Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Dadi Chikota (43 total)

MHE.ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 20 ni fedha ndogo sana inayopelekwa kijijini na kama wataamua kumlipa Mwenyekiti wa Kijiji, Serikali ya Kijiji haitafanya kitu chochote kingine. Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kubeba jukumu hili la kuwalipa Wenyeviti wa Vijiji?
Swali langu la pili, kutokana na umuhimu sasa wa kundi hili na malalamiko yaliyopo kila kona nchini Serikali sasa haioni ni muda muafaka wa kutoa waraka maalum ambao utatoa maelekezo kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhusu malipo ya Wenyeviti hawa na kuweka kiwango cha chini cha posho hiyo, badala ya kila Halmashauri kutekeleza jinsi wanavyoona wao inafaa.
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukiangalia kwa tathmini, maeneo mbalimbali posho hizi huwa hazilipwi na hoja ya Mbunge ni kwamba asilimia 20 ni ndogo. Ina maana ukiirejesha Kijijini, ikimlipa Mwenyekiti wa Kijiji mwisho wa siku ni kwamba fedha ile haitatosheleza hata kufanya kazi zingine za vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu Serikali za Mitaa safari hii ndiyo maana tumeweka Specification katika bajeti ya mwaka huu. kila Halmashauri wakati ikipitia mchakato wa bajeti tuione inakidhi jinsi gani itahakikisha mapato yake ya ndani kwa kupitia vyanzo mbalimbali ili mwisho wa siku iweze kuhakikisha kwamba inapeleka fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tumesisitiza kuanzia Julai Mosi lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba hili jambo tunalolifanya, jinsi gani kila Halmashauri iweze kukusanya pesa za kutosha. Lengo ni kwamba Wenyeviti wa Vijiji waweze kupata posho, hali kadhalika pesa nyingine iende katika shughuli zingine za Maendeleo ya Kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili juu ya kupanga kiwango maalum, ni kweli. Sehemu zingine wanalipa sh. 20,000, sehemu nyingine wanalipa sh. 10,000, tutaangalia lakini, tutafanya utafiti wa kutosha kuona jinsi gani hii hali iende sawasawa. Kwa sababu tunajua wazi kwamba kila mtu hapa katika Bunge hili anategemea kazi ya Mwenyekiti wa Kijiji au Mwenyekiti wa Mtaa katika kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni sambamba na mikutano yetu ambayo tunaenda kuifanya katika Jumuiya hizo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Swali langu la nyongeza namba moja, ni kwa nini sasa kwa kuwa, kila kitu kimekamilika na mchakato wa manunuzi umekamilika na barabara hii ni muhimu kwa usafirishaji wa korosho, ujenzi wa barabara hii usianze mara moja badala ya kusubiri mwaka wa fedha 2016/2017, hii maana yake tutaanza Julai na wakati wananchi wanasubiri ujenzi huu uanze mara moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba Naibu Waziri atupe Kauli ya Serikali kuhusu kilometa 160 zilizobaki, kwa sababu barabara hii ina kilometa 210 na amesema ujenzi utaanza kwa kilometa 50. Naomba majibu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilipangiwa bajeti yake kwa mwaka huu wa 2015/2016. Kwa hiyo, kuanza ujenzi kwa mwaka huu wa fedha, fedha zake hatuna. Fedha zimepangwa kwa mwaka wa fedha ujao na naamini Bunge lako Tukufu litaidhinisha bajeti hiyo na hivyo hatuna namna nyingine zaidi ya kuanza kujenga barabara hiyo kuanzia mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili naomba nimhakikishie kwamba dhamira ya Awamu ya Tano ya Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ya dhati na ndiyo maana tumeanza na kipande hiki cha kilometa 50. Mtakumbuka barabara nyingi tumekuwa tukianza na vipande vidogo vidogo sana, lakini katika Awamu hii ya Tano tutachagua miradi michache ili tupeleke rasilimali iweze kukamilika kwa haraka na baadaye tunaendelea kwenye miradi mingine, huo ndiyo mkakati wa jumla.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la usambazaji wa maji linalokabili mradi wa Mbwinji, Nachingwea, linafanana na tatizo la usambazaji wa maji wa mradi wa Makonde hususan chanzo cha maji Mitema. Kwa hiyo, nataka niulize, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati mkubwa ili Miji inayonufaika na mradi ule; Nanyamba, Kitangari na Tandahimba wapate maji ya kutosha.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo swali dogo, ni swali kubwa la Mheshimiwa Chikota kuhusu mradi wa Mitema kupitia Mamlaka ya Maji ya Makonde.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa Chikota unawahisha shughuli na wakati unajua kwamba mradi ule tumeutengea zaidi ya Dola milioni 84, mradi wa Makonde, fedha ambayo inapatikana kutoka Serikali ya India. Nikuhakikishie tu kwamba wakati wowote, inawezekana kwenye mwezi wa Saba au wa Nane fedha hiyo itakuwa imeshaidhinishwa na utekelezaji wa mradi wa Makonde na pamoja na vyanzo vya Makonde na Mitema vitafanyiwa kazi nzuri kukarabati ule mfumo wote wa maji tuhakikishe kwamba wananchi wa maeneo ambayo yako chini ya Makonde wanapata maji safi na salama.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Mchinga linafanana sana na tatizo la Halmashauri ya Tandahimba iliyopo Mkoani Mtwara, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kugawanya Halmashauri ya Tandahimba ili kuwe na Halmashauri mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, Wilaya ya Mtwara sasa hivi ina Halmashauri tatu, Mtwara Manispaa, Halmashauri ya Mtwara na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, je, Serikali ina mpango gani kumpunguzia mzigo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, ili kuanzisha Wilaya mpya ya Nanyamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali katika jibu langu la msingi ni kwamba mgawanyo huu wa Halmashauri na halikadhalika uanzishaji wa kata mpya, uanzishwaji wa vijiji halikadhalika uanzishwaji wa Wilaya una taratibu zake. Na nilizungumzia kwamba, kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 145 Ibara ya 146 inayoanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa, lakini kwa mujibu wa Sheria ya 287 inaainisha jinsi gani mchakato huu unaenda.
Sasa kwa Wilaya, Halmashauri ya Tandahimba, kwa mujibu wa Mheshimiwa Mbunge alivyoshauri ni kwamba mimi ninamshauri kwa sababu najua Mheshimiwa Chikota ni Mtaalamu mkubwa sana wa Serikali za Mitaa, tukimkumbuka katika reference yake alipokuwa katika ngazi ya mkoa hapo awali. Kwa hiyo, naona kwamba yeye awe chachu kubwa ya kutosha na mimi naona jambo hili halitamshinda. Mchakato ule utakapokamilika katika maeneo yake akija katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI sisi hatutasita kufanya maamuzi sahihi kulingana na vigezo vitakavyokuwa vimefikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika suala zima la hizi Halmashauri sasa kupata Wilaya Mpya ya Nanyamba ni kama nilivyosema awali. Nakuomba Mheshimiwa Chikota fanya utaratibu huo, wataalam watakuja site, wata-survey kuangalia vigezo vinafikiwa vipi; na mimi najua Kanda ile ukiangalia eneo lake ni kubwa sana siku nilipokuwa natoka Songea kwenda mpaka Masasi hapa katikati jiografia ya maeneo yale unaona kwamba, jinsi gani maeneo ya kiutawala mengine yako makubwa sana. Kwa hiyo, fanyeni hayo, baadae sasa Ofisi ya TAMISEMI itafanya tathmini na kuona kufanya maamuzi sahihi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mamlaka za Maji Mijini ndiyo vyombo vyenye dhamana ya kuhakikisha upatikanaji wa maji mijini na kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imeanzishwa kisheria mwaka 2015, je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha uundwaji wa Bodi ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Nanyamba ili kuhakikisha maji katika Mji wa Nanyamba yapatikana kwa kirahisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chikota, Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala analolizungumzia Mheshimiwa Chikota ni jambo la msingi na hizi Bodi za Mamlaka za Maji za Halmashauri ziko chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mwanzo Ofisi hii ilikuwa chini ya Waziri Mkuu. Tulichokifanya ni nini? Mwezi mmoja uliopita tulikuwa na mkutano mkubwa wa wadau mbalimbali kuhusiana na suala la uundwaji wa Bodi za Mamlaka za Maji ili ifike wakati halmashauri ziweze kuhudumiwa vizuri. Sasa Ofisi yetu inafanya uratibu kutokana na mabadiliko ya Serikali yetu kwamba sasa iko chini ya Ofisi ya Rais na tunafanya mchakato mpana, siyo kwa Bodi ya Mamlaka ya Maji ya Nanyamba peke yake isipokuwa ni Bodi za Mamlaka za Maji za halmashauri mbalimbali ambapo nyingi sana hatujaziunda, si muda mrefu sana zoezi hili litakamilika na Nanyamba Mamlaka yenu itakuwa rasmi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
16
Kwa kuwa hapo awali Serikali ilikuwa na chombo ambacho kinadhibiti education materials yaani EMAC na kwa kuwa ilivunjwa rasmi huko nyuma na kutamka kwamba wataunda chombo kingine kwa ajili ya kudhibiti vifaa vinavyoingia katika mfumo wa elimu pamoja na vitabu.
Je, Serikali inaukakasi gani wa kuunda chombo hicho maana mpaka leo hakijaundwa bado?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hapo mwanzo Wizara yenyewe ilikuwa inahusika katika kudhibiti kwa kutumia Kitengo hiko cha EMAC, lakini baadaye kupitia Waraka Na. 4 ambao niliutaja kulikuwa kumeundwa Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo kwa sasa ndiyo inashughulikia masuala hayo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa elimu kwa wakati wa Mtwara na Lindi ili wapate uelewa juu ya mradi huu?
Lakini pili, waweze kujiandaa kutumia fursa zitakazopatikana baada ya ujenzi wa kiwanda hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili, maeneo ambayo yalianishwa na mradi huu ni mawili, eneo la kwanza ni kwa ajili ya ujenzi wa kile kiwanda cha LNG, eneo la pili ni industrial park kwa ajili ya viwanda vingine ambavyo vitajengwa hapo baadaye.
Sasa nataka nijue hatua iliyofikia katika kutwaa eneo hili ambalo litajegwa viwanda vingine yaani eneo la industrial park kwamba je, wananchi wameshafidiwa au bado hawajafidiwa hadi sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mradi wa LNG ni mardi mkubwa sana, na nipende tu kusema kwa niaba yako na kwa niaba ya Wabunge; kati ya miradi mikubwa ambayo Serikali tumeitekeleza ni pamoja na mradi huu utakapo kamilika. Mradi huu kwa nchi za Afrika, Tanzania itakuwa ni nchi ya tatu katika kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, lakini kujibu swali la msingi ambalo Mheshimiwa Chikota anataka kujua ni hatua gani imefikiwa katika kutoa elimu kwa wananchi; hatua tatu zimeshafanyika hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza ilikuwa ni kuwapa ufahamu na utambuzi wa manufaa ya mradi huu kwa viongozi wa Mikoa ya Lindi pamoja na Mtwara ambao vikao vimefanyika na kikao cha mwisho kilifanyika jana pamoja na juzi.
Mheshimiwa Spika, lakini hatua ya pili kulingana na hilo TPDC pamoja na wakandarasi na wazabuni waliopewa kazi hii wameshaanza kutoa elimu katika Vijiji vinavyoambaa katika mradi huu. Vijiji ambavyo vimeshatoa elimu hadi sasa ni pamoja na Kijiji cha Likong‟o ambapo mradi utachukuliwa, eneo la Kikwetu pamoja na Kijiji cha Mtomkavu. Hayo ni maeneo ambayo elimu wananchi wameshapewa kwa ajili ya umuhimu wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba ni maeneo gani yamechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hiki. Kwa niaba ya wananchi ni vizuri niwatangazie kwamba eneo lililochukuliwa na mradi huu kimsingi ni eneo kubwa sana, ni jumla ya ekari 20,000 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu, hata hivyo kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa LNG ni hekta 2,071 zitatumika.
Mheshimiwa Spika, na kwa niaba ya wananchi ni vizuri nikiwaeleza, mradi huu utakapokamilika utakuwa na manufaa mengi kwa sababu wawekezaji mbalimbali watatumia maeneo haya. Kwa mujibu wa swali la Mheshimiwa Chikota, nikushukuru sana Mheshimiwa Chikota kwa sababu mradi huu ni vizuri sana Watanzania tukauelewa. Tunapozungumza kujenga uchumi wa viwanda ni pamoja na viwanda vikubwa kama kiwanda hiki ambacho nimekieleza.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba miundombinu ya kiwanja cha ndege ni pamoja na barabara inayoingia uwanjani na barabara hii sasa imechakaa. Sasa nataka kuuliza kwamba Serikali ina mpango gani wa ukarabati wa barabara inayoingia uwanja wa ndege wa Mtwara kutoka Magomeni Mjini Mtwara hadi uwanja wa ndege?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amesema kwamba kuna master plan ambayo inaandaliwa; sasa nilitaka kuuliza kwamba kwa kuwa Serikali ina mpango gani wa kutwaa eneo la ardhi kwa sababu sehemu kubwa ya uwanja huo wa ndege imepakana na eneo la Jeshi; sasa kwa vyovyote vile watahitaji eneo la kijiji cha Naliendele; wamejiandaaje kutwaa eneo hili ili kuepusha migogoro ya wananchi wa Naliendele hapo baadaye?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ukarabati wa barabara, ni sehemu ya mpango ambao nimeueleza katika swali langu la msingi. Tunapoongelea kukarabati uwanja huu ni kurekebisha njia za barabara za kurukia na kutua ndege pamoja na maingiliano na nyumba vilevile za abiria. Kwa hiyo, ni mpango wote, unaunganisha kila kitu ikiwa ni pamoja na barabara zinazoingilia uwanja huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, namwomba Mheshimiwa Mbunge asubiri kwanza tupate taarifa kamili ya mpango kabambe huo ambao unakamilika mwezi Julai kama nilivyosema katika jibu langu la nyongeza, baada ya hapo ndiyo masuala ya kutwaa ardhi na mipango mingine ya kutekeleza mpango huo yatafuatia.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, kipo! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa Mfuko wa Mawasiliano umenufaisha Kata chache sana katika Jimbo la Nanyamba; je, Serikali ipo tayari sasa kuingiza Kata ya Nyuundo na Kata nyingine ambazo hazina mawasiliano katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 badala ya kutuambia siku za usoni ambazo hatujui itakuwa ni lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kuna Makampuni ya Simu yamefunga minara katika baadhi ya kata zetu lakini upatikanaji wa mitandao bado ni hafifu kama vile Kata ya Njengwa na Milangominne.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari sasa kuyaagiza sasa makampuni hayo kutuma wataalamu ili wakaangalie matatizo ya minara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vijiji vya Kata vya Nyuundo ambavyo vimeainishwa katika awamu itakayofuata nimelichukua na tutaliangalia kama linaweza likatekelezeka kwa namna ambavyo ameeleza kwa sababu anafahamu kwamba bajeti imeshapita na tutaliangalia kwa namna itakavyowezekana. Naomba tu nimhakikishie kwamba Kata hii ya Nyuundo kwa vyovyote vile tutaishughulikia na mawasiliano tutayapeleka. Suala ni lini, itategemeana na fedha kama zitapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la maeneo Njengwa na Milangominne, minara kutofanya kazi, nimelichukua tutalifanyia kazi. Nitawafuatilia wahusika nione hasa kuna tatizo gani.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kuhusu uboreshaji wa elimu lazima tuzingatie mafunzo kazini kwa walimu. Sasa nataka niulize, Wizara ina mpango gani wa kufufua Vituo vya Walimu ambavyo vilianzishwa huko nyuma chini ya Mpango wa Kuboresha Elimu Ngazi ya Wilaya (District Based Support to Education(DBSPE) ambavyo kwa sasa hivi havitumiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili morale kwa Walimu ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba, dhana hii ya elimu bure inafanikiwa. Kwa hiyo, sasa nataka kujua kwamba, Serikali ina mpango gani kuhakikisha madeni kwa Walimu hayajirudii pamoja na kwamba, tupo kwenye sera ya kubana matumizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu ya maswali haya ya nyongeza.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunazo Teachers Resource Centers ambazo ni kweli zimekuwa zikisaidia sana katika harakati za kuanza kuwajengea Walimu taaluma ya kutosha katika kuhakikisha kwamba, wanafundisha masomo yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Chikota, kwamba Serikali katika mpango wake mpana wa sasa hivi; licha ya kufanya ukarabati wa maeneo mbalimbali katika shule kongwe pia itahakikisha kwamba vile vituo vinakuwa centers nzuri kama ilivyokula pale awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba, vituo vile vinasaidia kuweka mbinu bora. Kwenye hii Sera mpya ya Elimu tutaweka mbinu bora kwa Walimu. Kwa hiyo, vituo vile vitaendelea kutumika vizuri zaidi, lakini vile vile TAMISEMI na Wizara ya Elimu tuna mpango mpana katika kuhakikisha kwamba, wanafundisha vijana wetu katika mazingira mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la morale kwa wafanyakazi hasa Walimu, suala la malimbikizo ya madeni, ni kweli na tumesema hapa, hata Waziri wa Elimu siku ile alipokuwa anahitimisha hoja yake alizungumzia jinsi gani madeni yaliyokuwepo mwanzo na madeni yaliyolipwa na madeni gani ambayo yako sasa yanahakikiwa ili waweze kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nikiri wazi kwamba, madeni ya Walimu hayawezi kwisha kwa sababu kila siku ya Mungu lazima kuna Walimu wanakwenda likizo na lazima kuna Walimu ambao wakati mwingine wanahama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la dhana ya kulipa madeni mpaka ibaki sifuri kabisa, jambo hilo litakuwa gumu kwa sababu kila siku lazima kutakuwa na watu wanaendelea kudai. Jambo la msingi ni kwamba, ni lazima madai yanapojitokeza tulipe. Tukiri wazi kwamba Serikali ilijitahidi kwa kadri iwezekanavyo kuhakikisha Walimu hawa wanalipwa madeni yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, si kulipa madeni tu, hali kadhalika sasa hivi tunapambana katika kuboresha mazingira ya Walimu wanaofanyia kazi hususani ujenzi wa nyumba ili Walimu hawa wajisikie wako katika mazingira rafiki ya kufanya kazi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali la nyongeza, kwa kuwa, hali ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango, FDC inafanana na kile cha Mtawanya, kilichopo Mkoani Mtwara, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha miundombinu ya chuo hicho lakini pia kuboresha utoaji wa taaluma katika Chuo hicho cha Maendeleo ya Wananchi Mkoani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Serikali ina mpango mkakati mpya kabisa wa kufanya maboresho kwenye Vyuo vyote vya Maendeleo ya Wananchi hapa nchini. Mpango wetu ni kwamba, tayari tumeanza mazungumzo na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili tuweze kuvihamishia kwenye Wizara hiyo badala ya kubaki navyo sisi kwenye Wizara yetu. Lengo hasa ni kuboresha mitaala inayotolewa kwenye vyuo hivi lakini kuboresha administration ya vyuo hivi na kuongeza bajeti. Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Chikota, mpango tulionao ndiyo huo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwaa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la vyoo katika shule zetu za msingi linafanana na tatizo la nyumba za Walimu kwa shule zetu na tatizo hili sasa hivi kama limeachiwa Halmashauri ndiyo watatue tatizo hili, lakini kwa mapato ya Halmashauri nina uhakika mkubwa kwamba tatizo hilo haliwezi kupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumuuliza Naibu Waziri kwamba Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hili katika kipindi kifupi kijacho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niweke wazi kwamba Serikali kwa sasa imejipanga vema. Imejipanga vema kwanza hata ukiangalia mchakato wa bajeti ya mwaka huu tumemaliza madawati, lakini tumetenga takriban bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba katika shule za msingi na bilioni 11 katika shule za sekondari. Tukishirikiana TAMISEMI na wenzetu wa TEA jambo hili tumekuwa na mkakati mpana sana, lengo siyo nyumba za Walimu peke yake, bali ni madarasa, nyumba za Walimu, maabara na kufanya mpango kabambe wa ukarabati wa shule kongwe. Mwaka huu peke yake, shule kongwe 33, kila shule tunaipatia bilioni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu, Watanzania waone kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano, ina lengo la kuweka msukumo wa mbele katika kuboresha elimu yetu ya Tanzania.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama alivyosema kwenye jibu lake la msingi kwamba kituo hiki kinafanya tafiti mbalimbali lakini wanashindwa kuhaulisha yale maarifa wanayopata kwenye tafiti zao kwa wakulima kwa sababu hawana fedha za kutosha za kuweza kwenda kwa wakulima Mtwara, Lindi na Pwani na kuwapa matokeo mapya ya utafiti. Serikali ina mpango gani wa kukiongezea fedha kituo hiki ili waweze kuwafikia wakulima wengi wa korosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kiuatilifu muhimu katika uzalishaji wa zao la korosho ni sulfur dust. Napenda kujua mpango wa muda mfupi wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inawashawishi wawekezaji wakubwa waje kujenga kiwanda cha kutengeneza sulfur Mikoa ya Lindi na Mtwara ili sulfur hiyo iuzwe kwa bei ya chini kama ilivyo sasa hivi kwa viwanda vya mbolea badala ya kuagiza sulfur hii kwa fedha nyingi za kigeni kutoka nchi za nje?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto ya kibajeti itakayowezesha Kituo cha Naliendele kuhaulisha teknolojia ya korosho kwa wakulima na Serikali mwaka hata mwaka bado inaendelea kuongeza bajeti, lakini lazima niseme kwamba mafanikio makubwa ambayo tumepata kwenye zao la korosho na hasa katika msimu uliopita umechangiwa vilevile na teknolojia ambayo imetoka Naliendele. Kwa hiyo, nakubali kwamba kuna haja ya kuongeza bajeti na Serikali iko tayari kufikiria katika bajeti inayokuja lakini lazima vilevile tuseme kwamba pamoja na changamoto hiyo Naliendele imesaidia sana katika kukuza zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa kiwanda cha sulfur, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba namna mojawapo ya kupunguza gharama kubwa za sulfur kwa wakulima wetu ni kuhakikisha kwamba tunazalisha katika viwanda vyetu vya ndani. Nipende tu kumhakikishia Mheshimwa Mbunge kwamba tayari Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anafuatilia ujenzi wa kiwanda cha sulfur akishirikiana na Mheshimiwa Hawa Ghasia. Kwa hiyo, tunatumaini kwamba kitakapojengwa changamoto hii itakuwa imeondoka.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mosi, kuhusu Mradi wa Kitere pamoja kwamba majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanasema mradi umekamilika, lakini mradi huo umekamilika lakini haufanyi kazi kama unavyotakiwa na mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri shahidi amepita pale na hakuona hizi ekari 3,000 zimelimwa.
Kwa hiyo, naomba kauli ya Serikali kwamba, kuna mkakati gani wa kukamilisha mapungufu yaliyopo ili mradi huo sasa uweze kufanya kazi pasavyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kupitia Ofisi za Umwagiliaji Kanda, kuna miradi mingi hapa nchini ambayo haifanyi kazi. Juzi Kamati yetu ya LAAC ilikuwa Tabora, kuna mradi haufanyi kazi, kuna mradi Liwale, kuna mradi Mkuranga na miradi mingine. Sasa Serikali ina kauli gani kuhusu ushauri unaotolewa na ofisi hizi za umwagiliaji kanda ambazo miradi mingi ambayo inabuniwa na ofisi hizi huwa haifanyi kazi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Chikota, ambayo yote ni kama swali moja kwamba, miradi hii haifanyi kazi vizuri. Lakini pia ameonesha kuwa na utata kidogo katika ushauri wa taasisi yetu inayohusika na umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza
katika swali la msingi, Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba sasa hivi miradi yote hii ya umwagiliaji tunaifanyia mapitio. Na tulichokibaini ni kwamba tulijenga skimu za umwagiliaji, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi zile skimu za umwagiliaji
zimekuwa ama zinafanya kazi mara moja kwa mwaka na wala sio mara mbili kutokana na ukosefu wa huduma ya maji kwa kuwa miradi hiyo hatukuijengea mabwawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutapitia katika mpango
huu kabambe wa mwaka 2002 tuhakikishe kwamba, miradi hii sasa inafanyiwa usanifu na kutekelezwa kuhakikisha kwamba, inafanya kazi ile iliyotarajiwa. Lakini mapungufu pia yaliyojitokeza katika miradi hiyo tutayapitia, ikiwa ni pamoja na kuimarisha tume yetu ambayo Waheshimiwa Wabunge ninyi wenyewe mmeunda Tume ya Umwagiliaji kwa ajili ya kusimamia moja kwa moja shughuli ya umwagiliaji.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri
ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Ni wazi kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mfumo huu una upungufu na una changamoto nyingi ambazo nimeelezea mojawapo. Sasa nataka commitment ya Serikali kwamba hiyo Version 11 itaanza kutumika lini? Swali langu la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; changamoto nyingine ya mfumo huu ni kwamba, unasimama peke yake (stand
alone system) na wakati ukiangalia kwenye taasisi zetu, kwa mfano Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kuna mifumo mingi, tulitegemea kwamba mifumo hii ingekuwa inaongea; kuna EPICA, kuna LGMD, sasa je, Mheshimiwa Waziri atanihakikishia kwamba mfumo huu mpya Lawson Version 11 utakuwa unaongea na mifumo mingine?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nimpongeze sana kwa namna ambavyo amekuwa akisimamia suala zima la management ya rasilimali watu katika utumishi wa umma na yeye mwenyewe pia alikuwa katika utumishi wa umma na tunafahamu mchango wake na tunauthamini.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza, kwamba sasa Toleo hili la 11 ( Lawson Version 11) litaanza lini; nimhakikishie tu kwamba, katika Mwaka huu wa Fedha tumeshatenga Shilingi milioni 486 katika Idara yetu ya
Usimamizi wa Rasilimali Watu pamoja na Idara yetu ya TEHAMA na nimhakikishie tu kwamba katika Mwaka huu wa Fedha suala hili litakamilika. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, tumewakabidhi suala hili Wakala wa Serikali Mtandao ili waweze kusanifu na kusimamia usimikaji wake.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, kwamba ni lini sasa mfumo huu wa usimamizi wa rasilimali watu au
taarifa za kiutumishi na mishahara utaweza kuzungumza na mifumo mingine kama mifumo ya kifedha kama EPICA na mingine; nimwambie tu kwamba tunaiona hoja yake na hata e-government wamekuwa wakifuatilia suala hili kwa makini sana, si tu katika suala zima la kuongea, hata katika kuhakikisha pia gharama za mifumo yenyewe na udurufu wa kuwa na mifumo mingi wakati kunaweza kukawa na mifumo michache ambayo inaweza ikazungumza.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu kwamba pamoja na faida nyingine tutakazozipata tutakapoingia katika
Lawson Version 11 ni pamoja na kuunganisha mifumo mingine kama EPICA lakini pia kuhakikisha Mifumo kama ya NECTA, NIDA, RITA pamoja na mingine nayo pia ni lazima izungumze na Mfumo wetu wa Lawson.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Matatizo ya Mawasiliano ambayo yanalikabili Jimbo la Kilwa Kaskazini yanafanana na yale ya Jimbo la Nanyamba kwa sababu kuna kata za Njengwa, Nyundo, Nitekela na Kiyanga ambayo hayana mawasilinao. Na nilishawahi kuuliza swali hili hapa Bungeni nikaambiwa kwamba Mfuko wa Mawasiliano utapeleka mawasiliano huku na mradi huo bado mpaka sasa hivi haujatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipate majibu ya Serikali kuhusu miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO):
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Mawasiliano upo na huu unatekelezwa moja kwa moja na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini pia kuna programu nyingine ambayo ni ya watu binafsi ambao wamependa kuja kuwekeza katika nchi yetu. Kwa hiyo, kama hukupata kwenye mradi wa mawasiliano, basi tarajia pia unaweza ukapata kwenye hawa wawekezaji ambao wamekuja kufanya biashara kwenye eneo letu la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika hoja yako tayari umesema tayari ulishaahidiwa kupitia kwenye huu Mfuko wa Mawasiliano, Mheshimiwa Mbunge, niseme tu kwamba hebu tuvute subira kidogo, kama umeshaahidiwa hili lazima litatekelezwa.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa suala la udhibiti wa elimu huwezi kutofautisha na udhibiti wa vitabu vinavyoingia kwenye mfumo wa elimu na kwa kuwa imeonekana wazi kwamba taasisi ya elimu ambayo imepewa jukumu la kuthibiti ubora wa vitabu vinavyoingia kwenye mfumo wa elimu imeonekana kuna dosari kubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha chombo cha ithibati kama ilivyokuwa EMAC huko nyuma ili kudhibiti vitabu vinavyoingia katika mifumo yetu ya elimu na kuacha madudu yanayoendelea sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kurudisha mamlaka zilizokuwa zinafanya juu ya utungaji wa vitabu za wakati huo ni suala ambalo linabidi kuangaliwa zaidi. Kimsingi mapungufu yaliyojitokeza kwa mwaka huu Wizara ya Elimu imeanza kutunga vitabu kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, chombo kama hicho inabidi lazima kijengewe uwezo na ndio maana katika kufanya tathmini ya matatizo yaliyojitokeza, moja ya mambo yatakayoangaliwa ni uwezo wa chombo chenyewe, vilevile hata ushirikishwaji mpana wa wadau mbalimbali ikiwemo watu binafsi na wataalam kutoka katika maeneo mbalimbali.
Kwa hiyo, mimi nadhani kiujasiriamali tunasema kwamba kujifunza ni pamoja na kufanya makosa, lakini yasiwe ya kudhamiria yawe ni ya bahati mbaya. Kwa hiyo, tutaendela kuboresha na kushirikisha wadau wengi zaidi ili kuona kwamba tunapata vitabu vilivyo sahihi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Changamoto ya huduma ya afya iliyopo Kigamboni na Ubungo inafanana na ile iliyopo Jimbo la Nanyamba ambako hakuna kituo cha afya hata kimoja, hakuna hospitali ya wilaya, hakuna ambulance na hakuna DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya). Sasa nataka kujua Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kutatua changamoto hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba Mheshimiwa Chikota tulikuwa wote site na tulifika eneo ambalo wao wameweka kipaumbele kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakarabati eneo lile ili kupata kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ziara ile nimhakikishie Mheshimiwa Chikota kwamba Serikali imefanya commitment ya kutosha na pale muda si mrefu kuanzia sasa tutawekeza fedha nyingi takribani milioni mia saba katika kile kituo chake ambacho alikiwekea kipaumbele siku tulipofika pale. Kwa hiyo, naomba niwaambie wananchi wa Nanyamba kwamba Mbunge wao amepigana na Serikali imesikia na muda si mrefu tutakwenda kufanya uwekezaji mkubwa sana wa sekta ya afya katika eneo hilo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa wananchi wa Majimbo ya Mtama, Newala Vijijini na Newala Mjini kwa ajili ya usafirishaji wa korosho, choroko na mihogo. Je, ni lini sasa Serikali itaanza maandalizi haya ya ujenzi kwa kiwango cha lami, yaani kwa kufanya feasibility study? Watuambie ni lini wataanza sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; naipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala na Masasi. Hata hivyo, barabara hii ni kilometa 210, lakini ujenzi ambao umeanza ni kilometa 50 tu, wananchi wa Nanyamba, Tandahimba na Mtwara wanataka kusikia Serikali ina kauli gani kuhusu kilometa 160 zilizobaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kwamba Serikali imeiwekea umuhimu sana barabara hii kwa sababu ya mazingira ya korosho na jinsi wanavyopata shida katika kusafirisha katika yale maeneo kutoka Newala mpaka kuja kuunga Mtama. Kwa hiyo nimhakikishie tu kwamba mara fedha zitakapopatikana suala la feasibility study and detailed design tutaanza kulishughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuendeleza ujenzi Barabara ya Mtwara – Newala hadi Masasi nimhakikishie tu, tumeanza na hizo kilometa 50 hatutasimama, tutaendelea mpaka barabara hii itakapokamilika. Alikuja ofisini Mheshimiwa Chikota tulimwambia kuhusu hilo. Nimpongeze sana kwa jinsi anavyoendelea kufuatiliam nilitegemea kwa kuwa tulishamaliza ofisini asingerudia kuuliza, lakini kwa sababu anajua umuhimu wa barabara hii bado amerudia kuuliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana na jibu ni hilo, kwamba tutaendelea kuijenga barabara hiyo, hatutasimama. Tutamaliza hizi kilometa 50, baada ya hapo tutaendelea na kilometa zilizobaki mpaka tumalize kilometa zote 200.
MHE ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa shahidi kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria kwa sababu kuna watendaji wengi wa hizo AMCOS ambao hawana sifa zilizotajwa kisheria. Kwa hiyo, napenda kujua Serikali inatoa kauli gani kuhusu AMCOS ambazo zimeajiri watendaji ambao hawana sifa?
Mheshimiwa Spika, pili, kutokana na kazi kubwa ambazo wanazifanya watendaji hawa wa AMCOS hasa wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi ambao sasa hivi wanashughulikia zao la korosho na wanashughulika na fedha nyingi sana, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo kwa kuandaa mafunzo maalum ili kupunguza ubadhirifu na upotevu wa pesa ambao siyo wa lazima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu, naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Chikota ni mmoja kati ya Waheshimiwa Wabunge wanaofuatilia sana masuala ya ushirika kwa niaba ya wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu kwamba kama kuna mfanyakazi yeyote na mtendaji wa Chama cha Ushirika ambaye hajakidhi matakwa ya kisheria, kimsingi huyo amekaa mahali ambapo siyo pake. Kama ana ushahidi wa watendaji ambao wameajiriwa kinyume na taratibu au kinyume na sifa ambazo nimezitaja kwa mujibu wa sheria, naomba anipe orodha yao na mimi nitashughulika nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anasema kwa nini Serikali haitoi mafunzo au kuwajengea uwezo watendaji wa vyama vya ushirika, naomba nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja kati ya kazi ya Vyama vya Ushirika, hasa Vyama Vikuu, ni kuhakikisha vilevile kwamba watendaji wa Vyama vya Msingi wanajengewa uwezo. Kwa hiyo, tunaendelea kusisitiza kwamba Vyama Vikuu vishirikiane na Vyama vya Msingi kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ya mara kwa mara kwa watendaji wa Vyama vya Msingi. Vilevile, nitumie fursa hii kuwaagiza Maafisa Ushirika katika wilaya zote wahakikishe kwamba wanatekeleza jukumu lao la msingi la kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo viongozi pamoja na watendaji wa Vyama vya Ushirika.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa pembejeo za ruzuku hazitoshelezi mahitaji yote ya zao la korosho, Serikali inampango gani sasa zile pembejeo zingine ambazo mkulima atahitaji azipate sokoni kuagiza kwa pamoja (bulk purchase) kama itakavyofanya mbolea katika msimu huu kwa mwaka 2017/2018?
Swali la pili, ni ukweli usiopingika kwamba korosho mwaka huu imeingiza fedha nyingi sana za kigeni ni zao ambalo linaongoza, je, Benki ya Maendeleo ya Wakulima Tanzania ni lini itafungua tawi Mkoani Mtwara ili iweze kuwahudumia wakulima wa korosho wa Mikoa ya Mtwara na Lindi. Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, pembejeo hasa ya korosho ambayo inatumika zaidi ni hiyo sulphur na sulphur dust imekuwa ikiagizwa kutegemea na fedha ambayo imekuwa inapatikana katika ule Mfuko wa WAKFU wakati ule wa uendelezaji wa zao la korosho, pamoja na ile iliyokuwa inaagizwa kwa ruzuku na kuuzwa kwa wakulima kwa asilimia 50 bado wafanyabiashara binafsi walikuwa wanaagiza hii sulphur na kuiuza kwa wakulima ambao walikuwa hawapati fursa ya kununua ile inayoletwa kwa ruzuku ya Serikali. Kwa hivyo, sasa hivi tulichokifanya kwanza tumeongeza volume ya kuagiza kutoka tani 13,000 zilizoagizwa katika msimu uliopita mpaka tani 18,000 mwaka huu na lengo letu ni kwamba kwa msimu ujao wa korosho tutaongeza kutoka tani 18,000 mpaka tani 25,000 ambazo zinahitajika kwa ajili ya wakulima maeneo yote nchini.
Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao umekuwa unatumika ni uleule ambao tunau–introduce sasa kwenye mbolea ni wa bulk importation, umetusaidia sana katika kushusha bei ya sulphur dust yenyewe.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini TADB itafungua tawi huko Mtwara, nadhani mipango ipo na tulisema katika hotuba yetu ya bajeti kwamba, kwa kuanzia TADB wanataka wafungue matawi katika Kanda Saba hapa nchini, tulizitaja na jinsi kadri mtaji wao unavyoongezeka wataendelea kufungua matawi katika maeneo mengine nchini.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa upungufu huo wa Maafisa Ugani ni mkubwa sana kwenye Halmashauri ambazo zimeanzishwa hivi karibuni, kama Halmashauri ya Mji wa Nanyamba; je, Serikali ina mpango gani wa upendeleo kwa mamlaka hizi mpya za Serikali za Mitaa ambazo zimeanzishwa hivi karibuni?
Swali langu la pili, ukiangalia takwimu za ajira zilizotolewa hivi karibuni kwa Maafisa Ugani, na kwa kuwa nchi yetu ina takribani vijiji zaidi ya 12,000 utaona kwamba kuna vijiji vingi sana vinakosa Maafisa Ugani.
Je, Serikali ina mpango gani au mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba kila kijiji katika nchi yetu kinakuwa na Afisa Ugani ili kuleta mapinduzi ya kweli katika kilimo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Utumishi inatambua kwamba Mamlaka mpya za Serikali za Mitaa zilizoanzishwa zinahitaji upendeleo mpya, hasa katika kupanga watumishi. Nataka nimuahidi kwamba siyo Nanyamba tu, Nanyamba ni Mamlaka mpya ya Serikali za Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Mji wa Newala ni mpya, Halmashauri ya Mji wa Tarime ni mpya, Halmashauri ya Mafinga ni mpya, maeneo yale yote ambayo tumeanzisha Halmashauri mpya najua wakati wa kugawana watumishi zile mamlaka mpya hazikupata watumishi wengi. Kwa hiyo, nitakachofanya ni kuhakikisha zile mamlaka mpya zote zinapata watumishi wa kutosha ili zilingane, kama ni upungufu ulingane na zile mamlaka zilizokuwepo kabla.
Swali lake la pili, ni kweli kwamba vijiji vingi havina hawa Maafisa Ugani, hili limetokea kwa sababu muda mrefu katika nchi yetu, vile vyuo vinavyofundisha vyeti vya kilimo vilikuwa vimesimama, lakini baadae vimefufuliwa, sasa hivi kazi kubwa inaendelea. Nataka nimhakikishie kwamba tutaanzisha programu maalum kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha kwamba vyuo vile wanachukua wanafunzi wengi zaidi ili wanapomaliza waweze kuajiriwa na Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hatua inayochukua katika kusimika mifumo mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kurahisisha uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pamoja na pongezi hizo, nampongeza vilevile Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, changamoto kubwa katika utumiaji wa mifumo hii ni upatikanaji wa wataalam wa TEHAMA katika Mamlaka za Serikali zetu za Mitaa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri wataalam wa kutosha wa TEHAMA hasa katika halmashauri mpya ambazo zimeanza hivi karibuni kama Nanyamba na Halmashauri ya Mji wa Newala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba kwenye Mfumo wa EPICOR kuna changamoto nyingine ambayo inapatikana hususan wakati wa kutayarisha final account katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kiasi kwamba wataalam hulazimika kutafuta taarifa nyingine nje ya mfumo. Je, Serikali ina mpango gani wa ku--repair changamoto hii ili tunapoandaa hesabu za mwisho kwa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa wataalam wategemee taarifa za kwenye system tu na si kuchukua nyingine kutoka nje?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, Mwalimu Mstaafu, Mkurugenzi Mstaafu, RAS Mstaafu, mdogo wangu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuwaajiri wataalam wa TEHAMA, Wizara ya Utumishi na Utawala Bora tutakuwa tayari kuajiri watumishi hao kulingana na mahitaji. Katika zile nafasi 52,000 ambazo zilipitishwa na Bunge ambazo karibuni tutaanza kuajiri, zipo baadhi ya Halmashauri ambazo zimeweka maombi ya kuajiri wataalam hao. Sasa kila Halmashauri inawahitaji hawa kulingana na mahitaji yake yanahitilafiana.
Naomba nishauri, kwa hiyo, kama mdogo wangu Mheshimiwa Chikota, kule Nanyamba uliweka katika maombi, basi itakapofika kuajiri tutaajiri na kama hawakuwekwa tunashauri Nanyamba na Halmashauri nyingine zote katika bajeti inayokuja kutuwekea maombi hayo mkishirikiana na Wizara mama ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la pili la Mheshimiwa Chikota linahusu mfumo wa EPICOR ambao unasimamiwa na Wizara ya Fedha. Kwa sababu Kwa muuliza swali anapaswa kupata majibu sahihi ninaomba nimuombe Waziri mwenzangu wa Fedha ajibu suala la EPICOR kwa sababu linasimamiwa na Wizara yake, kwa ruhusa yako.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Chikota kwa kweli kwa kujali umuhimu wa mifumo hii kuingiliana na kufanya kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambayo anaisema ambayo sasa wataalam wanajikuta wakitegemea taarifa kutoka nje badala ya ndani ya mifumo kimsingi inatokana na madiliko ya teknolojia ambayo tunaenda nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Chikota atakumbuka kwamba tulianza na platnum wakati ule, tukajikuta kwamba mifumo hii na ina hitilafu tukaamia kwenye EPICOR 7.0; lakini nayo kulikuwa na modules ambazo ni friendly kwa mtumiaji, lakini ikawa na changamoto nyingine tukahama tena tukaenda 7.35 tukaenda 9.05 na sasa tumefika EPICOR 10.20. Kwa hiyo, kwa kweli changamoto anayoisema ni ya kiteknolojia zaidi. Tunatarajia kwamba huu mfumo wa EPICOR 10.2 sasa to zero itajalibu kushughulikia hizi changamoto ambao zinajitokeza katika utumiaji.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya matibabu kwa magonjwa ya UKIMWI na TB yanafanana sana na magonjwa ambayo yameibuka siku hizi, yale ambayo yanatokana na mtindo wa maisha hususani kisukari na shinikizo la juu la damu. Nataka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwenye dawa za magonjwa hayo kwa sababu mgonjwa akishapata ugonjwa huo ataendelea kutumia dawa hizo mpaka mwisho wa maisha yake. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku au kutoa bure kabisa dawa za magonjwa hayo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Chikota kwa kupunguza kitambi chake yeye mwenyewe. Kwa sababu alipokuja hapa alikuwa ana kitambi kirefu, lakini kadri siku zinavyoenda kitambi kimepungua. Sijui kama ni kwa changamoto za Ubunge ama ni kwa mazoezi makali anayoyafanya kwenye viwanja vya Jamhuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao hawajajiunga na timu ya Mheshimiwa Ngeleja wafanye hivyo haraka kwa sababu wanatupunguzia gharama za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna mikakati ya kitaifa ambayo tumeizindua, Mheshimiwa Makamu wa Rais alituzindulia mwaka jana mwezi Desemba na nchi nzima sasa hivi kuna siku ya mazoezi kila mwezi na inafanya vizuri sana. Kwenye Serikali, tiba kwa magonjwa yote chronic yakiwemo magonjwa hayo yasiyoambukiza na magonjwa mbalimbali ambayo yanatokana na magonjwa yasiyoambukiza ni bure kwa mujibu wa Sera ya Afya.
Kwa hivyo, ukiugua ugonjwa wa hypertension ama waswahili tunapenda kuita pressure, kisukari na saratani unatibiwa bure kwa mujibu wa sera, kwa sababu magonjwa yote sugu ama chronic illnesses kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 yanapaswa kutibiwa bure kwa gharama za Serikali. Kwa hivyo, hakuna gharama yoyote kwenye matibabu ya magonjwa haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto inakuja pale unapoenda kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kukawa hakuna baadhi ya dawa ambazo unazihitaji. Pale wenye kituo wanakuwa hawana namna zaidi ya kukuambia uende ukanunue mwenyewe kwenye private pharmacies. Hata hivyo, kwa mujibu wa sera matibabu ya magonjwa haya ni bure na tumeendelea kuboresha huduma zetu ili kama tutafikia uwezo wa kuwa na dawa zote ambazo watu wanazihitaji basi waweze kuzipata huduma hizo bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisisahau kukupongeza wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuamka kila siku asubuhi kwenda kushiriki mazoezi pale Jamhuri. Pia nikupongeze kwa ku-keep figure yako kuwa ya kiingereza (english figure). Nasema haya kuwatia moyo Waheshimiwa Wabunge wengi zaidi waweze kutamani kuwa na figure ndogo kama ya Mheshimiwa Naibu Spika. (Kicheko/ Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo la Nanyamba kuna kata saba ambazo hakuna mawasiliano ya uhakika ya simu, Kata ya Hinju, Nitekela, Nyundo, Mnima, Kitaya, Kilomba na Kianga. Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea mawasiliano ya simu wananchi wa maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na Kijiji cha mwisho hicho cha Kianga, Kitaya, Nitekela na kadhalika nimhakikishie kwamba majina haya tumeyapata na bahati nzuri hayo maeneo anayoyaongelea nayo yapo katika maeneo ya mpakani ni maeneo ambayo yanatakiwa yapewe kipaumbele. Kwa hiyo, nimwahidi katika kwamba katika Zabuni inayofuata ya kuhakikisha vijiji vyote Tanzania tunapeleka mawasiliano, zabuni ya mwezi wa Kumi vijiji hivyo navyo tutavifikiria. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kila tunapouliza kuhusu ukarabati mkubwa wa Mradi wa Makonde tunaambiwa kwamba kuna dola za Kimarekani milioni 84 ambazo ni za mkopo kutoka Serikali ya India, lakini kila siku tunaambiwa majadiliano yanaendelea. Sasa nilitaka nipate commitment ya Serikali, majadiliano hayo yataisha lini na mkataba utasainiwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mradi huu wa Makonde unahusisha Halmashauri nne; Newala Vijijini, Newala Mjini, Tandahimba na Nanyamba, lakini majibu ya Naibu Waziri yanazungumzia Halmashauri tatu tu. Sasa nilitaka nipate maelezo ya Serikali kuhusu mpango wa Serikali kutoa maji Mitema na kupeleka Halmashauri ya Mji wa Nanyamba.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Chikota kwa namna ya kipekee anavyowatetea wananchi wake, lakini kikubwa ni kuhusu suala la fedha za India.
Sisi kama Wizara ya Maji, kwa kuwa huu ni mpango mkubwa na mpango wowote mkubwa wenye mafanikio makubwa lazima uchukue muda. Sisi kama Wizara tunafuata taratibu lakini tunaamini utekelezaji wa mradi huu utaondoa kabisa tatizo la maji. Kwa hiyo, sisi kama Wizara ya Maji tutafanya jitihada za haraka ili jambo hili liweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala zima la chanzo cha Maji cha Mto Mitemba, sisi kama Wizara tumeshapokea andiko kuhusu suala zima la kutumia chanzo cha Mitemba ambacho kitaweza kutatua tatizo la maji kwa Halmashauri tatu, kwa maana ya Halmashauri ya Tandahimba, Newala na Nanyamba pamoja na maeneo ya jirani. Kwa kuwa andiko lile tumelipata, tunalifanyia kazi katika kuhakikisha tunalitekeleza kwa wakati kama ilivyopangwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ameonesha kwamba huduma hizi sasa zinaanza kutolewa kuanzia Hospitali ya Wilaya, na ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wetu wengi wapo vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha huduma hizi katika vituo vya afya ili kupunguza adha ya wananchi wetu kutembea kwenda Hospitali ya Wilaya?
Swali la pili, miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na kisukari, hivi sasa kuna ujenzi unaoendelea wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kule Mtwara, amesema kwamba hospitali za rufaa za kanda zitatoa vilevile huduma hii katika ngazi ya kanda.
Je, Serikali imejiandaaje sasa itakapofunguliwa Hospitali ya Kanda ya Kusini ambayo inajengwa Mtwara, kwamba huduma ya saratani pia itatolewa katika hospitali hiyo ili kuwapunguzia adha Wanamtwara kwenda Hospitali ya Ocean Road iliyopo Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Abdallah Chikota kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya na kwa kuwapigania wananchi wake wa Jimbo lake na Mkoa wa Mtwara katika masuala yote yanayohusiana na afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukizwa, siyo tu kisukari, lakini hata vilevile kiharusi, masuala ya pressure, magonjwa ya figo. Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga uwezo katika mnyororo wake wa utoaji wa huduma, sasa hivi tuko katika ngazi ya Wilaya lakini tunaendelea kuboresha kushuka katika ngazi ya vituo vya afya na mwisho tutashuka mpaka katika dispensaries.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba huduma za awali kwa magonjwa kama haya ya upimaji wa sukari, upimaji wa pressure, yote yanafanyika katika ngazi zote za mnyororo, lakini dawa kwa mfano, insulin ambazo zinahitaji utaalam zaidi zinapatikana katika ngazi ya Wilaya. Lakini tutaendelea kuboresha utaratibu huu kadri tutakapokuwa tunajenga uwezo katika mnyororo wetu wa utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza, je, Serikali itakuwa tayari kuanzisha huduma za saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ambayo inajengwa Mtwara. Kwa mujibu wa taratibu katika ngazi hiyo ya Rufaa ya Kanda, moja ya huduma ni pamoja na upatikanaji wa huduma za saratani. Kwa hiyo, pindi hospitali hii itakapokuwa tayari huduma hiyo nayo tutaiweka. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza naishukuru Serikali kwa kufanya tathimini ya ujenzi wa madaraja haya. Eneo hili ni muhimu sana kwa uzalishaji wa zao la korosho na wananchi wanapata shida kweli wakati wa kusafirisha korosho kupeleka mnadani. Sasa je, Serikali leo inatoa tamko gani kwamba ni lini ujenzi huu unaanza hata kama ni kwa awamu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kikwazo kikubwa cha ujenzi huu ni bajeti ndogo ambayo wamepewa TARURA. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha ambazo zinaenda TARURA ili ujenzi wa madaraja nchini uweze kwenda kwa kasi inayotakiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavo nimekiri kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba umuhimu wa madaraja haya haina ubishani; lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba ili kujenga madaraja haya kwa kiasi cha pesa kama tulivyotaja kwenye tathmini, bilioni 3.5 ni kiasi kingi cha fedha. Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge aiamini Serikali kwamba ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba changamoto hii inatatuliwa ipo kinachogomba ni bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anauliza uwezekano wa TARURA kuongezewa fedha ili iweze kufanya kazi kubwa. Jana nilijibu swali la nyongeza, kwamba ni vizuri pia tukazingatia kazi kubwa ambayo inafanywa na TANROADS na TARURA ndiyo tumeanza kuijenga, tuipe muda tuone namna ambavyo inatenda kazi kwa sababu pia itakuwa si busara kusema kiasi kingi cha fedha kitoke TANROADS kiende TARURA kwa sababu nao wana kazi kubwa ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza hapo hapo awali tulikuwa na chombo ambacho kilikuwa kinapitia hivi vitabu na vifaa vya elimu EMAC kabla ya kwenda mashuleni. Na kwa kuwa EMAC ilifutwa rasmi, sasa niulize Serikali ina mpango gani wa kuanzisha chombo kingine au chombo mbadala ambacho kitakagua vitabu na vifaa vya elimu kabla ya kwenda mashuleni? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni dhahiri kwamba sasa hivi kuna upungufu mkubwa sana wa vitabu kwa shule za msingi hasa darasa la kwanza mpaka la tatu; je, Serikali ina mpango gani wa haraka ili kutatua changamoto hii?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli Serikali ilivunja EMAC ambayo ni Education Management Approve Committee iliyokuwa inahusika na kupitisha machapisho na vitabu vya elimu baada ya chombo hicho kushindwa kutekeleza wajibu wake vizuri na tulishuhudia kwamba pamoja na kuwepo kwa chombo hicho, lakini bado vitabu vilikuwa na makosa mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba sasa hivi kazi ya kupitisha vitabu inafanywa na Taasisi ya Elimu Tanzania, lakini niseme kwamba Serikali itaangalia namna ya kuangalia utaratibu mwingine, baada ya kuondoa EMAC kwa sababu pia Taasisi ya Elimu inakuwa inaelemewa na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa vitabu, naomba nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba sasa vitabu vimekwishafanyiwa marekebisho na zaidi ya nakala 9,000 za vitabu vya kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu vimekwishasambazwa shuleni, kwa hiyo, sasa hivi tatizo hilo Serikali imekwishasambaza vitabu vilivyorekebishwa.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Changamoto ya maji ya Mji wa Handeni inafanana na Miji ya Nanyamba, Tandahimba na Newala, ambao wanategemea sana Mradi wa Makonde na hivi karibuni tuliwaambia miradi 17 financial agreement imeshasainiwa kwa mkopo kutoka Serikali ya India. Ningependa kupata kauli ya Serikali, je, ni nini kinaendelea baada ya kusainiwa ile financial agreement?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kabisa jinsi ambavyo amefuatilia sana kuhusu mkopo huu wa Serikali ya India pamoja na Mheshimiwa Mkuchika, kwa sababu wanajua kwamba wana-share kubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba, kuanzia jana shughuli imeanza, wataalam tumewaweka mahali maalum na katika muda wa siku 14 watakuwa wameshakamisha nyaraka ili hatua zingine ziendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa jibu fupi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa maeneo ya Makonde na Nanyamba, mwaka ujao wa fedha tunaanza utekelezaji wa huo mradi mkubwa tatizo la maji sasa litakuwa ni historia kwa maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa Mkoa wa Mtwara una vituo vingi sana vya kitalii, kwa mfano, ile beach ya Msimbati ambayo inaweza kuendesha gari, kuna Shimo la Mungu kule Newala, lakini vilevile Newala kuna Kituo cha Utamaduni wa Kimakonde na Mji maarufu wa asili Mikindani.
Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kutangaza vivutio hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika sehemu za Newala pamoja na Mikindani na maeneo mengine ya Mtwara yana vivutio vingi vya asili, maliasili na vitu vingi kwa kweli, hivi sasa naomba niseme tu kwamba tumechukua jitihada za kuhakikisha tunatangaza vyote kwa kushirikiana na Halmashauri zilizopo katika Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatangaza maeneo yote hayo na Mji wa Mikindani tutahakikisha kwamba tunautangaza ipasavyo kwa sababu una historia ndefu na nzuri ambayo nina uhakika watalii wengi watavutiwa kwenda kutembelea katika hilo eneo. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Changamoto za huduma za afya zilizopo Rorya zinafanana na Jimbo la Nanyamba. Naishukuru Serikali imetupa ujenzi wa vituo vitatu na kituo kimoja cha Dijecha ujenzi umekamilika. Je, ni lini Serikali italeta watumishi kwa sababu kituo kile kina watumishi saba na mahitaji ya sasa ni watumishi 41?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ridhaa yako, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata concern hii na kwa sababu tunajenga hivi vituo vya afya vipya 208 au tunaviboresha lengo letu kubwa ni ili viweze kufanya huduma ya upasuaji, tunajua tuna mahitaji makubwa ya wataalam. Hata hivyo, takribani wiki mbili zilizopita tumeshatangaza ajira zipatazo 6,180. Lengo kubwa ni kwamba watu wale tutakapowaajiri tuwapeleke katika vituo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, imani yangu Mheshimiwa Chikota wala asihofu kwa sababu Nanyamba vilevile ni miongoni mwa eneo ambalo tunalenga kuja kujenga Hospitali ya Wilaya tunajua mahitaji yatakuwa ni makubwa zaidi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba ni mpango wa Serikali wale watumishi 6,180 tutawagawanya maeneo mbalimbali lakini hata hivyo hatutaishia hapo itabidi tuongeze watumishi wengine kwa lengo la kuwasaidia Watanzania.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuulizwa maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tulitegemea kwamba baada ya kuanzisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ingekuwa Mkombozi wa mazao mengine ambayo hayana bodi, lakini kuna changamoto ya fedha kwenye bodi hii.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha nyingi za kutosha ili Bodi ya Nafaka na Mazao iweze kununua mazao mengine pamoja na mbaazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa soko la India limeonesha kulegalega na kwenye zao la korosho tulipoachana na soko la India tumeona kuna mafanikio baada ya kuja Waturuki na Wavietinam; Serikali ina mpango gani wa kuingia kwenye masoko mengine ili kuacha utegemezi wa soko la India?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge RAS Mstaafu na kaka yangu Mheshimiwa Chikota maswali yake madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kama Serikali ni kwamba tumeielekeza na kusisimamia Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko kwamba kuanzia sasa wajikite zaidi katika kufanya biashara ile ya kilimo cha ushindani. Tayari tumeshaanza kufanya mazungumzo na NSSF na mazungumzo hayo yamefanikiwa na tayari tumeshapata shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kununua mashine zile kwa ajili ya viwanda vya mahindi na alizeti kwa maana ya mashine mbili na tayari zimeshafika bandarini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili la nyongeza, ni kwamba ni vyema sisi kama Serikali; naomba niwaase Halmashauri zote nchini kwamba tutoe elimu kwa wakulima wetu kuweza kufanya kilimo cha kibiashara (commercial farming) kwa sababu unapokuwa kwenye commercial farming, utaweza kujua ulime kilimo cha aina gani? Mazao gani? Kwa bei gani? Utauza wapi? Kwa maana hiyo, hakutakuwa na hasara yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwamba mbaazi ni chakula kama vyakula vingine, tena ina protini zaidi kuliko maharage na inaongeza damu mwilini kuliko maharage. Vilevile nawaomba hata wale wanaofanya vyakula vya mifugo, ni kwamba hizi mbaazi zetu pia zinatumika vizuri sana katika vyakula vya mifugo kama ilivyokuwa soya. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D.CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa siku za nyuma Serikali ilijenga Vituo vingi vya Walimu (TRC) na kwa kuwa sasa hivi havitumiki kwa kukosa fedha, je, Serikali ina mpango gani wa kutumia sehemu ya fedha za elimu bure kupeleka kwenye Vituo vya Walimu ili ziendeshe semina kwa walimu hao katika maeneo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Abdallah Chikota kwa jinsi ambavyo anasimamia maendeleo kwenye Jimbo lake la Nanyamba na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla na hata kulisaidia Bunge zima na Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda nilichukue hili kama sehemu muhimu sana ya mchango wa mawazo mazuri na maoni Serikalini kwa ajili ya kulifanyia kazi. Ahsante.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kusuasua kwa ujenzi wa hospitali ya rufaa Mkoa wa Mwanza, kunafanana na kusuasua kwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini ambayo inajengwa Manispaa ya Mtwara. Sasa ningependa kujua Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ya rufaa Kanda ya Kusini ili ianze kutumika haraka iwezekanavyo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika jibu langu la swali la msingi kuna kiasi cha shilingi bilioni 10 ambazo zimetengwa mahususi kwa ajili ya kwenda kufanya ukarabati na kumalizia majengo ambayo tayari yalishaanzishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie na hasa baada ya kutenganisha kwamba hospitali za rufaa zinakuwa chini ya Wizara ya Afya, kasi itaongezeka tofauti na ambavyo mwanzo zote zilikuwa chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuondoa huu mzigo naamini ni rahisi sana kwa Wizara ya Afya, kusimamia na kuhakikisha kwamba hiyo hospitali ambayo ilishaanza kujengwa inakamilika kwa wakati.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba mkulima mdogo wa korosho hawezi kufanya hujuma hizi na hujuma hizi zinafanywa na makampuni makubwa na msimu wa korosho unatarajia kuanza mwezi wa tisa.
Kwa nini Serikali inakuwa na kigugumizi cha kuwataja makampuni hayo ili msimu ujao wasiingie katika soko la korosho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dada Hawa Ghasia, nimesema kwamba Serikali hatuoni na hatujapata kigugumizi chochote, ni kwamba tayari tume ya wataalam tumeshawasilisha ile taarifa ya uchunguzi kwenye vyombo vya dola, vinalifanyia kazi na mara tu ule uchunguzi wa uhakiki utakapofanyika na wa kina basi wote watatajwa na hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa. Ahsante.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Changamoto ya minara inayokabili Jimbo la Lulindi, inafanana na ile ya Jimbo la Nanyamba. Unapozungumzia mpaka wa Tanzania na Msumbiji ni pamoja na Kata ya Kitaya na Kilomba iliyopo katika Jimbo la Nanyamba; na Kampuni ya TTCL imepewa dhamana ya kujenga minara minane, katika Jimbo langu la Nanyamba; sasa nataka nipate kauli ya Serikali.

Je, ujenzi huo utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwenye Kata ya Kitaya na Kilomba Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) ilipewa tenda ya kufunga minara maeneo yale. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkandarasi tayari ameshaanza kukusanya vifaa kwa ajili ya kuvipeleka pale na hivi karibuni kazi itaanza; na ametuhakikishia kwamba ndani ya miezi sita, pale minara itakuwa imeshawekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni sambasamba na kwa Mheshimiwa Nape Nnauye kule Chiuta ambako wanahitaji mnara ili wananchi wa kule na wenyewe wawekewe mawasiliano.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kutimiza ahadi yake kupeleka gesi kwenye Kiwanda chetu cha Saruji cha Dangote. Pamoja na pongezi hizi, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na kupeleka gesi kwenye Kiwanda chetu cha Dangote, kuna viwanda vingine Mkoani Mtwara hususan viwanda vya kubangua korosho. Je, Serikali imejipangaje kupeleka gesi kwenye viwanda hivyo ili itumike katika shughuli za uzalishaji katika viwanda hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni kuhusu usambazaji wa gesi majumbani kwa sababu gesi inayozalishwa ni nyingi lakini matumizi ni kidogo. Je, Serikali imejipangaje kuongeza idadi ya watu watakaotumia gesi majumbani kwa Wilaya ya Nanyamba, Newala, Masasi na Mikoa mingine ili tutumie gesi yetu ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipokee pongezi zake kwa niaba ya Wizara baada ya kukamilisha ahadi yetu ya kumpelekea gesi Kiwanda hiki kikubwa cha Dangote kinachozalisha saruji. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Chikota kwa kazi nzuri anayofanya katika kufuatalia matumizi ya gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake mawili ya nyongeza anauliza ni lini Serikali itasambaza gesi katika viwanda ambavyo viko Mkoani Mtwara ikiwemo vya kubangua korosho. Napenda nimtaarifu Serikali yetu inatambua umuhimu wa gesi katika kuwezesha viwanda kuzalisha malighafi kwa kutumia gesi na ina mpango kabambe wa kusambaza gesi katika maeneo ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tuna viwanda zaidi ya 27 ambavyo vinatumia gesi na sasa hivi kuna mradi ambao unatekelezwa wa kusambaza gesi majumbani na viwandani na hasa maeneo ya Mtwara na Mkuranga. Hivi ninavyozungumza tayari TPDC imeshakamilisha mazungumzo na mkataba wa mauziano ya gesi ya viwanda vya KNAUF Gypsum Mkuranga na Lodhia Mkuranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye viwanda vya kubangua korosho, naomba niwataarifu wawekezaji wetu wote wenye viwanda katika ukanda huo ambao bomba la gesi limepita kutoka Mtwara kwamba fursa hiyo ipo, waje tu tuzungumze na TPDC. Serikali imejipanga katika uwekezaji huo na hata katika Mpango wa Matumizi ya Gesi kiasi cha trilioni 8 cubic fit zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya viwanda tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili alikuwa anauliza ni lini usambazaji wa gesi asilia majumbani utafanyika. Nataka nimtaarifu sasa hivi hata Waziri wetu Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani alizindua Mradi wa Usambazaji wa Gesi Asilia katika Mkoa Mtwara na Dar es Salaam. Kazi inayoendelea ni ununuzi wa vifaa mbalimbali na mpaka sasa vimeshanunuliwa vifungashio, vifaa vya kupunguza mgandamizo wa gesi, vifaa vya kupimia gesi majumbani. Vifaa vyote hivi vitakamilika ifikapo Mei, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kazi ya kusambaza gesi katika Mikao ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam inaendelea. Ahsante sana.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ujenzi huu wa reli utakuwa na maana sana endapo upanuzi wa Bandari yetu ya Mtwara utakuwa umekamilika. Kwa sasa hivi mpango ulikuwa ni kujenga gati tatu lakini kinachoendelea sasa hivi Bandari ya Mtwara ni ujenzi wa gati moja tu. Je, hizo gati mbili zilizobaki ujenzi wake utaanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ili reli hii itumike vizuri, tunatarajia hata Mkoa wa Lindi utumie vizuri Bandari ya Mtwara lakini barabara ya kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja imejengwa miaka 50 iliyopita. Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi mpya siyo ukarabati wa kuweka viraka viraka kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Chikota, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunashukuru kwa pongezi alizotupatia kutokana na jitihada mbalimbali ambazo Serikali inafanya kuhusu ujenzi wa reli kutoka Mtwara mpaka Mbambabay. Tunajua kwamba ili ujenzi wa reli hiyo uwe na tija, ni lazima tuanzie Mtwara kwenye bandari yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sasa hivi tumekwishaanza utekelezaji wa upanuzi wa Bandari ya Mtwara kwa awamu ya kwanza na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea na awamu ya pili na ya awamu ya tatu mpaka tutakapokamilisha upanuzi wa Bandari yetu ya Mtwara ili iwe ya kisasa kuweza kuhudumia mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua kuhusu upanuzi wa barabara ya Mtwara mpaka Mnazi Mmoja. Jibu lake ni kwamba mpaka sasa hivi tayari taratibu zote za kuanza ukarabati mkubwa wa barabara hiyo zimeshakamilika na tumekwishatangaza tenda hivi karibuni mkandarasi ataingia kazini kwa ajili ya kurekebisha barabara hiyo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kama alivyosema kwenye jibu lake la msingi kuna kiasi cha fedha kimetengwa katika bajeti ya 2019/2020; na kwa kuwa, barabara iliyojengwa kwa sasa imeishia Mnivata na kutoka Mnivata hadi Nanyamba ni kilometa 20; na kwa kuwa, kuna mkandarasi yuko pale.

Je, ni kwa nini sasa, bila kuathiri taratibu za manunuzi, kipande hicho asingepewa mkandarasi ili ajenge kwa kiwango cha lami hadi Nanyamba Mjini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Masasi kuna barabara pacha tunaita Barabara ya Ulinzi ambayo inakwenda mpaka Mahurunga, Kitaya, Mnongodi na Michenjele. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, ukizingatia sasa hivi kuna changamoto ya kiulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chikota, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Chikota kwa ushirikiano. Kwa kweli, mara zote nimefanya ziara mara nyingi sana kukagua barabara hii Mtwara – Mnivata, lakini muda wote Mheshimiwa Chikota alikuwepo na tumefanya kazi kwa pamoja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Chikota namshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kama ambavyo nimetoa jibu langu la msingi kwamba, harakati za ujenzi kwa maana ya shughuli za manunuzi zinaendelea ili kujenga kilometa 160 ambazo zimebakia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Chikota anafikiria kwamba, ili twende haraka ni kumruhusu mkandarasi aendelee kwa vile tulivyotenga fedha kidogo, lakini nimwombe Mheshimiwa Chikota avute subira na sisi mpango wetu ni kuhakikisha kwamba, tunafanya ujenzi wa haraka, ili wananchi wake kwenye Vijiji vya Malanje, Mnivata, Nanyamba, Mtimbwilimbwi, Mbambakofi, Mtopwa na majirani wa Tandahimba, Newala na kule Lulindi na Masasi waweze kupata huduma hii nzuri ya barabara.

Kwa hiyo, avute subira kwa sababu ziko taratibu za manunuzi zinafuatwa, sasa mkandarasi huyu kama ataomba na atakuwa na sifa basi anaweza akapewa, ili aanze kukamilisha upande ambao ameutaja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara pacha, hii barabara ya ulinzi kilometa 310; nimeitembelea baadhi ya maeneo katika sehemu hii ili kuona kwamba, tunafanya maboresho makubwa katika maeneo ambayo ni korofi, maeneo ambayo yanahitaji madaraja na makalavati. Kwa hiyo, cha kwanza ni kuhakikisha kwamba, tunaifanyia maboresho makubwa barabara hii kuhakikisha inapitika, kwa sababu ni muhimu sana katika shughuli za uchumi, lakini na za ulinzi.

Mheshimiwa Spika, sasa tutakwenda kwa kufuata vipaumbele. Tukimaliza barabara hii ambayo nimeitaja tutakwenda kuitazama sasa Barabara ya Ulinzi, ili iweze kuwasaidia wananchi wanaoishi maeneo haya. Ahsante sana.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti ukiangalia hiyo takwimu utajua wazi kwamba bado kiwango chetu cha ubanguaji ni kidogo kwa sababu msimu wa 2017/2018 Tanzania tulifikisha mavuno ya korosho Tani 312,000, kwa hiyo kinachobanguliwa ni kiasi kidogo sana. Sasa kwa kuwa Mkoa wa Mtwara na Lindi wameshatenga maeneo ya uwekezaji hususani viwanda vya korosho, je, Serikali itatoa vivutio maalum ikiwemo kufuta baadhi ya kodi ili wawekezaji hawa waje Mikoa ya Mtwara na Lindi kuwekeza Viwanda hivyo vya Korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mavuno ya korosho hutegemea sana upatikanaji wa pembejeo na niipongeze Bodi ya Korosho kwa sababu wale wakulima ambao hawajalipa fedha zao za korosho inatoa mkopo, lakini kuna urasimu mkubwa sana wa kupata hiyo pembejeo. Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa badala ya mkulima kuzaminiwa na AMCOS na Serikali ya Kijiji na Mkurugenzi waondoe huo mlolongo mrefu ili wakulima wadhaminiwe na AMCOS na kupewa hiyo sulfur (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa jitihada kubwa anayofanya katika kufatilia juu ya maendeleo mazuri ya zao hili la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusiana na kuweka vivutio kwa ajili ya uwekezaji kimsingi Serikali imekuwa ikifanya hivyo hasa kwa viwanda vyote ambavyo vinatumia malighafi inayozalishwa hapa nchini; na hivi karibuni tumeshuhudia kwamba kodi zimeondolewa kwa ajili ya kuwezesha viwanda hivyo viweze kufanya kazi. Hali kadhalika tunajaribu kuendelea kuona kwamba vile Viwanda ambavyo vilikuwa kwa siku za nyuma vinabangua korosho lakini kwa sasa vimekuwa havibangui na vitaendelea kuwa kama maghala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunajaribu kuwaunganisha sasa na Wawekezaji wengine ili waweze kutumia viwanda hivyo katika kuwekeza mashine na waweze kubangua korosho pasipo kulazimika kuanza kujenga upya pamoja na maeneo hayo ambayo yametengwa. Niupongeze sana Mkoa wa Lindi wa Mtwara kwa jitihada ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la pili, kuhusu pembejeo suala lake alivyolizungumza nimelisikia. Niseme tu kwamba tungependa zaidi kuona kwamba pembejeo hizo kwa wale wanaoagiza na kuzileta waweze wao wenyewe kuziuza kwa kulingana na uhalisia wa maeneo kuliko tu kutegemea kwamba Serikali yenyewe iwe inaingilia halafu badala yake pengine kutokuwa na usimamizi unaotakiwa. Hata hivyo mawazo yake tunayachukua na yataendelea kufanyiwa kazi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika mipango yetu ya Halmashauri ya Mji wa Nanyamba kuna vijiji tumeviacha kwa sababu vipo jirani na mradi huu na sasa hivi havijapangiwa mradi wowote. Sasa napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwa kuwa amesema marekebisho yatafanywa wakati Mtaalamu Mshauri atakapopatikana, je, Serikali ipo tayari kutoa meelekezo maalum kwa Mtaalam Mshauri ili vijiji 20 vikiwemo Maembe Chini, Maembe Huu, Kiromba na vijiji viingizwe kwenye mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kuhusu utekelezaji wa mradi. Ni muda mrefu sasa Serikali inasema inatafuta fedha, je, haioni muda umefika sasa hivi kutekeleza mradi huu kwa kutumia fedha za ndani? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chikota, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeweka mwongozo sasa hivi ambao unaeleza waziwazi kwamba vijiji vyote vilivyoko kwenye vyanzo vya maji ndivyo vitapata huduma ya maji kwanza wakati wa kutekeleza mradi. Pili, kila linapopita bomba la maji kilomita 12 pande zote za bomba hilo la maji vijiji vilivyo pembeni vitapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vijiji alivyosema Mheshimiwa Mbunge, kwanza, tuna mpango wa kupeleka maji vijiji, kwa mfano, Maembe Chini na Maembe Juu, Kirombo, Kirombo Chini, Mchanje na Mji Mwema. Vijiji vyote hivi pamoja na vijiji 14 vitapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza, je, Serikali tusianze mradi huu kwa kutumia pesa za ndani. Mradi huu gharama yake ni kubwa, kama nilivyosema ni shilingi bilioni 400. Wizara ya Maji bajeti yake takribani ni shilingi bilioni 673. Kwa kutumia pesa za ndani maana yake miradi yote sasa itashindwa kutekelezwa. Kwa hiyo, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi tunahakikisha kwamba tunatafuta pesa hiyo ili mradi huo uweze kuanza mara moja.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Wizara, napongeza viongozi wa Wizara hii; Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wamekuwa wakifanya safari nyingi kuja Mtwara ili kukabiliana na changamoto za hospitali hii. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa imeonekana hali ni tete kwa sababu hospitali yetu ya Rufaa ina Daktari Bingwa mmoja tu, sasa ningependa kujua kwamba: Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi kuhakikisha kwamba tunapata angalau Madaktari Bingwa watatu kwa kipindi hiki ambacho tunasubiri hao ambao wameenda vyuoni wahitimu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri kama alivyojionea alivyotembelea hivi karibuni Ligula kwamba majengo mengi yamechakaa yanahitaji ukarabati: Je, Wizara ina mpango gani kuyakarabati majengo hayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Abdallah Chikota, Mbunge ambaye naye anatoka Mtwara kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya, lakini katika ufuatiliaji wa karibu katika masuala mbalimbali ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusudio la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora za afya katika mikoa yote nchini na ndiyo maana Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa kuhamisha Hospitali za Rufaa za Mikoa kuja chini ya Wizara ya ili ziweze kupata usimamizi wa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuweza kujibu swali lake la kwanza, ni mikakati gani ambayo tunayo ya muda mfupi kuhakikisha kwamba tunapata hizi huduma za kibingwa, nimeeleza katika jibu langu la msingi kwamba katika hiki kipindi cha mpito, Wizara kwa kushirikiana na Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wamekuwa wanaendesha kambi mbalimbali za huduma za udaktari bingwa katika baadhi ya mikoa na tumekuwa na mizunguko hiyo ili kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo hayana huduma hizo kwa sasa zinaweza kufikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wale madaktari ambao wanamaliza sasa hivi,tumeweka utaratibu wa kuwafanyia kitu kinaitwa borning kwamba daktari ambaye amesoma kwa fedha za Serikali, atapangwa pale ambapo Serikali itamhitaji kwa kuwa ametumia fedha za Serikali na kwa chini ya utaratibu huo, madaktari ambao tunawapanga sasa hivi kwa sababu tumefanya tathmini ya Ikama, basi tutawapeleka katika maeneo ambayo wanahitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tumefanya tathmini ya kina ya miundombinu ya uchakavu wa majengo katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa na sasa hivi tumeanza kujielekeza kama Wizara katupitishia fedha ambazo ziko kwenye bajeti kufanya ukarabati mkubwa, nami nilikuwa pale Ligula tunafanya ukarabati wa jengo la bima, tumefanya ukarabati wa corridor, tunataka tukamilishe ile wodi ya grade one na vile vile tunataka sasa kuhamisha ile majengo ya theatre ili wananchi wa Mkoa wa Mtwara waweze kupata huduma nzuri na yenye ubora.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa ambalo tunataka tulifanye sasa Mtwara ili kufuta kilio cha wananchi wa Mtwara cha muda mrefu, kusudio la Serikali ni kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini.