Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Pascal Yohana Haonga (40 total)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwa kuwa walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi walisimamia mtihani wa kidato cha Nne mwaka jana 2015 hawajalipwa fedha zao. Je, Serikali haioni ni mwendelezo wa kuwanyanyasa walimu na kuwaonea?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika asante. Mheshimiwa Pascal juzi wakati anajadili hapa nadhani alizungumzia suala la Mbozi, na ofisi yetu inalifanyia kazi kushirikiana na Hazina na katika mchakato tunaoondoka nao walimu wote ambao malipo yao yalikuwa bado hayajakamilika basi yataweza kusawazishwa na jambo hili likaweza kukaa vizuri, Serikali inafanyia kazi jambo hilo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, japokuwa swali langu halijajibiwa kifasaha na imekuwa ni mwendelezo wa kukiuka Kanuni namba 46(1) na hii ni kawaida tumeona sijui inamaanisha nini. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:
Kwanza, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kupunguza bei ya mbolea ili kuwapunguzia wananchi gharama za kilimo?
Pili, ni lini Serikali itapunguza ushuru na tozo mbalimbali katika zao la kahawa ili kuwapunguzia wakulima mzigo maana wakulima wametwishwa mzigo kwa muda mrefu sana. Wamekuwa na tozo nyingi, ushuru mkubwa kwenye kahawa mwisho wa siku hawanufaiki. Sasa ni lini Serikali itapunguza ushuru na tozo mbalimbali katika zao la kahawa ili kuwapunguzia wakulima mzigo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanzaa kuhusu kupunguza bei ya mbolea, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba inachukua hatua zinazotakiwa ili kuhakikisha kwamba bei ya mbolea inayotumika katika mazao mbalimbali inapungua. Kwa wiki za hivi karibuni Wizara yangu imekuwa ikikutana na wataalam wake kuangalia ni namna gani tunaweza tukaondoa kero mbalimbali zilizopo katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuondoa kero ya bei ya mbolea ambayo kwa kweli imelalamikiwa na wananchi wengi.
Mheshimiwa Spika, lakini (b) ameulizia kuhusu kuondoa tozo mbalimbali zinazokabili mazao mbalimbali katika sekta yetu ya kilimo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara imekuwa ikipitia upya tozo zote zinazotolea ili kuona ni namna gani tunaweza kupunguza.
Mheshimiwa Spika, katika kufanya hivi nafikiri yeye mwenyewe ameshiriki katika Mkutano ambao Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi ameuitisha hivi karibuni wa Wabunge wanaotoka maeneo ya mazao haya ili kuangalia changamoto zilizopo lakini vilevile kupata mapendekezo yao ya namna ya kutafuta suluhu. Nimhakikishie tu kwamba, Wizara inapitia upya kuhusu hizo tozo kwa sababu ni kweli wananchi wanalalamikia na muda siyo mrefu tutapata mrejesho kamili kuhusu namna gani Serikali itapunguza au kuondoa moja kwa moja baadhi ya hizo tozo. Nashukuru sana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Waziri swali dogo. Ni lini Serikali itaacha kuagiza toothstick maana tuna miti mingi ya kutosha kule Mbeya na sehemu nyingine. Ni lini Serikali itaacha kuagiza toothstick? Ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mambo yanayoninyima raha ni kama kuona watu wanaagiza toothpick. Mimi nimeleta bajeti yangu hapa lakini haina maana hata ningeisoma kwa mbwembwe namna gani kama ninyi msipoikubali. Ninyi Wabunge mniambie kwamba toothpick zisipite Dar es Salaam muone kama zitaingia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtambo wa kutengeza toothpick ni dola 28,000, ni jukumu lako Watanzania kuwekeza. Kuna Mtanzania mmoja, nawaomba asiyetaka kuwekeza kwenye viwanda na nimelisema mara tatu, kuna Wabunge, kuna watu wanakuja kila siku wanataka kuwekeza, Mtanzania anayeagiza toothpick anaagiza container 100 ni mtu wa Makete. Mtambo wa kutengeneza toothpick ni dola 28,000. Kuna Mbunge Mheshimiwa Lema anafuatilia kuleta mtambo wa toothpick kupeleka Kilimanjaro. Watu wanahangaika, msikosoe, msilalamike twende tufanye kazi. Toothpick inatumia mabaki ya miti haitumii ubao, the reject, the unwanted material ndiyo inatumika. Tuchangamke, twende wote kwenye behewa la viwanda msibaki nyuma. Viwanda ni vita Bwana Msigwa twende kwenye viwanda. Toothpick mkiamua zisiagizwe hazitaingia, TBS ni yangu nitazizuia lakini na ninyi muwekeze watu wanapenda toothpick.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa shamba hili ni kubwa sana takribani ekari 12,000; na wazalishaji wa mbegu hata ekari 1000 hazijafika katika kuzalisha mbegu kwenye shamba hili. Wananchi wamehangaika kwa muda mrefu wanaharibu mazingira wanatafuta maeneo mapya ya kulima.
Je, Waziri sasa yuko tayari kwenda kuyapitia upya yale maeneo angalau kuwarudishia wananchi eneo angalau hata kidogo ili waendelee kulima kwa maana wanaharibu mazingira hawana maeneo ya kulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, NFRA walipokuwa wananunua mahindi msimu wa mwaka 2015; Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi inawadai ushuru wa shilingi milioni 420, hawajalipa fedha hizo.
Je, Serikali ipo tayari kupeleka fedha hizo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, shilingi milioni 420 ambazo hazijapelekwa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Wabunge wa Mbeya kwa kufuatilia suala hili, nakumbuka tuliambatana na Mbunge wa Mbozi pamoja na pacha wake Mheshimiwa Hasunga, Mbunge wa Vwawa. Niseme tu maeneo ya aina hii yapo, ambayo yamekuwa yakivutia wananchi kutaka wagawiwe. Nakumbuka hata suala la Bugaga ambalo Mheshimiwa Nsanzugwanko amekuwa akilihangaikia, naelewa concern ya Wabunge kutaka wananchi wapate maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge tukubaliane kwamba zoezi la kuwagawia wananchi mashamba ya Serikali siyo endelevu kwa sababu uhitaji wao ni mkubwa kuliko ukubwa wa maeneo yanayopatikana. Kwa hiyo leo hii hata tungesema tunatoa ekari 2000, kwa sababu hatutoi kwenye shamba la ujamaa, ni dhahiri kwamba wale vijana hawataweza kupata wote eneo hilo ambalo litakuwa tunaligawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, utaratibu endelevu ni kuwaweka vijana kwenye vikundi, halafu washirikiane na taasisi na Serikali, kutimiza lengo lile la kupata mbegu kutoka katika eneo hilo, huku wakisimamiwa na kutimiza vigezo ambavyo vinatakiwa katika suala hilo la mbegu. Nimeelekeza wataalam wangu wanipe mashamba yote ambayo yalishageuka kama mapori ambayo yanatamanisha wananchi kuona hayatumiki ili tuweze kutengeneza ushirika wa vijana wanaotaka kwenda kwenye kilimo waweze kuyatumia na Serikali itimize lengo lake la kupata mbegu kutoka katika mashamba hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kulipa fedha zile ambazo hazikuwa zimelipwa, nimelipokea na nitawaelekeza wataalam wangu wa NFRA waweze kutimiza jambo hili, kwa kulipa deni hilo ili Halmashauri iweze kutekeleza miradi yake ya maendeleo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kutokuwepo kwa gari ya zimamoto Tunduma, kumeleta madhara makubwa sana kwa wakazi wa Tunduma. Kwa mfano, siku za hivi karibuni kumetokea suala la moto ambalo liliteketeza karibu maduka 500. Hali hii kwa kweli imesababisha wafanyabiashara wengi na wajasiriamali, hali yao kuwa mbaya sana, mitaji yao imepotea. Je, kwa kuwa Serikali leo hii kipaumbele chake ni kununua magari ya washawasha badala ya kununua magari ya zimamoto, iko tayari sasa kuwafidia wale wananchi ambao maduka yao yaliungua kwa sababu ya uzembe wa Serikali? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuna tatizo pia kubwa ambalo maaskari wetu pale hawana nyumba na nyingine ambazo nyingi zimejengwa kipindi cha Ukoloni na nyumba nyingi zina nyufa na kituo chenyewe cha Polisi kipo kwenye hali mbaya sana. Je, Serikali itaanza lini ujenzi wa nyumba za maaskari wetu pale Mbozi na Kituo cha Polisi ambacho kwa kweli kimejengwa tangu kipindi cha ukoloni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Magari ya washawasha nimelizungumzwa hapa mara mbili, tatu kwamba tunatarajia kuyatumia magari haya vile vile kwa ajili ya kuzimia moto. Tupo katika huo mpango, mazungumzo yameshaanza kati ya Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Magereza. Haya magari machache ambayo nimezungumza juzi, yatasaidia. Kwa hiyo, hoja yako Mheshimiwa Frank Mwakajoka imekuja wakati muafaka kwamba hukupaswa kulaumu badala yake upongeze tu kwamba una tatizo la upungufu wa magari ya kuzimia moto, usilaumu kuhusu magari ya washawasha, upongeze kwamba haya washawasha yatakusaidia vilevile. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na nyumba za askari nalo hili tumelizungumza katika Bajeti yetu vizuri tu kwamba tuna mpango wa kujenga nyumba 4,316 katika mikoa kwa awamu ya kwanza takribani 16. Kwa hiyo, umesema kwamba eneo lako la Tunduma pia unahitaji. Labda nilichukue hili nione jinsi gani katika mgawanyo ule tunaweza kuzingatia ombi lako pia. Siwezi kukuahidi sasa hivi, lakini nalichukua ombi hili tulifanyie kazi.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ambayo sijaridhika nayo hata kidogo, naomba sasa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mmiliki wa shamba hili ndugu Joseph Meier alimiliki shamba hili kwa njia za ulaghai ikiwa ni pamoja na kuwapatia viatu Wenyeviti wa Vijiji wa kipindi hicho kwa tiketi ya CCM na akamilikishwa shamba hilo, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuchukua hatua za kinidhamu kwa mmiliki huyu ambaye ni mmiliki haramu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Serikali katika majibu yake imesema kwamba mmiliki wa hili shamba analihudumia kwa kiwango kidogo sana, kwa maana ya kwamba katika ekari 1,000 ekari zinazoendelezwa ni kama ekari 10 tu kati ya 1000; je, Serikali haioni kwa kigezo hiki tu ni muda muafaka sasa wa kumpora huyu bwana hili shamba lirejeshwe kwa wananchi wa Jimbo la Mbozi ambao hawana maeneo ya kulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza la nyongeza anasema kuwa huyu mwekezaji alichukua shamba hili kwa njia ya ulaghai. Sisi tunasema kwamba kama mwekezaji yeyote na ndiyo maana Msajili wa Mashirika ya Umma (TR) anapitia mikataba yote ya wawekezaji wetu ambavyo wameweza kumilikishwa mashamba na wengine ambao waliingia kwenye ubia wa mikataba mbalimbali ili kuweza kujua kama kuna tatizo lolote lile katika umiliki. Kwa hiyo, pale tunapogundua kwamba mwekezaji au mbia wetu ambaye tumeingia naye kama Serikali, kuna ubadhirifu wa aina yoyote ulifanyika, hatua zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaguzi hizo zinaendelea kwenye Mashirika yetu ya Umma yote kuhakikisha kwamba kuna usahihi wa umiliki, lakini vilevile hakuna ulaghai wa aina yoyote na hivyo kama itabainika kwamba kuna ulaghai ulitumika katika kujipatia shamba hili hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; kwamba huyu mwekezaji amekuwa akiendeleza shamba hili kwa kiwango kidogo sana, ambapo according to yeye Mheshimiwa Mbunge ni kama asilimia moja au mbili ya shamba alilokuwa amekabidhiwa la hekta 830, lakini ameweza kuendeleza kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hapa kwamba kinachotakiwa sasa Mheshimiwa Mbunge ajue jukumu hili liko kwenye halmashauri yake, yupo Afisa Mteule wa Ardhi pale ambaye ana jukumu la kufanya ukaguzi kwenye shamba hilo kuona maendelezo ambayo yamefanyika na akigundua kwamba hakuna maendelezo yoyote yaliyofanyika kwenye shamba hilo, basi amwandikie notice ya siku 28 ya kufanya marekebisho na baadaye amwandikie notice ya siku siku 90 ya kujieleza kwa nini asinyang‟anywe ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kama yote haya yatafanyika, mwekezaji huyu atakuwa ameshindwa kukidhi matakwa yanayotakiwa, basi atashauriwa Waziri wa Ardhi ili aweze kulitwaa shamba hilo na Waziri wa Ardhi atamshauri Mheshimiwa Rais afute hati husika. Baada ya hapo taratibu zikikamilika, basi hati itafutwa, umiliki utafutwa na umiliki wa shamba hili utarejeshwa kwenye halmashauri ambapo halmashauri ndiyo watapanga matumizi ya namna gani shamba hili litumike baada ya kuwa limerudishwa na Serikali mikononi mwa halmashauri.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Barabara ya kutoka Mji Mdogo wa Mlowo Wilaya ya Mbozi kuelekea Kamsamba ni barabara muhimu sana kwa kuwa inaunganisha Halmashauri ya Mbozi lakini pia na Halmashauri ya Momba. Pia barabara hii inaunganisha Mkoa mpya wa Songwe na Mkoa wa Rukwa na Katavi. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nadhani amewahisha swali hili kwa sababu anajua kuna swali lingine zuri kabisa la Mheshimiwa Silinde linakuja; lakini nimhakikishie tu kwamba kila ambapo Serikali hii imeahidi itatekeleza.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, kumekuwa na vijana wengi sana wa bodaboda nchini maeneo mbalimbali wamejiajiri kwa kubeba abiria, lakini bodaboda hao wengi hawana leseni. Je, Serikali ipo tayari kuwasaidia bodaboda kuwapatia leseni, kwa kuwa wengi walikuwa wanajihusisha na matukio ambayo siyo mazuri sasa wameamua kujiajiri. Sasa Serikali ipo tayari kuwapatia leseni bodaboda ili kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kuendesha bodaboda au chombo chochote cha usafiri bila leseni ni uvunjifu wa sheria. Hatutakuwa tayari kuendelea kulea uvunjifu wa sheria. Hatuwezi kuwapa leseni watu kwa kisingizio kwamba walikuwa wanaendesha bila leseni kuhalalisha uvunjifu wa sheria.
Tunachokisisitiza hapa ni kwamba Mheshimiwa Mbunge uendelee kuhamasisha wananchi wote kufuata sheria ikiwemo hao vijana ambao wanaendesha bodaboda bila leseni. Wafuate utaratibu wa kupata leseni kwa kufanya test ili waweze kupata leseni kisheria, siyo kupata leseni kwa sababu wamekiuka sheria. Sisi tutawachukulia hatua za kisheria wale wote ambao tutawabaini kwamba wanaendesha gari na pikipiki kinyume na sheria. Tunaomba ili sheria isiweze kuwakumba basi wafuate sheria kwanza.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mpango wa Serikali kwa sasa ni kuelekea Tanzania ya viwanda na hakuna viwanda ambavyo tunaweza kuvipata bila kuboresha kilimo. Hii ni sawa na kwamba unapanda mchicha unategemea kuchuma machungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pia hauwezi kuboresha kilimo bila kuwekeza kwenye vyuo vya kilimo. Je, Serikali ipo tayari kuboresha kituo cha mafunzo ya wakulima ambacho kipo kijiji cha Mbozi, kata ya Igamba, Jimbo la Mbozi ili kiwe chuo kamili, kwa maana tayari kituo hiki kipo na wakulima walishaanza kupata mafunzo pale tangu mwaka 2012?
Swali la pili, kwa kuwa vyuo vingi vya kilimo nchini kikiwepo Chuo cha Kilimo cha Uyole, vipo katika hali mbaya sana, Serikali imevitelekeza, miundombinu ni mibovu, havina wataalamu. Je, Serikali ipo tayari sasa kuboresha vyuo vyote vya kilimo nchini ili sasa tuweze kwenda na hii suala la nchi ya viwanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu ya swali la msingi, Serikali ina nia ya kuendelea kuboresha vyuo vyetu vya kilimo, kuboresha kule ni zaidi tu ya kuviongeza idadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba tukiweza kuimarisha na kuboresha huduma zinazotolewa na vyuo vilivyopo sasa sio lazima kuongeza vyuo vingine. Kwa sasa nchini kwetu tuna vyuo 14 vya kilimo katika kanda sita za kilimo. Sasa tunachofanya ni kuendelea kuziboresha ili ziweze kutoa huduma nzuri zaidi badala ya kuelekea kujenga utiriri wa vyuo ambavyo havina quality nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge nimuelekeze tu kwamba kituo anachozungumzia wakati huko mbele tunaweza kufikiria kufanya chuo kamili lakini kwa sasa vyuo vitatu ambavyo vipo mkoa jirani wa Mbeya tutaendelea kuviimarisha na kuviboresha ili viweze kutoa huduma kwa watu wa Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, jibu hilo pia linatumika kwa vyuo vyote nchini, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi. Serikali sasa inaanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Mifugo awamu ya pili ya ASDP II, moja kati ya matarajio katika kutekeleza mpango huu ni kuendelea kuboresha vyuo vyetu vya kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza kukarabati majengo, kuajiri rasilimali watu ya kutosha ili viweze kudahili wanafunzi wengi na kutoa elimu ya kilimo ambayo ni bora.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mji Mdogo wa Mlowo uliopo Wilaya Mbozi, tangu mwaka 2016 umetangazwa kuwa mji mdogo lakini hakuna shughuli yoyote pale inayoendelea kuonesha kwamba ni mji mdogo; bado vitongoji kama kawaida vipo na tayari ile asilimia 80 inayokusanywa na Halmashauri ya Wilaya inaendelea kukusanywa kama kawaida na asilimia 20 inarudi kwenye kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nijue ni lini rasmi sasa Mji Mdogo wa Mlowo utaanza kufanya shughuli zake kama Mji Mdogo na kama siyo kijiji kama ilivyokuwa kwa sasa japokuwa tangu mwaka 2016 tumeshapewa kuwa hadhi ya Mji Mdogo lakini shughuli zinazoendelea siyo za Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, mji anaouzungumzia Mheshimiwa Haonga ni kweli ni mji ambao sasa hivi eneo lake bado lipo katika suala zima la vitongoji, lakini kuna utaratibu ule kwamba vile vijiji tufanye ule uchaguzi wa Serikali za Vitongoji, then wachague Mwenyekiti wa Vitongoji kwa mujibu wa taratibu, then atachaguliwa TEO, then mchakato huu utaenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu katika eneo lake kuna baadhi ya Vitongoji vingi sana havijafanya uchaguzi na hii nakumbuka alikuja ofisini kwangu tulikuwa tunatoa maelekezo kwa Mkurugenzi kwamba aangalie utaratibu wa kufanya yale maeneo ambayo uchaguzi haujafanyika, ziweze kufanya uchaguzi maeneo yote sawa sawa na eneo la Vwawa kule kwa Mbunge wetu wa Vwawa. Maana yake zikifanyika chaguzi zote, basi utaratibu mwingine utafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kwamba vile vitongoji vyote viwe na hadhi ya vitongoji na Wenyeviti wake wa vitongoji baadaye wachague Mwenyekiti wao Kitongoji, then achaguliwe TEO, baadaye ule mji sasa unakuwa na mamlaka kamili kufanya kazi yake. Kwa hiyo, ni jambo ambalo tutaendelea kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi wetu, waendelee na michakato ile ya kufanya mamlaka ile inaweza kufanya kazi vizuri kama ilivyokusudiwa.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na wizi unaofanywa na baadhi ya makampuni ya simu, yanakata fedha za wateja yakidai kwamba tumekuunganisha na huduma fulani ambayo mteja hakuomba. Je, Serikali imejipanga vipi kudhibiti hali hii ya wizi unaofanywa na makampuni haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni namna tunavyotumia simu hizi. Mara nyingi sana huwa tunaulizwa maswali fulani na tunapojibu tunahalalisha makato bila wenyewe kujijua au unapobonyeza baadhi ya button unajikuta unakubali ukatwe bila mwenyewe kujua. Kwa hiyo, tumewataka watu wa TCRA wahakikishe wanatoa elimu ya kutosha ili wananchi wasifike mahali fedha zao zinakwenda bila ridhaa yao wakati wao wana utaalam wa kuwajulisha wananchi na wakatuelewesha ni namna gani tuzitumie hizi gadgets hasa hizi za android za siku hizi…
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Scheme ya Umwagiliaji ambayo ipo Kijiji cha Mbala Wilaya ya Mbozi, imetengenezwa tangu mwaka 1971 na miundombinu ya scheme hii imeharibika sana na hadi sasa haifanyi kazi. Naomba nijue Mheshimiwa Waziri atakapokuja Songwe yupo tayari kuongozana na mimi kuelekea kwenye scheme hiyo ya umwagiliaji na baada ya hapo sasa Serikali iweze kutengeneza miundombinu miundombinu ya scheme umwagiliaji ili wananchi hao waweze kunufaika na scheme hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba zipo scheme nyingi ambazo hazifanyi kazi, lakini tumesema mara nyingi kwenye Bunge hili kwamba tumeshatuma watu wanafanya mapitio ya scheme zote ili kuweza kuainisha mahitaji yake. Kwa hiyo, kwenda tu bila kuwa na jibu haisaidii, kwa sababu ameshasema kwamba haifanyi kazi. Kwa hiyo, tunaleta watu wataalam ili waainishe ni vitu gani vinatakiwa vifanyike kwa ajili ya kufanya ile scheme ifanye kazi. Kwa hiyo, naomba tusubiri ripoti ile itakavyoandikwa halafu tutaona hatua za kuchukua. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la miundombinu ya barabara katika Mji Mdogo wa Rujewa linafanana kabisa na ubovu wa miundombinu ya barabara katika Mji Mdogo wa Mloo, Jimbo la Mbozi.
Je, nini ahadi ya Mheshimiwa Waziri kwa wananchi wa Mloo kuhusu miundombinu mibovu ya barabara ambayo ni tatizo la muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Haonga unapozungumza suala la Mloo nafahamu kwamba changamoto kubwa ya Wabunge wengi humu ni suala zima la miundombinu ya barabara katika Halmashauri zetu. Ndiyo maana nawashukuru sana katika Mpango ule wa bajeti mwaka huu mmeona tumetenga bajeti kubwa karibuni ya shilingi bilioni 263. Lengo kubwa ni kwamba barabara za vijijini zenye vikwazo na zile barabara nyingine tuweze kuzihudumia.
Kwa hiyo, naomba niseme kwamba katika eneo la kwako ulilozungumza na kwa sababu tumeshawaajiri watu tena tunawapa performance contract ya jinsi gani kila meneja katika Halmashauri anapoenda kule afanye kazi yake na tutaipima na meneja atakaposhindwa ku-deliver maana yake hatokuwa na hiyo nafasi atapewa mtu mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ondoa hofu ni kwamba tutakuwa katika mkakati wa kutofanya kazi tena kimazoea katika utaratibu wa sasa, na kwa sababu jambo hili liliahidiwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi lazima tuwe na TARURA tutaenda kutekeleza kwa nguvu zote, naomba ondoa hofu katika eneo la Mloo tutalifanyia kazi haraka iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa mji mdogo wa Mlowo uliopo Jimbo la Mbozi ambao una idadi ya watu karibu 60,000 tangu uhuru hawajawahi kupata maji safi na salama ya kunywa licha ya kwamba Marais wote wanaopita huwa wanaahidi kutatua tatizo hili la maji.
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili la maji katika Mji Mdogo wa Mlowo ambapo mwaka jana wametangaza tenda lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea katika Mji ule wa Mlowo? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si kweli kwamba wananchi wale hawajawahi kupata maji toka uhuru. Sema maji yaliyopo pale Mlowo hayatoshelezi kwa wingi wake lakini wanapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nikupe taarifa kwamba sasa hivi Serikali imeamua kuanzisha huu Mkoa wa Songwe na tutakuwa na mamlaka moja. Kwa hiyo, Mlowo na Mbozi tutaunganisha mamlaka moja ya maji na tutaipa uwezo zaidi wa kuweza kusambaza maji ya kutosha. Sasa hivi tayari tender imeshatangazwa katika kuboresha upatikanaji wa maji Mlowo pamoja na Mbozi.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, siku za hivi karibuni tumeisikia Bodi ya Mikopo imeongeza masharti au vigezo vipya kwa wakopaji, kwa mfano wale viongozi wanaojaza fomu za maadili ya viongozi wa umma wakiwepo Madiwani nao pia ni miongoni mwa watu ambao watoto wao wananyimwa mikopo. Kwa kuwa tunajua kabisa kwamba Madiwani hawana mishahara na wanategemea posho ambayo ni kidogo sana je, Serikali haioni kwamba, huu ni unyanyasaji ambao kwa namna yoyote hauvumiliki na hitakiwi kuufumbia macho unaofanywa na Bodi ya Mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, siku za hivi karibuni wote tunajua kabisa kwamba Bodi ya Mikopo imeongeza makato kwa wanufaika wa mikopo. Kwa mfano awali ilionekana kwamba, wanufaika wa mkopo walikuwa wanalipa wanarejesha asilimia nane ya mkopo waliokuwa wamekopa kwa maana ya makato ya asilimia nane, lakini kwa sasa wanakatwa asilimia 15. Hali hii imesababisha wale wanufaika wa mkopo kama walimu na watumishi mbalimbali ambao walikuwa wamebakisha fedha kidogo ambazo walikuwa wanapata mwisho wa mwezi, leo hawana mshahara hata kidogo na kuna watumishi wanaacha kazi. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kurudi kwenye asilimia nane ya makato, ili angalao watumishi hawa waliocha kazi waweze kurudi makazini na maisha yaweze kwenda vizuri? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli alivyosema kwamba katika mwaka huu wa masomo kuna vigezo vimeongezwa kwa ajili ya watu ambao hawastahili kupata mikopo, ikiwa ni pamoja na viongozi wa umma wanaojaza fomu za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma. Lengo la kufanya hivyo ni kwamba, tunajaribu kuhakikisha kwamba mkopo ule unatumika kwa wale ambao hawana uwezo kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhusu Madiwani kama wana uwezo au hawana uwezo tunajaribu kuangalia kipato chao wanachoweza kupata kwa mwaka na kulinganisha na Watanzania wengine wengi ambao hawana kipato kabisa. Kwa hiyo, lengo ifahamike tu ni kwamba ni kujaribu kutoa fursa kwa wale ambao hali yao ni mbaya zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hitaji la sasa la kwamba waombaji wa mikopo ambao wanatakiwa kurudisha wanakatwa asilimia 10 inatoka kwenye mshahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba mkopo ule ukishachukua kigezo cha pekee cha kwamba unatakiwa kurudisha fedha ni kwamba wewe umekopa, maana yake ilitakiwa pale unapomaliza shule uanze kurudisha.
Sasa kwa muda mrefu sana ule mkopo umekuwa unashindwa kuwanufaisha watu wengi kwa sababu watu wengi hawarudishi na ndio maana sasa tumelazimisha kwamba, ni lazima kwamba, mtu ambaye atakuwa amepata ajira aweze kulipa kwa asilimia 15 ya mshahara wake, lakini vilevile kuna kigezo kingine ambacho tumeweka kwamba, tunatoa kipindi cha mpito au grace period ya miezi 24 toka mwanafunzi amalize shule, lakini baada ya hapo kama hajaanza kulipa tunaanza vilevile kutoza riba ya asilimia
10. Lengo ni kwamba tunahitaji kuufanya mfuko ule uwe endelevu ili wananchi wengi waweze.
Waheshimiwa Wabunge nafahamu kuna baadhi ambao nao wanadaiwa mikopo, katika siku hizi za karibuni tunakuja na orodha ya wale ambao ni wadaiwa sugu. Kwa hiyo, nawaombeni ushirikiano…
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwaka jana Serikali ilipunguza tozo 17 kutoka kwenye zao la kahawa. Lakini kwa bahati mbaya sana tozo 17 hizi hazimgusi mkulima wa zao la kahawa moja kwa moja na hivyo haijamletea mkulima unafuu hata kidogo.
Je, Serikali sasa iko tayari kupitia upya tozo zile ambazo zitamgusa mkulima moja kwa moja ambazo ni kero na iweze kuzipunguza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimezungumzia kwamba Serikali imepunguza au imetoa tozo 80 zaidi ya tozo 139 katika msimu huu wa fedha wa bajeti ya mwaka 2017/2018 zao la kahawa likiwemo. Sisi kama Serikali tunasema zao la kahawa na lenyewe ni mojawapo ya mazao mkakati ya biashara kwa nchi yetu na tumezingatia sana kuhakikisha kwamba tunaendelea kupunguza tozo katika zao la kahawa. Ahsante.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Mbozi ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe inapakana na Wilaya ya Songwe lakini Wilaya hizi mbili hazijaunganishwa kwa barabara na hivyo wananchi wa Wilaya ya Songwe hulazimika kupita Mkoa mwingine wa Mbeya kupitia njia ya Mbalizi kwenda Makao Makuu ya Mkoa ambayo yako Mbozi.
Naomba sasa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini Wilaya ya bozi na Wilaya ya Songwe zitaunganishwa kwa barabara ili kuwasaidia wananchi wa maeneo haya yote mawili kuweza kurahisisha mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge nikupongeze tu kwa kufuatilia na unajua umuhimu wa barabara ina mchango mkubwa sana kwenye maendeleo. Kwa vile sijapata fursa ya kutembelea wa Mbeya mimi napenda tu nilichukue hili ni jambo la kufanyia kazi na mimi nitatembelea Mbeya ili niweze kufika maeneo haya ili tuweze kushauriana vizuri na Mheshimiwa Mbunge wakati Serikali inafanya harakati za kufanya makusanyo na kuboresha barabara nchini. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ambayo pia inatumika kama Hospitali ya Mkoa wa Songwe akina mama ambao hujifungua pale ni wastani wa akina mama 18 hadi 20 kwa siku, lakini kwa bahati mbaya sana hospitali ile haina wodi ya wazazi.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ambayo hutumia kama Hospitali ya Mkoa kwa sasa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu, comrade wangu hapa kuhusu swali la Hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna changamoto kubwa ya wodi ya wazazi na jukumu la Serikali yetu ni kuhakikisha kwamba hizi Hospitali za Wilaya zote tunahakikisha tunaziimarisha vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunachukua hoja hiyo halafu kwenda kufanya analysis kupitia wataalam wetu kwenda pale kuangalia mapungufu yaliyokuwepo ili tuboreshe hospitali ile na hatimaye wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma nzuri. Kwa hiyo, nalichukua hili kwa ajili ya kuhakikisha tunalifanyia kazi.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, lakini kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza ninaomba kufanya marekebisho kidogo. Jimbo sio la Mbozi Mashariki ni jimbo la Mbozi, kwa hiyo, naomba liingie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Skimu za Umwagiliaji za Wilaya ya Mbozi zimechukua muda mrefu sana, kwa mfano Skimu ya Mbulu Mlowo imechukua zaidi ya miaka mitano haijakamilika na skimu hii ina urefu wa mita 1,125, zimejengwa mita 700 tu bado mita 400 kukamilika, miaka mitano mita 700, hizi zilizobaki 400 sijui zitakamilika lini. Sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri aniambie ni lini hizi mita 400 zilizobaki zitakamilika katika Skimu hii ya Umwagiliaji ya Mbulu Mlowo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wilaya ya Mbozi ni maarufu sana kwa uzalishaji wa zao la kahawa aina ya Arabica, ni kahawa ambayo ni tamu sana na ina soko sana duniani. Lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi mikahawa mingi inakauka Mbozi, hali imekuwa ni mbaya na muda si mrefu mikahawa hii inaenda kupotea Mbozi hatutakuwa na kahawa tena. Mheshimiwa Waziri, ninaomba sasa Serikali iweze kutoa commitment hapa; je, mko tayari kuweza kujenga mabwawa ya umwagiliaji wa kahawa maeneo yote yanayolima kahawa Mbozi ikiwepo Isansa, Igamba, Iyula, Msia na maeneo mengine ya Wilaya ya Mbozi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, anasema kwamba hizo skimu zimechukua muda mrefu; ni kweli, utaratibu uliokuwepo hapo mwanzo ulikuwa kwamba washirika wa maendeleo, JICA wamekuwa wanatekeleza wenyewe moja kwa moja, sasa tumeanzisha Tume ya Umwagiliaji ambayo ndiyo itasimamia miradi yote ya umwagiliaji na tulichopanga ni kwamba kwa kuanzia tutafanya mapitio ya miradi yote ya umwagiliaji tuikamilishe ile ambayo inaendelea.
Kwa hiyo, na huo mradi ambao tayari unaendelea tutaukamilisha kwanza kwa fedha ambazo tumezitenga kwenye bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lako la pili kuhusu tabianchi; tabianchi haina jibu la moja kwa moja ila ni lazima sisi tuchukue hatua kwanza ya kukabiliana nalo. Kwanza, tuweze kuona namna gani tutatunza mazingira, hii ni kazi ambayo lazima hata Halmashauri ya Mbozi ishughulike, ukataji wa miti, uchomaji wa mikaa ni lazima uachwe kwa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la kujenga mabwawa, tulichokipanga ni kwamba kwanza tutafanya kila Wilaya imeainisha maeneo ya kujenga mabwawa, tunafanya usanifu kwanza tuweze kujua gharama na tuweze kuona mahitaji jinsi bwawa lile linaweza kuwasaidia wananchi kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, suala lake tunalishughulikia na Serikali kupitia Tume ya Umwagiliaji. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Miradi ya World Bank, miradi ya maji mikubwa ya World Bank Kijiji cha Rungu, Wilaya ya Mbozi lakini pia kuna mradi mwingine Kijiji cha Ihanda tangu imezinduliwa na Mwenge miradi hii haijawahi kutoa maji. Sasa naomba niulize kwa nini miradi inazinduliwa na mwenge lakini haitoi maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa hoja siyo miradi ya kuzinduliwa na Mwenge haitoi maji, nafikiri hoja ya msingi ni kwa nini mradi umezinduliwa lakini hautoi maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika,i naomba niwasihi Wabunge sisi ni Wajumbe wa Kamati za Fedha, Wajumbe wa Baraza la Madiwani. Tusikubali hata siku moja, mradi ambao tunasimamia katika Kamati ya Fedha watu wanakuja kufanya kanyaboya, mradi unazinduliwa hautoi maji na wewe Mbunge upo, niseme kwamba jambo hili ni la kwetu sote. Mheshimiwa Haonga naomba niseme kwamba hili la kwetu sote hatuwezi tukakubali katika jambo hili, kama mradi huo hautoi maji na kwa vile tumekubaliana kwamba baada ya Bunge hili tunakwenda kupiga kazi ngumu Mkoa wa Songwe, tupitie huo mradi twende tukabaini kitu gani kinachoendelea hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku tulinde fedha hizi ambazo wananchi wana shida kubwa ya maji hatuwezi kukubali, sio mbio za mwenge peke yake isipokuwa kiongozi yoyote au mradi wowote unaozinduliwa ni lazima ufanye kazi kama unavyokusudiwa. Kwa hiyo, naomba nimsihi nikifika pale, hata kama ratiba yangu haijawekwa huko naomba aniambie kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri ule mradi uko hapa, lazima tufike hapo site twende kuangalia nini kinaendelea.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mbozi na Wilaya ya Songwe hazijaunganishwa kwa barabara licha ya kwamba Wilaya ya Mbozi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe, lakini wananchi wa kutoka Wilaya ya Songwe kwenda Makao Makuu ya Mkoa ambayo yako Mbozi wanalazimika kupita mkoa mwingine ambao ni Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize sasa, ni lini barabara ya kutoka Kata ya Magamba ambayo inapitia Kata ya Magamba Wilaya ya Mbozi; na hili niliweke vizuri, Magamba hiyo inapatikana Songwe, lakini Magamba nyingine pia inapatikana Mbozi. Kuna uwezekano wa kutengeneza njia kwenda Makao Makuu ya Mkoa kutoka Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini barabara hii itatengenezwa licha ya kwamba Naibu Waziri wa Ujenzi alisema kwamba angeweza kuja Mbozi kuangalia uwezekano na hadi sasa amewadanganya wananchi wa Mbozi, hajafika. Naomba sasa jibu la Serikali.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaunga mkono kabisa mambo ambayo yanaendelea hapa Bungeni, kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge katika kuuliza maswali. Nadhani wakati mwingine ni vizuri tuwe tunawasiliana kimkoa kwanza kujua status ya mambo ambayo tunakuja kuyauliza huku Bungeni. Siyo kitu kibaya wananchi wakifahamu kwamba umekuja kuuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kuna taratibu za ujenzi wa barabara ambazo zinaendelea kupitia TANROADS Mkoa wa Songwe. Ninaamini kama Mbunge angewasiliana na Meneja wa TANROADS Mkoa, asingekuja kuuliza swali kama alilouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Haonga kwamba detailed design tayari, sasa hivi tunafanya utaratibu baada ya kupitia hizo details kuanza kutafuta Mkandarasi wa kujenga hicho kipande cha barabara kutoka Mbozi kwenda Songwe. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mwaka jana mahindi yalishuka bei sana kutokana na Serikali kufunga mipaka hivyo kuwasababishia wananchi hasara kubwa sana kutoka bei waliyouza mahindi awali shilingi 20,000 wakauza shilingi 3,500.
Je, Serikali ipo tayari sasa mwaka huu kuhakikisha kwamba haifungi mipaka ili wananchi waweze kuuza mahindi kwa bei nzuri? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si kweli kwamba Serikali ndiyo inasababisha mahindi yashuke bei bali ni kwa sababu mahindi ni mengi yamezalishwa across region yote wamezalisha vizuri msimu uliopita lakini kwa sababu hili jambo linahitaji umakini katika kulishughulikia majibu mazuri tutayatoa katika hotuba yetu ya bajeti.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mashamba mengi ya kahawa Wilayani Mbozi katika Kata za Magamba, Nambinzo, Iyula na Igamba yameendelea kukauka. Ni lini Serikali itachimba mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji wa kahawa katika maeneo haya ambapo kahawa sasa inaendelea kukauka na hali imekuwa ni mbaya sana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza sisi nchi yetu tunataka kwenda kwenye kilimo lakini kimekuwa na changamoto nyingi sana. Wizara yetu ya Maji na Umwagiliaji tumeona haja sasa ya kuingia katika kilimo cha umwagiliaji. Kama nilivyoeleza, tuna Tume yetu ambayo inapitia maeneo mbalimbali kubainisha yale maeneo ambayo tunaweza tukahakikisha kwamba tunajenga hayo mabwawa. Namwomba kaka yangu Mheshimiwa Haonga, sisi kama Wizara ya Maji na Umwagiliaji hatutakuwa kikwazo kwa wananchi hao katika kuhakikisha tunatengeneza mabwawa hayo ili yaweze kuwa na faida kwa wananchi wao.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani haijawahi kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma, lakini Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ambacho ni chombo cha Serikali kimeongeza makato kutoka asilimia nane hadi asilimia 15. (Makofi)
Je, Serikali iko tayari sasa kusitisha nyongeza hiyo ya makato hadi pale ambapo itaongeza mshahara kwa Watumishi wa Umma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa ongezeko la makato kutoka asilimia nane hadi 15 limewaathiri sana watumishi wa umma maudhurio kazini kwa kukosa nauli.
Je, Serikali haioni kwamba ni muda muafaka sasa kusitisha makato haya ya kutoka asilimia nane hadi 15 kwa kuwa watumishi wengi sasa hawana nauli na suala hili limeweza kuathiri maudhurio watumishi kazini na kupunguza ufanisi wa kazi? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza katika majibu yangu ya msingi Serikali haina mpango wowote wa kusitisha makato ya asilimia 15 ya wanufaika wa mikopo. Naomba kwamba watu wasichanganye mambo kwa sababu unapokata asilimia ya mshahara italipwa kulingana na kiwango chako cha mshahara wewe kama unapata shilingi 100,000 asilimia 15 itakuwa ni ya 15,000 na anayepata milioni moja atalipa 150,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, makato haya yanazingatia uwiano na ukubwa wa mishahara, lakini Serikali haitasitisha kama ambavyo nimesema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaasa na kuwaonya watumishi ambao wanataka kusingizia makato ya asilimia 15 kwa kuchelewa kazini Serikali itachukua hatua za kinidhamu. Kwa sababu watumishi wote wa umma wanapaswa kuzingatia sheria kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi wa umma.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa ni suala la kisera kutengeneza kwa kiwango cha lami barabara zinazounganisha mikoa lakini pia ukizingatia ahadi ya Rais wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Mkapa na ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Kikwete na ahadi ya Waziri Mkuu wa sasa Mheshimiwa Majaliwa kuhusu kutengeneza barabara hii ya kutoka Mlowo Mkoa wa Songwe kupitia Kamsamba kwenda Kwera Mkoa wa Rukwa, ni kwa nini barabara hii imecheleweshwa? Je, hatuoni kama vile tunawadhalilisha viongozi wetu walioahidi ujenzi wa barabara hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali inasema mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 1,439.021 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. Kama fedha hizi zilitengwa mwaka 2017/2018 zaidi ya shilingi bilioni 1.4 yako maeneo mbalimbali ambayo wakati wa mvua yalikuwa hayapitiki, mfano Vijiji vya Sasenga, Itaka, Nambizo, Utambalila na maeneo mengine...
Mheshimiwa Spika, naomba niuliza swali. Je, fedha hizi zilifanya kazi gani ikiwa maeneo mbalimbali yalikuwa hayapitiki msimu wa mvua? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Haonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nakubaliana naye kwamba ni sera ya Serikali kuunganisha mikoa na mikoa na kuunga mikoa na nchi za nje na utekelezaji wake unaendelea katika maeneo mbalimbali. Nafurahi kusikia Mheshimiwa Haonga anakumbushia ahadi za Waheshimiwa Marais na Waheshimiwa viongozi wetu. Kwa kweli akubaliane na mimi tu kwamba zile ahadi zilizotolewa kipindi cha nyuma ndiyo zimesababisha hata ujenzi wa hili daraja kuanza na pia usanifu na hatua mbalimbali za manunuzi zinaendelea. Kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi kwamba ule utekelezaji wa ujenzi wa barabara kama ahadi zilivyokuwa unaendelea kutekelezwa na tutaendelea kutekeleza na nimhakikishie tutaendelea kutekeleza kwa kasi zaidi.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho tumepita, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kuhakikisha madeni mengi sana ya wakandarasi maeneo mbalimbali ya nchi yanalipwa. Kwetu sisi ni fursa sasa ya kuongeza kasi kwa ajili ya kuendeleza kukamilisha huu ujenzi. Kwa hiyo, tutaenda kuungana na wenzetu wa kule Rukwa kupitia barabara hii. Nimhakikishie Mheshimiwa Haonga baada ya Bunge hili nitaipita barabara hii ili niweze kuona pia hali ilivyo tuweze kushauriana vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili anasema kwamba katika kipindi kilichopita tulikuwa tumetenga fedha lakini wakati huu wa mvua kumekuwa na uharibifu na haoni sababu kwa nini sasa maeneo hayapitiki. Mheshimiwa Haonga ajue mwaka huu ulikuwa wa neema kwa upande mwingine lakini kwenye miundombinu kumekuwa na uharibifu. Ilikuwa siyo rahisi wakati mvua zinaendelea kunyesha twende kufanya matengenezo. Baada ya mvua kupungua, nimhakikishie Mheshimiwa Haonga, tunarudi sasa kurejeshea sehemu ambazo zilikuwa korofi wakati hatua ya kuimarisha barabara na kujenga katika kiwango cha lami inaendelea, maeneo yote ambayo yalikuwa yameharibika tunaenda kuyafanyia marekebisho.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, zile fedha ambazo zilikuwepo kwa ajili ya emergency zitatumika kwa ajili ya kuhakikisha barabara hii inatengenezwa. Kama nilivyosema, nitapita maeneo ambayo yatakuwa maalum zaidi tutaendelea kuzungumza kuona namna nzuri ya kushirikiana. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, naskushukuru sana. Naomba na mimi niulize swali la nyongeza. Skimu nyingi za umwagiliaji ambazo ziko Mbozi, Kata ya Bara kuna Skimu ya umwagiliaji ambayo ni ya miaka mingi sana, miundombinu yake imechoka na skimu hii haifanyi kazi vizuri. Sasa Mheshimiwa Waziri yuko tayari kukarabati skimu hii ya umwagiliaji ambayo iko Kata ya Bara ili iweze kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Bara, Kata ya Bara, Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, awali ya yote kama nilivyokuwa nimeeleza kwamba, katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji tumeona kabisa tumekuwa na changamoto katika suala zima la umwagiliaji. Moja ya changamoto tumekuwa na miradi mingi lakini haijakamilika, tunapitia mapitio yetu kabambe lakini nataka nimhakikishie, maeneo yote ambayo miradi haijakamilika sisi kama Wizara ya Maji na Umwagiliaji tutahakikisha tunaikamilisha ili wananchi wale waweze kufaidika katika suala zima la umwagiliaji.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo la barabara katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu linafanana kabisa na tatizo la barabara katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo katika Jimbo la Mbozi. Naomba kuuliza, ni lini sasa Serikali itatengeneza barabara ambazo zipo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo, Jimbo la Mbozi, ambazo wakati wa mvua mara nyingi zimekuwa hazipitiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli. Tatizo alilolisema Mheshimiwa Mbunge katika eneo lake ni tatizo ambalo limekuwa likiikabili nchi nzima wakati wa masika wakati mvua kubwa zikinyesha, hasa barabara zetu ambazo huwa zinaathirika sana ni barabara za udongo na barabara za changarawe, ukiacha barabara za lami ambazo maeneo machache, hasa ya madaraja ndio huwa yanaathirika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimpe ndugu yangu comfort kwamba, suala hilo linatambulika Serikalini. Katika tathmini ambayo tunaifanya tumezingatia hilo ili tuwe na backup ya kutosha wakati wa mvua kuweza kukabiliana na changamoto ambazo huwa zinajitokeza wakati wa masika.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Jimbo la Mbozi lenye kata 11 kuna kata mbili ambazo karibu vijiji 14 havina umeme kabisa. Sasa naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa hizi kata mbili za Magamba na Kata ya Bara zitapatiwa umeme wa REA? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme mpango wa Serikali ni kupeleka umeme katika maeneo yote ambayo yamesalia, vijiji 7,873. Kwa hiyo, kwa kuwa swali lake limejielekeza kwenye kata mbili ambazo zina vijiji 14 na hakuna umeme kabisa, nataka nimuarifu kwa kipindi hiki cha 2018/2019 – 2019/2020 Serikali itakamilisha upelekaji wa umeme katika maeneo ya hizo kata mbili na vijiji vyake kwa mradi huu kabambe wa REA Awamu ya Tatu unaoendelea kutekelezwa ndani ya mwaka huu wa fedha na unaoendelea. Ahsante.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Changamoto za zao la tumbaku zinafanana kabisa na changamoto zinazokabili zao la kahawa. Suala hili la pembejeo hasa mbolea imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa sababu wakulima wa kahama wengi wanashindwa kulima kahawa vizuri, wanashindwa kuhudumia mashamba ya kahawa kwa sababu ya bei kubwa ya mbolea. Licha kwamba Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea wa Pamoja lakini bado haijawa suluhu kwa wakulima wa zao la kahawa. Je, ni lini sasa Serikali itajenga viwanda vya mbolea nchini ili angalau sasa mbolea iweze kushuka bei na wakulima wa kahawa waweze kunufaika na uzalishaji uweze kuongezeka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumkaribisha Mheshimiwa Haonga pamoja na Wabunge wengine, leo tuna kikao cha wadau wa kahawa kinafanyika hapa Dodoma, kimeanza saa mbili na nusu. Kwa hiyo, baada ya maswali na majibu tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge kushiriki kikao hiki na tuweze kupata maoni yenu ili kuboresha mfumo wa ununuzi wa kahawa hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Mheshimiwa Haonga la lini Serikali itajenga viwanda vya mbolea, majibu ya Serikali ni kwamba inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha tunajenga viwanda vya mbolea hapa nchini ikiwemo utumiaji wa gesi asilia ambayo tumeigundua ili kutengeneza mbolea na kusaidia wakulima wetu waweze kupata mbolea hapa hapa nchini na kwa bei nafuu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mwaka 2016, Serikali ilitutaka sisi Wabunge kuorodhesha vijiji, vitongoji pamoja na mitaa yote ambayo haina mawasiliano na sisi Wabunge tulifanya hivyo, tukaorodhesha vijiji vyetu vingi sana. Jimbo langu la Mbozi niliorodhesha vijiji vingi sana kikiwepo Kijiji cha Mbozi Mission ambacho kina hospitali kubwa na taasisi nyingi kama vyuo, hakina mawasiliano, Kijiji cha Maninga, vijiji vingi sana Jimbo la Mbozi havina mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijue kwa nini Serikali ilituambia sisi Wabunge tupeleke orodha ya vijiji na maeneo ambayo hayana mawasiliano lakini mpaka sasa maeneo hayo hatujapata mawasiliano. Je, Serikali ilikuwa inadanganya Wabunge?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwaka 2016 tuliwaomba Waheshimiwa Wabunge waorodheshe maeneo mbalimbali ya majimbo yao ambayo hayana mawasiliano. Kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tulifanyia kazi maeneo mengi sana na ndiyo maana mpaka sasa hivi kwa mawasiliano takwimu zinasema Watanzania tunawasiliana kwa asilimia 94. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yake ya Mbozi Mission na mengine aliyoyazungumza inawezekana kabisa kwenye orodha ambayo tunategemea kuitangaza mwisho wa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi wa tano yakawemo na hivyo atapata mawasiliano. Hiyo ndiyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mtumishi anapokuwa anaajiriwa, mara ya kwanza na kwenye salary slip yake inaonesha muda atakaostaafu, hivyo inakuwa siyo suala ambalo ni la ghafla, lakini Serikali imekuwa ikichelewa sana kuwalipa watumishi hawa: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka inapokuwa wamesababisha ucheleweshwaji wa mafao kwa watumishi wa Umma inataikiwa walipe kwa riba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Halmashauri ya Mbozi kuna watumishi 35 wamestaafu toka Septemba, 2018, hadi sasa hawajalipwa fedha zao na wanaidai Serikali na wanaishi maisha magumu sana: Je, ni lini sasa Serikali itaacha kuwatesa watumishi hawa wanaoishi maisha ya taabu sana kwa sababu ya ucheleweshaji wa fedha zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Haonga amezungumza kuhusu ucheleweshwaji wa ulipaji wa mafao. Kwa mujibu wa sheria ambayo tumeipitisha hapa ndani Bungeni hivi sasa, inautaka mfuko kulipa mafao ya mstaafu ndani ya siku 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zilikuwepo changamoto nyingi hapo awali, nyingi sio kwambwa zinasababishwa na mfuko husika lakini pia wale wastaafu katika namna moja ama nyingine katika uandaaji wa nyaraka na kufuatilia taarifa zao imekuwa pia ikileta changamoto. Baada ya kuunganisha mifuko hii na kwa kutumia sheria mpya, hivi sasa PSSF wameweka utaratibu na motto wao ni kwamba wanalipa mafao tangu jana.

Mheshimimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa zoezi la ulipaji wa mafao kwa wastaafu linafanyika kwa kiwango kikubwa sana na kwa idadi ambayo nimesema tayari imeshalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu watumishi katika Jimbo lake la Mbozi, kwa sababu hii inakwenda case by case, nisilisemee kwa ujumla, lakini nichukue tu fursa hii kumwambia Mheshimiwa Haonga kwamba ofisi yetu iko wazi, kama kuna madai ya watumishi ambao mpaka hivi sasa bado hawajalipwa mafao yao, basi anaweza kuyasilisha ili sisi Ofisi ya Waziri Mkuu tuweze kufuatilia mkoa husika tujue changamoto ni nini na baada ya hapo tuweze kutatua changamoto yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kulipa mafao yao kwa wakati kabisa ili kuwafanya watumishi hawa waishi katika maisha ya amani.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mwaka 2018 kwa maana ya mwaka uliopita Serikali ilipora fedha za wakulima wa korosho zaidi ya bilioni 300 ambazo zilikuwa ni za export levy na kusababisha wakulima wa korosho kushindwa kununua sulphur. Mwaka huu tumeona uzalishaji wa korosho ulikuwa wa chini sana kwa sababu wakulima wanashindwa kununua sulphur.

Je, Serikali ipo tayari sasa msimu huu wa korosho unaokuja kuweza kugawa sulphur bure kwa wakulima wa korosho ili tija iweze kuongezeka katika uzalishaji wa korosho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa bei ya kahawa imeendelea kuwa chini mwaka hadi mwaka na hali hii imetokana na suala la pembejeo kuwa juu sana wakati bei ya kahawa imeendelea kuwa chini kabisa. Je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha mfuko wa kuimarisha bei kwenye zao la kahawa yaani Price Stabilization Fund ili pale kahawa inaposhuka bei Serikali iweze kufidia kupitia mfuko huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua kuhusu suala la export levy, kwanza sio kweli, Serikali haijapora pesa za wakulima wa export levy, wakulima wa korosho kule Mtwara. Haya yalikuwa ni mapato ya Serikali kama mapato mengine na tulileta mapendekezo hapa na yalipitishwa na Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, Serikali ilichofanya ni utekelezaji wa sheria ile ambayo ilipitishwa na Wabunge akiwepo Mheshimiwa Haonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu kahawa kwamba tuanzishe mfumo wa price stabilization kwa ajili ya kufidia pale bei zinapoanguka. Kwanza, ni wazo zuri ambalo na sisi Serikali tunalipokea. Lakini katika mazao sio la kahawa peke yake ambayo yanaanguka katika masoko ya dunia, ni suala la msingi, sio bei. Hatuna uwezo wowote wa ku-control bei katika soko la Kimataifa. Uwezo wetu sisi ambao tumegundua kama Serikali ni tija ndogo wanayoipata wakulima katika mazao kwamba wanatumia gharama kubwa lakini wanachokipata ni kidogo na ndiyo maana sasa hivi tunaimarisha mfumo wa upatikanaji pembejeo ili kuongeza tija kwa wakulima, watumie gharama ndogo wapate mavuno vizuri ili tuweze kushindana katika masoko ya ndani na ya nje ambayo hatuna uwezo wa kupanga bei.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Mji Mdogo wa Mlowo ulioko Wilaya ya Mbozi una wakazi wapatao elfu 70 na zaidi, lakini bahati mbaya sana mji huu una zahanati tu ambayo inahudumia watu hao zaidi ya 70,000.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kujenga kituo cha afya ili kuweza kuwahudumia wale wananchi ambao ni wengi na wanapata tabu sana na wanasumbuka wakati wa kupata matibabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mwalimu Paschal Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanza kujenga vituo vya afya awamu ya kwanza bajeti hii ya 2019/2020 awamu ya pili, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge awamu ya tatu tutazingatia maeneo yote ambayo hayajapata huduma hii, likiwepo Jimbo lake la Mbozi na hasa eneo mahususi ambalo amelitaja hapa asubuhi.
MHE. PASCAL Y. HAO NG A: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa katika majibu ya Serikali ni kwamba zimetengwa milioni 37 zitakazotumika katika kuboresha wodi ya akina mama wanaojifungua; na kwa kuwa wodi hiyo ni wodi ambayo kwa kweli akina mama wanapata shida, wanalala akina mama wawili katika kitanda kimoja na kuna msongamano mkubwa sana;

Je, Serikali sasa inaweza ikatupa majibu rasmi wana Mbozi na wana Songwe kwamba hizo fedha ni lini sasa zitakwenda rasmi? Kwasababu tatizo hili si dogo, ni kubwa sana. Akina mama wanapata shida na wanaweza kupata magonjwa kwasababu kuna msongamano ambao kwa kweli si wa kawaida?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa pia katika Hospitali hii ya Wilaya ya Mbozi ambayo pia inatumika kama Hospitali Teule ya Mkoa wa Songwe kuna tatizo la ufinyu wa OPD; na OPD iliyopo pale ni ndogo sana na kuna msomngamano mkubwa sana.

Je, Serikali ipo tayari sasa kufanya upanuzi wa ile OPD ili iweze kuboreshwa na ichukue wagonjwa walio wengi zaidi kuliko hali iliyoko sasa ambayo wagonjwa ni wengi na OPD ni ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kujibu maswali yote mawili ya Mheshimiwa Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nimemwmbia Mheshimiwa Mbunge commitment ya Serikali kwamba katika bajeti ya mwaka 2020/2021 milioni 37 zimetengwa. Tafsiri yake ni nini? Ni kwamba hiyo inaonesha seriousness ya Serikali katika kuahidi na kuweka katika maandishi. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali, tukiahdi tunatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaongelea juu ya suala zima la ufinyu wa wodi, kwa maana kunakuwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa katika ile hospitali ambayo inatumika kama ndiyo hospitali ya rufaa ya Mkoa. Ni ukweli usiopingika kwamba hospitali ile mwanzo haikuwa imekusudiwa kuwa hospitali ya Mkoa; lakini pia ni ukweli usiopingika Serikali imekuwa ikifanyakazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba huduma ya afya inasogezwa na ndiyo maana hata ukienda kwa Mheshimiwa Haonga unakuta kuna kituo cha afya cha Kisansa ambacho tukienda tukafanya shughuli nzuri na yeye ni shuhuda. Aendelee kuiamini Serikali, kwamba tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba pale ambapo inahitajika tufanye upanuzi tutafanya pasi na kusita.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana mwaka 2016 Serikali ilituambia sisi Wabunge tuweze kuorodhesha maeneo yote ambayo hayana mawasiliano Wabunge tulifanya hivyo na tena mwaka huu Serikali ikatuambia tuweze kufanya hivyo tena, na mimi baadhi ya maeneo yangu kwa mfano kata ya Halungu, Kata Nambizo, Bara Magamba, Itaka na maeneo mengine hayana mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali sasa itapeleka mawasiliano ya simu katika maeneo hayo ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, niseme tu kama nilivyozungumza, tumekuwa tukiwasiliana na Waheshimiwa Wabunge vizuri ili kutatua tatizo la changamoto ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali. Na kupitia huu utaratibu ambao tunaufanya kupata maoni na ushauri wa Wabunge ndiyo maana katika Awamu ya IV tumekuja na orodha kubwa sana ambayo tunaendelea kutatua matatizo yaliyokuwa maeneo yetu, vijiji 1222, ni vijiji vingi sana lakini kupitia kwenye awamu zilizopita tumeendelea kufanya hivi ninavyozungumza iko miradi mingine ambayo inaendelea wakati tutakuja na awamu nyingine ya nne. Kwa hiyo, Mheshimiwa Haonga nikutoe hofu tu kwamba ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba suala la mawasiliano litakuwa kwa wote kama tulivyoanzisha mfuko na nishukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Bunge lako kuanzisha Mfuko wa mawasiliano kwa wote umekuwepo kwa miaka kumi na kazi kubwa sana imefanyika ili kuhakikisha mawasiliano yanakuwa bora katika maeneo ya nchi yetu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli aliahidi kwamba kabla ya kufika mwaka 2020, barabara hiyo ya kutoka Mlowo kwenda Kamsamba hadi Kibaoni itakuwa imekamilika. Ukiangalia kuanzia sasa hadi mwaka 2020 bado miezi michache tu. Je, ni lini sasa ahadi hii ya Serikali itatekezwa kwa vitendo badala ya maneno?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika majibu ya Serikali kwamba kukamilisha usanifu wa kina hawajataja kwamba ni lini usanifu wa kina utakamilishwa. Je, Serikali kutotaja muda wa kukamilisha usanifu wa kina haioni huku ni kutowatendea haki wananchi wa Mikoa ya Songwe, Katavi, pamoja na Rukwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, umetaja ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni, lakini ujenzi wa barabara ni mchakato, lazima ufanye upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, baadaye uingie mikataba uanze kujenga. Hauwezi ukafanya kabla ya kukamilisha hizo hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vipande vya barabara ambavyo unavizungumzia tayari kuna kimoja mwezi huu wa tisa cha kutoka Mlowo kwenda mpaka pale tulipokamilisha daraja, mwezi wa tisa usanifu wa kina utakamilika baada ya hapo mambo mengine yanaanza. Upembuzi yakinifu umeanzia kule Muze unakuja kuunga Kamsamba, na tuna matarajio ya kuendelea huko na pia tumeshaanzia Inyonga kuja mpaka Maji ya Moto. Kwa hiyo, utaratibu unaendelea ahadi ya Mheshimiwa Rais inatekelezwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi na wananchi jirani zangu wa kule wawe na uhakika kwamba barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Kwa kuwa barabara hii inapita eneo muhimu sana eneo ambalo wanachimba makaa ya mawe, Kijiji cha Magamba, na kwa kuzingatia pia kwamba barabara hii inaunganisha wilaya mbili kwa maana ya Wilaya Mbozi pamoja na Wilaya ya Songwe, je Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuanza kufikiria kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa sehemu (b) ya swali hili haikujibiwa, inayohusu vivuko pamoja na madaraja Kata za Itumpi, Halungu, Itaka pamoja na Bara, je, Serikali inawaambia nini wananchi wa maeneo haya ambao wanakosa mawasiliano ya vivuko na wanakosa maeneo ya kuvukia; je, Serikali inawaambia nini na kwa kutokujibu vizuri swali hili, je, Serikali haioni kwamba wananchi hawa wataendelea kuteseka kwa kuwa maeneo mengi hawa wananchi hata kuvuka kutoka kijiji kimoja kwenda kingine inakuwa ni shida kubwa sana? Je, Serikali haioni kuwa ni kuwatesa wananchi wa maeneo haya?.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, Mheshimiwa Mbunge Sera ya Chama cha Mapinduzi, Sera ya Wizara ni kuunganisha mikoa kwa lami; lakini tunaendelea kuziunganisha wilaya kwa barabara za changarawe. Itakapofikia tumemaliza kwanza sera yetu ya kuunganisha mikoa kwa lami; na nishukuru kwamba Mkoa wako tayari umeshaunganishwa kwa lami tutaendelea sasa na barabara za wilaya, kwa hiyo uvute subira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madaraja na vivuko, sijui tofauti yake ni nini, lakini nafikiri umezungumzia madaraja; suala la madaraja tunaendelea kujenga kwenye barabara zote za TANROADS pamoja na barabara za TARURA pia. Kwa hiyo tutaendelea kujenga kadiri ya ukusanyaji wa fedha kutoka kwenye Mfuko wa Barabara. Nina imani na wewe mwenyewe unafahamu, TARURA sasa hivi inakwenda vizuri, matatizo yake tu ni kwamba fungu halijawa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwa sababu linatokana na Mfuko wa Barabara na kuna Kamati inaendelea sasa ili iweze kuweka uwiano ambao ni mzuri kulingana na barabara za TARURA baada ya muda tutakuwa na hela ya kutosha madaraja hayo ambayo unayaita vivuko pia yatajengwa.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, Mbozi katika Kijiji cha Harungu Wilaya ya Mbozi tuna mradi mkubwa wa maji ambao karibu milioni 600 ya World Bank na mradi huu una vituo kama 24 ilikuwa iwe na vituo 24 vya kuchotea maji lakini kwa bahati mbaya sana ule mradi wanasema kwamba umekamilika wakati vituo vinavyotoa maji kati ya 24 ni vituo vinne tu.

Je, Mheshimiwa Waziri, nini tamko lako kuhusu mradi huo ambao ni wa fedha nyingi lakini vituo vingi havitoi maji na tenki lile linavuja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutupa taarifa. Nimuagize tu Mhandisi wa Mkoa wa Songwe atupatie taarifa kama ulivyosema ili kuhakikisha kwamba tunalichukulia hatua haraka hili jambo. Ahsante sana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa fedha zote ambazo zinakusanywa kutokana na utalii wa Kimondo Mbozi huwa zinachukuliwa na Serikali kuu na hakuna hata shilingi moja ambayo imewahi kurejeshwa kwa wananchi wa Kijiji husika cha Ndolezi na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi: Je, Serikali haioni kwamba huu ni ubaguzi kwa wananchi wa Wilaya ya Mbozi kwa sababu maeneo mengine yenye utalii, wananchi hurejeshewa sehemu kidogo ya fedha zilizotokana na utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Vivutio vya Utalii vya Majimoto pamoja na Mapango ya Popo vimekuwepo kwa muda mrefu sana tangu uhuru. Je, Serikali kwa nini inaendelea kusuasua kutenga bajeti ya kuviendeleza vivutio hivi vya utalii ambavyo vipo katika Kijiji cha Nanyala, Kata ya Nanyala, Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu ni kwa nini Serikali imekuwa ikikusanya pesa hizi na kutokuzirudisha Halmashauri? Jambo hili siyo kweli.

Mheshimiwa Spika, unafahamu kwamba maduhuli yote yanayokusanywa na Taasisi mbalimbali za Setikali yanachangia katika mfuko Mkuu wa Serikali na pesa hizo ndizo zinazorudi kwa ajili ya uendeshaji wa huduma mbalimbali za jamii zikiwemo hospitali, kulipa walimu pamoja na mambo mengine na ujenzi wa miundombinu. Kwa hiyo, makusanyo haya yanayofanyika katika Serikali siyo lazima yarudi kama token kwenye Halmashauri, bali yanarudi kwa style ambayo wananchi wote katika Mkoa wa Songwe wanapata.

Mheshimiwa Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kimsingi jukumu la kuleta watalii na kuongeza mapato kwenye Halmashauri yake linaweza pia kufanywa na yeye. Kama mnavyofahamu, pamoja na kwamba tunapata watalii milioni 1.5 Tanzania, sehemu kubwa ya watalii hawa wanaokuja Tanzania wanatafutwa na wadau wa utalii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhamasishe Mheshimiwa Mbunge kuihamasisha Halmashauri yake na yeye mwenyewe kukitangaza kivutio hiki cha utalii, lakini pia kuweka miundombinu kwa kushirikiana na Halmashauri ili kuweza kuingiza mapato mengi zaidi kwenye Wilaya yake.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amesema kwamba tumekuwa tukisuasua katika kutangaza Majimoto. Hatujasuasua, nimemweleza katika jibu langu la msingi Mheshimiwa Mbunge kwamba Majimoto haya na Pango la Popo tumeviingiza katika kumbukumbu za Serikali. Jukumu la kuvitangaza na kuvifanya vilete watalii linaweza kufanywa na mtu mmoja mmoja. Kama mnavyofahamu, ni kwamba sisi kama Serikali tunasimamia sera lakini jukumu la mtu mmoja mmoja linaweza kutangaza kituo kile na kuleta watalii na kuongezea Serikali mapato.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, katika Wilaya ya Mbozi kumekuwa na usumbufu mkubwa sana kwa vijana wa bodaboda ambao wameamua kujiajiri ili kuweza kujikimu katika maisha na wamekuwa wakinyanganywa pikipiki hasa katika Mji Mdogo wa Mlowo pamoja na Mji wa Vwawa na maeneo mengine wamekuwa wakisumbuliwa sana na pikipiki zao zimekuwa zikichukuliwa kupelekwa Vituo vya Polisi.

Je, Serikali haioni kwamba huko ni kuwanyanyasa vijana ambao wameamua kujiajiri kupitia kazi hii ya bodaboda inayo wapatia kipato wao na wengine wameamua kuachana na maisha yao ya awali ambao hayakuwa mazuri wameamua kujiajiri. Sasa ni lini Serikali itakataza askari wasiwanyanyase vijana hao ambao wanafanya kazi hii ya bodaboda katika Wilaya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, hatukubali kuona wala haturuhusu kuona askari wakinyanyasa wananchi. Si jukumu la askari kunyanyasa wananchi, lakini kuhusiana na suala ambalo amelizungumza kuhusiana na jimbo la Mbozi kuhusu vijana hawa ambao anadai kwamba wananyanyaswa na waendesha bodaboda nisema yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza hili tulishalitolea maelekezo hapa Bungeni kwamba kuna aina ya makosa ambayo pikipiki zikikamatwa zinakuwa katika Vituo vya Polisi kuanzia sasa na tumeshatoa waraka huo katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ili wautekeleze. Sasa sina hakika kama hawa anaowazungumzia Mheshimiwa Haonga wapo katika yale makosa ambayo tumeyaruhusu waweze kukamatwa ama katika makosa ambayo tulishakata yasikamatwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachoweza kumhakikishia ni kwamba tutafuatilia kujua kama yatakuwa makosa ambayo tulishaelekeza yasikamatwe vijana hao basi tutachukua hatua kwa kushindwa kutekeleza maelekezo ya Wizara. Lakini kama itakuwa ni makosa ambayo yanaruhusika na tumeruhusu waweze kukamatwa basi tutamuelimisha Mheshimiwa Haonga ili aweze kuelimisha wananchi wake wafahamu na waepuke kufanya makosa kama hayo.