Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Mwita Mwikwabe Waitara (2 total)

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nampongeza kiongozi wa Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa swali zuri ambalo wewe mwenyewe Naibu Spika, umesaidia kuiua CCM humu ndani. Watu wataamini hizo hela mmekula, bora ungeacha ajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nimwulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nitatumia maneno ambayo watawala wanapenda kuyasikia kwamba Serikali hii haijafilisika kabisa na Serikali hii ina mikakati mizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika Ubunge wangu wa muda mfupi huu, ile Sheria ya Mfuko wa Jimbo ndiyo sheria ambayo nimeona imekaa vizuri kweli kweli kwa sababu ni fedha ambazo Mbunge anapewa kwa taarifa tu zinaingia kwenye Halmashauri halafu Kamati yake inakaa, miradi inaibuliwa halafu wanapanga inaenda kwa wananchi moja kwa moja, Mbunge hagusi hata shilingi mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali haijafilisika, tangu bajeti ya Serikali yenu hii ya Awamu ya Tano imepitishwa, Waheshimiwa Wabunge hawajapewa fedha hii ya Mfuko wa Jimbo. Sasa naomba unieleze, kama Serikali haijafilisika, Waheshimiwa Wabunge wameahidi miradi mbalimbali katika maeneo yao ya kiuongozi na wananchi wakawa wanasubiri miradi ile, Waheshimiwa Wabunge wanaonekana waongo kwa sababu fedha hazijaenda na Wabunge hawawezi kufanya maamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini kauli yako juu ya hili? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimwambie kwamba Serikali hii haijafilisika. Mfuko wa Jimbo wa Mbunge ni miongoni mwa fedha zilizoandaliwa kwa bajeti ambayo tuliipitisha mwezi Julai, lakini Mfuko huu unapelekwa mara moja kwa mwaka kwenye Majimbo yetu. Nawe ni shahidi kwamba toka tumemaliza Bunge sasa tuna miezi mitatu. Bado tuna miezi kama saba ili kuweza kuhakikisha kwamba fedha yote tuliyokubaliana hapa inaenda kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo yana kipaumbele chake, yapo yale ambayo yanaweza kutekelezwa ndani ya mwaka mzima, lakini nataka nikukumbushe kwamba mfumo wa fedha zetu ni cash budget, tunakusanya halafu pia tunapeleka kwenye miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe Mheshimiwa Mbunge faraja kwamba suala la Mfuko wa Jimbo bado unatambulika na fedha tutazipeleka kwenye Majimbo na Waheshimiwa Wabunge wote tutawajulisha tumepeleka kiasi gani ili sheria zile ziendelee kutumika na Mheshimiwa Mbunge kama Mwenyekiti wa Mfuko wa Jimbo utaendelea kuratibu mipango yako ya Jimbo lako na fedha ambayo tutaipeleka. Kwa hiyo, endelea kuwa mtulivu, fedha tutazipeleka na tutawajulisha Wabunge wote. Ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni sera ya Serikali kulinda raia na mali zao. Lakini mnamo tarehe 24 na tarehe 25, askari wa FFU katika Kambi ya Ukonga, Mombasa, walifunga barabara wakapiga akina mama, vijana na wazee na wakawatesa sana abiria na kuleta madhara makubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nipate tu, na wananchi wangu wasikilize, Serikali inatoa kauli gani juu ya matukio kama haya ambayo yanafanywa na viongozi na vijana ambao kimsingi tunatakiwa tuishi kama ndugu na kushirikiana kwa ajili ya kulinda raia na mali zetu? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunazo taarifa kwamba pale Ukonga kulikuwa na mgongano mkubwa kati ya Jeshi letu la Polisi na raia, na mgongano huu umesababisha pia kuuawa kwa askari mmoja na watu wengi kupigwa, lakini hatua nzuri zimechukuliwa. Mkuu wetu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Mjema, aliingilia kati na kuchukua hatua ya kuunda tume ambayo inafanya ufuatiliaji kuona chanzo na madhara yaliyojitokeza na wahusika katika jambo hili. Baada ya tume kumaliza kazi yake, ikibainika nani ametenda kosa hatua kali zitachukuliwa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu wewe ni Mbunge wa eneo lile lazima utashirikishwa pia katika kupata taarifa za matokeo ya tume iliyoundwa na Mkuu wetu wa Wilaya ya Ilala, Mama Sophia Mjema.