Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Dr. Haji Hussein Mponda (1 total)

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wakazi wa Wilaya ya Malinyi, Wilaya ya Ulanga na Kilombero, tunaishukuru Serikali na tunawapa pongezi kutekeleza ahadi ambayo wametuahidi ya ujenzi wa daraja la Kilombero ambayo imekuwa jawabu kubwa la kero ya miundombinu katika Wilaya hizo tatu. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ujenzi huo wa daraja la Kilombero unahusisha pia na barabara za maingilio na barabara hiyo ya maingilio inaunganisha barabara inayotoka Ifakara, Lupilo, Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo, Lumecha, Namtumbo mpaka Songea. Barabara hii kipindi cha masika inachafuka sana kutegemea na mazingira ya mvua maeneo yale na inakuwa inapitika kwa tabu sana. Sasa, je, Serikali inajipangaje na ukarabati wa kudumu wa maeneo korofi katika barabara hiyo niliyotaja?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; barabara hii niliyotaja inajulikana kwa T16, barabara hiyo iko katika upembuzi yakinifu unaosanifu kwa kina ambao umekamilika. Barabara inatakiwa ijengwe kwa kiwango cha lami. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo inayotoka Ifakara, inatobokea mpaka Songea ambayo itakuwa sio kwa ajili ya mkaazi wa Morogoro itasaidia pia na ndugu zetu majirani wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea kwa niaba ya Serikali pongezi alizotupa na kwa kweli ni wajibu wetu kutekeleza ahadi zote ambazo tumezitoa katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoongelea nayo iko katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015 hadi 2020 ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi na usanifu wa kina haujakamilika – physically umekamilika lakini taarifa bado haijakamilika na tunatarajia hiyo kazi itakamilika mwezi Mei, 2017. Kwa sasa taarifa ya rasimu imeshawasilishwa TANROADS wanaipitia kwa kina ili hatimaye wamrudishie maoni yule Mhandisi Mshauri ambaye ni kampuni ya Kyong Dong na baada ya hapo ndio atakuja kukamilisha kuandika taarifa ya mwisho. Kwa ratiba ilivyo ataiwasilisha taarifa ya mwisho mwezi Mei, 2017. Baada ya hapo Serikali itaanza kujipanga kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la ukarabati wa maeneo korofi kwa sasa ili iweze kupitika muda wote; nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Hadji Mponda Mbunge wa Malinyi na wananchi wote wa Malinyi hadi Kilosa kwa Mpepo kwamba Serikali ina mkakati kabambe na kila mwaka tunatenga fedha na nafahamu mwaka huu kuna wakandarasi wawili wako site katika maeneo korofi wanafanyia ukarabati wa hali ya juu ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika mwaka mzima bila matatizo.