwepo, kuna Watu wamesimama wanachangia kwenye Bunge hili, wanasema kuna Wabunge wanahusika na wizi wa fedha hizo. Kama wapo, kwa nini wasichukuliwe hatua? Kama kweli kuna Mbunge anaonekana kwenye documents zao anahusika na mambo hayo, Wabunge hao wanatokana na vyama vyetu. Vyama vina taratibu zao na Serikali ina taratibu zake. Kama kweli kuna Mbunge anahusika, ndiyo maana nasema tunapokuja Bungeni tuje kwa nia njema. Tusije kutengeneza hoja ya kushawishi watu kwa sababu kuna jambo watu wanashawishi iaminike kwamba kuna Wabunge wamefanya biashara na hizo Bodi.

Mheshimiwa Spika, Serikali huwa inazungumza maneno haya chini chini. Kama kweli watu hao wapo na ushahidi upo, ndiyo sababu tumeunda Mahakama watu wapelekwe Mahakamani badala ya kuja hapa bila kuwa na hoja na ushahidi. Ukiwauliza waliotoa hoja zile kwamba lete ushahidi; Mheshimiwa Mwambe amezungumza habari ya hiyo kesi, ameleta na document kwamba Mahakama iliamua moja, mbili, tatu.

Mheshimiwa Spika, mtu anasimama tu hapa anasema kitu, ukimwuliza ni Mbunge gani? Hataji Mbunge. Kwa hiyo, unakuta kabisa kwamba kuna nia isiyo njema kwa wakulima wa korosho wa Tanzania, sio wa Mtwara. Sisi wa Mtwara tunazungumza maneno haya kwa sababu asilimia karibu 85 ya korosho zinatoka Mtwara na Lindi. Ni lazima tuseme, lakini hatusemi kwa maana kwamba tuna chuki na maeneo mengine, tuna chuki na Serikali. Ndiyo maana tumeshauri. Mfano, nimeshauri hapa kwamba fedha hizo hamsini iende huko kwenye Consolidated Fund, nyingine ibaki kwenye tasnia ya korosho.

Mheshimiwa Spika, sasa linapokuja suala watu wakajenga vitu ambavyo havipo, sisi tunazungumza kwa ajili ya kuitetea Serikali hiyo hiyo. Wakulima hawa wa korosho tunaowasema ni wakulima wa kipato cha chini sana. Ungepata fursa ya kwenda maeneo ya korosho, ni shida. Kuna kitu kwa Kimakonde kinaitwa uhangu. Uhangu ni kitu kimoja cha hatari sana, ni upupu kwa Kiswahili. Huu ukikuwasha wewe Mheshimiwa Spika ambao hujakutana nao, utajua balaa la korosho lipoje. Wallah hizi fedha ungeomba kabisa kwamba hizi shilingi bilioni 200 ambazo Mheshimiwa Dkt. Mpango amezihifadhi (mimi najua kuna mahali alipozihifadhi) awapelekee basi, ziende zikalipe yale madeni, halafu baadaye ndiyo aje na nia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisema mwanzo kwamba hii amendment ingeletwa kwa nia njema zaidi kama tungekaa; ulizungumza mwanzo kwa hekima sana kwenye Kiti chako. Mwanzo ukasema twende kwenye Kamati ya Bajeti. Tumekaa zaidi ya siku tatu sisi. Mwanzo alipata dharura, alifiwa, tukakubali amefiwa, akaitwa kikao kingine ambacho yupo, hakuja. Yaani hiyo yote, nia njema ya pamoja kabisa kwamba hili jambo kabla hatujafika huko kupiga makelele tungekuwa tumemaliza na Mheshimiwa Dkt. Mpango, hakuja. Ukakaa, jambo ambalo mpaka leo sijui majibu yake yako wapi mpaka leo?

Mheshimiwa Spika, siku hiyo hiyo ukazungumza kwamba Waziri Mkuu hayupo, akija Waziri Mkuu mwenye jambo hili mtakaa kulizungumza. Hata lenyewe sikuona hata huo muda wa kupata kukaa kulizungumzia jambo hili.

Mheshimiwa Spika, mwanzo tumeanza na Wizara ya Kilimo kwa nia njema. Mheshimiwa Dkt. Mpango angejua nia njema ya kwetu wala tusingefika hapa kwenye mgawanyiko usiokuwa na sababu. Kwa sababu leo analigawa Taifa kwa misingi ya watu kupandikiza chuki kwamba Wabunge wa Kusini labda kuna maslahi fulani wanayatetea, kumbe sisi tunatetea kitu ambacho kipo kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, mnaodhani kwamba kuna watu wana maslahi kwa Wabunge wa Kusini, vyombo vya sheria vipo, kama mna ushahidi, hao watu wachukuliwe hatua. Hata ningekuwa mimi ninayezungumza nikaonekana nahusika kwenye huo ubadhirifu mnaosema, nichukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakulima wale, watu wale wa Bodi ya Korosho ambao wana madeni, fedha hizi ziende ili kunusuru matatizo yaliyokuwepo kwenye tasnia ya korosho. Nawaomba sana, ukipata fursa kwenda Ivory Coast, ninyi wakati mnaondoa hii Export Levy ya kwenye korosho, Ivory Coast wao wanatoa asilimia 85 wakulima wa Korosho. Sijui sisi tunajifunza wapi haya mambo.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tumeshauri na nimeendelea kushauri kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango, tunajua kwamba Serikali ina shida ya fedha, basi tuchukue hamsini wapelekeeni watu wa korosho, hamsini chukueni Serikali, tuendelee kuiendeleza nchi yetu kwa nia njema ile ile ambayo tunaikusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru pia kwa kunipa fursa hii. Nitaanza na suala la utawala bora ambalo lipo kwenye mapendekezo ya mpango huu tunaozungumza. Wakati tunazungumza suala la utawala bora sisi Watanganyika ambao tumejipa mamlaka ya kuwa Tanganyika sasa kuwa Gereza la Guantanamo Bay kwa kuwachukua Wazanzibari na kuwaleta Tanganyika bado watu mkazungumza suala la utawala bora, hatuwezi kuiendesha nchi na tukawa na mipango mizuri kama kuna watu wanadhulumiwa, kuna watu wanaonewa, bado mkaendelea kuzungumza mipango hii. Na kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, hili nalo lazima uliangalie sana kwa sababu linakugusa pia, ulione kwamba ni jambo la msingi tunapozungumza suala la mipango, suala la utawala bora na wa sheria ni lazima lizingatiwe kwa namna yoyote ile, ndiyo tutakwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati nasoma ukurasa wa 62, mmezungumzia suala la Benki ya Maendeleo ya Kilimo, niliona miaka ya nyuma Benki ya Maendeleo ya Kilimo ikiwa Dar es Salaam, wakulima wenyewe wanapatikana Tandahimba, sasa ni mambo ya ajabu na vichekesho kwa Taifa hili, mnazungumza benki ambayo iko Dar es Salaam, wakulima wa Rujewa kule Mbarali, wakulima wa korosho wa Tandahimba hakuna wanachonufaika na benki hiyo ambayo inayokaa Dar es Salaam, ni jambo la ajabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nina ushahidi wakati hata mmeleta trekta, watu wangu wa Tandahimba mpaka leo, wajanja wachache wameshachukua matrekta, wenyewe wakulima wa Tandahimba hawajachukua. Sasa wakati mnazungumza suala hili la Benki ya Maendeleo ya Kilimo basi mhakikishe na watu wa Tandahimba, watu wa Rujewa kule vijijini wananufaika na jambo hili la Benki ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mnazungumza mambo haya mmezungumza suala la barabara ambalo nimeliona, suala la barabara ile ya Masasi – Mtwara – Newala – Tandahimba, ukaizungumzia ile ya Masasi – Songea – Tunduru, bahati nzuri hii ya Masasi – Songea – Tunduru inakwenda vizuri sana. Lakini hii ya kwetu ya kutoka Mtwara – Tandahimba – Newala, pamoja na kwamba umepitisha bajeti na wananchi wakakubali kubomoa mabanda yao yaliyo barabarani, mpaka leo hakuna kinachoeleweka na tunaandaa sasa mpango wa mwaka unaofuata. Hili ni jambo la ajabu na linaweza likawaangusha Serikali ya CCM, sasa kama mnataka mipango iende, tutekeleze kwanza tuliyokubaliana halafu ndiyo mlete mipango ambayo inaweza ikawasaidia Watanzania hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezungumza suala la viwanda. Suala la viwanda, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikwambie tu kwamba Kusini, kwa maana ya Mtwara na Lindi tulikuwa na viwanda vya korosho vya kutosha, viwanda ambavyo mmeuza kwa bei chee, tena kwa njia za panya, zaidi ya viwanda vinane tulikuwa navyo, sasa kama mna dhamira ya dhati muone namna gani mnakwenda kuvichukua vile viwanda. Na hili linawezekana kwa Serikali yenu, kwa sababu ni Serikali tu ikiamua jambo inafanya, sasa tuone viwanda vile vya korosho kule mnavichukua ili watu wa Mtwara na Lindi waweze kunufaika na viwanda vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza hapa, suala la single customer territory, napata shida kwenye jambo hili, kama makusanyo ya ndani yametushinda, tunakuja kujibebesha mzigo wa kukusanya na pesa za watu wa Kongo, Zambia, hii ni akili ya wapi? Una mzigo wa magunia wa kilo 200 umeshindwa kuubeba mwenyewe unasema niongezee kilo 400, hili ni Taifa la ajabu sana. Nikuombe sana, mlikwenda kwenye jambo hili mkiwa mmeshirikiana na watu wa Kenya kwenye suala la VAT kwenye suala la utalii, Wakenya wakatukimbia, leo tumeingia mkenge kwenye jambo hili tayari bandari yetu inadorora ambayo inaleta zaidi ya asilimia 60 ya Pato la Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, wewe ni msomi mzuri na mara zote tukiwaambia muwe mnapokea ushauri, sio kila kinachozungumzwa na upinzani ni maneno ambayo tunaiudhi Serikali, sisi tunajua nchi hii ni ya Watanzania wote na tunazungumza kwa maslahi ya Taifa la Tanzania hatuzungumzi kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi, hatuzungumzi kwa maslahi ya Chadema, hatuzungumzi kwa maslahi ya CUF. Tunapotoa hoja za msingi za Kitanzania pokeeni hoja na mzifanyie kazi badala ya kukaa hapa mnatuletea ngonjera, mnazungumza majungu, mnazungumza mipasho, tuzungumze kauli za Kitanzania, tuwakomboe Watanzania wachache ambao wanapata shida huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Tandahimba ina hospitali moja ya Wilaya na vitu viwili vya afya ambavyo ni vya zamani. Hata hivyo, tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha shilingi milioni 400 za Tanzania kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Mahuta. Fedha hizi zimetumika vizuri. Kwa hiyo, ombi langu ni kupata fedha kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kituo hiki ambacho kinahudumia zaidi ya kata kumi zilizopo jirani. Hata hivyo, Wilaya ya Tandahimba jiografia yake ni ngumu kidogo, kwa hiyo, naomba Wizara itusaidie fedha kwa ajili ya kujenga na kuendeleza vituo vya afya vipya vilivyojengwa na wananchi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Mnyawa wananchi kwa kupenda maendeleo wamejenga vituo vya afya ambavyo vinahitaji msaada wa Serikali ili tuweze kumalizia. Kata ya Mndumbwe nayo wananchi wamejitolea kujenga kituo cha afya. Tunaomba msaada kwa Serikali iweze kutusaidia tumalize ujenzi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Wizara itujengee Kituo cha Afya katika Tarafa ya Litehu ambayo inahudumia wakazi zaidi ya 30,000. Tunaomba tupate kituo cha afya katika Kata ya Kitama I. Kituo ambacho kitasaidia kuboresha huduma za afya katika maeneo jirani kama Kata ya Miute, Michenjele, Mihambwe na Mkoreha. Wananchi wako tayari kujitolea, nami kama mwakilishi wa Jimbo la Tandahimba na mzaliwa wa Kitama, naahidi kuchangia mifuko 600 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Kwa unyenyekevu mkubwa naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana lakini pia niombe nitumie dakika saba ili dakika tatu atumie ndugu yangu Hamidu Hassan Bobali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Wizara hii ya Kilimo, kwanza nianze na suala la mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umetumika kwenye korosho. Kwa namna moja au nyingine tumeona kabisa kwamba kwa wakulima wa korosho mfumo huu umewasaidia sana. Naishauri Serikali na Wizara kwamba mfumo huu usiwe kwenye korosho tu, kwa sababu Mikoa ya Kusini tunalima ufuta, mbaazi na mazao mengine. Sasa kwa sababu mfumo huu kwenye korosho umekuwa bora sana ingependeza sasa mfumo huu uelekezwe pia kwenye mazao mengine kama ufuta, mbaazi na mazao mengine kama tumbaku ili uweze kuwanufaisha na Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na jambo kwenye korosho linaitwa export levy, ushuru huu ni ushuru mkubwa sana. Kwenye korosho Serikali inachukua asilimia 15 ya market price, lakini kwenye maelekezo wakati wanaunda mfuko ule wa kuendeleza zao la korosho katika mambo ambayo wameyasahau sana sikuona pesa zinatengwa kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima wa korosho kwenye suala la elimu. Leo kama kungekuwa na mkakati mzuri kwenye suala la elimu, ilivyotokea wanafunzi wa vyuo vikuu wamekosa mikopo na kwenye korosho kuna pesa asilimia 15 za export levy zingeweza kusaidia Mikoa ya Lindi na Mtwara kuongeza wadahiliwa wale wanaokwenda vyuo vikuu kwa kupata pesa za kutosha zinazotokana na hii export levy. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto nyingine kwenye Vyama vya Msingi vya Ushirika ambavyo vinachukua shilingi 60 kwa kila kilo moja kama ushuru wao. Pesa zile hazina maelekezo. Sasa ningemuomba Waziri kwa sababu jamii zetu zina matatizo mengi sana, wakati anatoa maelekezo yake aweke mkakati kwenye pesa za Vyama vya Msingi tuone zinaweza kusaidia jamii kwenye mambo ya msingi, leo tunakaa kuhangaika kutafuta pesa shilingi 10,000 kwa ajili ya CHF, wakati kwa mfano Mkoa wa Mtwara tuna Vyama vya Msingi ambavyo vinakusanya mamilioni ya pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano chama kimoja cha kwangu KITAMA kina uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 80,000 pesa ambazo ukienda kwenye mkutano mkuu wa chama cha msingi watu wanagawana shilingi 5,000 au 10,000 ambazo hazimsaidii chochote mkulima wa korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mapendekezo yangu kwa Wizara na kwa Waziri mwenye dhamana, aone ni namna gani pesa zile za Vyama vya Msingi za ushuru, inachukuliwa angalau kiasi fulani cha pesa zinawekezwa kwenye mambo ambayo yanaweza kusaidia jamii mfano hiyo CHF au la, hata wale watoto wanaofaulu kidato cha tano na kwenda cha sita kama wanakosa ada basi ielekezwe kwamba kila Chama cha Msingi cha Ushirika angalau kisomeshe watoto watano kuwapeleka form five na six. Ingesaidia sana, badala ya pesa hizi kuendelea kutumika kwa malengo ambayo siyo ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulikaa hapa tukawa tumezungumza jambo la stock exchange, jambo hili Mheshimiwa Waziri nilidhani kwenye majaribio haya tusiyafanye kwenye korosho tu kwanza. Mfumo wenyewe wa stakabadhi ghalani Mheshimiwa Waziri kama utakumbuka umeanza mwaka 2007 tumekuja kutekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani 2016/2017 mwaka huu ambao wewe ndiyo Waziri! Maana yake miaka iliyopita yote mfumo wa stakabadhi ghalani haujatekelezwa Mkoa wa Lindi na Mtwara na maeneo mengine yote. Wakulima walikuwa wanaendelea kwa kutumia Vyama vya Msingi, kukopa pesa benki wakawa wanalipa pesa nyingi ambazo mpaka leo ukienda Tandahimba kule kuna vyama vinadai pesa nyingi kwa sababu ya mfumo ule mbovu ambao hatukuutekeleza kama tunavyoenda sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tumeanza mwaka huu kuutekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani hii stock exchange naomba Mheshimiwa Waziri tuendelee kwanza na mfumo huu, tuwe tumejifunza vya kutosha angalau miaka mitatu, minne, tukijiridhisha kwamba tunakwenda vizuri ndiyo twende kwenye mifumo hii ya kisasa ambayo inahitaji capacity kubwa ya uelewa mkubwa, tofauti na watu wetu wa Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sasa kwenye Wizara ya Ardhi. Alizungumzia Kaka yangu Mchengerwa pale. Nilipata fursa kukaa na wakulima pamoja na wafugaji. Suala linalozungumzwa na Mheshimiwa Mchengerwa pale lile la Rufiji ni jambo zito sana. Waziri wa Ardhi aangalie namna ya pekee sana na Wizara nyingine muone namna gani jambo hili la migogoro ya wafugaji na wakulima mnaweza mkalimaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu akiwa Waziri wa Kilimo kipindi kifupi kile alianza michakato ya kuona migogoro hii inaishaje. Sasa siyo vibaya Mheshimiwa Waziri ukamfuata Mheshimiwa Mwigulu ukaangalia mikakati ambayo alikuwa anaiweka badala ya kila Waziri anaekuja anakuja na mkakati mpya, na mambo mapya mkayasahau hata yale mazuri ambayo wengine walianza kuyafikiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuomba Mheshimiwa Waziri kwenye jambo hili la Vyama vya Ushirika ambalo nilizungumza mwanzo uliangalie kwa mapana sana. Tuna madeni ya wakulima ambao wanadai pesa za korosho za mwaka 2012/2013 na mwaka 2013/2014 na hii kwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wanachi hatuna neno jema kwao ambalo tunaweza tukawajibu. Tumeshadanganya sana na ikiwezekana urudi mwenyewe uje Jimboni kwangu Tandahimba kuna wakulima wanadai pesa zao za mwaka 2012/2013, mwaka 2014/2015 mpaka leo hawajui hatma ya pesa zao zinapatikana namna gani. Kwa hiyo, niombe sana wakati wa majumuisho uone jambo hili unaliwekaje ili tuwe na majibu hata tunaporudi majimboni tuseme tulifikisha kwa Serikali na Serikali imetujibu moja, mbili, tatu, nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri vizuri, ninapenda kusema si ajabu Waziri mwenyewe akawa chanzo cha matatizo ya askari wa Jeshi la Polisi. Hili nazungumza wazi kwa sababu kuna matukio ambayo yametokea polisi wakiwa wanatimiza wajibu wao, baadaye wanatengua walichokiandika wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nazungumza sana kutokana na mgogoro ulioandaliwa na chama fulani ndani ya CUF. Tarehe 16 Novemba, 2016, nikiwa na Wabunge wenzangu wa CUF ambao ni Wajumbe wa Baraza kuu la Uongozi, tuliokwenda Newala kwa kibali cha polisi kwamba tunaruhusiwa kufanya mkutano wa ndani. Asubuhi tuko kwenye mkutano wa ndani, ghafla askari polisi wanakuja


na defender na washawasha wanakuja kutuondoa kwenye mkutano wa ndani, eti kuna mtu mwingine amewaambia kwamba haturuhusiwi kuendelea kufanya mkutano wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sisi haturuhusiwi kufanya mkutano wa ndani ni siku tano nyuma Ibrahimu Lipumba aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF alifanya mkutano na wakamlinda. Tarehe 19 tulienda Mtwara…

TAARIFA...

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa, pia Kiti chako kisiyumbe. Kuna watu wameomba taarifa hapa umewakatalia mara kadhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa mnaowabeba, ndiyo pamoja na hawa wengine hawa. Tarehe 19 Novemba Katibu Mkuu wa Chama changu cha CUF alikwenda Mtwara, anapaswa kufanya kikao cha ndani, tumelipia ukumbi na kila kitu, mwisho wa siku tunaambiwa haturuhusiwi kufanya kikao cha ndani.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukampigia Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, tukamwambia tatizo hili, lakini mwisho wa siku hatukupata maamuzi sahihi ya mambo haya. Mambo haya ya kihuni yanaendelea kufanywa na kundi hili la akina Lipumba na watu wake hawa akina Mheshimiwa Magdalena Sakaya, polisi wakiwa wanaendelea kuwalinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF Taifa, Mheshimiwa Julius Mtatiro amekwenda Tanga katika vikao vya ndani, hakuna mgogoro, polisi wameendelea kuzuia wasifanye vikao vya ndani.

Polisi hawa pia wakati tuko mahakamani wanaona mtu anapigwa kwa kisu, yule aliyepiga mpaka leo hajakamatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko Mabibo Mwenyekiti wetu wa Wilaya ya Kinondoni, Juma Mkumbi, ameitisha kikao na waandishi wa habari, wameingia wavamizi na bastola, hawajakamatwa mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio yote haya na Waziri ana barua ya chama ya kulalamika juu ya matukio haya ambalo Jeshi linaendelea kuwakumbatia hawa mungiki. Hata mkutano wa tarehe 21 Agosti, 2016, Lipumba kaingizwa kwenye mkutano na polisi kuvamia mkutano ambao mwenyewe Lipumba amekiri hakualikwa. Kama uliangalia kipindi kile cha 360 cha Redio Clouds, Lipumba mwenyewe anakubali hakualikwa, amevamia mkutano akiwa naOC- CID wa Magomeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mnakaa hapa mnazungumza, nikuombe Mheshimiwa Waziri, ulitia nia kubwa ya kutaka nafasi kubwa mwaka juzi ya Urais wa nchi hii, si ajabu Mungu kwa makusudi kabisa aliona bado na ndiyo haya unayoyafanya. Kwa sababu haiwezekani, watu wanaofanya matukio wapo, tumesharipoti kesi nyingi, matukio anayoyafanya Lipumba anasindikizwa na polisi. Tumeomba juzi kwenda kufanya usafi Buguruni, Mbunge wa Temeke mmemzuia, Lipumba mlikuwa mnamlinda pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri dhamana uliyopewa ni dhamana kubwa sana. Mwanadamu kuna muda anavumilia na kuna muda uvumilivu pia unashindikana. Mimi nasema hawa mnaowatumia, mmemtumia Sakaya anakwenda kushtaki watu polisi anasema tunataka kumshughulikia, watu ambao hatukuwepo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemalizika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kutuongezea kilomita 50 za barabara ya lami kutoka Mnivati – Tandahimba. Ombi langu kwa Serikali ni kwamba kwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Mtwara ambao unategemea sana zao la korosho huku asilimia 47% ya korosho zote Tanzania zikiwa zinatoka maeneo hayo, Serikali iwape wakandarasi zaidi ya mmoja ili tupate matokeo ya haraka sana.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe tu kuwa tunazo kilomita 50 za awali za kutokea Mtwara kuelekea Mnivati lakini barabara hii ambayo mkataba wake ilikuwa uwe umekamilika ndani ya miezi kumi na saba mpaka sasa ni kilomita 8 tu ndiyo zimewekwa lami. Hii ndiyo kusema kwa kusuasua huku tutahitaji miaka 10 kukamilisha barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba maeneo yafuatayo yapate minara ya simu; Kata za Mdimiba, Michenjele, Nganja, Mkwiti, Mkoreha na Chaume. Kata hizi hazina mawasiliano ya simu, naomba suala hili lishughulikiwe.

Mheshimiwa Spika, niombe kuzungumzia suala la reli ya kutoka Mtwara – Mbambabay - Mchuchuma - Liganga. Reli hii kama itejengwa italeta fursa za kibiashara Kusini mwa Tanzania na nchi za Malawi, Zambia na Msumbiji.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru wewe lakini pia nimpongeze Mzee wangu Mheshimiwa George Huruma Mkuchika kwa kupewa dhamana hii ya kuongoza Wizara ya Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la Wizara hii ya Ulinzi, kwangu kule Tandahimba kuna mambo yanafanywa na Askari wa Jeshi la Polisi, mambo ya hovyo kabisa. Mfano mdogo miezi mitatu iliyopita Askari Polisi wa Usalama Barabarani wamekuwa wakiwakamata vijana na kuwapiga. Sasa sijajua PGO ndiyo inataka hivyo au namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo mara kadhaa nimewahi kumwambia Waziri mwenye dhamana kwamba DTO wa Tandahimba mambo anayofanya Tandahimba hayako sahihi. Sasa sijui kama kuna sheria inamwongoza Askari Polisi anapokamata mtuhumiwa ampige. Hili limekuwa ni jambo ambalo linalojirudia kwa Jimboni kwangu, mara kadhaa anawachomekea magari vijana wa bodaboda. Hii ni hali ya hatari sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wakati atakapokuja atatuambia kwamba maelekezo aliyoyatoa sasa yamekaa namna hii au namna gani. Hata hivyo, ukienda Dar es Salaam pale sijajua au operation au ni kitu gani, ukiingia Mtaani Askari ambao hawana uniform wanakamata dereva bodaboda, ananyang’anya funguo kabla ya kumwambia jambo lolote lile, wakati mwingine hawajulikani kama hawa ni Askari au lah! Sasa ni vema kwa sababu mna bodaboda ambazo Askari wake wanavaa uniform wale wanafahamika vizuri mnaporuhusu Askari wanakwenda mtaani hawana uniform, wanakamata hovyo, mnahatarisha hata usalama wa raia wale wanaoishi mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa hapa wakati wanazungumza suala la ulinzi wa Wabunge, jambo lililotokea kwa Mheshimiwa Lissu ni jambo la fedheha kubwa sana kwa Taifa letu. Ni jambo ambalo kwa namna moja au nyingine sijui kama Wabunge tunaona uzito wake. Limezungumzwa sana kwenye Bunge hili, lakini bado Wizara mpaka leo waliofanya matukio yale hakuna maelezo yanayojitosheleza kwamba wale watu wakoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo ambayo yako clear kabisa, eneo la tukio ambalo Mheshimiwa Lissu amepigwa risasi ni eneo ambalo wanakaa Mawaziri, Mheshimiwa Naibu Spika unaishi pale, lakini vyombo vya ulinzi vinakuwepo pale, lakini mpaka leo jambo hili la Mheshimiwa Lissu limekuwa kizungumkuti halizungumzwi kwa mapana na kuonekana ufumbuzi wake unakuwaje. Leo kama Mheshimiwa Waziri jambo la Mheshimiwa Lissu analiona ni la masihara hili leo linatokea kwa Wapinzani kesho inawekana Wapinzani tukachukua nchi. Je, likitokea kwenu tuliangalie kama tunavyoliona hili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati nimeona imeshauri jambo jema sana na nione sasa kuwe na umuhimu kama wenzetu wa Kenya, Wabunge wanalindwa mpaka majumbani kwao kuna ulinzi wa Jeshi la polisi kwa nini Tanzania tusiige majirani zetu pale. Kamati imeshauri vizuri imezunguza kwa uhalisia kwamba Wabunge wakati mwingine tunapotekeleza majukumu yetu tunapotetea rasilimali za nchi, wapo watu wanaoiba hawawezi kutuacha salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vema tuone kwamba Bunge hili linaona na Wizara zione kabisa kwamba kuna umuhimu wa Wabunge kuwa na ulinzi wanapokuwa Majimboni lakini ikiwezekana hata tunapokuwa Dodoma hapa. Haya matukio mengine yanayotokea kama tunakuwa na ulinzi wa Jeshi la Polisi yawezekana kabisa yasitokee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine zipo Balozi zetu ukienda China kule kuna Maafisa wa Ubalozi hawapo, lakini bado hakuna hawajawapeleka watu wa kwenda kuziba nafasi zile. Sasa sijui kwenye Diplomasia ya uchumi kwenye jambo hili likoje, Waziri wa Mambo ya nje nadhani anaweza kutusaidia na hii siyo China tu, zipo nchi hata ukienda South Africa, mambo haya yako hivyo.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru lakini pia napenda nichangie muswada kama:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma muswada huu kifungu cha 5(3) utagundua kuna mapungufu makubwa ambayo tunapaswa kuyarekebisha kama Bunge na Napata shida kidogo kwasababu Waziri wa Sheria ni mtu ninaye muamini. Na ukisoma kifungu kile kimeeleza wazi, kimetoa tafsiri ya mtu; mtu anasema ni raia yeyote wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania. Lakini muswada huu tunaochangia unahusu Tanganyika. Sasa labda wakati tunataka kuchangia na kuendelea na muswada huu labda utoe tafsiri sasa kwamba mtu ni raia yeyote wa Jamhuri ya Tanganyika kama tulivyotaka Serikali tatu; inaweza ikawa tafsiri sahihi kabisa, maana inaleta shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumza Serikali tatu watu mkazikataa; leo tunazungumza suala la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunazungumzia na watu wa Zanzibar, na mmetoa tafsiri hiyo hiyo ya mtu; lakini kwenye muswada huu mnasema itumike Tanganyika tu; hili ni jambo ambalo nadhani Waziri kwasababu ni mtaalam sana wa sheria uone ikiwezekana kwa safari hii huu muswada tusiendee nao kwasababu una mapungufu makubwa ili muulete wakati mwingine tuujadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda kifungu cha sita nacho utaangalia; kuna mapungufu makubwa yanaendelea pale. Mmetoa mamlaka ya baadhi ya vyombo vya kiuchunguzi, wakati wanaendelea kuchunguza mambo yao; hamjatoa duration kwamba muda gani muda gani watachunguza. Kwa maana kuna uwezekano mkubwa ikachukua miaka hata mitano, kumi, kumi na tano kwasababu hakuna muda mle ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri wakati mnaangalia hili jambo msije mkawa mna tengeneza jambo kwa ajili ya uchaguzi wa 2019/2020. Maana nahisi kabisa mnatengeneza kitu cha 2019/2020 ili kubana uhuru wa watu kutoa taarifa zao vizuri kwa maelezo tu kwamba mnaweza mkasimama na vifungu hivi vidogo vya kusema kuna uchunguzi, kuna hili; watu wakakosa fursa ya kupata haki zao za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, niombe kama kuna marekebisho ya kifungu kile cha 5(3) mfanye marekebisho hayo, lakini kifungu kile cha sita ikiwezekana chote tukiondoe ili tuweze kwenda sawa kwa ajili ya haki ya watanzania hawa. Asante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru lakini kabla sijaendelea kuchangia niseme tu kwamba siungi mkono hotuba hii ya Wizara ya Kilimo. Kama mimi ningekuwa Waziri mwenye dhamana kwa namna mambo yalivyo ningejiuzulu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Na. 18 ya mwaka 2009 ukiisoma pamoja na Sheria ya Fedha Na.15 ya mwaka 2010, kifungu cha17A(2) kinaeleza wazi kuwa asilimia 65 ya export levy inakwenda kwenye tasnia ya korosho. Msimu wa korosho 2016/2017, asilimia 65 ya export levy ambayo ni shilingi bilioni 77, ukijumlisha na maduhuli ya nyuma jumla ya shilingi bilioni 91 haijaenda kwenye tasnia ya korosho. Msimu huu tuliomaliza wa 2017/2018, asilimia 65 ya export levy ni shilingi bilioni 115 haijaenda kwenye tasnia ya korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atuambie kama fedha hii ya korosho shilingi bilioni 206 imekwenda kulipia Bombardier wakulima wa korosho wajue. Leo hakuna pembejeo wakati fedha hizi asilimia 65 ndizo zinatumika kwenye pembejeo. Wapo watu wamezalisha miche inayokuja mpaka Dodoma mpaka leo hawajalipwa, wapo watu mwaka jana wamegawa pembejeo mpaka leo hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 30 Mei, 2017, TRA ilitoa taarifa na walimuandikia Katibu Mkuu Fedha kwamba export levy shilingi bilioni 75 imekusanywa, inatakiwa iende Bodi ya Korosho, haikwenda. Tarehe 15 Desemba, Katibu Mkuu wa Kilimo kaandika barua kumpelekea Katibu Mkuu wa Fedha, fedha haijaenda. Juzi amekuja Waziri wa Fedha anatupa blabla, anasema kuna shilingi bilioni 10, hakuna shilingi bilioni 10, ni sanaa tu, hii Serikali imekuwa ni Serikali ya kubeti. Kwenye kilimo tunabeti? Ndugu zangu kilimo si suala la kubeti mnalolifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ukurasa 30, ili ujue kwamba hii fedha haipo, Waziri anasema:-

“Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2018/2019 kiatilifu aina ya sulphur pamoja na vifungashio vya korosho (magunia) havitatolewa kwa njia ya ruzuku kama ilivyokuwa msimu wa kilimo 2017/2018. Wakulima watauziwa kwa bei ambayo itatangazwa na Bodi ya Korosho.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mpaka leo bei haijatangazwa. Hata hivyo, ukienda kwa wakulima wa korosho sulphur inauzwa Sh.32,000. Ukiendelea kusoma ukurasa huu, utaona mchakato unaendelea unawahusisha na watu wa benki kwenye kukopa huko. Kwa hiyo, inaonyesha wazi kabisa kwamba fedha za korosho zile za export levy ambavo zipo kisheria hazipo, ndiyo maana Mheshimiwa Waziri ameandika haya. Atakapokuja ku-wind up atuambie kama fedha zimelipa Bombardier, shilingi bilioni 206 miaka miwili mfululizo, tunakwenda mwaka wa tatu hazionekani mtuambie. Mnacheza kwenye kilimo mnawadanganya Watanzania, mnawadanganya wakulima wa korosho. (Makofi)

Mhesimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ukienda Mtwara, Tandahimba na Newala kuna Chama Kikuu cha Ushirika kinaitwa TANECU. Hiki Chama wenyewe hawa wanadanganywa, Chama hakifanyi vizuri, kinaendeshwa na Serikali. Nami nakuwa na mashaka, inawezekana TANECU Waziri ana hisa nacho. Moja, mwaka jana TANECU imekopa fedha TIB imeshindwa kulipa Waziri ameindikia Bodi ya Korosho wameikopesha TANECU shilingi bilioni 2 za Bodi ya Korosho, huyu huyu Waziri Tizeba, shilingi bilioni 2. Leo Waziri amekuwa mtu wa benki, wameshindwa kuilipa benki halafu anakaa anakuja anakwambia TANECU wanafanya vizuri kwa kuwapa fedha Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 Waziri Kikwete ameinusuru TANECU ikiwa inadaiwa. Mwaka 2008, 2009, 2010 wameshtakiwa na River Valley wamechukua fedha za wakulima zaidi ya shilingi bilioni moja na kitu wamemlipa River Valley, nimekwambia na kwenye takwimu za korosho zenyewe nimemuonyesha tofauti Mheshimiwa Waziri. Msimu wa korosho wa 2016/2017 ukienda kwenye Bodi ya Korosho Tandahimba wamekusanya tani zaidi ya 70,000 lakini maelezo ya TANECU aliowakopesha fedha wametupa maelezo kwamba tumekusanya tani 68,000, kuna tani zaidi ya 2,500 zimepigwa, ziadi ya shilingi milioni 600 za wana-Tandahimba, anajua, nimempa na takwimu wanaendelea kuibeba TANECU. Kumbe nilikuwa sijajua kwamba wanaibeba TANECU kwa sababu kuna maslahi, wameikopesha shilingi bilioni 2 wanatafuta namna ya kurejesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ambazo zina matatizo makubwa ni kwenye tasnia ya korosho. Leo Waziri huyu hawezi akatuambia sababu ya msingi ya kumuondoa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho. Kama fedha hawapeleki, kama yeye ndiye amemuandikia Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho akopeshe shilingi bilioni 2 lakini juzi wamemtoa kafara Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho. Kama tatizo lilikuwa Bodi ya Korosho kwa nini wasingeondolewa watumishi wote wa Bodi ya Korosho? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya si ya leo, Mkurugenzi wa kwanza ameondolewa hakuna maelezo yanayojitosheleza, Mkurugenzi huyu ameondolewa hakuna maelezo yanayojitosheleza, kumbe maelezo ndiyo yale wanatuma vikaratasi wenyewe maana nina barua yake ya kumuagiza Mkurugenzi kuwakopesha shilingi bilioni 2 TANECU ambapo mpaka leo wamekusanya shilingi bilioni 3 kwa wakulima wamerejesha shilingi bilioni mbili CBT. Kwa hiyo, wana maslahi yao na inawezekana kuna biashara ndani yake wanafanya, mwisho wa siku wanakaa wanatuambia unajua, TANECU ile, kumbe wenyewe wana mipango yao kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakulima wa korosho tuwaonee huruma sana. Mnasema mna nia njema kwenye mazao haya, juzi mtu mmoja sijui ni Waziri sijui ni nani anauliza suala la mbaazi hapa anasema mbaazi ni chakula. Sisi Lindi na Mtwara mbaazi ni chakula na ni zao la biashara na siyo chakula tu. Mnawavunja moyo wakulima, mwishowe mtawaambia watu wa Rukwa kwamba mahindi ni zao la chakula tu na si zao la biashara. Ni Serikali ya namna gani hii? Serikali ya kubetibeti, inakuwaje? Inakuwaje tunabeti kwenye masalhi ya wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapozungumza kumekuwa na danadana kwenye sulphur, kumekuwa na danadana kwenye mambo haya, wanakaa Bodi ya Korosho na...

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kwa tafsiri yako, maana ungenitaka tafsiri yangu ningeifafanua, nakubaliana na tafsiri yako, niendelee kuchangia. Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta ili niweze kuendelea kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayazungumza maneno haya, mfano mzuri kwa nini tunasema tunabahatisha bahatisha. Mheshimiwa Pascal Haonga akiwa anatoa rekodi ya bajeti tunayoipanga humu na namna ya fedha inavyopelekwa kama si kubahatisha ni kitu gani?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru sana, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuja kwangu tarehe 18 Oktoba,2018 kujionea adha ya maji ambayo ipo kwenye Jimbo langu la Tandahimba. Mheshimiwa Waziri alivyofika nadhani ameona kwa machoyake, lakini kwenye mpango huu wa maji Tandahimba tunazungumza sana Mradi wa Maji wa Makonde ambao utahudumia Wilaya ya Newala, Tandahimba na Nanyamba. Shida yangu kwenye huu mradi wanaosema waKitaifa, tulipoingia Bungeni 2016/2017, kwenye kabrasha la kitabu cha bajeti ya maji, ukisoma ukurasa ule wa 78 umezungumzwa Mradi huu wa Makonde tukiwa tunatarajia fedha za mkopo kutoka Benki ya India. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyorudi Bungeni 2017/ 2018, tumekuja tena kwenye ukurasa wa 80, tumeuzungumzia tena Mradi wa Maji wa Makonde tukiwa tunasubiri fedha kutoka kwenye fedha ya mkopo kutoka India. Tumekuja kwenye bajeti iliyofuata 2018/2019, ukurasa wa 64,Mradi huo wa Maji wa Makonde tunaozungumza, tunazungumzia fedha za kutoka kwa wafadhili. Tumekuja kwenye bajeti hii ya leo hii tunayoisema ya 2019/2020 ambayo inawezekana kwa sisi wengine ikawa bajeti ya mwisho tunazungumzia fedha ambazo wanataka kukopa tenasijui wapi, are we really serious tunataka mradi huu uendelee?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia kila tukija kwenye bajeti fedha za Mradi huu wa Makonde tunazungumzia fedha za kutoka kwa wafadhili, kwa miaka minne mfululizo, hizo fedha za wafadhili hakuna, hazitoki, hawa watu kweli watapewa maji? Hebu niwaulize ndugu zangu Serikali ya Chama cha Mapinduzi wanayosema Serikali ya wanyonge,ni mnyonge gani kama mwananchi hapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ndiyo bidhaa pekee ambayo wangekuwa wanawapa Watanzania shukurani yake ingekuwa ni kubwa kuliko kitu chochote kile. Leo zinatengwa fedha mabilioni zinakwenda kwenye Stiegler’sGorge ambao watumiaji wake si wote, fedha zinakwenda kwenye reli watumiaji wake sio wote, fedha zinakwenda kwenye bombardierwapandaji wa bombardier sio wote, waweke fedha kwenye miradi ya maji ambayo itawagusa Watanzania wote. Huu ndio ukomo wa huruma kwa Serikali ya CCM kwa Watanzania. Niwaambie kabisa, kama tunataka kupima ukomo wa huruma kwa Watanzania. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia alichokisema, lakini nimkumbushe hata wakati tunazungumza Mradi waGesi ya Mtwara tulisema ndio itakuwa mwisho wa tatizo la umeme Tanzania. Leo bado tunalia na umeme, kwa hiyo sitaki kuipokea taarifa yake ile akakae nayo kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Taifa la Tanzania ambalo hatuna shida ya maji yenyewe, tuna Ziwa Victoria, kwangu Mtwara tuna Mto Ruvuma, tuna Ziwa Malagalasi amezungumza Mheshimiwa Hasna pale, tuna Ziwa Tanganyika, tuna kila vyanzo vya maji ukienda Kilimanjaro kuna maporomoko yanamwaga maji, miaka 59 toka tumepata uhuru tunarudi Bungeni tunazungumza tatizo la maji kweli miaka 59 ya uhuru!(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,niombe sana, alizungumza hapa Mzee Mheshimiwa Chenge kwamba tunayoyaazimia Bungeni basi tuyasimamie, ile Sh.50 iliyozungumzwa, niombe Jumatatu Waheshimiwa Wabunge wote kwa tatizo la maji namna lilivyo, tusimamie kuona ile 50 inaongezwa ili watu wapate maji. Watu wamezungumza vyanzo vingi tu hapa, ukienda leo watumiaji wa simu bando tu, ukichukua fedha za kwenye bando ni matrilioni ya fedha, kwa nini tusichukue fedha tukapeleka kwenye maji?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,kwenye Mradi wangu mdogo ule waMkwiti, leo nimshukuru sana ameupa fedha, lakini ule mradi una lots tatu, lot ya kwanza ndio hii ambayo amepeleka fedha ya kutoa maji kule kwenye Mto Ngwele ambako pana tanki moja. Lot ya pili utatoa Mto Ngwele kupeleka Mangombyanalot ya tatu inatoka Mangombya kupeleka vijijini, lakini fedha iliyopata ni ya lot moja. Sasa ukiangalia hii lot moja maana yake tutakaa miaka tisa ndio kukamilishe lot tatu watu wapate maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kamatuna lots tatu na fedha ikawa ipo ni bora wakaunganisha fedha wakawapa wakandarasi tofauti ili watu waone social impact ya maji ambayo wanafanya. Leo tutawaambia tuna Mradi waMaji wa Mkwiti lakini si ajabu tukamaliza miaka 10 watu hawaoni matunda ya mradi ule ambao Mheshimiwa Waziri mwenyewe amejionea kwa macho yake. Kwa hiyo nimwombe sana ule mradi utawasaidia wale watu ambao wanatembea kilomita 58 kutoka Mkwiti kwenda Tandahimba ni kilomita 58. Kwa hiyo nimwombe sana kwa unyenyekevu mkubwa, najua wanachapa kazi vizuri, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri lakini na watumishi wa Wizara ya Maji pia wanafanya kazi kwa usiku na mchana waone namna wanavyoweza kutusaidia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kuchangia katika Wizara hii. Mimi nianze kidogo kuweka sawa baadhi ya mambo ambayo yapo kwenye Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Nitaendelea kuunganisha pale alipochangia ndugu yangu Mheshimiwa Antony Komu suala la wasaidizi wa Mheshimiwa Rais kumpotosha kwa mambo mengi sana. Kwenye korosho, hili limetokea, watu wamempotosha sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Mheshimiwa Rais akiwa Arusha alizungumzia suala la kangomba ambalo nataka nikwambie, kwa sisi Waislam hiyo biashara inayoitwa kangomba siyo dhambi, kwa sisi Waislam. Kwa sababu ipo hadithi sahihi kabisa inatoka kwa Ibn Abbas Radhiya Allahu- Anhu, Ibn Abbas anasimulia, alikuta Mtume amefika Madina na alipofika Madina akakuta watu wanafanya biashara ya matunda kwa makubaliano, kwa uwiano wanaokubaliana wenyewe. Mtume alipokuta biashara ile inakwenda, akasema hii biashara siyo haramu. Hadithi hii imepokelewa vizuri kabisa na wapokeaji wazuri kwa sisi Waislam ambao ni Bohari pamoja na Muslim. Kwa hiyo, kangomba siyo haramu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Waziri wa Biashara ambaye upo hapa, kwenye korosho tunajua watu hawajapata fedha mpaka leo; wapo waliopata fedha na upo utaratibu ambao umetumika labda huujui, nikukumbushe tu kwamba mwezi wa Nne zimetoka fedha, mtu anadai shilingi milioni 59 ili ku-rescue situation ionekane wakulima wamelipwa fedha, anaingiziwa shilingi milioni tisa anadai shilingi milioni 41. Hicho ndicho kichokuwepo kwenye korosho. Ukitaka ushahidi, mimi ninayo simu hapa, nimeingiziwa fedha mwenyewe. Nadai shilingi milioni 48, nimeingiziwa shilingi milioni nane, nyingine naendelea kudai na hili unalijua vizuri, unalifahamu vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wakulima wa korosho wameanza kufanya palizi, hawana fedha. Kama hawana fedha, wanatafuta watu wanaingia makubaliano, mtu anampa shilingi 100,000/= wanakubaliana wenyewe kwamba atampa gunia moja la korosho. Mnakaa mnamshauri Mheshimiwa Rais kwamba aliyefanya vile ni kangomba. Hii ni biashara halali kwa sisi Waislam. Kwa hiyo, kangomba siyo haramu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya msingi ya biashara hii ni kwamba Serikali hamjajipanga. Leo Serikali imezungumza kwamba inachukua fedha kuwalipa wakulima, lakini mpaka wakulima wanadai fedha za korosho. Je, mkulima asilime korosho? Anapatikana mtu ambaye amekubaliana naye mwenyewe kwa hiari yake anampa fedha, mwingine anachukua trekta anaenda kulima shamba la mikorosho. Akishalima ekari moja kwa makubaliano kwamba atampa korosho kilo 50, lakini mkikaa mnamwambia Mheshimiwa Rais kwamba wale watu ni kangomba. Wale siyo kangomba. Kwa hiyo, jambo hili lazima Mheshimiwa Waziri alijue vizuri sana ili akitokea, isije mwakani tena watu mkakurupuka mkamshauri Mheshimiwa Rais ndivyo sivyo kwenye korosho.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Katani, ongea nami ujumbe wako uwafikie. Kwa sababu ukiongea nao moja kwa moja sasa, hakuna namna wao wataupata. Wewe ongea na kiti ili wao waupate.

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa hiyo, naomba sana suala hili wakati wanamshauri Mheshimiwa Rais waende kufanya research kwanza, wajue matatizo ya wakulima yakoje? Mwaka huu tutakuwa na tatizo la dawa. Kuna tatizo la wakulima, kulima korosho yenyewe. Leo ukienda Mtwara, mikorosho watu wanawekeza. Shamba lenye ekari 10 mtu anawekeza kwa shilingi 500,000/= tu. Yule aliyewekezwa shamba, akivuna gunia 50 kwa sababu amewekeza na hana shamba, kesho kutwa anataka akuoneshe hati ya shamba, maana yamefanyika mwaka huu. Mtu alikuwa hatakiwi kulipwa fedha, mpaka alipokwenda Mheshimiwa Rais juzi, akasema watu wote walipwe. Huu ni ushauri ambao wasaidizi wa Mheshimiwa Rais wanamshauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye hili, naomba sana Bunge lifahamu vizuri, kwamba kwenye biashara hizo za mazao na siyo kwenye korosho tu, hata kwenye mpunga. Mimi nina trekta Ifakara pale, nalimisha mashamba, mwisho wa siku wananilipa magunia ya mpunga. Ukija kutafuta shamba langu, mimi sina shamba Ifakara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nataka niombe sasa Mheshimiwa Waziri ajaribu kutueleza kama alivyokuwa anazungumza ndugu yangu Mheshimiwa Komu; ile kampuni, baada ya kampuni kushindwa sasa kuilipa Serikali zile tani 100,000 za korosho walizokuwa wameingia makubaliano ya kisheria, watuambie hao INDO Power wanatufidiaje kwa kutudanganya? Maana wamelidanyanga Taifa. Ni lazima tuone INDO Power moja wanashtakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili watulipe fidia kwa sababu Watanzania walikuwa na matumaini kwamba korosho tani 100,000 zimepata mnunuzi, kumbe ni matapeli, Wakenya wamekuja kututapeli na wametudhalilisha wakulima wa korosho ambao mpaka leo hatujapata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la viwanda. Kule Kusini tulikuwa na viwanda vya kubangua korosho takribani 12. Vile viwanda vimeuzwa. Waliouziwa vile viwanda, maelezo yalikuwa waendeleze vile viwanda kwa ajili ya kubangua korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajua, vipo viwanda leo ni maghala ya kutunzia korosho, siyo viwanda vya kubangua korosho. Wakati ana windup atuambie Serikali ina mpango gani kwa wale walionunua viwanda kwa dhamira ya kubangua korosho kwa kubinafsishwa wana mpango gani kuhakikisha wale walioshindwa wana mpango gani kuhakikisha wale walioshindwa kupangua korosho viwanda vinataifishwa, virudi kwa watu ambao wanaweza kupangua korosho ili tuweze kuendelea na tasnia ya viwanda Tanzania? Atusaidie na bahati nzuri alikuwepo kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais na haya ameyasikia mwenyewe na mengine amejionea mwenyewe kwa macho, ajaribu kutusaidia kujua viwanda vile vya korosho mambo yake yanakuaje?(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema lakini nikushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi hii kuchangia mapendekezo ya mpango huu. Niende moja kwa moja kwenye suala la kilimo ambapo ndio pananigusa sana kwa sababu natoka sehemu ya kilimo. Ukisoma mapendekezo ya mpango ipo sehemu inazungumzia kujenga maghala kwenye mazao ya mpunga lakini niliwahi kutoa pendekezo mwaka jana na leo narudia tena wakati anachangia Mheshimiwa Musukuma alisema ipo miradi inapelekwa maeneo ambayo haina return binafsi nilimwelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo unajenga soko lakini return ya soko unalolijenga inarudi kwa muda gani, kuna eneo kama Tandahimba ambalo tunazungumza la korosho unashindwa kupeleka fedha ya kujenga ghala wakati kutunza korosho ghalani ni shilingi 38 kwa kilo moja. Yaani ukiwekeza bilioni 5 Tandahimba return yake kwa Serikali ni miaka miwili kama umewapa mkopo wanakuwa wamerejesha hiyo fedha. Lakini unapeleka kujenga soko sehemu ambayo hakuna hata wafanyabiashara wenyewe. Nilizungumza hizi mwaka jana na leo narudia tena kwenye huu mpango mnazungumza kujenga maghala ya mpunga kwenye kuhifadhi korosho ghalani shilingi 38.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tandahimba wakizalisha tani 74,000 kama walivyozalisha msimu iliyopita maana yake wanakusanya bilioni 2 na milioni mia nane na, ukipeleka fedha hii inaweza kurudisha kwa miaka miwili tu. Niwaombe kwenye mpango wenu muangalie factor hizi mupeleke fedha maeneo ambayo wanaweza kuzirejesha kwa wakati zikaenda kutawanywa maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hapa nataka nilikumbushe sitaki kukumbusha yaliyopita lakini nikumbushe kwenye bajeti ya mwaka jana wakati tunabadilisha sheria ya fedha ile ya korosho sheria namba 203 ninukuu maelezo ya Waziri wa Fedha alisema “ kufatia pendekezo hili shughuli za uendelezaji wa zao la korosho pamoja na gharama za uendeshaji wa bodi ya korosho zitagharamiwa kupitia bajeti ya Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo kama inavyofanyika hivi sasa kwa mazao mengine ikiwemo pamba, kahawa na pareto.” Jambo la kusikitisha tarehe 07 mwezi wa Kumi tulivyokuwa kwenye kikao cha wadau pale, bodi ya korosho na wizara imeleta mapendekezo kwa wadau ya mkulima kukatwa shilingi 25 kupeleka TARI Naliendele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima akatwe 25 kupelekwa Bodi ya Korosho, OC ya bodi ya korosho itozwe kwa mkulima na haya yalikuwa ni maelezo mazuri ya Waziri japo mwanzo tulikuwa tunafanya argument ya kukataa ile 15% kwamba ibaki bodi ya korosho lakini Serikali ilivyoshawishi tukakubali tukaona kabisa kwamba hiyo 15% ya export levy ambayo inapoinunua korosho leo 2700 maana yake kuna zaidi ya 380 na inakwenda kwenye mfuko mkuu, leo wanakatwa mkulima shilingi 50 inakwenda TARI ambayo mmeingia makubaliano na Ox-farm mnapata zaidi ya bilioni 70 leo mnakwenda kumnyonya mkulima huyu tena. Kikao kimekataa lakini wizara mnasema mmetumwa na wakubwa, wakubwa gani ambao hawana huruma na mkulima? Ni wakubwa gani ambao wamewatuma ambao hawana huruma na mkulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwenye mapendekezo ya mpango mwaka jana mmezungumzia uzuri mara nyingi tunaenda mbele tunarudi nyuma. Ni mwaka juzi Waziri Mkuu alisimama hapa akasema kumwondolea mzigo mkulima anaondoa tozo tano, tozo tano leo zimerudi tena mkulima yupi anayesaidiwa Tanzania? Niombe sana kwenye mpango huu tunapotafakari mapendekezo ya mpango wa maendeleo tuguse maslahi ya watu kwanza.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Katani kuna taarifa, Mheshimiwa Naibu Waziri kifupi

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi tu nilitaka nimpe taarifa ndugu yangu Katani kwamba tozo hii imejadiliwa kwenye kikao cha wadau ni kwa mujibu wa sheria na hakukuwa na mkubwa yoyote aliyeongoza kile kikao, kikao kile kiliongozwa na wadau wa kilimo.

Kwa hiyo, hakuna maagizo kutoka kwa mkubwa yeyote. Kama kuna any concern kuhusu tozo hii, utaratibu upo wazi, kikao cha wadau kikae kifanye maamuzi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Katani unapokea hiyo taarifa?

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake lakini pia na wewe nataka upate uelewa pia. Wadau wanaozungumzwa ndio walikataa kwenye kikao na clip ya audio ya mazungumzo yale yapo hili ni jambo limeletwa na Serikali sio jambo ambalo wadau wamelipitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unayo Mamlaka, unayo nafasi tukisubiri wadau tu, wadau ndio walileta baadhi ya sheria ambazo tunazibadilisha humu, wadau hao ndio wamekataa, huu ni mpango wa Serikali kutaka kumnyonya mkulima, tusitengeneze maneno mengine. Wabunge walikuwepo hao waulize wote tulikataa pale sasa hili ni jambo ambalo inawezekana ulikuwa hulijui, nimeamua niliweke hapa kwa sababu nimeona kwenye suala la mapendekezo ya mpango na hili lilizungumzwa na Serikali mwaka jana vizuri kwamba fedha za bodi zinatoka wapi, fedha za kuendeleza zinatoka wapi hao TARI wana bilioni 70, dola milioni 32 ox-farm wameshafikia makubaliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unakwenda kwa mkulima huyu mnyonge na ninyi mawaziri mnajua kwamba tunatoka kwenye mazingira magumu mliangalie hili kwa namna pana sana wala halihitaji majibu ya mhemuko, linahitaji kufanyiwa kazi kwa kuwajali wakulima wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ana dhamira njema na wakulima. Waziri Mkuu ametoa tozo ambazo zimerudi hapa kwa namna nyingine, kwa mlango wa nyuma. Naomba sana, kwenye mapendekezo haya ya mpango mwangalie mambo ambayo yanaweza yakatupa tija kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, mimi natoka vijijini. Naendelea kuungana na wenzangu walioshauri, fedha zile zinazokwenda TARURA kwa kweli hazikidhi mahitaji. Mfano mzuri, leo ukienda Jimboni kwangu ambako korosho zinatoka vijijini ili zifike bandarini pale, vijiji vile havipitiki. Fedha zinazokwenda TARURA, mbovu. Toka Nanyanga, pita pale unaenda Mdimba barabara haipitiki, lakini ni sehemu ambayo uzalishaji wake wa korosho wanazalisha zaidi ya tani 3,000 za korosho kwenye kata moja, lakini barabara ni mbovu, magari yanachakaa.

Mheshimiwa Spika, sasa badala ya kuzipeleka fedha TANROADS kuwe na uwiano aidha unaofanana, nusu kwa nusu; nusu mpeleke TARURA kwa sababu wanahudumia wananchi wengi kuliko hata TANROADS ambayo tunaitumia au 60 kwa 40. Asilimia 60 iende TARURA ili barabara za vijijini nazo ziweze kupitika. Mtakuwa mmewasaidia Watanzania wengi kuliko sisi ambao tunapata fursa tunapita kwenye ndege, siku nyingine kwenye magari, lakini vijijini wao kila siku shughuli zao zinahitaji barabara ziwe zinaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tafakari kwenye hili ikiwezekana mnavyoleta Mpango wenyewe sasa, basi tukute TARURA inakwenda asilimia 60, TANROADS inabaki asilimia 40 ili tusogeze mbele gurudumu la maendeleo la Taifa letu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwanza kukushukuru, lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo. Moja niipongeze Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambayo iko Mtwara kwa kiasi kikubwa kwa fedha ndogo ambazo wamepewa wameweza kusimamia vizuri na kuwafikia watu japo tatizo la fedha ya korosho kwa wakulima limekuwa kubwa. Na hili nadhani linafahamika vizuri nilizungumza wakati nachangia Wizara ya Viwanda lakini leo narudia tena kwa Wizara yenyewe ya Kilimo. Leo tunapozungumza simu yangu hapa nikikuletea ina message zaidi ya 700 watu wanalalamika hawajapata fedha, tatizo limekuwa ni fedha. Sasa Wizara ya Kilimo mtusaidie mkishirikiana na wenzenu wa Biashara tatizo la fedha ya korosho kwa wakulima lini zitapatikana fedha zikawafikia wakulima wakaweza kupalilia mikorosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliwaambia leo mikorosho watu wanakodisha shamba la heka 100, heka 80 mtu anakodisha kwa milioni tatu ili mradi tu aone kwamba sasa sina cha kufanya, watu wameshindwa kuwapeleka watoto shule kwa ajili ya fedha ya korosho hakuna, watu wameshindwa kufanya parizi la mikorosho kwa sababu ya fedha hakuna, lakini kuna shida ambayo naiona, nilisema ukienda maeneo ya Lindi kwa Mheshimiwa Nape, ukienda Kata ya Nachunyu leo korosho zinahitaji kupulizwa watu wale hawana dawa kwa sababu hawana fedha sijui Serikali inataka kutueleza nini wakati mna- wind up mtuambie mkakati thabiti wa fedha za wakulima wa korosho zitakwenda lini. Tunajua kazi mnaifanya kubwa kwa sababu jambo lenyewe hamkujiandaa nalo, kazi mnayoifanya kubwa lakini tatizo la fedha ni kubwa kuliko linavyodhaniwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hata maelezo na takwimu niliwahi kukwambia Mheshimiwa Waziri kwamba takwimu mnazozitoa mara nyingi haziko sahihi, ukienda Tandahimba rejection ya Benki imekuwa kubwa. Kwa hiyo, kitakachozungumzwa kimelipwa ukienda kwenye uhalisia ni tofauti kabisa Watanzania hawa wakulima wa korosho dhamana yao na azma yao ya kupata fedha ni lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikubaliane na mawazo yenu mliyosema kwamba tuweke bima. Bima inaweza ikasaidia kwenye mazingira kama haya tunayokuwa nayo, ingetusaidia sana lakini bahati mbaya sisi Wabunge tuna bima za kila aina lakini kwa wakulima wa korosho ambao ndio nguvu kazi ya nchi hii hawana bima. Linapotokea anguko la biashara ya korosho kama hili hatuna kwa kukimbilia sasa niwaombe sana muone utaratibu na namna nzuri ambao mnaweza mkaweka jambo hili sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumza Wizara ya Biashara suala la Kangomba na nyie ndio wenye korosho wenyewe nataka niwaambie kwenye korosho kule wakati wa korosho kuna wakinamama wanauza mchele wanabadilisha kwa korosho yaani ni butter trade system ipo, Mheshimiwa Mgumba umekaa kwenye korosho unayajua haya mnapokaa mkazungumza mambo ya kangomba na nyie watu wa kilimo mpo na mpo mliokaa kwenye korosho Mheshimiwa Omary umekaa kwenye korosho unajua, wakinamama wanapika maandazi wanabadilishana korosho.

Mheshimiwa Spika, kesho akipeleka korosho unatka kuonesha shamba ni kweli haya mambo mnayoyafanya? Haya kweli mnayoyafanya yako sahihi? Butter trade system ipo kwenye Mpunga, ipo kwenye Kahawa, ipo kila mahali ambapo mkulima anafanya biashara, sitarajiii itatokea miujiza tena ya kukaa mtu ukazungumza Kangomba japo Mheshimiwa Waziri unasema utatafutwa mfumo rasmi wa kurasimisha kangomba iwe jambo ambalo lipo kisheria. Lakini kwenye biashara hii hakuna jambo hilo haliwezekani yaani haupo utaratibu ambao utaupata ukasema hili unataka uliweke kisheria kwa sababu sheria hiyo itakataa tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ulivyosema kangomba haya huna dawa mkulima asipulize korosho, unataka mkulima asizalishe korosho huna dawa anapatikana tajiri anasema bwana chukua 100,000 anakwenda kununua salfa akienda kununu salfa muda wa msimu yule aliyetoa fedha anapewa korosho unamwambia akuoneshe shamba la korosho alitoe wapi wakati yeye amemsaidia mkulima, nyie Serikali leo mnashindwa kumsaidia mkullima, kama hela yake ya korosho hajapewa unataka alime na nini? Mimi nilikuwa nataka ingewezekana ufanye uombe siku tatu tu Bungeni hapa kusiwe na posho au kitu gani tuone kama tutajaa humu. (Makofi)

SPIKA: Hiyo haikubaliki Mheshimiwa Katani.

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, labda tungepata uchungu wa watu wa korosho ukoje siku tatu tusema hamna posho hamna nini viti hapa kama havikubaki vinane hapa, lakini kwa wakulima hawa wana dhambi gani? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nikushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, nami niungane na wenzangu kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya. Lakini nina mambo kadhaa ambayo ningependa nipate ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, sisi Mtwara pale tuna mitambo ya kuzalisha umeme, tunayo mitambo 11. Na Mheshimiwa Waziri unajua kila mtambo mmoja unazalisha megawati mbili kwa maana ya mitambo yetu 11 inazalisha megawati 22, japo miwili ni mibovu, na ninajua una taarifa hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye matumizi ya Mkoa wa Mtwara na Lindi kwa maelezo ya nyie wataalam wa umeme mnasema tunatumia megawatts 15 na tunakuwa na ziada ya megawats tatu, mara nyingi huwa napata shida mnaposema tunaziada ya megawatt hizo tatu kwasababu kama leo Tandahimba yenye vijiji 156 ina vijiji takriban 88 havina umeme lakini ukichukulia hesabu ya mkoa mzima wa Mtwara una vijiji vingi havina umeme kuliko vyenye umeme. Sasa sijui hii extra inaonekana kwamba inapelea, inapelea namna gani wakati watu kule hawapati umeme mtatusaidia kitaalamu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nirudi kwenye suala la mradi huu wa REA Mheshimiwa Waziri nashukuru sana tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara juu ya mkandarasi ambaye tunaye Mtwara, kwenye Jimbo langu nina vijiji 30 ambao vilitakiwa viwe na umeme na mkataba baina ya Serikali na yule Mkandarasi unaishia tarehe 30 Juni ya kesho kutwa lakini mpaka sasa ninapozungumza na wewe vijiji vitatu ndiyo wamewasha umeme sina hakika hizi siku zilizobaki anaweza kuwasha umeme kwa vijiji 27 ambavyo vimesalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niliwahi kukwambia kwa Jiografia ya kwetu kwa Jimbo langu la Tandahimba maeneo makubwa yenye watu wengi nikakwambia juzi nilikutumia na meseji Kata kama Mdimba ina wapiga kura tu elfu nane na kitu. Maana yake hiyo sehemu ina watu zaidi ya 12,000 au 13,000 na Kata nyingi za Tandahimba zina uwingi wa watu ukienda Tandahimba kwa uzalishaji wa korosho wa miaka mitatu, nyumba nyingi zimeshafanya wiring zinasubiri mapokeo ya umeme ukienda nyumba nyingi zimefanya wiring. Leo watu wanapata shida ya umeme ambao tuliamini kabisa kwa sisi watu wa Mtwara ambao gesi ambao tunasema asilimia 50 ya umeme tunaotumia ndiyo unatokana na gesi, lakini Mkoa wa Mtwara ndo unalalamika hauna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliwahi kwenda kwa Mheshimiwa Simbachawene nikapata maajabu makubwa vijiji vyake vyote vinawaka umeme. Lakini Mtwara ambako gesi inatoka leo tunakaa kulalamika umeme, umeme, umeme sasa hili Mheshimiwa Waziri niombe mnafanya kazi kubwa sana lakini kwa watu wale wa Mtwara ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na mradi ule tukazungumza habari ya mabomba hayo wale hawana umeme wapelekeeni umeme basi iwe kifuta jasho chetu tumepata umeme na wale wanauwezo wa kulipa hiyo 27,000 hata mngesema walipe 50,000 wanauwezo wa kulipa lakini umeme haujawafikia watu wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, nimuombe sana kwenye jambo hili tunapoenda kwenye REA hii basi uingize vijiji vile vilivyobaki tuone suala la umeme kwa namna mlivyoandika hiyo 2021 watu wawe wamepata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwanzo mlizungumza suala la viwanda ambavyo mama Ghasia amegusia suala la kiwanda cha Mbolea Msanga Mkuu, lakini mlizungumza suala la kiwanda cha Mbolea Kilwa Masoko kwenye kitabu chote cha Wizara sijaona hilo jambo sasa wakati una-windup utatuambia kwamba haya mambo ya viwanda hivi vya mbolea Kilwa Masoko, Mtwara kama vimepotea tujue vimepotea na kama vipo tujue vipo kwenye hatua gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la LNG ambayo wenzangu wamepongeza. Nipongeze lakini napata mashaka makubwa sana jambo hili limekuwepo tangu tunazungumzia suala lenyewe la gesi 2010 likazungumzwa suala la LNG Lindi, na tukaamini tutakuwa miongoni mwa maeneo ambayo uchumi wake ungepanda kwa kasi kusini ni pamoja na kama mngekweli mngejenga hii LNG. Leo mmehuisha mazungumzo kama mnavyosema tuone sasa haya mazungumzo mnayoyasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. KATANI A. KATANI: MheshimiwaSpika, nikushukuru sana na nadhani unajua kwamba mimi nikizungumza bajeti ya Wizara ya Fedha mimi naangalia sana kwenye kilimo kwa sababu asilimia 95 ya watu wangu wa Tandahimba ni wakulima.

Mheshimiwa Spika, ukisoma Fungu 43 la Wizara ya Kilimo fedha iliyokuwa imetengwa ilikuwa kama shilingi bilioni 98.11 ya kugharamia miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi, 2019 fedha iliyokwenda ni asilimia 42 tu. Sasa kwa sisi wakulima maana sisi wengine ni wakulima typical kama imekwenda asilimia 42 Waziri wa Fedha nadhani hapa si sawa, pana namna ambayo unapaswa uangalie uone sekta hii ya kilimo ambayo kwa Taifa la Tanzania asilimia 85 ni wakulima, fedha inayotengwa ya maendeleo inakwenda angalau asilimia 70 ili kilimo hicho tunachokisema tukione kimekuwa.

Mheshimiwa Spika, lakini mmezungumza suala la ukuwaji wa asilimia tano kwenye sekta ya kilimo ambayo mimi napata mashaka kidogo, kwa sisi wakulima wa korosho ambao tulizalisha tani zaidi ya 300,000 mwaka 2017/2018 na msimu uliopita tumezalisha tani laki mbili na kitu tukaona kwamba kuna ukuaji unaongezeka kidogo ninyi wataalamu wa hesabu mnaweza mkatupa tathmini hiyo mnaitoa kwa vigezo gani.

Mheshimiwa Spika, lakini limezungumzwa hapa kwenye suala la kilimo tulikuwa na mfumo ule wa fedha ile export levy ambayo iliondolewa na mzee wangu pale Kamala alikuwa ameomba kwamba Serikali sasa ione namna bora ya kuleta pembejeo za ruzuku kwa ajili ya kusaidia wakulima. Hili nadhani Mheshimiwa Waziri uangalie kwa namna ya pekee sana, itakuwa jambo muhimu na busara sana kwa wakulima suala la ruzuku. Kwetu sisi kwenye korosho mfano msimu huu tusipopata ruzuku kutoka tani 200,000 hizo zinazozungumzwa kuna uwezekano mkubwa msimu huu tunaokwenda tunakwenda kuzalisha tani 80,000.

Kwa hiyo, ni ombi langu kwa Wizara ya Fedha ambayo mwaka jana fedha zetu zimechukuliwa, tumesamehe, zimekwenda, tuone basi namna ya ku-recover hili jambo at least wakulima wapate ruzuku ya pembejeo ya korosho ili tuende kuanza msimu vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini nizungumze suala la miradi ya mikakati, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kuna siku nilikuandikia memo pale nikiwa nakwambia Tandahimba ambayo ndiyo wazalishaji wakubwa wa korosho mradi wa mkakati ambao walishaleta na mradi ule godown mmeshindwa kupeleka Tandahimba ambako wanazalisha tani zaidi ya 70,000 unakwenda kujenga ghala sehemu inayozalisha tani 10,000 hizo fedha mnazopeleka kwenye tani 10,000 return yake itakuwa kwa muda gani? Kwa sababu hizo fedha mngepeleka Tandahimba wanakozalisha tani 70,000 maana yake baada ya miaka miwili, mitatu kulikuwa na possibility kubwa ya fedha zenu kurudi, lakini unapopeleka fedha, mmepeleka fedha Mkuranga ambako wanazalisha tani 4,000 ukaacha kupeleka fedha Tandahimba wanakozalisha tani 74,000 ninyi wenyewe wataalamu wa uchumi sijajua, sijajua kitaalamu mnafanya utaalamu wa namna gani? Mnataka fedha zirudi ziweze kuwasaidia watanzania wengine au mnapeleka sehemu ambako fedha zitakaa miaka 15, 20 tukawa tunaendelea kulalamika matatizo ya fedha.

Ombi langu kwa Serikali, miradi hii ya mikakati pelekeni kwenye Halmashauri ambazo zinaweza kurudisha fedha, mfano Tandahimba ambayo inazalisha korosho zinauwezo wa kuzalisha tani 70,000 ina uwezo wa kuzalisha tani 80,000 ungepeleka mradi wa mkakati kama wa godown ambao Halmashauri ishawaletea mradi huo na bahati nzuri ulikuwa vizuri sana, return yake ilikuwa ya muda mfupi, leo inawezekana tungekuwa tumeshaanza kurejesha. Niwaombe sana muangalie mambo haya kwa namna ya kibiashara na kuona namna mnavyoweza kuzichukua fedha kupeleka sehemu nyingine.

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana watu wa Wizara ya Fedha tumeona Benki ya Kilimo, Mwanza wakati tumeenda wakati wa Kamati ya Kilimo tumeona wenzetu mmewapelekea tawi kule, lakini nimesoma kitabu chako Mheshimiwa Waziri nimeona Dodoma pana tawi, lakini nimeona mna maandalizi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kule Mbeya, nione sasa kuna umuhimu wa makusudi kabisa kwa sehemu yenye uzalishaji mkubwa mfano wa korosho Mtwara nako kuwe kwenye mpango wa kupeleka Benki ya Kilimo ili at least watu wale wapate mikopo…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Katani.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nimshukuru Mheshimiwa Rais ambaye ni Mjumbe namba moja wa Chama Cha Mapinduzi na wajumbe wengine kwa kupendekeza jina langu kurudi kwenye kinyang’anyiro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikishukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi kwa sababu ndicho chama kinachotekeleza ilani na mambo yanakwenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia dada yangu Mheshimiwa Halima akipongeza watu mkawa hamumuelewi. Amesema Awamu ya Tano yapo yanayofanyia mazuri, ndicho alichosema, msipate shida sana, wataelewa tu, wamekuja na wataendelea kuja wala msipate shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasimu hii ya Mpango iliyoletwa kuna mambo ambayo at least nataka niishauri Serikali. Ukisoma maelezo ya rasimu ya Mpango wa 2021 na ile yenyewe ya 2021-2026, kwenye suala la kilimo ambalo tumelizungumza na mimi nagusa sana kilimo kwa sababu asilimia 98 ya jimbo langu ni wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Waziri wa Mipango, tunapokwenda kuileta bajeti yenyewe ya mpango kabisa Wizara yetu ya Kilimo ambayo ukisoma Bajeti ya mwaka 2019/2020 ilitengewa asilimia moja tu ya bajeti kuu. Kilimo ambacho kwa maelezo yenyewe ya mpango yanasema kinaajiri watu zaidi ya asilimia 65, sasa reflection yake Watanzania wanaotegemea kilimo ni wengi bajeti inayokwenda kwenye kilimo ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda kusoma hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo amekielezea kilimo kwa mapana yake sana ukurasa ule wa 13 ameelezea vizuri sana. Nami hapa nataka Waziri wa Kilimo anisikilize vizuri sana. Mwaka 2017/2018 waliondoa fedha ya export levy ambayo ilikuwa inawapelekea wakulima pembejeo. Rais kwenye ukurasa huu wa 13 ametoa maneno ambayo nadhani Wizara ya Kilimo wana kitu cha kufanya na nataka ninukuu ili yawe mwongozo kwa Wizara. Mheshimiwa Rais anasema; “Kwa msingi huo, kwenye kilimo tunakusudia kuongeza tija na kukifanya kilimo chetu kuwa cha kibiashara. Lengo ni kujihakikishia usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwandani na pia kupata ziada ya kuuza nje. Ili kufanikisha hayo tutahakikisha pembejeo na zana bora za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea na viuatilifu vinapatikana.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Wizara wanatakiwa waende kwenye extra mileage na ndiyo maana tunataka mpango u-reflect na bajeti zao. Mheshimiwa Rais ameshaonesha dira hii kubwa, hii dira iwafanye watu wa kilimo sasa, kwa wakulima wetu tatizo la pembejeo tuone limekwisha, wakulima wetu tuone suala la dawa limekwisha. Rais amekwenda mbali mpaka matrekta, matrekta haya ya wakulima yanaishia mijini tu. Ukienda vijijini hakuna mtu anajua trekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wizara ya Kilimo waende mbali zaidi. Hii nchi ina ardhi ya kutosha. Wakulima hawa wanapaswa sasa waache kutumia jembe la mkono. Tunapokwenda kwenye uchumi wa kati wa viwanda ni lazima twende mbali ambako wakulima tutawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo hiki zao la korosho ndiyo zao pekee duniani lenye makato makubwa na mengi kuliko zao lingine. Sasa Wizara hapa wana jambo la kutusaidia. Kwenye korosho peke yake mapato yanafika 745, ukiacha hayo ambayo wanayaona kwenye mjengeko wa bei wa 226, lakini ukienda ukaangalia export levy, ukaenda ukaangalia ndani kuna waendesha maghala shilingi 38. Jumla ya makato tu kwenye korosho ni zaidi ya 745, hakuna zao lolote Tanzania ambalo lina makato makubwa kama korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima wafike mahali waone kwamba wakulima hawa wa korosho waende kwenye makato wanayoyakata kwenye pamba, alizeti, mahindi kuliko mzigo huu mkubwa. Tutaendelea kulalamika bei ya korosho ni ndogo kumbe makato makubwa wanayachakata Serikali. Tuone namna ya kuendelea kuyapunguza makato ya wakulima hawa kwa sababu yamekuwa mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Rais alivyokuja kwenye kampeni alishatuahidi watu wa kusini, kuna barabara ile ya kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala na ipo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Tuone sasa tunapokwenda kwenye bajeti barabara hizi zinatengewa fedha za kutosha ili tunapofika 2025, story ya barabara kwa eneo lile iwe imekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji; tumekuwa kwenye tatizo la maji kwa muda mrefu sana. Kuna wakati amekuja Makamu wa Rais akatuahidi tungepata fedha za Mradi wa Maji wa Makonde. Badala yake tumerudi hapa miaka mitano Mradi wa Makonde umesogezwa umekuja kwenye miji 28. Tuone sasa Serikali inatenga fedha kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Makonde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kuungana na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini asiyeshukuru kwa kidogo hawezi kushukuru kwa kingi. Nishukuru sana kwa huduma aliyotupa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa Taifa hili la Tanzania. Bado alama aliyoiacha itakuwa kumbukumbu kwa vizazi na vizazi. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii ya bajeti ya Waziri Mkuu nitajikita sana ukurasa wa 30 ambao umezungumzia sana suala la kilimo. Moja, nipongeze watu wa Wizara ya Kilimo ambao wanaleta pembejeo kwa wakulima, lakini ombi langu kwao walete pembejeo hii kwa wakati. Maeneo ya Masasi korosho zinaanza kupuliziwa dawa kuanzia mwezi wa sita mwanzoni kabisa. Hata baadhi ya maeneo ya Lindi ukienda kule Nachunyu Lindi korosho zinapuliziwa dawa mapema sana. Sasa ni matarajio yangu mkakati huu wa kuleta pembejeo ni vyema ziletwe kwa wakati sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nishauri sana Wizara hii ya Kilimo wakati wanaleta pembejeo wawaambie wakulima mapema sana ni kiasi gani cha fedha watakatwa ili wawe na awareness kwamba hizi pembejeo wanazopewa leo bure siyo kwamba wanapewa bure ni ili baadaye waweze kulipa. Sasa ni vizuri mkatoa mchanganuo wanachotakiwa kulipa kwa wakati huu kabla ya kufika wakati wamelima, wamevuna then ukaleta tu mchanganuo ambao unaweza ukawachanganya wakulima. Hili nishauri sana lifanyike sasa mapema ili liweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa ule wa 30 umezungumziwa mfumo wa TMX, niipongeze Serikali imesema mfumo ule kwa sasa hautatumika. Kwenye hili nataka nitoe takwimu ili Wizara ione kwamba TMX kwa sasa haifai. Msimu wa korosho 2016/2017 tumeuza korosho mpaka Sh.4,000, msimu wa korosho 2015/2016 tumeuza korosho mpaka Sh.3,700. Hata hivyo, TMX ambayo imeanza kufanyiwa majaribio kwenye korosho na ufuta msimu wa mwaka jana kwenye korosho za Tandahimba zile za TANECU kwenye tani 51,000 TMX imeuza tani 4,600. Ukioanisha na bei TANECU wameuza bei kubwa zaidi ya Sh.2,700 ukilinganisha na TMX ambayo imeuza kwa Sh.2,500.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanunuzi wake wa TMX ni wale wale wanaokwenda kwenye mnada wa kawaida. Sasa kwa namna hiyo tumeshaona wazi kwamba TMX imefeli. Kama kuna majaribio ya kwenda kufanyabiashara TMX isiwe kwenye korosho na ufuta huku kwenye korosho na ufuta uachwe utaratibu ule ambao umezoeleka ambao ni mfumo wetu wa Stakabadhi Ghalani ambao wenyewe umeleta tija kwa wakulima, kwa misimu mitatu wakulima wamepata neema imekuja TMX hamna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nipongeze hotuba maana Waziri Mkuu amesema TMX isitumike nisisitize haimfai mkulima siyo wa korosho tu hata wa pamba, watu wa pamba msiingie kwenye huu mtego. TMX ni mtego mkubwa sana, sisi wa kwenye korosho tumefanya majaribio tumeona kati ya mnada wa kawaida na mnada wa TMX, wa kawaida umekuwa bei juu kuliko TMX. Kwa hiyo hii, TMX ni ugonjwa ambapo naomba Wizara ya Kilimo msiujaribu kabisa, uondoeni kwenye mfumo, hauwafai wakulima hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasisitiza sana hili kwa sababu hii tumeiona. Niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwenye korosho kuna kitu kinaitwa moisture ni unyaufu ambapo korosho ikiwa mbichi ukienda kuipima unapokwenda kwenye mfumo wa TMX kwa ajili ya kusema unapeleka sales catalogue kule mnunuzi anaporudi huku akakuta korosho iko tofauti TMX hana msaada wowote kwa mkulima. Mfumo wetu wa kawaida mnunuzi anakwenda anaiona korosho, tunaposema korosho hii auta ni 51 anaiona site pale, huyu TMX kwanza wanunuzi wake ni hawa hawa madalali siyo wenyewe wa Ulaya, hawa wanaofanya TMX ni akina Alibaba wako Ulaya na mambo yao yanaenda hivi. Kama mnaweza kuleta viwanda vya kubangua korosho mka- process korosho, mnaweza mkafanya TMX, lakini kwa hii raw cashewnut tuacheni kwenye mfumo huu tuliokuwa nao na tuliouzoea tutamsaidia mkulima kwa namna kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, hili mtatusaidia ninyi watu wa TRA, kuna mashine hizi za EFD, sisi wengine kule tunafanya biashara kidogo. Tuliambiwa tukinunua mashine zile tutarejeshewa fedha baadaye. Tumelipia Sh.590,000 mpaka Sh.600,000 lakini ukikaa baada ya muda fulani unakwenda ku-upgrade ile mashine unalipia shilingi 80,000. Sasa mbona tunapokwenda kwa wenzetu hawa wa TANESCO wakishatupa meter tumeshamaliza, sisi tunalipia tu kila wakati kwa nini? Sasa hawa wa TRA na EFD, moja, waturudishie fedha kama walivyosema maana ni mali yao ile siyo mali ya mfanyabiashara, EFD machine ni mali ya TRA, ni mali ya Serikali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, nami nitumie fursa hii kukushukuru kwanza wewe. Vile vile nisiwe mchoyo wa shukrani, nami nawashukuru sana Waziri wa Maji, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu wa Maji pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana. Ni imani yangu kwa michango hii ya Wabunge, bajeti yenu itapitishwa bila mihemko yoyote kwa sababu mnafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Wizara ya Fedha, tunakaa hapa Wabunge kwa sababu ni ukweli wa dhahiri kwamba tatizo la maji kwenye nchi yetu bado ni kubwa. Sasa ni vyema Wizara ya Fedha, hii bajeti ambayo Wabunge tunakaa kuwasifia Mawaziri wanafanya kazi kubwa, wanatembelea miradi, wanajua changamoto, kama hawakupewa fedha hizi sifa zote tunazowapa hazitakuwa na tija kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuchangia pale alipochangia dada yangu, Mheshimiwa Agnes Hokororo. Sisi watu wa Mtwara ukiangalia kwenye bajeti tunao mradi ule wa miji 28, nasi tupo kwenye mradi wa Makonde. Napata mashaka makubwa; mimi na Mheshimiwa Waziri tumeingia Bungeni pamoja mwaka 2015, mradi huu wa miji 28 mnaousema tumeanza kuimba nao mwaka 2015. Miaka mitano tumemaliza tunazungumzia habari ya mradi wa miji 28, fedha zinatoka India. Huu mradi hebu mtuambie ukweli wake. Maana tusije tukawa tunaimba ngonjera ambayo tunajitekenya wenyewe, tunacheka wenyewe. Miaka mitano mradi huu wa miji 28, kila tunapokuja mnauzungumzia. Ukweli wa mradi huu uko wapi? Tusiwape matumaini wananchi.

Mheshimiwa Spika, 2017, Rais wa sasa, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan alikuja Tandahimba, akazungumzia mradi huu wa miji hii na akasema tunapata fedha kutoka Exim Bank ya India. Leo tunaingia miaka sita tunazungumza story ile ile, Watanzania wanataka maji.

Mheshimiwa Spika, Mtwara dada yangu amewaambia, tunao Mto Ruvuma. Jimbo langu mimi la Tandahimba kutoka Tandahimba Mjini kwenda Mto Ruvuma hazizidi kilometa 16, lakini watu wake hawana maji. Kama mmeweza kutoa maji Ziwa Victoria mkayatembeza zaidi ya kilometa 400 na uchafu, yanakwenda mpaka Tabora, yanakuja mpaka Dodoma, mnashindwaje kutengeneza mpango Mto Ruvuma ukatoa maji ukapeleka kilometa 16, 60, 70 hadi 100 Mkoa wa Mtwara tukawa tumemaliza kabisa tatizo la maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimegundua ninyi mna dhamira njema, lakini kule chini, alipokuja DG wa RUWASA Tandahimba, tumekwenda kwenye chanzo cha maji Mauta, kulikuwa na Mradi wa Maji Mkupete, maji yalikuwa hayatoki. Amekuja, baada ya siku tatu watu wale wameanza kupata maji. Kumbe hapa juu ninyi mko vizuri sana, hebu mulikeni kule chini. Tuleteeni wataalam ambao wataleta matokeo ya maji kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto ni ndogo, wataalam mliowaleta chini wengine wamezeeka, wapumzike. Lete damu mpya msogeze gurudumu watu wapate maji. Kama watu walikuwa wanakosa maji muda wote, DG kaja siku ya tatu maji yanatoka mpaka Maheha. Kumbe wakati mwingine changamoto ni watendaji hawa.

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamechangia hapa kwamba watendaji wa RUWASA ni wachache. Kama ni wachache mwone namna ya kuajiri watu wengine kwa sababu tunapozungumzia Jimbo kama Tandahimba lenye vijiji 147 na vitongoji 60 ukawa na wafanyakazi wanne, sidhani kama kukitokea changamoto Mkwiti kwenye mradi mkubwa wa maji wanaweza kuukimbilia kwa haraka kule.

Mheshimiwa Spika, pia watu hawa wa RUWASA hawana vitendea kazi, na lenyewe mliangalie. Sisi tunaokaa Wilaya ambazo zenyewe ziko scattered, yaani ukitoka Tandahimba unakwenda Jimbo la Mheshimiwa Nape, kilometa 61, una wafanyakazi watatu, wanajigawaje? Hawana pikipiki, hawana magari, hata ikitokea changamoto hawa watu wanakwenda kutatua tatizo Mkwiti kwa namna gani?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana, kwenye Mradi wangu wa Mkwiti kama mkiangalia kwenye maandiko yenu, ule mradi ulipaswa kukamilika mwaka 2018, lakini nimesoma kwenye bajeti bado fedha mliyoitenga kwenye Mradi wa Maji wa Mkwiti haiendi kutatua tatizo la maji kwenye Kata zile ambazo kipindi cha mwezi Juni mwananchi ananunua maji shilingi 1,500 kwa ndoo. Ikifika mwezi Juni tu hapo, watu wa Mwangombya, Mkwiti, Likolombe, Namindondi, Ngunja, Mmeda, Litehu, wanapata shida kubwa ya maji.

Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna dhamira ya dhati ya kuona kwamba tunataka tukamilishe tatizo la maji, basi wekeni fedha inayojitosheleza. Kama mradi ulipaswa kukamilika 2018 haukukamilika, leo malizieni fedha ili watu wale wawe wamepata maji na tumtoe mzigo mama ambaye anakunywa maji ambayo siyo salama.

Mheshimiwa Spika, nikwambie tu, sisi wanadamu bahati tuliyokuwa nayo, katika matumbo yetu kuna zahanati. Maana maji wanayokunywa watu wetu, usiku wanakunywa mbweha, asubuhi wanakunywa binadamu. Mungu ametujalia kuwa na zahanati tu, tunajitibu wenyewe. Vinginevyo, matatizo yangekuwa makubwa sana.


Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, niungane na Wabunge wenzangu wanaotoka mikoa ya kusini. Moja niunge mapendekezo ya Kamati ya Kilimo kuhusu Sheria ile ya Mfuko wa kuendeleza zao la korosho ambao mwaka 2018 Spika ukiwa kwenye Kiti hicho ililetwa sheria ile tukaibadilisha Sheria Na.17A. Kamati imependekeza vizuri kwamba sheria ile irejeshwe ili kumlinda mkulima huyu ambaye asilimia 65 ya fedha ile ilikuwa inakwenda moja kwa moja kwenye pembejeo, Bodi ya Korosho na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, mheshimiwa Nape amezungumza jambo mahususi hapa kwa sababu kwa matamko ya Serikali yenyewe ilisema fedha zile bilioni 200 ilizichukua baada ya kuona Bodi ya Korosho imeshindwa kuzisimamia vizuri. Sasa na Serikali nayo imeshindwa kuzisimamia vizuri mara tatu kuliko yale yaliyokuwa yanafanywa na Bodi kwa sababu kwa miaka minne au mitatu tumeishi hatuna Bodi ya Korosho, fedha zimechukuliwa na Serikali, wakulima hawana pembejeo na uzalishaji umepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sana kwa sababu fedha zilitunzwa, tunajua zimetumika mahali pengine lakini Serikali igharamie pembejeo hizi ambazo leo Wizara imefikiria jambo jema lakini approach yake inakwenda kumuongezea mzigo mkulima. Unaposema mkulima aendelee kuchangia 110 wakati Serikali imechukua bilioni 200 ya fedha za wakulima, nadhani Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Bashe ulikuwepo na ulikuwa unaunga mkono kwamba wakulima wanadhulumiwa, sasa ukae na Serikali hiyohiyo umepewa dhamana ya unaibu Waziri, Profesa ufanye kazi hii muiombe Serikali itupe bilioni 55/60 iende kulipa pembejeo wakulima wapate pembejeo mtakuwa mmewasaidia sana wakulima wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali inachukua bilioni 200 ilisema ingelipa gharama zote yenyewe, mwaka jana Serikali imechukua tena shilingi 25 kuchangia gunia za fedha ya korosho 2017/2018. Fedha ambayo wameikata kwenye mjengeko wa bei toka mwezi wa kumi lakini mpaka leo hao wenye magunia hawajalipwa hiyo fedha, fedha imechukuliwa wanaodai magunia hawajapewa lakini ni Serikali ilibeba mzigo wote kwamba tungeweza kulipa korosho hizi fedha, tungelipa magunia; wenye magunia wanadai, watu wa pembejeo wanadai na fedha zimechukuliwa.

Mheshimiwa Spika, niombe kwa sababu tuna Serikali Sikivu sana, na Mawaziri mpo makini kwelikweli lakini sijui shida mnaipata wapi, shida mnaipata wapi? Kaeni na Serikali muiambie kwamba tulikopa fedha za wakulima wa korosho maana zile mlisema matumizi sio mazuri, haya matumizi sio mazuri mmeshindwa kuunda Bodi ya Korosho, kwa miaka mitatu hakuna Bodi ya Korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkaja na ngonjera nyingine ambayo siiafiki kabisa eti uunganishe bodi za mazao haya ipatikane bodi moja, tuache bodi za kila zao libaki lenyewe litashughulika vizuri kuliko hayo mambo anayokuja nayo yaani Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba, Bodi ya Nini utengeneze dubwana moja Mheshimiwa Rais ndiyo maana alimuondoa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuona kwamba unatengeneza mtu amekaa tu pale kama picha, acheni tupate Bodi ya Korosho ambayo itasimamia zao na Sekta ya Korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana, Mheshimiwa Nape kawakumbusha hapa miche ya korosho ambayo imekuja mpaka Dodoma watu wake hamjawalipa, fedha zilikuwepo za kutosha, zilikuwa zinaweza kugharamia Sekta ya Korosho, lakini hatuna cha kujifunza. Msumbiji ambao wamekuja Tanzania kujifunza mfumo wa stakabadhi ghalani wanatoa pembejeo kwa wakulima bure kwa miaka 13 sasa, wamekuja kujifunza Taifa hili nyinyi waliokuja kujifunza ndiyo kwanza mnawaza tupate 110 tumkate mkulima, tufanye hivi, tunajifunza kutoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbona Ethiopia tulikojifunza sisi wanampa mkulima pembejeo bure, magunia bure, mabomba ya kupuliza korosho bure kila kitu wanafanya bure Serikali, mnapokusanya asilimia 15 ya export levy kwenye tani zile ulizokusanya 2016/2017/2018 laki tatu mnakusanya zaidi ya bilioni 144 ambazo mkichukua bilioni 55 mnaweza kugawa mapembejeo hayo na bado Serikali mkabakiwa na bakaa, mkawa mnamnyonya ng’ombe maziwa huku unamlisha.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali hii unamnyonya mkulima humlishi, mkulima huyu ataendeleaje? Mnasema asilimia 65 ya watanzania ni wakulima, wakulima ambao hawapewi pembejeo, wakulima ambao hawapewi magunia, wakulima ambao wakati wa kilimo hakuna mafunzo mnawapa, wakulima ambao kila jambo wanafanya wenyewe (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana, Mheshimiwa Waziri translate sasa u-professor wako kwenda kwenye vitendo vya kumsaidia mkulima, tusiwe tunajisifia ma- professor mpo tunakata ma-professor mtafsiri elimu yenu ije kwenye manufaa add value addition kwa wakulima wa korosho tutakaa tutapongeza tunama-professor chungu nzima, tuna madaktari chungu nzima, tafsiri elimu yenu kwenda kwenye value addition ya wakulima wa korosho, kwenye value addition ya wakulima wa mahindi, wakulima wamekuwa wakilalamika kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Taifa hili linautajiri wa kutosha kutoka kwenye kilimo, korosho tunayoisema hata Marehemu Mheshimiwa Rais, Mungu amrehemu alishasema kwenye korosho kama leo mtaamua kuwekeza vizuri kwenye korosho mkaleta viwanda, maganda ya korosho yanatengeneza brake pad ya kwenye magari tena Mercedes – Benz, maganda. Mafuta yanayotokana na korosho unaenda kutibu mbao zile za Mufindi haingii na mchwa hata mmoja hawezi kuharibu mbao, mabibo ya kwenye korosho leo mkiamua kufanya yawe na thamani tunaweza kutengeneza juisi, tunaweza kutengeneza pombe, Ulaya mkauza mapombe, mkulima wa Tanzania asingekuwa maskini hata dakika moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri kaeni mtafakari jambo hili, Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake amesema vizuri sana anataka kuona wakulima wakinufaika, Waziri onyesha mfano huo, tuanze na kwenye korosho huku, ombeni fedha, pembejeo hizi mtoe bure, lakini mkiangalia tathimini mliyoifanya natoa tani 8730 za Sulphur. Lakini nenda kwenye jedwali zenu 2017/2018 ambapo tumezalisha tani 313 Sulphur iliagizwa tani 18,000, nyinyi mmeagiza tani 8730 maana yake hatuendi kuongeza uzalishaji mnaoukusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye dawa za maji tuliagiza lita laki tatu na, leo mmeagiza lita 82,438 hamuendi kutoa majibu ya wakulima, hamuendi kutoa majibu na hiyo ipo kwenye hotuba zenu, mkae mfanye tafakari ya kina, tunahitaji mkusaidia mkulima huyu, mkulima ambaye anapata shida watu wamezungumza hapa adha ambazo mkulima anapata. (Makofi)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Katani.

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, shukurani sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nikushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na ushauri. Kwenye Bajeti hii ya Wizara ya Fedha kwenye Sekta yetu ya Kilimo bajeti yake yote ni 0.93 ya bajeti kuu. Kwa hiyo, nashauri sana, Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha kwenye jambo hili mnapokuja na bajeti ya mwakani kwenye Wizara yetu hii ya Kilimo ambayo inachangia pato la Taifa kwa asilimia 26, vile vile inachangia chakula kwa asilimia 100, basi mlete mpango ambao utakuwa endelevu, utakaoifanya Wizara hii iweze kukimbia. Hii tumeshapitisha, lakini naomba sana Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo mtakapokuja mwakani, msije tena na bajeti ya kilimo ambayo haifiki hata 1% ya gross budget ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote mnajua kabisa kwamba kwenye kilimo ndiyo tunategemea malighafi zote za kiwanda, kwenye kilimo ndiyo huko tunakotegemea kwenye chakula, kwenye kilimo ndiyo hiyo asilimia 26 ambayo kama inaleta pato la asilimia 26 halafu unawekeza asilimia 0.93 maana yake hatukitendei haki kilimo. Kwa hiyo, ni rai yangu na ombi langu kwa Serikali mwakani mnapoleta bajeti ya kilimo, leteni bajeti iliyojaa ili itusaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasisitiza tu kuwaomba Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo wanapoleta bajeti ya kilimo mwakani, basi waongeze fungu la bajeti ya kilimo kwa kuwa kilimo kinachangia pato la Taifa kwa asilimia 26 na kinachangia chakula kwa asilimia 100. Sasa ukilinganisha bajeti yetu hii ya kilimo ya 0.9 percent haioneshi kwamba tunakwenda kukifanyia kilimo yale mabadiliko ambayo tunayahitaji. Kwa hiyo, ni maombi yangu sana kwa Serikali hii ya CCM Sikivu, kwenye hili mlibebe kwa ajili ya bajeti ya mwakani, mlifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana bajeti hii. Tarehe 31 ya mwezi wa 12 mwaka 2020, watu wa TRA waliandika barua kupeleka kwenye vyama vyetu, kwa Wakuu wa Mikoa wakitaka wakulima watoe tozo kwenye korosho ya Income Tax ya 30 percent. Sasa kwa sababu Wizara imekwishatoa maelekezo na wanaopaswa kulipa Income Tax pato lao ni lazima lianzie shilingi 270,000/= na kuendelea, ukifanya overall ya wakulima wa korosho wote, kwa maelezo ya Wizara kupitia Naibu Waziri Mheshimiwa Bashe, mkulima wa kawaida anazalisha shilingi 1,400,000/= kwa mwaka. Maana yake pato la kawaida kwa mwezi halizidi hata shilingi 120,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Fedha iiambie TRA, wakulima hawa ambao wanachangia Export Levy kama korosho inakuwa shilingi 3,000/=, 15 percent Export Levy ni shilingi 400/= na kidogo. Ukijumlisha na cess shilingi 50/=, mkulima huyu anachangia zaidi ya shilingi 506/=. Sasa unapokaa ukawataka wakulima tena walipe Income Tax hii ni kutaka kuigombanisha Serikali na Chama cha Mapinduzi ambacho kinaongoza dola, kwa sababu hawa ni watu ambao ni wa chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Wizara ya Fedha na Msaidizi wako, mwaambie watu wa Mamlaka ya Mapato maana ninanyo hapa barua waliyoiandika tarehe 31 kutaka wakulima walipe Income Tax; mwaambie wakulima hawa pato lao haliwafanyi wao kulipa Income Tax. Kwa hiyo, nawaomba sana. Hawa wakulima kuna tozo nyingi ambazo wanapita kulipia bila hii ambayo mnataka kuwatoza tena. Kwa hiyo, mtoe maagizo kwa TRA waiondoe hii kitu kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kwa Wizara, nimeona mnaleta Miswada ya Sheria ya Fedha hapa, ile Export Levy tunayoiomba ambayo 2017 tuliondoa kifungu kile Na. 17(a) tunaomba mnapoleta Mabadiliko ya Sheria ya Fedha, kwa sababu na yenyewe iko ndani ya Mabadiliko ya Sheria ya Fedha, basi na ile muilete tena ili tuirudishe Export Levy wale watu wa CIDTF wapate fedha ili kwenye korosho mpunguze mzigo wa haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu walishagusia hapa mambo ya Madiwani. Naiomba Wizara, wakati mnajiandaa kufanya maboresho ya mambo haya, hata ile posho kama mnaweza, bajeti ya mwakani itawaruhusu vizuri, basi mwongeze posho ya Madiwani, at least wao ndio wanafanya kazi kubwa na ndio wasaidizi wetu kule chini wakati wote tunapokuwa tuko kwenye shughuli zetu hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena Wizara ya Fedha kama itawapendeza, wenzangu wamesema sana, zile fedha ambazo mmesema kuwapa wale watendaji wetu wa Kata, basi ikiwezekana mzitoe moja kwa moja na kama hamna hizo fedha, mwandike waraka kwa Wakurugenzi. Wakurugenzi hawa na Watendaji wetu wa Kata; Mtendaji wa Kata hawezi kwenda kwa Mkurugenzi kumwomba hiyo shilingi 100,000/=. Hata ingepita miezi mitano hajapewa, hawezi kwenda kumwomba. Fuatilieni mifano rahisi sana kwenye ofisi hizi za ma-DC, Maafisa Tarafa hizo posho walishakaa na Mheshimiwa Rais Marehemu Dkt. Magufuli lakini hizo posho bado hawapati kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana, mnapokwenda kutekeleza hii sheria mbayo mmetaka wapewe posho hizi la shilingi 100,000/=, basi ikiwapendeza Wizara ya Fedha mzipeleke ninyi wenyewe moja kwa moja ili kuondoa conflict baina ya Watendaji wa Kata na Wakurugenzi na mara nyingi Wakurugenzi wanaweza wasiwape kabisa kwa sababu tunajua hali za Halmashauri zetu. Wakati mwingine wanafanya bila kukusudia kwa sababu mapato yao na makusanyo yao siyo mazuri. Nawaombeni sana kwenye hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuomba, kilio cha Wenyeviti wetu wa Serikali ya Vijiji kwa kweli kimekuwa kikubwa sana. Hata hiyo posho ndogo ya shilingi 10,000/= ambayo baadhi ya maeneo wanasema wapewe, unaweza ukashangaa miezi minane hajapata hata shilingi 10,000/= moja. Kwa hiyo, naiomba Serikali na Wizara, kama itawapendeza hawa Wenyeviti wetu wa Serikali za Vijiji nao mwaandalie posho, siyo hii shilingi 10,000/=; mtakayoona inafanana na maisha ya sasa ili wafanye kazi zao kwa uadilifu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Allah Azza wa Jallah kwa kunipa afya njema, lakini nikushuru wewe pia kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze kwa kuipeleka Kamati ya Bajeti kule Mtwara hususan walipokwenda kwenye Bandari ya Mtwara. Ukisoma mapendekezo ya Mpango, Kamati ya Bajeti kuna mambo imependekeza kuhusu Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kuboresha Bandari zetu zote za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga kwa zaidi ya bilioni 328 leo kwenye mpango huu ambao unapendekezwa, nimeona Waziri wa Fedha amefanya kazi nzuri sana kwenye Mradi ule wa Liganga na Mchuchuma, lakini wakati tunaweka mpango huu wa Liganga na Mchuchuma tumesahau reli ambayo itasafirisha hayo makaa ya mawe na bidhaa nyingine ambayo reli hii inakwenda Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inanipa mashaka kama Waziri amesahau au la. Mapendekezo yangu kwenye jambo hili kwa sababu Serikali ina nia njema ya kutanua wigo wa biashara na kutoa fursa, basi wanapoleta mpango sasa tuone reli hii ya kutoka Mtwara Kwenda Mbambabay nayo inakuwepo kwenye mpango wetu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona pia Kamati ya Bajeti imependekeza vizuri kwenye Mpango hususan kwenye suala la zao la korosho kwenye kuongeza thamani. Leo bei ya korosho ukiitazama haiwezi kuwa na tija kwa mkulima kwa bei ya 1,800, 1,900. Kamati ya Bajeti imependekeza kuongeza thamani. Hata hivyo, wakati imependekeza kuongeza thamani, ni Serikali hii hii iliuza viwanda vya kubangua korosho. Leo tunashauri tena turejeshe viwanda ambavyo ndio mwarobaini wa kuongeza thamani kwenye korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mkataba wa kuuza viwanda vile ambavyo vimeuzwa zaidi ya viwanda vitano, mkataba ulikuwa wazi, ulikuwa unasema wanunuzi wa viwanda vile wanapaswa kubangua korosho. Matokeo yake vile viwanda havijaenda kubangua korosho hata kipindi kile cha hayati Daktari Magufuli aliposema askari waende wabangue korosho wamekwenda pale Lindi, viwanda vilivyouzwa kwa bei chee hakuna hata malighafi ya viwanda mle ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwa Serikali kwa jambo hili kwa sababu alionunua viwanda wamevunja mikataba. Moja Serikali ichukue vile viwanda, wapitie makubaliano ya Serikali ya kuuza viwanda na hao walionunua waweze kurejesha viwanda mikononi mwa Serikali ili tunaposema tunataka kuiongezea soko korosho, basi tuwe tuna viwanda tayari vya kubangua korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza pia kwenye Wizara hii ya Kilimo, walikuwa na mpango mzuri, tulikuwa na mapendekezo ya kujenga viwanda vikubwa vitano. Walisema wanajenga Pwani, Mtwara, Tunduru, Ruangwa, leo fedha zile wamechukua bilioni 210. Mheshimiwa Bashe anakumbuka vizuri, sasa kwa sababu amerudi kwenye Wizara hii tunataka tuone sasa tunaleta viwanda maeneo yanayolima korosho, hii ndio tija kwa mkulima. Kama juzi wakulima wanaona kwamba mfanyabiashara mmoja anakwenda Marekani kilo moja ya korosho iliyobanguliwa inauzwa kwa dola 40 zaidi ya Sh.90,000 ya kitanzania, maana yake imeongezwa thamani na ni ukweli usiopingika kwamba kama tutakuwa na viwanda vya kubangua korosho leo mkulima wa Mikoa wa Kusini, Lindi Mtwara na Ruvuma hawa watu watakuwa multi- trillionaire.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matajiri wanaozungumzwa wa Tanzania wa kwanza atatokea Mtwara kama tutaboresha viwanda vya kubangua korosho. Ni matarajio yangu kwenye mpango huo Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo wapo hapa. Wanapokuja sasa kwenye mpango wenyewe tuone mkakati madhubuti wa Serikali unaoelezea namna ya kumsaidia mkulima aidha wa korosho, kahawa kwa sababu bei hizo ukienda Songea kule bei ya kahawa na yenyewe ni kama ya korosho, haieleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna pekee ni kuwekeza kwenye kubangua, kuwekeza kwenye viwanda. Ushauri wangu kwa Serikali, Wizara ya Kilimo na Waziri wa Fedha ambaye ni msikivu, kama aliweza kuiongezea fedha Bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka jana, nadhani bajeti ijayo anaweza akaiongezea mara tatu ili tuone tija kwenye sekta ya kilimo inakaa sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu tunalo Bonde la Mto Ruvuma na hapa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo nataka anisikilize sana. Ameweka mipango yake vizuri kwenye Sekta ya Umwagiliaji, lakini ametusahau watu ambao tuna bonde lenye floor ya maji wakati wote. Ukija Jimboni kwangu nina Bonde pale Namahonga la Nacha, ukienda Mchichira nina Bonde pale la Ng’apa. Mabonde yale ni mazuri kwa uwekezaji huu wa umwagiliaji unaosema. Nione kwenye mpango sasa na sisi watu wa Mtwara tupo. Kaka yangu Chikota nadhani ana bonde ambalo naye ukitazama ukanda ule unakwenda mpaka Ruvuma. Kuna jambo wanaweza wakalifanya kwenye umwagiliaji na tukazalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda hata Mtama kuna mabonde pale, wasitusahau watuweke kwenye mpango tuone bajeti ya 2023/2024, sisi watu wa Kusini kwenye Sekta ya Umwagiliaji tupo kwa sababu maji tunayo. Hakuna sababu ya kuona kwamba umwagiliaji unawekaweka tu maeneo ya Tabora huko ambako hakuna maji. Watuletee sisi ambao tuna maji tumsaidie uzalishaji, Taifa lipate vitu vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado najikita hapo hapo kwenye sekta ya kilimo. Mheshimiwa Waziri kuna jambo amelifikiria ambalo ni jema sana la kuwasajili wakulima. Jambo hili ukilizungumza na hakuna bajeti ya kufanya jambo hili tutazungumza story miaka 10 na hatutaweza kusajili wakulima. Mheshimiwa Waziri akiwaambia watu wa Bodi wasajili wakulima watamwambia wanaotaka kutumika kule ni Maafisa Kilimo hawana fedha za kuwawezesha kwa ajili ya mafuta ya kwenda mashambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tandahimba peke yake inao zaidi ya wakulima Laki Moja na kitu, ili uweze kwenda kuwasajili wale inapaswa ufanye kazi mahsusi kabisa ambayo haina tofauti na Sensa. Sasa kwa sasabau umeamua kumsaidia mkulima niombe kwenye Mpango unaokuja nione umeweka package kabisa inayokwenda kufanya kazi ya kusajili wakulima ili unapoteleta mbolea yako ya ruzuku usipigwe mchanga wa macho. Utakuwa na takwimu sahihi utamjua Katani huyo ambaye ana namba ya NIDA, ana cheti cha kuzaliwa kila kitu ambacho umekitaka lakini ukiweke kwenye mpango, ukizungumza nadharia tutarudi tena hapa tunazungumza habari ya kusajili wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwako Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha upo wekeni bajeti ya fedha tuende tusajili wakulima. Tuwasaidie kwenye mazingira tunapotoa pembejeo za Serikali watu wasiweze kuwarubuni, watu wasiweze kuwaibia na mtaona mnapoweka projections’ kwamba mnataka korosho mzalishe tani Laki Saba, Laki Nane kama mtakuwa mmesajili wakulima, kwakweli mtakuwa hamuwezi kuibiwa pembejeo lakini hata mnapopanga mipango yenu mtakuwa mnapanga mipango ya kulima ambayo mnaijua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mapendekezo yangu machache yalikuwa ni hayo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kama alivyozungumza ndugu yangu Mheshimiwa Saashisha, leo sitaki kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri. Nitampongeza baada ya matokeo ya kile atakachokileta baadaye, baada ya michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge na namna atakavyokuja kuleta maboresho wakati wa kuweka mipango hii sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ukisoma Mpango wa Miaka Kumi wa Serikali ambao tunakwenda kwenye viwanda na sera ambayo tunayo ya elimu ya leo hatuendi kutoa majibu ya kile tunachokwenda kukifanya kwenye Mpango huu wa Uchumi wa Viwanda. Hii iko wazi ukienda leo Shule ya Ufundi Mtwara ambapo tunatarajia tungepata mafundi hao watakaokwenda kufanya kazi viwandani kutoka kwenye mashule yetu, shule zetu za ufundi zinaendelea kufa. Mtwara Tech ukienda pale wamebadilisha badilisha mambo, kwa hiyo shule zetu za ufundi zinakwenda kufa, wakati tunakwenda kwenye uchumi huu wa viwanda maana yake ni lazima tuwe polytechnic schools.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali, wenzetu Kenya wamefanya; ukienda Kenyatta University leo hata mitaala wamejaribu kubadilisha. Kozi zile nyingi ambazo zilikuwa za utawala ambazo sisi leo ndiyo tunazo; Vyuo vyetu vya kati vingi vinafundisha kozi za utawala badala ya kozi za ufundi. Maana yake yake ni nini? Ndiyo yale matokeo ambayo leo ukienda kwenye kuajiri utakuta bahasha 150,000 watu wanatafuta ajira kwa sababu tulishindwa kutengeneza mifumo ya shule za ufundi ambazo Watanzania wengi wangekwenda kufanya kazi kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye hili nimwombe sana Mheshimiwa Waziri. Leo vyuo vyetu vikuu; vipo vyuo vikuu na vyuo vya kati wanaendelea kutengeneza mitaala na kutengeneza kozi ambazo hata ukienda kwenye Ajira Portal hukutani na hicho kitu. Nenda Mipango pale kuna kozi unakutana na Bachelor Degree ya Development Finance and Economics; ukienda kwenye Ajira Portal, hicho kitu hukikuti kabisa na mzazi wa Tandahimba ameshampeleka mtoto chuoni, ame-grauduate pale, ana degree yake lakini kwenye Ajira Portal ya Serikali huioni hiyo kozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nenda Mwalimu Nyerere utakutana na wanafunzi wa namna hiyo chungumzima. Nenda TRA huko utakutana na makozi hayo wametoa ajira lakini wametengeneza kozi ambazo ukienda kwenye Ajira Portal hazitambuliki kabisa. Maana yake nini? Tunaendelea kutengeneza mitaala ambayo haiendi kumsaidia Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakuja kulisaidia Taifa hili kama watakaa chini sasa, tukatoka kwenye mitaala ya kikoloni ambayo ndiyo tunaitumia; maana ndiyo ukweli wa wazi huo. Tunaendelea kutumia mitaala ya kikoloni, mwanafunzi unampa masomo 11, anapokwenda form five, six anakwenda kuchagua masomo matatu, lakini ulimpa mzigo wa masomo 11 au 12. Cheti cha form four mtu ana division one ukiangalia imejichanganya changanya hivi, wala hujui kwamba mtoto huyu uwezo wake halisi ni upi? Maana mwingine ana ‘A’ zote saba; kwa hiyo, unaamua wewe tu kwamba huyu mtoto sasa nimpeleke HGK lakini kumbe uwezo wake labda ni PCB.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa umefika wakati tuone siyo tu kuanzia darasa la saba watakapokaa kuandaa mitaala vizuri ikiwezekana tuwe na foundation hii ya darasa la kwanza na la pili, lakini kuanzia la tatu mtoto tayari aingie kwenye combination kama mtoto atakayesoma sayansi akasome sayansi; kama ni mtoto anakwenda kusoma arts akasome arts, kuanzia darasa la tatu watakuja kulisaidia Taifa. Tutoke kwenye kutoa hizi kozi nyingi ambazo ni za utawala wakati ni kozi ambazo zinakosa fursa za soko la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye sera ya elimu, niseme hatuna sera ya kudumu ya elimu. Ukiangalia sera ya 2006 tulikuwa na sera ya exclusive education. Kabla hatujaitekeleza 2012 tukaja na jambo lingine elimu ya msingi iishie darasa la sita na lugha ya kufundishia iwe Kiswahili; toka 2012 ilishapitishwa huko. Leo tunarudi nyuma tunakaa hapa tunamwambia Waziri akae kutafakari sera sahihi ambayo tutakwenda nayo. Maana yake ni kwamba bado tunaendeshwa na sera za kikoloni ambazo kama tutaendelea na sera hizi za kikoloni, mitaala hii ya kikoloni maana yake Taifa hili tutaendelea kutumikishwa na wenzetu waliopo nje. Kwa sababu watakachokitaka wao ndicho tutakachokifanya. Sasa Profesa aende akatafsiri, elimu yake ije isaidie Watanzania na Taifa hili kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu Walimu wana kazi ngumu sana. Januari Walimu walishajiandaa tayari na scheme of work zao. Baadaye ukaja waraka ikaja kitu kinaitwa Kalenda ya Elimu; Walimu wakatakiwa wakae tena chini kuandaa scheme of work. Haijakaa vizuri kalenda, likaja jambo la sensa, Walimu wakakaa tena kutengeneza scheme of work nyingine, yaani ndani ya mwaka huu mmoja, Walimu wametengeneza scheme of work zaidi ya tatu. Hivi tunavyozungumza, Walimu wanafundisha kwa uzoefu tu siyo kufuata scheme of work; kwa sababu wanazo nne ambazo hawakuwahi kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye jambo hili Walimu hawa ambao tunawapa kazi kila dakika wanakaa kuandaa scheme of work inabadilika, wanakaa tena inabadilika, wawape mahitaji yao ya msingi kwama ilivyo askari. Askari tarehe 15 wanawapa allowance na walimu nao waanze kupata allowance kwa sababu kazi wanayoifanya ni kubwa kwenye Taifa hili. Hakuna watu wanaofanya kazi kubwa kama Walimu na wenyewe waingizwe kwenye allowance kama wanavyofanya majeshi kwa sababu wanabadilikabadilika, kila wanavyosema wanabadilika na walimu wanabadilika hivyo hivyo.

Kwa hiyo, niombe sana sana ikifika tarehe 15 Walimu nao wale allowance zao vizuri, lakini wapandishiwe mishahara yao, posho zao na kama kuna wanaowadai wawalipe Walimu hawa ili walete tija kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, wenzangu wamezungumza sana juu ya Baraza la Ushauri; hiki chombo Mheshimiwa Waziri akifanyie kazi kwa haraka sana. Atakuwa na chombo cha wataalam ambacho kitamshauri mambo ya msingi yanayohusu elimu ya Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa hili na kitamsaidia sana kupeleka elimu yetu mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)