Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Janet Zebedayo Mbene (15 total)

MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Ileje iliwahi kuwa katika Wilaya zilizoongoza kwa ufaulu wa wanafunzi, lakini miaka ya hivi karibuni ufaulu umeshuka na hii ni kutokana na miundombinu mibovu ya mazingira ya kufundishia:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa inaboresha miundombinu yote muhimu kwa utoaji wa elimu?
(b) Je, Serikali iko tayari kujaza pengo la Walimu liliko hivi sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha miundombinu ya shule, Halmashauri ya Wilaya ya Ileje katika mwaka wa fedha 2015/2016, ilitengewa shilingi milioni 798.0 ambazo zilipokelewa kwa ajili ya ukarabati, ujenzi na umaliziaji wa miundombinu ya shule nne za Msomba, Luswisi, Itale na Bupigu. Vile vile, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imetengewa shilingi milioni 130.8 ili kuendelea na uboreshaji wa mindombinu ya shule ya sekondari ya Ngulilo. Aidha, kupitia mapato yake ya ndani Halmashauri imetenga shilingi milioni 60.0 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za Walimu, ukarabati wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa matundu ya vyoo na matengenezo ya madawati. Jitihada hizi zinakusudia kuinua kiwango cha elimu inayotolewa kwa wanafunzi katika Wilaya ya Ileje.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya Walimu wa shule za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ni 819, waliopo sasa ni Walimu 567 na upungufu ni 252. Kwa upande wa shule za sekondari mahitaji ya Walimu wa sayansi na hisabati ni 156, waliopo ni 61 na upungufu ni 95. Hata hivyo, Wilaya ina zaidi ya Walimu wa masomo ya sanaa 105. Ili kuziba pengo la Walimu katika Halmashauri hiyo, Serikali imepanga kuajiri Walimu 35,411 waliohitimu kuanzia mwaka 2013/2014 na miaka ya nyuma ambapo sehemu ya Walimu hao watapangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Wilaya ya Ileje haina vyuo vyovyote vya Serikali vya ufundi zaidi ya vile vichache vya taasisi za dini na chuo cha ufundi ambacho kinamaliziwa kujengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan:
Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa chuo hicho cha ufundi ambacho bado kinahitaji jengo la utawala, vyoo, mabafu, kantini ya chakula, vifaa vya kufundishia pamoja na fedha ya kuwalipa wanafunzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba uongozi wa Wilaya ya Ileje mwezi Februari, 2016 uliiomba Wizara yangu kuangalia uwezekano wa kukabidhi kwa Serikali kupitia VETA Chuo cha Ufundi Stadi kilichopo Ileje kinachomaliziwa kujengwa ili kiwe cha Wilaya. Wizara yangu kwa kutambua juhudi zilizofanyika hadi sasa iliagiza wataalam wa VETA Makao Makuu na VETA Kanda ya Kusini Magharibi kwenda Wilaya ya Ileje na kufanya tathmini ya majengo na kutoa ushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya wataalam kufanya tathmini na kutoa ushauri wameiwezesha Wizara tarehe 17 Machi, 2016 kutoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya ya Ileje kupitisha suala la kukabidhi chuo hicho kwenye vikao vya kisheria ikiwemo DCC na RCC ili liweze kuridhiwa. Uongozi wa Wilaya ya Ileje pia ulielekezwa kuongeza eneo la ardhi kulingana na miongozo iliyopo ya VETA juu ya ujenzi wa chuo cha ufundi stadi. Pia halmashauri imeshauriwa ilipime eneo hilo na hatimaye kupata hati ya kiwanja kilipo chuo hicho na kisha makabidhiano rasmi yafanyike.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ridhaa ya vikao vya kisheria na kupatikana kwa hati ya kiwanja kilipojengwa chuo hicho Wizara itakuwa tayari kukipokea. Napenda kumuomba Mheshimiwa Mbunge kuhimiza viongozi wa Wilaya ya Ileje kutimiza maelekezo ya Wizara yangu ili makabidhiano ya chuo hicho cha ufundi cha ufundi kwa Serikali yafanyike kwa wakati na mapema iwezekanavyo.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Ileje inatambuliwa kuwa ndiyo inayokalia ardhi inayotoa makaa ya mawe yanayoitwa Kiwira Coal Mine lakini mgodi huu haujawanufaisha wananchi wa Ileje kwa muda wote uliokuwa ukifanya kazi mpaka ulipofungwa:-
(a) Je, ni lini mwekezaji mpya ataanza uzalishaji tena kwenye mgodi?
(b) Je, ni lini tutakaa na mwekezaji huyu kama halmashauri ili kufahamiana?
(c) Je, ni lini tutapata mwekezaji wa kutumia makaa haya kuzalisha umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira (Kiwira Coal Mine) unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 na kusimamiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). STAMICO wanamiliki leseni maalum ya uchimbaji mkubwa yenye usajili namba SML.233/2005 itakayodumu kwa miaka 25. STAMICO wanatarajia kuzalisha umeme megawati 200 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 500.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2015/2016, shirika liliweza kukamilisha Rasimu ya mwisho ya Upembuzi wa Mazingira kwa mradi wa Open Cast, wa kuzalisha megawati 200. Hata hivyo, mradi huo, pia unahusisha usafirishaji wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilometa 100 kutoka Kiwira hadi Mwakibete, Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa STAMICO ipo katika hatua za kumtafuta mzabuni kuendeleza mgodi huo lakini taratibu za kumpata mwekezaji zinaendeleza na zinatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2016. Mara tu mwekezaji atakapopatikana, atatambulishwa kwa viongozi wa Halmashauri za Rungwe na Ileje ambazo sehemu ya mradi huu unapatikana.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Jumuiya za kiuchumi za Kikanda zimekuwa sehemu ya mkakati mkubwa katika kuratibu masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kimazingira. Ileje ni Wilaya ya mpakani mwa Nchi za Malawi na Zambia lakini haina kituo cha forodha. Hakuna miundombinu ya soko la Kimataifa, hakuna kituo cha uhamiaji, hakuna kituo cha kudhibiti mazao, mifugo wala silaha. Hii inasababisha wahamiaji haramu na wahalifu kutumia mipaka kinyume cha sheria na taratibu:-
Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha forodha, kituo cha uhamiaji, soko la Kimataifa na kituo cha kukagua mifugo na silaha kwa ufanisi na maendeleo ya Ileje?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa kuwa katika Wilaya ya Ileje hakuna kituo cha forodha na uhamiaji wala soko la Kimataifa na vituo vya kukagua mifugo na silaha. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge ambaye ameendelea kufuatilia jambo hili kwa nguvu sana na kwa kutambua umuhimu huo, Mamlaka ya Mapato na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tayari tumefanya jitihada tumepata kiwanja kwa ajili hiyo lakini bado tunafanya mashauriano na nchi jirani na hususani Zambia na Malawi kwa sababu ya utaratibu wa kujenga kituo cha pamoja lakini pia tutahitaji maandalizi kwa ajili ya kuamua jengo lenyewe hilo la kituo cha pamoja liweje.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kazi hizo kukamilika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaanza utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho mara baada ya kuwa shughuli hiyo imekamilika, lakini kwa sasa natoa rai kwa niaba ya Serikali kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje na Wilaya zinazofanana na hizo kuendelea kutumia huduma zilizo katika Wilaya na Mikoa jirani wakati tunafanya utaratibu wa kujenga vituo hivyo.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Wilaya ya Ileje ni kati ya Wilaya zinazozalisha sana mazao mbalimbali ya nafaka, pia ina fursa nyingi sana za kilimo cha cocoa, vanilla, tangawizi, iliki na pilipili manga lakini hakuna viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza thamani ya mazao hayo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha viwanda vidogo hivyo ili kuongeza ajira kwa wananchi na pia mapato ya Serikali?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza mkakati wa ujenzi wa viwanda, Mamlaka za Mikoa na Wilaya zimeelekezwa kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Pia katika maeneo hayo, Mamlaka za Wilaya zinapaswa kutenga sehemu za hifadhi ya mazao au bidhaa na sehemu za masoko pale inapohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri za Wilaya pamoja na kutenga maeneo, zimehimizwa katika mipango yao ya maendeleo kuhusisha ujenzi wa miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi katika maeneo hayo ya ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nilizonazo ni kwamba Halmashauri ya Ileje imetenga mita za mraba 9,832 sawa na hekta 0.98 katika eneo la Itumba na mita za mraba 43,615 sawa na hekta 4.36 katika eneo la Isongole ambazo ni kidogo sana. Pia tathmini ya Wilaya moja, bidhaa moja (ODOP), ilionesha Ileje inaweza kufanya vizuri zaidi katika zao la alizeti. Tathmini hiyo hiyo inaonesha Ileje haijafikia kiwango cha kuzalisha cocoa, vanilla, tangawizi, iliki na pilipili manga kwa kiasi cha kukidhi mahitaji ya viwanda vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Ileje iko katika Mkoa mpya wa Songwe ambao kwa sasa hauna Meneja wa SIDO, Wizara imemwagiza Meneja wa SIDO Mbeya awasiliane na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ili watathmini fursa zilizopo na kusaidiana nao katika kuandaa mpango mkakati wa ujenzi wa viwanda vidogo ikiwa ni pamoja na mipango ya uzalishaji wa malighafi ya kutosha.
Aidha, Wizara inakamilisha mwongozo utakaotumika katika Mikoa na Wilaya katika kutenga maeneo, kuyaendeleza na kuhamasisha uwekezaji.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Mto Songwe umekuwa ukihama hama kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi huku ukiharibu rasilimali za wakazi wanaoishi karibu na mto huo na kingo zake kutokana na mafuriko.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudumu kudhibiti uharibifu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira na maumbile ya Bonde la Mto Songwe pamoja na mgawanyiko wa unyeshaji wa mvua katika bonde hilo ndio sababu kubwa inayofanya kuwepo kwa mafuriko ya mara kwa mara kila mwaka. Inakadiriwa kuwa takribani hekta 9,000 za ardhi huathiriwa na mafuriko katika kila msimu wa mvua na kufanya Mto Songwe kubadili mkondo wake mara kwa mara, hivyo kuathiri pia mpaka kati ya nchi za Malawi na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hali hii, tatizo hili linakuwa kubwa zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko kubwa la watu katika bonde. Aidha, matumizi mabaya yasiyo endelevu ya rasilimali zilizoko katika bonde husababisha uharibifu mkubwa wa ardhi, vyanzo vya maji, mifumo ikolojia na kutokewa kwa bioanuai zilizo katika bonde hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Malawi imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na matatizo katika Bonde la Mto Songwe. Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha Kamisheni ya Pamoja (Songwe River Basin Commission), ambayo itashughulikia masuala yote ya bonde hilo. Mpaka sasa kuna sekretarieti ya mpito iliyoanzishwa ambayo inaratibu shughuli ya bonge hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tayari programu ya kuendeleza Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Program) imeshaandaliwa kwa ajili ya utekelezaji. Masuala yaliyoainishwa kwenye programu kwa ajili ya utekelezaji ni kama ifuatavyo; kuendeleza kilimo endelevu, uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu ya maji, kudhibiti mafuriko ya mto pamoja na kudhibiti kuhamahama kwa mto, uboreshaji wa upatikanaji na usambazaji wa maji, maendeleo ya uvuvi, kukuza utalii na uboreshaji wa mazingira na kuiwezesha kamisheni usimamizi wa pamoja wa rasilimali za Bonde la Mto Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za mafuriko Sekretarieti ya Mpito ya Bonde kupitia programu hii (Songwe River Development Program) itajenga mabwawa matatu ambayo ni Songwe Chini, Songwe Kati na Songwe Juu. Pamoja na mabwawa hayo kutumika kudhibiti mafuriko pia yatatumika katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, usambazaji wa maji na shughuli za uvuvi. Vilevile, kutakuwa na mradi wa mazingira ambao utadhibiti kingo za mto (River Banks Stabilization) ili kuufanya mto usihame hame.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Serikali imetenga maeneo kadhaa kwa ajili ya uwekezaji nchi nzima:-
Je, ni lini Serikali itatafuta fedha za kutosha kuweka miundombinu muhimu katika maeneo haya ili kuvutia uwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia EPZA na halmashauri za wilaya na mikoa imetenga maeneo ya uwekezaji sehemu mbalimbali nchini. Kama alivyosema Mheshimiwa Janet Mbene maeneo ya namna hii ni muhimu katika kuvutia uwekezaji katika sekta ya ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uendelezaji wa maeneo hayo kwa kuweka miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi, Serikali imebuni mpango wa kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza maeneo hayo kama ilivyofanyika kwa Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo. Kwa maeneo yatakayokuwa na uhitaji wa haraka wa kuendelezwa kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina tutayatengea fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa viwanda vidogo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya kujenga miundombinu ya SIDO kwenye mikoa mbalimbali nchini.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Wilaya ya Ileje imejaliwa kuwa na rasilimali ya makaa ya mawe ya Kiwira na Kabulo na STAMICO imekaririwa kuanza rasmi kuuza makaa hayo kwa kasi ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya saruji na kukuza pato la Taifa, aidha, STAMICO ilianza uzalishaji wa majaribio ya makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo tarehe 30/04/2017.
(a) Je, Mgodi wa Kabulo utaendelea kuchimba baada ya majaribio hayo na ni nani anayefanya uchimbaji huo?
(b) Je, kuna makubaliano gani na Wilaya ya Ileje juu ya mrahaba na uchumi kwa wana Ileje?
(c) Je, ni lini Mgodi wa Kiwira utaanza kufanya kazi na ni nini hasa kinachokwamisha?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba sasa nijibu swali la mama yangu, Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Jimbo la Ileje, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lilianzishwa mwaka 1972 likiwa na jukumu la kushiriki na kusimamia maslahi ya Serikali katika sekta ya madini pamoja na rasilimali ya madini. Aidha, mwaka 2005 Mgodi wa Kiwira ulibinafsishwa kwa kampuni binafsi ya wazawa ya Tan Power Resources Ltd. (TPR) kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme na kufikia megawati 200. Mnamo tarehe 30, Juni, 2014 Serikali iliikabidhi STAMICO Mgodi wa Kiwira kutokana na mbia mwenza kukosa mtaji wa kuendesha mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ilianza uchimbaji wa majaribio katika leseni yake ya makaa ya mawe ya Kabulo mnamo mwezi Aprili, 2017 ambapo katika kazi hiyo jumla ya tani 8,674 za makaa ya mawe zilichimbwa. Baada ya kukamilisha majaribio ya awali STAMICO imeanza mchakato wa kumpata mkandarasi atakayefanya uchimbaji. Lengo ni mkandarasi huyo aanze kazi ya uchimbaji utakaozingatia taratibu zote za uchimbaji, mazingira na usalama mgodini katikati ya mwaka huu wa fedha yani 2018/ 2019.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO kama ilivyo kwa wamiliki wengine wenye leseni za uchimbaji wa madini inawajibika kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri wa asilimia 0.3 ya mapato ghafi yatokanayo na mauzo ya makaa ya mawe. STAMICO tayari imeanza kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na mauzo ya makaa yaliyofanyika ambapo kiasi cha shilingi 57,600 kimelipwa. Aidha, jumla ya shilingi 1,735,900 zimelipwa kama ushuru wa barabara kwa Halmashauri. Manufaa mengine ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje na kuchangia huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ilikabidhiwa Mgodi wa Kiwira mnamo mwezi Juni, 2014 ili kuendesha na kuusimamia kufuatia Kampuni ya Tan Power Resources kuurejesha Serikalini. Aidha, STAMICO imeendelea na jitihada mbalimbali za kutafuta fedha ikiwa ni pamoja na kutafuta wabia wenye uwezo watakaoshirikiana na shirika katika uendeshaji wa mradi huu.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
(a) Je, mradi wa Tanzania na Malawi wa kujenga mabwawa matatu makubwa kandokando ya Mto Songwe umefikia wapi?
(b) Mradi huo ulikuwa uanze kwa awamu tatu, na ya kwanza ilikuwa iwe Ileje lakini unaanzia Kyela kisha uende Malawi na kumalizia awamu ya tatu Ileje, je, ni nini kilifanya utaratibu wa awali ubadilishwe?
(c) Wananchi wa Kata za Bubigu na Ileje walishaambiwa wasifanye shughuli zozote katika eneo hilo ili kupisha mradi huo, je, kuna mpango gani wa kuwalipa fidia au kuwaruhusu waendelee na shughuli zao?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Jimbo la Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa mabwawa matatu katika Bonde la Mto Songwe. Kwa sasa utekelezaji huo upo katika awamu ya tatu inayohusisha ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini litakalotumika kwa ajili ya kuzuia mafuriko, kuzalisha umeme pamoja na shughuli za umwagiliaji. Makubaliano ya utekelezaji wa awamu hii ya tatu pamoja na mkataba wa uanzishwaji wa Kamisheni ya Kudumu ya Bonde la Mto Songwe yalitiwa saini katika kongamano la wawekezaji lililofanyika tarehe 18 Mei, 2017 nchini Malawi. Mkataba huo uliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 7 Septemba, 2017 Jijini Dodoma. Kwa sasa Serikali hizi mbili zinatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa utekelezaji wa miradi haujabadilishwa. Ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini utaanza baada ya kupatikana kwa fedha za ujenzi. Mabwawa mengine ya Songwe Kati na Songwe Juu, usanifu kina na ujenzi wake utaanza baadaye. Taratibu za kuwahamisha wananchi wa Kata ya Bubigu kutakakojengwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa ya Songwe Juu na Songwe Kati zitafanyika kwa mujibu wa sheria. Kwa sasa wanaruhusiwa kuendelea na shughuli zao hadi itakapotangazwa vinginevyo.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-

Kumekuwa na ongezeko la matumizi ya dawa za kupunguza maumivu zenye Codeine, Valium, Morphine, Amphetamine, Phenorbabitone ambazo zinauzwa bila cheti cha daktari na zinatumiwa kama mbadala wa dawa za kulevya:-

(a) Je, Sheria zinasemaje kuhusu hilo linalosababisha vijana kuwa mateja wa dawa za kawaida?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hakuna prescription drugs inauzwa bila cheti cha daktari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Sheria ya Chakula na Dawa, Sura Na. 219 katika kifungu chake 77(2) inatambua makundi matatu ya dawa ambayo ni:

(i) Dawa zinazodhibitiwa ama kwa jina la kigeni inaitwa controlled drugs kama Morphine, Pethidine na Diazepines kama vile valium:-

(ii) Dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari, prescription only medicines mfano dawa za antibiotic, shinikizo la damu, kisukari, za saratani na dawa zenye viambata vya Codeine; na

(iii) Dawa za kawaida ambazo kwa lugha ya kigeni tunaita Over the counter/general medicine dawa hizi hazihitaji cheti cha daktari. Mfano kama dawa za kikozi, mafua na maumivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria hiyo ya Mamlaka ya Chakula na Dawa, Sura 219 kifungu cha 77(4) kinatoa adhabu ya faini au kifungo kwa mtu yeyote atakayekutwa akitoa dawa za zinazodhibitiwa na zinahitaji cheti cha Daktari.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa pamoja na uwepo wa sheria na adhabu hizo bado kumekuwa na changamoto za uuzwaji wa dawa zinazohitaji cheti cha daktari pasipokuwa na chetu hicho. Wizara imeandaa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na suala hili kwa kufanya yafuatayo:-

(i) Kuandaa kanuni za usimamizi na udhibiti wa dawa za cheti ambapo pamoja na mambo mengine zitaainisha namna dawa zinazodhibitiwa (Tramadol, Diazepam, Pethidine na Morphine) ambapo kwa sasa rasimu ya awali imeshakamilika. Aidha, adhabu kali zimebainishwa kwa watakaokiuka taratibu hizo;

(ii) Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeandaa mifumo ya udhibiti ukaguzi katika meneo yanayotoa huduma za dawa nchini; na

(iii) Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara yanayoweza kupatikana kutokana na matumizi holela ya dawa.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-

Serikali ilinunua mashine ya kujengea kutoka Marekani kwa fedha nyingi sana kwa lengo la kuitumia kujenga nyumba nyingi za watumishi, ofisi na taasisi na kadhalika kwa haraka zaidi, mashine hiyo kwa muundo wake ina uwezo wa kujenga nyumba kwa bei nafuu zaidi na hivi sasa kuna upungufu mkubwa wa nyumba za walimu, madarasa, maabara, mabweni, nyumba za wauguzi, madaktari na vituo vya afya:-

(a) Je, ni nyumba ngapi na kwa gharama gani zilizojengwa na Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa kwa kutumia mashine hiyo na kama zimejengwa kwa ujenzi wa kawaida zingetumia kiasi gani?

(b) Je, ni kwa nini mashine hiyo haitumiki kujenga nyumba zinazohitajika wakati kuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za Serikali?

(c) Je, Serikali iko tayari kufanya tathimini na kutuletea Bungeni mpango mzima wa kuanza kutumia mashine hiyo kujenga nyumba zinazohitajika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba nne zilijengwa wakati wa mafunzo kwa gharama ya shilingi 1,325,000,000 na majengo matano yalijengwa baada ya mafunzo kwa gharama ya shilingi 9,216,653,699.50. Gharama za majengo yote jumla yake ilikuwa ni shilingi 10,541,653,699.50. Majengo haya ni pamoja na ukumbi (multipurpose hall) na nyumba za kuishi katika Kambi ya Twalipo Dar es Salaam; Banda la Jeshi la Wananchi wa Tanzania la Maonesho Sabasaba; na Ofisi ya muda ya Kitengo cha Uwekezaji TIC. Nyingine ni Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Kihangaiko; Kiteule cha Kijeshi Tarime; Karakana ya Wakala wa Vipimo na Mizani Misugusugu Kibaha; ghala la kuhifadhia nafaka la SUMA JKT kule Chita; na kumbi za burudani za SUMA JKT Mwenge Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo haya kama yangejengwa kwa ujenzi wa kawaida gharama zingefikia shilingi 11,981,649,808.70. Mbali na teknolojia hii kuwa ya nafuu katika gharama za ujenzi uliofikia asilimia 15%, unafuu mkubwa upo katika ujenzi unaokadiriwa kuwa na asilimia 70%.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango kikubwa mashine hizi hazitumiki ipasavyo kutokana na ukosefu wa fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa substructure yaani ujenzi toka chini hadi usawa wa msingi. Malighafi inayotumka ni steel coil ambayo kwa matumizi ya Kijeshi kama fedha za maendeleo zingepatikana ingeweza kukidhi mahitaji.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, mitambo ya UBM (Ultimate Building Machine) ilinunuliwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za ujenzi ndani za Wizara. Hata hivyo, Wizara ya Ujenzi na Jeshi la Kujenga Taifa liko tayari kushirikiana pamoja na taasisi nyingine za Serikali katika ujenzi wa majengo hayo. Aidha, Wizara iko tayari kuandaa mpango kabambe kwa kutumia teknolojia hiyo ili kuwezesha ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali. Ahsante.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. JANET Z. MBENE) aliuliza:-

Uchomaji wa mkaa kwa kiasi kikubwa unatumia miti ya asili pamoja na mapori ya akiba, ukataji wa miti hauendi sambamba na upandaji wa miti na hii ina athari kubwa sana kwenye mazingira yetu ikiwemo kupungua kwa mvua na kukauka kwa vyanzo vya maji:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutoza ada kwa mkaa unaosafirishwa nchi za nje ili iweze kurejesha mazingira katika hali yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene Mbunge Ileje kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli uchomaji wa mkaa hutokanao na miti kwa kiasi kikubwa unatumiamiti ya asili pamoja na mapori ya Akiba na nidhahiti ukatajia wa miti hauendi sambamba na upandaji wa miti na hii ina athari kubwa sana katika mazingira yetu. Ikiwemo kuendelea kupotea kwa Bionuai, kupungua kwa mvua na kukauka kwa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya mkaa inafanyika katika kwa mujibu wa sheria ya misitu ya mwaka 2002 kanuni za mwaka 2004 ni miongozo mbalimbali. Aidha, usafirishaji wa mkaa nje ya nchi umezuiliwa kwa mujibu wa kifungu Na. 16 cha sheria inayozuia usafirishaji wa baadhi ya bidhaa nje ya nchi yaani The export control Act cape 381RE 200 pamoja na makatazo mengine. Vilevile tangazo la Serikali Na. 417 la tarehe 24 Mei, 2019 kifungu Na. 21(1) limetoa zuio kwa mtu yoyote kusafirisha mkaa kwenda nje ya nchi isipokuwa mkaa mbadala yaani charcoal briquettes na kwa kibali maalum kutoka kwa Waziri mwenye dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa Serikali haisafirishi mkaa unaotokana na miti kwenda nje ya nchi kama ilivyotoa ufafanuzi hapo juu gharama za kurejeleza au kung‟oa kuondoa maeneo yaliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo mkaa zitatokana na mapato yanayopatikana kupitia tozo mbalimbali zilizoainishwa kwenye sheria ya misitu ya mwaka 2002 ikiwepo asilimia tano ya ushuru wa halmashauri inayotozwa kwa wafanyabiashara kwa mazao ya misitu. Aidha, tozo nyingine zinazotokana na tozo za ukaguzi wa biashara ya mkaa unaotokana na mabaki ya miti au mimea kwa maana ya briquettes ambao unaruhusiwa kwenda nje ya nchi.
MHE. JANET Z. MBENE Aliuliza:-

Geological Surveys za Wilaya au Mikoa mingi ni za miaka mingi tangu enzi za ukoloni. Surveys hizi nyingi zimejikita kwenye aina moja ya migodi kwa mfano Mkoa wa Songwe Survey imezungumzia machimbo ya mawe peke yake:-

(a) Je, ni lini Serikali itafanya mapitio ili kupata Geological Surveys zenye kujumuisha aina nyingine za madini ambayo yanapatikana katika Mkoa wa Songwe hususan Ileje?

(b) Je, Serikali ipo tayari kwenda kuwaelimisha wananchi wa Ileje juu ya madini yaliyopo na kuhamasisha uwekezaji kwa wachimbaji wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za jiolojia kwa ajili ya kuainisha madini mbalimbali yaliyopo nchini tangu kipindi cha mkoloni hadi sasa. Aidha, GST kwa ushirikiano na ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa Korea imeanza kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia ili kuongeza na kuboresha taarifa za uwepo wa madini mengine katika Mkoa wa Songwe na mikoa mingine nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zilizofanyika Mkoa wa Songwe zinaonesha kuwa Wilaya ya Ileje ina madini yafuatayo; moja ikiwa ni madini ya metali aina ya dhahabu yanayopatikana katika maeneo ya Mwalisi na Ikinga, Madini ya Viwandani aina ya Ulanga, yanayopatikana katika maeneo ya vilima vya Bundali na Ileje, madini ya nishati aina ya makaa ya mawe (Coal) yanapatikana katika maeneo ya Songwe, Kiwira na madini ya apatite na niobium yanayopatikana katika miamba ya carbonatite iliyopo maeneo ya kilima cha Nachendazwaya, ikiwa ni pamoja na madini mengine kama marble na madini mengine ya ujenzi.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania itaendelea kufanya tafiti mbalimbali za madini katika Wilaya ya Ileje na maeneo mengine ya nchi kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali ya fedha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya upatikanaji wa madini katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya madini kwa wachimbaji wadogo.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-

Serikali iliingia Mikataba na Uwekezaji na Wadau mbalimbali kwenye Sekta tofauti ambayo kwa sababu mbalimbali imesitishwa na Serikali?

(a) Je, ni Mikataba mingapi imesitishwa na ni sekta zipi zinaongoza?

(b) Je, Serikali imeingia gharama kiasi gani, katika kesi zilizofunguliwa Mahakamani na kusitishwa kwa Mikataba hiyo?

(c) Je, Serikali imepata faida au hasara gani kwa kusitisha Mikataba hiyo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene Mbunge wa Ileje, lenye sehemu (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ni kweli Serikali imekuwa ikisitisha Mikataba ya Uwekezaji kutokana na sababu mbalimbali, moja ikiwa ni kwa upande mmoja mwingine ni Mkataba wa kushindwa kutimiza masharti kwa mujibu wa Mkataba au makubaliano ama inapobainika kuwa kulikuwa na udanganyifu ambao haukuweka wazi taarifa za msingi wakati wa kuingiwa katika Mikataba hiyo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali bado inaendelea na mapitio ya Mikataba yote, iliyoingiwa na Serikali ili kutambua kama vigezo na masharti kama ya Mikataba hiyo vinatimizwa ipasavyo. Mara zoezi hili, likikamilika Serikali itakuwa na takwimu sahihi ya Mikataba yote, iliyosainiwa sambasamba na kuifanya tathmini ya gharama zake zilizotumika kwa kesi zilizofunguliwa kutokana na usitishwaji wa Mikataba husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Hati Idhini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyochapishwa katika gazeti la Serikali kwa Tangazo namba 48 la mwaka 2018 na Sheria ya marekebisho mbalimbali ya Sheria ambayo pamoja na mambo mengine imerekebisha majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeboreshwa zaidi, kwa kuanzishwa kwa Idara itakayoishughulikia utekelezaji wa Mikataba yote baada ya kufanyiwa mapitio yaani vetting. Jukumu hili litawezesha kutambua na kupata takwimu sahihi za Mikataba yote iliyositishwa, inayotakiwa kusitishwa na inayotakiwa kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pia, mabadiliko ya Sheria hiyo yameanzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo kwa sasa inasimamia mashauri yote ambayo Serikali inashtaki au kushtakiwa. Kwa sasa Ofisi hii inaendelea na kazi ya utambuzi wa mashauri yote dhidi ya Serikali kutoka katika Wizara na Taasisi zote za Serikali. Jitihada zote hizi, zina malengo ya kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi na mashauri yaliyofunguliwa kutokana na usitishwaji wa Mikataba na kutambua faida na hasara zake.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-

Ileje ina miradi iliyobuniwa kwa ajili ya kuzalisha umeme wa maji Mradi wa Luswisi na Ibaba, umeme huu ukizalishwa utaiwezesha Ileje kuwa na umeme wa kutosha kwa mahitaji yake yote na ziada na kuuza:-

(a) Je, Serikali itawasaidia vipi wananchi wa Ileje katika kukamilisha miradi hii?; na

(b) Je, Serikali itawasaidia vipi kuhakikisha usambazwaji wa umeme Ileje unaharakishwa?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuzalisha umeme wenye uwezo wa Megawati 4.7 katika eneo la Luswisi Wilayani Ileje. Gharama za mradi ni Shilingi Bilioni 19.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Umeme Ibaba unafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Kanisa la Moraviani – Tukuyu ambapo mradi huu ulibuniwa kuzalisha umeme kupitia jua na kusambaza kwa wanakijiji. Hata hivyo, utekelezaji wa mradi ulisuasua kutokana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka umeme wa grid katika Kijiji hicho mwaka 2017. Kwa sasa mradi huo unasambaza nishati ya umeme katika maeneo ya Shule ya Msingi Ibaba na Kituo cha Afya Ibaba.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kuhakikisha Vijiji vyote vya Wilaya ya Ileje vinapata huduma ya umeme kupitia Miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya pili na awamu ya tatu inayoendelea. Utekelezaji wa miradi ya REA awamu ya tatu utakamilika mwezi Juni, 2021.