Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Saul Henry Amon (6 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu. Vilevile niwashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Rungwe kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, sina mengi lakini vilevile siko mbali na Profesa Norman alichokizungumza, kwamba, utalii na hata mzungumzaji aliyepita ameongea hicho hicho, utalii umeangaliwa sehemu moja, hilo ndilo langu la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu misitu. Pamoja na kwamba kuna historia na jiografia ya misitu iliyopo na inayovunwa lakini naona ni Mufindi, Mufindi, Mufindi wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msitu pale Mbeya ulikuwepo siku zote, siku hizi naona ni jangwa. Msitu wa Kawetele, toka ulivyovunwa sijui mwaka gani lakini mpaka leo hii Kawetele hakuna miti, Kawetele ni jangwa, hatujui kwa nini wanafanya hivi na kwa nini Maliasili na Utalii wameamua kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina sababu ya kujiuliza, tunashangaa hata Mbeya, Iringa tuna matatizo ya madawati, lakini hiyo miti ingeweza kusaidia madawati kwa ajili ya thamani ya ofisi zetu na shule zetu. Mimi kwa Mheshimiwa Waziri nina ombi kwamba, ningependa kuona mapema iwezekanavyo Kawetele inarudishwa kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna watu wanaoshambulia misitu ambayo imewekwa kama hifadhi. Rungwe na misitu mingine ya asili bado haihifadhiwi inavyotakiwa, sijajua ni wapi ambako mnaangalia, ni nchi nzima au kuna kipande ambacho mmeamua kukiangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utalii, tunapozungumza maliasili, ni lazima tuzungumzie nchi yote kwa ujumla; kwa sababu pamoja na kwamba, ina faida kwa ajili ya kupata fedha, lakini vilevile kuna faida kwa ajili ya mazingira yanayoharibika na kupotea bure kwa sababu tu wahusika hawafuatilii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali haiwezi itupe wananchi wa Mbeya tupande ile miti tuweze kuitumia ile ardhi; kwa sababu Mbeya kuna watu wengi. Ukiangalia Mbeya misitu mingi imepandwa na wananchi na bado inavunwa vizuri na wananarudishia iweje Serikali ambayo inapata faida, kwa sababu ile ni kama biashara ya Serikali. Chukueni faida yenu lakini rudisheni mtaji pale pale, kwamba wakati wa kuvuna vilevile irudishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye Sekta ya Utalii. Mchangiaji hoja aliyepita ameongea habari ya kwamba, kuna service mbovu, lakini hiyo yote ni kwa sababu ya kutokuwa na utamaduni. Hatuna chuo ambacho ni thabiti kwa ajili ya kufundisha watu watakaohudumia hoteli zetu ili kuwe na kiwango cha Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunacho chuo lakini hakitoi na tumebakia kugombana na kusema hawa hawafai. Angalia wenzetu wanaotoka nje standard zao wanavyofanya, ni kwa sababu wamewekeza kwenye vyuo vya utalii. Huko wanapata ma-manager wazuri, wapishi wazuri, wahudumu wazuri. Sisi hivyo vyuo viko wapi? Kweli mtu atoke Mwanza, aje ajifunze Dar es Salaam peke yake ni kweli? Mtu atoke Mbeya aende Dar es Salaam kujifunza habari ya chuo. Vyuo vilivyopo havikidhi haja ambayo inaweza ikatoa international services.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo bado kwenye utalii. Utalii hautangazwi Nyanda za Juu Kusini na kusini mwa Tanzania na maeneo mengine, watu mmejikita maeneo ya kaskazini peke yake. Mheshimiwa Waziri aende Malawi, akaone utalii unavyofanya kazi kwenye Ziwa Nyasa. Sisi hapa tuna Ziwa Nyasa na tuna fukwe ambazo ni nzuri, ambazo hazichafuki, hazina takataka, lakini hatuzitangazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuunga mkono asilimia mia moja mchangiaji aliyepita kwa uchangiaji wake, ametoa mchango wa kizalendo. Naomba Wizara na vitengo vyake, viweze kutangaza utalii uliopo. Kwa mfano, Nyanda za Juu Kusini wameongea habari ya barabara kwenda kwenye mbuga za wanyama, vilevile tunaongea habari ya barabara kwenda Mlima Rungwe, hakuna barabara watu waende wakatembelee Mlima Rungwe. Hatuna barabara kwenda kwenye fukwe nzuri za Nyasa, kuna Ziwa Ngozi ambalo haliingizi maji wala halitoi maji, hamna anayetangaza. Tuna Ziwa Kisiba, kuna ziwa zuri sana ambalo halichafuki, halitoi maji na wala haliingizi maji lakini hatulitangazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtazamo wangu ninavyojua ni kwamba, hii Wizara inafanya biashara, tunaweza kufikiria kwamba, inafanya biashara kwa kulipa Serikali mapato ya bilioni 10 au15, lakini si biashara ambayo watu tungejiwekeza zaidi kwenye hayo maeneo kama ingekuwa zaidi ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingi sana ambazo ningeweza kuchangia, lakini kufikia hapo haya yalikuwa ni mawazo yangu na kwamba, tuchukulie umuhimu wa hali ya juu kutangaza vitega uchumi vyote, vivutio vyote ambavyo vipo maeneo yote ya Tanzania bila kujali ni wapi, watu waende kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimempa Mheshimiwa Waziri mfano wa kwenda Malawi akaangalie, wanatoka watu sehemu mbalimbali lakini fukwe tulizonazo sisi ni nzuri zaidi kuliko zilizoko Malawi. Haya ni yangu machache kwa leo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hii Wizara ya Miundombinu, vilevile namshukuru Mungu kwa kunipa huu muda wa kuchangia Wizara hii ya Miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niaze kushukuru na kumpongeza Rais kwa uamuzi wa kuanzisha hii standard gauge. Nimpongeze Rais vilevile kwa ununuzi wa ndege bila kujali watu watasema nini, kuna watu wanakebehi kwamba ndege hazina maana, lakini tunavyojua kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi zile ndege zilizonunuliwa ni manufaa ya Taifa zima pamoja na utalii wa ndani kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Waziri wa Miundombinu ambaye nimemwona kwenye tv akizunguka kila kona ya Tanzania kuangalia ujenzi wa miundombinu ya nchi hii, nakupongeza sana. Vilevile nimpongeze Naibu wake na Katibu wake ambao wote huwa nawaona kwenye vyombo vya habari wakizunguka na kuzungukia kuangalia miundombinu ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nipongeze pia ujenzi wa flyover zilipo Dar es Salaam kwani zitapunguza msongamano mkubwa uliopo Dar es Salaam ambao umesababisha shughuli nyingi za kimaendeleo zisiende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa standard gauge ambao utaharakisha maendeleo ya nchi yetu kwa kubeba mizigo, abira na sasa Mwanza tutakuwa tunaenda kwa saa nane badala ya siku mbili. Kigoma tutakuwa tutakwenda kwa saa nane mpaka tisa badala ya siku mbili. Hivyo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake na watendaji wake wakuu wakiwemo Mawaziri pamoja na Manaibu wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, nia yangu ambayo nimeijia hapa hasa kwa Mkoa wangu wa Mbeya. Mkoa wa Mbeya kama mnavyoujua na wote Mawaziri mmeshafika pale, barabara ya kuingia katikati ya mji ni tatizo kubwa sana. Kama alivyozungumza mchangiaji aliyepita amesema kwamba mahali pa dakika kumi tunatumia saa mbili, ni kweli mtu ukifika Uyole kama ndege itaondoka baada ya saa mbili na nusu itakuacha, mahali ambapo tunaweza kutumia nusu saa tu kutoka Uyole mpaka Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya bypass ya Mbeya ambayo ni Uyole bypass kwenda mpaka Songwe tunaomba wananchi wa Mbeya ifanyiwe upembuzi yakinifu haraka ili iweze kujengwa kwani Mbeya ni lango kuu kabisa ambalo linatumia nchi zaidi ya nane kwa kutumia barabara hiyo. Barabara hiyo ni kwa ajili ya kwenda Zambia, Malawi, Congo, Zimbabwe wote wanapita njia hiyo lakini usumbufu ni mkubwa sana, naomba mtusaidie.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nina ombi kwa Waziri kuhusu uwanja wa ndege tumewahi kurudi zaidi ya mara mbili, kwa sababu tu uwanja hauna taa za kuongozea ndege pale chini. Gharama yake sijajua ni kiasi gani kikubwa, mwaka huu naona ni mwaka wa pili tukizungumzia suala hilo wakati huo huo Serikali ilishaahidi kwamba itatoa hela ingawa nimeona bajeti ya mwaka jana sijaona hata senti tano iliyoenda Songwe, kama ipo nitaomba kuiona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudi kwenye Jimbo langu la Rungwe. Jimbo la Rungwe ni moja kati ya majimbo ambayo yanatoa chakula, viazi vingi mnavyoviona vinatoka Rungwe pamoja na ndizi zote zinatoka Rungwe, lakini Katika Wilaya ya Rungwe kuna kata tatu hazina barabara kabisa, hivi ninavyozungumza saa hizi zimekatika ukienda kata ya Swaya, kata ya Kinyala hakupitiki. Matokeo yake wakulima wa kule wanapata taabu kweli, tungeomba hizo barabara badala ya kuendelea kushughulikiwa na Halmashauri barabara ya kutoka Igogwe - Lubala - Vibaoni - Malangali mpaka Mbeya Vijijini tungeomba iwe barabara ya mkoa kwani pale pana mazao mengi, nazungumza sasa hivi hata tukiongozana na Waziri ataenda kukuta mazao yanavyoharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuyatoa mazao katika eneo hilo inabidi urudi umbali mrefu kilometa 40 halafu ndiyo uanze kupandisha nayo kwenda Mbeya kiasi kwamba wakulima wa eneo hilo pamoja na kwamba wanalima sana viazi, mahindi, maharage yananunuliwa kwa bei rahisi kiasi kwamba hawapati faida na gharama ya kilimo kile inakuwa ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba hiyo barabara uiangalie. Narudia hiyo barabara kama hujaiandika, barabara ya Igogwe kwenda Lubala - Vibaoni - Malangali ambayo inakwenda Swaya kwenda kutoka Mbeya Vijijini.

Hiyo ni barabara muhimu sana na kuna vyakula vingi sana, wakati kuna sehemu zingine watu wanakufa kwa njaa wanaumia kwa njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ambayo imepandishwa daraja, ninawashukuru sana Waziri pamoja, Naibu Waziri na Watendaji wako kwa kuipandisha daraja kuwa ya Mkoa. Barabara ya kutoka Pakati - Njugilo - Masukuru kwenda mpaka mpakani. Ile barabara wenzetu upande wa Kyela wamefika mpaka kwenye mpaka. Ni sehemu ndogo ili uweze kwenda Kyela kutoka eneo la Matwebe inabidi uzunguke utumie saa mbili badala ya kutumia dakika 20, vyakula, matunda, mpunga hapo vinaaribika kwa sababu hakuna mtu ambaye anaweza akazunguka kwa kiasi kikubwa wakati huu wa mvua. Ikifika kipindi cha mvua pale mahali panakuwa ni kisiwa, huwezi tena kuenda, hizo Kata mbili zinakuwa zimebaki na kila tunapokwenda kwa ajili ya kampeni tatizo ni hilo hilo.

Naomba Waziri kwa vile umeipandisha hadhi hiyo barabara naomba uifanyie angalau ukarabati kwa sababu kule hata material ile moram ni nyingi sana maeneo yale ambayo ni kazi ndogo, kwa sababu daraja ni moja na sehemu korofi hazizidi tatu ambazo ukisizimamia zinaweza zikawa zinakapitika moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine haya ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendeleza kujenga barabara ya Tukuyu kwenda mpaka Lwangwa kujenga barabara ya njia panda mpaka Matema hiyo nashukuku na tunaomba kila mwaka tuendelee kuzitafutia hela zile barabara, kwani zitafunguka, utalii ni mkubwa ukizungumza Matema ni utalii mkubwa sana na pale mnajenga bandari kwa ajili ya meli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka niishukuru na kuipongeza Wizara hii ni kwa kutengeneza na kutimiza ahadi. Ahadi ya kutengeneza meli katika Ziwa Nyasa. Zile meli tumeziona zimeshaingia majini na meli ya tatu ya abiria inakaribia kuisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwashukuru sana na kuwapongeza sana
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Fedha. Kwanza nimshukuru Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha bajeti yake, mimi nina mambo mawili makubwa. Wakati wa kukusanya kodi, kodi ni sawa na biashara nyingine yoyote lakini hapa kuna vikwazo ambavyo wafanyabiashara wengi tunavipata na kama Waziri hajalisikia hilo atume timu yake kwa wafanyabiashara, hasa wanaoingiza mizigo kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna huu mfumo wa TBS na tukiangalia kwamba nchi ya Tanzania sio nchi yenye viwanda kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara wa Tanzania sio wakubwa wa kila mmoja kwenda kutafuta kiwanda chake cha kuleta mizigo. TBS kuna tatizo, hasa la ile faini ya asilimia 15 ya invoice value ya mzigo anapoleta hapa Tanzania. Hilo ni tatizo kubwa sana ambalo naomba Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha iliangalie upya ni namna gani wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna Wizara mbili, kuna Wizara ya Afya kupitia TFDA kwa mambo ya vyakula na dawa na TBS ambayo inafanya sehemu zote. Hata hivyo, utaratibu wa TFDA ni mzuri, unaeleweka, pamoja na kwamba ni ghali, unakwenda unasajili bidhaa zako hapa Tanzania na wanakupa certificate. Ukishapewa mara moja huna usumbufu tena baada ya hapo, kwa hiyo TFDA hawana matatizo ukishasajili bidhaa zako, lakini TBS tatizo lake ambalo linawafanya Watanzania wengi wasiweze kuingiza mizigo, Watanzania wengi wapite porini ndiyo maana unasikia, Mheshimiwa Bashe ameongea hapa kwamba watu wanapita Kenya, wanapita Kenya kwa sababu ya kuikimbia TBS, wanaingizaje, haijulikani.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS wangechukua mfumo wa TFDA nina uhakika kwamba ingepunguza usumbufu mkubwa sana, kwamba mimi nilete bidhaa zangu, TBS wazikague kwa sababu viwanda vinavyotengeneza mizigo inayopita TFDA ndiyo hivyohivyo vinavyotengeneza kupita TBS, lakini TBS kila unapoingiza mzigo unakuwa na certificate yake. TFDA wakikusajili utaisajili tena hiyo mizigo yako baada ya miaka miwili, unakuta usumbufu wa TFDA unakuwa haupo lakini TFDA anakwambia chakula ingiza, unaingiza TBS anakwambia hujasajili na kama hujasajili TBS ulipe asilimia 15 ya invoice value. Kwa kweli imewafanya wafanyabiashara wengi sana wawe na manung’uniko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri na timu yake awaulize wafanyabiashara nini kikwazo kikubwa cha biashara. Kama anavyojua tunavyoingiza mizigo ndivyo tunavyoweza kuuzia nchi nyingine za jirani, na ukiuzia nchi nyingine za jirani tutapata faida si moja tu kwa ajili ya kuingiza mizigo, kwanza wanakuja kuchukua mzigo, wanakuja wanalala, wanatumia usafiri wa nchi wa ndani wa kwetu na mambo mengine, akina mama lishe wanapata vyakula, wanapata hela. Kwa hiyo kupitia TBS kwa kweli hilo ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba Serikali iliangalie hilo, kwa nini kazi za TFDA zisiwe za kwake. Tumepita nchi nyingi, ukiangalia Nigeria, Marekani na kwingineko, ukiambiwa kwamba hawa wanashughulika na mambo ya vyakula na dawa ni Wizara nyingine na ambao wanashughulika na mambo ya viwango ni Wizara nyingine na viwango vingekwenda kwa viwango na TFDA wangeendelea na kazi yao ya kukagua kwamba hivi vyakula na madawa viko salama kwa mlaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mapato ya nchi yataongezeka, watu watapungua. Kwa sababu ukiangalia TRA hakuna usumbufu kabisa kama ilivyokuwa zamani, ukiangalia bandarini hakuna usumbufu kama ilivyokuwa zamani lakini ukifika unakwama, kwa sababu sisi wafanyabiashara wa Tanzania wengi ni wadogo, ni watu ambao hatuna mitaji mikubwa, tunavyoenda kununua mizigo iwe ni Ulaya, iwe ni Marekani, iwe ni China au Dubai, tunachanganya, hivyo huwezi kupata na usumbufu wake ni mkubwa mno. Wakati unanunua mzigo utachukua zaidi ya wiki sita ili kupata certificate ya TBS. Hilo naomba waliangalie walipe umuhimu wa hali ya juu, watu wanatoroka na mizigo kupita sehemu nyingine kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hapo Mheshimiwa Waziri amenielewa na kama nilivyomwambia, sehemu nyingine zake zote ziko sawasawa; TRA ambako watu walikuwa wanaogopa pako sawasawa, vitu vinakwenda sawasawa wala ndani hatuingii. Ukienda TFDA unakwenda na certificates zako nimeleta mzigo huu, hatusumbuliwi, unapewa invoice. Hata hivyo, ikifika sasa, kama ninavyomwambia, ni kweli nikikaguliwa nitakwenda kukaguliwa wiki sita, badala ya kuondoka siku tatu nitakwenda kukaa zaidi ya miezi miwili nikisubiria ukaguzi na mizigo, lakini kibaya zaidi, kwa nini hawa TBS ambao wana jukumu wasichukue kwamba wewe unachukua kiwanda gani, mimi nitasema nauza vipodozi nachukua Procter and Gamble, basi lete hivyo vitu tuvipime kama viko sawasawa, au nimechukua Unilever, tuvipime viko sawasawa, wanipe certificate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai kuvipima kama viko salama, lakini na wenyewe watupe certificate ili tusiwe tunasumbuka kila mara tunapoingiza mizigo. Huu usumbufu Mheshimiwa Waziri ataona sasa hivi umetengeneza monopoly, maana ukizungumza atakuwa analeta mtu mmoja, ukimwambia huyu ndio anayeleta chuma basi ataleta huyo huyo kwa sababu ndiye aliye na nafasi na access ya kwenda kwenye kiwanda hicho kinachohusika na kumpimia mizigo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hilo ambalo watu wengi wameliongelea, nadhani ni la kuongezea tu, kuhusu hizo milioni 50. Kwa kweli ni matatizo, Waziri akakae na timu yake, milioni 50 watu tuliwaahidi na zilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kila tukienda kwenye mikutano tunaulizwa kama vile tuliwakopa. Kwa hiyo, wakae wakijua kwamba ahadi ni deni, hilo waliangalie kwa uzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wameliongelea watu na mimi nasisitiza tu, kwamba Serikali iangalie kwamba kuzichukua zile hela waangalie namna ya kuzirudisha na namna ya kuzifuatilia lakini zirudi benki tuendelee kukopa. Mambo yetu yamekwama, benki wanakataa kutupa hela, benki kama CRDB ambayo walikuwa wanaweza kukupa mara moja, hawana hela. Tafuteni utaratibu, zirudisheni kule kama na ninyi mnataka riba basi chukueni riba kutoka benki ili tuendelee kukopeshwa na ndiyo uchumi wenyewe, hakuna uchumi mwingine, kama wananchi hawana hela utapata wapi hiyo kodi, maana hawanunui, utapata wapi hiyo kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hayo ndiyo niliyokuwa nayo. Ahsante kwa kunipa nafasi hii kutoa mchango huu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi adimu ndani ya Bunge hili kuchangia. Kwanza kabla ya yote, naunga mkono hoja nisije nikasahau. Pili, naomba ku-declare interest kwenye uchangiaji wangu kwa sababu nitachangia kuhusu biashara nami ni mfanyabiashara, kwa hiyo na-declare interest mapema kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza, nataka kutoa pongezi kwa Serikali yangu ya Tanzania hasa kwa Mheshimiwa Rais kwa ununuzi wa ndege. Pamoja na kwamba kuna watu wanaopinga, lakini nawashangaa kweli kweli kwamba nchi inaweza kuwa bila ndege! Hata nchi ndogo zina ndege, sisi tusiwe na ndege; kwa kweli nampongeza sana na hili wanipelekee hiyo taarifa kwamba nampongeza kutoka ndani ya moyo wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, kuna wenzangu wamechangia kuhusu property tax. Nataka nimkumbushe tu Mheshimwa Waziri wa Fedha kwamba wakumbuke hili alilochangia mchangiaji mwingine simtaji jina, lakini Mheshimiwa Rais alilizungumza, akawaambia nyie wakusanya kodi mnafanya kodi zisikusanywe kwa sababu mnaweka kodi zisizobebeka. Hili amezungumza mchangiaji mwenzangu amesema kwa sisi viongozi; kiongozi akizungumza yanakuwa ni maamuzi sahihi na kama lina matatizo au ukakasi, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, basi lije hapa lizungumzwe ili hizo kodi za property tax ziweze kupunguzwa.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka aliongea Mheshimiwa Rais, sio mtu mwingine; akaongea bei mpaka akaongea akaweka mfano, nyumba ya ghorofa changisheni Sh.100,000/= sijui Sh.50,000/= lakini wanawaambia watu kodi ambazo haziwezi kubebeka. Ndiyo kweli aliyokuwa anazungumza mchangiaji mwingine aliyepita, wanaleta makadirio ya ajabu. Anakwambia ulipie kodi shilingi milioni 30 wakati hilo jengo wewe hupati hata shilingi milioni 30 kwa mwaka. Wanawatwisha watu mizigo ambayo haiwezi kubebeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, aliyeongea ni Mheshimiwa Rais na watu wote walisikia. Tunachotakiwa ni kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na naamini kwamba kodi hii ikiwa ni ya kiasi ya watu kutaka kwenda kulipa wenyewe italipika, lakini kwa haya mamilioni yanayotajwa kwa kweli sidhani kama watu wengi, kama alivyozungumza mchangiaji mwingine, mzee kastaafu, unamwambia akalipie Sh.200,000/=, ndivyo walivyoenda kukagua na kutoa tathmini ya hiyo nyumba yake. Kwa kweli ni ghali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kuna haya matatizo na vikwazo katika biashara tunazozifanya na ndiyo maana nime- declare interest. Kuna hizi taasisi za umma zinaingiliana mno na zinaenda zote kwa pamoja; lakini nitazungumza mojawapo ambayo ni hii ya uingizaji wa mizigo. Unakuta, TFDA, kwa mfano, tunaweza kuiondoa TRA. Sasa hivi katika watu wanaofanya kazi nzuri kupita maelezo, ni TRA lakini vikwazo vinavyowekwa na hizo Idara nyingine za Serikali ndizo zinazofanya uchangiaji wa uchumi kukua upungue. Kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumza katika eneo langu la vipodozi. Nchi nyingi kwenye vipodozi wanaoshughulikia ni watu wanaoshughulika na afya. Hapa kwetu naamini kwamba TFDA ndiyo wanaoshughulika na mambo ya dawa, vyakula pamoja na vipodozi. Unakuta TFDA wamekupa certificate, hawana matatizo. Wamekupa, wanakwambia kabla hujaingiza mzigo wako, lete tuukague, tuupime, tunakupa certificate.

Mheshimiwa Spika, unapewa certificate na TFDA, unayo. Unaenda kuleta mizigo, TBS wanakwambia huu mzigo haufai. Hapo wanakinzana mno na ndiyo maana wamesababisha watu wengi wapite porini. Siyo watu wote wana nguvu za kuweza kupita moja kwa moja. Naomba hilo liangaliwe na hapa siwezi kulizungumza sana kwa sababu nilikuwa nimekuja na hayo mawili. Pongezi kwa Mheshimiwa Rais kuhusiana na property tax na hiyo ya mambo ya kupingana kwa Idara za Serikali. Kwa kweli zinapingana sana kiasi kwamba wale wadogo wadogo ambao wamekuja kabisa na kwamba wamelipia wana karatasi za DFTA, lakini huyu anakataa. Kwa hiyo, unakuta wanakinzana.

Mheshimiwa Spika, TRA wako very efficient, unakwenda unafika siku tatu. Maana tulikuwa tunachukua wiki tatu au nne, lakini sasa hivi TRA siku mbili au tatu wamemaliza kazi yao. Unaanza kupiga kwata huku TFDA, wamemaliza; unaanza na TBS. TBS umemaliza nao wanakwambia kuna vipimo. Jamani, Kampuni iliyotengeneza hiyo mizigo ni ya Kimataifa, nitatoa tu mfano labda Procter and Gamble, watengenezaji wakubwa ambao wako katika kila nchi na vipimo vinajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu anakwambia lazima tupime tu hii chupa kama kweli ni mills 50, naye umlipe. Tupime hii chupa ni mills 100 naye umlipe. Ni kweli kabisa na siyo kwamba nazungumza kwa kuambiwa, ni vitu ambavyo navisikiliza. Kwa hiyo, wangekaa pamoja ili wahakikishe kwamba tunafanya shughuli za uzalishaji na kukusanya kodi iwe rahisi. Itakuwaje rahisi? Ni kwa kuchukua hizi mamlaka kwamba wewe ndio utashughulika na hili, wewe ndio utashughulika na hili, kuliko kila mmoja huyu kikwanzo, huyu hapana.

Mheshimiwa Spika, nitampa Mheshimiwa Waziri mifano mingi lakini hapa muda sina, kwa hiyo, muda nitautafuta mwenyewe nimpelekee mifano nimwambie kwamba na hawa wanamkwamisha kukusanya mapato na ndiyo sababu ya watu kupita porini, siyo kwamba watu hawapiti porini na vitu havingii.

Mheshimiwa Spika, nchi hii ni kubwa, mipaka yake ni mikubwa. Wewe mwenyewe ukiangalia kutoka Mombasa uje ufike Mtwara, utoke Mtwara umalize yote Malawi; utoke Malawi uende Zambia; yaani mpaka ni mkubwa sana. Nakumbuka tukirudi huko nyuma, kulikuwa na uongozi uliwahi kulegeza, walikuwa wanakusanya mapato makubwa sana. Vikwazo havileti mapato, wala kodi kubwa haileti mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu, naomba kumalizia, nalo hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakushukuru kwa sababu kwanza namfahamu ni rafiki yangu kwa muda mrefu, mkaliangalie. Vipodozi siyo kweli kwamba ni anasa, vipodozi siyo sigara wala siyo pombe. Kama siyo sigara wala pombe na kila aliyepo hapa ndani hakuna ambaye hakupakaa kipodozi. Wanapoweka tax kubwa namna ile mpaka na excise duty utafikiri unauza sigara au pombe kali, hawamtendei haki huyu mlaji wa mwisho. Mimi nitaleta, lakini atakayeumia ni huyu aliyemo humu. Sasa wanaponiwekea hiyo kodi kubwa, siamini hata kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango anataka watu wanuke vikwapa humu ndani, haiwezekani. Kwa hiyo, vipodozi, nataka nimwambie kabisa siyo kitu cha anasa. Nenda nchi yoyote; nenda Amerika, nenda Ulaya vipodozi vinaingizwa kwa sababu wanajua faida yake, hakuna asiyepakaa. Kwa hiyo, waangalie hilo na waliangalie vizuri sana. Hayo mambo matatu; Idara zinazokinzana wakae pamoja...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza naomba niungane na wenzangu kupongeza uongozi wa Rais wetu Magufuli kwa kazi anayoifanya, kwa wote nadhani wanaona hakuna ambaye haoni na jinsi anavyotekeleza amekuwa ni mzalendo wa nchi hii pamoja na Mawaziri wake wote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naenda ninayo yangu matatu kwa Mheshimiwa Mpango. La kwanza kuna hili la mazao ghalani ambalo limeanzishwa kwenye kahawa, korosho na pamoja na kokoa. Kuna baadhi ya haya mambo ni mageni sana sana kama haya ya kahawa na kokoa yameanza sasa hivi, lakini yameanza kwa kishindo wananchi hawatuelewi, tunashindwa kupita vijijini, naomba mpeleke ushauri ni namna gani hizi haya mazao ghalani yatakuwa yanafanywa yanawekwa na watu wana nunua namna gani. Sababu ya kuzungumza hivo kwa sababu unakuta mkulima yeye amelima amechuma na hana hela za kuwapa wale vibarua waliokuwa wanamsadia, hata mimi mwenyewe nikiwemo, lakini tumepeleka kahawa yetu hatujue bei yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo nyuma wakati tunakua kulikuwa na mauzo ya kahawa ambayo tulikuwa tunalipwa kwanza hela, lakini ikienda kuuzwa tulikuwa tunaletewa hela iliyobaki tulikuwa inaitwa mabaki. Lakini sasa hivi hawajui itauzwa bei gani, itauzwa na nani, lakini tumekusanya tumeshaipeleka kwenye vyama vyetu vya ushirika, hilo nilikuwa najaribu tu kwamba kama Serikali iliangalie hilo ili tuepukane na hayo mabomu na maswali mengi tunayoshindwa hata kuyajibu kwa hao wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu kuna kodi ambayo kwa kweli si rafiki sana hii najaribu tu kukumbusha Bwana Mpango mwaka jana niliongelea na leo nazidi kuongelea. Kuna kodi ya mahoteli ya vyumba watu waliokuwa/wanaokusanya VAT kawaida walikuwa hawadaiwi hii kodi ya chumba ya asilimia kumi kwenda kwenye Halmashauri zetu au kwenye miji yetu. Lakini imekuja baadhi ya Halmashauri zimekuwa zikidai lakini huyo mfanyabiashara ambaye atakusanya asilimia kumi ya Serikali Kuu, asilimia kumi ya Halmashauri na vilevile kuna kodi zingine nyingi kuna city service levy zote zinakusanywa na huyo huyo, je, huyu ambaye akusanyi VAT maana yake watu wote watakimbilia kwake na hili suala naomba liangaliwe kuna baadhi ya Halmashauri zimeanza hizo fujo, kuna baadhi ya Halmashauri zinataka kukusanya na kuwapeleka watu na mbaya zaidi hawatumii kama TRA wanavyosema kwamba sisi ni asilimia 18 anakuja anakuhesabia vyumba anahesabu na vyumba 50; mara 50,000, mara mwaka mzima hajui walilala watu au hawakulala anaku-charge na kukupeleka mahakamani, kwa kweli hilo ni kubwa na ni baya zaidi kwenye masuala ya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hilo uliangalie ulisimamie kwamba je, huyu anayekusanya VAT je, naye anatakiwa alipe hiyo asilimia kumi ya city service levy naomba hilo uliangalia make pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ambalo hili ni kukumbusha ndugu yangu Mpango mmefanya kazi kubwa sana nchi hii na hela zinazolipwa na wafanyabiashara na kodi zinazolipwa zinaonekana zinatumika namna gani. Alie na macho haambiwi tazama, mimi nina macho natembea nchi naona jinsi Serikali inavyofanya kazi. Lakini siamini kwamba Bwana Mpango na timu yako yote ya ukusanyaji mapato mmewahi kujiuliza kwanini watu wakimbie na kodi, kwa mfano SADC kodi zote ni sifuri, lakini mtu anashindwa kulipa, hamjiulizi ni kwa nini. Mimi nitakupa hapa kwa nini na nakukumbusha kwasabau mwaka jana nilizungumza na mwaka huu najaribu kukumbusha mamlaka zilizopo, TRA haina tatizo unapeleka wanakulipisha kodi yako, ukitoka TRA kwa mimi nizungumze mimi kama ndio mdau wa hiyo eneo nazungumza kwa upande wangu utakuja TFDA ndio waliopewa kwenye chakula na dawa kuangalia usalama wa chakula na dawa. Na wanautaraibu ambao unaeleweka vizuri, anakwambia bidhaa yako unataka kuingiza ulete tuipime tuisajili tutakupa kwa miaka mitatu, vizuri kabisa TRA anakwambia ingiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka TRA unakutana na TBS anakwambia upitishi huu mzigo sasa siuji nani ni nani hizi mamlaka zingejaribu kupewa kila kitu kila mamlaka nafasi yake ili watu wasiweze kukimbia, wanakimbia kwa sababu mamlaka ni nyingi, TBS ukimalizana nao anakwambia sasa kuna vipimo sasa sisi tunaoleta vikolokolo ni hatari kweli kweli, mtu wa weights and measures naye anataka apime kila chupa ya mafuta uliyoleta kila ceiling board uliyoleta, kila kigae ulicholeta mzigo hautoki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mzigo wa kutoka siku moja uliotolewa na TRA na TFDA utakwenda miezi miwili, miezi mitatu bado uko hapo hapo. Naomba hizi mamlaka na ningependekeza hizi mamlaka kila mamlaka ifanye kazi yake, lakini katika nyongeza hatutawakuza hawa wafanyabiashara wadogo, hapo Bwana Mpango uliangalie kwa kupitia mamlaka zako uangalie hasa TBS anakwambia ukifika kwenye nchi husika unatakiwa ukapate certificate ya kila aina ya mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nishazungumza tena na hili nakukumbusha tu, wewe ni mfanyabiashara mdogo umeenda ku-consolidate container una bidhaa aina kumi utafute makampuni kumi yote yakupe certificate na wewe ulikwenda kununua kwa supplier hukunua direct kutona kwa manufacturer. Kwa kweli hiyo ni kazi ni ngumu hatuta hawa Watanzania tunaotaka kuwainua kibiashara hawataweza kuinuka au kuwe na sababu moja tu kwamba hakuna kuagiza mizigo au mizigo mbadilishe utaratibu wafanye kama wanavyofanya TFDA tusajili kwa sababu hakuna kilichofichika. Kwa mfano tunazungumza habari ya SADC, ipo SADC, Uniliver ipo SADC, hivyo unapokwenda kununua au kiwanda cha ceiling board kipo SADC sisi tuchukue kiwanda cha ceiling board kinachoelewaka na address inayoeleweka tulete TBS waisajili ili kesho na kesho kutwa nisiendelee kutaka certificate ya kila wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo mimi naamini tutawafanya Watanzania hawa ambao ni wadogo wanaotaka kukua kwa sababu amini usiamini, hakuna aliyekua, wote tulizaliwa, tukawa na siku, mwezi, mwaka, miaka mpaka tukafika ikawa S.H. Amon ikawa brand badala ya kuwa jina ikawa ni brand. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo Bwana Mpango, kwa hiyo kama mimi nimefika pale nina vifurushi vyangu vya tani moja kwa nini nisiende porini pamoja na kwamba ni zero rated hata kama ni zero rated kwa nini mimi niende nikasumbuke nikae miezi kufuatilia? Nitapita porini na ndiyo maana unakuta watu wanapita porini, mngejiuliza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka yetu iko wazi, hilo ulielewe na ndiyo maana nakuambia kwamba TRA wewe kwa mfano umenunua mzigo South Africa hujashuka hapa unakuta karatasi zako zipo tayari za kwenda kulipia ushuru na unalipa. TFDA tayari ulishafika unalipa, lakini ukianza kusema kila item uende ukalipie, ununue ceiling board waende wakakague, ununue sijui kigae waende wakakague. Naomba sana sana ili watu wasiende porini, kwa sababu hapa nchi zote za SADC hakuna kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ukiniambia VAT ni kodi mimi kwangu VAT sio kodi, mimi nakukusanyia na kukuletea, kwa sababu nitakuja kukudai, lakini unavyoniambia nikae wiki tatu na mtaji wangu ni shilingi milioni mbili haiwezekani na huwezi kuwafanya Watanzania wadogo waanze biashara na wakue. Naomba mliangelie hilo, mkae, tuweze tuwe tunapata certificate kutoka TBS kama tunavyopata kutoka TFDA na kama tunavyopata kutoka TRA hatuna matatizo nako lakini hapa pana matatizo makubwa. Mimi huo ndiyo mchango wangu na ilikuwa ni ombi langu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja iendelee. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja zilizopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulize kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa hatua za makusudi za kuanzisha na kulifufua Shirika la Ndege Tanzania ambalo limefanya tuwe na usafiri wa uhakika na kupunguza ajali nyingi ambazo tungepata hasa viongozi kwa kutembea kwa barabara. Vilevile kwa hatua zake za makusudi kujenga reli ya Standard Gauge pamoja na Mradi kubwa kabisa wa Umeme wa Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo vilevile nataka kuongea mimi machache kwa Mheshimiwa Waziri Mpango - Waziri wetu wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ina usumbufu hasa katika uingizaji wa mizigo na hili ninalizungumza na nitakuwa nalizungumza ili uweze kuliangalia. Mimi maombi yangu ni kumwomba Mheshimiwa Waziri Mpango na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara wajaribu kuwaita wafanyabiashara wanaoingiza mizigo ndani ya nchi hii, kwa sababu hatuwezi kuzungumza kwamba sisi tunajitosheleza kwa viwanda na kuwekewa vikwazo vilivyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama wanasikiliza sana mimi mara nyingi Mheshimiwa Rais huwa namsikiliza sana, lakini wangesikiliza na kufuatalia kwa nini anasema punguzeni vikwazo? Amewaambia kuhusu majengo, amewaambia kwamba kodi hizi za juu mnazong’ang’ani watu hawana na ndiyo maana mnashindwa kuzikusanya. Muangalie vile alivyoondoa riba kwenye malimbikizo ya kodi watu wamelipa kiasi gani. Kwa hiyo, zile riba kubwa zikiondoka watu watalipa bila matatizo. Vilevile kuna vikwazo vingi na vikubwa sana kwenye taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali kwenye uingizaji wa mizigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uingizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi; na ndiyo maana nimeomba viwanda na biashara pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukiwaita wafanyabiashara nikiwemo na mimi mwenyewe kwa sababu na-declare interest kwa sababu nafanya hizo biashara tuzungumze kwa nini watu wanakwenda porini kwa nini watu mipaka ni mingi, mikubwa na mirefu sana. Mfanyabiashara anahangaika na muda, hakuna mfanyabiashara anayehangaika na kingine, anahangaika na faida yake na muda. Sasa unapomkalisha mfanyabiashara kwanza Serikali haipati faida na mfanyabiashara hapati faida. Matokeo yake ni kwamba tunarudisha na kufifisha uchumi wa nchi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwa nini nazungumza kuhusu vikwazo vya biashara ambavyo vipo wakati wa uingizaji mizigo. Unakuta idara ni nyingi za Serikali zinazotoa vikwazo, TRA anakwambia mimi nimemalizana na wewe ingiza, TBS anakwambia mimi na wewe tumemalizana ingiza, anakuja mtu wa vipimo anakwambia hapana mimi kwangu hujamaliza vipimo, nianze kutumia vipimo. Hujamaliza anakuja mtu wa mionzi anakwambiwa tunataka tuangalie hizo peremende ulizoleta kuhusu mionzi. Kwa hiyo, unakuta tunarudisha nyuma sana uingizaji wa mizigo na kusababisha watu kuona kwamba ni kero kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo naomba mngekaa kama Serikali. Vilevile kama hiyo sheria ilitungwa hapa na imetengeneza vikwazo, kwa nini msiirudishe hiyo sheria hapa ili iondolewe vikwazo? Hilo nalizungumzia la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili hawa wafanyabiashara mnawatengenezea monopoly, kwa sababu haiwezekani kwamba kila mfanyabiashara atakayekwenda kununua mizigo nje ya nchi atakwenda kwenye viwanda moja kwa moja, si rahisi hata kidogo. Nitajitolea mfano mimi mwenyewe, mimi nauza vipodozi, nijitolee mwenyewe, nisimpe mtu mwingine. Vipodozi ni aina 40; nikatafute makampuni 40 waje wafanye inspection mahali niliponunulia mizigo imetoka Uingereza, Canada, Marekani, Italy na kote huko wakague? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Serikali Tukufu, na ninaamini hata Mheshimiwa Rais angeambiwa angesema tuje tukagulie hapa hapa Tanzania. Mtu anende akanunue alete mizigo yake akaguliwe hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani mnataka kuniambia kwamba kule ndiko wanajua kuangalia bora kuliko Tanzania ambayo nyie ndio mnaiona physically? Hilo ningelifanyia kazi na hilo watu wanakimbia na kunung’unika sana; hawawezi kuwaambia kwa sababu hawawezi kuwafikia, lakini mimi niliowafikia nataka mlielewe hilo mlizungumze mkae viwanda na biashara pamoja Mheshimiwa Waziri wa Fedha ili kuwarahisishia wananchi na kurahisisha ukusanyaji wa kodi. Kwa sababu mfanyabiashara hawezi kukubali, ametoka South Africa umemzua mpakani, mpaka ni mrefu ukiliangalia Ziwa Nyasa lote lile ni mpaka. Ukienda moja kwa moja Mto Songwe – Tunduma - Zambia mpaka wapi kote ni mpaka, mtu ataamua kupita mahali pengine popote ili aweze kungiza kwa sababu yeye biashara yake anataka ifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimesimama kuchangia nakuomba kwa hilo tu kwamba naomba Mheshimiwa Waziri Mpango na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara muwaite wafanyabiasha kama alivyofanya Mheshimiwa Rais kuangalia kero za wafanyabiashara ya madini juzi ilipendeza sana mbele ya watu. watu waliongea wakaongea mpaka sasa hivi nina imani mnalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini vilevile hili mkilizungumza, mkalipeleka kwa Mheshimiwa Rais kwamba kikwazo cha watu kuingiza mizigo ndani ya nchi hii ni hiki hapa; wanavyozungumza watu wote kwamba Serikali sikivu ni kwamba Mheshimiwa Rais wetu ni msikivu kwa mambo yetu yanayotusumbua ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, nami nimesimama kwa ajili ya hilo. Otherwise napongeza sana na ninaunga mkono Taarifa ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuongea. Ahsanteni sana. (Makofi)