Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Leonard Haule (40 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Waziri wa Elimu, lakini kuna baadhi ya wasaidizi wake wanamwangusha sana. Kwa mfano, VETA Mikumi imefanya jambo baya sana kwa wananchi wa Jimbo la Mikumi, kwani VETA-Mikumi wakishirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) wameanzisha utaratibu mbaya sana na unawanyima haki wananchi wanyonge kwa sababu wananchi wanaambiwa ili mtoto aweze kupokelewa kuingia VETA - Mikumi ni lazima awe na kadi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekasirika sana na wako mbioni kuandamana kudai haki yao ya msingi ya kujiunga na Chuo hiko cha VETA – Mikumi, kwani mpaka sasa fomu zote za VETA zinagawiwa na makada wa Chama cha Mapinduzi na kuwanyima fursa wananchi wengine wa vyama vingine na hata wale wasiokuwa na vyama. Maana tunavyojua, Vyuo vya VETA siyo mali ya CCM bali ni vyuo vya umma na vinatakiwa kutoa fursa sawa kwa wananchi wote bila kuangalia itikadi zao, dini wala makabila yao. Cha msingi wawe wamekidhi vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka na utendaji wa kazi wa Mheshimiwa Waziri kwa wananchi. Naomba sana atakapokuja kuhitimisha atoe karipio kali kabisa kwa VETA - Mikumi na wasitishe zoezi wanalolifanya mara moja na watupe majibu ni nani aliyewatuma kunyanyasa wananchi kwa kuwabagua kwa vyama vyao? Mwisho wale waliohusika na zoezi hili, wawajibishwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waziri hatatoa majibu ya kueleweka, nakusudia kushika shilingi ya mshahara wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Awali ya yote nashukuru sana kwa ziara za Mheshimiwa Rais, Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji katika Jimbo letu la Mikumi. Natumaini mmezisikia changamoto za watu wa Mikumi kuhusu maji na ninashukuru sana baadhi ya changamoto hizo zimepata ufumbuzi. Baada ya kutoa shukrani hizo, naomba nichangie changamoto kadhaa za muhimu Jimboni Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mradi wa Maji wa Madibira, huu ni mradi wa muda mrefu sana tangu mwaka 1974 hadi 1975 na miundombinu yake imechakaa sana. Nashukuru Serikali imetenga shilingi 300,000,000 ili kukarabati na kutanua intake pamoja na upanuzi wa mitandao ya kuunganisha wateja. Ila nasikitika kuwa karibu mwaka mmoja sasa mzabuni amepatikana ila bado hajapewa kibali cha kuanza kazi kutoka Wizarani. Tunaomba sana apatiwe kibali ili aanze kazi hiyo ya kukarabati miundombinu mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Sigaleti (Kata ya Ruaha); chanzo hiki cha maji kilifanyiwa usanifu na wataalam wa maji wa Wilaya ya Kilosa baada ya kuagizwa na Mheshimiwa Waziri ambaye alifanya ziara Jimboni Mikumi mwaka 2017. Wataalam walijiridhisha kuwa chanzo hiki kina maji mengi na salama na uhakika na pia yanaweza kusaidia sana wananchi wa kata kubwa ya Ruaha yenye wakazi 35,000 pamoja na kata za jirani za Kidodi, Vidunda na Ruhembe. Pia wataalam walifanya tathmini kuwa kiasi cha shilingi bilioni mbili kinatakiwa ili kufanya mradi huu uweze kuhudumia wananchi hawa wanaoteseka na tayari tathmini hiyo nilishaikabidhi kwa Waziri husika. Tunaomba sana mradi huu uweze kuingizwa katika bajeti ya mwaka huu ili kumtua mama wa Ruaha ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Bwawa la Dachi (Kata ya Malolo); bwawa hili ni muhimu sana kwa umwagiliaji katika Kata ya Malolo, mradi huu ulifadhiliwa na JICA ya Japani kwa fedha shilingi 600,000,000 ili kujenga makingio ya mchanga unaotishia kuupoteza kabisa Mto Mwega unaotumiwa sana na kutegemewa sana na wananchi wa Kata ya Malolo kwa kilimo. Kumetokea ubadhirifu mkubwa sana wa fedha hizo na makingio yaliyojengwa yamejengwa chini ya kiwango na kusababisha mchanga kuendelea kumwagika kutoka milimani na kwenda kujaza Mto Mwega. Nilishawahi kuomba Serikali iingilie kati na Mheshimiwa Waziri aliahidi kulifuatilia jambo hili, lakini naona hakuna majibu mpaka sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha atuambie amefikia wapi na tunaomba sana Wizara iweze kuingilia kati na kusikia kilio hiki cha muda mrefu sana cha wananchi wa Kata ya Malolo kwani tegemeo lao la kilimo linategemea sana Mto huu wa Mwega.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana tusaidiwe visima virefu katika Jimbo la Mikumi kwani tumekuwa tukisahauliwa sana katika uchimbaji wa visima virefu hasa katika kata za Ruhembe, Vidunda, Mhenda, Tindiga, Zombo, Malolo, Uleling’ombe, Kisanga, Mabwerebwere, Kilangali, Mikumi, Ruaha, Kidodi, Masanze na Ulaya. Tunaomba sana kata hizi za Jimbo la Mikumi zifikiriwe kwa jicho la huruma maana wananchi wetu inafika mahali wana-share kunywa maji kwenye mito na wanyama kitu ambacho kinahatarisha sana afya zao na magonjwa ya maambukizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mikumi tumebarikiwa kuwa na vyanzo vingi sana vya maji. Mwisho kabisa niiombe sana Wizara itume wataalam wake kwenye Jimbo la Mikumi kwa kuwa pamoja na taabu na changamoto kubwa sana ya maji tunayokabiliana nayo lakini Jimbo la Mikumi limebarikiwa vyanzo vingi sana vya maji ambavyo vingeweza kumaliza kabisa kero ya maji.

Mhshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu la Mikumi tunaomba sana wataalam waje kuviangalia vyanzo vifuatavyo; Mto Iyovi, Mto Simbalambende na Kisanga. Natumaini tukifanikiwa kuvitumia vyanzo hivi tutakuwa kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kumtua mama ndoo kichwani. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii nyeti na muhimu kwa Taifa letu, Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia, ningeomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi na uwezo huu lakini niwashukuru sana wananchi wa Mikumi kwa kuweza kuniamini na kunikopesha kura zao, nawaahidi nitawalipa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzo kabisa naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole sana ndugu zangu wa Kilosa ambao siku mbili zilizopita tumepata maafa makubwa ya mafuriko. Wenzetu wawili wamefariki dunia, Mungu awalaze mahali pema peponi lakini pia familia nyingi zimetaabika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie hapo hapo ni kwamba katika Wilaya ya Kilosa imekuwa kama ni kawaida sasa hivi ikifika kipindi cha mvua basi mafuriko yanakuwa ni lazima. Hii imesababisha kuleta matatizo makubwa. Hivi ninavyozungumza mpaka sasa Watanzania wenzetu 4,765 wameathirika na mafuriko hayo, kaya zilizoathirika ni 1,238, nyumba 144 zimebomoka kabisa na heka za mashamba 3,707 zimeharibika kabisa na wenzetu wapo kwenye hali mbaya sana. Pia visima 18 vimeharibika kabisa, kwa hiyo, wenzetu wanapata taabu ya maji na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, imekuwa kama kawaida kwa kule Kilosa ambapo inaonekana tatizo kubwa ni miundombinu ya barabara, madaraja pamoja na kingo za mito ambazo zinazidiwa na maji. Sasa hivi tunapozungumza ile barabara ya Mikumi - Kilosa ya kilometa 78 haipitiki kabisa. Ukitaka kutoka Mikumi kwenda Kilosa inabidi uzunguke mpaka Morogoro, ufike Dumila halafu ndiyo uelekee Kilosa kitu ambacho kinaleta taabu sana kwa wananchi wengi wa Jimbo la Mikumi. Taarifa hii tumeileta Ofisi ya Waziri Mkuu na imeahidi kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ombi kubwa katika Kata ya Masanze tatizo kubwa ya mafuriko haya yaliyoleta maafa makubwa yamesababishwa na tuta la Mto Miyombo ambalo kila siku mvua zikinyesha zimekuwa zikileta taabu sana katika maeneo yale. Kwa Kilosa kwa ujumla wake Bwawa la Kidete ambalo limekuwa likimwaga maji kwenda pale Kilosa limekuwa likileta matatizo sana na ndiyo maana unaona kila mwaka tunakuwa na kazi ya kukarabati reli maeneo ya Godegode na Fulwe ambapo kila siku imekuwa ikisombwa na haya maji. Kwa Kata ya Tindiga kingo za Mto Mkondoa ndiyo zimebomoka na kuleta athari kubwa sana kwa wananchi wetu wa Kata ya Tindiga.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Serikali tujaribu sana kuboresha miundombinu hii ili tuache kupiga zile kelele za kuomba misaada kila siku. Mwezi wa kwanza tu hapa nilimuomba Mheshimiwa Waziri, Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama akatusaidia tani 200 na sasa hivi tena tumeleta maombi tusaidiwe tani 100, tutakuwa tukiomba hivi mpaka lini? Tunaomba tutafute solution, tuangalie jinsi ya kukarabati mito au miundombinu hiyo. Nawaomba sana mngeiwezesha Wizara ya Mazingira kwa kuuboresha Mfuko wa Mazingira ili uweze kutumika katika kuboresha vitu kama hivyo. Vinginevyo kila siku tutakuwa tukilia ndugu zetu wanakufa na tunapeana pole.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kata ya Ruhembe tumekuwa tukipiga kelele kuhusu kuvuka Daraja la Ruhembe ambapo ndugu zetu wamekuwa wakitaabika. Ndilo hilo daraja ambalo kuna mwalimu mmoja ambaye ni Afisa Elimu amefariki dunia kwa sababu alikuwa anataka kumuokoa kijana aliyekuwa anabebwa na maji. Serikali ilishafanya upembuzi yakinifu wa daraja lile, ni daraja muhimu na la msingi, naomba itengeneze daraja hili ili kuokoa Watanzania wa Kata ya Ruhembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nataka niongelee kuhusu utawala bora. Utawala bora ni pamoja na ushirikishwaji, uwazi na uwajibikaji. Tumekuwa kila siku tukisema na kupiga kelele tukiwaomba Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji watusaidie kwenye kampeni mbalimbali kwa sababu wenyewe ndiyo wanahusika na wananchi moja kwa moja. Mfano suala la elimu bure wahusika wa kwanza ni Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji. Tumekuwa tukiomba walipwe posho lakini imekuwa ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi sasa hivi imefika kipindi viongozi wetu wa Serikali katika Wilaya zetu, mfano sisi Kilosa kuna Mkuu wa Wilaya ya Kilosa amekuwa akiingilia sana madaraka ya Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji kiasi kwamba amewafanya wakae na woga na kuwa na hofu kubwa. Hapa napozungumza Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuyuni amesimamishwa na ofisi imefungwa na hili suala nililipeleka kwa Waziri wa TAMISEMI. Pia Mkuu wa Wilaya amefungia shimo la mchanga la Ruaha na kutisha kijiji cha Ruaha na kusema kwamba atauondoa uongozi wa Ruaha ni kwa sababu tu za kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Ruaha ina vijiji vinne na vyote vimechukuliwa na CHADEMA, huo ndio ukweli. Ina vitongoji 21 na vitongoji 20 vimechukuliwa na CHADEMA, huo ndio ukweli na Diwani ni wa CHADEMA. Sasa msitake kuzuia haya maendeleo ya watu wa Ruaha kwa sababu tu za kiitikadi. Siku zote mmekuwa mkituomba tuonyeshe ushirikiano na tuwe pamoja lakini mnapokuwa mnanyanyasa viongozi wa vitongoji na vijiji inatuwia vigumu kuweza kupata yale maendeleo ambayo tumekusudia kuyapata. Ili kuboresha suala la utawala bora tuendelee kushirikiana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ameenda mbali zaidi, nilimuomba ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kuja kutusaidia kule kwa wakulima wa miwa ambapo aliingilia uozo uliokuwa unaendelea katika chama cha RCGA. Kwa sababu alisoma ripoti ya Tume iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya ilikuwa ikisema kwamba ule uongozi haufai, Mheshimiwa Mwigulu kwa ujasiri na kuwapenda Watanzania aliuondoa ule uongozi na kuweka uongozi mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotustaajabisha ni kwamba yule Mkuu wa Wilaya anapinga maamuzi ya bosi wake yaani anasema Waziri alikurupuka…
MHE. JOSEPH L. HAULE: Anasema Waziri alifanya haya mambo bila kumshirikisha. Mkuu wa Wilaya ni nani mbele ya Waziri wake? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri ripoti hiyo ndiyo ipo vile, wakulima wale wa miwa wanakushukuru sana kwa sababu hata bei ya miwa imepanda kutoka 72,000 mpaka 79,000. Sasa hivi inavyoonekana hata percentage ya kuingiza miwa imepanda kutoka asilimia 45 kwenda asilimia 60 yaani wakulima wa nje wanaingiza asilimia 60 na wenye kiwanda wamekubali asilimia 40. Haya yote ni matunda ya wewe kutembelea kule lakini Mkuu wa Wilaya anataka kukukwamisha anasema wewe ni jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niende mbali zaidi, Mheshimiwa Mwigulu umeonyesha ushirikiano mzuri na kweli umeonyesha kwamba sio mzalendo wa tai bali ni mzalendo kutoka moyoni, nakupongeza sana ndugu yangu.
Nimshauri tu Ndugu yangu Mheshimiwa Nape kwa sababu Mheshimiwa Mwigulu alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Tawala na anafanya haya mambo kwa ajili ya Watanzania basi na wewe kwa sababu ulikuwa Mwenezi hebu achia TBC ionekane wazi na Watanzania waweze kukuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye suala la afya. Suala hili kwenye Wilaya yetu ya Kilosa limekuwa ni zito kwani hospitali yetu ya Wilaya imekuwa na taabu nyingi, dawa zinachelewa kufika, tunapoomba dawa MSD zinachelewa na nyingine hawana kabisa na malipo yanakuwa yameshafanyika hatuwezi kupata dawa nyingine. Kitu ambacho kimetuumiza ni kwamba tumekosa misamaha ya kodi. Hospitali ya Kilosa iliagiza ambulance na kuiomba Serikali isamehe kodi ili waweze kuingiza ambulance ile lakini Serikali ilikataa kutoa kodi hiyo kwa kitu ambacho kingeweza kuwasaidia Watanzania wenzetu kule. Watanzania wanataabika na wanahitaji msaada mkubwa, inapofika sehemu tunaagiza vifaa tiba vya hospitali za Serikali ambazo zinakimbiliwa sana na Watanzania walalahoi basi tuangalie uwezekano wa kuweza kuwasaidia Watanzania kwa kuruhusu na kusamehe kodi zile. Kwa Kilosa haijafanyika hivyo na hili limekuwa ni pigo kubwa sana kwa sababu Hospitali ya Kilosa inahudumia wananchi wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi katika Zahanati ya Mikumi, zahanati ile ni kama haipo. Nilipoongea na Daktari wa zahanati ile ameniambia ile zahanati ipo lakini kama haipo. Tunategemea Hospitali ya St. Kizito ambayo ni ya private, ni ya mission na inapewa milioni sitini kwa mwaka lakini bado walalahoi wanashindwa ku-afford gharama za matibabu pale. Naomba Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aweze kuboresha Hospitali ya Mikumi ili walalahoi wajisikie kwamba ni hospitali yao na waweze kutibiwa kwa bei rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Hospitali ya St. Kizito kuna kaya maskini ambazo zinapata msaada lakini imeonekana zikienda pale zinakuwa charged kwa pesa nyingi, maskini mnamsaidia kwa kumpa chakula inakuwaje unamuomba hela za dawa? Mtengenezee hospitali yake ya pale Mikumi ili aweze kwenda akajisikia yupo kwake. Pale kwenye Zahanati ya Mikumi sasa hivi hata kupima malaria ni shida na watu wanalalamika, tumewashawishi sana waingie kwenye mfuko wa afya lakini wakienda pale hata kupima inakuwa ni shida wanaambiwa kapime dirisha lile kachukue dawa dirisha lile as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihamie kwenye suala la elimu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niweke yangu tena ya muhimu katika hoja hii iliyopo mezani ya bajeti ya Wizara muhimu na uti wa mgongo ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze na suala zima la VETA-Mikumi. Kwa kuwa Chuo cha VETA - Mikumi ndiyo chuo pekee kilichopo katika Jimbo la Mikumi na kwa kuwa ukombozi wa vijana wengi wanaohitimu shule za sekondari zilizopo Jimboni kila mwaka hukosa mwelekeo, hivyo ni muhimu kukipa kipaumbele chuo hicho kwa kukiboresha katika maeneo yafuatayo:-
(i) Kupanua wigo katika fani zinazotolewa ili ziendane na mazingira ya Jimboni, kuongeza fani ya ufundi-kilimo (agro-mechanics);
(ii) Kukiongezea uwezo wa udahili kwa kuongeza idadi ya mabweni hasa kwa ajili ya wasichana ili kuendana na sera ya kuleta uwiano katika udahili kati ya wasichana na wavulana;
(iii) Kuongeza idadi ya madarasa na karakana za kujifunzia, pia kupanua wigo wa mafunzo kwa vitendo; na
(iv) Kuongeza na kuboresha vifaa vya kujifunzia ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kuwajengea vijana uwezo wa kitaalamu unaoendana na mabadiliko yanayotokea sokoni kila wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite kwenye changamoto zinazoikabili VETA-Mikumi kama ifuatavyo:-
(i) Baadhi ya watumishi kukaa muda mrefu sana bila kuhamishwa, wapo waliokaa zaidi ya miaka 20, hii inaathiri sana utendaji wa kazi kwa kuwa wanafanya kazi kwa mazoea na ufanisi kupungua;
(ii) Kuna upendeleo katika udahili hasa katika chaguo la pili hivyo kupelekea aidha ndugu wa viongozi au watu wao wa karibu kujaza nafasi hizo huku wananchi wazawa wa Mikumi wakikosa fursa hiyo. Katika udahili mwaka wa masomo 2016, wananchi wa Mikumi waliopata fursa ni asilimia 10 tu ingawa tunatambua kuwa usaili huwa unajumuisha waombaji kutoka kila kona ya nchi lakini vijana wa Mikumi walipaswa kupewa kipaumbele hasa katika chaguo la pili;
(iii) Kuwepo kwa uongozi usiofuata tararibu, kanuni za utumishi wa umma na utawala bora. Uongozi wenye mfumo kandamizi usiokubali kufanya kazi na watu waadilifu, uongozi unaofanya ubadhirifu na maamuzi yasiyokuwa na tija kwa VETA na Taifa kwa ujumla;
(iv) Chuo kimepeleka mini-bus kwa matengenezo Dar es Salaam zaidi ya wiki moja katika gereji bubu katika kipindi cha mwezi Mei 2016 bila kufuata taratibu za manunuzi. Pia kukiuka maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka magari yote ya umma kwa matengenezo TEMESA;
(v) Uongozi wa chuo (Afisa Rasilimali Watu na Mkuu wa Chuo) kuwa na mtandao mpana kuanzia VETA-Makao Makuu wa kuwakataa, kuwapinga na kuwahamisha watumishi wanaonekana kutokubaliana na mawazo yao ya kibadhirifu.
Kwa mfano Salum Ulimwengu (Mratibu Mafunzo) aliyekaa kwa kipindi cha miaka miwili na kuhamishiwa Arusha baada ya kuvutana na menejimenti baada ya Mkuu wa Chuo kukiuzia chuo gari bovu lililokuwa likimilikiwa na rafiki yake, pamoja na ununuzi wa spea hewa za magari ya mafunzo. Suala hili lilichunguzwa na ofisi ya CAG na hakuna ripoti yoyote iliyotoka. Hata hivyo, uuzwaji wa gari hilo haukuhusisha ofisi ya Afisa Mafunzo ila Kitengo cha Ufundi magari bila kufuata taratibu za mamlaka;
(vi) Kukataa kumpokea na kushindwa kumkabidhi ofisi Mratibu wa Mafunzo kwa kipindi cha mwaka mzima kinyume cha section 3.13 ya VETA Staff Regulations and Conditions of Service ambayo inatamka kuwa mabadiliko yoyote ya kiutumishi lazima yafanyike kwa makabidhiano ya kimaandishi (Rejea Internal Audit Report VETA- Mikumi, March- December 2014);
(vii) Mkuu wa Chuo na Afisa Rasilimali Watu kushinikiza uhamisho ili kulinda wizi wa mali za umma na ubadhirifu. Mfano mwingine, Msuya (Stores Officer) aliyekaa kwa kipindi cha mwezi mmoja na kupelekwa Morogoro. Joseph Riganya (Stores Officer) aliyevutana na uongozi wa chuo na kuhamishiwa Ofisi ya Kanda kwa kisingizio cha matibabu. Riganya alipinga ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi na ubadhirifu katika manunuzi unaofanywa na Mkuu wa Chuo na Afisa Rasilimali Watu; mfano katika ripoti ya ukaguzi wa ndani (internal Audit report) ya Machi hadi Desemba 2016 inaonyesha kuwa Afisa Rasilimali Watu, Mhasibu na Mwalimu mmoja walipokea vifaa vya thamani ya shilingi milioni 35 kinyume na taratibu kwani Kamati ya Mapokezi ndiyo yenye dhamana ya kupokea vifaa hivyo. Walifanya hivyo ili kulinda maslahi yao binafsi;
(viii) Ukiukwaji wa taratibu za ajira kwa kumpa mkataba Neema Bui ambaye hana sifa na anafanya kazi za manunuzi kwa maslahi ya Mkuu wa Chuo na Afisa Rasilimali Watu kwa kuwa kila Afisa Manunuzi anayeletwa anaondolewa kwa hila ili asizibe mianya ya wizi; na
(ix) Afisa Manunuzi Rogate aliyehamishiwa mwezi Februari 2016 kutoka Tabora amepewa vitisho kwenye kikao cha menejimenti na sasa anafanya mpango wa kuhama kuwapisha wanaojiita wenye chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuwasimamisha kazi Afisa Rasilimali Watu na Mkuu wa Chuo ili kupisha uchunguzi;
(ii) Kuwahamisha watumishi waliokaa muda mrefu sana katika chuo hiki ambao ndiyo chanzo cha kulea ubadhirifu;
(iii) Kuangalia kama ilikuwa halali kumhamisha Afisa Mafunzo, Ndugu Salum Ulimwengu aliyekaa kwa kipindi cha miaka miwili na ambaye amehamishwa mwezi mmoja tu tangu amhamishe mke wake katika Sekondari ya Mikumi, hivyo mtu aliyepigania maslahi ya Taifa kuteswa kisaikolojia na kifamilia;
(iv) Kufanya uchunguzi maalumu juu ya masuala ya manunuzi na fedha katika chuo cha VETA-Mikumi; na
(v) Kufuatilia ilipoishia ripoti ya CAG ya Oktoba 2015 juu ya Mkuu wa Chuo kukiuzia chuo gari chakavu kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee suala zima la elimu bure ambapo kumekuwa na changamoto nyingi kama ifuatayo:-
(i) Ruzuku inayotoka Serikalini ya kila mwezi haikidhi mahitaji ya shule mfano mpaka sasa Walimu Wakuu hawana fungu la mlinzi, umeme na maji;
(ii) Idadi kubwa ya wanafunzi ukilinganisha na Walimu, madarasa na miundombinu mingine kuna vyoo, madawati na kadhalika;
(iii) Huduma ya chakula shuleni irudishwe ili kuhamasisha watoto waende shule; (iv) Upungufu mkubwa wa Walimu wa sayansi kwenye Jimbo la Mikumi;
(v) Walimu kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu na pia wengi kuchelewa kupandishwa madaraja; na
(vi) Hakuna nyumba za Walimu na pia hawalipwi posho za uhamisho na pesa zao za likizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni baadhi tu ya changamoto nyingi za elimu kwenye Jimbo la Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia machache katika hoja hii iliyo mezani inayohusu Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa tumekuwa tukipanga mikakati mingi na kujinasibu kwamba tunataka kuipeleka nchi yetu kwenda kwenye uchumi wa kati ili tuweze kuipata Tanzania ya viwanda, wakati tunasahau kuwa hatuwezi kuwa na nchi ya viwanda nchi nzima kama bado tuna tatizo sugu na kubwa la nishati ya umeme katika sehemu zetu nyingi za vijijini ambako ndiko tunataka na tunapaswa kupeleka viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tutakuwa tunafanya kazi bure kama hatutaweka mkakati wa dhati huku tukisukumwa na dhamira ya mioyo yetu ya kufufua sekta ya kilimo. Yatupasa kuwekeza zaidi kwenye kilimo mfano, pamba, kahawa, korosho, miwa na kadhalika ili tuweze kutimiza dhamira yetu ya kuipata Tanzania ya viwanda ambayo pia itatusaidia kutoa ajira kwa watu wetu na kuongeza kipato kwa wakulima wetu na kujiletea maendelea ya nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumekuwa kila siku tukisema tunataka kufufua viwanda ambavyo vimekufa lakini hatutaki kusema ni nini kimeua viwanda vyetu. Mfano Mkoa wetu wa Morogoro ulikuwa ni moja ya mikoa iliyoshamiri kwa viwanda kadha wa kadha ambavyo sasa vimebinafsishwa, vingine vimeshakufa kabisa na kuwa mabanda ya kufugia mbuzi na kuku na vingine vipo njiani kufa maana kama ni mgonjwa basi yupo ICU anapumulia mipira kupata hewa na ndugu wapo mbioni kuzima mashine yenyewe ya kupumulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana kwa niaba ya wananchi wa Mkoa mzima wa Morogoro, Mheshimiwa Waziri kabla ya kusema ni vipi atafufua hivi viwanda, pia atuambie hali halisi ya viwanda vyetu vya Mkoa wa Morogoro ambavyo vilikuwa vinatoa fursa ya ajira kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Morogoro. Mfano, nataka kujua viwanda vyetu vya Mang’ula Mechanical and Machine Tools Limited (MMMT), Morogoro Canvas Mill Limited, Tobacco Processing Factory na MOPROCO vipo kwenye hali gani na vinasaidia nini kwenye ubinafsishaji uliofanyika na kama vina tija kwa Taifa letu. Pia kwenye Jimbo langu la Mikumi kuna kiwanda cha Kilombero Sugar Company Ltd. ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa sukari lakini kilibinafsishwa Aprili mwaka 1998 kwa Kampuni ya ILLOVO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuwasisitiza wakulima wa Wilaya ya Kilosa walime miwa na kuacha kulima mpunga na mahindi lakini wakulima hao wa miwa wamekuwa wakilalamika sana kunyonywa kuhusu idadi ya asilimia ya miwa inayoingizwa kwenye kiwanda hicho cha ILLOVO. Lakini pia wakiwa na malalamiko mengi ya upimaji wa utamu wa miwa hiyo (sucrose) na pia mabaki ya miwa hiyo (buggers) ambayo ni mabaki ya miwa yamekuwa yakitengeneza umeme na pia kuna morales ambayo inatengenezea pombe kali (spirits) lakini wakulima wamekuwa hawalipwi zaidi ya tani za utamu wa sukari tu ambapo sasa ndani ya kiwanda cha ILLOVO pia kuna kiwanda kingine cha kuzalisha pombe na bado wanasema kiwanda kinapata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kupata sukari ya kutosha kama hatutaweka mazingira mazuri na salama kwa wakulima wa miwa. Wakulima wa miwa wa nje wanataabika sana na wanayonywa sana na wanahitaji sana msaada wa Serikali kuwasaidia wakulima wao wapate mzani wao wa uhakika ili waweze kupima na kuingiza miwa yao kwa haki badala ya sasa kuwekewa mzani wasiouamini. Wapimaji ndio hao hao wenye kiwanda ambao pia ndio wanaopanga bei ya zao hilo, nasisitiza na naomba sana Serikali ifanye mpango wa kuwaletea wakulima mzani ili wapate haki yao na kufutwa machozi yao ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko makubwa sana ya wafanyakazi wa Kiwanda cha ILLOVO ambapo kumekuwa na mateso na unyanyasaji mkubwa sana wa wafanyakazi wa ngazi ya chini wa kiwanda hicho. Nakushauri siku moja uende pamoja na mimi kwenye Kiwanda cha ILLOVO ili tukasikilize kilio cha wafanyakazi wao na ninakuomba usiende kuonana na uongozi wa kiwanda bali tuonane na viongozi wa vyama vya wafanyakazi au wafanyakazi wenyewe ambao wamekuwa kama watumwa ndani ya ardhi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, lakini pia kumekuwa na malalamiko makubwa ya ajira za kindugu, ajira za kirafiki na ajira za rushwa ya ngono. Vyeo vinapandishwa kwa upendeleo mkubwa, lakini mbaya zaidi ni mishahara midogo sana ambapo Kampuni ya Sukari Kilombero (ILLOVO) imekuwa ikiwadanganya wafanyakazi kwamba wanapata hasara pindi linapokuja suala la majadiliano ya mishahara ingawa ukweli ni kwamba hakuna mwaka waliopata hasara bali ndiyo kwanza wanaendelea kuongeza kiwanda kingine cha tatu cha pombe, pamoja na ununuzi wa vifaa vyote vya usafiri kama magari, pikipiki ambavyo kila mtu akitumia kwa miaka mitatu tu viongozi hao wanauziwa kwa shilingi 100,000 tu.
Hii ni kama ile kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa John Magufuli, ni kwamba viongozi wa Kampuni ya ILLOVO wanaishi kama malaika na wafanyakazi wa chini ambao kimsingi wamekuwa wakifanya kazi ngumu kwa jasho na damu wanaishi kama mashetani. Sasa kuna wafanyakazi wa kigeni 23 pale ILLOVO, wakati wafanyakazi wa kigeni hawakutakiwa kuzidi wafanyakazi watano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo kubwa sana la wafanayakazi zaidi ya 2000 waliokuwa wanafanya kazi kwenye kiwanda cha Kilombero Sugar Company, kwa masikitiko makubwa sana nataka nipate majibu ni lini watatendewa haki zao na kulipwa mafao yao kama wanavyostahili kwa kupitia mkataba wao na mwajiri Na. 4/1995 ambapo walilipwa miezi kumi badala ya miezi 40 kadri ya Kifungu Na. 10.3.7 kinachohusu upunguzwaji kwenye mkataba huo wa hali bora za wafanyakazi, hivyo basi walipunjwa kiasi cha miezi 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri aje na majibu ya hoja hii ya msingi sana ambapo pia wafanyakazi hao walifutiwa malipo ya utumishi ya muda mrefu kama wanavyostahili kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na malalamiko mengi sana juu ya vipimo vya kazi kwa wafanyakazi wanaofanya kazi za vipimo. Sera waliyonayo ni kuhakikisha wanawapa vipimo vikubwa ili wasiweze kumudu kumaliza, hivyo kwao inawasaidia kubana matumizi kwani mfanyakazi asipomaliza kipimo kile alichopewa hawezi kulipwa hata kama kazi imebaki robo. Huu ni utumwa wa kiwango cha juu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inabidi ilifuatilie kwa kina na kuchunguza makampuni haya ya sukari yenye mashamba kwani wananchi hawa wanateseka sana. Serikali inaweza kufurahia kwamba wananchi wanapata ajira kumbe wamo utumwani ndani ya ardhi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ningeiomba Serikali ituambie ni lini itaanza kujenga viwanda vya kusindika viazi ambapo kilimo hicho cha viazi kimeshamiri sana katika Kata ya Kisanga ambapo tumebarikiwa kulima viazi kwa msimu mzima kwa wingi kushinda hata Gairo. Na pia napenda kuishauri Bodi ya Sukari itimize wajibu wake wa kuhakikisha inasimamia haki stahiki za wakulima wa miwa kuanzia kwenye mikataba yao dhidi ya makampuni ya sukari na wamiliki wa viwanda maana kwa sasa unyonyaji umezidi kwa wakulima wa miwa na kilio chao kikubwa ni kuwa na mzani wa kupimia sukari unaomilikiwa na wakulima wenyewe, tofauti na sasa ambapo mwenye kiwanda ndiye anayemiliki mizani hiyo na kuleta malalamiko ya miwa mingi kutupwa kwa kukosa ubora na utamu wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Waziri aje na majibu, ni tani ngapi za wakulima maskini zimeshatupwa mpaka sasa na ni hasara gani ambayo wakulima wameipata mpaka sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niongeze kidogo kwenye mchango wangu niliowasilisha jana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri wa Ujenzi aipe barabara ya Ruaha Mbuyuni - Mlolo (Chabi) - Ibanda - Mlunga - Ileling‟ombe mpaka Mpwapwa ya kilometa 74 ambapo inaunganisha Wilaya mbili za Kilosa na Mpwapwa. Hii inamaanisha kuwa inaunganisha mikoa ya Iringa, Morogoro na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mfuko wa Barabara wa Mkoa wa Morogoro walifanya tathmini na kuipitisha barabara hii kuwa chini ya TANROADS na pia waliwaalika wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi ambao nao waliipitisha na kusema inafaa kufanyiwa kazi haraka sana kadri inavyowezekana. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri akija ku-wind up aje atupe majibu, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hii ili kuunganisha wananchi hawa wa mikoa ya Dodoma na Morogoro na Iringa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Moja kwa moja nianze mchango wangu nikiuelekeza kwenye kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kata ya Malolo ambao wapo kwenye Jimbo la Mikumi wakilalamikia fidia yao ya uharibifu mkubwa sana wa mazao na mashamba yao uliosababishwa na kupasuka kwa bomba kubwa la mafuta ya TAZAMA Pipeline.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2011 bomba la TAZAMA lilipasuka na kusababisha hasara kubwa sana siyo tu kwa mazao bali zaidi kwenye afya za wananchi wa Kata hiyo ya Malolo hasa kwenye Vijiji vya Mgogozi, Chabi, Malolo „A‟, Malolo „B‟ na maeneo mengine yaliyozungukwa na bomba hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na wataalam walikuja kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea na walikubaliana na wananchi wa Kata ya Malolo kuwa watalipwa fidia ya sh. 320,000,000/= kwa madhara hayo. Tofauti na walivyokubaliana, wananchi wakaambiwa na Halmashauri ya Kilosa kuwa watalipwa sh. 50,000,000/=. Sasa wananchi wa Malolo wanataka kujua ni lini watalipwa sh. 320,000,000/= zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Malolo kwa masikitiko makubwa sana wanaiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi iwape majibu, ni lini itawafuta machozi yao kwa kuwalipa haki yao hii muhimu ya fidia hii ambayo hawajalipwa tangu mwaka 2011?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, napenda sana kuchangia kuhusu mradi huu wa REA. Inasikitisha sana kuona Jimbo la Mikumi halijaguswa kabisa kwenye mradi wa REA I na REA II na sasa tunaingia kwenye REA III tukiwa na sintofahamu kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mikumi limebatizwa jina na sasa kuitwa Jimbo la giza kwa sababu ya vijiji vingi sana vya Jimboni Mikumi kukosa umeme. Nilishaandika na kuipeleka barua kwa Mkurugenzi wa REA na kumwelezea hali halisi ya Jimbo langu la Mikumi lakini pia baada ya kuuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini ambaye naye alinijibu kwamba atahakikisha mradi wa REA III vijiji vyangu vya Jimbo la Mikumi vyote vitaingizwa kwenye mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Waziri akija kwenye majumuisho yake atuambie ni lini vijiji vifuatavyo vya kwenye Jimbo langu la Mikumi vitapata umeme?
(1) Kata ya Maloo – Vijiji vya Mgogozi, Malolo A & B, Chabi, Itipi;
(2) Kata ya Vidunda – Vijiji vya Vidunda, Udungu na Chonwe, Itembe;
(3) Kata ya Uleling‟ombe – Vijiji vya Uleling‟ombe, Mlunga, Lengewaha;
(4) Vijiji vya Mhenda – Vijiji vya Mhenda, Kitundueta, Ilakala, Maili 30;
5. Kata ya Masanze – Vijiji vya Munisagara, Chabima, Dodoma Isanga;
6. Kata ya Tindiga – Vijiji vya Malui, Tindiga, Kwalukwambe, Malangali;
7. Kata ya Ulaya – Vijiji vya Nyameni, Mbuyuni, Kibaoni, Ng‟ole, Nyalanda;
8. Kata ya Kilangali – Vijiji vya Mbamba, Kiduhi;
9. Kata ya Mikumi – Vijiji vya Ihombwe, Tambuka Reli, Msimba;
10. Kata ya Zombo – Vijiji vya Kigunga, Madudunizi, Nyali, Zombo; na
11. Kata ya Ruhembe – Kijiji cha Kielezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nijielekeze moja kwa moja kwenye migogoro mbalimbali iliyopo katika Jimbo langu la Mikumi ambapo pamoja na mimi mwenyewe kuileta kwenye Ofisi ya Waziri wa Ardhi mkono kwa mkono lakini cha kusikitisha ni kuwa sio tu kwamba haijaorodheshwa kwenye kitabu cha Waziri alicholeta na kukigawa kwa Wabunge, lakini pia migogoro hiyo haijatajwa kabisa mahali popote.
Naomba Mheshimiwa Waziri akija kwenye majumuisho anipe majibu ni lini na ni nini hatma ya migogoro hii ya ardhi na mashamba pori yafuatayo ambayo yapo kwenye Jimbo la Mikumi na kusababisha Watanzania wenzetu wazalendo kukosa ardhi na nyingi kupewa wanaoitwa wawekezaji ambao wameyafanya mashamba pori na mengine kuyabadilisha matumizi.
(i) Kata ya Mikumi - mgogoro kati ya wananchi wa Kitongoji cha Vikweme na JWTZ na wananchi wa Kikwalaza na Hifadhi.
(ii) Kata ya Ruhembe – mgogoro wa wananchi wa Kitete Msindazi na Hifadhi; wananchi wa Ruhembe na Hifadhi; wananchi wa Kielezo na Hifadhi na wananchi wa kijiji cha Kidogobasi na wavamizi wa ekari 98.
(iii) Kata ya Kilangali - mgogoro wa muda mrefu kati ya Kijiji cha Kilangali na Kijiji cha Tindiga; mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Mbamba na Kijiji cha Kiduhi ni wa muda mrefu sana; mgogoro wa kijiji cha Kilangali na Shamba la Mbegu la ASSA, huu nao ni wa muda mrefu sana na mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye Kata nzima ya Kilangali.
(iv) Kata ya Uleling‟ombe - kuna mgogoro mkubwa sana kati ya wananchi wa Uleling‟ombe na Msitu wa Ukwiva ambapo eneo hili lilihamishwa mpaka mwaka 1972 na wananchi wanaomba warudishiwe mpaka wa zamami (awali) wa mwaka 1957 ili wapate maeneo ya kulima na kujiletea maendeleo.
(v) Kata ya Ulaya - mgogoro wa ardhi kati ya Basso Masumin na Serikali ya Kijiji cha Ng‟ole; mgogoro wa ardhi kati ya wafugaji na wakulima wa Kijiji cha Mbuyuni; mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Mbamba; mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Ulaya Kibaoni, mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Mhenda na mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ng‟ole na Nyalanda.
(vi) Mgogoro mkubwa wa shimo la mchanga kati ya Kata ya Ruaha na Kata ya Ruhembe (Kijiji cha Kitete).
(vii) Mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Kitundueta (Mhenda) na Kijiji cha Ihombwe kilichopo Mikumi.
(viii) Kata ya Kidodi - mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji cha Lumango na hifadhi.
(ix) Kata ya Tindiga - mgogoro mkubwa sana na unaopoteza maisha ya Watanzania wengi sana kati ya wakulima na wafugaji na umedumu kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda Mheshimwa Waziri atuambie ni lini mashamba makubwa yaliyotelekezwa na wanaoitwa wawekezaji yatarudishwa kwa wananchi. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ilileta orodha ya mashamba pori 38 kwenye ofisi ya Waziri wa Ardhi bila mafanikio. Baadhi ya mashamba hayo ni:-
(i) Kata ya Kilangali - shamba Na.120 la Kivungu.
(ii) Kata ya Kisanga - shamba la SAS (Kisanga).
(iii) Kata ya Masanze - shamba la Miyombo; shamba la Dodoma Isanga na shamba la Changarawe.
(iv) Kata ya Ulaya - shamba la Ulaya.
(v) Kata ya Tindiga - shamba la Sumagro.
(vi) Kata ya Ulaya - shamba la Nyaranda
(vii) Shamba la Kilosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu kilicholetwa na Mheshimiwa Waziri hakina takwimu shahihi ukilinganisha na hali za mashamba pori hayo yaliyopo Jimboni Mikumi. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aje mwenyewe Jimboni Mikumi ili ashuhudie mapori makubwa yasiyoendelezwa wala kulimwa kama ambavyo amepewa taarifa na kusababisha wananchi wengi kukosa sehemu za kujiletea maendeleo na kuleta tija na maendeleo kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza sana naomba Mheshimiwa Waziri anipe ahadi ya kwenda pamoja na mimi Jimboni Mikumi ili akajionee mwenyewe. Ahsante sana, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Maliasili na Utalii maana ukizungumzia Jimbo la Mikumi moja kwa moja unazungumzia masuala haya muhimu ya utalii na maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa niongelee jinsi ambavyo wananchi wa Mikumi wamekuwa wakilia kutokana na jinsi ambavyo wanabanwa na migogoro mbalimbali ambayo inasababishwa na kuongezwa mara kwa mara kwa mipaka ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana wananchi wa Jimbo la Mikumi waliokuwa wakiishi katika maeneo ya Kipogoga pamoja na Mgoda walihamishwa mwaka 1963 na kupelekwa kwenye Vijiji vipya vya Vikweme, Rwembe maeneo ya Tindiga na sehemu nyingine. Hiyo ilisaidia kuifanya hifadhi ya Mikumi iweze kuanza mwaka 1963, lakini sasa hivi mipaka hiyo imeonekana kuwa inaongezwa na sasa hivi wananchi wamefuatwa kwenye vijijji, kwa mfano Kijiji cha Vikweme wanaambiwa tena waondoke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Vikweme wamekuwa na kilio cha muda mrefu sana ambapo upande mmoja wanakabwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na sasa hivi wameambiwa wahame maeneo yale kwa sababu ni ya Jeshi, lakini upande wa pili Hifadhi ya Mikumi inasema ni eneo lao, mnataka wananchi hao wa Mikumi waende maeneo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wazee ninaozungumza wamehamishwa mwaka 63 ni pamoja na akina mzee Leonard Haule ambaye tulimzika mwaka 1981, ambaye ni babu yangu. Wazee mwenzake akina mzee Mbegani mpaka leo wamekuwa wakitaabika na wakiililia Serikali kwamba mnataka waende wapi wakati wenyewe ndiyo watu wa Mikumi wazawa waliokuwa pale?.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na migogoro mingi kutokana na hifadhi kuongeza mipaka katika maeneo mengine kama ya Uledi, Ng‟ombe ambapo inaonekana kuna heka karibu 200 za wakazi wa Lugawilo ambao hifadhi pia imesema huu mpaka ni mpya. Wananchi wa huku wamekuwa wakilia kwa muda mrefu wakiitaka Serikali iweze kurudisha ule mpaka wa zamani wa mwaka 1957 uliokuwa ukiwawezesha kupata ardhi ya kulima na kujenga nyumba zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi kama wa Vikwema, Kitete Msindazi, maeneo ya Mululu, maeneo ya Msange pamoja na maeneo ya Lumango wameonekana kuwa wanataabika kwa sababu wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara na watu wa hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna suala la buffer zone. Eneo la Buffer Zone limekuwa likiongezeka kila siku. Eneo hili wananchi hawatakiwi kuingia kabisa. Mama zetu wamekuwa wakipigwa kwa sababu ya kuingia kuokota kuni kwenye maeneo haya. Ndugu zetu wamekuwa wanataabika na sasa tumesema kuwa Mikumi mpya ya Profesa J. tunataka haya mambo yakome na tuweze kukaa chini na wananchi ili tuweze kusuluhisha. (Makofi)
Mheshimwia Mwenyekiti, tunapozungumzia masuala ya hifadhi tunazungumzia ujirani mwema. Hapo zamani sisi tulipokuwa tunakua tulikuwa tunaingia kwenye mbuga ya wanyama ya Mikumi kwenda kuona wanyama, lakini pia tukicheza michezo pamoja na Maaskari wa Wanyamapori na vitu vingine kama hivyo. Pia walikuwa wakitusaidia kujenga zahanati, shule na wanafunzi walikuwa wakibadilishana uwezo. Sasa hivi kumekuwa na uadui mkubwa kati ya watu wanaokaa katika vijiji vinavyopakana na hifadhi na wahifadhi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiongelea suala la ujirani mwema kwa sababu tunasema wananchi kama watathaminiwa watapewa thamani wanaostahili na fidia lakini pia watashirikishwa kwenye mambo mbalimbali, hii itawasaidia sana kulinda rasilimali zetu na wanyama wetu. Kwa hiyo, tunataka tusisitize suala la ujirani mwema ili tuweze kuwatumia wananchi kuweza kulinda wanyama wetu na rasilimali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa style hii mnayosema kila siku kuna ujangili, wananchi wanawachukia tembo, wanawachukia askari wa wanyamapori na ndiyo wamewaweka kama maadui, kwa hiyo hata wakiona majangili wanaingia hawawezi kuwapa ripoti ndugu zangu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli mnataka tulinde rasilimali zetu, tuwape nafasi hiyo wananchi wa Tanzania tuwaoneshe umoja na ushirikiano, tuwaoneshe jinsi ya kucheza michezo ya pamoja; na kama inahitajika tuwape elimu ili wajue kitu gani cha kufanya na kipi sio cha kufanya, lakini sasa hivi ndugu zetu wanaokaa kwenye vijiji vinavyopakana na mbuga wameonekana kuwa wanateswa. Niwaambie tu Mikumi kuna watu wengine tumezika nguo kwa sababu hata maiti zao hatujaweza kuzipata kwa sababu wamepigwa risasi ndani ya hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kutokana na hilo tunataka tuisisitize Serikali kama kweli mnataka tulinde rasilimali za Mikumi tupunguze uadui huu kati wa wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi na watu wa hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tuzungumzie pia masuala ya tembo. Wanyama hawa sasa hivi imekuwa kama fashion kila mtu anayekaa karibu na hifadhi anazungumzia masuala ya tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa juzi, karibu wiki mbili katika kijiji kilicho katikati ya Kilosa na Mvomero kinachoitwa Mangae mtu mmoja ameuawa na tembo. Sasa ndugu zangu Serikali kila anapokufa mtu ndipo mnataka mje? Kila siku tunalia, tunapaza sauti ndugu wanakufa lakini hakuna linalochukuliwa lolote. Tunataka tuwaambie tunawapenda tembo, tunapenda ralisilimali zetu, tunaomba mtusikilize na sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wanalima mashamba makubwa ya mpunga, watu wanatumia hela nyingi, lakini tembo wanakula zile mali. Wananchi wanapata tabu, sasa hivi kuna mafuriko huko Mikumi, watu wana njaa, wanajitahidi kulima lakini tembo wanakula, Serikali imekaa kimya. Kuna Kata inaitwa Kilangali kila siku wimbo ni kuhusu tembo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, tunaomba watuangalie kwa jicho pevu, itafika kipindi hawa wananchi watachoka na tutaamua kufanya jambo litakalokuwa baya, watatuongeza kwenye magereza yao. (Makofi)
Mheshimimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kinatakiwa kusema ni kwamba, tunaangalia sana utaratibu wa kuwatunza tembo wetu lakini pia kuna suala la mamba, ambapo katika mto Mwega kwenye Kata ya Maloyo, mamba wameonekana kujeruhi sana ndugu zetu na watu wengine wamekufa. Kitu cha kustaajabisha ni kwamba, Halmashauri ya Kilosa imenunua bunduki mbili kwa ajili ya kuongezea nguvu kwenye maliasili, lakini cha ajabu ni kwamba mpaka leo wameshindwa kupata vibali kutoka mkoani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atumie nafasi hii. Halmashauri ya Kilosa imenunua bunduki, lakini vibali vinaonekana kupigwa chenga. Sasa tusije tukawafanya wananchi na sisi tukawaambia watumie mbinu mbadala ili kuweza kukabiliana na wanyama hao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa pale Mikumi tozo lote limeonekana kuwa linakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, wananchi wa Mikumi wamekuwa lonely, pesa ya pale haiwahusu, ni kama wamekaa kisiwani hata mbuga imekuwa kama sio mali yao tena. Tunataka wananchi wa Mikumi wasikie ownership, waone ile mbuga kama ni ya kwao, tuwashirikishe wakae pale wajione kwamba ile mbuga ni ya kwetu na sisi ni watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hivi kila kitu kinatolewa kinapelekwa Dar es Salaam, Mikumi hakuna kitu. Waheshimiwa Wabunge mnapita sana Mikumi pale mnaangalia wanyama mnapiga selfie, lakini mnashindwa kujua hata mnawasaidiaje wananchi wa Mikumi ambao mbuga ipo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Serikali iliangalie kwa jicho pevu mnawaachaje watu wa Mikumi? Maana imekuwa kama kisiwa, tunakuwa maskini wakati tumebarikiwa kuwa na mbuga nzuri ya wanyama ndugu zangu. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali tunataka tutengeneze kijiji cha makumbusho. Kama Zanzibar wameweza kuwa na mji mkongwe, watu wakishafanya utalii pale wanakaa tunacheza ngoma tunakula misosi, tunakula vyakula vya asili na kuuza vitu vyetu ambavyo vitakuwa pale Mikumi. Kwa hiyo tunataka tutengeneze kijiji cha makumbusho pale Mikumi wazungu na ninyi mkitoka mbugani kuzunguka mnaweza kuzunguka Mikumi ili ku- boost uchumi wa watu wa mikumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Wizara wanatuacha kama kisiwa, hakuna shughuli yoyote ya utalii inayoendelea Mikumi. Tena nimesikia wametenga bilioni moja ambazo zimeenda kwenye vijiji vinavyohusika na mbuga, kwa Mikumi sijasikia, mimi ndiye Mbunge lakini sijasikia hayo madawati sijui walimpa nani au hiyo michango imekuwaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipouliza kuhusu giving back kwenye society kuchangia vitu vingine wamesema sasa hivi hawataki kujadili kuhusu majengo, hospitali na vitu vingine bali wanataka sasa hivi kuweka hela inayozunguka zunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine. Kuna ile Mikumi Lodge ambayo ilikuwa pale Mikumi, ndiyo iliyokuwa tegemeo la watu wa Mikumi kwenda kutalii, lakini sasa hivi ile hoteli ilibinafsishwa tukasikia imechomwa moto. Nataka Waziri akirudi hapa aje atuambie nini mustakbali wa ile Mikumi Lodge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye barabara inayopita Mikumi ya kilomita 50, takwimu zinaonesha mnyama mmoja anagongwa kila siku, wanyama 956 wanagongwa kwa miaka mitano, tangu 2011 mpaka 2015 wamegongwa wanyama 956. Nataka Serikali ije na majibu ituambie wanataka kufanya jambo gani kuhusu kukomboa hawa wanyama wa Kitanzania na ina mpango gani na hawa wanyama ambao wanagongwa kila siku na wanawaona na takwimu wanazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumaliza na hayo, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niweze kuchangia kidogo katika hoja hii muhimu iliyokuwa mbele yetu. Kwanza na-declare, ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na nimeshiriki kikamilifu na nipongeze sana hotuba hii ya Kamati kwa asilimia zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya ziara kadhaa katika mashirika kadhaa ya umma lakini pia tuliweza kufanya ziara kadhaa katika makampuni hapa na pale ili kuangalia uwekezaji ambao taifa letu imefanya. Nishukuru sana Mashirika hayo aliyoonesha ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza nijikite moja kwa moja katika hoja iliyopo ambapo bado inaonekana kuna tatizo kubwa sana la kusaini mikataba ambayo taasisi zetu za umma zimekuwa zikifanya na wawekezaji mbalimbali. Mfano; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilisaini mkataba na kampuni kutoka Botswana inaitwa Mlimani GH na mkataba huo ni wa miaka 50 ambapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Serikali itakuwa inapata asilimia 10 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha jinsi gani ambavyo tumekuwa tukisaini mikataba hiyo, lakini pia inaonesha kwamba baada ya matumizi hayo na uwekezaji huo na Serikali kupata hiyo asilimia 10 baada ya miaka 50 ndiyo Serikali itakuja kunufaika na kupewa hayo majengo. Kwa mtaji huo tunarudi kule kule kwenye business as usual kwa sababu hakuna mtu ana guarantee kwamba Mlimani City kwenye miaka 50 ijayo itakuwa kwenye hali gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii inapelekea Taifa letu kukosa magawio, lakini pia imekuwa ikipata hasara kubwa na kushindwa kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali na mwisho wa siku kuleta mzigo mzito sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, moja kati ya Kamati ilipopitia na kuona, imeona kwamba mkataba kama huu uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umekuwa ni mkataba ambao ni mzigo mzito sana kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tangu sijawa Mbunge wa Mikumi, nilikuwa nikisikia mkataba uliokuwa ukiendelea kati ya TANESCO na IPTL, tunaweza kuona kwamba mkataba huu pia umeonekana kuwa mzigo mzito na sisi tulikuwa tukisikia katika Bunge la 2014, Novemba. Bunge hili liliamua kwamba ule mkataba usitishwe na zile mali ziweze kutaifishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri atakapokuja hapa tuweze kujua mkataba huo umeishia wapi kwa sababu umeonekana kuwa mzigo mzito sana kwa Watanzania, kwa sababu Tanzania inaonekana kulipa shilingi milioni 300 kwa IPTL. Kwa hiyo, inaonekanaka milioni 300 kwa siku, ni mzigo mkubwa sana kwa Taifa letu ambalo kila siku tunasema bado liko kwenye hali ya checheme checheme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hiyo, mashirika mengi ya umma yamekuwa yakiilalamikia Serikali, imekuwa ikiyapa madeni mazito, inakopa katika masuala haya ya msingi. Mfano, katika taasisi za umma kama TANESCO, inaidai Serikali pesa nyingi, lakini pia suala la maji safi na taka inadai pesa nyingi. Vile vile mifuko ya kijamii imekuwa ikidai pia pesa nyingi sana kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Juni 2016 imeonekana kwamba Serikali inadaiwa trilioni mbili nukta sita na PSPF. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi gani Serikali imekuwa ikipeleka mizigo mizito sana kwa hii mifuko ya kijamii ambayo sasa ili kuweza kututumka imeanza kupeleka hili gao la mafao sasa hivi watu wanaambiwa mpaka wafikishe miaka 55. Mpaka hapa ninavyoongea nimepigiwa simu na watu wangu wa Kilombero Sugar Company wananiambia walikuwa wakitaka kusaini na PPF kwenye fomu zao lakini wameambiwa wasubiri mpaka miaka 55. Huo ni mzigo mzito sana kwa Watanzania ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iweze kulipa madeni yake ambayo inadaiwa na taasisi zake. Hiyo nimetaja mfano tu wa PSPF lakini mifuko mingi ya kijamii inaonekana kukopwa na Serikali bila kulipwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, tunajaribu kuangalia migongano ya Sera na Sheria. TR ndiyo msimamizi wa mashirika yote ya umma lakini inaonekana mifuko hii ya kijamii inapotaka kwenda kufanya manunuzi au inapotaka kufanya michanganuo ya kujiendesha na kuweka uwekezaji imekuwa ikipata miongozo kutoka sehemu tofauti. Mara huku wanaambiwa na BOT, mara huku wanaitwa na SSRA miluzi mingi inampoteza mbwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifuko hii ya jamiii inaonekana kwamba inashindwa jinsi ya kwenda kwa sababu TR anakuwa hana taarifa rasmi za kuhusu uwekezaji unaotaka kufanyika kwa sababu viongozi wa sehemu mbalimbali wakiwemo BOT pamoja na SSRA wameonekana kuwa wakitoa miongozo tofauti kitu ambacho kinapelekea mashirika haya kwenda kununua bidhaa au kununua viwanja na ardhi kwa bei kubwa ambayo inapelekea mashirika haya yajenge nyumba kwa pesa nyingi ambazo mwisho wa siku Mtanzania maskini ndiyo anataabika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Shirika la Nyumba kama NHC linataka kujenga nyumba ambazo zitakuwa na uwezo na kumfanya mwananchi wa kawaida aweze kumudu lakini kwa gharama ambazo zipo hadi sisi Wabunge tunaanza ku-beep kwamba jinsi gani tunaweza tukanunua hizo nyumba hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo nyumba zinazosemwa za bei nafuu tumeenda kukagua juzi mradi wa NHC kule Chamazi ni hela nyingi sana ambayo kiukweli kwa maskini wa Kitanzania itakuwa ngumu sana kuweza kuchukua nyumba kama hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana pamoja na yote, lakini pia kwenye Bodi za Wakurugenzi wameonekana wakichaguliwa watu ambao hawana uwezo kiasi kwamba wanapeleka mashirika mengi kufa na mashirika mengine pia kuweza kuwa na watendaji ambao ni wabovu. Wakurugenzi wengi wanaoteuliwa wanateuliwa kirafikirafiki na wengine wanapewa ahsante ahsante, kitu ambacho kinapelekea mashirika yetu ya muhimu kwa Taifa letu kuweza kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Kwa hiyo tunashauri upatikanaji wa Watendaji hao uweze kufanyika kwa recruitment ili waweze kushindanishwa na wafanyiwe interview ili majina matatu yaweze kupelekwa kwenye mamlaka ambazo zinaweza kuteua mmoja atakayekuwa na tija na kusaidia mashirika yetu ya umma kwa ajili ya kwenda kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mambo mengine yanayosumbua ni pamoja na wanasiasa kuingilia mashirika haya ya umma ambayo mengine yanafanya biashara. Utasikia kuna miongozo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara fulani mara Naibu Waziri anasema hiki na hiki, fungu liende huku, kitu ambacho kinapelekea matatizo makubwa sana kwenye haya mashirika yetu ya umma na kufanya mengi yaweze ku-stuck na kushindwa kuendelea na kazi ambayo wamekuwa wakiifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nisisitize tunahitaji kuwaachia watendaji wetu wakuu ambao tumewapa madaraka na mamlaka ya kuweza kuongoza ili waweze kutupeleka kwenye sehemu nzuri itakayopeleka uwekezaji wenye tija kwa sababu tumeshuhudia sehemu mbalimbali watendaji hao walikuwa wanafanya kazi chini ya kiwango lakini tumeendelea kucheka na nyani na mwisho wake Tanzania inaendelea kuvuna mabua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu nitakapokuja hapa mtupe majibu jinsi gani ambavyo mtaweza kuwezesha Ofisi ya TR ili aweze kuwa na meno na nguvu ya kuweza kuyasimamia mashirika haya ambayo sasa hivi madaraka yake TR anaonekana kuwa ameporwa na sasa hivi anafanya kazi nusu nusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami niweze kuchangia kidogo kwenye Wizara hii nyeti ya Sheria na Katiba. Kumekuwa na malalamiko na kilio cha muda mrefu sana cha wafanyakazi walioachishwa kazi Kilombero Sugar Company mwaka 2,000. Wafanyakazi hao karibu 3,000 walipoachishwa kazi hawakulipwa stahiki zao na wamekuwa wakidai stahiki zao hizo kwa muda mrefu sana, wengine wameshatangulia mbele za haki na wengine bado wapo hai. Wafanyakazi hao walipoona hawatendewi haki walikwenda Mahakamani na kukawa na Jalada la Kesi Namba 50/2000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi hao wamekwenda mara kadhaa Wizara ya Katiba na Sheria wakiomba wapewe nakala ya hukumu ya jalada lao la kesi Namba 50/2000 bila mafanikio. Pia, waliandika barua kwa Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 24 Machi, 2016 na nakala kupelekwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye mnamo tarehe 25 Julai, 2016 (Kumb. Na. PM/P/1/569/82), Katibu wa Waziri Mkuu alijibu kuwa ameipata na ataisisitiza Wizara ya Katiba na Sheria ishughulikie kikamilifu kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwaka 2014 Mahakama Kuu iliwapatia tamko la kuvumilia na kwamba, walikuwa wakilifanyia kazi, mpaka sasa hakuna majibu. Ndipo walipoamua kulipeleka Wizara ya Katiba na Sheria mwezi Julai, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa niaba ya wafanyakazi walioachishwa kazi Kilombero Sugar Company 2000, namwomba Waziri atakapokuja kwenye majumuisho yake aje atupe majibu kwamba, ni lini sasa wananchi hao watapata haki yao ya kupata nakala ya hukumu ya kesi Namba 50/2000. Ni matumaini yangu mtawasaidia kilio cha wanyonge hawa, ili wapate haki yao ya kulipwa mafao yao wanayostahili ambayo wamekuwa wakiyapigania kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nichangie kidogo kwenye hoja hii iliyo mezani.
Kwanza kabisa ningependa kupata majibu ya Waziri, barabara ya Dumila – Rudewa - Kilosa – Mikumi ya kilomita 142 tu nashukuru imetengewa shilingi bilioni 5.207 ili kumaliza kipande cha Rudewa – Kilosa kilomita 18. Je, ni lini sasa Serikali itatenga pesa za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Kilosa – Mikumi kilomita 78 ambayo ni barabara iliyoahidiwa na Rais aliyepita Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Mheshimiwa Magufuli wakati wa kipindi chao cha Kampeni. Hii ni barabara muhimu sana ili iweze kusaidia Kata zaidi ya 10 na kukuza uchumi wa watu wa Mikumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba barabara ya Ruaha Mbuyuni – Mololo Chabi – Ibanda – Uleling’ombe ipandishwe hadhi lakini siioni katika mpango huu wa bajeti hii ya 2017/ 2018 na hii ni barabara inayounganisha Mikoa ya Iringa – Morogoro na Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia reli ya kutoka Kiwanda cha Sukari Kilombero – Kidatu mpaka Kilosa, ilikuwa inachangia sana kuboresha uchumi wa watu wa Mikumi na kuwaunganisha na reli ya kati. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufufua reli hii kama ilivyokuwa zamani ambapo pia kulikuwa na bandari kavu pale Mikumi ambayo ilikuwa inasaidia sana kukuza uchumi wa wananchi wa mikoani na wananchi wa Wilaya ya Kilosa kwa ujumla. Tunaiomba sana Serikali iturudishie bandari kavu ya Mikumi ili iweze kwenda na kasi ya maendeleo ya nchi yetu na kufikia uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kuhusu mawasiliano, Jimbo la Mikumi limekuwa na matatizo makubwa sana ya mawasiliano, mfano Kata za Vidunda, Uleling’ombe, Chabima, Munisagala, Mhenda, Chonwe, Udungu, Itembe, Tindiga, Malangali, Nyameni na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali ituletee mawasiliano ya simu kwenye vijiji hivi na vingine vingi Vya Jimbo la Mikumi ili wananchi nao wapate fursa ya kupata mawasiliano na kukuza biashara zao na kukuza uchumi wao kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii nyeti iliyopo mbele yetu. Kabla ya kuanza niwape pole sana Watanzania wenzangu wa Jiji la Arusha na Watanzania wote kwa ujumla kwa msiba huu mkubwa. Wananchi wa Mikumi tupo pamoja nanyi na tunaendelea kuwaombea marehemu walale mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia na- declare interest mimi ni Mwanamuziki, ni mwanamuziki bora kabisa wa hip hop Afrika Mashariki na kati na kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa hiyo hii Wizara inanihusu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, historia ya nchi yetu inaonesha tangu waasisi wa nchi hii walipokuwa wakifanya harakati kadha wa kadha walikuwa wakitumia sana sanaa. Nakumbuka Mwalimu Nyerere alikuwa akatumia wasanii mbalimbali akina Mzee Mwinamila, akina Mzee Moris Nyunyisa ambao mpaka leo midundo yao inatumika kwenye taarifa za habari huko TBC wakati anafanya harakati za ku-promote vijiji vya ujamaa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia akina Mzee Mkapa walikuwa wakitumia sana wanamuziki wa mashairi kama akina Mzee Tambalizeni na watu wengine kama hao. Inaonesha ni jinsi gani ambavyo sanaa ni kitu muhimu na ni nyenzo muhimu sana katika Taifa kuonesha utamaduni, kuonesha mila lakini pia kufikisha ujumbe kadha wa kadha. Tunajua kwamba sanaa inatumia sana mafundisho lakini pia inakanya, inaonya na inasifia inapobidi; lakini kwa sasa kwa siku za usoni imeonekana wasanii kadha wa kadha wameonekana kuwa wakibanwa kutoa yale mawazo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamependa kuwa wakisifiwa tu na wasanii wanapotoa mawazo mbadala wamekuwa wakipata rabsha kama ilivyotokea kwa msanii Roma ambaye ametekwa na akaja kuachiwa katika mazingira ya kutatanisha, lakini pia Msanii Ney wa Mitego ambaye alishikwa na baadaye akaja kutolewa kwa msamaha wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii inawapa hofu sana wasanii kuweza kutoa kile walichokuwa wanakifikiria kwa sababu tunaamini msanii yupo huru na anatakiwa kutoa mawazo huru katika kulisaidia Taifa letu. Hata sisi tulipokuwa tukifanya muziki tulikuwa tunaimba nyimbo kama ‘Ndiyo Mzee”, “Siyo Mzee” na vitu vingine wengi mnavijua, Mheshimiwa Waziri ulisema wewe ni shabiki wangu mkubwa, kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba mlikuwa mnajua jinsi ambavyo tumetumia sanaa hii kufundisha, kukanya, kuonya na kuburudisha pia.

Mheshimiwa Spika, wasanii wa Tanzania wamekuwa kwenye mazingira magumu sana na wamekuwa kwenye umasikini mkubwa. Mara nyingi tumekuwa tukiwatumia wasanii katika kampeni mbalimbali; tumekuwa tukiwatumia katika kampeni za malaria na hata katika chaguzi zilizopita
mmeona jinsi wasanii walivyokuwa wakitumika na baadaye mmewatumia kama Makarai na kuyaweka uvunguni.

Mheshimiwa Spika, tunajua Makarai yanatumika kwenye kujenga maghorofa na vitu vingine kama hivyo lakini tayari nyumba ikishakamilika yanawekwa uvunguni hayatakiwi hata kuonekana kwa wageni. Wasanii wa Tanzania wamekuwa wakitumika kwa style hiyo na wengi wamekuwa wakiwa maskini sana na hali yao ya uchumi imekuwa ngumu kwa sababu wamekuwa hawathaminiwi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa nikipiga kelele na kupaza sauti ya wasanii kwa sababu nataka niwaambie, katika nchi zilizoendelea kama Marekani, Uingereza Taifa lao linapata mapato makubwa sana kupitia sanaa zao. Takwimu iliyofanywa hapa Tanzania na Rulu Art Promoters inaonesha kwamba muziki peke yake unachangia takribani asilimia moja na zaidi ya pato la Taifa la Tanzania. Kwa hiyo, tunaona kabisa muziki umekuwa katika hali mbaya lakini bado inachangia asilimia moja. Naamini Wizara ikitumia umakini na ikijaribu kuwekeza zaidi katika Wizara hii, wasanii wa Tanzania wataweza kuchangia pato kubwa sana katika Taifa. Pia imesaidia sana kwenye kutoa ajira, wasanii wamejiajiri na kuajiri vijana wengi zaidi katika sekta hii ya sanaa.

Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali ilitenga pesa kidogo sana ambayo ni bilioni tatu tu na katika hali ya kustaajabisha ni bilioni 1.19 ambayo ilikwenda kwenye nyanja hii na sasa hivi tunaweza tukaona katika bajeti hii imetengwa pesa ndogo ambayo kiukweli kabisa tunaona kama utani shilingi bilioni sita kwa sekta nzima ya Habari, Utamaduni na Michezo.

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa kama kweli tuko makini kwenye kusaidia sanaa ya Tanzania ambayo imekuwa ikitoa ajira kubwa sana kwa wasanii na vijana wa Kitanzania, ilitakiwa tuweke pesa nyingi na hiyo pesa iweze kufika kwenye maeneo yanayohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na malalamiko sana ya wasanii mfano wa filamu. Wasanii wa filamu wameandamana juzi wakiwa wanapaza sauti zao wakiwa wanataka haki zao za msingi. Hata hivyo niwaulize tu wasanii wenzangu wa filamu, huyu Bashite ameonekana kuwa na matatizo mengi na vyombo vya habari, amekuwa na matatizo mengi na Watanzania wengi wameonekana ambao wameonekana kuwa wanampinga, inawezaje mkamuweka akawa front line katika kutetea haki zenu za msingi? Tunaamini movement yoyote ambayo inatakiwa ifanyike kwenye kutetea haki inahitaji muungano wa watu wengi.

Mheshimiwa Spika, iwapo mngetaka kufanikiwa kwenye hili jambo mngemtumia kama Waziri wa habari kama alivyofanya press conference yake na Roma, tuliona vyombo vyote vikionesha mshikamano na umoja wao lakini sasa hivi tumeona mnamtumia Bashite ambaye anataka kujiosha kupitia ninyi na matokeo yake sasa Watanzania hawajawaelewa na ninyi wenyewe mmemeguka kwa sababu amekuwa na matatizo mengi na watu tofauti tofauti.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu, sanaa ya filamu ya Tanzana inatoa ajira na sisi tuko hapa kwa ajili ya kuitetea na tunajua kwamba mna shida nyingi. Kwa mfano mdogo tu; kabla ya kufanya filamu, inabidi utoe shilimgi 500,000 kwenye Bodi ya Filamu kwa sababu tu ya kupeleka script yako, lakini ukishatoa script yako inabidi utoe tena shilingi 300,000= kwa ajili ya kupewa kibali cha ku-shoot. Ukishamaliza kutoa shilingi 300,000 na ukisha-shoot unapeleka shilingi 1,000 kukagua kila dakika ambayo unakuwa umeifanyia ile filamu. Ukitoa hiyo unakuja kupeleka tena unafunguliwa file pale COSOTA, unalipa zaidi ya shilingi 40,000. Baada ya hapo unapeleka TRA wanakupa sticker ambayo ni shilingi nane ndani, shilingi nane nje, jumla shilingi 16 kwa kila copy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukimaliza hapo unaenda tena ku- negotiate na yule distributor ambaye ni Mhindi na ukishakubaliana naye kwa bei ambayo mliyokubaliana, anakata asilimia 30 kwa ajili ya kupeleka kwenye kodi ya Tanzania. Unaweza ukaona jinsi ambavyo wasanii wa filamu wanaumia. Hata hivyo strategy waliyoitumia kwenye kutetea haki zao, wametumia mlango mwingine wa kutokea badala ya kutafuta strategy ambayo wangepata support yote. Kwa hiyo, nimwombe Waziri huu ni muda sasa wa kukaa chini na wasanii kuunganisha nguvu zote, tunahitaji Waziri wa Mambo ya Ndani, tunahitaji COSOTA, tunahitaji BASATA na Waziri wa Habari na Michezo tuweze kukaa chini na wasanii tuweze kujua shida zao ambazo zinawasumbua.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tatizo la hati miliki; katika hii Sheria ya Hati Miliki namba Saba ya mwaka 1999 imepitwa sana na wakati. Wasanii wanaibiwa sana kazi zao, piracy imekuwa kubwa lakini wezi wanaokamatwa na kazi hizo hamna adhabu kali ambayo wanapata. Tumeona kwamba kuna mtu alikamatwa na container zaidi ya bilioni sita zilikuwa zimetumika lakini baadaye anakuja kupigwa fine ya milioni tano. Mnaweza mkaona kwamba huu ni mzaha na inakatisha sana tamaa ya wasanii wa Tanzania katika hali kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi msanii Diamond alikuwa analalamika, TRA wamempelekea kodi ya milioni mia nne. Unaweza ukajiuliza kwamba adaiwa milioni mia nne kwa kiasi gani alichoingiza? Downloads ambazo inafanyika, mnaweza mkaona kwamba sasa hivi wasanii wanabawanwa, TRA wanatamani kuvuna kutoka kwa wasanii kitu ambacho bado hawajakipandikiza. Tumekuwa na ule msemo kama wa zamani kwamba shamba likiwa na bangi ni lako lakini likiwa na dhahabu ni la Serikali. Tunataka kuchuma kitu ambacho hatujakipanda. Ndiyo maana nasema, inabidi Serikali sasa ianze kuweka na kuwekeza kutoka kwenye shule za msingi mpaka Chuo Kikuu tuanze kuwajenga wasanii.

Mheshimiwa Spika, hata juzi, msanii Darasa alienda Arusha, TRA wakavamia show yake, wakasema kwamba haya mapato inabidi tugawane asilimia 18 yaani wameibuka tu from nowhere. Darasa ameenda Arusha kwa gharama zake, ameenda kufanya matangazo, amelipa Ukumbi, wameenda wamefunga mageti saa 12 wanamwambia lazima tukate asilimia 18 pale Arusha, matokeo yake wamekuja kufungua mageti saa sita usiku, kijana wa watu aliyejiajiri kupitia muziki amepata hasara, amepata watu 200, 300 TRA wakakata hela zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo TRA kama mnataka pesa kaeni chini na wasanii tutengeneze strategy nzuri itakayosaidia wasanii wa Tanzania wanapowekeza kupitia kitu kama hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuanza kuchangia kwanza nitoe pole kwa wananchi wa Mikumi kwa tahayari kubwa na mshtuko mkubwa ambao umetokea jana baada ya vijana saba kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha kwenye Hifadhi ya Mikumi. Hatuna uhakika kama hawa wenzetu wako salama huko waliko au itakuwa ule utaratibu wa kuzika nguo ndugu zetu hatuwaoni. Niwaambie tu ndugu zangu wa Mikumi kwamba tupo pamoja, na mimi nitaungana nao kesho kuangalia ndugu zetu wana hali gani. Niwatoe hofu tu kwamba tumeshalifikisha kwenye sehemu zinazohusika, naamini watatumia muda wao na upendo wao kama Watanzania kuweza kujua wenzetu wapo wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kwenye Wizara hii nyeti, Wizara ambayo ni uti wa mgongo wa Tanzania, ambayo inatoa zaidi ya asilimia 75 ya ajira, lakini pia kwa mwaka 2016 imeweza kutoa asilimia 29 ya pato la Taifa. Pia katika Wizara hii ambayo tunasema ni nyeti kumekuwa na changamoto nyingi sana, lakini changamoto kubwa ambayo tunaiona ni changamoto ya bajeti yenyewe. Kwa kuwa kwa mwaka 2016/2017 tunaona kwamba fedha za maendeleo zilikuwa zimetengwa shilingi bilioni 100 lakini mpaka Mei 4, 2017 ilikuwa imekwenda asilimia tatu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona ni jinsi gani ambavyo bado kama nchi tuna tatizo. Hii ni shida kubwa sana kama kweli tunasema kilimo ni uti wa mgongo na unatoa ajira kubwa kwa Watanzania kama hivi; nadhani tunapaswa kujiongeza zaidi ili tuweze kuona jinsi gani tunaweza kuwasaidia wakulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hizo pesa ambazo ni shilingi bilioni 100 kuwa zimetengwa, lakini fedha za ndani zinaonekana ni shilingi bilioni 23 tu na fedha ambazo tunategemea wafadhili ni shilingi bilioni 78. Kwa hiyo, hapo napo unaweza ukaona kwamba wafadhili wakileta migomo kama ambavyo inaonekana sitofahamu nyingi, hii nchi inaelekea pabaya zaidi na ndiyo maana kila siku na kila kona unasikia watu wanalia njaa, watu wanalia kuna uhaba wa chakula ingawa visingizio ni vingi kwamba tabianchi nayo inachangia. Hata hivyo pia sisi wenyewe kama nchi hatujajipanga ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2017/2018 inaonekana bajeti kwa ujumla imetengwa shilingi bilioni 267 na kati ya hizo shilingi bilioni 156 ni za maendeleo, shilingi bilioni 150 zipo kwenye Kilimo, shilingi bilioni nne kwa ajili ya Mifugo na shilingi bilioni mbili kwa ajili ya Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninatokea kwenye Mkoa wa Morogoro ambao Serikali ina mpango wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Taifa, kwa sababu Morogoro tumebarikiwa ardhi nzuri, lakini pia ina rutuba na pia inalima aina nyingi za mazao na kila mmea unakubali, na ndiyo maana tumeamua kuwa hivyo, na sababu pia Morogoro ni center na vitu kama hivyo. Lakini kwa style hii ya kutenga bilioni nne kwa ajili ya mifugo si dhani kama tunakwenda kumaliza tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji. Pia kwenye bajeti hiyo kwa miaka mitatu mfululizo pale Wilayani kwangu Kilosa pesa za bajeti hiyo hazijaweza kufika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri, utakapokuja utuambie ni kwa nini Kilosa inakuwa inasahaulika sana na kuna upendeleo wa maeneo mengine mengine, lakini Wilaya ya Kilosa ambayo ni Wilaya nyeti yenye ardhi nzuri na yenye rutuba, imekuwa ikiwa nyuma sana ikipelekewa pesa za maendeleo basi ni kwa miaka mitatu mfululizo. Na kwa style hii Mheshimiwa Waziri nataka nikuahidi tutakabana sana mashati kwa sababu sasa tumeamua kuwekeza kwenye kilimo na tunajua ndicho kitakachotutoa kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo wananchi wa Tindiga, Mabwerebwere, Kilangali, Masanze, Muhenda, Malolo ambao wanategemea sana kilimo wamekata tamaa kwa sababu wanaona kama Serikali inawaacha peke yao. Hata zile pembejeo pamoja na madawa, mbolea zinaonekana hazifiki kwa wakati, na ndiyo maana wananchi wa kule wamekuwa na tabu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni kuhusu wakulima wa miwa ambao ni asilimia kubwa sana katika jimbo letu la Mikumi kwenye kata za Ruhembe, Kidodi pamoja na Ruaha, lakini pia hata watu wa Vidunda na Mikumi wameonekana kulima kilimo hiki cha miwa. Kilimo cha miwa kimetoa ajira kubwa sana kwetu na ninashukuru sana kiwanda cha Ilovo juzi wametangaza bei ya muwa kutoka shilingi 79,000 sasa hivi ni shilingi 101,000, hilo Mheshimiwa Waziri nitakupongeza kidogo; hii ni kwa sababu wakulima wamekuwa wakilia kwa muda mrefu. Hata hivyo bado haitoshi, tunataka kusema kwamba wakulima wa miwa bado wamekuwa na shida kubwa na Mheshimiwa wanakusubiri kwa hamu kwa sababu kilio chao kimeonekana bado hakiwezi kupata solution ya kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa miwa sasa hivi wameambiwa na wamepata agizo kutoka Serikalini watoke kwenye vyama vyao vya hiyali vyama vyao vya kiraia waweze kujiunga na vyama vya ushirika. Hilo ni wazo zuri ni wazo jema na mimi kama Mbunge nali-support lakini naona kama muda ambao tumewapa wale wakulima ku-shift kutoka kule kwenda huku bado ni muda mdogo sana wanahitaji kupata elimu kwa sababu tumeona vyama vingi vya ushirika vikiwa na matatizo kadha wa kadha lazima tuwaeleze faida na hasara hiyo iliwakiweza kujitoa wajitoe kwa umuhimu na wajue jinsi gani ya kushirikiana na sisi, maana naamini tukiwapa elimu ya kutosha wanaweza nao kushirikiana na sisi. Lakini sasa hivi kuna mgomo baridi Mheshimiwa Waziri wakulima wengine wanagoma wengine wanaenda lakini tunasema tukienda kwa pamoja tukawapa elimu tunaweza tukafanikiwa kwenye hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa miwa wamekuwa na tatizo lingine, wananchi wengine na wakulima wa nchi zingine wanalipwa pia masuala ya bagasse lakini na wanalipwa masuala ya molasses. Bagasse ni tatizo kubwa ambalo pia kiwanda kinawalipa utamu peke yake yaani sucrose. Lakini ingeweza kuwalipa bagasse ambayo inatengeneza mashudu, mbolea, pia umeme lakini wakulima hawapati faida yoyote kupitia hiyo. Vilevile molasses ambayo inatengeneza spirit na inatengeneza pombe, pale pale ilovo kwa pembeni kuna kiwanda cha pombe; lakini wakulima wa kule bonde la Ruhembe hawanufaiki kwa njia yoyote na vile vitu, wanalipwa utamu peke yake, yaani sucrose. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hata huo utamu wenyewe umekuwa ukionekana kuwa na walakini, inaonekana gauge yenyewe inakwenda kwenye saba mpaka nne wakati wataalamu waliokuja kule wanasema hakuna gauge ya saba wala ya nne bali utamu unatakiwa kwenye gauge 11 na kuendelea Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbuke kwamba wakulima wa bonde la Ruhembe wanalalamikia kuhusu utamu na wanalalamika sana kwa kusema kwamba hakuna gauge nne wala gauge saba bali wanapunjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wana tatizo lingine la mzani, wamekuwa wakiomba kila siku kwamba wanataka wakulima wa nje wawe na mzani wao binafsi kabla ya kuingiza kule kiwandani kwa sababu mtu wa kiwanda yeye ndiye anayepima, yeye ndiye anayepanga bei na yeye ndiye anayefanya kila kitu inawaumiza sana wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa sababu nchi hii inajua umuhimu wa sukari na inatoka kwa wingi kule Kilombero basi jaribu kuwashika mkono wakulima wa miwa wa kule Kilombero ili waweze kufanya na kulima kwa bidii, naamini wakilipwa kwa uwiano huo itawasaidia sana. Ndiyo maana juzi Mheshimiwa Waziri mmekamata magari ya kupeleka miwa ya kutoka Kilombero kwenda Kenya, ni kwa sababu watu wanakimbilia bei nzuri, na hawalipwi utamu peke yake wanalipwa bagasse, wanalipwa molasses na vitu vingine. Kwa hiyo na sisi naamini tukijiongeza tutaweza kuwatengeneza wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wakulima wamekuwa wakilalamika kuhusu DRD, wanasema zile asilimia za kuingiza miwa mule kiwandani zimekuwa ndogo, iko 40 kwa 60 angalau ingekuwa 50 kwa 50 au 55 kwa 45 ingeweza kuwasaidia kidogo ili miwa iweze kuwa inapatikana kwa wingi. Lakini pia kulikuwa na wazo la kutengeneza kiwanda kingine kule Mfilisi, sasa hatujui hicho kiwanda kimefikia wapi sasa nategemea Mheshimiwa Waziri utakuja kunijibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji. Nashukuru sana wakati ndugu yangu Augustine Mtitu alipopigwa mkuki wa mdomoni ukatokea shingoni, baada ya kilio kidogo Mheshimiwa Waziri ulifika ingawa ulininyatianyatia, hukufika kwa wakati na hukanishtua vizuri nilisikia tu kwamba umetokea na ukaingia mitini. Napenda siku nyingine ukija jimboni unitaarifu nikiwa kama Mbunge na muwakilishi wa wananchi ili tuweze kujadiliana kwa kina na tuweze kujua jinsi gani tunaweza tukawasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini migogoro ya wakulima na wafugaji halijakwisha, bado kuna migogoro mingi na ninaamini hili suala ni mtambuka linahitaji Waziri wa Ardhi, Waziri wa Maliasili na Utalii lakini pia na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani tuweze kukaa na kulijadili kwa sababu inaonekana upimaji wa ardhi imekuwa ni tatizo kubwa kule Kilosa, lakini pia yale maeneo tengefu yamekuwa yanaongezwa kila siku, vile vile ardhi imekuwa ni tatizo sana kwa wananchi wa Jimbo la Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla. Kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, tumekuomba sana, utakapokuja uturudishie yale mashamba makubwa, mashamba kama Sumagro, Kisanga, Kilosa Estate, Miyombo Estate ni mashamba ambayo yameachwa mengi nimashmba pori tunaomba uturudishie iliwananchi waweze kufanya kazi yake yao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwa dakika hizi tano ulizonipa katika Wizara hii nyeti Wizara muhimu sana kwa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara hii tumeona kuna changamoto kubwa sana za miradi mbalimbali kuweza kufika kwa wakati katika maeneo ambayo yanastahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni-declare interest, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Kitu kikubwa ambacho naweza nikakizungumza kwa haraka, baada ya lile zoezi la kutumbua wafanyakazi wa vyeti fake, tumekuwa na athari kubwa sana ya watumishi katika maeneo yetu hasa Mkoa wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wilaya yetu ya Kilosa uhitaji wa watumishi ulikuwa ni 1,025 kwenye kada mbalimbali kama Wauguzi, Madaktari, Wafamasia, Ustawi wa Jamii na Maafisa Afya, lakini waliopo ni 474 tu, sawa na asilimia 46. Pia tuna upungufu wa watumishi 551 sawa na asilimia 54. Unaweza ukaona jinsi ambavyo Wilaya ya Kilosa imekuwa nyuma sana katika sekta hii ya afya na watu wamekuwa wakitaabika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu kwa Serikali, tunaomba itusaidie sana watumishi hawa waweze kufika katika Wilaya yetu ya Kilosa lakini pia tuweze kuokoa maisha ya mama na mtoto ukizingatia jiografia ya Wilaya ya Kilosa imekuwa iko mbali mbali sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kabisa tumeona kwamba kuna upungufu mkubwa wa vituo vya afya ambapo sasa hivi Serikali imetoa shilingi milioni 400 pale kwenye Kituo cha Afya cha Kidodi, tunashukuru sana. Pia kituo hiki ni muhimu kwa sababu kinaenda kuhudumia wananchi wa Kata ya Ruaha, Vidunda, Kidodi pamoja na Rwembe. Kwa jiografia iliyoko pale tunaona pia kuna umuhimu wa kusisitiza na kuiomba Serikali iweze kutupatia gari ili liweze kusaidia wananchi wa Jimbo la Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upungufu huu wa Madaktari Bingwa katika Wilaya yetu ya Kilosa, mwaka 2017 tulisikia Serikali inataka kupeleka Kenya Madaktari 500, basi kwa upungufu huu tunadhani mngetudondoshea pale Mikumi kidogo Madaktari Bingwa kadhaa ili waweze kutusaidia katika Wilaya yetu ya Kilosa, hii ingeweza kusaidia sana. Pia dawa zimekuwa zinafika chini ya kiwango; dawa zimekuwa chache. Unaposikia kuna shilingi trilioni 1.5 hazieleweki zimekwenda wapi kwa kueleweka, nadhani zingeweza kuwa zimepangiwa mkakati maalum katika kitengo hiki cha afya na kuweza kuwasaidia mama na mtoto, tungeweza kupata hesabu nzuri sana na Serikali ingeweza kutimiza malengo ya kuwasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna kitu ambacho Serikali inabidi iongeze nguvu. Katika Maafisa Maendeleo wa Jamii wamekuwa pungufu sana. Kwa nchi nzima tunaona kwamba uhitaji ni watumishi 4,000 lakini waliopo ni 1,700. Kwa hiyo, unaona kwamba asilimia 57.5 kuna upungufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Maendeleo ya Jamii ndiyo wahamasishaji wakubwa katika Wilaya zetu, katika maeneo yetu kuwahamasisha wananchi waweze kujiletea maendeleo yao. Unapokuwa huongezi msisitizo katika kada hii na kufanya upungufu katika watumishi wa Maafisa Maendeleo ya Jamii inakuwa inashindwa kuwa-connect Watanzania na wananchi katika kujiletea maendeleo yao katika maeneo yao. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iongeze nguvu katika kuongeza Maafisa Maendeleo ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo tumevitembelea, bajeti haziendi kwa wakati na vyuo vimekuwa katika hali mbaya. Namuomba sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy, waongeze nguvu kwa kuongeza Maafisa Maendeleo ya Jamii ili waweze kuwa chachu na kuwakusanya wananchi pamoja, waweze kujadiliana nao ili kujiletea maendeleo katika maeneo yao. Maana huwezi ukaongelea maendeleo katika Jimbo, Wilaya na katika Mkoa bila kuwahusisha Maendeleo ya Jamii. Hao ndio wanaoweza ku-connect Serikali na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapokuja kuongelea suala la barabara, suala la wananchi kulima, watu kufanya programu mbalimbali katika nchi yetu, Maafisa Maendeleo ya Jamii ni watu wa muhimu sana. Naiomba sana Serikali iongeze nguvu zake katika kuajiri watu hawa. Asilimia 57, unaweza ukaona upungufu huo ni mkubwa sana na inatia damage kubwa sana kwa Serikali.

heshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa sababu nina dakika tano, nami ni mwanamuziki bora kabisa wa hip hop nitakwenda kwa style ya rap kidogo, yaani mbio. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikazie alipoishia mwenzangu Mheshimiwa Devotha Minja. Ni masikitiko makubwa sana kwa Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Morogoro na wadau wote wa maendeleo Mkoa wa Morogoro kwa kitendo cha Mkoa wa Morogoro kushindwa kukaa katika Bodi ya Barabara na kushindwa kukaa katika Kamati ya Mashauriano ya Mkoa, ni aibu kubwa sana kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie, tumekuja hapa Dodoma ndiyo tunaletewa makabrasha makubwa yaani kama hivi ili tuanze kuyasoma wakati hatujapitisha na hatujui bajeti ya Mkoa wa Morogoro imepitishwa na nani? Mnaweza mkapata picha, Waheshimiwa Wabunge mnajua umuhimu wa Road Board na mnajua umuhimu wa RCC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisogeza hilo kwa Mheshimiwa Waziri ili aweze kuangalia jinsi atakavyotusaidia kama inawezekana kweli wanasema wanaweza kutumbuana, wajaribu kuangalia hili jambo watali-handle vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema nitakwenda haraka kidogo. Jambo la kwanza ninalotaka nianze nalo, kilio cha wana Kilosa na Mikumi ni barabara ya kutoka Dumila kwenda Kilosa kuishia Mikumi. Hii barabara ni muhimu sana na mpaka sasa imejengwa kwa kilometa 45 tu. Nimeona kwenye kabrasha la Wizara hapa, wanasema wametenga shilingi bilioni sita na zenyewe ni kwa sababu ya kulipa madeni ya mwanzo huko ya watu wengine. Hatujui kimetengwa kiasi gani cha kukamilisha kilometa 24 za kutoka pale Ludewa mpaka Kilosa, lakini pia kilomita 78 za kutoka Kilosa mpaka Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni barabara ni ya msingi, inakwenda kuunganisha watu wa kaskazini wanaopita Korogwe wanaokuja kutokea Turiani wanakuja Dumila, wanatokea Kilosa – Mikumi wanakwenda kwa Mheshimiwa Lijualikali kule Kilombero, wanakuja kutokea Mlimba lakini wanaenda kuingia Njombe pamoja na Songea. Unaweza ukaona jinsi ambavyo barabara hii ni ya muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumeomba pia kupandishwa hadhi kwa barabara yetu inayotoka pale Ruaha Mbuyuni, inaenda Malolo – Uleling’ombe inakuja kutokea Kibakwe kwa kaka yangu Simbachawene, lakini mpaka leo hatujapata majibu hii barabara itakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Daraja la Ruhembe. Nilishaongea mara nyingi hapa, hili daraja ni la muhimu, ndugu zetu wanakufa mara kadhaa. Mheshimiwa Waziri alisimama na kuniambia kwamba wametenga shilingi milioni 700, sizioni sehemu yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walituambia watatupa daraja la muda pale kutoka Kiberege, limeshakuja, machuma yamewekwa chini, ndugu zangu wa kule Ruhembe bado wanaendelea kufa, watu na mama zetu wanataabika sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, akija atuambie mpango gani wanao kuhusu Daraja ya Ruhembe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu uchukuzi. Jimbo la Mikumi mnajua ni la utalii lakini sasa hivi ukimaliza tu pale kwenye vibao vya kuingia Mikumi, upande wa kulia wote Railway wamepiga X, maana yake nyumba zote na vitega uchumi vyote na mahekalu yote yaliyojengwa kule inabidi yabomolewe. Wananchi wa Mikumi wanaishi kwenye taharuki kubwa sana. Hii siyo Mikumi peke yake, bali Kata ya Kidodi na Kata ya Ruaha ambayo ni Kata mama katika Jimbo la Mikumi, nao wanaishi katika sintofahamu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijaribu kuwasiliana na viongozi wa Railway wakatuambia kwamba wanajua kwamba pale Mikumi kulikuwa na reli inatoka Kilosa kuja pale kwenye kiwanda cha sukari, lakini hiyo reli yenyewe mpaka leo mataruma yameshang’olewa. Hakuna dalili ya reli yoyote, wanawafanya wananchi wa Mikumi wanaishi kwa wasiwasi, wanashindwa kuendeleza biashara zao, watalii wanashindwa kuwekeza kwa sababu ya kuwa na alama za X na tunaambiwa tutabomolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri wawaambie watu wa TRL waje kukaa na watu wa Mikumi kwa sababu watu wamepewa hati na wamejenga pale wamewekeza kwa ajili ya utalii, lakini wanakuwa katika hali ya sintofahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu suala la TARURA. Tunajua umuhimu wa TARURA. Mama yangu Mheshimiwa Kiwanga hapa amegusia kuhusu barabara ya pale Kilosa Mjini, shilingi milioni 600 imepigwa, lami imewekwa pale miezi sita haijafika inatimka vumbi, lakini bado hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA Kilosa bado wana hali ngumu sana, fedha zinazokwenda ni ndogo lakini pia hawana usafiri. Wilaya ya Kilosa ni Wilaya kubwa sana, lakini pia jiografia yake ni mbaya sana. Tujaribu kuangalia jinsi ya kuwawezesha hawa TARURA ili waweze kufanya kazi nyingine za kutosha kusaidia wananchi wa Mikumi, maana kuna barabara zime… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na wenzangu kumpa pole sana Mbunge mwenzetu John Heche kwa kufiwa na mdogo wake kwa kuchomwa kisu na Polisi kule Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kuchangia Wizara hii muhimu ambayo inahusisha Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa. Jambo la kwanza ambalo ningependa kuchangia leo ni kuhusu suala la Bunge Live. Bunge ni chombo muhimu sana cha uwakilishi, chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi hapa Tanzania na tunaamini Bunge ni kama mkutano wa wananchi wote kwa sababu kuna wawakilishi kutoka pande zote za Tanzania humu ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo nadhani ilikuwa ni muhimu sana Serikali yetu iliangalie upya hili suala la kuondoa Bunge Live ili wananchi waweze kutuona wawakilishi wao tunavyowawakilisha ndani ya Bunge ili iweze kuwafikia moja kwa moja na kujua vitu gani vinavyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi inaongozwa na Mihimili mikuu mitatu, kuna Serikali Kuu, Mahakama na Bunge. Tumeona jinsi ambavyo viongozi wa Serikali wakifanya ziara mara kwa mara na wanaoneshwa live maeneo mengine. Hii inaonesha ni jinsi gani ambavyo ni muhimu sana kwa

wananchi kuweza kuona viongozi wao wanafanya na kutekeleza vitu gani ambavyo wametutuma.

T A A R I F A . . .

MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina haja ya kuijibu hiyo taarifa kwa sababu mimi naongelea Bunge Live yaani hapa ninavyoongea watu wawe wanashuhudia live kule, Dada yangu vipi? Hiyo saa tatu watu wanakuwa wamechoka, watu wanaangalia Bunge hadi usiku mkubwa na siyo live, hiyo ni recorded. Kwa hiyo, hilo lilikuwa jambo langu la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wiki iliyopita niliongea jambo la msingi sana kuhusu Chama cha Mapinduzi kupora viwanja vingi vya michezo ambavyo vimekuwa vikimilikiwa na Serikali lakini sasa vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi na wameshindwa kuviendeleza. Hapa ninavyoongea na wewe ni kwamba hapo kwenye Kata ya Ruaha kwenye Jimbo la Mikumi kuna utata mkubwa na taharuki kubwa sana kati ya wananchi na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambao kwa kutumia mabavu wameupora uwanja wa shule ya msingi Ruaha ‘A’ ambao pia unatumia na Ruaha ‘B’ pia unatumika na shule ya sekondari ya Kidodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya elimu inasema kwamba kila shule lazima iwe na uwanja wa michezo. Pale Ruaha wanafunzi wa shule ya msingi Ruaha ‘A’ na Ruaha ‘B’ pamoja na shule ya sekondari ya Kidodi wanatumia uwanja huo, Chama cha Mapinduzi kimeupora na kinaanza kusema sasa hivi ni wa kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja huo ulijengwa mwaka 1986 ambapo wananchi walijitokeza na kufanya harambee kwa ajili ya huo uwanja na wakajenga vibanda pembeni ambapo mkataba walioingia na mkataba wanao mpaka leo inasema kwamba Serikali itamiliki ule uwanja lakini yale maduka ya pembeni yatakuwa ni haki ya wamiliki au wananchi ambao walikuwepo na mkataba wamesaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha ajabu juzi Chama cha Mapinduzi wamekuja pale Ruaha wakiorodhesha majina na kuwaambia wale wananchi waondoke. Kwa kweli kuna hali mbaya sana na niwambie kitu kimoja, iwapo Chama cha Mapinduzi kitafanikiwa kuchukua ule uwanja maana yake tunakwenda kufunga shule ya msingi Ruaha ‘A’, Ruaha ‘B’ pamoja na shule ya sekondari ya Kidodi kwa sababu hawana uwanja wa michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka niongee kuhusu suala la BASATA, inasikitisha sana hii Wizara kwamba hadi sasa imetimiza asilimia 59 tu ya bajeti yake na asilimia 41 mpaka leo tunavyoongea haijakamilika. BASATA ni chombo cha msingi na tunaichukulia BASATA kama wazazi lakini BASATA imegeuka na kuwa kama chombo cha hukumu kwa Wasanii wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, BASATA ni kama mlevi na mtoto akijisaidia kwenye mkono wako huukati, unauosha na unaendelea na shughuli zingine. Niliamini kwamba BASATA inatakiwa iwape elimu hawa wasanii wa Tanzania waweze kujifunza, waweze kupata ushauri lakini pia waweze kuangalia jinsi gani ambavyo wanaweza kuisaidia tasnia ya muziki hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie wenzetu wamefanyaje, Uingereza kwa mwaka 2015 muziki peke yake umechangia GDP paundi bilioni 4.1 katika Pato la Taifa la Uingereza. Marekani mwaka 2015 muziki peke yake umechangia GDP ya dola milioni 15. Kwa hiyo, naamini kabisa kama Wizara inataka kuwekeza kwa vijana maana huwezi ukamkamua ng’ombe ambaye hujamlisha majani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwaambia Serikali waweke bajeti kwa wasanii, wana matatizo makubwa tofauti na hayo wanayoyafanya maana wanadhani kwamba kuwasaidia wasanii wa Tanzania ni kuwaalika sehemu za maofisi zenu kupiga nao picha, kupiga selfie na vitu vingine. Wasanii wa Tanzania wana matatizo makubwa, hawahitaji kula ubwawa na wao. Wanahitaji wawasaidie masuala ya kazi zao zinazoibiwa, wanahitaji wasaidiwe masuala ya masoko na mitaji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie ndugu zangu, BASATA mpaka sasa katika hali ya kustaajabisha ndiyo imepewa mamlaka ya kusimamia hii kitu lakini bajeti yake ni milioni 23 kwa mwaka mmoja, mwaka 2016…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH L. HAULE. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, awali ya yote nitoe pole sana kwa Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Jesca David Kishoa, ambaye amepata ajali mbaya sana asubuhi hii tunamuombea kwa Mungu aweze kumpa nguvu na uponyaji wa mapema aweza kurudi kuendelea kulitumikia Taifa. Lakini pia nitoe pongezi kubwa sana kwa pacha wangu Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu kwa kuhitimu mafunzo ya huko ndani ambayo yameongeza sana ujasili na cv yake ya kisiasa natumaini sasa hivi hatokuwa Rais wa Mbeya bali anaenda kwenye mchakato wa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko siku za mbeleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa haraka kidogo, kwenye Wizara hii ya Viwanda kama wenzangu walivyosema Mkoa wa Morogoro ulibarikiwa kuwa na viwanda vingi sana ambavyo vingi vilibinafsishwa, na tukiwa tunategemea wawekezaji waweze kuviboresha kwa zaidi, lakini kwa masikitiko viwanda vingi vya Mkoa wa Morogoro vimekufa. Hapo ninavyoongea na wewe viwanda vya Moproco, Komoa, Canvas, Morogoro Leather Shoes na viwanda vingine kadha wa kadhaa viko ICU na sasa hivi zimekuwa kama Magodauni na vingine vinafugiwa mpaka mbuzi vitu ambavyo kiukweli sidhani kama ni lengo la Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi . (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe Waziri kabla hatujaenda kwenye viwanda vipya tuangallie wapi tulijikwaa na viwanda vyetu vilifanywaje ili tuweze kuvirudisha na kuangalia jinsi gani ambavyo tunaweza kuirudisha Morogoro kwenye ramani, kwa sababu sasa hivi pia Serikali ilitangaza kwamba muda si mrefu Morogoro inakwenda kuwa ghala la Taifa la chakula. Kwa hiyo, tunahitaji viwanda vingi, tunahitaji kufufua malighafi nyingi, kwa sababu morogoro imebarikiwa sana kilimo na ina ardhi nzuri na kila sifa ambayo inastahili kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nijikite katika jimbo langu la Mikumi. Mikumi tumejikita na tuna kiwanda kikubwa sana cha Sukari cha Kilombero, kiwanda hiki kila mmoja anajua kwamba ni moja kati ya viwanda vikubwa sana Tanzania ambavyo vinatoa ajira kubwa na ni tegemeo kubwa sana kwa sukari hapa nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1999 kwenda 2000 wakati kiwanda hiki cha Kilombero Sugar Company kikimilikiwa na Serikali kilipunguza wafanyakazi takribani 3000, na ilipoingia Illovo kwenda kama mwekezaji. Hawa wafanyakazi mpaka leo hawajalipwa fidia zao. Kilio hiki cha wafanyakazi ni kikubwa sana na kimeleta taharuki kubwa. Wazee wetu walitumikia kiwanda hiki kwa nguvu zao zote, kwa uwezo wao wote, kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini wengine wamekufa bila kulipwa mafao yao, na wengine wanataabika kupata mafao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, juzi tulikuwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na nilimuuliza swali hili. Kiwanda hiki ni muhimu sana kwa wakazi wa Mikumi, lakini Jimbo la Kilombero, Jimbo la Mlimba na Wilaya nzima ya Kilosa. Wafanyakazi wengi sana wameajiriwa kwenye kiwanda hiki, ni kiwanda kikubwa tunakipenda na kinaonesha ushirikiano. Lakini tunaomba sana Waziri, Rais alisema kwamba wakati mnabinafsisha kiwanda kwenda Illovo Serikali ilifanya makosa na wawekezaji walifanya makosa, hakusema kwamba wale wafanyakazi wana makosa yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iwalipe fidia hawa watu walioachishwa kazi zaidi ya watu 3000 ambao kiukweli kabisa inaonesha hii ni haki yao ya msingi. Na niombe kuwaambia kwamba hata Kiwanda cha Makaratasi cha Mgololo na wenyewe walikuwa na kesi hii

lakini wenzetu wamelipwa hivi karibuni niwaombe Serikali mtupie jicho na Mheshimiwa Waziri wewe ni rafiki yangu kila nikikutana na wewe unaniambia nakupiga na kiwanda kimoja hapa nina viwanda kama vitatu mfukoni. Siku utakapokuja kule Ruaha watu wanakusubiri wapate majibu kwamba ni lini Serikali inakwenda kuwalipa fidia hawa wazee wetu ambao wametumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Kiwanda cha Sukari Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja hilo, ili tuweze kutunza viwanda vyetu tunahitaji kuwa na mahusiano mazuri tunasema kiwanda cha Ilovo wanafanya vizuri sana wametoa ajira kubwa sana kwa Watanzania pale. Lakini mahusiano yamekuwa mabaya sana kati ya wakulima wa nje pamoja na kiwanda na Ilovo. Bado tunakuwa na matatizo ya mizani, bado wakulima wanalipwa sucrose kwa kiwango kidogo, lakini pia tunasema kwamba ili tuweze kuwa na uwiano ni lazima tuwe na mzani huru kwa sababu mpimaji ni huyo huyo, mpanga bei ni huyo huyo wakulima wetu wanaumia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hivi kumekuwa na taharuki kubwa sana na changamoto kubwa wale wafanyakzi wa kiwanda cha pale cha Ilovo wamekuwa na mgogoro mkubwa sana na mfuko wa jamii wa NSSF. Kwa sababu wale wafanyakazi wanafanya kazi ki mikataba na kila msimu wanaweza kuajiriwa kwa miezi nane mpaka 10 na ile baada ya miezi 10 inaahirishwa wanakuwa na mapumziko ya miezi miwili na wanaporudi kwenye msimu mpya kiwanda kinaweza kikawaajiri tena au kisiwaajiri. Kwa hiyo, inasababisha wale wafanyakazi ambao wamefanya kazi na hawarudishwi tena kwenye kiwanda hawawezi kupewa pension yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nijielekeze kusoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 13(1) inasema: “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”. Vilevile Ibara ya 14, inasema: “Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye Wizara ya Utawala Bora. Wiki iliyopita nilisimama katika Bunge lako Tukufu nikizungumzia kwamba kuna upotevu wa watu kumi katika Jimbo la Mikumi maeneo ya Ruhembe, Kidodi pamoja na Ruaha na niliongea hapa kwenye Bunge nikiamini kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imo humu ndani. Pamoja na kuongea hapa Bungeni na kumfuata Waziri wa Maliasili na Utalii na kuwafuata wahusika wote mpaka leo watu wamenyamaza kimya kana kwamba hakuna kilichotokea katika Hifadhi za Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimekuwa nikijiuliza, Serikali hii inajipambanua kwamba inajali utu, haki lakini pia utawala bora, pamoja na hayo kila siku tunaimba kwamba Tanzania ina amani lakini ni jambo la kushangaza sana unapoona kwamba kuna watu kumi na tunaripoti kwenye Serikali wamepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu tarehe 2 Aprili, leo ni tarehe 12, siku kumi hakuna mtu yeyote amezungumzia lolote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii imetusikitisha sana na bado majonzi yamekuwa makubwa sana katika Jimbo la Mikumi maeneo Ruhembe na niseme kitu kimoja kwamba hali hii inaendelea kuleta taharuki na imani ya wananchi kwa Serikali imekuwa ndogo na inazidi kushuka kila siku. Kwa kuwa tunajua kwamba TANAPA na Polisi wana helikopta au helikopta hizo zinakuwa kwa ajili ya intelijensia kuwakamata wapinzani tu na kushindwa kuelewa Watanzania wengine wasiokuwa na hatia wanaopotea katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku kumi ni nyingi watu wanapokuwa hawaonekani. Tukasema labda tupeleke kwa Serikali itatafuta namna ya kutupa majibu ya jambo kama hilo, inasikitisha sana kuona mpaka leo siku ya kumi watu wamekuwa na majonzi. Basi hatuombei labda wamekufa tuseme lakini hatuombei hivyo, kama wamekufa basi mtupe hata nguo zao ili tukazizike au tukaendelee na misiba katika Jimbo la Mikumi, labda huo ndiyo utawala bora mnaoujua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana imeundwa Kamati imekwenda kule, RCO pamoja na watu wa hifadhi, you can’t be a judge of your own case, huwezi kuwapeleka watu ambao tunahisi na wananchi wanalia kwamba watu wamepotea katika hifadhi yao, halafu bado wao wao ndiyo wakaenda kuangalia na kufanya uchunguzi mpaka leo hakuna majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo tunaomba mliangalie kwa kina na tupate majibu ya Serikali hawa watu kama wamekufa tujue, kama wamepotea tujue, tunatakiwa tujue ripoti yao. Nina nia ya kuomba Bunge lako Tukufu liunde Tume ambayo itakwenda kufanya uchunguzi katika maeneo hayo ya Ruhembe ili tuweze kuwapa haki hawa wananchi ambao ndugu zao wamepotea katika hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu Tume ya Uchaguzi. Kila siku tumekuwa tukizungumza Tanzania ni kisiwa cha amani lakini naona watu wana nia ya kupoteza kisiwa cha amani cha Tanzania. Labda niwashauri tu Wabunge wa CCM ambao mnashabikia sana kuhusu hii Tume ya Uchaguzi, muangalie sasa hivi katika TV za kimataifa, CNN, Al-Jazeera na sehemu nyingine, jinsi ambavyo kumekuwa na unrest katika dunia kwa sababu ya mambo kama haya. Watu wamefungwa mikono, watu wanashindwa kusema lakini Tume imekuwa haitendi haki kwa wapinzani wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Sudan mmeona kimemtokea nini Al-Bashir lakini ukiangalia Algeria na Venezuela kuna vitu kama hivyo na hapa Tanzania kama tutaendelea kucheka na hii Tume ya Uchaguzi ambayo sasa matokeo yamekuwa yakitangazwa vice versa, leo tu Mahakama ya Mbeya imetoa hukumu kwamba katika Kata ya Ndalambo ambapo alitangazwa mgombea wa CCM lakini wameona ni jinsi gani ambavyo Serikali ya CCM imekuwa ikiiba kura kila siku na sasa hivi wameonekana wameiba na mgombea wa CHADEMA ametangazwa kushinda pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wanasema Tume hii ni huru kwa sababu akina Profesa Jay walitangazwa; hamjui mbilinge tulizozifanya huko mpaka tukatangazwa. Tumefanya uchaguzi tarehe 25, tarehe 26 unaona magari yanakuja yanaondoka, tarehe 27 CCM wanabeba magari ya matangazo wanataka kujitangaza kwa nguvu, nyomi linaongezeka pale na pale kweli asingetoka mtu. Napenda kusema kwa Wanamikumi kwamba nitaendelea kusimama pamoja nanyi na niombe watu wote wapenda amani hapa Tanzania wasimame pamoja kuhakikisha kwamba Tume hii inabadilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwanamuziki wa hip hop lakini pia napiga ngumi mbili, tatu, napenda boxing; kama wewe ni referee kama Tume ya Uchaguzi, basi usinifunge mikono mimi halafu ukamuacha jamaa anipige mangumi mengi mengi usoni, unanifunga kamba halafu unamwambia jamaa apige, haiwezekani. Ipo siku hizi kamba zitakatika na nitawapiga manondo ya kutosha ndugu zangu kwa sababu tunakwenda kushinda na tunaamini tutakwenda kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu watu wote ambao wamepitia katika nyanja na matatizo mbalimbali waamini kwamba haya mambo ni ya kupita tu. Watu wangu wa upinzani tulizeni ball, mwaka huu ni wa uchaguzi tunakwenda oya oya na mzuka kama kawaida maeneo ya katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niende kwenye Wizara ya TAMISEMI kwa Mheshimiwa Jafo. Nashukuru sana ulifanya ziara Jimboni Mikumi lakini kiukweli kabisa ni kwamba katika Kituo cha Afya cha Mikumi baada ya ziara yako ndiyo mambo kidogo yameanza kwenda vizuri na mimi kama Mbunge nimechangia mifuko 200 kuonesha kwamba nina-support kile kinachotokea kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya ni kwamba wale wafanyakazi waliopewa kazi za ziada bado hawajalipwa mpaka leo na wameniagiza nikwambie kwamba wameshaleta barua kwako wanasubiri uwasaidie. Wale ni walalahoi wa Mikumi wamefanya kazi pale wanataka uwasaidie wapate haki yao ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wananchi wa Malolo wanajenga Kituo cha Afya kwa nguvu zao wenyewe na mimi kama Mbunge nimepeleka tena mifuko 200 ku- support juhudi hizo. Tunaomba Serikai nayo ituongezee hela kidogo ili tuweze kukamilisha nia yao ya kuweza kuwa na kituo chao cha afya kama ambavyo sera inasema kila kata iwe na kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Ulaya, nilishaongea muda mrefu kimechakaa, tunaomba Serikali ipeleke pesa kule. Pia Waziri wa Nishati alishafanya ziara pale, aliona kwamba hakuna umeme na alisema atatuletea umeme, watu wanasubiri maeneo ya Mikumi, Ulaya pale tuweze kupata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwamba tuliomba magari, kwa sababu Mikumi pale kuna ajali nyingi sana Mitaa ya Msimba, Ng’apa mpaka Ruaha Mbuyuni lakini sasa hivi kinajengwa pale kituo cha dharura kwa ajili ya ajali na kwamba tutaletewa magari mawili kama ambavyo Mbunge niliomba. Kwa sababu tumegundua kwamba pale Mikumi kuna matatizo mengi ya ajali mbugani na sehemu nyingine na tukasema kwamba tukipata magari ya wagonjwa yatasaidia kukimbiza wale watu wanaopewa rufaa. Maana kutoka Mikumi mpaka Kilosa ni kilometa 78; Mikumi mpaka Morogoro kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ni kilometa 120; Mikumi mpaka Iringa ni zaidi ya kilometa 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani kwamba tumeambiwa haya magari yapo, Wanamikumi wanayasubiri kwa nguvu na kwa hamu kubwa ili tuweze kuwasaidia Watanzania. Maana Mikumi pale inapita barabara kubwa inayotoka Tanzania kwenda Zambia mpaka South Africa, tunaamini hata watu wa Nyanda za Juu wanaopata ajali maeneo yale watapata nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye TARURA. Kwa kweli TARURA bajeti yao ni ndogo na ndiyo maana mwaka jana nilipiga kelele hapa nikisema Wilaya ya Kilosa ni kubwa lakini imekuwa na bajeti ndogo sana, TARURA hawana hata gari. Nashukuru tumeletewa gari lakini bado TARURA uwezo wake ni mdogo. Kuna barabara kutoka Ruaha Mbuyuni - Malolo - Kibakwe; kuna barabara ya kutoka Dumila - Kilosa - Mikumi lakini pia kuna barabara nyingine ya kutoka Ulaya – Madizini - Malolo, hizo zote ziko chini ya TARURA, tunaamini inaweza kutusaidia. Hii barabara ya Dumila – Kilosa iko chini ya TANROADS, naamini nao watatusikia waweze kutusaidia kwa sababu ni barabara muhimu sana kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuongelea kuhusu upungufu wa watumishi na kwa Wizara ya Elimu katika Wilaya yetu ya Kilosa tumekuwa na upungufu mkubwa sana wa walimu. Mfano shule ya msingi ina wanafunzi wa awali wa darasa la kwanza hadi la saba 107,000 lakini walimu wako 2,393 tu na tuna upungufu wa walimu 929. Pia tuna maboma 39 tunaomba Serikali itusaidie; sekondari tuna madarasa pungufu 129, majengo ya utawala 28, nyumba za walimu 689 lakini pia tuna upungufu wa hostels 27. Wananchi wamefanya juhudi kubwa sana ya kujenga maboma tunaamini Serikali itatusaidia ili tuweze kuboresha elimu katika Wilaya yetu ya Kilosa ambayo ni wilaya kongwe sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme kwamba tuko pamoja na Kambi Rasmi ya Upinzani na nimheshimu sana Mheshimiwa Japhary Michael ambaye amewasilisha hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nichangie kwenye hoja iliyoko Mezani ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niungane na Taarifa ya Kambi ya Upinzani na ninaiunga mkono kwa asilimia zote, lakini pia ni Mjumbe wa caucus ya Bunge ya Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGS). Na nitapeleka mchango wangu katika sehemu tatu, nitaanza na masuala ya SGR, lakini nitaongelea Barabara ya Dumila – Kilosa – Morogoro – Mikumi, halafu nitaunganisha na masuala ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya ziara pamoja na hi caucus yetu ya SDGS kutoka Dar-es-Salaam kwenda Morogoro mpaka Kilosa ambapo mradi huu wa SGR umefika. Tuliona jinsi ambavyo kumekuwa na changamoto mbalimbali katika mradi huu pamoja na sifa nyingi ambazo wenzetu wamekuwa wakizisema, lakini kuna changamoto kubwa sana. Na ninasema naunga mkono Taarifa ya Kambi kwa sababu imejaribu kutoa uchambuzi jinsi gani ambavyo tungeweza kuboresha reli hii ya SGR, ili kuleta manufaa yenye tija kwa Watanzania ambao ndio pesa zao zinatumika mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika SGR tumegundua kwamba, malighafi nyingi zinazotumika zinanunuliwa kutoka nje. Unaweza uka-imagine ukiangalia vitu kama cement pamoja na chuma ambacho kinatumika kwa wingi sana katika mradi huu vyote vinaagizwa kutoka nje. Na maana yake ni kwamba, kama tunaagiza hivyo vitu kutoka nje tunatumia pato letu la Taifa na pesa zote za kigeni zinakwenda kwenye mradi huu. Na ndio maana mara nyingi tumekuwa tukisema tumekuwa hatuna vipaumbele katika nchi yetu kwa sababu, mambo ambayo tunayafanya sasa hivi tungeweza kuyafanya na kuyatambua kwa wenzetu walipopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunagundua kwamba, katika Awamu iliyopita ya Nne kipaumbele kilikuwa ni Liganga na Mchuchuma kabla sisi wengine hatujaingia kwenye Bunge hili Tukufu tulikuwa tukisikia Liganga na Mchuchuma, Liganga na Mchuchuma, lakini sasa hivi hicho kipaumbele hatukioni kabisa. Mradi wa Liganga na Mchuchuma ungeweza kutumika chuma chake katika Mradi huu wa SGR ungeweza kupunguza gharama za mradi huu na ungeweza kuwana tija zaidi kuliko sasa hivi tunapotumia pesa nyingi za Watanzania katika mradi wa SGR. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika kipindi sasa kila mtu anakuja na vipaumbele vyake, imekuwa kama ile hadithi ya zamani kwamba, kuku na yai nani ameanza kuzaliwa na vitu kama hivyo. Ndio maana tunasema ili tuweze kufanikiwa ni lazima tukae chini na tuendeleze yale wenzetu waliyoanza Awamu ya Tano ilipaswa kuendelea na jambo hili la Liganga na Mchuchuma, ili kuweza kufanya Mradi wa SGR uwe na tija zaidi kwa Watanzania wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kutembelea huko huu Mradi wa SGR umepita katika Jimbo la Mikumi na SGR Makao yake Makuu pale Kilosa yapo katika Kijiji cha Muungano, Kata ya Mabwerebwere katika Jimbo la Mikumi. Kumekuwa na malalmiko makubwa sana ya wananchi wa pale kwamba, pamoja na kwamba, pale ndio imewekwa kambi, lakini pia wale watu hawajapata vile vipaumbele. Tunatambua kwamba, mradi wowote ambao tunakuwa tunasaini lazima vipaumbele viangalie wananchi waliokaa maeneo yale kwa ajili ya ajira na mambo madogomadogo yanayoenda katika ajira zile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye SGR Wananchi wa Kilosa wamekuwa wanalalamika sana kwamba, wanaachwa katika mradi huu, kazi za udereva, kazi zile za kutumia nguvu na vitu kama hivyo, wamekuwa wanawekwa pembeni na kilio chao kimekuwa kikubwa. Lakini pia, tulitegemea kutakuwa na kipengele katika mkataba wowote tunajua kuna kipengele kile ambacho kinahusu social responsibilities na vitu kama hivyo, lakini tumeona CSR katika mradi huu katika maeneo ya Mikumi na Kilosa yamekuwa hayazingatiwi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, Wananchi wanaokaa pale Mabwerebwere wana changamoto nyingi mradi huu tunategemea kwamba, walivyokuwa pale wangeweza kuwasaidia kwenye masuala ya shule ambapo Wananchi sasahivi wanalalamika na wanachangishana mia mbili mia mbili kwa ajili ya kujenga shule, wana changamoto kubwa ya maji, wana changamoto kubwa ya zahanati. Tulitegemea mradi mkubwa kama huu ungeweza kurudisha kidogo kwa wananchi wa maeneo yale ambao waliacha mashamba yao na vitu vingine mradi huu uweze kupita, lakini wamekuwa na kilio kikubwa sana kwa kusahauliwa na mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, mradi huu umepita katika Kijiji kinaitwa Umunisagala. Hawa watu wa Umunisagala wamekuwa wakilia na malalamiko yao yamekuwa makubwa sana kwa sababu, nao wamesahaulika katika mradi kama huu na wamesahaulika kwa sababu, wametoa ardhi yao. Reli ya zamani ile meter gauge ilikuwa inapita pale, lakini sasahivi SGR imepita eneo lingine kwa sababu ya kukwepa mmomonyoko wa ardhi pamoja na mafuriko ambayo yanatokea maramara kwa hiyo, wamechukua eneo kubwa la Kijiji cha Umunisagala, lakini hawajawazingatia katika masuala mengine ya kijamii kama hayo ya shule, zahanati, maji na vitu vingine kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitegemea hawa wakandarasi ambao wanahusika Yapi Merkezi wangeweza kutoa japo kidogo ili kuweza kuwapoza wananchi wa maeneo yale nao wajisikie kwamba, wana ownership ya mradi ule maana tunaamini kabisa, ili tufanikiwe tunahitaji kuwa na ujirani mwema kati ya wawekezaji pamoja na wananchi wanaoishi maeneo haya. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali izingatie sana kuwaangalia Wananchi wa Wilaya ya Kilosa ambao wengi wamebomolewa nyumba zao, mradi umepita huko; Polisi imebomolewa na ratiba inaonesha kwamba, hata viwanja vya michezo vitabomolewa, itapita reli hii. Sasa hawa watu lazima tuwafikirie na tuwe na jinsi ya kuwa-compensate ili waweze kukaa na kupenda mradi kama huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie suala la reli. Wakati tumeenda kwenye ziara ya SGR pale Kilosa nilizungumza na Mkurugenzi wa Reli Tanzania kwa sababu kulikuwa na changamoto kubwa sana Wananchi wa Mikumi, Kidodi pamoja na Ruaha waliwekewa alama za X kwa muda mrefu. Na pia kulikuwa na reli ya zamani iliyokuwa inatoka kwenye kiwanda cha Sukari Kilombero pale Ruaha inaenda mpaka Kilosa na kubeba mizigo kupeleka sehemu nyingine, kwa kweli, ile reli imekwisha hata mataluma hayapo. Na tulipoongea na Mkurugenzi kwa nini watu wamewekewa reli kama wana nia ya kufufua, walituambia bado hawajapata mtu wa kuweza kuwawezesha kutengeneza hiyo reli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo ninavyoongea hapa leo watu wa reli wamekuja pale Mikumi kuna maeneo ya kikwaraza Mji Mdogo wa Mikumi ambao ni Mji wa Kitalii wameweka na wameweka barrier wamezuia wananchi wasipite na magari yao kwenda kwenye maeneo ya Kikwaraza, maeneo ya Tambukareli ambayo kwa kweli ni sehemu ambayo ardhi yake sasa ndio wawekezaji wengi wa masuala ya Campsite wamenunua maeneo hayo. Kama mnaona kwenye Tv kuhusu Mji Mpya wa Mikumi ni maeneo hayo ambayo watu wa reli leo wameziba na kuzuwia Wananchi wasiende. Sasa unaona watu wa Campsite wanashindwa kuwekeza kwenye Mji wa Kitalii. Tutapata wapi pesa za utalii kama tunaanza kushindwa kuwekeza na kuweka vitu vizuri katika mpangilio kama huo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana watu wa reli waliangalie hilo. Huo Mji Mpya wa Mikumi unahitaji sana kuweza kuzingatiwa na kutoa nafasi kwa Wananchi, ili waweze kuwekeza zaidi kwenye jambo la utalii ambalo litaongeza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo tangu nimeingia kwenye Bunge lako Tukufu nilikuwa nikizungumzia Barabara ya Dumila – Kilosa – Mikumi. Hii ni barabara ya kilometa 142 na ilikuwa ni ahadi ya tangu Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Awamu ya Nne na alipokuja Rais Dkt. Magufuli pia kwenye kampeni zake aliahidi kuijenga kwa lami. Nashukuru nimeona kwamba, kuna bilioni mbili zimetengwa, lakini bado kuna nafasi kubwa sana ambayo bado haijazingatiwa maana katika kilometa 142 zilizojengwa kwa lami ni kilometa 45 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwenye kitabu cha Waziri katika ukurasa wa katikati hapa 166 inaonesha kwamba, watatengeneza kwa kilometa 20 tu, lakini awamu hizi zilisema kwamba, itatoka Dumila mpaka Ludewa kwa kilometa 45 halafu itatoka Ludewa mpaka Ulaya halafu ikitoka Ulaya itamalizia Mikumi, lakini wamesema watatengeneza kilometa 24 tu ambazo zitatoka Ludewa mpaka Kilosa. Sasa ninataka Waziri akija atuambie ni lini wataanza kujenga awamu ya kilometa 78 kutoka pale Kilosa mpaka Mikumi ambapo kuna kata nyingi zipo katikati zinazotegemea barabara hii kwa ajili ya kujenga uchumi kwa Wananchi wa Wilaya ya Kilosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kata ambazo ziko njiani katika barabara hii ya kilometa 78 ni Kata ya Magomeni, Kata ya Masanze, Kata y Zombo, Kata ya Ulaya, Kata ya Muenda na Kata ya Mikumi. Unaweza ukaona jinsi ambavyo kama barabara hii itatengenezwa itaweza kusaidia na ku-boost uchumi wa Wananchi wa Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nilitaka nizungumze kuhusu mawasiliano. Niliuliza swali wiki mbili zilizopita na Naibu Waziri alinijibu kwamba, hawawezi kupeleka mawasiliano kwenye vijiji ambavyo vina mtandao wa aina moja, lakini hivyo vijiji nilivyovitaja havina mtandao kabisa katika Jimbo la Mikumi na niko mbioni kuandika barua kukuletea Naibu Waziri, ili uweze kuona vijiji ambavyo namaanisha. Vijiji hivi vipo kwenye Kata za Vidunda maeneo ya Chonwe, Naudung’u, Itembe, lakini Kata ya Kisanga, kuna Kata ya Tindiga, Malangali kule kwa Lukwambe pamoja na Malui, lakini Uleling’ombe, maeneo ya Mlunga na Lengewaa, lakini pia kuna maeneo ya Masanze, Munisagala, Chabina na Dodoma Isanga, lakini pia kuna Kata ya Muenda ambapo bado mawasiliano hayajafika katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa ulisimama na kunijibu hapa na kusema bado unaendelea na tathmini na nia yenu ni kuleta mawasiliano kwa Wananchi wa Jimbo la Mikumi, mtusaidie kuzingatia maeneo haya ambayo yanahitaji sana mawasiliano kwa ajili ya uchumi wao. Asante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, nami nichangie kidogo kwenye Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Jimboni kwangu Mikumi kuna kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambacho kinafanya kazi nzuri sana ya uzalishaji wa sukari, lakini kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu sana kutoka kwa wafanyakazi zaidi ya 3,000 waliofukuzwa kazi bila kulipwa mafao yao mwanzoni mwa mwaka 2000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha afafanue ni lini hawa wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi Kilombero Sugar Company kabla haijabinafsishwa kwa Illovo watalipwa mafao yao? Pia kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wakulima wa nje (outgrowers) ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu kupunjwa sana kwenye mzani ambao unamilikiwa na wenye kiwanda. Je ni lini Serikali itawaagiza wenye kiwanda cha Illovo kuweka mzani utakaokuwa wa uwazi ili kuwafanya wakulima kupata haki yao ya kujua mazao yao yanayoingizwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wakulima wa miwa wa Bonde la Ruhembe wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya kipimo cha Sucrose (utamu) ambayo wamekuwa wakipunjwa kwa kuambiwa utamu wa miwa yao ni mdogo sana hivyo kulipwa fedha kidogo sana pia. Wakulima wa bonde la Ruhembe wamekuwa wakiomba sana kwamba pamoja na kulipwa sucrose pia walipwe na molasses na buggers ambazo zinatumiwa na watu wa kiwanda cha Illovo kutengeneza mashudu, mbolea, spirit na hata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakulima wa Bonde la Ruhembe wanalia sana bila matumaini kwa nini wanalipwa utamu (sucrose) peke yake wakati mazao yao yanatoa pia products zingine ambazo wenye kiwanda cha Illovo wanazitumia na kuuza bila kuwalipa tofauti na nchi za jirani kama Kenya na Malawi ambako wakulima wanalipwa pia fedha za bugger na molasses na kuwasaidia sana kufaidika zaidi na kilimo hicho cha miwa na kuwaongezea zaidi uchumi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri, atakapokuja ku-wind up atuambie ni kwa nini Serikali haiwaagizi wamiliki wa viwanda kwanza kuwalipa wakulima wa miwa bei nzuri za Bugger na molasses? Sambamba na hilo kwa nini bado bei ya tani ya miwa kutoka kwa wakulima wa nje bado inasuasua?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa kuwa pale Kijiji cha Mufilisi kingejengwa kiwanda kingine kidogo cha Sukari ifikapo mwaka huu wa 2017, lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya kujengwa kwa kiwanda hicho cha sukari pale Mufilisi ambacho kingesaidia sana kuleta ajira na pia kurahisisha usafirishaji wa miwa kutoka Kata za Mikumi na Kisanga. Je mpango huo wa kiwanda cha sukari cha Mufilisi kimefikia wapi na ni lini kitakamilika na kuanza kazi? Au ndiyo yale yale ya kwenye utaratibu bila kutekelezeka?

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa kwenye Jimbo la Mikumi Kata za Malolo, Masanga, Mhenda, Mabuerebuere, Kilangali na Tindiga kuna mazao ya aina mbalimbali tena kwa wingi sana, nadhani sasa Serikali ili iweze kufikia malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda basi ingeangalia sana umuhimu wa kujenga viwanda vidogo vidogo kwenye Jimbo la Mikumi, ambayo pia vingeenda sambamba na kuhakikisha umeme unafika kwenye kata hizi za Jimbo la Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika kurekebisha miundombinu ya barabara, naamini kabisa kilimo kinacholimwa Jimboni Mikumi kitasaidia sana kufanikisha kutoa ajira kwa wananchi wengi zaidi; pia kufikia malengo ya Serikali hii ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini vile vile kufanikisha kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa ghala la Taifa. Tumebakiwa na ardhi nzuri, kubwa na yenye rutuba na Wanamorogoro wapo tayari kulima kwa bidii; cha msingi ni kuwawekea viwanda ili wapate uhakika wa masoko ya mazao yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara hii nyeti na muhimu sana ya Maji na Umwagiliaji. Ni ukweli ulio dhahiri kabisa kwamba Wizara hii ni muhimu sana na ni uti wa mgongo wa Taifa hili na pia ninaunga sana ule msemo wa maji ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitoe shukrani zangu za dhati kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mheshimwa Engineer Kamwelwe kwa kufanya ziara muhimu kabisa Jimboni kwangu Mikumi na Wilayani kwetu Kilosa kwa ujumla. Mheshimiwa Kamwelwe alipokuwa Jimboni Mikumi alifanya na kuahidi mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha maji cha Sigareti kilichopo kata ya Ruaha, Mheshimiwa Naibu Waziri alituma wataalam wa Wilaya ya Kilosa wakakague chanzo hiki na wataalam walifanya hivyo na kunipa report ya kitaalamu kuwa chanzo hiki cha Sigareti ni chanzo cha mserereko chenye maji mengi, safi na salama, kinaweza kutoa huduma kwa wananchi wa kata ya Ruaha yenye wakazi zaidi ya 30,000 na kata za jirani za Ruhembe na vijiji vyake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulikadiriwa kufikia kiasi cha pesa cha shilingi bilioni mbili na kidogo na nilipomletea Mheshimiwa Naibu Waziri aliahidi kuwa kiasi hicho cha pesa kitawekwa kwenye bajeti hii ya mwaka 2017/ 2018. Niliwaambia wananchi wasikivu wa kata ya Ruaha ambao walifurahi sana na kutoa pongezi nyingi kwa Serikali hii kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu, lakini cha kusikitisha bajeti ya chanzo hiki muhimu cha maji cha Sigareti haipo kwenye taarifa ya bajeti hii.

Naomba Waziri atimize ahadi yake kwa wananchi wa kata ya Ruaha na kuwawekea au kutenga pesa hizo shilingi bilioni mbili ili mradi huu muhimu wa maji uweze kuanza kujengwa na kuokoa vifo vya akina mama na watoto wa kata ya Ruaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Madibila katika kata ya Mikumi niliwahi kuuliza ni lini Serikali itakarabati miundombinu na intake ya chanzo cha maji cha Madibila ambacho kilijengwa mwaka 1975 wakati idadi ya wakazi wa Mikumi ni watu 6000 tu na sasa imepita miaka 40 miundombinu ni ile ile chakavu sana na wakazi wa Mji Mdogo wa Mikumi wamefikia watu 30,000 na zaidi, Naibu Waziri alianiahidi kwenye majibu yake kuwa wanalitambua tatizo hilo na watalifanyia kazi kuanzia mwezi Julai mwaka huu, lakini sijaona pesa zikiwa zinatengwa specifically kwa ajili ya chanzo hiki muhimu cha maji cha Madibila kwa wakazi wa Mji Mdogo wa Mikumi. Naomba majibu je, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya mradi huu wa chanzo cha Madibila.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vya maji vya Iyovi na Mto Mholanzi ni wazi Mji wa Mikumi ni mji wa kitalii na unakua kwa kasi sana kwa kupata wageni na watalii mbalimbali kutoka kona zote za dunia. Tatizo sugu la maji linapunguza sana kasi ya wawekezaji wa mahoteli na sekta mbalimbali za kukuza uchumi wakati Mikumi ina vyanzo vingi sana vya maji kama Mto Iyovi na Mto Mholanzi. Je, ni lini sasa Serikali itavifanyia kazi vyanzo hivi vyenye maji mengi tena ya gravity au mserereko vyenye gharama nafuu kabisa kuokoa wananchi wa Mikumi na kukuza mji na uchumi wa wananchi wa Mikumi kama ambavyo wenzetu wa Kanda ya Ziwa walivyotumia vizuri Ziwa Victoria kupunguza tatizo hili sugu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mradi wa maji wa vijiji kumi katika kata ya Mikumi na Kidodi. Mradi wa Maji wa Visima wa World Bank kata ya Mikumi bado unasuasua na haujakabidhiwa kwa wananchi kama iliyoahidiwa na Mkandarasi Malaika Construction, pamoja na Serikali kumpatia shilingi milioni 208 alizoomba. Pia vituo vya maji 52 vimeanza kuharibika kwa kuwa vilijengwa muda mrefu na tanki la lita 300,000 bado wananchi hawaoni mwanga wa kupata maji safi na salama ingawa majaribio yalifanyika na akinamama na watoto wa Mikumi walifurahi sana kuona maji yanatoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kustaajabisha mpaka leo mradi huu haujakabidhiwa kwa wananchi. Tunataka kujua ni lini mkandarasi Malaika atakabidhi mradi huu kama alivyokuahidi wewe na wananchi wa Mji Mdogo wa Mikumi? Pia Mradi wa Msowero uliopo kata ya Kidodo ulikabidhiwa kwa wananchi wa kata ya Kidodo tangu mwaka 2015, lakini cha kushangaza ni kuwa tangu mradi huu umekabidhiwa kwa wananchi maji hayatoki, naomba kauli ya Serikali kuhusu mradi huu muhimu wa Msowero uliopo kata ya Kidodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Lengewaha kata ya Uleling’ombe, tunaomba sana Serikali imlipe pesa mkandarasi wa mradi huu ili arudi site, maana hayupo kwa muda mrefu na tunaomba tujue tatizo liko wapi na kama ameshindwa kazi basi afukuzwe na kuvunja naye mkataba, na kama anadai basi alipwe pesa zake ili aendelee na umaliziaji wa mradi huu muhimu kwa wananchi wa Uleling’ombe, ambao wanakunywa maji machafu ya mto huku waki-share na wanyama na kusababisha magonjwa ya mara kwa mara ya mlipuko na kusababisha vifo kwa mama zetu na watoto wa Kata ya Uleling’ombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu visima, tunaiomba sana Serikali itukumbuke kutuchimbia visima virefu na vifupi hasa kwenye kata za Mhenda, Malolo, Ulaya, Msanze, Kilangali, Mabwerebwere, Tindiga, Ruhembe, Vidunda, Ruaha, Kisanga Zombo, Mikumi, Uleling’ombe na Zombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nimalizie na suala la umwagiliaji, nilishawahi kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji ni lini Serikali itatoa tamko na kutuma wakaguzi wakakague mradi wa umwagiliaji wa Bwawa la Dachi lililopo kwenye kata ya Malolo, ambapo Serikali kupitia ufadhili wa Shirika la Kijapan la JICA ambao walitoa zaidi ya shilingi milioni 600 ambazo zimeliwa na bado makingio ya mchanga unaohatarisha Mto Mwega kujaa mchanga, na kupoteza kabisa nia njema ya wananchi wa Kata ya Malolo wanaoutegemea kwa kilimo cha umwagiliaji vitunguu, mboga mboga na mazao mengine muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, makingio hayo yamejengwa chini ya kiwango, michanga bado inajaa kwenye mto mwega, shilingi milioni 600 zimeliwa na hakuna mtu yeyote anayehoji kuhusu ubadhirifu huu mkubwa sana unaohatarisha maisha ya wananchi wetu wa kata ya Malolo. Naomba Waziri akija kuhitimisha atuambie ni lini atakuja kata ya Malolo akiongozana na mimi ili kusikia kilio kikuu cha wananchi hawa kuhusu Bwawa la Dachi na shida yao ya maji ambayo yanahatarisha maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kumalizia Naibu Waziri akijibu swali langu alijibu kuwa mkandarasi wa Bwawa la Kidete lililopo Wilayani Kilosa mkataba wake umesitishwa na tender itatangazwa hivi karibuni, nimeona kwenye ukurasa wa 47 wa hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji kuwa ni moja kati ya mabwawa yatakayojengwa kwenye bajeti hii ya mwaka 2017/2018. Wananchi wa Wilaya ya Kilosa wanataka kujua ni kiasi gani kimetengwa kwenye ujenzi wa bwawa hili muhimu la Kidete ambalo linasababisha mafuriko ya mara kwa mara Wilayani Kilosa yanaharibu makazi ya watu. Vifo vya wakazi wa Wilaya ya Kilosa na pia mafuriko yanayosababishwa na Bwawa la Kidete yanasababisha uharibifu mkubwa sana, reli yetu ya kati ambayo Serikali inajitahidi kuijenga kwa kiwango cha standard gauge na lini ujenzi huu wa Bwawa la Kidete utaaanza. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara hii ya Afya na Maendeleo ya Jamii. Kwanza kabisa naunga mkono mapendekezo ya Kamati maana na mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa kabisa ni upungufu na uchakavu wa zahanati na katika jimbo zima la Mikumi lenye kata 15 lina vituo vya afya viwili tu; yaani Kituo cha Afya cha Ulaya na Kituo cha Afya cha Kidodi ambacho tunashukuru sana tulipokea shilingi milioni 400 kwa ajili ya kukitanua na kukiboresha ili kiweze kuokoa maisha ya mama zetu na watoto pia kufanya upasuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vituo viwili tu vya afya kwenye jimbo zima la Mikumi havitutoshi, Kituo cha Afya cha Ulaya kina hali mbaya sana, kimechakaa sana lakini pia kina upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya, wananchi wanateseka sana, wengi wanakimbilia hapo lakini kusema ukweli huduma zimekuwa mbaya sana na kuumiza sana wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati zetu katika Jimbo la Mikumi zina hali mbaya sana na mimi kama Mbunge nimeshirikiana bega kwa bega na wananchi wenzangu wa Kata ya Malolo (vijiji vya Chabi na Mgogozi) kujenga zahanati mbili na tupo kwenye umaliziaji, lakini pia kwenye Kata ya Masanze zahanati ya Kijiji cha Dodoma Isanga niliezeka kwa Mfuko wa Jimbo pia. Zahanati ya Kijiji cha Muungano na Nyali ambapo nimezikarabati pia kwa kupitia Mfuko wa Jimbo mwaka 2016/2017 lakini bado tuna changamoto kubwa sana kwenye Jimbo la Mikumi na tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia kuunga mkono jitihada hizi za wananchi wa Jimbo la Mikumi.

Lakini pia Mji Mdogo wa Mikumi ambao kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 inaonesha kuwa kuna idadi ya watu wapatao 21,113 lakini Zahanati ya Mikumi imechakaa sana na ina uwezo mdogo sana wa kuhudumia wananchi hawa ambao wengi ni akina mama. Hivyo tunaomba sana Mheshimiwa Waziri na Serikali iweze kuboresha na kutanua ujenzi wa Zahanati ya Mikumi kuwa Kituo cha Afya ili kuondokana na adha ya huduma ya afya wanayoipata wakazi wa Mji Mdogo wa Mikumi; lakini pia Serikali iweze kusaidia ukarabati wa Zahanati za Uleling’ombe, Zombo, Kisanga, Tindiga, Vidunda, Mhenda, Ruhembe na Mabwerebwere na pia jiografia ya Jimbo la Mikumi ni mbaya sana hivyo tunaomba sana Serikali iweze kutusaidia magari ya wagonjwa ili tuweze kuokoa maisha ya akina mama na watoto ambao wengi sana wanapoteza maisha kwa sababu ya ukosefu wa ambulance na usafiri wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mji Mdogo wa Mikumi una hopsitali ya taasisi ya dini ya St. Kizito ambayo imekuwa ikitoa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa mji wa kitalii wa Mikumi, lakini pia watu wa mataifa mbalimbali wanatumia barabara kuu ya Tanzania mpaka Zambia mpaka Afrika Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na umuhimu wa hospitali hii ya St. Kizito, Serikali ilikuwa inatoa ruzuku na kulipa mishahara ya baadhi ya watumishi, lakini katika hali ya kusikitisha hospitali hii haijapata ruzuku hii kwa miaka kadhaa mfululizo na nilipokwenda kuzungumza nao walisema walikuwa wanapewa shilingi milioni 60 kwa mwaka ambazo kwanza zilikuwa hazitoshi. Lakini pia kwa sasa hawajazipata kwa miaka mitatu mfululizo, lakini pia kuna tetesi kuwa Serikali imeamua kusitisha mikataba na hospitali hizi muhimu za taasisi za kidini ambazo kwenye Wilaya yetu ya Kilosa zipo mbili yaani St. Kizito na Hospitali ya Berega ambayo ipo pia kwenye Wilaya yetu ya Kilosa. Tunaomba sana majibu ya Mheshimiwa Waziri ili tujue wameamua kuvunja mikataba yao na hospitali hizi za taasisi za kidini? Na kama jibu ni hilo Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Kilosa hasa Jimbo la Mikumi ambao wengi ni maskini na gharama za huduma ya afya zimekuwa kubwa sana na wameshindwa kuzimudu kutokana na taasisi hizo kutoza pesa nyingi kwa wananchi ili ziweze kujiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna upungufu mkubwa sana wa Maafisa Maendeleo kwenye kata zetu nyingi za Jimbo la Mikumi, lakini pia kwa masikitiko makubwa sana nifikishe malalamiko makubwa sana kwa Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kilosa kwa kufanya kazi zake kisiasa zaidi na kushindwa kushirikiana na taasisi zinazotaka kuja Wilayani Kilosa hasa Jimboni kwangu Mikumi kwa kushindwa kutoa vibali kwa taasisi hizo zinazotaka kuja kutoa elimu kwa wananchi hasa vijana, akina mama na wazee ili waweze kujiunga kwenye vikundi na kushirikiana na Ofisi ya Mbunge na Serikali ya Wilaya ili waweze kujiletea maendeleo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ambayo inaitwa Tanzania Bora Initiative ambayo ilionesha nia njema ya kuja kutoa elimu na kuwaunganisha vijana kwenye Jimbo la Mikumi na Handeni na walifuata taratibu zote za Kiserikali ili waweze kusaidia wananchi wa maeneo hayo, lakini katika hali ya kusikitisha Afisa Maendeleo ya Wilaya ya Kilosa mpaka sasa anawapiga chenga kuwapa kibali cha kufanya kazi hii njema ya kuwafanya wananchi wajiunge pamoja na kujiletea maendeleo, tena kwa kushirikiana na Serikali bila sababu za msingi na wamefuatilia kibali hicho cha kuja kufanya shughuli hizo muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa, Jimboni Mikumi ili waweze kushirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo yao. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii nyeti ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Sukari cha Illovo – Kilombero; kumekuwa na malalamiko makubwa sana ya wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi kwenye Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kilichobinafsishwa na Serikali mwaka 1999-2000 ambapo wafanyakazi zaidi ya 3000 mpaka leo hawajalipwa fidia zao na wanapigwa danadana na hawapewi majibu ya kueleweka ya fidia zao, wengi ni watu wazima wengine wanakufa bila kulipwa haki zao na wengine wanategemea fidia hiyo ili waweze kusomesha watoto wao na pia kujiendeshea maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri atakapokuja atupe majibu ni lini wananchi hawa waliokuwa wanafanya kazi Kiwanda cha Sukari Kilombero watalipwa fidia zao ambazo ni haki yao ya msingi? Pia kwenye Kiwanda cha Sukari cha Illovo kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu sana ya wakulima wa miwa kuhusu upimaji wa sucrose, upimaji wa mzani na bei ya miwa yao wanayokipeleka kiwandani kutokuwa ya uwazi kabisa, maana vitu vyote muhimu vinafanywa na kiwanda yaani upimaji uzito, utamu na upangaji wa bei wote unafanywa na kiwanda na kuwabana sana wakulima wa nje (out growers). Je, ni lini Serikali itawaamuru wawekezaji hawa kuwapa wakulima mzani huru wa tani za miwa, utamu na ni lini wakulima hawa wataanza kulipwa kutokana na buggers na sprit ambapo sasa hivi wanalipwa utamu wa muwa peke yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kidogo cha sukari cha Mufilisi – Mikumi; Serikali kwenye bajeti ya 2015/2016 ilikuja na bajeti na kusema wametenga pesa za kuanzisha Kiwanda cha Sukari cha Mufilisi. Je, zoezi hili limeishia wapi? Maana sasa kwenye bajeti hatuoni tena likizungumzwa na halipo kabisa. Je, Serikali inaweza kutuambia tumekwama wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya kusindika nyama, nyanya, ngozi, maziwa, viazi na matunda na mboga mboga, mbaazi; Mheshimiwa Waziri Wilaya ya Kilosa tumebarikiwa mifugo mingi sana na wingi huo wa mifugo unasababisha changamoto kubwa sana ya mapigano ya wakulima na wafugaji, kwa sababu wafugaji wamezidiwa sana na mifugo mingi na hawana pa kuwapeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali iangalie umuhimu wa kuanzisha viwanda vya kusindika nyama, ngozi, maziwa ili wafugaji hawa wapate uhakika wa soko la kuuza mifugo yao na kupunguza mifugo yao tofauti na sasa ambapo tunawaambia wafugaji wapunguze mifugo yao. Je, waipeleke wapi wakati hawana masoko ya uhakika ya kuuza mifugo yao, naomba Waziri uliangalie sana hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya kusindika nyanya, viazi, mbogamboga, mbaazi na matunda; wakulima wengi wa Wilayani Kilosa wanalima sana mazao haya na mengine mengi, kitendo cha kukosa soko la uhakika kinawapa umaskini mkubwa sana na kuwakatisha tamaa ya kuendelea kulima wakati wote, tunajua kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu. Tunaomba sana Serikali itusaidie jimboni Mikumi tupate viwanda vya kusindika mazao haya ili tuweze kumkomboa mkulima wa Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla hasa kwenye kata zinazoongoza kwa kilimo kama Kata za Kisanga, Tindiga, Mabwerebwere, Vidunda, Malolo, Kilangali, Mhenda, Zombo, Ulaya, Masanze, Ruaha, Mikumi, Kidodi, Ruhembe na Uleling’ombe. Hili naomba majibu ya Waziri ni lini watatujengea viwanda vya kusindika mazao jimboni Mikumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, COSOTA; bajeti inayopelekwa na kutengwa kwenye taasisi hii muhimu ni ndogo sana na inapelekea COSOTA kushindwa kutimiza wajibu wake sawasawa. COSOTA ni chombo muhimu sana kinapaswa kiangaliwe kwa jicho la kipekee sana maana ndicho chombo kinachoweza kuwasaidia wanamuziki wetu wa Tanzania kwenye wizi wa kazi zao ambacho kimsingi wizi wa kazi za wasanii ndicho kilio kikubwa sana cha wasanii wetu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Sheria ya Hakimiliki na Hakishirika Namba 7 ya mwaka 1999 imepitwa sana na wakati na imekosa meno kabisa, niiombe sana Serikali kama kweli ina nia thabiti na dhamira ya kweli ya kuwasaidia wasanii wa nchi hii basi ilete muswada wa sheria hii Bungeni ili tuweze kuirekebisha na kuipa nguvu ili tuweze kuwakomboa wasanii wetu wengi waliojiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji, Jimbo la Mikumi lina ardhi nzuri na bora tena kubwa sana na tumebarikiwa sana kuwa na vyanzo mbalimbali na vingi vya maji kwenye mito mbalimbali na ardhi yetu maji yapo juu kabisa kwa maana ya water table. Tunaomba sana Serikali iweze kutupatia ardhi kubwa sana ambayo imetekelezwa na wawekezaji ambao wanahodhi mashamba hayo makubwa bila kuyaendeleza. Kurudishwa kwa mashamba hayo kutawezesha sana wawekezaji wengi kuweza kuja jimboni kwetu Mikumi na Wilayani kwetu Kilosa ili tuweze kutoa ajira zaidi kwa Wanamikumi na pia kuweza kuleta maendeleo kwa wanakilosa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho tunaomba sana Serikali itupie macho kwenye Jimbo la Mikumi ili waweze kutuletea wawekezaji maana Mikumi inajitosheleza katika kila sifa inayotakiwa na wawekezaji ili waje na kufanya uwekelezaji hasa kwenye masuala ya kilimo, utalii na viwanda. Ahsanteni sana na karibuni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe nichangie kidogo kwenye Wizara hii nyeti ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mawakala wa pembejeo, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelezo Bungeni kuwa wanafanya uhakiki wa mawakala wanaopaswa na kustahili kulipwa. Je, hili suala limefikia wapi na lini mawakala hawa wa pembejeo watalipwa stahiki zao maana wengi wamefilisika na wengi wanakufa maskini huku haki zao zikiwa mikononi kwa Serikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, kwanza ni masikitiko makubwa sana kuendelea kuona kwa miaka miwili mfululizo sasa pesa za maendeleo katika sekta ya mifugo – Fungu 99 na sekta ya uvuvi – Fungu 64 hazijapelekwa mpaka sasa. Naiomba sana Serikali kama kweli ina nia thabiti ya kuwasaidia wafugaji wetu na wavuvi wa nchi yetu, basi ipeleke pesa za maendeleo kwenye sekta hizi muhimu ili tuweze kuwakomboa Watanzania wenzetu wanaoteseka sana ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Spika, Ranchi ya Mkata kwa muda mrefu sana imekuwa kama kichaka cha wahalifu na kushindwa kusaidia wafugaji wetu kufuga, kulima, malisho na kukodishia wafugaji na kusababisha wafugaji wengi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Kilosa kukosa njia mbadala ya kupata njia bora ya kufuga mifugo yao. Tunaomba Serikali iangalie sana ranchi hii.

Mheshimiwa Spika, bado kuna migogoro mingi ya wakulima na wafugaji kwenye Wilaya ya Kilosa na hii inatokana na ufinyu wa ardhi bora na wingi wa mifugo. Wafugaji wana mifugo mingi sana hata wanakosa maeneo ya malisho na maji ya kutosha (malambo) na kusababisha kuingiliana sana na mashamba ya wakulima na kusababisha migogoro isiyokwisha ya wafugaji na wakulima. Tunaiomba sana Serikali ipunguze maeneo ya ranchi na maeneo tengefu na kuyagawa kwa wafugaji ili waweze kupata maeneo ya kufugia, malisho, malambo na majosho.

Mheshimiwa Spika, lingine ni mipaka ya vijiji vya ufugaji na maeneo tengefu na hifadhi. Kuna migogoro mikubwa sana kati ya maeneo (vijiji) vya wafugaji kama Mufilisi na Mkaa Endelevu na vijiji vingine kama Kiduhi na mipaka ya Hifadhi ya Mikumi na vijiji vingine vya wafugaji kama Parakwiyo, Mbande na Twatwatwa vilivyopo Wilayani Kilosa na ambavyo vimekuwa na migogoro ya mipaka na hifadhi na baadhi ya vijiji vya wakulima. Tunaomba sana Serikali itupie jicho jambo hili na kumaliza migogoro hii ya muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kilosa ina upungufu mkubwa sana wa majosho, malambo na malisho ya mifugo. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali iweze kuwasaidia wafugaji wetu hao pamoja na madawa ya mifugo yao ambayo mingi inakufa kwa magonjwa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukiwaomba sana wafugaji wapunguze mifugo yao kwenye Wilaya ya Kilosa lakini hatujawaandalia masoko ya mazao yao ya mifugo. Tunaiomba sana Serikali kujenga viwanda vya mazao ya mifugo kama viwanda vya kusindika nyama, maziwa na viwanda vya ngozi katika Mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Kilosa ili kuweka mazingira wezeshi na rahisi kwa wafugaji wetu kuweza kufuga mifugo michache na yenye tija kwa Taifa letu. Ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, nianze na suala la migogoro isiyokwisha kati ya Hifadhi ya Mikumi na Vijiji vinavyopakana na hifadhi.

Mheshimiwa Spika, jana tu kumetokea mauaji ya vijana wawili katika Kijiji cha Ilakala kilichopo kwenye Kata ya Jimbo la Mikumi. Huu ni muendelezo tu wa mauaji ya watu wetu wengi katika Jimbo la Mikumi. Tunaiomba sana Serikali iweze kuingilia kati na kutoa adhabu kwa wahusika ambao wanasababisha mahusiano mabaya kati ya hifadhi zetu na vijiji vinavyopakana na kusababisha migogoro ya muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, tembo wamekuwa kero sana katika Vijiji vya Kilangali, Mhenda, Mululu na kadhalika na kusababisha uharibifu mkubwa sana wa mazao, mali na hata watu kupoteza maisha. Njia hii inayotumiwa na Serikali ya Awamu ya Pili imeshindwa kabisa kwa kiasi kikubwa kusaidia kudhibiti tembo hao. Tunaomba sana Serikali ianzishe vituo vyenye askari katika maeneo haya muhimu ili waweze kusaidia kudhibiti tembo hawa ambao wanaleta madhara makubwa sana kwa wananchi wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia kidogo kwenye Wizara hii muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipouliza swali mara kadhaa hapa Bungeni kuhusu ni lini Serikali itajenga daraja muhimu la Mto Ruhembe lililopo kwenye Kata ya Ruhembe Jimboni Mikumi, aliyekuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI ambaye sasa ni Waziri aliahidi kututengea Sh.700,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo kwa kuwa wanatambua umuhimu wake na vifo vingi vinavyosababishwa na maji mengi ya mto huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha mpaka leo bado hakuna kinachoendelea maana mpaka sasa hata yale machuma ya daraja yaliyoletwa kutoka Chekeleni yamewekwa chini na hakuna kinachoendelea na madhumuni yake yalikuwa yaletwe ili lijengwe daraja la muda wakati tunasubiri kuletewa fedha za ujenzi wa daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu aweze kutujibu ni lini pesa hizo Sh.700,000,000/= zitaletwa na je, vyuma vya daraja la muda ni lini vitaweza kuunganishwa na kusaidia wananchi kwa muda muafaka maana vinapokaa pale kwa muda mrefu vinasababisha hali ya wananchi kuwa mbaya na pia watu wenye nia mbaya wanaweza kuviiba na kuitia hasara kubwa sana Serikali na wananchi wa Jimbo la Mikumi kwa ujumla. Tunaomba sana tupate majibu ni lini Serikali italijenga daraja hili muhimu la Ruhembe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imekuwa ikiahidi mara kwa mara kumalizia ujenzi wa barabara ya lami kuanzia Dumila – Kilosa mpaka Mikumi ambayo imekuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano kuwa barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho Mji Mdogo wa Mikumi unakua kwa kasi sana na ni mji wa kitalii, je ni lini Serikali itajenga kituo cha afya kwenye Mji Mdogo wa Mikumi? Maana Zahanati ya Mikumi ni chakavu sana na imezidiwa kabisa uwezo na idadi kubwa sana ya watu wengi pale Mikumi na vitongoji vyake, hivyo tunahitaji sana kuwe na kituo cha afya ili kiweze kuhudumia wananchi na watalii na wanaotumia barabara ya Tanzania - Zambia ambapo kuna ajali nyingi sana maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao ya wafanyakazi wa iliyokuwa Kilombero Sugar Company ambayo mwaka 1999 ilibinafsishwa kwa mwekezaji wa Illovo. Wafanyakazi zaidi ya 3,000 ambao walifanya kazi kwa weledi mkubwa walishastaafishwa mwaka 1999 – 2000. Kampuni ya Kilombero Sugar ilipobinafsishwa mpaka sasa wanapigwa danadana kuhusu mafao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge nilishafanya jitihada za kuwaleta wawakilishi wa wazee hawa mpaka kwa Waziri Jenista Mhagama, lakini mpaka leo bado hawajapatiwa ufumbuzi wa malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilileta mara kadhaa swali la msingi hapa Bungeni, lakini cha kustaajabisha swali hili limekuwa haliletwi kabisa kwenye order paper, jambo ambalo linatupa wasiwasi kwamba, Serikali haina majibu ya swali lao kwamba ni ni lini watu hawa maskini watalipwa mafao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli alipofanya ziara kwenye uzinduzi wa barabara ya Kidatu – Kilombero, nilimwomba atusaidie ili wafanyakazi hawa ambao wengi wao wameshakuwa watu wazima sana na wengine wameshatangulia mbele za haki, bila kulipwa stahiki zao kitu ambacho kwa kweli kinawafanya waishi kwenye maisha duni sana huku wengine wakiwa hawana hata uwezo wa kuhudumia familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa kabisa, Mheshimiwa Rais ambaye aliwapa moyo sana wananchi hawa kwa kuwaambia kuwa atahakikisha wanapata stahiki zao na atazungumza na Mawaziri husika lakini mpaka leo wananchi hawa bado hawajapata majibu yoyote na hawajui leo yao wala kesho yao. Namwomba sana Waziri akija kwenye majumuisho ya hoja yake, atupe majibu; Je, ni lini hasa waliokuwa wafanyakazi 3,000 wa Kilombero Sugar Company watalipwa mafao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wa Serikali waliopunguzwa na baadaye kurudishwa kwenye zoezi la vyeti feki; kuna idadi kubwa sana ya watumishi katika Wilaya ya Kilosa ambao walipunguzwa kwenye zoezi la vyeti feki, lakini baadaye wakaonekana wanastahili kuendelea na kazi lakini mpaka sasa hawajalipwa pesa zao walizokuwa wanastahili, kupokea kipindi walipokuwa Watendaji wa Vijiji, Walimu, Watumishi wa Afya, Madereva na kadhalika. Nakumbuka Waziri wa Utumishi alisema, watu wote waliosimamishwa kimakosa watalipwa stahiki zao, ningependa kujua, je, watumishi hawa wa Serikali watalipwa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya TARURA ni ndogo sana, lakini pia TARURA wanafanya kazi yao ya kutengeneza barabara za ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa kusuasua sana, kwa mfano, barabara ya Ruaha Mbuyuni – Malolo – Kibakwe ambayo ni muhimu sana kwa wakulima wetu na kwa umuhimu huo pia, barabara hii inaunganisha Mikoa ya Morogoro – Iringa na Dodoma. Tuliomba ipandishwe hadhi ili ihudumiwe na TANROAD lakini mpaka sasa barabara hii inaharibika sana na kuna kipindi haipitiki kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya muhimu ya Ulaya – Madizini – Malolo – Kibakwe pia ni muhimu sana inayounganisha Mikoa ya Morogoro – Iringa na Dodoma, lakini imekuwa haipitiki hasa kipindi kama hiki cha masika, naomba sana waifikirie ili iweze kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kusuasua sana kwa zoezi la uunganishwaji wa nishati ya umeme kwenye Jimbo la Mikumi, ningependa kujua; je, ni lini Serikali itaweka umeme kenye barabara kuu ya Tanzania – Zambia hasa maeneo ya kona za Msimba, Ng’apa na kadhalika ambapo panaunganisha na maeneo ya Ruaha Darajani lakini umeme unapita juu na kushindwa kuunganishwa umeme kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeshauliza mara kadhaa hapa Bungeni kuhusu jimbo letu lenye sifa kubwa ya utalii, lakini maeneo mengi ni ya giza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi yake ya kuwaunganishia umeme wananchi wa Kata za Vidunda, Ulelingombe, Malolo, Wedo
– Kisanga, Zombo, Ulaya, Mhenda, Tindiga, Mbamba, Kiduhi, Tambukareli, Kikwalaza, Munisagala, Dodoma Isanga, Udung’u Mgogozi, Chabi, Kielezo, Gezaulole, Dinima na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mikumi tumekuwa na matatizo makubwa sana ya mawasiliano ya simu. Mfano, barabara ya TANZAM (Tanzania – Zambia), pale maeneo ya Msimba, Iyovi na Ng’apa kumekuwa kuna ajali nyingi sana na sehemu hii ina kona kali nyingi sana na ajali nyingi sana zimekuwa zinatokea, lakini jambo baya kabisa ni kuwa, maeneo haya kuanzia Msimba mpaka Ruaha Mbuyuni hakuna mawasiliano yoyote yale ya simu na hakuna umeme kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali ilitupie jicho la huruma eneo hili ambapo wasafiri wengi sana wa ndani ya nchi na wengi wa nje ya nchi wanapata matatizo mbalimbali lakini hawawezi kuwasiliana na wenzao na kusubiri kudra za Mwenyezi Mungu tu. Pia, katika Jimbo la Mikumi kwenye Kata za Vidunda, Malolo, Tindiga, Kisanga, Kilangali, Ulelingombe, mabwerebwere na eneo la muhimu kabisa la katikati ya Hifadhi ya Mikumi ambalo ni muhimu sana kwa watalii na linaongeza sana pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa tuta la Mto Miyombo/Bwawa la Kidete; nashukuru sana Ofisi hii ya Waziri Mkuu kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakitusaidia pale tunapopata maafa ya mafuriko kwenye Wilaya yetu ya Kilosa na Jimbo la Mikumi. Kubwa ni kupasuka kwa kuta za Bwawa la Kidete ambalo Serikali kila siku imekuwa ikituahidi kuwa, imetenga pesa kwa ajili ya kujenga bwawa hili muhimu la Kidete kuzuia mafuriko hayo. Pia, kingo za Mto Miyombo zimezidiwa na wingi wa maji na mvua inapozidi, maji hufurika kwa wananchi na kuleta maafa. Naomba majibu ya Serikali, ni lini itajenga Bwawa la Kidete na lini itajenga tuta la Mto Miyombo?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kuchangia kwenye Wizara hii nyeti na muhimu ya Muungano na Mazingira. Wilaya yetu ya Kilosa ni Wilaya Kongwe sana hapa nchini; na kwa kweli changamoto kubwa sana tunayoipata kila mwaka ni mafuriko ya mara kwa mara ambayo yanasababisha vifo, uharibifu mkubwa wa mashamba, mali na miundombinu mbalimbali katika Wilaya ya Kilosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya mafuriko hayo ni kupasuka kwa bwawa la Kidete ambapo mvua zinaponyesha kidogo tu yanamwagika kwa wananchi lakini pia kupoteza ulekeo wa mto Miyombo ambao ni mto unaopita kwenye kata nyingi za Wilaya ya kilosa yenye Majimbo ya Kilosa kati na Mikumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali itusaidie pesa ili kujenge bwawa hili muhimu la Kidete kwa kuwa Waziri wa Maji alishafanya ziara na kuahidi kuwa pesa zimeshatengwa na wapo kwenye mchakato wa kumalizana na mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mto Miyombo tunaomba sana tujengewe tuta katika Kata ya Masanze iliyopo Jimbo la Mikumi ambapo kwa ujenzi huu wa tuta ni muhimu sana na utasaidia sana kuzuia maji yasiende kwenye makazi ya wananchi na kuepusha maafa ambayo yanatokea mara kwa mara kwenye kata hii pamoja na Kata Magomeni na kuleta maafa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaiomba sana Serikali kuchonga kingo za Mto Miyombo hasa kwenye maeneo ya Kata ya Kilangali ili kuzuia maji kuingia kwenye maeneo ya wananchi (makazi na mashamba yao) na kuyaharibu vibaya sana kutokana na mto huu kupoteza uelekeo mara kwa mara kwa kuzidiwa na maji mengi ambayo yanatiririka kwa wingi sana hasa kipindi kama hiki cha masika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba sana Serikali iongeze bajeti ya Wizara hii hasa kwenye mfuko wa mazingira ili kuwezesha Wizara hii kutimiza majukumu yake muhimu sana kwa Taifa hili kwenye masuala muhimu yahusuyo mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo la Mikumi lina Kata 15 na katika Kata hizo zinapata taabu sana ya kutokuwa na Mahakama na zile zenye Mahakama zinachangamoto zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama nyingi hazijapimwa au kurasimishwa na kusababisha wananchi kuingilia na kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu kwenye maeneo ya Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uchakavu mkubwa wa majengo ya Mahakama za Jimbo la Mikumi. Mahakama nyingi zimechakaa sana na hazina umeme wala vyoo kitu kinacholeta usumbufu kwa watumiaji wa Mahakama zetu na watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ofisi kutokuwa na nembo ya Taifa na Bendera. Mahakama zetu za Jimbo la Mikumi, mfano Kata ya Mikumi na Kata ya Malolo hazina nembo ya Taifa na kupunguza heshima ya Mahakama zetu. Mahakama zetu hazina samani za ofisi, mfano computer, mashine za kurudufu hukumu, makabati ya kuhifadhia nyaraka mbalimbali muhimu. Hii inasababisha malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi maana wanakosa haki yao ya kupata hukumu ya kesi na kuambiwa waje siku nyingine hata kama hukumu imeshatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, linginei ni mahabusu. Mahakama nyingi ziko mbali na vituo vya Polisi au Magereza na kusababisha Mahakama kupata shida ya kuwahifadhi watuhumiwa, mfano Mahakama ya Kata ya Malolo ipo zaidi ya kilomita 200 kutoka Kituo cha Polisi na kusababisha usumbufu mkubwa wa kusafirisha wafungwa. Inabidi mtuhumiwa atoe shilingi 60,000/= kwa nauli wakati ni wajibu wa Serikali na ikishindwa inabidi hakimu alipe hela yake ya mfukoni inakuwa ngumu sana. Tunaomba Polisi waje kuwachukua wafungwa ili kupunguza mzigo kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nichangie kuhusu upungufu wa watumishi wa Mahakama. Kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mishahara ya Mahakimu na watumishi wa Mahakama ni midogo. Vile vile posho za nyumba; Mahakimu ni watu muhimu sana kutokana na aina ya kazi zai wanazofanya wanastahili sana kupata posho za nyumba kama wanayopata waendesha mashtaka, maana mahakimu wengi wanaishi mbali sana na maeneo ya Mahakama ambapo hawajapewa na Serikali nyumba za kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokakana na kazi yao ya kutoa haki sawa na kuhukumu, Mahakimu wanastahili sana wapewe ulinzi wa kutosha maana kutokana na kazi yao watuhumiwa wengi wanaokutwa na hatia wanawatisha sana Mahakimu wetu na kutishia usalama wao hasa kwa kuzingatia Mahakimu wengi wanaishi mitaani bila ulinzi wa uhakika na usalama wao na kuhatarisha maisha yao. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kidogo kwenye Wizara hii muhimu ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kwamba wasanii wa Tanzania wanapata shida sana kutokana na usimamizi mbaya kwa maana ya ulinzi wa kazi za wasanii. Je Serikali haioni umuhimu wa kuileta kwenye Bunge lako Tukufu Sheria ya Hati Miliki na Hati Shiriti, Na.7 ili tuipitie upya na kuifanyia marekebisho? Kwani sheria hii imeshapitwa sana na wakati na inaonekana kuwa ndiyo chanzo cha wasanii wa Tanzania kuwa maskini na wengine kupata stress (msongo wa mawazo) na kujikuta wanajingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na unywaji wa pombe kupitiliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, urasimishaji wa sanaa. Serikali haioni ikirasimisha rasmi wasanii itaweka mambo mengi kuwa rasmi na kusaidia Serikali kujua kipato cha kila msanii anachoingiza kupitia sanaa na kuweza kukusanya kodi yake vizuri tofauti na sasa ambapo vipato vya wasanii havijulikani na kusababisha Serikali kupoteza pesa nyingi kupitia kodi.

Mheshimiwa Spika, tumeona Serikali ikihangaika na mikataba mibovu waliyoingia wasanii na kunyonywa kwa kiwango cha ajabu na cha kusikitisha sana lakini mikataba kati ya wasanii na mashirika mbalimbali ingekuwa wazi ingesaidia sana mbali ya Serikali kupata kodi pia wasanii wangepata nafasi ya kuweza kukua zaidi na pia ingepelekea kupata ushauri mbalimbali juu ya kuwekeza (kuji-brand) zaidi ili kuwafanya wawe professional zaidi na kuepuka hali za wasanii wengi wa Tanzania ambao wengi wao wanakufa maskini kutokana na kutokuwa na msaada wowote wa kifedha na ushauri na mwisho wao kuwa mbaya na wa kusikitisha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iache kuwatumia wasanii kisiasa na ijikite kuwasaidia wasanii wawe neutral na kufanya shughuli zao za kitaifa na siyo kichama zaidi. Kwa kuwatumia wasanii kisiasa inawaumiza sana kwenye jamii kwani siyo kila shabiki wa muziki anaipenda CCM, hivyo kupelekea wale wasioikubali CCM kutowa-support kwa sababu wanatumiwa na CCM na mwisho wao kuwa mbaya, mfano, msanii Marlaw.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iongeze bajeti ya BASATA maaana hawa ndiyo walezi wa sanaa ya Tanzania na pia ndio kama baba na mama wa sanaa ya Tanzania. Bajeti ya shilingi milioni 22 kwa mwaka ni ndogo sana na haitoshi kuwawezesha kuwafikia wasanii wote nchi nzima na kuwaelimisha na kuwasimamia kama majukumu yao yanavyojieleza.

Mheshimiwa Spika, lakini pia BASATA waache kufungia hovyo kazi za wasanii bila kufuata sheria kwani hakuna sheria inayoruhusu BASATA kufungia kazi za wasanii wa Tanzania. Kwa kufingia hovyo kazi za wasanii BASATA wanavunja sheria na wasipoangalia ipo siku watajikuta Mahakamani wakishtakiwa na wasanii wanaojielewa na itaharibu sana mahusiano kati ya wasanii na BASATA kitu ambacho kitadidimiza zaidi ukuaji wa sanaa yetu ambayo inategemea sana mahusiano mazuri kati ya wasanii na BASATA.

Mheshimiwa Naibu Spika, ieleweke BASATA ni mlezi wa sanaa ya Tanzania na siyo Mahakama ya kuwasulubu wasanii wa Tanzania. Naomba sana waitumie vema nafasi na heshima ya kuwa mlezi wa sanaa ya Tanzania na washirikiane vizuri na wasanii wa Tanzania kwa maslahi mapana zaidi ya sanaa ya Tanzania, Taifa letu na kizazi hiki na kizazi kinachokuja.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, zoezi la Vitambulisho vya Taifa kwenye Jimbo la Mikumi, zoezi la uandikishaji wa hivi vitambulisho vya Taifa limesimama kabisa. Jimboni Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla watu walishalipa fedha zao, shilingi 500/= kila mmoja lakini mpaka leo bado hawajapewa Vitambulisho vyao vya Taifa na mbaya zaidi hili tamko la Serikali kuhusu kusajili namba zote za simu nchini ukiwa na kitambulisho cha Taifa imeleta sintofahamu kubwa sana kwa wananchi wetu na Watanzania kwa ujumla. Naomba Waziri wa Mambo ya Ndani akija kuhitimisha atoe kauli ya Serikali kuhusu zoezi hili la vitambulisho na usajili wa namba za simu kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, upotevu wa wananchi kumi wa Kijiji cha Ruhembe Jimbo la Mikumi; niliripoti Bungeni na kwenye vyombo mbalimbali vya usalama na vyombo vya habari kuhusu watu 10 waliopotea wakiwa pembezoni wa Hifadhi ya Mikumi, lakini mpaka leo tarehe 24 bado hakuna majibu ya Serikali kama hawa watu ni wazima, wamekamatwa au wamekufa tangu walipopotea tarehe 2 Aprili, 2019. Je, Waziri wa Mambo ya Ndani na vyombo vyake vya ulinzi na usalama wanatoa kauli gani juu ya upotevu wa ndugu zetu hawa?

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa na migogoro mfululizo ya wakulima na wafugaji Wilayani Kilosa, Serikali iliahidi kujenga vituo vya Polisi kwenye Kata za Tindiga, Ulaya, Kilangali, Malolo na Mabwerebwere: Je, Serikali itatimiza lini ahadi yake hiyo ya kulinda wananchi na mali zao kwenye kata hizi?

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Mikumi ni muhimu sana na kina kazi kubwa sana ya kulinda wananchi wa Tarafa nzima ya Mikumi yenye Kata saba za Mikumi, Malalo, Uleling’ombe, Mhenda, Ulaya, Kisanga na ukizingatia Mikumi ni Mji Mdogo wa Kitalii na idadi kubwa sana ya watu, kituo hiki hakina gari ya doria na mbaya zaidi Cell yao ni ndogo sana. Hakuna choo na mpaka leo watuhumiwa wanajisaidia kwenye ndoo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akitupie jicho la huruma kituo hiki cha Mikumi ili Askari wetu waweze kufanya kazi yao kwa weledi na watuhumiwa wapate haki yao ya mazingira salama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu kwa ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure (bila malipo). Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wanafunzi katika kujiandikisha kujiunga na shule mbalimbali lakini kuna tatizo kubwa sana la miundombinu kwani miundombinu imezidiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na elimu msingi, mfano, vyoo, madarasa, ofisi za walimu na nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pamoja na idadi ya wanafunzi kuongezeka lakini kuna uhaba mkubwa sana wa walimu kwani uwiano wa wanafunzi na walimu kwenye shule zetu haulingani kabisa. Hivyo basi inapelekea ile dhamira njema ya kukuza na kusaidia kila mwenye uwezo wa kwenda shule aende shule isiwe na tija kwa maana uchache wa walimu unadumaza hiyo nia njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa fedha za miradi na maendeleo. Tumekuwa tukipitisha fedha na bajeti mara kwa mara lakini cha kusikitisha ni kwamba fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo zimekuwa zinatolewa kwa asilimia ndogo sana. Niiombe sana Serikali iwe inatoa fedha zinazopitishwa na Bunge lako Tukufu ili kuweza kufikia yale malengo ambayo Wizara na Serikali kwa ujumla zinakuwa zimejiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa walimu. Tumekuwa na upungufu mkubwa sana wa walimu nchini. Mfano kwa wilaya ya Kilosa peke yake, kwenye upande wa shule za msingi, tuna wanafunzi 107,000 lakini tuna walimu 2,393 kwa hiyo tuna upungufu wa walimu 929. Nitumie nafasi hii kuiomba sana Serikali itusaidie kwa kutuongezea walimu zaidi kwenye shule za msingi Wilayani Kilosa. Pia ituongezee walimu wa sayansi kwenye Wilaya yetu ya Kilosa kwani napo tuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Ni vyema sana Serikali ikaona umuhimu wa COSTECH ili tuweze kusaidia Taifa letu kwenye masuala ya ubunifu wa mambo mbalimbali kwenye nchi yetu. Tanzania tumebarikiwa sana kuwa na watu mbalimbali wanaovumbua vitu vingi lakini tuna tatizo kwa COSTECH kushindwa kuwafikia na kuwasaidia kutokana na ufinyu wa bajeti. Bila bajeti ya kueleweka COSTECH haiwezi kuvumbua, kubuni na kusaidia vipaji mblimbali ambavyo kama vingeweza kusimamiwa ipasavyo vingeweza kutuletea maendeleo makubwa sana na kututoa kimasomaso kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya Afya. Kama inavyojulikana ni ngumu sana nchi yoyote kupata maendeleo kama wananchi wake hawana afya bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watumishi wa Afya; pamoja na jitihada za kujenga mahospitali na vituo vya afya, lakini tumekuwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya nchini. Mfano mpaka mwezi Machi, taarifa za Wizara zinaonesha zina upungufu wa watumishi kwa asilimia 48 na hii inaonesha kuwa kasi utoaji wa vibali vya kuajiri uko chini sana ukilinganisha na ongezeko la wagonjwa. Pia, ongezeko hili la ujenzi wa hospitali na vituo vya afya ni vema sana ungekwenda sambamba na ajira mpya za watumishi wa afya sambamba na kuwalipa watumishi wa afya waliopo wanaodai stahiki zao ili kuweza kuongeza tija ya utendaji kazi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la magari ya wagonjwa Jimboni Mikumi; Jimbo la Mikumi lina jiografia mbaya sana na katika kata 15 za Jimbo la Mikumi tuna vituo vya afya vinne tu navyo ni kuwa viwili, yaani Kituo cha Afya cha Kidodi na Kituo cha Afya cha Ulaya na vituo vipya vya afya vya Mikumi na Kituo cha Afya cha Malolo. Kwa hali hiyo inasababisha wananchi wengi kufia njiani wakati wanasafirishwa umbali mrefu sana ambapo ni kutokana na ukosefu wa magari ya wagonjwa. Jimbo zima halina gari hata moja la wagonjwa kwenye zahanati zote pamoja na vituo vya afya vyote. Tunaiomba sana Serikali itusaidie magari ya wagonjwa mawili au zaidi ili tuweze kuwaokoa wananchi hawa wa Jimbo la Mikumi, hasa mama na watoto. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Dada Ummy Mwalimu, atusaidie na kuokoa maisha ya wanawake na watoto wa Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, NHIF; uandikishaji wa Bima ya Afya ya NHIF umekuwa mdogo sana. Mfano, mwaka 2016/ 2017, walisajili 27% tu; mwaka 2017/2018, walisajili 32% tu; mwaka 2018/2019, walisajili 33%; na kusuasua huku kunatokana na ufinyu wa bajeti. Tunaomba sana Serikali izingatie sana bajeti ya afya kwa ujumla. Pia, Serikali iharakishe kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote yaani Universal Health Coverage ili tuweze kuupitisha na kuleta tija zaidi ya kuwasaidia na kuwaokoa Watanzania wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuajiri Maafisa Maendeleo ya Jamii; ni vema sasa tukajikita zaidi kwenye kinga kuliko tiba na watu wanaoweza kutusaidia zaidi kwenye jambo hili la kinga ni Maafisa Maendeleo ya Jamii ili waweze kusaidia jamii zetu huko chini ili wapate elimu zaidi ya afya kwani ni kweli tupu kwamba, kinga ni bora kuliko tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu, nashukuru sana nami nichangie katika Wizara hii muhimu ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, COSOTA; kwanza kabisa ningependa kuishauri Serikali ihamishe COSOTA kutoka kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara na kuipeleka kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hii itasaidia sana kuifanya kuwa kwenye Wizara inayohusiana kabisa na masuala yao ya sanaa ambayo ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, changamoto inayowakabili wasanii wa nchi hii ni wizi wa kazi za wasanii na sheria inayolinda kazi za wasanii Sheria Na.7 ya mwaka 1999 imepitwa na wakati na kwa kweli imekosa meno kabisa na imeshindwa kabisa kuwalinda na kuwasaidia wasanii wa Tanzania ambao kila kukicha kazi zao zinaibwa na kuuzwa kiholela na hakuna sheria inayowabana wezi wa kazi za wasanii. Naiomba sana Serikali kama kweli inataka kuwasaidia wasanii wa Tanzania basi iilete hapa Bungeni Sheria ya Hati Miliki na Haki Shiriki Na.7 ya mwaka 1999 tuifanyie marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao ya kilimo na vya kuchakata mazao ya mifugo; Jimbo la Mikumi linalima sana mazao mbalimbali, lakini tuna tatizo kubwa sana la viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao hayo ambayo yangeweza sana kutoa nafasi kwa wananchi wa Mikumi kuweza kupandisha thamani ya mazao yao kwa kuyachakata kwenye viwanda hivyo. Naiomba sana Serikali iweze kulitilia mkazo hili ili tuweze kuwasaidia wakulima wetu ambao wanalima kwa bidii zote, lakini masoko yamekuwa ni kitendawili kikubwa sana kwao, hasa kwenye Kata za Tindiga, Kilangali, Kisanga, Uleling’ombe, Mhenda, Ulaya, Masanze, Zombo, Vidunda, Ruhembe, Mikumi, Kidodi, Mabwerebwere na Kata ya Malolo. Hivyo tunaomba sana Serikali iangalie suala hili muhimu kwa kutusaidia tupate viwanda vidogo vya kuchakata mazao ya kilimo na viwanda vya mazao ya mifugo kama viwanda vya nyama, ngozi, maziwa na kadhalika ili tuweze kuwasaidia wakulima na wafugaji wa Jimbo la Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kidogo kwenye Wizara hii nyeti, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu sana kati ya Jeshi la Wananchi Mikumi na wananchi wa Kitongoji cha Vikweme. Nilishalifikisha jambo hili kwa Mheshimiwa Waziri na nilishauliza swali hili mara kadhaa hapa Bungeni bila mafanikio, Mji Mdogo wa Mikumi wapo tayari kabisa na wameshatenga eneo kwa ajili ya kuwapa Jeshi ili wakafanyie huko mazoezi, lakini Jeshi letu limekataa na kuendelea kuling’ang’ania eneo la Vikweme ambalo wananchi wengi wa Jimbo la Mikumi wanalitegemea kwa kilimo na pia kuna nyumba za wananchi kwa makazi, shule, nyumba za ibada na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Waziri aweze kulitatua hili na pia afanye ziara jimboni Mikumi kama alivyoniahidi wakati akijibu swali langu Bungeni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo ambayo kimsingi ni uti wa mgongo wa taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Wakulima wa Miwa. Kumekuwa na kilio cha muda mrefu sana cha wakulima wa miwa wa bonde la Ruhembe Jimboni Mikumi ambao ni wakulima wa miwa wa nje (out growers) katika ukanda wa Bonde la Ruhembe ambapo malalamiko yao ya muda mrefu ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, idadi ya miwa inayoingizwa kiwandani kutoka kwa outgrowers bado imekuwa ndogo sana hivyo tunaomba sana Wizara iliangalie suala hili kwa kuwa tumewashauri sana wakulima na watu wengine walime miwa kwa wingi, lakini miwa inayochukuliwa na kiwanda ni kidogo. Hali hii inasababisha miwa mingi ya wakulima wa nje kutochukuliwa na kiwanda, hasa ukizingatia pia kuwa kiwanda nacho kina mashamba yake.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Mzani. wakulima wa miwa wamekuwa wakilalamikia sana mzani unaotumika na kiwanda cha Illovo kwa kuwa mzani ni wa Illovo na wanaopimia ni watu wa Ilovo hivyo wakulima wanakosa wawakilishi wa kuwawakilisha ili kuhakikisha kuwa kiwango cha miwa na utamu kweli vinaendana na uhalisia. Hivyo wakulima wanaomba sana wapate mzani wao au wawe na uwakilishi wa kutosha katika mzani unaotumiwa na kiwanda cha sukari cha Ilovo.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utamu wa Muwa (sucrose). Kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wakulima wa miwa kwamba kwa kuwa hawana wawakilishi wakati wa upimaji wa utamu wa sukari, basi wamekuwa wanapewa takwimu ambazo si sahihi, hivyo kuwafanya walipwe pesa kidogo sana kutokana na vipimo vya sukari vinavyoonesha kuwa miwa yao ina utamu kidogo tofauti na uhalisia. Kwa kuwa kuna wakati wanaambiwa miwa yao ina sucrose mpaka nne (4), kitu ambacho wataalamu wanasema hakuna kiwango hicho kwa miwa ya bonde la Ruhembe, bali inakuwa kwenye 10 -11 na si hizo takwimu ambazo wanaambiwa na watu wa kiwandani.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Mabaki (Maganda ya Miwa – Bagasse). Wakulima wameendelea kulalamika kuwa wanalipwa utamu tu wa miwa na hawalipwi mazao mengine yanayotokana na miwa kama mashudu (bagasse) ambazo zinatengenezewa umeme na nyingine zinatumika kama mbolea. Pia wamekuwa hawalipwi molasses ambazo zinatumika kwa ajili ya kutengeneza sprit, hivyo kilio kikubwa cha wakulima kwa Serikali ni kuhakikisha wakulima hawa wa miwa wanalipwa na vitu vingine vinavyotokana na miwa kama bagasse na molasses sambamba na sucrose (utamu) ili kuuinua uchumi wa wakulima wetu wa nje.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Pembejeo. Kama Kambi Rasmi ya Upinzani ilivyoshauri, kilio kikubwa cha wakulima ni ukosefu wa pembejeo kwa wakati. Ili tupate kilimo bora ni vema sana Serikali ikahakikisha kuwa upatikanaji wa pembejeo unapatikana kwa wingi na kwa haraka
iwezekanavyo. Kwa mfano kwenye Wilaya yetu ya Kilosa pia tumekuwa na ucheleweshaji mkubwa sana wa pembejeo. Pia zimekuwa na tatizo la kupatikana kwa bei ya juu sana na inapanda kila mwaka na kufanya wakulima wetu wa Wilaya ya Kilosa kushindwa kulima kwa tija ilhali wilaya yetu imebarikiwa sana kwa kuwa na ardhi nzuri ya kilimo na ni moja ya wilaya bora kabisa hapa nchini kwetu kwenye sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba sana Serikali ili wakulima wetu waweze kulima kilimo bora na cha kisasa, ihakikishe upatikanaji wa pembejeo, usambazaji wa pembejeo na matumizi yake. Pembejeo zinazohitajika sana kwa wakulima wetu wa Wilaya ya Kilosa ni mbegu bora, mbolea na madawa, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii nyeti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kupotea kwa ndugu zetu kumi katika Hifadhi ya Mikumi. Wananchi wa Mikumi hususan wananchi wa Kata ya Ruhembe Kata ya Kidodi na Kata ya Ruaha bado wana masikitiko makubwa sana ya kupotelewa na ndugu zao wapatao kumi tangu siku ya tarehe 02, Aprili, mwaka huu wa 2019; mpaka leo bado hawajapatikana wala hakuna taarifa wala dalili yoyote ya kuwaona tena ndugu zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii imekuwa ni tabia ya muda mrefu sana ya ndugu zetu kupotea kwenye Hifadhi ya Mikumi. Kwa taarifa ambazo si rasmi zinasema watu hao huwa wanauliwa na askari wa wanyamapori, hasa wakiwakamata wananchi wanaookota kuni au shughuli yoyote ya kijamii pembezoni au ndani ya hifadhi hii. Tunajiuliza askari hawa wanatumia sheria gani kuua watu wetu hata kama wamewakamata kwa makosa yoyote? Je, wana haki ya kuwaua binadamu wenza bila kuchukuliwa hatua yoyote?

Mheshimiwa Naibu Spika, Tembo Waharibifu wa Mashamba. Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la tembo ambao wanatoka ndani ya mipaka ya hifadhi na kwenda kuharibu mashamba ya wakulima wetu na pia kuwajeruhi wananchi wetu. Hivi karibuni kumekuwa na tembo wengi sana wanaoharibu mashamba ya wakulima kwenye maeneo ya Kata ya Tindiga, Kata ya Kilangali, Kijiji cha Doma (Mvomero) na kuharibu sana mazao ya wananchi na kusababisha hasara kubwa sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejitahidi kutoa taarifa kwa Afisa Maliasili wa Wilaya ya Kilosa lakini wilaya nzima kuna askari mmoja tu, tunaomba sana Serikali iwasaidie sana wananchi wa maeneo haya hasa Kata ya Tindiga na Kilangali ambao wana kila dalili ya kukumbwa na baa la njaa kama hawatapata msaada wa mapema ili kuzuia hawa tembo wasiendelee kuharibu mashamba yao ili baadaye waweze kuvuna kile walichopanda na kuwaepusha na baa la njaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kifuta Jasho kwa Wananchi wa Jimbo la Mikumi. Wananchi wa Jimbo la Mikumi ambao mashamba yao yalivamiwa na tembo bado wamekuwa hawalipwi kifuta jasho chao.

Namuomba Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha atuambie katika Jimbo la Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla, je, ni wananchi wangapi wamelipwa kifutajasho kwa mwaka huu na wangapi hawajalipwa na lini watalipwa? Pia ninataka kupata majina ya wahanga wote waliolipwa na ambao bado hawajalipwa kifuta jasho ili tuweze kufuatilia zaidi haki hii ya wanachi wetu kwa Wilaya ya Kilosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Migogoro ya Mipaka Kati ya Vijiji Vinavyopakana na Hifadhi ya Mikumi. Bado kuna migogoro mingi sana katika Jimbo la Mikumi kati ya vijiji vya Mikumi vinavyopakana na hifadhi yenyewe. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri afanye ziara ya kikazi Jimboni Mikumi ili aweze kutusaidia kuhusu changamoto hii ya muda mrefu kati ya wananchi na Hifadhi ya Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana muda unavyozidi kwenda wananchi wanaona kama wanaonewa na wanaona kama kuwa na neema ya kuwa na hifadhi kwao imekuwa laana, maana badala ya kujivunia kuwa na hifadhi sasa wamekuwa wakiuliwa, wakiteswa na kunyang’anywa maeneo yao ya kilimo na shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo, kitu ambacho wanaona kama wanaonewa, kunyanyaswa na hawatendewi haki ilhali wao walistahili kuwa ni wanufaika wa kwanza na muhimu wa Hifadhi hii ya Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali iliangalie hili la mahusiano ya wananchi na hifadhi kwa jicho pevu ili kuwafanya wananchi wajivunie kuwa na neema ya kuwa na hifadhi, wailinde Hifadhi yetu ya Mikumi na wanyama wake na pia waweze kushirikiana na watu wa hifadhi kuwatambua na kuwataja majangili na watu wenye nia ovu na mbaya kwa Hifadhi yetu ya Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote yanawezekana tu kama tutakuwa na ujirani mwema kati ya wananchi na askari wanyamapori ili kuweza kujenga jamii inayopendana, kuheshimiana na kushirikiana ili kuilinda Hifadhi yetu ya Mikumi na kuifanya Mikumi sehemu salama ya kuishi na kuchangia pato zaidi la utalii katika taifa letu. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia Wizara hii muhimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu umeme wa REA III Jimbo la Mikumi. Ninatambua kuwa mkandarasi wa REA III katika Jimbo la Mikumi ni State Grid lakini bado kazi ya kuleta umeme kwenye Jimbo la Mikumi inasuasua sana.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Kijiji cha Udung’u kilichopo katika Kata ya Vidunda ambacho kipo kwenye mpango huu; na awamu hii mkandarasi ameshindwa hata kwenda kufanya survey na hakuna shughuli yoyote iliyofanyiwa kazi. Tunaomba kujua, ni lini wananchi hawa watapelekewa huduma hii muhimu?

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Vidunda bado hakijafanikiwa kwa namna yoyote ile, hata nguzo bado hazijapelekwa; wananchi wanataka kujua tatizo ni nini? Maana walinisikia nikiuliza swali Bungeni na walimsikia Naibu Waziri Mheshimiwa Subira Mgalu akiwahakikishia kuwa nguzo zipo.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Ulaya. Mheshimiwa Waziri amekuwa akituahidi mara kwa mara kwamba Kata hii ya Ulaya itafikiwa, na alifanya ziara kwenye kata hii na akatembelea na Kituo muhimu cha Afya cha Ulaya ambacho hakina umeme na kinahudumia Tarafa nzima ya Ulaya yenye Kata za Ulaya, Mhenda na Zombo. Hata hivyo mpaka leo hii hakuna shughuli yoyote inayohusu umeme inayoendelea katika Kata hii muhimu ya Ulaya.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Kata ya Tindiga. Kwenye Kata ya Tindiga hakuna shughuli yoyote inayohusu umeme inayoendelea ingawa nayo ipo kwenye mpango wa REA III, kwenye awamu hii; Kata ya Tindiga ina Vijiji vya Tindiga A, Tindiga B, Malui, Kalukwambe na Malangali. Tunaomba kujua, ni lini kata hii na vijiji vyake vitapatiwa umeme?

Mheshimiwa Spika, Kata ya Zombo. Nguzo zimeanza kushushwa katika Kata ya Zombo lakini zoezi hili bado linasuasua na Serikali ilituambia itaunganisha umeme huu kutoka Kata ya Masanze kwenye Kijiji cha Changarawe. Kata ya Zombo ina vijiji vitano, ambavyo ni; Zombo Lumbo, Kigunga, Nyameni, Nyali na Madudumizi. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea umeme kwenye vijiji hivi?

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Kata ya Mhenda. Kata ya Mhenda ipo katikati ya Kata ya Mikumi maeneo ya Ihombwe na Kata ya Ulaya. Sasa tunaomba sana Serikali itusaidie kutuletea umeme kwenye Kata hii muhimu ya Mhenda yenye vijiji vya Mhenda, Ilakala, Nyaranda na Maili 60. Tunaomba sana Serikali itusaidie tupate umeme kwa wakati kama walivyotuahidi.

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Chonwe. Kijiji hiki kipo katika Kata ya Vidunda na kipo kwenye mpango huu wa REA III awamu ya kwanza, lakini mpaka leo hakuna jitihada zozote zilizooneshwa na Serikali na mkandarasi hajawahi hata kufika.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mikumi. Ikumbukwe kuwa Mikumi ni Jimbo la Kitaliii na kwenye Kata ya Mikumi kumekuwa na uwekezaji mkubwa sana wa hoteli za kitalii na camp sites. Pamoja na hayo, kwenye Kata ya Mikumi, katika hali ya kustaajabisha na kusikitisha maeneo ambayo yana uwekezaji wa hoteli za kitalii hayana umeme. Maeneo haya ni; Kikwalaza na maeneo ya Tambukareli ambako kuna Mji Mpya wa Kiserikali wa Mikumi. Kwenye maeneo ya Kikwalaza wenye hoteli wanalalamika sana kwamba wanapata gharama kubwa sana za kuendesha hoteli zao kwa kukosa umeme, kiasi kwamba inawalazimu kutumia majenereta makubwa sana, kitu ambacho kinawagharimu sana kwenye uendeshaji wa hoteli zao.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya Tambukareli kuna maeneo ambayo leo watu wa TANESCO – Mikumi wamekuwa kimya na wamesababisha wananchi kushikwa na butwaa. Sasa wananchi wanataka kujua; Serikali ilipojibu swali langu Bungeni waliahidi kwamba kwa kuwa kuna shughuli za kitalii na zinaongeza Pato la Taifa letu basi wangetoa kipaumbele kwenye Kata hii ya Mikumi na maeneo yake haya ya Kikwalaza na Tambukareli. Je, ni lini tutapatiwa umeme kwenye maeneo sambamba na maeneo ya Barabara Kuu ya Tanzania kwenda Zambia, hasa maeneo ya Msimba na Ng’apa?

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Umeme Jazilizi (Densifications). Maeneo ya Ruaha Mbuyuni, Malolo A, Malolo B. Mgogozi na Chabi yaliyoko kwenye Kata ya Malolo yamepitiwa na nguzo za umeme uliopo karibu. Nilishawahi kuuliza swali na Mheshimiwa Waziri alinijibu kuwa kuna pesa zimepatikana kutoka kwa wahisani na kwamba maeneo haya pamoja na maeneo ya PWD, Dodoma, Kipekenya, Dodoma Isanga, Munisagala na Chabima yaliyopo kwenye Kata ya Masanze na maeneo ya Gezaulole, Mbamba, Kiduhi vilivyopo kwenye Kata ya Kilangali; je, ni lini wataunganishwa na umeme?

Mheshimiwa Spika, Kata ya Uling’ombe. Hii ni kata ambayo ni muhimu sana kwa kilimo na madini na inapakana na Jimbo la Kibakwe ambalo lina umeme. Tunaiomba sana Serikali itupatie umeme kwenye Kata hii muhimu yenye vijiji vya Uleling’ombe, Mlunga, Ibanda na Lugawilo ili nishati hii ikatumike kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo haya kwa kuchakata mazao na shughuli za madini.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.