Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Saul Henry Amon (7 total)

MHE. FREDY A. MWAKIBETE (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza :-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya maji Mji Mdogo wa Tukuyu kwani hali ya maji ni mbaya sana na miundombinu iliyopo ni ya zamani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Rungwe Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tukuyu wenye wakazi wapatao 61,975 unapata maji kwa asilimia 40 ukilinganisha na mahitaji halisi. Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka katika chanzo cha Masoko wenye gharama za shilingi bilioni 4.7. Kazi zitakazotarajiwa kufanyika ni ujenzi wa vyanzo viwili vya Mbaka na Kigange kwa ajili ya kupeleka maji katika Mji wa Tukuyu pamoja na vijiji 15, ujenzi wa matanki manne (4), ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 13.6 na ujenzi wa vituo vya maji 125. Hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 1.7.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika Bajeti ya mwaka 2015/2016, imetumia shilingi milioni 144, kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya mradi wa maji kutoka katika chanzo cha mto Maswila ili kukidhi mahitaji ya maji kwa wakazi wa Mji wa Tukuyu. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi milioni 295.3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji katika Mji wa Tukuyu.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza:-
Mradi wa Masoko Group Water Scheme umeshughulikiwa kidogo na
miundombinu tayari imeshaharibika.
Je, ni lini mradi huu utamaliziwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na
Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa
Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Masoko Wilayani Rungwe
unatarajiwa kuhudumia jumla ya vijiji 15. Mradi huu ni miongoni mwa miradi
inayojengwa chini ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji kwa fedha za
ndani. Mradi huu ulisimama baada ya Halmashauri kuvunja mkataba na
Mkandarasi ajulikanaye kwa jina la Osaka Store.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kwa sasa umeanza tena kutekelezwa
na Mkandarasi Multi Professional Limited, aliyeanza kazi mwezi Februari, 2016
ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa chanzo cha Mbaka, ujenzi wa
tenki la kuhifadhi maji Kijiji cha Lufumbi, kulaza mabomba yenye urefu wa
kilomita 12.6 na kujenga vituo vitano vya kuchotea maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe tayari mwezi
Disemba, 2016 ilitangaza zabuni ya kuwapata wakandarasi watakaotekeleza
ujenzi wa awamu ya pili utakaohusisha ulazaji wa bomba kilomita 92.1 na ujenzi
wa vituo 135 vya kuchotea maji. Mradi huu ukikamilika utagharimu jumla ya
shilingi bilioni 5.3 na utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika Vijiji vya
Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa,
Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.
MHE. SAUL H. AMON aliuliza:-
Barabara ya Pakati – Njugilo – Masukulu – Matwebe hadi mpakani ni barabara kubwa na inapita katika Kata nne ambazo ni Masoko, Bujela, Masukulu na Matwebe, barabara hii ilishapandishwa daraja na kuwa ya TANROADS:-
Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa ili kuondoa adha kwa wananchi kwa kupoteza kipato kwa mazao kuharibika njiani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Pakati – Njugilo – Masukulu hadi Mpakani mwa Wilaya ya Rungwe na Kyela yenye urefu wa kilometa 24.5 ni barabara ya wilaya. Katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa Muhtasari Na.2016/2017/ 01 cha tarehe 6/12/2016, kilipendekeza ipandishwe hadhi na kuwa barabara ya mkoa. Baada ya mapendekezo kupelekwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, barabara hiyo iliidhinishwa na kupandishwa hadhi kwa urefu wa kilometa 4.4 kutoka Njugilo hadi Masukulu katika Wilaya ya Kyela.
Mheshimiwa Spika, matengenezo ya barabara hii yanatarajia kuanza Agosti 2018, kufuatia kuwekwa kwenye Mpango wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Barabara za Vijijini kupitia ufadhili wa watu wa Marekani (USAID), chini ya programu ya Irrigation and Rural Roads Infrastructure Project – IRRIP II ambapo kwa sasa zipo kwenye hatua ya usanifu.
MHE. COSATO D. CHUMI (K.n.y. SAUL H. AMON) aliuliza:-
Jimbo la Rungwe ambalo lina kata 29 lina vituo viwili tu vya afya ambavyo ni Masukulu na Ikati; wananchi wa Kata ya Mpuguso na Isongole kwa nguvu zao wameanzisha ujenzi wa vituo vya afya:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia kumaliza ujenzi huo ili kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ambayo baadhi ya maeneo ni takriban kilometa 50 na usafiri usio wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na uboreshaji wa vituo vya afya 208 nchi nzima ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa karibu na wanapoishi. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 1, yaani mwezi Septemba, 2017 ilipeleka Sh.500,000,000 kwenye Kituo cha Afya cha Ikuti kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD), chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya akina mama wajawazito, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia la kisasa, mtambo wa oxygen na kukarabati miundombinu ili kuhakikisha huduma za upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito na huduma nyingine zinapatikana katika Kata ya Ikuti badala ya kufuata huduma hizo kwenye hospitali ya wilaya ambayo iko mbali. Aidha, mwezi Aprili, 2018 Serikali imepeleka Sh.500,000,000 kwenye Kituo cha Afya cha Masukulu ili kujenga na kukarabati miundombinu itakayoboresha huduma kama ilivyo kwa Kituo cha Afya cha Ikuti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Kituo cha Afya cha Mpuguso kimetengewa shilingi milioni 100 kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kumalizia jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Sambamba na kuitaka halmashauri itenge fedha za mapato ya ndani ili kuendeleza ujenzi kwenye Kituo cha Afya cha Mpuguso na kuanza ujenzi kwenye Kituo cha Afya cha Isongole, napenda kutoa ahadi kwamba Serikali itavipa vituo hivyo kipaumbele cha juu ili ikiwezekana vikamilike mwakani.
MHE. DKT. TULIA ACKSON (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza:-

Wilaya ya Rungwe ina vyanzo vingi vya maji ambavyo vinatiririsha maji.

Je, ni lini Serikali itarekebisha miundombinu ili kuongeza kiwango cha maji ambayo kwa sasa hayatoshi kiasi cha kufanya Idara ya Maji kufunga baadhi ya maeneo kama vile Vijiji vya Ibungila, Lubiga na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe inakadiriwa kuwa na jumla ya wakazi wapatao 291,176. Huduma ya maji imegawanyika katika maeneo makuu mawili; eneo la kwanza ni huduma ya maji Mjini Tukuyu inayotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tukuyu na eneo la pili ni huduma ya maji vijijini inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la mijini, watu wapato zaidi ya 32,074 wanapata huduma ya maji kati ya watu 50,000 sawa na asilimia 63. Katika maeneo ya vijijni, watu wapatao 157,750 wanapata huduma ya maji kati ya watu 240,250 sawa na asilimia 55.7. Vyanzo vya maji vinavyotegemewa na wananchi wa Rungwe ni vijito, mito na chemchemi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Ibungila na Lubiga vilikuwa vinapata huduma ya maji kutoka katika mradi wa maji wa Mji wa Tukuyu, uliojengwa tangu mwaka 1984 ambapo kuanzia mwaka 2002 unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tukuyu. Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa watu na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji maji, kwa sasa huduma ya maji katika Vijiji vya Ibungila na Lubiga haipatikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya maji katika Mji wa Tukuyu ambao katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetoa shilingi milioni 3,087 kupitia Mamlaka ya Maji Mjini Tukuyu ili kuongeza upatikanaji wa maji. Fedha hizo zitafanya kazi ya ujenzi wa tank lenye mita za ujazo 200 na kukarabati mtandao wa bomba kilomita tisa. Utekelezaji wa mradi huo unaendelea. Hadi sasa ujenzi wa tank umekamilika na bomba za inchi sita zenye jumla ya urefu wa mita 750 zimelazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utekelezaji wa mradi huu kukamilika vijiji vya Ibungila na Lubiga vitaweza kupata huduma ya maji kutokana na ukarabati unaoendelea kufanyika hivi sasa.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza:-

Hakuna barabara ya kuunganisha Daraja la Nyubati na Kata ya Kisondelea hadi Nzunyuke umbali wa zaidi ya kilomita 30 kufika kijiji cha Nyubati:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya kuunganisha Kijiji cha Nyubati na Kata ya Kisondelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-


Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa wananchi wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilometa 30 kwa kuzunguka kutoka Nyubati hadi Nzunyuke kutokana na kukosekana kwa daraja. Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) umefanya usanifu na tathmini ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo kiasi cha shilingi milioni 847.36 kinahitajika ili kuitengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, TARURA imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nyubati – Lutete yenye urefu wa kilometa 6 inayounganisha Kijiji cha Nyubati na Kata ya Kisondelea.
MHE. DKT. TULIA ACKSON (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza:-

Umeme wa REA umepita katika vijiji vya Unyamwanga, Kisonidzela na Mpuga lakini wananchi wa maeneo hayo hawajaunganishiwa huduma ya umeme.

Je, ni lini wananchi hao wataunganishiwa huduma ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ni miongoni mwa halmashauri zilizonufaika na utekelezaji wa mradi wa REA II uliotekelezwa na mkandarasi kampuni ya SINOTEC Ltd. kutoka nchini China ambapo vijiji vya Unyamwanga na Kisonidzela ni miongini mwa vijiji vilivyopatiwa huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kupitia utekelezaji wa mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa na Mkandarasi STEG International Services jumla ya vijiji 26 katika Wilaya ya Rungwe vitafikishiwa umeme ikiwemo kijiji cha Mpuga.

Mheshimiwa Spika, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilomita 20 za njia ya umeme wa msongo kilovoti 33, kilomita 42 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4, ufungaji wa transfoma 25 na kuunganisha wateja wa awali 1,195. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 2.25

Mheshimiwa Spika, baadhi ya vitongoji ambavyo havikufikiwa na umeme katika utekelezaji wa REA II katika vijiji vya Unyamwanga na Kisonidzela vitapatiwa umeme kupitia mradi wa ujazilizi Awamu ya II Densification II utakaoanza na kutekelezwa kuanzia mwezi Julai, 2019 ahsante sana.