Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Saed Ahmed Kubenea (24 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Nami niungane na wengine kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ubungo kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mbunge wao, kwa kura zaidi ya 87,000 dhidi ya yule ambaye upande wa pili wanamwita hajawahi kushindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja katika hoja yangu katika kuchangia Mpango wa Maendeleo, katika ukurasa wa 50(6)(a) ambayo ni Vihatarishi katika Mpango. Vihatarishi katika utekelezaji wa Mpango, vimeelezwa kwamba ni pamoja na kumekuwa na changamoto katika upatikanaji wa mikopo kwa wakati, na riba kubwa hivyo kuathiri uwezo wa nchi kukopa, kwa upande wa misaada kumekuwepo na masharti magumu na utayari wa washirika wa maendeleo kutoa fedha kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa hapa kwamba vihatarishi vya Mpango ni pamoja na Washirika wa Maendeleo kukataa kutoa fedha kwa wakati. Washirika wa Maendeleo nchi ya Marekani, Taifa kubwa duniani, tayari limekataa kutoa fedha za MCC, na Umoja wa Ulaya uko njiani kuzuia misaada. Sababu wanasema kwamba kuna tatizo Zanzibar, uchaguzi wa Zanzibar umefanyika na kuna tatizo kubwa la msingi ambalo linapaswa kutatuliwa, sisi tuko hapa Bungeni tunajifungia ndani ya Bunge hili, tunajifanya hamnazo, tunaona kwamba Zanzibar hakuna tatizo tunashangilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasimama katika Bunge, wanajipa mamlaka wa kuwa Maamiri Jeshi Wakuu, na wanatangaza kwamba Zanzibar hakuna tatizo. lakini ukweli ni kwamba, uchaguzi wa Zanzibar utatuletea matatizo makubwa kama Taifa, tusipokuwa makini katika kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna namna yoyote ya Bunge hili kukwepa kuzungumza suala la Zanzibar. Uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika tarehe 25 Oktoba na matokeo yote yakawa yameshakusanywa na yapo.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo...
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba ulinde muda wangu. Iwapo matatizo haya Zanzibar hayatatatuliwa kwa umakini vinginevyo mpango huu mzima hautatekelezwa.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Taarifa...
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba ulinde muda wangu, lakini nimepokea maelezo ya Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, nimemshangaa kwamba anataka tusizungumzie masuala ya Zanzibar, wakati yeye ametoka Zanzibar amekuja hapa kuiwakilisha Zanzibar. Yuko kwenye Bunge hili kwa sababu ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Mpango wa Maendeleo na ninapozungumzia maendeleo, tunazungumzia maendeleo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zanzibar ikiwemo, Katiba hii imeitaja Zanzibar kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; asome vizuri. Matatizo ya Zanzibar ya uchaguzi yasipopatiwa ufumbuzi wa kudumu tukakaa humu ndani tukajifanya hatujui kama Zanzibar kuna tatizo, Maaskofu wanahubiri katika Madhabahu, Mashehe wanasema katika Misikiti, wadau wa maendeleo wanatukanya, kwamba Zanzibar kuna matatizo sisi tunakaa hapa tunajidanganya. Nchi yetu tunaipeleka pabaya na Mpango huu wa Maendeleo hautafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tokea mwaka 1964 mpaka mwaka 1980 hakuna Mpango wowote wa Maendeleo uliofanikiwa kwa zaidi ya asilimia hamisini kwa sababu wadau wa maendeleo walikataa kutoa fedha. Fedha za maendeleo kutoka kwa nchi wahisani zilikuwa hazitoshi na huu mpango mzima unaokuja hapa unategemea fedha za wahisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa thelethini na moja wa kitabu hiki, kimeelezwa juu ya suala zima la utawala bora. Bunge hili ambalo Mpango unasema kuimarisha utawala bora, lilifanya kazi kubwa sana katika Bunge la Kumi, kulipitishwa maazimio hapa juu ya fedha za escrow, Tume zikaundwa, Majaji ambao walituhumiwa kuhusika na kashfa ya Escrow wakaundiwa Tume za uchunguzi, ilitangazwa. Mawaziri wanne wakajiuzuru katika Bunge hili, Wenyeviti wawili wa Kamati za Bunge wakajiuzuru. Serikali ikasema inaunda Tume lakini Tume ya majaji haikuundwa, Mawaziri waliojiuzuru mmoja Profesa Sospeter Muhongo amerudishwa katika Bunge hili akiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliyeondolewa na Bunge leo anaongoza Bunge kama Mwenyekiti wa Bunge. Hii maana yake nini, maana yake suala zima la rushwa lililotajwa katika ukurasa wa 34 kwamba ni tatizo katika nchi yetu linaonekana halina tatizo kabisa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa! Nampa taarifa Mheshimiwa Saed Kubenea...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kubenea endelea.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nilikuwa naeleza na bado nasisitiza kwamba suala la utawala bora ni jambo la muhimu sana katika Taifa letu. Hatuwezi kukaa hapa tukawa tunahubiri amani na utulivu wakati Taifa letu halina utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana mmoja wa wachangiaji katika Bunge hili alisema kwa sauti kubwa kwamba Chama ambacho kimegombea uongozi kwa vipindi vitatu mfululizo kikishindwa kitaingia kuwa chama cha ugaidi. Hata hivyo, namsamehe kwa sababu hasomi historia anaishia hapa hapa Tanzania. Ukienda India, Uingereza, Canada na Newzealand vyama vyote vikubwa vilivyoshindwa uchaguzi vimebaki kuwa imara, Chama kinachoshindwa uchaguzi lakini kinaendelea kuimarika kwa kushinda Majimbo mengi na kuchukua Halmashauri nyingi na kile ambacho kinashinda uchaguzi, lakini kinaendelea kuporomoka siku hadi siku kipi kinachoelekea kwenye ugaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila shaka Chama kile ambacho kinashinda uchaguzi lakini kinaendelea kuporomoka siku hadi siku ndicho kinachoelekea katika ugaidi. Hayo yanaonesha ni jinsi gani Taifa letu leo usalama wa raia wetu ulivyokuwa mashakani. Mimi mwenyewe ni muhanga wa usalama wangu na nimetajwa katika Bunge hili la Kumi katika ripoti ya richmond.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanauwawa, watu wamepigwa na Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kulinda raia na mali zao. Waandishi wa Habari kina Mwangosi, Mwandishi wa Habari mwenzangu ameuwawa, Absalom Kibanda amepigwa, Dkt. Steven Ulimboka ametekwa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande, lakini Serikali imekaa kimya na inasema hawa watu wasiojulikana. Serikali ni lazima ichukue hatua madhubuti kulinda usalama wa raia na mali zao ili kuimarisha utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu wanazungumza sana mambo ya reli ya kati na mimi naomba nizungumze kuhusu reli ya Kati.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mpango mzima wa reli ulioletwa hapa na Serikali, wakati sisi tunaonya kwamba nchi wahisani zimekataa kutoa fedha na kwamba mipango hii ya maendeleo haiwezi kutekelezwa. Kuna Mpango umekuja hapa wa reli. Reli hii inahitaji dola bilioni saba, karibu shilingi trilioni kumi na tano. Serikali ya Tanzania ilikuwa inaomba fedha kutoka Serikali ya China. Naomba niwapeleke shule, Serikali ya China imekataa kutoa fedha kwa ajli ya kujenga reli ya kati, mtafute fedha kutoka maeneo mengine.MWENYEKITI:
Mheshimiwa Kubenea muda wako umekwisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kupongeza hotuba ya Msemaji wa Upinzani Bungeni aliyoitoa leo asubuhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeambiwa na nimemsikiliza Waziri wa Viwanda akizungumza jinsi ya kuifanya Tanzania iwe ya viwanda, lakini katika hotuba nzima sijasikia Serikali ikisema kwa nini viwanda vyetu vilikufa? Nchi hii ilikuwa na viwanda vingi, ilikuwa na mashamba, ilikuwa na migodi na mabenki, yamegawanywa na yameuzwa kwa bei ya kutupa, halafu leo Serikali inakuja inasema inaanzisha viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwamba wangekuja na mkakati wa kutueleza kwanza viwanda vyetu vilikufaje. Tumeambiwa, baadhi ya Wabunge wamezungumza humu kwamba viwanda vyetu vimekufa kwa sababu Taifa hili halina uzalendo. Nikiangalia Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri waliomo humu ndani upande huu wa pili, asilimia kubwa sio wazalendo. Viwanda hivi hata vikianzishwa vitakufa! Hata kuanzishwa, havitaanzishwa! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna fedha kwenye bajeti hii ya kuanzisha viwanda. Bajeti nzima imetengewa shilingi bilioni 80. Kiwanda kimoja zaidi ya shilingi bilioni 60, unajenga wapi hivyo viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimwangalia huyu Waziri na mbwembwe alizokuja nazo asubuhi kwamba ataanzisha viwanda, namfananisha na yule aliyekuwa Waziri wa Habari wa Iraq wakati wa vita vya Ghuba ya Pili Al-Sahaf; ndiye mwenye mbwembwe kama hizi. Anaweza kukuaminisha pepo wakati bado uko hai, hujafa, akakwambia kuna chakula kiko hapo, kula, chakula hakipo! Huyu anafaa kuwa Waziri asiye na Wizara Maalum, ahamasishe kuzibua mito, ahamasishe kuzibua mitaro, hiyo ndiyo kazi anayoiweza, siyo kazi kubwa kama hii. Viwanda haviwezi kujengwa kwa namna hii. Huyu anaweza kufanya kazi ya uhamasishaji, ile ambayo inaweza kufanywa na watu wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 nilipata nafasi ya kwenda Uingereza. Nikiwa pale Uingereza nilitembelea kituo chetu cha biashara cha London. Nilikwenda Ubalozi, wakatueleza, pale London kuna kituo chetu cha biashara kinaitwa London Trade Center.
Kituo hiki kilianzishwa baada ya maelekezo ya Rais wa wakati huo mwaka 1989. Hali ya kituo cha London inasikitisha! Wafanyakazi wa Kituo cha London hawajalipwa mishahara toka Disemba mwaka 2015. Mkurugenzi wa Kituo cha London, nyumba yake inadaiwa kodi, hajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameandika barua chungu nzima kwenye Wizara, Mheshimiwa Waziri anazo barua hizo, wanakumbushia juu ya malipo ya mishahara, wanakumbushia malipo ya pango, lakini Serikali haijapeleka fedha London. Wakati Waziri anajibu hoja za Wabunge nataka alieleze Bunge hili Tukufu ni lini Serikali itapeleka fedha za mishahara London?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki kimefanya kazi kubwa sana ya kuitangaza Tanzania nje, lakini wafanyakazi wa kituo hiki wameachwa solemba, wameachwa yatima. Wameandika barua, kuna barua hapa ya tarehe 22 Februari, 2016. Kuna barua wanaeleza jinsi ambavyo wasivyokuwa na fedha, wako hoi, hata kazini hawawezi kwenda, hawana nauli, halafu mnaweka watu nje wadhalilike! Wamekopa, mpaka mzigo wa madeni umewazidi! Kama hamuwezi, warudisheni Tanzania, badala ya kuja na mbwembwe hapa mtaanzisha viwanda; mnashindwa kulipa wafanyakazi wenu waliopo London, mtaanzishaje viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni mchungu. Bahati mbaya sana, tukizungumza sisi tunaitwa wapinzani. Amezungumza Mheshimiwa Bashe, amewaambia mnahitaji miujiza ili muweze kutekeleza hii bajeti. Sisi tunazungumza kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kujenga nchi kama huna bandari. Sisi Mungu ametujalia tuna bandari, lakini bandari yetu tumeiua. Leo mizigo inayopita bandarini asilimia 40 ya mzigo imeshuka kwenye makontena. Matokeo yake, badala ya kuiendeleza bandari, kila siku tunakwenda kuvunja Bodi ya Bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Harrison Mwakyembe amekuwa Waziri wa Uchukuzi, amekwenda kuvunja Bodi ya Bandari, akamfukuza na Mkurugenzi wa Bandari Mheshimiwa Mgawe; amekuja akaunda Bodi yake. Akaja Mheshimiwa Sitta akafukuza Bodi ya Mwakyembe; akaja Waziri Mkuu akafukuza Bodi ya Mheshimiwa Sitta na miongoni mwa Wajumbe waliofukuzwa ni Naibu Spika. Sasa haya ni mambo gani? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo bandari miezi mitano haina Bodi, haina Management, unaendeshaje nchi? Bandari haina Mkurugenzi, unaendeshaje nchi? Halafu unasema unaweza ukaleta Tanzania ya viwanda; viwanda vipi bila bandari? Ndiyo maana Waziri katika bajeti yake yote, anazungumza juu ya bomba la gesi linalotoka Uganda kwenda Tanga. Pia kuna reli inajengwa kutoka Uganda kwenda Rwanda. Katika mipango hii ya Waziri hakuna reli ya kutoka Kagera ambako ndiko karibu na Uganda, lakini hakuna mpango mkakati wa biashara katika mkoa huu; na huo ndiyo mkoa Waziri anakotoka! Mkoa wake! Hakuna biashara! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi afanye upendeleo, lakini hii ni kuonesha kwamba hakuna connection kati ya Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Miundombinu, hakuna! Hiyo ndiyo Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika mwaka 2015 wakati wa kampeni, mimi sio mwenyeji sana huko, Rais Magufuli aliongelea Special Economic Zone Kagera. Katika eneo alilolisema nadhani ni Omukanjuguti, labda akina Mheshimiwa Tibaijuka na Mheshimiwa Lwakatare wanaotoka huko, wanaweza kujua zaidi. Utueleze basi katika majibu yako, mipango gani ya kibiashara unayopanga kwa ajili ya kilimo cha mboga na matunda kinachohitajika uwanja wa ndege? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ya kuzungumza bila kuleta hoja nzuri hatutafika. Hapa tunazungumza juu ya mradi wa Mchuchuma na Liganga, lakini wale Wachina, nyaraka zilizopo na Serikalini mnazo, zinaonesha Wachina hawana fedha ya kuendesha huu mradi, wanataka kukopa dola milioni sita kutoka Benki ya Exim na dhamana yao ni Mchuchuma na Liganga.
Sasa mali yetu inachukuliwa dhamana halafu Mheshimiwa Nagu anasimama hapa anasema tuwe na viwanda. Alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na ripoti ya CAG imesema ule mkataba ni fake, uvunjwe; Mheshimiwa Mama Nagu akiwa Waziri. Mambo gani? Mnaambiwa mnasema tunatukana. Sisi tunawaeleza! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii haitaenda kwa ngonjera na usanii na kwa mtu kuwa Al-Sahaf. Nchi hii itakwenda kwa uchumi endelevu kwa watu kukaa kwenye meza, kuchora uchumi, kuendesha nchi kwa data, hesabu, numbers. Bila hesabu, bila namba, hakuna uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kusema kwamba Taifa letu limebahatika, lina utajiri mkubwa, lakini tusije tukarudia makosa wakati wa ubinafsishaji. Tuliuza mabenki, tukauza viwanda…
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Kwanza nampongeza kabisa kwa dhati Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Wananchi la Tanzania limefanya kazi kubwa sana katika Jamhuri ya Muungano na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaposema hapa kwamba jeshi lisitumike kisiasa, hatuna maana kwamba sisi sio wazalendo, tunalipenda jeshi letu lakini tunaonya kwamba vitendo vinavyofanyika Zanzibar na vilivyofanyika wakati wa uchaguzi na sasa vinaashiria uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu. Hiyo haina maana kwamba watu hawa siyo wazalendo au hawalipendi jeshi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizotoa askari kulinda amani katika Jeshi la Umoja wa Mataifa. Ripoti iliyowasilishwa tarehe 3 Machi inazungumzia matukio 99 ya ubakaji na udhalilishaji wa watoto yaliyofanyika mwaka 2005 na walinzi wa amani Umoja wa Mataifa katika nchi 69. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 6 Machi, 2016, kwa mujibu wa vyombo vya habari vilimnukuu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi akisema kwamba ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya yaliyotokea katika Afrika ya Kati na maeneo mengine, hajaipata. Leo ni tarehe 10 Mei, takribani miezi miwili tokea Waziri alipowaambia umma kwamba ripoti ile hajaipata. Tunaomba Mheshimiwa Waziri wakati anapojibu alieleze Bunge hili Tukufu, ni hatua gani zimechukuliwa kama askari wetu wa Jeshi la Ulinzi na Usalama walihusika na mambo yaliyotokea katika Jeshi la Kulinda Amani?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni muhimu sana kwa kuwa jeshi letu limefanya kazi nzuri, linaheshimika duniani, ili lisiweze kuchafuliwa kwa mambo ambayo hayawahusu. Jambo hili ni muhimu pia likawekwa wazi kwa kuwa taarifa hizi zilitolewa hadharani na ziko katika mitandao na zipo katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Jijini Dar es Salaam. (Makofi)
Jambo la pili, kuna taarifa kwamba Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania limeingia mkataba wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi na Kampuni ya Henan Guijo Industry Investment Co. Ltd. Katika mkataba huo, Jeshi la Wananchi wa Tanzania litatoa ekari za mraba 26,082.87 katika eneo la plot number 1255 Masaki, Jijini Dar es Salaam. Katika mkataba huu mjenzi akikamilisha mradi kwa mujibu wa taarifa zilizopo, ataendesha eneo hili kwa muda wa miaka 40 na baada ya hapo eneo litarudi jeshini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri atueleze kama mkataba huo umesainiwa; na kama haujasainiwa nitaliomba Bunge hili Tukufu lielekeze kwamba mkataba huu ambao unaweza ukawa wa kinyonyaji upelekwe katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ili uweze kupitiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi letu limewahi kuingia mikataba ya aina hii na ambayo baadaye ilikuja kuonekana imedhalilisha Jeshi, imedhalilisha Serikali ukiwemo mkataba wa Meremeta. Sasa ni vizuri tukajihadhari, lakini kibaya zaidi, ni kwamba kampuni ya Henan Guijo Industry Co. Ltd. ambayo imeingia mkataba na Jeshi la Wananchi au inataka kuingia mkataba na Jeshi la Wananchi, inajifunga mkataba mwingine na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hiyo itajenga pia nyumba ya Dkt. Hussein Mwinyi iliyopo plot number 2435/5 eneo la Sea View, Upanga Jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo ndiyo itakayolipia gharama za ujenzi...
TAARIFA
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.....
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema mita za mraba, labda hakusikia vizuri. Naomba pia unilinde kwenye muda wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mkataba huu, kama ambavyo unaweza kuwa ama umesainiwa ama haujasainiwa, ni kwamba mjenzi ndiye ambaye atajenga pia nyumba ya Dkt. Mwinyi. Sasa kama madai haya ni ya kweli, tunaomba Mheshimiwa Waziri atuambie huu siyo mgongano wa kimaslahi? Je, kwa mkataba huo, haina maana kwamba jeshi letu linaingizwa kwenye mkataba wa kinyonyaji kwa kuwa Waziri ananufaika? (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema kwamba uchunguzi ufanyike na vyombo vinavyohusika, vimchunguze Mheshimiwa Waziri na vipeleke taarifa kwenye Bunge hili Tukufu kwa kuwa uchunguzi huu ni muhimu kwa sababu unahusu hoja muhimu kabisa iliyopo mbele ya Bunge lako Tukufu.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kumalizia hoja yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi letu la Wananchi tunalipenda sana, Taifa letu tunalipenda sana, Bunge letu Tukufu tunalipenda sana, lakini mambo ya namna hii yanatia doa Jeshi letu na Taifa letu. Kuna mambo yanazungumzwa mengi sana kwenye Taifa hili. Baadhi ya kampuni ambazo zinatuhumiwa katika maeneo mengine kwamba zimefanya biashara na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi nazo pia zinatajwa kufanya biashara na Jeshi la Wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Kampuni ya Lugumi, baadhi ya nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba Kampuni ya Lugumi iliwahi pia kufanya biashara na Jeshi la Wananchi na iliwahi kuuza silaha kutoka Taiwan lakini Jeshi letu lilizikataa kwa kuwa zilikuwa chini ya kiwango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sana kwamba…
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri jeshi letu likajiepusha na makampuni kama haya. Kwa nini vitu hivi vinajirudia mara kwa mara? Tunalipongeza sana kwa kazi nzuri ambayo Jeshi limefanya katika Taifa hili, limefanya kazi kiuadilifu, kiuaminifu na kwa kweli mambo mengi limepakaziwa. Jeshi linashinikizwa kufanya mambo kwa sababu za kisiasa. Mikataba mingi ambayo Jeshi hili limeingia ikiwemo Meremeta ni kwa sababu za kisiasa. Mambo mengi ambayo yanatokea Zanzibar, yamefanyika kwa mashinikizo ya kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema haya, tunataka jeshi letu liondoke huko, likafanye kazi ya kulinda amani katika Taifa letu na kufanya kazi ya kulinda mipaka yetu. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kubenea muda wako umekwisha.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Kwanza niseme kwamba siungi mkono bajeti hii kwa sababu haitekelezeki.
Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI na nilisema kwenye Kamati kwamba baadhi ya Mikoa iliyoleta bajeti kwenye Kamati, bajeti yao walipunguza kwa zaidi ya asilimia 60. Kwa hiyo, kwa maoni yangu, bajeti hii haitekelezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie suala zima la Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA) pamoja na mradi wa mabasi yaendayo kasi ya DART. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kikao cha Baraza la Madiwani cha Kamati ya Uongozi cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali yenyewe na Msajili wa Hazina, zimejiridhisha kwamba hisa za UDA ziliuzwa kinyume cha taratibu kwa anayejiita mwekezaji Kampuni ya Simon Group Limited. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali za UDA zinazohamishika na zile zisizohamishika, zimetapakanywa katika mabenki mbalimbali kwa kuwekwa dhamana. Naye Mwanahisa mkubwa Hazina, hakuridhishwa na uamuzi wa kuuzwa UDA. Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa tarehe 10 Juni, 2011, uliosimamiwa na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuidhinisha uuzaji wa UDA haukuwa halali. Serikali inalijua hili, Bunge la Jamhuri wa Muungano linalijua hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkutano uliitishwa na watu wanne, haukutimiza akidi na ulisimamiwa na mtu mmoja anayeitwa Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam; Robert Kisena, Mkurugenzi wa Simon Group; Mwanasheria wa Jiji, Issack Nassoro na Mkurugenzi wa Jiji, Philips Mwakyusa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mkutano huo, ndipo ikatangazwa kwamba UDA, Simon Group imetimiza masharti. Taarifa ya Serikali ya Agosti 3, mwaka 2011, kwenda kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, naomba niinukuu na inasema: “Mkutano ulikuwa batili kwa kuwa ulikiuka Katiba ya UDA Kifungu 45 kutokana kwa kutotimia kwa akidi na kukosekana kwa Msajili wa Hazina. Serikali inakiri kikao hicho hakikuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi na maazimio yoyote yaliyofikiwa yalikuwa batili.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi wakati kikao cha kugawa hisa za UDA kinafanyika, Meya wa Jiji alipokea barua ya tarehe 28 Februari, 2011 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, iliyomwagiza kusitisha mara moja mchakato wa kuuza hisa za UDA ambazo hazijagawiwa. Barua kutoka Serikalini (Ofisi ya Waziri Mkuu) ilibeba Kumb. Na. 185/295/07/27.
Barua hii ipo Ofisini mwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ipo Hazina, lakini Serikali imeendelea na mchakato wa uuzaji wa UDA kinyume cha taratibu; Serikali imeendelea kumilikisha mali ya umma kinyume cha sheria. Wanakiri katika nyaraka zao zote kwamba mbia hakutimiza masharti yote ya mkataba, lakini bado Serikali inaridhia na tayari Simon Group amelipa shilingi bilioni tano kwenye akaunti ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kumiliki hisa za UDA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba maamuzi yaliyofikiwa na Kikao cha Kamati ya Uongozi na Fedha, kilichofanyika juzi cha kuzuia hisa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuuzwa ninaunga mkono kwa asilimia mia moja. Fedha zilizowekwa katika akaunti ya Jiji hazitarudishwa mpaka hapo Jiji la Dar es Salaam litakapofanya hesabu zake na kuona Simon Group ametumia leseni ya UDA na mali za UDA, ameweka Benki, amepata faida. Tufanye ukaguzi wa ndani kujua ni kiasi gani cha faida alichopata, hapo ndipo tunaweza tukarudisha hizo hela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli uuzaji wa hisa za UDA na UDA yenyewe na DART yenyewe imegubikwa na udanganyifu, ulaghai, utapeli na Serikali inakiri katika nyaraka zake; na Waziri anakiri na anajua kwamba mchakato wa UDA haukufuata taratibu; lakini wanaendelea na mradi wa uendeshaji wa mabasi yaendayo kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu umetokana na mkopo wa fedha ambazo Serikali imekopa kutoka Benki ya Dunia, lakini anayetumia barabara zile ni mtu mmoja. Kampuni ya UDA inaulizwa hawa wenye daladala watatumia nini? Wanasema tutawaingiza katika huo mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri anapojibu alieleze Bunge hili Tukufu kwa nini mkopo huu ubebwe na Watanzania wote wakati barabara zinatumiwa na mtu mmoja? Ni vizuri mkopo huu ukabebwa na yule anayetumia barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimeona hapa Bungeni, baadhi ya Wabunge wenzangu wanasimama macho yakiwatoka, wakiunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kupambana na vita dhidi ya ufisadi. Baadhi yao ukiwaangalia, hawafanani na wanachokisema. Wengine sisi hatukuvamia hili treni la ufisadi, records zipo! Tumepambana Mwenyekiti unajua na Bunge hili Tukufu linajua. Kwa hiyo, sisi wengine tupo tayari kupambana na vita hii hadi mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja hapa imejitokeza na inazungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge, juu ya kuzuia vyombo vya habari kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge. Naomba niseme machache mawili na moja, naona Waheshimiwa Wabunge wanamtupia mzigo mkubwa, ndugu yangu Mheshimiwa Nape. Mheshimiwa Nape hahusiki na hili jambo, mnambebesha mzigo asiohusika nao; siyo wake! Tafuteni mwenye mzigo huu. Huu ni uamuzi uliofanywa na vikao vya juu, Mheshimiwa Nape ni wakala tu hapa. Shikeni hao! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba Bunge hili linafuata nyayo za Bunge la Uingereza, lakini chini ya Bunge hili, TBC ndiyo ambayo inaendesha hii studio ya Bunge. Kinachoitwa studio ya Bunge ni koti la TBC lililovaa Bunge. Wafanyakazi 15 waliopo hapa nawajua kwa majina, ni waajiriwa wa TBC.
Kwa hiyo, ni hatari sana kuona kwamba Bunge letu linaacha utaratibu wake wa kawaida. Hata huko Uingereza, Bunge linaonyeshwa live, vyombo vya habari vinaonyesha Bunge Live. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kusema kwamba mimi nadhani uamuzi huu ni lazima uangaliwe vizuri na busara itumike kuutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, jana Mheshimiwa Zitto amezungumza juu ya hoja ya watu ambao wanapata…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa!.....
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee nimalize...
Mheshimiwa Mwenyekiti, namaliza kwa kusema kwamba Mheshimiwa Zitto jana…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kubenea, muda wako umekwisha.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.
Mheshimiwa Spika, leo Bunge hili linakutana kwa pamoja kuamua kusitisha au kusaini Mkataba wa EPA. Lakini juzi wakati tunapata semina juu ya mkataba huu baadhi ya Wabunge tuliomba tuletewe watu wengine ambao waliufikisha mkataba huu mahali hapa ili waje kueleza uzuri wa mkataba huu. Ni bahati mbaya sana kwamba kilio hicho hakikusikilizwa.
Mheshimiwa Spika, mpaka hapa tulipofika, mambo yote haya yamefanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Leo hii kutuambia kwamba huu mkataba ni wa ajabu, ni mbaya, ni mchafu, ni wa kikatili na hili lenyewe nalo ni la ajabu. Ndiyo maana tunasema kwamba baadhi ya watu wanaposema kwamba Chama cha Mapinduzi kimechoka, kimezeeka, wanasema kwa sababu ya mambo kama haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inawezekana kabisa kwamba mkataba huu ukawa ni mbaya, lakini kuna faida kubwa kwenye mkataba huu ambazo hazijaelezwa na watoa mada. Kwa mfano, mkataba huu unatupa sisi kama nchi upendeleo maalum wa kupeleka bidhaa katika nchi za Ulaya bila kulipa kodi. Jambo hili halielezwi mahali popote na watu waliotoa mada. Binafsi inawezekana tukawa na maoni yanayokinzana, na ndiyo mjadala. Hoja ya msingi hapa ni nani aliyefikisha mkataba huu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkataba huu ulijadiliwa katika Kikao cha Baraza la Mawaziri cha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kabla mkataba kuingia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulipitia kwenye Kikao cha Makatibu Wakuu, baada ya Kikao cha Makatibu Wakuu mkataba uliingia kwenye Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu mkataba kabla ya kwenda katika Baraza la Afrika Mashariki ulipitia katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa watu wanakuja hapa leo kusema mkataba mbaya, mchafu kana kwamba nchi hii ndiyo kwanza inaanza upya, si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana kwamba Bunge hili likaelezwa taarifa sahihi kutoka pande zote mbili. Upande unaopinga mkataba na upande unaotaka mkataba ili maamuzi sahihi yafanyike kwa manufaa ya Taifa letu. Tusifanye mambo ya ushabiki hapa. Tulipitisha miswada na sheria mbalimbali hapa za kuuza mabenki yetu, tukauza mashamba, tukabinafsisha lakini hao hao waliobinafsisha wamerudi wamesema uamuzi ule haukuwa sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni lazima na ni muhimu sana kabla ya Bunge lako Tukufu halijaingizwa katika mgogoro huu, wapatikane watu wa upande wa pili, wakaeleza uzuri wa mkataba huu ili Bunge hili liweze kuamua kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bunge limeelezwa kwamba nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Rwanda, taarifa zinasema hata Rwanda wameshasaini mkataba huu. Sasa kama sisi tuko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya na Rwanda wameshasaini mkataba, sisi ndani ya Jumuiya hiyo tunabaki wapi kama kisiwa? Nchi za SADC ambazo zimeshasaini sehemu ya mkataba huu na sisi tumo katika Jumuiya ya SADC kama washirika wa biashara, tunakuwa wapi kama nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni jambo muhimu sana kwamba kabla ya uamuzi wa kufunga, kusaini au kutokusaini kwa mkataba, ni muhimu kwa maoni yangu kwamba huu mkataba haiwezekani wote huu kama ulivyo ukawa mbaya, haiwezekani. Haiwezekani kwamba dudu lote hili likawa baya kwa sababu watu wetu, wazalendo kabisa walitumwa kutoka Serikalini kwenda kushiriki kwenye vikao vya majadiliano hadi wakatengeneza kitu hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Bunge hili lingetoka na Azimio kwamba kabla ya mkataba huu kusainiwa vile vifungu ambavyo ni vibaya viondolewe tukajadiliane, vile vifungu ambavyo havifai viondolewe tukajadiliane, si kusema kitu chote hiki ni kibaya, tutaonekana watu wa ajabu duniani, yaani hata sisi kupeleka bidhaa zetu nje likawa jambo baya? Kwa nini tumejiunga na AGOA? Kwa nini kila mwaka tunapeleka maafisa kwenye mikutano ya AGOA? Ni kwasababu kuna vitu vizuri vimo humu ndani ya mkataba. Hivyo vitu vizuri hivyo, tuiagize Serikali ikafanye majadilinao upya ili vile vizuri tuvichukue na vibaya tuvitupe, si kusema kila kitu kibaya, haiwezekani. Haiwezekani kwamba vitu vyote vilivyomo humu vikawa vitu vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo rai yangu ni kwamba Serikali ambayo iliingia mkataba huu, watalam ambao walishiriki mkataba huu, Baraza la Mawaziri ambalo limeshiriki mkataba huu mpaka kutufikisha nchi mahali kwenye njia panda, Mabunge ya nchi za wenzetu yamesharidhia, sisi tukiwa tuko nyuma hawa watu waliotumwa kwenda kusaini mkataba huu ni lazima wawajibike.
Waliokwenda kufanya mazungumzo ya mkataba huu, kama mkataba huu ni mchafu ni lazima wawajibike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo hili lisichukuliwe kwa ushabiki. Sote hapa tunaweza tukawa Wazalendo, na hakuna mtu asiependa nchi yake lakini ni lazima tupime uzuri na ubaya.
Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii.
Kwa ufupi sana, kwanza naunga mkono hoja ya Kamati iliyopo mbele ya Bunge lako Tukufu na pili, naunga mkono pia hoja iliyoletwa kwenye Bunge hili ya kuvunja RUBADA na kuleta shughuli zote za RUBADA katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, katika ripoti imeelezwa kwamba Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa linajenga nyumba na kuweka miundombinu ya umeme, maji na barabara na matokeo yake nyumba hizo zinazojengwa zimekuwa za gharama kubwa. Pamoja na wito wa Kamati wa kutaka Serikali na wadau wengine wachukue hatua za kuweka miundombinu ya maji na barabara katika maeneo ambayo miradi ya National Housing inapelekwa, lakini kuna jambo moja muhimu sana ni muhimu Bunge lako Tukufu hili likaazimia kwamba Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba mpya za kisasa ambazo zinauzwa kwa watu binafsi, lakini zipo nyumba katika nchi hii ambazo zimejengwa tokea wakati wa ukoloni na nyingine zimejengwa mwanzoni mwa uhuru zipo katika maeneo ambayo siyo ya biashara, lakini Shirikala Nyumba la Taifa halitaki kuuza kwa wapangaji walioishi katika nyumba zile kwa zaidi ya miaka 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba hizo nyingine ziko Ilala Sharrif Shamba kwenye Jimbo lako la uchaguzi, nyingine ziko Temeke, nyingine ziko Ubungo na maeneo mengine mengi katika nchi hii. Kama Serikali inauza nyumba kwa wananchi wa kawaida, kwa wafanyabiashara wakubwa, kama shirika linaingia mikataba ni muhimu shirika hili likauza hizi nyumba kwa wakazi ambao wameishi katika hizo nyumba kwa zaidi ya miaka 20 au 30. Hili ni jambo muhimu sana kwa sababu litawasaidia wananchi wetu kupata nyumba za makazi. Tayari Serikali ilishakiri Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifungua nyumba mpya Iringa mwaka 2008 alikubali kwamba Serikali yake itauza nyumba zote hizo ambazo zinakaliwa na wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ripoti hii kuna suala zima la utalii, lakini Bodi ya Utalii haikutengewa fedha katika bajeti, Bodi ya Utalii haina fedha, Serikali imefunga kituo cha biashara, kituo cha utalii cha uwekezaji kilichopo London na imefunga kituo cha biashara kilichopo Dubai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo hivi vilikuwa vinafanya kazi ya kuutangaza utalii wa Tanzania nje ya nchi, lakini sasa vituo vimefungwa na utalii hauwezi kutangazwa tena. Vituo hivi vilikuwa vinatangaza mambo ya TANAPA, mambo ya Ngorongoro, Zanzibar Island, Mafia na maeneo mengine ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Leo Bodi ya Utalii haina fedha, utalii hautangazwi matokeo yake Mlima Kilimanjaro unaambiwa uko Kenya wakati uko Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila uwekezaji, bila Serikali kuwekeza katika maeneo haya haiwezi ikapata faida, utalii unazalisha asilimia 17.5 ya bajeti ya Taifa, lakini Serikali imetupa utalii inasubiri Mwenyezi Mungu awaletee neema wakati neema haiwezi kuja bila kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana kwamba Bodi ya Utalii lazima ipewe fedha, ni lazima utalii utangazwe ili Taifa hili liweze kupata mapato mazuri kwenye utalii wetu. Bila kuweka fedha kwenye utalii wakati Serikali inafunga taasisi za utalii nje ya nchi hatuwezi kufika mbele, ni muhimu sana kwamba Bodi ya Utalii, Shirika la Utalii, Ngorongoro na kodi ya VAT kwa watalii iondolewe ili kuweza kuvutia watalii nchini, watalii waweze kuja wengi nchini na utalii uweze kutoa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wengi kabisa wametumbukia katika utalii lakini utalii katika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wakati anazungumza Bungeni akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani, alisema Serikali yetu hii tuiamini sana ifanye uchunguzi wa mambo haya ya utekaji na utesaji na sisi humu ndani ukiuliza nani haiamini hii Serikali hayupo atakayetokea. Kwa sababu Serikali hii ni yetu sote ndiyo maana tuko hapa tunaisimamia Serikali, tuko hapa tunaishauri Serikali, lakini Serikali inayotaka kuaminika ni lazima iwe wazi. Hivi kwa mfano mtu aliyetaka kumpiga risasi Mheshimiwa Nape hajulikani, Serikali haimjui, kama inamjua basi ijitenge naye, kama haimjui iseme, lakini tunavyojua Serikali inamjua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makosa ya kijinai yametendwa katika nchi hii na watendaji wa Serikali. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ameingia kwenye chumba cha habari akitumia silaha, kwa mujibu wa sheria zilizopo ule ni unyang’anyi, wizi wa nguvu. Amekwenda kupora CD za chumba cha habari. Kamera zimeonesha, Tume ya Mheshimiwa Nape Nnauye imeripoti. Ripoti ya Tume ya Mheshimiwa Nnauye imeundwa na waandishi wa habari na imekuwa submitted kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayetenda jinai, DPP yuko pale, moja ya majukumu yake ni kuendesha kesi za jinai mahakamani, lakini pia kuangalia ni nani anayetenda jinai kuagiza DCI wafanye uchunguzi, hiyo ndiyo kazi ya DPP. Sasa DPP yupo amenyamaza, polisi wapo wamenyamaza. Mtu anatumia jina ambalo sio lake, ametenda makosa mengine yenye adhabu ya zaidi ya miaka 30 gerezani. Watu wamekwenda mpaka Kolomije, wamekwenda nyumbani kwao kijijini kwake wamezungumza na mama yake, vyombo vya habari vimefika huko, Waziri Mkuu anasema tuiamini Serikali, tunaiamini kweli lakini Serikali lazima iwe wazi iache double standards. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watumishi wa umma kwenye nchi hii wamefukuzwa kazi wengine wameshtakiwa wamefungwa lakini mtu mmoja anaitwa Paul Makonda jina lake Daudi Bashite anaachwa kwa sababu gani, who is Makonda? Mtu anaingia kwenye chumba cha habari akiwa na silaha za moto na polisi, who is Makonda? Halafu Serikali inasema iaminike, waandishi wa habari wanafanya kazi kwenye mazingira magumu halafu Waziri wa Habari ananyamaza, inasikitisha. Waziri wa Habari ananyamaza, ameona waandishi wa habari wananyanyasika kwenye nchi hii anatetea uhalifu halafu anasema tuamini Serikali, tunaaminije? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makosa zaidi ya nane wanasheria wanasema. Rais wa Chama cha Wanasheria yuko humu ndani, TLS haichukui hatua dhidi ya Makonda, Tume ya Haki za Binadamu haichukui hatua dhidi ya Makonda halafu mnasema Serikali tuiamini. Bunge limenyamaza linapigwa pini, linapigwa kufuli lisimzungumzie Makonda, jamani, halafu mnasema tuamini Serikali, Serikali inaaminikaje ikiwa imejifunika kwenye blanketi. Kutoa silaha hadharani ni kosa la jinai. Leo Kamishna Siro amesema ni kosa la jinai, Mheshimiwa Nape ametolewa silaha hadharani. Juzi watu wametoa silaha hadharani, aliyetoa silaha Mheshimiwa Nape anamjua, dunia inamjua, vyombo vya habari vinamjua, waandishi wa habari ndio waliozuia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie mjadala huu.

Kwanza kwa niaba ya Waandishi wa Habari wenzangu, wamiliki wa vyombo vya habari, Wahariri na wadau wote wa habari, natoa pole kwa msiba mkubwa uliolikumba Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, napenda nizungumzie suala la uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam. Uwanja wa Taifa umekabidhiwa ndani ya kipindi cha miaka mitano. Uwanja ule umejengwa kwa dola za Kimarekani milioni 50. Ni uwanja wa tatu kwa ukubwa katika Bara la Afrika, lakini uwanja wa Taifa umekabidhiwa ukiwa haujakamilika. Kwenye eneo la jukwaa kuu ambalo linaitwa VIP, ikinyesha mvua watu wote waliokuwepo pale wanaloa kana kwamba umesimama kwenye mnazi. Ushahidi ni mvua hii inayonyesha Dar es Salaam sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zilizopo ni kwamba mkandarasi alitakiwa ajenge ule uwanja kwa kuweka paa maalum ambalo litakuwa linafunga na kufungua ili wakati wa mvua lile paa liweze kutumika kuzuia mvua isinyeshee. Sasa uwanja umekabidhiwa, sherehe zimefanyika bila eneo hilo kukamilika.

Mheshimiwa Spika, pia katika eneo hilo, ulikuwepo mfumo wa ukusanyaji mapato na uwanja ulikabidhiwa bila mfumo huo kukamilika, lakini Serikali hii ya sasa hivi ikafuatilia utaratibu huo na ikaona kwamba ule mfumo unaweza ukawekwa na wajenzi na umewekwa na tumeokoa zaidi ya shilingi milioni 900 bila fedha za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa nini usifanyike utaratibu mzuri, waliojenga uwanja ule wakaukamilisha tukaendelea na shughuli zetu bila mgogoro? Inawezekana kwamba ama waliopewa mamlaka ya kusimamia uwanja hawakuwa na uwezo wa kusimamia uwanja ule vizuri wakati wa ujenzi ama walihongwa ili uwanja ule usikamilike vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa hatuna sababu ya kufukua makaburi, lakini ni muhimu Uwanja wa Taifa ukaangaliwa vizuri kwa sababu watazamaji au watu wanaofika uwanja wa Taifa wanaloa mvua na ushahidi wa mechi ya juzi kati ya Simba na Azam watu wote waliokuwepo pale uwanjani waliloa kama vile wamesimama kwenye mnazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala hapa ambalo Mheshimiwa Waziri wakati anazungumza sikuwepo, lakini nimesoma vyombo vya habari. Gazeti la Habari Leo limesema Mheshimiwa Waziri amesema Waandishi wa Habari asilimia 90 hawana sifa. Sasa najiuliza, sijui utafiti gani ambao Mheshimiwa Waziri ameufanya kwamba asilimia 90 ya Waandishi wa Habari waliopo hawana sifa na sijui sifa ambayo Mheshimiwa Waziri anaizungumzia ni ipi? Kwa sababu wapo Waandishi wa Habari ambao wamepata mafunzo mazuri kwenye vyombo vya habari na wao leo wamekuwa Waandishi wa Habari, wanafanya kazi na wanaongoza vyombo vya habari.

Mheshimwa Spika, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwakyembe, Mwandishi wa Habari, anafahamu hili. Alipomaliza masomo yake ya Kidato cha Sita alikwenda kufanya kazi kwenye chombo cha habari. Wakati huo au mpaka sasa sina hakika, ila nahisi mpaka sasa Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe hajawahi kusomea Uandishi wa Habari. Kama nakosea, Waziri wangu, kaka yangu atanikosoa, lakini ndivyo ninavyofahamu mimi.

Mheshimiwa Spika, elimu peke yake haitoshi kuwa na Waandishi wa Habari wazuri na mzungumzaji aliyepita hapa alizungumzia mambo ya ukocha kwamba kuwa na vyeti tu hakumfanyi mtu awe kocha mzuri. Kwa hiyo, ni vizuri kauli kama hizi…

SPIKA: Mheshimiwa Kubenea, sikukatishi lakini nia yangu ni kukupongeza tu. Hii habari ya vyeti tu halafu mkija hapa, ooh Bashite, Bashite!

Mheshimiwa Kubenea endelea tu. (Makofi)

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ninachotaka kusema ni kwamba tunaweza tukazungumzia vyeti na hatukatai vyeti, lakini tunachozungumzia, misingi, uadilifu, uaminifu mzuri wa mtu, elimu peke yake haitoshi. Ni lazima tujenge Waandishi wa Habari. Sasa kauli hizi zinaweza zikachukuliwa na Waandishi wa Habari na zimetolewa na Waziri mwenye dhamana ya tasnia ya habari ambaye anapaswa kwa vyovyote vile kulinda Waandishi wa Habari kwa gharama yoyote ile, sio kuwakatisha tamaa.

Mheshimiwa Spika, kuna suala hapa la Waandishi wa Habari kufanya kazi katika mazingira magumu sana. Waandishi wa Habari wanatishwa, hawako huru, wanaminywa na sheria nyingi mbaya ambazo zinaminya uhuru na haki ya Waandishi wa Habari kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano hai ni huo ambao wewe umeuchukulia wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye aliingia kwenye chumba cha habari akalazimisha habari itoke. Ripoti imeandaliwa na Mheshimiwa Nape, Kamati ya Mheshimiwa Nape iliyoundwa na Mheshimiwa Nape inaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo, ni Doctor, ni Mwanasheria, ni Mhariri, amefanya kazi Mashirika ya Kimataifa. Haiwezekani mtu wa namna hii akafanya kazi bila weledi kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati imeongozwa na Jesse Kwayu, Mhariri wa magazeti mengi nchi hii amepitia. Amekuwa kwenye media zaidi ya miaka 20; kizazi kingi hapa cha Uandishi wa Habari amekifundisha. Haiwezekani Jesse Kwayu akafanya kazi chafu isiyo na weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliitwa kwenye Kamati; akakataa, Kamati ilitaka kutoa ripoti kesho yake, ikasitisha ili imhoji Mkuu wa Mkoa. Mkuu wa Mkoa akakimbia Kamati. Uandishi wa Habari unaelekeza, tafuta source, akikosekana unasema. Huwezi kuua story kwa sababu mtu amekosekana. Makonda ameikimbia mwenyewe Kamati. Mheshimiwa Waziri anasema hawezi kutumia Ripoti ya Kamati ambayo haina weledi.

Mheshimiwa Spika, mimi sina ugomvi na Dkt. Mwakyembe, akikataa kutumia ripoti, huo ni utashi wake, lakini nina ugomvi naye anapochanachana na kuikosoa hii ripoti. Akatae kutumia, aseme sitaki, basi! Asibeze kazi ya kitume iliyofanywa na Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati hii imefanya kazi ya kitume. Serikali hii ambayo Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe anaongoza, haikuhoji watu ambao walikuwa na vyeti feki. Wanalalamika, lakini ripoti ya vyeti feki imetolewa hadharani. Magazeti yameagizwa yaandike hiyo ripoti na magazeti hayo yamechapisha hadharani. Waziri wa Habari anayekataa ripoti ambayo haikusikiliza watu, ameruhusu magazeti anayoyaongoza yachapishe ripoti ambayo upande wa pili haukusikilizwa. Hii ni double standard. Kama tunataka kuongoza Taifa hili, ni vizuri tukafanya kazi bila kuonea watu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nime-note ulichoongea. Nasisitiza kwamba nchi inaendeshwa kwa misingi ya haki. Hatuwezi kuwa upande huu, jambo tunalikubali tunalifuata, upande huu...

TAARIFA...

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa hiyo na kwamba gazeti kwa mujibu wa mhariri alifuata kuchapisha kwa sababu Rais aliagiza majina yale yachapishwe kwenye magazeti. Kwa hiyo, asingeonekana mzalendo kama angekataa kufanya kazi hiyo, naye amekuwa mzalendo amechapa, lakini haituzuii sisi kukosoa utaratibu uliotumika. Nami sio Mhariri wa hilo gazeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la Mkataba wa TBC na Kampuni ya Kichina. Jambo hili limezungumzwa hapa Bungeni mara kadhaa, tumeliandika kwenye vyombo vya habari kwamba mkataba kati ya TBC na Kampuni ya Kichina ni wa kinyonyaji. Mheshimiwa Waziri wa habari aliyetangulia kabla ya Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, aliahidi mbele ya Bunge hili kwenye mkutano uliopita kwamba ripoti ile itakuwa hadharani na Serikali itaiangalia upya suala zima la mkataba wa TBC na Kampuni ile ya Kichina. Nataka Mheshimiwa Waziri wakati anajibu atueleze mkataba kati ya TBC na Kampuni ya Kichina umefikia wapi?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwepo hoja ndani ya Bunge na tokea jana na leo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wanazungumza mambo mengi juu yetu sisi upande wa pili ambao tunaambiwa hatuungi mkono juhudi za Serikali au za Rais za kutetea rasilimali za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya msingi ni kwamba sisi hatuhusiki kwa namna yoyote ile na mikataba yote ya madini iliyofungwa na Serikali hii. Hatujawahi kuwa kwenye Serikali hiyo na hatujawahi kuingia katika hiyo Serikali na kwa hiyo, hatujawahi kusaini mkataba wowote ule. Kwa hiyo, hiyo mikataba yote iliyofungwa ni ya Chama cha Mapinduzi na Serikali yao. Wasichukue kesi isiyotuhusu wakatutupia sisi. Hiyo ni kesi yao, hilo ni dudu lao, wameliamsha, wamalizane nalo wenyewe. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwepo hoja ya msingi sana kwamba eti tumeibiwa katika rasilimali zetu, kwamba tumeibiwa na watu waliokuja kuwekeza. Mikataba iliyofungwa imefungwa kwa mujibu wa sheria zilizopo. Waliofunga mikataba na ambao bahati njema mmoja wao amezungumza hakamatiki, anasema, mikataba hiyo imefungwa baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kukutana na kuwepo minutes za vikao hivyo. Hatuwezi kusema tumeibiwa wakati tumeruhusu mali yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningewaelewa sana kama tungesema mikataba iliyofungwa ni ya kinyonyaji, mimi hiyo ningewaelewa. Siyo wizi, hapa hakuna wizi! Wizi ni mtu anayeondoka ndani ya nchi yako, anagonga stempu, analipa ushuru, anakulipa hela yako, anaondoka unasema anakuibia! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kuthibitisha kwamba hakuna wizi, Rais amekaa na aliyemwita mwizi jana Ikulu. Mlango wa Ikulu jana ulifunguliwa ukawa wazi, mwizi akaingia Ikulu, Rais mwenye vyombo vya dola…

TAARIFA . . .

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huyo ndio mwizi aliyeitwa na Mheshimiwa Rais kwamba kampuni hii haikusajiliwa nchini, inatudhulumu, wamekaa naye Ikulu wakazungumza naye. Nilitegemea Mheshimiwa Rais angeenda kumweka ndani huyu mtu na akamzuia asizungumze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima yako, naomba niliache hilo jambo, lakini message imefika. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu kwenye Wizara ya Nishati na Madini nilizungumza juu ya kuwepo mgongano wa maslahi kwa baadhi ya viongozi wetu waandamizi kwenye Serikali. Bahati njema au bahati mbaya nilimtaja kaka yangu, rafiki yangu Mheshimiwa Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa. Naye juzi akajibu hapa, akanieleza mimi binafsi nilivyo na akasema amenichangia matibabu, akasema ameninunulia kompyuta yeye na rafiki zake. Kwa kweli kama nisingelelewa katika misingi ya Uislamu ningerejesha fedha ya Mheshimiwa Mwambalaswa aliyonichangia matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sikumwomba Mheshimiwa Mwambalaswa anichangie, nilikuwa kitandani ninaumwa, watu wakaomba mchango wakanichangia, lakini nimesikitika kwamba mchango alioutoa sirini amekuja kuusema hadharani ndani ya Bunge hili. Ni masikitiko makubwa sana, kwamba ukiwa na kiongozi wa namna hii siku akikuchangia maziko atakuja kukudai sanda au kuja kukudai jeneza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe onyo kwa Waheshimiwa Wabunge mnaochangisha michango ya harusi humu ndani ya Bunge, mkimchangisha Mheshimiwa Mwambalaswa, kuna siku atakuja kuwadai wake mnaooa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgongano wa maslahi upo katika viongozi wetu wakubwa katika nchi hii. Mheshimiwa Ame Mpungwe alikuwa Balozi wetu wa Afrika Kusini, akawa dalali katika makampuni ya Makaburu yaliyonunua NBC, yaliyochimba Tanzanite na magazeti yaliandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gazeti la Rai lilihoji Balozi Mpungwe ni Balozi mzalendo au muuza nchi? Mara baada ya Balozi Mpungwe kustaafu akawa mmoja wa wamiliki wa makampuni makubwa ya uwekezaji wa madini katika nchi hii, AFGEM ya Tanzanite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Daniel Yona aliyekuwa Waziri wetu wa Nishati na Madini alichukua dokezo akapeleka kwenye Baraza la Mawaziri la kuuza Kiwira. Kiwira ikauzwa akaanzisha Kampuni inaitwa TanPower, nayo ikaingia ubia na Kampuni nyingine inaitwa ANBEN Limited wakauziana Kiwira. Ilivyoenda Kiwira, mnaijua. Leo tunakaa hapa tunazungumza kana kwamba hayo mambo hayapo! Eti tusijadili watu waliohusika kuiingiza nchi hii katika migogoro ya kifisadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwambalaswa amesema kwenye Bunge hili kwamba yeye hakuwa na maslahi binafsi na mradi wa umeme wa upepo wa Singida, akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, mimi natoa ushahidi hapa, alikuwa na mgongano wa maslahi. Mwaka 2011 kuna invitation letter, hii hapa, inatoka China inamwalika Mheshimiwa Victor Mwambalaswa mwenye Passport number AD002021 iliyotolewa Januari, aliyezaliwa tarehe 08, issued Januari, 2006. Hii hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaliko huu anakwenda China akifuatana na William Mhando ambaye alikuwa Mkurugenzi wa TANESCO; na wengine ni Timothy Njunjua Kalinjuna na Machwa Kangoswe, hii hapa. Wanasema wanakwenda kufunga mkataba kati ya TANESCO na Kampuni ya China na Kampuni ya Power East Africa Limited ambayo ni yake. Anasafiri kwa fedha za Tanzania, anasafiri kwa passport ya Tanzania, analipwa posho ya TANESCO, anakwenda kufunga mkataba wa kampuni yake, halafu anakuja hapa anasema lile lilikuwa wazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hapa taarifa ya NDC inasema Mradi wa Umeme wa Upepo wa Singida PT 33162, mradi umeanza mwaka 2010. Maelekezo ya mradi; mradi unatekelezwa kwa Kampuni ya Seawind Power Limited na NDC; na hiyo Power Pool East Africa Limited, ya kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2010 Mrindoko Bashiru anakuja kutoa barua hii ya kuipa kazi kampuni ya akina Mheshimiwa Mwambalaswa. Mwaka 2010, Mheshimiwa Sitta anafunga mjadala wa Richmond Bungeni kwa ubabe tu. Mwaka 2011 Mheshimiwa Mwambalaswa anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, mwaka 2010 Mheshimiwa Mwambalaswa anakuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo, tunapozungumza mgongano wa maslahi ndiyo huu. Mnazungumza vitu gani humu ndani? Halafu watu wanasema hapa mnafukua makaburi, fukueni haya. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgongano mkubwa wa maslahi. Nina orodha ndefu ya viongozi wa Serikali hii ambao mikataba iliyofungwa nyuma yao wana mgongano wa maslahi. Hatuwezi kukaa hapa tunadanganyana kwamba Taifa hili ni letu wote wakati wengine wananufaika, wengine wanaliibia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja hapa amesimama asubuhi anasema nampongeza Mheshimiwa Rais. Namwomba Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akaangalie fedha iliyotumika kulipa Kampuni ya IPTL; na Waziri wa Fedha na Mipango akaangalie. Mwaka 2010 kuelekea kipindi cha Uchaguzi Mkuu, shilingi bilioni 46 kulipia mafuta IPTL; kwa mwezi shilingi bilioni 15, Mheshimiwa Ngeleja akiwa Waziri wa Nishati na Madini na ndiye aliyesaini hiyo hoja; yule, Mheshimiwa William Ngeleja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyaraka zipo, ushahidi upo! Aende, Mheshimiwa Rais ana faili huko Ikulu afungue faili la IPTL aangalie mwaka 2010 kipindi ambacho tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. IPTL imelipwa shilingi bilioni 15 kwa mwezi kuwasha mitambo ya IPTL. Halafu mnakaa hapa tunadanganyana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kabisa, naviomba vyombo vya ulinzi na usalama viwachunguze hawa watu, hatuna maslahi binafsi, tunatetea maslahi ya Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme wazi baada ya mjadala kufungwa jioni, nitatoa taarifa kwa Kiti chako kwamba kwa kutumia Kanuni zetu nitaleta Hoja ya Kuundwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza Operation Sangara yote ilivyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina square meter zaidi ya 800 eneo la bahari, kutoka Mtwara mpaka Tanga, kutoka Pemba mpaka Mafia lakini eneo la uvuvi linachangia sehemu ndogo sana ya pato la Taifa letu kwa sababu hatujawekeza kabisa katika uvuvi. Wananchi wa Dar es Salaam sisi tunaishi kwa nyama, kuku na samaki lakini nchi yetu haiangalii kabisa katika eneo zima la nyama, hivi Tanzania inaagiza kuku, nyama na samaki kutoka nje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania ambayo tuna bahari ya kutosha, meli za nje zinakamatwa ndani, tunazitaifisha, tunapelekwa mahakamani, tunadaiwa fidia ya mabilioni, lakini sisi tunaagiza samaki kutoka nje, hii ni aibu! Ni aibu miaka 50 baada ya uhuru Tanzania yenye bahari, maziwa na mito inaagiza samaki kutoka nje. Halafu Wabunge wa CCM wanasimama hapa wanasema tutazuia bajeti, hakuna Mbunge wa CCM mwenye uwezo wa kuthubutu kuzuia bajeti, hayupo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama akiwepo na bajeti hii ikazuiwa, mshahara wangu wa mwezi huu nisilipwe, wapeleke kwenye majimbo ya hao Wabunge. Mheshimiwa Spika, nisilipwe. Hakuna Mbunge wa CCM anaweza kusimama katika maneno yake mpaka mwisho.

Mheshimiwa Spika, hiki kilichoandaliwa na Mheshimiwa Mpina, mimi namfahamu sana Mheshimiwa Mpina. Mwaka 2012 akiwa Mbunge alizuia bajeti hapa, alikataa bajeti ya Serikali, leo Mheshimiwa Mpina anakaa kwenye Wizara, anachukua hela za wafugaji, anachukua hela za uvuvi, halafu harejeshi fedha kwa wananchi. Nashangaa nikimuona Mheshimiwa Mpina wa leo nikimuangalia na Mheshimiwa Mpina wa miaka saba iliyopita, siyo huyu, siyo kabisa. Ni rafiki yangu, ni kaka yangu, tunaheshimiana lakini nikimuangalia yule Mheshimiwa Mpina wa miaka ile siyo huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi ni tatizo kubwa sana katika nchi yetu. Kuna Sheria ya Hifadhi ya Bahari ya mwaka 1999, zaidi ya miaka 30 leo haijafanyiwa marekebisho. Wavuvi wetu katika maeneo ya pwani na visiwani, ukienda kule Mafia na Rufiji, utakuta eneo limetengwa kwa ajili ya hifadhi ya bahari lakini hifadhi ya bahari inaweka boya mita 100 inazuia wavuvi wasifanye kazi zao za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, leo uvuvi katika visiwa kama vya Mafia, Kware na Koma kwa Mheshimiwa Ulega, asilimia 99 ya wananchi wanategemea uvuvi. Pale Kware na Koma kwa Mheshimiwa Ulega wananchi hawalimi, wanategemea bahari lakini hifadhi ya bahari imeenda kuchukua maeneo ya bahari, imezuia wananchi wasivue, imeleta matatizo makubwa.

Mheshimiwa Spika, katika baadhi ya maeneo Jeshi la Wanchi linatumika na hifadhi ya bahari kukimbiza wavuvi na kuzamisha boti za watu na kunyang’anya nyavu za watu, Jeshi la Wananchi. Nchi gani hii mnaongoza? Nchi hii tuliomba uhuru ili wananchi wawe huru, wafanye mambo yao huru kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, baada ya kuwa huru Watanzania wamekuwa watumwa katika nchi yao. Wanazungumza Wabunge wa CCM hapa unaona uchungu, mnaenda kwenye uchaguzi kesho mtasemaje? Mtawaambia nini wananchi au ndiyo mtatumia dola na polisi kushinda? Hoja hizi za Mheshimiwa Bulembo hazijibiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana kuna mtu ameniambia, sijui kama kweli, kwamba Waziri wa Mifugo anatoka Kanda ya Ziwa, hafahamu kabisa mambo ya Pwani. Mheshimiwa Ulega anatoka Mkuranga, lakini anatoka Kimanzichana, hata bwawa kwake hakuna. Mkurugenzi wa Uvuvi anatoka Kanda ya Ziwa. Sasa hiki kilio cha wananchi wa Pwani ambacho kilianza toka enzi za akina Mheshimiwa Mudhihir Mudhihir, Mheshimiwa Bakari Mbonde, Mheshimiwa Ayoub Kimbau…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwamba umenipa nafasi ya kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Simbachawene tuko Kamati moja ya Katiba na Sheria na anajua jinsi gani Serikali ilivyoshindwa kupeleka fedha za maendeleo katika Wizara nyingine na Ofisi ya Makamu wa Rais iliyolazimishwa kuhamia Dodoma ilivyopewa fedha nyingi sana kinyume/ zaidi ya bajeti iliyoomba. Ni kwa sababu mipango ya kuhamia Dodoma, mipango ya kuufanya uwe Mji Mkuu haikuandaliwa. Tumekurupuka bila kuwa na vigezo, tumekurupuka bila kuwa na takwimu na tunafanya mambo haya kama vile nchi hii inakufa kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kuufanya Dodoma kuwa Mji Mkuu ambayo ndiyo hoja ya Mheshimiwa Simbachawene. Mji Mkuu umetangazwa kabla ya sheria kuja Bungeni. Jiji limetangazwa bila sheria kuja Bungeni. Sasa tunatangaza jiji halafu ndiyo tunaleta sheria, halafu tunapongezana hapa. Tunatangaza Makao Makuu ya nchi Dodoma wakati Jiji la Dodoma halijawa na sheria ya kuifanya Dodoma kuwa Jiji. Maana yake ni kwamba kumbe Mheshimiwa Rais alikuwa anakuja kuhamia kijijini, haji kuhamia kwenye Jiji. Hakuna sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo ni zuri na hakuna anayelipinga, lakini ni lazima tufuate taratibu. Kuna mikoa nchi hii imetimiza vigezo vyote vya kuwa jiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro, Manispaa ya Moshi imetimiza vigezo vyote vya kuwa jiji, lakini Mheshimiwa Rais amekataa Moshi kuwa jiji na Mheshimiwa Simbachawene unajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine kwa sababu amesema watu wa Kaskazini wasimame kwanza, maendeleo yaende mikoa mingine, yawezekana amekataa Moshi kwa sababu watu wa Kaskazini wasimame kwanza.

T A A R I F A . . .

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya sana kwamba mtu aliyesimama wala hajui historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wakubwa wa Moshi ni Baraza la Madiwani, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kupitia Baraza la Madiwani na Meya wao Japhary Michael ambaye leo ni Mbunge wa Moshi Mjini walipitisha Azimio la Moshi kuwa Jiji. Vikao vya RCC vyote viliamua Moshi iwe Jiji. Anazungumza nini? Nimemsamehe kwa sababu hajui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya kukurupuka, tunapozungumza hivi leo tunataka Dodoma iwe Jiji, tumeomba msaada wa kujenga uwanja wa mpira kutoka Morocco ili kuifanya Dodoma iwe na hadhi ya Jiji. Madhara yake ni nini? Madhara yake ni kwamba Morocco msimamo wa CCM hawa na Serikali hii kwa miaka yote tokea Baba wa Taifa tunatambua Sahara Magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dodoma hii watumishi wa umma wameletwa Dodoma. Ndoa zimevunjika, waume wako Dar es Salaam, wake wako Dodoma; wake wako Dar es Salaam, waume wako Dodoma, ndoa zimevunjika. Watu wameshindwa kuhama na wake zao na familia zao, mtu amebakisha miaka minne, leo analazimishwa aje Dodoma kabla ya kustaafu, imekuwa ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Dodoma ambayo imetangazwa Mji, Dodoma ambayo imetangazwa Makao Makuu ya nchi haiwezi kuunganisha na nchi za Jumuiya ya Afrika MAshariki. Leo kutoka Rwanda, Waziri akitaka kufanya miadi ya Waziri Mkuu hapa Dodoma akitokea Rwanda hawezi kufika kwa haraka kuliko akifika Dar es Salaam. Hakuna connection kati ya Mkoa wa Dodoma na Mikoa mingine kwa usafiri wa haraka wa anga. (Makofi)

Sasa mnataka Dodoma iwe Mji, Dodoma iwe Makao Makuu, hakuna international schools hapa za kusoma watoto wa Mabalozi. Dodoma haijawa tayari na ninyi mnajua kwamba wapo watu waliofanya research wakasema baada ya miaka 10 ijayo kwa kutenga shilingi trilioni nne kwa kila mwaka kwa muda wa miaka 10…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze tu na alipoishia Profesa, ndugu yangu kwamba mimi nashangaa na sielewi kama Taifa tunataka nini? Tunataka ujamaa au ubebepari? Tunataka umeme wa maji au wa makaa ya mawe? Yaani nashangaa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina taarifa hapa ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ya tarehe 3 Juni, 2016 anasema kwamba Serikali inawekeza katika Mradi wa Mchuchuma na Liganga ambao utazalisha megawatt za umeme na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Mradi huu navyofahamu ulikuwepo miaka mingi sana lakini haujatekelezwa na ulikuwa ndiyo ukombozi wa nchi hii katika umeme na ndiyo tulivyokuwa tunaambiwa hapa. Sasa tunakwenda katika umeme wa maji ambao tuna Mabwawa ya Nyumba ya Mungu, Kihansi, Mtera, Hale na Pangani na yote haya yanazalisha chini ya kiwango chake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka nchi hii inapatwa na ukame, hatuna uhakika huo umeme wa maji tunaoenda kuzalisha kama utaweza kumudu tabianchi. Umeme wa makaa ya mawe na chuma cha Liganga una uhakikika kwamba hauwezi kuadhiriwa na tabianchi. Kuna umeme wa upepo wa Singida tumeshindwa kuuendeleza. Mradi wa Umeme wa Singida Benki ya EXIM ya China, Mheshimiwa Waziri anajua, ilishakubali kutoa mkopo kupitia NDC ili umeme ule uweze kuendelezwa, umeshindwa kuendelezwa. Sasa unashangaa kwa nini tunachukua vitu nusu nusu? Leo tunaanzisha hiki, hatufikishi mbali tunakiua; kesho tunaibuka na kitu kingine. Fedha za Watanzania zinazama kwenye miradi ambayo siyo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi watu wamezungumza hapa juu ya Kiwanda cha Urafiki ambacho kilikuwa ni mali ya Watanzania kwa asilimia 100. Wamekichukua kiwanda, wakakiuza kwa mwekezaji, mwekezaji akawa hana mtaji, wakamkopesha fedha za Serikali, Serikali ya Tanzania ikamdhamini kwenye benki za nje, akaenda kukopa na fedha hakurudisha na hisa anazo yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Alhaj Ally Hassan Mwinyi aliwahi kuita timu yetu ya Taifa Kichwa cha Mwendawazimu kwamba kila mtu anajifundisha kunyoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli unashangaa kwamba jambo tunalianzisha, tumeanzisha umeme wa gesi, wamekuja hapa Maprofesa, Profesa Muhongo alitembea na agenda ya umeme wa gesi nchi nzima, ndiyo ilikuwa agenda. Leo tumeacha gesi, tunazungumza umeme wa maji. Umeme wa maji ulikuwepo wakati wa Mwalimu Nyerere yakajengwa hayo mabwawa makubwa, tukahama tukaenda kuanzisha umeme wa mashine za kukodi; Songas, APTL, Richmond, DOWANS, tumeona huko nako; yaani sijui tunaelekea wapi? Sijui Taifa hili wataalam wetu wanafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha, kaka yangu namheshimu sana, nimemsoma akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, amefanya kazi nzuri, naomba asimame kama Waziri wa Fedha, amshauri Mheshimiwa Rais vizuri. Rais wetu siyo mchumi na hakuna binadamu yeyote aliyekamilika mahali popote pale. Waziri amshauri Rais, awe kama Mawaziri wa Fedha waliopita. Alikuwepo Mheshimiwa Mgimwa, alikuwa Waziri wa Fedha anayejiamini alikataa mpaka kulipa hela za Escrow, record zipo. Mheshimiwa Waziri Mpango amshauri Rais, hivi kweli mnachukua fedha shilingi bilioni 211 za korosho za wananchi wa Mtwara hamzirudishi, mnarudisha shilingi
bilioni 10, mnakuja na Muswada leo wa kuzuia hizo fedha zisirudi tena Mtwara. Jamani, huu ni wizi wa fedha za wananchi. Hii ni dhuluma! Hawa ni wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mama yangu Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti nilikuwa India wakati naumwa ni miongoni mwa watu wa kwanza waliokuja kuniangalia. Mama simamia hii kitu, itakuondoa Bungeni. Wananchi wa Mtwara hawatakuelewa. Hawakukuelewa kwenye gesi, hii ndiyo hawatakuelewa kabisa. Simama mama, fedha za wananchi hizi zinataka kuondoka, simama zitetee ili wananchi wa Mtwara, Kusini, Mafia na maeneo mengine wanaolima korosho wapate matunda ya zao lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, unakuta kodi kwenye ndizi zinazotengenezea pombe, matunda, mimi nilitegemea tuletewe fedha za makinikia zile shilingi trilioni 409, tuzione humu ili wananchi wetu waachane na hizi kodi na TRA iache kukimbizana na Wamachinga Kariakoo. Shilingi trilioni 409 ni fedha nyingi kweli ambazo zinatosha kuendesha nchi hii kwa zaidi ya miaka 10. Sasa badala yake hizo fedha hazipo, wimbo wa makinikia hatuusikii tena, tuachane na hivi vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema hivi, ukikuta Serikali inakimbizana na Wamachinga mtaani, haikusanyi kodi kwa wafanyabiashara wakubwa, ujue kuna tatizo. Sisi kodi zetu zote ni kwa wafanyabiashara ndogo ndogo; wauza vitumbua, bodaboda, Machinga, tuachane na vitu hivi, tuleteeni kodi za migodi, ondoeni misamaha ya mafuta kwenye migodi, tuleteeni vitu vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti nzima hii wanasema haitekelezeki, mimi sijui kama haitekelezeki, lakini Mheshimiwa Waziri anajua kwamba mapato yetu yanashuka mwezi hadi mwezi na kwenye mwezi Mei na Aprili mwaka huu, mapato yetu yalipungua na yalikuwepo mapendekezo ya kupunguza fedha za maendeleo katika baadhi ya maeneo. Ni lazima Serikali itafute mpango madhubuti wa kuendesha uchumi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkiwa mnakwenda kulia, mnajiita wajamaa wakati Serikali haimiliki hata benki moja kwa asilimia 100, inamiliki asilimia 30 au asilimia 31 kwenye NMB na NBC, halafu Serikali inajiita ya ujamaa. Mtu mmoja anasimama anajiita mjamaa lakini ukimwangalia kwa nyuma ana shamba heka 150 halafu anasema ni mjamaa. Sasa sijui ni mjamaa au Kijiji cha Ujamaa, mimi sielewi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Taifa ni letu wote na likididimia, tunadidimia sote, hakuna atakayekuwa salama. Mheshimiwa Waziri analeta mapendekezo na amesema kwenye Muswada na analeta humu kwamba kutakuwa na akaunti moja ya kuhifadhi fedha. Mkipata Rais anayefanana na Sani Abacha tutakuja kulia huku. Ni lazima tuweke mipaka ya madaraka. Ninyi mlikuja na mapendekezo ya kupunguza madaraka ya Rais katika Katiba Mpya. Mapendekezo ya Katiba Pendekezwa ni kupunguza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema Mheshimiwa Waziri wa Fedha amshauri Rais vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-wataala kwa kutujalia kufika siku ya leo na kutoa mchango wetu Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nimpe pole Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wananchi wa Buyungu, wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na familia ya Mheshimiwa Mwalimu Kasuku Bilago kwa kuondokewa na mpendwa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini humu ndani kuna tatizo kubwa la STAMICO (Shirika letu la Madini la Taifa). STAMICO haina mtaji, imekabidhiwa jukumu kubwa sana la kusimamia madini katika nchi hii lakini Serikali haijawahi kuipa STAMICO mtaji wa kutosha wa kufanya shughuli zake. Matokeo yake nchi imekuwa kichaka cha watu kupora madini yetu kwa sababu hatujaijengea uwezo mkubwa STAMICO wa kusimamia rasilimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shirika hili la umma ambalo ndiyo lilikuwa linatarajiwa kubeba dhamana kwa makampuni yote yanayokuja kuwekeza kwenye madini kwenye nchi hii, angalau shirika hili liwe ndiyo shirika kiongozi, lakini limetupwa na limeachwa yatima. Jambo ambalo limesababisha sasa kuzaliwa kwa makampuni mengi feki na kuchukua rasilimali za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ilianzisha Kampuni inaitwa Meremeta ambayo siku za nyuma aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Kayaza Pinda aliliambia Bunge mwaka 2008 kwamba Kampuni hii ni ya Usalama wa Taifa na Kampuni hii inamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, akakataa kutoa taarifa ya Kampuni ndani ya Bunge hili. Kampuni ya Meremeta ilithibitika kwamba asilimia 50 ya wanahisa wake ni watu kutoka nje na kwa hiyo kwa vyovyote vile haiwezi ikawa Kampuni ya Jeshi la Wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Wananchi lilishajiondoa tokea mwaka 2002 baada ya Kampuni ya Meremeta kurudishwa Hazina kwa Msajili wa Hazina. Hadi kufikia Juni, 2008 kampuni ya Meremeta ilikuwa na Dola za Marekani zaidi milioni 80 katika akaunti yake iliyofunguliwa Benki ya NBC kule Musoma, karibu zaidi ya bilioni 200. Fedha ambazo ni za walipa kodi wa nchi hii na hazijulikani zilivyotumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa makampuni ya nje kujiingiza katika biashara ya ndani bila kuisaidia STAMICO kusimamia miradi ya madini nchini hatutaweza kufika popote. Kila mwaka tutakuwa tunaibiwa, kila mwaka tutakuwa tunapiga kelele lakini njia pekee ya kusaidia Taifa hili ni kuimarisha STAMICO. Njia pekee ya kuondoka hapa tulipo ni kuimarisha STAMICO.

Mheshimiwa Naibu Spika, wageni wanakuja hapa wanachimba madini yetu wanaondoka, wanaacha mashimo, wanaacha uharibifu wa mazingira hakuna mtu nyuma anayeweza kusimamia. Kama STAMICO ingekuwa ndiyo shirika letu umma, linamiliki zaidi ya asilimia 50 ya hisa kwa makampuni ambayo yanakuja kuchimba, maana yake kwamba jukumu hili angekabidhiwa STAMICO. Leo ukienda kule Nzega kuna kampuni imechimba madini imeondoka imeacha mashimo, imeacha uharibifu wa mazingira, wananchi wanateseka, leo mzigo unabebwa na Serikali na kampuni haikulipa kodi imeondoka, mambo kama haya nchi hii haiwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma ripoti ya Kamati, kuna mgodi mmoja uko Mara umetajwa humu, Jeshi la Wananchi limezuia ile kampuni iliyopewa kazi ya kuchimba madini isifike kwenye mgodi. Mimi nilipongeze Jeshi kwa hatua hiyo, nchi yetu Jeshi letu limetumiwa kama kichaka cha watu kuja kuchukua fedha zetu. Kwa hiyo, ni lazima uchunguzi ufanyike kama Jeshi limefunga mkataba na kampuni fulani, huo mkataba uonekane, maslahi ya Taifa letu yaangaliwe kwanza kabla ya kitu chochote kile. Tusije tukatumia Jeshi tukaonekana tunaficha baadhi ya vitu kutumia Jeshi ili vitu hivyo viweze kuondoka kiurahisi kwa sababu Bunge hili au Wabunge hawa hawana mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya Jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kusikitisha sana kwamba katika kitabu kizima cha Waziri na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, hakuna mahala popote palipozungumzwa makinikia kwa ufasaha wake. Tulitegemea Bunge letu lipewe taarifa ya kina ya mazungumzo yanayoendelea kati ya Serikali na makampuni ya Accacia na mengine ambayo yaliambiwa na TRA hayakulipa kodi ya zaidi ya shilingi trilioni 424. Dola za Marekani bilioni 190 ambazo tuliambiwa nchi hii ingepata kutokana na makinikia, bajeti nzima ya Serikali iliyokuja haizungumzii mahali popote jambo hilo na katika ripoti ya Waziri hakuna mahali popote ambapo amezungumzia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mmoja wa Wajumbe au Mwenyekiti wa hiyo Kamati yumo humu ndani Profesa Kabudi atuambie makinikia yamefikia wapi. Mchanga ambao ulizuiwa bandari umeondoka? Kama bado upo, upo mpaka lini? Je, leo migodi inasafirisha mchanga kwenda nje ya nchi? Kiwanda cha kuchakachua ule mchanga kinajengwa lini ili Watanzania ambao walikuwa na matumaini ya kupata elimu bure, kila Mtanzania aendeshe Noah yake mwenyewe kwa fedha hizi, kila Mtanzania apate matibabu bure kwa fedha hizi, kila Mtanzania aweze kuishi maisha mazuri kama ambavyo nchi nyingine zinaishi kwa fedha hizi, fedha hizi shilingi trilioni 424 zinapatikana lini? Bajeti ambayo ni zaidi ya miaka 10 ya bajeti ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni muhimu sana tukaelezwa Watanzania makinikia yako wapi. Mazungumzo yamefikia wapi, fedha hizi zinapatikana lini ili sisi tupate kuwaambia wapiga kura wetu kwamba kila Wilaya, kila Kata itapata Kituo cha Afya kwa sababu kuna shilingi trilioni 424 bajeti ya miaka 10 ijayo ya Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi ni nyingi sana na kama tumeibiwa kwa kiasi hiki ni lazima Serikali ijiangalie vizuri. Mimi niwashauri njia pekee tusipige danadana, tuimarishe Shirika la Taifa la Madini (STAMICO), tulipe mtaji...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja ambazo ziko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kunukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sehemu ya Utangulizi ambayo inasema: “Kwa kuwa sisi Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, undugu na amani. Na kwa kuwa misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi, na pia wenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa, na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimenukuu msingi huu wa Katiba nikirejea kesi mbalimbali ambazo zimepelekwa Mahakamani na zimecheleweshwa kwa makusudi kabisa. Moja ya kesi ambayo nataka niitolee mfano ni ya Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye alifungwa na Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, akakata rufaa kwenda Mahakama Kuu na aliomba awe nje kwa dhamana wakati shauri lake linasikilizwa lakini Mheshimiwa Mbilinyi alikaa gerezani kwa kipindi chote cha kifungo chake hadi pale alipotoka baada ya kupata msamaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu inasema Mahakama itende haki bila kuangalia sura ya mtu lakini wapo watu ambao wamekosa haki zao kwa makusudi kabisa kwa utaratibu ambao Mahakama imeshindwa kuwapa haki hizo. Taarifa zilizopo ni kwamba Jaji aliyekuwa Incharge kwenye kesi ya Mheshimiwa Mbilinyi alikiri kwamba alishinikizwa kuendelea na shauri lake kulipeleka mbele.

MWENYEKITI: Mheshimiwa kubenea haya maneno unaweza ukayathibitisha?

KUHUSU UTARATIBU

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Bunge hili lilipokea Muswada wa Mobile Court, uliletwa kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, Serikali katika mvutano wa adhabu ambazo zilikuwa zimependekezwa katika Mahakama hiyo ikaondoa ule Muswada. Hata hivyo, juzi wakati wa uzinduzi wa Siku ya Sheria tumesikia kwamba Mahakama imezindua Mobile Court.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mashaka ya Wabunge yalikuwa Mobile Court ina gharama kubwa sana. Gari moja lilikadiriwa kuwa na thamani kati ya shilingi milioni 200 mpaka milioni 490. Tukasema gharama za kuendesha Mobile Court ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia ni kubwa kuliko tukiamua kujenga Mahakama za Kata. Pia tukasema katika baadhi ya maeneo gari hili haliwezi kufika na tukatoa mfano kwa Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, kule juu milimani, gari hili la Mobile Court haliwezi likafika. Lingine lilikuwa ni eneo la maamuzi yenyewe na hasa katika eneo la fine ambazo zitaenda kutozwa kule na haki ya watu kupewa wakili na kusikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Muswada unaletwa Bungeni tayari tenda au magari yalishaagizwa kutoka nje. Kwa hiyo, Bunge lilikuwa linatumika kuhalalisha kitu ambacho tayari kilikuwa kimeshafanyika.

T A A R I F A

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana kaka yangu, rafiki yangu, Mheshimiwa Mwakasaka, nikizungumzia Kamati ya Bunge nazungumzia Bunge Dogo. Nimesema Muswada ulikuja kwenye Kamati ya Katiba na Sheria na ukaondolewa na Serikali, sasa sijui, aah, naomba niendelee tu.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu.

T A A R I F A

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, alikuwa anazungumza hapa juzi akasema sisi Wabunge tuwe wavumilivu, tuwe tunasikiliza na wenzetu, usikilize kile ambacho pengine wewe hutaki kukisikia. Huyu mwenyewe hapo nje alikuwa analalamika na wenzake wawili na wenzake watasimama sasa hivi kwamba Rais Magufuli hasikilizi watu, sasa wewe unapata wapi moral authority ya kuniambia mimi. Kwa hiyo, taarifa yake nimeikataa.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ibara ya 74(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inazungumzia juu ya uwepo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo tunayo sasa imeundwa na kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Na.1 ya mwaka 85 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia muundo na mfumo wa Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ujao na jinsi Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wanakatazwa na Katiba hii kwamba watu wanaojihusisha na vyama vya siasa (makada) wasiwe wasimamizi wa uchaguzi lakini ukiangalia huko chini muundo wa Tume, ukiacha pale juu unatutia mashaka kwamba tunaweza tukaenda kwenye uchaguzi mkuu wa 2020 tukiwa na amani na usalama. Niishauri Serikali na niiombe sana kwamba ifanye marekebisho ya Tume yetu ya Uchaguzi ili yale mambo ambayo yametokea Zanzibar mwaka 2001, yametokea Kenya na katika mataifa mengine yasije yakatupata na sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina picha za Wakurugenzi wa Halmashauri ambao walikuwa makada wa CCM na walikuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Wengine asubuhi wanakuwa makada wa CCM na mchana wanaenda kusimamia uchaguzi, kinyume na Katiba yetu, kinyume na Sheria ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Jecha Salim Jecha, kuamua tu binafsi kufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/2018 ambayo sasa tunaelekea kuandaa bajeti mpya unakuta katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali ilikusanya takribani shilingi trilioni 17 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 18, hii ni kwa mujibu wa kitabu hiki. Kama mapato yalikuwa shilingi trilioni 17.9 matumizi yakawa shilingi trilioni 18.7 maana yake ni kwamba nakisi ya bajeti yetu ilikuwa inakaribia shilingi trilioni 1 na hiyo ama ipatikane kutokana na mikopo ama misaada kutoka nje, matokeo yake bajeti imeshindwa kutekelezwa. Ukisoma bajeti yote, mishahara na matumizi mengine ya Serikali karibu fedha zote zilizokusanywa zimetumika katika matumizi ya mishahara na matumizi mengine ya madeni ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isiyofikia malengo ya makusanyo yake haiwezi kutekeleza bajeti yake kikamilifu. shilingi trilioni 6 ambazo zilitengwa kwa ajili ya maendeleo hizi zote maana yake hazipo katika makusanyo ya Serikali, zenyewe ni lazima zipatikane ama kutokana na mikopo ama kutokana na misaada kutoka nje. Misaada sasa imekuwa shida kutokana na mahusiano yetu kuwa siyo mazuri na nchi wahisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye bajeti, kwa mfano, uvuvi, makadirio yalikuwa shilingi bilioni 7.1, fedha za ndani shilingi bilioni 3, fedha za nje shilingi bilioni 4, zilizotoka shilingi bilioni 4 maana yake pengine Serikali haikutoa hata shilingi katika uvuvi. Matokeo yake Serikali imeenda ku-deal na wanaoitwa wavuvi haramu, uvuvi watu hawawezi tena. Hatukuweza kutoa mafunzo tumeishia kulipa mishahara, matokeo watu wanalipwa mishahara, wanakaa ofisini wanasoma magazeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye kilimo, makadirio ni shilingi bilioni 98.1, zilizotoka ni shilingi bilioni 41.2 sawasawa na asilimia 42 plus. Sasa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili. Kwenye kilimo ndiko kwenye miwa, kwenye sukari; kwenye kilimo ndiko kwenye chakula, Serikali inashindwa kuwekeza kwenye kilimo, tunategemea wahisani, halafu matokeo yake tunasema tumetekeleza bajeti yetu, tunakaa hapa tunajisifu, tunasema mwakani kusiwe na uchaguzi, tunatumia shilingi milioni 800 Dola za Marekani kuagiza chakula nje, karibu shilingi trilioni 1.8.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kubenea, subiri kidogo. Taarifa Mheshimiwa Ulega.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Kubenea, kwa faida yake na kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wengine kutokana na kauli aliyoisema kuwa Serikali haiwekezi na hivyo kupelekea wataalam katika Wizara kama vile ya Uvuvi, wanakaa wanasoma magazeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa kuwa katika Wizara ambazo Serikali imetenda vyema, hata kupelekea kuvuka malengo katika utekelezaji wa kazi, ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika mwaka wa 2018/2019 ambao sasa tupo katika robo ya mwisho. Idara Kuu ya Mifugo imetengewa kukusanya pesa za maduhuli ya Serikali takriban shlingi bilioni 18. Mpaka hivi sasa tunavyozungumza, tumeshakusanya shilingi bilioni 26. Maana yake ni kwamba tuko zaidi ya asilimia 140. Idara kuu ya Uvuvi ilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 16, mpaka sasa hivi tumeshakusanya zaidi ya shilingi bilioni 24. Maana yake tuko zaidi ya asilimia 110. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mbunge anaposema kuwa watu wamekaa wanasoma magazeti, ni kwa sababu sio mfuatiliaji wa haya mambo. Nampa nafasi afuatilie zaidi ili aweze kuona mchango chanya unaotokana na Idara kubwa hizi mbili kwa mapato ya Taifa letu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kubenea.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu. Anaposema maduhuli, maana yake ni kodi, maana yake ni faini. Haya siyo makusanyo yanayotokana na fedha za kodi, ni faini. Ndiyo maana Ziwa Victoria Tanzania inamiliki zaidi ya asilimia 50 ya Ziwa Victoria; Uganda wanamiliki asilimia 33; na Kenya wanamiliki asilimia 6. Tokea Serikalli ya Awamu ya Tano iingie madarakani, viwanda saba vipya vimefunguliwa Uganda na Watanzania, kwa sababu ya urasimu uliopo kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi; kwa sababu ya kuweka sheria za operesheni hizo za wavuvi. Watu wamekimbia nchi wameenda kuwekeza Uganda kwa sababu ya faini hizo za shilingi bilioni 20 anazodai hapo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapozungumza, hii niliyosoma, shilingi bilioni tatu ni ya Wizara yenyewe, kwamba fedha iliyopelekwa ni shilingi bilioni tatu, siyo ya kwangu mimi. Sasa anapozungumza kwamba wamekusanya, kukusanya maduhuli, maduhuli sijui anaelewa maana ya maduhuli? Maduhuli siyo kodi ya kila siku ya Serikali, ni vyanzo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona niachane naye.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ndiyo uti wa mgongo. Pembejeo zote zinazopatikana kwenye kilimo…

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Agness, taarifa.

T A A R I F A

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mwongeaji, pale aliposema kwamba Tanzania hatuna mahusiano mazuri na nchi wahisani. Labda kama hana kumbukumbu nzuri.

Mheshimiwa Mwenuekiti, majuzi Chancellor Merkel, Rais wa Ujerumani, aliipongeza Tanzania kwa kuwa na mahusiano mazuri na nchi nyingine na kwamba uchumi wetu umekua sana. Pia nampa taarifa kwamba juzi tumefungua Ubalozi mpya…

MWENYEKITI: Imetosha, taarifa ni moja tu bwana.

MHE. AGNESS M. MARWA: …Cuba ambao yeye anapaswa kuji…

MWENYEKITI: Hapana taarifa ni moja tu.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kubenea, taarifa moja tu ile ya kwanza.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi hiyo taarifa wala sina sababu nayo kuipokea kwa sababu mimi nimepokea taarifa ya Serikali yenyewe, Mheshimiwa Waziri ameeleza ndani ya bajeti kwamba mahusiano yao siyo mazuri na wahisani, kwa hiyo, wahisani hawatoi hela vizuri. Hata hii inathibitisha.

MWENYEKITI: Kwenye ripoti gani hiyo wewe Mheshimiwa?

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ni…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kubenea, hebu nisaidie na mimi ili record ikae vizuri. Kwenye taarifa ipi?

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mradi wa Mheshimiwa Zitto Kabwe, alikuwa na mradi kule Kigoma, ambao...

MWENYEKITI: Hapana. Mheshimiwa Kubenea, hapa tuna hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, wewe niambie tu katika andiko.

MHE. SAED A. KUBENEA: Nimeiondoa, nichangie. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nimemsikia Mheshimiwa Rais anasema kwamba viwanda vyote ambavyo vimebinafsishwa na Serikali na wale ambao walipewa kazi ya kubinafsisha viwanda hivyo ambao walibinafsishiwa viwanda hivyo, hawakuviendeleza wavirejeshe Serikalini. Mheshimiwa Rais akaomba radhi kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya watangulizi wake kwa mambo ambayo yalifanyika katika nchi katika uuzaji na ubinafsishaji wa mali za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesahau jambo moja kubwa sana ambalo limefanyika katika nchi hii. Nyumba za Serikali zilizouzwa Rais hajasema zirejeshwe, tunaomba nyumba zote za Serikali zilizouzwa kiholela na kienyeji, zirejeshwe mikononi mwa Umma. Nyumba hizi waliouziwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie jioni ya leo. Kwanza nianze mchango wangu kwa kunukuu maneno ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, liyoyatoa kwenye Bunge hili tarehe 7 Februari, 2008.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lowassa alisema, “Bunge hili ndio chombo kikuu cha kusimamia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba hapa ndipo mahali pekee ambapo tunapaswa kuonesha umahiri wetu na utayari wetu wa kudumisha kwa vitendo demokrasia ya hali ya juu katika Taifa letu.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mijadala yetu ndani ya Bunge na ukiangalia kazi yetu sisi kama Wabunge unapata shida kwamba Mbunge anasimama ndani ya Bunge anapongeza kwa asilimia mia moja halafu analaumu kwa asilimia mia moja. Anasema tokea mwaka 1967 nchi hii ilikuwa haijawahi kujenga hospitali, lakini imejenga baada ya mwaka 1977. Sasa unauliza hicho chama kilichokuwa kinaongoza hiyo Serikali ni kipi? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapata shida ukiangalia, mtu anajaribu kuweka ushabiki wa vyama badala ya kuweka maslahi ya nchi mbele. Kwa hiyo, ni rai yangu tu kwamba sisi Waheshimiwa Wabunge tujikite zaidi kuangalia Taifa letu na maslahi yake badala ya kuangalia ushabiki wa vyama vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 18 ya Katiba yetu ambayo ni mchango wangu katika Kamati ya Huduma za Jamii, inaeleza wazi kwamba kila mtu anayo haki ya kupata habari na kutoa habari na ni wajibu wa Kikatiba wa kila raia. Sasa Kamati imeleta mapendekezo juu ya uboreshaji wa Kituo cha Television ya Taifa cha TBC. Walisema TBC iboreshwe ili iweze kutoa matangazo yake vizuri na iweze kusikika vizuri. Ni jambo zuri sana na tunaliunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, TBC ya sasa hivi siyo chombo cha Umma tena. Kimejaa ushabiki na hakiendeshi mambo yake kwa weledi ambapo upande wa pili wa watu wengine ambao wako ndani ya Bunge hili au wanaunda vyama ambavyo viko ndani ya Bunge hili au kwenye Taifa hili, hawapewi nafasi ya kutosha ya kutoa maoni yao. Sheria zilizopo, Kamati inapendekeza TCRA wasimamie leseni za TV za online na television za kawaida. Ni jambo ambalo binafsi silipingi. Ila kuna shida kidogo. Ukienda upande wa magazeti; na katika hili naomba ni-declare interest kwamba mimi ni Mwandishi wa Habari na mmiliki wa chombo cha habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, magazeti katika nchi hii sasa hivi yanapewa leseni ya kuendesha kwa kila mwaka, jambo ambalo limeondoa uwezekano wa wawekezaji wakubwa wenye fedha kuja kuwekeza kwenye nchi, kwa sababu mtu hana uhakika kwamba baada ya leseni yake kumalizika atapata muda wa kupewa leseni nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yalikuwepo magazeti, yaliyumba kwenye uchumi, lakini wawekezaji wa ndani na nje walikuja kuyachukua wakayanunua, wakayaendesha na sasa yametoa ajira kubwa, yameleta mitambo ya kuchapisha magazeti, yameajiri watu wengi sana Watanzania wako hapa, wamepata kazi. Kwa hiyo, nitoe ushauri kwa Kamati na Serikali kwamba, ile sheria ambayo inatumika angalau kwenye television wanapewa leseni ya miaka mitano. Angalau basi kwenye magazeti wangeweka kipindi cha miaka mitano mpaka kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ardhi kuna miaka 33 mpaka miaka 99. Sasa tuangalie kwenye madini sheria zimebadilishwa, mambo haya yamebadilika; ili sasa tuweze kufungua uwanja mpana sana wa watu kupata habari kwa uwazi, kupata habari sahihi na kwa wakati sahihi, ili haki ya kila raia isivurugwe kwa sababu ya sheria tunazotunga hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haki hii ya Kikatiba ni haki ambayo mtu haiombi ni yake amepewa kwa mujibu wa Katiba yetu. Ni muhimu sana haki hiyo ambayo tumepewa kwa msingi wa Katiba yetu ikalindwa na kudumishwa. Tunapata shida leo, tunalaumiwa dunia nzima kwamba Taifa letu haliheshimu uhuru wa watu kujieleza, haliheshimu uhuru wa watu kutoa maoni, haliheshimu uhuru wa watu kutoa habari. Sasa baadaye sisi tunakimbizwa na tuko porini…

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kubenea, kuna taarifa. Mheshimiwa Stanslaus Mabula.

T A A R I F A

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuokoa muda sitaisoma kanuni husika, lakini nataka nimpe Taarifa mzungumzaji kwamba suala la uhuru wa kujieleza ni suala ambalo liko wazi; na kwa sababu, Serikali ya Awamu ya Tano inasimamia jambo hilo, ndiyo maana rafiki yangu Mheshimiwa Kubenea pamoja na wenzake wakiwemo akina Mheshimiwa Mwambe, Mheshimiwa Komu na wengine ambao sitawataja kwa majina, wameukosa uhuru huo wa kujieleza ndani ya chama chao kufikia hatua ya kusema; na wameambiwa sumu haionjwi kwa kulamba na ulimi. Sasa ni haki ipi ya kujieleza anayoitaka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu nimpe taarifa. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kubenea.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ni majungu tu. Kwa hiyo, taarifa kama hiyo nimemwachia yeye mwenyewe. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haki hizi ambazo tumezizungumza ni haki za kisheria, kama zipo basi zinawezekana zipo kwa pande zote katika nchi. Hata kwenye chama ambacho naye anatoka hizo haki inawezekana zikawa zinavurugwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo la muhimu ni kwamba tumekubaliana kwa mujibu wa sheria zetu na Katiba yetu. Mnalaumiwa sana na yeye anajua kwamba leo ukienda kwenye mitandao ya kijamii, ukienda kwenye ripoti mbalimbali za Amnesty International, World Bank, IMF, wanatulaumu na tunanyimwa misaada kwa sababu ya kuzuia hizi haki. Sasa hili jambo siyo geni, linafahamika na kila mmoja. Rai yangu, kwa nini tunakaa kwenye pori tunakimbizwa na simba, badala ya kurukia faru anaweza kukuokoa unaenda kurukia swala, anakuua? Simba anachukua wewe na swala pamoja. Tusifike huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vya habari Tanzania vinapita katika wakati mgumu sana. Vyombo vya habari havipati matangazo kutoka Serikalini, vinabaguliwa hasa vile vya binafsi, kuna urasimu mkubwa wa kutoa habari hata ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi kwamba baadhi ya mijadala inayofanyika humu ndani haichukuliwi na vyombo vya habari. Kwa hiyo, sisi badala ya kwenda mbele sana, miaka 100 mbele, tunarudi nyuma miaka 50 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakushukuru sana. Ahsante sana, Mungu akubariki. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayofanywa na Kamati ya Sheria Ndogo ni kazi nzuri sana, nasi kama Wabunge tunaipongeza sana Kamati hii chini ya Mheshimiwa Adrew Chenge mzoefu, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Miswada au Sheria nyingi zinazoletwa hapa Bungeni zinakuwa na matatizo makubwa sana. Jana tumepitisha sheria hapa ya kumpa mamlaka Mkurugenzi wa EWURA ambaye atakuwa na mamlaka ya kushtaki, kufuta mashtaka na kuharibu mali. Sasa huko tulishatoka, vyombo kama TAKUKURU kwa mfano, tulivitungia sheria humu ndani visiweze kupeleka mashtaka Mahakamani bila kupeleka kwa DPP. Polisi tuliwaondolea mamlaka ya kupeleka kesi Mahakamani bila kupata kibali cha DPP ili kuondoa upendeleo na kukomoa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe tuna- balance hivi vitu, hatuwezi kuchukua mamlaka ya mtu yote tukakabidhi kwa mtu mmoja yeye mwenyewe ndiyo akawa Mwendesha Mashtaka, yeye mwenyewe ndiyo akawa Hakimu, yeye mwenyewe ndiyo akawa mlalamikaji, haya ni mambo yanayokwenda kinyume cha Katiba yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali inapotaka kuleta Miswada au Sheria Ndogo katika Kamati zetu za Bunge ni lazima izingatie Katiba yetu ambayo ni msingi mkuu wa sote tuliopo hapa tuliapa kuilinda na kuitetea, tukija humu Bungeni tukiweka ushabiki wa kivyama, tukiweka ushabiki wa kukomoana hatutaitendea haki nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri sana kwamba hii kazi ambayo inafanywa humu Bungeni na Kamati zetu za Bungeni na Bunge lenyewe ni kazi nzuri lakini Serikali ilete mambo haya yawekwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hili jedwali asilimia karibu 70 ya sheria ndogo zilizoletwa humu zina makosa makubwa ya kiuandishi na mengine yanapingana na Katiba yetu. Kwa mfano, kuna Sheria hii ya Madaktari hata Kamati inasema inapingana na Ibara ya 13(3) ya Katiba ambayo inatoa uhuru wa kila mtu kutobaguliwa kwa mujibu wa sheria. Serikali ambayo imeapa kulinda Katiba lakini inatunga Kanuni na inaleta sheria ndani ya Bunge inayopingana na Katiba unashangaa kwamba Mheshimiwa Waziri ameapa kulinda Katiba, Manasheria Mkuu wa Serikali ameapa kulinda Katiba, Kamati inasema sheria hiyo mnayoleta humu ndani inapingana na Katiba! Wao wamo ndani wanataka mpaka watu waende Mahakamani waka-challenge hivi vitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitengemea Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawaziri waliopo humu na bahati njema Waziri Mkuu yumo humu ndani wangelichukuwa hili jambo wakaliondoa kabisa wakakubaliana na mapendekezo ya Jedwali la Kamati ya Sheria Ndogo ili jambo hili lisituletee matatizo. Hatuwezi kutunga sheria humu ambazo zinapingana na Katiba. Unashangaa kwamba sisi tumekuja humu tumeapa kulinda Katiba lakini tunapitisha Sheria na Kanuni zinazopingana na Katiba na Kamati inatuelekeza humu kwamba hii inapingana na Katiba Ibara ya 13(3) wameainisha sasa tunafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata sheria tunazotunga humu ndani ya Bunge, Serikali inaleta sheria wakati mwingine unashangaa baada ya miezi sita sheria inabadilishwa. Wakati wa kuipitisha vigelegele, hoihoi utadhani unakomoa, unatunga sheria dhidi ya wakoloni, kumbe unatunga sheria dhidi ya Watanzania wenzako. Yaani utadhani unatunga sheria dhidi ya makaburu kumbe unatunga sheria dhidi ya Watanzania wenzako, halafu baada ya miezi sita unakuja unasema sheria hii tumeshauriwa tumeona tuondoe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, tuliwaambia leteni sheria zenye maslahi ya nchi, msilete sheria kwa kukomoa watu, sisi sote ni Watanzania. Leo mnaweza mkawa chama tawala kesho mkawa chama cha upinzani; leo mnaweza mkawa mko madarakani, kesho hamko madarakani. Wapo wengi ambao walikuwa madarakani jana – siyo juzi, jana – leo hawapo, jana siyo juzi wala majuzi, mifano ipo na mnaijua, hatutaki kuyasema humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikushukuru sana kwamba vyombo hivi ambavyo vimetungwa kwa mujibu wa kanuni zetu tuvitumie vizuri, siyo kwa kukomoa watu. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri, kwa kazi kubwa ambayo imefanyika kwenye Jimbo la Ubungo hasa kwenye eneo la urasimishaji wa maeneo ya watu ambao walikuwa wanakaa kwenye maeneo yasiyo rasmi. Mheshimiwa Wazri, hongera sana kwa kazi hiyo na tunaomba ile kazi ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru kwa master plan ya Dar es Salaam ambayo sisi kama wadau tumeshirikishwa kwa sehemu kubwa. Tunaomba ile master plan ikamilishwe ili Dar es Salaam mpya iweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la migogoro katika ardhi mingi inachangiwa na wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi ambao sio waaminifu na sio waadilifu. Hapa naomba ni- declare interest kwa sababu jambo hili na mimi linanigusa kidogo kwamba kuna kiwanja katika maeneo ya viwanja 20,000 vilivyopimwa Dar es Salaam kuna mmoja wa wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi alienda kumega lile eneo na akajimilikisha na Mheshimiwa Waziri, taarifa hizi zimefika Wizarani kwake lakini kwa mshangao mkubwa ameshindwa na kigugumizi kushindwa kuchukua hatua.

Mheshimiwa Spika, nashangaa kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekuwa jasiri kwelikweli wa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo mengi lakini migogoro kama hii inayomgusa kwenye Wizara yake yeye mwenyewe anashindwa kuchukua hatua. Kwa hiyo, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mheshimiwa Lukuvu ufanye hii kazi ambayo tumekuletea na kama unataka ukumbushwe zaidi umesahau tukuletee hizo nyaraka ili uweze kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu National Housing ambalo limezungumzwa kidog na mzungumzaji aliyepita. National Housing imefanya miradi mikubwa Dar es Salaam na miradi mikubwa mitatu imesimama. Mradi wa Kawe na ule mradi wa Victoria. Mradi wa Kawe ulikadiriwa kutumia shilingi bilioni 114 wakati unaanza, karibu dola za Marekani milioni 63.9. lakini sasa hivi baada ya kusimama unakadiriwa kutumia shilingi bilioni 142. Mradi haujaenda mbele, National Housing imekopa kwenye taasisi za fedha. Mkopo ule unalipwa kutokana na mradi wenyewe, mradi umesimama. Matokeo yake National Housing wanalipa kutokana na mapato ya ndani ya kila siku ya kodi ambazo tunalipa sisi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana Serikai ikachukua hatua za dharura kuruhusu National Housing waendelee kukopa ili kukamilisha miradi waliyoanzisha. Mradi kama ule wa Victoria, umekamilika kwa karibu asilimia 95 lakini National Housing wamezuiwa kuendelea kujenga kwa sababu wamezuiwa kukopa na baadhi ya benki zilishahamisha matawi yao kwa mfano Benki ya NBC ilikuwa na tawi Kinondoni pale eneo la Manyanya, wamefunga lile tawi wakitegemea watahamishia huduma zao kwenye tawi la Victoria na walishamaliza mkataba na yule mwenye jengo. Leo wamezuiwa kuendelea na Victoria NBC wamehamishia tawi lao pale Victoria. Kwa hiyo, wanapaswa kuhamishia hapo kwenye hilo jengo jipya, hawawezi kuhamishia kwa sababu jengo limesimama, jengo haliwezi kuendelea kwa sababu National Housing wamezuiwa kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa jambo hili litaifanya National Housing isambaratike kabisa. Kwa hiyo, mikopo hii ni mikubwa kweli kweli sio mkopo wa bilioni moja au mbili, tunazungumzia mkopo wa bilioni 244, sio fedha ndogo kwa shirika kama hili! Na shirika limefika kikomo cha kukopa, limeomba ruhusa ya Serikali liruhusiwe kukopa kwa dharura. Serikali haitaki kutoa kibali. Mheshimiwa Waziri, jitahidi sana shirika hili lisije kufa mikononi mwako, utapata aibu. Limetoka mbali National Housing ilikuwa haijulikani kabisa, limejengwa vizuri, leo ina miradi mikubwa, ina miradi mpaka hapa Dodoma, isije ikafa mikononi mwako. Jitahidi sana.

Mheshimiwa Spika, nadhani kuna matatizo makubwa sana kwenye Bodi zetu za Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma. Ni vizuri tunapoteua Bodi kwa sababu haiwezekani mkopo huu wote ukapita tu hivi hivi bila bodi kuangalia na kama Serikali inakuja kuona leo maana yake Bodi ilishindwa kuwajibika na ndiyo maana Serikali ilivunja Bodi ya National Housing. Kwa hiyo, nafikiri tunapounda Bodi zetu tuache kuingiza ushabiki wa urafiki, tuache kuingiza ushabiki wa siasa…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SAED A. KUBENEA: …tujenge Bodi imara. Nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii muhimu ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha ya Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali. Kwanza niseme masikitiko yangu kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anawasilisha hotuba yake hapa Bungeni, aliacha jukumu lake la msingi la kusimamia sera za Serikali juu ya bajeti akajikita kwenye ushabiki wa kushabikia Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu ni Taifa changa sana na sisi wengine hatuna mahali popote pa kwenda, tumezaliwa hapa, tumekulia hapa, tumeishi hapa. Hatujawahi kwenda hata nchi za watu kuishi miaka mitano, miaka kumi, kwa hiyo hatuna mahali pa kwenda, bila kuheshimu utulivu wetu, amani yetu na busara zetu hakika Taifa hili tunaweza tukalipeleka mahali pabaya sana. Kwa hiyo Mheshimiwa Mpango jukumu lako kubwa ni kuisimamia Serikali juu ya mapato na kututoa hapa tulipo na kuachana kabisa na huu ushabiki wa kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye ukurasa wa 87 na 88 anasema; fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya maendeleo ni shilingi trilioni 12.25 ambayo ni sawa karibu na asilimia 37 ya bajeti. Ukiangalia kwenye hiki kitabu fedha karibu zote zimekwenda kwenye miradi isiyozidi minne,

wametaja hapa reli ya kati (standard gauge), umeme wa Mto Rufiji, REA na maji. Ili uchumi wetu uweze kukua tungewekeza katika kilimo, tungewekeza katika viwanda, tungewekeza katika umwagiliaji, lakini bajeti za Wizara hizo zote ziko chini ya asilimia tano ya bajeti yote. Sasa unajiuliza tunapojenga reli kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, tumewezaje kuunganisha uchumi wa nchi na kule Congo - Lubumbashi ambapo Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma wanapigania kwamba reli yetu iende? Unajiuliza hiyo mizigo tunaibebaje ikifika Dodoma tunaunganishaji uchumi wetu na nchi za nje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashangaa sana, nashangaa kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Mpango kabla hajawa Waziri wa fedha alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango na huu mpango wa miaka ishirini pengine umeandaliwa akiwa ofisini au alishiriki kuuandaa, miaka 25. Sasa leo anakuja na mpango mwingine kabisa wa umeme, na mimi najua kwamba nchi hii kipaumbele chake kikubwa ulikuwa umeme wa makaa ya mawe wa Linganga na chuma cha Mchuchuma, lakini kwenye bajeti nzima Serikali haizungumzi lolote juu ya Mchuchuma, haizungumzi lolote juu ya Liganga, haizungumzi lolote juu ya umeme wa gesi ya Mtwara haina kitu kabisa. Wanakuja na miradi mipya kila siku kitu kipya, kila siku kitu kipya, tunakwenda wapi! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri ni vizuri sana Serikali ikaangalia kwamba miradi ambayo tumeanza nayo mwanzo kama kipaumbele ifanyiwe kazi vizuri ili tusije tukawa tunakwenda kila mtu anakuja na kitu chake. Mheshimiwa Kikwete alikuja na umeme wa gesi hatujamaliza, hata gesi yenyewe hatujazalisha, hata deni hatujalipa leo tumeachana kabisa na gesi tunakuja na umeme wa maji. Huu umeme wa maji tuliuacha kwa sababu tulipata matatizo makubwa kwenye Kihansi, kwenye Nyumba ya Mungu, kwenye Mtera na Hale. Mabwawa yalikauka na Serikali ikalazimika kuingia kwenye mikataba na makampuni ya kufua umeme wa dharura, nchi ikaingia kwenye matatizo makubwa. Huu umeme wa Rufiji tunaofua hatuna uhakika kama mabadiliko ya tabia nchi hayataweza kutuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri Serikali badala ya kuangalia miradi kwa pupa pupa, ifanye uchambuzi yakinifu kwa kila mradi ili tunapoenda kwenye mradi, tunapoingiza fedha za walipa kodi wa nchi hii kwenye miradi mikubwa lazima tuitekeleze. Hii bajeti ukiisoma yote, fedha za maendeleo zinategemea fedha nyingi kutoka nje na fedha za nje hazina uhakika wa kuzipata. Tayari wafadhili kwa mujibu wa Kamati ya Bajeti imesema haiweze tena kuchangia bajeti ya Serikali, inakwenda kujenga miradi moja kwa moja, ni kwa sababu hatuaminiki tena. Usimamizi wetu siyo mzuri wa miradi ya watu na tunakuja hapa baada ya kuwashukuru hawa wanaotupa fedha, tunawakebehi na kuwaita mabeberu, siyo jambo jema hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti inazungumzia uchaguzi mkuu ujao, bajeti inazungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hapa ni mahali pazuri kabisa muhimu pa kurejesha heshima ya nchi yetu na utulivu wa nchi yetu. Nchi yetu hii imewahi kuingia kwenye matatizo makubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000; mamia ya wananchi wa Zanzibar, wa Pemba walilazimika kuwa wakimbizi katika nchi yao. Nchi hii ambayo ilikuwa kimbilio la wakimbizi ikaacha ikazalisha wakimbizi kutokana na misingi mibaya ya kusimamia chaguzi zetu. Hata leo ukisoma matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi mwaka 2015 ukachukua kura zote zilizotangazwa kwamba zimepigwa, ukachukua kura halali, ukachukua na kura ambazo siyo halali ukijumlisha kwa pamoja hazifungamani kabisa, ni mbingu na ardhi, na hata idadi ya iliyoandikishwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 na waliopiga kura ni tofauti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu Serikali ikaiboresha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na ikaachana na hii biashara ya kukata rufaa kwa ajili ya Wakurugenzi wa Halmashauri walioondolewa na mahakama kusimamia uchaguzi. Kitendo cha kukata rufaa peke yake kimeonesha hila, kinaonesha nia mbaya iliyopo, kwa hiyo, ili tuondoke huko watu waweze kuaminiana, yaliyotokea Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka 2015 yasijirudie tena katika uchaguzi ujao wa 2020. Tuipe uwezo Tume ya Uchaguzi ya kusimamia uchaguzi ulio huru na haki ili anayeshindwa huo uchaguzi aseme ahsante sana. Watu wapeane mikono, waache uhasama wa kisiasa, lakini kwa hii tabia ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango ameionesha humu Bungeni nachelea kusema nina hofu na uchaguzi ujao kwamba unaweza ukawa huru na haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu hili limejengwa na wazazi wetu kwa misingi imara kabisa ya demokrasia ya hali ya juu sana, na hili Bunge ndiyo chombo kikubwa kabisa katika Jamhuri ya Muungano cha kuonesha umahiri wetu katika demokrasia. Tusiposimama hapa tukataka Tume yetu ya Uchaguzi ikaendesha chaguzi yetu vizuri na haki, yaliyotokea kwenye nchi za wenzetu yalitokana na mambo haya haya ya kufanya uchaguzi kuwa usanii fulani na wananchi baadae wakakataa uchaguzi huo, tusifike huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya nchi za wenzetu za Afrika ziliingia kwenye matatizo makubwa baada ya Tume zao za Uchaguzi kufanya kazi za kisanii, leo Tume yetu ya Uchaguzi haiaminiki katika macho ya dunia. Wanatokea wenzetu wanatuambia boresheni haki za binadamu, boresheni demokrasia, utawala bora, tunawabazaza. Wakati hao wanaotuambia baadhi yetu tumeishi kwenye nchi zao miaka kumi, tumesoma huko, tumeishi huko, wametupa scholarship za kusoma kwao na kuishi kwao tunakuja tunawatukana, siyo haki hata kidogo. Uhusiano wetu na mataifa ya nje ungekuwa ndiyo huo unaombiwa hapa ndani ya Bunge hili hakika isingekuwepo miradi ya SIDA, isingekuwapo JICA, isingekuwa miradi ya Wajapani wala miradi ya Waingereza hapa nchi hii isingekuwepo, lakini imekuwepo kwa sababu tulisahau yaliyopita tukaganga yajayo na ndivyo nchi zote zinavyojengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda South Africa leo, kama Afrika Kusini wangekubali kurudishwa nyumba kwenye ubaguzi wa rangi nchi yao isingeenda pale. Ukienda Rwanda, kama Wanyarwanda wangekuwa wanakubali mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 yawe kumbukumbu kwenye kichwa chao nchi yao isingefika hapo ilipoenda, lakini walisahau. Hata kama walitufanya watumwa, walitutawala, tuachene na hivyo vitu tusonge mbele kwa manufaa ya nchi yetu ili kile walichokichukua waweze kukirudisha hapa, kiweze kutusaidia kwenye maendeleo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo la mwisho kabisa ni juu ya kodi ya pad ya kina mama ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameiondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa Kubenea, sekunde thelathini.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utafiti uliofanywa na Shirika la UNICEF kati ya wanafunzi 10 wanaosoma shuleni mmoja ameacha shule kwa sababu ya kukosa taulo ya kujihifadhi. Badala ya Serikali ku-deal na wafanyabiashara ambao wananufaika na huo msamaha, wanakuja kuondoa kodi kwa watu wote, hili jambo sio sahihi na ninalipinga kwa nguvu zote. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mchungaji Peter Msigwa kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni weledi na busara. Aidha, nampongeza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine duniani ni sharti uendane na utii wa Serikali yetu kwenye mikataba ya kimataifa. Mwaka 2016 Bunge la Kumi na Moja katika mikutano mbalimbali pamoja na mambo mengine lilipitisha Sheria ya Huduma ya Habari (Media Services Act of 2016) na Sheria ya Upatikanaji wa Habari (The Access to Information Act, 2016). Serikali ilieleza hapa Bungeni kwamba utungwaji wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa au wengine wanaita The Access to Information Act kuwa utoaji wa taarifa siyo tena jambo la hiari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizo mbili hazikidhi matarajio ya wananchi na zimesheheni maneno matamu lakini yakiwa hayatekelezeki. Kinyume na matarajio ya wengi, sheria hazioneshi kwamba kutakuwa mwarubaini wa ukiritimba wa mamlaka za Serikali katika kutoa taarifa. Hii ni kwa kuwa zimepingana na dhana ya haki ya kupata taarifa na zimezika haki ya kikatiba ya raia kupata taarifa. Badala ya kusaidia wananchi kupata habari, sheria hizo zilizotungwa zitatumika kama kichaka cha kuficha udhaifu wa viongozi wasio waadilifu na zinaweza zikatumika hata kufungia baadhi ya vyombo vya habari. Hii ni kwa sababu ndani ya sheria hizo kumewekwa vifungu vinavyompa mamlaka mwenye taarifa kutotoa taarifa alizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 6(3) cha Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa kimetaja mambo ya Usalama wa Taifa yasiyopaswa kutolewa kuwa ni taarifa ya nchi au Serikali ya kigeni inayohusiana na Usalama wa Taifa na uhusiano wa mambo ya nje au shughuli za mambo ya nje yakiwemo masuala ya kisayansi na teknolojia yanayohusiana na Usalama wa Taifa, mathalani, taarifa juu ya ununuzi wa rada; udhaifu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU); uuzaji wa hati fungani za Serikali kwa benki ya Stanbic na unyonyaji kwenye mikataba ya madini na gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, udhaifu wa TAKUKURU uliripotiwa na mtandao mashuhuri wa WikiLeaks. Ulimnukuu aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini, Michael Retzer akisema, Edward Hoseah ambaye kipindi hicho alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alizuiwa na bosi wake, Rais Jakaya Kikwete, kuwashtaki vigogo wa wizi wa fedha za EPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uuzaji wa hati fungani uliibuliwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO). Kiasi cha shilingi trilioni 1.3 zimedaiwa kupotea katika sakata hilo. Kifungu cha 5(3) cha sheria kimetaja taarifa ambazo hazipaswi kutolewa ni upelelezi unaofanywa na vyombo vya uchunguzi, faragha binafsi na taarifa za Usalama wa Taifa lakini nani asiyejua udhaifu wa vyombo vya uchunguzi? Vingi vinatuhumiwa kubebana kwa njia ya upendeleo au rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria mpya ya Upatikanaji wa Taarifa imerejesha kwa mlango wa nyuma sheria katili ya magazeti (Newspaper Act ya mwaka 1976) na ndivyo ilivyotarajiwa pia kwenye mikataba. Taifa hili limenyonywa kwa miaka mingi na limekumbwa na migogoro lukuki inayotokana na kuwapo mikataba iliyofungwa kinyemela na watendaji wa Serikali. Wengi walitarajia kuwa mikataba hiyo ingekuwa wazi angalau kwa Bunge, mambo mengi yangekuwa tofauti na yalivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu, Ibara ya 19; Ibara ya 19 ya Mkataba wa Haki za Kijamii na Kisiasa wa mwaka 1966 (ICCPR), Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu wa 1981 na kifungu cha 18 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 kinatoa uhuru wa maoni bila kikwazo cha aina yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kilio hiki cha Wabunge na wananchi hakijasikilizwa na hivyo kinaishia kuipaka matope Jamhuri ya Muungano mbele ya macho ya kimataifa. Baada ya Serikali na Bunge kutunga sheria hizi zinazoratibu shughuli za waandishi wa habari nchini, je, Wizara haioni kuwa sheria hizo zinaharibu taswira ya nchi yetu kimataifa?

Je, Serikali haioni haja ya kuwahusisha wadau wa habari ili kuanza kufanyia kazi malalamiko yao na hatimaye kuleta muswada ili sheria hizo zifanyiwe marekebisho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ubalozi wetu kule Washington DC kumepatikana taarifa kuwa kumelipwa kiasi cha dola za Marekani milioni 1.05 (karibu shilingi bilioni 2.4), kwa mwanamke aliyepelekwa nchini humo kuwa mtumishi wa nyumbani wa Afisa wetu wa Ubalozi, Dkt. Allan Mzengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vya habari vimenukuu taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania mjini Washington DC zinasema, Serikali ililipa kiasi hicho cha fedha kwa makosa binafsi yaliyofanywa na Dkt. Allan Mzengi na alituhumiwa kumsafirisha kinyume cha sheria hadi nchini Marekani Bi. Zipora Mazengo. Dkt. Mzengi alishtakiwa kumfanyisha kazi kwa saa 15 kila siku na kushindwa kumrejesha nchini kwa miaka minne hata pale alipofiwa na ndugu yake Bi. Zipora Mazengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya sheria za Marekani, upelekaji mtu yeyote (mwanamke au mwanaume) kutoka eneo moja hadi lingine kwa shabaha ya kumtumikisha linakuwa ni kosa baya sana nchini humo la usafirishaji haramu wa binadamu (human trafficking offence). Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Bi. Mwanaidi Maajar ananukuliwa akieleza wasiwasi wa kuharibika uhusiano kati ya nchi hizi mbili wakati akiwasiliana na Sanze Salula, aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barua ya Balozi Maajar kwa Salula yenye Kumb. Na. WEPC.179/53 ya tarehe 4 Februari, 2011 ilinakiliwa pia kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo na aliyekuwa Katibu wa Rais Prosper Mbena. Alisema ingawa kwa sasa Serikali ya Marekani imeonyesha karidhika kutokana na Mawakili wa Bi. Zipora kupunguza deni na Dkt. Mzengi kukubali kuanza kulipa kwa awamu, suala hili litabaki kuwa tete kutokana na hatua ya Mawakili wa Bi. Zipora kupinga utaratibu wa kulipa. Balozi Maajar anasema Mawakili hao wameanza tena kampeni za kuichafua Tanzania katika Congress, pamoja na kuishinikiza tena Serikali ya Marekani ili nayo iishinikize Serikali yetu kulipwa deni hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akiandika kwa njia ya tahadhari, Balozi Maajar alieleza Sheria ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Watu ya Marekani ina kipengele kinachoipa mamlaka Congress kuiamuru Serikali kusimamisha misaada kwa nchi ambayo imethibitika kuvunja sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata maelezo ya Waziri kama fedha hizo zimeshalipwa zote ili kuiondolea nchi yetu aibu katika nyanja za kimataifa na kuyumbisha uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba maelezo ya Waziri kuwa ni hatua gani za kinidhamu alizochukuliwa Dkt. Mzengi kutokana na kosa alilolifanya ambalo limeiaibisha Tanzania mbele ya nchi wahisani? Tatu, Serikali inachukua tahadhari gani ili kuzuia kosa kama hili lililofanywa na Dkt. Mzengi lisijirudie tena?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii na naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu wa Habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mwandishi wa habari na mmliki wa vyombo vya habari na pili, muswada uliopo mbele yetu naomba tuweke rekodi sawa sawa kwamba haukushirikisha wadau wakuu wa vyombo vya habari.
Mheshimiwa Menyekiti, hoja ya wadau wa vyombo vya habari ambayo imeelezwa vizuri na Waziri asubuhi ililenga kwamba Jukwaa la Wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari walipopata muswada huu wakati wa kujadili washirikishe waandishi wa habari waliopo wilayani na mikoania kupitia Umoja wa Waandishi wa Habari (Press Clubs). Umoja wa press club waliomba kwamba muswada huu uletwe katika Bunge lijalo kwa kuwa muda wa kutoa maoni ni mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya sana kwamba rekodi hiyo inapotoshwa kwa maksudi. Kwamba wadau wakuu ambao wako mikoani na wilayani hawakushirikishwa katika muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi, Bunge hili limekuwa linalaumiwa kwamba linachukua maoni ya watu waliyopo Dar es Salaam peke yake. Safari hii wadau wanataka kushirikisha wenzao waliyopo vijijini na Wilayani, Bunge linakataa, ni bahati mbaya sana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 8(1) cha muswada kinataka wawepo waandishi wa habari wa ndani na kimataifa, watangazaji na kitatoa leseni kwa waandishi wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uandishi wa habari ni tofauti na udaktari, ni tofauti na uuguzi, ni tofauti na engineering; vitu hivi visichanganywe kwa pamoja. Ndiyo maana Ibara ya 18 ya Katiba yetu inatoa uhuru kwa kila raia kupata na kutoa habari. Katiba yetu haijasema kwamba kila mtu anayo haki ya kuwa daktari, engineer, nesi au mwanasheria; huko kwingine huko, siyo huku. Ndiyo maana leo gazeti likitaka kuandika habari nzuri za madini, kwa mfano, nani aliyepewa leseni ya kwanza ya madini nchi hii? Mgodi gani ulianza kuchimba Tanzanite hapa? Mgodi gani ulianza kuchimba dhahabu? Chombo cha habari kitamtafuta Dkt. Dalaly Kafumu, ambaye alikuwa Kamishina wa madini anajua nani aliyetoa mikataba. Dkt. Kafumu siyo mwandishi wa habari, lakini kwa sheria hii Dkt. Kafumu hataruhusiwa kuandika mpaka awe na leseni. Ni vitu tofauti kabisa na ambavyo waandishi wa habari wanavitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada unakataza kuingilia kesi ambazo zinasemwa zinachunguzwa na vyombo vyetu vya uchunguzi; ni jambo la kusikitisha sana. Rekodi zipo, kama vyombo vya habari vingekuwa vinazuiwa kuchunguza kesi wakati wa sheria ya mwaka 1976, leo Dkt. Mwakyembe huyu asingekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond. Richmond ni zao la waandishi wa habari, tusingechunguza kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Morogoro na dereva teksi mmoja wa Dar es Salaam isingepelekwa mahakamani bila gazeti la Mwananchi kufanya uchunguzi kwa jambo ambalo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam alisema tayari vyombo vya uchunguzi vinachunguza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusingekuwa na Escrow, tusingekuwa na Vitambulisho vya Taifa; kesi hizi zisingekwenda mahakamani kama waandishi wa habari wangezuiwa kuandika habari za uchunguzi ambazo vyombo vyetu vya usalama vinasema vinachunguza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kifungu hiki pamoja na vingine vinakinzana na utawala bora na utawala wa sheria na mikataba yetu tuliyosaini na Jumuiya za Kimataifa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 47(1) na (2)(a), (b), (c) na (d) vya muswada vinazungumzia kwamba kutakuwa na makosa kusambaza taarifa zilizokatazwa. Na asubuhi Waziri anasema kwamba mtambo wa kuchapia, wameondoa lile eneo la kwamba mtambo wa kuchapishia gazeti unaweza ukataifishwa au ukauzwa au ukawekwa bondi na badala yake ikiwa; anasema kwamba mhusika alijulishwa na akathibitika kwamba alipokea hiyo taarifa ndipo kwamba huo mtambo hautachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni nani anayetoa hiyo taarifa? Mtambo mmoja unachapa magazeti zaidi ya sita, haiwezekani kuchukua suala hili zima la kuwahusisha watu wengine wasiohusika na waandishi wa habari, wasio na taaluma ya uandishi wa habari, wasio na nyenzo za kuingia kwenye chumba cha habari kuwaambia kwamba wao waangalie content ambazo zinaandikwa kwenye magazeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa hapa asubuhi, tena bahati mbaya sana wazo hili limeletwa na Kamati, kwamba eti waandishi wa habari wavae mavazi rasmi kama madaktari, wanasheria. Waandishi wa habari wanakwenda kuandika habari za vita unataka avae suti? Anakwenda kuandika habari za sports, habari za Miss Tanzania avae suti? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilidhani jambo hili lingebaki kwa waandishi wa habari wenyewe, wao wanajua kwamba huwezi kumtuma mwandishi wa habari Ikulu akavaa jeans au akavaa kaptura akaja hapa ndani ya Bunge kuna mavazi yake. Lakini mnataka tuweke kwenye sheria eti waandishi wa habari wavae nguo maalum, jamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la leseni kwa waandishi wa habari. Ni jambo zuri, linaletwa hapa linazungumzwa, lakini ni muhimu kama kuna leseni kwa waandishi wa habari basi zitolewe kwa wahariri ambao wako chumba cha habari, ambao wao kazi yao ni kupokea kila taarifa, kupokea habari kutoka mikoani, vijijini na wilayani, ambapo watazipima na kuziangalia hizi habari zinapaswa kutangazwa au hazipaswi, lakini siyo leseni kwa watu wote ambao hata wachangiaji wa makala kwenye magazeti ambao watu wanataka kuchambua uchumi nao wawe na leseni za kuandika habari, hilo siyo jambo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ikibidi Mheshimiwa Waziri leseni ziwe kwa wahariri ambao wamesajiliwa wakati wa usajili wa magazeti, isiwe kwa waandishi wote wa habari, muhimu sana jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada unaelekeza kwamba utatoa marufuku kwa waandishi wa habari wasiokuwa na ithibati, kufanya kazi za habari. Hii ni hatari kubwa mbeleni kwa kuwa kama Bodi ya Ithibati itatoa vibali kwa waandishi wa habari wenye diploma na degree maana yake ni kuwa waandishi wa habari wenye elimu ya ngazi ya cheti hawatakuwa na kazi za kufanya wala kujihusisha na kazi za uandishi wa habari. Ni kinyume kabisa, kabisa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifungu vingi, kifungu cha 50 (4)(5)(6)(7)(8) (a)(b)(10) na (11), vingi vinapingana kabisa kabisa na mikataba ya kimataifa na dhamira ya Serikali ya kuleta muswada huu mbele ya Bunge hili. Suala la muda lilikuwa ni jambo jema na ambalo lilipaswa kabisa kufikiriwa na kuwa sehemu nzuri kabisa ya kupatikana muswada mzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu ukiusoma kwa undani unaona kwamba muswada unataka wamiliki watu wa nje wamiliki asilimia 49 ya hisa ya kwenye magazeti na kwenye televisheni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hivi kwa sasa unaweza ukasema jambo hili lina nia njema, lakini kuna mtu analengwa yupo hapa, raia wa kigeni anamiliki gazeti na gazeti hili lilikuwa linamilikiwa na wazawa. Gazeti la Mwananchi lilikuwa linamilikiwa na kina Rostam Aziz, biashara imewashinda wameuza, ametokea mwekezaji kutoka nje amewekeza kwenye gazeti la Mwananchi, leo gazeti lile sheria inataka kwamba mwekezaji wa nje aje kumiliki asilimia 49 na wazawa wamiliki asilimia 51. Hao wazawa wako wapi? Mtaji uko wapi? Na kama wapo si waanzishe ya kwao nani amewazuia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiuangalia muswada wote unakuta kwamba hawa watu wanaoitwa wa kutoka nje wanatakiwa wamiliki asilimia 51, lakini katika maeneo mengine nchi hii madini yetu yote yanamilikiwa na wawekezaji wa nje kwa asilimia 100, gesi inamilikiwa na wawekezaji wa nje kwa asilimia 100, Serikali imeuza mabenki, imeshindwa; NBC imeuzwa na Serikali na haimiliki asilimia 51, NMB Serikali imeuza hisa kwa wageni, benki pekee iliyobaki ya Twiga imefilisika na inaongozwa na Serikali. Kwa nini mnawalazimisha waandishi wa habari vyombo vyao vimilikiwe na wazawa wakati wazawa wenyewe hawana uwezo wa kumiliki na hawana interest?
Mheshimiwa Mwenyekiti, anzisheni vyenu mmliki asilimia 100, hakuna atakayewauliza. Kampuni ya kwangu namiliki asilimia 100 sina mwekezaji, Habari Corporation inamilikiwa na watanzania asilimia 100 haina mwekezaji kutoka nje, waacheni watu. Uhuru linamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi kwa asilimia100 halina share na UKAWA wala mtu yeyote na watu wengine wamiliki vyombo vyao wanavyotaka wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata baadhi ya magazeti ambayo yalikuwa yanachapishwa humu ndani nayo yalikuwa yanamilikiwa kwa kwa asilimia100 na watu wenyewe waliomo humu humu ndani, hayakuwa na mwekezaji wala hayakuwa na watu kutoka nje, likiwemo gazeti la Mwafrika. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo haya mambo haya tusirithi vitu kutoka nje. Ni vizuri tukarithi vitu vyetu wenyewe na tusiingize vitu ambavyo vinatufanya tuchukiwe na wananchi. Wananchi muswada huu wanasema haujakidhi matakwa ya waandishi wa habari na wao kwa ujumla wao. Kwa hiyo, ninakusudia kuleta marekebisho mbalimbali katika muswada huu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilianza kutekeleza Sheria ya Ubinafsisshaji wa Mashirika ya Umma mwaka 1993. Ambapo ilisema imeamua kujitoa katika uendeshaji wa mashirika ya umma kwa sababu mashirika hayo yamekuwa mzigo kwa Taifa na yamekosesha ajira mamilioni ya wananchi. Sasa leo Mheshimiwa Waziri amekuja na shirika jipya la umma la bandarini kuja kufanya kazi ile ile iliyokuwa inafanywa na NASACO miaka 20 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Serikali kujiondoa katika biashara lilifanyiwa utafiti wa kina na wakaruhusu na mchakato mzima ukapitishwa kwenye vikao halali vya Chama Cha Mapinduzi na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na mwaka 2015 bado inazungumzia ubinafsishaji wa mashirika ya umma. Leo Serikali iliyojiondoa kwenye biashara inarudi kwa mlango wa nyuma kutaka kufanya biashara na haituambii biashara hii inayofanya imefanya utafiti wapi, ilishindwa wapi na sasa itapata nini.

Mheshimiwa Spika, meli hizi ambazo zinakuja bandarini sio meli za Tanzania, Shirika la Meli la Taifa lilishakufa na halina meli, meli hizi ni za watu wa nje. Chombo hiki kinachotungwa hapa hakiko Mozambique, South Africa wala hakipo Kenya. Sasa matokeo yake, tutahamisha wafanyabiashara wakubwa wa meli ambao hawatataka kuwa hodhi na NASACO au hicho chombo kinachoundwa tutafukuza wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hoja ya msingi inayojengwa hapa ni kwamba, bandarini kumekuwa na wizi mkubwa na kumekuwa na ufujaji wa mali ya umma. Ukisoma hotuba nzima ya Waziri unakuja kuona kwamba Muswada huu
umekuja kwa sababu kuna ufisadi bandarini lakini ufisadi uliofanyika bandarini ndugu zangu, hakuna ufisadi wowote mkubwa uliofanyika bandarini ambako Serikali hauujui chanzo chake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, makampuni ya biashara kama Home Shopping Centre ambayo imepigiwa kelele humu ndani bado inapiga deal bandarini na sasa hivi wameshafungua njia nyingine china kama ilivyofungua zamani. Sasa hata mkianzisha NASACO mkaanzisha NASA sijui Chama cha Upinzani cha Kenya au nini bado kama hamjatatua matatizo ya bandari, hamjaweza kupata solution kwa kufanya biashara.

Mheshimiwa Spika, chombo kinachoundwa Msemaji wa Upinzani amesema na Kamati imesema kwamba chenyewe ndicho kitachokuwa kinasimamia biashara, kitafanya biashara na kitasajili mawakala wa biashara, ni kinyume kabisa na utawala wa ushindani wa biashara duniani. Haiwezekani mtu huyo mmoja akawa yeye anafanya biashara, anatoa leseni za biashara, anasimamia biashara za wengine na yeye ndiye anayefuta wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jamani, hata mahakama hazifanyi hivyo mnavyofanya nyie. Ni lazima uwepo utawala unaokidhi, kama Serikali inataka NASACO ifanye biashara, kiundwe chombo kingine cha kudhibiti makampuni mengine ikiwemo NASACO ndani ili haya makampuni yaweze kufanya biashara huria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anakuja na Muswada anakuja kufuta kifungu cha pili cha Muswada ambao unahusu mambo ya Muungano akisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeidhinisha kifungu hicho kifutwe. Katika Sehemu ya Nne ya Muswada anasema pia kwamba Muswada huu utasimamia Sheria ya Bahari ya mwaka 2003.

Mheshimiwa Spika, mimi nashangaa kwamba Waziri anatoka Zanzibar, Waziri amechaguliwa kwenye Baraza la Mawaziri kukidhi matakwa ya Muungano. Waziri anasimamia maslahi ya Zanzibar pamoja na Muungano; anakuja na Muswada Bungeni, kifungu kinaondolewa na Kamati badala ya kuondoa yeye mwenyewe kwenye eneo la Baraza la Mawaziri. Wakitokea watu humu ndani wakizungumza kwa uchungu maslahi ya Zanzibar anasimama anawa-attack personally, hili ni lazima tujadili vitu hivi.

Mheshimiwa Spika, mimi nashangaa Waziri anafika mahali ukizungumza haya mambo kwa uchungu wa nchi, anakwambia, kule hayo mambo yanazungumzwa na wananchi wa Kijijini kule Pemba sio wa hapa. Hao wananchi wa Kijijini wa Pemba ndio alienda yeye kuomba kura wakamnyima, nadhani walikuwa sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. Sheria inajenga fursa ya shirika kufanya biashara badala ya kuwa msimamizi, ni kinyume na misingi ya biashara, utawala bora, haki za biashara na ni kinyume kabisa na dhamira ya Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015. CCM ilisema wazi kwamba biashara itakuzwa na sekta binafsi na itatoa ajira kwa vijana kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, leo Muswada unatoa udhibiti kwa chombo kinachoundwa cha NASAC kudhibiti biashara nzima na yenyewe ndio itakuwa inaangalia huyu apewe leseni, huyu asipewe na huyu afanye kazi hii. Sijaona utafiti wowote kwamba kazi hii ambayo inaenda kufanywa na NASACO au NASAC itawezaje kutokuingilia kazi zinazofanywa na kampuni ya utoaji mizigo bandarini TICTS, sijaona. Inawezekana kabisa tukaanzisha mgogoro mwingine mkubwa humu na makampuni binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi sipingi kuundwa chombo chochote cha kusimamia biashara ya meli bandarini, mimi hilo sipingi. Ninachopinga ni kwamba, NASAC haiwezi ikafanya kazi zote; ikawa mshindani, ikafanya biashara, ikatoa leseni kwa wengine na ikawa na mamlaka ya kufuta wengine, hiyo kitu haiwezekani. Ni lazima tuwe na vyombo viwili tofauti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama Waziri ana nia njema ya kutaka kufanya NASAC ifanye biashara, alete Muswada mwingine wa kuunda chombo kingine cha kusimamia ili kazi ya NASAC iwe ni kufanya biashara na kushindana, hao wengine wafanye baishara.

Mheshimiwa Spika, hii itasaidia uwajibikaji, security kwa wenye meli na itasaidia ushindani kwenye biashara zetu. Vinginevyo tutakuwa tunarudi nyuma kule kule, tunarudisha makampuni haya ambayo yameshakufa, yameshazikwa, hayana mtaji na hayana watu, tunawapa mzigo mwingine Watanzania wa kwenda kuyafufua.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji na biashara huria ni sehemu ambayo Serikali hii imejifunga kwenye mikataba ya kimataifa. Leo ukianza kuanzisha biashara ya ukiritimba, ukitaka sukari inazalishwa Kagera halafu uisafirishe uirudishe Dar es Salaam kwenye SUDECO halafu SUDECO ndio wairudishe tena Kagera ili watu wa Kagera, hiyo sukari itakuwa bei kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, NASAC inaenda kuanzishwa hii italeta gharama kubwa sana kwa watu ambao wanafanya biashara za meli au wakala binafsi, matokeo yake mizigo yetu bandarini itakuwa ya bei juu sana. Kodi bandarini zitaongezeka na hatimaye watu watakimbia Bandari ya Dar es Salaam na kukimbilia kwenye bandari nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana, hakuna mtu anayewapinga au anepinga kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia biashara ya bandarini, tunachopinga ni chombo kimoja kuwa na kazi zote kwa pamoja. Hapa hakutakuwa na haki na uwazi na sisi hata wewe ndani ya Bunge hili umetoa mamlaka kwa Kamati nyingine, umetoa mamlaka kwa vyombo vingine vifanye kazi; sasa ukibeba kila kitu wewe mwenyewe mambo hayaendi. Huwezi kuwa wewe mwenyewe ndio unasafirisha, unasambaza, unasaga, unalima, unapanda na unasambaza mbegu, hii biashara ya wapi.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi humu ndani wanajua kwamba makampuni mengi yaliyofanya biashara bandarini yanafahamika na wamiliki wake ni akina nani. Ufisadi wa wakina Masamaki ule sio wa kwao peke yao, ndio maana hata ile kesi mahakamani imekuwa hivi, imekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu wanajulikana na hata Waziri anawajua, lakini sasa badala ya kushughulikia tatizo la msingi la watu wanaofanya ufisadi bandarini na ufisadi katika nchi, unatunga sheria; sheria peke yake haiwezi kumaliza ufisadi kwenye nchi. Sheria itakuwa tu inaelea na hili shirika litakufa, shirika litakufa ama bandari tutaipoteza. Tukinga’ang’ania NASAC kwa mfumo huu tutapoteza biashara ama shirika lenyewe litakuja kufa na walioua NASACO ya mwanzo si wapo? Rekodi si zipo?

Mheshimiwa Spika, wewe umekuwepo kwenye Bunge hili, unayajua haya mambo vizuri. Historia ya NASACO inajulikana, mgogoro wa wafanyakazi wa NASACO unafahamika; wafanyakazi wa NASACO wenyewe hawajalipwa mafao yao mpaka hivi sasa. Mnakuja kuanzisha shirika, wafanyakazi wa NASACO bado wanadai, wengine wamekufa wameacha watoto na wajukuu hawajalipwa haki zao. Tulipe hawa watu kwanza, tutapata laana bure ya kuanzisha shirika wakati tunadaiwa. Historia ipo wazi, tuache kuleta mambo haya ya juu juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri ajikite katika Muswada, aangalie bandarini tunahitaji kitu gani; fanya utafiti mzee. Kabla ya utafiti asije hapa Bungeni, yaani hana utafiti wowote kwa nini NASACO imeshindwa, hajatupa NASACO ya zamani kwa nini imeshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Shirika moja kubwa lilikuwa la peke yake nchi nzima, lenyewe ndilo linaloleta meli, linatoa mizigo bandarini, lilikuwa na jengo la NASACO pale mjini limekufa, majengo, magari na mali za NASACO wameuza na wafanyakazi wanawadai. Leo wanakuja na shirika jipya wanataka kuanzisha biashara upya, biashara watafanyaje wakati mwanzo wameshindwa. Sasa hivi ni wakati wa digital yaani atashindwa biashara asubuhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri angekuja sisi Wabunge angetushawishi sana kwamba tulishindwa kwa sababu hii. La pili ili sisi tuwaamini kwa sababu wamewaambia Watanzania Sera ya Ubinafsishaji inawezekana na kwamba uchumi wa nchi utakua kwa ubinafsishaji, leo wanarudisha NASACO na wanaacha ubinafsishaji wakati sera hiyo hawajaifuta kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Mheshimiwa Spika, Chama cha Mapinduzi bado kinaamini katika uwekezaji, ubinafsishaji, urasimishaji na kutoa ajira kwa vijana. Kwa njia hii imani hiyo wanaiweka kando na wanataka kurudisha ukiritimba wa mfumo wa dola kushika hatamu na kufanya biashara. Biashara imewashinda na sio kwa maneno yangu, ni kwa maneno ya Chama cha Mapinduzi yenyewe, Mheshimiwa Abdallah Kigoda, wakati huo akiwa Waziri, aliliambia Bunge hili kwamba Serikali imeshindwa kufanya biashara, inafanya ubinafsishaji na uwekezaji katika viwanda, siyo mimi, yako kwenye maandishi.

Mheshimiwa Spika, sasa nimalizie tu kwa kukushukuru.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala kwa kunijalia afya nzuri na kuniwezesha kuwepo hapa Bungeni kushiriki katika kupitisha Muswada huu muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Simu la Taifa linaloundwa ni zao la Kampuni au Shirika la Posta na Simu ambalo lilikuwepo huko nyuma. Serikali hii imeleta Muswada huu bila kufanya utafiti wa wapi tulipoanguka wakati wa Kampuni ya Simu ya Taifa (TTCL). Tulikuwa na Shirika la Posta na Simu, lilikuwa shirika moja lenye nguvu nchi nzima, Serikali ikaligawa hilo shirika wakatengeneza Kampuni ya Simu ya Taifa na Shirika la Posta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo tunarudi kuja kuanzisha Shirika la Simu la Umma bila kuangalia kitu gani ambacho Serikali ilikosea katika kubinafsisha Kampuni ya Simu ya Taifa. Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wakati TTCL inabinafsishwa, Mheshimiwa Profesa Mark Mwandosya, alisema yafuatayo, naomba nimnukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwandosya anasema:-

“Pamoja na nia njema ya kuanzisha Mashirika ya Umma, hatimaye yalikuja kuwa mzigo mkubwa kwa Hazina yetu. Asilimia kubwa yalitegemea ruzuku ya Serikali na baadhi yalikuwa mufilisi. Teknolojia ilikuwa imebadilika sana na ili kuyafufua ingegharimu Serikali na umma wa Watanzania kiasi kikubwa sana cha fedha. Uchumi wa nchi wakati ule usingeweza kubeba mzigo huo, ndipo Chama cha Mapinduzi wakati ule kiliporidhia Serikali ibakie na shughuli zake za msingi za utawala, ulinzi na usalama.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ilivyokuwa wakati Kampuni ya Simu inabinafsishwa ndivyo hali ilivyo hivi sasa. Kampuni ya Simu inaenda kuanzisha Shirika la Umma mwekezaji kwa mujibu wa taarifa zilizopo aliyepewa kuendesha TTCL kwa hisa asilimia 35, aliposhindwa kuendesha alifanya hujuma ya kung’oa mitambo yote iliyokuwepo katika Chuo cha TTCL kilichopo eneo la Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. Alikifunga chuo hicho na kung’oa mtambo wa kutoa ankara kwa wateja ambao kwa mujibu wa wahandisi wa kampuni hiyo ulikuwa bado una uwezo mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilitegemea Serikali ije na majibu ya hujuma iliyofanyiwa TTCL kabla ya kuanzisha Kampuni ya Umma ya TTCL, majibu hayo hayajaja. Hakuna majibu kwa nini mwekezaji aling’oa mitambo, kwa nini mwekezaji hakuja na mtaji na kwa nini Serikali inanunua hisa kwa fedha ambazo yenyewe iliweka kwenye kampuni ya simu. Ubinafsishaji mzima waTTCL ulitawaliwa na ulaghai, ubinafsi na mchezo mchafu wa kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya watu waliokuwemo wakati wa ubinafsishaji walichafuliwa majina yao kwa mbio za Urais kwa sababu tu walisimamia kitu ambacho kila mtu alikiona TTCL inafilisika. Kwa hiyo, hoja ya Waziri kwamba TTCL inaanzishwa ili kutoa huduma kwa umma, TTCL iliyopo sasa ni kaburi. TTCL haina nyenzo na haiwezi kuingia katika ushindani wa biashara wa sasa hivi. Serikali haina uwezo wa kuweka mtaji mkubwa kabisa wa kuifanya TTCL iweze kuingia kwenye ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini hizi hatua zinazofanyika bila kufanya utafiti, tutarudi hapa ndani ya miaka mitano au baada ya miaka mitano na historia itatuhukumu, tutarudi kuja kubinafsisha upya Shirika hili la Umma tunalolianzisha leo. Kwa sababu utafiti yakinifu, katika hotuba nzima ya Waziri hajaeleza Serikali imefanya utafiti wapi ilipokosea na kwa nini sasa inarudi kuja kumiliki shirika lake la umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea kwamba Serikali ingekuja na Muswada wa kuuza hisa za TTCL kwa wafanyakazi wa Kampuni ya TTCL ambao wamelitumikia Taifa hili na shirika lao tokea lilipoanzishwa baada ya kuvunjwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini Serikali inasema inamiliki hisa asilimia 100 bila kuwa na mipango endelevu ya kulikokoa Shirika hili la Simu la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo matatizo yaliyokuwepo kwenye uwekezaji, Waziri, kampuni ya MCI ambayo ndiyo ilikuwa wamiliki wa hisa asilimia 35 za TTCL waliuziwa hisa hizo kinyemela, mchakato haukufuata utaratibu na waliahidi kujenga njia za simu 800,100 pamoja na kulipa dola za Marekani milioni 120. Fedha hizo hawakulipa na njia za simu hawakujenga na Serikali ikatoa fedha nyingine kununua hisa zenyewe za TTCL. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwekezaji alitakiwa kuonesha waziwazi zabuni ya kununulia asilimia 35 za hisa za TTCL, pamoja na kueleza njia watakazofunga katika kipindi cha miaka minne hadi mwaka 2003. Kampuni inayoshinda zabuni haikuweza kufanya yote ambayo walikubaliana katika mkataba, lakini Serikali iliendelea kumbeba, kumkumbatia na kumpakata mwekezaji wakati ameshindwa kulinda masharti yote ya mkataba wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Serikali inatoa fedha za umma ambazo zilipaswa kwenda katika vijiji vyetu kulipia umeme, kulipia maji, kuhudumia wananchi wetu, lakini zinatumika kununua hisa ambazo ni mali ya Serikali. Jambo hili sisi hatuliungi mkono, pamoja na nia njema iliyopo lakini tunafikiri kwamba ni lazima tungeanzia pale ambapo Serikali iliishia, ilishindwa kuliendesha shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na nitachangia kwa kifupi sana. La kwanza, sisi kwenye Kamati ya Katiba na Sheria na jambo hili umemuuliza Mwenyekiti wetu kwamba hayo marekebisho ya mwisho ya Serikali yalikuja kwenye Kamati? Sasa mimi sitaki kuwa Jaji, lakini nikuombe utumie mamlaka uliyonayo ufanye uchunguzi Serikali walileta marekebisho ya mwisho kwenye Kamati? Kwa ufahamu wangu mimi hawakuleta; sasa nakuachia wewe, vyombo unavyo, kamera zipo kwenye Bunge, Mawaziri wapo hapa, Mwenyekiti yupo, Katibu wa Kamati wapo, waulize maelekezo yako walitekeleza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Sheria yoyote inapotungwa huwa ni lazima iwe inatafuta tiba na imetolewa mifanoi hapa nchi ya Ghana, ya Kenya na humo mote Sheria ilipotungwa kulikuwa na matatizo ambayo yalilazimisha kutungwa hiyo Sheria; Rwanda walipotunga Sheria ya Vyama vya Siasa walikuwa wanazuia mauaji ya kimbali yasiendelee, Kenya walikuwa wanazuia mauaji ambayo yalitokea mwaka 2007 ambayo yalizaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Sasa kumbe hapa nilivyosikia Waheshimiwa Wabunge sijui kama ndiyo dhamira ya Serikali, lakini nilivyomsikia Mheshimiwa Simbachawene na nilivyowasikia Wabunge wengine kumbe kuna tishio la nje ambalo mimi silioni la kuletwa Muswada huu Bungeni. Kwa sababu ukiuangalia huu Muswada ulivyokuja kwenye Kamati mwanzo unashangaa kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametambulishwa leo Bungeni hapa ni Profesa, Waziri wa Katiba na Sheria ni Profesa, Msajili wa Vyama vya Siasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, hawa watu wanaletwa Muswada Bungeni unapingana na Katiba ya nchi yaani sisi ambao siyo Wanasheria ndiyo tunakuja kuona vifungu vinavyopingana na Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inawezekana ikawa ni nia ovu na wamesema Mheshimiwa Ally Saleh amesema. Wameleta kifungu ambacho sasa hivi kwenye jedwali la marekebisho la mwisho kimeondolewa na Serikali ambalo limeletwa hapa mchana. Kifungu ambacho kilikuwa kinaruhusu vyama viungane, lakini Mheshimiwa Rais aliyepo madarakani alikuwa anapoteza madaraka yake, tunawauliza kwenye Kamati ninyi mnaruhusu vyama viungane, wanasema wote watapoteza nafasi zao, lakini Rais atabaki. Tunawauliza kwa Sheria ipi? Wanasema kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 42(3) lakini Ibara ya 42(3) wanaoitaja inasoma pamoja na masharti ya Katiba hii, masharti yaliyomo kwenye Katiba ni lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tungekuwa tunaingia kwenye nchi ambayo Mheshimiwa Rais akiamua kuunganisha vyama watu wakienda Mahakamani wanamzuia wanamwambia wewe siyo Rais. Hivyo vitu hawavioni! Sasa hivi wameondoa kabisa maana yake nini, maana yake wanataka Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa mfano akitaka kuhama chama kwa sababu Mwalimu Nyerere alisema kwamba nafuata chama kwa sababu ya sera na usafi wake na uadilifu wake, nikikikuta chama hiki CCM kimepoteza malengo hayo mimi nitakihama kwa sababu CCM, siyo baba yangu mzazi, wala siyo mama yangu mzazi. Sasa Mheshimiwa Rais Magufuli leo kwa Muswada huu hata akiiona hii CCM chafu kweli kweli na haisafishiki hawezi kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo inawezekana hawa watu walioleta huu Muswada wameona kwamba pengine wapo watu wanataka kumpinga Mheshimiwa Rais 2020 ili Mheshimiwa Rais akitoka aende na chama chake na wale awaache kule wamemzuia, yaani Muswada, dhamira inayoonekana. Kwa hiyo… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kubenea, naomba ujielekeze tu kwenye Muswada maana hayo unayoyasema utapata tabu, sasa hivi watasema uthibitishe yatakupa tabu kwa sababu siyo ya kweli. Endelea Mheshimiwa Kubenea.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni jambo la ajabu kwamba Msajili wa Vyama ndiye anakuwa mlalamikaji, Mheshimiwa Zitto ameeleza kidogo, Msajili wa Vyama anakuwa mwendesha mashtaka, Msajili wa Vyama anakuwa Jaji na Msajili wa vyama anakuwa bwana Jela. Tumewaambia kwenye Kamati kwamba mnatoa mifano ya vyama vya mipira; ulitolewa mfano na mdau mmoja kwamba hata Chama cha Mpira wa Miguu kinaadhibu, tukasema sawa, lakini kwenye Chama cha Mpira wa Miguu kuna Kamati za Nidhamu, Kamati za Rufaa na Kamati mpaka za ligi, kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa hata Baraza la Vyama vya Siasa halikushirikishwa katika Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamekuja kwenye Kamati wakati wa kutoa maoni yao, wamekushukuru sana, sana na shukrani hizo zilitolewa na Mheshimiwa Shibuda kwamba wewe ulifanya juhudi kubwa za kuwaita Viongozi wa Vyama vya Siasa na ukawawezesha kuishi Dodoma kutoa maoni yao, lakini Msajili wa Vyama ambaye anaunda Baraza la Vyama kwa mujibu wa Sheria alikataa kukutana nao na Muswada huu haukupitia kwenye baraza kwa mujibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Msajili wa Vyama vya Siasa ni mlezi wa vyama, Msajili anapogeuka kuwa Hakimu, anapogeuka kuwa mwendesha mashtaka, anapogeuka kuwa Polisi, anapogeuka kuwa bwana Jela, dhamira njema…

MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

SPIKA: Mheshimiwa Kubenea kuhusu utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, muda wangu umebaki mwingi na naomba niendelee. Muswada huu amekuja kwenye Kamati Waziri kuhusu kipindi cha mpito cha utekelezaji wa Sheria hii, tukasema Serikali ilikuja na mapendekezo kipindi cha mpito kiwe miezi sita tukawaambia hivi miezi sita unaweza ukaitisha mkutano mkuu wa chama kwa sababu Muswada huu ukipita hapa Bungeni vyama vyote vinalazimika kubadilisha Katiba zao na hali ya vyama vyetu tunaijua, hata chama tawala kimebadilisha ratiba za vikao vyake kwa sababu ya uwezo wa kiuchumi, ndivyo tulivyoambiwa. Sasa tukasema angalau basi uwe mwaka mmoja, angalau basi iwe tarehe 30 ya Septemba mwaka 2020 ili vyama vinapoitisha mikutano yao mikuu ya uteuzi wa wagombea zifanye pia mabadiliko ya Katiba zao, lakini maoni yale hayakuzingatiwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeambiwa kwamba vyama vinaweza vikashirikiana, vyama vinaweza vikaungana, hiyo ya kuungana wameitoa wapi?

SPIKA: Ni kengele ya pili Mheshimiwa Kubenea, nakushukuru sana kwa mchango wako.