Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Azza Hilal Hamad (13 total)

MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Mradi wa maji kisima kirefu katika Mji Mdogo wa Tinde umechukua muda mrefu sana kukamilika:-
Je, ni lini sasa mradi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua tatizo hilo la maji, Serikali katika mwaka fedha 2014/2015 ilitenga shilingi milioni 100 ambazo zilitumika kwa ajili ya kulipia gharama za uchimabaji wa kisima kirefu katika Mji wa Tinde, ujenzi wa vituo vinne vya kuchotea maji na ujenzi wa nyumba ya pampu. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imepeleka jumla ya shilingi milioni 200 ambazo zimepokelewa mwezi Novemba, 2015 na zitatumika kwa ajili ya ununuzi na ufugaji wa pampu na mfumo wa umeme wa jua pamoja na miundombinu yake yote. Kazi nyingine zinazofanyika ni ujenzi wa msingi wa kitako pamoja na ununuzi wa matenki ya kuhifadhia maji yenye ukubwa wa mita za ujazo 20, na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa mita 5,200. Aidha, kazi hii inafanywa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Shinyanga na inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2016.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisja ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu, jana tulipata ajali mbaya lakini kwa uwezo wake na mapenzi yake alitunusuru. Shukrani zote zinamstahiki yeye kwa sababu ndiye muweza wa kila jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga unaendelea ambapo kazi zilizofanyika ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje yaani OPD, ujenzi wa wodi 2 za kulaza wagonjwa ambazo zipo katika hatua ya “renta”, ujenzi wa nyumba moja ya watumishi ambayo ipo katika hatua ya ukamilishaji, ujenzi wa jengo la vyumba vya madaktari yaani Doctors Consultation Rooms ambalo limeshapauliwa na uwekaji wa miundombinu ya maji na umeme katika jengo la OPD. Kazi zote hizo zimegharimu jumla ya shilingi 368,000,000.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imeidhinishiwa shilingi 40,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa wodi mbili za kulaza wagonjwa, umaliziaji wa nyumba moja ya mtumishi pamoja na jengo la vyumba vya madaktari. Halmashauri imetakiwa kuhakikisha inaipa kipaumbele Hospitali hiyo kwa kutenga bajeti kila mwaka ili kukamilisha miundombinu iliyobaki.
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. AZZA H. HAMAD) aliuliza:-
Je ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya kuchimba Bwawa la Mradi wa Umwagiliaji Masengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, skimu ya umwagiliaji ya Masengwa ambayo ilijengwa kati ya mwaka 2004 na 2006 chini ya Programu Shirikishi ya Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji, ina eneo lililoboreshwa lipatalo hekta 325. Hata hivyo, eneo linalolimwa linafikia hekta 800. Aidha, kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, tumeshuhudia ukame hali ambayo imewafanya wakulima wawe na hitaji la kujengewa bwawa kwa ajili ya kutunza maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hitaji hilo, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Mwanza, imetenga fedha kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kutoa gharama halisi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo. Aidha, Wizara ilikwishaainisha maeneo yote nchini yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kuandaa mpango kabambe wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji wa mwaka 2002 (National Irrigation Master Plan). Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, hivi sasa Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Japan inaendelea na mapitio ya mpango huo ambao utahusisha ujenzi wa mabwawa madogo, ya kati na makubwa kwa nchi nzima.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga makazi bora katika Kituo cha Wazee cha Kolandoto kwa kuwa makazi haya yamekuwa ya muda mrefu na yamechakaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Makazi ya Wazee ya Kolandoto yaliyopo Manispaa ya Shinyanga yalianzishwa mwaka 1917 kwa lengo la kutoa huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa ukoma ambao walikuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kolandoto. Aidha, baada ya kupona maradhi hayo waliendelea kubaki eneo la Kolandoto kwa sababu ya kuepuka unyanyapaa uliokithiri katika jamii zao. Tangu kipindi hicho, Serikali ilichukua jukumu la kuwatunza wananchi hao na kuwapokea wazee wengine wasiojiweza ambao walihitaji huduma za ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Spika, napenda nikiri kuwa makazi haya ni miongoni mwa makazi ambayo yanahitaji ukarabati kutokana na uchakavu wa nyumba za makazi ambazo zilijengwa miaka mingi iliyopita.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hali hiyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa kipaumbele cha kuboresha hali ya Makazi ya Wazee wa Kolandoto kwa kujenga bweni lenye uwezo wa kuchukua wazee 20, wa kiume 10 na wa kike 10. Ujenzi huo utakamilika ifikapo Oktoba mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, pia Wizara imejenga jiko ambalo limefungwa majiko yanayotumia nishati ya gesi. Majiko hayo yameanza kutumika kupikia chakula cha wazee badala ya kutumia kuni.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapelaka fedha za kutosha kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga ambao umeanzishwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kupitia fedha za ruzuku kutoka Serikalini imekamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), nyumba moja ya mtumishi pamoja na jengo la kutolea huduma za ushauri nasaha ambalo liko katika hatua ya upauaji. Jumla ya shilingi milioni 365 zilitumika kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa mchanganuo ufuatao:-
Ruzuku kutoka Serikali Kuu shilingi milioni 267; mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya shilingi milioni 86; nguvu za wananchi shilingi milioni saba na mchango wa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu shilingi milioni tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 110 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo ambapo kati ya hizo shilingi milioni 40 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi milioni 70 ni ruzuku kutoka Serikali kuu. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 zitatengwa shilingi milioni 110 kwa ajili ya kendeleza ujenzi wa hospitali hiyo ambapo shilingi milioni 50 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi milioni 60 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu. Serikali itaendeleza ujenzi wa hospitali hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha ili wananchi waweze kupata huduma.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Kituo cha Watoto wenye ulemavu cha Buhangija kimekuwa kikijiendesha kwa kusuasua:-
Je, Serikali ipo tayari kupeleka fedha kwa asilimia mia moja katika kituo hiki hasa ikizingatiwa kuwa kinachukua
watoto kutoka Kanda yote ya Ziwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Buhangija ni Shule ya Msingi jumuishi inayochukua watoto wasio na ulemavu na wenye ulemavu wa aina mbalimbali na siyo kituo cha kulelea Watoto wenye ulemavu. Shule hii huchukua watoto wenye ulemavu kama vile wasioona, bubu, viziwi, weye ualbino, ulemavu wa viungo na pia watoto wasio na ulemavu kama nilivyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uendeshaji wa kusuasua kwa utoaji wa huduma katika shule hii kulitokana na ongezeko la ghafla la watoto na vijana wenye ualbino kukimbilia shuleni hapo kuanzia miaka ya 2009 kutokana na sababu za vitendo vya ukatili, mauaji, unyanyasaji na unyanyapaa uliokithiri dhidi ya watu wenye ualbino katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Hali hiyo ilisababisha ongezeko la watoto na watu wazima hapo shuleni kufikia 407 kutoka 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya Buhangija kama shule nyingine nchini zenye mahitaji maalum, itaendelea kupatiwa mgao wa fedha na Serikali pamoja na mahitaji mengine ya kimsingi kwa mujibu wa taratibu za Serikali. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa wanafunzi wanapata elimu bila mashaka yoyote kwa kuwa tatizo la msongamano limepungua sana na kufanya wanafunzi kubaki 228 tu, idadi ambayo shule inamudu kuwahudumia.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka maji katika Sekondari ya Masengwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza ahadi yake ya kupeleka maji kwenye Shule ya Sekondari Masengwa. Serikali imeandaa mradi wa kutoa maji Kijiji cha Bugweto Manispaa ya Shinyanga kwenda katika Kijiji cha Masengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tararibu za kumpata Mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kupeleka maji katika Kijiji cha Masengwa zimekamilika. Utekelezaji wa mradi huo utaanza katika mwaka wa fedha 2018/2019. Matarajio ni kwamba mradi huu utakapokamilika utawanufaisha wakazi wa Kijiji cha Masengwa ikiwemo na Shule ya Sekondari Masengwa.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji katika Kijiji cha Ishololo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa Bwawa la Ishololo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ni moja kati ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo chini ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Utekelezaji wa mradi huo ulifikia ukomo wake mwezi Desemba, 2013 ambapo Benki ya Afrika ilisitisha kutoa fedha za utekelezaji wa mradi wakati utekelezaji wake ulikuwa bado haujakamilika.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina dhamira ya dhati ya kukamilisha skimu zote za umwagiliaji ambazo utekelezaji wake haujakamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha. Kwa sasa Serikali inakamilisha mapitio ya Mpango kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ambao unabainisha hali ya skimu za umwagiliaji nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji nchini Serikali itatoa kipaumbele kwa miradi yote itakayobainishwa ukiwemo mradi wa umwagiliaji katika Kijiji cha Ishololo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inakabiliwa na upungufu wa Madaktari Bingwa.
Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Shinyanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Azza Hillal Hamad kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kuwatetea wananchi wa Shinyanga hususani katika sekta ya afya nataka kumpongeza sana kwa jitihada zake hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwezesha kutoa huduma za kibingwa Hospitali za Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inahitaji kuwa na Madaktari Bingwa wa fani sita muhimu ambazo ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akinamama na Wajawazito, Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Daktari Bingwa wa Mionzi, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto. Aidha, Serikali inatambua kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa sasa ina Madaktari Bingwa watatu tu ambao ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akinamama na Wajawazito, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Daktari Bingwa wa Watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuzihamisha Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya kina kujua hali halisi ya mahitaji ya Madaktari Bingwa na fani zao katika Hospitali zote za Mikoa, Kanda Maalum na Hospitali ya Taifa Muhimbili. Baada ya kukamilisha tathmini hii Wizara itawapanga upya madaktari bingwa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya kila hospitali ya mkoa, kanda, hospitali maalum na zile za Taifa, lengo ni kuwa kila Hospitali ya Mkoa iwe na Madaktari Bingwa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji katika Kijiji cha Ishilolo, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa Bwawa la Ishololo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ni moja kati ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo katika Wilaya (DASIP) chini ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Utekelezaji wa mradi huo ulifikia ukomo wake mwezi Desemba, 2013 ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika ilisitisha kutoa fedha za utekelezaji wa miradi wakati utekelezaji wake ukiwa haujakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo dhamira ya kukamilisha skimu zote za umwagiliaji ambazo utekelezaji wake haujakamilika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa fedha. Skimu hii ipo miongoni mwa skimu za umwagiliaji zitakazopewa kipaumbele katika kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji (Irrigation Master Plan 2018 - 2025) ambapo kwa sasa umeanza kutekelezwa. Kwa kuzingatia umuhimu wa miradi hii ukiwemo mradi wa umwagiliaji wa Ishololo, tayari Serikali imekwishaanza mazungumzo na wadau mbalimbali, ikiwemo Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA kwa lengo la kuboresha miradi yote ambayo haijakamilika na ile inayofanya kazi chini ya ufanisi uliokusudiwa.
MHE. AZZA HILALY HAMAD aliuliza:-

Je, lini Serikali itachimba bwawa kwa ajili ya kuboresha Mradi wa Umwagiliaji Nyida.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilaly Hamad Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa Kuendeleza Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo ikiwa ni pamoja na Skimu ya Umwagiliaji ya Nyida. Katika kutekeleza Mradi huo, Kampuni ya Shekemu Construction Ltd. inafanya kazi ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuboresha mfumo wa usambazaji maji mashambani ambapo utekelezaji wa Mradi huu kulingana na Mkataba umefikia asilimia 68 ya kazi zote za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Disemba 2019 jumla ya Shilingi za Kitanzania 282,154,880.68 zimelipwa kwa Mkandarasi kati ya Shilingi za Kitanzania 466,594,981.81 zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza Skimu ya Nyida. Mradi huo kwa sasa umesimama kupisha msimu wa kilimo kwa wakulima na mvua zinazoendelea kunyesha. Hivyo, Mkandarasi ataendelea na kazi iliyobakia kulingana na Mkataba mara baada wakulima kuvuna mazao yao na msimu wa mvua kumalizika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mvua zisizotabirika pamoja na wakulima kuwa na mwamko mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji kwa kutaka kuongeza tija na uzalishaji kwa kulima misimu miwili kwa mwaka; na kwa kuzingatia kuwa chanzo cha maji cha skimu hiyo ni Mto Manonga ambao ni wa msimu; na hivyo Serikali iliona umuhimu wa ujenzi wa Bwawa ili kuendeleza skimu hiyo.

Aidha, ili kutekeleza mradi huo, mwaka 2013 Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya ya Shinyanga na Nzega zilifanya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa awali kwenye eneo linalokusudiwa kujengwa bwawa la Nyida eneo la Lyamalagwa litakalokuwa na uwezo wa kumwagilia maji mita za ujazo 4,167,825 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.5 kwa wakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kutokana na mabadiliko ya kimuundo ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, na miradi mingi ya umwagiliaji kujengwa chini ya kiwango wakati huo, Serikali haikuweza kutekeleza mradi huo kwa wakati kutokana na kufanya tathmini ya kina ya ufanisi ya miradi hiyo na hivyo kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati. Aidha, kwa kuwa muda mrefu umepita tangu tathmini hiyo ifanyike, Serikali itafanya mapitio upya ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata mahitaji na gharama halisi ya ujenzi wa bwawa na athari zake kwa sasa na itaanza kujenga ujenzi wa bwawa hilo baada ya tathmini hiyo kukamilika.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA (K.n.y. MHE. AZZA H. HAMAD) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawapa huduma ya umeme wananchi wa Vijiji vya Buyubi, Itwangi, Imenya, Nyambui na Mwankanga ambao muda mrefu wamekuwa watazamaji wa nguzo za umeme unaokwenda maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vijiji 126 vya Wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 22 kati ya vijiji 126 katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini vina umeme. Vijiji 50 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III, Mzunguko wa Kwanza unaotekelezwa na Mkandarasi Angelique International Limited ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti, 2019 jumla ya vijiji 19 vimeshawashiwa umeme na ujenzi wa miundombinu unaendelea katika vijiji vilivyobaki na wateja zaidi ya 211 wameunganishiwa umeme. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 50 vya Wilaya ya Shinyanga Vijijini inahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 170.9; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 156; ufungaji wa transfoma 78 za KVA 50 na KVA 100 na kuunganisha umeme wateja wa awali 2,241. Gharama za mradi ni shilingi bilioni
10.7 na mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 54 vilivyobaki vikiwemo vijiji vya Buyubi, Itwangi, Imenya, Nyambui na Mwankanga vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III, Mzunguko wa Pili unaotarajia kuanza mwezi Januari, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Mabweni katika shule za sekondari zilizoanzishwa Kitarafa ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kupata elimu iliyo bora Mkoani Shinyanga?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa shule za sekondari kuwa na mabweni ili kuboresha elimu. Kwa sasa mpango wa Serikali ni kuziboresha shule za sekondari zilizopo ambapo kipaumbele ni katika ujenzi wa miundombinu muhimu wa vyumba vya madarasa, vyoo mabweni na maabara ili kuboresha mazingira ya kufundishi na kujifunzia. Ukarabati wa shule hizo unahusisha miundombinu ya mabweni hasa kwa watoto wa kike ili kuweza kupata elimu iliyo bora. Hadi sasa, shule za sekondari 1241 zimejengewa mabweni kati ya shule za sekondari 3634 zinazotumia ruzuku ya Serikali Kuu, mapato ya ndani ya Halmashauri na mchango wa jamii. Serikali itaendelea kujenga mabweni na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu.