Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Saed Ahmed Kubenea (16 total)

MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Serikali imetoa ahadi nyingi za kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam lakini sasa ni takribani miaka sita tangu Serikali itoe ahadi hizo na tatizo hilo bado liko pale pale:-
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kumaliza tatizo hilo la maji?
(b) Je, ni kwa nini Serikali imekuwa ikitoa ahadi za kuwapatia wananchi wake maji wakati haina uwezo wa kutekeleza ahadi zake hizo?
(c) Je, ni nini kimesababisha kutokamilika kwa mpango wa kusambaza maji toka Ruvu ambao ulitarajiwa kuwa ungemaliza tatizo la maji katika maeneo mengi ya Jiji hasa Jimbo la Ubungo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, lenye vipengele (a), (b), (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza ahadi zote ilizoahidi kuhusu kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam. Tayari ahadi ya kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini na ulazaji wa bomba kubwa lenye kipenyo cha milimita 1800 kutoka Ruvu Chini hadi Jijini lenye urefu wa kilomita 56 imekamilika. Mtambo wa Ruvu Chini umeanza kuzalisha lita milioni 270 kutoka lita milioni 180 za awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu umekamilika na sasa una uwezo wa kutoa maji lita milioni 196 kutoka lita milioni 82 za awali kwa siku. Kazi za ulazaji wa mabomba mawili kutoka Mlandizi hadi Kimara, ujenzi wa tenki jipya la maji la Kibamba na ukarabati wa matenki ya Kimara zimefikia wastani wa asilimia 98. Uendeshaji wa majaribio umeanza mwezi Aprili, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea kutekeleza mradi wa Kimbiji na Mpera ambapo hadi sasa Mkandarasi amekamilisha uchimbaji wa visima tisa kati ya visima 20 vilivyopangwa, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2016. Visima hivyo vyote vikikamilika vitatoa lita milioni 260 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa ujenzi wa mabomba ya kusambaza maji Jijini Dar es Salaam ulisainiwa tarehe 11/12/2015 na Mkandarasi yuko kazini akiendelea kutambua njia za mabomba na maeneo ya kujenga matanki na kuchukua vipimo yaani survey. Matarajio ni kuanza ujenzi mwezi Mei, 2016 kazi hii itakamilika June, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam kwa sasa umefikia lita milioni 390 kwa siku, ukilinganisha na mahitaji ya maji lita milioni 450 kwa siku za sasa. Miradi yote ikikamilika uzalishaji wa maji Jijini Dar es Salaam utafuikia lita milioni 750 ambapo yatakidhi mahitaji hadi kufikia mwaka 2032.
MHE. FREEMAN A. MBOWE (K.n.y MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne ilikopa fedha kwenye Benki za Nje na zile za biashara kwa mfano mwaka 2011 Serikali ilikopa shilingi trilioni 15 na kufanya Deni la Taifa kufikia shilingi trilioni 21, kabla ya mwaka 2015 ilikopa tena kiasi cha shilingi trilioni 9 na kufanya Deni la Taifa kuongezeka kufikia shilingi trilioni 39.
(a) Je, mpaka sasa Deni la Taifa linafikia kiasi gani?
(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya makusudi ya kudhibiti ongezeko hilo la Deni la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali ilipokea mikopo ya nje yenye masharti nafuu na ya biashara kiasi cha shilingi bilioni 1,333.28 na mwaka 2014/2015 Serikali ilipokea mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 2,291.6. Mikopo hiyo haikufikia kiasi cha trilioni 15 kwa mwaka 2011 na trilioni tisa kabla ya mwaka 2015 kama ilivyotafsiriwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Juni, 2016, Deni la Taifa lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 23.2 ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni 19.69 mwezi Juni, 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 20.5 na deni la sekta binafsi lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 2.7.
Aidha, deni la Serikali lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja nchini, mradi wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafishia gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na mradi wa maji Ruvu Chini na Ruvu Juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya makusudi kabisa ili kudhibiti ongezeko la deni hilo. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa miradi yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa Pato la Taifa, kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa wakandarasi na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mikataba inayoweza kusababisha mzigo wa madeni kwa Serikali. Aidha, Serikali inaendelea na mchakato wa kukamilisha zoezi la nchi kufanyiwa tathmini (sovereign rating) kwa lengo la kupata mikopo nafuu.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Kituo cha Biashara cha Taifa - Tanzania Trade Center kilichopo London, Uingereza kimeripotiwa kuwa kinakabiliwa na uhaba wa fedha za kukiendesha na kulipa watumishi wake kutokana na kukosa fedha kutoka Hazina jambo ambalo linasababisha kuzorota kwa kazi za kituo hicho na kukabiliwa na mzigo mzito wa madeni.
(a) Je, Serikali inaweza kueleza hali ya kituo hicho kwa sasa ikoje?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hali ya kifedha na kiutendaji ya kituo hicho ambacho kimesaidia sana kutangaza Tanzania nje ya nchi inakuwa imara na kufanya kazi zake kwa ufanisi?
(c)Je, ni kiasi gani cha fedha kinachodaiwa na kituo hicho na watu mbalimbali nchini Uingereza na hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Biashara cha London kilianzishwa mwezi Oktoba, 1989 kufuatia uamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais mwaka 1989. Lengo la kituo hicho lilikuwa ni kuhamasisha biashara baina ya Tanzania na nchi za Ulaya, hususan Uingereza kwa kutangaza fursa za biashara na uwekezaji na kuvutia wawekezaji kutoka Tanzania na Ulaya kuchangamkia fursa hizo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwake kituo kimefanikiwa sana katika kutekeleza majukumu yake licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zitokanazo na ufinyu wa bajeti na upungufu wa rasilimali watu. Changamoto hizo zimefanya kituo hicho kushindwa kuendana na kasi inayotakiwa ya mabadiliko duniani yanayotokana na matumizi ya teknolojia katika mifumo ya uenezaji wa taarifa na habari ulimwenguni. Ili kulinda heshima ya Taifa na watumishi waliokuwepo katika kituo hicho, Serikali imeamua kukifunga rasmi kituo hicho na kuhamisha majukumu yake kutekelezwa na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Mjini London.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kituo kimefungwa na majukumu yake kutekelezwa na Ofisi yetu ya Ubalozi Mjini London, Serikali itaangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya Ubalozi wetu ili kukidhi majukumu ya ziada yaliyoongezeka.
(d) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Novemba, 2016 Wizara ilipokea na kulipa deni la jumla ya shilingi 129,896,360 kutoka kituo hicho cha London ikiwa ni madai ya pango, maji, simu, umeme na gharama za kufunga kituo hicho.
MHE. JOHN J. MNYIKA (k.n.y MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali iliahidi kuhamisha Kituo cha Mabasi cha Ubungo na kukipeleka eneo la Mbezi katika Jimbo la Kibamba lakini mpaka sasa jambo hilo halijatelekezwa.
(a) Je, Serikali imefikia hatua gani ktaika kutekeleza ahadi hiyo?
(b) Je, mradi wa kuhamisha Kituo cha Mabasi unatarajiwa kutumia kiasi gani cha fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hadi sasa tayari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Serikali za Mitaa (LAPF) umeanzisha kampuni ya ubia ya Mzizima Properties Limited ambayo itahusikana usimamizi na uendeshaji wa shughuli za kituo za kila siku. Kazi inayoendelea ni kutafuta Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kuthibitisha usanifu wa mwisho wa kina wa mradi ili kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi.
Mheshimiwa Spika, gharama za ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi cha Mbezi Luis zinakadiriwa kuwa shilingi bilioni 28.71 zitakazotolewa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Jiji na LAPF. Gharama halisi zitajulikana baada ya usanifu wa kina (detailed design) utakapofanywa na Mtaalam Mshauri.
MHE. MWITA M. WAITARA (K. n. y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali imetangaza kukabidhi rasmi kazi ya kufufua kiwanda cha kutengeneza tairi cha Arusha kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) baada ya kusitisha rasmi uzalishaji mwaka 2009.
Je, mpaka sasa kazi ya kufufua kiwanda hicho imefikia wapi na inatarajiwa kugharimu fedha kiasi gani?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kiwanda cha kutengeneza matairi cha Arusha kilisimamisha uzalishaji mwaka 2009 kutokana na Serikali kukosa fedha kwa ajili ya kukiendesha na mbia mwenza (Kampuni ya Continental AG) hakuwa tayari kuendelea kuwekeza katika kiwanda hicho. Hivyo, Serikali iliweka dhamana ya kukisimamia kiwanda hicho chini ya NDC. Dhamira ya Serikali hivi sasa ni kuona kiwanda hicho kinaanza kuzalisha matairi mapema iwezekanavyo.
Mpaka sasa Serikali imenunua asilimia 26 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na mbia mwenza na hivyo kukifanya kiwanda hicho kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Ili uwekezaji mpya katika kiwanda uwe wenye tija, katika mwaka 2016/2017 Serikali imefanya utafiti wa kubainisha aina ya teknolojia itakayotumika, uwezo wa uzalishaji, upatikanaji wa malighafi, upatikanaji wa soko na athari za mradi na teknolojia itakayotumika kwa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya awali imebaini kuwa kwanza, mitambo iliyopo ambayo ilifungwa kwenye miaka ya 1960 ikiwa imetumika haifai kwa uzalishaji wa kiushindani, pili, inatakiwa kufungwa mitambo inayotumika teknolojia ya kisasa itakayowezesha kiwanda kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira. Tatu, kiwanda kipanuliwe ili kiweze kuzalisha matairi ya aina mbalimbali na kwa wingi ili kupata faida ya uzalishaji kwa wingi (economies of scale). Nne, kiwanda hicho kiundeshwe na sekta binafsi, Serikali ikiwa mbia kwa hisa zinazolingana na rasilimali za kiwanda zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali kwa mwaka 2017/2018 kutafuta mbia atakayekidhi vigezo tajwa hapo juu ili uwekezaji uanze.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Serikali iliingia ubia na kampuni kutoka Jamhuri ya Watu wa China ya kumiliki na kuendesha Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kilichoko Ubungo Jijini Dar es Salaam lakini mbia huyo ameshindwa kutoa mtaji wa kuendesha kiwanda hicho.
(a) Je, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha kuwa mbia huyo anaweka mtaji wa kutosha wa kukiendesha kiwanda hicho?
(b) Je, kwa nini Serikali inafikia maamuzi ya kukibinafsisha kiwanda cha umma kwa mtu ambaye hana mtaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sued Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya Serikali ni kukiendeleza Kiwanda cha Urafiki ili kizalisje nguo na mavazi ya aina mbalimbali. Kutokana na mwekezaji aliyepo kutozalisha kwa ufanisi, mazungumzo ya wanahisa yalifanyika mwezi Machi, 2017 ambapo mbia mwenza, Kampuni ya Changzhou State Owned Textile Assets Operations Limited imeonesha kuwa tayari kumiliki kiwanda kwa kupunguza hisa zake kutoka 51 za sasa na kuipatia Tanzania hisa nyingi zaidi. Katika mpangilio huo mpya, tutakuwa na uwezo mkubwa wa maamuzi ikiwemo kusimamia kampuni kimkakati na kuweka mtaji wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Nguo cha Urafiki ni kiwanda cha kihistoria kilichoanzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1966. Kutokana na historia ya kiwanda hicho wakati wa ubinafsishaji, Serikali ya Tanzania iliitaka Serikali ya China iliyotusaidia kujenga kiwanda hicho kutupa mbia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya China ilikasimu ombi hilo kwa Jimbo la Liangsu ambalo ni bingwa katika sekta ya nguo. Serikali ikateua Kampuni ya Dieqiu Textile Dyeng (DTD)na Printing Group Company ambayo haikufanya vizuri na ikaletwa Kampuni ya Changzhou State Owned Textile Limited tuliyonayo sasa. Kampuni hii nayo haifanyi vizuri hali iliyopelekea kushinikiza ongezeko la hisa za Serikali na mamlaka katika uendeshaji wa kiwanda kama nilivyoeleza hapo awali.
MHE. MWITA M. WAITARA (K. n. y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali imetangaza kukabidhi rasmi kazi ya kufufua kiwanda cha kutengeneza tairi cha Arusha kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) baada ya kusitisha rasmi uzalishaji mwaka 2009.
Je, mpaka sasa kazi ya kufufua kiwanda hicho imefikia wapi na inatarajiwa kugharimu fedha kiasi gani?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kiwanda cha kutengeneza matairi cha Arusha kilisimamisha uzalishaji mwaka 2009 kutokana na Serikali kukosa fedha kwa ajili ya kukiendesha na mbia mwenza (Kampuni ya Continental AG) hakuwa tayari kuendelea kuwekeza katika kiwanda hicho. Hivyo, Serikali iliweka dhamana ya kukisimamia kiwanda hicho chini ya NDC. Dhamira ya Serikali hivi sasa ni kuona kiwanda hicho kinaanza kuzalisha matairi mapema iwezekanavyo.
Mpaka sasa Serikali imenunua asilimia 26 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na mbia mwenza na hivyo kukifanya kiwanda hicho kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Ili uwekezaji mpya katika kiwanda uwe wenye tija, katika mwaka 2016/2017 Serikali imefanya utafiti wa kubainisha aina ya teknolojia itakayotumika, uwezo wa uzalishaji, upatikanaji wa malighafi, upatikanaji wa soko na athari za mradi na teknolojia itakayotumika kwa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya awali imebaini kuwa kwanza, mitambo iliyopo ambayo ilifungwa kwenye miaka ya 1960 ikiwa imetumika haifai kwa uzalishaji wa kiushindani, pili, inatakiwa kufungwa mitambo inayotumika teknolojia ya kisasa itakayowezesha kiwanda kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira. Tatu, kiwanda kipanuliwe ili kiweze kuzalisha matairi ya aina mbalimbali na kwa wingi ili kupata faida ya uzalishaji kwa wingi (economies of scale). Nne, kiwanda hicho kiundeshwe na sekta binafsi, Serikali ikiwa mbia kwa hisa zinazolingana na rasilimali za kiwanda zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali kwa mwaka 2017/2018 kutafuta mbia atakayekidhi vigezo tajwa hapo juu ili uwekezaji uanze.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Serikali katika Bunge la Kumi iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ambayo ilidhihirika kuwa na upungufu na baadhi ya wadau waliona kuwa kama sheria ikipita inaweza kuifanya nchi kuwa adui wa matumizi ya mtandao wa teknolojia ya habari na mawasiliano na sheria hiyo sasa inawaathiri watumiaji wa mitandao, kompyuta, simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyofanana na hivyo:-
Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa kuifanyia Marekebisho Sheria hiyo inayobana uhuru wa mwananchi wa kupata habari?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na marekebisho madogo kwenye jibu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya Mwaka 2015 ni sheria adhibu kwa maana ya penal law ambayo inaainisha makosa na adhabu dhidi ya uhalifu unaotendeka mtandaoni. Sheria hii imeanisha makosa yanayotokana na matumizi mabaya ya mitandao na adhabu zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa sheria hii una manufaa makubwa kwani imesababisha kupungua kwa makosa ya mtandao, upatikanaji wa haki pale mtu anapotenda kosa, kwani kabla ya hapo kulikuwa na changamoto katika uainishaji wa makosa na adhabu hali iliyopelekea haki kutopatikana. Pia uwepo wa sheria hii umewezesha kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao kama vile, Serikali Mtandao, Elimu Mtandao, Biashara Mtandao na hivyo kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ni muhimu sana katika nchi yetu na badala ya kuwaathiri watumiaji au wananchi, imesaidia kupunguza uhalifu wa mitandao, kwani wananchi wameanza kujua na kuelewa faida na hasara ya kutumia mitandao. Mfano, wahalifu wanaoiba fedha kwa njia ya mtandao wanashughulikiwa na sheria hii na haki kupatikana tofauti na ilivyokuwa hapo awali, kwani wananchi wengi walikuwa wakipoteza haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za hali ya uhalifu kuanzia Januari hadi Desemba, 2017 iliyotolewa na Jeshi la Polisi inaonesha kuwa uhalifu kwa kipindi hicho ni matukio 4,824 yaliyoripotiwa, ukilinganisha na matukio 9,441 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2016 ambapo ni sawa na upungufu wa asilimia 48.9. Hivyo kwa sasa Serikali haina mpango wa kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria hii hadi hapo kutakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi kutumia fursa chanya zinazotokana na matumizi sahihi ya mtandao kuliko kutumia mitandao kwa ajili ya kufanya mambo ambayo ni kinyume na sheria za nchi na tamaduni za Kitanzania.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Kumekuwepo na vitendo vingi vya uhalifu hapa nchini kwa watu kuvamiwa, kupigwa, kujeruhiwa na kuporwa mali zao na hata kuuawa:-
• Je, Serikali ina mpango gani wa kukomesha vitendo hivyo vya uhalifu ambavyo vinatishia usalama wa raia na mali zao?
• Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza juhudi za ulinzi wa raia na mali zao ili kudumisha amani na utulivu nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
i. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina mipango mbalimbali ya kukomesha vitendo vya uhalifu kwa kuimarisha doria za miguu, pikipiki na magari, pia kufanya misako dhidi ya uhalifu na wahalifu. kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu za kukabiliana na uhalifu, kufanya operation za mara kwa mara na kushirikisha jamii kwenye ulinzi wa maeneo yao kupitia dhana ya Polisi Jamii.
ii. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao kwa kuendelea kuajiri askari na kuongeza vitendea kazi pia, kwa kutumia falsafa ya kugatua madaraka. Serikali imeshapeleka wakaguzi katika tarafa, jimbo, kata, shehiya ili kushiriki kikamilifu kwa kuyabaini maeneo tete ambayo huwa ni vyanzo vya uhalifu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Kituo cha Afya cha Palestina kilichopo Kata ya Sinza alitangaza kukipandisha hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, bado Serikali inaendelea kuipatia fedha hospitali hiyo kama Kituo cha Afya.
Je, ni lini Serikali itaitambua hospitali hiyo kama Hospitali ya Wilaya kwa kuipa fedha na vitendea kazi vinavyofanana na hadhi yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Palestina kimekuwa kinafanya kazi kama Hospitali ya Wilaya kufuatia tamko la Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne la tarehe 11 Disemba, 2012.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tamko hilo, ukaguzi ulifanyika na kubaini uhitaji wa kuongezewa eneo kwa ajili ya upanuzi wa huduma. Ifahamike wazi kuwa kituo hiki kilianzishwa ili kitoe huduma kama Kituo cha Afya, hivyo hakiwezi kuwa Hospitali ya Wilaya. Kwa kutambua umuhimu wa kituo hiki, hatua zifuatazo zimechukuliwa kutatua baadhi ya changamoto:-
(a) Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ruzuku ya ununuzi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imeongezeka hadi kufikia shilingi milioni 69 kutoka shilingi milioni 57.4 kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
(b) Madaktari Bingwa watatu wameshapelekwa katika kituo hiki kati ya watano wanaohitajika, kwa maana ya Madaktari Bingwa wa Watoto, wawili na Daktari wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi mmoja.
(c) Katika mwaka wa fedha 2018/2019, kiasi cha shilingi milioni 160 kimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la ghorofa moja ambalo lina wodi ya wanaume, wanawake na watoto.
(d) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kituo kimetengewa asilimia 25 ya fedha za Mfuko wa Pamoja wa Wafadhili (Health Sector Basket Fund) ambayo ni sawa na shilingi milioni 357.73 ya mgao wa Manispaa ya Ubungo ambayo ni shilingi bilioni 1.43. Fedha hizi ni kwa ajili ya utawala na ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako tukufu, napenda kuelekeza Halmashauri ya Ubungo kutenga eneo lisilopungua ekari 25 litakalowezesha kuwepo katika eneo moja majengo yote ya msingi ya Hospitali ya Wilaya. Aidha, Serikali itaendelea kupeleka Madaktari Bingwa na kuboresha huduma zaidi katika kituo hiki kadri bajeti itakavyokuwa ikiruhusu.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete iliahidi kujenga kwa lami barabara ya kutoka Kimara Mwisho kupitia Mavulunza – Bonyokwa Segerea hadi kuungana na barabara ya Nyerere yenye urefu wa Kilomita 4.7 na ambayo imekasimiwa kwa TANROADS:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa lami kama ambavyo iliahidiwa miaka mitano iliyopita?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara hiyo ili kupunguza tatizo la foleni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, lenye kipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Kimara Mwisho kupitia Mavulunza - Bonyokwa hadi Segerea hadi kuungana na barabara ya Nyerere yenye urefu wa kilomita nane (8) unategemea kuanza mara baada ya kukamilisha utekelezaji wa mpango wa sasa wa ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano unaoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano Jijini Dar es Salaam unaendelea vizuri. Mpaka kufikia mwezi Aprili, 2018, ujenzi wa barabara ya Banana - Kinyerezi – Kifuru – Marambamawili - Msigani hadi Mbezi Mwisho yenye urefu wa kilomita17, ambayo inaunganisha barabara ya Nyerere na Morogoro umefikia asilimia 90. Kwa sasa ujenzi unaendelea ili kukamilisha sehemu ya barabara iliyobaki yenye urefu wa kilomita mbili (2) kuanzia Msigani mpaka Mbezi Mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa barabara hii kutaunganisha barabara ya Nyerere, Morogoro na Bagamoyo kupitia barabara ya Mbezi Mwisho, Goba, Tangi Bovu ambayo ujenzi umekamilika.hata hivyo, Serikali inaendelea kutenga fedha za matengenezo ya barabara ya kutoka Kimara Mwisho – Bonyokwa - Segerea ili kuhakikisha inapitika vizuri wakati wote.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-

Gesi asilia iliyogundulika nchini ni takribani ujazo wa trilioni feet 56:-

(a) Je, uwekezaji wa viwanda vinavyotumia gesi asilia kwa ukanda wa Kusini umefikia wapi na ni wa kiwango gani?

(b) Je, mpango wa kujenga kiwanda cha kuchakata gesi asilia bado upo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi asilia iliyogundulika nchini hadi sasa ni futi za ujazo trilioni 57.54. Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam ni maeneo yaliyonufaika na shughuli za uwekezaji katika viwanda vinavyotumia gesi asilia. Matumizi ya gesi asilia nchini yalianza tangu mwaka 2004 ambapo kufikia mwezi Oktoba, 2019, jumla ya viwanda 48 vimeunganishwa na mtandao wa gesi asilia. Viwanda hivyo vinatumia gesi asilia kama nishati na vingine vinazalisha umeme kwa matumizi ya viwanda.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) unaendelea. Kwa sasa utekelezaji wake umefikia hatua ya majadiliano ya mkataba wa nchi husika (Host Government Agreement) kati ya wawekezaji na Serikali. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-

Ni ukweli kwamba bei ya bidhaa za Viwandani kwa kiwango kikubwa zinatokana na gharama za uzalishaji kama vile maji, umeme, nguvu kazi na kadhalika:-

Je, kitendo cha kutoa kibali kwa Viwanda vya Sukari kuagiza sukari kutoka nje, siyo kuua kabisa Kilimo cha zao la miwa ambacho wakulima wanategemea kuuza kwenye viwanda vya ndani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Sukari imeakuwa ikifanya tathmini ya mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka na kwa kuzingatia matumizi ya kawaida na matumizi ya viwandani. Aidha, tathmini hiyo hufanyika sambamba na kujua uwezo wa viwanda vya kuzalisha sukari hapa nchini ambapo nakisi kati ya uzalishaji na mahitaji ndiyo kiasi cha sukari inayohitajika kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tathmini ya mahitaji ya sukari kwa miaka miwili iliyopita, yaani 2017/2018 na 2018/2019 ilibaini kuwepo na utengamano wa soko la ndani kwa bei na upatikanaji wa sukari nchini. Aidha, utengamano huo ni matokeo ya maamuzi ya Serikali ya kutumia mfumo wa kuwapa leseni wazalishaji wa ndani kuagiza sukari kutokana na mahitaji badala ya mfumo wa kutumia wafanyabiashara kuagiza sukari toka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mfumo huo umeweza kudhibiti uingizaji wa sukari ya ziada nchini kwani wazalishaji huagiza kuliangana na kiasi kilichoainishwa kwenye leseni husika. Aidha, kabla ya utaratibu wa kuwapata vibali wenye viwanda kuagiza sukari, nakisi ya sukari (Gap Sugar) ilikuwa ni zaidi ya tani 130,000 nchini, lakini baada ya utaratibu wa kuwapa wenye viwanda kuagiza, upungufu umepungua hadi kufikia tani 38,000.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho uzalishaji wa miwa kwa wazalishaji wadogo umeongezeka kutoka tani 568,083 msimu wa 2017/2018 hadi tani 708,460 msimu wa 2018/ 2019. Ongezeko la uzalishaji wa miwa kwa wakulima madogo limekwenda sambamba na ongezeko la kipato cha mkulima ambapo mapato ghafi kwa wakulima wa Kilombero, kwa mfano wakulima wa Kilombero yamefikia thamani ya shilingi bilioni 68.7 msimu wa 2018/2019 kutoka shilingi bilioni 48.1 misimu wa 2017/2018.

Aidha, kutokana na ongezeko la uzalishaji wa miwa kwa wakulima wadogo, uzalishaji wa sukari nchini umeongezeka kwa asilimia 16.8 kutoka wastani wa tani 307,431.26 hadi tani 359,219.25 katika msimu wa 2018/2019 wa kilimo.
MHE. TUNZA I. MALAPO (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-

Uvuvi katika nchi yetu ni shughuli inayohusu wakazi wengi sana ikiwa ni ya pili kutoka kwenye kilimo kwa kutoa ajira kwa Watanzania wengi:-

(a) Je, ni lini na ni wapi kiwanda cha samaki kwa ukanda wa Pwani kitajengwa?

(b) Je, mpango wa ujenzi wa Bandari ya Samaki umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na kuhamasisha Sekta Binafsi kuwekeza katika Sekta ya Uvuvi kwa kuweka mazingira mazuri ikiwemo uwepo wa malighafi kwa viwanda vya kusindika mazao ya uvuvi. Hadi sasa kuna viwanda vitano vya kusindika mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani. Vilevile, Serikali inatarajia kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kujenga viwanda vya kusindika mazao ya uvuvi nchini ikiwa ni moja ya mikakati yake.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeingia mkataba na mshauri elekezi Kampuni ya Sering Ingegneria kutoka Italia kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari ya uvuvi katika mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi. Kampuni hii ilianza kazi tarehe 2 Agosti, 2018 na tayari imekabidhi taarifa ya awali (inception report) na kazi inaendelea ambapo hatua ya pili ya ukusanyaji wa taarifa muhimu (interim report) inaendelea. Aidha, upembuzi huo utakapokamilika utawezesha kutambua maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa bandari na gharama za ujenzi wa bandari ya uvuvi.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-

Serikali ilitangaza kuwa wanasheria wote walioko kwenye mashirika ya umma watafanya kazi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi na kuwapa ufanisi kwenye ufuatiliaji wa kesi zinazofunguliwa dhidi ya Serikali.

(a) Je, utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu mawakili binafsi kutosimamia kesi za Serikali limefikia wapo?

(b) Je, ni kiasi gani cha fedha kilichookolewa tangu mashirika ya Serikali yaache kutumia mawakili wa nje?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yaliyofanywa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2018 yaliyopitishwa na Bunge lako tukufu, yaliwezesha kufanya wanasheria wote katika utumishi wa umma kuwa chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mabadiliko hayo yalitokana na Tangazo la Serikali Na. 50/2010 lililotambua kuwepo kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo amepewa jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendesha mashauri yote ya madai ambayo Serikali inashtaki au inashtakiwa.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tayari imeshatoa maelekezo kwa Wizara na Taasisi zote za Serikali kuwasilisha mashauri yote ya madai dhidi ya Serikali katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uratibu, usimamizi na uendeshaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uwezeshaji wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa sasa mashauri yote ya madai dhidi ya Serikali yanasimamiwa na ofisi hii isipokuwa kama itaonekana kuwepo kwa ulazima wa kuhusisha mawakili binafsi. Hii hutokea iwapo mashauri husika yamefunguliwa katika mahakama za nchi za nje zisizokuwa za Kimataifa ambazo kwa baadhi ya nchi sheria zake za ndani na taaluma ya uwakili haziruhusu mawakili wa nchi nyingine kufanya shughuli za uwakili hasa uwakilishi mahakamani ndani ya nchi husika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, inapotokea hitaji la kutumia mawakili binafsi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali hulazimika kutoa kibali cha Serikali cha kuajiri Wakili kutoka ndani ya nchi hiyo itakayoshirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kusimamia uendeshaji wa shauri husika.

Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kumesaidia kupunguza gharama zilizokuwa zinalipwa na wakili binafsi ambazo kwa tathmini ilifanyika uendeshaji wa kila shauri moja hapa nchini zilikuwa hazipungui shilingi 5,000,000 na kwa upandea mashauri yaliyofunguliwa nje ya nchi gharama za kumlipa wakili kwa kila shauri ilikuwa hazipungui dola za Marekani 300,000 mpaka 2,500,000 kwa kila shauri.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu ya bajeti 2019/2020 kwa mwaka 2018/2019 Serikali iliokoa kiasi cha shilingi 9,018,957,011 ambazo zingelipwa kwa mawakili binafsi. Ninapenda kulithibitishia Bunge kuwa Serikali itaendelea kuokoa fedha nyingi zaidi ambazo zitasaidia kuleta maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea na kazi ya ukusanyaji wa mashauri yote ya madai kutoka kwa Wizara na Taasisi zote za umma/Serikali. Zoezi hili litakapokamilika litasaidia kufanya tathmini ya kina na kupata thamani halisi ya fedha zilizookolewa na Serikali kupitia maboresho haya mapya. Ahsante.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-

Kuna taarifa kwamba ubadhirifu bado unaendelea katika Shirika la NIC; vilevile taarifa zinaonesha kuwa Shirika hilo halina mipango thabiti ya kukabiliana na washindani wake kibiashara:-

(a) Je, ukweli juu ya taarifa hizo ni upi?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuisaidia NIC kifedha na kitaalam ili kuliwezesha shirika hilo kukabiliana na ushindani wa kibiashara?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, hakuna ubadhirifu wowote unaoendelea katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Shirika limeendelea kuboresha mifumo yake ya udhibiti wa mapato na matumizi ili kukabiliana na washindani wake kibiashara katika sekta ya bima. Katika kujiimarisha kibiashara, Shirika limechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mapato yote yanakusanywa kwa kutumia Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) ambao ulianza kutumiwa na Shirika mwezi Novemba 2019 na kuondoa ukusanyaji wa mapato kwa fedha taslimu (cash); kuongeza udhibiti katika ulipaji wa madai ikiwepo kufanya ukaguzi maalum wa madai yote ya Bima za Maisha ili kujiridhisha juu ya uhalali wa madai haya; Shirika lipo katika hatua za mwisho za kuunganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kihasibu na Malipo katika Taasisi za Umma (MUSE) ambao utaongeza udhibiti katika malipo yote yanayofanyika; kusitisha matumizi ya hundi (cheque) ambapo kuanzia mwezi Desemba 2019, Shirika lilisitisha matumizi ya hundi (cheque) katika malipo yake yote na kuanza kutumia mfumo wa malipo wa kielektroniki hivyo kuongeza uthibiti wa matumizi na kuzuia uwezekano wa matumizi ya hundi feki (forged cheques).

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua mbalimbali kuliimarisha Shirika la Bima la Taifa (NIC) kitaalam kwa kufanya yafuatayo: Kuliondoa Shirika kutoka kwenye mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa na kuliwezesha kushiriki katika biashara ya bima kwa ushindani; imelifanyia mabadiliko ya kiuongozi Shirika ili kuongeza tija na kuleta mabadiliko chanya kwenye utendaji na usimamizi wa shughuli zake; na imelisaidia Shirika kwa kuwapatia wataalamu mbalimbali katika nyanja za mifumo ya TEHAMA, mifumo ya utendaji kazi na mifumo ya utunzaji kumbukumbu (e-Office) ili kuweza kuongeza ufanisi wa Shirika na kuweza kukabiliana na ushindani wa kibiashara.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeliimarisha Shirika kifedha kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kupata biashara za Serikali na kushinikiza malipo ya hapo kwa hapo ya premium ambayo yamesaidia kupunguza malimbikizo ya premium kutoka kwa Taasisi za Serikali kutoka zaidi ya shilingi bilioni 20 hadi milioni 500 kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maendeleo mazuri ya Shirika, Serikali inaendelea kuliimarisha Shirika hili la kimkakati kwa kulisaidia katika kupitia upya Mpango Mkakati wake ili uendane na mahitaji halisi ya biashara ya ushindani; kuongeza uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA ili kuwafikia wateja wengi zaidi; kuongeza ubora wa huduma zake na kulipa madai haraka na kwa urahisi; kujitangaza zaidi na kuongeza uwekezaji wenye tija ili kutoa gawio kubwa kwa Serikali na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Taifa.