Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja kwa hotuba hii ya 2016. Kwa vile Hotuba ya Waziri mpya na Awamu mpya ya Tano, lakini uhalisia Wizara hii. Umuhimu wa Wizara hii kwa miaka mingi sasa imekuwa haina msaada kwa wakulima hasa wa Mkoa wa Morogoro na zaidi Wilaya ya Gairo. Wilaya ya Gairo ni moja ya Wilaya zinazolima sana nchini pamoja na kuwa haipo kitakwimu na umaarufu cha ajabu Wilaya hii haipati ruzuku za pembejeo na ikipata zinakuja nje ya muda wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwaka huu mbegu imekuja mwezi wa Kwanza katikati, wakati kilimo cha Gairo mbegu inatakiwa mwezi Novemba. Gairo ina Tarafa mbili, Tarafa ya Gairo na Nongwe, Tarafa ya Nongwe yote ina maji ya kutosha, mito ya kudumu mingi, lakini hakuna mpango wowote wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika maeneo haya pamoja na Halmashauri ya Gairo kuomba pesa, lakini imekuwa haipewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuna nia ya kuondoa nchi katika matatizo ya chakula na mazao ya biashara, wataalam wa Wizara wajiongeze na kujua kila sehemu inayofaa kwa kilimo. Siyo kunakili kila siku kuwa maeneo fulani ndiyo wanafaa au yanafaa kwa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija upande wa mifugo Wilaya hii ina mifugo mingi lakini kuna uhaba wa mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo, hasa katika Vijiji vya Kitaita, Ngayaki, Chogoali, Misingisi, Mkalama, Meshugi, Ndogomi, Kumbulu, Chilama. Tunaomba sana huduma hii ya mabwawa ichukuliwe kwa jicho la huruma na haraka, kwani wafugaji hawa wanapata tabu sana kwenda zaidi ya kilomita kumi hadi kumi na tano kwa ajili ya maji na mara nyingine wasipate maji ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nategemea mtashughulikia suala hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia. Kwanza nimpongeze dada yetu, Waziri wa Afya pamoja na msaidizi wake, Ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kuwakilisha hotuba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika sehemu chache tu na za muhimu sana kwa watu wetu wa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na huu Mfuko wa Afya ya Vijijini (CHF). CHF ukiiangalia sana muundo wake na jinsi ilivyoanzishwa iko ki-theory sana. Ukiiangalia utajua labda huu mfuko ni ukombozi wa wananchi wanaoishi vijijini. Lengo lake kwa wanachama wake ni kuchangia ili kupata huduma za dawa pamoja na vifaa vinavyohusiana na tiba.
Ukiangalia kiundani katika practical hakuna kitu kama hicho. Utakuta vituo vya afya au zahanati zinachangia Mfuko huu wa CHF, zile pesa zinakwenda CHF makao makuu, badala ya watu kuletewa dawa hawaletewi dawa, utakuta wanaletewa condom au vitu vingine tu havina hata msingi, hata chanjo za watoto vijijini zinashindikana. Mimi sioni huu mfuko wa CHF maana yake nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia katika muundo wake kwa kweli una maana kubwa sana. Mwanachama wa CHF akienda kwenye kituo cha afya au kwenye zahanati kitu atakachoambulia kupata pale ni kipimo tu kama akiambiwa ana malaria hicho kipimo kidogo basi ameshamaliza, zaidi ya hapo dawa nenda kanunue, hakuna dawa. Sielewi mpango huu wa CHF una faida gani!
Mimi nitoe ushauri kama huu mpango wa CHF umeshindikana kwa nini msiunganishe hii mifuko ili mfuko wa bima uwe mmoja? Nina maana kwamba CHF na NHIF uwe mfuko mmoja, kuna faida gani ya kuwa na mifuko mingi ambayo haina faida yoyote? Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu madaktari, kwa mwaka wanahitimu zaidi ya madaktari 1,000 lakini wanaoajiriwa hawazidi 300. Halafu tunakwenda vijijini na kwenye vituo vya afya tunawaambia watu wachangie kujenga vituo vya afya na zahanati. Kwa mfano, pale Gairo kuna zahanati zaidi ya sita zimeshajengwa, vituo vya afya viwili mpaka leo havina Muuguzi wala Daktari sasa maana yake nini? Tukija hapa tuna kazi ya kuambiwa tu tuwashawishi wananchi. Mimi kama Mbunge kwa kweli sasa hivi nimechoka simshawishi mtu hata mmoja ajiunge CHF, namwambia kwanza achana nayo nenda na hela yako cash, haina maana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba dada yangu aliangalie sana hili kwa sababu ni Waziri mgeni uwe makini sana na suala hili. Tunapozungumzia habari za afya za watu basi Madaktari muwape ajira na mhakikishe kwamba wanafika Wilayani. Kwa mfano, Wilaya ya Gairo mpaka sasa hivi haina Madaktari kabisa na Wauguzi. Mwaka huu mmetupangia Wauguzi wanne Wilaya nzima na hao Matabibu watano Wilaya nzima kwa kweli haina maana ya aina yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nataka kufahamu, hii Wizara ya Afya iko tu kazi yake kutengeneza sera au iko kwenye majukumu? Maana mimi naona iko kwenye kutengeneza sera kwa sababu yenyewe inapohudumia inahudumia mwisho Hospitali za Rufaa tu, lakini ukija huku kwenye Hospitali za Wilaya utakuta ziko chini ya Halmashauri. Ukiuliza ambulance, utaambiwa ambulance kwani ninyi hamna mapato? Sasa hizi Halmashauri zinatakusanya wapi mapato ya kutosha wakati ambulance moja ni zaidi ya shilingi milioni 150 au 200! Hizi Halmashauri zitawezaje kupata vitu vyote hivi, zihudumie elimu, maji, majengo yao na ambulance? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu maana inaonekana hii Wizara ingekuwa Bodi tu ingekuwa hamna tena Wizara ya Afya iwekwe Bodi fulani tu basi kwa sababu ukiangalia huduma zake zote ziko chini ya TAMISEMI. TAMISEMI ndiyo imebebeshwa kila aina ya mzigo. Ukiangalia TAMISEMI siyo imebebeshwa mizigo tu imebebeshwa hata majitu mabomu mabomu yale yote yasiyojua kazi yote yako TAMISEMI, sasa kuna huduma gani hapo itakayofanyika ya ukweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumza kile kitu cha ukweli, ndiyo ukweli huo. Huduma za afya ni mbovu na utakuta Halmashauri za Wilaya kama kituo cha afya kiko mjini manesi pamoja na upungufu kama wako watano au sita, utakuta wanne wako kwenye kituo cha mjini, kule kijijini utakuta wakati mwingine kama kuna Daktari mmoja ndiyo huyo mpaka anazalisha akina mama, tunawadhalilisha akina mama. Sasa mimi sielewi, kama iko kisera, mimi nataka kujua kisera tu kwa sababu ukija kwenye TAMISEMI ndiyo ina mambo yote ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia pale Gairo, namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii alizungumza kwamba unaweza ukatoka hapa unaenda Morogoro ukapata accident, sasa ukiangalia katikati ya Tumbi ya Morogoro hapa ni Gairo, kilomita 131 kutoka Dodoma na kilomita 131 kwenda Morogoro, kila siku tunapiga kelele pawepo na madaktari na ambulance lakini mpaka leo hakuna. Mimi nashangaa hapa mkitoa mifano mnatolea Kanda ya Ziwa tu sijui wapi hakuna madaktari mbona hamtolei mfano Gairo, Gairo Madaktari hawapo na ndiyo barabara kuu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee MSD. Naomba pesa zao wanazodai walipwe zaidi ya shilingi bilioni 130, wapewe hela zao ili watoe huduma safi. Ule mpango wa MSD kuweka maduka ya dawa kwenye Hospitali ya Rufaa isiwe hivyo, waweke maduka yao mpaka Hospitali za Wilaya. Kinachotakiwa kufanyika pale wao wapewe nafasi tu lakini waweke maduka yao. Wanaopenda huduma za afya siyo kwamba wako mijini tu, wako vijijini na Wilayani basi angalau wapewe nafasi kwenye Hospitali ya Wilaya ili nao waweke maduka ili wananchi nao wa sehemu za vijijini na kwenye Halmashauri wapate huduma za MSD. Naona kila atakayezungumza au kwenye vyombo vya habari utasikia MSD imeweka duka Muhimbili sasa hivi ina mpango wa kuweka Morogoro, ina mpango wa kuweka wapi, huku Wilayani vipi au MSD haiko Kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kugongewa kengele ya pili nafikiri kwa haya machache nimeeleweka, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wa hotuba hii ya TAMISEMI. Kwanza kabisa, niwapongeze Mawaziri wote wawili katika Ofisi hii ya Rais (TAMISEMI) na nasema bado mapema kabisa naunga mkono hoja hii isipokuwa tu kuna sehemu nataka nitoe ushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 16 tumeona kwamba sasa hivi Halmashauri zetu zote zinataka zitumie mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, jambo jema sana. Pia tumesikia hotuba mbalimbali za Mheshimiwa Waziri Mkuu ambazo zinahitaji sana msaada wa kutoka katika Wizara hii. Tunajua Serikali ina nia nzuri sana na ndiyo maana inaanzisha maeneo mapya kama vile mikoa na wilaya. Hata tunaposema kwamba hotuba ya Waziri Mkuu inahitaji msaada mkubwa kutoka TAMISEMI, kwa mfano ile kusema kwamba tutafuta Halmashauri zile ambazo hazikusanyi mapato yanayotakiwa, naiomba Wizara ya TAMISEMI imsaidie Waziri Mkuu, kwanza ianze kufuta wafanyakazi wabovu kwenye hizi Halmashauri za Wilaya kabla ya kufuta Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukianza kufuta Halmashauri kabla ya kufuta wafanyakazi wabovu mtakuwa hamjatutendea haki. Wafanyakazi kwenye Halmashauri ni wabovu, wamechoka hasa ukichukua kwa mfano Halmshauri yangu ya Gairo, kuanzia Mkurugenzi, Afisa Mipango, Mweka Hazina wote hakuna kitu. Sasa kwa kweli utategemea Diwani au Mbunge atatoa ushauri gani wa kitaalam ili hiyo Halmashauri iwe na mapato? Cha msingi kwanza tuangalie hawa watendaji wetu, watendaji ni wabovu, lazima tukubaliane.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata nikisoma kwenye hiki kitabu cha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kusema kwamba kuna Halmashauri zingine zina hati nzuri, zingine hati kidogo za mashaka, zingine hati chafu, ukiangalia ukweli Halmashauri zote zina hati chafu tu. Huo ndiyo ukweli. Ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene nakujua uhodari wako, naomba uziangalie kwa umakini sana Halmashauri, ndiyo kwenye mchwa, wanapewa pesa nyingi na Serikali na zote zinaishia huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tujaribu kuziangalia hizi Halmashauri mpya kwa jicho la huruma, tumeanzisha Halmashauri nyingi sana. Nitoe mfano wa Halmashauri yangu ya Gairo toka ianzishwe mpaka sasa hivi haina hata gari. Wakati tuko Halmashauri mama ya Wilaya ya Kilosa tunagawana pale, tumepewa magari sita na mpaka sasa hivi linalotembea ni moja tu na lenyewe ukipanda kilometa saba unasukuma kilometa saba. Kwa hiyo, Mkurugenzi hana gari, kituo cha afya hakina ambulance, hebu mtufikirie, mtuonee huruma hizi Halmashauri mpya, tupeni vitendea kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika ukurasa wa 32 wa hotuba ya Mheshimiwa Simbachawene amezungumzia kuhusu habari ya Hospitali za Wilaya, hapa nchini Hospitali za Wilaya ziko 84 tu, wilaya 97 zinatumia hospitali za taasisi za umma au za dini. Kwa mfano, kama pale Gairo, Wilaya ya Gairo inategemewa na wilaya nyingi za pembeni kwa mfano Kiteto, Kilindi, Kongwa na Mvomero wote wanategemea sana pale Gairo lakini Gairo pana kituo cha afya na toka tuanzishiwe wilaya ile hatujapata fungu la aina yoyote la kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Gairo tuna kituo cha afya ambacho kinatoa huduma za hospitali pamoja na operesheni pamoja na vitu vingine lakini hatuna ambulance na Gairo ni kama Tumbi pale maana ni katikati ya Morogoro na Dodoma. Sasa mnataka mpaka kiongozi aje avunjike miguu pale ndiyo muone umuhimu wa Gairo kwamba panatakiwa ambulance? Tunaomba tupate ambulance na tupewe fungu la kijenga Hospitali ya Wilaya ya Gairo. Tumeshaomba sasa hivi ni zaidi ya miaka miwili, huu wa tatu, hatujapata. Tunaomba sana mtufikirie kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye upande wa barabara, sasa hivi kila Mbunge anataka barabara yake ihame kutoka TAMISEMI ipandishwe hadhi iende TANROADS. Ilitakiwa TAMISEMI mjiulize ni kwa nini Wabunge hawataki barabara zao ziwe TAMISEMI au ziwe chini ya Halmashauri? Utakuta kilometa tano inayotengenezwa na TANROADS na kilometa tano inayotengenezwa na Halmashauri ni vitu viwili tofauti na ndiyo maana Wabunge wote hawataki barabara sasa hivi ziwe chini ya Halmashauri. Kuna maombi zaidi ya 3,400 ya kupandisha daraja barabara ili ziwe chini ya Barabara za Mikoa kwa sababu huku kwenye Halmshauri ndiyo kwenye mchwa wa kula pesa zote za barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata mgao wa pesa ukiangalia utakuta Wilaya kama ya Gairo na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri anaifahamu vizuri sana Wilaya ya Gairo, anafahamu kuanzia Gairo mpaka Nongwe, anaijua vizuri sana milima yake ile ilivyo inazidi hata milima ya Lushoto. Mwaka jana tumeomba shilingi bilioni 1.5 tunakwenda kuwekewa shilingi milioni 400 na katika hizo mpaka sasa hivi imefika shilingi milioni 22. Sasa hata huyo mama aliyeko hapa TAMISEMI, anayeangalia hizi barabara za Wilaya sijui mmemuweka tu akae, hatembei au hajui mazingira ya hizi wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nashauri itengenezwe agency ambayo itakuwa ina mamlaka ya kuzisimamia barabara za TAMISEMI na kuangalia ubora wake ili Wabunge tusiwe tunaomba barabara nyingi ziwe chini ya TANROADS. Pawe na kitu ambacho kinasimamia ufanisi wa barabara vinginevyo tunakuwa tunaacha watu wanakula hela tu. Utakuta barabara ya TANROADS ina shilingi milioni 200, ya Halmashauri ina shilingi milioni 300 lakini ya TANROADS ina kiwango cha juu na hao hao Ma-engineer bado wapo, usimamizi mbovu, lazima kitengenezwe chombo ambacho kitasimamia hizi barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye bajeti hii, nikisoma katika hiki kitabu, Ofisi ya TAMISEMI, fedha za 2016/2017, ukienda kwenye kilimo hapa utakuta Wilaya ya Ilala imetengewa shilingi milioni 100, Wilaya ya Kinondoni shilingi milioni 148, Wilaya ya Temeke shilingi milioni 113, halafu ukija hapa Wilaya ya Gairo shilingi milioni 15, ina maana Temeke wanalima sana kuliko Gairo? Kinondoni, Ilala wanalima sana kuliko Gairo, haiwezekani! Angalia, ukisoma humu utakuta miji mikuu imewekewa hela nyingi sana za kilimo kuliko zile wilaya. Sasa nafikiri haya mambo tujaribu kuyaangalia hayako sawasawa kabisa. Hivi hapa kuna sehemu inalima viazi kuliko Gairo katika nchi hii, kuna sehemu inalima mahindi mazuri kuliko Gairo, acha mahindi ya wapi sijui huko hayakoboleki hayo. Kwa hiyo, naomba hili liangaliwe kwa umakini zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kunipa nafasi na mimi kuwa mmojawapo wa wachangiaji katika hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wetu Profesa Sospeter Muhongo pamoja na Naibu wake. Pamoja na kuwa ni mgeni lakini tunaona ana nia njema katika Wizara hii na Taifa hili. Vilevile nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na wote katika Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitaanza na REA, cha kwanza nitapingana kidogo kuunga mkono juu ya hoja ya ndugu yangu Mheshimiwa Ally Mohamed Keissy, kwamba REA wanafanya vizuri kwa sababu moja. REA katika mipango yao ya kugawa umeme vijijini wana upendeleo, hili liko wazi, kwa wale Wabunge waliopita, Bunge lililopita wameona, katika ile miradi ya awamu ya pili. Kuna baadhi ya wilaya na majimbo yana vijiji mpaka sitini; kwa mfano Majimbo ya Karagwe na Bunda.
Mheshimiwa Spika, ukija Jimbo la Gairo lina vijiji vinne na havijawaka umeme hata kimoja. Karagwe kuna vijiji 110, ukija Bahi kuna vijiji viwili, hapa Dodoma hakijawaka hata kimoja, sasa nataka kujua, hawa REA wanafuata vigezo gani? Wanataka sisi Wabunge tukashinde ofisini pale kwa Meneja au kwa ndugu yangu yule Msofe tuanze kuomba umeme, tusifanye kazi nyingine? Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri ameliona hili ndiyo maana safari hii hata vijiji hajavitaja humu kwa sababu nafikiri nia yake labda ni kwenda kugawa keki hii kwa kila mwananchi na kila Wilaya au kila Jimbo wapate sawa, wasirudie yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka jana wameandika Gairo vijiji 27 ndani ya kitabu cha Wizara, nimekwenda kule na Waziri aliyepita, Mheshimiwa Charles John Mwijage, nimekwenda na Mheshimiwa Simbachawene, hawaelewi, wala watu wa REA hawajui wakati wapo Wizara ya Nishati wanaishia vijiji vinne. Kwa kweli mwaka huu ndio utakuwa wa mwisho wangu kuunga mkono hii habari ya REA.
Mheshimiwa Spika, REA hawana maana kabisa katika ugawaji wa umeme vijijini. Hata kama pesa hawapewi basi tupewe hata maneno kwamba utawekewa kijiji hiki, kijiji hiki, tubaki tunadai, sasa hata pa kudai hakuna. REA ni tatizo kubwa na ninyi Wabunge wageni mtaliona tatizo hilo, bado hamjaliona. Mwaka huu nasubiri kwa sababu nimeangalia sana kwenye hotuba ya Waziri hivi vijiji sijaviona humu mwaka huu tumetajiwa tu idadi ya pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine, mimi ni mfanyabiashara na katika biashara zangu nafanya biashara nyingi mojawapo ikiwa ya mafuta. Na-declare interest na humu ndani kuna watu wengi kuna Walimu, wakulima, wafugaji, kila mtu ana fani yake. Kwa hiyo nisipozungumzia habari ya biashara ya mafuta wakati najua na na-declare interest nitakuwa sijajitendea haki. Kwa wale waliopita Bunge lililopita wanajua kabisa vituko vya EWURA, wanavifahamu, na ndiyo maana hata Mbunge, Mheshimiwa David Silinde nafikiri alikuwa anataka kuizungumzia lakini muda ulikwisha.
Mheshimiwa Spika, kwanza lazima tukumbuke hata neno chakachua aliyelileta Bungeni na Tanzania nzima ni mimi hapa wakati nazungumzia habari ya kuchakachua mafuta ya taa, diesel na petrol ndiyo hilo likaingia chakachua matokeo, sijui chakachua kitu gani, chakachua kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, EWURA ilianzishwa wakati ule mafuta ya taa yalikuwa hayana kodi, petroli na diesel zilikuwa na kodi ziliyazidi mafuta ya taa karibu shilingi mia sita. Kwa hiyo, wafanyabiashara wengi wakawa wanachukua mafuta ya taa wanayafanya malighafi wanachanganya na diesel au na petroli kwa ajili ya kujipatia kipato. Tukaanzisha mfumo wa kuweka vinasaba kwenye mafuta ili mtu akichanganya mafuta ya taa na petroli au na diesel anaona kwamba amechanganya na mafuta ya taa.
Mheshimiwa Spika, baadaye EWURA walishindwa kabisa kuondoa ule uchakachuaji kwa vinasaba vyao kwa ajili ya rushwa iliyoko EWURA. Kwa hiyo, Bunge hili likaamua kupandisha mafuta ya taa kwa kuweka kodi kwa sababu EWURA walishindwa kufanya kazi yao. Lakini cha ajabu EWURA wakahamia sasa wakawa wanaendelea kuweka vinasaba kwenye petroli na diesel. Sasa wakija kwenye petrol station wanakwambia vinasaba vimepungua, kwa hiyo, umeshusha mafuta yanakwenda mgodini au yanakwenda transit. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vinasaba wanawekaje? ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge nataka niwaeleze. Mtu yuko Dodoma ananunua mafuta anapiga simu BP, nataka kununua mafuta, BP anamwambia bei yangu hii, anamwambia nimekubali, anamwambia weka hela Dodoma kwenye benki nitaziona kwa internet hapa Dar es Salaam. Unaweka hela Dodoma benki mtu wa BP anakwambia lete gari, nampigia simu nikiwa Dodoma Transporter peleka gari yangu BP kanipakilie mafuta.
Mheshimiwa Spika, Transporter anamtuma dereva wake nenda kapakie mafuta labda ya Shabiby BP, dereva akifika pale yuko mtu aliyepewa tenda na EWURA wanaitwa GFI, mtu wa GFI anakuja anamwambia dereva, wakati huo dereva hana elimu yoyote wala hajui vinasaba au anawekewa mkojo wa punda au anawekewa juice, anaambiwa umeona hii hivi ndiyo vinasaba hivi usinuse, nakuwekea hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumbuka vile vinasaba havibadilishi mafuta rangi wala nini, unaletewa Dodoma. Siku ya pili anakuja mtu na gari la EWURA na havionekani kwa macho ameshaambiwa na yule mwenzie kwamba kule nilikoweka nimeweka kidogo nenda kapime. Anakuja anapima kwako, kwanza anakwambia kabisa nipe milioni tatu kama hutaki napima, usipotoa hiyo pesa na sisi Wabunge wabishi kutoa rushwa anapima, anakwambia vinasaba vipo lakini vimepungua kidogo wakati huvioni kwa macho, hujahusishwa kwenye kuviweka, wala havikuhusu; sasa huu ni wizi.
Mheshimiwa Spika, nikwambie kwa Tanzania kwa mwezi inaingiza meter tones laki mbili na elfu hamsini, sawasawa na lita mia tatu na vinasaba mtu wa mwisho anayeweka mwenye gari anachajiwa shilingi kumi na mbili na senti themanini na nane, kila lita moja unayoweka wewe mafuta. Kwa mwezi yule aliyepewa tenda analipwa bilioni tatu na milioni mia nane, kwa mwaka bilioni arobaini na sita, umenielewa.
Mheshimiwa Spika, hii kampuni ya GFI imepewa tenda bila kutangazwa kwenye magazeti na mpaka leo tenda hiyo inaendelea. Tafuteni GFI imepewa wapi hiyo tenda, haijawahi kutangazwa na imepewa tenda mpaka leo hii. Tusizungumze hapa tunasema sijui hii kampuni ya nani, hii kampuni ni ya wao wenyewe na ukimchukua leo Kalamagozi wa EWURA na yule Kaguo utaona anavyojieleza, wanajieleza kuliko hata waandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadhi ya magazeti hayawezi kuandika EWURA vibaya, baadhi yao, yanayopewa matangazo, kwa sababu ukiandika vibaya tangazo hupewi. Ukiandika vibaya habari ya EWURA, hupati tangazo. Hivi leo bilioni arobaini na sita hii ukiigawanya hata kama tununue madawati tu tunapata madawati laki saba.
Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja hii mpaka nipate jibu sahihi la hawa watu wa EWURA. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye hotuba ya Wizara ya Fedha. Kwanza nitaanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, maana kwenye ukweli lazima tuseme ukweli. Mimi huwa sipongezaji sehemu ambazo naona zina matatizo, lakini kama sehemu ni ya ukweli, tutapongeza sehemu ya ukweli na tutasema ukweli. Nitampongeza kwenye kufuta misamaha ya maduka ya majeshi. Hapa nampongeza. Kwa nini nasema nampongeza?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao hawajatembelea haya maduka au hawajawahi kupitia haya maduka, wanaweza wakaona wamefanya kosa kubwa sana, lakini kama ulishawahi kwenda kwenye haya maduka ukajionea kinachofanyika pale, utagundua alichokifanya ni sahihi kabisa. Niwapeni mfano mmoja tu, hapa Dodoma kuna duka la Magereza, liko hapa Magereza na hata sasa hivi ukienda liko wazi muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia wanunuzi wa vile vitu, mtu yeyote pale ananunua kwa msamaha wa kodi na kibaya zaidi viwango vya vile vitu ni vibovu vilivyopindukia. Unaweza ukaenda ukapata kitu cha Sumsung, labda TV ya Sumsung lakini ukiingalia ile inafanya kazi miezi sita, imekufa. Kwa hiyo, siyo kuwasaidia wanajeshi au siyo kuwasaidia watu askari wetu, hapo ni kuwaumiza na kuzidi kuwalia fedha zao kwa kutumia exemption. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hilo, niko tofauti kidogo na baadhi ya wenzangu kwa sababu naona kwamba hilo ni tatizo, liwekewe utaratibu mzuri ambao utawanufaisha hawa askari wetu, nao wataridhika, ndiyo cha msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 64 anazungumzia kodi za magari na pikipiki. Mimi ni mfanyabiashara wa magari lakini leo sizungumzii habari yangu, nitazungumzia habari ya Watanzania. Amezungumzia usajili, sasa hapa hatujaelewa ni ule usajili wa mara moja, ukishasajili gari hulipii tena au ndiyo road licence?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni road licence, ukiangalia hapa kwenye pikipiki sh. 95,000/= kwa mwaka, hii ni pesa nyingi mno kwa mtu wa bodaboda. Kwa gari ni sh. 250,000/=, hiyo siyo shida. Kwa nini usiweke utaratibu mwingine? Ubadilishe utaratibu! Utaratibu huu ndiyo ule ambao ulileta matatizo miaka ya nyuma; na Bunge la nyuma watu walilalamika sana. Mabunge ya miaka iliyopita, TRA haiwezi ikaanza kufukuzana na watu wa bodaboda, hawana askari wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Polisi wetu hawatoshi kufukuzana na watu wa bodaboda kisa hawajalipa hiyo sh. 95,000/=. Ibadilisheni system yake, iwekeni angalau katozo kadogo kwenye mafuta ili msiwe mnapata usumbufu wa kufukuzana na hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pikipiki moja ikitumia lita saba tu kwa siku, kwa mwezi ina lita 210 kwa mwaka ina lita 2,520; kwa hiyo, ukimwekea shilingi kumi, atalipa 25,200/=. Ukienda kwenye magari kwa mfano, malori yanayokwenda nje na yanayotembea mikoani, kwa safari moja tu au tuseme kwa mwezi, weka kima cha chini, litatumia lita 4,800 pamoja hata na mabasi, kwa kima cha chini kabisa kwa mwezi. Ukiangalia kwa mwaka litatumia lita 57,600/=; ukiweka kwa shilingi kumi tu utakusanya sh. 576,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kuwa bodaboda atakuwa amelipa kiasi kidogo cha pesa, lakini hawa wengine huku watakuwa wamefidia ile gharama na kufikia lengo la Serikali, kuliko kwenda kusukumana na hawa wafanyabiashara wadogo wadogo kufukuzana nao.
Nakumbuka mwaka juzi 2014 kilichotokea Morogoro, kutaka kuuana watu wa TRA na hawa watu wa bodaboda kwa ajili ya hayo mambo ya kufukuzana na watu wa bodaboda. Kamua ng‟ombe wako huku unamlisha majani, unamkamua polepole kuliko kwenda kufukuzana fukuzana huko. Wekeni tozo hii ya sh. 10/= tu kwenye mafuta imalize haya matatizo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, sasa hivi hakuna asiyejua nchi hii ukame wa pesa ulioko mitaani. Kuna ukame mbaya sana wa pesa huko mitaani, nani asiyefahamu? Kama mfanyabiashara mkubwa leo hii ataweza kwenda kukopa Standard Bank, City Bank, Stanbic, lakini je, hao walipa kodi mnaowatarajia kuwaongeza, watakopa wapi? Watakopa NMB, watakopa CRDB, watakopa NBC, watakopa TIB na ukiangalia hizi Benki zina asilimia ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wanachukua pesa zote; pesa za bandari, Mashirika ya Umma, wanazipeleka zote BOT; mzunguko wa pesa utatoka wapi ili hao watu wadogo wakope? Ni sawasawa na binadamu unaitoa damu yote unaipeleka kwenye kichwa ikae huko huko isizunguke, haiwezekani hiyo! Huo ndiyo ukweli wenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnaona mabenki yanafaidika, basi wapeni hizo pesa at least kwa interest, nao muwapangie interest kiasi cha kuwakopesha wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini ukichukua pesa ukizipeleka BOT ambapo haina mzunguko wa aina yoyote kifedha, BOT Gairo haipo, BOT haipo Ngara, BOT haipo Sengerema, haipo Kaliua wala Kasulu, wanaenda kukusanya pesa zote wanaziweka. Wafanyabiashara nao wakiamua kukusanya pesa zao waweke kwenye madebe, kutakuwa na pesa nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuangalie, wakizizuia pesa sehemu moja kama BOT, wanazuia mzunguko wa pesa kwenye hili Taifa, maana yake itafikia sasa wafanyabiashara nao watachukua pesa nao wataweka kwenye debe lake hapeleki Benki. Wa bajaji naye ataweka kwake, sasa mzunguko utatoka wapi? Hao watu wanaokopa shilingi milioni mbili, shilingi milioni 10, watakopa wapi? Maana mfanyabiashara mkubwa ataenda kwenye mabenki ya nje, atapata pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiangalie, kama tunaona mabenki yanafaidika, basi hizi pesa tuziwekee mpango mwingine angalau hata tuwape hawa mabenki kwa interest lakini siyo kuzizuia sehemu moja hizi pesa. Tukizuia huo mzunguko, pesa itakuwa shida nchi hii, nakwambieni ukweli kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la mafuta, nashukuru kwamba kuongeza mafuta kwenye mafuta ya nje ni jambo jema kwa asilimia 10, lakini aangalie na viwanda vya ndani toeni kodi ya VAT kwenye viwanda vya alizeti vya ndani ya nchi na viwanda vingine vya mafuta. Kwa sababu mpaka sasa hivi ukiona mafuta ya nje yako sh. 50,000/=, ujue ya alizeti itatofautiana sh. 2,000/= tu bei yake, kwa sababu bado kuna kodi. Kwa hiyo, bado hujamsaidia mkulima hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wakulima wadogo wadogo wote wana viwanda vyao vidogo vidogo; lakini katika vile viwanda vimetofautiana; yuko yule ambaye hajafikisha kodi ya shilingi milioni 100 ambaye haingii moja kwa moja kwenye VAT, anasaga alizeti na yuko yule wa kwenye shilingi milioni 20, 30 anasaga alizeti hiyo hiyo lakini hana VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa usawa uko wapi? Usawa haupo. Ili upate usawa, viwanda vya ndani vyote vitolewe hiyo kadi ya VAT. Mimi sina kiwanda, lakini ukweli ndiyo huo; ili pale tuweze kupata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kwenye ngano pale, mmezungumzia ngano kutoka asilimia 35 kuja asilimia 10. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo imegusa kila sekta na kila kona ya nchi yetu. Vile vile namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake kwa kuwezesha vijana zaidi ya 1,000 kupata ajira katika Kiwanda cha Nguo cha Morogoro wakiwepo vijana wa Wilaya yangu. Nawashukuru kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo nitaanza na pombe ya viroba. Najua wengi watashangaa, watasema huyu jamaa Muislam; na najua wale watu wanaopenda kuweka maneno kwenye midomo ya watu wengine, wataweka maneno mengi. Siyo kwamba naunga mkono watu wanywe viroba, napinga na viroba visiwepo kwa sababu vinaathiri hali za watu na hata sasa hivi watu wananenepa baada ya viroba kuacha kuwepo mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashauri kitu kimoja; kwa sababu katika bajeti ya mwaka 2016 wakati tunaweka kodi katika vinywaji na katika bajeti yetu na mapato yetu, hata viroba navyo tulivihesabu na vilikuwepo kihalali.
Mheshimiwa Spika, ni kweli pombe hii inadhuru watu, lakini naomba au nashauri kwa wakati mwingine utaratibu utakaotumika kuzuia vitu kama hivi, basi uchukuliwe kwa umakini sana. Waanze kuzuia kwenye production ili huku zinakouzwa, basi ziishe.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mfanyabiashara sikuingia hapa kama nachunga ng’ombe wala kama mkulima au nani, nimeingia kama mfanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni lazima nizungumze habari ya biashara na kama sisi Wabunge wa vyama vyote hapa tusipozungumza wenyewe basi tujue biashara kwenye nchi hii itakufa. Kwa sababu mtu amenunua mali ya shilingi bilioni moja, shilingi milioni 300 halafu amenunua kisheria, ana risiti zote za TRA na amelipa kodi leo unakuja unamwambia kuanzia sasa hivi hii mali ni haramu. Tayari ameshaingia kwenye matatizo amekopa katika mabenki huko na biashara yake imeshafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba mnielewe vizuri, siungi mkono unywaji wa viroba lakini utaratibu uliotumika naomba usirudiwe tena. Kwa sababu leo anaweza akaja mtu hapa akasema tena kitu kingine kikaleta madhara. Kwa hiyo, tuangalie utaratibu mzuri wa kufanya mambo haya. Hilo la
kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, wewe mwenyewe Spika ni shahidi kwa sababu kati ya watu wanaoathirika na jambo hili ni mimi na wewe. Wakulima wetu ambao wanalima katika upande wa Wilaya ya Kiteto wamekuwa wananyanyaswa kupita kiasi hasa na vyombo vya dola ambavyo viko pale wilayani na mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mbuga ya Murtangos wanasema ile ni hifadhi. Hawawazuii watu kulima wakati wanakwenda kulima, wanangoja mahindi yameshafika labda mwezi mmoja, wanakuja ng’ombe wanachungia mule wakienda wale wakulima kushtaki na wao wanawekwa
ndani. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza wapo watu wa Pandambili ambayo ni wilaya yako na wapo watu wa Gairo wapo ndani mpaka sasa hivi na wale Wamasai ambao wanachungia kwenye ile mbuga wapo nje, hao jamii ya kifugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama mnataka kuzuia, hatukatai kuzuia, kwa nini msizuie wakati wanalima mnakuja kuzuia wakati mahindi yameshakuwa makubwa? Kama hiyo ni hifadhi, hifadhi gani ambayo ng’ombe wanachungwa lakini wakulima hawaruhusiwi, hiyo ni hifadhi ya aina gani?
Naomba viongozi wetu na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu ambaye ni mtiifu na msikivu akienda pale asisikilize masuala ya wilayani wala mkoani, aangalie tu yeye mwenyewe atume watu wake wachunguze atapata jibu ambalo lipo sahihi. Akitaka na majina nitampa ya wakulima wetu ambapo zaidi ya heka 3,000 watu wamechungia na wako nje halafu tunasema zaidi ya asilimia 80 ya wananchi ni wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hizi pesa, watu wanasema tu, pesa zimepotea, hamko kwenye mzunguko wa kibiashara, ukiujua vizuri mzunguko wa kibiashara pesa imepotea kwa sababu wakulima wa mwaka jana hawajapata mazao. Hawa wakulima wadogowadogo wangeweza kuvuna
mwaka jana kila mtu hapa angefanya biashara na mzunguko wa pesa ungekuwa mkubwa. Tunasema tu aah Magufuli kazuia pesa, Magufuli kafanya nini, Serikali imezuia pesa, wakulima hawakuvuna mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni mfanyabiashara sasa hivi nina zaidi ya miaka 25, najua mwaka wowote mkulima mdogo anayelima heka mbili au tatu akipata mazao atakwenda kwa fundi cherehani atanunua sare, atakwenda kwa huyu atanunua maji, atakwenda kwa huyu atanunua
hiki, ndiyo mzunguko. Yule naye biashara yake ikitoka atapanda basi, ataenda Dar es Salaam, kwa hiyo kila mtu atafanya biashara. Wakulima hawa wasipopata pesa ina maana mzunguko haupo, kila kitu kitakuwa kibaya tu, tutalalamika tu. Hata ukiachiwa hizo pesa za benki, unasema
mkopo hakuna, hata ukiachiwa, security zenyewe unazo? Maana yake mabenki siyo rafiki wa mtu maskini, huo ndio ukweli.
Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine la matrekta. Tunashukuru matrekta 1,860 yale ya SUMA JKT yamekuja na waliwakopesha wananchi kwa kulipa asilimia 30. Hata kwangu Gairo pale nimepata matatizo makubwa sana maana niliambiwa Mbunge weka dhamana, nimeweka
dhamana nyingine badala ya kuandika jina la niliyemkopea limeandikwa jina Ahmed Shabiby ndiyo kakopa. Sawa watu wangu nawajua najua tu yatalipwa lakini wakati SUMA JKT anapewa auze matrekta hajui hata sheria za kuuza, kwanza na yeye mwenyewe akatafuta tena dalali mwingine ndio amuuzie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halafu baada ya hapo haya matrekta hata ukilipa hupewi kadi wala halina namba, kwa hiyo, linatembea tu kama mkokoteni wa ng’ombe. Tafuteni watu wote wenye matrekta haya, waliopewa kadi hawazidi 300. Mkulima akiomba kadi anaambiwa hebu soma engine number, wewe angalia namba yoyote bandika, sasa anabandika namba ipi, atakataje insurance? Kwa hiyo, matrekta yale hayana namba sasa sijui ni utaratibu gani. Halafu leo tena mnakwenda mnakamata, mnafanya kuangalia rangi, lile la bluu wanakimbiza wanakamata
yamejaa pale, hii ni dhuluma? Mkulima anataka umpe kadi yake akumalizie deni humpi, kwa sababu ameshaambiwa na wenzake waliomaliza madeni kwamba hatupati kadi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa matrekta yote ya Manyara, Tabora na Tanzania nzima kwa ujumla yamekamatwa halafu watu tunasifia tunasema hawa wameshindwa kulipa madeni, wameshindwa nini, jamani tusiwaangushe hawa wakulima wetu tuwaombee tena yaje matrekta mengine wakope, tuangalie kosa liko wapi. Naomba Waziri anayehusika aende akachunguze kama SUMA JKT wanazo registration cards za haya matrekta. Hakuna namba, hata insurance atakataje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni maji. Leo maji nimeamua kuzungumzia chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Toka mwaka 2007, Gairo imepewa Sh.6,600,000,000, lakini kilichofanyika wamekwenda kuchimba visima vile vya maji tisa vinatoa maji lakini yale maji hata akinywa ndege anatapika. Haijawahi kutokea. Wamekwenda kupima kwa Mkemia hayafai. Nimewapa ushauri wa kila aina hawajafuata ule ushauri, sasa miaka 10 na mimi Mbunge nakwenda hiki kipindi cha tatu, kwa hiyo, hata wale wananchi wangu kwa sababu wengine hawana uelewa wanasema Mbunge amekula pesa alipewa yeye hela za mradi kafanyia biashara zake sasa maji hakuna. Nimewaambia basi huu
mradi kama mmefeli hizi pesa zilizobakia kuna chanzo cha maji kiko pale karibu tu, kilometa kama 25, nunueni basi mabomba tupate maji ya mserereko lakini imekuwa hadithi. Ukiongea hapa unajibiwa hiki lakini hakuna linalofanyika. Tunakwenda kwenye uchaguzi hiyo miaka ijayo, pesa zipo lakini hazitumiki, ndiyo maana leo nimeamua kumwachia Mheshimiwa Waziri Mkuu alifuatilie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu niende naye Gairo, hapa na Gairo saa moja tu, aende akashuhudie matenki yamejengwa, mitandao ya matenki ipo lakini kuvuta tu maji kupeleka pale sasa hivi mwaka wa kumi hakuna kinachofanyika. Ndiyo na pesa ipo. Kila siku ukiwaambia kaleteni maji ya mserereko hakuna kinachofanyika. Wamekuja watu ambao wameletwa na Wizara ya Maji wamechora ramani wamefanya kila kitu lakini bado hatupati maji. Kila nikiongea na Mheshimiwa Waziri anasema subiri kidogo safari hii tayari wewe maji umepata, sasa maji nimepata yako wapi, haya maji nitasema mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama unavyojua Jimbo la Gairo watu wanalima sana, wanapata sana mazao lakini tatizo maji yake chini ya ardhi yako mbali na hasa pale Gairo Mjini huwezi kupata maji matamu hata ufanye nini, utapata tu haya maji ya chumvi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu safari hii angalau aje Gairo pale kwa sababu yeye kidogo wakimwona na akifahamu maendeleo ya pale ya miaka kumi na asilimia iliyofikiwa mpaka sasa hivi kwa kuona kwa macho itasaidia. Ndiyo maana leo hili suala la maji nimeona naweza nikakosa nafasi kwenye Wizara ya Maji nimuachie Waziri Mkuu ili siku nyingine mwakani kama hakuna maji mimi nitachangia tena Wizara hii hii nimuulize Waziri Mkuu imekuwa vipi. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziiri pamoja na timu yake yote katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili ni kuhusu barabara zangu za jimbo la Gairo ambayo ni ahadi ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ambayo aliitoa tarehe 26 Juni, 2014 tarehe 26. Kwanza ni shukuru, maana usiposhukuru na kidogo basi ujue wewe shukrani huna tu hata ukienda mbinguni huko ni hivyo. Ukiangalia hata kwenye youtube ukiandika tu Magufuli Gairo au Magufuli aitwa jembe Gairo utaona hotuba yake inakuja pale. Alitoa ahadi ya barabara ya kutoka Gairo kwenda Chakwale kwenda Kilindi kwa kiwango cha lami. Alitoa ahadi ya kuweka Mji wa Gairo kilometa 5 za lami Gairo Mjini. Alitoa ahadi ya Gairo - Nongwe kilometa 76 kuchukuliwa au kukasimiwa na TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nasema hivyo kwanza na mpongeza Mheshimiwa Rais, na ninamshukuru Mheshimiwa Rais na ninamshukuru Waziri wa ujenzi kwamba; nikiangalia katika hotuba ya kitabu cha Waziri wa Ujenzi ukurasa wa 339 naiona barabara ya Nongwe imetengewa zaidi ya milioni 900 na kwa bahati nzuri mkandarasi wa kuweka lami Gairo Mjini tayari yupo kazini pale na anaendelea kazi ya kuweka zile kilometa tatu za lami.
Nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri, kwamba katika ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilomita 5 zimebakia kilometa mbili, na wakati Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi anatupa ahadi ya unjezi wa kilometa tano alikuwa anaelewa matatizo yaliyopo pale. Kwa hiyo, tumepewa kilometa tatu lakini tunaomba hizi kilometa mbili zimaliziwe haraka, kwa sababu mwaka huu sijaziona kwenye bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ukiacha hizi kilometa tatu peke yake ni sawa sawa na mtu kumvalisha koti la suti halafu chini umemvalisha kaptula. Kwa hiyo naomba tumalize hizi kilometa mbili. Vilevile nikiangalia ile barabara ya kutoka Gairo kwenda Kilindi kwa ndugu yangu Kigua, ambayo ingesaidia hata watu wanaotoka Iringa kupitia Dodoma, Zambia wapi kwenda bandari ya Tanga kwa sababu pale ni karibu sana kutoka Gairo mpaka Kilindi ni kilometa 100 tu nayo haimo kwenye bajeti. Kwa hiyo na washauri na najua hii Wizara ni sikivu mtaweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha zaidi ambacho nilitaka kukiongea kwa leo ni kuhusu habari ya mashirika ya umma. Watu wengi wamepongeza sana mashirika yote ya umma ambayo yako chini ya Wizara hii ya Ujenzi. Wizara hii ya Ujenzi ni moyo wa nchi, Wizara hii ina taasisi 37, na moja ya hizo Taasisi kubwa nizitaje chache kuna TTCL, Posta, Bandari, ATC, TRA, hizo nikutajie tano ambazo zote ni kubwa kabisa. Nataka niseme kwamba namshukuru Mheshimiwa Rais, nimpongeze pamoja na Mheshimiwa Wazari na Mheshimiwa Naibu Waziri na Makatibu wa Wizara hii wote kwa kupata Bodi ambazo zinaongozwa na watu ambao wana weledi, wajumbe wenye weledi na ma-CEO. Ukichukua taasisi zote nilizozitaja ma-CEO ni vijana na ni wazuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu uko wapi? Haya mashirika ambayo yako kwenye hii Wizara ukiangalia sana ya natakiwa yaendee kibiashara. Shirika la Reli lazima liende kibiashara, TTCL lazima iende kibiashara, ATCL lazima iende kibiashara, Posta lazima iendee kibiashara, bandari lazima iendee kibiashara hata Mheshimiwa Rais wakati ananua ndege alijua kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika hakuna watu wanafiki kama baadhi ya sisi Wabunge. Miaka ya juma tunapiga kelele tunafananishwa na Rwanda. Rwanda wana ndege sisi hata kimoja hichi kibovu bovu, leo ndege zimekuja mnaanza kusema ndege sio kipaumbele cha kwanza. Mimi nasema vyote ni vipaumbele, lakini viongozwe kwa mujibu wa sheria za kibiashara, hicho ndio cha msingi. Kwa mfano, unaunda
Bodi, zina madaktari, zina maprofesa zina wajumbe safi halafu baadaye tena hapo hapo yanatoka maagizo, matamko kutoka huku ya naingilia kwenye ile Bodi. Sasa kuna faida gani ya kuweka Bodi mpya? Acheni watu wafanye kwa kutumia utaalamu wao. Kama mmeweka Bodi basi acheni Bodi pamoja na ma-CEO wao na Menejimenti zifanye kazi yake; lakini kutakuwa na faida gani ya kuweka bodi mpya halafu mnaziingilia ingilia? Hii ni biashara jamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni wapeni mfano mmoja hili shirika letu la TTCL; hili ni shirika ambalo lingekuwa linachangia uchumi wa Taifa. Tuchukue mfano wa shirika la simu la Ethopia, kwa mwaka wanatengeneza dola bilioni 3.3, ukitoa kodi wanabaki na dola bilioni 1.5. Kwenye mfuko wa Serikali wanachangia karibu dola milioni 300, hiyo ni sawa sawa na bilioni zaidi ya 700 za Tanzania. Sasa haya sio tunawategemea TRA lazima tuwe na mashirika ambayo yataingiza hela kwenye Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia uwekezaji wa TTCL, ili ifike Tanzania nzima itachukua zaidi ya miaka, na ikimaliza kufika huko vijijini na sehemu nyingine hawa Vodacom na kampuni zingine kama Tigo, watakuwa tayari wana mitandao mipya. Wakati huko huko Serikali tena ina asilimia 40 kwenye Shirika la Airtel, kama Wabunge hawafahamu. Asilimia 40 ya Airtel ni hela ya Serikali ya Tanzania, lakini toka hizo asilimia 40 ziwekwe kwenye Airtel kila siku Airtel wanapata hasara hawaleti faida hata shilingi moja kwenye Serikali. Sasa kwa nini hizo hisa za kwo 60 zilizobakia tusizinunue ziwe za Serikali (TTCL) halafu tutakuwa tayari tumeshajigawanya, tumeshachukua mitambo ya Airtel tunakuwa tayari tuko Tanzania nzima na tunaingia kwenye compentintion? Kuliko kuacha asilimia 40 wakati ilie asilimia 40 kila siku hawapati faida. Kwa hiyo, hela ya Serikali imekaa tu Airtel. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye shirika la ndege; uwekezaji wa ndege si mchezo. Ukiwa bilionea ukitaka kuwa milionea ingia kwenye biashara ya ndege. Inataka lazima muwe na mtaji na lazima uweke mtaji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ila hilo shirika linatakiwa lipewe hela lijiendeshe, TTCL.

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba hii iliyopo mbele yetu. Leo nilikuwa sitaki kuchangia habari za haya mambo ya Road License lakini imenibidi nichangie kidogo tu ili tuelewane vizuri tu siyo labda kwa kushindana au nini ila kueleweshana tu.

Mheshimiwa Spika, nafikiri kama Waziri wa Fedha angefuata yale mawazo yetu ambayo tulikuwa tunampa siku tano za nyuma basi ina maana kwamba angepandisha Sh.140/= kwenye bei ya mafuta, asingepandisha Sh.40/=. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu Wabunge wengi tuliokuwa tunachangia humu, mimi sikupata nafasi lakini wengi walikuwa wanasema kwamba, Sh.50/= weka kwenye maji, Sh.50/= weka REA na Road License weka kwenye mafuta. Sasa leo kwa busara zake tu akaamua kuweka Sh.40/= tu peke yake ile Sh.100 akaiacha lakini bado na hii nayo tunamgeuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ndugu yangu hapa Mheshimiwa Kamala yeye ni Mwalimu, ameeleza vizuri sana na mimi sasa ni Mwalimu wa huko mtaani nitawaeleza kidogo. Kwa hesabu tu nyepesi, niwape hesabu nyepesi tu, Road License gari lenye CC2500 ilikuwa inalipiwa Sh.200,000/= kwa mwaka. Sasa tuchukue mfano tu mwenye gari hiyo, maana yake tuangalie kwanza hawa watu wa kawaida, kila siku akijaza lita 10 ya mafuta kwa mwezi atajaza lita 300. Akijaza lita 300 ukiweka mara ile Sh.40/= kwa mwezi analipa Sh.12,000/=, ukiweka ile Sh.12,000/= kwa mwaka analipa Sh.144,000/=. Kwa hiyo, hata hiyo Sh.200,000/= bado hajafika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapeni mfano mmoja, tunaposema kwamba usafiri utapanda sijui kilimo kitapanda, Mungu ananisaidia mimi ni mkulima na msafirishaji, lazima ku-declare interest, bei ya EWURA ya mwezi huu tuliomaliza nao ilishusha dizeli kwa Sh.81/= na petroli kwa Sh.30/=, kwa mwezi huu wa Tano tuliomaliza. Mwezi huu bei iliyotangazwa juzi, dizeli imepanda Sh.43/= na petroli imepanda Sh.25/=. Kwa hiyo, hata ukiweka na hii Sh.40/= hatujafika bei ya mwezi wa Nne na bado hizo nauli zipo pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mtu jana alizungumza, nataka nizungumze kweli, bei ya mabasi iliyotolewa na SUMATRA imetolewa miaka mitano iliyopita lakini mpaka leo hakuna basi limefikisha ile bei waliyopangiwa na SUMATRA, hakuna. Dar es Salaam – Arusha ni Sh.33,000/= lakini watu wanaenda kwa Sh.25,000/=; Dodoma – Dar es Salaam ni Sh.24,000/= watu wanaenda kwa Sh.17,000/= mpaka Sh.20,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme hii kodi, hata Wabunge wengine wapo upande wa CCM na wengine wapo upande mwingine, walikuwa wanasema iingie kwenye maji, tumetoa Road License na gharama za Road License zilikuwemo kwa wasafirishaji hata msingepandisha mafuta walikuwa wanalipa Road License, kwa hiyo gharama ilikuwa ipo pale pale tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, gharama hii ya Road License ibaki kama Road License kwenye mipango yake ya Serikali. Kama kuna mpango mwingine wa kupandisha maji basi tuweke tena Sh.50/= nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusiingize hii huko kwamba tuitoe kwenye mipango yake ya Serikali, sijui ifanye hiki na kile kwa sababu hata usipopandisha mafuta, ukiacha Road License si ni pesa msafirishaji ataingiza tu ile.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze tu ili watu walielewe hili suala vizuri, hii ni nchi yetu. Kule China watu walikuwa wanavaa chunlai siyo kwamba walikuwa wanapenda, leo wanavaa bluu watu wote kesho kijani, walikuwa wanafunga mikanda ili wafike mahali wanapohitaji. Kwa hiyo, twendeni tufunge mikanda tufike mahali tunapotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine huyu Ndugu yangu Mheshimiwa Mpango leo nampa shikamoo. Mara ya kwanza humu tulikuwa tunakujadilijadili, tukaona huyu jamaa mpole sana kwa sauti lakini mbona kama haelewielewi, hataki ushauri.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi kwenye Bunge hili tumegundua kwamba katika watu wanaopenda ushauri Mheshimiwa Mpango naye mmojawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwa nini nimempa shikamoo. Ukiangalia taarifa ukurasa wa 54…

TAARIFA....

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Taarifa yake naipokea kwa sababu ni rafiki yangu huyu najua ananichangamsha tu, hakuna hata matatizo lakini najua nilishamwambia kwamba ni mkulima na mfugaji, ni rafiki yangu Waitara hakuna matatizo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nilikuwa nasema Mheshimiwa Mpango shikamoo, amerudi pale pale kwenye vile viwanda vya Mwalimu Nyerere. Hii ni kwa sababu ukiangalia ukurasa wa 54, kipengele cha tatu, amezungumzia kupunguza ushuru wa vile viwanda vitakavyoletwa kwa ajili ya kuunganisha matrekta, boti na magari. Ametoa ushuru huu wa Corporate Income Tax kutoka asilimia 30 mpaka 10. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nataka nitoe ushauri, mpaka leo hakuna mtu aliyefikia rekodi ya mzee wetu Mwalimu Nyerere. Wakati ameanzisha kile Kiwanda cha TAMCO pale Kibaha cha kuunganisha magari ya Scania, pamoja na kuwaambia wawekezaji waje lakini aliwapa masharti ya kununua bidhaa zinazotengenezwa Tanzania ili kuunganisha yale magari.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, rejeta zote zilizokuwa zinatumika kwenye magari yote yaliyokuwa yanaunganishwa Tanzania zilikuwa zinatoka kwenye Kiwanda cha Serikali kinaitwa Afro Cooling, betri zote zilikuwa zinatoka kwenye Kiwanda cha Serikali kinaitwa YUWASA, wiring zote zilizokuwa zinafanyika kwenye magari zilikuwa zinatoka East African Cable, matairi yote yalikuwa yanatoka General Tyre, spring zote zilikuwa zinatoka Tasia Spring na muffler zote zilikuwa zinatoka Tanzania kwenye kiwanda cha Serikali. Sasa hapo ndiyo unaongeza ajira kwa sababu bila kufufua viwanda kama General Tyre, Afro Cooling na viwanda vyote nilivyovitaja na vingine viko vingi tu bado kuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ulikuwa ukiangalia ile gari ilikuwa inatengenezwa na Watanzania kwa asilimia zaidi ya 18. Kwa hiyo, ile gari ili ifanyiwe assemble hapa hivi viwanda vingine vyote vilikuwa vinafanya kazi na vinatoa ajira nyingi sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, naomba kwenye huu ukurasa wa 54 hapa basi aweke hayo masharti ya kwamba mwekezaji yeyote atakayekuja kuunganisha magari hapa Tanzania basi lazima atumie bidhaa za Tanzania. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ajitahidi juu chini ahakikishe hivi viwanda vinafufuka kama General Tyre, Afro Cooling… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo namwomba Mheshiiwa Waziri afufue hivi viwanda ili hii dhana yake iende vizuri.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, nianze kumpongeza Mheshimiwa Mawaziri wote wawili pamoja na Naibu Mawaziri wao na Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kujikita kwenye Jimbo langu na hasa kwenye Kituo cha Afya cha Gairo kwa sababu Gairo ni Wilaya lakini bado haina hospitali ya Wilaya. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri baada ya kufika Gairo na kuona kwamba kile kituo cha afya kina umuhimu sana na kiko katikati ya barabara ya Morogoro Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile kinapokea majeruhi wengi sana na wagonjwa wengi kutoka Wilaya ya Kongwa ambayo imepakana nayo, Wilaya ya Kilindi pamoja na Wilaya ya Kiteto. Kituo kile kimekuwa ndiyo sehemu yao ya hospitali yao ya rufaa pamoja na kuwa ni kituo cha afya. Namshukuru pia kwa kutupa pesa milioni 400 kwa ajili ya kujenga majengo ya operesheni na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja cha ajabu sijui huku TAMISEMI kwa hawa Wakurugenzi wa hizi Idara nini wanafikiria, nini wanafanya na wanaangalia kwa vigezo gani kugawa watumishi kwenye wilaya, bado sipati jibu, leo nimeheshimu tu, lakini siku nyingine kwa kweli hatutoelewana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mheshimiwa Waziri anajitahidi, lakini Wilaya ya Gairo kituo hicho cha afya na Wilaya nzima wametuletea mwezi wa Novemba mwaka jana Wauguzi Wasaidizi watatu, wakati upungufu ni zaidi ya Wauguzi 70. Wametuletea Matabibu wametuambia ni Matabibu baada ya kuwachunguza kumbe ni Matabibu Wasaidizi, tumewarudisha huko watubadilishie mpaka leo hakuna kibali cha kubadilisha ili waajiriwe. Kwa hiyo, ina maana hatukupata mtumishi yoyote kwenye kituo cha afya cha Gairo na Wilaya nzima ya Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mpango wa kufungua vituo vya afya vitano, lakini hatuna Matabibu wala hatuna Wauguzi. Ukija kwa wale Madaktari pale ni sehemu ya barabarani nimesema ile ndiyo ‘Tumbi’ ya Dodoma - Morogoro kwa sababu mtu yoyote akipata matatizo na ukiangalia hata idadi ukisoma ya accident nyingi zinazotokea katika maeneo yale, Madaktari wenyewe operesheni na Madaktari wengine tunahitaji zaidi ya wanne au watano lakini hatujapata hata mmoja. Sasa sielewi ni nini kinachofanyika hapa kwenye hizi Idara zenu za TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija hata watumishi katika Halmashauri ya Gairo; ukienda uhasibu hakuna watumishi wa daraja la pili, halafu leo tukipata hati chafu watatufungia hiyo Halmashauri kama alivyozungumza Waziri Mkuu? Haiwezekani kwa sababu watumishi Wahasibu hawapo! Utumishi kwenyewe hamna kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru dada yangu hapa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametupatia gari la wagonjwa, Wilaya ile haina kabisa magari ya wagonjwa. Bahati mbaya ina Tarafa nyingine kutoka Gairo ni kilometa 100 inaitwa Tarafa ya Nongwe, hii Tarafa milima yake ni kuliko milima ya Lushoto, nako wanahitaji gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo gari lililoletwa na Wizara ya Afya nalo halina Madereva. Halmashauri imeomba kuajiri Madereva watano lakini kutoka Wizara ya Utumishi hakuna kibali mpaka leo. Kwa hiyo sasa mnataka hiyo gari aendeshe Mbunge? Matatizo tupu! Naomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu shule za Msingi wale wengine wenye vyeti feki wameondoka wengi na mwaka huu wanastaafu Walimu 50 na sasa hivi pana upungufu wa Walimu zaidi ya 270. Kwa hiyo, shule za msingi utakuta kuna shule sasa hivi ina Walimu wawili ama Mwalimu mmoja. Sasa ndugu zangu wa TAMISEMI sielewi ni vigezo gani wanavyotumia kutafuta hawa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, wakati tunatoka Wilaya ya Kilosa kugawanya kuwa Wilaya mbili tuliangalia ukubwa wa eneo Wilaya ya Kilosa ilikuwa na Tarafa saba, tukakubaliana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwamba ianzishwe Wilaya ya Gairo kuwa na Tarafa tatu, Tarafa ya Nongwe, Tarafa ya Gairo na Tarafa ya Magole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikatokea baada ya ile Wilaya kuanzishwa uchaguzi wa 2010 ulishafanyika, kwa hiyo Mheshimiwa Rais aliyepita akasema sasa itabidi kwa sababu huku wamechagua Mbunge na huku nako wameshachagua Mbunge kwa hiyo NEC wametuambia baada ya zoezi hili likishapita wakati wa uchaguzi 2015, ile Tarafa ya Magole irudi Wilaya ya Gairo kama ilivyoamuliwa hapo mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, 2015 ile Tarafa haijarudishwa, kwa hiyo utashangaa wa pale Gairo ukitoka kilometa sita unakuta tena kijiji kipo Wilaya ya Kilosa, Berega yote, Kiegeya yote hata pale wanakouza viazi kwa mbele pako Wilaya ya Kilosa, kwa hiyo wanawatesa wananchi bila sababu. Wale Wapinzani sasa wameingia na majungu wanasema kwamba Mbunge wa Gairo hawapendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lingine liko kwenye Utumishi; hili lazima tulizungumze wazi mimi ni Mbunge wa CCM na nimepitia kwenye ngazi nyingi nimekuwa Kamanda, nimekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, nimekuwa Mbunge miaka mingi sana kwenye hiki Chama. Sasa hivi kuna watu kwenye ofisi za Serikali huku kwenye utumishi wanatafuta mbinu ya kujifanya watu wanafanya kazi zao lakini kuichafua Chama cha Mapinduzi na kuchafua Viongozi wa Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kijana yule Abdul Nondo ana umaarufu gani mpaka wamwite kwa kutumia vyombo vya habari, hawawezi kufanya investigation, wafanye investigation, wamwandikie barua anaitwa, lakini hapo ni kutaka kuichafua tu wanataka kuichafua Serikali ya CCM kwamba aambiwe yule kuna mbinu ya aina yoyote anatafutiwa, ana umaarufu gani mpaka yule mtu wa Immigration aende akakae anaanza anataka cheti cha bibi, cheti cha mjomba, cheti cha babu mpaka aandike kwenye vyombo vya habari? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapa watu umaarufu wakati kesi iko Mahakamani mtu anapatikana, kuna watu wengine watatumia ile kusema mmeona sasa, Serikali ya CCM ikimtaka mtu inaanza kumwambia siyo raia, wakati siyo kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwenye utumishi waambieni watu wenu, televisheni kila mtu anaipenda, lakini uwe na mambo ya maana ndiyo uende ukajiangalie kwenye televisheni. Sasa itakuwa basi kila mtu akitaka kitu anatoa taarifa kwenye televisheni au kwenye mitandao siyo sawa! Wanachafua Serikali yetu wakati hakuna mtu mwenye habari na mtu mdogo kama yule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye utumishi tuangalie haya masuala, mnayaona ya kawaida lakini kuwapa watu maneno na mambo mengine ya kuongea au watu kufikiria au kuwasababisha watu wajue kwamba Serikali inamtafuta yule kijana, wakati Serikali nina uhakika kabisa haina mpango na mtu mdogo kama yule kwa sababu hana madhara yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo yangu, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mmoja wa wachangiaji katika Wizara yetu hii nyeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisimama mara nyingi sana kuchangia Wizara hii Wizara ya Maji. Pale Gairo pana mradi wa maji sasa hivi una muda mrefu, lakini kila nikisimama au kila Wizara ikileta bajeti ule mradi uko asilimia tu 84 na mwaka unaofuata unashuka unakuwa asilimia 75. Kwa hiyo, sasa sielewi mwaka mwingine unapanda bado haujaisha mwaka mwingine unashuka. Kwa leo sitaongelea sana huu mradi ila nitatoa ushauri kwa sababu nimeona kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 3 kwamba sasa hivi anatafutwa mzabuni wa kuweza ku-supply pump pamoja na mashine ya kuchuja chumvi ambayo ina uwezo wa kuchuja zaidi ya lita nafikiri kulingana na matenki zaidi ya mita milioni moja au zaidi kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa mpango huo nimeona kwenye gazeti la juzi hapa la terehe tatu, naomba iwe kweli kwa sababu huu mradi kwanza utakuwa ni mradi wa mfano kwa sehemu zingine za nchi yetu, kukuta maji mengi chini ya ardhi ni suala lingine na
kukuta maji salama ni suala lingine, unaweza ukachimba maji lakini ukakuta yana chumvi na ukienda kupima hayafai kwa matumizi ya binadamu. Kwa hiyo, siyo kila sehemu yenye maji mengi kwamba ni baraka unaweza ukakuta maji lakini yana chumvi ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule wa Gairo itakuwa ni mwanga kwa Wziara na sehemu zingine zote ambazo zina maji chini lakini hayafai kwa matumizi ya binadamu, nafiki ni mradi wa kwanza Tanzania ambao maji yatachunjwa sasa na kuwa maji salama na wananchi kutumia, naomba utekelezaji. Kwa sababu ule mradi ni wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na Wabunge wengine waliotangulia, siwezi nikasema Wizara ya Fedha haijaleta pesa haijaleta nini, tayari ule mradi wa shilingi 6,666,000,000 mkandarasi amechukua zaidi ya asilimia 80 ya pesa ameshachukua tayari, lakini haujakamilia sasa mimi siwezi kulaumu, siwezi kusema hapa pesa iko wapi haiwezekani! Hata huyo Waziri wa Fedha kama amezuia pesa bora azuie tu, kama asilimia 80 imechukuliwa na bado utekelezaji wake hata hauna dalili sasa hizo pesa zinakwenda wapi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wangu hapa amejitahidi sana pale Gairo na nushukuru tumemuomba aje pale Gairo na anakuja na nafikiri atakuja kwa ajili ya miradi ile ya maji kuja kuangalia. Atakuja Mvomero, atakwenda Gairo anaangalia miradi kwa sababu pesa tayari Kilosa, Mvomero, Turiani, Gairo, lakini kasi iko wapi ndugu zangu? Ingekuwa pesa haijatoka mngesema kweli hapa pesa haijatoka kuna matatizo, labda Wizara fulani haijaleta pesa hizo pesa zipo, maji yako wapi, tumekaa sasa hivi pale unajua kuna watu wengine duniani hawapo, mbinguni hawapo hawaelewi wanajua labda Mbunge huwa anapewa hela anaweka mfukoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu kabisa wanasimama pale wanakuambia Mbunge huyu wa Gairo amekula pesa zetu za maji, wanajua labda Wabunge tunapewa pesa kwa hiyo sisi ndiyo tunatoa toa pesa kwenye miradi. Wabunge hatupewi pesa, pesa ziko kwenu na ninyi ndiyo mnahudumia hizo au kama mmeshindwa mtu ukweli basi fedha zetu tuwe na account zetu za Mfuko wa Jimbo halafu tuweke watu muangalie nchi nzima kama haina maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa maji wa mradi huu maji hakuna, lakini ukiangalia hapa kwenye bajeti utaona usimamizi tu wa maji Gairo, Mvomero, Turiani na Kilosa ni shilingi milioni 490, usimamizi tu! Sasa si ulaji huu?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu namuomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Katibu Mkuu wamekuja pale, huu mradi wa Gairo utakuwa na gharama kubwa sana kwa wananchi. Nawakumbusha kwamba mradi huu wakati wa Waziri Maghembe alishasema ukiwa na gharama kubwa Serikali/Wizara italipia yenyewe gharama zile za pale siyo wananchi maana tuwekane sawa kabisa, muangalie kwenye Hansard. Ukiwa na gharama Wizara kama alivyosema Waziri aliyetangulia kwamba ninyi ndiyo mtakaowalipia gharama hizo wananchi wa Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewapa plan nyingi, tumewapeleka kwenye vyanzo vya Mserereko lakini kila watalaam wenu wakifika unasikia ooh! maji haya hayatoshi. Hivi maji haya ndiyo Mto Mkondoa yanasumbua watu kila siku yanaleta mafuriko pale Kilosa halafu unasema hayatoshi kusambaza Gairo? Tumewapeleka kwenye chanzo cha Mto Mkondoa unapotoka Gairo kila siku mafuriko pale Kilosa, Mto Ludewa, Mto Mvumi yote inatoka Gairo pale juu, kwa hiyo hata macho na sisi hatuoni kwa macho? siyo watalaam wa maji lakini hata kwa macho hatuoni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tumeomba pesa mtupe kile chanzo tunachotumia sasa hivi cha mserereko kina bomba za nchi tatu, tupeni bomba za plastic tu ambazo hazifiki hata shilingi bilioni moja tutoe pale kwenye chanzo cha Mserereko tulete pale. Mwaka jana mmetoa milioni 312 hazijatumika popote. Mnaweka tu hapa, litatumika bomba la chuma yaani mnapiga plan za ulaji ulaji, pesa ipo lakini plan za ulaji tu! Mwaka huu tena ukiangalia kuna shilingi milioni 300 eti hizi kufunga mita Mijini, kwanini msikusanye ile shilingi milioni 300 ya mwaka jana haijatumika na hii shilingi milioni 300 ongezeni hapo.

Waheshimiwa Wabunge, hatufuatilii tu mkiangalia, lakini kwenye Wilaya pesa za maji zinakuja nyingi, miradi ya utapeli mingi. Mimi mtu akiniambia hela haziji labda Wabunge wenyewe tu hatufuatilii tu, lakini ukifuatilia kwa makini, mimi pale Gairo naangalia pale na kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Saddiq na sehemu nyingine nyingi tu hata Mheshimiwa Mabula nimeongea nao hapa, kuna miradi mingi! Hata ya kwenye Halmashauri mnatoa hela, lakini Wizara hamsimamii siyo tuende mpaka TAMISEMI ile si mambo ya maji? Wizara ninyi mmetoa labda Gairo maji, kwa mfano pale Chakwale na Kibedi kuna mradi wa karibia shilingi milioni 500 lakini maji mpaka leo hayatoki na wakandarasi wameshakabidhi. Ukifungua yale maji mabomba yote yanapasuka, kwa hiyo mnataka sisi kama anavyokuja Mheshimiwa Magufuli hata haya mambo ya maji tukamlalamikie Rais? Sasa hawa wataalam wamewekwa kwa ajili ya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani, halafu mnajua kabisa Mji kama Gairo ni mji mkavu kama Dodoma, kwenye kutenga pesa mnatufananisha sisi na sehemu ambayo watu wakichimba hata na mkono kama panya hapa wanapata maji, huu utalaam unatoka wapi? Muwe mnaangalia, lazima muwe na usawa kwamba sehemu zingine maji hayapatikani kirahisi. Kwa hiyo Ndugu zangu tunaombeni sana... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Leo nitachangia kiasi tu. Kwanza nianze na ile shangwe ya akinamama kwa kuondolewa kodi ya taulo za kike. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kutoa kodi hii, lakini bado tuna wasiwasi na sio wasiwasi kwamba bei itakuwa ipo pale pale. Kwa sababu ametoa kodi kwa nia nzuri, lakini cha msingi lazima aangalie aweke na bei, kwamba itauzwa bei gani? kwa sababu ukitoa kodi yule mwenye duka hawezi akajua hiyo kwamba imetolewa kodi wala haitofahamika na hivyo yeye atauza bei ile ile; kwa hiyo manufaa kwa wananchi hayatakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba aangalie namna ya kurekebisha, kwamba waweke na kiwango cha bei, kwamba hii itauzwa kiasi fulani ili wale wenye maduka wasiweze kujipatia faida hii ya ushuru ambao umetolewa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwenye Viwanda, kwa kweli ameonesha nia nzuri sana ya kuweza kunyanyua viwanda vya nchi hii; na wale watu ambao kweli wana nia ya kuanzisha viwanda huu ndio wakati wao. Nasema hivi kwa sababu bajeti hii imeonesha kabisa na ipo wazi kabisa, kwamba kama unaweza kuanzisha viwanda anzisha na Serikali inakuunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano kwenye mafuta, ameongeza ushuru kwenye crude oil na viwanda vya Tanzania vya ndani ya nchi kama mawese ametoa ushuru. Ila tunamshauri, hata kwenye mashudu nayo hajayaekezea vizuri, nayo atoe ushuru wake ule wa ongezeko la thamani (VAT).

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huu nataka niwaambie wafanyabiashara, wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano ndio wakati wa kufanya biashara. Kwa sababu bado watu wanadanganyana danganyana hali mbaya, TRA inafilisi, sijui nini, huku na benki nazo ndio zimeshusha Interest. Sasa huu ndio wakati wa kukopa, hela zimejaa, wakati watu wanaogopa sasa ndio wakati watu kukopa na kufanya biashara, ukichelewa hapa ndio biashara imekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha msingi tu, nataka nitoe ushauri na nataka niseme ukweli; kwamba hapa inaonekana kabisa Mawaziri wetu wanafanya kazi lakini ushirikiano haupo, ni zero. Kwa sababu unataka kuanzisha viwanda vya mafuta lakini ushirikiano wa Waziri wa Viwanda na Waziri wa Kilimo uko wapi? Maana unapiga kelele uanzishe kiwanda cha mafuta ya alizeti wakati kwa wakulima hamna lolote wala hakuna support ya aina yoyote ili wazalishe alizeti kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaanzisha kiwanda, kwa mfano kama hapa Dodoma ukiweka kiwanda inatakiwa kiwe kimoja tu na hata hivyo hakitoshi kwa sababu alizeti yote hii ya Dodoma inakwenda Singida. Kwa hiyo hata ukianzisha kiwanda kingine hawatoweza kupata alizeti za kutosha. Mbegu ya alizeti inayotumika Tanzania inatoa 22 percent ya mafuta wakati South Africa kuna mbegu inatoa 60 percent. Nataka kusema hapa Mawaziri hapa maneno mengi, ushirikiano hakuna, vitendo hakuna; huu ndio ukweli na lazima tuambiane ukweli; tusipoambiana ukweli hapa, tukianza kuogopana, tutasalimiana, tutakunywa chai lakini ukweli ndio huo; wengine ndio maana sasa wanafikia hamna sifa wanaenda kupima samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafanya tu, ukiangalia ile video inakuangalia hamna kitu. Nataka nimtafute Mheshimiwa Rais kwa wakati wangu, ntamwambia mzee hawakusaidii hawa pangua tena, si dhambi kupangua pangua Mawaziri mara nne, mara tano. Waangalie, maana Mawaziri ukiangalia kwenye nchi hii wanaofanya kazi kwa moyo kabisa hawazidi watano. Wengine nao wamekuwa walalamikaji kama sisi Wabunge, tukikutana humu, aaa’ nchi hii’, mimi naogopa’, yaani hawahawa ndio wanaichafua, halafu mnapiga kelele; hawa ndio wanaomchafua Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bora hata upate adui mpinzani wa chama kuliko mpinzani wa ndani ya Serikali, mbaya zaidi kwa sababu humjui. Kwa hiyo, naomba Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Mpango ana shida sana, ana shida sana kutokana na Mawaziri wengine kutokupa support, huo ndio ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nilisikia kina tajwatajwa hapa, mimi nafanya biashara, kwa hiyo nitakiongelea kila siku kama nitaona kinaenda tofauti. Kuna Mbunge mmoja hapa nilikaa naye hataki yeye TIPER itumike, anataka mafuta yakija yaingie moja kwa moja kwenye madepo ya kampuni binafsi, hicho kitu hakiwezekani. TIPER imejengwa tangu enzi ya Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kudhibiti kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mfumo unaotumika sasa hivi ndio mfumo sahihi, wakati ule hizi kampuni nyingi hazikuwepo. Ili Serikali ijue mapato yake lazima mafuta yote yaende sehemu moja, yakitoka kwenye meli moja kwa moja yaende TIPER. Wakati huo ndivyo ilivyokuwa, hizi kampuni nyingine zote; Oryx, Gapco, zote hazikuwepo hizi. Puma zilikuwa hazipo, Oilcom, nani, hawakuwepo hawa. Kwa hiyo wakati ule yakienda TIPER ndio yanaenda Esso,Agip na Shell. Sasa hivi anakuja mtu anasema hiyo italeta leakage, sijui na nini. Yakifika pale TIPER, wewe kama una lita milioni tano utasubiri Milioni tano zako utapata zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie kwa nini wanafanya hivi? Wanafanya hivi kwa sababu kampuni chache hizi zinapanga hata bei, kwamba hawa sasa tuwagonge hivi. Sasa hivi vikampuni vya Watanzania vidogo vidogo hivi ndivyo vinavyoshusha, vinasababisha na wao washuke. Kwa hiyo nia yao ni kuuza kampuni ndogo ndogo ili wabaki wao; na kila mtu akiweka mafuta kwao wanachukua karibu kwa metric tons wanachukua dola ishirini. Kwa hiyo wanajua yakienda kule wao watakosa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na wakuu wote wanaoongoza taasisi kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu mimi nianze na barabara ya Gairo – Iyogwe ambayo inakwenda mpaka Mkoa wa Tanga kwenye Wilaya ya Kilindi pale kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kigua. Nafikiri hii barabara Mheshimiwa Waziri amefika muda si mrefu kama miezi miwili iliyopita na Mheshimiwa Naibu Waziri naye amefika kwenye barabara hii kama miezi mitatu iliyopita na kwa bahati nzuri wakati unafika Mheshimiwa Waziri ulishuhudia pale magari yakiwa yamekwama watu hata kwa miguu wanashindwa kupita, ulijionea kwa macho. Kwa bahati nzuri ukaongea na Eng. Mfugale ukaahidi kwamba patakuwa na madaraja ya temporary angalau barabara hii ipitike lakini katika kitabu changu cha bajeti hapa sijaona matengenezo ya barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikumbukwe kwamba iko katika ahadi ya Rais ya kuwekwa lami kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga kupitia Wilaya ya Gairo na Wilaya ya Kilindi na ni barabara muhimu sana na wote mnaifahamu. Hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi pale Gairo tarehe 26 Juni, 2014 aliitaja sana barabara hii, mpaka leo iko Youtube humu bado sijajua ni kwa nini haipo lakini nafikiri ataangalia namna ya kufanya ili iweze kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ile barabara ya Gairo Mjini ambayo toka mwaka jana ilipewa shilingi bilioni 1.5, mwaka jana ilitolewa shilingi milioni 500 mkandarasi amejenga madaraja lakini mwaka huu mmetoa hela chache kabisa shilingi milioni 120. Kwa hiyo, nina wasiwasi kama kuna mkandarasi atakayekubali kuanza kutengeneza barabara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ile barabara pale Gairo Mjini haipitiki tena ya kutoka pale njiapanda ya hospitali mpaka Magoeka kwa sababu TARURA tena hawamo na TANROADS nao hawaishughulikii, sasa haipitiki. Kwa hiyo, naomba hii barabara ya Gairo Mjini iweze kupangiwa pesa ya kutosha ili iweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ile barabara ya Gairo – Nongwe. Ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu imepangiwa vihela hela vingi vingi sana vidogo vidogo. Kweli lazima nishukuru, mara nyingi imekuwa inapangiwa pesa lakini hakuna hata mara moja imeshawahi kuwekewa changarawe. Kila mwaka tunaitengeneza na mvua za mwanzo tu imeharibika. Pesa zinazopangwa hata nikiangalia hapa ni nyingi zinatosha hata changarawe lakini haijawahi kuwekewa changarawe hata mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri mliangalie hili la barabara ya Gairo – Nongwe kwa sababu pesa mnazozipangia ni nyingi lakini hakuna sehemu iliyowekewa changarawe. Kwa hiyo, hata manyunyu kidogo haipitiki na ile barabara imekaa kama ya Lushoto, unavyoona milima ya Lushoto au zaidi ya milima ya Lushoto ndiyo inakopita barabara hii ya Gairo – Nongwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia minara ya simu, nilikuwa nataka ndugu zangu Mheshimiwa Waziri na Naibu wako Mheshimiwa Nditiye muangalie sana. Minara ya kijiji cha Masenege na Idibo ipo siku nyingi na ni ahadi ya siku nyingi na hata katika vitabu vyenu kila siku ipo. Mnara katika Kata hii ya Idibo, Makao Makuu ya Kata mpaka leo hauna hata dalili ya kujengwa. Tukiweka minara hii ya Gairo pale Idibo, Masenge na Chogoa katika Kata ya Chogoa tutakuwa tumemaliza kabisa shida katika wilaya ya Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka nikizungumzie ni habari ya bandari. Lazima niseme ukweli au nikiri Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa hivi inafanya vizuri sana, wizi wote uliokuwa pale katika Bandari ya Dar es Salaam sasa hivi haupo. Mmoja ambaye alikuwa hatumii Bandari ya Dar es Salaam ni mimi hapa lakini sasa hivi nina mwaka wa tatu natumia Bandari ya Dar es Salaam na huwa naweka mpaka mitego, naweka vitu loose nione kama vitaibiwa lakini iko vizuri sana. Haina wizi na ina speed ya hali ya juu sana na ndiyo maana mnaona sasa hivi inaleta changamoto ya malori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzuri wa bandari hii sasa hivi kumekuwa na malori ambayo yamepita kiasi kwenye barabara zetu. Tulizungumza sana na mimi bahati nzuri ni mjumbe wa Kamati kwa muda mrefu katika hii Kamati ya Miundombinu kwamba tuanzishe dry port ya pale Vigwaza ili haya malori yote yawe yanaishia pale. Ukifika pale mzigo wote wa bandari uwe unachukuliwa na ile reli ambayo sasa hivi hata haifanyi kazi ya kwenda Tanga na Arusha, mizigo iletwe mpaka pale Vigwaza, malori yote yaishie pale Vigwaza yasiende mjini. Tumelizungumza sana suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba muangalie malori yamezidi, sasa hivi foleni ya Dar es Salaam sio ya kawaida. Pamoja na kuwa tunatengeneza reli ya standard gauge kuja Dodoma lakini suala hili hata tukitengeneza dry port hapa Ihumwa itasaidia tu mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Burundi, Rwanda na Uganda. Hata hivyo, bado ile bandari kavu (dry port) ya pale Vigwaza itasaidia sehemu zote za Malawi, Congo, Zambia na sehemu nyingine na cha zaidi ni kuondoa msongamano ambao upo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa TPA walishatoa mpaka pesa zaidi ya USD 2,000,000 kwa ajili ya kutengeneza kichwa cha treni na tulikiona pale Morogoro kwa ajili ya kufanya kazi kama hizi. Je, kile kichwa cha treni kiko wapi? Kwa sababu ukiangalia dry port za Dar es Salaam zinavyochaji usafiri ule tu wa kutoka pale bandarini kwenda kwenye dry port pale Mandela Road au sehemu nyingine ni pesa nyingi kuliko hata kukodisha hiyo treni kutoka mjini mpaka pale Vigwaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mjitahidi kuhakikisha kwamba ile dry port inaisha. Sisi tulienda kuikagua na ilishaanza kujengwa, tunaomba haraka sana ifanye kazi na malori yote yaishie Vigwaza ili kuondokana na foleni. Maana sasa yanasababisha vifo, mara utasikia kontena limeangukia hiace na limeua watu, mara limefanya nini, tunaombeni sana mtusaidie kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, mimi si Mbunge wa Wilaya ya Mpwapwa, lakini kwa usafiri nafanya biashara na ndiyo nilikoanzia kwenda katika biashara yangu ya mabasi, kwenda Mpwapwa, Dar es Salaam, jamani huyu mzee Mheshimiwa Lubeleje mtamuua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka na miaka analalamikia habari ya barabara ya Mpwapwa kuja Kongwa, kipande kile kidogo cha lami, kila siku mzee mpaka sasa hivi mzee meno yameng’oka bado anaongea lakini hamtaki kumsikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni sana, kwa uwezo wako Mheshimiwa Mfugale, barabara ya Mpwapwa ni barabara muhimu sana, kulinganisha na barabara zingine za wilaya zingine. Tunaomba jamani kwenye bajeti hii nimeangalia na mzee wangu, lakini hatujaiona hii, na imo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020. Lakini haina dalili yoyote mpaka leo. Tunaomba sana hii barabara ya Mpwapwa, nayo iwemo kwenye mpango huo na ninajua Mheshimiwa Waziri ni Engineer na bahati nzuri na wewe Mpwapwa huwa unakwenda mara nyingi, kwa hiyo, nayo mtaishughulikia, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Naunga mkono hoja, asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuwa mwongeaji kwa siku ya leo kwenye hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwanza nataka niseme tu kwamba, humu ndani Wabunge tumeingia kila mtu ana fani yake, wako wakulima, wako wafugaji, wako Walimu, tuko wafanyabiashara, wako Wanasheria. Kwa hiyo, kila mtu anaijua sekta yake vizuri, pamoja na kuwa wapo wengine wanajua kila sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, Wizara ya Viwanda na Biashara, kama inavyoitwa, Waziri wa Wizara hii anachotakiwa ni kuhakikisha kwamba anatengeneza biashara inakwenda vizuri kwenye nchi yetu ya Tanzania, asiwe ni mmoja wa sehemu ya kubomoa biashara kwenye nchi hii. Kwa nini nasema hivyo? Inaonekana kabisa wazi Wizara hii ya Viwanda na Biashara haielewi chochote kuhusu biashara kwenye hii nchi. Kabisa, hili ni suala la wazi, kwenye ukweli lazima tuseme ukweli, na ndiyo maana sasa hivi Rais wetu anapata tabu sana, kila anapokwenda anaelezea mambo, anakuwa yeye ndiye Waziri, yeye ndiye Rais. Kwa kweli, Rais mwishowe atapasuka kichwa, watu aliowaweka hawamsaidii! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwenye ukweli huwa sipindishi maneno, ukweli ni ukweli tu. Hivi, mimi nauliza Wizara ya Biashara, leo hii ukiangalia kodi kila Wizara inaanzisha kodi kuhakikisha kwamba inakomesha biashara au inakomoa biashara, kila Wizara. Leo hii ukienda kwenye Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira, unakuta kuna WCF, hawa wanaambiwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, wao wana chaji zao kibao. Ukienda kuna OSHA, (Usalama wa Mahala pa Kazi), wao wana kodi zao nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano mmoja tu wa hawa OSHA, mimi nafanya biashara zote, ya mafuta nafanya na biashara zingine. Nitolee mfano kwenye biashara ya mafuta, wanachukua kodi kwa mwaka laki tano, OSHA. Mwaka huu wanataka milioni tatu na laki tano, kwenye kituo cha kijijini. Kituo cha mjini mpaka milioni sita, kwa mwaka, ada. Sasa imekuwa kila mtu anakusanya fedha na anaona sifa, kwamba akimkomesha, akimfungia mfanyabiashara, yeye anaona sifa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niulize, hapo hapo kuna WCF, wako hivyo hivyo. Ukija Halmashauri kuna service levy, anachukua kwenye mauzo, siyo kwenye faida, kwenye mauzo, 0.3%. Sasa ukiangalia kwenye viduka vidogo, nendeni hapa Dodoma tu, viduka vyote vidogovidogo hivi, mtu anaanzisha kiduka chenyewe kina thamani ya milioni tatu, nne, anapigwa mpaka laki tatu, laki nne, hiyo service levy, halafu sasa Waziri wa Viwanda na Biashara yupo. Sasa yeye biashara yake ni ipi, ni kuua biashara au kukuza biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ukweli, nini biashara ambayo anaitetea, maana yake anatakiwa atetee wafanyabiashara wawe wengi, aingilie kila sehemu ambapo anaona wafanyabishara wanaonewa. Ndiyo maana ya biashara, lakini sasa kila mtu amekuwa sasa mchukua kodi, ukija vipimo, anakwenda dukani mtu wa vipimo, ameshapima ule mzani wa dukani, kagonga na label yake, kila kitu, kwenye duka dogodogo tu linauza mchele na nini, kesho anakuja tena, anasema mbona huu mzani wako unapunja, wakati yeye ndiye kagonga ule muhuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijue, ndugu yangu, Mheshimiwa Kakunda, maana ya kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara maana yake lazima ahakikishe kwamba anakuza biashara, si kuua biashara. Kwa hiyo, inatakiwa kila sehemu ambako mfanyabiashara anaonewa, yeye aingilie, kutetea, lakini wamejielekeza sana kwenye viwanda, viwanda, viwanda, sawa, kuna kiwanda cha General Tyre, kilikuwa namba moja katika East and Central Africa kwa ajili ya kutengeneza matairi bora. Wote hakuna mtu ambaye hajapenda tyre la General Tyre, mpaka leo hiki kiwanda kipya hakifufuki! Kiwanda cha Serikali, leo hii tunashindwa na firestone ya Kenya, inaingiza mpato makubwa sana kwenye Serikali ya Kenya, lakini sisi General Tyre, tumeingia tu tunapiga siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mbunge wa kushangilia, kwenye ukweli nitasema ukweli kutetea maslahi ya nchi yangu. General tyre ni muhimu, mimi siwezi kukaa hapa nasema tu haya tu Mheshimiwa Waziri, umeanzisha kiwanda fulani, umeanzisha kiwanda fulani wakati viwanda havipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Yuasa, Yuasa mpaka Uingereza walikuwa wananunua betri za Yuasa, kiwanda cha Serikali, kimebinafsishwa, mpaka leo, wameangalia kinafanya kazi gani! Kuna viwanda vingapi vilibinafsishwa nchi hii, vinafanya kazi gani, watu wamevikalia tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vimekaliwa tu, kwa hiyo, naomba…

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze ndugu yangu, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, asimamie Wizara yake ya Viwanda na Biashara na hasa upande wa biashara, ahakikishe kwamba biashara anaisimamia katika Wizara zote….

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa muhimu.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Sasa wewe naona, ungekaa kwanza kidogo, unanichanganya.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani, taarifa!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby naomba uendelee.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante. Kwa hiyo, ninachoomba, kwamba hatua zichukuliwe, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara aangalie biashara, kila Wizara sasa hivi, wanasema TRA tu, TRA kweli inachukua kodi yake, lakini kuna kodi zingine kubwa kuliko za TRA, tozo zimekuwa nyingi sana sana kuliko hata hizo za TRA. Kwa hiyo, naomba sana waangalie sana na Waziri afanye vikao na wadau ili apate hayo matatizo, siyo kila siku tunamwona tu naangalia tiles, anaangalia mbolea, ajaribu kukaa na wadau wamwambie, wampe changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji. Kwanza niunge hoja mkono na niishukuru Wizara hii na niwashukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na wote wanaohusika kwenye Wizara hii. Labda na mimi sana sana ni kutoa ushauri na ushauri wangu utajikita katika sehemu za biashara hasa katika wafanyabiashara wa kati na wa chini na hii katika ushauri tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nitaanza na mashine za EFD kwa sababu tupo kwenye Wizara hii ya Bajeti na Fedha. Hizi mashine za EFD lazima zitafutiwe mikakati katika hawa wafanyabiashara wadogo na hata wale wakubwa ambao wanatumia mashine za EFD. Mashine za EFD sasa zimekuwa kero sasa sijafahamu ni makampuni yaliyopewa hii tender za ku-supply kwa sababu utakuta mtu ana duka dogo lakini ile mashine kila siku ni mbovu na sasa imekuwa ni mataji kwa wale watu wenye mashine, utakuta sasa unatakiwa ubadilishe mashine leta hela nyingine, uiboreshe lete pesa nyingine. Sasa hii imekuwa tatizo kwa wafanyabiashara kwa hiyo zingaliwe upya. Hawa-supply au model ya hizi mashine zinazotumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ni kwenye biashara ya transportation na hasa malori, mimi sina malori. Lakini nafikiri uchunguzi haujafanyika kwa kina kwamba sasa hivi tunazidi kupoteza Watanzania wote ambao wanafanyabishara ya transportation ya malori. Mheshimiwa Rais pamoja na sisi Wabunge tulijitahidi sana wakati ule wa VAT na ile single customer ili bandari yetu ifanye kazi, lakini sasa hivi bandari yetu inafanya vizuri sana, custom pale wanafanya vizuri sana, lakini transportation yote wanafaidika watu wa nje Burundi, Zambia na Rwanda.

Mheshimiwa Spika, watu hawalifahamu lakini sasa hivi magari yote ya Watanzania yanasajiliwa Zambia, Rwanda Burundi na Uganda. Ukitaka kufanya uchunguzi huo kaa barabarani zikipita gari za transit nne; tatu au mbili zina namba ya Rwanda, Burundi au Uganda au Zambia na kwa ushahidi zipo gari zinakuja mpya gari 100/gari 50 zinaenda Zambia zinasajiliwa lakini za Watanzania zinakuwa namba ya kule, kwa hiyo, kodi yote inalipiwa nchi za nje. Na ukitaka kujua kwa akili nyepesi ukiangalia gari za Rwanda, Rwanda wanatumia left hand drive utaona gari ina right hand drive unajua hii gari ya Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo gari zote za transit sasa hivi zinahamia nchi jirani, tatizo ni nini? Lazima hapa tujiulize hapa kuna shida gani. Nilikuwa naomba watu wa TRA hasa ndugu yangu aliyepewa ukamishna sasa hivi kwa sababu najua ni msikivu, ajaribu kukaa na hawa wafanyabiashara angalie kuna shida gani hadi watu sasa wanahama kupeleka kodi kwenye nchi zingine na nilikuwa nashauri sehemu kama hii ni lazima waweke limit kwa mfano kama income tax, najua ukiweka kwenye mambo ya transportation iwe mabasi iwe malori kwamba kodi yetu tukipiga mahesabu kwa jumla ya transportation zote zilizopo Tanzania idadi ya magari labda tunapata kiasi fulani, lakini tuwekea limit kila gari iwe inalipa kiasi hiki najua kabisa mtapata zaidi ya mara kumi ya kodi ya sasa hivi. Kwa sababu wafanyabiashara watanzania ukitaka wafanye hesabu saa nyingine hata tunalaumu TRA, lakini wafanya mahesabu wenyewe wa Tanzania nao ni fake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaweza ukawa mfanyabiashara unafanyiwa mahesabu unampekea consultant wa mahesabu anakufanyia mahesabu anaonesha unadaiwa wewe sasa TRA atafanya nini? Wakati huo unayemuamini kwenye mahesabu yeye ndio aliyekufanyia mahesabu anaonesha unadaiwa wewe sasa TRA atakwambia hudaiwi? Kwa hiyo, lazima tuangalie hizi biashara watu wanazozifanya wengi ni watu wa kawaida na watu wa kati. Kwa hiyo, lazima tuangalie namna gani yakuwasaidia na namna gani Serikali itakusanya kodi yake bila kupunguza kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuja kwenye EFD za kwenye mafuta, hizi ni wizi mtupu kwenye petrol station na wewe nafikiri ni sahidi kwa sababu unafanya hii biashara, hizi ni za wizi na ninajua kabisa Dkt. Mpango, Ndugu Kichere...

MHE. RICHARD M. NDASSA: Kichere hayupo.

MHE. AHMED M. SHABIBY: ... Ndugu Kidata na wote walikuja hawakushiriki katika mchakato wa kuleta hizi EFD walikuta ule mchakato upo, hatuwezi kuwalaumu hao watu.

Mheshimiwa Spika, lakini unanunua lile dubwasha kwa dola 3,000 mpaka 5,000; unalifunga kwenye petrol station kwa mwaka unalipa shilingi 1,200,000 kwa ajili ya yule fundi. Halafu mkoa mzima kuna fundi mmoja, halafu ikiharibika unatoa ripoti TRA kwamba mashine imeharibika, unaendelea kuuza, ile mashine haifanyi kazi, kesho na kesho kutwa anakuja fundi anakwambia kadi imekufa, anachukua shilingi 300,000 kwenye kila pump, yale makaratasi yanayotumika pale ni ya mamilioni kila siku halafu haina faida yoyote kwa sababu EWURA wanatoa bei, tuna chombo cha Serikali kinaitwa EWURA kinajua kabisa mfanyabiashara wa rejareja kwenye kila lita anapata kiasi gani.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano mtu anaendesha Kituo cha Engen au Total au Oryx au Gapco au nani anajulikana kabisa kwa lita anapata shilingi 72. Huyo mwendeshaji wa kituo na mafuta yote yanatoka depot. Kwa nini msichukue huko mkate kwenye ile profit ya huyo muuzaji kwa nini msikate pesa yenu huko? Mkatie huko Dar es Salaam kama hii ni shilingi 72 tunachukua tunakata shilingi 15 kwa lita, kusanyeni huko. Kwa sababu mnapotaka kukusanya mafuta yakuja kwa muuzaji wa retail, sasa hivi Wilaya zote kuna boda boda na kuna nini na kuna watu wanauza kwenye mapipa na wanashindwa kudhibitiwa, mtu wanamshushia kutoka kwenye tenki la gari, ana mapipa yake 20 chumba cha 4,500 yanaenda moja kwa moja kwenye mapipa.

Mheshimiwa Spika, mtu ana malori yake, anashusha gereji, haipitii kwenye petrol station, sasa hiyo EFD inafanya nini? Kwa sababu mtu anaamua kuiba anavyotaka yeye, sasa hiyo EFD inafanya nini? Leo mimi nina mabasi, naamua kushusha gereji kwangu na EFD gereji? Kwa hiyo nimechukua mafuta lakini hayakupita kwenye EFD nataka kumuuzia mtu anaenda kuuza kwenye mapipa natoa kwenye gari direct moja kwa moja mpaka kwenye mapipa, kuna EFD? Napeleka shambani kuna EFD? Kwa hiyo kateni huko angalieni kwamba katika vituo vyote tunapata milioni ngapi na tukikata hapa huku basi hatupotezi wala hatupunguzi yale mapato tunayopata.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukilichukua hilo utapata hela nyingi sana, hizi EFD machine yaani ni kupoteza muda tu kabisa kabisa. Endelea Mheshimiwa Shabiby. (Makofi)

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ndio cha msingi.

SPIKA: Kata kule kule Dar es Salaam upate hela yako.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, juzi nimekwenda Kiteto unakuta fundi anaambiwa amemuita fundi ana wiki tatu hajafika kutengeneza mashine za EFD wakati kuna njia rahisi kabisa za kukusanya mapato. Halafu sisi tunawashauri na tunasikia kwa wafanyabiashara wenzetu ili Serikali ipate fedha, basi tunaomba muwe wasikivu hata kwenye haya magari wangeamua tunasema labda kila gani fulani linakwenda transit tunachukua kodi yetu milioni mbili au tatu kwa mwaka wewe shauri yako.

Mheshimiwa Spika, sasa utakuta mtu akiwa ana gari nne hafanyi hesabu, analipa labda milioni moja, mwenye gari tano kwenda mbele anafanya hesabu analipa milioni tatu. Mtu akifikia uwezo wa kununua gari huyo ana uwezo wa kulipa kodi. Kuna haja gani ya kumwambia asifanye hesabu au kama mtu anafanya hesabu afanye lakini pawe na bei inayoeleweka kwamba gari hii mtaondoa hata vyanzo vingine sababu ya kutoa rushwa si kukamata. Hata uweke wakamataji wawe wa wangapi utakamata wote? Sababu ya utoa rushwa ni kutoa vyanzo vya rushwa, kwamba nini kinasababisha hapa ndio unatoa rushwa. Kwamba hiki kinasabaisha rushwa tukiweke mazingira kitakuwa hakina rushwa, hiki kina sababisha kero hii tukiondoa kitakuwa hakina kero, lakini tusitegemee TAKUKURU, TAKUKURU atakamata watu wangapi? Hii kitu haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya kuna ile watu hapa mwaka jana ilifutwa ilikuwa milioni tatu sijawahi kufanya hiyo. Wala kwa mimi siipendi kuweka jina langu kwenye gari, lakini kuna watu wanapenda kuweka majina kwenye magari, unakuta mtu anaandika King Musukuma, nitolee mfano Musukuma gari yake imeandikwa King Musukuma alikuwa nalipa shilingi milioni tatu lakini wakaja wakapandisha, sasa mwingine haweki lile jina la kwenye plate namba kwa sababu labda ni starehe. Mwingine ana kama akina dada hapa Wabunge na wadada wengine walioko mtaani gari zao wanazitumia vizuri ana TZB hataki hiyo gari ionekane ni TZB anaamua kuandika jina lake pale ili afute ile namba gari isijulikane kama ni gari zamani au gari mpya. Kwa sababu gari yake bado ni nzuri. Wewe unaenda unaweka kodi kubwa, sasa hata nikiangalia sasa hivi kama mapato yapo pale pale lakini waliosajili ni wachache, eeh, tuweke bei ndogo watu wawe wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna yale bango yalikuwa kwenye malori hatuna sisi viwanda, lakini mabango ya kwenye viwanda hata sasa hivi ukiangalia unasema malori ya bakhresa yako wapi mbona hayapo, malori ya fulani yapo wapi mbona hayapo, sio kwamba hayapo yale mabango yalikuwekewa sijui milioni nne kwa mwaka ukiandika kwenye lori tu kwamba hii bidhaa fulani inauzwa unalipia milioni nne/ milioni ngapi sasa mwishowe watu wameamua kufuta tu wamebakiza magori mawili/matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, weka pesa kidogo upate mapato mengi. Kuna hii...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Nimekuongeze dakika kidogo endelea Mheshimiwa Shabiby. (Makofi)

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Kwa hiyo, utakuta tunachotakiwa sisi kufanya tusizungumze sawa tunasema kwamba kuna biashara zimefungwa labda 1,000 zimefunguliwa biashara 14,000. Lakini biashara zilizofunguliwa 14,000 na zilizofungwa zipo sawa? Inawezekana biashara wamefungua 14,000, 12,000 lakini biashara za briefcase, mtu akenda BRELA kasajili, kaenda TRA kachukua clearance, kaenda Halmashauri kachukua leseni, kafungua biashara, lakini hata duka lenyewe hana. Ukingalia biashara zinazofungwa na zinazofunguliwa na kero nyingine haijatajwa kwenye bajeti hii watu tumeng’ang’ania kero za TRA, lakini kuna watu wengine wana kero kuliko hiyo TRA.

T A A R I F A

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Susan.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nimpe taarifa mzungumzaji Mbunge Mheshimiwa Shabiby kwamba anasema kwamba biashara za kuandika bango na hii imepoteza hela nyingi sana katika nchi yetu kwa mfano mtu ana salon yake akiandika bango ama hoteli wanam-charge hela nyingi, matokeo yake watu wanafuta. Kwa hiyo biashara nyingi hata sasa hata hoteli, maduka, salon wote wameondoa mabango kwa hiyo TRA wanapoteza hela nyingi sana. Bora wapunguze bei ili hawa watu waendelee kuweka bango katika biashara zao. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Shabiby ilikuwa ni taarifa kwako tu.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa sababu ni taarifa ya kujenga na tupo pamoja. (Makofi)

Kwa hiyo sisi tunaishauri TRA na nina uhakika kabisa hata watu wanapoizungumzia habari ya TRA lazima tuseme ukweli. Ukiangalia huko juu kwa Makamishna huko hakuna matatizo kabisa, huku chini na ndio maana Rais alisema. Hapa Dodoma mlikuwa mnashuhudia wenyewe mtu anakwenda anafunga duka anasema hapa kazi tu. Kumbe ana roho mbaya, huyo anakuwa ana roho mbaya na Rais Magufuli tu wala hana kitu kingine, hapa kazi tu tumetumwa, wanasema.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi bahati nzuri tunashukuru kuna Meneja wa TRA amekuja mpya hapa Dodoma ameondoa hilo tatizo, kwa hiyo, mimi ushauri wangu ni huo. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Shabiby.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Wizara hii na kwa viongozi wake wote. Natambua Wizara hii ni kiungo muhimu kati ya wafanyabiashara na Serikali. Bila Wizara hii kufanya kazi kwa umakini na uweledi, basi ndoto ya Serikali yetu ya kuwa na viwanda itakuwa ndoto isiyotimia. Kwa sababu kumekuwa na kila aina ya matamko na sheria za ovyoovyo za kuua biashara ndani ya nchi hii hasa kutoka katika mamlaka zilizopo kama EWURA, TBS, NEMC, SUMATRA na zinginezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ili mtu apate leseni ya NEMC ya Petrol Station, kwanza lazima apate consultant ambaye amepitishwa na NEMC na baada ya hapo asajili mradi, consultant pekee analipwa shilingi millioni saba (Sh.7,000,000/=) na kusajili mradi napo fedha. Ukimaliza consultant, ili watu wa NEMC waje kukagua ripoti ya consultant nao unalipa gharama zao za kuja site.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo wakiridhika kukupa leseni, unalipa shilingi milioni kumi (Sh.10,000,000/=) na baada ya hapo utaendelea kulipa ada ya kila mwaka shilingi laki tatu (Sh.300,000/=). Utakuta inagharimu zaidi ya shilingi milioni ishirini na tano kupata Leseni ya NEMC kwa kituo kimoja na bila kujali kipo kijijini au mjini. Je, kwa faida ya Sh.90 kwa lita kuna biashara hapo, bado gharama za kodi, upungufu wa mafuta, mishahara na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii nimetoa mfano kwa kituo cha mafuta lakini ndiyo hivyo hivyo kwa hoteli au viwanda ukitaka kupata leseni ya NEMC. Kwa mfano huu mdogo, Wizara hii inachukua hatua gani kuhakikisha mamlaka zilizopo zinafanya kazi zake kwa ufanisi na siyo kuwa wakusanya faini na watoza kodi au Wizara hii ni jina tu? Kwa nini chochote kinachofanywa na mamlaka kuhusu biashara ndani ya nchi hii kisihusishe Wizara kwanza kabla ya sheria na kanuni zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu.