Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joseph Leonard Haule (10 total)

MHE. JOSEPH L. HAULE aliuza:-
Wanachi wa Mikumi upande mmoja wamebanwa na Hifadhi na upande wa pili ardhi kubwa wamepewa Wawekezaji ambao hawajafanya uendelezaji wowote katika mashamba ya Kisanga, Masanze, Tindiga na hiyo kupelekea wananchi kukosa ardhi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuirudisha ardhi hii kwa wananchi ili waweze kujiletea maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Jimbo la Mikumi ni miongoni mwa maeneo ambayo yana ardhi nzuri kwa kilimo na ambalo pia lina wakulima na wawekezaji wenye mashamba makubwa.
Mheshimiwa Spika, ili kuitwaa ardhi kwa yeyote ambaye ameshindwa kuiendeleza utaratibu ufuatao unapaswa kufuatwa:-
Mheshimiwa Spika, kwanza sheria inataka mmiliki apatiwe ilani ya ubatilisho ya siku 90 na mamlaka (Halmashauri) husika ambapo shamba lipo. Ilani hiyo inatakiwa kueleza masharti yaliyokiukwa na kwa nini miliki yake isifutwe. Vile vile muda huo unampa mmiliki muda wa kuwasilisha utetezi wake kwa mujibu wa kifungu cha 47, 48 na 49 cha Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999.
Pili, muda wa ilani ya ubatilisho utakapokuwa umekwisha mapendekezo ya ubatilisho yatatumwa kwa Kamishna ambapo kama Kamishna atakubaliana na sababu za mapendekezo ya ubatilisho, Kamishna atawasilisha mapendekezo kwa Waziri mwenye dhamana ambaye naye atawasilisha mapendekezo hayo kwa Mheshimiwa Rais na kumshauri afute miliki hiyo.
Mheshimiwa Spika, naishauri Halmashauri husika ifanya ukaguzi wa mashamba yote makubwa yaliyomo ndani ili yale yaliyokiuka sheria hatua zinazofuata zichukuliwe.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Serikali ilifanya tathmini na kuona umuhimu wa kujenga daraja kwenye Kata ya Ruhembe kwa shilingi milioni mia sita lakini mpaka sasa shilingi milioni 100 tu zimepelekwa kwenye Halmashauri ya Kilosa.
Je, ni lini kiasi cha shilingi milioni 500 kilichobakia kitapelekwa ili kukamilisha daraja hilo na kuwasaidia wananchi wa Ruhembe wanaozunguka umbali mrefu ili kupata mahitaji yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zilizoidhinishwa na Serikali katika bajeti ya mwaka 2014/2015, kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Ruhembe zilikuwa ni shilingi milioni 300 fedha zilizopokelewa hadi Juni, 2015 zilikuwa shilingi milioni 100 ambazo zilitumika kwa ajili ya usanifu wa ujenzi wa daraja hilo. Mkandarasi aliyeomba fedha hizo anahitaji shilingi milioni 600 na hivyo kusababisha mradi huo kutotekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, zimetengwa shilingi milioni 700 ambazo zitatumika kujenga daraja hilo na kuchonga njia inayounganisha daraja hilo.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Kilio kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji kimekuwa ni cha muda mrefu sana kwa Wilaya ya Kilosa, lakini pia Jimbo la Mikumi, Kata za Tindiga, Kilangali na Mabwegere jambo linalosababisha wakulima kushindwa kwenda mashambani.
Je, ni lini Serikali itakomesha migogoro hiyo isiyo na tija kwa ustawi wa Taifa letu?
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kata za Tindiga na Kilangali, inatokana na wakulima kukinga maji ya Mto Miyombo kwa ajili ya umwagiliaji na hivyo kusababisha yasitiririke na kuikosesha mifugo maji. Aidha, mipaka ya vijiji vya Kiduhi na Kilangali haijawekwa bayana kiasi cha kufanya mifugo kushindwa kupita kwenda kwenye maji. Chanzo cha mgogoro wa kijiji cha wafugaji cha Mabwegere ni vijiji jirani kutotambua mipaka ya kijiji hicho.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya maji kwa mifugo katika Kata za Tindiga na Kilangali kwa kuanzia katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imetenga fedha kwa ajili ya kuchimba lambo katika kijiji cha Kiduhi, Kata ya Kilangali.
Mheshimiwa Spika, jitihada mbalimbali zimefanyika katika kushughulikia migogoro ya Mabwegere hadi kuhusisha mahakama. Kwa sasa suala hili linashughulikiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo Waziri mwenye dhamana kwa mamlaka aliyonayo kisheria amemteua Jaji wa Mahakama Kuu ili kufanya uchunguzi wa mgogoro wa Kijiji cha Mabwegere.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa tatizo la migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliandaa mkutano wa Wakuu wa Mikoa mwezi Julai 2016, kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kutenga maeneo ya malisho ya mifugo ikiwemo itakayotolewa kwenye mapori ya akiba na hifadhi. Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kufanya tathmini ya umiliki wa Ranchi za Taifa kwa lengo la kubaini maeneo ambayo hayatumiki kikamilifu ili wapewe wafugaji. Pia Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya tathmini ya Mapori ya Akiba na Hifadhi yaliyopoteza sifa ili yatumike kwa shughuli nyingine ikiwemo ufugaji, hii ni pamoja na kutambua kuwa mapori mengi tengefu ni ardhi za vijiji kwa mujibu wa sheria na hivyo kuendelea kuwa maeneo ya malisho. (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE Aliuliza:-
Mradi wa maji Madibira ulianzishwa mwaka 1975 na sasa miundombinu yake imechakaa sana na banio (intake) lake imekuwa dogo sana wakati idadi ya watu imeongezeka sana.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukarabati miundombinu hiyo ili kuwaokoa wananchi wa Mikumi na taabu ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikwishabaini changamoto zinazoukabili mradi wa maji wa Madibira unaotumiwa na wananchi wa Mikumi. Changamoto hizo kwa sehemu kubwa zinachangiwa na uchakavu wa miundombinu ya mradi pamoja na ongezeko la watu, hivyo kusababisha kiasi cha maji kinachozalishwa kutokidhi mahitaji ya maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali imechukua hatua za kutatua changamoto ya maji katika eneo la Mikumi, ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji chini ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji inatekeleza ujenzi wa mradi mpya wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 809.4, hadi kufikia Machi, 2017 mradi huo umekamilika kwa wastani wa asilimia 86 na unatarajiwa kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi Mei, 2017 kukamilika kwa mradi huo, kutaboresha hali ya huduma ya maji katika Mji wa Mikumi. Baada ya kukamilika kwa mradi huo mpya, Serikali itaanza pia kufanya ukarabati wa mradi wa maji wa Madibira ili kuuwezesha uendelee kutoa huduma ya maji katika Mji wa Mikumi.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Wanyama hasa Tembo wamekuwa wakiharibu sana mazao ya wananchi kwa fidia ndogo sana ya Sh. 20,000 kwa heka na hii hupunguza ushiriki wa wananchi katika kuzuia ujangili ndani ya Hifadhi:-
Je, Serikali imejipangaje kukaa vizuri na wananchi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ili kuwa na ushirikiano katika kuzuia ujangili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa maisha ya binadamu, mazao na mifugo imeweka utaratibu wa kulipa kifuta jasho na machozi kwa uharibifu unaosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia halmashauri zake za Wilaya na taasisi zilizo chini ya Wizara ya maliasili na utalii imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi na sheria zake ikwemo za kufukuza wanyamapori mara inapotokea wameingia katika makazi ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa uhifadhi kutoa elimu kwa wananchi juu ya kutumia pilipili na ufugaji wa nyuki kandokando ya mashamba ili kuzuia wanyama hususani tembo kuingia mashambani. Elimu hii ilianza kutolewa katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ili kufanya zoezi hili kuwa endelevu vikundi 23 vilisaidiwa kuanzisha Mfuko wa Kuweka na Kukopa na fedha wanayopata isaidie kununua baadhi ya vifaa vinavyotumika kuzuia wanyama kuingia mashambani pamoja na kuviwezesha vikundi kiuchumi ili visaidiwe katika kuzuia ujangili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya vikundi vilivyoanzishwa, kumi vimepata usajili toka halmashauri ya wilaya na vingine 13 bado vinaendelea kushughulikia usajili wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imetoa mizinga 180 kwa wananchi wa Kijiji cha Maharaka ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi katika kutekeleza maazimio ya kutumia pilipili na mizinga ya nyuki kuzuia tembo kuingia katika mashamba yao. Vilevile elimu inaendelea kutolewa katika Vijiji vya Mikumi, Mkata na Ihombwe ili nao kutumia mfumo wa pilipili katika mashamba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzishauri Halmashauri za Wilaya kuajiri Askari Wanyamapori na kuwapatia vitendea kazi ili waweze kusaidia wananchi pale kunapojitokeza tatizo la uharibifu wa mazao na mifugo kuvamiwa na wanyamapori.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Kumekuwa na migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na wananchi kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi hizo kama vile Ruhembe, Kitete, Kikwalaza, Mji Mpya, Ihambwe, Mululu na sasa Kitongoji cha Lugawilo, Kata ya Uleling’ombe:-
Je, ni lini Serikali itaweka mipaka ili wananchi hao wasiendelee kunyang’anjywa ardhi yao kwa kisingizio cha kuwa wameingia kwenye Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hakuna mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Taifa Mikumi na Vijiji vya Ruhembe na Ihambwe wala na Vitongoji vya Kikwalaza na Mji mpya ambavyo vimepakana na Hifadhi ya Taifa Mikumi. Mgogoro uliokuwepo ulishughulikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilosa, Viongozi wa Hifadhi, Viongozi wa Vijiji na wajumbe wane kutoka kila kijiji. Uhakiki wa mpaka wakati wa usuluhishi wa migogoro hiyo ulisimamiwa na viongozi wa Ardhi wa Mji Mdogo Mikumi, wataalam wa Ardhi Wilaya ya Kilosa, Mshauri wa Ardhi Mkoa wa Morogoro na wataalamu wa mipaka wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kufuatia utatuzi huo, eneo la mpaka unaotenganisha vijiji na hifadhi, ulifwekwa na vigingi vya kudumu (beacons) kuwekwa pamoja na vibao vya kuonesha mpaka wa hifadhi katika baadhi ya maeneo. Vilevile hifadhi imeendelea kusafisha mpaka wake na vijiji vyote kila Mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Mikumi haina mgogoro wa mpaka na Kijiji cha Kitete Msindazi, kwani mpaka uliobainishwa na Tangazo la Serikali Na.121 la mwaka 1975 ulitafsiriwa ardhini kwa usahihi na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo uliridhiwa na pande zote husika zilishirikishwa katika uhakiki wa mpaka huo ambao ni viongozi wa vijiji na Hifadhi ya Mikumi chini ya usimamizi ya Kamati ya Ulinzi wa Usalama ya Wilaya ya Kilosa. Hata hivyo, lipo eneo la ardhi (general land) ambalo siyo sehemu ya hifadhi wala kijiji kati ya mpaka wa hifadhi na Kijiji cha Kitete Msindazi. Kisheria eneo hilo liko chini wa Kamishna wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mikumi na Kitongoji cha Lugawilo, Kata ya Uleling’ombe kwa kuwa hifadhi haipakani na kijiji chochote cha Kata ya Uleling’ombe. Aidha, naomba Mheshimiwa Mbunge atakapopata nafasi atembelee Hifadhi ya Taifa Mikumi kupata uhalisia wa kile kinachofanyika.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-

Jimbo la Mikumi linaitwa Jimbo la giza kutokana na kata zake nyingi kutokuwa na umeme, kama Kata ya Ulaya, Zombo, Tindiga, Mhenda, Kilangali, Vidunda na kadhalika:-

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Jimbo hilo ambalo limebarikiwa kuwa na Mbuga za Wanyama na vivutio kadha wa kadha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mikumi lina vijiji 57, kati ya vijiji hivyo vijiji 16 vina umeme. Katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2021, vijiji 41 ambavyo havijafikiwa na umeme katika Jimbo la Mikumi vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoendelea sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Mikumi kwa sasa inafanyika katika vijiji nane vya Ihombwe, Kwalukwambe, Vidunda, Madizini, Zombolumbo, Malui, Udung’hu na Kigunga. Kazi za kupeleka umeme katika vijiji hivyo vinahusisha ujenzi wa kilomita 26 za njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 na kilometa 32 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4, ufungaji wa transfoma 16 na kuunganishia umeme wateja wa awali 533 na gharama za mradi ni shilingi bilioni mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Tatu, mzunguko wa kwanza katika Jimbo la Mikumi pamoja na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla ulianza mwezi Julai, 2018 ambapo Kampuni ya State Grid Electical and Technical Works Ltd. inatarajia kukamilisha kazi hizo mwezi Juni, 2019. Vijiji vilivyobaki 33 vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu unaotarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2020/2021.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-

Jimbo la Mikumi lina uhaba mkubwa wa Vituo vya Afya na hata pale ambapo kuna Kituo, basi dawa na Wataalamu ni tatizo:-

Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo hilo sugu la uhaba wa Vituo vya Afya na dawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ina jumla ya vituo vya afya vitano. Kati ya vituo hivyo viwili vipo katika Jimbo la Mikumi ambavyo ni Kituo cha Afya Kidodi na Ulaya. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Kituo cha Afya cha Kidodi kilipatiwa jumla ya shilingi milioni 400 za ukarabati na kwa sasa kinatoa huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito. Vilevile Kituo cha Afya Kidodi kimepatiwa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 95 ili kukiwezesha kuanza kutoa huduma. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 zahanati ya Mikumi ilipewa jumla ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuongeza majengo ili iweze kukidhi vigezo vya kupandishwa hadhi kwa Kituo cha Afya na mpaka sasa kazi ya ujenzi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wa Kata ya Malolo inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya Malolo kwa kutumia mapato ya ndani ambapo ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo la upasuaji na wodi ya wazazi yapo katika hatua ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 1.07 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi. Vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi Februari, 2019 Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imepokea shilingi milini 849 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na 2017/2018 Serikali iliajiri jumla ya wataalam wa afya 8,238 ambapo Halmashauri ya Kilosa ilipata jumla ya wataalam 42 wa kada mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kujenga vituo vya afya kote nchini pamoja na kuajiri wataalam wa afya kulinga na upatikanaji wa rasilimali fedha.
MHE. CONCHESTER RWAMLAZA (K.n.y MHE. JOSEPH L. HAULE) aliuliza:-

Aliyekuwa Waziri wa Maji, Mheshimiwa Eng, Isack Kamwelwe, alitembelea chanzo cha maji cha Sigaleti kilichopo Kata ya Ruaha ambacho kimepimwa na kuthibitishwa na Wataalam wa Idara ya Maji kwamba, kina maji mengi na salama na kinaweza kuhudumia ipasavyo Kata za Ruaha, Kidodi na Ruhembe. Na kwamba, zinatakiwa shilingi bilioni 2 ili maji hayo yaweze kupatikana kwenye kata hizo:-

Je, Serikali ipo tayari kutenga kiasi cha fedha kwenye bajeti, ili kuokoa maisha ya wananchi zaidi ya 35,000?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata za Ruaha, Kododi na Ruhembe ni miongoni mwa kata 18 zilizopo katika Jimbo la Mikumi. Upatikanaji wa huduma ya maji katika Jimbo hilo umefikia asilimia 68.

Mheshimiwa Spika, Kata za Ruaha, Kidodi n Ruhembe zina jumla ya vijiji 12, hata hivyo vijiji vinane tayari vimejengewa miundombinu ya miradi ya bomba; aidha vijiji vinne katika Kata ya Ruhembe vinatumia visima vifupi vilivyofungwa pampu za mkono, hivyo uboershaji wa huduma ya maji katika kata hizo bado ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wakazi na kukua kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, ni kweli chanzo cha maji cha Mto Sigaleti ni miongoni mwa vyanzo vya maji vinavyopendekezwa kutumika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Mikumi, zikiwemo kata hizo. Baada ya kupata makisio ya awali ya kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo, kwa sasa Wizara yangu inafanya mapitio ya kina ya usanifu na alama na tayari kiasi cha shilingi milioni 658 kimetengwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafuta umiliki wa mashamba pori ya muda mrefu ya Mauzi Estate, Miyombo Estate, Sumagro Estate Kisanga Estate (Lyori Estate) yaliyopo kwenye kata za Tindiga, Masanze, Kilangali na Kisanga na kuyagawa kwa wananchi wanyonge ili waweze kupata maeneo hayo wanayoyahitaji sana ili kufanya shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wote wa ardhi nchini ambao wameendelea kukiuka masharti ya kumiliki ardhi ikiwemo kutoendeleza ardhi kwa mujibu wa sheria na taratibu; kuendeleza ardhi kinyume na masharti ya umiliki; na kutolipa kodi ya pango la ardhi.

Kwa upande wa mashamba, katika kipindi cha kuanzia Disemba, 2015 mpaka sasa, jumla ya milki za mashamba 45 zimebatilishwa katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa Mkoa wa Morogoro, jumla ya mashamba 15 yamebatilishwa ambapo mashamba 10 kati ya hayo yapo katika Wilaya ya Kilosa anapotoka Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliunda timu ya kupitia mashamba yote yaliyobatilishwa katika Mkoa wa Morogoro pamoja na kukagua mashamba yenye sifa za kubatilishwa. Mashamba ya Mauzi Estates, Sumagro Estates, Kisanga Estates na Miyombo ni miongoni mwa mashamba ambayo timu yangu iliweza kuyakagua na hatua za ubatilisho wa milki zinaendelea. Jumla ya mashamba yaliyokaguliwa na kupendekezwa kubatilishwa ndani ya Mkoa wa Morogoro ni 23 na yote yapo katika Wilaya ya Kilosa. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeelekezwa kufanya taratibu za ubatilisho kwa mashamba hayo haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambazo zimebaini kuwepo kwa mashamba yasiyoendelezwa katika maeneo yao, kuwasilisha Wizarani mapendekezo ya kubatilisha milki za mashamba husika ili taratibu za kuyabatilisha zikamilishwe kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (Sura113).