Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Peter Ambrose Lijualikali (12 total)

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Naam!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuzungumza kidogo. Naomba nizungumzie kwamba kama tunataka kutengeneza nchi ya viwanda ili twende kwenye uchumi wa kati mimi nafikiri kiwanda ni matokeo ya uwekezaji katika umeme. Lazima tuwe na umeme utakaoweza kufanya viwanda vifanye kazi. Kwa hiyo, niishauri Serikali kwamba ijitahidi sana kuwekeza katika umeme ili tuwe na umeme wa uhakika. Tukiwa na umeme wa uhakika viwanda ambavyo tunataka vije ama tuvifufue basi viweze kupata uwezo wa kufanya kazi vizuri. Huo ulikuwa ni ushauri wa kwanza. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nizungumzie hoja hii ya sukari. Tanzania kuna viwanda vinne ambavyo vinazalisha sukari. Kuna kiwanda cha Ilovo, kipo Jimboni kwangu Kilombero, kuna kiwanda cha Mtibwa, kuna cha TPC na kuna Kagera. Kiwanda cha Ilovo kimefunga uzalishaji wake tangu mwezi wa kwanza na hii ni kwa sababu ya maintenance, lakini leo ajabu karibu tani nane za sukari kutoka Ilovo zilikuwa kwenye godown hapo Tabata zimeuzwa leo. Hili godown lipo Tabata limeuza tani nane. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba tuna sukari ambayo imefichwa na wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais akiwa na nia safi, mimi nasema safi kwa sababu anazungumza vizuri ya sisi tuweze kupata sukari na viwanda viendelee, watu wanaficha sukari, wanasubiri maintenance za viwanda zikifanyika wao ndiyo watoe mzigo. Kibaya zaidi baada ya huu upungufu wa sukari hawa watu wanataka wapewe vibali vya kwenda kuagiza sukari yaani watu wanaoficha sukari kwenye ma-godown leo wanataka wao ndiyo wapewe vibali vya kwenda kuagiza sukari. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba hao watu kwa tabia yao hii ya kuficha kwanza hatuna uhakika kama wataagiza ambacho wameruhusiwa, maana yake ni kwamba wataongeza. Wakiongeza viwanda vyetu hivi vinne vya Ilovo, Mtibwa, TPC na Kagera vikianza production vitakuta tayari kuna mzigo mkubwa upo kwenye soko vitapunguza uzalishaji. Vikipunguza uzalishaji maana yake hawa wakulima wetu mfano wakulima wangu kule Sanje, Kidatu, Mkula wataathirika. Tunakwenda kuua hawa wananchi ambao wanaendesha kilimo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa, niiombe Serikali isiruhusu kabisa wafanyabiashara waagize sukari nje. Mimi najua kuna watu wamewekwa humu ndani waweze kuongea maneno haya, wamewekwa humu ili waweze kusema kwamba wafanyabiashara waruhusiwe, niombe Serikali, hivi viwanda vinne na kwa sababu Serikali hii inaweza sana, hawa Mawaziri wanafanya kazi bila kuwa na sheria, hawana kazi, basi niombe kama huo ndiyo utaratibu wetu hata kama viwanda hivi watasema kwamba sijui havina mamlaka haya, tuendelee hivi hivi tu, tufunike hivi hivi hawa wenye viwanda, viwanda hivi ndiyo viagize sukari ili kulinda viwanda hivi na wakulima. Nilikuwa nataka hili niliweke sawa watu wajue na Serikali ijue kwamba kuruhusu wafanyabiashara binafsi kuagiza sukari ni kuua viwanda na kuuwa wananchi watu wa Sanje na sehemu zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu Morogoro. Morogoro ina viwanda vingi sana lakini viwanda hivi watu wanafuga mbuzi, hapa ndipo wanaposema we have killed our past and we are busy killing our future. Tumeua past yetu na tuko busy kuua future yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi huwa najiuliza hivi nia ya Serikali ya privatization (kubinafsisha) hivi viwanda ilikuwa ni nini? Ilikuwa ni kuwapa watu nafasi ya kupata maeneo ya kufuga, kuuza mashine zetu kama scraper au nia ilikuwa tuongeze uzalishaji na ajira?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nia ilikuwa ni kuongeza ajira na uzalishaji hivi inakuwaje tunakuwa na viwanda yaani kama Taifa tumejiminya, tumepata viwanda, tukasema wenzetu mviendeleze halafu wanachukua hivyo viwanda wanaanza kufugia mbuzi, wanakata mashine, wanauza kama scraper, kama Taifa hii ni aibu! Sidhani kama Serikali hii ya Awamu ya Tano inayosema Hapa Kazi Tu itaruhusu kwamba hizi ndizo kazi zenyewe. Yaani kazi ya Mwalimu Nyerere ilikuwa kuunda viwanda halafu watu wengine waje kukata scraper! Sidhani kama hii ndiyo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mifano hapa, pale kwangu Mang‟ula pana kiwanda kinaitwa MMT, nina handover letter hapa ambayo hii Serikali ilikabidhi hiki kiwanda kwa Mama Rwakatare, Mama Rwakatare huyu huyu ambaye alikuwa Mbunge, handover hii hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu walikuwa hawajui kama mlikuwa mnaona vifaa kama mapanga na kadhalika vyenye picha ya mamba ilikuwa ni Mang‟ula. Kiwanda tumekabidhiwa kikiwa kizuri, kikiwa kina kila kitu lakini pale sasa hivi kuna mbuzi tu ndiyo wanachungwa pale lakini unakuta eti mtu naye anajiita mwekezaji, amewekeza nini huyu? Umewekeza kwa kuua uchumi wa nchi? Kile kiwanda kilikuwa kinatoa ajira pale, Serikali ikaamua kutoa, ikasema endeleza na nimuombe Waziri twende kule akaone kiwanda hiki ambacho kilikuwa kina manufaa katika nchi yetu leo kimekuwa cha kufunga mbuzi. Hatuwezi kujenga Taifa la hivi na tukiongea hivi hatumuonei mtu, tunaongea ukweli kwa sababu ya faida ya Taifa letu. Kuna watu huko hawana ajira, tumetoa viwanda watu wanafugia mbuzi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kama haitoshi, kuna kiwanda kingine kilikuwepo pale Mang‟ula, wengine mnafahamu vizuri wakati reli hii ya TAZARA inajengwa vifaa vya kutengeneza yale mataruma vilikuwa pale Mang‟ula. Mwalimu Nyerere kaacha viwanda vizuri, kiwanda vya Ilovo, kiwanda vya Mtibwa spare zake ilikuwa wanazipata Mang‟ula. Leo kiwanda mtu anachukua semi-trailer anapakia chuma chakavu anapeleka kuuza, sisi tupo tu hapa, Taifa lipo, Serikali ipo! Kiwanda kinahujumiwa, nchi inaliwa tunasema wawekezaji, what kind of this business? Are we serious?
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: We are not serious and never be serious. We have killed our past and we are busy killing our future. Ukiuliza, anaongea mpinzani, anaongea UKAWA, come on lets be serious! Tunazungumzia uchumi wa nchi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri twende tukaone kule! Kiwanda ambacho mnasema mmempa mtu mkaone…
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Peter Lijualikali, siyo Juakali. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutimiza jukumu langu la Kikatiba kuwepo mahali hapa na nitaanza na TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango wa kuisaidia miji ili iweze kuendelea nimeona hapa kuna miji 18 ambayo Mheshimiwa George Simbachawene ameiweka kwenye hotuba yake, kwenye hii miji siuoni Mji wa Ifakara, ni mji mpya ambao ninadhani kwa changamoto ambazo mji huu unao kama za barabara na juzi tulikuwa na mafuriko makubwa sana ambapo Mto Rumemo umekuwa na kawaida ya kumwaga maji kuja Mjini Ifakara, sasa nimeshangaa tangu bajeti ya 2016 miji ni ile ile 18, kuna miji mipya mwaka jana imetangazwa na Ifakara ikiwemo, lakini mji wangu wa Ifakara hauonekani kwenye huu mpango.
Sasa nichukue wakati huu kumuomba Mheshimiwa Waziri Simbachawene aweze kukumbuka Mji wa Ifakara kwa maana ni mji mpya, mji ambao una changamoto, ningependa kuona unaingia kwenye huu mpango ili mji uweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye suala lingine la utawala bora na hapa nitasema kidogo. Mwaka jana wakati tunakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na mara zote tumekuwa tukisema Tume hii siyo huru na mfano hapa upo; kwamba Tume ya Uchaguzi ilikuja Ifakara, Kilombero ilikuja kuhakiki majimbo mapya na huu ni mpango wa kila baada ya miaka mitano. Mwenyekiti wa Tume hii akasema Ifakara kwa kuwa ni Halmashauri ya Mji ina-qualify automatic kuwa Jimbo la Uchaguzi, sehemu ikishakuwa Halmasahauri maana yake ina-qualify kuwa Jimbo automatic. Kile kigezo cha population hapa hakipo tena kwa sababu hii ni mamlaka inayojitegemea. Kunakuwa na Baraza la Madiwani, Halmashauri, Mkurugenzi na Idara kamili which means ina-qualify kuwa na Mbunge hapa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Jaji Lubuva kukiri kwamba Ifakara ina-qualify kuwa jimbo nikashangaa anakuja kutangaza majimbo mapya Ifakara haipo. Nikashangaa sana na nikasema kama Serikali ya CCM inaongoza mambo yake kisheria na kwa miongozo ya Katiba ni kwa nini Ifakara iachwe, wakati sheria na vigezo vya Ifakara kuwa Jimbo vilikuwa vinaipa Ifakara kuwa jimbo. Na nikasema kama Tume ya Uchaguzi inao wataalam, ina wanasheria na wanajua fika kwamba Ifakara ina-qualify kuwa jimbo lakini kwa makusudi wakanyima Ifakara kuwa jimbo tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi siyo huru, haifanyi kazi zake kisheria ni uhuni unaofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho tumekuwa tukisema upinzani kwamba hii Tume hii irekebishwe nafikiri kuna haja ya hii kitu kufanyiwa kazi na katika mazingira kama haya kama Tume inakubali kabisa kwamba Ifakara inapaswa kuwa jimbo halafu wanashindwa kulifanya jimbo kwa nini tusikubali kwamba pia Lowassa mlimwibia? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kitu kipo wazi, yaani kitu kipo wazi tu kisheria kwamba hii sehemu inafaa kuwa jimbo Mwenyekiti wa Tume anakubali kwamba hii sehemu inafaa kuwa jimbo lakini anafanya lisiwe jimbo kihuni tu, kwa nini tusikubali kwamba Tume hii CCM mmekuwa mkiitumia kihuni ili mfanikiwe ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye hii hii utawala bora yametokea mpaka mimi nakuja kukamatwa na polisi wananikwida kwa sababu ya huu uhuni leo eti polisi mwenye „V‟ koplo anakuja kumkamata Mbunge kihuni kabisa. Leo hii kila mtu anasema Lijualikali ulionewa unastahili kwenda Kilombero na bahati yangu kwenda Kilombero nazuiwa na polisi na nina kesi mahakamani kwa sababu hiyo, halafu mnasema eti hapa kuna utawala bora!Huo utawala bora uko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo nadhani Taifa hatupaswi kuyaendeleza. Ninadhani tuna kila sababu ya kurekebisha siasa zetu. Kama sehemu inastahili haki zake sehemu inastahili na haya unakuta hata katika Mkoa wa Dar es Salaam, Madiwani wengi ni wa UKAWA, lakini Serikali ya CCM mmetafuta namna zozote mnazoziweza ili mshinde Jiji. Mmefanya kila namna mnahangaika, mnajua kabisa hamna haki hiyo, lakini mnahangaika mnavyoweza ili muweze tu kushinda.
TAARIFA....
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli unabaki pale pale kwamba tumetumia miezi mitano, tumefanya vurugu, mpaka zimekuwa forged hati za mahakama ambazo mahakama imekataa. Nabaki kwenye msingi ule ule kwa nini mpaka mahakama isingiziwe? Kwa nini mpaka tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nimekosea kusema Rais, na Rais anisemehe sana na ninyi mnisamehe lakini nina hoja ya msingi hapa, hii hoja hatuwezi kuidharau, kwa nini mpaka tufikie huku? labda nimesema hivi kwa sababu nimekwazwa moyoni, nimeumia moyoni yaani ni kwa nini nifanyiwe hivi, Rais yupo, Waziri Mkuu yupo, mpo wote kwa nini vitokee hivi? Kwa hiyo, ni kweli naomba mnisamehe, najua mnajua kwamba mlikosea na Mungu awasamehe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye hoja nyingine, kuna kitu...
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda umeisha jamani.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ndiyo nimeyasema sasa hivi hapa, this is not fair, haya nimeyasema sasa hivi tu, ameongea mbele yangu muda amechukua hapa na umeona kabisa, ndiyo nimesema sasa hivi mambo haya, hamsikii tunasema hapa ndani lakini hamsikii, hatuwezi kwenda hivi kama Taifa!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa leo ni mara ya kwanza nasimama ndani ya Bunge lako kuzungumza tangu nimetoka Gereza la Ukonga, ambako nilikuwa natumikia kifungo batili cha miezi sita, nashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kilombero, kwa namna ambavyo wananipenda, wananiheshimu na wanajua mchango wangu kwao, kiasi ambacho nilipokuwa nimefungwa hawakukata tamaa, walikuwa wanakuja kuniona, walikuja kwa wingi Idete, mpaka ikaonekana wanaweza wakavunja Gereza, maana walikuwa wengi sana, ikabidi nihamishwe. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe shukrani za pekee kwa Chama changu, Mwenyekiti wangu wa Chama Taifa Mheshimiwa Mbowe, Wakili wangu msomi Mheshimiwa Tundu Lissu, pia ninawashukuru watu wote waliokula njama, walionifanyia fitna na uhuni ili nifungwe, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mhehsimiwa Mwenyekiti, vilevile niwashukuru Wabunge wa CCM wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB) Mheshimiwa Mbowe anazungumza yanayonisibu gerezani na kutaka Bunge lichukue attention nawashukuru kwa kumzomea, ila mjue mlikuwa hamzomei Mwenyekiti, hamkuwa mnamzomea Mbowe ila mlinizomea mimi, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kabisa ninawashukuru wafungwa wa Gereza la Ukonga na wale wa Gereza la Idete, maana naamini maisha yangu yalikuwa mikononi mwao. Wangeweza kufanya ubaya wowote lakini waliniheshimu, wakanitunza na niseme Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu programu ya Parole ambayo ni misamaha kwa wafungwa. Misamaha hii ambayo inatumika vibaya na vizuri. Gerezani nimekuta kuna wafungwa wazee ambao wamefungwa miaka ya 1970 mpaka leo bado wapo gerezani, lakini Serikali mmekuwa mkitoa msamaha kwa wafungwa wanaofungwa miezi sita, vifungo vidogo. Nataka nimwambie Waziri, nilimwambia tukiwa wawili na leo ninasema mbele ya Bunge, vifungo hivi vya miezi sita, wahalifu wakubwa wa Taifa hili, wanatumia vifungo vidogo kufanya uhalifu wanakuja gerezani, wanakaa kwa muda mchache, halafu wanatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mtu anajipa kesi ndogo ambayo anajua atafungwa miezi sita, anajua atakaa miezi mitatu, atapata msamaha. Anakuwa na kesi hiyo mahakamani, anakwenda anafanya tukio kubwa la mauaji au ujambazi ile kesi ndogo inamfunga, anakuwa amejikinga na lile tukio kubwa ambalo amelifanya mtaani. Waziri wa Mambo ya Ndani unatoa msamaha kwa huyu mfungwa pasipokujua umemsaidia kuficha kesi kubwa ambayo alikuwa nayo mtaani.

Kwa hiyo, mnawafunga watu kwa miezi michache mnawatoa, baada ya muda mfupi kumbe walitakiwa wapate msamaha watu wenye vifungo vikubwa, hii ingesaidia kuwafanya watu wenye vifungo vya muda mfupi peke yao waone kwamba hii siyo kinga.

Mheshimiwa Waziri, hili nilikwambia na leo nasisitiza Parole muwe mnaangalia vifungo, msijali kwamba hiki ni kikubwa mkaona hawa hawafai, hawa wenye vidogo basi ndiyo tuwatoe, vidogo vinatumika kuficha maovu makubwa. Kwa hiyo, naomba hili muangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ukiwa Ukonga na magereza mengine, nimeshuhudia askari wakifanya njama pamoja na maafisa wa mahakama, wale admission officers wafungwa wanakosa kupata haki zao za kupata Hati za Hukumu pamoja na upande wa mashtaka, kunakuwa na uhusiano mzuri kati ya mahakama pamoja na askari wa admission. Mfungwa akiomba apate nakala ya hukumu akienda kule mahakamani anaambiwa muone askari fulani, askari yule anamwambia mfungwa lazima utoe hela, ndiyo upate hati ya mashtaka na mwenendo wa mashtaka. Hii maana yake ni kwamba askari wako lazima uwaangalie. Vitengo vya Admission vinatenda rushwa, vinazuia wafungwa kupata haki yao, naomba hilo Mheshimiwa Waziri uangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu hii programu mnasema ya urekebishaji. Mimi nilipokuwa gerezani nilitegemea ningeona huo urekebishaji mnaousema, kwamba wafungwa mnawarekebisha kwa programu ambayo ni tangible. Nione kuna programu ya urekebishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho nimekiona sasa sijui kama huu ndiyo urekebishaji wenyewe, nimeona marungu, mfungwa anapigwa marungu mpaka mguu unageuka. Unapigwa rungu mpaka mguu unashindwa kutoka.Nimeona wafungwa wanafanyishwa, labda niseme nilipoingia mara ya kwanza gerezani, askari wako walinikamata wakanipiga mitama, sijafanya chochote nimeingia hapo. Sasa sidhani kama Mbunge naweza nikafanyiwa hivyo wafungwa wa kawaida sijui wanafanywaje na siamini kama huu ndiyo urekebishaji au nilifanyiwa hivyo kwa sababu mimi ni Mbunge wa Upinzania labda, lakini kama hizo ndiyo programu za urekebishaji, vile ambavyo wafungwa wanafanyiwa mle ndani, wafungwa wanauwawa, wanapigwa risasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,mimi nimefanyiwa mambo ajabu kama hayo katika Gereza la Idete, askari ananiambia nitakuuwa. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri uliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuambie wewe ni Waziri mpaka wa wafungwa, usifikiri kwamba wewe ni Waziri tu kwa watu ambao wako mtaani, nenda gerezani kasikilize vilio vya wafungwa. Wafungwa wana matatizo makubwa sana nenda kawasikilize, wanavyofanyiwa mambo ya ajabu mle ndani. Nilikwambia tukiwa wawili na leo nakwambia, nenda kasikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoamini kabisa mtu yeyote wa Mungu anajua kabisa vitabu vinasema waonee huruma wafungwa, wagonjwa, walemavu na wajane. Hizi kauli za wamenyeke tu, Mheshimiwa Rais anasema hawa wafungwa wamenyeke hawafai, wafanye kazi mpaka wachubuke,mimi nilifungwa kihuni, nimeonewa, sina kosa, lakini Rais alisema kwamba nimenyeke. Ningekuwa sina Wakili msomi kama Mheshimiwa Tundu Lissu maana yake yake na mimi ningebaki ninamenyeka. Sasa kuna watu wangapi ambao nchi hii wanamenyeka kwa uhuni tu ambao wamefanyiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri, wale wafungwa ni binadamu, wafungwa ni watu. Yeyote aliyepo hapa ipo siku chochote kinaweza kikatokea. Sheria mnazotunga hapa, wakati mimi nasema haya wewe umevaa crown upo juu unafikiri uko sahihi, ipo siku na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena kuhusu maisha ya askari. Mheshimiwa Waziri nikuulize, hivi leo ukiambiwa uchague, ukae kwenye choo chako au ukae kwenye nyumba wa Askari wa Magereza wa Idete wewe utachagua ukae wapi? Kati ya choo chako wewe Waziri, choo chako wewe Mbunge na chumba cha Askari wa Magereza uambiwe ukae kwa siku moja utakaa wapi?

Utakaa chooni kwako. Nyumba ya askari wa nchi hii wa magereza ni mbaya choo chako ni kizuri. Wabunge vyoo vyenu ni vizuri, vyoo vya askari wenu, na hawa askari pamoja na yote haya mnayofanyiwa, bado sisi ambao tunaongea haya maneno mnatupiga virungu, Mungu anawaona ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza tangu mwaka 2012 mpaka leouniform hawajapewa. Nimekuta askari wanajinunulia wenyewe uniform.Wananiambia Mbunge hii uniform nimenunua mwenyewe kwa fedha zangu na hivi unavyoona hivi haifanani na nguo za askari wengine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo fair, package allowance mnawapa askari wengine, wanajeshi wengine mnawapa package allowance leoMagereza wale mpaka leo hamjawapa, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru lakini askari polisi msitumike vibaya na hawa jamaa, Mungu anawaona.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nataka nizungumzie ushuru wa mazao ambao Mheshimiwa Waziri ametoa kwa mazao ya kilimo. Alisema kwa hawa wakulima ambao wanasafirisha mizigo yao kwa maana ya mazao kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine, kama ni mzigo usiozidi tani moja wasitoe ushuru.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana mimi nina Halmashauri mbili, ya Ifakara na Kilombero. Wananchi wangu hasa wa Ifakara wengi wanalima Halmashauri ya Kilombero wanakuja Ifakara hapa katikati huwa kuna barrier ambapo huwa wanawekwa pale Askari Polisi wenye bunduki kwa ajili ya ushuru. Kama Halmashauri ya Kilombero tulisema mkulima kutoka Ifakara anayelima Kilombero, akirudi na magunia yasiyozidi 20 anapita bure.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa hili agizo kwamba tani moja ndiyo ipite, tani moja ni wastani wa magunia 10 maana yake ni kwamba tayari tumesha-confuse utaratibu wetu kule Ifakara. Maana yake tunawaambia wananchi wa Ifakara kama tulikuwa tunasema wapite na magunia 20 sasa wapite na magunia 10 tu kwa mujibu wa sheria hii, tayari ni confusion. Maana yake ni kwamba hapa sasa hatusadii.

Mheshimiwa Spika, mimi nasema tani na ningependa unisikilize mpaka mwisho kwa sababu katika hicho kizuizi wanapokaa askari hapo, mkulima hata kama ana gunia tano za mpunga, hawezi kuchukua fuso au usafiri mkubwa kwa ajili ya kubeba hizi gunia tano, maana yake lazima wakulima watachanga, watakodi usafiri mkubwa waweke kwenye hilo gari waweze kuja Ifakara. Haiwezekani mkulima atoke na mzigo Idoko akiwa na gunia 10 atembee nazo mpaka Ifakara, hawezi kukodi maana yake lazima wachange wawe wengi. Wakifika pale wanaambiwa huu mzigo ni wa mtu mmoja wakati wale ni wakulima wengi wamechanga gari.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili Mheshimiwa Waziri aliangalie, aende kule Ifakara aweke sawa, haiwezekani mkulima mmoja akodi gari wakati ana magunia matano au sita maana yake lazima wakulima wengi wachange kwenye hili gari moja ili wawe na mzigo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niseme nina shida ya barabara pale, barabara yangu ya kutoka Kidatu mpaka Ifakara ni mbovu kwa miaka mingi. Sasa Mheshimiwa Waziri nimeambiwa imetengwa shilingi milioni 300 kwa ajili ya fidia, maana barabara hiyo sasa hivi ndiyo inataka kujengwa, hivi kutoka Kidatu mpaka Ifakara pale kuna nyumba ngapi, ni nyingi sana. Hii fidia ya shilingi milioni 300 ni takribani nyumba mbili tu hizi, hawa wengine fidia yao iko wapi? Kwa hiyo, naiomba Serikali kama ina ya dhati ya kujenga barabara hii, fidia iongezwe siyo hii hela ndogo ambayo imewekwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo lingine, hotuba ya Mheshimiwa Msigwa, hii hotuba ya akili ndogo nafikiri itaishi milele. Kwa sababu mambo yanayotokea leo katika nchi hii yameshasemwa miaka mingi sana na hata Msigwa alisema akili ndogo haiwezi kuongoza akili kubwa. Leo ambacho kinatokea hapa ni kwamba akili ndogo ile ambayo ilikuwa inapiga makofi wakati sheria mbovu zinatungwa hapa Bungeni, ile akili ndogo wakati akina Zitto wanasema hawa Mawaziri wanakwenda kusaini mikataba nje, Waziri anapewa ndege aende nje akaingie mkataba mlikuwa mnapiga kelele nyie mnasema kwamba huyu Zitto mwongo, hafai na ametumwa, Zitto akafukuzwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati haya yanatokea huyu Rais wetu alikuwa pale amekaa. Wakati Mnyika anaongea haya maneno kwamba nchi hii inaibiwa, nchi hii inafilisiwa, mlikuwa mnapiga makofi nyie, akili ndogo hiyo inapiga makofi. Akili kubwa akina Msigwa, Zitto na Mnyika wakati wanasema haya maneno walionekana wabaya.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu unakuja hivi, kwa kuwa tumeshasema na kama Taifa tumeona kwamba Acacia ni wezi na kwa kuwa na Rais amesema hawa watu wanatakiwa wafanyiwe kazi, kwanza lazima kinga ya Rais itolewe, tufanye amendment hapa, Marais wa nchi hii wasiwe na kinga ya kutokushtakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu hainiingii akilini wakati leo unamwambia Karamagi, unamwambia mzee wangu Chenge kwamba wahojiwe Marais waliopita wanaachwa. Haiwezekani Chenge alifanya makosa Rais asijue, haiwezekani Cabinet ilikuwa haijui. Tufanye amendment ya sheria Marais wote na hii vita siyo iwe ni one man army, isiwe vita ya jeshi la mtu mmoja ndiyo lipigane iwe vita ya Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ni kuomba radhi, CCM lazima muombe radhi kwa hasara ambayo mmeleta kwenye Taifa hili. Leo hapa mnajifanya mnapiga makofi, mnashangilia wakati nyie mmeua watu, watu wamekosa madawa kwa sababu ya uamuzi wenu wa hovyo. Kwa hiyo, huo ndiyo ushauri wangu, amendment ije, Rais aombe radhi, Bunge liombe radhi na CCM muombe radhi kwa maamuzi mliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Awali ya yote, nitoe pole kwa familia ya Diwani, Marehemu Godfrey Luena ambaye aliuawa kwa kupigwa mapanga nyumbani kwake. Natoa pole lakini nataka niiambie familia yake kwamba Luena hajafa, Luena anaishi. Kile ambacho alikiamini kitaishi, ambacho alikipigania kitaishi hakitafika kwake Kilombero. Tunamheshimu Luena kwa kazi aliyoifanya na tunaamini kazi yake haitapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana hekima ya upinzani wa nchi hii ni upumbavu kwa Serikali ya CCM. Kwa bahati mbaya sana, hekima yetu ni upumbavu; hekima yetu ni tafsiri kwamba ni waoga. Ni bahati mbaya, lakini hekima yetu haitalala, itafanya kazi siku zote ingawa inaonekana ni upumbavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo katika Taifa letu kuna jambo ambalo kwa kweli linaniuma sana. Nichukue mfano tu, watu wana-post kwenye mitandao kwamba Mheshimiwa fulani anaumwa au anakaribia hivi, watu wanasema bora aende, bora afe, tumechoka. Kama sisi ni watu wazima wenye akili timamu, wenye upendo wa Taifa letu, unapokuwa na Taifa ambalo kiongozi mkubwa wa Taifa anaumwa halafu wananchi wanasema bora afe; hii inatoa tafsiri mbaya kwa Taifa. Taswira ya nchi yetu inaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema haya maneno kwamba kuna shida, huu ni upumbavu. Tunaposema kuna uonevu katika nchi hii, kwa sababu tumesema, tunaonekana sisi ni waoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu ambaye hajui hapa, Bunge lililopita Mheshimiwa Nape na wenzake walisema usalama wa nchi ni mbovu, Kamati ya Bunge iundwe, ile Kamati ikafanya kazi kubwa, ikaenda huko, mpaka leo majibu hakuna. Kwa nini hamna majibu? Hekima hii ni upumbavu kwenu. Mnadhani kuwa mambo ni mazuri?

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mama yangu, nimwambie kwamba lengo langu haikuwa kumuudhi mtu yeyote kati yenu, ama yeyote aliyepo humu ndani, siyo lengo langu. Nami sijafundishwa kumuudhi mtu yeyote. Nimejaribu kutumia labda neno ambalo naweza nikaeleweka, ila kama limekuudhi, nisamehe. Naamini kwamba umenielewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani watu wazima tumekaa wote hapa, tunaona kabisa viashiria vya nchi kuharibika, tunajifanya hatuoni. Ninyi ndio wazee wetu. Tulitegemea muwe wa kwanza kuona haya mambo kwamba yanaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunahubiri mshikamano, umoja na upendo; na mwenzangu Mheshimiwa Mwakyembe alikuja kwenye Kamati, akasema sasa hivi tuna mpango tulete sijui kampeni ya uzalendo kwanza. Unawezaje kuwa na uzalendo kwenye Taifa ambalo Diwani wangu anauawa, kiongozi wangu wa chama anafanyiwa uhuni, mpaka leo kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona mfano, haya magazeti, jambo hilo hilo likiandikwa kwa ajili ya Mheshimiwa Mbowe kwa maneno hayo hayo, Serikali inakaa kimya; Mheshimiwa Waziri anaona raha, anatulia. Jambo hilo hilo, neno hilo hilo likiandikwa kwa kiongozi wa Serikali, gazeti linafungiwa. Huu umoja unatoka wapi? Huu upendo mnaotaka kuhubiri unatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu jambo baya; hata hii sheria wanayosema ya mtandaoni, watu wote ambao wamekamatwa nayo ni watu ambao wanaaminika wanaongea jambo ama wame-post kitu ambacho kinakwenda kinyume na Serikali, lakini jambo hilo hilo mtu wa CCM aki-post, husikii shida yoyote. Sasa tutajidanganya hapa; amani, amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikia niwaambieni, nchi zozote zile ambazo mambo yameharibika, haikuanza tu siku mambo yakaharibika, mambo yanaanza hivi. Wazee mpo hapa mnaona mambo yanaharibika kwa sababu mnadhani mtakuwapo milele, mnaacha mambo yaende. Mtaharibu nchi yetu ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa. Niongelee sasa kuhusu elimu. Taifa lolote lazima likitaka maendeleo liwekeze kwa watu. Investment ya nchi ya kwanza ni kwenye aina ya watu inayotengeneza Taifa. Hii nitasema siyo kwamba nafurahia, Taifa ambalo tunazindua ndege watu wanakwenda kukimbilia kupanda eti kupiga picha. Come on! Hii nchi gani? Yaani Watanzania tumekuwa, yaani, khaa! Haya bwana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti, asilimia 70 ya fedha ambazo zimeingia kwenye elimu ni fedha za wafadhili. Fedha zetu za walipa kodi hazijaingia kwenye elimu. Maana yake ni kwamba Taifa letu halijawekeza kwenye elimu. Kama Taifa haliwekezi kwenye elimu, tunawekeza kwenye Bombadier na vitu vingine, its okay. Tutakuwa na Bombadier, tutakuwa na standard gauge, vitu vizuri vizuri vitakuwa vinaonekana, lakini vina-bring impact gani kwa watu wetu?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampa pole Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Heche kwa kufiwa na mdogo wake ambaye ameuawa akiwa Kituo cha Polisi. Kauawa ndani ya mikono ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, Wizara yetu ya Michezo pamoja na mambo yake yote inayofanya; na leo ameongea mwenzangu hapa, anasema viwanja ambavyo CCM ilivichukua kwa kuwa wameshindwa kuvifanyia kazi iwasaidie kuviendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala kwanza haliwezekani. Kama mmeshindwa kuviendeleza viwanja ambavyo mmepora kwa wananchi, tena mpaka sasa wananchi tuwape fedha za kuviendeleza, this is not fair. Kama vimewashinda, mvirudishe kwetu tuviendeleze kwenye Halmashauri zetu ili wananchi wetu waweze kufanya michezo na Taifa liendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hata kule kwangu Ifakara, nina kiwanja kikubwa sana, CCM wamekipora. Kile kiwanja kimejengwa na wananchi kwa jasho la wananchi. Leo hii eti ni cha CCM. CCM hawana nyaraka yoyote, wame-forge nyaraka, haiwezekani. Kwa hiyo, naomba kwamba kama vimewashinda, mvirudishe kwetu tuvifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Taifa lolote linatakiwa liwe na taswira ambayo inajenga heshima kwake. Taifa kama lina mambo ambayo hayaeleweki linakosa heshima kama ambavyo sisi kama hatueleweki tunakosa heshima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenye Taifa letu tumeweka kanuni mpya za mitandao. bloggers leo wanaambiwa wachangie Sh.100,000/= ili waweze kupeleka habari. Sisi kama Taifa kama tunashindwa kuwasaidia wananchi wetu wapate taarifa kama Taifa, watu wanajitegemea wenyewe, wanaweka mipango yao, tunakuja tunawakatisha tamaa, hatuwezi kuendelea. Juzi hapa Mheshimiwa Rais amesema hatuwezi kuwa na mitandao kama China. Kama tunaweza kuiga ya China hayo, tuige pia na kunyonga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, China kule kama mtu anafanya makosa ya rushwa mashtaka yao ni kifo tu. Hukumu ni kifo. Sasa kama hili la China ni zuri, pia wachukue na hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wananchi wetu wanashindwa kupata taarifa za kimsingi, magazeti wanayafungia, tena wanayafungia kwa jambo hilo hilo ambalo linafanywa na mtu wa kawaida. Likifanywa kwa ajili ya kuisema Serikali jambo hilo hilo Mheshimiwa Waziri anasimama anachukua hatua; jambo hilo hilo likisemwa kwa ajili kumtukana Mwenyekiti ama Kiongozi wa Upinzani, Serikali wanakaa kimya. This is not fair. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kujenga Taifa ambalo watu wanakuwa treated kwa mujibu wa matakwa ya kiongozi aliyeko madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu linaongozwa kwa mujibu wa sheria; Taifa letu haliongozwi kwa mujibu wa maneno ama kwa mujibu wa kauli za kiongozi yeyote yule. Tuna sheria zetu, lazima tuzifanyie kazi. Haiwezekani tu mtu anasimama anasema kuanzia leo... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PETER A.P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kuna mambo ambayo yanafanyika kwenye nchi yetu mimi natafsiri ni kama vile yanaleta fedheha kwa Jeshi la Polisi. Mambo haya yanafanya jeshi letu lionekane kama vile halina weledi, sijui ni kwa nini. Kwa mfano, utaona kuna bwana mmoja alimtishia Nape bastola, Waziri akasema huyu mtu tutamshughulikia, huyu mtu atafutwe, lile suala jinsi lilivyoenda mpaka leo kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yule anaonekana mtaani, yupo na hata juzi amefanya kazi mbele ya kamera. Sasa sielewi matamko haya huwa yanatoka kwa nia gani, ina maana Polisi hawaoni kwamba haya mambo yanachafua Jeshi letu la Polisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo amekamatwa akiwa ofisini kwake mpaka leo amepotea, haifahamiki yuko wapi. Taarifa zinasema aliyemkamata ni DSO, Mzee Mkuchika hapa anasema siyo wao, anasema hii ni kazi ya Polisi, Polisi wako kimya hawasemi chochote. Hii inafanya Jeshi letu lionekane kama vile halina taaluma hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, RPC wa Iringa anasema Nondo alikwenda mwenyewe Polisi kwenda kusema kwamba yeye hakutekwa wakati Kanda Maalum ya Dar es Salaam inasema Nondo amekamatwa. Haya mambo yanaonesha hili Jeshi letu linafanya kazi siyo kwa taaluma. Niwaombe sana Polisi wetu, kama wanapewa mashinikizo kwenye kazi yao, wajue kabisa kwamba wao ndiyo wanakuwa answerable mambo yanapoharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine ni Roma Mkatoliki. Roma ametekwa, akasema ameteswa na akasema anashindwa kuongea kwa sababu anaogopa maisha yake yako hatarini, Polisi wanasikiliza tu hawasemi chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni huyu Ndugu yangu Musiba. Musiba anaongea maneno hapa mabaya kabisa, Polisi wanasema wanachukua hatua. Mheshimiwa Lissu alisema maisha yake yapo hatarini, yapo kwenye shida, Polisi wanasema kama Mheshimiwa Lissu hakwenda Polisi kushtaki wenyewe hawana mpango lakini Musiba anaongea mambo ya hovyo kabisa, Polisi wanasema wao wanafanyia kazi, this is so unprofessional na hii inasababisha Jeshi letu kuonekana halina weledi. Watu wamekaa juu hapo wamesoma, wana uwezo mkubwa, kwa nini wanafanya vitu ambavyo vinaonesha kwamba hawana uwezo, kwa nini wasioneshe uwezo wao ambao sisi tunaamini wanao? Kwa nini wanafanya hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo yana-brand Taifa letu kuwa ni Taifa ambalo lina taasisi ambazo hazijielewi. Taifa letu lilikuwa linaheshimika duniani kwamba ni sehemu ya amani, ni sehemu nzuri ya kuishi. Leo Taifa letu linakuwa branded ni sehemu moja ya hovyo kwa sababu watu ambao mmepewa kazi za kufanya mnashindwa ku-act professionally mnafuata maagizo ambayo ni politically. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili likienda sehemu mbaya, juzi hapa Mkuu wa Polisi wa Arusha alipata ajali watu wana-comment bora afe tu, no, no, no! Wazee huko juu msifurahie mambo haya. Mheshimiwa Waziri asifurahie mambo haya, ni lazima wajiulize kuna shida wapi? Kwa nini mtu afurahie kifo chako? Wanakosea wapi? Kama Taifa tunakosea wapi? Haya mambo lazima wajiulize! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kusema maneno yafuatayo. Diwani wangu Luena alifariki, taarifa zinasema treni ama kipisi kilipiga honi mara tatu kwenye eneo la tukio. Hii inaleta picha kwangu inawezekana ile treni ilikuwa imewachukua watu ambao walimuua Diwani wangu kwa sababu ni kwa mara ya kwanza tangu kipisi kimeanza kazi ndiyo imepiga honi mara tatu nusu saa baada ya tukio, haiwezekani! Naomba hili walifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, nimwombe Mheshimiwa Waziri amwambie IGP wetu aje Ifakara aongee na Polisi wangu Ifakara, asikie na wao wana shida gani, asiende tu sehemu zingine anaongea nao, kule kuna shida nyingi sana, kituo kibovu. Aje, akae na sisi hata kama ni kuchanga, tuchange, kama ni kusaidia tusaidie, kama ameshindwa kujenga, sisi hela zipo, wananchi watatoa. Kwa hiyo niwaombe hilo, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Sikuwa nimepanga kusema haya maneno, lakini nitasema kidogo. Kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha sana kuona katika Bunge letu kuna Wabunge wana mawazo ya kufanya Rais aliyeko madarakani aendeleze kipindi ambacho kipo katika Katiba.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ni jambo ambalo kama tunaweza kuruhusu Katiba yetu ianze kufanyiwa marekebisho makubwa kama haya na kama haya ndiyo mawazo ambayo tunayo, yaani CCM wote ninyi mlioko humu ndani na nje, yaani hamjaona mtu mwingine Tanzania nzima, kwa kweli ni masikitiko makubwa sana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Kwa hiyo, kwa kweli ni jambo la fedheha. Mimi binafsi nimesikitika sana.

MBUNGE FULANI: Haukuwa mpango.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Aah, kwa sababu hata huo nao haukuwa mpango na alisikika, kwa hiyo, ni vyema mkanisikiliza tu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anaongea, alizungumzia maendeleo mengi, mipango ya Serikali ambayo inafanywa na kwenye Sekta ya Barabara ya miundombinu akaizungumzia barabara yangu ya Ifakara Kidatu kwamba inaendelea vizuri na katika moja ya vipaumbele vya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hii barabara ya Ifakara – Kidatu, jambo la kwanza ni barabara ambayo inafadhiliwa na wafadhili mbalimbali na tayari mikataba yake imeshasainiwa na fedha zipo. Rais mwaka 2018 alikuja kule Ifakara, Kidatu akazindua, akaweka jiwe la msingi, lakini hii barabara ni kama vile haifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Spika, site yupo Mkandarasi, ni kweli, lakini huyu Mkandarasi ni kama hafanyi kazi yoyote, amekaa tu, analalamika fedha hapati, mambo hayaendi, mizigo yake na vifaa vyake viko kule Bandarini. Akiomba vitoke anaambiwa alipe kodi.

Mheshimiwa Spika, Bunge la mwezi wa Pili, Bungeni hapa niliuliza swali nikamwomba Mheshimiwa Waziri anayehusika twende Ifakara, Kidatu akaangalie maendeleo ya ile barabara na kwa nia, nami niliona kabisa alikuwa na nia njema akasema tutakwenda mbele ya kiti chako, wananchi wakasikia, Taifa likasikia, lakini ukimpigia simu hapokei, ukimtumia message hajibu. Sasa hii maana yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, ukimwangalia Rais Dkt. Magufuli, ukiwa makini ukamsikiliza vizuri, analalamika sana. Huyu Rais wetu amekuwa Rais wa kulalamika. Tena imefikia hatua analalamikia mpaka Mawaziri. Juzi hapa alisema Mawaziri ham-communicate. Sasa hii maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nafikiri labda sijui kuna kitu Mheshimiwa Rais watu wanamtegea hawamuungi mkono, kwa sababu kama tuna Mheshimiwa Waziri anakubali atakwenda Jimboni kwenda kutekeleza kitu ambacho Rais wake alikwenda tena nchi nzima ikawa live kwenye TV, watu wote wanaona kabisa, Mheshimiwa Rais anasema kabisa, “natoa miaka mitatu barabara hii iwe imeisha” na akasema fedha zipo.

Mheshimiwa Spika, mimi nasema kule kazi haziendi, Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba twende tukaone. Mheshimiwa Waziri hapokei simu, hajibu message, anaingia mitini. Maana yake nini? Sasa sijui ni kumgomea Mheshimiwa Rais, sijui ni maneno ya kampeni tu, sijui maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, kama tunataka kweli kukomboa Taifa letu, kuna vijitabia kama hivi lazima tuviache. Sisi ni viongozi humu ndani, tabia hizi nami niseme kabisa kutoka moyoni, mimi Rais Dkt. Magufuli namwonea huruma sana. Mheshimiwa Spika ni shahidi, Rais Magufuli kila anaposimama ni kulalamika, anasema Wizara hii, Wizara hii, jambo hili, jambo hili, hili niliagiza, hili nilisema, hili nilisema, watu wote hawa hivi Rais wenu hamumpendi, mbona analalamika sana, ninyi manafanya kazi gani, mbona hamsaidii? Kila siku ni kulalamika tu yaani vitu ambavyo anatakiwa alalamike Mbunge, analamika Rais, mpo Mawaziri, kuna Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya wote mpo. Nyie Magufuli hamumpendi ila tu hamsemi ukweli, kama mnapenda kwa nini hamumsaidii?

Mheshimiwa Spika, niombe, kama fedha za barabara hii hakuna mseme, hizi fedha hakuna, kama fedha zimeenda kwenye Stiegler’s Gorge mseme, zimekwenda Stiegler’s Gorge, kama zinafanya kazi mseme, watu wa Ifakara, watu wa Kilombero, watu wa Kidatu, watu wa Mkula, watu wa Sanje tumechoka. Tunahitaji barabara hii ijengwe, kama fedha hakuna mseme, sisi tumechoka jamani, mbona nyie mna raha, mnakaa kwenye lami sisi tumewakosea nini? Kwa upande huu nilikuwa na hili.

Mheshimiwa Spika, ukija kuangalia kwenye Wizara ya Kilimo, nimeangalia randama ya kilimo, lakini fedha ya pembejeo, hakuna. Rais Dkt. Kikwete ameondoka madarakani kwenye bajeti ya 2015/2016 aliweka bilioni 78, bajeti hii kwenye randama ya Wizara ruzuku ya pembejeo nil, hata mia hakuna, yaani wanataka kuwaambia Watanzania kile ambacho Rais Kikwete alikifanya wao kwa miaka miwili wameshindwa tayari, yaani wameshashindwa. Mwaka 2016/2017 asilimia 89 ya bajeti ya Kilimo haikutoka, wamepeleka only 11, halafu sasa wanahuburi nchi inakwenda mbele, nchi inasonga, pembejeo tu zimewashinda, wataweza kweli.

Mheshimiwa Spika, kama Rais wetu hawamsaidii kumwambia ukweli kwenye haya mambo, hii nchi ilipofikia inategemea with due respect tunaongea hapa unasikia sauti za kunikejeli, is not fair, sisi tukifanya vitu kama hivi kidogo tu kama hivi toka nje, ondoka, lakini Msukuma na mwenzake wanaongea kejeli kabisa, as if mimi hapa naongea ujinga, lakini kwa sababu mnasema nchi ni ya kwenu, lakini nataka niwambie jambo moja CCM, hamtakaa hapa milele, hamtakaa milele, mtatoka na tutawatoa…

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali kidogo tu, utaratibu wa humu ndani unaongea na mimi, wewe hao usiwasikilize, wewe niambe mimi tu, utajikuta hugombani nao, endelea kuchangia ili dakika zako zisipokee.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, naongea na wewe na hata sisi wakati tunaongea na wewe, watu wanapofanya mambo kama haya, wewe unatakiwa unilinde, ni haki yangu kuwaambia wanyamaze niseme, lakini wewe kuwaachia is not fair.

SPIKA: Sasa nimekupa nafasi ya kusema na unapaswa kusema na mimi, badala lake unanifokea, unanifundisha si ndio hapo tunapokosana na ninyi ndugu zangu. Wewe umepewa nafasi changia hiyo bajeti, ongea na mimi usisikilize watu wangine, wewe ongea na mimi.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika ninachosema ni kwamba kama unahisi, kama unafikiri…

SPIKA: Hivi ngoja nikwambie, unajua kwenye Bunge hubishani na Spika mnafahamu, ndio haya yanafanyika, kujua kwingi ndio tatizo, yeyote anayesimama hapa anaongea na Spika. Ongea na Spika kama una cha kuongea, kama huna cha kuongea, pumzika.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika naomba unisamehe kama ambacho nimekiongea, unadhani kwamba nimekufokea au nimekusema, sio lengo langu wala sio kusudi langu. Naomba unisamehe kwa hilo, lakini ambacho mimi namaanisha, naomba kwamba mtu anapoongea watu wote tuheshimiane. Hilo ndio ombi langu, naomba hili litusaidie ili twende vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa nasema, ruzuku ya pembejeo 2000 kwenye randama ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, inaonekana ni nil, haipo. Mheshimiwa Rais Dkt. Kikwete aliondoka akacha bilioni 78, sisi miaka miwili tu ya Rais Magufuli akiwa madarakani, miaka miwili tu, wameshindwa kutenga bajeti ya pembejeo, maana yake wanawaambia wakulima kule mtaani, wapambane wenyewe. Sasa huko mtaani ajira hakuna, vijana hawajaajiriwa kwa 98%, kitu pekee labda ambacho kingeweza kuwasaidia kilikuwa ni kilimo na utaratibu wa nchi ulitenga ruzuku, wao wametoa, hawa watu wanafanya kazi gani?

Mheshimiwa Spika, wanasema wanakwenda katika nchi ya viwanda, sijui nchi ya nini, mimi nimeangalia style nyingi, wakati wenzetu wanafanya revolution za uchumi, walianza na agriculture revolution, walianza kupata kwanza mazao, kilimo kikaimarishwa ndio viwanda vikaja, sasa kilimo kinakufa, wategemee kutakuwa na viwanda, vitatoka wapi? Hivyo viwanda vita-feed kitu gani? Yaani unakuwa na kiwanda cha nini kama hakuna raw materials na lazima kuwa na mkakati wa nchi. Kuna siku nilisema hapa development lazima kwanza ingalie watu na 89% au 80% ya Watanzania wapo kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, katika jambo ambalo naamini lilikuwa zuri ambalo pengine lilifanyika, ile sheria ambao tuliipitisha hapa ya tani moja kwa mkulima apite bila ushuru, wale wakulima wadogo kabisa, nilijua kwamba itakomboa na sincerely kabisa naamini hivyo, lakini ukienda field wakulima hawa wanafanya nini? Wanafanyiwa nini, ni kweli kwamba ile tani moja wakipita hawatozwi ushuru? Ni kweli unakuta wakulima wanatozwa ushuru, vibibi, vimama, ambavyo wanalima heka moja, heka mbili kupata substance, tumetunga sheria hapa Bunge ya kazi gani? Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli alikuja Ifakara, nilimwambia kwamba Rais ile sharia, ile amri yako hapa haitekelezeki, akasema marufuku nchi nzima, nini kinafanyika? Wakuu wa Mikoa wapo, Mawaziri wapo, Wakuu wa Wilaya wapo, Serikali ipo, as if hamna mtu anayeona, yaani hatuumii.

Mheshimiwa Spika, jana ulisema hapa Lema alipata mkopo milioni mia sita na ngapi, ni kweli kapata kwa sababu hiyo ni haki yake, hawa wakulima wa nchi hii wanapata nini? Mbona hatuwapendi?

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nashukuru na Mungu akubariki, uendelee vizuri, ufanye kazi zako vizuri, ingawa Mwenyekiti wangu wa chama leo hakufanya kazi yake hapo ya kuwasilisha bajeti yetu ya Kambi, lakini kwa sababu alitoka Bungeni na wewe ukatoa ile amri yako, lakini anasikitika sana. Nashukuru. (makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 4 Machi, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Ikulu alizungumza sakata la Mo Dewji na akasema anashangazwa na namna ambavyo polisi wameshughulikia. Pia akasema kabisa Watanzania sio wajinga, picha iliyochezwa haiingii akilini; ni maneno ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa IGP akasema ndani ya siku nne atatoa taarifa, atasema kinagaubaga nini kilichotokea, leo ni siku ya 42, IGP kachuna, kakaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azory Gwanda amepotea, ama amepotezwa hatufahamu, hayupo duniani ama sijui yupo wapi hatujui. Mheshimiwa Lissu kapigwa risasi mchana kweupe, Ben Saanane mpaka leo hajulikani yupo wapi. Watu wameokotwa kwenye mifuko ya sandarusi kwenye fukwe za bahari ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia maneno ya Rais aliyomwambia IGP na akasema Watanzania sio wajinga, kwenye kitu ambacho kilikuwa wazi, ambacho hakijajificha cha Mo Dewji, Rais akasema hapa haiko sawa na IGP akasema kwamba hili ndani ya siku nne nitalishughulikia, hivi kama hivi imefanyika kwa Mo Dewji, jambo lipo wazi kiasi hiki, hawa akina Mheshimiwa Lissu, hali ikoje, akina Ben Saanane, watu wa kawaida hali ikoje? Ni mambo mangapi yanafanyika katika nchi hii kwa taswira hii ambayo watu hawapo accountable kwa hayo mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jambo hili ni fedheha, kitendo cha IGP kutamka hadharani atatoa majibu ndani ya siku nne halafu mpaka leo amekaa kimya na Serikali wamekaa kimya, jambo zito kama hili, hii inamaanisha kabisa kwamba nchi yetu haina utawala wa kisheria. Hii inamaanisha kabisa kwamba Serikali ya CCM hawawajibiki kulinda raia wa Tanzania; ni mfano wa dhahiri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivyo ndivyo jinsi ilivyo, naomba iundwe tume maalum ya kufuatilia mambo yote haya na tume hii iwe na hadhi ya kimahakama. Kama Rais anaweza akatoa jambo na akasema Watanzania wana akili, wameona kuna matatizo na IGP akasema ni kweli ndani ya siku nne nitatoa maelezo, leo siku ya 42 amekaa kimya, maana yake kuna mambo mengi katika nchi hii hayapo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa tume ikiundwa yenye nguvu ya kimahakama, ipitie mambo yote; ipitie jambo la Ben Saanane, Azory Gwanda, Akwilina na Mheshimiwa Lissu. Mambo yote haya yaje na ikiwezekana hii tume ije iripoti Bungeni ili Wabunge tuweze kusema way forward nini kifanyike kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Sheria ya Uhujumu Uchumi na Utakatishaji wa Fedha. Hii sheria inawezekana kabisa iliundwa kwa nia njema kabisa lakini kwa jinsi ambavyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, tangu mwanzo wa Bunge hili linaanza 2015 nimekuwa nikizungumzia sana ujenzi wa barabara yetu ya Ifakara - Kidatu ambayo inatakiwa itoboe iende mpaka Songea. Hii barabara inafadhiliwa na wafadhili katika mradi wa Sagoti wafadhili kama wanne hivi USA Aid na wengine.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli Rais wetu mwaka 2017 aliweka na akasema anaamini hizi km 75 ndani ya miaka mitatu itakuwa zimeisha yaani ilitakiwa mwezi huu 4 barabara iwe imeisha. Lakini mpaka dakika hii barabara imefanyiwa kazi kwa almost asilimia tano au sita. Leo ni miaka mitatu wafadhili wanalipia kila kitu asilimia 98 ni ufadhili serikali ya Tanzania inatakiwa itoe asilimia mbili tu kwa ajili ya fidia kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mpaka leo barabara inasuasua na juzi nikamwona RAS baada ya daraja kuwa limekatika pale kutokana na hizi mvua, anakwenda anamshutumu mkandarasi, anasema mkandarasi ni mzembe, anazembea, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga barabara hii iishe lakini wewe mkandarasi unazembea kitu ambacho siyo kweli, anajua ukweli. Ukweli ni kwamba Serikali yetu inataka mkandarasi yule atoe kodi (VAT) wakati mikataba haitaki kodi kutoka. Kumekuwa na ubishani wa kodi itoke au isitoke, tangu mwaka 2017 mpaka leo miaka mitatu, kitu ambacho tunapewa bure. Yaani wazungu wanatuambia wanataka watujengee barabara na fedha wanatupa, wazungu, mabeberu, ninyi hamtaki barabara ijengwe mnataka kodi. Hii ni aibu kabisa, ni aibu na ni kitu kibaya na sielewe commitment ya Serikali katika hili maana yake ni nini. Yaani tafsiri ni nini! Hapa napata mashaka hivi ni kweli wizara zinaweza zikagombana na mkandarasi kama Mheshimiwa Rais Magufuli hajui, kweli!

Mheshimiwa Spika, wnataka watu wa Kilombero tuamini kwamba nyuma ya kwenye huu mpango, kwenye huu ukwamishwaji Mheshimiwa Rais yupo? Kwa sababu kama Mheshimiwa Rais amekuja kuzindua barabara na akasema ndani ya miaka mitatu barabara iishe, leo ni asilimia tano na Mheshimiwa Rais ana vyombo vyake, ana watu wake wote. Ana Mawaziri, ana Waziri Mkuu, ana Wakuu wa Majeshi, ana TAKUKURU, ana vyombo vyote, kweli hajui. Hivi kweli nyie hamjui!

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hili ni jambo la aibu na hiyo commitment ya Awamu ya Tano wanayosema wao wapo hapa kutetea maslahi ya watu yako wapi kwenye hili jambo. Barabara yetu hiyo sisi huo ni uchumi, sisi kwetu ni uchumi ule.

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Kamwele tafadhali.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Lijualikali ambaye ana dakika za kuendelea kuchangia katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, barabara ya Kidatu-Ifakara ujenzi unaendelea, lakini tulikabiliwa na changamoto za hali ya hewa. Mkoa wa Morogoro tangu tarehe Mosi Oktoba, mwaka jana, mvua ilianza kunyesha haijasimama mpaka leo na kwa asili ya ukandarasi anatumia udongo. Mvua zikishanyesha kuna moisture content inayotakiwa ili aweze kujenga barabara, sasa kutokana na hayo mazingira ameshindwa kuendelea.

Mheshimiwa Spika, tutakuwa na vitu vingi tunavyoviongea lakini sisi wasimamiaji, mimi ndiye ninayesimamia ule mradi, sehemu kubwa ambayo imefanya hii barabara isikamilike ni kwa sababu ya hali ya hewa na yale maeneo yana mvua nyingi kila wakati na yeye anaishi kule. VAT siyo sababu, VAT ni suala la kiutawala wala halina mgogoro wowote, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ifakara kule niwaaminishe kwamba Serikali ina nia nzuri ya kuijenga barabara ile yote mpaka Malinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana imeshaanza lakini kutokana na hali ya hewa haiwezi ikajengwa katika kipindi cha hali ya hewa mbaya, hivyo ubora wa barabara unaotarajiwa hautapatikana na tutakuja tena kuleta lawama nyingine. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge suala hili tusubiri mvua ikishakatika ataona speed tutakayokwenda nayo, hatuna mgogoro mwingin,e mambo mengine ni ya kiutawala tu. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali, taarifa hiyo.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, utakumbuka Bunge la mwezi wa Tisa mwaka jana nilikuwa humu peke yangu, nilikaa kiti hicho baada ya wengine kuwa wametoka nje kutokana na ambacho kimetokea, niliongea hii hoja. Nakumbuka uliniambia sasa umeona umetoa ya moyoni sasa utulie umeongea umesikika na unakumbuka, hoja ilikuwa ni hii hii. Bunge lililopita mwezi wa Kwanza nimeuliza swali na hansard zipo, Mheshimiwa Waziri kwa mdomo wake anasema tatizo ni VAT, Serikali kutaka kodi na akasema mgogoro wa kodi umeisha. Amekiri mwenyewe na hansard zipo kama ni uongo mimi leo naacha ubunge, hansard ije hapa, kama ni uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuendesha nchi kwa ujanja ujanja, huwezi kuwa Waziri unakuwa mjanjamjanja, uongouongo hauwezekani. Majibu ya Serikali lazima yawe ya ukweli, watu wanaiamini Serikali, wanaamini jibu la Serikali; leo unapokuwa unajibu hili, kesho jibu hili maana yake commitment yako wewe haipo. Kwa hiyo niseme kwenye hili nasema wazi Mheshimiwa Waziri ametudanganya, amedanganya Bunge kwa sababu tayari kuna hansard za majibu yake akisema shida ni VAT. Haiwezekani Serikali ambayo wanasema wana fedha wanaanza kugombania fedha za msaada, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kila siku wanasema hapa, nchi hii ina fedha, nchi iko vizuri, wazungu wanatujengea barabara wao hawataki, haiwezekani, haiwezekani. Nimwambie Mheshimiwa Waziri asisingizie habari za mvua, mvua tangu mwaka 2017 mpaka leo, mwaka 2017 mpaka leo mvua gani hiyo, Mvua ya Nuhu! Ni gharika! Ni gharika nasema! (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sisi tunaumia sana, nyie kama mnakaa huku kwenye viyoyozi barabara safi, sisi kule tuna shida hatujihisi kama tuko Tanzania. Haiwezekana halafu Mheshimiwa Waziri anakuja hapa anaongea vitu vya uongo kabisa, haiwezekani, haya mambo yanaudhi, Mheshimiwa Waziri namwomba sana aheshimu kiti alichokaa hapo na mwaka huu tunawang’oa. (Makofi)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, mwongozo.

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali ni kengele ya kwanza, lakini naona yuko juu sana nataka nimpe likizo kidogo, nimrudishe baadaye ili atulie kidogo. (Kicheko)

Unaonaje dakika tano zako nikikupa baadaye.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ni sawa haina shida.

SPIKA: Ili upoe kidogo.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ni sawa haina shida.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ameniudhi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa tena dakika zangu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa kwenye issue ya barabara ingawa ndugu yangu Kibajaji pale anasema huu siyo muda wa barabara na kwamba muda umeisha. Mimi nataka nimwambie tu kwamba mimi ni Mbunge kwa miaka mitano na nimeapa kukaa hapa mpaka nitakapofika mwisho.

Kwa hiyo, mimi nitasema mambo ya Kilombero mpaka siku ya mwisho. Mimi kazi yangu ni kusema mambo ya Kilombero. Ninyi Serikali ya CCM na Rais Magufuli kazi yenu ni kutenda yale mimi nayoyasema kuhusu Kilombero. Kwa hiyo, mimi hapa nitafanya kazi yangu mpaka siku ya mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike hatua kule kwenye sheria ya sifa za kuingia Bungeni kidogo zibadilike, shule pia inatakiwa itumike angalau hata form four hivi. Mambo mengine ni kutokana na shule inawezekana ikawa watu hawaelewi mazingira ya humu ndani. Kwa hiyo, niombe ifike hatua shule pia iingizwe, mtindo wa kusema kwamba tu mtu ajue kusoma na kuandika kama Taifa sasa hii issue ifike mwisho, shule itajwe form four, form six. Kama dereva wa Serikali anaambiwa lazima awe form four…

SPIKA: Dakika tatu zinaisha…

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ni bora ziishe lakini nchi ijue ukweli. Kwa sababu kama kuna Mbunge anakambia eti bwana wewe muda umeisha wakati anajua kabisa tumeapa miaka mitano…

T A A R I F A

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuzingatie elimu kwenye kuchagua Wabunge.

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Lijualikali naomba ukae upokee taarifa. Mheshimiwa Deo Sanga.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji ajue hata waliomaliza form four na wenye degree wapo failures. Kwa hiyo, form four siyo maana yake ndiyo inayokuingiza hapa. Wapo watu hawana form four lakini vichwa vyao ni sawa na mtu mwenye PhD. (Makofi)

SPIKA: Na huo ni ukweli wa maisha. Mheshimiwa Lijualikali pokea taarifa.

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, issue siyo kufeli au kufaulu; kama tunasema madaktari wawe na level fulani, kama madereva wetu tu lazima wawe na form four, wewe unakaa hapa upitishe sheria za nchi, uisimamie Serikali halafu uwe tu darasa la pili au shule huna kabisa. Lazima tuitendee haki nchi yetu. Huyu nimwambie kabisa mimi sijakimbia shule, kwa hiyo, lazima tubadilishe twende kwa style hiyo, shule itumike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilombero iwe ni mwaka huu au mwakani kwa sababu wahisani wameshatoa fedha na fedha mnazo, mimi kama Mbunge wa Kilombero nawataka mfanye kazi yenu ya kutuletea barabara yetu. Haiwezekani mmepewa fedha za bure kabisa, fedha mnazo mmekalia hamtaki kazi ifanyike kwa sababu zozote zile. Halafu Mheshimiwa Waziri alikuwa anasema suala la VAT ni suala la kitaalam tu wakati mmeshikilia mitambo ya mwekezaji, mmeshikilia mitambo ya mkandarasi asifanye kazi leo hii unasema kwamba hili suala ni la kawaida tu, maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, nimtake Waziri iwe kesho, keshokutwa ama mwakani Kilombero tunataka barabara yetu tuliyopewa na mabeberu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilombero haina Hospitali ya Wilaya, Hospitali inayotumika ni Mtakatifu Fransisco lakini gharama zake ni kubwa kidogo kwa watu wengi kuweza kumudu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna Vituo vya Afya vya Kibaoni, Mang’ula na Kidatu. Vituo hivi havikidhi mahitaji ya kihuduma na tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Kilombero ni zaidi ya 500,000. Bila ya kupata Hospitali ya Wilaya, bado bituo hivi vitakuwa na kazi kubwa hivyo kupunguza ufanisi. Tunaomba kupatiwa Hospitali ya Wilaya ya Kilombero.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.