Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Mwita Mwikwabe Waitara (135 total)

MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali kupitia Halmashauri itakamilisha majengo ya madarasa yaliyotokana na nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Abdala Kigoda, Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua juhudi za wananchi na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Elimu ikiwa ni pamoja na kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule kama vile vyumba vya madarasa, madawati, matundu ya vyoo, nyumba za Walimu, mabwalo na maabara.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Handeni ina maboma yapatayo 15 ya vyumba vya madarasa yaliyoanza kwa nguvu za wananchi na kati ya hayo, maboma sita yako katika hatua ya lenta. Hadi Januari, 2019 Halmashauri imepokea jumla ya shilingi 46,600,000/= kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma yaliyoanza kwa nguvu za wananchi ili yaanze kutumika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Wadau kupitia Programu ya Lipa kwa matokeo (EP4R) na Programu ya kuimarisha ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T) itaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.

Aidha, Halmashauri zinahimizwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma yaliyopo kabla ya kuanzisha miradi mipya. Naomba kuwasilisha.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-

Serikali imeanzisha sera nzuri ya viwanda nchini ili kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo kwa wananchi.

(a) Je, Serikali haioni upungufu wa mafundi mchundo na mafundi sadifu kuwa ni kikwazo cha ufanisi wa sera ya viwanda?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuziimarisha shule za ufundi za Moshi, Ifunda, Tanga na Mtwara ili kuwaandaa na kuwapatia mafundi sadifu kufanikisha sera ya viwanda nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa mafundi mchundo (technicians)na mafundi stadi (artisans)katika kutekeleza azma ya Serikali ikifikia uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025. Hadi kufikia Desemba 2018, kulikuwa na vyuo vya ufundi stadi 449 nchini ambavyo vilidahili wanafunzi 119,184 kujiunga katika fani mbalimbali za ufundi ili kuwa na wataalam wa kutosha kuendana na mageuzi ya viwanda nchini. Vilevile, kupitia programu ya taifa ya kukuza ujuzi kwa vijana, jumla ya vijana 10,858 wamefaidika na mafunzo mbalimbali ya ujuzi katika fani za useremala, uashi, terazo, uchongaji vipuri, ufundi umeme, ufundi bomba, uchomeleaji, ushonaji, upishi, huduma za hoteli, ufundi magari na kutengeneza viatu vya ngozi. Mikakati hiyo inakusudia kuwa na wataalam wa kutosha ili kufanikisha utekelezaji wa sera ya viwanda.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuborsha mazingira ya elimu nchini ikiwemo ukarabati wa shule na miundombinu ambapo kupitia mradi wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) kati ya mwaka wa fedha 2015/2016 hadi Desemba, 2018 Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 11.2 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za ufundi. Shule zilizokarabatiwa ni shule ya Sekondari Moshi kwa shilingi bilioni 2, Ifunda shilingi bilioni 2.8, Tanga shilingi bilioni 1.8, Musoma shilingi bilioni 1.2, Bwiru Wavulana shilingi milioni 825 na Iyunga shilingi milioni 978. Lengo la Serikali ni kuhakikisha shule hizo za ufundi zinaimarishwa ili kuwa na wataalam watakaoshiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-

Halmashauri ya Geita DC ina Majimbo mawili ya Geita Viijini na Busanda ambayo kiutawala husababisha usumbufu na hali tete kwa wananchi kijiografia na mkoa ulishapitisha kuomba Serikali iigawe kuwa na Halmashauri ya Busanda:-

Je, ni lini Serikali itaridhia ombi hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura Na. 287 (Mamlaka za Wilaya) na Sura Na. 288 (Mamlaka za Miji) pamoja na Mwongozo wa Serikali kuhusu Uanzishaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Mwaka 2014, mapendekezo ya kuigawa Halmashauri yanapaswa kujadiliwa kwanza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa uamuzi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeshajadili suala hili katika Kikao cha Baraza la Madiwani ingawa bado halijapelekwa kwenye Vikao vya Ushauri vya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC). Mara mchakato utakapokamilika na maombi kuletwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tathmini itafanywa na kuona kama kuna haja ya kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Mheshimiwa Spika, aidha, kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha maeneo yaliyokuwa yameanzishwa ili yaweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa badala ya kuendelea kuanzisha maeneo mapya ambayo hayaondoi kero ya kusogeza huduma kwa wananchi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Waheshimiwa Madiwani wana majukumu mengi ya kufanya katika kata zao; na posho wanayolipwa kwa mwezi hailingani kabisa na majukumu yao na ni ndogo sana:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza posho ya Waheshimiwa Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiongeza posho na maslahi ya Madiwani nchini kwa awamu kulingana na uwezo wa halmashauri kukusanya mapato ya ndani. Serikali ilipandisha posho za mwezi za Madiwani kutosha Sh.120,000 kwa mwaka 2012/2013 hadi shilingi 250,000 kupitia Waraka wa tarehe 16, Agosti, 2012 na posho za madaraka kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2014/2015 kupitia Waraka wa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa wa Tarehe 23, Desemba, 2014, Serikali ilipandisha posho za Madiwani kutoka Sh.250,000 hadi Sh.350,000 kwa mwezi kwa Madiwani na Sh.350,000 hadi Sh.400,000 kwa mwezi kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya pamoja na posho nyingine kama ilivyoainishwa kwenye Waraka wa tarehe 26, Novemba, 2007.

Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la posho na maslahi ya Madiwani inatokana na halmashauri kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani. Hivyo, natoa wito kwa halmashauri kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri ili kujenga uwezo wa ndani na kulipa posho hizo kwa Madiwani.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-

Serikali imekuwa na utaratibu wa kukarabati shule zake za sekondari na za msingi nchini:-

Je, ni lini Serikali itafanyia ukarabati Shule za Sekondari Masagulu, Lwande, Mkuyu na Shule za Msingi Songe na Masagulu zilizopo Wilayani Kilindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA C. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ina jumla ya Shule za Msingi za Serikali 111 na Sekondari 22. Kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imepatiwa kiasi cha Sh.122,823,097 kwa ajili ya ujenzi na umaliziaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari ambapo shule tatu za sekondari na 14 za msingi zimenufaika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuboresha miundombinu mashuleni ikiwemo ukarabati wa shule kongwe 89 nchini. Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na wadau wengine wa maendeleo itaendelea kuweka kipaumbele cha ukarabati wa miundombinu ya shule ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza. Aidha, natumia fursa hii kuzielekeza Halmashauri zote kutenga bajeti kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Moja ya mkakati wa EQUIP – Tanzania ni kuinua ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa kike ili waweze kuhitimu Shule ya Msingi na kuendelea na Sekondari, lakini mtoto wa kike ana vikwazo vinavyoweza kukatiza ndoto hii:-

(a) Je, mpango huu umejikita vipi katika kutokomeza mimba na ndoto za utotoni, udhalilishaji kingono, ukeketaji na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto?

(b) Je, ni upi usaidizi wa mpango wa wanafunzi walio katika hatari zaidi kwa makundi kama vile waliotelekezwa, walio katika umasikini wa kupindukia, yatima na walionusurika kutokana na unyanyasaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, udhalilishaji kongono na ukeketaji, Serikali kupitia programu ya EQIP Tanzania imeanzisha clubs za wanafunzi ziitwazo Jiamini Uwezo Unao (JUU) kwenye Shule za Msingi 4,476. Malengo ya clubs hizo ni kuwajengea wanafunzi hasa wa kike uwezo wa kujiamini, kujieleza na kujitambua. Kupitia clubs hizo, wanafunzi wanajifunza masuala mbalimbali ikiwemo hedhi salama na athari za kupata mimba katika umri mdogo.

Aidha, ili kuboresha mazingira ya watoto wa kike, mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kwa kupitia programu hii ilitoa ruzuku ya jumla ya shilingi bilioni 2.46 kwenye shule 4,476 ambazo kila shule ilipewa shilingi 550,000/=. Kupitia ruzuku hiyo, elimu ilitolewa kwa wanafunzi wa kike na wazazi kupitia ushirikiano wa Wazazi na Waalimu (UWAWA), kuhusu namna ya kutengeneza taulo salama za kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali kupitia programu ya EQUIP Tanzania imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii wakiwemo wanafunzi, wazazi na Walimu kupiga vita vitendo vya ukatili kwa watoto na kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia kwa makundi maalum wakiwemo watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia programu ya EQUIP Tanzania, Serikali imeongeza fursa ya kujifunza kwa watoto wa kike sawa na wa kiume na kuwakinga na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto. Jumla ya shilingi bilioni 6.8 zimetumika kuwajengea uwezo Walimu 50,446 kuhusu mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo matumizi ya mbinu zinazojali jinsia na ujenzi wa mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huo umeboresha mbinu rafiki na zinazozingatia jinsia katika ufundishaji na ujifunzaji kutoka asilimia 54 mwaka 2014 hadi aslimia 65 mwaka 2016 katika shule zilizo katika Mikoa iliyotekeleza programu hiyo ya EQUIP Tanzania. Tathimini inaonesha kuwa wasichana waliopata wastani wa juu katika kumudu stadi za kusoma na kuandika, walifikia asilimia 26.7 ikilinganishwa na wavulana asilimia 18 katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-

Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa hupata posho shilingi elfu ishirini kwa mwezi kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na kazi kubwa wanayoifanya:-

Je, ni lini Serikali itaongeza posho kwa Wenyeviti hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS – TAMISEMI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji katika shughuli za maendeleo. Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Mitaa, vitongoji na Wajumbe wa Serikali za Vijiji pamoja na Wajumbe wa Mitaa za mwaka 2014 zilizotolewa kupitia Tangazo la Serikali Na. 322 na Na. 323, sifa zinazomwezesha mkazi wa
Mtaa, Kijiji na Kitongoji kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti au mjumbe wa Serikali za Mitaa ni pamoja na kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, Serikali inalipa posho ya Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa kwa kutumia asilimia 20 ya mapato ya ndani inayorejeshwa na Halmashauri kwenye ngazi za Serikali za Mitaa. Hata hivyo, kiasi hicho kinategemea hali ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri yanayokusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Mkakati uliopo ni kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha makusanyo katika vyanzo vya mapato vilivyopo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ili kujenga uwezo wa kulipa posho kwa viongozi hao. Aidha, viwango vya posho inayolipwa vinatofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine kulingana na uwezo wa kifedha uliopo.
MHE.DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-

Katika Ilani ya CCM kuhusu huduma za afya nchini ni kujenga zahanati katika vijiji na kituo cha afya katika kila kata; kwa sasa Jimbo la Igunga lina vituo vya afya viwili tu katika kata 2 kati ya 17 na zahanati kwenye vijiji 19 tu kati ya vijiji 68:-

(a) Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye kata 15 zilizosalia?

(b) Je, ni lini Serikali itajenga zahanati kwenye vijiji 49 vilivyosalia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa NaibuSpika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 kwa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya kote nchini kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo. Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ilipokea shilingi milioni 800 kwa mwaka wa fedha 2018 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya Igurubi na Simbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kituo cha Afya cha Simbo ambacho ujenzi wake upo asilimia 97, fedha hizo zilitumika kumalizia majengo mawili ambayo ni jengo la upasuaji, nyumba ya mtumishi pamoja na ujenzi wa majengo mapya manne ambayo ni maabara, jengo la uzazi, jengo la kufulia na jengo kuhifadhi maiti. Aidha, kituo hicho kimeanza kupokea vifaa tiba kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Kwa upande wa Kituo cha Afya Igurubi, ujenzi unaendelea na umefikia asilimia 70. Jumla ya majengo manne mapya yamejengwa ambayo ni maabara, jengo la uzazi, jengo la kufulia na jengo la kuhifadhi maiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa awamu katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha. Ahsante.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-

Wakati wa ziara ya Kampeni za Uchaguzi Mheshimiwa Rais aliahidi kujenga daraja la kuunganisha Tarafa tatu za Luoimbo, Suba na Nyancha na tayari Halmashauri imeshapeleka makadirio Wizarani:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja linalounganisha Tarafa za Luoimbo, Suba na Nyancha ni miongoni mwa ahadi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozitoa maeneo mbalimbali nchini wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umefanya tathmini ya gharama za ujenzi huo na wamepata kiasi cha shilingi bilioni 1.15. Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo. Azma ya Serikali ni kuhakikisha ahadi hiyo pamoja na ahadi nyingine zilizotolewa na viongozi wakuu wa kitaifa zinatekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitao ijayo. Ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-

Barabara ya Vikindu – Vianzi hadi Sangatini ni muhimu kwa wakazi wa Jimbo la Mkuranga na Kigamboni:-

Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynab Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Vikindu - Vianzi hadi Sangatini yenye urefu wa kilomita 18.65, inaanzia Kijiji cha Vikindu -Vianzi na Kitongoji cha Sangatini (Mkuranga) Mkoa wa Pwani na kuungana na barabara ya Kibada, Mwasonga hadi Tundisongani iliyopo Wilaya ya Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa upande wa Wilaya ya Mkuranga inahudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijiji na Mijini (TARURA) na kwa upande wa Wilaya ya Kigamboni inahudumiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, TARURA Wilaya ya Mkuranga wameiomba Serikali shilingi milioni 270 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 za kuifanyia matengenezo maeneo korofi kwa urefu wa kilometa 18 na kujenga boksi kalvati moja lenye midomo miwili. Aidha, TARURA watafanya tathmini ya ujenzi kwa kiwango cha lami kipande wanachokisimamia na itakapokamilika, Serikali itazingatia matengenezo hayo kwa kutegemea na upatikanaji wa rasilimali fedha. Ahsante.
MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:-

Tarafa ya Mtinko Jimbo la Singida Kaskazini yenye Kata sita haina kituo cha afya cha Serikali:-

(a) Je, Serikali ipo tayari kukamilisha jengo la kituo cha afya katika Kata ya Makuro lililojengwa na wananchi ili wananchi waweze kupata huduma za rufaa kutoka katika Zahanati zilizopo?

(b) Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha za majengo ya ziada katika kituo cha afya Kata ya Makuro ili kutoa huduma bora kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mnweyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Joseph Monko Mbunge wa Singida Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Mtinko yenye Kata sita ina zahanati tisa na haina kituo cha afya. Hata hivyo, wananchi wa Tarafa hiyo hupata huduma za afya za rufaa kwenye hospitali teule ya Wilaya ya St. Carols Council Designated Hospital.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri ya Singida imepokea jumla ya shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya na kukarabati vituo vya afya viwili yaani kituo cha afya cha Msange na kito cha afya cha Mgori ili kuweza kutoa huduma za upasuaji kwa mama na mtoto. Serikali itaendelea kujenga na kukamilisha maboma ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyowezeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha afya cha Makuro kimejengwa kwa nguvu za wananchi na mpaka sasa jengo la wagonjwa wa nje lipo katika hatua za ujenzi kwenye ukuta. Nazielekeza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma na vituo vya kutolea huduma kwenye maeneo yao ya kiutawala. Serikali itaendelea kukamilisha maboma na kujenga kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA) aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa Mkuu wa Wilaya ya Ikingu amekuwa akijichukulia sheria mkononi na kuwanyanyasa wananchi wa Kata za Ighombwe, Iglansoni na maeneo ya Wilaya ya Ikungi.

Je, Serikali inaweza kutoa majibu ni mamlaka yapi aliyonayo Mkuu huyo wa Wilaya ya kuwanyanyasa na kuamrisha mali za wananchi kuchomwa moto au kuporwa na Serikali bila utaratibu wowote wa kisheria kwa kisingizio kuwa wanaishi maeneo yasiyoidhinishwa kwa makazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Igombwe, Iglasoni na maeneo ya Wilaya ya Ikungi zinapakana na hifadhi ya Msitu wa Minyughe yenye ukubwa wa hekta 264,600. Kwa nyakati tofauti shughuli za kibinadamu kwenye vijiji vinavyozunguka msitu huu zilianza kuhatarisha mazingira ya hifadhi hasa baada ya wananchi kadhaa kuhamia eneo la hifadhi na kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kupitia vikao vya kisheria vya Baraza la Madiwani liliazimia kuulinda msitu huu na kuwaondoa wavamizi, hivyo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambayo ndiyo yenye mamlaka aliyopewa na Sheria ya Tawala za Mikoa ya Regional Administrative Act ya mwaka 2002, chini ya Kifungu cha 15 kutoa amri halali, iliwataka wananchi hao kuondoka katika maeneo ya Hifadhi ya Msitu wa Minyughe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuwaondoa wavamizi lilifanyika kwa awamu mbili, yaani Mei na Oktoba, 2017 ambapo watu 119 waliondolewa kwenye hifadhi hiyo pamoja na ng’ombe 2,243, mbuzi 455 na kondoo 169. Zoezi hili lilishirikisha Askari wa Jeshi la Polisi waliofanya kazi yao kwa weledi wa hali ya juu kwa sababu hakuna raia aliyejeruhiwa wala kupoteza mali zake. Ni dhahiri uwepo wa Askari Polisi ambao ni wasimamizi wa sheria uliwezesha operesheni hiyo kufanyika salama na hakuna kielelezo wala ushahidi kwamba haki zao za msingi zilivunjwa.
MHE. OMARI M. KIGUA (K.n.y. MHE. MENDRAD L. KIGOLA) aliuliza:-

Sekondari za Jimbo la Mufindi Kusini zinakabiliwa na tatizo la hosteli kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka mbali:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga hosteli kwa kila sekondari katika Jimbo la Mufindi Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ina shule za sekondari 43 ambapo kati ya hizo shule 21 zina daharia (hostel). Katika mwaka wa fedha 2018/2019, shule nyingine mbili za sekondari za Ihowanza na Mninga zinaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa hosteli ili kufanya idadi ya shule zenye hosteli kufikia 23.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imetenga kiasi cha shilingi milioni 60 kupitia mapato ya ndani ili kusaidia ukamilishaji wa daharia zilizopo katika hatua ya ukamilishaji. Vilevile Lyara in Africa wamepanga kusaidia ujenzi wa hosteli katika Shule za Sekondari za Kiyowela na Idunda na CAMFED wamesaidia ujenzi wa hosteil ya Ihowanza.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Wanawake Mkoani Kigoma wameitikia wito wa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali kama vile vikundi vya kilimo cha muhogo, kurina na kuchakata asali na VICOBA:-

Je, Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kigoma zimechangia kiasi gani kwa vikundi hivyo kama sheria inavyotamka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri za Mkoa wa Kigoma zilitoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 129 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi Februari 2019, Mkoa wa Kigoma umetoa shilingi milioni 249 kwa ajili ya vikundi 171 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 181 zimetolewa kwa vikundi 120 vya wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais - TAMISEMI itaendelea kusimamia sheria inayozitaka Halmashauri kutenga, kutoa mikopo na kusimamia marejesho ya fedha hizo kutoka kwenye vikundi vilivyonufaika. Ahsante.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Mara ni mkoa ambao una makundi makubwa ya jamii ya wafugaji, wakulima na wavuvi lakini kwa sasa kuna shida kubwa ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji:-

Je, ni lini wafugaji watapatiwa eneo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara unakadiriwa kuwa na ng’ombe 1,305,075, mbuzi 733,321, kondoo 437,387,
nguruwe 5,802, punda 11,757 na kuku 1,524,653. Upande wa Nyanda za Juu katika Wilaya za Serengeti, Tarime, Rorya, Butiama na Bunda ndizo zenye ufugaji mkubwa wa mifugo ambapo Wilaya za Musoma, Rorya na Bunda kwa kiasi kikubwa zinashughulika na uvuvi hasa kwenye vijiji vya mwambao wa Ziwa Viktoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara kupitia Halmashauri 9 umeshatenga maeneo yenye jumla ya ukubwa wa hekta 15,588.55 kwa ajili ya malisho ya mifugo kupitia mpango wa matumizi ya ardhi ya vijiji. Mkoa kupitia Halmashauri utaendelea kutekeleza mpango wa matumizi ya ardhi kwa vijiji ili kuainisha matumizi ya ardhi kwa makundi mbalimbali wakiwemo wafugaji na wakulima ili kuepusha migogoro. Ahsante.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-

Mabadiliko ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 yameleta nafuu sana kwa wakulima, lakini wakati huo huo Halmashauri za Wilaya zenye wakulima wadogo zimeathirika kimapato na kusababisha kushindwa kutatua kero za wananchi kwa wakati.

(a) Je, Serikali inaweza kuangalia upya suala la utaoji ruzuku za maendeleo?

(b) Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo imeathirika kwa kiwango kikubwa: Je, Serikali ipo tayari kuipatia ruzuku ili kutoa huduma za elimu na afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290 imefanyiwa marekebisho na Bunge Mwezi Juni, 2017 kwa kupunguza kiwango cha ushuru wa mazao kutoka asilimia tano hadi asilimia tatu kwa mazao ya chakula na biashara. Hata hivyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha makusanyo katika vyanzo vilivyopo ili kuongeza mapato na kuboresha utaoji huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mikakati hiyo, mapato ya ndani ya Halmashauri yameendelea kuongezeka kila mwaka. Mfano, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya shilingi bilioni 687 na zilikusanya shilingi bilioni 553.39 sawa na asilimia 81. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri zimeidhinishiwa kukusanya shilingi bilioni 735.58 hadi Februari, 2019 zimekusanywa shilingi bilioni 401 sawa na asilimia 55. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri zimekadiria kukusanya shilingi bilioni 765.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi kwa ujumla inaonyesha makusanyo ya Halmashauri yameendelea kuongezeka pamoja na kupungua kwa ushuru wa mazao kutokana na Halmashauri kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato na vyanzo mbadala. Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea kuzisimamia Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuimarisha makusanyo na kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwaka 2019, Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 416 kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa ajili ya kugharamia Elimu Msingi Bila Malipo, shilingi milioni 250 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 20 ya shule za sekondari na shilingi 411 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba. Serikali itaendelea kuongeza utoaji wa ruzuku kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Serikali imekuwa na utaratibu wa kukarabati shule zake za msingi na sekondari nchini:-

Je, ni lini Serikali itazifanyia ukarabati Shule za Msingi Kwemashai, Bandi, Milungui, Kilole na Shule za Sekondari za Ntambwe, Ngulwi - Mazashai na Mdando?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2018/2019, Serikali kupitia Program ya Lipa Kulingana na Matokeo (EPforR) imepeleka jumla ya shilingi milioni 467 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, matundu sita ya vyoo na madarasa mawili katika Shule ya Msingi Shukilai (Shule ya Elimu Maalum) na ujenzi wa mabweni mawili Shule ya Sekondari Magamba, ujenzi wa bweni moja na madarasa mawili Shule ya Sekondari Umba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa Fedha 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 2,392 ya madarasa nchi nzima ambapo kati ya fedha hizo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imepewa kiasi cha Sh.512,500,000 kwa ajili ya kukamilisha maboma 46 ya madarasa shule za sekondari. Serikali itaendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya elimu kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY atauliza:-

Serikali ina nia njema ya kuuweka Mji Mkongwe wa Mbulu kwenye mpango kabambe wa maboresho ya Miji na Majiji, Mikoa na Wilaya na kwenye Awamu ya Pili ya mpango huo kwa ajili ya miundombinu ya masoko, barabara, vituo vya mabasi na taa za barabarani:-

(a) Kwa kuwa Mji wa Mbulu ni mkongwe toka kuanzishwa kwake, je, ni lini sasa nia hiyo njema itatekelezwa?

(b) Je, mpango huo wa maboresho ya Mji utasaidiaje miundombinu ya barabara za mitaa ya Mji wa Mbulu ambazo ni zaidi ya kilomita 40 za changarawe kwa kuwa ni kilomita 1.8 za lami kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikalli kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI inatekeleza miradi ya uboreshaji Miji Tanzania ambayo ni Urban Local Government Strengthening Programme (ULGSP) na Tanzania Strategic Cities Project (TSCP) na Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP) kwa fedha za mkopo nafuu toka Benki ya Dunia. Mpaka sasa miradi hii inatekelezwa katika Majiji 6, Manispaa 19 na Halmashaurui za Miji 6. Utekelezaji wa Programu ya Kuzijengea Uwezo Mamlaka za Miji (Urban Local Government Strengthening Programme-ULGSP) ulianza katika mwaka wa fedha 2013/2014 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2019/2020. Wakati wa maandalizi ya programu hii, Mji wa Mbulu ulikuwa haujapata hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji na hivyo kukosa vigezo vya kujumuishwa kwenye programu. Serikali itatoa kipaumbele kwa Mji wa Mbulu kwenye awamu nyingine za mradi huu.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Programu ya Kuzijengea Uwezo Mamlaka za Miji inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya msingi katika miji, kujenga uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuwezesha uandaaji wa mipango kabambe ya uendelezaji wa miji na kuboresha uwajibikaji na utawala bora. Hivyo Mji wa Mbulu ukijumuishwa utanufaika na mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara katika Mji wa Mbulu. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara, Serikali inajenga barabara yenye urefu wa kilomita 0.4 kwa kiwango cha lami nyepesi (double surface dressing) kwa gharama ya shilingi milioni 300 na kazi ya ujenzi inaendelea.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza:-

Hakuna barabara ya kuunganisha Daraja la Nyubati na Kata ya Kisondelea hadi Nzunyuke umbali wa zaidi ya kilomita 30 kufika kijiji cha Nyubati:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya kuunganisha Kijiji cha Nyubati na Kata ya Kisondelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-


Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa wananchi wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilometa 30 kwa kuzunguka kutoka Nyubati hadi Nzunyuke kutokana na kukosekana kwa daraja. Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) umefanya usanifu na tathmini ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo kiasi cha shilingi milioni 847.36 kinahitajika ili kuitengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, TARURA imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nyubati – Lutete yenye urefu wa kilometa 6 inayounganisha Kijiji cha Nyubati na Kata ya Kisondelea.
MHE. KIZA H. MAYEYE (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni cha muda mrefu na pia kimetumika kuandaa viongozi wa nchi yetu na nchi jirani:-

(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi Chuo hicho kuwa Chuo Kikuu?

(b) Je, kwa nini Serikali haipeleki fedha za maendelo katika Chuo hicho kama zilivyopangwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y. WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali Mbunge wa Mchinga, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni Taasisi ya Elimu ya juu iliyoanzishwa na Sheria Na.6 ya mwaka 2005. Chuo kinatekeleza majukumu yake makuu kuendesha mafunzo ya Kitaaluma katika fani ya Sayansi ya Jamii katika ngazi za Cheti, Stashahada, Shahada ya Kwanza na umahiri. Aidha, Chuo kinaendesha mafunzo ya Uongozi, Maadili na Utawala Bora, Mafunzo ya Elimu ya kujiendeleza, kinafanya tafiti na kinatoa ushauri kwa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Serikali kwa sasa si kupandisha hadhi Vyuo vilivyopo, bali ni kuboresha mazingira ya Vyuo Vikuu vilivyopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu, kwa kuwa na vifaa vya kisasa na kuwa na Wahadhiri wengi zaidi wenye Shahada ya Uzamivu. Hatua hizo zitawezesha kuongeza nafasi za Udahili na kuimarisha ubora wa elimu itolewayo. Jitihada zinazofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni pamoja na zifuatazo:-

(i) Kupata wataalam zaidi katika fani zenye uhaba ambapo Chuo kimepeleka wataalam 33 kwenda kusoma Shahada za Uzamivu; na

(ii) kuongeza miundombinu ya Chuo kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa na kumbi za mihadhara ambapo, ujenzi wa ukumbi wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 330 kwa wakati mmoja umekamilika na kuzinduliwa tarehe Mosi Aprili, 2019.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikipeleka fedha za maendeleo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kadri fedha hizo zinavyopatikana, mfano mwaka 2017/2018, Serikali ilitoa fedha zote zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maendeleo kiasi cha shilingi Bilioni 1 nukta 89 ambazo zilitumika kukamilisha ujenzi wa hosteli ya wanafunzi, ahsante.
MHE. SUSAN P. MASSELE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu cha Umma au Vyuo Vikuu vya Umma vyenye hadhi ya juu katika Mkoa wa Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NASERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Peter Massele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu katika kuandaa rasilimali watu itakayochangia katika kufikia azma ya Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa Serikali inatekeleza Mpango wa kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza nafasi za udahili na kuimarisha ubora wa elimu itolewayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa tuna idadi ya Vyuo Vikuu 11, Vyuo Vikuu vishiriki viwili na Taasisi za Elimu ya juu 32 zinazotoa Elimu ya juu nchini. Mkoa wa Mwanza una matawi ya Taasisi ya Elimu ya juu za Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Aidha, Mkoa una Tawi la Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT) mbali na Vyuo Vikuu vya Mtakatifu Augustino na Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Bugando ambavyo vinamilikiwa na taasisi binafsi. Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu ni za Kitaifa ambapo hupokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaboresha mazingira vya Vyuo vilivyopo lakini kama itaona kuna umuhimu wa kuongeza Vyuo vingine itafanya hivyo katika maeneo yatakayoonekana yanafaa. Wito wangu kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine ni kuendelea kutumia Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo katika Mkoa wa Mwanza. Ahsante.
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-

Serikali imekuwa ikiwapandisha madaraja walimu lakini haitoi malipo stahiki kwa madaraja hayo mapya kwa kipindi kirefu tangu walipopandishwa madaraja yao:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao mara wanapopandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilisitisha kupandisha walimu na watumishi wengine madaraja katika mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017 kutokana na uhakiki wa watumishi uliohusisha uhalali wa vyeti, elimu na ngazi za mishahara. Lengo la uhakiki ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Serikali inabaki na watumishi wenye sifa na wanaostahili kulipwa mishahara. Kutokana na sababu hiyo, ni kweli wapo watumishi ambao walipandishwa madaraja ambao hawajalipwa mishahara mipya, wapo waliopata mishahara mipya na baadaye kuondolewa na wapo ambao hawakupandishwa kabisa pamoja na kwamba walikuwa na sifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kurekebisha changamoto hizo, Serikali ilitoa maelekezo kuanzia Novemba, 2017 kwa waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhuisha barua za kupandisha madaraja watumishi hao ili waweze kulipwa stahiki zao. Aidha, kwa wale ambao walikuwa na barua lakini taarifa zao zilikuwa hazijaingizwa kwenye mfumo, waajiri walielekezwa kuhuisha barua zao kuanzia tarehe 1 Aprili, 2018 ili waanze kulipwa stahiki zao. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha watumishi wenye sifa na kupanda madaraja wanalipwa stahiki zao.
MHE. BONNAH M. KALUWA aliuliza:-

Wananchi wa Kata za Kinyerezi, Bonyokwa, Segerea Liwiti, Kipawa, Kimanga, Kisukulu na Tabata wamekuwa wakitumia fedha na muda mwingi kwenda kutafuta bidhaa na huduma katika masoko ya Buguruni na Kariakoo kutokana na kukosa huduma hizo katika maeneo yao:-

(a) Je, kwa nini Serikali isijenge soko kubwa katika eneo mbadala lililo katikati na linaloweza kufikiwa na wananchi hao kwa wakati?

(b) Je, kwa nini Soko la Kinyerezi lililozinduliwa na Mwenge mwaka 2017 lisifunguliwe ili kutoa huduma kwa wananchi wanaozunguka soko hilo na maeneo ya karibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Kamoli, Mbunge wa Segerea, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala iliweka kipaumbele cha kutekeleza mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Soko la Kisutu utakaogharimu takribani shilingi bilioni 12.17. Mpaka sasa mradi huo umepatiwa jumla ya shilingi bilioni 3.92 na ujenzi unaendelea. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga masoko mengine ndani ya Manispaa ya Ilala. Halmashauri inashauriwa kutumia fursa ya miradi ya kimkakati na kuandaa andiko la mradi wa kujenga masoko katika Kata ya Kinyerezi, Bonyokwa, Segerea, Liwiti Kipawa, Kimanga, Kisukulu na Tabata ili kupata fedha za utekelezaji.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Kinyerezi lililozinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 limepangwa kuanza kutumika Mei, 2019 baada ya matengenezo ya choo ambacho kilikuwa hakijakamilika kwa wakati huo.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-

Walimu wa hesabu na sayansi ni changamoto kubwa ndani ya Wilaya ya Buhigwe:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu katika wilaya hiyo na waliopo sasa ni wangapi?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika shule za Buhigwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo.

(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ina jumla ya shule 19 zenye wanafunzi 6,622. Jumla ya Walimu waliopo wa hisabati na sayansi ni 83 sawa na asilimia 54 ya Walimu 155 wanaohitajika. Mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri Walimu wa masomo hayo kwa awamu na kwa sasa kibali cha kuajiri Walimu 4,549 kimekwishatolewa ambapo kati ya hao, 1,374 ni wa Masomo ya Sayansi na Hisabati. Utaratibu wa kuajiri Walimu hao unaendelea na watapangwa kwenye halmashauri zenye upungufu mkubwa ikiwemo Halmashauri ya Buhigwe.

(b) Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/ 2018, Halmashauri ya Buhigwe ilipokea vifaa vya maabara kwa shule mbili za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara. Vilevile katika Mwaka 2018/2019 Serikali inatarajia kununua na kusambaza vifaa vya maabara kwenye shule za sekondari 1,250 zikiwemo shule za sekondari katika Halmashauri ya Buhigwe zilizokamilisha vyumba vya maabara.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Madiwani nchini wanafanya kazi kubwa sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea posho na mishahara au maslahi yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kazi kubwa wanayofanya Waheshimiwa Madiwani katika kusimamia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao. Kwa kuzingatia ukweli huo, Serikali imekuwa ikipandisha posho na maslahi ya Madiwani kwa kadri mapato ya Halmashauri yanavyoongezeka. Kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali ilipandisha posho ya Madiwani kupitia Waraka wa mwaka 2012 kutoka shilingi 120,000/= hadi 250,000/= kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 108.3. Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilipandisha tena posho za Madiwani kupitia Waraka wa mwaka 2014 kutoka 250,000 hadi 350,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inalipa pia posho ya madaraka kwa Wenyeviti wa Kamati kiasi cha shilingi 80,000/= kwa mwezi na posho ya kikao kiasi cha shilingi 40,000/= kwa mujibu wa Waraka wa Mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo kikubwa kinachotumika kupandisha posho za Madiwani ni uwezo wa Halmashauri kukusanya mapato ya ndani ya Halmashauri husika. Serikali itaendelea kuthamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayotekelezwa na Waheshimiwa Madiwani na kuongeza posho hizo kadri makusanyo ya mapato yanavyoongezeka.
MHE. FELSTER A. BURA aliuliza:-

Mkoa wa Dodoma una upungufu wa Walimu 527wa Sayansi:-

Je, ni lini Serikali italeta Walimu wa kutosha wa sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Dodoma una shule 221 za sekondari zikiwa na wanafunzi 72,254. Mahitaji ya Walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati ni Walimu 1,641 na Walimu waliopo ni 916, hivyo pungufu ni Walimu 527 sawa na asilimia 32 ya mahitaji halisi.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri Walimu wa masomo hayo kwa awamu na kwa sasa kibali cha kuajiri Walimu 4,549 kimetolewa ambapo kati ya hao Walimu 1,374 ni wa masomo ya Sayansi na Hisabati. Taratibu za kuajiri Walimu hao zinakamilishwa ili kuwapanga Walimu hao katika Halmashauri zenye upungufu ikiwepo Halmashauri za Mkoa wa Dodoma. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali inatenga na kutumia fedha kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, tuna majibu yake. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba nimjibu Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, madhumuni ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama ilivyotajwa kwenye Katiba, Ibara ya 146(2)(a) mpaka (c) ni kuimarisha demokrasia na kutumia demokrasia katika kuharakisha maendeleo. Katika kutekeleza jukumu hili muhimu, viongozi wanaoongoza vyombo vya Serikali za Mitaa huchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji.

Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa Serikali za Mitaa unahitaji rasilimali fedha ili kuwezesha upatikanaji wa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi ikiwemo vifaa vya uchaguzi yani masanduku, lakiri, fomu na kadhalika. Pamoja na vifaa hivyo, zipo gharama mbalimbali zinazohusiana na uendeshaji wa uchaguzi huo ikiwemo mafuta ya magari, matengenezo ya magari na posho mbalimbali kwa ajili ya watu watakaoshughulikia mchakato mzima wa uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, vilevile zipo taratibu za kisheria ambazo zinapaswa kufuatwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kama vile kutoa matangazo ya Kiserikali yanayohusu uchaguzi, kufanya vikao mbalimbali na wadau wa uchaguzi, kuhakiki maeneo au majimbo ya uchaguzi na kuandaa Daftari la Wapiga Kura, kuratibu shughuli hizo zote zinahitaji rasilimali fedha. Hivyo, kukamilisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni lazima Serikali itenge fedha za kugharamia shughuli hizo, kama ilivyo kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Ahsante.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-

Madeni ya Halmashauri hususan mikopo ya vijana na wanawake ya miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2016 yamekuwa hayalipiki kutokana na Halmashauri nyingi kutokuwa na mapato ya kutosha kuendesha Halmashauri hizo hasa miradi ya maendeleo.

Je, ni kwa nini madeni hayo yasifutwe ili kuondoa hoja za ukaguzi kwenye Halmashauri hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikitoa fedha za mikopo kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali. Katika kipindi chote cha utekelezaji hakukuwa na sheria kwa ajili ya kusimamia utengaji na utoaji fedha hizo na kusababisha kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya fedha ambazo hazikutolewa kwa walengwa katika kipindi husika na kusababisha hoja za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutungwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Fedha hizo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inakusudia kuyafuta malimbikizo hayo kama ilivyoelekezwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kazi ya kuhakiki takwimu, kubaini kiasi ambacho kimelimbikizwa katika Halmashauri zote nchini inaendelea na Mara tu itakapokamilika, taratibu za kufuta malimbikizo hayo zitafanyika. Aidha, kwa sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI inazisimamia kwa karibu Halmashauri ili kuhakikisha zinatoa fedha hizo kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakarabati Shule ya Sekondari ya Mpanda Girls?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya ukarabati wa Shule za Sekondari Kongwe nchini kwa awamu kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha. Katika Awamu ya kwanza, Serikali imekarabati shule za sekondari 53 kwa gharama ya shilingi bilioni 53.6 ikijumuisha ujenzi wa Shule za Sekondari za Nyakato na Ihungo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya pili Serikali imepanga kukarabati shule 17 kongwe za Sekondari nchini ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda. Jumla ya shilingi bilioni 16 zimetengwa kukarabati shule hizo. Miongoni mwa fedha hizo shilingi milioni 986 zimetengwa kwa ajili ya Shule ya Wasichana ya Mpanda. Ahsante.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA aliuliza:-

Kuna uhaba wa watumishi na vitendea kazi katika Idara ya Ardhi na Maliasili – Wilaya ya Muheza kunakosababisha kuazima watumishi na vifaa kutoka Halmashauri nyingine:-

(a) Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi na kununua vitendea kazi katika Idara hiyo?

(b) Je, Serikali iko tayari kuwawekea wananchi Wanasheria ili kusaidia kutatua migogoro ya ardhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yosepher Ferdinand Komba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza inao watumishi 12 kati ya 20 wanaohitajika. Halmashauri imeendelea kuomba vibali kwa ajili ya kuajiri watumishi hao. Hata hivyo,ili kukabiliana na upungufu huo Halmashauri imeajiri watumishi watatu (3) wa Ardhi kwa mkataba ili kutatua changamoto mbalimbali za ardhi. Vile vile katika mwaka wa fedha 2017/2018, kupitia mapato yake ya ndani Halmashauri ilinunua GPS- RTK (Real time Kinematic) kwa ajili ya upimaji ardhi kwa gharama ya shilingi milioni 37. Aidha, Halmashauri imetoa gari Toyota Land Cruiserkwa ajili ya Idara ya Ardhi na Maliasili. Halmashauri itaendelea kununua vitendea kazi kwa awamu kadri ya upatikanaji wa Fedha.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mfumo wa kisheria wa utatuzi wa Migogoro ya Ardhi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao umeainishwa katika Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi, Na. 2 ya mwaka 2002 na Kanuni zake. Migogoro ya ardhi iliyopo Wilayani Muheza imegawanyika kwenye makundi makuu matatu; migogoro ya kiwilaya ambayo inahusisha mipaka ya vijiji vya Wilaya ya Muheza na Tanga Jiji pamoja na Vijiji vya Muheza na Pangani. Migogoro hii inashughlikiwa katika ngazi ya Mkoa na itapatiwa ufumbuzi wakati wowote.

Kundi la pili la migogoro ni migogoro ya mipaka ya vijiji iliyotokana na zoezi la upimaji wa mipaka nchi nzima uliofanyika mwaka 2007. Vikao kwa ajili ya kumaliza migogoro hii vinaendelea na vimefikiwa hatua nzuri. Migogoro mingine ni migogoro ya viwanja ambayo hupokelewa na kutatuliwa kwa utaratibu wa kawaida wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Suluhisho la kudumu kwa aina hii ya migogoro ni kukamilisha mpango wa matumizi bora ya ardhi, kupima viwanja na kurasimisha makazi ambapo mpaka sasa makazi 4,768 yamerasimishwa Wilayani Muheza. Serikali itaendelea kutekeleza Mpango waMatumizi Bora ya Ardhi, kurasimisha makazi, kupima viwanja na mashamba ili kumaliza migogoro ya ardhi.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:-

Kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa Shule za Msingi Wilayani Mwanga:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu 384 wanaohitajika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Jumanne Abdallah Maghembe, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna changamoto ya upungufu wa walimu wa shule za msingi nchini, na Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ina jumla ya shule za msingi 110, za Serikali zenye jumla ya walimu 590, hadi kufikia Novemba, 2018 kulikuwa na upungufu wa walimu 384.

Mheshimiwa Spika, Mwezi Aprili, mwaka 2019, Serikali imeajiri walimu 4,549 wa shule za msingi na sekondari ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Halmashauri ya Mwanga, na kati ya walimu hao 3,089 ni kwa shule za msingi na walimu1,460 ni shule za sekondari. Walimu hawa wameshapangwa katika halmashauri mbalimbali nchini na walipaswa kulipoti kuanzia jana mpaka tarehe 21 na wale ambao hawataripoti, nafasi zao zitapewa watu wengine ambao wana uhitaji kama huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri ya Mwanga imepelekewa walimu 21 wa shule za msingi nawalimu watano wa shule za sekondari. Serikali itaendelea kuajiri walimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Wananchi wa Manyoni Magharibi kwa kushirikiana na Serikali kupitia miradi mbalimbali ikiwemo TASAF wamejenga zahanati katika Vijiji vya Gurungu, Sanjaranda, Kitopeni, Ipande, Doroto, Itagata, Kalangali, Makale, Mwamagembe na Kintanula, lakini mpaka sasa zahanati hizi hazina Waganga:-

Je, ni lini Serikali itazipatia zahanati hizo Waganga, ili wananchi wapate huduma kufuatana na sera yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika kwa Mwaka wa Fedha 2017/ 2018 na 2018/2019 Serikali imeajiri watumishi 8,444 wa afya katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambapo watumishi 46 walipangwa kwenye vituo vya afya na zahanati katika Jimbo la Manyoni Magharibi. Zahanati za Gurungu, Sanjaranda, Kitopeni, Ipanda, Doroto, Itagata, Kalangali, Makale, Mwamagembe na Kitanula zimepatiwa Waganga na wataalam mbalimbali wa afya ambao wanatoa huduma hadi hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya afya vya kutolea huduma za afya sambamba na kuajiri wataalam wa afya kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Chilonwa iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ambayo kwa sasa imefikia kwenye linta?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Chilonwa ni miongoni mwa Kata 36 za Wilaya ya Chamwino, ina vijiji viwili vya Nzali na Mahama, Kata ina huduma za Zahanati moja iliyopo katika Kijiji cha Nzali. Wananchi wa kijiji cha Mahama walianzisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji ambayo kwa sasa jengo limefikia hatua ya lInta. Katika kuunga mkono juhudi za wananchi, Halmashauri ya Chamwino katika mwaka wa fedha 2019/2020 kupitia mapato yake ya ndani imetenga shilingi milioni 30 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo katika Kijiji cha Mahama. Ahsante.
MHE. HASNA S. MWILIMA aliuliza:-

Jiografia ya Halmashauri ya Uvinza ni mbaya na kusababisha wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Nne kutoka mwambao wa Ziwa Tanganyika kusafiri zaidi ya kilometa 200 kufuata Shule za Kidato cha Tano na Sita zilizopo katika ukanda wa Reli:-

(a) Je, kwa nini Serikali isianzishe Shule za Kidato cha Tano na Sita kwenye Kata nane za Ukanda wa Ziwa Tanganyika ili kuwapunguzia usumbufu wanafunzi hao?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati na kuongeza miundombinu katika Shule za Kidato cha Tano na Sita Rugufu Wasichana na Wavulana ambazo miundombinu yake ni chakavu na haitoshelezi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katumba Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza inaundwa na Tarafa tatu za Nguruka, Ilagala na Buhingu. Shule za Sekondari za Kidato cha I – IV ziko 20 (18 za Serikali na 2 za binafsi) zote zikiwa na jumla ya wanafunzi 11,622. Shule za Kidato cha Tano na Sita zipo tatu ambazo ni Lugufu Wavulana, Lugufu Wasichana, zote za Tarafa ya Nguruka na Kalenge iliyopo Tarafa ya Ilagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uanzishaji wa Shule za Kidato cha Tano na Sita ni la kisera, lakini Serikali inaendelea kuboresha na kupanua miundombinu katika Shule za Sekondari Buhingu katika Tarafa ya Buhingu na Sunuka katika Tarafa ya Ilagala ambazo zinatarajiwa kupandishwa hadhi na kuanza kutoa elimu ya Kidato cha Tano na Sita ifikapo Julai, 2020.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Shule za Sekondari za Lugufu Wavulana na Wasichana ni miongoni mwa Shule za Sekondari zilizoanzishwa kwenye maeneo yaliyokuwa Makambi ya Wakimbizi Mkoani Kigoma. Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri imekuwa ikitumia mapato ya ndani ya Halmashauri na kukamilisha vyumba vitatu vya maabara za Sayansi.

Vile vile Serikali Kuu kupitia progrmu ya EP4R imepeleka fedha za ukarabati wa matundu manane ya vyoo na shilingi milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili mapya kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-

Kwa muda mrefu tumepigania kuboreshwa kwa maslahi ya Madiwani ikiwepo posho za vikao na Serikali imekuwa ikisisitiza kuongeza mapato ili halmashauri ziweze kuwalipa Madiwani vizuri kadri ya uwezo, wito ambao umeitikiwa vizuri, mwezi Februari, 2019 tumepokea barua toka TAMISEMI ikielekeza Madiwani walipwe posho za vikao shilingi 40,000 na si vinginevyo.

Je, kwa nini Serikali isiache halmashauri kulipa posho kadri ya uwezo kama ambavyo msisitizo umekuwa toka awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imetoa ufafanuzi kupitia barua Kumb. Na. CCB. 215/443/01 ya tarehe 02 Januari, 2019 juu ya ulipaji wa posho mbalimbali za Madiwani ikiwemo posho za kuhudhuria vikao. Sheria ya Serikali za Mitaa Sura Namba 288 Kifungu cha 42 na Sura ya 287 Kifungu cha 70, inamtaka Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kupitisha viwango vya posho za Madiwani. Hivyo posho hizo zinapaswa kulipwa kwa kuzingatia miongozo na maelekezo ya Waziri mwenye dhamana wa Serikali za Mitaa. Maelekezo yanayotolewa yanasaidia kuweka usawa wa viwango vya posho za Madiwani katika halmashauri zetu nchini, hivyo kuondoa malalamiko kutoka wa Waheshimiwa Madiwani.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na udhibiti wa mapato na itendelea kuongeza posho na maslahi ya Madiwani kulingana na kuimarika kwa uwezo wa halmashauri kwa kukusanya mapato yake ya ndani.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-

Fedha za kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF), zimekuwa msaada mkubwa katika kusaidia Maendeleo Majimboni.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza viwango vya fedha hizi ili kuleta ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge Konde kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo yaani Constituency Development Catalyst Fund, ulianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 16 ya Mwaka 2009 yaani The Constituency Development Catalyst Fund Act, 2009. Lengo la Mfuko ni kuhakikisha miradi ambayo ni vipaumbele vya wananchi katika Jimbo husika na ambayo haikupata fedha katika bajeti inapata fedha za utekelezaji. Kwa tafsiri ya Sheria iliyoanzisha Mfuko, fedha za Jimbo ni kwa ajili ya Majimbo ya uchaguzi ambayo yameanzishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania. Vigezo vinavyotumika kugawa fedha ni ukubwa wa eneo, idadi ya watu na kiwango cha umasikini katika Jimbo husika.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiongeza fedha hizi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha ambapo mwaka 2018/ 2019, Serikali iliongeza kiasi kinachotolewa kutoka shilingi bilioni 10 zilizokuwa zikitolewa kipindi cha nyuma mpaka shilingi bilioni 12.5 na Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha fedha kinachotolewa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo umeainishwa katika Sheria ya Mfuko Kifungu Na. 10(1) kwamba kutakuwa na Kamati ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo katika kila halmashauri ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Jimbo husika. Miongoni mwa majukumu ya msingi ya Kamati hii ni kuchambua miradi inayowasilishwa kutoka kwenye jamii na kuidhinisha miradi itayotekelezwa na jukumu la Mkurugenzi Mtendaji ni kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Kamati hii. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Moja kati ya vigezo vya “Capital Development Grant Assessment”ni namna Halmashauri inavyoweza kutoa taarifa kwa wananchi juu ya mtiririko wa fedha ambazo Serikali imepeleka katika Halmashauri na miradi iliyokusudiwa kutekelezwa:-

(a) Je, kwa nini mchakato huo ulisitishwa?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kurejesha mchakato huo ambao utakuwa ukiongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa wa viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa Halmashauri ulikuwa ni kigezo cha kuziwezesha Halmashauri kupata ruzuku ya maendeleo isiyo na masharti (Local Government Development Grant) kuanzia mwaka 2005. Miongoni mwa vigezo vilivyozingatiwa ni kuwepo kwa uwazi katika mapokezi na matumizi ya fedha kwenye ngazi ya Vijiji, Kata na Mitaa kwa kuhakikisha mapato na matumizi yanabandikwa kwenye mbao za matangazo. Mradi huo ulitekelezwa kupitia fedha za wafadhili ambapo Serikali pia ilikuwa na mchango katika fedha hizo. Mradi huo ulifikia ukomo mwaka 2013, baada ya wafadhali kujitoa na Serikali kuendelea kutekeleza mradi huo kuanzia mwaka 2014/2015 na 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuziwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo afya na elimu. Wananchi wanachangia nguvu kazi na vifaa mbalimbali kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hiyo. Serikali inakubaliana na wazo la kuzipima Halmashauri katika matumizi ya ruzuku hiyo inayotolewa na Serikali kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo liko kwenye mjadala ndani ya Serikali ili kuona namna bora ya kulitekeleza katika kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwenye Halmashauri hadi ngazi ya vijiji.
MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-

Katika Jimbo la Solwa tayari kuna maboma 158 ikiwemo shule za msingi, sekondari na afya na tayari tumeomba fedha ili kukamilisha maboma hayo:-

Je, ni kiasi gani cha fedha Jimbo hilo limepata ili kukamilisha maboma hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya kukamilisha maboma 2,392 ya shule za sekondari ambazo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 87.5 kwa ajili ya kukamilisha maboma saba ya shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na ukarabati/ujenzi wa vituo vya afya na zahanati 352 kwa gharama ya shilingi bilioni 184.6 ambapo kipaumbele ni ukamilishaji wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi. Ukarabati wa vituo 352 unahusisha ukamilishaji wa maboma 199 ya vituo vya afya na zahanati.

Katika Halmashauri ya Wilaya Shinyanga, Serikali imefanya ukarabati wa Kituo cha Afya Samuye na Tinde kwa gharama ya shilingi milioni 900. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/2020 kupitia mapato yake ya ndani Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imetenga kiasi cha shilingi milioni 140 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Barabara za Mji Mafinga hazipitiki kwa mwaka mzima na kati ya kilomita 407 kwa mujibu wa DROMAS lami ni kilometa 5.58.

Je, Serikali ipo tayari kuongezea fedha TARURA ili ijenge barabara za kupitika kwa mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa DROMAS Mji wa Mafinga una Mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 325.67. Aidha, urefu wa mtandao wa barabara unatarajiwa kuongezeka pindi zoezi la uhakiki wa mtandao wa barabara linaloendelea litakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Mji wa Mafinga ili kuhakikisha zinapitika wakati wote na imeongeza bajeti ya matengenezo ya barabara kwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga kutoka Shilingi milioni 876.81 mwaka kwa fedha 2017/2018 hadi Shilingi bilioni 1.036 mwaka wa fedha 2019/2020. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini yaani (TARURA) unakamilisha zoezi la kuhakiki mtandao wa barabara zake na itaweka vipaumbele vya ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja kwa kuzingatia urefu na umuhimu wa barabara husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kupitia formula ya mgao wa fedha za Mfuko wa Babarara ili kuona namna bora ya kuiwezesha TARURA kwa kuiongezea fedha ili iweze kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika halmashauri mbalimbali nchini, ahsante.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Mvumi Mission itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Barabara wa mwaka wa fedha 2019/2020 imetenga kiasi cha shilingi milioni 375 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mvumi Mission kwa kipande chenye urefu wa kilometa moja kwa kiwango cha lami. Maandalizi ya ujenzi yameshaanza na ujenzi unatarajia kukamika ifikapo mwezi Agosti, 2020.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika Jimbo la Mtera kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:-

Shule ya Msingi Vikindu katika Wilaya ya Mkuranga ina mikondo miwili (A na B) darasa la kwanza hadi la saba na mwaka 2019 darasa la kwanza na la pili yalikuwa na wanafunzi 300 kila darasa.

(a) Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha uwiano wa mwalimu na mwanafunzi wa 1:45 unazingatiwa kwa mujibu wa Sera ya Elimu ya Msingi?

(b) Je, kwa msongamano huo tunaweza kupata wanafunzi walioelimika na kukidhi malengo ya Tanzania ya viwanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo swali lake ambalo lina sehemu (a) na (b):-

(a) Mheshimiwa Spika, ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi katika Halmashauri ya Mkuranga limetokana na juhudi za Serikali za kuhamasisha wananchi kuandikisha wanafunzi shuleni kupitia mpango wa elimu msingi bila malipo. Ili kukabiliana na msongamano wa wanafunzi katika Shule za Msingi Vikindu, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kujenga Kituo Shikizi cha Juhudi, Kitwangi, Mitawa na Muungano. Kituo Shikizi cha Muungano kilichopo katika Kijiji cha Vikindu kinatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2020 na kitakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 300. Mkakati mwingine ni wanafunzi kusoma kwa kupokezana yaani double section ambapo kuna madarasa ya asubuhi na ya mchana.

(b) Mheshimiwa Spika, kama ilivyoelezwa kwenye sehemu (a) hatua mbalimbali zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuhakikisha msongamano wa wanafunzi madarasani unapungua na kuwezesha kupata elimu bora. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Ipo ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kilometa nane oinayopita katikati ya Mji wa Itigi.

Je, ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mhehsimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kukamilisha usanifu wa barabara inayopita katikati ya Mji wa Itigi yenye urefu wa takribani kilometa nane. Usanifu huo umefanywa kama sehemu ya usanifu wa barabara ya Mkiwa - Itigi - Rungwa - Makongolosi yenye urefu wa kilometa 413 uliosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania yaani TANROADS. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara inayopita katikati ya Mji wa Itigi kwa kiwango cha lami itakayojengwa chini ya mradi wa ujenzi Mkiwa -Itigi - Rungwa - Makongolosi ili kufungua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Barabara ya Meimosi Nanenane katika Manispaa ya Morogoro imegharimu fedha nyingi sana za Serikali lakini barabara hiyo haikujengwa katika viwango vinavyofaa.

Je, kwa nini Wakandarasi waliohusika na ujenzi wa barabara hiyo wasichukuliwe hatua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Raisi TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maluum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Meimosi-Nanenane yenye urefu wa kilometa 5.1 (Meimosi (2.6 km), Meimosi 2 (1km) na Meimosi 3 (1.5 km) ilijengwa kwa kiwango cha lami nzito (asphalt concrete) kwa gharama ya Shilingi bilioni 11.81. Ujenzi ulianza Julai, 2015 na kukamilika mwaka 2017 chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri Ms DOCH Ltd ambaye alikabidhi mradi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro mnamo tarehe 30 Aprili, 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zote zilizoainishwa kwenye mradi huu zilifanyika kwa viwango vya ubora vilivyoelekezwa na upimaji wa ubora kwa kila hatua ulifanyika. Tangu barabara hii ilipokabidhiwa, haijaonesha udhaifu wowote na inatumika kama ilivyokusudiwa hivyo, Serikali haina sababu yoyote ya kuchukua hatua kwa Mkandarasi aliyejenga barabara hiyo, ahsante.
MHE. ANDREW J. CHENGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi yake ya kujenga barabara za Mji wa Bariadi kwa Kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa barabara katika Mji wa Bariadi kwa kiwango cha lami kwa kujenga barabara zenye urefuwa kilometa 7.76 kwa kiwango cha lami, njia za waenda kwa miguu kilometa 9.4, mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 10.11 na uwekaji wa taa 302 chini ya mradi wa uendelezaji miundombinu katika miji (Urban Local Governments Strengthening Project-ULGSP).

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja katika Mji wa Bariadi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI (K.n.y. MHE. SIXTUS R. MAPUNDA) aliuliza:-

Tangu mwaka 2016, Serikali iliahidi kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga ikiwa ni pamoja na kujenga wodi ya watoto, chumba cha upasuaji na gari la wagonjwa:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sixtus Raphael Mapunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mbinga ambapo kupitia mapato yake ya ndani Halmashauri ya Mji Mbinga imefanya ukarabati wa jengo la „Grade A‟ kwa gharama ya Shilingi milioni 45 na kununua jokofu la kuhifadhia maiti lenye thamani ya Shilingi milioni 29.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetoa kiasi cha Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kalembo ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mbinga, ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL (K.n.y. MHE. GODFREY W. MGIMWA) aliuliza:-

Tatizo la ukosefu wa nyumba za Walimu kwenye maeneo mengi ya Jimbo la Kalenga kumesababisha Walimu kuhama na hivyo kudhoofisha ukuaji wa elimu kwa ujumla: -

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuisaidia Halmashauri ya Iringa Vijijini ili kuhakikisha inajenga nyumba za kutosha kwa Walimu?

(b) Mapato ya ndani ya Halmashauri hii hayatoshi kujenga nyumba za Walimu. Je, nini mkakati wa Serikali juu ya tatizo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali tayari imetoa Shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba 2 za walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Serikali inaendelea kutafuta fedha kupitia vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule zikiwemo nyumba za walimu.

(b) Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Serikali ni kuziwezesha halmashauri kuandaa maandiko ya miradi ya Kimkakati itakayoongeza mapato ya halmashauri ili kukidhi mahitaji yaliyopo ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu. Aidha, Halmashauri zimeelekezwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani na usimamizi wa vyanzo vilivyopo ahsante.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Wananchi wa Wilaya ya Lushoto wamejitahidi kujenga maboma mengi ya maabara lakini mpaka sasa Serikali haijawaunga mkono:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kumalizia maboma haya?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi imekamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara 13 katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kati ya maabara 159 zinazohitajika.

Aidha, maabara 138 zinaendelea kujengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri na nguvu za wananchi. Katika mwaka wa fedha 2019/20, Halmashauri inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji wa maabara katika Shule za sekondari za Mlongwema, Kwemalamba, Lukozi, Ngwelo na Shume zilizopatiwa shilingi milioni 5 kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-

Maboma mengi ya maabara kwenye Shule za Sekondari za Kata nchini hayajakamilika na hata pale yanapokamilika hakuna vifaa vya maabara na tunahitaji sana wanasayansi kuelekea uchumi wa viwanda:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha maabara hizo na lini zitakamilika?

(b) Je, ni lini vifaa vitapelekwa katika maabara zilizokamilika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na Washirika wa Maendeleo imekamilisha ujenzi wa maabara 5,801 kati ya maabara 11,369 zinazohitajika. Hivyo, upungufu uliopo ni maabara 5,568. Serikali inaendelea na ukamilishaji wa vyumba vya maabara kupitia ruzuku ya Serikali Kuu na mapato ya ndani kwa kushirikisha nguvu za wananchi. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya Kondoa Mji, imeidhinishiwa jumla ya Sh. 8,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara katika Shule ya Sekondari Bicha.

(b) Mheshimwa Spika, Serikali imenunua na kusambaza vifaa vya maabara vyenye thamani ya shilingi bilioni 19.13 katika shule 2,948 za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara. Serikali kwa kushirikisha wananchi na wadau wa maendeleo itaendelea kuboresha maabara za masomo ya sayansi ili ufundishaji wa masomo hayo ufanyike kwa vitendo na siyo nadharia.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Kufuatia majibu ya Swali langu Na. 17 lililojibiwa tarehe 07/11/2018 kuhusu Bagamoyo kupata hadhi ya Halmashauri ya Mji, Serikali ilielekeza kwamba tusubiri wasilisho la Kamati ya ushauri ya Mkoa wa Pwani (RCC) ili Ofisi ya Rais (TAMISEMI) iweze kulifanyia kazi ombi hilo; na suala hilo limeshajadiliwa na RCC na taarifa kuwasilishwa Ofisi ya Rais (TAMISEMI):-

Je, ni lini sasa Serikali itaipa Bagamoyo hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA C. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo ya kupandisha hadhi Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji yaliwasilishwa kwenye barua yenye kumbu Na. CAB.51/222/01/56 ya terehe 23 Januari, 2019 kutokq kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, maombi hayo yalichambuliwa kulingana na mwongozo wa kuanzisha maeneo ya utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Wilaya ya Bagamoyo ilikosa vigezo viwili muhimu ili kuiwezesha kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji. Vigezo vilivyokosekana ni kukosekana kwa mpango kabambe wa uendeshaji wa Mji (Master Plan) na eneo lake lililopimwa kuwa na chini ya asilimia 75. Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani amejulishwa kwa barua yenye kumbu Na. CCB.132/394/01B/30 ya tarehe 14 Machi, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi na wananchi wa Mkoa wa Pwani wakati wote na jitihada zao ili kukamilisha vigezo ili kuiwezesha Bagamoyo kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-

Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwahi kupewa jukumu la nyongeza la kusimamia kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba kwa Sheria iliyotungwa na Bunge kwa kutumia Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba ya Nchi:-

(a) Je, ni kwa nini Ibara ya 74(6)(e) isitumike ili Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa Mwaka 2019 usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI)?

(b) Je, ni kwa nini Serikali haijatekeleza makubaliano na Vyama ya mwaka 2014 ya kuwezesha Uchaguzi wa Vitongoji na Mitaa kutumia Daftari la Wapiga Kura lililoboreshwa badala ya Orodha ya Wakazi?

(c) Je, ni hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 unakuwa huru na wa haki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika Mbunge wa Kibamba lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaliyoainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Jukumu la kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa Katiba isipokuwa ni jukumu la Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288. Hivyo, masharti ya Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba hutumika tu pale ambapo kuna Sheria iliyotungwa na Bunge inayoipatia Tume ya Taifa ya Uchaguzi majukumu mengine.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kueleza, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina Mamlaka ya kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kutokana na msimamo huo wa Kikatiba uchaguzi wa Serikali za Mitaa hauwezi kutumia daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuwa daftari hilo lipo chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 12 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343. Kwa msingi huo, makubaliano yoyote yaliyowahi kufanyika kuhusu matumizi ya daftari la kudumu la wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa yanapaswa kuzingatia masharti ya Kikatiba na sheria za nchi.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unakuwa huru na haki Serikali imeandaa Kanuni na Miongozo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 ambazo zimezingatia maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu Tanzania pamoja na asasi za kiraia.
MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:-

Katika mitihani ya Taifa ya Vitendo kwa Kidato cha Nne utaratibu mpya ulioanzishwa mwaka 2017 ambao ni bora zaidi ulibadilika na kupelekewa checklist ambayo sasa inahitaji vifaa vingi zaidi na practical nyingi ikilinganishwa na hapo awali ambapo ‘instructions’ ya mwezi mmoja ilitolewa kabla:-

(a) Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha za vifaa vya Maabara kufidia ongezeko la gharama za vifaa hivyo ambavyo vinazidi fedha iliyoingizwa kwa mwaka?

(b) Shule nyingi sasa zimelundika madeni ya Maabara na hushindwa kulipa: Je, Serikali iko tayari kulipa madeni haya yaliyosababishwa na utaratibu huu mpya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Joseph Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ilitekeleza Sera ya Elimu Msngi bila malipo tangu mwaka 2016 ambapo kila mwezi takribani shilingi bilioni 23.8 zimekuwa zikitumwa moja kwa moja shuleni. Kati ya fedha hizi, takribani shilingi bilioni 1.645 zinatolewa kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji wa shule (Capitation Grand). Matumizi ya fedha za ruzuku ya uendeshaji ni pamoja na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ikiwa ni pamoja na vifaa vya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia programu ya EP4R, Serikali imekuwa ikinunua vifaa vya maabara kwa shule mbalimbali za sekondari nchini. Mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya shule 1,800 za sekondari zilizokuwa zimekamilisha ujenzi wa maabara zao, hazikuwa na vifaa, vilipelekewa vifaa hivyo. Aidha, mwaka 2018/2019, jumla ya shule 1,258 zilizokamilisha maabara, zimeainishwa na ununuzi wa vifaa hivyo upo kwenye hatua za mwisho. Pindi taratibu zitakapokamilika, shule hizo zitasambaziwa vifaa hivyo vya maabara, ambapo katika Mkoa wa Singida kuna shule 59 zitakazopatiwa vifaa vya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianza kutekeleza utaratibu wa kupelekea fedha moja kwa moja shuleni mwaka 2016 na hivyo madeni mengi yanayozungumziwa ni ya kabla ya mwaka 2016, ambapo shule zilikuwa zikikusanya ada na kuruhusiwa kutumia kwa ajili ya uendeshaji wa shule ikiwemo ununuzi wa vifaa vya maabara. Hivyo Serikali imeelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kulipa madeni hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, ni lini Halmashauri ya Mji wa Mafinga itaingia katika mpango wa uendelezaji na uboreshaji wa Miji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) iliingia makubaliano ya mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha miji nchini. Programu hii ina maeneo mawili katika uboreshaji; uboreshaji wa miundombinu na kuzijengea uwezo Halmashauri hizi ili ziweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vigezo vilivyokuwa vimewekwa katika programu hii ni kuwa, ili Halmashauri iweze kuingia katika utekelezaji wa programu ni lazima iwe Manispaa au Mji. Hivyo, Mafinga ilikosa sifa za kuwa katika programu hii kwa wakati huo, ambapo ilianza kutekelezwa mwaka 2012, bado Mafianga haikuwa na hadhi ya Mji. Utekelezaji wa programu hii ulipaswa kukamilika Desemba, 2018. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali programu hii imeongezewa muda hadi Juni, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika utekelezaji wa programu hii, Serikali imeanza mazangumzo na Benki ya Dunia ili kuwa na programu nyingine ya uboreshaji na uendeshaji wa miji nchini itakayoanza baada ya kwisha kwa programu hii ya sasa. Serikali itatoa kipaumbele kwa Miji na Manispaa ambayo haikuwepo kwenye programu awamu ya kwanza ikiwemo Mafinga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI (K.n.y. MHE. ESTHER N. MATIKO) aliuliza:-

Serikali imekuwa ikitoa vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya Tsh. 4,000,000/= kila baada ya miezi mitatu kwenye zahanati za Halmashauri za Mji wa Tarime kupitia Wakala wa dawa (MSD); kwa miaka miwili iliyopita Serikali imepunguza ugawaji wa dawa na vifaa tiba kutoka thamani ya Tsh. 4,000,000/= mpaka Tsh. 166,000/=; mfano zahanati ya Gamasara imepokea dawa na vifaa tiba vyenye thamani hiyo:-

Je, ni kwa nini Serikali iliamua kupunguza mgao wa dawa kutoka Tsh. 4,000,000/= mpaka Tsh. 166,000/= ilhali idadi ya watu inazidi kuongezeka katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na Majimbo ya jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama Ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupungua kwa bajeti ya dawa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kunatokana na tathmini ya uwezo wa kuagiza na kutumia dawa wa vituo vya kutolea dawa katika Mji wa Tarime. Mfano, Zahanati ya Gamasara, ilitengewa na kupatiwa kiasi cha shilingi milioni
17.25 katika mwaka wa fedha 2018/2019 na tarehe 30 Juni, 2019, zahanati hiyo ilikuwa imetumia kiasi cha shilingi milioni
4.25 pekee na hivyo kiasi cha shilingi milioni 13 ilichopewa kutumia katika mwaka husika kubakia Bohari ya Dawa (MSD). Hivyo tunazielekeza Halmashauri zote na vituo vya kutolea huduma za afya, kwamba wawe wanazingatia mipango yao ya bajeti katika manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuweza kuhudumia wananchi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. WILLY Q. QAMBALO aliuliza:-

Mabaraza ya Ardhi ya Kata ni chombo muhimu sana katika kutatua migogoro ya ardhi. Hata hivyo, changamoto kubwa ni uwezeshaji (chakula na nauli) na wajumbe wa mabaraza hayo ili wafanye kazi zao kwa weledi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wajumbe wanawezeshwa ili waweze kutoa haki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha 7 cha Sheria ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata kinazipa Halmashauri wajibu wa kutengeneza utaratibu wa namna ya kuwezesha Mabaraza ya Ardhi na Kata kiutendaji na kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Mikoa na Wilaya imeelekezwa kuzisimamia Halmashauri kuhakikisha Mabaraza hayo yanawezeshwa ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu. Kila Halmashauri inatakiwa kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia Mabaraza ya Ardhi ya Kata. Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji ili kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi, ahsante.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-

Wananchi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori waliopo Namtumbo miaka 14 iliyopita walikubaliana kuacha ardhi yao kwa shughuli za hifadhi na kwamba ardhi hiyo isitumike kwa makazi wala kilimo cha mazao ya kudumu isipokuwa mpunga pekee. Wananchi washiriki kutunza njia za asili za wanyama hususan tembo na walikubaliana kwamba mipaka ya ardhi husika ingepitiwa upya baada ya kupita miaka 10 kuanzia mwaka 1996 walipoingia makubaliano:-

(a) Je, kwa nini Serikali imekiuka makubaliano hayo na kuwakaribisha wafugaji kwenye maeneo ya wananchi yaliyokuwa yakitumika kwa kilimo cha mpunga?

(b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wakulima ambao mashamba yao ya mpunga yameathiriwa na ng’ombe wanaochunga katika mashamba hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo zilizoanzishwa kwa kushirikisha wananchi wenyewe na kutangazwa katika Gazeti la Serikali. Aidha, Serikali haijabadili matumizi ya ardhi hiyo na kuwapatia wafugaji isipokuwa wapo baadhi ya wafugaji waliovamia maeneo hayo bila kufuata taratibu. Serikali inaendelea kuwabaini na kuwaondoa wafugaji ambao wamevamia maeneo yasiyoruhusiwa na kuwapeleka katika maeneo yaliyotengwa rasmi kwa shughuli za ufugaji.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, wapo baadhi ya wakulima waliovamia na kufanya shughuli za kilimo katika eneo la Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori kinyume na sheria. Hivyo, hakuna fidia itakayolipwa na Serikali kwa wakulima waliovamia na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yasiyoruhusiwa. Viongozi wa Mkoa na Wilaya wanaelekezwa kusimamia na kuhakikisha yanatengwa maeneo rasmi kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo kuepuka uvamizi wa hifadhi.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y. MHE. HASSAN S. KAUNJE) aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itawadhamini Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili waweze kupata mikopo kama ilivyo kwa Madiwani na Wabunge?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho/mishahara Wenyeviti wa Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inalipa posho ya Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayorejeshwa na Halmashauri kwenye Vijiji na yanayokusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Madiwani, Wabunge hudhaminiwa kupata mikopo kwenye mabenki na taasisi za kifedha kupitia posho za kila mwezi ambacho ni kipato chenye uhakika kuwezesha kurejesha mikopo hiyo waliyokopa.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuziwezesha Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha makusanyo ya ndani katika vyanzo mbalimbali na kuimarisha uwezo wa Halmashauri kulipa posho hizo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Soko la Mji wa Mpwapwa, ni dogo, limechakaa na halifanani kabisa na hadhi ya Mji wa Mpwapwa ambao idadi ya watu ni zaidi ya laki moja?

Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi wa soko jipya na la kisasa katika mji huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa inafahamu changamoto ya udogo wa soko la Mji Mpwapwa na imekwishaandaa mikakati ya kujenga soko hilo la kisasa linaloendana na hadhi ya idadi ya watu katika eneo hilo. Halmashauri imetenga eneo katika Kiwanja Na. 61 Kitalu B Mazae chenye ukubwa wa mita za mraba 15,000 kilichopo katika Kata ya Mazae.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri inaendelea kuandaa Andiko la Mradi pamoja na kufanya usanifu ili iweze kuwasilisha andiko hilo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na hatimaye Wizara ya Fedha na Mipango kupitia utaratibu wa Miradi Mikakati, vilevile Halmashauri inaendelea na mazungumzo na uongozi wa Mradi wa Local Investmest Climate ili kupata fedha za ujenzi wa soko. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. SALOME W. MAKAMBA) aliuliza:-

Je, kuna sababu gani za kitaalam zinazosababisha Walimu wa Shule za Sekondari kuhamishwa Shule za Msingi wakati ufaulu kwa Shule za Sekondari kwa masomo ya sanaa upo duni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilihamisha baadhi ya walimu waliokuwa wanafundisha shule za sekondari kwenda kufundisha shule za msingi katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo walimu 8,693 walihamishwa. Walimu hao walihamishwa kutokakana na ziada ya Walimu wa masomo ya sanaa waliokuwepo katika shule za sekondari za Serikali nchini ambapo wakati huo shule za msingi za Serikali zilionekana kuwa na upungufu mkubwa wa Walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitaalam Walimu wote wa shule za msingi na sekondari wameandaliwa na wana mfanano katika maeneo ya mbinu za kufundisha, ya kisaikolojia na malezi na makuzi ya watoto wetu. Maeneo hayo ambayo kimsingi ni muhimu kwa kila Mwalimu na hufundishwa katika ngazi zote za vyuo vinavyotoa taaluma ya Ualimu nchini.

Naomba pia nilifahamishe Bunge lako Tukufu kuwa, suala la ufaulu duni husababishwa na sababu mbalimbali zikiwemo za kimazingira, ushiriki wa wazazi na jamii katika mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto. Hivyo, wingi wa Walimu pekee hautoshi kumfanya mwanafunzi afanye vizuri katika mtihani wake. Ahsante.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-

Katika kutekeleza mpango wa kutuma fedha za elimu moja kwa moja mashuleni Serikali hutuma shilingi bilioni 18 kila mwezi kwenye akaunti za shule nchini kwa mujibu wa maelezo ya viongozi kwa umma?

(a) Je, Serikali imeshatuma kiasi gani cha fedha kati ya Januari – Desemba, 2016, 2017 na 2018 kwenda kwenye shule nchini?

(b) Je, Serikali imefanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo na kama zilizotoka Hazina zilifika kwenye shule husika; Je, Serikali ipo tayari kuleta Bungeni Ripoti za Ukaguzi huo?

(c) Kama Serikali haijafanya ukaguzi huo; Je, ipo tayari kuagiza ukaguzi maalum utakaofanywa na CAG na kuweka Taarifa ya Ukaguzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Mpango wa Elimu msingi Bila Malipo kuanzia Januari, 2016 hadi Disemba, 2018 jumla ya Sh.798,170,400,005.04 zimetolewa na Serikali na kutumwa moja kwa moja shuleni. Fedha hizo zimejumuisha chakula kwa wanafunzi, fidia ya ada, uendeshaji wa shule, posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu na Maafisa Elimu wa Kata. Fedha hizi zinajumuisha pia fedha zinazokwenda Baraza la Mitihani kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya Kitaifa kwa ngazi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utaratibu wa kawaida wa ukaguzi wa fedha za Serikali, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali hufanya ukaguzi katika Wizara, Taasisi, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kila mwaka. Kwa kuwa, fedha za Elimu Msingi Bila Malipo ni sehemu ya fedha zinazotumwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwa kuwa fedha hizo hutengwa kwenye bajeti kila mwaka wa fedha, ni dhahiri kuwa fedha hizo hukaguliwa na CAG pale anapofanya ukaguzi kwenye mamlaka husika. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-

Wananchi wa Msalala kwa juhudi zao wamejenga mabweni katika Shule za Sekondari za Bulige, Busangi, Baloha, Mwalimu Nyerere, Lunguya, Ntobo na Isaka.


(a) Je, Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kuyatambua mabweni hayo na kuzipatia shule hizo ruzuku za uendeshaji wa mabweni kwa ajili ya umeme, maji, chakula na ulinzi?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuongeza miundombinu kama mabwalo ya chakula na nyumba za matron katika Shule hizo?

(c) Je, ni lini Serikali itasaidia wasichana wa Msalala katika Kata nyingine kama Mwanase, Mwalugulu, Jana, Bugerema na Bulyanhulu kwa kuwajengea Mabweni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa Serikali kugharamia shule za bweni na shule za kutwa ni tofauti. Shule zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge ni za kutwa ambazo hupelekewa fedha za fidia ya ada na fedha uendeshaji. Ili shule hizo ziweze kupelekewa fedha kwa ajili ya chakula, ni lazima ziwe zimesajiliwa kama shule za bweni za Kitaifa. Shule za Kitaifa zina sifa ya kuchukua wanafunzi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na hushindanishwa kutokana na ufaulu wao.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza miundombinu ya mabweni na mabwalo ya chakula kwenye shule hizo, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuongeza mabweni na mabwalo kwenye shule za bweni na kuongeza madarasa, maabara na matundu ya vyoo kwenye shule za kutwa. Katika mwaka fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa nane katika shule nne za sekondari. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 kupitia program ya EP4R, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 58.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za sekondari nchini.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Serikali ni kuboresha miundombinu katika shule zote za Serikali. Nazielekeza Halmashauri ziendelee kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kujenga hosteli kwenye shule zilizoko katika maeneo yao ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujifunzia kwa watoto wa kike nchini. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2019:-

Je, Serikali inasema nini juu ya ushirikishwaji wa Vyama vya Siasa katika mkakati wa kutoa elimu ili kufikia lengo la uchaguzi huru na haki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa za mwaka 2019, chini ya Matangazo ya Serikali ya Na. 371, 372, 373 na 374 ya mwaka 2019, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeandaa Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019. Mwongozo huo umevitambua Vyama vya Siasa kama mdau muhimu katika suala la utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura.

Aidha, katika hatua za maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, wadau wote muhimu vikiwemo Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu vilishirikishwa katika hatua zote na kutoa maoni yao ili kuwezesha kuwa na Uchaguzi Huru na Haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yetu kuwa Vyama vyote vya Siasa vitashiriki katika kutoa elimu ya mpiga kura kwa wanachama wao kwa kuzingatia miongozo na Kanuni zilizotolewa.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA (K.n.y. MHE. ROSE K. SUKUM) aliuliza:-

Mpango wa Serikali kupeleka fedha za afya moja kwa moja kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya umesaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na stahiki za watumishi, lakini Waganga Wafawidhi hufanya kazi za Wahasibu na Maafisa Manunuzi na hivyo kusababisha kutotoa huduma kwa wagonjwa kwa wakati:-

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuajiri Wahasibu na Maafisa Manunuzi kwa kila Zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SRIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Rose Kamil Sukum, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Mpango wa Serikali wa kupeleka fedha za afya moja kwa moja kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya umesaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na stahiki za watumishi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali iliajiri kwa mkataba Wahasibu Wasaidizi 535 na kuwapanga katika Vituo vya Afya vya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mkataba wa kwanza kumalizika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI iliwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuwaombea kibali cha ajira ambapo yalitolewa maelekezo kuwa Wahasibu Wasaidizi hawa waajiriwe na Halmashauri kwa mikataba na walipwe kwa kutumia mapato ya ndani hadi hapo Serikali itakapokuwa imewaajiri. Aidha, wahasibu hawa wana jukumu la kuhudumia Kituo husika na Zahanati zake zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijaajiri wataalam wa manunuzi kwa kuwa manunuzi mengi katika Vituo vya Afya yanafanywa na Pharmacists ambao wapo katika Vituo vyote vya kutolea huduma ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya fedha kwa Vituo hivyo ni kwa ajili ya manunuzi ya dawa, vifaa vya tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa ya Serikali (MSD).

Serikali itaendelea kuajiri Wahasibu Wasaidizi kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:-

Inapotokea Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa/Kijiji amefariki au kupoteza sifa ya kuwa Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji husika huongozwa na Kaimu Mwenyekiti:-

Je, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuwepo uchaguzi mdogo kama ilivyo kwa Madiwani na Wabunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Joseph Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 yaani Kanuni ya 43(1) – (4) na Kanuni ya 45 zinatoa fursa ya kufanya Uchaguzi Mdogo kujaza nafasi iliyoachwa wazi endapo Mwenyekiti wa Kitongoji, Kijiji, Mtaa atafariki au kupoteza sifa za kuendelea kuwa katika nafasi hiyo kutokana na sababu zilizoainishwa kwenye Kanuni ya 44(1) na (2). Uchaguzi Mdogo hautafanyika endapo muda uliosalia kabla ya muda wa Mwenyekiti kuwa kwenye madaraka kukoma ili kupisha uchaguzi ni miezi sita au pungufu yake. Ahsante.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-

Ikiwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inawahudumia na kutatua kero za wananchi, kero hizo zisipotatuliwa katika ngazi za Mitaa, Kata, Wilaya na Mkoa wananchi hao hulazimika kuandika na kushika mabango kila Mheshimiwa Rais anapofika majimboni ili kupaza sauti zao:-

(a) Je, ni kwa nini Viongozi wa Wilaya na Mkoa huzuia mabango hayo yasionekane na kusomwa na Mheshimiwa Rais?

(b) Je, wananchi watumie njia gani kufikisha ujumbe wao kwa Mheshimiwa Rais pale matatizo yanaposhindwa kutatuliwa katika ngazi ya chini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Serikali kwa ujumla inaamini katika uwazi na uwajibikaji na kwamba, ni haki ya msingi ya wananchi kueleza matatizo yao kwa sauti au kwa maandishi pindi wanapotembelewa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Rais. Kama kuna Viongozi wa Mikoa au Wilaya wanawazuia wananchi, hayo sio maelekezo ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI wala Serikali na wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa, wananchi wana haki ya kueleza changamoto zao kwa Viongozi wa Kitaifa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao utaratibu na mfumo wa kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa na viongozi. Mfumo huo unaanzia ngazi ya Kitongoji hadi Taifa, utaratibu ambao unawawezesha wananchi kufikisha kero zao kwenye ngazi mbalimbali kwa ajili ya kuzitafutia utatuzi. Nazielekeza Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa kuimarisha madawati ya kupokea kero na malalamiko katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kufikisha kero na changamoto zao kwa wakati. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami Barabara ya King’ori kutoka Malula Kibaoni hadi King’ori Madukani, Maruvango, Leguruki, Ngaranyuki hadi Uwiro?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Meru imekamilisha usanifu wa barabara ya Malula-King’ori-Leguki-Ngarenanyuki yenye urefu wa Kilomita 33 ili kuijenga kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.259 ili ipitike majira yote ya mwaka. Serikali inaendelea kutafuta fedha za kukamilisha ujenzi huo. Aidha, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni mpango wa muda mrefu ambao utekelezaji wake utategemea upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya barabara hiyo katika mwaka wa fedha 2017/2018 kiasi cha shilingi milioni 221 kilitumika kufanya matengenezo ya kawaida katika barabara hiyo. Vilevile mwaka wa fedha 2019/2020 kiasi cha Shilingi milioni 35.7 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE (MHE. AMINA S. MOLLEL) aliuliza:-

Shule ya Viziwi Mwanga hutoa Elimu ya Msingi kwa Watoto wasiosikia na wasioongea kwa Mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Arusha; wanapohitimu Elimu ya Msingi, Wanafunzi hao hujiunga na Shule za Sekondari za kawaida ambazo hazina Walimu wenye Taaluma Maalum, vifaa na mazingira rafiki kwa Watoto wenye ulemavu:-

Je, ni lini Serikali itajenga Shule ya Sekondari Maalum kwa Watoto Viziwi (wasiosikia na wasioongea)?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Jumanne Abdallah Maghembe Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu kwa wanafunzi viziwi inatolewa katika Shule maalum 17 za Msingi na vitengo maalum 120. Shule hizi za Msingi zina jumla ya wanafunzi 7,212 na jumla ya walimu 885 wataalam wa kufundisha wanafunzi viziwi. Vilevile, ipo Shule maalum moja ya Sekondari na vitengo maalum 23 vya sekondari. Shule hizi za sekondari zina jumla ya wanafunzi viziwi 1,778 na jumla ya walimu 302 wataalam wa kufundisha wanafunzi viziwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Maalum ya Viziwi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru katika eneo la Tengeru (Patandi), ambayo mwaka 2020 kwa mara ya kwanza itaanza kudahili wanafunzi viziwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kutoa wito kwa wadau wote wa elimu wenye nia ya kujenga Shule za Watoto wenye ulemavu wakiwemo viziwi, wafanye hivyo, Serikali itatoa vibali husika kwa kuzingatia taratibu na sheria husika.
MHE. RICHARD P. MBOGO Aliuliza:-

Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290 yameleta nafuu sana kwa wakulima, lakini wakati huo huo Halmashauri za Wilaya zenye wakulima zenye wakulima wadogo zimeathirika kimapato na kusababisha kushindwa kutatua kero za wananchi kwa wakati:-

(a) Je, Serikali inaweza kuangalia upya suala la utoaji Ruzuku za maendeleo?

(b) Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo imeathirika kiwango kikubwa: Je, Serikali ipo tayari kuipatia ruzuku ili kutoa huduma za Elimu na Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITAIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa ruhusa yako kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mbogo, naomba uniruhusu niwatakie heri vijana wetu, watoto wetu wa Darasa la Saba ambao leo na kesho wanafanya mitihani yao ya kumaliza Darasa la Saba na wanafunzi hao wapo takribani 947,221 wa kawaida na wale wenye mahitaji maalumu.

Nawaomba watu wote ambao wanahusika na zoezi hili la mitihani, wazingatie taratibu na kanuni na miongozo na kamwe wasijihusishe na udanganyifu kwa namna yoyote ile ili matokeo yawe yawe mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI nijibu swali la Mheshimiwa Richard Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290 kwa kuondoa kodi ambazo zilikuwa ni kero hasa kwa wakulima wadogo. Takwimu za jumla zinaonesha makusanyo ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yamekuwa yakiongezeka kila mwaka. Mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 665.4 na zikakusanya shilingi bilioni 544.8; mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri zilipanga kukusanya shilingi milioni 687.3 na zikakusanya kiasi cha shilingi bilioni 553.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani hizi zisomeke bilioni, siyo milioni. Mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 723.7 na zimekusanya shilingi bilioni 661.36. Hivyo, kwa tathmini ya jumla, inaonesha kuwa uamuzi wa kuondoa kodi kero haujaathiri ukusanyaji wa mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya afya katika kipindi cha Mwaka 2017/2018 na 2018/2019, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya Kamoge na Katumba na shilingi milioni 220 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nsimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya elimu, mwaka wa Fedha 2018/2019, Serikali imeipelekea Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa 20 ya shule za sekondari. Vilevile katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 kupitia Programu ya EP4R Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kiasi cha shilingi milioni 205.7 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, ukamilishaji ma maboma ya madarasa saba na ujenzi wa matundu ya vyoo 12 katika shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia EP4R, Serikali imeipatia Halmashauri ya Nsimbo kiasi cha shilingi milioni 100.6 kwa ajili ya ujenzi wa maabara na matundu sita ya vyoo shule za sekondari. Aidha, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020, Serikali imeitengea Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kiasi cha shilingi milioni 421 kwa ajili ya elimu msingi bila malipo.Ahsante.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Jimbo la Masasi lina Shule moja tu ya Sekondari ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita ambayo ni ya Kitaifa ingawa mahitaji ya Wanafunzi wanaofaulu kwenda Kidato cha Tano na Kidato cha Sita yameongezeka sana, Shule pekee ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita iliyopo Masasi ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi:-

(a) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi Shule za Sekondari za Mwenge Mtapika na Anna Abdallah ili ziweze kupokea Wanafunzi wa Kidato cha 5 na 6;

(b) Jimbo la Masasi linahitaji vyumba 27 vya maabara ambapo hadi sasa vyumba Saba tu ndiyo vina vifaa vya maabara katika shule Nne; Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika Shule zote za Sekondari?

(c) Ikama ya Walimu wa Sayansi katika shule za Sekondari Tisa zilizopo Jimbo la Masasi ni Walimu 84 japokuwa waliopo ni 24 tu; Je, Serikali inaweza kulifanya jambo hili kama dharura inayohitaji utatuzi wa haraka kwa kutuletea Walimu 60 wa Sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi Mjini, lenye sehemu (a), (b), na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Masasi Mji inafanya jitihada kuziwezesha shule tatu za Sekondari ambazo ni Sululu, Mtapika na Anna Abdallah ili ziweze kupandishwa hadhi na kuanza kutoa elimu ya Kidato cha Tano na cha Sita. Tayari shule hizo zilishakaguliwa na wadhibiti ubora wa shule na kukutwa na mapungufu kadhaa, hasa ya miundombinu ya maji, umeme na mabweni na hivyo kukosa sifa. Halmashauri kwa kushirikiana na wadau inafanyia kazi mapungufu hayo ili shule hizo ziweze kupandishwa hadhi na kutoa elimu tarajiwa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya shule za sekondari 1,800 zilizokamilisha ujenzi wa maabara zilipelekewa vifaa vya maabara, na kati ya hizo shule sita ni za Halmashauri ya Mji wa Masasi. Vilevile katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, jumla ya shule 1,258 zilizokamilisha ujenzi wa maabara zitapelekewa vifaa vya maabara na taratibu za manunuzi zinaendelea ambapo shule tatu kati ya shule zitakazopatiwa vifaa hivyo zipo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2018/2019, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 7,515 katika shule za sekondari nchini. Kati yaoWalimu ni 7,218 na Fundi Sanifu Maabara ni 297. Kati ya walimu walioajiriwa walimu wenye mahitaji maalum ni 29, walimu wenye elimu maalum ni 50, walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni 7,089 na walimu wa lugha (Literature in English) ni 100. Ambapo walimu 15 wa sayansi walipangwa katika Halmashauri ya Mji wa Masasi. Ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa Sayansi katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi 2018/2019, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 7,515 katika shule za sekondari nchini. Kati yao, Walimu 7,218 na Fundi Sanifu Maabara 297. Kati ya walimu walioajiriwa walimu wenye mahitaji maalum walikuwa 29, walimu wenye elimu maalum ni 50 na walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni 7,089 na walimu wa lugha (Literature in English) walikuwa 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2018/2019 Serikali ilipanga jumla ya Watumishi 121 katika shule za sekondari Mkoani Katavi. Kati yaoWalimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati walikuwa 115 na Fundi Sanifu Maabara walikuwa Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo walimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-

Mwaka 2012 Mahakama ilitoa hukumu kuwa wakulima na wafugaji wote waondoke ndani ya Hifadhi ya Jamii ya Emborley Murtangos iliyoko Wilayani Kiteto lakini baadhi ya wananchi walipinga amri hiyo na kuendelea kufanya shughuli zao na kusababisha mgogoro baina ya wakulima na wafugaji:-

(a) Je, Serikali imeshughulikia kwa kiasi gani mgogoro huo uliodumu kwa miaka 8?

(b) Je, Serikali ilichukua hatua gani kuwadhibiti na kuwaadhibu waliokiuka amri hiyo?

(b) Je, nini kauli ya Serikali juu ya matumizi ya Hifadhi hiyo ili kumaliza mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kibali chako, naomba kabla ya kujibu swali la msingi la Mheshimiwa Mbunge, uniruhusu niwapongeze na kuwashukuru sana Kamati za Mitihani ya Darasa la Saba ngazi ya wilaya na mikoa, walimu wetu, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu Tanzania kwa juzi na jana kumaliza zoezi la mitihani ya darasa la saba. Taarifa njema ni kwamba mitihani hiyo imetoka salama hakuna mtihani uliovuja. Tnawashukuru sana Kamati na hasa Baraza la Mitihani, Wizara ya Elimu na TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014/2015, Serikali iliunda Kikosi Kazi cha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mipango na Fedha (Ofisi ya Taifa ya Takwimu), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kwa lengo la kuhakiki mipaka ya hifadhi, kupima na kuweka alama za mipaka na kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Baada ya kufanyika kwa kazi hiyo, eneo la hifadhi lilibaki na ukubwa wa hekta 75,394.6 kutoka hekta 133,333 za awali na kusajiliwa kwa namba 79667.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuwaondoa wananchi wa makundi ya wakulima na wafugaji wanaondelea kuingia kwenye hifadhi. Kuanzia mwaka 2014-2019, wananchi 49 wamefikishwa mahakamani kwa kukiuka amri ya Mahakama na makubaliano ya matumizi ya ardhi yaliyoidhinishwa.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Hifadhi ya Emborley Murtangos litabaki kuwa eneo la hifadhi ya jamii kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi kama ilivyoidhinishwa na kwa kuzingatia maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa. Aidha, hali ya ulinzi na usalama katika eneo hilo itaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha panakuwepo na amani na utulivu wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazielekeza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya kuchukua hatua stahiki pale inapobainika ukiukwaji wa matumizi ya ardhi kwenye eneo la hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA) aliuliza:-

Shamba la uzalishaji wa Mitamba Kibaha lipo katikati ya Mji wa Kibaha na limezungukwa na makazi ya watu:-

Je, Serikali ina mpango gani juu ya matumizi ya eneo hili kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali uliopo ni kutumia shamba la mitamba lililoko katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa ajili ya uzalishaji wa chanjo za mifugo na kuendelea kuimarisha kituo cha uhalishaji cha kanda ili kuendeleza Sekta ya Mifugo. Tayari Halmashauri imepima eneo la hekta 1,037 ambalo halijavamiwa na kupatiwa hati yenye namba 395140 ya mwaka 2011. Kwa sasa eneo hilo linatumika kwa majaribio na Tanzania Veterinary Laboratory Agency (TVLA) kwa ajili ya kufanya majaribio ya kuzalisha chanjo za magonjwa ya mifugo na kuweka kituo cha kanda cha uhamilishaji na tayari mitambo ya kuzalisha kimiminika cha hewa baridi ya nitrojeni imesimikwa. Ahsante.
MHE. MARY P. CHATANDA (K.n.y. MHE. RASHID A. SHANGAZI) aliuliza:-

Mkoa wa Tanga ndiyo Mkoa wenye halmashauri nyingi zaidi kwa sasa ukiwa na jumla ya halmashauri kumi na moja:-

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuugawa mkoa huo ili kurahisisha shughuli za utawala na maendeleo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa Mkoa wa Tanga ndio mkoa wenye halmashauri nyingi zaidi kwa sasa ukiwa na jumla ya halmashauri 11. Hata hivyo, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuimarisha maeneo ya utawala yaliyopo yaliyoanzishwa katika miaka ya hivi karibuni kwa miundombinu na huduma mbalimbali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kabla ya kuanzisha maeneo mengine mapya. Hivyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati Serikali ikitekeleza azma ya kuimarisha maeneo yake yaliyopo ambayo yana upungufu wa miundombinu na huduma mbalimbali muhimu kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wetu.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuza:-

Je, ni lini Serikali itaifanya Halmashauri ya Itigi kuwa Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Massare Mbunge wa Manyoni Mangharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza wakati majibu swali la Bunge Na. 287 kuhusu pendekezo la kugawa Mkoa wa Tanga, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikalli inatambua umuhimu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala kwa ajili ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha maeneo yalianzisha hivi karibuni yanaboresha na kuendelezwa kwa miundombinu na huduma mbalimbali zikiwemo Ofisi, makazi ya viongozi na watendaji, huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano, barabara na umeme ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia mamlaka hizo.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ufaulu wa wanafunzi katika maomo ya Sayansi na hisabati yanaonekana kushuka kila mwaka, mathalani mwaka 2015 asilimia 85 ya wanafunzi walifeli somo la hisabati matokeo ya kidato cha nne. Aidha, katika masomo mengine ya Kemia, Fizikia na Biolojia ufaulu bado ni duni sana.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuinusuru Halmashauri ya Mji wa Tarime na janga hili la ufulu duni katika masomo ya sayasi?

(b) Je, nini mkakati wa Serikali katika kuiwezesha maabara za shule za sekondari zilizojengwa kwa nguvu kubwa ya wananchi ndani ya Jimbo la Tarime mjini kuweza kupata wataalam na vifaa vya maabara ili kuinuka ufaulu kwenye masomo ya Sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko Mbunge wa Tarime Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifutavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mipango mbalimbali ya uboreshaji wa elimu ya sekondari nchini ili kuinua kiwango cha ufaulu na ubora wa elimu kwa ujumla. Serikali imeipatia Halmashuri ya Mji wa Tarime walimu 59 wa masomo ya sayansi ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2019/20 imepanga kutumia shilingi bilioni 58.2 kupitia EP4R kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu ya sekondari nchini ikiwemo Halmshauri ya mji wa Tarime. Vilevile kupitia mradi mpya wa uboreshaji wa Elimu ya Sekondari nchini, Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 48.9 kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari nchini.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika shule zote tisa za sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime wanafunzi wanafanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa vitendo kwa kutumia maabara zilizopo. Hata hivyo, maabara hizo ni kweli zinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya maabara na huduma nyingine kama maji na gesi. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia mpango wa EP4R imepanga kutumia bilioni 58.2 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari ambapo jumla ya shule 70 zitapatiwa vifaa vya maabara zikiwemo shule za Halmashauri ya Mji wa Tarime.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:-

Serikali inafanya juhudi katika kuendeleza elimu hapa nchini kwa kutoa elimu bure na hata kujenga Shule nyingi zikiwemo za kata.

Je, lini sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha Maabara za Sayansi katika Shule zote za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMIESEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Jumanne Abdallah Maghembe, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi katika shule za sekondari kwa kushirikisha wananchi na wadau wa maendeleo wa ndani na nje. Katika mwaka wa fedha 2019/ 2020, Serikali imetenga kiasi cha jumla shilingi bilioni 107.1 zikiwemo shilingi bilioni 58.2 kupitia mpango wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) na shilingi bilioni 48.9 kupitia mgango wa kuboresha shule za sekondari (SEQUIP) ambapo sehemu ya fedha hizo zitatumika kukamilisha ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kwa shule za sekondari za kata nchini. Ahsante.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-

Serikali imeziagiza halmashauri zote nchini kutenga asilimia tano ya vijana na asilimia tano ya wanawake kutoka mapato ya ndani ili kuchangia mfuko wa maendeleo wa wanawake na vijana:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa halmashauri ambazo hazizingatii takwa hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMIESEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hapo awali utekelezaji na usimamizi wa mfuko wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ulikuwa na changamoto kutokana na kutokuwepo kwa sheria na kanuni. Baadhi ya Halmashauri zimekuwa zikitenga asilimia 10 kutoka katika mapato yake ya ndani bila kujali vyanzo lindwa na fedha zenye maelekezo maalumu kama vile CHF na fedha zenye maelekezo maalumu.

Mheshimiwa Spika, mwezi Juni, 2018, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa sura Na. 290 kwa kuongeza kifungu cha 37(a) ambacho kimeelekeza namna bora ya kusimamia fedha hizo. Kufuatia marekebisho ya sheria hiyo, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) imeandaa kanuni ambazo zimefafanua namna bora ya kutenga fedha hizo, kutoa mikopo na kusimamia utekelezaji wake. Kwa mujibu wa kanuni hizo, asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu itatengwa baada ya kutoa vyanzolindwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais (TAMISEMI) itaendelea kuzismamia halmashauri kuhakikisha zinatekeleza sheria hii na kanuni zake za mfuko wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa kwa halmashauri zitakazoshindwa kutekeleza sheria hiyo na kanuni zake. Ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-

Majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Ulanga ni machache, madogo na machakavu hasa yale ya kulaza wagonjwa:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo na ujenzi wa majengo mapya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuikarabati na kuipanua Hospitali ya Wilaya ya Ulanga ambapo mwezi Mei, 2019, Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 400 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ulanga. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri imetenga shilingi milioni 60 kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kukarabati Hospitali ya Wilaya hiyo. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA (k.n.y. MHE. MASHIMBA M. NDAKI) aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa kila shule ya msingi au ya sekondari kunakuwa na walimu wa kike kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa kike hasa katika masuala yanayohusiana na hedhi salama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inao utaratibu kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa katika kila shule ya msingi na sekondari wanateuliwa walimu wa kike wa kuwasaidia wanafunzi wa kike hususan katika masuala yanayohusiana na ushauri nasaha na unasihi likiwemo suala hilo. Lengo la kuwa na walimu hawa shuleni ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kike wanapatiwa elimu ya afya na usafi itakayowawezesha kutambua mabadiliko yanayotokana na kupevuka kwa miili yao na kuelimishwa njia bora na salama za kujistiri pale wanapopatwa na hali hiyo. Aidha, wanafunzi hawa wanahitaji mlezi wa kike wa kuweza kuwasaidia wanapokuwa na changamoto mbalimbali kuhusiana na masuala ya kike.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (Education Performance for Results - EP4R) imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kusawazisha ikama ya walimu wakiwemo walimo wa kike katika Halmashauri ili kukabiliana na tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Shule za watoto wenye mahitaji maalum hupokea wanafunzi wenye matatizo mbalimbali kama vile ulemavu wa viungo, viziwi, uoni hafifu na wenye ualbino; baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatekeleza wototo wao wakishawapeleka kwenye shule hizo:-

(a) Je, ni kwa nini Serikali haitoi fedha kwa shule hizo iliziweze kuhimili mahitaji ya watoto hao?

(b) Je, ni kwa nini Serikali inaziachia majukumu Halmashauri kuendesha shule hizo wakati zinapokea wanafunzi kutoka nje ya mkoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wanafunzi wenye mahitaji maalum wana haki sawa ya kupata elimu kama wanafunzi wengine wasio na mahitaji maalum. Kwa kutambua changamoto wanazokutana nazo wanafunzi hawa, Serikali kupitia mpango wake wa elimu bila malipo, imekuwa ikigharimia huduma za chakula kwa wanafunzi wote wenye mahitaji maalum wanaosoma katika shule za bweni na za kutwa. Vilevile Serikali imekuwa ikinunua vifaa na visaidizi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha kisha kuvigawa kwa wanafunzi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019, Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 3.87 kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu shuleni. Changamoto kubwa kwenye utaratibu huu ni upatikanaji wa takwimu sahihi za wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa upatikanaji na utoaji wa takwimu sahihi za wanafunzi wenye mahitaji maalum. Serikali itaendelea kusimamia utoaji bora wa elimu kwa wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum bila kujali mkoa au eneo ambalo anatoka.

Mhehimiwa Spika, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA (K.n.y. MHE. MARTIN A. MSUHA) aliuliza:-

Uhaba wa walimu wa Hisabati na Sayansi umeathiri sana matokeo ya darasa la saba mwaka 2017 Wilayani Mbinga.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka walimu wa masomo hayo Wilayani Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA W. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Alexander Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, zipo sababu mbalimbali zilizopelekea kushuka kwa ufaulu wa wanafuzi wa darasa la saba wa mwaka 2017 Wilaya ya Mbinga ikiwemo. Upungufu wa walimu, ushiriki hafifu wa wazazi husasani kufatilia maendeleo ya watoto wao, utoro na nyingine nyingi. Walimu wa shule za msingi wanaoajiriwa wanaweza kufundisha masomo yote yaani Sanaa na Sayansi pamoja na Hisabati.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Serikali imeajiriwa walimu 14,422 ambapo 10,695 ni walimu wa shule za msingi za 3,727 ni walimu wa shule za sekondari. Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imepatiwa jumla ya walimu 143 kati hayo walimu 112 ni wa shule za msingi na walimu 31 ni wa shule za sekondari. Kati yao 28 ni wa Sayansi na Hisabati, mmoja masomo ya biashara na wawili ni walimu wa fasihi kiingereza (English Literature). Serikali itaendelea kuajiri walimu na kuwapanga kwenye Halmashauri hasa zenye upunugufu wa walimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-

Mkoa wa Dodoma una mahitaji ya walimu 11,676 kwa uwiano wa 1:40 kwa shule za msingi. Kwa sasa walimu waliopo ni 7,382 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 4,410 sawa na asilimia 38.

Je, ni lini Serikali itaajiri mwalimu wa kutosha Mkoani Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA W. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Bura, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiajiri na kuwapanga walimu kwenye Halmashauri kwa awamu. Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Serikali imeajiri walimu 14,422 ambapo 10,695 ni walimu wa shule za msingi na 3,727 ni walimu wa shule za sekondari. Mkoa wa Dodoma umepatiwa walimu 699 wa shule za msingi kati ya walimu 10,695 walioajiriwa wa shule za msingi. Serikali itaendelea kuajiri walimu kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JANETH M. MASABURI Aliuliza:-

Nchi yetu imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwemo bahari, maziwa, mito na mabwawa mengi ya asili pamoja na rasilimali watu kubwa ambao hawana ajira.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha vijana na akina mama kwenye kila Halmashauri nchini kutenga maeneo maalum ya kujenga mabwawa ya kufugia samaki ili makundi hayo yapate kujiajiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya ardhi kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya kufugia samaki, kuendeleza ufugaji wa samaki kwenye vizimba na kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali kwa ajili ya uzalishaji bora na endelevu wa samaki.

Mheshimiwa Spika, jitihada zetu nyingine za Serikali za kuwasaidia wavuvi nchini wakiwemo vijana na akinamama ni kuondoa kodi katika zana za malighafi yaani uvuvi kwa engine za kuvulia, nyavu, kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani yaani VAT kwenye engine za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio ili kupunguza gharama za zana na vyombo vya uvuvi na kutoa ruzuku kwenye zana za uvuvi ambapo mvuvi anatakiwa kuchangia asilimia 60 na Serikali ni asilimia 40.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote nchini zimekuwa zikipewa mafunzo ya uvuvi endelevu kwa wavuvi wakiwemo vijana na akinamama kupitia semina, warsha, vipeperushi, makala, redio na luninga kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wadau mbalimbali. Pia Maafisa Uvuvi katika Halmashauri zote nchini wamepatiwa mwongozo wa ugani katika sekta ya uvuvi kwa lengo la kutoa elimu kwa wavuvi na ukuzaji wa viumbe kwenye maji na kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo jumla ya nakala 1,000 zilisambazwa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kwamba Serikali ni pamoja na Serikali za Mitaa na mtu yeyote anayetekeleza madaraka au mamlaka kwa niaba ya Serikali au Halmashauri.

Je, kwa nini katika kipindi chote cha uwepo wa Katiba hiyo Serikali haijatunga Sera ya Ugatuaji Madaraka ambayo ingewezesha kuweka mfumo wa kisheria unaoelekeza mipaka, majukumu na utaratibu wa utekelezaji wa matakwa hayo ya Kikatiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Jimbo la Mchinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali za Mitaa zipo kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Mwaka 1998 Serikali iliandaa andiko la kisera la maboresho ya Serikali za Mitaa ambalo ndio mwongozo wa utekelezaji wa Sera ya Ugatuzi wa Madaraka nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hata hivyo, kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuandaa Sera ya Taifa ya Ugatuzi wa Madaraka ambayo inatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika katika mwaka wa fedha 2019/2020. Sera hiyo itaweka mfumo wa kisheria unaoelekeza majukumu na mipaka ya wadau mbalimbali kwenye utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika utoaji wa huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-

Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yamekuwa ni chanzo cha migogoro badala ya kutatua migogoro.

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kutoa mafunzo ya muda mfupi ili waweze kumudu majukumu yao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaraza ya Kata ni vyombo vya kisheria vya utatuzi wa migogoro katika ngazi ya chini ya jamii vyenye nguvu ya kisheria katika kutatua migogoro ya wananchi. Mabaraza hayo yaliyoanzishwa mwaka 1985 kwa Sheria ya Mabaraza ya Kata, Sura ya Namba 206 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika utekelezaji wa majukumu yake, baadhi ya Mabaraza yamekuwa na changamoto za kiutendaji zinazotokana na uelewa mdogo wa masuala ya kisheria kwa wajumbe, maadili na kutofahamu mipaka ya majukumu yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilitoa mafunzo kwa Wanasheria wa Halmashauri kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Mabaraza ya Kata. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo ilitoa mafunzo kwa Wakurugenzi na Wanasheria wa Halmashauri. Mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa mafunzo kwa Mabaraza hayo kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Katika kujenga Tanzania ya viwanda, Serikali imekuwa na mikakati ya muda mrefu.

Je, ule mkakati wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI wa kujenga viwanda 100 kwa kila Mkoa ni sehemu ya mkakati na umeainishwa kwenye waraka gani wa Serikali ili kuwapa wananchi rejea ya pamoja ya kitaifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa kujenga viuwanda 100 kila MKoa ni sehemu ya mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa viwanda uliofungamanishwa na maendeleo ya watu. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeandaa mwongozo kubainisha majukumu Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika utekelezaji wa Sera ya viwanda. Lengo la mkakati huo ni kutoa hamasa kwa viongozi na wananchi kushiriki kikamilifu kuwezesha uwepo wa viwanda katika maeneo yao hivyo mkakati huo haupaswi kutenganishwa na mipango mingine ya Serikali inayohamasisha ujenzi wa viwanda nchini. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Mwaka 2019 kutafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa sheria.

Je, Serikali ina mkakati gani unaoendelea katika maandalizi ya mchakato wa uchaguzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 unafanyika kwa ufanisi, Serikali imekamilisha maandalizi ya Kanuni za uchaguzi zitakazotumika kuendesha uchaguzi huo. Kanuni hizo zimetangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 26 Aprili, 2019 kwa kupewa namba kama ifuatavyo:-

(i) Tangazo la Serikali Namba 372 kuhusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika mamlaka za Miji.

(ii) Tangazo Namba 371 linalohusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji.

(iii) Tangazo Namba 373 linalohusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya na

(iv) Tangazo Namba 374 linalohusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Halmashauri za Miji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imehakiki maeneo ya utawala na kufanya mafunzo na mikutano kwa wadau wa uchaguzi huo. Vilevile Serikali inaendelea na maandalizi ya ununuzi wa vifaa vya uchaguzi na imetenga kiasi cha shilingi 82,975,994,000.148 Kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo. Ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-

Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji na Vitongoji wanafanya kazi kubwa na ngumu sana hasa Mtwara Mjini na maeneo mengine ya nchi yetu.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwalipa mishahara kama ilivyo kwa Watendaji wa Vijiji na Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji katika shughuli za maendeleo. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Wajumbe wa Serikali za Vijiji pamoja na Wajumbe wa Mitaa za mwaka 2014 zilizotolewa kupitia Tangazo la Serikali Na. 322 na Na. 323, sifa zinazomwezesha mkazi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti au Mjumbe wa Serikali za Mitaa ni pamoja na kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji siyo watumishi wa umma na hivyo hawaajiriwi na kulipwa mishahara kama ilivyo kwa Watendaji Vijiji na Mitaa. Hata hivyo, kwa kuzingatia kazi kubwa inayotekelezwa na viongozi hawa katika kusimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao, Serikali inawalipa posho kutokana na asilimia 20 ya mapato ya ndani ya Halmashari kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Ulipaji wa posho ya viongozi hao unategemea hali ya makusanyo ya kila Halmashauri. Serikali inatoa wito kwa Halmashauri zote ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kuthamini mchango mkubwa wa viognozi hao na kuwalipa posho kutokana na mapato ya ndani. Ahsante.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Chuo cha FDC kilichoko Shirika la Elimu Kibaha ambacho hakina vifaa vya kujifunzia, karakana zimechoka pamoja na miundombinu mibovu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (Kibaha Folk Development College -KFDC) kilianzishwa mwaka 1964 kikijulikana kama Farmers Training Centre kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya Mradi wa Tanganyika Nordic Project. Baada ya mradi huu kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania mwaka 1970, jina la mradi lilibadilika na kuitwa Shirika la Elimu Kibaha na hivyo chuo kikawa chini ya Shirika hili. Mwaka 1975 wakati huo Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilipoanzishwa nchi nzima, chuo hiki kilianza kuitwa Kibaha FDC chini ya Wizara ya Elimu kikiwa miongoni mwa vyuo 55 nchini. Kwa kipindi kirefu chuo hiki hakijafanyiwa ukarabati mkubwa, hata hivyo, kupitia mapato yake ya ndani chuo kimekuwa kikifanya ukarabati mdogo mdogo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupitia Chuo Kikuu cha Ufundi cha Dar es Salaam (DIT) imekifanyia chuo tathmini na kuandaa mpango mkubwa wa ukarabati. Vilevile chuo kiliandaa andiko la mradi na kuomba fedha kutoka Serikali ya Uholanzi ili kuboresha chuo ambapo vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 70 vilipatikana na kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa vifaa chuoni.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kukarabati chuo hicho utakaotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA (K.n.y. MHE. OMARI A. KIGODA) aliuliza:-

Kuna mgogoro mkubwa wa ardhi unaondelea katika Wilaya ya Handeni ambao kama hatua za haraka hazikuchukuliwa unaweza kusababisha ugomvi mkubwa kati ya wananchi.

Je, nini tamko la Serikali katika kuzuia tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawaagiza viongozi na watendaji wote wa Serikali katika Wilaya ya Handeni kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uendelezaji wa ardhi ili kuzuia migogoro ya ardhi. Aidha, wananchi wanasisitizwa kuzingatia sheria za ardhi na kujiepusha kuvamia maeneo yasiyoruhusiwa ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima. Tathmini inaonesha ipo migogoro inayohusisha mipaka baina ya halmashauri moja na nyingine, migogoro baina ya wamiliki wa ardhi na wananchi na baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya ardhi yasiyoruhusiwa. Viongozi wa Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Handeni wanaelekezwa kutatua migogoro hiyo kwa kushirikisha wananchi na kwa kuzingatia sheria za ardhi. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa viongozi na watendaji watakaobainika kukiuka sheria za ardhi na kusababisha migogoro ya ardhi. Ahsante.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA aliuliza:-

Sekondari ya Lanzoni iliyopo Wilayani Mkinga ilianzishwa mwaka 1995 kwa lengo la kuchukua wanafunzi wa chaguo la pili lakini inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme, maji, usafiri pamoja na makazi ya watumishi:-

Je, Serikali ina Mikakati gani ya kushirikiana na Halmashauri ya Mkinga katika kutatua changamoto hizo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yosepher Ferdinand Komba Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Shule ya Sekondari ya Lanzoni ina changamoto nyingi za kimazingira ikiwemo kutokuwa na umeme wa grid, maji na uhaba wa nyumba za walimu. Pamoja na changamoto hizo, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri kupitia Mpango wa MMES II, ilifanikiwa kujenga nyumba mbili (2) mpya za walimu, vyumba viwili vya madarasa na maabara moja ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga imefanya tathmini ya kupeleka maji katika shule ya Lanzoni kutoka katika Mto Zigi na kubaini kuwa kiasi cha shilingi milioni 7.6 zinahitajika. Halmashauri kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutafuta fedha ili kukamilisha kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Shule ya Sekondari Lanzoni haina umeme wa grid na inatumia umeme wa jua. Hata hivyo tayari imeshaingizwa kwenye Mpango wa REA III hivyo muda wowote itaunganishwa kwenye umeme wa grid Taifa, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OSCAR R. MUKASA) aliuliza:-

Kata ya Biharamulo Mjini imetangazwa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo hivi karibuni; kwa sasa kuna mahitaji makubwa ya upangaji wa ardhi na makazi hasa katika hadhi ya kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo:-

Je, Serikali ipo tayari kuwaunga mkono wananchi wa Biharamulo Mjini wakati huu ambapo wao wenyewe wanaendelea na jitihada za ndani kuhakikisha wanakuwa na upangaji wa makazi unaoendana na hadhi mpya ya Mamlaka ya Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kuwaunga mkono wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo Biharamulo katika upangaji wa makazi ya mji huo. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imekamilisha michoro elfu tisa ya mipango miji yenye jumla ya viwanja 6,356 vyenye ukubwa wa ekari 8,753.7 kati ya viwanja hivyo, viwanja 2,337 vimepimwa na upimaji unaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha. Mpango wa baadaye ni kujenga barabara ya lami yenye urefu wa mita 700 ili kuboresha utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Spika, upangaji na upimaji wa makazi unawawezesha wananchi kupata faida mbalimbali ikiwemo kuongeza thamani ya ardhi, kupunguza migogoro ya ardhi, wananchi kupatiwa hati miliki ambazo zinawawezesha kuzitumia kupata mikopo katika taasisi za fedha na kuwawezesha wananchi kuishi kwenye makazi yaliyopangwa hivyo kurahisisha uwekaji wa huduma kama barabara, umeme na maji. Nazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuhamasisha wananchi na kuwashirikisha katika upangaji, upimaji na urasimishaji wa ardhi na makazi yao.
MHE. ANDREW J. CHENGE (K.n.y. MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE) aliuliza:-

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akikemea sana baadhi ya kodi ambazo zimekuwa ni kero kwa wananchi:-

Je, ni kwa nini baadhi ya Halmashauri zimekuwa zikikaidi agizo hilo la Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kodi kero zilifutwa na Serikali kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 mwaka 2017. Hivyo, Halmashauri yoyote inayoendelea kuwatoza wananchi kodi ambazo zilifutwa na Serikali kwa mujibu wa sheria ni kukiuka maelekezo ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kuziagiza Halmashauri kuacha kutoza kodi ambazo zimefutwa kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Rais, TAMISEMI haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa Halmashauri ambayo itabainika kuwatoza wananchi kodi ambazo zimefutwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, endapo Mheshimiwa Mbunge anazo taarifa za Halmashauri inayotoza kodi zilizofutwa, tunaomba taarifa hizo ili Seriali iweze kuchukua hatua. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Mji wa Kibaha unakua kwa kasi hivyo mahitaji ya Watumishi yameongezeka ikiwemo Watendaji wa Mitaa, Maofisa Mifugo, Walimu pamoja na Watumishi:-

Je, ni lini Serikali itatoa kibali cha ajira na kuajiri Watumishi pungufu ili kuleta ufanisi zaidi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa ikama ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 Halmashauri ya Mji wa Kibaha ilikuwa na uhitaji wa Watumishi 1,854 ambapo waliopo ni 1,713 na upungufu ni watumishi 140 sawa na asilimia 7.7. Hivyo, Halmashauri ya Mji wa Kibaha ni miongoni mwa Halmashauri zenye tatizo dogo la upungufu wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuajiri Watumishi wa Kada mbalimbali na kuwapanga kwenye halmashauri kwa kuzingatia mahitaji ya halmashauri kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JOSESPH M. MKUNDI aliuliza:-

Kituo cha Afya Bwisya kimekarabatiwa na kuongezewa miundombinu muhimu kufikia kiwango cha hospitali:

Je, kwa nini Serikali isipandishe hadhi kituo hicho na kuwa Hospitali ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa visiwa vya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuanzia Julai, 2017 hadi Machi, 2020 Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 800 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya Bwisya na Muriti. Vilevile Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, alielekeza baadhi ya kiasi cha fedha za maafa ya ajali ya Kivuko cha Ukerewe kiasi cha shilingi milioni 860 zitumike kupanua na kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya Bwisya. Hivyo kituo hicho kimejengwa na kukarabatiwa kwa jumla ya shilingi bilioni 1.26.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha taratibu za kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Bwisya kilichopo kwenye Kisiwa cha Ukara ili kiwe na hadhi ya Hospitali ya Halmashauri.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH Aliuliza: -

Je, ni fedha kiasi gani Tanzania imeomba na kupatiwa kutoka katika mfuko wa fedha za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa, ndio mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako tukufu naomba kwa kibali chako niruhusu niseme angalau maneno mawili kabla ya kwenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, la kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na uzima, lakini la pili nashukuru sana Chama Cha Mapinduzi, chama changu kuendelea kunianimi na kunipa dhamana hata kuniruhusu kwenda kugombea kwenye Jimbo la Tarime Vijijini, lakini pia nawashukuru sana wapiga kura wa Tarime Vijijini, Kanda Maalum kule Tarime Mara kwa kunipa ridhaa hii na hatimaye ahadi yangu ambayo nilitoa mbele yako imetimia. Lakini mwisho lakini sio kwa umuhimu namshukuru sana Mheshimiwa Rais kuendelea kuniamini kuniteua kama Naibu Waziri. Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya maelezo hayo mafupi ninaomba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, nijibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeomba na kupokea fedha kiasi cha dola za Marekani 8,488,564 kutoka katika Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi. Fedha kutoka Mfuko huo huombwa kwa kuandaa miradi inayokidhi vigezo vilivyokubalika. Fedha huombwa kupitia taasisi ya utekelezaji ya kitaifa au kimataifa, fedha hizo husajiliwa na Bodi ya Mfuko huo. Kwa Tanzania taasisi ya kitaifa iliyosajiliwa na Mfuko huo ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambao walipata ithibati ya Mfuko huo Oktoba, 2017.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa miradi ifuatayo imeomba na kupata fedha kutoka mfuko huo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa ajili ya utekelezaji hapa nchini.

Mradi wa kwanza ni Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Mkoa wa Dar es Salaam. Gharama za mradi huo ni dola za Marekani 5,008,564. Mradi ulitekelezwa mwaka 2013 hadi 2019 na Fedha zilizotolewa kupitia UNEP. Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa ukuta wa kukinga maji ya bahari Kigamboni na Barabara ya Barrack Obama na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua Ilala na Temeke na kupanda mikoko maeneo ya Mbweni na Kigamboni, Dar es Salaam.

Mradi wa pili ni Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa jamii za pwani ya Zanzibar. Gharama za mradi huo ni dola za Kimarekani 1,000,000. Mradi uliidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha dola za Marekani 30,000 kilitolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi. Fedha zitatolewa kupitia NEMC ambayo iliwasilisha kwa mtekelezaji wa mradi huo ambaye ni Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar. Aidha, andiko la mradi liliidhinishwa na sasa taratibu za kusaini mkataba kati ya NEMC na Mfuko wa Adaption Fund zinaendelea chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mradi wa tatu ni Mradi wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa Jamii za Wakulima na Wafugaji Wilaya ya Kongwa. Gharama za mradi ni dola za Marekani 1,200,000. Mradi umeidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi. Fedha zitatolewa NEMC na kuwasilishwa kwa mtekelezaji ambaye ni NGO ya Foundation for Energy Climate and Environment.

Mradi wa nne ni Mradi wa Kimkakati wa Teknolojia ya Kuvuna Maji Kuimarisha Uwezo wa Jamii za Vijijini katika Maeneo Kame ya Mikoa ya Singida, Tabora na Dodoma. Gharama za mradi ni dola za Marekani 1,280,000. Mradi umeidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi.

Mradi wa mwisho na wa tano ni Mradi wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi wilaya ya Bunda. Gharama za mradi n dola za Marekani 1,400,000. Mradi huu bado haujaidhinishwa na Bodi ya EF, lakini kiasi cha dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi. Naomba kuwasilisha.
MHE. KAVEJURU A. FELIX Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Standard Gauge Railways kutoka Tabora kwenda Kigoma?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Aliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219. Kutokana na gharama kubwa za ujenzi na ili kurahisisha ujenzi, awamu ya kwanza inajengwa katika vipande vitano ambavyo ni Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300), Morogoro – Makutupora (kilometa 422), Makutupora – Tabora (kilometa 368), Tabora – Isaka (kilometa 165) na Isaka – Mwanza (kilometa 341).

Mheshimiwa Spika, ujenzi katika vipande vitatu vya Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300), Morogoro – Makutupora (kilometa 422) na Mwanza – Isaka (kilometa 341) unaendelea na Serikali inakamilisha taratibu za manunuzi ya makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge kwa vipande vya Makutupora – Tabora (kilometa 368) na Tabora – Isaka (kilometa 165).

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa reli ya Tabora – Kigoma (kilometa 411) Serikali imemuajiri Mshauri Elekezi wa Kampuni ya COWI kwa ajili ya kufanya upembuzi na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli hii kwa kiwango cha Standard Gauge. Kazi hii inaendelea na inatarajiwa kukamilika Septemba, 2021.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya kupata mkopo wenye masharti nafuu kwa lengo la kukamilisha ujenzi wa mtandao mzima wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge ikiwemo reli ya Tabora – Kigoma (kilometa 411), Kaliua – Mpanda – Karema (kilometa 316.7).

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa bandari kavu inayojengwa Katosho Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bandari Kavu ya Katosho Kigoma ni kituo kilichosanifiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ajili ya kuhudumia tani laki tano (500,000) kwa mwaka ili kusaidia kampuni za usafirishaji kuhifadhi makasha kwa muda kabla na baada ya kusafirishwa ndani au nje ya nchi kupitia Bandari ya Kigoma.

Mheshimiwa Spika, kwa hivi sasa upitishaji wa shehena katika bandari ya Kigoma umekuwa ukiongezeka kutoka wastani wa tani 180,000 hadi 200,000 kwa mwaka. Hata hivyo, ongezeko hili la upitishaji wa shehena katika bandari hiyo ni chini ya asilimia 50 ya uwezo uliosanifiwa wa kupitisha tani 700,000 kwa mwaka katika bandari hiyo na hivyo kuifanya bandari Kavu ya Katosho Kigoma kutokuwa na matumizi ya kuweza kusaidia bandari ya Kigoma kwa kuwa bado haijaelemewa katika kuhudumia shehena iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, TPA imekwishalipa fidia wananchi wanaopisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho Kigoma yenye ukubwa wa hekta 69 na kazi ya ujenzi wa uzio kwa eneo lote la bandari hiyo imekamilika. Usanifu wa ujenzi wa sakafu ngumu na majengo ya huduma umekamilika na tutaanza kuijenga kwa awamu kuendana na ongezeko la upitishaji wa shehena kuanzia mwaka ujao wa fedha (2022/ 2023). Aidha, uendelezaji wa Bandari Kavu ya Katosho Kigoma upo katika Mpango Kabambe wa TPA kwa mwaka 2009 hadi 2028.
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI Aliuliza:-

(a) Je, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina Taasisi ngapi na zipi zina uwezo wa kujiendesha zenyewe?

(b) Je, ni zipi kati ya Taasisi hizo zinapeleka gawio Serikalini?

(c) Je, gawio ni takwa la kisheria?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Captain Abbas Ali Hassan, Mbunge wa Fuoni lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inasimamia jumla ya Taasisi 25, kati ya hizo, Mamlaka za udhibiti zipo nne, Taasisi za Utendaji zipo 14, Bodi za Usajili wa Kitaalamu zipo tatu, Vyuo vya Mafunzo ya Kisekta viwili, na Mabaraza ya Walaji ni mawili. Aidha, kuna Vyuo vya Mafunzo ya Kisekta vinne vinavyosimamiwa moja kwa moja na taasisi za kiutendaji. Kati ya hizo, jumla ya taasisi saba zinajitegemea. Taasisi hizo ni TASAC, TCAA, LATRA, TPA, SINOTASHIP, KADCO na CRB.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali ni mmiliki katika Taasisi na Mashirika ya Umma kwa kuwa imewekeza kiasi kikubwa cha fedha. Umiliki wa hisa unatofautiana kulingana na kiasi cha mtaji kilichowekezwa. Kuna taasisi zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 na nyingine chini ya hapo.

Mheshimiwa Spika, mchango hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha, Sura Na. 348 ambayo inataka taasisi ambazo shughuli zake zinahusisha kukusanya maduhuli ya Serikali, kutoa asilimia 15 ya makusanyo ghafi kwa mwaka kama mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, Mashirika ambayo hufanya biashara na Serikali ni mwanahisa mwenza, yanapaswa kutoa gawio kwa serikali kama mbia katika biashara hiyo. Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi isipokuwa TAZARA na SINOTASHIP zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Taasisi hizi mbili ndizo zinapaswa kutoa gawio Serikalini na zilizobaki zinatakiwa kutoa mchango kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, kutokana na utendaji usioridhisha, TAZARA imekuwa haitoi gawio la asilimia 50 inayopaswa kutolewa kwa Serikali ya Tanzania. SINOTASHIP ambayo Serikali inamiliki asilimia 50 imekuwa inatoa gawio Serikalini.

Aidha, Taasisi nyingine zilizobaki chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zimekuwa zinatoa michango yao kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Taasisi ambazo zimekuwa zinakusanya maduhuli na kutoa asilimia 15 ya mapato yao ghafi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ni pamoja na LATRA, TASAC, TCAA, TPA, TAA na KADCO. Taasisi zilizobaki hazizalishi mapato na nyingine zimekuwa zinapata ruzuku kutoka Serikalini.

(c) Mheshimiwa Spika, suala la utaratibu wa matumizi na mgawanyo wa gawio na michango ni la kisheria. Suala la gawio limeainishwa kwenye Sheria ya Makampuni Sura Na. 212 ambapo faida inayopatikana baada ya kutoa matumizi yote, Serikali hupata gawio kulingana na kiwango cha hisa kilicho kwenye Kampuni au Taasisi husika. Ahsante.

Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza:-

Je ni lini Serikali itaacha kuwatoza shilingi 600 wakati wa kuingia na kutoka Bandarini wananchi wa Visiwa vya Kasalazi, Yozu, Gembela na Soswa katika Jimbo la Buchosa kwa kisingizio cha uwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kiwango cha tozo ya abiria wanaopita katika bandari ndogo zilizopo katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa bahari na maziwa ni shilingi 600 kama ambavyo imeainishwa katika kitabu cha tozo cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA). Hata hivyo, TPA baada ya kupokea malalamiko ya wadau mbalimbali kuhusu tozo hizo, imeanza kuchukua hatua za kufanya marejeo ya tozo hizo kwa bandari zote ndogo nchini kwa kushirikisha wadau katika maeneo mbalimbali. Vikao vya wadau ikiwemo wananchi katika Visiwa vya Kasalazi, Yozu, Gembela na Soswa vitafanyika kwa lengo la kupokea maoni yao kabla ya kuidhinishwa kwa tozo mpya. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya ujenzi wa barabara ya Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi hadi Nachingwea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini TANROADS ilikamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mtwara -Tandahimba – Newala - Masasi hadi Nachingwea yenye urefu wa kilometa 255 mwaka 2015. Mpango wa Serikali ni kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu kulinganana upatikanaji wa fedha. Hadi sasa Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi huo katika sehemu ya Mtwara hadi Mnivata yenye urefu wa kilomita 50 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 89.591.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na mipango ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu iliyobaki ya Mnivata – Tandahimba – Newala - Masasi hadi Nachingwea kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021 jumla ya Shilingi Bilioni 10 zilitengwa kwa ajili ya malipo ya mkandarasi wa barabara kwa sehemu ya kwanza ya Mtwara - Mnivata na kuanza maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya Mnivata - Tandahimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini imeendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hiyo ili kuhakikisha kuwa inapitika kwa majira yote. Pia napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa, baada ya Mheshimiwa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu wa Tano kuiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kutukopesha fedha za ujenzi wa sehemu hii ya Mnivata – Tandahimba – Newala - Masasi yenye urefu wa kilometa 160, benki hiyo tayari imetembelea barabara hiyo na kuna dalili nzuri benki hiyo kugharamia ujenzi wa sehemu hiyo ya barabara. Ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:-

Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi huchangia Pato la Taifa kutokana na shughuli za utalii.

Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa kuukarabati Uwanja wa Ndege wa Same Mjini ili ndege ndogo na za kati ziweze kutua kuleta watalii wa ndani na nje ya nchi katika Hifadhi ya Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ushauri wa Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kuhusu ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Same, Serikali itaangalia uwezekano wa kukifanyia ukarabati kiwanja hicho kwa kadri ya upatikanaji wa fedha ili kuongeza Pato la Taifa kupitia sekta ya utalii. Ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza:-

Visiwa vilivyopo katika Ziwa Victoria, Wilayani Muleba havina usafiri salama na wa uhakika, na vilevile Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi haina miundombinu stahili.

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka kivuko ili kurahisisha usafiri kati ya Visiwa vilivyopo Ziwa Victoria na Miji ya Mwambao ya Ziwa hilo Wilayani Muleba?

(b) Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu muhimu ikiwemo maghala ya kuhifadhia bidhaa katika Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi ili kuwavutia wafanyabiashara kutumia bandari hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Uchukuzi tayari imepeleka wataalam maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, hususan Wilaya ya Muleba kufanya tathimini ya maeneo yanayofaa kuwekewa huduma ya usafiri wa vivuko. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Ujenzi, imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa maegesho ya Muleba – Ikuza na Ngara – Nyakiziba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kwa kuuona umuhimu wa huduma hiyo kwa wananchi wa maeneo hayo, inaangalia uwezekano wa kuboresha huduma za usafiri zinazotolewa na Kivuko MV Chato II – Hapa Kazi Tu, kwa kuongeza njia (route) ya kutoka Chato hadi kwenye visiwa vinavyoweza kufikiwa na kivuko hicho katika Wilaya ya Muleba.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekamilisha zoezi la utwaaji wa ardhi katika Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi kwa lengo la kujenga miundombinu muhimu ili kuwavutia wafanyabiashara pamoja na kutoa huduma za usafiri wa kuelekea maeneo mengine ya Ziwa Victoria kupitia Bandari hiyo. Hadi sasa kazi ya kuainisha mahitaji ya miundombinu inayofaa kujengwa katika Bandari hiyo imekamilika. Miundombinu husika ni pamoja na ghala la kuhifadhia mizigo, jengo la kupumzikia abiria, kantini na chumba cha walinzi. Utekelezaji wa mradi huu unatarajia kuanza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022. Ahsante.
MHE. SIYLVESTRY F. KOKA aliuza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kumaliza mradi wa ujenzi wa barabara ya Makofia - Mlandizi - Vikumburu kupitia Mbwawa kwa kiwango cha lami ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Siylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Makofia – Mlandizi – Vikumburu yenye urefu wa kilometa 135.97 ni barabara ya mkoa inayounganisha Wilaya ya Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uhakiki wa mali zitakazoathiriwa na mradi kwa sehemu ya Makofia – Mlandizi – Maneromango yenye urefu wa kilometa 100 umekamilika. Kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii zitaanza kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara ya Ujenzi itaendelea kuihudumia barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 1,524.07 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanja cha Ndege cha Mwada Mkoani Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege yaani TAA na kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara wameainisha eneo la Mwada katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege katika mkoa huo. Aidha, Serikali imeendelea na taratibu za kutwaa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja hicho cha ndege. Baada ya hatua hii, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi yaani Sekta ya Ujenzi kupitia TANROADS, itatangaza zabuni ya kumpata Mshauri Mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo hapo juu, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali ina nia thabiti na imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa uwanja huo unajengwa ili kuweza kutoa huduma muhimu katika Mkoa huo wa Manyara na maeneo ya jirani. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Daraja la Mto Bubu ili wananchi wa upande wa pili wa mto waweze kuvuka na kupata huduma mbalimbali za kijamii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Daraja la Mto Bubu lijulikanalo kama Munguri B lipo katika barabara ya Kondoa – Nunguri – Mtiriangwi – Gisambalang – Nangwa yenye jumla ya urefu wa kilomita 81.4. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara kupitia Wilaya za Kondoa na Hanang.

Mheshimiwa Spika, mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2019/2020 zilisababisha Mto Bubu kutanuka na kufanya Daraja la Munguri B kutopitika wakati wa mvua. Kwa kutambua changamoto hii, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imetenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021 kwa ajili ya kufanya usanifu wa Daraja jipya katika Mto Bubu.

Mheshimiwa Spika, taratibu za ununuzi wa kumpata Mhandisi Mshauri zipo katika hatua za mwisho ambapo kazi hiyo inatarajiwa kuanza Juni, 2021. Aidha, katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, daraja hili limetengewa shilingi bilioni sita kwa ajili ya kukamilisha kazi ya usanifu. Baada ya usanifu kukamilika, ujenzi wa daraja hili utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:-

Je ni lini Serikali itajenga barabara inayounganisha Jimbo la Ukonga na Mbagala kwa mkupuo badala ya kujenga kilometa moja kila mwaka ili kuondoa kero ya usafiri kwa wakazi wa Majimbo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti, kuanzia mwaka 2000 Serikali imekuwa ikiijenga barabara hii ya Chanika - Mbande inayounganisha Jimbo la Ukonga na Mbagala kwa kiwango cha lami kwa awamu. Hadi sasa jumla ya kilometa 14.34 kati ya kilometa 19.29 sawa na asilimia 74.5 zimejengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami. Aidha, kilometa 4.95 zilizosalia zitaendelea kujengwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Handeni- Kiberashi-Kiteto – Mrijo – Chemba – Kwa mtoro hadi Singida kwa kiwango cha lami kwa kuwa ipo kwenye Ilani na pia Ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujua Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Handeni – Kiberashi – Kwa mtoro – Singida ni barabara ya mkoa yenye urefu wa kilometa 461. Kati ya urefu huo, kilometa 111 zipo Mkoa wa Manyara, kilometa 171 Mkoa wa Dodoma na kilometa 47.1 Mkoa wa Singida. Barabara hii nikiunganisha muhimu cha Mikoa ya Singida, Manyara, Dodoma na Kanda ya Pwani hasa bandari ya Tanga na Dar es salaam. Kukamilika kwa barabara hii kutapunguza idadi ya magari ya nayopita katika barabara kuu ya kati Central Corridor kuelekea Kanda ya Kati na Kanda ya ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), imekamilisha Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara hii. Kwa sasa Serikali ipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii. Katika Mwaka wa Fedha 2021 jumla ya Shilingi bilioni 6 zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2021/22 barabara hii itazingatiwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Bulamba – Bukonyo hadi Masonga yenye urefu wa kilometa 32.23 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri ya Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bulamba – Bukonyo hadi Masonga yenye urefu wa kilometa 32.23 ni barabara ya mkoa inayounganisha mji wa Nansio na Ziwa Viktoria kupitia vijiji vya Murutunguru - Bukonyo hadi Masonga. Barabara hii inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inaendelea kuiimarisha kwa kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka ili kuhakikisha kuwa inapitika kipindi chote cha mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga jumla ya shilingi milioni 757.94 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii. Kazi za matengenezo hayo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hii kila mwaka ili kuhakikisha kuwa inaendelea kupitika wakati wote kabla ya kuijenga kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka ujao wa fedha wa 2021/2022, barabara hii imeombewa shilingi milioni 219.159 kwa ajili ya matengenezo ya vipindi maalum na shilingi milioni 510 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya Daraja la Nabili lililopo katika barabara hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, mpango wa Serikali wa ujenzi wa uwanja wa ndege eneo la Kisumba, Wilayani Kalambo umefikia hatua gani kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa imejikita katika kukamilisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga kilichopo Mkoani Rukwa ambacho ni miongoni mwa Viwanja vya Ndege vinne (4) vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kupata ufadhili kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB). Aidha, Serikali imekamilisha taratibu za kupata Mkandarasi na kupewa Idhini (No Objection) kutoka EIB, kinachosubiriwa ni kupata fedha baada ya taratibu za kimkataba kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege kwamba, baada ya Serikali kukamilisha Ujenzi wa Viwanja vya Ndege vya mikoa vilivyosalia ikiwemo Sumbawanga, Serikali itaendelea na ujenzi wa viwanja vidogo vya ndege kwa hadhi ya airstrip ikiwa ni pamoja na Kiwanja cha Ndege cha Kalambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashauri wananchi wa Kalambo kutumia Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga mara ujenzi wake utakapokamilika.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-

Je, ni lini Wananchi wa Idofi watalipwa fidia baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Serikali kwa ajili ya kujenga Mradi wa Idofi One Stop Centre?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi ya ujenzi wa vituo vya pamoja vya ukaguzi wa magari ya mizigo (One Stop Inspection Station) katika shoroba mbalimbali za barabara nchini, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi Makambako katika eneo la Idofi.

Lengo la ujenzi wa vituo hivyo ni kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha kwa wasafirishaji wa nchi za SADC na EAC wanaotumia barabara zetu. Vituo hivyo vitakapokamilika vitakuwa na Ofisi ya Polisi, TRA, Afya, Uhamiaji na Vituo vya Mizani katika eneo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kituo cha Makambako hadi kufikia Aprili, 2021 jumla ya shilingi 870,182,049 zimelipwa kwa wananchi 39 kati ya 275 wanaopisha ujenzi wa mradi huo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta jumla ya shilingi 3,758,635,767 ili kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi 236 waliosalia. Ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Kivuko katika Mto Ruvuvu ili kuunganisha Vijiji vya Mayenzi na Kanyinya vilivyopo Wilayani Ngara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuendelea kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji ikiwa ni pamoja na kuunganisha maeneo yenye mahitaji ya vivuko ikiwemo Mayenzi na Kanyinya kila inapopata fedha. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Ujenzi, ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga maegesho ya Mayenzi na Kanyinya, ili iweze kupeleka kivuko ambacho kitaunganisha wananchi wa maeneo hayo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maegesho hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) uko kwenye hatua za ununuzi wa kumpata mkandarasi wa kufanya ujenzi wa maegesho ya kivuko hicho na mkandarasi wa kufanya ukarabati huo chenye uwezo wa kubeba abiria 60 na magari mawili ambacho hapo awali kilikuwa kinafanya kazi eneo la Rusumo
– Nyakiziba, yaani MV Ruvuvu ya zamani, ambacho kwa sasa kimeegeshwa katika Mto Ruvuvu. Baada ya ukarabati huo kukamilika, kitatoa huduma kwenye eneo la kati ya Mayenzi hadi Kanyinya. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mbalizi – Shigamba kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mbalizi – Shigamba yenye urefu wa kilometa 52.2 ni barabara ya mkoa inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Songwe kupitia Wilaya ya Mbeya Vijijini na Wilaya ya Ileje. Barabara hii ni ya changarawe na udongo ambayo hupita sehemu zenye miinuko na miteremko mikali, hivyo kupitika kwa shida wakati wa mvua kutokana na utelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa katika Kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2020, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, alipokuwa akiongea na wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi aliahidi kuijenga Barabara ya Mbalizi – Shigamba kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, utekelezaji wa ahadi za Viongozi, ikiwemo ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Mbalizi – Shigamba hufanyika kwa awamu kulingana na upatikanji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inatafuta fedha ili kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Wakati Serikali inatafuta fedha za kuanza taratibu za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali kwa kiwango cha changarawe ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. IRENE A. NDYAMKAMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakarabati Meli ya Mv. Liemba pamoja na kujenga meli mpya ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, asante. kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Irene Alex Ndyamkama, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli imetenga kiasi cha shilingi bilioni 135 katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya kutekeleza miradi tisa ya ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli katika Ziwa Victoria na Tanganyika. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ukarabati wa meli ya Mv. Liemba ambayo tayari umeshapata mkandarasi na taratibu za kusaini mkataba zinakamilishwa na itasainiwa mwanzoni mwa mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kutekeleza mradi wa ukarabati wa meli ya Mv. Liemba katika Ziwa Tanganyika, Serikali pia imepanga kutekeleza miradi ya ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli mpya ya kubeba shehena ya mizigo katika Ziwa Tanganyika na ukarabati mkubwa wa meli ya kubeba shehena ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika. Mikataba ya miradi hiyo ipo katika hatua za mwisho kusainiwa mapema mwanzoni mwa mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumai yangu kuwa, kukamilika kwa miradi hii kutaondoa adha ya usafiri kwa njia ya maji katika Ziwa Tanganyika na mikoa jirani na Kigoma. Aidha, kutaimarisha na kuifanya nchi yetu kuwa kiungo kikubwa cha soko pana la pamoja linalokisiwa kuwa na idadi ya watu takribani milioni 10 wanaoishi pembezoni mwa ziwa hili katika nchi za Mashariki na Kati ya Afrika ikijumuisha nchi ya Tanzania, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurasimisha Bandari ya Mbweni kuwa Bandari ndogo?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbuge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekamilisha kazi ya kutambua Bandari bubu zote zilizo katika mwambao wa Bahari ya Hindi ikiwemo bandari ndogo ya Mbweni kwa ajili ya kurasimishwa kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kwa kushirikaina na Manispaa ya Kinondoni, zipo katika hatua ya kutambua mipaka ya eneo la bandari hiyo kwa upande wa bahari na nchi kavu ili kuweka miundombinu rafiki kama vile maegesho ya majahazi, barabara, ofisi, choo, maji, umeme na ghala la kuhifadhia mizigo.

Mheshimiwa Spika, tangu mwezi Februari, 2020, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imepeleka wafanyakazi na mashine za POS katika bandari ndogo ya Mbweni ili kusimamia shughuli za kibandari na kukusanya mapato. Katika miezi tisa ya mwaka wa fedha 2020/2021 (Julai 2020 hadi Machi 2021), TPA imeweza kukusanya kiasi cha shilingi milioni 117. Mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka baada ya kuirasimisha bandari hiyo na kuiwekea miundombinu muhimu.

Mheshimiwa Spika, kwa hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi Mshauri ambaye pamoja na mambo mengine, atafanya usanifu katika Bandari za Mbweni na Kunduchi na kushauri aina ya uwekezaji wa miundombinu itakayofaa katika bandari hiyo. Ahsante.
MHE. MARIAM D. MZUZURI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za viongozi waandamizi wa Serikali kama Makatibu Wakuu na Mawaziri katika Mji wa Dodoma kwa ajili ya makazi ya viongozi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Ditopile Mzuzuri, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tangu Serikali kuhamishia shughuli zake makao makuu ya Serikali hapa Jijini Dodoma kumekuwepo na juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa viongozi waandamizi wa Serikali wanapata makazi bora ya kudumu na yenye usalama. Katika kutekeleza hilo, Serikali imeanza mkakati wa kujenga nyumba za viongozi katika jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2020/ 2021 Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi - Sekta ya Ujenzi, imetenga kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 20 za viongozi na shilingi bilioni nne kwa ajili ya ukarabati wa nyumba 40 za viongozi jijini Dodoma. Hivi sasa kwa kutumia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) hatua za ubunifu na usanifu wa nyumba hizo pamoja na makadirio ya gharama za ujenzi zimekamilika. Aidha, ukarabati wa nyumba za viongozi jijini Dodoma unaendelea.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi - Sekta ya Ujenzi, imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba 20 za viongozi jijini Dodoma. Aidha, pamoja na ujenzi wa nyumba hizi, Serikali pia imetenga fedha kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa nyumba nyingine 40 za viongozi zilizopo jijini Dodoma katika maeneo ya Kisasa, Area D na Kilimani. Ahsante.
MHE. REUBEN N. KWAGILWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Handeni, Mziha hadi Turiani, Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Handeni – Mziha – Turiani yenye urefu wa kilometa 109.36, inahudumiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Handeni – Mziha – Turiani umekamilika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kulipa sehemu ya madai ya mkandarasi wa barabara ya Magole – Turiani yenye urefu wa kilometa 45.2 na kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Turiani – Mziha – Handeni yenye urefu wa kilometa 104.0 kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, nini kinazuia kukamilika kwa ujenzi wa Barabara ya Makutano – Sanzate kwa kiwango cha lami ambayo ina miaka tisa sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara kutoka Makutano hadi Sanzate yenye urefu wa kilometa 50, ulianza mwezi Mei, 2013 na ulitarajiwa kukamilika Mei, 2015. Ujenzi wa sehemu hii ya barabara, unatekelezwa na Kampuni ya Mbutu Bridge JV Contractors ambayo ni Muungano wa makampuni ya kizalendo 11 kwa gharama ya shilingi bilioni 46.1. Mbutu Bridge JV Contractors walipata mradi huu kwa njia ya ushindani baada ya kumaliza mradi wa mafunzo kwa Makandarasi Wazalendo wa Ujenzi wa Daraja la Mbutu ambao ulifanyika kwa ufanisi mkubwa. Hivyo, Serikali iliona ni fursa nyingine kwa kampuni ya kizalendo kuongeza uzoefu katika ujenzi wa barabara za lami.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu, kulijitokeza changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa changarawe kwa ajili ya tabaka la barabara (G45), kuongezeka kwa kiasi cha upasuaji miamba na kuongezeka kwa kiasi cha ukataji udongo. Hali hii ilisababisha kubadilishwa kwa usanifu wa barabara na kulazimu Mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji wa mradi hadi Februari, 2021.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mkandarasi hakuweza kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa. Kwa sasa kazi iliyobaki ni asilimia 12 maana yake imefanyika asilimia 88. Kufuatana na mpango mpya wa ujenzi, Mkandarasi amepanga kukamilisha ujenzi ndani ya miezi minne kuanzia sasa. Mkandarasi ameshapeleka katika eneo la kazi vifaa muhimu vya ujenzi ikiwa ni pamoja na malori, kokoto na lami.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itahakikisha mapema iwezekanavyo baada ya kuhakiki madai ya mkandarasi shilingi bilioni 1.7 anazodai ili kumrahisishia kukamilisha kazi hii ndani ya muda nilioutaja. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Singida ili ndege za ATCL zianze kutua na kurahisisha usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanja cha ndege cha Singida ni miongoni mwa viwanja 11 vilivyofanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ufadhili wa fedha kupitia mradi wa Benki ya Dunia. Viwanja hivyo 11 ni kama ifuatavyo; Lake Manyara, Musoma, Songea, Kilwa Masoko, Tanga, Iringa, Lindi, Moshi, Singida, Njombe na Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hatua ya awali ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kukamilika, Serikali imejipanga kuanza hatua ya ujenzi kwa viwanja vyote vya ndege kwa awamu kwa kutumia fedha za ndani kutokana na ukweli kwamba gharama za ujenzi wa viwanja hivyo ni kubwa ukilinganisha na bajeti inayotolewa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia bajeti, Serikali kupitia TANROADS imejipanga kuanza na ujenzi wa viwanja vya Iringa na Songea. Ujenzi wa viwanja vilivyobaki kikiwemo cha Singida utaanza mara Serikali itakapopata fedha. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo ili kuweza kupata fedha za kujenga viwanja hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo hapo juu, namuomba Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu na wananchi wa Singida waendelee kuvuta subira kwani Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina nia ya dhati ya kujenga kiwanja hicho cha Singida. Ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa uwanja mpya wa ndege katika Mji wa Njombe utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): alijibu

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanja cha ndege cha Njombe ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Transport Sector Support Project (TSSP). Viwanja hivyo 11 ni pamoja na Lake Manyara, Musoma, Songea, Kilwa Masoko, Tanga, Iringa, Lindi, Moshi, Singida, Njombe na Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hatua ya awali ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali imejipanga kuanza ujenzi kwa hatua mbalimbali kwa awamu kwa kutumia fedha za ndani, lakini kutokana na ukweli kwamba gharama za ujenzi wa viwanja hivyo ni kubwa ukilinganisha na bajeti inayotolewa kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia bajeti, Serikali kupitia TANROADS imejipanga kuanza na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Iringa na Songea. Ujenzi wa viwanja vilivyobaki kikiwemo cha Njombe utaanza mara Serikali itakapopata fedha. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo ili kuweza kupata fedha za kujenga viwanja hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo hayo hapo juu, namuomba Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika pamoja na wananchi wa Njombe Mjini waendelee kuvuta subira kwani Serikali ina nia ya dhati ya kujenga kiwanja hicho.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Mbagala Kokoto hadi Kongowe wanaopisha ujenzi wa barabara ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara Ujenzi na Uchukuzi ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara kwa lengo la kushughulikia tatizo sugu la msongamano wa magari, hususan katika barabara kuu za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo barabara ya Kilwa kuanzia Mbagala Rangitatu mpaka Kongowe yenye urefu wa kilometa 3.8. Utekelezaji wa mpango huu unahusisha upanuzi wa barabara kutoka njia mbili kuwa njia nne pamoja na ujenzi wa Daraja la Mzinga.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha ujenzi huo unafanyika bila vikwazo, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha hatua za awali za kupitia jedwali la fidia na kuhakiki mali za wananchi wanaostahili kulipwa fidia. Aidha, zoezi hili liliwahusisha pia viongozi wa Serikali za Mitaa husika ili kuhakikisha wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia wanalipwa stahili zao kwa mujibu wa sheria zilizopo. Hivyo wananchi wa Mbagala eneo la Kokoto hadi Kongowe wanaombwa kuwa wavumilivu wakati zoezi la kuhakiki taarifa za fidia linaendelea. Mara uhakiki utakapokamilika wahusika wote watalipwa fidia kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Tarime hadi Serengeti kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Tarime – Mugumu (Serengeti) ina jumla ya urefu wa kilometa 87.14 ambapo sehemu ya barabara hiyo yenye urefu wa kilometa
10.7 tayari imejengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 76.44 zilizobaki zimejengwa kwa kiwango cha changarawe. Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la Mara lililopo katika barabara hii lenye urefu wa meta 94 na barabara za maingiliano za daraja hilo zenye urefu wa kilometa 1.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilometa 25 nje ya kilometa 76.44 zisizokuwa na lami za barabara hiyo imetangazwa tarehe 4 Juni 2021. Taratibu za manunuzi zikikamilika kazi za ujenzi zitaanza mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa sehemu itakayobaki kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyopatikana.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther N. Matiko, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakaetekeleza mradi huu. Aidha, mkataba kati ya Serikali na mkandarasi Beijing Construction Group Co. Ltd umesainiwa Disemba, 2020 na utekelezaji wa mradi huu utakamilika kwa kipindi cha miezi 18, baada ya kuanza hatua za utekelezaji. Hivi sasa Serikali imemaliza awamu ya pili ya malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huu ili kuruhusu mkandarasi kuanza hatua ya utekelezaji wa ujenzi. Hata hivyo, Serikali imeshamkabidhi mkandarasi eneo la mradi.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Esther N. Matiko kwamba, Serikali ina nia ya dhati ya kukarabati na kupanua Kiwanja cha Ndege cha Musoma na utekelezaji wake utakamilika baada ya miezi 18 kama nilivyosema nilivyosema. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Bypass ya Mji wa Maswa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya mchepuo katika mji wa Maswa (Maswa Bypass) yenye urefu wa kilometa 11.3 ulisainiwa tarehe Mosi Juni, 2021 kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Kampuni ya M/S CHICO ya China kwa gharama ya shilingi 13,446,688,420.00 na muda wa ujenzi ni miezi 15 ambapo ujenzi wa barabara hii unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Julai, 2021. Ahsante.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Kyetema – Katoro – Kyaka utaanza na kukamilika kwa kiwango cha lami kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kyaka 2 – Kanazi – Kyetema yenye urefu wa kilometa 60.7 amepatikana na anatarajiwa kusaini mkataba mwishoni mwa mwezi Juni, 2021. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 500 zimetengwa kwa ajili ya kuanza kazi hiyo. Baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamlika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

(a) Je, kwa nini kipande cha reli ya kati kutoka Manyoni hadi Singida hakipo kwenye mpango wa ukarabati?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukarabati kipande hicho cha reli ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na mpango wa ukarabati wa mtandao wa reli iliyopo na kufufua njia za reli zilizofungwa kwa awamu kwa kuanzia na njia kuu (main line). Katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali inazingatia Mpango wa Miaka Mitano wa Taifa ambao unaanzia 2021/ 2022 – 2025/2026. Aidha, Serikali itaendelea na ukarabati wa matawi ya reli ikiwemo kipande cha reli kutoka Manyoni hadi Singida kulingana na mahitaji ya ukuajiwa uchumi na uwezo wa kifedha. Lengo la Serikali ni kuboresha miundombinu ya reli ili kurahisisha huduma za uchukuzi nchini.

Mheshimiwa Spika, sehemu (b); Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo na miundombinu ya reli imara katika kuchochea uchumi wa nchi. Hata hivyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi sehemu (a), Serikali itaendelea kufungua njia zote zilizokuwa zimefungwa ikiwa ni mkakati wake wa kurejesha huduma za usafiri wa reli wenye uhakika nchini na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia TRC imepanga kufanya tathmini kwa ajili ya ufunguaji wa njia zilizokuwa zimefungwa kwa lengo la kujua gharama za ukarabati. Maeneo ya reli yatakayohusika ni pamoja na Kilosa – Kidatu na Manyoni – Singida. Hivyo, naomba Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba Serikali inafanya kazi eneo la reli Manyoni – Singida, ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa kipande cha barabara ya lami kilichoanzia Sanya Juu kuelekea Kamwanga ambayo kwa sasa imeishia Kijiji cha Elerai wakati zimebaki takribani kilometa 44 kuunganisha na kipande kingine cha lami kilichotoka Tarakea na kuishia Kijiji cha Kamwanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushkuru, kwa niaba ya Waziri Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Bomang’ombe – Sanya Juu – Kamwanga yenye urefu wa kilometa 97.2 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami imekamilika. Ujenzi umepangwa kutekelezwa katika awamu tatu. Ujenzi katika awamu ya kwanza (Lot 1) wa sehemu ya Sanya Juu - Elerai kilometa 30.2 umekamilika. Serikali inatafuta fedha za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu ya pili (Lot 2) wa sehemu ya Elerai - Kamwanga kilometa 42 na awamu ya tatu (Lot 3) ya Bomang’ombe – Sanya Juu ambayo ni upanuzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha za ujenzi wa barabara tajwa, barabara hii itaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 728.878 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Nyashimo Wilayani Busega hadi Dutwa Wilayani Bariadi kupitia Shigala, Malili, Ngasamo na Imakanate yenye kilometa 47 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nyashimo –Dutwa ni barabara ya Mkoa yenye ureu wa kilometa 47 inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nyashimo –Dutwa ipo katika mpango mkakati wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mwaka 2021/2022 – 2025/2026 kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Barabara hii inaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali pamoja na ujenzi wa madaraja ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetengewa shilingi milioni 1,102.607 kwa ajili ya matengenezo pamoja na ujenzi wa Daraja la Shigala na la Malili. Ahsante.
MHE. ERIC J. SHIGONGO K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

(a) Je, ni lini Jimbo la Sengerema litapata Kivuko kipya angalau kimoja kati ya vivuko vitano ambavyo Serikali imepanga kujenga katika Ziwa Victoria kwa bajeti ya mwaka 2021-2022?

(b) Je, Serikali inafahamu adha ya usafiri wanayoipata wananchi wa Mji Mdogo wa Buyagu Wilayani Sengerema pamoja na wananchi wa Wilaya za Misungwi na Nyang’hwale kwa kukosa chombo madhubuti cha usafiri wa majini?
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamisi Mwagao, Mbunge wa Sengerema, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imepanga kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini aina na ukubwa wa kivuko kinachohitajika katika eneo hilo. Mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na gharama za kivuko hicho kujulikana, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya katika Jimbo la Sengerema kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea changamoto ya adha ya usafiri iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mbunge. Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2021/2022 itatumia wataalam kufanya upembuzi yakinifu katika eneo la Buyagu Wilaya ya Sengerema na Nyang’wale Wilaya ya Misungwi. Upembuzi yakinifu huo utasaidia kubaini aina na ukubwa wa kivuko kinachofaa ili kiwekwe kwenye mpango wa utekelezaji katika mwaka wa fedha 2022/2023. Ahsante.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi anayetengeneza kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Loliondo hadi Mto wa Mbu ili iweze kukamilika na kurahisisha maisha ya Wakazi wa Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa barabara ya Loliondo – Mto wa Mbu sehemu ya Wasso – Sale yenye kilometa 49 ulianza Oktoba, 2017 ambapo hadi kufikia Julai, 2021 utekelezaji wa kazi ulikuwa umefika asilimia 83. Serikali inaendelea kumlipa Mkandarasi wa mradi huu pamoja na Makandarasi wa miradi mingine ya maendeleo inayoendelea hapa nchini kulingana na hati za madai zinazowasilishwa na kuhakikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Hadi kufikia Juni, 2021, Mkandarasi wa ujenzi wa barabara hii amelipwa jumla ya shilingi bilioni 38.07. Ahsante.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Igowole – Nyigo kilomita 54 ambayo imetajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara ya Mkoa ya Igowole - Kasanga – Nyigo yenye urefu wa kilometa 54.51, inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Igowole – Kasanga – Nyigo yenye urefu wa kilomita 54.51 kwa Wananchi wa Wilaya ya Mafinga. Kwa sasa, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimaye kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii, ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi milioni 66 kimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Ulyankulu – Uyui hadi Tabora Manispaa kwa kiwango cha lami ikizingatiwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya hizo tatu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Ulyankulu – Uyui –Tabora yenye urefu wa kilometa 77 kwa wananchi wa Wilaya za Kaliua, Uyui na Manispaa ya Tabora ambapo kwa sasa inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimae kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika Mwaka wa Fedha 2021/22 kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia tano kimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kugharamia matengenezo ya Reli ya TAZARA ambayo miundombinu yake imechakaa na ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na hata nchi jirani za SADC?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya TAZARA Na. 23 ya mwaka 1975 iliyorekebishwa kwa Sheria ya TAZARA Na. 4 ya mwaka 1995. Reli hiyo inamilikiwa kwa uwiano wa hisa hamsini kwa hamsini baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kugharamia matengenezo ya reli ya TAZARA na ndiyo maana inaendelea na jitihada za kukamilisha marekebisho ya Sheria Na. 4 ya mwaka 1995 ambayo kukamilika kwake kutaondoa changamoto zinazoathiri uwekezaji katika reli hiyo kwani uwekezaji unaofanyika sasa hauongezi thamani ya hisa za nchi inayowekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo, Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa TAZARA inaendelea kutoa huduma wakati jitihada za marekebisho ya sheria zikiendelea. Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Serikali ya Tanzania iliipatia TAZARA jumla ya shilingi bilioni Kumi kwa ajili ya ununuzi wa vipuri vya kutengenezea vichwa saba vya treni na vifaa vya kuongeza uwezo mgodi wa mawe na kiwanda cha kutengenezea mataruma ya zege vilivyopo Kongolo Mkoani Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vipuri na mashine hizo vimeshanunuliwa na matengenezo ya injini yamekamilika mwaka 2020 na hivi sasa zinafanya kazi. Mashine kwa ajili ya Kongolo zinafanya kazi pia. Aidha, Serikali ya Tanzania inaendelea kulipa mishahara ya wafanyakazi wa TAZARA upande wa Tanzania ambapo katika Bajeti ya mwaka 2021//2022 zimetengwa jumla ya shilingi bilioni 14.98.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini ya Serikali kuwa mchakato wa kurekebisha Sheria ya TAZARA utaisha hivi karibuni baada ya Serikali ya Zambia kukamilisha zoezi linaloendelea la uteuzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali na kuwa tayari kwa kikao cha pande zote mbili kwa ngazi ya Makatibu Wakuu na hatimaye Mawaziri ili kuridhia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria tunayoyasubiri. Ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza Viwanja vya Ndege ndani ya Hifadhi ya Serengeti kwa kujenga Uwanja wa Ndege katika Mji wa Mugumu nje kidogo ya Hifadhi pamoja na kukamilisha ujenzi wa barabara ya lami ya Makutano Sanzate Natta na ile ya Tarime Mugumu Natta?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri na Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kujenga Kiwanja cha Ndege cha Serengeti katika eneo la Mugumu, kitakachotoa huduma za usafiri ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Aidha, kiwanja hicho kitakapojengwa na kukamilika kitapunguza matumizi ya viwanja vya ndege ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwani ndege nyingi zitakuwa zikitumia kiwanja kitakachokuwa kimejengwa nje ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Makutano – Sanzate – Natta yenye urefu wa kilometa 90, ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea na umegawanyika katika awamu mbili. Sehemu ya kwanza ni Makutano – Sanzate yenye urefu wa kilometa 50; kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami zinaendelea na hadi Oktoba 2021 ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2022. Aidha, sehemu ya pili ni Sanzate – Natta yenye urefu wa kilometa 40; ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea. Hadi Oktoba, 2021 kazi za ujenzi zilikuwa zimefikia 7% na zinatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Barabara ya Tarime – Mugumu – Natta yenye urefu wa kilometa 122.97 itajengwa kwa awamu. Zabuni kwa ajili ya kupata Mkandarasi wa kujenga sehemu ya Tarime - Nyamwaga yenye urefu wa kilometa 25 zimefunguliwa mwishoni mwa Oktoba, 2021 na uchambuzi unaendelea ili kumpata Mkandarasi wa ujenzi. Serikali itaendelea na ujenzi wa sehemu iliyobaki kadiri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, ni lini tatizo la upungufu wa mabehewa ya abiria na mizigo litatatuliwa katika Kituo cha Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Shirika la Reli Tanzania (TRC) linakabiliwa na uhaba wa mabehewa ya abiria na mizigo. Ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa mabehewa katika kituo cha Mpanda na sehemu zingine, Shirika linaendelea na ukarabati wa mabehewa na tayari limesaini mkataba wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa 37 ya abiria na 600 ya mizigo. Aidha, mwezi Juni, 2021, Shirika limesaini mkataba wa ununuzi wa mabehewa mapya 22 ya abiria utakaotekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 na katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 18.8 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa mapya 100 ya mizigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda, pamoja na wananchi wa Mpanda, kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na zoezi la ukarabati na ununuzi wa mabehewa ya abiria na mizigo. Ni matumaini yetu kuwa pindi mabehewa yatakapowasili nchini na ukarabati kukamilika, tatizo la uhaba wa mabehewa kwa sehemu kubwa litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ahsante.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha uwepo wa marubani wawili kwenye ndege ndogo za abiria?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ndege zote kwa mujibu wa vyeti vya utengenezaji (type certificate) huwa zina taarifa inayoelekeza mambo muhimu ya kifundi na usalama yahusuyo operesheni za ndege hizo. Pamoja na hizo nyaraka mbili, pia kuna kitabu cha maelekezo ya matumizi. Ndege zote zenye uzito wa kilogramu 5,700 kwenda chini ni ndege za rubani mmoja kwa mujibu wa nyaraka za mtengenezaji.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga na Sheria ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga, haizuii ndege hizo kuendeshwa na rubani mmoja na ni salama kufanya hivyo. Hata hivyo, nchi yetu imeweka sheria ya kuwa na marubani wawili kwa ndege yoyote ya abiria yenye uzito unaozidi kilogram 5,700 hata kama mtengenezaji wake anaruhusu rubani mmoja mmoja, katika kujiwekea wigo mpana wa kuweka usalama wa anga.

Mheshimiwa Spika, aidha, Mamlaka ya Usafiri wa Anga imeweka utaratibu wa kuhakiki afya za marubani mara kwa mara kwa mujibu wa sheria. Uhakiki wa kati na mkubwa hufanyika kila baada ya miezi sita kwa marubani wenye umri unaozidi miaka 40 na kila baada ya miezi 12 kwa marubani wenye umri wa chini ya miaka 40. Uhakiki wa mara kwa mara na wa kushtukiza pia hufanyika. Aidha, rubani yeyote anayekutwa na changamoto za kiafya huwekewa sharti la kutoruka peke yake au kuzuiwa kuruka kabisa. Ahsante.