Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdulaziz Mohamed Abood (2 total)

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.

Kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 niliwahi kumwambia Mheshimiwa Waziri kuhusu matatizo ya hospitali ya Mkoa wa Morogoro, kuhusu x-ray machine, majokofu ya kuhifadhia maiti na upungufu wa madaktari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila iwapo nisipomshukuru Waziri na Naibu Waziri. Walishughulikia tatizo ya x-ray machine, walitutumia Wataalam ambao machine yetu ilikuwa ni analogue wakaibadilisha kuwa digital na sasa inahudumia wagonjwa 50 mpaka 70 kwa siku. Pia tumeweza kuunganishwa katika mfumo wa tele-medicine ambao wanapata ushauri zaidi kwa Madaktari Bingwa.

Kuhusu majokofu tunamshukuru Mheshimiwa Waziri ametupatia na sasa katika wiki hii yanaanza kutolewa ya zamani na kuwekwa mapya katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Upungufu wa madaktari tunashukuru Mheshimiwa Waziri umetutimizia kiasi kikubwa ila tuna tatizo bado moja kubwa la specialist wa ENT ambaye hatuna hata mmoja.

Pili, tuna tatizo vilevile la wafamasia ambao walitakiwa wawe 14 lakini tunae mmoja tu msaidizi. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri katika hilo naamini kwa kazi unazozifanya na Naibu Waziri kwa speed ya Awamu ya Tano mtatumalizia kero hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero nyingine ni wodi ya wazazi katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Hospitali ya Mkoa inapokea wazazi 40 kwa wastani kwa siku na wodi inaweza kupokea wagonjwa 20 mpaka 25 tu kwa siku. Kwa hiyo, tungeomba Mheshimiwa Waziri atuongezee wodi nyingine katika bajeti yake ili tuweze kutimiza mahitaji ya wazazi katika wodi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero nyingine tuliyonayo Morogoro ni ambulance. Tunayo ambulance moja tu na wagonjwa wanakuwa ni wengi mno kiasi ambacho wengine wanaandikiwa rufaa ya kwenda Muhimbili, ambulance moja inashindwa kufanya kazi yake. Kwa hiyo, tunakuomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo na nitakupa ushirikiano ili tuweze kupata ambulance mpya nyingine kwa ajili ya hospitali ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine la gharama za wanaovunjika viungo kwa maana ya wanaovunjika mifupa kwenye ajali na matatizo mengine. Gharama zile katika Hospitali ya Mkoa ambao hawana bima ya afya ni kubwa mno kuanzia shilingi 500,000 mpaka shilingi 700,000, lakini ukiuliza unaambiwa kwa sababu ya gharama ya vyuma.

Kwa hiyo, tunakuomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo kwa sababu gharama hizi kwa watu wa hali ya chini wanashindwa kumudu, tungeomba mtufikirie juu ya hili ili tuweze kupata vyuma na vifaa vingine kwa ajili ya kuweza kupunguza gharama hizo ili wananchi waweze kugharamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya ya kutekeleza ahadi za maji katika Jimbo letu la Morogoro Mjini. Tunamshukuru alituahidi atatupa mradi wa maji na kweli sasa tumepata mradi wa maji, naishukuru sana Serikali, ila ninachoomba kwa Mheshimiwa Waziri tuharakishe huu mradi wa maji ambao tulimepewa na Wafaransa ili kuondoa kero hii ya maji, na hasa wakazi wa Morogoro wanazidi kuongezeka wakiwemo Wabunge wengine humu wakihamia Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna eneo la uwekezaji ambalo linahitaji maji mengi kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda na wawekezaji wengi wakija kitu cha kwanza wanachouliza ni maji. Kwa hiyo, tunaomba Wizara iharakishe kazi hii ya mradi huu wa maji ili tuweze kupata maji kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Morogoro bado kuna tatizo la maji. Huu mradi ni mradi wa muda mrefu lakini sasa hivi bado tuna tatizo la maji. Bwawa la Mindu limejaa lakini miundombinu inayokwenda na kusambaza katika maneo mbalimbali ya Morogoro bado ni tatizo. Kwa hiyo, naomba Wizara iliangalie hilo ili kuongezea bajeti upande wa Morogoro kwa ajili ya kuweza kutengeneza miundombinu mipya ambapo maeneo mengi kuna miundombinu chakavu; na hasa maeneo ya Kihonda, Tungi, Lukobe, Mkundi na Kiyegeya. Cha kushangaza zaidi wananchi wa Mindu ambao wanalilinda lile bwawa la maji kwao hakuna maji wala miundombinu ya maji, kwa hiyo, naomba Wizara waliangalie hilo ili tuweze kuondoa kero hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya World Bank ambayo wananchi wamechangia. Sasa kuna tatizo ambalo Mheshimiwa Waziri naomba hili mlifanyie kazi, kuna kata mbili kata ya Bigwa na Kingolowila, kuna mitaa minne ambayo wananchi wamechangia mradi huo lakini mradi huo unataka kuchukuliwa na kupewa MORUWASA. Ila wananchi sasa wanadai wanasema miradi wameshachangia wao wanahitaji wao wenyewe waendeshe hiyo miradi ya maji kwa kutumia vikundi vyao vya ushirika. Tatizo linalokuja ni kusema kuwa sheria hairuhusu. Mimi nadhani wakati wananchi walipokuwa wakichangia ilitakiwa waambiwe kwamba mradi huu hamtoweza kuendesha wenyewe. Sasa hivi kuna mgogoro mkubwa sana katika maeneo haya. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri, elimu ya kutosha inatakiwa kwa wananchi ili kuepukana na tatizo hili la kudai kuendesha mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wamepewa MORUWASA na bei wanayowapangia sasa hivi ni kubwa, kwa hiyo, hawakubaliani nao na mradi umesimama na wananchi bado wanaendelea kukosa maji. Tunaomba hili tatizo lifanyiwe kazi ili tuweze kulimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine kubwa bado linaendelea na hasa tunategemea kupata mradi mkubwa wa maji, Mjini Morogoro. Tatizo ni bili za maji wananchi wanalipa maji ambayo kwa mwezi mzima au miwili hajapata lakini anapata bili ametumia maji, ni kutokana na mita zenyewe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.