Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata (15 total)

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Kirando katika Wilaya ya Nkasi kinatoa huduma kwa vijiji zaidi ya ishirini katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na katika kituo hicho wodi za watoto na akina mama zimekuwa ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya watoto na akina mama wanaohudumiwa katika kituo hicho.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi hizo ili kuondoa kero kwa akina mama na watoto wanaohudumiwa katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha wodi ya akina mama na watoto katika kituo cha afya cha Kirando, tathmini ya awali imefanyika na kubaini kuwa zinahitajika shilingi milioni 250 ili kukamilisha ujenzi huo. Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo Serikali itaweka katika mpango na bajeti wa Halmashauri ili kuanza ujenzi wa wodi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umbali wa kituo hicho kutoka Makao Makuu, Serikali imepeleka gari la wagonjwa ili kuboresha huduma za Rufaa kwa akina mama na watoto. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri imeweka kipaumbele katika ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Kabwe ili kiweze kuhudumia wananchi wa Korongwe na Kabwe ambao wanahudumiwa na kituo cha afya cha Kirando.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Asilimia kumi ya bajeti ya Halmashauri nchini hutengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia fedha hizo zitolewe kwa kila Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyojibu hoja hii mara kadhaa hapa Bungeni, Serikali imejipanga kuhakikisha asilimia kumi ya fedha za vijana na wanawake zinatengwa na zinapelekwa kwa njia ya mikopo. Usimamizi wa suala hili uliwekewa mkazo katika mwongozo wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo Halmashauri zote zimetenga shilingi bilioni 56.8 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake kutokana na mapato ya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ili kuhakikisha fedha hizo zinatengwa na kupelekwa kwa vijana na wanawake. Maamuzi ya kutenga fedha hizi ni kadri ya makusanyo kila robo mwaka yanafanywa na Halmashauri kupitia Kamati ya Fedha na Mipango na Baraza la Madiwani.
Hivyo, naomba kutoa wito kwenu Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika kusimamia suala hili ambalo liko kwenye Halmashauri zetu ili kila tunapofanya maamuzi ya kugawa rasilimali fedha kutokana na mapato ya ndani, tuweke kipaumbele katika kutenga fedha hizo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali ilipanga kujenga na kupanua Uwanja wa Ndege wa
Sumbawanga Mjini.
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika pamoja na kuwalipa fidia wananchi
wanaozunguka uwanja huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata,
Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kujenga Kiwanja cha Ndege
cha Sumbawanga kwa kiwango cha lami pamoja na jengo jipya la abiria
(Terminal Building). Kiwanja hiki ni miongoni mwa viwanja vinne ambavyo
vitajengwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Rasilimali ya Ulaya (European
Investment Bank). Viwanja vingine vitakavyojengwa kwa mkopo kutoka
European Investment Bank katika kundi hili ni Viwanja vya Shinyanga, Kigoma na
Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi
zilitangazwa mwezi Agosti, 2016 na kufunguliwa mwezi Oktoba, 2016 ambapo
Mkataba na Mkandarasi wa kujenga kiwanja hiki utasainiwa baada ya kupata
idhini (no objection) kuhusu taarifa ya uchambuzi wa zabuni ambayo watu wa
EIB (European Investiment Bank) tunatarajia kuipata. Aidha, napenda
kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa zoezi la uhakiki wa mali za wananchi
ambao wataathirika na mradi huo lipo katika hatua za mwisho.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali inatambua uwepo wa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji ambao wanatekeleza majukumu yao moja kwa moja
na wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa posho viongozi hao kama inavyofanya kwa Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia kila Halmashauri imeweka utaratibu wa kuwalipa posho Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri. Katika makusanyo ya mapato kupitia vyanzo vya ndani kila Halmashauri hupeleka asilimia 20 kwenye vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba 3% hutumika kwa ajili ya maendeleo na 17% hutumika kwa ajili ya utawala ikiwemo kuwalipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa. Viwango vya kulipa posho hizo hutofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine kulingana na makusanyo ya mapato ya ndani katika vyanzo vilivyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa fedha hizo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imependekeza kulifanya suala la asilimia 20 kuwa la kisheria katika marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Maandalizi ya sheria hii yako katika hatua za mwisho na Muswada huo utawasilishwa na kujadiliwa hapa Bungeni.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Lengo la Serikali ni kuwainua kiuchumi wananchi maskini vijijini hasa wanawake ambao hawana dhamana ya kuweka benki ili waweze kupata mikopo kwa sababu nyumba nyingi za vijijini hazina Hatimiliki ambazo zingeweza kutumika kama dhamana benki.
Je, Serikali inawasaidiaje wananchi na hasa wanawake kwa kuzungumza na benki ili zikubali kukpokea Hatimiliki za kimila kama dhamana ya mikopo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa Hatimiliki za kimila ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 na kanuni zake. Utoaji wa hati za Hakimiliki ya kimila ulianza mwaka 2004 Wilayani Mbozi na baadae uliendelea katika Wilaya zingine ambapo hadi sasa takribani hati za Hakimiliki za kimila 400,761 zimekwishatolewa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999, hati za Hakimiliki za kimila zina hadhi sawa kisheria na hati inayotolewa na Kamishna wa Ardhi. Hadi sasa hati za Hakimiliki za kimila zimewezesha wananchi kupata mikopo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 59 kutoka taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo NMB, CRDB, TADB, Stanbic Bank, Meru Community Bank, Agricultural Trust Fund Bank, SIDO, NSSF na Mfuko wa Pembejeo katika Wilaya ya Mbozi, Iringa, Babati, Bariadi, Arumeru, Mbarali, Manyoni, Kilombero, Bagamoyo, Mbinga na Tandahimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baadhi ya taasisi za fedha zimekuwa hazikubali kupokea hati za Hakimiliki ya kimila kama dhamana kwa wananchi kupata mikopo. Sababu ambazo zimekua zikitolewa na taasisi hizo ni pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na thamani au ardhi husika kutoendelezwa; vikwazo katika kuuza dhamana pale mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo kutokana na sharti la kutaka ardhi iuzwe kwa mkazi wa kijiji husika na baadhi ya wamiliki wa ardhi kutokuwa na sifa za kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hizo, Wizara yangu kupitia marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 yanayoendelea inaangalia uwezekano wa kuondoa vikwazo vinavyozuia uuzaji wa dhamana pale mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo pamoja kuzungumza na taasisi za fedha kuwa hati ya Hakimiliki ya kimila ina hadhi sawakisheria na hati inayotolewa na Kamishna wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wananchi hawana budi kuyaendeleza maeneo yao hususani yale yaliyopatiwa hati za Hakimiliki za kimila ili kuyaongezea thamani na hivyo kuzishawishi taasisi za fedha kuyakubali maeneo hayo kama dhamana ya mikopo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Halmashauri za Wilaya ya Nkasi na Sumbawanga Mjini hazina Hospitali ya Wilaya; wanawake na watoto wanapata shida ya matibabu wakati wa kujifungua na huduma za watoto.
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali katika Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa umeanza taratibu za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika eneo la Milanzi. Hospitali ya Mkoa inayotumika sasa itabaki kuwa Hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga wanapata huduma za afya katika Hospitali Teule ya Dkt. Atman inayomilikiwa na Kanisa ambayo imeingia mkataba na Serikali wa utoaji huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Taratibu za kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo zinakamilishwa. Kwa sasa wagonjwa wanapata huduma katika Hospitali Teule iliyopo pamoja na vituo vya afya na zahanati. Serikali itajitahidi kutafuta fedha na kushirikiana na wananchi wa Nkasi ili kufanikisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali ilipanga kujenga na kupanua Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini:-
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika pamoja na kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka uwanja huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ukarabati wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga upo kwenye hatua ya manunuzi. Mkataba wa usimamizi wa kazi ya ujenzi ulitiwa saini baina ya Serikali na kampuni ya SMEC kutoka Australia mwezi Oktoba, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mwezi Juni, 2017 Serikali ilitiliana saini mkataba wa ujenzi wa ukarabati wa uwanja huo na Kampuni ya Sino-Shine Overseas Construction and Investment East Africa Limited kutoka Nchini China. Utekelezaji wa mradi huo utakapoanza unategemewa kukamilika ndani ya miezi 18. Kazi ya ujenzi wa uwanja huo zitaanza mara baada ya Serikali kukamilisha taratibu za malipo ya fidia kwa wananchi wanaostahili kulipwa ili waondoke kupisha ujenzi wa uwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaoathirika na mradi huo yapo katika hatua ya uhakiki wa mwisho kabla ya ulipaji wa fidia kuanza.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia vikundi vya wanawake waliopo katika Mkoa wa Rukwa katika suala la mikopo na kuwapatia elimu ya ujasiriamali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vya wanawake vinawezeshwa kupitia mfuko wa wanawake unaotokana na asilimia tano ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Sambasamba na hilo Serikali inawahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu ya ujasiliamali kwa vikundi vya wanawake ili kuwajengea uwezo, kuibua miradi yenye tija itakayosaidia kupata kipato na kurejesha mkopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 vikundi vya wanawake 55 vyenye wanachama 698 vimepatiwa mikopo ya shilingi milioni 56.87 kati ya shilingi bilioni 6.5 zilizokusanywa kutokana na mapato ya ndani katika Mkoa wa Rukwa.
Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 vikundi 33 vya wanawake vimepatiwa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 118 kati ya shilingi bilioni 4.2 ya makusanyo ya mapato ya ndani hadi machi, 2017 sawa na asilimia 2.78.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kutoa maelekezo kwa Halmashauri kuimarisha makusanyo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki iliyowekwa katika Halmashauri zote 185 na kuhakikisha kwamba fedha zinapelekwa kwenye mfuko kila zinapokusanywa.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Wanawake ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kusimamia nchi yetu na kwamba ukimwezesha mwanamke umeiwezesha familia na Taifa kwa ujumla.
Je, ni lini Serikali itafikiria kuboresha huduma za kibenki zitakazoweza kuwahudumia akina mama walio mikoa ya pembezoni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa mwanamke katika familia na Taifa kwa ujumla. Kwa kutambua hilo, Halmashauri zote nchini zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana. Suala hili lipo kisera na ni maamuzi ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wanawake wanawezeshwa na kujengewa uwezo kiuchumi. Aidha, Serikali itaendelea kuibua programu wezeshi kwa wanawake kwa kadri itakavyoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za kisera za Serikali za kuwawezesha wanawake kiuchumi, jukumu la msingi la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili watu binafsi, taasisi za umma na binafsi ziweze kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kuzalisha mali pamoja na huduma zikiwemo huduma za kibenki. Badala ya Serikali kujiingiza moja kwa moja kusambaza huduma za kibenki hapa nchini, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, upatikanaji wa maji, umeme, mawasiliano na usalama wa watu na mali ili kuvutia wawekezaji kusambaza huduma za kibenki katika maeneo mbalimbali hapa nchini yakiwemo maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara, hususan sera, miundombinu na usalama yamevutia wawekezaji binafsi wa ndani na nje kuwekeza hapa nchini na hivyo kuimarisha huduma jumuishi za kifedha kwa njia ya simbanking, wakala wa benki, mobile money, NGO’s, SACCOS na benki za kijamii. Jitihada hizi zimesaidia kuongeza matumizi ya huduma rasmi za fedha kutoka asilimia 58 mwaka 2013 hadi asilimia 65 mwaka 2017. Aidha, matumizi ya huduma zisizo rasmi za fedha zimepungua kutoka asilimia 16 mwaka 2013 hadi asilimia saba mwaka 2017. Hivyo basi, ni wajibu wetu kuendelea kuwashawishi wawekezaji binafsi kusogeza huduma za fedha karibu na wananchi badala ya kuitegemea Serikali.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA (K.n.y. MHE. BUPE MWAKANG’ATA) aliuliza:-
Vijana wengi wamejiajiri katika shughuli mbalimbali ikiwemo waendesha bodaboda, lakini waendesha bodaboda hao wamekuwa wakisumbuliwa sana na askari wa barabarani kwa kutozwa faini ambazo muda mwingine hazina maana na hivyo kuwakatisha tamaa.
Je, Serikali inachukua hatua gani ili kudhibiti vijana hawa wasinyanyaswe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa biashara ya pikipiki kwa huduma ya usafiri kwa jamii ambapo vijana wengi wamepata ajira hivyo kukuza kipato chao. Umuhimu mkubwa wa usafiri huu hauwaondolei wahusika wa usafiri huu wajibu wa kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani ili kuufanya usafiri huu kuwa salama kwa watumiaji.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua wale wote ambao wanakiuka Sheria na Kanuni za usalama barabarani, ni rai yangu kwa wale wote ambao wanahisi kuonewa ama kunyanyaswa wakati wakitumia usafiri huu kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa shamba la Efatha Mkoani Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa matumizi ya Shamba Na. 48/1 la Malonje kati ya mmiliki ambaye ni Mdhamini wa Efatha na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hili, hususan Vijiji vya Songambele, Sikaungu na Msanda Muungano. Madai ya wananchi hao ni kuwa sehemu ya shamba hili imeingia ndani ya vijiji vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo awali Shamba la Malonje lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo likiwa halina upimaji ambapo lilipimwa mwaka 1997 likiwa na ukubwa wa hekta 15,000. Mwaka 2007 shamba hili liligawanywa ambapo hekta 10,000 ziliuzwa kwa wamiliki ambao ni Efatha Ministry na hekta 5,000 zilizobaki zilipimwa vitalu na kugawiwa wafugaji. Mwaka 2010 baada ya kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi, ilibainika kuwa upimaji wa vijiji uliofanyika umeingiliana na mipaka ya shamba husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa, imefanya jitihada mbalimbali za kumaliza mgogoro huo. Baada ya jitihada hizo kutozaa matunda, tarehe 7 Novemba, 2017 nilikutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma ya Efatha na baadhi ya Watendaji wake kwa lengo la kukubaliana namna bora ya kumaliza mgogoro huu ili kuboresha mahusiano ya ujirani mwema kati ya mmiliki na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo. Wizara yangu ilipendekeza kwamba Efatha iridhie kuachia sehemu ya ardhi ya shamba yenye ukubwa wa ekari 8,392.9 na kuigawa kwa wananchi wa vijiji husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Bodi ya Wadhamini kukaa, waliridhia kutoa ekari 3,000 kwa Vijiji vya Songambele, Sikaungu na Msanda Muungano kwa maana ya kila kijiji kigawiwe ekari 1,000. Hata hivyo, Kijiji cha Sikaungu kimekataa kupokea ekari hizo kwa kuwa wao wanataka kiasi cha ardhi kama ilivyoonekana kwenye vyeti vyao vya ardhi ya kijiji.

Aidha, majadiliano bado yanaendelea kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Efatha na Serikali ya Kijiji cha Sikaungu. Baada ya majadiliano hayo kukamilika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri itasimamia upimaji wa ardhi hiyo.
MHE. BUPE N. MWAKANG‟ATA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga visima virefu vya maji katika Wilaya ya Nkasi ili kutatua changamoto ya maji iliyopo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua tatizo la maji lililopo katika Wilaya ya Nkasi Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020 imepanga kuchimba visima virefu 9 katika maeneo ya Masolo, Katogolo, Mpata, Mienge, Itindi, Kacheche, Lyele, Mbwendi na Kakoma. Kiasi cha shilingi milioni 315 kimetengwa katika bajeti ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kazi hiyo. Hadi kufikia mwezi Disemba 2019, Visima 7 vimechimbwa katika vijiji vya Masolo, Katogolo, Mpata, Mienge, Kanazi na Ipanda na kiasi cha shilingi milioni 220 kimetumika katika upimaji na uchimbaji wa visima hivyo ambavyo vitatumika kama vyanzo vya maji katika vijiji husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mrefu wa kutatua tatizo la maji katika Wilaya ya Nkasi, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imepanga kutumia zaidi ya bilioni 1.3 kwa kupitia Programu ya PforR kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Nkasi. Wizara imeshatuma fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji 6 Wilayani Nkasi ambapo miradi yote hiyo itatekelezwa kwa mfumo wa wataalam wa ndani (Force Account).
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-

Mkoa wa Rukwa una wilaya nne na hakuna Hospitali ya Wilaya:-

Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali za Wilaya katika wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imeupatia Mkoa wa Rukwa kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo ambapo kila Halmashauri imepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5. Vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, Mkoa wa Rukwa umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali za Halmashauri za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo, ambapo kila Halmashauri itapewa kiasi cha shilingi milioni 500. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 500 kimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-

Je, ni lini Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa itaanza kujengwa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa unao Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga inayotoa huduma za rufaa kwa halmashauri nne za mkoa huo hadi sasa. Hata hivyo hospitali hiyo inayo changamoto ya ufinyu wa nafasi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya ya kutolea huduma za afya ili kukidhi mahitaji ya wananchi. Kutokana na changamoto hiyo Ofisi ya Mkoa wa Rukwa imeshapata eneo jipya la ukubwa wa hekari 100 lililopo Milanzi ndani ya Manispaa ya Sumbawanga litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya rufaa ya mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu utaanza baada ya kumalizika ujenzi wa hospitali za rufaa katika mikoa mipya ya Katavi, Songwe, Njombe, Simiyu na Geita.
MHE. JACQEULINE N. MSONGOZI (K.n.y MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA) Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ni miongoni mwa viwanja vya ndege vinne (4) ambavyo ni Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga vinavyotarajiwa kujengwa na kukarabatiwa kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB).

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za makubaliano ya mkataba wa miradi hiyo baina ya Serikali (kupitia Wizara ya Fedha na Mipango) na Mfadhili (Benki ya Uwekezaji ya Ulaya – EIB) tayari zimekamilika na idhini (No Objection) ya kuanza utekelezaji wa miradi yote minne (4) imetolewa na Mfadhili wa miradi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Mkandarasi (M/ s Sino Shine Overseas Construction & Investment East Africa Limited) na Mshauri Elekezi (SMEC International PTY Limited) ikishirikiana na Kampuni ya SMEC International Tanzania Limited) kwa ajili ya kutekeleza kazi hii, wamepatikana. Hivyo hivi sasa, Serikali iko katika hatua za awali za kuanza utekelezaji wa mradi huu.