Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dua William Nkurua (7 total)

MHE. DUA W. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri na yanayotia moyo kwa wananchi wangu wa Nanyumbu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Nanyumbu tulikuwa na bahati mbaya ya gari la Programu ya Maji kupata ajali, gari ambalo sasa haliwezi kutumika kabisa.
Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango gani sasa kuipatia Wilaya ya Nanyumbu gari ili wataalam waweze kutoa huduma hizo kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ingawa swali hili limepata majibu kidogo hafifu kutoka kwa Mheshimiwa Nkamia, lakini nataka pia tuna tatizo la wakandarasi kuzidai Halmashauri pesa za maji za Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini hasa tutawalipa hawa Wakandarasi ili kuondokana na kero ya mgogoro kati ya Halmashauri na Wakandarasi hao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la gari ambalo limeharibika, tutaliangalia na tutakapopata fedha tutalifanyia matengenezo na kama matengenezo yatashindikana, basi tutafanya utaratibu wa kununua gari lingine jipya ili wananchi wa Mangaka waendelee kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kabisa kwamba kuna miradi mingi ambayo imechelewa kukamilika kwa sababu ya fedha zinazoitwa fedha za Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matatizo ya kifedha katika nchi ambayo yamesababisha miradi mingi ya maji isikamilike. Hata hivyo, tunamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia sasa fedha zinaanza kutolewa ambazo zitahakikisha kwamba miradi yote ambayo ilikuwa haijakamilika, inakamilika pamoja na miradi ya Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DUA W. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika wale ambao walifanyiwa tathmini ya awamu ya kwanza, wapo ambao mpaka sasa hawakulipwa, Majina yao yalirukwa katika Kijiji cha Misawaji, lakini pia wapo ambao walifanyiwa tathmini kwamba nyumba zao zitabomolewa nusu lakini zimebomolewa zote na hivi ninavyokwambia wamechanganyikiwa kabisa.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuma watu tumuoneshe watu ambao wameathirika ili wapate haki yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara kutoka Masasi mpaka Mangaka imekamilika, hadi sasa magari yenye uzito mkubwa kutoka Songea kuelekea Masasi yanatumia hiyo barabara.
Je, Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu wa kuleta mizani katika Mji wa Mangaka ili kuokoa barabara ambayo Serikali imetumia gharama kubwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana nae kwamba tutatuma watu waende wakalichunguze hilo suala na hatimaye tuweze kulipatia ufumbuzi stahiki. Ninachoomba kumhakikishia tu ni kwamba Serikali hii inafuata sheria na yeyote mwenye haki ya kulipwa fidia atalipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili nadhani anafahamu kwamba hizo barabara anazoziongelea bado hazijakamilika na hivi karibuni nimepiata katika eneo lake ingawa kwa bahati sikumjulisha kwa sababu ilikuwa ni dharura wakati natokea Jimbo la Namtumbo. Ninamhakikishia mara barabara hizi zitakapokamilika na umuhimu utakapoonekana kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mizani, Serikali itafanya maamuzi stahiki. (Makofi)
MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi tena ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa barabara hii ya kutoka Nangomba kwenda Nanyumbu imetolewa majibu ambayo yanatia moyo na sina mashaka kabisa na ahadi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano; lakini kwa kuwa barabara hii inaunga barabara kubwa inayotoka Songea mpaka Mtwara, kwa jina maarufu inaitwa Mtwara Corridor. Barabara hii kutoka Songea mpaka pale ilipo mizani, Mnazi Mmoja ni zaidi ya kilometa 500.
Je, kwa kuwa Mangaka pana pacha ya kuelekea Msumbiji, Serikali haioni umuhimu wa kuweka pale mizani ili kuweza kudhibiti magari yote yaelekeayo Msumbiji na Mbamba Bay ili kulinda barabara zetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Mheshimiwa Spika, nimepata taarifa hiyo kwamba kuna mchezo unafanywa na wasafirishaji wanaotumia magari makubwa kusafirisha bidhaa kutoka Songea kwenda Mtwara kwa sababu hakuna mizani kati ya Songea hadi Mangaka, hivyo wanabeba mizigo mikubwa, wanapofika Mangaka au kukaribia Masasi huwa wanapunguza mizigo kwa sababu mbele watakutana na mizani.
Mheshimiwa Spika, nimepata hiyo taarifa na ninaomba kuchukua nafasi hii kuwaagiza TANROADS wahakikishe wanaangalia mahali gani waanze kuweka mizani ya kutembea ili tuanze kudhibiti wakati kituo maalum cha kuweka mizani kitakapokamilika.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kwa sasa sehemu mbalimbali za vipande hivi vya barabara kati ya Mtambaswala, Mangaka hadi Songea havijakamilika. Inawezekana kwamba mahitaji hayo ya kuweka mizani yatafanyika baada ya kukamilika kwa wakandarasi wote katika barabara hiyo ya Mtwara Corridor. Ninaomba kazi hiyo ya kuweka mizani inayotembea (mobile) ifanyike haraka ili kuweza kuhakikisha kwamba barabara zetu hazianzi kuharibika kabla kazi haijakamilika. (Makofi)
MHE. DUA W. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru
kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Miundombinu, lakini nataka
nifanye marekebisho kidogo siyo Kata ya Mnauje ni Kata ya Mnanje.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya majibu yake mazuri, nina swali dogo
la nyongeza. Katika Kijiji cha Marumba, Kata ya Mkonona kulijengwa mnara wa
TTCL na mnara ule uliwashwa, lakini utendaji kazi wa mnara huu siyo mzuri. Kijiji
hiki kipo mpakani kabisa mwa Tanzania na Msumbiji na sote tunafahamu
umuhimu wa mawasiliano mipakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, kijiji hiki kinahudumia mpakani na
mnara huu haufanyi kazi vizuri. Je, Serikali itafanya nini kuhakikisha kwamba,
mnara huu unafanya kazi haraka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, nimepokea taarifa yake na nitatafuta muda nizungukie huo mpaka
ili tuone vijiji vyote vya mpakani hali ikoje, ikiwa ni pamoja na hiyo Kata ya
Mkonona.
MHE. DUA W. NKURUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Akbar amekuwa akiliuliza swali hili mara kwa mara, je, Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu wa kutembelea Jimbo lake ili aweze kujionea hali halisi ya kule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Vijiji vya Masuguru, Mtambaswala, Nanderu, Ngonji na Marumba vimepitiwa na Bonde hili la Mto Ruvuma katika Jimbo la Nanyumbu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia wananchi hawa skimu ya umwagiliaji ili kuwakwamua katika hali ya maisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Akbar kwa namna anavyowatetea wananchi wake. Ni kweli amekuwa akiliuliza swali hili na amekuwa akilifuatilia mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jukumu la Naibu Waziri ni kufuatilia miradi na kwenda kuangalia uhalisia. Niko tayari kwenda kuona mradi huo kama alivyoomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkakati wa kilimo cha umwagiliaji Nanyumbu, sisi kama Wizara ya Maji tuna eneo la hekta milioni 29.4 linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na katika mikakati yetu ambayo tunataka kuhakikisha kwamba umwagiliaji unakuwa na tija kubwa kwenye uzalishaji, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Nanyumbu, hatutawasahau wala hatutawaacha wananchi wa Nanyumbu katika kuhakikisha tunawapa kilimo cha umwagiliaji. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nitoe shukrani zangu kwa Serikali kwa sababu Wilaya yetu ya Nanyumbu pia tulikuwa na matatizo ya usafiri kwa Jeshi la Polisi lakini siku za hivi karibuni Serikali imetupatia na sasa polisi wana uwezo wa kufanya kazi kiurahisi. Hata hivyo, pamoja na shukrani hizo, nataka niongeze swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekiri kwamba Nanyumbu ni miongoni mwa wilaya mpya na hatuna jengo lenye hadhi ya kuwa na hadhi ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya. Sasa kwa kuwa Serikali inajua hilo.

Je, nitarajie sasa kwenye bajeti ijayo kuona haya maandalizi ambayo Serikali imesema ipo katika maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho; je, kwenye bajeti hii ijayo nitarajie kuona hiyo bajeti inasomwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa William Dua, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba kama ambavyo alivyokuja kulizungumzia suala la mapungufu ya usafiri na tukalifanyia kazi, basi na suala la kuhakikisha kwamba tunafanya kila linalowezekana ili kuimarisha kituo cha polisi katika Wilaya ya Nanyumbu nacho vilevile tutachukulia kwa uzito kama ambavyo tumechukulia uzito wa suala la changamoto ya gari katika wilaya yake.
MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba TARURA naikubali na nafahamu uwezo wake lakini ni kwamba kuna maeneo TARURA inakuwa na uwezo mdogo ndiyo maana tunakuja na haya maswali.

Sasa nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini barabara kutoka Mangaka hadi Matekwe Wilaya ya Nachingwea mpaka Liwale Wilaya ya Liwale itaweza kupandishwa hadhi kwa sababu tayari Wilaya zote tatu zimeshaombea kupanda hadhi? Naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kama nilivyozungumza muda mfupi kwamba kulikuwa na changamoto ya mgao wa fedha kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika na hali ya jiografia ndiyo maana baada ya TARURA kuwepo tumelazimika kufanya uratibu na kuzitambua barabara zote ili sasa ziweze kupata huduma kadri inavyostahili kutokana na uwiano wa namna pia tunavyopata fedha. Kwa hiyo, hilo zoezi limeenda vizuri na ninaamini kabisa kati ya maeneo ambayo labda wakati mwingine hayakupata allocation nzuri, baada ya zoezi hili yatapata mgao kulingana na uwezo wa kifedha, lakini pia kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ya Mangaka - Nachingwea kwenda Liwale zipo hatua kadhaa zinaendelea, kutoka Nachingwea kwenda Liwale kilometa 129 tumeanza usanifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami, lakini nafahamu kutoka Nachingwea kuja Mangaka kwamba liko zoezi wakati wote tumetenga fedha tutaanza ujenzi wa lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dua na kwa vile pia ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu tukutane tu hata baadae pia uweze kuona mpango mzima wa maeneo tulivyojipanga kwa ajili ya kuboresha barabara zetu katika mkoa huu wa Mtwara pamoja na barabara zetu upande wa Lindi.