Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA) (15 total)

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Tatizo la ajira katika nchi yetu, na hasa kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu limekuwa ni kubwa sana, kama kwa mwaka mmoja inaonyesha idadi hiyo bado hawana ajira.


Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuliambia Bunge hili ni lini hasa watakuja na mkakati wa kuanza kutoa labda mikopo midogo midogo ambayo itakuwa ni mitaji kwa hawa vijana ambao wanamaliza Vyuo vya Elimu ya Juu ambao hawana kazi kwa muda mrefu?, hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa inaonekana kwamba Serikali bado haina orodha kamili ya wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana kazi.


Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kukubaliana na mimi kwamba umefika wakati sasa kuanza kuwa na data bank ya kujua wahitimu wote wa Vyuo vya Elimu ya Juu ili kuweza kujua ni ujuzi wa aina gani na weledi wa namna gani ambao upo katika nchi hii, na kuweza kuwashauri waajiri mbalimbali na sehemu mbalimbali? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, katika hoja ya kwanza ya mikopo midogo midogo Serikali inatambua ya kwamba asilimia kubwa ya wahitimu hawa ambao wengi wangependa pia kufanya shughuli za kujiajiri wanakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa programu ambayo itasaidia katika upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi waliohitimu elimu ya vyuo vikuu ambapo ziko fedha, ambazo zitatolewa kwa ajili ya wahitimu hao kupitia vikundi vyao na kampuni mbalimbali ambazo zitaundwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ipo Kampuni ya Wahitimu kutoka SUA ambayo inaitwa SUGECO, wenyewe walipatiwa fedha za mikopo na wanaendelea na shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, mipango hiyo ipo na itaendelea kuwepo.

Pili, katika suala la orodha kamili ya wahitimu, Serikali imekuwa ikifanya tafiti kila mwaka kuweza kubaini ni asilimia ngapi ya vijana ambao hawana kazi waliohitimu Elimu ya Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu. Ilianza kuanzia mwaka 2006 kutumia utafiti wa labour force survey ambayo ilifanyika mwaka 2006/2014. Utafiti huo unahitaji fedha, kila mara fedha inapopatikana utafiti huu umekuwa ukifanyika na huwa unafanyika kila baada ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufanya utafiti kupata taarifa kamili ya vijana hao ambao wamehitimu elimu ya juu na hawana ajira ili tuone hatua stahiki za kuchukua.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, ulipaji wa kodi ili kuiwezesha Serikali kuweza kutoa huduma nzuri kwa wananchi ni wajibu wa kila raia wa nchi hii na kwa kuwa kumekuwa na matatizo mengi katika mfumo wa ulipaji wa kodi katika Serikali Kuu na Halmashauri, kodi usumbufu mkubwa kwa walipa kodi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mfumo wa ulipaji kodi ili uwe wazi zaidi na kuwawezesha wananchi kuweza kulipa kodi zile zinazotakiwa kulipwa?
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa wananchi wengi hawajui umuhimu wa kulipa kodi, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi na hasa walipa kodi ili waweze kuzijua aina zote za kodi na kuweza kulipa kama inavyotakiwa.ambazo zimekuwa zikileta
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza mpango gani wa kurekebisha mfumo wa ulipaji kodi. Sasa hivi kama mlivyoona na kwa kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya „SASA KAZI TU‟ tumeimarisha mfumo wa ulipaji kodi kuanzia katika ngazi ya Taifa mpaka Halmashauri zetu na mmeona jinsi ambavyo sasa tunaweza kukusanya kodi kwa kiasi kikubwa.
Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuimarisha na Mamlaka yetu ya Mapato Tanzania imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba hilo linafanyika katika ngazi ambayo wanafanyia kazi wao na pia mpaka Halmashauri zetu kule wanakokusanya uimarishaji wa ukusanyaji kodi utakuwa wazi kabisa na kila mmoja ndani ya Halmashauri mwenye jukumu hilo anayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu kutoa elimu, mpaka sasa hivi tayari tuna kitengo cha utoaji elimu ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na elimu hii huwa inatolewa moja kwa moja kupitia televisheni zetu mbalimbali tuna vipindi ndani ya wiki na pia utoaji huu wa elimu ya kodi pia hufanywa kwa semina mbalimbali na warsha zinazofanywa na watoa elimu wetu kutoka Mamlaka ya Kodi Tanzania.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa imeonekana taasisi nyingi hazifuati mfumo huu wakati Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 iliweka ni lazima kwa kila mtumishi kujaza hizo fomu na kutekeleza mfumo huu. Je, ni hatua gani ambazo Serikali imekusudia kuchukua kwa taasisi na watumishi ambao hawafuati huu mfumo ambao ni wa lazima kwa mujibu wa sheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kutangaza hadharani taasisi ambazo zimefanya vizuri katika kutekeleza mfumo huu kungesaidia sana kuwapa motisha wafanyakazi wanaofanya kazi katika taasisi hizo. Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba umefika wakati sasa taasisi zinazofanya vizuri na zile ambazo zinafanya vibaya zitangazwe moja kwa moja hadharani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza, kuhusiana na hatua gani ambazo Serikali inakusudia kuchukua kwa watumishi ambao hawazingatii mfumo huu, nipende tu kumwambia kwamba, kuanzia mwaka 2012, Katibu Mkuu Utumishi alitoa Waraka na ilielekeza kwamba kuanzia kipindi hicho hakuna mtumishi wa umma atakayepandishwa cheo endapo hajaweza kujaza fomu ya OPRAS. Vile vile tunakusudia kuweka tozo maalum kama adhabu kwa ajili ya watumishi ambao hawatazingatia sharti hili.
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili alitaka kufahamu endapo Serikali iko tayari kutangaza hadharani taasisi zinazofanya vizuri. Nipende tu kusema kwamba, tunafikiria pia kuweka tuzo, lakini tunapokea ushauri na tutaangalia ni kwa namna gani suala hili linaweza kutekelezwa kwa kutangaza hadharani.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu haya ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mazingira ya kimondo chenyewe yako kwenye hali mbaya sana, na ukiangalia miundombinu na barabara zinazoenda kule ziko kwenye hali mbaya sana, hivi sasa hivi kimondo kile hata uzio wa kukizunguka kimondo kile ku-protect haupo. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya kimondo kile ili kiwe ni kivutio kizuri sana kwa utalii pamoja na kuinua pato la Mkoa mpya wa Songwe na Jimbo langu la Vwawa?
Mheshimiwa MWenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ilishaandika barua ya kuomba Wizara hii ikikabidhi kimondo kwenye Halmashauri ili waweze kukiendeleza na kuweka vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na migahawa, hoteli na vitu mbali mbali vitakavyowavutia watalii wa ndani na nje, Serikali ni lini sasa itakubali kukikabidhi kimondo hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linahusu changamoto ya miundombinu kutokuwa bora au kutokuwa rafiki kwa shughuli za utalii kwenye eneo hili ambako kimondo chetu kipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua wazi kwamba ili kuweza kuboresha utalii miongoni mwa maeneo ambayo yanatakiwa kutiliwa mkazo, na kwakweli yanatiliwa mkazo na Serikali, ni pamoja na kuboresha miundombinu kwenye maeneo yenye vivutio kama hili la kwenye kimondo cha pale Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya Serikali ambayo ametaka kuifahamu Mheshimiwa Mbunge ni kuboresha miundombinu hiyo kwa kutumia bajeti zake lakini pia kwa kushirikisha wadau. Kwa hiyo wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kutumia fedha zake za bajeti kuboresha miundombinu bado mheshimiwa Mbunge kwa kuungana na Serikali aweze kutafuta namna ambayo anaweza kushirikiana na Serikali kuweza kuwafikiwa wadau mbalimbali kwenye eno la Mbozi ikiwa wanaweza kufanya jitihada kuungana na Serikali katika kuboresha miundombinu kama alivyoitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kimondo kukabidhiwa kwa Halmashauri, suala hili haina tofauti kubwa sana kiuendeshaji, Serikali ni ile ile, Halmashauri bado ni Serikali na Serikali kuu bado ni Serikali. Mawazo mema na mazuri yanaweza kupokelewa kulingana na ubora wake na wakati. Kwa hiyo nimshauri mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Halmashauri na washauri waweze kutuandikia Wizarani tutaweza kupima kuona ikiwa sababu hizo za kukabidhi kimondo hicho kwa Halmashauri linaweza likafanya eneo hilo likafanyika utalii kwa namna bora zaid na kwa tija zaidi kuliko ilivyo sasa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Ningependa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna taasisi nyingi za Serikali ambazo zinafanya kazi zinazofanana na hii inasababisha kwamba bado gharama ziendelee kubaki kuwa kubwa. Serikali ina mpango gani wa kupitia upya taasisi zake zote ili kuhakikisha kwamba zile zinazofanana zinaunganishwa, kusudi kuweza kupunguza matumizi zaidi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme tu kwamba, kama alisikiliza vizuri jibu langu la msingi, hiyo ndiyo azma na mwelekeo wa Serikali. Hata hivyo, nimpongeze na kumshukuru sana, kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia masuala mazima ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba tayari Katibu Mkuu Kiongozi, kupitia Ofisi ya Rais, alishatoa maelekezo kwa Wakuu wote wa Taasisi za Umma na tayari Taasisi zote, Wizara zote zimekwishawasilisha mapendekezo katika Ofisi ya Rais, kuhusiana miundo na mgawanyo wa majukumu ambayo wao wangeipendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya hivi sasa tayari Ofisi ya Rais tumeishaunda timu ya wataalam na wameanza kupitia ili kuangalia endapo majukumu yaliyopo kwa taasisi fulani fulani, kama yanaweza kuhalalisha uwepo wake. Lakini vile vile kuangalia ni majukumu gani, nitolee tu mfano ziko Wizara unakuta zimeunganishwa Wizara mbili, Wizara moja ilikuwa tayari ina kitengo chake cha mawasiliano, ina kitengo chake cha mambo ya teknohama, lakini na Wizara nyingine vile vile, ilikuwa na kitengo kama hicho na idara zingine zinazofanana na mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba ni lazima itabidi kufanyia mapitio idara moja tu ndiyo iwepo. Vile vile watumishi hao wengine itabidi waangaliwe sasa ni wapi watapelekwa, katika sehemu zingine ili waweze kuleta tija zaidi na kupunguza gharama kwa Serikali.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naomba niulize maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mfumo wa ugatuaji wa madaraka ulikuwa na lengo la kuwapa madaraka wananchi kuweza kuwa na maamuzi yao na kutekeleza masuala yao yanayohusiana kufuatana na mazingira yaliyopo; na kwa kuwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu hayo katika maeneo husika: Je, Serikali haioni haja ya kuupitia upya huu mfumo ili Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wabaki badala ya kuwa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji, Halmashauri za Wilaya pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri za Majiji ambao kidogo wamekuwa wakiongeza gharama kwenye Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa kuwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya sasa hivi zimekuwa zikikabiliwa na upungufu mkubwa sana wa mapato na kwa sababu Serikali kuu imekuwa haina fedha za kutosha kuweza kuzipatia hizo Wilaya. Je, Serikali haioni haja kwamba Wakuu wa Wilaya sasa iwe ni sehemu ya kutegemea mapato yanayotokana na hizo Halmashauri ili waweze kuendesha majukumu yao na kusimamia sera vizuri katika maeneo husika?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeelezea pale awali maeneo haya mawili; nafasi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 61 na ile ya Serikali za Mitaa Ibara ya 145 na 146.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ikiwezekana basi hizi nafasi nyingine zitolewe. Kutokana na Katiba hiyo sasa zimekwenda kutungwa sheria. Kuna Sura namba 287 na 288, ambapo 287 inaelekeza katika Halmashauri, kuonyesha structure, jinsi gani kama Mwenyekiti wa Halmashauri, Diwani na kiongozi wa ngazi ya Kijiji anayechaguliwa ndiyo maana ya ile dhana kubwa ya D by D kushusha madaraka kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema uondoe hilo, maana yake umetoa dhana ya D by D. Kwa hiyo, maana yake ni Katiba sasa imetupeleka katika utengenezaji wa sheria ambapo leo hii kijiji kinahakikisha kina Mwenyekiti wake wa Kijiji na Mwenyekiti wake wa Vitongoji, wanafanya maamuzi katika maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, jukumu lao kubwa ni kusimamia utaratibu na kanuni kuhakikisha kwamba unaendelea kama ilivyo. Kwa hiyo, kitendo cha kuondoa kimojawapo, maana yake, kwanza utakuwa umevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Sheria za Bunge ambazo zimewekwa humu kwa mujibu wa sheria itakuwa inaonekana hatuko sawasawa. Naamini kwamba mfumo tuliokuwa nao hivi sasa uko sawasawa. Kama kutakuwa na mawazo mengine, basi tutaendelea kuboresha kwa kadri siku zinavyoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la Wakuu wa Wilaya kwamba hawana mapato na mapato yao ikiwezekana yanayotoka kwenye Halmashauri ndiyo yangeweza kuwasaidia kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kwamba, tunajua Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wakati mwingine wanakuwa na changamoto kubwa sana kwenye OC. Jukumu letu kubwa sisi kama Ofisi ya Rais ni kuhakikisha tunaziwezesha ofisi hizi. Kitendo cha mfano, hata hatukipendi sana, saa nyingine kitendo cha Mkuu wa Wilaya kwenda kuomba kwa Mkurugenzi kupewa pesa ya mafuta, mwisho wa siku anashindwa hata kuisimamia Halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni jukumu la Serikali Kuu na sisi tutajitahidi, ndiyo maana tunasema kwamba tufanye collection ya mapato. Serikali Kuu inavyopata fedha za kutosha zitasaidia ku-facilitate kazi zake kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ziweze kufanya kazi vizuri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, nataka niongezee majibu hayo katika swali lililoulizwa na Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwava kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, amesema yeye angependekeza kwamba hawa Wenyeviti wa Halmashauri waondoke na badala yake, kazi zile kwa sababu zinafanywa kwa pamoja katika dhana ya ugatuaji wa madaraka kwenye Halmashauri, basi Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawa wachukue nafasi ile. Nataka tu niseme kwamba kusema ukweli hapa itakuwa imekiuka dhana ya checks and balances kwa sababu Wenyeviti ni Wawakilishi wa wananchi na wao ndiyo political figures kwenye maeneo yale, kwa maana ya uwakilishi wa wananchi per se.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ni Wawakilishi wa Serikali Kuu. Kazi yao, pamoja na kazi nyingine ni kuziangalia hizi Halmashauri kama zinafuata sera, sheria za nchi, kanuni, taratibu na maagizo mbalimbali ya Serikali Kuu, pale chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanamwangalia nani? Wanamwangalia huyu Mwakilishi wa wananchi ambaye yuko pale na wataalam wake hawa kuanzia Mkurugenzi na wataalam wengine kama wanafanya vizuri. Ndiyo maana tunasema, hakuna mwingiliano kwa sababu mwingiliano ni pale ambapo Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anaingilia jambo ambalo linakwenda vizuri. Huo ni mwingiliano; lakini anapofanya intervention ya jambo linalokwenda vibaya ili sheria izingatiwe, hii inaruhusiwa kwa sababu ndiyo kazi yake iliyomweka pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niongezee majibu haya na niwahakikishie kwamba mfumo wetu sisi Watanzania wa ugatuaji wa madaraka ni mfumo mzuri ambao nchi nyingi za Kiafrika zinakuja kujifunza hapa kwa sababu ni mfumo uliokaa vizuri na unasababisha amani na utulivu katika nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tuendelee nao huu hadi hapo baadaye ingawa tunakubali kwamba huwa kuna reforms zimekuwa zikifanyika kuanzia mwaka 1982, mwaka 1992, mwaka 1998, lakini ipo haja ya kuendelea kuboresha lakini siyo katika eneo hili la checks and balances. Tutaharibu system nzima ilivyokaa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ningependa kuuliza swali dogo tu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa hapo nyuma, shule nyingi zilikuwa zinategemea sana michango ya wazazi ili iwasaidie katika kuweza kutoa mafunzo hasa katika zile fani ambazo hazikuwa na Walimu wa kutosha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fungu maalum kwa ajili ya wale Walimu ambao watakuwa wanatoa mafunzo hasa ya masaa ya ziada baada ya ule muda wa kazi kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba tutafanyaje katika kuongeza fungu maalum kwa ajili ya Walimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunaanza, maana tumepata mahali pa kuanzia. Kama nilivyosema kwamba mgawanyiko wa fedha unapelekwa katika jinsi gani kugharamia elimu hii na naamini kama nilivyosema kwamba kila jambo lina changamoto yake. Jambo hili limekuwa na mafanikio makubwa sana na ndiyo maana kwa kadri tunavyoenda tunafanya tathmini vile vile ili kuangalia na changamoto zilizojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi tutaangalia jinsi gani tutafanya, lakini lengo kubwa ni kuweza kuwaajiri Walimu ili waweze kutatua tatizo la upungufu wa Walimu hasa Walimu wa sayansi katika maeneo yetu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007/2008 Serikali kupitia Ofisi ya Rais - Utumishi ilikipa Chuo cha Utumishi wa Umma kikishirikiana na chuo kimoja cha Macintosh cha Canada kuandaa framework ya kuwandaa viongozi ambayo ilijulikana kama Leadership Competence Framework. Na katika framework hiyo ilikuja na sifa 24 yaani leadership competencies 24. Sasa, je, ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kuziingiza hizo competencies katika mafunzo ambayo tayari yameandaliwa na Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika utaratibu wa majeshi yetu kuna utaratibu kwamba mtu hawezi kupata cheo chochote mpaka kwanza apate mafunzo fulani. Sasa kwa kuwa Serikali imesema inaandaa utaratibu wa kozi ambazo zitakuwa ni lazima kwa watumishi wa umma waandamizi. Je, ni lini sasa tamko la Serikali hizo kozi zitaanza ili watumishi hawa wawe wanafundishwa na wanaandaliwa ili wawe mahiri kabla hawajapata uteuzi wa madaraka ya aina yoyote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hasunga, alikuwa ni mtumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kwa hiyo, anaifahamu sekta hii vizuri sana na anakifahamu chuo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuingiza zile sifa 24 za uongozi katika mafunzo yake; nisema tu kwamba sasa tunaandaa utaratibu katika hayo mafunzo ya lazima, utakapokamilika na zile sifa zote 24 katika leadership competence zitaweza kuingizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, ni lini sasa katika mafunzo ya in-service, kabla watu hawajapandishwa cheo yataweza kuwekewa utaratibu, nipende tu kusema kwamba pamoja na haya tumeandaa pia, utaratibu wa kuwa na assessment centre ambao tutaweza kuweka kuwa na pool ya watu mbalimbali ambao wana-managerial positions ambazo wakati wowote wanaweza wakateuliwa. Watakuwa tested, lakini pamoja na hayo pia, kutakuwa na yale mafunzo ya lazima ambayo niliyaeleza awali yatakapokamilika basi wataweza kupatiwa na tutakuwa hatuwezi kupandisha cheo mtu kabla hajapata mafunzo hayo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya swali hili yanafanana kabisa na mazingira ya wakulima wa Wilaya ya Mbozi na hasa katika Jimbo la Vwawa. Kwa kuwa, moja ya gharama kubwa ambazo wakulima wa kahawa wanazipata ni pamoja na kusafirisha kahawa yao kupeleka kwenye mnada kule Kilimanjaro. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba Mnada wa Mloo unafunguliwa ili kupunguza ushuru na tozo mbalimbali ambazo zinawakabili wakulima wa zao la kahawa wa Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba mnada mkubwa wa zao la kahawa upo Moshi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya zao la kahawa suala la minada na mahali panapofanyika ni moja kati ya masuala tunayofanyia kazi. Kwa hiyo, avute subira, nina hakika muda sio mrefu tutakuwa na suluhisho katika hili.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kwamba Watanzania ambao ni zaidi ya miaka 15 na ambao hawazidi miaka 54 wako takribani milioni 25 na kuendelea; na kwa kuwa asilimia 22.4 ni kubwa sana, maana yake ni kwamba karibu takribani watu 5,813,066 hawajui kusoma na kuandika.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha sasa vituo vya kufundishia kama ilivyokuwa zamani katika kila kijiji, kwa sababu tatizo hili ni kubwa sana na hasa katika Jimbo la Vwawa na maeneo mengine nchini?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri umesema kwamba mmeziagiza Halimashauri kutenga fedha ili wahakikishe kwamba huo mfumo wa KKK unatekelezwa.
Je, mmeweka mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kutakuwa na uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Hasunga kwa kuridhika na majibu yetu ya awali, pia kwa majibu yanayofuata ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kwamba kila mahali kwenye taasisi ya elimu, iwe ni shule ya msingi, iwe ni sekondari, iwe ni chuo ni kituo halali cha watu wasiojua kusoma na kuandika kuweza kupata elimu au mahali pa kujifunza.
Vilevile Wizara baada ya kutembea na kuona kwamba eneo hilo bado lina uhitaji mkubwa, tumeshaweka mikakati ya kuona kwamba elimu ya watu wazima inapewa kipaumbele na kuona kwamba wananchi wetu wa Tanzania tupungue ikiwezekana angalau tufikie asilimia tano mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ufuatiliaji katika Halmashauri ili kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa sisi sote ni Madiwani kwenye Halmashauri zetu, basi tuone umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya shughuli hiyo ya kuhakikisha wenzetu wote wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata hii nafasi. Kwa kuwa Mheshimiwa waziri amesema kwamba wana mpango wa kupeleka vitendea kazi na magari katika Ofisi za Ukaguzi wa Elimu, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa fedha za uendeshaji, unaweza ukapeleka magari kama hakuna fedha za uendeshaji bado hawataweza kufanya kazi; na kwa kwa muda mrefu wakaguzi wamekuwa wakifanya ukaguzi katika shule ambazo ziko jirani tu kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea OC ofisi hizo zote za kanda ili ziweze kufanya kazi yao sawasawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema awali ni kwamba kimsingi Wizara imedhamiria kuboresha eneo hili la ukaguzi. Suala la OC limekuwa likiimarishwa kila wakati na ndio maana tunataka kuangalia mfumo mzima, hata ikiwezekana mafungu yao ya upatikanaji wa OC yaende moja kwa moja bila kupitia katika ngazi nyingine.
Vilevile ukaguzi tunaotaka kuuzingatia si tu ule wa kuangalia masomo peke yake, mpaka miundombinu, shule iko wapi? Inafundisha vipi na imesajiliwa katika sura ipi? Kwa hiyo, tunataka kwenda kwenye ukaguzi kwa njia ambazo ni pana zaidi ili kuwezesha kuona kwamba mambo ambayo tunaagiza kupitia sera zetu na miongozo yanatekelezwa pia katika shule zetu za Serikali.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya walimu wamekuwa wakijiendeleza wao wenyewe katika vyuo mbalimbali na kupata vyeti lakini kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikivikataa vyeti hivyo, imekuwa haivitambui. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvitambua hivyo vyeti ili waweze kupandishwa madaraja zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kujiendeleza ni kujiendeleza tu aidha Serikali imekusomesha ama umejiendeleza mwenyewe kinachotakiwa ni kujiendeleza. Ndiyo maana katika jibu la msingi mwanzo nimesema mtu akijiendeleza maana yake ana-submit cheti chake, kinapitiwa na kuhakikiwa na Afisa Utumishi mtu huyo anastahili kupanda daraja na kuwekwa katika nafasi yake anayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna kesi kama hiyo, maana wakati mwingine hatuwezi tukajibu kesi hapa zote kwa ujumla, inawezekana kuna case by case, kama likiwa hilo basi tunaomba tujulishane hiyo kesi imejitokeza wapi tuweze kuifanyia kazi. Mtu yeyote aliyesoma provided kwamba amesoma na ana cheti halali jambo hilo halina mashaka la kuwekwa katika muundo anaostahili. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na hatua ambazo zimechukua katika kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo ambalo limekuwa na matatizo makubwa katika taasisi za umma ni eneo linalohusu ununuzi wa vipuri na matengenezo ya magari pamoja na mafuta.
Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wote walioko katika Menejimenti za Mashirika hayo wanakopeshwa magari badala ya kutumia magari ya Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndiye mwenye wajibu wa kukagua hesabu zote za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma, lakini kwa muda mrefu tumeona kwamba hesabu za taasisi za umma, Mkaguzi Mkuu amekuwa akizipatia sekta binafsi zimekuwa zikikagua kwa niaba yake, lakini sekta hizo binafsi zimekuwa ziki-charge fedha kubwa sana ya ukaguzi. Je, ili kupunguza matumizi Serikali ina mpango gani wa kuimarisha ofisi ya CAG ili iweze kufanya kazi hiyo sawa sawa badala ya kutumia sekta binafsi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ununuzi wa vipuri na matengenezo na watumishi kukopeshwa magari, tunapokea wazo lake zuri na tutalifanyia kazi kuona ni jinsi gani utekelezaji wake ili kuona tunapunguza matumizi haya kama alivyosema kwenye magari. Tusisahau pia ni taratibu na kanuni za utumishi ndizo ambazo zinaelekeza haya yote ambayo yanatendwa na Serikali yetu, pale ambapo itaonekana inafaa tofauti na uamuzi uliopo sasa, basi Serikali yetu haitasita kufanya hivyo ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama ambavyo Serikali imekusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu Serikali yetu inatambua umuhimu wa ofisi hii ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na imekuwa ikiimarisha kila mwaka hatua kwa hatua kuhusu wafanyakazi kupewa ujuzi lakini pia kuhusu na bajeti yake. Sote ni mashahidi tumeona juzi tumepitisha bajeti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na imeongezeka kama Bunge lako Tukufu ambavyo ilipendekeza, ni imani yangu ofisi hii itakagua ofisi zetu na taasisi zote za umma pale ambapo inaonekana inafaa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Mazingira ya swali hili yanafanana kabisa na hali halisi iliyopo katika Jimbo la Vwawa hasa katika Wilaya ya Mbozi. Kwa kuwa, Wilaya ya Mbozi inajishughulisha sana na kilimo na niwazalishaji wakubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Tawi la Benki ya Kilimo ili liweze kutoa mikopo kwa wakulima hawa wa Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumekuwa tukisema hapa, Benki ya Kilimo sasa inaelekea kufungua Ofisi za Kanda na ofisi mojawapo ya Kanda itakayofunguliwa katika Mkoa wa Mbeya, ambapo najua ni karibu kabisa na Wilaya ya Mbozi. Ni imani yangu wananchi wetu na wakulima wetu wa Wilaya ya Mbozi watapata faida za kupata mikopo nafuu kutoka katika benki hii.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.

Kwa kuwa katika Jimbo la Vwawa kuna Kituo cha Afya ambacho kimejengwa kwenye Tarafa ya Iyula ambacho kimekamilika karibu miaka miwili iliyopita, lakini mpaka sasa hivi hakina watumishi wa kutosha na hakina vifaa.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba watumishi wa kutosha wanapelekwa na vifaa vya kuweza kuwasaidia kutoa huduma mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sote tunafahamu kazi kubwa sana iliyofanywa na Serikali yetu katika kuboresha miundombinu ya huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya takribani 487 ndani ya miaka mitano iliyopita, lakini harakati hizo za ujenzi zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika maeneo mbalimbali bado tuna changamoto ya idadi ya watumishi wanaohitajika kuanza kutoa huduma, lakini pia tuna changamoto ya vifaa tiba, na ndiyo maana katika mpango wetu wa vituo vya afya katika mwaka wa fedha ujao tunatarajia kuomba takribani shilingi bilioni 22.5 kwa ajili kwanza ya kuhakikisha vituo vyote na hospitali za halmashauri zilizojengwa zinapata vifaa tiba kwa kushirikiana na mapato ya ndani ya halmashauri. Lakini pili, mpango upo wa kwenda kuwaajiri watumishi kwa ajili ya kuwapeleka katika vituo hivyo.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Hasunga na Waheshimiwa Wabunge wote wenye hoja kama hiyo, kwamba Serikali ina takwimu za kutosha za mahitaji ya vifaa tiba katika vituo vyetu vya afya, za mahitaji ya watumishi katika vituo hivyo vya afya na itakwenda kuajiri watumishi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha lakini pia tutakwenda kupeleka vifaa tiba. Kwa hiyo, Mheshimiwa Hasunga nikuhakikishe kwamba kituo hicho cha afya kipo kwenye mpango na tutahakikisha kinaanza kutoa huduma bora kwa wananchi.