Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Mary Machuche Mwanjelwa (45 total)

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Katika Mpango wa Kilimo Kwanza Serikali ilihamasisha Watanzania kuongeza uzalishaji katika kilimo ili Serikali itoe mikopo ya matrekta kwa wingi.
(a) Je, kumekuwa na mafanikio kiasi gani kwa mazao ya biashara na chakula?
(b) Kama kumekuwa na mafanikio, je, kuna utaratibu gani wa kuendeleza mpango huo kwa wananchi wanaohitaji kukopeshwa matrekta wakiwemo wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru sana Mungu. Vilevile ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa dhamana hii. Ninakushukuru sana wewe binafsi kwa kunilea vyema na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Kilimo Kwanza umekuwa na mafanikio katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini ambapo uzalishaji wa jumla wa mazao ya biashara katika msimu wa 2016/2017 umeongezeka kufikia tani 881,583 ikilinganishwa na tani 796,562 mwaka 2015/2016. Aidha, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka hadi kufikia tani 16,172,841 kwa msimu wa 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya chakula kwa Mkoa wa Singida umeongezeka kutoka tani 453,097 mwaka 2013/2014 hadi tani 481,452 kwa mwaka 2015/2016. Aidha, uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kutoka tani 184,066 mwaka 2012/2013 hadi tani 293,873 kwa mwaka 2015/2016. Uzalishaji wa mazao ya chakula katika Wilaya ya Manyoni umeongezeka hadi kufikia tani 42,554 kwa mwaka 2015/2016 ambapo uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka tani 1,342 mwaka 2011/2012 hadi kufikia tani 6,212 mwaka 2015/2016. Alizeti uzalishaji umeongezeka kutoka tani 4,464 mwaka 2010/2011 hadi tani 21,871 mwaka 2016/2017, na ufuta umeongezeka kutoka tani 2,285 mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 8,874 kwa mwaka 2015/2016.
• Mheshimiwa Spika, jumla ya matrekta 18,774 yanafanya kazi nchini ambapo kati ya matrekta hayo, matrekta makubwa ni 11,500 na matrekta madogo ya mkono ni 7,274. Aidha, Wilaya ya Manyoni ina matrekta makubwa 32, matrekta madogo ya mkono 39 na wanyamakazi 14,782 ambapo kilimo cha kutumia maksai ni maarufu katika Wilaya ya Manyoni.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali Kuu katika kuhakikisha wakulima wanapata zana bora za kilimo, halmashauri za wilaya pia zimeelekezwa kuhamasisha wakulima kujiunga au kuanzisha vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) ambavyo vitakopesha wanachama wake au kuwadhamini kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kununua matrekta na zana zake.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Tunatambua juhudi za Serikali za kujenga Chuo cha Kilimo na Mifugo katika Kata ya Lufyilo.
Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa bwalo la nyumba za walimu ili chuo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa majengo ya madarasa yalishakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mbunge wa Jimbo la Busokelo kama ifuatavyo:-
Wizara ya Kilimo ina jukumu la kusimamia na kuviendeleza vyuo vya kilimo hapa nchini. Hiki ni kituo kidogo cha kutoa mafunzo ya kilimo kwenye scheme za umwagiliaji kwa maana ya World AgricultureResource Center. Kituo hiki kilijengwa kwa jitihada kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki Profesa Mark Mwandosya ambapo mwisho alikabidhi kituo hicho kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ili wakamilishe sehemu iliyobaki.
Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua uwepo wa kituo hicho na inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ili kupata fedha za kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa ajili ya kutumika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, vyuo vya kilimo vinavyosimamiwa na Wizara ya kilimo vipo 14. Vyote hivi vimejengwa muda mrefu na hivi sasa vinakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ikiwemo ofisi za walimu, madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu, maktaba pamoja na karakana. Changamoto nyingine ni uhaba wa wakufunzi na watumishi wa kada nyingine pamoja na vifa vya kufundishia.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizo Wizara imeweka kipaumbele cha kuboresha vyuo vilivyopo badala ya kufikiria kuongeza vyuo vingine. Vyuo hivyo vikikarabatiwa vitaweza kuchukua wanafunzi wengi hivyo kuwezesha Serikali kufikia lengo la kuwa na mtaalam mmoja wa kilimo katika kila kijiji na pia kuzalisha maafisa ugani wenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa wakulima. Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 Serikali imeshatenga shilingi 773,208,000 kwa kuanzia kwa ajili ya kufanya ukarabati katika Vyuo vya MATI.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali iliahidi kuanzisha mfumo wa commodity exchange ili kuwasaidia wananchi wanaolima korosho kupata bei nzuri katika msimu husika
– Je, Serikali ina kauli gani huu ya kuanza kwa mfumo huo?
– Je, Serikali itatatua vipi suala la kodi nyingi kwa wakulima wa korosho inayosababisha kupata bei ndogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya soko la bidhaa (commodity exchange) yalianza mwaka 2011 kwa lengo la kufanya biashara ya mazao kuwa ya wazi na yenye ushindani kulingana na nguvu ya soko. Aidha, mfumo huu umelenga kupunguza gharama za uendeshaji wa masoko yote ya mazao yote ya chakula na biashara ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri na yenye tija.
Mheshimiwa Spika, hatua ambazo zimeshachukuliwa hadi sasa ni pamoja na kupitishwa kwa waraka wa soko hilo, kuundwa kwa bodi ya soko, kutungwa kwa sheria ya mwaka 2015 ya soko la bidhaa pamoja na kanuni zake, kufanya uzinduzi wa kuanzisha soko hili, kutoa mafunzo kwa madalali watakaoendesha soko hilo na kutoa mafunzo kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na sekta binafsi ili kujenga uelewa wa pamoja. Vilevile ofisi na jukwaa la soko hilo vimefunguliwa kwenye jengo la LAPF lililo kijito nyama Jijini Dar es Salaam. Kazi za uwekaji wa vifaa katika ofisi na jukwaa zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, elimu ya soko la bidhaa inaendelea kutolewa kwa baadhi ya viongozi wa ngazi za Mkoa na Wilaya na maafisa kilimo, ushirika, biashara na maendeleo ya jamii katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Dodoma na Singida. Aidha, elimu hiyo imeshatolewa kwa viongozi wa vyama vikuu vya ushirika na viongozi wa vya msingi na vyama visivyokuwa vya kiserikali ili kujenga uelewa wa somo hili. Pia elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima na wananchi wka ujumla ili wadau waufahamu mfumo huo wa soko.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeondoa ushuru na tozo an kubakiza makato ya usafirishajia korosho kulingana na umbali halisi. Mchango wa kuendeleza zao na ushirika na kuondoa shilingi 50 kwa kila kilo zilizokuwa zinatozwa kwa ajili ya kufungashia korosho. Aidha, Serikali imepunguza ushuru wa Halmashauri za wilaya kutoka asilimia tano hadi tatu.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Kwa takwimu za miaka ya hivi karibuni uzalishaji wa kahawa Wilayani Mbinga umeonekana kushuka kwa mkulima mmoja mmoja (out growers). Na sababu mojawapo ya kushuka kwa uzalishaji huo ni kuzeeka kwa miti ya kahawa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea wakulima wa Mbinga mbegu mpya ili kuinua uzalishaji?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mnada wa kahawa Wilayani Mbinga, badala ya minada hiyo kuendelea kufanyika Moshi?
(c) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupiga marufuku kabisa uuzaji wa kahawa mbichi ikiwa shambani, maarufu kama “magoma” Wilayani Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martin Msuha, Mbunge wa Mbinga, swali lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali wa kuwapelekea wakulima wa Mbinga mbegu mpya ili kuinua uzalishaji ni kwa kutekeleza mpango mkakati wa kuendeleza zao la kahawa kwa miaka kumi (2011 – 2021). Katika mpango huo utafiti na usambazaji wa miche bora, ili kuondokana na miche yenye tija duni na iliyo zeeka ni mojawapo ya kipaumbele. Utekelezaji wake unafanyika kwa kushirikiana na wadau, hususan Tanzania Coffee Research Institute (TaCRI). Kituo cha utafiti na uzalishaji miche cha Ugano kilichoko Wilayani Mbinga katika mwaka 2016/2017 kilizalisha na kusambaza miche bora ya kahawa 270,869 na kazi inaendelea. Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Kahawa (Tanzania Coffee Development Fund) umefadhili na kupunguza bei kutoka shilingi 300 kwa mche mmoja hadi shilingi 150 kwa vituo vyote nchini vilivyoko chini ya TaCRI ili miche hiyo isambae kwa kasi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mnada wa kahawa huendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Kahawa Namba 23 ya mwaka 2001. Serikali haina mpango wa kuanzisha Soko la Mnada wa Kahawa - Mbinga au mahali pengine nchini kwa sababu, uwepo wa miundombinu ya mashine ya kielektroniki ya kuendesha mnada iliyopo Moshi, maabara ya kuonjea kahawa, wataalam wa kuendesha mnada hu, gharama za mnunuzi ambapo atalazimika kwenda katika kila mnada, kama utawekwa kila mahali ambapo kahawa inazalishwa uzoefu unaonesha kuwa nchi nyingi duniani huweka mnada sehemu moja tu, ili kurahisisha uendeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tangu kuanzishwa kwake kabla ya uhuru mnada uliwekwa Moshi kwa kuwa ndiko kulikua na wanunuzi na biashara ukilinganisha na maeneo kama Kagera, ingawa uzalishaji unafikia hadi asilimia 40 ya nchi nzima. Mnada unauza kahawa ikiwa kwenye maeneo ya uzalishaji kwa mfano kule Mbinga na Mbeya, n.k. KInachopelekwa Moshi ni sampuli tu kwa ajili ya uonjaji.
Aidha, Serikali imeanzisha soko la bidhaa (Commodity Exchange) ili kupunguza gharama za uendeshaji wa masoko ya mazao ikiwemo kahawa.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kifungu Namba 29(ii) cha Kanuni za Kahawa 2013, ni kosa kwa mtu yeyote kununua matunda ya kahawa (ripe cherry) kwa hiyo, Serikali inakataza biashara ya kahawa mbichi. Naomba nitoe agizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, wote kwa pamoja na wahusika wengine wote kwamba, hairuhusiwi kabisa uuzaji wa kahawa mbichi.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Zao la tumbaku lina tozo nyingi ambazo ni mzigo kwa wakulima.
(a) Je, ni lini Serikali itapunguza tozo hizo?
(b) Je, kama itapunguza, itaanza kupunguza tozo ngapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto mbalimbali katika uzalishaji wa mazao ya biashara nchini ikiwemo zao la tumbaku. Changamoto hizo ni pamoja na kuwepo ada na tozo mbalimbali zinazotozwa kwa wakulima na wadau wengine wanaojishughulisha na mnyororo wa thamani wa zao hilo ambazo zimekuwa na athari katika mapato ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 imefuta, ada na tozo zipatazo 80 kati ya tozo na ada 139 zilizokuwa zinatozwa katika mazao ya kilimo nchini ambazo zilibainika kutokuwa na tija kwa wakulima. Kutokana na maamuzi hayo kwenye tasnia ya tumbaku, jumla ya tozo 10 zilifutwa na tozo mbili zilipunguzwa viwango na tasnia ya kahawa jumla ya tozo 17 zilifutwa na tozo moja ilipunguzwa kiwango, tasnia ya sukari jumla tozo 16 zilifutwa, tasnia ya pamba tozo mbili zilifutwa, tasnia ya korosho tozo mbili zilifutwa, tasnia ya mbegu tozo saba zilifutwa, tasnia ya mbolea tozo tatu zilifutwa na tozo moja ilipunguzwa kiwango. Aidha, tozo 20 zilikuwa zinatozwa na Vyama vya Ushirika katika ngazi mbalimbali nazo zilifutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika orodha ya tozo ambazo zilitamkwa kufutwa katika tasnia ya tumbaku kwenye Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2017/2018 ni pamoja na mchango kwa Chama cha Ushirika cha Msingi kiasi cha USD 0.072 kwa kilo na mchango wa Chama cha Ushirika cha Mkoa kiasi cha USD 0.030 kwa kilo.
Hata hivyo, baada ya majadiliano ya wadau katika tasnia ya tumbaku, tozo hizo zilirejeshwa kutokana na umuhimu wake katika kuwezesha usimamizi unaofanywa na Vyama vya Ushirika katika tasnia ya tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mukhtadha huo, ada na tozo zilifutwa katika tasnia ya tumbaku ni pamoja na ada ya fomu ya maombi ya leseni za kununua tumbaku, ada ya leseni ya kununua tumbaku kavu, ada ya leseni ya kuuza tumbaku nje ya nchi, ada ya leseni ya kununua tumbaku mbichi kiwandani, tozo ya leseni ya kununua tumbaku mbichi kwa kila Wilaya, tozo ya Baraza la Tumbaku (Tobacco Council) na tozo ya dhamana ya Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya mikopo.
Aidha, mpango wa Serikali ni kuhakikisha tozo na ada mbalimbali ambazo ni kero kwa wakulima wa tumbaku zinafutwa na kubakia zile ambazo zina mahusiano na uendelezaji wa zao husika.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD aliuliza:-
Je, Serikali imejipanga vipi kukidhi mahitaji ya viuwadudu kwa wakulima wa pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Hassan Aboud, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa viuwadudu katika kudhibiti magonjwa na visumbufu vya mazao nchini.
Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 wakulima wameitikia kwa vitendo azma ya Serikali ya kuimarisha kilimo cha pamba nchini kwa kuongeza eneo linalolimwa pamba kutoka wastani wa ekari 1,000,000 hadi wastani wa ekari 3,000,000. Kutokana na mwitikio huo, hadi tarehe 22 Desemba, 2017 jumla ya ekari 1,500,000 zilikuwa zimelimwa na kupandwa zao la pamba na kwa kuhitaji chupa zile (acrepacks) 4,500,000 za viuwadudu. Hata hivyo, kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha wakulima wameendelea kuhakikisha kwamba zao hili linafanyika na vilevile suala la viuatilifu linafanikiwa. Nakushukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y MHE. PETER J. SERUKAMBA) aliuliza:-
Bei ya kahawa ni ndogo ikilinganishwa na gharama za uzalishaji.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha bei ya zao la kahawa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima kwa kuwapatia ruzuku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, lene sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya kahawa duniani ikiwa ni pamoja na kahawa ya Tanzania hutegemea bei katika masoko mawili ya rejea duniani ambayo ni Soko la Bidhaa la New York (New York Commodities Market) kwa kahawa ya Arabica na Soko la London International Financial Futures and Options Exchange kwa kahawa ya Robusta.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenendo wa bei katika masoko hayo huathiri moja kwa moja bei kwa nchi zote wazalishaji wa kahawa ambapo mwenendo huo pia huathiri bei katika soko la mnada wa kahawa na bei ya wakulima Tanzania. Bei ya kahawa katika masoko ya rejea pia hutokana na kiasi kilichopo na mahitaji (demand and supply) ya kahawa duniani kwa wakati husika. Aidha, kwa kuwa wanunuzi hununua kahawa kwa bei ya mwali pwani (FOB) ambayo hujumuisha bei ya mkulima na gharama, zao za ununuzi kwa hivyo bei ya kahawa haizingatii kabisa gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la kahawa pia hukabiliwa na ada na tozo mbalimbali ambazo huongeza gharama za kufanya biashara na hivyo kusababisha wanunuzi wengi kwenda kununua kahawa katika nchi jirani ambako hakuna ada na tozo nyingi na hivyo kutoa bei nzuri ukilinganisha na bei za ndani. Hali hiyo husababisha wakulima kutorosha kahawa nje ya nchi ili waweze kupata bei nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haiwezi kupandisha bei ya kahawa kwa kuwa bei hiyo hutokana na masoko rejea ya dunia. Hata hivyo, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuwaongeza kipato wakulima. Mikakati hiyo ni pamoja na kufuta ada na tozo zipatazo 17 katika sekta ya kahawa ili kumpunguzia mkulima mzigo wa malipo ambayo wanunuzi huweka kwenye gharama zao za ununuzi; kuongeza ushindani katika mnada kwa kuwaondoa wanunuzi wa kahawa vijijini ili wakanunue kahawa mnadani kwa ushindani, kuimarisha, kufufua na kuanzisha Vyama Vikuu vya Ushirika katika kila Mkoa unaolima kahawa na Vyama vya Msingi kwa maana ya AMCOS katika kila kijiji ili kukusanya kahawa ya wakulima, wanachama na kuipeleka mnadani. Aidha, AMCOS zimehamasishwa kuanzishwa viwanda vya kuchakata kahawa ili kupata kahawa bora na yenye bei nzuri na kuimarisha usimamizi kwa zao la kahawa katika ngazi na hatua zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali huwapatia wa kahawa ruzuku kwa kupunguza bei ya miche bora ya kahawa inayozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania, vilevile Mamlala za Serikali za Mitaa zinazolima kahawa nchini zimeagizwa zote kuanzisha bustani za kuzalisha miche bora kulingana na mahitaji ya wakulima wao na kuigawa bure na pia kuhakikisha inapandwa na kutunzwa. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Halmashauri ya Mji wa Babati inaidai NFRA ushuru wa zaidi ya shilingi milioni 90 katika kipindi cha mwaka 2014/ 2015.
Je, ni lini fedha hizo zitalipwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa ununuzi wa nafaka mwaka 2014/2015 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulinunua tani 1,127.826 za mahindi zenye thamani ya shilingi 6,063,913,000 kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima katika Mji wa Babati. NFRA ilipaswa kulipa kwa Halmashauri ya Mji wa Babati ushuru wa shilingi 181,917,390 ambazo ni asilimia tatu ya thamani ya mahindi yaliyonunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Wakala ulilipa ushuru wa mazao kwa tani 4,400,000 zenye thamani ya shilingi 66,000,000 na kubaki na deni na deni la ushuru wa mazao kwa tani 7,727.686 zenye thamani ya shilingi 115,917,390.00. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti wakala ulishindwa kulipa kiasi chote cha ushuru kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa ununuzi wa mahindi zaidi ya melengo yaliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016 Wakala ulilipa deni lote la ushuru wa mazao kwa Halmashauri ya Babati kwa awamu mbili ambapo tarehe 10 Agosti, 2015 ulilipa shilingi 23,000,000 na kumalizia deni la shilingi 92,917,390 tarehe 27 Januari, 2016. Aidha, kwa sasa Wakala umelipa ushuru wa mazao kwa Halmashauri zote ilikonunua mahindi na hakuna deni lolote kuhusu ushuru wa mazao.
MHE. MARWA R. CHACHA (K.n.y. MHE. JOYCE B. SOKOMBI) aliuliza:-
Katika Msimu wa mwaka 2017/2018, wananchi wa Wilaya ya Serengeti na Bunda wanaoishi kandokando ya Mbuga ya Serengeti wameathirika sana kwa mashamba yao kushambuliwa na tembo na hivyo kukumbwa na baa la njaa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuyafanya maeneo hayo kuwa kipaumbele cha kuwapa msaada wa chakula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mnamo mwezi Mei, 2017 ilichukua hatua madhubuti ya kupeleka mahindi kiasi cha tani 400 kwa Wilaya ya Serengeti na tani 253.6 kwa Wilaya ya Bunda na kuyauza kwa bei nafuu kwa wananchi walioathiriwa na ukame pamoja na uharibifu wa mazao uliosababishwa na wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki na za haraka za kukabiliana na upungufu wa chakula katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Wilaya ya Serengeti na Bunda. Aidha, Wizara ya Kilimo itashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuweka mkakati wa pamoja wa kudhibiti tembo wanaoharibu mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali mnamo mwezi Mei, 2018 kupitia Wizara ya Kilimo ikishirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Taifa ya Takwimu itafanya tathimini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2017/2018 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019 (Preliminary Food Crop Production Forecast) katika Wilaya zote nchini ikiwemo Wilaya ya Serengeti na Bunda ili kujua hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine Wilaya ya Serengeti na Bunda zimekuwa zikifanya tathmini za athari za uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo mara unapojitokeza ili kubaini ukubwa wa tatizo na idadi ya wakulima walioathirika. Taarifa za tathmini hizo huwasilishwa Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo wakulima waliobainika kuathiriwa hulipwa kifuta jasho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine matokeo ya tathmini hii yataainisha Wilaya zenye viashiria vinavyopelekea uwepo wa upungufu wa chakula kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa mazao unaosababishwa na wanyampori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa chakula katika maeneo yatakayobainishwa kuwa na viashiria vya upungufu wa chakula na kuchukua hatua stahiki ikiwamo ya kufanya tathmini ya kina ya chakula na lishe (Comprehensive Food and Nutrition Security Vulnerability Assessment).
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya kina itaainisha hali halisi ya upatikanaji wa chakula, idadi ya watu walioathirika, viwango vya athari, kipindi cha athari, sababu zilizosababisha na hatua stahiki za kuchukuliwa na Serikali na wadau wengine katika kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Lengo ni kuhakikisha uwepo wa hali endelevu na ya utengemano wa hali ya usalama wa chakula na lishe nchini.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Pamoja na kuishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kumwondolea mkulima matatizo ya zao la tumbaku:-
• Je, Serikali imechukua hatua zipi katika kuimarisha utendaji kazi wa Bodi mpya ya Tumbaku ili ifanye kazi kikamilifu?
• Je, Serikali inawahakikishiaje wakulima wa tumbaku upatikanaji wa mbolea kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania ilizinduliwa rasmi tarehe Mosi Disemba, 2017. Ili kuimarisha utendaji kazi wake kikamilifu, Serikali imeiagiza kuwa tumbaku iendelee kuwa miongozi mwa mazao mkuu yanayowanufaisha wakulima ili kuliingizia Taifa fedha za kigeni kwa kuhakikisha kuwa ubora wa tumbaku unaongezeka kwa asilimia 15 ifikapo mwaka 2021 na uzalishaji wake kufikia tani laki moja na ishirini kutoka tani elfu sitini na tatu za sasa.
Mheshimiwa Spika, tumbaku inazalishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na wakulima wanazalisha kwa mkataba ili kuwa na soko la uhakika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tumbaku ni moja ya zao la kimkakati, Bodi imelekezwa kuyataka makampuni ya ununuzi kufanga mikataba na Bodi ya Tumbaku Tanzania na kisha kuyapangia maeneo ya kwenda kununua badala ya utaratibu wa sasa ambapo makampuni hujichagulia maeneo ya kwenda kununua.
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine ni kutafiti na kubaini aina nzuri za tumbaku zinazopendwa na wanunuzi ili zilimwe na kuwauzia wanunuzi wa aina hizo za tumbaku; kuwachukulia hatua za kinidhani watendaji wasiowajibika kikamilifu na kufuata vizuri kalenda ya uzalishaji wa tumbaku.
(b) Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka wa 2017/2018, mbolea ya tumbaku ilichelewa kutokana na kuchelewa kwa maafikiano ya bei ya kununulia tumbaku ambayo ni kigezo kwa kila kampuni kuahidi kiasi cha tumbaku itakachonunua na hivyo kubaini kiasi cha mbolea itakayotumika kuzalisha kiasi hicho cha tumbaku.
Mheshimiwa Spika, ili mbolea ianze kuagizwa maafikiano ya bei yanatakiwa kukamilika kati ya Machi na Mei kila mwaka. Katika msimu wa kilimo wa 2018/2019, Bodi ya Tumbaku Tanzania inaendelea kuratibu majadiliano ya bei kati ya wanunuzi na wakulima ili uagizaji wa mbolea ufanyike mapema. (Makofi)
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
• Je, ni lini Serikali itaondoa kabisa malalamiko yanayotokana na makato, rushwa, uwazi na matatizo mengine yaliyopo katika mfumo mzima wa ununuzi wa zao la korosho?
• Je, ni lini Serikali itaondoa utaratibu wa wakulima kulipwa mara mbili na badala yake walipwe pesa zao mara moja na wasubiri bonus baadae?
• Ni lini Serikali itadhibiti usambazaji wa pembejeo kwa watu ambao siyo wakulima wa korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, makato yanayotokana na biashara ya zao la korosho yapo kwa mujibu wa sheria na mjengeko wa bei ambayo huamuliwa na wadau wa zao la korosho. Aidha, makato mengine ni kwa ajili ya maendeleo ya Mikoa na Halmashauri za Wilaya zao la korosho linakozalishwa.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilifuta tozo tano na katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Serikali imefuta tozo mbili zilizokuwa zinatozwa kwenye biashara ya zao la korosho. Vilevile Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria Namba. 6 ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 pamoja na sheria nyingine za nchi ikiwemo kuwavua madaraka na kuwachukulia hatua za kisheria viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wanaotuhumiwa kushiriki katika vitendo vya ubadhirifu, rushwa na ukiukwaji mwingine wa sheria, kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa malipo kwa wakulima wa zao la korosho kwa sasa hivi hufanyika mara moja tu. Aidha, malipo kwa wakulima waliouza korosho hulipwa kwenye akaunti za vyama vikuu vya ushirika kutoka kwa makampuni yanayonunua korosho kupitia minada. Baadae fedha hutumwa kwenye akaunti za benki za vyama vya ushirika vya msingi na hatimae kulipwa kwa mkulima mmoja mmoja kupitia akaunti yake ya benki.
Mheshimiwa Spika, Serikali inadhibiti usambazaji wa pembejo za zao la korosho kwa watu ambao sio wakulima wa korosho kwa kutumia sensa ya wakulima wa zao la korosho (wanachama na wasio wanachama wa vyama vya ushirika). Sensa hii inawezesha kujua mahitaji halisi ya pembejeo kwa wakulima wa korosho.
Aidha, pembejeo inayoonekana kwa watu ambao sio wakulima wa korosho, inatokana na wakulima wa zao la korosho ambao siyo waaminifu.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua za makusudi kutenga mitaji kwa wakulima wadogo wadogo wa mazao ya vitunguu na alizeti katika Wilaya mpya ya Mkalama kupitia benki za mikopo au ruzuku toka Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa wakulima ni mhimili muhimu katika maendeleo ya kilimo. Hata hivyo upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wakulima unakabiliwa na changamoto kutokana na sekta ya kilimo kukabiliwa na majanga mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na milipuko ya wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea. Aidha, kumekuwepo na changamoto ya kukosekana kwa hatimiliki zinazoweza kutumika kama dhamana (collateral) pamoja na riba kubwa isiyoendana na msimu wa uzalishaji mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali ilianzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo inayotoa mikopo ya riba nafuu kati ya asilimia 7-15 ambapo kwa Benki za Biashara riba ni kati ya asilimia 18 - 24. Aidha, masharti mengine kwa waombaji mkopo katika vikundi ni kutumia mashamba yao kama dhamana ya mikopo ambapo muda wa kuanza urejeshaji mikopo (grace period) hufika hadi miezi sita na kipindi cha kurejesha mkopo kufikia hadi miaka 15 kulingana na aina ya mkopo. Aidha, benki hiyo, hadi kufikia mwezi Machi 2018, imeidhinisha mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 38.79 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kilimo nchini, ambapo kwa Mkoa wa Singida peke yake, benki inatarajia kutoa mikopo kulingana na maombi yatakayowasilishwa na wakulima kwa kuzingatia vigezo na masharti.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea kutoa mikopo kupitia Mfuko wa Pembejeo (Agriculture Input Trust Fund – AGITF) ambao unalenga kukopesha wakulima pembejeo na zana za kilimo kwa gharama nafuu, ambapo riba ya mikopo ya AGITF ni kati ya asilimia sita hadi nane ambapo waombaji wa mikopo katika vikundi vilivyosajiliwa hawahitajiki kuwa na dhamana ya hati au mali isiyohamishika.
Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 Mfuko wa Pembejeo umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 789,650,000 kwa wakulima wa Mikoa ya Singida na Dodoma ambapo mikopo hiyo ilijumuisha matrekta, pembejeo za kilimo, nyenzo za umwagiliaji na usindikaji.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa mitaji kwa wakulima, Serikali imekuwa ikiimarisha Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuhamasiasha benki za biashara na wadau mbalimbali ikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka mikopo kwa wakulima nchini.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio ya Serikali kwamba mikakati hiyo itasaidia katika upatikanaji wa mikopo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kwa riba na masharti nafuu ili kuwawezesha wakulima wadogo kuendesha kilomo chenye tija. (Makofi)
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
Uzalishaji wa pamba Mkoani Mwanza umepungua kutoka tani 350,000 kwa mwaka 2009 hadi tani 120,000 kwa mwaka 2016:-
Je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi ili kulifufua zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji wa pamba umekuwa ukishuka katika miaka ya hivi karibuni, sio kwa Mkoa wa Mwanza tu, bali pia katika maeneo yote yanayozalisha pamba nchini. Miongoni mwa sababu ambazo zilichangia kushuka kwa uzalishaji ni bei ndogo ya pamba kwa wakulima, kukosekana kwa mfumo bora wa usimamizi wa ununuzi wa pamba ambao ulisababisha baadhi ya wakulima kukopwa, matumizi madogo ya pembejeo hususan viuadudu, mbegu bora na mbolea. Aidha, kutozingatiwa kwa kanuni bora za kilimo cha pamba na matumizi madogo ya zana bora za kilimo vimeathiri uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekusudia kuinua kilimo cha zao la pamba kwa kuimarisha usimamizi kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya kitaifa. Katika usimamizi huo, mkazo umewekwa katika upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi za wakulima, eneo wanalolima, kiasi cha pembejeo hususan viuadudu, mbegu bora na mbolea. Aidha, Serikali inasimamia kikamilifu vyama vya msingi ili viwe imara na pale ambapo havipo vianzishwe ili huduma za pembejeo na masoko zipatikane kupitia vyama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhamasishaji na usimamizi imara, msimu wa 2017/2018, uzalishaji wa pamba unategemewa kuwa zaidi ya tani 600,000. Hii ni kutokana na wakulima kuhamasika na Serikali kupeleka pembejeo hususan viuadudu ambapo chupa milioni 7.3 zenye thamani ya shilingi bilioni 29.2 zimenunuliwa na kupelekwa kwa wakulima ikilinganishwa na chupa 700,000 katika msimu uliopita. Aidha, vinyunyizi 16,500 vyenye thamani ya shilingi milioni 495 vimenunuliwa. Pia vinyunyizi vibovu 6,000 vilivyokuwa kwa wakulima vimekarabatiwa bila malipo pamoja na wakulima kufundishwa namna ya kupulizia viuadudu hivyo ili kudhibiti visumbufu vya zao hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa muda wa kati na mrefu kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 121,639 mwaka 2016/2017 hadi kufikia tani milioni moja ifikapo mwaka 2020. Lengo hilo litafikiwa kwa kuongeza matumizi ya mbegu bora ambapo katika msimu wa 2018/2019, bodi itazalisha tani 40,000 za mbegu aina ya UKM08 ambayo ni zaidi ya mahitaji ya tani 25,000 kwa mwaka. Mbegu mpya aina ya UKM08 ina sifa za kipekee ikiwemo tija kubwa ya uzalishaji ikilinganishwa na mbegu ya zamani aina ya UK91.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati mwingine ni kuongeza uzalishaji wa mbegu mpya aina mbili zilizothibitishwa kwa ajili ya kuzipeleka kwa wakulima na kutenga maeneo maalum ya kuzalisha mbegu bora. Aidha, maeneo yaliyoainishwa na Serikali kupitia Bodi ya Pamba katika kutekeleza mpango wa uzalishaji wa mbegu bora aina ya UKM08 ni Wilaya za Igunga, Uyui, Urambo, Nzega na Meatu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Zipo taasisi bado zinaendelea kununua mazao kwa mkopo, jambo linalosababisha malalamiko kwa wakulima.
(a) Je, Serikali inalijua jambo hilo?
(b) Je, ni lini utaratibu huu wa kununua mazao kwa mkopo utaisha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi za Serikali zinazohusika na ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima ni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB). Hata hivyo, taasisi hizi kwa miaka mitatu ya 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018 zimeweza kununua mazao toka kwa wakulima bila kuwakopa hivyo kutopata malalamiko yoyote kutoka kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ulinunua mahindi tani 22,335,157, mwaka wa fedha 2016/2017 tani 62,099,319 na mwaka wa fedha 2017/2018 tani 26,038,643.
Aidha, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilinunua mahindi tani 3,300 kwa mwaka wa fedha 2015/2016, tani 1,971.5 mwaka wa fedha 2016/2017 na tani 2,250 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kutoka kwa wakulima. Manunuzi yote haya yalifanyika kwa fedha taslimu bila ya kuwakopa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, Serikali inaendelea kusisitiza uimarishwaji wa vyama vya Msingi vya Ushirika na Vyama Vikuu vya Ushirika ili kupitia vyama hivyo wakulima waweze kuuza mazao yao na kujihakikishia soko. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa uuzaji wa mazao katika Soko la Bidhaa za Kilimo (Tanzania Mercantile Commodity Exchange) kupitia mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani (Warehouse Receipts System) unaosimamiwa na Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi (Warehouse Receipts Regulatory Board).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali itasimamia uuzaji wa mazao ya wakulima kwa njia ya minada ili kuweka ushindani wa bei na kumwezesha mkulima kupata bei kubwa kama ilivyo katika zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hizi zitamhakikishia mkulima kuwa na soko la uhakika na hivyo kuongeza kipato chake. Aidha, Serikali inapenda kuwaomba wanunuzi binafsi wa mazao mbalimbali ya wakulima kujizuia au kuacha kabisa kuwakopa wakulima kwani vitendo ya namna hiyo huwakatisha tamaa wakulima na kusababisha kushuka kwa uzalishaji.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Zao la Pamba limeendelea kupoteza mwelekeo kila kukicha na hivi karibuni mbegu walizoletewa wakulima wa Geita hazikuota kwa asilimia 30. Je, ni nini juhudi za Serikali katika kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO allijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba ulibadilika kuanzia miaka ya 1990 baada ya soko huria kuanza. Kutokana na kutokuwepo mfumo rasmi wa utayarishaji wa mbegu za pamba kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003, wakulima walikuwa wakiendelea kutumia mbegu aina ya UK 91 ambayo kwa mara ya kwanza ilitolewa mwaka 1991 na imekuwa ikitumika kwa zaidi ya miaka 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuwepo kwa magonjwa na wadudu, aina hii ya mbegu ya UK 91 imekwisha poteza sifa za kuendelea kutumika hivyo kuendelea kutumia aina hii ya mbegu ndio chanzo kikubwa cha uzalishaji na tija duni ya zao la pamba. Aidha, kwa kuwa mbegu hiyo hutunzwa na viwanda vya kuchambulia pamba, mara nyingine utunzaji wake huwa duni, hali ambayo hufifisha ubora wa mbegu na kusababisha utoaji wake pia kuwa hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kurekebisha mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba kwa kufuata vigezo vyote vya ubora kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Na. 18 ya mwaka 2003. Aidha, juhudi zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika sasa ni kuzalisha kwa wingi mbegu aina ya UKM 08 chini ya uratibu wa Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru kwa kushirikiana na sekta binafsi na Bodi ya Pamba. Vilevile aina mbili za mbegu mpya za UK 171 na UK 173 zitaanza kupatikana kwa wakulima kuanzia msimu wa 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa tulizonazo ni kwamba mbegu iliyosambazwa kwa wakulima Mkoani Geita haikuwa na tatizo lolote la kuota na hatukuwahi kupokea malalamiko kutoka kwa mtu yoyote kuhusu kutoota kwa mbegu hizo. Tumuombe Mheshimiwa Mbunge pia kama anao ushahidi wa mbegu wa hizo kutoota utupatie ili tufanye utafiti kujua tatizo hilo litakuwa limetokeaje. Aidha, maoteo ya uzalishaji wa pamba msimu huu wa 2017/2018 yanatarajiwa kuwa makubwa sana ambapo kiasi cha tani 600,000 zinatarajiwa kuvunwa.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha inasambaza pembejeo kwa wakati na kwa kuzingatia msimu na jiografia ya maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya pembejeo hufanywa na sekta binafsi, hususan makampuni na wafanyabiashara wadogo wa pembejeo za kilimo huhakikisha kuwa husambaza na kuuza pembejeo za kilimo kwa wakulima kulingana na mahitaji. Jukumu la Serikali katika kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati ni kuratibu mahitaji, upatikanaji na matumizi yake na kuelekeza aina za pembejeo zinazofaa kwa kuzingatia msimu wa kilimo katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuandaa mifumo ya kuhakikisha kwamba pembejeo za kilimo zinasambazwa na kuwafikia wakulima wengi kwa wakati na kwa bei nafuu. Ili kutekeleza azma hiyo, kuanzia mwaka 2017/2018 Serikali imeanzisha na kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (Fertilizer Bulk Procurement System) ili kuhakikisha mbolea inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa BPS umeleta faida nyingi zikiwemo kuongezeka upatikanaji kutoka tani 277,935 mwaka 2016/2017 hadi tani 310,673.7 mwezi Aprili, 2018 na kupungua kwa bei za mbolea kwa kati ya asilimia 11 hadi 39.5 ikilinganishwa na bei ya mbolea kabla ya Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mbolea tani 109,000 ikiwemo mbolea ya kupandia (DAP) tani 55,000 na mbolea ya kukuza (Urea) tani 54,000 zimeingizwa na kusambazwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Mbolea hizo hutumika kwa zaidi ya asilimia 62 kwa mwaka.
Aidha, siku ya Jumapili, tarehe 13 Mei, 2018, tutawapitisha Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani katika semina ambayo inahusu Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja ili tujenge ufahamu kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mbegu bora, kuanzia mwaka 2017/2018 Serikali imefuta tozo saba kwenye mbegu. Mpango huu umelenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza upatikanaji na kupunguza bei ya mbegu bora kwa mkulima. Kwa kufuta tozo hizo, Serikali inategemea bei ya mbegu bora itapungua na wakulima wengi wataweza kununua na kutumia.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha pamba yote iliyopo katika Jimbo la Bunda inanunuliwa kwa bei nzuri na kwa wakati muafaka?
(b) Katika Jimbo la Bunda kuna kilimo cha mkataba kwa kampuni moja na wakulima wana hofu kuwa huenda kampuni hiyo isifanye vizuri kwa wingi wa pamba iliyopo, je, Serikali inatoa kauli gani juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bunda katika msimu huu imelima ekari 71,668 na inatarajia kuvuna pamba tani 21,000 za pamba mbegu. Kampuni mbili za Olam Tanzania Ltd. na S&C Ginning Company Ltd. ndizo zitakazonunua pamba katika Wilaya ya Bunda. Kutokana na uchunguzi uliofanywa na Bodi ya Pamba, kampuni hizi zina uwezo mkubwa wa kifedha na kwamba tayari zimekwishapata fedha kutoka vyombo vya fedha tayari kwa ajili ya kuanza kununua pamba baada ya msimu kuzinduliwa tarehe 1 Mei, 2018. Aidha, nichukue fursa hii kipekee kabisa kuwahakikishia wakulima wa pamba wa Wilaya ya Bunda na maeneo yote yanayolima pamba kwamba pamba yao yote itanunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa kilimo wa 2017/2018 Wilaya ya Bunda na Wilaya nyingine 38 zimetekeleza kilimo cha mkataba baada ya kupewa idhini na Serikali ya kuingia mikataba na makampuni ya pamba. Katika Wilaya ya Bunda makampuni mawili ya Olam Tanzania Ltd. na S&C Ginning Company Ltd. ndiyo yaliyoingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Bunda Mji kwa ajili ya kutekeleza kilimo cha mkataba. Makampuni hayo yamekopesha pembejeo wakulima ambapo fedha hizo inabidi zirejeshwe wakati wa kipindi cha mauzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya wakulima 42,000 wamenufaika na mfumo huu wa kilimo katika Wilaya ya Bunda. Kwa kuwa makampuni haya yamewezesha wakulima kulima kwa tija na kwa ubora unaotakiwa na soko ni muhimu, mkataba katika maeneo haya lazima uheshimiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejiridhisha na uwezo wa makampuni haya na kwamba pamba yote katika Wilaya ya Bunda itanunuliwa kwa wakati na bei ya kuanzia itakuwa bei elekezi ya shilingi 1,100 kwa kilo na bei inaweza kupanda kulingana na hali ya soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Kampuni ya Olam Tanzania Ltd. ambayo itanunua pamba katika Jimbo la Mheshimiwa Boniphace Getere ni kampuni kubwa na imejipanga vizuri kuhakikisha itawahudumia wakulima wa pamba ipasavyo kama ilivyofanya katika ule msimu wa ununuzi wa 2017/2018. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Serikali imezuia biashara ya BUTURA na wanunuzi wa kahawa kwa watu binafsi (moja kwa moja kwa wakulima) na kuagiza yote iuzwe kwa Vyama vya Msingi wakati vyama kama KDCU vilishindwa kuwapa bei nzuri wakulima:-
• Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha inakuja na mbinu mpya ya kuwapa bei nzuri wakulima wa kahawa?
• Je, ni hatua zipi zimechukuliwa haraka ili kuhakikisha wale walioua Vyama vya Ushirika wanashtakiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka 2018/2019, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imejipanga kuhakikisha kuwa biashara ya zao la kahawa itaendeshwa na kusimamiwa na Vyama vya Ushirika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali chini ya mfumo wa stakabadhi za ghala. Aidha, kupitia mfumo huu, kahawa ya mkulima itakusanywa na kukobolewa na kisha kuuzwa mnadani chini ya usimamizi wa Vyama Vikuu vya Ushirika, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bodi ya Kahawa na Bodi ya Stabadhi za Ghala ambapo kahawa itanunuliwa kwa bei ya ushindani na yenye tija itakayowezesha mkulima kulipwa malipo ya pili na ziada.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), imeendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara na kaguzi za kiuchunguzi katika vyama vya ushirika na kuchukua hatua mbalimbali za kisheria pindi inapobainika kuwepo kwa ubadhirifu. Aidha, wahusika wa ubadhirifu wamekuwa wakichukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na Bodi za Uongozi na Menejimenti zake kuondolewa madarakani na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ambapo baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hushtakiwa Mahakamani na kuwataka kurejesha fedha walizoiba.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Zao la Katani linalimwa kwa wingi Mkoani Tanga hususan Wilaya ya Muheza na ni zao tegemeo la Uchumi Mkoani humo na bei ya zao hili katika Soko la Dunia limeongezeka sana:-
• Je, Serikali ina mpango gani katika kuongeza ulimaji wa zao hilo Wilayani Muheza?
• Je, kwa nini Serikali isitafute mwekezaji mkubwa wa kuwekeza katika kilimo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa zao la mkonge linalimwa kwa wingi zaidi Mkoani Tanga. Kwa sasa Wilaya ya Muheza ina jumla ya wakulima wadogo wapatao 211 ambao hadi kufikia mwezi Desemba walikuwa wamepanda hekta 975 na kuzalisha tani 1,462.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni kweli kuwa bei ya Mkonge katika Soko Dunia kwa sasa ni nzuri na inaendelea kuimarika, mathalan mkonge ule wa daraja UG, bei yake kwa sasa imefikia Dola za Marekeni kati ya 1,600 hadi 1,800 kwa tani. Hali inatoa fursa kubwa kwa wakulima wa mkonge kunufanika na kilimo hiki na kupata mazao makubwa na hivyo kuimarisha hali zao za maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania inatekeleza Mpango wa Miaka 10 ya Uendelezaji wa zao wa mwaka 2012/2013 – 2021/2022 (10 Years Sisal Development Plan). Mpango huu pamoja na mambo mengine unalenga pia kuongeza idadi ya wakulima wadogo wa mkonge kwa kuhamasisha ushiriki wa wananchi wengi zaidi kwenye kilimo hiki katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilayani Muheza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imetoa maelekezo kwa Bodi ya Mkonge ya kuhakikisha wadau wa mkonge wanaongeza uzalishaji kufikia tani 100,000 mwakani kwa kupanua na kutunza vyema mashamba yakiwemo yaliyomo Wilayani Muheza ili kuongeza tija. Pia kuhamasisha wakulima wapya kujiunga na kilimo hiki, hususan wakulima wadogo wa maeneo ya Tanga, Kilimanjaro, Singida na Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaunga mkono kabisa wazo la kupata wawekezaji wakubwa wengi zaidi wa mkonge Wilayani Muheza kama ilivyo kwa mashamba ya Kigombe, Muheza/Kitisa na Kumburu ili kupanua wigo wa ajira na mapato kwa Halmashauri. Wilaya ya Muheza ina mashamba makubwa yaliyofutiwa hati na Serikali kwa kutoendelezwa na kwa kuzingatia hali nzuri ya soko la mkonge pamoja na mabadiliko ya tabianchi ambayo mkonge huwa hauathiriki nayo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na uongozi wa Mkoa wa Tanga wa kupanga matumizi ya mashamba haya ikiwemo kuhamasisha uwekezaji mpya katika mashamba hayo kwa kuyaendeleza kwa kilimo cha mkonge. Ni vyema Mheshimiwa Mbunge akashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakatumia fursa hii kwa kutenga maeneo kwenye mashamba hayo kwa ajili ya wawekezaji wakubwa na wa kati wa mkonge.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Tanzania ni nchi yenye mazao ya biashara kama pamba, korosho, tumbaku na kahawa. Zao la pamba linazidi kuporomoka kutoka wastani wa ekari moja kilo 400 hadi kilo 120 kwa ekari moja ikilinganishwa na nchi kama China ekari moja kilo 2,000, India kilo 1,500, Burkina Faso kilo 1,200 na wastani wa uzalishaji wa dunia ni kilo 1,200 kwa ekari moja:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mkakati wa Kuendeleza Zao la Pamba unaoratibiwa na Bodi ya Pamba Tanzania kwa lengo la kuhakikisha kuwa tija na uzalishaji wa pamba nchini vinaongezeka. Kutokana na utekelezaji wa mkakati huo, uzalishaji wa pamba msimu 2017/2018 unatarajiwa kufikia zaidi ya tani 600,000. Aidha, mafanikio hayo yanatokana na upatikanaji wa mbegu bora, viuatilifu, huduma za ugani, uchambuaji na uongezaji thamani wa zao hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeanzisha Mkakati wa Kuzalisha Pamba hadi Mavazi kwa maana ya (Cotton to Clothing Strategy 2016-2020) ambao unatarajia kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka wastani wa kilo 600 hadi 700 kwa ekari kwa sasa na kufikia kilo 1,800 kwa ekari ifikapo mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika, aidha, mkakati huo unalenga kuongeza utengenezaji wa nyuzi kutoka wastani wa tani 30,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 90,000 ifikapo mwaka 2020 pamoja na kuongeza mauzo ya bidhaa za pamba nje ya nchi kutoka wastani wa Dola za Marekani milioni 30 hadi kufikia milioni 150 kwa mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha ongezeko la tija na ubora wa pamba, Serikali imechukua hatua ya kuimarisha mfumo wa uzalishaji wa mbegu za pamba ambapo kuanzia msimu 2018/2019, maeneo yote yanayolima pamba yatatumia mbegu aina ya UKM08 na kuachana kabisa na mbegu aina ya UK91 ambayo haina ubora. Aidha, aina mpya ya mbegu za pamba UK171 na UK173 zilizoidhinishwa mwezi Januari, 2018 zinaendelea kuzalishwa kwa wingi na zitaanza kuwafikia wakulima kuanzia msimu wa kilimo cha pamba wa 2021/2022. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa wakulima 435 wa kahawa waliodhulumiwa katika Jimbo la Buhigwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabalika, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2011/2012, Kikundi cha Wakulima wa Kahawa cha Kalinzi Organic kilipeleka jumla ya tani 15.8 za kahawa yenye thamani ya Dola za Kimarekani 74,397.24 kwa Kampuni ya Tanganyika Coffee Curing Co.Ltd kwa ajili ya kukobolewa na baadaye kuuzwa mnadani. Hata hivyo, baada ya kukoboa kampuni ya TCCCo Limited ilitambulisha kimakosa kahawa ya Kikundi cha Kalinzi Organic kuwa ni kahawa ya Kikundi cha Kalinzi Coffee Farmers kwa maana ya (KACOFA) na hivyo Bodi ya Kahawa Tanzania kukilipa fedha za mauzo ya kahawa kikundi cha KACOFA badala ya Kikundi cha Kalinzi Organic.
Mheshimiwa Spika, baada ya kugundulika mkanganyiko huo, taratibu za usuluhishi zilifanyika na maamuzi yalitolewa ambapo kikundi cha KACOFA kilikubali kurejesha fedha hizo kwa Kikundi cha Kalinzi Organic kupitia mauzo ya kahawa yao ya msimu ule wa 2012/2013. Hata hivyo, katika msimu wa 2012/2013 na 2013/2014 Kikundi cha KACOFA hakikupeleka kahawa ya kuuza kwenye soko la mnada hivyo fedha hizo hazikuweza kurejeshwa kwa Kikundi cha Kalinzi Organic kama ilivyoamuliwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya mashauriano kati ya uongozi wa kiwanda, Bodi ya Kahawa, Wizara ya Kilimo na viongozi wa Mikoa ya Kilimanjaro na Kigoma iliamuliwa kuwa suala hilo liwasilishwe kwenye vyombo vya usalama kwa ajili ya uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, upelelezi wa suala hilo umekamilika na jalada la shauri hilo lipo kwa Mwanasheria wa Serikali ili atoe uamuzi na mapendekezo ya hatua za kuchukua kwa kikundi cha KACOFA. Aidha, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba haki ya Kikundi cha Kalinzi Organic itapatikana. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Idadi kubwa ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo ili kujipatia mapato na moja kati ya changamoto kubwa wanayokabiliwa nayo ni ukosefu wa mitaji ya kuwezesha shughuli zao kuwa na ufanisi na tija zaidi:-
Je, Serikali ina mikakati gani kupitia Benki ya Kilimo kuwasaidia wananchi hao kupata mitaji ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Jimbo la Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto za upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo kutokana na taasisi nyingi za fedha kuweka masharti magumu hususan kwa waombaji kutoka sekta ya kilimo. Kutokana na umuhimu wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali, kama kuhamasisha uanzishwaji wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOs), VICOBA na Mfuko wa Taifa wa Pembejeo. Mikakati mingine ni pamoja na kufungua Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali (TIB) na kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo iliandaa Mpango wa Biashara ambao umeainisha mikakati na hatua za kuchukua. Benki pia inatoa mikopo kwa muda mfupi, muda wa kati na mrefu kwa riba nafuu kupitia vikundi vya wakulima wadogo. Benki imejikita katika utafuta vyanzo vipya vya mtaji ili kuimarisha uwezo wa benki. Aidha, Serikali imeshaipatia benki hiyo mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika wa shilingi bilioni 103.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ambayo imeshaanza ni pamoja na kuratibu utoaji wa dhamana kwa mikopo itakayotolewa na mabenki na taasisi nyingine za fedha kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (Smallholder Farmers Credit Guarantee Scheme) ambapo kiasi cha fedha USD milioni 20 kimetengwa; kufadhili miradi ya ubunifu vijijini kupitia Mfuko wa Ubunifu Vijijini (Rural Innovation Fund) ambapo kiasi cha fedha USD milioni 5 kimetengwa.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ni kuanzisha Progaramu za Uwezeshaji wa Vijana wa Wanawake na kupanua huduma za kibenki kwa kuanzisha Ofisi za Kanda sita (6). Hadi sasa Benki imefungua Ofisi ya Kanda ya Kati Jijini Dodoma na Ofisi ya Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 itafungua Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Jijini Mbeya na Ofisi Ndogo ya Kanda ya Magharibi Mjini Kigoma. Aidha, Kanda tatu zilizobaki ambazo ni za Kusini, Kaskazini na Zanzibar zitafunguliwa baadaye.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Julai, 2018, Benki imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 48.67 ambayo imewanufaisha wakulima 527,291 katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Morogoro, Tanga, Manyara, Kagera, Arusha, Zanzibar na Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Aidha, Serikali itaendelea kuongeza mtaji wa Benki ya Kilimo na kuhamasisha uanzishwaji na usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima.
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itaunda Bodi ya zao la Mchikichi kama ilivyoanzisha kwenye mazao mengine?
(b) Je, Serikali imefanya utafiti wowote kuhusu kuendeleza zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Na.19 ya Mwaka 2009 ilianzisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambayo ina jukumu la kuhamasisha uzalishaji na kufanya biashara ya mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko. Kwa sasa Bodi imeanza kufanya biashara ya zao la mahindi na alizeti kwa kununua, kusafisha na kusaga unga wa mahindi na kukamua mafuta ya alizeti. Bodi itakuwa inaongeza mazao mengine kulingana mahitaji, uzalishaji na uwepo wa biashara (commercial viability) ya zao husika. Aidha, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa zao la mchikichi katika ukuaji uchumi wa Taifa na kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi itatoa kipaumbele kwa zao hilo ili liweze kushughulikiwa na Bodi hii katika awamu ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa usimamizi wa mazao ya nafaka na mchanganyiko katika uzalishaji na masoko, Serikali inatarajia kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko, kwa maana ya (Cereals and other Produce Regulatory Authority). Kwa maana hiyo, mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kudhibiti na kusimamia biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko ili kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo cha mazao husika ikiwemo zao la mchikichi.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa zao la michikichi nchini unaratibiwa na Kituo cha Utafiti cha Mikocheni kilichopo Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti cha Tumbi kilichopo Tabora. Aidha, Kituo cha Utafiti Tumbi kimeweza kukusanya hifadhi nasaba (germplasm) za michikichi iliyoko nchini, wakati Kituo cha Utafiti cha Mikocheni kinatafiti namna ya kuzalisha miche ya michikichi kwa njia ya tissue (tissue culture) na baadaye kuisambaza kwa wakulima. Vilevile kituo hicho cha Mikocheni kina mpango wa kuingiza mbegu mama bora toka nje ya nchi na kuzitathimini ili kuona uwezekano wa uzalishaji wake hapa nchini.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Wakulima wa mbaazi Mikoa ya Mtwara na Lindi wameshuhudia kuporomoka kwa bei katika msimu wa mwaka huu pamoja na kwamba walihamasika kulima kwa wingi.
(a) Je, ni nini kilisababisha kuporomoka kwa bei ya mbaazi?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha hali hiyo haijitokezi msimu ujao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli bei ya mbaazi iliporomoka kutoka wastani wa bei ya shilingi 2,750 kwa kilo mwaka 2014/2015 hadi shilingi 700 kwa msimu wa mwaka 2016/2017 na kufikia wastani huo na katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Hali hii imesababishwa na ongezeko la uzalishaji wa mbaazi katika nchi za India, China, Brazil, Myanmar, Canada, Msumbiji, Sudan na Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ongezeko hilo la uzalishaji, mwezi Agosti, 2017 nchi ya India ambayo ndio wanunuzi wakuu wa mbaazi zetu ilizuia uingizaji wa mbaazi kutoka nje ya nchi hiyo kwa kuwa walikuwa na uzalishaji mkubwa wa kukidhi mahitaji yao na hivyo kusababisha ukosefu wa soko la uhakika kwa mbaazi zilizozalishwa nchini msimu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika, Serikali imeandaa mikakati mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao hususan mbaazi. Mikakati ya muda mfupi ni pamoja na Wizara kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwamba itaongeza idadi ya mazao yatakayonunuliwa ambayo ni pamoja na mazao ya jamii ya mikunde (mbaazi, choroko na dengu), mbegu za mafuta (ufuta, alizeti na karanga) na nafaka kwa (mtama, ulezi na uwele) katika mwaka 2018/2019. Kwa sasa bodi hiyo imepata soko la tani 100,000 za soya, tani 20,000 za ufuta na tani 3,500 za mbaazi ambazo zitauzwa kwa wadau ndani ya nje ya nchi. Pia itanunua tani 6,000 za alizeti kwa ajili ya kukamua mafuta katika kiwanda chake kilichopo Kizota, Jijini Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati mwingine wa muda mfupi ni kuuza zao la mbaazi katika soko la bidhaa kwa maana ya commodity exchange na kuhamasisha utumiaji wa mbaazi hapa nchini katika maeneo mbalimbali hususan katika mashule na majeshi yetu (Magereza na JKT). Aidha, Serikali kupitia Maafisa Lishe waliopo katika Halmashauri zote nchini, watatoa mafunzo ya namna bora ya kuandaa vyakula vinavyotokana na mbaazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya muda mrefu ni pamoja na kampuni kutoka India kujenga Kiwanda cha kiitwacho Mahashree Agro Processing Ltd kitakachosindika aina zote za mazao jamii ya mikunde, korosho na ufuta katika Kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mkambarani, Wilayani Morogoro kitakachokuwa na uwezo wa kusindika tani 200 za aina mbalimbali ya mikunde kwa siku na kuuza katika soko la ndani na nje. Kiwanda hicho kitasaidia wakulima kupata bei nzuri na soko la uhakika mara kitakapoanza uzalishaji mwaka 2019.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Mradi wa Kilimo wa RUBADA - Rufiji, umekuwa mradi wa kitapeli ambao watu wachache wanajinufaisha na rasilimali za Rufiji bila ya Wana-Rufiji kupata maendeleo yoyote.
Je, ni lini Serikali itafikiria kuleta mradi wa kilimo katika Bonde la Mto Rufiji ambalo kwa miaka mingi liko tupu bila shughuli yoyote ya kilimo hasa ikizingatiwa kuwa bonde hilo lina kila kitu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu mbili, naomba nianze kutoa maelezo ya utangulizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rubada siyo mradi, bali ilikuwa ni Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Rufiji kwa maana ya Rufiji Basin Development Authority.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya, sasa naomba nianze kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema nikiri tu kwamba kulikuwepo upungufu wa kiutendaji ndani ya RUBADA. Kutokana na hali hiyo, Wizara ilifanya uchunguzi mwezi ule wa Oktoba, 2014 na tarehe 8 Aprili, 2015 Wakurugenzi watatu wa RUBADA walisimamishwa kazi na hatimaye tarehe 21 Januari, 2016 Bodi ya RUBADA iliwafukuza kazi rasmi Wakurugenzi wawili.
Aidha, kutokana na mabadiliko ya kisera, kisheria na kimfumo, imeonekana kuwa RUBADA imekosa uhalali wa kuendelea kuwepo. Hivyo Serikali mnamo mwezi Septemba, 2017 ilileta Muswada wa Sheria Bungeni ukipendekeza kuifuta RUBADA. Bunge liliridhia kuifuta RUBADA na shughuli zake kuhamishiwa taasisi nyingine za kiserikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaelewa fursa zilizopo katika Bonde la Rufiji. Hatua kadhaa zimechukuliwa kutumia vizuri fursa hizi. Mathalani, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa Bwawa Stiegler’s Gorge kwa ajili ya umeme wa megawati 2,100. Bwawa hili pia litawezesha kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji, mifugo na uvuvi. Pia upo mradi wa Bwawa la Maji la Kidunda ambalo pamoja na kutoa uhakika wa maji ya kunywa kwa Jiji la Dar es Salaam litatumika pia kwa umwagiliaji, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya sekta ya kilimo imeandaa programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili kwa maana ya (ASDP II) ambapo ina maeneo ya kipaumbele 23 na jumla ya miradi ya uwekezaji kwa maana ya Investment Projects 56 ya kipaumbele ambayo inajumuisha miradi iliyopo katika Bonde la Mto Rufiji ambayo ilikuwa ikiratibiwa na RUBADA chini ya uliokuwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Miradi hiyo ni kama vile iliyopo maeneo ya Muhoro, Tawi, Bumba na Msoro. ASDP II inalenga kuendeleza miradi hiyo iliyopo Bonde la Mto Rufiji kama kuweka miundombinu ya umwagiliaji ambapo wananchi wengi watanufaika kupitia programu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu kuwa miradi hii ikikamilika italifanya Bonde la Mto Rufiji kuwa lulu ya maendeleo. Kwa maana hiyo, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa avute subira kidogo kuona mabadiliko haya tarajiwa na yenye matokeo chanya.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Shirika la Kilimo Uyole lina Kituo cha Utafiti katika Kitongoji cha Nkena, Kata ya Mtanila, Wilayani Chunya; na kwa kuwa kituo hicho kimehodhi eneo kubwa sana na hakijafanya kazi kwa zaidi ya miaka kumi na tano (15):-
Je, ni lini Serikali italiacha eneo hilo kwa wananchi kwa shughuli zao za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa kilimo, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, nianze kutoa maelezo ya utangulizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lililokuwa linajulikana kama Shirika la Kilimo Uyole sasa hivi ni Kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole ambacho makao yake yapo Uyole Mbeya. Kituo hiki kiko chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI - Tanzania Agricultural Research Institute) chini ya Wizara ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Utafiti Tumbaku Tanzania (TORITA - Tobacco Research Insitute of Tanzania) inatumia maeneo ya ardhi yaliyopo Tumbi, Tabora pamoja na Mtanila, Chunya na Seatondale kule Iringa kwa ajili ya shughuli za utafiti wa tumbaku kwa lengo la kuwapatia wakulima wa tumbaku teknolojia bora ikiwemo mbegu bora zinazostahili visumbufu vya tumbaku na ujengaji wa mabani bora. Aidha, watafiti kutoka Uyole Mbeya wamekuwa wakitumia kituo hiki kwa nyakati tofauti kufanya utafiti kwa mazao mbalimbali ikijumuisha mahindi na maharage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya utafiti wa Tumbaku Tanzania TORITA bado inahitaji rasilimali ardhi hiyo kwa ajili ya shughuli za utafiti kwa mahitaji ya sasa na ya baadaye. Ikumbukwe rasilimali ardhi kwa ajili ya matumizi ya utafiti huwa inatengwa kwa kuzingatia mahitaji ya miaka mia mbili ijayo. Taasisi hii ina mikakati mikubwa ya kuwezesha wakulima kupata mbegu bora suala ambalo litahitaji eneo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hivi sasa inaendelea kuboresha huduma zake mbalimbali za utafiti kupitia TARI ambayo itakuwa na msukumo mkubwa na kujiendesha yenyewe ikishirikiana na sekta binafsi. Hivyo, kuhitaji eneo hilo kwa ajili ya kupanua shughuli zake zote za utafiti.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Kituo cha mafunzo ya Wanyamakazi na utengenezaji wa zana za kilimo katika Kata ya Upuge, Wilayani Uyui, Mkoani Tabora kimechakaa sana na hakifanyi kazi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukifufua Kituo muhimu sana kwa mafunzo na zana zake vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2002/2003 hadi 2006/2007, ilikarabati vituo sitini na nane vya mradi wa wanyamakazi katika mikoa kumi na nane nchini kikiwemo Kituo cha Upuge kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na kupewa zana kwa ajii ya kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wakulima. Zana hizo ni pamoja na plau, majembe ya palizi, majembe ya matuta, tindo (rippers) na mikokoteni kwa ajili ya kutoa mafunzo na kufanya maonesho kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la ukarabati huo ni kuvifanya vituo hivyo kuendelea kutoa mafunzo kwa wakulima katika maeneo yao kwa kushirikiana na Maafisa Ugani waliopatiwa mafunzo juu ya wanyamakazi kwa ajili ya kufundisha wakulima katika vijiji. Aidha, eneo linalolimwa na wanyamakazi limeongezeka kutoka asilimia ishirini hadi asilimia ishirini na nne hivyo, kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia sabini hadi asilimia 62.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia lengo la kuongeza uzalishaji na tija, Wizara ina jukumu la kusimamia upatikanaji wa Zana za Kilimo, utoaji mafunzo yahusuyo Zana za Kilimo, udhibiti wa ubora wa zana zinazoingia nchini kwa kushirikiana na CAMARTEC, utafiti na huduma za ugani, pamoja na kuainisha zana mbalimbali kwa matumizi ya mashamba kabla na baada ya kuvuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Wanyamakazi cha Upuge kwa sasa kina maksai ishirini na mbili na eneo lenye ukubwa wa hekta themanini kwa maana ya (ekari 200), hivyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Uyui inakusudia kufanya ukarabati wa zana hizo na kuanza kutoa mafunzo kwa Maafisa Ugani ishirini na Wakulima mia moja katika msimu wa 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ya Kilimo inaishauri Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kukitumia Kituo cha Upuge kwa mafunzo na uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kupata fedha zitakazosaidia kumudu gharama za kuendesha kituo hicho. Wizara ya Kilimo inasisitiza kuwa Halmashauri za Wilaya zote nchini ni lazima zisimamie na kuendeleza vituo vya wanyamakazi vilivyopo katika Halmashauri zao.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Tumbaku inayolimwa Mkoani Tabora inachangia pato kubwa la Taifa:-
Je, Serikali ipo tayari kuboresha mazingira ya kilimo hicho ili kisiathiri mazingira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la tumbaku hulimwa katika Mikoa 11 ambayo ni Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Shinyanga, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Mara, Songwe na Morogoro. Uzalishaji wa zao hili husimamiwa na Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania na kwa kufuata taratibu na kanuni za kilimo kinachojali hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora unazalisha tumbaku nyingi zaidi kuliko mikoa mingine inayozalisha tumbaku hapa nchini, na hivyo kuchangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa. Aidha, katika msimu wa 2015/2016 Mkoa wa Tabora pekee ulizalisha asilimia 47 ya tumbaku yote iliyozalishwa nchini na asilimia 48 kwa ule msimu wa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania inasimamia taratibu na kanuni zote ambazo zinahamasisha kilimo bora cha tumbaku na kinachozingatia hifadhi ya mazingira. Pamoja na mambo mengine, Kanuni zinaelekeza kila mkulima wa tumbaku asajiliwe na awe na eneo la kupanda miti isiyopungua 250 au zaidi kwa kila hekta moja ya tumbaku anayolima.
Miti inayopandwa pamoja na kuwa chanzo cha nishati ya kukausha tumbaku pia husaidia kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Tumbaku Tanzania imeendelea kuhamasisha na kusimamia ubadilishaji wa mabani ya kukaushia tumbaku kutoka ya awali yanayotumia magogo ya miti na kutumia mabani ya kisasa ambayo yameongezeka kutoka mabani 101,982 mwaka 2014/2015 na kufikia mabani 172,405 mwaka 2016/2017. Aidha, mabani ya zamani yamepungua kutoka mabani 192,975 mwaka 2014/2015 hadi mabani 135,410 mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuhamasisha wakulima wote wa tumbaku nchini kutumia mabani ya kisasa kuanzia msimu wa mwaka 2018/2019 ikiwa ni pamoja na kuendeleza juhudi za kutafuta nishati mbadala. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Wilaya ya Hanang ni miongoni mwa Wilaya zinazozalisha kwa wingi nafaka za mahindi, ngano na shayiri lakini inashangaza kuona kuwa ruzuku ya pembejeo imepungua kutoka vocha 20,000 kwa mwaka 2012/2013 hadi vocha 10,000 mwaka 2014/2015:-
• Je, ni kwa nini vocha zimepungua na lini Serikali itaanzisha mfumo mpya wa pembejeo?
• Je, Serikali inatumia utaratibu gani kuhakikisha kwamba Mawakala wa pembejeo hawawauzii wananchi kwa bei kubwa kuliko bei ya soko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2012/2013, bajeti ya ruzuku ya pembejeo kwa utaratibu wa vocha ilitokana na mchango wa fedha za Serikali na Benki ya Dunia hivyo kupelekea kuwa na vocha nyingi ambapo Wilaya ya Hanang kaya 20,000 zilinufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mwaka 2015/2016 bajeti ya ruzuku ya pembejeo kwa kutumia vocha ilitokana na mchango wa Serikali pekee na hivyo kupungua kwa idadi ya vocha zilizotolewa, ambapo idadi ya kaya katika Wilaya ya Hanang ilipungua na kufikia kaya 10,000 ikilinganishwa na mwaka ule wa 2012/2013.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha mfumo wa usambazaji wa pembejeo kwa wakulima, kuanzia msimu wa 2017/2018, Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja kwa maana ya Bulk Procurement System, ambao umeongeza upatikanaji wa mbolea kwa wingi, bei nafuu na kwa wakati. Aidha, kwa kutumia utaratibu huo, bei za mbolea aina ya DAP na Urea zimepungua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja hutoa bei elekezi kwa kuzingatia umbali kutoka makao makuu ya wilaya kwenda kwenye kata na vijiji. Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na pindi ukiukwaji wa bei elekezi unapobainika hatua stahiki zinachukuliwa kwa wahusika.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Wakulima wa Vijiji vya Vikonge, Bugwe, Majalila na Kupanga wako tayari kulima kilimo cha pamba katika Wilaya ya Tanganyika, tatizo lililopo ni Serikali kutoa kibali cha idhini ya kulima kilimo hicho.
Je, ni lini Serikali itatoa kibali hicho ili wananchi waanze shughuli za kilimo cha pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba niwatakie Waislamu wote nchini Ramadhan Kareem. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliweka marufuku ya kilimo cha pamba katika badhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Katavi ili kuzuia kuenea kwa mdudu anayeitwa funza mwekundu. Zuio hilo ni mojawapo ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya kuzuia kuenea kwa wadudu ambao hawako kwenye maeneo mapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ilipokea taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Kakoso kuhusu uwepo wa wakulima wa pamba katika Wilaya ya Tanganyika. Kutokana na taarifa hiyo, timu ya wataalam kutoka Chuo cha Utafiti cha Ilonga na Bodi ya Pamba ilitumwa kwenda Wilayani Tanganyika na Mpanda ili kupata uthibitisho kuhusu uwepo wa wakulima wa pamba na kufanya tathimini ya mwenendo wa funza mwekundu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa iliyoandaliwa na wataalam hao imeainishwa kwamba mdudu huyo hayupo katika maeneo ya Mkoa wa Katavi yanayokaliwa na watu. Aidha, taarifa ilibainisha kwamba Wilaya za Tanganyika na Mpanda hazipatikani na eneo lenye zuio na kupendekeza Wilaya hiyo na Wilaya zote hizo ziruhusiwe kulima pamba.
Kutokana na taarifa hiyo, Serikali kwa msimu wa mwaka 2017/2018 imetoa kibali cha kuruhusu zao la pamba lizalishwe katika Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi na uzalishaji umeanza katika Wilaya hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo fedha zao ambazo walikopesha Serikali tangu mwaka 2014/2015?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, wifi yangu kama ifuatavyo:-
Mhesimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo kupitia vikundi vya wakulima na benki jamii badala ya utaratibu wa vocha za pembejeo uliokuwa unatumika awali. Utaratibu huu ulitumika kwa lengo la kuwajengea uwezo wakulima kuweza kukopa na kujipatia pembejeo wao wenyewe. Serikali ilitakiwa kuchangia asilimia 20 ya gharama za pembejeo zinazotosheleza ekari moja tu. Utaratibu huu ulikuwa utumike nchi nzima, lakini Mikoa iliyotekeleza ilikuwa ni Morogoro, Njombe, Iringa, Manyara, Mbeya, Ruvuma, Rukwa na Tabora tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu ilipokea na kupitia nyaraka mbalimbali za Makampuni na Mawakala wa Pembejeo 23 zenye madai ya jumla ya shilingi 7,180,914,669 waliofanya kazi ya kusambaza pembejeo zenye ruzuku msimu ule wa kilimo 2014/2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhakiki wa awali umefanyika kwenye mikoa kumi. Kupitia uhakiki huo wa awali imejiridhisha pasipo shaka uwepo wa upungufu kwa baadhi ya Makampuni na Mawakala kwa madai waliyowasilisha ikiwemo kukosekana kwa nyaraka za manunuzi, kutokuwepo kwa mikataba ya kazi, kukosekana kwa orodha ya wakulima wanufaika katika vijiji husika na kukiukwa kwa taratibu za utoaji wa pembejeo kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na matokeo ya uhakiki huo wa awali kuwa na upungufu mkubwa katika madai hayo, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uhakiki wa kina katika Mikoa yote na kwa Mawakala wote ili kubaini uhalali wa madai hayo ili madeni halali yaweze kulipwa. Taarifa rasmi ya uhakiki huo itatolewa mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa pembejeo zilizogawiwa kwa msimu wa mwaka 2016/2017 ambapo Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ilipewa jukumu la kusambaza mbolea na baadhi ya Kampuni na Mawakala wa Mbegu walisambaza mbegu bora, uhakiki pamoja na ukaguzi wa mahesabu unaendelea. Uhakiki huu utakapokamilika, taarifa itatolewa mapema. Ahsante.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, Serikali imechukua hatua gani kwa walioruhusu korosho zilizochanganywa na mawe kusafirishwa nje ya nchi bila kuchanguliwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Korosho ghafi katika msimu wa 2017/2018 lilikuwa zuri hususan kutokana na kupanda kwa bei ya korosho na kuuzwa kuanzia shilingi 3,500 hadi shilingi 4,000 kwa kilo. Bei ilipanda kutokana na Serikali kuimarisha minada ya korosho na kuwahamasisha wanunuzi kutoka nchini Vietnam kuja kununua korosho moja kwa moja Tanzania badala ya kupata korosho hizo kupitia India kama ilivyokuwa imezoeleka kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo, baadhi ya watu wasio waaminifu katika tasnia ya korosho wameanza kuchanganya korosho na vitu visivyokuwa korosho yakiwepo mawe na kokoto au kuchanganya korosho nzuri na mbovu kwa lengo la kuharibu Soko la korosho nje ya nchi. Suala hili lilibainika baada ya makontena mawili ya korosho ghafi kutoka Tanzania kugundulika kuwa zimechanganywa na kokoto huko Vietnam. Timu ya uchunguzi iliyoundwa na Serikali imebaini kuwa korosho hizo zilitoka Tanzania na zilipitia katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuwafanyia uchunguzi wa kina wale wote walioripotiwa katika taarifa ya timu ya uchunguzi iliyoundwa na Serikali ili hatua stahiki zichukuliwe kwa watakaobainika kuwa waliruhusu korosho zilizochanganywa na kokoto kusafirishwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua nyingine ni pamoja na kuitaka Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi ya Ghala, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Mamlaka za Serikali za Mitaa kushirikiana katika kuimarisha usimamizi wa ubora wa korosho katika mnyororo wake wote kudhibiti uhalifu huo. Pia kusimamia kikamilifu na kuhakikisha kwamba korosho zinazosafirishwa nje ya nchi zinakuwa na ubora unaostahili na kuweka nembo ya utambulisho kwa maana ya kuzi-brand na mfumo wa kuzitambua korosho zake nje ya nchi na hivyo kulinda soko lake na kuzitaka kampuni za ndani na nje ya nchi kuwasilisha malalamiko yao Serikalini pindi yanapotokea matatizo katika biashara zao kabla ya kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari kwa kuwa huchafua jina la biashara ya korosho za Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchunguzi unaofanywa sasa na vyombo vyetu vya dola umeshapelekea watuhumiwa kadhaa kukamatwa na kwa manufaa ya uchunguzi huo Serikali itatoa kauli mara itakapokuwa tayari kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Serikali imedhamiria kufufua tena Ushirika wa Mazao na Kuweka na Kukopa:-
Je, kwa nini Serikali isiwe inawasilisha Bungeni ukaguzi wa Hesabu za Vyama vya Ushirika unaofanywa na COASCO kila mwaka ili Bunge lipate nafasi ya kuzijadili kama inavyofanyika kwa ripoti za CAG?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) ni shirika la umma lililoanzishwa kwa Sheria Na.15 ya mwaka 1982 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2005 kwa lengo kuu la kufanya ukaguzi wa hesabu za Vyama vya Ushirika Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya ukaguzi unaofanywa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) inawasilishwa kwa chama cha ushirika husika na kujadiliwa na wanachama katika Mkutano Mkuu kwa mujibu wa kifungu cha 55(5) cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 pamoja na kifungu cha 4(1)(b) cha Sheria ya Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika Na. 15 ya mwaka 1982 iliyorekebishwa mwaka 2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013, vyama vya ushirika nchini husajiliwa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika. Sheria hii inaelekeza pia kuwa vyama vya ushirika vinapaswa kukaguliwa na COASCO au taasisi zingine za ukaguzi zilizoidhinishwa na Mrajisi. Aidha, ukaguzi wa vyama vya ushirika hufanywa pia katika vipindi tofauti kulingana na misimu ya mazao na shughuli za vyama ambapo ripoti za ukaguzi huwasilishwa katika mikutano mikuu ya vyama husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vyama vya ushirika ni taasisi za kijamii, hivyo ripoti za ukaguzi huwasilishwa katika mikutano mikuu ya vyama husika na kujadiliwa na wanachama wake wenyewe. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJABU aliuliza:-
Chuo cha Kilimo cha Utafiti cha Mlingano Wilaya ya Muheza kipo katika hali mbaya:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwenye Kituo cha Kilimo Mlingano ili kiweze kufanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uchakavu ya miundombinu katika baadhi ya vyuo vya kilimo ikiwemo Chuo cha Kilimo cha Mlingano. Changamoto hizo ni pamoja na uchakavu wa ofisi, madarasa, mabweni ya wanachuo, maabara, nyumba za watumishi, maktaba pamoja na Karakana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuvikarabati vyuo vya kilimo kupitia Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (SDP II) ili viweze kutoa mafunzo ya kilimo kwa ufanisi. Uboreshaji huo unatarajiwa kuviwezesha vyuo kuzalisha wataalam wenye umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika sekta ya kilimo. Aidha, uboreshaji huo pia utavutia wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati kujiunga na vyuo kama ilivyokuwa zamani na hivyo kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2018/2019, Serikali imepanga kuvifanyia ukarabati vyuo vya kilimo vyote nchini ikiwemo Chuo cha Kilimo cha Mlingano ambapo jumla ya shilingi bilioni nne zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya vyuo vya kilimo nchini.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Vitongoji vingi katika Jimbo la Bagamoyo havijafikiwa na mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini nchini:-

Je, ni lini TASAF itaviingiza vitongoji hivyo katika mpango wake wa kunusuru kaya maskini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Manajimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Bagamoyo ulianza mwaka 2013 ambapo vijiji/mitaa 66 vilijumuishwa katika mpango huo. Hadi sasa jumla ya walengwa katika kaya 12,081 wamenufaika na mpango huo. Aidha, jumla ya fedha zilizotumika katika mpango huo ni kama ifuatavyo:-

(a) Uhaulishaji fedha kwa (conditional cash transfer) Sh.9,709,631,300.

(b) Miradi ya kutoa ajira za muda 277 yenye thamani ya Sh.3,560,991,100 imetekelezwa.

(c) Vikundi 536 vya kuweka akiba na kuwekeza vyenye jumla ya wanachama 7,591 vimewezeshwa na hadi sasa wanachama wa vikundi hivyo wameweza kuweka akiba ya Sh.27,277,100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Sehemu ya Pili ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Bagamoyo inatarajia kuanza kabla ya Juni, 2019 kwa maana ya mwaka huu ambapo jumla ya vijiji na mitaa 44 vitafikiwa. Hivyo, jumla ya vijiji na mitaa 110 katika Wilaya ya Bagamoyo vitakuwa vimenufaika na mpango huo.
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:-

Kumekuwa na upungufu wa rasilimali watu katika taasisi za umma na baadhi ya watumishi kushindwa kufanya maamuzi:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo ndani na nje ya nchi kwa watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo na kuleta tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwapatia mafunzo watumishi wa umma ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi. Kwa kutambua hilo, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora huandaa sera, kanuni na miongozo inayohusiana na mafunzo katika utumishi wa umma na kufuatilia utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Menejimenti ya Ajira ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2008 kifungu 4.8; Sera ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2013 kifungu 4.2; na Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 kifungu G 1 (vifungu vidogo 7, 9, 10 na 11) zinasisitiza kuhusu umuhimu wa kila mwajiri katika utumishi wa umma kuandaa na kutekeleza Mpango wa Mafunzo kwa mujibu wa tathimini ya mahitaji ya mafunzo kwa maana ya (Training Needs Assessment).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 kupitia Wizara, Idara zinazojitegemea pamoja na Wakala, Serikali ilitenga jumla ya Sh.54,470,327,822 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya ndani na nje kwa watumishi wa umma. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, jumla ya Sh.39,839,347,632 zimetengwa kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo hususani Australia, India, Japan, China, Indonesia na Jamhuri ya Korea ambapo katika mwaka ule wa 2016/2017 kupitia wadau hao jumla ya watumishi wa umma 654 walipatiwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika nchi hizo. Aidha, katika mwaka ule wa 2017/2018, fursa za mafunzo zilizotolewa na washirika hao ziliongezeka hadi kufikia 827. Fursa hizo zimewezesha watumishi wa umma kupata uelewa, ujuzi na maarifa mapya ya kumudu majukumu yao katika kutekeleza malengo ya Taifa. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-

Rushwa ni adui mkubwa wa haki. Aidha, rushwa ikishamiri husababisha athari hasi kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiteknolojia na hivyo kuchangia ongezeko la umasikini:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kulinusuru Taifa dhidi ya Rushwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba rushwa ni adui wa haki, kwani ni kikwazo katika kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi kwa haki na usawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua athari za rushwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, Serikali imeandaa kutekeleza mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa na mpango wa utekelezaji Awamu ya Tatu kwa maana ya NACSAP III ule wa mwaka 2017 hadi 2022.

Mkakati huu unalenga kuzuia na kupambana na rushwa katika Sekta za uchumi za kimkakati zenye mazingira shawishi ya rushwa ambazo ni manunuzi ya Umma, ukusanyaji wa mapato, uvunaji na matumizi ya maliasili, madini, nishati, mafuta na gesi, utawala, vyombo vya utoaji wa haki na shughuli za Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa malengo ya mkakati huu ni kuimarisha na kuboresha mifumo ya utawala ya vyombo vya utoaji wa haki, kuimarisha elimu ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa na kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za Umma na vilevile za binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba wala rushwa na wahujumu uchumi wanachukuliwa hatua za kisheria, Sheria ya Uhujumu Uchumi ile Sura ya 200 imefanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 ya Mwaka 2016 kwa kurekebisha vifungu kadhaa kwa kupanua wigo na kuongeza makosa ya uhujumu uchumi pamoja na kuanzisha Division ya Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi katika muundo wa Mahakama Kuu na Mahakama hii imeshaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapambano dhidi ya rushwa yameonesha mafanikio ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kitengo cha urejeshaji mali chini ya TAKUKURU kwa ajili ya urejeshaji mali zilizopatikana kwa njia za rushwa kwa maana ya Asset Tracing and Recovery Unit. Kupitia kitengo hiki, Serikali imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 127.9 na kutaifisha au kuzuia akaunti za fedha zenye shilingi bilioni 4.5. Kesi 1,340 zimefunguliwa Mahakamani na Serikali imeshinda kesi 685.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, miradi ya maendeleo 899 yenye thamani ya shilingi 1,642,522,950,825.10 ilifuatiliwa ambapo miradi ipatayo 111 yenye thamani ya shilingi bilioni 23,256,624,083.40 iligundulika kuwa na kasoro au kufanyiwa ubadhirifu. Hivyo, uchunguzi unafanyika na upo katika hatua tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-

Tatizo la ufisadi na wizi nchini limeachwa likaendelea kwa muda mrefu sana:-

(a) Je, ni kwa nini TAKUKURU wasiachiwe kuendesha mashauri makubwa ya ufisadi na wizi Mahakamani moja kwa moja bila ya kuomba kibali cha DPP?

(b) Je, DPP amezuia majalada mangapi ya uchunguzi kufikishwa Mahakamani na ni kwa nini?

(c) Je, Serikali haioni kwamba DPP anaweza kutumika kulinda maslahi ya viongozi ambao kwa kiwango kikubwa wanajihusisha na vitendo vya wizi na ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, lenye sehemu (a),(b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007, TAKUKURU wanayo mamlaka ya kufikisha watuhumiwa waliotenda makosa ya hongo kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria Na.11 ya mwaka 2007 moja kwa moja Mahakamani bila kupitia kwa Mkurugenzi wa Mastaka (DPP). Makosa mengine yaliyosalia yanapaswa kupata kibali cha DPP kabla ya kupelekwa Mahakamani kama ilivyoelekezwa kwenye kifungu cha 57(1) cha Sheria Na.11 ya mwaka 2007.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 57(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007, DPP anapaswa kutoa au kutotoa kibali kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani ndani ya siku 60 tangu Jalada la Uchunguzi kumfikia. Hata hivyo, DPP anapokea majalada ya uchunguzi kutoka vyombo mbalimbali vya uchunguzi vikiwemo TAKUKURU, Polisi, na Uhamiaji. Kwa siku DPP hupokea takribani majalada 10 kutoka TAKUKURU. Hivyo, kuna kila sababu DPP akaongezewa rasilimali watu na fedha ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa wakati. Dhana ya kuwa DPP anazuia Majalada ya Uchunguzi yasifikishwe Mahakamani siyo sahihi.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba DPP ni Ofisi inayojitegemea na mamlaka yake yako kwa mujibu wa Katiba. Hata hivyo, sote tumeshuhudia kwamba viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri wakifikishwa Mahakamani na kuhukumiwa kwenda jela. Naomba nitumie fursa hii kuwaasa watumishi na viongozi wote wa umma mkiwemo ninyi Waheshimiwa Wabunge kutojihusisha na vitendo vyovyote vile vya rushwa. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-

Halmshauri ya Longido inatakiwa kuwa na watumishi 1,660 wa kada mbalimbali lakini kwa sasa wapo 1atumishi 1,117 tu, hivyo, kuna upungufu wa watumishi 543 na wengi wao ni Watendaji wa Vijiji, Kata, Madereva na Makatibu Muhtasi:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vibali vya kuajiri watumishi wanaohitajika ili kuondoa upungufu uliopo?

(b) Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuwathibitisha maafisa wanaokaimu wenye sifa za kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kuwepo kwa tatizo la upungufu wa watumishi kwa waajiri mbalimbali hapa nchini na siyo kwa Halmashaui ya Wilaya ya Longido pekee. Upungufu huu umesababishwa kwa kiasi kikubwa sana na zoezi la kuwaondoa katika Utumishi wa Umma watumishi waliobainika kutumia vyeti vya kughushi katika ajira zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Serikali imetoa kibali cha ajira mbadala nafasi tano (5). Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Longido itapatiwa nafasi za Walimu na Fundi Sanifu Maabara kutoka kwenye mgawo wa nafasi 4,549 za Ajira Mbadala za Walimu ambazo mchakato wake unaendelea chini ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine, Halmashauri ya Wilaya ya Longido imetengewa jumla ya nafasi 177 za kada mbalimbali zikiwemo Watendaji wa Vijiji, Kata, Madereva na Makatibu Muhtasi katika mwaka wa fedha ule 2018/2019. Katika kuhakikisha suala la upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido linapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Serikali itaendelea kutenga nafasi za ajira mpya pamoja na kutoa vibali vya Ajira Mbadala kwa kada za kipaumbele katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sehemu (b) ya swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wa umma wanaothibitishwa katika nafasi za uongozi kwa maana ya madaraka ni wale walioteuliwa rasmi katika nafasi hizo baada ya taratibu za upekuzi kukamilika. Aidha, hakuna utaratibu wa kuthibitisha watumishi wa umma wanaokaimu nafasi za uongozi kwa maana ya madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hufanya upekuzi kwa watumishi wa umma wanaokaimu nafasi za madaraka ili kubaini iwapo wanafaa au la. Uamuzi iwapo mtumishi husika anafaa kuteuliwa kwenye nafasi anayokaimu hutegemea na matokeo na upekuzi. Hivyo, pamoja na kuwa na sifa za kitaaluma, Serikali hailazimiki kumthibitisha mtumishi iwapo anakosa vigezo vingine vya uongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa watumishi wa umma wote nchini wanaokaimu nafasi za uongozi wafanye kazi kwa bidii, weledi, umahiri, uzalendo kwa kuzingatia maadili ya kazi ili waweze kukidhi vigezo vya kuteuliwa na kisha waweze kuthibitishwa kwenye nafasi za uongozi ambazo ni madaraka wanazoteuliwa kuzishika. Ahsante.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-

Serikali katika kuhakikisha inapata watumishi bora na wenye sifa iliamua kuwaondoa watumishi wasio na sifa pamoja na wenye vyeti feki, lakini zoezi hilo lilikumbwa na changamoto mbalimbali ambapo Afisa Utumishi aliwaondoa watumishi kwenye payroll bila sababu maalum na walipofuatilia Wizarani walirudishwa kazini:-

(a) Je, kwa nini Serikali isiunde timu maalum ili ipite kila Halmashauri kupitia taarifa juu ya zoezi hili ili haki itendeke hasa kwa wale ambao hawana uwezo wa kwenda Wizarani?

(b) Wapo watumishi ambao baada ya kuajiriwa kwa kutumia vyeti feki walijiendeleza kielimu zaidi ya Darasa la Saba na wameondolewa kwa kosa la udanganyifu wa vyeti: Je, Serikali haioni kuwa hao ni bora kuliko wale ambao hawakujiendeleza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kushirikiana na waajiri na Baraza la Mitihani la Taifa, Serikali iliendesha zoezi maalum la kuhakiki vyeti vya ufaulu mtihani wa Kidato cha Nne, Kidato cha Sita na Ualimu. Kupitia zoezi hilo, watumishi 15,189 walibainika kuwa na vyeti vya kugushi na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mshahara (payroll).

Hata hivyo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watumishi na vyanzo vingine kuhusu watumishi kuondolewa kimakosa au kwa uonevu katika orodha ya malipo ya mishahara, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa karibu ikiwa ni pamoja na kuunda timu za ufuatiliaji wa utekelezaji wa zoezi hili. Jumla ya watumishi 4,160 waliobainika kuondolewa kimakosa au kwa uonevu wamerejeshwa kazini. Kati ya watumishi waliorejeshwa kazini 3,057 ni Watendaji wa Vijiji/Mtaa na Kata.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wanaojiendeleza zaidi ya Darasa la Saba wanafanya vizuri na Serikali inahimiza watumishi kujiendeleza kielimu. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ile ya D.12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009, ni makosa kwa mtumishi kujipatia ajira kwa njia ya udanganyifu.

Hivyo Serikali ilielekeza waajiri kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara Watumishi wa Umma wote walioajiriwa kabla ya tarehe 20, Mei, 2004 ambao katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi walijaza taarifa za udanganyifu kwamba walifaulu mitihani ya Kidato cha Nne, lakini hawakuthibitisha taarifa zao kwa kuwasilisha vielelezo vya sifa hizo kama vile taarifa binafsi (personal records).

Hivyo, pamoja na watumishi hao kujiendeleza kielimu, uamuzi wao wa kutoa taarifa za udanganyifu unawaondolea sifa ya uaminifu na uadilifu kwa Serikali na hivyo wanakosa sifa za kuendelea kuwa Watumishi wa Umma. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-

Je, Serikali inatumia Sheria ipi kutowapa wafanyakazi stahiki zao zinazohusu kupandishwa madaraja na ongezeko la mwaka (Annual Increment) kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Barua ya Katibu Mkuu – Utumishi yenye Kumbukumbu Namba CAC. 45/257/01/E/83 ya tarehe 9 Septemba, 2013 kuhusu upandishwaji wa vyeo kwa madaraja kwa watumishi wote nchini wa umma huzingatia vigezo muhimu sana kama vile sifa za kitaaluma, uzoefu wa kazi, utendaji mzuri wa kazi kwa maana ya OPRAS, tange au ukubwa kazini kwa maana ya Seniority, uwepo wa ikama na bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka husika wa fedha, vilevile bila kusahau nidhamu na mwenendo wa mtumishi huyo wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ile ya E. 9(1) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009, Toleo la Tatu, nyongeza ya mwaka ya mishahara haipaswi kuombwa au kudaiwa na watumishi wa umma bali Serikali ndio yenye uamuzi wa kutoa au kutokutoa nyongeza hiyo. Hivyo, katika utumishi wa umma hakuna sheria inayoainisha kwamba, mtumishi anatakiwa kupata nyongeza ya kawaida ya mshahara kwa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya E.2 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 viwango vya mshahara ikiwa ni pamoja na nyongeza ya mshahara kwa kila mwaka kwa maana ya annual increment hupangwa kulingana na uwezo wa Serikali kulipa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitoa nyongeza ya mshahara ya kila mwaka kwa maana ya annual increment kwa watumishi wote wa umma kuanzia mwezi Novemba, 2017. Vilevile Serikali imewaelekeza waajiri wote kuendelea na upandishwaji vyeo kwa watumishi 193,166 waliokasimiwa katika ikama ya bajeti ya mwaka 2017/208 kuanzia tarehe 1 Mei, 2019 na barua zinaendelea kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahimize watumishi wote wa umma kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuleta tija katika utumishi wa umma na Serikali itaendelea kutoa nyongeza ya mshahara pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kadri uwezo wa Serikali kulipa utakavyoruhusu. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI (K.n.y. MHE. ENG. RAMO M. MAKANI) aliuliza:-

Utekelezaji wa Mpango wa Kaya Maskini katika Jimbo la Tunduru Kaskazini una changamoto nyingi sana zinazolalamikiwa na Wananchi:-

Je, Serikali itachukua hatua zipi za makusudi kurekebisha kasoro hizo ili wananchi wapate kunufaika vema zaidi na huduma za Mfuko huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, naomba kujibu swali la Eng. Ramo Matala Makani kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa Mheshimiwa Eng. Makani hakutaja waziwazi changamoto za utekelezaji wa mpango kwenye Jimbo lake, Serikali kupitia TASAF, changamoto kubwa ambayo Mpango unakumbana nao ni kilio kutoka kwa baadhi ya wananchi maskini ambao hawajafikiwa na huduma za Mpango huo kwenye Vijiji/ Mitaa/Shehia takribani 5,693 ambavyo havikufikiwa katika Awamu ya Kwanza ya Mpango huu wa kunusuru kaya maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Makani na Wabunge wengine kwamba utaratibu umeshaandaliwa wa kuweza kufika kwenye Vijiji/ Mitaa/Shehia hizo mara tu baada ya mpango kuanza utekelezaji. Katika awamu hii, TASAF imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa yale malalamiko ya upendeleo, ubaguzi na kuachwa kwa watu maskini kuandikishwa kwenye Mpango huu hayajirudii na mifumo ya kielekroniki itatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi wote kwamba muda utakapofika wahakikishe wanalisimamia vizuri zoezi la utambuzi wa walengwa ili wale wanaostahili basi waweze kuwa wameandikishwa kwenye mpango huu. Hatua kali zitachukuliwa kwa viongozi na watumishi katika ngazi zote ambao katika maeneo yao watabainika kuwepo watu au kaya zisizo na vigezo kwenye Awamu ya Pili ya Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni malalamiko ya walengwa kuhusu makato ya fedha kipindi cha malipo. Suala hili walengwa wanaendelea kuelemishwa kwa nini makato yanatokea. Sababu ya kukatwa fedha zao ni kutokana na kutotimiza masharti ya kupokea ruzuku hasa kwa kaya zenye watoto walio shuleni halafu hawaendi shule na wale wanaotakiwa kuhudhuria kliniki ambao ni watoto wenye umri wa miaka mitano na hawafanyi hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kaya itashindwa kutimiza masharti ya kutimiza watoto hao kutohudhuria shuleni au kutopeleka watoto kliniki fedha hizo zinakatwa kama adhabu. Nimuombe Mheshimiwa Makani na Wabunge wengine wote, mnapoenda kwenye ziara katika Majimbo yenu ndugu zangu tusaidiane kutoa elimu hii ili kuepusha malalamiko ambayo sio ya lazima. Ahsante.
MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa baadhi ya wananchi wamekuwa wakinufaika na mradi wa TASAF ambao kwa kiasi umekuwa ukifanya vizuri, aidha mradi huu umefika vijiji vichache tu na vijiji vingine bado havijafikiwa na Serikali iliahidi kuwa vijiji vyote vitanufaika na mradi huu.

(a) Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya mradi wa TASAF kufikia vijiji vyote nchi nzima?

(b) Kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya viongozi kukata fedha za walengwa wa TASAF moja kwa moja kwa kuwakatia bima, michango mbali mbali ya vijiji na kadhalika bila ridhaa yao. Je, Serikali inatoa kauli gani katika jambo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Ahmad Badwel Mbunge wa Bahi lenye maswali mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulipoanza mwaka 2013 uwezo wa fedha uliokuwepo ulitosheleza kufikia Vijiji/Mtaa/Shehia 9,986 ikiwa ni asilimia 70 ya Vijiji/Mitaa/Shehia zote nchini. Vijiji/Mitaa/Shehia ambavyo havijafikiwa ni 6,858.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshakamilisha hatua zote za maandalizi ya Kipindi cha Pili cha Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini ambacho kinatarajia kuanza utekelezaji mwishoni mwa mwaka huu 2019 baada ya Serikali kupata fedha. Kipindi cha Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kitatekelezwa kwenye Halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar katika Vijiji/Mitaa na Shehia zote ikiwa ni pamoja na kufika kwenye Vijiji/Mitaa/ Shehia 6,858 ambavyo bado havijafikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ufafanuzi kuhusu matumizi ya fedha za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. Fedha hizi ambazo ni ruzuku zinatolewa ili kaya iweze kugharamia mahitaji ya msingi kama chakula, gharama za elimu na afya na kuwekeza kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kuongeza kipato. Hivyo, ni maamuzi ya kaya husika kupanga matumizi ya fedha hizi ili mradi haziendi kwenye matumizi ambayo hayaisaidii kaya kujikwamua na umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya maeneo, viongozi wa vijiji wanalazimisha kukatwa kwa ruzuku za walengwa ili kukatiwa bima ya afya au kulipia michango mbalimbali. Hii si sawa na haikubaliki. Napenda kusisitiza, lakini vilevile niagize, kwamba walengwa wasikatwe fedha zao moja kwa moja bali walipwe stahiki zao na iwapo kuna michango inayotakiwa kama ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya kijiji basi michango hii itozwe kwa wananchi wote wa kijiji husika na siyo kukata moja kwa moja kutoka fedha za walengwa wa TASAF peke yao. Nimalizie kwa kusisitiza kwamba viongozi wote waliokuwa wanatoa amri ya kukata fedha za walengwa wa TASAF moja kwa moja bila ridhaa ya walengwa hao, waache kufanya hivyo mara moja, kwa kuwa huu siyo utaratibu na wala siyo sahihi na vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba, baadhi ya halamshauri zilishawahi kufanya hivyo na Wakurugenzi waliagizwa warudishe fedha hizo na tayari wamesharudisha. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kuna utaratibu wowote wa kuajiri watu wote waliohitimu Vyuo na kukidhi vigezo vya kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu Serikali imekuwa Mwajiri Mkuu, wa Wahitimu wa Vyuo mbalimbali kutoka katika soko la Ajira nchini. Ajira hizi zimekuwa zikitolewa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya raslimali watu katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali kwa kuzingatia ikama na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kugharamia ajira mpya katika Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, Serikali ilianzisha Sekretarieti ya ajira katika Utumishi wa Umma, kwa lengo la kuratibu mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma kwa uwazi na ushindani kwa njia ya usaili wa nadharia na vitendo pale inapobidi. Hivyo, wahitimu wanaofaulu usaili ndiyo wanaokidhi vigezo vya kuajiriwa na huwa wanaajiriwa kwa kada zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Duniani kote, Serikali siyo mwajiri pekee wa wahitimu wa vyuo mbalimbali vya elimu, kwani pamoja na kuajiriwa Serikalini, wahitimu hao huajiriwa pia katika Sekta binafsi, Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, Asasi za Kiraia na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wahitimu wengine huamua kujiajiri wenyewe na hivyo kutoa mchango wa maendeleo kwa Taifa kwa njia moja au nyingine. Aidha, kuhitimu Elimu ya juu, siyo kigezo pekee cha kuwezesha muhitimu husika ila sifa na ushindani wa kutosha ili kuweza kuajiriwa na Serikali. Hivyo, Serikali haina utaratibu wa kuajiri wahitimu wote wa vyuo vya Elimu ya juu nchini. Ahsante.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST Aliuliza:-

Je, ni likizo ya muda gani wamekuwa wakipewa wazazi (watumishi wanawake na wanaume) pale wanapopata watoto mapacha zaidi ya wawili au watoto njiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni H. 12(2) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, mtumishi wa umma mwanamke anapojifungua mtoto hupewa likizo ya uzazi ya muda wa siku 84 mara moja kila baada ya miaka mitatu. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni H. 12(3) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009, mtumishi husika anapojifungua watoto zaidi ya mmoja hupewa siku 14 zaidi za likizo ya uzazi na hivyo kuweza kuwa siku 98. Kanuni tajwa haikubanisha muda wa likizo ya uzazi kwa mtumishi anayejifungua mtoto njiti.

Mheshimiwa Spika, matukio ya uzazi wa mapacha zaidi ya wawili (triple) na watoto njiti ni nadra kutokea mara kwa mara. Hivyo, Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 hazikuainisha masharti ya likizo ya uzazi kwa matukio kama hayo. Hivyo, natoa wito kwa waajiiri na wasimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma kutoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Utumishi na kuomba kibali cha kuongezewa muda wa likizo ya uzazi kwa watumishi wa umma walio chini yao pindi wanapojifungua watoto mapacha zaidi ya wawili au watoto njiti.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni H.13 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009, Mtumishi wa Umma mwanaume hupewa likizo ya uzazi ya angalau siku tano kuanzia siku ya kuzaliwa mtoto ili aweze kuhudumia familia yake. Hata hivyo, iwapo kuna sababu za msingi zinazomlazimisha kuendelea kuhudumia familia kwa ukaribu, mtumishi husika anaweza kuomba ridhaa kwa mwajiri wake ya kuongezewa ili siku kadhaa kuhudumia familia.

Mheshimiwa Spika, hivyo, inapotokea mtumishi wa umma kajifungua watoto mapacha zaidi ya wawili au watoto njiti na kulazimika kuwa na muda wa zaidi wa kuhudumia watoto hao, mwajiri wake anapaswa kuwasilisha hoja kwa Katibu Mkuu (Utumishi) ilia toe kibali cha kuongeza muda wa likizo ya uzazi. Ahsante.