Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia (17 total)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya uchumi kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba - Newala – Masasi, itaanza kujengwa baada ya upembuzi yakinifu kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahmani Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi, yenye urefu wa kilometa 210 pamoja na Daraja la Mwiti ulikamilika mwezi Aprili, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi utaanza kwa sehemu ya Mtwara hadi Mnivata, yenye urefu wa kilometa 50. Taratibu za kumpata Mkandarasi wa kujenga sehemu hii ya barabara zimekamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu hii ya Barabara ya Mtwara hadi Mnivata umepangwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-
Uwanja wa Ndege wa Mtwara ulijengwa mwaka 1965.
(a) Je, ni lini uwanja huo utafanyiwa ukarabati mkubwa ili kuwezesha ndege kuruka na kutua bila matatizo?
(b) Je, ni lini uwanja huo utawekewa taa ili ndege ziweze kutua wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya Kiwanja cha Ndege cha Mtwara. Ikiwa ni mpango wa muda mfupi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inafanya tathmini ya uchakavu wa matabaka ya lami ya njia ya kuruka na kutua ndege ili kubaini ukarabati stahiki unatakiwa na mahitaji ya fedha ya kufanya ukarabati huo. Katika kutekeleza jukumu hili, shilingi milioni 290 zimetengwa na mamlaka katika mwaka 2015/2016 na kazi hiyo ya tathmini inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2016. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imetenga shilingi bilioni kumikwa ajili ya ukarabati wa kiwanja hiki.
Katika mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege katika mwaka wa fedha 2015/2016 ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho kutoka Daraja III(C) la sasa kwenda daraja IV(E) ili kiweze kuhudumia ndege kubwa zaidi na hivyo kuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa Ukanda wa Kusini. Ukarabati na upanuzi wa kiwanja utahusisha miundombinu yote ya kiwanja ikiwemo taa na mitambo ya kuongozea ndege pamoja na majengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo ya uandaaji wa mpango kabambe wa usanifu wa awali inatarajiwa kukamilika Julai, 2016. Kukamilika kwa mpango huu kutaiwezesha Serikali kutafuta fedha za kukarabati na upanuzi wa kiwanja ikiwemo ufungaji wa taa za kuongoza ndege wakati wa kutua na kuruka nyakati za usiku.
(b) Ikiwa ni mpango wa muda mfupi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeingia makubaliano na Kampuni ya British Gas (BG) kwa ajili ya kutumia taa zake ambazo ni za kuhamisha (portable airfield ground lighting) kwa ajili ya kuongozea ndege pale ambapo ndege itatakiwa kutua usiku.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Halmashauri za Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Kampuni ya HELM wanakusudia kujenga Kiwanda cha Mbolea huko Msanga Mkuu, Mtwara Vijijini.
Je, ni lini Serikali itaridhia mradi huo kuanza?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Awa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kiwanda cha mbolea na ni mshirika mkuu wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea huko Msanga Mkuu-Mtwara Vijijini. Baada ya kufanya tathmini ya kitaalamu juu ya mahitaji ya gesi kwa ajili ya kiwanda hicho na kwa kuzingatia matumizi ya gesi nchini (Gas Utilization Master Plan) pia kwa kuzingatia hazina ya gesi tuliyonayo kwa sasa katika visima vya nchi kavu na baharini, kampuni ya HELM imealikwa kuwasili nchini kwa ajili ya majadiliano ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Awa Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na nilihakikishie Bunge lako Tukufu na Watanzania wote kuwa kwa hazina ya gesi tuliyonayo sasa Tanzania ya TCF 57.25 tuna uwezo wa kuwapatia HELM kiasi cha million cubic fit 104 kiasi wanachohitaji kwa siku wamalizapo kujenga kiwanda hicho.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, Serikali imeweka mikakati gani ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini inayojengwa Mikindani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini, Wizara inaendelea kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya afya ili waweze kuchangia gharama za kukamilisha mradi huu. Vilevile Wizara inaendelea kufanya majadiliano na taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zinaweza kutoa mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi huu.
Hata hivyo, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017, Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza kwa awamu nyingine ya ujenzi wa majengo mengine ya kutolea huduma baada ya kukamilika kwa jengo la matibabu ya magonjwa ya nje (Out Patient Department) na mapokezi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A.
GHASIA) Aliuliza:-
Wananchi wa Kitere na Bonde la Mto Ruvuma wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha mpunga kwa miaka mingi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima hao kuwa na kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Umwagiliaji wa Kitere ulianza kutekelezwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambapo shughuli zilihusisha ujenzi wa bwawa, mifereji na vigawa maji mashambani. Ujenzi huu ulifanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na kukamilika Disemba, 2015. Mradi una jumla ya eneo la hekta 270 na wananchi wanaonufaika ni takribani 3,300 ambao kwa sasa wanajihusisha na kilimo cha mpunga na mbogamboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya Bonde la Mto Ruvuma, mwaka 2012 Serikali kwa kushirikiana na SADC iliajiri mtaalam mshauri Kampuni ya SWECO toka Sweden aliyepewa kazi ya kuainisha matumizi mbalimbali ya Bonde la Mto Ruvuma ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme, umwagiliaji na uhifadhi wa mazingira. Kazi hii tayari imekwishafanyika na taarifa ya mtaalamu mshauri imeainisha maeneo yote ambayo yatafanyiwa upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Umwagiliaji wa Kitere na ile iliyopo katika Bonde la Mto Ruvuma tayari imekwisha ingizwa katika Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ambao hivi sasa unafanyiwa mapitio ili uendane na hali halisi ya sasa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara yangu imeyaweka maeneo hayo katika bajeti kwa ajili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kuendeleza maeneo hayo.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wavuvi wa Mtwara Vijijini ili waweze kufanya uvuvi wa kisasa zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya uvuvi nchini kwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kuendeleza wavuvi wakiwemo wavuvi wa Wilaya ya Mtwara Vijijini ili waweze kufanya uvuvi wa kisasa zaidi. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuwapatia zana bora za uvuvi, elimu kuhusu masuala ya uvuvi na ujasiriamali, pamoja na kuboresha miundombinu ya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kuwapatia mitaji wakulima, wavuvi na wafugaji, itawawezesha kupata mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Benki ya Rasilimali Tanzania na benki za kibiashara kama NMB na CRDB kupitia vyama vya ushirika ili kuboresha shughuli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi kununua zana bora za kisasa kama boti, mashine na nyavu ambapo wavuvi wa Mtwara Vijijini pia watanufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka 2017/2018 Serikali itaanza kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili (ASDPII) ambapo miradi ya kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia zana bora imeainishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Elimu ya Uvuvi (FETA) inaendelea kutoa elimu ya uvuvi wa kisasa kwa wavuvi na imefungua kituo cha mafunzo Mikindani Mtwara. Pia, Serikali itatoa mafunzo ya uvuvi wa Bahari Kuu kwa wavuvi 50 kutoka Halmashauri za Pwani ya Bahari ya Hindi ikiwemo Mtwara Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu matumizi ya zana bora za uvuvi, ufugaji wa samaki, ukulima wa mwani na uongezaji wa thamani ya mazao ya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mpango kabambe wa uvuvi (fisheries master plan) inaendelea kuboresha miundombinu ya uvuvi ikiwemo mialo na masoko. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini, imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki la kisasa katika Kata ya Msanga Mkuu.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Tohara kwa wanaume imethibitika kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kiasi kikubwa.
(a) Je, kwa nini Serikali isiagize tohara kuwa ya lazima kwa wanaume wote?
(b) Je, elimu kuhusu tohara imefikishwa kwa wananchi kwa kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, si rahisi kwa Serikali kuagiza tohara kuwa lazima kwa wanaume wote nchini japokuwa tohara ina faida kubwa sana kiafya kwa wananchi wetu. Wizara iliweka mikakati ya kubaini mikoa ya kipaumbele ambayo haina utamaduni wa kutahiri na ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kutoa huduma ya tohara kama afua rasmi. Mikoa hiyo ni 14 ambayo ni Iringa, Njombe, Tabora, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera na Musoma. Itakapofika mwezi Oktoba, 2017 mikoa mipya minne ambayo ni Singida, Kigoma, Mara na Morogoro itaongezwa na hivyo kufikisha idadi ya mikoa 17. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Spika, elimu kuhusu tohara imefikishwa kwa wananchi kwa kiasi kikubwa ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau wake katika mikoa ya kipaumbele imekuwa ikitoa elimu kabla na baada ya huduma ya tohara katika vituo vya kutolea huduma za afya na wakati wa huduma mkoba zinazotolewa ngazi ya jamii kupitia kampeni mbalimbali. Serikali iliendesha Kampeni kubwa ya Tohara maarufu kama Dondosha Mkono Sweta ambapo elimu kuhusu tohara ilitolewa kupitia matangazo na vipindi vya redio na televisheni, mabango, machapisho, vijarida mbalimbali, filamu na waelimisha rika.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne ilianza ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini katika eneo la Mitengo Mikindani – Mtwara.
• Je, kuna mikakati gani ya kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa hospitali hiyo?
• Je, ni lini wananchi wategemee kuanza kutumia hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wizara ipo kwenye hatua ya kuandaa awamu nyingine ya kumalizia sehemu iliyokwishaanzishwa ya jengo la mapokezi ya wagonjwa wa nje yaani Out Partient Department (OPD) pamoja na kukamilisha majengo mengine kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ambapo kiwango cha kazi kilichoingiwa mkataba kwa awamu ya kwanza kimekamilika na kukabidhiwa kwa Wizara. Mwaka 2011 Wizara ilijenga uzio wa ukuta wenye kilometa 2.7 kwa ajili ya usalama na uhifadhi wa eneo la hospitali. Sanjari na hilo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wamekubali kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la Wagonjwa wa nje OPD na ujenzi huo utaanza mapema pindi taratibu za ndani zitakapokamilika.
(b) Mheshimiwa Spika, matarajio ya Wizara kwamba kipindi cha mwaka mmoja baada ya kumpata mkandarasi wa awamu ya pili sambamba na upatikanaji wa fedha za kuendelea na ujenzi, jengo la wagonjwa wa nje litakamilika na kuweza kuanza kutumika wakati majengo mengine yanaendelea kukamilishwa.
MHE. JEROME D. BWANAUSI (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati mifereji ya maji na matuta ambayo yalijengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita katika Mji wa Mikindani ili kupunguza athari ya maji ya bahari kwenye mitaa na makazi ya watu hasa kipindi cha mvua kali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mipango ya ukarabati wa mifereji ya maji ya mvua na matuta katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani. Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imekuwa ikifanya ukarabati wa mifereji ya maji ya mvua inayoingia baharini katika mji wa Mikindani kila mara mahitaji yanapojitokeza kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na Serikali Kuu.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imetuma kiasi cha shilingi milioni tatu kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri katika kufanya ukarabati wa mfereji uliopo Kata ya Magengeni. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 37 zilitumika kufanya ukarabati wa mfereji katika Kata ya Mtonya, Magengeni na Mitengo kupitia fedha za Mfuko wa TASAF.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa ukarabati wa mifereji na matuta, Halmnashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati huo. Hivyo, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imetenga kiasi cha fedha shilingi milioni 50 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mifereji kata za Mtonya, Magengeni na Kisungule.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, ni lini Kivuko cha MV Mafanikio kitalala upande wa Msangamkuu ili kuwezesha dharura zinazojitokeza za wagonjwa hasa akinamama wajawazito kuhudumiwa wakati wa usiku?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahaman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kivuko cha MV Mafanikio ambacho hutoa huduma ya kuvusha magari na abiria kati ya Msangamkuu na Mtwara Mjini eneo la Msemo, wakati wa usiku kinaegeshwa kwenye boya lililopo upande wa Mtwara Mjini. Kivuko hiki huegeshwa upande wa Mtwara Mjini kutokana na eneo hilo kuwa na kina kirefu cha maji hivyo kufanya kivuko kuwa salama wakati wa kupwa kwa maji ya bahari (low tide).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imenunua boti ndogo iitwayo MV Kuchele yenye uwezo wa kubeba abiria nane ambayo inatumika kutoa huduma ya dharura kati ya Msangamkuu na Mtwara Mjini nyakati za usiku, ikiwemo huduma ya kuvusha akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Boti hiyo kwa sasa huegeshwa upande wa Mtwara Mjini kwa sababu za kiusalama na endapo huduma ya dharura itahitajika upande wa Msangamkuu, mawasiliano hufanywa kwa njia ya simu ili boti hii iweze kutoa huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati wa Serikali ni kuweka miundombinu itakayowezesha boti hiyo kuegeshwa upande wa Msangamkuu wakati wa usiku ikiwemo nyumba ya kulala kwa ajili ya Nahodha wa boti hiyo.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, Serikali inaweza kutuambia ni nini hasa kinachosababisha uharibifu wa mazingira kwa kiwango kikubwa kati ya sheria na usimamizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 Kifungu cha 11(1), 13(1), 14, 16(1) na 30 imeainisha mfumo wa kitaasisi wa usimamizi wa mazingira nchini. Ofisi ya Makamu wa Rais ina jukumu la kuratibu na kuna wasimamizi mbalimbali wa utekelezaji katika ngazi tofauti. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linasimamia utekelezaji na uzingatiaji wa sheria kwa ujumla. Aidha, Wizara za Kisekta na Serikali za Mitaa zina jukumu la kusimamia hifadhi ya mazingira kulingana na wajibu na maeneo wanayosimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo sheria za kutosha zinazohusu usimamizi wa mazingira. Pamoja na Sheria Mama ya Mazingira Na.20 ya mwaka 2004, pia tunazo sheria zifuatazo ambazo ni muhimu katika hifadhi ya mazingira. Sheria ya Madini (2010); Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji (2009); Sheria ya Afya ya Jamii (2009); Sheria ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi (2003); Sheria ya Viwanda vya Kemikali na Wanunuzi wa Kemikali (2003); Sheria ya Uvuvi (2003); Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi (2003); Sheria ya Misitu (2002); Sheria za Ardhi Na.4 na Na.5 (1999); Sheria ya Ulinzi wa Mimea (1997); na Sheria ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (1994). Hivyo, tunahimiza usimamizi wa sheria hizi ili kulinda mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, uharibifu wa mazingira kwa kiwango kikubwa unasababishwa na kukosekana kwa usimamizi thabiti wa shughuli za hifadhi ya mazingira katika ngazi za halmashauri unaochangiwa na kutokuwa na GFS Code kwa ajili ya kutenga fedha za hifadhi ya mazingira katika bajeti za Serikali za Mitaa. Aidha, uelewa wa wananchi kujua wajibu wao wa kuhifadhi mazingira bado ni tatizo. Pia uharibifu wa mazingira huchangiwa na ongezeko la idadi ya watu linalopelekea kuongezekana kwa mahitaji ya rasilimali kama vile matumizi ya ardhi katika vyanzo vya maji, ukataji wa misitu na pia uelewa mdogo wa jamii kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Hifadhi ya Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitumie fursa hii kuwaagiza watendaji wa ngazi zote kuchukua hatua kadri itakavyowezekana kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa sheria hizi ili kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa ujumla.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Je, Serikali imechukua hatua gani kwa walioruhusu korosho zilizochanganywa na mawe kusafirishwa nje ya nchi bila kuchanguliwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Korosho ghafi katika msimu wa 2017/2018 lilikuwa zuri hususan kutokana na kupanda kwa bei ya korosho na kuuzwa kuanzia shilingi 3,500 hadi shilingi 4,000 kwa kilo. Bei ilipanda kutokana na Serikali kuimarisha minada ya korosho na kuwahamasisha wanunuzi kutoka nchini Vietnam kuja kununua korosho moja kwa moja Tanzania badala ya kupata korosho hizo kupitia India kama ilivyokuwa imezoeleka kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo, baadhi ya watu wasio waaminifu katika tasnia ya korosho wameanza kuchanganya korosho na vitu visivyokuwa korosho yakiwepo mawe na kokoto au kuchanganya korosho nzuri na mbovu kwa lengo la kuharibu Soko la korosho nje ya nchi. Suala hili lilibainika baada ya makontena mawili ya korosho ghafi kutoka Tanzania kugundulika kuwa zimechanganywa na kokoto huko Vietnam. Timu ya uchunguzi iliyoundwa na Serikali imebaini kuwa korosho hizo zilitoka Tanzania na zilipitia katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuwafanyia uchunguzi wa kina wale wote walioripotiwa katika taarifa ya timu ya uchunguzi iliyoundwa na Serikali ili hatua stahiki zichukuliwe kwa watakaobainika kuwa waliruhusu korosho zilizochanganywa na kokoto kusafirishwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua nyingine ni pamoja na kuitaka Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi ya Ghala, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Mamlaka za Serikali za Mitaa kushirikiana katika kuimarisha usimamizi wa ubora wa korosho katika mnyororo wake wote kudhibiti uhalifu huo. Pia kusimamia kikamilifu na kuhakikisha kwamba korosho zinazosafirishwa nje ya nchi zinakuwa na ubora unaostahili na kuweka nembo ya utambulisho kwa maana ya kuzi-brand na mfumo wa kuzitambua korosho zake nje ya nchi na hivyo kulinda soko lake na kuzitaka kampuni za ndani na nje ya nchi kuwasilisha malalamiko yao Serikalini pindi yanapotokea matatizo katika biashara zao kabla ya kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari kwa kuwa huchafua jina la biashara ya korosho za Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchunguzi unaofanywa sasa na vyombo vyetu vya dola umeshapelekea watuhumiwa kadhaa kukamatwa na kwa manufaa ya uchunguzi huo Serikali itatoa kauli mara itakapokuwa tayari kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakarabati mifereji ya maji ya mvua na kuta za mito inayoingiza maji ya bahari katika Mji wa Mikindani ili kuirejesha katika hali yake ya awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 129(1) kinaeleza wajibu wa kila mamlaka ya Serikali za Mitaa kwenye eneo lake itajenga au kuandaa mifereji ya maji ya mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kumekuwepo na changamoto ya kujaa kwa maji katika maeneo mengi nchini yanayopakana na bahari kunakosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kufanya baadhi ya mifereji kushindwa kumudu athari zake. Kufuatia hali hii, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imeanza kuchukua hatua zinazolenga kuzuia na kupunguza madhara yaliyojitokeza katika maeneo yaliyoathirika nchini ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya jumla ya maeneo haya ikiwemo Mikindani ili kuwezesha kuandaa Mpango wa Taifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ipo katika hatua za kuandaa Mpango Endelevu wa Kitaifa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (National Adaptation Plans) wenye malengo ya muda wa kati na muda mrefu ili kuboresha usimamizi wa mabadiliko nchini kwa kushirikiana na halmashauri zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi, tunashauri halmashauri za maeneo husika kuingiza gharama za ukarabati wa mifereji kwenye bajeti zao ili kupunguza athari zilizozidi kuongezeka kwa kuiga mfano wa Jiji la Dar es Salaam.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAWA A. GHASIA) aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa reli kutoka Mtwara – Mbambabay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali (feasibility and preliminary design) wa ujenzi wa reli kutoka Mtwara – Mbambabay kupitia matawi ya Mchuchuma-Liganga zenye urefu wa kilometa 1,092. Mshauri Mwelekezi wa kifedha na uwekezaji (transaction advisor) tayari amepatikana, mkataba na mshauri wa uwekezaji unatarajiwa kusainiwa ifikapo Juni, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mshauri wa Uwekezaji atakuwa na jukumu la kuunadi mradi huu kwa wawekezaji mbalimbali, ikizingatiwa kuwa mradi huu unatekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP). Hii ni katika kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa reli nchini kwetu. Hivyo, baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kumpata mwekezaji kwa njia ya PPP, ujenzi wa reli hii utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa hata sasa tumekuwa tukipokea wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika reli hii ambapo tumekuwa tukiwaelekeza kufuata sheria na taratibu za ununuzi kwa miradi inayotekelezwa kwa mfumo wa PPP. Taratibu hizo zinawaelekeza kuandaa na kuwasilisha wazo lao (proposal) la kufanya uwekezaji kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambalo litawasilishwa katika Wizara yetu baada ya kuwa wamejiridhisha. Aidha, baada ya kuchambuliwa kwa kina na Wizara, litawasilishwa katika kitengo cha PPP kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uchambuzi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kitengo hicho, wakimaliza uchambuzi na kuridhia, mwekezaji atatakiwa naye kufanya upembuzi yakinifu wake ambao baadaye utalinganishwa na upembuzi yakinifu uliofanywa na Serikali kabla ya kukamilisha taratibu za uwekezaji.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-

Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuendeleza eneo EPZA Mkoani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, eneo la Special Economic Zone Mtwara (SEZ) lipo katika eneo la Msanga Mkuu. Eneo hilo litaendelezwa kwa ajili ya bidhaa zinazotokana na mafuta na gesi ambapo litajengwa Petrochemical Complex pamoja na kiwanda cha kuzalisha mbolea. Mkoa wa Mtwara kupitia Baraza la Ushauri la Mkoa Mtwara (RCC) umeingia mkataba na kampuni ya Helm AG na Proman A.G kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha mbolea.

Mheshimiwa Spika, eneo la Mtwara SEZ linahusisha kuanzishwa kwa viwanda vitano vya kuzalisha methanol, kiwanda cha kuzalisha ammonia kutengeneza petrochemical, mbolea na urea na melamine. Mradi huo ambao umepangwa kutekelezwa katika awamu tatu utagharimu Dola za Kimarekani Bilioni Tano ambapo awamu ya kwanza itagharimu dola za Kimarekani Bilioni Moja. Utekelezaji wa mradi wa kutengeneza mbolea unatarajiwa kuanza mara muafaka wa bei ya gesi asilia kati ya Serikali na Mwekezaji utakapofikiwa. Juhudi za kuhitimisha majadiliano zinafanyika.

Mheshimiwa Spika, uendelezaji wa eneo hili unaendelea na kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 Serikali ilitoa shilingi bilioni 3.95 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya maji na usanifu wa barabara za kuingia eneo la mradi. Kazi hizi zimetekelezwa na TARURA pamoja na Mamlaka ya Maji Mtwara (MTUWASA). Hadi sasa kazi ya kujenga miundombinu ya maji imekamilika, na kazi ya ujenzi wa barabara na jengo la utawala zinaendelea na matarajio ni kukamilika mwezi Desemba 2019.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Ligula inakabiliwa na upungufu wa Madaktari Bingwa:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Ligula inapata Madaktari Bingwa wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Hawa Abdulrahamani Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula) inahitaji kuwa na Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ili kuwezesha kutoa huduma za kibingwa. Aidha, Wizara inatambua kuwa, Hospitali hii kwa sasa ina Madaktari Bingwa mmoja tu wa fani ya Udaktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi na wakawake (OBGY).

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia uamuzi wa Serikali kuzihamishia Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara imefanya tathmini ya kina kujua hali halisi ya mahitaji ya Madaktari Bingwa na fani zao katika Hospitali zote za Mikoa, Kanda, Maalum na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tathmini hii, itawezesha utekelezaji wa uamuzi wa kuwapanga upya Madaktari Bingwa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya kila Hospitali ya Mkoa, kanda maalum na Taifa. Lengo ni kuwa, kila Hospitali ya Mkowa iwe na Madaktari Bingwa wa fani nane za kipaumbele ambazo ni Daktari Bingwa wa Uzazi na Wanawake, Daktari Bingwa wa Watoto, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa, Daktari Bingwa wa Huduma za Dharura na Magonjwa ya Ajali, Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi na Daktari Bingwa wa Huduma za Radiolojia katika Hospitali za Mikoa ikiwemo Hospitali ya Ligula.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara imewapeleka Madaktari Bingwa wa fani za Upasuaji wa kawaida na Upasuaji wa Mifupa 125 katika Chuo cha MUHAS ambao wanatarajia kumaliza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021. Madaktari hawa watapangwa katika Hospitali ya Rufaa za Mikoa ikiwemo Ligula. Wizara itaendelea kutenga bajeti ya kuwasomesha Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha Hospitali zote za Rufaa zinakuwa na Madaktari Bingwa wa kutosha. Kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 Serikali inagharimia masomo ya madaktari bingwa 127 katika Chuo cha MUHAS.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kipindi hiki cha mpito, Serikali imekuwa ikiendesha kambi za udaktari bingwa ikiwa ni pamoja na upasuaji kwa lengo la kufikisha huduma za madaktari bingwa kwenye mikoa isiyokuwa na huduma hizo.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-

Tatizo la maji Mkoani Mtwara limeendelea kuwa kero kubwa kwa wananchi wa Mkoa huo:-

(a) Je, mradi wa kutoa maji mto Ruvuma hadi Mtwara Manispaa umefikia hatua gani?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ukarabati wa Mradi wa Maji wa Mbuo Nkunwa?

(c) Je, ni nini hatma ya Mradi wa Maji Makonde?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa mradi wa kutoa maji katika chanzo cha maji cha Mto Ruvuma kwa ajili ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuajiri mtaalam atakayefanya usanifu wa kina na kuandaa makabrasha kwa ajili ya kuanza utekelezaji katika mwaka wa fedha 2020/2021. Mradi huu ni mkubwa, ukitekelezwa utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara.

(b) Mheshimiwa Spika, ukarabati wa mradi wa maji Mbuo – Nkunwa unaendelea kufanyika na Mkandarasi anaendelea na kazi. Mpaka sasa bomba la njia kuu lenye urefu wa kilomita 3.6 limelazwa na wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji.

Pia mkandarasi amechimba kisima kingine kipya ili kuongeza kiasi cha maji. Kazi ya kufunga miundombinu ya bomba la mtandao wa maji inaendelea. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2020. Usimamizi wa mradi huu unafanywa na wataalam wa ndani (force account) wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA).

(c) Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mradi wa Makonde, Serikali imepanga kufanya ukarabati kwa awamu. Awamu ya kwanza ya ukarabati inaendelea ambapo tayari njia ya bomba kuu yenye urefu wa kilomita 17 kutoka chanzo cha maji Mitema hadi Mjini Newala imekamilika.

Mheshimiwa Spika, kazi ya ufungaji wa pampu inaendelea ili majaribio ya mradi yafanyike kwa ajili ya Mji wa Newala. Aidha, katika awamu hii upo mpango wa kuongeza njia nyingine kubwa kutokea Mitema hadi eneo la Nambunga ambapo tenki lenye uwezo wa lita milioni tano litajengwa na maji yatasambazwa katika Mji wa Newala na vijiji jirani. Awamu ya pili itahusisha ukarabati wa mtandao wa mabomba katika eneo la Tandahimba ili kutoa huduma ya maji ya uhakika.