Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abdallah Dadi Chikota (17 total)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa wana majukumu mengi ikiwemo kuhakikisha amani na usalama katika maeneo yao:-
Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho ya mwezi ya Wenyeviti hawa ili kutoa motisha kwa kazi yao?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa katika kusimamia shughuli za Maendeleo Nchini. Katika kuzingatia uzito huo wa majukumu, Serikali imeweka utaratibu wa kila Halmashauri kurejesha katika Vijiji na Mitaa asilimia 20 ya mapato ya ndani ambapo sehemu ya fedha hizo zinatakiwa kulipa posho ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kuwa baadhi ya Halmashauri hazipeleki fedha hizo katika Vijiji na Mitaa na hivyo kuwanyima haki Viongozi hao kulipwa posho zao. Changamoto kubwa ya Halmashauri ilikuwa ni makusanyo yasiyoridhisha ya mapato ya ndani ambayo yalisababisha kushindwa kulipa posho hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia sasa Serikali inaimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ambapo imethibitika kuongeza makusanyo kwa zaidi ya asilimia mia moja. Kwa njia hiyo, Halmashauri zitakuwa na uwezo wa kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa ambao sote tunatambua mchango wao mkubwa katika Taifa hili wa kuhamasisha shuguli za maendeleo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI, itaendelea kusimamia suala la makusanyo ya mapato ya ndani kwa nguvu zake zote ili kujenga uwezo wa Halmashauri kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Kampuni ya BG-EXXON MOBIL, OPHIR na washiriki wenzao wako tayari kuanza ujenzi wa LNGPlant.
(a) Je, ni nini kinachokwamisha kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo?
(b) Je, ni hatua gani za makusudi zinachukuliwa ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG) ulibuniwa mwaka 2014 kufuatiwa ugunduzi wa gesi asilia nchini ambao umetoka katika bahari ya kina kirefu. Mradi huo unatekelezwa katika na kampuni za kimataifa ya Statoil ya Norway, BG ya Uingereza, Exxon Mobil ya Marekani pamoja na Ophir ya Uingereza. Kampuni nyingine Pavilion ya nchini Singapore pamoja na shirika la TPDC ambalo ni la Serikali hapa nchini. Kutokana na umuhimu wa wa mradi huo katika kujenga uchumi wa gesi asilia nchini Serikali inachukua hatua za utekelezaji wa mradi kwa awamu tofauti. Lakini Serikali inachukua tahadhari muhimu sana katika kuandaa mradi huu.
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri. Hatua zilizofikiwa kwa sasa ni pamoja na kupata eneo la LNG litakalojengwa kwa umbali wa kilometa 2,000 na katika eneo lingine ambalo litakamilika mpaka 2020.
Mradi huu unatekelezwa kama nilivyosema na TPDC ambapo kufikia mwaka 2015 Serikali ilikabidhi TPDC hatimiliki ya eneo ambalo kwa sasa tafiti mbalimbali za kihandisi, kijiolojia, kimazingira na kijamii zinaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya mikataba mbalimbali yameanza baada ya Serikali kukamilisha uundaji wa timu ya kufanya majadiliano (government negotiating team). Majadiliano kati ya government negotiationteam yameanza na yatakamilika mwezi Septemba mwaka huu. Mahojiano hayo pamoja na mambo mengine yanafanya pia ifikapo mwaka 2020 kukamilika kwa ufasaha kabisa. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini hukutana na wawekezaji hao kila baada ya miezi mitatu ili kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa mradi huu.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu ya mkononi kwenye Kata za Mbembaleo, Nyuundo, Mnima na Kiyanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Mbambakofi, Mwamko na Mwang’anga kutoka katika Kata ya Mbembaleo, vijiji vya Namahukula, Namambi na Namgogoli kutoka katika Kata ya Mnima na vijiji vya Mkahara, Mnongodi, Mwamko na Tulia kutoka katika Kata ya Kiyanga vimo katika orodha ya vijiji vitakavyopata huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa awamu ya pili na awamu ya tatu ya mradi wa mawasiliano ya Viettel (Halotel).
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa awamu ya pili na awamu ya tatu ulioanza Novemba, 2015 na unategemewa kukamilika Novemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Kata ya Nyuundo vimeainishwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na vitaingizwa katika miradi ya siku za usoni kwa kadri ya upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi zitakavyopatikana.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Zao la korosho linakabiliwa na changamoto kadhaa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Chuo cha Utafiti wa Kilimo – Naliendele kinapanuliwa ili kiweze kufanya tafiti mbalimbali za magonjwa yote ya korosho badala ya sampuli kupelekwa nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Utafiti Naliendele ni kituo mahiri cha kufanya utafiti wa kugundua na kutathmini aina bora za korosho zinazotoa mavuno mengi na zinazopendwa katika soko. Vilevile kituo kinafanya utafiti kuhusu mbinu bora za uzalishaji, magonjwa na wadudu wanaoshambulia korosho na utafiti wa kuongeza thamani ya zao la korosho. Pia ni kituo cha kwanza Afrika kutoa mbegu bora za korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naliendele ilipeleka sampuli za korosho nje ya nchi ili kupata ufafanuzi kama vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa ukungu au blight ni aina moja au tofauti. Ufafanuzi wa aina hii wa aina za vimelea utasaidia kuweza kupata viatilifu vya ugonjwa huu. Maabara za nje ya nchi ni maalum (specialized laboratories) ambazo hufanya uchunguzi wa magonjwa ya mazao mbalimbali ikiwemo zao la korosho kutoka katika nchi tofauti. Maabara za aina hizi ni ghali kuendesha hivyo kuwa na maabara ya aina hii hapa nchini itakuwa ni hasara kwa vile matumizi yake yatakuwa chini yaani underutilized ukilinganisha na fedha zitakazotumika kujenga na kutunza maabara hiyo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA Aliuliza:-
Je, ni lini Mfumo wa Taarifa za Watumishi LAWSON utaboreshwa na kuondoa dosari zilizopo sasa hivi kama vile watumishi wa Umma kuondolewa kwenye makato ya mikopo wakati hawajakamilisha malipo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management Informaton System) au kwa version nyingine ya LAWSON Version 9 unaotumika sasa kwa ajili ya kukusanya taarifa za kiutumishi na malipo ya mishahara ulianza kutumika mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mfumo huu una changamoto ambazo zinasababisha watumiaji wasio waadilifu kuutumia vibaya kinyume na utaratibu ikiwemo kusitisha makato ya mkopo kabla mkopo wote haujamalizika kulipwa. Hii ilibainika kutokana na kaguzi za mara kwa mara zinazofanywa na Serikali ambapo hadi sasa watumishi wa aina hiyo wapatao 65 kutoka katika mamlaka za ajira 32 wamechukuliwa hatua mbalimbali baada ya kugundulika kuwa wametumia vibaya dhamana walizokabidhiwa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii, Serikali inaendelea na hatua za kuhamia kwenye toleo jipya la mfumo huu (LAWSON Version 11) ambao unatarajia kuwekwa mifumo zaidi ya udhibiti ili kuhakikisha kwamba maafisa wenye dhamana ya usimamizi wake hawafanyi
mabadiliko yoyote bila kugundulika.
Mheshimiwa Spika, usanifu wa mfumo huu ili kuweza kuhamia katika toleo jipya la LAWSON Version 11 unaendelea ambapo wataalam wetu wa Wakala wa Serikali Mtandao (EGA) ndio wamepewa jukumu la kusimamia usanifu na usimikaji wake. Baada ya maboresho haya miundombinu madhubuti ya kuzuia matumizi mabaya ya mfumo itaimarishwa.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Watendaji wa Vyama vya Msingi vya Mazao (AMCOS) wanapatikana kwa njia ya ushindani na wanakuwa na sifa zinazostahili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatayo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuwapata Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao na Masoko (AMCOS) upo kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 pamoja na Kanuni za Ushirika za mwaka 2015. Utaratibu umeelekezwa kwa mujibu wa kifungu cha 134 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika katika Jedwali la Pili, vifungu vya 14, 15, 16 na 18 kuwa panapotokea nafasi za kazi za Watendaji wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote, vikiwemo vile Vyama vya Ushirika vya Mazao na Masoko, nafasi hizo hutangazwa kwa wananchi kwa muda wa siku 30 ili waombe nafasi hizo kwa ajili ya ushindani.
Mheshimiwa Spika, sifa zinazotakiwa kwa waombaji wa nafasi za Watendaji wa Vyama vya Msingi vya Ushirika, vikiwemo Vyama vya Msingi vya Mazao na Masoko ni kama ifuatavyo; kiwango cha elimu kuanzia kidato cha nne; uelewa wa lugha za kiswahili na kiingereza; uwezo wa kufundishika; majina na anuani za angalau wadhamini wawili (referees); aina ya biashara na shughuli inayofanywa na mwombaji na taarifa nyingine yoyote inayohusika kutoka kwa mwombaji. Hivyo, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania inahakikisha kuwa Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao na Masoko wanapatikana kwa njia ya ushindani na wanakuwa na sifa zinazostahili kama zilivyotajwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.
MHE. ABBDALAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za kuzalisha korosho zinazosababishwa na pembejeo kuuzwa kwa bei ya juu.
Je Serikali ina mpango wa kutoa mikopo midogo midogo kwa wakulima wa korosho ili waweze kumudu gharama hizo?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima ikiwemo ruzuku ya kununua viuatilifu vya zao la korosho. Lengo la kutoa ruzuku hizo ni pamoja na kuwapunguzia wakulima gharama ya bei ya soko ya pembejeo hizo ambazo zinachangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoa ruzuku ya pembejeo, Serikali pia imeanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumiwa kuuzia korosho, utaratibu ambao umesaidia kupata soko la uhakika na kuongeza bei ya korosho kutoka shilingi 2,900 kwa kilo moja msimu wa mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi 4,000 kwa kilo moja msimu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, kupitia Tume ya Ushirika, Serikali imeandelea kuwahimiza wakulima kujiunga kwenye vyama vya ushirika na vikundi vya wakulima ili kurahisisha kupata mikopo itakayo wawezesha kumudu gharama za uzalishaji. Aidha, mwaka 2015 Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ambayo inatoa mikopo ya muda mfupi miaka miwili, muda wa kati miaka miwili hadi mitano na muda mrefu miaka mitano hadi miaka 15 kwa wakulima, kwa riba nafuu ya kati ya asilimia nane hadi asilimia 12. Benki hii imeendelea kutoa elimu ya mikopo kwa wakulima, kwa hali hiyo napenda kuwashauri wakulima kote nchini kupitia vyama vya ushirika na vikundi kutumia fursa hiyo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Ili kuleta mapinduzi ya kweli ya kilimo, ujuzi na maarifa ya wataalam wa kilimo unatakiwa uwafikie wakulima mara kwa mara.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani wa kutosha na kuwapeleka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa baada ya uteuzi, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyoonesha juu yangu, wananchi wa Wilaya ya Newala na kwa hakika wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara, wamepokea uteuzi wake kwa shangwe kubwa. Na mimi nataka nichukue nafasi hii kumuahidi Rais nitatekeleza majukumu yangu ya kumsaidia bila upendeleo wala woga na siku zote nitamuomba Mwenyezi Mungu anisaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuleta mapinduzi ya kweli ya kilimo, ujuzi na maarifa ya watalaam wa kilimo unatakiwa uwafikie wakulima mara kwa mara. Serikali imekuwa ikitoa vibali vya ajira za Maafisa Ugani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kila mwaka wa fedha kutegemea uwezo wake wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2013/2014 hadi 2016/2017 jumla ya Maafisa Ugani 5,710 waliajiriwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimwa Mwenyekiti, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani 1,487. Aidha, Serikali itaendelea kutoa nafasi za ajira kwa Maafisa Ugani kadri ya mahitaji na uwezo wa bajeti.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, ni lini Mfumo wa EPICOR, LGMD na ule wa LAWSON iliyopo kwenye halmashauri itaanza kuwasiliana na si kuwa stand alone system kama ilivyo sasa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo hii; ule wa Usimamizi wa Fedha za Umma (Intergrated Financial Management Systems – IFMS) au EPICOR, Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management Information System) au Lawson na Mfumo wa Ukusanyaji Takwimu za Utoaji Huduma (Local Government Monitoring Database) ilinunuliwa kwa nyakati tofauti kutegemeana na teknolojia iliyokuwepo wakati huo na kwa madhumuni tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na teknolojia zake, ni kweli mifumo hiyo ilikuwa haiingiliani au kubadilishana taarifa (automatic data exchange). Hali hii imesababisha kuwepo kwa changamoto ya kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na usimamizi. Gharama hizi ni pamoja na mafunzo kwa watumiaji, leseni za mifumo, ununuzi wa mitambo na vifaa pamoja na gharama nyingine za uendeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa mifumo hii inaunganishwa ili kuleta ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa sasa teknolojia imekuwa na pia uwezo wa Serikali kiutaalam umeongezeka hususan baada ya kuanzisha Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) na Idara/ Vitengo vya TEHAMA katika Ofisi za Serikali kuanzia miaka ya 2010.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa mifumo hii inawasiliana hatua zifuatazo zimechukuliwa:-
(a) Kuandaa miongozo ya viwango (technical specifications) kwa kuzingatiwa wakati wa kusanifu, kujenga na kuimarisha au kuhuisha mifumo kwa lengo la kufanya maandalizi ya kuunganisha na kuimarisha.
(b) Kutengeneza mfumo maalum wa ubadilishanaji taarifa kutoka mifumo mbalimbali.
(c) Kuweka miundombinu ya TEHAMA ambapo mtandao mkuu wa mawasiliano Serikalini ambapo taasisi, tumeziorodhesha 72 za Serikali, Wizara 26, Wakala wa Serikali 29, Idara zinazojitemea 17 zilizopo Dar es Salaam, Dodoma na Pwani. Aidha, Serikali imeunganisha katika mtandao huu taasisi za Serikali zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 77, Sekretarieti za Mikoa 20, Halmashauri za Majiji, Miji, Wilaya 38 na Hospitali za Mikoa 19 kwa lengo la kuwezesha kuunganisha mifumo inayotumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kulingana na mpango kazi uliopo kazi iliyobaki ya kuunganisha mifumo mbalimbali ndani ya Serikali, ikiwemo mifumo hii mikuu inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari ambapo matibabu yake ni ya muda mrefu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa dawa za ugonjwa wa kisukari bure kama ilivyofanya kwa ugonjwa wa kifua kikuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya ya mwaka 2007 inatambua uwepo wa wagonjwa wasio na uwezo wa kuchangia gharama za huduma za afya ikiwa ni pamoja na wale waliokuwepo katika makundi maalum ya kijamii, wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 60 ambao hawana uwezo wa kipato, watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, watoto walio katika mazingira hatarishi, wanawake wajawazito na watu wasiojiweza kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kundi hili pia wapo wagonjwa wenye magonjwa sugu kama saratani, wanaoishi na virusi vya UKIMWI, kisukari, magonjwa ya moyo, pumu, selimundu, kifua kikuu, ukoma na magonjwa ya akili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wataalam wa Ugonjwa wa Kisukari Nchini, inaendesha Programu ya Kitaifa ya Kisukari ambayo inajulikana kama National Diabetic Program, ambapo imeanzisha vituo vya matibabu ya kisukari vipatavyo 169 katika Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Aidha, jumla ya madaktari na wauguzi 1,925 wamepatiwa mafunzo maalum ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa kisukari. Lengo ni kuwapatia wagonjwa wote wa kisukari huduma bora na za bure za matibabu kama ilivyoainishwa katika Sera ya Taifa ya Afya. Hadi hivi sasa Serikali imetoa matibabu na dawa ya bure kwa wananchi wapatao 5,386.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko katika mchakato wa kuainisha idadi na mahitaji ya wagonjwa wa kisukari nchini. Pindi kazi hii itakapokamilika Serikali itatoa mwongozo utakaosimamia vizuri zaidi matibabu ya wagonjwa wa kisukari nchini.
MHE. HAWA A. GHASIA (K.n.y MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA) aliuliza:-
Wadhibiti wa Ubora wa Elimu ngazi ya Wilaya wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa vitendea kazi.
• Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia changamoto za ofisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yao?
• Je, ni lini Wizara itapeleka Wadhibiti Ubora wa Elimu katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba badala ya kutegemea wale wa Halmashauri ya Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule kama chombo cha udhibiti wa ubora wa elimu. Kutokana na ongezeko la Halmashauri na Wilaya mpya nchini, kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika idara hii ikiwemo upungufu wa Wadhibiti Ubora wa Shule, ofisi na vitendea kazi kama vile magari. Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo ununuzi wa magari, ujenzi na ukarabati wa ofisi pamoja na kuongeza idadi ya wadhibiti ubora wa shule.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imehuisha mfumo wa udhibiti ubora wa shule ambapo kiunzi cha udhibiti ubora wa elimu kimeandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wadau mbalimbali wa elimu ili washiriki kikamilifu katika kusimamia ubora wa elimu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa idara ya udhibiti ubora wa shule inajengewa uwezo ili itimize majukumu yake kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Nanyamba ni miongoni mwa Halmashauri ambazo hazijafunguliwa ofisi ya udhibiti ubora wa shule. Katika kukabiliana na hii, Serikali imepanga kuanzisha huduma ya udhibiti ubora wa shule katika Halmashauri zote nchini ambazo hazijafunguliwa ofisi, ikiwemo Nanyamba pindi zoezi la kuongeza Wadhibiti Ubora wa Shule litakapokamilika.
Mheshimiwa Spika, aidha, nasisitiza kuwa Wadhibiti Ubora wa Shule waliopo katika Halmashauri mama waendelee kudhibiti ubora wa shule katika Halmashauri hizo mpya wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kuanzisha huduma hii katika Halmashauri hizo. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Hivi karibuni Serikali ilikusanya vitabu vyenye dosari vilivyosambazwa shule za msingi nchini.
i. Je, Serikali imepata hasara kiasi gani kutokana na dosari hiyo?
ii. Je, ni hatua zipi zimechukuliwa kwa waliosababisha hasara hizo?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali imeondoa vitabu ambavyo vilikuwa shuleni ambavyo vilisambazwa mwaka 2017 ambavyo vilibainika kuwa vina makosa. Katika utekelezaji wa hatua hiyo Serikali ilizingatia taarifa ya tathimini iliyofanyika kuhusu vitabu hivyo na taarifa hiyo iliainisha vitabu vilivyokuwa na makosa ya kimaudhui na vile ambavyo havikuwa na makosa ya kimaudhui. Vitabu ambavyo vimeondolewa shuleni ni vile ambavyo vina makosa ya kimaudhui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania limeiagiza Menejimenti ya Taasisi kupitia vitabu vyote vilivyoondolewa shuleni na kufanya tathimini ya ukubwa wa makosa ili hatimaye kukokotoa hasara iliyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania iliwasimamisha kazi watumishi 29 ili kupisha uchunguzi wa chanzo cha dosari mbalimbali za vitabu. Uchunguzi huu umefikia hatua ya watumishi hao kuandikiwa mashitaka ya kinidhamu ambapo yakithibitika hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Wakulima wa mbaazi Mikoa ya Mtwara na Lindi wameshuhudia kuporomoka kwa bei katika msimu wa mwaka huu pamoja na kwamba walihamasika kulima kwa wingi.
(a) Je, ni nini kilisababisha kuporomoka kwa bei ya mbaazi?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha hali hiyo haijitokezi msimu ujao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli bei ya mbaazi iliporomoka kutoka wastani wa bei ya shilingi 2,750 kwa kilo mwaka 2014/2015 hadi shilingi 700 kwa msimu wa mwaka 2016/2017 na kufikia wastani huo na katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Hali hii imesababishwa na ongezeko la uzalishaji wa mbaazi katika nchi za India, China, Brazil, Myanmar, Canada, Msumbiji, Sudan na Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ongezeko hilo la uzalishaji, mwezi Agosti, 2017 nchi ya India ambayo ndio wanunuzi wakuu wa mbaazi zetu ilizuia uingizaji wa mbaazi kutoka nje ya nchi hiyo kwa kuwa walikuwa na uzalishaji mkubwa wa kukidhi mahitaji yao na hivyo kusababisha ukosefu wa soko la uhakika kwa mbaazi zilizozalishwa nchini msimu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika, Serikali imeandaa mikakati mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao hususan mbaazi. Mikakati ya muda mfupi ni pamoja na Wizara kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwamba itaongeza idadi ya mazao yatakayonunuliwa ambayo ni pamoja na mazao ya jamii ya mikunde (mbaazi, choroko na dengu), mbegu za mafuta (ufuta, alizeti na karanga) na nafaka kwa (mtama, ulezi na uwele) katika mwaka 2018/2019. Kwa sasa bodi hiyo imepata soko la tani 100,000 za soya, tani 20,000 za ufuta na tani 3,500 za mbaazi ambazo zitauzwa kwa wadau ndani ya nje ya nchi. Pia itanunua tani 6,000 za alizeti kwa ajili ya kukamua mafuta katika kiwanda chake kilichopo Kizota, Jijini Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati mwingine wa muda mfupi ni kuuza zao la mbaazi katika soko la bidhaa kwa maana ya commodity exchange na kuhamasisha utumiaji wa mbaazi hapa nchini katika maeneo mbalimbali hususan katika mashule na majeshi yetu (Magereza na JKT). Aidha, Serikali kupitia Maafisa Lishe waliopo katika Halmashauri zote nchini, watatoa mafunzo ya namna bora ya kuandaa vyakula vinavyotokana na mbaazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya muda mrefu ni pamoja na kampuni kutoka India kujenga Kiwanda cha kiitwacho Mahashree Agro Processing Ltd kitakachosindika aina zote za mazao jamii ya mikunde, korosho na ufuta katika Kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mkambarani, Wilayani Morogoro kitakachokuwa na uwezo wa kusindika tani 200 za aina mbalimbali ya mikunde kwa siku na kuuza katika soko la ndani na nje. Kiwanda hicho kitasaidia wakulima kupata bei nzuri na soko la uhakika mara kitakapoanza uzalishaji mwaka 2019.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Je, ni lini kiwanda cha Saruji cha Dangote kitapewa gesi asilia na TPDC?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petrol Nchini (TPDC) imekamilisha kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kupeleka gesi asilia katika mitambo ya kuzalisha umeme wa muda katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote umbali wa mita 100 kutoka katika Toleo la Kwanza la Gesi (Block Valve Station No. 1).

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ya mradi wa kuwezesha matumizi ya gesi kuzalisha umeme kwa Kiwanda cha Dangote ilikamilika na kuanza kufanya kazi Agosti, 2018 ambapo hadi kufikia Aprili, 2019, Kiwanda cha Dangote kimeanza kutumia wastani wa futi za ujazo milioni tano kwa siku kwa kuzalisha umeme.

Awamu ya pili ya mradi inahusu ujenzi wa miundombinu ya bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka BVS 1 kwenda kwenye Kiwanda cha Dangote, umbali wa kilimita 2.7 kwa ajili ya kuwezesha gesi asilia kutumika kama nishati ya kuchoma malighafi ya kuzalisha saruji. Jumla ya gharama za mradi ni shilingi bilioni nane na milioni mia mbili. Awamu ya pili ya mradi ilikamilika Desemba, 2018 na sasa Kiwanda cha Dangote kinatumia gesi ya wastani wa futi za ujazo milioni 15 hadi 20 kwa siku kwa ajili ya uzalishaji wa saruji.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Ujenzi wa Barabara ya Mtwara – Newala – Masasi (kilometa 210) umeanza kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara hadi Mnivata (kilometa 50).

Je, Serikali ina mpango gani kwa kilometa 160 zilizobaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara yote ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi, kilometa 210, pamoja na Daraja la Mwiti ulikamilika mwaka 2015. Mpango wa Serikali ni kujenga barabara yote kwa kiwango cha lami kwa awamu. Awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya Mtwara – Mnivata, kilomita 50, ambayo utekelezaji wake hadi kufikia Desemba, 2019 ulikuwa asilimia 76. Jumla ya shilingi bilioni 3.4 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.

Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami kwa kilometa 160 zilizobaki pamoja na Daraja la Mwiti utaanza katika mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

(a) Je, Viwanda vilivyopo nchini vina uwezo wa kubangua korosho kiasi gani?

(b) Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuongeza ubanguaji wa korosho?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota Mbunge wa Nanyamba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa sasa Tanzania ina jumla ya Viwanda vikubwa vya kati na vidogo vya kubangua korosho vipatavyo 34 ambavyo vikubwa na vya kati ni 18 na vidogo ni 16. Viwanda 18 vikubwa na vya kati vina uwezo uliosimikwa (installed capacity) wa kubangua tani 63,400 kwa mwaka na 13 kati yake vinafanya kazi. Viwanda vidogo ni 16; tisa kati yake vinafanya kazi na vina uwezo wa kubangua tani 9,610 kwa mwaka. Viwanda vyote 34 vya korosho vina jumla ya uwezo uliosimikwa wa kubangua tani 73,010 kwa mwaka na uwezo unaotumika kwa sasa ni tani zisizozidi 50,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imehamasisha sana sekta binafsi kuanzisha viwanda vya kubangua korosho, ambapo imefanikiwa kuwabadilisha wafanyabiashara wakubwa watatu wa kuuza korosho ghafi kujenga viwanda vya kubangua korosho. Wafanyabiashara hao ni Al Andalus Company Mnazi Mmoja Lindi, Mkemi Agrix Company na Fuzzy International Company vyote vya Mkuranga, Pwani. Pamoja na jitihada hizo, pia tumefanikiwa kupata mwekezaji mmoja Mkoani Mtwara yaani Yalin Company Limited ambaye Kiwanda chake kiliwekewa Jiwe la msingi na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Aprili, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hicho kinatarajia kuanza kubangua tani 6,000 na kitaendelea na kuongeza uwezo wake mpaka kufikia tani 10,000 kwa mwaka. Aidha, Kiwanda hicho chenye teknolojia ya Kisasa kinatarajia kutoa ajira zipatazo 250.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Wizara ya Maji ilikubali kurekebisha mchoro wa Mradi wa Maji kutoka Mto Ruvuma hadi Mtwara ili vijiji vingi vya Halmashauri ya Nanyamba vipate maji toka Mto Ruvuma:

(a) Je, marekebisho hayo yamefikia hatua gani?

(b) Je, ni vijiji vingapi vya Halmashauri ya Mji wa Nanyamba vitanufaika na mradi huo

(c) Je, ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilikubali kufanya marekebisho ya mchoro wa Mradi wa kutoa Maji kutoka Mto Ruvuma kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani ili kuongeza idadi ya vijiji zaidi vikwemo vya Halmashauri ya Nanyamba.

Mheshimiwa Spika, usanifu wa mradi huo ulishakamilika, hivyo, mabadiliko ya mchoro yatafanyika wakati wa utekelezaji wa mradi huo kabla ya kuanza kwa ujenzi wa kazi hiyo. Idadi ya vijiji vitakavyoongezwa itajulikana baada ya mabadiliko ya mchoro yatakayofanywa na Mtaalam Mshauri atakayesimamia ujenzi wa mradi huo.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa mradi huo unakadiriwa kugharimu kiasi cha Dola za Marekeni milioni 189.9. Kwa sasa Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za utelekezaji wa mradi huo na unategemea zaidi upatikanaji wa fedha ili kazi iweze kuanza.