Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. David Ernest Silinde (482 total)

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la kwanza kwenye Bunge lako hili la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Spika, suala la madawati limekuwa ni suala sugu sana katika nchi yetu. Swali langu la kwanza, nataka kujua Serikali ina mpango gani sasa wa kuwa na mfuko maalum au mfuko wa kudumu ambao utafanya hili tatizo la madawati liweze kupungua katika nchi yetu na hasa katika Jimbo langu la Bunda, upungufu wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari ni mkubwa sana?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa hivi nchi yetu kuna wanafunzi wanaenda shuleni hasa sekondari. Kuna mkanganyiko wa kusema twende na madawati, wengine wananunua wazazi, wengine wanasema Serikali inaleta.

Mheshimiwa Spika, nini tamko la Serikali kwenye suala hili la madawati katika shule za sekondari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE: DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimjibu Mheshimiwa Boniface Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, maswali yake mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, ametoa kama pendekezo la Serikali kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kutatua tatizo la madawati. Jambo hili nafikiri ni jambo jema na sisi kama Serikali tunalipokea. Hata hivyo, pamoja na kupokea wazo ambalo amelileta la kuwa na mfuko maalum, lakini bado naweza kueleza kwamba hili suala la upungufu wa madawati mashuleni Serikali imeendelea kukabiliana nalo, lakini na sisi kama Wabunge tuna wajibu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, moja, kwanza sisi Wabunge ni Madiwani katika Halmashauri zetu. Pia katika halmashauri tunapswa kuwa na mipango ya kutumia fedha za ndani kuhakikisha kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la madawati.

Mheshimiwa Spika, vilevile sisi ni Wenyeviti wa Mifuko ya Jimbo. Kwa hiyo, kama kuna changamoto katika halmashuri yako sehemu ya fedha za Mfuko wa Jimbio unaweza kuzitumia katika kutatua tatizo la madawati. Aidha, unaweza kutafuta wadau mbalimbali ambao wanaweza kusaidia kuhakikisha kwamba tunaondoa changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusiana hoja kwamba watu wengi wamekuwa wakilazimishwa ili mwanafunzi aingie darasani lazima mpaka ulipe mchango wa dawati ama utoe dawati. Msimamo wa Serikali ambao aliutoa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kwamba wanafunzi wote wanapaswa kujiunga bila kuwa na masharti, kama hilo linaloletwa la kusema kwamba lazima mtu atoe dawati ndiyo asajiliwe shuleni.

Kwa hiyo, msimamo wa Serikali bado uko palepale na tutaendelea kusimamia huo msimamo wa Serikali kama ambavyo Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameagiza. Ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kila baada ya miaka 10 tumekuwa tukifanya sensa ambapo sensa hii pamoja na mambo mengine inaonesha mtawanyo wa umri na kwa hiyo, ni rahisi kufanya maoteo ya watoto wanaoingia shuleni. Kwa kuwa, tatizo hili la mawati limekuwa likitokea kila mwaka inapotokea tunaanza msimu mpya wa masomo, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kutumia takwimu zinazotokana na sensa kujiandaa vizuri kulimaliza tatizo hili badala ya kutokea mwaka hadi mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimuondoe hofu, Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inatumia takwimu sahihi kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto za madawati na wanafunzi mashuleni. Ndiyo maana nimeeleza katika moja ya mpango wa Serikali ambao sasa hivi upo ni kwamba kila darasa linavyokuwa linajengwa ni lazima liwe na madawati ama kama ni shule lazima iwe na miundombinu yote. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu tu ya kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto ya madawati mashuleni.

Mheshimiwa Spika, lakini pili na kwa kifupi ni kwamba sisi tuna huo mpango na nimhakikishie kabisa kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano, hiyo kero ya madawati mashuleni tunayo na tutaieleza katika mpango wetu wa bajeti wakati utakapofika.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi tena ya kuweza kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Wilaya ya Chemba tuna upungufu wa walimu wa kike chini ya asilimia 50. Huyu mwalimu ambaye amepelekwa Shule ya Msingi Donsee ametolewa kwenye shule nyingine, wamemhamisha kutoka shule hiyo wamempeleka shule nyingine, lakini nataka kwenye mpango wa Serikali nimeambiwa hapa Serikali iko kwenye mpango.

Ni lini Serikali itatuletea walimu wa kike kwa ajili ya kunusuru maisha ya watoto wetu wa kike?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, changamoto zinazosababisha walimu wetu wa kike wasikae kwenye shule zetu hizo ni ukosefu wa nyumba za walimu, miundombinu ya barabara, ukosefu wa umeme, kuna changamoto nyingi kadha wa kadha. Walimu wakifika kule kwa mfano Shule ya Msingi Birise iko umbali wa zaidi ya kilometa 160, bodaboda ni shilingi 45,000 mwalimu wa kike unampeleka pale, hawezi kukaa mazingira ni magumu. Hata zahanati tu hawana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali, ni lini itakwenda kujenga nyumba za walimu, kuboresha miundombinu ya barabara, lakini pia suala zima la umeme ili tunapopeleka walimu wetu wa kike waende wakakutane na mazingira rafiki wapate kuishi kule na hatimaye watoto wetu wa kike waweze kupata na wao fursa ya kuhudumiwa na walimu hawa wa kike? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba nitumie fursa hii kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza lini Serikali itapeleka walimu wa kike katika Halmashauri ya Chemba? Kama ambavyo nilijibu katika swali langu la msingi, Serikali bado imeendelea na utaratibu wake wa kawaida wa kuajiri walimu mara kwa mara na bahati nzuri sasa hivi tuko katika mpango wa mwisho wa kutoa ajira mpya kwa walimu kwa hiyo, hilo suala lake tutalizingatia na tutaangalia zaidi jinsia, ili kuhakikisha kwamba, tunawasaidia watoto wa kike katika shule zote nchini.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, alikuwa anauliza moja ya changamoto kubwa ni ukosefu wa miundombinu, hususan nyumba za walimu, na ndio sababu ambayo imesababisha walimu wengi kutokufika katika baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inatambua kwamba changamoto hiyo ipo na katika moja ya mkakati wa Serikali ambao umekuwepo sasa hivi, Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, imekuwa ikijenga miradi mingi kwa maana ya miundombinu katika sekta ya elimu. Tumekuwa tukijenga mabweni, madarasa, mabwalo, miundombinu ya vyoo pamoja na nyumba za walimu za two in one.

Mheshimiwa Spika, sasa lini tutajenga, mimi niseme tu kwamba, kwa sababu tuna mpango mwingine wa tatu ambao tutaueleza katika bajeti na kwa sababu umeelezeka huko ndani kulingana na bajeti, tutapeleka hizo nyumba za walimu katika yale maeneo ambayo yana shida zaidi ili kuhakikisha kwamba walimu wa kike wanafika maeneo hayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya kutoa Elimumsingi Bila Malipo kwa miaka mitano mfululizo, kuna changamoto ambazo zimejitokeza kutokana na zoezi hili. Moja ya eneo kubwa ni kwamba vigezo vinavyotumika kupeleka fedha kidogo vinasumbua, hasa kwa shule ambazo zina wanafunzi wachache wakati baadhi ya mahitaji hasa ya utawala yanafana. Je, Serikali haioni umefika wakati wa kupitia upya vigezo hivi na kuona namna bora ya kupeleka fedha hasa kwenye eneo la utawala ili kutatua tatizo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Elimumsingi kwa definition ambayo imekuwa ikitolewa ni kuanzia Chekechea mpaka Kidato cha Nne. Hapa pana Kidato cha Tano na cha Sita ambapo hakuna facility na Elimu ya Juu kuna mikopo.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuhusisha kidato cha tano na cha sita kwenye elimumsingi ili nao wapate elimu hii ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli alichoeleza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina vigezo vyake ikiwemo idadi ya wanafunzi na ndiyo mfumo ambao tunautumia kupeleka hiyo ruzuku ya fedha katika shule zote nchini. Bahati mbaya sana kwenye zile shule ambazo wanafunzi wake ni wachache tumekuwa tukipeleka fedha kulingana na mahitaji ama kulingana na idadi yao ambayo ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na nia njema na ndiyo maana moja ya nia njema yake ni kuanzisha Elimu Bila Malipo. Kutokana na hiyo nia njema, sasa hivi nafikiri ninyi nyote mmejua, moja ya jitihada kubwa ya Serikali ilikuwa ni kuboresha miundombinu hususan katika yale maeneo ambayo shule nyingi zimekosa uhitaji na Wabunge wote ni mashuhuda sasa hivi, Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, mabwalo pamoja na maabara. Ndiyo maana nimeeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba, kulingana na bajeti na mahitaji tutaendelea kutenga fedha. Hata hivyo, hiyo changamoto anayoielezea Mheshimiwa Mbunge tunaipokea na kutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita ambao Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba hawahusiki na Elimu Bila Malipo. Moja nipokee, lakini hili ni suala la kisera; na kwa sababu Serikali ipo hapa ndani, tumelipokea hilo na tutalifanyia kazi tuone mahitaji yake kulingana na mazingira tuliyonayo. Ahsante sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi lakini niulize swali la kwanza. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa maamuzi aliyoyatoa siku ya Jumatatu ya kuruhusu kuajiriwa kwa walimu 6,000 kwa haraka, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni ukweli kwamba walimu 6,000 wanaokwenda kuajiriwa bado wanakwenda kufanya replacement; mahitaji ya walimu katika shule bado ni makubwa sana. Maamuzi ya Serikali ya kutoa elimu bure kwa nia njema yamefanya kuwe na uhaba mkubwa sana wa walimu katika maeneo hasa ya vijijini. Kwa hiyo, pamoja na mipango ambayo imeelezewa lakini bado kuna tatizo kubwa na ninapenda kujua, je, Serikali inaweza bado ikatoa commitment kwamba itaajiri walimu wa kutosha? Kwasababu hii namba iliyotajwa hapa bado haitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; naelewa kuna vigezo ambavyo vinatumika kwenye ugawaji wa walimu kwenye maeneo mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa yale maeneo ambayo ni miji ambayo iko ndani ya halmashauri vigezo ambavyo vinatumika kwa kweli havina uhalisia kwasababu maeneo hayo unakuta yanaangaliwa sana kwasababu yana miji lakini vilevile yana maeneo mengi sana yenye shule nyingi sana ambayo wananchi wamejitoa wakajenga shule ambazo zipo katika maeneo ya vijijini. Wanapoangalia vigezo vya reallocation unakuta kwamba hawaangalii hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali; je, Wizara itakuwa tayari kupitia upya vigezo vya ku-allocate walimu ili maeneo ya halmashauri za miji ambayo yana maeneo makubwa ya zaidi ya kilometa 25 yaweze kupata walimu ili elimu yetu iwe na tija? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri wazi kabisa kwamba alichozungumza Mheshimiwa Mbunge ya uhaba wa walimu nchini pamoja na replacement ya walimu 6,000 ambayo tunakwenda kuifanya hivi karibuni bado upo. Na Serikali imeji-commit hapa katika statement yangu ya awali kwamba tutaendelea kuajiri kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Na mpango huo upo na ni endelevu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ondoa wasiwasi kwenye hilo kwa sababu Serikali iko makini, na Serikali ya Rais wa Sita, mama Samia Hassan Suluhu, imejipanga kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumzia kuhusu Wizara kama tutakuwa tayari kupitia vigezo vya ugawaji wa walimu upya. Nikubali kabisa hilo tumelipokea, moja, ni kama ushauri, lakini pili, tutaendelea kulizingatia kuhakikisha kabisa ugawanyaji wa walimu wote nchini unafuata usawa na haki katika maeneo yote. Ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Tatizo ambalo linaikumba Njombe Mjini la uhaba wa walimu, ndilo tatizo hilohilo ambalo linaikumba Wilaya ya Chunya kwa uhaba wa walimu. Ajira mara ya mwisho iliyopita Wilaya ya Chunya tulipata takribani walimu 26 tu ambao ni idadi ndogo ukilinganisha na ukubwa wa Wilaya ya Chunya.

Je, Serikali inatuhakikishia vipi kwamba kwenye awamu hii ya ajira itakayokuja tutapata walimu wa kutosha, hasa maeneo ya vijijini, ili kuweza kukidhi mahitaji ya watu wa Wilaya ya Chunya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, moja, nikubaliane na yeye kwamba kweli hata Chunya nakufahamu vizuri. Eneo ni kubwa na kuna idadi ndogo sana ya walimu. Lakini kwa sababu ameleta hapa ombi na sisi kama Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumelipokea hilo ombi na katika mgawanyo wa walimu 6,000 tutalizingatia hilo. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na tatizo kubwa la walimu katika nchi nzima, na kuna walimu ambao wanajitolea kufanya kazi za kufundisha katika maeneo mbalimbali nchini, zinapojitokeza ajira walimu hawa hawapewi nafasi; je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha walimu wanaojitolea wanapewa kipaumbele pale nafasi zinapotoka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya vigezo ambavyo sasa hivi Serikali imekuwa ikitumia katika kuajiri walimu ni pamoja na kuzingatia walimu wote ambao wamejitolea kwa muda mrefu katika shule wanazofundisha. Kwa hiyo, hata katika hizi nafasi 6,000 ambazo tunakwenda kuzijaza zitazingatia vigezo hivyo. Na tumetoa maelekezo kwa maafisa elimu wote ngazi za wilaya kuleta taarifa za walimu wote wanaojitolea katika shule zao ili tuweze kuwazingatia katika ajira mpya. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yako ya msingi ameonesha kabisa changamoto ya walimu pamoja na kuajiri hawa waliopo bado changamoto itakuwepo, hasa kwenye walimu wetu wa sayansi. Na technology inakua, hasa matumizi yetu ya simu. Sasa kama Serikali, mna mkakati gani wa kuhakikisha sasa tuna-link, hasa zile shle zilizopo vijijini tukatumia hii mitandao ili wakawa na access ya wale walimu wanaofundisha wenzao mjini wapate elimu sawa na kule vijijini? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwenye masuala haya ya TEHAMA bado kuna changamoto kubwa sana hususan vijijini, na hata kwenye mitandao ya simu sisi wote ni mashuhuda kabisa kwamba networking ya mjini na vijijini ni tofauti kabisa. Lakini sasa hivi Serikali tuna mitandao, tuna mfumo ambao unawezesha walimu wa vijijini na mijini kuwa na access iliyo sawa. Kwa hiyo, pamoja na kwamba ameleta kama moja ya mapendekezo ama maoni na ushauri, basi sisi tutalipokea na moja ya kazi kubwa tutakazozifanya ni kuboresha mifumo iliyopo ili kuondoa hii changamoto ambayo ipo kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, miaka ya mwanzo ya 2000, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi ilikuwa na miradi ya viwanja 20,000, ambapo kwenye Jimbo la Kawe ilihusisha Kata ya Mbweni na Kata ya Bunju.

Mheshimiwa Spika, wananchi wakati wanalipia viwanja moja kati ya ahadi ya Serikali ilikuwa ni kutengeneza barabara za ndani. Hata hivyo, mpaka sasa hivi barabara nyingi za ndani za Kata hizi za Mbweni na Bunju kwenye mradi wa viwanja 20,000 bado ipo katika hali mbaya. Ninataka tu commitment ya Serikali kama itaenda kufanya uchunguzi na kuweza kwenda kufanya utaratibu wa kutengeneza barabara moja baada ya nyingine, kwa sababu wananchi walilipia kwenye viwanda.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima James Mdee kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alichokuwa anakitaka hapa ni ahadi ambayo ilitolewa na Serikali katika miaka ya 2000 ya kutengeneza barabara za ndani katika maeneo ya Bunju na Vijibweni. Mimi nimwambie tu kwamba tumepokea kile alichokisema, kwamba anataka commitment ya Serikali, na sisi tunakubali kwenda maeneo hayo, tutakwenda kufanya tathmini kujionea hali ili tuone na bajeti jinsi ambavyo tutakavyopanga kutekeleza ahadi ya Serikali ambayo ilikuwa imepangwa kwa wakati huo. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nimfahamishe Mheshimiwa Mdee kwa swali lake kwamba, ni kweli mradi huo ulikuwepo, lakini baadaye miradi yote kutoka kwenye Wizara tumeirudisha kwenye mamlaka za upangaji. Kwa hiyo ni jukumu pia la Halmashauri husika kuwasiliana na watu wa TARURA kwasababu zile zinakuwa zipo chini ya TARURA ili TARURA waweke kwenye mpango ili ziweze kufunguliwa kama ambavyo ilistahili kuwa.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru ahsante.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii niipongeze na kuishukuru Serikali ya CCM ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuweza kukubali mradi huu ambao wananchi wa maeneo haya wameteseka kwa miaka mingi sana. Siyo tu kwamba mradi huu unakwenda kupata suluhisho la mafariko kwa watu wa Kigogo, Hananasifu, Magomeni na Mzimuni, lakini pia makazi yao yanakwenda kuboreshwa na uoto wa asili unakwenda kurudi, nina maswali mawili ya nyongeza;

Mheshimiwa Spika, pale Kigogo kuna mito mingine miwili midogo ambayo inaitwa Tenge na mwingine Kibangu, mito hii sambamba na mto Msimbazi wakati wa mvua maji yanakuwa ni mengi sana na wananchi wanataabika sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa tuko katika hatua za awali za upembuzi wa jinsi gani Mto Msimbazi unakwenda kujengwa; Je, Serikali inakubaliana na mimi ni wakati sasa wa kwenda kupeleka wataalam ili wakausanifu Mto Kibangu uchepushwe maji yake yahamie kwenye Mto Msimbazi ili kuwanusuru wananchi wa maeneo hayo na adha hiyo ya mafuriko?

Swali langu la pili, kwa kuwa katika Kikao cha Tatu cha Mkutano wa Bunge lililofanyika tarehe 29 Aprili mwaka huu, Serikali ilikubali kumpeleka Mheshimiwa Naibu Waziri kwenda kujionea mwenyewe maeneo yale. Je, sasa Serikali iko tayari kuniambia ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri nitakwenda naye kule Kinondoni akajionee mwenyewe changamoto hizi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge amelileta kama ombi kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama tuko tayari kupeleka wataalamu wakafanye tathmini juu ya mito midogo ambayo inapeleka maji ikiwemo Mto Kibangu na Tenge, niseme tu kwamba jambo hili tumelipokea na tutatuma wataalam wakafanye tathimini waone namna ambavyo lile eneo limeathirika jinsi hiyo mito itakavyoleta maji tuone na gharama jinsi zitakavyokuwa na mwisho wa siku, baada ya hapo maana yake tutatoa taarifa kama litafanyika kwa wakati gani kulingana na bajeti itakavyopatikana kulingana na tathimini ambayo tutakuwa tumeifanya.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ameomba tuongozane kwenda Kinondoni nafikiri mara ya Bunge hili kuisha tutakwenda tutafanya ziara katika eneo la Kinondoni pamoja na maeneo yete ya Dar es Salaam, kwa hilo niko tayari kwenda kujionea hizi athari zote zinazotokea. Ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, matatizo ya Mto Msimbazi ni sawa kabisa na matatizo ya yaliyoko kwenye Mto Milongo katikati ya Jiji la Mwanza, ninataka tu kufahamu mto huu umekuwa unasababisha maafa mara kwa mara mvua zinaponyesha.

Je, ni lini Serikali inao mkakati wa kuhakikisha mto huu unajengwa upya na kuwekewa tahadhari zote kuepusha maafa yanayowakuta wakazi wa Kata za Mabatini, Milongo, Mbugani pamoja na Kata yenyewe ya Nyamagana. Ni lini Serikali itachukua hatua kuhakikisha mto huu na wenyewe unakuwa kwenye hesabu ya kushughulikiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameleta ombi jipya la Mto Milongo ambao na wenyewe umekuwa na athari zinazofanana na Mto Msimbazi. Kwa hiyo, tunalipokea kwa sababu Serikali muda wote iko kazini, kama ambavyo tunakwenda kufanyia kazi Mto wa Msimbazi maana yake na la kwake vilevile tunalipokea na tukishalipokea maana yake tutafanya tathimini na katika mipango ya baadaye tutaliweka katika mipango yetu. Ahsante sana.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ahadi ambazo Hayati Dkt. Magufuli aliahidi wakati wa kampeni ilikuwa ni pamoja na kujenga soko kuu la Mji wa Bunda pamoja na stendi mpya.

Je, kati ya stendi na soko kuu, ahadi hii yenyewe itatekelezwa lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKO ANA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Bunda Mji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hapa nimeelezea kwa chini kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa TACTIC, uendelezwaji wa miundombinu katika miji yetu. Na ule uendelezaji wa miundombinu kwenye TACTIC haihusu barabara peke yake, ni pamoja na masoko, stendi, madampo ya taka yaani tunatengeneza mji kuwa wa kisasa. Kwa hiyo, hata hiki anachokizungumza kuhusu soko kuu pamoja na stendi mpya katika Mji wa Bunda nafikiri itakuwa ndani ya package katika mradi huu wa TACTIC ambao mara utakapotekelezeka ni sehemu ya huo mradi, ahsante sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Tunduru, na kwa Kata hizi zilizotajwa; Tinginya, Malumba, Kalulu, Mindu, Narasi Mashariki na Narasi Magharibi, ni kata ambazo hazina vituo vya afya. Lakini pia zinazungukwa na Selous Game Reserve. Wakati mwingine unakuta wale akinamama wanaokwenda kujifungua, haja ya kujifungua inawapata wakati wa usiku ambapo sasa kutoka maeneo waliyopo mpaka kufika kwenye hospitali ya wilaya pana zaidi ya takribani kilometa 80 mpaka 100 na wakati mwingine sasa wamekuwa wakipata majanga ya kuvamiwa na tembo, wanyama wakali kama simba na chui.

SPIKA: Swali.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa wananchi hawa kujengewa vituo vya afya ili waweze kuondokana na adha hiyo?

(b) Mheshimiwa Spika, maeneo hayo yote niliyoyataja yana zahanati tu, na zahanati zao wakati mwingine unakuta hazina watumishi wa kutosha. Zahanati moja ina mtumishi mmoja na kwamba akiumwa huyo mtumishi ni wiki nzima hakuna huduma ya afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba zahanati hizo zinapelekewa wahudumu wa afya ili waweze kupata huduma inayostahili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza kwamba lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga vituo vya afya katika maeneo hayo. Na nilishalijibu katika jibu langu la msingi kwamba kwa kadri ya upatikanaji wa fedha Serikali tutaendelea kujenga katika maeneo husika, na nimhakikishie kabisa kwamba Serikali inazingatia umuhimu wa maeneo hayo ambayo wananchi wanatokea. Kwasababu kama alivyoeleza hapo awali kwamba kuna changamoto nyingi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tutayaingiza katika mpango na fedha itakavyopatikana ataona matokeo yake.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ameeleza kwamba katika maeneo hayo watumishi/wahudumu wa afya hawapo wa kutosha. Na sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tuna huo mpango, kwa kadri tunavyokuwa tunaajiri kutokana na vibali ambavyo tunapatiwa tutaendelea kuwatenga. Kwa hiyo, hata maeneo hayo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kupeleka kulingana na vibali vya ajira ambavyo serikali itakuwa inatupatia. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Changamoto zilizoko Tunduru zinafanana sana na changamoto zilizoko kule Arumeru Mashariki, hususan Kata za Maruvango, Kikatiti, Malula na Majengo. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya afya kwenye hizo kata ambazo nimezitaja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi kwamba kwa kadri Serikali tutakavyokuwa tunapata fedha ya kutosha na bajeti yetu tutakavyokuwa tunaitenga, tutaendelea kujenga. Kwa hiyo, hata maeneo ya Arumeru Mashariki nayafahamu na ninajua umbali wake. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri fedha itakavyopatikana basi tutazingatia na maeneo husika. Ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, bado hali ya Urambo ni mbaya kuhusu upimaji wa afya ya akinamama na watoto kwa kuwa X- ray ni mbaya. Na wakati huohuo, pamoja na jitihada nzuri ya kupata ultrasound mbili, bado ultrasound hizo hazina watumishi, zimekaa bure. Kwa hiyo, sasa kwa kuwa hakuna X-ray kama alivyojibu Mheshimiwa Waziri, ultrasound tumejitahidi tumepata mbili, hazina watumishi. Je, lini Serikali italeta watumishi wawili angalau zile ultrasound zianze kupima akinamama na watoto? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; pamoja na nia nzuri ya Serikali yetu ya kutujengea kituo cha afya Mlimani katika Kata ya Uyumbu, jengo la akinamama na watoto linakaribia kuisha lakini limepungukiwa milioni 100. Suala hili tulizungumzia Mheshimiwa Waziri mhusika alipokuja kutembelea, Mheshimiwa Dkt. Festo, bado ile hospitali inahitaji kumaliziwa jengo. Je, lini Serikali itatuletea milioni 100 ambazo tumekisiwa zimalize ili wodi ya akinamama ianze kutumika badala ya sasa wanakwenda mbali kwa lengo la kujifungua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza na ameomba hapa kwamba walau wapelekewe watumishi wawili katika maeneo ambayo tumepeleka ultrasound na X-ray katika Wilaya yake ya Urambo. Nimhakikishie kabisa kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tumekubaliana kwamba Waziri husika anaendelea kufanya utafiti na kuhakikisha ndani ya kipindi hiki kifupi wanapeleka mtaalam katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, commitment ya fedha ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia jengo lililoko katika Jimbo la Urambo ambayo inahitajika kuhakikisha hilo jengo linaanza kutumika kwa wakati. Nimhakikishie kabisa kwamba nimewasiliana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ameniagiza kwamba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutapeleka wataalam wetu wakaangalie hiyo tathmini na baada ya hapo tutatoa majibu ya msingi kuhakikisha hilo jengo linakwisha na linaanza kutumika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, japokuwa ntaendelea kubakia kuwa mwananchi mtiifu wa Jangwani, na chini ya GSM naamini kwamba tutavuka salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja katika Jimbo la Kilombero na Mheshimiwa Job Ndugai akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu alipokuja katika Jimbo la Kilombero, waliwaahidi wananchi wa Jimbo la Kilombero juu ya ujenzi wa Hospitali ya Jimbo la Kilombero. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, dada yangu, Mheshimiwa Ummy, ametuahidi kwamba tutapata milioni 500 za kuanza ujenzi huu.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, ni lini ujenzi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kabisa katika bajeti inayokuja ya mwaka 2021/ 2022, Serikali imehakikisha kuanza hospitali mpya katika halmashauri zote nchini ambazo hazina hospitali za wilaya.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, natambua mchango wa Serikali kwa kupeleka fedha kwenye ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi lakini kilio cha Wanankasi ilikuwa ni kupata huduma kwa level ya Wilaya. Mpaka sasa jengo lipo lakini huduma inayotolewa hailingani na huduma inayotakiwa kutolewa katika Hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba pamoja na madaktari kulingana na level ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika eneo lake kuna jengo ambalo bado kutumika kwasababu ya vifaa tiba. Na hilo nimwambie tu kabisa kwamba mimi kabla sijafika hapa nilikuwa nazungumza na Waziri anayehusika na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na katika bajeti yake ambayo tutakwenda kuipitisha, kuna fungu ambalo tumetenga kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya hospitali zote ambazo majengo yake yako tayari lakini hayajakamilika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukishapitisha bajeti, ninaamini kabisa kwamba mara baada ya Bunge hili na mara baada ya bajeti kupita, basi hivyo vifaa na vifaa tiba vitatengwa na kupelekwa. Suala la watumishi basi tutaendelea kutenga kulingana na vibali vya ajira ambavyo tunapatiwa na Serikali. Ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Kata hizo ambazo nimezitaja Kata ya Maboga, Kata ya Kalenga, Kata ya Ulanda, Kata ya Wasa wananchi ni wakulima ambao wanalima mali mbichi nyingi sana; viazi, njengere, maharage na mengine mengi na barabara imekuwa ni kikwazo katika kusafirisha hizo mali zao, na wamekuwa wakipata tabu mali zinaharibikia njiani. Mwaka 2020 pesa alizosema zimetolewa walikwangua sababu ilikuwa ni wakati wa uchaguzi, na sasa hivi baraba hazipitiki.

Je? Kwa nini Serikali haioni kwamba hii barabara sasa imekuwa ni kubwa na inahudumia watu wengi ambayo inaweza ikaenda mpaka ikatokea Madibila Mbeya ili iingie katika mpango wa TANROADS na itoke TARURA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna barabara ambayo wananchi wametumia nguvu zao ambayo imetobelewa kutoka katika Kata ya Kihanga ikaja katika Kata ya Maboga ambako kuna Zahanati na kuna Hospitali ya Wilaya iliyoko Tosamaganga, wananchi wanashindwa kufika kupata hudama hizo.

Je, ni lini sasa Serikali itaifanyia kazi barabara hii ili wananchi hawa waweze kupata huduma hizo za afya na kuweza kufika katika maeneo hayo kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Victor Tendega Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza kwamba kwa nini Serikali sasa isione umuhimu wa kuihamisha barabara ambayo inapita Maboga, Kalenga, Wasa, Kihanga mpaka kutokea Madibila kutoka TARURA kwenda TANROADS.

Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie kabisa kwamba si barabara zote zinahitaji kupandishwa kwenda na kuhudumiwa na TANROAD, lakini jambo kubwa ambalo naweza nikamuhakikishia ni kwamba kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Serikali itaendelea kuzitengea fedha barabara zote za muhimu.

Mheshimiwa Spika, na kikubwa ambacho alikuwa amekisema Serikali haifanyi kazi wakati wa uchaguzi peke yake, Serikali inafanya kazi muda wote, na katika bajeti hizi tumetenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili ameuliza vilevile barabara ya kutoka Kihanga kwenda Maboga ambako amesema kuna kituo cha afya ni lini Serikali itahakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa, nimeeleza hapa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na kwa sababu fedha tumetenga katika bajeti na kwa sababu bajeti tunakwenda kupitisha sisi sote hapa nikuombe Mheshimiwa Mbunge tupitishe hiyo bajeti ili barabara zetu zitengenezwe, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Leo tutajadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na sehemu ya hotuba hiyo tutajadili suala la ajira hususan kwa vijana. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali iliruhusu tusafirishe mazao ya misitu kwa saa 24 na hivyo kusisimua na kuchechemua uchumi sio wa Mafinga tu na maeneo mengine. Je, Serikali iko tayari kufanya upendeleo maalum kwa Mji wa Mafinga kutokana na nature yake ya kibiashara kuruhusu baadhi ya maeneo watu kufanya biashara saa 24 na yenyewe ikabaki na suala la ulinzi ambayo ni kazi kuu ya Serikali?

Mheshimiwa Spika, swali pili, katika jibu la msingi Serikali imesema kuna changamoto ya miundombinu muhimu kama vile taa, kamera na kadhalika. Sisi kama Halmashauri tuko tayari kujenga baadhi ya miundombinu lakini je, Serikali iko tayari kutusaidia japo taa za barabara katika maeneo muhimu katika njia panda za Itimbo, Madibila, Mufindi na Sokoni ili kuwawezesha wananchi hawa kuendelea kujiajiri na kujipatia kipato na hivyo kuwa na mchango katika Serikali na mifuko yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Mbunge alikuwa anataka upendeleo maalum kwa Mji wa Mafinga ili uweze kufunguliwa. Katika jibu langu msingi nilieleza kabisa moja ya jukumu kubwa la Serikali ambalo tunalifanya sasa ni kuhakikisha tunajenga miundombinu na usalama unakuwepo. Baada ya kutathmini ndipo tunaweza kuruhusu Mji wa Mafinga ili uweze kufanya biashara kwa saa 24.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ni la msingi kabisa Mheshimiwa Mbunge ameainisha commitment ya Halmashauri yake kwamba wao kama Mafinga Mji wako tayari kujenga baadhi ya miundombinu muhimu na sisi kama Serikali tuweze kusaidia katika kuweka hizo taa za barabarani. Nafikiri wazo hilo ni jema na mimi niungane kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kusema kwamba tunaomba Halmashauri ya Mji Mafinga waanze hiyo hatua ya kutengeneza hiyo miundombinu muhimu na sisi tutatuma wataalam wetu waende kufanya tathmini, ili tuweze kuwaruhusu waweze kufanya hiyo biashara yao kwa saa 24 na sisi tutawasaidia katika hiyo sehemu itakayobakia.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imejenga mifereji katika baadhi ya maeneo, lakini mfereji wa kutoa maji kutoka Kata ya Shangani, maeneo ya Kiangu kwenda baharini haufanyi kazi vizuri, maji yanajaa sana kwenye majumba ya watu. Sasa swali langu, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kwenda Mtwara kuuona mfereji ule na kufanya utaratibu wa kuhakikisha mfereji ule unatengenezwa kwa kiwango kizuri ili kusudi wananchi wale wasiweze kupata adha hiyo maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, maeneo mengi ambayo yanajaa maji katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ni ambayo Serikali imepima viwanja ikawagawia wananchi, siyo kwamba wamevamia. Katika kujaa maji kule kunasababisha uharibifu na wakati mwingine vifo vya wananchi.

Je, Serikali sasa iko tayari kwenda kukaa na wananchi wale waone wanatatua vipi changamoto hizi kwa sababu kadri miaka inavyokwenda tatizo ni kubwa, linaharibu mali na wakati mwingine kugharimu maisha ya wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza alilokuwa ameliomba, anaomba sisi kama Ofisi ya Rais – TAMISEMI hususani Waziri kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda katika eneo husika kushuhudia anachokieleza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, niko tayari mara baada ya kupitisha bajeti yetu, nitaongozana naye pamoja na Mbunge wa Jimbo husika kuhakikisha tunaipatia ufumbuzi kero hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ameuliza kama Serikali ipo tayari kukaa na wananchi, nimhakikishie tutakavyokwenda kule tutakaa na wananchi ili tuweze kupata suluhisho la tatizo hilo. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Changamoto ya kujaa kwa maji yanayotokana na mvua iliyoko Mkoa wa Mtwara haina tofauti kabisa na changamoto iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam hususan eneo la Jangwani. Kujaa kwa maji katika eneo la Jangwani imekuwa ni changamoto ya muda mrefu na haijawahi kupatiwa tiba ya kutosha. (Makofi)

Mhesimiwa Spika, swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani au inatueleza nini kuhusiana na changamoto hii ya kujaa maji pale Jangwani hasa ikizingatiwa kwamba Jangwani ni kiunganishi kikubwa sana cha wafanyabiashara wanaoelekea Kariakoo eneo ambao limebeba uchumi mkubwa sana wa nchi? Naomba Serikali basi itoe majibu ni lini itaweza kukomesha changamoto hii ya kujaa maji Jangwani. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Agnesta Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuoanisha eneo la Jangwani na maeneo yaliyoko kule Mtwara katika Manispaa ya Mikindani kwamba na lenyewe linajaa sana maji na anataka kufahamu mkakati gani ambao Serikali inao kuhakikisha tunatatua tatizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuna mradi mkubwa wa DMDP ambao unajenga miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam. Sehemu ya miundombinu hiyo ambayo tumekuwa tukiijenga ni pamoja na mifereji mikubwa ambayo imekuwa ikihamisha maji kutoka katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kupeleka baharini.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, sasa hivi tuna Mradi mkubwa wa Mabasi Yaendayo Kasi na moja ya jukumu lao kubwa ni kuhakikisha lile eneo la Jangwani linapandishwa tuta kubwa ambalo litahakikisha ile kero ambayo inawapata wananchi inaondolewa. Kwa hiyo, nimhakikishie kabisa Serikali ipo kazini na ile kazi itakamilika na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam hawatajutia kuichagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Halmashauri ya Meru nayo ilikuwa victim ya withdraw ya mradi mkakati ambayo ilikuwa imetengenezwa mwaka ule wa 2019. Naomba kuuliza: Je, Serikali sasa iko tayari kuja kutekeleza ule mradi?

Mheshimiwa Spika, Mradi huo uko eneo la Tengeru mahali panaitwa Sadak, ulikuwa umeshatengenezwa na Serikali ilikuwa imeshachakata lile andiko na nilipofika kule Hazina nikakuta karibia pesa zinatoka, kuja hapa Bungeni nikaambiwa mradi umekuwa withdrawn: Je, ni hatua gani zinazoendelea kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Meru nayo inawezeshwa, kwa sababu sasa hivi inashindwa kuhudumia wananchi kwani haina mapato ya kutosha?Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ni kweli mwaka 2019/2020 Serikali ilijaribu kusitisha kwa muda miradi yote ile ambayo ilikuwa inasuasua. Sasa hivi nikuhakikishie kwamba, Serikali imejipanga na tumekubaliana tui-review; na miradi yote ile ambayo ilisitishwa, ile miradi ya kimkakati katika Halmashauri zote ambazo zilikuwa zimepangiwa awali, inakwenda kufanya kazi. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, changamoto ya Hanang inafanana sana na changamoto iliyopo kwenye mji wetu wa Chemba. Ni bahati mbaya sana uwezo wa Halmashauri yetu, ni mdogo: sasa naomba kujua, ni lini Serikali itajenga stendi kwenye Mji wetu wa Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nieleze tu kwa kifupi kwamba, ile miradi ya kimkakati katika Halmashauri ilikuwa na vigezo kwa kila Halmashauri kupata. Tuliainisha vigezo 13 ambavyo Halmashauri ikivikamilisha inapata ile miradi. Moja ya vigezo ikiwemo ni; katika miaka mitatu mfululizo, Halmashauri hiyo iwe imepata hati safi. Kwa hiyo, kama ulikuwa unakosa baadhi ya vigezo, basi ulikuwa hau-qualify kupata hiyo miradi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge kuhimiza Halmashauri zenu kutimiza vigezo vyote. Vigezo ambavyo vimekamilishwa, vinaletwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI nasi tukiona kwamba Halmashauri ina-qualify, basi tunawa-guarantee kupata huo mradi kwa ajili ya kusaidia Halmashauri zetu kuongeza mapato yao ya ndani. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya barabara hiyo, lakini barabara hiyo imechukua muda mrefu sana, zaidi ya miaka mitano haijatengenezwa kabisa na madaraja yote yamekatika kabisa. Wananchi wa Kata ya Isaba, Kazovu, Bumanda, Korongwe, Katete wanapata tabu sana wakati wanapotaka kwenda kupata huduma za afya katika Kata ya Kirando. Swali la kwanza; nataka kujua, ni sababu zipi zimesababisha kusimama kwa ujenzi wa barabara hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami mguu kwa mguu kwenda kuona tatizo lililopo katika wilaya hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunakiri kabisa kwamba sababu kubwa ya kuchelewa ama kutokukamilika kwa wakati kwa barabara hii kwa muda mrefu ni kutokana na kuwa na bajeti finyu. Hivyo tumeendelea kufanya matengenezo ya kawaida kwa kipindi hiki cha miaka hii ambayo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaieleza. Hata hivyo, tunaahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Serikali bado itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hii kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa sababu ya kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Mbunge ya kuwapigania wananchi wa maeneo ya Nkasi pamoja na Mkoa mzima wa Rukwa na najua kila siku amekuwa akitukumbushia katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye barabara hizi, nimuahidi kabisa mara baada ya Bunge hili nitaongozana naye tukawasikilize wananchi na kupatia ufumbuzi barabara hizo. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto ya barabara ambayo imetoka kutajwa ya Kirando – Katete ni sawasawa na changamoto ya kutoka Wanging’ombe kwenye Jimbo la Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, kutoka Wanging’ombe kuelekea Kipengele, Lupira, Kijombo hadi Lumbira ile barabara ambayo iko chini ya TARURA. Naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa sababu hadi dakika hii ninavyozungumza wakazi wamekuwa wakilala njiani wakati wanaposafiri kutokana na changamoto ya barabara hiyo? Kwa hiyo, naomba majibu ya swali hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Festo Sanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu na bahati nzuri ameainisha katika eneo ambalo Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, jimboni kwake ndiko barabara ilikoanzia, lakini kwa sababu mimi na Mheshimiwa Mbunge pamoja na yeye mwenyewe anafahamu katika bajeti fedha ambazo tumekuwa tukitenga na tunaahidi mbele yako kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa kadri zinavyopatikana kuhakikisha hii barabara inapitika wakati wote. Ahsante. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa majibu ambayo yanaeleza zaidi barabara za kawaida kwa sababu milioni 900 haina uwezo wa kujenga kilometa ya lami hata moja. Kwa hiyo naomba sasa kujua kwa sababu Mji wa Ikungi ni mpya kwa maana ya wilaya ni mpya na kwa sababu Makao Makuu ya Wilaya tunategemea yawe na lami. Sasa naomba nijue kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu alituhakikishia tangu 2019 na leo ni 2021; je, ni lini hasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga hizo kilometa tano ya lami ili wananchi wa Ikungi nao waweze kupata lami na kufaidi matunda ya uhuru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu ni lini sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga kilometa tano za lami katika Makao Makuu ya Wilaya yake katika eneo la Ikungi. Ni kwamba, kama katika jibu letu la msingi tumeainisha hapa kwamba katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, tumepanga kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini kwa maana ya TARURA kutenga fedha kwa ajili ya kufanya usanifu na tathmini za gharama ya ujenzi kwa kiwango cha lami katika eneo hilo. Kwa hiyo mara baada ya usanifu na tathmini ya kina ambayo itakwenda kufanyika katika mwaka huu wa fedha maana yake katika mwaka wa fedha unaofuatia tutaanza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami katika eneo la Ikungi. Nimhakikishie, Serikali ya Rais wa Sita, mama Samia Suluhu Hassan iko tayari kukamilisha ahadi hiyo kwa vitendo. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kufahamu kwamba, ni lini barabara ya kutoka Mlowo kwenda Kamsamba ujenzi wake utaanza, ikizingatiwa kwamba, suala zima la upembuzi pamoja na usanifu limeshakamilika, lakini pia ni barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya Awamu ya Tano pamoja na Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipokuja kwenye kampeni. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA – MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, barabara hii naifahamu vizuri ni barabara ambayo inasimamiwa na TANROADS. Ni kutoka Mloo mpaka Kamsamba ambapo ni nyumbani kwetu kabisa ni kilometa 166.6 na miaka yote imekuwa ikihudumiwa na TANROADS. Bahati nzuri kwasababu Serikali ni moja na ndio maana iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ninaamini mimi na yeye tukishirikiana kwa pamoja ile barabara itajengwa kwa kiwango cha lami na ninajua Serikali imeipangia fedha kwa ajili ya ujenzi utakaoanza hivi karibuni. Ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Wazir nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara Miyuyu - Ndanda kimekuwa kimetengewa fedha mara kwa mara za matengenezo ya kawaida, lakini fedha hizo hazitibu shida iliyoko kwenye mlima pale na barabara ile ni barabara ambayo inatumika kwa wagonjwa kutoka Wilaya za Newala na Tandahimba wanaopata rufaa kwenda Hospitali ya Ndanda. Hali ya pale ni mbaya, ni mlima kumbwa na korongo kubwa kiasi kwamba inahatarisha usalama kwa watumiaji wa barabara ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupata kauli ya Serikali. Ni lini itajenga kwa kiwango cha lami barabara ile hasa kipande kile ili wananchi wanaotumia hospitali ya Ndanda kama hospitali ya Rufaa waweze kupata urahisi wa kufika hospitalini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jimbo la Newala Vijijini, zimesababisha athari kubwa sana ya barabara kukatika magari hayapiti, hata pikipiki zinapita kwa shida, kwa mfano barabara kutoka Malatu Shuleni - Namkonda hadi Chitekete, barabara ya Maputi - Meta, barabara ya Likwaya Nambali, barabara ya Mtikwichini - Chikalule, barabara ya Mtikwichini - Lochino na Chikalule.

Mheshsimiwa Naibu Spika, upi mpango wa Serikali wa kupeleka fedha kwa ajili ya dharura ya kutengeneza barabara hizo ambazo kwa sasa hazipitiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge aliuliza eneo korofi la Mlima Miyuyu mpaka Ndanda na amesema kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha, lakini bahati mbaya tatizo hilo limekuwa halitatuliki, kwa hiyo, alikuwa anaiomba Serikali ni lini itajenga lami katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu peke ninachoweza kumuhakikishia ni kwamba kutokana na ombi alilolileta na sisi Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutakwenda tufanye tathimini na baada ya hapo tutaleta majibu ya eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sehemu ya pili barabara ambazo amejaribu kuzitaja Mheshimiwa Mbunge ambaye ninaamini anafanya kazi hii kwa nia njema ya kusaidia wananchi wake wa Jimbo la Newala, ameainisha maeneo mengi sana na kutaka mpango wa dharura na lenyewe nimuhakikishie kwamba Serikali tumesikia na kwa sababu katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha yakiwemo hayo maeneo ambayo ameyaainisha, lakini Serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta vyanzo vingine.

Kwa hiyo kulingana na bajeti itakavyopatikana na sisi tutaakikisha kabisa kwamba tunatatua matatizo ya wananchi wa Newala na maeneo mengine ya Tanzania. Kwa hiyo, ahsante sana Mheshimiwa Mbunge tumepokea maombi yako na nikupongeze kwa kazi nzuri kwa wananchi wako, ahsante sana. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na jiografia ya Mkoa wa Kilimanjaro, niseme ukweli kwamba changamoto yetu kubwa kule Kilimanjaro ni barabara hasa Jimbo langu la Moshi Vijijini na wakati wa mvua kama huu kuna mafuriko makubwa sana. Naomba nimuulize Naibu Waziri ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya TPC – Mabogini – Kahe yenye urefu wa kilometa 11.4 na kumalizia zile za Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School - Kiboriloni - Sudini – Kidia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ilishasema ingeanza upembuzi yakinifu wa barabara ya Uru – Mamboleo - Materuni yenye kilometa 10.2, ni lini Serikali itafanya zoezi hilo. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ulivyoniongoza, umeniomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kuhusu ni lini upembuzi yakinifu utaanza katika barabara ya Uru – Mamboleo – Materuni yenye urefu wa kilometa 10.2.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais makini kabisa Mama Samia Hassan Suluhu, tumesikiliza maombi ya Mheshimiwa Mbunge. Kwa sababu ameomba tu upembuzi yakinifu na nafahamu mpaka muda huu TARURA wananisikiliza ni agizo langu kwao kwamba sasa watenge fedha waanze upembuzi yakinifu kwa ajili ya barabara hiyo ili iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia hizo barabara nyingine zote ambazo ameziainisha, Serikali imesikia tutaziweka katika Mpango kuhakikisha zinakamilika kwa wakati. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mpaka sasa kuna kaya kumi ambazo maji yameingia ndani na hawana pa kuishi katika Mtaa wa Ununio, Serikali ina mkakati gani wa dharura kabla ya kutekeleza mradi huu alioutaja ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata mahali pa kuishi na sehemu zile nilizoainisha zinapata majibu mapema? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilio hiki ni cha nchi nzima kwa maana matatizo haya yamekuwa yanajirudia kila eneo la nchi; ni lini basi Serikali itaweka mikakati madhubuti ya kujenga mifereji imara ili basi maeneo haya maji yaweze kuelekezwa kwenda kwenye maziwa, mito hata bahari ili kuepuka adha ya magonjwa ya milipuko pia na adha kwa wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza alikuwa anaomba kujua upi ni mkakati wa dharura katika eneo la Ununio ambao Serikali imeuweka kuhakikisha tunatatua tatizo hilo la mafuriko. Nimuambie tu kabisa kwamba Serikali iko kazini na baada ya janga hili inafanya tathmini ya mwisho kuhakikisha kwamba tunasaidia maeneo hayo hususan maeneo ya Ununio katika Kata hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza ni lini Serikali itaweka mikakati madhubuti kuhakikisha kwamba tunaondoa majanga haya hususan kwa kujenga mifereji. Nimhakikishie kabisa kwamba sasa hivi moja ya mkakati mkubwa ambao Serikali unao katika kila barabara tunayoijenga tunaambatanisha na ujenzi wa miundombinu hususan mifereji. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu ya mikakati ambayo ipo na tutaendelea kufanya hivyo. Kwa kadri fedha zitakavyopatikana tutajenga mifereji mikubwa pamoja na midogo kuhakikisha janga la mafuriko nchi nzima katika maeneo yote ambayo tunayasimamia hayapatwi na hii adha ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha. Ahsante sana.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ujenzi huu ni ahadi ya muda mrefu, ni miaka sita sasa lakini kama ambavyo ameweza kutoa majibu utekelezaji wake umeanza kwa kuweka kifusi katika Mji ule wa Kakonko. Ni miezi minne sasa shughuli za biashara katika Mji ule hazifanyiki, je, Serikali iko tayari angalau kifusi kiweze kusawazishwa katika maeneo yale ili wananchi waendelee na shughuli zao wakati taratibu hizo nyingine zikifanyika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya Kakonko – Kinonko – Nyakayenze - Muhange na Kasanda - Gwanumpu - Mgunzu ni barabara ambayo iko chini ya TARURA. Barabara hii imeharibika sana pamoja na kwamba ni maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa, wananchi hawawezi kusafirisha mazao yao. Je, nini jibu la Serikali kuhusiana na suala hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anaiuliza Serikali kwamba ni kwa nini sasa tusisambaze kile kifusi ili shughuli zingine ziendelee. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi ni kwamba barabara ile inajengwa kwa kiwango cha lami, kwa hiyo, kile kifusi ni sehemu tu ya process za kukamilisha barabara ile. Kama tulivyojibu kwenye jibu la msingi kwamba kufikia mwezi Mei, yaani mwezi ujao ile barabara itakuwa imekamilika kwa kiwango cha lami kwa sababu TARURA wako kazini. Hapa napozungumza wanasikia, nina hakika hilo zoezi litakuwa linaendelea na kazi inafanyika.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ameainisha barabara ambazo zimeharibika sana na kuiomba Serikali iweze kuzifanyia kazi. Nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmini na baada ya hapo nafikiri sisi na TARURA katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko tutakaa pamoja kuhakikisha barabara hiyo inajengwa ili kuondoa hiyo adha ambayo wananchi wanaipata. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara kule Kakonko inafanana kabisa na ahadi ya Mheshimiwa Rais katika barabara ya Boay – Gidas hadi Getasam, Wilaya ya Hanang, lakini barabara ya Boay –Gidas, barabara ya Babati Vijijini: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huu wa barabara kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, sasa hivi barabara hiyo imekuwa ni chakavu kabisa na haiwezi kupitika: Je, Serikali inatuahidi nini hata kutusaidia kwa kiwango cha changarawe? Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ambacho amejaribu kukiainisha Mheshimiwa Mbunge; ni lini Serikali itaanza kukamilisha ahadi za Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Marais wote waliotangulia na hapa amejaribu kuainisha barabara katika maeneo ya Hanang na Babati Vijijini.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie kwamba mpaka sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Serikali kwa ujumla tumeanza mchakato wa kuziainisha ahadi zote zilizotolewa na viongozi wakubwa nchini. Baada ya hapo tutazifanyia tathmini, tutazitenga katika mipango yetu na kuziwekea bajeti ili kuhakikisha kila ahadi ambayo kiongozi mkubwa aliahidi inatekelezwa na kwa wakati ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi, hususan maeneo yale ambayo yana-involve sana uzalishaji mkubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Jimbo la Tabora Mjini ya walimu na madawati yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Jimbo langu la Kaliua nilikuwa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja; Kaliua katika shule zetu za Usenye, Usinge, Ufukuto na maeneo mengine tuna upungufu wa walimu wa msingi na sekondari wapatao 873.

Je, Serikali ni lini itatupatia walimu hao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Kaliua tuna upungufu wa takribani madawati 4009. Je, Serikali ni lini itatupatia madawati hayo au fedha kwa ajili ya kukamilisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE.DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kwezi, Mbunge wa Kaliua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza la Mheshimiwa Mbunge alikuwa anazungumzia kwamba katika Jimbo lake kuna upungufu wa walimu 873 na akataka kufahamu ni lini Serikali tutapeleka walimu hao? Mimi nimuahidi tu kabisa kwamba katika mgawanyo ambao tutakwenda kuajiri wale walimu 6000 basi sehemu ya walimu wale baadhi tutapeleka katika Halmashauri yake na Jimbo lake la Kaliua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili kuhusu madawati, changamoto ya madawati kama tulivyoahidi na tumetenga katika bajeti yetu ambayo Waheshimiwa Wabunge mliipitisha kwamba katika yale madawati 710,000 sehemu ya hayo madawati tutapeleka katika jimbo lako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi na hilo. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kuandikisha watoto kuingia darasa la kwanza kunakuwa na sharti la Watoto kwamba ni lazima waje na certificate ya kumaliza elimu ya awali; na changamoto hii imekuwa ni kubwa sana katika maeneo ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam katika shule kama za Mbande, Majimatitu, Charambe, Nzasa na maeneo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam:-


Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kuondoa changamoto hii kwa wananchi au wazazi ambao wanapeleka watoto wao kuwaandikisha darasa la kwanza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa uwiano wa darasa la kwanza utakuta kuna mikondo minne au mitano ya lakini darasa la awali linakuwa moja tu, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa watoto wote ambao wanaanza darasa la kwanza kwenda kujiunga na elimu ya awali katika shule husika:-

Je, Serikali imejipangaje sasa kuweka bajeti ya kutosha katika kuimarisha elimu ya awali katika shule zote za msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali hapa kwamba kumekuwa na sharti la certificate ya Elimu ya Awali; na anataka kufahamu Serikali inatoa kauli gani? Kwanza nieleze tu kabisa kwamba katika ngazi ya awali, Serikali haina utaratibu wa certificate. Hizo ni taratibu ambazo watu wamejitungia huko chini. Mara nyingi sana ni hizo shule za private zaidi ndiyo wamefanya hivyo, lakini huo utaratibu haupo.

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali ni moja tu; certificates zilizopo ni za darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita na kuendelea, lakini kwa shule za awali certificate hakuna. Huo ni utaratibu ambao Serikali haiutambui. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, uwiano wa wanafunzi, hususan darasa la kwanza na shule ya awali; na kwa sababu hiyo niseme tu kwamba kutokana na umuhimu wa kuongeza wanafunzi katika shule za awali, ndiyo maana sasa hivi katika mipango yote ya Serikali ambayo tunayo, ikiwemo EP4R, Boost, Lens, RISE, miradi yote, tumehakikisha kabisa kwenye kila mradi tunaweka na component ya kujenga madarasa ya shule za awali ili kuhakikisha watoto wetu wanapata madarasa bora na tunaongeza madarasa ili watoto hao waweze kupata mazingira bora ya kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na vile vile nampongeza Mheshimiwa Mariam Kisangi. Nataka tu kuendelea kutoa tamko la kisera; ni marufuku shule kudai certificate ya awali kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni kwamba bado hatujafanya vizuri katika kuongeza access ya watoto kuanza elimu ya awali. Kwa hiyo, haileti mantiki kusema kila mtoto ili aanze Darasa la Kwanza awe na certificate ya awali. Tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwenda kuweka nguvu za kuboresha watoto wetu hususan wa masikini kupata elimu ya awali, hususan katika maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona niweke hiyo; na wote ambao wanadai certificate ya elimu ya awali wajue kwamba wanatenda kinyume na maelekezo na miongozo ya Serikali.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe shukurani kwa majibu, lakini nataka niseme kwa mradi ambao unazungumzwa wa TACTIC mradi huu nadhani ulishapangiwa fedha, lakini mpaka sasa hivi jinsi ninavyozungumza kuhusu Kata ya Magomeni na Ufukoni bado hali ni mbaya. Je, Serikali ni lini ujenzi wa barabara hizi utakua tayari?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ni lini miundombinu ya mifereji ambayo tulikua tunaizungumza toka mwanzo Serikali itakua tayari kuweza kuboresha mifereji ambayo sasa hivi mara kwa mara kunapatikana mafuriko makubwa na wananchi inatokea hali sinto fahamu kwenye majumba ya watu na wengine kupoteza maisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ambazo ameziainisha zilizopo katika mradi wa TACTIC kwa kifupi ni kwamba mradi wa TACTIC bado katika hatua za mwisho za makubaliano na mahafikiano na Serikali ili zianze kutekezwa.

Kwa hiyo, Mbunge nikuhakikishie kabisa kwamba mara baada ya huu mradi kuwa umekamilika na Serikali kumaliza hatua zote, barabara hizo ambazo umeziainisha zitaanza kujengwa kwa sababu ziko katika mradi wa TACTIC.

Mheshimiwa Spika, vile vile, katika sehumu ya ule mradi wa TACTIC miongoni mwa component ambazo ziko ndani yake ni pamoja na ujenzi wa mifereji kwa hiyo, mradi huu utakapokua umefikia hatua za mwisho na ninaamini Serikali ipo katika mazungumzo na ninahuhakika kabisa mara itakavyokamilia basi barabara zako pamoja na mifereji ya wananchi wa Mtwara Mjini itajengwa kama ambavyo imeainishwa katika huo mradi ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru changamoto iliyopo Mtwara ya barabara inafanana sana na changamoto Nkasi. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alituahidi wana Nkasi kipande cha barabara kutoka Chala mpaka Mpalamawe, ningependa kupata commitment ya Serikali kwa kuwa ahadi zote zinakua recorded ni lini ahadi hiyo itatekelezwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ametaka kujua tu ni lini ahadi ya Mheshimiwa Hayati Rais ama niseme ahadi zote za viongozi ni kwamba sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ipo katika hatua ya mwisho tunakusanya na kuandaa mpango wa namna ya kutekeleza ahadi zote za viongozi na nikuhakikishie tu kwamba kuanzia mwaka wa fedha ujao tutaanza kutenga pole pole fedha kwa ajili ya kuhakikisha zile ahadi zote ambazo viongozi wakuu walikua wamezitoa zinaanza kutekelezeka.

Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali makini na imeshazungumza hadharani kwamba kazi inaendelea yale yote yaliyozungumzwa tutayaendeleza kuhakikisha kwamba tunawahudumia wananchi wetu vizuri. Kwa hiyo, waambie wananchi wa Nkasi Kaskazini kwamba zile ahadi zilizoaidiwa Serikali itazitekeleza kwa vitendo ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanatia moyo, sasa nataka kujua; kwa kuwa Sera ya Serikali ni kuwa na Sekondari katika kila Kata: Je, ni lini sasa Serikali itajenga Shule za Sekondari katika Kata ya Mbagala, Kilungule na Kibonde Maji ambapo Kata hizo hazina Sekondari kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami kwenda katika Jimbo la Mbagala kujionea hali ya msongamano wa wanafunzi darasani katika Shule ya Mbande, Chamazi, Mianzini, Kilamba, Nzasa, Mbagala, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kilungule na Kijichi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha baadhi ya Kata hususan Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kibonde Maji ambazo mpaka sasa hivi hazina Sekondari; na Sera ya Serikali ni kwamba kila Kata lazima iwe na Sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Mbagala ambako anawapigania kwamba hizo Kata zote zitapata Sekondari za Kata ambazo zipo katika mpango wetu. Kwa sababu sasa hivi Serikali tuna mpango wa kujenga sekondari 1,000 nchi nzima katika zile Kata zote ambazo hazina sekondari. Kwa hiyo, miongoni mwa Kata tutapeleka Shule za Sekondari ni pamoja na Kata alizoziainisha; Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kiponde Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tuongozane tukaone msongamano katika shule ambazo ameziainisha hapa ikiwemo Mbande, Chamazi, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kijichi na Kilungule; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari, hata akisema baada ya maswali na majibu twende, mimi nitakwenda kwa ajili ya hiyo kazi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami siko mbali sana. Madhara yaliyopo katika Jimbo la Mbagala ni sawa sawa na Jimbo langu la Temeke.

Nimeona hapa Shule nyingi za Sekondari zimeenda kujengwa Mbagala, lakini Temeke bado tuna kiu; kama nilivyosema siku zote, Temeke tunazaliana sana na sasa tuna watoto wengi wa Darasa la Kwanza. Tutakapofika mbali, naamini kabisa sekondari hizi zilizopo haziwezi kutosha hasa kule Vituka, Tandika, Kurasini, Mtoni, Temeke 14, kote tunatamani sekondari hizi ziwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kwamba kama atakwenda naye Mbagala, basi twende pamoja na Temeke tufike. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge naye kwamba tutakavyopanga safari ya Pamoja, Mbunge wa Mbagala pamoja na Mbunge wa Temeke tutakwenda. Niliainisha Kata za Mbunge wa Mbagala na wewe tutakwenda wote katika maeneo ya Vituka, Tandika, Kurasini, Temeke 14, kuhakikisha tunafanya kazi ya wananchi. Nanyi wote mnafahamu, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuondoa tatizo la Madarasa nchi nzima, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, na kwa niaba ya Mbunge wa Ulanga Mheshimiwa Salim, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa lazima ukitaka kwenda Ulanga upite Jimbo la Kilombero na kwa kuwa Wilaya ya Malinyi, Ulanga, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilombero ni ukanda mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba ni muhimu kuwa na timu ya dharura ya TARURA ikaenda kwenye eneo hilo kwa sababu Wilaya ya Kilombero, Jimbo la Mlimba, Ulanga na Malinyi hakuendeki?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili: Je, Mheshimiwa Waziri pia haoni kwa udharura huo akatafuta haraka iwezekanavyo gari la kuwapelekea wananchi wa Wilaya ya Ulanga kwa maana ya timu ya TARURA ikapata gari la dharura wakati huu wa mvua ambapo njia hazipitiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jambo la kwanza ameiomba Serikali kupeleka timu ya dharura kwa ajili ya kwenda kupitia zile barabara ambazo zimebadilika na kufanya tathmini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hivi ninavyozungumza sasa hivi kuna timu zipo huko kwa ajili ya kuangalia zile barabara zote mbovu ambazo zilipitiwa na hili janga la mvua yakiwemo maeneo ya kule Malinyi. Kwa hiyo, watu wapo kazini na hiyo timu inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu katika Bunge hili wengi huwa wanatusikiliza sasa hivi, ninaagiza wapitie tena upya waangalie hiyo tathmini ya barabara ya Kilombero kupitia Ulanga inafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameomba kwamba tuwe na gari la dharura kwa ajili ya Ulanga. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba, tumeshatengewa fedha na katika hizo fedha tutanunua magari 30 na miongoni mwa maeneo ambayo tumeyapa kipaumbele, tutapeleka gari kwa ajili ya TARURA ni katika Jimbo la Ulanga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshmiwa Mbunge, Ulanga watapata hilo gari.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Barabara za Ulanga ni sawa sawa na barabara za Mlimba:-

Je, ni lini barabara ya kutoka Mlimba Mjini mpaka Tanganyika Masagati ambayo inatengenezwa na TARURA itaweza kukarabatiwa na kutengenezwa kwa sababu kutokana na mvua ni mbaya sana kiasi cha kuleta taabu ya kupitika? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge anauliza ni lini barabara ya kutoka Mlimba kwenda Tanganyika Msagati itajengwa kwa sababu ipo katika hali mbaya?

Mheshimiwa Naibu spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumelipokea ombi lake na Ofisi ya TARURA watafanya tathmini na watatafuta fedha kwa ajili ya matengenezo ya eneo hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, Mji wa Mbinga unakua kwa kasi na kipindi cha mvua barabara nyingi ambazo zimejengwa kwa kiwango cha changarawe huwa zinaharibika. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuongeza kiasi kilichotengwa katika msimu wa 2020/2021 na 2021/2022 ili kuhakikisha kwamba angalau kipande kirefu kijengwe ili kukidhi matakwa ya wananchi wa Jimbo la Mbinga Mjini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Serikali imefanya vizuri sana katika program ya ULGSP na TSCP na kuna uwezekano mradi wa TACTIC, je, Halmashauri ya Mbinga Mjini itakuwepo katika programu hii ya TACTIC?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tu kwamba katika bajeti ya mwaka 2021/ 2022 Serikali iweze kuongeza fedha katika Mji wa Mbinga Mjini ili angalau Serikali iendelee kujenga barabara nyingi za kutosha. Kwa sababu bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilishapitishwa na kiwango tulichokitenga kwa ajili ya fedha kipo kulingana na ukomo, lakini katika majibu yetu ya msingi tumeainisha hapo kwamba kwa kadri fedha zitakavyoendelea kupatikana, udharura na kadhalika, tutaendelea kupeleka fedha katika Halmashauri ya Mji Mbinga ili wananchi wake waweze kupata barabara nzuri na zinazopitika wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameuliza kama Mji wa Mbinga upo katika ule mradi wa TACTIC. Nimwambie tu kabisa kwamba katika ule mradi, Halmashauri ya Mji Mbinga ipo. Ni sehemu ya ile miji 45 ambayo imeainishwa.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema wataendelea kujenga barabara kadri wanavyopata fedha, lakini kuna maeneo ambayo yana changamoto kubwa. Napenda kujua, kuna maeneo ambayo hayapitiki kabisa ikiwemo kule kwangu Nkasi, Barabara ya Kasu – Itindi ambayo mpaka sasa wanawake wanajifungulia njiani kutokana na uharibifu wa barabara :-

Je, ni lini Serikali itakuwa na kipaumbele kwa maeneo ambayo yana changamoto kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge amejaribu hapa kuainisha kwamba tutaendelea kujenga kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Katika yale maeneo ambayo kuna shida kubwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI (TARURA) tuna fungu la dharura kwa ajili ya kurekebisha maeneo korofi kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, endapo patakuwa na shida basi tumekuwa tukipeleka timu ya wataalam kufanya tathmini na baada ya hapo tumekuwa tukitoa fedha kama ambavyo tunaendelea katika maeneo mbalimbali nchini hivi sasa. Kwa hiyo, katika hilo eneo ambalo ameliainisha, naiagiza Ofisi ya Raisi, TAMISEMI (TARURA) kwamba waende wakafanye tathmini halafu baada ya tathmini wailete kwetu tuone namna gani tunaweza tukasaidia wananchi wa Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Changamoto ya barabara iliyopo Mbinga ni sawa sawa na changamoto iliyopo kwenye Jimbo langu la Hanang hasa Mji wa Katesh. Ule ni Mji ambao una umri zaidi ya miaka 30 na kitu ukiwa ni Makao Makuu ya Wilaya lakini hakuna kilometa hata moja ya lami :-

Je, Wilaya ina mpango gani angalau kuweka kilometa 10 za lami ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuainisha hapa barabara ambazo ni ahadi za viongozi na sasa hivi nikuhakikishie tu kwamba Serikali ipo katika Mpango wa Kukusanya ahadi zote na kuziweka pamoja, kuzifanyia tathmini pamoja na kuzitengea bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hicho ambacho amekieleza katika Mji wa Katesh ambapo mahitaji yao yapo, nimhakikishie kuwa ahadi zote za viongozi tutaziainisha, tutazitenga katika bajeti kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo katika mji wake wa Katesh.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niseme kwamba katika Jimbo la Kawe kuna barabara kama hizo ambazo ni sugu kama Barabara ya Ununio – Malindi, Mbweni – Teta mpaka Mpiji. Barabara hii inajengwa lakini inasuasua kwa muda mrefu: Ni lini sasa Serikali itamalizia barabara hii ili wananchi hawa waweze kupata nafuu?

Swali la pili, ni mkakati gani endelevu wa Serikali ambao sasa baada ya barabara hizi kujengwa wataweka mitaro ambayo haitaathiri barabara hizi kwa sababu imeonekana barabara nyingi zinaharibika kwa sababu ya mitaro? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuainisha baraba nyingine katika Jimbo la Kawe ambazo ni mbovu ikiwemo barabara ya Ununio – Malindi, Mbweni – Teta mpaka Mpiji na akaiomba Serikali izitengeneze. Najua Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi nzuri na mimi nimwahidi kabisa kwamba kama tulivyozungumza katika swali letu la msingi, tutaendelea kufanya tathmini na kadri tutakavyopata fedha hizo barabara zitatengenezwa. Hiyo ndiyo nia ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na mama yetu Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili amejaribu kuainisha kwamba ni mkakati gani ambao unaweza kusaidia zile barabara zetu zisiharibike ikiwemo kujenga mitaro itakayopitisha maji nyakati za mvua? Hata hivyo, Mheshimiwa Mbunge anatambua kabisa kwamba kuna mpango mkubwa wa DMDP wa ujenzi wa barabara kwa maana ya miundombinu yote katika Jiji la Dar es Salaam. Sehemu ya fedha ambazo zipo ni pamoja na kujenga mitaro ili kuhakikisha barabara zetu zote zinakuwa na ubora katika muda wote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie mkakati wa Serikali ni pamoja na kuendelea kujenga mitaro, madaraja na kuziboresha barabara zetu kwa kipindi chote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya Barabara ya Kairuki ni sawa kabisa na changamoto iliyopo katika barabara ya kutoka Ndala kwenda Mwawaza kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kukamilisha barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Christina Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha Barabara ya Ndala – Mwawaza kuelekea Hospitali ya Shinyanga. Ameuliza ni lini Serikali itaikamilisha. Niseme tu kwamba, tutaikamilisha kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na tathmini ambazo zinaendelea kufanyika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na subira, hiyo barabara itajengwa kwa kadri tutakavyopata fedha. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, ndani ya Jimbo la Kibamba ipo barabara ya Temboni – Msingwa kwenda Kinyerezi ina changamoto kubwa sana kwa muda mrefu. Je, mchakato unaoendelea kupata mkandarasi ni lini utakamilika na barabara hiyo kuanza kujengwa chini ya TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha kwamba, barabara ya Temboni – Msimbwa kwenda Kinyerezi imeharibika na anataka kujua lini barabara hii itaanza kujengwa. Nimwambie tu kwamba, mchakato unaendelea na mchakato utakapokamilika kama ambavyo yeye ameainisha, tutakapomaliza huu mchakato hii barabara itaanza kujengwa mara moja kwa sababu, tumeshaitenga katika bajeti. Ahsante sana.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ukweli usiopingika kwamba ni barabara ambayo haipitiki kipindi chote cha mvua. Ni barabara ambayo inaleta manufaa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa madini ya jasi ya Makanya yanalisha viwanda vya Tanga Cement, Twiga Cement, Moshi Cement, Doria Arusha na nchi za Rwanda na Burundi na kuiingizia Serikali mapato. Serikali haioni haja ya kuiboresha barabara kwa kuitengea fedha ili iweze kufanya kazi muda wote na kuongeza mapato ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika machimbo haya wako wanawake ambao wamewekeza kule ambao wamepata fursa ya kuendesha biashara ya mama lishe na biashara ndogondogo. Je, Serikali haioni kwamba kwa kusimama kwa machimbo haya kutokana na barabara korofi wanawake hawa wanadhoofika kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza maswali mawili ya msingi kabisa ambayo yana nia njema ya kuwasaidia wanawake wote wa Same mpaka Mkoa mzima wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza la msingi ambalo ameuliza hapa, amesema barabara hii haipitiki na ameomba Serikali tutenge fedha. Kwa kuwa maombi haya yametoka kwa mtu ambaye ameshakuwa kiongozi ndani ya chama na ni maombi muhimu sana,
nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu wa Ofisi ya Rais, TARURA, waende katika eneo hilo wakafanye tathmini ya kina na kuileta ofisini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia barabara hii iweze kupitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amesema kwamba kusimama kwa machimbo ya jasi kunasababisha uchumi kwa akina mama kuyumba na kuomba watu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kusaidia ili barabara hiyo iweze kujengwa. Kama nilivyojibu katika jibu la msingi kwamba tutahakikisha barabara hiyo inatengenezwa na inapitika kwa wakati wote kuhakikisha tunasaidia akina mama hao wanaoendesha biashara zao maeneo yale lakini vilevile tunawasaidia wananchi wa Same.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika majibu ya msingi, Naibu Waziri ametueleza kwamba kwa kipindi kifupi Serikali imewekeza pale takribani shilingi milioni 130 hivi kwa kuweka changarawe na kukarabati. Hata hivyo, kila baada ya ukarabati huo, mvua ikija inazoa changarawe zile na shida inabakia palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na shida ambazo mwenye swali alishazizungumzia, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kuanza kuweka lami katika kilometa chache chache ili shida hiyo ya kupoteza hela za Serikali iishe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba tunatuma wataalam wa TARURA pale wakafanye tathmini na baada ya tathmini hiyo watakayotuletea ndiyo tutafanya maamuzi ya kwamba sasa ijengwe hilo lami kama ambavyo nilimjibu mwenye swali la msingi, ama tuweke kiwango cha changarawe. Kitu ambacho nina uhakika nacho ni kwamba Serikali yetu ni makini na inasikia, lengo lake ni kuhakikisha barabara hiyo inapitika kwa wakati wote. Ahadi zetu siyo za uongo, tuko hapa kwa ajili ya kufanya kazi na tutahakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa akina mama wa Jimbo la Same Magharibi wengi wao nao pia wako katika Machimbo haya ya Jasi na wanachimba jasi kwelikweli. Je, Serikali haioni kwamba ni muhimu hawa akina mama kupata mikopo maalum kwa sababu uchimbaji wa jasi unatumia pesa nyingi? Kama inawezakana, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuwapa mikopo akina mama wote wa Tanzania ambao wanachimba madini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali la msingi lilikuwa linataka tujenge barabara tuwasaidie, lakini miongoni mwa majibu ambayo tulikuwa tumetoa ni pamoja na kuwainua akina mama ambao wanafanya kazi katika machimbo hayo ya jasi.

Mheshimiwa Mbunge wa Same Mashariki amependekeza Serikali itenge fedha kwa ajili ya kupeleka mikopo na sisi sasa hivi katika moja ya sheria ambazo tulipitisha ndani ya Bunge ni kuhakikisha zile asilimia kumi za mikopo kutokana na mapato ya ndani zinakwenda katika hayo makundi ya akina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na nafikiri moja ya kipaumbele ambacho tutakizingatia ni hicho. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa majibu mazuri. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Mama Anne Kilango, ame-raise humu ndani hoja ya msingi sana ya kutambua makundi maalum na hasa ya wanawake yenye mahitaji maalum ya mikopo kwa ajili ya shughuli za kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mama Anne Kilango, pia niwatangazie na Wabunge wengine wote, kupitia mpango maalum wa Serikali, tayari tumeanzisha mfuko maalum wa SUNVIN; tunauita hivyo kwa ajili ya ku-support shughuli hizi za akina mama na wafanyabiashara wadogo na wa kati ili waweze kuji- transform na kufanya biashara kubwa na hasa za uwekezaji kwenye viwanda, madini na shughuli nyingine zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, mnaweza kuwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili mpate taarifa ya mfuko huo akina mama na Watanzania wengine waweze kuanza kuutumia. Tayari mfuko huo umeshakuwa na fedha na umeshaanza kutumika kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa hali ilivyo katika eneo la Makanya huko Same inafanana moja kwa moja na hali ilivyo katika Kata za Mwabomba na Mwandu katika Jimbo la Sumve, ambapo barabara za kutokea Mwabomba kupitia Chamva - Mulula mpaka Manawa hazipitiki katika kipindi chote cha mvua:-

Je, lini sasa Serikali itaamua kuzijenga kwa kiwango barabara hizi ili ziweze kupitika katika mwaka wote ili watu hawa waweze kufanya shughuli zao za maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Kasalali Mageni ameainisha maeneo ya Kata kadhaa, kama nne hapa ambazo hazipitiki kabisa. Nami tu niwaagize TARURA Makao Makuu, ninaamini hapa wananisikiliza, wakafanye tathmini kama ambavyo nimeagiza katika eneo la Same ili walete hiyo taarifa. Kwa sababu sasa hivi tunahitaji tathmini za kina ili tuhakikishe hizi barabara tusiwe tunazungumza tu hapa, tunaleta maneno maneno. Tuzungumze kwa data na tuhakikishe kabisa kila barabara, hususan zile ambazo hazipitiki kabisa tunazitengea fedha na kila fedha inayopatikana inajenga ili kuhakikisha barabara zote zinapitika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nilichukue hilo jambo na tayari nimeshaagiza sasa hivi, watafanya tathmini na nitaleta majibu kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wananchi wa Isulwabutundwe, Dubanga, Isamilo, Mkolani, Busekeseke ni wananchi wavumilivu sana. Barabara hizi hazijalimwa kwa miaka 10 sasa; na tunaishukuru Serikali tumepata kiasi cha shilingi milioni 580 kwa ajili ya kulima kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika barabara hizi, barabara ya Isamilo - Mkolani – Busekeseke ina urefu wa kilometa 18, tumepata morum kilometa 7; hii nyingine ya Mkoba Bridge – Isulwabutundwe – Mkolani – Dubanga tumepata kilometa tano. Sasa Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kuuliza: Serikali haioni umuhimu wa kuweza kuongeza fedha kwa dharura ili kipande kilichobaki kuwekewa moorum kilimwe kwa pamoja, maana kukilima nusu kitaondoka, halafu tena mwakani tutaanza upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wananchi wa Nyamikoma kupitia daraja la Kimilawinga, daraja hili inaponyesha mvua halipitiki kabisa na wananchi hawa ni lazima wapite Kimilawinga waende Lwenge, waende Kamwanga kwa ajili ya kupata mahitaji na mpaka Nzela:

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga pesa sasa kwa ajili ya kwenda kujenga daraja hili kwa dharura? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza dogo ambalo aliuliza Mheshimiwa Kasheku Musukuma ni kutaka Serikali iongeze fedha katika zile barabara tulizozitoa ili kuhakikisha yale maeneo ambayo Moorum haijawekwa, basi yawekwe na yalimwe kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimjibu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha huu unaokuja, kuna fedha vile vile imetengwa kwa maana ya mwaka 2021/ 2022 kwa ajili ya barabara hizo. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwamba zimepelekewa fedha na itafanya kazi kwa mwaka wa fedha unaokuja kwa sababu huu mwaka sasa tunaumalizia na ndiyo kazi ambazo zinazoendelea kwa wakati uliopo.

Mheshimwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumzia daraja linalopita Kinilawinga na amehitaji kwamba Serikali ilijenge kwa dharura. Nafikiri suala la madaraja siku zote, ninyi wote hapa mnatambua kabisa kwamba daraja linahitaji tathmini kwanza, baada ya tathmini ndiyo ujue gharama yake ni kiasi gani? Kwa hiyo, niagize tu TARURA wakafanye tathmini katika eneo hilo halafu walete Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kufuatia mvua nyingi ambazo zimenyesha katika Jimbo la Serengeti, barabara nyingi zilizo chini ya TARURA sasa zimeharibika sana ikiwemo barabara ya kwenda Iselesele, barabara ya kwenda Mosongo lakini pia barabara ya kuzunguka stendi ile. Pia barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kuzunguka soko la Mji wa Mugumu nayo haijajengwa muda mrefu:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hizi na zile za kufanyiwa marekebisho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, ameainisha barabara kadhaa ambazo zinahitajika zitengenezwe; na kwa kuwa nafahamu changamoto za barabara kama ambavyo Wabunge wamekuwa waki- debate humu ndani ya Bunge; niseme tu, jambo hilo tumelipokea na sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika ule mchakato wetu wa pamoja, tunaandaa plan ambayo itahakikisha barabara zote nchini tunazipitia, tunafanya tathmini ya kutosha na kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha hizo barabara zinatengenezwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, awaambie tu wananchi wa Serengeti wakae mkao wa kula, hizi barabara tutazifanyia kazi na kazi yake mtaiona kabla ya miaka hii mitano kwisha.Ahsante. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna umuhimu sana katika barabara ya Singida – Supuka – Ndago ambayo kimsingi inapita katika Jimbo la Waziri wa Fedha pia.

Je, ni lini sasa Serikali itaichimba angalau kwa kiwango cha changarawe barabara hii ambayo zaidi ya miaka kumi haijafanyiwa marekebisho yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza barabara ya Supuka – Ndago ambako ni Jimbo la Iramba Magharibi ambapo anatokea Waziri wa Fedha wa sasa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Niseme tu kabisa kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Nami pia niungane na swali la msingi kama ilivyo Wilaya ya Geita Mjini, kulikuwa na matatizo ya barabara zilizo chini ya TARURA. Wilaya yetu ya Chunya pia ina matatizo mengi ya barabara zilizo chini ya TARURA zilizoharibika vibaya kutokana na mvua zilizonyesha mwaka huu.

Mheshimwa Naibu Spika, barabara ya kuanzia Lupa kwenda Nkunungu – Lupa - Lwalaje zimeharibika vibaya na kwenye fedha zilizokuwa zimetengwa, zilitengwa maeneo korofi:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za dharura ili barabara hizo ziwewe kutengenezwa ikizingatiwa kuwa maeneo haya zinalimwa Tumbaku na msimu wa soko la Tumbaku unaanza wiki ijayo kwa hiyo, itashindwa kutoka kule? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Masache ameainisha baadhi ya barabara ambazo zimeharibika sana wakati wa mvua yakiwemo madaraja; na sehemu ya hizo barabara TARURA walipeleka fedha kwa ajili ya kutatua hizo changamoto za udharura kwa maana ya uharibifu wa hizo barabara. Sasa hivi ameomba tu kwamba Serikali ni lini tutatenga fedha kuhakikisha hizo barabara zinapitika?

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu la msingi ni kwamba kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyokuwa tutazitengeneza na bahati nzuri maeneo hayo mimi nayafahamu na nimeahidi kufika kujionea mwenyewe hali halisi. Nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge na tutazungumza na wananchi. Ninaamini kabisa kwamba kutokana na bajeti ambayo Bunge lilipiga kelele na Serikali ikaongeza, tutafikia maeneo mengi sana mwaka huu wa fedha kuhakikisha tunapunguza hizo changamoto ambazo zinawakabili wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, majibu haya yaliyotoka ni ya Wilaya ya Geita, nami maswali yangu yalikuwa yanaelekea Jimbo la Busanda. Kwa hiyo, nilipokee tu kwa sababu Jimbo la Busanda liko ndani ya Wilaya ya Geita, lakini mgawanyo wake inawezekana Wilaya ya Geita usiwe ule ambao tunautarajia kuupata kule Busanda.

Swali langu la kwanza la nyongeza: Je, Serikali ina mpango gani; kwa sababu sasa hivi kuna ramani mpya ya vituo vya afya na vituo vingi vinavyotajwa vina ramani ya zamani ikionekana wazi kwamba kuna upungufu mkubwa wa wodi za wanaume na wodi za wanawake: Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya hivi vituo vya afya vijengwe kwa ramani hii mpya ya sasa? (Makofi)

Swali la pili; pamoja na vituo vilivyotajwa, kuna upungufu mkubwa sana wa uimarishaji wa upatikanaji wa dawa kwenye vituo hivyo: Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba vituo hivi sasa vinaweza kuwahudumia wananchi na upatikanaji wa dawa ukawa kama uliokuwa unapatikana awali; kwa sababu, kwa miaka miwili sasa wananchi wana vituo vya afya lakini hawapati dawa kwa ajili ya kuwahudumia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge alilokuwa anahitaji kufahamu ni juu ya ramani ambazo zimekuwa zikitolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye ujenzi wa vituo vya afya kwamba, wakati mwingine haziendani na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikubwa ambacho naweza nikamwambia Mheshimiwa Mbunge, zile ramani zilizoletwa katika maeneo husika ni minimum standards. Maboresho yanaweza yakafanyika kulingana na maeneo husikwa. Kwa hiyo, endapo kutakuwa na hitaji fulani, watu wa eneo husika wanaweza kufanya maboresho pamoja ikiwemo kuijulisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nasi tutawapa ruhusa hiyo ili kuhakikisha hivyo vituo vinajengwa kulingana na mahitaji husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amezungumzia kwamba, tumekuwa na vituo lakini bado mahitaji ya dawa hayapatikani vya kutosha. Jambo hili nafikiri karibu Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto tumekuwa tukilijadili hili kila wakati na tumekuwa tukilitolea ufafanuzi. Kikubwa, wote tunafahamu kwamba, mahitaji kama bima za afya, fedha ambazo wananchi wanatoa pale pale, lakini kwa hivi karibuni Serikali imeongeza bajeti kubwa kwenye madawa na usimamizi wake mzuri. Kwa hiyo, tutaendelea kuongeza dawa katika vituo vyetu na tutaongeza vile vile usimamizi ili ziweze kuwafikia walengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Kwa kuwa, Mkoa wa Kilimanjaro asilimia 40 ni Wilaya ya Same; na kwa kuwa Wilaya ya Same ina majimbo mawili; na Wilaya nzima ina Hospitali ya Wilaya moja: Je, Serikali haioni kwamba lile eneo ni kubwa sana, sasa upande wa Mashariki nao wapate japo Hospitali ya Wilaya moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu ya sasa ni kwamba kila Halmashauri ya Wilaya ipate hospitali yenye hadhi ya wilaya na ndio maana kwenye bajeti hata ya mwaka huu ambayo tumeipitisha mwaka 2021/2022 Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha hata zile Halmashauri ambazo hazikuwa na hospitali za Halmashauri tutazijenga mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili alilolileta hapa ni wazo kwamba angalau jimbo kwa imbo liweze kupata lakini tutaendelea kuzingatia kuleta huduma bora za afya katika maeneo yote ikiwemo kujenga vituo vya afya na zahanati kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunamaliza kwanza Halmashauri zote halafu maombi mengine tutakuja kuyazingatia kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini bado niseme kwamba Arumeru Mashariki kuna shida nyingi sana hususan katika sekta ya afya. Wananchi wanahangaika sana kujijengea zahanati wenyewe, mimi mwenyewe tangu nianze harakati za kurudisha jimbo kwenye jengo, nimezunguka kwenye jimbo kushoto, kulia, kusini, magharibi, kaskazini kuhakikisha kwamba, wananchi wanajua kwamba tunahangaika nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana nami kwamba Wabunge hatupitwi na changizo lolote jimboni, kwa hiyo, kila zanahati inayojengwa kila kituo cha afya kinachojengwa Mbunge anahusika.

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, je, ni lini Serikali itaingilia kati ujenzi wa Zahanati iliyoko Katiti, Zahanati ya Kolila, Zahanati ya Zengon, Zahanati ya Majengo na sehemu nyingine nyingi jimboni. (Makofi)

Pili, je, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya Kikao hiki cha Bajeti tukakague aone ninalolizungumza hapa kama ni la kweli au la? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge amejaribu kulieleza ili Serikali iweze kutoa ufafanuzi, ni kwa namna gani Serikali inatoa mchango katika maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakianzisha ujenzi, hususan wa maboma ya afya; na ameainisha baadhi ya maeneo ikiwemo Kikatiti, Kolila na maeneo mengineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana Serikali katika mwaka huu wa fedha tumeamua kutenga shilingi milioni 150 mpaka 200 kwenye kila jimbo ili kwenda kusaidia kumalizia zahanati ambazo zimeanzishwa na wananchi. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kulingana na fedha tunazopata na tutaendelea kuzingatia mchango mkubwa ambao unatolewa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali dogo la pili la nyongeza lilikuwa, kama niko tayari kuongozana naye Mheshimiwa Mbunge; nimhakikishie, nipo tayari na nitaifanya hiyo kazi kwa uaminifu mkubwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza, lakini pia nitumie fursa hii kuishauri Serikali kwamba, kwa kuwa barabara zetu za vijijini haziachi kuharibiwa na mvua kila wakati, nashauri kila Wilaya ambayo haina mtambo wa kutengeneza barabara, wapewe mtambo ili kuweza kunusuru barabara hizi badala ya kungojea makandarasi wapatikane ndipo barabara zifanyiwe repair? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza. Kuna mkandarasi anaitwa Balcon Construction Tanzania Ltd. ambaye amepewa contract ya shilingi 115,357,520/= kutengeneza barabara ya kwenda Kitongoji cha Esokonem mlimani Gelai kwenye Kata ya Gelailumbwa, ambaye ametelekeza barabara, baada ya kuiharibu barabara hiyo ambayo imetengenezwa kwa nguvu ya wananchi na kutifua mawe makubwa kiasi kwamba haipitiki tena. Tangu mwezi wa Kumi na Moja mwaka 2020 barabara hiyo imesimama, haipitiki. Naomba Serikali iseme neno kuhusu hilo: Je. Serikali itamchukulia hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna barabara za mitaa ya Mji Mdogo wa Longido na ambazo zilikuwa ni sehemu ya ahadi ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kutoka pale kwa DC kwenda Makao Makuu ya wakazi wa Halmashauri ya Longido, ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami na tangu mwezi wa Kumi na Moja mwaka 2020 kazi imesimama kwa sababu mkandarasi hajalipwa certificate ambayo amewasilisha; je, Serikali itatimiza lini takwa lake la kumlipa mkandarasi huyo ili kazi imalizike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuitaka Serikali tueleze ni hatua gani tutachukua kwa Mkandarasi ambaye ameitelekeza barabara aliyoitaja iliyopo jimboni kwake. Kwa kuwa taarifa hizi ndio nazipata hapa, naomba niiagize TARURA Makao Makuu kwa kushirikiana na Mkoa wa Arusha waweze kutuletea taarifa haraka iwezekanavyo ili sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tujue ni hatua gani tutachukua. Endapo itabainika kwamba Mkandarasi huyo ametelekeza barabara basi tutamnyang’anya hiyo contract na tutatangaza upya ili tupate mkandarasi mwingine atakayemalizia hiyo barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ahadi ambayo ilitolewa na Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ya barabara kutoka DC kwenda Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido eneo hilo ambalo ametaja Mheshimiwa Mbunge, kazi hiyo imesimama na amesema sababu ya kusimama ni yule Mkandarasi kutokulipwa fedha. Naomba hili nilifuatilie ili tuone ni hatua gani ambazo ofisi zetu zimekuwa zinachukua kwa sababu mpaka Mkandarasi labda hajalipwa maana yake kutakuwa labda wana-process zile certificates ambazo amekuwa amezileta katika Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kwa hiyo naomba nilifuatilie ili tuweze kui-fast truck na kuirahisisha ili waweze kulipwa na hiyo barabara iweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kata ya Udekwa, Kata ya Ukwega, Kata ya Kimara na Kata ya Idete hazina mawasiliano kabisa kutokana na mvua ambazo zimeharibu kabisa barabara.

Je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura kwa ajili ya barabara ya kata hizi ambazo zina mazao mengi ili ziweze kutengenezwa na wananchi waweze kuendelea na shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba fedha za dharura katika barabara ambazo ameziainisha hapa. Nimwambie tu moja ya kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na TARURA katika kipindi hiki ni pamoja na kupeleka fedha za dharura katika maeneo yote ambayo yalikuwa yemeathirika sana na mvua kubwa ambazo zilikuwa zimenyesha. Pamoja na fedha ndogo ambayo tunayo kwa sababu katika fedha za dharura ambayo tunayo kwa mwaka huu ambayo unakwisha ni kama bilioni 12 ambazo tulikwenda kuziainisha katika yale maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ameainisha maeneo hayo, niseme tu kabisa Ofisi ya Rais, TAMISEMI itapitia hayo maeneo na ione kama kuna udharura wa haraka kabisa ili tuweze kupeleka fedha na hizo barabara ziweze kupitika. Ahsante sana.
MHE. DAVID M. KIHENZILE Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nataka niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, hospitali hiyo iko mbali na makazi ya watu, ni upi mpango wa Serikali sasa katika kujenga makazi kwa ajili ya watumishi wa hospitali hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, ni upi mpango wa Serikali katika kutatua kero kubwa ya wataalam wa sekta ya afya katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika Jimbo letu la Mufindi Kusini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa David Kihenzile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza hapa ni lini Serikali itajenga makazi kwa ajili ya watumishi wa afya wa Hospitali ya Halmashauri ya Mufindi. Nimueleze tu kwamba katika jitihada za Serikali, moja ya jitihada kubwa ni kama tulivyoeleza katika jibu letu la msingi tumekuwa tukiongeza fedha kuhakikisha tunaboresha hospitali hiyo na kila mwaka tumekuwa tukitenga fedha. Kwa hiyo, nimueleze tu kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo kuanzia wodi, OPD pamoja na nyumba za watumishi kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi, Serikali ina nia njema kwenye suala hili na tutalifanyia kazi ombi lake na siyo tu kwa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi bali kwa nchi nzima katika vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusiana na kero ya wataalam, Serikali inaendelea na ajira na katika kipindi hiki Serikali itaajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya zaidi ya 2,600. Katika mgawanyo huo, sehemu ya watumishi hao tutawapeleka katika Halmshauri ya Wilaya ya Mufindi kwa ajili ya kupangwa kwenye vituo vyake vya afya. Ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa changamoto zilizoko katika swali la msingi ni sawa na zilizoko katika Jimbo langu la Kinondoni katika Kata ya Makumbusho ambako kuna dispensary ilianza kujengwa tangu mwaka 2019 na ilikuwa imalizike Aprili, 2020, sasa hivi ni mwaka mmoja haijamalizika.

Pamoja na juhudi za Manispaa kusimamia ujenzi ule na Mfuko wa Jimbo, je, Serikali haiwezi ikatia mkono sasa kuhakikisha kwamba dispensary ile inamalizika ili wananchi wa Kata ya Makumbusho, Jimbo la Kinondoni waweze kupata huduma? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameiomba Serikali kuweka mkono katika Kata ya Makumbusho kwenye eneo ambalo limejengwa dispensary ambayo ilikuwa imepaswa kumalizika Aprili, 2020. Tunatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Halmashauri ya Kinondoni hususan katika sekta ya afya, tunatambua kazi kubwa anayofanya Mbunge katika Jimbo la Kinondoni na tunatambua kazi nzuri inayofanywa na Serikali kuboresha sekta ya afya nchini.

Kwa hiyo, tumelipokea ombi lake lakini tutaendelea kusisitiza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni sisi pamoja na wao kwa pamoja tuimalize dispensary hii ili wananchi waanze kupata huduma za afya.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Serikali kwa kukubali kuitengeneza barabara hiyo ya Bujela – Masukulu - Matwebe.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni lini Serikali itaisaidia Sekondari ya Lake Ngozi iliyopo Kata ya Swaya ambapo ni ngumu kufikika majira ya mvua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inajipangaje kuhusiana na barabara zote na madaraja ambayo yanaunganisha kati ya barabara na shule ambapo imewafanya wasichana wengi washindwe kwenda shuleni kutokana na mvua nyingi zinazonyesha zaidi ya miezi nane katika Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu ni lini Serikali tutasaidia kujenga barabara inayoelekea Sekondari ya Lake Ngozi kuhakikisha inapitika ili kusaidia wanafunzi ambao wanatumia barabara hiyo ili iweze kupitika kwa kipindi chote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi kwamba Serikali tunaendelea kutenga fedha kuhakikisha barabara hizo zinapitika kwa wakati wote na tunazingatia maombi maalum kama haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu barabara na madaraja yote ni ajenda yetu sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA kuhakikisha safari hii tunayashughulikia. Ndiyo maana katika bajeti ambayo mlitupitishia hapa, moja ya malengo yetu makubwa na ya msingi sasa hivi ni kuhakikisha tunakwenda kujenga madaraja hususan katika yale maeneo korofi, kujenga mifereji pamoja na zile barabara ambazo hazipiti ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ya barabara muda wote. Kwa hiyo, nimwambie tu kwamba akae mkao wa kutulia Serikali ipo kazini. Ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyogeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Singida Mjini kupitia Kinyeto hadi Sagala eneo la Kinyagigi linalounganisha Kijiji cha Minyaa na Kinyagigi ilikatika kabisa na wakati wa mvua ilikuwa haipitiki ambapo maji hujaa inakuwa kama bwawa vile. Pia barabara inayotoka Makuro kuelekea Jagwa nayo pia ilikatika kabisa na ilikuwa haipitiki kutokana na utengenezaji wa chini ya kiwango. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha barabara hizi zinapitika wakati wote hasa wakati wa masika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Naibu Waziri yupo tayari kuambatana na mimi wakati wowote kuanzia sasa kwenda kutembelea jimbo zima kuona uhalisia wa barabara zake zilivyo hoi na ambavyo hazipitiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge ameuliza upi ni mpango mkakati wa Serikali wa kusaidia hizi barabara ziwe zinapitika wakati wote. Nimwambie tu Mheshimiwa kwamba Mpango Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakarabati, tunatengeneza na tunaanzisha barabara mpya ili kuhakikisha tunatoa huduma hiyo kwa wananchi kwa wakati wote. Ndio maana katika bajeti ambayo mmetutengea sasa hivi kuna ongezeko la fedha na kazi mojawapo ya hizo fedha zilizoongezeka ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kushughulikia barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara za aina tatu; za lami, changarawe na udongo na zaidi ya asilimia 80 za barabara zetu ni za udongo. Kwa hiyo, lengu letu sisi kwa awamu ya kwanza chini ya Rais wetu wa Awamu ya Sita ni walau tuifikie nchi nzima kwa kiwango cha changarawe kwa asilimia 50. Tukijenga kwa kiwango hicho cha changarawe na tukijenga na madaraja, naamini kabisa huu uharibifu ambao unasababisha hizi barabara zisipitike wakati wote tutakuwa tumeutatua ikiwemo za Jimbo lake la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili la kuongozana naye, naomba kusema kwamba nipo tayari. Bahati nzuri nilishafika Singida Kaskazini, nafahamu miundombinu yake na changamoto zake na nilikwenda wakati ni msimu wa mvua. Kwa hiyo, tutarudi tena tukafanye kazi kwa sababu huo ndiyo wajibu ambao tumedhamiria kuufanya. Ahsante.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Changamoto ya wananchi wa Singida ni sawa na changamoto wanayopitia watu wa Kyerwa na hasa Kata ya Songambele, eneo la Kitebe ambalo wanazalisha sana mahindi lakini kuna changamoto ya barabara tangu lile eneo limekuwepo kwenye Kijiji cha Kitega. Nataka kupata commitment ya Serikali kuhakikisha wanaiunganisha hiyo Kitega na Kata nzima ya Songambele ili tuweze kufanya biashara na Jimbo la Karagwe lakini pia na Rwanda kwa sababu ni mpakani mwa Rwanda pia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tunatambua mchango mkubwa ambao wamekuwa wakiutoa, tunatambua umuhimu wa barabara zote nchini na ndiyo maana tunaendelea kuongeza fedha na tumekuwa tukizitenga ili kuhakikisha kwamba tunazitengeneza na zinapitika. Hata wananchi wa Kitega katika hiyo Kata ya Songembele tutahakikisha tunawaunganisha ili kuwaondolea hiyo adha ambayo ina wakabili. Kwa hiyo, tutatafuta fedha ili tuzipeleke katika eneo husika. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kituo cha Afya pekee kinachotegemewa na watu zaidi ya 300,000 pale Vunjo ni cha Kilema. Kwenda kwenye kituo hiki, barabara iliyopo ni hiyo ya Mandaka – Kilema au barabara ya Nyerere. Sasa hivi barabara ile haipitiki kabisa, wagonjwa hawawezi kwenda kwenye kituo hiki cha afya. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri, chonde chonde atoe tamko la dharura watu waende kushughulikia barabara hii. Nitashukuru sana akitoa tamko hilo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei ameelezea hiyo barabara inayoelekea katika Kituo cha Afya Kilema kinachohudumia zaidi ya wananchi 300,000 kwamba haipitiki wakati huu na ameitaka Serikali itoe tamko. Niiagize TARURA kwamba waende wakafanye tathmini watuletee katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kusaidia, tuone namna gani tunapata fedha na kuitengeneza hiyo barabara kwa dharura ili wananchi waweze kupita.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kifupi sana uniruhusu. Ninafahamu kwamba mradi wa TACTIC ni mradi mbadala baada ya mradi wa TSP. Mradi wa TSP umekuwa mkombozi mkubwa sana kwenye nchi yetu kwenye miji, majiji na Serikali kwa pamoja. Utakumbuka hata ukiitazama Mbeya leo ukaitazama Mwanza, Tanga, na Manispaa nyingine za Kigoma, Ujiji na maeneo mengine, zaidi ya kilometa 457 zilijengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu toka Juni, 2019 barabara nyingi sana zilitangazwa na wakandarasi wakahitajika, wakajaza fomu ili wapate kazi. Sioni jitihada za Serikali ambazo zitatusaidia kuhakikisha barabara hizi zinatengenezwa kwa wakati. Barabara ziko nyingi, mfano ukienda hata Mbeya leo barabara ya kutoka machinjio ya Ilemi kwenda Mapelele inategemea fedha hizi ili ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda barabara ya Buswelu ambayo itakwenda kuunganisha soko la mbogamboga mpaka stendi mpya inategemea barabara hii. Barabara ya Mkuyuni kwenda Nyakato inategemea fedha hizi. Soko jipya la Kirumba linategemea fedha hizi. Hata ukienda kule kwa Mheshimiwa Ummy, barabara ambayo inakwenda Masiwani kwenda Hospitali ya Wilaya inategema fedha hizi. (Makofi)

Sasa jitihada za Serikali za Serikali kuhakikisha fedha hizi zinapatikana: ni lini Serikali itahakikisha mradi huu unaanza mara moja ili fedha hizi zipatikane tuone matokeo?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inafahamu kwamba TARURA haina uwezo wa kujenga barabara hizi bila fedha hizi tunazozitegemea leo zipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali lake la kwanza la msingi Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula Mbunge alijaribu kuainisha umuhimu wa mradi huu wa uendelezaji wa miundombinu katika miji kwa maana ya TACTIC kwa kutaja maeneo mbalimbali ikiwemo katika Jimbo ambalo anatokea Naibu Spika wetu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Ametaja Jimbo ambalo anatokea Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Jimbo lake Mheshimiwa Mbunge, Jimbo la Nyamagana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunatambua umuhimu wa barabara hizi na tunatambua umuhimu wa mradi huu. Ndiyo maana tumesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na hata katika ile miji yote ambayo imeainishwa kwenye huu mradi mtaona tumetuma wataalam katika kila Halmashauri, wameshafika huko kujadiliana mambo gani ya msingi yaingizwe katika huo mradi. Hiyo yote ni nia njema ya kuhakikisha kwamba huu mradi unakamilika kwa wakati. Ninaamini chini ya uongozi wa Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Hassan Suluhu; chini ya uongozi wa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Ummy Mwalimu jambo hili litakamilika kwa wakati na huu mradi utatekelezeka kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amesema kwamba TARURA haina uwezo wa kuzijenga barabara hizo. Ni kweli, ndiyo maana tumekuja na huu mradi wa TACTIC kuhakikisha zile changamoto za barabara katika hayo maeneo yote yaliyotajwa tunazitatua. Kwa hiyo, lengo letu ni kuhakikisha tukidhi vigezo, tumalize majadiliano na mwisho wa siku barabara zianze kujengwa kwa sababu hilo ndiyo lengo la Serikali. Ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi huu wa TACTIC, Singida mjini pale unatarajiwa kujenga soko la kisasa la vitunguu, soko la Kimataifa. Pia, wananchi wa Singida Mjini wanataka kujua ni lini mradi huu utakamilika? Kwa sababu feasibility study imekwishafanyika. Sasa ni lini, ili waweze kuendelea na soko lao la Kimataifa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama nilivyojibu katika maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana na ndivyo ambavyo nitamjibu Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mussa Sima, kwamba nafahamu kwamba kulikuwa na awamu ya kwanza ya majadiliano, sasa hivi tuko katika majadiliano awamu ya mwisho. Ndiyo maana katika sehemu ya huo mradi tumewatuma wataalam kuhakikisha wanaainisha maeneo yale muhimu yanayojengwa na mradi huu ni component ya mambo mengi ndiyo maana kuna masoko, barabara, kuna madampo ndani ya huu mradi wa TACTIC. Huu mradi utakapokamilika maana yake utasaidia mambo mengi ikiwemo mpaka kujenga stendi za kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba awe na subira kwa sababu tuko hatua za mwisho na hii kazi itafanyika. Ondoa wasiwasi. Chini ya Awamu ya Sita, barabara hizi zitajengwa, mradi huu utafika na wananchi wa Singida Mjini na maeneo yote ambayo yameainishwa katika huu mradi watafaidika na mradi huu. Ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imepeleka vifaa vya maabara kwenye shule 18 kati ya 19: Je, sasa wana kauli gani kuhusu kupeleka walimu wa kutosha wa sayansi katika huu mgao unaokuja wa walimu ili vifaa hivi viweze kuwatendea haki wanafunzi wetu wa Mkalama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa Wilaya ya Mkalama ina High School moja tu na ambayo iko kwenye mchepuo wa Sanaa: Je, Serikali ina mpango gani kuhusu kuongeza hostel katika Sekondari ya Gunda ambayo sasa wana hostel moja ili angalau sasa tuweze kuanzisha mchepuo wa sayansi katika sekondari hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tunapokea pongezi ambazo amezitoa kwa sababu, Serikali imefanya kazi nzuri katika jimbo lake na Halmashauri yake ya Mkalama kwa kupeleka vifaa vya maabara katika sekondari 18 kati ya 19 za jimbo lake. Swali lake la msingi ambalo ameiliza ameuliza tu ni lini Serikali itapeleka Walimu wa Sayansi wa kutosha katika shule hizo zenye maabara, ili angalau sasa pamoja na vifaa basi pawepo na basi pawepo na Walimu wa kutosha kwenye huo mgawo unafuatia. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepokea ombi lake na tutazingatia wakati wa mgawanyo ambao tutautoa hivi karibuni kabla ya mwisho wa mwezi Juni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameomba tujenge hostel ya Sekondari ya Dunga ili angalau na wao waweze kupata kidato cha tano na cha sita. Niseme tu ombi lake limepokelewa na tutalifanyia kazi kulingana na mahitaji ya jimbo lake.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika baadhi ya shule zetu za sekondari zilizoanzishwa kabla ya Serikali kuweka mkazo kwamba, lazima shule kabla haijasajiliwa iwe na maabara, kuna shule chache zimebaki zikiwa hazina maabara kabisa kama Shule ya Flamingo iliyoko katika Wilaya ya Longido, Tarafa ya Ketumbeine, Kata ya Meirugoi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha za kutosha, ili kila shule ya kata iwe na maabara ukizingatia kwamba, sayansi ni muhimu? Pia wananchi wanajitahidi kuchanga, lakini bajeti ya TAMISEMI imetoa 25,000/= tu kama umaliziaji wa maabara ambazo zimeshafikia hatua ya juu; hii ambayo haina kabisa Serikali ina mpango gani kutusaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anataka kufahamu upi niseme ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha katika zile shule zote, yaani ikiwemo Shule yake ya Flamingo iliyopo katika jimbo lake, ambazo hazina maabara tunazikamilisha. Moja ya mpango wetu na ndio maana katika bajeti mtaona kabisa tumetenga fedha, moja kwa ajili ya kuhakikisha tunamalizia maabara zote ambazo wananchi walikuwa wamezianzisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tumezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha katika yale maeneo ambayo kuna shule za sekondari za kata ambazo hazina maabara zinaanzisha ujenzi, ili sisi tuweze kuongezea fedha. Kwa hiyo, moja ya huo mkakati ni pamoja na kumalizia katika sekondari ya Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, nimhakikishie kabisa kwamba, hata hiyo Sekondari ya Flamingo itakuwa na maabara, tutapeleka vifaa na watoto watasoma sayansi kwa vitendo. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, nilikuwa na swali la nyongeza.

Kwa vile migogoro hii kwa sehemu kubwa inachangiwa sana na kutokamilika kwa utengenezaji wa mipango bora ya matumizi ya ardhi katika Mikoa, Wilaya na Vijiji vyetu. Ni lini basi Serikali itakamilisha upimaji na utekelezaji wa sera ya kuwa na mipango ya kuwa na matumizi bora kwa kila Kijiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Mhagama, Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge alikuwa anauliza kwamba moja ya sababu kubwa ya hii migogoro ni sisi ama Serikali kushindwa kwa wakati kukamilisha hii mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwambie tu jambo moja kwamba ili Serikali iweze kupima hizo ardhi katika maeneo mengine yote. Ni lazima ngazi za Halmashauri zote nchini zipange bajeti ili watu/sisi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi tuje tupime hayo maeneo ili kuhakikisha kabisa tunaondoa hiyo kero iliyopo.

Kwa hiyo, nizitake Halmashauri zote nchini kuhakikisha katika bajeti zao wawe wanatenga fedha kwa ajili ya upimaji wa ardhi ili kuhakikisha kwamba hii migogoro tunaiondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu matumizi ya ardhi katika ngazi za vijiji nafikiri ni kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba tutaendelea kuhamasisha ngazi za Halmashauri kuhakikisha wote wanafuata sheria lakini tutaendelea kutenga fedha na kuainisha maeneo yote ili kuondoa hii migogoro ambayo inaendelea kujitokeza kila wakati. Kwa sababu hilo ndiyo lengo la Serikali kuhakikisha kwamba migogoro hii ya mipaka pamoja na maeneo inatatuliwa kabisa. Ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Barabara hiyo ili iweze kukamilika inatakiwa yajengwe madaraja mawili; je, Serikali haioni kwamba kiasi cha fedha cha shilingi milioni 10 kilichotengwa hakitatosheleza kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza, kwa nini Serikali isijenge pamoja na daraja lingine kwa sababu hiyo barabara ina madaraja mawili na fedha tuliyotenga ni ndogo kukamilisha hiyo barabara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kufanya tathmini na baada ya hiyo tathmini tutatafuta fedha ili tuweze kumalizia na hilo daraja lingine ili liweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nasikitika sana swali langu halijajibiwa, swali limeuliza juu ya kilometa 58.2, nimejibiwa juu ya kilometa 23 tu. Naomba nirudi tena, ni lini Serikali itajenga barabara yote ya kilometa 58.2 kwa sababu sehemu kubwa ya barabara hiyo tayari imekatika kwa sababu ya mvua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; barabara pia ya Larta – Lahoda – Handa imekatika kabisa hakuna namna watu wanaweza kupita. Naomba kupata majibu ya Serikali barabara hizi ni lini pia zitajengwa ili watu wapiti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza kwamba ni lini barabara inayopitia Lahoda na maeneo ambayo ameyaainisha kwamba itajengwa. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, TARURA kwa maana ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini umepanga kufanya tathmini ya barabara zote nchini pamoja na madaraja ili tuweze kuwa na database ya kutosha kuangalia zile barabara ambazo zinaharibika sana tuzipe kipaumbele katika mipango yetu inayokuja. Ndiyo maana nimeahidi kwamba moja ya barabara ambayo tutaipa kipaumbele ni hizi barabara ambazo ameitaja ikiwemo hii barabara ya Kwa Mtoro -Sanzawa – Mpendo ambayo tulikuwa tunaijenga kwa awamu kulingana na fedha inavyopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, Serikali ipo kazini na hatupo hapa kwa ajili ya kumdanganya mtu yeyote, lengo la Serikali ni kuwahudumia wananchi ili waweze kupata huduma bora kabisa ya usafiri na usafirishaji. Ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri yaliyotolewa mbele hapa, lakini ninalo swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Kigoma Kusini linao urefu wa barabara hii ya Simbo kwenda Kalya ndio hiyo ambayo inazalisha hizo barabara tatu nilizozisema. Barabara ya Kalya kwenda Sibwesa inatoka nje ya nchi kwa sababu kuna bandari pale Sibwesa, lakini barabara hii pia ya Lubalisi inatoka nje ya mkoa na hii ya Kalya – Ubanda inatoka nje ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali iangalie kuweza kuipa kipaumbele barabara hizi kwa sababu zinaufungua mkoa kupitia Halmashauri ya Kigoma Kusini kwa maana ya Jimbo la Kigoma Kusini, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alichoomba ni kwamba Serikali tuizingatie ile barabara na mimi nipokee ombi lake kwa sababu tumeshakiri katika jibu letu la msingi kwamba moja hiyo barabara tumeitambua na kuiingiza katika mpango. Awali TARURA wakati inaanzishwa tulikuwa tulikabidhiwa barabara zenye urefu wa kilometa 108,000; kwa hiyo sasa hivi kuna ongezeko la barabara karibu 36,000 mpya.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa barabara hizo ambazo zimetambulika ni pamoja na hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge umeziainisha. Kwa hiyo, kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na tutakavyoendelea kuziweka katika mpango basi barabara hiyo tutaipa kipaumbele katika mwaka wa fedha unaokuja.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali haioni umuhimu sasa wa kupeleka majina ya waajiriwa moja kwa moja kwa Wakurugenzi ili Wakurugenzi wawapangie vituo vya kufanya kazi badala ya kupangwa moja kwa moja kutoka TAMISEMI?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wakurugenzi ndio wanaofahamu idadi ya upungufu wa walimu, ukiangalia Jimbo la Ndanda Wilaya ya Masasi kwa mfano, sasa je, Serikali haioni haja ya kuwapa nafasi Wakurugenzi kupendekeza nafasi za ajira kutokana na watu wanaostaafu au kufariki kwenye maeneo yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tumekuwa na taratibu tofauti hususani kwa walimu ambao wamekuwa wakiajiriwa kuwapeleka katika maeneo yao husika na moja utaratibu ni kwamba sisi tumekuwa tukiwatuma katika halmashauri husika katika vituo ambavyo wao wenyewe wamekuwa wakiomba. Kwa hiyo, wao wanaoomba zile ajira huwa wanaainisha maeneo gani wanataka kwenda kufanyia kazi na sisi tumekuwa tukitekeleza kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kuwapa mamlaka Wakurugenzi ni taratibu za kiutumishi na Serikali inafanya kazi baada ya kupata kibali kutoka Ofisi ya Rais (Utumishi) ambao wanatuletea namna, vigezo na sababu mbalimbali za mtu kuajiriwa. Kwa hiyo, kama kuna mapendekezo hayo ya kutaka kubadilisha ni Bunge lako Tukufu ndio lenye mamlaka hiyo, ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna uhaba mkubwa wa walimu nchini na Serikali imekuwa inawaajiri kwa awamu kidogo kidogo na bado pengo ni kubwa, imebidi shule nyingi zitumie walimu wa kujitolea na ajira zinapotangazwa unakuta mwalimu aliyejitolea amepangiwa kwenda shule mbali na ile aliyojitolea.

Je, Serikali haioni sasa ni muhimu wale walimu wote waliojitolea na walimu wale wakuu wamewapendekeza kwamba ikitokea ajira waajiriwe palepale walipojitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tungetamani walimu wote ambao wanajitolea katika maeneo yao husika wapangiwe maeneo hayo lakini bahati mbaya inatokana na ule uhaba ambao unatokana. Kwa mfano kama sasa hivi tuliomba taarifa za walimu wote wanaojitolea mashuleni tukaletewa nafasi walimu wanaojitolea 70,000 na nafasi ambazo zimetangazwa na Serikali ni 6,000 kwa hiyo nafikiri unaweza kuona ni changamoto kiasi gani tunapitia katika kukabiliana na janga hili.

Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina nia njema kuhakikisha kwamba itaendelea kuajiri walimu kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na bajeti ambayo tutakuwa tunajipangia na kila mwaka tutakuwa tunaendelea kufanya hivyo walau kuhakikisha kwamba tuna accommodate hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelieleza. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Kiruswa kwa swali lake la nyongeza kwa nini tusiajiri walimu ambao wanajitolea. Ni kweli kigezo kikubwa ambacho tutakitumia katika kuangalia wenye vigezo ni wale ambao wanajitolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kukiri sasa hivi yapo malalamiko hata hao wanaojitolea kuna wengine wameleta barua za fake za kusema kwamba wanajitolea wakati hawajitolei. Kwa hiyo, jana tumepokea pia maelekezo yako suala hili ni tete, nafasi ni 6,949 mpaka juzi walioomba wameshafika 89,958. Kwa hiyo, suala hili naomba utuamini Serikali tutatenda haki; hata hao wanaojitolea tutawachambua kama ni kweli wanajitolea.

Mheshimiwa Spika, pia kuna walimu wamemaliza 2012, 2013, 2014, 2015 hawajaajiriwa kwa hiyo upo pia mtazamo ndani ya Wizara labda tuangalie hawa ambao wamemaliza siku nyingi wanajitolea na hawajapata ajira kwa sababu muda wao wa kuajiriwa pia unapungua kwa sababu lazima waajiriwe kabla ya miaka 45. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana uiamini Serikali suala hili ni tete, walioomba wenye vigezo ni wengi, nafasi ni chache lakini tutatenda haki kama ulivyoelekeza bila kubagua dini, kabila, jinsia wala upendeleo wa nafasi yoyote. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, shule hizi ziliahidiwa tangu 2019/2020 kwamba zingeanza high school; na madarasa yalishakamilika Shule ya Bombo na bweni lilikuwa ni moja tu ambalo lilikuwa lijengwe ili wavulana nao wapate nafasi. Cha kusikitisha ni kwamba sasa yamepelekwa tena mpaka Septemba 2022. Swali langu ni kwamba: Kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuona kwamba high school ni muhimu sana katika shule zetu ili wanafunzi wetu waweze kuendelea na masomo ambayo yatawapa ujuzi zaidi katika maisha yao? (Makofi)

Swali la pili ni kwamba, kwa kuwa somo la Stadi za Kazi mashuleni linafanywa zaidi kinadharia: Je, Serikali ina mpango gani kuongeza nguvu katika kufanya masomo ya vitendo kusudi wanafunzi wanapomaliza shule wakaweze kujiajiri kwa kuzingatia kwamba Serikali haiwezi kuajiri wanafunzi wote wanaomaliza shule? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Naghenjwa amejaribu kuainisha, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kufungua shule hizo kama ambavyo ilikuwa imeahidi katika mwaka wa fedha 2019/2020? Nimweleze tu kabisa kwamba Serikali inafahamu umuhimu wa kuanzisha Kidato cha Tano na Sita katika shule hizo na ndiyo maana tumekuwa tukipeleka fedha kila mwaka ili kuhakikisha kwamba shule hizo zinakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa. Kwa sasa kuna upungufu wa miundombinu ya msingi; madarasa bado hayajajitosheleza, hakuna maabara na hakuna maktaba katika maeneo hayo. Kwa hiyo, tunataka tukamilishe ili tuweze kuzifungua shule hizo zikiwa na vigezo vyote vilivyokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusu stadi za kazi mashuleni kwamba wanafunzi kwa sasa wanasoma nadharia, nieleze tu kwamba Sera ya Serikali ni kuhakikisha kwamba stadi zote za kazi mashuleni wanafunzi wanafanya kwa vitendo. Ndiyo maana unaona katika mwaka uliopita 2020 kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, watoto waliomaliza Kidato cha Nne kwa mfano kwenye masomo ya sayansi hawakufanya ile alternative to practical, walifanya ile real practical kwenye mitihani yao.

Mheshimwia Naibu Spika, kwa hiyo, hii inaonesha tu kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaondoa hii dhana ya nadharia na ndiyo maana katika bajeti zetu unaona tumejenga maabara karibu katika shule zote nchini na tutahakikisha tutazikamilisha kwa wakati ikiwemo kuzipelekea vifaa. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Serikali, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa mapokeo ya wananchi kupitia matamko mbalimbali ya Serikali na kwenye swali langu nimeuliza elimubure kama ilivyotamkwa mara ya kwanza tofauti na waraka. Mapokeo ya wananchi kulingana na kwamba ni elimubure wamekuwa na uitikio hafifu wa kuchangia michango wakiamini elimu ni bure kama ilivyotamkwa. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kulieleza Bunge lako na wananchi wakajua sasa kwamba kilichobadilika ni elimu bila ada na utaratibu wa michango umebadilishwa tu kwa kwenda kuomba kibali wanapaswa kuchangia maendeleo ya shule?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa nia ya Serikali ilikuwa ni kuwapunguzia wazazi mizigo au changamoto ambazo wanazipata na shida ya huko sio ada peke yake, Serikali kwa nia hiyo hiyo njema hawaoni sasa ni muda muafaka wa kurudi kufanya tathmini kwa kuwashirikisha kikamilifu wadau wa elimu wakawaambia changamoto kubwa iliyopo badala ya ada peke yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka Serikali tueleze kwamba, hii sio elimubure ni elimu bila ada. Niseme tu kabisa kwamba Waraka wa Elimu Na.5 wa mwaka 2015 ulishazungumza, kwamba tulichokisema elimumsingi ni elimu bila ada wala sio bila kitu kingine chochote, elimu bila ada, lakini, Serikali ilitoa tena Waraka mwingine Na.3 wa mwaka 2016, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba, katika ule waraka tumeainisha wajibu; kuna wajibu wa Serikali na vilevile wa mwananchi. Wajibu wa mwananchi ni pamoja na kushiriki katika miradi ya maendeleo ya Kiserikali ikiwemo kujenga miundombinu kama madarasa, vyoo na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeainisha pale, lakini sasa tuliweka option ya kwamba wale wananchi wasilazimishwe, wachangie kwa hiari yao kwa kushikirikishana na Bodi za Shule. Huo ndio msimamo wa Serikali mpaka sasa hivi kwamba, elimu bila ada bado inaendelea kwa sababu lengo letu ni kuwasaidia watoto wale wa chini ili watoto wote waweze kupata elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Serikali tufanye tathmini upya; tunaendelea kufanya tathmini kila wakati na tunaendelea kuangalia au kuboresha kadri muda unavyokwenda. Kwa hiyo, tumepokea kwa sababu ndio wajibu wa Serikali kuhakikisha kama kuna mahali kuna upungufu, basi tunarekebisha. Hili katika jibu la msingi ni kwamba, nchi nzima sasa hivi tuna watoto wa sekondari zaidi ya milioni 14. Kwa hiyo, ni lazima Serikali tufanye upya tathmini ili kuangalia namna gani tunasaidia Sera ya Elimu na elimu kwa ujumla nchini. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Kama alivyoeleza Waraka Na.3 wa mwaka 2016, umeainisha bayana wajibu wa wazazi katika kushiriki kwenye kuchangia maendeleo ya shule. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wazazi kuendelea kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali kwa sababu mazingira ya shule yanapokuwa mazuri na watoto wao wanakuwa na uhakika wa kupata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa tunasisitiza kwamba mwanafunzi asifukuzwe shule kwa sababu ya michango. Hilo ndio jambo ambalo lazima katika kutekeleza Waraka huo, wazingatie kwamba ni marufuku kumfukuza mwanafunzi yeyote shuleni kwa sababu ya michango. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza nitangulize shukrani za pekee kwa sababu Serikali yetu imeendelea kutambua umuhimu wa kujenga shule za bweni katika wilaya za wafugaji ambapo kwa wastani mtoto hutembea hadi kilometa 13 kwa siku kufika shuleni.

swali langu la kwanza; kwa kuwa kuna shule kadhaa za bweni kongwe ikiwepo Shule ya Bweni ya Longido ambayo ilikuwepo kabla ya uhuru na ya Keitumbeine, Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati shule hizi za msingi ambazo baadhi ya miundombinu yake ni chakavu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa idadi ya watu inaendelea kuongezeka na hizi shule za bweni tulizonazo za msingi zinazidi kuwa ndogo, Serikali ina mpango gani wa kuongeza miundombinu ya madarasa na nyumba za walimu na mabwalo ili watoto waendelee kusoma katika mazingira mazuri na rafiki? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la msingi amejaribu kuainisha kwamba mpango upi wa Serikali wa kuhakikisha tunakarabati shule kongwe za msingi nchini. Wakati tunapitisha bajeti yetu moja ya jambo ambalo tulizungumza hapa Bungeni ni kwamba tumeshazitambua shule 726 kongwe zilizojengwa kabla ya uhuru na zile ambazo zilijengwa mara baada ya uhuru ambazo zimechakaa.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali sasa hivi ni kutafuta fedha kuhakikisha kabisa kwamba tunazikarabati shule zote kongwe na ahadi ya Serikali ipo palepale kwamba tutazikarabati ikiwemo Shule ya Msingi ya Longido ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, mpango mkakati wa Serikali ni upi kutokana na ongezeko la idadi ya watu na linapelekea wanafunzi vilevile kuongezeka hususan katika kujenga mabweni, mabwalo na madarasa ya kisasa. Kama nilivyoeleza awali kwamba na Wabunge wote ni mashahidi katika hili, kwamba sasa hivi Serikali tumekuwa tukijenga au tukikarabati mabweni, madarasa pamoja na miundombinu mingine ambayo inaboresha elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kabisa kwamba bado tuna mipango mingi. Miongoni mwa mipango tuliyonayo sasa hivi, tuna mpango mpya wa shule bora, lakini vilevile tuna mpango wa BEST, SEQUIP na EQUIP. Mipango ipo mingi sana, yote lengo lake ni kuhakikisha kwamba tunaongeza miundombinu mashuleni na kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wabunge wote waondoe wasiwasi, Serikali ya Awamu ya Sita tutahakikisha tunawafikia wote katika Majimbo yao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba katika Wilaya ya Karatu, Tarafa ya Eyasi kuna Shule ya Msingi Endamaghan ambayo ni maalum kwa ajili ya hawa watoto wa kifugaji kwa maana ya Wahadzabe ambao wanatoka kwenye hii Tarafa ya Eyasi, lakini wapo wengine wanatoka Wilaya ya Mbulu, lakini shule hiyo ni ya muda mrefu inahitaji marekebisho kimiundombinu ili hawa wanafunzi waweze kupata hiyo huduma muhimu ya elimu. Je. Serikali sasa ipo tayari kutazama shule hiyo na kuipatia fedha kwa ajili ya maboresho hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalichukua jambo hilo na tutafanya marekebisho na tutaboresha hiyo shule. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana; pamoja na majibu mazuri ya Serikali, majibu ambayo yanaeleza ni walimu kumi tu wa sayansi walioajiriwa kwa muda wa miaka mitano hali inayopelekea wanafunzi wengi wa Jimbo la Mbulu Mji na maeneo mengine nchini kushindwa kufanya mazoezi ya sayansi, na kwa kuwa tatizo hili limewagharimu wananchi kwa muda mrefu kwa ajili ya kuwachangia walimu wa kujitolea katika shule za Halmashauri ya Mji wa Mbulu.

Nini kauli ya Serikali ya kutusaidia walau tatizo hili linapungua katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu pamoja na maeneo mengine nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa tupo kwenye mchakato wa ajira na majibu ya awali nilipofuatilia Wizarani walikuwa wamesema tuna walimu wengi wa sayansi na tatizo hili limewagharimu wanafunzi hao wasifanye vizuri.

Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa nafasi pekee ya kuondoa walau kiasi kikubwa cha upungufu wa walimu kwa shule za sekondari katika Jimbo la Mbulu Mji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza alikuwa nataka kujua kauli ya Serikali ya kupunguza tatizo la walimu wa sayansi hususan katika eneo lake lakini na maeneo mengine nchini; ni kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba Serikali itaendelea kuajiri walimu na tutaendelea kuangalia kada mbalimbali hususan kada za walimu wa sayansi pamoja na wataalam na mafundi sanifu wa maabara ili tuweze kuwasaidia.

Kwa hiyo, miongoni mwa vigezo ambavyo tumevizingatia sana ukiacha vile vigezo vya awali ambavyo tulivitaja ikiwemo watu kukaa muda mrefu ambao hawajapata ajira, lakini miongoni mwa vigezo ambavyo tunavitumia sasa hivi ni pamoja na ku-consider walimu wa sayansi katika ajira hizi ambazo tutazitoa hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nimtoe wasiwasi tu kwamba Serikali tutaendelea kuwapanga katika maeneo yote ikiwemo katika eneo lako la Mbulu Mji. Kwa hiyo, hilo niahidi kwa Wabunge wote kwamba tutazingatia Majimbo yote katika kipindi hiki kuwaletea walimu wa sayansi lakini hatutawaacha na walimu wa arts ambao wamesoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba alitaka tu kujua ni namna gani tunawasaidia kuwatoa. Jukumu kubwa ni kwamba Serikali itaendelea kuajiri kulingana na upatikanaji wa fedha na kadri tutakavyoajiri ndivyo ambavyo tutaendelea kuwapanga, ahsante sana. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Ndugu yetu pia:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza nauliza kwa kuwa, tayari barabara ya Mferejini – Narumu – Takri – Lyamungo hadi Makoa imeshatengewa shilingi milioni 500 kwa ujenzi wa kiwango cha lami. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa hivi kuongeza pesa mwaka huu wa fedha, ili hiyo barabara ikamilike kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na swali la pili, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa International School kwa Raphaeli, Umbwe, inayounganisha na hii Barabara ya Mheshimiwa Mafuwe kule Lyamungo kwa kiwango cha lami? Ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa hii barabara inayoishia pale Mto Sere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameeleza, kwanza ametambua kwamba, Serikali tumepeleka fedha milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami. Na kikubwa ambacho ameomba tu ni kwamba, je, Serikali ni namna gani tutaongeza fedha kwa ajili ya barabara hiyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, moja, tuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Samia Hassan Suluhu kwa kutoa fedha milioni 500 kwa majimbo yote nchini kwa ajili ya barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili kwenye jambo hili tuombe Bunge lako tukufu mpitishe bajeti kuu, ili yale mapendekezo yaliyoletwa na Wizara ya Fedha ya kuongezea TARURA fedha katika kile chanzo cha shilingi 100 iweze kupita maana tutapata fedha. Na hizi fedha tutakazopata maana yake tutakwenda kuongeza barabara katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo hili ejeo ambalo mmeliainisha hapo. Kwa hiyo, ombi letu kwenu mpitishe bajeti kuu na sisi tutafanyia kazi maombi yote ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeyaleta kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ameeleza hii Barabara ia International School kupitia Umbwe na hayo maeneo ambayo ameyaainisha ambayo yako katika jimbo lake:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hivi ninavyozungumza kazi nzuri ambayo ulikuja Ofisini kwetu na ukatuomba tumeanza kwanza kujenga mifereji katika barabara hiyo na itakavyokamilika maana yake tutaipandisha hadhi kwa kuiongezea viwango vile ambavyo vinastahili. Kwa hiyo, ndio kazi ambayo tumedhamiria kuifanya na tutaifanya kwa wakati wote, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninakubaliana na aliyosema Naibu Waziri:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hizi ziko kwenye tambarare ya Kilimanjaro na mvua zote zinazonyesha mlimani zinashuka chini na kufagia changarawe yote iliyowekwa na TARURA. Na kwa kuwa, Barabara ya kutoka Hai kwenda Rundugai inaunganisha Barabara ya TPC ambayo ni ya lami.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kabisa kuanza barabara hiyo kwa lami kuliko kila wakati kumalizia hela za Serikali kwenye changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Kilimanjaro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameeleza concern njema kabisa yenye nia njema. Niseme kwamba, tumelipokea ombi lako tutakwenda kufanya tathmini, ili tuingize katika mipango inayofuatia ya kuhakikisha tunaiondoa hiyo adha. Sio kila wakati tu hizi barabara zetu zikawa zinaondolewa na mvua kutokana na ile changamoto ya udongo au kifusi kwa hiyo, tunachokitaka sisi ni kuhakikisha kwamba, hizi barabara zinatengenezwa katika kiwango ambacho muda wote zitakuwa zinapitika.

Kwa hiyo, nilipokee hilo na tutaliingiza katika mpango, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hizi ahadi yake ni ya muda mrefu na zimetengewa kiasi kidogo sana cha pesa. Na tuna barabara nyingi sana ambazo katika Mji wa Bagamoyo zinahitaji kupata huduma ya lami, mfano.

Je, ni lini Serikali itachukulia umuhimu Barabara ya Makofia – Mlandizi kwa sababu ni barabara muhimu sana ambayo inapita katika chanzo cha maji ambayo wanakunywa watu wa Dar-es-Salaam pamoja na pwani ambapo panaitwa bomu. Ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami hii njia ili kunusuru magari yanayonasa kupeleka dawa wananchi waweze kunusurika afya zao katika mikoa hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatatvyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa, moja kwamba hizi barabara imekuwa ni ahadi ya muda mrefu na fedha inayotengwa ni ndogo, lakini pili ameanisha Barabara ya Kofia – Mlandizi ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wake wa Jimbo la Bagamoyo kwamba, ni lini sasa Serikali tutatenga fedha:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama nilivyojibu katika majibu ya awali kwamba, moja ya wajibu wetu sisi ni kupokea mapendekezo yanayoletwa na Wabunge, lakini la pili ni kuhakikisha kwamba, zile ahadi zote ambazo viongozi wetu wakuu walizitoa zinatekelezwa. Na tutaendelea kuzitekeleza kwa kadiri ya upatiakanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana katika jibu langu la msingi nikasema niwaombe Wabunge wote wapitishe Bajeti Kuu ya Serikali ili kile chanzo kilichokuwa kimetengwa zile fedha maana yake zitaongeza kuna kitu tutakwenda kukifanya. Na haya maombi mnayoleta maana yake tutayatekeleza. Hakuna barabara yoyote inaweza kutekelezeka bila kuwa na fedha. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge muweze kufanya hivyo, ili tuweze kufanya kazi nzuri ya kuwasaidia wananchi wetu. Kwa hiyo, tunayapokea hayo tutayafanyia tathmini na tutayaweka katika mipango yetu, ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa ahadi ya barabara hizi imetolewa pia kwenye Jimbo la Kibaha Vijijini kwenye Mji wa Mlandizi na tayari kuna barabara ya kilometa moja imeanza kutekelezwa na miezi sita sasa haijalipwa chochote. Je, Serikali haioni ni muda sahihi sasa kumalizia ile fedha ili mkandarasi amalizie ili hata ile kazi ambayo ameshaanza kufanya isiharibike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara zote ambazo wakandarasi wako site zitaendelea kulipwa fedha ili ziendelee kukamilika, ikiwemo hii barabara ambayo umeitaja hapa.

Kwa hiyo, haitakwama kwa sababu ninaamini kabisa kwamba, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kupitia TARURA tunapitia zile certificates ambazo wakandarasi wanazileta kwetu na tunazitolea fedha. Kwa hiyo, na hili tumelisikia na nikuhakikishie kwamba, itaisha kwa wakati kama ambavyo iliahidiwa na viongozi wetu wakuu, ahsante.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, nakushkuru Mheshimiwa Waziri, uzuri umejibu halafu umefanya ziara kwangu, hizo barabara zote ulizozisema ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza ambayo ni hatarishi sana, daraja la Budoda halipitiki toka kwenye kampeni. Je, Serikali haina mfuko wa dharura kwenda kurekebisha madaraja ambayo yanawafanya wananchi kupoteza Maisha? Kuna Kata ya Ngemo, Mtonya pamoja na Ludembela, kuna madaraja mpaka sasa hivi hayapitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wewe Mheshimiwa Naibu Waziri, ulifika kwenye jimbo langu na ukajionea na tulizama mara tatu. Je, kwa sasa hivi na bunge linakwenda kuisha, nikawaambieje wananchi kulingana na ubovu wa barabara hizi ambazo hazipitiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemus Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ameuliza kwamba daraja la Budoda halipitiki kwa muda mrefu tangu kipindi cha kampeni, kwa hiyo akauliza kama hakuna fedha za dharura. Niseme tu Mheshimiwa mbunge nimelipokea jambo lako na ninalikabidhi kwa TARURA Makao Makuu, ili waende wakafanya tathmini hiyo na watuletee taarifa ili tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la Pili ameuliza atawaambi nini wananchi, kwa kuwa bunge linakwisha na barabara zake bado hazipittiki. Nenda kawaeleze tu kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunamaliza matatizo ya barabara maeneo mengi nchini. Na katika hatua ya awali ambayo tulioichukuwa ni kupeleka fedha milioni 500 kwenye kila Jimbo, ambazo zitakwenda kujenga barabara za lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili waeleze wananchi wako kwamba, mara baada ya bajeti ya Serikali kupita, kikiwemo kile kifungu maalum cha kuongezea fedha za TARURA, tutaongeza fedha katika Jimbo lako ambazo zitasaidi zaidi zile barabara ambazo ni mbovu. Ahsante sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala yapo katika Kata ya Ntobo na ukizingatia Kata zake zilivyokuwa mbalimbali hususan Kata za Isaka, Mwalugulu, Jana na Mwakata kupata taabu sana kupata huduma za ki- Halmashauri. Sasa nini mpango wa Serikali wa kuanzisha Mamlaka ya Mji mdogo katika Kata ya Isaka ili kuwawezesha wana Isaka nao sasa waweze kupata huduma kwa urahisi. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba tu kwamba kwa nini sasa Serikali isianzishe Mamlaka ya Mji Mdogo katika eneo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala kwenye Kata ya Ntobo kama alivyoeleza. Kwa hiyo, ametaka kujua ni lini lakini jibu langu la msingi utaratibu ni uleule kwamba mkitaka tuanzishe haya Mamlaka maana yake mfuate taratibu hizi ambazo tumezianisha, mlete maoni yapitie katika ngazi zote na sisi tutafanya tafakuri na tathmini na baadae tukishajiridhisha basi maomba hayo tutayapeleka kwa Mheshimiwa Rais ambaye ndiye ana mamlaka ya mwisho kabisa ya kutangaza maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo ndilo jibu la Serikali anzisheni mchakato nasi tutakuja tufanye tathmini. Ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza Mamlaka ya Mji wa Vwawa inahudumia Mkoa wa Songwe. Je, ni lini Serikali itaupandisha hadhi Mamlaka ya Mji wa Vwawa kuwa Halmashauri ya Mji.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru sana kwa kunisaidia kujibu. Kikubwa ni kwamba kwanza na mimi mwenyewe nina interest kwa sababu natokea katika Mkoa huo huo wa Songwe na ninaufahamu vizuri Mji Mdogo wa Vwawa ambao unahudumia kwa sasa Makao Makuu ya Mkoa wetu wa Songwe.

Kwa hiyo, kikubwa mimi na wewe pamoja na Mkuu wa Mkoa wetu ambaye anatusikia sasa hivi nafikiri tuanzishe tu mchakato mapema halafu ikishafika katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI ninaamini tuki-meet vigezo vyote basi tutafanya hilo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliomba, ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya ya kusema kwamba huu wa fedha unaoanza keshokutwa hapo tumetengewa shilingi milioni 182 kwa ajili ya kutengeneza kalavati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi lilikuwa linazungumzia kwamba ni lini Serikali itatengeneza daraja, kama katika maelezo yake alivyosema kwamba eneo hili lina kilometa 38 zinazounganisha Wilaya ya Kiteto na Wilaya ya Kilindi. Eneo hili lina changamoto kubwa kwa sababu daraja ni kubwa sana, kiasi hiki kilichotengwa hakitoshi hata kidogo kwa ajili ya kujenga daraja.

Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakwenda yeye au wataalam wake kwenda kuangalia upana wa daraja hili ili Serikali iweze kutenga fedha za kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; miaka ya nyuma Serikali ilishatenga pesa kwa ajili ya daraja hili, lakini nina uhakika thamani ya fedha kwenye daraja hili haikufanyika.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutuma timu kuona kama fedha hizi zilitumika ipasavyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anachokieleza Mheshimiwa Mbunge, kwamba daraja lile ni kubwa na Bonde la Mto Sambu kama alivyokuwa amelianisha hapa ni bonde ambalo limeongezeka na linakadiriwa kuwa urefu wa mita 75. Na kwa tathmini ya awali ambayo ilikuwa imefanyika kwenda kufanya matengenezo katika eneo hilo ambalo linahusu hilo daraja, kuna makaravati kama 18, pamoja na drift yaani vile vivuko mfuto vidogo zaidi ya 30 na kitu. Na ilivyofanywa tathmini ya fedha ya awali ni kwamba eneo hilo linahitaji zaidi ya bilioni 2.9 ili kuhakikisha hiyo barabara iwe inapitika muda wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi tu niseme kabisa kwamba Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema mimi mwenyewe nitafika eneo hilo ili niweze kushuhudia, na vilevile nitaituma timu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenda katika eneo husika. Lakini kikubwa ni kwamba kwa sasa tuna ufinyu wa bajeti ndio maana umeona tumetenge hizi fedha chache. Lakini Bajeti Kuu ya Serikali ikipita, na kile chanzo kipya ambacho tunapelekea fedha kuongezea TARURA ninaamini tutazingatia hili ili barabara hii iweze kupitika kwa wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Splika, kwa hiyo tunaomba Waheshimiwa Wabunge mpitishe Bajeti Kuu ya Serikali ili tupate kile chanzo cha uhakika na ninaamini katika mwaka ujao wa fedha hili swali halitaulizwa tena, tutakuwa tumeshalifanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niishukuru Serikali kwa kazi inayofanyika kwa upande wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kyerwa ni miongoni mwa Wilaya ambazo zina vipindi virefu vya mvua, barabara zake zinatengenezwa kwa udongo, sasa Serikali ina mpango gani wa kuongeza bajeti ili barabara hizi ambazo hazipitiki kipindi cha mvua ziweze kutengewa bajeti ya changarawe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; niishukuru Serikali kwa ombi langu lla kujenga lami katika Mji wa Nkwenda, kazi ambayo tayari imekamilika lakini nilileta ombi kwa sababu ya umuhimu wa ule Mji wa Nkwenda kuweka taa pale. Je, Serikali imefikia wapi ombi ambalo nimelileta kwenu kuweka lami katika Mji wa Nkwenda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKLIA ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anaomba tu, amejaribu ni ombi vilevile ni ushauri, upi ni mpango wa Serikali wa kuongeza bajeti. Nafikiri baada ya Wabunge wengi kuzungumza ndani, Serikali katika bajeti kuu imekuja na mpango wa kuongeza fedha kwa TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuseme tu kwa ongezeko hilo la fedha ambalo Bunge lako Tukufu likiwapendeza wakapitisha, basi tutaongeza bajeti katika halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Kyerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; ameshukuru kwamba Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami katika eneo la Mji wa Nkwenda na hiyo lami imeshakamilika lakini sasa hivi alileta ombi Serikalini na nimhakikishie tu kwamba ombi lake linatekelezwa na Serikali kwa sababu mkandarasi ameshapatikana, yupo site na taa zitawekwa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kawaambie wananchi wa Kyerwa katika Mji wa Nkenda kwamba ombi ulilolileta basi linaanza kutekelezwa; hivi niavyozungumza mkandarasi amekwenda site, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; nataka kujua pesa hizo za vitambulisho ambavyo wajasiriamali wanavitoa huwa zinaingia akaunti gani na mahesabu yake ni yapi, swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wanaonaje wakaweka utaratibu hasa wafanyabiashara wa mbogamboga na mama ntilie ambao mitaji yao ni midogo wakahakikisha kwamba chaji yao inakuwa moja kwa nchi nzima badala ya bei inakuwa juu zaidi kwa sababu wengi mitaji yao ni midogo, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKLI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ametaka kujua tu fedha za wajasiriamali wadogowadogo zinaingia katika mfuko gani, ni kwamba zinaingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, huko ndiko ambako fedha zinakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili alikuwa tu anataka kujua ukomo. Nieleze tu kwamba wakati Serikali inapanga ukomo wa shilingi 20,000 ilikuwa imezingatia vipato vya wananchi wetu na ndio maana awali hawa wakina mama ntilie, wafanyabiashara wadogowadogo walikuwa wanalipa fedha nyingi zaidi kwa kuchangia kidogokidogo kila siku lakini ilipowekwa shilingi 20,000 maana yake tulikuwa tumewasaidia kupunguza hiko kiwango. Kwa hiyo, hiki kiwango ambacho kipo kwa sasa bado kinazingatia hali halisi iliyopo lakini sisi tutalipokea ombi lako na tutaendelea kulizingatia kwa kadri ya mahitaji ya wafanyabiashara wetu, ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yanaonesha kwamba kazi inaendelea. Lakini niiombe Serikali, pamoja na kazi, kasi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mtwara una Kata 191 na kati ya Kata hizo, 137 zina shule za sekondari na Kata 57 hazina shule za sekondari. Na jambo hili linasababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu sana kufuata shule za sekondari, na matokeo yake ni upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa katika Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, je, katika shule hizi 310 Mkoa wa Mtwara umetengewa shule ngapi katika kipindi hiki? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba shule ni walimu pamoja na mambo mengine yote. Sasa Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu wa sayansi wa asilimia 41. Sasa nina wasiwasi kwamba kama hakutakuwa na maandalizi ya kutosha, kukamilika kwa madarasa au kwa shule hizi zitakazojengwa kutaongeza tena upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba baada tu ya kukamilika kwa shule kunakuwepo na walimu wa sayansi wa kutosha ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari umeshanipa mwongozo kuhusu takwimu sahihi na mimi nitampatia takwimu sahihi katika mwaka huu wa fedha tutajenga shule ngapi. Lakini niwahakikishie wananchi wa Mtwara kwamba Kata zote zilizobaki 57 zitajengwa sekondari za Kata kwa sababu zipo katika mpango wetu kwa sababu idadi ya shule tulizonazo zinatosheleza Kata zote nchini ambazo hazina shule hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anasema Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu, hususan wa sayansi, na alitaka kujua mpango wa Serikali ni upi kuongeza. Ni kwamba Serikali itaendelea kuajiri kama ambavyo tulitangaza hizi ajira ambazo muda mfupi, ndani ya wiki mbili hizi tutakuwa tumeshatoa hayo majina. Lakini vilevile Serikali itaendelea kuajiri walimu wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu kwamba tutaendelea kuangalia hivyo vigezo ambavyo amevitaja, wakiwemo walimu wa sayansi, na masomo mengine hatutayaacha kwa sababu yote yanahitajika katika elimu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, wakati unajibu hapo umesema fedha zinatosheleza kwenda kwenye kata zote ambazo hazina shule, na Mtwara wanazo 57. Hizo sule zote zitajengwa mwaka huu wa fedha?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ambacho nilikuwa nakieleza kwa kifupi ni kwamba Mradi wetu wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari Nchini ni ujenzi wa shule za sekondari 1,000. Na awamu ya kwanza Mwaka huu wa Fedha ambao tunakwenda, 2021/ 22, tunaanza kujenga shule 310.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hizi 310 ni kwa mwaka huu. Halafu mwakani tutakuwa na idadi nyingine ya shule kwa Mwaka mwingine wa Fedha kwa maana ya 2022/2023, tutaleta fedha nyingine. Lakini mradi wetu unatosheleza kujenga shule zote kwa sababu tuna upungufu katika Kata kama 780 ambazo hazina sekondari za Kata hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bado tutajenga na bado zile kata ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi tutapeleka vilevile sekondari nyingine, yaani kutakuwa na sekondari mbili katika Kata moja ili tuweze ku-accommodate idadi kubwa ya wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilichomwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba awe na uhakika kwamba Kata zote za Mtwara zitafikiwa. Lakini kwa mwaka huu nitampa idadi kamili ya shule ngapi tunajenga na mwakani tutajenga shule ngapi na mara ya mwisho tutamaliza kwa ngapi. Ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara hii iliahidiwa na Mheshimiwa Rais na umepita muda mrefu sana, na wananchi wamekuwa wakihoji, na katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri sijaona commitment. Je, ni lini hasa fedha zitapatikana kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa tunakwenda kuahirisha Bunge keshokutwa na wananchi wamekuwa wakiniuliza kila siku na kila saa kwa sababu hospitali hiyo inatumiwa na wagonjwa wengi sana kwenda kwenye hospitali ya wilaya. Ni nini nitakwenda kuwaambia wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibu nitakaporudi Jimboni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza tu kwamba lini hasa fedha zitapatikana kwa sababu ahadi hii ni ya muda mrefu, na katika jibu letu la msingi tumeeleza hapa kwamba mara fedha zitakapopatikana basi barabara hii tutaiingiza katika mipango yetu ya kujengewa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa kuwa Serikali ilisikia kelele ama maombi ya Wabunge ambayo waliyatoa katika Bunge lako Tukufu na kusababisha Serikali kutaka kuanzisha chanzo kipya cha fedha ili TARURA iweze kuongezewa, ninaamini tutakavyopata ongezeko la fedha hiyo tutazingatia ombi la Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ameuliza ni nini akawaambie wananchi. Akawaambie tu wananchi kwamba ahadi ambayo viongozi wetu wakubwa waliitoa itatekelezwa mara hapo fedha itakapopatikana. Ahsante.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa lakini kusema ukweli matengenezo yanayofanyika hayatoshelezi kitu. Unafanya matengezo mwezi huu, mwezi ujao mvua kubwa ikinyesha unarudia tena matengenezo. Kusema kweli ahadi ambazo zilitupa ushindi sisi wana-CCM ni ahadi hii ya barabara ya Mandaka – Kilema ambayo Mheshimiwa Rais aliitoa. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze ni lini au anafanya commitment gani kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna taswira kwamba kule Kilimanjaro kuna barabara nzuri. Nataka niwahakikishie wananchi kwamba Kilimanjaro hatuna barabara nzuri, barabara zilizokuwepo ni zile za zamani zilizojengwa na Ushirika na zingine zinaenda mpakani. Sasa namuomba Mheshimiwa anayehusika, Waziri wa TAMISEMI, hajawahi kufika kwenye jimbo langu akaona hali ya usafiri ilivyo ngumu, najua kwamba tumeshapewa hela lakini hazitoshi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Kimei uliza swali lako.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Je, Waziri atakubali kuongozana nami nikamtembeze aone hali ya barabara za Vunjo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza Mheshimiwa Mbunge amesema anataka kujua commitment ya Serikali juu ya ahadi ya barabara ya Mandaka – Kilema itaanza kujengwa lini kwa kiwango cha lami. Niseme tu kwamba tumelipokea kwa sababu moja ya wajibu wetu ambao tulikuwa tunaufanya hapo awali ilikuwa ni kuchukua ahadi zote za viongozi ili tuziweke katika Mpango. Kwa sababu jana tumepitisha Bajeti Kuu na kuna ongezeko la fedha ambalo limetokea, naamini katika Mpango unaofuata tutakuwa tumeingiza na tutafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili kufika katika Jimbo lake, nimwambie tu hapa katika Bunge lako Tukufu kwamba niko tayari kwa sababu mara baada ya Bunge nitakuwa na ziara ya kuzunguka katika maeneo mbalimbali ikiwemo zile ahadi ambazo nimezitoa hapa kwa Wabunge mbalimbali kufika katika maeneo yao. Kwa hiyo, moja ya eneo ambalo nitafika ni pamoja na Vunjo. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini barabara ya Mzumbe – Mgeta itajengwa kwa kiwango cha lami ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Awamu ya Nne? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, alichozungumza hapa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya utekelezaji wa Barabara ya Mzumbe mpaka Mgeta, niseme tu kama nilivyojibu katika jibu la msingi na la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kimei kwamba, na yenyewe tunaiingiza katika mpango, tutaizingatia. Barabara nyingi tutaziongeza katika mpango baada ya kupata ongezeko la fedha hii ambayo jana Bunge lako Tukufu lilipitisha. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mchakato wa kuanzisha Wilaya ya Ukonga ulifanywa mwaka 2015 sambamba na uazishwaji wa Wilaya ya Kigamboni na Ubungo katika halmashauri mbili ambazo wakati huo Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na Halmshauri ya Temeke, Ilala na Kinondoni. Kwa hiyo, Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam zilifanya mchakato wa kutaka kuongeza halmashauri ikiwemo Halmashauri ya Wilaya Ukonga. Je, Serikali haioni haja sasa ya kurudia kwenye kumbukumbu zake kuangalia jambo hilo ili lifanyiwe utaratibu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwanza, niipongeze Serikali kwa kuanzisha Jiji la Dar es Salaam lakini kwa kuwa Ofisi za Halmashauri ya Jiji ziko katika Mtaa wa Morogoro Road na Drive In kwa kifupi mjini Posta na kwa mkazi wa Chanika, Msongora, Mzinga, Kitunda, Zingiziwa, wana changamoto kubwa ya kufika kwenye Halmashauri hizo za Wilaya ili kuweza kupata huduma za kijamii. Je, Serikali haioni haja ya kusisitiza jambo hili la kupata Wilaya mpya ya Ukonga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza Mheshimiwa Mbunge anasema mchakato ulifanyika mwaka 2015, wakati wa mchakato ule Halmashauri za Ubungo na Kinondoni ndizo zilizokuwa na sifa za kupata Halmashauri za Wilaya na anasema twende tuka-review mchakato wa mwaka 2015. Nafikiri jibu la Serikali ni la msingi, kama kuna maombi mapya ni lazima muanze upya mchakato na kila kipindi kinapopita kinakuwa na sababu zake. Kwa hiyo, maombi yote ya nyuma kwa sasa hivi tunasema ni maombi ambayo hayatambuliki kwa sababu zoezi lile lilifanyika kwa wakati mmoja na halmashauri ambazo zilikidhi vigezo zilipewa hiyo hadhi za kuwa wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu utabaki palepale kwamba kama kuna nia hiyo anzeni upya watu wa Ukonga mfuate taratibu zote za kisheria, mlete maombi na sisi tutayapeleka kwa Mheshimiwa Rais. Rais ndiye atakayekuwa na maamuzi ya mwisho ya kuanzishwa either kwa Wilaya ya Ukonga ama kusitisha kwa kadri atakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili amerudia jambo lilelile kwa sababu Makao Makuu ya Ofisi za Jiji yapo mjini sana na anaona kwamba kuna haja ya kuwa na wilaya mpya ili kusogeza huduma. Kikubwa ni kwamba Serikali tutaendelea kupeleka huduma kwa wananchi, lakini hayo maombi yenu kama yatakidhi basi Serikali itaendelea kuangalia. Hilo nafikiri ndiyo jibu sahihi kwa wakati huu. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Makambako kuhusiana na masuala ya Polisi na TANESCO ni wilaya na taasisi zingine ni wilaya. Serikali haioni sasa ni muhimuMakambako tupewe wilaya kwenye Halmashauri ya Mji wa Makambako kwa sababu taasisi zingine zote zipo kiwilaya kasoro halmashauri kutamka kwamba ni Halmashauri ya Wilaya ya Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, kama ifuatavyo:
-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba Halmashauri ya Mji wa Makambako ambapo yeye ndiye Mbunge wa eneo hilo kwamba kipolisi ni wilaya. Nieleze tu kuna wilaya za kipolisi na wilaya za kiutawala ambapo sisi Ofisi ya Rais - TAMISEMI tunasimamia. Ndiyo maana unajikuta kuna maeneo mengine ni Mikoa ya Kipolisi, kwa mfano Ilala ni Mkoa, lakini ni wilaya, kulikuwa na Kinondoni wakati fulani zilikuwa Wilaya za Jiji la Dar es Salaam wakati ule lakini bado zilikuwa zinatambulika kama ni Mikoa ya Kipolisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huwezi kuniambia tu kwa sababu Kinondoni ni Mkoa wa Kipolisi basi tutamke leo kutakuwa na Mkoa wa Kinondoni. Niseme tu hizo ni taratibu za kiutendaji za kiserikali endapo wao wanaona wanahitaji kuwa na halmashauri basi wafuate taratibu kama ambavyo tumejibu katika swali la msingi. Ahsante.
MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Waziri yupo tayari kutembelea baadhi ya zahanati, vituo vya afya pamoja hospitali ya wilaya ili kujionea changamoto hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa upungufu wa watumishi katika jimbo langu umefikia asilimia 67, je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi wa afya katika Jimbo la Ulanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Salim Alaudin Hasham, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kama ombi, je, tupo tayari kutembelea jimbo lake na kujionea changamoto hizo zinazolikabili. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge tupo tayari mimi na mwenzangu Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya Mheshimiwa Dkt. Dugange na tutafika katika eneo lake na kushuhudia haya ambayo ameyazungumza na tutachukua hatua za kimsingi kuwasaidia wananchi wa jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, ameuliza kama tupo tayari kuongeza watumishi. Niseme tu kwa kadri tutakapokuwa tunaendelea kupata kibali cha kuajiri kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi tutaendelea kuajiri na kuongeza watumishi. Kwa hiyo, katika nafasi chache tunazozipata kama ambazo tunakwenda kuziajiri nafikiri kabla ya mwisho wa mwezi huu tutakuwa na watumishi kwenye kada ya afya karibu 2,700. Kwa hiyo, miongoni mwa watumishi hao wengine tutawaleta katika jimbo lako ili waweze kusaidia kuongeza ile ikama ya watumishi wa kada ya afya. Ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tatizo walilonalo Ulanga ni sawasawa na tatizo tulilonalo katika Wilaya Bunda hasa katika Jimbo la Mwibara. Je, ni lini Serikali itatusaidia kuondoa tatizo la madawa na vifaatiba katika zahanati zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA ((MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kajege, Mbunge wa Mwibara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, anachouliza Mheshimiwa Mbunge ni lini Serikali sasa tutasaidia kuondoa tatizo la vifaatiba na dawa katika jimbo lake. Ukiangalia katika bajeti za Serikali kila mwaka tumeendelea kuongeza fedha ili kuhahakisha tunasogeza huduma hizi kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri, sisi wote ni mashuhuda bajeti ya vifaatiba na dawa kwa mfano katika mwaka 2015/2016 nchini ilikuwa ni shilingi bilioni 31, lakini katika mwaka 2021/2022 tunazungumzia bajeti ya dawa na vifaatiba nchi nzima ni shilingi shilingi bilioni 270. Kwa hiyo, niseme tu, tumeongeza bajeti tutaendelea kuongeza na kuboresha ili kuhakikisha tunaliondoa kabisa tatizo hili la huduma ya afya katika maeneo yetu yote nchini. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa dawa na vifaatiba imekuwa ni changamoto karibia nchi nzima. Je, ni kwa nini Serikali basi isihamasishe uwekezaji mdogo na mkubwa wa viwanda vya dawa na vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kuondoa Kodi ya Forodha pamoja na masharti mengine ili basi viwepo viwanda vingi ambapo mwisho wa siku dawa hizi zitakwenda kuwasaidia Watanzania na hususani walio wengi huko vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Agnesta Lambert ameleta pendekezo kwamba ni kwa nini sasa Serikali isione haja ya kuongeza uwekezaji kwenye viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba nchini ili kupunguza hii adha? Jambo hili ni jema, ndiyo maana sasa hivi sera ya Serikali ni kuhimiza watu wote wanaotaka kuwekeza nchini waje, ikiwemo kwenye sekta hii ya dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunawaruhusu watu wote na katika kipindi sahihi kabisa cha kuwekeza ni
sasa, kwa sababu Serikali imeboresha mazingira bora ya kufanya biashara nchini ambayo yanaruhusu wawekezaji wote kuwekeza ndani ya nchi. Ninaamini hao watakaokuja kuwekeza kwenye maeneo ya dawa na vifaa tiba wanapewa kipaumbele zaidi. Kwa hiyo, mazingira ya Serikali yako sahihi na tunawaruhusu na Serikali itaendelea kuwekeza zaidi. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa bajeti ya dawa ya Serikali imeongezeka kama ambavyo taarifa zinaonyesha kutoka shilingi bilioni 31 mpaka shilingi bilioni 270 na kwenye makabrasha ya Serikali inaonekana upatikanaji wa dawa umeongezeka kwa kiwango kikubwa lakini uhalisia kwenye Vituo vya Afya na Zahanati siyo sawa na hizi taarifa kwa sababu bado kwenye Jimbo la Sumve katika Vituo vya Afya na Zahanati tatizo la upatikanaji wa dawa bado ni kubwa sana: - (Makofi)

Je, Wizara haioni sasa umefika wakati muafaka wa kutengeneza utaratibu mahususi ambao utaisaidia Serikali kwenda kutatua tatizo hili kwa uhalisia kwa kupata taarifa halisi kutoka kwenye vituo na siyo makabrasha ambayo yanapatikana kwa wataalam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Kasalali Mageni ame-suggest jambo jema ambapo ukiangalia katika hotuba ya Wizara ya Afya wakati wanaisoma hapa pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye Idara ya Afya ambayo sisi tunasimamia, katika moja ya changamoto ambayo imekuwa ikitukumba ni kwamba Serikali imekuwa ikipeleka dawa lakini haziwafikii walengwa kama ambavyo imekusudiwa. Sababu kubwa ilikuwa ni baadhi ya watumishi, sio wote, kutokuwa waaminifu; aidha kwa kuuza zile dawa ama wengine kutokuzitumia mpaka zina-expire, matokea yake wale wagonjwa wanaotakiwa wapatiwe zile huduma za kimsingi wanashindwa kuzipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hizi Serikali tuko katika hatua za mwisho za kuandaa mfumo ambao sasa hivi utakuwa unajua dawa inayoingia na dawa inayotoka kiteknolojia. Kwa hiyo, naamini hiyo ndio itakuwa mojawapo ya suluhisho la kuondoa hii changamoto iliyopo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mgawanyo huu ulifanyika mwaka 2015/2016, ni miaka mitano, sita sasa; na kwa kuwa hadi sasa hakuna tamko la wazi la Wizara kuwasilishwa mbele ya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri zote mbili ili kuondoa hali ya madeni mbalimbali na rasilimali nyingine na mkanganyiko uliopo: -

Je, ni lini sasa Wizara itawasilisha mgawanyo huu kwa waraka maalum wenye GN mbele ya Mabaraza hayo mawili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika mgawanyo wa rasilimali tulizopokea ni pamoja na watumishi; Halmashauri ya Mji Mbulu sasa inakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi takribani miaka sita sasa kwa ajili ya hizo asilimia 40 ambapo wengine wamestaafu na wengine wamefariki kwa sababu mbalimbali: -

Je, lini sasa Serikali itaondoa tatizo hili la upungufu wa watumishi hawa angalau kwa awamu katika sekta mbalimbali katika Halmashauri yetu ya Mji wa Mbulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay katika swali lake la kwanza alikuwa tu anataka kwamba kujua ni lini Serikali itatoa tamko la wazi ambalo litawasilishwa katika mabaraza ili kutoa waraka maalum ili hizi Halmashauri mbili ziweze kujua sasa zimeshagawanyika rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, kwa sababu jambo hili limefanyika muda mrefu, ninaiagiza Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba waandike hili tamko la wazi haraka iwezekanavyo na ndani ya miezi mitatu jukumu hilo tutakuwa tumeshalifanya na mabaraza hayo mawili yatakuwa yamekaa ili wawe wanajua kabisa rasmi wameshaganyika. Kwa hiyo, ndani ya miezi mitatu tutakuwa tumeshalitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni kero ya watumishi wachache katika eneo lake na anataka kujua Serikali itatatua lini tatizo hili; niseme tu Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, tutashirikiana kwa Pamoja, kwa sababu wanaotoa kibali cha kuajiri watumishi ni Ofisi ya Raisi Utumishi na Utawala Bora na sisi jukumu letu ni kupata hao watumishi na kuwapangia vituo na maeneo ya kwenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale ambao tunaendelea kuwajiri kama ambavyo tumekuwa tukiendelea kuajiri walimu, tumekuwa tukiendela kuajiri watumishi katika kada ya afya, tunaendelea kuwaleta katika Halmashauri zetu nchi kwa kadri tutakavyokuwa tunapata kulingana na kibali tunavyopewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuleta watumishi katika eneo lako kwa kadri tutakavyokuwa tunapewa kibali na bajeti ya Serikali inavyohitaji. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa
kuwa mgawanyo wa Halmashauri hizi mbili ulitangazwa kwenye GN ya mwaka 2015, kwa nini sasa ichukuwe miezi mitatu wakati tangazo liko wazi na sheria hii iko wazi sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Flatei Massay ameeleza kwamba GN ni kweli ilitoka mwaka 2015 lakini bahati mbaya sana tamko la wazi lilicheleweshwa kuwasilishwa. Kwa hiyo, nikiri kabisa kwamba nafikiri kulikuwa na kupitiwa kwenye utekelezaji wa jambo hili na ndiyo maana, kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita tuko hapa, tumeahidi kulitekeleza ndani ya miezi mitatu ili kuhakikisha jambo hili limeisha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mgawanyo wa mali iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam haukuhusisha wadau wakiwepo Waheshimiwa Wabunge: -

Je, Serikali haioni sasa haja ya kuu-review ule mgao hasa katika ile mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu?

NAIBU SPIKA: Nataka kuamini ukisema Wabunge, unamaanisha pia na Madiwani hawakushirikishwa. Kwa sababu kama walishirikishwa Madiwani halafu Wabunge ndio hamkuwepo, ni ninyi ambao hamkuwepo. Hebu fafanua kidogo.

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam hayakushirikishwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jambo alilolita Mheshimiwa Abdallah Chaurembo ni kubwa sana ambalo linahitaji kwanza tufuatilie, tujiridhishe kwa sababu ninaamini kila jambo linapofanyika kunakuwa na muhtasari ambao huwa unaandikwa na vikao na idadi ya watu waliohudhuria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, endapo jambo hilo halikufanyika, basi ninaamini Ofisi ya Rais, TAMISEMI itazingatia namna bora kabisa ambayo itasaidia jambo hili liweze kufanyika kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunalipokea na tutakwenda kulifanyia kazi, ahsante sana.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja tu la nyongeza.

Kwa kuwa Jimbo la Kawe lina barabara nyingi sana ambazo zinaunganisha Wilaya na Wilaya kwa mfano, Wilaya ya Ubungo pamoja na Kindondoni huko kwa juu.

Ni lini sasa Waziri atakwenda pamoja nami ili ukaone hali halisi katika Jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mara baada ya Bunge nitaongozana na wewe pamoja na wale Wabunge ambao niliahidi katika Mkoa wa Dar es Salaam kuzungukia barabara zote za Mkoa huo, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza, niishukuru sana Serikali kwa kutusaidia pesa na kuweza kumalizia ujenzi wa madarasa ya Form Five na Six pale Nzela.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, majibu ya Serikali kuhusiana na Shule ya Sekondari Lubanga hayajajitosheleza vizuri kwa kuwa tumekuwa tukisuasua, hata hayo madarasa mawili yamejengwa na Mbunge pamoja na nguvu za wananchi. Kwa sababu maombi nimeshaleta zaidi ya mara tano, ni lini Serikali mtatupatia pesa kwa ajili ya kujenga madarasa na mabweni kwa ajili ya Form Five na Six pale Lubanga? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ili Mheshimiwa Naibu Waziri aone nachokiomba kina umuhimu, naomba commitment yake baada ya Bunge twende wote akaone ule umbali wa kutoka Lubanga kwenda kwenye hiyo shule ya Form Five na Six ambayo itafunguliwa mwezi waliopanga, ni kilometa 105, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ametaka tu commitment ya Serikali kwamba ni lini sasa Shule ya Lubanga itapelekewa fedha ili yale madarasa mengine yakamilike na shule hii tuweze kuifungua kwa wakati. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge tumelipokea suala hili, tutatafuta fedha na tutaziweka katika miradi ambayo inafuatia ili kuhakikisha katika mwaka wa fedha unaokuja shule hii iwe imekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili alikuwa ananiomba tuweze kuongozana mara baada ya Bunge, nimpe taarifa kwamba nitakuwa na ziara katika Mkoa mzima wa Geita. Kwa hiyo, niseme tu kabisa kwamba nitakwenda pamoja naye mpaka katika eneo hili analolisema kujionea kwa pamoja. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa huwa Shule ya Sekondari Msalala tumeweza kujenga madarasa na miundombinu yote kwa ajili ya Kidato cha Tano na cha Sita na pia Kata ya Nyangh’wale tumeweza kukamilisha ujenzi huo.

Je, ni lini sasa Serikali itatoa kibali ili tuweze kufungua shule hizo kwa Kata za Nyang’wale na Msalala? Tumeshakamilisha miundombinu, ni lini Serikali itatoa kibali ili tuweze kufungua shule hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema katika eneo lao wameshamaliza ujenzi wa shule za sekondari katika Kata za Nyang’wale pamoja na Msalala na anachotaka kujua tu ni lini Serikali itatoa kibali. Kwa sababu ameshalizungumza hapa nitaagiza wataalam wangu waende wakafanye tathmini pale wajihakikishie kama miuondombinu yote imeshakamilika. Wakishajiridhisha na hilo maana yake tutatoa kibali mara moja na shule hiyo itafunguliwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kipande cha barabara ya Mashua – Jiweni ni kipande muhimu sana kwa sababu kinahudumia Kata tatu; Kata za Masama Kusini, Romu na Masama Magharibi lakini Vijiji vikubwa vya Lukani, Kiu, Lwasaa na Jiweni. Barabara hii kwa sasa haipitiki, je, Serikali haioni ipo haja ya kupeleka fedha za dharura ili barabara hii ambayo inatuletea mazao huku Dodoma, iweze kupitika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tangia tumepata Uhuru, Jimbo la Hai hatujawahi kupata taa za barabarani, ni lini sasa Serikali itatuletea taa za barabarani kwenye Mji mkubwa unaokua wa Boma Ng’ombe, Maili Sita na Njia Panda ya kwenda Machame? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza hapa kwamba barabara ya Mashua mpaka Jiweni ambayo inahudumia Kata kubwa tatu haipitiki na ameomba fedha za dharura. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge tumelipokea ombi lake na tutakachokifanya sasa hivi tutatuma wataalam wakafanye tathmini na baada ya hapo tutatafuta fedha ili barabara hiyo iweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni lini sasa Serikali itapeleka taa za barabarani katika Miji Mikubwa ya Boma Ng’ombe, Njia Sita pamoja na Kata nyingine ambazo ameanisha hapa. Niseme tu najua jitihada kubwa za Mheshimiwa Mbunge kwa Jimbo la Hai na najua ana dhamira ya kweli ya kuwasaidia wananchi wake, kwa sababu ameleta ombi hili niseme na lenyewe tunalipokea kwa ajili ya kulifanyia kazi. Naamini kabisa kwa ufuatiliaji wake mzuri na fedha ikipatikana basi taa zitaletwa na Serikali kwa wakati kulingana na bajeti itakavyopatikana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniona. Nadhani mtakubaliana nami kwamba hizi barabara zinajengwa ili kuwapa watu urahisi wa maisha na kuwawezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kalali – Nronga ni barabara ambayo ina kona nyingi, ni ndefu na ina milima, ni chini tu ya Mlima Kilimanjaro. Huko Nronga ndiyo kwenye kile kiwanda kikubwa cha maziwa ya mgando ambayo pia yananywewa hapa Dodoma. Swali langu kwa Wizara, ni lini sasa barabara hiyo itaanza kutengenezwa kidogokidogo kwa lami ili wamama wale waweze kuteremsha maziwa yao mpaka mjini na kufika huku Dodoma kwa ajili ya afya za watu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachokieleza Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara ya Kalali – Nronga ambayo inapita pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro kule chini imeharibika na tunahitaji fedha ya kutosha kuendelea kuijenga na ombi la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba wanahitaji sasa ianze kujengwa polepole kwa kiwango cha lami. Niseme tu kwamba kulingana na bajeti yetu kadri itakavyoongezeka, tutalipokea na tutaliweka katika mipango yetu ya baadaye kuhakikisha barabara hii inatengenezeka ili iweze kutoa huduma kwa urahisi kwa wananchi wa eneo husika. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Sote tunafahamu kwamba ni adhma kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kumaliza changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi. Pia tunafahamu kwamba kwenye mwaka huu wa fedha Serikali imetenga zaidi ya bilioni 1.5. Lengo ni kuhakikisha kwamba baadhi ya majengo katika Hospitali hii ya Tunduma yanakamilika. Hata hivyo changamoto kubwa ni kwamba mpaka sasa hivi hakuna jengo la wazazi. Kwa hiyo mimi nilitaka nitoe ombi kwa Serikali, kwamba iangalie sasa namna, kwamba kwenye mwaka huu wa fedha iharakishe kupeleka fedha hizo kwa haraka ili majengo hayo yatakapokamilika yasaidie pia kutoa huduma za uzazi kwa wanawake wa Mji wa Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu; kwa kutambua jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Mbunge wa Jimbo la Tunduma na Naibu Waziri Mheshimiwa David Silinde katika kuhakikisha kwamba hospitali hii inakamilika kwa wakati; nilitaka tu niweze kufahamu na wananchi wa Tunduma, Maporomoko, wa Muungano wa Kaloleni wanataka kumsikia Mbunge wao kwamba anasemaje, kwamba ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa hii hospitali kwa maana ya majengo, vifaa Pamoja na watumishi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa wanawake wa Mkoa wa Mkoa wa Songwe, hususan kwenye kupigania masuala yao ya afya, anafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hili swali nasema nina interest nalo kidogo kwa sababu ni jimbo langu, na bahati nzuri leo nalijibu mimi mwenyewe. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya mama yetu Samia Hassan Suluhu ina dhamira ya dhati kabisa ya kusaidia sekta ya afya nchini. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka wa fedha huu 2021/2022 katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetengewa bilioni 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nimhakikishie tu kama Mbunge wa Jimbo husika fedha hiyo itafika na tutahakikisha kwamba inajenga kama amabvyo imekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ni kwamba anauliza ni lini hospitali ile itakamilika. Ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais imeshatoa fedha awamu ya kwanza imepeleka bilioni nne ambazo zimeshajenga jengo la kwanza na ambalo linatumika sasa hivi. Awamu ya pili tunapeleka bilioni 1.5, kwa hiyo itakuwa imebaki bilioni kama nne ya mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati kwenye hilo na ile hospitali itapelekewa fedha zote, kwa sababu muda bado upo na itajengwa na itakamilika kama ambavyo imekusudiwa. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba pia nishukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali yanakiri kwamba upembuzi yakinifu ulifanyika mwaka 2018 ambapo aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye ndiye Rais wa sasa naye alikuja kutoa ahadi. Swali; natakiwa kuikumbusha mara ngapi Serikali ili ujenzi uanze?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni ukweli usiopingika kwamba pale ambapo maeneo yetu na mikoa yetu inapopata fursa ya kutembelewa na viongozi wa Kitaifa kuna mambo ambayo tunanufaika ikiwa ni pamoja na ahadi za viongozi hao wa kitaifa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba hawa viongozi wa kitaifa wanapangiwa ziara ili kutembelea mikoa yote ili na sisi tuweze kufaidika katika ahadi ambazo wanatoa viongozi hao?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tunakubaliana na mawazo yake Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli Serikali imeshafanya kazi ya awali ya kuandaa detail design na imeshakamilika; na kama ambavyo nimemjibu katika swali langu la msingi hapa, nilimwambia kwamba sasa hivi kazi ambayo tunaifanya Serikali ni kutafuta fedha tu ili daraja hilo lianze kujengwa, hicho kivuko ambacho tumekitaja hapo. Kwa hiyo nimwambie tu kwamba hahitaji kuikumbusha Serikali mara kwa mara kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali makini inakumbuka kila ahadi ambayo tumeitoa. Kwa hiyo na kwenye hili nimwondoe shaka kabisa kwamba fedha itakapopatikana tutakamilisha ujenzi huo, na ninaamini ndani ya kipindi hiki cha miaka 5 ya Mheshimiwa Rais wetu tutalitekeleza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili linalohusu ziara za viongozi, ninaamini hapa anazungumzia Mawaziri, Naibu Mawaziri, na hususan Ofisi yetu ya Rais TAMISEMI. Nimuahidi tu kwamba nitafika katika eneo lake na tutafanya ziara ya pamoja kwenda kujionea shughuli za kimaendeleo zinazofanyika eneo lile ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Mungaa ina shule zaidi ya nane za O-level na kwa sababu shule hii ya Mungaa ni kongwe ndiyo maana niliomba shule hii iweze kujengwa ili kuwapatia fursa wanafunzi wanaokosa nafasi ya kwenda kidato cha tano na sita kama ambavyo imekuwa ni tatizo kwenye maeneo mengine.

Kwa hiyo, naiomba Serikali katika tathmini hiyo iweze kuchukua umuhimu wa pekee kuhakikisha shule hiyo inajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika vikwazo ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza ni pamoja na vikwazo vya watoto wa kike katika shule zetu za sekondari zikiwemo shule za kata. Ni nini mkakati wa Serikali kujenga hosteli za kuweza ku-accommodate wanafunzi wote wa kike katika shule zetu ambazo ziko katika Jimbo la Singida Mashariki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza alikuwa ameelezea tu kwamba Tarafa ya Mungaa ina shule nane za O-level na hivyo alikuwa anasisitiza tu kwamba tuiweke kwenye tathmini. Katika jibu la msingi tumekubali kwamba kwenye tathmini ya zile shule 100 ambazo tunakwenda kuzifanyia upanuzi nchi nzima kwa ajili ya kupokea watoto wa kidato cha tano miongoni mwa shule tutakayoifanyia tathmini ni Shule ya Mungaa. Kwa hiyo, hilo tumelikubali litafanyika katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili kuhusu vikwazo kwa watoto wa shule ambao wanatembea umbali mrefu kuelekea shuleni, moja ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kujenga hosteli. Ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha nyingi tu kuhakikisha kwamba tunajenga hosteli katika maeneo mbalimbali na ninyi mmepitisha bajeti hiyo. Kwa hiyo, tunachosubiri tu ni fedha zitakapotoka tutaainisha maeneo mbalimbali na tutazingatia Jimbo la Singida Mashariki. Ahsante. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini ukiangalia majibu yake yanasema kwamba bado wanafanya tathmini ina maana hawajaanza na robo tayari ya mwaka tumeshapita.

Sasa swali langu ni lini watakwenda kujenga shule hizo ili watoto wa kike wasiweze kupata adha hizo kwa sababu tumeona adha wanazozipata watoto wa kike hasa Mkoa wa Iringa wanapata changamotoo kubwa sana. Kwa hiyo, tunaomba majibu ni lini wanaanza, tumeshapitisha robo sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba robo ya kwanza ya mwaka imepita na bado inaonesha kama hatujafanya tathmini, kwa hiyo anachotaka kujua exactly ni lini? Ni kwamba Serikali ina mipango na mikakati yake na mimi nimwambie tu kwamba kabisa Serikali ya Awamu ya Sita hatutashindwa kukamilisha haya majengo kwa wakati. Moja ambacho hafahamu tunapojenga kwa mfano darasa ni muda wa miezi mitatu darasa linakuwa limekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachokisubiri sasa hivi tu baada ya robo ya kwanza na mifumo ya fedha kufunguka kinachofuatia baada ya hapo ni fedha kuanza kuzitenga na kuzipeleka katika maeneo husika yaliyopangwa katika bajeti. Kwa hiyo, ninyi ondoeni wasiwasi Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan hii kazi tunaiweza na tutaimaliza kwa wakati. Ahsante. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi nilitaka niulize swali. Serikali ilikuwa na programu ya kukarabati shule kongwe nchi nzima ikiwepo Shule ya Sekondari Iringa Girls na Lugalo Secondary zilizopo Iringa ambazo ni za bweni kwa watoto wa kike na hasa watoto wenye ulemavu wa ngozi, viungo na wasioona. Pale hapakufanyika ukarabati wa mabweni mawili; moja katika shule ya Iringa Girls na nyingine Lugalo Secondary.

Je, ni lini sasa Serikali itatukamilishia mabweni yale ili watoto wale wenye ulemavu wasiendelee kupata shida ya mahali pa kulala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri anazungumza kitu ambacho anakifahamu kwamba hizi shule alizozitaja ziko katika mipango yetu. Kwa hiyo, aondoe wasiwasi tu kwamba tutatekeleza ahadi ya kuwasaidia wanafunzi wote sio Iringa Girls na Lugalo ni shule zote kongwe tulizozikusudia zitafikiwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ilishaahidi kujenga shule bora ya mfano ya wasichana katika kila mkoa nchini; na kwa kuwa shule hiyo ya mfano katika Mkoa wa Arusha tulikubaliana kwamba itajengwa katika Jimbo la Longido; na kwa kuwa tulishatenga eneo la kujengwa shule hiyo katika Kata ya Angekahang, ni lini ujenzi wa shule hiyo ya mfano kwa ajili ya wasichana wetu itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mpaka sasa hivi tumeshaainisha maeneo yote 26 ambayo shule hizi zitajengwa baada ya kupata mapendekezo kutoka katika kila mkoa. Kwa hiyo, kinachosubiriwa sasa hivi tu ni fedha itoke na baada ya hapo tutapeleka fedha kwa awamu ya kwanza katika mikoa 10 ambayo tumeainisha mwaka huu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge atupe muda eneo lake halitabadilishwa na kazi hiyo itafanyika kama ambavyo imekusudiwa. Ahsante sana.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali imejipangaje kutatua mgogoro unaofanana na huo katika Vijiji vya Magara na mashamba ya wawekezaji kule Kiru?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali itakuja lini kutatua mgogoro katika vijiji vya Kata ya Kaiti ambavyo ni Vijiji vya Minjingu, Vilima Vitatu na Kakoi kati ya wafugaji na Jihubi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali lake la kwanza na la pili ameainisha baadhi ya maeneo akisema Vijiji vya Magara na mashamba ya wawekezaji na hilo eneo lingine katika Mkoa wa Manyara. Katika maagizo ambayo sisi Serikali tumeyatoa ni kwamba tutaagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na haya maeneo aliyoyataja, basi waende kutafutia ufumbuzi na watatuletea taarifa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tujue hatua zaidi za kuchukua. Hata hivyo, tunaamini kwamba yapo ndani ya ofisi ya mkoa na wanaweza kuyamaliza na hii migogoro isiendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Silinde, Naibu Waziri TAMISEMI, na kwa niaba ya Waziri, nataka niongeze kidogo majibu kwa Mheshimiwa Mbunge kwa kumpa taarifa kwamba viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa wa Manyara wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa walikuja kuniona juzi kueleza hayo matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewaahidi kwamba mwezi Oktoba tutakwenda kuitisha mkutano wa Viongozi wote wa Mkoa watuambie kwa pamoja matatizo yote yanayowasibu juu ya migogoro yao yote, halafu tupange ratiba ya kutekeleza kwa pamoja, pamoja na haya aliyoyasema. Hii ni nyongeza ya haya. Maagizo ya kwa Mkuu wa Mkoa tutayapeleka, lakini na mimi mwenyewe nitakwenda mwezi Oktoba. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nishukuru kwa majibu yanayoridhisha ya Serikali. Ni kweli kituo hiki cha Mapera kuanzia mwezi Julai kimeanza kutoa huduma. Kituo cha Muungano, wananchi hawa kituo hiki wamekijenga wenyewe kwa asilimia 100 kwa kusaidiwa na mapato ya ndani kidogo sana, hiyo shilingi milioni 60, lakini sasa wanahangaika kujenga jengo la wazazi. Je, Serikali ina mpango gani kuunga jitihada hizi mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kata ya Kipololo imejenga Zahanati ya Kipololo, Kata ya Mbuji imejenga Zahanati ya Mnyao, Kata ya Litembo imejenga Zahanati Lituru lakini pia Kata ya Mkako Kiukuru wamejenga zahanati. Zahanati hizi zimekamilika, zingine sasa zina miaka mitatu, miwili mpaka leo hazijaanza kazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi katika zahanati hizi ili ziweze kuanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba tu Kituo cha Afya Muungano ambacho kimejengwa na wananchi kwa asilimia 100 na sasa hivi kuna jitihada za kujenga jengo la wazazi, anataka commitment ya Serikali. Niseme tumelipokea na tutaliweka katika mipango inayofuata ili kuhakikisha tunaingiza katika bajeti zetu hiki Kituo cha Afya cha Muungano ili kiweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu kata alizozitaja katika vijiji alivyoviainisha kama Kata ya Kipololo, Mbuji, Litembo na Likako ambazo zimejenga zahanati na mpaka sasa hivi bado hazijafunguliwa. Niseme tunalipokea na naamini watendaji wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambao wanasimamia Idara ya Afya wamelisikia hili, hivyo sasa tutajua namna ya kupanga watumishi waliopo na vile vile kama Serikali itaajiri hapo mbele kidogo tutapeleka watumishi ili vituo hivi vianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mengine mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa sasa halmashauri na wananchi kwa kweli wamewekeza nguvu kuboresha miundombinu ya mabweni, vyoo, madarasa, mabwalo katika shule hizi za Dosidosi, Dongo, Ndedo na Lesoit, nini commitment ya Serikali sasa kama kuwaongezea nguvu katika jitihada hizi za kuboresha miundombinu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kwenda na mimi Kiteto kwa siku ambazo sio nyingi sana tutembelee shule hizi za Dongo, Lesoitd, Ndedo, Dosidosi na Sunya ili kuona mazingira yalivyo ili tuweze kushauriana? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edward Olelekaita Mbunge wa Jimbo la Kiteto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anataka tu commitment ya Serikali kutokana na jitihada kubwa iliyofanywa na wananchi wake katika Jimbo la Kiteto. Nikiri tu kwamba moja ya mpango wa Serikali katika Mwaka huu wa Fedha ni kuongeza upanuzi wa shule 100. Katika hizo shule 100 lengo letu ni ili ziweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, miongoni mwa shule tutakazozingatia ni pamoja na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha katika ule mpango wetu wa shule 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili la kwenda Kiteto, nitakwenda. Nitaongozana na Mheshimiwa Mbunge ili tukajionee hayo maeneo husika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Shule ya Sekondari Ngh’oboko Halmashauri ilishajenga majengo ya kidato cha tano na sita, madarasa manne yakiwa na ofisi tatu na vyoo 16 vya ndani. Je, Serikali iko tayari kujenga bweni na kukamilisha bwalo ambalo liko usawa wa Hanam likiwa na store ili shule hii iwe na kidato cha tano na sita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge hili ombi lake ameshalileta ofisini kwetu na nimeshalikabidhi kwa wataalam waweze kuangalia kwamba wanaweza kusaidia nini. Maombi aliyoyaainisha hapo ni bweni na bwalo, kwa hiyo, nilishalikubali tangu jana alipokuwa ameniletea yale maombi. Kwa hiyo, nimwambie tu kwamba aondoe wasiwasi, Serikali chini ya Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu itafanya hii kazi na tutaifungua hiyo shule ili wanafunzi waanze kusoma.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pale katika Jimbo la Kinondoni tuna shule za sekondari tisa zenye wanafunzi zaidi ya 11,000 na pass rate pale pamoja na wale wanaokwenda kidato cha tano na sita ni zaidi ya asilimia 80. Hata hivyo, hawa ni watu wa hali ya chini sana, wanapelekwa shule za mbali. Kwa kuwa hatuna high school, naiomba Serikali ikubaliane na mimi kwamba itujengee hata day school ya high school ambayo itaweza kuwasaidia wananchi wa vipato vya kawaida kabisa katika jimbo lile badala ya kuwapeleka mbali wanafunzi wetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba moja ya maelekezo moja ya maelekezo aliyotoa Waziri wa Nchi katika Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo Kinondoni ambazo zina mapato mengi na haya maelekezo tumewaagiza Wakurugenzi kuhakikisha wanatenga fedha kupitia fedha zao za ndani kujenga shule za sekondari ikiwemo kumalizia madarasa katika maeneo ambayo hakuna.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ambalo wameliomba hapa namwagiza Mkurugenzi wa Kinondoni kuhakikisha hili linatekelezeka nami nitakwenda kufuatilia kuhakikisha hii ahadi ambayo nimeiahidi hapa Bungeni inafanya kazi, Kinondoni wana huo uwezo wa kutekeleza kwa kutumia mapato yao ya ndani. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kuna changamoto kubwa sana katika maeneo ya wafugaji; na kwa sababu wana utamaduni wa kuhama; na changamoto hii iko katika baadhi ya Kata katika Wilaya ya Karatu na Mbulu Vijijini katika eneo linaitwa Yaeda Chini; je, Serikali sasa iko tayari kutazama maeneo haya na kuhakikisha wanajenga mabweni kuanzia Shule za Awali, Msingi na hadi Sekondari ili kuhakikisha kwamba jamii hii ya kifugaji na wenyewe watoto wao wanapata haki ya kupata elimu kama ambavyo walivyo katika maeneo mengine nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anaomba kwamba tuendelee kuyazingatia maeneo ya wafugaji na ameainisha hapa eneo la Yaeda Chini na anataka commitment ya Serikali ikiwemo kujenga shule kuanzia awali, msingi na sekondari ili tuweze kuwasaidia maeneo hayo. Nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikizingatia kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, katika eneo ambalo anatokea Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kwamba Serikali ilijenga kule shule. Kwa hiyo, hata maeneo yote ya wafugaji tutaendelea kuyazingatia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuyaweka kwenye mpango kwa kadri fedha inapopatikana na kuhakikisha kwamba tunahudumia wananchi wote ili wapate huduma ya msingi ya elimu ikiwemo hayo maeneo ambayo ameainisha. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; nini kauli ya Serikali kwa kuwa Daraja la Gunyoda limepoteza maisha ya wakazi wa Jimbo la Mbulu Mji hasa nyakati za masika? Kwa kuwa daraja hilo ni kubwa na linaunganisha halmashauri mbili imekuwa kikazo kikubwa sana kwa huduma za kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa tatizo la kuongezeka kwa makorongo katika nchi yetu limekuwa kubwa na tatizo hili linachochewa na mabadiliko ya tabianchi. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutuma Watalaam wa Wizara, Mkoa na Halmashauri zote nchini ili wafanye mapitio upya katika maeneo haya ili waandae mpango wa kuzuia kuongezeka kwa makorongo, lakini pia na ujenzi wa maeneo ambayo yatapewa kipaumbele katika bajeti za Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza anataka kauli ya Serikali juu ya hilo korongo ambalo linatakiwa kujengwa daraja. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi Serikali ya Awamu ya Sita, moja ya kazi yake kubwa ambayo tumekubaliana kuifanya sasa hivi ni kuunganisha maeneo yote kwa kujenga madaraja hususani katika maeneo korofi. Kwa hiyo na daraja hili katika mpango wa fedha wa mwaka unaofuatia tutaliweka katika vipaumbele vyetu kuhakikisha daraja hili na lenyewe linapatiwa fedha ili liweze kujengwa kwa umuhimu ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema hapa kwamba daraja hili linaunganisha halmashauri mbili kwa maana ya Mbulu Mji na Halmashauri ya Mbulu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, lilihusu maongezeko ya makorongo, akawa anataka Serikali tufanye tathimini upya kwa kutuma watalaam ili tuweze kuzuia uendelezaji huu. Moja; nipokee kama ushauri kwamba sisi kama Serikali tumepokea, lakini la pili; ni kwamba kwa hivi karibuni tulishawatuma wahandisi wetu nchi nzima kukagua na kuanisha maeneo yote korofi hususani madaraja ili tuweze kuyatengea bajeti na yaweze kupitishwa. Kwa hiyo na hili ni sehemu ya mapendekezo ambayo ameyatoa na sisi tunaendelea kuyapokea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa swali la msingi linazungumzia korongo lililopo katika Wilaya ya Mbulu Mji ambalo linaenda mpaka Wilaya ya Karatu na katika Tarafa ya Yasi ambako kuna wakulima wa vitunguu katika maeneo hayo. Sasa je, Serikali haioni ipo haja ya kuikutanisha TANROADS Mkoa wa Arusha kwa maana ya Wilaya ya Karatu na TANROADS Mkoa wa Manyara ili kwa pamoja kuwe na nguvu ya kuhakikisha haya madaraja ambayo yanaathiri wilaya mbili yanapatiwa ufumbuzi ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kama inavyotakiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nikubali na nipokee ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwa sababu Serikali ni moja na tunafanya kazi kama wamoja, basi kwa kutumia hadhara hii niahidi tu kwamba tutakaa pamoja na watu wa ujenzi kuhakikisha, hao TANROADS Arusha na Manyara wanakutana na kufanya tathmini katika maeneo hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha. Kwa hiyo tumepokea ushauri wake na tutaufanyia kazi. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo. Jimbo la Mji Korongo hili la Gunyoda linalosemwa lipo kwenye barabara moja hiyo hiyo kuja Jimbo la Mbulu Vijijini, lipo korongo la Hudaya ambalo lina thamani kubwa ya 1,200,000,000.

Je, Serikali ipo tayari sasa na hii ya Hudaya kuweka kwenye mpango kwa sababu ukiweka hili la Gonyoda la Hudaya utakuwa hujaweka kwenye mpango wa kujengwa barabara hiyo itakuwa haitumiki kabisa.
Je, Waziri yupo tayari na hili ili barabara itumike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa sababu na hili ni ombi jipya na bahati nzuri lilishafanyiwa tathmini na gharama ya fedha na jukumu letu sisi kama Serikali ni kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa hayo madaraja. Kwa hiyo na lenyewe nilipokee tutaenda kushauriana na wataalam ili na lenyewe tuliingize katika mpango wa awamu inayofuatia. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kuuliza swali la nyongeza moja. Rais aliyepita, Mheshimiwa Magufuli alituahidi kutujengea daraja kutoka Kata ya Ifunda kwenda Kata ya Lumuli sasa napenda kujua, je, tumefikia hatua gani kutekeleza hiyo ahadi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, moja ya mpango wetu ni kwamba ahadi zote za Viongozi Wakuu na Viongozi wetu Wastaafu na ile ambayo ilitolewa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, zote zipo katika mipango ya utekelezaji wa Serikali. Kwa hiyo, aondoe shaka zipo pale na Serikali inachosuburi tu ni namna ya kuzitekeleza. Ahsante sana.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba na wewe umeweza kuona hili swali halijajibiwa na mimi nimegundua hivyo, lakini nimpongeze Waziri kwa majibu mazuri yanayoonyesha namna gani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanga bajeti kuendelea kuhakikisha maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yakamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu nipatiwe majibu mazuri, ambayo yanaendana na swali langu ili niweze kuridhika sasa kwamba ni lini Serikali inaweza ikaona kuna mpango mzuri kwenye hizi Kata ambazo ni kubwa hazina zahanati ili wananchi hawa waweze kupata zahanati na siyo kwamba kuna maboma hakuna hata hayo maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yaani ni ujenzi mpya, Serikali ina mpango gani na njia ipi madhubuti kuhakikisha kwamba Kata ambazo ni kubwa mfano, Kata hii ya Ng’ambo ambayo iko Tabora Mjini na zingine nyingi ambazo sijaziainisha zinaweza kupata ufumbuzi huo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwanza tunamaliza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa zote nchini. Tangu uhuru tulikuwa tuna Tarafa 570 na tulikuwa na Tarafa 363 tu pekee ambazo zilikuwa na Vituo vya Afya na katika Awamu ya sasa hivi tulikuwa na Vituo vya Afya kama 207 ambavyo Serikali tayari imeshapeleka fedha kwa awamu mbili ambazo nafikiri kila Mbunge anazo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukija kwenye level ya zahanati kwa kila Kijiji lengo la Serikali ambalo tumeliweka na ndiyo maana nimejaribu kuelezea hapa fedha ambazo tumezitenga ni kwa ajili ya kwenda kumalizia zahanati ambazo zimeanzishwa na nguvu za wananchi na nyingine zimeanzishwa na mapato ya ndani ya Halmashauri na ndiyo maana kwenye swali hili la msingi lilipokuwa linaulizwa, tumemshauri Mbunge wa Jimbo na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Tabora kwamba, hamasisheni wananchi mkishirikiana na vyanzo vya ndani muanze ujenzi ili sisi kutoka Serikali Kuu tulete fedha kwa ajili ya kumalizia hiyo zahanati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukisema kwamba tutajenga zahanati vijiji 12,000 kwa wakati mmoja kwa sasa hivi hatuwezi kudanganya kwenye hilo, ukweli wetu ni kwamba tunamaliza Vituo vya Afya Tarafa zote, tunamaliza Hospitali katika Halmashauri zote halafu kwenye ngazi ya vijiji tutapeleka fedha, kwenye vijiji vyote ambavyo zahanati wananchi wamepeleka nguvu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo ndiyo jibu letu, ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kuishukuru sana Serikali kwa jitihada kubwa ambazo zimeshaanza katika kuboresha Mji huu wa Mbamba Bay. Lakini pamoja na shukrani hizo, ninapenda kupata majibu kutoka Serikalini, Mji huu wa Mbamba Bay ni mji ambao ni wa muda mrefu sana takribani miaka mia moja, lakini vilevile ni kitovu cha utalii katika Mkoa wa Ruvuma, lakini hiki kiasi cha kilometa moja, moja na nusu kinachotengwa ni kidogo kulinganisha na mahitaji yaliyopo kwa sababu mji huu umedumaa kwa muda mrefu.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba katika bajeti inayofuata angalau tupate hata kilometa mbili ili kuendana na kasi ya kukuza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Jimbo la Nyasa ni kubwa sana kwa ukubwa wake na jiografia milima mikali kiasi kwamba hawa TARURA ambao wanasimamia hizi barabara wanapata shida sana katika usimamizi kutokana na kuwa na gari bovu ambalo kila wakati linaendea matengenezo kutokana na hali halisi ya mazingira.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza gari jipya moja angalau kuwawezesha hawa watumishi wa TARURA waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mji wa Mbamba Bay ni Mji mkongwe na Mheshimiwa Mbunge kama alivyozungumza nafahamu jitihada kubwa ambazo anazifanya katika Jimbo lake na anahitaji tuongeze bajeti kuhakikisha ule mji unaongezewa lami.

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika swali letu la msingi kwamba tutaendelea kutenga fedha na katika mwaka wa fedha unaokuja kwa maana ya 2022/2023 basi Mji wa Mbamba Bay tutauongezea bajeti kwa ajili ya ujenzi wa kilometa walau moja ya lami nyingine ili kuongeza mtandao wa lami katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili ameeleza kwamba Halmashauri ya Nyasa gari lake watu wa TARURA ni bovu na wanashindwa kufika katika maeneo korofi ni muhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini tumeshaagiza magari mia moja ambayo tutayagawa katika Halmashauri za Wilaya 100 nchini ikiwemo Halmashauri ya Nyasa.

Kwa hiyo, hilo tunauhakika nalo atapata gari jipy. Ahsante. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Sengerema tunazo shule 31 za Sekondari na katika hizo shule 31 Sekondari mbili ndiyo zina kidato cha Tano na Sita, Sengerema Sekondari na Nyampurukano Sekondari na zimeelemewa wanafunzi na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja aliona ile hali ya Sengerema kwa watoto walivyowengi na wananchi wa Sengerema wanamshukuru Mwenyezi Mungu wanaendelea kufanya kazi ya ziada kwa ajili ya kuwashughulikia akinamama kupata watoto wengi kuijaza dunia.

Mheshimiwa Spika, sasa hili jambo la Sengerema kutokukosa Sekondari hizi za Kidato cha Tano, Sengerema wanafunzi wanakosa nafasi na Mheshimiwa Naibu Waziri aliona na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alikuja kule na akaona hiyo hali. Lini sasa hili jambo litafanyika kwa haraka kwa ajili ya huyo Mdhibiti Ubora kwenda kukagua hizi shule kwa sababu zimekaguliwa mwaka huu na mwaka kesho tunategemea wanafunzi watakuwa ni wengi nini msaada wa wizara katika jambo hili, la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili ni kwamba Sengerema Sekondari imeelemewa na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alikuja pale na akatoa ahadi ya kutupa vitanda kutokana na watoto alivyoona wanalala katika mazingira magumu na Nyampurukano Sekondari pia imeelemewa ni nini msaada wa Serikali katika jambo hili ili waweze kutusaidia kwa haraka sasa katika kuzisajili shule hizi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Tabasamu Mbunge wa Jimbo la Sengerema niweze kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ameeleza kwamba katika halmashauri yake ya Sengerema kuna Sekondari karibu 31 na katika hilo eneo kuna shule mbili tu za kidato cha tano sita na anataka kwamba tuwaagize watu wa Udhibiti Ubora kwamba waende wakakague hizi shule tuone kama zinakidhi vigezo.

Mheshimiwa Spika, na ni nitumie fursa hii najua kwamba kazi nzuri ambayo anaifanya Mheshimiwa Mbunge na bahati nzuri nilifika pale na niliona jitihada yake kubwa kujenga shule 15 kwa mpigo. Niwaagize tu Halmashauri ya Sengerema kwamba waende sasa hivi huko walipo kuanzia wiki ijao wakague na watuletee taarifa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kama maeneo haya yanakidhi vigezo ya kuanzishwa kidato cha tano na cha sita na kwa sababu tunaile programu yetu ya kuzipanua shule 100 kwa ajili ya kuziongezea madarasa na miundombinu ili kuzifanya kuwa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo, tutazingatia katika ule mpango ili tuone tunaweza tutaongeza shule ngapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwamba Mheshimiwa Waziri alifika kule na aliahidi nimwambie tu kabisa kwamba najua alifika shule eneo la Sengerema na aliahidi kutoa baadhi ya vitanda kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya wanafunzi ama waweze kupata malazi bora. Kwa hiyo, ahadi ile ipo pale pale na itatekelezeka kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alikuwa ameahidi na nikuhakikishie tu kwamba shule zote ambazo zitakidhi vigezo basi tutaziingiza katika mpango. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto la Jimbo la Sengerema ni sawa sawa na Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Igalula hatuna shule ya kidato cha tano na sita, lakini baada ya kutambua hayo wadau na wanachi tumeweza kujikongoja na tumepata mabweni na miundombinu salama ya kuweza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Je, lini Serikali itaitambua shule ya Sekondari ya Tula ili iweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili kupunguza uhaba wa shule katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Venant Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba katika maeneo yale ambayo yanahitajika kuanzishwa kidato cha tano na cha sita ni lazima halmashauri husika kupitia Ofisi za Elimu pamoja na watu wa Udhibiti Ubora wanakwenda katika eneo husika wanakagua ile shule, wanatuletea hayo mapendekezo tunaona kama ina meet vile vigezo.

Kwa hiyo, kama inafikisha vile vigezo basi sisi tutakuwa tayari kuongeza fedha na baadhi ya miundombinu ili kuhakikisha tunaisajili na kupokea. Kwa hiyo, na yeye Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tutawaagiza watu katika halmashauri yake watatuletea hiyo taarifa na baada ya hiyo taarifa maana yake tutaleta majibu ya msingi kama inakidhi kupandishwa au itasubiri katika mwaka mwingine wa fedha. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, shule ya Sekondari Farukwa ilipandishwa hadhi na ikawa ya kidato cha tano na sita lakini baadaye wakasitisha na sababu walizofanya wasitishe tumezimaliza tayari ni lini sasa wataturudishia shule yetu ya kidato cha tano na sita. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Monni Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, anasema kwamba Shule ya Farukwa ambayo ipo katika Jimbo la Chemba wameshamaliza zile changamoto kwa hiyo wanataka kujua ni lini sasa Serikali itairudisha ile shule ili sasa ianze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tutawatuma wataalam kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI watakuja kukagua kujiridhisha kama hizo vile vigezo vyote mmeshamaliza na kama itakuwa imekamilika basi nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mwaka unaokuja hiyo shule itafunguliwa na wanafunzi wataenda kusoma hapo. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru sana, kwanza naipongeza Serikali kwa kazi inayoondelea, lakini pia nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maporomoko haya ya Kalambo Falls ni kivutio kikubwa sana kwa Mkoa wa Rukwa, sasa Serikali ina mpango gani wa kujenga lami kwa sababu wawekezaji na watalii wanapenda sana vitu vizuri kama lami, vitu vizuri kama umeme. Sasa Serikali ina mpango gani wa kutengeneza miundombinu kwenye maporomoko hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba hili alilolileta Mheshimiwa Mbunge ni ombi kwa sababu ya umuhimu mkubwa wa maeneo haya ya maporomoko ya Kalambo Falls. Kwa hiyo na sisi tuseme tu kwamba tumelipokea tutafanya tathimini na tutaangalia mfuko wetu jinsi ulivyo kama fedha itapatikana basi tutailekeza Ofisi ya Rais kupitia TARURA Kalambo waweze kwenda kujenga huko. Lakini kwa sasa tutakwenda kufanya tathimini halafu tuone jinsi tutakavyopata fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Kwa sababu mahitaji ya wananchi wa Mchinga ni kufanya biashara na kuongeza kipato, na kivuko hiki ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa jimbo hili. Ningependa kupata tamko rasmi la Serikali kwamba ni lini hasa watarajie kwamba ahadi hii ya Serikali itatekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshi mi wa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Shigongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi, Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ni lini hasa. Nimemueleza hapa kwamba tulishafanya tathmini, na daraja hilo linahitaji shilingi milioni 147, na imetengwa katika bajeti ambayo tutapitisha katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika mwaka wa fedha unaokuja daraja hili litajengwa, na hiyo nina uhakika kwa asilimia 100. Ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo Mchinga zinafanana sana na Changamoto za Wilaya ya Nkasi katika Kata ya Isunta na Kata ya Namanyele ambako kivuko hicho kimekuwa kikiathiri sana wanafunzi wanaokwenda Mkangale primary pamoja na sekondari ya Mkangale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itajenga kivuko hiki ili kuwasaidia watoto ambao wamekuwa wakipata shida sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kijibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, kama nilivyoeleza awali, madaraja yote yakiwemo yaliyo katika jimbo lake tumeshayafanyia tathmini, na mengi tunatarajia kuyaweka katika bajeti hii inayokuja ya mwaka 2022/2023. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatekeleza ahadi hii ambayo Serikali imeahidi. Ahsante sana.
SPIKA: Ahsante sana. Waheshimiwa Wabunge, tukiwa hapo kwenye Ujenzi na Uchukuzi, nilikuwa nimesema habari ya TARURA, naona Naibu Mawaziri wameshaingia humu ndani, Naibu Waziri anayehusika na TARURA aseme jambo kwa sababu huko tunapigiwa sana simu barabara zimekatika kwenye majimbo.

Sasa kila Mbunge hapa hawezi kupata nafasi ya kueleza, sasa toeni maelekezo ya jumla kwa TARURA nchi nzima ili barabara zinazosimamiwa na TARURA ambazo zimekatika na hazipitiki wao waende wakazitazame ili wananchi waweze kupata huduma ya barabara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu mwongozo ama maelekezo ambayo Ofisi yako imeyatoa kwetu Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nimelipata suala hili vizuri, nawaagiza Mameneja wote wa Mikoa wa TARURA pamoja na halmashauri zote nchini kuanzia siku ya kesho waende katika maeneo yote nchi nzima kwenda kufanya tathmini haraka iwezekanavyo na kutupatia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia kitengo chetu cha TARURA ili angalau tuweze kutoa fedha katika zile fedha zetu za dharura. Katika yale maeneo ambayo bajeti yake ipo maana yake tutapeleka zile fedha kuhakikisha zinakwenda kufanya hiyo kazi ambayo imekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie tu kabisa hili agizo ambalo tumelitoa litatekelezeka na hiyo taarifa ikishafika tutaileta katika Bunge lako Tukufu kabla ya Bunge hili kwisha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwa kuwa bado changamoto ni kubwa sana katika hospitali ya Wilaya ya Mbozi, na fedha ambazo tayari zimepelekwa hazijatosha kumaliza changamoto katika wodi ya wazazi. Nilikuwa nataka kufahamu, kwa nini sasa Serikali isifikirie kutuongezea fedha katika mwaka ujao wa fedha ili kuweza kumaliza changamoto zilizopo katika wodi ya wazazi likiwemo suala la upanuzi pamoja na ukarabati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wanawake wa Mkoa wa Songwe katika Wilaya za Mbozi, Ileje, Songwe pamoja na Momba tuko vizuri sana katika suala la kuijaza dunia. Kitakwimu, katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi wastani wa watoto 450 huzaliwa kwa mwezi. Kutokana na changamoto hiyo Hospitali hii ya Wilaya ya Mbozi iko katika Kata ya Vwawa, na kata hiyo mpaka sasa hivi ninapoongea hakuna kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, kwa nini sasa Serikali isifikirie kutujengea kituo cha afya katika Kata ya Vwawa ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue mchango wa Mheshimiwa Mbunge kwa wanawake wa Mkoa wa Songwe; amekuwa akifanya kazi. Ndiyo maana kama unavyoona, katika swali lake la kwanza ambalo ameliuliza hapa, anasema Serikali ifikirie kuongeza fedha kwa ajili ya kusaidia ile wodi ya akina mama na watoto ya Hospitali ya Mbozi ambako yeye mwenyewe safari iliyopita kabla ya Bunge hili alikuwa hapo na ameahidi kulikarabati jengo hilo. Kwa hiyo nimpongeze kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ninaweza nikakisema ni kwamba Serikali imepokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge ambapo katika swali letu la msingi tumejibu kuwa katika mwaka unaofuata tutaweka milioni 50, lakini pia tutazingatia kwa kuangalia vyanzo vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, kuhusu kujenga kituo cha afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Kata ya Vwawa, na hili tumelipokea. Kwa sababu moja ya malengo la Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma kwa wananchi. Kwa hiyo, ombi lake nalo tumelipokea ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wanawake wa Mkoa wa Songwe na kazi nzuri ambayo wanaifanya ili kuhakikisha tunakisaidia Chama chetu Cha Mapinduzi pamoja na kuwasaidia wananchi ambao wana imani na Serikali yao. Ahsante sana.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa watu wenye ulemavu wanahitaji privacy zaidi na miundombinu rafiki wakati wa kujifungu. Je, Serikali inaonaje ikatenga vyumba maalum ambavyo vitatumika na wanawake hawa wenye ulemavu wakati wa kujifungua pale wanapojitokeza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Ikupa, Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha watu wenye mahitaji maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naye nimpongeze kwa kuwa anafanya kazi nzuri ya kufuatilia watu wenye mahitaji maalum nchi nzima. Hili alilolileta hapa kama swali. Ameeleza vizuri, kwamba watu wenye mahitaji maalum wanahitaji privacy, na je, Serikali tunalionaje hili kama moja ya mahitaji yetu ya msingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba tumepokea mawazo na mapendekezo yake, na tutalipeleka katika timu yetu ya wataalam ili kuhakikisha kwamba walau katika baadhi ya hospitali na maeneo yote ambayo huduma ya afya inahitaji tuweze kutenga hivi vyumba maalum ili kuwasaidia wenzetu wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, tumelipokea na tutalifanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulize masikitiko makubwa ya majibu ya Serikali. Mheshimiwa Naibu Waziri aliyejibu swali hili alijibu swali hili hili katika Bunge lililopita. Leo nilipoona swali hili limerudishwa kwa makosa kutoka swali lile la kwanza nililopenda kuuliza nikaacha kwa sababu nimetumiwa jana jioni. Lakini majibu yaliyotolewa ni tofauti kabisa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri aliyoyatoa kule mwanzo kwenye Bunge lililopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi niiombe tu Serikali kwamba, tunachouliza hapa ni ujenzi wa Daraja la Bunyoda ambalo Serikali imepigiwa kelele kwa miaka tisa. Na Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa majibu mazuri sana kwenye Bunge lililopita, kwamba usanifu wa daraja hili ni bilioni moja na milioni mia mbili. Leo jibu lililokuja ni kwenda kufanya usanifu upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani kama Mheshimiwa Waziri atarejea kwenye majibu yake arejee, lakini kwa Bunge hili linalokuja daraja hili lisipowekwa kwenye bajeti, nadhani nitakuwa naunga mkono bajeti ambayo haina tija kwa wananchi wa Mbulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, ninaomba majibu ya kina ya daraja hili kujengwa kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu ndani ya Bunge hili, akisema katika mwaka wa bajeti wa 2022/2023 daraja hili litatengewa fedha bilioni moja na milioni mia mbili ambapo usanifu wake uko tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pil; eneo la Mbulu Mji lina kata 10 vijijini na kata saba mjini. Eneo lote la vijijini lina makorongo makubwa. Ni lini wataalam wa TARURA na TAMISEMI watakwenda katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ili waweze kujua namna ya kuweza kutatua tatizo la makorongo linalokabili maeneo ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu katika maeneo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, baadhi ya maelezo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyatoa tuliyatoa katika Bunge lako Tukufu, na nilishatoa maelekezo katika ngazi za chini. Kwa hiyo kitu ambacho walikuwa wameshatueleza ni kwamba walikuwa bado hawajafanya usanifu, isipokuwa walitupatia zile gharama za awali, kwamba wanakadiri daraja lile litagharimu bilioni moja nukta mbili. Kwa hiyo sisi ambacho tunahitaji ni exactly figure ili tuweze kuliweka katika bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nipokee maoni na maelezo ambayo ameyatoa Mheshimiwa Mbunge, na niahidi kwamba nitalifanyia kazi, kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu haitakuwa tayari kulidanganya Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo hilo hatutalipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto nyongine za wananchi wa Jimbo la Mbulu kumaliza matatizo ya makorongo kwa kujenga madaraja pamoja na kurekebisha barabara, Mheshimiwa Mbunge na hili tumelipokea, tutaendelea kufanya usanifu pamoja na tathmini na kama ambavyo kiti chako kilieleza siku zilizopita uliopita, tathmini ya awali tumeshaifanya, bado tunakwenda kufanya tathmini ya kina ili kujua ukubwa wa matatizo katika maeneo yote nchini ikiwemo Jimbo la Mbulu, na sisi tutachukua hatua ya kuyakamilisha. Ahsante sana.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo katika Halmashauri au Jimbo la Mbulu halitofautiani na tatizo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambapo Daraja la Godegode halipitiki kwa muda mrefu sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nipate kauli ya Serikali kuhusiana na ujenzi wa daraja hili ambalo limekuwa ni kiungo katika kata za jirani lakini wananchi wamekuwa wakipata shida sana katika kupata usaifiri. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fatma Toufiq Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja ambalo Mheshimiwa Mbunge amelieleza liko katika barabara ambayo inahudumiwa na TANROADS. Lakini kwa kuwa Serikali ni moja na sisi Ofisi ya Rais-TAMISEMI tunafanya kwa ukaribu sana na watu wa TANROADS tumelipokea hilo, na kwa sababu kama ni tathmini ya pamoja tunaifanya wote kwa pamoja, hususan katika zile barabara ambazo zina mwingiliano; kwa hiyo nilipokee na hili, nalo tuahidi tu kwamba tutalifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo hayo wanapatiwa huduma. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nishukuru sana Serikali kwa kuleta fedha za TARURA zinazojenga Barabara ya kutoka Kambanga kwenda Ifinsi na kutoka Majalila kwenda Ifinsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani zote hizo barabara ile haitakuwa na umuhimu wa aina yoyote kama hakutakuwa na bajeti ya Daraja la Mto Mnyamasi eneo la Ifinsi.

Je, ni lini Serikali itajenga daraja hilo ili iweze kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Bugu ambao hawana mawasiliano kabisa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naye ameomba daraja, na kiukweli madaraja mengi ndiyo hayo ambayo sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tuliahidi kwamba tunayafanyia tathmini ili kuhakikisha kwamba tunarahisisha usafiri katika maeneo mbalimbali nchini. Na ahadi hiyo tuliitoa ndani ya Bunge kwa sababu maeneo mengi nchi hii yanasumbuliwa zaidi na madaraja, kwa sababu, moja, ya kuharibika, lakini pili, maeneo mengine yana madaraja ambayo wakati wa misimu ya mvua yanakuwa hayafikiki kabisa kwa sababu ni mabovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunatakiwa tukajenge madaraja ya kudumu ili kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanapata huduma hiyo ya usafiri na usafirishaji wa wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo ambalo amelieleza Mheshimiwa Kakoso lipo katika mipango yetu, na asubiri tu kwamba baada ya mwaka huu wa fedha, naamini yale yako ndani ya bajeti tutayatekeleza. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa sababu alipofanya ziara jimboni kwangu tuliweza kwenda eneo moja ambako mto umekatika, mawasiliano hayakuwepo na akaahidi kutoa fedha, na bahati nzuri fedha imeshatolewa, lakini mkandarasi aliye pale ni jeuri na hafanyi kazi kama inavyotakiwa, na fedha tayari anayo.

Je, Waziri yuko tayari kutusaidia kumsukuma huyo mkandarasi aifanye hiyo kazi mara moja ili kuepusha shida ya upitaji ya pale kwa sababu sasa hivi mvua zinaendelea kunyesha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilifika jimboni kwa Mheshimiwa Hussein na nilishuhudia hayo madaraja mabovu siyo moja tu mengine yameshaanza na kutekelezeka na baadha ya madaraja ambayo nilikuta katika jimbo lake ni madaraja ya miti, ambayo wananchi walikuwa wanalipishwa fedha. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tuliagiza fedha hizo ziende, sasa changamoto ambayo imetokea hapa ni mkandarasi kushindwa kufanya kazi kwa wakati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge moja nimelipokea, lakini pili kutumia Bunge lako Tukufu namuagiza huyu Mkandarasi afanye kazi kwa wakati kinyume na hapo tutavunja mkataba na kupeleka mkandarasi mwingine ili akamalizie hiyo kazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri ambayo imeifanya na hasa kwa barabara hizi kilomita sita na kilometa 3.5 kama alivyosema kwenye jibu la msingi zimejengwa. Kabla sijakwenda kwenda kwenye swali, nimshukuru Waziri wa TAMISEMI, Ndugu yetu Bashungwa alipopita kwenye kazi zake katika Mkoa wetu wa Njombe alikuta tuna maafa pale katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, akatoa fedha zake mfukoni kuwasaidia wahanga wale, namshukuru sana sana na wananchi wanakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, kwa kuwa kazi ni nzuri na kwa kuwa kilometa zilizobaki ni kilometa 2.5. Ni lini wataanza kuzijenga ili wananchi wa Makambako wawe na imani kubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini katika kilomita hizo zilizobaki zitamaliziwa kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa moja ya jitihada kubwa ambayo Mheshimiwa Mbunge anaifanya ni kuhakikisha hii ahadi ya Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kilomita sita inakamilika na kilomita zilizobaki ni 2.5 ambazo sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tunapaswa kuzitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishazungumza na Mheshimiwa Mbunge, tulishazungumza na TARURA Mkoa wa Njombe kuwaambia kwamba barabara hizi ziwekwe katika mpango wa kila mwaka wa fedha ili hizi kilometa 2.5 tuzimalize kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025. Kwa hiyo, matarajio yetu kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 barabara hizi kilometa 2.5 zitakuwa zimeshakamika. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo. Nauliza kuwa, je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga barabara ya kuanzia Gairo hadi Kata za Chagongwe na Nongwe kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa ahadi ambayo imeahidiwa katika Awamu ya Nne ya Serikali na anataka Awamu ya Sita tuikamilishe kwa wakati. Jibu moja kubwa la msingi ambalo Wabunge wote wanapaswa kufahamu ni kwamba Ahadi zote za Viongozi, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumeziainisha na zote zinathamani halisi ya fedha ambayo tumeziwekea kila ahadi, kama ni barabara, maji, Kituo cha Afya zote zipo katika vitabu vyetu na utekelezaji wake ni kwamba tumekuwa tukitenga fedha katika kila mwaka wa fedha. Kwa hiyo, hata hili la Awamu ya Nne na lenyewe lipo katika utekelezaji huo. Kwa hiyo, ninachoweza kukisema ni kwamba, litatekelezwa kulingana na fedha tunavyokuwa tunazipata kila wakati ili kuhakikisha tunamaliza ahadi zote za viongozi zilizopo. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Kwa kuwa nimeshatoa machozi ya kutosha mbele ya viongozi wetu wakuu kuhusiana na uhitaji wa lami kwenye barabara zetu tatu fupi pale Vunjo ambazo ni Barabara ya Uchira-Kisomachi-Kolalie, Barabara ya Pofo-Mandaka-Kilema na Barabara ya Himo Sokoni- Lotima. Nataka nimwombe Waziri kama ataridhia kuambatana nami kwenda kutembelea barabara hizi ili aweze kuona uhalisia wa hadhi ya barabara hizi na kero ambazo wananchi wanapata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu kwa kifupi swali la Mheshimiwa Dkt. Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari kuambatana na Mbunge kwenda kuziona hizo barabara ili tuhakikishe kwamba tunawapatia ufumbuzi wa kudumu. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama unavyojua Mji wa Bunda unakua kwa kasi na Serikali ya Awamu ya Nne iliji-commit kujenga kilomita 10 katika mitaa ya Mji wa Bunda na hasa ukizingatia sasa kuna barabara moja tu ya lami kutoka pale Mjini kwenda Bomani. Nataka nijue ni lini Serikali itakamilisha ahadi hii ya kilomita 10 ili Mji wa Bunda ufanane na Miji mingine kwa lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu awali kwamba ahadi zote viongozi zipo na tunachokifanya sasa hivi zote zimeshatengewa fedha yaani kwa maana thamani halisi. Kwa hiyo, tunavyopata fedha ndipo ambavyo tunatekeleza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nimwahidi najua Mji wa Bunda na bahati nzuri na mimi mwenyewe nimefika, kwa hiyo ninachokiahidi ni kwamba zile barabara zitajengwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye nia ya dhati kabisa kuondoa adha kubwa ambayo wananchi wa wilaya hizi mbili, mikoa hii miwili ya Ruvuma na Njombe, kwa sababu mto huu una mamba wengi lakini ni mto mkubwa sana. Kwa hiyo, ni hatari kubwa sana kwa wananchi pale, kwa hiyo kwa majibu nashukuru sana. Ombi tu kwamba waharakishe ili daraja hili liweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ombi hili, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Barabara ya Unyoni kuelekea Maguhu inapitika kwa shida sana lakini ipo barabara kutoka hapo Maguhu Mapera kuelekea Kambarage, barabara hii iko hatarini kutoweka. Kuna korongo kubwa sana kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha.

Sasa je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura ili kuokoa ile barabara iweze kutumika kama inavyotumika siku zote? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu dogo la pili, jiografia ya Wilaya ya Mbinga hususan Jimbo la Mbinga Vijijini ni milima na mabonde hali ya kwamba inahitaji madaraja mengi lakini na barabara zinapitika kwa shida sana. Nahitaji commitment ya Serikali, je, iko tayari kuongeza fedha tofauti na ile hali ya kawaida katika Jimbo la Mbinga Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Liuka Kapinga Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, bahati nzuri nilifika jimboni kwake, niliona kazi nzuri anayoifanya na jinsi wananchi wanavyomkubali kwa kuwa anafuatilia kwa ukaribu zaidi matatizo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba swali la kwanza alilouliza ni kwamba je, tupo tayari kutoa fedha za dharula ili kusaidi hili korongo kubwa linapita katika hizi barabara ambazo ameziainisha. Niseme tu katika Bunge lako Tukufu baada ya agizo la Mheshimiwa Spika tumeshafanya tathmini ya awali ya kugundua maeneo yote ambayo ni korofi nchi nzima. Kwa hiyo, ambacho tutakwenda kuangalia tu katika eneo lako la Mbinga kama maeneo hayo yametengwa. Kama halipo maana yake tutamuagiza meneja wa TARURA katika halmashauri yako afanye tathmini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu kuongeza fedha, tumewaagiza Mameneja wote wa TARURA Mikoa pamoja na katika Halmashauri. Katika mwaka huu wa fedha, watakavyoleta zile bajeti zao walete bajeti kulingana na uhalisia wa maeneo husika kwa hiyo, hilo ndiyo agizo. Kwa hiyo, naamini kwamba maeneo haya ambayo

Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha yatakuwepo katika bajeti hizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Naibu Waziri na Waziri wake kwa majibu mazuri ya Serikali. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwenye Jimbo langu la Nanyumbu, sasa hivi kuna kadhia kubwa ya korongo kubwa ambalo limesababisha wananchi wa Kijiji cha Kiuve wawe kisiwani. Jambo ambalo limesababisha mama mmoja kujifungua kwa sababu ya kushindwa kufika hospitalini kutokana na korongo hilo.

Swali, je, Waziri atakuwa tayari kufuatana nami kwenda kuona kadhia kubwa iliyopo ambayo wananchi wa Kijiji kile cha Chiuve wanashindwa kufika hospitalini kutokana na lile korongo ili tutafuta majawabu sahihi ya wananchi wale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hiyo changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza hapa, alinieleza hata kabla hajauliza hili swali la nyongeza na akawa ananiomba kwamba twende wote pamoja. Kwa hiyo, nafikiri amelileta hapa ili nimthibitishie kupitia Bunge. Nipo tayari kuongozana naye ili tukashuhudie hili eneo na tuweze kupata majawabu ya haraka kuhakikisha tunawasaidia wananchi wa eneo la Chiuve. Ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Wilaya hii ya Newala ni kati ya wilaya kongwe hapa nchini na shule zake mfano Shule ya Makukwe II, Nakaako na Babati ni shule ambazo zina hali mbaya na mapaa yake yake yanavuja hivi sasa. Kipindi hiki cha masika, vijana wetu wanasoma katika mazingira magumu sana. Swali la kwanza, Serikali itakuwa tayari kuzifikiria shule hizi katika mwaka ujao wa fedha kuipangia bajeti ya kutosha ili kufanya ukarabati?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; linakwenda ndani ya jimbo langu. Katika Kata ya Mikangaula, Wilaya ya Nanyumbu kuna shule ya Mikangaula ambayo ina wanafunzi 1,500 na kuna darasa lina wanafunzi 300. Kwa kutambua adha hii wananchi wa Kata hii wameamua kutumia nguvu zao ili kujenga madarasa katika vijiji vingine. Je, Serikali ipo tayari kushirikiana na wananchi wa Kata hii kuipatia fedha ili vijiji hivi ambavyo vimetoa nguvu zao waweze kupata fedha na kuwanusuru wananchi wao? (Makofi) Je, ni lini Serikali itakabidhi majengo yaliyokuwa ya Hospitali ya Muhimbili kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili kupunguza uhaba wa majengo katika Hospitali hiyo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli nimweleze tu kwamba Serikali ipo tayari kuingiza katika mpango Halmashauri ya Newala na kuhakikisha hizo shule kongwe zote zinafanyiwa ukarabati. Hapa nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka sasa hivi tathmini ya awali tumeshapata tathmini ya Shule 750 za Msingi Kongwe ambazo zimejengwa kabla ya mwaka 1950, yaani kabla ya uhuru wa nchi yetu ambazo tunatakiwa kuzifanyia tathmini.

Mheshimiwa Spika, katika mpango wetu ni ndani ya miaka mitano shule zote kongwe nchini tutazikarabati kwa kujenga madarasa mapya, ndiyo maana katika mwaka wa fedha 2022/2023 tuna ujenzi wa madarasa kwenye Shule za Msingi 12,000 nchi nzima kwa ajili ya kwenda kufanya hayo maboresho. Kwa hiyo, tuko tayari kwa hilo ikiwemo na katika eneo la jimbo la Mheshimiwa katika Kata ya Mikangaula ambayo umeianisha kwamba tutaingiza katika mpango na tutawapatia fedha ili kumalizia hayo majengo. Ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa lengo ni kuboresha elimu yetu nchini. Ni kwa nini sasa Serikali isipandishe hadhi Shule ya Sekondari Sepuka ambayo ipo Jimbo la Singida Magharibi ambayo kwa sasa ndiyo shule kongwe kuliko shule zote katika Tarafa ya Sepuka ambayo imebeba nusu ya Kata za Jimbo la Singida Magharibi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba ombi la Mheshimiwa Mbunge ni Shule ya Sepuka sijajua ni sekondari ama msingi, lakini naamini ni Sekondari kwenda Kidato cha Tano na cha Sita ambao wanataka tupandishe hadhi na kuwa kidato cha tano na cha sita kwa sababu inapokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali. Moja ya mpango wa Serikali ni kufanya upanuzi wa shule za sekondari za Kata 100 katika mwaka 2022 ili tuongeze wigo wa kuongeza wanafunzi wa kwenda kujiunga na kidato cha tano na cha sita.

Mheshimiwa Spika, naamini kama lipo katika mpango, basi maana yake tutalifanyia kazi katika mwaka huu fedha 2022/2023, lakini kama halipo maana yake tutalifanyia kazi katika mwaka wa fedha unaokuja 2023/2024. Kwa hiyo, nitayapitia ili niweze kujiridhisha nione kama halipo katika mwaka huu, kama litakuwepo mwakani maana yake tutaliingiza, kwa hiyo ni hilo tu. Ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, hali ilivyo kwenye Wilaya ya Newala ni sawasawa na Kibaha Vijijini kwenye shule za Dutumi, Madege na Magindu. Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati sahihi na kule kulifanyia ukarabati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kumjibu Mheshimiwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba mwakani tuna madarasa zaidi 12,000 kwa ajili ya ukarabati wa shule za msingi nchini. Kwa hiyo, naamini kwa sababu moja ya utaratibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunayafikia majimbo nchini, likiwemo Jimbo la Kibaha Vijijini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aondoe wasiwasi kwa sababu tutaweka katika mpango na wananchi wake watapata hiyo faida ya yeye kuwepo ndani Bunge. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. Ahsante sana.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa shule ya Sekondari ya Sumve ni moja ya shule kongwe ambayo ina historia kubwa sana kwenye nchi yetu ambapo mama Maria Nyerere alipata elimu yake pale na ni shule ambayo imechakaa sana. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuipa kipaumbele shule hii ya Sumve Sekondari katika kuanza ukarabati wa shule kongwe katika bajeti inayokuja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kumjibu kwa kifupi sana Mheshimiwa Kasalali kwa swali lake; ni kwamba shule aliyoitaja Sumve ambayo ina historia kubwa amesema tuipe kipaumbele basi na mimi nilipokee ombi lake tutazingatia, tutampa kipaumbele na kama tutakavyowapa Wabunge wote katika Bunge hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alifika katika Mtaa wa Ubungo Kisiwani tarehe 14 Mei, 2022 akafanya mkutano na wananchi pale na kulikuwa na mgogoro wa kiwango. Aliagiza kwamba wataalam wakafanye tena tathmini ili warudi kwa wananchi waelewani kuhusu kiwango ambacho kinastahili. Je, ni lini hiyo ripoti itapatikana?

Mheshimiwa Spika, la pili. Kwa kuwa muda mrefu umepita na wananchi pale hamna kinachofanyika na hata anuani za makazi hazijafanyika pale kwa sababu ya suala hili: Kwanini Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri msitoe tamko kwa sababu fidia hii haijulikani italipwa lini na wananchi wanaendelea na maisha yao kama kawaida? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili, Mthamini Mkuu alishamaliza kazi yake na alishasaini. Kwa hiyo, baada ya hili zoezi kukamilika, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, ni kutafuta fedha. Kwa hiyo, kikubwa ni kwamba tutarudi kukaa na wananchi na kuwaeleza haya yote ambayo yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Waziri kwamba kauli ya Serikali ni kwamba bado tunahitaji kuendelea kulitumia lile eneo, na ndiyo maana tunatafuta fedha ili tuwalipe kwa wakati. Kama muda utakuwa umepita, maana yake kuna options mbili kwenye sheria. Moja, kurudia uthamini; na pili, kunaweza kukawa na interest ili kuhakikisha kwamba wale wananchi wanapata fidia stahili kutokana na kutoa eneo lao. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya ulipaji wa fidia inawakumba pia wakazi wa Mbagala, maeneo ya Kokoto mpaka Kongowe na Tuangoma, bado wanadai fidia kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Kilwa Road; na kwa kuwa toka imefanyiwa tathmini mwaka 2019 mpaka leo hii hakuna malipo yoyote yanayofanyika kwao: Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia hiyo kwa wananchi wa Mbagala – Kokoto mpaka Kongowe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wote ambao wamefanyiwa tathmini yao watalipwa haki zao kwa sababu Serikali haina muda wa kutaka kwenda kumtapeli mwananchi yeyote. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi huo. Kwa sababu Serikali ni moja, barabara ile najua iko upande wa TANROADS, basi tutafanya kazi hiyo kwa pamoja kuhakikisha jambo hili linawafikia. Ahsante sana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Katika kuboresha ufaulu katika shule zetu za kata; je, Serikali ina mpango gani sasa kuweza kukamilisha maabara?

Lakini swali la pili, ni lini Serikali itamaliza upungufu wa walimu hasa wa sayansi katika shule zetu za Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni kwamba lengo la Serikali kwa sasa ni kuhakikisha shule zote zinakuwa na maabara na ndiyo maana katika kila mwaka wa fedha tumetenga fedha kujenga maabara katika shule zetu za sekondari za kata nchini. Kwa hiyo, hilo ni kipaumbele chetu ambacho Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ametuagiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, upungufu wa walimu wa sayansi tunautambua na ndiyo maana katika ajira zote ambazo tumekuwa tukizitoa sasa hivi tunawapa vipaumbele pia zaidi walimu ambao wamesoma masomo ya sayansi na tutaendelea kufanya hivyo ili kuondoa hili tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi katika shule zetu. Ahsante sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba shule zote za kata na za Serikali kwa ujumla zinapata hatimiliki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha shule zote zinakuwa na hati iliki na ndiyo mpango uliopo sasa na tumehamasisha halmashauri zote kutekeleza jambo hilo. Kwa hiyo lipo katika mpango wa Serikali. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni kweli barabara hii kwa muda mrefu imekuwa na shida na haipitiki, ni barabara ambayo ni ya ulinzi, inaunganisha kati ya Msumbiji na Tanzania. Kwa mazingira yaliyoko Msumbiji, barabara hii ni muhimu itengenezwe kwa sababu kipindi cha kifuko haiptiki kabisa: -

Je, ni lini sasa Waziri wa TAMISEMI, au Naibu wake wataenda katika eneo hili kuangalia hii kero ambayo inapatikana katika eneo lile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Kwa kuwa barabara hii iliweza kupitishwa kwenye michakato mbalimbali kabla TARURA haijaanzishwa; na baada ya TARURA kuanzishwa, barabara hii ikabaki kwenye TARURA peke yake; na maombi yale yalifika mpaka kwenye RCC: Je, lini Serikali itaangalia ma-file yake kuona mapendekezo yale ili yaweze kupitishwa kwa haraka kunusuru hali iliyoko pale Msumbiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daimu Idd Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko tayari Kwenda katika jimbo lake muda wowote na tuko flexible kwa sababu huo ndiyo wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba, jukumu la kupandisha hadhi hizi barabara liko chini ya TANROADS kupitia Wizara ya Ujenzi. Kwa hiyo, nafikiri kwa sababu Serikali tunafanya kazi kwa pamoja, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba jambo hili linafanyika kwa haraka. Ahsante sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Mlalo kwenye Ngwelo, Mlola, Mashewa hadi Korogwe inaunganisha wilaya mbili; na barabara hii iko chini ya wakala wa barabara vijijini kwa maana ya TARURA na imeshaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kilomita 2.7: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuipandisha hadhi hii barabara na kuwa ya mkoa?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kazi nzuri ambayo inafanyika katika Jimbo la Mlalo, hususan hii barabara ya Mlalo – Nachiwa mpaka Korogwe na ndio maana sisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tulitenga fedha kwa ajili ya kuanza sasa kutekeleza kwa ujenzi wa lami. Sasa kwa kuwa, maombi yao ni kupandisha hadhi, nafikiri tutaiagiza Halmashauri ya Mlalo ifuate taratibu kama ambavyo tumeiagiza Halmashauri ya Tunduru, ili barabara hiyo nayo iweze kufikia hivi viwango ambavyo Mheshimiwa Mbunge anahitaji. Ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii pamoja na mwongozo uliotolewa na Serikali lakini bado utekelezaji wake ni mdogo kwenye halmashauri zetu zote.

Je, Serikali ina mkakati wa kusimamia mwongozo huu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, Serikali haioni haja sasa ya kutunga sheria ya kuhusu jambo ili basi kuwanusuru wanafunzi wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba huu mwongozo unasimamiwa na jukumu letu sisi kama Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ni kufuatatilia utekelezaji wa mwongozo huu na tathmini yake. Kwa hiyo, niseme tu tutarudi tena tutawaagiza Maafisa Elimu kuhakikisha kwamba agizo la Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu la wanafunzi wote waliokatishwa masomo wanarudi shuleni linatekelezwa kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, kuhusu sheria, tumelipokea wazo hili ni jema, na sisi kama Serikali tukishirikiana na Bunge tutafanya mchakato kuhakikisha kwamba sheria hiyo inaletwa Bungeni ili tuweze kuwalinda Watoto hao ambao wameacha shule. Ahsante sana.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la moja la nyongeza; kwanza nichukue nafasi hii nimshukuru sana kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Mvomero, Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kutupa fedha nje ya bajeti ya TARURA.

Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuiongezea TARURA bajeti ya matengenezo ya barabara, kwa kuwa barabara nyingi zilizoko vijijini ambako kule yanapotoka mazao ya wakulima wetu, barabara zile ni mbovu.

Je, Serikali ni lini itaongeza fedha za bajeti ya TARURA ili barabara hizi ziweze kutengenezwa vizuri na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Jimbo la Mvomero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ofisi ya Rais – TAMISEMI, tunapokea pongezi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini suala la pili la msingi ni kwamba nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu kipenzi, Mama yetu Samia Suluhu Hassan inazingatia jambo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amezungumza hapa la kuongeza bajeti kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimuondoe shaka tu kwamba fedha bahati nzuri iliyopo ipo na tutaendelea kuifanyia kazi na nyongeza yoyote tutaendelea kuileta kwa wananchi.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii, naomba kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga, barabara ya Maswa – Kadoto, kupitia Mnadani kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy Sabu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba bahati nzuri maeneo aliyoyataja yapo katika mipango yetu na kadri tutakavyoweka fedha maana yake tutayajenga na yatakamilika. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na pia napongeza majibu mazuri ya Serikali hasa hiyo tathmini ambayo inaenda kufanyika ni tathmini nzuri ya school mapping.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili. Swali la kwanza, hivi karibuni kuanzia miaka ya 2017 kumekuwa na ujenzi wa madarasa, mabweni na kadhali na hiyo ni miundombinu ya shule. Je, tuna uhakika gani kama hizi Shilingi Bilioni 230 nazo zitaendeleza tu utaratibu huo wa kujenga madarasa badala ya shule mpya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye taarifa ya jana ya sensa, katika Wilaya ya Sikonge, wananchi wameongezeka mara mbili, maana yake ni kwamba hata idadi ya wanafunzi imeongezeka mara mbili.

Je, kwa nini Serikali isiweke kipaumbele ya kujenga shule mpya Nne katika Wilaya ya Sikonge kwenye hayo maeneo ambayo nimeyataja kwa mwaka huu wa fedha? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba katika tathmini tunayoifanya ya ujenzi wa shule mpya za msingi na katika fedha ambayo imetengwa sehemu ya hiyo fedha itakwenda kujenga shule mpya sehemu nyingine tutakwenda kukarabati maboma ya madarasa ambayo yamekwisha muda wake, na maeneo mengine tutabomoa kabisa na kuanza upya ujenzi katika mabwawa ambayo yamekwisha kabisa. Kwa hiyo, huo ndiyo mpango wa Serikali ambao upo, kwa hiyo nimuondoe hofu kwenye hilo.

Mheshimiwa Spika, suala lake kuhusu shule nne mpya za msingi, nikuhakikishie tu fedha ipo kwa sababu mradi peke yake wa BOOST ambao tunautekeleza kwa miaka mitano, thamani yake ni trilioni 1.15. Kwa hiyo ni fedha ipo ya kutosha ambayo tutahakikisha changamoto ya elimu msingi tunazimaliza nchini. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nitakuwa na swali moja dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo, mamlaka ambayo imeahidiwa kwa muda mrefu kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Mwaka 2009 Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake Mheshimiwa Mizengo Pinda, aliahidi; pia imetajwa kwenye awamu karibu tatu za Ilani ya Uchaguzi ya Chama changu cha Mapinduzi. Mwaka 2020 Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyepo naye aliahidi kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo. Nilitaka nijue tu Mheshimiwa Waziri kama yuko tayari sasa kuongozana nami kwenda kujiridhisha sababu hizi zinazosema kwamba uanzishwaji wake unacheleweshwa kwa sababu ya mapato ya ndani. Tuongozane ili twende kujiridhisha kwa kukaa na wataalam na Halmashauri ili tuweze kupata jibu la pamoja la uanzishwaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Shirati.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge ndani ya wiki mbili tutakaa na Baraza la Madiwani pamoja na Wakurugenzi katika Halmashauri yake, kuainisha na kutangua vyanzo vyote vya mapato ili tuone kama vinaweza kuhudumia ili mamlaka hii ndogo iweze kuanza.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ili kuepusha hii migogoro: Je, ni lini sasa Serikali itaweza kwenda kuweka mipaka halisi ya ile sehemu ili tuendelee na shule kwa sababu mgogoro huu umekuwa ukijirudia mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nawaagiza Halmashauri ya Temeke kwamba baada ya rufaa hii kwisha, mara moja waanze mchakato wa kuweka mipaka halisi ili watu wasiende kuvamia hilo eneo. Kwa hiyo, mchakato uanze mara moja kuanzia sasa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Barabara ya Getifonga - Mabogini hadi Kahe, iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kujengwa kwa kiwango cha lami na huko ndiko ilikojengwa hospitali ya wilaya: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?

Mheshimiwa Spika, barabara ya International School - Kibosho KCU hadi kwa Raphael imebakiza kilomita nane kukamilika kwa kiwango cha lami: Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba barabara aliyoitaja mwanzo ya kutoka Getifonga – Mabogini Kahe, ipo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara hii kwa sasa iko katika usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami. Usanifu unaofanyika ni wa kilomita 31.25, kwa hiyo, tupo katika hatua nzuri kwenye hiyo.

Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka International School – Kibosho - KNCU mpaka kwa Raphael na yenyewe kilomita 8.42 tayari imeshajengwa kwa kiwango cha lami. Kiwango ambacho kimebakia ni kilomita 5.49, kwa hiyo na yenyewe tunatafuta fedha ili tuanze ujenzi kwa kiwango hicho.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka kuuliza ni lini sasa Serikali itajenga daraja linalounganisha Halmashauri ya Msalala, Kijiji cha Namba Tisa na Halmashauri ya Nyang’hwale? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya kazi kubwa ambayo sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumekubaliana kuifanya sasa ni pamoja na kutambua madaraja korofi yote ambayo tunahitaji kuyahudumia sasa ili tuunganishe moja na eneo lingine. Kwa hiyo, hata hili daraja alilotaja Mheshimiwa Mbunge la kuunganisha Halmashauri ya Msalala na Halmashauri ya Nyang’hwale liko katika mpango wetu, hivyo, nimuondoe hofu katika hilo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Wizara kupitia TAMISEMI, kupeleka fedha nyingi katika Kata ya Swaya. Naomba kujua kama ni lini watawaongezea ili waweze kujenga daraja linalounganisha wananchi na hasa wanafunzi kuelekea kwenye Shule ya Sekondari ya Swaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukipeleka fedha mara kwa mara, uzuri yeye mwenyewe amekuwa ni shuhuda na nimhakikishie tu kwamba sisi tunazingatia maoni ya wananchi na jambo lake tumelipokea. Ahsante sana.
MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Swali la kwanza; kwa kuwa Kyela ni sehemu ambayo ina mvua nyingi sana na huwa inakumbwa na mafuriko kwa kipindi kila mwaka. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta fedha ambazo zimekosekana kwa muda mrefu kwa maendeleo ya barabara Wilayani Kyela?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa inajulikana barabara haziwezi kudumu kwenye mafuriko hasa hizi za changarawe na udongo. Je, Serikali imewahi kufanya utafiti wa kutafuta namna nyingine ya ujenzi wa barabara kwa mfano, kutumia enzymes katika kitengo chake cha utafiti hapo TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kupeleka fedha kwa ajili ya barabara na nimwondoe shaka tu. Bahati nzuri Serikali sasa hivi imeongeza bajeti yake na sisi tumekuwa tukitekeleza vya kutosha. Kwa hiyo, hilo aondoe shaka kabisa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tafiti katika maeneo ambayo barabara hazidumu kutokana na mvua nyingi kama ilivyo Kyela, utafiti huo umefanyika na moja ya mipango yetu ni kuja na majibu ambayo yatasaidia barabara za maeneo hayo ziweze kupitika muda wote. Kwa hiyo, Serikali ipo kazini na inafanya hii kazi kwa umakini kabisa ili kuwasaidia wananchi wake.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa zoezi hili alilolisema Mheshimiwa Waziri hapo awali lilishawahi kufanyika na halikuwa na mafanikio na barabara hii ni muhimu sana kwa Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Mwanza. Je, nini maelekezo yake ya haraka kwa wafanyakazi wa TARURA ili zoezi lifanyike haraka ili tuweze kuunganisha barabara hii katika mikoa hii miwili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimeshatoa maelekezo kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Busega kupitia TARURA waanze mara moja mchakato huo ili nia ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka huduma kwa wananchi na nia ya Mbunge wa jimbo lile kuhakikisha barabara hiyo inapitika muda wote ifikiwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maelekezo haya nimeshayatoa na nayarudia tena na nitakuwa wa kwanza kuyafuatilia maelekezo hayo ili yaweze kutekelezeka.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi. Tuna Barabara ya kutoka Makambako – Mlowa – Kifumbe ambako inakwenda kutokezea kule Ilunda. Barabara hii tumekuwa tukiiomba ipandishwe hadhi na kuwa ya TANROADS na kwa kuwa kule mbele inakotokezea barabara hii tayari ni ya TANROADS. Je, kwa nini sasa barabara hii inakoanzia isiwe ya TANROADS ikaunga na kule mbele ambako inatokea kwai le iliyo ndani ya TANRAODS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotoa maelekezo katika swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Busega, niielekeze vilevile Halmashauri ya Makambako na Mkoa wa Njombe, kuhakikisha wanaanza na wao mchakato rasmi sasa ili barabara hii na yenyewe watu wa TANROADS, wakishapitisha vile vigezo vyao na wakaona inakidhi, iweze kupandishwa hadhi na kuwa barabara ya Mkoa ili iweze kusaidia wananchi wa eneo hilo.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa
Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi barabara ya kutoka Bashineti – Lukumanda – Seche – Basodeshi – Ibadalu – Zinga, kutoka TARURA Kwenda TANROADS? Kwa sababu barabara hii upande wa Singida iko TANROADS na upande wa kutoka Babati kwenda Mbulu iko upande wa TANROADS.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hhayuma, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maelekezo yetu katika halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Hanang na mikoa yote, ni kuhakikisha zile barabara ambazo zinaunganisha kati ya halmashauri moja na nyingine, mkoa mmoja na mwingine ambazo zinaangukia katika upande wa TARURA ili ziunganishe mkoa, ni kuanza mchakato wa kuhakikisha sasa zinakuwa na vigezo vya kupandishwa hiyo hadhi.

Mheshimiwa Spika, maelekezo yangu kama katika swali la msingi na kwa Waheshimiwa Wabunge ni hayo na tutafuatilia maelekezo hayo kwa nia moja tu ya kutaka kuwasaidia wananchi katika maeneo yenu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara inayotoka Mangaka Wilaya ya Nanyumbu - Nachingwea Tarafa ya Kilinalondo - Liwale katika Kata ya Ilombe, tumeshaiombea iingie TANROADS, lakini mpaka leo tunapigwa danadana.

Je, ni lini barabara hii itaweza kupandishwa hadhi kuwa barabara ya TANROADS kwa sababu barabara hiyo imepita katika wilaya tatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ameshasema Mheshimiwa Mbunge walishaomba na mchakato upo katika ngazi husika na wenye jukumu la kufanya hivi ni watu wa TANROADS, naamini sisi Serikali ni moja tutalifuatilia ili kuharakisha huo mchakato uweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itamalizia kipande kilichobakia kwenye Kawawa Road kufikisha Marangu Mtoni kwa hadhi ya lami, tulipewa ahadi na Mheshimiwa Rais Kikwete awamu zile na iko kwenye Ilani ya CCM?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimwondoe hofu kwa sababu tumeshajenga awamu ya kwanza na kilichobaki nikumalizia katika eneo la pili na uzuri barabara hii iko katika mipango ya TARURA. Kwa hiyo, kwa sasa tunatafuta fedha tutakapopata mara moja naamini kabisa kwa sababu iko katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi barabara hii tutaitengeneza. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Mchakato wa kupeleka barabara za TARURA, kutoka TARURA kwenda TANROADS ni barabara ya kutoka Bukama – Mikulusanga – Mikomalilo tulishafanya mchakato na umekamilika. Sasa hoja ya kujiuliza ni kwamba TANROADS na TARURA wakitaka kupeleka barabara, vigezo vya kuwapelekea TANROADS wanasema sisi mpaka tupelekewe na Wizara. Sasa ni lini muunganiko huu wa TARURA na TANROADS utakuwepo ili barabara za TARURA ziondoke kwenye TARURA ziende TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna muunganiko mzuri kati ya TANROADS na TARURA na tunafanya kazi kwa kushirikiana pamoja. Kwa hiyo, kinachofanyika tu ni kwamba kwenye zile barabara ambazo ziko chini yetu, huwa tunazipeleka kwao na wao wanaangalia vile vigezo vinavyostahili. Kwa hiyo, siyo kwamba wana nia ya kuchelewesha hizo barabara, ni kwa sababu wanaangalia vile vigezo, vikashakamilika wanatafuta fedha na ndiyo wanatangaza hizo barabara na kuwa za mkoa.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuimarisha ushirikiano wetu ili haya maswali ya Waheshimiwa Wabunge tuweze kuyajibu kwa wakati na kwa urahisi zaidi. Ahsante sana.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Mwanga haina mapato ya kutosha, je, Serikali haioni umuhimu wa kuisaidia halmashauri hii ili kujenga uzio katika shule hii muhimu ya wasichana ambayo inapata adha kubwa sana kutokana kutokuwa na uzio, usumbufu, changamoto ya wanyama pamoja na miti kuharibika wakati ambapo ndiyo inaoteshwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Athuman Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeielekeza Halmashauri ya Mwanga na natambua kwamba Mheshimiwa Mbunge anajua, sawa kiwango chao bado sio kizuri sana. Sasa hivi sisi kama Serikali tumekuwa na mipango mingi ikiwemo kumalizia miundombinu ili wanafunzi wetu waweze kukaa katika maeneo salama ambayo yatawasaidia wao waweze kuwa na ufaulu mzuri katika masomo yao. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tulipokee kwa mipango ya baadaye ili tuweze kuja kulifanyia kazi baada ya kumaliza hili jukumu la kwanza ambalo tumejipangia kama Serikali.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana pia nashukuru kwa majibu ya Serikali, ninalo swali moja tu la nyongeza.

Wakati Waziri mwenye dhamana akilisukuma jengo hili, je, Serikali haioni umuhimu wa kuigeuza barabara hii kuwa ya mzunguko au ya pete ili kuepusha Mji wa Mpanda na msongamano wa magari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba hii barabara ni ya mzunguko kwa maana ya ring road ikiunganisha Halmashauri ya Nsimbo, Mpanda Manispaa pamoja na Halmashauri ya Tanganyika. Kwa hiyo, kwa umuhimu huo tunaitambua na ndiyo maana tunai-push zaidi ili iweze kupandishwa hadhi na iweze kuhudumia watu wote kwa wakati wote. Kwa hiyo, jambo hilo Mheshimiwa Mbunge tumelipokea. Ahsante sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, bado kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa wataalam wa kusoma vipimo hivi; je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea wataalam hao?

Swali langu la pili; je, Serikali haioni umuhimu wa kutusambazia vipimo vikubwa kwenye zahanati zetu pamoja na hospitali yetu ya Wilaya Nanguruwe ili tuweze kupima na magonjwa mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nimuondoe hofu, kadri Serikali itakavyoendelea kuajiri na kuongeza wataalam katika kada ya afya maana yake na mgawanyo huo utafika mpaka katika Jimbo lake la Mtwara Vijijini na maeneo mengine ya Taifa. Kwa hiyo, lipo katika mpango wa Serikali na tunaendelea kuajiri kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, umuhimu wa kuongeza vipimo vikubwa hilo lipo na ndiy kazi kubwa anayofanya Rais wa sasa Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Sasa hivi Ofisi ya Rais – TAMISEMI tukishirikiana na Wizara ya Afya, tunatarajia kupokea shilingi bilioni 169.7 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, vifaa tib ana vitendanishi kwa ajili ya maabara. Kwa hiyo tutaendeela kuvileta kwa kadri ambavyo vinapatikana. Ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa kuzingatia maelekezo yako ya maswali ya nyongeza yawe mafupi, nakushukuru sana swali langu kuwa la kwanza katika Bunge lako hili la kwanza ikiwa Simba imeshafanya yake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wakati Simba ikifanya yao tayari Yanga Sport Club ikiwa inaongoza ligi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa naomba kuuliza maswali yangu mafupi madogo mawili ya nyongeza.

Kwanza, kwa kuzingatia majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba tumekosa fedha kutokana na ripoti ya wataalam wetu au andiko la wataalam wetu kutokukidhi vigezo. Je, Mheshimiwa Waziri anatuhakikishia kwamba ataweza kutupatia wataalam ili tuandike upya andiko hili?

Swali la pili, wananchi wa Mji wa Ifakara wanateseka sana kutokana na soko hasa msimu huu wa mvua. Je, Mheshimiwa Waziri mwenyewe wa TAMISEMI atakuwa tayari katika Bunge hili kutafuta hata siku moja kutembelea soko hili na kuzungumza na wananchi wa Mji wa Ifakara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza aliuliza kwamba kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaweza kuwapatia wataalam. Tuko tayari kuwapatia wataalam ambao watashirikiana na Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuhakikisha wanakamilisha andiko lao, kwa hiyo hilo tuko tayari.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu kwenda Ifakara. Mheshimiwa Mbunge mimi niko tayari hususani wakati wa weekend tunaweza tukaongozana kwenda kushuhudia hiyo kero ya wananchi katika eneo lako. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuwa hali ilivyo Kilombero inafanana kabisa na ilivyo katika Jimbo la Sumve katika eneo la Bungulwa ambapo Halmashauri tumeshaleta andiko la kujenga soko la kisasa katika mnada wa Bungulwa.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuleta pesa ili mradi huu muhimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ufanyike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, anasema Halmashauri yake imeshaleta andiko katika ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa sasa anachohitaji tu ni kwamba fedha sasa itolewe kwa ajili ya soko hilo. Mimi tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kupitia hilo andiko na kuangalia namna bora ambayo tunaweza tukatafuta fedha kuhakikisha kwamba tunaleta katika Halmashauri yake.

Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo commitment ya Serikali, ahsante.(Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Changamoto iliyopo Mkoa wa Songwe inafanana kabisa na changamoto iliyopo Mkoa wa Dodoma katika Wilaya ya Chamwino na Wilaya ya Chemba.

Ni lini Serikali itajenga barabara ya kutokea Itiso, Zajirwa mpaka Kimaha kwa maana ya Kata ya Kimaha kuunganisha na Wilaya ya Chemba?

Pili, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutokea Kimaha – Soya – Msada mpaka Wilaya ya Kondoa? Ninakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa hizi barabara ikiwemo Itiso – Kimaha na nyingine Kimaha – Soya na maeneo yote ambayo ameyaainisha kwamba, anataka kujua tu commitment ya Serikali ni lini itajenga barabara hizo.

Mheshimiwa Spika, ninaamini katika bajeti ya fedha ya mwaka unaokuja ziko sehemu za hizi barabara alizoziainisha tumezitengea fedha na nyingine tutaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha barabara hizi zote zinapitika kwa wakati wote. Kwa hiyo, hilo ndio jibu la Serikali. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusiana na barabara hiyo, ombi langu ni kwamba, Serikali haioni haja katika kipindi ambacho tunasubiri matengenezo ya hiyo barabara tupate daraja la dharura ambalo limefanya kusiwe na mawasiliano kabisa ya wananchi hawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, ni kwamba, katika jibu letu tumeshaweka commitment ya kutenga fedha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Bahati nzuri mwaka wa fedha huu unaoanza, ambacho naweza nikamhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Momba ni kwamba, daraja hilo litajengwa katika mwaka wa fedha unaokuja, kabla ya msimu wa mvua kuanza. Kwa hiyo, hiyo ndio commitment ya Serikali. Ahsante. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Kilolo ambayo ilikuwa ni kilometa 33, lakini inapita Jimbo la Kalenga kutoka Ipogolo kwenda Kilolo, lini itajengwa kwa sababu imekuwa ni muda mrefu haijajengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anahitaji tu commitment ya Serikali ya ujenzi wa barabara kilometa 33 kutokea Iringa kwenda Kilolo ambayo inapitia Kalenga ambayo muda mrefu haijajengewa. Ni kwamba barabara hii tumekuwa tukiitengea fedha za matengenezo; na kwa sababu, Serikali inazingatia umuhimu wa hayo maeneo, na ninafahamu katika mwaka unaokuja kuna fedha imetengwa kwa ajili ya kuhakikisha yale maeneo korofi yote yanatengenezwa. Ahsante sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza kwamba, hii barabara ambayo inazunguka fence ya kwa Waziri Mkuu; fence ile imepakwa rangi nyeupe, lakini ina vumbi na kipindi cha mvua ina tope. Ni lini mtajenga kwa kiwango cha lami ili kuweza kutunza ile fence nzuri inayozunguka kwa Waziri Mkuu yenye rangi nyeupe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge anachozungumza kwamba, hii barabara ya nyuma inayozunguka fence ya Waziri Mkuu ni ya vumbi na tumekuwa tukiitengeneza kwa kiwango cha changarawe. Kwa hiyo, sasa anahitaji commitment ya Serikali ya kujenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, niwaagize TARURA Mkoa waende wakafanye tathmini ya ujenzi wa kiwango cha lami. Wakishakamilisha hiyo tathmini, basi watuletee Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutajua wapi ambapo tutatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. Ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Kituo hiki cha Afya Kiloleli kinahudumia zaidi ya Kata tatu kwa maana ya Kiloleli, Nyaruhande pamoja na Rubugu, lakini kina kituo cha afya kimoja: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa wodi ya wanawake, watoto pamoja na wanaume ili kukidhi mahitaji ya kituo cha afya hiki?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Waziri yuko tayari kutembelea Kituo cha Afya Kiloleli ili kuona mahitaji ya wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, alichoomba Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, pamoja na kwamba kituo hiki cha afya kinafanya kazi, ameomba tu tuongeze fedha kwa ajili ya wodi tatu ili kuhakikisha kwamba kiwe full kwenye matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu sasa hivi tumekuwa tukipata fedha karibu kila mwezi na zile fedha tumekuwa tukizielekeza kule, kwa hiyo, fedha nyingine tutatenga kwa ajili ya kuhakikisha tunapata wodi tatu katika kituo hiki ili kiwe full katika matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, la pili, ameomba kwenda kutembelea. Najua ni rafiki yangu na anaelewa kwamba nikitembelea pale atapata mambo mengi na mema. Nimhakikishie tu kwamba tutakwenda pamoja, tutatafuta moja ya weekend tukiwa katika kipindi cha Bunge hili refu tufike ili tuone hizo kero ambazo amezizungumza. Ahsante sana.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nini mpango wa Serikali kuhusu kuongeza vifaa tiba kwenye Kituo cha Afya Nyamwaga, Wilaya ya Tarime ili kipandishwe hadhi kiwe Hospitali ya Wilaya, ikizingatiwa Wilaya ya Tarime ina uhitaji mkubwa kutokana na jiografia ilivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ambacho Mheshimiwa Mbunge ameomba tu hapa ni kwamba, lini Serikali tutaongeza fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Nyamwaga ili kiweze kuendelea kuhudumia watu? Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imesikia ombi lake na tutafanya tathmini tuone ni vitu vingapi ambavyo vinahitajika kwa wakati huu ili viweze kutoa ile huduma stahiki. Ahsante sana.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aliyetangulia, Mheshimiwa Ummy, alipita Jimbo la Kalenga na akaahidi kunipa shilingi milioni 300 katika Kituo cha Magulirwa pamoja na cha Kibena: Je, ni lini hizo fedha zitakuja ili tuweze kumalizia vituo hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ambacho amekiainisha hapa Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, Mheshimiwa Waziri alienda akatoa commitment ya kupeleka fedha. Nasi tuna mpango wetu pale Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba ahadi zote za viongozi zipo katika mipango yetu. Kwa hiyo, litakapokuwa limekamilika hili, basi hizi fedha ambazo zimeahidiwa zitapelekwa katika hayo maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri aliahidi. Ahsante sana.
MHE. ANNA K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kuuliza Serikali, Kata ya Vunta katika Jimbo langu la Same Mashariki lina kituo cha afya ambacho kina jengo moja tu. Sasa Serikali naomba niulize kwamba, mnafanya mpango gani wa kurekebisha ili kiwe kituo cha afya hasa chenye majengo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli hayo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge anaeleza, mimi mwenyewe nimefika katika Tarafa ya Mamba Vunta kule, ni milimani kweli kweli; na nimeona changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiainisha. Nami nikiwa kule niliwaahidi wananchi kupitia maombi ya Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali kutokana na mahitaji na umbali wa eneo lile tutapeleka kituo cha afya katika Tarafa ile nyingine. Kwa hiyo, ile ahadi ambayo nimeizungumza ipo katika bajeti inayokuja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ondoa shaka katika hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Serikali ilijenga Kituo cha Afya Mtakanini na kumaliza mwaka 2020, lakini mpaka leo hakina vifaatiba hasa katika majengo ya upasuaji: Je, ni lini Serikali itanunua vifaatiba katika Kituo cha Afya cha Mtakanini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, vile vituo tulivyoanza navyo, kuna vituo vya mwanzo ambavyo tulitoa fedha na ambavyo vimeshakamilika, tumeshaanza kupeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba ili vile vituo vianze kukamilika; na tutapeleka hivyo katika awamu ya pili. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, lipo katika mpango na watapata hivi karibuni. Nimhakikishie kwamba hicho kituo cha afya na chenyewe kinaanza kufanya kazi kwa sababu nafahamu kwamba hii ni commitment ya Serikali na fedha ipo na tumekuwa tukifanya hivyo. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa changamoto iliyoko Busega inafanana kabisa na changamoto iliyoko Wilaya ya Kiteto: Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ujenzi wa vituo vya afya katika Tarafa zifuatazo: Tarafa ya Dosidosi, Tarafa ya Makame pamoja na Tarafa ya Kibaya? Ahsante sana kwa kunipa nafasi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, yeye ameomba kwamba, vituo vitatu katika Tarafa tatu ambazo ameziainisha hapo.

Mheshimiwa Spika, unatambua kabisa kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, moja ya kazi kubwa ambayo tumeifanya sasa hivi ni kuhakikisha Tarafa zote ambazo hazikuwa na vituo vya afya, tumepeleka fedha na ujenzi unaanza.

Kwa hiyo, miongoni mwa maeneo ambayo ameyataja, zipo baadhi ya Kata, sehemu ya hizi Tarafa alizozitaja, tumepeleka vituo vya afya na ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, nimwondoe shaka kwamba hivyo vituo vitakamilika na tutaleta na vifaa tiba ili kuhakikisha wale wananchi wanapata huduma ya afya kama ambavyo Serikali imekusudia. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Halmashauri ya Mbulu Vijijini haina vifaatiba. Je, Serikali ina mpango gani kuleta vifaatiba kwenye Halmashauri hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu kwa Wabunge wa awali kuhusu vifaatiba ni kwamba, sasa hivi moja ya jukumu kubwa ambalo tunalifanya sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ni kupeleka fedha kwenye hospitali na vituo vya afya ambavyo vimekamilika kwa ajili ya kununua vifaatiba; na hilo limekuwa likifanyika. Kwa hiyo, hata yeye katika Halmashauri yake najua kwamba akiwasiliana nao kule kuna fedha nyingine tumepeleka Machi, mwaka huu kuhakikikisha wananchi wale wanapata vifaatiba. Kwa hiyo, hilo ndiyo jibu la Serikali kwa ujumla katika maeneo yote ambayo yanahitaji vifaatiba. Ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi: Kituo cha afya cha Lupa Tingatinga ndiyo kituo cha afya kikubwa zaidi kwenye Tarafa ya Kipembawe, lakini kituo hiki hakina wodi yoyote kwenye Tarafa hii. Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kujenga wodi kwenye Kituo cha Afya cha Lupa Tingatinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa kwamba, kwenye Kituo cha Afya cha Lupa Tingatinga, na bahati nzuri hili eneo nalifahamu na changamoto zake nazijua, ninajua kazi ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akipambania pale ni wananchi wake kupata wodi. Nimhakikishie tu kwamba, tutaliweka katika mipango ya Serikali ili tuhakikishe wanapata wodi na hicho kituo kiendelee kutoa huduma. Ahsante sana.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kibiti kwenye Kata ya Bungu tuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kutupa shilingi milioni 250 kumalizia kituo cha afya. Ni lini Serikali italeta fedha hizo ili tuweze kumalizia kile kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba, tulishatoa fedha awamu ya kwanza shilingi milioni 250 katika vituo ambavyo asilimia kubwa ya Wabunge walipata, ikiwemo katika Jimbo la Kibiti ambalo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Nimhakikishie tu kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha tutatoa fedha nyingine shilingi milioni 250; na katika awamu ya kwanza tayari vituo vya afya 100 tumeshapeleka shilingi milioni 250 kumalizia ile shilingi milioni 500 na bado vituo vya afya kama 123 ambavyo tutamalizia kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha watapata hiyo fedha, shilingi milioni 250 ili waweze kumaliza vyote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Zahanati ya Mabwepande imechakaa na kusababisha wananchi na watumishi kuhudumiwa nje ya kituo chini ya mti: Je, ni lini Serikali itaenda kukarabati zahanati hiyo au kujenga kituo cha afya ili wananchi wa Mabwepande waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya mpango ambao sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tulikaa na Halmashauri zenye mapato makubwa ikiwemo Halmashauri ya Kinondoni, Jiji la Dar es Salaam pamoja na Ilala na Temeke. Tuliwaambia kwamba, kwa sababu maeneo yenu yana fedha kubwa, basi mhakikishe mnatenga fedha kwa ajili ya ukarabati. Kwa hiyo, kupitia swali hili ambalo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa, nimwagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kuhakikisha kwamba anapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya cha Mabwepande. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaishukuru Serikali kwa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imepita miaka minne tangu Serikali Kuu ilipobaini kwamba andiko la mradi wa Stendi ya Madaba halikukidhi vigezo. Ni hatua gani za haraka ambazo Serikali Kuu ilizichukua wakati huo ili kuhakikisha kwamba stendi hii inajengwa na inawanufaisha wananchi wa Madaba ili kuongeza mapato kwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kama upembuzi yakinifu unakusudiwa kufanywa kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023, ni lini sasa kwa uhakika stendi ya Madaba itajengwa? (Makofi)
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge aliuliza tu kwamba andiko la awali ambalo limechukua takribani miaka minne na alichotaka kufahamu ni hatua gani ambazo Serikali ilizichukua baada ya hili andiko kukataliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ambacho tulikifanya kwa kutumia wataalam wetu tulilirudisha lile andiko katika Halmashauri ya Madaba na baada ya kufanya hivyo waliainishiwa maeneo ya kufanya marekebisho. Kwa hiyo, jukumu la kuandika andiko ni la Halmashauri ya Madaba na ndio maana hata sasa hivi tumewarejea tena ili waandike upya haraka iwezekanavyo ili sisi tutafute fedha hii stendi iweze kukamilika. Kwa hiyo, mara watakapokuwa wamekamilisha kwa wakati basi na sisi tutatafuta fedha ili tuweze kujenga stendi hiyo kwa manufaa ya wananchi wa Madaba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu upembuzi yakinifu mara utakapokamilika ameuliza lini, ni kwamba watakavyomaliza andiko na mimi naamini tutajiridhisha kwamba kama andiko linakidhi vigezo likishakamilishwa mara baada tutakapopata fedha tutaanza mara moja kuhakikisha mradi ule unaanza. Ahsante. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiuliza Serikali ni lini itaisaidia Wilaya ya Ngara kuweza kujenga stendi mpya na ya kisasa? Ahsante.
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachotaka kujua tu ni lini tutawasaidia kujenga stendi mpya na naamini kwamba moja ya miradi ya kimkakati katika Halmashauri nyingi ni pamoja na kuwa na stendi mpya. Kwa hiyo, kama Halmashauri yake itakuwa imewasilisha andiko maana yake kazi kubwa ambayo tunaifanya sasa ni kutafuta fedha, mara tutakapopata fedha maana yake ujenzi huo na wenyewe utaanza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kufahamu hivi karibuni Makamu wa Rais alivyokuwa pale Bukoba Mjini aliwasilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba Bukoba Mjini sasa tutajengewa stendi kuu ya mabasi. Kwa hiyo, ninataka kufahamu ni lini hiyo ahadi itatekelezwa na Bukoba tutapata stendi kuu ya mabasi ili kufungua Mkoa wetuwa Kagera na nchi za jirani? (Makofi)
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa ambacho Wabunge wote wanapaswa kufahamu wakiwemo Mheshimiwa Neema Lugangira ni kwamba ahadi zote za Viongozi zipo katika hatua ya utekelezaji. Kikubwa tumeshaziainisha, tumeshazipa vipaumbele, jukumu letu sasa hivi ni kutafuta fedha kuhakikisha hizo ahadi zinatekelezeka.

Kwa hiyo, pesa itakapokuwa imepatikana hii ahadi ya Makamu wa Rais na yenyewe itatekelezeka kama ambavyo ameahidi. Kikubwa ni kwamba ahadi zote za viongozi zitatekelezwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale ilikuwa na mradi wa kimkakati wa stendi lakini fedha zililetwa zikarejeshwa baada kukwama kwenye manunuzi.

Je, fedha zile zitarejeshwa lini ili mradi ule uendelee?
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka Mbunge wa Jimbo la Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hatujabadilisha sheria na ninyi mnakumbuka mwaka jana, fedha zote ambazo zilikuwa zinavuka mwaka zilikuwa zinarejeshwa Hazina, maana yake mnatakiwa kuanza kuomba upya.

Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nimesikia maombi hapa ambayo ameyainisha na tutakwenda pale Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kuona namna bora ya kusaidia kwa zile fedha ambazo awali zilikuwa zimeshapelekwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ahadi hii sasa ina miaka Sita na inaenda mwaka wa Saba, ahadi zote zinazotolewa na Viongozi wetu wa Kitaifa wanatoa kwa sababu ya hali ilivyo ngumu kwenye Majimbo yetu yaliyo mengi. Ninavyojua kwa Viongozi wa Kitaifa ni sehemu ya maelekezo ya Serikali, ahadi hii hata hayati marehemu John Kwandikwa aliifuatilia sana lakini utekelezaji wake mpaka leo haujafanyika.

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ahadi hii na kwa nini Serikali isitafute fedha za ziada kuhakikisha kituo cha afya hiki kinajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichoeleza ni kwamba hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nieleze tu Bunge lako tukufu kwamba moja ya mpango mkubwa wa Serikali ambao ulikuwepo awali ni kuhakikisha kwamba zile Tarafa zote nchini ambazo hazikuwa na vituo vya afya tulikuwa tunapeleka vituo vya afya, ndiyo maana katika mwaka wa fedha huu unaokwenda kuisha Serikali imepeleka fedha za ujenzi wa vituo vya afya 233 ikiwemo katika Jimbo la Ushetu ambapo tumepeleka fedha awamu ya kwanza, fedha za tozo Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho wao wamepeleka katika eneo lingine.

Meshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika eneo hili ambalo liko katika ahadi baada ya kumaliza huu mkakati ambao tumeuainisha kumaliza Tarafa zote nchini basi na eneo lako tutaliweka katika kipaumbele kuhakikisha kwamba hii ahadi haichukui muda mrefu ili kuwasaidia wananchi wa Kata ya Ulowa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL E. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Tabora Mjini wananchi kwa nguvu zao wamejitahidi sana kujenga vituo vya afya ambavyo vingi viko kwenye maboma lakini wengine wamekusanya mawe na kujitolea nguvu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kusaidia kumalizika kwa hivi vituo vya afya ambavyo wananchi wamejitoa nguvu zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatambua maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Tabora Mjini wananchi wameshiriki kwa nguvu zao kuchangia ujenzi wa vituo vya afya na maboma yako mengi karibu kila Mbunge hapa anaweza kuyaainisha. Kwa hiyo, wakati wa sasa ukiwa ni mpango wa kuhakikisha kwamba Halmashauri zote zinapata hospitali za Wilaya, ambapo tulikuwa na Halmashauri 28 hazikuwa na hospitali za Halmashauri ambapo mwaka huu wa fedha Serikali imepeleka fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa pili ilikuwa ni kumaliza Tarafa zote nchini, tulikuwa na Tarafa 570, karibu Tarafa 233 zilikuwa hazina ambapo Serikali tumepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa maeneo hayo. Kwa hiyo, mpango wa tatu utakuwa sasa ni kwenda kumalizia katika yale maeneo ambayo wananchi wameweka nguvu zao. Kwa hiyo, haya masuala ni yanakwenda kwa mipango na kwa muda kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalitambua hilo na tutatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapeleka fedha ku-support wananchi nguvu zao walizozitoa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza kwamba Tarafa ya Matamba kuna kituo cha afya cha Matamba kina takribani miaka 30, hakina jengo la Mama na Mtoto na wala hakina jengo la mochwari. Huduma ya mochwari tunaenda kupata kwenye Wilaya ya jirani inaitwa Chimala. Sasa tunaomba ni lini Serikali itatupatia fedha tuweze kujenga jingo la mama na mtoto lakini eneo la kuhifadhia wenzetu kwa maana ya mochwari, kwa sababu ni umbali mrefu tunaenda kuhudumiwa kutoka kwa Jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameainisha kwamba Tarafa ya Matamba ina kituo cha afya lakini hakina huduma ya mochwari pamoja na mama na mtoto, kwa hiyo alichoomba tu ni kwamba Serikali lini tutapeleka fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu kwamba tumelipokea hili ombi na tutaliweka katika mipango yetu ya baadaye ili tuhakikishe kwamba hizi huduma mbili ambazo ameziainisha Mheshimiwa Mbunge zinapatikana. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango ambayo Serikali imeainisha hapa ya ujenzi ya vituo vya afya lakini hakuna mpango wa wazi wa kuonesha namna gani sasa tunajenga vituo vya afya lakini tunaajiri watumishi wa sekta ya afya tukizingatia kwamba tuna upungufu wa takribani asilimia 50 ya watumishi wa afya kwenye sekta zetu za afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inajenga na moja ya mkakati tulionao ni kuajiri na hata katika mwaka huu wa fedha nafikiri kama wiki ijayo Mheshimiwa Waziri wa Nchi atatangaza nafasi za ajira ambazo tutakwenda kuajiri katika maeneo haya ya afya pamoja na elimu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali imejipanga kuajiri na Waziri wa Nchi atatangaza hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni Mashariki tuna Kituo cha Afya cha Kintiku ambacho tayari Serikali ilishajenga jengo la maabara, jengo la x-ray, wodi ya mama na mtoto na mochwari, lakini hatuna jengo la OPD. Ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba wanatupatia jengo la OPD?
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Chaya Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameainisha kwamba katika Kituo cha Afya cha Kintiku kinachokosa tu ni jengo la OPD na nimhakikishie tu kwamba maeneo yote ambayo yana mapungufu na sisi tulipeleka fedha tutamaliza majengo, kwa sababu maeneo mengine yanakosa mochwari, maeneo mengine yanakosa maabara, mengine yanakosa wodi za akina mama, kwa hiyo lipo katika mpango ikiwemo katika eneo hili la Kintiku ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliainisha. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika Kituo cha Afya cha Ukuge ulijengwa mtambo mkubwa uliokusudiwa kutengeneza oxygen kwa ajili ya Kanda yote ya Magharibi, lakini bahati mbaya mtambo ulipowashwa, ukawa unatengeneza nitrogen.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuchukua mpango huo unaotengeza nitrogen ili watuletee unaotengeneza oxygen?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichokielezea kuhusu huo mtambo ili Serikali ichukue najua suala hili linahusu zaidi Wizara ya Afya. Kwa hiyo, kwa niaba ya Wizara ya Afya, tuseme tumelipokea hilo na Serikali italifanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu ambayo yametolewa na Serikali na mpango mzuri wa Serikali katika kupeleka watumishi katika maeneo mbalimbali hasa Wilaya ya Kakonko, bado watumishi hawa wamekuwa wakihama kutokana na upungufu wa miundombinu hasa nyumba za watumishi katika maeneo hayo.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi hawa wa kada ya afya wanabaki katika maeneo hayo hasa kwa kujenga nyumba za watumishi hao?
(Makofi)

(b) Kutokana na changamoto hiyo: Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kufuatana nami kwenda Wilaya ya Kakonko ili hiki ambacho nakieleza kama changamoto aweze kuona na hatimaye aweze kutafuta njia sahihi za kuweza kumaliza changamoto hiyo? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge ameainisha kwamba tunapeleka watumishi katika maeneo kama Buyungu, Halmashauri ya Kakonko, lakini asilimia kubwa ya hawa watumishi wamekuwa wakihama.

Kwa hiyo, alichokuwa anaainisha Mheshimiwa Mbunge ni kutaka Serikali moja, tujenge nyumba za watumishi ili watu wabaki; nafikiri kuongeza zile incentives kwa ajili ya watumishi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mkakati wa Serikali sasa hivi ni kuhakikisha watumishi wote wapya tunaowaajiri hawaruhusiwi kuhama katika maeneo yao, walau siyo chini ya miaka mitatu. Hiyo ni moja ya sehemu ya mikataba ambayo tumeiweka. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha mazingira kwa kutenga fedha ili kujenga nyumba za watumishi na kuongeza mahitaji mengine ambayo wanayahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili la kwenda Kakonko, niko tayari, hiyo nguvu ninayo na uwezo ninao na tuko tayari kwa ajili ya kuwatumikia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi nzuri ya kutuletea fedha za kujenga vituo vya afya na hospitali za Halmashauri: Je, katika Kituo cha Afya cha Lyamkena na Hospitali iliyoko Mlowa katika Mji wa Makambako, inafanya kazi na inahudumia wagonjwa asubuhi mpaka jioni; ni lini Serikali italeta watumishi ili kiweze kuhudumia masaa 24? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ameomba tu ni watumishi na katika jibu la msingi nililolijibu awali ni kwamba Serikali inatarajia kuajiri na tangazo la ajira litatolewa na Waziri wa Nchi na nafikiri inawezekana ikawa kabla ya wiki ijayo. Mara atakapolitoa, ajira zitakavyoombwa, sehemu ya watumishi tutakaowaajiri, baadhi tutawapeleka katika eneo hilo ili kuweza kusaidia. Ahsante.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itapeleka mtaalam wa meno katika Hospitali ya Somanda Wilaya ya Bariadi kwa kuwa aliyekuwepo amestaafu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachohitaji ni mtaalam wa meno na ninaamini tunapokuwa tunaajiri, tunazingatia maeneo yenye upungufu. Kwa hiyo, ninaamini pamoja na eneo analolitaja, litakuwa katika hizo sehemu za ajira ambazo zitatangazwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na pongezi kubwa kwa Serikari kwa ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea sasa, vipo vituo vya afya ambavyo vimejengwa kipindi cha nyumba lakini mpaka sasa havina watumishi wa kada ya afya wa kutosha: -

Je, ni lini sasa Serikali itapeleka watumishi hao ili wananchi wapate huduma inayostahili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilijibu swali hili kama ulivyoelekeza. Tunatambua kwamba kuna changamoto ya uhaba wa watumishi katika kada ya Afya.

Moja ya mikakati ni pamoja na Serikali kuajiri. Katika mwaka wa huu wa fedha 2021/2022 Serikali inatarajia kuajiri. Waziri wa Nchi atakapokuwa ametangaza ajira hizi, maana yake tutaainisha na kupeleka maeneo yale ambayo yana uhaba mkubwa wa watumishi kuhakikisha kwamba huduma za afya huduma za Afya zinaanza. Kwa hiyo, hilo ndilo jibu la msingi na niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tutazingatia maeneo yote ambayo hayana watumishi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri kwa kuwa muwazi na kuwa mtu mzuri. Alitembelea Vunjo baada ya kuahidi hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni hivi, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuinua hadhi ya OPD Himo kuwa Kituo cha Afya kwa kutekeleza majengo matatu yanayostahili pale, pamoja na watumishi wanaohitajika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho anahitaji tu ni kwamba kwenye eneo hilo la Himo tupandishe hadhi, tuongeze watumishi, tujenge jengo la OPD na anachotaka kufahamu tu, ni lini sasa ile huduma ambayo ameikusudia Mheshimiwa Mbunge itatekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali imelipokea na tutalifanyia kazi kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita moja ya ajenda yake kubwa kabisa ni kuhakikisha tunaboresha huduma za afya nchini. Ahsante sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nimesikiliza hapa maswali kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI takribani Wabunge wengi ambao wamekuwa wakiuliza maswali ya nyongeza wamekuwa na hofu ya uhaba wa watumishi na hasa kwenye sekta ya elimu na sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama hapa kwa heshima kubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba niwaarifu Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais na Serikali yake wametambua tatizo hili la uhaba wa watumishi na hasa kwenye miradi ya sekta ya afya na sekta ya elimu. Hivyo basi, Mheshimiwa Rais ametoa kibali. Ahadi ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha ilikuwa tuajiri watumishi 44,000; tayari Serikali ilishaajiri watumishi wapya na wa ajira mbadala 12,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais ameridhia na wiki ijayo nitatoa tangazo rasmi la ajira 32,000 na utaratibu wa ajira hizo na mgawanyo wake katika sekta ambazo zinaongoza kwa uhaba wa watumishi, maelezo yote nitayatoa wiki ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, Serikali ya Awamu ya Sita inajali tatizo la uhaba wa watumishi nchini. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, barabara hizi nyingi za Nyanda za Juu Kusini zimekuwa na changamoto ya mvua ya muda mrefu, na barabara nyingi hazijafikiwa kiwango cha changarawe. Ni upi mkakati wa Serikali? Na ukifuatilia maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa anazungumza na watu wa TARURA kwamba maeneo ya Kusini ambayo ni ya uzalishaji barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha changarawe kwa wingi.

Je, ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa kwa kiwango cha changarawe, hususan kwenye Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Njombe hususani Wilaya ya Makete?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kwamba moja tunataka kuwahakikishia tunapandisha hadhi barabara za udongo kwenye changarawe na pili, zile za changarawe kuzipeleka katika kiwango cha lami; na tunafungua barabara nyingi mpya. Kwa hiyo sehemu ya miradi mikubwa ambayo tumeielekeza katika Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Agri-connect ni ujenzi wa lami ili maeneo hayo yaweze kupitika muda wote na shughuli za kiuchumi ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali ipo kazini na tutaendelea kuongeza fedha ili kuhakikisha hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja zinafanyiwa kazi.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali; nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na watoto wengi wa kike kukosa masomo siku tano mpaka saba kwa hiyo kunasababisha kwa mwaka kukosa masomo kwa siku 50. Nini commitment ya Serikali katika madarasa haya mengi mapya ambayo hayana mfumo huu wa vyumba maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ameianisha hiyo changamoto, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi Ofisi ya Rais – TAMISEMI tunazielekeza halmashauri zote sasa kujenga vyumba ambavyo vinaweza vikawasaidia watoto wa kike kujistiri wakati wa hedhi. Lengo ni kuhakikisha kwamba Watoto hawa hawakosi masomo wanapokuwa katika kipindi chao ili kuweza kuwasaidia kama ambavyo katika michoro yetu mipya ambayo tumeianisha.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake kama anavyosema mwenyewe Milioni 100 kwa upungufu ambao upo ambao ni zaidi ya asilimia 62 itatuchukua muda mrefu sana kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi, kwa sababu walimu wetu wanafanya kazi nzuri na tuliwajengea madarasa mazuri huko vijijini mbapo tunatakiwa wakae karibu.

Je, ni mkakati upi wa haraka wa kutafuta fedha za kutosha kuweza kumaliza tatizo hili ambalo limekuwa kubwa na linapunguza ari ya walimu kufanya kazi? (Makofi)

Swali la pili ni pamoja na kwamba juhudi zinaendelea za kupata Walimu lakini walimu nao ni wachache sana ambao hawa-fit idadi ya wanafunzi ambao tunao, kwa sababu Serikali imetangaza ajira za Walimu na kwa sababu Halmashauri ya Ikungi ina upungufu mkubwa.

Ni nini Serikali itafanya kuhakikisha kwamba inapunguza kabisa tatizo la idadi ya walimu ambao wapo katika Halmashauri yetu ya Ikungi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua kwamba kuna changamoto na fedha ambazo zimetolewa katika Halmashauri ya Ikungi ni ndogo. Mkakati wa Serikali kwa mfano, kama sasa hivi moja ya mikakati ya Serikali ni kuhakiksha kila sekondari mpya tunayoijenga ama shule mpya tunajenga na nyumba za walimu na ninyi mmekuwa mfano three in one. Yote hii ni katika kukabiliana na changamoto ya nyumba za walimu.

Mheshimiwa Spika, tuna mikakati mingi ikiwemo kutafuta fedha na jukumu letu kubwa la sasa ni kuhakikisha tunamaliza kwanza ujenzi wa madarasa na shule latika maeneo yote yenye uhitaji, mara baada ya kumaliza hiyo hatua yetu ya pili ni kuhakikisha tunajenga nyumba kwa Walimu hususan katika yale mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu upungufu wa Walimu katika Halmashauri ya Ikungi nimhakikishie tu Mhehsimiwa Mbunge katika hatua ambazo tumeshatangaza ajira, Ofisi ya Rais, TAMISEMI sasa hivi tutaajiri Walimu 9,800 na katika hizo ajira 9,800 tutakazoajiri sehemu ya Walimu tutapeleka katika Halmashauri yako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuondoe shaka na hilo.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba za Walimu kidogo kidogo na kwa kuwa, zipo nyumba za Walimu ambazo zimejengwa kabla ya uhuru na mara tu hata baada ya uhuru na sasa hivi ni chakavu sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati angalau zile zilizopo ili kuboresha makazi ya Walimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Zodo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya maelekezo ambayo ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeyatoa katika Halmashauri zote nchini ni kuhakikisha wanatenga fedha za ndani katika mapato yao ya ndani ili kufanya ukarabati wa nyumba zote ambazo zipo za Walimu katika Halmashauri husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata hichi anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ninaendelea kuagiza Halmashauri kutekeleza yale maelekezo ambayo Ofisi ya Rais TAMISEMI iliyatoa ya kutenga fedha ili kukarabati hizo nyumba za Walimu katika maeneo yote ambayo zimechakaa.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya nyumba za walimu ambayo iko kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ni sawa na changamoto iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ambapo angalau tumeanza hatua ya kwanza tumejenga maboma.

Je, ni nini mkakati wa Serikali kukamilisha maboma haya ambayo ni nyumba za walimu kwa ajili ya kuwapatia malazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya mkakati wa Serikali ni kuendelea kutoa fedha na tumekuwa tukifanya katika maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakijenga maboma, ikiwemo nyumba za walimu vituo vya afya pamoja na madarasa, kwa hiyo tumekuwa tukifanya hivyo. Hata hili analolisema ni kwamba Serikali tutaendelea kutekeleza na ndiyo maana moja ya kazi yetu kubwa sasa hivi ni kutafuta fedha kuhakikisha maboma mengi tunayafikia kwa kadri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, kuna upungufu mkubwa wa nyumba za Walimu katika Mkoa wa Simiyu kwenye shule za sekondari.

Je, ni lini Serikali itajenga nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi ni kwamba, moja ya mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha ili tuendelee kujenga nyumba, hususan katika yale mazingira magumu huo ndiyo mkakati wetu.

Mheshimiwa Spika, hata katika bajeti ambayo tutakwenda kuipitisha kuna fedha tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika maeneo yale ambayo ni magumu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kupeleka fedha kwa kadri ya mahitaji na tutagawanya kwa nchi nzima ili kuhakikisha tunaleta usawa kwenye hilo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo Ikungi na Wilaya ya Mbogwe lipo. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea walimu wa Wilaya ya Mbogwe nyumba ili na wao wapate pa kuishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Maganga Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, mkakati wa Serikali sasa hivi ni kutafuta fedha, kadri tunavyopata fedha maana yake tunajenga. Nimeainisha hapa kwamba siku hizi tunajenga Sekondari na kila Sekondari tunaweka nyumba za walimu three in one, yote hiyo ni mkakati wa kuondoa hii adha ya nyumba za walimu. Kwa hiyo. hata hapo Mbogwe nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, Serikali tutaendelea kuleta fedha kwa kadri zitakapopatikana, kwa hiyo aondoe shaka kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Lengo la barabara hii ni kufungua mawasiliano kati ya Burundi na Tanzania. Kufuatia hili, katika kikao cha ushauri cha Bodi ya Barabara iliamuliwa barabara hii ihamishwe, kipande hiki cha Gwarama – Muhange, kitoke TARURA kwenda TANROADS . Nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili?

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa kuwa barabara hii ni muhimu, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami, aweze kuiona hii barabara? Nina hakika akishaiona atakuwa tayari kuchukua hatua za muhimu kujenga barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Kigoma imeipendekeza kupandishwa hadhi; na kwa kuwa Serikali tunafanya kazi kwa pamoja, basi jambo hili tumelipokea na ninaamini wenzetu wa TANROADS na wenyewe wanalo. Kwa hiyo, endapo hii barabara itakuwa inakidhi vigezo vyote, basi Serikali italifanyia kazi na itekeleze kama ambavyo Bodi ya Barabara ya Mkoa imependekeza.

Mheshimiwa Spika, suala la mimi kuongozana naye, nipo tayari mara baada ya Bunge lako Tukufu tutakapomaliza. Ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Barabara ya kutoka Irula katika Jimbo la Kilolo kwenda Image mpaka Kata ya Ibumu ni barabara mbaya sana, haijawahi kuchimbwa hata siku moja: Ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango hata cha changarawe tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Tendega ameainisha hii barabara ya kutoka Irula mpaka Ibumu kwamba ni bararaba ambayo haijajengwa, basi tutakwenda kufuatilia ili tuone kama imeanishwa kwenye bajeti ili tuweze kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Napenda kujua ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara inayounganisha Wilaya ya Shinyanga Mjini na Shinganya Vijijini kutoka Old Shinyanga kwenda Solo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Dkt. Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba kila kitu kipo katika mipango na Serikali tumeainisha maeneo yote yenye vipaumbele. Kwa hiyo, kadri tutakavyoyafikia, maana yake yote yataainishwa. Umuhimu wa hii barabara unafahamika na ndiyo maana mara zote tumekuwa tukifanyia matengenezo. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii na yenyewe itafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya kutoka Chala kwenda Mpalamao imekuwa ni ahadi ya viongozi wengi na iliwekwa kwenye ilani lakini mpaka sasa hatuoni kinachoondelea. Ni lini mtatekeleza ahadi hiyo ya barabara ya Chala - Mpalamao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya kutoka Chala mpaka Mpalamao ni kweli tumekuwa tukiizungumza mara kwa mara, na nimemwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ipo katika vipaumbele ambavyo tumeviweka. Kwa hiyo, tunatafuta fedha ili ianze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri kuwa Kata ya Kidatu kuelekea Kata Msola Stesheni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, barabara haipitiki kwa sasa: -

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kutengeneza barabara ile angalau kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoanisha Mheshimiwa Mbunge ipo katika mipango ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inajengwa. Kwa hiyo, tusubiri tu muda utakapofika na barabara hiyo itafanyiwa kazi.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Barabara ya Tabora - Mwambali imeshafanyiwa usanifu tangu mwaka 2020, lakini mpaka leo haijaanza kujengwa. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu baadhi ya maswali, barabara zote ambazo tayari zimefanyiwa usanifu na ambazo zipo katika mpango wa Serikali ni kwamba sasa hivi kitu kimoja ambacho tunakitafuta ni fedha ili tuanze kuzitekeleza. Kwa hiyo, ninaamini kwamba mara fedha itakapopatikana, basi na hii barabara itaanza kujengwa. Ahsante sana.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Serikali barabara yetu Bigwa na barabara yetu Ngerengere, Matuli, Matulazi:-

Je, lini Serikali itatuangalia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Ngerengere kwenda Matulazi ni moja ya barabara muhimu na ya kipaumbele. Moja ya kazi kubwa ambayo tunaifanya sasa hivi, ni kufanya usanifu ili sasa tuiweke katika mipango yetu ya kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo. Ahsante sana.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Barabara ya Kisesa, Bujola kwenye Makumbusho ya Machief wa Kisukuma imebaki kilometa 1.3.

Je, ni lini itakamilishwa na Serikali kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Boniventura Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya ambayo ameianisha ni kwamba mpaka sasa Serikali imeshafanya kazi sehemu kubwa. Kwa hiyo, sehemu ndogo ya kilomita 1.3 iliyobakia na yenyewe ipo katika mpango ili iweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nilitaka kujua kuna barabara yetu ya Chemba - Soya ambayo kwa muda mrefu imekuwa na shida kubwa na mara kadhaa viongozi walipokuja waliahidi kuijenga walau kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, naomba kujua commitment ya Serikali katika hili.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ahadi zote ambazo viongozi wamezianisha zipo katika mpango. Kwa hiyo, hata hii ambayo barabara ameiainisha Mheshimiwa Mbunge ya kutoka Chemba mpaka Soya ni miongoni mwa barabara zetu, zipo katika mipango yetu. Ahsante sana.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Lakini Wilaya ya Mbozi ina shule za sekondari 44, Serikali imepelekea vifaa vya maabara kwenye shule za sekondari 12 tu. Sasa je, nini commitment ya Serikali katika hizi bilioni tano ambazo zimetengwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kusaidia shule ambazo katika Wilaya ya Mbozi hususan Jimbo la Mbozi ambazo hazijapata vifaa vya maabara? Naomba kuuliza.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mbozi ni kwamba tutapeleka fedha kwa ajili ya shule za sekondari ambazo ameziainisha katika jimbo lake, zile zote ambazo zitakuwa zimemaliza maabara katika mwaka wa fedha unaokuja na zile nyingine ambazo tumeshanunua vifaa tunasubiri tu zile shule ambazo zitaleta taarifa tupeleke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natambua kazi njema anayoifanya katika Jimbo la Mbozi na ninajua ameji-commit kwa kiwango gani kwa wananchi wake. Kwa hiyo, nimuondoe shaka kwenye hilo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Mbulu Vijijini ziko sekondari 16 lakini sekondari 11 hatuna vifaa vya maabara ya sayansi.

Je, Mheshimiwa Waziri lini utapeleka vifaa hivyo ili wanafunzi waweze kujifunza vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba kama nilivyojibu katika swali la awali na swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, ni kwamba katika maeneo yote ambayo wameshamaliza ujenzi wa maabara sisi tutapeleka vifaa ikiwemo katika Jimbolake la Mbulu Vijijini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aondoe wasiwasi katika hilo.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo kwenye shule ya msingi Ng’ambo Tabora ni sawa na changamoto iliyopo kwenye shule ya msingi Igurubi ambayo ni Makao Makuu ya Tarafa ya Igurubi Jimbo la Igunga. Tunayo shule ya msingi ambayo kwa sasa ina wanafunzi wengi mpaka imezidiwa, kwa hiyo tunaomba pia Serikali katika utatuzi wa changamoto hizi iweze kuangalia pia shule ya msingi Igurubi ili iweze kulipatia ufumbuzi wa tatizo hili na changamoto hii ili wanafunzi wetu wasome kwa uhuru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus Ngassa Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nae ameeleza tu kwamba katika Jimbo lake la Igunga Tarafa ya Igurubi kuna Shule ya Msingi Igurubi ambayo na yenyewe ina wanafunzi wengi. Nimhakikishie tu kwamba moja ya mpango wa Serikali sasa hivi ni kutapisha shule zote zenye wanafunzi zaidi ya 2000 na ndio maana tuko katika mkakati wa kutafuta fedha na tumezitambua shule zote ambazo zina changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo mpango huu utakapokamilika maana yake tutawafikia na wao. ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ningependa niongeze hapo swali la nyongeza, kwa kuwa Serikali imekiri hapa kwamba shule nyingi zimezidiwa na wanafunzi kwa nini Serikali sasa isitangaze kwamba hapa Tanzania tuna upungufu wa shule badala ya kuendelea kutangaza kwamba tuna upungufu wa madarasa peke yake?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Kakunda Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mbunge tu ni kwamba anataka kufahamu tutangaze kwamba tuna uhaba wa shule na siyo madarasa. Nimhakikishie tu kwamba Serikali inatambua changamoto zote, katika baadhi ya maeneo tuna changamoto ya madarasa na kuna baadhi ya maeneo tuna changamoto ya shule, ndiyo maana katika maeneo ambayo yana changamoto ya shule Serikali tunapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, kwa hiyo hatuwezi kutangaza kama janga kwa sababu Serikali ipo kazini na inafanya kazi kutatua hizi changamoto ambazo Mheshimiwa Mbunge ameainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.

Ili kuweka taarifa sahihi kwa wananchi wangu wa Bukoba Mjini. Je, Serikali kupitia TARURA ina maana kuwa barabara hizi zimehamishiwa TARURA badala ya TANROADS nilitaka kujua hilo maana hizi barabara ni za TANROADS siyo za TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kumekuwepo na malalamiko mengi ya fidia kwenye miradi ya aina hii. Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wananchi wangu wa Bukoba Mjini endapo wakipitiwa katika hii barabara watapata fidia kwa uharaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba anasema barabara hii huenda imehamishwa kutoka TANROADS kwenda TARURA, nimwambie tu kwamba hapana ni kwa sababu Serikali hii ni moja na inafanya kazi kwa pamoja nasi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA na TANROADS tunafanya kazi kwa umoja. Kwa hiyo, kikubwa katika swali lake la msingi alilouliza hapa juu ya kuhakikisha usanifu unakamilika na ujenzi wa barabara unaanza vitafanyika kama ambavyo ameainisha hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu fidia anataka tu mara baada ya usanifu ni wananchi wale walipwe fidia kwa wakati, Serikali italipa fidia kulingana na tathmini ambayo itafanywa katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naishukuru Serikali; mwezi Julai mwaka jana tumepokea shilingi milioni 192 kwa ajili ya uendelezaji wa shule hiyo kuwa kidato cha tano na sita. Ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya kukamilisha bwalo na kujenga makataba ya high school?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa fedha hizi zilikuja zikaanzisha majengo mapya na kuacha yaliyokuwepo. Ni lini Serikali itakamilisha nyumba nne za watumishi zilizopo pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tulishaanza hatua ya awali na tumebakisha tu ujenzi wa bwalo pamoja na maktaba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tutakapopata fedha za mradi ambayo tunayo sasa hivi, tutazitenga kwenye bajeti na kupeleka katika shule hiyo.

Mheshimiwa Spika, na kuhusu majengo mapya ni kwamba kwa sababu sasa hivi tuna miradi mikubwa miwili ya SEQUIP pamoja na BOOST ambapo sehemu ya fedha hizo ni pamoja na kumalizia majengo, kujenga majengo mapya, pamoja na nyumba za walimu. Tutafanya hivi mara tutakapopokea fedha hizo, ahsante.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada ya kujenga madarasa katika Jimbo la Buchosa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Jimbo la Buchosa lina kata 21 na watu takribani 400,000 lakini ina high school moja tu. Nilishapeleka maombi Wizarani kwa ajili ya kuomba Shule ya Sekondari Kakobe, Bupandwa na Nyakahilo ziweze kupandishwa hadhi kuwa high school.

Je, Mheshimiwa Waziri, anaweza kutamka wananchi wa buchosa wamsikie ni lini shule hizi zitapandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mpango tulionao Ofisi ya Rais- TAMISEMI, ni kuziongezea, yaani kwa maana kuzipanua, shule mia moja nchini ili kuzipa hadhi za kidato cha tano na sita kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi iliyoongezeka. Miongoni mwa shule ambayo ipo ni pamoja katika Jimbo la Buchosha. Kwa hiyo nimuhakikishie tu kwamba kuna fedha ambayo tunaisubiria, ikishafika tu tutatekeleza hilo, ahsante sana.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa muda niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kuiuliza Serikali, Jimbo la Songwe lina tarafa mbili na kwenye Tarafa ya Kwimba kuna shule moja ya A-level pale Maweni Sekondari, lakini kutoka Maweni Sekondari mpaka ukafike mwishoni kabisa karibu na Ziwa Rukwa kuna Shule ya Sekondari ya Kapalala ambayo ina vigezo vyote vya kuwa na hadhi ya kupata kidato cha tano na imezungukwa na shule sasa takriban nne, Gua Sekondari, Phillipo Mulugo Sekondari, Ngwala Sekondari, na Kapalala yenyewe.

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi katika shule hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la mheshimiwa Phillipo Mulugo, Mbunge wa Jimbo la Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Mheshimiwa Mbunge, aliyoyatoa hapa mimi nimhakikishie kwamba tutatuma wataalamu waende kukagua na kujiridhisha kama vigezo vimetimia ili tuanze mchakato wa kuipandisha hadhi, ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Shule ya Sekondari ya Mogabili ni shule kongwe na ya bweni ambayo inagharamiwa na wazazi na inachukua wanafunzi wengi sana. Imekidhi vigezo ambavyo vimetajwa na Mheshimiwa Naibu Waziri hapa. Nataka tu kujua kama hii shule ya sekondari itapandishwa hadhi kuwa kidato cha tano na sita katika hizo shule 100 ambazo Waziri amezitaja hapa, anatarajia kuzifanya mwaka huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sio shule zote zimeomba kuwa kidato cha tano na sita. Kwa hiyo nitaangalia katika mpango, kama ipo maana yake tutaiweka katika mipango yetu ili iweze kukamilisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya kusema maneno hayo naamini Mheshimiwa Mbunge amenielewa.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sisi pia kule Namtumbo tuna Shule ya Sekondari ya Sasawala iliyopo katika Tarafa ya Sasawala ambayo iko kilometa 220 kutoka Makao Makuu ya Wilaya na imekidhi vigezo kwa kuwa imeongezwa ina madarasa na mabweni. Tunaomba na sisi tuorodheshwe katika hizo orodha ya Shule za Sekondari 100 kwa kuwa imekidhi vigezo. Je, linawezekana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama Shule imekidhi vigezo jambo hilo linawezekana. Hata hivyo niwathibitishie Wabunge wote kwamba tutapitia maeneo yote ambayo yamekidhi vigezo ili tuweze kuyapa kipaumbele. Ahsante sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, sisi tuliomba tangu mwaka jana kwenye Shule ya Makong’onda hatujajua mpaka sasa hivi hali ikoje?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, Mbunge wa Masasi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, shule zote ambazo zipo katika maombi ndio tunazifanyia kazi. Tutakapopata hiyo hela maana yake kuna baadhi ya miundombinu ambayo tunatakiwa tukamilishe ili sasa ziweze kupandishwa. Ahsante sana.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni ukweli usiopingika kwamba Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi imepeleka fedha nyingi sana za kujenga vyumba vya madarasa na sasa watoto wote wanaenda mashuleni. Hata hivyo bado kuna tatizo kubwa sana la nyumba za Walimu. Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mkakati thabiti wa kuhakikisha kwamba kunakuiwa na nyumba za Walimu za kutosha ili vijana wetu waweze kusoma vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ndio maana kwa sasa Serikali katika mipango yake kila mahali ambapo tunapeleka shule, tunahakikisha tunajenga na nyumba za Walimu katika kila shule ambayo tunaianzisha. vile vile mikakati mingine tuliyo nayo ni pamoja na kutafuta fedha ili kusogeza huduma hiyo ya makazi kwa Walimu, lakini tumeziagiza halmashauri kutenga fedha katika bajeti zao za ndani kuhakikisha katika kila bajeti ya mwaka wanaweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu. Ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ikumbukwe kwamba Halmashauri hizi za Geita ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zinachangia mapatao makubwa sana Serikalini kutokana na masuala ya uchimbaji wa dhahabu. Kwa hiyo, barabara hizi zinapokuwa hazitengenezwi vizuri hazitoi taswira nzuri kwa wananchi wa maeneo hayo. Kwa hiyo, naomba kuisisitiza Serikali kuongeza jitihada katika kuikamilisha vizuri barabara hii.

Mheshimiwa mwenyekiti, swali la pili ni kwamba, inaonekana katika Halmashauri nyingi amabazo ziko Vijijini na zile ambazo zinaanza kuchipukia zisizo na mapato makubwa, ugawaji wa fedha inayopelekwa kwa ajili ya barabara hizi za TARURA ni mdogo sana kiasi kwamba barabara nyingi zinashindwa kufunguliwa.

Je, ni lini Serikali itaeweka utaratibu mzuri wa kuongeza jitihada za kufungua maeneo haya ya vijijini ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Halmashauri ya Geita kutokana na shughuli za kiuchumi ambazo ziko pale na ndiyo maana ukiangalia kwenye jibu letu la msingi tumetenga fedha na tutakacho hakikisha ni kwamba fedha hizo zinakwenda na zile barabra zinarekebishika, kwa hiyo hilo halina shaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu ugawaji wa fedha za barabara ambazo zimekuwa zikionekana kuwa chache na kwa sababu ya ukubwa wa mtandao wa barabara tulionao nchini Serikali tunalipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalizingatia kulingana na bajeti ambavyo tutakuwa tukizitenga, ahsante. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, barabara hii ya kutoka Ruaha Mbuyuni kupitia Malolo, Ibanda, Mlunga, Uleling’ombe, Kinusi mpaka Wilaya ya Mpwapwa ndiyo kiungo kati ya Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Dodoma, na kwa kuwa Kata ya Uleling’ombe ndiyo Kata ambayo kiuchumi inalisha maeneo mengi ya Jimbo la Mikumi pamoja na Wilaya ya Mpwapwa.

Je, Serikali haioni kwamba wakati umefika sasa wa kuiweka barabra hii katika vipaumbele vya kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa mwenyekiti, tumetambua umuhimu wa barabara hiyo na ndiyo maana umeona katika mwaka wa fedha unaokuja tumeitengea fedha, kwa sababu awali barabara hii ilikuwa haipo katika mtandao wetu. Kwa hiyo, nimthibitishie Mbunge wa Jimbo la Mikumi, barabara hiyo tutaitengea fedha na itajengwa kama mapendekezo ya Mbunge lakini kutokana na umuhimu wa kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Dodoma. Ahsante sana.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Barabara ya Mahenge inayopita Udekwa inatokeza mpaka Ilula ni barabara muhimu sana, ni barabara mbadala ya barabara ya Mlima wa Kitonga kama magari yakikwama.

Je, ni lini Serikali itaipa umuhimu mkubwa sana ili barabra hii ijengwe kusiwepo na matatizo inapotokea katika barabra ya Kitonga, magari yaweze kupita katika hii barabra? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Iringa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabra ya Mahenge mpaka kwenda Ilula kama barabara ya mchepuko tunatambua umuhimu wake na tutawatuma TARURA Mkoa wa Iringa waende wakafanye tathmini halisi na watuletee ili tutafute fedha kwa ajili ya utengenezaji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Tunduru Kusini lina shule za sekondari kumi, katika hizo zote hamna high school na Shule ya Sekondari Mchoteka ina maabara tatu, ina mabweni mawili na moja linajengwa, ina vyoo 20, kumi na moja vya kike na tisa vya kiume, halafu ina madarasa 16; kati ya hayo manne hayatumiki. Kigezo kilichobaki ni bweni pamoja na jiko.

Kwa nini sasa Serikali kwa kutilia umuhimu wa kutokuwa na high school katika Jimbo langu isitilie mkazo wa kupewa fedha kwa haraka ili Jimbo la Tunduru Kusini lipate high school?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja tumepokea ombi lako, kwa sababu kwa kuizingatia hiyo shule itatupunguzia gharama za kwenda kuanzisha high school mpya, kwa hiyo tumelipokea na tutalifanyia kazi ili sasa tulete shule ya Kidato cha Tano na Sita katika Jimbo lako, ahsante sana.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia niendelee kuipongeza Serikali kwa fedha walizotuletea tulizipokea na barabara inaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeshasema kwamba itaendelea kuihudumia barabara hiyo mpaka itakapopandishwa hadhi, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni hatua gani imefikiwa ya barabara hiyo kupandishwa hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS kwa sababu ina vigezo vyote vinavyostahili?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, ni nini mkakati wa Serikali kwa barabara za namna hiyo ambazo zina vigezo na zinaunganisha Nchi ya Tanzania na nchi za jirani ili ziweze kuwekwa katika mkakati wa kuzipandisha hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara zikishatoka katika ngazi ya TARURA ili zipandishwe hadhi zinakwenda Wizara ya Ujenzi ambao ndio wasimamizi wa TANROADS. Kwa hiyo, hatua ya sasa zipo huko ambapo wanafanya uchambuzi wa mwisho, wakishamaliza nafikiri watatangaza kwenye Gazeti la Serikali kwa taratibu ambazo zimewekwa.

Mheshimiwa Spika, la pili, mkakati wa Serikali ni kuhakiksha barabara hizo kwanza kwa sasa zinapitika wakati wote na kulingana na mahitaji ya wakati uliopo na wakati ujao, maana yake tutaendelea kuzingatia ili kama zinahitaji kupandishwa hadhi zitafanyika hivyo, kama haitahitajika basi tutaendelea kuzihudumia ili zipitike wakati wote, ahsante sana.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Ni lini Serikali itahamisha barabara ya Bashnet – Bassodesh – Hirbadaw - Singida kutoka TARURA kwenda TANROADS kwa kuwa upande wa kutoka Bassodesh - Hirbadaw ipo TANROADS na Singida ipo TANROADS matengenezo yake huwa yako tofauti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Xaday Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nizielekeze tu halmashauri zenye mahitaji hayo zifuate taratibu na utaratibu unaeleweka unaanzia ngazi za halmashauri baadaye zinaenda katika Bodi ya Barabara Mkoa halafu zinapelekwa Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya uthibitisho. Kwa hiyo sisi tunapokea tu kama ombi ili hizo taratibu ziweze kufuatwa, ahsante sana.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kuna pesa ambazo zinakuja sasa hivi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Swali la kwanza; je, ni kwa nini Serikali wakati inaleta hizo pesa ilete pamoja na hizo pesa za kujenga ofisi za walimu kwa sababu kumekuwa kuna tofauti kubwa kati ya madarasa ambayo yanakuja kujengwa lakini Walimu wanakuwaqa hawana ofisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je ni lini Serikali itanunua furniture za ofisi ambazo zimejengwa na manispaa zipo tu na hazina furniture za walimu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Jimbo la Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa sasa wa Serikali ni kujenga na kuongeza madarasa katika maeneo ambayo yana uhitaji na ndio maana katika miradi mikubwa ambayo tunayo sasa kwa maana Mradi wa SEQUIP pamoja na BOOST yote miwili kwa pamoja ina thamani karibU trilioni 2.35.

Mheshimiwa Spika, katika yale madarasa maeneo mengine wanajiongeza, ukipeleka madarasa mawili wanajenga na ofisi katikati ambalo ni jambo jema. Tumekuwa tukipeleka fedha kwa ajili ya majengo ya utawala. Kwa hiyo sisi tutaendelea tu kuziagiza halmashauri kutenga fedha kujenga maeneo ya utawala, lakini ofisi nyingine waendelee kujiongeza kwa kuweka ofisi katikati ya madarasa ambayo tumekuwa tukiyapeleka huko. Kuhusu fanicha nafikiri ni maelekezo yetu pia kwa halmashauri zote nchini kuwapatia furniture kwenye staff rooms zote za shule katika maeneo yao, ahsante sana.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kuishukuru Serikali kwamba katika Mkoa wa Simiyu tuna madarasa mengi sana, lakini kuna upungufu wa Ofisi za Walimu. Walimu wetu hawafanyi kazi kwa furaha kwa sababu hawana ofisi wengi wanakaa kwenye miti. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu ujenzi wa Ofisi za Walimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Minza Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumeziagiza halmashauri kujenga ofisi kwa kila halmashauri kutenga mapato yao ya ndani kwa sababu moja ya jukumu letu sasa ni kujenga madarasa, mabweni, mabwalo ya chakula ambayo ndio kazi kubwa tunayoifanya sasa ikiwemo na majengo ya utawala kwa baadhi ya shule. Kwa hiyo kwa kadri tutakavyokuwa tunatafuta fedha tutakuwa tunapeleka, lakini tumeziagiza halmashauri kutumia mapato yao ya ndani kufanya hivyo. Kwa hiyo tunafanya hivyo kwa Mkoa wa Simiyu na mikoa yote nchini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Walimu wengi wanakosa viti na meza nzuri za kukaa na kuweza kufanya kazi zao vizuri. je, Serikali inalijua hilo na ina mkakati gani wa kulitatua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mtwara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto hizo katika baadhi ya shule na tunazifanyia kazi. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, Halmashauri ya Mji wa Mbulu iliko soko na stendi ni mahali pamoja kwenye kiwanja kimoja hali inayohatarisha watumiaji wa huduma na wapokea huduma katika eneo hilo.

Swali la kwanza; je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu mkubwa wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu kusogezwa kwenye kundi la pili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa tatizo hili ni kubwa na tumesubiri mradi huu kwa muda mrefu, Mheshimiwa Waziri ana kauli gani ya kuweza kufika Mbulu na wataalam wa TAMISEMI ili waone tatizo lenyewe kwa undani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini , kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kikubwa ni kwamba makundi yote matatu yatapatiwa hizo fedha za TACTIC na miradi yote iliyoainishwa itajengwa. Jukumu kubwa tunalolifanya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sasa ni kuhakikisha miradi hii inatekelezeka kama ambavyo imepangwa katika mkakati tulionao. Niwahakikishie tu hata wale wa tier one kwa maana ya kundi la kwanza, miradi yao inaanza kutekelezeka katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu miradi kuchelewa, niko tayari kwenda Mbulu pamoja na wataalam kwenda kujionea haya ambayo Mheshimiwa Mbunge anayazungumza, ahsante sana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kwa maana ya Mradi huu wa TACTIC kilometa 15 Mji wa Mpanda, Soko la Kazima na kilomita 29 kutoka Mwankulu mpaka Mpanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Kapufi Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Mpanda ipo katika kundi la pili ambalo kwa sasa mwezi wa Pili huu tulioanza zabuni za kutafuta wataalam washauri zinaanza na utekelezaji wa miradi hiyo kwa wenzetu watu wa Mpanda utaanza mwakani mwezi Aprili, 2024. (Makofi)
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mradi wa TACTIC pia upo kwenye Jimbo la Arusha Mjini na mnategemea kujenga stendi ya kisasa Bondeni City na lami maeneo ya Engosheraton na Olasiti na kwa kuwa mradi huu ulitegemea kuanza toka Julai, 2022. Je, ni nini changamoto inayochelewesha mradi huu kuanza kwa wakati maana miezi saba imeshapita mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulichelewa kidogo kwa sababu ya zile taratibu ambazo tulipaswa kuzifuata, lakini mpaka sasa tuko katika hatua nzuri. Kwa mfano, Jiji la Arusha lipo katika kundi la kwanza ambalo mwezi Februari, mwezi huu ambao tuko sasa, Serikali inatangaza kuwapata Wakandarasi watakaoanza kutekeleza na tunatarajia mchakato huu utakamilika mwezi Aprili na wakandarasi watakuwa site kujenga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba utekelezaji katika kundi la kwanza unaanza mwaka huu. (Makofi)
MHE. JERRY W. SLAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya Banana – Kitunda – Kivule - Msongola inayoenda hospitali ya wilaya kilometa 11.7 ina hali mbaya sana.

Je, Waziri na nimemwona Waziri mwenye dhamana yupo atakuwa tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi kwenda kutoa majibu ya Serikali, lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Slaa kuhusiana na barabara ya kilometa 11 ya kutoka Banana kwenda Msongola na nimhakikishie kwamba mwezi huu wa Februari tutakapomaliza Bunge atakapokuwa tayari tutaongozana naye kwenda kuangalia barabara hiyo na kuitekeleza, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante mwanzoni nilisema Spika, nafanya marekebisho. Kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa walimu wa hisabati, na wanafunzi wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri kutokana na ukosefu wa walimu wa hisabati. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha shule zote nchini zinapatiwa walimu wa hisabati kama ilivyowahi kufanya kwenye somo la sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kuna shule hazina walimu hususani wa somo la hisabati na upungufu umekuwa mkubwa. Ndiyo maana katika mpango wetu, ambapo tumeomba kibali Utumishi, tutakapokuwa tumepata sehemu yake ni kuajiri walimu wa sayansi hususani walimu wa hisabati ili kuhakikisha kwamba tunakabiliana na hii changamoto iliyopo, ahsante sana.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimwa Naibu Spika, na mimi napenda kuuliza swali la nyongeza; kwa maana ya kwamba tunafahamu changamoto ya walimu wa sayansi kwenye Jimbo la Arusha Mjini ni kubwa sana na hata kwa nchi nzima. Je, Serikali ina mpango gani wa kuja na mkakati Madhubuti wa kuondoa changamoto ya walimu wa sayansi wa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba mpango wa Serikali namba moja ni kuajiri ajira mpya ambazo sehemu kubwa itakuwa ni kuchukua walimu wa sayansi. Mpango wa pili ni kuhakikisha kwamba sasa hivi sisi Ofisi ya Rais-TAMISEMI tukishirikiana na Wizara ya Elimu matarajio yetu ni kuanza kuwatumia hao walimu waliomaliza ambao watakuwa wanajitolea wenye professional hiyo kuhakikisha kwamba tunaondoa hiyo changamoto. Kwa hiyo tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba masomo ya sayansi tunapaa walimu na vifaa vilevile ili kuhakikisha wakati wote yanakuwa yanafundishwa, ahsante sana.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini bado kumekuwa kuna changamoto kubwa hususan kwa shule shikizi ambazo zilipata msaada kupitia maswala la UVIKO pamoja na kupitia Kapu la Mama.

Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na shule hizo kupatiwa walimu ikiwa shile hizo zimesajiliwa lakini nyingi zina mwalimu mmoja mmoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, pamoja na kuonekana kwamba kada ya walimu imekuwa ikiajiri sana walimu wakike lakini kwa Mkoa wa Katavi imekuwa ni tofauti. Katika Mkoa wetu wa Katavi kuna changamoto kubwa sana ya walimu wa kike katika shule za Sekondari; mfano katika shule ya Majalila, shule ya Mwamapuli ambapo shule hizo zimekuwa hazina kabisa walimu wa kike.

Je, Serikali inatoa tamko gani ili Watoto wetu waweze kupata mahitaji ambayo mtoto wa kike anayapata akiwa na mwalimu wa kike shuleni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua uwepo wa vituo shikizi ambavyo vinasaidia shule mama. Tulishatoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wote mikoa nchini kuhakikisha kwamba wanafanya msawazo na sehemu ya msawazo huo ni pamoja na kupeleka walimu kwenye hivo vituo. Kwa hiyo nirudie tena jmabo hili litekelezwe kama ambavyo Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais- TAMISEMI amekwishalitolea maelekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu walimu wa kike Mkoa wa Katavi kukosekana, tumelipokea ili tulifanyie kazi kwa kuongeza idadi ya waalimu katika ajira zinazofuatia, na katika maeneo ambayo kuna walimu wengi tutafanya msawazo vilevile kuwapeleka katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha, ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nishukuru sana kwa majibu ya Serikali lakini nilikuwa na ombi. Naiomba Serikali kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa mapema kwa sababu ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa kata ya Luwaita kwa ajili ya kusafirisha mazo yao kwenda kwenye maeneo ya soko, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea tutafanya hivyo, kwa sababu awamu ya kwanza na ya pili ziko katika utekelezaji kwa hito na hii ya tatu tutaitekeleza, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa menyekiti, ahsante kwa swali lanyongeza. Barabara ya kutoka Mapera kuelekea Ilela iliyopo Mbinga Vijijini imeharibika sana na kukwamisha shughuli za maendeleo za wakazi wa Kata za Mapera, Kambarage pamoja na Mikaranga.

Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura kwa ajili ya kurekebisha barabara hii ili wakazi wa maeneo haya shughuli zao za maendeleo ziweze kuendelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, niagize tu TARURA mkoa wake waende waipitie hii barabra ya Mapera mpaka Ilela waangalie uharibifu ambao upo na watoe tathmini ili tutafute fedha iweze kurekebishwa, ahsante sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu haya ambayo yanaleta faraja kwa watu wa Same, kati ya mtandao wote wa barabara hizi za Same za kilometa 874 asilimia 80 ya barabara hizo zina-connect watu wa milimani ambao wao ndio wakulima wengi na kule ndiko kwenye mvua kubwa ambazo hizi barabara huharibika mara kwa mara.

Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba wakati umefika sasa barabara hizo zitengenezwe kwa kutumia aidha mawe au zitumie zege hasa zile sehemu mbaya ili wananchi waweze kupeleka mazao sokoni kwa wakati wote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri maeneo ambayo ameyaainisha ya milimani katika Halmashauri ya Same na mimi nimefika na ninatambua hali ngumu ambayo wanapata wananchi wa maeneo hayo na Serikali tumepokea ushauri na tutashauriana katika ngazi za chini ili waweze kutekeleza sehemu ya mawazo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyatoa, ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga haina kabisa mtandao wa barabara ya lami; je, nini kauli ya Serikali kuhusu kuipatia halmashauri hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christine Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ndio maana moja ya mkakati wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika bajeti zilizopita ilikuwa ni kutoa shilingi milioni 500 katika kila jimbo ili waanze sasa kujenga mtandao wa lami.

Kwa hiyo, kwa sababu hiyo ahadi inaendelea kutekelezeka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi tutafanya hivyo, lakini mapendekezo makubwa mnayatoa ninyi wenyewe, lakini wazo la Serikali ni kuweka mitandao ya lami katika maeneo yote, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa mafuriko au maporomoko yale ya milimani kipindi cha mvua yanaleta maji yote tambarare na barabara inayotoka Same mpaka Bendera inakuwa haipitiki, wakati mwingine hasa kuanzia Ndungu mpaka Bendera kwenyewe.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuifanya na kuipasisha barabara hiyo ijengwe kwa lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua adha ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza na ndio maana katika mkakati wa Serikali tumeongeza fedha ili tuhakikishe kwamba hizi changamoto ambazo Wabunge wamekuwa wakizieleza humu ndani tunazitatua. Kwa hiyo, na hilo tumelipokea tutaliweka katika mipango yetu, ahsante sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nampongeza mlezi wetu Mheshimiwa Zuberi Ali Mauridi, Spika Baraza la Wawakilishi kule Zanzibar kwa kufanya ziara katika Mkoa wetu wa Lindi na Jimbo la Mchinga. (Makofi)

Sambamba na hilo wakati anaelekea kwenye ile shule maalum ya wasichana ambayo Mama Samia Suluhu Hassan ametoa pesa shilingi bilioni nne. Mheshimiwa hakuweza kufika kule kutokana na ubovu wa barabara; barabara ile ni ya matope; na kwa kuwa mwezi wa saba shule ile itaanza, imeshapewa kibali cha usajili.

Je, je ni lini barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Jimbo la Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba moja ya jitihada kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kwamba ni kujenga shule maalum za wasichana katika kila mkoa zenye wastani wa thamani ya shilingi bilioni nne na katika maeneo hayo tunatambua tunahitaji mtandao ya barabara. Kwa hiyo, kwa hatua ya awali tutawaelekeza TARURA Mkoa wa Lindi, kwanza waijenge kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika wakati wote wakati sisi tunatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, changamoto zilizoko kule Same zinafanana sana na changamoto za Meru ambako barabara nyingi zinakwenda mlimani na barabara ni za vumbi.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara ili tuweze kuwa na barabara ambazo ni za hard surface?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaona haja hiyo ya kuongeza fedha kwa ajili ya bajeti za matengenezo na ujenzi mpya na ndio maana kila mwaka imekuwa ikiongeza bajeti. Kwa hiyo, sisi tulishukuru Bunge kwa kutuongezea na tutafanya hivyo kuhakikisha barabara za jimboni kwako na Tanzania nzima kwa ujumla zinapitika wakati wote, ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la Kwanza; kwa kuwa, Rais wa Awamu ya Tano Dokta John Pombe Magufuli Hayati, alipotembelea eneo la Kaengesi aliahidi ujenzi wa kilomita Saba za lami kutoka Kaengesa junction mpaka Chitete. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kuanza ujenzi wa barabara hiyo ya lami ambao usanifu na utambuzi wa barabara hiyo umekamilika?

Swali la pili; kwa kuwa, Jimbo langu la Kwela lina Miji mingi midogo, ukianza Mji wa Laela, Mpuyu, Kaengesa, Mji Mdogo wa Muze, Ilemba na Kilyamatuni, Miji hiyo ina barabara za mitaa ambazo hazijatambuliwa bado.

Je, Serikali mna mpango gani wa kuzitambua hizo barabara ili ziweze ku-qualify kupata bajeti kutoka Serikalini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Clement Sangu Mbunge wa Jimbo la Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ahadi zote za Viongozi Wakuu wa nchi yetu ambazo zimeainishwa zote zipo katika mipango yetu ikiwemo barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha ya kilomita Saba ambayo Hayati Dokta John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Awamu ya Tano alitoa. Kwa hiyo, ipo katika mipango yetu na tunatafuta fedha ili utekelezaji wake uanze.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la barabara ili ziweze kutambuliwa jambo hilo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa Miji hiyo inakuwa kwa kasi na bahati nzuri ni maeneo ambayo hata mimi mwenyewe nayafahamu, basi nikuahidi tu kwamba tutatuma wataalamu wetu ili waweze kuzitambua na kuzisajili ili sasa zianze kupatiwa huduma. Ahsante sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali katika suala la mgawanyo, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri katika mgawanyo uliopita wa Walimu ajira zilizopita, Halmashauri yangu ya Mkalama ilipata walimu 12 tu ikilinganisha na Halmashauri zingine ambazo zilipata zaidi ya walimu 40.

Je, unatuambia nini katika mgawanyo huu unaokuja kuhusu Halmashauri yangu ya Mkalama kwani tuna upungufu wa Walimu zaidi ya 800 katika Halmashauri yangu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuzingatia vigezo vya kupeleka Walimu ambao watapata nafasi hiyo katika Halmashauri zote nchini kulingana na mahitaji. Tunatambua kwamba changamoto bado ni kubwa na mahitaji ya walimu bado ni makubwa lakini kwenye hizi tutaendelea kutenda haki. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaleta kulingana na idadi na mahitaji ya eneo husika. Kwa hiyo, siyo wote 800 lakini ni wale ambao watatosheleza kwa wakati wa sasa. Ahsante sana.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ni kweli wiki moja iliyopita tumepokea Milioni 43 kwa ajili ya kuanza kazi zilizoainishwa hapo. Kutokana na umuhimu wa daraja katika mto huo uliosababisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kuahidi daraja la juu mwaka 2015.

Je, Waziri uko tayari kufika katika Kijiji hicho ukajionea adha inayokata mawasiliano ya Kata Nne na Wilaya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Maafisa kutoka Wizara ya Ujenzi walifika kukagua hilo daraja pamoja na barabara. Ninataka kujua Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi hilo daraja kuwa TANROADS ili tuweze kupata fedha za kutosha kuihudumia barabara hiyo kutokana na umuhimu wa kiuchumi wa Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari nitakwenda katika eneo lake kama alivyoahidi, kwa hiyo nitafika kwenda kujionea hiyo hali halisi anayoizungumza Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea maombi yote na tunatambua kwamba kuna maombi mengi sana ambayo Halmashauri na Mikoa kupitia Bodi ya Barabara yameyafikisha kwa ajili ya kupandishwa hadhi. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuyafanyia kazi na mara watakapokuwa wamemaliza kujiridhisha maana yake barabara hizo zitapandishwa hadhi. Kwa hiyo, siyo kwamba Serikali inapuuza ni kwa sababu tunafanya tathmini tunaangalia uwezo wa kifedha ili kazi hiyo inapokamilika maana yake na hizo barabara iweze kutengenezwa kulingana na hiyo hadhi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Daraja la Mto Nabili linalounganisha Kata ya Bukindo, Kata Nkilinzia ni muhimu sana kwa mawasiliano ya wananchi wa maeneo haya.

Ni lini Serikali itatupatia pesa kujenga daraja hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimwondoe tu hofu kwamba tumepokea hiki kilio chake na tutakifanyia kazi, kwanza tutawatuma watu wetu wakafanye tathmini na kuona fedha kiasi gani zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili. Ahsante sana.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za dharura tayari tulishaandika andiko kwa ajili ya barabara ya Kambarage – Mapera – Litoho - Mgumbo pamoja na Mkongotingisa kwenda Muungano, kwa sababu mvua bado zinanyesha na barabara hizi zinataka kutoweka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ambayo ameainisha Mheshimiwa Mbunge ambayo ipo katika mpango wa Serikali ninaamini kabisa kwamba tuko katika hatua za mwisho za kutafuta fedha ili kuhakikisha hiyo barabara inafanyiwa kazi. Kwa hiyo, nimwondoe hofu mara tutakapopata hiyo fedha maana yake tutaanza ujenzi. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali yenye matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Bahi, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Kata ya Mwangoi na Kata ya Dule Mlalo ambako linaunganishwa na Mto Umba, mto ule umehama na kusababisha kina cha maji kushuka chini zaidi na hivyo daraja limezama katika eneo lile, lakini Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA wameshafanya tathmini.

Sasa nauliza ni lini ujenzi wa daraja jipya linalounganisha Kata ya Mwangoi na Kata ya Dule katika Kijiji cha Chamlesa litaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo ameianisha pamoja na hilo eneo ambalo daraja linahitajika, kati ya Mwongoi na Dule, daraja hilo lipo katika mpango na tutalitekeleza katika mwaka wa fedha 2022/2023 yaani mwaka unaofuatia.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika Kata ya Isalalo kwenda kwenye Kata ya Ikunga, kuna mto mkubwa wa Nkana.

Je, Serikali ina mpango gani ili kuwafanya wananchi wa Isalalo waweze kuvuka kwenda Kata ya Ipunga kwenye Kijiji cha Ipanzya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri eneo ambalo amelianisha Mheshimiwa Mbunge ninalifahamu na bahati nzuri niko huko huko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshawaagiza watu wa TARURA Mkoa wa Songwe waende wakafanye tathmini katika eneo hilo ili watupe tathmini ili tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika eneo hilo.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, Serikali ina mpango gani na barabara ya Kisukulu - Maji Chumvi ambayo imeharibika sana sasa hivi na wananchi hawawezi kupita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bonnah Kamoli, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo ameianisha Mheshimiwa Mbunge inafanyiwa tathmini kwa wakati wa sasa na watakapomaliza tathmini tutampatia taarifa Mheshimiwa Mbunge, ni lini sasa tunaanza rasmi ujenzi katika eneo hilo.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, nimepokea wito wa Serikali kwamba tuendelee kushirikiana na wananchi kujenga shule; na kwa kuwa mwaka jana tulileta maombi ya kujengewa/kumaliziwa shule 58 za shikizi tukapata shule kumi tu kati ya 58 bado shule 48 zimeongezeka sasa hivi ziko 55.

Je, Serikali itatupatia lini fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa shule hizo shikizi 55 ambazo zipo sasa hivi? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, usajili wa shule za msingi na usajili wa shule za sekondari hufanywa kwa mikondo, mkondo mmoja wa shule za msingi una watoto 45 na mkondo mmoja wa shule za sekondari nadhani una watoto 40. Sasa maana yake ni kwamba shule yenye mikondo minne inatakiwa iwe na wanafunzi kwenye darasa moja wanafunzi 180 katika shule ambazo zimeshazidi idadi ya wanafunzi wanaohitajika kwenye mikondo. Kwa nini Serikali isiwe na mkakati maalum wa kitaifa wa kujenga shule mpya karibu na maeneo ambayo shule zimezidi idadi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mbunge kwamba moja ya mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunamalizia shule shikizi zote na kwa awamu ya kwanza katika mwaka wa fedha huu hapa ambao tupo, Mheshimiwa Rais alitoa fedha na tukajenga madarasa 3000 nchi nzima kwenye maeneo ya shule shikizi.

Kwa hiyo, hizo shule kumi ambazo tulileta katika maeneo yako, na sasa hivi tuna mipango mingine ambayo tuna fedha, na baadhi ya fedha tutazielekeza katika maeneo ambayo bado yanaupungufu na yana mahitaji hususani katika shule shikizi, kwa hiyo, katika kipaumbele tutakachotoa ni pamoja na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatapisha shule zote ambazo zina wanafunzi wengi na ikiwemo kusajili katika maeneo ambayo sasa idadi ya wanafunzi ni kubwa hususani katika hizi shule shikizi ambazo zimezidi.

Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge haya yote yapo katika mpango wa Serikali na tunaendelea kuyatekeleza na mfano mzuri katika mwaka huu wa fedha na katika bajeti ambayo tumeipitisha hapa ya mwaka 2022/ 2023.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na program ambayo imeitoa. Ila nina swali moja dogo la nyongeza. Kwa vile wahenga walisema seeing is believing, je, Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili, uko tayari tuongozane, mguu kwa mguu twende tukatembelee hizo shule ambazo nimezitaja ili uone jinsi ambavyo zimechakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari kwenda na Mheshimiwa Mbunge hata kabla ya Bunge kwisha, ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa shule kongwe zinajumlisha pia shule ya Zombo, shule ya msingi pale Jimbo la Mikumi pamoja na Kidodi. Je, Serikali haioni wakati umefika sasa wa kuona namna bora ya kuboresha shule hizi kwa kuzikarabati.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango ambao tunao sasa hivi miongoni mwa shule ambazo zitafanyiwa ukarabati ni pamoja na hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilikuwa nataka commitment ya Serikali ni lini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilikuwa nauliza kwa kuwa sasa hivi mfumo ndiyo unaochagua wapi nyumba ziende. Kwanini sasa Wizara isipeleke hizi nyumba kwa majimbo badala ya mfumo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Jimbo la Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali imeshaweka commitment ya kwa kutenga fedha katika bajeti yake, na ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha ambao tumepitisha bajeti ya TAMISEMI, tumetenga jumla ya bilioni 81.48 ambazo zitatumikwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za misingi na sekondari.

Kwa hiyo, ni commitment kubwa ya Serikali. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tutafanya hivyo katika maeneo yote nchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, ni kwamba amekuja tu mfumo kwamba tupeleke katika majimbo. Niseme tutaendelea kuzingatia maeneo yote yenye uhitaji mkubwa ikiwemo katika jimbo lake kama ambavyo ameainisha. Kwa sababu lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba tunamaliza hii kero kwa kadri fedha itakavyokuwa inapatikana. Ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Longido ina changamoto kubwa sana ya nyumba za walimu ambayo inasababisha ukosefu mkubwa wa walimu katika wilaya hii. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba fedha tumetenga kwa mwaka huu unaokuja lakini vile vile tutazingatia maeneo ya pembezoni ikiwemo Longido kama ambavyo ameainisha. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Chemba ina jumla ya shule za msingi 103 za Serikali na tumeongeza shule nane kwa matokeo ya fedha za UVIKO, lakini asilimia 70 ya shule zote hizi zipo vijijini ambavyo ni ngumu sana kupata nyumba za kupanga, naomba kujua mna mkakati gani wa maksudi wa kujenga nyumba za Walimu kwenye shule hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Monni Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Serikali ni kujenga nyumba maeneo ya pembezoni na miongoni mwa mikakati ambayo nimeainisha ni pamoja na kutenga fedha, vilevile tuna miradi mbalimbali ambayo tumeiainisha ikiwemo BUST, EP4R, EQUIP 2 yote hii lengo lake ni kuhakikisha kwamba tunapunguza hiyo adha kwa hiyo tutazingatia maeneo hayo ikiwemo Jimbo la Chemba. Ahsante. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, Ahsante. Sambamba na nyumba za Walimu Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga ofisi za Walimu au kukarabati ofisi zilizopo kwa ajili ya Walimu na kuweka samani zake ndani ya ofisi hizi, hasa katika Jimbo letu la Temeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama tulivyojibu kwenye upande wa nyumba za Walimu sasa hivi moja ya mkakati wetu mkubwa ni kuhakikisha kila tunapokenga madarasa tunaweka na ofisi za Walimu, kwa hiyo huo ndio mkakati wa Serikali ili kuhakikisha kwamba walimu wanakuwa na maeneo mazuri ya kukaa ambayo yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku. Hivyo, hilo lipo na limezingatiwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Hili linahusu Majimbo yote ya Vijijini hasa hasa kule ambako kumejengwa shule shikizi, nyumba nyingi za Walimu zilizopo zimejengwa kwenye maeneo ambayo angalau Mwalimu anaweza akapata nyumba za kupanga, sasa hizi shule ambazo ziko kwenye maeneo ambayo Mwalimu hapati hata nyumba za kupanga.

Je, kwa nini hizo shilingi bilioni 43 zisielekezwe kwenye maeneo kama hayo badala ya kuangalia maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa George Kakunda Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nilipokuwa najibu swali nimeainisha kwamba maeneo ambayo tutayazingatia zaidi ni maeneo yenye uhaba, maeneo ya pembezoni kwa hiyo ni moja ya jambo ambalo sisi tumelizingatia. Ahsante sana.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niongezee maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 12 kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri ni ya muhimu sana kwa wananchi wa eneo hilo ikitokea Lubira, Kyabunaga, Bugango mpaka mpakani.

Je, sasa ni lini Serikali itaona umuhimu wa barabara hiyo kwakuwa inakidhi vigezo vyote vya kuhudumia na TANROAD ipandishwe hadhi kwenda kule iwe imepata bajeti ya uhakika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, barabara ya kutokea Kiwanda cha Kagera Sugar kwenda Kijiji cha Bubali imekuwa ina changamoto kwa muda mrefu na inahitaji matengenezo makubwa.

Je, ni lini barabra hiyo itatengewa bajeti ili iweze kutengenezwa na wananchi waweze kutumia barabara hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mbunge ameomba barabara hiyo kupandishwa hadhi na jukumu hilo kubwa linafanywa na wenzetu wa TANROADS, kwa kuwa Serikali ni moja basi sisi tutalipokea hilo ombi ka niaba ya TANROADS na watakwenda kulifanyia kazi kwa kufuata zile taratibu ambazo zinatakiwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Kagera Sugar kwenda Bubali ambapo ameainisha hapo ni lini itapangiwa fedha, mimi nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitawaagiza Maneja wa TARURA wa Wilaya na Mkoa wa Kagera waende wakafanye tathmini ili sisi tutafute fedha kwa ajili ya barabara hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

La kwanza; uhitaji wa vyumba vya madarasa na mabweni katika shule za sekondari ambazo ziko pembezoni katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini ni mkubwa kama vile Shule ya Sekondari Kasanga, Bwakila Juu na Singisa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Morogoro Vijijini katika kata tajwa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na mabweni ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea mwendo mrefu, lakini vilevile msongamano darasani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuona ni kuamini; je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi kwenda katika kata tajwa ili kujionea kwa uhalisi tatizo kubwa tulilokuwa nalo na kuweza kutusaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa Serikali ni kuhakikisha kata zote za pembezoni tunazifikia kwa kujenga shule, lakini vilevile kwa kuongeza madarasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kata hizo tutazifikia, na mimi niseme tu kwamba nitakwenda na nitaongozana naye kwenda kushuhudia katika hayo maeneo. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa halmashauri zilizopata fedha nyingi za Serikali kwaajili ya ujenzi wa madarasa; je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kuongeza mabweni kwenye Shule za Sekondari za Bulamata, Kakoso na Kabungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, katika maeneo ya Tanganyika ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha nimhakikishie tu kwamba Serikali ni kuhakikisha na yenyewe tunayafikia; na ndiyo maana sasa hivi tuna programu mbalimbali kuwafikia katika maeneo ambayo hayafikiki. Kwa hiyo, nimuondoe hofu kwenye hili analolizungumza. Ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Wilaya ya Hai ina shule 13 chakavu sana na Mheshimiwa Rais alipotembelea Wilaya ya Hai, aliahidi kutupa fedha kwa ajili ya kujenga maboma ya shule hizi chakavu, lakini wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri pia ametembele Wilaya ya Hai na amejionea shule zilivyo chakavu. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuondoe wasiwasi, kwamba mpango wa Serikali wa marekebisho ya shule tutaanza katika mwaka wa fedha wa 2022/2023. Najua moja ya shule niliahidi ni Makeresho na ipo katika huo mpango, ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imejitahidi kujenga shule za sekondari katika kila kata na kuna watoto wengi hasa wasichana wanatoka wanatembea kilometa zaidi ya tano; je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba shule zinakuwa na mabweni angalau kunusuru watoto wa kike na hawa fataki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunajenga shule na mabweni katika maeneo ya pembezoni hususani maeneo yale ya wafugaji zaidi kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata ile huduma ya shule bila kwenda umbali mrefu. Kwa hiyo, hilo lipo katika mpango wa Serikali, ahsante.

NAIBU SPIKA: Haya katika mipango yako uweke vilevile na Kisutu Secondary School.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, sawasawa.

NAIBU SPIKA: Imeingia kwenye Hansard hiyo.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, imeingia hiyo.
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Sindeni – Kwedikwazu ni barabara muhimu na kuna idadi kubwa ya watu na vilevile inatumika kutoa mazao mengi; na kipindi cha mvua inasumbua sana. Je, ni lini Serikali itaitengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Saluu, Mbunge wa Jimbo la Handeni Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba Serikali ina mpango wa kuhakikisha barabara zile zenye shida kutafuta fedha ili tuzitengee na kuzijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge najua anafanya kazi nzuri ya kuwatetea wananchi wake katika Jimbo la Handeni Vijijini, kwa hiyo katika hilo nimwambie tu kwamba kadri tutakavyopata fedha basi eneo lake tutalizingatia sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutenga shilingi 1,140,000,000 kwa ajili ya kujengwa shule 57 katika Jimbo la Kiteto.

Je, Serikali ni lini itaharakisha sasa usajili wa shule hizi ili wananchi waweze kupata huduma kama ambavyo nia ya Mheshimiwa Rais imeweza kulenga kutatua changamoto?

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana na Mbunge wa Jimbo la Kiteto ili kwenda kuona hali halisi ya vituo hivi ambavyo vinajengwa kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kwanza kabisa niseme kwamba napongeza kazi nzuri anayoifanya, na nimhakikishie tu kwamba Serikali ipo tayari kusajili shule zote ambazo zimekamilika na maeneo yote ambayo yanahitaji. Kwa hiyo, wayafuate tu yale maelekezo ambayo tumeyatoa na sisi tutazisajili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kuhakikisha tukajionee hizo kero za wananchi. Ahsante sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nasikitika kwa kupata majibu ambayo sio; niseme tu kwa lugha nyepesi kwamba siyo ya ukweli. Barabara haziwezi zikakosa wakandarasi.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na kucheleweshwa kwa mikataba hiyo juu ya kuwepo taratibu nyingi za manunuzi: Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kupunguza milolongo hiyo ya manunuzi ili mikataba hii iweze kusainiwa kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Serikali itaanzisha au itarudisha mfumo wa kila Halmashauri kuwa na Meneja wa TARURA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tu nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu za manunuzi kwenye kandarasi zozote tunazozifanya ni lazima zifuatwe. Nasi hatutaruhusu mtu yeyote kukiuka hizi taratibu za kimanunuzi. Kikubwa tu ni kwamba tunaendelea kuboresha mifumo ili kuhakikisha kwamba tenda zote zinazotangazwa ziweze kupatikana kwa muda ili kazi ambazo zimekusudiwa zifanyike kwa haraka. Kwa hiyo, tumekuwa tukiboresha na ndiyo maana sasa hivi watu wote wanaomba kupitia mfumo.

Mheshimiwa Spika, la pili, utaratibu uliopo sasa ni kwamba kila Halmashauri tumeweka Meneja wa TARURA ambaye anasimamia barabara katika eneo lake. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Eneo la Mto Mori linalounganisha Kata nne Kata ya Nyabulongo, Nyatorogo, Kigunga na Milale ni eneo ambalo wananchi wamekuwa wakipoteza maisha kwa muda mrefu sana hasa pale wanapojaribu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine. Hivi ninavyozungumza, wananchi watano wamefariki na mpaka sasa tunaendelea na maombolezo ambapo walijaribu kuvuka kwa kutumia vyombo kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Spika, nilitaka nijue Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mkataba wa dharura angalau kwa kujengewa daraja kwa kutumia mkataba wa dharura ili kunusuru maisha ya hawa wananchi ambao hawana namna, wanalazimika kuvuka kwenda upande wa pili kutafuta huduma za kijamii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri jambo ambalo amelieleza Mheshimiwa Mbunge ninalifahamu. Nasi tumeshamwagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA kupeleka timu ya kwenda kufanya tathmini na baada ya hapo, watatuletea taarifa ili sasa tuandae mchoro kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu katika eneo hilo. Tathmini ya awali ambayo tafanyika sasa, itapelekea sasa angalau tuweke kivuko cha muda wa dharura ili wananchi wale waweze kuvuka katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Waziri Mkuu alifanya ziara pale Wilayani Nyang’hwale na akatoa ahadi ya ujenzi wa kilometa mbili Makao Makuu ya Wilaya; na Mheshimiwa Waziri Silinde alikuja pale akajionea lile vumbi ambalo linatimka pale katikati ya mji: -

Je, ni lini Serikali itajenga ama kukamilisha ahadi ya Waziri Mkuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mimi nimefika pale na ni kweli kabisa kwamba kuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za viongozi wakuu ikiwemo ya Waziri Mkuu ambayo ameitoa, itatekelezeka kwa vitendo. Kwa hiyo, nimwondoe shaka na bahati nzuri nafahamu lile eneo. Kwa hiyo, lipo katika mpango wetu, tumeliweka, na tutalifanyia kazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa kumekuwa na baadhi ya wakandarasi ambao wanaacha madeni kwa wananchi kwa kazi za kujitolea na kokoto: Nini kauli ya Serikali kwa wananchi hawa wanaoachwa na madeni na Mameneja wa TARURA kuzuia hili lisitokee siku nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa tukipata hiyo changamoto na tumekuwa tukielezwa na wananchi katika maeneo mbalimbali kwamba wakandarasi wamekuwa wakiacha hayo madeni katika maeneo husika. Moja ya utaratibu wetu sasa hivi, kabla ya kumaliza ule mkataba, hatutalipa fedha zote za mwisho mpaka pale ambapo watakuwa wamemaliza madeni ya watu katika maeneo husika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka 2018 aliahidi kujenga kilometa tano za lami ndani ya Mji wa Mangaka katika Wilaya yangu ya Nanyumbu: -

Je, ni lini ahadi hii ya kiongozi wetu itatekelezwa ndani ya wilaya yangu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu swali la awali la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, ndivyo ambavyo naweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi zote zipo katika mpango wetu na bahati nzuri Bunge lako Tukufu kupitia kauli ya Mheshimiwa Rais mlituongezea fedha Ofisi ya Rais ya TARURA.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi angalau tuna wigo mpana wa kuhakikisha kwamba tunatekeleza hizi ahadi za viongozi kwa wakati. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi kwamba kabla ya mwaka 2025 tutakuwa tumeanza utekelezaji wa ahadi hiyo ya Waziri Mkuu. Ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Lakini kutokana na umuhimu wa shule hii, kama ilivyoelezwa hapa; kwamba ni ya muda mrefu sana; na naona hapa majibu yote yaliyotoka ni ya jumla jumla.

Mheshimiwa Spika, nachotaka kuomba ni commitment ya Serikali; je, Shule hii ya Kingurungundwa ni lini italetewa fedha kufanyiwa ukarabati? Kwa sababu hali ya shule hii ni mbaya zaidi kuliko hizo shule nyingine ambazo umezijumuisha kwenye majibu yao. Naomba kupata commitment ya Serikali, hii Shule ya Kingurungundwa ni lini italetewa fedha ili ifanyiwe ukarabati mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI
ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tulijibu katika jibu la msingi, kwamba, mpango wetu wa sasa ni kuzifanyia tathmini shule zote ikiwemo shule ya Kingurungundwa. Tukishamaliza mchakato; maana yake ni kuanzia mwaka huu wa fedha mpaka mwaka 2025/2026. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tutafanya mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha shule hiyo inafanyiwa ukarabati, ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Na mimi napenda kuuliza swali moja la nyongeza; Shule ya Msingi Chunya Mjini pamoaja na Shule ya Msingi Chunya Kati ni shule kongwe ambazo zilikuwepo tangu kabla nchi yetu haijapata uhuru. Shule hizi zimechakaa sana baaddhi ya majengo yameanguka.

Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili ukarabati wa majengo hayo uweze kufanyika na ziweze kurudi katika hali kama shule nyingine ambazo zinajengwa sasa hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kitu kikubwa ambacho nikukuhakikishie tu kwamba miongoni mwa shule ambazo ziko katika mpango hizi ni mbili ambazo umezianisha Mheshimiwa Mbunge, na tutahakikisha baada ya tathmini tutazipa kipaumbele ili kuhakikisha kwamba zinajengwa. Ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni lini Shule ya Msingi SUA ambayo ina matatizo ya upungufu wa vyuo itafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tathmini yetu itaisha mwezi Julai 2022 na tutakuwa na shule zote nchini, ikwemo ya Shule ya Msingi SUA ambayo ameiainisha hapa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba mara baada ya hiyo tathmini kila mmoja atajua shule yake inahudumiwa lini. Ahsante sana.
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu maziuri ya Mheshimiwa Waziri, na ya kueleweka nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa mchakato wa huu ni mrefu, je, Serikali itakubaliana nami kwamba kuna ulazima wa kuongeza vyombo vya usafiri katika Halmashauri ya Mbarali, hasa kwenye sekta ya elimu, afya, TASAF na kadhalika ili waweze kuwahudumia wananchi kikamilifu?

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa TARURA ipo chini ya TAMISEMI, je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kuwa kuna ulazima wa kuhamasisha hii TARURA sasa ikarabati zote zilizoharibiwa na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha kipindi kilichopita, ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii kwa urahisi na pia kusafirisha mazao yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Leornard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni kuhusu usafiri. Nimhakikishie tu kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI tumeshaanza huo mchakato. Mwaka jana tuligawa magari, kwa maafisa elimu sekondari, na mwaka huu vilevile tumeshaagiza magari mengine 184 kwa ajili ya maafisa elimu wa shule za msingi ambayo tumeshapata awamu ya kwanza 35 na mengine yanakuja, lakini yote yameshalipiwa.

Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo tunatoa magari kwa ajili ya wahandisi wa TARURA wa halmashauri, lakini vilevile tutapeleka ambulance katika halmashauri zote nchini ambazo zina hospitali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jukumu hili la kusadia Halmashauri nchini ikiwemo ya Mbarali lipo katika utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusu kumalizia ukarabati wa barabara za TARURA, tumelichukua hilo katika bajeti yetu na kwamba tutahakikisha kwamba zinajengwa kulingana na mahitaji. Ahsante sana.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo tangu mwaka 2017, ilipitia taratibu na vigezo vyote vya kuweza kugawa jimbo. Lakini changamoto iliyorudishwa ni Kamba kuna idadi ndogo ya watu. Je, Serikali itakuwa tayari kuigawa hii halmashauri, baada ya sensa ya mwaka huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Kilolo, ilikuwa imekidhi vigezo vingine isipokuwa ya idadi ya watu; na kinachosubiriwa ni kujua hiyo idadi watu. Mimi ninaamini kwamba kama vigezo vitafikiwa basi mapendekezo yatapelekwa huko mbele na mamlaka husika italiangalia. Kwa hiyo, tusubiri vigezo vikishakuwa vimekamilika, basi hatua hiyo inaweza kukubalika baadaye. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni lini sasa Serikali italigawa Jimbo la Sumbawanga Vijijini ambalo hata Mwenyezi Mungu aliligawa kati kati, Ufipa wa Chini kata 13 na Ufipa wa Juu kata 14. Sasa ni lini Serikali italigawa jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi, ni kwamba wafuate tu utaratibu na sisi tutazingatia endapo hizo halmashauri zimetimiza vigezo vyao, na baada ya hapo maana yake sisi tutapeleka katika mamlaka husika kwa ajili ya maamuzi. Kwa hiyo, kikubwa tu waanze mchakato halafu mamlaka husika italiangalia hilo. Ahsante.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa uamuzi wa mwisho wa Serikali kugawa halmashauri, wilaya na mikoa ulifanyika mwaka 2012, takribani miaka kumi iliyopita, na kwa kuwa maeneo mengi sasa hivi yana sifa kabisa za kugawiwa, mfano Mkoa wa Tabora, Morogoro, Tanga na mikoa mingine mikubwa na baadhi ya wilaya ambazo ni kubwa kama Sikonge na Mbeya.

Je, maamuzi mengine ya Serikali tuyategemee lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Josephat Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kwamba Serikali ilifanya maamuzi ya mwisho, mwaka 2012, na muda ambao umepita mpaka sasa hivi ni miaka kumi na bado Serikali inapitia na kutathmini kuona haja ya kuongeza endapo maeneo ya utawala, ama tuendelee na sasa ili tuendelee kuyaboresha na kuwa bora. Kwa hiyo, naamini kabisa Serikali uamuzi wake mpaka sasa hivi upo sahihi na bado tunazingatia; na siyo kwamba mwaka 2012 ndiyo ilikuwa mara ya mwisho. Bado huo mchakato utaendelea baada ya kuona mahitaji ya wakati wa sasa. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Wilaya ya Tunduru ilianzishwa mwaka 1905 na mpaka leo bado ni kubwa kulinganisha na wilaya zingine; na kwa kuwa vikao vyote vinavyohusu kugawa halmashauri ile limefanyika mpaka ngazi ya mkoa; na kwa kuwa Tunduru Kusini ndilo jimbo ambalo linaathirika sana kwa kutokuwa na halmashauri. Je, Serikali itaanzisha lini halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Idd Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, kwamba halmashauri ambazo zimeshamaliza mchakato, bado Serikali inaendelea kupitia vigezo na kutathimini, ili kuona kama haja ya kutangaza kwa wakati uliopo ama tuendelee kuboresha zile halmashauri ambazo ni changa. Kwa hiyo jambo hilo lipo katika ofisi zetu na wasubiri wakati ambapo itakuwa tayari kufanya hivyo, tutafanya hivyo.
MHE. FURAHA MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi. Je, ni lini Serikali itaongeza idadi ya tarafa katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela kwa kuwa zina kata zaidi ya kumi na tano na zina tarafa moja moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuongeza maeneo ya utawala ni moja ya jukumu la Serikali ambalo tumekuwa tukilifana mahali ambapo pana vigezo vyote. Kwa hiyo, kama kunakuwa na eneo halina vigezo maana yake tunakuwa hatuna hiyo fursa ya kuongeza. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Furaha Matondo kwamba endapo maeneo hayo yaliyoainishwa yakifuata taratibu zote na zikafika katika Serikali Kuu, basi Serikali itazingatia kulinga na vigezo vilivyowekwa kikatiba. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwanza nishukuru sana majibu ya Mheshimiwa Waziri, na nimpongeze, huwa anatembelea sana Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, ninakiri hizo fedha milioni 250 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mkunwa, zimefika na zinaendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba wananchi wa Mangopacha Nne, tayari walishaandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya muda mrefu tu, zaidi ya miaka mitano. Kwa hiyo, niombe sasa Serikali itoe kipaumbele fedha zitakapopatikana.

Mheshimiwa Spika, hii Kata ya Mangopacha Nne ni moja ya kata katika Tarafa ya Dihimba, ambapo tarafa hii haina hata kituo kimoja cha afya lakini kuna zahanati katika baadhi ya vijiji. Kuna tatizo kubwa sana la wanawake…

SPIKA: Swali lako Mheshimiwa.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nauliza swali, katika kutatua tatizo la wanawake kujifungua hasa nyakati za usiku. Je, Serikali itakuwa tayari kuboresha huduma katika hizi zahanati ili kusudi akina mama waweze kupata huduma bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninatambua kwamba anafanya kazi nzuri kwa Mkoa wa Mtwara na ndiyo maana amekuwa akitetea sana katika huduma za afya, hususan wanawake katika mkoa wake. Nimhakikishie tu kwamba Serikali ipo tayari kuboresha huduma katika tarafa hiyo, na tutalifanyia kazi, ahsante sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa Njombe walishakamilisha ujenzi wa vituo vya afya viwili kwenye Kata mbili, Kata ya Mamangolo na Kata ya Kifanya; na tumekuwa tukiomba sana hapa. Nini kauli ya Serikali kuhusu kutoa vifaa tiba kwenye hospitali ili mama mtoto aweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, baada ya ukamilishaji wa vituo hivyo kinachofuatia ni kutafuta vifaa tiba na ambavyo vipo katika mpango. Kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunanunua vifaa tiba kwa ajili ya vituo vya afya ambavyo vimeshakamilika. Vitakapokuwa vimepatikana tutavipeleka pale kwa wananchi, ahsante sana.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na vibali na eneo lililotengwa, lakini bado kadhia ya magari makubwa hupaki, kupakua na kupakia mizigo katika Barabara kama za Nyati, Faru, Tembo na kadhalika inaendelea.

Je, Serikali inaelewa kwamba wafanyabiashara hawa wa mizigo wanawakosesha haki ya kimsingi wanye makazi ya kulala, pia kuharibu utaratibu mzima wa afya ya akili?

Je, ukitokea moto, wakati barabara zote zimezibwa na magari makubwa haya ya mizigo, Serikali haioni kama hilo janga in the make, ina mpango gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, cha kwanza tunatambua haki za msingi za wananchi wa maeneo hayo wanayokaa na kero wanayoipata. Kwa hiyo, kutokana na umuhimu wake, sisi kama ofisi ya Rais TAMISEMI, tunaomba tulipokee na tuangalie namna bora ambayo tunaweza tukaifanya kuchukua hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la msingi, kuhusu majanga ya moto, tumesema moja ya mkakati wetu na mkakati wa Jiji la Dar es Salaam ni kujenga eneo jipya katika eneo la Mnazi Mmoja kwaajili ya maegesho ya magari. Kwa hiyo, kwa kuuliza hili swali la msingi maana yake sasa tutaiharakisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ianze huo mkakati hara iwezekavyo ili muondokane na hiyo kero. Ahsante.

Mheshimiwa Naibu Waziri tunakushukuru sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Wizara ya Maji, Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya sasa ulize swali lake.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, je, ipo ruzuku ama mikopo nafuu ya kuwezesha miradi hii ya vizimba ili kufanya uvuvi kuwa wa kisasa zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Wizara ina mpango gani wa kuendelea kutoa elimu kuwawezesha wavuvi au wananchi wanaozunguka Ziwa Victoria kuwa na uelewa zaidi na haswa Mkoa wa Mara ambao bado hawajapata elimu hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba Mheshimiwa Mbunge ni mvuvi na ni Mchuuzi na ni mtu ambae anaipenda sana hiyo kada. Nimhakikishie tu kwamba Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunazo fedha ambazo ni za masharti nafuu kwa ajili ya wafugaji wa samaki kwa vizimba kwa vijana. Eneo la pili ni kwamba mpango wa kutoa elimu upo na sasa hivi tumeanza na programu za vijana atamizi ambao wanakuwa wakifundishwa juu ya ufugaji wa samaki na elimu ya viumbe maji katika maeneo ambayo yanazungukwa na bahari, maziwa ambapo vijana wengi wanahusika na kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, hivyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Agnes Marwa kwamba kazi hiyo itafanyika. Ahsante sana.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa; nini mkakati wa Serikali kutoa kipaumbele kwa vijana wenye ulemavu wenye sifa kwenye mradi huu wa uvuvi wa vizimba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Stella Ikupa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango na katika mipango yetu tumewapa vipaumbele watu wote wenye ulemavu na katika elimu ambayo tunaitoa sasa hivi moja wapo ya kigezo ni kuwa na wavuvi ambao wanatokana na watu wenye mahitaji maalum, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi kwanza nitoe shukrani na pongezi kwa majibu mazuri na ambayo yanaenda kutoa matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini ambao wanasubiri skimu hizi kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; katika Skimu ya Msange wananchi wanatumia mfumo wa mafuta, yaani diesel, kwa ajili ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji na tayari wananchi wameshatuma maombi kwa ajili ya kubadilishiwa mfumo kwenda…

SPIKA: Swali.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, je, Serikali iko tayari sasa kuwasaidia wananchi kubadilisha mfumo kutoka kwenye generator ili waepuke mafuta mengi na sasa watumie umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna Bwawa la Mgori pamoja na Kisisya ambayo yamejaa tope na mifumo ya umwagiliaji imeharibika;

Je, Serikali iko tayari sasa kwenda kuyafufua mabwawa haya ili yaweze kuwasadia wananchi kuongeza kipato katika kilimo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Kilimo itakaa pamoja na Wizara ya Nishati ili kuhakikisha wanafanikisha jambo hili kuondoa wananchi kutoka kwenye generator kwenda kwenye umeme. Kwa hiyo, hilo tutakaa pamoja ili kulifanikisha hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Bwawa la Mgori na Kisisya ambayo yamejaa tope na yanahitaji kufufuliwa, nimhakikishie tu, kwamba nimezungumza na Waziri wa Kilimo na Wizara ya Kilimo itawatuma wataalam wake waende kufanya tathmini ili waweze kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hiyo, ahsante sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata majibu ya swali hilo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa utafiti uliofanywa na Tanzania National Carbon Center mwaka 2018 unaonesha kwamba mifugo ya kuchungwa – siyo ile ya kusafirishwa, ya kuchungwa inachangia asilimia 28 ya uharibifu wa mazingira. Je, Serikali ilitoa maagizo kwa halmashauri kwamba zitenge maeneo ya hao wafugaji ili wapate maeneo makubwa ya kufugia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ranchi zetu zilizopo Tanzania haziwezi kutumika kama mashamba darasa ya wale wakulima wetu wakubwa wasiojua faida ya ufugaji ambao siyo wa kuswaga?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninashukuru kwa maswali madogo mawili ya msingi ambayo Mheshimiwa ameyaeleza, nimhakikishie tu kwamba kwa sasa Serikali ina mpango wa kutenga maeneo na tumeanza kufanya hivyo, katika hatua ya awali mpaka sasa tumetenga hekta Milioni 3.38 ambazo zitachangia katika malisho na zimeelekezwa katika halmashauri za vijiji, lakini kutumia ranch kama eneo la mashamba darasa jambo hilo ndiyo lipo katika mkakati wa sasa na tumekuwa tukifanya hivyo katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, moja ya mipango mikubwa tuliyonayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni pamoja na hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na pia atupelekee shukrani nyingi Serikalini kwa kutuletea milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Samaki pale Manda. Pamoja na Shukrani hizo naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kule Ludewa wananchi wana ng’ombe kama 33,871 wa kienyeji na 687 wa kisasa ambao sio bora sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea madume bora kwa ajili ya kuboresha uzao wa ng’ombe kule Ludewa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kurekebisha, Sheria Sera na Kanuni ili ziweze kusimamia Sekta ya Uvuvi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tunapokea shukrani na pili Program ya Uboreshaji wa Mifugo inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni program endelevu inayotumia njia ya madume bora na njia ya uhimilishaji. Yeye ameomba madume bora na katika mwaka huu wa fedha tunaoelekea 2023/2024, mkakati huu utaendelea na Ludewa tutaiweka kwenye eneo mojawapo la kunufaika na program hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya Sera, Sheria na Kanuni zetu tumekuwa tukifanya hivi na kila mara panapotokea hitaji, tutaendelea kuboresha Sheria na Kanuni zetu. Kwa hiyo kama Mheshimiwa Mbunge analo jambo mahususi tunamkaribisha kwa ajili ya kufanya maboresho hayo. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Serikali imewahi kwenda kutoa elimu ya ufugaji wa vizimba vya samaki kwa wananchi wanaozunguka Ziwa Basutu. Je, kwa kuwa imekwishakuwa ni muda mrefu ni lini Serikali itapeleka fedha ili wananchi hao waweze kunufaika na mafunzo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tayari wananchi wa Basutu wamekwishapata elimu naomba nimuahidi kuwa Serikali inalichukua jambo hili na kwenyewe tutakwenda kufanya tathimini ya kimazingira ili waweze kunufaika na program hii na kujiongezea kipato na kutengeneza ajira. Ahsante sana.
MHE. DKT. FAUSTINE NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika majibu ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba kuna nguvu kubwa sana imepelekwa katika ukanda wa Maziwa katika suala zima la ufugaji wa samaki kwa vizimba. Je, nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba na Ukanda wa Pwani ikiwa ni pamoja na Kigamboni zinanufaika na uvuvi wa samaki kwa njia ya vizimba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa 2022/2023 upande wa Mikoa ya Pwani kwenye programu hii ya ufugaji wa samaki tulipeleka pesa zaidi upande wa ukulima wa mwani Takribani Bilioni 2.1zimenufaisha wakulima wa mwani kutoka Tanga kule Moha mpaka Mtwara kule Msimbati, sasa katika mwaka wa 2023/2024 kupitia programu maalum ya blue economy tunatarajia kupeleka tena nguvu kwa maana ya uwezeshaji, kwa lengo la mwani vilevile unenepeshaji wa Kaa na ufugaji wa Majongoo Bahari. Kwa hivyo, wakulima na wavuvi wa ukanda wa Pwani wakiwemo wa Kigamboni na wenyewe makundi ya vijana na akina mama yatapata kunufaika na programu hii. Ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu hayo yenye kuleta matumaini. Pamoja na kwamba wamechukua hatua mbalimbali za upimaji wa eneo na kuchukua tathmini ya hati ya mazingira, ninaomba niulize swali moja la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Lindi Manispaa limejengwa mwaka 1950, kwa hiyo ni soko ambalo tumerithi kutoka kwa wakoloni, ni la muda mrefu tangu Lindi ikiwa eneo dogo na sasa hivi Lindi Manispaa ina kata 31 na makusanyo ya manispaa ni shilingi bilioni tatu kwa mwaka. Makusanyo ni madogo lakini tunatoa huduma katika kata 31.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lini Serikali itaona umuhimu mkubwa wa kutupatia fedha katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kutekeleza mradi huu wa kimkakati wa ujenzi wa soko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua shauku ya Mheshimiwa Mbunge juu ya soko hili, na amekuwa akilipambania tangu akiwa Mbunge wa Viti Maalum na mpaka sasa ni Mbunge wa Jimbo. Na ukweli ni kwamba Manispaa ya Lindi ipo katika Tier II katika miradi ambayo inaanza kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2023/24, kwa hiyo nimuondoe shaka tu na wananchi wake kwamba utekelezaji wao utafanyika kama ambavyo watu wa Tier I sasa hivi wako katika hatua za mwisho, ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale kwenye bajeti ya 2018-2020 tulitengewa fedha kwa ajili ya kujenga stendi ya kisasa kama mradi wa kimkakati, lakini fedha zile zilirudishwa kutokana na sababu zisizojulikana. Je, ni lini Serikali itatuletea fedha hizo tena ili mradi ule wa kimkakati uweze kukamilika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Bunge lako lilipitisha hapa sheria ya kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo zimeelekezwa katika miradi na kuvuka mwaka wa fedha ziendelee kubaki ili zitekeleze miradi ambayo imekusudiwa. Na jambo hili alilozungumza Mheshimiwa Mbunge maana yake sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI italifanyia kazi kulipitia ili ione namna bora ya kuhakikisha fedha zile zinarudi na kufanya kazi ambayo imekusudiwa, ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Soko Kuu la Bukoba Mjini ni chakavu na dogo kwa matumizi ya sasa, je, lini Mradi wa TACTIC utaanza ili soko hilo lijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Manispaa ya Bukoba iko katika awamu ya pili ya utekelezaji wa Mradi wa TACTIC (Tier II). Kwa hiyo nimwondoe hofu, kama ambavyo Mbunge wa Jimbo, Mheshimiwa Stephen Byabato analifuatilia na jambo hili linakwenda kutekelezeka. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye Jimbo la Ukonga tarehe 23, Februari, alitoa maelekezo ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanza mchakato wa ujenzi wa soko kwenye Kata ya Gongo la Mboto, soko ambalo litatumiwa na wafanyabiashara ambao kwa sasa wanafanya biashara barabarani na kutumiwa na zaidi ya kata tano. Je, Serikali imefikia wapi kwenye utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Waziri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo aliyatoa ni maelekezo ambayo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alishaelekezwa kuyatekeleza. Kwa hiyo, ninarudia tu kumwelekeza mkurugenzi wa manispaa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kwa muda mrefu nimekuwa nikifwatilia juu ya ujenzi wa soko la mazao pale Vwawa;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba lile soko linajengwa kama ambavyo imekuwa ikiahidi kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Hasunga tunatokea katika mkoa mmoja na anatambua kabisa Soko la Vwawa liko katika Mradi wa TACTIC Tier III kwa hiyo, utekelezaji wa mradi utakapoanza ambapo mimi na yeye tuko katika kundi moja, maana yake na yeye atapatiwa hiyo huduma. Ahsante sana.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa ajili ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa majibu hayo ingawaje kuhusu Lyamahoro Secondary School limejibiwa hivi zaidi ya miaka miwili, kwamba inaanza mwezi ujao, lakini haijaanza. Sasa swali: -

Je, Serikali inafahamu kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba nzima haina shule ya ngazi ya kidato cha tano na sita? Inafahamu hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali inafahamu kwamba tukipata shilingi milioni 80 kila shule, kwa Lyamahoro 80 na Rubale 80, shule hizi zinakamilika kuwa na kidato cha tano na sita, zinaweza zikaanza?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua shauku ya Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha katika Halmashauri yake ya Bukoba wanapata shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita. Na ndiyo maana katika jibu la msingi Shule ya Sekondari ya Lyamahoro imeshapata sifa. Kwa hiyo, nimhaikishie tu kwamba Julai inapokuwa inaanza maana yake na shule hii itatekelezeka; kwa hiyo tunatambua kwamba hakuna na ndiyo maana utekelezaji wake unakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu kupeleka hizo shilingi milioni 80 katika hizo shule mbili ni sehemu ya fedha ambayo nafikiri itatosha tu kukamilisha baadhi ya miundombinu kwa sababu ili shule iwe na kidato cha tano na sita inahitaji bweni, bwalo, jengo la utawala pamoja na madarasa ya ziada na vyoo. Kwa hiyo kuna bajeti kidogo ambayo inahitajika kwa hiyo nimhakikishie tu kwamba Serikali itatafuta fedha ikishirikiana na halmashauri pamoja na yeye Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahasante sana. Shule ya sekondari Ifaru iko katika jimbo la Chemba mwanzoni ilikuwa na kidato cha tano na sita baadaye wakasitisha kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu. Sasa uchakavu ule tayari Serikali imefanya ukarabati. Ni lini sasa itarejesha kusajili wanafunzi wa kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mohamed Monni Mbunge wa Chemba kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI imelipokea jambo hilo na italifanyia kazi; kwa sababu moja ya malengo ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kuhakikisha halmashauri zote nchini zinakuwa na shule za kidato cha tano na cha sita kwa sababu ya ongezeko kubwa la wanafunzi ambao wanawekwa sasa, kwa hiyo lipo katika mchakato na linafanyiwa kazi.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimuulize Naibu Waziri swali dogo; Halmashauri ya Mji wa Bunda wananchi wamehamasika na wameanza ujenzi wa Sekondari mpya katika kata ya Nyamakokoto. Ni lini sasa mtamalizia majengo manne ya shule ya sekondari Nyamakokoto ili watoto wetu wa Bunda nao wapate nafasi ya kusoma vizuri?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu pia Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Ester Amos Bulaya ambaye amewazungumzia wananchi wa Bunda, kwamba moja ya malengo makubwa ya serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba shule zote ambazo zimeanza zinapata fedha na kumaliziwa. Kwa hiyo na hilo lipo katika mpango itapelekwa fedha kwa ajili ya kuhakikisha shule hiyo inakamilika.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Halmashauri ya Wilaya ya Hai tayari imeshapeleka maombi ya kupandisha hadhi shule nne kutoka kidato cha nne kwenda cha tano na sita, ambazo ni shule ya Lemila, Masikia, Longoi na Mkwasa. Je, ni lini Serikali itasajili shule hizi ili ziweze kutoa elimu ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mafuwe Mbunge wa Jimbo la Hai kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI baada ya kuona shule zote zinakuwa zimeshakamilisha na kufikisha vigezo maombi ya usajili wa shule kuwa kidato cha tano na sita yanapelekwa Ofisi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwa hiyo jambo hilo nafikiri lipo huko. Ofisi ya Rais TAMISEMI itashirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuhakikisha jambo hilo linakamilika kwa zile shule ambazo zimekidhi vigezo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali hili nimeliuliza mwaka 2020, 2021 na nikajibiwa majibu haya haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametaja kwamba halmashauri ya Geita ina shule za sekondari tatu sisi halmashuri ya Geita tuna majimbo mawili, jimbo la Busanda na Jimbo la Geita. Shule mbili ziko jimbo la Busanda. Jimbo la Geita lina population ya zaidi ya watu laki saba na nusu, kwangu, tuna shule moja. Watoto wanalazimika kutembea kilometa 80. Sasa, bado nahitaji majibu sahihi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Nkome ina wanafunzi 9500 ina shule nne; na miundo mbinu yote ya madarasa tumejitosheleza, tunapungukiwa tu ujenzi wa bweni kwa ajili ya kufungua kidato cha tano na cha sita.

Je Serikali iko tayari kupeleka pesa kwenye kata ya Nkome ili tuweze kufungua pia kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba majibu tuliyotoa kwa sasa ni sahihi kwa kuwa ni kweli Halmashauri ya Geita ina majimbo mawili, kwa maana ya Geita na Busanda ambao wana hizi shule za kidato cha tano na sita tatu. Ninajua mahitaji makubwa ambayo yako pale, ndiyo maana kwa sasa tumesema tunaendelea kuziimarisha ili kuongeza idadi ya wanafunzi wakati tunatafuta fedha kuhakikisha tunaongeza shule nyingine. Kwa hiyo nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inapopata fedha itafanya hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu hii Shule ya Sekondari Nkome ambayo ina idadi kubwa ya wanafunzi na wanahitaji Bweni tu. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI niseme ombi hili tumelipokea na litafanyiwa kazi. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kakonko inayo shule moja tu ya kidato cha tano na sita, ambayo ni Shule ya Sekondari Kakonko, lakini tunazo Shule za Sekondari Nyamtukuza, Mhange, Shuhudia, Kasanda na Gwanum ambazo zina sifa, kwa maana ya kwamba zina madarasa lakini hatuna hosteli.

Je, ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya kujenga hosteli ili wanafunzi waanze kupokelewa kidato cha tano na cha sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Kakonko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba mahitaji ya shule za sekondari kidato cha tano na sita yanapewa kipaumbele kwenye takriban majimbo mengi kwa sasa; na ndio maana katika jitihada zake Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha mliona, kwamba kwa kushirikiana na kampuni ya madini African Barrick walipewa dola milioni, takriban bilioni 70, ambazo ni kwa ajili ya ku-support elimu nchini. Fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na sita. Kwa hiyo lengo la Serikali ni kuhakikisha hii adha inaondolewa. Kwa hiyo Mheshimiwa Kamamba nikuondoe hofu kwa sababu iko katika mipango ya Serikali.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina shule moja tu ya sekondari ya kidato cha tano; lakini inazo shule mbili ambazo zina sifa ya kuwa kidato cha tano, Shule ya sekondari ya Mpotola na Shule ya Sekondari Makukwe, lakini tuna shindwa kwa sababu hatuna mabweni au hosteli.

Je, ni lini Serikali itatuunga mkono kutujengea hosteli ili tuanze kidato cha tano na cha sita katika shule hizo mbili?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda Mbunge wa Newala vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe hofu na yeye, kwamba Serikali imesikia na imepokea hayo maombi na itayafanyia kazi kwa kadri ambavyo tunatafuta fedha ili kuhakikisha wananchi wake wanapatiwa hiyo huduma ya kidato cha tano na sita na Watanzania wote kwa ujumla, ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusukuru kwa kunipa nafasi. Shule ya Sekondari ya Mkonoo iliyopo katika Jiji la Arusha ina madarasa kumi yaliyojengwa kwa fedha za uviko. Madarasa hayo yamekamilika na yana samani zote; lakini kwa sababu ya umbali madarasa haya hayajaanza kutumika hadi leo, takribani miezi sita sasa.

Je, Seikali haioni haja sasa kujenga hosteli kwenye shule hii ili madarasa haya yaanze kutumika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa shule hiyo madarasa yameshakamilika na miongoni mwa halmashauri ambazo zina mapato makubwa ni pamoja na Jiji la Arusha. Kwa hiyo nimwelekeze tu Mkurugenzi wa Jiji kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo ili shule hiyo iweze kupata usajili na kusajiliwa kama ambavyo maombi ya Mheshimiwa Mbunge, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa tatizo hili la uhaba wa hosteli katika shule za Serikali nchini limekuwa kubwa sana;

Je, Mheshimiwa Waziri haoni kuwa una haja kubwa ya kupeleka timu katika halmashauri zote ili kuratibu na kuona upungufu ulivyo mkubwa na hatimaye kuja kuiweka kwenye mipango ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimpongeze Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kwa maoni ambayo ameyatoa. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeyasikia na hivyo itayafanyia kazi kwa kuunda timu maalum ambayo itazunguka maeneo yote ili ipitie na kugundua ukubwa wa changamoto ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza. Ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Shule ya Sekondari ya Busagara na Shule ya Sekondari Kumgogo zilizoko katika Jimbo la Muhambwe zina miundombinu ya madarasa kwa ajili ya kuanzisha kidato cha tano na cha sita.

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga hosteli ili tuweze kuanza huduma ya kidato cha tano na sita katika shule hizi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Jimbo la Mhambwe. Kama ambavyo nimeeleza hapo awali katika majibu mbalimbali ambayo nimeyatoa kwa waheshimiwa Wabunge, nimwondoe hofu kwamba sehemu ya timu ambayo itatumwa nafikiri itatumwa kupokea maoni yote ambayo Wabunge wote wameeleza; mapungufu katika shule ambazo tunaweza kuongeza aidha hosteli, bweni ama jengo la utawala na zikatumika kama kidato cha tano na sita zikiwemo za jimbo lako. Kwa hiyo waondoe hofu wananchi wa Muhambwe kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazi na itafanya kazi hiyo, ahsante. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga hosteli katika Shule za Sekondari za Meatu na Kimali ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu kwa kifupi Mheshimiwa Minza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaeleza nia ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza shule za kidato cha tano na cha sita nchi nzima ikiwemo katika Mkoa wa Simiyu. Kwa hiyo niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge wote kwenye dhana hii, kwa sababu fedha inatafutwa na sehemu ya fedha imeshapatikana ambayo itaelekezwa katika halmashauri zenu kwa ajili ya kuongeza mabweni sehemu zingine mabwalo ya chakula sehemu nyingine madarasa na vyoo ili tuweze kuzisajili na kuzifungua. Kwa hiyo hofu hiyo iondolewe kwa waheshimiwa wote.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika inazo shule za Kalema, Kabungu pamoja na Bulamata, ambazo zina tatizo kubwa sana la ukosefu wa mabweni.

Je, ni lini Serikali watapeleka fedha ili waweze kujengewa mabweni?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti,ni kwamba Serikali bado inaendelea kutafuta fedha, na sehemu ya fedha ambayo imeshapatikana katika awali tayari kuna maeneo ambayo tayari imeshaelekeza kuhakikisha kwamba zinafunguliwa shule za kidato cha tano na sita na zianze kufanya kazi. Kwa hiyo hata haya maombi yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa yatawekwa katika mpango ili Serikali iweze kuyatekeleza kwa kutafuta fedha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga hosteli katika Shule ya Sekondari ya Nasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu kama ifiatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa shule ambazo ziko katika mpango wa Serikali kuongezewa hosteli ni pamoja na shule ya Sekondari Ngaza ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha hapo, ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Kwa kuwa, mawakala ambao walitakiwa kutoa mbegu katika Jimbo la Arumeru Magharibi wamekataa kutoa mbegu kwa madai kwamba Serikali haijawalipa fedha zao na kusababishia wakulima kutopata mbolea katika maeneo husika. Je, nini kauli ya Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wakulima hawa kwa haraka ili waweze kupata mbolea hasa katika msimu huu wa kilimo?

Swali la pili, kwa kuwa Mawakala hawa wanateuliwa na Wizara moja kwa moja kwenda kwenye Majimbo au Halmashauri.

Je, Serikali haioni sasa ifanye jambo la haraka kuwateua mawakala wa uhakika watakaokwenda kutoa huduma hiyo kwa wananchi hawa ili waendelee kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Mawakala hawajalipwa fedha zao na ndiyo sababu ya kutokupeleka mbolea ya ruzuku kwa wananchi jambo hilo sidhani kama lina ukweli wowote, isipokuwa ni kwamba Serikali inafanya taratibu za kumalizia malipo kwenye baadhi ya Mawakala ambao watalipwa na kazi yao itafanyika, lakini kigezo cha kutokulipwa kwa sababu hiyo ni kigezo ambacho Serikali kupitia Wizara ya Kilimo haioni kama ni njia muafaka wa kuwasaidia wakulima na wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawataka Mawakala wote kutekeleza yale maelekezo ya mikataba ambayo walisaini kati ya Mawakala na Wizara ya Kilimo. Pia kuteua Mawakala wa uhakika jambo hilo tumelipokea na ndiyo maana katika awamu hii iliyofanyika, maana yake imetoa somo kwa Wizara ya Kilimo ambalo katika mwaka unaokuja maana yake itazingatia yale mapungufu yaliyojitokeza mwaka huu ili yasiweze kujitokeza katika msimu ujao wa kilimo. Ahsante. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa niombe radhi uliniita lakini sikuwa nimeuliza swali. Naomba niulize swali la nyongeza.

Kwa kuwa, kuna baadhi ya viwanda vinazalisha mbolea hapa nchini kikiwemo kiwanda cha Intracom pale Nara, kiwanda cha Minjingu na viwanda vinginevyo. Je, nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba viwanda hivi na vinginevyo vinazalisha mbolea ya kutosha ili kuweza kukabiliana na upungufu wa mbolea nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA
KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuleta wawekezaji wengi nchini ili waweze kuzalisha mbolea ya kutosha kwa ajili ya kusaidia usambazaji wa mbolea kwa wakulima wote nchini, ndiyo maana ukiangalia moja ya mwekezaji wetu ni hawa Intracom kutoka Burundi ambao wao watazilisha karibu tani 60,000 na moja ya mkakati mwingine wa Serikali ni kuhakikisha Minjingu inaongeza uzalishaji kutoka tani 30,000 mpaka tani 100,000 kwa mwaka. Lengo ni kuahakikisha kwamba wakulima wanapata mbolea zote kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu huo ni mkakati wa Serikali na Serikali iko kazini kuhakikisha tunaongeza wawekezaji vilevile tunaongeza wigo wa viwanda vilivyopo kuongeza uzalishaji nchini. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, napenda kujua sasa kwa miradi ambayo inaendelea itakamilikalini?

Swali langu la pili, Bukoba Manispaa mradi wake una chanzo cha uhakika ambacho ni Ziwa Victoria. Je, Serikali haioni kwamba kwa kushirikiana na BUWASA wanaweza kutazama uwezekano wa kutumia mradi huu ambao una maji mengi, ambao unaweza kupeleka maji katika Kata za Bujugo na Maruku? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ambayo imeanza kama ambavyo tumeainisha hapa, mingine ipo asilimia 88 maana yake iko katika hatua za mwisho za utekelezaji wake, kwa hiyo kikubwa tu nimhakikishie kwa niaba ya Waziri wa Maji kwamba Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu ili miradi yote itekelezeka kama ambavyo tumesainiana katika mikataba kati ya Wizara na Mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chanzo cha uhakika cha Ziwa Victoria na maoni ambayo umeyatoa Wizara imeyapokea na itayafanyia kazi ili kuhakikisha tutumie hicho chanzo kuwaletea huduma wananchi wa Bukoba Manispaa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Nina swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Nkasi Kusini lina idadi kubwa sana ya mifugo na wananchi wa Kata ya Ntuchi pamoja na Chala wameshaandaa maeneo ya ujenzi wa majosho. Je, ni lini Serikali itakuja kujenga majosho hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, natambua kazi kubwa anayoifanya katika ufuatiliaji wa kuhakikisha maeneo yake yanapata majosho pamoja na malambo. Kwa bahati nzuri tulishakaa ofisini na kukubaliana jambo hili kwamba, katika mwaka wa fedha kwa sababu tunaendelea na mazungumzo na Wizara ya Fedha, fedha itakayotoka tutapeleka katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha, ahsante sana.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na Mheshimiwa Ally Kassinge kutembelea eneo la Kilwa Kivinje ili kujiridhisha na mahitaji ya soko hilo na kuharakisha ujenzi wake?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Ziwa Bassotu ukanda upande wa Kata ya Mulbadaw miundombinu ya msingi imeishajengwa ya mwalo. Je, yupo tayari kutoa tamko ili watendaji wake ndani ya Wilaya Hanang’ wafungue Mwalo huo mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili kuhairishwa na ratiba yetu tutapanga kuanzia mwezi ya saba kwa hiyo hilo limekubalika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tamko la ziwa niseme tu kwamba, nimelipokea jambo hilo na ninakwenda kulifanyia kazi na baada ya hapo tutatoa tamko rasmi, ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ili kuzifanya juhudi hizi ambazo Mheshimiwa Waziri amezieleza hapa kuwa endelevu, Je, hatuoni haja ya kuja na mkakati wa pamoja ambao utazishirikisha sekta za maliasili, kilimo, mifugo pamoja na sekta ya maji ili kulimaliza kabisa tatizo hili ambalo ni la muda mrefu?

Swali la pili, kwa kuwa kuna good practices kwa wenzetu Uganda ambao wanawashurutisha wafugaji wenye mifugo wengi kutenga maeneo ya malisho toshelezi kwa ajili ya mifugo yao. Je, Serikali haioni haja ya kuiga mfano huu mzuri ili kuweza kupambana na changamoto hii ambayo inaleta migogoro kati ya wakulima, watu wa maliasili pamoja na mifugo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ni kwamba mkakati upo wa Wizara zote ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Maji, tukiungana na watu wa Wizara ya Ardhi, kuandaa mipango endelevu kwa ajili ya kusiadia wafugaji wetu ili kuondoa hii migogoro ambayo imejitokeza. Kwa hiyo, jambo hilo lipo Mheshimiwa Mbunge, na tutaendelea kuliboresha zaidi ili tuondoe hii dhana ambayo imekuwa ikijengeka kila wakati ya migogoro inayotokana na wafugaji pamoja na wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutenga maeneo, hilo tayari ni agizo ambalo Serikali ilishalitoa katika Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji, hususan wale wenye mifugo wengi ili kuondoa hii kuhamahama kutafuta malisho pamoja na maji. Utaratibu huu kwanza utaboresha mifugo wetu wa kisasa na kuongeza ubora wa malisho na mifugo ambao tunao. Ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwaka 2006 Serikali iliridhia mifugo kuhamishwa kutoka Bonde la Ihefu kupelekwa Mkoani Lindi, hivi ninavyozungumza katika Wilaya za Liwale, Kilwa na Nachingwea kuna mafuriko makubwa ya mifugo na hivyo kusababisha kuwa na uhaba wa malisho, maji pamoja na huduma nyingine za mifugo.

Je, kuna utaratibu gani ambao Serikali imeupanga kwa ajili ya kidhibiti mifugo hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge amelieleza hapa lina ukweli kwa sababu idadi kubwa ya mifugo sasa hivi wamekuwa wakielekea upande wa kusini, ndiyo maana moja ya mipango mikakati ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunayo sasa hivi ni kuongeza maeneo ya malisho, tunapeleka mabwawa ili ku-control sasa ule ufugaji holela. Kwa hiyo, jambo hilo tumelipokea kwa umuhimu mkubwa na tutaleta mpango kazi kwa ajili ya maeneo hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yanayoonesha kwamba kikundi kimoja Jimboni Busanda kitapata shilingi milioni 69.4 hivi, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Jimbo la Busanda katika maeneo ya Ziwa Viktoria yana vikundi vingine katika Kata ya Nyamwilolelwa, Kata ya Bukondo na Kata ya Nyachiluluma: Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba, inaweza kuongeza vikundi vinavyokopesheka kwenye maeneo hayo ili huduma hii iweze kuwasaidia wananchi wengi kwa ajili ya maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nini mkakati wa Serikali kuhamasisha ufugaji wa samaki kwenye maeneo ambayo yako mbali na Ziwa Victoria? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza Mheshimiwa
Mbunge amezungumzia kuhusu kuongeza idadi ya vikundi katika jimbo lake. Bahati nzuri katika mwaka wa fedha tutaongeza idadi ya vikundi kufikia 893. Kwa hiyo, katika mwaka huu unaokuja basi na jimbo lake tutaongeza hivyo vikundi ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kuhusu maeneo ambayo yako mbali na Ziwa Viktoria, ni kwamba, tumeanzisha programu maalum ya ufugaji wa samaki kwa njia ya mabwawa ambayo sasa hivi katika mwaka uliopita tulikuwa na mashamba darasa kumi. Kwa hiyo, matarajio yetu ni kwamba mwaka wa fedha unaokuja, tutafanya hivyo. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati wa sasa na tutaendelea kuhimiza. Mfano mzuri, hata hapa Chamwino tunafanya shamba darasa katika maeneo ambayo ni kame. Kwa hiyo, huo ni mkakati ambao upo na ni endelevu, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wavuvi wa Mkoa wa Mara na hasa wale waliounda vikundi kwa ajili ya ufugaji wa vizimba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Zoezi la kutoa elimu ni endelevu. Kwa kuwa, vikundi bado viko vingi, basi tutawatuma tena wataalamu wetu waende kuwasaidia wafugaji wa Ziwa Victoria katika Eneo la Mara ambalo Mheshimiwa Mbunge ameainisha, ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Buyungu, wapo wafugaji wa samaki ambao wapo katika vikundi, lakini wapo wengine ambao ni mmoja mmoja, lakini wanapungukiwa maarifa na mtaji kwa ajili ya kuwawezesha kufuga kwa tija. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawawezesha hawa wafugaji waweze kufuga kwa tija? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge. Mkakati wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni pamoja na kuwezesha vikundi mbalimbali vya wavuvi na wavuvi binafsi. Ndiyo maana ukiangalia katika mwaka huu wa fedha tumetoa fedha nyingi na tunaenda kutoa mikopo ya maboti. Kwa hiyo, waliwemo wavuvi wa Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, Buyungu kule na wenyewe tutawafikia. Kwa hiyo, tuwaondoe shaka kwenye hilo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Nini mkakati wa Serikali wa kuhamasisha wanawake wengi zaidi wafuge kwa kutumia vizimba ili wawezekuepukana na umasikini? (Makofi)

NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inazingatia sana na imekuwa ikihimiza wanawake kujiunga katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba. Ndiyo maana sasa hivi katika kila programu ambayo tunaianzisha tumeweka pale threshold ambayo lazima kwenye kila program pawepo na wanawake wanaojiunga na shughuli hizo. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu yetu na tutaendelea kuisimamia kuhakikisha kwamba wanawake wanaingia katika shughuli hizi, ahsante sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika Wilaya ya Manyoni tuna kata tatu za Majiri, Maweni na Kijiji cha Kibumagwa ambako kuna uvuvi wa Samaki: Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba, tunaboresha uvuvi huu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni ambako na kwenyewe wanaendesha uvuvi wa samaki, anachotaka ni sisi kwenda kuboresha. Jukumu letu kubwa ni kwamba, moja, tutaendelea kuleta elimu pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa kupitia hii mikopo ya masharti nafuu. Kwa hiyo, tutafika katika kila eneo ambalo watu wetu wanajishughulisha na hizi shughuli za uvuvi pamoja na mifugo, ahsante sana.

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; je, Serikali ina mkakati gani wa kuvisaidia vikundi ambavyo vilikuwa vimeathirika na kutumia nyavu za wiring?

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Vikundi ambavyo vimeathirika na matumizi ya hizo nyavu, kwanza Serikali siyo waumini wa nyavu zile ambazo hazijaruhusiwa nchini. Pili, sasa hivi tumekuwa tukikaa na kampuni zinazotengeneza nyavu kuhakikisha kwamba wanatengeneza nyavu ambazo zime-meet kiwango ili kuondoa vurugu ambazo zimekuwa zikijitokeza na wavuvi wetu kupata hasara. Kwa hiyo, moja ya sehemu ya mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba, zana za kisasa zinapatikana kwa wavuvi wetu ili waweze kuvua kisasa, ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kule kwetu Mtwara wananchi wamehamasika kufuga majongoo Bahari kwenye vizimba, lakini tatizo kubwa ni vifaranga. Nataka kujua ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wafugaji wale wanapata vifaranga kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, namshukuru sana Mheshimiwa
Mbunge, amezungumzia suala la majongoo bahari ambayo ni moja ya bidhaa kubwa ambayo sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunaitangaza. Niwaondoe shaka wananchi wa ukanda ule. Sasa hivi moja ya mkakati wa Serikali, tunaanzisha kituo cha kuzalisha vifaranga katika Mkoa wa Mtwara ili kuhakikisha kwamba uzalishaji wake unakuwa wa haraka na kwa ukaribu zaidi. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati wa sasa na tunalifanya hilo kwa haraka iwezekanavyo.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba katika ziwa inaonekana ni njia moja nzuri ya kusaidia kupumzisha ziwa kwa wavuvi kuvua katika ziwa. Nini mkakati wa Serikali kusaidia wavuvi katika Ziwa Tanganyika kupata vizimba vya kutosha vya ufugaji wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bahati nzuri Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda anajua kabisa mkakati wa Serikali sasa hivi, baada ya kuwekeza sana katika Ziwa Victoria sasa tutafanya hivyo katika Ziwa Tanganyika pamoja na Ziwa Rukwa na Ziwa Nyasa. Ziwa Tanganyika tumeshakaa na Wabunge wa eneo hilo, na mwaka wa fedha unaokuja, mpango wetu kwa asilimia kubwa utakuwa katika ziwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kule Mufindi Kusini kuna Mabwawa ya Nzivi, Ngwazi pamoja na Kihanga; na mabwawa mengine kama yale ya Ihoanza ambayo yanachimbwa. Changamoto kubwa ambayo ilikuwepo pale ni mambo mawili; suala la vifaranga takribani milioni tano na zana za uvuvi: Je, Serikali iko tayari kupeleka vifaranga takribani milioni tano pamoja na mikopo ya vifaa vya uvuvi vya kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Uzuri ni kwamba, jambo hili ambalo amelizungumza Mheshimiwa Kihenzile, alishafika mpaka ofisini kwetu na tulizungumzanaye mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri na wataalamu wetu. Tulishamuahidi kwa sababu, kwa sasa tuna vifaranga kama milioni 15 na tuliahidi katika jimbo lake kupeleka minimum ya vifaranga milioni nne. Kwa hiyo, hilo lipo katika mpango, ikiwemo zana za kisasa kulingana na tutakavyovipata katika mwaka wa fedha unaokuja, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa mradi huu ulianza 2012 na 2013 mkandarasi akaondoka na gharama yake ni takribani bilioni 1.4 je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wakazi wa Ishololo Usule? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa mradi huu ni muhimu sana kwa wananchi wa Ishololo Kata ya Usule je, Waziri uko tayari kutembelea mradi huu ukaone ni jinsi gani wananchi wa Ishololo – Usule wanauhitaji wa mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Waziri yuko tayari kufika katika eneo la Ishololo – Usule ili kujionea hali halisi ya huo Mradi. Commitment ya Serikali ni kama katika jibu la msingi lilivyoandikwa kwamba katika mwaka wa fedha huu unaokuja 2023/2024 tutafanya tathimini na utekelezaji wa huu mradi utaanza 2024/2025.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa naomba nimtaarifu Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba hiyo miche ya migomba Hai haijafika kwa hiyo niombe sasa commitment ya Serikali kwa kuwa zao hili ni zao muhimu sana katika Jimbo la Hai ni lini mtatuletea miche mipya ya migomba kuondoa changamoto tuliyonayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa zao la mgomba linaenda sambamba na zao la vanila lakini zao la vanila kwa sasa bei imeshuka sana ukilinganisha na ile ya Dunia sasa hivi kilo moja ni shilingi 20,000 lakini inatokana na mazao yanayotokana na vanila inayotoka nje ya nchi yanakuja kwa wingi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia mazao ya vanila yanayotoka nje ya nchi ili zao hili liweze kuongezeka bei hapa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa kuwa sasa hivi Serikali inaendelea na utaratibu wake wa teknolojia ya chupa kwa maana ya tissue culture kwenye zao la mgomba kama ambavyo ameeleza na anataka commitment ya Serikali kwenye kupeleka miche hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu kwamba Serikali itapeleka kulingana na mahitaji ya eneo husika, kwa hiyo kusema lini exactly kwa wakati huu hatuwezi kutaja moja kwa moja lakini tuwahakikishie wananchi wa Hai kupitia Mbunge wao Serikali itapeleka miche katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Hai.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vanila ni kwamba tumechukua wazo la Mheshimiwa Mbunge Serikali itafanya tathimini ili kuweza kusaidia zao hilo la vanila.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali la nyongeza. Kumekuwa na hasara kubwa kwa wakulima wa migomba kwa sababu ya ugonjwa wa mnyauko. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa huu ili wakulima wa migomba wapate faida? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mkakati wa Serikali ndiyo pamoja na hizi tafiti ambazo zinafanyika za kuja na aina mpya ya mbegu ambayo itakuwa na uwezo wa kukabiliana na magonjwa mnyauko na huo ndiyo mkakati sahihi kwa sasa, kwa hiyo tuwahakikishie tu wananchi kwamba Serikali ipo kazini ili kuondoa hii adha ya wakulima ususani katika zao la mgomba.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nimesikiliza majibu ya Serikali na kwa takwimu alizozitoa Naibu Waziri ni wazi kabisa kwamba bado atujawa na dhamira ya dhati ya kuwasaidia wavuvi wa Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kufahamu ni mkakati upi wa Serikali kwa sasa kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi wa Ziwa Tanganyika kwa sababu na ninyi mmekili kuna changamoto ya zana ya kisasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika wanakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo utitiri wa leseni lakini changamoto ya vizimba pamoja na changamoto ya kanuni zilizopo. Mheshimiwa Waziri uko tayari kwenda kukutana na wavuvi uwasikilize ili mtakapo kuja na kauli au na utekelezaji uendane na uhalisia wa Ziwa Tanganyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu spika, ahsante sana. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwanza niko tayari kuambana pamoja na yeye Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika kwenda kujionea hizi adha ambazo Mheshimiwa Mbunge anazieleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili; mkakati wa Serikali ni pamoja na kuongeza zana za kisasa najua kwenye suala ya uwiano ndiyo ambalo limeleta changamoto. Lakini mwaka wa fedha ujao tumepanga hivyo hivyo maana yake tutaongeza kulingana na mahitaji ya maeneo husika ikiwemo mikopo, tutaleta vilevile vizimba ili kuongeza sasa wigo mpana wa wavuvi katika ziwa hilo, ahsante sana.
MHE. MAIMUNA SALUM MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kabisa kwamba asilimia kubwa ya wakulima wa zao hili ni wanawake, je, mkakati wa kutoa elimu pia kuwahusisha wanaume ili na wao waweze kujiongezea kipato kupitia zao hili ukoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa product itokanayo na zao la mwani ni muhimu sana kwa afya ya wananchi wote wakiwemo wanaume pamoja na wanawake. Je Serikali haioni haja sasa ya kutumia Vyombo vya Habari kuujulisha umma umuhimu wa zao hili ili wananchi wengi waweze kulilima na kupata mazao au kupata ajira zitokanazo na zao hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua umuhimu wa zao hili na jitihada mojawapo ya sasa na mkakati ambao tulionao katika maeneo ambayo yanazunguka Ukanda wa Pwani na wamekuwa wakituona maeneo mbalimbali ni kutangaza kwa makundi yote mawili wanawake na wanaume kuhakikisha wanashiriki katika zao hili la mwani. Kwa hiyo kazi hiyo tunaifanya na tutaongeza jitihada kuifanya ili ongezeko la watu wanaojihusisha na shughuli hizo wawe wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutumia Vyombo vya Habari, sasa hivi tumekuwa tukifanya ukiangalia TBC kuna vipindi vinavyohusisha kilimo cha mwani, lakini tutaongeza mara dufu zaidi ili tutanue wigo mpana ili vyombo vya Habari viweze kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo jambo hilo tumelipokea na tutalifanya, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Kigamboni ina ukanda wa bahari takribani kilomita 70, nataka kujua nini mkakati wa Serikali wa kukuza kilimo cha mwani na jongoo bahari katika Wilaya ya Kigamboni kama mkakati wa kuchochea uchumi wa bluu na kuongeza ajira nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mkakati wetu mkubwa ni kuhakikisha tunafikia maeneo yote ya ukanda wa pwani na ndio maana hivi karibuni tumepata fedha kutoka maeneo mbalimbali. Juzi tumesaini mkataba wa fedha karibu dola milioni 13 na watu wa USAID na sehemu ya hizo fedha ni pamoja na kuhamasisha kilimo cha mwani na majongoo bahari katika Ukanda wa Pwani ikiwemo Kigamboni. tumefanya hivyo Ifani, Tanga, kwa hiyo ni jambo ambalo lipo katika mchakato. Ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa, mnada huo hakuna choo, hakuna maji na wananchi wanapeleka mifugo yao mara kwa mara pale na mnakusanya fedha nyingi pale. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuchukua hatua ya dharura kujenga choo na kupeleka maji pale ikisubiria mpango mkubwa?

Swali la pili, je, kwa kuwa mnada huo pia Wizara ndiyo inakusanya fedha, kwa nini fedha hizo ambazo mnazikusanya isitumike kwa ajili ya kukarabati mnada huo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, jambo la kwanza tukiri changamoto ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza na akiwa anahitaji hatua za dharura. Nimuondoe shaka kwamba hizo hatua za dharura kwa mahitaji hayo kama ya vyoo pamoja na maji basi tutawaelekeza wataalamu katika maeneo hayo waweze kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, pili kuhusu makusanyo ya fedha ambazo zinakusanywa pale kwamba ndiyo zifanye ukarabati, nimwambie tu kwamba mnada ule unahitaji ukarabati mkubwa na ndiyo maana tunataka tufanye tathmini na tuujenge kwa viwango ambavyo vinastahili. Kwa hiyo tutalietekeleza hili kama ambavyo Serikali imepanga katika mipango yake, ahsante. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nimekuwa nikiuliza mara kadhaa kuhusu ujenzi wa Soko la Samaki katika Jimbo langu la Mchinga, Kata ya Mchinga lakini mara zote nimekuwa nikipewa tu ahadi, ahadi, ahadi! Sasa naiomba Serikali inipe commitment kuhusu suala la ujenzi wa hilo soko la Samaki, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza ninakiri kwamba Serikali ni kweli imekuwa ikitoa ahadi kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki katika Jimbo la Mchinga na jambo hilo mpaka sasa hivi bado halijafanyika, sababu za kutofanyika ni kwamba mpaka sasa Serikali tunatafuta fedha ili tufanye usanifu wa kina na baadae tulijenge soko hilo. Kwa hiyo, commitment ya Serikali iko pale pale kwamba soko hilo tutalijenga na wakati uliopo sasa ni kutafuta fedha, ninaamini kabla hatujamaliza hii miaka yetu miwili kuna hatua ambayo tutakuwa tumeifanya na kufikia. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii.

Kwa kuwa, Waziri wa Mifugo alishatembelea mnada wa Duka Bovu katika Wilaya ya Monduli na akaahidi ukarabati utaanza mara moja; je, ukarabati huu utaanza lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mnada katika eneo la Monduli ambalo Mheshimiwa Mbunge ameutaja upo katika mipango ya Serikali, tunachosubiri tu ni malipo ambayo tukiyapata kutoka Hazina basi sehemu ya fedha hizo zitakwenda kwa ajili ya ukarabati. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini mtaboresha miundombinu kwa minada ya Kibaya, Dosidosi na Sunya?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu awali, kwa sasa tunatafuta fedha ili tuhakikishe kwamba hiyo minada ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja tunaikarabati na kuitengeneza kwa viwango ambavyo vinavyotakiwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge waondoe shaka wananchi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itatekeleza kama ilivyoahidi. (Makofi)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Mnada wa Kata ya Soya ni kati ya minada mikubwa ambayo inafanya shughuli za uuzaji wa mifugo kwa maana ya mbuzi, ng’ombe, kondoo pamoja na punda lakini mnada ule miundombinu yake ni chakavu.

Je, Serikali mko tayari kuutembelea mnada ule nakujionea halia halisi ili muweze kutenga fedha itakayoweza kukarabati mradi huo ili wakulima wa mifugo waweze kuutumia mnada ule kwa tija na kwa maana ya afya kwa watumiaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko tayari kufika katika eneo la Soya, bahati nzuri ni karibu hapa tunaweza tukapanga tu baada ya muda wa Bunge tukafika na kujionea hali halisi ili tuweze kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati huo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. IDD K. IDD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa Halmashauri ya Msalala imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa mnada wa Kata ya Burige, sasa ni lini Serikali italeta fedha kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika mnada huo wa Burige?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwanza tuipongeze Halmashauri ya Msalala kwa kutenga fedha kwa ajili ya uzio wa mnada ambao Mheshimiwa Mbunge ameuainisha. Serikali tulishaweka commitment yetu kwa ajili ya kumalizia mnada huo, commitment yetu iko pale pale isipokuwa kwa sasa hivi tunaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha mnada huo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE.JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri kutoka Serikalini lakini napenda kuuliza swali moja la ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya uvuvi inaonekana kama sasa hivi ina mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi. Je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kujengwa mabwawa maeneo ya Malula na maene ya Majengo ambako kila mwaka mvua zinaleta mafuriko, yale maji yavunwe yajengwe mabwawa kwa ajili ya kufugia Samaki?
NAIBU WAZIRI WA UVUVI NA UFUGAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Kwanza nibampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua mchango wa Uvuvi katika uchumi wetu na hata maoni ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza hapa kwamba tuanze sasa kujenga mabwawa kwa ajili ya kuboresha sekta ya uvuvi ni sehemu ya mpango tulionao sasa hivi. Kwa hiyo, tunachokifanya sasa hivi ni kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba tunafika kwenye maeneo yote hususan maeneo ambayo hayana maji mengi kwa maana ya Maziwa na Bahari, ahsante sana.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa mamalishe wengi waliokuwepo katika soko la zamani wamekosa nafasi katika soko jipya. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya ujenzi wa dharula katika jengo la mamalishe ili kuwanusuru mamalishe waweze kufanya shughuli zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Bagamoyo ina wavuvi wengi ambao wanavua bila kuwa na utaalam. Je, Serikali ina mpango gani wa kutuma watu kuja kutoa mafunzo ya ubora na dhana bora ili wavuvi wasiweze kugombana na Serikali mara nyingi katika uvuvi wao?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza ni mpongeze vile vile Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo kwa kufatilia sana jambo hili na bahati nzuri katika soko analolieleza mimi binafsi nimefika na nimejionea hali halisi. Kwa hiyo, sisi kwa kushirikiana na Halmashauri yake tutazungumza na Halmashauri ili tuone namna bora ya kutekeleza huo udharura wa kuwasaidia wale mama lishe ambao walikosa nafasi katika soko la awali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu wataalam, nimhakikishie tu kwamba wataalam tunao na tutawatuma ili waweze kupeleka elimu ya utaalam wa uvuvi kwa wananchi wake, ahsante sana.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga soko la kisasa la samaki katika Kata ya Mbweni ili wananchi waweze kujipatia kipato lakini kuiletea Serikali mapato?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mheshimiwa Mbunge ameeleza jambo jema kuhusu soko la kisasa la uvuvi katika Kata ya Mbweni ambalo lipo katika sehemu ya mipango yetu kama Wizara, kikubwa tu sasa hivi ni kwamba tunatafuta fedha na tukishapata fedha katika maeneo yote ya kimkakati tutajenga kama ambavyo tunataka kutekeleza. Ahsante sana.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo na kuonesha jinsi gani Serikali ina wajali wavuvi. Maswali yangu mawili ya ziada ni kama ifuatavyo: -

Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu ya mikopo kwa wavuvi wadogo ili iende sambamba na mafunzo ya uvuvi wa kisasa?

Swali langui la pili; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha masharti ya mikopo hiyo haiwakwazi na kuwabana wavuvi wadogo? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Angelina Adam Malembeka kwa maswali mazuri na ya msingi.

Kwanza nimwondoe shaka kwa sababu haya ni maelekezo ambayo tumepewa na Marais wetu wawili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Mwinyi kwamba kabla ya mikopo hiyo ni lazima sasa tuwapatie watu elimu ambayo itawasaidia kutumia kwa usahihi mikopo hiyo ambayo itatolewa, kwa hiyo jambo hilo tutalitekeleza kabla mikopo hiyo kuwafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la masharti, jambo hilo ndio la msingi ambalo sasa hivi tumekuwa tukifanya kwamba tumepunguza masharti kwa kiwango kikubwa na asilimia kubwa ya hii mikopo haina riba, ni mikopo ambayo tunawawezesha tukianza na kuwapatia utaalam wa kisasa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wadogowadogo hasa Wilaya ya Ukerewe tayari wameshaunda vikundi na taratibu zote za mikopo wameshafata. Je, ni lini Serikali itawapatia mikopo ili waweze kununua nyavu na kuvua kwa halali na kuachana na uvuvi haramu?( Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge Dada yangu Mheshimiwa Furaha Matondo kwamba sehemu ya mikopo ya awamu ya kwanza ambayo tulitoa karibu asilimia 80 ya mikopo ilienda Kanda ya Ziwa kwa maana ya Ziwa Victoria, ni kwa sababu tu waombaji ni wengi na kiwango cha mikopo kilikuwa kidogo. Kwa hiyo sisi tutaendelea kuwazingatia kwa kadri ambavyo tunakuwa tukipokea fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hilo lipo katika mapango wa Serikali. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia matumaini hususan kwenye Balozi zetu. Ila tukumbuke kwamba tuna takribani zaidi ya miaka 30 sasa tokea mwani huu uletwe hapa kwetu Tanzania ambayo ni nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha mwani mwingi, lakini bado hatujaona jitihada kubwa za kuhakikisha mwani utambulika nchini na kuwa na thamani kwa wakulima wetu: Je, ni upi mpango wa Serikali sasa wa kushirikiana na taasisi ya sayansi na teknolojia iliyokuwepo Dar es Salaam pamoja na ile taasisi ya Zanzibar ambayo inashughulika na masuala ya mwani ili kuhakikisha mwani unakuwa na thamani nzuri na unatambulika? Hilo swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wizara imejipangaje sasa ili kutoa elimu kwa wakulima wetu ili wafahamu faida zinazopatikana kwenye huo mwani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kwa ukaribu zao la mwani. Zao la mwani ni moja ya mazao ya kimakakati katika Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi ambayo yanatokana na mazao ya bahari. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni pamoja na kuzitumia hizi taasisi ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge hapa kwa maana ya COSTECH pamoja na ZSF iliyoko upande wa Zanzibar. Malengo haya tutaendelea kuyasisitiza kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha sasa huu mwani unakuwa maarufu siyo kwa Tanzania peke yake, ni mpaka nchi za pembezoni ili kuongeza biashara kubwa na pato la Taifa kwa ujumla kwa pande zote mbili; Tanzania Bara pamoja na Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, hilo ndiyo mpango wetu wa sasa kuhakikisha kwamba tunaongeza engagement ya watu katika zao hili la mwani ikiwemo vijana, akina mama pamoja na wanaume ambao watahitaji kuingia katika zao hili. Kwa hiyo, tutatoa elimu na tutaongeza wataalam kwa ajili ya kusaidia zao la mwani. Ahsante. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwani ni zao ambalo likisanifiwa linaweza likatoa bidhaa nyingi ambazo zinatoa faida kwa wakulima: Je, ni lini Serikali itawapelekea viwanda vidogo vidogo katika yale maeneo ambayo yanazalisha mwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Moja ya mpango wa Serikali ni pamoja na kuwawezesha wakulima wa mwani na ndiyo maana ukifuatilia katika Hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambayo aliitoa hapa Bungeni, moja ya mikakati tuliyonayo ni pamoja na kuwanunulia vifaa vya kisasa na kuongeza tija katika zao la mwani ikiwemo kuwapatia viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuzalisha kama sabuni, mafuta yanayotokana na mwani. Kwa hiyo, hayo ni sehemu ya mpango ambao Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunayo. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina swali dogo tu la nyongeza. Tunafahamu kwamba mwani ni muhimu sana na unaleta fedha za kigeni lakini mwani unalimwa sana na wanawake na hata kule Jimboni kwangu Mchinga, wanawake wanalima mwani, lakini bei yake ni ndogo ndogo sana. Serikali ina mpango gani juu ya hili jambo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nampongeza Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa Jimbo la Mchinga kwa kuwa Halmashauri yake ya Mchinga hapa nchini ni moja ya halmashauri ambazo zinaongoza kwa uzalishaji wa zao la mwani. Kwa hiyo, hilo linafahamika, na ni kweli zao la mwani wakulima wakubwa ni akina mama. Sisi kama Serikali tunakiri kwamba bado changamoto ya bei ipo chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati yetu tuliyonayo ni pamoja na majibu ya swali la msingi kama tulivyojibu kwamba, ni kutangaza zao la mwani, kutafuta masoko nje ya nchi hususan katika nchi ya China ambapo ndipo wanunuzi wakubwa wa zao hili ili kuhakikisha kwamba sasa tunaongeza bei kwa wakulima wetu wa ndani ili kupata tija na kuongeza pato la Taifa kwa nchi nzima. Kwa hiyo, hilo liko ndani ya mipango yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kuendelea kuwapatia vijana wetu ajira; na kwa kuwa tumeona sehemu kubwa ya ranchi bado hazitumiki.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawia vijana wetu maeneo ya kufuga na wakawafundisha ufugaji bora ili waweze kuwekeza sawa na wale wenzetu katika sekta ya kilimo walivyofanya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mpango tulionao sasa hivi ni pamoja na kuongeza maeneo na kugawa maeneo ambayo hayatumiki kwa vijana ambao sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumepanga kufanya hivyo katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo, liko kwenye mpango na tunakwenda kulitekeleza, ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa, mradi huu wa skimu ya umwagiliaji ya Karema umechukua muda mrefu zaidi ya miaka kumi na swali kama hili nimeliuliza hapa Bungeni zaidi ya mara tano.

Je, Serikali sasa ina mkakati gani wa kwenda kubomoa ile miundombinu ambayo waliiweka ambayo haiwasaidii wananchi na kabla ya kuweka mradi ule wananchi walikuwa wakinufaika wanapata mazao yao. Lini Serikali wataenda kubomoa ule mradi?

Swali la pili, kwa kuwa ndani ya miaka kumi wananchi wamekuwa wakilima wakipata hasara kwa sababu ya miundombinu iliyowekwa mibovu. Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa fidia wakulima hao ambao wamelima kwa miaka kumi wakiteseka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kwa ukaribu juu ya ujenzi wa mradi wa Karema wa umwagiliaji, lakini nimuondoe shaka kwamba ndiyo maana ukiona katika jibu la msingi tumeandika hapa kwamba mradi huu wa Karema ambao sasa hivi uko katika hatua za mwisho za usanifu wa bwawa pamoja na miundombinu ya umwagiliaji na tumeahidi kabisa hapa kwamba utakamilika katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Kwa hiyo, nimuondoe shaka kwa sababu Serikali imeona hiyo kero ya wananchi na katika mwaka wa fedha unaokuja litatekelezeka kama ambavyo Wizara ya kilimo imeahidi na itafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu hasara ambayo wananchi wameipata kutokana na kushindwa kulima vizuri katika eneo lao, nimwambie tu kwamba ukweli ni kwamba hatuwezi kulipa fidia kwa hasara ambazo zilitokana na wao kulima eneo lile, lakini Serikali imekuwa ikizingatia umuhimu wa wakulima nchini na ndiyo maana umeona Serikali katika ku-boost kilimo ikawa imekuja na mradi wa kutoa ruzuku za pembejeo, yote hii ni kutaka kuwanufaisha wananchi ambao wanapata faida kutokana na ruzuku hizo. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha kilimo nchini ili kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kupata faida. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kondoa, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu majosho haya yanalenga katika kuboresha afya za mifugo ambayo mwisho wa siku tunapata kitoweo kizuri. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba ujenzi huo unasimamiwa vizuri na majosho yale yakamilike kwa muda uliopangwa?

Swali la pili, kwenye Jimbo la Singida Mashariki katika Kata ya Siuyu tulikuwa na josho ambalo sasa hivi limeingiliwa na eneo la Kanisa la RC pale Siuyu na tuliomba lihamishwe liende eneo lingine kwa sababu linakosa sifa ya kutumika pale. Tumeshatenga eneo katika Kijiji cha Siuyu na tuliomba muda mrefu zaidi ya miaka mitatu sasa. Ni lini Serikali itajenga josho kwa ajili ya kutoa huduma ya mifugo katika Kata ya Siuyu. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba amepongeza hii jitihada ambayo tumeifanya lakini vilevile ametaka kuona kwamba kunakuwa na usimamizi mzuri na kuhakikisha haya majosho yanakamilika ili kuimarisha afya ya mifugo. Kwa hiyo, nimuondoe hofu kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Waziri Ulega pamoja na mimi Msaidizi wake tunaahidi kabisa kwamba haya yote yaliyopangwa katika mwaka wa fedha unaokuja na yale ambayo hayajakamilika tutahakikisha katika mwaka wa fedha unaokuja yanakamilika kwa wakati kwa sababu hili ndiyo lengo letu na ndiyo lengo la Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa josho katika Kijiji cha Siuyu ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja hapa basi naomba jambo hilo nilipokee kwa sababu nitaangalia katika orodha ambayo tunayo hapa kama tumelitenga katika mwaka huu fedha na kama halipo tuone namna gani tunatafuta fedha ili kuliweka katika moja ya vipaumbele vyetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Wilaya ya Liwale ndiyo Wilaya katika Mkoa wa Lindi imepokea wafugaji wengi sana lakini hakuna miundombinu ya majosho wala malambo. Je Serikali iko tayari kutujengea majosho na malambo kwenye Kata ya Lilombe na Kata ya Ndapata, Kata ambazo ndizo zimetengwa kwa ajili ya kupokea wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Liwale ni miongoni mwa Wilaya ambazo zipo katika mpango wetu katika huu mwaka. Kikubwa tutaangalia katika orodha ili tuone maeneo gani ambayo tutayapa kipaumbele. Ahsante.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kuna swali nauliza.

Mheshimiwa Spika, wale Mawaziri nane walikuja kufanya nini? Leo tunapokuja kusema kwamba Serikali haikuelekeza, haya kama huo ni mgogoro, je tutautatua lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; jambo la kwanza kwenye ile Kamati ya Mawaziri nane ambayo ilizunguka maeneo mbalimbali nchini, kila eneo lilikuwa linapelekewa taarifa kuhusiana na mahitaji ya eneo husika, sasa katika shamba la Kitaraka Holding maamuzi ya Serikali ambayo Kamati ya Mawaziri nane iliyatoa pale ni kwamba sasa ifanyike tathmini ambapo katika ile tathmini tutajua lile shamba wananchi wameingilia kwa kiwango gani ili sasa tuweze kumega sehemu ya lile eneo kuwakabidhi wananchi na sehemu ya eneo ibaki katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kazi ambayo ilikuwa inaifanya hapo awali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa hivi kinachofanyika, Kamati ya Mawaziri tulikaa na Mheshimiwa Waziri ikaundwa tume maalum ambayo inafanya hiyo tathmini na baada ya hiyo tathmini kukamilika sisi tutakwenda katika eneo hilo kwenda kutoa maamuzi ya mwisho kwa ajili ya wananchi. Kwa hiyo, hiyo ndio kazi kubwa ambayo imefanyika.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru Serikali, majibu ni mazuri sana. Sasa swali la kwanza, kwa kuwa ujenzi umefanyika kwa muda mrefu na sasa kuna cracks nyingi zimetokea pale. Je, Wizara iko tayari kwenda kufanya ukarabati eneo lile ili uzinduzi utakapofanyika eneo lile liwe linafaa kwa ajili ya mnada, swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba kukuuliza Mheshimiwa Waziri uko tayari kuambatana na mimi baada ya Bunge hili twende pale Ngara, Murusagamba tukazindue huo mnada? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; cha kwanza nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kwamba mnada umekamilika na hayo mapungufu machache ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha tutayarekebisha kabla ya kuzindua na mimi niko tayari kwenda mara baada ya Bunge lako tukufu kuahirishwa, ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na mkakati wa jumla wa Serikali wa kukarabati zahanati 18 ndani ya Jimbo la Kwela lakini katika Kijiji cha Kavifuti, Kata ya Miangalua na Kijiji cha Kiandaigonda zahanati zake ni kama magofu kabisa zimechakaa. Je, Serikali wana mpango gani wa dharura kunusuru walau wananchi wapate huduma sehemu iliyo salama?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wa Kijiji cha Kapewa, Mtetezi, Mumba pamoja na Mtapenda wametumia nguvu kubwa kujenga zahanati ambayo imebaki fedha kidogo kumalizia. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka fedha ili wananchi wapate huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa anafanya kazi nzuri sana kuwasaidia wananchi wa Jimbo lake la Kwela hususan katika kufatilia haya masuala ya zahanati. Bahati nzuri maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge, anayataja hata mimi binafsi nimewahi kufika na nimeona hiyo changamoto na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilishaahidi kuyafanyia kazi. Katika sehemu ya mpango wa dharura hususan katika maeneo ya Miangalua, maeneo ya Mpui hayo yapo katika mpango wa Serikali. Kwa hiyo kikubwa sasa ni kuendelea kuyafuatilia ili yaweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya Mtapewa ambapo kuna nguvu kubwa ya wananchi moja ya mpango wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ambayo wananchi wameweka nguvu yao, itapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia maboma hayo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa afya za wananchi ni muhimu na ni uwekezaji wa Serikali kwa ajili ya nguvu kazi, kumekuwa na jitihada za wananchi kujenga zahanati katika maeneo mbalimbali kwa nguvu zao na kumekuwa na bajeti ndogo kwenye halmashauri baadhi ambazo hazina uwezo. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuweza kutenga fedha kwa ajili ya kumalizia zahanati zilizojengwa na wananchi katika maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kama nilivyojibu kwenye swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, kwamba moja ya mkakati wa Serikali hususan katika maeneo ambayo kuna nguvu za wananchi ni kupeleka fedha na kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni kutafuta fedha kwa ajili ya kumalizia maeneo ambayo wananchi wameweka nguvu zao. Kwa hiyo katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge, ameyaainisha yapo katika mpango ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Barabara ya Kalenga – Wasa - Mafinga ni barabara muhimu sana kwa uchumi katika Mkoa wetu wa Iringa. Je, katika kilometa 100 za Mradi wa RISE kwa nini wasipatiwe japo kilometa 10 tu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Barabara ya Itimbo – Kitelewasi inapita katika milima na miteremko mikali, hivyo inahitaji kujengewa makalavati. Je, Serikali ipo tayari sasa kujenga makalavati ili wananchi wa Kitelewasi na Itimbo waweze kupita kwa uraisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Sika, ahsante sana. Kwanza natambua kwamba kuna mahitaji makubwa ya ujenzi wa barabara hususani katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Barabara ya Kalenga mpaka Mafinga ambayo ina urefu wa kilometa 100 hususani hizi za RISE na amekuwa akiomba kilometa kumi, niseme tu kwamba zile barabara zimeshawekwa katika mpango wake. Kwa hiyo kikubwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI itazingatia katika mipango ijayo ili kuona sasa tunatafuta hizo kilometa 10 waweze kujenga katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Barabara ya Itimbo – Kitelewasi ambayo ina mteremko mkali, mahitaji ya Kalavati, nafikiri kwa kutumia fedha za Mfuko wa Dharura, Ofisi ya TARURA Mkoa wa Iringa tuwaelekeze tu kwamba kulingana na mahitaji ya maeneo hayo, waipe kipaumbele barabara hii, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuona potential iliyoko kwenye Ziwa Viktoria na haja ya kulitumia ziwa hili kuweza kutatua changamoto za kiuchumi na ajira kwa vijana walioko katika Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza fedha hizi zimetengwa takribani Shilingi bilioni 20 kwa mwaka wa fedha 2022/2023; na tunavyozungumza sasa utaratibu ulianza tangu mwaka 2022 na sasa tumebakiwa na kama siku saba tu kumaliza mwaka huu wa fedha 2022/2023; naomba commitment ya Serikali: Ni lini hasa utekelezaji wa mradi huu utaanza kwa sababu, taratibu zote za awali zimeshatimia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa vile tayari kuna sintofahamu na changamoto fulani kwa vijana wa Mwanza na Mikoa yote ambayo inahusika na mradi huu ambazo baadhi yake nilizungumza jana: Je, Serikali au Waziri na wasaidizi wake wako tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili la Bajeti kwenda kuwasikiliza vijana wanaonufaika na mradi huu juu ya changamoto na sintofahamu zao kuweza kuzitatua? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia jambo hili kwa ukaribu kabisa. Nimhakikishie tu kwamba tuko katika hatua za mwisho za maandalizi za ugawaji wa hivi vifaa, hususan maboti kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa Victoria. Uzinduzi huu tutafanyia huko huko ukanda wa Ziwa Viktoria. Kwa hiyo, tuko katika hatua za mwisho na ninaamini ndani ya muda mfupi Wizara ya Mifugo na Uvuvi itataja hiyo tarehe rasmi ya lini sasa tunatoa vifaa hivyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuambatana na Mheshimiwa Mbunge, mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri tuko tayari muda wowote mara baada ya Bunge lako kuahirishwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kuhusiana na eneo hili, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mkakati wa Serikali umejikita kwenye wafugaji wapya wanatoka vyuoni. Ni nini mpango wa kuwawezesha wafugaji hawa wa sasa ambao wengi wanafuga kienyeji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; upande wa nyama ya kuku kumekuwa na tatizo la vifaranga mara nyingi. Nini mpango wa Serikali kuhakikisha vifaranga vinapatikana ndani vyenye ubora ambao nyama yake inaweza pia kuuzwa nje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia tasnia hii ya nyama nchini kwa umakini mkubwa. Nimwondoe shaka tu kabisa kwamba mipango ya Serikali siyo kwa vijana wanaotoka vyuoni, ama vijana wa kisasa pekee, ni pamoja na wale ambao wamezoea kufuga kwa mifumo ya kiasili. Kwa hiyo, mipango yetu inajumuisha makundi yote mawili na tunaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba tunaboresha mbari za mifugo kwa wafugaji wote nchini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa vifaranga, ndiyo moja ya mikakati ambayo sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunayo sasa hivi kuhakikisha tunaongeza uzalishaji ili vifaranga vipatikane kwa wingi na tuwasaidie wafugaji wetu, hususan wa kuku, na mifugo mingine, ili tuweze kuuza nje ya nchi kwa wingi mkubwa, ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize Wizara, kwa nini katika jimbo zima hakuna josho la kuogeshea wanyama?

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mikakati ambayo tunayo katika mwaka wa fedha unaokuja, 2023/2024, Halmashauri ya Tarime ni miongoni mwa halmashauri ambazo zitapata majosho katika yale majosho ambayo tuliyatangaza katika fedha ambazo tuliziweka katika mpango, shilingi bilioni 5.7.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wazee wa Wilaya ya Nyasa walipokutana tarehe 5 Machi, 2023, waliniagiza na walisema kwamba wanaona Wilaya ya Nyasa inadharaulika kwa sababu miradi yake inachelewa kupatikana na ikianza haiishi kwa wakati na hata kama ikionesha dalili ya kuisha haipewi vifaa vinavyotakiwa.

Je, Serikali haioni haya mawazo ya wazee wa Wilaya ya Nyasa yana ukweli kiasi fulani? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa pia kulikuwa kumejengwa karakana kwa ajili ya kutengeneza boti toka mwaka 2015 mpaka leo karakana hiyo haifanyi kazi iliyokusudiwa. Je, ni lini sasa na hiyo karakana itaweza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Jambo la kwanza nitambue maoni ya Mheshimiwa Mbunge ambayo yametolewa na wazee wake na nimhakikishie tu kwamba Serikali haidharau wananchi wa Nyasa wala wananchi katika maeneo yoyote yale. Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo maana tumemuelezea kwanza katika jibu la msingi, kuhakikisha kwamba soko hilo linafunguliwa na ndiyo maana zabuni imeshafunguliwa. Tunamaliza tu mchakato atakwenda atajenga na baada ya kujenga tutalifungua soko hilo ili liweze kuhudumia wananchi wa Jimbo la Nyasa kupitia Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Spika, suala la karakana na lenyewe basi tumelipokea, mimi mwenyewe binafsi nitafanya hiyo jitihada binafsi ya kuhakikisha inafunguliwa kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ningependa kufahamu ni lini Serikali mtapeleka fedha kumalizia ujenzi wa soko la Samaki Kata ya Mkinga, toka mmeahidi mwaka jana hakuna kitu kinaendelea?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunatambua kuhusu mahitaji ya Soko la Mkinga na tuliahidi katika bajeti. Changamoto ambayo ilikuwepo ni kwamba fedha zilikuwa hazijatoka lakini jambo hilo liko katika mpango na nafikiri Wizara ya Fedha itakapokuwa imeleta fedha kwa wakati huu, tutazileta kwa wakati na kuhakikisha soko hilo linajengwa.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ningependa niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tunafahamu katika shule zetu nyingi za msingi miundombinu muhimu kama maji na umeme haipo. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha miundombinu hii inapewa kipaumbele katika shule zetu hizi hususan katika Mkoa wangu wa Songwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; natamani kufahamu, huko kwetu shule nyingi za msingi zimekuwa hazina vyoo, hususan kwa Mkoa wangu wa Songwe na hasa zaidi katika Wilaya yangu ya Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baadhi ya miundombinu ya maji pamoja na umeme ambayo tunayo ina changamoto kubwa. Moja ya Sera ya Serikali ni kuhakikisha sasa hivi kwenye taasisi zote hizo za kielimu zinapatiwa umeme pamoja na maji. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hilo lipo katika mpango wa Serikali na ndio maana sasa hivi unaona katika usambazaji wa umeme wa REA, wamekuwa wakiwapa vipaumbele taasisi hizo ambazo nimeziainisha hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na maeneo mengi kukosa vyoo hususan shule zetu, katika bajeti ya mwaka huu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo. Miongoni mwa vyoo tutakavyojenga ni katika Mkoa wa Songwe ambao yeye Mheshimiwa Mbunge ni Mbunge ambaye tunawakilisha pamoja. Ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Shule nyingi za Msingi za Mkoa wa Lindi ni za zamani, zimejengwa mwaka 1947 na zingine kabla ya hapo, ikiwepo ya Lionja, Ngunichile, Kivinje, Ntua na kwingineko. Je, Serikali ina mkakati gani katika shule hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu katika mpango ambao tathmini inafanyika ni pamoja na hizo shule ambazo ameziainisha katika Mkoa wa Lindi na tathmini yetu itakapokamilika tutaainisha maeneo yote kila mmoja ni wakati gani utatekelezeka. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwenye hilo. Ahsante sana.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Tabora Mjini lenye kata 29 lina matatizo kama hayo, lina shule nyingi sana za msingi ambazo ni kongwe na wananchi wamekuwa wakifanya juhudi ya kuzikarabati kwa juhudi zao wenyewe. Je, ni lini hasa huo mpango utaanza huu wa kuzisaidia kukarabati hizi shule kongwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu umeanza mwezi Aprili mwaka huu na utakamilika mwezi Julai mwaka huu. Mara baada ya kukamilika, tunaanza utekelezaji. Nimhakikishie tu kwamba tuko ndani ya mwaka wa utekelezaji na tutafikia shule zote ikiwemo hizi ambazo yeye ameziainisha. Ahsante sana.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Mbozi ni moja ya Wilaya inayoongoza kuwa na shule nyingi za msingi, shule 179, lakini kiasi cha fedha za miundombinu na ukarabati zinazotoka Serikali Kuu kuja Wilaya ya Mbozi ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya shule 179. Sasa kwa nini Serikali isiangalie Wilaya ya Mbozi kwa jicho la tatu na kuangalia idadi ya hizi shule nyingi za msingi na kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya miundombinu na ukarabati kwa ajili ya shule hizi za msingi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba Jimbo la Mbozi lina shule nyingi na lina majengo mengi ambayo bado hayajakamilika. Nimhakikishie Mbunge tu kwamba moja ya vigezo ambavyo tutavitumia sasa hivi ni kuhakikisha yale maeneo yenye uhitaji mkubwa tunayapa kipaumbele ikiwemo Jimbo la Mbozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanz; Mji wa Kondoa Mjini una hali mbaya sana hasa kipindi cha mvua kwa kuwa na mafuriko katikati ya mji. Je, Serikali inaweza ikatupa fedha kwa ajili ya kujenga mitaro kuzuia yale mafuriko kutokea mitaa ya Uwanja wa Puma mpaka katikati ya mji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tuna barabara ya kilomita kama moja kutoka barabara kuu kwenda katika Ofisi za Mkurugenzi maana yake majengo ya halmashauri . Je, Serikali ipo tayari kusaidia fedha kwa ajili ya kuweka lami kwa sababu ya ule muundombinu uliowekwa pale, jengo zuri la thamani kubwa lakini barabara ya tope?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba katika bajeti ambayo tumepitisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, sehemu ya fedha ambazo tumeziweka ni pamoja na Jimbo la Kondoa na sehemu ya fedha hiyo itahusika katika ujenzi wa mitaro ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Kwa hiyo nimwondoe shaka tu kwamba kwa kuwa tumeshapitisha bajeti, basi tutakwenda kutekeleza kama ambavyo yeye amehitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusiana na mahitaji ya kilomita moja kutoka barabara kuu ya lami kwenda katika jengo lao la halmashauri, niseme tu ombi hili tumelipokea japo tunatambua kwamba Mradi wa TACTIC sehemu mojawapo ni kutekeleza mradi huu ambao Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wakati ule ilijenga Barabara ya Mombasa- Mazini-Moshi Bar na kipindi hiki barabara hii imeharibika sana hasa kipande cha kuanzia pale Mombasa mpaka Transfoma. Je, Serikali haioni ni wakati sasa kufanya ukarabati wa dharura wa kipande kile cha barabara ili kuwapunguzia wananchi kero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba ni kweli barabara ile ilijengwa na sasa hivi kwa kweli imeharibika kutokana na adha za mvua. Nimhakikishie Mbunge tu kwamba, tunawaagiza watu wa TARURA, Mkoa wa Dar es Salaam waende wakafanye tathmini na kutafuta fedha kwa ajili ukarabati wa barabara hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali la kwanza; kwa kuwa majibu ya Serikali yanaonesha kabisa fedha iliyotengwa ni ndogo kulinganisha na miradi ya wananchi. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kuongeza fedha ili kuweza kumalizia miradi ambayo nguvu za wananchi zimetumika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuona miradi hiyo ama nguvu hizo za wananchi kwa kuanzia tuanze na Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba wananchi wamefanya kazi kubwa sana ya ujenzi wa maboma na fedha ambayo tumetenga bado haikidhi, lakini Serikali inaendelea kutafuta fedha kuhakikisha kwamba tunakamilisha na kuongeza jitihada ambazo wananchi wamezifanya. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwamba, tutaendelea kuongeza kwa mfano mwaka huu na mwakani mwaka wa fedha unaofuatia, Serikali itaongeza fedha ili kuhakikisha maboma hayo yanakamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, niko tayari kwenda kujionea hiyo miradi Mkoa wa Manyara nikiongozana na Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum pamoja na Wabunge wote wa Mkoa wa Manyara. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kumalizia zahanati na kuna baadhi ya zahanati ambazo tumeshakamilisha katika Wilaya ya Nyangh’wale. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kupeleka vifaa tiba na kuweza kuzifungua zahanati hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Nassoro Amar, Mbunge wa Nyangh’wale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna maeneo mengi ambayo mpaka sasa wameshamaliza vituo vya afya pamoja na zahanati. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumeshafanya uagizaji wa vifaa tiba na baadhi ya tender zipo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuagiza hivyo vifaa. Kwa hiyo mara vifaa hivyo vitakapofika basi tutapeleka katika vile vituo ambavyo vimekamilika ili kuhakikisha kwamba zahanati hizo pamoja na vituo vya afya vinafunguliwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamalizia Hospitali ya Wilaya Sumbawanga Mjini inayoitwa Isyofu, ambayo bado wodi hazijaisha. Ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili wodi zijengwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hospitali ya Sumbawanga Mjini nilifika mimi mwenyewe pale na nilijionea adha ambayo inaendelea pale na najua bado haijakamilika. Commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha ili tuongezee na kuikamilisha ile hospitali kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Halmashauri wa Mji wa Mafinga Kata ya Bumilainga kwa kufuata maelekezo ya Serikali kwamba tutenge fedha za mapato ya ndani kujenga kituo cha afya, tumetekeleza na tuko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha Kituo cha Afya cha Bumilainga. Je, Serikali mpo tayari kutuletea vifaa ili kituo hichi cha afya kianze kazi, ambacho kinahudumia pia Halmashauri ya Mufindi anakotoka Mheshimiwa Mwenyekiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mhheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Cosato Chumi Mbunge wa Mafinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kwamba mara baada ya kituo hicho cha afya kukamilika tupo tayari kupeleka vifaatiba pamoja na Wauguzi ili kiweze kufunguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. SYLVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Pwani ni mkoa mkongwe toka mwaka 1975 na maombi haya yalipelekwa Serikalini hadi kwa Katibu Mkuu Kiongozi toka mwaka 2016 tukiwa ni pamoja na Geita na Kahama.

Mheshimiwa Spika, hawa wenzetu walikwishapata Manispaa, vigezo alivyovizungumzia Mheshimiwa Naibu Waziri vinanipa utata, kwa sababu ukiangalia Manispaa ya Kigamboni wana kata nane, lakini wamepewa Manispaa na hadi sasa vigezo vyote alivyovizungumza hapo Mji wa Kibaha umekwishavitimiza. Sasa je, ni kwanini hatujapatiwa manispaa na ni lini tutapata Manispaa ya Mji wa Kibaha ili tuweze kufikia hadhi tunayostahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, sababu ambayo imechelewesha Halmashauri ya Mji wa Kibaha kupewa hadhi ya Manispaa ni kutokukidhi vigezo ambavyo tumeviainisha na Halmashauri inavifahamu. Kwa hiyo, ndiyo ilikuwa sababu kubwa ambayo imesababisha kuchelewa kwa Halmashauri hiyo.

Lakini lini itapewa hadhi ya Manispaa kwa sasa hivi kwanza Serikali tunajikita katika kuboresha maeneo yaliyopo na naamini kwamba mara baada ya Halmashauri ya Kibaha itakavyokuwa imekidhi vigezo na mamlaka husika kuona haja ya kuipandisha, tutafanya hivyo. Ahsante sana.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Mji wa Vwawa una Mamlaka Ndogo ya Mji wa Vwawa na Mkoa wa Songwe kwa muda mrefu umekuwa hauna Manispaa.

Je, ni lini Serikali utaupandisha hadhi Mji wa Vwawa ili iwe Manispaa kwa ajili ya kuhudumia Mkoa mpya wa Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge anayezungumza anajua kabisa katika eneo alilolitaja na mimi mwenyewe nina interest nalo kwa sababu ni mkoa wangu. Ni moja ya mjadala ambao tumekuwa tukijadili katika vikao vya RCC. Kwa hiyo, ambacho tulishauri Mkoa wa Songwe ni kwamba wafuate zile taratibu ambazo zimeianishwa kuleta maombi, halafu yatapelekwa kwa mamlaka, wakati huo sasa hivi mamlaka imejikita zaidi kwenye kuboresha. Kwa hiyo, tufuate taratibu na baada ya taratibu kukamilika basi tutashauri mamlaka kuona namna bora ya kulitekeleza hili. Ahsante.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, Serikali haioni haja ya kushughulikia mkanganyiko na mtanziko uliopo kuhusu dhana na mipaka ya Jiji la Dar es Salaam, na kama inaona haja hiyo lini itafanya hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ameainisha dhana ya kuangalia upya mipaka katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na ukubwa wake na umuhimu wake kwa Taifa, sisi tumepokea jambo hilo na tutakwenda kushauriana na timu yetu tuone muda gani tunaweza tukalitekeleza ili tuangalie hivi vigezo ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha ahsante.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Iringa Vijiji ina majimbo mawili ambayo ni Kalenga pamoja na Isimani na tayari upande wa Isimani mwenzangu alishaomba tupate Halmashauri. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ombi hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kupandisha hadhi majimbo kuwa Halmashauri yanafuata vigezo, na Halmashauri ambazo hapo nyumba zilikidhi vigezo zilipewa hayo mamlaka. Kwa hiyo, hili lililoombwa na Halmashauri ya Isimani maana yake lipo katika utekelezaji, kwa hiyo, sisi kazi yetu ni kuendelea kupitia vigezo na jambo hili litakapokuwa limekamilika maana yake tutatangaza kupitia sheria ambazo ziko nchini. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ofisi ya jimbo ni nyenzo muhimu sana katika utekelezaji majukumu ya jimbo. Ofisi nyingi sana za jimbo zimekuwa hazina samani wala vitendea kazi vya ofisi. (Makofi)

Je, Serikali haioni sababu ya kuimarisha ofisi kusudi iwe inafanya kazi zake kikamilifu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itatoa fedha ya kutosha kuhakikisha Mfuko wa Jimbo unafanya kazi inayostahili jimboni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba ofisi nyingi za Wabunge katika majimbo yao hazina samani na tunaziagiza Halmashauri zote nchini kupitia kwa Wakurugenzi kutenga fedha na kuzikamilisha ofisi hizo ili Wabunge waweze kuzitumia. Kwa hiyo, hilo ni agizo kwa Halmashauri na wakurugenzi wote.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili amezungumzia kuhusu ongezeko la fedha katika Mfuko wa Jimbo. Nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiyo anasimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuongeza fedha za Mfuko wa Jimbo kwa mwaka huu kutoka shilingi bilioni 11 ambazo zilitumika mpaka shilingi bilioni 15.99 kwa hiyo ni ongezeko kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika mwaka unaouja huu kutakuwa na ongezeko la fedha za Mfuko wa Jimbo katika majimbo yote nchini. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na majimbo ambayo hayana ofisi kabisa mpaka sasa ikiwa ni sambamba na kuona kama wanaweza wakaziboresha ofisi ambazo zilijengwa na Bunge na zimechakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Wabunge wengi bado hawajafikiwa kupata ofisi kamili katika maeneo yao na Serikali tumekuwa tukitenga bajeti kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha kuhakikisha tunajenga. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwa muda ambao Serikali imejipangia, ninaamini Wabunge wote watapata ofisi kulingana na hadhi yao. Ahsante sana.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii nzuri na muhimu sana, naomba kuuliza swali la nyongeza kwamba muda mwingi Wabunge wako hapa Dodoma kwa shughuli za Kibunge na kama unavyofahamu Mbunge wakati wote anafanya kazi za wananchi. Lakini kwa hapa Dodoma Wabunge hawana ofisi, ofisi zao zimekuwa ni magari, ukienda kwenye gari unakuta amerundika makabrasha mengi ambayo angepaswa kuwa na ofisi ili aweze ku-attend issues mbalimbali za kibunge.

Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea ofisi Wabunge hapa wawapo kwenye shughuli zao za Kibunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameleta mapendekezo, na kila mapendekezo yanahitaji bajeti, tunahitaji kwanza kufanya tathmini na kuona uwezekano wa utekelezaji wa jambo hilo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tumepokea jambo hilo, tutakwenda kulifanyia tathimini, ahsante.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza ninasikitika kwamba majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni ya uwongo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Geita una master plan na ilizinduliwa na Mheshimiwa Waziri mwaka 2020 na zoezi hilo ni la siku nyingi zaidi ya miaka miwili na kitu iliyopita na Mji wa Geita umepimwa zaidi ya asilimia 70, kwa hiyo, kwa kuwa majibu yake ni ya uwongo, labda ni ulize tu swali.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni lini sasa wataenda kuangalia upya vigezo kwa sababu jibu alilokuja nalo siyo sahihi wataenda kuangalia upya vigezo vya kuupandisha Mji wa Geita kuwa Manisapaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Miji mingi iliyopanishwa kuwa Manispaa suala la vigezo vya kupimwa halikuwepo na iko Miji mikubwa kwa asilimia kubwa ni squater, hili sharti la kupimwa ni sharti jipya, ni lini wataliondoa sharti hilo?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vigezo ambavyo Ofisi ya Rais, huwa tunaviweka, kupitia vigezo vyetu, hayo ni maeneo ambayo tulikwenda tukaikabidhi Halmashauri ya Mji Geita na tukawaeleza kwanini hawajatimiza hivyo vigezo. Tulikuwa tumeainisha moja ya mpango wa master plan, walikuwa wamepata Mkandarasi ambaye alikuwa bado hakumaliza hatua nne za mwisho kwa hiyo, kama wamemaliza sasa hilo linakuwa ni jambo lingine, lakini kabla ya hapo walikuwa hawajakidhi vigezo. Kwa hiyo, tumepokea wazo la Mheshimiwa Mbunge la kupitia upya hivyo vigezo, lakini kwa sasa hii ndiyo hali halisi ambayo iko chini kwenye ground.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha manispaa au halmashauri zote ambazo zinakuwa na hadhi, zikikidhi vigezo, jukumu letu litakuwa ni moja tu kupeleka kwa mamlaka na mamlaka ndiyo itakuwa na uamuzi wa mwisho.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Makao Makuu ya Mikoa mingi yamepewa Manispaa. Nataka kufahamu ni lini Serikali itatupatia Manispaa katika Mkoa wa Songwe kwa maana ya Vwawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kama hili nililijibu siku ya jana, ambako nilisema Mbunge wa Jimbo la Vwawa, Mheshimiwa Japhet Hasunga. Nimhakikishie tu kwamba Mkoa wa Songwe ni moja kati ya Mikoa ambayo imeiomba kupewa hadhi ya kuwa na Manispaa, kinachofanyika sasa hivi ni kuhakikisha kwamba vile vigezo ambavyo vimewekwa vinapitiwa na wakishakidhi vile vigezo maana yake tutaishauri mamlaka iweze kama kuipatia ama yenyewe itaona vingenevyo. Kwa hiyo, huo ndiyo msimamo mpaka sasa wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.(Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro iko katikati ya Majiji ya Dodoma, Arusha na Dar es Salaam. Je, ni lini Manispaa ya Morogoro itakuwa Jiji?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Dkt. Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, endapo Manispaa ya Morogoro itakuwa imekidhi vigezo na itakuwa imefuata taratibu zote, jukumu letu kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ni kufanya tathmini na kupeleka mapendekezo hayo kwa mamlaka ili iweze kufanya maamuzi. Ahsante.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itapandisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kateshi, kuwa Mamlaka kamili ya Mji wa Kateshi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Eng. Samweli Mbunge kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachohitaji katika Halmashauri yake ya Hanang’ ni kufuata tu vile vigezo halafu baada ya kumaliza hivyo vigezo watuletee nasi tutakuja kufanya tathmini tuone kama inakidhi ili tuweze kupandisha hadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kuna Mamlaka za Miji Midogo hapa nchini imekaa kwenye wadhifa huo kwa muda mrefu na sasa vinakidhi kwenda kwenye hatua nyingine. Je, ni lini Serikali sasa itazipandisha ikiwemo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Karatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba kuna mamlaka nyingi ambazo zinahitaji kupanda hadhi, moja ya jukumu kubwa la Serikali sasa hivi ni kuhakikisha kwanza tunaboresha miundombinu katika Halmashauri ambazo bado hazijakamilika. Lakini pili, kulingana na mahitaji tutapandisha hadhi, na sisi tutapendekeza kulingana na vilevile mahitaji ya wakati husika. Kwa hiyo, hilo ndiyo jibu la Serikali kwa sasa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Kwa kuwa, Serikali imekiri kwamba inatafuta fedha kulipa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na umeelekeza kwamba Halmashauri ifanye utaratibu huo. Je, uko tayari kuelekeza Halmashauri zote ili hela hizi zilipwe kwenye Mfuko Mkuu ili watu hawa wakapate kulipwa katika bajeti ya mwakani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ameona na amesikia kilio cha wafanyakazi ameongeza asilimia 23 kwenye mshahara. Je, huoni kwamba sasa ndiyo muhimu kuona kwamba watumishi wengine na hasa hawa niliowataja kwenye asilimia hii wapo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na hili ni agizo kwa Halmashauri zote kuhakikisha sehemu ya mapato ambayo yanashuka kwenda katika vijiji ni sehemu ya posho ambazo wenyeviti wa vijiji wanapaswa kulipwa. Kwa hiyo, tutakachokifanya tu ni kufuatilia kuona agizo hili ama utaratibu huu unatekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu asilimia 23 linahusu wale ambao ni Watumishi wa Umma ambao wako kwenye mishahara, kwa hiyo, kwa madiwani bado wako katika sehemu ya posho, ndiyo maana tumesema tunatafuta vyanzo vingine ili kuhakikisha kwamba tunawaongezea posho Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Tatizo lililopo Kyerwa linafanana kabisa na tatizo lililoko Mtwara Vijijini. Kata ya Mpapura Kijiji cha Nanyani tokea Julai, 2017 ujenzi wa zahanati ulishakamilika. Mpaka leo ninapozungumza takribani ni miaka minne. Ni lini sasa Serikali itakwenda kufungua zahanati hiyo ili wananchi waweze kupata huduma kwa sababu wamesubiri kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu kwa kutoa agizo la jumla kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Ma-DMO kuhakikisha wanatuletea taarifa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya zahanati zote ambazo zimeshakamilika na zinahitaji usajili ili ziweze kufunguliwa na sisi tuweze kujua namna bora ya kuchukua hatua za kuzifungua mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtaa wa Mpamaa ambao uko Kata ya Miyuji katika Jiji la Dodoma wananchi wamejenga zahanati, lakini hadi sasa zahanati ile haifanyi kazi. Nini kauli ya Serikali katika kuifanya zahanati hii ifanye kazi ili wananchi wapate huduma ya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ameainisha eneo la Mpamaa kwamba kuna zahanati ambayo imejengwa na bado haijafanya kazi. Nitoe kauli ya jumla kwa Serikali kwamba maeneo yote ambayo zahanati zimekamilika tungeomba tupate taarifa, ziletwe Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kufanya tathmini ya jumla kwa ajili ya usajili, vifaa tiba pamoja na wauguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Ni lini Serikali itafungua zahanati katika Kijiji cha Pomelini Kata ya Ng’uruhe Jimbo la Kilolo kwa sababu wananchi walichangia na Serikali imeshamalizia kile kituo kwa muda mrefu; na wananchi wanakuwa wakifuata matibabu umbali mrefu sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kwa swali hili ambalo ameliuliza nitamwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilolo pamoja na DMO waende wakafanye tathmini ili watuletee ili ifanyiwe usajili na ili tuweze kuifungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kata ya Itela ina zahanati mbili; Itera pamoja na Chanya. Zahanati hizi zimekamilika kila kitu lakini bado hazijasajiliwa. Ni lini zitasajiliwa ili wananchi waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Tarafa ya Nkwenda ina kata saba na ina kituo kimoja cha afya na ina zaidi ya wakazi 150,000; na msongamano umekuwa mkubwa katika kituo kile cha afya, lakini tulileta ombi Wizarani la kujenga kituo kingine cha afya katika Kata ya Songambele: Je, ni lini Serikali italeta pesa ili tuweze kujenga kituo cha afya ili kuondoa msongamano uliopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hizo zahanati mbili ambazo zimekamilika katika eneo la Itera ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliainisha, nimwakikishie tu kwamba zipo katika mchakato wa usajili na usajili utakapokamilika manake na sisi tutapeleka wahudumu ili zianze kutoa huduma. Kwa hiyo, nimwondoe shaka kwenye hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuhusu Tarafa ya Ikwenda ambayo walileta maombi ya kuongezewa kituo cha afya kingine, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba jukumu la kwanza la Serikali ilikuwa ni kuhakikisha tarafa zote tunazipelekea vituo cha afya. Jambo hilo tumelifanya na sasa hivi ujenzi unaendelea. Jukumu la pili la Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yenye uhitaji kulingana na umbali na ukubwa wa maeneo tutapeleka vilevile vituo vya afya ikiwemo katika Tarafa yake ya Ikwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini pia kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Arumeru, naishukuru Serikali kwa kutenga kiasi hiki cha fedha Milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, ni lini ujenzi wa daraja hili utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Wilaya ya Ngorongoro, kuna mto, unaitwa Mto Yuhe, mto huu ni hatari sana hasa kipindi cha mvua kwa kuwa watoto wetu wanashindwa kwenda shule upande wa pili vilevile akina Mama wajawazito wanashindwa kwenda kujifungua upande wa pili.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kujenga daraja hili ili kunusuru Maisha ya wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kumuahidi Mheshimiwa Mbunge ni kwamba daraja hili litajengwa katika mwaka fedha unaonza na tutalipa kipaumbele kuhakikisha kwamba linakuwa ni moja ya madaraja ambayo yatajengwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, katika Halmashauri ya Ngorongoro ambako kuna daraja la Nyuki ambalo na lenyewe linahitaji kujengwa, ninamuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatafuta fedha na tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmini ili na daraja hilo tulitafutie fedha ili liweze kujengwa, ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali kwa majibu mazuri, ingawa shule hii ya Kalenga tayari imeshatimizi vigezo. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Kata nyingine ya Sekondari ya Isimila ambayo ina Kidato cha Tano na Kidato cha Sita, hii ina wasichana na wavulana. Mwaka 1999 aliyekuwa Rais wakati huo Mheshimiwa Hayati Mkapa alipita pale na akaahidi kujenga ukuta ili kuwalinda wanafunzi pale lakini mpaka leo haujakamilika.

Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunafahamu kule Marekani wameanzisha kitu kina Ben Carson Reading Clubs, huyu mwana sayansi Ben Carson alipata maarifa yake kwa kusoma kwenye maktaba.

Je, Serikali ni lini sasa itajenga Maktaba kwenye shule za Kata zote katika Jimbo la Kalenga.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ambayo ilitolewa ya ujenzi wa ukuta katika shule ya sekondari Isimila bado ipo na sisi niseme tu kwamba katika mipango yetu tumeiweka, kikubwa ambacho tunatafuta sasa hivi kwa sababu tuna mipango mingi sana ya kutafuta fedha, tutakapopata fedha kwa ajili ya kujenga maana yake tutaanza haraka iwezekanavyo. Lengo la Serikali kwa sasa ni kuhakikisha shule zote nchini zinapata maktaba zikiwemo hizo za Kalenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kikubwa tu ambacho tunabanwa sasa hivi ni bajeti lakini tunaendelea kutafuta fedha na ninaamini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan tunaweza tukalifikia hili kama tulivyofanikiwa kwenye madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa jitihada kubwa ilizozifanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi hawa wa Kata ya Mnanje, Wilayani Nanyumbu, wanapata ukombozi kwa kupata hii consent ambayo itaweza kupunguza pakubwa sana adha na changamoto katika Kata hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali iko tayari kufanya jitihada za haraka kuleta hizi Milioni 250 ili kukamilisha ujenzi huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali itakuwa tayari kuleta watumishi wa kutosha ikiwa ni pamoja na vifaatiba ili kituo hiki kiweze kuanza kufanyakazi haraka na kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia tu kwamba hizi fedha Milioni 250, kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu Kata zote, maeneo yote ambayo tulipeleka fedha nusu, yatakuwa yamefikiwa ikiwemo katika Jimbo la Nanyumbu la Mheshimiwa Mhata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mara baada ya kukamilika moja ya lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunanunua vifaatiba pamoja na kupeleka watumishi katika vituo vyote ambavyo Serikali imeanzisha, ahsante. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Waziri Mkuu alipotembelea Kata ya Jangalu kwenye Kijiji cha Itolwa aliahidi kujengwa kituo cha afya. Naomba kujua ni lini sasa kituo hicho kitajengwa maana sasa ni miaka minne, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya Serikali kwanza ilikuwa ni kuhakikisha tunamaliza ujenzi katika Tarafa zote, lakini lengo la pili, ni kuhakikisha zile Kata ambazo hazifikiwa na zenyewe tunazijengea vituo vya afya. Kwa hiyo, hayo ndiyo malengo ya Serikali. Tatu, ahadi zote za Viongozi ambazo zimetolewa ziko katika mpango wetu tutahakikisha kabisa kwamba zinafikiwa ikiwemo katika Jimbo la Chemba, ahsante. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aweke kumbukumbu sawa ni Jimbo la Nanyumbu, naona maelekezo yako mengi yanazungumza Jimbo la Nanyamba, ni Jimbo la Nanyumbu, liko Mkoani Mtwara na Jimbo la Nanyamba pia liko Mkoani Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza kumekuwa na ucheleweshaji wa fedha hasa kwenye hii miradi ambayo wananchi wanaiibua. Sasa katika Jimbo langu nina maboma zaidi ya Kumi ambayo mpaka sasa hivi hayajapata fedha.

Je, Serikali ina kauli gani juu yama boma hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya lengo la Serikali ambalo hata kwenye bajeti tumepitisha, kila mwaka tumekuwa tukitenga fedha kwa ajili ya umaliziaji wa maboma ambayo yameanzishwa huko chini na wananchi pamoja na Serikali zetu kule chini. Kwa hiyo, tumekuwa tukitenga labda kwa kiwango fulani. Sasa hatuwezi kuyamaliza yote kwa wakati mmoja ila kwa wakati. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mhata kwamba hata katika Jimbo la Nanyumbu, tutafanya hivyo katika mwaka wa fedha unaokuja kuongeza baadhi ya maboma ili tuhakikishe yanakamilika yote kwa wakati.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Serikali inajenga hospitali pale Ukerewe ambayo ikikamilika itakuwa na hadhi ya Mkoa na ikikamilika itakuwa inahudumia cases kubwa za rufaa. Sasa nataka kuiuliza Serikali haioni umuhimu sasa kuimarisha kituo cha afya cha Nakatungulu ambacho kitasaidia kuhudumia wagonjwa magonjwa ya kawaida na kikikamilika kitahudumia Kata zaidi ya Sita kwenye eneo la Mjini pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumekuwa tukiboresha vituo vya afya ambavyo vimekuwa na idadi kubwa ya watu na zile ambazo zinahudumia Kata nyingi ikiwemo katika hii Kata ya Nakatundu ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Kwa hiyo, bado iko katika mipango yetu na sisi tutaendelea kuziboresha kuhakikisha tunapeleka huduma za afya karibu na watu.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kufahamu ni lini Serikali itatujengea kituo cha afya katika Kata ya Vwawa ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha kwamba Tarafa zote zinapata vituo vya afya, hilo eneo ambalo analianisha ndiyo Makao Makuu ya Mkoa ambako tunayo hospitali ya Mkoa ambayo tumeipandisha hadhi kutoka hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, baada ya kumaliza hizo process zote ambazo tunazo sasa hivi, maana yake ndiyo tutafuatia hiyo hatua ambayo Mheshimiwa Mbunge anaainisha, ahsante. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Elimu bila malipo imeweza kuibua vijana wenye vipaji kutoka familia zenye mazingira magumu. Mfano, Bariadi mwaka juzi alitokea kijana aliyepata ‘A’ zote katika masomo yake. Wanafunzi hao wamekuwa wakipangwa shule maalum au shule zilizo mbali zaidi na kushindwa kumudu gharama za kusafiri na zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kuwabaini wanafunzi wa aina hii ili waweze kuwasaidia na kutimiza ndoto zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tumekuwa tukiomba mabweni kwa ajili ya shule zetu za Kata na zinapokamilika shule hizi zinakuwa za Kitaifa. Je, Serikali haioni haja ya kuona kuwa na catchment area kama vile katika Mkoa au Wilaya kuwe na shule ya bweni ili tuweze kuwanusuru vijana wanaokatisha masomo kwa kutembea umbali mrefu. Kwa mfano, mwanafunzi anayetokea Lukale kilomita 40 kwenda Bukundi na kurudi kilomita 40? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba wanafunzi wote wenye vipaji Serikali inawazingatia, na inapotokea wanafunzi waliofanya vizuri kama huyo na bahati mbaya anakuwa ameenda katika maeneo ambayo hakustahili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumefungua dirisha, mnatuletea hayo maombi na tunaweza tukafanya mabadiliko mengine. Kwa hiyo, hilo liko wazi na liko ndani ya uwezo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ujenzi wa shule za bweni katika ngazi ya mkoa kwa kuzingatia hayo; umbali, mahitaji na vipaji, ndiyo maana kwa mwaka huu wa fedha na mwaka 2021, Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ameamua kujenga Shule za Kimkoa kwa wasichana. Mwaka 2021 tumeshapeleka fedha shule 10 na mwaka huu vile vile tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule nyingine 10 za kimkoa ambazo zitapokea wasichana wenye vipaji katika mikoa husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba lengo la Serikali litafikiwa na tunafanya hivyo kupunguza umbali pamoja na kuongeza tija ya elimu katika maeneo husika, ahsante. (Makofi)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza niishukuru Serikali kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari.

Swali langu la nyongeza, Mheshimiwa Waziri majibu yako yamejumlisha fedha zote zilizopo ndani ya Wilaya ya Igunga, hivyo basi nilikuwa nataka kuomba kwa shule zetu shikizi kwa maana ya Shule za Kazima, Mwakipanga, Mwamakingi pamoja na Shule ya Msingi Shikizi Mwasung’o. Je, ni lini Serikali itatuunga mkono kutupatia fedha kwa shule hizi shikizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Shule ya Sekondari ya Mwisi pamoja na Shule ya Sekondari ya Choma tuna uhaba wa mabwalo la chakula. Je, ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya mabwalo kwa watoto wanaotumia kidato cha tano na cha sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shule Shikizi ambazo amezianisha Mheshimiwa Mbunge lini tutapeleka fedha, nimuhakikishie tu kwamba zipo katika mipango yetu na bahati nzuri siku ya Jumatatu tumezindua mradi wa BOOST na mradi ule unagharimu karibu trilioni 1.1. Kwa hiyo, fedha zile zitakapokuwa zimekuja maana yake tutazipeleka katika shule zote nchini ikiwemo ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi huo katika Shule ya Sekondari Mwisi ambazo hazina mabweni ni sehemu ya mpango ambao sisi kama Serikali tutapeleka maana yake ni component nzima ni pamoja na mabweni. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Kata ya Mwasubi iliyopo katika Tarafa ya Mondo, Wilaya ya Kishapu ni kata mpya na haina madarasa ya kutosha katika shule ya sekondari. Je, ni lini Serikali itajenga ili kuongeza madarasa katika shule hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge tutaongeza madarasa kwa kuwa moja ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha shule zote tunazifikia kwa kuongeza madarasa na kuzikarabati. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru pia Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha Shilingi Bilioni Moja mwaka jana ambazo ndizo zimetumika kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Spika, swali, barabara hii ni moja ya ahadi ya Mheshimiwa Rais ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Je, Serikali inasemaje kuhusu hilo, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hatua ya awali ni hii ambayo tunarekebisha hii barabara ili walau iweze kupitika kipindi chote wakati ambapo tunatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza hiyo ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itatekeleza ahadi yake kwa vitendo. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninamshukuru Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, kwanza; kwa kuwa sasa tuna elimu bure ya sekondari na mpaka Kidato cha Sita. Ninashukuru kwa hilo kwa Serikali, nimshukuru Mama Samia kwa kutoa elimu bure kwa Kidato cha Tano na cha Sita. Sasa lipi Serikali itafanya kusamehe michango ya sekondari 20,000? Kusamehe michango ya Kidato cha Sita na cha Tano ya 70,000 au kutoa michango ya sekondari ambayo inafikia Shilingi Laki Tano au michango ya Kidato cha Sita ambayo inafikia Shilingi Milioni Moja, kipi kifanyike sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa swali lake lilikuwa ni la jumla na nimwambie tu kwamba baada ya elimu bila ada maana yake wanafunzi wale hawalipi ile ada ambayo walikuwa wanalipa ya Shilingi 20,000 kwa Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne. Maana yake na hivi tunavyokwenda kwa Kidato cha Tano na Kidato cha Sita ambapo ada kwa miaka yote imekuwa ni Shilingi 70,000 maana yake sasa hivi wazazi hawatalipa hiyo ada ya Shilingi 70,000. Kwa hiyo, huo ndiyo msimamo wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi wote wa Tanzania ili waweze kupata elimu bila malipo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hiyo michango mingine tunaendelea kuiangalia ili kuhakikisha kwamba haiathiri masomo ya wanafunzi na wazazi kuhakikisha watoto hawa wanapata elimu bora. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kumekuwa na michango mingi sana hasa kwa hawa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano. Nina mwanafunzi ambaye hana wazazi hana familia, alikuwa anaenda Bwiru Sekondari, nimelazimika kutoa fedha nyingi mara nne zaidi ya ile fedha ya ada.

Nini sasa tamko la Serikali leo juu ya shule hizo ambazo michango ni mikubwa mara Nne zaidi ya fedha ambazo unatozwa za ada?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monnie Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kwamba yote lazima iwe imepitishwa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo. Kama kuna shule ama kuna eneo lolote lina michango mikubwa tunaomba taarifa hizo ofisi ya Rais TAMISEMI ili tuweze kuchukua hatua katika hayo maeneo ambayo wamezidisha michango.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, michango ambayo imezidi kiwango ni michango ambayo haikubaliki na Serikali tulishatoa kauli yetu.(Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Waziri kumekuwa na lugha ya pre-form one ambayo inatumika sana kwenye shule binafsi na ina michango mingi sana kwa wazazi wanaopeleka watoto kwa masomo hayo. Mnatoa tamko gani kama Serikali kuondoa hili neno la pre-form one kwa sababu inaongeza gharama kwa familia na wazazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, masuala yote yanayohusu shule binafsi yanashughuliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nasi kama wadau tunatambua mchango mzuri ambao unatolewa na shule binafsi katika kukuza elimu bora nchini. Kwa hiyo, nimuelekeze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumelipokea na tutalifikisha Wizara ya Elimu ili waweze kuchukua hatua ambazo zinastahili.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini kwa kuwa Wabunge wote katika swali hili linaonesha ni namna gani wananchi wanakerwa pamoja na kuwa na huo mwongozo.

Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuwaelekeza Walimu na hizo Bodi wasitumie mwongozo huo kama uchochoro wa kuwapatia wazazi mzigo mzito?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tumepokea wazo la Mheshimiwa Mbunge na tunatoa maelekezo kuwakumbusha shule zote nchini juu ya utekelezaji wa mwongozo huo. Ahsante sana
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda nielekeze swali langu katika Mkoa wa Simiyu Wilaya ya Busega: Ni lini Serikali itapeleka mashine ya X-Ray katika Wilaya ya Busega? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Minza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa hivi tuko katika mchakato wa kufanya manunuzi ya vifaa tiba, ninaamini mara baada ya mchakato huu kukamilika, basi tutalizingatia hilo nao tutawapatia hiyo X-Ray.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Utakubaliana nami kwamba katika jibu ambalo limetolewa na Serikali, wanaongelea suala la kuajiri watumishi 7,612; na kitakachoenda kufanyika ni kugawa kwa kuzingatia quality na siyo equity. Katika swali langu la msingi nimeongelea juu ya upungufu mkubwa wa watumishi wa kada ya afya katika Halmashauri yetu. Hivi karibuni wamehama watumishi 33 na wakahamishiwa watumishi watatu tu: Je, Serikali katika mgao huu itaenda kuzingatia equity badala ya equality?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa watumishi ambao wamekuwa wakipelekwa katika maeneo yanayoonekana kama ya pembezoni wanaenda kuishi kule kama kupata confirmation na kupata ukuu wa idara na baadaye kuhama; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi wote ambao wanapangwa katika maeneo hayo wanaenda kuishi kwa kipindi chote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, baada ya kumaliza mchakato wa ajira, maana yake kitakachofuata ni kugawanya katika Halmashauri zote nchini na tutagawa kulingana na mahitaji katika maeneo husika. Kwa hiyo, hatutakuwa na ile namba kwamba tutagawa Halmashauri zote kwa usawa, Hapana, tutagawa kulingana na mahitaji. Tunatambua kabisa kwamba katika maeneo kama Kalambo kuna uhitaji mkubwa, kwa hiyo, tutawapa kulingana na hiyo idadi.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwenye suala la kuhusu kuhama watumishi baada ya kwenda katika maeneo ya pembezoni, moja, ya utaratibu ambao tumeweka sasa, mtumishi haruhusiwi kuhama siyo chini ya miaka mitatu, lazima afanye kazi katika eneo alilopangiwa na baada ya hapo, labda kuwe na sababu za msingi sana ambazo zinapelekea mtu huyo apaswe kuhama. Kwa sasa ni kwamba tunafunga na wote wanakuwa na commitment letter ya kuhakikisha wanabaki katika maeneo hayo, ahsante. (Makofi)
MHE. AYSHROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Singida unakabiliwa na upungufu mkubwa wa wauguzi ambako zaidi ya wauguzi 800 wanahitajika: Je, ni lini Serikali itatuletea wauguzi wa kutosha ili kusaidia mkoa wangu kutoa huduma za afya na hususan kusaidia huduma ya mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Aysharose Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Singida, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali tunaajiri kulingana na bajeti na mapato kadri ambavyo tunapata na mahitaji yaliyoko. Kwa hiyo, tutakavyoajiri ikiwemo ajira 7,612 maana yake katika ule mgawanyo na Singida nao tutawapatia, ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Serikali kwa kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Babati Vijijini wamekamilisha ujenzi wa zahanati za Guse, Hayamango na Yasanda, lakini zahanati hizo zimeshindwa kufunguliwa kwa sababu ya upungufu wa watumishi wa afya: Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuwapeleka watumishi ili zahanti hizo ziweze kufunguliwa na kuhudumia wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba kuna zahanati nyingi hazijafunguliwa kwa sababu ya kukosa watumishi, nasi kama Serikali tunalijua hilo na katika watumishi ambao tutawapeleka, tutawaagiza Wakurugenzi wawapangie katika zile zahanati ambazo zimekamilika ili ziweze kutoa huduma, ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina changamoto kubwa sana ya watumishi hasa kada ya afya na elimu: Je, ni lini Serikali itapeleka walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ili kukabiliana na changamoto kubwa sana ya watoto wetu kukosa elimu na elimu kushuka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ajira ziko katika hatua za mwisho na hizi ajira ni pamoja na kada ya afya na elimu, kwa hiyo, katika ule mgawanyo Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe vilevile tumeizingatia na itapata katika ule mgawanyo wa walimu pamoja na kada ya afya, ahsante.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nikiwa Mbunge wa Kawe, tumejenga hospitali kubwa sana ya mfano kupitia fedha za Halmashauri eneo la Mabwepande ambayo sasa hivi iko katika hatua za mwisho kabisa: Je, katika mchakato wa kugawa watumishi wa kada ya afya, Serikali mtazingatia hospitali hii kubwa ambayo itasaidia Wilaya za Bagamoyo na Kawe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika sehemu ya ajira ambazo tutazipanga na kupeleka katika Hospitali ya Mabwepande ni pamoja na hizi ajira mpya ambazo tutazitoa, ahsante. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kata hizi ambazo nimezitaja kwenye swali langu la msingi ziko mbali sana na mojawapo ina mto katikati, kwa hiyo wanafunzi wanapata shida sana kwenda shuleni. Shule inayo-accommodate wanafunzi wa kata hizi ambazo hazina kabisa sekondari ni Shule ya Sekondari Mkindo. Sasa je kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifanya hii sekondari ya Mkindo kuwa ni sekondari ya bweni ili iweze kuwasaidia wanafunzi ambao wanatoka maeneo ya mbali waweze kufikia ndoto zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali iliona umuhimu wa kujenga vituo vya afya kwa kupitia pesa za tozo lakini pia pesa za COVID-19. Je, kwa kata hizi zenye maeneo ambayo hayana sekondari, kwa nini isilete mpango mahsusi kama ilivyofanya kwenye Wizara ya Afya ili kuhakikisha na hizi kata ambazo hazina sekondari na zenyewe zinapata sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amehitaji kwamba katika Kata ya Mikindo tuifanye kuwa shule ya bweni, tulipokee wazo hili na tutakwenda kufanya tathmini tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hii.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ina mpango mahususi na mpango wetu ni kujenga sekondari 1,000. Mwaka wa fedha huu ambao unaisha 2021/2022 tumeshapeleka fedha katika kata 232, karibu bilioni 109.57 na katika mwaka wa fedha ambao Wabunge wameshatupitishia bajeti kwa maana ya 2022/2023 tutajenga shule za sekondari 234, manake tutapeleka katika kata zote katika majimbo ambayo bado hawajapata. Mwakani vilevile na mwaka kesho kutwa tutafanya hivyo hivyo. Kwa hiyo ndani ya miaka ya Mama Samia tutamaliza shule zote 1,000 ambazo Mheshimiwa Rais ameahidi kupitia mradi wa SEQUIP. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwenye hilo. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Nyamagoma ni miongoni mwa Kata za Wilaya ya Ngara ambazo hazina shule ya sekondari. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nyamagona? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George, Mbunge wa Jimbo la Ng’ara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata ya Nyamagona ipo katika mpango ambao tunakwenda kujenga katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwamba itajengwa katika mwaka wa fedha unaokuja wa 2022/2023.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nikiri wazi kweli wataalam wako katika Kata ya Loya, wanafanya usanifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maswali yangu mawili ya nyongeza la kwanza, tarehe 17 Mei, Mheshimiwa Rais alipokuwa Mkoa wa Tabora nilimfikishia kero hii ya wananchi wa Loya na akamuagiza Waziri wa Ujenzi aweze kushughulikia daraja hilo.

Je, Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI, hamuoni kuharakisha huo usanifu ili mpeleke Wizara ya Ujenzi ili muweze kusaidia kujenga daraja hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, kwa kuwa daraja hili litachukua muda mrefu kukamilika na wananchi wanaendelea kupoteza maisha, hamuwezi kuona uharaka kwa kujenga daraja la watembea kwa miguu ili wananchi wasiendelee kupoteza maisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho nina uhakika nacho ni kwamba tuko katika hatua za mwisho za kukamilisha usanifu ambao mpaka sasa hivi tumebakiza kama wiki tatu tu kukamilika. Kwa hiyo, mara baada ya kukamilika basi tutakabidhi kwa wataalam kwa ajili ya hizo fedha ili sasa zipatikane na ujenzi wa daraja uanze. Kwa hiyo, uharaka wa kujenga daraja la miguu kwa sababu hizi kazi zinaenda sambamba, nimhakikishie tu kwamba tutafanya haya yote kwa pamoja kuhakikisha kwamba wananchi wale wanapata huduma, ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona daraja la Zihi – Mlambalasi kwenda Kiwele ambalo ni Jimbo la Kalenga ni daraja ambalo ni muhimu sana linatakiwa lijengwe kwa sababu linakwenda kwenye makumbusho ya Mkwawa.

Ni lini Serikali italijenga daraja hilo kwa sababu sasa hivi watu wanapita tu, ni kasehemu kadogo wanapita kwa pikipiki tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunajenga madaraja ambayo yamekuwa sumbufu katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa hiyo, niwaagize tu Mkandarasi wa TARURA Mkoa wa Iringa waweze kwenda kufanya tathmini na baada ya tathmini tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Ahsante.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, Mto Bubu umekata katikati kati ya Kijiji cha Mpendo - Hamia na hivyo kipindi cha mvua kuna na ugumu sana wa kupata mawasiliano ya barabara kuja Dodoma.

Nini mkakati wa Serikali walau wa kujenga daraja la muda ili watu wapate mawasiliano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmnini waone ni namna gani linaweza likatekelezeka ndani ya muda mfupi. Ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa taarifa ambazo nimepewa taarifa hii na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ni kwamba tayari marekebisho yao yameshafanyika na imeshawasilishwa kwenye mamlaka ya ofisi yake. Swali langu, itakapofika kwenye meza yako, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa soko hili likikamilika litahitaji sana mizigo mingi kutoka pembezoni kwenye maeneo mbalimbali na kata mbalimbali. Serikali ina mpango gani sasa wa kutekeleza ahadi ya Rais kwa kujenga barabara ya Shilinjoro - Mijengweni, Arusha Road – Ngalawa; na barabara ya Jiweni – Lukan - Losaa - Nakyungu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Hai ambayo tulikuwa tumeiadikia kufanya marekebisho, wapo kwenye hatua na kwa maelezo ya Mheshimiwa Mbunge ni kama wamekabidhi. Ninachoweza kumhakikishia ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, itakapopata andiko hilo maana yake tutaanza mara moja kutafuta fedha ili sasa tutekeleze ahadi ambayo ipo ya kujenga soko hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kukamilika kwa soko maana yake tutafuta fedha zaidi sasa kurekebisho hizo barabara ambazo zinaelekea katika eneo la soko ili kurahisisha uchumi wa wananchi wa Hai. Kwa hiyo, hicho ndicho nachoweza kusema ahadi ya Serikali ya Awamu ya Sita.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kwa fedha hizi ni revolving funds lakini bahati mbaya sana baadhi ya vikundi vinashindwa kufanya mrejesho. Je, Serikali inawachukulia hatua gani vikundi ambavyo vinashindwa kufanya mrejesho ili vikundi vingine vipate mikopo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa biashara nyingi zilizoanzishwa na vikundi hivi vina-fail. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya uchambuzi wa kina na ushauri kabla hawajatoa mikopo katika vikundi hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba wale wote ambao hawalipi mikopo kuna hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa katika kila Halmashauri, ikiwemo kuwafuata, kuwaelimisha, lakini vilevile wale ambao wamekuwa wagumu kesi zao za madai zimekuwa zikipelekwa mpaka mahakamani na wengine wamekuwa wakilipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaandaa mpango ambao utafanya sasa watu wote wanaokopa waweze kulipa kwa wakati ili fedha zile ziwasaidie na watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tumepokea ushauri na sasa hivi tunajaribisha kuwapa elimu Maafisa Maendeleo wa Jamii ili waweze kufanya uchamuzi wa kina pamoja na ushauri sahihi wa wale wote wanaokop ili mikopo hii iwe na tija. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kwa kuwa mikopo hii mara inapotolewa wakopaji uanza kulipa mara moja, lakini wapo wakulima wa mazao ya muda mrefu kama parachichi na mazao mengine yanayochukua muda mrefu.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa kipindi cha kusubiria yaani grace period kabla hawajaanza? Uko tayari kutoa agizo hilo Mheshimiwa Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hii inaongozwa kwa kanuni na sheria iliyotungwa na Bunge. Kwa hiyo, mpaka muda huu ninapozungumza bado kanuni zinazotumika ni zile ambazo zimetungwa. Kwa hiyo, ili kuongeza grace period maana yake tunahitaji mabadiliko ya kisheria ili tuweze ku-accomadate. Kwa hiyo, Bunge lako tukufu litakavyoona wakati unafaa basi mnaweza kufanya marekebisho na sisi tutatekeleza.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, katika Jimbo la Manyoni Mashariki kuna Kata ya Makutupora ambayo ilipangiwa kujenga shule mpya, lakini mpaka sasa hivi fedha ya kujenga shule mpya katika Kata ya Makutupora haijapelekwa. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha hii ili shule ianze kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa utoaji wa elimu ya awali katika Mkoa wa Singida bado ni hafifu; je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba sasa tunaajiri walimu wa elimu ya awali hususani katika maeneo ya vijijini ya Mkoa wa Singida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi ya Serikali na ujenzi wa shule ya sekondari katika Kata ya Makutupora iko pale pale na tutajenga kata hiyo kwa sababu fedha zipo katika bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili kuajiri walimu wa awali katika ajira hizi zilizotangazwa moja ya kigezo ambacho tumezingatia ni kuajiri walimu wapya ambao wana shahada ya elimu ya awali na stashahada ambao tutawapeleka katika shule zote nchini ili kusaidia hii elimu ya awali nchini.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uhaba mkubwa wa watumishi katika Wilaya ya Liwale, lakini hata hivyo mgao tunapata watumishi, lakini idadi ya watumishi wanaohama na wanaohamia kubwa ni ile ambayo wanahama bila kufanyiwa replacement. Je, nini kauli ya Serikali juu ya kuhamisha watumishi bila kutupatia replacement kuziba nafasi hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatambua changamoto za maeneo ya pembezoni walimu wengi wanaoajiriwa huwa wanapenda kuhama na sasa hivi mkakati wa Serikali ni kwamba watu wote ambao tunawaajiri tunawapa na ile barua kwa maana ya commitment letter ambayo itawafanya wakae maeneo siyo chini ya miaka mitatu mpaka watakavyoomba kuhama. Lengo la Serikali ni kuhakikisha maeneo yote nchini yanakuwa na usawa wa walimu wote ambao tunawaajiri, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru na kuipongeza Serikali kutenga hiyo fedha ambayo itakuwa na matumaini makubwa kwa wananchi wa Mtowiso wanaosubiri barabara hiyo ya Ng’ongo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza la nyongeza; kwa kuwa Serikali mmetumia shilingi milioni 900 kujenga barabara ya Msia - Mawezuzi, kwenda Sumbawanga Mjini na bado haijakamilika.

Je, ni lini mtaleta shilingi bilioni 1.5 zilizobaki ili kukamilisha barabara hii ipitike?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la nyongeza; kutokana na mvua nyingi mwaka huu barabara za Kijiji cha Kamsamba ambayo inaunganisha Kijiji cha Kavifuti na Miangalua ilibebwa na maji na mpaka sasa tumeandika andiko liko Wizarani. Nataka kujua je, ni lini fedha hizo za dharura zitakuja ili kutengeneza Daraja hilo la Kamsamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilikuwa imetoa fedha milioni 900 na mpaka sasa tunahitaji kuongezea fedha ambapo ziko katika mchakato na mchakato ukikamilika fedha ile itapelekwa ili barabara hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha hapa iweze kumalizia hicho kipande kilichobakia.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili, wameomba fedha kwa ajili ya barabara ambayo imeharibika kutokana na mvua na fedha hizo ni za dharura, na ni kweli hilo andiko lipo Ofisi ya Rais, TAMISEMI (TARURA) na sisi tuko katika hatua za mwisho kuhakikisha kwamba hiyo fedha tunaipata ili tulete na turekebishe barabara hiyo, kwa hiyo, hayo ndiyo majibu.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mfano jimbo lake lile la Tunduma, linaingia mara sita kwa jimbo langu, lakini wote tunapata fedha sawa za mgao wa barabara, sasa haoni kama hiyo siyo sawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli ukichukulia Jimbo la Mbozi, ukifananisha na Jimbo la Tunduma, Jimbo la Mbozi ni kubwa zaidi kuliko Jimbo la Tunduma na utaratibu ambao ulikuwa unatumika mwaka uliopita ni utaratibu ambao tulikubaliana wote Wabunge humu ndani na ndiyo maana sasa hivi tunarekebisho hiyo formula ili majimbo yote yapate kulingana na ukubwa wa eneo na mahitaji ya eneo husika. Ahsante sana.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa pesa nyingi kwa ajili ya miradi ya barabara hizi zinazosimamiwa na TARURA, bado miradi mingi kwenye maeneo imesimama au inasuasua ikiwemo Jimbo la Ukerewe kwa sababu wakandarasi ama kutokuwa na uwezo au kuwa na mrundikano wa kazi nyingi.

Nini kauli ya Serikali juu ya hali hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali katika maeneo yote ambayo wakandarasi hawafanyi vizuri ni kuhakikisha kwamba wanamaliza ndani ya muda kwa sababu tumetoa muda kamili wa kufanya ile kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kama kuna maeneo ambayo wakandarasi wamekuwa hawatekelezi kabisa wajibu wake tunaomba maeneo hayo mtuletee sisi ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia TARURA, ili tuweze kuchukua hatua zikiwemo kuvunja mikataba kwa sababu wanachelewesha hizo kazi. Ahsante sana.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anaongea na Mameneja wa TARURA nchini, alisema kuna mikoa kama Njomba na Mbeya ambayo hali ya barabara ni mbaya lakini ni mikoa ya uzalishaji, TARURA lazima muwape kipaumbele kuwapa fedha; kwa mfano Makete, hali ya barabara ni mbaya.

Ni lini mtaongeza fedha kwa ajili ya mikoa hii ya uzalishaji katika Taifa letu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuonesha kwamba Serikali inazingatia maeneo yenye uzalishaji mkubwa ndiyo maana utaona katika hizo nyanda ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha kuna miradi maalum ikiwemo miradi ya RISE ambayo haiko maeneo mengine, lakini iko katika maeneo ambayo yanazalisha. Tumepeleka huko ili kuongeza fedha nyingi kwa ajili ya uzalishaji katika maeneo hayo. Kwa hiyo, hilo ndiyo jibu sahihi, sio tu fedha za TARURA, ni pamoja na miradi husika. Ahsante sana.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, nauliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kutokana na uelewa wangu halmashauri zote zilizo nchini zinatofautiana mapato na Serikali imekuwa ikitangaza tu mafunzo ili halmashauri zijihudumie; je, hamuoni sasa kuna umuhimu wa Serikali kupeleka fedha kwa uwiano sawia?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kumekuwa na mfululizo wa hati chafu ambazo ni zaidi ya miaka kumi mfululizo; je, Serikali haioni kwamba inaendelea kupoteza fedha za wananchi kwa kutokuwa na watu wenye weledi au ufanisi mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja ya lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaongeza fedha kwa ajili ya mafunzo na tutazigawa kulingana na uwiano katika halmashauri moja na nyingine, kwa hiyo, hilo ndiyo lengo la Serikali, lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunazuia wizi kwa kuwapa mafunzo ya kuweza kuzuia vitendo hivyo vya kihalifu katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili kuhusu hati chafu katika maeneo mengi nchini, moja ya kazi kubwa ambayo tumeifanya sasa hivi ni kuhakikisha moja tunawaondoa watu wote wanaosimamia fedha katika maeneo hayo wakiwemo wahasibu, ma-DT pamoja na wakurugenzi. Kwa hiyo, hizo ni hatua ambazo tunachukua, lakini sasa hivi tutakkuwa tunaleta watu ambao ni waadilifu katika maeneo yetu na hatutakuwa tunahamisha kama ambavyo ilikuwa awali mtu anafanya tukio baya upande mmoja tunahamisha katika halmashauri nyingine. Ahsante sana.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwa kuwa katika halmashauri kwanza Serikali imetoa mafunzo kwa maafisa 210 ambao ni wachache sana ukilinganisha na halmashauri zilizopo hapa nchini mikoa iliyopo; na kwa kuwa uandaaji wa hesabu unahitaji ujuzi na maarifa maalum ambayo yanatakiwa yatolewe na wafanyakazi wengi wamekuwa hawana maarifa hayo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wahasibu pamoja na Wakaguzi wa Ndani wanapatiwa mafunzo wanayostahili katika utayarishaji wa hesabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tumejibu hawa tumetoa mafunzo kwa maafisa 210 sasa hivi tumeongeza fedha katika bajeti yetu, kuhakikisha tunawafikia watu wote wa vitengo, wahasibu pamoja na wakaguzi wa ndani ili kuhakikisha kwamba sasa wanafanya kazi ambayo imekusudiwa. Kwa hiyo, fedha zimeongezeka na mwakani tutafanya hivyo kwa watu wote wa idara hiyo.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria za uandaaji wa hesabu zimekuwa zimekubadilika mara kwa mara kulingana na mahitaji ya kimataifa; je, sasa Serikali haioni ni wakati sahihi sasa wa kutenga fungu rasmi kwa ajili ya hawa wahasibu ili wakaweze kuhudhuria classes za NBAA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe, Mbunge wa Jimbo la Busega kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali tutaendelea kutenga fedha kadri inavyopatikana lakini kwa sasa tutaendelea na mafunzo ili kuhakikisha kwamba haya yanayotokea sasa hayaendelei. Ahsante sana.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri, lakini mwaka 2020 wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliposimama pale katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Geita aliahidi kilometa tatu na mwaka 2021/2022 TAMISEMI, ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilometa moja, lakini mpaka leo tunaenda mwaka wa Serikali kumalizika hatujawahi kuiona hiyo kilomita moja.

Je, kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba sasa mtatekeleza kilomita mbili na sio kilometa moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kasheku Musukuma, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama fedha hizi zipo katika bajeti ambazo zimetengwa, nitalifuatilia na nimelipokea ili kuhakikisha kwamba linatekelezeka kama ambavyo limeainishwa katika bajeti, ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kutokana na tozo mbalimbali; ni lini sasa itaweka vipaumbele kwenye majimbo ambayo yana changamoto kubwa sana za barabara ikiwemo Jimbo la Nyamagana Jijini Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inazingatia vipaumbele kulingana na mahitaji ya kila jimbo ikiwemo Jimbo la Nyamagana.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Kituo cha Afya cha Upugi kiko kilometa nne kutoka barabara kubwa ya Tabora - Nzega. Mheshimiwa Rais alipopita pale wananchi walimuomba awawekee barabara ya lami kwa sababu wagonjwa wakizidiwa kutoka kituo cha afya kwenda mjini inakuwa taabu sana. Je, Serikali iko tayari kuanza kujenga barabara hiyo ya kilometa nne?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari kwa ajili ya kutekeleza maeneo yote yenye utata wa barabara ikiwemo eneo ambalo amelianisha Mheshimiwa Mbunge, isipokuwa kwa sasa tunatafuta fedha ili tuzitenge katika bajeti ili tuanze utekelezaji. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kuniona kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Liwale ni mji unaokua kwa kasi sana na ni miaka 42 sasa umri wa mji ule, lakini una kilometa 1.8 tu za lami pale mjini. Je, Serikali iko tayari kutuongezea mtandao wa barabara ya lami kwenye mwaka huu wa bajeti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuambie tu kwamba Serikali iko tayari na tumetenga fedha na ninaamini eneo la Liwale ni sehemu ambayo tumewaanishia katika bajeti ya mwaka huu 2022/2023.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, lakini pia napenda kuipongeza Serikali kwamba sasa imeanza kutenga fedha za dharura kwa ajili ya barabara zetu za TARURA, naipongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, barabara ya kutoka Changarawe kwenda Kisada ambayo inapita maeneo ya Matanana na Bumilayinga kutokana na miti ambayo wananchi walipanda kwa wingi na sasa imekomaa, inatumika sasa na malori makubwa.

Je, Serikali iko tayari kuitazama barabara hii kwa macho mawili kwa sababu inaharibika mara kwa mara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tunafahamu kwamba na wewe Naibu Spika ni mmoja wa wanufaika wa Mradi wa DMDP kama utakuja kukamilika, na sisi watu wa miji 45 tuna Mradi wa TACTIC. Mimi na wananchi wa Mafinga tunapenda kufahamu, je, katika huu Mradi wa TACTIC ambao utanufaisha kata nyingi za pale Mjini Mafinga, Upendo, Isalavanu, Kinyanambo na kadhalika, je, unaanza lini kwa sisi wa tu wa Mafinga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari kuiangalia kwa umakini barabara ya Changarawe – Kisada ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiainisha hapa ili tuhakikishe kwamba inafanyiwa matengenezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lini Mradi wa TACTIC utaanza. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Mjini ipo katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi huo ambao utaanza katika mwaka wa fedha unaokuja wa 2022/2023. (Makofi)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupata tatizo la mafuriko, madaraja mengi ndani ya Wilaya ya Hai yaliezuliwa yakiwemo Madaraja ya Marire na Kikafu. Daraja hili limekuwa kero kubwa kwa wananchi jambo linalomlazimu Mheshimiwa Diwani Martin Munisi kila siku asubuhi kuamka kwenda kuwavusha watoto wa shule kwenye daraja hili.

Je, Serikali ni lini itakarabati madaraja haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa daraja hili lina changamoto nyingi, niwaagize TARURA Mkoa wa Kilimanjaro wafike eneo la tukio wafanye tathmini na kuchukua hatua za haraka ikiwemo kujenga daraja dogo la dharura ili eneo hilo liweze kupitika, ahsante sana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, Manispaa ya Mpanda nayo ni kati ya Manispaa ambazo zipo kwenye Mradi wa TACTIC. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie na sisi Mpanda ni lini tutaanza Mradi huu wa TACTIC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Manispaa ya Mpanda ipo katika Awamu ya Tatu ya Utekelezaji wa Mradi wa TACTIC ambao utaanza mwaka wa fedha 2022/2023, ahsante sana.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mbogwe ina barabara nyingi, ukizijumlisha upana wake ni zaidi ya kilometa 3,000, hivyo basi barabara nyingi mpaka sasa hazipitiki Mheshimiwa Naibu Waziri na wewe ni shahidi, tulishawahi kwenda pamoja kwenye hilo jimbo.

Je, ni lini sasa hizi barabara nyingine ambazo haziko kwenye mpango utanipa bajeti ili TARURA ya Mbogwe iweze kuzitengeneza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wilaya ya Mbogwe ina madaraja manne na mpaka sasa hivi madaraja hayo hayapitiki, likiwemo Daraja na mpaka wa Bukombe, Kata ya Masumbwe ambalo linaunganishwa na Kata ya Bugerenga.

Naomba kujua sasa Mheshimiwa Naibu Waziri umejipangaje ili kuweza kunisaidia wananchi wangu waendelee kufaidika na Serikali hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajenga barabara hatua kwa hatua na ndiyo maana hatua ya kwanza Mji wa Mbogwe umeingizwa katika Mpango wa RISE. Hatua nyingine Mheshimiwa Rais alifanikisha kuongeza bajeti ya TARURA ambapo tunafika maeneo mengi. Kwa hiyo, hata hizo barabara ambazo zimebakia tutaendelea kuzijenga kwa kutenga fedha za bajeti katika kila mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madaraja ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa vilevile lengo la Serikali kupitia TARURA ni kufungua barabara hususani katika yale madaraja mabovu yakiwemo hayo aliyoyataja. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya tathmini na tutatenga fedha ili kuhakikisha kwamba yanajengwa kwa wakati, ahsante sana.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza niishukuru Serikali kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari.

Swali langu la nyongeza, Mheshimiwa Waziri majibu yako yamejumlisha fedha zote zilizopo ndani ya Wilaya ya Igunga, hivyo basi nilikuwa nataka kuomba kwa shule zetu shikizi kwa maana ya Shule za Kazima, Mwakipanga, Mwamakingi pamoja na Shule ya Msingi Shikizi Mwasung’o. Je, ni lini Serikali itatuunga mkono kutupatia fedha kwa shule hizi shikizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Shule ya Sekondari ya Mwisi pamoja na Shule ya Sekondari ya Choma tuna uhaba wa mabwalo la chakula. Je, ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya mabwalo kwa watoto wanaotumia kidato cha tano na cha sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shule Shikizi ambazo amezianisha Mheshimiwa Mbunge lini tutapeleka fedha, nimuhakikishie tu kwamba zipo katika mipango yetu na bahati nzuri siku ya Jumatatu tumezindua mradi wa BOOST na mradi ule unagharimu karibu trilioni 1.1. Kwa hiyo, fedha zile zitakapokuwa zimekuja maana yake tutazipeleka katika shule zote nchini ikiwemo ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi huo katika Shule ya Sekondari Mwisi ambazo hazina mabweni ni sehemu ya mpango ambao sisi kama Serikali tutapeleka maana yake ni component nzima ni pamoja na mabweni. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Kata ya Mwasubi iliyopo katika Tarafa ya Mondo, Wilaya ya Kishapu ni kata mpya na haina madarasa ya kutosha katika shule ya sekondari. Je, ni lini Serikali itajenga ili kuongeza madarasa katika shule hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge tutaongeza madarasa kwa kuwa moja ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha shule zote tunazifikia kwa kuongeza madarasa na kuzikarabati. Ahsante sana.
MHE. DANIEL T. AWACK: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ahadi hii ya kilometa kumi ni toka Rais wa Awamu ya Nne, na leo tuko na Rais wa Awamu ya Sita; je, ni lini ahadi hii ya kilometa kumi itatekelezeka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mji wa Karatu uko center ya mji wa kiutalii, kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Lake Manyara, National Park na hifadhi ya Serengeti. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kujenga kilometa kumi ili kuimarisha mji uwe wa kiutalii katika Mji wa Karatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Awack, Mbunge wa Jimbo la Karatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali tutaendelea kutenga fedha kila mwaka kuhakikisha ahadi za viongozi wetu wakuu ambazo walizotoa zinatekelezeka katika Jimbo la Karatu. Serikali inaona haja muhimu kabisa ya kuhakikisha kwamba barabara hizo zinakamilika kwa sababu ya umuhimu wa eneo la Karatu hususan katika sekta ya utalii.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, katika Mji wa Mbalizi, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami; je, ni lini barabara hizo zitajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oran Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika mchakato wa kutafuta fedha, na mara utakapopata fedha hizo maana yake tutaanza ujenzi ili kukamilisha ahadi za viongozi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeahidi kujenga barabara kilometa tano kwenye Mji wa Hyadom; je, ni lini Serikali watatimiza ahadi ya kujenga kilometa hizi za lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua ahadi ambazo viongozi wametoa ikiwemo katika eneo la Hyadom, katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambako hadi sasa tunatafuta fedha na tumeendelea kutenga kila mwaka hizo fedha ambapo tutakuwa tunapeleka katika maeneo hayo ili kukamilisha ahadi hizo.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Mji wa Nkwenda ni moja kati ya miji ambayo iliahidiwa kujengewa kilometa tano za lami, hata hivyo kilometa tano hazikujengwa ndani ya mji zilijengwa katika barabara ya TANROADS ambayo inapita nje ya mji.

Sasa nataka kujua ni lini kilometa tano zilizoahidiwa kujengwa katika barabara za ndani ya Mji wa Nkwenda zitajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua ahadi za viongozi hususan katika maeneo yote ikiwemo eneo la Kwera ambalo umeliainisha hapa Nkwenda na kwa hili ambalo amelieleza ni kwamba Serikali itaendelea kutekeleza kadri ambavyo tutapata fedha, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba kuiuliza Serikali; ni lini kilometa tano zilizoahidiwa na Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano katika Mji wa Nguruka zitajengwa?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon Bidyanguze, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa ahadi zote za viongozi tumeshazichukua pale Ofisi ya Rais – TAMISEMI na jukumu letu la sasa ni kuzitafutia fedha ili kuhakikisha kwamba zinaanza kutekelezeka.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa kuwa Jimbo letu la Temeke limepata kilometa 53.10; je, huoni haja ya Serikali kufanya mazungumzo na Benki ya Dunia mapema ili kweli Julai hii hizo barabara zianze kujengwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika jibu lako la msingi umenijibu kwamba kuna kata ambazo tayari zimeshafanyiwa ukarabati na barabara hizo zinatumika. Niombe kusema kwamba katika Kata ya Chang’ombe, Sambali, Keko, Azimio, Temeke 14 na Miburani sijapata kuona hizo barabara.

Je, uko tayari kuandamana na mimi twende tukazione hizo barabara katika jibu lako la msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mapendekezo hayo yameshapelekwa na yapo Wizara ya Fedha, na mazungumzo yanaendelea, ni imani yangu kwamba haya mazungumzo yataisha kama ambavyo tulikubaliana mwezi wa saba ili sasa huu mradi wa kwa Halmashauri ya Temeke na Jiji la Dar es Salaam uweze kufanya kazi. Nimhakikishie niko tayari tunaweza tukaongoza na yeye siku ya Jumamosi, weekend hii kwenda kuziona barabara hizo.

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuwa Jimbo la Temeke linapakana na Jimbo la Ukonga na sisi ni wanufaikaji wa mradi kwenye Kata za Ukonga na Gongolamboto.

Naomba sasa kujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mradi huu kwa awamu ya tatu unazinufaisha Kata za Majoe, Kivule, Kitunda na Chanika katika barabara za Pugu, Majohe – Gwera katika barabara ya Kitunda, Kivule, Msongola…

SPIKA: Mheshimiwa Jerry Silaa hilo ni swali la nyongeza unataka kumaliza barabara zote kweli? (Kicheko)

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, aondoe shaka, kuhusu utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa ni mradi unaohusu jiji zima la Dar es Saalam ikiwemo katika Jimbolake la Ukonga. Kwa hiyo mara utakapokamilika barabara alizozianisha ziko katika huo mpango, ahsante sana.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, Mji wa Mafinga ni miongoni mwa miji 45 itakayonufaika na mradi wa TACTIC ambayo pia Jiji la Mbeya lipo.

Je, Mheshimiwa Waziri, uko tayari kukutana na Wabunge wa miji hiyo 45 ili kutueleza maendeleo ya mradi huo kama tulivyofanya kwenye miji 28 maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, nitamwambia Waziri wa Nchi na tutakutana na Wabunge wote katika hiyo miji 45 ili kuwaelezea juu ya utekeleza wa mradi huo. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, je, Serikali ina mpango gani wa kuzitumia fedha zilizobaki katika utekelezaji wa mradi huu wa DMDP Awamu ya Kwanza katika kuziboresha barabara za Jimbo la Mbagala na Jimbo la Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri na tutakwenda kushauriana na wataalam juu ya utekelezaji wa mabaki wa hizo fedha ambazo zimebakia, ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Kwa kuwa Jimbo la Kawe, katika Wilaya ya Kinondoni lina mtandao mkubwa wa barabara kuliko majimbo yote ya Dar es Salaam; je, Serikali inaweza kusema ina mkakati gani kuongeza nguvu kuongeza barabara kutengeneza kupitia DMDP awamu ya pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba tunatambua ukubwa wa Jimbo la Kawe kama ilivyo katika majimbo mengine na tunatambua umuhimu wa kuongeza bajeti. Na katika mradi DMDP moja ya vigezo ambavyo umezingatia ni pamoja na ukubwa wa maeneo. Kwa hiyo, mgawanyo utalizingatia ukubwa wa maeneo husika, ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru pia Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha Shilingi Bilioni Moja mwaka jana ambazo ndizo zimetumika kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Spika, swali, barabara hii ni moja ya ahadi ya Mheshimiwa Rais ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Je, Serikali inasemaje kuhusu hilo, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatua ya awali ni hii ambayo tunarekebisha hii barabara ili walau iweze kupitika kipindi chote wakati ambapo tunatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza hiyo ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itatekeleza ahadi yake kwa vitendo. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninamshukuru Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, kwanza; kwa kuwa sasa tuna elimu bure ya sekondari na mpaka Kidato cha Sita. Ninashukuru kwa hilo kwa Serikali, nimshukuru Mama Samia kwa kutoa elimu bure kwa Kidato cha Tano na cha Sita. Sasa lipi Serikali itafanya kusamehe michango ya sekondari 20,000? Kusamehe michango ya Kidato cha Sita na cha Tano ya 70,000 au kutoa michango ya sekondari ambayo inafikia Shilingi Laki Tano au michango ya Kidato cha Sita ambayo inafikia Shilingi Milioni Moja, kipi kifanyike sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa swali lake lilikuwa ni la jumla na nimwambie tu kwamba baada ya elimu bila ada maana yake wanafunzi wale hawalipi ile ada ambayo walikuwa wanalipa ya Shilingi 20,000 kwa Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne. Maana yake na hivi tunavyokwenda kwa Kidato cha Tano na Kidato cha Sita ambapo ada kwa miaka yote imekuwa ni Shilingi 70,000 maana yake sasa hivi wazazi hawatalipa hiyo ada ya Shilingi 70,000. Kwa hiyo, huo ndiyo msimamo wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi wote wa Tanzania ili waweze kupata elimu bila malipo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hiyo michango mingine tunaendelea kuiangalia ili kuhakikisha kwamba haiathiri masomo ya wanafunzi na wazazi kuhakikisha watoto hawa wanapata elimu bora. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kumekuwa na michango mingi sana hasa kwa hawa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano. Nina mwanafunzi ambaye hana wazazi hana familia, alikuwa anaenda Bwiru Sekondari, nimelazimika kutoa fedha nyingi mara nne zaidi ya ile fedha ya ada.

Nini sasa tamko la Serikali leo juu ya shule hizo ambazo michango ni mikubwa mara Nne zaidi ya fedha ambazo unatozwa za ada?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monnie Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kwamba yote lazima iwe imepitishwa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo. Kama kuna shule ama kuna eneo lolote lina michango mikubwa tunaomba taarifa hizo ofisi ya Rais TAMISEMI ili tuweze kuchukua hatua katika hayo maeneo ambayo wamezidisha michango.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, michango ambayo imezidi kiwango ni michango ambayo haikubaliki na Serikali tulishatoa kauli yetu.(Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Waziri kumekuwa na lugha ya pre-form one ambayo inatumika sana kwenye shule binafsi na ina michango mingi sana kwa wazazi wanaopeleka watoto kwa masomo hayo. Mnatoa tamko gani kama Serikali kuondoa hili neno la pre-form one kwa sababu inaongeza gharama kwa familia na wazazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, masuala yote yanayohusu shule binafsi yanashughuliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nasi kama wadau tunatambua mchango mzuri ambao unatolewa na shule binafsi katika kukuza elimu bora nchini. Kwa hiyo, nimuelekeze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumelipokea na tutalifikisha Wizara ya Elimu ili waweze kuchukua hatua ambazo zinastahili.

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini kwa kuwa Wabunge wote katika swali hili linaonesha ni namna gani wananchi wanakerwa pamoja na kuwa na huo mwongozo.

Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuwaelekeza Walimu na hizo Bodi wasitumie mwongozo huo kama uchochoro wa kuwapatia wazazi mzigo mzito?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumepokea wazo la Mheshimiwa Mbunge na tunatoa maelekezo kuwakumbusha shule zote nchini juu ya utekelezaji wa mwongozo huo. Ahsante sana.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza. Pia napenda kuipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na yenye kutia matumaini kwa wananchi wa Kata ya Kwamsisi pamoja na Kwamngumi kwa kuwa hiki kilikuwa kilio chetu sisi sote.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza, ninahitaji commitment ya Serikali kwamba ni kweli mwaka huu tutaenda kujengewa Skimu hii ya Kwamsisi na mwakani tutaenda kujengewan Skimu ya Kwamngumi maana imekuwa ahadi ya siku nyingi. Kwa hiyo, naomba commitment ya Serikali kwamba jambo hili linaenda kutokea mwaka huu na mwaka ujao.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, ahadi ya Serikali tulivyoahidi hapa itatekelezeka kwa asilimia mia moja. Hiki ninachokizungumza, nina uhakika nacho, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kahawa yenyewe ni bidhaa ambayo ni malighafi, swali langu ni kwamba: Ni upi mkakati wa Serikali kuvutia sekta binafsi katika kuongeza thamani kwa maana ya kuzalisha bidhaa ambazo zitachukua kahawa kama malighafi kwa mfano perfume, dawa na bidhaa nyinginezo ndani ya nchi yetu? Ni upi mkakati wa Serikali kuvutia uwekezaji wa aina hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali la msingi ambalo lina tija katika kuongeza thamani katika zao la kahawa. Miongoni mwa mikakati yetu ambayo tulikuwa tumeiweka ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi kuja nchini.
Mheshimiwa Spika, moja ya sababu ambayo tumeiweka hapo, mwekezaji yeyote atakayekuja nchini kuwekeza kwenye viwanda vyetu hususani vya kahawa, maana yake tumepunguza baadhi ya kodi ambazo zilikuwa ni kodi kero kwa wawekezaji ikiwemo kuzuia baadhi ya bidhaa ambazo zinatoka nje, zinazoweza kuua soko la ndani, pamoja na kuwapa vivutio vya muda wa kufanya kazi hizo pamoja na mazingira ya kibiashara kuyaongeza katika soko letu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mkakati wa Serikali yetu ni kuvutia wawekezaji na kila mwekezaji atafanya biashara zake hapa katika hali ya usalama zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara hii kwa kipindi cha miaka mitatu imetumia zaidi ya Bilioni Moja kuijenga na Serikali imeashaweza kutoa fedha hizo, hii ni dhahiri kwamba Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la barabara hii. Haa hivyo, barabara hii bado kuna kipande cha kilomita 18 kutoka Ifinga Mjini kuelekea Kitongoji cha Muungano na Ruhuji kilometa 18.

Je, ni lini sasa Serikali itaifungua barabara hii kuelekea eneo hilo la Ruhuji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inafanyakazi kubwa na kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameomba ongezeko la eneo la barabara la kilomita 18 kutoka Ifinga kwenda kwenye Kitongoji cha Muungano, basi naawagiza TARURA Mkoa wa Ruvuma pamoja na Halmashauri ya Madaba waende wakapitie barabara hiyo na wafanye tathmini na baada ya hapo watuletee fedha ili tuweze kui-extend. Ahsante sana.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga soko la kisasa katika Wilaya ya Bariadi, Mkoani Simiyu ukizingatia Wilaya ya Bariadi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Lucy Sabu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tulishatoa maelekezo katika Halmashauri zote ambazo zinahitaji miradi ya kimkakati kuandika maandiko ili Ofisi ya Rais TAMISEMI tutafute fedha na kuileta katika hayo maeneo ili waweze kupata masoko ya kisasa ikiwemo hiyo Halmashauri ya Bariadi. Kwa hiyo, niwape tu hilo agizo kwamba walete hayo maandiko yao nasi tutayafanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, katika swali langu la msingi naomba kuongeza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Wampembe ina Kata Nne ambazo kuna biashara kubwa sana ya samaki ambayo inafanyika na nchi jirani hakuna soko. Je, ni lini Serikali itawajengea soko kwa ajili ya biashara zao za samaki Kata ya Wampembe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mimi ningemuomba Mheshimiwa Mbunge, kwanza tumalize soko la Chala halafu baada ya hapo kama vipaumbele vinavyofuatia, maana yake linalofuatia ni hilo eneo ambalo amelifikisha hapa Mheshimiwa Mbunge. Ahsante sana.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba sasa kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itaanza kuwajengea wananchi wa Jimbo la Ngara soko la kimkakati eneo la Kabanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George, Mbunge wa Jimbo la Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninatambua kwamba Halmashauri ya Ngara imeshaleta andiko lake na wataalam katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI wapo kulipitia ili tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo, niwaagize tu wafanye haraka kwenye mapitio ya hilo andiko na kutafuta fedha ili eneo hilo la Mheshimiwa Mbunge alilolianisha waweze kujengewa soko. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Skimu ya Umwagiliaji ya Njage ilisanifiwa kutoa huduma kwenye hekta 1,750, mpaka sasa ni hekta 750 tu ambazo miundombinu ya umwagiliaji imefika.

Je, ni lini Serikali itakamilisha hizi hekta 1,000 zilizobaki?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Skimu ya Idete ni skimu inayonufaisha Jeshi la Magereza tu na Idete, wananchi wa Kata ya Idete hawanufaiki; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi pia wa Idete wawe sehemu ya kunufaika kwenye mradi huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kumjibu Mheshimiwa Kunambi Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja, tunatambua kwamba Skimu ya Njage ambayo hekta ambazo zinatumika mpaka sasa hivi ni 750 na 1,000 bado hazijafanyika. Nimwondoe hofu kwamba nimezungumza na DG wa Tume ya Umwagiliaji kuhusu expansion ya mradi huu kumalizia hizi 1,000. Kwa hiyo, amesema tutaliweka katika mipango yetu ya kibajeti ili kuhakikisha tunalikamilisha kwa wakati ili wananchi wake waweze kupata faida ya kulima katika eneo kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Skimu ya Idete ambayo inatumika na Magereza na yenyewe tumekubaliana kwamba tutakwenda kufanya usanifu wa kina kuongeza expansion ili wananchi wa Kata ya Idete waweze kufaidika. Magereza watumie na wananchi wa kawaida wa Kata ya Idete na wenyewe waweze kunufaika na skimu hiyo. Ahsante sana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona, kwa sababu Serikali imefanya kazi nzuri ya kuhimiza umwagiliaji na kadhalika. Njombe tumepata miradi hiyo na wananchi wamefaidika, wamelima mahindi na wamepata mazao mengi sana. Serikali imenunua mahindi tunaishukuru. Je, Serikali ni lini itawatamkia wananchi wa Mkoa wa Njombe itakuwa tayari kuwalipa hela walizouza mahindi yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kumjibu Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali ilinunua mahindi karibu tani 202,000 na thamani ya tani ambazo tulikuwa tumenunua ilikuwa ni karibu bilioni 187 na tumeshalipa na mpaka sasa hivi tudaiwa kama bilioni 56 ili kumaliza katika deni la awali. Tuko katika mchakato wa mwisho wa kuwalipa wakulima wote nchini wenye thamani ya hilo deni ambalo nalizungumzia la bilioni 56. Kwa hiyo nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge na baada ya kumaliza malipo, Serikali kupitia NFRA tutaendelea kununua tena mahindi ili kutimiza lengo ambalo tumejiwekea kwa mwaka, ahsante sana.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa wananchi wa Kata ya Muhamo na Msange katika Jimbo la Singida Kaskazini wamesubiri kwa muda mrefu mradi wa umwagiliaji. Je, ni lini Serikali itatangaza mradi huo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni kwamba Mradi wa Muhamo upo katika mpango wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na nimwondoe tu shaka Mbunge kwamba, sasa hivi tuko katika mchakato na tukishakamilisha tu watapata matokeo, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii, niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Umwagiliaji wa Luamfi ni mradi muhimu sana kwa wakulima wa Ziwa Tanganyika. Je, ni lini mradi huu utakamilika kwa kuwa umekuwa unasuasua sana?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimwondoe tu shaka Mheshimiwa Mbunge Aida Khenani kwamba, maeneo yote yanayofaa kwa umwagiliaji ikiwemo mradi ambao ameutaja wa Luamfi ni kwamba yote tumeweka katika mipango yetu, ambayo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaitekeleza. Nimhakikishie pia kwamba, bahati nzuri Mheshimiwa Rais anatuunga mkono sana na ameweka jitihada kubwa pamoja na fedha kuhakikisha maeneo yote yanayofaa yanafikiwa. Kwa hiyo hata hilo lenyewe tutalikamilisha kwa wakati, ahsante sana.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa, Mheshimiwa Waziri wakati akihitimisha bajeti hapa alisema kwamba hiyo tozo atakuwa analipa mnunuzi, na kwa hiyo wakulima wa arabica nchini hawatalazimika kulipa shilingi 200.

(a) Je, kwa nini bodi bado inaendelea kuwatoza?

(b) Je, kwa nini basi mnunuzi asiambiwe rasmi kwamba awe analipa hiyo, na ijulikane kwenye Hansard?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli Mheshimiwa Waziri alipokuwa anazungumza hapa wakati wa Bunge alilitolea ufafanuzi, na ndiyo maana hii bei ya shilingi 200 ikawa inawekwa katika bei ile ya jumla ya soko, kwa maana mnunuzi analipa moja kwa moja na katika ile sehemu mkulima anakatwa. Hata hivyo, mapendekezo yake sisi tunayapokea na tutayapitia upya ili tuone namna bora ambayo mkulima ataona athari za moja kwa mojo za makato hayo ya shilingi 200. Ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza, naomba niishukuru Serikali kwa kuweka mpango wa kufanya usanifu pamoja na kujenga miundombinu katika skimu ya umwagiliaji kwenye eneo la Kata ya Kihungu kwa Mwaka 2024/2025. Nina swali moja la nyongeza. Katika Kata ya Mpepai eneo la Mtuwa na Ruvuma Chini nayo ni maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya kujenga za umwagiliaji;

Je, Serikali inampango gani wa kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanajengewa skimu za umwagiliaji?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Moja, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba kilimo tunachokipeleka sasa ni kile ambacho kitakuwa kinategemea maji badala ya mvua. Yaani tunataka Mtanzania alime katika misimu yote, yaani kwa maana kipindi cha kiangazi awe na shughuli ya kufanya ya kilimo lakini na kipindi cha msimu wa mvua afanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo haya maeneo ambayo ameyaainisha Mheshimiwa Mbunge ni maeneo yote ambayo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inayapitia ili kuhakikisha kwamba yote tunayatafutia fedha na yanaingia katika mpango ili yaweze kutekelezeka, ahsante sana.

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule katika Jimbo la Mlalo Tarafa ya Umba kwa maana ya Kata ya Mng’aro, Lunguza, Mnazi lakini na Kijiji cha Kivingo tumeshatenga maeneo kwa ajili ya skimu hizi za umwagiliaji;

Je, lini miradi hii itaanza?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nimjibu Mheshimiwa Rashid Shangazi Mbunge wa Jimbo la Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba haya maeneo yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja ya Mng’aro, Lunguza, Mnazi na Kivingo wameshayaandaa kwa ajili ya shughuli hiyo. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inayafanyia kazi; na tukishamaliza kazi hiyo basi miradi hiyo itatekelezeka. Kikubwa ambacho niwaondoe shaka Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais ameweka commitment kubwa kwenye miradi yote ya umwagiliaji na fedha ipo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii. Kwa hiyo, tutafikia takriban miradi yote nchini, ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itajenga skimu za umwagiliaji kwenye Kata za Minepa, Mazimba na Lupiro Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kama nilivyojibu swali la msingi, lakini vilevile swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, nimjibu tu Mheshimiwa Christine Ishengoma kwamba maeneo yote haya ambayo yanafaa kwa ajili ya umwagiliaji tumeiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuyapitia yote nchini kuyaweka katika mpango makakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mpaka sasa hivi tumeshafikia takriban asilimia 70 ya maeneo yote ambayo yanafaa kwa kilimo. Kwa hiyo, hata haya nayo mengine yamefikiwa mengine tunaendelea na utekelezaji wake. Kwa hiyo nimuondoe shaka kazi hiyo inafanyika. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Skimu za mifereji ni skimu ambazo zilikuwepo na kule kwetu Vunjo zimekuwa zinaweza zikaleta matokeo chanya kwenye kuongeza tija kwenye kilimo. Kwa kuwa Tume ya Umwagiliaji imeshafika kutafiti na kuziangalia skimu hizi, je, Waziri anaweza akanihakikishia kwamba wataenda haraka na kuanza kukarabati mifereji ile?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Vunjo Dkt. Charles Kimei kwamba hiyo kazi tutaifanya kwa haraka iwezekanavyo kwa sababu tumepewa rasilimali zote kutekeleza jambo hili; kwa hiyo, liko ndani ya uwezo wetu. Ahsante sana.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Serikali kupitia Tume ya Umwagiliaji ya Taifa ilifika Ngara ikaanza kujenga Skimu ya Umwagiliaji ya Vigondo ila ikaitelekeza kwa miaka saba iliyopita. Naomba commitment ya Serikali;

Je, ni lini Serikali itafika Vigondo, Rulenge na Ngara kuja kukamilisha mradi wa Skimu ya umwagiliaji ya Vigondo?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nimjibu Mheshimiwa Ndaisaba Mbunge wa Jimbo la Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri jambo lake tumelizungumza jana na tumeshalifikisha kwa Mkurugenzi wa Tume; kwamba miradi yote ya nyuma ambayo ilikuwa imesimama tunaipa kipaumbele itekelezeke na ikamilike kwa wakati, na miradi mipya ambayo tunataka isaidie wakulima wote nchini nayo itakamilika. Ndiyo maana nimesema kwamba bahati nzuri Mheshimiwa Rais kama ni fedha ametupa kwa ajili ya kutekeleza miradi hii na sisi tutaitekeleza kama maelekezo ya Mheshimiwa Rais na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ahsante sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Ni muda mrefu sasa tangu serikali itoe ahadi ya kupeleka wataalam ili wakafanye upembuzi na usanifu kwa ajili ya Skimu ya Umwagiliaji ya Makangaga Kata ya Kiranjeranje katika Jimbo la Kilwa Kusini kazi hiyo bado haijafanyika mpaka sasa; je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake ya kwenda kufanya usanifu huo?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Mradi wa Makangaga uko katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa ajili ya kufanyiwa usanifu, kwa hiyo unatekelezeka katika mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa mradi huu ulitumia shilingi bilioni 1.2 na haukukamilika; je, Serikali haioni haja ya kuangalia kilichosababisha kutokukamilika ikiwemo halmashauri kutohusishwa kusimamia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa Wilaya ya Meatu hatujanufaika na Miradi ya Umwagiliaje je, Serikali pia ipo tayari kutupatia eneo la umwagiliaji katika Kata ya Mwamalole na Mwabuzo eneo moja ambalo tumelipa kipaumbele kama wilaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba tu nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na changamoto ambazo zilijitokeza awali na mapendekezo ambayo ameteyatoa sasa hivi tu miradi yote tunahakikisha kwamba inashirikisha watu wote ikiwemo halmashauri, Wabunge wa maeneo husika pamoja na Sekretarieti za Mikoa ili kuhakikisha kunakuwa na ufanisi katika kutekeleza. Kwa hiyo, tumelipokea hilo jambo na tutalifanyia kazi na hata hivyo karibuni tulikaa na Wabunge kuanisha kwenye maeneo ya miradi hiyo kuona namna gani watashiriki katika miradi yao.

Mheshimiwa Spika, la pili, kutoa kipaumbele katika maeneo ambayo ameyataja hapa ikiwemo Mwamalole. Kata ya Mwamalole nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga kwamba maeneo yote yanayofaa kwa ajili ya umwagiliaji tutayafikia na tutajenga miradi kwa ajili ya Skimu za Umwagiliaji na Mabwawa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwakunipa nafasi niulize swali. Naomba niulize swali moja ni lini Skimu ya Usense itakamilika Kata ya Ulurwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba tu nimuhakikishie Mheshimiwa Anna Lupembe kwamba kwa kuwa ujenzi unaendelea. Sisi tutakachohakikisha ni kum-push Mkandarasi aweze kukamilisha kwa wakati mradi huo kama ulivyopanga, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri suala la bei ya chai tumekuwa tukilisemea kwa muda mrefu sana ni kweli katika jibu lako la msingi mnasema kuna mnada wa chai kule Mombasa. Sisi kama Taifa tunajitosheleza kwa chai ya Rungwe, chai ya Njombe na kule Lushoto kwa nini msiweke mnada katika Taifa letu kwa sababu tunao wateja wa kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Umehamasisha Wawekezaji kuwekeza katika chai lakini wapo wawekezaji ambao hawaendi sawa na wakulima maeneo ya Rungwe kwa kutokuwapa pesa zao kwa wakati lakini tu si hivyo wanajiita Wakulima Estate lakini wakulima kama wakulima wahausiki ni mradi wa mtu binafsi. Serikali mtachukua hatua gani kuhakikisha jina hilo litumike sawa sawa na wakulima wanavyohitajika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Mwakagenda kwa kufuatilia suala hilo la chai na kama tulivyojibu katika jibu letu la msingi, kwamba mkakati wa sasa wa Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na mnada ndani ya nchi na kama alivyoainisha yale maeneo yote kwamba tuna maeneo mengi na chai inatosheleza na huo mkakati na ndiyo njia pekee ambayo itatusaidia kuongeza bei na kuimarisha soko la ndani la chai. Kwa hiyo, tumelipokea na tunalifanyia kazi na tutapata majibu haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, hukusu hawa wawekezaji ambao hawaendi sawa na Wakulima nitoe tu rai kwamba sisi kama Wizara tutakwenda tutakaa nao ili kuhakikisha kwamba hizi changamoto ambazo zinajitokeza haziendelei tena, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali la nyongeza. Shamba hili la Kisasiga lenye ukubwa wa ekari 48,000 zoezi la kupima udongo lilishafanyika na lilifanywa na watalamu wa Taasisi ya Kilimo ya TARI Mlingano tangu mwezi Agosti, 2021 na majibu yakaja kwamba shamba lile linafaa kwa Kilimo cha Alizeti. Kwa hiyo upimaji umeishafanyika, majibu yameishakuja.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni Serikali haioni kwamba sasa hivi kinachotakiwa ni kupeleka Watalam wa Miundombinu ya Ujenzi wa Block Farm ili washirikiane na Watalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kufanya tathimini ya Ujenzi wa Miundombinu ya Block Farm ili mwaka huu wa fedha unaokuja ibaki tu kutafuta fedha ili kazi ya ujenzi wa block farm ianze kwa sababu ekari 48,000 zimekaa idle na majibu tangu mwaka 2021 yameishapatika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kama ambavyo tumejibu katika jibu la msingi kwamba kuna Timu ya Watalam wa Wizara na yenyewe imefika katika eneo la Nzega na baada ya hiyo taarifa hatua zote ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema Wizara itazifanyia kazi. Bahati nzuri sana katika kipindi ambacho Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza msukumo mkubwa katika kilimo ni kipindi cha Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nimthibitishie tu kwamba shamba hilo litajengwa na Watalam watapelekwa kwa ajili ya kufanya hiyo tathimini ya miundombinu na katika mwaka wa fedha tutaliweka katika bajeti, ahsante sana. (Makofi)