Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia (44 total)

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, kwa kawaida viongozi wa kisiasa hawapati pensheni bali sisi kama Wabunge tunapata gratuity. Isipokuwa viongozi wetu hawa wakuu ambao muuliza swali amewazungumzia kwamba wao wanapewa pensheni wakiamini kwamba wameshamaliza kazi na wanatulia na wanapewa pensheni ili wasitapetape na kuhangaika kwenda hapa na pale kuhemea.
Je, huoni sasa ni wakati wa kuirekebisha sheria kwamba pensheni hiyo itolewe pale tu ambapo tumeshajiaminisha kwamba kiongozi huyu sasa ameshastaafu kweli, anastahili pensheni na kwamba hatatapatapa tena mpaka kufikia hatua ya kukataa kwamba hajafanya kazi yoyote? (Makofi)
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, ukiangalia stahili mbalimbali ikiwemo na pensheni au pensheni ya mwaka, iko kwa mujibu wa sheria; Sheria Na. 3 ya mwaka 1999 lakini vilevile iko kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria Na.11 ya mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza, bado mtu anayo haki. Nami nitoe tu rai kwamba kwa wale Viongozi Wakuu Wastaafu ambao wanahudumiwa kwa mujibu wa sheria hii ambayo niliitaja ya mwaka 1999 pamoja na mwaka 2005, wajitahidi kuenenda na misingi ya Kifungu Na. 6(j) aya ya tatu, imeweka masharti kwa Viongozi wa Umma, ni masuala gani wanatakiwa wayafuate.
Mheshimiwa Spika, hawatakiwi kutoa siri za Serikali walizozipata wakati wakitumikia; hawatakiwi kutoa masuala mbalimbali ambayo waliyapata wakati wakitumikia kama viongozi wa umma; hawakatazwi kujiunga na masuala mengine kwa sababu Sheria haijakataza.
Mheshimiwa Spika, mimi naomba kwa wale viongozi wa umma wa kisiasa, basi wajikite katika misingi ya kifungu Na. 6(j)(3) cha Sheria ya Maadili; Sheria Na. 13 ya mwaka 1995. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, MACEMP Awamu ya Kwanza, ilipeleka nguvu nyingi sana katika udhibiti kwa maana ya ununuaji wa boti, ujenzi wa majengo kwa ajili ya watumishi na kupeleka nguvu ndogo sana kwa wavuvi. Ukiangalia kilimo ni pamoja na uvuvi, lakini upande wa wakulima wanawezesha pembejeo na elimu.
Je, ni lini wavuvi na wenyewe watawezeshwa kwa kupewa zana bora na elimu badala ya kila siku kuwadhibiti, kuwafukuza na kuwatoza faini kama ambavyo tunafanya?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa kazi anayoifanya nzuri ya kufuatilia kazi ya wananchi wake ya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inajipanga katika hatua za kuboresha sekta ya uvuvi kuwaangalia na wavuvi wenyewe ikiwemo kuanzia shughuli yenyewe ya uvuvi, ikiwemo adha wanayokutana nayo yakiwemo makato, tozo wanazotozwa lakini pia na uhitaji wa vitendea kazi na kuhakikisha pia kwamba tunawaondolea manyanyaso wanayopewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitoe kauli tu kwa wale ambao wanawanyanyasa wavuvi, wanawanyanyasa akina mama sambamba na yale ambayo tumetoka kuyasikia, ni vema wakazingatia sheria na misingi ya kazi walizotumwa. Kumekuwepo na utaratibu wa baadhi ya watu wanaopewa dhamana, wakipewa mgambo wanatumia kigezo cha sheria, lakini wakiwapokonya maskini wale kama ni chakula wanakula wao wenyewe, wakipewa kazi ya kuzuia sehemu ya kuuzia nguo wakienda pale kuzuia wanapokonya nguo zile wanachukua wanazitumia wao wenyewe. Hivyo hivyo, na kwenye samaki wanawapoka samaki wanachukua wao wenyewe, tabia hiyo waiache na ikitokea katika eneo lolote tupate taarifa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anayenyang‟anya wananchi wanaofanya kazi fulani, akawanyang‟anya kwa kigezo cha kutumia sheria na akatumia yeye kwa manufaa yake binafsi ni mwizi kama mwizi mwingine anayenyang‟anya katika kipindi ambacho wananchi hawaoni. Kwa hiyo, tabia hiyo iachwe na kwa wale watakaoendelea watafikishwa katika mkono wa sheria ili kuweza kukomesha tabia hiyo nchi yetu iweze kuendeshwa kwa misingi ya sheria na utawala bora.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la tabia nchi linakabili maeneo mengine. Mji wa Mikindani ni mji ambao uko chini ya usawa wa bahari na kwa miaka mingi maji yakijaa baharini huwa yanaingia mpaka katikati ya mji lakini yalikuwa hayaleti madhara kwa sababu kulikuwa na kingo ambazo zimejengwa ili kuzuia maji yasilete athari kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kingo hizo zimeharibika kwa kiasi kikubwa na kufanya maji yanapojaa baharini kwenda kule kwenye mji mpaka katika makazi ya watu. Je, Serikali ina mpango gani wa kurejesha tena zile kingo ambazo ziliwekwa hasa kipindi hiki ambacho maji katika usawa wa bahari yamekuwa yakiongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua tatizo kubwa la kuongezeka kwa kina cha bahari. Siku zilizopita nilieleza kwamba sasa kina cha bahari kimeongezeka kwa sentimeta 19. Serikali yetu inachukua hatua za kuhakikisha kwamba tunakabiliana na tatizo hili. Moja, ni pamoja na kuzikarabati zile kuta na tayari tuna miradi inayoendelea. Mwezi wa nne mwaka huu, tutaanza rasmi kuzikarabati zile kuta za bahari ili kuhakikisha kwamba tunadhibiti ule mmomonyoko ambao umefanyika kwenye kuta hizo na kuziwezesha kuwa bora zaidi ili kutokuendelea kumomonyoa kingo za bahari yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niseme kwamba hata kwenye mkutano huu wa juzi wa Paris, Serikali yetu ilipata dola za Marekani 1,052,000. Fedha zote hizi kazi yake kubwa ni kwanza kutupatia uwezo mkubwa wa kupata fedha zaidi kutoka kwenye vyanzo vya fedha vya mabadiliko ya tabia nchi kama Adaptation Fund, Least Developed Countries Fund, Green Climate Fund na maeneo mengine kama UNEP na tumejipanga vizuri tutakapopata fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine pia fedha hizi tutazitumia kufanya tathmini ya kina katika maeneo ambayo yameathirika sana na suala zima la mabadiliko ya tabia nchi ili tuweze kuchukua hatua mahsusi ya kutatua tatizo hili. Tutatumia fedha za wahisani lakini vilevile tutatenga fedha zetu za ndani ili kukabiliana na tatizo hili la mabadiliko ya tabia nchi ambalo sasa linatishia dunia, linatishia nchi yetu.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yake kimesema kwamba shule ni bure kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuyaachia matokeo ya wanafunzi ambao wanadaiwa na NECTA kwa sasa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa hoja yake, niseme kwamba hilo suala tumelipokea, tutalifanyia kazi, halafu tutakuja kutoa majibu
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nilitaka kwanza afanye marekebisho ya jina, naitwa Hawa na siyo Awa. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, napenda kujua huo mwaliko wa HELM umetumwa lini ili tuweze kufuatilia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri amekuwa akituhamasisha sana Wabunge kuwahamasisha wawekezaji katika mikoa yetu. Napenda kufahamu ni vivutio gani anavyo ambavyo angependa pale tunapohamasisha tuviseme ili tusikwame kama ambavyo viongozi wa Mkoa wa Mtwara walivyokwama katika suala hili la kiwanda cha HELM?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Nahitaji kutoa maelezo kidogo kwa lile la kwanza hata home boy wangu amuita hivyo hivyo. Lile jina ambalo siwezi kulisema hata home boy wangu huwa anamwita hivyo hivyo. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kwamba kampuni ya HELM imealikwa na TPDC siku 10 zilizopita. Mimi pamoja na yeye Mheshimiwa tutawasiliana na TPDC na kwa kauli yangu nawaagiza TPDC wawasiliana na huyo mwekezaji na watoe taarifa wakati tukiwa hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie vivutio wanavyovizungumzia, tatizo hasa siyo vivutio ni ucheleweshaji wa mradi walioupata watu wa Mtwara. Kilichopelekea ucheleweshwaji wa mradi ni taarifa za kisayansi. Wakati tukiwa na TCF 2 Mtwara tulikuwa hatuna uhakika kama gesi ile ingeweza kutosha mahitaji yetu hasa mahitaji ya umeme. Uvumbuzi wa gesi TCF 2.17 za Ruvu, zimetupa kiburi na kujidai kwamba tunaweza kuwasha mitambo. Ndiyo maana tarehe 10 Julai, kuna mwekezaji nakwenda kuzindua mtambo wake wa megawati 400 pale Bagamoyo. Kwa hiyo, hayo yaliyopita yamekwisha, ukitaka vivutio vinapatikana kwenye Investment Policy, viko wazi na vingine nitaandika kwenye jedwali. Ninyi njooni mnione mimi, mwekezaji akikwama mje mnione, ikikwamishwa na Wizara yoyote njooni mnione mimi. Mimi ndiyo receptionist, nitaweza ku-clear matatizo yanayokwamisha uwekezaji.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa anafahamu kwamba tangu ulivyomalizika mradi wa MACEMP hakuna juhudi zozote ambazo zimechukuliwa na Serikali za kuwawezesha wavuvi katika masuala mazima ya zana pamoja na utaalam wa uvuvi na ndiyo maana wavuvi sasa wanatumia zana ambazo siyo sahihi. Je, anakubaliana na hilo na wanachukua hatua gani katika kulitatua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tokea uishe mradi wa MACEMP kumekuwepo na changamoto nyingi sana lakini naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba uvuvi haramu au wa kutumia zana ambazo haziruhusiwi za uvuvi hauwezi kuruhusiwa kwa sababu yoyote ile kwa sababu kimsingi ni vitu ambavyo vinapingana na sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nieleze tu kwamba wavuvi wote kabla hawajapewa leseni ya uvuvi wanakuwa wamefahamishwa na wamefundishwa kuhusu uvuvi haramu ni nini na kwamba ni nini kinatakiwa watekeleze. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuwaomba wavuvi wote nchini kufuata taratibu ambazo tayari wanafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na mradi wa MACEMP kwisha bado jitihada za Serikali za kuwapatia wavuvi mafunzo pamoja na nyenzo bora za uvuvi zinaendelea na ndiyo maana katika bajeti yetu ambayo mliipitisha Waheshimiwa Wabunge tuliainisha kabisa namna ambavyo tutajaribu kugawa na kusaidia vikundi kuweza kuwa na zana bora za uvuvi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini, maeneo ya Moma na Dihimba kote, usikivu wa simu za mikononi siyo mzuri.
Je, ni lini atakwenda kufuatilia yale makampuni ambayo yalipewa kazi ya kuweka minara huko ambapo mpaka sasa hivi kwa kweli kwingine wamejenga, haisikiki na kwengine hawajafika kabisa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, CHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hawa Ghasia kama Mwenyekiti wa Kamati, vilevile amemwona Waziri wangu kutetea maslahi ya watu wa Jimbo lake. Namshukuru sana kwa juhudi kubwa anazozifanya, kwanza kutusaidia sisi wote kama nchi kupitia Kamati ya Bajeti, lakini vilevile kuwatetea wananchi wa Wilaya ya Mtwara, Jimbo la Mtwara Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia nitafika kukakagua hilo eneo na baada ya hapo tutampa majibu sahihi, siyo majibu tu, lakini vilevile kujibu kwa vitendo.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, NHIF wamekuwa wakitafuta viwanja kule Mtwara kwa ajili ya kujenga kituo kwa ajili ya kutolea huduma za kisasa. Kwa nini wasishirikishwe katika ujenzi huu wa Hospitali ya Kanda ya Kusini badala ya kufanya duplication ya kujenga huduma ambazo zinafanana?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa nini Serikali isitenge pesa zake yenyewe kwa kiasi cha kutosha ili kuhakikisha kwamba ujenzi huu unakamilika kwa haraka kwa sababu umeanza tangu mwaka 2009 na sasa hivi tuko 2016, ni karibia mika saba sasa. Je, wako tayari kutenga pesa zake za kutosha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 badala ya kuendelea na mazungumzo ambayo yanaonyesha kutokuzaa matunda?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii, pia namshukuru sana Dada yangu, Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini kwa maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana kwa jitihada anazofanya kufuatilia ukamilishaji wa mradi huu wa hospitali, yeye pamoja na Mheshimiwa Abdallah Chikota wamekuwa wakinisumbua sana kuhusu utekelezaji wa mradi huu.
Kwa msingi huo mimi mwenyewe nilifanya ziara kwenye mradi huu na mpaka sasa nimekwisha kufanya ziara mbili za kazi na katika ziara moja tuliongozana na wenzetu wa NHIF ambao ni Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa ambao upo chini ya Wizara yetu na kuwapa ushauri badala ya wao kujenga hiyo Center of Excellence ambayo wamekusudia kuijenga kule Kusini wafanye tathmini na watazame namna ya kutumia fedha zile ambazo walizikusudia kwa mradi wao kuwekeza kwenye kukamilisha mradi huu wa Hospitali ya Kanda ya Kusini, hivyo wazo lake na sisi tulikwishaanza kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lile swali la pili kwamba kwa nini Serikali haitengi pesa za kutosha kwenye bajeti yake; ni kwamba tayari mradi huu umekuwa ukitekelezwa kwa kasi kidogo na Serikali na majengo kwa sehemu kubwa ya kuanzia yamekwisha kukamilika yako takribani asilimia 95 kuanza kutumika na mimi katika ziara zangu nimewaelekeza namna ya kuanza utekelezaji wa mradi wenyewe hivyo hivyo ulipofikia kuliko kuusubiria mpaka ukamilike ili walau huduma za mapokezi, huduma za dharura lakini pia huduma za out patients (huduma za wagonjwa wa nje) zianze kutolewa kwa kutumia majengo ambayo tayari yanaelekea kukaimilika kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa tumekwisha kuwekeza takribani shilingi 1,782,000,000, na katika Bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali kwenye bajeti yake imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi kwamba tutaendelea kuitazama hospitali hii Ili kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 tuweze kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi huu.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kwanza niulize swali linalohusiana na Halmashauri yangu ambayo inavyo Vituo vya Afya, cha Mahurunga na Kitere, ambavyo vinavyo vyumba vya upasuaji na vifaa vyote vinavyohitajika; lakini mpaka sasa hivi havijaweza kufanya kazi kwa sababu hakuna watalaam wa kuweza kufanya hizo huduma suala ambalo linakatisha tamaa kujenga vituo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika bajeti iliyopita tuliiomba Serikali itenge pesa kupitia mafuta kwa ajili ya kujenga Zahanati na Vituo vya Afya, Serikali ikatuahidi kwamba tuipe muda ifanye tathmini nchi nzima ili kujua mahitaji halisi na kujua majengo mangapi hayajakamilika. Tulitaka kufahamu, je, Serikali sasa imeshakuwa tayari, imeshafanya hiyo tathmini ili iweze kuingizwa katika bajeti inayokuja?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kujibu maswali matatu; kwanza, la Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Hawa Ghasia la kuhusu Kituo chake cha Afya, ambacho kina kila kitu, lakini hakina watalaam; ana vituo viwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, sekta ya afya ina upungufu wa watalaam takriban asilimia 48, lakini tayari Mheshimiwa Rais juzi amezungumza kwamba tutaajiri watalaam katika Sekta ya Afya, kwa hiyo, tutapanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunasubiri kuajiri watalaam, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa wawapange upya watalaam walionao. Unaweza ukaenda katika Kituo cha Afya ukakuta kina watalaam 18, lakini kituo kimoja cha afya katika Wilaya hiyo hiyo kina watalaam watatu. Kwa hiyo, hili ni jukumu la Makatibu Tawala wa Mikoa kufanya redistribution.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Hawa Ghasia kwamba, je, ule mpango wa kufanya tathmini ya maboma ya Vituo vya Afya, tumefikia wapi? Ni kweli Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais (TAMISEMI), baada ya kupitisha bajeti ya mwaka 2015, tulifanya tathmini na tumesha-identify kuna maboma mangapi ya Zahanati, kuna Vituo vya Afya vingapi ambavyo havijakamilika; na tayari Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango yuko hapa, tumekubaliana badala ya kusema tunaenda kuvimaliza vyote katika mwaka mmoja, ndiyo narudi katika swali la Mheshimiwa Zacharia. Tuta-pick angalau Kituo cha Afya kimoja katika kila Halmashauri badala ya kusema tutafanya Kituo cha Afya katika kila Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mkakati wetu kila mwaka angalau Kituo cha Afya kimoja kwa kila Halmashauri baada ya miaka mitatu tutakuwa na Vituo vya Afya takriban 500, asilimia 100 zaidi ya Vituo vya Afya 500 ambavyo vimekuwepo nchini miaka 50 baada ya uhuru, sisi tutavipata katika kipindi cha miaka mitatu. Kwa hiyo, tutaleta katika bajeti ya mwakani hivyo, kituo kimoja cha afya kwa kila Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Gekul, ni kweli hii sera ya msamaha kwa wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano, ndiyo mojawapo ya sababu ya changamoto katika upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba katika Vituo vya Afya vya Umma. Sasa ni takriban asilimia 60 kwa kweli ya watu ambao wanahudumiwa katika hospitali zetu za umma, ni hawa watu wa msamaha. Kwa hiyo, hawachangii wakati Sera ya Afya inasema, huduma za afya ni kuchangia. Mkakati wetu ni upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema, nilitaka kuongeza, tunazungumzia financing for the health sector, jinsi gani tutatengeneza, jinsi gani tutagharamia Sekta ya Afya. Kwa hiyo, tunaenda kwenye Bima ya Afya kwa kila Mtanzania; maana yake, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuwakatia Bima ya Afya wanawake, wazee na watoto wa chini ya miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa Pili tutakuja kwako Bungeni, tulete mapendekezo yetu na tunategemea moja ya vyanzo vya fedha hizi ni zile kodi zinazotokana na mambo ya madhambi; sin taxes. Kwa mfano, pombe, sigara na bia na naamini Waziri wa Fedha na Mipango atatukubalia kwa ajili ya kufikia Universal Health Coverage itakapofika mwaka 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi napenda niulize swali la nyongeza.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini tayari imeshapanua kituo chake cha afya cha Nanguruwe, ambapo pia kinacho chumba cha upasuaji cha kisasa, chenye vifaa na kimeanza kutoa huduma kwa lengo la kuifanya iwe hospitali ya Wilaya, ambapo majengo yote yanayotakiwa yamekamilika.
Je, ni lini Serikali itaibadilishia hadhi kutoka kituo cha afya na kuwa hospitali ya Wilaya baada ya kuwa kila kitu kimekamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli katika mpango wa bajeti tulipokuwa tunajadili na watu wa Mtwara kule Nanguruwe, mwaka huu kwamba wameonesha demand ya kituo hiki, na ni kweli walihakikisha kituo hiki kimekamilisha vitu vyote vya msingi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Hawa Ghasia, tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Afya kuangalia zile taratibu za kikawaida kuhakikisha kituo hiki sasa kinapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya, tukijua wazi kwamba ikiwa hospitali ya Wilaya hata kasma ya bajeti itabadilika eneo hilo na wananchi wataendelea kupata huduma nzuri baada ya kituo hicho kupanda kuwa Hospitali ya Wilaya.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumza ni Februari tunaelekea Juni, mwaka wa fedha unaishia na Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa ambayo ina tatizo kubwa la watumishi na hasa wa sekta ya afya. Nilitaka kufahamu ni lini hicho kibali kitatolewa na ajira hizo zitaajiriwa? Kwa sababu ninavyo vituo viwili vya afya vyenye vyumba vya upasuaji, lakini hakuna upasuaji unaofanyika kwa sababu hakuna watumishi na Wilaya nyingine zote za Mkoa wa Mtwara hali ni hiyo hiyo, ni lini kibali kitatolewa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna anavyofuatilia masuala mazima ya utumishi na tunatambua pia, na yeye alishakuwa Waziri wa Utumishi na alifanya kazi kubwa na nzuri sana hapo alipokuwa na sisi tumeweza kuvaa viatu vyake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sasa, kama nilivyoeleza, tumeanza na watumshi wa sekta ya elimu pamoja na mafundi sanifu wa maabara na tunatarajia ifikapo mwezi wa tatu wataweza kuingia katika ajira. Kwa upande wa watumishi wa sekta ya afya, muda si mrefu tutaanza pia awamu yao na ninadhani kati ya mwezi wa tatu mpaka wa nne watakuwa wameshaingia katika utumishi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi nilulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Mtwara hadi Newala – Masasi kipande cha kutoka Mtwara hadi Nnivata tender ilishatangazwa, na kwa mujibu wa maelezo ya Meneja TANROADS Mtwara ni kwamba mkataba ulisainiwa tarehe 16 Januari, lakini ukimuuliza Waziri anasema hajui, Naibu Waziri hajui na wengine wanakwambia mara mkataba uko kwa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali. Sasa nilitaka kujua mkataba umesainiwa au haujasainiwa na inachukua muda gani kujua ndani ya ofisi hiyo hiyo inamchukua Waziri muda gani kupata taarifa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ghasia na kupitia kwake na wananchi wake wa Mtwara Vijijini kwamba Serikali kama ambavyo imepanga kwenye bajeti ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami katika mwaka huu wa fedha itatekeleza ahadi hiyo na tofauti ambayo ameieleza kati ya tunachokifahamu sisi na anachoambiwa na TANROADS Mkoa kule kimetokana na sintofahamu iliyotokea kwa mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kila kitu kukamilika na document kuwa tayari kusainiwa kuna kipengele ambacho ilibidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali akikamilishe kukiangalia na kukiweka sawa kabla mkataba haujasainiwa.
Kwa hiyo, ninavyofahamu mimi na kwa namna Mheshimiwa Waziri wangu alivyonieleza na namna nilivyoambiwa na TANROADS pamoja na Katibu Mkuu mkataba huu utasainiwa muda wowote katika wiki hii kwa sababu Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu namshukuru ametusaida kulitatua lile tatizo ambalo lilikuwa linatusumbua, kwa hiyo mkataba utasainiwa muda wowote kati ya wiki hii na wiki ijayo. Kikubwa na cha msingi fedha tumetenga, tuko tayari kuanza ujenzi, process za kumpata mkandarasi wa kujenga tayari sasa zimefikia mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba Mheshimiwa Ghasia pamoja na mengi anayotushauri kwenye hili atuvumilie kidogo, lakini kubwa ni kwamba zile fedha tulizozitenga shilingi bilioni 21 zitatumika katika mwaka wa fedha kuanza ujenzi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo; zipo hisia kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwamba Wizara ya Nishati na Madini haina nia ya dhati na kiwanda cha mbolea
cha Msanga Mkuu cha HELM ambacho amekielezea uwekezaji wake. Kwa sababu majadiliano yamechukua muda mrefu na ujenzi ambao ameusema utakamilika mwaka 2020 kuanza kwake ujenzi itategemea makubaliano ya bei ya kuuziana gesi.
Je, anatoa kauli gani juu ya hisia za wananchi wa
Mtwara kwamba kiwanda hcho hakitazamwi vizuri ndani ya Wizara yake hasa ukizingatia hata kwenye jibu lake la msingi hakukitaja kiwanda hicho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Hawa Ghasia katika jibu langu la nyongeza nimeeleza mikakati ya Serikali ya kujenga kiwanda hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimeeleza hatua ya majadiliano ya gesi kwa sasa nikupe taarifa Mheshimiwa Hawa Ghasia na mimi nakushukuru sana unavyohangaikia maendeleo ya wananchi wa Mtwara Vijijini, Kampuni ya
Helmo kutoka Ujerumani inapendekeza kwa sasa hivi ichukue gesi kwa dola 2.6 wakati ukifanya hivyo Mheshimiwa Hawa na wewe unajua makadirio ya gharama ya chini kabisa
katika standard price ulimwenguni kote na hapa kwetu ni dola 4.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Ghasia nikuhakikishie tu jitihada za makusudi zinafanyika kuhakikisha kwamba wananchi wa Mtwara wanapata gesi, lakini matumizi ya mbolea pia. Kwa hiyo, hatua tunayochukua majadiliano kati ya Kampuni ya HELM kwa kiwanda cha mbolea pamoja na Serikali yatakuwa yamekamilika na kiwanda cha mbolea kitaanza sasa kutekeza katika ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020 waliosema ni makadirio yao ya kampuni kuwa wamesha-set taratibu zote na ujenzi wa kiwanda hicho kukamilika. lLakini jitihada za Serikali ziko pale pale. Ahsante sana.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tatizo hili la migogoro baina ya wakulima na wafugaji siyo la Mkoa wa Morogoro peke yake, tumelishuhudia katika Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Lindi, sasa kwa nini Wilaya zote tatu za majaribio zimekuwa katika mkoa mmoja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, je, Mkoa wa Pwani na Lindi
zoezi hilo litafanyika lini ili kuondoa changamoto ya wakulima na wafugaji hasa katika Wilaya za Rufiji, Kilwa na yale maeneo ambayo wafugaji wapo kwa wingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza napokea pongezi zake ambazo ametoa na mimi nashukuru, ni kutokana na ushirikiano wetu sote. Katika maswali yake mawili aliyozungumza; la kwanza, amesema tatizo la migogoro lipo katika mikoa mingi nchini na kwa nini tumeamua kuanzia Mkoa wa Morogoro peke yake na Wilaya zote tatu za mfano zipo Mkoa wa Morogoro?
Mheshimiwa Spika, napenda nilithibitishie Bunge lako hili, nadhani wote ni mashahidi kwamba katika ile migogoro ya wakulima na wafugaji kwa Mkoa wa Morogoro ilikuwa ni kama imekithiri.
Mheshimiwa Spika, mauaji mengi yalikuwa yanatokea kule na kila leo kulikuwa na changamoto za hapa na pale na ndiyo maana tukasema sasa kwa sababu maeneo hayo yamekuwa na mgogoro mkubwa tuanzie pale ili tuweze kupata uzoefu pia wa kuweza kutatua migogoro ya aina hiyo katika maeneo mengine.
Kwa hiyo, kuanzia Morogoro lengo lake kubwa ilikuwa tu ni katika kuhimili ile migogoro iliyokuwepo na kuona namna gani tutaweza kuisitisha ili tuweze kufanya kazi hii vizuri zaidi katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema, ni lini tutakwenda katika Mkoa wa Pwani na Lindi na hususan Rufiji na Kilwa, kama alivyotolea mfano.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu, kwa sababu utatuzi wa migogoro hii na upangaji na upimaji utafanyika kwa awamu mbili na tumekwishaanza, mimi niseme pale ambapo tutakuwa tumepanga ratiba inayofuatia, basi tutaweka na mikoa ambayo ina migogoro ukiwemo na Mkoa wa Pwani ambao nao pia unaonekana una migogoro mikubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafanya hivyo kutegemeana na uzoefu tulionao katika migogoro iliyopo lakini pia katika kuhakikisha migogoro mingine haiibuki.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda niulize swali la nyongeza. Mikakati ya Serikali ni kuboresha afya katika maeneo yote na kupandisha hadhi baadhi ya Vituo vya Afya kuwa Hospitali. Katika Mkoa wa Mtwara tulikuwa tunapandisha hadhi Kituo cha Afya Nanguruwe na Kituo cha Afya Nanyumbu, kuhakikisha inakuwa Hospitali na tumefikia hatua nzuri ya kufungua kuwa Hospitali. Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu kutoka TAMISEMI alipokuja alisema Vituo vya Afya viendelee kuwa Vituo vya Afya na tuanze ujenzi upya. Sasa nataka kujua ile ni kauli yake au ni kauli ya Serikali? Kwa sababu Serikali siku zote imekuwa ikitusaidia kufikia hapo ili vituo hivyo viwe hospitali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Kituo cha Afya cha Nanguruwe na Nanyumbu, Mheshimiwa Mbunge anakumbuka nilivyofika pale, Nanguruwe, Kituo cha Afya ambacho kina facilities nyingi sana, kilikuwa na suala zima la ahadi ya Mheshimiwa Rais kuifanya kuwa Hospitali ya Wilaya. Maana yake nini? Naibu Katibu Mkuu wetu alizungumza technically kwamba nini tunatakiwa kufanya? Kwamba tukiwa tuna upungufu wa mambo ya hospitali, lazima tujiwekeze katika suala zima la ujenzi wa hospitali zetu za Wilaya. Siyo kama ni kauli yake, isipokuwa ni kauli ya Serikali sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kwamba tuvi-convert Vituo vya Afya kuwa Hospitali za Wilaya, maana yake tunafifisha baadhi ya juhudi, lakini kuna maeneo mengine yana special preferences. Kwa mfano, pale Nanguruwe, Nanyumbu au maeneo mengine niliyotembelea, unakuta Vituo vya Afya vingine walikuwa katika program ya kufanya kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimesema tuna-treat maeneo mengine case by case. Kwa case kama pale Nanguruwe au Namyumbu ambapo hata Mheshimiwa Rais mstaafu alipopita pale alitoa ahadi, ahadi ile itaendelea kuwepo pale pale. Lengo kubwa ni kuwasaidia wananchi wale na kwa kiwango kikubwa Serikali imesha-invest vya kutosha kukodi na vifaa vingine kuwasaidia wananchi wa eneo lile.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu marefu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kwa kweli nashindwa hata kusema kama Mbunge ninayewakilisha wavuvi yaani nikirudi Jimboni sina hata cha kuwaambia kufuatana na haya majibu ambayo yapo, kwa sababu ukiangalia nilitegemea aniambie angalau bajeti ya mwaka huu zimetengwa fedha kiasi fulani kwa ajili ya wavuvi angalau wa Jimbo lako au wa Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ninaweza kwenda kuwaambia wakulima mwaka huu kiasi cha pembejeo kilichotengwa kwa sulphur na dawa za maji, kila kitu nina uwezo wa kwenda kusema, lakini kwa wavuvi sina.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la mabenki aliyozungumza, mabenki ni ya kibiashara na wavuvi hawana dhamana yoyote ya kuwaunganisha. Katika haya mafunzo, unataka kutoa mafunzo ya Bahari Kuu kwa mwambao wa bahari kutoka Moa mpaka Mtwara wenye Wilaya zaidi ya 14, wavuvi 50 ambao kwa mimi naona ni sawa na kijiji kimoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda Mheshimiwa Waziri aniambie mgawanyo wa hao 50; wavuvi ambao anataka kuwapatia mafunzo ya uvuvi wa Bahari Kuu kila Wilaya wanawapa wangapi ili na mimi ninavyorudi Mtwara Vijijini nikaseme kwamba watapewa kiasi hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tulikuwa na mradi wa MACEMP ambao ulifanya vizuri sana katika kuwasaidia wavuvi, hivi mpango huo umefikia wapi au umekufa au kwa nini tusichukue mafunzo tuliyoyapata kutoka kwenye MACEMP tukahamishia Serikalini, tukatekeleza sisi wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anaposema Mheshimiwa Hawa Ghasia kwamba imekuwa ni vigumu kuweza kusema ni fedha gani zimetengwa kwa ajili ya Wilaya yake ya Mtwara Vijijini, lakini natambua kwamba Mheshimiwa Ghasia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, kwa hiyo, ana uelewa zaidi wa namna bajeti katika sekta ya uvuvi inavyotengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tu wanaoshikilia hasa bajeti ya kuendeleza uvuvi ni Halmashauri. Kwa hiyo, kama Diwani anayeshiriki katika mijadala katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini najua kwamba itakuwa ni rahisi yeye kufuatilia zaidi. Niliyoyazungumza mimi ni ya kisera zaidi kwa sababu amezungumzia kuhusu mipango, lakini pale nimeonesha kidogo fedha ambazo zinasimamiwa na Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niko tayari kukaa naye tujadiliane niweze kumwonesha hiyo mikakati kwa ufasaha zaidi. Kuhusiana na MACEMP ni kweli kabisa kama anavyosema, MACEMP umekuwa ni mradi ambao umekuwa na mafanikio makubwa na ndiyo maana yale tuliyojifunza kutoka MACEMP tumeweza kuweka katika Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili ili kuweza kuyachukua yale mazuri na kuweza kuyajengea mkakati ili wavuvi wetu waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la namna gani wale wavuvi 50 watakavyogawanywa, niko tayari vilevile kukaa naye tuangalie namna gani katika hao kuna ambao watatoka Mtwara Vijijini, lakini niseme kigezo ni uwezo wa kuvua katika Bahari Kuu. Tunaweza tukafikiri kwamba ni wachache, lakini sio Watanzania wengi, sio wavuvi wengi wa kawaida ambao wanaweza wakajihusisha na uvuvi wa Bahari Kuu.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi napenda kuuliza swali la nyongeza.
Swali ambalo Mheshimiwa Kikwembe ameuliza ni kwamba katika shule nyingi ikiwemo Ndanda Sekondari, Loleza na shule nyingi ambazo zilibadilishwa, zilizokuwa za wasichana na wavulana zikawa za wavulana. Hata hivyo, hizo shule hazijai kwa sababu shule ambayo ilikuwa kidato cha kwanza mpaka cha sita, leo unaifanya ya kidato cha tano tu na cha sita. Mabweni ni mengi. Nenda Loleza, hayajai; Ndanda hayajai; Mtwara Girls na shule nyingine nyingi. Maombi tayari yalishakuwa yamefika TAMISEMI na mchakato wa kufanya tathmini ulishaanza.
Je, ule mchakato ulisimama kwa tatizo gani? Nilichokuwa namuomba Mheshimiwa bado warudi wakalifanyie tathmini suala hilo kwa sababu majengo mengi yako idle na wanafunzi hasa wa kike wanakosa pa kwenda?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa ku-raise concern ambayo na sisi Serikalini tunajaribu kuitafakari. Maamuzi haya yalipofanyika pengine hatukufanya uchambuzi vizuri. Kuna faida kubwa shule inapokuwa na O-level na A- level kwa pamoja kuliko unapoamua A-level wakawa peke yake na O-level wakawa peke yake.
Hata hivyo, tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa Wizara ya Elimu ili tuweze kuona namna ya kurudisha kwa haraka tu, kwa sababu ni suala dogo tu; kurudisha ile miundombinu ipo na pengine maeneo mengine miundombinu imekuwa ikiharibiwa kwa sababu haitumiki. Kwa hiyo, concern ya Mheshimiwa Hawa Ghasia ni ya kweli na tutajaribu kuchambua kwa shule zote nchi nzima tuweze kuona namna ya kuzirudisha shule katika mfumo ule wa zamani ulivyokuwa. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kama vitabu vyetu vyote vya dini vinasisitiza tohara, na pia tafiti zinaonyesha katika maeneo ambayo hakuna tohara ya wanaume maambukizi ya UKIMWI ni makubwa kushinda viwango vya Kitaifa, sasa kwa nini Serikali inapata kigugumizi katika kulazimisha suala hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; kama magonjwa mengine yote yanapewa chanjo, yaani chanjo inakuwa ni lazima kwa ajili ya kukinga magonjwa haya, kwa nini tohara kwa upande wa wanaume isiwe lazima ili na yenyewe iwe kinga ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kupunguza gharama kubwa kwa Serikali ya kuhudumia ugonjwa huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali inapata kigugumizi, Serikali haina kigugumizi chochote kwenye jambo hili. Tunachokifanya kwanza kwa ujumla ni lazima ieleweke dhana ya ridhaa, kwenye huduma za afya, kwenye huduma za tiba, kuna kitu kinaitwa consent, sasa kunaweza kukawa kuna ridhaa ambayo inatolewa kwa mtu moja kwa moja kwenda hospitali yeye mwenyewe kwa ridhaa yake kwa sababu anaumwa na amefika hospitali. Pale hatutamuuliza kama anaruhusu tukutibu kwa sababu yeye mwenyewe amekuja hospitali na kwa msingi huo anataka kutibiwa, kwa hiyo yule ameshatoa ridhaa ambayo ni ya yeye mwenyewe kutaka kwenda hospitali kwa sababu amefika hospitali kwa sababu anaumwa. Lakini kwenye mambo yote yatakayohusu upasuaji, vipimo, ni lazima pia kuwe kuna ridhaa kutoka kwa mgonjwa na kama mgonjwa hajitambui kutoka kwa ndugu zake, huo ndiyo msingi wa huduma za tiba duniani kote.
Mheshimiwa Spika, sasa kwenye suala hili la tohara, kwa sababu ni jambo la hiari kama vile ilivyo kwa matibabu mengine yote, ni lazima mtu atoe ridhaa yake ndiyo aweze kupatiwa huduma ya kufanyiwa tohara, na haiwezi hata siku moja kuwa ni jambo la lazima na kwa msingi huo, Serikali haina kigugumizi chochote kwenye jambo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini nitumie nafasi hii kutoa rai kwa akina mama wote nchini kutumia fursa ya kuwashawishi wenza wao watafute…

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa akina mama wote nchini kutafuta wakati muafaka wakiwa na wenza wao kuzungumza nao kwa upole, kwa heshima na upendo wa hali ya juu wale akina baba ambao wanashiriki nao tendo la ndoa ambao hawajafanyiwa tohara. Hii itasaidia kuwashawishi wanaume wao wenyewe kwa hiari yao waende kwenye vituo vinavyotoa huduma za tohara ama kwenye huduma mkoba ambazo zinazunguka kwenye mradi wetu kama nilivyosema hapo, kwa sababu tohara inapunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kiwango cha asilimia 60, sio kitu kidogo, ni kitu kikubwa. Lakini pia tohara inaepusha maambukizi ya vinasaba vya Human Papilloma Virus (HPV) ambavyo vimekutwa kwa zaidi ya asilimia 80 kwa akinamama ambao wana saratani ya shingo ya kizazi. Kwa hiyo, ni muhimu sana akina baba wakafanyiwa tohara. Na akina mama watumie fursa wakati muafaka wawasihi wenza wao waende wakafanyiwe tohara kwa hiari.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa chanjo ni lazima why not tohara? Nafikiri majibu yangu kwenye jibu langu la awali yanajitosheleza. Tohara hata kama ni kitu ambacho kingesaidia kupunguza maambukizi ya Saratani kama hivyo nilivyosema ama kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI lakini bado ili kumfanyia mtu ni lazima kuwe na hiari yake na hatuwezi kufanya vinginevyo.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kuuliza swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Mwijage. Mkoa wa Mtwara na hasa Manispaa ya Mtwara na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara tayari tumeshatengeneza Master Plan na tumeshatenga maeneo kwa ajili ya viwanda. Tunayo EPZA, lakini tunayo maeneo ambayo hayahitaji fidia wala nini. Wizara yake inasaidiaje huo mkoa kuhakikisha kwamba na wenyewe unakuwa wa viwanda kwa sababu fursa zote zipo? Gesi, bandari, mazao kama korosho yapo. Je, Wizara yake ina mkakati gani wa kusaidia Mkoa wa Mtwara? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo. Nina taarifa kwamba tarehe 2 Mei, 2017 Master Plan ya Mtwara ilikamilika. Kilichobaki au jukumu nililonalo na Wizara yangu ni kuendelea na jitihada za uhamasishaji. Nimeshaanza uhamasishaji Mheshimiwa Mbunge, juhudi zako za kunipa kwanja cha bure kwa ajili ya kujenga Kiwanda cha Sulphur siyo kwamba nimenyamaza, tunapambana kuweza kuwaleta hao wawekezaji. Niseme kilichobaki ni uhamasishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara naendelea kuhamasisha, iko kwenye ramani yangu, ni eneo ambalo liko tayari kwa ajili ya uwekezaji. Wawekezaji watakuja Mtwara.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawapatia wakulima pembejeo kwa ajili ya kilimo na wafugaji hivyo hivyo. Kwa upande wa uvuvi Serikali mna mkakati gani wa kuhakikisha na wenyewe mnawawezesha badala ya kila siku kuchoma nyavu zao na kuacha wakiwa maskini? Mwisho, naipongeza timu yangu ya Yanga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hilo la Yanga, sitalijibu, siyo sehemu ya swali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ruzuku ya kilimo, wavuvi hawajasahauliwa. Wizara ina utaratibu ambapo inatoa ruzuku kwa wavuvi wanaotaka kununua injini za boti. Kwa hiyo, kama kuna Mheshimiwa Mbunge yeyote ambaye ana vikundi vyake vya wavuvi ambao wanataka kununua boti, Serikali inatoa ruzuku ya asilimia 40 kwa vikundi vinavyonunua injini za boti. Kwa hiyo, ruzuku ipo. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza maswali mengine ya nyongeza kwa sababu swali la msingi kwa kweli Mheshimiwa limejibiwa kwa ujumla zaidi kiasi kwamba linaninyima matumaini.
Mheshimiwa Spika, swali langu niliuliza kuna mkakati gani wa kuharakisha, sasa suala la uzio wa mwaka 2011 nadhani hilo si sehemu ya kuharakisha ujenzi wa hiyo hospitali. Suala la kama Bima ya Afya pia wamekubali kusaidia katika ujenzi huo tumelisikia zaidi ya miaka miwili sasa.
Je, ni lini taratibu za ndani zitakapokamilika ambazo zilichukua zaidi ya miaka miwili?
Swali la pili, hivi majengo ya OPD peke yake yanatosha kuifanya kuwa ni Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dada yangu Hawa Abdulrahman Ghasia kwa ufuatiliaji wa karibu sana wa suala hili. Ninadhani wananchi wa Mtwara Vijiji wananisikia kwamba suala hili amekuwa akilifuatilia kwa ukaribu na hii ni mara yake ya zaidi ya tatu kuuliza suala hili.
Majibu ya swali lake la kwanza kwamba ni lini mchakato wa ndani utakamilika naomba nisitoe time frame mahsusi kwa sababu sina uhakika ni lini mchakato huu utakamilika lakini nimuahidi tu kwamba nitalifuatilia mimi mwenyewe kwa ukaribu na nitamjulisha pindi nitakapokuwa nimepata jibu la uhakika kwamba ni lini haswa mchakato wa ndani utakamilika kabla NHIF hawajatoa pesa kwa ajili ya kwenda kumalizia jengo la OPD.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linalohusu mchakato wa kuanzisha hospitali yenyewe kwamba je, inatosheleza tu kwa kuwa na OPD ili iwe hospitali ya Kanda, hapana. Tunachokifanya ndicho alichokiuliza kwenye swali la msingi kwamba, tunataka hospitali walau ianze kutoa huduma sasa katika kuanza kutoa huduma ili ikamilike zinahitajika pesa nyingi sana. Kwa kuwa pesa zote hazipatikani siku moja na mahitaji ya hospitali hii ni makubwa na sote tunakubaliana kwamba kuna umuhimu wa kuwepo na hospitali hii na huduma hizi kuanza kwa haraka, ndiyo maana tumeona kuliko kusubiria mpaka hospitali yote ikamilike wakati tuna majengo ya awali yameshakaribia kukamilika kabisa na tunaweza tukaanza kutoa baadhi ya huduma, tumeona tuanze kutoa huduma kwa awali, lakini zitatoka katika kiwango hicho hicho cha ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kuuliza swali la nyongeza kwa kaka yangu, Mheshimiwa Kapteni Mkuchika kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la watumishi katika sekta ya kilimo ni sawasawa sana au zaidi ya katika sekta ya afya. Sasa hivi maeneo mengi, hasa vijijini, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya afya.
Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuajiri watumishi wa sekta ya afya ili kunusuru maisha ya Watanzania, hasa akina mama na watoto? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba maeneo muhimu ambayo wananchi wanategemea kupata huduma ni upande wa afya, maji, hayo ni mambo yanayogusa maisha ya kila siku pamoja na elimu na barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka yote Serikali inapoajiri imekuwa ikiweka umuhimu mkubwa sana upande wa watumishi wa afya, kwa sababu Waziri wa Utumishi anaajiri hawa Maafisa Afya baada ya kuwa tayari wameshafunzwa na kuhitimimu, nataka niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba nitazungumza na Waziri mwenzangu wa Elimu na Wizara ya Afya wapate mafunzo watumishi wengi zaidi katika fani ya afya ili wakazibe mapengo haya yaliyopo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante na mimi napenda kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mtwara Vijijini, Kata ya Mambo Pacha Nne na Kata ya Tangazo, Kijiji cha Kilambo, wameanza mchakato wa kujenga vituo vya afya na michango ya wananchi inaenda kwa kasi kubwa.
Je, Serikali itatusaidiaje katika kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya katika Kata ya Tangazo, Kijiji cha Kilambo na Kata ya Mango, Pacha Nne?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu, miongoni mwa maeneo ambayo alileta kama request katika Jimbo lile la Mtwara ni eneo hilo kwa sababu liko linapakana na Msumbiji.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika vipaumbele vyetu vya sasa katika programu tunayoanza nayo kabla ya mwezi wa pili, maeneo yale tumeyapa kipaumbele na tumeyaingiza katika mpango wetu wa bajeti ya muda katika hizi funds ambazo tunazipata kutoka kwa wafadhili mbalimbali. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante viwanda vyote ambavyo vilibinafsishwa kwa maana viendelee kubangua korosho sasa hivi vimegeuka maghala tofauti na mikataba iliyoingiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni juhudi gani Serikali hasa Wizara ya Viwanda na Biashara inasimamia kuhakikisha kwamba vinaendelea kuwa viwanda na sio maghala ya korosho kwa sababu vibali vya kufanya maghala vinatolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara. Lini wataacha kuwapa vibali ya kufanya maghala na wafanye viwanda?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni juhudi gani, kama swali la msingi ilivyoelezwa Kiwanda hiki cha Masasi kimekwama kwa sababu ya shauri lililopo mahakamani. Lakini katika mfumo huo kuna viwanda vingine vipo mahakamani, katika sekta ya korosho ninavyo viwanda ambavyo nimehakikisha mwenyewe wamiliki wake wameshaanza kutengeneza mipango ya kuviendeleza ikiwemo kuleta mitambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mitambo nimeiona mwenyewe kuanzia hivi vya Kibaha mpaka vya Liwale one, kwa hiyo juhudi zinafanyika kuendelea kuwafuatilia hawa wawekezaji ili waweze kuvirudisha katika njia ya kufanya kazi viwanda hivi, ikiwa ni pamoja na kutafuta mitaji, kwa hiyo, juhudi hizi za kuhakikisha vinafanya kazi tutahakikisha zinaendelea.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ina umri wa zaidi ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake, je, mchakato wa kuanzisha ofisi mpya ya udhibiti ubora inachukua muda gani ikiwemo ni pamoja na kupata vitendea kazi pamoja na watumishi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Halmashauri mama ambayo ni Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, bajeti ambayo imetengewa na imepelekwa na Serikali imeweza kukagua shule 18 tu kati ya shule 106; je, Serikali inapoilekeza ikakague Nanyamba kwa bajeti ipi ambayo imeipeleka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni muda gani inahitajika kazi ya kuanzisha ofisi ya udhibiti ubora itachukua, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna muda maalum, yote inategemeana na upatikanaji wa fedha na tunachosema tu ni kwamba kwa sasa tumejipanga kwamba tutahakikisha kwamba Wilaya zote zinakuwa na wadhibiti ubora. Kwa hiyo, tutaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba ofisi hizo zinakuwepo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili kwamba Halmashauri mama ya Mtwara yenyewe bado haijaweza kufanya ukaguzi kwa kiwango kikubwa.
Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo letu ni kuhakikisha kwamba kadri tunavyoendelea tunapanua uwezo wa wadhibiti ubora wetu kuweka kufanya udhibiti ubora. Kwa hiyo, hata kama sasa kiwango cha udhibiti ubora kilichofanyika bado ni kidogo lakini lengo letu ni kuendelea kuongeza fedha ili tuhakikishe kwamba tunaweza tukafanya hiyo kazi kwa ufanisi na kwa wingi zaidi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa nini tusitumie uzoefu ambao tuliupata katika mradi wa MACEP ambapo zoezi la kuzuia uvuvi haramu lilikuwa linaenda sambamba na kuwawezesha wavuvi wetu kwa vifaa na zana bora ili waondokane na uvuvi haramu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia, kwamba kwa nini tusitumie uzoefu tulioupata katika mradi wa MACEP. Mradi wa MACEP ulikuwa ni mradi maalum uliofadhiliwa na Benki ya Dunia. Mradi ule ulikuwa unahusianisha vipengele vingi ikiwemo kuwawezesha wavuvi wetu ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani.
Mheshimiwa Spika, tunao Mradi unaoitwa SWIOFish hivi sasa ambao pia upo kwenye Ukanda wa Pwani. Moja ya jambo ambalo unafanya ni pamoja na kuwawezesha wavuvi, kuwafanyia capacity building kwa maana ya uwezo wao wa pamoja wa kijamii, lakini vilevile na kujenga miundombinu. Kwa hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu upo katika hatua za kati na katika hatua zake za mwisho nina imani tutafika katika hii hatua ambayo yeye ameipendekeza hapa.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri na niipongeze Serikali kwa kununua boti ndogo ya MV Kuchele. Hata hivyo, MV Kuchele itatumika vizuri sana kama Serikali itajenga majengo katika pande zote mbili au itajenga upande wa Msangamkuu ili kuwezesha kuwa na mtu ambaye analala pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo sasa hivi kama kuna mgonjwa ni lazima ile simu ipigwe na Mganga wa kituo cha Msangamkuu na wakati mwingine mganga wa Msangamkuu anakuwa hayupo Msangamkuu hivyo kuleta changamoto kubwa sana kwa wagonjwa kuweza kuvushwa upande wa pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huu upande wa pili hakuna nyumba ambayo kuna mtu analala pale, huyo ambaye anavusha kwenye hiyo boti analala nyumbani kwake na yeye kama binadamu huwa inachukua muda mrefu sana kuweza kutatua changamoto hiyo. Swali je, Serikali ni lini itajenga hiyo nyumba ya kuwezesha kulala mtu pale upande wa Msangamkuu ili dharura inavyojitokeza iweze kutatuliwa kwa haraka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa nini upande huu wa Msangamkuu ambapo MV Kuchele na MV Mafanikio zinalala kwa nini kusiwe na mtu analala pale ili simu inapopigwa aweze kuvuka kwa haraka na kuweza kutatua changamoto inayojitokeza?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeingia Bungeni lakini wakati tunamaliza Bunge lililopita nilikuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji leo hii ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake nimeendelea kumwomba anielekeze na kuniongoza nitende yaliyo mema yanayompendeza. Pili nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini, lakini tatu, nijibu sasa hoja za Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru kutokana na uzoefu alionao, aliyoyataja ndio ambayo sasa hivi tunayapanga, kwamba tuliona changamoto ya kivuko kilichokuwepo kwamba ni kikubwa na ule upande wa Msangamkuu wakati mwingine maji yanakuwa yapo chini sana, tukanunua kivuko kidogo ambacho kinabeba watu nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kivuko hiki usiku kina-park upande wa Mtwara Mjini, lakini ni kweli tunajipanga kujenga nyumba ili walinzi wakae upande wa pili kuweza kuondoa hili tatizo ambalo Mheshimiwa Mbunge analizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ndio nimeingia nitampa majibu Mheshimiwa Mbunge kabla hatujatoka katika hili Bunge kuangalia fedha ambazo tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ili nyumba iwepo askari wakae pale na kuangalia jinsi gani kile kivuko sasa kitakaa ule upande wa pili. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nataka kuuliza swali la nyongeza.
Nimesikia katika majibu yake ametaja Mikoa ya Pwani, Tanga na Unguja, lakini Mtwara na Lindi ni miongoni mwa mikoa ambao wavuvi wapo na uvuvi unafanyika kwa wingi. Je, ni lini hiyo miradi ya majaribio itafika katika Mkoa wa Lindi na Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mama Hawa Ghasia ya kwamba baada ya kuonesha mafanikio katika maeneo tuliyoyataja mradi huu utatanuka hata kuelekea katika Mikoa ya Lindi na Mtwara ili wavuvi wa Lindi na Mtwara na wenyewe waweze kwenda kuvua na kupata mafaniko makubwa badala ya kutumia muda na rasilimali nyingi bila ya sababu.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naipongeza sana Serikali katika kuhakikisha inaboresha miundombinu ya sekta ya afya. Hata hivyo, je, Serikali iko tayari kwenda sambamba na uongezaji wa watumishi katika maeneo hayo? Kwa sababu sasa hivi changamoto kubwa sana ni watumishi katika zahanati zetu na vituo vya afya pamoja na hospitali.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Hawa Ghasia, ninafahamu kwamba siyo muda mrefu tutaimarisha kituo chake cha Mahulunga pale katika Jimbo lake ambalo najua kwamba changamoto ya watumishi itakuwa kubwa. kwa bahati nzuri Naibu Waziri alishasema awali kwamba tunaajiri watumishi 6,180.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutawapa kipaumbele katika miundombinu hii wananchi waweze kupata huduma ya afya katika Jimbo la Mtwara DC.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Wizara inayo dira na inayo dira na mpango mkakati ambapo inatambua matatizo yaliyopo na hayo matatizo yanaiwekea katika mipango yake mikakati. Je, kwa mujibu wa mpango mkakati wake hizo nyumba za Askari wa Masasi zitajengwa lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa mujibu wa mpango wa mkakati huohuo na dira yake haya magari mawili au zaidi kwa Wilaya ya Masasi yatatolewa lini badala ya kuacha tu bila kuwekewa muda?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwamba kulingana na mipango tuliyokuwa nayo kuhusiana na ujenzi wa nyumba za Polisi Masasi pamoja na kupeleka gari, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba mipango hii inategemea na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la nyumba bahati njema ni kwamba tayari tumeshapata fedha za kuanzia ambayo tunatarajiwa kujenga nyumba 400. Kwa hiyo, katika Mkoa wa Lindi pia nyumba hizo zitajengwa, naomba baada ya Bunge hili niangalie ili niweze kumpa takwimu halisi za wilaya ya Masasi kuhusiana na nyumba hizo zipoje.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la gari nimezungumza kwamba, kulingana na hali ya uhalifu, hasa kubwa zaidi jiografia ya Masasi ilivyo inastahili kupata gari. Nikaeleza kwamba, pale ambapo magari yatapatikana basi katika maeneo ya vipaumbele vilevile Wilaya ya Masasi ni mojawapo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira magari yakipatikana tutapeleka na bajeti ikikaa vizuri nyumba tutajenga. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa nini Serikali kama inaona umuhimu wa mazingira inashindwa kutenga fedha kwa ajili ya kutengeneza GFS Code? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Wizara inao mkakati wa kusimamia hizi sheria kwa sababu sheria ni nyingi na zinajitosheleza lakini kinachoonekana hapa ni udhaifu katika usimamizi wa sheria. Je, mkakati upo wa kuzisimamia hizo sheria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Abdullahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na kule kwao Naumbu karibu na Mkunguni wanamuita mama ambaye hakubali kushindwa, mama ambaye tunaamini kwa namna anavyowawakilisha Mtwara huyu mama mpaka mwenyewe atakaposema kwamba sasa basi nipumzike lakini anawawakilisha vizuri wananchi wa Mtwara Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana wakati mwingine yeye kama mchezaji huwa ana-overlap anasaidia mpaka Jimbo la Mtwara Mjini. Juzi juzi ameuliza maswali ambayo yalikuwa yanahusu mifereji pale Mtwara Mjini, anamsaidia rafiki yetu ndugu Mheshimiwa Nachuma. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kulikuwa na tatizo la kupanga bajeti au kuanzisha code maalum (kasma) kwenye Halmashauri zote katika nchi yetu lakini Mheshimiwa Waziri amekwishatoa mwongozo na kuomba Halmashauri hizi waweze kuanzisha hiyo kasma na kutenga fedha. Hii ni sambamba na Wizara zote za kisekta kuanzisha kitengo maalum ambacho pia kinatakiwa kwa mujibu wa sheria kusimamia mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, kwamba tuna mikakati na pengine anadhani ni udhaifu wa usimamizi wa sheria. Nimhakikishie Mheshimiwa Hawa Ghasia, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 27 imetoa wajibu kwa kila Mtanzania kulinda na kuhifadhi rasilimali za nchi yetu. Pia tuna Sera hii ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 1997 na yenyewe ni sera ambayo inahakikisha kwamba mazingira yetu yanalindwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ghasia tuna sheria hii hapa Sheria Mama Na.20 ya 2004 ambapo Kifungu cha 6 kimewapa wajibu wananchi waweze kulinda na kuhifadhi mazingira. Tuna Ilani ya CCM hapa Ibara ya 152 ambapo tunakwenda kupambana na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Ndiyo maana sasa kutokana na yote haya hata juzi hapa nilielezea tulivyo na mikakati ya 2007 ya kitaifa ya kuhimili katika masuala ambayo ni ya uharibifu wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge ni mashahidi hapa, suala ni mindset ya wananchi, tuna sheria nzuri na mikakati lakini mindset ya wananchi ndiyo tatizo. Mungu amemuumba mwanadamu kwa mfano wake lakini bado wanadamu hawahawa wanamuangusha pamoja na kwamba Mungu alimweka kuanzisha mazingira kwenye bustani ya Eden. Kwa hiyo, nitoe wote kwa wananchi wote na Wabunge, sisi wenyewe tuhakikishe kwamba tunalinda na kuhifadhi mazingira, ahsante.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa korosho ambazo zimegundulika kuwa zimechanganywa na mawe zilipitia Bandari ya Dar es Salaam na tatizo hilo halipo katika Bandari ya Mtwara: Kwa nini Serikali isitoe kauli kwamba kwa korosho za Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ni marufuku kupitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, huu uchunguzi unaonekana umechukua muda mrefu sana na swali langu niliuliza walioruhusu, ni rahisi sana kukamata walioruhusu korosho hizo ziende kwa sababu kulikuwa na uwezekano kabisa kuzigundua kabla hazijasafirishwa kwenda nje ya nchi. Kwa nini Serikali inasita kuwataja waliohusika ili iwe fundisho kwa wengine katika msimu ujao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uhalifu hauna destination lakini sisi Kama Serikali hilo tumelipokea, tutalifanyia tathmini na tuangalie jinsi gani Bandari ya Mtwara inaweza ikatumika pia badala ya ile ya Dar es Salaam ingawa pia hao watu wabeba mizigo hata meli unakuta wakati mwingine anataka apeleke mzigo mahali ambapo pia anaweza akarudi na mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, Serikali sisi sio kwamba tunapata kigugumizi. Tume ya kitaalam ilimaliza kazi yake na tumeshawasilisha hili jambo kwenye vyombo vya dola, inafanyia kazi na mara tu ule uchunguzi wa kina na wa uhakika utakapofanyika wote waliohusika watatajwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Ahsante.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, asante nilitaka kuuliza swali la nyongeza, suala la ununuzi wa Korosho unaendana sambasamba na ulipaji wa wadau wanaoshiriki katika suala zima la Korosho, ununuzi unaoendelea mpaka sasa hivi halmashauri hazijapewa pesa yao ya ushuru hata senti tano. Nilitaka kuiuliza Serikali yangu, kwa kuwa Serikali imeamua kununua Korosho ni lini italipa ushuru wa halmashauri ili Bajeti zetu ziende kama tulivyozipanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia Mbunge wa Mtwara Vijijini, kwanza ni kweli kuna watoa huduma mbalimbali katika zao la Korosho, na sisi kama Serikali tuliona mwanzoni kutokana na mkanganyiko uliokuwepo tuliweka mkazo zaidi kulipa kwamba wakulima kabla ya watoa huduma.

Mheshimiwa Spika, na mpaka sasa tulishalipa wakulima zaidi ya asilimia 59 sasa hivi tumeshaanza kulipa na watoa hudma wengine wakiwemo hao watu wa halmashauri, mpaka jana tulishalipa zaidi ya bilioni nne kwa wasafirishaji lakini tumeshalipa watunza maghala zaidi bilioni sita na tushalipa pia watoa huduma wengine wasambazaji wa magunia zaidi ya bilioni nne nukta nane.

Kwa hiyo na hiyo ya Halmashauri tunaifahamu tushawaambia watu wa vyama vikuu na vyama vya msingi watunze rekodi zao vizuri wote tutawalipa kwa sababu halmashauri na Serikali kuu wote ni wadau katika hili, Serikali kuu export levy na hawa hizo fedha za halmashauri zote Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi zipo kwenye mikakati na tutazilipa. Lakini la mwisho, nitoe ufafanuzi katika hili, ni kweli Serikali tunanunua Korosho lakini sio kwamba Serikali yenyewe ndio inanunua Korosho ni Taasisi ya Serikali ya Bodi ile ya nafaka ya mazao mchanganyiko ndio inayonunua Korosho, kama zinavyofanya biashara Taasisi zingine kama TTCL na zingine sio Serikali kuu.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami naomba kuuliza swali la nyongeza. Ni kwa kiasi gani Serikali imefikisha taarifa ya uwepo wa soko la muhogo huko China katika mikoa yetu, kwa sababu katika RCC iliyopo Mkoa wetu wa Mtwara ajenda ambayo ilikosa majibu ya uhakika ni ajenda hii. Je hizo taarifa walizonazo za uhakika wa masoko wamezifikisha mikoani?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kimsingi kama nilivyosema kwamba kwanza kuliundwa Kamati ya Wataalam kwa ajili ya kutathmini changamoto mbalimbali juu ya zao hilo. Vilevile TANTRADE iliwaita wadau ambao nilikaa nao katika mkutano na kuwaelimisha juu ya upatikanaji wa masoko hayo. Kwa misingi hiyo kwa sababu Mheshimiwa Hawa Ghasia amezungumzia katika eneo maalum la Mtwara; nimwahidi tu kwamba, watumia fursa hiyo kwenda kuelimishwa ili waweze kushiriki kikamilifu.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri wa Viwanda kwa majibu mazuri aliyoyatoa kwa niaba ya Serikali. Katika nyongeza ya swali hilo kwamba, ni kweli kama Serikali tarehe 1 mwezi huu tumekaa na mnunuzi mkubwa wa mhogo kampuni ya Epoch Tanzania Limited ambaye tumeshampa kibali kama uthibitisho ili kwenda kukionesha kwenye Serikali ya China. Tumefanya hivyo, kwa sababu mnunuzi yoyote anatakiwa kwanza athibitishwe na Serikali wazalishaji wa zao hilo na tumempa jana na hiyo taarifa imeshafika Ubalozi wa China maana Serikali ya China kuthibitisha hilo. Kwa hiyo, baada ya mkataba huo sasa tunakuja maana yake tumepata soko la uhakika na linalotambulika kisheria. Kwa hiyo mwaka huu 2019 tutakuja kuwatangazia rasmi ni lini sasa tutaanza usafirishaji.

Mheshimiwa Spika, sambamba na kampuni hiyo ya Epoch Limited, kuna kampuni zingine tatu tumeshawapa
vibali, zote zimeshapata idhini ya kuuza mhogo katika soko la China, kwamba siyo kazi rahisi kwa utaratibu waliojiwekea wenzetu China, kwamba mtu yeyote tu ukiwa na mhogo sehemu unauingiza, hapana ni lazima upate uthibitisho kwenye Serikali ya uzalishaji ili kupata uhalali kama mzigo huo ni salama kwa matumizi ya nchi yao.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri; hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Mji wa Mikindani ni miongoni mwa miji ambayo iko chini ya usawa wa bahari; kwa hiyo hii mifereji ninayoizungumzia ni ile ambayo maji ya bahari yakijaa inapitisha maji kuingia katikati ya mji na iko mingi na tangu zamani hii mifereji ilikuwa imejengewa lakini kutokana na uwezo mdogo wa halmashauri imeshindwa kuifanyia ukarabati mara kwa mara. Swali, je, Serikali iko tayari kuisaidia Manispaa ya Mtwara – Mikindani katika kukarabati mifereji hii ya Mji wa Mikindani kwa sababu kuiachia manispaa peke yake ni kuiongezea mzigo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kwenda Mikindani kuona hicho ninachokizungumzia ili aweze kunielewa zaidi na hatua za haraka ziweze kuchukuliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika,
nichukue fursa hii kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijajibu swali na mimi nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake na ushirikiano mkubwa ambao anatupa sisi Wizara ya Mazingira katika kukabiliana na hali hii ya mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali lake la kwanza; kwanza nipo tayari na tupo tayari pia kusaidia maeneo yote kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la swali la msingi, kuhakikisha kwamba maeneo yote haya tunajitahidi ili tunakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia mifuko ambayo tunapata fedha kutoka kwa wenzetu, kwa maana ya Global Climatic Change.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu kwenda Mtwara. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ninayo ziara ya kuanzia tarehe 18 Iringa, lakini pia kwenda Mtwara, Njombe, Ruvuma, Lindi na baadaye nitakwenda Mtwara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba najionea mazingira halisi ya hiyo mifereji ambayo ameitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Dihimba yenye vijiji zaidi ya 30 haina kituo cha afya hata kimoja na Kata ya Mangopachanne tayari wameshaanza ujenzi wa kituo cha afya. Je, Serikali iko tayari kuwaunga mkono katika kukamilisha kituo cha afya katika Kata ya Mangopachanne?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi ipo tayari sana kuunga mkono wananchi hawa. Tuendelee kuwasiliana, tutatafuta fedha, zikipatikana tupeleke kukamilisha maboma yote na sio kule kwa Mheshimiwa Hawa Ghasia peke yake ila ni nchi nzima kwa Majimbo mbalimbali kukamilisha maboma yaliyojengwa na nguvu za wananchi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante ningependa kuuliza swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini tumechimbiwa visima 11 na kati ya visima hivyo, visima vitatu tayari Serikali imeridhia mchakato wa kutafuta mkandarasi uanze.

Je, ni lini Serikali itaridhia na visima vinane vilivyobaki navyo mchakato wa kutafuta mkandarasi uanze, ili huduma ya upatikanaji wa maji Jimbo la Mtwara Vijijini iboreke?

SPIKA: Majibu ya swali hilo Mheshimiwa Naibu Waziri Maji, tafadhali.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, lakini la kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, mama yangu Hawa, kwa kazi kubwa anayofanya katika jimbo lake, lakini kikubwa nimuagize Mhandisi wa Mkoa kwa maana ya Meneja wa RUWASA katika kuhakikisha analifuatilia hili jambo na ahakikishe lianze kwa haraka. Na sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari kuwapa msaada, ili mradi huu uanze kuwaka kwa wakati.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami napenda kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri yangu ya Mtwara Vijijini ninazo kata mbili za Moma na Muungano ambazo mpaka sasa hivi mkandarasi hajaweka umeme hata kijiji kimoja. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba anawapelekea wananchi hao umeme kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika masuala ya kuweka umeme kuna hatua. Hatua ya kwanza ni mipango kama kawaida na ku-plan network kama itakavyokuwa. Hatua ya pili ni ya kujenga kwa mfano kujenga line kubwa au line ndogondogo na baada ya hapo kuweka transforma na kuwasha. Katika misingi hiyo niseme tu kwamba nalichukua kama ambavyo umeeleza kumfuatilia huyo mkandarasi tuone kwamba hajafanya kitu kabisa au yuko kwenye hatua ambazo zimebakiza kuweka transforma tu na kuwasha.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wakandarasi wote nchini kwamba suala la umeme katika vijiji kama ambavyo Serikali inategemea kusambaza umeme katika vijiji vyote Tanzania ni la muhimu hasa ikizingatiwa katika kipindi hiki ambacho Watanzania wanahitaji kuwekeza katika viwanda na shughuli mbalimbali za kibiashara na maisha yao.

Kwa hiyo, niwaombe wakandarasi, Serikali imewapa heshima, hasa wakandarasi wa ndani kuwapa nafasi ya kufanya kazi hizo badala ya kuwategemea wakandarasi wakubwa kutoka nje, watumie wakati huo mzuri na watumie nafasi hiyo kuhakikisha kwamba hawaiudhi Serikali na kusababisha kuwanyang‟anya kazi na kuwapa kazi wakandarasi kutoka nje jambo ambalo walikuwa wakililalamikia siku zote.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kuuliza swali moja la nyongeza. Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa sana baina ya zana zipi zinaweza kutumika katika uvuvi na zipi hazifai. Miongoni mwa maeneo ambayo mkanganyiko huo upo ni pamoja na katika Jimbo langu la Mtwara na mara nyingi tumekuwa tukimwomba Waziri au Naibu Waziri mwenyewe waje ili wakae na wavuvi wakubaliane kipi ni sahihi na kipi si sahihi lakini suala hilo limekuwa gumu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuniambia ni lini atakuja Mtwara ili kuongea na wavuvi wa Mtwara kwa sababu kwa zaidi ya miaka mitatu hawajawahi kumwona Waziri wala Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza kwa kufuatilia kwa karibu sana hali za wavuvi wa Mtwara na naomba tu nimhakikishie kwamba Serikali iko makini sana katika kuwafuatilia wavuvi wetu.

Mheshimiwa Spika, nimefika Mtwara, nimefanya mkutano na wavuvi wa Mtwara katika Mji wa Mikindani katika Chuo tulichokijenga cha Wavuvi cha FETA ambako ni mji wa asili wa kwake yeye mwenyewe Mheshimiwa Hawa Ghasia. Nataka nimwambie kwamba nilikutana na wavuvi na nikazungumza nao mwaka jana na katika kesi walizonipatia moja ya kesi ni matumizi ya zana aina ya nyavu za ring net, mgogoro wao ni muda gani utumike mtando huu kwa maana ya mtego huu wa ring net na ugomvi wao ni kina cha kutumika kwa zana hii ya ring net.
Naomba nimhakikishie kuwa katika jambo lingine lililotokea pale Mikindani ni choo ambacho wavuvi walikilalamikia cha pale sokoni ambacho tulitoa maelekezo kwa Halmashauri waweze kukirekebisha na taarifa tuliyonayo ni kwamba tayari wameshafanya marekebisho hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hii dhana ya kutumia kutokana na kina wavuvi walio wengi wangependa sana kuona wanatumia zana hizi nje maji mepesi, maji mafupi ambapo kwa kufanya hivyo wanakwenda katika uharibifu wa mazingira ya bahari kwa sababu huku katika maji mafupi, ndiko samaki wanakozaliana na wanapokuja kuweka nyavu zile maana yake ni kwamba wanaharibu maeneo ya mazalia. Naomba nimhakikishie kwamba nitarudi tena Mtwara kwenda kuzungumza na wavuvi na kuweza kupata hatima ya shughuli zao.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Barabara ya kutoka Mangamba - Kilambo - Msimbati itajengwa lini kwa kiwango cha lami kwa sababu ni Sera ya Serikali barabara zinazounganisha nchi kuzijenga kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba usanifu wa barabara hiyo ya kutoka Mtwara Mjini - Kilambo tumeshakamilisha. Ni nia ya Serikali kuhakikisha tumeijenga kwa kiwango cha lami pamoja na daraja ili tuweze kuungana kwa daraja la pili kwa ajili ya kwenda Mozambique.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kwa zaidi ya miaka mitatu imeshindwa kuongeza hata asilimia tatu ya upatikanaji wa maji pamoja na Serikali kuleta pesa nyingi na ipo miradi ya Mayaya na Liyo ambayo kwa zaidi ya miaka mitano haijakamilika:-

Je, Serikali ipo tayari kuunda Tume na kufuatilia kujua kwenye wilaya hiyo kuna tatizo gani ambalo linashinda kutekeleza miradi ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo nilishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kutupitishia Sheria (Na. 5) ambayo imetupa nafasi sisi kama Wizara ya Maji na rungu la kuwawajibisha Wakandarasi lakini hata kuwawajibisha Wahandisi wetu wa maji. Ninachotaka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tumeshaunda kikosi kazi katika kila mkoa. Labda niagize kikosi kazi hicho kihakikishe kwamba kinafika katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini katika kuhakikisha inatatua tatizo la maji, nami nitafanya ufuatiliaji wa kufika mwenyewe.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo ameyatoa. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza eneo ambalo amelizungumzia zaidi siyo eneo la Msanga Mkuu, ni eneo la Mtwara Mjini. Kwa upande wa Msanga Mkuu hakuna kazi yoyote ambayo mpaka sasa hivi imefanyika ambayo inaweza kubeba ujenzi wa viwanda ambavyo amezungumzia. Je, ni lini majadiliano ya bei ya gesi asilia yatakamilika ili hivyo viwanda vianze kujengwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, inapotokea kwamba mchakato wa majadiliano unachukua muda mrefu sana kama ambavyo Helm na TPDC wamechukua tangu mwaka 2011 mpaka leo 2019 majadiliano hayajakamilika. Nini nafasi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuwasaidia wawekezaji ili waweze kutoka katika huyo mkwamo ambao wameupata. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kwanza ninashukuru kwa niaba ya Wizara kwa pongezi alizotupa kwa majibu, pili niseme tu kwamba Serikali imekuwa ikiendeleza juhudi ya kukamilisha mazungumzo hayo, suala la gesi ni utajiri wa Tanzania ambao unapaswa kutumika kwa uangalifu mkubwa. Kwa hiyo, kabla ya kuingia mkataba, ni muhimu sana kwa Serikali kuangalia kwamba inampa mwekezaji gesi hiyo kwa bei ambayo kwanza itakuwa ni bei inayokubalika lakini vilevile kumhakikishia upatikanaji wa malighafi hiyo kwa wakati wote.

Mheshimiwa Spika, nikiendelea na swali lake la pili la kuchukua muda mrefu niseme tu kwamba Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji pamoja na Wizara ya Nishati na Madini tutahakikisha kwamba hilo zoezi la kukamilisha kwa bei inayotakiwa ili aweze kupewa mwekezaji linafanyika mapema iwezekanavyo. Kwa hiyo, nalichukua hili kama commitment ya kushirikiana na Wizara nilizozitaja kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi mapema ili nchi iweze kunufaika na gesi ambayo inapatikana Mtwara.(Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakumbuka Mheshimiwa Waziri alipotembelea Mkoa wa Mtwara alionyesha huu mradi kutokuwa katika mipango yake. Je, amebadilisha mawazo lini kwamba huo mradi utatekelezwa sasa hivi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mipango mingi ya kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali. Nami kama Waziri siwezi nikabadilisha mpango wowote wa Serikali kwani natekeleza mipango ya Serikali. Mradi bado upo kwa sababu ulipangwa na Serikali na utatekelezwa. Hata hivyo, kwa wakati huu tuna miradi mingine ambayo itatekelezwa huko Mtwara na mipango inaendelea vizuri.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kama ambavyo ameeleza kwamba maeneo yenye makazi wamepanua barabara kwa ajili ya kuangalia usalama wa raia na sasa hivi tunaweka zebra na matuta, lakini kumejitokeza matumizi mabaya ya zebra kwa sababu wakati mwingine unakuta waenda kwa migu ndio wanapewa muda mrefu sana kuliko hata magari na hivyo kusababisha msongamano.

Je, kwa nini Serikali isiweke taa za kuruhusu waenda kwa miguu, ili wao wawe wanapita pale kwa zamu badala ya kuwa wanapita wakati wote?

Mheshimiwa Spika, pili, matuta nayo imethibitika kwamba, kwa kuweka matuta mengi barabarani na matumizi ya madereva wetu imesababisha matatizo ya mgongo, hasa kwa wanaotumia magari.

Je, hakuna utaratibu mwingine wa kuweka usalama kwa waenda kwa miguu zaidi ya kuweka matuta barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge na kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Hawa Ghasia kwa namna anavyofuatilia mambo mbalimbali ya maendeleo. Na niseme kuhusu matumizi ya zebra na matuta ni kwamba ni kweli kumekuwepo na changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini utakubaliana na mimi kwamba tunaweka zebra na matuta ni kwa ajili ya kuhakikiha wananchi wetu wanakuwa salama kutokana na baadhi ya watumiaji wa barabara kuwa wanatumia barabara zetu bila kuzingatia utaratibu na masharti yaliyowekwa ili kuwafanya wananchi wetu waweko salama. Kwa hiyo, nilikuwa napenda Bunge lako litambue kwamba uwekaji wa zebra na matuta haya ambayo saa nyingine yameonekana kuwa ni usumbufu, lakini ni nia njema ya Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wake wanabaki kuwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwa siku za hivi karibuni tumejipanga vizuri maeneo mengi nchini tunaendelea kuweka taa. Kwa hiyo, iko mipango ambayo imefanyika na Halmashauri zetu, kuna taa nyingine wanaweka kupitia halmashuri zetu za wilaya na miji tunaendela kuweka taa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hilo nimelichukua kwa maana ya kuweka msukumo mkubwa zaidi ili maeneo mengi tuweke taa kutoa usumbufu ambao unajitokeza, ili matumizi ya barabara yaweze kwenda sawasawa na watumiaji wa magari pia waweze kwenda vema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme kuhusu matuta, kipindi sio kirefu sana nilijibu hapa swali kuhusu matuta kwamba, sisi Serikali tumeendelea kuyapunguza matuta maeneo mengi. Tuliweka matuta kwa sababu ya usalama wa wananchi, lakini tumegundua baada ya kuweka matuta elimu imeendelea kuwa kubwa kwa wananchi wetu wanaotumia barabara pale tunapothibitisha kwamba sasa eneo fulani hali ya hatari ya wananchi imepungua matuta hayo tumeyaondoa. Tumeondoa matuta mengi sana kwa hiyo, Mheshimiwa Hawa Ghasia kubaliana na mimi hilo, lakini kama kuna maeneo ambayo ni mahususi tutaona kuna matuta yanaleta shida mtufahamishe na sisi Serikali tutakuwa tayari kwenda kufanya marekebisho, ili kutoa usumbufu wa watumiaji wa barabara hususan wanaotumia magari.