Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Prosper Joseph Mbena (16 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliompongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na timu yake yote ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa uwasilishaji mzuri wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla sijachangia, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wote wa Jimbo langu la Morogoro Kusini kwa imani kubwa waliyonionesha kwangu na kunichagua kuwa Mbunge wao kwa kura nyingi sana, nawashukuru sana. Ninachoomba tushikirikiane kwa pamoja tuondoe umaskini ambao kwa kweli uko mwingi sana katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo haya yaliyoletwa mbele yetu na Waziri wa Fedha ni mazuri na kwa kweli tunahitaji tumsaidie kuboresha ili aje na Mpango utakaokuwa mzuri zaidi kwa nia ya kuondoa umaskini katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo, yangu zaidi ni ushauri katika maeneo machache ambayo nimeona yakiboreshwa pengine tutakuja na Mpango mzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni eneo zima na falsafa nzima ya uchumi wa viwanda. Napata picha kwamba mapendekezo haya yameogopa kuja na mpango mkubwa zaidi ya mapendekezo haya yaliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumza kuwa na uchumi wa viwanda nilitegemea nione mapendekezo mazito zaidi ya viwanda vitakavyotukwamua ili uchumi huu sasa kweli uitwe uchumi wa viwanda, lakini humu ndani sikuona sana. Nimeona viwanda vinavyozungumzwa ni vile vilivyobinafsishwa, vichache ambavyo havionekani moja kwa moja kama kweli tumedhamiri sasa kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Pia nimeona hata teknolojia inayozungumzwa humu inazungumzwa teknolojia nafuu na ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tukitaka tujifananishe na wanyonge wenzetu wale, tutabakia hapa hapa. Yupo Mheshimiwa Mbunge mmoja ameeleza kwamba kuna wakati tulifanana na nchi kama za Malaysia, leo hii wenzetu wametuacha sana, wao sasa wanakuwa wafadhili. Ni lazima tutoke hapa tulipo na sisi tuzungumze kwa nguvu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nashauri, kwa nini kwa mfano Serikali isichukue model kama ya China. China ya sasa hivi walifanya uwekezaji mkubwa sana miaka ya 1990. Wali-phase out viwanda vyao vile vilivyokuwepo wakati ule. Viwanda vyao vingi havikuwa na efficiency kubwa katika uzalishaji, wakavi-phase out. Wakachukua technology kutoka nchi za Magharibi na wakaingia kila sekta wakafanya uwekezaji mkubwa sana. Hivyo ndivyo viwanda vinavyozalisha sasa hivi ambavyo vinaifanya China iwe hii tunayoijua leo. Nashauri na sisi tufanye hivyo, tusiogope.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye maamuzi ya uhakika kabisa ya makusudi, yatakayotuwezesha tutoke hapa. Tutafute teknolojia, tutafute mashine ili tuwe na viwanda ambavyo ni vya kisasa, tuwekeze humo. Returns zitakuja baada ya miaka 10, 20, lakini tukienda kiunyongeunyonge kama tunavyoonekana kwenye mapendekezo haya, tutaendelea ndugu zangu kuwa bado tuna tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumzie upande wa miundombinu iliyoelezwa. Miundombinu ni muhimu sana katika nia nzima ya kutaka kutoka kwenye umaskini lakini pia kujenga uchumi wa viwanda. Kama walivyosema wenzangu, miundombinu ya barabara, mathalani bado haijagusa sehemu nyingi ya kuwatoa hawa maskini ambao ndio tunawazungumzia sasa hivi. Kwenye Jimbo langu ni tatizo kubwa sana pamoja na kwamba ni potential areas za kuleta uzalishaji sana hasa kwenye mambo ya kilimo. Yapo maeneo ya Kongwa yanalima sana, Waheshimiwa Wabunge wengi mna mashamba yenu kule, lakini njia mbaya sana, barabara hakuna, hizi ni sehemu za uzalishaji, unaziachaje bila miundombinu ya namna hiyo, haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia viwanda vitakavyokwenda kwenye eneo kama hilo la kilimo kutumia malighafi ya mazao kuweza kusindika na kuondoa tatizo la ajira kwa vijana wetu wengi. Hivyo, nashauri, barabara hizi ziende kwenye sehemu za vijiji, walipo watu, kwenye sehemu za uzalishaji, huko ndiko tuweke misisitizo. Nazungumzia maeneo ya kwangu kule, kama Kisaki, Mvuha na Uponda, hizo ni sehemu ambazo ni potential lakini hazina barabara pia na Bwira Juu, Bwira Chini, kote huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuzungumzie suala la umeme. Umeme wamejitahidi sana, lazima tuwapongeze. Nampongeza sana Mheshimiwa Profesa Muhongo, lakini tunayo maporomoko madogo madogo. Kwangu kule yapo maporomoko ya maji ya Mlulu katika Mto wa Kibana, Kijiji cha Lugeni. Ni potential kutoa megawatt nadhani moja, ambayo ni lilowatts 1000. Tukiweza kujenga uwezo wetu kwa vijiji vya namna hiyo vyenye maporomoko, tukawekeza kule, tutawasaidia sana hata wakazi wa kule, hata watu wa vijijini kule. Kwa hiyo, nashauri sana Serikali iangalie miradi kama hiyo pia iipe umuhimu mkubwa kuliko kuendelea kutegemea umeme ghali ambao tunatumia kwa ajili ya hawa wanaotumia mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumzie pia tatizo kubwa la ng‟ombe. Ng‟ombe tunawahitaji na viwanda tunavihitaji, lakini niishauri Serikali, moja ya njia ya kuondoa tatizo hili la migogoro ya wafugaji na wakulima kwa sasa hivi ni kuwekeza katika viwanda, hata kama vidogovidogo, kwenye maeneo hayo yenye matatizo ili wafugaji wasikae sana na ng‟ombe zao na kukosa malisho. Nitafurahi sana kama Mheshimiwa Waziri wa Kilimo utakapofika wakati wake akaja kutueleza mkakati ambao unatekelezeka wa kuondoa tatizo hilo once and for all.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie suala la viwanda vidogo vidogo, kwa sababu uchumi wa viwanda, nazungumzia uchumi wa viwanda kwa nia ya kuondoa umaskini kote. Tunahitaji kuwa na viwanda vidogo vidogo kwa kila Jimbo. Hii itasaidia ku-address tatizo la ajira kwenye Majimbo yetu na kwangu kule tayari nimeshatenga maeneo manne kwa ajili ya kuanzisha viwanda hivyo. Nitashukuru sana kumsikia Waziri wa Viwanda, muda utakapofika, atatusaidiaje kushawishi na kuweka viwanda vidogo vidogo katika maeneo ya kwenye Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika,, naunga mkono hoja. Kujenga msingi wa uchumi wa viwanda utawezesha nchi kukuza uchumi wake haraka na kutoa ajira nyingi kwa vijana wetu. Muhimu hapa ni kuangalia aina gani ya viwanda tunavyovihitaji, masoko yapi ya nje na ndani tunayalenga na lazima viwanda hivi visambazwe kwenye mikoa na wilaya mbalimbali kuwepo na uwiano tusifanye makosa ya upendeleo katika kusambaza viwanda. Fursa iwe sawa kwa wote, sasa tofauti iwepo tu kwenye upatikanaji wa malighafi husika kwa mahitaji ya viwanda, hapo uwekezaji utaangalia eneo lipi lina comparative advantage na hivyo kusukuma maamuzi ya wapi kiwanda kijengwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ili kujenga viwanda hivi, tunahitaji miundombinu ijengwe pale ambapo haipo na pale ambapo ipo, miundombinu hii iimarishwe. Miundombinu ya barabara, umeme, maji, simu na mawasiliano mengine ya usafirishaji. Jimbo la Morogoro Kusini lina comparative advantage kwa ujenzi wa viwanda vikubwa na vidogo vidogo vitakavyotumia malighafi zinazopatikana hapo hapo Jimboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Morogoro Kusini kuna maeneo makubwa ya kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kama vile mpunga, mahindi, ufuta, alizeti, karanga, pamba na mazao mengine, matunda aina zote nanasi, maembe, papaya, machungwa, avocado na kadhalika, viwanda vya kusindika vyakula vinaweza kujengwa humo Jimboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo pia lina mchango mkubwa wa kutoa kwa faida ya nchi kwenye eneo la madini, misitu, lakini barabara kutoka Bigwa hadi Kisaki kwa kiwango cha lami, ndio itakuwa mkombozi. Mradi huo wa kupanua barabara hiyo ya Bigwa – Kisaki na kuwekwa lami ni muhimu kutekelezwa na ni jukumu la Serikali kutoa fedha za kutekeleza miradi hii muhimu, sio suala la kukabidhi wahisani, hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni fursa za nchi yetu kufanya biashara nje ya nchi. Mpango wa AGOA ambao Serikali ya Marekani imekubali kuongezea muda zaidi wa miaka 15? Sasa lazima nchi yetu inufaike na mpango huu. Utekelezaji wa miaka 10 iliyopita ya AGOA, haukuwa mzuri. Nchi yetu haikunufaika sana na AGOA. Sasa Serikali isimamie vizuri zaidi tuweze kunufaisha nchi angalau kwa asilimia 90 ya AGOA.
Mwisho, kuwepo na mpango maalum kwenye Mpango wa Serikali utakaowasaidia wananchi wetu wanaopatwa na majanga ya mafuriko ya mvua hususan vjijini. Msaada wa chakula, madawa unapaswa kupelekwa kwa waathirika haraka sana. Maeneo hatarishi kwa wananchi kuishi ni vizuri yasiruhusiwe wananchi kuishi humo, lakini liwe jukumu la Serikali kuwagharamia wananchi hao kuhamishiwa maeneo salama. Kata ya Selembala yenye vijiji vya (i) Magogoni (ii) Kiganila (iii) Bwira juu (iv) Bwira Chini (v) Kiburumo, katika Jimbo la Morogoro Kusini sasa ni Kata hatari ya mafuriko ya mvua kila mwaka na ni hatarishi kwa maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafuriko makubwa yaliyotokea tarehe 6 Aprili, 2016 na 16 Aprili, 2016 ni ushahidi tosha, vijiji vyote vitano sio salama tena. Serikali ilipe fidia na kuwaondoa wananchi wote wa vijiji vitano vya Kata ya Selembala (na siyo vijiji vitatu vilivyochaguliwa) ili wote wahamie eneo salama ili Kata yote ya Selembala sasa itumike kwa mradi wa bwawa la maji Kidunda. Napendekeza hata zao la miwa sasa lingeweza kupandwa eneo lote hilo kwa ajili ya viwanda vya miwa katika Jimbo la Morogoro Kusini. Mpango wa Maendeleo lazima uangalie usalama na ustawi wa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri Mheshimiwa Nape Moses Nnauye kwa uwasilishaji mzuri. Michezo na sanaa ni ajira kubwa sana duniani. Wizara ije na mipango thabiti ya kukuza michezo hususan mpira wa miguu kwa timu za wanaume na wanawake ili kuwapa vijana wetu fursa kubwa ya kupata ajira.
Suala la rushwa katika maamuzi ya mpira wa miguu ni janga la Taifa, aibu hii lazima ikomeshwe na Wizara husika. Kushinda mchezo na kushindwa katika mchezo ni haki ya timu zinazocheza. Mwamuzi anapofanya maamuzi kwa upendeleo anawanyima haki waliostahili ushindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu TFF itumie ushahidi wa video za michezo inayolalamikiwa kwa kutumia wachunguzi wenye kutenda haki ambao hawafungamani na upande wowote, ikithibitika kwamba kweli mwamuzi amependelea basi adhabu iwe moja tu, kumuondoa mwamuzi huyo asichezeshe mchezo wowote wa mpira wa mguu kwa miaka mitano. Pasiwepo na nafasi ya kuomba msamaha, rushwa ni adui wa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Morogoro Kusini kuna mwamko wa hali ya juu kwenye michezo na sanaa. Jimbo limeanzisha ligi ya jimbo ya mpira wa miguu. Timu kumi na saba za kata zitashindana. Mbunge ndiye amegharamia vifaa vya awali vya mipira, jezi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ligi hiyo ni kwa wavulana mpira wa miguu na wasichana upande wa netball. Lakini pia kuna timu mbili za timu ya mpira wa miguu (soka) kwa wanawake. Naomba Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini akubali kuwa mgeni rasmi wakati wa fainali za mechi hizi za ligi ya jimbo la Morogoro Kusini kwa tarehe tutakayokupatia hapo baadaye. Lakini pia tunaomba Wizara ichangie kata hizi kumi na saba zinazoingia kwenye ligi vifaa vya michezo kususan mipira ya kutosha, jezi na viatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la timu zetu za mpira wa miguu kutofanya vizuri chanzo chake ni uongozi. Viongozi wengi wa michezo wamejawa na ubinafsi, wasio na weledi na wanaotengeneza makundi ndani ya timu yao badala ya kujenga umoja kwenye timu.
Ushauri wangu Wizara iwaangalie viongozi wa timu zetu na kuwataka waongoze timu kwa misingi ya katiba na sheria, kanuni na kujenga umoja kwenye timu wanazoziongoza badala ya kubagua wanaowaongoza. TFF lazima ijiangalie yenyewe kiuongozi ili itende haki kwa timu zote bila ya kubagua. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa maoni na mchango wangu wa mawazo kwenye hotuba ya bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama ilivyowasilishwa kwetu na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Madelu, Waziri wa Wizara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri na hotuba nzuri ambayo imesheheni maeneo yote muhimu ya sekta hii. Pia nimpongeze kwa jinsi ambavyo anajituma katika kufanya kazi zake. Yeye na Mawaziri wengine wamekuwa mstari wa mbele katika kutatua matatizo ya wananchi wetu, nakushukuru na nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ninachokifanya hapa ni ushauri tu katika nia ya kuboresha lakini pia ni mawazo, Mheshimiwa Waziri anaweza kuyachukua na anaweza kuyachuja. Katika bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama nilivyosema maeneo mengi yameguswa lakini mimi ningependa nione linajitokeza zaidi ufumbuzi wa tatizo kubwa la migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Nasema ningetamani nilione hilo limejitokeza kwa sababu kwa kweli kwa sehemu kubwa katika baadhi ya Majimbo langu likiwa mojawapo Morogoro Kusini, migogoro hii inatishia usalama wa wananchi wetu. Wapo walioumizwa, wapo ambao wametengeneza uhasama mkubwa sana na chanzo ni migogoro hiyo. Nafahamu Wizara zaidi ya moja inahusika katika kutafuta ufumbuzi wa jambo hili mojawapo ikiwa ni Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nyingine zikiwa ni Ardhi na TAMISEMI. Napenda Wizara hizi zote zinazohusika zituonyeshe na kutueleza waziwazi jinsi watakavyoweza kutatua migogoro hii iwe historia, tumechoka nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufumbuzi wake uko kwa namna nyingi, moja kiutawala ambayo naamini kabisa Mheshimiwa Waziri anafanya hivyo kwenda kuzungumza na makundi haya lakini lingine kusema ukweli ni la kiuchumi na hapa ndipo napenda Mheshimiwa Waziri ajielekeze zaidi. Mifugo hii imeshaingia hata kwenye maeneo ambayo siyo ya ufugaji. Wakati mwingine kutoa mifugo ile yote ni nadharia, kiutekelezaji ni ngumu. Ufumbuzi wake upo katika kuanzisha viwanda vitakavyoweza kutumia malighafi za mifugo ile kutengeneza bidhaa ambazo zinaweza kuwa nyama za kusindika, ngozi na mifano mingi. Tunaposema uchumi wa viwanda katika eneo hili vielekezwe kwenye maeneo hayo ambayo kwa kweli mifugo tayari imeshakuwa mingi na sasa tunahitaji hata wale wafugaji wanufaike zaidi na mifugo yao. Hii itatupunguzia uhasama kwa sababu sasa wakulima mashamba yao yatakuwa salama na wafugaji watakuwa na mahali pa kupeleka ng‟ombe zao, soko la karibu litakuwa viwanda vitakavyojengwa, hivyo Mheshimiwa Waziri ningependa sana hili lijitokeze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni ushauri tu kama nilivyosema na kwenye eneo hili naomba nitumie fursa hii kuwapa pole sana wananchi wangu wa Jimbo la Morogoro Kusini hususani kata zile ambazo zimepata mafuriko makubwa sana, Kata ya Serembala, Mvuha pamoja na Konde. Wananchi wameathirika sana, wamepoteza nyumba zao, mashamba yao, mazao yao yaliyokuwa shambani na mengine nyumbani na kwa kweli mazingira yale ni magumu kwa mtu yeyote. Nawapa pole lakini Serikali inajua, mimi mwenyewe nimelifikisha kwa Waziri anayehusika na naamini ufumbuzi wa kudumu utapatikana. Ikiwezekana na hapa ndipo ninapotaka kuchangia Wizara ione inaweza ikafanya nini kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo Mheshimiwa Waziri ametueleza ambayo yamebainishwa katika mradi ule wa BRN, ni maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kilimo cha miwa pamoja na mpunga. Katika Jimbo langu yapo maeneo mawili, Kisaki na Mvuha, ni maeneo mazuri kwa ajili ya kilimo cha miwa. Mimi napendekeza liongezwe eneo lingine la tatu lile la Serembala ambalo ni hatarishi kwa wananchi na ni eneo kubwa sana. Wananchi wale wangeweza kutolewa wakapelekwa sehemu iliyo salama kwao ili sasa eneo lile lilimwe miwa, ni eneo zuri sana kwa ukulima wa miwa. Tuondoe tatizo hili kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nitapenda nilichangie ni lile ambalo wenzangu wamelisema, lakini labda mimi niliseme kwa maana ya kuongezea tu uzito. Miundombinu yetu si rafiki sana kwa wakulima na kwa ajili ya kuongeza kilimo. Yapo maeneo katika jimbo langu yana historia ya kutoa mazao mengi sana lakini hayapitiki kwa barabara kipindi kama hiki na mazao yanaharibika bure. Ni vizuri Serikali ikawa na strategic, yale maeneo ambayo wanajua kabisa kwamba ni potential kwa ajili ya kilimo, mazao yanapatikana mengi watengeneze pia na miundombinu bora na ile ambayo mwaka mzima inapitika ili wakulima kweli waweze kulima. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, pia tupatiwe zana, Mheshimiwa Waziri amesema hapa kuna mpango wa Serikali wa kupata matrekta, nadhani kutoka Poland au kwa kutumia msaada wa Poland, matrekta zaidi ya 2,000, ni jambo zuri. Jimbo langu la Morogoro Kusini linajulikana kwa ukulima hebu tupatiwe hata matrekta 20, tunahakikisha tutalisha sehemu kubwa ambayo wenzetu wanakuwa na upungufu wa chakula mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono hoja kama nilivyosema na nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi niungane na waliompongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya kutoka Kisaki kuja Morogoro, Bigwa kilometa 151, ni barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ni barabara ambayo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ameahidi wananchi wa Morogoro Vijijini, ni barabara ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu hii ya Tano ameahidi wananchi kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami na ni barabara ambayo ilipitishwa kwa ajili ya mpango wa MCC, lakini hata bila MCC kupita bado Serikali iliipa umuhimu kwamba ingeanza na kipande cha kilometa 78 cha kutoka Bigwa hadi Mvuha kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kwamba barabara hiyo haipo humu kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri, hiyo haikubaliki, itatuletea ugomvi usiokuwa wa lazima na wananchi wa Morogoro Vijijini na niwe mkweli kabisa mimi nitakuwa upande wao, tunaihitaji barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madaraja yaliyomo katika njia hiyo; lipo daraja la Ruvu, lipo daraja la Mvuha na lipo daraja la Dutumi. madaraja ya Mvuha na Dutumi yanatitia, yanadidimia chini madaraja yale. TANROADS wana habari, wameagizwa washughulikie, lakini mpaka ninavyosema hivi hakuna kinachofanyika na hayamo kwenye mpango huu, inasikitisha. Lakini napenda nimkumbushe Waziri kwamba hilo litaleta ugomvi usiokuwa na lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuriko yaliyotokea hivi karibuni sehemu ya Mvuha yamesababishwa kwa sehemu kubwa na matatizo ya madaraja haya kwa sababu yanaenda chini, mvua inayesha, mafuriko yanajaa juu, watu hawawezi kupita, hakuna ukingo, yanaleta ajali kwa watu na magari yanayopita, Mheshimiwa Waziri tusaidie.
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyowasilishwa kwenye Hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni vizuri ikatekelezwa ipasavyo ili kuweza kuleta matokeo mazuri yaliyotabiriwa. Tatizo kubwa la bajeti za Wizara mbalimbali ni kutopatikana kwa fedha zinazoidhinishwa na Bunge kwa wakati ili utekelezaji wa mipango iliyotengewa fedha kwenye bajeti uweze kufanyika kwa wakati uliopangwa. Ni muhimu Hazina izingatie hili na kutoa fedha kwa wakati unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje na Serikali kwa ujumla haikutoa tamko lolote kwenye Hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje, kuhusu vitendo vya ubaguzi na udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya wananchi wa India dhidi ya Waafrika waliopo India. Matukio ya udhalilishaji wa Mtanzania mwanafunzi, aliyevuliwa nguo zake na kuburuzwa mtaani, raia mwingine wa Congo ambaye aliuawa kikatili na matukio mengi dhidi ya Waafrika huko India, haya ni mambo makubwa ya kidiplomasia ambayo hayapaswi kuachwa yapite bila kukemewa na kuyatolea tamko na Waziri mwenye dhamana ya mahusiano na nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 23 Juni, 2016, Uingereza itapiga kura ili wananchi wake waamue ama kuendelea kuwemo ndani ya Jumuiya ya Ulaya (EU) ama kutoka kwenye Jumuiya hiyo, mpango ulio mashuhuri kwa kujulikana kama BREXIT. Ni vizuri Wizara hii ingefanya tathmini na kushauri je, nchi yetu itaathirika vipi na kunufaika vipi na hatua hiyo ya Uingereza hasa kwa kuwa Uingereza imekuwa na ushawishi mkubwa kwa baadhi ya sekta za maendeleo ndani ya Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini hizi ni muhimu ili kuiandaa nchi yetu ipasavyo. Je, kama Uingereza itajitoa kwenye Jumuiya ya Ulaya bila Uingereza kwa nchi yetu itapungua au itaongezeka? Haya ndiyo maswali ambayo wananchi wa Tanzania wangependa kupata majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inabidi kuratibu kwa weledi zaidi mahusiano ya nchi za nje ili nchi wahisani wasiathiri mipango ya maendeleo ya wananchi wetu Watanzania kwa kuvunja makubaliano tunayoyafanya kwa sababu za kisiasa. Uamuzi wa Marekani kusimamisha mpango wa MCC II kwa Tanzania ni mfano mzuri. Hali ya kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili na marafiki zetu ina gharama zake. Tusipoweza kuratibu kwa weledi wa hali ya juu tutavuruga mipango mizuri ya maendeleo ya wananchi wetu. Tanzania ni nchi huru ina heshima yake hatutaki mahusiano ya kudharauliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naunga mkono hoja, hata hivyo yapo mambo machache yanahitaji maboresho kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mchezo wa mpira wa miguu ndiyo mchezo unaopendwa sana duniani kote, uongozi wa TFF unasababisha matatizo makubwa kwa makundi mbalimbali ya wapenzi wa mpira wa miguu hususan pale wanaposhindwa kusimamia haki za vilabu vya mpira na wanachama wake kwa kupotosha maamuzi yanayolenga kufanya upendeleo, kunyima haki na kuonesha kuegemea upande fulani. Jambo hili ni aibu, tunahitaji viongozi walio juu ya ubinafsi na upendeleo wowote kwenye maamuzi yao.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni viwanja vya mpira wa miguu. Upo utaratibu wa TFF kutumia msaada wa FIFA unaotolewa kwa wanachama wake kuweka nyasi za bandia kwenye viwanja vinayoteuliwa. Ni busara kuweka utaratibu mzuri wa viwanja gani tunadhani vianze kuwekewa nyasi hizi kabla ya kufikiria labda viongozi wetu TFF wanapeleka nyasi bandia katika mikoa wanayotoka. Viwanja vya mpira vya Jamhuri Dodoma, Jamhuri Morogoro, Majimaji Songea vingestahili kuwekewa nyasi za bandia kwanza kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tunahitaji viongozi wa TFF wasio na upendeleo wa ovyo ovyo. Nchi hii yetu wote, wote tunayo haki sawa, ni vema viongozi wawe watenda haki kwa wanaowaongoza. Kwenye mpira wa miguu TFF ni tatizo, wajirekebishe.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kutoa maoni yangu katika kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hotuba ya Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze pia kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Philip Mpango kwa hotuba yake ambayo kwa ujumla ni nzuri na kama wenzangu wengi walivyosema, ni bajeti ya kwanza hii, anachukua mambo mengine ya nyuma, anaangalia huko tunakokwenda mipango iko vipi, pamoja na ushauri mwingine, naamini na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge atauzingatia, kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nielezee masikitiko yangu makubwa kwa kusema kweli, kwamba Jimbo langu la Morogoro Kusini tulijipanga sana katika kipindi hiki tuweze kukuza uchumi, hasa wa kilimo na kwa sababu hiyo tulitegemea sana kupata miradi ya miundombinu ya barabara. Tumezungumza sana, tumeomba sana, tumeeleza sana, lakini kwa bahati mbaya sana haikupewa umuhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalisema wazi kabisa, limenisikitisha na litawasikitisha wananchi wengi sana wa Morogoro Kusini. Hata hivyo, naamini Serikali itakuwa na jicho lingine la kuangalia ukweli kwa sababu huko ndiko kwenye kuzalisha mazao, huko ndiko kwenye vijiji, huko ndiko kwenye nafasi ya kutengeneza viwanda hivi tunavyovizungumza, lakini bado haki haitendeki, bado wenzetu hawaoni hicho ambacho sisi wengine tunaona, bado hawaoni hata umuhimu wa ile barabara ya Bigwa kwenda Kisaki kwa kiwango cha lami ambacho watu kama Wamarekani waliiona na wameiweka kwenye Mpango wa MCC II, lakini Serikali yangu hii hawataki kukubali, hawataki kuona, hakuna haki inayotendeka na hili si jambo jema, hatulikubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizunguzie hali ya uchumi wa Taifa, nimesoma hali ya uchumi wa Taifa katika mwaka huu tulionao 2015, kwa sehemu kubwa, kwa sekta nyingi hatukufanya vizuri ukifananisha na hali ilivyokuwa mwaka 2014. Yapo maeneo tumefanya vizuri sana, ukuaji wa Sekta kama za Ujenzi, hususan barabara na ujenzi wa nyumba za makazi, tumefanya vizuri na kwenye eneo hili nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ni eneo ambalo yeye mwenyewe akiwa Waziri wa Ujenzi amelisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nipongeze Sekta Binafsi, niipongeze pia Serikali upande wa TBA, pamoja na mashirika na taasisi za kifedha ambazo ziliweza kwa sehemu kubwa kujenga hizi nyumba za makazi ambazo tunazizungumzia sasa hivi na sehemu nyingi ni mfano. Ni nzuri, ni za kisasa zinafurahisha hata kwa kuziangalia, nawapongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hilo halitoshi, hatukufanya vizuri kwenye upande wa biashara. Kwenye upande wa biashara hatukufanya vizuri, kwenye biashara kwenye ranking zetu Kimataifa kwa upande huu, malalamiko ni yale yale. Kunakuwa na usumbufu kidogo wakati wa kuomba leseni, kunakuwa na mzunguko sana, hata wakati wa kulipa kodi tu hizi bado watu wanazungushwa. Sasa Serikali ifike mahali tuweke utaratibu mzuri, tujirekebishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sababu nchi kama Rwanda kila siku wenzetu wanasifiwa kwamba wao wanarahisisha sana mambo yao kuliko sisi na viongozi wetu hawahawa, Mawaziri wetu hawahawa wana uwezo mkubwa sana, lakini bado tatizo hili linaonekana kuwa linatusumbua. Nawaomba sana tujipange kwa makusudi kabisa, tuondoe tatizo hilo, tuondoe tatizo la rushwa, tuondoe tatizo la ukiritimba, watu wafanye biashara. Tunahitaji hawa watu wengi wa biashara waongeze mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie maeneo machache machache ambayo nayaona pengine yataleta tija kidogo kwenye hii bajeti. Wengi wamezungumzia suala la uvuvi kutopata nafasi inayostahili. Ni kweli, ukisoma kwenye vitabu hivi huamini kwamba hii ni nchi yetu ambayo imezungukwa na maziwa na bahari, hatujaweza kutumia vizuri nafasi yetu. Inanifanya nikumbuke kwamba inawezekana tulifanya makosa sana tulipoliharibu Shirika letu la TAFICO, naamini kabisa uvuvi tunaoufanya huu ni mdogo sana, lakini bado tumepata mapato haya, tungeweza kupata zaidi ya mara nne kama tungeweza kufanya uvuvi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Msumbiji wamenunua meli kubwa za uvuvi kwa ajili ya bahari hii ambayo tuna-share nao, wamenunua meli 34 zinafanya uvuvi wa viwanda na sasa hivi nyingine wanazitengeneza ili sasa wa-meet zile standards za kuuza samaki wao kwenye soko la Ulaya, sisi hakuna, huoni kama kuna jambo la namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningewaomba sana twendeni kwa spidi, twendeni na sisi kama vile si Taifa dogo hivi. Tuchukue uzito wetu, ukubwa wetu hata kwa jiografia tu, hawa wenzetu wanashinda vipi sisi tushindwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo linanihusu moja kwa moja ningependa nichangie, nisije nikalisahau, ni hili la milioni 50 za vijiji. Wengi wamelizungumza, kila mtu ana mawazo yake, wengine wanataka waanzishie benki, wengine wanataka waanzishie vitu vingine. Hizi ni pesa ziko maalum kwa ajili ya wajasiriamali wetu vijijini, ni vizuri tusiende nje ya malengo ya hizi pesa zilipowekwa. Tugawiwe kwa utaratibu mzuri lakini ulenge kule ambako ilani ilisema na Mheshimiwa Rais alisema, tuwasaidie wajasiriamali kule, hili ndilo lengo kubwa la hizi pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mikoa 10 itakayoteuliwa mwanzo sina uhakika nayo, vigezo gani mtatumia sina uhakika, nitashindwa majibu ya kuwaambia watu wangu kule jimboni. Ninachoomba hizi pesa zigawiwe, vijiji vipate ili na wao waweze kufanya shughuli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la ununuzi wa ndege tatu za Air Tanzania (ATCL) jambo zuri, limekuja wakati muafaka, ushindani mkubwa kwenye eneo hili. Sikatai pendekezo linalozungumzwa la kuangalia partners tunaoweza tukafanya nao, lakini hilo halizuii sisi kuanza na hizo ndege ambazo tunataka tuwe nazo. Wasiwasi wangu ni madeni ya ATCL, kama bado yapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma nilihusika kwenye vikao vidogo vidogo, nafahamu vitu vingine. Upo wakati ndege zao zilitaka zikamatwe wakiwa nje ya nchi, sasa kama madeni haya hayajamalizika, wanaweza wakanunua ndege mpya, wakaanza safari, hukohuko zikawa grounded, zinachukuliwa na wenye madeni. Kwa hiyo, tahadhari naiweka tu kwa Serikali waangalie, je, suala hilo limekaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie…
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa maoni yangu au mchango wangu kwenye hotuba hii muhimu ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango. Kabla sijatoa maoni yangu na mimi niungane na wenzangu waliokupongeza wewe kwa msimamo sahihi, haki na kutokubali kuyumbishwa. Nadhani ni mmoja kati ya watu ambao tayari nilishakupongeza na uendelee na msimamo huo. Ningekuwa nina uwezo wa kukupangia basi ningesema umalize ngwe hii yote mpaka tutakapoondoka, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie maeneo machache tu katika Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, nikianza na lile la mafanikio ya MKUKUTA II.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema vizuri kwamba mafanikio makubwa yameonekana katika MKUKUTA II na moja ya mafanikio hayo ni pale ambapo umaskini umepungua kwa karibu asilimia 6.2. Sasa tukiangalia mmoja mmoja kwenye Majimbo yetu basi ndipo tunapoona kwamba kipimo kile kumbe sisi wengine bado hatujakifikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu mimi vijiji vyangu nikianza na pale nilipozaliwa Lugeni niende maeneo mengine ya Konde, Kisaki Station, Nyingwa ni ndoto ukisema kwamba umaskini umepungua; umaskini umeongezeka. Sasa hii maana yake ni kwamba mpango huu haukuwanufaisha wale waliolengwa na inawezekana sana Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na watendaji wengine wa karibu na wananchi hawakuhusishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwenye mpango mwingine unaokuja na matayarisho yake yaanze sasa, tuwe na takwimu sahihi ya hao walengwa, tuwe na utaratibu mzuri wa kuwafikia hawa walengwa, Wabunge wahusishwe kikamilifu, sisi ndiyo tunaojua watu wetu wanaohitaji msaada mkubwa, tunaojua umaskini umekaa wapi ili mafanikio haya yanayozungumzwa sehemu nyingine yaweze kufika kwenye maeneo yetu haya ambayo kwa bahati mbaya kwenye MKUKUTA II hatukuweza kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la hili la Sheria ya Manunuzi. Wenzangu wamesema na mimi niongeze tu sauti. Nashukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Chenge ametuonesha ukubali wake na utayari wake wa kulifanya hili kama Serikali itakuwa bado ina kigugumizi cha kuleta hapa mbele ya Bunge. Sidhani kama Serikali inaona ugumu; ninachojua kwa sababu nimetoka huko Serikalini, muda wote nilipokuwa pale Serikalini kilio ni hicho hicho kwamba sheria hii ni mbaya, itokee nafasi tuibadilishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nashangaa fursa hiyo tunaiacha inapita lakini hata Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alituahidi hapa Bungeni kwamba sheria hii italetwa ili tuweze kuibadilisha; nawaomba sana Serikali, Waziri wa Fedha , ashughulikie hili tulimalize. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu naomba nilizungumzie hili ambalo pia wenzangu wamelizungumza, pesa hii shilingi milioni 50 kwa kila Kijiji. Hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Mkuu wa nchi, imetangazwa nchi nzima, dunia nzima inajua hakuna shortcut yake, ni utekelezaji tu unaotakiwa hapa. Mheshimiwa Waziri utafute hizi pesa tutengeneze utaratibu mzuri ili pasiwepo na ufujaji wa pesa hizi ili kwa kweli wananchi wetu maskini waweze kunufaika na mchango huu mkubwa uliotolewa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Wabunge wenzangu wawili wamezungumzia kuhusu mikopo ya benki za biashara. Mikopo hii inayotolewa kwa wananchi na kwa kweli mwananchi anapokwenda kukopa ni kwamba, ana shida, lakini mabenki haya yanatumia shida za hawa wananchi kuwabana. Dhamana wanayoweka ya nyumba, mikopo hii masharti yake ni magumu sana, utekelezaji wa mkopo huu ukijumlisha na riba, mkopo unakuwa ni mara mbili. Wapo wananchi wengi sana wamepoteza nyumba zao za kuishi, wengine wamejiua, wengine wamepata maradhi ya kusononeka na wengine ndoa zao zimeharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, yote haya yameletwa kwa sababu nadhani Serikali haikuangalia sana. Faida zinazotengenezwa na benki hizi kutokana na mikopo hii, wote sisi ni mashahidi, baada ya mwaka utasikia wametengeneza bilioni 10 wanagawana; lakini wamefanya hivi kwa kumgandamiza huyu mwananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu Wizara ya Fedha ikishirikiana na Benki Kuu iangalie upya mwenendo wa benki hizi na mikopo yao kwa wananchi na hasa kama inawezekana, dhamana hii ya nyumba itolewe katika mpango mzima wa kuwakopesha watu. Kwa sababu kwa kusema ukweli tunawarudisha wananchi wetu kwenye umaskini mkubwa sana kwa ajili ya matatizo haya ya mikopo ya kibenki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametuelezea kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali, na katika hotuba yake ameeleza kwamba wafadhili kwa mwaka 2015/2016 wameweza kupunguza ahadi yao ya mchango kutoka Shilingi bilioni 660 hadi kufikia Shilingi bilioni 399, punguzo hilo ni karibuni asilimia 40. Hili jambo linanisikitisha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa ni wafadhili ambao tuliona ni marafiki zetu, tumekaa nao katika meza, tumewaeleza mipango yetu na wao wala si kwa kushurutishwa wamekubali kuchangia hicho walichoahidi. Leo hii kwa sababu yoyote ile wanafika mahali wanajitoa anavuruga kabisa bajeti na mpango mzima wa maendeleo wa nchi yetu, haikubaliki. Serikali inatakiwa iwaeleze, Serikali inatakiwa ifike mahali ijulishe dunia kwamba hawa ni marafiki ambao wametuangusha katika nia yetu ya kufika mahali fulani kwenye maendeleo, haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na-declare interest, nilikuwa Kamishna wa External Finance pale Wizara ya Fedha, nimefanya kazi kwa muda mrefu sana. Mahusiano ni muhimu lakini mahusiano hayo yana heshima ya nchi na nchi. Inapofika mahali dharau inaoneshwa namna hii ni juu ya Serikali kuonesha kwamba mwenendo huo hatukuupenda katika mahusiano yetu. Kwa hiyo, nawaomba sana Serikali hebu tusiwe wanyonge hivyo, dalili ninazoziona ni kwamba kuna unyonge unyonge hivi, ndiyo maana tunachezewa hivyo, ndiyo maana barabara nyingine sasa zimeachwa kwa sababu tu wafadhili fulani hawakutoa pesa ambazo waliahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2016/2017. Kumekuwa na ongezeko la watoto walioandikishwa kuanza shule, Serikali imebeba gharama kubwa za kumsomesha mtoto na kushirikiana na wazazi na walezi wa wanafunzi hawa kupitia programu ya elimu bila malipo. Bado changamoto zilizopo za upungufu wa madarasa kwa shule zote za sekondari na shule za msingi, upungufu wa nyumba za walimu kwa shule zote hizi za sekondari na shule za msingi,

Pia upungufu mkubwa wa matundu ya choo kwenye shule hizi za sekondari hasa zaidi kwenye shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upungufu wa walimu kwenye baadhi ya shule za sekondari na shule za msingi na upungufu wa vitabu vya kufundishia na vitabu vya wanafunzi haya ni mambo muhimu ambayo Serikali inayashughulikia kwa nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limetokeza suala la watoto wa kike kupewa mimba mashuleni. Serikali inapaswa kuendelea kulikataza na kulisimamia suala hili kwa kuhakikisha wanaume wanaokatisha masomo ya wanafunzi hao wa kike kwa kuwapa mimba wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Pia ni muhimu kwa Serikali na hususan Halmashauri za Mikoa na Wilaya kuhakikisha zinajenga hostel za kutosha kwa ajili ya wanafunzi wote wa kike na kuwakinga wanafunzi hao. Hostel hizi zitapunguza sana tatizo lililopo la wanafunzi wasichana kupata mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Morogoro Kusini kuna shule nyingi za sekondari ambazo zimejengwa kwa nguvu kubwa za wananchi lakini zina changamoto hizi za mimba. Tunaomba Wizara itoe fedha za kutosha kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ili tuondoe tatizo hili la aibu la wanafunzi wa kike kupewa mimba mashuleni. Mazingira ya wanafunzi hawa ni mabaya sana na yanasababisha kupata mimba hizo. Tukiwezeshwa kujenga hostel za wanafunzi wa kike kwenye shule hizi, tutaondoa tatizo lililopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jimbo langu la Mororogo Kusini tunalo eneo tayari la kuanzisha shule za VETA. Bado naikumbusha Serikali iweze kutupa msaada tuweze kuanzisha chuo hicho kwa kipindi kijacho cha mwaka 2017/2018 - 2018/ 2019. Sambamba na hilo jimbo la Mororogoro Kusini imeziteua shule za sekondari Matombo na shule ya sekondari Misewesewe ya wasichana iliyopo kata ya Mngazi kuanzisha kidato cha tano (form five) kuanzia mwaka 2017/2018. Matayarisho yamekamilika kwa shule hizi hususan shule ya sekondari ya Matombo ili ianze kupokea wanafunzi wanaoingia kidato cha tano kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2017/2018. Nimepata taarifa kwamba kumekuwa na ucheleweshaji wa kuwezesha mpango huu kutokana na urasimu Wizarani. Naomba Wizara ihakikishe tunalikamilisha mapema ili wanafunzi waweze kupata elimu ya form five ndani ya Wilaya ya Morogoro Vijijini kupitia shule zetu hizo mbili zilizoteuliwa ambazo kwa kiasi kikubwa zimecheleweshwa kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Bunge kwa Mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mkuu wetu wa Nchi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kutuletea maendeleo ya kiuchumi nchini. Kufufua zana za uchumi wa viwanda, ununuzi wa ndege za usafiri kwa ajili ya Shirika letu la Ndege la Taifa (ATCL), kutekeleza kwa vitendo maamuzi ya Serikali ya kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kuja Dodoma, kutekeleza ujenzi wa reli ya kisasa ya standard gauge, kutekeleza ujenzi wa barabara ya juu (flyovers) katika maeneo ya makutano ya barabara Jijini Dar es Salaam, kutekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Stiegler’s Gorge, ni mifano ya juhudi hizo za kujenga uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuzaji ujuzi. Katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelezea umuhimu wa kukuza ujuzi wa nguvukazi tuliyonayo na kusema ni miongoni mwa ajenda muhimu za kisera. Naomba kupendekeza kwamba wataalam wastaafu wazalendo watumike katika kusambaza ujuzi na elimu kwa vijana wetu. Wapo Watanzania wengi wenye ujuzi mkubwa katika fani mbalimbali za uzalishaji uchumi na kadhalika ambao ni wastaafu ambao bado wana nguvu na uwezo mkubwa wa kushauri. Serikali iwatumie wastaafu wetu hawa pamoja na wataalam wengine ambao bado hawajastaafu, ili kuweza kupata matokeo ya haraka ya ukuzaji ujuzi na kuwajengea vijana wetu uwezo mkubwa (capacity building).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta Binafsi. Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji uchumi. Suala hili ni muhimu sana kulisimamia na kuliendeleza kwa nia ya kujenga uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo juhudi za mara kwa mara zifanyike na hatua kuchukuliwa za kuwawezesha wafanyabiashara Watanzania na wazalendo kunufaika na uchumi wa nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo. Serikali imekamilisha maandalizi ya awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo. Bado uzalishaji katika kilimo ni wa kiwango cha chini ukizingatia ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo cha kumwagilia, haitumiki. Nashauri katika maandalizi hayo iwe ni pamoja na kupanga mikakati ya kulima maeneo yote yanayolimika na kutafuta masoko ya nje na ndani kwa mazao yote yatakayolimwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; Serikali imetoa fedha za kutekeleza ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu ya vituo vya afya na maabara ya upasuaji kwa akinamama wanaojifungua. Jumla ya vituo vya afya 100 vimepatiwa jumla ya shilingi milioni mia saba, kila moja ikiwa shilingi milioni mia nne; ni kwa kazi za umaliziaji miundombinu na shilingi milioni mia tatu zinanunulia vifaa na madawa MSD. Nimeomba Serikali ijumuishe Vituo vya Afya vya Mvuha, Mtamba (Kisemu) na Tawa vilivyomo kwenye Jimbo la Morogoro Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya kiongozi wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kubwa ya kukuza uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka huu wa 2016/ 2017, haukuwa mzuri hasa bajeti ya maendeleo kutokana na fedha kidogo zilizotolewa na Hazina ambazo ni asilimia
3.31 tu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge. Naishauri Serikali yetu ihakikishe fedha zote za maendeleo zinazoidhinishwa na Bunge kwa Wizara hii zitolewe kwa wakati ili tulete mabadiliko makubwa ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya bajeti ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi haikueleza kwa namna gani Serikali itamaliza migogoro ya wafugaji na wakulima. Jimbo langu la Morogoro Kusini limekumbwa kwa kiasi kikubwa sana na migogoro ya wafugaji na wakulima na wananchi wanaathirika, wapo waliopoteza maisha yao, waliopata ulemavu na waliopata umaskini. Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi haijasema Serikali imejipanga vipi kuitafutia ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufugaji wa sasa wa ng’ombe kwa utaratibu wa kuchunga mashambani hauna tija. Wizara ijipange kufanikisha ufugaji wa kisasa wa zero grazing. Nchi za Botswana na Namibia zinaweza kuwa mfano mzuri wa kuigwa, tujipange na sisi kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo katika bajeti hii bado hakijapewa umuhimu unaostahili kwa kuzingatia rasimali zinazotengwa, kilimo cha trekta na umwagiliaji ndicho kitakacholeta mapinduzi ya kilimo nchini. Kwenye bajeti hii, mikopo ya kununua trekta ni kidogo mno. Mfuko wa Taifa wa Pembejeo umepanga kutoa mikopo ya matrekta 71 tu kwa nchi nzima, kiasi hiki ni kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima ijenge miundombinu ya kilimo, barabara, trekta nyingi za kutosha, vifaa vya umwagiliaji pia Serikali ihakikishe mbegu bora na mbolea ya kutosha inapatikana kwa wakati. Kwa upande wa Jimbo la Morogoro Kusini tunayo maeneo mazuri sana ya kilimo cha trekta na umwagiliaji mfano eneo la Kongwa, Kilengezi, Selembala, Magogoni, Lundi, Dutumi na Kisaki ni maeneo makubwa yanayolima mahindi, mpunga, ufuta, mihogo, viazi na kadhalika. Tunaomba Serikali ituwezeshe wakulima wetu wapate mikopo ya nyezo hizo za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa upande wake itengeneze barabara za kwenda mashambani ili zipitike muda wote wananchi watalima sana. Taarifa ya Serikali kuwa zao la muhogo limepata soko China ni habari njema kwetu, tunaomba kufahamu utaratibu utakaotumika na chombo gani kinachosimamia hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeeleza dhamira yake ya kuifanya nchi ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Hivyo, nashauri Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi itengeneze mpango wa uzalishaji wa mazao yatakayoingia katika viwanda vitakavyojengwa nchini kuandaa upatikanaji wa raw materials za viwandani mfano miwa kwa viwanda vya sukari, matunda kwa viwanda vya juisi na vinywaji baridi na kadhalika. Mashamba ya mazao haya yatakuwa makubwa na ni vema kuanza kuandaliwa vinginevyo viwanda vyetu vitajengwa hakuna raw materials. Kwenye uzalishaji huu, matumizi ya sayansi na teknolojia uongezeke ili tupate mazao mengi ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, sekta ya uvuvi bado kuimarika tunahitaji mapato yaongezeke mara dufu. Nashauri tuingie ubia na makampuni ya nje yenye meli kubwa za uvuvi kwenye uvuvi wa bahari kuu badala ya utaratibu wa sasa wa kutoa leseni kwa makampuni hayo ya nje kutoka China, Hispania, Seychelles, Taiwan, Ufaransa na Mauritania. Serikali haipati mapato ya kutosha kwa utaratibu huu kuliko kama tungeingia nao ubia. Msumbiji wanafanya hivyo na wamekuwa na mapato mazuri. Wanayo matatizo mengi ya jinsi walivyotumia fedha zao kununulia meli za uvuvi lakini hiyo ni tofauti na mpango wa ubia ninaoushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kuliletea Taifa letu maendeleo ya kiuchmi. Miradi ya barabara ni muhimu sana katika kuleta maendeleo nchini. Kwa bahati mbaya sana katika hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 barabara muhimu kwenye Jimbo la Morogoro Kusini hazikupewa fedha za kutekelezea miundombinu hiyo muhimu. Barabara ya kutoka Bigwa - Kisaki tulishakubaliana kwenye bajeti ya miaka miwili ya nyuma kwamba barabara hiyo itapanuliwa na kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo ilikuwa igharamiwe ujenzi wake kwa kiwango cha lami na Marekani kwenye mpango wa MCC II, lakini kutokana na sababu za kisiasa Marekani ilisitisha utekelezaji wake. Serikali yetu ikathibitisha kwamba itachukua jukumu la kugharamia mradi huo muhimu kwa faida ya wananchi na kuahidi Bungeni kwamba ndani ya miaka mitano, Serikali itajenga barabara hiyo ya Bigwa - Kisaki kwa kiwango cha lami. Inasikitisha kuona huu ni mwaka wa tatu wa miaka mitano Serikali bado haijaanza kutekeleza mradi huu. Kinachofanyika ni matengenezo tu, hili halikubaliki, fedha zilizotengwa kwenye bajeti ni matengenezo kwenye barabara ya udongo na changarawe, naiomba Serikali itekeleze ahadi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Morogoro Kusini, tunashida sana na barabara za udongo na changarawe zinazowatesa wananchi hususani wakati wa mvua. Barabara ya kwenda Kongwa, barabara ya Mvua – Magogoni – Selembala, barabara ya Mtombozi – Lugeni – Nemele, barabara ya Kangazi – Mtombozi, barabara ya Konde - Mlono (kilometa 4.5), barabara ya Matombo shuleni - Tawa, Matombo – Uponda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Morogoro Kusini bado lina matatizo na mawasiliano ya simu. Haiwezekani katika karne hii, tunakuwa na wananchi kwenye vijiji vyetu vya Tanzania, haiwezekani kutumia simu zao kwa kukosa mtandao. Wengine inabidi wapande mitini ili kuzungumza na simu zao. Maeneo ya Kolero, Singisa, Bungu, Lugeni, Lusangalala, Uponda, Kasanga, Tandali na kadhalika wanahitaji huduma za simu hususani TTCL, Tigo, Airtel, Vodacom kilometa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Serikali itende haki kwa kugawa maendeleo kwa wananchi wetu sawa kwa sawa. Jimbo la Morogoro Kusini tunahitaji barabara za lami, fedha zinapotea nyingi kufanya matengenezo kwenye barabara za udongo kila mwaka, hiyo si sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada kubwa anazofanya katika kutuletea maendeleo katika nchi yetu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa jitihada kubwa anazofanya katika sekta hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwa kweli kumshukuru kwa dhati, kulikuwa na tatizo la muda mrefu la fidia ya watu wa Selembala katika Jimbo langu, fidia ambayo zaidi ya miaka minne tumekuwa tunahangaika nayo lakini kwake yeye amelifanikisha na wananchi wamelipwa jumla ya shilingi bilioni 3.3. Siyo pesa ndogo, amejitahidi namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto ndogo ndogo ambazo bado sekta hii tunaiomba itusaidie kupitia kwa Waziri. Moja, yapo maeneo katika Jimbo la Morogoro Kusini ambayo kwa kweli yanapewa maji ya visima, lakini hayastahili kunywa maji ya visima. Zipo sehemu za Sesenga na maeneo ya Kisaki, nashauri tuwe na mradi wa kupeleka maji ya bomba. Hili linawezekana kwa sababu tuna mito mikubwa tu ambayo ipo maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nitaliomba kwa Mheshimiwa Waziri ni kuangalia uwezekano wa kuwa na mradi ndani ya Jimbo lile wa kueneza mabomba ya maji, yachukue kutoka kwenye vyanzo vya mito ili wananchi wapate maji safi na ya uhakika, tuachane na visima. Yapo maeneo kweli yanastahili visima lakini sio katika jimbo lile ambalo limezungukwa na mito mikubwa, sehemu nyingi hizo na details zake nitampatia Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu nitakaloomba kwa Waziri, atakapokuwa anangalia uwezekano wa kutengeneza miradi mikubwa ya namna hiyo, aone wataalam waliopo katika halmashauri zake. Halmashauri zetu wakati mwingine tunakosa kuwa na miradi mizuri kwa sababu ya kukosa watu wenye uwezo wa kubuni na hili ni suala la utaalam. Nitamuomba sana aliangalie kwa upande wa Morogoro Vijijini ili tuweze kuwa na wataalam wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, langu mimi kubwa ilikuwa nimshukuru Waziri amefanya jitihada kubwa sana, ahsante sana.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada kubwa anazofanya za kutuletea maendeleo nchini.

Mheshimiwa Spika, sekta ya maliasili na utalii ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Ni vyema Serikali ikaweka mipango yake vyema ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika kutokana na maliasili zilizopo nchini.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Morogoro Kusini lina mchango mkubwa katika kulinda na uhifadhi wa maliasili kama vile misitu ya asili, wanyamapori, hifadhi za taifa hususani Selous Game Reserve upande wa Kata ya Kisaki, mito ya maji na kadhalika. Yapo malalamiko makubwa ya baadhi ya wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini ambao kwa masikitiko makubwa mimea yao ya mpunga waliyolima kwenye maeneo ambayo baadae yametambulika kuwa ni ya hifadhi ya Taifa iliharibiwa kwa makusudi. Wananchi hawa waliomba waachiwe ili waweze kuvuna mpunga wao na baada ya hapo wasingelima tena maeneo hayo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, wakati mwingine wananchi waelekezwe na kuwasaidia wanapokosea. Pia yapo malalamiko ya mifugo ya ng’ombe kuteketezwa na askari wa hifadhi. Yupo mwananchi anayedai ng’ombe wake zaidi ya 200 kuteketezwa. Barua yake ya kukumbushia malalamiko hayo ya tukio lililodaiwa kutokea mwezi Aprili, 2015 nimeletewa nakala yake ambayo nimeikabidhi kwa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii hapa Bungeni jana tarehe 21 Mei, 2018. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kushughulikia malalamiko hayo na muhusika ajibiwe ipasavyo, kuendelea kukaa kimya si sahihi.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Morogoro Kusini lina maeneo mengi ya vivutio ambavyo vinaweza kutumika kuvutia watalii. Jiwe lenye umbo la matiti makubwa ya mama kwa lugha ya Kiluguru tunaita Matombo, jiwe hilo ndilo lililopelekea Tarafa nzima iitwe Matombo. Jiwe lile lipo, ninasikia ziwa lake moja limekatwa na mgeni mmoja aliyekuwa anakata mawe. Hii ni sehemu ya utamaduni na utalii, tuhakikishe historia kama hii inatunzwa na kutumika kuvutia watalii.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Bwakila Juu ipo nyumba aliyoishi chifu wa zamani wa Waluguru. Nyumba ile ingeweza kuwaleta watalii na wenye kufuatilia historia kuja na kuandika zaidi kuhusu taarifa za maisha ya chifu huyo. Barabara kutoka Bigwa hadi Kisaki ndiyo hiyo inayotumika na watalii kwenda kwenye Hifadhi ya Selous kupitia Morogoro. Miundombinu ya barabara hii si mizuri. Lazima tutambue umuhimu wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, TANAPA ni shirika muhimu katika kukuza na kuendeleza sekta hii ya maliasili na utalii. Misaada ya TANAPA kwa Jimbo la Morogoro Kusini bado inahitajika na kwa kweli bado haijaonekana kwa kiwango cha juu. Eneo lote la Kisaki, Sesenga na kadhalika TANAPA ingeweza kusaidia miradi yao ya maendeleo, maji, shule, barabara na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, mahusiano kati ya wananchi na askari wa hifadhi sharti yawe mazuri kwa ustawi mzuri wa nchi yetu. Naomba Serikali isimamie ili kuhakikisha wananchi wanatendewa haki.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote anayotutendea sisi viumbe wake hapa duniani. Hata tunayopitia hivi sasa ya COVID-19 ni matakwa yake yeye Mola wetu, tunamuomba atuepushe na janga hilo la kimataifa na kutupatia hali ya furaha, amani na upendo, Amen.

Mheshimiwa Spika, nampongeza kiongozi wetu wa nchi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuongoza vema wananchi wake na kuletea maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita ya uongozi wake. Miradi mikubwa mikubwa ya maendeleo imeandaliwa na kuanza kutekelezwa. mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge railway), ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, ununuzi wa ndege nane na ya tisa inakuja kwa ajili ya shirika letu la ndege (Air Tanzania), ujenzi wa Hospitali za Wilaya kwa nchi nzima, ujenzi wa Vituo vya Afya nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Morogoro Kusini tumenufaika kwa kupata Hospitali ya Wilaya inayojengwa Mvuha, vituo vitatu vya afya kwenye Kata za Duthumi, Kisemu na Kisaki. Ujenzi wa majengo yote matano kwa kila kituo katika vituo viwili vya afya vya Duthumi na Kisemu, vimekamilika. Tunasubiri vifaa na mashine zipelekwe pamoja na madaktari na wauguzi na wafanyakazi wengine ili vituo hivyo vianze kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Kisaki fedha zake za ujenzi zimekwishatolewa na Serikali, kwa kweli kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais mwenyewe alipotembelea Kisaki na maandalizi ya ujenzi umeshaanza. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa moyo wake wa huruma, upendo na kututhamini. Tunasema asante.

Napenda pia kumshukuru Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Janeth Magufuli, kwa upendo mkubwa alionao moyoni mwake kwa kutupatia baiskeli kumi kwa ajili ya watoto walemavu katika jimbo langu la Morogoro Kusini. Namshukuru sana mama yetu Mwenyezi Mungu amzidishie, Amen.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb), kwa hotuba yake nzuri aliyoiwasilisha hapa Bungeni kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kwa ufasaha na ustadi mkubwa mafanikio yaliyopatikana katika Awamu ya Tano chini ya kiongozi wetu mkuu, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kazi kubwa na nzuri umefanyika, hongera sana.

Mheshimiwa Spika, nakupongeza wewe binafsi na wasaidizi wako kwa kutuletea Bungeni maendeleo ya kidijitali. Mheshimiwa Spika umekuwa mstari wa mbele kwenye mabadiliko haya ya kisayansi ndani ya Bunge la Tanzania lakini pia umekuwa mfano wa kuigwa wa kuimarisha mahusiano mazuri kati ya Bunge na mihili mingine miwili hapa nchini; Serikali na Mahakama. Kuwepo kwa mahusiano haya mazuri kati ya mihimili yetu mitatu hapa nchini kunatuletea uhakika wa kuwepo maendeleo, amani na ufanisi mzuri katika jamii yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeelezea mambo mengi yanayomgusa kila mwananchi. Mvua zinazonyesha kwa nguvu nchini kote jimboni kwangu imeleta madhara makubwa kwenye miundombinu ya barabara, mashamba na nyumba za wananchi. Kwa bahati mbaya mafuriko haya kwenye maeneo kama Kata ya Selembala huwaibua mamba wanaotoka Mto wa Mvuha na kuwadhuru wananchi. Mwanafunzi wa miaka kumi na moja anayeitwa Rahma Ramadhani Nemelagani wa darasa la nne wa shule ya Msingi Kiganila aliuawa kwa kuliwa na mamba. Mwenyezi Mungu amuweke mahala pema peponi, Amen.

Mheshimiwa Spika, barabara yetu ya Bigwa - Mvuha - Kisaki kujengwa kwa kiwango cha lami, Serikali inasubiri nini? Naomba tuanze kujenga. Barabara za ndani la Jimbo la Morogoro Kusini ambazo ndizo zinakwenda kwa wananchi vijijini kwenye mashamba zimeharibiwa na mvua. Tunaomba Serikali itusaidie fedha za kutengeneza barabara hizi kwa kiwango cha kustahimili mvua hizi. Pengine wakati umefika sasa Serikali ifanye tathmini kama gharama za kila mwaka za kuweka vifusi vya udongo katika baadhi ya barabara zetu za vijijini kuna tija ikilinganishwa na gharama ya mara moja ya kuweka lami.

Mheshimiwa Spika, janga la COVID-19 Wabunge wenzangu wameeleza na Serikali imetoa maelezo muhimu ya jinsi ya kujikinga. Mungu azidi kutusimamia. Ni ugonjwa hatari. Niombe tu jamii yetu kutopuuza maelekezo yanayotolewa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuheshimu na kutii masharti ya quarantine. Wanaoambukizwa ugonjwa huu sio kwa makusudi hivyo tusiwaone kama ni watu wahalifu bali wapelekwe hospitali na kwa kweli tunahitaji kuwaonesha upendo na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapate nafuu na kurudi kwenye afya zao za kawaida.

Mwisho, Jimbo la Morogoro Kusini linakumbushia ombi la kutupatia chuo cha ufundi - VETA na kinaweza kujengwa katika mojawapo ya Kata za Lundi, Duthumi au Kisaki. Vijana wengi wanamaliza masomo yao ya msingi na sekondari na wakipatiwa mafunzo hayo ya ufundi wataingia katika mfumo wa uchumi wa viwanda na kutoa mchango wao mkubwa. Naunga mkono hoja.