Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saed Ahmed Kubenea (18 total)

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, naomba Mheshimiwa Waziri jina langu amelitamka vibaya naitwa Saed siyo Sadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na tatizo la mtambo wa Ruvu kupatiwa ufumbuzi lakini tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa hasa katika Jimbo la Ubungo, Kibamba, Segerea, Kigamboni, Ukonga, na hata Temeke.
(a) Mheshimiwa Waziri tatizo hili linatokana kwa kiasi kikubwa na uchakavu wa miundombinu hasa yale mabomba yanayosambaza maji katika majumba. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kukarabati miundombinu ya maji katika Jiji la Dar es Salaam?
(b) Kwa kuwa, majibu ya Mheshimiwa Waziri yamekuwa ya jumla, kwamba mtambo umekamilika, majaribio yameanza, ukarabati unafanyika, Mheshimiwa Waziri anaweza akataja kwa majina mitaa ambayo mradi huu wa maji utafanyika katika kipindi hiki cha haraka?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba msamaha nimetamka Sadi kumbe ni Saed, basi nitafanya marekebisho Mheshimiwa Kubenea.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maswali ya Mheshimiwa Kubenea mawili ni kwamba, Serikali kupitia Wizara ya Maji inao mpango mkubwa sana wa kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ukarabati na upanuzi wa mfumo wa kusambaza maji safi katika Jiji la Dar es Salaam, unaohusisha maeneo ya Tegeta-Mpiji, Mpiji-Bagamoyo na Mbezi-Kiluvya. Mradi huu unagharimu dola za Marekani milioni 23.927 na ujenzi unatarajiwa kukamilika tarehe 21/4/2017. Mradi huu utakapokamilika maeneo yatakayopatiwa maji ni pamoja na Mji wa Bagamoyo na vitongoji vyake, eneo la uwekezaji la Bagamoyo EPZ, Mpiji, Bunju, Mabwepande, Boko, Mbweni, Tegeta, Ununio, Wazo, Salasala, Kizundi, Matosa, Mbezi Juu, Goba, Changanyikeni, Makongo, Kiluvya, Kibamba, Mbezi Msakuzi, Makabe, Marambamawili na Msigani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali kwa kutambua kwamba kuna maeneo mengi ambayo hayatofikiwa kwa haraka na mtandao wa mabomba ya maji, imefanya utaratibu wa kuchimba visima 51, katika hivyo visima 51 visima 24 vimekamilika, na maeneo ambayo tayari yameanza kupata huduma hiyo ni pamoja na Mavurunza A, Kilungule A na B, King’ongo I, King’ongo III, Sandali, Mpogo, Mwemberadu, Mburahati, Kipunguni, FFU, Ukonga, Mongo la Ndege, Segerea, Chanika na Yombo, Saranga na Saranga II. Chang’ombe A, Ununio, Chang’ombe Toroli, Keko Magurumbasi na Keko Mwanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Mheshimiwa Kubenea uwe na uhakika matarajio yetu ni kwamba, ikifika mwaka 2017 maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam yatakuwa tayari yameshapatiwa maji.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Matatizo yaliyopo katika Jimbo la Moshi Vijijini yanafanana na matatizo yaliyopo katika Jimbo la Ubungo maeneo ya Kilungule, Kimara Baruti, Korogwe na Golani, Kata ya Kimara pamoja na Makoka, Kajima na Nova Kata ya Makuburi. Je, Serikali ni lini itawapatia maji wananchi wa maeneo hayo? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Ubungo maeneo mengi tunategemea yatapata maji baada ya kukamilisha huu mradi wa Ruvu Juu ambao tayari umeshakamilika. Tatizo lililopo ni kwamba umeme uliopo pale Ruvu Darajani ni mdogo tuna pump kubwa sana ya kuleta maji Dar es Salaam; tumeshaanza kuvuta line ya umeme kutoka Chalinze kuleta pale. Tutakapomaliza line ya umeme maeneo yote ya Ubungo yale yatapata maji kutoka Ruvu Juu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na shaka.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kituo hiki kilipoanzishwa mwaka 1989 tayari Tanzania ilikuwa na Ubalozi Mjini London ambao ulianzishwa mwaka 1961, na moja ya jukumu la kituo hiki ni kuvutia uwekezaji na hasa suala la utalii ambao unachangia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa. Je, nini kilionekana kimeshindikana wakati huo kufanywa na Ubalozi na ambacho sasa kinaweza kufanywa na Ubalozi huo?
(b) Kwa kuwa kituo kimefungwa na miongoni mwa madai makubwa ambayo Serikali ilikuwa inadaiwa ni posho za wafanyakazi wa kituo waliopo London, mishahara ya wafanyakazi na kodi za nyumba za wafanyakazi wetu waliopo London.
Je, Serikali inaweza kutoa tamko gani juu ya madai ya wafanyakazi wa kituo hiki waliopo London kama wameshalipwa fedha zao na kama wamerejeshwa nchini, je, wamelipwa fedha zao za kujikimu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema yalikuwa ni maagizo ya Mheshimiwa Rais lakini pia naomba ikumbukwe kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imesema na inatekeleza sasa kuboresha na kupeleka watumishi wote katika balozi zetu zote duniani ili kuhakikisha wao wanafanya kazi husika na zinazostahiki kufanywa na balozi setu.
Kwa hiyo agizo lile halikuwa la makosa na sasa Serikali ya Awamu ya Tano imerejesha jukumu hili ndani ya Ubalozi ambalo ni moja ya majukumu yake na Ubalozi wetu unaendelea kufanya vizuri.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, niseme kama Naibu Waziri wa Fedha, madai tuliyoyapata ni shilingi 129,896,000 na ndiyo ambayo tunayalipa kama kuna watumishi ambao wanadai posho zao na haki zao zozote naomba watuletee ili tuweze kuhakiki na tutaweza kulipa kama ambavyo tumelipa deni lililotangulia.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuuliza swali langu la nyongeza kwa ruhusa yako naomba niweke rekodi
sawasawa, kwamba hisa za Jiji la Dar es Salaam hazikuuzwa jana, ziliuzwa toka mwaka 2009 wakati sisi hatujawa katika uongozi wa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa kuwa Waziri ameliambia Bunge kwamba ule mkataba wa uendeshaji wa usafirishaji wa Jiji la Dar es Salaam ni wa muda na kwamba wao Simon Group ndio wameshinda hiyo zabuni, lakini kwa kuwa mkopo uliojenga
miundombinu ya barabara za Jiji za Dar es Salaam umetolewa na Benki ya Dunia, na kwa kuwa mkopo ulionunua magari yaendayo kasi Dar es Salaam umetolewa na Benki ya NMB, na Serikali ndiyo dhamana wa Benki hiyo haoni kwamba sio halali kwa mtu mmoja kumiliki uendeshaji wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam na kuacha wananchi wengine ambao wana mabasi madogo madogo kuachwa nje ya utaratibu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza NMB ni ya nani? Serikali tuna hisa kwenye NMB. Kwa hiyo hakuna hata dhambi yoyote kwa NMB ku-facilitate, maendeleo ya usafiri wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini zile arrangement za NMB na huyu mwekezaji ambaye anaendesha mradi wa mabasi
yaendayo kasi Dar es Salaam ambaye ni Serikali na mwekezaji binafsi it is a PPP, ni mradi ambao una-arrangements zake.
Arrangements zile ni za kati ya UDART ambayo Serikali imo na Simon Group na benki na ujenzi wa miundombinu ni makubaliano ya Serikali na World Bank wala utaratibu wa uendeshaji haukuwa ni jambo muhimu sana, hapa ilikuwa ni kuboresha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, Watanzania wanafahamu adha ya foleni ya Dar es Salaam, Watanzania wanafahamu namna
tunavyopoteza uchumi katika Jiji la Dar es Salaam, hivi kwa nini sisi Watanzani tuna-tend kuchukua PPP. Hatuwezi kujenga hii nchi kwa kutegemea Serikali peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda sana fikra za baadhi ya Wabunge, fikra za kuamini kwamba private sector ni muhimu
katika ujenzi wa uchumi, na siogopi mimi kum-quote Mheshimiwa Zitto Kabwe kwamba ni mtu anayejua sana
eneo hilo la uchumi. Lakini Waziri wa Fedha amekuwa akieleza hapa eneo hilo, lakini bado sisi Watanzania
anaposhiriki mswahili katika shughuli yoyote ya PPP ni nongwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yetu haiwezi kuendelea kwa msingi huu, ila angekuja mgeni kutoka nje angeshangiliwa
kweli kweli, kwani hamjui kwamba kuna hisa nyingi zinachukuliwa kwenye makampuni ambayo Serikali ilitakiwa
kushiriki lakini tumeshindwa.
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuendelea na msingi huu wa kuendesha uchumi na uchumi ukaenda kama mawazo
yenyewe ndiyo haya.
Mheshimiwa Spika, Serikali inafahamu, imelinda maslahi yake na inafahamu mradi huu umuhimu zaidi si faida
bali huduma kwa wananchi wa Dar es Salaam.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, majibu ya Serikali yameonesha kwamba eneo pekee lililopimwa katika Jimbo la Ubungo ni eneo la Kimara ambalo kumepimwa viwanja 3,196 au nyumba 3,196; je, Serikali inasemaje katika maeneo yaliyobaki ya Makuburi, Manzese, Ubungo na maeneo mengine ya Jimbo la Ubungo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri amejibu vizuri. Maswali haya yanapaswa kuwa ndani ya mipango ya Halmashauri husika, kama tunavyopanga mipango juu ya shughuli nyingine za maendeleo ndani ya Wilaya basi tujipangie mipango ya namna ya kupima na kupanga miji yetu ndani ya Wilaya zetu, haiwezi kuanzia hapa. Nataka niwaambie wote wawili hata huo mnaosema Mheshimiwa yangu Kubenea tulikuwa wote hapa Kimara, hatupimi pale tunarasimisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam ni moja ya miji ambayo imejengwa siku nyingi, imejengwa vibaya ni makazi holela. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa ni kurasimisha angalau wananchi waweze kupata barabara za kupitisha huduma zao, waweze kupata hati kidogo ili angalau nyumba zao thamani zile zisipotee, angalau thamani ya mali waliyowekeza pale na zile hati ziwasaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imekuja na mpango mbadala wa kuwawezesha hawa maskini kurasimisha mali zao ili angalau ziwasaidie katika kujitegemea. Kwa hiyo, tunafanya zoezi la urasimishaji, hapa unaposema ndugu yangu Kubenea tulienda wote Kimara tunafanya zoezi la urasimishaji na haya anayosema ndugu yangu tunafanya zoezi la urasimishaji, upimaji mpya utafanywa Dar es Salaam baada ya kumaliza master plan, tuliyonayo ni ya mwaka 1979, sasa hivi tunaandaa master plan tume-engage wataalam, tukishamaliza master plan ambayo itashirikisha viongozi wote wa Dar es Salaam na wananchi wa Dar es Salaam, Dar es Salaam itapangwa upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ni zoezi la urasimishaji kuwawezesha wananchi kutoka kwenye hadhi ile ya makazi holela angalau waitwe nao wanaishi kwenye makazi rasmi. Hilo ni zoezi ambalo linaendelea sasa na zoezi hili ni shirikishi, wananchi kwenye mitaa wanashiriki wenyewe, wanachangia gharama wenyewe, kupanga maeneo yao katika mitaa yao. Kwa hiyo naomba zoezi hili tushirikiane na ninyi tuanzie kwenye mitaa kujadili halafu Wizara hizi mbili tushirikiane na mipango yenu. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika majibu yake ameeleza kwamba uwekezaji ni lazima uende pamoja na manufaa kwa wananchi waliopo katika eneo ambalo uwekezaji umefanyika. Katika Jimbo la Ubungo kuna maeneo ya EPZ yaliyopo eneo la Ubungo External na kuna Kiwanda cha Urafiki ambacho Serikali imekibinafsisha kwa mwekezaji wa nje. Maeneo hayo mawili hayana manufaa yoyote kwa wananchi wa Ubungo na eneo la EPZ lina migogoro mikubwa, wafanyakazi wanalipwa mishahara midogo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itatatua matatizo ya EPZ yaliyoko katika Jimbo la Ubungo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo kwetu unasema mwenye shibe hamjui mwenye njaa. EPZA kuna viwanda vinaajiri vijana zaidi 3,000, mimi naomba kama kiwanda hicho kingehamia kwetu nikaajiri vijana 3,000. Urafiki inatoa ajira, inaweza kuwa na upungufu yale specific uyalete kwangu niyashughulikie. Wawekezaji wote ni wazuri yule aliye mbaya mumlete kwangu, lakini hao 1,800 na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu upande wa Ajira wanaajiri vijana 400 kila baada ya miezi minne. Narudia tena na sifichi ningeomba hao watu wangekuwa kwenye Jimbo langu naajiri vijana wangu 400 kila mwezi, usikufuru Mheshimiwa Kubenea.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza jina langu ni Saed Kubenea tofauti na Mheshimiwa Waziri alivyolitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kiwanda cha Urafiki kinaendeshwa kwa hasara kuanzia mwaka 1998 na kusababisha malimbikizo ya hasara yanayofikia shilingi bilioni
18.04 hadi tarehe 30 Juni, 2011. Na kwa kuwa mwekezaji aliyepita kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Hodhi la Taifa alichukua mkopo kwenye Benki ya Exim ya China unaofikia shilingi bilioni 56.1 na riba ya shilingi bilioni 4.04; na kwa kuwa Serikali imeamua kuwanyang’anya wafanyabiashara wazawa viwanda ambavyo walivinunua kutoka Serikalini kwa kushindwa kuviendesha. Je, Serikali iko tayari kumnyang’anya mbia huyu Kiwanda cha Nguo cha Urafiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ya Tanzania ilituma ujumbe China ambao uliongozwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Viwanda na Biashara, Shirika la Hodhi la Taifa na FTC kati ya tarehe 17 na
23 Desemba, 2011; na kwa kuwa ujumbe huu ndio uliopendekeza mwekezaji mpya kupewa kiwanda na kuhamisha hisa za Serikali kutoka asilimia 49 ambazo ilikuwa inamiliki. Je, Serikali iko tayari kuwawajibisha wafanyakazi hao wa umma waliotuletea mwekezaji fake? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, hatunyang’anyi watu viwanda, hakuna mtu aliyebinafsishwa kiwanda atanyang’anywa, ila kama kiwanda kikikushinda nakushauri na nakuambia umpe jirani yako. Nimekuwa nikilisema ni kama tulivyolelewa sisi na nyanya zetu, ukiwa na nguo ikikubana usiichane, mpe mwenzio avae na viwanda hivi vitafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kiwanda cha Urafiki nimesema ni kiwanda cha kihistoria, tulipobinafsisha viwanda, viwanda viwili vilikuwa na maneno na Mwalimu alivisemea, Mwalimu alipinga kubinafsisha Kiwanda cha Bora akasema gharama ya kubinafsisha Bora inazidiwa hata na bei ya plot pale Pugu Road wakampa majibu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, alipokuja kwa Urafiki akasema mwende kwa Wachina na katika jibu langu nimeeleza mlolongo tunaoufuata kupata partner mpya. Partner mpya sitaki kuendelea zaidi kwa sababu sasa tuna- negotiate na chini ya uongozi wa Kamati yangu ya Biashara unakwenda kupata deal nzuri, Kamati ya Viwanda na Biashara tumiliki zaidi na Mchina amekubali kutupa percent kubwa karibu 75 percent. Kwa hiyo, tutakuwa na umiliki tutaweza kuamua kiwanda kiwanda kiende vipi, tutakujengea Urafiki nzuri Mheshimiwa Kubenea, nataka kuona watu 8,000 wanafanya kazi pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala la waliokwenda, hili suala limetolewa maamuzi na CAG. CAG aliyoyaona ukiyaona utalia Kubenea. Kwa hiyo, kila mtu ambaye alihusika katika kutuingiza kwenye dhahama hii rungu litamshukia kama mwewe. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Kesi Na. 9 iliyofunguliwa na Jebra Kambone katika Mahakama Kuu ya Tanzania iliyokuwa ina-challenge baadhi ya vifungu vya sheria hii, Mahakama Kuu ilisema kifungu Na. 50 kinachozungumzia nguvu ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuunganisha makosa na kumpa mtu haki ya kukiri mbele yake inakiuka Katiba na hadi sasa sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kesi iliyofunguliwa na Jamii Forum, pia Mahakama ilisema sheria hii inatafsiriwa vibaya na Jeshi la Polisi. Swali la kwanza, je, kwa maelezo hayo ya Mahakama, Serikali haioni kwamba kuendelea na sheria hii ni kukiuka Katiba ambayo yenyewe imeapa kuulinda na kuitetea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sheria hii imeleta mgogoro mkubwa na malalamiko mengi ndani na nje ya nchi wakiwemo nchi wahisani. Kwa nini Serikali inatafuta ugomvi mwingine na makundi mengine ambayo inaweza kuepukana nayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kubenea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge akubaliane nami kwamba sheria hii imesaidia sana na imetatua matatizo mengi. Kama zilivyo sheria nyingine, upo utaratibu wa kufanya marekebisho. Lazima Serikali ipitie hatua kadhaa kabla haijaleta marekebisho Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kujibu swali lake, niseme tu kwamba hizi kesi ambazo amezitaja ni mahsusi na yumkini inaweza ikasaidia pia kufanya marekebisho. Kwa hiyo, tunaichukua tu kama ni kitu ambacho lazima tupitie kama Serikali kwa maana ya kutazama mbele ya safari. Ni kawaida sheria ambazo zipo kufanyiwa marekebisho mbalimbali. Kama ilivyozoeleka, zipo sheria nyingi kila wakati inapohitajika, kwa sababu sheria siyo static, inavyotazamwa na marekebisho yataweza kuja kwenye Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili aliposema ni kwamba yapo malalamiko ambayo yanaweza yakaleta ugomvi. Niseme kwamba siyo kweli kwa sababu sisi ni kama Taifa na kama nchi, lazima tuangalie taratibu zetu. Ni lazima tuhakikishe kwamba sheria tulizonazo wa kwanza kunufaika nazo ni wananchi wenyewe na Taifa. Kwa hiyo, hili ni suala la kulitazama tu kwa upana wake, lakini hatuwezi kwenda kutunga sheria kwa kufuata shiniko la mtu, tutatunga sheria ili kuleta haki kwa wananchi na Tanzania kwa ujumla.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, swali langu msingi wake ni kwamba, wananchi ambao wameumizwa, wametekwa, wamepotea, sio suala la kuimarisha Vituo vya Polisi kwenye ulinzi shirikishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu je, Serikali ina mpango gani wa kushikika wa kulinda raia hawa ambao wamekuwa wakijitolea kutetea nchi yao kwa maslahi ya Watanzania wote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itakamilisha uchunguzi na kuleta ripoti Bungeni ya matukio ya kihalifu yanayofanana na ugaidi ambayo wamefanyiwa watu mbalimbali, akiwemo Mheshimiwa Tundu Lissu, Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi, Abisalom Kibanda na Dokta Stephen Ulimboka na wengineo? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nataka nichukue fursa hii kumpinga na kumkosoa vikali kabisa Mheshimiwa Saed Kubenea, kutokana na utangulizi wa swali lake ambalo ameuliza; na kimsingi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Jeshi la Polisi, imekuwa ikihakikisha inalinda usalama wa raia wote na mali zao. Hakuna matabaka katika kusimamia ulinzi wa raia na mali zao, hiyo ndio kazi ya Jeshi la Polisi ya kila siku kwa hiyo, kusema kwamba kuna watu wanakosoa Serikali, sijui kuna watu wana nini, hizo ni kauli potofu na si sahihi na nadhani kwa mamlaka yako ungeelekeza hata zifutwe katika Hansard. Kwa sababu, ni upotoshwaji mkubwa kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hilo suala la kulinda usalama wa raia na mali zao jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika. Imani yangu ni kuwa kwa kadri ambavyo tunakwenda mbele tumekuwa tukifanya hivyo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kitaalam, kukusanya taarifa za kiintelijensia, kufanya doria, kuangalia maeneo tete, kuangalia takwimu, kumbukumbu za uhalifu nchini na ndio maana mpaka leo nchi yetu imeendelea kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoelekea katika Serikali ya Uchumi wa Viwanda, Serikali ya Uchumi wa Kati, tunaamini kabisa kutakuwa kuna mabadiliko makubwa sana ya kiteknolojia katika utekelezaji wa majukumu yake kwenye vyombo vyetu vya dola. Kwa hiyo, tutakapoimarisha na kuwekeza katika maeneo ya teknolojia tunaamini kabisa kazi hii itafanywa katika mazingira mepesi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu uchunguzi. Kazi ya uchunguzi imekuwa ikiendelea kufanyika, ingawa kazi ya uchunguzi kama alivyozungumzia yeye katika eneo mahususi la ugaidi, lina changamoto nyingi kwa sababu, tuhuma za ugaidi zinahusisha taarifa nyingine ambazo zinatoka katika mamlaka za nchi nyingine, lakini na taasisi nyingine nje ya Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, katika kufanya uchunguzi ambao unahitaji taarifa kupata katika nchi nyingine, kupata katika mamlaka nyingine, si jambo ambalo linaweza likawa limefanyika kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mpaka sasa kutokana na matukio mengi yaliyojitokeza kuna hatua kubwa imeshafikiwa katika uchunguzi wa kesi mbalimbali, ziko ambazo zimeshafika mwisho, ziko ambazo zinaendelea kuchunguzwa. Pale ambapo uchunguzi utakamilika hatua zitachukuliwa kwa wahusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa watu wote ambao wanahusika kutoa ushirikiano kwa mamlaka katika kutekeleza majukumu yake. Mfano huu ambao ameuzungumzia wa kesi ya Mheshimiwa Tundu Lissu, tumekuwa mara nyingi tukitaka ushirikiano kutoka katika chama hiki ambacho Mheshimiwa Kubenea anatoka, ili tuweze kupata watu ambao wanaweza kutusaidia kutupa taarifa, ikiwemo dereva yule ambaye alikuwa na Mheshimiwa Tundu Lissu, lakini wenyewe wamekuwa wakifanya jitihada za kufifisha kupatikana kwa dereva huyo. Kwa hiyo, ushirikiano kwa wananchi ikiwemo na wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge na chama chake ni muhimu katika kukabiliana na kuharakisha uchunguzi wa kesi yetu. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hoja ya msingi ni wazazi pia kuna suala la wake. Baadhi ya madhehebu ya kidini na makabila yanakuwa na mke zaidi ya mmoja. Kwa kuwa Mfuko wa Bima ya Taifa unatambua mke mmoja, je, Serikali iko tayari kuruhusu watu ambao wana wake zaidi ya mmoja waweze kuingizwa katika Mfuko wa Bima ya Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KAKUNDA):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saed Kubenea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nadhani katika nchi hii kwa sababu Serikali inatambua kwamba wananchi wake wana dini na baadhi ya dini na mila zinaruhusu mke zaidi ya mmoja, hili amelileta kama mchango wa Mbunge na ushauri kwa Serikali, wacha tulichukue kwa ajili ya kulifanyia kazi zaidi. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru. Kwa kuwa tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa, katika Majimbo karibu yote ya Jiji la Dar es Salaam; na kwa kuwa Serikali imekuwa inasema Bungeni karibu miaka mitano sasa kwamba imepata fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha mfumo wa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Je, ni lini hasa mradi huu wa Benki ya Dunia utaanza rasmi katika Jiji la Dar es Salaam?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza mwaka ujao wa fedha kwa sababu tayari tumeshatangaza tender.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna tatizo la maji kwa wananchi wa maeneo ya Rombo na suala hili limekuwepo tokea miaka ya 1960, ni lini Serikali itaruhusu uchepushaji wa hayo maji ili wananchi wa Rombo ambao wanapata maji kutoka Mlima Kilimanjaro kwa wingi sana waweze kutatua tatizo hilo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la Rombo linafanana kabisa na suala la Ubungo, hasa katika maeneo ya Kajima, Kimara na Makoka, je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa Ubungo kukamilisha mradi mkubwa wa maji ambao umetokea Kibamba hadi maeneo hayo ya Kimara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini natumia nafasi hii kutambua kwamba tuna changamoto kubwa sana katika maeneo mbalimbali kuhusu suala zima la maji. Serikali kwa kuona haja ya kutatua changamoto hii ya maji, katika Wilaya ya Rombo tumetenga kiasi cha Sh.1,530,000,000 ili kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Ubungo nilifanya ziara pamoja na Mheshimiwa Mbunge na kuna mradi mkubwa wa upanuzi ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. Kubwa, mimi kama Naibu Waziri pamoja na viongozi wote wa Wizara tutausimamia mradi huu ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuulizwa swali la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali nyingi za Wilaya kama Hospitali ya Sinza, Dar es Salaam ambayo ilikuwa Kituo cha Afya cha Sinza Palestina kimepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, hospitali hiyo haipati fedha kama Hospitali ya Wilaya na kukosekana kwa fedha hizo kumesababisha hospitali kushindwa kukidhi mahitaji yake ikiwemo kuwa na chumba cha kuhifadhia maiti. Je, Serikali iko tayari kupeleka fedha za Hospitali ya Wilaya katika Hospitali ya Sinza Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kukumbusha kwamba swali hili limekuwa likiulizwa la Sinza Palestina, naomba nimjibu Mheshimiwa Said Kubenea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilishawahi kujibu hapa, Kituo cha Afya cha Sinza Palestina siyo Hospitali ya Wilaya. Katika jibu langu ambalo nililitoa siku ile nilitaka Halmashauri wahakikishe kwamba wanatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Nikajibu pia kwamba katika kituo cha afya na hii ni changamoto katika vituo vya afya vingi ambavyo viko mijini tunakosa jina hasa ambalo tungeweza kusema kwa sababu viko juu ya vituo vya afya vya Kata za vijijini lakini pia havifikii hadhi ya Hospitali ya Wilaya. Ndiyo maana ukienda Sinza Palestina pale tumepeleka mpaka Madaktari Bingwa lakini bado hiyo haitoi mwanya kwamba tuseme ni Hospitali ya Wilaya. Kwa sababu Hospitali ya Wilaya inahitaji eneo la ukubwa usiopungua ekari 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishawaambia Halmashauri yake watenge eneo hilo ili tujenge Hospitali ya Wilaya kama ambavyo tunafanya kule Kivule kwa Mheshimiwa Waitara ili tuwe na hospitali za Wilaya kupunguza msongamano katika hospitali zingine.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo ya wavuvi wa Pemba yanafanana na matatizo ya wavuvi wa maeneo mengine ya kKusini mwa Tanzania vikiwemo Visiwa vya Mafia na Mtwara. Matatizo ya wavuvi pia yanafanana na matatizo ya wafanyabiashara wa Tanzania hasa wa malori ambao wanakamatwa katika nchi ya Congo.
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kulinda raia wake waliopo nje wanaopata matatizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama tulivyosema katika nchi ya DRC Congo tuna Ubalozi wetu na Mabalozi wetu kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba haki kwa ajili ya wananchi wa Tanzania walioko nje ya nchi inatekelezwa. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba watafanya kazi hiyo na huo ndiyo wajibu wao wa msingi, hatutawaacha na tumefanya hivyo siku zote.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongeza swali la nyongeza. Kwa kuwa miongoni mwa viwanda ambavyo vimebinafsishwa na Serikali, ni Kiwanda cha Nguo cha Urafiki. Katika Kiwanda cha Nguo cha Urafiki mwekezaji hakuja na mtaji, badala yake Serikali ndiyo ilikwenda kukopa katika Benki ya Exim ya China na ikampa mwekezaji mtaji wa kuendesha Kiwanda cha Urafiki. Je, ni lini Serikali itakirejesha Kiwanda cha Urafiki mikononi mwa wananchi wa Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kubenea kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo umezungumza, Kiwanda cha Urafiki kinatokana na urafiki kati ya nchi ya China na Tanzania. Ni Kiwanda ambacho msingi wake ulijengwa katika mahusiano hayo ya nchi mbili ya Kidiplomasia. Kwa hiyo, tunatamani kuona kiwanda hicho kikifanya kazi vizuri zaidi na wote tumekifuatilia na kujua kwamba kuna maeneo yanayohitajika kufanyiwa marekebisho. Hivyo, Serikali hizi mbili zinashughulika kwa pamoja kuona ni namna gani kiwanda hicho kitaendelezwa vizuri zaidi. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoka na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa miundombinu ya Dar es Salaam na ukatikaji wa umeme, TANESCO imekuwa haitoi taarifa ya kuwepo kwa tatizo la ukatikaji wa umeme katika baadhi ya maeneo ambayo miundombinu hiyo inatekelezwa, jambo ambalo linasabisha kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotumia umeme, lakini hasa katika maeneo ya umma, ikiwemo hospitali ya Sinza Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kwamba miundombinu ya TANESCO haiathiriki ya umeme kutokana na utengenezaji wa barabara zinazotengenezwa katika eneo hilo la Dar es Salaam?

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, ambayo hayapati umeme wa kutosha, ni pamoja na katika Jimbo la Mheshimiwa Mwita Mwaikwabe Waitara, Jimbo la Ukonga, Mheshimiwa Ndugulile Jimbo la Kigamboni, Mheshimiwa Kubenea mwenyewe Jimbo la Ubungo na Majimbi mengine likiwemo la Kibamba.

Sasa Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam, ambalo ndiyo kitovu cha biashara, linapata umeme wa kutosha na wakati wote bila usumbufu wowote na hasa ukizingatia kwamba, mradi mkubwa wa umeme wa gesi uko Kinyerezi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Kubenea ameulizia taarifa, endapo, pindi umeme unapokatikatika. Nataka nimtaarifa Mheshimiwa Kubenea, kwamba Serikali kupitia TANESCO tulitoa maelekezo ya kutumia maendeleo ya teknolojia katika kuhakikisha wananchi inawafikia taarifa haraka na maendeleo hayo ni kupitia pia uundwaji wa ma-group mbalimbali na katika Mkoa wa Dar es Salaam, Kanda zote zimeundiwa ma-group na hata mimi mwenyewe nipo kwenye group la Kibamba la utoaji taarifa za huduma ya TANESCO na mikoa yeto ina ma-group ya whatsapp.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sambamba na hilo pia, hata katika kikao cha maafisa habari nchi nzima kilichofanyika Mwanza, Shirika la Umme TANESCO na Wizara ya Nishati ni miongoni mwa taasisi na Wizara zilizofanya vizuri katika kuwahabarisha wananchi taarifa mbalimbali zinazohusiana na sekta ya nishati. Kwa hiyo, nataka niwape, pengine kama Mheshimiwa Mbunge hajaungwa kwenye haya ma-group nataka nielekeze kwamba Mbunge wa Ubungo sambamba na Wabunge wengine wote waungwe kwenye ma-group na viongozi wote ili iwe kiungo katika kutoa taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ameulizia namna ya uboreshaji wa miundombinu ya usafiri wa umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Kubenea, katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwanza kuna mradi mkubwa wa upanuzi wa Kituo cha Ubungo, kituo hiki kinapokea umeme kutoka mitambo ya Kidatu kwa msongo wa kilo vote 220 na inapoza kwenye mashine za MVA 125 na inafanya kwamba, megawatts 200 kusambaza katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, kituo hiki kinapokea umeme kutoka mitambo ya SONGAS megawatts 189, mitambo ya Ubungo ll megawatts 129 na Kituo cha Tegeta megawatts 45. Mahitaji ya Mkoa wa Dar es Salaam ni megawatts 500, lakini Kituo cha Ubungo kina uwezo wa megawatts 655. Lakini lazima niseme kwamba mitambo hii inafanyiwa ukarabati, wakati mwingine inafikia ukomo, inatakiwa ibadilishwe vipuli, kwa hiyo, inapotokea hiyo, ndiyo maana changamoto ya kukatikakatika umeme kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya nini? Serikali ya awamu ya tano kupitia TANESCO inaendelea na upanuzi wa Kituo cha Ubungo, imeshaagzia na imefika mashine ya MVA 300 ambayo itaongeza megawatts 240 kwenye msongo wa kilovoti 132 na kufanya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa na upatikanaji mkubwa wa megawatts za kutosha kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ameyataja Majimbo ya Ukonga, ametaja Jimbo la Kigamboni, kwamba lina changamoto. Nataka nimtaarifu, Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo haya, akiwemo Mheshimiwa Waitara, Mheshimiwa Ndugulile, wamefanya jitihada kubwa ya kufuatilia maeneo ambayo hayana umeme na ndiyo maana Serikali ikabuni mradi wa Peri-urban na imetenga bilioni 86 na sasa hivi hatua iliyokuwepo ile mikataba ya wakabdarasi ilishafikishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, niwatoe hofu wakazi wa maeneo ya Ukonga, ambako mimi mwenyewe nimefanya ziara kata sita, ikiwemo Zingiziwa, Buyuni, Kivule, lakini pia maeneo ya Somangila, maeneo ya Pembamnazi, maeneo ya Kisarawe ll, maeneo ya Msonga, maeneo ya Buyuni, yote hayo yametengewa bajeti na mradi utafanyika na kwa gharama za REA elfu 27. Wakazi wa Dar es Salaam wakae mkao wa tayari, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imejipanga kutekeleza miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Shirika la Reli la Taifa linamiliki hayo maeneo kihalali, lakini kwa kuwa Wizara ya Ardhi na Halmashauri za Wilaya mbalimbali zimetoa hati za umiliki wa ardhi katika maeneo hayo hayo ambayo ni maeneo ya reli; kwa mfano kule Moshi Kiwanda cha Serengeti kiko chini ya eneo ambalo linamilikiwa na reli.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa msuguano uliopo kati ya hati halali zilizotolewa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na zile hati ambazo ziko chini ya Shirika la Reli la Taifa ili wananchi hawa na maeneo haya yaweze kuendelezwa kwa haraka iwezekanavyo? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Kubenea kwa kutambua kwamba maeneo haya yanamilikiwa kihalali na Shirika la Reli na ndio maana niendelee kumsihi Mheshimiwa Mbunge Kubenea na Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwasaidia wananchi wetu kwa sababu maeneo ambayo unatambua ni halali na kama inatokea makosa ambayo ni ya kiuadilifu, wananchi wanapewa maeneo ambayo ni halali kwa ajili ya miundombinu ya reli kwamba sio vema. Kwa hiyo, tuwasaidie wananchi wetu na tuchukue hatua mnapema, ili Wananchi wasidumbukie kwenye shida ambayo inajitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu hakuna msuguano, hakuna msuguano kwa sababu kama maeneo haya ni halali kwa ajili ya shirika la reli msuguano haupo, isipokuwa ni ile hali tu ya utovu wa nidhamu uliotokea kusababisha baadhi ya wananchi wachache labda wakamilikishwa maeneo sio kihalali. Kwa maana hiyo niendelee kutoa wito tu kwa watumishi wote wa umma kwamba tunapotekeleza majukumu yetu tutekeleze kwa kuzingatia sheria, ili tusiendelee kuwasumbua wananchi wetu kama tutakuwa tumevunja sheria.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri yenye tija.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa baadhi ya mashirika ya umma yanaendelea kutumia mawakili binafsi katika kuendesha kesi am bazo imeshtakiwa na wadai. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mashirika ya umma na taasisi zake zinazoendelea kutumia mawakili binafsi katika kuendesha kesi za umma?

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa moja ya malengo ya kubadilisha kuagiza kesi binafsi, kesi zilizoshtakiwa Serikali zisimamiwe na mawakili wa Serikali ni kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi. Sasa gharama za kuendesha kesi nchi za nje zimekuwa kubwa sana na sababu moja inayosababisha Serikali ishtakiwe nje ni pamoja na kuvunja mikataba kiholela.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inalipa wadai wote, wakandarasi wote ambao wamei-supply Serikali kwenye mikataba ya Kimataifa ili kuiondoa Serikali na mzigo mkubwa wa madeni na kushtakiwa nchi za nje? (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kubenea.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, baadhi ya Mashirika ya Umma kuendelea kutumia mawakili binafsi hii inawezekana ni kwamba wakati maelekezo haya ya kesi zote kusimamiwa na Wakili Mkuu wa Serikali yanatolewa yale mashirika yalikuwa tayari yameshawa-engage wale lawyers, lakini kwa vyovyote vile kwa sasahivi wanafanya kazi pamoja na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kuanzia pale lilipotolewa lile agizo kwamba kesi zote za haya mashirika ya umma zisimamiwe na Wakili Mkuu wa Serikali hakutakuwa na kesi yoyote ambayo itasimamiwa tena na Mawakili binafsi isipokuwa katika mazingira ambayo Mheshimiwa Waziri ameyaeleza. Kama iko kesi nje ya nchi na iko katika mahakama ambayo kuna taratibu ambazo haziwezi zikawaruhusu wanasheria wetu kusimama katika zile mahakama basi tutapata mawakili binafsi wa kusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ambalo linagusa kesi mbalimbali zilizoko na zinazotokana na kuvunjwa kwa mikataba na kadhalika, nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa hivi tunao umakini mkubwa sana tunapoingia hii mikataba kiasi kwamba hatutaingia katika mazingira ya kuweza kushtakiwa kwa sababu ya kuvunja mikataba.

Kwa hiyo sasa hivi tunazingatia mambo yote ya muhimu, maslahi ya nchi na kadhalika na kuhakikisha kwamba mikataba yetu inategengenezwa vizuri kabisa kiasi kwamba hatutakuwa na matatizo ya kesi hizi mbalimbali. Na kwa kesi ambazo ziko tayari kwa kiasi kikubwa tumeingia katika majadiliano na mashauriano tuone namna gani tunaweza tukazimaliza kesi hizo kwa njia ya mashauriano badala ya kuendelea na njia ya mahakama. Naomba kuwasilisha.