Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. David Ernest Silinde (30 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa na kwa sababu umempa alert, ngoja tu tumwache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu mpaka tulipofikia leo ni mwaka wa 55 tangu tumepata Uhuru. Wakati tunapata Uhuru na mpaka Baba wa Taifa anatoka madarakani, nchi yetu ilikuwa na viwanda karibu 366 ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilivibinafsisha, ikaviua kabisa na tuna mifano thabiti.
Kwa mfano, mpaka 1984 viwanda vya nguo vilikuwa 12 leo hakuna kiwanda cha nguo hata kimoja kinachozalisha. Tulikuwa na viwanda vya kubangua korosho 12 leo hakuna kiwanda hata kimoja kinachosimamiwa na Serikali kwenye kubangua korosho. Tulikuwa na viwanda vya sukari, mkonge, viwanda mbalimbali vilikuwa 366. Tulikuwa na Shirika la Ndege mwaka 1984 tulikuwa na ndege 12 au 11 leo Shirika letu la ATC halina ndege hata moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunasema tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda ni wazo jema, lakini Mpango wa miaka mitano uliopita ndiyo ulitakiwa uondoe vikwazo vya kuelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda. Ukipitia kwenye Mpango wa miaka mitano uliopita, viwanda vinahitaji umeme, tuliwaambia na tulilieleza Taifa kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano lazima tuzalishe megawatts 2,780. Leo tuna megawatts 1,247 ambazo zimetoka mwaka 2010 - 2015 yaani tumepata ongezeko la megawatts 347 kwa miaka mitano. Bado hatujafikia lengo la miaka mitano hapo tunakwenda kwenye uchumi wa kati wa viwanda ambao upo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, unaona kabisa kwamba kikwazo hiki bado hatujaondokana nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweka lengo la barabara zaidi ya kilomita 5,000 lakini mpaka sasa ni kilomita 2,773 sawa na asilimia 53 ndizo ambazo zimejengwa. Sasa unajiuliza kwamba huu uchumi wa viwanda ambao vikwazo vyake tulipaswa kuvitatua katika Mpango wa awali wa Miaka Mitano haujakamilika, je, tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda wa namna gani? Hayo ndiyo maswali ambayo Serikali inapaswa kutujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaangalia tu focus ambayo Wizara imetuletea, inasema tuna matarajio mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 kuwa na bajeti ya shilingi trilioni 22.9 bajeti ya mwaka jana ilikuwa ni shilingi trilioni 22.45 yaani tumeongeza shilingi bilioni 450 kutoka katika bajeti ya mwaka uliopita. Ukiangalia watu wa Kenya, jana na wenyewe walikuwa wanatoa Mpango wao wa Taifa, bajeti yao ni Kenyan money trillion 2.19 ambazo ni sawasawa na trilioni 44.5 za Kitanzania. Kenya wana bajeti ya trilioni 44.5 sisi Tanzania tuna bajeti ya trilioni 22 halafu unasema tunakwenda kwenye uchumi wa kati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tukisema ni maagizo mtatulaumu lakini unaona kabisa haileti sense. Bajeti ya Maendeleo ya Kenya ni nusu, asilimia 47 ya bajeti ya Taifa, trilioni 20.195 ya Kenya ndiyo bajeti ya maendeleo sisi bajeti yetu ya maendeleo haifiki hata trilioni 10. Kila mwaka tukikaa ndani ya Bunge tunaishauri Serikali kwamba angalau bajeti ya maendeleo ifikie asilimia 35 ya bajeti husika ya nchi lakini hicho kiwango hatujawahi kufikia katika historia ya hili Taifa.
Sasa unajiuliza tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda ama tunapiga propaganda za kuwaambia Watanzania kwamba matarajio yetu ni haya, maana tumekuwa ni watu wa kubadilisha slogan ili kuwateka wananchi katika mambo ambayo tunashindwa kuyafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumekuwa ni watu wa kuwashauri tu, tumekuwa ni watu wa kuwaambia lakini mmeshindwa kuyatekeleza haya. Sasa leo tunawauliza kwenye hizo trilioni 22 bajeti ya maendeleo ina-reflect viwanda? Unakuta hai-reflect viwanda ambavyo tunatarajia kuwekeza. Kwa hiyo, mwakani Waziri wa Fedha atakuja na visingizio hivi hivi kwamba bajeti ilikuwa ndogo ndiyo maana tumeshindwa kufikia malengo. Tunahitaji kujenga reli ya kati, tunahitaji kujenga viwanja vya ndege na kununua ndege, nchi yetu haijawahi kuwa katika vikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Iran juzi wametoka kwenye vikwazo wamekwenda Ufaransa kwenye Shirika la Airbus wameagiza Boeing 108, hawa watu walikuwa kwenye vikwazo sisi ambao tumekuwa kwenye amani kwa kipindi chote tunazungumza stori za namna ileile. Unajiuliza hivi Watanzania tunayoyasema ndiyo tunayoyatekeleza? Tunaulizana kila siku kwa nini tunashindwa kutekeleza masuala ya msingi ambayo kama Taifa tumekuwa tukiyahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuzungumze…
TAARIFA
MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Silinde naomba uketi....
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, this is the fact ipo kwenye taarifa ya Wizara ya Fedha, taarifa yenyewe imesema kwamba mpaka 2010 tumezalisha megawatts 900, kutoka 2010 - 2015 tumeongeza megawatts 347 tu. Kama Wabunge ndiyo jukumu letu kuieleza Serikali. Kwa hiyo, hayo matarajio ambayo tulikuwa tumeyapanga tufikie 2,780 ifikapo 2015 ambayo bado hatujafikia. Kwa hiyo, that is the fact Mheshimiwa Waziri. Kwenye upande wa viwanda, the same applies, Taifa linaelewa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumalizia, kama Taifa na Bunge nashauri katika bajeti ya mwaka 2016/2017, lazima tutunge sheria kwenye Sheria ya Bajeti tuingize provision ya kuhakikisha kwamba Serikali inaweka at least 40 percent ya bajeti ya nchi kuwa ya maendeleo, tuiwekee sheria. Hii asilimia 35 ambayo tumekuwa tukiizungumza haina sheria ndiyo maana utekelezaji wake haupatikani. Kwa hiyo, nalishauri Bunge na hata Wizara mnapotengeneza ile Finance Bill, moja ya provision ni kuhakikisha kwamba asilimia 40 ya fedha inayotokana na bajeti nzima inakwenda kwenye maendeleo na tunaitungia sheria ili utekelezaji wake upatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine bandari tumeeleza, Bunge hapa lilitunga Sheria ya Mawasiliano (Telecom Act) ya 2009 na kuna Sheria ya Madini ya 2010 ambayo zinaitaka Serikali kuhakikisha Makampuni ya Madini pamoja na Makampuni ya Simu yanajisajili kwenye Soko la Hisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia Makampuni ya Simu yana mapato makubwa, angalia mzunguko wa Mpesa, angalia wateja ambao wako kule lakini angalia kodi wanayolipa kwenye Serikali! Makampuni ya Simu tangu 2009 mpaka leo miaka saba yameshindwa kujisajili. Kodi wanayopata Serikali siyo stahili kwa sababu tumewaambia kabisa mkiyasajili tutakuwa tunaona uendeshaji wao lakini Serikali miaka yote haifanyi. Sisi kama Wabunge jukumu letu ni kuwashauri na tumekuwa tukiwashauri lengo letu kuhakikisha Serikali inapata mapato sahihi na mkipata mapato maana yake haya yote tunayoyazungumza hatutayajadili tena kwa maana ya mdomo tutajadili utekelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokuwa tunawashauri wakati mwingine muwe mnapoekea siyo mnabisha tu. Uwezo wa kujenga hoja tunao na uwezo wa kusema Tanzania ni mkubwa kweli kweli, tatizo la Tanzania ni utekelezaji wa yale ambayo tumekubaliana ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri mnapokuja Mpango na mnajua kabisa haya mapendekezo ama mwongozo wa Mpango tunaoujadili leo ilitakiwa iwe ni extract kutoka kwenye Mpango wa Miaka Mitano kwa sababu hatuna ule Mpango wa jumla wa Miaka Kumi na Tano. Tunasema tuna Strategic Plan ya miaka kumi na tano lakini…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umekwisha.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa sababu muda tunagawana, niende moja kwa moja kwenye ripoti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti mbili zimeandikwa vizuri sana na kwa ufasaha na Kamati husika. Hata hivyo, kuna mambo ambayo kwa ujumla tunahitaji sisi kama Bunge kuya-adopt na mengine kutoa ushauri kama Azimio la Bunge kwa Serikali juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mambo mengine katika Halmashauri na taasisi zetu huko mtaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo yanakwamisha miradi mingi sana katika ngazi za Halmashauri kutokukamilika. Jambo la kwanza ni maagizo ya mara kwa mara yanayotoka kwa viongozi wa juu bila kuwekwa katika bajeti za Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa katika Halmashauri zetu kumekuwa na maagizo ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa yaani Mkuu wa Wilaya anaweza kuja katika Halmashauri akatoa agizo ambalo halipo katika bajeti za Halmashauri. Matokeo yake maagizo hayo yamekuwa yakisababisha kuwepo na reallocation. Haya ni matumizi mabovu ya fedha kwani fedha ambazo zilikuwa zimepangwa kufanya kazi nyingine zinaenda kufanya kazi nyingine na matokeo yake anapokuja mkaguzi wa fedha zinaonekana fedha za Halmashauri zimetumika kinyume na vile ambavyo zilikuwa zimepangiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili nilikuwa nashauri ni lazima liingie kama moja ya pendekezo na watu wa Serikali za Mitaa pamoja na taasisi nyingine wajaribu kulichukua na sisi kama Bunge ni lazima sasa tuiambie Serikali, Wakuu wa Wilaya wajue mipaka yao ya kazi, Wakuu wa Mikoa lazima wajue mipaka yao ya kazi na wala siyo kupanga miradi ya maendeleo katika Halmashauri. Infact hata kwa ninyi viongozi wa juu kabisa wakiwemo Mawaziri na Mheshimiwa Rais, tuwashauri vizuri tu kwamba wanapotoa maagizo, kwa mfano unasema tunakwenda kwenye operation ya madawati, ni jambo jema lakini tuseme hiyo operation ya madawati ianze katika mwaka wa fedha ujao siyo katika mwaka wa fedha husika kwa sababu inatuvuruga kabisa katika ngazi ya Halmashauri. Kwa hiyo, hilo naomba tupeleke kama moja ya pendekezo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, moja ya jambo ambalo linakwamisha sana utendaji kazi huku chini katika Halmashauri zetu, huu mfumo wa uteuzi sasa hivi umekuwa ni mbovu sana. Nalisema hili kwa sababu moja, nimeshuhudia mwaka huu tumekuwa na idadi kubwa sana ya Wakurugenzi ambao hawakupitia katika utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yamekuwa yakisemwa na hili ni vizuri tukalisema vizuri. Watu wetu kule chini wanaoanza kazi katika Serikali za Mitaa kwa mfano wanaanza with an intention, anaanza kama Afisa Msaidizi Daraja la II, baadaye anapandishwa Daraja la I, baadaye anakuwa Afisa Mwandamizi, siku inayofuatia anakuwa Mkuu wa Idara, with an intention siku moja nitakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya fulani ama nitapandishwa na nitakuwa RAS. Huu mwenendo wa sasa hivi ambapo watu wamekuwa wakitolewa from no where, mtu alikuwa tu mgombea wa Chama cha Mapinduzi anateuliwa moja kwa moja kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri, imeondoa ile morale na motisha kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii niwaambie kabisa ni moja ya jambo ambao Chama cha Mapinduzi ni lazima mjirekebishe kwenye hili, limeondoa motisha kabisa kule chini. Watu wanalalamika na wananung‟unika sana kwamba yaani sisi huku tuliko tumetumikia zaidi ya miaka 30, 20, 18 nategemea siku moja nitapandishwa cheo kumbe pamoja na utumishi wangu wote uliotukuka katika Serikali za Mitaa lakini leo thamani yangu haionekani. Matokeo yake anakuja mtu from no where na mtu yule ambaye humjui uwezo wake wala utendaji wake wa kazi, ile imeondoa sana morale, hata sasa hivi morale imeshuka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima hili lieleweke kabisa kwamba kwenye masuala ya uteuzi yabaki kama Sheria ya Utumishi inavyosema, lazima mtu atumikie kwa kiwango fulani na akifikia labda miaka saba huyu anaweza kuwa qualified kuwa Mkurugenzi Mtendaji ama kuwa DAS katika Halmashauri husika. Kwa kuendelea na mwenendo huu kitakachotokea ni nini? Wale walioko wanaweza wakawakwamisha hawa wapya ambao wanateuliwa. Wakiwakwamisha hawa wapya wanaoteuliwa zinazoathirika ni Halmashauri na wananchi katika maeneo yetu tunayoongoza. Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika Serikali zetu za Mitaa moja ya jambo ambalo linakwamisha sana kutokamilika kwa miradi ni Serikali kuchukua vyanzo vya mapato katika ngazi ya Halmashauri. Kwa sekunde mbili ni kwamba tabia ya hii Serikali kujirundikia, sasa hivi tumekuwa tukiona Serikali ikijisifu kuwa na mapato mengi lakini ukweli mapato yako mengi lakini yanatokana na vile vyanzo vya Halmashauri, haijaanzisha vyanzo vyake vipya. Kwa hiyo, tunachotaka waanzishe vyanzo vipya tofauti na kwenda kunyang‟anya katika ngazi ya Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo dogo la mwisho ni kwamba nimepitia ripoti ya PAC, imeandikwa vizuri lakini watu wa Benki ya TIB walikataa kuleta majina ya wadaiwa sugu ambao wanadaiwa kutokana na kukopa fedha kutoka Benki ya Maendeleo. Matokeo yake ni nini? Kama wameikatalia Kamati ya PAC maana yake wamelikatalia Bunge na hii ni dharau kubwa sana kwenye Bunge lako Tukufu. Hofu hii inatokana na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wasiwasi kwa sababu Mwenyekiti wa sasa wa Bodi hii ni Profesa Palamagamba Kabudi, ni mtu mwenye heshima lakini inapotokea watu wanakataa kuleta majina ya wadaiwa sugu wakati benki ina madeni chechefu ambayo hayalipiki zaidi ya shilingi bilioni 78, kitakachotokea ni kama kilichotokea kwenye Twiga Bancorp. Kwa hiyo, kwa vile hizi benki ni za Serikali na hizi fedha zinatokana na kodi za wananchi, nashauri Kiti chako lazima kichukue hatua dhidi ya taasisi zozote zinazokataa kutekeleza maagizo ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa hayo machache, nafikiri dakika zangu nyingine atamalizia mwingine. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hususan katika mpango wake wa Makadirio ya Mapato na Matumizi wa mwaka unaofuatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo napenda kuanza nalo, maana nina mambo kama sita hivi ya kuzungumza kwa haraka haraka. Jambo la kwanza ni utekelezaji wa miradi ya barabara. Hii imekuwa ni kilio kwa Wabunge wote ndani ya Bunge, nami kama Mbunge wa Jimbo la Momba nimekuwa nikilalamikia hivi kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kawaida tu ambayo hata Waheshimiwa Mawaziri wanasema, tumekuwa tukilalamikia juu ya ahadi wanazotoa Viongozi wetu Wakuu hususan Marais, zinachukua muda mrefu sana kukamilika. Nimezungumzia barabara ya kutoka Kamsamba, yaani Kibaoni – Kilyamatundu – Kamsamba unakwenda mpaka Mlowo zaidi ya kilometa 200. Aliahidi Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete mwaka 2009, lakini barabara ile mpaka leo imekuwa ni story ambayo haibadiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri hapa, ukiangalia kwenye ukurasa wa 269, fedha iliyotengwa mle ndani, unakuta tu ni rehabilitation, sijui feasibility study, yaani shilingi milioni 120, shilingi milioni 200; kwenye zaidi ya kilometa 200, ni sawa na kazi bure. Kwa hiyo, tunataka Serikali iwe na mpango maalum kukamilisha hizi ahadi za Waheshimiwa Marais wanazozitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuendana na barabara hiyo msisahau lile Daraja la Momba. Mmelitengea shilingi bilioni tatu, wananchi sasa tumeshachoka kusikia zile story za kila mwaka; fedha inatengwa, feasibility study, tuko site; tunataka daraja, hatutaki story hizo ambazo zimekuwa zikijirudia kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu kwa haraka haraka ni usimamizi wa huduma za usafiri na uchukuzi hususan majini na kwenye maziwa. Sana sana mnachokuwa mnazungumzia kila mara, Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa; lakini kuna maziwa madogo madogo yaliyoko kule kwetu, kwa mfano Ziwa Rukwa liko mpaka kule Momba; kuna Ziwa Manyara, watu wanakufa kule kila siku, maboti yanaua watu, lakini taarifa zake huku huwezi kuzikuta na hakuna hatua yoyote ambayo inakuwa ikichukuliwa na Wizara yako. Kwa hiyo, tungependa mnapotoa ufafanuzi muyajadili pamoja na maziwa haya madogo likiwemo Ziwa Rukwa na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kuyajadili hayo machache ya Jimbo langu, nizungumze sasa masuala ya Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia Shirika la Ndege (ATCL) ni kama vile hatujawahi kuwa na shirika nchi hii. Yaani ni kama vile ndiyo limeanza mwaka 2016, lakini ukweli ni kwamba Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati anaondoka madarakani aliacha ndege 11. Hii kila mtu anajua kwamba ziliachwa ndege 11 ambazo zilipotea katika mazingira ambayo hayaeleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nia njema inaonekana kwamba tunahitaji kufufua shirika letu la ndege na kuna sababu za msingi zimeelezwa, hakuna mtu anayebishana nayo; lakini kuna mambo tunahitaji kuwashauri kama wachumi. Kununua ndege cash kwa kulipa asilimia 100 siyo sifa nzuri sana kiuchumi tofauti na utaratibu ambao duniani watu wote wanatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimeona kwenye bajeti mmetenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa ndege, ni jambo jema hakuna mtu anayekataa. Nunueni ndege kama utaratibu wa watu wengine wanavyofanya. Lipa ten percent, ndege inakuja nchini inafanya kazi. Kwenye hiyo fedha mnaweza kununua zaidi ya ndege kumi tofauti na sasa hivi mnavyotaka kwenda kulipa cash. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa sisi hatukatai, lakini tunachojaribu kuwashauri, jaribuni kufanya mambo kwa utaratibu wa kawaida wa kichumi ambapo fedha moja inaweza ikasaidia mambo mengine wakati jambo lingine na lenyewe linafanyika. Kwa hiyo, hicho ni kitu ambacho nasema ni muhimu tukawa tunakizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tuelezeni kuhusu deni ambalo lilikuwa linaikumba ATCL, kwamba mnasema ndege zitakuja, hofu yetu ni kwamba kwa mfano hiyo ndege ambayo itakuwa inakwenda mpaka huko Uchina sijui wapi; tunafahamu kuna kesi Mahakamani kuhusu Shirika la ATCL, madeni yanayodaiwa; ikitokea sasa ndege ikaenda kule, ikakamatwa ikazuiwa kule, maana yake hasara kwa Taifa itaendelea kubaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka tujue kwa nini Serikali imechukua hatua ya namna hii kwa sababu mpaka sasa hivi hizi ndege zimekuwa zikinunuliwa kwa utaratibu mmoja tu; wa Mheshimiwa Rais kununua na kuzileta ndani ya nchi, lakini ule utaratibu wa kishirika wa kiuendeshaji ambao unaweza kuwaathiri huko nje kutokana na deni ambalo shirika lilikuwa nalo tangu awali utatupeleka wapi? Kwa hiyo, tungependa tupate ufafanuzi juu ya hili jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza jambo la tatu kwa haraka haraka kuhusu Shirika la TAZARA. Kila mwaka tumekuwa tukilalamika kuhusu TAZARA, kwamba TAZARA haifanyi kazi vizuri, sasa hivi ukiangalia kwenye rekodi zao wanasema mwaka huu angalau umebeba mizigo tani laki moja. Wakati Shirika la TAZARA linaanza lilikuwa linabeba mizigo tani milioni moja kwa mwaka, sijui kama umenielewa, lakini leo tunajisifu kwa tani laki moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jibu ni moja tu, kwamba nchi mbili wanachama, zinategeana juu ya hili shirika, ndiyo maana hili shirika haliwezi kuendelea. Kila siku mgogoro kwenye hili shirika umekuwa ukisemekana ni management, lakini ukweli ni kwamba hapa kuna kutegeana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama mnashindwa, kuna plan B vilevile. Mnaweza mkazungumza na Zambia pamoja na Tanzania mkakubaliana kwamba sisi tunafikiri hii reli kutokea Tunduma mpaka Dar es Salaam, sisi watu wa Tanzania tuwe tunaihudumia wakati huu kuna matatizo. Watu wa kutokea Tunduma mpaka kwenda New Kapiri Mposhi kule wahudumie watu wa Zambia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu mizigo siyo tu ile inayotoka Kongo, kuna mizigo ambayo inatoka Mbeya pale kuja Dar es Salaam; kuna mizigo inayopitia Iringa na maeneo mengine; tunaweza tukaitumia hii kama sehemu mojawapo ya reli ya kati, yaani mkavunja mkataba, kila mmoja wa kipande chake akatumia huku na wao watu wa Zambia wakatumie kule. You can go on that way, inaweza kusaidia kuliko sasa hivi mnatumia fedha nyingi na shirika halionekani likienda mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka nizungumzie hapa, nimeona kwenye hotuba, Serikali inataka kufufua Shirika la TTCL. Shirika hili lilikuwepo tangu mwaka 1993, lakini kwenye records hapa wanasema tunataka tutoke wateja laki mbili mpaka kufika milioni moja; mpaka mwaka 2020 wanahitaji kufikisha wateja milioni nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Master plan ya investment yao, fedha wanazohitaji ni Dola 663,000 kwa miaka hiyo mitano ili wafikie wateja milioni nne lakini ukiangalia Kampuni dogo kabisa la Hallotel ambalo limeanza Oktoba, 2015 wenyewe within mwaka mmoja na kidogo wame-invest dola bilioni moja, wana wateja 2.7 million.
Mheshimiwa Naibu Spika, mindset ya Watanzania bado imekaa ile ile kwamba sisi ni Serikali, tutaliendesha Shirika Kiserikali; sasa imegeuka mashirika yote Serikali ihudumie; haiwezekani! Kwa hiyo, lazima tu-change mtazamo huu ambao umeenda; na ndiyo maana unakuta hata Shirika la ATC sasa hivi linakwenda katika huo mtazamo wa Kiserikali Serikali, siyo mtazamo wa Kikampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi biashara ni ushindani! Sasa huwezi kwenda kwenye ushindani wa kimawasiliano unaona kuna Vodacom pale, kuna Tigo, kuna Airtel halafu na wewe unakuja TTCL kwanza una-invest kidogo, pili hamna marketing strategies ambazo unaweza uka-penetrate kwenye market, lakini mtu atakuja atasema hawa Hallotel wanatumia mkongo wetu. Yes, wanatumia minara ya TTCL, lakini at the end of the day gharama yao wao Hallotel iko chini kuliko gharama ya wao wanaomiliki huo mtambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo unakuwa unajiuliza, hapa utakuwa unafanya nini katika hili Taifa? Yaani we don’t think big! Bado mitazamo yetu kufikiri juu ya biashara ni mitazamo ya kijima. Tunafikiri bado kule nyuma kwamba Serikali inaweza kufanya kila kitu, lakini sasa hivi dunia inaendeshwa na market forces; soko huru ndiyo linaloamua juu ya uendeshaji wa uchumi wa nchi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda haya mashirika na hizi taasisi ndogo ambazo tunataka Taifa lifanye biashara, zisibaki na huu mtazamo; hii mindset ya sasa kwamba kila kitu Serikali ita-inject fedha pale, kwamba Serikali ndiyo itaendesha hiyo kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Shirika la ATC, Serikali ikitoa mkono maana yake na Shirika lenyewe linakufa kwa sababu mtazamo wetu si ule ambao kwamba tunaweza kujiendesha wenyewe tukafika kule tunapotakiwa, kwa sababu sasa hivi kila kitu tunataka investment ya Serikali. Kwa, kwa hiyo, ni lazima tubadilishe mtazamo wetu dhidi ya haya mashirika ambayo Serikali inahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, nashukuru na naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kupata fursa ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango. Sisi kama Taifa tuna tatizo kubwa sana la kiuchumi yaani kwa lugha nyepesi tunaweza tukasema tuna economic crisis na ndiyo tatizo la ki-mindset kwa watu wote. Tatizo tulilonalo kama Taifa tunataka kutatua matatizo ya kiuchumi kwa majibu ya kisiasa, hilo ndilo tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mapato kila siku yanashuka. Hata kule TRA mapato yanashuka mpakayameachwa kutangazwa sasa hivi. Lakini majibu yanayokuja ya kisiasa. Niseme tu kwamba hata bajeti ya mwaka 2017 ambayo sisi kama Wabunge hususan Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tumekuwa tukiita ni bajeti ya kihistoria. Mimi nasema ni bajeti ile ile kwa sababu hakuna jambo jipya ambalo unaweza ukajifunza kwenye hii bajeti. Na niseme tu kwa mara ya kwanza hii bajeti ina tone ya kisiasa yaani siasa ni nyingi kuliko hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa huu utaratibu tutashindwa kupata suluhu ya tatizo na ndio maana siku mbili/ tatu uliona issue ya makinikia sasa badala ya ku-solve kitaalam suala la makinikia linatakiwa li-solve kisiasa kwa hiyo ikawa sasa politics inatawala kwenye jambo ambalo linatakiwa watu walijadili kitaalam, hilo ndilo tatizo tulilonalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye bajeti karibu kila kitu ni kile kile, nchi za wenzentu kwa mfano nchi ya Kenya wanapoandika bajeti kama hii wanakukambia bajeti yetu kwa mwaka huu itapunguza tatizo la ajira kwa kiasi fulani. Sisi bajeti yetu imezungumzwa yote, lakini haikuambi mwaka huu wa fedha 2017/2018 tutapunguza ajira kwa kiwango gani. Majibu ni yale yale tatizo la kiuchumi linatafutiwa suluhu ya kisiasa. Hilo ndilo tatizo tunalokabiliana nalo. Bajeti za wenzetu inapojadili namna ya kupunguza umaskini inaeleza vizuri kabisa, bajeti ya mwaka huu shilingi trilioni 31 kwenye bajeti ya maendeleo shilingi trilioni 11 tutapunguza umasikini kwa kiwango cha asilimia moja, wenzetu wanaeleza bajeti hii haielezi, hata mpango wenyewe haulezi hauende direct kwenye haya mambo. Tatizo ni lile lile, matatizo ya kiuchumi tunataka kuyatatua kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu nchi nyingine Bunge halijadili madawati au sijui Halmashaluri yangu haina vyoo, hayo ni mambo yanayotakiwa yajadiliwe kwenye ngazi za Halmashaluri. Bunge tunatakiwa tuzungumze mambo makubwa sera za kiuchumi za kitaifa. Tuishauri Serikali namna ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, haya ndiyo mambo ambayo tunapaswa kuyajadili. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kimoja, mwaka 2014 Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Kinana alipokuwa Mbeya katika uwanja ule wa CCM akasema vizuri kabisa kwamba CCM tunapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa sababu tumewakosea sana. Haya maneno hata ukienda kwenye YouTube utaikuta ile hotuba ya Mheshimiwa Kinana alieleza vizuri sana kwa sababu alikuwa anajua na aliainisha kwa nini tuwaombe radhi Watanzania, sasa hapa hakuna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii bajeti ya kihistoria, mimi nilijadili hapa namtafuta mtu maskini anaondokaje kwenye wimbi la umaskini, sioni, ndiyo zinaongezeka hizi sera. Wamekuja hapa na kufuta hiyo annual motor vehicle license ya shilingi 40 halafu unasema kwamba itaongeza tu shilingi bilioni 27.

TAARIFA

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kangi Lugola ni rafiki yangu wa karibu sana na anapozungumza kauli kama hizi unajua ukimjibu kisiasa atapotea kabisa kwa sababu nchi hii tumeshawahi kuwa na Rais Mwamba wa Afrika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Sasa ukisema Nyerere unaweza ukamtoa kwenye hiyo reli unakuwa unakosea sana na siyo majibu mazuri. Akumbuke vizuri kabisa kwamba wapo akina Mkapa na Kikwete hatujawahi kupuuza mchango wao pamoja na kwamba wamewahi kuwa na makosa. Kwa hiyo, ni vizuri Mheshimiwa Kangi ukatambua mchango wa wale wazee wengine maana yake wakikusikia wewe uliyekuwa unawaunga mkono leo ni kama vile unaona hawakuwepo, siyo jambo jema kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna shida na uwepo wa Rais Magufuli, hatuna shida na jambo hilo lakini tunachokijadili, tunajadili ni namna gani Chama cha Mapinduzi kinavyotekeleza hizi sera ambazo hazitekelezeki. Unajua kuna kitu kimoja watu wanasema ametoka Kikwete amekuja Magufuli lakini wote wanatekeleza Ilani ya chama kimoja. Magufuli hatekelezi sera za kwake binafsi, anatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ndivyo alivyofanya Kikwete, Mkapa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huwezi kuwatofautisha Magufuli na Chama cha Mapinduzi ama Kikwete na Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, jibu jepesi ni kwamba Serikali iliyokuwepo madarakani kwa kipindi chote ni ya chama kimoja ya Chama cha Mapinduzi tu. Kwa hiyo, makosa yote ambayo tunayataja yameletwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, hicho ndicho tunachokijadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu vizuri kwamba tunahitaji kujadili mambo ya msingi, kwa mfano Waziri wa Fedha hapa amekuja ameongeza shilingi 40, kuna watu wameeleza hapa wanaona kama vile ni kisenti kidogo lakini cha ajabu sisi tume-question pale unaongeza shilingi 40 kwenye mafuta ya taa, hebu Mheshimiwa Waziri wa Fedha nieleze kwenu Buhigwe ni gari gani inatumia mafuta ya taa

ama kuna Bajaji inatumia mafuta ya taa yaani unakuta hakuna majibu. Sasa of all kwenye ile lita moja ya mafuta ya taa bado Serikali inapata shilingi 425, tozo inatoka pale. Kwa hiyo, ukiongeza shilingi 40 maana yake mwananchi wa kijijini atalipa tena shilingi 465 nyingine, sasa hayo ni maswali ambayo tunapaswa kujiuliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda watu hawajui, kwa siku sisi kama Taifa tunatumia lita 8,300,000; lita 5,000,000 zinatumika kwenye mafuta ya dizeli, lita 3,000,000 tunatumia kwa ajili ya mafuta petroli na lita 300,000 yanatumika kwenye mafuta ya taa. Sasa jaribuni kukokotoa ndiyo mtajua kiwango ambacho kinakwenda kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuli-propose hata kwenye Kamati hata Mheshimiwa Waziri wa Fedha anaweza kujua, tulisema ni bora ikaongezeka shilingi 50 kwenye mafuta iende kwenye maji ili wananchi wa vijijini wapate maji kwa sababu tatizo la nchi hii ni maji. Waziri akakataa akasema hiyo Sh.50 ikiongezeka itaongeza gharama ya mafuta na wananchi maskini watapata shida. Sasa leo kafanya kitu kile kile kwenye angle nyingine, sasa maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine ni kutokuaminika, sijui ni kutojielewa au kijichanganya, hayo ndiyo mambo ambayo sisi siku zote tumekuwa tukiyapinga na tunalieleza Bunge lijaribu kuyaangalia. Ingekuwa vizuri sisi kama Bunge kwa umoja wetu tukakubaliana hapa kwamba pamoja na kwamba motor vehicle imefutwa, kwa kifupi siyo kwamba imefutwa isipokuwa tumebadilisha tu utaratibu wa kulipa. Kufuta maana yake hicho kitu hakitakiwi kuonekana mahali popote, ni kwamba tumebadilisha kutoka kulipa direct inakwenda kulipwa indirect, mfumo ni ule ule yaani kupunguza maumivu ya namna ya kulipa, haijafutwa. Ieleweke vizuri haijafutwa ila tumebadilisha utaratibu, kama ni kufuta unaoindoa pale.

Sasa hii shilingi 40 kama Bunge tuidhinishe humu ndani iende kwenye miradi ya maji vijijini ili wananchi wote wapate maji safi na salama lakini ikienda huko huko itaishia tu kuwa katika matumizi ya kawaida na mwisho wa siku haitafanya jambo lolote la msingi kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa angalia trend za bajeti zote za miradi ya maendeleo, kwa miaka nenda rudi bajeti za miradi ya maendeleo zimekuwa zikitekelezwa kwa kiwango kile kile chini ya asilimia 40. Sasa leo unapokuja na bajeti ya tone ya namna hii, mwakani sisi tutakuhoji tu vilevile. Maana yake hapa tumeficha uso wetu kwamba mwaka jana ni kama vile hakukuwa na jambo lolote lililofanyika lakini ukweli mwaka jana Wizara ya Fedha na Mipango mmefeli kwa kiwango kikubwa tofauti na matarajio ambayo tulikuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alipokuja bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri akajisifu akasema mimi ni ndiyo nimeingia, nisikilizeni, mambo yatakavyokuwa motomoto basi sisi tukakosa mpaka hoja, iwe ni Wapinzani na Chama Tawala tukakaa kimya tukasema ngoja tusubiri kinachokuja, kilichotokea ni nini? Ni yale yale ambayo miaka ya nyuma yamekuwa yakifanyika, utekelezaji wa bajeti ya maendeleo upo chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba Serikali itakapokuja kuhitimisha ituonyeshe namna gani inaweza kutekeleza ile bajeti yake ya miradi ya maendeleo na iainishe vyanzo vipya. Kitu kingine tunakushauri chukua kwenye bajeti yetu mbadala, kuna vyanzo tumekushauri ikiwemo Euro Bond, float Euro Bond utapata karibu shilingi trilioni 2.2 itakusaidia kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo. Ni ushauri wa bure ambao kama ukitaka unaweza kuchukua na usipotaka basi lakini kwa maslahi ya Taifa, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii nami kujadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019. Mapendekezo ya mpango ambayo tunayajadili leo hayana tofauti na mapendekezo tuliyopitisha mwaka jana, hakuna tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hauna tofauti kwa sababu tone yake ni ileile ya mwaka jana, ndiyo ambayo ipo katika kitabu hiki cha mwaka huu, ukikipitia chote kama kilivyo, kina tone inayofanana. Sasa changamoto yake ni nini? Changamoto ya mpango wote ni utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakwenda kwenye hoja ambazo zipo kwenye kitabu. Mimi leo najadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Serikali ya Awamu ya Tano ina sifa moja imejinasibu kama Serikali ya kubana matumizi, lakini kwenye kitabu hikihiki unarudi unakuta deni la Taifa limeongezeka toka dola milioni elfu 22 mpaka dola milioni elfu 26115.2 ambayo ni sawasawa na trilioni hamsini na tisa. Sasa wewe unasema umebana matumizi, deni limeongezeka, unawachanganya wananchi, kwa hiyo sasa ndiyo vitu tunavyokwenda kuvijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda kuuliza sababu za kungezeka kwa deni ni nini Mheshimiwa Waziri amekuja sababu za kuongezeka kwa deni la Taifa ni ujenzi wa reli ya standard gauge, SGR, Strategic Cities mradi wa Usafirishaji Dar es Salaam (DART), sasa the question ni nini? Mheshimiwa Rais anapozunguka huko mtaani anatueleza kwamba tutajenga reli kwa fedha zetu za ndani, unakuta kwenye kitabu, kitabu kinasema tofauti kwamba tutajenga reli kwa mkopo, tuelewe nini, yaani tuelewe nini, kinachoandikwa na kinachozungumzwa ni vitu wiwili tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni mambo lazima tukubali kuyarekebisha, yaani siasa siyo kupiga fiksi muda wote au siasa sio kutafuta kiki muda wote hamna, wakati mwingine wananchi wanahitaji kuelewa ukweli. Tuwaeleze tu ukweli, tutajenga reli kwa mkopo, tutakopa kiasi hiki zitalipwa na wananchi, unapata sifa kwa sababu wananchi wanachotaka ni miradi ya maendeleo, sasa unawaambia tutajenga, kitabu kimeandikwa na ushahidi wetu unaotumaliza ni hiki kitabu. Hilo nimelimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni matumizi ya fedha nje ya bajeti tulizozitenga. Tumekaa hapa zaidi ya miezi mitatu tunapitisha bajeti, tunapitisha vifungu na mwisho wa siku kuna kitu kinaitwa Appropriation Bill, Sheria ya Matumizi ya Fedha. Ile sheria inatufunga kwamba tutumie kulingana na kile ambacho tumekipanga humu ndani. Sasa unakwenda kwenye kitabu unakuta sasa kuna miradi mipya tu kwamba miradi ya ujenzi wa bwawa wa mitambo ya kufua umeme Stiegler’s Gorge siyo jambo baya wala sikatai, lakini unarudi Sheria ya Bajeti inataka nini? Ukiangalia kifungu cha 43 cha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 inataka Serikali inapotaka kuongeza bajeti ije hapa. Ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Chato sio kosa, ni nia njema ile, lakini usipofuata sheria...

T A A R I F A . . .

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ni vizuri nimweleze kabisa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, mimi sipingani na kutenga fedha ya bilioni mbili ipo kwenye bajeti. Hiyo ilikuwepo na ndio maana hakuna mtu anayejadili, lakini sisi tunachojadili ile bilioni 39, ambayo iko nje na kinyume cha bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunajadili. Ni mambo mema Sheria ya Bajeti kifungu cha 43(1) ya mwaka 2015 inaruhusu Serikali kuomba nyongeza ya bajeti na inawekewa mkazo na Sheria ya Fedha za Umma, kifungu namba 18(3) na cha (4) ya mwaka 2000; vyote hivyo inataka Serikali inapotaka kufanya jambo kwa mfano unataka labda kuli-allocate ama kuongeza jambo lingine jipya ambalo halikuwepo kwenye bajeti unaleta ndani ya Bunge. Sasa mambo mengi hapa ndani yanayofanyika sasahivi na Serikali hayajapitishwa na hili Bunge, hayajapitishwa na tumekaa humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoeleza ni nini? Leo unayafanya haya in good faith unasema unatumia kwa nia njema, lakini kesho atakuja Rais mwingine, Mheshimiwa Mpango utakamatwa kwa kutumia madaraka yake vibaya huo ndio ukweli. Kwa sababu hapa Mheshimiwa Simbachawene juzi alijiuzulu kwa sababu tu aliingia mkataba wa TANZANITE, lakini kwenye maelezo yake alisema kabisa ametumwa juu, lakini leo amewajibika yeye. Kumbukeni watu wanaowatuma wana kinga, wao hatuwafungi, wala hatutawakamata. Kesho nakueleza ukweli sio lazima atoke Upinzani huyo Rais, atakwambia nani alikupa mamlaka ya kuidhinisha fedha za Stiegler’s Gorge, nani alikupa mamlaka ya kupitisha fedha nanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachotaka sisi hapa, tunataka tu Serikali ifuate utaratibu, kwani tatizo liko wapi? Ni jambo jema, ni kwa nia njema tunakutakia mema na tunakuonea huruma wewe kwa sababu baadaye mimi nitakuwa shahidi kwamba ulikuwa unakataa ushauri ndani ya Bunge na nitataka, hiyo kamati ya uchunguzi utakapokuwa unaenda ndani mimi nitakuja kutoa ushahidi kwa sababu tulishauri, kwa sababu tunayajua haya, sheria zipo na uzuri wa hii nchi ni kwamba sheria zipo, unless otherwise, leo Sheria ya Manunuzi iko likizo yaani iko likizo kabisa hakuna mahali inapotumika yaani mambo yanajitokeza tokeza tu huko, unashangaa tu kitu kimefanyika, baadaye procedure ndio zinafuata, yaani unaanza ku-take action halafu baadaye unafuata procedure. Haya yote yataundiwa Kamati ya Uchunguzi na tawala zinazokuja, miaka minane au mitatu sio mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili nataka tu nimwambie Mheshimiwa Waziri. This is politics, politics lazima ujue namna ya kui-handle, kwa sababu politics ina repercussion, utabaki peke yako na hakuna mtu atakayekuja kukuangalia muda huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukijadili hapa issue ya maji, maji ni kero kwa nchi nzima. Unapitia Mpango hapa unakuta imeandikwa sijui visima kumi na tano; Mpiji, issue za Halmashauri tu, hizi ni issue ndogondogo kabisa. Sera ya Maji inazungumzaje, sera ya maji inataka Mtanzania akichota maji mbali ni mita mia nne, lakini sasa hivi uhalisia ni upi? Wananchi wanapata shida, ukija ukisoma takwimu za Wizara watakwambia maji mijini wanapata kwa aslimia zaidi ya themanini; maji vijijini zaidi ya asilimia sitini na tano, lakini je hali halisi maji yanapatikana? Kauli mbiu ya Serikali inasema tumtue mama ndoo kichwani, ndoo hiyo imetuliwa, tuwe wakweli, ndoo imetuliwa? Jibu unakuta kwamba haijatuliwa na kila mmoja anatafuta mahali pa kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni mambo tunayohoji ya msingi kwa nia njema tu, tengenezeni bajeti ambayo inatekelezeka. Sasa haya yote haya ndio mambo ambayo tumekuwa tukiwaeleza humu ndani na nafikiri Waziri wa Maji aliyekuwepo anajua haya mambo, nini kimemtoa pale sasa hivi? Sasa haya yote ndiyo haya tunayoyazungumza watu wanataka maji, hawataki stori za kwenye vitabu, hizi tumeshachoka nazo. Kwa hiyo sasa hayo ni mambo yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Sekta binafsi, Serikali imeijadili kidogo sana yaani ka-paragraph kamoja tu, lakini ukweli Sekta binafsi imeporomoka. Mabenki yanapata hasara, mzunguko wa fedha umeshuka, mikopo chechefu imeongezeka, watu wanashindwa kulipa madeni, Serikali haijajadili mpango wa namna ya kuiwezesha Sekta binafsi ili iweze kuwa imara, inakuja na sheria, sasa hivi kila siku wanaleta sheria, sasa hivi wanaleta Sheria ya NASACO, yaani kila kitu unataka Serikali ifanye biashara na Serikali yenyewe. Hiyo principle ya wapi, duniani ilishashindwa, kama unafuata policy ya China hawaendi namna hiyo na namna China walivyobadilisha uchumi wao sio kwa staili tunayokwenda nayo, hii ni staili ya kutuvuruga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya yote hatutaki kuyasema lakini ni kwenye vitabu, leo unazungumza ili uchumi ukue ni lazima watu wakose hela, hiyo siyo interpretation sahihi. Kufanya biashara na sekta binafsi sio chanzo cha ubadhirifu wa fedha, kunatakiwa kuwe na namna ya ku- handle wale watu, kuna namna ya kufanya nao kazi na tueleze tu ukweli watu wanahitaji ajira wote tumekuwa tukijadili hapa kuna tatizo kubwa sana la ajira nchini, lakini ajira sio lazima ajiriwe na Serikali; mtu hata akiajiriwa benki pale CRDB anasema nimeshapata ajira yangu; mtu akiajiriwa pale na Mohamed Dewj anasema mimi nimepata ajira; mtu akiajiriwa na Coca Cola anasema mimi nimepata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo nenda kwenye hayo Makampuni yote Coca Cola wamepunguza wafanyakazi, ukienda Mabenki wanapunguza wafanyakazi, lakini yote hapa bado Serikali haijaja na mpango makini wa kuhakikisha kwamba sasa tuna-revamp sekta binafsi iweze kusaidia kwenye uchumi wetu. Sasa haya yote tunajaribu kumwelimisha lakini anakuwa mgumu wa kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimweleze Mheshimiwa Waziri this is politics na ndio iko hivihivi, utakuwa hapo utaondoka, utawala uliopo uko leo, kesho utaondoka, ndiyo maisha yanavyokwenda, tusikilizane, tuelimishane ili tuweze kuelewa wapi tunapotaka kuelekea, kwa sababu tunataka uchumi imara. Sasa hizi sera mnazokuja nazo hizi na NASACO kila siku tunapitisha sheria mpya sisi tunawaangalia tu, zinafukuza wawekezaji, lakini haziruhusu mazingira ya watu kurudi nchini kuwekeza ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya yote ni masuala ya kiuchumi ambayo tunayakwepa kwa sababu na bahati mbaya nchi yetu tunataka nchi ya kijamaa halafu tunataka matunda ya kibepari, haiwezekani! Ni biashara ambayo haipo yaani na hicho ndicho ambacho mimi nakiona kwamba tuko wajamaa lakini tunataka matunda ya kibepari, biashara hiyo haipo.

Sasa Mheshimiwa Waziri lazima akubali na nasoma hotuba yao, tumekwenda tumefuata mpango wake kwa umakini sana na uzuri kitu kimoja tu Mheshimiwa Mpango ndiye yeye aliyeandaa mpango alikuwa Katibu Mkuu wa Mipango, makosa yote anayoyakosoa ya Serikali ya nyuma yeye ndiye aliyeyafanya. Kwa hiyo, akifitisha fito au kufanya nini ni yeye ndiye mwenye haya makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifurahia sana Mheshimiwa Rais alivyomweka Mheshimiwa Mpango pale, nikajua sasa huyu aliyetengeneza mpango sasa atausimamia vizuri. Eeh, bwana eee, kila kitu hamna kitu, biashara hakuna, yaani mambo yanafanyika chini ya standard. Bahati mbaya sana wanataka sifa, yaani kakitu kadogo wanataka wasifiwe, tulieni mambo yanajifanya yenyewe, tekeleza wajibu wako, watu watakupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nashukuru sana. Nafikiri elimu imemwingia, atayafanyia kazi. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bunge limekuwa kila siku moja ya ajenda yake ni kupata semina elekezi kupeleka kwa ma-RC pamoja na ma-DC. Lengo la hizi semina ni kwa sababu ya haya mambo yanayotokea, haya tunayoyasema kama hawa watu wangepatiwa semina elekezi wakajua mipaka ya mamlaka yao naamini yasingetokea. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, mercury ina tabia moja, ukiifukia chini ya ardhi hata kama ni kilometa tano chini ya ardhi, itapanda itaibuka juu. Sasa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ana tabia za mercury yaani ananyanyuka. Hali iliyopo sasa hivi ni kwamba yaani akitoka Rais anayefuatia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam yaani Waziri wa Mambo ya Ndani hayupo, IGP hayupo, Waziri Mkuu hayupo, hakuna mtu yeyote, Bunge kama mhimili halipo, yaani imefikia mahali…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni vizuri nikali-clarify kidogo. Nafikiri Mheshimiwa Waziri hajaelewa au hajanisikia vizuri, hata akirudi kwenye Hansard ataona kitu ambacho nimekizungumza. Ninachokifanya hapa ni kutetea Baraza la Mawaziri pamoja na Waziri Mkuu, ndicho ninachokifanya hapa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM kabla ya mwaka 2015 ndiyo chama kilichokuwa kinasifika kwa protocol, chama ambacho kilikuwa kinajua kiongozi gani afanye nini kwa wakati gani, suala la protocol lilikuwepo. Hata hivyo, sasa hivi protocol ile ambayo tulikuwa sisi wachanga wa vyama tunajifunza kwenu leo haipo kabisa, protocol imevurugika, hicho ndicho nilichokuwa nakielekea. Ndiyo maana nikasema ni kama vile, yaani mambo anayoyafanya ni kama vile anaona kama hakuna Waziri Mkuu, tena nimetumia neno ni kama. Wewe leo unakuta mtu ana-suspect mtu mmoja, huyohuyo ana-arrest, huyohuyo ana-interrogate, huyohuyo anahukumu just one person! Hakuna utaratibu huo katika nchi hii! Ndiyo maana ya hiki tunachokifanya hapa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kitu kimoja, Rais anasikia, Wabunge tumelalamika kuhusu Tume leo ameteua Tume, anasikia. Rais akishauriwa vizuri mimi nina uhakika, akishauriwa vizuri kwa mawazo mtangamano akayasikiliza, atakuwa the best President lakini Rais akisikiliza mawazo ya upande mmoja hawezi kuwa Rais mzuri. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachokifanya hapa tunataka Bunge kama mhimili ufanye kazi yake na tunataka Mawaziri wafanye kazi yao. Mimi niwapongeze, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa busara uliyoionesha, nakupongeza sana Waziri wa Mambo ya Ndani kwa busara uliyoionesha katika kipindi hiki, hii lazima tupongeze, nampongeza sana Kiongozi wa Upinzani pamoja na IGP kwa busara waliyoionesha. Wangekuwa hawana busara nina uhakika sasa hivi hili jambo lingekuwa limeshaharibu utaratibu wote wa nchi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunasema kwamba hatutaki mgongano wa haya mambo. Ndiyo maana tangu mwanzoni nikaelezea tabia ya mercury ukiidumbukiza hata kilometa tano itanyanyuka sasa hizi tabia ndiyo wanazo watu. Sisi tuliokwenda Jeshini kule tunafahamu zile 22 critics. Sasa tunachotaka wapelekeni na hawa vijana kule Jeshini wakajifunze, wapeni semina elekezi, kinyume na hapo mnaharibu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wasanii, mmejadili kuhusu wasanii, tumewatumia kwenye kampeni za uchaguzi pande zote mbili, leo unawalipa wema kwa ubaya watu ambao wamezunguka nchi nzima kufanya kampeni kwenu. Wafanyabiashara waliochangia vyama vyetu vya kisiasa kwa ajili ya kushinda uchaguzi leo unawalipa wema kwa ubaya, hatuwezi kuendesha nchi katika huo mfumo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi ya Taifa letu kama Tanzania au moja ya sifa kubwa ya Tanzania ni utu, kuheshimiana, busara, hekima na kusikilizana. Hayo ndiyo mambo ambayo tumekuwa tukiyahitaji, ndiyo misingi ya Utanzania. Kwa hiyo, tunachokifanya hapa siku zote tunataka muende mkamrekebishe Mkuu wa Mkoa asijigeuze yeye mamlaka zaidi ya Bunge…
Hatuwezi kukubaliana na jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, Asante sana kwa kunipatia fursa hii ya mimi kuwa mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Momba na niwashukuru sana vilevile Mahakama Kuu kwa kuhalalisha Ubunge wangu siku ya tarehe 16, baada ya Mgombea wa Chama cha Mapinduzi kunikatia rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hayo yote. Sasa niwambie wananchi kwamba tumerudi kwa ajili ya kazi moja tu kuhakikisha Momba inaendelea mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesoma Hotuba ya Waziri kidogo ilichelewa, lakini nimepitia Hotuba ya Kamati pamoja na Hotuba ya Kambi ya Upinzani. Kwa mara ya kwanza katika Bunge hili niseme kabisa kwamba Kamati ya Nishati na Madini imejitahidi sana kutoa taarifa inayoelezea matatizo yaliyopo kwenye Sekta nzima ya Nishati pamoja na Madini, niwapongeza sana Kamati ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukizungumza kila mara na Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na kaulimbiu ikisema itakapoingia madarakani itapitia mikataba yote na makampuni yote yanayochimba na kuzalisha madini ndani ya nchi yetu, lakini mpaka sasa, hatujasikia mapitio ya mkataba kwenye kampuni yoyote. Hatujasikia na ni kauli ambayo ilitoka kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Sasa kwa nini tunaliulizia hili jambo kwa sababu sekta ya madini ndiyo sekta ambayo sisi kama Taifa tumeibiwa sana! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, makampuni haya tangu yameanza kuzalisha madini hayajawahi kupata faida na haya yamekuwa yakizungumzwa ndani ya Bunge tangu Mabunge yaliyopita. Bunge la Tisa, la Kumi mpaka hili la Kumi na Moja tunajadili mambo yaleyale na mifano midogo tunayo. Tuna mfano wa Mgodi unaozalisha Almasi wa Williamson Diamond pale Shinyanga, umeanza kuzalisha mwaka 1940, leo tunapojadili ni miaka 76, lakini mpaka leo hawajawahi kupata faida, hawajasitisha uchimbaji wa madini na ukiangalia kwenye malipo yao ya kodi ndani ya hili Taifa hakuna chochote kinachofanyika. Haya ndiyo tunayosema, kile kilichoahidiwa na Serikali ya Awamu ya Tano cha kupitia mikataba, ndiyo kilitakiwa kifanyike sasa, kwa sababu haiwezekeni watu miaka 76 hawapati faida, lakini hawaondoki, wako pale pale.
Mheshimiwa Spika, sasa haya ndiyo maswali ambayo tulikuwa tunahitaji kupata majibu kutoka kwenye Wizara ya Nishati na Madini ambayo iko chini ya Mheshimiwa Waziri Sospeter Muhongo. Kwa hiyo tunahitaji hayo majibu. Tunahitaji majibu juu ya kampuni ya ACACIA ambayo hata Kamati imeeleza, Mahakama ya Usuluhishi imewaambia walipe kodi ya mapato karibu bilioni 89 ambazo walikuwa wamezikwepa kwa kipindi cha miaka minne, lakini mpaka leo kampuni hiyo hiyo inashindwa kulipa na Serikali haijasema, haijatoa kauli na haijachukua hatua yoyote. Sasa haya ndiyo mambo tunayosema, huwezi kuita hapa kazi tu, wakati unashindwa kusimamia makampuni ya namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya tunataka kazi iendane na kukamata hawa watu, walipe hizo bilioni 89 ambazo zimeamuriwa na Mahakama ya Usuluhishi kuhakikisha kwamba Taifa letu linapata hiyo faida. Kwa hiyo, nategemea Mheshimiwa Waziri Sospeter Muhongo atatupatia majibu kwenye majumuisho yake hizi bilioni 89 zilizoamriwa kulipwa kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nini mpaka sasa hivi, Serikali inashindwa kuzipata fedha hizi?
Mheshimiwa Spika, lakini, kuna mambo mengine ambayo tulikuwa tumeyajadili. Kwenye Mabunge yaliyopita Bunge liliamuru kwamba makampuni ya uzalishaji wa madini yajisajili kwenye soko la hisa la ndani ya nchi, siyo yafanye cross listing. Unajua, watu wanashindwa kuelewa haya makampuni yamejisajili London yamejisajili kwenye masoko ya nje ambako sisi Watanzania wa ndani hatuwezi kupata taarifa juu ya mwenendo wa haya makampuni, huku ndani tunapata tu taarifa za kawaida na kinachotokea nini? Kule wanapata faida, lakini kwenye taarifa za ndani za Taifa letu hakuna faida yoyote inayoonekana juu ya makampuni haya yanayochimba madini katika hili Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunahitaji kupewa majibu juu ya maazimio ya Bunge, juu ya kauli ya Rais ambayo ndiyo ahadi kwa Watanzania lini mtapitia mikataba ya makampuni yote yanayozalisha madini nchini. Kwa sababu madini yaliyoko ndani ya nchini yetu yanakwisha wala siyo kwamba yatakaa milele, ni Non Renewable Resources na kila mmoja anajua hiki kitu. Kwa hiyo, sasa hatutaki kupata mashimo kama yalivyo kwenye Resolute kama tunavyoona kule Tulawaka kwamba Taifa limebakiwa tu na mashimo ambayo sisi kama Taifa hatukupata faida ambayo tulikuwa tunatarajia kutoka na mikataba ambayo sisi tulikuwa tumeingia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo tungependa kupata ufafanuzi, Rais wakati anazindua mradi wa pili, kule Kinyerezi aliahidi kwamba atahakikisha mkataba wa IPTL wa kulipa capacity charge, yeye katika Serikali yake, huo mkataba anauvunja na hatalipa ameyasema hayo Mheshimiwa Rais. Sasa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaliona hili kwamba mpaka sasa ni hatua gani mmechukua kuhakikisha haya Makampuni hayaendelei kulipwa capacity charge yawe yanazalisha umeme, yasiwe yanazalisha umeme? Hebu fikiri, milioni 300 za Kitanzania zinapotea kila siku kampuni izalishe umeme ama isizalishe, hii hasara hatuwezi kuendelea kuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, makampuni haya yalikuja kwa lengo moja tu, kuzalisha umeme wa dharura, lakini mpaka sasa hivi siyo kwamba tuna udharura, udharura haupo sana kama kipindi ambacho kilikuwepo. Sasa hivi tuna uhakika na kile tunachokifanya, lakini mpaka leo haya mambo yanaendelea, sasa tunataka tuambie, maana yake tunajua kauli ya Rais ndiyo kauli ya Serikali, ndiyo msimamo wa wananchi, kwamba tunataka kuona makampuni yote yanafungiwa na maazimio yote ya Bunge yanafuatwa na yanapatiwa mkakati wake.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambolo ningependa kulizungumzia, Kamati vile vile imelisema na mimi nilitaka niliseme. Kampuni ya Dangote ilikuja kwa lengo zuri kabisa na naamini bado lengo ni zuri. Imekuja kwa lengo la kuzalisha saruji ndani ya nchi yetu, lakini mpaka leo tunapojadili kampuni ile haitatumia gesi ya nchini, haitumii na wala haitatumia gesi kwa sababu mitambo yake ile imetengenezwa kwa ajili ya kutumia makaa ya mawe. Lakini cha ajabu ambalo Watanzania hawajui, makaa ya mawe yale sio yanayotoka Liganga na Mchuchuma kule. Makaa ya mawe yale yatatoka Msumbiji ambako ni karibu kabisa na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, sasa unajiuliza haya maswali kila siku kwamba tunazalisha gesi na gesi ipo kwa wingi lakini tunashindwa kwa sababu moja tu, tumeambiwa wameshindwa kukubaliana juu ya bei halisi, kwamba Dangote anataka senti kadhaa tu. Tunaamini sasa gesi ili iwe faida kwa Taifa, gesi hii ndiyo itumike kwenda kwenye Kampuni ya Dangote, Serikali ipate faida kutokana na mauzo ya gesi ili sisi kama wananchi tuweze kujitegemea huko tunakokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la nne, miradi ya REA. Waziri hapa amesema kumeongezeka kwa bajeti, nakubaliana, kwamba imetoka karibu bilioni 357 mpaka mnakwenda kwenye 500. Hata hivyo, changamoto ni nini, mwaka jana, mwaka 2015/2016, tulitenga karibu bilioni 357 kwenye Bunge hili hili la bajeti, lakini mpaka sasa hivi tunapojadili kwenye bajeti ile fedha zilizotoka hazijafika hata asilimia 70. Sasa leo unaleta tena 534, of course umeongea vizuri kwamba hapa hakuna cha MCC, its okay, lakini hela hizi zitafika kwa asilimia 100?
Mheshimiwa Spika, Momba kule mlipeleka miradi ya umeme tukaahidi Halmashauri ya Momba itapata umeme wa REA kufikia mwaka jana 2015 Juni, lakini mpaka leo tunapojadili, mwaka mzima, Momba hakuna umeme. Nguzo zipo pale zimesimama, miradi ya REA haiendelei. Sasa hii changamoto tusiwadanganye Watanzania kwa kutaja viwango vya fedha, tunataka utekelezaji unaoendana kwa vitendo, tuambiwe hela inayokwenda kufanya kazi, kwa hiyo hicho ndicho tunachokitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unaweza kusema hapa REA tumetenga trilioni moja, its okay, trilioni moja itafikiwa mwisho wa mwaka? Je hizo Bilioni 357 za mwaka 2015/2016 zimefika kwa asilimia 100? Mheshimiwa Muhongo kwenye facts za data najua yeye ni mzuri sana, lakini ngoma ipo kwenye utekelezaji, twende tufanye utekelezaji, ndiyo Taifa tunachotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kwenye issue ya vinasaba, tumekuwa tukiijadili kila mwaka. Vinasaba vilikuwa vimeletwa kwa kazi moja tu, lengo ni kupunguza uchakachuaji…
SPIKA: Mheshimiwa…
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la kitongoji cha Mchangaji au kwa jina jingine Ishinizya Kijiji cha Senga, Kata ya Kamsamba Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, kuna tatizo kubwa sana la mpaka kati ya Mkoa wa Rukwa (Wilaya ya Sumbawanga Vijijini-Kwela) na Wilaya ya Momba maana kijiji hicho cha Mchangani/Ishinizya kila upande unadai ni wake kwa sababu za mipaka. Naomba Wizara yako ikalitatue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa sababu ya muda kuwa mfupi nitachangia kama mambo mawili au matatu kwa ajili ya kuisaidia Serikali kwenye huu mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninalokwenda moja kwa moja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba ukipitia hotuba yake, hususan maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2017/2018 utagundua hapa kuna maeneo mengi kweli kweli, hii miradi ya kielelezo ipo karibu kumi na kitu, ukienda kwenye kila sekta wameweka miradi mingi sana. Ninalisema hili kwa sababu unajua standard za priority unazifahamu, ukitaka kuweka vipaumbele maana yake unatakiwa uchague viwili, vitatu, maximum vitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukishakuja na vipaumbele zaidi ya kumi na huu unakuwa ni uwongo, ni jambo ambalo halitekelezeki. Kwa hiyo, jambo ambalo nataka kuishauri Serikali, ili waondoe ugomvi na Wabunge, dunia hii ilivyo hata ufanye nini watu hatuwezi kuridhika lakini namna ambavyo unaandika unataka uridhishe, huku na huko tunapeleka mradi, kwa fedha gani? Kwa hiyo, at the end of the day, mwisho wa mwaka ni kwamba tutawalaumu tena mwakani kwa sababu haitekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi wewe mwenyewe unajua, miradi sisi tangu tunasoma shule ya msingi, mfano makaa ya mawe Mchuchuma na Liganga, yaani ipo tu kila mwaka hai-mature, every year hai-mature, unaweka miradi ya kielelezo, mwakani tutazungumza yale yale, miradi kama hii wewe unaondoa unapeleka kwenye Wizara husika itekeleze katika ile miradi ya miendelezo ya kila siku. Unaweka mradi unaandika kwa mfano, uanzishaji wa Kituo cha Kibiashara cha Kurasini, wawekezaji hawapo, wale Wachina walishaondoka, sasa ukishaweka kielelezo maana yake what are you doing?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unakuta ni miradi ambayo tunajua kabisa ikifika mwakani tutamweka kwenye 18 Mheshimiwa Mpango atalalamika tena, jamani mimi mgeni kwenye Wizara mnanionea, mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kwenu Wizara nendeni mkachague miradi mitatu, minne, unajua hata ukitekeleza hapa kwa asilimia 100, 98, watu tutakupongeza, huo ndiyo utaratibu wa kuongoza nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo nililiona kwa sababu nikaona kabisa kwamba sasa tuache kuwapiga tuwape solution. Sasa changamoto ni kwamba mkiamua kuyapuuza up to you, lakini hiki ninachokwambia, leta mitatu, minne, nina uhakika mnaweza kutekeleza kwa kiwango cha pesa ambacho kinakusanywa, hilo linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, utekelezaji wa mpango umekuwa ukikutwa na changamoto nyingi sana, na changamoto kubwa ya utekelezaji wa mpango ni fedha. Asilimia kubwa ya mambo ambayo tumekuwa tukikutana nayo hizi fedha mara nyingi zinahusu wahisani, sasa wahisani ndio hao, leo wanaweza wakasema mwakani tutailetea Serikali dola milioni 900 na ikifika mwakani mmekwaruzana kwa sababu fulani wanasitisha ile misaada, na ukija Bungeni sisi kama Wabunge tunakwenda kuwaambia wananchi kwamba Serikali ilitenga kiasi hiki kwa ajili ya mradi huu, wahisani wamejiondoa, anayebeba lawama baada ya hapo ni Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii miradi ya msingi ambayo tunataka kupeleka kwenye utekelezaji lazima kwanza Serikali iwe na uhakika imepata fedha kwanza, halafu ndiyo inaleta kwamba huu mradi tunakwenda kuutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachoshauri ni kwamba mnaweza mkakopa huko, mkishakopa ndiyo unakuja hapa. Nazungumza kama Waziri wa Viwanda na Biashara, kiwanda hiki kitaanza kujengwa kufikia mwezi wa kumi, hela ipo kwenye akaunti, usizungumze kwamba jambo litafanyika wakati hela haipo huo tunaita ni uongo na ni jambo ambalo halitekelezeki. Huu ni ushauri ambao naipa Serikali leo, ikiyafuata haya mambo mwakani hamtalaumiwa, lakini msipoyafuata haya mambo mtaendelea kulaumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, nataka nizungumzie TRA, kwenye ukusanyaji wa mapato TRA wamekuwa wakilalamikiwa sana. Leo ukisikia kila kona ya nchi TRA wanakamata, sibishani na watu wanaokwepa kodi, nataka TRA wakusanye kodi, lakini kinachofanyika kule nje, wanaenda kwa mtu, ana biashara yake wakimkuta mtu kwa mfano hajalipa kodi wanamkamata, wanafunga biashara yake, sasa matokeo yake nini? Unapomfungia mtu biashara yake na unamdai kodi, maana yake yeye mwenyewe hapati kipato, Serikali inakosa fedha kwa kumfungia yule mtu biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu wamekopa mabenki wanashindwa kurudisha mikopo, kwa hiyo, hapo TRA kumfungia mfanya biashara ni kukomoa Watanzania, ni mambo ya kawaida ni madogo madogo sana yanaweza kutekelezeka humu ndani. Serikali inachotakiwa kifanye wale wote wanaodaiwa kodi watengeneze utaratibu waweke kama malipo benki, benki ukishindwa kulipa fedha zako zikiwa nyingi wanakuambia tunakupunguzia ama tunakuongezea muda wa kulipa, utakuwa unalipa kiasi hiki in installment. Sasa TRA wanataka wao ….
MHE. DAVID E.SILINDE: Haya ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo nilikuwa nashauri kwa sababu mmepigwa sana na ukiona watu wanasema sana ujue kuna tatizo sio kwamba watu wanawaonea.
Kwa hiyo, ushauri wangu naomba hayo mambo matatu myafanyie kazi mwakani hatutawalaumu, mkiendelea kutaka kufanya yote kuridhisha kila mtu hamtafanikiwa. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Wizara ya Fedha na Mipango. Kwa lugha nyepesi kabisa adui namba moja wa maendeleo ya Taifa hili ni Wizara ya Fedha na Mipango. Adui namba moja na nina sababu, sababu namba moja Wizara ya Fedha inashindwa kutoa fedha ambazo zipo kisheria namba moja.

Mheshimiwa Spika, hili nalisema, nenda kwenye ripoti ya Mkaguzi, angalia fedha ambazo Wizara kwa kupitia TRA wamekusanya na ambazo wamepeleka na zile ambazo hawajapeleka, hawapeleki fedha. Leo ukienda kuangalia watu wa korosho wanalalamika, wamekuja watu wa Bodi ya Korosho kwetu wamelalamika juu ya Wizara ya Fedha wamekusanya bilioni 91, wamepelekewa bilioni 10, fedha yao halali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, railway development levy, hakuna hata senti iliyopelekwa kule, angalia kila kifungu Wizara ya Fedha wana sababu moja tu wanasema siku hizi uhakiki, yaani Serikali hiyo moja kigezo chao ni uhakiki na ndio kichaka cha kujifichia kutokupeleka fedha.

Mheshimiwa Spika, Mawaziri hapa wanakuja wanalia fedha hakuna na fedha zao ambazo zipo kisheria, wao jukumu lao ni kuchukua, kukusanya na kurudisha kule, hawafanyi wanalitakia mema Taifa hili, the answer is no, hawatakii mema Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha za miradi ya maendeleo angalia kilimo chini ya asilimia 10, miradi ya maendeleo; viwanda ambavyo ndio tunahubiri, Wizara ya Viwanda na Biashara asilimia tisa, leo uchumi wa Taifa ambao tunalia kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda
unapeleka asilimia tisa na Wizara hawawezi kuleta majibu hawa na tunawaona. Pia wana sababu za ajabu, maagizo kutoka juu, maagizo gani, yaani huko juu ni wapi mbinguni yaani ambako sisi kama Taifa hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Spika, hivyo tuulizane swali dogo, unapoagizwa kutoka juu, hivyo mtu anayekuagiza kuvunja sheria you need to know one thing. Leo mpo ninyi, kesho utawala utakuja awamu nyingine, itakuja Awamu ya Sita atakayekuwa responsible ni ninyi Mawaziri kwa sababu sisi hatutamgusa Mheshimiwa Rais ana kinga Mheshimiwa Rais yoyote yule awe ni Mheshimiwa Dkt. Magufuli, afanye chochote kibaya ana kinga, ninyi hamna kinga tutawachukulia hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa haya ndio ambayo yanapelekea haya madudu kuendelea kufanyika na tumekuwa tukishuhudia kila wakati, sasa kuna maamuzi ambayo Wizara inayafanya ambayo sisi kama Taifa ndiyo tunaingia hasara, kwa mfano unajua unapojenga reli ya standard gauge ni jambo jema na sisi kama wananchi hatupingiki tunakubaliana na hilo jambo, lakini unapoamua kukopa mkopo wa kibiashara kwenda kuhudumia reli ambayo malipo yake ni baada ya miaka 20 ni kuliingizia Taifa hasara, yaani unatumia current asset to finance the long term liability, ni nini ninachokisema? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mikopo ya mabenki wanakupa muda wa grace period ya miezi sita, mradi wako hujakamilika unaanza kulipa fedha, lakini ukitumia concessional loan ni watu wanakwenda kwenye mradi, wanatekeleza mradi, mradi unakwisha, baada ya mradi kuisha unapewa muda fulani miaka mitatu, baada ya hapo ndio unaenda kuwalipa. Sasa leo hii miradi ni mema Kwa Taifa lakini tutaanza kulipa kabla miradi haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, baada ya miaka 20 ndio mradi ile pay back period yake kuanza kutoa faida ndio unaanza kuiona, unajua matokeo yake ni nini? Hakuna maendeleo yatakayoendelea kufanyika, ndio maana leo tukija humu ndani kilimo wanalia, afya wanalia, elimu wanalia, maji wanalia, hakuna mradi unaofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa haya wanaosimamia ni Wizara ya Fedha, sijawahi kuona Wizara ambayo inashindwa kuelewa kama Wizara ya Fedha na hii inabidi uwe mkali sana, bila kuisimamia Wizara ya Fedha kupeleka fedha hizi zote tunazosema hapa ni ngonjera, kwa sababu kila kilichoandikwa mwisho wa siku lazima kitafsiriwe na fedha iende pale. wanatamka mapato yameongezeka, sisi tunashangilia huko mtaani, haya tuonyesheni hela basi, hazionekani.

Mheshimiwa Spika, lLeo unakwenda angalia tu mfano mdogo tu deni la Taifa ndani ya miezi 12 wamekopa trilioni saba, hilo deni limeingia kwenye deni la Serikali, trilioni saba, haya waambieni hili deni la trilioni saba hela zake basi tuonyesheni na zile mlizokusanya ndani tuonyesheni vilevile tuone hii miradi na utekelezaji wake mnafanyaje wanakwambia tu hili ni himilivu kwa asilimia 34.4 ukomo wetu ni 56%, hawazungumzii tax to GDP yaani makusanyo ya kodi against pato la Taifa, tuko kwenye 14.5%, ndio ambayo tuko sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa duniani kote siku hizi watu walishaacha kutumia mfumo wa debt to GDP siku hizi watu wanatumia mfumo wa kodi kwa pato ghafi la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana umenielewa. Tunakumbushana, ni Mwalimu lakini ni mwananadharia. Mimi nayaishi haya maisha practically. Hii ndiyo changamoto inayo-face nchi. Maprofesa wengi wamefeli kwenye uongozi duaniani kote walipokabidhiwa. Kwa sababu hivi vitu, unajua kuzungumza na kutekeleza ni vitu viwili tofauti. Sasa hilo tumezungumza, tunaona hali halisi. Sasa kuna mambo mengi ambayo hawa wanasimamia, leo wanasimamia rufaa za kodi, angalia kule, kuna rufaa kibao; lakini wanasema ili tumsikilize mtu tupokee ombi lake lazima ulipe moja ya tatu ya kodi. Ndiyo kazi ya Wizara ya Fedha, yaani ni kukandamiza.

Mheshimiwa Spika, angalia mikakati yao Wizara ya Fedha. Mikakati yote ni kodi, kodi, ongezeko la kodi. Hakuna mahali popote wanayoweza kukuonesha namna watakavyozalisha ama namna ya watakavyotengeza mkakati wa wale watu wetu kwenda kulipa kodi. Hawa ndio wanaosimamia, sisi tunawahoji kila siku. Kuna majibu mengine tunayavumilia, lakini kiukweli wanataka kuvuna mahali ambapo hajawapanda, ndiyo kitu kibaya sana ambacho hawa watu wanacho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine ambalo wanalo, ni kutokutaka kuelewa. Kama walichokipanga wao wameshakipanga, maelezo yote tutakayotoa ndani ya Bunge hakuna jambo lolote watakalolisikia. Hilo ndilo tatizo. Wizara ya Fedha ina kiburi cha hali ya juu, sijawahi kuona katika nchi hii!

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa hapa awali, wamejikita kwenye fedha, kwenye mipango ni kama hamna. Hiyo ndiyo imekuwa changamoto katika nchi hii kwa miaka mingi. Yaani inapofika suala la mipango, waulize hawa Mipango, ndiyo hii mipango inakuja mambo mapya. CAG ameshatoa mapendekezo mengine, wao wenyewe wanayakimbia. Haya yote ni kwa sababu wanashindwa kutusikiliza, wanashindwa kuelewa.

Mheshimiwa Spika, ubaya sana kwenye hizi nchi, inafika mahali watu wanawaachia haya nendeni basi tuwaone, mtafikia wapi? Mtashindwa! Sasa ninachofahamu, Mheshimiwa Rais anahitaji kushauriwa vizuri. Yeye ni binadamu, hata kama kuna wakati ana-push jambo ukimwelewesha usiku atalala peke yake, atasema lakini lile jambo Mheshimiwa Waziri Mpango alinimbia kweli. Sasa ile akikwambia tu “nimesema kuanzia leo, toa hela hizi peleka huku.” Unasema sawa mzee. Hakuna Taifa la namna hiyo! Lazima umwambie hapana Mheshimwa Rais. Nitatekeleza hilo jambo lako, lakini lazima tufuate utaratibu. Ni mambo ya kawaida. Hata Mbinguni kule kwa Mungu ili uende Mbinguni lazima ufuate utaratibu, hakuna dunia inaendeshwa bila utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ndiyo yaliyotufikisha leo hapa. Ni kwa sababu mambo mengi na fedha nyingi, zinakwenda bila utaratibu. Mwisho wa siku wanasema mali bila daftari huishia bila habari. Kwamba unaweza ukakusanya mali nyingi, lakini kama unashindwa kurekodi, kuwa na mipango, yaani hutafanya kitu chochote. Miaka mitano; imebaki miwili, itakwisha, mtakuja na the same story. Mtaishia kupiga kelele tu kwamba tumetekeleza; tuonesheni mlichokitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi milioni 50 kila kijiji, ipo kwenye rekodi hapa; leo mwaka wa wangapi? Wa tatu huu, ndiyo bajeti ya tatu; tumebakiwa na bajeti mbili tu. Wanatenga, lakini hawajapeleka hata shilingi mia. Ipo kwenye taarifa yao. Walitenga shilingi bilioni 59, wakasema tunakwenda kwenye pilot study; hawajapeleka hata shilingi mia. Mwaka 2017 wakatenga shilingi bilioni 60, hawajapeleka hata shilingi mia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tukija tukiwahoji tunaonekana tunakosea, lakini ni kweli hizi takwimu wameziandika wenyewe; wanaotudanganya ni wao wenyewe; lakini yote hii ni kwa sababu wanaamini sisi hatuelewi. Sisi tunajua, tunaweza kuwa katika ujinga wetu tunaelewa kidogo, lakini kwenye hiki cha ujinga kinatoka kwa wananchi. Wewe unafika Jimboni mtu anakuuliza, Mheshimiwa Mbunge shilingi milioni 50 hazijaja hapa kwa sababu wewe Mbunge ni mzembe, lakini unajua kabisa ni kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Fedha kasema hela itakuja. Namwuliza hela iko wapi? Anakwambia hela itakapopatikana. Si mmetuelezaa hela zipo nyingi huku! Sasa hilo ndiyo tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijazungumzia miradi ya kimkakati ya Kitaifa nitazungumzia mambo mawili madogo tu ya jimboni kwangu. Jambo la kwanza pamoja na shukrani ambazo zimetolewa za ujenzi wa Daraja la Momba ambalo limekamilika kwa karibu asilimia 97 na linatumika, sisi wananchi wa Momba tumefurahi sana, lakini tunaomba sasa ile barabara ya kutoka Mlowo – Kamsamba – Kiliamatundu ijengwe kwa kiwango cha lami kama ilivyo Ilani ya CCM ilivyoahidi, kama ilivyo ahadi ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Kikwete na Mheshimiwa Mkapa, wote waliahidi kujenga hiyo barabara lakini mpaka sasa hawajakamilisha. Barabara ya Kakozi – Kapele – Ilonga ambayo wameipandisha hadhi na hawajaifanyia kazi mpaka sasa, tunaomba ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nahitai kuzungumzia masuala ya Kitaifa ambayo kimsingi yanaweza yasieleweke vizuri na ndiyo maana unajikuta mara nyingi tumekuwa tukigongana. Mradi wa SGR, thamani ya mradi wote wa reli ya SGR ni dola za Kimarekani 7,000,000,000 na maamuzi yameshafanyika ya kujenga reli yetu kutoka Dar es Salaam - Morogoro mpaka Dodoma kwa awamu ya kwanza kabla ya kwenda kwa awamu ya pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulishawaeleza Tanzania kwamba hatuna shida na reli inayojengwa, shida yetu ni namna mambo yanavyotekelezwa na nikasema hapa reli ambayo imejengwa, maamuzi ya awali yaliyofanyika chuma chote kinatoka China – nje ya nchi. Chuma kidogo ambacho kimekuwa kikinunuliwa hapa ndani ya nchi wamekuja watu wenye viwanda kwetu, watu wa viwanda vya chuma wamepewa vile vitani kama vya kudanganyishia, tani 1,000 au 2,000 basi, lakini chuma chote kimetoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya tunasema ni makosa ambayo tumeshayafanya kabla hatujawaza mapema. Nimeamua kulizungumzia hili kwa sabbau najua awamu ya pili ya kutoka Makutupora kwenda mpaka Mwanza itafuatia, lakini kabla hatujaenda katika huo mradi tuna mradi wa Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma endapo tungewekeza kwenye kutengeneza chuma chetu maana yake hii fedha ambayo tunaitumia kwa ajili ya reli yetu hapa nchini tungekuwa tunanunua chuma ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa juzi ulisikia ripoti ya IMF. Ripoti ya IMF imeshusha uchumi wa Tanzania kutoka kasi ya kukua ya asilimia saba mpaka asilimia nne na sababu walizozitoa nafikiri kila mmoja amejaribu kuzisoma na Serikali walituambia hapa tusiwahishe shughuli, tukakubaliana na hilo jambo, lakini Serikali wamekuwa wakitaja hizo argument zao huko mtaani kwamba mbona IMF hawaja-include miradi mikubwa kwa mfano reli ya SGR katika uchumi wetu pamoja na ndege.

T A A R I F A

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba pamoja na kwamba tunapokea taarifa aliyopewa, lakini hicho kilichozungumzwa hakiondoi taarifa zilizokuwepo mle ndani, hakiondoi! That’s the fact! Yaani bado ni asilimia nne, haiwezi kuondoa hiyo fact!

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambacho nilikuwa najenga, nafikiri Mheshimiwa Waziri ambacho alitakiwa anielewe ni kitu kimoja na hii ndiyo shida ya hili Taifa. Moja ya ambacho nilikuwa nakizungumza maelezo ambayo wamekuwa wakiyatoa kwamba kwa nini hiyo miradi mikubwa haiwi included kwenye ile Taarifa ni kwa sababu kumekuwa na capital outflows kubwa yaani tunatumia fedha ya ndani, tunanunua kila kitu nje ya nchi na ndiyo maana uchumi wetu unashuka kwa sababu hatu-inject fedha ndani ya uchumi wa Tanzania. Tumepata mradi lakini fedha kwenye circulation haipo! Hiyo ndiyo tofauti ya kwetu sisi na Kenya. Kenya…

NAIBU SPIKA: Sawa, sasa Mheshimiwa Silinde ngoja twende vizuri kwa sababu Taarifa uliyokuwa umeizungumzia umesema ni ya IMF na barua tuliyosomewa ni ya IMF. Mimi naomba tuji…

(Hapa Mhe. Esther N. Matiko alikuwa akizungumza na Mhe. David E. Silinde)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther muache asikilize Taarifa ninayompa mimi hapa ili aweze kufuata maelekezo, ukimwongelesha atakuwa hanisikii, subiri mimi nimalize na wewe utazungumza.

Mheshimiwa Silinde kwa sababu Taarifa uliyokuwa unaizungumza umeanza kwa kusema Taarifa iliyotolewa na IMF imesema hivi. Taarifa aliyotoa Mheshimiwa Waziri inatoka huko huko IMF ikisema haijasema hivyo, kwa hiyo weka mchango wako vizuri ili taarifa zetu zikae sawasawa. Weka mchango wako vizuri Taarifa zetu zikae sawasawa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naona hili jambo, labda kama nchi tuna-complicate sana kwa sababu ya facts ambacho kinaelezwa pale hawajakanusha kuhusu ukuaji wa uchumi wala hawaja- comment juu ya ile Taarifa na sisi hapa tunachojaribu kutaka ku-rescue hili Taifa hapa lilipo, ndicho ambacho tunachohitaji kukifanya. Sijui kama umenielewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeweza kumwambia sijapokea, lakini ni taarifa kutoka IMF, ni barua ameandikiwa. Ukisoma ile taarifa yote utaona Maofisa wote wa Serikali wako pale. Sasa mimi najaribu kueleza kwamba tofauti ya kwa nini hawaja-include miradi yetu na ni kwa nini wenzetu Wakenya, mradi wao wao walikopa bilioni 5.5 US dollar wakaingiza kwenye mradi wao, kilichosababisha uchumi wao kukua kwa asilimia 1.5 kwa sababu fedha ilitoka nje ya nchi ikaingia ndani ya Kenya. Sisi Tanzania ni vice versa, fedha inatoka Tanzania, inakwenda nje ya nchi, hiyo ndiyo tofauti yetu sisi na watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa hapa ambacho nataka nishauri, makosa yaliyofanyika awali kwenye kutoa fedha nyingi nje ya nchi, ndiyo nataka yasifanyike katika Mradi wa kutoka Makutupora kuelekea Mwanza kwa maana gani? Mradi wa Liganga na Mchuchuma gharama yake unahitaji kama dola bilioni tatu za Kimarekani, lakini ukishaukamilisha ule mradi kwenye mradi wa Liganga utapata chuma, utapata makaa ya mawe, utapata umeme na utachenjua madini mengine. Kwa hiyo tunapoanza kujenga mradi kutoka Dodoma kwenda Mwanza maana yake chuma kitakuwa cha ndani ya nchi. Kwa hiyo hela yetu hii ya ndani itatumika hapa hapa, hatutaendelea kununua tena machuma kutoka huko China. Kwa hiyo hapo hata IMF watakavyokuja watakuambia kwa sababu fedha yote inabaki kwenye mzunguko, maana yake nchi yetu uchumi wetu utakua

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa unaweza ukajiuliza swali dogo, kwa miaka minne mfululizo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mpaka sasa tumeiingizia shilingi trilioni 13.8. Mwaka huu wa fedha wanaomba shilingi trilioni 4.9, maana yake in total ni karibu shilingi trilioni 18.7, ndani ya miaka minne. Asilimia 40 ya fedha za miradi yote ya maendeleo ya Tanzania zipo Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa jiulize swali, tume- inject fedha inakwenda kwenye shilingi trilioni 18 lakini matokeo ya kiuchumi yanakwenda vise versa. Badala ya uchumi kutoka asilimia 7 kwenda 8, matokeo yake inatoka 7 inakwenda 4, inakwenda vise versa. That is the question tunahitaji kupata majibu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashauri Serikali kwamba tumieni fedha ambayo inaingia ndani ya uchumi kwa ajili ya kubadilisha maisha ya Watanzania, hicho ndicho ambacho tunakitaka. Changamoto ambayo ipo watu wetu hawa hawapendi kusikiliza ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, SGR bado inaendeleoa, itatoka Dar es Salaam, itakuja Morogoro, returning on investment ni nini? Hili ni swali ambalo tunapaswa kujiuliza. Je, itabeba tu watu peke yake mpaka Morogoro? Jibu ni kwamba kubeba watu haiwezi kurudisha gharama ya fedha ambayo tumeiweka mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotakiwa kufanya ni nini? Ndiyo maana nawashauri, sasa hivi wakati reli inakuja jengeni bandari kavu pale Morogoro. Ukishaweka bandari kavu pale Morogoro maana yake mizigo yote ambayo inakwenda nchi za SADC…

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Pamoja na inayokwenda Mikoa ya Kusini reli ile itayopita pale itaibeba. Kwa sababu mradi wote…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Silinde, kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, hamna taarifa hapa, hawataki kusikiliza ukweli tu. Sisi tunajaribu kuwashauri, shida mliyonayo Chama cha Mapinduzi mkishauriwa hamtaki, mkikosolewa hamtaki, mnataka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho najaribu kukieleza hapa ni kwamba kwa sasa mnatakiwa mjenge bandari ya nchi kavu Morogoro ambayo itasaidia kupeleka mizigo yote ya nchi za SADC, hicho ndicho kitu ambacho tunakihitaji kwa sasa. Nimesoma ile package ya kwanza ya mradi kutoka Dar es Salaam - Morogoro - Dodoma, nimeona tuna lengo la kuweka bandari ya nchi kavu hapa Dodoma, sasa kabla hatujaanza hapo, kwa hii awamu ya kwanza tuweke bandari kavu pale Morogoro ili tuhakikishe kwamba return on investment iweze kujibu mapema kabla ya jambo lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye jambo linguine maana kengele ya kwanza imeshalia ni barabara. Tanzania barabara ndiyo chanzo kikubwa cha ajali kuliko hata uzembe wa madereva, namba moja hiyo. Kwa sababu barabara zetu ni ndogo lakini hazirekebishwi kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuwe wakweli, Serikali haiwezi kufanya kila kitu kama ambavyo mmekuwa mkijiaminisha mbele za watu, haiwezekani! Kulikuwa na mradi hapa wa Dar-Moro Express Way, mradi ule ulitakiwa tu uendeshwe kwa mfumo wa PPP ama kuwapa private sector. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaulize Serikali, unapomleta mtu akakujengea barabara, mkopo amekopa mwenyewe akajenga Dar es Salaam - Morogoro, barabara ile wanapita watu hata kwa kulipa fedha. Tunakwenda nchi za watu, tumekwenda South Africa, Ulaya na nchi zote, watu wanalipia gharama (road toll). Sasa mnasema kwa sababu ya reli, hatujengi Dar-Moro Express Way kwa sababu imekuwa taken by event, kwamba kwa sababu kuna reli basi hiyo barabara haiwezekani, yaani unaona ni thinking ya kurudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yetu, ukijenga barabara kwa kutumia mfumo wa PPP, ukijenga madaraja kama Kigamboni, sifa inabaki kwa Serikali na haiendi kwa mtu mwingine tofauti. Tofauti yenu na sisi ninyi mnafikiri kwamba Serikali italeta maji, itajenga shule na kadhalika na ndiyo maana miaka yote, tangu mmekuwa madarakani kwa miaka 58 mambo yanakwenda polepole tofauti na kasi inayohitajika na mnataka pongezi kwa vitu ambavyo mnaviweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri sasa watu wa TISS wafanye vetting ya watu wanaoweza kuongoza hii nchi ili kuhakikisha wanaipeleka mbele. Kuna watu wanafikiri kijamaa kuliko miradi inavyotaka kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni ATCL. Hakuna mtu hata mmoja anayepinga ATCL lakini menejimenti lazima iwe huru, hiyo namba moja, wasiingiliwe wafanye kazi kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, kuna vitu ambavyo sisi tutaendelea kuwakosoa kila siku hapa ndani. Wewe Dreamliner imekuja tangu Julai, 2018, karibu mwaka mzima imepaki pale, tunakaa tunaiangalia pale, ile ni hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sawa na mtu umenunua coaster yako kutoka Japan umeiweka nyumbani kwako unaiangalia, haiingizi kitu chochote. Kwa nini usisemwe, kwamba wewe unafikiri kibiashara au unafikiriaje? Hayo ndiyo tunayolalamikia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia watu wa Rwanda, pamoja na kwamba wana Shirika la Rwanda Air lakini menejimenti ya Rwanda wamechukua watu wa Ethiopia, ndiyo wanao-run lile shirika halafu watu wa chini kule ndiyo watu wa Rwanda. Kwa sababu watu wa Ehiopia ndiyo wana uwezo mkubwa wa kuendesha mambo haya. Sasa na ninyi msione aibu kwenda kumchukua mtu Ethiopia, Rwanda akaja kuwasaidia. Hata KQ sasa hivi, miongoni mwa mabadiliko yao wamefanya hivyo. Msifanye maamuzi mkafikiri kwamba kila kitu kinawezekana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ambaye ndio Mwenyekiti wetu wa kikao kwa siku ya leo, kunipa fursa kujadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza michango mingi na mingi ni mizuri. Kwa sababu mpango wetu huu ni wa mwisho, mimi nitajielekeza kwenye Kitabu cha Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano ambacho Bunge lako Tukufu lilipitisha na miradi ambayo mpaka sasa haijatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa 2016 tulipokuwa tunajadili kitabu hiki kuna miradi ya kielelezo ambayo sisi kama Taifa tulipanga itekelezwe. Katika miradi ya kielelezo, ipo ambayo tumefanikiwa kwa kiwango fulani na ipo ambayo tumeiondoa kabisa na Serikali inashindwa kuleta majibu ya msingi kulieleza Bunge lako Tukufu kwa nini tumeshindwa kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi Na.1, ukisoma ukurasa wa 83, miradi ya kielelezo inayohusiana na Kanda za Maendeleo, kuna ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo, amezungumza Mheshimiwa Mtemi Chenge hapa. Ni kwamba bandari hii, lile eneo lote lilikuwa lina uwezo wa kuongeza ajira zile zisizo rasmi na kufikia 100,000. Sasa hebu fikiria leo katika nchi ambayo wananchi wanalalamika hakuna ajira, hii bandari ambayo ilipaswa iwe tayari imetekelezwa, tangu mpango wa pili tumeanza kuuandika, mpaka leo hakuna majibu ya kutosha, Serikali inashindwa kutueleza ni kwa nini jambo hili linashindwa kutekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni uanzishaji wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini. Hii ipo kwenye Mpango ukurasa huo huo wa 83(e). Jambo hili mpaka leo halipo popote na Serikali imelipa fidia lile eneo, limekaa pale halina kazi yoyote. Maana yake tulipitisha Mpango ambao tumeshindwa kuutekeleza na leo Serikali haijatoa majibu. Mradi huu vilevile ulikuwa unaongeza ajira ambazo zinafikia walau zile zisizo za moja kwa moja pale, zaidi ya 100,000 zingeweza kupatikana kwa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa Mji wa Kilimo Mkulazi. Tuliandika kwenye Mpango huu wa Miaka Mitano na mpaka leo tunakwenda kwenye mpango wetu wa mwisho, huwezi kuona Serikali inakuja kutoa maelezo, huo mradi wetu wa ujenzi wa Mji wa Kilimo wa Mkulazi mpaka sasa tumefikia wapi na matokeo yake ni nini kulingana na mpango tulivyoupitisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine tulioupitisha kwenye Mpango ambao mpaka sasa hivi haujatekelezwa ni uanzishaji wa viwanda vya vipuri na kuunda magari. Hii ipo kwenye kitabu hiki cha Mpango wetu ukurasa wa 84. Mpaka leo huo mradi haujatekelezwa, hakuna viwanda vya vipuri vya kutengeneza magari hapa ambavyo vimeanzishwa; wala viwanda vya kuunda magari ambayo tulikuwa tunahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya uchimbaji wa makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma, hii imekuwa story. Mimi tangu nasoma sekondari miaka ya 1990 mpaka nimeingia Bungeni, sasa nafanana na akina Mheshimiwa Mkuchika sasa hivi, bado story ni ile ile ya Liganga na Mchuchuma. Mheshimiwa Mtemi Chenge amezungumza, tunashindwa kuingia mikataba ambayo inaeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweka malengo sisi kama Taifa letu; malengo na viashiria kwa ajili ya utulivu wa kufanya biashara katika Taifa letu. Kwa mfano, mwaka 2015/2016 urahisi wa kufanya biashara Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 139 kati ya nchi 189 na malengo tuliyoweka katika mpango tulisema inapofika mwaka 2020/2021 tuwe katika nafasi ya 100. Yapo kwenye vitabu hivi, lakini unapozungumzia leo, nchi yetu iko nafasi ya 144. Lengo lilikuwa nafasi ya 100, lakini mpaka sasa tuko wa 144 kati ya nchi 190. Ni malengo tuliyojiwekea ambayo mpaka leo katika huu Mpango hayajateklezwa. Sasa unaweza…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde kuna Taarifa.

Mheshimiwa Angella Kairuki.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo anapotosha. Ukiangalia kwenye nafasi ambayo Tanzania kwa sasa tumeishikilia kwa ripoti iliyotoka mwezi wa Kumi, tumetoka nafasi ya 144 kwenda nafasi ya 141. Nami nilitarajia angeweza kupongeza kwa sababu, ukiangalia siyo nchi nyingi ambazo zimeweza kupata mafanikio hayo; na hii ni hatua katika kuelekea katika maboresho makubwa kwa ajili ya kuweza kuboresha nafasi ya Tanzania katika tathmini hii ya Benki ya Dunia. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa hiyo Taarifa. Labda nimweleze tu. Ndiyo maana nimezungumzia Mpango. Mpango wetu tulisema tunavyozungumza leo, tuwe nafasi ya 100. Uko nafasi ya 141. Au unataka tukupongeze wakati Mpango huu tumeandika sisi wenyewe? Issue ni malengo. Tumesema mwisho wa mwaka utafanya mtihani utapata marks 90, umepata 54, unataka upongezwe. Wewe uko ume-under score. Sijui kama umenielewa! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ndiyo upungufu wa kutokukubaliana na hali halisi. Mwaka 2010 Tanzania ndiyo ilikuwa katika nafasi bora kabisa ambayo yumewahi kufikia. Mwaka 2010 tulikuwa nafasi ya 125 ya urahisi wa kufanya biashara katika nchi 189. Kwa hiyo, tumerudi nyuma, hatuwezi kujipongeza katika vitu ambavyo hatujafanya vizuri sana. Kwa hiyo, nasi haya tumeyatoa ili Serikali iweze kuyafanyia kazi, sio ku-counter attack tu kila kitu, hamwezi kufanikiwa katika hicho kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mapendekezo yangu ya Mpango, nini ambacho Serikali sasa inapaswa kukifanya ili kuhakikisha baadhi ya mambo wanaweza kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo namba moja kama Taifa ambalo tunapaswa sana kuliwekea mkazo ni kutumia nafasi yetu ya kijiografia kuhakikisha tunatumia huu ukanda wetu, kwa maana sisi kama Tanzania tunazungukwa na nchi zaidi ya nane. Hizi nchi ndiyo tunapaswa kuzifanyia biashara kuliko hizi porojo ambazo tumekuwa tukifanya hivi sasa. Hiyo ndiyo namba moja. Nilitegemea kwenye Mpango, Serikali ingekuja na Mpango huu unaokuja watueleze ni namna gani tutafanya biashara na nchi zote zinazotuzunguka kwa kutumia Tanzania kama sehemu ambayo ndiyo itakuwa kituo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa nasoma ripoti ya wiki iliyopita, Kenya peke yake kwa kutumia bandari yao tu wamesema wamepunguza asilimia 50 ya ushuru kwa wafanyabiashara wote watakaotumia Bandari ya Mombasa. Hao Kenya, yaani wameshaweka incentives ya kuhakikisha wanatunyang’anya hata hizi biashara tunazofanya na nchi nyingine. Sasa Serikali na Mheshimiwa Dkt. Mpango hapa, nataka aieleze nchi kwamba nasi tunafanya nini kuvutia hizi nchi wanachama zinazotuzunguka kuhakikisha tunapata faida ya kuwa katika nafasi bora kabisa katika…

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde kuna Taarifa. Mheshimiwa Eng. Isack Kamwelwe.

T A A R I F A

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kuhusiana na uwongo ambao umetembea kwamba Bandari ya Mombasa imepunguza ushuru kwa asilimia 50. Jambo hilo halipo, ilikuwa ni uwongo, uchochezi tu wa wafanyabiashara. Bei iko pale pale kule Mombasa. Dar es Salaam ndiyo tunaendelea kupunguza bei ili tuwe na meli nyingi na ndiyo maana sasa hivi zinaanza kuingia meli kubwa za mita mpaka 300 zinazobeba ma-container mpaka 5,000. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri huwa tukizungumza tunapowapa data huwa wanaelewa na wanafuatilia na huwa hawayatolei majibu mpaka tuwakumbushe humu ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni kuhakikisha tunatumia nafasi, geographical position advantage tuliyonayo kuhakikisha tunafanya kuwa incentives ya ku-promote biashara kushirikiana na nchi nyingine. Hiyo ndiyo hoja yangu kubwa. Hata kama Mheshimiwa Waziri hapa anasema ni speculation, lakini hiyo haiondoi mantiki ya kwa nini watu wamepeleka hizo speculations Kenya badala ya kuzileta hapa Tanzania, kwamba kwa kufanya biashara hapa Tanzania, maana yake unaweza ukapata hizo benefits na kuondoa hiyo migogoro inayoendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuwe wa kweli. Nchi yetu kwa sasa bado tunashindwa kuwekeza katika mifumo ya PPP. Hii tumeieleza muda mrefu sana, nami nitaieleza kwa kifupi sana. Mheshimiwa Mtemi hapa amejaribu kuzungumzia, lakini sisi nchi yetu tukiruhusu PPP ninaamini mambo mengi makubwa yanaweza kufanikiwa kuliko tunavyofanya sasa hivi. Nami ninachokitaka hapa, PPP ielekezwe kwenye miundombinu na wala siyo kitu kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi unapoleta sekta binafsi ikashirikiana na Serikali, ikajenga barabara kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, Dar Express Way, muundombinu ukakaa pale, ile sifa inakwenda kwa Serikali, haiendi kwenye sekta binafsi kwa kujenga ile barabara. Ukichukua hela hizo hizo, kwa mfano reli tumeigawanya maeneo mengi, fedha hizi hizi ukachukua PPP ukajenga reli, faida ya ile reli inakwenda kwa wananchi na wala siyo kwa ile sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi sana, ukiangalia wenzetu wa Malaysia walipokuwa wanaanza huu mfumo wa PPP, katika phase ya kwanza waliingia mikataba ya hovyo ambavyo na wao wenyewe wanakiri, lakini pamoja na kwamba walifanya mikataba ya hovyo wakasema phase ya pili walirekebisha phase ya kwanza. Sasa sisi hapa kama uling’atwa na nyoka zamani, unasema sasa hiyo njia sisi hatutaki kuelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja yangu kwa Serikali katika huu Mpango, tujikite kuwekeza kwenye PPP katika miradi ya miundombinu. Ukijenga reli hapa hakuna mwekezaji ataondokanayo, mtu akijenga barabara hapa hata akiingia hasara hakuna mtu ataondokanayo, lakini kitu pekee ambacho nisingekubaliananacho, PPP isifanyike kwenye masuala ya service only. Yaani kwenye upande wa huduma, nchi ijitegemee yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa sababu sasa hivi tuna ndege, tunataka tuone sasa katika Mpango wetu hapa, service industry tunaiwekeza kwa kiwango gani katika nchi yetu? Tufanye kama wanavyofanya wenzetu wa Rwanda pale, yaani wana Conference Tourism, wana Business Tourism. Sasa hivi dunia nzima iwe ni vikao vya FIFA, iwe ni vikao vya Mabunge ya Afrika, iwe ni vikao vya Mabunge ya Dunia, wote wanakwenda Rwanda kuwekeza kwa sababu wanaona ka- nchi kao ni kadogo, hawana rasilimali za kutosha kwa hiyo, wana-promote watu kwenda Rwanda kufanya mikutano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, shirika lao la ndege linapata faida, lakini na nchi vilevile inapata mapato kwa sababu, watu wengi wanakwenda pale. Sasa hayo ndiyo mambo ambayo tulitegemea Mpango wetu uwekeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo tu cha mwisho, tumenunua Dreamliner mbili ambazo nafikiri ninyi wenyewe mmeziona. Tusingependa kuziona zinakaa pale, tunataka tuone kwenye Mpango hapa route za Kimataifa. Route kubwa ziwe zinaainisha kama ambavyo wale wote wanaopanda ndege kwenda Kimataifa ukisoma vile vitabu vyao vinakuonesha destination ambazo wanatarajia kwenda, destination za sasa. Sasa na haya tuyaone hapa ili walau hizi ndege zisiwe hasara kwa Taifa, badala yake zilete faida. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii na mimi nichangie hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoijadili Wizara ya Kilimo tunajadili wakulima namba moja, wafugaji pamoja na wavuvi. Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo chama pekee ambacho kwenye bendera yake kuna nembo ya jembe na nyundo. Jembe linamwakilisha mkulima ambae ndiyo leo tunamjadili hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamechangia humu ndani. Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa hili Taifa, Serikali kwenye bajeti zake wamepeleka asilimia tatu za miradi ya maendeleo ya kilimo. Asilimia tatu ambao wako kule ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba katika kila shilingi 100/= Serikali imepeleka shilingi 3/= kwa ajili ya kumwezesha mkulima ambaye yupo kwenye bendera ya Chama cha Mapinduzi, mkulima mnyonge. Tanzania ukizungumzia mnyonge, tunamzungumzia mkulima, hatumzungumzi mtu yeyote. Mkulima ndio tunajadili kwamba ndio mnyonge. Mpaka kwenye Chama cha Mapinduzi, ndiyo tulitumia kama silaha ya kumuondolea mkoloni, mnyonge mkulima, asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magazeti baada ya kusoma hotuba, yalipongeza sana hotuba yakaisifu kwa kuondoa tozo, lakini hizi tozo hatujazijadili kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imeondoa tozo, kwa mfano, tozo 80 kwenye mazao ya biashara, kwenye tumbaku wameondoa tozo kumi, kwenye Kahawa wameondoa tozo 17, kwenye sukari tozo 16, kwenye pamba tozo mbili, kwenye korosho tozo mbili na kwenye chai tozo moja. Sasa nataka tujadili tozo moja baada ya nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia tozo za sukari 16, zote kwenye kitabu zinamhusu mnunuzi na wala siyo mkulima moja kwa moja. Tozo zinamsaidia mtu wa kati, siyo mkulima wa kawaida wa chini. Tozo hazijadili kuhusu miundombinu ambayo wakulima wanahitaji. Wanahitaji soko la uhakika, wanahitaji miundombinu kwa maana ya umwagiliaji na wanahitaji mbolea. Hayo ndiyo mambo ambayo Wizara ya Kilimo ingekwenda kujadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye tozo ya pamba, yenyewe inasema, wameondoa pale tozo mbili; ukija kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema kwa mfano, kuna tozo ya kituo cha kununulia pamba katika ngazi ya Halmashauri ambayo Wizara ya Kilimo mpaka sasa hivi inasema tozo hii Wizara itawasiliana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya utekelezaji wa suala hili. Maana yake mpaka sasa hivi Wizara haijawasiliana na TAMISEMI. Tulitegemea nini hapa? Tulitegemea kwamba Wizara wanapokuja hapa, hili suala liwe limeshakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo ya pili inasema tozo ya maendeleo ya elimu kwenye pamba inayotoza kwa kiwango cha shilingi 10/= kwa kilo katika Halmashauri ya Meatu, Halmashauri moja, wao Meatu waliweka hii tozo ili wachangie elimu wapate mapato ya ndani. Wizara ya Kilimo inasema, Wizara itawasiliana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya utekelezaji. Maana yake bado hawajatekeleza, lakini ilivyoandikwa ni kama jambo limekwisha, hiyo ni kwenye tozo ya pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija tozo ya korosho; tozo mbili zote zinahusu wanunuzi wa korosho. Hapo utaona tu kwamba tozo zinazoondolewa; gharama za magunia na kamba shilingi 56/=. Ni nani anahitaji hayo magunia na kamba? Ni mkulima wa kawaida? Ni yule anayenunua, anayepeleka huko mbele. Ada ya Leseni ya kununua korosho kwa kiwango cha dola 1000, siyo mkulima hapa. Wakulima wa korosho wanataka wahakikishiwe kwamba yale madawa kwa ajili ya mbolea pamoja na korosho ndiyo yanayotakiwa na ndicho ambacho tumekuwa tukikijadili hapa. Hapa ukiangalia, ni mtu wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokisema hapa ni kwamba tumesaidia watu, wale middle men kwa maana wafanyabiashara badala ya wakulima wa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye tozo ya tumbaku, ni hivyo hivyo. Kati ya tozo kumi ni tozo mbili tu ndizo zinawahusu wakulima wa kawaida moja kwa moja. Ukienda kwenye tozo za kahawa kati ya 17 ni tozo mbili peke yake ndizo zinazohusu wakulima moja kwa moja. Sasa tunapojadili tozo, tujadili kwa kuwasaidia wakulima wa chini na ndiyo maana siku zote tumekuwa tukisema kwamba hapa Serikali ingekuja ingejadili uhakika wa mbolea kwa wakulima wa kawaida, uhakika wa masoko kwa wakulima wetu, miundombinu ya umwagiliaji kwa mwaka mzima. Hayo ndio mambo ambayo tungesema kwamba tunamyanyua mkulima wa kawaida tunampeleka juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo sukari ni kwamba baada ya kuona ime-mess up na hata ukisoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, inaonesha uagizaji wa mwaka huu, sukari inaonekana mazao yameongezeka kweli kweli kuliko mwaka 2016. Kwa hali halisi kwenye soko la humu humu ndani ni kwamba hali ya sukari ni mbaya kuliko hata ile ya mwaka uliokuwa umepita. Sasa ukipitia hizi takwimu, zinaji- contradict.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ambayo tunayahitaji hapa tuyajadili. Ukijadili takwimu kwa spin, magazeti yakakusifu lakini ulichokiandika ndani hakitekelezeki na wala hakitamgusa mwananchi wa kawaida na ndicho ambacho mimi baada ya kukisoma hivyo, ndiyo maana ukienda hata kwenye hotuba ya Kamati, Kamati imeeleza vizuri, kilimo siyo moja ya vipaumbele vya Serikali. Maoni ya Kamati ndiyo maoni ya Bunge zima maana yake Bunge tunaiambia Serikali kwamba kilimo mnachokifanya ni sawa sawa na kazi bure, haya ni maoni ya Bunge yaani Kamati ni Bunge, ndicho tunachokijadilia hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji majibu juu ya haya masuala. Moja, tunahitazi ufafanuzi juu ya tozo moja baada ya nyingine, hizi ambazo zimeandikwa. Kwenye Kamati hizi hazikupelekwa, zimeletwa tu hapa ndani ya Bunge na ndiyo maana tunahitaji ufafanuzi juu ya hili jambo. Jambo lingine tunahitaji uhakika kwamba hawa wakulima ambao tumekuwa tukiwajadili kila mwaka iliwemo kule Momba, mwaka 2016 Serikali imeshindwa kununua chakula na tishio la njaa la mwaka 2016 ndilo ambalo sasa mwaka huu lilitakiwa tunapokuja katika mwaka huu mpya wa fedha, tishio lililokuwa linaoneka mwaka wa fedha uliopita lilitakiwa mwaka huu sasa Wizara ije na bajeti ambayo tutasema kwamba tutanunua chakula ambacho kitaweza kusaidia nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu, usalama wa Taifa siyo kuwa na bunduki nyingi. Usalama wa Taifa ni kuwa na chakula. Ukiwa na bunduki na mabomu, lakini mwisho wa siku watu wako wakiwa na njaa, hiyo vita huwezi kushinda. Ukisikia Marekani wanakwambia kwamba tuna uwezo wa kupigana vita tatu ama nne kwa wakati mmoja, ama mpaka vita sita, siyo kwamba kwa sababu wana mabomu ama wana teknolojia, wana uhakika wa kuweza ku-feed wanajeshi wao wakaendeleza mapambano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi uhakika wenyewe wa chakula ndani ya hili Taifa haupo, lakini ukiangalia mazingira yaani geographically position ya nchi yetu, ipo vizuri kabisa. Kwa maana, ukiangalia kama ni maziwa, yapo ya kutosha, kama ni mito ipo ya kutosha; lakini mwisho wa siku ni kwamba, miradi ya umwagiliaji haifanyi kazi vile inavyotakiwa. Miradi ambayo ilikuwa imeanziswa na Serikali, leo wananchi ndio wamekuwa wakilalamika.

Mheshimiwa Mewnyekiti, mwisho wa siku ni kwamba miradi hii ambayo ilikuwa imeanzishwa kwa mfano, miradi ya umwagiliaji badala ya kuwasaidia wananchi wa chini wa kawaida, sasa ile miradi anakuja mwekezaji mmoja anaambiwa sasa wewe huu mradi wa maji ndiyo utakaotumia. Kwamba anakuja mwekezaji, ameshaona miundombinu pale ya Serikali, anaambiwa ninyi mtatumia huu mradi na wananchi wa kawaida hawapewi ile namna ya kutumia yale maji kwa ajili ya kilimo cha mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo nilitaka kabisa lazima Serikali inapokuja itoe ufafanuzi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, tuelezwe, unapotaka kununua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kujadili hizi report zetu zote tatu, lakini zaidi nitajikita kwenye masuala ya uchumi, hususan kwenye Kamati yetu ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na report kuandikwa na kuelezwa ndani ya Bunge; pamoja na majibu ya Serikali kwa kipindi cha huu mwaka uliopita 2017, kwamba hali ya uchumi ni nzuri, lakini ukipitia kwenye records na taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoka; kwa mfano, kwenye Taarifa ya Easy of Doing Business kwa maana ya wepesi wa kufanya biashara, kwenye viashiria 11 ambavyo vimetoka nchi yetu imeporomoka kwa viashiria saba, yaani kwamba, kila mwaka tumekuwa tukiporomoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye kiashiria kimoja tu, upitishaji shehena bandarini na usafirishaji wa bidhaa. Sasa hivi tuko nchi ya 182 kati ya nchi 190 na bandari ndiyo sehemu pekee katika nchi hii ambayo inatuongezea mapato mengi. Asilimia 40 ya mapato ya nchi hii yanapatikana bandarini, lakini hali ilivyo mpaka sasa hivi hali ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukienda pale bandarini makontena mengi yamezuiwa pale kwa sababu ya contradictions ambazo ziko pale. Watu wa TBS wanasema hawawezi kutoa vibali vya kuruhusu makontena yatoke mpaka wapate certification kutoka TRA. Watu wa TRA hawawezi kuwaruhusu watu kutoa makontena mpaka wapate certification kutoka TBS, unashindwa kujua contradictions za kimamlaka ya watu wawili wanaofanya kazi kwenye Serikali moja zinavyosababisha wananchi waweze kuumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo mnajikuta kuna masuala ya storage mle ndani, ambayo ni non statutory fee ambayo mtu yeyote angeweza kuachiwa akafanya biashara, lakini leo imekuwa Serikali kama kuwakwamisha wafanyabiashara, ili walipe storage fee, ili kuongeza mapato ambayo yamekuwa yakiendelea. Kwa hiyo ni vizuri Serikali ikaja ikatueleza mikakati na namna ambavyo inaweza kukabiliana na hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, kutokana na muda najitahidi kukimbia kimbia. Jambo la pili, ukipitia Taarifa ya IMF na World Bank ambayo wameitoa mwisho wa mwaka, taarifa inatueleza kabisa kwamba, ukipitia Sera yetu ya Kifedha kwa maana ya Monetary Policy pamoja na Fiscal Policy, hizi sera moja inamtafuna mwingine. Kwamba, benki unajikuta kama sasa hivi Benki Kuu inajitahidi kushusha riba, ili mabenki yapate fedha yaweze kukopesha wananchi, lakini ukweli wananchi wanashindwa kukopa pamoja na Benki Kuu kupunguza riba kule ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini; kwa sababu, ukija kwenye Fiscal Policy ndio Sera ambayo inakula. Yaani kodi ni nyingi kwa maana mtu anashindwa kukopa kwa sababu, anajua nikikopa nitashindwa kulipa, kwa hiyo, inabidi kuangalia hapa je, tunatengeneza uchumi wa namna gani katika hili Taifa na ukiangalia kama sasa hivi tangu Taarifa ya Benki ya Dunia imetolewa, sisi kama Taifa tumeshindwa kutoa maelezo ya kutosha ambayo yanaweza kulisaidia Taifa namna gani ambavyo tunaweza kukabiliana na hii hali ya ukwasi kupungua zaidi hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuonesha uchumi kwamba umeendelea kuyumba; ukiangalia sasa hivi Serikali imefunga mabenki, inajitetea yale mabenki wigo wake ni mdogo, lakini ukweli ni kwamba, ukiangalia zile community bank 12, benki karibu nane zinatakiwa zifungwe kwa sababu na zenyewe bado zina-run under profit, kila mwaka zinapata negative ukiangalia kwenye report ambazo wao wenyewe wamezitoa. Kwa hiyo, napenda na jambo hilo vile vile Serikali iweze kukaa na kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukwasi kupungua; sasa hivi mzunguko wa fedha nchini umepungua kwa zaidi ya asilimia 45. Watu hawawezi kuagiza nje ya nchi na sisi wenyewe tumekuwa tukiiona hiyo hali, lakini bado Serikali imekuwa ikijinasibu kabisa kwamba, fedha zipo zinatosha, lakini hali ya uchumi wa nchi yetu bado umeendelea kuyumba kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zimeendelea kuonesha kwamba, ili sera na uchumi uwepo bado ufisadi ndani ya nchi yetu umeendelea kuwepo. Jana Mheshimiwa Heche alijaribu kuzungumzia kidogo tu kuhusu Mradi wa Passport Nchini. Mradi ule umekuwa inflated kwa 40 million US Dollar. Nina taarifa ambazo tumezipata, ni kwamba ule mradi thamani yake halisi ulikuwa ni dola milioni 16, sawasawa na paundi milioni 11, lakini umekuwa inflated to dollar karibu milioni 58, forty million plus.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna taarifa hizi, kuna kampuni ambayo ilishakuwa imepewa Memorandum of Understanding ambayo walipewa vile vile mkataba ambao haukusainiwa mpaka dakika ya mwisho, lakini mwisho wa siku waliingia kampuni mpya ambayo inaitwa ya HID. Hii Kampuni ya HID ambayo ndiyo imefanya hii kazi haijawahi kufanya mradi wa Passport duniani mahali popote. Ni kampuni ambayo kazi yake ni moja tu, inatengeneza hizi security doors, yaani zile kazi ambazo za ku-swap. Sasa ndio kampuni ambayo imeingilia hiyo kazi na ndio imefanya. Imeingia ubia na watu ambao walikuwa NIDA katika kile kipindi ambacho kimepita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ufisadi bado upo na uchumi umeendelea kuyumba, lakini watu wamekuwa wakifichaficha tu kwa namna fulani. Tuna documents zote kama ambavyo watu wakihitaji sisi tutazikabidhi. Kwa hiyo, tungependa vilevile tunapojadili Sera ya Uchumi na haya mambo lazima vilevile yaweze kujadiliwa, kama tunapinga ufisadi lazima hatua ichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naamini kabisa sisi humu ni Wanasiasa na tunaweza hata tukawa ni Mawaziri, tunaweza tukawa hatulijui hili, lakini taarifa za ndani tulizonazo ni juu ya hili jambo kuna ufisadi wa kutisha kwenye mradi wa passport za hapa nchini. Kwa hiyo, ni jambo ambalo linahitaji lipatiwe ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa ni kuhusiana na transfer pricing. Nchi yetu pamoja na kwamba, tumekuwa tukipambana kuwakamata wananchi wa kawaida walipe kodi, lakini ukweli ni kwamba, makampuni makubwa yamekuwa yakikwepa kodi katika namna ambayo Serikali haiwezi kupambana nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami hili nataka Wizara ya Fedha ijaribu kwenda kuangalia zile regulations (kanuni) zao kuhusiana na haya makampuni makubwa kwenye issue nzima ya transfer of pricing. Nilitoa mfano mmoja, wakati tunapitia kwenye moja ya Kamati, kwa mfano, kampuni ya Petra Diamond, ambayo inafanya kazi ya uchimbaji wa almasi, yenyewe…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii kuchangia hoja iliyoko mbele yetu ambayo ni uwasilishaji wa hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ningependa kutolea ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo zilijitokeza wakati Waheshimiwa Wabunge wanachangia katika hotuba ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi walichangia kuhusu miundombinu katika shule zetu na miongoni mwa mambo ambayo walikuwa wamechangia; moja walipendekeza kwamba kwenye hizi shule kongwe za msingi ambazo nyingi ni mbovu, walikuwa wanaomba Serikali izingatie na izifanyie ukarabati. Mpaka ninavyozungumza sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeshazitambua shule 722 nchi nzima, shule kongwe na shule hizi ni zile ambazo zilijengwa kabla ya uhuru na nyingine zilijengwa mara baada ya kupata uhuru. Tumekubaliana kwamba wanafanya tathmini na baada ya kumaliza tathmini tutatumia hii miradi ambayo tuko nayo; tuna Mradi wa GPE-LANES II, Mradi wa Shule Bora, Mradi wa Boost na Mradi wa EP4R kuhakikisha hizi shule zinakarabatiwa kama Bunge linavyohitaji.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuonyesha kwamba Serikali bado inahangaika na miundombinu na kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira bora. Mwaka huu wa fedha ambao tunakwenda kuupitisha kama Bunge lako litaidhinisha, tumedhamiria kujenga shule 300 kati ya shule 1,000 complete school na shule hizi zitajengwa katika zile kata ambazo hazina sekondari. Shule hizi zitakuwa za kidato cha kwanza mpaka cha nne, madarasa yatakuwa nane mpaka 12 na shule hizi shule moja itagharimu shule milioni 650 mpaka 700 mpaka inakamilika.

Mheshimiwa Spika, na zoezi hili ni endelevu tutalifanya Mwaka huu wa fedha, tutalifanya mwakani, tutalifanya mwaka kesho kutwa. Baada ya kukamilika kwa shule zote hizi maana yake tunatarajia kuwasaidia watoto wa masikini 400,000 kwa kujenga shule 1,000 katika safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, Serikali kwenye kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu na tunamsaidia mtoto wa kike, tumekubaliana kwamba tutajenga shule 26 maalumu za kimkoa na mwaka huu tunaanza shule 10 kati 26 na mwakani tutafanya 16 kuhakikisha kwamba kila mkoa unakuwa na shule ya wasichana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shule hii ya wasichana itakua inachukua watoto 1,000 mpaka 1,200 nchi nzima, shule itakuwa complete itakuwa na kila kitu na tunajenga shule ya kisasa kweli kweli, kwasababu gharama ya shule moja hizi ni bilioni nne, ni kitu ambacho nafikiri kwa mara ya kwanza katika Serikali yetu tunafanya kitu kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walijaribu kuzungumzia kuhusu ujenzi wa mahabara, ninafikiri kama kuna kazi kubwa Serikali imefanya ni kujenga mahabara za kisasa kwenye shule zote nchini. Na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Mwaka 2020, hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyefanya mtihani wa alternative to practical, kwa hiyo, haya ni mapinduzi makubwa kabisa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana utaona kabisa kwamba kwenye bajeti yetu tumetenga pale, mwaka huu wa fedha tunakwenda kufanya ukamilishaji wa mahabara 1,043, tunakwenda kumalizia maboma yale ambayo wananchi wameanzisha na kila boma litagharimu milioni 12.5 na mahabara moja tumepeleka kwa ajili ya kwenda kuzikamilisha milioni 30 na shule sekondari 1,841 na kwenye bajeti yetu, tumetenga bilioni 89.9 kuhakikisha zoezi hili linakamilika. kwa hiyo, tumedhimiria kabisa kuibadilisha sekta ya elimu katika ngazi ya elimu msingi ambayo tunaisimamia.

Mheshimiwa Spika, kwenye uhaba wa nyumba za walimu ni hoja ambayo hata Mheshimiwa Spika ulizungumza hapa na sisi tumeipokea kwakweli kuna changamoto kubwa. Tulikuwa tunazungumza na wataalam pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumekubaliana kuangalia namna bora ambayo tunaweza kuwasaidia walimu hasa walioko katika mazingira magumu kuhakikisha kwamba, sasa hii adha tunawaondolea. Kwa hiyo, tumedhamiria na tumekubaliana baada ya bajeti yetu tutakwenda kuanda mpango maalumu ili tuwasaidie walimu ambao zaidi wanakaa katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ajira za walimu ni kweli kabisa kwamba bado tunachangamoto ya walimu katika maeneo mengi, lakini tukiri wazi kwamba Serikali itaendelea kuwaajiri walimu kila mwaka kulingana na mahitaji na hali alisi ya kibajeti. Kwa hiyo, hilo ni kwamba kwa sasa hivi na ndiyo mpango wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwamba kila mwaka tutaajiri moja kwa kufanya replacement ya wale walimu ambao wanastaafu, wanafariki, wanaacha kazi, au wanafukuzwa kwa mambo mengi yaani hatutakua tunaacha kwamba wanastaafu halafu atuajiri, sisi tumesema kila mwaka tutaajiri kwa kufuatia hivyo.

Mheshimiwa Spika, jingine bajeti na mahitaji tutaongeza namba kulingana na mahitaji yaliyopo kuhakikisha kwamba tunaongeza ajira za walimu nchini. Katika kuondoa urasimu, tumeanzisha mfumo wa ajira ya mambo ya kazi unaitwa Online teacher application system na lengo la mfumo huu, moja ni kuondoa urasimu, pili ni mfumo ambao unawapangia walimu vituo moja kwa moja yaani unakwenda pale unapo- apply unaona mpaka shule unayotaka kuchagua. Kwa hiyo, kama kuna halmashauri zimeja maana yake ule mfumo utakuwa unakuonyesha huku kumejaa Kongwa au maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawasaidia watu wote. Tumekubaliana kwamba tutaendelea kuzingatia walimu wanaojitolea mashuleni kwa muda mrefu, tutazingatia mwaka wa masomo wa wa wale wanafunzi kwa maana walimu wanafunzi waliohitimu, kuna walimu wameitimu 2012,2013,2014, hawajaajiriwa. Kwa hiyo, tumesema sasa hivi tutakwenda kuwazingatia hao kwanza, lakini wote tunahakikisha tuna wa-accommodate katika mfumo wetu na watu wote wanapata hiyo ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye issue ya uhamisho ni moja ya ajenda ambayo ilizungumzwa sana na Wabunge, nieleze tu kweli kuna changamoto kubwa sana ya uhamisho hususani wa walimu na ndiyo moja ambayo imekua kero kubwa sana. Kwa hiyo, tumekubaliana Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi, tumeandaa mfumo unaitwa Human Capital Management Information System. Mfumo huu ni kwamba mtumishi atakuwa na uwezo wa kujiamisha online yani straight bila kuja huku chini uonge, fedha sijuwi ufanye kitu gani ndiyo upate uhamisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na huu mfumo uko katika hatua za mwisho na sasa hivi tunachokifanya, tumemaliza kutoa mafunzo katika ngazi za halmashauri sasa tunakuja katika ngazi ya juu ili watu wote waanze ku-apply kupitia huu mfumo. Kwa hiyo, lengo moja mtumishi atahama kupitia online; lakini pili taarifa mara yule mtumishi atakapokua amedhibitishwa kuhama zitaamishwa mara moja ikiwemo na mshahara wake yaani tukimuamisha tunamuhamisha moja kwa moja. Kwa hiyo, tunaamini kwa hili tutaondoa changamoto ya watumishi kuchelewa kupata majibu yao ya kuomba utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, tutoe rai tumesema kabisa katika huu mfumo ni lazima tuweke masharti vile vile, moja ya sharti tukalo liweka sasa hivi tumekua tukiajiri walimu, mwalimu akishafika kwenye kituo kwa mfano amepangiwa Kasulu, akishapata check number kesho yake anataka kuhama, tumeweka condition kwamba mtumishi hatahama kituo mpaka amalize miaka tatu kwenye kituo chake cha kazi. Kwa hiyo, na mfumo uta detect hili jambo kwamba huyu mtumishi bado muda wake wa kuhama, kwa hiyo ataendelea kukaa kwa hiyo mfumo utamkataa direct, tumekubaliana tutafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu ya mwaka 2021/2022 tumetenga bilioni 50 kwa ajili ya kununua vitabu vya kujifunzia na kujifundishia kwasababu kumekua na changamoto kubwa sana na Wabunge wamezungumza, shule zetu nyingi hazina vitabu katika maeneo husika na mawili ya mwisho ni kwamba kumekua na madeni ya wastaafu ambayo yamezungumziwa. Na ninavyozungumza sasa hivi kuna baadhi ya halmashauri zimeanza kuwalipa watumishi baada ya kusikia mjadala unavyoendelea Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, na Waziri husika tumesha pitia yale madeni tuna wastaafu walimu 2,822 ambao wanadai Serikali bilioni 3.9 kwa hiyo tunamalizia hatua za mwisho ili kuhakikisha watumishi wote waliofanya kazi kwa Amani kulitumikia Taifa letu nawenyewe wote wanalipwa kuhakikisha kwamba hatuendelei kuwasumbua kama ambavyo imekua ikitokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho mwaka huu Serikali inatarajia kupandisha madaraja, watumishi zaidi ya 90,000 nchi nzima, lakini kwenye hao watumishi wako na walimu kuna fifty-three, percent asilimia 53 ya hao watumishi ni walimu, kwa hiyo tuseme tu jamani Serikali imesikia mambo ya Wabunge, Serikali inafanya kazi, Serikali inajiamini kwa kitu ambacho tunajipanga na sisi tunawaomba Waheshimiwa Wabunge mtupitishie hii bajeti yetu ili twende tukatekeleze tumejipanga na tuko tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru naunga mkono moja ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi fursa ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma hotuba hii yote kwa ujumla imeonesha kama vile yaani Tanzania kwenye mambo ya barabara na nini hakutakuwa na tatizo lolote, ndiyo hotuba nzima ilivyokuwa imeonesha. Lakini nitatumia kama dakika mbili kuelezea Jimbo langu la Momba halafu mengine ntayazungumza ya kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza swali hapa Bungeni miaka yote kuhusu kupandishwa hadhi kwa barabara ya Jimboni kwangu Momba kutoka Kakozi – Kapele kwenda Ilonga, Sumbawanga na Serikali ikaniahdi hapa kwamba tutaipandisha hadhi, wakakiri imekidhi vigezo na nini, lakini mpaka leo ile barabara huu ni mwaka wa nne tangu ahadi ya Serikali ndani ya Bunge, haijatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna barabara ya kutoka Mlowo kwenda Kamsamba mpaka Kiliamatundu, barabara ile imekuwa kwenye ahadi ya kila mwaka ukosoma kwenye hotuba hii kila mwaka iko mle ndani kwamba tutaijenga kwa kiwango kinachoridhisha itakuwa na uhakika wa kiwango cha lami, lakini ile barabara imebaki kuwa story ambayo haikamiliki. Kwa hiyo, sasa ukiangalia haya mambo ndiyo inashindwa kuelewa kwa nini Serikali inashindwa kutekeleza kile inachokizungumza kila mwaka kwa sababu imekuwa ikichukua miaka mingi. Sasa hayo ndiyo maeneo makubwa ambayo sisi jimboni kwangu wakati wa sasa ndiyo yanayotusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nizungumzie mambo ya kitaifa. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina deal na Shirika letu la Ndege la Taifa. Hivi karibuni ndege yetu ya tatu ya Bombadier imewasili nchini na baada ya kuwasili kulikuwa na taarifa za kukamatwa kwa ile ndege ya tatu, ilikuwa inadaiwa. Hata hivyo pamoja na kwamba imewasili Serikali haijatueleza imelipa kiasi gani kwenye kuikomboa ile ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka majibu kwa sababu zile fedha ni kodi za Watanzania. Masuala kama haya yanapoachwa kimya sisi Watanzania tutaendelea kuyauliza bila kupatiwa majibu kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata taarifa, Mamlaka ya Anga Tanzania pamoja na Shirika la Ndege Tanzania limeondolewa kwenye yale mashirika ya anga (IATA) umesikia hiyo taarifa hivi karibuni, kwa sababu ya madeni na inashindwa kujiendeleza. Sasa haya tunahitaji majibu ili tujue hili shirika letu ni kweli linajiendesha vile inavyotakiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukisikia taarifa zinazotoka Serikali zinaeleza Shirika la Ndege la Taifa kwamba linapata faida; wao wanasema tumepata faida. Nakumbuka mara ya mwisho waliainisha kwamba wamekusanya karibu shilingi bilioni 20, lakini hawatuelezi running cost za ili shirika; hawaelezi wanaendeshaji; maana unatajiwa tu mapato ghafi. Atueleze kuhusu faida iliyopatikana baada ya kuondoa gharama za uendehaji wa shirika. Kwa hiyo tunahitaji kufahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye report ya Kamati ya wakati uliopita ilikuwa inaonesha kabisa kwamba Shirika la Ndege lina madeni makubwa, kuliendesha ni gharama kubwa. Sasa kumekuwa na contradiction kati ya kinachotolewa na Serikali na maelezo yanayokuwa yanatoka kwenye Kamati. Kwa hiyo, jambo hili tunahitaji kupatiwa ufafanuzi ili tuweze kufahamu hivi shirika letu lipo katika kile kiwango tunachohitaji, yaani ili liweze kuendelea na kulishauri vizuri. Kwa hiyo, tulikuwa tunahitaji kupata ufafanuzi kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu kwenye shirika hili la ndege, hatujawahi kuona taarifa ya ukaguzi ya CAG juu ya hili shirika la ndege. Sasa tunahitaji majibu; kuna usiri gani wa kushindwa kuleta taarifa ya CAG ya ukaguzi wa Shirika la Ndege ndani ya Bunge? Tunahitaji hayo ili tuweze kujua namna gani tunaweza tukawashauri, lakini pia tunahitaji kujua hizi kodi za Watanzania zisingekuwa zinapigwa huko kimya kimya halafu sisi watu hatujui; kama ambavyo leo Watanzania wote wanahoji kuhusu zilipo shilingi trilioni 1.5 hatutaki kufika huko na ndiyo maana, Mheshimiwa Waziri atakuja kutueleza hapo kwenye ku-wind up, atueleze kwa nini taarifa zake hazionekani? Yaani zinakuwa ni siri ilihali mradi huu ni kwa maslahi ya Taifa? Tunahitaji majibu juu ya jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka yote upande wa barabara (TANROADS). Wakala wa Barabara kwa miaka ya hivi karibuni tumeshindwa kupata ripoti ya ukaguzi ya TANROADS (Wakala wa Barabara wa Taifa). Tunazitaka hizo taarifa kwa sababu kuu mbili; kumekuwa na maneno uko mtaani watu wananon’gona nong’ona kwamba kulikuwepo na barabara hewa zenye thamani ya shilingi bilioni 252. Sasa unapoelezwa hizi taarifa halafu Serikali inakaa kimya; sisi kama Wabunge jukumu letu kuhoji tunahitaji kupata ufafanuzi ili tujue kweli hiki wanachokizungumza ni kweli ama ni uongo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini CAG haruhusiwi ama taarifa zake haziletwi kwa Wakala wa Barabara wa Taifa? Kwa sababu tunaziona barabara zetu, tunataka kujua value for money ya hizi barabara. Je, barabara inayojengwa thamani yake inalingana na pesa iliyokuwa imetolewa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo majibu ambayo Serikali inapaswa kutuletea sisi Wabunge ili tuweze kuishauri namna ya kuliendesha hili taifa. Kwa hiyo, hilo tunahitaji kufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine; sasa hivi kuna TARURA. Najua TARURA inategemea Mfuko wa Barabara fedha zake nyingi zote, niseme fedha zote zinatoka kwenye Mfuko wa Barabara. Hata hivyo bado kumekuwa na mkanganyiko, fedha kule kwenye TARURA hazipelekwi. Kuna barabara ambazo kwa sasa TARURA haiwezi kuziendesha. Nataka kujua namna gani ambavyo watu wa TANROADS wanaweza yaani tunatafuta yaani kama ule ushirikiano wa namna kupandisha hadhi zile barabara ambazo TARURA hawawezi, lakini fedha nyingi zimekuwa zikipelekwa upande wa TANROADS kuliko upande wa fedha za miradi ya barabara vijijijini hususani kupitia TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimeona nilizungumzie, najua liko kwenye upande wa TAMISEMI zaidi, lakini wana deal na barabara kwa hiyo unazungumzia barabara lazima kuwepo na connections, kwamba huyu anakuleta kwenye ngazi ya Wilaya na Mkoa huyu anakupeleka kwenye ngazi ya kitaifa zaidi. Kwa hiyo, na hili nilikuwa nataka tupate ufafanuzi kutoka kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Simu la Taifa (TTCL), shirika hili lina miaka mingi lakini ukuaji wake, yaani linakua katika tunasema in a negative growth. Sasa hivi wanasema rudi nyumbani, lakini rudi nyumbani hawana uwezo wa kujiendesha, yaani kwenye Taifa hili wapo kwenye Mikoa kumi tu peke yake. Tuliwauliza hapa siku moja, Halotel amekuja ana muda usiopungua miaka miwili, lakini ndani ya muda mfupi Halotel ana wateja zaidi ya milioni moja. Lakini TTCL lenye miaka na miaka lina wateja hawafiki hata laki mbili, ukiwauliza Serikali wanakwambia hiki ndicho kitu cha kujivunia, hiyo ndiyo changamoto iliyopo kwenye Serikali yetu. Tunataka kuanzisha mambo mengi lakini hatuwezi ku- compete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia hapa kwa nini Serikali isikubali kushiriki kwenye ubia wa PPP juu ya namna ya ku-run hizi kampuni. Amekuja Waziri hapa anasema kwenye miradi ya PPP Serikali ya Awamu ya Tano haioni kama ni kipaumbele. Sasa unajiuliza, mtawezaje kuendesha kila kitu kwa gharama ya fedha za ndani? Sasa haya dunia ya sasa huwezi ku-run miradi mikubwa bila kuingia katika mfumo PPP haiwezekani, na bahati mbaya sana Awamu hii ya Tano inafiiri kila jambo linaweze kutekelezeka kwa fedha za ndani, kitu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii na mimi nichangie hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tukiwa ndani ya Bunge lako tukufu kipindi tunapitisha bajeti humu ndani kama hii Bajeti Kuu, nakumbuka makofi yaliyokuwa yanapigwa humu ndani kwamba bajeti hii haijawahi kutokea yaani haina mfano! Mwaka jana tukajenga hoja tukaonekana sisi kama vile mwaka jana hatueleweki. Sasa mwaka huu siku ya Alhamis wakati Waziri Mpango anawasilisha bajeti yake, nakumbukua maneno ya Spika mwishoni ana-windup anasema jamani haya ni mapendekezo ya bajeti, siyo bajeti haijawahi kutokea ni mapendekezo. Kwa sababu gani, kwa sababu yale yote waliyoyaahidi mwaka jana with confidence, hayajatekelezeka. Kwa kifupi kwa mara ya kwanza ukisoma hotuba yake yaani unaona kabisa ni bajeti ya kukiri kushindwa, bajeti ya kuomba msaada anaomba Simon wa Kirene kwenye bajeti aje ashuke, abebe msalaba wa zege humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 81 wametajwa viongozi humu ndani, mashuhuri. Alipowataja mimi nilikuwa nawakumbuka ikabidi nirudi tena nisome upya, ili niainishe hawa viongozi waliotajwa kwenye dunia, viongozi mashuhuri na uchumi wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu wa kwanza aliyewekwa Deng Xiaoping, Rais wa Pili wa Jamhuri ya China, wakati anaingia madarakani alisema, to embrace people to be rich (kuwafanya wananchi kuwa mtajiri). To be rich is something to be glorious, Deng Xiaoping. Haya yapo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Mpango haya kayasema, sasa tu- compare na kwetu, sisi tunataka watu wetu wawe matajiri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kauli tumezisikia wote, tunataka matajiri waishi kama mashetani. Akatajwa Rais wa Pili, Lee Kuan Yew wa Singapore, huyu aliibadilisha Singapore kutoka dunia ya tatu kuwa dunia ya kwanza. Jambo la kwanza baada ya kupata madaraka, alifanya jambo moja, alisema lazima tuhakikishe watu wetu wanapata ajira (to promote stable employment jobs) kwa sababu Singapore unemployment ilikuwa iko juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya msingi ya kujifunza kwa huyu Rais wa Pili wa Korea, moja yeye ali- promote private sector, Singapore uchumi wake ni private sector. Sisi angalia private sector inavyolia leo, inalia siyo kawaida. Nenda kwenye mabenki angalia uchumi wake kule, mabenki yameporomoka, tumekaa na NBC wanakwambia imeshuka mpaka faida, dividend ya Serikali hakuna. Tumekaa na NMB, tumekaa na watu wa private sector wanailalamikia Serikali kwamba hatuwekezi kwa private sector. Haya aliyasema Rais wa Pili huyu ambaye amekuwa compared hapa, hizi sifa hizi yeye ali-promote private sector. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lee alikuja Tanzania mwaka 1973 pale UDSM, miaka hiyo akina Mheshimiwa Chenge walikuwepo pale, akaja pale na Mwalimu Nyerere akamwambia Mwalimu hii sera yako ya ujamaa na kujitegemea njia hii siyo sawasawa, alizomewa kweli na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati huo. Alipozomewa akasema mimi nilichokisema ndiyo hiki, hii njia mliyochukua siyo sawasawa. Juzi nikamsikia Katibu Mkuu wako wa chama anasema turudi ujamaa na kujitegemea! Mnakotupeleka siko. Kama unatumia mifano ya watu ambao waliwajali watu wa chini kuinua uchumi halafu comparison how? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Mahathir Mohamed wa Malaysia, unajua kabisa Malaysia imeendelea kwa mfumo wa PPP (Public Private Partnership). Haya tueleze sisi public private, tunasema reli tutajenga wenyewe, ndege tutanunua wenyewe, Stieglers’ Gorge tutanunua wenyewe, kwa nini, tutakopa, mwisho wa siku huu mfumo unaotumika sasa uko Tanzania tu. Duniani kote miradi mikubwa Serikali ina engage miradi mikubwa ya kiuchumi pamoja na private sector, lengo ili gharama zinazobakia, baadhi ya gharama ziende kusaidia wananchi. Sasa mikopo tunayochukua ni ipi, mikopo ya kibiashara na hii mikopo ya kibiashara tunayoichukua unajua maturity yake ni ndani ya muda mfupi miezi sita. Nilizungumza wakati wa Wizara ya Fedha kwamba, jambo la reli (standard gauge) siyo baya, lakini matokeo yake reli kabla haijaisha tunaanza kulipa mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii nakueleza ukweli, Waziri wa Fedha asipodhibiti Deni la Taifa tunakwisha. Kwa sababu, mwisho wa siku angalia kwenye hotuba yake kwenye ule ukurasa ambao ameainisha ile bajeti yake nafikiri ni kama ukurasa wa 78, soma mapato anayoyapata. Mapato ya Serikali Kuu ya ndani anategemea kupata trilioni 20, lakini kwa miaka yote hawajawahi kuzidi trilioni 14, hapo ni kama amekusanya asilimia 100. Ukija ukiangalia kwenye matumizi, Deni la Taifa, trilioni 10, mishahara trilioni saba, matumizi mengineyo trilioni tatu, trilioni 20, hayo ni first and second charge, jukumu la kwanza na jukumu la pili, wana uhakika wa kukamilisha? Kuna miradi ya maendeleo, hakuna? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana ukipitia bajeti nzima mwaka huu trilioni 10 hawajakusanya, miradi ya maendeleo haijafanyika, Halmashauri zina-suffocate! Haya tunawaambia kwa nia njema. Sasa unamgusa mtu kama Nelson Mandela amekaa jela miaka 27, mtu wa kwanza, hebu fikiria mtu aliyekufunga ndiyo unamuweka kuwa Makamu wako wa Rais, Frederik Willem de Klerk. Halafu yule aliyekuwa anamtesa Mandela ndiyo alikuwa bodyguard wake mpaka anakwenda kabirini, ndiyo alikuwa Chief bodyguard, yule gerezani aliyekuwa anamtesa miaka 27, anayemfanyisha Mandela kazi ngumu mpaka akaumwa TB ndio alikuwa bodyguard wa Mandela. Niambie wa kwetu angefungwa hata miezi sita ingekuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani mnakimbia vitu. Hebu kwa mfano unataka umuige Mandela, tumekuletea hotuba ya kurasa 521 unakimbia hotuba, mtaweza tabia za Mandela? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua wakati mwingine kama unakimbia maoni halafu unataka kuwa Mandela, hizi ndio tunaita nadharia. Utekelezaji ni tofauti na nadharia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere huyu sifa zake hazielezeki, ana sifa kweli na mimi ninakiri kwamba Mwalimu Nyerere anapaswa kuwa Mwenye Heri kama Kanisa Katoliki wanavyotaka, kwa sababu gani, aliunganisha Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akina Mtei wale wa Kaskazini walikuwa Magavana wake. Watu wale wa Usalama wa Taifa, Mkuu wa Usalama walikuwa ndiyo watu wake waliokuwa wanamsaidia, akina Ndugu Kombe wale na akina nani, leo huwezi kusema Taifa moja la upande huu, sijui Kaskazini wasubiri, hawa hivi, haiwezekani!

Mheshimiwa Naibu Spika, it is ok. Sina shida na suala la ETS, mkitaka kushughulika nendeni mpaka kwenye simenti, sigara na mafuta.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipa fursa hii kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kum-quote Makamu wa Rais wa Ghana, Dkt. Mahamudu Bawumia, anasema; “Huwezi kuendesha uchumi kwa propaganda.” Never, haijawahi kutokea, haitakuja kutokea, kwa sababu hali halisi ya maisha ya wananchi itakuumbua. Maswali madogo tu sisi mioyoni mwetu tunaridhika na namna Wizara ya Fedha inavyoendesha uchumi wa nchi hii? Mioyoni mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge tukiwa tumekaa kantini, tukiwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti kila taasisi inayokuja tumewapelekea bango kitita, taasisi zote, hakuna inayoridhika, watu wanalalamika. Tuna uwezo wa kusema propaganda kadri tunavyoweza, lakini uchumi hauendeshwi kwa propaganda, uchumi ni fact. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha iliyo chini ya Mheshimiwa Dkt. Mpango. Dkt. Mpango yule wa Tume ya Mipango leo wakikutana na Mheshimiwa Dkt. Mpango wa Wizara ya Fedha leo, ni watu wawili tofauti. Hakuna mahali wana-merge, yaani huwezi kuwakutanisha, yaani yule wa Tume ya Mipango wana-differ kwenye kila kitu, ndiyo ukweli, whether mnakubali ama mnakataa, ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Wizara ya Fedha na Mipango, mwaka jana mimi nilizungumza hapa Bungeni, inafanya mambo ya reallocation ya fedha bila mamlaka ya Bunge. Kosa hilo hilo wamelirudia tena mwaka huu, wametengeneza revised budget zaidi ya bilioni 355, Bunge halijapitisha wala hakuna reallocation warrant kwenye vitabu vyetu. Huko wamekiuka Sheria ya Bajeti… (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
naomba tu nimpe taarifa mchangiaji, pamoja na hizo personal attacks kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Dkt. Mpango hapa yuko kama Waziri na kanuni zinamtaka amu-address kama Waziri na siyo Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Spika, lakini nataka nimpe taarifa kwamba kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Bajeti, Sura ya 439 kimempa Waziri wa Fedha mamlaka ya kufanya uhamisho baina ya mafungu kwa kiasi kisichopungua asilimia tisa. Hiyo bilioni 355 anayoisema ni asilimia moja tu ya hizo asilimia tisa ambazo Mheshimiwa Waziri wa Fedha amepewa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninataka nimpe taarifa Mheshimiwa Silinde, asi-take advantage ya haya yanayojiri kupotosha fulani hivi, hiki kiasi cha fedha cha hizo bilioni 355 kiko ndani ya sheria na kanuni hiyo niliyoisema ambayo inampa mamlaka Waziri wa Fedha kufanya hayo aliyoyafanya. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Silinde ni taarifa kwako hiyo, iko ndani ya uwezo wake.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Bahati mbaya Waziri hakuelewa na Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Waziri wa Fedha unajua.

Mheshimiwa Spika, hawa watu hii ni sheria, Sheria ya Bajeti iko wazi, Sheria ya Fedha iko wazi. Sisi baada ya muda wako kuisha tutakutana mahakamani kule kwa hii kazi. Wasikudanganye, utafungwa kwa mambo haya. Sheria haifi, criminal huwa haifi. Mheshimiwa Waziri hajaelewa ni bahati mbaya sana. Watu wanaokushangilia sana usiwafurahie kuliko wanaokuambia ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba mimi niendelee na hoja za msingi ambazo nilikuwa nazungumza, kwamba makosa haya ya revised budget bila kuleta kwenye Bunge mamlaka aliyonayo ya kwenye mafungu ile asilimia moja hayo yanaeleweka. Lakini tutakwenda mwisho wa siku haya, sisi tunarekodi tu, tunaweka kwenye rekodi, utawala utakavyobadilika watakuja kusema akina Mheshimiwa Silinde mlituambia na mlitushauri vizuri na utawala siyo lazima aje CHADEMA nawaambia huko huko ndani, umenielewa. Kwa hiyo, hicho ndicho tunachokisema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Wizara ya Fedha imeshindwa kusimamia sera zake nyingi za fedha na tunapojadili hapa, tatizo la nchi hii, sera za nchi tulizonazo lazima ziendane na malengo (objectives) ambayo tumejiwekea. Sasa leo ukiangalia Sera ya Fedha, Sera ya Biashara, Sera ya Kilimo zinatofautiana kabisa when it comes to industrialization. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajadili uchumi wa viwanda lakini nenda kaangalie Sera ya Fedha, angalia Sera ya Biashara na Kilimo yaani hivi vitu vitatu tu vinatofautiana. Sasa unajiuliza unafikiaje malengo ya uchumi wa viwanda ambao tunauhubiri humu ndani wakati sera zenyewe zinatofautiana.

Mheshimiwa Spika, Serikali ikaja na blueprint, mkaleta opinion hapa kwamba twende na blueprint; leo kila unayemuita sasa twendeni tukatekeleze hakuna hata mmoja ambaye yuko tayari. Kuna mikanganyiko kibao mule ndani.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Silinde, taarifa, Mheshimiwa Angellah Kairuki nimekuona.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Silinde aache kupotosha. Tayari tumeshatoa taarifa, mpango kazi wa blueprint uko tayari na kuanzia Julai mwaka huu utekelezaji unaanza na hakuna anayepinga hilo na hata sekta binafsi yenyewe, bahati nzuri tarehe 28 Mei, nilikuwa nao, wanasubiri kwa hamu utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini si hilo tu, yako maeneo ambayo tayari utekelezaji umeanza. Ukiangalia katika kufuta tozo mbalimbali za OSHA, zaidi ya tozo tano; ukiangalia katika Wizara ya Madini katika uzalishaji wa chumvi zaidi ya tozo tisa zimefutwa. Lakini pia Wizara ya Afya kupitia TFDA, TBS, kwenye Bodi ya Nyama na Maziwa na bodi nyinginezo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe sana kwa kweli Mheshimiwa Silinde asitumie hadhara hii kuweza kufanya upotoshaji huo na niwahakikishie wananchi na wafanyabiashara wawe macho, Serikali inatambua kwamba wao ndiyo engine ya ukuaji wa uchumi, tuko pamoja nao, tunawathamini, tutawalea na kuhakikisha kwamba wanafanikiwa na hata Mheshimiwa Rais muda si mrefu anakutana nao kuhakikisha kwamba mambo yao yanakwenda vizuri. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Silinde taarifa hiyo ipokee.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, uzuri hawa watu ukipiga kwenye fact huwa lazima wajitokeze. Mimi napokea taarifa yake, naipokea kwa sababu ndicho ninachokizungumza. Hii taarifa ya blueprint tangu mwaka 2016, leo nasema hata Bunge halijui ndiyo taarifa inatolewa humu ndani kwa kushtukiza. Hii biashara ya kushtukiza kila kitu itaendelea mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mimi nasema naipokea, lakini bado ukiona vitu anavyovitaja ni vitu petty, yaani vitu vidogo vidogo. Kuna haja na ndiyo maana moja ya proposal yangu kwenye mchango wangu kabla huyu haja interfere nilitaka nikuombe uunde Kamati Maalum itakayopitia ile blueprint kuishinikiza Serikali ianze utekelezaji wake kwa sababu mambo mengi yanakwama, ndilo jambo ambalo nilikuwa nauliza.

Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana kuna vitu hapa tunaweza tukaulizana maswali, nchi hii kwenye masuala ya sera kuna swali tumewahi kujiuliza siku moja, hivi leo kwa mfano Wizara ya Kilimo isingekuepo watu wasingekuwa wanalima humu ndani, hii nchi watu wasingekuwa wanalima? Au Wizara ya Viwanda na Biashara isingekuepo watu wasingefanya biashara? Wangefanya. Sijui kama umenielewa.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa angalia hawa wataalam walikokaa kule, ndiyo wanatumika kama kuvuruga utaratibu. Sasa ukipitia, hii nilikuwa najaribu kuiunganisha kwa sababu sera yetu ya sasa ni sera ya uchumi wa viwanda. Sasa hivi vitu vitatu vikubwa nilikuwa naona ni vitu ambavyo lazima ilikuwa tuvi-merge ili kuhakikisha tunaisaidia.

Mheshimiwa Spika, kwenye Kamati ya Bajeti amekuja Waziri wa Viwanda na Biashara wanalalamikia kuhusu mtiririko wa makodi, amekuja Waziri wa Fedha na wenyewe wanawalalamikia watu wa upande mwingine. Kwa hiyo, imekuwa ni lawama juu ya lawama ya kila moja wao. Kwa hiyo, hilo nikasema ni bora kulisema.

Mheshimiwa Spika, lakini cash economy is very expensive na Mheshimiwa Dkt. Mpango anajua. Wakati Dkt. Mpango anaanza kuwa Waziri alisema bajeti yetu ni kasungura, sasa hivi amebadilisha kutamka yeye mwenyewe sasa hivi anatamka kwamba unajua uchumi wetu sasa ni kasimbilisi, kwamba makusanyo ya fedha ni madogo. Sasa tunapoiambia Wizara ya Fedha irekebishe, iongeze uzalishaji maana yake tunataka kodi, wigo wa kodi uongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana lengo letu lilikuwa ni nini, Wizara ya Fedha ni lazima i-promote, iweke incentives kwenye private sector ili kuongeza uzalishaji na wigo wa kodi. Lakini Wizara ya Fedha inajikita kwenye kodi peke yake, yaani yenyewe inafikiri kwamba kodi baada ya kodi ndiyo suluhisho.

Mheshimiwa Spika, kuna maswali ya kujiuliza hapa, swali namba moja, kwa mfano hivi kupunguza kodi ndiyo suluhu ya kupata kodi nyingi? Jibu linaweza kuwa ndiyo au hapana. Kwa sababu gani, moja, unaweza kuangalia efficiency, kama kukiwa na efficiency nzuri mtakusanya kodi, lakini efficiency ikiwa mbovu kodi itakuwa hakuna.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, uchumi unakwendaje? Kama uchumi ni mbovu hiyo kodi haiwezi kupatikana, mtahangaika haitakusanywa mahali popote. Ni masuala ambayo tunapaswa tuangalie. Jambo la tatu, compliance, mazingira ya kibiashara. Wakati mwingine wafanyabiashara hawataki wapunguziwe hata kodi, ni bureaucracy iliyokuwepo mle ndani, kuna kanuni zinakwenda contrary na sheria ambazo tumepitisha ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, sasa haya yote ndiyo kazi yetu sisi kuishauri Wizara ya Fedha iyafanyie kazi ili ku-rescue uchumi wa nchi. Lakini hapa watu wanataka kusikia zile lugha za kupendeza tu, jamani reli imepata, Stiegler’s imekwenda hivi, sijui nini; hizo lugha hazisaidii, tunaangalia mapungufu ili yarekebishwe, nchi iende mbele na hiyo ndiyo kazi yetu kubwa ambayo tunaifanya humu ndani. Sasa bahati mbaya binadamu huwa hapendi kusikia maneno mabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere wakati anaondoka madarakani…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Silinde.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipatia fursa hii kuchangia hotuba ya bajeti kwa mwaka 2019/2020. Mimi napenda kuanza kwa kusema kwamba duniani kote maendeleo ya nchi hayategemei kodi peke yake na ninalisema hili kwa sababu wimbo humu ndani sasa hivi imekuwa ni kodi, kodi, kodi, taratibu za kikodi, sasa leo mimi nitazungumza zaidi kwenye kushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kodi ni moja ya kitu ambacho kinasaidia maendeleo, lakini kodi asilimia kubwa ya nchi nyingi inatumie kwenye kulipa mishahara na recurrent budget kwa maana hizi OCs, matumizi mengineyo.

Mheshimiwa Spika, dunia ya sasa kama unataka kuendelea, kuna njia kubwa mbili tu za kufanya; jambo la kwanza ni Foreign Direct Investment na jambo la pili ni Private Public Partnerships. Hayo ndiyo mambo makubwa ambayo yanaweza kukutoa kwenye kasi ile ambayo dunia inaitaka ya sasa.

Mheshimiwa Spika, leo tumepitia hotuba ya Wizara ya Fedha na kwenye hotuba ya Wizara ya Fedha na baadhi ya hotuba zilizotangulia, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, imeainisha baadhi ya miradi ambayo bado haitekelezeki.

Mheshimiwa Spika, wameelezea Mradi wa LNG wakati wa Nishati na Madini kwamba uko kwenye negotiation, wameelezea mradi, kwa mfano mradi ambao mwingine umekufa wa Bandari ya Bagamoyo, kuna Mradi wa Liganga na Mchuchuma, kuna Mradi wa SGR na kuna Mradi wa Stiegler’s Gorge. Miradi hii ingetumia mfumo wa FDI na PPP, hebu fikiri leo uchumi wa Tanzania, tumekuwa katika level gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, LNG dola bilioni 30, unazungumzia trilioni 70 za kitanzania; Bandari ya Bagamoyo, endapo tungeingia mkataba vizuri kabisa, dola bilioni 10, sawasawa na trilioni 24, Liganga na Mchuchuma - dola bilioni tatu, sawa na trilioni saba, SGR trilioni 17 yaani ukimaliza phase nzima na Stiegler’s Gorge trilioni sita. Yaani unazungumzia uchumi ungeongezeka kwa wakati mmoja kwa trilioni 124. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo pato letu la Taifa ni trilioni 125, fikiria hizi fedha zingeingia ndani ya uchumi wetu, trilioni 124 kwa wakati mmoja, nakuhakikishia leo Serikali ya awamu ya tano ingekuwa ime-double GDP ya Taifa letu, lakini tatizo liko wapi, watakwambia mikataba mibovu na weakness ambayo tumekuwa tukiifanya kila siku kwenye miradi mikubwa kama hii, yaani wewe ukigundua kifungu kibovu na mkataba wote huutaki, wakati utaratibu wa dunia nzima, kama kuna mahali pana shida, unakwenda una renegotiate. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hebu angalia trickle down effect kwenye masuala kama haya, leo ajira zingekuwa bwerere kila mahali, kwa sababu kila mtu angepata ajira kwenye maeneo hayo kwa mfumo huo kwa hizo fedha ambazo karibu trilioni 124 zingeingia ndani. Viwanda vingekuwepo vingi nautolea mfano, Bandari ya Bagamoyo peke yake, ilikuwa tu siyo bandari, the whole project ilikuwa na viwanda zaidi ya 1,000 pale. Sasa haya yote yangekuwa yanafanyika kwa wakati mmoja, leo maendeleo yote yangebadilika. Sasa sisi tunatumia fedha za ndani na wakati mwingine tunakopa kwenye mabenki ya kibiashara ku- finance miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mfano mzuri, SGR tunakopa kwenye mkopo wa kibiashara, Stiegler’s vilevile, tunakopa vilevile humo ndani, tutaanza kulipa kabla hii miradi haija- mature!

Mheshimiwa Spika, na ninayasema haya kwa sababu moja tu, SGR awamu ya kwanza, Dar es Salaam - Morogoro, mpaka sasa umetekelezeka kwa asilimia 48. Bado hatujafika Morogoro, 48% tutakuja kumaliza mwaka gani na tunakwenda kwenye uchaguzi mwakani. Morogoro - Makutupora mpaka sasa umetekelezeka kwa asilimia saba tu, bado asilimia 93! Kwa mwendo huu Rais Magufuli anaweza kuondoka madarakani miradi hii haijakamilkka bado. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili, Stiegler’s Gorge mpaka sasa hivi mradi ni kwamba upo tu kwenye ma-study, wametoa bilioni 700, haujaanza ku-mature na tunahitaji umeme ambao ile reli itakapokamilika inatakiwa ianze kutumia ule umeme. Sasa haya yote ni kwamba tunakwenda lakini tunakwenda in a slow, very slow yaani mwendo wa konokono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni vizuri na Mheshimiwa Rais, nakwambia anataka kusikia maneno kama haya, hataki kusikia vitu vingine. Sasa kinachotokea ni nini, Bunge tunashauri, lakini haya mambo hayamfikii!

Mheshimiwa Spika,na mimi kuna kitu kilinishangaza sana, siku ile Mheshimiwa Rais wakati anazungumza na wafanyabiashara, nikawa najiuliza swali, hivi yale yaliyozungumzwa na wafanyabaishara, humu ndani Bungeni hatujawahi kuyasema? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kama humu ndani hatujawahi kusema, basi sisi wote hatustahili kuwa Wabunge. Kama hatujawahi kuyasema maana yake hatustahili kuwa Wabunge na kama tumeyasema, hayafiki, tafsri yake ni kwamba kuna watu ni washauri wabovu kabisa wa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii ninaisema kwa sababu moja, mwaka 2006 nikiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Rais Thabo Mbeki wakati ule alikuja pale, akafanya mdahalo Nkrumah, sasa pale Nkrumah alituambia hivi, kazi ya Urais inaweza kuwa ngumu kama una washauri wabovu na inaweza kuwa rahisi kama una washauri wazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ukisikia huko mtaani, unamsikia Rais Magufuli analalamika, Urais mgumu, Urais mgumu! Kumbe jibu ambalo Mbeki alituambia pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2006 ndiyo leo naliona kwamba amezungukwa na washauri wabovu, ndiyo maana anaona kazi ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Rais anakutana na wafugaji, Rais anakutana na wafanyabiashara, Rais anakutana na wachimba madini wadogo, Rais ata…, yaani Rais anafanya kila kitu mwenyewe! Bunge tunafanya kazi gani? Hasa hayo ndiyo maswali ambayo yanamnyima… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimelisema hili kwa sababu mwaka jana kwa mfano Kamati ya Bajeti tulikuja hapa na mapendekezo 11, Serikali ilikataa mapendekezo yote ndani ya Bunge hili! Baada ya miezi mitatu mambo hayajaenda vizuri, mchuzi wa zabibu, katikati ya mwaka wa fedha tukaletewa sheria ya mabadiliko hapa, Rais kule alishapigwa fix, katikati ya mwaka wa fedha tumekuja kubadilisha mapendekezo, mwaka huu wameleta mengine kama matatu, bado kama manne hivi. Sasa haya yote, ndiyo matokeo ya watu kumshauri vibaya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Rais anapaswa kushauriwa kwamba unajua na Mheshimiwa Mpango hili unajua, haya mambo ndiyo Rais anakiwa aelimishwe beyond reasonable doubt! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukizungumzia, mimi kila siku, siku moja nilizungumzia Rwanda, nimesoma mfumo wa Rwanda. Rwanda Rais Kagame, kabla hajafanya jambo, anaruhusu watu wafanye study analysis, wanakwenda zaidi ya mara tatu, yaani watu wanasoma mfumo sawasawa. Sasa study ya kwanza, study ya pili, study ya tatu, wanajiondoa na wasiwasi wa kutekeleza mambo, baada ya hapo, wanakwenda kutekeleza wakishakuwa wameondoa doubts zote katika ule mkataba. Sasa leo Tanzania, nikawa najiuliza hii mikataba tunayoikimbia, ina maana sisi hatuna hata wasomi/wanasheria wanaoweza kuandika mikataba vizuri! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ee, tunakaa na watu ambao wanafikiri tu kodi ndiyo inaweza kuleta maendeleo nchi hii, fedha za ndani ndiyo zinaweza kuleta maendeleo nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaani, with this, namna, hata ukiwapa miaka 100 hakuna chochote watakachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa we have to think in a different way na haya mamabo mmpelekeeni Mheshimiwa Rais aweze kuyafanyia kazi, kinyume na hapa, tutakwenda tu, tutabidi tu kwamba Bunge basi limalize kazi yake, awe anafanya mwenyewe pale Ikulu awe anaita sijui viongozi wa dini, asikilize maoni yao, na haya mengi tunayoyasema hapa!

Mheshimiwa Spika, waambie watu wako waache kuchujachuja sana haya mambo, yaani wanayakata sana, watu wanataka kusikia huko, taarifa haziji kama zilivyo, kwa hiyo, matokeo yake ni nini, lazima watu muwe na uwezo wa kusikiliza both sides, mambo mazuri na mambo mabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili niliamua niliseme kwa sababu ndiyo namna pekee ambayo tunaweza tukatoka hapa tulipo, tukaenda mbele zaidi, lakini kitu kingine tulizungumzia kuhusu kilimo. Mimi nimejaribu kusoma, Tanzania sasa hivi tunataka uchumi wa viwanda, lakini hatuwekezi kwenye kilimo! Jana mimi nimejaribu kupitia kwenye mitandao, kwenye kusoma journals nyingi, nchi zote zilizokuwa kiviwanda, kwenye first generation ya agriculture revolution, second generation ya agriculture revolution na third generation ambayo ilikuwa ni ya China, wote kabla ya kwenda kwenye viwanda, waliwekeza kwenye kilimo. Kilimo kilipozidi, ndipo wakaenda kwenye viwanda. Sisi tumekwenda kwenye sera ya viwanda wakati hatuna malighafi na ndiyo maana mnaona, sera ya viwanda haitekelezeki! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wewe mwenyewe unajiuliza, leo, hivi unaenda kuanzisha kiwanda, wakati huna pamba ya kutosha, unakwenda kuanzisha kiwanda wakati tumbaku yenyewe imeshuka kutoka uzalishaji wa tani milioni 150 mpaka tani 350,000. Pamba yenyewe imeshuka, korosho imeshuka, tunaanzisha kiwanda kwa malighafi ipi? Za kuagiza kutoka nje ya nje ya nchi! Kasome First Agriculture Revolution, kasome Agrarian Economy, kasome The Green Economy ya China, wote watakwambia causative ya viwanda, causative ya mabadiliko ya viwanda ilitokana na kilimo kikubwa na cha kisasa, ndiyo wakaenda katika uchumi wa viwanda. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kunipa fursa hii kuchangia Mapendekezo ya Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamezungumza ndani ya Bunge lako Tukufu walau kuna waliotoa mchango wa maana kuna wengine wameingiza kidogo siasa, lakini ndio maana ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niende kwenye mpango na ninataka Dkt. Mpango unisikilize vizuri kweli kweli ukipitia hotuba yako ukurasa wa 34 ambapo unajadili changamoto za utekelezaji wa mpango wa maendeleo na bajeti:-

(i) Serikali inasema ugumu wa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara waliopo katika Sekta isiyo rasmi kwa kuwa hawana sehemu rasmi za kufanyia huduma ya Kibiashara, hiyo ni moja Serikali imekiri.

(ii) Kutofikiwa kwa lengo la Kodi zinazotokana na ajira (Pay As You Earn) kilichosababishwa na kutofikiwa kwa malengo ya ajira mpya na kutokuongezeka kwa mishahara kwa wafanyakazi kama ilivyokuwa imetarajiwa haya Serikali inakiri. Hebu imagine Serikali ilikuwa inaanzisha chanzo haijui kama mishahara itaongezeka halafu leo tunakaa ndani tunajadili, Serikali yenyewe inakiri kwamba jamani tumeshindwa kwa sababu mishahara haijaongezeka kama tulivyokuwa tunatarajia tulikuwa tunapitisha mpango wa nini?

(iii) Sasa unakuja inakwambia kushuka kwa biashara za Kimataifa kulikopelekewa kutofikiwa malengo ya uagizwaji wa bidhaa kutoka nje, Serikali imekiri, watu wanazungumza yenyewe imekiri, imeandika ukurasa huu wa 35.

(iv) Upungufu wa Wafanyakazi na Vitendea kazi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tazania yaani mpaka leo Serikali yaani wakusanyaji mapato hawana Vitendea kazi mnajadili nini yaani hapa tunajadili nini?

(v) Kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo wakati wa utekelezaji wa bajeti.

(vi) Changamoto ya masoko na bei ndogo za mazao kwa wakulima, Serikali imekiri yenyewe mapungufu.

(vii) Kuendelea kuwepo kwa madai mbalimbali yakiwemo ya wakandarasi, watoa huduma, wazabuni na watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria malalamiko ya Serikali ambayo yalivyo genuine. Sasa kazi ya Bunge ambayo ilipaswa leo tuijadili hapa cha kwanza ilikuwa ni kwa namna gani tunaweza tukatoka hapa, that was number one. Mimi nimejaribu kupitia mpango hapa tangu jana napitia nimeangalia kila nikijaribu kuangalia sasa Serikali imekuja na mpango itautekelezaje mwakani kwa sababu mpango bila fedha ni kazi bure, is a nonsense. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi zote zinazopigwa hapa zitabaki kuwa stori tuu sasa unakuja kugundua, mimi wiki iliyopita, wiki mbili nilikuwa Rwanda kuna kitu nimejifunza na ningependa Tanzania ikajifunza. Nchi ya Rwanda kabla Mawaziri hawajateuliwa na Rais Kagame wanapewa perfomance contract unasema mimi Waziri wa Fedha nikiwa Waziri nitafanya moja, mbili, tatu, nne, tano, ukishindwa kutekeleza unaondoka automaticaly, hakuna mjadala.

Sasa leo kwetu humu ndani unakuta mtu analinda Uwaziri kwa kusifia sio kwa kutenda kazi, leo tukiwapima Mawaziri hapa tukasema Waziri gani number one na wa mwisho ni nani? Sisi wenyewe Wabunge tunajua nani anapiga porojo hapa ni waongo tu, nani wanamdanganya Rais tunawajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tunawajua hapa wote ninyi mlivyo, sasa matokeo yake mtu anayejua kusifia sana ndio anayeonekana anafanya kazi, tunaliangamiza Taifa hili. (Makofi)

Sasa ukipitia hapa unaenda unaangalia mafanikio ya utekelezaji wa mpango unakuta Serikali imeandika pale kwamba ulipaji wa madai, eti Serikali mafanikio kulipa madai mlikuwa mnakopa mlikuwa hamjui hamtalipa? Yaani ipo kabisa kwenye hotuba ukurasa wa 31 eti madai, kulipa madai kweli jamani? Kwenye hotuba kabisa unaandika kabisa kabisa yaani na watu wanavuka kama hawaelewi unakuta mtu anakuja anaandika hapa kwamba huduma za maji, kwa mfano soma ukurasa wa 31 mimi imenishtua ndani ya miaka mitatu kwamba ukurasa wa 31 wa hotuba inasema; “Miradi 1595 ya maji vijijini imekamilika inayohudumia watu milioni 31,652,000” uongo uliotukuka, is a complete lie, kila Mbunge hapa analalamika maji watu milioni 31 jamani over sixty percent ya wananchi ndani ya miaka ya tatu kweli tunajadili mambo ya namna hii? A total lie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo unaweza kuyakuta Tanzania tu lakini muangalieni mwenzenu Mheshimiwa Rais Kagame, Kagame is a different man, pamoja na matatizo yake mengine lakini nimeona ni mtu tofauti. Rais ana bodi ya ushauri ambayo inamshauri, hiyo ina vikao viwili tu, mwezi wa sita wanakaa Kigali, mwezi wa kumi wanakaa Washington, Marekani. Bodi yake aliyounda kuna Rais Clinton, kuna kina Tony Blair kuna ma-CEO wa makampuni makubwa yote yanamshauri kuhusu uchumi wa Rwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mradi unatekelezwa Rwanda bila kupitia level tatu za utathmini, anaitwa consultant number one, anakuja namba mbili, anakwenda namba tatu akishauriwa Rais Kagame hapo arudi nyuma ndio mtu akipinga atapotea katika mazingira ya kutatanisha, sio mawazo tu ambayo mtu mmoja anaweza akatoa wazo likaanza kutekelezeka halafu tathmini baadae, this is a nonsense, hatuwezi kuendesha nchi katika huo mfumo. (Makofi/Kicheko)

Sasa leo tuna SGR (reli), Kenya wakati wanaanzisha SGR walihakikisha wanapanua bandari ya Mombasa, that was they did Kenya, leo una SGR Tanzania bandari wanasema tunarekebisha gati one wakati mipango ya miaka yote tunapitisha ndani ya Bunge tumepitisha gati 13, gati 14 yamefutwa kwenye mpango sasa unategemea hii reli ikishakamilika fedha tunaturudisha vipi za miradi ya reli? Tumeshindwa kuiga Kenya wanavyofanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unasema mradi unaanza Disemba unakwenda mpaka Isaka sijui baada ya hapo unakwenda Makutupora wakati Rwanda mwenzako anakwambia Mradi wa SGR ataufadhili kwa kutumia PPP, wewe unasema nitaufadhili kwa kutumia fedha za ndani yaani unakuja kugundua yaani sijui tuna watu wa namna gani kwenye nchi yaani tuna watu they can not think unaweza kuwa Ph.D holder you can be a Professor lakini real life inakuwa determined na uwezo na capacity namna ambavyo mtu anavyoweza kutekeleza na kusikiliza. Kwa hiyo, mimi niliona nilisemee hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ukiifananisha na Rwanda ni vitu viwili tofauti strategically sisi tumezungukwa na nchi karibu tisa ambao hizi zote zinategemea Tanzania. Nchi ya Rwanda hawana rasilimali mtu atajenga hoja wanaiba Congo, lakini si kweli mtu anasema Rwanda ni kanchi kadogo si kweli mtu atakuja anahoja Rwanda kuna vision, Rwanda kuna commitment watu wako tayari kutumikia Taifa lao Tanzania hakuna commitment iko labda kwa mtu mmoja tu the rest ni blaa blaa tu kudanganya wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali inapokuja mwishoni ije na mpango, itueleze hapa namna gani tunaweza tukakusanya trilioni 22 ili tuweze ku- finance mpango, lakini ukiangalia hapa nilikuwa naangalia vilevile kwenye huo ukurasa uliokuwa unafuatia namna ambavyo mkakati wao hamna mkakati tutaimarisha TRA kwa kukusanya kodi yaani ni kile kile waje watuambie namna gani sasa tutapata fedha kwenye vyanzo vya uhakika ili nchi iweze kufaidika.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia Taarifa ya Kamati ya Bajeti. Nianze kwa kusema jambo moja tu; moja ya vitu ambavyo ninamwonea huruma sana Rais, Dkt. Magufuli, ni anazungukwa na watu wanaompa taarifa za uongo sana. Bahati mbaya sana, tunapokaribia kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, watu wanaongea uongo sana, yaani unaweza kumwambia mtu jambo ambalo hata yeye mwenyewe anajua kabisa unamdanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hoja zilizokuwa zinajadiliwa tangu tulipoanza Bunge hili, hususan siku ya jana na mwendelezo wa siku ya leo, bado hatujibu maswali ya msingi wanayohitaji Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuiangalia Taarifa ya Kamati ya Bajeti, unaweza ukapata maelezo ambayo sisi Wajumbe tulikuwa tunapewa ndani ya Kamati ya Bajeti. Kuna vitu havipo kwenye taarifa yetu ambavyo ndivyo vingekuwa vina uwezo wa kujibu maswali ya msingi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa tulipewa ya Mfuko wa Maji. Mfuko huu ambao Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilisema inakwenda kumtua mama ndoo kichwani, kati ya shilingi bilioni 299.9 ambazo Serikali ilitakiwa itoe kupeleka katika Mfuko wa Maendeleo ya Maji, imetoa shilingi bilioni 1,637 sawa sawa na asilimia 0.6. Haya hampendi kuyasikia, lakini ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wahisani waliahidi kutoa shilingi bilioni 284, mpaka sasa wametoa shilingi bilioni 4,320, sawa sawa na 4%. Haya sasa hebu niambie, unatatuaje tatizo la maji? Unamtuaje mama ndoo kichwani katika kipindi hiki cha miaka minne, kuelekea uchaguzi, hili haliwezi kuzungumzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi ndani ya Bunge kwamba itamalizia majengo yote ya wananchi wa Tanzania waliyoyajenga kwa nguvu kazi yao; kwenye shule na afya; kwa maana ya Shule za Sekondari na Msingi, maboma yote, waliahidi. Ikapigwa hesabu fedha iliyokuwa inahitajika katika mwaka wa fedha uliokuwa unapita, shilingi bilioni 251. Sisi kwenye Kamati ya Bajeti tulipambana na Wizara ya Fedha tukawaita mbele ya Kamati ya Uongozi Serikali ikaji-comit kwamba katika Mwaka wa Fedha unaokuja robo ya kwanza tutatoa shilingi bilioni 29. Mpaka leo tunavyozungumza, hawajapeleka hata senti moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ndiyo maswali ya msingi ambayo wananchi wanataka majibu ya moja kwa moja. Sasa unakwenda kujadili mambo makubwa. Amezungumza vizuri sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Kamala, ukuaji wa uchumi. Kwenye takwimu za Serikali zinaji- contardict zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati ya Bajeti, niwaeleze, katika mwaka wa fedha uliopita, ukisoma taarifa yao, inasema, mwaka wa fedha kipindi kama hiki kilichopita, ukuaji wa uchumi ulikua kwa asilimia 5.8, yaani Julai – Desemba na mwaka huu uchumi umekuwa kwa 6.0% yaani imeongezeka 2%. Ukirudi nyuma ukapitia taarifa ya mwaka 2018, uchumi wa Tanzania ulikua kwa 6.8%; yaani ni uongo uliopindukia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 kwenye taarifa yao ambayo ipo; sasa bahati mbaya sana, taarifa ambayo iko ndani ya Hansard ambayo Wabunge wote tunazo, mimi ninazo na Wabunge wote mnazo, labda kama hamsomi, inaonesha 6.8%. Taarifa ya leo imebadilisha matokeo ya mwaka 2018, halafu wanakuja wataalam wanakwambia huwa tuna-adjust, yaani what a fix? Yaani can you fix a country like this? I wonder! Hii ndiyo bahati mbaya. Sasa ndio watu waliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda kuangalia DSE, ndani ya mwaka mmoja Soko la Hisa la Dar es Salaam limepoteza mtaji wa shilingi trilioni nne. (Makofi)

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya hayazungumzwi na ndiyo yanayohusu mzunguko wa fedha wa Taifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Ndiyo Mheshimiwa Obama.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi huwa sina muda wa kudanganya na sipendi kumjibu Mheshimiwa Obama, nafikiri alikuwa anatafuta tu nafasi ya kuzungumza humu ndani. (Kicheko/Vigelegele/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzunguko wa fedha ni asilimia 3.2, mfumuko wa bei ni asilimia 3.3. Uki-calculate namna ya ukuaji wa Pato la Taifa, tunakua kwa asilimia moja, wala siyo sita. Ukiwauliza Serikali juu ya hizi takwimu, soma taarifa ya Benki Kuu, soma taarifa wanayotoa Serikali, yaani ni vitu viwili contrary. Nami najua kwa nini BoT wanataja taarifa ya ukweli, ni kwa sababu inasomwa na IMF, inasomwa na World Bank, inasomwa na watu ambao wanajua. Taarifa ya wanasiasa inakuja kisiasa kweli kweli na hilo ndilo tatizo kubwa sana ambalo linalikabili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Watanzania wanataka kujua maswali madogo madogo; mfumuko wa bei umeshuka kwa nini bei za vyakula, bei za bidhaa zinapanda? Serikali inapaswa kujibu mambo madogo madogo. unataka u-deal na micro economy ambayo hujaifanyia feasibility study, ni kama tu umekurupuka, hujui jambo lolote inavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa angalia matumizi; ukienda kuangalia kwenye Fungu la matumizi huku, unakuta Hazina, ndani ya nusu mwaka tulitakiwa tuwape bilioni 144 mpaka sasa wamepewa bilioni 414 asilimia 286. Ukiangalia Tume ya Uchaguzi 1.2 wamepewa 8.3 billion sawasawa na asilimia 674. Kaangalie yale Mafungu yaliyozidishiwa fedha, narudia kusema, siku Mheshimiwa Dkt. Magufuli atakapomaliza utawala wake, mtu wa kwanza kwenda Jela atakuwa ni Katibu Mkuu wa Hazina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,na msimdanganye, atakwenda, kwa sababu Mheshimiwa Rais akishaondoka madarakani hana power tena ya kumlinda mtu aliyeko. Anayekupenda anakwambia ukweli, ukipitia matumizi kwenye hivi vitabu, mwakani CAG akipitia haya taarifa itakayoletwa ndani ya Bunge kutakuwa na zaidi, yaani matumizi ya fedha, mtakuja kuambiwa hapa, safari hii mmetajiwa 1.5 trillion, itakuja trillion nane, kwa sababu fedha zilizokuwa misallocated, is too much na Bunge hatuletewi kile kitabu cha kuonesha Serikali inafanya reallocation kila mara, hakiji humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungependa kufahamu, Serikali ni kwa nini hailipi fedha za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na mashirika ya umma, ni kwa nini Serikali katika robo ya kwanza mwaka 2018 tulipitisha kwenye fungu kwamba Serikali kama bilioni 60 za kulipa milioni 50 kila kijiji kwenye pilot study, mpaka sasa hivi, ni kwa nini hawjapeleka na ndiyo ahadi yao katika Uchaguzi Mkuu? Tunahangaika na uchumi mdogo ili kuutengeneza uchumi mkubwa, hilo ndilo ambalo tunalihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na yote haya machache niliyoyasema, lakini naiomba Serikali pamoja na Kamati ya Bajeti tuliyopendekeza, siyo tu ije iyajibu, lakini tunataka commitment ya Serikali kwenye kutekeleza haya na wala siyo…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Silinde.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kunipatia fursa hii ya kujadili Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa. Nianze tu kwa kusema kwamba yaliyoanza kuzungumzwa kuhusu Katiba, tukilalamika Katiba ni mbovu, haina maana ubovu wake ndiyo uendelee kukiukwa, hicho ndicho ambacho tumekuwa tukisimamia kila siku. Pamoja na kwamba hatujapata Katiba mpya hii Katiba iliyopo ifuatwe kama ambavyo tumeapa ndani ya Bunge na walioapa nje ya Bunge kutekeleza wajibu wao. Ni hilo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisoma hii sheria kuanzia kifungu cha kwanza (1) mpaka cha 24. Jambo la kwanza lililonishangaza ni Serikali kubadilisha jina la Muswada ndani ya Bunge leo. Hii maana yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba Serikali yenyewe inajua kuna jambo ilikuwa imeficha, inajua watu wa vyombo vya habari walikuwa wamejiandaaje na hii taarifa! Ukweli ni kwamba habari ni zao la taarifa, huo ndiyo ukweli yaani huwezi kutoa habari bila kupata taarifa mahali fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna magazeti yamekuwa yakiandika habari ambazo zinahusisha taarifa za kiuchunguzi. Sasa leo unamwambia yule mtu ambaye alikuwa anaandika taarifa za kiuchunguzi aende kwa Afisa Habari wa Halmashauri fulani ama Mkoa fulani ndiyo apewe taarifa husika. Hapa tunasema funika kombe mwanaharamu apite lakini ukweli ni kwamba mnaficha na mnakwenda kuua Taifa kwa Muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe amesoma hapa mwanzoni, ameanza kwa mbwembwe nzuri na niisifu sana Serikali hii ya Awamu ya Tano huwa mnaanza hivi, wananchi maskini, wananchi wananapata shida, tuko hapa kwa ajili ya kuwatumikia, that’s the way mnavyokwenda. Sasa kwa mfano ameanza hapa unajua wananchi tunataka waombe taarifa kwa Mtendaji, ukisoma hii sheria kifungu cha kwanza (1) hadi cha 24 hakuna mahali pameandikwa Mtendaji wa Kata, hakuna mahali pameandikwa sijui vitu gani yaani ni tactics za kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa ujumla taarifa nzima inayozungumza hii sheria inazungumza mambo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi, taarifa za umma ambazo mwananchi wa kawaida hatakiwi kupata. Taarifa zisizopaswa kutolewa amesema, moja inayohusu usalama wa Taifa tunakubaliana. Jambo la pili, ni taarifa inayohusu maslahi halali ya kibiashara, tunafichwa nini? Mikataba mibovu ambayo tumekuwa tukilalamikia hapa. Serikali ya Awamu ya Tano ilijinasibu ndani na nje ya Bunge, ilisema mkituchagua mikataba tutaweka wazi, Watanzania watapata taarifa kwa uwazi, leo unakuja unasema taarifa zisizopaswa kutolewa ni zenye maslahi halali ya kibishara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi haiendeshwi kwa mfumo huu. Hatuwezi kuji-contradict sisi wenyewe. Kwa hiyo, ndiyo maana kila siku tumekuwa tukiwaeleza ndugu zetu Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tumieni wingi wenu kwa faida ya hili Taifa, msitumie wingi wenu kwa kukandamiza Taifa hili. Naelewa kabisa na naona understanding za Wabunge wengi wa CCM, tukienda nje hapo mnasema ila pale mmegonga kwelikweli. Canteen tukikaa pamoja, mnasema ninyi jamaa mna hoja pigeni nyundo, tukipiga mkija hapa unashangaa hata wewe unadanganya hapa lakini ukweli ni kwamba tunaangamiza Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano taarifa nawapa kwamba mkubwa mmoja alisema wafyatue watoto kwa sababu elimu bure, nawapa taarifa, umenielewa? Leo kuna Mbunge anakuja anasema aah hamkuielewa vizuri, ile ilikuwa ni utani, sijui umenielewa, lakini kuna watu tayari wameshatwangwa mimba, watu wanazaa kwa sababu elimu ni bure. Sasa haya kuna watu wataendelea kuyatetea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mtu amekuja ametoa taarifa, akasema jamani eeh hebu wale mnaofichaficha hela ziruhusuni kinyume na hapo mimi ndani ya siku mbili nachapa pesa zote mpya, nawapa taarifa sijui kama mmenielewa? Sasa taarifa ni kwamba fedha zimefichwa maana yake ni nini? Ni hali ngumu ya maisha. Sasa ukisema hali ngumu ya maisha unaambiwa wewe ni mchochezi, wewe ni mvunja amani ya nchi, watu wanakamatwa kwenye vyombo vya habari. Hatuwezi kuendesha Taifa kwa style hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapa taarifa, Mheshimiwa Rais anasema jamani mnajua kuanzia sasa mchanga wa madini usisafirishwe nje ya nchi, very abruptly. Tunajua kabisa wana mikataba halali ambayo leo mnasema tuizuie, can you see the contradiction hapo? Wewe ni lawyer Chenge umenielewa hapo na ninyi wengine mmenielewa. Hii nchi hatuwezi kuiendesha kwa ujanja ujanja kwa kutunga sheria kila siku, haiwezekani, lazima tukubali kubadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana wakati tunawasikiliza hapa kwa makini, wanasema fumbo mfumbie mjinga, mwerevu ataling‟amua, sasa sisi wajanja tumeling‟amua kwamba hamuwezi kutuingiza kwenye 18 kirahisi. Ukiangalia kuanzia mwanzo mpaka mwisho sisi hatutaki kubadilishabadilisha mambo, kila siku mnatengeneza sheria za kukandamiza watu, kila siku sheria. Unatengeneza sheria unamkomoa nani? Cha ajabu, amezungumza Mheshimiwa Lema na Mheshimiwa Msigwa, sheria yenyewe inayozungumzwa adhabu yake, penalty yake not less than ten years. Ten years taarifa za Mtendaji wa Kijiji? Ten years taarifa ya Mwenyekiti wa Kijiji? Ten years Mwenyekiti wa Kitongoji? This is wonderful! Huyu anayekataa kutoa taarifa hapewi adhabu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine tunaulizana, nani anayepotosha taarifa? Mtendaji akileta taarifa ya uongo maana yake tukubaliane nayo? Waziri akileta taarifa ya uongo ndani ya Bunge maana yake tukubaliane nayo? Kwa hiyo, jibu unakuta hii ni kudanganya danganya tu, lakini tunagundua kabisa kwamba hii ni janja ya nyani, mnataka kubana vyombo vya habari na mwisho wa siku tunajiumiza sisi wenyewe. Tunajenga Taifa ambalo siku moja Rais mmoja anaweza kuwa na power ya kuvunja Bunge na kuondoa mtu dakika yoyote, sekunde yoyote, tutatengeneza sheria sisi wenyewe na huku ndiko tunakoelekea. Leo system yote ime-frustrate, watu wanaogopa kumwambia Rais ukweli. Hii sheria hamuipi tafsiri sahihi na ilipokuwa kwenye Cabinet hamkumueleza ukweli Mheshimiwa Rais. Sisi tumesema huyu Rais bila kuambiwa na kuelezwa ukweli hii nchi haitakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema wananchi wakapewe taarifa mmezuia mikutano wa hadhara, nani atakwenda kuwaelemisha kuhusu kupata taarifa?
KUHUSU UTARATIBU....
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kumuelimisha Mheshimiwa Mbunge Musukuma. Haya ndiyo mambo tunayoyakataa kutetea ouvu na uongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikutano imezuiwa na Rais amezungumza kila mahali, hakuna mahali ambapo hatujayasikia. Sasa sisi tulikuwa tunasema, haya mambo aliyoyazungumza Mheshimiwa Rais ni mema kweli, sijui kama umenielewa, tunataka sasa tukawaelimishe wananchi tupeni fursa ya kuzungumza kwa sababu sisi ndiyo wenye watu na watu ndiyo wana mamlaka ya kuweza kutusikiliza kule ndani.
Leo kwa hofu tu unasema sasa wewe Silinde hapana kwenda mahali fulani. Leo mimi natakiwa niende nikawaambie sikilizeni hapa Mbozi taarifa ziko moja, mbili, tatu, nne, tano mnatakiwa mfuatilie hivi. Bungeni tulipitisha moja, mbili, tatu kwa sababu kuna baadhi ya Wabunge hawatekelezi majukumu yao, hiyo ndiyo kazi tunayotakiwa tuende kuifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu hii sheria yenyewe mlivyoitunga kijanjajanja itatumika Tanzania Bara tu angalia mmewabagua Wazanzibar. Leo Zanzibar siyo Tanzania ile? Kifungu ya 2 unaandika tu itatumika Tanzania Bara pekee wakati ndani ya Bunge tuna Wabunge kutoka Tanzania Zanzibar. What is this? Kwa hiyo, Zanzibar kule tukaneni, fanyeni mnavyoweza, mpewe taarifa mnavyokwenda lakini Tanznia Bara tu peke yake. Kwa hiyo, unakuja kugundua haya ndiyo matatizo ambayo yamekuwa yakitokeza katika huu mfumo wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili Waziri uende kurekebisha kwamba hii sheria mkitaka itumike kote japo sisi tunaipinga kwa nguvu zote nendeni na Zanzibar kwa sababu ni nchi moja ipelekeni kule na kwenyewe ikafanye kazi lakini sisi hatukubaliana na hii sheria kwa wakati uliopo na vyombo vya habari visikie na haya tunayoyasema. Hii taarifa leo Mawio, Mwanahalisi hawatakuwa na mamlaka maana mtawahoji hii taarifa umetoa wapi, chombo gani kimekupa hii taarifa, Nape anafungia kwa sababu alikuwa anakosa ile mwanya wa kuyafungia, sasa leo atakuwa anawafungia kweli kweli, amekupa Afisa Habari gani?
Kwa hiyo, leo taarifa sahihi za nchi hii zitakuwa zile zinazotoka kwa Gerson Msigwa tu na watu wengine hawatakuwa na taarifa sahihi ndicho tunachokwenda kukiona. Sasa tunaomba hii ngoma irudishwe tu kwa sababu leo tunapata taarifa tunazotaka, Mbunge nina mamlaka ya kupewa taarifa wakati wowote, ninapokwenda mahali popote wala huhitaji kunitungia sheria na wajibu huu tumekuwa tukiutekeleza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la mwisho nisisitize kwamba nchi hii ni yetu sote na hakuna mamlaka iliyowahi kushindwa kukaa madarakani milele. Wanasema empire ya Rome ndiyo empire pekee iliyotawala dunia miaka mingi na hakuna watu waliowahi kuwaza kama inaweza kuanguka. Ninyi Chama cha Mapinduzi fikirini mara mbili kwamba there is a day mtakaa huku sisi ndiyo tutakuwa tunakaa huko tunatekeleza hizi sheria mtalia na kusaga meno kwa sababu tunaona maumivu mnayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano midogo, tulikuwa na Waziri Mkuu Edward Lowassa, leo anapata yale maumivu ya kutengeneza sheria alipokuwa huko upande wenu kwa sababu leo naye anakamatwa kama sisi, anagongwa virungu, maji ya kuwasha anamwagiwa, yote haya ni matokeo ya sheria mbovu tunazozitunga sisi wenyewe. Kwa hiyo, tunawaasa tengenezeni sheria ambazo zitatusaidia sisi wenyewe. Ndugu Mramba na Yona wote wanajuta kwa kutengeneza sheria hizi ambazo zinawafunga wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia hii fursa, nafikiri Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe emeelewa kwamba tunazungumza kwa hoja tukitaka mustakabali wa Taifa letu. Tujenge Taifa lenye kufuata sheria, haki na siyo kutengeneza sheria kwa ajili ya kuwakomoa watu fulani na ninyi kuna siku mtakuwa huku backbencher. Bahati mbaya sana Mheshimiwa Rais wa sasa dakika yoyote, sekunde yoyote hana rafiki anakufumua unarudi backbencher na tunawaona wengine mnavyojuta mliokuwa Mawaziri. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii angalau kutoa ufafanuzi wa hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano, kwa maana ya 2021/2022 – 2025/2026 pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wakati wanachangia waligusia mambo mengi sana ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI. Nami kwa niaba ya Waziri, Mheshimiwa Suleiman Jafo, naomba nitoe baadhi ya ufafanuzi katika mambo ambayo tumeyasikia na tunaendelea kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo Waheshimiwa Wabunge walizungumzia ni mapendekezo ya kuiongezea fedha TARURA ili waweze kujiwezesha kujenga hizi barabara za vijijini. Kwa hiyo, kitu kikubwa ambacho Waheshimiwa Wabunge wanapaswa kufahamu, ni kwamba Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kushirikiana na TARURA pamoja na TANROAD, imeandaa andiko linalopendekeza upya kupitia chanzo hiki cha mafuta ili tuone kama kinaweza kikasaidia. Pendekezo hili tunakwenda kuliwasilisha Serikalini kwa hatua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali inaendelea kupitia formula wa mgao wa fedha chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kupitia Bodi yake ya Mfuko wa Barabara. Kwa hiyo, hili tuliona tulizungumze kwa sababu ni Wabunge wengi walikuwa na nia njema kutaka kuona kuna ongezeko la mapato kwenye Mfuko wa TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la lingine ni kwamba watu wa TARURA hawawajibiki katika Halmashauri kwa maana ya Madiwani. Nieleze tu kwamba, Mwongozo wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini, unaelekeza vizuri kabisa kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambao ulitolewa na Katibu Mkuu mwaka 2018, inaitaka TARURA kufanya kazi moja kwa moja na Serikali za Mitaa. Pia Mheshimiwa Waziri alishalitolewa mwongozo kwamba miradi mingi inapaswa kuibuliwa na Madiwani ambapo watashirikiana na TARURA ili kuitengenezea bajeti na hivyo iwe inatekelezeka. Kwa hiyo, bado msimamo wa Serikali uko pale pale kwamba TARURA itaendelea kufanya kazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, lilikuwa ni kuimarisha miundombinu. Hili tumelipokea, nafikiri litakuwa affected zaidi baada ya yale mapendekezo ya awali ya ongezeko la mapato ambayo tunayapeleka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya nne, Waheshimiwa Wabunge walielezea kuhusu uendelezaji wa Mradi wa Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya DMDP. Kwa kifupi tu ni kwamba Serikali inaendelea kukamilisha utaratibu kwa ajili ya uendelezaji wa mradi huu na kwa awamu ya pili tunatarajia huu mradi wa DMDP utatumia dola za Kimarekani milioni 120.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la afya, Waheshimiwa Wabunge walipongeza jitihada kubwa ambayo imefanyika katika ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali katika ngazi za Wilaya na wakataka kuhakikisha kwamba Serikali inamaliza miradi yake kama ambavyo ilikuwa imepangwa hususan yale maboma ambayo yameibuliwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu kwa kifupi kwamba kwa mwaka 2021, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 27.5 kuhakikisha kwamba tunakamilisha maboma 555 ya zahanati zote nchini. Kwa hiyo, tumeamua tuliseme. Tumetenga shilingi bilioni 33.5 kuhakikisha tunanunua vifaa tiba katika hospitali 67 za halmashauri ambazo zilikuwa zimejengwa katika mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu, Waheshimiwa Wabunge walieleza kwamba pamoja na jitihada nzuri ambazo Serikali imezifanya kwenye kujenga miundombinu mizuri, lakini walikuwa wanataka ihakikishe kwamba inaongeza idadi kubwa ya Walimu katika shule zetu. Sasa katika kukidhi jambo hilo, tueleze tu kwamba Serikali itaendelea kuajiri Walimu kama ambavyo tumefanya mwaka 2020, tulitangaza ajira 13,000; ajira 8,000 tayari zilikuwa zimeshatolewa na 5,000 ziko katika hatua ya mwisho. Vile vile ni kwamba tutaendelea kufanya hivyo, kulingana na mahitaji kama ambavyo tumeyaainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Waheshimiwa Wabunge walikuwa wamezungumzia ushirikishaji wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi. Sasa hili tumeliainisha vizuri kabisa kwamba kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, tumeandaa Mkakati wa Miaka Mitano, kwa maana ya 2017 mpaka 2025 kuhakikisha kwamba tunawa-accommodate wananchi wote. Ndiyo maana unaona Serikali imeanzisha utaratibu wa kutumia force account ku-accommodate wananchi wa kawaida kushiriki katika uchumi wa nchi yao.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni miradi ya maendeleo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde, kengele imegonga. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii nami kuchangia Sheria ya Fedha ya Mwaka, 2018.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo napenda kuanza nalo ni hii sheria ambayo Serikali inakwenda kufuta Tume ya Mipango. Katika jambo ambalo kwa mara ya kwanza katika Taifa linashangaza kweli kweli, ni uamuzi wa Serikali kwenda kufuta Tume ya Mipango. Hii kwa mara ya kwanza ni kitu ambacho kinashangaza.

Mheshimiwa Spika, miaka yote hii sheria imekuwepo, tangu mwaka 1994 kumekuwepo na Tume ya Mipango kwa maana ya The Planning Commission. Cha ajabu katika mwaka huu wa fedha kwenye Sura hii ya 13, Serikali imekuja na amendment ya kufuta Tume ya Mipango. Sasa unajiuliza, hivi lengo la Serikali kufuta Tume ya Mipango ni nini? Wanakwambia unajua hii sheria iliyopo ni kama inamlazimisha Rais kuitekeleza. There shall be establishment ya hii Planning Commission.

Mheshimiwa Spika, sisi kwenye Kamati jana tulikaa, tukabishana na Serikali tukawaeleza kuna ubaya gani ama
kuna athari gani za kiuchumi za kufuta Sheria ya Tume ya Mipango? Serikali ikasema tunatakiwa tuifute kwa sababu mwenye mamlaka hataki kutumia.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa mkali sana kwenye hili na haya maneno alizungumza Waziri wa Fedha ndani ya Kamati ya Bajeti. Nikamwambia kama mwenye mamlaka hataki tuhoji jambo hili, mmelileta kwenye Kamati ya Bunge kufanya nini? Yaani unaleta kufuta sheria halafu unatuambia tusihoji mamlaka. Tukasema hatuwezi kuishi katika huu mfumo. Kwa hiyo, kumbe haya maamuzi hatutungi sheria kwa ajili ya kusaidia nchi, ni kwa ajili ya kumsaidia mtu. Imenisikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa unajua kabisa umuhimu wa Tume ya Mipango, nchi zote duniani zina Tume ya Mipango hata kama zinatengenezwa katika majina tofauti. Kuna nchi nyingine wanaita National Development Plan, National Development Vision, yaani majina tofauti.

Mheshimiwa Spika, leo Tanzania kwa mara ya kwanza tunakwenda kuifuta sheria ya mwaka 1994 baada ya miaka 24, tunaona haina umuhimu. Ukimuuliza huyo mtu ambaye anakwenda kuifuta, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndio ambaye alikuwa Katibu wa Tume ya Mipango; yaani miaka mitano ya Jakaya Kikwete ndio alikuwa Katibu wa Tume ya Mipango. Leo wanasema majukumu ya Tume ya Mipango yanahamishiwa Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuambiane ukweli, Wizara ya Fedha na Mipango imejikita zaidi upande wa fedha kuliko mipango, yaani kama kina kitu ambacho Wizara ya Fedha haifanyi ni Mipango. Leo unapokwenda kuifuta hii Sheria ya Mipango, maana yake ni kwamba tunawaachia sasa Serikali yaani Wizara ya Fedha, uamuzi wa wao kuamua kujipangia mambo na kutekeleza wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa maoni yangu ni nini? Kwa nini wanakwenda kuifuta hii Tume ya Mipango? Hata hivyo wameshaifuta, kwa nini? Ni kwa sababu wamekuwa na mipango ya kushtukiza ambayo haipo na wala Bungeni hatukupangia Bajeti. Sasa kutokana na kuona kwamba wamekuwa ni watu ambao hawajui mwelekeo unakwendaje, wameamua kwenda kufuta ili wawe wanapanga mambo wanayotaka wenyewe. Huo ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Taifa bila Tume ya Mipango ni sawa na gari ambalo lipo kwenye mwendo kasi halafu limekosa break, linakwenda kuanguka. Sasa napendekeza na ndiyo maoni ya Kamati, hakuna tatizo lolote Serikali ikiiacha Tume ya Mipango ikabaki kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunawaomba sana muiache hiyo Tume, kwa maana ya sheria, kwa sababu hii sheria tangu imekuwepo Mheshimiwa Mkapa hakuitumia, Mzee Mwinyi hakuitumia lakini Mzee Kikwete alipokuja akaitumia, ndiyo hii mipango mnayoona leo.

Mheshimiwa Spika, hii Mipango ya Maendeleo ya miaka 2025, Mipango ya Maendeleo ya 2063, inatengenezwa na think tank ya pamoja. Kitendo cha Serikali kwenda kuua Tume ya Mipango, nafikiri moja ya uamuzi wa ovyo kabisa ni huu hapa wa kufuta hii Tume. Kwa sababu wanasema, tukawauliza maswali, ikitokea sasa ninyi mmeondoka, Rais mwingine amekuja madarakani, atafanyaje kama ndiyo anataka kuitumia Tume ya Mipango. Akasema atatengeneza sheria nyingine.

Mheshimiwa Spika, yaani tunakuja tena kulipa kazi Bunge lijalo litengeneze sheria mpya katika hatua zake zote tatu wakati sheria ipo. Ambacho kilitakiwa kifanyike hapa na Wizara ni kuboresha tu hii sheria ama kuianza kwa sababu hata ikikaa dormant mtu yeyote anaruhusiwa kuitumia hii sheria pale anapotaka. Sheria iko wazi tu, haijamlazimisha Mheshimiwa Rais kuitumia kama hahitaji kuitumia. Kwa hiyo, nataka na hilo nilizungumzie na Serikali ielewe kwamba uamuzi huu ni moja ya uamuzi wa ovyo kabisa ambao nafikiri wakiendelea kuufanya utaligharimu Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nataka kuzungumzia Sheria ya Fedha za Umma, Sura 334. Sheria hii inahusu kuanzishwa kwa Akaunti Jumuishi ya Pamoja, hiyo tunaita TSA. Alitangulia Mheshimiwa Zitto akazungumza hapa. Kuanzishwa kwa hii Sheria ama kuanzishwa kwa Akaunti moja Jumuishi siyo kosa katika nchi, lakini utaratibu tunaokwenda kuuanzisha Tanzania, nasema hivi, tunaweka Taifa kwenye risk ambayo siku moja Taifa linaweza lika- paralyse.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nalizungumza hili? Nimepitia nchi ambazo zinatumia mfumo wa TSA. Mfumo wa hizo nchi ni kwamba nchi inakuwa na fedha, kwa mfano, kuna fedha ziko Momba, ziko kule Ruangwa na Kongwa. Inapofika mwisho wa siku, taarifa za fedha zinaletwa Benki Kuu, zinakwenda kwenye Akaunti ya Pamoja kwamba leo Momba tumebakiwa na kiwango kadhaa cha fedha. Kwa hiyo, wamekuwa wakiendesha mfumo huo kwamba inapofika jioni nchi inajua ina ukwasi kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, sheria yetu inavyokwenda kuonesha na ukiipitia tu vizuri kabisa, ni kwamba fedha zote za nchi hii mpaka zile za kwenye Halmashauri zinakwenda Mfuko Mkuu halafu baada ya hapo zinakwenda katika Mfuko wa Akaunti moja. Yaani hela za nchi nzima zinakwenda kwenye Akaunti moja. Ukipitia kwenye sheria utaona sheria inampa mamlaka Waziri wa Fedha kutunga regulation juu ya namna ambavyo Paymaster General atautekeleza ule mfuko, matumizi yake yatakuwaje na namna atakavyokuwa ana-limit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachokwenda kutokea ni nini? Hii Akaunti moja inakwenda kusimamiwa na watu watatu tu katika nchi. Hela zote tunapeleka katika chungu kimoja. Sasa mimi nikawaambia, hivi ikitokea siku moja system hiyo ya kifedha, hiyo Akaunti moja system yake ikafa, maana yake siku hiyo nchi imepotea.

Mheshimiwa Spika, ikitokea akaja Rais mzalendo, mmemwekea fedha zote peke yake, akiamua kutoroka nchi, akiondoka na hizo hela zote nchi itakuwa katika usalama gani? Sijui kama wamenielewa! Kwa sababu akaunti hii inaenda kuwa controlled na watu tatu. Ninachokueleza, hii ndiyo halisi. Najua unacheka, lakini ndiyo hali halisi.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba hizi hela hazihamishwi kwa kubebwa kwenye ndege ni ku- transfer ni ku-transfer tu. Watu wana-transfer fedha kwenda kwenye akaunti ya nchi nyingine. Watu wanafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, Nigeria wakati wa mfumo wa Jonathan walipoanzisha huu mfumo; leo Serikali ya Buhari wanakwambia mfumo wa TSA kwa sababu haukutengenezwa vizuri, ndiyo ulipelekea fedha zote na ufisadi mkubwa ulifanyika, kwa sababu fedha zote zilipelekwa pamoja. Cha ajabu, sasa hivi kinachokwendwa kwenye hii TSA kunakwenda kupitishwa fedha ambazo hazipo kabisa, Bunge hatujapitisha. Ukipitia kwenye sheria, utaona hapa kuna kitu kimeandikwa unspent. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukipitia hapa kwenye schedule ya Waziri utaona ameelezea hapa kwamba moja ya fedha zinazokwenda kwenye hii Akaunti ya TSA kuna kitu kimeandikwa unspent balances na ukienda mwanzoni kwenye yale mawazo yao ya mwanzo kwenye sheria utaona kuna fedha imeandikwa non voted fund. Fedha hizo sisi kama Bunge hatupitishi. Sasa matokeo yake, fedha ambazo hazijapitishwa na Bunge, fedha zilizopitishwa na Bunge, zote zinakwenda katika akaunti moja.

Sasa ukichanganya na Serikali ambayo haina Tume ya Mipango, maana yake kesho tutakapokuwa tunawahoji
wanatekeleza mipango, watakwambia hela tulizozitoa ni zile unspent balances ambazo ninyi Bunge hamna mamlaka nazo. Sasa imekiuka Katiba, vifungu tumeviuliza katika Bajeti yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunachokitaka, Serikali ipate muda wa kuipitia ili hili jambo liwe kwa faida ya Taifa na siyo kwa ajili ya kunuifasha watu wachache ambao wanafikiri ni wazalendo kwa wakati wa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kunipatia fursa hii kuchangia hotuba ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumeona tutolee ufafanuzi baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wakati wanachangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamejaribu kuzitoa hapa ambazo sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunazigusia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja namba moja ambayo Wabunge wengi walichangia walikuwa wanaiomba Serikali ama kuitaka Serikali kukamilisha maboma ambayo ni nguvu ya wananchi, ambayo yalitokana na nguvu za wananchi huko katika maeneo husika. Na sisi kama ambavyo bajeti yetu ilivyopita, tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha hayo maboma nchi nzima lakini kwa awamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika mwaka wa fedha 2021/2022, kwenye maboma ya maabara peke yake kwa shule za sekondari tumetenga bilioni 26.07 kwa ajili ya maboma 1,043. Lakini vilevile kwa ajili ya kukarabati na kukamilisha majengo ya shule za msingi tumetenga bilioni 23.154 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya shule za msingi 1,852. Na kwa ajili ya sekondari tumetenga bilioni 23 kwa ajili ya maboma 1,840. Kwa hiyo, hiyo ni hatua ya awali kuhakikisha kwamba tunaunga mkono nguvu za wananchi ambazo wamekuwa wakijitolea katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Waheshimiwa Wabunge walijenga hoja hapa wakitaka mkakati wa Serikali wa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wa sekondari wanaotokana na elimu bila ada au elimu bila malipo ambao sasa tunaamini katika mwaka wa keshokutwa, kwa sababu sasa hiivi ukiangalia watoto wa darasa la sita tulionao ambao wanatokana na Sera ya elimu bila ada wako milioni moja na laki nane. Kwa hiyo, watakavyofika mwaka 2022 tutakuwa na watoto ambao wanatakiwa kwenda kidato cha kwanza mwaka 2023, ukifuatilia ili pass rate ya kila mwaka ya zaidi ya asilimia 80, zaidi ya watoto milioni moja na laki mbili wanatakiwa wajiunge na kidato cha kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana kwenye bajeti yetu tumetenga fedha, kwa mwaka huu tutaanza na ujenzi wa shule mpya 300, lakini ndani ya miaka mitatu tutajenga shule 1,000 ambazo zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400,000 kwa hiyo, maana yake ukichanganya na idadi ya sasa tutakuwa walau tumeshapunguza hiyo kero ya wanafunzi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezielekeza halmashauri zote nchini kulingana na mapato yao ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Na tumeweka categories, kwa mfano halmashauri zenye kipato chini ya bilioni 1.5 kujenga madarasa 20 kila mwaka kwa kutumia fedha za ndani, kwenye halmashauri ambazo mapato yake ni kati ya bilioni 1.5 na bilioni 5 watajenga madarasa 40 kwa kutumia mapato ya ndani, na katika halmashauri zenye mapato zaidi ya bilioni 5 watajenga madarasa 80. Kwa hiyo, yote hii ni mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaondoa hiyo kero ya madarasa katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la taulo za kike tuliona Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia, na sisi TAMISEMI tukaona ni vizuri tuka-respond. Tumeziagiza shule zote na tumeandika mwongozo kuhakikisha kwamba kwenye ile fedha ya capitation grant, asilimia kumi itatumika kwa ajili ya kununulia taulo za kike shuleni. Kwa hiyo, hilo nimeona tuliseme kwasababu ndiyo dhamira ya Serikali, na litakwenda kutekelezeka na sisi kama wasimamizi tutahakikisha hilo linafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi mbalimbali ambayo ipo sasa hivi; tunakamilisha majengo, tunakarabati, tunaboresha, zikiwemo shule kongwe na zingine ambazo tumeziainisha kupitia Miradi kama ya EQUIP, SEQUIP, Boost na Shule Bora; tuna Miradi vilevile ya EP4R pamoja na LINES II. Kwa hiyo hii yote ni sisi Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI tukishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tunataka kuhakikisha mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora na anakuwa na mazingira bora na sahihi.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rwamlaza.

T A A R I F A

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde, kwamba hiyo capitation inayopelekwa shuleni, shilingi 4,000 inabaki Wizarani, inabaki shilingi 6,000 kwenye shule. Nina mashaka kama shilingi 6,000 hiyo ambayo haitoshelezi hata kununua chaki katika shule kama inaweza kusaidia watoto katika kupata taulo za kike.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Silinde, unaipokea taarifa hiyo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nafikiri Mheshimiwa Mbunge anafikiri labda ni shilingi 6,000 peke yake ndiyo inayokwenda shuleni kwa mwanafunzi mmoja; fedha tulizotenga kwenye bajeti kwa ajili ya capitation ya kwenda kule ni zaidi ya bilioni 298. Kwa hiyo fedha hiyo wewe calculate asilimia 10 ya hiyo fedha kwa ajili ya kwenda kununulia hizo taulo za kike kwa ajili ya kusaidia wananchi, kwa hiyo hilo ndilo lengo la Serikali na tumejipanga kulitekeleza kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, niwaombe mtakapokuwa mnapita kwenye ziara zenu katika shule waombeni taarifa, kila mkuu wa shule na mwalimu mkuu wamenunua taulo za kike kiasi gani kwa kutumia fedha ya capitation. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwasababu katika shule siyo kwamba inakwenda 6,000 peke yake, hiyo 6,000 ni kwa mwanafunzi mmoja. Kwa hiyo, kama shule ina wanafunzi zaidi ya 1,000 na kuendelea maana yake unachukua ile 6,000 unazidisha mara 1,000. Kwa hiyo, kuna shule zinapata zaidi ya milioni 30, kuna shule zinapata milioni 12, kwa hiyo inategemeana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa hivi kwenye hiyo formula ya capitation grant tunakuja na formula mpya kuhakikisha kunakuwepo na minimum amount. Kwasababu shule nyingine zina idadi ndogo ya wanafunzi lakini mahitaji ya kishule yanalingana. Kwa hiyo, tumeliangalia vizuri na tuko makini katika kulikamilisha hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimeona niyatolee hayo ufafanuzi, na niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kwa kunipatia fursa hii kuchangia taarifa za kamati mbili zilizoletwa hususan kamati ya USEMI ambayo ndiyo wasimamizi wakuu wanaotusimamia sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya USEMI na nikiri wazi kabisa moja ya kamati ambayo imekuwa ikitushauri vyema kabisa sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni Kamati ya USEMI imekuwa karibu nasi nyakati zote na sisi bila kinyongo chochote haya yote waliyoyaandika hapa tumeyapokea na tutayafanyia kazi kama ambavyo yameletwa na kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na mambo machache sana ya kuchangia kwa maana ya kuongezea tu. Jambo la kwanza ni kwamba kuna hizi fedha za maendeleo 40% kwa 60% zinazotokana na mapato ya ndani katika halmashauri zetu na sasa hivi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni alitupatia fedha kupitia fedha za Mradi wa Mapambano Mhidi ya UVIKO-19 na fedha nyingi tulipeleka katika madarasa na inaonyesha kabisa kuna baadhi ya halmashauri kule wanataka kujifichia humu ndani ili miradi ya maendeleo iliyopangwa katika asilimia 40 na 60 waingizie katika hizi fedha za UVIKO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kamati ilivyoagiza na sisi tumeshaziagiza halmashauri zote nchini kuleta taarifa ya fedha za maendeleo ya zile asilimia 40 kwa 60 zinazotokana na mapato ya ndani zisihusishwe na fedha ambazo alizozitoa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, hilo tulishaliagiza na kabla ya mchakato wa Bunge la Bajeti kuanza taarifa hiyo tutakuwa tunaileta kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili suala la 10% ambazo zinatokana na mikopo katika makundi maalum kwa maana ya wanawake, vijana pamoja na watu wenye mahitaji maalum kamati imeomba kwamba tulete marekebisho ya sheria pamoja na kanuni zake kwa sababu hilli tumeliona ni changamoto kwetu sote na Waziri wangu Mheshimiwa Bashungwa ameniambia kwamba tulipokee na kwamba hili tutaleta marekebisho ya sheria kamati itatushauri pamoja na Bunge lako tukufu ili tupate namna bora ambayo hizi fedha kila wakati zitakapokuwa zinatoka ziende zikafanye kazi ama tija ile ambayo imekusudiwa na Serikali pamoja na Mheshimiwa Rais mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni kuhusu ajira ambalo tayari Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ameshalizungumzia. Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba ajira sasa hivi kama nafasi 10,000 tumeomba kibali ambapo tukishapatiwa maana yake tutazitangaza ili ziende zikaongeze idadi ya walimu katika yale madarasa 15,000 ambayo Mheshimiwa Rais ameyatoa. Kwa hiyo, tusubiri Serikali ipo katika mchakato wake na inafanya kazi kwa kusikilizana litakapokuwa limekamilika Bunge lako Tukufu litapewa hiyo taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusu TARURA watu wengi wameizungumzia sana na Bunge lilishatuagiza hapa wiki iliyopita kwamba tulete taarifa ya tathmini ambayo tayari taarifa ya awali tumeshapatiwa kwa hiyo sasa hivi tunaandaa taarifa ya kina na tutaleta kwako katika Bunge Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tu niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge moja ya kazi nzuri ambayo amefanya Mheshimiwa Rais ni kupeleka fedha za kutosha kwenda kwenye halmashauri zetu pamoja na Majimbo hizi hela kwa ajili ya ujenzi wa barabara, na mfano mzuri zile shilingi milioni 500 kwenda kwenye Majimbo Mheshimiwa Rais ametoa fedha zote milioni 500 kwenda katika Majimbo 214 sawa sawa na bilioni 107. Kwa hiyo, zile ambazo tulishapitisha ndani ya Bunge kupitia mfuko wa Hazina Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ametimiza ahadi yake na zipo katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kinachofanyika huko tu ni kuhakikisha zifanye ile kazi iliyokusudiwa na Wabunge hawa wanapaswa na wao kutusaidia kuhakikisha kwamba wanazifuatilia hizi fedha zifanye ile kazi ambayo Mheshimiwa Rais amekusudia ifanyike kwa watanzania wote. Tuwaahidi tu kwamba tutakuwa tunatoa taarifa kwa kila Mbunge na sasa hivi tunaandaa mfumo ambao utasaidia sasa kuwa tunatoa taarifa kila fedha ambayo inatoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI iwe ni kama kwenye darasa iwe ni kama kwenye barabara iwe ni kama kwenye zahanati tunataka tutoe taarifa kama unavyopata zile automated mesages za kwenye simu zile tunataka tuwe tunawafikishia Wabunge ili wahakikishe wao wanauwezo wa kufanya hiyo kazi na kufuatilia hizo fedha kwa urahisi. Kwa hiyo nikushukuru sana na ninaunga mkono hoja za kamati zote mbili. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kunipatia fursa hii kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini shukrani zangu vilevile ziende kwa Viongozi wetu Wakuu kuanzia kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, vilevile niwashukuru Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi wamekuwa washauri wakubwa na washauri wazuri sana kwa Mheshimiwa Rais. Hata haya mafanikio makubwa unayoyaona ni matokeo ya ushirikiano mzuri wa viongozi wetu na sisi kama Wasaidizi wao tumekuwa tukifata miongozo ambayo wamekuwa wakitupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia hoja kubwa mbili, hoja ya kwanza ni kwa upande wa elimu. Mwaka wa fedha huu unaokuja Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu anatarajia kupitia hotuba ya bajeti ya TAMISEMI tutajenga shule nyingine mpya 234 nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa unaona haya ni mafanikio makubwa sana, mwaka jana tulijenga 232, Mwaka wa Fedha 2022/2023 tunajenga 234, kwa hiyo ndani ya miaka miwili tu ya Mheshimiwa Rais tutakuwa na shule 466, kwa hiyo ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani hapa kuna shule zile za kimkoa, mwaka jana tulijenga shule 10 ambazo zinaendelea na ujenzi shule 10 za kimkoa za wasichana na mwaka huu vilevile tumetenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa shule 10 nyingine za kimkoa kwa wasichana katika mikoa 10 nchini, kwa hiyo ni kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu kupitia bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Rais anakusudia vilevile kujenga madarasa zaidi ya 7,600 mapya nchi nzima, lengo lake ni kuona kwamba mwaka huu tunatarajia watoto wa Darasa la Saba watamaliza zaidi ya Milioni Moja Laki Tano na Elfu Sitini, sasa kwa wastani wa pass rate ya asilimia 80 mpaka asilimia 85 ambayo imekuwepo kwa miaka mitano mfululizo, tunatarajia wanafunzi zaidi ya Milioni Moja na Laki Mbili watakwenda kujiunga na kidato cha kwanza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais bado anaendelea na azma yake ya kuhakikisha hakuna mtanzania yoyote anabaki nyumbani kwa kukosa nafasi ya shule. Kwa hiyo, bajeti hii itakapopita maana yake tunakwenda kutekeleza hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi Mheshimiwa Rais amezingatia maombi ya Waheshimiwa Wabunge wengi ambao walikuwa wameyatoa hapa, kwamba tumekuwa na upungufu ndiyo bado tunahitaji nyumba za walimu maeneo ya pembezoni lakini mwaka huu kupitia bajeti yetu tumetenga Bilioni 81.48 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za misingi na sekondari nchini. Kwa hiyo, unaona ni kazi njema na nzuri ambayo inakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia bajeti hii tutaendelea kukarabati shule kongwe za msingi zile ambazo zimeainishwa katika maeneo mengi. Tumezitambua nyingi lakini kwa awamu hii ya kwanza tutaanza karibu na shule 100 na tuna miradi mingi ambayo tutaipeleka kwa ajili ya kukarabati shule, kujenga madarasa mapya pamoja na kumalizia yale ambayo wananchi wameweka nguvu zao. Kwa hiyo miradi kama SEQUIP, EP4R, GPE LENS yote ni sehemu ya miradi ya kuhakikisha kwamba kwenye upande wa elimu tunatekeleza vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliona niliseme hili ili Waheshimiwa Wabunge watambue kabisa kwamba tunapokwenda kupitisha bajeti hii maana yake tunakwenda kupeleka haya maono ambayo Mheshimiwa Rais anayo kwa nchi yetu. Kwa hiyo, mpaka itakapofika 2025 ninaamini kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kila Mbunge ataacha alama katika Jimbo lake na atakuwa na kitu cha kusema. Kwa hiyo, niseme tu maono haya ya viongozi wetu wakubwa yataleta tija kwenye hili Taifa kuliko kipindi chochote ambacho kimewahi kutokea katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni kwenye upande wa barabara tumeona kabisa kwamba, moja Mheshimiwa Rais ametuongezea fedha nyingi sana kwa mara ya kwanza na ndiyo maana unaona hata Wabunge wengi safari hii wamepongeza upande wa TARURA kwa sababu TARURA kwa umri wake TARURA imeanzishwa mwaka 2017 mwaka huu ndiyo itakuwa inatimiza mwaka wa tano tangu kuanzishwa kwake. Kwa hiyo, kwa mara ya kwanza mwaka jana walau imepata bajeti ambayo imewafikia Majimbo yote kwa hiyo, vivyo hivyo hata mwaka huu tutafika katika maeneo yote nchini na tutahakikisha yale maeneo korofi na moja ya mkakati wa kwanza ambao tulionao ni kuhakikisha tunakwenda kurekebisha madaraja korofi katika maeneo yote ambayo tumeyafanyia tathmini hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu cha kwanza ni kuhakikisha tunawaunganisha wananchi wetu kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Pili ni kuhakikisha kwamba maeneo korofi yote yale na yenyewe yanafikiwa kama ambavyo tumekuwa tukikusudia. Kwa hiyo, tutakachokifanya ni kuhakikisha tunakwenda kusimamia vizuri fedha ambayo itapitishwa na hili Bunge na sisi hapa pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu Bashungwa tumekubaliana tu kwamba, moja wa wajibu wetu ni kuhakikisha tunazunguka kila eneo nchi hii na tutafika karibu Majimbo yote ndani ya Mwaka mmoja ili kuangalia value for money na kuangalia kazi inafanyika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kabisa huo uwezo tunao, hiyo nguvu ya kufanya hiyo kazi tunayo kwa sababu Mheshimiwa Rais ametuamini na ametuwezesha kufanya hii kazi kwa urahisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Bunge lako Tukufu liweze kutupitishia hii bajeti ili iende ikatekeleze yale ambayo yamekusudiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na yale ambayo Mheshimiwa Rais pamoja na Wasaidizi wake kwa maana ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wamekusudia kwa ajili ya Watanzania naisi tuahidi tu kwamba tutafanya kazi kwa uaminifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa umuhimu mkubwa nimshukuru sana Mheshimiwa Bashungwa sisi Wasaidizi wake amekuwa akitupa ushirikiano mzuri kabisa, kiukweli kabisa tumekuwa tukijifunza sana kutoka kwake ni Waziri ambaye anasikiliza, Waziri ambaye hajinyanyui, kwa hiyo ukija kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI pale utaona kama wote ni Mawaziri lakini kumbe yeye ndiye Waziri wetu na sisi ni Wasaidizi wake, kwa hiyo anatuheshimisha sana, kwa hivyo nimpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kabisa kwamba kwa kuwa tunae hapa tutafanya mambo mengi, tuwakaribishe sana Waheshimiwa Wabunge wakati wowote muda wowote mkiwa na jambo lolote, sisi tuko tayari kufanya kazi kwa ukaribu na Bunge hili tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tunaamini bila Bunge hili mambo mengi hayatakwenda kwa hiyo hilo tuliona tuliseme hapa. Mwisho tunalipongeza Bunge lako tukufu, mjadala wa TAMISEMI kwa hizi siku zote ambazo zimejadiliwa ni mjadala ambao ulikuwa wenye mantiki, uliokuwa unaonyesha dira umetukosoa vizuri na kutupa mwelekeo, nasi tumekubaliana hapa kwamba yale yote ambayo yamejadiliwa hapa tumeyapokea tutayafanyia kazi na yale ambayo kama kuna mtu analo kwa wakati wowote aje kwetu tutalipokea. Kwa hiyo, haya nimeyasema kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nichangie makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2019/2020. Jana wakati wajumbe wanachangia ilinifanya nikumbuke miaka mitano iliyopita tukiwa ndani ya Bunge lako Tukufu, wajumbe wengi waliokuwa wanachangia baadhi walikuwepo kwenye Bunge lililopita ambalo ilikuwa ikifika kwenye hotuba ya Wizara ya Nishati, wakati huo ilikuwa inaunganika na madini, jambo moja lilikuwa ndio wimbo wa Taifa, lilikuwa gesi; kila mtu alikuwa gesi, gesi.

Mheshimiwa Spika, wakati huo Waziri wa wakati huo Mheshimiwa Muhongo, Profesa, alikuwa akisimama hapo mbele anakwambia sasa Tanzania inaenda kuwa kama Dubai. Sisi wajumbe wa Kamati ya Nishati wakati huo tulikuwa tunasafirishwa kwenda kujifunza gesi. Kila mwisho wa mwezi Waziri anasimama anasema leo gesi imegunduliwa trilioni kadhaa, sasa Tanzania ina gesi zaidi ya trilioni kadhaa, mbili imegunduliwa, tatu, mpaka ikafika hamsini na saba. Tangu ameondoka Mheshimiwa Prof. Muhongo hatujasikia tena taarifa ya ugunduzi wa gesi nchini ambazo zilikuwa zinatangazwa mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili, ile gesi ambayo tulikuwa tunaambiwa Tanzania inabadilika kuwa kama Dubai leo hakuna hata mmoja anayeizungumzia tena, tumesahau leo. Sasa leo, jana wajumbe wamechangia nitarudia tena, wakati ule wa gesi imepamba moto Serikali ikaleta mpango kwamba, sasa tunatengeneza bomba refu ambalo lili-cost karibu US Dollar 1.2 billion mpaka Ubungo. Gesi hii italeta umeme wa kutosha, leo bomba lilelile tuliloliimbia wimbo ndani ya Bunge, yaani kila mmoja alikuwa anaimba wimbo, bomba lile linatumika kwa asilimia 6. Six percent mtu ana- justify kwamba, hiyo ndio iko sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa haya ndio mambo ambayo leo mimi nataka tuyajadili na Serikali itupe majibu. Serikali hapa imeomba kwenye hotuba yake, inaomba trilioni 1.86 ile ya bajeti ya ndani ambayo itakwenda kwenye maendeleo, sawa na 95.1%. Kati ya hizo trilioni 1.44 zinaombwa kwa ajili ya Stiegler’s Gorge, megawati 2,115 ukisoma chini wanakwambia wanaomba bilioni 60 kwa ajili ya extension ya megawati 185. Sasa nataka to think beyond the box na niko tayari kukosolewa; Kinyerezi Extension megawati 185 bilioni 60, hesabu ya kawaida in a layman language ukiwa na bilioni 600 ukafanya extension ya Kinyerezi maana yake una uwezo wa kuzalisha megawati 1,850. Hesabu ya kawaida, ukiwa na trilioni 1.2 una uwezo wa kufanya extension ukapata megawatt 18,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutumia hela iliyotengwa, kwa mfano ukinipa hela ile ya Rufiji trilioni 1.44 mwakani Tanzania kwa kufanya extension tu itakuwa na megawatt 18,500. Hii trilioni 1.44 ni kwa ajili ya megawatt 2100 ambazo ili zije zikamilike unahitaji trilioni 6. Kwa trilioni 6 unapata megawatt 2115, kwa kufanya extension ya Kinyerezi kwa trilioni 6 unapata megawatt 18,500. Hivi ukijiuliza Tanzania tumerogwa na nani kwenye kufikiri? (Makofi)

MHE. MAULIS S. A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Nani amesimama taarifa?

MHE. SAID M. MTULIA: Mtulia.

T A A R I F A

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, namheshimu sana mchangiaji na mchango wake ni mzuri lakini nataka nimpe taarifa kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya umeme wa maji na umeme wa gesi.

Mheshimiwa Spika, pesa tunazotumia pamoja na wingi wake kwenye kuzalisha umeme wa maji, yale maji hatutayalipia, hatutalipa bili ya maji, ni maji ya mto. Na umeme utakaotumika wa Kinyerezi I kuzalisha gesi, ile gesi ina gharama tunalipa gesi; kuna pesa kwanza unalipa gesi halafu kuna pesa ya kutengeneza mtambo ambao utatoa umeme. Gesi ni ya TPDC na umeme ni wa TANESCO, lazima ulipe na bei ya gesi, hilo nampa taarifa.

SPIKA: Taarifa hiyo Mheshimiwa David Silinde, unaipokea?

WABUNGE FULANI: Ngoja kwanza, haiwezekani.

SPIKA: Utaratibu hauendi hivyo, tunaenda na mmoja mmoja, aipokee taarifa; hajaongea chochote sasa taarifa yako labda kama unampa taarifa yule aliyeongea kule mwanzo, sasa inakuwa tabu kidogo, Mheshimiwa Silinde.

Waheshimiwa Wabunge, tuokoe muda, leo muda dakika zenu chache sana hapa

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, taarifa ile aliyotoa ndugu yangu Mheshimiwa Mtulia ni suala la kutokusoma na hili ndilo tatizo kubwa sana la nchi yetu, watu hawasomi na poverty mentality imekaa Tanzania, watu hawafikiri. Gesi yenyewe ni mali yetu, siyo mali ya mtu mwingine, ukitumia gesi ukazalisha megawatt 18,500 tutauza Burundi, Rwanda, Kenya na nchi zote kwa kutumia fedha hizi hizi, hela hii inayopatikana tuna uwezo sasa wa kurudi tukaanzisha Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa una-ignore jambo moja, unakwenda jambo lingine; unajiuliza tumerogwa wapi? Ndiyo hizi hoja mtu anakuja bwana mnapinga kila kitu kwa sababu ya uchaguzi, kushinda uchaguzi siyo hoja ambayo inatuleta hapa, ni kuishauri Serikali ili iweze kufikia yale malengo. (Makofi)

MHE. CHARLES M. KITWANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ambacho nilikuwa nataka kukizungumzia, hoja ya kusema…

SPIKA: Mheshimiwa Silinde naomba, Mheshimiwa nakuruhusu.

T A A R I F A

MHE. CHARLES M. KITWANGA: Mheshimiwa Spika, namuheshimu sana Mheshimiwa anayezungumza ni mdogo wangu lakini asifanye direct costing kwamba ukiwa umetengeneza umeme kwa mwanzo wa shilingi 10 kwa eneo hilo hilo ukifanya kitu kilekile unazidisha mara mbili inakuwa 20. Kuna exponential, kuna extra cost zinazokuwa pembeni ambazo yeye hana details. (Makofi)

SPIKA: Unapokea taarifa ya Mheshimiwa Charles Kitwanga? Makatibu mlinde muda wa Mheshimiwa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nashukuru Wabunge wamenielewa na hata Mheshimiwa Kitwanga amenielewa. Pamoja na kwamba nakubaliana na hoja yake kwa maana ya kunakuwa na other overhead cost it’s true lakini pamoja na hivyo, sikilizeni muwe mnakubali kusikiliza kwanza msiwe mna haraka, sikilizeni muelewe. Hapa tunachoshindana ni ku-think beyond the box, nimefikiria nje na mnavyofikiria ninyi. Kwa hela yenu tutapata umeme mdogo tofauti na hiki ambacho tayari tulishakuwa tumekianza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa mmekuja na mpango mzuri tu, kwa mfano issue ya LNG. LNG baada ya ugunduzi wa gesi mwaka 2010, mwaka 2014 Serikali ikasema sasa lazima tuunde LNG ili tuanze kusafirisha gesi. Makampuni yakajitokeza; British Gas, State Oil, Exxonmobil Tanzania, Ofil Energy wakasema sisi kwa umoja wetu tunaweza tukafanya.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 mwezi Agosti, Mheshimiwa Rais Magufuli akawaagiza TPDC kuharakisha mchakato kwa kuhakikisha LNG inaanza kujengwa, unakuja unasoma ripoti ya Mheshimiwa Waziri anakwambia ndiyo kwanza government negotiation team inakwenda kuanza mazungumzo. Miaka mitano tangu wazo la kuanzishwa kwa LNG, we are still discussing with this mindset Haki ya Mungu hatuwezi kwenda popote, with this mindset hatuwezi kwenda popote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unajiuliza, nini kinakwamisha? Mwaka 2017 tulitunga sheria nzuri za kulinda rasilimali zetu lakini kuna baadhi ya vifungu havitekelezeki, huo ndiyo ukweli. Juzi juzi nilikusikia ulitoa mfano mzuri tu na nakumbuka juzi wakati Mheshimiwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Mheshimiwa Mahiga wakati anajibu swali moja akasema mnapoangalia hii mikataba, msiangalie tu upande wa negative, wakati mwingine muangalie mazuri ya mikataba… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi fursa ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Thamani ya mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nami niseme tu kwamba muswada umekuja mahali pake na ni muswada ambao utakuja kulisaidia sana Taifa ikiwa baadhi ya mambo ambayo nitakwenda kuyazungumza vilevile yatapewa kipaumbele hususan kwenye utekelezaji wa hii sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utathimini, maana yake tunajadili jambo linalohusu mali; thamani ya jambo fulani, hapo ndipo tunapokuwa tunajadili maana ya utathimini. Mara nyingi kwenye masuala yanayohusu utathimini hususan kwenye Taifa letu, ndilo eneo ambalo limekuwa likijenga migogoro mingi sana kwa wananchi pamoja na Serikali, hususan kwenye hii miradi ambayo tumekuwa tukiisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka jambo la kwanza ambalo nilitaka nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, wameainisha sifa za mtu kuwa Mtathimini wa ardhi; na pamoja na kwamba wameainisha mtu anayepaswa kusajiliwa kuwa valuer, inaonesha kwamba sasa hivi kumekuwa na contradiction nyingi sana huko tunakoelekea. Kwa mfano, jibu ninalotaka ni kwamba endapo kutakuwa na ripoti mbili za watathimini wawili kuhusiana na jambo moja ripoti ipi ndiyo itachukuliwa na kufanyiwa kazi? Kwa sababu kuna haya makampuni ambayo yanafanya kazi ya kutathimini na vilevile kuna watathimini wa Serikali. Sasa kwenye mradi ukiwaleta watu wawili tofauti kwenye mradi mmoja, watakupa ripoti mbili za thamani tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa ninachotaka kufahamu kutoka kwako Mheshimiwa Waziri, endapo kutatokea contradiction hii kwa Watathimini wenye vigezo vinavyofanana, je, ripoti ipi ndiyo itakayotumika kwa ajili ya tathimi ya thamani ya hilo eneo? Kwa hiyo, nilitaka nilifahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa kwamba kwenye utathimini huu wamesema hawa Watathimini wamepewa mamlaka ya kufanya tathimini kwenye mambo mengine. Sasa hivi umejua kabisa kwamba kumekuwa na tathmini, kabla hujachukua mkopo hususan kwa watu wa kawaida kule mtaani, unafanyiwa tathimini; una-mortgage labda nyumba, shamba ama gari. Kwa mfano, unawekeza nyumba yako kwamba nyumba yangu ni shilingi milioni 800 na unalipa deni baada ya kufanyiwa tathimini labda shilingi milioni 700 na mwisho wa siku unaposhindwa kulipa shilingi milioni 100, benki inakuja kuuza nyumba yako kwa thamani ya shilingi milioni 100 na wewe unakuwa umepoteza ilhali katika kipindi chote cha mkopo wako umejitahidi kulipa shilingi milioni 700 na umeshindwa shilingi milioni 100 tu ambayo imebakia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka nijue hapa, Serikali na yenyewe kwenye maeneo kama haya, inawezaje kuwasaidia hawa watu ambao watakuwa wanakutana na adha kama hii ili kuondokana na kero ambazo zimekuwa zikitokea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba moja ya changamoto kwenye masuala ya tathmini kwenye nchi yetu ambayo mimi nimekuwa nikayashuhudia ni kwamba sisi kama Taifa la Tanzania, kwa mfano, mtu anakuja anaomba kibali cha ujenzi, tunashindwa kupata thamani, yaani kujua thamani ya nyumba mtu anayokwenda kujenga? Ukienda kwa mfano nchi za Uarabuni pale Saudi Arabia na nchi zote za Uarabuni, pale mtu anapotaka kujenga cha kwanza unaleta ramani, unatoa thamani ya ile nyumba ambayo unataka kujenga. Labda unasema, hii nyumba yangu kabla sijapata vibali, nategemea hii nyumba kuanzia mwanzo mpaka mwisho itatumia shilingi milioni 600. Wao tayari kwenye database yao wanaweka ile dhamani ya mali. Kwa hiyo, mwisho wa siku ni kwamba hata ikitokea baadaye Serikali inataka kutumia eneo lile inakuwa inajua thamani ya kitu ambacho kiko eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la nchi yetu ni kwamba sisi hatuna huo utaratibu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, moja ya mapendekeo ambayo ningetaka ni kwamba sasa hivi mnapotoa vibali vya ujenzi kwa nyumba ya aina yoyote ile, jambo la kwanza watu waainishe na thamani ya nyumba anayotaka kujenga. Kwa hiyo, mnakuwa mnajua. Kwenye kutathimini ni kwamba kila hatua ya ujenzi, ramani inatakiwa ifuatiliwe, hatua ya msingi mnafuatilia mpaka nyumba inapokuwa inakamilika ama mradi husika unapokuwa unakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mkifanya hivi, maana yake sasa hata hao Watathimini wenyewe tutawapunguzia gharama. Kwa mfano, kama sasa hivi tumekuja na hii sera ya Property Tax ambayo inakwenda kukusanywa na TRA. Hao watu wa TRA watakuwa na urahisi wa kukusanya mapato kwa sababu watakuwa wanajua thamani ya kila nyumba ama ujenzi, ama jambo lolote ambalo limefanyika katika eneo husika. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri naye atakapokuja ajue namna gani wanaweza kuja kuliweka ili kuweza kusaidia hii tasnia ya Watathimini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba kuna ulazima sasa wa kupima ardhi nchi nzima, hili tumekuwa tukililia kila siku. Tukipima ardhi, tukapanga miji vizuri, maana yake ni kwamba migogoro hii ambayo inatokea, haitatokea tena. Leo ukiangalia Serikali inapotea fedha nyingi sana kwenye kulipa fidia. Kila mradi unaotolewa ni kwamba watu wanadai fidia kubwa na wakati mwingine inazidishwa mara tatu tofauti na thamani ya kitu ambacho kiko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri, jambo la kwanza ni lazima tukubali kupima ardhi; ni lazima tukubali kupanga maeneo, hii itarahisisha suala la utathimini; lakini tukubali kuweka reserve ya maeneo ya miradi. Sasa hili sisi linatushinda. Leo watu wengi mnaweza kuwa na mifano mizuri. Ukitembea ukaenda Marekani leo, ukitembea ukaenda hata South Africa, nchi ya jirani kabisa hapo, utakuta wenzetu kwenye barabara, kwanza barabara ziko nane, lakini bado wana reserve ya kutengeneza barabara nane nyingine. Sasa hapo unaona kabisa kwamba vision ya nchi ni ipi?
Kwa hiyo, sisi tunachotakiwa kukifanya sasa hivi ni kuhakikisha na hapo tunapokwenda kufanya hii miradi tuhakikishe tunatenga hayo maeneo ili kupunguza hizi gharama ambazo zinatokea. Niseme tu kwamba sasa hivi moja ya changamoto kubwa ambayo tunaipata kwa upande wa Serikali, ni kushindwa ama niseme kung‟ang‟ania kutumia maeneo; hao Watathimini wanatumia maeneo ambayo watu wanakaa, yaani kuna wakazi. Mfano, mdogo ni mradi wa Kinyerezi, umekwenda maeneo ambayo tayari wakazi wako pale. Sasa leo Serikali inabidi itumie gharama kuwaondoa wale watu.
Kwa mfano, kama sisi kama Serikali tungekuwa tumetenga ama tumefuata maeneo ya maporini, maeneo ambayo hayana wakazi wengi, ninaamini hii gharama ambayo tunaiingia sasa kupitia kwa hawa Watathimini Serikali isingeipata na hii fedha ingetumika kwa ajili ya miradi mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashukuru sana, hayo ndiyo yalikuwa maoni yangu katika huu muswada. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili nami nichangie Miswada miwili iliyoko mbele yetu. Miswada iliyoko mbele yetu ni Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi wa mwaka 2016 pamoja na Sheria ya Utafiti wa Kilimo wa mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi mbili ambazo ziko mbele yetu zimesainiwa na watu wale wale. Utaona hapa kuna Balozi Kijazi pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo wa wakati ule, Mheshimiwa Mwigulu; sheria zote mbili wamesaini watu hao na mwezi uliosainiwa hizi sheria ni mwezi wa Tano. Sheria hizi ukizipitia hapa mbele baada ya Muswada wa Sheria, wanasema; moja, “imetungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” Hiyo ni Sheria ya Kilimo na ukija kwenye Sheria ya Uvuvi na yenyewe imetungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia kwenye Sheria ya Uvuvi, Kifungu cha (2) kinachozungumzia matumizi ya sheria, kinasema: “sheria hii itatumika Tanzania Bara tu.” Wakati ukija kwenye hii Sheria ya Kilimo, hii inatumika kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hapa nafikiri unajaribu kuona concept ambayo najaribu kuizungumza hapa. Sheria mbili zimezungumzwa na watu wale wale kwa nyakati zile zile zinazofanana. Zinaigawanya Tanzania kibaguzi kwenye makundi mawili. Swali hili kwa mfano, Sheria ya Uvuvi, Zanzibar peke yake ndiyo imezungukwa zaidi na maji, yaani Kazanzibar kenyewe kamemezwa na maji na shughuli yao moja kubwa ni uvuvi, lakini hapa tunazungumzia suala la Tanzania Bara peke yake, kwa maana nyepesi, Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya ndiyo maswali ambayo kila siku tunasema. Humu ndani tuko kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunahitaji majibu yanayohusu Muungano, yaani kwa maana ya Zanzibar pamoja na Tanganyika. Sasa kama ni hivyo, ndiyo tunakuja na ile hoja yetu ya kila siku kwamba hapa hoja ya Serikali tatu haiepukiki kutokana na mwenendo wa sheria tunazotunga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwenye hii sheria itabidi hii Sheria ya Kilimo, huo upande wa Kiswahili huo, jina hili la Sheria, juu mmekosea kote, kuanzia ukurasa wa 34 mpaka ukurasa wa mwisho wa 63, huku juu mmeandika Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi. Hii header, huku juu kote.
Sasa hii inaonyesha unseriousness, yaani vitu vidogo kama hivi. Unajua watu wanapimwa uwezo wa kufanya mambo kwa vitu vidogo vidogo. Miezi minne unakosea mambo kama haya, mwisho wa siku utakosea; ndiyo maana nchi inaingia kwenye mikataba ambayo kila siku ina matatizo. Mambo madogo madogo kama haya!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nina swali la kujiuliza la jumla; tatizo la nchi hii ni sheria? Maana kila siku tunatengeneza sheria kama ndiyo solution ya matatizo yetu, maana yake hilo ndilo swali Mheshimiwa Waziri utuulize. Maana yake ukiangalia tumekuwa na institute kwa miaka yote; na hizi taasisi za kufanya utafiti zimekuwa zikifanya tafiti mbalimbali na zile tafiti hazifanyiwi kazi. Kwa hiyo tatizo lililoko hapa, siyo sheria, ni mtu anayeweza kuratibu hizi tafiti kufanya kazi zake na hizi tafiti zikatekelezwa. Hilo ndiyo tatizo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia, Wizara ingekuwa na utaratibu mzuri wa ku-coordinate hizi taasisi, leo hata hii sheria tusingekuwa tunaijadili. Wala tukisema kwamba sheria itakuja kutusaidia, siamini kwamba sheria ndiyo inaweza kutoa solution ya matatizo ya kilimo katika nchi yetu. Siamini kitu kama hicho! Ninachoamini ni utayari ambao sisi kama viongozi tukiwa nao ndiyo utakaopelekea solution ya tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapozungumzia tafiti za kilimo, maana yake ni nini? Maana yake tunatafsiri kwamba, kilimo kinachohitajika ni kwamba ziletwe mbegu bora, wananchi wazalishe wapate mazao mengi. Leo bila hata hizo tafiti, bado Watanzania wanazalisha sana na inafikia mahali Serikali inashindwa kununua mazao ya wakulima wa kawaida. Kwa hiyo, hapo huwezi kutueleza kwamba tatizo ni sheria, ndiyo Watanzania wanakosa soko; tatizo ni sheria, ndiyo Watanzania wanakosa mbolea; tatizo ni sheria, ndiyo Watanzania wanashindwa kutabiri hata hali ya hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuja kugundua kabisa kwamba tutaendelea kutengeneza sheria kila siku kupata utaratibu, lakini hatutapata majibu sahihi kama tutashindwa kuwa tayari kulitumikia hili Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitaendelea kusisitiza juu ya hili, kwamba uratibu wa shughuli zote, lazima pawepo sasa na commitment ambayo tunaweza kutekeleza majukumu haya ambayo tumeyapangia. Ila jukumu la kisheria lipo tu ambalo nina uhakika ukipata watu ovyo kabisa, hawataweza kutekeleza na tutarudi hapa tutatengeneza sheria nyingine ambayo ita-supersede sheria ambayo sasa hivi tumeipitisha. Kwa hiyo, hilo linatakiwa lifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria imeeleza hapa, financing; tatizo la hizi tafiti zetu, moja, ni financing. Financing kwa maana ya kupata fedha kwa ajili ya kuwasaidia watu wafanye tafiti, lakini pili, hizo hizo fedha kutekeleza zile tafiti ambazo zimetekelezwa, yaani ambazo zimefanyiwa kazi.
Kwa hiyo, hayo ndiyo matatizo makubwa. Sasa hapo unasema, Waziri atatoa kibali; kwa mfano, kuna sheria moja nimeipitia hapa, inasema Waziri ataidhinisha fedha ambazo hata kama hazipo kwenye matumizi ya mwaka wa fedha uliopita, zitaidhinishwa baada ya maandishi ya Mheshimiwa Waziri. Sasa pale unakuja kugundua Waziri anaweza akapitisha tu mwanya wake wa fedha kwa sababu tu hazipo katika mwaka ule wa fedha. Yaani ipo ndani ya sheria ambayo imeandikwa humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachotakiwa tukizungumze sisi sote, tafiti lengo lake ni nini? Maana yake kuna tafiti zinazojulikana na kuna tafiti ambazo hazijulikani na kuna tafiti ambazo tayari katika Taifa letu tulitakiwa tupewe majibu; kuna tafiti zimefanyika ambazo mpaka sasa hivi hatujaelezwa zimeleta majibu gani tofauti.
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante,