Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Pascal Yohana Haonga (13 total)

MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
(a)Je, ni lini Serikali itaweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo kama vile mbolea ili kuwapunguzia Wakulima ghaarama za uzalishaji?
(b)Je, ni lini Serikali itaanzisha Mfuko Maalum wa Zao la Kahawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya mbolea na mbegu za kilimo tangu mwaka 2007/2008. Kwa lengo la kumpunguzia mkulima gharama. Mathalani katika msimu huu wa kilimo Serikali imetoa ruzuku kwenye mbegu bora na mbolea za kupandia na kukuzia kwa mazao ya mahindi na mpunga kwa utaratibu wa vocha kwa kaya laki tisa tisini na tisa elfu mia tisa ishirini na sita mikoani. Aidha, Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya madawa na mbegu bora kwenye mazao ya pamba na korosho. Vilevile kwa mazao ya chai na kahawa ruzuku imekuwa ikitolewa kwenye miche bora ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao hayo.
(b) Mheshimiwa Spika, tasnia ya kahawa tayari imekwishaanzisha Mfuko wa Zao la Kahawa kutokana na azimio la Mkutano Mkuu wa wadau wa kahawa uliofanyika Mei, 2011. Mfuko huu ulizinduliwa rasmi Januari, 2013 na tangu kuanzishwa kwake Mfuko unaendelea kutekeleza majukumu yake kutokana na michango ya wadau.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayokabili Mfuko huo ni kukosa mitaji ya kutosha kutoa huduma zote zilizokusudiwa kwa kuwa michango ya wadau ni midogo. Mfuko unaandaa mkakati wa kutafuta mtaji kutoka taasisi za fedha ili waweze kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa ikiwa ni pamoja na mikopo ya pembejeo kwa wakulima wa kahawa.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Shirika la NAFCO Magamba limeshindwa kuyaendesha mashamba yaliyochukuliwa kutoka kwa wananchi na kuwakosesha maeneo ya kulima na mara nyingine kuwakodishia kwa gharama kubwa.
Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka wa kuyarejesha mashamba hayo kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, kwa sasa Serikali haiwezi kulirejesha shamba hilo kwa wananchi kwa kuwa lipo kimkakati kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mbegu za kutosha ili kukidhi mahitaji ya mbegu nchini. Vilevile kupitia shughuli za uzalishaji mbegu, wakulima hupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na madawa ya kilimo na utunzani wa shamba, pia kusambazia teknolojia mpya za kilimo bora.
Aidha, tayari Serikali ilichukua hatua za kurejesha mashamba nane ya kahawa ya Ngamba, Shishiwanda, Ihanda, Ndugu I, Ndugu II, Tukumbi, Ruanda na Ishera ambayo yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ili kuyagawa au kuyauza kwa wananchi kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ambapo baadhi yao wamepatiwa hati miliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, tayari alishatembelea shamba hilo, akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa, Mbunge wa Mbozi mwenyewe, wataalam wa ASA na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi. Katika ziara hiyo, wataalam wa ASA na Halmashauri walitoa maelezo kuwa kuna kipindi cha kupumzisha shamba kwa mwaka mmoja au miwili ili kuongeza rutuba ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu hizo za kitaalam zinaweza kutafsiriwa kuwa shamba hilo halitumiki ipasavyo. Aidha, baada ya ASA kukabidhiwa shamba hilo na Shirika Hodhi la CHC, hakuna wakulima waliowahi kukodishwa shamba hilo, bali ASA imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu kwenye shamba hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliopo wa kuzalisha mbegu ni pamoja na kupanua wigo wa ushirikiano ili Kampuni zaidi zishiriki katika uzalishaji wa mbegu kwa kutumia shamba hili. Vilevile kuhamasisha vikundi vya vijana ili washirikiane na ASA katika uzalishaji wa mbegu. Mwisho, kuweka miundombinu muhimu iliyohitajika katika uzalishaji ikiwemo kuunganisha umeme wa gridi na kujenga miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Katika Kijiji cha Isenzanya Wilayani Mbozi, shamba lenye ukubwa wa hekari 1,000 linalohodhiwa na Mzungu aitwaye Joseph Meya halijaendelezwa kwa miaka mingi sasa huku wananchi wa kijiji hicho wakiwa hawana maeneo ya kilimo:-
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kulirejesha shamba hilo kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwana Joseph Meier na Bi. Enala Mgala kwa pamoja wanamiliki shamba lenye ukubwa wa hekta 330.16 ambayo ni sawa na ekari 825.4 kwa Hati Na. 257 MBY LR lililopo katika Kijiji cha Isenzanya, Wilaya ya Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wamiliki hawa wameendeleza kipande kidogo cha shamba hili kwa kupanda kahawa na mazao ya msimu kama mahindi na maharage. Hata hivyo, kutokana na mahitaji ya ardhi kuongezeka, wananchi wa Kijiji cha Isenzanya kwa nyakati tofauti kupitia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi wamekuwa wakiiomba Serikali kuwapatia ardhi hiyo ili waitumie kwa kilimo. Katika kutekeleza azma hiyo, November 2015 Mkurugenzi wa Halmashauri alifanya mkutano uliojumuisha wamiliki na wanakijiji wa Kijiji cha Isenzanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mkutano ukaguzi wa shamba kufanyika mpaka sasa mazungumzo na wamiliki wa shamba yanaendelea. Aidha, Sheria ya Ardhi, Namba 4 ya Mwaka 1999 imeeleza wazi namna ya utoaji wa maeneo pale ambapo mmiliki anakiuka masharti yake. Halmashauri kupitia Afisa Ardhi Mteule inayo mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa sheria husika. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati Serikali ikiendelea na utaratibu wake.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha Chuo cha Kilimo Wilaya
ya Mbozi ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi wanaohitimu kidato cha nne na cha sita Mkoa wa Songwe na maeneo mengine nchini ili waweze kupata mafunzo kwenye chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa Chuo cha Kilimo katika Wilaya, Mkoa na Taifa ni muhimu kwa kuwa kinasaidia kujenga nguvukazi wataalam na wakulima kifikra na kimtizamo katika kuongeza uzalishaji na tija katika nyanja ya kilimo kwenye eneo husika. Hivyo chuo cha kilimo kikianzishwa katika Wilaya ya Mbozi kinaweza kuchochea maendeleo ya uzalishaji na usindikaji wa mazao yanayozalishwa Wilayani hapo ikiwemo kahawa, mahindi, maharage na matunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuanzisha chuo
cha kilimo kuna gharama kubwa kwa ajili ya kujenga miundombinu, kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuajiri rasilimaliwatu kwa ajili ya kazi za mafunzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wakati huu vipo vyuo vitatu vya Serikali Mkoani Mbeya vinavyotoa mafunzo ngazi ya Stashahada na Astashahada. Vyuo hivi ni Uyole, Igurusi na Inyala vyenye uwezo wa kuwa na wanafunzi takribani 700 kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP II) Wizara itaboresha Vyuo vya Kilimo vya Uyole, Igurusi, Inyala pamoja na vyuo vingine kwa kujenga miundombinu, kuongeza upatikanaji wa vifaa, kuongeza rasilimali watu na kadhalika ili viweze kudahili wanafunzi wengi zaidi wakiwepo wanaotoka Wilaya ya Mbozi.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Kigezo kimojawapo cha kuwanyima mkopo waombaji wa mkopo ya elimu ya juu ni kama muombaji alisoma shule za binafsi.
(a) Je, Serikali haioni kuwa baadhi ya wanafunzi hulipiwa ada ya shule za binafsi na ndugu, jamaa, marafiki na NGO’s hivyo wanafunzi hao wanapofikia elimu ya juu hushindwa kumudu gharama za elimu hiyo?
(b) Je, Serikali ipo tayari kufuta kigezo hicho ili kuwapatia waombaji wa mikopo haki yao ya kupata elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga Mbunge wa Mbozi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa za msingi za kupata mkopo wa elimu ya juu zinaainishwa katika kifungu cha 17(1) cha Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya 2004 (Sura ya 178) ya Sheria za Tanzania kama ifuatavyo; awe Mtanzania, awe amedahiliwa kwenye chuo kinachotambulika, awe ameomba mkopo kwa njia ya mtandao, awe hana chanzo kingine cha kugharamia elimu yake. Mbali na sheria, vigezo vingine ni uyatima, ulemavu, uhitaji na mahitaji ya rasilimalwatu kwa ajili ya vipaumbele vya maendeleo vya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuwasilisha maombi ya mkopo wa elimu ya juu muombaji hutakiwa kuwasilisha taarifa muhimu zikiwepo shule au vyuo alivyosoma kabla ya kujiunga na elimu ya juu. Bodi ya Mikopo hutumia taarifa hizi ili pamoja na mambo mengine kubaini historia ya uchangiaji wa gharama za elimu katika ngazi ya sekondari au chuo ili kumpangia mkopo stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale inapothbitika kwa maandishi kwamba mwanafunzi husika alisaidiwa au kufadhiliwa na ufadhili huo umekoma Bodi ya Mikopo huwakopesha kwa kuzingatia hali zao za kiuchumi kwa wakati huo. Kwa mfano, katika mwaka wa masomo wa 2016/2017 jumla ya wanafunzi 719 waliothibitika kufadhiliwa au kusaidiwa katika masomo yao ya sekondari walipata mkopo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Wakulima wa Wilaya ya Mbozi wamekuwa wakitegemea mvua za msimu zisizotabirika katika kilimo chao.
Je, Serikali haioni kwamba huu ni wakati muafaka wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya hivi karibuni, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeanza kuathirika na vipindi vya ukame hata wakati wa msimu wa mvua, tofauti na ilivyokuwa miaka ya huko nyuma. Kutokana na hali hiyo, halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilikwishaanza kutekeleza mipango ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika wilaya hiyo kupitia mipango ya kuendeleza kilimo cha wilaya. Kupitia mipango hiyo, Skimu za Umwagiliaji za Sasenga (hekta 540), Iyula (hekta 180), Songwe (hekta 250), Bara (hekta 300), Mbulu Mlowo (hekta 100), Mkombozi (hekta 150), Ikumbilo Chitete (hekta 60), Ruanda Mbulu (hekta 52) na Wasa (hekta 45) ziliainishwa na kuanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ina mpango wa kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo yanayofaa kujengwa mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa maji ya umwagiliaji kwa ajili ya Skimu za Nambizo, Msia na Hamwelo katika Halmashauri hiyo.
Aidha, kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Halmashauri zote zinazotekeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.
MHE. JOESPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. PASCAL Y. HAONGA) aliuliza:-
Shule za Watu Binafsi zinatoa huduma ya elimu kama zilivyo Shule za Umma, lakini kwa muda mrefu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo (property tax), tozo ya fire, kodi ya ardhi na kodi nyinginezo:-
(a) Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuondoa baadhi ya kodi zisizokuwa na tija ambazo zimekuwa kero kwa shule za watu binafsi?
(b) Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kuzipatia ruzuku shule binafsi kwa sababu zinashirikiana na Serikali kupunguza tatizo la ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Hasunga, Mbunge wa Mbozi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya elimu nchini ambapo hadi sasa jumla ya shule za msingi 1,432 kati ya shule 17,583 zinamilikiwa na sekta binafsi. Aidha jumla ya shule za sekondari 1,250 kati ya shule 4,885 zinamilikiwa na sekta binafsi. Vilevile kati ya vyuo vikuu 34, vyuo 22 vinamilikiwa na sekta binafsi. Kwa mchanganuo huo ni dhahiri kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuongeza fursa na ubora wa elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikishirikiana na wamiliki wa shule binafsi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kodi na tozo. Katika kutatua changamoto hizo hadi kufikia sasa Serikali imeweza kuondoa tozo ya uendelezaji ujuzi (Skills Development Levy-SDL) tozo ya zimamoto, kodi ya mabango na tozo ya usalama mahali pa kazi (OSHA).
Mheshimiwa Spika, hii ikiwa ni hatua ya Serikali kuhakikisha kuwa sekta binafsi inakuwa na mazingira rafiki na wezeshi katika kuwaletea Watanzania maendeleo. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na umoja wa wamiliki wa shule binafsi itaendelea kujadiliana na kutatua changamoto zinawakabili ili kuvutia uwekezaji katika sekta ya elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuzipatia ruzuku shule binafsi, Serikali itaendela kuboresha mazingira ya Taasisi za Fedha ili sekta binafsi iweze kupata mitaji kwa gharama nafuu huku Serikali ikiendelea kupunguza changamoto zilizopo katika shule za umma.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imeongeza makato kwa wanufaika wa mikopo kutoka asilimia 8 hadi 15 bila kuwashirikisha wadau mbalimbali pamoja na wanufaika wa mikopo.
• Je, Serikali haioni kwamba imevunja mkataba wa makubaliano kwa kuwa wakopaji walisaini mkataba wa asilimia 8 na siyo asilimia 15?
• Ongezeko la makato limewaathiri sana wakopaji na kuwafanya kuwa ombaomba na kuishi maisha magumu sana. Je, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu haioni kama litakuwa jambo la busara kusitisha makato hayo ya 15% mara moja ili kunusuru maisha ya watumishi waliokopa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Paschal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijavunja mkataba wowote na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu. Kilichofanyika mwaka 2016 katika marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura ya 178 ni kuiboresha sheria hiyo kwa kutaja kiwango mahususi cha asilimia 15 kinachopaswa kukatwa kutoka mshahara ghafi wa wanufaika. Kabla ya marekebisho hayo kifungu cha 7(1)(h) kiliipa Serikali mamlaka ya kupanga kiwango cha makato na kubadilisha kiwango pale itakapoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kukuhakikishia kuwa Serikali inafahamu umuhimu wa kuwashirikisha wadau katika marekebisho ya sheria yoyote, hivyo basi, katika mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Sura ya 178 ya mwaka 2016 wadau mbalimbali walishirikishwa na wadau hao ni pamoja na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi TUGHE na TUCTA, Chama cha Mawakili nchini (TLS) pamoja na wanafunzi kutoka Taasisi za Elimu ya Juu kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Elimu ya Biashara Dodoma pamoja na Chuo cha Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makato ya asilimia 15 kutoka kwenye mshahara ghafi wa wanufaika wa mikopo yamewekwa kisheria kwa lengo la kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinarejeshwa kwa wakati ili ziweze kuwasomesha Watanzania wengine ambao wanauhitaji. Hivyo kwa sasa Serikali haina mpango wowote wa kusitisha makato hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu nchini kuhakikisha kwamba wanarejesha mikopo yao kwa wakati kwani wapo Watanzania wengi ambao wanahitaji mikopo hiyo ili iweze kuwanufaisha wahitaji wengine. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mji wa Mlowo kuelekea Rukwa kupitia Kamsamba imekuwa muhimu katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Songwe, Rukwa na Taifa kwa ujumla:-
Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka wa kuitengeneza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mlowo – Kamsamba yenye urefu wa kilometa 130 ni barabara ya Mkoa inayohusumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Songwe. Wizara yangu kupitia TANROADS imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ambapo TANROADS Mkoa wa Songwe imeshatangaza zabuni ili kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Baada ya kukamilisha hatua hiyo, ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, imekuwa ikitenga fedha kila mwaka za kufanyia matengenezo mbalimbali, ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/18 imetenga shilingi bilioni 1.439 na kwa mwaka wa fedha 2018/2019 zimetengwa shilingi bilioni 1.089 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Vilevile, Wizara inaendelea na ujenzi wa daraja la Momba katika Kijiji cha Kamsamba na kazi inatarajiwa kukamilika Agosti, 2018.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA aliuliza:-

Kuna watumishi katika Halmashauri nyingi za Wilaya nchini walikuwa wanachama wa PSPF wamestaafu zaidi ya mwaka mmoja na hawajalipwa fedha zao za kiiunua mgongo (pension) na kwa sasa wanaishi maisha ya taabu na mateso makali:-

(a) Je, ni lini sasa Serikali itawalipa wastaafu hawa?

(b) Inasemekana kwamba Serikali imetumia vibaya fedha za PSPF ikiwa ni pamoja na kukopesha baadhi ya watu na taasisi: Je, Serikali haioni kwamba hii inaweza kuwa sababu mojawapo ya kucheleweshwa mafao kwa wastaafu?

(c) Fedha za kiinua mgongo ni mali ya Mtumishi anayestaafu: Je, kwa nini Mifuko ya Pensheni isiwakopeshe wastaafu watarajiwa angalau 40% ya fedha hizo bila riba pale inapobaki miaka 10 kabla ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Paschal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka kufikia tarehe 28 Februari, 2019 Mfuko mpya wa PSSF ulikuwa umekamilisha kulipa malimbikizo ya deni la wastaafu lilorithiwa kutoka Mfuko wa PSPF ambapo jumla ya wastaafu 9,971 wamelipwa stahiki zao zilizofikia kiasi cha shilingi bilioni 888.39. Aidha, Mfuko umekamilisha mfumo wa ulipaji mafao utakaowezesha kufanya malipo katika ngazi ya mkoa na hivyo kuwezesha mfuko kulipa mafao ndani ya muda uliowekwa kisheria wa siku 60 tangu mwanachama anapowasilisha madai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge iliyoanzisha mfuko husika. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inasimamia muundo wa utawala na mfumo wa maamuzi na usimamizi wa uwekaji wa fedha za mifuko. Aidha, sheria inaipa Bodi ya Wadhamini ya mfuko jukumu la kusimamia uwekezaji wa fedha za mfuko kwa uhuru. Hivyo basi, siyo kweli kwamba Serikali inaweza kuingilia uendeshaji wa mifuko au kufanya maamuzi ya uwekezaji ikiwemo kukopesha taasisi au watu binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, imekuwa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanachama wake kupitia vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) katika maeneo ya kazi. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa mwaka 2015, Mifuko inaweza kutoa mikopo kwa SACCOS hadi asilimia 10 ya rasilimali za mfuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zinaruhusu wanachama kutumia sehemu ya mafao yao kama dhamana kwa ajili ya kujipatia mkopo wa nyumba kutoka katika mabenki na taasisi za fedha nchini ili kuwawezesha kuboresha makazi wakati wa kipindi cha utumishi wao.

Aidha, Kanuni Na. 24 na 25 ya kanuni mpya za Mafao ya Hifadhi ya Jamii za mwaka 2018 zimetoa wigo mpana zaidi kwa wanachama waliochangia kwa miaka isiyopungua 10 kuweza kupata huduma hii tofauti na hapo awali ambapo ni wanachama waliokuwa wametimiza umri kuanzia miaka 55 ndio waliweza kupatiwa mikopo ya kujenga vyumba.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-

Wastani wa akinamama wanaojifungua kwa siku ni 18 - 20 katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi; licha ya idadi kubwa ya akinamama wanaojifungua, kuna ufinyu wa majengo mbalimbali ikiwepo na wodi ya akinamama:-

(a) Je, ni lini Serikali itashughulikia ujenzi wa wodi ya akina mama katika hospitali hii?

(b) Hospitali ya Wilaya ya Mbozi inatumika kama Hospitali ya Mkoa wa Songwe na haina maji safi na salama. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya maji safi na salama katika hospitali hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imefanya tathmini na kubaini zinahitajika jumla ya shilingi milioni 37 kwa ajili ya upanuzi wa wodi ya akina mama wanaojifungua. Mradi huo umepewa kipambele katika mpango wa bajeti wa mwaka 2020/2021 ili kuanza ujenzi.

Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri imeidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 12 kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji katika hospitali ya Wilaya ya Mbozi ili kutatua changamoto ya maji katika hospitali hiyo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-

Wilaya ya Mbozi ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe inapakana na Wilaya ya Songwe; Wilaya hizi mbili hazijaunganishwa kwa barabara hivyo Wananchi wanaotoka Wilaya ya Songwe kwenda Makao Makuu ya Mkoa hulazimika kupitia Mkoa wa Mbeya?

(a) Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara ya changarawe kutoka Kata ya Magamba ambayo ipo Wilaya ya Songwe kupitia Kata ya Magamba ambayo ipo Mbozi?

(b) Kata za Magamba, Itumpi, Bara, Itaka na Halungu hazina vivuko na madaraja hali inayosababisha usumbufu kwa Wananchi; Je, ni lini Serikali itajenga vivuko katika Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kabla ya kujibu swali naomba kufanya marekebisho ya kiuchapaji kidogo katika ile sehemu ya swali sehemu ya (b) sehemu ya Kata ya Iyempi isomeke Itumpi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga Mbunge wa Mbozi lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara anayozungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara inayoanzia Kijiji cha Mlowo na kupitia Vijiji vya Zelezeta, Isansa, Nafco, Magamba, Itindi hadi Galula. Sehemu ya barabara inayoanzia Kijiji cha Mlowo, Zelezeta, Isansa, Nafco hadi Magamba yenye urefu wa km 34 ni barabara ya Mkoa inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe. Aidha, sehemu hii inayoanzia Magamba, Itumpi hadi Galula yenye urefu wa km 32 inahudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mkoa wa Songwe na inapitika vizuri majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kwenye Sekta ya Kilimo, biashara na madini ya makaa ya mawe Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekuwa ikiifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine za barabara alizouliza Mheshimiwa Mbunge zinasimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Songwe iliyopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha za kutosha kuiwezesha TANROADS na TARURA kuihudumia barabara hii pamoja na kuimarisha madaraja aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-

Wilaya ya Mbozi ina vivutio vingi sana vya utalii, baadhi yake ni Kimondo kilichopo Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali, Majimoto na Mapango ya Popo katika Kata ya Nanyara, lakini baadhi ya vivutio hivyo hasa Majimoto na Mapango ya Popo havitambuliwi na havipo hata kwenye orodha ya kumbukumbu za Serikali:-

(a) Je, ni lini Serikali itavitambua rasmi vivutio hivyo?

(b) Je, kivutio cha Kimondo kimeingiza shilingi ngapi kwenye Halmashauri ya Mbozi na Serikali Kuu tangu kigunduliwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inavitambua vivutio vilivyopo Mkoani Songwe ikiwemo vinavyopatikana Wilaya ya Mbozi vya Majimoto na Mapango ya Popo na tayari vimeorodheshwa katika kumbukumbu za Serikali. Vivutio hivyo vilitambuliwa rasmi katika maadhimisho ya siku ya Kimondo Duniani yaliyofanyika katika Kituo cha Kimondo cha Mbozi kilichopo Kijiji cha Ndolezi, Kata ya Mlangali tarehe 28 - 30 Juni, 2018.

Mheshimiwa Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kufanya utafiti wa kina kwa lengo la kukusanya taarifa sahihi na vivutio vilivyopo Mkoani Songwe kwa lengo la kuvitangaza katika gazeti la Serikali. Vivutio vitakavyokidhi vigezo kuwa urithi wa utamaduni wa Taifa tutavitumia kiutalii.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Mwaka wa Fedha 2013/ 2014 hadi 2017/2018 Serikali imekusanya kiasi cha shilingi milioni 14,378,000/= kutoka katika kituo cha Mbozi kutokana na watalii waliokwenda kuona Kimondo. Kwa kutambua umuhimu wa kituo hicho, Serikali inaendelea kukiboresha kwa kujenga Kituo cha Kumbukumbu na Taarifa na kuandaa maadhimisho ya Siku ya Kimondo Duniani. Aidha, jitihada za kukitangaza kituo hicho zitaongeza idadi ya watalii ndani na nje ya nchi na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)