Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omary Tebweta Mgumba (61 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nitoe mchango wangu katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa letu. Nichukue nafasi hii kuwashukuru Wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kwa dhamana kubwa waliyonipa kuwawakilisha ndani ya Jimbo hili. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya na uhai wa kufika siku hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nijielekeze katika suala la miradi mikubwa ile, hasa suala lile la miradi mkubwa wa Village City ambao uko Mkulazi unapatikana katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ndani ya Morogoro Vijijini katika Jimbo ninalotoka mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema nijielekeze hapa kwa sababu huu siyo mradi wa kwanza kupewa ndani ya Jimbo hili lakini utekelezaji wake unachukua muda mrefu. Kwa mfano, tuna mradi wa bwawa la Kidunda mpaka sasa hivi unaenda una suasua. Hata hivyo, tunaishukuru sana Serikali kwa kutupa mradi huu, lakini naomba nisisitize katika utekelezaji ufanyike haraka iwezekanavyo; hasa katika kuandaa miundombinu rafiki kwa ajili ya uwekezaji. Kwa mfano, sasa hivi Mkulazi vijiji vyake vyote vinne ambavyo ni Usungura, Chanyumbu, Mkulazi yenyewe na Kidunda vyote havina mawasiliano, vyote barabara haipitiki mwaka mzima, lakini pia hata maji yenyewe ndiyo hayo ya kubahatisha pia havina umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeiomba Serikali ingekuja na mpango kabla ya kuwekeza huo mradi mkubwa kuandaa hayo mazingira ili kuwavutia wawekezaji, hata wale watu wenye nia ya kuja kuwekeza ndani ya Morogoro vijijini, ndani ya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki wawe na moyo kwamba mazingira yanaruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu suala la viwanda, Morogoro ambayo ndiyo Mji wa mwanzo kabisa baada ya uhuru Serikali iliamua kabisa kuitenga mahsusi kwa ajili ya viwanda. Tunashukuru kwa hilo na kulikuwa na viwanda vingi tu ambavyo viikuwa vinasaidia ajira ndani ya Morogoro vijijini, Morogoro Mjini na Taifa kwa ujumla, lakini viwanda vile vingi havifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kabla ya kuja na Mpango wa Pili wa viwanda wangekaa na hawa ambao waliobinafsishiwa ili kujua changamoto gani ambazo zimewakabili mpaka sasa haviwezi kuzalisha vile viwanda na kutoa ajira kwa Watanzania. Tulikuwa na viwanda vya Moro Shoes, Viwanda vya Ngozi, Viwanda vya Mafuta, Viwanda vya Nguo vyote hivyo vimekufa vimebaki vya Tumbaku na vile vya Sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwauliza wale wa wawekezaji wanatuambia jambo moja tu, wanasema kwamba viwanda tukizalisha hapa havilipi, kwa hiyo, ndiyo maana rai yangu Serikali ni vizuri mkakaa na hawa mliowabinafsishia mkajua changamoto zao, hata kama mnataka tuvichukue tena lakini itatusaidia kubaini changamoto mapema ambazo zitatusaidia katika Mipango mipya kwa hapo kuanza kwenda mbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu viwanda hivyo hivyo, suala la Viwanda vya Tumbaku kuwa Morogoro. Morogoro kwanza watu tusisahahu kwamba na sisi ni wazalishaji wa tumbaku, lakini pia unapoanzisha kiwanda mahali popote, wote humu Wabunge tungetamani kila Jimbo kuwe na kiwanda. Hata hivyo, kiwanda unaanzisha kwa kutugemea cost benefit, unatazama wapi nikiweke hiki kiwanda ambacho kitanilipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya makampuni Morogoro ilijaliwa kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe katika kuwa pale, kwa sababu ndiyo mikoa michache ambayo ilikuwa na rasilimali nzuri tangu wakati huo, lakini pia ndiyo sehemu iliyokuwa na maji ya uhakika, kulikuwa na umeme wa uhakika, lakini pia Morogoro ndiyo karibu na Dar es Salam ambako ndiyo kuna bandari kuu ya kusafirisha mazao. Kwa ushahidi huu ndiyo maana hata sasa hivi wafanyabiashara binafsi bado wanaitamani kuwekeza Morogoro kwa sababu ya jiografia na hali ya hewa iliyokuwepo Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii Serikali muendelee kutupa nafasi kubwa zaidi Morogoro kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kwa sababu mazingira ni rafiki ambayo yanavutia na yana gharama nafuu sana ya uendeshaji. Nitoe mfano tu, hiyo tumbaku inazalishwa songea, Morogoro, Iringa na Tabora na mikoa mingine. Siyo rahisi kwa mwekezaji kuweka kila kiwanda katika kila mkoa ni kwa sababu inategemea na wingi wa raw material. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie kuhusu wajasiriamali. Mpango huu umekuja lakini umeweka nje wajasiriamali, kwa sababu tukizingatia hivi maendeleo ya viwanda ambao ndiyo Mpango wa muda wa Pili huu unakuja utategemea sana maendeleo ya kilimo. Hata hivyo, wajasiriamali wa nchi hii, hususani wanaojishughulisha katika mazao ya kilimo wamewekwa kando ya mfumo wa soko letu hapa Tanzania. Leo hii mfanyabiashara au kijana aliyemaliza elimu ya Chuo Kikuu au elimu ya sekondari ambaye anataka kujiajiri mwenyewe hususani katika shughuli za kilimo hana fursa hiyo kwa mfumo wa soko uliokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana aneyesifiwa mfanyabiashara mzuri ni yule anayefanya importation, akienda nje ya nchi akinunua mazao kitu chochote bidhaa amuuzie mkulima huyo anaruhusiwa na atapewa vigelegele, lakini yule ambaye anakwenda kununua mazao kwa mkulima afanye exportation ataambiwa mwizi, kibaraka, mnyonyaji, kibaraka wa Wahindi na majina yote ya ajabu ajabu atapewa huyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali waje na Mpango mzuri jinsi ya kuliboresha soko letu ili sekta hii ya sehemu hii wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa waweze kushiriki kikamilifu katika ununuzi wa mazao ya biashara kutoka kwa wakulima moja kwa moja. Kwa sababu sasa hivi mfumo uliopo umewatenganisha kati ya mnunuzi na muuzaji. Leo hii mnunuzi hajui mzalishaji anahitaji nini na mzalishaji hajui mnunuzi anahitaji nini kwa viwango ambavyo wanavitaka. Matokeo yake baadaye biashara zetu zinakosa masoko baada ya uzalishaji na hatimaye wakulima wetu wanakuwa watu wa kuhangaika, leo wanazalisha zao hili, kesho zao lile, hakuna zao moja ambalo ana uhakika nalo la kumuinua kimaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nizungumzie mgogoro wa wafugaji na wakulima. Sisi Morogoro kiasili ni wakulima lakini sasa hivi tumevamiwa kwa kiasi kikubwa na wafugaji wasiofuata sheria, taratibu hata na kanuni zile za kufuga. Baada ya kuchunguza muda mrefu nimeona wanahama kwa sababu wanakosa malisho maji huko wanakotoka. Niiombe Serikali ije na mpango mkakati wakuboresha miundombinu ya wafugaji huko wanakotoka na kuwapa elimu ya kufuga kisasa ili waendele kubaki huko ili janga ambalo mnatuletea Morogoro limeshakuwa kubwa linatuzidi uwezo wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kwa mfano jana tu, wakulima wangu kule Kata ya Tununguo na Vijiji vyake wamepigwa na wafugaji. Mfugaji anakuja anaingia ndani ya shamba anamwambia mkulima kwamba, mifugo ni muhimu kuliko chakula wanageuza mazao ya wakulima ndiyo chakula cha mifugo. Wanawatandika bakora hata wakienda sehemu yoyote hawasikilizwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ije na Mpango mkakati wa kumaliza tatizo hili la wafugaji nchini, hasa kujenga miundombinu ya wafugaji sehemu za wafugaji na kupima ardhi yote ili tuweze kujua eneo la wafugaji lipi na wakulima? lakini hasa kuimarisha hiyo miundombinu ya kifugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho haina maana kwa umuhimu, kuhusu suala hapo hapo suala la kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo na najua maendeleo ya viwanda vinakuja baada ya maendeleo ya kilimo kuwa endelevu. Serikali kwenye Mpango wenu mmesema kabisa haijafanya vizuri kwenye kilimo, bila kuimarisha kilimo hata hivi viwanda tunavyotaka kuviweka vitakuja kukosa raw material baadaye italazimika tu-import raw material kwa ajili ya viwanda hivyo. Niishauri Serikali ije na Mpango Mkakati thabiti wa kuimarisha kilimo, kuongeza uzalishaji, kuwavutia masoko ili ku-adress matatizo ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza, kabla ya yote naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, maana yake nisije nikatiririka mpaka nikajisahau kama ule upande wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya bajeti ambayo inagusa, inakidhi na inajibu changamoto nyingi za Watanzania mpaka imewaogopesha upande wa pili kwa sababu watachangia nini wakati Waziri Mkuu amemaliza kila kitu na ukija kuchanganya na utendaji wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewamaliza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa wamekuwa kigeugeu sana. Tuwaambie kabisa CCM imejaa viongozi wa kila aina. Awamu ya Nne hawa hawa walikuwa wanalalamika Serikali haichukui maamuzi, ikichukua maamuzi inachelewa, tukawaambia sasa tunaleta Rais ambaye anachukua maamuzi haraka. Sasa wameanza kulalamika, wanalalamika nini, ni kwa sababu ameshawapiga Dokta John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza bajeti ya Waziri Mkuu kwa hali halisi, kuna Mbunge mmoja huku huwa anasema kwamba maneno yanadanganya lakini hesabu hazidanganyi. Nataka nimpeleke huko huko kwenye hesabu, hii bajeti imemaliza kila kitu, ukurasa wa mwisho kabisa kwenye fedha pale zilizopitishwa kwa sababu Waziri Mkuu ameonesha kwamba anaenda kutokana na maneno wanayozungumza Serikali ya Awamu ya Tano na vitendo vinaelekea vitakuwa hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tu kwenye fedha alizoomba tuzipitishe ni Sh. 236,759,874,706 wakati mwaka 2015/2016 fedha zilizopitishwa zilikuwa ni shilingi milioni 391.966 kwa kukaribisha, ni punguzo zaidi la asilimia 40 maana yake ni jinsi Serikali ilivyojipanga kubana matumizi na kuleta bajeti halisi ambayo inalingana na uwezo wa nchi yetu. Pia data hizo hizo, katika OC, mwaka 2015/2016 ilikuwa shilingi bilioni 349.288 mwaka huu OC imepunguzwa mpaka imekuwa shilingi bilioni 71.564, ni punguzo la asilimia zaidi ya 79.5, kujibana kwenye matumizi ya hovyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupunguza pesa hizo katika bajeti halisi ameenda kuziongezea kwenye masuala ya maendeleo. Suala la maendeleo mwaka 2015/2016 ilikuwa ni shilingi bilioni 42.6 lakini bajeti ya Waziri Mkuu hii aliyoileta hapa ni shilingi bilioni 165.196, ni sawa na ongezeko la asilimia 122.5. Ndiyo maana nimesema naunga mkono hoja siyo kishabiki kwa uhalisia na namba halisi alizoleta Waziri Mkuu. Inaonesha ni jinsi gani bajeti hii inavyoenda kuwakomboa Watanzania walio wengi ambao kama anavyosema Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwamba waliteseka muda mrefu sasa nao ni zamu ya kuteseka upande wa pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema upande wa pili unaona wanavyolalamika ni baada ya hii kasi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kutumbua majipu na hasa baada ya jipu kumfikia mkwe wao. Baada ya mkwe kuwekwa ndani ndiyo hawa wapambe wanaanza kulalamika na kujihami wanaona huu moto unakuja. Niwatoe shaka tu kwamba aliyekuwa msafi ataendelea kuwa msafi, wale wachafu mkono wa sheria utaendelea kuwafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya facts hizo, naomba nishauri Serikali katika mambo yafuatayo:-
Kwanza suala la ajira, naiomba Serikali izingatie sana katika kuweka mipango thabiti kwa ajili ya SME kwa maana ya wafanyabiashara wadogo na wa kati na hasa ukizingatia nchi yetu watu wengi wamejiajiri kwenye kilimo na kilimo ndiyo kinatoa ajira nyingi kwa maana ya kilimo na wafanyabiashara wa kilimo na watu wa namna hiyo. Kuna mambo mengine ambayo yako kisheria kwa mfano mfumo stakabadhi ghalani upo kisheria lakini ni mfumo ambao unawatoa SME na wafanyabiashara wadogo kushiriki katika biashara ya mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali itafute namna yoyote inavyowezekana ku-accommodate kundi hili kubwa la SMEs jinsi ya kushiriki katika mfumo huo ili kuweza kukabiliana na tatizo kubwa la ajira na ukizingatia Serikalini ajira hamna hata huko sekta binafsi siyo nyingi kiasi hicho kama tunavyofikiria, nyingi tunategemea watu wajishughulishe katika ujasiriamali, mambo ya biashara na mambo mengine. Ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu utaona hata kule anasema changamoto mojawapo ni urejeshaji wa mikopo kwa sababu vijana wanakwenda kujiajiri lakini wanakosa hizo fursa za kujiajiri kwa sababu fursa zimekuwa chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiwatengenezea vizuri namna ya kuwasaidia kwa ajili ya kushiriki katika ujasiriamali hata urejeshaji wa mikopo tutakuwa tumetatua tatizo hilo. Hata hizi fedha ambazo Serikali kwa nia nzuri inataka kuzi-allocate kwa ajili ya kukopeshana kwenye kila kijiji shilingi milioni 50, lakini lazima tuwatafutie kazi za kufanya la sivyo utawapa shilingi milioni 50 kama kazi hakuna watu watakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuishauri Serikali kwenye suala la maji hasa kwenye Bwawa la Kidunda. Bwawa la Kidunda nimeanza kulisikia hata shule sijaanza lakini mchakato wake umekuwa mrefu ukihusisha mambo ya mazingira na kadhalika. Tangu miaka 80 wazee wengine wananiambia tangu miaka ya 70 Kidunda inazungumziwa lakini sasa hivi Serikali imefika mahali pazuri naomba utekelezaji wake uende haraka sana. Kwa kumaliza utekelezaji wa mradi huu Jiji la Dar es Saalam ambalo linategemewa kiuchumi na Tanzania zaidi ya asilimia 70 utaweza kupata maji ya uhakika na viwanda vitaweza kwenda, lakini na sisi huku Morogoro tutaweza kuneemeka na fursa zinazokuja na Bwawa la Kidunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuishauri Serikali kuhusiana na migororo ya ardhi. Serikali imekuja na mpango mzuri wa majaribio katika Wilaya za Mvomero, Ulanga na Kilombero, naipongeza sana. Naomba katika mpango huu kwa sababu sasa hivi Morogoro ndiyo tunaongoza kwa migogoro ya ardhi na sababu kubwa ni kwamba ndiyo ardhi ambayo ina rutuba lakini kuna mashamba pori mengi na pia tuko karibu na soko kubwa la nyama kwa maana ya Dar es Salaam na kwenda nje, lazima mtu apitie Morogoro kwenda ku-export.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nia nzuri ile ya majaribio kwa Wilaya tatu tu ningeomba ingefanyika kwa Mkoa mzima wa Morogoro ili kuondoa hili tatizo, ukiwabana huku wanahamia upande wa pili. Mtamaliza huku watatoka upande wa pili wataenda kule kwa sababu ilishatokea katika ile Operesheni Tokomeza walianza Kilombero wote wakaja kwetu Morogoro Vijijini, operesheni ilivyokwisha wakarudi upande ule ule. Ni vizuri jambo hili lingefanyika kwa mkoa mzima ili kuwadhibiti vizuri hasa wale wavamizi waliokuja bila utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kushauri katika suala la afya. Wilaya ya Morogoro ni kongwe lakini mpaka leo haina Hospitali ya Wilaya. Wilaya hii ina Halmashauri mbili, Manispaa na Morogoro Vijijini lakini mpaka leo hii hatuna Hospitali ya Wilaya. Naomba katika mpango huu ingeingizwa pia na Hospitali ya Wilaya ili tuondoe adha ya watu wa Halmashauri hasa wa Morogoro Vijijini ambao wanatembea zaidi ya umbali wa kilometa 180 kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nataka niishauri Serikali katika suala la uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji. Wote tunakubaliana miongoni mwa vyanzo vya maji katika nchi yetu vipo katika milima ya Uluguru kwa maana ya kule Kinole na Tegetero mpaka Mgeta, lakini utunzaji wa vyanzo hivyo inaachiwa Halmashauri…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nachukua fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Kilimo kwa hotuba yao nzuri na mikakati waliyoiweka katika mipango yao ya kilimo. Kwanza, nachukua fursa hii kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini nina ushauri kidogo wa kuongezea nyama katika mipango ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Waziri anaposema kwamba ukitaka mali utaipata shambani na anasema vijana wengi tuelekee huko ndiko tutakapoipata mali. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, mali hiyo huko inapatikana ukiwa na ardhi tu na miongoni mwa matatizo makubwa yaliyopo sasa hivi nchini kwetu ni migogoro ya ardhi hasa kwa wakulima na wafugaji, kama alivyoielezea vizuri katika kitabu chake, lakini kwa bahati mbaya, na ninaisema kwa bahati mbaya kwa sababu naujua umahiri wa Mheshimiwa Waziri, lakini hakuiwekea mikakati wala mipango kwa ajili ya kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii mizuri yote ambayo mmeiweka bila kutatua tatizo la wakulima na wafugaji, yote ni sifuri kwa sababu tuna tatizo kubwa sana huko vijijini na waliosabisha tatizo hili la wakulima na wafugaji ni Wizara ambao wanahusika kwa namna moja au nyingine. Wanatoa hatimiliki, wanauza mashamba bila kuzingatia hali halisi ya field ikoje. Unakuta wananchi kwenye sehemu husika wameishi miaka 12, 15, zaidi ya 20 lakini anakuja mtu anapewa hatimiliki, ndiye mmiliki halali. Mifano iko mingi, hasa nichukulie Jimbo langu, labda ndipo unaweza kunielewa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shamba la Kidago ambalo zamani lilikuwa la Uluguru Tailors. Ni shamba ambalo wakulima pale wamekaa zaidi ya miaka 40. Leo hii kapewa mwekezaji na kesi iko mahakamani. Sitaki kulizungumza sana kwa sababu lipo, lakini nakuomba Mheshimiwa Waziri uje ili uone hali halisi ilivyo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili, kuna shamba la Pangawe, ambapo pale kuna mradi wa mfano, walikuwa wa KOICA (Corea) ndiyo wamewekeza. Leo hii tuna tatizo kubwa sana na mwekezaji. Nakuomba Mheshimiwa Waziri uje katika jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki ili tuweze kukaa na mwekezaji huyu tuone ni namna gani tunaweza kumaliza tatizo hili; kwa sababu nia nzuri mliyokuwanayo, bila kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji tatizo hili litakuwa kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine uko kule mpaka Kata za Maturi, Kidugaro, kwenye vijiji vya Ng‟ese huko matatizo ni hayo hayo. Kwa hiyo, ndiyo maana dhamira yako kuu ya kusema vijana twende huko, tunakwenda huko lakini ardhi hakuna. Nina ushahidi ndiyo maana unaona kuna migogoro ya ardhi kila siku nchini kote. Kwanza uje na mkakati, nafikiri baada ya kuja kutoa majumuisho yako, uje utuambie, Serikali na Wizara yako imejipanga vipi katika kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji ili tuwe salama tuweze kuongeza uzalishaji katika nchi hii? Leo hii wakulima wa nchi hii hususan wa Morogoro Kusini Mashariki, zamani tulikuwa tunalinda nguruwe na kima, sasa hivi tunalinda ng‟ombe ili wasile mavuno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Sisi Morogoro Vijijini ni wakulima wazuri wa matunda, lakini sijaona katika kitabu chako mpango mkakati kwa ajili ya viwanda vya kusindika matunda, kwa ajili ya kutengeneza soko la uhakika kwa matunda yanayooza katika sehemu kubwa ya nchi yetu hususan Morogoro Vijijini. Sisi ni wakulima wazuri wa ndizi, machungwa, machenza na maembe katika vijiji vya Tegetero, Kinole, Kiloka na sehemu nyingine zote, lakini leo hii matunda yanaoza mtini wakati mwingine kwa kukosa soko la uhakika, hasa viwanda vya kusindika mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, niende kwenye Jimbo langu tena kuhusu Shamba la LMU lililoko Ngerengere. Lile shamba ni la kuzalisha mifugo ya kisasa. Shamba lile lina ukubwa zaidi ya heka 11,000 lakini utaishangaa Serikali kuna ng‟ombe 900 tu, mbuzi 200, nguruwe 50 na eneo lote limebaki ni pori. Hapa ninashauri mambo mawili, kwanza, naiomba Serikali kuwekeza nguvu kubwa katika uendelezaji wa shamba hili ili lengo lililokusudiwa litimie liweze kutufaidisha watu wa Morogoro Kusini Mashariki hususan Tarafa ya Ngerengere.
La pili, ushauri wangu na ombi kwa Serikali, Ngerengere sasa hivi imekuwa Mji Mdogo, imekua na bahati mbaya hatuna eneo lolote la upanuzi kwa sababu tumezungukwa na vikosi vinne vya Jeshi. Tunamba ombi maalum Serikalini, angalau tupatiwe heka 1,500 katika shamba hili ili tuweze kuliendeleza na shamba hili pia vigawiwe vitalu kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili kuendeleza maendeleo ya watu wa Morogoro Kusini Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie katika Bodi ya Korosho na bodi nyingine za mazao nchini. Miongoni mwa majipu yaliyopo katika nchi hii, hizo bodi za mazao ndiyo matatizo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mmoja tu katika Bodi ya Korosho, hapa wadau wa korosho wamezungumza mengi kuhusu makato yanayotokea huko. Miongoni mwa kazi nyingi za Bodi ya Korosho ni pamoja na kuhamasisha uzalishaji, lakini pia usindikaji (processing), lakini pia kutafuta masoko. Haya yote matatu Bodi ya Korosho inakwenda kwa kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja, mwaka 1973 uzalishaji wa Korosho tulifikia tani 145,000 wakati wa Mwalimu Nyerere, leo hii baada ya miaka zaidi ya 30 tunazungumza uzalishaji tani 154,000. Kwa ushahidi hata nchi zilizokuja kuomba mbegu hapa, kama Vietnam leo zimeshatupita, lakini bodi hii kila mwaka wanakupa projection, wanakwambia tunazalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kuhusu kodi nyingi zilizokuwepo kwenye Bodi hii ya Korosho. Mkulima analipa zaidi ya shilingi 640 kwakilo moja ya korosho, ambapo tukichukua tu hesabu hii iliyokuwa ni projection ya mwaka wa 2015 ambayo ni tani 154,000, zaidi ya shilingi bilioni 99 wakulima wa korosho wanaiacha. Hiyo fedha bei ya korosho ingeachwa kwa mkulima ingekuwa kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mkulima wa Korosho anakatwa shilingi 207 huko kijijini, kwa maana ya five percent tunazungumza shilingi 60 kwenye ushuru wa Hamashauri, shilingi 50 ni Chama cha Ushirika, shilingi 10 ni kwa ajili ya mtunza ghala, shilingi 20 Cooperative Union, shilingi moja kwa ajili ya kikosi kazi. Makato hayo jumla yake inafika 207. Achana na hayo, anaambiwa kuna export levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa kuwa na export levy ni kwa ajili ya ku-encourage investment katika nchi yetu. Kwa miaka yote ambayo tumekuwepo hapa, Bodi ya Korosho inasema inafanya investment ya ubanguaji wa Korosho nchini. Inachukua 15 percent ya FOB price ambapo kwa mwaka wa 2015 kwa sababu FOB price ilikuwa ndogo, wakachukua bei elekezi ya shilingi 2,900 ni sawasawa na kukata shilingi 435 sawasawa na shilingi bilioni 69. Hakuna kiwanda chochote kilichowekezwa, kitu ambacho… (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kufika siku ya leo, kunipa afya na uzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba niwape pole Wapiga Kura wangu wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Vijijini kwa ujumla kwa mafuriko makubwa yaliyowakuta ya mvua ambapo mashamba yao yote yameharibika na mvua hiyo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Dkt. Kebwe na Mkuu wa Wilaya kwa hatua yao waliyoichukuwa ya kutusaidia chakula ingawa kidogo lakini siyo haba, kimesaidia sana waathirika hawa! Nachukua fursa hii kuiomba Serikali, tunaomba misaada zaidi ya chakula katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nampongeza sana Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hotuba yake nzuri ambayo inaonyesha dhamana aliyobeba ya kutimiza matakwa na ndoto za Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Kwa sababu Rais wa Awamu ya Tano tangu anaomba kura mpaka sasa anajipambanua kwamba Serikali yake itakuwa ni ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtie moyo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara angalau ameanza kuleta mpango. Pamoja na wengine wanasema kwamba umekuja na mpango lakini fedha ambazo umeziomba ni chache sana, kuna tatizo moja ambalo kama wazungu wanavyosema, ukitaka kumnyima kitu Mwafrika, kiweke kwenye maandishi. Kwa sababu umeongelea vizuri kwenye ukurasa wa 140 kwenye mikakati yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa naomba ninukuu na umesema; “kuhamasisha sekta binafisi, kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi za hapa nchini na kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya vifungishio (packaging) na kadhalika.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni nini maana yake? Maana yake ni kwamba siyo Serikali ndiyo itajenga viwanda, bali ni sekta binafisi ndiyo itajenga viwanda. Kazi ya Serikali itakuwa ni kuweka mazingira mazuri ya kuivutia sekta binafisi kuja kuwekeza katika viwanda na hatimaye kutoa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzetu wanaosema kwamba bajeti ni ndogo, nafikiri kwamba hiki kitabu kama ulivyosema au tulivyokiona ni kikubwa sana, watu wanaona uvivu kukisoma chote. (Makofi)
La pili, Mheshimiwa Waziri unalaumiwa na unaambiwa kwamba mpaka leo miezi sita haujaanzisha kiwanda chochote. Hawa wenzetu ndiyo maana tunasema wenzetu vigeugeu! Juzi tu hapa wamekuja walikuwa wanailaumu Serikali hii kuhusu kuhamisha fedha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kuwahudumia Watanzania. Leo hii ndani ya miezi sita, hili ndilo Bunge la Bajeti ya kwanza la Serikali ya Awamu ya Tano; kwa fedha gani ungeweza kuitumia kujenga viwanda hivyo ndani ya miezi sita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ndiyo maana ameleta hapa sasa tumpe ili mwakani akija ndiyo tumkabe koo. Kwa hiyo, niwaombe tu ndugu zangu kwamba pamoja na kwamba tunatamani sana hivyo viwanda vijengwe, lakini haviwezi kujengwa bila kupitisha bajeti na mipango aliyoileta katika Bunge hili na hiyo ndiyo kazi yetu sisi Wabunge, tumpitishie halafu tuje tumhukumu mwakani akija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, naomba nichangie katika mpango wenyewe aliouleta. Mheshimiwa Waziri kama ulivyosema, miongoni mwa changamoto zinazowakabili wawekezaji wengi ni malighafi isiyokuwa ya uhakika, maana yake nazungumzia viwanda ambavyo vipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangaze interest, maana unaweza kusema mimi nazungumzia korosho. Mimi niliwahi kufanya kazi katika kampuni inayohusika na mazao ya biashara miaka 19 kwa ajili ya exportation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoongelea nina uzoefu kidogo wa kujua ni changamoto gani ambazo wanakumbana nazo hususan kwenye korosho, pamba, kahawa, mbaazi, dengu, choroko, mpunga na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie changamoto zinazowakabili wawekezaji wa viwanda vya korosho, kwa sababu viwanda hivi vinabeba uchumi mkubwa sana hasa kwa wakulima wa Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na sehemu ndogo ya Mkoa wa Morogoro katika upande wa Mkulazi kule tulikopakana na Kisarawe. Ndiyo maana nafarijika na hili kulizungumzia mara nyingi kwenye upande wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi kama nilivyowahi kusema mwanzoni, sababu mojawapo ambayo wawekezaji wengi wamefunga viwanda vya kubangua korosho, miongoni mwa sababu mojawapo ni mfumo wa stakabadhi ghalani ambao hauwapi fursa wawekezaji wa ndani kupata raw materials.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mfumo unaoenda kuwashindanisha wawekezaji wa ndani wenye viwanda pamoja na wabanguaji wa India kwenye uwanja mmoja. Haiwezekani hata siku moja mwenye kiwanda cha ndani atafute raw materials mpeleke kwenye mnada akashindane na wabanguaji wa India, hawezi kupata raw material. Ndiyo maana uliona sababu, kulianzishwa viwanda zaidi ya 10, tulishafikia kubangua zaidi ya tani 50,000, nchini leo vyote vimefungwa vimebaki viwili tena vinasuasua!
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo jambo jepesi, mtu kawekeza mtaji wake, ka-run kiwanda zaidi ya miaka mitano, leo anafunga na Serikali tumekaa kimya, wanahamishia nchi za wenzetu za jirani, kuna tatizo! Naomba kushauri katika hili, kama kweli tunataka kuwavutia wawekezaji wengi waje kwenye kuwekeza Tanzania husasan katika viwanda vinavyotumia malighafi za Tanzania, kwa mfano kama korosho, ni lazima tuwatengenezee mazingira mazuri ya kuhakikisha wanapata malighafi hiyo, la sivyo itakuwa ni ndoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa mfano tu, kwa mfano, huwezi kushindana na India kwa sababu India wenyewe ukizungumza korosho, unazungumza siasa za India. Wale wana uwezo wa kubangua tani 1,600,000, lakini uzalishaji wao ni tani 600,000 tu. Kwa hiyo, ni lazima wanahitaji tani milioni moja kutoka nchi mbalimbali. Ndiyo maana wanawapa mpaka incentive ya 2% kwa ajili ya mtu ku-export korosho iliyobaguliwa kutoka India, Tanzania kwetu hakuna! Pia mtu akibangua kule, by product kwa maana ya vipande vya korosho, kwa maana ya maganda ya korosho, yote ni biashara lakini Tanzania hakuna. Kwa hiyo, kuna incentive kubwa zaidi India kuliko Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili, tuweke kabisa Sera ambayo inatambulika na itawavutia wawekezaji kwamba mtu yoyote anayewekeza kwenye Korosho hapa Tanzania, tutahakikisha anapata raw material kwanza kwa ajili ya kutosheleza kiwanda chake kwa mwaka mzima, ndiyo turuhusu mnada mwingine kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo watakuja, kwa sababu hata sera yetu nchini hairuhusu ku-import raw material kutoka nje, wakati nchi nyingine kama Vietnam na India wanaruhusu ku-import raw material kutoka nchi nyingine. Sababu ni nini? Kumpunguzia gharama za uzalishaji huyu mwekezaji. Kwa sababu usipomruhusu a-import raw material kutoka nchi nyingine, ukizingatia korosho ni biashara ya msimu ya miezi mitatu, maana yake unamlazimisha mwekezaji wa Tanzania, kama ana kiwanda cha kubangua tani 50,000 anunue hiyo raw material ya 50,000 kwa miezi mitatu na ai-store.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana nyingine gharama itakuwa kubwa kwenye storage, kwenye mtaji, kwenye weight loss, kwenye running na kwenye mishahara kwa ajili ya walinzi na wafanyakazi wengine kulinda hiyo, kitu ambacho kwingine hamna. Wanaruhusu ndani ya miezi mitatu kwa sababu biashara ya korosho ni rotation business in the world.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii biashara, watu wanazunguka, wanunuzi ni hao hao. Miezi mitatu wako Tanzania, baada ya Machi wanakwenda India mpaka Juni; baada ya Juni wanakwenda Afrika Magharibi kwa maana ya Nigeria, Guinea Bissau na Ivory Coast. Kwa hiyo, mtu ana fursa, atakuja kununua hiyo mwezi Oktoba kwa ajili tu ya kutumia hiyo miezi mitatu, baada ya hapo anakwenda sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda siyo rafiki sana, nitakuona Mheshimiwa Waziri nikupe mchango zaidi katika hili ili ukusaidie katika kuwekeza katika kilimo hususan mazao ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nisije kusahau nyumbani, sisi ni wakulima wa matunda na ninakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mwijage kwa juhudi zako kubwa unazozifanya kwa ajili ya kutukumbuka watu wa Morogoro hususan kwenye kilimo cha ndizi na kututafutia wawekezaji kwa ajili ya kiwanda cha ndizi ili tuweze kupata soko la uhakika kwa ajili ya matunda yetu, mananasi, ndizi na menginyo yanayopatikana ndani ya Morogoro Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nitoe ushauri mwingine. Kwa sababu hii korosho tukibangua hapa tutapata ile korosho iliyobanguliwa ambayo kitalaam inaitwa kernel, lakini baada ya kernel kuna vile vipande vipande. Hivi vipande vipande, soko hakuna kwingine zaidi ya India. Ila kudhibiti kutaka watu wakabangue kule, India wameweka import duty kubwa.
Nakuomba Mheshimiwa Waziri uende kwenye Ubalozi wa India ukawaombe angalau ili kuvutia wawekezaji waje wawekeze hapa, waondoe ushuru huu wa vipande ili tupate soko la hao wanaobangua hapa, vile vipande tukauze India.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nakuomba kwa sababu wewe ndio Waziri wa Uwekezaji na Biashara, katika suala la mchakato wa kupata leseni za biashara, ni vizuri ukafungua dawati moja ambalo litarahisisha hao wawekezaji kwa maana ya sehemu zote kupatikana katika…
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami kuchangia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Pia nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi hasa Awamu ya Tano, kwa mwanzo mzuri wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi hasa katika utumbuaji majipu na dhamira thabiti ya ukusanyaji mapato ambao unakwenda kujibu changamoto kubwa ambayo ilikuwepo kwa ajili ya ufinyu wa mapato Serikalini ambapo inatuonesha mwanga sasa miradi ya maendeleo itakwenda kwa maana ya fedha kupatikana kwa wakati na maendeleo kufika kwa wananchi.
Pia, nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango kwa Mpango mzuri aliouwakilisha leo wa miaka mitano ambao unaonesha mwanga wa Tanzania mpya ambayo Watanzania walikuwa wanasubiri mabadiliko tuliyowaambia watayapata ndani ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, nchi nyingi zimeendelea kwa kupitia mlango wa viwanda, nchi nyingi zimepiga hatua kwa maendeleo ya viwanda, lakini pamoja na maendeleo ya viwanda pia viwanda vinategemea maendeleo ya miundombinu kwanza, kwa sababu miundombinu ndiyo ufunguo wa maendeleo ya viwanda, pamoja kwamba maendeleo ya viwanda ndiyo ufunguo wa maendeleo ya uchumi, lakini bila miundombinu rafiki, miundombinu mizuri na wezeshi maendeleo ya viwanda yatakuwa yana walakini kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yangu kwa sababu ili kuwe na maendeleo ya viwanda, lazima Serikali ije na mpango mzuri wa kuboresha hii miundombinu ukizingatia Mheshimiwa Waziri anasema miongoni mwa changamoto ambazo awamu ya kwanza haikuweza kutekeleza vema katika maendeleo mazuri ya miundombinu, kwa mfano, katika miradi mitano ile mikubwa ya mpango huu, lipo suala la Mkulazi, Kijiji cha kilimo lakini miundombinu kule siyo mizuri. Matokeo yake kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, mradi ule unatakiwa kutekelezwa pamoja na ushirikishwaji wa private sector, sasa private sector nyingi zikienda kule kufanya ukaguzi zinashindwa kufika kwa wakati. Hivi ninavyosema sasa hivi mawasiliano yamekatika huko Mkulazi kwenyewe, tunakwenda miezi sita kipindi cha miezi mitatu hii ya mvua huwezi kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ili kuwavutia hao private sector waje, katika kuutekeleza mpango huu kwa uhalisia wake ni vizuri kuboresha miundombinu ya Mkulazi ukizingatia barabara, mawasiliano, umeme pamoja na maji ili lile eneo liwe rafiki, na liweze kuwavutia wawekezaji wengi kwa ajili ya mradi huu ambao utakuwa unajibu changamoto nzuri kuhusu maendeleo ya kilimo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nichangie katika suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo kinachangia asilimia 75 ya ajira ya Watanzania, kilimo kinachangia pato la Taifa zaidi ya asilimia 25, lakini pia kinachangia katika fedha za kigeni asilimia 30 na pia kilimo ndiyo source kubwa ya mapato katika Halmashauri zetu nyingi Tanzania...
MHE. KHATIB SAID HAJI: Taarifa....
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza unilindie muda wangu na pia taarifa yake siipokei, kwa sababu nilikuwa sisomi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nachangia katika umuhimu wa kilimo, lengo lilikuwa kwa sababu ya umuhimu wa kilimo kama nilivyosema, namwomba Mheshimiwa Waziri katika mpango wake anapokuja, ni vizuri akaongeza bajeti ya kilimo kutoka iliyopo sasa angalau ingefikia asilimia 10, kwa umuhimu wa kilimo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la kilimo, kilimo kinategemea ardhi na sasa hivi tumeona changamoto kubwa iliyopo hapa nchini ni migogoro ya ardhi, nilitegemea katika mpango huu, Serikali ingekuja na majibu ya kutatua changamoto hiyo, hasa katika kupima ardhi, kuzingatia matumizi bora ya ardhi, ili kila eneo lipate mmiliki na wale wananchi waweze kumilikishwa ile ardhi waweze kuitumia kwa ajili ya kupatiwa Hati Miliki kama Hati zile za Kimila, zinaweza zikawasaidia katika kujipatia mikopo katika taasisi za fedha na kuanza kulima kilimo cha kibiashara zaidi kama walivyojiajiri katika hicho kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, tatizo la kilimo katika nchi yetu hii siyo wakulima tu, tatizo kubwa ni miundombinu ya kilimo imeachwa nyuma. Ningeshauri Serikali iongeze bajeti ya kilimo katika miundombinu ya umwagiliaji, ili kilimo kiweze kuwa na uhakika wa mavuno na kiweze kuzivutia taasisi za fedha ili kuwakopesha wakulima badala ya sasa wanategemea mvua na ndiyo maana wakulima wanashindwa kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hata pale Serikali ilipokuja na mpango wa kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhia mazao, pesa zile zingetumika zaidi kwenye miundombinu ya kilimo, hasa umwagiliaji. Nafikiri tatizo la maghala wangekopeshwa tu, taasisi za fedha wangeweza kutoa kwa sababu, vile ni vifaa wezeshi tu vya kuhifadhia ambavyo vinavutia hata taasisi za fedha kukopesha wakulima, tofauti na sasa hawawezi kuwakopesha wakulima kwa sababu hawana uhakika mkulima huyu kama atavuna au atafanyaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali ingeelekeza zaidi kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo badala ya mambo mengine, nina uhakika kikiwepo kilimo cha uhakika hizi taasisi za fedha zote zitavutika kwenda kuwekeza kwenye kilimo kwa sababu wana uhakika mkulima atavuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tukiwezesha katika mipango bora hii ya ardhi kupima, tukiwatengea wafugaji eneo lao, kuwatengenezea miundombinu na kuwaweka pamoja nina uhakika hata hawa wafugaji wataweza kukopesheka na wataweza kuendelea na itawavutia wawekezaji wa viwanda vya maziwa waje kuwekeza katika maeneo yale, badala ya sasa wanashindwa kuwasaidia hawa wafugaji kwa sababu wamekuwa wachungaji badala ya wafugaji na mtu anajua kwamba hata akiwekeza katika kiwanda cha maziwa hana uhakika wa kupata raw material ya maziwa kwa sababu hawa wafugaji ni wa kuhamahama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la masoko ya kilimo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda hapa alizungumza neno la busara kabisa na ni ukweli, kwa sababu alizungumza vizuri akasema, ili bidhaa zetu za kilimo za viwanda ziweze kuuzika lazima bei zetu ziwe za chini, kuna watu wamembeza kwa sababu tunataka tulete siasa katika suala la kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli uliopo haya mazao ya kilimo tunayolima, yaliyo mengi sisi siyo watumiaji tunategemea soko la nje. Soko la nje wauzaji siyo peke yetu, lazima lina ushindani wa hali ya juu, kama bidhaa zetu zitakuwa na gharama kubwa wanunuzi wana nafasi kubwa ya kwenda nchi nyingine au kununua sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mchangiaji mmoja alizungumza hapa akasema wakulima hawana uhakika mwaka huu wanalima mbaazi bei imepanda, mwakani imeshuka analima ufuta! sababu kubwa haya ni mazao ya muda mfupi na kama mazao ya muda mfupi, mwaka huu Tanzania mkilima ufuta mkipata bei nzuri mwakani nchi nyingine nazo zinalima, matokeo yake supply inakuwa kubwa kuliko demand, ndiyo maana bei inashuka bei nyingine inapanda, sasa tukitaka tulete siasa katika mambo ya uchumi hatuendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Serikali kwa mipango mizuri inayokuja nayo, Waziri wa Viwanda tuelezane ukweli na ndiyo maana nilishauri siku moja ni vizuri kukaundwa taasisi ya utafiti wa masoko ulimwenguni ili kutoa taarifa kwa wakulima wetu kuwaambia nini kinachohitajika ulimwenguni sasa hivi kilicho na bei nzuri badala ya kilimo cha historia, umezaliwa baba yako analima kahawa, analima mkonge, unataka ulime kitu hicho tu, wakati mwingine zao hilo halihitajiki huko kwa walaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la migogoro ya ardhi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi kwa kazi kubwa aliyoifanya na mimi ni mnufaika mmojawapo. Alifika kijijini kwangu katika Kata ya Tununguo katika Kijiji cha Mliringwa na alichukua maamuzi hapo hapo baada ya kuona ubabaishaji. Aliweza kuirudisha kwa wakulima ardhi ya heka zaidi ya 3,500 kutoka kwa wawekezaji wababaishaji ambao waliipata kwa ujanja-ujanja. Nakuomba Mheshimiwa Waziri urudi tena, kama unavyoona Morogoro mkipita yote yale ni mapori, lakini siyo mapori ni mashamba ya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la mashamba pori, wenyewe wenyeji hatuna pakulima, kila shamba lina hati, lakini hayaendelezwi. Nakuomba sana urudi myahakiki, ili mturudishie tuweze kuendelea. Morogoro ilikuwa ndiyo hifadhi ya chakula, lakini kila mwaka uzalishaji wa chakula unapungua, sababu kubwa ni ardhi imeshikwa na watu ambao wameenda kukopea hela badala ya kuitumia kwa ajili ya uzalishaji mali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho, naomba katika mpango ule wa Mkulazi, shamba namba 217 lenye hekta 63,000, mpango wa Serikali hekta zote 63,000 mnataka muwape Wawekezaji, heka 3,000 tu ndiyo mmetubakizia watu wa Mkulazi, watu wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla, hizi heka 3,000 hazitoshi kwa Watanzania katika kijiji hiki cha mfano kinachotaka kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu na naishauri Serikali, tusiiuze hii ardhi kwa mgongo wa wawekezaji kwa watu wachache kama mpango unavyosema, heka 20,000 kwa mwekezaji mmoja wa miwa, heka 20,000 kwa mwekezaji wa pili wa miwa na heka elfu tano tano kwa maana ya 20,000 zilizobaki kwa wawekezaji wanne wa mpunga, halafu Watanzania tuliobaki au watu wa Morogoro heka 3,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ni vizuri ardhi hii ikagawanywa mara mbili, nusu ikaenda kwa outgrowers kwa maana ya watu wa Mkulazi, Morogoro na Watanzania kwa ujumla waje wapate elimu ya kilimo cha kisasa pale kwenda kusambaza kwingine badala ya kuiondoa ardhi hii yote kuwapa wawekezaji huko mbele tunakokwenda kutakuwa ni kweusi, tusije kupata madhara kama wanayoyapata nchi nyingine, huko mbele vizazi vyetu vikaja kugombea ardhi na kuuana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia kufika siku ya leo tuko ndani ya jengo hili tukiwa na afya njema na uhai.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa hotuba nzuri ambayo ina mipango inayoonesha dhamira ya dhati. Kuna Mbunge alizungumza jana akasema kwamba zaidi ya asilimia 46 ya bajeti ya maendeleo kwenye bajeti kuu inakwenda katika Wizara hii ya Ujenzi. Baada ya kupitia kitabu nimeona pesa nyingi imekwenda huku kuna sababu maalum ya kulipia madeni ya wakandarasi. Dawa ya deni ni kulipa na inaonesha ni jinsi gani Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri kuwalipa wakandarasi hawa ili waendelee kujenga zaidi barabara zetu na kufungua milango ya uchumi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge mmoja jana ametoa takwimu nyingi sana kuilaumu Serikali kwa kusema kwamba pale bandarini mizigo imepungua, mizigo inayoenda Malawi, Zambia, Congo lakini amesahau kusema jambo moja tu kwamba pamoja na kupungua huko lakini mapato yameongezeka. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali pamoja na kwamba mizigo inapungua lakini mapato yameongezeka. Hii maana yake ni kwamba imedhibiti uvujaji wa mapato na hapa tunajali ubora na sio uwingi, bora kiingie kichache lakini tunakusanya zaidi. Hii inatuhakikishia kwamba sasa barabara zetu ambazo tulikuwa tunaomba na zinapitishwa na Bunge lakini pesa hazipelekwi sasa zitapelekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo kwa Serikali nitoe angalizo tu, wenzangu wamezungumza lakini na mimi nisisitize kwamba Bunge hili kazi yake ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Tunapitisha hizi bajeti, lakini tunategemea hizi bajeti zitakwenda kwa wakati ili bajeti hii itekelezwe ili tuendelee kuaminiwa na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano mmoja tu katika Jimbo langu, bajeti zilizopitishwa mwaka jana kwa ajili ya matengenezo ya kawaida tu barabara ya Bigwa - Kisaki, Madamu - Kinole mpaka leo pesa hizo hazijafika na barabara hazijaanza kutengenezwa. Hiyo ni bajeti ya mwaka jana na tumebakiza mwezi mmoja na nusu kumaliza muda wa bajeti ya mwaka wa fedha.
Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ni vizuri mipango ambayo mmeileta hapa na tunaipitisha kuhakikisha kwamba inatekelezwa ili tuendelee kujenga uhalali wa kuongoza nchi hii miaka mingi ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu msongamano wa Dar es Salaam, Mbunge mwenzangu kutoka Morogoro kaka yangu Mheshimiwa Saddiq alivyozungumza lakini amesema mkoa wowote lakini mikoa ambayo ina nafasi kubwa ya kuwa na bandari kavu kama alivyosema ni Pwani au Morogoro, lakini Morogoro una nafasi kubwa zaidi ya kuwa bandari kavu kwa sababu zifuatazo:-
Kwanza, kijiografia inaunganishwa na kanda zote, Kanda ya Kati, Kusini na Kaskazini. Kwa hiyo, tukiweka bandari kavu pale itatuondoshea msongamano kule Dar e Salaam na kufanya shughuli kutekelezeka kirahisi. Pia tutafungua milango ya kiuchumi kwa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine ya jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze katika Jimbo langu katika Wilaya yangu ya Morogoro Vijijini. Wilaya ya Morogoro Vijijini hususani Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, siasa kubwa katika jimbo lile sasa hivi imekuwa ni barabara hususani barabara ya Bigwa - Kisaki. Ni barabara ya muda mrefu, Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi 2005 kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami akiwepo Waziri wa Ujenzi ambaye sasa hivi ndiye Rais aliyeko madarakani. Mwaka 2010 tena Rais, Dkt. Jakaya Kikwete akatoa ahadi ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Pia mwaka 2014 alipokuja kutuaga watu wa Morogoro Vijijini akiambatana na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Rais aliyeko madarakani, Dkt. John Pombe Magufuli akaahidi tena kwamba hii barabara itajengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hii sijaiona katika kitabu hiki, namwomba sana Mheshimiwa Waziri akija katika majumuisho yake atupe matumaini ahadi hii ya Rais itatekelezwa lini kujengwa kwa kiwango cha lami barabara?
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kwani inaunganisha mkoa wa Morogoro pale Kisaki na mkoa wa Pwani kupitia Wilaya ya Rufiji. Pia inakwenda katika mbuga ya Selous, lakini ndiyo barabara pekee katika Mkoa wa Morogoro ilikidhi vigezo vya MCC. Hii ndiyo barabara iliingia katika mradi wa MCC. Kama Wamarekani waliona barabara hii ni muhimu naamini kabisa Serikali yetu ya Awamu ya Tano itaona ni muhimu zaidi na itaitekeleza haraka sana kwa kuijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji mradi huu ulikuwa chini ya MCC. Namwomba Waziri akija atupe matumaini baada ya hao MCC kuleta madoido na kuweka pembeni Serikali ina mpango gani kuchukua jukumu hilo na kuimalizia kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la kupandisha hadhi barabara ya kutoka Ngerengere - Mvuha kuwa ya mkoa.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango huu katika mada iliyopo mbele yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze moja kwa moja kwenye asilimia kumi ya vijana na akinamama. Niungane na wajumbe wenzangu waliotangulia, wengi wameshachangia mada hii hasa kutilia msisitizo kwenye hii asilimia tano ya vijana na asilimia tano kwa akinamama. Pamoja na kuchelewa kwa fedha za OC kwenda Halmashauri kwa sababu jambo hili ni la kisheria na jambo hili ambalo kwa sisi ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tuliahidi kwa wananchi.
Naishauri Serikali ni vizuri ikafunguliwa akaunti maalum katika Halmashauri zetu kutenga fedha ili kila mwezi kwenye mapato bila kujali OC imekuja au haikuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kwenye bajeti zetu kule kwenye Halmashauri kama tulivyoona asilimia kumi inakwenda kwa vijana na akina mama, asilimia hamsini kwenye miradi ya maendeleo na asilimia arobaini kwenye matumizi ya ndani. Sasa mara nyingi wakati mwingine bajeti zinawekwa kubwa kwa ajili ya kupata hiyo asilimia 40 ya OC na matokeo yake kila hela inayokusanywa kwa kisingizio kwamba OC haijaja hela yote inatumika katika matumizi ya kawaida na matokeo yake hakuna mradi wowote wa maendeleo unakuwa umetekelezwa kwa kutumia fedha za ndani wala kwenda kwenye hii asilimia kumi kwa vijana na kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri kwamba kila mwezi kila fungu ambalo tulilolipangia kwenye mipango yetu katika Halmashauri likawekwa kwenye akaunti yake ili kama OC haijaja basi athari iwe kwenye OC, katika ile miradi ya maendeleo iendelee ili tukifika mwisho tunajua OC tumekwama wapi ili wajibane wapi na ile miradi yetu ya maendeleo asilimia ile hamsini iliyotengwa hata kama tusipoimaliza yote lakini angalau kwamba kwingine tutakuwa tunaipunguza, la sivyo itakuwa kila kitu inaishia kwenye OC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye suala la semina kwa viongozi. Ndugu zangu kama tulivyoona asilimia arobaini ya bajeti ya Serikali inakwenda kwenye miradi ya maendeleo. Hiyo miradi ya maendeleo inakwenda kule chini na watekelezaji na wasimamizi wakubwa ni Madiwani, lakini mpaka tunavyosema hivi hao wasimamizi wa miradi mikubwa na kutazama value of money kule chini hawana semina yoyote. Maana yake ni nini? Hawajui wanachoweza kukisimamia, kipi ni kipi. Ni vizuri pamoja na kujibana tukawapa mafunzo hawa Madiwani ili wawe na uelewa mpana wa kusimamia kile wanachopaswa kusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; pia hata wale Viongozi wetu kule wa Serikali za Vijiji, kwa sababu kule hela zote hizi zinakwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji na Afisa Mtendaji. Afisa Mtendaji ni mwajiriwa wa Serikali ana mshahara, lakini huyu signatory ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji hana posho wala mshahara na ukizingatia ile asilimia ishirini haiendi huko. Kwa hiyo, anasimamia kitu ambacho yeye hafaidiki na chochote, sasa matokeo yake hata kudanganywa na Watendaji ili miradi hii isitekelezwe kwa kiwango kilichokubaliwa inakuwa ni rahisi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yangu tukaangalia ni namna gani tunaweza kuwalipa chochote hawa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa au posho ili waweze kusimamia miradi yetu kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye utawala bora; suala hili la utawala bora hasa katika ngazi za Mikoa na Wilaya. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa uteuzi mzuri alioufanya kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya, lakini pamoja na uteuzi huo bado hawa watu wanahitaji semina elekezi. Nasema hivyo kwa sababu kuna mambo mengi yanatokea hasa kwenye mgongano wa kimadaraka kule katika Halmashauri zetu.
Nitoe mfano tu kwenye Halmashauri yetu, unakuta Baraza la Madiwani wakati mwingine limeamua kwa mujibu wa kanuni na sheria lakini anaweza kuja Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa akasitisha yale maamuzi ya Baraza la Madiwani yasifanyike na matokeo yake Mkurugenzi anakuwa katika wakati mgumu amsikilize nani, alisikilize Baraza la Madiwani au amsilikize Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tuna ushahidi dhahiri upo umetokea kwenye Halmashauri zangu na matokeo yake Mkurugenzi huko analaumiwa na huku analaumiwa. Wakati mwingine tunawalaumu Wakurugenzi siyo maamuzi yao lakini kwenye kutumikia mabwana wawili na wakati mwingine majukumu yao hawayajui na mipaka ya kazi zao hawaijui, wanakuwa wanayumba yumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja tu ambao ulifanyika ndani ya Baraza la Madiwani; tumefanya maamuzi sahihi ya kuhamisha Halmashauri yetu kutoka Morogoro Mjini kwenye vijijini kwamba kikwazo kilikuwa pesa, tumepata pesa baada ya kushauriana na Wizara ya TAMISEMI yenyewe kwa msaada mkubwa ambao ametupa Mheshimiwa Waziri Simbachawene na timu yake, yule mdaiwa sugu matokeo yake akatulipa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, jali muda wangu maana muda wenyewe mchache, siku yenyewe moja tunaijadili hii.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa hiyo, kwanza nampongeza Mheshimiwa Simbachawene kwa ushirikiano mkubwa sana alioipa Halmashauri ya Morogoro mpaka huyu mdaiwa sugu akatulipa hela zetu, tukapanga muda ndani ya mwezi mmoja tuhamie Makao Makuu kwenda Mvuha, kutoka Mjini kwenda Vijijini, lakini kabla ya maamuzi yale hayajafanyika, anajiandaa Mkurugenzi na timu yake anakuja Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa kupitia RAS anawabeba Wakuu wa Idara kawapeleka Mvuha kawabwaga pale anasema anayetaka kazi ndiyo hapa nimemfikisha, asiyetaka hamna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lile halina choo, halina ofisi wala kitu chochote, lakini kwa kukubali kwamba ni mkubwa amesema hawa watu wakakaa kule, matokeo yake nini? Huo ni mfano mmoja mdogo sana. Sasa ni vizuri hawa watu wakapewa semina elekezi ili kila mmoja ajue madaraka yake na kila mtu ajue mipaka yake. Kwa sababu hawa wananchi Baraza la Madiwani ndiyo tunatakiwa tutetee maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu watumishi kutokujiamini katika kutoa maamuzi, huu ni mfano hai upo ndani ya Halmashauri ya Morogoro, tuna tatizo kubwa sana kule la wakulima na wafugaji, lakini ni kosa kwa kiongozi wa kuchaguliwa, uwe Mbunge au Diwani kusema kuna tatizo la wakulima na wafugaji. Umetokea mfano Diwani mmoja wa Kolelo amewekwa ndani mara mbili na vyombo vyenye mamlaka kwa kusema kwenye Kata yake kuna tatizo la wakulima na wafugaji, anaonekana ni mchochezi, sisi Wabunge ndiyo tulienda kumtoa zaidi ya mara mbili. Tunasema haya ni nini? Lakini Mungu siyo Athuman baadae yakaja kutokea mapigano makubwa sehemu ile ile viongozi waliyokuwa wanakataa kwamba hakuna mapigano ya wakulima na wafugaji; hakuna tatizo la wafugaji kuvamia kwenye mashamba ya wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi ni kwa nini? Kwa sababu hawa viongozi wetu walishapewa miongozo kwamba sehemu yoyote kwenye tatizo la wakulima na wafugaji likitokea basi Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa hana kazi. Sasa wakati mwingine wanatumia kuficha maovu kwa kuogopa wao kuja kuchukuliwa hatua. Niombe sana tuwape moyo hawa viongozi, ni bora waseme ukweli ili tutatue tatizo kuliko kuficha baadaye mambo yanakuja kuharibika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TASAF; kwanza niipongeze sana Serikali kwa mradi huu wa TASAF umesaidia sana kaya maskini, lakini naomba sana elimu iongezwe hasa kule vijijini hakuna elimu, wananchi hawajapata elimu sawasawa, kwa sababu wanaamini hasa wazee kwamba huu ni mradi wa kusaidia wazee, hawajui kwamba ni mradi wa kusaidia kaya maskini. Sasa ni lazima iongezwe ijulikane kuna tofauti ya kusaidia wazee na kusaidia kaya maskini. Mara nyingine unaona kuna mgogoro wanakwambia kijana ana nguvu zake lakini yupo kwenye mradi wa TASAF, kumbe ni kijana lakini hana uwezo kiuchumi. Kwa hiyo, ni vizuri elimu ikaongezeka kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niongelee sasa kwenye Kamati ya Katiba na Sheria kuhusu suala la NSSF. Niungane na maoni ya Kamati kwa sababu ya utawala bora na kwa sababu tuna mihimili mitatu, Bunge, Mahakama na Serikali na Serikali imeshaanza kuchukua hatua katika wale watuhumiwa ipo kwenye vyombo vya uchunguzi, ni vizuri sana tukaipa nafasi Serikali ikamaliza uchunguzi wake, lakini naomba kuishauri baada ya uchunguzi huo walete taarifa hapa Bungeni ili ukweli ubainike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii ya Kamati ya Bajeti. Kwanza niunge mkono hoja ya Kamati ya Bajeti kwa sababu mambo mengi, changamoto ambazo zinaikabili nchi yetu kama Taifa, mengi Kamati imezingatia, kwa hiyo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa makusanyo makubwa ya mapato na kubana matumizi kulingana na mapato hayo halisi bila kutegemea misaada mingine. Baada ya pongezi hizo niwe na ushauri mdogo, kwa sababu tumeona pamoja na makusanyo makubwa ya mapato hayo item mbili ndio zinakula; mishahara pamoja na madeni. Kwa bahati mbaya sana madeni mengi ambayo yanalipwa kwenye kandarasi kubwakubwa na nyingi hizi zinatoka nje, maana yake ni nini? Serikali inatumia hizo bilioni zaidi ya 900 kwa mwezi lakini hela zile baadaye zinahama kutoka nchini zinakwenda nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeomba ushauri katika hili, Serikali sasa ni vizuri ili kusisimua uchumi ndani ya nchi nao kuwalipa wawekezaji wa ndani ili kwanza waweze kusisimua uchumi, wakiendelea kufanya biashara wataendelea kutoa ajira kwa wananchi wetu lakini pia mzunguko wa pesa utakuwepo ndani ya nchi lakini kuendelea kuwalipa na yale madeni ya nje tu maana yake zile hela zinakwenda kuimarisha mzunguko kwenye nchi za wenzetu. Tunajua dawa ya deni ni kulipa lakini tuwe na balance ya sehemu zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunasema tuna uchumi wa viwanda, ni kweli kabisa tuna uchumi wa viwanda lakini pamoja na uchumi huu wa viwanda Serikali peke yake lazima inaitegemea sana sekta binafsi. Sekta binafsi hizi zingine ziko ndani ya nchi, kwa hiyo tunapowalipa wadeni wa ndani tutakuwa tunawarahisishia kushiriki kwenye uwekezaji wa ndani ya nchi kwenye uchumi wa viwanda. Kwa mfano tu, Serikali leo ikiweza kulipa mifuko ya jamii ambayo wanaidai Serikali mifuko hii itakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda na sekta nyingine hapa nchini na kutoa ajira na kuimarisha uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye suala la kilimo; kama ukurasa wa 42 unavyosema kilimo ndio uti wa mgongo, kinaajiri zaidi ya asilimia 70, lakini kwa bahati mbaya sana kilimo hicho hicho ukuaji wake kila mwaka unakwenda chini, sasa hivi tunaambiwa ni asilimia tatu ambayo hata yale makubaliano tu ya Maputo kule tunatakiwa angalau tuchangie asilimia 10, lakini kwa mwendo huu inaonekana bado tuna safari ndefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye hili, kwa sababu huwezi kutatua matatizo ya kilimo au kilimo kipande bila kutatua matatizo yanayokabili Sekta yenyewe ya Kilimo, wenzangu wamezungumza mengi lakini lazima Serikali ije na mkakati mzito kwenye kutatua hili tatizo la mipango bora ya matumizi ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa kama zamani wakati wa Mwalimu Julius, ilikuwa inajulikana kabisa mikoa gani ya wafugaji na mikoa gani ya kilimo, kwa sababu hata tunapozungumza matumizi bora ya ardhi maana yake ni kwamba tukatenge ardhi zetu wapi panafaa kwa kilimo, wafugaji wakae wapi, makazi yake wapi. Sasa mpango huohuo uanzie ngazi ya Kitaifa kwanza kwa sababu haiwezekani ukawaweka pamoja wafugaji na wakulima, haiwezekani kukaa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tujue kabisa mikoa gani itatupa tija kwa ajili ya mifugo na mikoa gani itatupa tija kwa ajili ya kilimo. Nitoe mfano, Mkoa wangu wa Morogoro, tumeambiwa Ghala la Taifa, Ghala la Taifa maana yake ninyi mko zaidi kwenye mambo ya kilimo lakini hali inayoendelea kule kama hii mipango bora hatutaizingatia kuanzia ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya itakuwa ni hadithi. Kwa hiyo, niombe tu hii mipango bora ya ardhi ianze kuanzia ngazi ya Taifa, itangaze kabisa mikoa gani mahsusi kwa ajili ya kilimo na mikoa gani mahsusi kwa ajili ya mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo katika kilimo, leo kilimo hakivutii wakulima wapya, hakivutii mtu kwenda kuwekeza kwenye kilimo sababu kilimo chetu bado kinategemea mvua, huna uhakika wa kuvuna. Ndiyo maana leo bajeti ya kilimo kwenye mbolea kila mwaka inaongezeka lakini tija inapungua. Kwa nini? Mtu anaweza akapata mbolea, anaweza kupata trekta anaweza kupata mtaji lakini kama hana maji hayo yote ni bure, kama tunavyoona mwaka huu mvua haijanyesha, watu wamewekeza lakini watapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mfano mzuri ndiyo maana unaona hata Benki ya Kilimo yenyewe ina hela zaidi ya bilioni 59 lakini imekopesha bilioni tatu tu kwa sababu anaona kwamba hata akikopesha uhakika wa kulipa hamna. Ushauri wangu katika hili ni vizuri sasa Serikali tujielekeze zaidi katika mipango yetu kuwekeza kwenye maji, hasa kwenye mabwawa. Kwa hiyo, naungana na maoni ya Kamati kuongeza ile shilingi 50 kila lita ili iwe 100 ili Wizara hii iwe na Mfuko wa kutosha wa maji twende kutatua changamoto za maji na kukabiliana na hali halisi inayolikabili Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa hivi tuna ukame, mara nyingi tunakuja na mipango ya kukabiliana na matokeo hatukabiliani na chanzo kilichosababisha ni nini. Sasa hivi tuna tatizo hili la ukame sasa tukawekeze kwenye masuala ya mabwawa ya umwagiliaji ili kilimo chetu kiwe cha uhakika, mtu yeyote akienda kuwekeza kwenye kilimo awe na uhakika wa kuvuna kwa sababu maji ya kumwagilia yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi hata hizi benki za biashara tutakuwa tumetatua suala la mitaji kwa wakulima kwa sababu watawakopesha kwa sababu wanawafahamu kwamba wana uhakika wa kulipa kwa sababu wana uhakika wa kuvuna katika uwekezaji huo wa kilimo. Hata tukiongeza mbolea, hata tukiongeza madawa kama uhakika wa maji hamna, kama kilimo cha umwagiliaji hamna, hamna benki yoyote – iwe ya kilimo au iwe ya kibiashara ambayo inaweza kuwekeza kwenye suala la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuhusu kukopa zaidi ndani, ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wengi, kuna mmoja alikuwa anazungumza anasema kwa nini sasa hivi hatukopesheki huko nje, kuna sababu gani. Sababu ziko wazi tu, sababu ni kwamba sasa hivi demand imekuwa kubwa kuliko supply, hata hao wakopaji uwezo wao sasa hivi nao ni mdogo. Mfano mdogo tu tunauona sasa hivi hata Marekani wenyewe huyu Rais mpya aliyeingia anasisitiza viwanda vyao wawekezaji warudi kuwekeza ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limeishtua kidogo hata China. China wanasema sasa wanataka kubadilisha badala ya kwenda kuwekeza zaidi nje ya nchi wanaona ni bora kufanya innovation kwenye teknolojia yao ili kupunguza gharama za uzalishaji ili waendelee kuzalisha ndani ya nchi zao, maana yake wa-reduce production cost ili waendelee kulinda ajira yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni signal sio nzuri kwetu tunaposema kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda maana yake support kutoka kwa Mataifa makubwa itakuwa ni ndogo kwa sababu haya sasa na wao sasa hivi wataangalia zaidi Mataifa yao kuliko kuja kuwekeza kwetu kwa sababu wanaona kwamba kuja kuwekeza huku kama wanahamisha ajira za watu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii kama Serikali tuichukue na twende kwa tahadhari. Ni vizuri katika hili tukajielekeza zaidi katika yale mambo ambayo tuna uwezo nayo na tuko wazuri katika uzalishaji zaidi kuliko haya ya kutegemea wawekezaji kutoka nje. Hawatapenda kwamba tuendelee kama wao halafu tuje tuendelee kugombania soko lilelile, wao wanapenda waendelee kututumia sisi kama soko badala ya kuwa partner wazalishaji wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, katika suala la hizi milioni 50, ni vizuri kwamba Serikali ikaleta haraka sana, ndani ya bajeti hii kabla haijaisha ni vizuri hizi hela zikafika huko vijijini ili ziweze kwenda kusisimua hali ya uchumi na kuongeza mzunguko wa uchumi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ni vizuri Serikali tukawa na vipaumbele vichache ambavyo vinalingana na uwezo wetu badala ya kuwa na vipaumbele vingi ambavyo tunaviandika tu, wakati mwingine utekelezaji wake unakuwa hafifu. Ni vizuri tukavichagua vichache tukavitekeleza na kutokana na hali hali sasa hivi – kama alivyosema mwenyewe Waziri wa Fedha – upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu nje imekuwa ni michache sana, mikopo inayopatikana sasa hivi ni ya kibiashara. Kama mikopo inapatikana nje ya kibiashara maana yake itakuwa na masharti magumu na matokeo yake hata tukikopa zaidi itakuwa na riba kubwa na itakuwa ni mzigo mkubwa sana kwa Taifa na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Kamati, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Wenzangu wengi wametoa pongezi kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi Awamu ya Tano. Na mimi nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama sitashukuru kidogo walichonifanyia katika Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa nia ya dhati kwa mara ya kwanza ukiondoa ile Barabara ya lami ya Taifa, Dar es Salaam - Morogoro ya kwanza tangu miaka 50 ya Uhuru ndiyo Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja kuzindua Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa pale Kizuka, ametuzawadia kilometa zaidi ya 15 kutuwekea lami. Tunamshukuru sana nasi tunaanza kuona matunda ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa mara ya kwanza kuwa na barabara la lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Uongozi wa TANROADS Mkoa wa Morogoro ukiongozwa na Engineer Dorothy Mtenga na timu yake nzima, kwa usikivu mkubwa ambapo tulipopeleka maombi yetu ya kupandishwa barabara kutoka Wilaya kwenda Mkoa, barabara ya Ubena Zomozi - Ngerengere - Tununguo mpaka Mvuha, mwaka huu imepandishwa na nimeiona na imetengewa fedha. Nawashukuru sana huu ndiyo utekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi jinsi tulivyoahidi inaonekana namna inavyotekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni ombi kuhusu barabara hii ya Ubena Zomozi kwenda pale Kizuka ingawa cha kupewa hakina nyongeza na hii ilikuwa ni zawadi mahsusi kwa Mheshimiwa Rais kwa Jeshi letu, kwa walinzi wetu wale wa Kizuka, walinzi wa mipaka yetu, kama mnavyofahamu Mheshimiwa Waziri pale Kizuka tuna kambi nne, pamoja na ile ya Sangasanga ya wale wazee wa kazi mliowaona pale wakitoa burudani juzi pale uwanjani. Sasa wale barabara yao inaanzia Mdaula mpaka Sangasanga, ombi langu kwako na ninafikiri Serikali iko hapa, umfikishie Mheshimiwa Rais, tunaomba hawa nao ni wapiga kura wangu wasione kama wametengwa, basi hizi kilometa zao saba zingewekewa lami kama walivyowekewa wenzao wa Kizuka, litakuwa ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo niende kwenye barabara. Kama tulivyosema barabara ya kwanza ya lami ndiyo hiyo itakuja kilometa 15 kutoka ahadi ya Rais, lakini kuna barabara muhimu kuliko yote ya Bigwa - Kisaki. Ni barabara ambayo kila wakati tunaiongelea hapa lakini bahati mbaya sijaiona humu. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inapita katika tarafa nne za jimbo hili, inapita tarafa ya Mkuyuni, tarafa ya Matombo, tarafa ya Mvuha, tarafa ya Bwakila, lakini cha muhimu barabara hii inakidhi sera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani kwa upande wa Rufiji. Kutoka Kisaki kwenda Rufiji ni kilometa 60 tu na kutoka Morogoro Mjini kwenda Kisaki kilometa 170. Kwa hiyo, utakuwa umefika Rufiji kwa kilometa 230, itakuwa ina mchango mkubwa sana kitaifa badala ya mtu anayetoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu, Morogoro yenyewe akienda Mtwara analazimika mpaka atembee kilometa 200 kwenda Dar es Salaam, baadae atoke 170 kwenda Kibiti mpaka Rufiji, ndiyo hapo tutakuwa tumeokoa gharama kubwa sana kwa kutengeneza barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaokoa msongamano Dar es Salaam, tutaokoa gharama za usafirishaji pia barabara hii ikitengenezwa tutarahisisha kufika katika Mbuga yetu ya Selous kupitia Kisaki kwa ukaribu zaidi kwa hiyo, tutaongeza mapato ya kiuchumi kupitia utalii. Kwa hiyo, naomba sana barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa tangu 2005 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete, akarudia 2010 pia 2015 na nishukuru ipo kwenye ilani, basi utekelezaji ufanyike haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwenye barabara hii ya Bigwa - Kisaki, ningeomba hawa waliopisha barabara waliokuwa kwenye hifadhi, wamefanyiwa tathmini muda mrefu sana Mheshimiwa Waziri. Sasa ni wakati muafaka wakalipwa fidia mapema ili ikifikia wakati wa kutengeneza hiyo barabara basi iende kwa haraka sana. Naomba ukija kufunga mjadala wako ni vizuri tupate commitment ya Serikali tujue ni lini watu waliopisha barabara watalipwa fidia zao kwa sababu mpaka sasa hivi, zaidi ya miaka mitano wamekaa hawafanyi uendelezaji wowote, hawafanyi kitu chochote. Kama unavyojua nyumba yoyote ikiwa karibu na barabara inakuwa ni nyumba ya biashara siyo ya makazi, watu wana-frame zao, watu wana viwanda vyao vya matofali, vyote vimesimama kwa kusubiri kupisha hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu niende kwenye upande wa reli. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali nzima ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa reli ya kati. Hii reli ya kati ina manufaa makubwa sana katika Mkoa wa Morogoro, hususan katika Jimbo langu. Inapita Kidunda, Ngerengere, Mikese pamoja na Mkulazi. Kwa hiyo, itakuwa na manufaa makubwa sana kiuchumi, itaturahisishia gharama za uzalishaji, gharama za usafirishaji kwenda chini, matokeo yake itakuwa faida kubwa kwa wananchi wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu katika hili, kuna watu ambao wameathirika na maendeleo haya ya reli ya kati. Kuna watu wamekaa zaidi ya miaka 20 leo wamepewa notice wanatakiwa wahame ndani ya mwezi mmoja. Mheshimiwa Waziri, hata kama huyo mtu ahame ndani ya mwezi mmoja atapata wapi nafasi hiyo ya kwenda kujenga, muda ndani ya mwezi mmoja apate makazi. Ombi langu la kwanza wangeongezewa muda hata kama miezi sita, ili wapate nafasi ya kujenga kule ambako wanaenda, la pili kwa wale waliokaa zaidi ya miaka 12, Shirika la Reli lilikuwepo walikuwa wanaangalia, watu walishajua pale mahali pao, leo kuja kumhamisha mtu huyu bila chochote kama sheria inavyosema kwamba mtu akikaa zaidi ya miaka 12 mahali hapo anahesabika ni pake. Ni vizuri mngewapa kifutia jasho angalau waende kurudisha pale walipokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, linguine ni kuhusu mawasiliano. Kuna kata zangu zaidi ya tano kwenye tarafa ya Ngerengere, kata ya Maturi, kata ya Mkulazi, kata ya Seregete, kata ya Tununguo na kata ya Kibuko, tarafa ya Mkuyuni, zote hazina mawasiliano, zaidi ya vijiji 30. Nakuomba sana hivi vijiji tuvipatie mawasiliano hasa huku Mkulazi kwenye mradi mkubwa unakotekelezwa sasa hivi na wawekezaji NSSF kwa ajili ya kiwanda cha sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika mawasiliano niongelee kuhusu TTCL. TTCL ni shirika la kwetu, nilikuwa nasikia kuna baadhi ya wenzetu hapa walikuwa wanalifananisha na shirika la huko nje. Jamani hata hayo mashirika yanayosifika huko Ethiopia kwanza yaliwezeshwa mtaji na Serikali yao, pili, yalilindwa na ushindani kwa mashirika mengine kwa muda mrefu mpaka yalipokaa sawasawa ndiyo wakaruhusu mataifa mengine au mashirika mengine kwenda kufanya bisahara pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vizuri kwa sababu shirika hili ni letu, kupitia Serikali, Serikali ni vizuri ikaongeza mtaji kama inavyofanya kwenye ATC ili shirika hili li-take off baada ya hapo na ikiwezekana hata huu mtaji tuwape kama loan ili kuwapa uwajibikaji hawa wafanyakazi wa TTCL wajue kwamba tumekopeshwa na Serikali, ni hela za Watanzania zinapaswa zirudishwe kwa wakati na hata kama siyo kwa faida, lakini zirudi Serikalini zije zifanye kazi nyingine. Lakini kuwaacha kwenye ushindani huu mkubwa, tumeona hapa mashirika mengine yamekuja kuomba huku mtaji, tukiwaacha hawa TTCL washindane na ma-giant hao sasa hivi hatuwezi kuwatendea haki na halitaweza kwenda mbele sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili pia kwenye TTCL, wanatoa huduma zinatumika na Serikali na taasisi nyingine na sisi wengine, ni vizuri tukawalipa zile ankara zao. Mara nyingi mashirika mengi ya Serikali yanakufa ni kwa sababu hatuyaendeshi kibiashara, tunayaendesha kiserikali kama vile yanatoa huduma. Tunatumia huduma zao, wakati wa kulipa hatulipi, baadae madeni yanakuwa makubwa, shirika linashindwa kujiendesha kibiashara.

Naomba Serikali yangu ni vizuri kama tunadaiwa na TTCL ili tuipe nguvu i-take off hapo ilipo tuilipe madeni yao ili waweze kusimama na kwenda kwenye ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kuhusu TTCL ni kwamba sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nami kwa kunipa nafasi nichangie Wizara hii muhimu ya Kilimo, Wizara ambayo ni uti wa mgongo wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba uniruhusu nitoe pole nyingi sana kwa wananchi wangu wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hususan wananchi wa Kata ya Kinole, Tegetelo na Mkuyuni kwa athari kubwa ya mvua iliyowapata ambayo imesababisha uharibifu mkubwa wa barabara hasa ile ya Madam – Kinole na Bigwa – Kisaki. Niwaambie kwamba suala hili tumeshalifikisha kwa Serikali na naishukuru sana Serikali kwa kuanza kutengeneza, kurudisha miundombinu, ile ya barabara ya Bigwa - Kisaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni kwamba kutokana na hali halisi ya Kinole, leo ni siku ya 15 watu hawana mawasiliano ya barabara. Zaidi ya kilometa 30 watu wanatembea kwa miguu. Naomba na hii barabara itolewe jicho ili iweze kurudisha mawasiliano haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, kwanza naishukuru sana Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa hotuba yao nzuri ingawa tutatoa mchango kwa ajili ya kuboresha tu, lakini kila kitu kimekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niende moja kwa moja kwenye matatizo. Nianze na Jimbo langu kuhusu matatizo ya migogoro ya wakulima na wafugaji. Naipongeza sana Serikali kwa hatua ambazo imezichukua za kuunda Kamati za Wizara tano ili kutafuta suluhu la tatizo hili. Kama ulivyoshuhudia mwenyewe Mheshimiwa Waziri, kwenye kitabu chako kuhusu migogoro mingi, leo mauaji mengi ya mifugo kwa ajili ya ukame ni Morogoro; mapigano mengi ya wakulima na wafugaji ni Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawe unafahamu Morogoro kiasili ulikuwa kwamba siyo Mkoa wa wafugaji, leo neema hii iko Morogoro, maana yake kuna wafugaji ambao wamekuja, hawakuzingatia taratibu na Kanuni za Kisheria kufika pale Morogoro. Ndiyo maana migogoro imekuwa mingi na ndiyo maana mifugo iliyokufa imekuwa mingi kutokana na ukame na uvamizi wa ardhi bila kufuata taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu kwa Serikali, wakati tunasubiri hii taarifa kufanyiwa kazi, lakini tuliona Serikali hii ya Awamu ya Tano imewatoa kwa nguvu kubwa sana wafugaji waliovamia mbuga za wanyama katika Hifadhi za Serikali. Kwa sababu hizo hizo, basi tunawaomba wawatoe kwa nguvu wale wafugaji wavamizi wasio halali, walioingia katika maeneo ambayo sio yao. Isiwe na kisingizio cha kusema hakuna pa kuwapeleka. Kama wale waliotolewa kwenye misitu walipatikana pa kuwapeleka na hawa wavamizi watafutiwe sehemu ya kwenda ili kumaliza tatizo hili la wakulima na wafugaji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu madeni ya Mawakala wa Mbolea, huu ni mwaka zaidi ya wa pili na nusu sasa tunazungumza kwamba Serikali inafanya uhakiki. Nami naiunga mkono sana Serikali yangu kwa sababu sishabikii na siko tayari Serikali iwalipe watu ambao ni
wababaishaji na wadhulumaji ambao hawakutoa huduma Serikalini, walipwe kwa jasho ambalo hawajalitumikia. Niko pamoja na Serikali yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ucheleweshaji huu umeleta athari kubwa sana kwa watoa huduma hizi. Watu wameuziwa nyumba zao, ndoa zao zimesambaratika, yaani maana yake watu wameachana na wake na waume zao kutokana na migogoro kwamba hakuna kipato ndani ya nyumba, lakini pia watu wamefilisiwa. Wengine wamejiua na kupoteza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ombi langu kwa Serikali leo hii, kwa mfano, mtu aliyekopa shilingi milioni 100 benki, miaka miwili anadaiwa na benki zaidi ya shilingi milioni 40 kama riba aliyochukua asilimia 20. Itakuwa ni kuwaonea. Kwa wale watakaokuja kugundulika ambao ni halali na wametoa huduma kuja kuwalipa kiasi kile kile kama wanachoidai Serikali, kwa sababu siyo kosa lake kwa kuchelewa, ni kosa la mtu mwingine. Ni vizuri mkalichukulia hili kuwalipa pamoja na fidia na gharama za riba walizochukua mikopo kule benki ili kuwarudisha watu hawa katika sehemu tuliyowakuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kufanya hivyo, maana yake tumewapeleka kwenye umaskini mkubwa sana. Leo hii kuna watu wangu kule walikuwa wanatoa ajira ya kujiajiri kwa wenzao, lakini leo wamekuwa ombaomba, wameshafika zaidi ya mara nne hapa kufuatia madai haya Wizara ya Fedha, kwa Waziri Mkuu na Waziri wewe mwenyewe, mpaka leo hawajapata. Wanashindwa kujilipatia mpaka nauli. Leo huyo mtu aliyejiajiri mwenyewe anatakiwa asaidiwe! Jua kwamba tatizo hili ni kubwa na limesababisha ombaomba wengi miongoni mwa watu wengi waliokuwa na uwezo mkubwa wa kujihudumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, kwenye wabanguaji wa korosho, yaani kama Taifa mpaka sasa hivi ninachanganyikiwa; tunataka Tanzania ya viwanda au tunataka Taifa la kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya wenzetu? Kwa nini ninasema hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni zaidi ya mwaka wa 20 tangu tuanze kuingia kwenye private sector, lakini zaidi ya asilimia 90 ya korosho inayozalishwa nchini inapelekwa nje ya nchi huko India au Vietnam kubanguliwa. Wakati mwingine Mheshimiwa Waziri mwenyewe anasifia kabisa, tumeuza korosho tani 4,000 imeenda Vietnam. Tunaona kama sifa! Naona kwamba hatujaelewa mustakabali au nia kubwa ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisema anataka viwanda na alisema hakuna mtu yeyote atakayemzuia ndoto zake; yule atakayemzuia atakwama mwenyewe. Nimuulize Mheshimiwa Waziri, nani anayemkwamisha katika uwekezaji wa ndani wa Viwanda vya Korosho kubanguliwa? Maana korosho hizi kwenda katika raw form India ama Vietnam maana yake tunahamisha utajiri na ajira kwenda kwenye Mataifa mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kuwashindanisha wawekezaji wa ndani au wabanguaji wa ndani wadogo na wakubwa kwenye mnada na wanao-export kwa raw form, hakuna mwekezaji yeyote wa ndani ataweza kushinda mnada wowote ule. Kwa sababu nchi hizo za India na Vietnam, export levy yoyote wanayoiweka wenyewe wanaenda kurudishiwa. Nani ambaye atashinda mnada kwa hapa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ushahidi upo wazi na ndio maana 90% za kusafirisha raw form na viwanda vilivyokuwepo; natolea kwa mfano mdogo, kwamba tulisema Wahindi wanyonyaji; wamekuja Wachina, Sun Shine Group kampuni kubwa kuliko zote kule China imewekeza leo Lindi ina uwezo wa ku-process zaidi ya tani 5,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mnada wa mwaka 2016 tumezalisha korosho zaidi ya tani 264,000MTS, imenunua ni 180 tu, tena za mwisho wa mnada baada ya wanunuzi ma-giant kuondoka, unategemea huyo ni nani atakuja kuwekeza Tanzania kwenye korosho kwenye processing? Mtu wa nje anakuja baada ya kuona mafanikio kwa mtu wa ndani kwamba amefanikiwa vipi au mwenzie aliyetangulia kwenye biashara hiyo amefanikiwa nini; naye ndio atavutika kuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika hili kwa Serikali, la kwanza ni vizuri kuendesha minada miwili tofauti, tukaiga model kama ya Msumbiji. Korosho ukianza msimu, kipaumbele cha kwanza, mnada wa kwanza, wanaletwa Local Processors watupu washindane kwa ajili ya kuhakikisha wanapata raw materials kwa ajili ya ku-process ndani, kutoa ajira kwa wananchi wetu; lakini pia kuongeza thamani kwenye korosho zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunavyo-export raw, maana yake Wahindi ndio wanaingiza foreign currency nyingi zaidi kuliko Watanzania. Mfano mdogo tu, korosho hapa leo wameuza Sh.4,000/= lakini ikibanguliwa zaidi ya Sh.25,000/= kwa kilo. Sasa nani anapata korosho bei kubwa zaidi? Ninyi au Vietnam? Sisi au Wahindi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tuhakikishe tunawavutia wawekezaji, tuweke mazingira, wawekezaji wa ndani wapate korosho kwanza kama raw material kabla ya mtu mwingine yeyote. Wakishajaza ndiyo turuhusu ku-export, watu wa nje waje watoe. Katika kufanya hivyo tusije kumlalia mkulima. Serikali iangalie namna gani kwa zile bei watatoa kwa Local Processors ili twende sambamba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja ya bajeti kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi nichukue fursa hii ya dhati kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa nafasi ya kufika siku hii ya leo ya Ijumaa ndani ya Mwezi wa Ramadhani. Pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua kubwa alizozichukua na kwa kutanguliza uzalendo kwa nchi yake, ameweka uzalendo mbele kuliko maslahi yake binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya utendaji wa Wizara ya Fedha kwa kuleta bajeti nzuri inayoonyesha mwelekeo halisi wa Taifa letu kwa mwaka huu. Pia kama walivyozungumza wenzangu ni bajeti ambayo imetoka kwenye mawazo ya Watanzania na Wabunge wenyewe. Nakumbuka tulijadili kwa kina Mpango ulipoletwa hapa Bungeni kama Wabunge tukapendekeza mapendekezo mengi na Serikali imeyapokea. Kwa hiyo, hilo tunapaswa kushukuru kwa sababu kama alivyosema Mbunge mmoja mwaka jana Serikali haikutusikiliza lakini mwaka huu hii bajeti ni ya kwetu, michango mingi ilitokana na michango tuliyopendekeza wakati wa Mpango. Kwa hiyo, tunajisikia kwamba tunai-own bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa wanasema kwamba unapomsifia mwizi msifie na yule anayemfukuza. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete aliyetuletea chuma kama alivyosema yeye. Alituambia mimi naondoka nawaletea chuma hiki ili kitekeleze pale nilipochoka mimi yeye aende kwa kasi zaidi. Leo ndiyo tunamuelewa Mheshimiwa Dkt. Kikwete kwamba chuma kinatema cheche. Tofauti yake na Marais waliotangulia huyu wa sasa ni mpole sana, kwa hiyo, ni vizuri akaongeza kidogo ukali na usimamizi wa karibu katika mali za Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu tumechezewa vya kutosha. Nimuombe Mheshimiwa Rais, kwa sababu Serikali iko hapa, aende nje ya boksi, kama alivyosema mwenye ng’ombe amekwenda kumkagua Mchungaji kama ripoti anayomwambia ni sahihi, basi ni vizuri akaenda pia kukagua kwenye vitalu vya uwindaji. Huko nako mambo si mazuri kama tulivyokuwa tunasikia Mabunge ya zamani. Kwa kasi hiyohiyo aliyoifanya kwenye madini aende na upande wa huko ili tujiridhishe kama taarifa wanazotupa wachungaji ni sahihi ili mwenye ng’ombe wake ajiridhishe kwa sababu kama alivyosema tulimchagua Watanzania kwenda kusimamia rasilimali hizi ili ziweze kutunufaisha wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo makubwa sana huko vijijini, leo barabara za Kinole, Mkuyuni na Mkulazi hazipitiki. Tatizo kubwa hatuna rasilimali fedha ya kuweza kuzitengeneza, tunaambiwa maskini na tunadanganywa kwa misaada midogomidogo kumbe kama Taifa, kama anavyosema Mheshimiwa Rais, tuna uchumi mzuri na mapato mazuri. Kwa mwendo huu aliouanza naamini barabara zote hizo zitaweza kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, niende kwenye mchango wangu wa leo. Mchango wangu wa leo kitu cha kwanza naomba kuishauri Serikali, pamoja na bajeti nzuri na mipango mizuri na nia nzuri ya kuwatumikia Watanzania lakini nataka kupendekeza kwenye mfumo wetu wa bajeti. Sina tatizo na mfumo wetu wa cash budget kwa maana kwamba utekelezaji wake unategemeana na mfumo wa upatikanaji wa fedha, shida yangu kidogo iko kwenye huo utekelezaji.

Leo hapa kama Bunge tumekaa tumekubaliana au tulishakubaliana haya yaliyoletwa na Waziri kwenye bajeti kuu au bajeti za kisekta tunaamini ndiyo vipaumbele na ndiyo mipango ambayo wananchi wametutuma ili kwenda kuitekeleza. Kwa mfano inatokea wakati mwingine ile mipango tuliyokubaliana humu haikutekelezwa na mwaka wa fedha umekwisha, mwakani tukija ingawa tunaanza zero na ile mipango yote tuliyoipanga msimu uliopita tunaisahau kama vile tulishaikamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nataka nitoe mfano kabisa, nianze na mfano wa Kitaifa kabla sijaenda kwenye Jimbo. Kama Taifa katika kwenda kwenye uchumi wa viwanda au wa kipato cha kati tulikubaliana mwanzoni lazima tuongeze uzalishaji kwenye kilimo, kuboresha
miundombinu kwa miaka mitano iliyopita. Kwa bahati mbaya sana kilimo chetu hakikuboreka miaka mitano kuanzia 2010 mpaka 2015 lakini bado leo tulivyoanza 2015 Mpango wa Miaka Mitano tumeacha mambo ya kilimo, kuimarisha uzalishaji na kuongeza tija katika kilimo kama vile tulishakamilisha kila kitu na kilimo kinakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi upo katika kitabu chako mwenye Mheshimiwa Waziri umesema kabisa hali ya kilimo haiendi vizuri, kilimo kinashuka kutoka asilimia 2.3 kwenda asilimia 2.1. Nilitarajia kwamba sasa uje na mikakati mizuri ya kwenda kuimarisha kilimo lakini sasa tumekiacha kama vile tulishamaliza. Niseme kabisa Taifa hili tunategemea sana kilimo, zaidi ya asilimia 70 tunategemea kilimo, tukiacha sekta hii nyuma maana yake tumewaacha Watanzania wengi nyuma.

Kwa hiyo, kwa sababu hizi sekta nyingine ni consumption, ukizungumza afya na elimu zinahitaji fedha, lakini hii tukiiimarisha ni sekta ya kiuzalishaji, ni ya haraka sana kutubadilishia uchumi wa wananchi wetu mmoja mmoja lakini pia uchumi wa Taifa, itatuongezea mapato ya kigeni ili kuweza kuimarisha uchumi wetu kama Taifa. Pamoja na kwamba labda ilisahaulika, niishauri Serikali kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mapendekezo katika hili, miongoni mwa changamoto tunazozipata kwenye kilimo moja ni upatikanaji wa mbegu. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali kwa sababu resource ni ndogo tukawezesha vyombo vyote vya usalama, hususan Magereza tukatafuta mashamba yao kwa sababu wanayo ya kutosha tukawekeza bwawa kubwa la umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha kisasa ili tuzalishe mbegu. Tuanzie hapo tu, tuzalishe mbegu ili tuondokane kabisa na tatizo la upatikanaji wa mbegu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ili kuimarisha uzalishaji ni vizuri kuingia mikataba na makampuni wazoefu wenye teknolojia, wenye ujuzi, wenye ufahamu katika mazao kwa ajili ya kuzalisha miche kwa ajili ya mazao ya biashara. Kwa mfano, kama wanavyofanya Naliendele kwa ajili ya korosho, tutafute sasa watu wenye uzoefu ili wazalishe miche kwa ajili ya kahawa, kokoa, mazao yote ya muda mrefu na kuigawa bure kwa Watanzania yaani ruzuku ipelekwe kwenye kuzalisha tu hiyo miche halafu tuigawe bure kwa Watanzania ili tuweze kuongeza uzalishaji mkubwa sana katika mazao ya kilimo ili tuondoke hapa tulipo kwenda mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema tatizo kubwa la mfumuko wa bei ni suala la ukame na upatikanaji wa maji. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, ni vizuri mngeweka sasa mikakati ya kuondokana na kukabiliana na ukame na ukosefu wa mvua kwa kujenga mabwawa na majosho kwa ajili ya wafugaji na mambo yote ambayo yanahusiana na maji, hatuwezi kujenga nchi nzima lakini tunaweza tukaanza na sehemu fulani. Mheshimiwa Waziri anafahamu tuna Bwawa la Kidunda ni la muda mrefu sana. Kwa nini tusingeanza na hili ili liweze kutumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kulisha Taifa hili na tuwe na uhakika wa chakula, malighafi na ajira kwa watu wetu, hususan wanaoweza kuishi vijijini na sehemu nyingine zipo fursa nyingi za kutengeneza mabwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu katika suala la leo, nikupe mfano mwingine kuhusu mfumo ule wa bajeti. Kwa mfano, mwaka jana mlitutengea shilingi bilioni 17 kwa ajili ya kulipa fidia kwa watu waliopisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda pamoja na kutengeneza ile barabara ya kwenda Kidunda. Hata hivyo, mpaka leo hata senti tano haijafika na tumebakiza wiki mbili tunamaliza mwaka. Kwenye bajeti mmetutengea shilingi bilioni 1.5 kwa Bwawa hilo la Kidunda wakati fidia tupu inadaiwa shilingi bilioni nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wiki mbili hizo zikiisha tutawaambia nini wananchi maana mnatusababishia ugomvi mkubwa sana na wananchi Mheshimiwa Waziri kwa kushindwa kutekeleza bajeti kama ilivyopangwa. Kwa sababu sisi kama wawakilishi wa wananchi tukitumwa hapa

tumetumwa na wananchi kuja kuleta shida zao baadaye tukirudi tuwaeleze Serikali imewapangia kuwafanyia nini. Kama mwaka jana nimewaeleza wametengewa shilingi bilioni 17 kwa ajili ya kutengeneza barabara hiyo pamoja na kulipwa fidia yao. Mwaka jana nimewaambia watu wa Kinole wametengewa shilingi milioni 105 kwa ajili ya kutengenezea barabara yao, barabara ile haijatengenezwa mpaka leo na leo kuna ugomvi mkubwa sana inaonekana kama vile Mbunge hawasemei wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu utakwisha na mwakani hata nikimdai Meneja wa TANROADS atasema haipo kwenye bajeti, nikimdai Meneja wa Maji anasema kwamba haipo kwenye bajeti mwaka huu Mheshimiwa tumetengewa shilingi bilioni 1.5, kwa hiyo haiwezekani kutekeleza tusubiri mwakani. Nikuombe sana, ni vizuri muuangalie mfumo huu wa bajeti ili uendane na hali halisi kwa sababu yale mnayotuambia hapa tunakwenda kwa wananchi kuwaeleza, sasa isije kuonekana kama sisi viongozi tunasema uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nichukue nafasi hii tena kuunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. Ahsante sana, Mwenyezi Mungu ampe uhai mrefu na uzima Rais wetu ili aweze kuonesha maajabu ndani ya nchi yetu, ndani ya Afrika na ndani ya dunia. Rais Trump alisema Waafrika wengi tatizo tuna Marais wezi, lakini Mheshimiwa Dkt. Magufuli amemhakikishia hakuna Marais wezi, tuna Marais wazalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie Mpango wa Serikali uliokuwa mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nichukue nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Mpango, Naibu Waziri wake na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Doto kwa kuandaa Mpango huu na kuletwa hapa Bungeni ili sisi Wabunge tuweze kutoa mchango wetu na pale kwenye mapungufu tuweze kuongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze sana Serikali kwa kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA). Ni wakala ambaye anaenda kutatua changamoto za miundombinu, hususan kule vijini kwetu tunakotoka. Hii maana yake nini kwamba, mawasiliano kati ya wakulima kutoka sehemu moja mpaka sehemu nyingine yanakuwa ni rahisi zaidi, lakini pia wakulima tunapata nafasi nzuri ya kupeleka mazao yetu sokoni na kupunguza gharama na kuongeza vipato kwa wakulima wetu. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa kuanzisha na kuihamasisha Mifuko ya Jamii kuingia kwenye kuwekeza katika viwanda, hususan kiwanda cha kielelezo, Kiwanda cha Mkulazi. Nawapongeza sana, kwa sababu kinaenda kujibu tatizo la nchi la upungufu wa sukari. Baada ya kiwanda hiki kuisha matatizo ya sukari yatapungua sana nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo nianze kuchangia kwenye Mpango, na mi mi kwa sababu natoka kijijini, ninatoka Wilaya ya Morogoro Vijijini lazima nitajikita zaidi kwenye suala la kilimo kwa sababu ndiyo suala linalogusa wananchi walio wengi katika maeneo yangu ni suala linalogusa Watanzania wengi. Kwa sababu zaidi ya Watanzania asilimia 70 wako vijijini na wanategemea kilimo kwa chakula pamoja na shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Mawenyekiti, nataka tu ni-quote vitu kidogo kwenye Azimio la Arusha, kule mwanzo kabisa. Azimio la Arusha lilizungumza kabisa maendeleo ya nchi yataletwa na watu, hayaletwi na fedha. Fedha ni matokeo sio msingi wa maendeleo. Ili tuendelee tunahitaji vitu vinne, watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Watu tunao zaidi ya milioni 55, ardhi tunayo tena yenye rutuba na mito inayotiririka, siasa safi tunayo ambayo ni siasa ya ujamaa na kujitegemea, uongozi bora tunao, uongozi wenye sera nzuri za Chama cha Mapinduzi. Tatizo ni nini tunakwenda kwa taratibu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba tumewaacha watu wengi katika ushiriki wa kiuchumi katika Taifa letu. Watu hao ni nani? Ni wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najikita kwa wakulima kwa sababu kama nilivyosema ndiko ninakotoka huko, huwezi kusema nchi hii tutaendelea kama hatujaweza kuongeza kipato cha watu walio wengi wa Tanzania ambao ni wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu kilimo chenyewe kinakua taratibu sana, lakini pia hata uwekezaji wa kilimo kwa Serikali bado uko chini sana kwa hiyo, maana yake ni nini, tunawa-sideline watu wengi Watanzania wako nyuma. Kama kilimo kinakuwa taratibu maana yake kipato cha Watanzania wengi nacho kitakua taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Azimio la Arusha liliwahi kuzungumza kwamba tusipotahadhari kwa sababu watu wanasema ukizungumza unyonyaji watu wengi wanafikiria ubepari, lakini Azimio la Arusha lilizungumza kwamba, kuna unyonyaji mwingine kama hatukuchukua tahadhari na Serikali isipochukua tahadhari tunaweza kuzalisha unyonyaji mwingine ndani ya nchi kati ya wafanyakazi tunaoishi mjini na wafanyabiashara tunaoishi mjini na wakulima wengi wanaoishi vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu wakulima hawa ndio tunawategemea kwa ajili ya uzalishaji wa chakula. Wakulima hawa ndio tunawategemea kwa ajili ya uzalishaji wa malighafi za viwanda vyetu, lakini tutapata dhambi kama hatuwaangalii, hatuwatengenezei mazingira mazuri ya mazao yao kupata bei nzuri zaidi ili waweze kuwainua kimapato kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja, mimi natoka Morogoro ni wakulima wazuri sana wa mpunga, mahindi na mbaazi, lakini leo hii wakati wa msimu wakulima ukianzia kule Mikese, Tomondo, Kikundi na sehemu zingine tulikuwa tunauza mahindi debe moja zaidi ya shilingi 10,000, kilo zaidi ya shilingi 600, lakini leo hii mahindi ni shilingi 450. Wakati ule tunavuna ambapo kila sehemu Tanzania watu wanavuna sisi mahindi yalikuwa ni shilingi 600 leo hii hakuna msimu mahindi shilingi 450. Ndiyo maana ninaishauri Serikali kwamba tusipokuwa waangalifu tunazalisha unyonjaji, watu wa mjini kuwanyonya watu wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya wakulima yanayozalishwa mahindi tunawalazimisha wauze bei ya chini ili watu wa mjini na wafanyabisahara tupate chakula kwa bei nafuu, lakini wenyewe wakulima bidhaa zinazozalishwa mjini kwenda vijijini bei zake ziko palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia sukari bei iko palepale, tukizungumza sabuni bei iko palepale, tukizungumza nguo bei ziko palepale, tukizungumza mafuta bei iko palepale, tukizungumza tiles bei ziko palepale. Mkulima anachotoka kununua bei zinapanda, mkulima kitu kinachomuingizia kipato bei zinashuka, bora zingeshuka kwa nguvu za soko kuliko kushuka kwa kutengeneza mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hawa hawakulima mahindi haya kwa bahati mbaya, walilima kutokana na bei nzuri ya mwaka jana ambayo mahindi yalifika zaidi ya shilingi 2,000 ndiyo maana watu walihamasika mpaka wengine walichukua mikopo kwenda kununua, lakini leo kuna watu wanasema kuna wafanyabiashara wamenunua mahindi ndio wanaolalamika wanataka kufaidika, hili sio kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ina dhana kwamba, wamepiga marufuku kwa sababu wafanyabishara wamenunua mahindi wameyahifadhi watafaidika sio sahihi, kwa sababu mkulima huyu anayelima kama nilivyosema mwanzoni anategemea kilimo kwa sababu ya chakula, anategemea kilimo kwa sababu ya kipato chake, anachokihifadhi ni chakula tu. (Makofi)

Kwa hiyo, ukikataza kwamba mahindi yasiwe na bei nzuri unamuumiza mkulima auze bei ndogo kwa wafanyabiashara na watu wengine. Hamna namna yoyote ataacha kuuza kwa sababu ndio kipato chake, lakini pia hana mahali pa kuhifadhi. Mtu amelima amepata gunia 200 ama 300 kuna mkulima gani wa kijijini ana uwezo wa kuhifadhi gunia 200? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali inaona kwamba kumsaidia mkulima ni kuzuia mahindi yasiende nje ya nchi, basi ni kumuumiza kwa sababu wakulima ni lazima wauze. Ni kweli mahindi mengi yapo kwa wafanyabiashara na mahindi machache yako kwa wakulima, tangu lini imekuwa dhambi kufanya biashara kwenye nchi hii, tangu lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ajira hamna tunawahamasisha watu wakafanye biashara, wamechukua mikopo, wamechukua hela zao wamekwenda kununua, kwa mkulima anamuona ndio mwokozi wakati wa msimu ili kutatua changamoto zake, amemuuzia mahindi, ameyahifadhi, ana mkopo, leo unamwambia asiuze. Ndio maana Mheshimiwa Dkt. Mpango leo unaona mikopo chechefu inaongezeka kwenye mabenki. Inaongezeka kwa sababu miongoni mwa watu waliokopa benki ni hao wafanyabiashara wa mahindi na hao wafanyabiashara wa mazao tuliyopiga marufuku yasiweze kuuzwa nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali, na ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, tutumie fursa ya mahitaji makubwa ya mahindi yetu Kenya, fursa ya mahindi yetu Sudan Kusini, fursa ya mahindi yetu kuhitajika Uganda, tuziangalie kama fursa tusiziangalie kama changamoto. Tutanue soko letu la mahindi tupeleke zaidi ili tuongeze uzalishaji zaidi miaka ijayo na mwakani, kwa sababu vuli hizi tukifika mwezi wa pili/tatu mahindi watu wakianza kuvuna vuli, mahindi yatakuwa zaidi ya shilingi 300, sijui kama tumemsaidia mkulima, hatujamsaidia mfanyabiashara zaidi ni kuwarudisha watu kimapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu Serikali fanyeni tafiti. Waruhusuni wakulima wakubwa na wafanyabiashara wauze mahindi haya ili waweze kulipa mikopo waliyokopa na kurudisha tija kwa uwekezaji wao kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninalotaka kuzungumzia kwenye suala la mbaazi kwa sababu linatugusa, hapa ndiyo hii dhana ambayo ilikuwepo. Sasa hivi kuna baadhi ya watu wanafikiria kufanya biashara ni dhambi, akiambiwa kuna dalali ni mwizi, akiambiwa kuna wakala ni mwizi, akiambiwa kuna mfanyabiashara ni mwizi! Hatuwezi kujenga, hata hiyo kauli tunayosema kwamba tunataka tushirikiane na wafanyabiashara binafsi maana yake wafanyabiashara binafsi ni wafanyabiashara, sasa ukiwaweka kwenye kundi la wezi hatuwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dhana ilijengeka kwamba ukiongea na mnunuzi wa mwisho basi utapata bei nzuri, hili ni kosa kubwa ambalo tulilifanya kwenye mbaazi mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja hapa Waziri Mkuu wa India ambaye ndiye mnunuzi mkubwa na mwenye bei nzuri wa mbaazi. Serikali tukaongea naye, tukamwambia kwamba sisi ndiyo wazalishaji wakubwa wa mbaazi, tunazo mbaazi za kutosha ila walanguzi tu ndiyo wanakuja kutununulia hapa, njooni ninyi wenyewe. Kwa taarifa baada ya pale aliwaita wanunuzi wote 16 hapa nchini wa kununua mbaazi akawaambia naomba muanzishe wakala wenu, umoja wenu wa kununua mbaazi Tanzania na sitaki mtu yeyote anunue mpaka aje kwanza kupata kibali. Tumekiona mwaka huu, mbaazi kutoka shilingi 2,000 mpaka shilingi 150.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mjue kwamba biashara ni taarifa, kama mimi nina taarifa wewe huna ndiyo mimi nitafanya biashara na kupata faida. Kama mnunuzi wa mwisho amejua kwamba kumbe mbaazi inapatikana Tanzania ana haraka gani ya kuongeza bei? Kwa hiyo, alichokifanya amefanya syndicate kwa wafanyabiashara wote wakubwa akawaambia huwezi kununua, kwa sababu mwanzoni bei zilikuwa zinapanda kutokana na uzoefu, weledi wa hao wafanyabiashara kwa sababu wamewekeza, wamechukua mikopo, wana wafanyakazi lazima wanunue. Wao wanafanya tafiti, wanajua mbaazi hizi zinahitajika lini, nani anahitaji na kwa kiasi gani. Kwa hiyo, wanajua kucheza na yule mnunuzi wa mwisho. Wana uwezo wa kununua bei kubwa kuliko iliyoko katika soko la dunia lakini wanajua nae anahitaji lini, wanazi-hold wanamwambia hatuna mbaazi kama hutaki bei yetu hatuuzi, ndiyo maana bei inapanda. Lakini wafanyabishara wale kwa sababu wanajua wanamdanganya kumbe wakati mwingine mbaazi ni nyingi lakini wanamwambia sharti kwa ajili ya kufanya biashara, hakuna!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri katika hilo. Baada ya hapo Dkt. Mpango na Waziri wa Viwanda, kaeni na wadau/wafanyabiashara wa mazao mbalimbali mjue mahitaji ni nini, ubora gani unaohitajika, wakati gani. Kwa sababu wao wana uzoefu wa kutosha, wana mitaji hawategemewi Watanzania peke yake, wanategemewa dunia nzima wanunuzi ndiyo hao hao ukizunguka.

Kwa hiyo, wao wanaweza kujua kwamba kwa nini mbaazi zimeshuka na kwa nini mazao mengine yamepanda. Watu wengi wanataka kupotosha kusema kwamba biashara ya mbaazi imeshuka kwa sababu ya soko holela na biashara ya korosho bei inapanda kwa sababu ya udhibiti wa soko, siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya mbaazi inashuka kwa sababu ni zao la muda mfupi, zao la muda mfupi mwaka huu ukipata hela na nchi nyingine zitalima kwa sababu ni zao la miezi mitatu, miezi sita. Kwa hiyo, baadae supply inakuwa ni kubwa kuliko demand. Korosho, hata akikuta 4,000 huwezi kupanda leo ukavuna, tusubiri baada ya miaka mitano au kumi, hizi bei zilizoenda utakuja kuona hali itakuwaje. Ndiyo maana ushahidi unauona, Serikali ya India ndiyo wabanguaji wakubwa wa korosho baada ya Vietnam zaidi ya tani milioni moja lakini uzalishaji wao kila siku unashuka wanazidi ku-import...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Elimu.
Kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa nafasi hiyo aliyokuwa nayo. Kama ni mchezaji huyu ni wa kulipwa. Kwa sababu wachezaji local tulikuwepo Wabunge wa CCM wengi lakini kwa mamlaka yake Mheshimiwa Rais alisajili wachezaji wa kulipwa, wewe ni mmojawapo na alikupeleka katika Wizara hii si kwa bahati mbaya. Mimi nasema kama ni upele umepata mwenye kucha, hongera sana mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye mchango wangu ingawa wenzangu wengi wamesema lakini na mimi nirudie tu, hasa kwenye ubora wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, ukiangalia na records za nyuma bajeti ya elimu inaongezeka mwaka hadi mwaka, miundombinu inajengwa tukiwashirikisha wazazi, wananchi kwa mfumo uliopo sasa hivi wa D by D, walimu wanaongezeka, Serikali inajitahidi kuajiri walimu wengi na wanafunzi pia wameongezeka, kwa maana hata mwaka huu baada ya elimu bure tumeona wameongezeka wengi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa, output ya elimu na kiwango cha elimu kila siku kinashuka! Sasa ni suala la kujiuliza, kama vitu vyote hivi vinaongezeka, pesa zinaongezeka, madarasa yanaongezeka, vitabu vinaongezeka, lakini elimu inarudi nyuma; tatizo tumejikwaa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni shahidi; yeye mwenyewe amesema kwamba, yeye ni zao la shule za Serikali, Tabora Girls na ametokea huko. Jambo moja tu, hata yeye mwenyewe akienda Tabora Girls leo, ile aliyosoma yeye. Ndiyo leo inafanana na Tabora Girls? Elimu aliyopata pale Tabora Girls, ndiyo ile inayotolewa pale leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mwanzo nimesema, upele umempata mwenye kucha kwa sababu umepata elimu bora na kupitia Serikali hiyo hiyo, sasa umepewa jukumu la kusimamia Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa kabisa ambalo naliona kwa upeo wangu; moja ni kukosa uzalendo na kuzipenda shule hizi hasa kwa sisi viongozi. Nasema hili kwa sababu tulikuwa na Serikali yetu ya CCM ya Awamu ya Kwanza, tulikuwa na Awamu ya Pili na Awamu ya Tatu. Wengine sisi tulianza Awamu ya Pili mpaka ya Tatu, tulikuwa tunasoma huko na watoto wa viongozi. Wote! Yaani mtu akichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Serikali ni sherehe kijijini au kwenye familia. Leo hii mtu akichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Serikali, ni kilio! Anaambiwa mwanangu nitakutafutia Private uende. Tena mbaya zaidi, hata viongozi wenyewe waliokuwa hata Serikalini, watoto wao wanaosomesha kwenye Shule za Serikali wanahesabika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unategemea nini kama wewe mwenye jukumu la kusimamia na kuboresha hiyo elimu, watoto wako wote hawasomi pale? Wanasoma Ulaya na shule zile ambazo ni za private, zinatoa elimu bora. Kwa hiyo, wewe mwenyewe kiongozi unakubali kwamba zile shule zetu za Serikali hazitoi elimu bora. Sasa nawaomba, ili tuweze kuziboresha kwa ukweli hizi shule, kwanza sisi viongozi turudishe watoto huko; kwa sababu tunajifahamu, hata kule vijijini kwetu, ukisikia kesho mwenge unakuja, ndiyo barabara inachongwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kurudisha watoto wetu waende huko, hata Walimu, kwa sababu utakuwa unapata mrejesho kama kiongozi au Waziri, kila mtoto anapokuja kama anapata elimu bora au sivyo. Hata wale Walimu wa kule lazima wataboresha mazingira ya elimu kwa sababu wanajua mkubwa atafahamu. Kwa hiyo, ukosefu wa ubora wa elimu, output tunapata ndogo ni kutokana na sisi wenyewe dhambi hii tumeibeba. Kama ile ile ya kutokuthamini vyetu, tunathamini vya wageni, sasa tunathamini hata shule nyingine za private na nyingine, tunaacha za kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika suala la ada elekezi, nawezekana nikatofautiana kidogo na wengine. Wengi hapa walikuwa wanazungumza; walikuwa wanasema kwamba, Serikali haina haki ya kuweka ada elekezi katika suala la elimu. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hili suala la ada elekezi ni mjadala mpana.
Kama sisi humu humu Wabunge tulikuwa tunaisema Serikali hii hii, nitoe mfano mmoja hasa wa sukari; tumesema bei elekezi ya sukari ni shilingi 1,800/=. Kwanini Serikali hamsimamii bei iuzwe 1,800/=? Leo mazao ya wakulima iwe pamba, iwe korosho, iwe tumbaku yanawekewa bei elekezi; mafuta yanawekewa bei elekezi, umeme una bei elekezi, kwanini shule zisiwe na bei elekezi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali wateja wake ni wananchi masikini wa Taifa hili, zaidi ya asilimia 70 wanaishi vijijini, kama tukiacha tu tuseme, watu hawa hizi shule ni za kwao, wamekopa, ndiyo ile kwamba tumegeuza elimu ni biashara badala ya huduma. Kwa hiyo, ni vizuri, kwa sababu hata kwenye mazao, pande mbili za wadau wanakaa; wanunuzi, wazalishaji, wakulima na wadau wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali, wakae na wadau wa wamiliki wa shule na wazazi na Serikali yenyewe wapange bei elekezi kutoka na ubora wa shule, wazi-categorize katika qualities zake. Kwa sababu tunakubali kweli kuna shule nyingine zina hali ya juu zaidi, nyingine ni za kati, nyingine ni za chini, lakini zote bei haziwezi kufanana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hapa, kuna hoja ambayo ilikuja upande wa pili kule na ilitolewa mfano wa Shule ya Sekondari ya Almuntazir wanazungumza kwamba imepandishwa bei imekuwa kubwa kutoka shilingi1,600, 000/= mpaka shilingi milioni 1,900,000/=. Mimi nikajiuliza, yaani labda ni factor gani imetumika kuichagua shule hii moja badala kutolea shule nyingi? Kwa sababu kuna shule nyingine nyingi zina ada kubwa zaidi kuliko hii ya Almuntazir. Kuna shule zina ada mpaka shilingi milioni 70, nyingine shilingi milioni 35, nyingine shilingi milioni 20, nyingine shilingi milioni tano, nyingine shilingi milioni tatu; lakini amekuja kuichagua Almuntazir yenye shilingi 1,900,000/=. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tutende haki, tunapotoa maoni yetu, tuweke maoni ya jumla, tusionekane kama tunabagua jamii fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niongelee kuhusu Jimbo langu. Sisi ni Halmashauri ya Morogoro na jukumu moja la Wizara hii, linasema kwamba, ni kusimamia elimu ya ufundi. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, ukija hapa uniambie umejipanga vipi katika kutuunga mkono katika Chuo cha VETA katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini? Kwa sababu eneo tunalo, wananchi wameshajitolea, lakini tatizo tu hatujapata kushikwa mkono na Serikali kwa miaka mingi na Chuo hicho hatuna. Hii inasababisha wanafunzi wengi wanaoishia Kidato cha Nne na cha Sita kukosa nafasi ya kuendelea na elimu ya ufundi baada kukosa nafasi ya Chuo Kikuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi jioni hii nami niwe mchangiaji wa kwanza kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha uhai na uzima tumeonana jioni hii ya leo. Katika mchango wangu wa kwanza ninaishukuru Serikali kwa utendaji mzuri ambao wanaufanya na wanatutumikia watu wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nichukue nafasi hii kuwapa pole sana wananchi wa Kata ya Matombo, Halmashauri ya Morogoro Vijijini na wanachama wa CCM kwa ujumla kwa kuondokewa na Diwani wetu wa Viti Maalum asubuhi hii ya leo, Mheshimiwa Zuhura Mfaume aliyetangulia mbele ya haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwape pole wananchi wangu wa Kijiji cha Kisanga Stendi, Kata ya Tununguo, Tarafa ya Ngerengere ambao siku mbili zilizopita walivamiwa na majambazi na ndugu Mbaga amefariki dunia kwa kupigwa risasi na watu wengine sita wamepigwa risasi ni majeruhi bado wapo hospitalini. Waliotangulia mbele ya haki Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema na wale ambao wako kwenye majeruhi wapate nafuu wapone haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba nilitoa pongezi za awali lakini kuna watu wengine wanaona kwamba labda tukitoa pongezi ni kama kujipendekeza Serikalini au tunataka tuipake mafuta Serikali yetu, lakini mimi kama mwakilishi wa Morogoro Vijijini na watu wa Morogoro Vijijini tusipoishukuru Serikali hii ya Awamu ya Tano tutakuwa hatujatenda haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni mzoefu ni mmoja wa wakongwe nchi hii, unafahamu Morogoro ilikuwa ndiyo mji wa viwanda pamoja na Tanga, ilikuwa ni ndoto za Mwalimu Nyerere na Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa Mbunge wetu wa kwanza Mkoa wa Morogoro, wa pili alikuwa Ndugu Kambona, tatu alikuwa Ahmed Jamal, tangu aondoke Ahmed Jamal Morogoro ilirudi nyuma kiviwanda, hapo katikati tuliyumba sana, hata vile vilivyobinafsishwa vilikuwa havifanyi kazi sawasawa.

Sasa Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuja kuufufua Mkoa wa Morogoro ninyi wenyewe ni mashahidi kila akipita alikuwa akisimama Msamvu ni juhudi kuwahamasisha waliochukua viwanda wavifufue, hasa vile vilivyokuwa vinafugiwa mpaka mbuzi. Pia akatutafutia viwanda vipya vitatu, tena hivyo vitatu vimekuja kwenye Jimbo langu la Morogoro Vijijini, kwa nini nisimshukuru? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kujipendekeza ni ili kupewa kiwanda kikubwa cha sukari zaidi ya kuzalisha tani laki mbili ambapo kitaajiri watu laki moja acha nijipendekeze. Kama kujipendekeza kuletewa Kiwanda cha Kuchakata Mbaazi katika Jimbo langu acha nijipendekeze, kama kujipendekeza ni kuletewa Kiwanda cha Sigara cha kutengeneza Marlboro ambayo inakwenda kuuzwa Marekani kwenye Jimbo langu acha nijipendekeze, kama kujipendekeza ni kuletewa shilingi milioni 500 Februari mwaka huu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika Jimbo langu acha nijipendekeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kujipendekeza ni kuletewa zaidi ya bilioni nne kwa miradi ya maji katika Kijiji cha Fulwe - Mikese, Kijiji cha Kiziwa milioni 700, Kijiji cha Kibwaya milioni 600, Kijiji cha Nyumbu milioni 600 pamoja na Tulo-Kongwa acha nijipendekeze. Kama kujipendekeza ni kuja kuweka kambi ya ujenzi wa Standard Gauge reli ya kisasa katika Kata yangu ya Ngerengere nyumba zaidi ya 70 zinajengwa kwa ajili ya watumishi wakiondoka, acha nijipendekeze, kama kujipendekeza ni kutengeneza barabara ya kutoka Ngerengere - Maturi - Kwaba - Mkulazi mpaka Kidunda kwa thamani ya one point eight billion acha nijipendekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hapa mengi ambayo tumefanyiwa kwenye Jimbo langu sitaki Jimbo la mtu mwingine nitajipendekeza sana kwenye Serikali hii. Kama kujipendekeza barabara ya kwenda Stieglers Gorge ipitie kwenye Jimbo langu kutoka Ubena Zomozi - Ngerengere - Tunungua mpaka Mvua acha nijipendekeze. Kama kujipendekeza ni kuletewa 1.5 billion shillings kuweka kwenye mpango kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ambayo tuliiomba hapa Bunge lililopita acha nijipendekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kujipendekeza ni kujengewa kituo cha afya cha milioni 400 kwenye Kata yangu ya Mkuyuni acha nijipendekeze. Nayasema haya wenzetu hata kwenye mitandao wanapotosha sana, wanasema Wabunge wa CCM kazi yao wakifika ni kuisifia tu Serikali ya CCM kama imefanya nini. Nawaambia kama wale watu haya wanajua ni uwongo waje katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, ndani ya Halmashauri ya Morogoro, Mkoani Morogoro waje wayaone haya ambayo yamefanyika, kama hawajajipendekeza na wao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo pamoja na mafanikio ndiyo maana uongozi uko kwa miaka mitano na kila mwaka tunapanga bajeti tunakuja kuwasemea wananchi wetu Serikali inayachukua kwa kufanya maboresho kwa ajili ya kuondoa changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM katika Jimbo langu, katika Halmashauri yangu lakini nina maombi machache ndani ya Serikali yangu.

Kwanza katika yote ni barabara ya Bigwa - Kisaki kujengwa kwa kiwango cha lami, hii barabara iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini ni ya muda mrefu. Kama mnakumbuka ndiyo barabara mbili tu ambazo zilichaguliwa kujengwa kwa msaada wa Serikali ya Marekani, baada ya Serikali ya Marekani kujiondoa hii barabara Serikali imesema itaichukua na bahati nzuri Mheshimiwa Rais akiwa Waziri wa Ujenzi wakati Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, anakuja kutuaga katika Jimbo letu alimkabidhi kiporo hicho na aliahidi kwamba atakitekeleza.

Niwaombe sana, hii barabara uchambuzi yakinifu na usanifu wa kina umemalizika, hii barabara ni muhimu kwetu na sasa hivi umuhimu wake umeongezeka zaidi ukizingatia Serikali kupitia Wizara ya Maliasili inataka kufungua utalii kule Kusini kwenda Selous kupitia barabara hiyo. Niwaombe sana tuitengeneze barabara hii ili utalii wetu uende vizuri, lakini pia ni barabara mbadala kutoka Mjini kwenda huko Kisaki, kwenda Stieglers mpaka Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara hii ndiyo inakwenda Makao Makuu ya Wilaya ambayo Mheshimiwa Rais ametuhamisha kwa fedha zake na kwa amri zake sasa hivi tuko Vijijini. Ni kweli Morogoro Vijijini na Makao Makuu yetu yako Morogoro Vijijini, niwaombe sana barabara hii isiishe angalau ndani ya miaka mitano basi ianze angalau wananchi wale wawe na matumaini.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilishukuru kuhusu ujenzi wa kiwanda chetu cha sukari katika Jimbo langu. Hakuna mazuri ambayo hayaji na changamoto, kwa sababu kiwanda hiki kitaajiri watu zaidi ya laki moja, watu wenye ajira rasmi na wasiokuwa rasmi itaongeza mahitaji ya huduma za jamii makubwa kwa muda mfupi. Kwa taarifa kiwanda hiki mashine zake zilishaagizwa, zilishaanza kutengenezwa na kitaanza kujengwa mwishoni mwa mwaka huu na kitaanza kuzalisha mwakani Septemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana kwa sababu watakuwa ni watu wengi wanakuja kwa mara moja, tuziangalie Kata hizi za Maturi na Mkulazi kinapojengwa kiwanda kile hasa ujenzi wa kituo cha afya pamoja na shule ya sekondari ukizingatia ile Kata ya Maturi ni mpya, tumeshaanza wenyewe tumejenga madarasa mawili na tunaendelea lakini kwa ujio wa wakazi hawa wapya hatutoweza kumudu kwa mambo ya shule na vituo vya afya na zahanati kwa wakati mmoja kuwa-accommodate watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili pili; barabara hiyo ambayo imetengenezwa mwaka huu, niwaombe sijaiona kwenye mipango ya TARURA, barabara ni ndefu sana ina kilometa zaidi ya 80 ambayo kwa sasa tunasaidiwa na mwekezaji, lakini tukiiacha barabara hii iendelee kuhudumiwa na mwekezaji tutaongeza gharama za uwekezaji na ule uwekezaji utakuwa hauna tija au utakuwa na gharama kubwa kwa mwekezaji wetu.

Niwaombe sana Serikali muichukue barabara hii muiingize kwenye mipango yenu ili muitengeneze kurahisisha kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji ule na kuwavutia watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kwenye mkazo wa elimu. Hapa ninataka niongee Kitaifa zaidi, hapa nataka niiongelee UDOM. Serikali ipo hapa mimi ni mmoja ambaye nimepitia vyuo hivyo vyote viwili UDSM na UDOM, nimefika pale kama tunavyofahamu kile Chuo kilitakiwa kijengwe vitivo saba, vitivo viwili bado havijakamilika na Mheshimiwa Rais alishaahidi anatakiwa kukumbushwa tu, mara nyingi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akiahidi lazima anatekeleza, tuliona alifanya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa hiyo niwaombe sana mpelekeeni salamu ili amalizie atupatie fedha pale UDOM waweze kumalizia vile vitivo viwili ili lile lengo lililokusudiwa liweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu UDOM kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 45,000 lakini mpaka sasa kimedahili wanafunzi 30,000 tu, madarasa yapo, vyumba vipo, nyumba zipo kila kitu, tatizo kubwa liko kwa wahadhiri ni wachache. Ninakuomba Waziri wa Utumishi katika mipango yako uje utuambie umewaandalia nini watu wa UDOM kwa ajili ya kuongeza watumishi (wahadhiri) ili waweze kudahili wanafunzi wengi zaidi na yale majengo yote yaweze kutumika na lengo letu pale UDOM liweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la elimu niongelee kuhusu ubora wa elimu. Katika ubora wa elimu huu mara nyingi unashuka, matatizo yako mengi katika ngazi mbalimbali, ngazi za msingi, sekondari mpaka chuo lakini leo nataka nijikite kwenye vyuo vikuu. Elimu yetu mara nyingi watu wanasema kwamba wanatoka vyuo vikuu lakini hawaajiriki. Miongoni mwa changamoto nilizoziona ni usimamizi wa wale…….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kupata nafasi ya kuchangia mjadala huu kuhusu Hotuba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa afya na uzima tumekutana asubuhi ya leo kuchangia Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia viwanda vitatu vipya katika Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki, Mkulazi One, Philip Morris na Mahashree cha kuchakata mbaazi, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu kama Magufuli asingekuwa Rais, Mkulazi One isingekuja Mkulazi, kiwanda kile cha sukari kisingekuja pale na leo nitazungumzia hoja hii tu moja mwanzo mwisho, nikipata muda nitazungumzia ya pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa na ziara na Mheshimiwa Rais pale Morogoro na nilimweleza hili, nilimwambia mchakato wa kujengewa Kiwanda cha Sukari Mkulazi kilianza tangu mwaka 2016 mpaka leo Serikali yako ina mchakato, kiwanda hakijaanza kutengenezwa. Nilimwambia wanaokukwamisha wapo ndani ya Serikali na chama chako, tupo Bungeni na sehemu nyingine kwenye taasisi za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo habari zilikuwa za mtaani, leo nimezipata rasmi kwenye ukurasa wa 32 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri; anasema kiwanda cha kutengeneza sukari cha Mkulazi One kilichokuwa pale Morogoro Jimboni kwangu kitaanza kuzalisha mwaka 2025, miaka saba kuanzia sasa. Kiwanda cha Mkulazi II ambayo ni Mbigiri anasema kitaanza kuzalisha mwaka 2022 baada ya uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nilimwambia Dkt. Magufuli juzi kwamba lengo viwanda hivi vianze kuzalisha baada ya uchaguzi ili watu waje na ajenda wakwambie ulisema wewe Tanzania ya viwanda, viko wapi na leo inatimia kwa ushahidi wa kitabu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa simuelewi Mheshimiwa Rais siku zote anaposema wasaidizi wangu wengine hawanielewi, leo ndiyo nimemuelewa. Tunafahamu siyo wote walifurahia kiwanda hiki kujengwa Morogoro, kuna watu walitaka kijengwe sehemu nyingine. Vilevile tunafahamu kuna wengine hawakupendezwa kiwanda hiki kupewa NSSF na PPF kwa sababu kuna wengine washindani wa hiyo biashara ya sukari walitaka shamba lile waliendeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanapitia mlango wa nyuma kukwamisha kiwanda hiki kuanza kwa wakati ili kutoa ajira kwa Watanzania, kuongeza uchumi wa Watanzania na kuondoa tatizo la sukari nchini. Mungu anawaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi, walikuja na sababu zote, sababu ya kwanza walisema kwamba wakati Mheshimiwa Rais anaiomba mifuko ya jamii ijiingize kwenye viwanda, wanasema mifuko haina uzoefu wa sukari kwa hiyo kujiingiza kwenye viwanda ni kupoteza hela za wanachama, hilo limepanguliwa limekwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadae wanasema kwamba hapana, mkataba umesainiwa na mtu ambaye ni tofauti, kwenda wakagundua aliyesaini ni mtu sahihi. Mara nyingine wanasema kwamba hapana raw material haijakuwa tayari, hivi kiwanda na raw material kinaanza nini? Tulikuwa na Mheshimiwa Rais juzi Kilombero, wananchi wanalalamika soko la miwa halipo, Mtibwa, Turiani wanalalamika soko la miwa yao halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wawekezaji wako tayari, walishasaini mkataba tangu mwaka jana na mtengenezaji wa kiwanda kile, kile Kiwanda cha Mbigiri II kilitakiwa kifike mwezi wa kwanza mwaka huu. Kiwanda cha Mkulazi I kilitakiwa kifike Juni mwaka huu na Kiwanda cha Mkulazi II kilitakiwa uzalishaji kianze mwezi huu, lakini mpaka leo Serikali haijatoa kibali kwa mwekezaji. Ndiyo maana tunasema tatizo si pesa wakati mwingine, tatizo ni uzalendo na dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua, ni kweli kabisa mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake, lakini si lazima kila jani lililopo pale atakula. Tatizo la watumishi wengi huko ndani ya Serikali wanataka kila jambo lazima kuwe na cha juu ili na yeye anufaike, kama jambo hilo hanufaiki yeye yuko radhi lichelewe hata miaka kumi, hata mradi upotee kwa sababu tu yeye hajanufaika, hili halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wekeni maslahi yenu pembeni, tangulizeni Tanzania kwanza, wekeni uzalendo kama alivyouonesha Dkt. John Pombe Magufuli. Ninayasema haya, nafikiri ananisikia, ajue namna gani kwamba kuna watu wanamkwamisha katika Sera hii ya Viwanda. Nilimwambia na leo nimelirudia baada ya kuona kwenye kitabu hiki kwamba viwanda hivi vitaanza kutekelezwa baada ya uchaguzi 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana watumishi wa Serikali, sisi tulitoka sekta binafsi tulikua tunapimwa kutokana na matokeo, wenzetu wanapimwa kutokana tu na chochote ambacho hakina tija wakati mwingine.

Naomba majibu ukija kufunga hoja yako, kiwanda hiki tayari hela zipo na mwekezaji ameshawekeza, Kiwanda cha Mbigiri II mwekezaji ameshalima zaidi ya hekta 1000 za miwa, tunavuna kuanzia Juni, 2018. Lakini pia outgrowers (wakulima wadogo) walishapata mkopo kutoka Benki ya Azania zaidi ya 4.9 billion na wameshalima zaidi ya hekta 600, hawa wote baada ya kuvuna watapeleka wapi bila kiwanda hiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali toeni kibali haraka iwezekanavyo, kiwanda hiki kiagizwe kianze uzalishaji Mbigiri II mwaka huu na Mbigiri I mwakani; zaidi ya hapo hatutaelewana, nafuatilia mradi huu kwa karibu sana. Siku ile nilimwambia kama hatutapata kibali haraka nitaenda tena Ikulu kwenda kumueleza Mheshimiwa Rais na tutawataja hata kwa majina wale wanaomkwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili, Morogoro ndio uliokuwa mji wa viwanda na ninataka nimwambie Dkt. John Pombe Magufuli, nampongeza sana kwa sababu anatekeleza ndoto zote za Mwalimu, anajenga Stiegler’s, anajenga Kidunda, amehamisha Makao Makuu kuja Dodoma, lakini sasa kama alivyosema juzi, kuwa katikati kuna raha yake, lakini katikati hiyo Mwalimu Nyerere alimaanisha Morogoro ndiyo uwe mji wa viwanda. Na wakati ule aliunganisha na Pwani kwa sababu sehemu kubwa ya Pwani ilikuwa ni sehemu ya Mkoa wa Morogoro, hatukuwa na Mkoa wa Pwani, tulikuwa na Dar es Salaam na Morogoro na ndiyo maana alisema kwamba Morogoro uwe mji wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tulikuwa na viwanda vyetu zaidi ya 11 vile vya kimkakati, leo vinavyofanya kazi ni vinne tu. Vinavyofanya kazi ni Kilombero Sugar, Mtibwa pamoja na kile cha tumbaku, pia kinachechemea hiki cha 21st Century ambacho kinafanya kazi na Moproko imeanza.

Nataka majibu ya kina, nini hatima ya viwanda saba vilivyobaki? Morogoro Ceramic ambayo raw material ilikuwa inatumia mchanga tu, lakini mnafahamu mmewauzia watu kwa bei ndogo kwa kupeana kiujomba ujomba, matokeo yake wale waliochukua viwanda vile wakang’oa mashine kwenda kuuza kama scraper, naona kwa sababu wamenunua kwa bei rahisi, hata akiuza scraper yeye anapata faida kuliko ku-run kiwanda. Nataka mniambie Morogoro Ceramic iko wapi, Kiwanda cha Magunia kiko wapi? Mniambie Kiwanda cha Ngozi kiko wapi na mna mkakati gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mpaka kile la Mang’ula, kiwanda ambacho ndiyo uhai wa Reli ya TAZARA, na mnafahamu mpaka leo, Mang’ula hakipo, leo TAZARA tutaiendeshaje? Ilikuwa chuma chochote, spare yoyote ya gari au ya namna gani usipoipata mahali popote unaenda kuchongesha pale Mang’ula, leo Serikali kama hamuoni lolote, hamuoni umuhimu huo Wachina tafuteni namna gani ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana mlete majibu mazuri. Nilisikitika sana, nilitamani kulia siku ile wakati anaongea Mzee Kasori kuhusu historia na umuhimu wa kiwanda kile. Leo tupo tumepata Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, mzalendo, msaidieni. Kiwanda hiki ndio uhai wa TAZARA, nchi maskini kama hii Tanzania haiwezi kununua kila spare part kutoka China bila kukifufua kiwanda hiki kukirudisha katika hali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya najua mpaka uwe na roho ngumu kuyasema, na watu watanichukia lakini lazima ukweli niyazungumze kwa sababu mimi natoka Morogoro, viwanda hivi viko Morogoro, vina faida kubwa sana kwa watu wa Morogoro, kwa taifa, lazima tuambiane ukweli. Bila kuambiana ukweli hatutoki hapa tulipokwama. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kupata nguvu ya kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu ya Nishati na Madini. Pia, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Joseph Magufuli, kwa hekima kubwa ya kumteua Profesa Muhongo katika nafasi ya Uwaziri wa Wizara hii. Ni kweli ametundendea haki Watanzania kwa maana upele umempata mwenye kucha katika Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo, Naibu wake, Katibu Mkuu wa Wizara na Timu nzima ya Wataalam Wizarani kwa mipango yao na mwanzo mzuri wa utendaji katika Wizara hasa kuleta umeme wa uhakika kwa sisi wa vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali kuhusu leseni kwa makampuni ya uchimbaji wa madini; wakati wa kuitoa kwa wawekezaji hao (leseni) ni vizuri kuwashirikisha wananchi wa eneo husika kupitia viongozi wao, kwa maana ya wawakilishi katika vijiji, kata, jimbo na wilaya, ili kuondoa migogoro ya wananchi na wawekezaji katika meneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni vema ifahamike faida na manufaa ya uchimbaji huo kwa jamii na Taifa kwa ujumla, badala ya hali ya sasa mwekezaji anapata leseni Dar-es-Salaam na akifika maeneo husika halipi fidia wala service levies katika Halmashauri husika kwa kisingizio cha madini sio mali ya mtu na wao wameshalipia Serikalini kwa wamiliki wa madini hayo. Nashauri, kabla ya kutoa leseni, Wizara ni vizuri kufanya utafiti katika maeneo husika, ili kufahamu hali halisi ya eneo hilo la uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, machimbo ya marble katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, katika Halmashauri ya Morogoro, katika Vijiji vya Kivuma, Kata ya Kibuko, Tarafa ya Mkuyuni na Kijiji cha Masiyu, Kata ya Gwata. Wawekezaji hawajalipa fidia kwa wananchi na pia, kutolipia ushuru wa huduma katika halmashauri kwa miaka zaidi ya ya sita tangu waanze uchimbaji, Kampuni ya Zhong Fa!
Mheshimiwa Naibu Spika,Sababu hii imekosesha mapato stahiki kwa Serikali, kwa sababu mrabaha wanalipa katika mkoa uliosajili TIN zao, ambao uko mbali na machimbo husika, ambao hawajui kiasi halisi kinachopatikana. Nashauri katika suala la mrabaha washirikishwe TRA Wilaya na Mkoa husika wenye machimbo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba kupatiwa umeme katika Kata ya Mkulazi vijiji vinne, Kata ya Mafuli vijiji vinne, Kata ya Kidugalo vijiji saba, Kata ya Ngerengere vijiji viwili, Kata ya Kiloka kijiji kimoja, Kata ya Gwata vijiji viwili, Kata ya Mkambarani vijiji viwili, Kata ya Mkuyuni vijiji viwili, Kata ya Kinole vijiji vinne, Kata ya Tegetero vijiji vinne na Kata ya Kibuko vijiji vyote vinne.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya vijiji 64 ni vijiji 16 tu ndivyo vyenye umeme, naomba katika REA III tupatiwe umeme katika vijiji hivi na kata hizi kwa ujumla, kwani hata huko tunakotaka kwenda katika uchumi wa viwanda, hasa Kata ya Mkulazi kwenye mradi mkubwa flagship wa Mkulazi Village afya na Bwawa la Kidunda ambalo vijiji vyake vina umbali zaidi ya kilometa 50 toka kijiji kimoja kwenda kingine; mfano Usungwa, Mkulazi, Usangara mpaka Kidunda. Naomba tupatiwe umeme ili katika REA nasi tufanane na Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii kutoa mchango wangu katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ni muhimu sana na fahari ya kujivunia kwa nchi yetu sababu una manufaa kwa pande zote mbili za Muungano wetu na Watanzania walio wengi hatujui nchi nyingine zaidi ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, naomba kutoa mchango wangu kama ushauri kwa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kama ifuatavyo:-
Utunzaji wa mazingira ni muhimu sana hasa mustakabali wa nchi yetu kwa kizazi cha sasa na cha baadaye ukizingatia na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu unaotokana na shughuli za binadamu katika vyanzo vya maji, misitu na mbuga zetu za wanyama ambazo ni urithi wetu na zawadi toka kwa Mwenyezi Mungu kama zawadi kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu wa hilo la utunzaji wa mazingira na kutokana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na mikakati ya kuvuna na kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo na kwa matumizi ya kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na kuondokana na kilimo cha kubahatisha na kutegemea mvua ambazo kwa sasa hazina uhakika kutokana na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa ushauri kwa Serikali kuwa; tuwekeze katika kujenga mabwawa zaidi ili kuvuna na kuhifadhi maji kwa ajili ya kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mabwawa hayo ni bwawa la Kidunda ambalo andiko lake la kwanza lilikuwa mwaka 1955 kabla ya uhuru na la pili ni mwaka 1962 na la tatu ni mwaka 1994 ambalo lilibadilisha wazo la awali la matumizi ya bwawa kwa uzalishaji wa umeme, ufugaji wa samaki, kilimo cha umwagiliaji pamoja na uzalishaji wa maji safi na salama kwa Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri Serikali kurudi kwenye mipango ya awali ya Mwalimu Nyerere ya kujenga bwawa kwa ajili ya matumizi yote kwa ajili ya kukabiliana na uzalishaji wenye tija katika kilimo na kuwa na uhakika wa chakula na malighafi ya kiwanda ukizingatia kuna shamba kubwa la miwa na kiwanda cha sukari kinachojengwa kule Mkulazi ambao nao watahitaji maji kutoka katika bwawa hilo. Katika hili tutapata changamoto lakini tutangulize maslahi mapana ya Tanzania kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa afya na uzima tumeipata nafasi hii ya kuchangia katika sekta hii muhimu kwa Watanzania, sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, pia natoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu na nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo katika kumsaidia katika majukumu kwenye sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa pia shukrani za pekee kwa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Japhet Hasunga (Mb) kwa ushirikiano mkubwa anaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Vile vile ninamshukuru Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Naibu Waziri mwenzangu kwa ushirikiano mkubwa anaonipa katika kuwatumikia Watanzania; tunafanya kazi hii kwa pamoja kama timu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao. Aidha, nawashukuru wapiga kura wangu kwa kuendelea kuniamini na kunipa ushirikiano wa kutosha pale ambapo ninapokuwa katika Bunge hili na sehemu zingine kuwawakilisha. Nipo hapa kwa sababu yao, niko hapa ndiyo sauti yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nachukua nafasi hii kukishukuru chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa ushirikiano mkubwa kinachonipa katika kutekeleza majukumu haya hasahasa kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwenye Sekta hiyo ya Kilimo. Aidha, namshukuru Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na watendaji wa Wizara ya Kilimo na taasisi zilizokuwa chini ya Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya na ushirikiano wanaonipa katika kutimiza majukumu yangu.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, ninaomba sasa nichangie hotuba yangu ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa kutoa maelezo na ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika sehemu kuu mbili ambazo ni umwagiliaji na zao la kahawa na kama nitapata muda nitaenda kwenye miwa pia na mbegu za mafuta kwenye mafuta ya kula.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza na hoja hizo mbili, sisi kama Serikali niishukuru sana michango ya Wabunge. Wengi wamezungumzia kuhusu bajeti kwamba bajeti ya sekta ya kilimo ni ndogo. Pamoja na ukweli huo wengi wana- refer azimio la Malabo na lile la Maputo. Ni kweli lakini tuna maazimio mengi ambayo tumeingia kama nchi. Tutoe mfano tu, afya tunatakiwa tutenge asilimia 15, elimu asilimia 20, kilimo asilimia 10, tuna asilimia 45 kwa mambo matatu tu; lakini ukiangalia vipaumbele tulivyokuwa navyo viko vingi. Kwa hiyo hii bajeti kwa mazingira tuliyonayo na hasa uchumi wetu ni vizuri kwamba tukazingatia badala ya kujielekeza kwenye maazimio ambayo hayaendani na hali halisi ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, pia bajeti hii ya sekta ya kilimo tunaitekeleza kwa kupitia mpango wetu wa ASDP II. Kama tulivyoeleza bajeti hii kwenye ASDP II asilimia 40 ndiyo Serikali na asilimia 60 itatekelezwa na sekta binafsi. Kwa hiyo sekta binafsi nayo ina mchango mkubwa sana katika kuendeleza kilimo katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, kilimo ni kipana, ni kilimo mazao, kilimo mifugo, kilimo mifugo, kilimo uvuvi, na kilimo misitu, Kwa hiyo bajeti yake huwezi kuiona tu kwenye Wizara hii moja ya Kilimo, utaiona kwenye Wizara zote hizo zingine pamoja na Wizara zile za Kisekta. Kama mnavyokumbuka bajeti hii ni mwendelezo wa mipango wa Serikali tangu mpango ule wa mwanzo.

Mheshimiwa Spika, tulikubaliana kama Serikali, mpango wa mwanza ulikuwa kwanza kuondoa vikwazo vya kimaendeleo na ndiyo maana sasa hivi bado Serikali tunaendelea kuondoa vikwazo vya kimaendeleo ili kumkwamua mkulima; ndiyo maana tunaboresha hiyo miundombinu ya barabara, reli, pamoja na ndege, yote ni ili kuwezesha mazao ya wakulima ili yaweze kufika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Hoja Mahsusi Kuhusu Mambo ya Umwagiliaji. Kulikuwa na hoja kutoka kwenye Kamati yetu ya Kilimo lakini pia Kambi Rasmi ya upinzani na pia katika michango ya Wabunge mbalimbali. Ni kweli eneo la umwagiliaji kama nchi bado ni dogo sana ambalo eneo linalofaa kwa umwagiliai tuna hekta zaidi ya milioni 29 lakini mpaka sasa tumeendeleza hekta 475,000.

Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga ndani ya miaka 10 tuweze kuongeza eneo la uzalishaji kutoka hekta 475,000 mpaka hekta 1,000,000. Kama nilivyosema awali hiyo sisi kama Serikali pamoja na kushirikiana na Sekta Binafsi pia na Serikali za Halmashauri na kupitia Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo na Benki nyingine kwa sababu tukisema kwamba tunategemea hela za kibajeti, maeneo haya ya umwagiliaji yote hatutaweza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo na Benki nyingine za kibiashara kama CRDB, NMB, Azania, Benki ya Posta na zingine zote, hizi sasa tumesema kwamba kwa sababu tunaenda kwenye kilimo cha biashara, zinakwenda kwa maelekezo ya Serikali na mipango hiyo kwamba Serikali tunakwenda kudhamini asilimia 50 ya fedha zote zilizotolewa na benki hizi za biashara ili kwenda kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika nchi hii badala ya miradi yote ya umwagiliaji kusubiri pesa za kibajeti kwa udhamini wa Serikali kwa kushirikiana na Serikali za Halmashauri za Wilaya pamoja na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambao wao watahusika kwa ajili ya kutoa utaalam kwa ajili ya ramani na kusimamia ujenzi ili halmashauri hizi na miradi hii tuweze kuchukua mikopo ya masharti nafuu kuiendeleza miradi hiyo ili tuwe na kilimo cha uhakika cha umwagiliaji katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutakuwa kweli na miradi itategemea fedha za kibajeti lakini pia tutakuwa na miradi ya kibiashara ambayo itapata fedha kutoka kwenye taasisi zetu hizi za fedha kwenye benki hizo ambazo nimeziainisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mkopo huu utalipwa ndani ya miaka mitano mpaka miaka 15; na mingine iwe ni fursa kwa wafanyabiashara wakubwa kuchukua ardhi kwenda kuwekeza miundombinu ya umwagiliaji, baadaye tutaweza kuwakodisha kwa wakulima na wanufaika wengine utaweza kulipa tarayibu mpaka pale ambapo pesa itakaporudi. Mpango huu tunauweka katika ile mpango wetu wa kwamba jenga, endesha, baadaye unakabidhi baada ya malipo ya ujenzi ule kurudi.

Mheshimiwa Spika, la pili kwenye umwagiliaji, tumeona baada ya Wizara hii kuja kwetu cha kwanza ambacho kama Serikali tulichokifanya kwa pamoja ni kuielekeza mhasibu (CAG) kufanya ukaguzi maalum kwenye miradi yote ya umwagiliaji nchini.

Mheshimiwa Spika, na nikiri, baada ya taarifa hiyo ambayo tulishai-table hapa kwenye Bunge lako Tukufu, tutaijadili vikao vijavyo baada ya Bunge la Bajeti ambapo tumeona madhaifu mengi sana katika miradi hii; na ndiyo maana sehemu nyingine miradi kwamba imemalizika, maji haitoi au miradi imejengwa chini ya kiwango. Yote hayo sisi kama Serikali tumeyapokea na tumeshaanza kuyafanyia kazi hata kabla hatujaanza mjadala hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza, tumeunda timu maalum ya kiuchunguzi kwenda kuyathibitisha yale ambayo aliyoyagundua CAG kwa mujibu wa sheria ili sasa wale wote ambao waliotufikisha hapo kwanza tuwachukulie hatua lakini kubwa zaidi ni kujifunza wapi tulifanya vibaya ili kuja na mikakati ya kuweza ku-address tatizo lililokuwepo na kwenda kuwa na kilimo cha uhakika cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, pia, katika suala la umwagiliaji sasa tunataka kufanya mapitio ya kimuundo. Badala ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuwa tu kwenye kanda, sasa tunataka tuishushe mpaka kwenye ngazi ya kata, vijiji mpaa ngazi ya halmashauri. Kwa hiyo tutakuwa na wataalam Makao Makuu kwenye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji lakini pia tutakuwa na wataalam wa umwagiliaji kwenye kanda, tutakuwa na wataalam wawili kwenye mkoa na baadaye tutakuwa na wataalam wengine kwenye wilaya. Baadaye tutawajumuisha pamoja na wale wa halmashauri ili miradi hii isimamiwe maalum. Kila mradi ambao utasimamiwa, utakuwa na Meneja maalum au Mhandisi maalum wa kuusimamia mradi huo, badala ya sasa miradi mingi ilikuwa inasimamiwa na Engineers wa Kanda ambao wanaishi Makao Makuu Dar es Salaam, kitu ambacho kimechangia miradi mingi kujengwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na hoja za Wabunge mbalimbali, ambao wamezitoa. Kwa mfano, Mheshimiwa Deo Ngalawa, alikuwa anazungumzia mkakati wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua. Ni kweli, hoja yake ni ya msingi, lakini katika kilimo hiki cha umwagiliaji kama nilivyosema katika maelezo yangu, kwa sababu kilimo tunategemea mvua, tunategemea maji ya ardhini kwa kuchimba visima, lakini pia kwa ajili ya kuvuna maji kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa. Sisi kama Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima hawa wadogowadogo, mpaka sasa tuliagiza mitambo ya kuchimba na kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji na mitambo hiyo imeshafika na imeshafika hapa Dodoma. Lengo kwa wale wandarasi wa ndani wadogo wanaopewa, ambao uwezo wao wa vifaa ni mdogo, watakodisha kwa bei nafuu mitambo hii ili kurahisisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile kulikuwa na Mheshimiwa Neema Mgaya, alikuwa anasema kwamba Serikali iwekeze kwenye malambo, mabwawa ili kuongeza uzalishaji. Kama nilivyosema katika maelezo yangu kupitia mapitio ya mpangi kabambe, ambao tayari tulishauhaulisha, mpango wa umwagiliaji, yote lengo ni kwenda kujibu hoja za wananchi.

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili, ni suala la kahawa, ni kweli, kwenye suala la kahawa, kama walivyosema Wabunge wengi na Kamati yetu ya Kilimo, walikuwa wanataka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa soko la kahawa. Kwanza, tulichofanya katika msimu huu unaokuja, cha kwanza tumeyatambua makampuni yote ya ndani ambayo yananunua kahawa zetu kwa ajili ya kuwapa vibali Vyama vyote vya Ushirika na wakulima na makampuni yanayonunua hapa kahawa, kuuza moja kwa moja bila kupitia mnadani. Hilo limeonesha mafanikio makubwa zaidi, kahawa zaidi ya asilimia 80 tunavyoongea, tayari zilishakuwa kwenye makubaliano ya kuweza kuuzwa moja kwa moja kwa wale wanunuzi wa kahawa wa uhakika ambao wanakwenda kuuza nje.

Mheshimiwa Spika, la pili, tuliona kwamba ni busara, kwa sababu kahawa ni zao la muda mrefu, tunawahimiza wakulima wetu walime kahawa, lakini hii fursa inaangaliwa na nchi mbalimbali duniani. Wanavyoona bei ya kahawa inavyopanda au bei ya mazao mengine, nao wanaangalia. Cha pili, tumeona kwamba ni vizuri kuingia makubaliano maalum na nchi zile za walaji katika nchi mbalimbali ili tuwe na soko la uhakika. Kahawa hii tunawahimiza wakulima walie, tunakwenda kuiuza kwa nani, kwa bei gani na kipindi gani ili tupate mikataba ya muda mrefu kati ya miaka mitano mpaka 20 ili tusije kuzalisha kahawa kwa wingi, baadaye inafika kule muda unakuwa umekwisha. (Makofi)

Watu wengi hapa walikuwa wanajiuliza kwa nini Kenya ni kubwa na Uganda…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu…

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie dakika moja tu.

SPIKA: Ahsante, malizia dakika moja.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): …wanasema kwa nini Kenya bei ni kubwa na Uganda, sababu ni hiyo, wenzetu walishakuwa na bilateral sisi tulikuwa bado, ndiyo maana kwamba wenzetu walikuwa wanapata mikataba mizuri kabla ya sisi na sisi sasa tumeamua tunafanya hivyo ili kuboresha bei ya mazao yetu nchi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na uzima kujumuika hapa leo kwa pamoja kuchangia hoja hii muhimu ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu lakini pia nikushukuru wewe binafsi kwa umahiri katika uongozi wako katika kipindi chote tukiwa hapa na hasa kwa ubunifu na mabadiliko ya matumizi ya Bunge Mtandao ambao umeturahisishia Wabunge utendaji wetu wa kazi ya kuwawakilisha wananchi wetu tunaowawakilisha.

Vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja watendaji wote wa Wizara wakiongozwa na Makatibu Wakuu kwa hotuba na kazi nzuri wanayofanya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani na pongezi hizo naomba kutoa mchango wangu wa ushauri kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maboresho madogo kwa kuwa hotuba imebeba mambo mengi mazuri kwa Watanzania.

Kwanza ni uwekezaji wa shamba la Mkulazi I kwa zao la alizeti. Shamba la Mkulazi I lililopo Kata ya Mkulazi, Tarafa ya Ngerengere, Mkoani Morogoro lina ukubwa wa hekta zaidi ya 61,000. Kutokana na tafiti mbalimbali za udongo, maji, hali ya hewa na kadhalika, eneo linalokubali kilimo cha miwa ni hekta 28,000 ambazo zitazalishwa sukari kupitia kampuni tanzu ya NSSF ya Mkulazi Holding Company Limited. Na eneo lililobaki zaidi ya hekta 33,000 zinafaa mazao mengi kama vile mahindi, mtama, mihogo na alizeti.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa lengo kuu la Kampuni ya Mkulazi kwa sasa ni kuendeleza eneo linalolimwa miwa na kwa kuwa tuna tatizo kubwa la upungufu wa mbegu za alizeti kwa malighafi ya viwanda vya ndani na upungufu mkubwa wa mafuta ya kula. Naomba kuishauri Serikali kupitia Wizara kuliazima eneo hili kwa vijana, kina mama na wakulima kwa ujumla kwa utaratibu wa kilimo cha kitalu katika vikundi vya wakulima au wakulima wakubwa wenye uwezo wa kulima maeneo makubwa kilimo cha alizeti ili kutosheleza mahitaji ya viwanda vyetu ya tani zaidi ya milioni mbili kwa mwaka tofauti na sasa wanapata tani laki sita tu na kulazimika kufanya kazi chini ya kiwango na kulazimu kutumia fedha za kigeni kuagiza mafuta nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ukifanyiwa kazi kuanzia kilimo cha mwaka huu cha vuli utakuwa na faida kubwa kwa taarifa za kiuchumi na kijamii pia. Tutaongeza ajira kwa vijana, tutaongeza kipato na uchumi wa watu wetu, utainua uchumi wa tarafa, utaokoa fedha za kigeni tunazotumia sasa kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, tutaimarisha shughuli za kiuchumi na kuimarisha huduma za jamii katika eneo la uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, pili vibali vya kazi kwa wawekezaji wakubwa toka nje; pamoja na nia nzuri ya Serikali kulinda ajira za Watanzania kwa kudhibiti ajira za wageni nchini kwa utoaji wa vibali, lakini kuna nafasi za ajira lazima zishikiliwe na wenyewe au watu wa karibu wao wanaowaamini. Kwa mfano nafasi za kuu kama CEO na Ukurugenzi Mkuu na Fedha hii nafasi wawekezaji wanapenda kuwa watu wao kwa vigezo zaidi hasa cha uadilifu, historia, mahusiano na maono ya mtumishi binafsi na ya kampuni badala ya kuangalia utaifa pekee.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo naomba kuishauri Serikali kuangalia namna ya kuwapa na kuwaongezea muda wa vibali wenye makampuni hayo watu wao wa karibu wanawaamini kuendelea kubaki nchini kuendeleza makampuni yao, kinyume cha hapo inaweza kumlazimu mwekezaji kusitisha uwekezaji wake nchini na kuhamishia nchi nyingine kwa kutokuwa na mtu sahihi anayemuamini kumkabidhi kusimamia rasilimali zake alizowekeza hapa nchini.

Ushauri wangu waongezewe muda wa vibali kwa muda na haraka ili kuvutia uwekezaji nchini badala ya mtizamo hasi kuwa hatutaki uwekezaji wa watu kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, ajira kwa vijana na ujasiriamali na biashara kwa mazao ya kilimo; vijana ni nguvu kazi kubwa sana katika Taifa letu na kwa takwimu zilizopo nguvu kazi ya Taifa zaidi ya 67% ni vijana na zaidi ya vijana, lakini kila mwaka wanaingia katika soko la ajira na uwezo wa Serikali na sekta binafsi kuajiri ni vijana laki moja na hamsini na tano tu kwa mwaka. Kwa muktadha huu sekta yenye uwezo wa kutoa ajira kwa wingi bila kubagua wala kuchagua ni sekta ya kilimo kwenye mnyororo mzima wa thamani kuanzia uzalishaji mashambani, biashara ya mazao ya kilimo, kutoa huduma ya pembejeo za kilimo, usafiri, vifungashio, zana za kilimo, fedha za mitaji, usafirishaji na kadhalika, lakini kutokana ni mifumo ya masoko ya mazao hasa kwa mazao ya kimkakati inawaondoa vijana katika kujihusisha na biashara ya mazao ya kilimo kwa wakulima kuwa kwenye soko la nje moja kwa moja au kuwa kwenye minada yenye wanunuzi wa nje ambao kimsingi ndio walikuwa wanunuzi wa wajasiriamali vijana katika kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu ukiendelea tutaweza kutengeneza matajiri na wafanyabiashara wakubwa wa kesho wa Taifa hili kwa kuwa mazao ya kilimo ndiyo msingi wa kuwatengeneza kwa uzoefu na mitaji yao mikubwa na kubambia sekta nyingine baada ya mafamikio na kujenga uchumi imara kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hii naomba kushauri mfumo wa wanunuzi wa mazao ya wakulima wa stakabadhi ghalani na minada kufanyiwa mabadiliko na kuwa na masoko ya ngazi mbili. Ngazi ya kwanza ni soko la wakulima kuwa mazao yao kupitia vyama vya msingi ili kudhibiti ubora na bei kwa wakulima. Soko hili litawahusisha wakulima kwa maana ya wauzaji na wanunuzi wa ndani, wajasiriamali, wakulima wakubwa, vyama vikuu, wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara pamoja wenye viwanda vya ndani vya kuchakata mazao ili kivipatia malighafi kwa bei himilivu ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuweza kushindana katika solo la kimataifa na mataifa mengine. Hawa wote ndio wanunuzi katika soko la awali na kuwa katika solo la upili kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, soko la upili ni stakabadhi ghalani au TMX linalowakutanisha wafanyabiashara wa ndani, wakulima wakubwa na wanunuzi wa nje kwa mazao yanayosafirishwa nje ya nchi na yanayotumika kwa viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu utasaidia kutatua changamoto zilizopo katika mfumo wa ushirika na masoko ya mazao kwa sasa. Wakulima watapata malipo taslimu na kwa wakati, utaondoa rushwa kwenye ushirika, ukosefu wa malighafi kwa viwanda vya ndani mfano viwanda vya korosho na kahawa, kutoa ajira kwa vijana kwa kujiajiri katika biashara ya mazao ya kilimo na kuongeza mapato ya Serikali kwa wajasiriamali na wafanyabiashara ya kununua katika soko la awali na kuuza katika soko la upili.

Mheshimiwa Spika, naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake mahiri na miongozo yake kwangu katika kuwatumikia Watanzania kuwaletea maendeleo. Vilevile nimshukuru tena Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usimamizi mzuri wa shughuli za Serikali na jinsi anavyotusimamia na kutuelekeza mara kwa mara katika kutimiza majukumu yangu.

Mheshimiwa Spika, aidha nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja muhimu ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuridhia barabara kutoka Bigwa - Kisaki kujengwa kwa kiwango cha lami kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 kufuatia maombi ya watu wa Morogoro Kusini Mashariki kupitia mimi Mbunge wao hapa Bungeni na Bunge lake kupitisha.

Mheshimiwa Spika, baada ya bajeti hiyo kupita kwa barabara hiyo ya Bigwa - Kisaki kujengwa kwa lami na kuendelea kuomba Serikali na kushauri kuhimiza ujenzi kuanza haraka kutokana na umuhimu wa barabara hii kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali yangu kutoa kibali cha ujenzi wa barabara hii ili mchakato wa kutafuta mkandarasi ukaanza ili kuanza ujenzi mwaka huu. Pia nashauri kwa kuwa nafamu Serikali ina majukumu mengi na tatizo la kukabiliana na Corona kwa sasa basi naiomba Serikali barabara yote ya kilometa 78 basi inaweza kutoa kwa awamu, kwa mwaka huu Serikali ikatoa kwa awamu hata kwa kilometa 40 na mwaka mwingine kutoa sehemu iliyobaki kilometa 38 ili ujenzi wa barabara mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, umuhimu wa barabara hii kwa sasa umeongezeka sana pamoja na Makao Mkuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, kupita katika tarafa tano kati ya sita za Halmashauri ya Morogoro lakini barabara hii inakwenda kwenye mbuga nyeti ya Hifadhi ya Nyerere, Mbuga ya Hifadhi ya Wanyama ya Selous kwenda kwenye Bwawa la Kisasa la Nyerere pamoja na kuunganisha mikoa ya Morogoro na Pwani.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara hii utarahishia ujenzi wa Bwawa la Nyerere, kuimarisha shughuli za utalii kwa kuboresha barabara pamoja na kukuza uchumi wa watu wetu kwa kurahisisha mawasiliano yao na kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao na kuongeza kipato na uchumi wa watu wetu.

Mheshimiwa Spika, barabara hii kila mwaka Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa mwaka kwa matengenezo kwa kiwango cha changarawe lakini bado inaharibika hasa kutokana na madhara ya mbuga.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa mara nyingine Serikali kutoa kibali cha ujenzi mapema ili kuanza ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, mwisho niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kwa kuniunga mkono na ushirikiano wanaonipa na kuwatumikia kuwaletea maendeleo yanayoonekana jimboni kwa macho.

Mheshimiwa Spika, nakushuru wewe tena kwa kunipa nafasi na ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Ardhi. Kwa sababu kama alivyosema Mwalimu Nyerere, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne na ardhi ikiwa ni mojawapo. Siasa safi tunayo ya ujamaa na kujitegemea, watu tunao, uongozi bora tunao unaotokana na Chama cha Mapinduzi na sera zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ni mchakato, hayawezi kuja siku moja kama wenzetu wanavyotaka. Hatukuwepo mwaka 1961 wakati tunapata uhuru, lakini Tanzania ya mwaka 1961 siyo Tanzania ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wenzetu wanaosema kwamba hakuna dira; dira ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tena katika utangulizi tu, imezungumza Wazi kabisa nataka pale kunukuu aya ya 6(b) inasema: “kuongeza kasi ya kupima ardhi yao na kuwapatia hatimiliki za kimila ambazo watazitumia kama dhamana ya kuwawezesha kupata mikopo na kuendeleza shughuli zao za kilimo, uvuvi na ufugaji.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu akisema kwamba hatuna vision, achukue Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hii hapa, kila kitu kimo humu ndani. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu sasa katika Wizara hii ya Ardhi. Ardhi kama tulivyosema, ndiyo rasilimali muhimu sana kwa Taifa lolote lile ikiwemo Tanzania; ardhi na vitu vyake vinavyopatikana katika ardhi. Inawezekana tumepotoka. Kwa mfano tu, inapogundulika mafuta au madini sehemu yoyote ya ardhi, fidia pale kwa Mtanzania ambaye anaimiliki au kijiji atapewa tu labda kama ana migomba, minazi au nyumba yake, lakini mali ile yote ya pale iliyogundulika chini ya ardhi tunaimilikisha kwa wageni. Mtanzania yule anabaki maskini kwa kisingizio cha uwekezaji au tunasema tutapata mrabaha ambao ni mdogo mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri katika hili ili kuendeleza kuwaneemesha Watanzania na kutengeneza matajiri wazawa wa Kitanzania ama kwa kumiliki Serikali au kijiji au yule mwenye ardhi pale, popote pale inapogundulika rasilimali hiyo, basi tutengeneze sheria ije kwamba yule ambaye yupo pale apate hata asilimia fulani katika umiliki ule ili utajiri ule uendelee kubaki kwa Watanzania badala ya sasa kubaki na mashimo na michanga isiyokuwa na faida na mrabaha mdogo ambao tunapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu migogoro ya ardhi. Tena Mheshimiwa Waziri nafikiri labda amepitiwa katika hili. Katika kitabu chake sijaona migogoro yoyote ya ardhi katika Wilaya yangu ya Morogoro katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini na ukizingatia ndiyo tunaongoza kwa mashamba pori yanayomilikiwa na watu wanaojiita wawekezaji, wamekopea tu mapesa, lakini hawayaendelezi. Naomba kama nitaileta tena ile list aingize hiyo migogoro ili tuweze kupatiwa majibu na kuweza kurudishwa kwa wakulima waweze kuyaendeleza baada ya hawa wawekezaji kushindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la migogoro ya ardhi kama Mheshimiwa Waziri alipotuambia pale nyuma kwamba wameshaanza kuitatua, kwa mfano, wameanza kule Kilombero na Ifakara, basi kasi hii naomba iongezwe ili tatizo hili liweze kutatuliwa haraka. La sivyo, katika hatari ninayoiona ambayo inakuja mbele yetu, inayohatarisha umoja wetu, mshikamano na amani nchini, basi ni hii migogoro ya ardhi. Wote ni mashahidi, tumeona watu wenyewe, Watanzania sasa hivi wanavyopigana, wanavyouana, kwa hiyo, naomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itolee kauli hili suala la upimaji wa ardhi na kuwamilikisha ardhi watu wake ili tuweze kuiendeleza tuondoe hili tatizo la migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kutoa ushauri katika hili, migogoro mingi hii inasababishwa na viongozi waliopewa mamlaka kubwa lakini ufahamu mdogo wa kisheria, hasa viongozi wa vijiji na Mabaraza ya Ardhi, kwa sababu huko ndiko kuna migogoro mkubwa. Pia linachangiwa na kupewa dhamana kubwa wakati hawana posho wala mshahara, matokeo yake wanajikita kwenye vitendo vya rushwa kwa mtu ambaye anataka ardhi kwa sababu anajua hawa Wenyeviti wa Vijiji au Viongozi wa Vijiji ndio wenye mamlaka, anakwenda kuwanunua wanapata ardhi kiujanja ujanja, baadaye inatuletea matatizo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda huko vijijini utakuta mwekezaji au mtu yeyote kapata ardhi bila kuwashirikisha wananchi, lakini unakuwa muhtasari upo na sahihi zipo za initial na hati imetolewa mpaka Wizarani kwenye hiyo ardhi. Matokeo yake, hata tukienda Mahakamani, haki hiyo inakuwa hatuipati mpaka labda tumtegemee Rais atengue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, naomba Wizara ya Ardhi, niliwahi kusema hapa kwamba pale Ngerengere sasa hivi ni Mamlaka ya Mji Mdogo; na sera za ardhi zinasema mjini popote hapahitajiki kuwa na shamba, lakini pale tuna shamba la Serikali ya LMU (Livestock Management Unity). Naomba shamba hili tuwape ardhi mahali pengine nje ya mji, ili shamba hili tuweze kulitumia kwa matumizi ya makazi na huduma za kijamii, lakini pia tuweze kuliendeleza kama ukanda wa viwanda vidogo vidogo ndani ya Halmashauri yetu kwa sababu ndiyo sehemu ambayo ina miundombinu mizuri lakini pia lipo karibu na Dar es Salaam, itakuwa ni rahisi sana kupata wawekezaji kwa ajili ya kuendeleza viwanda, kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenda uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kujielekeza kwenye National Housing Corporation -NHC. Sasa hivi NHC wamejikita sana kwenye miji mikubwa na matokeo yake kutokana na ushindani uliopo, hata nyumba nyingine zinaanza kukosa wapangaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna Wilaya mpya, Halmashauri mpya na Mikoa mipya na tuna matatizo makubwa ya miundombinu ya majengo na wateja ni Serikali, wapo wa uhakika! Basi tunaomba kama wangeweza kuja kujielekeza huko kuanza kujenga nyumba kwenye mikoa mipya, Halmashauri mpya na Wilaya mpya ili tuweze kwenda kwa kasi na sisi tuwe na majengo na kuwa na ofisi na tutawalipa pango lao kwa kupitia Halmashauri zetu na Serikali Kuu kwa sababu jukumu hilo linatakiwa ni Serikali kujenga miundombinu. Nina uhakika wateja wa uhakika pale wapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kujielekeza kwa Mheshimiwa Waziri kumwomba tena kwa mara nyingine aje katika Halmashauri yangu ya Morogoro ili kutatua mgogoro mkubwa wa Mkoa wa Pwani na Morogoro katika Kata ya Magindu Pwani na Kata ya Seregete „B‟ kuhusu mpaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo ni la muda mrefu ambapo wenzetu wa Magindu wanaleta mifugo katika Halmashauri yetu na wanawauzia wawekezaji bila kufuata taratibu, matokeo yake inaleta migogoro mikubwa sana na uhasama kati ya watu ambao ni ndugu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aje katika Kata ile ya Kidugaro katika Kijiji cha Seregete hapo Magindu atusuluhishe kwa sababu tumeshakaa muda mrefu wenyewe hatujapata muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu katika mada yetu hii iliyokuwa mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukuke fursa hii kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na wataalam wao kwa kuleta bajeti nzuri kwa sababu ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano. Bajeti hii ndiyo inatoa mwelekeo wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na imeonesha anapita kutokana na maneno yake aliyokuwa anaahidi wakati wa kampeni. Aliahidi viwanda na kweli bajeti inatafsiri hivyo, inaanza kujiandaa kwa ajili ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme hii bajeti kubwa imejielekeza hasa kwenye miundombinu na elimu, miundombinu ni asilimia 25 na elimu asilimia 22, jumla 47. Hivi ni vitu muhimu sana katika maendeleo ya viwanda kwa sababu vikwazo vikubwa kwa wawekezaji wengi ilikuwa ni miundombinu sasa bajeti inaenda kutibu hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba kwanza nipate…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nichukue fursa hii nipate tu ufafanuzi kutoka kwa Waziri wakati akija kuleta majumuisho yake hasa kutokana na hotuba yake kwenye ukurasa wa 57 hasa kwenye ushuru wa mafuta ya kulainisha mitambo kutoka Sh. 665 hadi Sh. 699 kwa lita. Kwa sababu kwa ufahamu wangu ushuru wa sasa hivi ni senti 50 kwa lita na kama ushuru ndiyo huu ulioandikwa hapa Sh. 665, ni ushuru mkubwa sana. Kwa hiyo, namwomba tu alete ufafanuzi wakati anakuja kufanya majumuisho yake ipi ni sahihi, hii iliyoandikwa kwenye kitabu au ni hii inayotumika sasa hivi huko field 0.5 cent kwa lita moja ya mafuta ya kulainishia mitambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, naomba ufafanuzi pia kwenye takwimu, nimesoma kwenye kitabu hiki cha Hali ya Uchumi cha mwaka jana hasa kwenye ukurasa wa 149, uzalishaji wa mazao ya mafuta. Nimeona kwenye ufuta, alizeti, kwa mfano alizeti Tanzania tunazalisha tani milioni 2,878,500, karanga tani 1,835,933, ufuta tani 1,174,589. Nichukulie kwenye ufuta tu, hata nchi zinazoongoza ulimwenguni kama ni Myanmar kule na China hawajafikia kiasi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe tu Mheshimiwa Waziri na timu yake wakae vizuri waangalie hasa hii Idara ya Takwimu au hizi mlikozipata kwa sababu hizi data ziko kwenye mitandao na zinaenda, zinaweza zikapotosha wawekezaji wakaja hapa halafu malighafi hakuna au tunaweza kupanga mipango yetu kwa kuamini kwamba malighafi ipo kumbe hamna. Tunazo data za kutoka Custom kwenye Ofisi yake, mwaka jana usafirishaji wa ufuta kwenda nje ya nchi ni tani 133,000 kutoka mwezi Juni mpaka mwezi Desemba. Naomba tu wazipitie vizuri wakalete data halisi ambazo zinaweza zikawa kichocheo kwenye uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda ufafanuzi wa mwisho, kama nilivyosema mwanzoni hii bajeti ni ya miundombinu. Kwa bahati mbaya sana sijaona kwenye bajeti hii miundombinu ya kwetu kule, barabara hasa ile ya Bigwa - Kisaki kwa kiwango cha lami. Mradi ule ulikuwa ugharamiwe na MCC na hao MCC sasa hivi wamejiweka pembeni. Kwa ajili ya mradi ule na miradi mingine Tanzania iliyokuwa inagharamiwa na MCC sijui sasa Serikali imejipangaje kwa ajili ya kutekeleza pengo hili lililoachwa na hawa jamaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kwa sasa nijielekeze kwenye mchango wangu. La kwanza ni kuhusu Mfuko wa Maji. Wabunge wengi wamezungumzia suala hili kwa sababu maji ni uhai. Nami lazima nijikite hapa kwa sababu tuna tatizo kubwa sana la maji katika Jimbo langu la Morogoro Kusini hasa katika vijiji kama vya Mkuyuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa maji uko miaka 15 haujawahi kufanyiwa ukarabati na vijiji vile ambavyo vilikuwa vitongoji sasa hivi vimekuwa vijiji kama vijiji vya Kivuma, Kibuka na Mwalazi wanategemea maji ya mradi huo huo ambao uliwekwa tanki la 10,000. Tukiomba tunaambiwa kwamba vijiji vingine havijapata maji wakisema ni lazima wamalize vijiji vingine ndiyo waje kwenye ukarabati wakati sasa vile vitongoji vimeshakuwa kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kibuka kilikuwa Kitongoji cha Mkuyuni sasa hivi ni kata inategemea mradi wa kijiji hicho hicho. Kwa hiyo, nimwombe Waziri akubaliane na mawazo mengi ya Wabunge kuongeza hii Sh. 50 katika lita ya petrol na diesel ili twende kutatua tatizo la maji vijijini. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, Wabunge wote wana kilio cha maji na Sh. 50 kuongezwa. Wabunge kazi yetu ni kuishauri Serikali namwomba Waziri apokee ushauri huu ili tukatatue tatizo la maji na vituo vya afya na zahanati kwa sababu mzigo huu wananchi walishabeba muda mrefu sana kwa kuchangia zahanati na vituo vya afya huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuchangia ni kupunguza tatizo la msongamano Dar es Salaam ili kufungua fursa za uchumi na kuharakisha maendeleo ya uchumi. Tatizo la msongamano Dar es Salaam linaathiri sana uchumi wa Taifa letu kwa sababu watu wanatumia muda mrefu kufika kazini na wanatumia muda mchache kufanya kazi. Tatizo hili nilishawahi kusema siku moja, ni lazima tufungue vituo vikubwa vya kibiashara na bandari kavu nje ya Dar es Salaam na ukisema nje ya Dar es Salaam basi Morogoro ina sifa mojawapo ambayo baadhi ya mikoa mingine haina.
Mheshimiwa Naibu Spika, Morogoro ni mkoa ambao umepitiwa na reli zote mbili, reli ya kati na reli ya TAZARA. Tunaweza kutumia reli hizi ili kuingiza na kutoa mizigo bandarini kwa kutumia treni badala ya magari yote kutoka mikoani na nchi zingine zikapakia mizigo pale Morogoro. Pamoja na juhudi kubwa za Serikali kutatua changamoto ya foleni Dar es Salaam lakini kwa kuanzisha bandari kavu Morogoro tutakuwa tumepata suluhu ya kudumu kumaliza changamoto hii lakini pia tumeinua hali za uchumi wa sehemu hizo zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kuchangia katika sekta hii ni suala la kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu na wengi wamechangia umuhimu wa kilimo, unaajiri asilimia 70 ya watu wetu, pato la Taifa asilimia 25, hela za kigeni zaidi ya asilimia 30 inatoka kwenye kilimo, chakula asilimia 100, malighafi asilimia 65 lakini bajeti hii imejikita zaidi kwenye miundombinu badala ya kutatua uchumi wa watu wengi walikojiajiri kwenye kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba niliona kwenye Mpango kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo katika suala la Mkulazi, lakini sikuona kwenye Mpango wa 2016/2017, nilijua sasa kilimo ndiyo kitapewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri katika hili…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu ambayo ni ya Mipango na Fedha. Nichukue fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kufika siku ya leo. Pia nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sijampongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango na timu yake kwa hotuba nzuri na mipango ambayo tunaiona Tanzania mpya iko mbioni kuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nichukue fursa hii kukupongeza wewe binafsi. Nakupongeza kwa umahiri wako mkubwa, kwa weledi mkubwa na unavyoendesha Bunge hili la Kumi la Moja. Usitishike na hivi vitisho kutoka upande wa pili, simamia hapo kwa sababu ya kutenda haki. Walizoea kupindisha sheria, sasa wamekutana na nguli wa sheria ambaye ni wewe ndio maana wanagonga ukuta. Usivunjike moyo, sisi tuko nyuma yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nijielekeze katika kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii hasa kwenye Benki ya Kilimo kwa sababu kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili. Serikali kwa kuliona hilo walianzisha Benki mahsusi ya Kilimo na Bunge hili la Kumi ambalo sisi hatukuwepo lakini tulikuwa tunasoma kwenye magazeti na taarifa mbalimbali lilipitisha sheria ya Serikali kuweka mtaji wa kutosha katika benki ile ili kutatua changamoto za wakulima wa nchi hii. Kwa sababu tatizo kubwa la nchi hii, sekta kubwa inayoajiri watu wengi ambayo ni kilimo imekuwa haikopesheki na niipongeze Serikali kwa kuliona hilo kwa kuanzisha benki hii. Walitenga zaidi ya shilingi bilioni 300 iwe kwenye Benki ya Kilimo, lakini mpaka sasa nasikitika Serikali wamepeleka shilingi bilioni 60 tu. Hizi shilingi bilioni 60 hazitoshi kutimiza malengo na mipango ya Serikali iliyopanga kwa ajili ya kukwamua Watanzania walio wengi waliojiajiri katika sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili limekuwa ni kubwa sasa matokeo yake benki hii badala ya kujielekeza katika lengo kuu la kuendeleza sekta ya kilimo hasa zile skimu za umwagiliaji na kuwakopesha wakulima, wanafanya kazi kama za benki za biashara, kutoa mikopo ya muda mfupi kwa sababu wanaogopa kupata risk kubwa. Wanaweza kutoa mikopo ya muda mrefu na pesa ikazama na wakakinzana na masharti ya Benki Kuu ya mtaji unaohitajika. Kwa dhamira hiyohiyo ambayo Serikali mliiona mwanzoni na mipango mizuri iliyokuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hii benki iongezewe fedha ili iweze kujitanua na kuwawezesha wakulima wengi kufaidika wakiwepo na sisi huku wa mikoani katika Jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki na Tanzania kwa ujumla, hii benki ndio mkombozi wa mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ikiiwezesha benki hii inaweza kufungua matawi yake na kuongeza rasilimali watu. Kwa sasa hivi ule mtaji waliopewa hawawezi kujitanua zaidi ya kuwa Dar es Salaam ambapo ndiyo makao makuu, lakini kama mnavyojua Dar es Salaam siyo wadau wakubwa sana wa kilimo, kilimo kiko mikoani, Morogoro na sehemu nyingine. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu iongeze mtaji katika benki hii ili lengo na kusudio lililokusudiwa liweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili nijielekeze katika Tanzania Commodity Exchange. Ni wazo zuri kwa sababu utakuwa ndiyo muarobaini wa soko la uhakika la bidhaa zetu za kilimo hususan kwa wakulima wa Tanzania. Kwa sababu ni soko ambalo litatoa haki kwa wadau wote wa soko hili kuanzia mkulima, madalali, wafanyabiashara, mawakala lakini hata na wanunuzi wenyewe. Pia kutakuwa na uhakika wa ubora ambao unajulikana kwa sababu mambo yataenda kisheria na kimtandao, hawezi mtu yeyote kudanganywa, bei itakuwa wazi lakini hata na ubora utajulikana, ule udanganyifu mdogomdogo utaondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu tu katika hili na niiombe Serikali kwa sababu katika utaratibu wa soko hili miongoni mwa wadau wakubwa watakuwa wale madalali wa hilo soko, madalali wa wanunuzi na wa wauzaji. Katika kitabu cha hotuba nimesoma anasema mpaka sasa hivi kuna makampuni matano ambayo yameshajiorodhesha katika soko hili. Kwa hiyo, niombe wakati anakuja kujumuisha angetutajia angalau makampuni haya ni yapi ili tuwe na uelewa mpana zaidi na tuone ni makampuni yale yale ya kiujanja ujanja yameshakamata fursa au sasa ni makampuni ya ukweli yako kwa ajili ya kumkomboa mkulima halisi wa Tanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ni pana sana na imeajiri watu wengi kwa maana ya wafanyabiashara wadogo, wafanyabiashara wa kati, mawakala, madalali, ajira zao kubwa ziko hapa. Kwa hiyo, naomba kuishauri Serikali pamoja na kwamba tunaenda kwenye utaratibu huu wa soko ambao ni mzuri sasa makundi haya ni vizuri tukayatambua katika ushirika wao mbalimbali. Kwa mfano pale Dar es Salaam kuna Chama cha Madalali cha Mazao ya Mahindi na Ufuta lakini Morogoro pia viko vyama vya madalali na mikoa mingi vipo. Kwa sababu mitaji yao ni midogo ni vizuri tukawatambua kisheria kwenye umoja wao huo tukaweka utaratibu wakaingia kwenye soko hili nao wakatumika kama ndio madalali wa wakulima au wa wazalishaji. Badala ya kuwaacha nje tukaachia makampuni makubwa ndiyo yashike kazi hiyo basi tujue tutakuwa na kundi kubwa la vijana wa Kitanzania watakosa ajira jambo ambalo ni hatari. Sisi lengo letu kubwa ni kutengeneza ajira kwa ajili ya kuongeza vipato kwa wananchi wetu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu katika taratibu huu, Wizara hii ivitambue vikundi vyote au umoja wowote wa madalali Tanzania nzima. Kwa sababu kwanza itasaidia sana wakitambuliwa kisheria na kupewa leseni inaweza kuwa tax base nyingine kwa sababu nafahamu wanapata mapato makubwa hawa madalali wa mikoa mbalimbali. Suala la udalali mtu akienda kununua atatumia dalali na akiuza atatumia dalali. Wakitambuliwa kisheria na mapato yao yakijulikana watasaidia kuchangia katika pato la Taifa kwa maana ya kulipa kodi na kila kitu. Pia kama Serikali mkawatengenezea fursa ya kushiriki katika huu utaratibu mpya unaokuja ili tusiliache kundi kubwa nyuma baadaye tukaenda wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo siyo kwa sababu ya umuhimu, hii Wizara ndiyo Wizara nyeti inayogawa mafungu ya fedha. Sisi kama Bunge hapa tunapitisha bajeti lakini kuna changamoto kubwa pesa haziendi kama tulivyopitisha na pia hazifiki kwa wakati. Nimuombe Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango, ni mpya kwenye Wizara hii na ndiyo maana sasa hivi hatuwezi kuchangia sana tunampa nafasi, changamoto zilizotokea huko nyuma tunaomba uzirekebishe ili pesa hizi tunazopitisha zifike kwa wakati na zifike kama tulivyopitisha ili zile shughuli za maendeleo tulizopanga katika Majimbo yetu na Wilayani kwetu ziende kama zilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja tu, suala la MKUKUTA katika Halmashauri yangu ya Morogoro Vijijini mwaka wa tatu huu haijafika hata senti tano. Hata ile miradi ambayo ilianzishwa imeishia palepale badala yake tumeelekeza nguvu kwamba wananchi wajichangie, wameshajichangisha tumeshamaliza vyumba vya madarasa zaidi ya miaka mitatu lakini mafungu hayapo. Kwa hiyo, nimuombe kwa niaba ya Serikali hiyo basi walete haya mafungu ili tuweze kumalizia miradi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja kwa 100% na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango uliopo mbele yetu. Kwanza nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa kutendo cha kudhibiti matumizi hasa kwenye taasisi zake na mashirika ya umma. Kubwa kuliko lote hasa kitendo cha kuhamisha akaunti zote za taasisi hizi kuwa BOT, ni kitendo ambacho ni cha kizalendo sana na hili nalisema kwa kinaga ubaga na mifano ipo hai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna baadhi ya wenzetu wanasema kwamba hali halisi ya maisha yamekuwa magumu kwa sababu ya kitendo hiki, siyo kweli. Siyo kweli kwa sababu hizi benki zilianzishwa, kazi yake ni kuhudumia wateja, kutoa mikopo kwa wafanyabiashara. Lakini hujuma zilizokuwa zinafanyika nitoe mfano mmoja tu wa taasisi moja kama ya bandari, yenyewe iliweka bilioni 440, kwenye fixed account kwenye mabenki mbali mbali kwa rate ya 3.5%, bilioni 440. Halafu yenyewe tena ikaenda kukopa kwenye benki hizo hizo bilioni 100 kwa ajili ya miradi yake ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu hapa, baada ya Serikali kuona hujuma hizo, kupeleka hizo akaunti BOT anasema Serikali imenyonga wafanyabiashara, siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taasisi nyingine hizo hizo, hii mifuko yetu ya kijamii, inakusanya shilingi bilioni 38 kwa mwaka, shilingi bilioni 27 matumizi kwa sababu fedha zipo tu za kutumia, inachangia kwenye mfuko shilingi bilioni mbili tu kwa mwaka mzima, leo Serikali imeona hujuma hizo imepeleka hizi fedha zote zikapate udhibiti BOT mtu anasema wafanyabiashara wamenyongwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kitendo hiki cha kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima na ovyo ambacho sasa tuiombe tu Serikali ifanye mfumo mzuri ambao kama hizi benki zipo ziende sasa zikakope kule BOT kwa rate inayokubalika ya sokoni siyo ile ya kiwizi wizi ya 3.5 halafu fedha nyingine zinaenda kwa wajanja wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa sababu huu unasema ni wizi alafu hizo hizo benki zilikuwa zinaikopesha Serikali kwenye treasure bill, Serikali ikiwa na tatizo inakwenda kukopa kwenye benki zile zile kwa rate kubwa zaidi ya asilimia 15, 20. Kwa hiyo, niwaombe Serikali hapo msilegeze, msimamo ni huo huo ili kwamba tuwe na nidhamu katika matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili kuhusu makusanyo hasa kwenye TRA, nilikuwa naomba Waziri Mpango katika mapendekezo ya kuongeza tax base, kweli tumepata muhamasisho wa Rais na watu mbalimbali kwamba watu wajitolee kwenda kulipa kodi kwa hiyari, lakini kitendo cha Mtanzania, wengi wanahofia ukisema leo nataka kuanza kulipa kodi, TRA sasa hawaanzi pale, watakupa hizo kodi miaka kumi ijayo hata kulipika hazilipiki. Ni sawa sawa sasa wanakwenda kufilisi, matokeo yake watu wanaogopa na watu walipakodi wanaendelea kubaki walewale, ni kitu ambacho hakitaisaidia Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu, kama kuna uwezekano toweni muda maalum kwamba watu wajitokeze kulipa kodi ili muongeze wigo wa tax base, lakini mkasamehe hayo makando kando ya nyuma ili watu waanze kulipa kuanzia hapo kwenda mbele. Tutaongeza wigo mpana wa kulipa kodi kuliko kung’ang’ania kusema mpitie makando kando hayo watu hawana risiti, hawana uthibitisho zaidi ya kuwafilisi, matokeo yao watafilisika, hamtakusanya tena hizo kodi uko mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine sasa hivi kwenye makusanyo hayo ya kodi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ili nami nichangie katika Wizara hii muhimu kwa mustakabali wa afya na uzima wa Watanzania. Naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, hususan Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu ya Wizara hii kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ari na kasi kubwa hasa katika ongezeko kubwa la kibajeti na upelekaji fedha hususan za dawa katika Halmashauri zetu. Vilevile naishukuru Serikali kwa kuonesha nia na kutuweka katika mpango wa kuboresha huduma ya afya na upanuzi wa miundombinu katika Kituo chetu cha Afya Mkuyuni ili kiweze kutoa huduma za upasuaji na wodi za akinamama ili kuwa na uzazi salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi na shukrani hizo, naomba kutoa maombi yangu kwa niaba ya watu wa Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Vijijini kwa ujumla, kama ifuatavyo:-

(i) Ahadi ya Rais kuhusu gari la wagonjwa. Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, alituahidi kutupatia gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya Mkuyuni tangu mwaka 2010 na mwaka 2014 katika Kituo cha Afya, Kinole, mbele ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kupokea ombi hilo toka kwa watu wa Kinole kupita kwa Chifu Kingalu Mwana Banzi wa 14 lakini mpaka sasa magari hayo hayajapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu kupitia kwa Mheshimiwa Waziri kutekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais na kutupatia magari hayo mawili ili kuokoa maisha ya watu wetu hasa akinamama wakati wa kujifungua ukizingatia hatuna hospitali ya wilaya na hali ngumu ya kijiografia katika eneo letu kutokana na milima iliyoko kule Kinole. Pia, tunategemea Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ambayo iko mbali na jimbo na halmashauri yetu.

(ii) Ombi la Hospitali ya Wilaya. Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ni ya muda mrefu lakini mpaka sasa hatuna hospitali ya wilaya na kutegemea hospitali ya mkoa. Ombi langu ni kuomba Serikali kutujengea hospitali ya wilaya ili kutoa huduma karibu na wananchi na kupunguza msongamano katika hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri wangu, wakati tunasubiri ujenzi wa hospitali ya wilaya ambao utachukua muda, naomba Serikali iteue kituo kimoja cha afya kati ya Tawa, Dutumi, Mkuyuni ama Ngerengere kuwa hospitali ya wilaya ili kutoa huduma kwa wananchi kutokana na halmashauri kwa sasa kuhamia kijijini Mvuha ambapo ni mbali na hospitali ya mkoa.

(iii) Kutokana na hali ya kijiografia ya Jimbo letu, naomba Serikali kutujengea na kuzipandisha hadhi zahanati za Mikese Station, Mkulazi, Tununguo, Seregete, Kinole, Kibuko na Kiroka kuwa vituo vya afya ili kutoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie hoja iliyokuwa mbele yetu. La kwanza nijielekeze kwenye ukurasa wa 76 wa kitabu cha PAC. Kwanza nitangaze interest kuwa mimi ni Mjumbe wa PAC hasa kuhusu suala la muamala uliokwama wa shilingi bilioni 100 TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili kwa sababu ni suala mtambuka, TAMISEMI kama tunavyofahamu ni Wizara mama na inayobeba Halmashauri zetu. Tumewasikiliza Wajumbe waliotangulia wengi tulikuwa tunalalamika pesa haziji kwenye Halmashauri yetu kwa wakati, na tulikuwa tunatafuta mchawi ni nani? Katika hili ni vizuri Serikali ikachukua hatua stahiki kujua liko nini hapo Hazina, kwamba imetoa exchequer ya shilingi milioni 287 kwenda TAMISEMI, halafu wanarudisha nyuma shilingi bilioni 100 bila taarifa ya TAMISEMI wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI wanaandika cheque kuwalipa wateja wao wanakwenda benki wanakuta hewa, na hili sio jambo dogo. Katika Bajeti ile ambayo ilikuwa ya shilingi milioni 287 ambayo pesa zilizoletwa hizi ni sawasawa na asilimia 47, maana yake nini? Kama asilimia 47 pesa hazikuja TAMISEMI ukizingatia hata bajeti yetu mpya ya maendeleo ni asilimia 40 hii mpya, hiyo ya zamani ilikuwa chini ya hapo. Ndiyo maana kumbe tunalalamika kwenye Halmashauri zetu pesa haziji tatizo liko huku huku kwa watoa fedha wenyewe. (Makofi)
Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano, tuko pamoja kama alivyosema Mheshimiwa Rais alipokuja hapa Bunge tumsaidie na sisi Wabunge tuko tayari kumsaidia katika vita vyake vya kifisadi ili kuangalia hizi shilingi bilioni 100 ziko wapi. Kwa sababu bila kuchukua hatua stahiki mchezo huu utaendelea na hali itakuwa kama hivi, kila siku tutagombana, miradi haiendi, pesa haziji baadaye tunaweza kuweka rehani utekelezaji wetu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni kuhusu NFRA kupata hasara ya shilingi bilioni 6.7. Hasara hii ni kubwa sana. Nakubaliana na sababu zilizotolewa na Kamati lakini kubwa ni kuchanganya biashara na siasa. Kuna watu wamesimamishwa, lakini binafsi nasema wamesimamishwa kiuonevu kwa sababu sio makosa yao. Ilipitishwa hapa kwamba uwezo wa NFRA kuhifadhi ni tani 140,000 kwa ma-godown yao yote, lakini baada ya NFRA kununua mahindi haya viongozi hawa hawa wa juu na sisi viongozi wa kisiasa kila mtu anataka mahindi yake yanunuliwe katika eneo lake na kutoa maagizo kwa viongozi wa NFRA wanunue bila kuzingatia uwezo wa kuhifadhi waliokuwa nao.
Leo mahindi yameharibika, tunawatoa kama mbuzi wa kafara wakati kimsingi siyo waliosababisha tatizo hili. Kwa sababu wasingetekeleza maagizo ya wakubwa wao waliyokuwa wanaambiwa kwamba lazima mahindi ya wakulima yanunuliwe bado wangetambuliwa tatizo lingekuwa liko pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hili naomba Serikali ifanye uchunguzi hasa na kila mtu apate haki yake stahiki kwa sababu uwezo wa kuhifadhi ni tani 140,000 unamuambia mtu anunue tani zaidi ya 200,000, ataziweka wapi? Lazima aziweke nje na akiziweka nje mvua zikija lazima yaharibike. Sasa yakiharibika unakuja kumuadhibu wakati wewe ndiyo uliyemuelekeza kwamba anunue na hela umempelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nataka tu nilizungumze vizuri sana, Serikali siyo mnunuzi wa mahindi. Tunapowazuia wakulima wasiuze mahindi yao nje wakati tunajua uwezo wa kuzalisha mahindi Tanzania ni zaidi ya tani milioni tatu na uwezo wa Serikali kununua ni mdogo, kwenye bajeti mwaka huu tumetenga kununua tani 100,000, wewe utajihesabu ni mnunuzi? Matokeo yake wakulima wanaacha kuuza mahindi yao sehemu zenye wateja baadaye yanakosa soko, kipato cha wakulima kinaenda chini na kudhoofisha uchumi wa wakulima wetu. Kwa hiyo, naomba sana hata mwaka huu mnapokuja tena kununua hifadhi ya chakula tusije kuwazuia wakulima kuuza mahindi yao kwa wateja wengine kwa kusema Serikali itakuja wakati tunajua uwezo huo wa kununua mahindi yote ya wakulima wetu hatuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, niungane na maoni ya Kamati yangu hasa kuhusu suala la NSSF kwa sababu huu ni mfuko muhimu sana, ni mfuko wa wapigakura wetu, wastaafu wako huko, ni vizuri Bunge hili likaridhia Kamati hiyo ikaenda kujiridhisha na hali halisi iliyokuwepo huko NSSF. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwa hatua stahiki ilizochukua kukabiliana na matatizo na changamoto zilizokuwepo ndani ya NSSF.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe angalizo sana hasa kwenye ule Mradi wa Dege kwa sababu ile ardhi mpaka leo bado ni ya Azimio kwa mujibu wa title, lakini pia kuna mkataba ambao NSSF umeingia na mbia wake. Kwa hiyo, suala hili siyo la kukurupuka, ni vizuri kujipa muda wa kutosha kuangalia kwa kina na kujiridhisha mikataba inasemaje ili siku za usoni tusije kuingia kwenye matatizo makubwa zaidi ikiwa tutakurupuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wote wanaotuhumiwa bado ni watuhumiwa tu, tusije kuwahukumu kama wakosaji wakati chombo cha kuhukumu ni mahakama. Wote tujipe subira kama Kamati yangu ilivyosema, twende huko tujiridhishe, iletwe taarifa ambayo imekamilika. Kwa sababu jambo hili bado liko kwenye uchunguzi tuviachie vyombo vingine vya uchunguzi viendeee kufanya kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nataka kusema kwamba tumefanya kazi yetu katika mazingira ya kutegemea paper work na maelezo tu kutoka kwa management na Bodi tulizokutana nazo, lakini kiuhalisia PAC tumeshindwa kwenda kutembelea mradi wowote. Kama unavyofahamu siku hizi kuna watumishi hewa, wanafunzi hewa, tunaamini pia kuna miradi hewa. Kwa hiyo, ombi langu kwako kwa sababu tunakwenda kwenye mchakato wa bajeti ni vizuri bajeti ya Bunge ikaongezwa ili na bajeti ya PAC na LAAC zikaongezwa kuziwezesha kutembelea hii miradi tusije kuuziwa mbuzi kwenye gunia kwa sababu tunaweza kusema mradi fulani upo kumbe haupo. Ni vizuri tukatembelea miradi na mashirika hayo kwenda kujiridhisha zaidi. Pia tupate nafasi ya kutembelea hata makampuni au mashirika mengine ya umma yanayofanana na mifuko hii kwenda kujiridhisha kwa sababu mashirika mengi yanafanya mambo kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho niombe Serikali ifuatilie hii mifuko. Kwa mfano, NSSF wenyewe kama tunavyofahamu wana majengo mengi lakini cha ajabu majengo yao hawakai, wenyewe wanapanga, ni kitu cha ajabu kabisa. Wana majengo mazuri kwa nini wasikae kwenye majengo yao kuokoa fedha? Kwa hiyo, niishauri Serikali iwape mwongozo kwa sababu hivi vyombo vinasimamiwa na Benki Kuu na Mdhibiti wa Mifuko wawashauri NSSF na mifuko mingine yote warudi kwenye nyumba zao walizojenga wakae huko kuliko tafsiri ya sasa hivi inavyoonekana kwamba wanalazimika kwenda kupanga kwa sababu labda ya 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye miradi ya uwekezaji, mifuko mingi kwa ujumla inawekeza….
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa dakika tano na mimi nichangie hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze moja kwa moja kwenye ukurasa wa 24 wa kitabu cha Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji hasa kwenye miradi mikubwa ya mabwawa nchini ambayo haijatekelezwa kwa muda mrefu. Kama kuna mradi ambao haujatekelezwa muda mrefu kuliko yote hapa nchini basi ni mradi wa Bwawa la Kidunda. Huu mradi wa Bwawa la Kidunda kabla ya uhuru mwaka 1955 ndiyo wazo hili lilianza na andiko lake la kwanza usanifu ulifanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uhuru chini ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1962 akaubeba mradi huu akasema huu ndio ukombozi wa uchumi imara kwa sababu nchi yetu inategemea uchumi wake kwa kiasi kikubwa kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua Bwawa hili la Kidunda lilikuwa ndio liwe mkombozi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji lakini kwa ajili ya maji ya uhakika kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, ujazo wa wakati ule ulikuwa ukubwa wake zaidi ya cubic meter milioni 450, Serikali zote zilizokuja ziliendelea kuubeba mradi huu lakini haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya ukosefu wa pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu kuanzia mwaka 1994 pamoja na mahitaji ya maji kuendelea kuongezeka mradi huu ulibadilishwa matumizi kutoka katika multiple use maana ya kwamba mahitaji ya binadamu, mifugo pamoja na umwagiliaji yakawekwa tu kwa ajili ya single use yaani matumizi ya binadamu na kupunguza ukubwa wa bwawa kutoka cubic meter milioni 450 mpaka 190, kwa kusikiliza tu wadau wa maendeleo wasiotutakia mema kwa ajili ya maendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua wakati mwingine wadau wa maendeleo wakitaka kukuzuia wanaweza kukusingizia tu wakakwambia bwana hapo Selous hapo kuna nyoka hayupo ulimwengu mzima yupo hapo tu, mkilijenga hilo bwawa huyo nyoka atakuwa amepotea, na sisi tumekubali hiyo akili tukapunguza bwawa kutoka cubic meter milioni 450 mpaka 190. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila nchi ulimwenguni sasa hivi inatanguliza maslahi ya wananchi wake zaidi kuliko ya mtu yeyote. Wamarekani wanasema Marekani kwanza, Waingereza wanasema Uingereza kwanza na Wachina wanasema China kwanza ni lazima tufanye maamuzi magumu katika hili ili tukubaliane na changamoto zinazotukabili nchini kwetu hasa ya ukame. Lazima turudi kwenye usanifu wa awali wa ule ujazo wa 450 milioni badala ya huu wa 190 tu kwa ajili ya matumizi ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tuende na andiko lile la asili ambalo liliandikwa tangu mwaka 1955 wakati ule hata mahitaji ya maji yalikuwa machache sana kuliko sasa hivi mahitaji ya maji ni makubwa zaidi, hata Mto Ruvu unaanza kupungua maji hususan wakati wa kiangazi. Kwa hiyo, hili Bwawa la Kidunda utekelezaji wake ndiyo utakuwa ni uokozi kwa ajili ya uchumi wetu kama tunavyojua Dar es Salaam tunaitegemea zaidi ya asilimia 75 kwa uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili kwa Serikali ni kwa sababu miaka yote 62 mradi huu haujatekelezwa shida kubwa ni fedha. Leo hii kule Mkulazi ndiyo kinajengwa kiwanda kikubwa kuliko chote cha sukari kupitia kampuni ya Mkulazi Holding, lakini kwa tatizo la maji huu mradi hautatekelezeka. Bwawa hili ni lazima lijengwe ndiyo huu mradi wa Mkulazi nao u-take-off.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
HE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja hii muhimu ya ulinzi wa nchi yetu na mipaka yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumshukuru Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake hasa Waziri wa Ulinzi na wataalam wake kufika katika Jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki katika Wilaya ya Morogoro Vijijini kufuatilia uwanja wa ndege wa Jeshi letu pale Kizuka Ngerengere. Tunasema ahsante sana.

Mheshmiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufulu kwa maamuzi yake ya kuagiza kutujengea barabara ya lami kutoka Ubena – Zomozi – Kizuka mpaka Ngerengere kupitia uwanja wa Kizuka.

Mheshiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo za watu wa Morogoro Kusini Mashariki hususani wananchi wa Tarafa ya Ngerengere na Tarafa ya Mvuha, naomba sasa nitoe ombi langu rasmi kwa Serikali hasa kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tuna Kambi mbili za Jeshi pale Ngerengere yaani ya Kizuka na Sangasanga na kwa kuwa barabara itakayowekwa lami ni ya Ubena – Zomozi – Kizuka - Ngerengere na kwa kuwa umbali kutoka Kizuka - Ngerengere - Sangasanga siyo mbali na Kambi ya Sangasanga wanatumia barabara ya Mdaula – Sangasanga yenye urefu wa kilometa 10, kwa hiyo basi, naomba barabara hii nayo iwekwe lami kwani watoto hawa wa Sangasanga na Kizuka ni baba na mama mmoja ili wale Sangasanga wasione wametengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu kulipa uzito suala hili na hasa kwa umuhimu wa jeshi letu na hasa kikosi hiki cha Sangasanga kutokana na uzito wa majukumu yake. Naomba barabara ya Mdaula – Sangasanga - Ngerengere kuwekwa lami ili kuunganika na ile ya Ubena - Kizuka - Ngerengere na kurahisisha usafiri kwa jeshi letu na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata fursa ya kuchangia Kamati hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nitoe shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyetupa afya na uzima hata tumekutana jioni hii ya leo. Lakini pili, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa sera yake ya viwanda na kwa kuanza kwa vitendo, natoa mfano kwenye jimbo langu. Mwaka wa jana wakati nakuja hapa watu wengi majirani zangu hapa walikuwa wananiambia kwamba Mgumba Mkulazi, lakini kilio kile kimemfikia Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka mazingira mazuri na tumepata mwekezaji, Mkulazi Holding Company Limited, kampuni tanzu ya Mifuko ya Jamii ya NSSF na PPF inawekeza kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa sukari katika Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki, chenye uwezo wa kuzalisha tani 150,000 kwa mwaka na kuondoa adha ya sukari hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kwenda kwa vitendo utekelezaji wa sera ya viwanda. Haya sio maneno, kama mtu anabisha aje kule Mkulazi anaona ujenzi unavyoanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo sasa niende moja kwa moja kwenye ushauri. La kwanza, naomba kuishauri Serikali hasa kwenye suala hili la TFA (Shirika la Mbolea) na kama walivyosema Kamati, suala kubwa hili shirika ni muhimu sana hasa kwenye sekta ya kilimo. Hili shirika ndio tunalitegemea kwa ajili ya usambazaji wa mbolea kwenye zana za kilimo, lakini kama Serikali haiwezi kulilea vizuri lazima madeni haya yataendelea kuongezeka na shirika hili litakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe tu Serikali, leo hii kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati, shirika hili lilianza na mtaji wa shilingi bilioni 17.9 leo wana mtaji wa negative billion 12.3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini na sababu ni nini? Ni kwa sababu, mara nyingi Serikali, hasa kwenye taasisi zake hasa inapopata huduma kwenye ulipaji au fidia ya ile ruzuku ambayo inaagiza taasisi zake itumie inachelewa kwa muda mrefu sana, athari yake inakuwa kubwa na matokeo yake haya mashirika yanapoteza uaminifu kwa wadau na taasisi nyingine za fedha, hata kwa wasambazaji wengine wa mbolea kule wanakochukulia mbolea hizi na matokeo yake wanashindwa kukopesheka, athari kubwa inaenda kwa wakulima wetu kutokupata mbolea kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niishauri Serikali inapohitaji huduma kwenye shirika lake, kwa mfano kama hapa, shirika hili linaweza kwenda kununua mfuko labda wa mbolea shilingi 50,000 lakini Serikali kwa ajili ya kurahisisha ipatikane kwa bei nafuu, ikaiambia TFC uzeni shilingi 30,000 nyingine ni ruzuku. Sasa ile ruzuku ambayo Serikali ina top up ni vizuri ikaipeleka kwa wakati ili kufidia shirika liweze kujiendesha kibiashara na ziweze kulipa madeni yake kule ambako inakopa. Badala ya kutoa miongozo kwamba toeni ruzuku, shirika linatoa ruzuku, lakini hela haziendi kwa wakati, ndio matatizo haya ya negative ya mtaji yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili niishauri Serikali kuhusu kwenye Bodi za Mazao. Bodi za Mazao zimekuwa nyingi na mara nyingi tunavyoziona nyingine hazipo kwa ajili ya manufaa ya kilimo chetu wala kwa wakulima wa Tanzania. Sasa ushauri wangu kwa Serikali, ni vizuri tukaunda bodi mbili tu, moja ikawa kwa ajili ya mazao ya biashara ambayo itasimamia mazao yote ya biashara yale makubwa yaliyokuwa na bodi kwa sasa; kwa mfano labda ile Bodi ya Korosho, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Pareto, Bodi ya Pamba, zote zikaunganishwa zikawa bodi moja na bodi ya pili ikawa Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Hizi zikiwa mbili itakuwa ni rahisi, moja inashughulikia mazao mchanganyiko nyingine mazao ya biashara, kwa kufanya hivyo hata menejimenti yake inakuwa ni rahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu Mifuko ya Jamii. Katika hili nakubaliana na mapendekezo ya Kamati, wanapozungumza kwamba Msajili wa Hazina (TR) anatakiwa atambulike kisheria kwenye mifuko hii. Nilikuwa naomba tu Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuja kufunga hoja yake; bado mimi sijaelewa vizuri. Kwa uelewa wangu mdogo najua hii Mifuko ya Jamii ni mali ya wanachama. Sasa kama mali ni ya wanachama Serikali ipo kama mdhamini lakini si moja kwa moja kama ilivyo kwenye yale mashirika ya Serikali kwa mfano kama TTCL na mashirika kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia mali ya wanachama labda TR aingie moja kwa moja kule kama msimamizi mali ya Serikali wakati ile si mali ya Serikali moja kwa moja ni mali ya wanachama, naomba ufafanuzi katika hili ili tuweze kupata uelewa wa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa katika kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha na uwekezeji, lakini pamoja na nia nzuri ya kupunguza matumizi, bado utaalam na ubora unatakiwa uzingatiwe, sasa kumezuka tabia moja hasa kwenye mashirika haya ya Serikali, iwe NHC au TBA utakuta mwenyewe ndiye mkandarasi, wakati huo huo ni mshauri mwelekezi wa mradi na pia ndiye msimamizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali hii haipo kisheria, kwasababu pamoja na yote kuna mambo ya Kisheria. Lazima iwe kwamba engineer awe mwingine, msimamizi awe mwingine, ili kuonesha kama kazi inayotekelezwa inakidhi ubora unaotakiwa. Tukiachia hali hii iendelee, pamoja na nia nzuri ya kupunguza matumizi, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuja kupata miradi ambayo inakuwa chini ya kiwango, baadaye hata tija au value for money ikakosa kuonekena huko mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika mjadala huu wa kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya, uzima na uhai na kuwa hapa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa Kasim Majaliwa kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia shughuli za Serikali kwa weledi, maarifa na utulivu wa hali ya juu. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayofanya ya kumsaidia Waziri Mkuu na wao wenyewe kufika katika Jimbo langu la
Morogoro Kusini Mashariki kwa nyakati tofauti katika kusukuma maendeleo ya watu wa jimbo langu na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa ni mnyimi wa shukrani kama sitamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwatumikia Watanzania na hasa kwa kutuletea maendeleo katika Jimbo langu kama vile Kiwanda cha Sukari katika Kata ya Mkulazi, barabara ya lami toka Ubena Zomozi mpaka katika kambi yetu ya Jeshi la Ulinzi na Usalama, Kambi ya Kizuka na mradi wa maji katika Kijiji cha Fulwe Mikese na mengine mengi katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na cha kupewa hakina nyongeza na kwa kuwa katika kijiji na Kata hii ya Ngerengere kuna kambi tatu za Jeshi kwa maana ya Kizuka na kikosi namba 23 na Sangasanga na kwa kuwa vy ote ni vikosi vyetu na wote ni wapiga kura wangu na hawa wa kikosi cha Sangasanga wasijisikie wanyonge na kubaguliwa na kusahaulika, kwa niaba yao, naiomba Serikali hasa Mheshimiwa Rais kuweka lami pia barabara toka Kizuka mpaka Ngerengere Mjini kupitia Sangasanga mpaka Mdauli ili vikosi vyote vitatu viweze kufikiwa kiurahisi kwa barabara ya lami na walinzi wetu kufaidi matunda ya uhuru kama dhamira njema aliyoonyesha Rais wetu Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kuanza kuweka lami katika barabara ya Ubena-Kizuka. Naomba sana hii barabara ya Mdaula-Sangasanga- Ngerengere-Kizuka nayo kuwekewa lami kilometa kumi na tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuanza mchakato wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge ambayo inapita katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki katika Vijiji vya Kidunda, Ngerengere, Kimoko na Mikese ambayo italeta maendeleo
makubwa katika eneo la Morogoro Vijijini na Morogoro kwa ujumla ukizingatia sisi Morogoro ndiko inakoishia awamu ya kwanza ya mradi huu. Tunashukuru sana kwa mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo naomba kuishauri Serikali na kuiomba itoe ufafanuzi rasmi eneo la hifadhi ya reli ni kiasi gani sababu katika kuandaa utekelezaji wa mradi huu, wataalam wametoa notisi kwa wananchi kubomoa nyumba zao kupisha mradi lakini kila
sehemu ina umbali tofauti. Kwa mfano, Ngerengere wameambiwa umbali ni mita 120 kila upande, Mikese mita 90 na Morogoro Mjini mita 30 kila upande. Je, umbali wa hifadhi ni upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kutokana na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sheria Namba 4 na 5 na kanuni zake inasema kama mtu amejenga na kukaa zaidi ya miaka 12 bila kubughudhiwa eneo hilo ni halali yake. Je, kwa sheria hiyo Serikali haioni ina wajibu wa kuwalipa wananchi waliojenga na kukaa zaidi ya miaka 12 bila bugudha ili kutowarudisha nyuma kiuchumi wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia muda waliopewa wa mwezi mmoja kuhama ni mdogo sana kwa mwananchi wa kawaida kuhama tena bila ya fidia kupata fedha ya kujenga nyumba mpya. Naomba Serikali kuwapa muda wananchi wa miezi sita ili kupata muda wa kuhama kwa utulivu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ni muhimu, michezo ni afya na Bunge linatuhimiza kushiriki mazoezi lakini hatuna uwanja wa kufanya mazoezi kwa timu zetu za Bunge. Kwa kuwa Serikali imehamia Dodoma na kutakuwa na mahitaji makubwa ya viwanja vya michezo, naomba kuishauri Serikali na Ofisi ya Bunge kuwaona CDA na Mamlaka ya Halmashauri kulipatia Bunge eneo la michezo kwa Timu za Bunge badala
ya sasa kutangatanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika suala hili. Kwa sababu ya muda naomba nianze kumpongeza Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi na Naibu wake Mheshimiwa Angelina Mabula, pamoja na wataalam wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya kukabiliana na changamoto mbalimbali za ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa Kijiji cha Lukonde wana matatizo makubwa, wanapata kipigo kutoka kwa mwekezaji wa Shamba la Kidago alilopata kwa njia ambazo sio halali toka Uluguru Toiler aliyewanyang’anya wananchi bila ya kufuata taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu ni mkubwa sana kwa Kijiji na Kitongoji cha Kidago, Lukonde, nyumba zao zaidi ya sitini (60) zimechomwa moto zaidi ya mara tatu tofauti na kwa miaka tofauti na kuchoma mazao yao na mfugaji huyo aliyepewa ardhi hiyo. Ombi langu, Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili kumalizika naomba afike kidogo na kujionea hali halisi na kuwasaidia wananchi hawa ili waweze kuishi katika nchi yao kwa amani na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nataka kushauri Serikali kutenga Bajeti na kupima ardhi yote ya Halmashauri ya Morogoro Vijijini. Kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi, kupanga matumizi ya ardhi kwa ajili ya wakulima na wafugaji na hifadhi na kujenga miundombinu ya kiufugaji kama majosho, mabwawa katika maeneo ya wafugaji na kutoa elimu kwa wafugaji kufuga kisasa na umuhimu wa kuwa na mifugo kutokana na ukubwa wa ardhi waliyonayo na miundombinu ya mifugo iliyopo sehemu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwaondoa wafugaji wavamizi waliokuja Morogoro vijijini na Morogoro kwa ujumla bila kufuata sheria Kanuni na taratibu za kuhamisha mifugo toka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na kuharibu mazingira, mashamba ya wakulima, vyanzo vya maji na barabara zetu tulizojenga kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi hii ili nichangie katika Wizara hii ya Maji.

Kwanza, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uhai na uzima nimefika siku ya leo. Pili, niishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa inayofanya hasa kwa hiki kidogo ambacho kimekuja. Wengi hapa tumesimama tunalaumu kweli pesa ni ndogo,ni kweli nami nakubaliana kabisa pesa ni ndogo, hata ile bajeti tuliyopanga haijaenda ni kweli lakini nilikuwa najua kwa sababu pesa ni ndogo basi tungekuja na mawazo mengi zaidi ya kuishauri Serikali namna gani inaweza kuongeza pesa. Kwa kusema hayo, nami niungane na wenzangu waliotangulia, pamoja na mambo yote kutokana na umuhimu wa maji ni vizuri tukaongeza bajeti katika mafuta ile ya shilingi 50 kwa lita ili tuongeze Mfuko wa Maji uweze kuwa na fedha ya kutosha twende tukaongeze bajeti ya maji ili kutatua tatizo la maji nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo niende kwenye ukurasa wa 71 wa kitabu cha Waziri kuhusu Bwawa la Kidunda. Hili Bwawa la Kidunda mwaka jana tulipitisha bajeti hapa na tulilitengea shilingi bilioni 17 na baada ya kufuatilia mimi mwenyewe Hazina walishatoa shilingi bilioni 10. Madhumuni makubwa ya hiyo shilingi bilioni 17 ilikuwa ni kujenga ile barabara ya Ngerengere - Kidunda kwenda kwenye mradi lakini pia kulipa fidia ya shilingi bilioni nne kwa watu walioathirika kupisha barabara na sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sana, mpaka hivi tunavyoongea pesa hizo zimetolewa Hazina lakini hata senti tano haijalipwa kwa hao waathirika wa Kidunda, Chanyumbu na sehemu nyingine.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri akija anieleze, bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi, wiki mbili zilizopita watu walikuwa hawaamini kama Mbunge wao anafuatilia fedha hizi, walikuja hapa bila taarifa mpaka Wizara ya Maji kufuatilia hela hizi. Tulikutana na Waziri tunamshukuru sana alitupa ushirikiano na alituambia kwamba zipo hela nusu shilingi bilioni mbili. Cha kushangaza mwaka jana tulikwenda Wizara ya Maji, tuliambiwa ziko nusu shilingi bilioni mbili hizo hizo, mwaka huu tena mwezi wa tatu tumefika ziko shilingi bilioni mbili hizo hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba Serikali ije ituambie kwamba hizi shilingi bilioni mbili zitapatikana lini na hawa watu watalipwa lini ili waweze kuendelea na shunghuli zingine na pia hizi shilingi bilioni mbili zilizobaki Serikali ituambie itatoa lini ili mradi huu uweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya fidia hiyo kulipwa, pia huu mradi ni wa muda mrefu sana na una umuhimu mkubwa sana kitaifa, ni vizuri sasa tupate kauli ya Serikali. Kila kitabu cha bajeti kinachokuja, cha mwaka jana kimekuja wanasema tunatafuta fedha, mwaka huu kimekuja wanasema tunatafuta fedha, fedha zipo kwa watu binafsi. Kama pesa hakuna, tuishauri Serikali ikaingia ubia na private sector kutekeleza hii miradi mikubwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nasema hivyo mradi huu umeanzishwa tangu mwaka 1955 na wakoloni. Baada ya kupata uhuru mwaka 1962, Mwalimu Nyerere kutokana na umuhimu wake aliona tuendelee na mradi huu. Mwaka 1982 likaja tena andiko tuendelee, nashangaa sana mwaka 1994 Serikali kwanza imeupunguza mradi wenyewe kwa sababu wakati ule mradi huu ulikuwa ni zaidi ya lita milioni 430 leo umepunguzwa ni lita milioni 190.

Naomba niishauri Serikali, kutokana na umuhimu wa maji, kutokana na kilimo cha kubahatisha, kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni vizuri tukazingatia andiko lile lile la mwanzoni ili huu mradi uwe multi-purpose badala ya single use kwa ajili ya matumizi tu ya binadamu. Ni vizuri tukarudisha kule ili tuweze kutumia kwa ajili ya umwagiliaji pamoja na matumizi ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niende sasa kwenye suala la Jimbo, hii ilikuwa ni mradi wa kitaifa. Sisi mwaka jana hapa tunashukuru Serikali tulipata mradi mmoja pale Mikese ambao ulikuwa unachukua zaidi ya shilingi bilioni mbili na mwongozo Serikali ikautoa yenyewe wakasema hawawezi kutuma pesa mpaka kwanza mkandarasi aanze. Tunamshukuru sana huyu mkandarasi ameshafanya kazi zaidi ya asilimia 40 na juzi ameshusha zaidi ya semi-trailer tatu ya mabomba yote ya mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, tushaandika certificate zaidi ya tatu lakini bado hatujapata majibu, Mkurugenzi wangu hajapata majibu na pesa hazijakuja. Nimeona kwenye kitabu cha Waziri kwenye bajeti mwaka huu imeshushwa hii bajeti imewekwa shilingi bilioni
1.7 wakati mradi ule peke yake una shilingi bilioni mbili.

Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu Tukufu, ni vizuri tukaleta hela hizi mapema kabla hii bajeti haijaisha kwa sababu kama hizi hela hazijaletwa kabla bajeti haijaisha mkandarasi atasimama baadaye mtakuja kutuletea hizi hela shilingi bilioni 1.7 kama zitapatikana mwakani zitakuwa haziwezi kutosheleza kutekeleza mradi huu wala miradi mingine. Kwa sababu hii tunayotumia ni cash budget, naomba sana Serikali ikazileta hela hizi za kumlipa huyu mkandarasi ili ule mradi wa Mikese aumalizie kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka nichangie kwenye mradi wa Chalinze Awamu ya Tatu. Mradi wa Chalinze Awamu ya Tatu na sisi watu wa Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Vijijini ni wanufaika kwani kuna vijiji kama saba vitapata maji katika mradi huu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, nataka kujua tu Serikali mradi huu itaumaliza lini ili vijiji vyangu vya Bwawani, Ngerengere, Kidunda na Kidugalo na kambi zetu zote zile za Jeshi kwa maana ya Kinonko zipate maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. OMARY T. MGUMBA Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kununua ndege na kuimarisha Shirika letu la Ndege ili kuinua utalii wa ndani na nje kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya wataalam kwa wasilisho zuri la hotuba yao ya uchapaji kazi wao katika Wizara hii. Baada ya utangulizi huo, naomba kutoa mchango na ushauri wangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zuio la mkaa; zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanategemea matumizi ya mkaa na kuni katika maisha yao ya kila siku, kwa mfano vijijini. Kwa kuwa nishati mbadala mpaka sasa haijasambaa nchi nzima hasa kwa maeneo ya vijijini katika Jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki ambako zaidi ya asilimia 70 ya vijiji umeme haujafika na hata gesi hakuna na wananchi hutegemea kuni na mkaa kama nishati ya kupikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni kwa kuwa wananchi wengi vipato vyao ni vidogo kumudu gharama ya umeme ukizingatia umeme wenyewe ni mdogo ambao haukidhi mahitaji ya nchi na kwamba anayetumia zaidi analipa zaidi na gharama kubwa sana ambazo wananchi hawawezi kumudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri Serikali kusitisha zoezi la katazo la matumizi ya mkaa kusafirisha sehemu moja kwenda nyingine mpaka pale Serikali itakapokuwa na uwezo wa kuzalisha na kusambaza nishati mbadala nchi nzima kwa wananchi na pia kupata maandalizi ya kutosha katika kutoa elimu kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu ahadi ya Serikali ya kutupatia ardhi ya kulima kutoka katika msitu wa Mkulazi ulio karibu na Kijiji kipya Bwila Juu walikohamia watu waliopisha ujenzi wa bwawa la Kidunda. Watu waliopisha ujenzi wa bwawa kutoka Kidunda Kitongoji cha Manyanyu na vingine walikuwa na nyumba zao pamoja na mashamba katika maeneo hayo kama ilivyo kawaida sehemu za vijijini. Lakini Serikali aliwapa wananchi hawa katika eneo jipya viwanja tu vya kujenga nyumba bila ardhi ya kilimo ili kujitegemea kiuchumi kama eneo la awali lilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia changamoto hiyo na umuhimu wa kilimo na uchumi wa wananchi hao, Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajabu Lutengwe ilisema itawapa wananchi hawa ardhi yenye ukubwa wa ekari 50,000 iliyo karibu na vijiji vipya ili wananchi waweze kuhamia pale na kuendeleza shughuli zao za kilimo na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kutimiza ahadi hii haraka ili wananchi waweze kuendeleza shughuli za kiuchumi na kuepuka mambo kama yale yaliyotokea mwaka 1973 katika operation vijiji. Ni lini Serikali itatoa ardhi hii kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni mamba katika Mto Ruvu. Wakati wa kiangazi tunapata maafa mengi hasa katika Kata ya Tunanguo kutokana na mauaji yanayosababishwa na mamba wanaotoka katika Mto Ruvu. Ombi langu kwa Serikali, kwanza kuvuna mamba hawa kutoka Mto Ruvu kwa sababu wamekuwa wengi na pili kulipa fidia na matibabu kwa wananchi walioathirika na mamba. Pia Serikali kulipa wananchi wangu walioathirika na tembo miaka saba iliyopita katika kata ya Kidugala, Ngerengere, Mkulazi na Matuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake thabiti, makini na uzalendo mkubwa. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na wataalam na watendaji wa Wizara kwa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo nianze kwa kutoa mchango wangu na nianze na kuwasemea watu wangu wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na hasa kuhusu TRC kupitia RAHCO. Naipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Makutupora, Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maendeleo ya ujenzi huu wa reli kuna watu walioathirika kwa kupisha maeneo yao ili kujengwa kwa reli, lakini mpaka sasa watu hawa hawajalipwa fidia zao. Fidia hulipwa ndani ya miezi sita baada ya tathmini na hulipwa kabla ya eneo kuchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuchelewa kulipwa fidia hii kumeleta athari kubwa kwa watu wetu kwa sababu wananchi walikuwa wanategemea maeneo hayo kwa shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, mifugo na pia ni makazi yao kwa baadhi ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamebomolewa nyumba zao, mashamba yao, huduma za jamii kama zahanati, shule na kadhalika. Kwa mfano, watu wa Ngerengere na Mikese wamebomolewa nyumba zao bila kulipwa fidia na wengine kulipwa fidia ndogo isiyolingana na bei ya soko na hali halisi katika Kijiji cha Mikese Station, zahanati mpya inabomolewa na kutakiwa kulipwa shilingi milioni 70 ambayo ni ndogo kuliko gharama zilizotumika au kuhitajika kujenga upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali kulipa fidia kwa wakati na kiwango kinachostahili ili kuwainua wananchi kiuchumi au kuwalipa kwa kiwango kwa kuzingatia thamani halisi badala ya kuwarudisha nyuma zaidi kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kuwalipa fidia watu hawa walioathirika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya Elimu kwa umuhimu wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uzima kufika siku ya leo. Vilevile nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kupunguza changamoto za madawati nchini na kutoa elimu bila malipo ya ada toka shule ya chekechea mpaka shule za upili kidato cha nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya utangulizi huu nianze kutoa mchango wangu na ushauri kwa Serikali. Halmashauri ya Morogoro ina ukubwa zaidi ya kilometa za mraba 11,700 na umbali zaidi ya kilometa 180 toka Morogoro Mjini na shule ya kwanza ya sekondari ilijengwa mwaka 2000 na nyingine wakati wa ujenzi wa shule ya kata mwaka 2006 lakini hatuna shule ya fani hata moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Morogoro ina changamoto nyingi hasa ya miundombinu na uwezo mdogo wa mapato. Ili kukabiliana na changamoto hizo naiomba Serikali Kuu itusaidie katika ujenzi wa shule ya kidato cha tano na sita katika shule ya kata ya Mkuyuni, Ngerengere ama Nelson Mandela ambazo ni makao makuu ya tarafa za Mkuyuni, Ngerengere na Mikese kama zilivyofuatana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kudhibiti utoro na mimba za utotoni; kutokana na takwimu za BEST 2016 za utafiti wa kufahamu sababu mbalimbali za wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuacha shule mwaka 2015 ni vifo, mimba na utoro. Kutokana na takwimu hizo, mchanganuo wake ni kama ufuatao:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujauzito ni 3,637; utoro, 139,866 na vifo ni 3,917. Kutokana na takwimu hizo, utoro ni chanzo kikubwa cha watoto kuacha shule, ni zaidi ya 94% kuliko hata ujauzito. Katika hawa wapo watoto wa kiume na wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kuja na mkakati maalum kama ule wa ujenzi wa shule za kata na wa utengenezaji madawati nchi nzima, kumaliza ujenzi wa mabweni katika shule zote za kata ndani ya miaka miwili ili kukabiliana na tatizo la utoro na mimba za utotoni; kwa watoto kuishi shuleni chini ya uangalizi wa walimu na waangalizi wao wawapo mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe mwongozo shule zote za kata kujenga mabweni katika shule za kata kwa kutenga fedha katika bajeti zao na kushirikiana na wadau wa maendeleo na wananchi wa sehemu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Halmashauri wapewe mwongozo na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika kusaidiana na wadau kumaliza tatizo hili la utoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nataka kutoa ushauri pia katika ujenzi wa maktaba katika kila Wilaya na Tarafa nchini ili kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa ubora wa elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Afrika ikiwemo Tanzania, tuna tatizo kubwa kama Bara na kama nchi kwamba watu wengi hawapendi kusoma na kujifunza ili kupata uelewa na maarifa mbalimbali kutakakowezesha watoto kufanya vyema katika mitihani na pia mtu wa kawaida kupata uelewa wa kukabiliana na mambo ya kidunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wenzetu wa mataifa ya nje wanatuambia ukitaka kumficha kitu Mwafrika weka vitu katika maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata vijana na wanafunzi wengi wanasoma kwa ajili ya kufaulu mitihani na siyo kupata uelewa na ufahamu wa somo ama kwa kutopenda kusoma au kukosekana kwa miundombinu ya kujisomea na hata shule zetu zinakosa kuwapa mazoezi na mitihani ya mara kwa mara wanafunzi kwa kukosa miundombinu ya vifaa vya kuandalia mitihani hiyo mingi kwa mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ili kuinua elimu yetu na kujenga utamaduni kwa watoto kupenda kujisomea tangu wakiwa wadogo. Kwa kuzingatia uwezo mdogo wa Serikali wa kujenga maktaba katika kila kata; na kwa kuwa hakuna vitendea kazi vya kuandaa mitihani ya majaribio katika shule nyingi za umma; hivyo basi, naishauri Serikali yangu kuja na mkakati wa kujenga maktaba katika kila Wilaya na Tarafa ili zitumike kwa kujisomea. Hii itawasaidia watoto wa shule za msingi na sekondari katika tarafa husika na jamii husika, pamoja kutumia majengo hayo kama kituo cha elimu, mafunzo na miundombinu ya kuandaa mitihani, kuichapisha na kupeleka katika shule ya eneo lake kutokana na mahitaji ya shule husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kujenga maktaba na vituo vya elimu kwa jamii katika kila makao makuu ya tarafa, itasaidia sana kujenga utamaduni wa kujisomea kwa watoto wetu na jamii kwa ujumla, pia kupunguza gharama za kuandaa mitihani ya majaribio na ushindani kati ya shule kwa shule, kata kwa kata na tarafa kwa tarafa ili kuongeza uelewa na uwezo wa vijana wetu kuelewa masomo yao na kujiandaa vyema kushinda na kufaulu mitihani yao katika shule za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu kwa uchumi wa Watanzania wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu wa mdomo, niko hapa katika kuongeza mchango wangu huo wa awali nilioutoa kwa kuchangia kwa mdomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa viwanda nchini na kutokana na umuhimu wa ajira na fedha za kigeni na ushindani uliopo katika soko la kimataifa, naomba kuishauri Serikali kama ifuatavyo kwa kuongezea katika ule mchango wa mdomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kukutana na wawekezaji wa ndani wa kubangua korosho haraka iwezekanavyo ili kutambua matatizo wanayowakabili hususan kushindwa kupata malighafi, kushindwa kubangua korosho kutokana na uwezo wa viwanda vyao na wengine kufunga na kuhamia nchi za jirani kama Msumbiji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa kuwa tunayo makampuni ya ndani kama vile ETG, Sunshine Group, Hyseas, MECT na hata yale yaliyofungwa kama vile Olam (T) Ltd., Buko Agro Focus, Micronix, Premier Cashew, Lindi Farmer na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukutana nao, Serikali itabaini wana matatizo gani na aina ya msaada gani wanahitaji kutoka Serikali ili Serikali ije na mipango, sera na mikakati ya kuweza kubangua korosho zetu ndani ya nchi ili kuongeza thamani ya korosho zetu, kutengeneza thamani ya korosho zetu, kutengeneza ajira kwa vijana wetu na kuongeza mapato ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Serikali kuwapa kipaumbele wawekezaji wa ndani wa kuchakata mazao ya kilimo hususan wabanguaji wa korosho katika mnada wa Stakabadhi Ghalani kwa kuwa unaweza kushindana na wabanguaji wa nje na wafanyabiashara wa korosho ghafi kwenda nje, sababu mataifa ya nje wanatoa ruzuku kwa wafanyabiashara hao na gharama za uendeshaji ziko chini katika nchi ya India, Brazil na Vietnam na kusababisha korosho inayobanguliwa nchini kuwa na gharama kubwa na kusababisha kuwa na bei ya juu katika soko la kimataifa na kukosa ushindani wa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali itoe kipaumbele kwa wawekezaji wa ndani kupata korosho katika minada ya mwanzo ili kupata korosho bora ambazo zina viwango vikubwa vya ubora kabla ya zile korosho za mwanzo zinazoathiriwa na mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuongeza export toka asilimia 15 mpaka asilimia 20 na hili ongezeko kwenda kuwapa ruzuku wabanguaji wa ndani na kuvutia wawekezaji wengi zaidi na kutengeneza ajira na kuongeza thamani ya bidhaa zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na sababu za kihistoria na kwa sababu za ushindani wa soko la korosho katika soko la dunia, naishauri Serikali kutokujiingiza tena katika biashara ya kubangua korosho. Kama tulivyojenga viwanda 11 mwishoni mwa miaka ya 1970 vya kubangua lakini tulishindwa na kuua kabisa zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu suala hapa siyo kubangua tu korosho, suala la msingi ni soko la kuuzia korosho zilizobanguliwa katika soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lengo mojawapo la kubinafsisha na kupata mbinu na masoko ya kimataifa, soko la kimataifa lina ushindani mkubwa kwa kuwa walaji wanataka au wanapenda kununua kutokana na brand na jina la makampuni waliyoyazoea. Sasa wasiwasi wangu tutawekeza lakini tunashindwa kuuza katika masoko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba baada ya kuwekeza kama Serikali, ni bora kuwapa ruzuku na vivutio wawekezaji wa kubangua korosho nchini ili kupunguza gharama za uzalishaji ili kuweza kushindana na kwa kuwa wengi wana masoko katika masoko ya kimataifa, itakuwa ni rahisi kushindana kuliko Serikali au Bodi ambayo haina wateja kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na siyo kwa umuhimu, nataka kupata kauli ya Serikali kuhusu ununuzi wa ufuta mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hili kwa sababu tarehe 9 Mei, 2017 Mkuu wa Mkoa wa Lindi katika kikao cha wadau wa zao la ufuta alitoa tamko la soko la ununuzi wa ufuta msimu wa mwaka 2017/2018, utakuwa wa Stakabadhi Ghalani. Pia tarehe 17 Mei, 2017 Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kilwa ambalo ni sehemu ya Mkoa wa Lindi limekaa na kutoa tamko nalo kuwa mwaka huu soko la ufuta litakuwa ni soko huria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hizo ni kauli kutoka kwa viongozi wa Serikali halali, Serikali Kuu na Serikali ya Halmashauri ambazo zimeleta mkanganyiko mkubwa kwa wakulima na wafanyabiashara, ukizingatia msimu uko karibu kuanza na makampuni yameshaajiri wafanyakazi, mawakala na kuchukua maghala ya kukusanyia ufuta na kusababisha taharuki kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufunga hoja yake, aje atuambie nini kauli ya Serikali kuhusu mfumo wa ununuzi wa ufuta mwaka huu, utakuwa ni mfumo upi? Wa soko huria au stakabadhi ghalani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kupeleka fedha za maendeleo katika miradi mbalimbali na taasisi zake kwa asilimia 34, ni hatua nzuri ukizingatia zaidi ya miaka miwili kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia fedha za maendeleo hazikuwa zikipelekwa, lakini sasa zimeanza kupelekwa, ni hatua ya kupongezwa badala ya kubeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, sasa nianze kutoa mchango wangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Fedha za Usimamizi na Ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo. Serikali imetoa Mwongozo wa kusitisha miradi yote ya maji kutosimamiwa na Wakandarasi Washauri kwa kupunguza matumizi na badala yake kazi hiyo ya usimamizi wa utekelezaji wa miradi ifanywe na wataalam wa mkoa na halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia hiyo nzuri ya kubana matumizi, lakini Serikali imesahau kupeleka fedha katika halmashauri husika za usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya maji na mingine na kusababisha miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango na kuchukua muda mrefu kukamilika kwa kukosa usimamizi wa karibu wa kitaalam kwa watumishi wenye weledi wa kazi hii. Naomba kushauri Serikali yangu kupeleka fedha za usimamizi na ufuatiliaji kuwezesha halmashauri na mikoa kusimamia miradi hii ili kupata thamani halisi ya fedha ya miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Chalinze III. Mradi wa Chalinze III ni wa muda mrefu sana na mpaka sasa haujakamilika. Katika mradi huu na sisi watu wa Morogoro Kusini Mashariki ni wanufaika wa mradi wa Chalinze III katika Vijiji vya Kidugalo, Chiwata, Maseye, Kinonko, Ngerengere, Sinyaulime na Lubungo, pamoja na Kambi zetu za Jeshi za Kinonko, Kizuka na Sangasanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya usambazaji maji na matanki ya kuhifadhia maji imejengwa zaidi ya miaka tisa iliyopita kiasi kwamba mingine imeanza kuchakaa, lakini maji hayajawahi kutoka hata siku moja. Nataka kupata kauli ya Serikali kuwa ni lini watu wa jimbo langu katika vijiji hivi watapata maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mkandarasi yupo site kufuatilia na kukagua miundombinu ya maji na kutaka kujenga kidaka maji (intake) ya kupokea maji kutoka Ruvu Chalinze kwenye chanzo cha maji. Nataka kujua, ili mkandarasi aweze kujenga kidaka maji hicho, ni eneo gani litajengwa tanki ili aweze kujenga? Kwani mpaka sasa mkandarasi anashindwa kujua wapi ajenge kidaka maji kwa sababu hajui mwelekeo wa bomba kuu litatoka wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kulipwa wakandarasi wa maji. Katika Halmashauri yangu ya Morogoro tulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 5.19 mwaka 20/06/2017, lakini mpaka sasa tumepata shilingi bilioni 1.09 tu sawa na asilimia 19.84 ya bajeti ya mwaka na sasa tumebakiza miezi miwili muda wa mwaka wa fedha kibajeti kwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshapeleka madai ya Certificate zaidi ya mara tatu, lakini mpaka sasa hatujapata majibu yenye thamani ya shilingi milioni mia nane ya kumlipa mkandarasi wa Mradi wa Fulwe, Mikese na wengine, ili waweze kumaliza miradi hii kwa wakati. Ombi langu kwa Serikali ni kutuletea fedha hizi, ili kuwalipa wakandarasi kabla ya mwaka wa bajeti kwisha kwani, bajeti ya mwaka huu imekuwa ndogo kuliko ya mwaka jana, yaani ni shilingi bilioni
1.7 toka shilingi bilioni 5.1.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Bwawa la Kidunda mwaka wa jana ndani ya Bunge lako Tukufu, Serikali kupitia Wizara hii ya Maji iliomba bajeti ya shilingi milioni kumi na saba kwa sababu ya kulipa fidia kwa watu wangu waliopisha mradi wa Bwawa hili la Kidunda; Matuli, Kwaba, Mkulazi, Diguzi, Chanyumbu na watu wa Kitongoji cha Manyunyu na pia kutengeneza barabara ya kutoka Ngerengere mpaka Kidunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hakuna fidia iliyolipwa ya shilingi bilioni nne wala barabara iliyotengenezwa katika eneo hilo, ingawa barabara hii ilitengenezwa sehemu korofi na mwekezaji wa Shamba Number 217, Mkulazi Holding Company Limited. Kwa sasa barabara hiyo imejaa maji na kuharibika kabisa kutokana na kwamba haikutengenezwa yote na kwa kiwango kilichotarajiwa na DAWASA. Kwa kuwa, bajeti tulitenga ya shilingi bilioni 17 na Hazina wametoa shilingi bilioni 10 kati ya fedha hizo, lakini sasa Wizara wanasema wametenga shilingi bilioni 1.5 tu ya mwaka 2016/2017 na shilingi bilioni mbili katika bajeti ya mwaka 2017/2018 ambayo haitoshi kwa fidia wala ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kupata Kauli ya Serikali; kwanza, ni lini wananchi watalipwa pamoja na fidia kwa kuwa muda mrefu umepita? Pili, ni lini Serikali itajenga barabara hii ya kwenda Kidunda, ukizingatia bajeti tulishapitisha na fedha kutolewa na Hazina? Tatu, kwa kuwa, watu waliopisha mradi ni wakulima waliopoteza nyumba zao na mashamba yao yaliyokuwa katika sehemu walizopisha mradi, lakini walikopelekwa wamepewa viwanja tu kama vile wao ni watumishi wa Serikali au wafanyabiashara wakati ajira zao ni kilimo; na kwa kuwa bila mashamba maisha ya wananchi hawa yatakuwa magumu sana na kwamba haiwezekani kuishi, je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kumega Msitu wa Mkulazi ulio karibu na makazi mapya ili wananchi hawa wapate sehemu za kulima na kuendesha maisha yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Fedha. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya na uzima tumekutana siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mchango wangu nitajielekeza kwenye milioni 50 za kila kijiji. Mheshimiwa Waziri wa Fedha mwaka jana wakati alipokuja hapa alikuja na mpango mzuri na Bunge lako hili lilitenga zaidi ya shilingi milioni 59 kwa ajili ya kutekeleza azma hii ya kupeleka milioni 50 kila kijiji. Hata hivyo, mpaka muda huu tunaongea kutokana na ripoti ya Kamati na hali halisi hata kule kwenye vijiji vyangu, hakuna kijiji chochote ambacho kimeshapata milioni 50. Moja ya changamoto kubwa ambayo tunakutana nayo sasa hivi tukienda kwenye Majimbo swali la kwanza utaulizwa milioni 50 zitakuja lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida kubwa sana kule vijijini kwa sababu, niwapongeze sana UWT upande wa akinamama walifanya kazi kubwa sana pamoja na Wabunge kuhamasisha vikundi vingi sana vimeanzishwa kwa matarajio kwamba kuna milioni 50 zitakuja, kwa sababu tuliwaambia kwamba tutapitishia kwenye vikundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali wakati inakuja kufunga mjadala huu ni vizuri ikaja na kauli thabiti ya Serikali kwamba hizi fedha zitatoka au zimebadlishwa mpango mwingine ili tuwe na jibu la Serikali na Wabunge kuwapelekea wananchi wote tuwe na msimamo mmoja badala ya sasa hivi wananchi hawatuelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nikikumbuka ile bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri alisema tumetenga milioni 59, mwaka huu tungepeleka labda milioni 50, mwakani 50 mpaka miaka mitano vijiji vyote tungevimaliza. Sasa mwaka jana hatukupeleka hata senti tano, lakini bajeti ya mwaka huu inakuja na milioni 60. Nilitegemea kwa sababu hatukupeleka mwaka jana bajeti ya mwaka huu ingekuja na mia au zaidi ya mia ili twende na mipango ambayo Serikali ilipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nijielekeze kwenye mapato. Tatizo kubwa la nchi yetu hasa nchi hizi za dunia tatu ikiwemo na Tanzania tuna mahitaji makubwa sana lakini mapato yetu ni madogo. Katika hili niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, watu wengi walikuwa wanalaumu kwa nini tumepokea mpaka sasa asilimia 34 ya fedha za miradi ya maendeleo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa sababu kabla haijaingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano zaidi ya miaka miwili, Serikali Kuu ilishindwa kupeleka hela za maendeleo katika Halmashauri zetu. Sasa leo tumepata asilimia 34, kutoka sifuri unapata asilimia 34 ni suala la kupongeza sio kubeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema katika hili ni ukweli usiopingika, hali ya biashara sasa hivi nchini siyo nzuri, biashara nyingi zinafungwa. Maana ya biashara kufungwa ni kwamba ajira za Watanzania zinapotea, mapato ya mtu mmoja mmoja na wafanyabiashara yanapotea, mapato ya Serikali yanapungua. Huko mbele tusipochukua tahadhari ya kuongeza tax base ya walipa kodi nchi hii inawezekana walipa kodi watapungua na mapato ya Serikali yatapungua sana. Baadaye hata haya tuliyofikia sasa yatakuwa yanapungua, kwa sababu athari nyingine itakuja, tutawakandamiza wale wachache walipa kodi, tuwaongezee viwango badala ya kuisambaza hii kodi kwa watu wengi zaidi ili waweze kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili, nimeona katika ukurasa wa 77 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema kwamba, miongoni mwa mikakati yao ni pamoja na kurasimisha biashara nyingi zisizokuwa katika mfumo rasmi kuja kwenye mfumo rasmi wa kodi. Leo hii tuna tatizo katika nchi yetu, Mtanzania mfanyabiashara akisikia biashara yake imetembelewa na Polisi au imetembelewa na TRA anapumua zaidi ikitembelewa na Polisi kuliko TRA. Anajua leo sijui kuna shida gani? Au leo umaskini sasa umeshaingia kwenye biashara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili, niombe kama kweli tunataka kuwarasimisha na kupanua tax base katika hili, tupate walipa kodi wengi katika nyanja hizi, basi Serikali inapaswa itoe elimu ya kutosha kwa walipa kodi na Watanzania kwa ujumla, umuhimu wa kulipa kodi, manufaa kwa nchi na kwenye hii biashara yenyewe, watu waelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutoa incentive maalum kwa wajasiriamali wa ndani. Kuwaambia mtu yeyote yuko huru kurasimisha biashara yake kuingia kwenye mfumo wa kodi, tutaanza kudai kodi hapo alipoanza kurasimisha kwenda mbele. Tatizo sasa hivi zinafungwa biashara nyingi, sio kwamba hawapati faida, wakati mwingine mtu anaona anakuwa salama zaidi kufunga biashara aachane na Serikali kuliko aje ajitangaze kurasimisha anapewa madeni kuanzia miaka ilipoanza hiyo biashara, akija kuangalia uwezo wa kulipa hana, matokeo yake biashara inakuwa hohehahe na anafilisiwa kabisa. Sasa kwa nini mtu aje ajirasimishe kwa nini asifunge tu aachane nayo atafungua biashara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kama kweli tuna dhamira ya kuwasaidia wajasiriamali na kweli tuna dhamira ya Watanzania walipe kodi bila kushurutishwa basi ni vizuri tutoe incentive. Tuseme miezi sita au mwaka mtu yeyote tutaanzia kulipa kodi pale unapoanza kurasimisha biashara yako kwenda mbele. Nilishawahi kusema humu ndani tuchukue mfumo kama wa Wizara ya Ardhi inavyofanya, leo nikipima ardhi yangu mimi naanza kulipa leo, huwezi kusema kwamba miaka yote unatumia ardhi hii lazima ulipe, hakuna mtu atakuwa na huo uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwenye matumizi. Ni kweli mwenzangu mmoja alizungumza huku, sisi tuna tatizo kubwa sana la mapato ni madogo lakini hata hayo mapato yenyewe madogo, Serikali inajibana, TRA wanajibana yakifika kwenye Halmashauri zetu au taasisi zetu hayatumiki kwa makusudio ya Serikali iliyopanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano kwenye Halmashauri yangu ya Morogoro, kuna miradi kwa mfano miradi ya maji pale Kiroka na Tuluwakongo, hela zimekuja tangu 2015 milioni 700 mpaka zimeanza kutumika leo kwa mbinde kwelikweli, kwa sababu zile pesa zinatakiwa Mkandarasi zisimamiwe kule vijijini, sasa watu wa halmashauri hawana maslahi binafsi ya asilimia 10, kwa hiyo hawaoni umuhimu wowote wa kusaidia hilo jambo liende. Wako radhi wananchi wakose hiyo huduma kwa vile tu wao hawana maslahi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri Serikali mkaweka mifumo sahihi ya ufuatiliaji ili mjue fedha mlizozipeleka kule zinatumika? Kwa sababu sisi Madiwani tunadanyanywa sana na hawa wataalam na wao wanasema kila kitu tuwaachie wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapeni mfano mwingine. Kwenye hiyo hiyo Halmashauri juzi tu tumetoka kwenye Kamati ya Fedha, walileta pale pesa walizoleta zaidi ya milioni 360 kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini wakatuletea sisi shilingi milioni 170 wakasema zingine hamna, na bank statement wanakuletea kabisa unaambiwa haipo. Baada ya kubanana sana zikaja ikaletwa tena, tulizisahau milioni 190. Sasa mambo kama haya wakati mwingine kama mnavyofahamu wasimamizi wakubwa ni madiwani, lakini madiwani wenyewe hawa hawana mishahara. Sasa akirubuniwa kidogo ni rahisi sana kupitisha kwa sababu anajiangalia yeye na maslahi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, kwa sababu Madiwani ndio wasimamizi wakubwa wa Serikali kule chini wa pesa za wananchi, ni vizuri Serikali ikaangalia namna gani ya kuwalipa mishahara Madiwani ili waweze kusimamia pesa za umma zitumike kama zilivyopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Wakaguzi wa Ndani kule kwenye Halmashauri, kila akitaka kwenda kukagua miradi anaambiwa hatuna pesa Serikali haijagawa OC. Hizo pesa wakati mapato ya ndani yapo! Morogoro DC tumekusanya zaidi ya bilioni 1.6, haijawahi kufikiwa tangu uhuru ianze, tulikuwa tunaishia milioni 500, 600, lakini leo Mkaguzi wa Ndani anaaambiwa kwamba hakuna OC huwezi kwenda kukagua ile miradi, kwa sababu wanaficha mambo yao waliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kunipa nafasi kuchangia katika Taarifa za Kamati zetu zote mbili hizi. Kwanza nachukua nafasi hii kuzipongeza Kamati zote mbili kwa taarifa ambazo zinaakisi hali halisi iliyopo nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nijielekeze moja kwa moja kwenye masuala ya mbaazi pamoja na mahindi, kwa sababu sisi watu wa vijijini na ukizingatia nchi hii, watu zaidi ya asilimia 70 wanategemea kilimo, siku zote lazima tuwasemee wakulima ambao ndio tumekuja kuwawakilisha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbaazi limetikisa sana na limeathiri sana wakulima wetu Tanzania kwa ujumla. Tatizo kubwa kuna lugha inazungumzwa kwamba Serikali ilihamasisha sana. Mbaazi hatujawahi kuhamasishwa, tulikuwa tunalima siku zote kutokana na kuvutiwa na bei zilizopo sokoni, lakini kilichotokea mwaka 2017 tu alipokuja Waziri Mkuu wa India kuja kusema atanunua yeye mbaazi zote za Tanzania, ndiyo pale labda watu wengine tunachanganya kusema kwamba Serikali ilihamasisha tununue mbaazi hizi na leo hakuna mnunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea na kwa mbahati mbaya sana, kabla hatujafikia mwisho wa majadiliano na kusaini mikataba, baadaye India ikatokea kwamba wamezalisha mbaazi zaidi kuliko mahitaji yao. Kwa hiyo, wakawa hawahitaji tena kuingia mkataba na Tanzania wala na nchi nyingine kwa sababu walichozalisha wenyewe ni ambacho kilikuwa kinawatosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri tu kwa Serikali kwamba ni vizuri tukafanya utafiti mkubwa na mahitaji ya soko husika kabla ya kubeba hiyo kauli kuipeleka kwa wananchi. Wanaweza kuichukua na kuongeza uzalishaji wakati hitaji hilo kwa wakati huo hakuna. Ni vizuri tukawekeza zaidi kwenye research and development, kufanya utafiti kwa maana ya masoko, nini kinahitajika kwa wakati gani, hata ambacho tukizalisha tunakuwa na uhakika muda gani kinahitajika na wapi tunakipeleka na kwa bei gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano wa pili, sasa hivi kuna taarifa nyingi tunaletewa kwamba sasa hivi China inahitaji sana mihogo. Kama viongozi tunaweza kuichukua kauli hiyo tunapeleka kwa wananchi wetu, tukawaambia kwamba mihogo inahitajika, lakini mpaka sasa hivi nina uhakika kwamba hata mikataba haijafanyika na hatujui ni bei gani? Kwa hiyo, tusije kuchukua kosa lile lile tulilofanya kwenye mbaazi kwenda kuwahamasisha watu wakaanza kulima kabla ya kuingia mikataba rasmi na kujua bei yake.

Matokeo yake wakulima watakuja kuilaumu Serikali pasipokuwa na sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu suala la mahindi, ni vizuri Serikali mkaliweka vizuri suala hili kwa sababu wananchi wengi wameaminishwa kwamba Serikali ndiye mnunuzi mkubwa wa mahindi kupitia NFRA, kitu ambacho siyo sahihi kabisa, kwa sababu labda sisi wenyewe Wabunge tunasahau. NFRA tumepitisha wenyewe hapa bajeti ni shilingi bilioni 100 tu. Shilingi bilioni 100 unanunua mahindi hata tani 100,000 hayazidi. Sasa kuwaaminisha watu kwamba Serikali itakuja kununua mahindi wakati pesa yenyewe tuliyotenga ni chache, storage capacity ni ndogo kwenye uzalishaji wa tani zaidi ya 4,000,000 za mahindi Tanzania ni just a peanut. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza NFRA kama inavyofahamika yenyewe National Food Reserve Agency. Huyu ni wakala tu wa kuhifadhi chakula cha dharura cha msaada, kwa hiyo, sio mnunuzi wa mahindi yetu Tanzania. Katika hili naomba kuishauri Serikali, ni wakati muafaka sasa wa kuifufua na kuwekeza zaidi katika Shirika la Hifadhi la Chakula (National Milling Corporation) ili lichukue nafasi yake kama zamani ndiyo iwe kampuni mbadala ya kununua mahindi yetu na kuyahifadhi na kufanya biashara kwa niaba ya umma. Tuna uhakika tunatengeneza soko la mazao yetu ya nafaka badala ya kutegemea NFRA ambayo kazi yake ilikuwa ni kununua chakula cha hifadhi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali, ni vizuri tukawatafuta wadau au Serikali yenyewe kulifufua shirika letu la usagishaji ili lifanye kazi yake kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa sheria na ndiyo itakuwa mkombozi wa mazao yetu ya kilimo. Kama mnavyojua, Serikali au Watanzania wengi tumejiajiri kwenye kilimo, kuwaacha nyuma wakulima ni kuliacha Taifa na watu wengi zaidi maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu labda ni uwekezaji katika mabwawa. Mimi natoka Morogoro na kama mnavyojua sasa hivi mafuriko yako mengi sana, Kilosa, Morogoro Vijijini na sehemu nyingi tu ambapo yanatuathiri na kuturudisha nyuma kiuchumi. Sasa badala ya kutumia haya kama ni majanga, Serikali tuyageuze kama ni fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kuyaachia maji haya yaende baharini, ni vizuri sasa tukaanza kuwekeza na kuyavuna maji haya ya mvua kuanzia Manyara, Dodoma, Morogoro yote, kwa sababu maji haya yanayotuathiri Morogoro yanaanzia Manyara, yanapita Dodoma yanakuja huku, kote huko, tukijenga mabwawa halafu tukayatumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji tutakuwa tumepiga ndege wawili kwa jiwe moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumeokoa maafa yanayosababishwa na mafariko, lakini pia tumetengeneza uchumi, maji haya tunaweza kuyatumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Tukiwekeza hivyo tutakuwa tumewaondoa wananchi wetu kwenye lindi la umasikini na kuondoka katika kilimo cha kujikimu cha kutegemea kilimo cha mvua. Sasa hivi tutakuwa na maji ya uhakika na hawa wananchi wanaweza kukopesheka hata na taasisi za fedha kwa sababu watakuwa na uhakika wa kuvuna, kwa sababu maji yatakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nizungumze Bwawa la Kidunda. Naipongeza sana Serikali kwa juhudi na mikakati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango wangu katika hili. Niipongeze Serikali na Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo ina mwelekeo mzuri wa bajeti yetu ya 2018/2019. Kwa sababu ya muda naomba niongelee jambo moja tu na mengine nitaongelea kwenye Wizara zinazofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano hasa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu alioufanya ambapo Marais waliopita walikuwa hawajaufanya pamoja na kazi nzuri waliyoifanya kwa kutekeleza mradi wa Stiegler’s Gorge ambao unakwenda kutuhakikishia umeme wa uhakika zaidi ya megawatts 2,100 ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo siyo dogo, hili suala lilianza tangu miaka ya 60, Mwalimu Nyerere ilikuwa ni ndoto zake kulitekeleza, lakini kutokana na vikwazo mbalimbali wale wasioitakia mema Tanzania ndiyo waliokuwa wanaukwamisha mradi huu usitekelezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu una manufaa makubwa sana. Pamoja na uzalishaji huo wa umeme megawatts 2,100 lakini pia utatoa ajira kwenye uvuvi. Hili bwawa litakuwa ni sehemu ya utalii, liko bwawa karibu na mbuga yetu ya Selou lakini pia kutakuwa na heka zaidi ya 85,000 ambazo zitakuwa ni za kilimo cha umwagiliaji. Utaona ni namna gani unaona huu mradi una fursa nyingi na faida kubwa ambayo inakwenda kutekelezwa na Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia huu mradi utaboresha huduma za jamii. Nitoe mfano kwenye Jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki. Kupitia mradi huu, barabara ya Ubenazomozi – Ngerengere - Tununguo – Mvuha
- Kisaki - Stiegler’s Rufiji yote itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Unataka mafanikio gani zaidi ya haya? Niipongeze sana Serikali kwa kuliona hili, lakini hasa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuthubutu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine watu hawaelewi miongoni mwa sababu ya kuanzishwa NEMC na mambo mengine haya ilikuwa ni kuzuia miradi kama hii ya Stiegler’s na Kidunda kwa sababu walikuwa wanaona ni miradi ya kielelezo, inakwenda kuwakomboa Watanzania kwenye njia ya umeme pamoja na maji, wakatuwekea vikwazo chungu nzima tusiitekeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kutoa mfano humu ndani Mradi wa Bwawa la Kidunda andiko lake la kwanza lilikuwa tangu mwaka 1955, andiko la pili 1962, andiko la tatu 1982 baada ya Wajapan kushinda ile tenda ya kutengeneza ule mradi ndiyo pale Wajerumani wakatuletea mradi huu wa mazingira, nani asiyejua? Leo tumepata Rais anakwenda kutekeleza yale bila kusikia lolote kwa maslahi ya Watanzania halafu tunaubeza. Niwaunge mkono, tuko nyuma yenu na kwa kusema haya naamini kabisa Serikali itapaa na Watanzania tutakwenda mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kusema haya niwaambie, haina maana Serikali imeachana na miradi ya gesi. Nawapa mfano mmoja, Rais tumemwona kama miezi miwili iliyopita alienda kuzindua Mradi wa Umeme Kinyerezi II zaidi ya megawatts 168. Huu ni mradi wa gesi inatumika ile ile ya Mtwara haijasimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika ni kuchanganya hii yote, mradi wa maji na mradi wa gesi ukizingatia umeme unaozalishwa kwa maji una gharama nafuu zaidi. Megawatts moja katika kuzalisha umeme wa gesi ni zaidi ya milioni 1.2 USD wakati mradi wa kuzalisha maji megawatts moja tunatumia zaidi ya milioni 1.0 USD maana yake ni nini? Huu mradi ambao ni wa kuzalisha kwa maji una gharama nafuu kuliko wa gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Serikali haijaacha. Niwaambie suala la gesi ni la utafiti unaendelea mpaka leo, tuna neema tumeshagundua futi za ujazo zaidi ya trilioni 57…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa uhai wa wananchi wetu. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na uzima hata tumefika jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Wizara kwa kazi ya utekelezaji wa miradi ya maji katika jimbo langu na ziara ya Mheshimjiwa Waziri na Naibu wake kafika katika jimbo langu kuona changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama na miradi ya maji ya umwagiliaji. Naomba Serikali kutupatia fedha za ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji ya vijiji vya Mkuyuni, Pangawe na Kizinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Mkuyuni ni mradi chakavu na wa muda mrefu, tangu mwaka 2000 wakati huo mahitaji ni madogo na watu wachache. Naomba Serikali kutenga fedha za ujenzi wa tenki kubwa, kubadilisha mabomba kutoka nchi nne na kuweka ya nchi sita na kujenga kidaka maji kipya juu zaidi ya chanzo, ili kuwe na msukumo mkubwa zaidi kuwezesha maji kufika katika vitongoji vyote na kijiji cha Kivuma ambacho kipo juu zaidi ya Mkuyuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba upanuzi wa Mradi wa Maji wa Pangawe na Kizinga na ukarabati mkubwa, kwa sababu mahitaji ya maji yameongezeka, uelewa wa watumia maji safi na salama umeongezeka, idadi ya watu imeongezeka na ujio wa viwanda katika kata hii ya Mkambarani kama vile cha Phillip Morris na Mahashree yanaongeza idadi ya watu na mahitaji kuongezeka. Naomba mahitaji ya vifaa kama vya mradi wa Mkuyuni na Kivuma ipatiwe fedha kwa mradi huu wa Pangawe pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu la pili ni kukipatia maji kijiji cha Mfumbwe kwa sababu wana chanzo cha maji ya msereko karibu, pia vijiji vyote vilivyozunguka vina maji kasoro kijiji hicho kimoja kilicho katika kata Mkuyuni.

Pia naomba Serikali itupatie fedha katika mradi wa umwagiliaji katika shamba la kijiji cha Kibwaya katika Bonde la Mto Kibwaya, Kisemu mpaka Mfumbwe ili kuwawezesha wakulima kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka na kuongeza kipato cha wakulima na uhakika wa chakula katika kijiji hiki, Kata na Tarafa nzima ya Mkuyuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Serikali kufanya ukaguzi maalum katika mradi wa umwagiliaji wa kijiji cha Kwika sababu umechukua muda mrefu tangu mwaka 2005 mpaka sasa. Pamoja na kutuma kiasi kikubwa cha fedha, lakini bado mradi haujamalizika na kujengwa chini ya kiwango na kupoteza fedha za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na mchango wangu uzingatiwe pamoja na ule wa mdomo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie katika mjadala uliokuwa mbele yetu kuhusu hoja hii katika Wizara yetu hii ya Afya. Nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya na uzima tumeikuta jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi na shukrani, Wizara ya Afya hii imefanya mambo makubwa sana, hasa katika uimarishaji wa upatikanaji dawa pamoja na uboreshaji wa vituo vya afya nchi nzima. Nitolee mfano kwangu nimepata kituo kimoja pale kwenye Kata yetu ya Mkuyuni, pia tumepata kituo kingine katika halmashauri hiyo hiyo katika eneo la Dutumi, niwapongeze sana kwa hayo yote. Pia tumepata katika mgao unaokuja katika bajeti hii tutengewa 1.5 bilioni kwa sababu ya hospitali ya wilaya, tunaishukuru sana Serikali hasa Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri hayo kuna ombi ambalo nataka niombe. Mheshimiwa Waziri wa Afya, pamoja na mambo mazuri anayotufanyia lakini tuna ahadi za Mheshimiwa Rais tangu 2010 kuhusu upatikanaji wa magari ya wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Mkuyuni na Kituo cha Afya Kinole; ahadi hizi ni za muda mrefu, namwomba sana ikiwezekana aziingize ili atupatie turahisishe huduma ya afya katika jimbo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watumishi wa afya wako wachache; tuna zahanati ambazo tumeshazimaliza, kwa mfano Zahanati ya Bamba, tangu mwaka jana imekwisha, kuna Zahanati ya Tununguo, kuna Zahanati ya Kidugalo, zote hizi tunashindwa kuzifungua kwa sababu ya ukosefu wa watumishi wa afya. Nimwuombe sana atupatie hao watumishi ili tupeleke huduma karibu kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kidogo kwa umbali ile ripoti ya CAG; nimegundua, kuwa pamoja na kwamba wanafanya juhudi kubwa katika upatikanaji wa dawa lakini Shirika la Dawa la MSD linadai zaidi ya bilioni sitini na moja. Niwaombe sana hizi pesa kwa sababu zilikuwa zitolewe na global fund na hazijatolewa mpaka leo niwaombe sana Serikali muisaidie MSD ili fedha hizi zipatikane ili tuweze kuongeza upatikanaji wa dawa katika hospitali zetu, zahanati na vituo vya afya ili tuweze kuwahudumia wananchi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Serikali waisukume hii MSD, imekuwa ni msaada mkubwa sana na inatuletea sifa ndani ya nchi na nje ya nchi hasa baada ya kupata ule mkataba wa usambazaji dawa katika nchi za Afrika ya Mashariki pamoja na Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo katika ripoti ya CAG tumegundua pia kwamba sasa hivi kuna upungufu wa zaidi ya 1.5 trillion kwenye ripoti ile. Kwanza lazima nikiri, maana tusije kupotosha kitu ambacho CAG amekiweka ni kweli kuna mapungufu ya 1.5 trillion haionekani. Hii ni Serikali ya kwetu na tusiposema ukweli tutakuwa hatujaitendea haki, tusipende kona kona wakati jambo ni kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko chote CAG ndilo jicho la Wabunge na sisi Wabunge ni wawakilishi wa wananchi. Kwa hiyo anaposema CAG anatusemea sisi Wabunge na anawasemea wananchi wote wa Tanzania kwa sababu ndio wenye mali. Sasa leo CAG amezungumza kwamba kuna pesa ambazo hazionekani 1.5 trillion halafu sisi wenye mali tukisema tukishabikia tunakosea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa kirefu katika hili kwa sababu ndio umekuwa mjadala kwenye mitandao ya kijamii na kuna upotoshaji mkubwa kwenye hili. Hii ripoti ya CAG imekuja hapa Bungeni baada kwanza kukabidhiwa Mheshimiwa Rais pale Ikulu kwa mujibu wa Katiba na Sheria inavyotaka. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais kama angetaka isije au angetaka kufanya uchakachuaji wowote angeichakachua siku ile pale Ikulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimsikia kwa macho yetu Mheshimiwa Rais akimpongeza CAG mwenyewe Profesa kwamba wewe ni mtu mwema, ni mcha Mungu, naamini hukumwonea mtu katika ripoti hii na tutaifanyia kazi. Sasa akitokea mtu mwingine akianza kusema kwamba Rais anakumbatia haijulikani ni upotoshaji.

T A A R I F A. . .

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu na huyu ni ndugu yangu tunaheshimiana sana kwa sababu mimi naongelea taarifa ya 1.5 trilioni yeye anaongelea ATC ni vitu viwili tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo nilikuwa nazungumza kwamba Mheshimiwa Rais mwenyewe alijipambanua katika vita vya ufisadi na rushwa na kwa namna yoyote ile hawezi kufumbia macho hili na ninavyomjua Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli na ndio maana aliipokea na aliruhusu ile taarifa ije hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tulimwona Mheshimiwa Waziri Mkuu pia akipokea maelekezo kwa Mheshimiwa Rais baada ya kupokea taarifa hii kwamba wataifanyia kazi hasa pamoja na hayo mapungufu, maana yake ukisema unaifanyia kazi na huu upungufu upo lazima wamekubali kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali na niitake Serikali hili jambo si la kupuuza, ni jambo ambalo limezungumzwa na CAG katika ripoti yake ambayo sisi Wabunge na wananchi wa Tanzania ndio jicho letu. Kwa hiyo tunapoona 1.5 trillion haina maelezo ya kutosha tunapata mashaka. Nimtake Waziri wa Fedha na Serikali kwa ujumla atuletee majibu ya kuridhisha katika hili sio kuanza kupiga kona kona ili kwamba kweli tuone Serikali hii na Mawaziri wanamuunga mkono Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika vita hii ya ufisadi na rushwa iliyokuwepo nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna namna yoyote lazima tupate majibu ya uhakika, Bunge hili ni moja, katika maendeleo hakuna vyama iwe CCM, iwe CHADEMA, iwe CUF, iwe ACT hakuna mtu anayetaka ufisadi wowote. Tunamtaka Waziri wa Fedha alete hapa majibu ili tuone namna gani na huu ubabaishaji uishe, tumechoka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na ukarimu aliyetuwezesha kuwa na afya na uzima siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kuipongeza na kuishukuru Serikali kupitia Wizara hii ya Ujenzi kwa kusikiliza ombi langu na kujibu shida za barabara yetu ya Ubena Zomozi – Ngerengere – Tununguo – Mvuha - Kisaki mpaka Selous kwa kuipandisha daraja kuwa ya mkoa na kutengewa fedha katika bajeti hii shilingi bilioni tano kwa ajili ya kutengeneza barabara hii na kuiboresha ili iweze kupitika mwaka mzima na kutumika pia kupeleka vifaa vya ujenzi katika mradi Mto Rufiji. Vilevile nashukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa matengenezo mbalimbali katika barabara ya Bigwa – Kisaki, Madamu – Kinole - Msomvinzi – Mikese na madaraja na sehemu korofi katika Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na matengenezo hayo ya barabara ya Bigwa - Kisaki lakini barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa nchi na wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki, Morogoro Vijijini, Morogoro na Taifa kwa ujumla. Nasema ni muhimu kwa sababu ni barabara inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya Mvuha. Pia ni barabara inayokwenda katika Mbuga yetu ya Selous kwa lango la Kisaki. Ni barabara inayounganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani kupitia Kisaki - Stiegler’s Gorge na kufika Kibiti, Rufiji na kurahisisha mawasiliano na muingiliano wa watu wetu kati ya Morogoro na Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ipo katika Ilani ya CCM kutengenezwa kwa kiwango cha lami kwa umbali wa kilometa 78 toka Morogoro - Bigwa – Mvuha. Pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wa wakati huo ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwa barabara hii itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Naiomba sana Serikali yangu ya CCM kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuinua uchumi wa watu wa Mororgoro Vijijini na Taifa kwa ujumla na kutusaidia watu wa Morogoro Vijijini kufikisha bidhaa zetu za mazao ya kilimo kwenye masoko kwa urahisi na kuinua utalii katika pori na Mbuga yetu ya Selous.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imebeba imani ya wananchi wangu kama Mbunge, Chama cha Mapinduzi, Serikali yangu na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwa tukiahidi tutatekeleza na kuzingatia Ilani na sera zetu za kuunganishwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshamalizika muda mrefu na wananchi walishapisha na kuondoka katika maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii zaidi ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa sijaona dalili za kuanza ujenzi huo wa kiwango cha lami na tumebakiwa na miaka miwili kufika mwaka 2020 kipindi cha mwisho kutekeleza Ilani ya Chama chetu CCM ikiwamo hii barabara ya Bigwa – Kisaki kutengenezwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sijaona katika bajeti hii barabara za mkoa kwa mkoa kutengenezwa kwa kiwango cha lami kati ya Mkoa wa Mororgoro na Pwani. Pia barabara hii inakwenda kwenye mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s ambao una manufaa makubwa kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nataka kuiomba Serikali kupandisha hadhi barabara ya Ngerengere – Diguzi- Matuli – Kwaba - Mkulazi mpaka Kidunda ili iwe katika ngazi ya mkoa kwa sababu pamoja na uwepo wa TARURA, lakini ni changa na barabara hii ni ndefu ina urefu wa kilometa 75 na ina miradi mikubwa miwili ya kitaifa ya Bwawa la Kidunda na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi. Barabara hii haipo kwenye mipango ya bajeti hii wakati miradi ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi inatelekezwa mwaka huu. Naiomba Serikali kutenga fedha za matengenezo ya barabara hii ili kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa uwekezaji wa viwanda katika Kata ya Mkulazi na Matuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni suala la mawasiliano; hatuna mawasiliano ya simu katika Kata ya Mkulazi, Matuli, Tununguo, Seregete A&B pamoja na Kata za Kibuko, Tomondo, Tegetelo na Ludewa. Naomba sana mawasiliano kwenye kata hizi na mkazo zaidi katika Kata ya Matuli na Mkulazi sababu ni kata zenye miradi mikubwa ya kielelezo ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda na Kiwanda cha Sukari Mkulazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika hoja ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetusaidia afya na uzima tumefika jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, nichukue nafasi hii kumpongeza Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Hussein Ally Mwinyi kwa kazi yake nzuri na ya kizalendo anayoifanya katika Taifa hili. Pia niwapongeze wakuu wetu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi yao nzuri ya kulinda mipaka yetu pamoja na wataalam wote wa Wizara kwa utendaji wao mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kutenga fedha katika bajeti hii kwa utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami toka Ubena Zomozi mpaka Kizuka Ngerengere kwenye kiwanja chetu cha ndege na barabara tunayoitumia kufika Ngerengere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ujenzi wa barabara hii lakini nina maombi mawili. Ombi langu la kwanza ni kuiomba Serikali kujenga barabara hii toka Ubena Zomozi mpaka Ngerengere Mjini ili kipande kile cha kilomita kilichobaki pia kijengwe kwa kiwango cha lami ili kupeleka maendeleo kwa wananchi wa Tarafa nzima ya Ngerengere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la pili ni kwa kuwa tuna Kambi nyingine ya Sangasanga ambayo inatumia barabara ya Mdaula mpaka Sangasanga. Nichukue nafasi hii kuomba Serikali pia kutengeneza barabara hii toka Mdaula - Sangasanga mpaka Ngerengere Mjini kwa kiwango cha lami ili kuunganisha barabara toka Ubena Zomozi - Kizuka - Ngerengere na Ngerengere - Sangasanga - Mdaula na kurahisha mawasiliano ya kambi zetu za Jeshi toka katika uwanja wa kijeshi lakini pia kuimarisha mawasiliano na mwingiliano wa wananchi wetu kwa urahisi na kuboresha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nina ombi kwa Jeshi Kambi ya Kinonko kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya kambi na wananchi wa Kijiji cha Sinyaulime, Kitongoji cha Kipera ambapo wananchi walikuwa pale kabla ya Jeshi kuhamia pale. Naomba Jeshi liwaachie wananchi maeneo haya sababu wanatayategemea kwa makazi na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango kwenye Wizara hii muhimu inayogusa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali hasa kwa zuio la kuuza mahindi nje ya nchi. Nimesoma kitabu hiki kwenye ukurasa wa 61, nafikiri kilio cha Wabunge wengi mwaka jana, tuliolalamika kwamba Serikali isiingilie mfumo wa soko la mahindi, naona Serikali imesikia na mkatekeleze hili kama mlivyopanga. Isije sasa wakulima wanaanza linaanza tena zuio jipya la vibali watu wasiuze. Liacheni soko liwe huru, watu tukauze mahindi mahali popote panapohitajika. Naipongeza sana Serikali kwa ajili ya hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kuishauri Serikali hasa kwenye soko la mbaazi. Soko la mbaazi ni gumu sana, wengi wamezungumza, mimi bahati nzuri nilikuwa kwenye kampuni ya wanunuzi wakubwa wa mazao hayo duniani kwa miaka 19 lakini tulifanya miaka mitatu tu, miaka 16 yote hatukununua hata kilo moja na ni kampuni ya Wahindi wenyewe. Changamoto kubwa ni soko lina hatari kubwa sana kwa sababu mnunuzi mkubwa ni mmoja peke yake. Kwa hiyo, siku yoyote akibadilisha sera zake au siku yoyote uzalishaji kwake ukiwa mkubwa ni tatizo kwenye mbaazi kama tulichokiona mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, mnunuzi mkubwa ni Serikali ya India ni vizuri sana, kwa sababu biashara ni diplomasia, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara mkae pamoja ili hawa watu wa diplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje akae na Serikali ya India, tupate makubaliano ya awali ya kuwauzia mbaazi zetu kama walivyofanya Ethiopia na nchi zingine. Hata kukiwa na uzalishaji mkubwa hawawezi kubadilisha lazima watakuwa wanazingatia makubaliano, zaidi ya hapo, tutakuwa na soko la kubabaisha kwa sababu wao ndiyo wakulima wakubwa, wanunuzi wakubwa na walaji wakubwa wa mbaazi duniani. Lazima tukae na Serikali ya India, tupate ombi maalum la kuturuhusu kwamba mbaazi zetu tuuze kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu viwanda vya kubangua korosho. Naomba sana kuishaui Serikali, suala la viwanda vya kubangua korosho lilianza tangu mwaka 1978, Mwalimu Nyerere alifungua viwanda 11 na vyote havikubangua korosho na vilikuwa na uwezo wa kubangua zaidi ya tani 100,000. Kama mkikumbuka wakati ule uzalishaji wetu ulikuwa tani 174,000. Viwanda hivi havikununua hata kilo moja kwa sababu ya mabadiliko ya teknolojia, lakini ni kutokana na changamoto nyingi zilizokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 tukafufua makampuni mengi ambayo yalikuja hapa kuwekeza kwa ajili ya ubanguaji wa korosho. Olam Tanzania Limited ilikuwa na uwezo wa kubangua tani zaidi ya 30,000, wamebangua kwa miaka 10 lakini tulipoanza tu stakabadhi ghalani wakahamisha kiwanda chao kwenda Mozambique. Kiwanda cha Mohamed Enterprises kilikuwa na uwezo wa kubangua zaidi ya tani 2,000 kimefungwa, Kiwanda cha Premier Cashew au Fidahussein kilikuwa na uwezo wa kubangua zaidi ya tani 3,000 kimefungwa; Kiwanda cha Masasi Cashewnut kilikuwa na uwezo wa kubangua tani 1,000 kimefungwa; na Kiwanda cha Buko Masasi nacho kimefungwa, hii ni miaka ya 1990 mpaka 2012. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hivi tuna viwanda vitatu Export Trading Group (ETG) ana uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 5,000 lakini habangui hizo tani 5,000 kwa sababu raw material hapati, anasafirisha nje kama raw material. Sunshine Group pale Lindi kina uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 2,000 lakini raw material kwenye mnada anapata tani 200 tu; Haute ana uwezo wa kubangua tani 2,000 mwaka jana kapata tani 800. Kwa hiyo, unaona kuna shida ya upatikanaji wa raw material kwa viwanda vya ndani. Ni sababu sera zetu wakati mwingine haziruhusu au hazi-favour hawa wabanguaji wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Hivi viwanda vya ubanguaji vinahitaji hela nyingi sana. Mtu anakuja, anawekeza hela zake anajua kwamba atarudisha baada ya miaka mitano au kumi baada ya miaka miwili sera zimebadilika. Kwa mfano, hapa Tanzania haturuhusiwi kufanya importation ya korosho kutoka nchi zingine. Wakati dunia nzima ubanguaji wa korosho au soko la korosho ni la mzunguko yaani mwaka huu inakuwa miezi mitatu Tanzania, miezi mitatu India, miezi mitatu Nigeria na miezi mitatu Brazil. Kwa hiyo, mtu ananunua miezi mitatu, anabangua baada ya hapo anaenda sehemu nyingine. Kwa hiyo, jambo hilo sera inazuia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye sera zetu tuliweka export levy kwa sababu ya kuzuia korosho yetu isiende nje. Ombi, hii ya asilimia 15 inatosha sana, aidha, ibaki hapo au kuwahakikishia wabanguaji iende juu zaidi ili kuzuia hizi korosho zisiende kule. Kwa sababu akija mtu mwingine kesho akishusha hii export levy maana yake mbanguaji wa ndani huyu hawezi kupata raw material, korosho yote itaenda India, itaendelea kwenda Vietnam kwa sababu wana bei kubwa na wana gharama nafuu ya uzalishaji kuliko sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huo, naomba sasa niuombee sasa Mkoa wa Morogoro. Serikali ya Awamu ya Tatu iliamua wakati ule Waziri Mkuu akiwa Ndugu Sumaye na Rais Benjamin Mkapa kwamba Mkoa wa Morogoro ndiyo uwe Makao Makuu ya Nane Nane Tanzania na maonesho yote yafanyike pale kwa sababu ya hali ya kijiografia na uwepo wa Chuo cha Kilimo (SUA) pale Morogoro. Baada ya kuondoka, sera hiyo ikabadilishwa, sasa hivi Maonesho ya Nane Nane yanazunguka kila mkoa na kila kanda matokeo yake tunaongeza gharama kwa wadau, kujenga jengo kila mahali, hata yale majengo sehemu nyingi yamebaki magofu. Ombi langu, ni vizuri tuchague sehemu moja tuweke ndiyo Maonesho ya Nane Nane kwa nchi nzima kama tunavyofanya Sabasaba. Yako Maonesho ya Kibiashara Dar es Salaam, kila mtu anajua Dar es Salaam na Maonesho ya Nane Nane yawepo pale Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kuhusu suala la ushirika. Mheshimiwa Waziri, hizi taarifa za kusema Morogoro tuko tayari kwa ajili ya stakabadhi ghalani mnazitoa wapi? Mimi natoka Morogoro Vijijini, hata kikao cha RCC hatujawahi kukaa Wabunge wa Morogoro, kikao
cha kisheria hatujawahi! Jana unaniambia kwamba Morogoro Mkoa tumekubali stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri aachane na taarifa hizi za kwenye maandishi. Morogoro Vijijini au Morogoro kwa ujumla hatuna vyama vya msingi, hatuna maghala, hatuko tayari na msimu unaanza mwezi ujao (wiki mbili zinazokuja), katika hali kama hiyo tunaanzaje? Huna ghala, huna wataalam, huna vyama, hujavitengeneza, sasa kwa sababu maamuzi yanatoka Serikalini, tunaweza tukakubali kwa sababu Serikali ni chombo kikubwa lakini mngetusikiliza sisi wawakilishi wa wananchi tunaotoka kwa wannachi tunawashauri kwa nia njema, mfumo huu tuanze mwakani badala ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuhusu hizi data kwenye ukurasa wa 65, Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu ambayo iko kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu. Tunafahamu kazi moja ya Bunge ni kutunga sheria, pamoja na kazi nyingine, lakini nikuombe ili Bunge lako liingie kwenye historia. Wakati mwingine tusiwe tunatunga sheria tu, wakati mwingine ije sheria tuzifute zile sheria ambazo zinakinzana na maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu misingi ya sheria iko mitatu, kuna sheria ya katazo, kuna sheria wezeshi, kuna sheria ongozi. Sheria katazo zile sheria zinakataza katakata usifanye jambo hilo, lakini sheria wezeshi ni zile ambazo tunazitunga kwa ajili ya kutuwezesha kupata kitu fulani kwa faida ya watu wetu na sheria ongozi ni zile ambazo tunazitunga kwa ajili ya kutuongoza kutimiza jambo fulani, lakini kwenye kutimiza majambo hayo inawezekana tukakumbana na mambo mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nataka nichangie jambo moja tu kwa sababu sasa hivi Bunge zima pande zote tunakubaliana, kila mtu anakubali kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa mradi mkubwa huu aliouanzisha Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa Stiegler’s kwenda kuutekeleza ili kutatua changamoto za umeme zilizoko nchini kwetu. Tuko kwenye Wizara ya Utalii, tunaambiwa, tuliambiwa miaka mitatu nyuma nchi hii Tanzania kwa vivutio duniani ni ya pili, lakini leo hii sio ya pili ni ya nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi sio taarifa zangu, ni ya nane, sababu kubwa ni sababu miongoni mwa huduma zetu ni mbovu, miundombinu ni mibovu, umeme sio wa uhakika, ndege hakuna, mambo mengi ambayo yapo tumeshuka mpaka wa nane kwa kuwa na vivutio vya utalii. Kwa hiyo, niseme tu nitazungumza hapa kwa sababu, kuna upotoshaji mkubwa sana kama vile huu ukataji miti ambao unaenda kuiharibu Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe mwenyeji wa Dodoma, hata UDOM lilikuwa pori, lakini kwa maslahi ya umma tuliamua tujenge Chuo Kikuu na ndio maana mpaka leo unaona tembo kila ikifika msimu wake wanapita pale zilikuwa njia za tembo. Hata wale wazee wa zamani wanajua Dar es Salaam ilikuwa pori pia, lakini leo Dar es Salaam imejaa maghorofa, tumeharibu mazingira. Alisema ndugu yangu Mheshimiwa Getere hapa, kati ya mazingira na binadamu nini ni muhimu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi naumia sababu Wabunge wa Tanzania tunazozitoa ndio sababu zilezile wakoloni wetu walizitumia kutukwamisha kutengeneza miradi hii wakati wa Mwalimu Nyerere. Kama kuna Mtanzania anahisi kama walioendelea, nchi zilizoendelea zinafurahia siku moja nayo Tanzania waione imeendelea anajidanganya. Wanatamani sisi tuendelee kuwa hivi hivi maskini na wao waendelee kuwa matajiri. Ndio maana kwenye miradi yote mikubwa inayotaka kutuhakikishia kwenye kuongeza uzalishaji nchini kwetu na kujikwamua kwenye umaskini hawataki kuisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ingekuwa mradi ule kutekeleza condom ungesikia hela zinamiminika. Ingekuwa suala la vyandarua vya mbu hela zinamiminika, lakini mradi ule tunakwenda kuzalisha umeme zaidi ya megawati 2,100 ni umeme mwingi tutaupata ndani ya miaka mitatu ambayo tuna miaka 57 ya uhuru mpaka leo nchi hii tuna megawati 1,400 tu, leo mtu anakuja kukejeli pale, nashangaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri somo la uzalendo lianze kuanzishwa haraka sana kuanzia chekechea ili watu waijue nchi yao, waweze kuitetea nchi yao, pale tunapokandamizwa. Hivi kuna uharibifu unaofanywa kama mataifa yaliyoendelea? Iraq ilikuwa vile? Ule uharibifu uliofanyika Iraq, Libya, unafanana na uharibifu ule wa pale?

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu ambayo ni kioo cha nchi yetu katika uso wa kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na ukarimu kwa kuendelea kutupa ruhusa ya kupumua pamoja na maudhi tunayomfanyia kama binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo naanza na mchango wangu kwa kujielekeza hasa katika ukurasa wa 14; kuhusu Diplomasia ya Uchumi. Tanzania tunategemea kilimo kwa chakula, ajira, biashara na malighafi, lakini tatizo kubwa ni masoko ya uhakika na yenye bei nzuri na tija kwa wakulima wetu. Kwa mfano, zao la mbaazi kukosa soko mwaka jana 2017/2018 na bei yake kuanguka kutoka 2,000 ya mwaka 2016/2017 na kufikia 150 kwa kilo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii imeathiri uchumi wa Taifa na kipato cha wakulima wetu na kusababisha hasara kubwa. Pia imeleta madeni katika taasisi za fedha zikiwemo benki na SACCOS ambako waliwalichukua mikopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbaazi kuzingatia bei nzuri na ushindani wa soko kwa msimu wa mwaka uliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina ardhi kubwa na faida ya kijiografia katika mikoa mingi katika uzalishaji wa mbaazi ikiwemo Morogoro, hasa Morogoro Vijijini, Kilosa, Turiani na Ifakara na mikoa mingine kama Arusha, Manyara, Shinyanga, Pwani, Lindi na Mtwara ambayo ilikuwa inatoa ajira, chakula na kuongeza vipato vya watu wetu; ukizingatia kwamba zao hili la mbaazi kilimo chake hakina gharama kubwa na usumbufu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao hili si la kupuuza na kuliacha kwa sababu lina fursa nyingi za kiuchumi, lakini tatizo kubwa ni soko lake, kwamba linategemea jamii moja tu na sehemu moja ambayo ni India. Kutokana na kutegemea soko moja wakulima wetu wanaathirika zaidi kwa sababu mabadiliko yoyote ya sera ya soko hilo au uzalishaji mzuri wa mbaazi wa India kunaathiri soko la mbaazi la wakulima wetu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri katika Wizara hii katika Diplomasia ya Uchumi kutafuta soko la mbaazi kabla ya msimu kuanza katika nchi ya India na hasa mnunuzi mkuu ambaye ni Serikai ya India ili kuwa na uhakika wa soko na bei nzuri kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuishauri Serikali kuingia mkataba wa ununuzi na Serikali ya India kutoka kwetu kwa bei ya kiasi ili kutumia vizuri Diplomasia ya Uchumi na kuongeza fedha za kigeni na kipato kwa wakulima na kuepuka hasara kama mwaka jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie hoja iliyokuwa mbele yetu ya bajeti Kuu. Awali ya yote namshukuru Mwenyenzi Mungu aliyetupa afya na uzima, tumefika asubuhi hii ya leo. Nami pia naipongeza Serikali kupitia Wizara hii ya Fedha, Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango, Naibu wake, Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa utendaji wao nzuri na umakini na usimamizi mzuri katika taasisi hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nami nianze mchango wangu, kama muda utaniruhusu nitachangia mambo matatu. Jambo la kwanza, ni suala la Export Levy, kuvuja kwa mapato na lingine ni hili suala la tax stamp.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwa ajili ya Export Levy na ikiwezekana, naweza kutumia muda mwingi sana hapa kutokana na hali ninavyoiona na jambo hili tukiliachia liendelee kama hivi, linaweza kugawa Bunge letu, Serikali yetu, Taifa na upotoshaji ukikaa muda mrefu ambao siyo sahihi. Kuhusu Export Levy ina historia ndefu tofauti na hapa tunavyoanza kujadili. Sababu hizi ziko za kisheria. Kama unavyofahamu, kazi ya Bunge ni kutunga sheria; Serikali kazi yake ni kusimamia sheria na kutekeleza; na Mahakama ni kutafsiri sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hapa nina Finance Bill ya Mwaka 2010 ambayo ndiyo tunafanya reference Wabunge wengi, kwamba hizi pesa kama zinaonekana Serikali imeenda kuwapora watu wa Kusini ambao ni pesa zao, walikubali wakatwe kwenye korosho kwa ajili ya maendeleo yao, lakini Serikali hii bila huruma imeenda kuzichukua na kuzipangia matumizi bila kuwashirikisha wenyewe. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba niseme siyo kweli. Kwa mujibu wa Finance Bill ya Mwaka 2010 ambayo ninayo hapa, ilitunga Bunge hili. Naweza kunukuu, Sheria Na. 203 ilianza mwaka 1984 lakini marekebisho yake ya mwaka 2002, 2006 mpaka 2010. 17(a) inasema:

“A person who export raw cashew nut shall pay an export levy to be computed and collected by Tanzania Revenue Authority (TRA) at the rate of fifteen percent of the FOB value.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesitisha. Twende Na. 2 kwenye mgawanyo wake ndiyo kwenye matatizo hapa. Kifungu cha 2 (a) kinasema:

“Sixty five percent would be divided among district council which are cashew nut producer.” Asilimia 65 inakwenda kwenye Wilaya zinazozalisha zao la korosho, lakini bado ni hela ya Serikali. Ukisema inakwenda Wilayani, Halmashauri bado ni Serikali. Siyo hela ambayo unasema kwamba imeporwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba (b), “thirty five percent will be…

T A A R I F A . . .

. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ndugu yangu Mheshimiwa Zitto anavyoniheshimu, nami namheshimu sana, naye anafahamu hivyo, tunaheshimiana sana, nakubali sana maelezo yake, lakini sizungumzi maneno ya mtaani. Nimesema ninayo Finance Bill ya 2010 ndiyo naifanyia reference hapa. Hii hapa na nitai-table mezani ionekane nani anasema ukweli,. si ndiyo! Cap. 203 sawa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo taarifa yake siipokei kwa sababu mimi naongea mambo ya kisheria. Bahati nzuri, sasa ngoja nieleze kama anavyosema siijui, ni vizuri na Mheshimiwa anajua kabisa kwamba mimi nimeishi kwenye hii. Siongei jambo ambalo silijui siku zote. Nimekaa kwenye korosho miaka 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ilianza mwaka 1984 baada ya zao hili kudorora nchini. Tulifikia uzalishaji wa tani


zaidi ya 174,000, zilishuka mpaka tani 16,000 kwa mwaka. Ndiyo Serikali ya Awamu ya Kwanza ikaamua kuja na mkakati maalum ya kufufua zao hili mwa 1984. Mwaka 1985 ndiyo ikaanzishwa Sheria ya Kuanzisha Bodi ya Korosho (CBT) kwa ajili ya uendelezaji na kufufua zao hili. Mwaka 1990 tulianza kubinafsisha mashirika na kuwa-invite wafanyabiashara binafsi kutoka duniani kote kuja kushirikiana nao kulifufua na kuliendeleza zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 Kampuni niliyokuwa nafanyia kazi, Olam International ilikuja hapa nchini na ikaanza kununua. Wakati huo Export Levy hii haipo, tulikuwa tuna-export korosho zero rated. Lengo la kufufua hili zao, tuviwezeshe viwanda vyetu 12 alivyojenga Baba wa Taifa mwaka 1978/1979 kwa ajili ya kubangua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikopa mkopo wa World Bank, hivyo viwanda 12 vyote vinajulikana, havikubangua hata korosho. Korosho yote ikawa inaenda nje. Ndiyo likaja wazo la kusema ili tu-discourage kwa ajili ya usafirishaji ya raw nut kwenda nje kufaidisha Mataifa mengine na kuhamishia ajira kule, tuweke Export Levy. Ndiyo ikaja Finance Bill na kubadilisha sheria mwaka 1996. Ndiyo tuliweka ushuru wa kwanza Export Levy three percent. Lengo lilikuwa ni ku- discourage.

T A A R I F A . . .

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani amenipeleka nyumbani. Hili suala la kukusanya pesa zote kwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina haijaanza kwenye korosho. Tulianza EWURA, zote zinaenda Hazina, TCCRA, zote zinaenda Hazina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala waliloleta Finance Bill hapa, kuondoa kipengele namba mbili (2) kwenye matumizi ya pesa zile, nilisema mwanzoni. Kwa mujibu wa Sheria, asilimia 65 ilipaswa iende kwenye Wilaya zinazozalisha korosho zote, zile za Mtwata na Kusini.

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na ukizingatia, unitunzie muda wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1996 ndiyo ikawekwa 3% kwa ajili ya Export Levy Rate, bado korosho ikawa inaenda more than 90 percent nje. Lengo halijafikia. Ilipofika 2002, Serikali ya Awamu ya Tatu ikaongeza kutoka 3% kwenda 5%, lakini bado korosho ikawa inaenda nje. Ndiyo hapo ulipoanza mgawo. Wakasema kwa sababu lengo kwa kuzuia korosho hizi zisiende nje ni kwa sababu korosho hizi ni chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa tutungie sheria tuzigawanye, sehemu ya asilimia 65, iende kwenye Wilaya zilizochangia zao hili kufika mapato yao, asilimia 35 ziende CBT wakati huo mfuko ulikuwa haupo kwa ajili ya kuendeleza zao hili ili tunyanyue uzalishaji. Baadaye uzalishaji ukiwa mkubwa, korosho zitaenda nje na viwanda vyetu vitapata. Bado pamoja na na juhudi zote za Serikali hizo, korosho ilikuwa inaenda zaidi ya asilimia 90 nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipofika mwaka 20…

K U H U S U U T A R A T I B U . . .

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mchango mwingine mkubwa zaidi zaidi ya huu. Nimekuja kwa sababu lilianza kujadiliwa humu ndani kabla yangu. Sasa tukiacha jambo hilo likae kama lilivyo, umma kule wanaamini walichoongea ni sahihi. Ndiyo maana nimekuja na historia kwanza. Watu wanafikiria tu 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala lilianza 2002, ndiyo mgawo kwa mara ya kwanza ukaanza kuwekwa. Kabla ya hapo ilikuwa inakusanywa. Wakasema asilimia 65 iende kwenye Wilaya, asilimia 35 kwenye CBT kwa ajili ya kuendeleza. Tulipofika 2010, ikaonekana bado korosho zinaondoka nje. Ndiyo ikaja kuongezwa kutoka asilimia 10 iliyoongezwa 2006 kuja asilimia 15 ya sasa. Pamoja na hayo, kwa sababu lengo kubwa ilikuwa ni ku-discourage exportation ya raw, lakini bado korosho zinakwenda wakasema…

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo mfuko ambao ulianzishwa kwa ajili ya 2009 na 2010 baada ya sheria kutungwa kwa ajili ya kusimamia addition value na ku-procces hizo korosho hapa nchini, ukafeli na ukawa na matumizi mabovu sana ya pesa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa, Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika hoja ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na afya na kukutana siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na mchango wangu kuhusu Chuo chetu Kikuu cha Dodoma kwa kuongeza udahili wa wanafunzi kujiunga katika Chuo cha Umma baada ya kuongeza ajira ya Wahadhiri na vifaa ili waweze kujaza chuo chetu na kufikia lengo la kuwa na wanafunzi 45,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kutoa ushauri wangu kwa Serikali kutoa kipaumbele cha kwanza katika udahili wa wanafunzi na kutoa mkopo kwa wanafunzi wa vyuo vyetu vya umma. Kwa sababu hivi vyuo vilijengwa kwa fedha za umma kupitia kodi na mikopo iliyochukuliwa italipwa na umma huu wa Tanzania na kwa maana hiyo ni vizuri kujaza vyuo hivi kwanza ukizingatia tulishafanya uwekezaji mkubwa katika vyuo hivi vya umma na tunafanya mrejesho na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kutoa ushauri wangu katika usimamizi wa ubora wa elimu katika vyuo vikuu vyetu hasa ubora wa mitihani na ufundishaji kwa ujumla. Utakuta Mhadhiri anatakiwa kufundisha topic 12 kwa muda wa wiki14, lakini utakuta Mwalimu amefundisha topic mbili au tatu tu na kutoa mtihani katika topic hizo ili kuficha udhaifu wake wa kutokuwepo chuoni na kutofundisha kwa muda mrefu. Pia baadhi ya Wahadhiri hawahudhurii madarasani kwa muda mrefu na kuja ama mwisho wa muda wa muhula au mwanzo wa muhula na kufundisha vipindi na mada zilizotakiwa kufundishwa kwa wiki 14, badala yake anafundisha kwa wiki moja au mbili topic zote kwa muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tajwa hapo juu zinaathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu yetu kwa ngazi ya vyuo vikuu kwa sababu wanafunzi na Wahadhiri wanajali zaidi kupata cheti chenye alama za juu ili kupata ajira kwa urahisi sababu katika soko la ajira mahitaji ya soko yanaelekezwa katika wahitimu waliopata alama za juu badala ya dhamira, uelewa, utaalam, ufahamu na mahitaji. Ili kukabiliana na tatizo la kushuka kwa ubora wa elimu katika vyuo vyetu nina ushauri ufuatao:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuandaa chombo cha udhibiti ubora wa elimu katika ngazi ya Vyuo Vikuu ili kukagua ubora wa elimu katika upande wa Walimu, ufundishaji, mitaala na ubora wa mitihani inayotungwa kama ina tija inakidhi mahitaji katika soko la ajira nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuja na mpango mkakati wa kubadilisha mitaala ya elimu ya juu na chini ili ilingane na mahitaji ya sasa katika soko la ajira hasa kuwaandaa wahitimu kujiajiri wenyewe hasa mkazo kuwekwa katika elimu ya ufundi, ufundi stadi, kilimo, sayansi na elimu ya kiteknolojia na computer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuunda Tume ya Raisi ya Elimu kama ile ya Makwetta ili kufanya tathmini ya elimu yetu hasa katika ubora wake kuanzia ngazi ya elimu ya awali mpaka Chuo Kikuu ili kubaini upungufu,,fursa na mahitaji na kuja na mapendekezo ya kuboresha ubora wa elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na sio kama kwa umuhimu nirudi tena kusema changamoto zinazowakabili wananchi wenzangu wa Morogoro Kusini Mashariki ninaowawakilisha hapa Bungeni na kuiomba Serikali kuyapatia ufumbuzi wake. Naomba Serikali kutupatia magari mawili ya wagonjwa kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais katika Kituo cha Afya Mkuyuni kinachofanyiwa ukarabati na Kituo cha Afya Kinole chenye idadi kubwa ya watu. Kwa kutoa huduma kwenye kata tatu za Kinole, Tegetelo na Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magari hayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2010 kwa gari la Mkuyuni na mwaka 2014 kwa gari la Kinole na mbele ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na wakati huo ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kutupatia magari haya ili kuokoa vifo vya wagonjwa na hasa watoto na kwa mama. Pia naomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini ili kufungua mawasiliano ya barabara zifuatazo:-

 Mkuyuni – Ludewa – Mgozo;

 Mkuyuni – Kibuko – Tununguo

 Mkuyuni – Luholole – Kibuko;

 Mwalazi – Kibuko – Luholole;

 Seregefe B - Kuaba;

 Seregefe A – Lubumi – Mafulu;

 Mkulazi – Mvuha;

 Mbarangwe - Kisanga Standi;

 Kwoka – Mfumbwe - Kibwaya;

 Kizinga - Kimbwala – Kwika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Madini. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya na uzima wa kufikia siku ya leo na kutoa michango yetu katika Wizara hii muhimu kwa uchumi wa Taifa letu na tunafaidika na baraka hii aliyotupa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara hii kwa ujumla, kuanzia Waziri wa Madini, Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Biteko, pamoja na Katibu Mkuu na watendaji na wataalam wote wa Wizara kwa utendaji wao mzuri na weledi, hata kama Wizara hii ni mpya lakini wamefanya mambo makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani na pongezi hizo, sasa nianze kutoa mchango wangu. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa michache nchini yenye madini mengi na ya kila aina ikiwemo Wilaya ya Morogoro, hususan Morogoro Vijijini, lilipo Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Miongoni mwa madini yanayopatikana ni marble, ruby, dhahabu, graphite, manganese, garnet, emerald, corundum, ulanga, limestone, urani na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na wingi wa madini hayo katika maeneo yetu, lakini bado hayajatunufaisha ipasavyo wananchi wa maeneo hayo. Tumewahamasisha wachimbaji wadogo wadogo kujiunga pamoja ili kutambulika kisheria na kuweza kuaminika na kujipatia mtaji wa pamoja kutoka katika taasisi za fedha na mabenki na kuweza kujipatia vifaa vya kisasa na kuchimba kwa tija na faida kubwa na kujiongezea kipato chao na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo mpaka sasa vikundi hivi havijapata vibali na leseni kutoka Wizarani kwa muda mrefu na kurushwa kama mpira mara waende wilayani, mkoani, Dodoma au Wizarani Dar-es-Salaam. Namuomba Mheshimiwa Waziri wakati anafunga hoja anieleze tatizo ni nini hata inachukua muda mrefu kuvipa vibali na leseni vikundi hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni kuhusu Sheria mpya ya Madini ya kutosafirisha nje ya nchi madini ghafi mpaka yawe yameongezwa thamani ndani ya nchi. Pamoja na nia hiyo nzuri kwa Serikali yenye lengo la kuongeza ajira kwa Watanzania, pato la fedha za kigeni, pamoja na kuitangaza nchi yetu nje ya Tanzania katika soko la kimataifa, nashauri Serikali ikaliangalie suala hili kwa upana zaidi kwa sababu, kuna madini mengine kama ruby na marble yanatumika kutengeneza bidhaa za mwisho tofautitofauti. Ruby ukiikata unapunguza thamani na inapatikana sehemu mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu ya Maji. Nichukue nafasi hii kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa afya na uzima tumekutana jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, hakuna ziada mbaya na mimi niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara Profesa Kitila pamoja na watumishi wote wa Serikali katika Wizara hii kwa juhudi kubwa ambazo wanazifanya kwa kuwaletea maji wananchi wa Tanzania. Wote ni mashahidi tumeona kwamba wanachapa kazi na wanatembelea sehemu mbalimbali kujua changamoto za Watanzania lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa fedha kutoka Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niishukuru Serikali kwa miradi mbalimbali inayoendelea katika jimbo langu katika vijiji vichache. Pia nimeona humu nia ya Serikali kulijenga Bwawa la Kidunda, niipongeze sana na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutimiza ndoto za Mwalimu Nyerere za miaka ya 1960 ambazo anazitekeleza sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali, Kidunda siyo mara ya kwanza kuiona kwenye vitabu, nimeiona mwaka juzi wakati nikiwa mwaka wa kwanza hapa Bungeni, nimeona mwaka jana nikiwa mwaka wa pili hapa Bungeni na mwaka huu pia nimeiona, lakini utekelezaji wake haufanani na kinachoandikwa. Niwaombe sana mwaka twende tukatekeleze mradi huo, ni mradi wa miaka mingi na una manufaa makubwa sana katika nchi yetu hasa kwa upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam, Pwani na Morogoro hasa kwa hivi viwanda vyetu kuwa na uhakika wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni mipango ya muda mrefu ya Mwalimu Nyerere, nikikumbuka pale Morogoro alivyotujengea viwanda zaidi ya 11 kutoka msaada wa World Bank alijenga na Bwawa lile la Mindu kwa ajili ya ku-supply maji. Kwa hiyo, tunafuata nyendo zake hata huko aliko anafurahia namna gani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anatimiza ndoto zake alizoziacha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi na shukrani hizo, nianze kuomba maombi ya kwenye jimbo langu. Kama nilivyosema kuna miradi michache inatekelezwa lakini kuna mambo mbalimbali niwaombe. Kuna Mradi wa Chalinze III, ni mradi wa kabla mimi sijakuwa Mbunge tangu 2009, tulipata vijiji saba, miundombinu yote ilijengwa tangu 2009 lakini mpaka leo hiyo miundombinu imeshakuwa chakavu na imeanza kubomoka hatujaweza kupata maji. Mheshimiwa Waziri unapokuja kufunga hoja yako tunataka majibu ya Chalinze III maji yatatoka lini? Mwaka jana ulisema kuna mambo mnayafanya mchakato unafikika mwisho lakini tumebakiza miezi miwili kumaliza hii bajeti bado hatuna matumaini Chalinze III itaanza kutoa maji lini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika Chalinze III hiyohiyo kuna vijiji vitatu ambavyo vilisahaulika kujengewa miundombinu yake ambavyo ni Gwata, Masewe na Lubongo. Tunaomba sana hizo hela tukamalizie hiyo miundombinu ili ikianza kutoa maji Chalinze III na sisi pale tupate maji.

Mheshimiwa Spika, pia katika Tarafa ya Ngerengere karibu kata zote hatuna maji safi na salama. Niombe wataalam wa Wizara na Halmashauri waje wafanye utafiti wa kupata maji ardhini ili tuweze kupatiwa visima katika zile kata ambazo haziwezi kufikiwa na vyanzo vya maji vya mserereko ambavyo tunavyo kule Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi kuungana na wenzangu wengi waliopendekeza kwamba tuongeze shilingi 50 katika tozo ya mafuta kwa ajili ya kuongezea Mfuko wa Maji ili tuweze kusambaza vizuri maji huko vijijini. La pili niungane na wenzangu pia waliopendekeza kwamba Wakala wa Maji Vijijini ianzishwe.

T A A R I F A . . .

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, namheshimu sana ndugu yangu, lakini nikuombe wewe muda wangu uutunze ili na mimi niweze kutoa mawazo yangu kwenye Wizara hii. Suala la export levy tutakuja kulijibu Wizara ya Kilimo ikija hapa, lakini sasa tunazungumzia masuala ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema nikubaliane na wenzangu ambao wanataka tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini, lakini naomba nitofautiane kidogo au nitoe mawazo yangu kidogo. Tukianzisha wakala huu sasa hivi kabla hatujajua miradi ya maji imekwama wapi tutarithisha matatizo kutoka katika Mamlaka za Maji zilizoko sasa hivi na kupeleka kwenye huo wakala mpya.

Mheshimiwa Spika, pendekezo langu, kabla ya kuanzisha wakala huo, ni vizuri ama Serikali au wewe au CAG afanye ukaguzi maalum katika miradi yote ya maji nchi nzima ili tubaini tatizo la miradi hii kutekelezwa chini ya kiwango au miradi hewa ni nini? Baada ya hapo wakija na majibu na mapendekezo ndiyo Serikali ichukue na sisi Wabunge tutakuwa na uelewa mpana wa kuishauri Serikali kutoka hapa kwenye mkwamo twende wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Miradi mingi ambayo ilikuwa inaanzishwa na kandarasi nyingi watu walikuwa wanapeana kiujanjaujanja. Wakandarasi waliokuwa wanapewa hawana sifa wala vigezo, kwa sababu ni mtoto wa mjomba au mtu kwa sababu ana fursa hiyo iko pale anaanzisha kampuni yake, anamwambia ndugu yake weka hapa tender anashinda, uwezo hana, vifaa hana na ndiyo maana mpaka sasa hivi tuna miradi hewa na miradi mingine huko maji hayatoki.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kabla hatujaunda huu Wakala wa Maji ni vizuri kabisa kwanza tukabaini matatizo ni nini, nani alihusika na majina yao bila kujali vyeo vyao, yawe wazi ili tuisaidie Serikali tuondoke kwenye mkwamo huu wa maji tuliokwama.

T A A R I F A . . .

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Hiyo taarifa kwa sababu haina ushahidi wala uhakika nikiichukua atanirushia kesi ambayo haihusiki hapa, twende kwenye kuchangia maji tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kuhusu washauri elekezi wa miradi ya maji, hiki ni kichaka kingine cha kutafuna fedha. Utakuta mradi wa maji wa kisima kimoja mshauri elekezi anatoka Arusha, Dar es Salaam ndiyo anakuja kusimamia kwenye halmashauri. Ushauri wangu kwa Serikali kwa sababu wana wataalam wao ndani ya Halmashauri na mkoa hata kwenye Mamlaka ya Maji, kwenye miradi hii midogo midogo ni vizuri washauri elekezi wakatumiwa hao watumishi wa Serikali ili kuokoa fedha nyingi na hawa washauri elekezi wakatumika kwenye miradi mikubwa tu kama Kidunda, Chalinze III na mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, tunalumbana hapa tatizo ni sababu ya pesa kidogo na niipongeze sana Serikali kwa kuja na mikakati ya kujiongezea pesa. Tunafahamu biashara ni uwekezaji na katika uwekezaji huo inayotuingizia mapato mengi kuliko yote ni kilimo asilimia zaidi ya 25 lakini ya pili ni utalii, watalii wanaongezeka namna gani? Lazima tupate watalii wengi na ndiyo maana Serikali imekuja na jibu la kuongeza mapato kwa kununua ndege ili watalii hawa wawe wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tulikuwa kwenye semina na wanasema watalii wengi tunaopata ni wazee, huwezi kumsafirisha mtalii mzee kwa gari kutoka Arusha kama unakuja Selous, haiwezekani, lazima atumie ndege. Niishauri Serikali siyo hizi kubwa tu wanunue hata ndege ndogo, tunaona hata wakati wa uchaguzi kuna vyama CCM na vingine tunakodisha ndege kutoka Kenya maana yake tunahamisha uchumi kuwatajirisha Kenya, ni bora zinunuliwe ndege nyingi ndogo hapa nchini tunakodisha na uchumi huo utaendelea kubaki ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wale wanaobeza suala la ununuzi wa ndege jambo hili ni la kwenda kuimarisha mapato ya Serikali kwa sababu miongoni mwa kinachochangia mapato makubwa Serikalini ni utalii kwa zaidi ya asilimia 17.6. Kwa hiyo, kwa kununua ndege hizo tuna uhakika watalii wetu wataongezeka. Tuipongeze Serikali kwa ununuzi huu wa ndege na kwa ubunifu huu wa kuongeza mapato badala ya kuwabeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi kwa kunipa nafasi nichangie hoja hii iliyokuwa mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza na mimi niwapongeze sana Wizara ya Ardhi, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. Pamoja na changamoto kubwa ya migogoro mingi iliyokuwepo kabla lakini kwa kasi wanayoenda nayo tunaimani siku moja itakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme mimi ni mmoja wa Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, lakini ushirikiano tulioupata kutoka kwenye Wizara hii katika majukumu yetu ni mkubwa sana. Tulikuwa na ziara na Kamati ya Ardhi kukagua mipaka ya nchi, lakini huwezi kuamini tulipewa ushirikiano na Naibu Waziri, Katibu Mkuu siku zote tulivyokuwa kwenye safari wote tulikuwa nao mguu kwa mguu mpaka tumerudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulipokwenda Dar es Salaam siku tatu siku zote Waziri mwenyewe Lukuvi tukawa naye siku tatu, ni tofauti kabisa na wakati mwingine kwa watu wengine ambao wanasema wako busy. Tunashukuru sana waendelee na moyo huo ili kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nina machache leo na zaidi ni ushauri. La kwanza, dhuluma ya wamiliki ardhi hasa wanyonge hususani Manispaa ya Morogoro. Mheshimiwa Waziri ni mchapakazi na aliwahi kufika Morogoro kwa ajili ya kutatua migogoro hii ya ardhi. Hata hivyo, nataka nitoe mfano mmoja kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tatizo la njaa mwaka 1974, Mwalimu Nyerere alitaka tuwe na kilimo cha kufa na kupona na akasema kila Mkuu wa Mkoa asimamie suala la uzalishaji wa chakula, anayezembea basi kazi hana. Basi ilitokea siku moja akaenda Mkoa mmoja akakuta kwa sababu mtu anataka asipoteze kazi wakatafuta wafungwa Magerezani, wakatafuta shamba likalimwa, wakachukua mahindi ya wakulima wakayapanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyapanda ili kuonesha kwamba chakula hali safi akapelekwa pale Mwalimu. Sasa kwa sababu Mwalimu uzuri alikuwa anatafuta taarifa mbalimbali, kufika pale akanyofoa tu mhindi mmoja akaona ni feki na yule Mkuu wa Mkoa akapunguzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi, Mheshimiwa Waziri aliwahi kuja Morogoro Manispaa kutatua tatizo la ardhi na kusikiliza changamoto za dhulma ya ardhi Mkoa wa Morogoro hususani Manispaa; lakini alichofanyiwa hakijui na sasa leo nataka nimwambie. Watu wa Morogoro hasa wamiliki wa ardhi wanyonge walichonganishwa na Serikali yao, lakini sasa wamepata ukweli wanamwomba sana arudi tena akawasikilize ili atatute changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ile Mheshimiwa Waziri alipokuja Morogoro watu wenye migogoro ya ardhi wakakusanywa Ukumbi mwingine, halafu akapelekwa kwenda kuongea na watumishi. Watu walikasirika sana na hili jambo halipendezi, wanaleta chuki kugombanisha Serikali ya Awamu ya Tano na wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Morogoro Manispaa kuna dhuluma kubwa sana ya ardhi, kazi yote wanayofanya Mawaziri inaharibiwa na watendaji wao kule chini. Kule chini wakigawa ardhi wanajigawia wao halafu wanauza kwa watu wengine. Pia hata ile ardhi wanayogawiwa wanyonge, wale Maafisa Ardhi wanaowaleta na Wataalam wa Ardhi hawako kwa ajili ya kusaidia matatizo ya watu, badala yake ni kila siku kupora ardhi ya wanyonge na kuwauzia wenye pesa na wakija viongozi wakitaka kusema matatizo yao wanaminywa, wanakanyagwa kwenye Mikutano na Mabango yote yanachanwachanwa ili wasijue matatizo yanayowakabili Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aje, kuna mchezo mchafu mpaka wanachoma mafaili ya wamiliki halali wa ardhi wanatengeneza hati mpya na mafaili mapya. Mheshimiwa Waziri anione nimpe ushahidi mimi mwenyewe mwathirika, marehemu baba yangu mwathirika, dada yangu mwathirika, majirani zangu waathirika, watu wa Morogoro waathirika. Nitampa hivyo viwanja vyote ambavyo na watu wengine wenye matatizo kama ya kwangu na jamii ya Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu fidia ndogo wanayolipwa watu kupisha miradi ya maendeleo hususani vijijini. Kwanza tunashukuru sana Serikali inavyotuletea miradi mingi kwa ajili ya maendeleo hususani huu mradi wa reli inayoenda kasi. Wananchi wetu hasa Mikese Station, Ngerengere na Kidugalo ni miongoni mwa waliotoa ardhi yao kwa ajili ya kupisha miradi hiyo. Hata hivyo, fidia waliyolipwa ni flat rate 500,000 kwa heka, kitu ambacho ni tofauti na bei ya soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajiuliza; Serikali hii hii taasisi zake kama NSSF au ukikuta National Housing wakitaka kujenga nyumba kwenda kununua ardhi wananunua kwa bei ya soko na hiyo bei ambayo haipo popote pale. Natoa mfano tu, mradi kule wa Dege Beach ilinunua heka moja zaidi ya milioni 800, kwa kusema land for equity hata National Housing hivyo hivyo, matokeo yake zile nyumba zinakuwa na gharama kubwa na wanakuja kuumizwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wanajiuliza mbona Serikali hii ikitaka kujenga mjini au sehemu yoyote wananunua bei ya soko, lakini wakija kuchukua ardhi yetu huku vijijini wanasema tunalipa bei ya Serikali. Huku wanatuumiza wanalipa mapato madogo kitu ambacho leo hii aliyelipwa 500,000 pale kupisha miradi hii hawezi kupata ardhi kama ile ile pale hata nusu ya pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo bei ya ardhi pale Mikese ni zaidi ya shilingi milioni nane kwa heka. Natoa mfano, Kampuni ya Mahashree ambayo imewekeza pale Kiwanda cha Mbaazi ilinunua mwaka jana heka moja milioni nane, lakini yenyewe imekuja kulipwa 500,000 kwa heka na Serikali ardhi ile ile, ndani ya mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa tuwe kama msumeno. Kama bei inayotumika ni 500,000 kote hata huku kwenye taasisi za umma kama NSSF na National Housing inapotaka kujenga miradi ya maendeleo bei iwe hiyo hiyo ili nyumba hizi ziwe bei nafuu wananchi hawa wapate uwezo wa kuzimiliki hizo nyumba tofauti na sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bei kubwa ya kodi za ardhi, hili ni janga lingine, kwa sababu Mheshimiwa Waziri yeye mwenyewe ni shahidi, tumekwenda wote Kilungule amepima ardhi bure, lakini watu kwenda kulipia mpaka leo wameshindwa. Hili kama halitaangaliwa vizuri, basi tunakwenda katika njia nyingine ya kumilikisha ardhi kutoka kwa wanyonge kwenda kwa matajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipotahadhari ardhi hii itamilikiwa na wachache Tanzania kwa kisingizio cha Watanzania wengine kushindwa kulipa ardhi kwa sababu kama wanavyosema mtu akishindwa kulipa kodi watampeleka Mahakamani, watamnyang’anya ardhi na kweli watawanyang’anya wengi, lakini ndilo lengo la Serikali? Maana yake ni nini, ni kwamba ardhi hii tunaipokonya sasa kwa wanyonge walio wengi tunapeleka kwa matajiri wachache wenye uwezo wa kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri na bora Mheshimiwa Waziri akaweka bei inayoweza kulipwa na wengi ili watu wote walipe kuliko wakiweka bei kubwa watalipa wachache wengine hawataweza kumilikishwa ardhi, kitu ambacho itakuwa ni hatari sana huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Umiliki wa Ardhi Vijijini. Nnafahamu kwenye nyaraka zinaonekena ardhi kubwa inamilikiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ili kutoa mchango kwenye hoja iliyokuwepo mbele yetu. Kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru Wabunge wote waliopata nafasi ambao wametoa mchango wao na sisi kwa niaba ya Wizara ya Kilimo kuna hoja chache zimetugusa, mawazo yote waliyoyatoa tunayachukua na tunaendelea kuyafanyia kazi ili kuboresha biashara hii, sekta ya kilimo iende vizuri. Kuna hoja ziko kama tatu au nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ni hoja ya kurasimisha mfumo wa kangomba kwenye korosho. Kuna wengine Waheshimiwa Wabunge wamefananisha kilimo cha mkataba na biashara ya kangomba. Biashara ya kangomba imekataliwa kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Stakabadhi Ghalani, Sheria Na. 10 ya mwaka 2005; Sheria Tasnia ya Korosho Na.18 ya Mwaka 2009 na kanuni zake za Mwaka 2010, mwongozo Na. 13 wa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani wa mwaka 2018, lakini pia na Sheria ya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013, zote hizo zimevipa mamlaka Vyama vya Msingi vya Ushirika na vyama vya Vikuu ndio wenye jukumu la kukusanya korosho kutoka kwa wakulima na kuzifikisha kwenye maghala ya masoko yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sheria hizo nilizozitaja, hayupo yeyote mwingine anayeruhusiwa kununua au kukusanya korosho kutoka kwa wakulima isipokuwa wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya msingi na ushirika, hivi ni kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge au Wabunge wanaona sasa sheria hizi zimepitwa na wakati hazina manufaa labda kwa Taifa au kwa wakulima, basi kwa mujibu wa kanuni zetu, Kanuni ya 81 ya Toleo la Januari, 2016, inaruhusu Mbunge kuleta hapa hoja binafsi, ailete hapa, basi itachakatwa, ikionekana inafaa itapitishwa, lakini sisi kama Serikali kazi yetu kubwa ni kusimamia utekelezaji wa sheria kwa sababu sheria hii ilipitishwa na Bunge lako Tukufu hapa, tutaendelea kuisimamia ili sheria hii iendelee kutekelezwa. Mpaka sasa mfumo unaotambulika kisheria na kikanuni na kimwongozo ni mfumo wa stakabadhi ghalani na korosho zote zitaendelea kukusanywa na vyama vyetu vya ushirika na si vinginevyo.

Mheshimiwa Mwenyekti, pia kuna hoja nyingine imetolewa kuhusu kuna kesi ngapi ambazo zipo mahakamani au polisi. Labda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kesi zipo za kutosha na ushahidi upo na zipo ngazi mbalimbali, kuna kesi zipo ngazi ya polisi zingine ziko mahakamani. Kwa mfano, wiki moja iliyopita nimetoka Newala na nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Newala, walikuwa na kesi zaidi ya 47 na mojawapo ni korosho, mtu walipomkamata na tani 10 anasema korosho zile zimetoka Malinyi Morogoro, unaona namna gani kwamba udanganyifu upo na maana yake ametoka Morogoro amepita Pwani, amepita Lindi mpaka Mtwara na kufika Newala na Newala kwenyewe sio mjini kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizo kesi zipo na kama Mheshimiwa Mbunge bado ana nia ya kutaka takwimu sahihi kwa sababu ni suala la kitakwimu, tutampatia baada ya Bunge hili atuone afike pale Wizara tutampatia takwimu kesi ngapi na ziko mahali gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hoja imetolewa hapa kusema turuhusu uagizaji wa korosho kutoka Mozambique. Hilo haliwezekani kwa mujibu wa sheria kwa sababu korosho za Mozambique grade yao iko chini…

MWENYEKITI: Malizia.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):… zikija hapa zitatuharibia ubora wa korosho zetu na soko bei yake itapungua, hatuwezi kufanya hilo lazima tuwalinde wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye muswada uliokuwa mbele yetu.
Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai na uzima wa siku ya leo. Pia na mimi naungana na Wajumbe wenzangu wengi ambao michango mizuri iliyotolewa, kwanza nianze kwa kuunga mkono hii hoja kwa asilimia mia moja kwa sababu ni muswada ambao ni mzuri na umekuja wakati muafaka ambao utatua changamoto kubwa zilizokuwepo kwa Wathamini ambao walikuwa baadhi yao wengine ni wadanganyifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nasema ni muswada mzuri kwa sababu mpaka taasisi kwa mfano kama za kifedha zilikuwa zinakosa hata uaminifu kwa baadhi ya wathamini wengine na ndiyo maana walikuwa wanachagua hata Wathamini maalum wa kufanya kazi zao. Sasa hii ilikuwa inakosesha fursa kubwa sana kwa wananchi wetu kupata kile walichokuwa wanatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, wenzangu wameshachangia mengi lakini naomba tu kwenye kile kifungu cha 52(2) na tumeona hapa kwenye amendment ametuletea Mheshimiwa Waziri leo; kama tunavyojua tarehe ya uthamini ni siku ile ya uthamini na ardhi mara nyingi huwa inapanda bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu valuer, ule muda ambao valuation inakua kwa miaka miwili tunakubaliana ni sawa, lakini sasa inaanza kutumika mpaka pale valuer anapotia saini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba katika kipengele hiki tu hata huyu Valuer Mkuu baada ya kuthibitishwa ile, uwekwe muda maalum kuliko kuacha hivi hivi tu. Ni vizuri kupendekeza iwekwe kama miezi sita hivi, kwa sababu tukiacha hivi hivi kuna athari, wakati mwingine valuation inaweza ikafanyikakwa nia njema kabisa ikafika kwake na wakati huo labda hana uwezo au hana fedha ya kulipa akauchelewesha kwa makusudi hata miaka mitatu, minne, mitano, matokeo yake itamwathiri yule mwananchi au yule ambaye ni mnufaika wa valuation ile, kwa sababu anakuja kulipwa wakati ile value ya land au the property imeshapita muda wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri hata huyu valuer akawekewa muda maalum aseme kwamba, yaani ikifika mezani kwake ile document basi izungumze kabisa ndani ya miezi sita anatakiwa asaini, ili tusije kuondoa maana nzima ya ile evaluation report ambayo ilikuwepo mbele yetu. Nisema tu, ilikuwa mchango wangu leo ni huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu ya Wizara ya Ujenzi inayosimamia miundombinu ya barabara na mawasiliano nchini.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima na kupata nafasi ya kuwa mmojawapo wa Waheshimiwa Wabunge kutoa mchango wa kuboresha kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya hii ya CCM ya Awamu ya Tatu kupitia Wizara hii ya Ujenzi. Nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya usafiri nchini. Naipongeza Serikali kwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ya reli ya kati toka Dar es Salam mpaka Kigoma.

Mheshimiwa Spika, nashukuru Serikali kwa sababu reli hii ujenzi wa Awamu ya Kwanza toka Dar es Salam mpaka Morogoro unakamilika mwaka huu Desemba, 2019 na kwa kiasi kikubwa barabara hii inapita katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Jimbo ambalo naliongoza mimi. Reli itakuwa na msaada mkubwa wa kuinua hali ya vipato na uchumi wa wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro kwa ujumla kwa kuwa itapunguza gharama ya usafiri wa mazao ya wakulima wa Ngerengere, Mikese, Kinole, Tegetero, Tununguo, Mkuyuni, Kiroka, Tomondo, Mkulazi na Vijiji vya Kata zote za Morogoro kwa ujumla na kupunguza gharama za usafiri na kuongeza vipato vya wananchi wa Morogoro.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli kwa kuweka katika bajeti barabara ya Bingwa - Kisaki kuanza kwa ujenzi na kuanza kilometa 50 kwa kiwango cha lami. Naipongeza Serikali kwa sababu ni sikivu, baada ya kusikiliza maombi yangu ya ujenzi wa barabara kuanza ujenzi kila Bunge la bajeti tangu kuingia katika Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi na shukrani hizo kwa Serikali kuiweka katika bajeti barabara ya Bingwa - Kisaki lakini kiasi kilichotengwa ni kidogo sana cha shilingi milioni mia moja arobaini na tano (145,000, 000) kwa kujenga barabara ya kilometa hamsini ni kiasi kidogo sana ambacho hakiwezi kutosha kulipa hata fidia tu kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hii ya Bingwa Kisaki. Ushauri wangu kwa Serikali kuongeza kiwango cha fedha katika bajeti ya ujenzi wa barabara hii ya Bingwa - Kisaki ili ujenzi wake uanze mwaka ujao wa fedha unaanza mwezi Julai baada ya bajeti hii kupita.

Mheshimiwa Spika, kiasi hiki ni kidogo ambacho pia hakiwezi kutosha kulipa mkandarasi malipo ya awali ya asilimia 15 kwa mujibu wa sheria. Naomba Serikali iongeze fedha ili ujenzi uanze.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili naomba Serikali kutupatia minara ya mawasiliano katika Kata ya Tegetero, Rudewa, Seregete, Mkulazi, Tununguo, Kidugalo na Matuli na Vijiji vyote vya Kata hiyo pamoja na Vijiji vya Luholole, Mwarazi na Kibuko Kata ya Kibuko. Pia mnara katika Vijiji vya Newland Lubungo, Mhunga Mkola katika Kata ya Mikese. Pia naomba ujenzi wa madaraja katika Mto Ruvu kuunganisha Tarafa ya Mvuha na Tununguo kupitia Mbarangwe, Tununguo mpaka Kisanga Stendi. Pia naomba daraja la kuunganisha kati ya Kata ya Matuli na Kidugalo kwenye Mto Ngerengere.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, ndugu yangu, Mheshimiwa Kakunda; Naibu Waziri; Katibu Mkuu; Naibu Makatibu Wakuu, kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, ndani ya muda mfupi wa miaka mitatu matokeo tumeyaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kumsifia tu bila kutaja hata viwanda vichache ambavyo vinaonekana kwa kila mmoja. Niseme kwenye mambo ambayo ni ya msingi, tukianza kwenye viwanda vya matunda, Wizara hii imefanikisha kufungua viwanda vikubwa viwili, kuna Alvin kule Bagamoyo lakini kingine kiko pale Chalinze Mboga. Ni viwanda vikubwa saizi moja na Bakhresa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye viwanda vya mpunga, kuna viwanda vingi vinajengwa lakini kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki na kati kinajengwa pale Morogoro Mjini, Kihonda. Wengi mkipita pale Njiapanda ya Viwandani mkono wa kulia mtakiuona, ambacho kitakuwa kiwanda kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki na Kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kahawa viwanda vitatu; kipo cha AMIMZA kule Bukoba Mjini, KADERES pale Karagwe na OLAM pale Misenyi. Vyote hivi ni matunda ambayo yamekuja ndani ya muda mfupi katika kipindi cha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende kwenye chai pale Unilever. Juzi tu Mheshimiwa Rais alienda kukizindia kiwanda kikubwa ambacho kinatoa ajira na uhakika wa masoko ya mazao yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mpaka sasa tuna maombi chungu nzima ya walioonesha nia ya kuja kuwekeza kwenye viwanda vya korosho. Tuna matarajio makubwa mwaka huu tutaanza kubangua korosho kwa kiasi kikubwa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawapongeza kwa kazi hiyo. Nimetaja vichache, viko vingi, naamini nikianza kuvitaja muda wangu utakwisha hata mchango wangu nisitoe sehemu zingine, kwa hiyo, nawapongeza sana kwa hayo makubwa mnayoyafanya kuibea Serikali hii na kuwatumika wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingi hapa zimetolewa za Wabunge, hatuwezi kuzijibu zote kutokana na muda lakini naamini kabisa Wizara au Serikali italeta kwa maandishi majibu ya Wabunge wote mliochangia na michango yenu tunaithamini sana, mtapata majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya kulinda viwanda vyetu vya ndani, hoja ni ya msingi kwa sababu viwanda hivi tunagombeana na wenzetu, vinakuja, lazima tuweke mazingira mazuri ya kuvilinda. Waheshimiwa Wabunge, tumewasikia, tunavifahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano tu kwamba kuna viwanda hivyo kama vya alizeti, sio vyote vinafungwa kwa sababu ya mipango mibovu ya Serikali, hapana. Nitolee mfano viwanda viwili vya alizeti vilivyofungwa pale Singida, vimefungwa kwa sababu ya upungufu wa malighafi nchini. Kwa hiyo, tusichukulie hiyo kama ni changamoto, tuichukue kama ni fursa ya kwenda kuongeza uzalishaji wa alizeti ili viwanda vyetu vipate raw material ya kutosha. Ndiyo maana hata viwanda vingine vya alizeti vinachakata mbegu za alizeti kwa muda mfupi sana, miezi mitatu baada ya hapo mbegu nchini hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kila kiwanda kinachofungwa ni kwa sababu kuna mazingira mabaya, hapana, vingine vinafungwa kutokana na kwamba kama Watanzania hatujatumia vizuri fursa ya kuongeza uzalishaji kwa ajili ya ku-feed hivyo viwanda vyote kwa raw material. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tuchukue hii kama ni fursa tukawaambie wapigakura wetu tuongeze uzalishaji kwa sababu soko la uhakika lipo kwa viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujasiriamali umezungumzwa sana hapa katika suala la kangomba, mimi sipendi sana kuita kangomba, mimi nataka niwaite wajasiriamali. Mtoto wako usimfatafutie majina mabaya, hawa wajasiriamali ni Watanzania, ni watoto wetu na ndugu zetu na Serikali tumewasikia. Kinachogomba ni sheria ambayo Bunge hili ndiyo tulipitisha, kwa mfano, Sheria ile ya Korosho Na. 12 na Na. 15, ukikutwa na korosho kama huna kibali cha Bodi ya Korosho unatakiwa ukamatwe, yaani hata haya tunayoyafanya ni huruma na ubinadamu kwa Watanzania. Tukifuata sheria inavyosema basi hata wale wakulima wote ilipaswa tuwaweke ndani. Sasa hivi tuko kwenye mchakato kama Serikali kuipitia Sera ya Kilimo ya mwaka 2013 ili tuangalie mapungufu yote hayo na tuje na sera na sheria ambayo inakidhi mahitaji ya sasa na hali ya sasa ya masoko yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati mwingine haya tunayoyafanya ni kwa mujibu wa sheria ambazo zimetungwa na Bunge hili. Niwaombe ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tukileta sheria hiyo kuondoa hao mnaoita kangomba (wajasiriamali) wafahamike basi muweze kuipitisha ili sisi kwa wajibu wetu wa Serikali kwenye kusimamia sheria uwe sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo pia wanasema kwamba labda hatujalipa, tumewatesa wakulima, hapana. Ni kweli tunakiri kuna wakulima mpaka sasa bado hawajalipwa, tunadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 102 kati ya shilingi bilioni 724. Mpaka sasa tumeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 622. Sasa hivi Serikali tunaweka mazingira mazuri ili kuwezesha Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo kupata hizi shilingi bilioni 102 haraka iwezekanavyo ili kwenda kuwamalizia wakulima wachache hawa waliobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye soko la mbaazi, kwanza ni kweli miaka mitatu iliyopita soko la mbaazi lilikuwa siyo zuri. Sababu kubwa ni kwamba hatukuwa tumeingia mkataba maalum na walaji na soko kubwa la mbaazi katika nchi ya India. Baada ya kuona mapungufu hayo, Serikali tuko kwenye mchakato wa kuingia makubaliano maalum na watumiaji au wanunuzi wakubwa wa mbaazi duniani; India na nchi nyingine, ili tuwe na uhakika wa mbaazi zetu tukizalisha tunakwenda kuuza wapi, kwa bei gani na kwa nani ili haya mabalaa yote yaliyotukuta yasitokee.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha mwisho, bado tumeimarisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Omary Mgumba, muda wako umekwisha, ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami nitoe mchango wangu katika hoja hii muhimu ya Bajeti Kuu ya Serikali na Hali ya Uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na uzima ili kuwa miongoni mwa viumbe vyake kwa ajili ya kumuabudu na kupata nafasi ya kushiriki kutoa mchango wangu kweye hotuba hii ya muhimu kwa mustakabali na maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, dada yangu, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Ndg. Dotto James na watumishi wote wa Wizara ya Fedha kwa kuchapakazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo mkubwa na kufanikisha miradi mingi ya maendeleo mikubwa na midogo kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii inatekelezwa kwa sababu ya upatikanaji wa fedha kutoka Serikalini Kuu na Serikali ya Halmashauri nchini chini ya usimamizi mzuri wa Wizara hii ya Fedha kwa kusimamia makusanyo ya mapato ya Serikali vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kumpatia fedha katika Jimbo la Morogoro kwa kituo cha afya Mkuyuni, Mikese na Gwata, kila kimoja shilingi milioni 400; na pia uboreshaji wa barabara ya Bigwa – Kisaki, Mikese – Msombizi na Ubena Zomozi – Ngerengere – Tununguo – Mvuha – Kisaki Stiegler’s na Madamu – Kinole kwa kiwango cha changarawe na kuweza kupitika mwaka mzima kwa majira yote ya mvua na jua.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uboreshaji wa barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kiwango cha changarawe lakini bado ule umuhimu wa Serikali kuitengeneza barabara kwa kiwango cha lami uko palepale kwa sababu umuhimu wa barabara hii kwa shughuli za kiuchumi za wananchi wa Morogoro Vijijini umeongezeka, hasa shughuli za kilimo, uwekezaji wa kiwanda cha sukari cha Morogoro Sugar pamoja kuwepo kwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara hii ya Bigwa – Kisaki ndiyo inayotumika kufika kwenye mradi mkubwa wa kielelezo wa kufufua umeme wa Mto Rufiji (Stiegler’s). Kuwepo kwa mradi huu na Mbuga ya Selous kutaongeza wageni wa utalii na kuongeza mapato ya Serikali na uchumi wa taifa. Kwa umuhimu huo, barabara hii ina umuhimu na ulazima wa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kuweka barabara hii ya Bigwa – Kisaki katika bajeti ya mwaka 2019/ 2020 kujengwa kwa kiwango cha lami. Ombi langu kwa Serikali kuwahisha ujenzi wa barabara hiyo kwa haraka na kuongeza kiwango cha fedha za bajeti na kuzitoa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili ni maombi ya vituo vya afya Kata za Kinole na Tegetero kule milimani kwenye Milima ya Uluguru ambao wako mbali na Makao Makuu ya Tarafa Mkuyani Bondeni. Pia vituo vya afya katika Kata za Ngerengere, Tununguo, Kidugalo na Mkulazi katika Tarafa ya Ngerengere ambako hakuna hata kituo kimoja chenye hadhi ya kituo cha afya ilhali ni tarafa kubwa kuliko tarafa zote kwenye Wilaya ya Morogoro. Pia tuna kambi nyingi za jeshi kituo kikuu cha garimoshi ya kisasa (SGR) na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Serikali, vituo vya afya katika Kata ya Kibuko ambayo ni kata mpya, Kata ya Kiloka na Tomondo ambazo zina watu wengi sana katika Tarafa ya Mkuyuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba ujenzi wa mabweni na madarasa ya vidato vya tano na sita katika Shule za Sekondari Mkuyani, Nelson Mandela na Ngerengere ili kuwa na shule za vidato vya tano na sita kwenye makao makuu ya tarafa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Serikali kuboresha miundombinu ya Shule za Msingi za Mkunyani, Mikese na Njia Nne Ngerengere kwa sababu zina uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa vya ziada kila moja zaidi ya 20 kwa kila shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchago wangu kuwasemea watu wa Morogoro Kusini Mashariki, sasa naomba kushauri Serikali katika kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982, Sura ya 290, kifungu 7(1)(g) na kufanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2017 kupitia kifungu cha 32(a),(b) na (c) kuhusu produce cess na kifungu cha 13(4) kuhusu ushuru wa huduma. Sheria hizi zinainyima Serikali mapato makubwa. Ushauri wangu ni kama ifuatavyo:-

(i) Makampuni yanayolima na kuchakata mazao ya miwa na mkonge kulipa kodi ya kuzalisha mazao katika halmashauri wanazolima mazao na kusamehewa kodi ya huduma kwenye halmashauri hiyo.

(ii) Makampuni makubwa yanayolima na kuuza nje ya nchi mazao yao ambao hatuna uwezo wa kukusanya kodi ya mazao kwa wanunuzi, Sheria ya Fedha ya 2019/2020 itamke kuwa muuzaji wa mkonge akusanye kodi hiyo kwa mteja wake kwa niaba ya Serikali na asipokusanya atalipa yeye mkulima mkubwa.

(iii) Mwekezaji/mnunuzi anayenunua mazao halmashauri moja na kwenda kuchakata mazao yake katika halmashauri tofauti na aliyozalisha mazao hayo anapaswa kulipa tozo na ushuru, zote mbili, yaani produce cess na ushuru wa mazao kwa halmashauri aliyozalisha na kulipa ushuru wa huduma (service levy) katika halmashauri anakokwenda kuchakata mazao yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kuingiza mapendekezo haya katika Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019/ 2020 ili kuongezea mapato ya Serikali na kuimarisha mapato ya halmashauri na kusukuma maendeleo ya wananchi kwa haraka katika mikoa na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba Serikali kuboresha na kupanua miradi chakavu ya maji ya zamani ya Mkuyani na Kivuma pamoja na mradi wa Pangawe – Kizinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja hii muhimu iliyo mbele yetu kuhusu bajeti ya Serikali na hali ya uchumi. Nichukue nafasi kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya na uzima nimepata nafasi hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja asilimia 100 kwa sababu ya mambo mazuri yaliyokuwepo ndani ya suala hili. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalamu wote wa Wizara ya Fedha na taasisi zake.

Mheshimiwa Spika, nianze kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwenye hoja zile zinazohusu sekta ya kilimo na nitatoa ufafanuzi wa hoja chache lakini tuwaahidi kwamba michango yao yote ina umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa kilimo chetu nchini lakini kwa maendeleo ya Taifa letu. Michango yote tutaifanyia kazi na wale ambao hoja zao nitakuwa zijazigusa kutokana na muda basi Wabunge wote mtazipata kwa maandishi ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa hoja ya pamba uliyosema maana muda wenyewe ni mchache nisije nikamaliza kabla sijagusa suala hilo. Kwanza, ni kweli soko la pamba haliendi mwendo mzuri na tumefungua msimu tangu tarehe 2 Mei lakini mpaka sasa mwenendo wake sio mzuri. Tulishatoa bei elekezi ya Sh.1200 lakini kwa bahati mbaya wakati bei ile inatoka soko la dunia bei zilianza kushuka hasa kutokana na vita vya kibiashara kati ya nchi ya China na Marekani, kwa sababu nchi ya China ndiyo watumiaji na wanunuzi wakubwa wa pamba na nchi ya Marekani pamoja na kuwa ni wazalishaji wakubwa wa pamba nao wanawauzia China lakini pia ndiyo wanunuzi wakubwa wa nguo kutoka China.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na msuguano wao na kuwekeana vikwazo, huyu amekataa kununua nguo za kutoka China mwingine amekataa kununua pamba kutoka nchi ya Marekani. Kwa hiyo, wanapogombana mafahari wawili nyasi zinaumia na sisi huku nchi za Afrika ndiyo tunaumia ikiwemo Tanzania na bei imeendelea kushuka mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, wakati tunapanga bei pamoja na wadau na wanunuzi bei katika soko la dunia ilikuwa ni zaidi ya dola senti 0.75, leo hii tunapozungumza ni dola senti 0.66 zaidi ya dola senti 0.9 imepungua. Kwa hiyo, wanunuzi kama tunavyofahamu ni wafanyabiashara wameshindwa kuingia sokoni na wameshindwa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha hasa mabenki kwa sababu mabenki wamekataa kuwapa mikopo kwa sababu wanasema huwezi kuwapa mikopo wakati kwenye biashara hii anaenda kutengeneza hasara.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali tumefanya vikao mbalimbali na kikao cha mwisho kimefanyika siku tatu zilizopita Dar es Salaam na wanunuzi wote tumekubaliana kwamba wataingia sokoni kununua kwa bei ileile Sh. 1200 na Serikali tumeweza kudhamini mikopo yao kutoka kwenye benki na tumewaelekeza kwamba wasiuze pamba hiyo mpaka mwezi Agosti, kama watauza pamba hiyo kwa hasara Serikali tutafidia hilo gap la hasara lakini bei iendelee kuwa Sh.1200. Kwa hiyo, sasa hivi wako kwenye harakati mbalimbali za ku-finalize na benki ili wapate hela wataingia sokoni muda siyo mrefu.

Mheshimiw Spika, hoja ya pili ambayo imezungumzwa na watu wengi ni kuhusu bajeti ndogo ya sekta ya kilimo. Kwanza, tunavyofahamu bajeti yetu ni cash budget tunakwenda kutumia kutokana na tulichokipata lakini kama Serikali kila mwaka tumeendelea kuiongeza bajeti hii. Mwaka uliopita 2018/2019 katika Wizara ya Kilimo bajeti ilikuwa ni shilingi bilioni 204 lakini mwaka huu tumewekewa zaidi ya bilioni shilingi 254, kuna ongezeko la shilingi bilioni 50 kwa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, pia sekta ya kilimo ni mtambuka, usiangalie tu kwamba Wizara ya Kilimo. Tumesema mapinduzi ya kilimo yataongozwa zaidi na ASDP II ambaayo inatekelezwa na Wizara zaidi ya nane. Kwa hiyo, ni vema kuangalia na bajeti hizo za Wizara zingine ambazo zote zinakwenda kusherehesha suala la kilimo.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la bajeti ya Wizara ya Viwanda, Wizara ya Ardhi, kwa sababu kilimo huwezi kulima kwenye angani, unatakiwa kulima ardhini. Kwa hiyo wanapoenda kupima mashamba na maeneo ya kilimo wanatekeleza SDP II. Kuna Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Wizara ya TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, zote hizi bajeti zao pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii upande wa misitu ambao ndiyo kilimo chenyewe, zote zinatekeleza SDP II mapinduzi makubwa ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, katika sisi Wizara ya Kilimo tuna taasisi zaidi ya 22, bajeti zake haziko hapa kwenye bilioni 254, hizi bajeti zake ziko kwenye Mfuko wa Hazina kwa sababu hizi taasisi zetu nyingine zinaripoti kwenye Mfuko wa Hazina. Tuna bajeti zaidi ya bilioni 69 kuanzia Bodi za Mazao pamoja na taasisi nyingine. Pia tuna makusanyo mbalimbali, mapato mbalimbali kwenye Bodi zetu, kama wanavyofahamu kule kwenye pamba tuna Sh.100 kwa kilo kwa ajili ya Mfuko wa Pembejeo na Bodi nyingine ziko kama hivyo. Zote hizi zinakwenda kutekeleza bajeti ya kilimo, kwa hiyo kwa bajeti ya kilimo ni pana sana huwezi kuiona tu kwenye Wizara moja hii Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, la tatu, wamechangia Wabunge wengi kwenye suala la uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji kwamba ni kweli na wengine wamefika mbali, wanasema kwamba Serikali haijafanya jambo lolote kabisa, si kweli Waheshimiwa Wabunge. Kama wanakumbuka huko nyuma Serikali katika baadhi ya mikoa tulikuwa tunapeleka chakula cha msaada, upungufu wa chakula.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. OMARY T. MGUMBA: Nashukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika hoja iliyo mbele yetu.
La kwanza niipongeze Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuleta sheria hii katika Bunge lako, ili tuweze kuifanyia mabadiliko. Sheria hii ni muhimu sana tena imechelewa sana kuleta, kwa sababu ni sheria kandamizi ambayo ilikuwa inasababisha mzigo mkubwa kwa wananchi, Serikali kutumia fedha nyingi kuliko gharama halisi ya bidhaa ambazo zilikuwa zinatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Sheria hii ilikuwa inachelewesha maendeleo, hasa Serikali kuwahudumia wananchi wake kutokana na mchakato mrefu ambao ulikuwa unafanyika kupitia sheria hii; ambao zaidi siku 90 kwa maana ya zaidi ya miezi mitatu, kitu ambacho kilikuwa kina sababisha kuchelewa kupata huduma kwa wananchi wetu.
Baada ya utangulizi huo naomba kushauri vitu vichache kama ulivyosema nitumie muda vizuri kwa sababu muda siyo rafiki; nitaenda kwa haraka haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza kama sheria yenyewe inavyotaka lengo kubwa ni kwenda hasa kuzingatia value of money, ni kwa sababu ya kupata thamani halisi ya pesa ambazo zitatumika. Kwamba kama tukanunue bidhaa kutokana na bei ya soko ni kweli kabisa, lakini ni jambo zuri, ningeishauri Serikali sasa ijipange kuwa na fedha taslimu katika akaunti zake ili mtoa huduma huyu anapotoa huduma apate malipo yake kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, hutoweza kupata bei ya soko kama mtu utamlipa ndani ya miezi mitatu, miezi sita au mwaka mmoja wakati mwingine mpaka miaka miwili inachukua mtu hajalipwa, halafu unategemea upate huduma ya soko, matokeo yake tutaweka sheria lakini sheria ambayo itakuwa haitekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ninao mfano hai kabisa ambao umetokea kwenye Mawakala wa Mbolea kwa mfano, Mawakala wa Mbolea wametoa huduma kwenye Serikali lakini leo wengine wana zaidi ya mwaka hawajalipwa na hivi vimesababisha matatizo makubwa sana kwa ucheleweshaji wa pembejeo kwa wakulima wetu. Kwa sababu hawa mawakala wamekosa sifa za kukopesheka katika mabenki, lakini pia wamekosa sifa za kukopesheka kwa wasambazaji wakubwa kupewa zile mbolea kuzipeleka kuzisambaza kwa wakulima wadogo.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali kwa jambo hili limekuja zuri na tumaimani kabisa litapunguza gharama za bidhaa na litaleta unafuu mkubwa kwa wananchi wetu, lakini sasa kwa imani tuliyokuwa nayo ya Serikali ya Awamu ya Tano ukusanyaji huu wa mapato nayo ijipange hivyo hivyo kurahisisha ulipaji wa fedha kwa watoa huduma ili waweze kutoa huduma kwa wakati na haya malalamiko kwa wananchi na sisi wenyewe yaweze kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ambalo ushauri mwingine katika hili suala la mchakato wenyewe wazabuni ni hapa, kwa sababu ndio miongoni mwa matatizo makubwa kuna rushwa kubwa sana inafanyika katika mchakato huu wa manunuzi. Kwa sababu mchakato mrefu unahusisha watu wengi na lazima wale wanaosimama kwenye kutoa haki wanataka cha juu sasa watoa huduma wengi wanapigia hizo gharama zote kwenye bei ya bidhaa na bei hizi zote zinakuja kumlalia mlaji kule mwisho.
Kwa hiyo, ninaomba Serikali katika suala hili tuongeze uwazi ili bei ijulikane gharama halisi za bidhaa husika na ijulikane ni kipindi gani muhudumu akitoa huduma atalipwa na Serikali ili ikitokea serikali iki-default kumlipa yule basi kiwepo kipengele kabisa Serikali ibebe riba ya kulipa kwa kipindi chote ambacho itakaa na hizo hela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pamoja na kulipa hiyo riba ilipe fidia kwa mfanyabiashara yule ambaye katoa huduma na Serikali imechelewesha malipo, kwa sababu kwa kukaa na pesa ya mtoa huduma kwa kipindi kirefu unamsababishia yeye a-block yaani hafanyi biashara yoyote, hafanyi shughuli nyingine yoyote ya kiuchumi kwa ajili ya kujiongezea kipato, pesa zake unazo wewe kwa maana nyingine umesimamisha kila kitu yeye kwenda mbele kwaajili ya maendeleo. (Makofi)
Sasa sio kulipa riba tu lakini ni kumfidia ni faida gani angeipata kwa pesa ile kwa wewe kuwa nayo kwa kipindi kile lazima katika hili tuwe msumeno tusiwe visu tukate huku na huku. Kwa sababu mara nyingi watoa huduma waki-default kutoa huduma tuna-cancel mikataba yao na tunawafutia, lakini Serikali inapochelewesha kumlipa hata miaka mitatu anakuja kulipwa kiasi kile kile ambacho amechukua miaka mitatu iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunazungumza value of money tuzungumze value of money pande zote mbili hata kwa kuchelewesha pesa ile kwa muda mrefu Serikali inapaswa ibebe majukumu hayo ya kumlipa riba zake na pia faida aliyotaka kutarajia kuitengeneza ndani ya kipindi chote ambacho Serikali imeshikilia hela hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache nashukuru sana niwaachie wengine nao watoe mchango wao, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana nami kupata nafasi kutoa mchango wangu katika hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nijielekeze kwenye RUBADA. Nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kuleta Muswada huu hapa Bungeni ili ufanyiwe maboresho ili lengo hata madhumuni ya kuanzisha ile RUBADA yaweze kutimia. Niseme tu kwamba nakubaliana na Wabunge wengine, kazi ya Wabunge ni kutunga sheria lakini hizi sheria tunatunga binadamu, binadamu hamna aliyekamilika. Ndiyo maana tunatunga, tukiona kuna upungufu ni halali Serikali ilete hapa tufanye marekebisho ili iwe na tija ile tuliyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali msife moyo. Mkiona kuna makosa yoyote, kutunga hiii sio kwamba ni Biblia au Msahafu kwamba haubadiliki. Wakati wowote kwenye hitaji hilo iletwe, hii ndiyo kazi yetu tumeiomba miaka mitano. Hakuna kazi nyingine, ni hii ya kutunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naunga Serikali mkono sana kwa ajili ya kubadilisha hii Sheria ya RUBADA. Kwa kweli kama walivyosema wenzangu RUBADA waliacha jukumu lao la msingi kwa ajili ya kuendeleza Bonde la Mto Rufiji wakawa madalali kwa ajili ya kukamata wawekezaji na kuwatafutia ardhi kwa njia ambazo siyo halali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano halisi kabisa, kuna kampuni ya uwekezaji wa kiwanda cha sukari inaitwa Morogoro Sugar, imekuja kuomba ardhi kupitia RUBADA ndani ya Bonde hilo la Rufiji ambalo Bonde la Mto Rufiji maana linakuja mpaka kule Morogoro Vijijini hususan Kisaki, Mkulazi na sehemu nyingine. Wawekezaji hao wana zaidi ya mwaka wa pili hawajapata ardhi kwa sababu walienda RUBADA wakalipa hela zaidi ya dola 40,000, RUBADA wakaweka mfukoni, halafu RUBADA kwa hila wakaja kijijini kwetu kule wanahamasisha wananchi na Serikali za Vijiji itenge ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji tukatenga hiyo ardhi kwa ajili ya uwekezaji tunajua tutapata mwekezaji badala yake RUBADA wakija wanatumia nguvu kubwa kulazimisha kuwaambia hii ardhi wanawapa bure bila makubaliano yoyote na kijiji wakati wao wameshavuta. Matokeo yake mpaka leo ile kampuni haijapata hiyo ardhi mpaka pale walipojitambua kuanza kurudi, kufuata taratibu na sheria na kukutana na vijiji husika kwa ajili ya kupata ridhaa ya kupata ardhi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono hili wazo la Serikali kuifuta kabisa hii RUBADA ambayo sasa ije mamlaka nyingine tunayoweza kuendeleza Bonde letu la Mto Rufiji kwa faida ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri pia Serikali katika hili, kuna wengi ambao walinufaika kupata ardhi kupitia RUBADA. Hata hao wawekezaji walionufaika kupata ardhi kupitia RUBADA hawajaziendeleza ardhi hizo, badala yake walitumia ardhi hiyo kwenda kukopea kwenye mabenki mbalimbali na kufanyia biashara nyingine tofauti na lengo halisi walilokubaliana na RUBADA.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali katika hili, pamoja na kuvunja na kuhamisha majukumu haya ya RUBADA kwenye Taasisi/Wizara nyingine kupitia mikataba hii, kwa wale wawekezaji wachache ambao walipata ardhi kupitia RUBADA, tuone kama walitimiza yale masharti na makubaliano waliyokubaliana kwa ajili ya kuendeleza ile ardhi. Kwa sababu tuna ardhi kubwa imeachwa kuanzia Morogoro Vijijini mpaka Kilombero huko, haijaendelezwa kwa kisingizio kwamba hii ardhi inamilikiwa na mwekezaji ambaye amepata RUBADA ana hati kila kitu wakati wakulima na wananchi wengi hawana ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali ikapitia mikataba hiyo tuone ardhi hizo ambazo hazijaendelezwa, taratibu za kisheria zifuatwe kama wamekiuka ni kuitwaa ardhi hiyo irudi Serikalini ikapewa mamlaka hiyo mpya kwa ajili ya kuendeleza ardhi hii kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania badala ya wenzetu hawa wametumia kwenda kukopa na kuendeleza biashara zao ambazo hazina malengo na tija kwa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nijielekeze kwenye suala la transit goods kuhusu masuala ya VAT, ambapo nakubaliana na maoni ya Kamati ya Katiba na Sheria. Ni vizuri kwamba tukaongeza muda, muda huu wa siku 30 ni mchache sana, hauendani na muda wa wapinzani wetu kama kule Afrika Kusini wana siku 180, Mozambique wana siku 90. Sasa hii inawezekana sasa hivi tuko kwenye ulimwengu wa kibiashara ikawakimbiza watumiaji na wadau wengi wa Bandari yetu ya Dar es Salaam kukimbilia hizi bandari zingine kwenda kutumia kwa sababu ya muda mchache huu ambao tumeuweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali waangalie hili kama kuna uwezekano tuongeze muda kwa ajili ya mizigo inayoenda nchi zingine ili iwe kivutio kwa watu wengi kuitumia bandari yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilikuwa na hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nitoe mchango wangu kwenye mjadala uliokuwa mbele yetu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na mwingi wa ukarimu, aliyetuwezesha kufika jioni hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nami naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Sababu ya kuunga mkono ni kwa sababu Serikali ina lengo kubwa la kutaka kujenga uchumi wa Kitaifa ambapo haikuanza kuleta makusanyo yote ya fedha ya Serikali katika Mfuko Mkuu. Tuliona kwenye Finance Bill ya mwaka 2016 Serikali ilihamisha fedha za taasisi zake kama EWURA na TCCRA ambao walikuwa wanatakiwa kuchangia tu 15% kwenye Mfuko Mkuu, lakini 85% ilikuwa inabaki kwenye mifuko hii, lakini zote zilienda Mfuko Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, tuliona mwaka 2017 katika Finance Bill, pia tulihamisha fedha za bandari, zote asilimia 100 zilikuwa zinatumika huko. Nao walikuwa wanachangia 15% tu, lakini zote zilihamishwa. Kwa hiyo, wanapokuja mwaka huu kuhamisha fedha hizi kwenda Mfuko Mkuu naamini wana lengo lile lile la kuweka uchumi wa Kitaifa, mapato ya Kitaifa ili yaweze kutumika sehemu zote kutokana na mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu mazao ya kimkakati yako matano ambayo ni korosho, tumbaku, kahawa, mkonge na chai. Kwa hiyo, kwa kuweka katika Mfuko Mkuu na hela hizi zikarudi katika mikoa inayozalisha mazao haya kwa mujibu wa bajeti ambayo tutapitisha sisi Bungeni, maana yake zile hela zitawafikia wakulima kutokana na mahitaji yao kwa sababu wawakilishi wao tupo Bungeni, tutakuwa tumelifanya hilo.

Mheshimiwa Spika, pia zile hela tutakuwa na uhakika sisi Wawakilishi wa wananchi ambao ndio wenye jukumu la Kikatiba kuisimamia Serikali. Tunawezesha CAG kwenda kukagua chombo ambacho kitakuwa CBT, kwa hiyo, sisi tutakuwa na nafasi ya kuisimamia Serikali badala ya sasa hela hizi kutumika au kusimamiwa na chombo binafsi ambacho hakimpi fursa CAG kwenda kukagua. Maana yake hata sisi Bunge hatuna uwezo wa kuisimamia Serikali katika upande huo.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo na kuunga mkono hoja, nianze na mapendekezo yangu machache niliyokuwa nayo kaama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza; mazao ya kimkakati yaliwekwa wakati huo mwaka 1984 ni ili yatuletee fedha za kigeni na kutoa ajira kwa wananchi wetu. Sasa hivi kuna mazao mengine yameonekana yana umuhimu mkubwa sana na masoko yake yako ndani ya nchi na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, napendekeza kwa Serikali, katika hayo mazao matano ya kimkakati ni vizuri tungeongeza mazao mengine matatu. La kwanza, tungeongeza miwa kwa sababu ina mahitaji makubwa ndani ya nchi na nje ya nchi, kwa sababu, tunatumia kiasi kikubwa sana cha pesa za kigeni kuagiza sukari nje ya nchi. Ni vizuri ikaingia miwa ikiwepo miongoni mwa mazao ya kimkakati ili tuweze kuongeza uzalishaji wa miwa na kuzalisha sukari nyingi hapa nchini ili tuweze kutoa ajira pamoja na kuokoa fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao la pili; tungeongeza ngano kwa sababu, tunatumia kiasi kikubwa sana cha pesa kuagiza ngano na viwanda vyetu vyote vya ngano; aidha, Bakhresa, Monaban, Azania na vingine vingi vinaagiza ngano kutoka nje wakati tuna uwezo wa ardhi kubwa ya kuzalisha mazao yao hapa na kutoa ajira na kutengeneza soko la ndani. Nayasema haya kwa sababu biashara yoyote ukifanya kwanza angalia soko linalokuzunguka.

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu, kwanza tuna soko la ndani, lakini pia tuna soko la nchi za Afrika Mashariki na Kati, tukiyaingiza hayo badala ya kugombaniana kuzalisha mazao kama mbaazi tunategemea soko la nje ambapo mlaji naye akizalisha, hatuna soko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao la tatu; tungeongeza katika mkakati mbegu za mafuta kwa maana ya alizeti, ufuta na mazao mengine. Nayasema haya kwa sababu tuna viwanda vikubwa vya kusindika mafuta hapa nchini, kwa mfano, Mount Meru, Abood pale MOPROCO Morogoro. Kiwanda cha Abood kina uwezo wa kusindika mbegu za mafuta zaidi ya tani 70,000 kwa mwaka, lakini cha kusikitisha mwaka mzima ndugu yangu Abood anapata tani 5,000 tu. Unaona namna gani tukiweza kuzalisha mbegu za mafuta na kwa kuwa viwanda tunavyo tutaweza kutengeneza ajira, lakini pia tutaweza kuokoa fedha nyingi za kigeni tunazopoteza kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ambayo siyo safi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile hata ndugu zangu wa Kigoma maweze yale tukiyawekea mkakati mzuri, yataongezeka na tutazalisha hapa, tutatengeneza ajira nzuri na uchumi mzuri kwa watu wetu. Pia nitolee mfano Kiwanda cha Mount Meru, viwanda vyake vyote vina uwezo wa kusindika mbegu za mafuta zaidi ya tani 400,000, lakini kwa mwaka vinapata tani 40,000 tu. Maana yake ni 10% ya mahitaji yake. Unaona ni namna gani tuna fursa kama nchi au Taifa ya kuweza kuongeza uzalishaji zaidi kutengeneza ajira na kuweza kuokoa fedha za kigeni tunazotumia nje.

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu ya mazingira tuliyokuwanayo ambapo Soko la Kimataifa, Soko la Dunia, lina ushindani mkubwa sana. Sasa ni vizuri focus kubwa tukaangalia kwenye mazao ambayo bidhaa zake zina mahitaji makubwa ya ndani na nchi zinazotuzunguka kuliko kuendelea kuhangaika na mazao ambayo tunategemea soko la nje ambayo wauzaji siyo sisi peke yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, katika mchango wangu wa leo ni kwa ajili ya Serikali ilipovunja Mfuko wa Korosho mwaka 2017. Mfuko ule ulikuwa na balance ya shilingi bilioni 51 na hela zile zilihamishwa kwenye CBT, Mamlaka ya Korosho. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikajiridhisha, ikafanya ukaguzi maalum pale CBT ili kugundua hela hizi ambazo zilikuwa ni mapato ya Korosho ya Export Levy kwamba zilitumikaje kwa maana ya sulphur tu na mbegu za mwaka 2017 walizotoa bure kule Kusini kwa ndugu zetu? Siamini kama shilingi bilioni 51 zinaweza kuishia kwa ajili ya magunia tu, sulphur, pamoja na miche ya mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, Serikali imekuja na sheria, nami naipongeza hii Finance Bill, lakini sheria inaanza hapa kwenda mbele. Baada ya kumaliza mchakato wao, kuchakata, kuhakiki madeni yote yanayodaiwa na Mfuko wa Korosho, ni vizuri sana tukaanza kuyalipa madeni yale hela zikarudi kule Kusini, wote wanaodaiwa walipwe ili tuondoke na mkwamo huu tuanze sheria hii kuitekeleza kuanzia leo kwenda mbele badala ya kutumia zile fedha zilizokusanywa nyuma.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia moja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asilimia mia moja. Ahsante sana.