Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mbaraka Salim Bawazir (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SALIM M. BAWAZIR: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa kazi nzuri wanazofanya, Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wote wa Mashirika yaliyopo Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaelekeza mchango wangu kwa REA. Naomba Serikali iangalie jinsi ya kusambaza umeme katika Vijiji vya Kata zifuatazo – Kata ya Magubike „A‟ na „B,‟ Kidefe, Lumuma, Madoto, Kitete, Lumbiji, Mambaya, Kitonge 1 na 2. Muandi, Chaombele, Ifunde, Mwasa, Kitati, Mzaganza, Mkundi, Dumila Juu, Mkundi Matogolo. Msowero Shule ya Sekondari, Mayambaa Kitongoji cha Mkobwa, Sukutari, Kichangani, Majengo, Mfulu, Madudu, Mbigili, Mabawa, Mateteni, Peapea, Buyuni na Mabatini Unone.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyote hivyo havijapata umeme wa REA. Naomba Mheshimiwa Waziri utusaidie kupata umeme kwani wananchi wa maeneo hayo wana shida sana. Sambamba na wananchi, umeme pia ni muhimu ufike kwenye shule ya Sekondari ya Msowero. Umeme utasaidia wanafunzi kujisomea nyakati za usiku.
Mheshimiwa Naibu Spika, vinasaba viliwekwa kwa kuwa bei ya mafuta ya taa yalikuwa bei ya chini. Wafanyabiashara wakawa wanachakachua mafuta, lakini sasa bei ya mafuta ya taa iko juu kuliko diesel. Sasa vinasaba vya nini tena? Tunapoteza fedha za Watanzania ambazo zingeweza kutumika kwa kununua madawa na madawati kwa wanafunzi mashuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine ni leseni za mafuta. Upatikanaji wake unasumbua sana wafanyabiashara, masharti ni mengi mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBARAKA S. BAWAZIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kusaidia sana katika kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji katika Jimbo langu la Kilosa. Nashukuru sana kwa ushirikiano mliotupa japokuwa bado kuna matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mashamba ya Usagala A&B yaende kwa wakulima. Mashamba hayo yanamilikiwa na SINO Development Tanzania Limited (Usagara Sisal Estate). Wafugaji wapewe Mkata Ranch, Kandoro Ranch na Lukumai Ranch kwani maeneo haya yanafaa sana kwa wafugaji. Hali kwa sasa sio nzuri, watu wanalinda usiku na mchana mazao yao kuogopa wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali pamoja na mambo mazuri waliyoyafanya katika Jimbo la Kilosa wazingatie ushauri wangu kwa maslahi ya wananchi wa Kilosa. Naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua juhudi za Serikali katika kuwamilikisha wananchi ardhi. Aidha, natambua kwamba kwa kuwamilikisha wananchi ardhi na kuwapatia hati miliki tunaipa thamani ardhi hiyo na kwa maana hiyo wananchi wanaweza kuitumia ardhi hiyo kama dhamani na kukopa katika taasisi za fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado kumekuwa na uelewa mdogo miongoni mwa wananchi juu ya taratibu za kufuata hadi kuweza kumilikishwa ardhi. Kwa sababu hiyo, napenda kujua katika mchakato wa kuwamilikisha wananchi ardhi kwa kutumia hati za kimila, kutafanyika upimaji wa ardhi hiyo au mwananchi atamilikishwa moja kwa moja sehemu hiyo aliyokuwa akiishi au kuitumia tangu mwanzo? Aidha, napenda kujua ikiwa upimaji utafanyika, mwananchi atatakiwa kulipia kiasi gani cha fedha kwa ajili ya upimaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imeshaanza utekelezaji wa zoezi la kupima na kumilikisha ardhi katika Wilaya tatu za mfano; za Ulanga, Kilombero na Malinyi mkoani Morogoro, nadhani ingekuwa vyema Serikali ikatoa mrejesho wa maendeleo ya mchakato huo ili tuweze kujua mafanikio ni kiasi gani au kuna changamoto kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza kasi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi, ni kwa nini Serikali isiziagize Halmashauri za Wilaya husika kufanya kazi hiyo? Nadhani Wizara ikizipa Halmashauri ruhusa ya kufanya hivyo zoezi hilo litakwenda kwa kasi kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa viwanja vya makazi katika Manispaa ya Morogoro eneo la kutoka Nane Nane hadi Mkambarani katika barabara ya Morogoro – Dar es Salaam katika Manispaa ya Morogoro ni shamba la katani ambalo kwa muda mrefu sasa haliendelezwi licha ya kwamba shamba hilo halina tija kwa kilimo cha katani kutokana na kutoendelezwa, lakini lipo mijini kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ingekuwa vyema sasa Serikali ikabadili matumizi ya ardhi ile ili vipimwe viwanja vya makazi katika eneo lile ili kupanua mji wa Morogoro. Nasema hivi kwa sababu sera yetu ya mipango miji hairuhusu kuwa na mashamba makubwa katikati ya mjini, lakini pia ni mpango wa Serikali kubadili matumizi ya ardhi ikiwa ardhi hiyo haitumiki kikamilifu kwa shughuli iliyokusudiwa.
Mheshimwa Mwenyekiti, ipo migogoro mingi ya mipaka ya ardhi kati ya wananchi na Jeshi la Wananchi (JWTZ). Hali hii imesababisha wananchi wengi kubomolewa nyumba zao na kuondolewa kwa nguvu bila hata ya kulipwa fidia. Aidha, wananchi wanaokumbwa na madhila haya hawajui wapate msaada wapi kati ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi au Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 Kikosi cha Anga Namba 671 cha JWTZ kiliweka mabango katika makazi ya wananchi wa Mtaa wa Makoka, Uluguruni katika Kata ya Makuburi Dar es Salaam ya kuwataka wananchi hao wasifanye chochote katika eneo hilo kwa kuwa ni la Jeshi. Cha kushangaza ni kwamba eneo hilo lina shule za Serikali mbili; ya msingi na sekondari, lina huduma za jamii kama umeme, maji na barabara. Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni bado inakusanya kodi ya ardhi na majengo katika eneo hilo. Napenda Serikali itoe kauli kwa wananchi hao ili wajue hatma yao kwa kuwa wamechanganyikiwa kutokana na mkanganyiko kuhusu umiliki wa ardhi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema kama wananchi hao hawana haki katika eneo hilo waambiwe mapema ili wasije wakashtukizwa kuambiwa kuhama na kuwasababishia maafa makubwa. Aidha, kama wana haki ya kumiliki eneo hilo, basi Serikali iagize kikosi hicho kiondoe mabango yake ili wananchi hao waweze kuishi kwa amani na kuendeleza makazi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MBARAK S. BAWAZIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, NEMC wanachelewesha sana utoaji wa taarifa na kuruhusu ujenzi uendelee, Tanzania ya Viwanda haitaweza kupatikana kwa uratatibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za vibali kwa mtu anayetaka kujenga kituo cha mafuta ni kubwa sana na hapo hapo mteja anatakiwa amchukue mtaalam kwa gharama zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Viwanda vya Plastic kama vinafungwa vifungwe na kama wanatoa muda watoe kwa wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusimamisha uletaji wa mkaa mjini wakati utaratibu wa matumizi ya gesi kwa kupikia hayajakaa vizuri. Elimu itolewe kwa wananchi madhara ya ukataji wa miti na watumie nishati mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.