Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga (7 total)

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Chuo Kikuu cha Mzumbe ni chuo kikongwe chenye historia tangu mwaka 1953 kipindi cha ukoloni na mwaka 1972 kupandishwa hadhi kuwa Chuo cha Uongozi wa Maendeleo (IDM) kikiwa na miundombinu ya kukidhi wanafunzi wasiozidi 1,000. Kwa sasa chuo hiki kina jumla ya wanafunzi 11,282 ambapo idadi hii ni sawa na ongezeko la 874.3% wakati hali ya majengo na miundombinu kwa kiasi kikubwa bado ni ile ile ya mwaka 1972:-
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga miundombinu mipya ikiwemo madarasa, mabweni, ofisi za Wahadhiri, jengo la utawala na kadhalika ili kukidhi mahitaji ya ongezeko kubwa la wanafunzi na Wahadhiri waliopo na watakaokuja na kukifanya chuo hiki chenye historia kubwa kiwe na taswira ya chuo cha kisasa na hadhi ya kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tiisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaanza kujenga miundombinu mipya kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kudahili na kuleta tija kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kati ya mwaka 2010/2011 hadi 2015/2016, Serikali ilitenga na kutoa jumla ya Sh. 8,075,490,199 fedha za maendeleo kwa ajili ya ukarabati na kujenga majengo na miundombinu mipya katika Kampasi za Mzumbe, Mbeya na Dar-es-Salaam. Aidha, kwa mwaka 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na majengo katika Kampasi Kuu ya Mzumbe na shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya katika Kampasi ya Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilidhamini chuo kujenga jengo jipya la ghorofa tano lenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kumbi za mihadhara, maktaba, ukumbi wa mikutano na ofisi katika Kampasi ya Dar-es-Salaam ambalo limekamilika na linatumika. Katika Kampasi ya Mbeya jengo jipya la ghorofa mbili la maktaba lenye vyumba vya maabara ya computer na ofisi limekamilika na limeanza kutumika mwaka 2015/2016. Vilevile ujenzi wa jengo la taaluma na utawala lenye ghorofa mbili unaendelea na unafadhiliwa na Serikali pamoja na mkopo kutoka kwa Mamlaka ya Elimu (TEA) kwa thamani ya shilingi bilioni 2.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa juhudi hizi za ukarabati, ujenzi na mipango inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe ni dhahiri kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuinua hadhi ya chuo hiki na hivyo kuweka mazingira stahiki ya kufundishia na kujifunzia.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Hospitali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na changamoto zinazoikabili za kuwa na wagonjwa wengi, kukosekana kwa Hospitali za Wilaya, kupokea majeruhi wa ajali mbalimbali lakini hadi sasa hospitali hiyo inatumia X-ray za zamani ambazo ni chakavu hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Je, ni lini Serikali itapeleka x-ray ya kisasa (Digital X- ray) ili kuondokana na adha kubwa wanayopata wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali namba 13 lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua umuhimu wa huduma ya uchunguzi kwa kutumia mionzi ya rediolojia. Aidha, Wizara inatambua changamoto ya uchakavu wa mitambo ya radiolojia na gharama kubwa za matengenezo inayoathiri upatikanaji wa huduma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kuleta mashine mpya 34 za kisasa za digital ambazo zinatengenezwa na Kampuni ya Philips, na hii inatokana na mkataba wa matengenezo wa mwaka 2012 na 2016 ambao mbali ya matengenezo waliyotakiwa kufanya walitakiwa vilevile kubadilisha mashine chakavu na kuweka mashine mpya. Mashine hizi zitafungwa katika hospitali za rufaa zote za mikoa Tanzania Bara ikiwepo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Awamu ya kwanza ya kuletwa mashine hizi inatarajiwa kuwa ni Juni, 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na gharama kubwa ya kununua na kufanya matengenezo ya vifaa vya uchunguzi Wizara imeanza kufanya uchambuzi ikiwa ni pamoja na kuangalia uzoefu wa nchi nyingine ambazo zilishaanza kuweka utaratibu wa kukodisha vifaa na kulipia huduma. Wizara inatarajia kutumia uzoefu huo kuandaa miongozo itakayowezesha kutekelezwa kwa utaratibu huo kwa ufanisi.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Milima ya Uluguru ni chanzo kikubwa sana cha maji katika mito na vijito vingi ambavyo husaidia kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa maji safi na salama katika Mkoa wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam. Hata hivyo, kutokana na uharibifu wa mazingira uliosababishwa na ujenzi holela, kilimo na ufugaji, mito hiyo imeanza kukauka hivyo kusababisha adha kubwa ya upatikanaji wa maji kwa wananchi:-
Je, Serikali ina mipango gani ya kimkakati ya kuilinda milima hiyo isiendelee kuharibiwa na kuhakikisha miti iliyokatwa inapandwa mingine ili kuhifadhi vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tisekwa ambaye amekuwa akifuatilia sana masuala ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo sasa; Milima ya Uluguru ni mojawapo ya Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains) yenye ikolojia ya kipekee na bioanuai adhimu; ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya maji ya Mto Ruvu unaohudumia wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali kupitia taasisi zake na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuitunza na kuihifadhi Milima ya Uluguru. Jitihada hizo ni pamoja na:-
Kwanza, kuanzisha Mfuko wa Hifadhi ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains Conservation Endowment Fund) wa mwaka 2002 kwa lengo la kusaidia juhudi za uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki ikiwemo Milima ya Uluguru. Jumla ya dola za kimarekani milioni 2.4 zilitumika kuanzisha na kuendesha shughuli za mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Mfuko huu ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya fedha kwa taasisi za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Asasi za Kiraia na vikundi vinavyojihusisha na juhudi za uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki. Kila mwaka kiasi cha shilingi milioni 50 hutolewa kwa wadau wa uhifadhi wa mazingira kwa njia za ushindani.
Pili, mwaka 2008, Serikali ilitangaza kupitia gazeti la Serikali namba 296 eneo lenye jumla ya hekari 24,115 kuwa hifadhi asilia (nature reserve) na kuanzisha mamlaka rasmi ya kusimamia eneo hilo la Milima ya Uluguru. Kupitia mamlaka hiyo, uhifadhi wa Milima ya Uluguru umeendelea kuimarika kwa kuanzishwa na kuimarishwa kwa Kamati za Maliasili na Mazingira katika vijiji vyote 62 vinayozunguka hifadhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi nyingine ni pamoja na kuweka upya alama za mipaka (beacons), kufanya tafiti mbalimbali, kuimarisha utalii, kupanda miti na kuingia makubaliano ya ushirikiano wa uhifadhi wa vijiji hivyo.
Tatu, kupitia Mamlaka ya Bonge la Wami – Ruvu ambalo linahusisha Mlima Uluguru, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa miaka mitano (2016-2021) uitwao Securing Watershed Services Through Sustainable Land Management.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mradi huu, Serikali imetenga jumla ya dola za kimarekani 22,000,000 huku wafadhili wengine (UNDP na GEF) wakichangia jumla ya dola za kimarekani 5,648,858 na kufanya mradi huu kuwa na gharama ya dola za kimarekani 27,648,858. Sehemu ya fedha hizi zinatumika katika juhudi za uhifadhi katika maeneo yaliyo nje ya hifadhi asilia (Uluguru Nature Reserve). (Makofi)
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi sana vya utalii ambavyo vikitumika vizuri vinaweza kuchangia pato la Taifa na wananchi kwa ujumla; moja kati ya vivutio hivyo ni pamoja na Mbunga za Hifadhi ya Wanyama Mikumi ambayo inaongeza mapato mengi, lakini mbuga hizo hazina hoteli nzuri za kitalii zenye kukidhi viwango vya kimataifa, kutokana na kuungua kwa Hoteli ya Kitalii ya Mikumi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga hoteli kubwa za kitalii ndani ya Mbuga ya Mikumi ili kuvutia watalii wengi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuwa Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Mikumi. Baada ya kuungua kwa lodge ya Mikumi, Serikali kupitia TANAPA imeendelea na juhudi mbalimbali za kuhamasisha uwekezaji katika hifadhi hiyo, ambao fursa za uwekezaji hususan huduma za malazi zimekuwa zikitangazwa. Aidha, mwekezaji wa kuifufua lodge ya Mikumi alishapatikana na kazi ya ukarabati inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mikumi kwa sasa wanatumia kambi tatu za mahema (tented camps) zilizoko ndani ya hifadhi, lodge na hoteli kumi zilizopo Mikumi Mjini. Wizara kupitia TANAPA imetenga maeneo saba kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli na lodge ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi zenye hadhi na viwango vya kimataifa ili kuleta watalii wengi na kuongeza mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii katika Ukanda wa Kusini kwa ujumla, Serikali ilizindua rasmi mradi wa kuendeleza utalii Ukanda wa Kusini wa Tanzania ujulikanao kama REGROW tarehe 12 Februari, 2018 Mjini Iringa. Lengo la mradi huu ni kuwezesha maendeleo ya utalii kwa kuboresha miundombinu, kuhifadhi maliasili na mazingira katika hifadhi ya Ukanda wa Kusini ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutumia fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge, uongozi pamoja na wakazi wa Mikumi kwa ujumla kutenga maeneo ya uwekezaji wa huduma za malazi na utalii ili kunufaika na biashara ya utalii nje ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. (Makofi)
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-

Kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi dhidi ya Mamlaka za Maji Safi katika Halmashauri mbalimbali kwa kuwapatia wananchi bili kubwa za maji ambazo haziendani na uhalisia:-

Je, ni lini Serikali itaanzisha utaratibu wa kulipia maji kadri utumiavyo katika utoaji wa huduma hiyo kama ilivyo kwenye umeme?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza kutumia utaratibu wa kulipa maji kadri unavyotumia (pre-paid meters) katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa sasa utaratibu huo umeanza kutumika katika maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka za Arusha, Iringa, Songea, Dodoma, Tanga, Mbeya, Tabora, Mwanza, Moshi na DAWASA.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeagiza Mamlaka zote nchini kuendelea kuwafungia wananchi dira za maji za kulipa maji kadri watumiavyo ili kupunguza malalamiko ya wananchi pamoja na kupunguza tatizo la malimbikizo ya madeni ya matumizi ya maji.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-

Barabara zinazotoka Kidiwa hadi Tandali, Daraja la Mgeta hadi Likuyu, Visomolo hadi Lusungi na Langali SACCOS hadi Shule ya Sekondari Langali Tarafa ya Mgeta Wilayani Mvomero zimejengwa kwa nguvu za wananchi, lakini bado hazipitiki kutokana na vikwazo vya miundombinu na madaraja:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hizo ili kuondoa adha wanazopata wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine T. Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kidiwa – Tandali – Maguruwe yenye urefu wa kilometa 13.8 imefanyiwa upembuzi yakinifu na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kubaini zinahitajika shilingi bilioni 2.81 kwa ajili ya matengenezo makubwa (Rehabilitation Works) kwa kiwango cha zege katika sehemu za maeneo ya milimani na ujenzi wa miundombinu ya madaraja. Serikali inaendelea na mpango wa kutafuta fedha kwa kizingatia uwingi wa fedha zinazohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 34.6 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum (Periodical Maintenance) kwenye barabara za kibaoni – Lukuyu na barabara ya Visomoro – Bumu – Mwalazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja (vented drift) katika Mto Songa.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-

Baadhi ya watoto wakubwa wenye uwezo wameamua kuwatelekeza wazazi wao pasipo kuwapa matunzo wanayostahili:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawajibisha watoto waliotelekeza wazazi wao na kuhakikisha wanatoa matunzo stahili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ipasavyo:-

Mheshimiwa Spika, napenda kulithibitishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wazee katika ustawi wa Taifa letu. Sote tunatambua kuwa wazazi walitumia rasilimali walizokuwanazo kuhakikisha watoto wanapata huduma za matunzo na malezi ili kuwawezesha kukua na kufikia ndoto zao.

Mheshimiwa Spika, kufuatia mifumo ya hifadhi ya jamii ya asili, jukumu la kuwatunza na kuwalea wazazi au wazee ni la wanafamilia, hususan watoto. Kutokana kudhoofika kwa mifumo hiyo ya asili, mmomonyoko wa maadili na utandawazi, jukumu hilo limekuwa na changamoto nyingi na kusababisha wazazi kutelekezwa.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuhakikisha maslahi ya wazee yanalindwa na wanapata haki zao ikiwemo matunzo, Serikali iliandaa Sera ya Wazee ya mwaka 2003 ambayo inaelekeza jamii kuwajibika kutoa matunzo kwa wazee.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hakuna sheria ya kuwawajibisha watoto wanaotelekeza wazazi wao. Serikali itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutambua jukumu lao la malezi na matunzo kwa wazazi ambao ni hazina na tunu muhimu ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kutoa rai kwa watoto na jamii kwa ujumla kuhakikisha wazazi na wazee wanapatiwa malezi na matunzo yanayostahili.